Search This Blog

Thursday, 2 June 2022

MIKONO MICHAFU - 4

 





    Simulizi : Mikono Michafu

    Sehemu Ya Nne (4)





    **** ***** ***** *****



    KWA kweli pamoja na kutoka pale nyumbani, sikuwa na mahali pa kuanzia kumtafuta Tausi kwa kuwa mpango ule wote ulipangwa na Omari japo hakuna aliyekuwa anajua kama Omari ndiye anaratibu zoezi lile kwa kuwa alimtumia askari mmoja asiye na cheo chochote ambaye ni mmojawapo wa vijana wake waaminifu. Hiyo ilisaidia kuficha nguvu ya mtandao wetu. Uamuzi wangu wa kwanza ulikuwa ni kumtafuta Omari.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ghafla nikapokea simu iliyonishusha presha, nilipokea taarifa kuwa Tausi yuko salama…

    Kumbe alipoingia barabara kubwa tu kutoka pale nyumbani, Tausi alikutana na gari mbili zilizomuweka katikati na kulazimisha kumuongoza kuelekea Bagamoyo badala ya uelekeo wa mjini kama ilivyopangwa.

    Kutokana na aina ya kazi tunazozifanya na hatari inayotukabili kulingana na uadui tuliyojijengea, kuna baadhi yetu tunaoaminiana tulianzisha mtandao mdogo wa kulindana nje na utaratibu wa kiofisi. Na ndiyo uliniokoa siku hiyo mikononi mwa wanaojiita wanalinda maslahi ya taifa.

    Siku hiyo kwenye taarifa za habari za usiku huo zikatangazwa habari kuwa majambazi sita wameuawa na wananchi wenye hasira kali maeneo ya Mbagala Majimatitu usiku wa kuamkia siku hiyo na polisi wanaendelea na uchunguzi.

    Tukio la kuvamiwa nyumbani kwangu niliendelea kulikalia kimya, sikulitolea taarifa yeyote ofisini wala sikuilamu ofisi kwa kutochukua hatua ndani ya muda uliotakiwa ila tukio hilo na maneno ya yule lofa vilinipa ujumbe kuwa siko salama tena na ofisi inashiriki kwa namna moja au nyingine kwenda kinyume na mimi.

    Lakini pia kikubwa nilikuwa najaribu kuwapa ujumbe kuwa na mimi ni mtu wa aina gani. Chezea mimi wewe?

    Ila maneno aliyoniambia Mkuu siku aliyonitembelea yalirudi kichwani, “Nchi haitawaliki kijana wangu, kila kiongozi mwadilifu katika taasisi za ulinzi na usalama anatamani muda wake wa kustaafu ufike ili aachie ngazi kwa kuwa tunalazimishwa na wanasiasa kufanya watakavyo hata kama ni kinyume na taratibu na kanuni na sheria za nchi” aliniambia mzee yule kwa utulivu huku tukitembea pembeni ya bahari.

    Siku ile mzee yule aliendelea kunielezea kuhusu nguvu za kifedha walizonazo baadhi ya watu ambao wanajipanga kugombea urais, pia alinigusia kuhusu nguvu za vyama vya upinzani katika kubadilisha mawazo ya wananchi wa kawaida kiasi cha kutokea vurugu za mara kwa mara. Kwa jinsi alivyokuwa akiongea, hakuonyesha kama anahitaji nitoe mchango wowote wa mawazo.

    “Siasa na uroho wa madaraka ni sumu kubwa ambayo inaelekea kuangamiza taifa letu, watu wanajilimbikizia mali ili kupata nguvu ya kisiasa. Imefikia wakati taaluma zote zimemezwa na siasa, itafika wakati wanasiasa watalazimisha madaktari kuwaandikia dawa wagonjwa kwa namna wanavyotaka wao. Hii ni hatari sana” alinieleza mkuu.

    Baada ya kumsikiliza kwa muda, siku hiyo aliniambia sentensi moja ambayo ikawa inajirudia rudia kichwani mwangu kila mara “Epuka kutumiwa na wanasiasa, wewe ni mtoto wa Tanzania na hutakuwa na nchi nyingine ya kuiita nyumbani hata ukibadili uraia”. Sikujua aliniambia kwa sababu gani, ila alimaanisha alichoniambia.

    Nikaja kuelewa kwa ufasaha maneno ya Mkuu baada ya tukio lililonitokea. Inamaana kuwa Mkuu alikataa kutumika na hawa jamaa ndiyo wakamuua? Yuko wapi Mwajuma? Nilipowaza hivyo nilihisi damu ikikimbia kwa kasi isiyo ya kawaida mwilini, na kwa mara ya kwanza katika maisha yangu nikakihofia kifo.

    Siku mbili zilipita kukiwa na ukimya kama vile hakuna kitu kilichotokea lakini upande wangu nilikuwa katika harakati za kujiwekea hali ya usalama hasa kwa ajili ya Tausi. Nilijua wakati wowote wangeweza kumvaa labda kwa kumdhuru au kumuonyesha picha zangu na Mwajuma ambaye ni marehemu kwa sasa.

    Mpango wakumuweka Tausi katika hali ya usalama ulikamilika. Jioni moja tuliiweka kwa ajili ya utekelezaji.

    Yolanda aliwasili nyumbani kwangu na gari dogo yenye vioo vya giza. Huyu ni mmojawapo wa vijana waliokuwa wakiaminiwa na Mkuu japo alikuwa bado ni mpya kwenye kazi yetu lakini alikuwa na mwenendo wa kizalendo haswa japo aliwahi ‘kuniboa’ wakati nna ‘stress’ zangu kuhusu Tausi. Eti mimi nna mawazo yangu, yeye akawa anabusiana na kijamaa chake mbele yangu. Ah! Lakini ulikuwa wivu tu wa kibwege.

    Japo hakuwa kwenye mtandao wetu wa kulindana, tulimshirikisha Yolanda kwenye zoezi hilo kwa kuwa hatukubahatika kuwa na mwanamke kwenye mtandao wetu. Na Yolanda alionyesha kupenda kuwa karibu sana na mimi na Tausi kwa kuwa alijua ni kwa namna gani tunapendana akawa anatufurahia.

    Yolanda aliingia nyumbani kwangu akakaa kwa muda, kisha akatoka Tausi akiwa na mavazi ya Yolanda na kuondoka na lile gari kuelekea sehemu ambayo angekutana na Omari, yule rafiki yangu mpenda wanawake Malaya. Omari alikuwa tayari na maagizo juu ya sehemu ya kumpeleka Tausi ili awe salama.

    Zilipita dakika kumi bila kupata mrejesho wowote toka kwa Omari. Kwa mujibu wa makubaliano yetu na mpango ulivyo, ndani ya dakika tano tayari Omari angeshanihakikishia kuwa Tausi yuko katika mikono salama na mimi nianze kazi mara moja.

    Mapigo ya moyo yakaanza kwenda kama mishale ya saa mbovu huku mawazo mengi yakipita kichwani nikajikuta nimezama kwenye mawazo mengi huku akili yangu ikifanya kazi haraka haraka na kusahau uwepo wa Yolanda pale kwa muda. Ghafla mawazo yalirudi kwa Yolanda.

    Nilipogeuka kumwangalia Yolanda, tukakutanisha macho na kuangaliana kwa muda. Macho yetu yaliambiana mambo ambayo hayakua mazuri, ghafla Yolanda akapeleka mkono kiunoni kutaka kutoa bastola yake. Nikamrukia teke ambalo nadhani liliupa mkono wake ullpata ganzi kwa sababu kwa dakika mbili ambazo tulizicheza baada ya teke lile, sikuuona mkono huo kushiriki chochote.

    Yolanda alikuwa mzuri katika mapigano lakini sio kiasi cha kunipa tabu tena wakati sehemu ya moyo wangu imeguswa. Nilimdhitibi na kumuweka kwenye chumba kidogo kisicho na kitu baada kumfunga na nyaya nyembamba kwenye mikono na miguu ambazo zingeweza kumkata kama angefanya harakati zozote za kujinasua.

    Ilionekana dhahiri kuwa Yolanda amenisaliti na ana uhakika pale alipo analindwa na watu waliomtuma kwa hiyo hakuwa na wasiwasi.

    Kwa jinsi Yolanda alivyo mrembo, ingekuwa wewe usingethubutu kumpiga hata kibao na angekuua, ni aina ya warembo ambao huwa wanachorwa kwenye majarida yaani amekamilika kila idara lakini mwanamme nilichapa kama napiga paka aliyeiba kitoweo cha ngama ambacho tayari ushakisongea ugali.

    “Yolanda! Wewe ni wa kunisaliti mimi?” nilijikuta namuuliza kwa uchungu binti yule

    “Taifa ni zaidi ya wewe na Tausi” alinijibu kwa macho makavu.

    Niligundua kwa haraka haraka kuwa amelishwa maneno ya sumu kiasi cha kuniona mimi ni adui wa taifa hili. Sikujisumbua kumhoji chochote kwa sababu nilijua wazi kuwa hata ningemuua asingenipa taaifa yeyote nnayohitaji.

    Badala ya kumchukia nilimuonea huruma Yolanda, nikapekua kwenye mashine ya kuhifadhia sauti, nikapata maongezi ya mkuu na maongezi ya yule mwehu wa wanaojifanya wanatetea usalama wa taifa. Nikamrekodia kwenye kifaa maalumu na kumuwekea Yolanda asikilize akiwa mule mule kwenye kijichumba nilichomhifadhi mimi nikiondoka.

    Kifaa nilichokitumia kumrekodia, kina sehemu ambayo unaweza kukiamrisha kifute kumbukumbu zote baada ya muda fulani na ndivyo nilivyofanya. Nilikiamuru kirudie mara mbili halafu kifute kumbukumbu zote. Nilijua baada ya mimi kuondoka wenye Yolanda wangefika muda wowote kumchukua mtu wao.

    Niliamini kuwa ile ndiyo tiba pekee inayomstahili Yolanda, japo nilifanya kwa faida yangu pia katika kupunguza idadi ya maadui. Kawaida yangu huwa narekodi kila maongezi nnayofanya na ugeni wowote unaokuja pale nyumbani kwa kutumia saa yangu maaalum ambayo huivaa mara zote nikiwa pale nyumbani.

    Nilijiandaa haraka haraka na kutoka pale nyumbani nikitumia gari yangu. Moyoni nilijawa na chuki ya hali ya juu kutokana na kugusiwa Tausi wangu tena kwa jambo lisilomhusu halafu sio la haki. Chuki hiyo ilichanganyikana na woga fulani kwamba wanaweza kumuonyesha zile picha na kumjaza sumu zitakazomfanya anichukie.

    “Vipi kama watamuua kama walivyomuua Mwajuma” nilijisemea moyoni maneno hayo yaliyonitia ghadhabu na kuona dhahiri umuhimu wa kuushambulia mtandao alionidokeza Mwajuma kabla ya wao kunimaliza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa kweli pamoja na kutoka pale nyumbani, sikuwa na mahali pa kuanzia kumtafuta Tausi kwa kuwa mpango ule wote ulipangwa na Omari japo hakuna aliyekuwa anajua kama Omari ndiye anaratibu zoezi lile kwa kuwa alimtumia askari mmoja asiye na cheo chochote ambaye ni mmojawapo wa vijana wake waaminifu. Hiyo ilisaidia kuficha nguvu ya mtandao wetu. Uamuzi wangu wa kwanza ulikuwa ni kumtafuta Omari.

    Ghafla nikapokea simu iliyonishusha presha, nilipokea taarifa kuwa Tausi yuko salama…

    Kumbe alipoingia barabara kubwa tu kutoka pale nyumbani, Tausi alikutana na gari mbili zilizomuweka katikati na kulazimisha kumuongoza kuelekea Bagamoyo badala ya uelekeo wa mjini kama ilivyopangwa.

    Baada ya mwendo kama wa dakika nne, taarifa zilishasambaa kuwa binti ya rais katekwa na watu wasiojulikana na anatakiwa apatikane ndani ya nusu saa lakini namba za gari zikatangazwa ni zile za gari alilokuwamo Tausi. Ilikuwa ni kazi ya Omari kwa kutumia namna anayoijua mwenyewe alivujisha taarifa hizo za uongo.

    Hali hiyo iliwatisha sana mabosi wa watekaji ambao nao ni sehemu ya wakubwa walioko madarakani, wakaamua kutengua mpango wao kwa kuwa vyombo vyote vya usalama vilifungua macho na baada ya dakika zisizozidi kumi likajulikana gari lilipo na ndipo zikatolewa taarifa rasmi kuwa taarifa za awali zilitolewa kimakosa. Wakati huo vijana wa Omari walikuwa wameshamrudisha Tausi mikononi.

    Nilizipata habari hizo nikiwa njiani kwenda kwenye sehemu ambayo ningewasiliana na Omari bila yeyote kujua kama ni mimi ndiye nawasiliana na Omari. Nikajifikiria kurudi nyumbani lakini nikaona niwape muda maadui wamchukue Yolanda, nikatafuta sehemu yenye pilika pilika nikaegesha gari langu na kuingia nipate kinywaji.

    Mabosi wa watekaji walikuwa wamechanganyikiwa wasijue ni nani aliyetoa taarifa zile zilizouvuruga mpango wao. Ingawa mtu wa kwanza kumfikiria alikuwa Omari, muda wote wa pilika hizo Omari alikuwa akionekana kwenye hoteli moja akinywa na makahaba wawili. Na hakuwa anajishughulisha na mawasiliano yeyote. Wakajua hahusiki.

    Kitu ambacho mpaka wakati huo walikuwa na uhakika nacho ni kwamba nina nguvu kuliko walivyonifikiria awali kutokana na ukweli kuwa tayari walifeli katika mipango yao miwili dhidi yangu. Na kutofahamu huko ndiko kulifanya wasite kunipoteza duniani. Tuliamua katika mtandao wetu tusiwe na mawasiliano ya moja kwa moja nje na taratibu za kiofisi ili kuongeza wigo wa kujilinda, na sasa ndiyo tunaona faida yake.

    Wakati kinywaji changu kikiwa nusu, nikapokea simu toka kwenye namba nisiyoijua. Sauti niliyoisikia ndiyo iliyonishtua sana japo halikuwa jambo geni kutokea. Ilikuwa ni sauti ya Kazikanda Moluwi, mkuu mpya wa usalama wa taifa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akaanza kuniita kwa jina. Hakuna anachonikera bosi huyu kama anacholiharibu jina langu, yeye badala ya kuita Musa anaita Msa.

    “We Msa, uko wapi?” aliita kwa sauti yake nzito ya kishamba shamba.

    “Niko Jojiz, maeneo ya posta” nilimjibu bila kusita.

    “Subiri hapo hapo” aliongea KM na kukata simu.

    Nikabaki nimeishikilia simu yangu mkononi. Nikaanza kuangaza milangoni kuona ni nani ataingia.

    Nikajikuta nashikwa bega na mlevi mmoja aliyekuwa akipiga stori sana na wenzake kwenye meza ya jirani yangu. Nikageuka kumwangalia, akatabasamu kisha akaniambia tuondoke kama vile tulikuja wote. Nilielewa moja kwa moja anamaanisha nini, nikainuka bila kumalizia kinywaji changu na kutoka naye huku akininukisha harufu yake ya pombe.

    Baada kama ya dakika kumi nilikuwa uso kwa uso na Kazikanda Moluwi au KM. Huwa sina mazoea kabisa na Mkuu huyu kwa kuwa sipendi watu wenye mitazamo isiyobadilika na hali halisi iliyo. Huwezi kumwambiakitu tofauti na anachoamini.

    “Msa, kuna kazi maalum ambayo taifa linataka uifanye” aliniambia baada ya kunipa sifa za kijinga kibao.

    “Nakusikiliza mkuu” nilimjibu kwa heshima huku nikiongeza umakini.

    “Mkuu wa nchi anataka uingie kwenye siasa, utaelekeza chama cha upinzani cha kuingia na shughuli utakayoenda kuifanya. Ni chama ambacho kinasumbua na kuhatarisha usalama wa taifa” alinielezea kwa utulivu KM na kumalizia kuniuliza kama nina swali.

    Nikakumbuka maneno ya Mkuu aliponitembelea kuwa kuna kundi ndani ya chama tawala linalopigiwa kelele na wapinzani kutokana na kujilimbikizia mali ambalo linashindwa kushugulikiwa na mamlaka kutokana na mizizi yake ilivyosambaa. Kundi hilo ndilo linatumia vibaraka wao kufanya mambo ya ajabu yanayomchafua Rais na serikali yake.

    “Agizo hili kalitoa mwenyewe au umeambiwa tu kuwa mkuu wa nchi kaagiza na kwa nini nitumwe mimi?” nilimuuliza maswali mawili ambayo yalimfanya ajiweke sawa kwenye kiti chake. Japo nilishajua atakachojibu lakini nilitaka kumuonyesha kuwa nafanya kazi kwa kufikiri sio kufuata tu maagizo.

    “Unachotakiwa ni kufanya kazi unayopangiwa bila kuhoji” alitoa jibu nililotarajia ila alikosea kwa kuniuliza kama kazi zote nilikuwa napewa sababu ya mimi kuchaguliwa kuifanya kazi husika.

    Nilimuelezea kazi moja moja na kumalizia kazi ya kumchunguza baba yake Tausi, Mzee Nurdin kwamba ilitokana na ukweli kuwa sikuwepo nchini kwa muda mrefu hivyo watu wengi ambao walikuwa kwenye mtandao wake wasingenigundua.

    KM alikaa kimya kwa muda kisha akaendeleza desturi yake ya utemi, “Hapa ni amri tu hakuna siasa”. Jibu lake lilinifanya nichekee moyoni, maana ananituma kazi ya siasa halafu ananiambia hataki siasa.

    Kwa kadiri ya mazoea yangu na ufahamu nilio nao, ukiona mtu anatanguliza kumtaja mkuu wa nchi ujue anataka kufanya jambo kwa maslahi yake ila anataka tu kutumia jina la rais ili kuwatisha watu wasihoji.

    “Mkuu” nilianza kuongea kabla hajanikatisha kwa ukali.

    “Nini!”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Siku hizi watu ni wafuatiliaji wazuri, ili tufanikiwe itabidi nijifanye nimeacha kazi na nilipwe stahiki zangu zote kisha nijifanye nimegeukia siasa. Hapo kila kitu kitaenda anavyotaka mheshimiwa rais” nilifanya jaribio la kumjaza kwenye mtego wangu. Akaniomba muda ajifikirie.

    “Ila nitalipeleka kama wazo langu kwa mheshimiwa ili alichukulie kwa uzito” aliniambia KM. nilifurahi sana kwa uamuzi wake wa kulipeleka kama wazo lake. Pamoja na yeye kufanya vile ila apate sifa kuwa ana mikakati bora, wazo kama hilo kutoka kwake lisingewafanya wanaomtuma kulitilia shaka na kufikiri mara mbili.

    Unajua watu wanaofanya mambo kama hawa wanaojiita watetea usalama wa taifa huwa hawana akili japo mara nyingi hujiona ‘vichwa’ sana. Kwa kuwa mioyo yao imetawaliwa na tamaa za mali na madaraka, akili zao zinaangalia eneo hilo tu. Nilijua watakubali kwa vile kwa akili zao ndogo watajua nikiwa nje ya mfumo rasmi itakuwa rahisi kwao kunipeleka wanavyotaka na ikiwezekana kuniondolea uhai wangu.

    “Utapigiwa simu kupata maelekezo” aliniambia KM. Nikageuza kurudi nyumbani nikimuomba Mungu kuwa kila kitu kiende ninavyotaka mimi.

    Hakuna kilichonishangaza kwa hali niliyoikuta nyumbani kwangu, sehemu zote nilizotarajia zingepekuliwa zilipekuliwa na Yolanda wao walikuwa wamemchukua. Sikuthubutu kuwasiliana na Tausi kwa ajili ya usalama wake ila kusema kweli nilikuwa na hamu naye.

    Kwa haraka ya ajabu nikapata taarifa zote nilizokuwa nazihitaji juu ya Boimanda, hii inatokana na mahojiano waliyoyafanya watu wangu na wale walionivamia. Boimanda alikuwa mtumishi mwadilifu wa serikali katika wizara kadhaa na kumalizia utumishi wake ofisi ya rais ambako alikuja kustaafu. Hakuwa na utajiri kutokana na usimamizi mzuri wa sera ya ujamaa na kujitegemea, pamoja na kupitia kwenye nafasi hizo pia Boimanda alikuwa usalama wa Taifa aliyestaafu akiwa kwenye ngazi za juu.

    Wakati akiwa usalama wa Taifa aliwaingiza vijana wake wengi sana, na mmojawapo alikuwa Kazikanda Moluwi ambaye sasa ndiyo Mkuu mpya. Kwa mara ya kwanza nikawa namtazama Boimanda kwa mtazamo mwingine, na nikaona bayana kilichokuwa kikimpa jeuri yule bwege aliyekuja kunihoji nyumbani kwangu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog