Search This Blog

Wednesday, 1 June 2022

MOYO WA KUPENDA - 3

 







    Simulizi : Moyo Wa Kupenda

    Sehemu Ya Tatu (3)



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Rama na Faudhia walitoka pamoja ofisini kwa mkuu wa kituo wakiwa huru, wakaelekea katika gari yao na kabla hawajaingia kupanda ndani ya gari wakapigwa na butwaa!

    Kundi la waandishi habari liliwazonga na kuwatupia maswali mfululizo, Faudhia alipanda ndani ya gari yake haraka, Rama akafatia kuingia upande wa kushoto, wakafunga milango huku wakisonya Faudhia akawasha gari, na kuondoka eneo lile bila kuzungumza chochote yeye wala Rama. Waandishi wale waliisindikiza ile gari kwa picha za video na picha mnato.

    Gari ile ilipofika eneo la soko la Magomeni na Mahakama ya mwanzo ya Magomeni, ikapinda kushoto kukamata Barabara ya Morogoro wakapinda kulia wakatembea na njia ya watembea kwa miguu hadi katika kituo cha mafuta pale katika makutano ya Barabara ya Kawawa na Morogoro, maarufu kama magomeni mataa, akaingia katika barabara ya Kawawa akapinda kushoto kuelekea maeneo ya Kinondoni.

    Wale waandishi habari walikwenda kwa mkuu wa kituo kile kutaka habari zaidi ya muendelezo wa tukio lile lililokuwa limetawala katika vyombo vya habari, ndani ya siku mbili zile.

    Mkuu wa kituo akawakaribisha ofisini kwake, akafanya nao mahojiano ya kina kuhusu tukio lile akajibu maswali lukuki ya waandisha waliokuwa wakimuhoji kwa mpigo.

    “Ndugu waandishi nashukuru kwa kufika kwenu hapa leo, kwani wenzetu mtatusaidia sana katika jambo hili. Kuna mwanamke anasambaza virusi vya Ukimwi makusudi hapa jijini, ameshauwa watu sita na sasa watu wawili zaidi ameshawaambukiza virusi hivyo. Kwa hiyo tunaomba mtusaidie kuwatangazia uma kuwa makini na mtu huyo ambae picha yake nitawapa ili muitoe katika vyombo vyenu. Pia nitaomba muelewe kuwa huyo mwanamke jana tu amefunga ndoa na Bwana mmoja anaejulikana kwa jina la Faridi Kacheche, mzaliwa wa Ujiji kigoma. Huyo mwanamke anaitwa Rebeka John Makuka mzaliwa wa Tanga, na hii ndiyo picha yake. Mwanamke huyo tunamtafuta popote alipo wananchi watoe ushirikiano kwa kutupigia katika namba zetu za simu ambazo nitawapa baadae, ili popote watakapomuona watoe taarifa katika namba hizo na sie tutamshughulikia ipasavyo.”

    Mkuu wa kituo cha Polisi Magomeni, alizungumza na waandishi wa habari wale kwa kina na akatowa namba zake mbili za simu ili kupokea taarifa ya Rebeka John Makuka.

    Waandishi waliipiga picha ile picha ya Rebeka , wakaandika jina lake katika vijitabu vidogo walivyokuwa navyo mikononi mwao, wakamshukuru mkuu wa kituo kwa kuwapa ushirikiano wa kutosha wakataka majina ya wale watu walioondoka na gari ile iliyovunjwa kioo, na mkuu wa kituo akawapa majina yao, wakaaga na kuondoka kuwahi katika vyumba vya habari kwa ajili ya kuipeperusha habari ile.

    Faudhia Baddy Mnyone aliendesha gari yake huku akiwa amenyamaza kimya kabisa hadi alipofika maeneo ya Kinondoni Mkwajuni, akapinda kushoto kuelekea katika Baa ya masai akaegesha gari yake pembeni na kumgeukia Rama akamwambia.

    “Rama kaka yangu tumekutana katika matatizo yanayofanana, tena wote tumeumizwa na wapenzi wetu tuliowapenda sana ambao sasa hivi wapo pamoja wakiwa wametusaliti, wapo pamoja wakifurahi wametuacha sie tukiumia. Hivyo leo ndiyo hatma yetu kwani mie inanibidi nifike nyumbani kwangu ili nikapange vitu vyangu ili nitokomee pasipojulikana, nataka tuagane kaka yangu”

    Faudhia alisema maneno yale huku moyo wake ukimuuma sana, machozi yakimlenga lakini akiwa hana jinsi nyingine ila kwenda ambapo moyo wake umedhamiria, kwani amedhamiria kubadilisha mazingira japo aweze kusahahu mambo mazito yaliyomtokea.

    Rama alimtazama Faudhia nae moyo wake ukaingia simanzi kwani alimzowea Faudhia kwa muda mfupi sana, amemuokoa na kifo kibaya alichokusudia kujiuwa leo anaagana nae akiwa hana furaha katika moyo wake. Ametambuana na huyu dada akiwa hana furaha na leo anaachana na huyu dada pia akiwa hana furaha, alimpa mkono wake Faudhia akaushika kisha huku machozi yakimtoka akamwambia;

    “Faudhia dada yangu asante kwa kuwa nawe, kwani kwa muda mfupi niliokuwa na wewe japo katika matatizo lakini nilifarijika sana, leo unaniacha hapa moyo wangu unaniuma sana kuwa mbali nawe, sina mtu wa kunifariji katika matatizo yangu, nani atakaeweza kunifariji hadi nirudi katika furaha, nani Faudhia simuoni, maisha yangu yashakuwa yametawaliwa na vilio tu, sidhani kama nitafanya kazi tena, haya kwa heri ya kuonana sina maisha marefu tena Faudhia, ukisikia nimekufa usiache kuja kunizika, usiache kuja kaburini kwangu, japo nitakuwa maiti lakini nitaipata faraja kuwa umenitembelea asante sana kwa heri yakuonana.”

    Rama alisema maneno yale huku machozi yakimtoka akateremka ndani ya gari ile akawa anatembea kwa miguu asijue wapi aendapo.

    Faudhia alilia kwa uchungu akiwa bado yupo mle ndani ya gari, akamtazama Rama aliekuwa anatembea kwa miguu kuelekea usawa wa Mwananyamala, mwisho akaendesha gari taratibu hadi akamfikia Rama akamwambia huku machozi yakimtoka kama maji.

    “Rama nashindwa kukuwacha peke yako, nashindwa Rama naomba upande humu kwenye gari ili tuondoke sote.”

    Rama alimtazama Faudhia kwa macho yenye machozi akasimama na kutafakari kisha akamwambia.

    “Hapana Faudhia nenda tu dada yangu niache nimalize pumzi zangu za mwisho, niache nimalize hatua zangu za mwisho, niache Faudhia sitoweza kuwa na wewe kwani mie nimuathirika, bora wende Faudhia pengine nitazoea tu, na kama ikiwa nitakufa nakusihi ufanye kama nilivyokuagiza, maradhi yangu yananifanya niwe mbali na wewe Faudhia huo ndiyo ukweli, nenda tu sina kinyongo na wewe, mie nalia na Moyo wangu, nalia na Moyo wa kupenda ndiyo ulonifikisha hapa.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Faudhia alizidi kulia machozi Rama alipomwambia maneno yale kwani japo alikuwa amewachukia wanaume wote, ila kwa Rama alimuona ni tofauti katika moyo wake hakika aliathiriwa nae, nafsi yake imetokea kumpenda Rama, amemuona ni kijana anaependa kwa dhati, amemuona ni kijana mtanashati, waliofanana vimo vyao, waliofanana maumivu yao, waliokuwa wamepata matatizo pamoja, Faudhia hakutaka kuamini kwama Rama ameathirika akafikiri labda vipimo vimekosea, sasa afanyaje akaona waende katika sehemu nyingine tofauti ili akapime tena, asaa kheri anaweza kuonekana mzima, wazo hilo lilipotawala akashuka ndani ya gari akamfata Rama pale chini akasimama mbele yake na kumueleza azma yake kwa upole.

    “Rama hebu twende sehemu nyingine yenye vipimo vya uhakika ili tukapime tena wote, pengie kile kipimo ni kibovu, huwezi juwa unaweza kujiweka roho juu bure kumbe kipimo kikawa siyo kizima, twende pale Agha Khan Hospital tukapime upya twende tukapime damu kubwa, siyo damu ya vidoleni tena labda mungu anaweza akatubadilishia matokeo, akatupa matokeo mazuri”

    Rama alisikiliza yale maneno kwa makini yakamuingia hadi ndani ya mifupa yake, matumaini kwa mbali ya kuwa labda anaweza kuwa mzima kama akipima kwa kutoa damu kubwa damu ya mshipa ilimuingia, akamkumbatia Faudia na Faudhia akamkumbatia yeye wakakaa vile kwa sekunde kadhaa huku Faudhia akimpigapiga mgongoni. Wakaachiana wakawa wanatazamana usoni, kila mmoja akamfuta machozi mwenzake, wakaingia wote ndani ya gari na Faudhia akaendesha gari ile huku akizungumza kwa utulivu.

    “Rama kwanza itabidi nifike nyumbani kwangu ili nioge na kupiga mswaki kisha nibadili nguo, twende kwako pia uoge na kujisafi ubadili na nguo, tutae mahali tule ili turudishe nguvu katika miili yetu ndiyo twende katika vipimo Agha Khan Hospital, kwani wale wanavipimo vya kitaalamu zaidi, huwezi kujua matokeo yanaweza kubadilika ikawa vinginevyo”

    Rama alitikisa kichwa kukubaliana na maneno ya Faudhia huku ndani ya moyo wake akimuomba Mungu apate majibu mazuri ili amuoe Faudhia.

    “Sawa mie sina amri juu yako Faudhia, nipo kama bendera vile mie nafata upepo tu utalo amua wewe mie maridhia tu sina ubishi kwako.”

    Faudhia alimtazama Rama kwa jicho la ajabu, alimshangaa maneno yake yalikuwa yakimuathiri katika nafsi yake, akashangaa kwa muda mfupi aliokuwa amekaa nae, moyo wa kupenda ulikuwa unamuelemea yeye, ila kitu pekee kilichokuwa kinamuwekea pingamizi ni kule kuathirika kwa Rama, ndiyo maana akamwambia waende wakapime tena ili wapate kuona kama kunaweza kuwa na mabadiliko.

    Aliona Rama moyo wa maumivu anaujuwa na amemuona kuwa anapenda kwa dhati anapopenda sehemu huwa moyo wake wote unapenda, hajui kupenda nusu kwake nusu apende mwengine, alikuwa hajui kuugawa moyo wake katika kupenda.

    “Sawa Rama nimesikia na nimependa kuwa umenisikiliza mie ninavyosema, basi tuanze kwangu kisha kwako, halafu kwenda kula na hatimae Hospital kupima upya”

    Faudia akarejesha uso wake mbele, akaigeuza gari yake akaifata barabara ya Kawawa akapinda kushoto kuitafuta Moroco, alipofika pale katika makutano ya barabara zenye majina ya viongozi mashuhuri, Barabara ya Kawawa na Ali Hassani mwinyi akanyoosha moja kwa moja kama anaekwenda kule Shoppers Plazza, kabla hajafika katika maduka yale akapinda kushoto katika barabara ile ya vumbi, akatembea taratibu hadi nyumbani kwake. Alisimamisha gari akapiga honi, mlinzi wa kampuni binafsi akachungulia kupitia katika tundu ndogo ya geti kubwa la chuma, akamuona mwenyeji muhusika wa nyumba ile Yule mlinzi akafungua geti lile, na Faudhia akaiingiza ndani gari ile akaiegesha katika uwa mpana uliokuwa na magari mengine madogo matatu yameegeshwa.

    Faudhia alimwambia Rama washuke, wakateremka kutoka katika gari ile, Faudhia alikwenda katika sehemu wanayohifadhi funguo, akachukua funguo akafungua mlango wa nyumba ile ya kisasa iliyokuwa na kila kitu ndani yake wakaingia ndani.

    Rama alitembeza macho yake huku na kule akaona jeuri ya pesa ilivyofanya kazi. Kila kitu kilichokuwamo katika nyumba ile kilikuwa ni cha thamani sana, hata gari alizoziona pale uwani zikiwa zimeegeshwa, zilikuwa ni gari za thamani kubwa gari za bei mbaya, kwani hakukuwa na gari ya milioni saba wala nane pale.

    Rama akajilinganisha na uwezo wake ambao amediriki kujenga nyumba ya kawaida tu yenye vyumba vitatu na sebule isiyohimili hata kuwekwa seti za sofa tatu kwa pamoja , kwani kiwanja chake kilikuwa kidogo, uwezo wake ulikuwa wa mtanzania wa kawaida, hadi nyumba yake kufikia ilivyo imemchukua miaka karibu mine anajenga tu, hata sasa bado kulikuwa na sehemu ambazo zilihitaji kujengwa, ama kweli nyumba ya masikini haishi kujengwa.

    “Rama mbona umezama katika mawazo namna hiyo? Hapa ndiyo kulikuwa nyumbani kwangu maisha haya yote unayoyaona sina hamu nayo tena, yameshanitumbikia nyongo bora uzima tu na mie Mungu atanipa maisha yangu hata kama yakulalia kitanda cha ukambaa, karibu mie nakwenda kujimwagia maji ili niwe mtu manaake hapa sina amani kabisa nanuka jasho.”

    Rama alimtazama faudhia akaitikia kwa kichwa kuwa amemuelewa kisha macho yake yakarudi katika kutalii mle ndani, katika kichwa chake kulikuwa kumejaa lindi la mawazo kuwa itakuwaje mtalaka wa Faudhia ikiwa ataamua kuja nyumbani kwake akamkuta. Moyo wake ukaanza kupiga kwa kasi ikawa moja haikai wala mbili haiingii, woga ulimtanda katika mwili wake vipele vya baridi vilizagaa mwilini mwake akajishangaa kwa nini iwe vile, kwa nini awaze kitu kama kile kisha mwili wake upate woga namna ile, akasema ndani ya moyo wake;

    “Hapa ipo namna siyo bure, kwani haijawahi kunitokea hali kama hii maishani mwangu.”

    Rama alitaka amwite Faudhia ili amuage kuwa atamsubiri nje, lakini hakujua hata ameingia chumba gani jinsi nyumba ile ilivyokuwa kubwa, wasiwasi ulimzidi akapoteza amani kabisa, haja ndogo aliisikia ikimbana. Ama kweli woga mbaya.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mlango ulifunguliwa pale sebuleni, Rama akageuza shingo yake kwa haraka sana kutazama kule mlango ulipofunguliwa, macho yake yakamtoka pima akamuona Faudhia aliekuwa amejipamba amepambika, ananukia uturi siyo mchezo pale sebuleni alipokuwa Rama pote kulihanikizwa na harufu ya manukato yale, alikuwa amevalia jinzi iliyombana ya rangi nyeusi, juu akavaa fulana kubwa iliyoshuka hadi katika makalio, nayo pia ilikuwa na rangi nyeusi, alikuwa amevaa viatu virefu vyekundu, mkononi mwake alikuwa amekamata mkoba wa thamani wa rangi nyekundu, usoni mwake alibandika miwani pana iliyomkaa vyema usoni mwake, mdomo wake aliupaka rangi ya mdomo nyekundu, shingoni mwake alichafuka na kidani kipana cha dhahabu kilichokuwa kimefungwa lakti yenye alama kubwa ya herufi F.

    Rama akajikuta anatamka bila kupenda”Waaaaooo”

    Faudhia aligeuka nyuma akafunga mlango wa chumba kile akawa anapiga hatua kuelekea pale alipo Rama, huku milio ya viatu ya “Ko ko ko” ikisikika katika sakafu ile ya vigae vya thamani visivyoteleza.

    Rama alimlaki Faudhia akamwambia “Umependeza mashaallah”

    Faudhia huku akitabasamu akamjibu” Asante na uzuri unachangia”

    Wote kwa pamoja walitoka kuelekea uwani Faudhia alikuwa na funguo nyingine ya gari akabonyeza kitufe katika funguo zile, na moja kati ya zile gari tatu zilizokuwapo pale ikawasha taa huku ikitoa mlio.

    Faudhia akamwambia Rama. “Hii pia ni gari yangu na hizo mbili hapo ni gari za Faridi”

    Rama akatikisa kichwa kukubaliana nae, Faudhia alifungua mlango wa gari ile na Rama akafanya hivyo akakaa kiti cha pembeni, gari ikawashwa ilikuwa ni gari aina ya Toyota Alteza, Faudhia akaelekea getini mlinzi akafungua geti lile, lakini kabla Faudhia hajaitoa gari yake nje kabisa ya geti, gari aina ya Lange Rover New Model, ilisimama mbele ya geti ile ikitaka kuingia mle ndani, ikaizuia gari ya Faudhia kutoka nje.

    Faudhia, na Rama wakaitazama gari ile ndani yake wakawaona Faridi aliekuwa amekaa upande wa kushoto na Rebeka aliekuwa amekaa katika usukani akiendesha wakawa wanatizamana uso kwa uso.



    Kila mmoja hakulitegemea lile tukio la kukutana na mwenzake namna ile, hivyo lilikuwa limewachanganya sana, walibaki katika kutazamana vile kwa muda, bila shaka kila mmoja akitafakari hatua za kuchukua.

    Faridi alifungua mlango wa gari akashuka na kupiga hatua kadhaa kuelekea katika gari ya Faudhia huku akiwa amekasirika.

    Kuona vile kitendo bila kuchelewa Faudhia nae alishuka mle ndani ya gari akenda kusimama mbele ya Boneti ya gari yake akiwa na mkoba wake mkononi.

    Faridi alitembea hadi pale mbele ya gari ya Faudhia akasimama mbele yake akamtazama kwa ghazabu kisha kikamtoka kibao kikali cha kelbu, na kumpata Faudhia shavuni kwake. Faudhia alihisi maumivu makali sana akashika shavu lake kwa mkono mmoja na mkono wa pili akiwa amekamatia ule mkoba wake madhubuti.

    Rebeka alifungua mlango wa gari akashuka chini, akamfata Faridi pale alipokuwa akimnasihi asimpige Faudhia.

    Rama mle ndani ya gari aliiona ile hali kwa macho yake, moyo wake ukamuuma sana kwa kitendo cha Faudhia kupigwa kibao mbele yake, lakini Rebeka alipoteremka ndani ya gari na kwenda kumshika Faridi kilimuuma zaidi, kwani aliona mtu alietia dosari maisha yake na akaweka ahadi ya kulipiza kisasi yupo mbele yake, hivyo hakuwa tena na sababu yakuendelea kukaa ndani ya gari kisha akadharauliwa namna vile, aliterema ndani ya gari ile akawa anapiga hatua ili kwenda kumalizana na Rebeka, lakini alifanikiwa kupiga hatua tatu tu akasimamishwa.

    Faridi aliekuwa anavutana na Rebeka alimuona Rama akishuka ndani ya gari ya mtalaka wake, akitembea kuwafata walipo, ndipo kufumba na kufumbua bila kutarajiwa na mtu yeyote awae alichomoa Bastola kiunoni mwake akamuelekezea Rama, huku akimwambia kwa ghazabu.

    “Wewe mpumbavu unaeingilia ndoa za watu, unadiriki kuingia nyumbani kwangu? Umechupa mipaka sana na lazima nikushikishe adabu mpumbavu mkubwa wewe!”

    Rama alimtazama Faridi kwa hasira kisha akamjibu kwa kumwambia.

    “Faridi mie na wewe wote ni marehemu watarajiwa kama ulikuwa hujui hilo nataka ujuwe tangu sasa. Huyo Malaya ulieoa alikuwa ni mchumba wangu na kwa taarifa yako huyo ni Mua…….!”

    “Koma tena ukome kama ilivyokoma ziwa la mama yako! Acha kunipakazia mjinga mkubwa wewe, unaweza kuwa na mwanamke kama mimi wewe? Hunijuwi sikujuwi usinijazie Inzi bure siwezi kutembea na malofa mie, usinipakazie tafadhali eee usiniharibie siku yangu!”

    Rebeka alimkatisha Rama asimalizie kusema kama ameathirika kwani bado kabisa azma yake haijatimia kwa asilimia mia moja, hivyo alimkana kuwa hamtambui kweupe kabisa.

    Rama alimtazama Rebeka aliekuwa akimwambia maneno yale huku akiwa anamnyali vibaya. Kitendo kile cha kunyaliwa kikazidi kumpandisha hasira. Akataka kupiga hatua kumvamia Rebeka pale alipokuwa, lakini ile Bastola ya Faridi safari hii ikakokiwa ikawekwa tayari kwa kufyatuliwa.

    Kelele za chuma kile cha silaha inayochukua maisha ya mwanaadamu ndani ya sekunde ilimuhofisha Rama.

    Siyo kama Rama aliogopa kufa laa, kufa kwa risasi angependa zaidi kuliko kufa kwa mateso ya maradhi ya Ukimwi. Ila kitu alichokichelea ni kwamba asingependa kufariki kabla Rebeka hajamtia katika mikono ya sheria kwa uhalifu wa kuambukiza wanaume virusi vya Ukimwi anaoufanya kwa makusudi mazima. Wakiwa katika kutazamana baina ya Rama na Faridi, mara walisikia yowe la woga kutoka kwa Rebeka, wote wakamtazama Rebeka ili kujua nini kilichomfanya apige yowe namna ile, hakika wote walipigwa na mshangao mkubwa sana, na kushindwa kuamini kitendo wanachokiona machoni mwao.

    Rebeka alikuwa amewekewa bastola kichwani na Faudhia, Rebeka akawa anatetemeka vibaya sana.

    “Malaya mkubwa wewe, unadiriki kuuwa watu makusudi mjinga wewe! Unamkana huyo bwana kuwa humjuwi wewe? Ule ujumbe uliomuachia yule wa kuwa umeshauwa watu sita kwa Ukimwi ulimuachia paka kama huyo humjuwi? Eee sema au sasa hivi nakisambaratisha kichwa chako unamjuwa huyo bwana au humtambui?!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Rebeka alimtazama Faridi akiwa anatetemeka vibaya sana, akihitaji msada kwani alikuwa ameshikika vibaya.

    Faridi aligeuka kumtazama Faudhia akampa ubavu Rama pale aliposimama. Akamtazama Faudhia kwa jicho la husda akamwambia.

    “Fau unafanya kosa kubwa sana shusha hiyo silaha yako chini, utaweza kuua upate kesi bure shusha silaha hiyo.”

    Rama alishangaa sana kumuona Faudhia kuwa ndani ya mkoba wake alikuwa amebeba silaha ya moto, ila haikushangaza kwa Faridi hata kidogo kwani yeye mwenyewe ndiye aliemshughulikia serikalini kumilikishwa silaha ya moto kihalali kutokana kuwa mke wa mtu mkubwa na hata kuhitajika kuwa na ‘Self Defence’ yeye na mkewe lakini siku moja tu toka waachane leo anaonja uchungu na ubaya wa chombo kile kinapokuwa mikononi kwa mwenzako hasa akiwa na dhamira mbaya.

    “Nyamaza kimya marehemu mtarajiwa wewe, unaambukizwa Ukimwi na Malaya huyu unaona umepata mwanamke wa maana siyo? Kwa taarifa yako huyo Malaya wako ameathirika na huyo umuonae hapo mbele ya uso wako alikuwa ni mchumba wake alietarajia kumuoa mwezi huu. Basi ni vyema ukatambua kuwa yaliyompata Beku na Ungo yatampata, kama huyo mwanaume mwenzako amekimbiwa ukafatwa wewe, basi naamini ipo siku na wewe utakimbiwa atafatwa mwengine kwani utakuwa umeshaambukizwa Ukimwi tayari na itakuwa ni zamu ya kuambukizwa mwanamme mwengine”

    Mahasimu wale wakiwa wanatazamana vile, mlinzi wa Faridi alitoa simu akapiga Polisi kituo cha ostabey na kuelezea hali ilivyo kuwa kuna hatari ya damu kumwagika kwani silaha za moto zipo waziwazi zikielekezewa watu. Akawafahamisha askari wale mtaa na nyumba namba kwenye tukio lile.

    Askari wa doria waliokuwa jirani na pale, walipewa taarifa ile wakawa wanaelekea eneo la tukio kwa kasi kubwa.

    “Faudhia hayo ni maneno ya mkosaji tu, rebeka hana Ukimwi wala hamtambui huyu bwana, ila kwa kuwa unataka kupindua muradi ndiyo maana unataka mke wangu kumpa mtu huyo asiemfahamu. Unapomuwekea silaha kisha ukamlazimisha kumkubali huyo mtu, atamkubali kwa kuwa kuna silaha ila ukweli bado utabaki palepale kuwa hamfahamu kabisa huyo bwana.”

    Faridi alisema maneno yale huku akimtazama Faudhia kwa jicho baya.

    Faudhia alicheka kicheko cha dharau akamtazama Rebeka aliekuwa amefadhaika sana, kwani katika maisha yake hakuwahi kuwekewa silaha kama ile popote katika mwili wake, kitendo kile cha kuwekewa silaha ile ya moto kichwani, kilimfadhaisha sana.

    Faridi hasira zilimjaa kwa kicheko cha faudhia cha dharau, akataka kuonesha ubabe kwa kumkomboa mpenzi wake, akamsahau Rama akaielekeza Bastola yake kwa Faudhia huku akimtaka Faudhia aweke silaha yake chini.

    Faudhia akakaidi amri haramu ya Faridi, ikawa Faudhia amemuelekezea silaha ile aina ya Balleta Rebeka, na yeye akaelekezewa silaha aina ya Star (Chinese) na Faridi, kila mmoja akitaka kuitumia silaha yake kwa mlengwa.

    Rama alipopewa ahueni ile ya kutoelekezewa mtutu wa Bastola, akamuhami Faudhia ili asidhuriwe na risasi za silaha ya Rama hivyo akakata shauri.

    Alirusha teke moja la nguvu katika mkono wa Rama ukaitoa ile Bastola mikononi mwake na kudondoka chini huku ikifyatuka risasi moja na kutoa mlio uliosikika sehemu kubwa katika eneo lile.

    Rama alimvamia Faridi kwa kumbo akadondoka nae chini kwa kishindo, wakawa Faridi yupo chini na Rama yupo juu wakikabana kabali katika shingo.

    Rebeka alipiga kelele aliposikia sauti ya risasi iliyofyatuka katika Bastola ya Faridi, akahisi kama ile bastola aliyowekewa kichwani kwake na Faudhia imefyatuka kwake yeye. Mwili wake ulikufa ganzi akaishiwa nguvu akanyong’onyea akaanguka chini kama mzigo.

    Faudhia alimuona Rebeka akianguka chini huku akitwetwa, pumzi zikimpaa. Akapiga hatua hadi pale katika Bastola ya Faridi ilipoangukia akauweka kwapani mfuko wake, akaiokota ile Bastola ya Faridi kwa mkono mwingie pale chini kwa tahadhari kubwa, akawa ameshika silaha mbili mikononi mwake. Akamkimbilia Rama pale juu alipokuwa ambapo alikuwa akitupa makonde ya uso kwa Faridi kama hana akili nzuri.

    Mara wakiwa katika mbilinge mbilinge zile, zikasikika sauti za milio mikubwa ya risasi zilizohanikiza eneo lile.

    Askari polisi wa Anti Robari walikuwa wameshuka eneo lile, wakawaweka chini ya ulinzi watu wote wane waliokuwa pale, Faudhia akakutwa na silaha mbili mikoni mwake akatakiwa kuzisalimisha zile silaha pale chini alipokuwa.

    Hali ilikuwa tete sana kwa Rebeka kwani kitendo cha Faudhia kumwaga hadharani kuwa yeye ni muathirika kimemtia aibu na kule kuoneshwa kwake silaha zile kumemfanya Presha ishuke, akawa anahangaika kuitafuta pumzi yake iliyokuwa ikimjia kwa kusuasua.

    Faudhia aliziweka zile silaha chini akaiinua mikono yake juu, askari mmoja alimfata akatoa pingu akamfunga nazo kwa nyuma. Wakati huo huo akazichukua zile silaha zilizosalimishwa akazitoa risasi zilizokuwa zipo chemba tayari kwa kufyatuka, akaziweka katika Megazin zake.

    Rama baada ya kusikia milio ya risasi na sauti ya askari ikimuamuru kujisalimisha, alitii amri ile huku akimuacha Faridi akivuja damu mdomoni mwake, pia akiwa ameumka uso mzima kama alieumwa na manyigu. Chezea ngumi za uso wewe?!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Askari mnaona lakini, nashambuliwa nyumbani kwangu? Mnaona huyu bwana na huyo bibie wanataka kutuua? Nyie mashahidi hivyo mjuwe.”

    Faridi aliongea maneno yale huku akisema na mikono yake ikiwa katika hali ya kuuliza askari wale.

    Rama alifungwa pingu akaingizwa ndani ya gari ya Polisi pamoja na faudhia, wakiwa na pingu mikononi mwao. Faridi alijifuta mavumbi akawaambia wale askari huku akitowa kitambulisho chake cha kazi na kuwaonesha askari wale.

    “Nimekuja kushambuliwa mimi na mke wangu nje ya nyumba yangu, huyo mwanamke nimemuacha sasa ameniletea bwana wake ili kunifanyia fujo nyumbani kwangu kweli hii ni haki jamani?”

    Askari wale wakamwambia, “Uje kituoni kufungua kesi ya kupigwa na kufanyiwa fujo nyumbani kwako, hawa sie tunakwenda nao kituoni hapo Ostabey.”

    Askari wale walisema maneno yale huku wakimuinua Rebeka pale chini aliekuwa amepandwa na presha, wakamuinua huku Faridi akimpa msada wakampakia ndani ya gari yake waliokuja nayo.

    Faridi akawaambia wale askari kuwa anamuwahisha mkewe hospitali kisha atakwenda kituoni kwa ajili ya kufungua shitaka lile.

    Akairudisha ile gari ya Faudhia uwani kwenye maegesho yake, kwani funguo za gari ile zilikuwa sehemu yake katika gari ile iliyokuwa haikuzimwa mashine yake.

    Askari Polisi walirukia gari yao aina ya Toyota Land Cruser Pick up wakaelekea kituo cha Polisi Ostabey na Faridi akiwa na Rebeka akaelekea Hospitali ya TMJ iliyokuwa jirani na pale kwake.

    Rama na Faudhia walifikishwa katika kituo cha Polisi cha Ostabey wakaingizwa katika chumba cha wapelelezi kuhojiwa wakafunguliwa pingu mikononi mwao, Faudhia akatakiwa kueleza uhalali wa silaha zile alizokutwa nazo.

    Faudhia akaeleza uhalali wa silaha zile, akatoa risiti yake kutoka katika mkoba wake, ikaionesha silaha anayoimiliki kuwa ni ya halali, pia akaeleza ile silaha nyingine kuwa siyo yake bali inamilikiwa na Mtalaka wake. Akaeleza namna ilivyotokea hadi kukutwa nayo mikononi mwake silaha ile.

    Askari alizichukuwa zile risiti akazikagua kwa makini jina la mmiliki wa silaha ile, aina ya silaha iliyoandikwa katika risiti ile pamoja na namba ya silaha ile zote zikawa zinalingana hakuna mushkeli wowote na silaha waliyokuwa nayo pale mbele yao, ikiwa imefungwa usalama wake..

    “Kwa nini unatembea na risiti za silaha wakati hii silaha inaonesha katika risiti hii umemilikishwa miaka miwili nyuma?”

    Askari mpelelezi alimuhoji swali la kizembe Faudhia lakini akiwa na maana yake ndani ya nafsi yake.

    “Kwani kutembea na risiti ni makosa ninayostahili kushitakiwa nayo?!”

    Faudhia alijibu kijeuri swali lile kwani hakuona umuhimu wa swali lile kwake.Kakini njaa iliyokuwa imemkamata sana, ilipoteza kabisa busara katika kinywa chake.

    “Samahani Afande naomba niwasiliane na mkuu wa kituo cha Polisi Magomeni, kwani leo hii asubuhi tulikuwa pale na kuna majukumu muhimu aliniagiza naomba mnipigie niongee nae.”

    Rama aliwaambia wale askari wa upelelezi waliokuwa pale katika chumba chao kwenye gorofa ya kwanza.

    Wale askari walitazamana kwa muda wakamuuliza Rama.

    “Wewe upewe mikakati na mkuu wa kituo umekuwa ni askari? Mkuu wa kituo ni nani wako hata akupe mikakati wewe?”

    Rama aliwaeleza wale askari kuhusu watu waliopelekea kuwaleta pale mkuu wa kituo anamuhitaji yule mwanamke alieachiwa kule katika eneo la tukio.

    Wakamuuliza kama namba za mkuu wa kituo anazo, nae aliingiza mkono mfukoni kwake akatoka na kikaratasi kilichokuwa na namba ya mkuu wa kituo cha Polisi magomeni, akawakabidhi wale askari kikaratasi kile.

    Wale askari wakakichukuwa kikaratasi kile wakakiangalia hakika waliziona namba za simu mbili katika karatasi ile.

    Askari mmoja alitowa simu yake, akaziandika zile namba za simu kisha akapiga namba ya mtandao wa Voda akasikiliza upande wa pili.

    “Halow mkuu wa kituo cha Polisi magomeni hapa nani ninaongea nae?

    Simu ile iliitika upande wa pili, na Yule askari alimsalimu mkuu Yule kwa heshima kisha akajitambulisha na kituo chake cha kazi, akamwambia kuna mtu anataka kuzungumza nae. “Mkuu kuna mtu anataka kuzungumza na wewe, anasema ulimpa namba zako ili muwasiliane hivyo tulitaka kuhakikisha tu Afande. Yule mkuu wa kituo akamwambia ampe azungumze nae. Rama alipopewa ile simu hakufanya makosa alifikisha ujumbe sawasawa.

    Mkuu wa kituo cha polisi magomeni alifahamishwa kuonekana kwa Rebeka pia kutaka kufunguliwa kesi kwao pale Polisi. Hivyo akamtaka mkuu yule kuchukuwa hatua za haraka sana ili kumtia mokononi Rebeka kabla hajatoweka katika mji huu hasa ukizingatia kuwa tayari Rebeka ameshafahamu kuwa mumewe ameambiwa matatizo yake. Hivyo mwanamke Yule anaweza kufanya uhalifu ule zaidi na zaidi kisha akatoroka na kuendeleza kufanya maafa. Mkuu wa kituo cha Polisi Magomeni akamuahidi kwenda pale wakati uleule. Simu ile ikakatwa askari wale wakapata mwanga wa tukio lile.

    Nje ya jengo lile la polisi katika maegesho ya magari ya raia gari aina ya Lange Rover New Model, lilikuwa likiegeshwa kituoni pale na dereva wake aliekuwa amejaa hasira sana.

    Faridi aliteremka ndani ya gari yake akaifunga mlango akaioneshea rimoti na kubonyeza kitufe, kilichofunga loki za milango ile pia ikiwasha taa ya kuonesha kuwa ulinzi wa gari ile upo macho.

    Akapiga hatua hadi pale mapokezi ya Polisi, akasimama ubaoni na kuomba PF3 (POLICE FORM NAMBER 3) pia akitaka kufungua kesi kwa kupigwa na kufanyiwa fujo nje ya nyumbani kwake, pia akieleza kuwa watu waliomfanyia tukio lile wameshakamatwa wapo pale kituoni, ambao ni mwanamke na mwanamme.

    Wale askari wa kaunta waliokuwa zamu, wakamuelekeza apande juu gorofa ya kwanza akikutana na korido, apinde kulia kisha atakiona chumba cha upelelezi mkono wake wa shoto, hapo atawakuta wahusika na watuhumiwa wake wanahojiwa hivyo kila kitu atafanyiwa na askari waliowakamata watuhumiwa wale.

    Faridi akapanda ngazi kuelekea kule alipoelekezwa, na alipofika pale akawaona watuhumiwa wake wakiwa wamekalishwa kitako na yeye akapokelewa akahojiwa kuhusu silaha aliyokutwa nayo mtalaka wake kama anaifahamu, akajibu kuwa ni yake ila aliporwa na mtuhumiwa wake wa kiume ili kutaka kumshambulia lakini katika kupambana nae, silaha ile ikaanguka chini ikafyatuka ndipo mtalaka wake alipoikimbilia na kuiwahi wakamuweka chini ya ulinzi yeye pamoja na mkewe aliekuwa ameshukwa na presha, nay eye akaanza kushambuliwa na bwana wa mtalaka wake, hata wale askari walipofika katika eneo la tukio wakamkuta akiwa chini akishambuliwa.

    Wakiwa katika mahojiano na Faridi askari wale, mara aliingia bwana mmoja mrefu mwenye mwili uliojaa, aliejengeka kikakamavu akiwa na sharubu nyingi juu ya mdomo wake zinazogusana na pua . Askari wale wote walisimama wakatoa heshima kwa mkubwa yule, na yule bwana aliipokea heshima ile kisha akaketi kitini bila kukaribishwa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alikuwa ni mkuu wa kituo cha Polisi Magomeni, aliekuwa amevaa nguo za kiraia nguo ambazo Rama na Faudhia walishamuona nazo asubuhi walipotolewa kutoka hospitali ya taifa Muhimbili. Mkuu wa kituo cha Polisi Magomeni alitaka maelezo ya kesi ile ilivyokuwa hadi Rama na Faudhia kuwekwa chini ya ulinzi, askari wale wakaeleza kila kitu tangu walipopigiwa simu wakiwa doria na kupewa taarifa ya tukio lile walipokwenda eneo la tukio hali halisi waliyoikuta, pamoja na silaha walizozikamata, ingawa silaha zile moja imeshatambulika kuwa inamilikiwa kihalali na Faudhia Baddy Mnyone kutokana na kibali chake ambacho alikuwa akitembea nacho. Ila silaha nyingine mlalamikaji ameitambua ni yake anayoimiliki kihalali ingawa bado hajawapa vielelezo vinavyothibitisha umiliki wake.

    Mkuu wa kituo akasema kuwaambia wale askari kwamba; “Hawa watuhumiwa ninawapa dhamana mimi, ila huyu Faridi nendeni nae nyumbani kwake akawaoneshe vielelezo vyake vya kumiliki silaha, pia Rebeka huko hospitali akiruhusiwa tu na dakitari namtaka ofisini kwangu haraka, huyo Faridi mpeni PF3 akatibiwe ila hiis ni kesi za mapenzi mtu na mtalaka wake, hivyo watakwenda kumaliza nyumbani kwao kifamilia, kwani kunaweza kuleta mlolongo wa kesi tele hapa”

    Mkuu wa kituo cha Polisi Magomeni baada ya kusema maneno yale aliwageukia Rama na Faudhia, akawaambia mnaweza kwenda ila kesho asubuhi mripoti ofisini kwangu.

    Rama na Faudhia walishukuru sana, Faudhia akaelezwa kuwa silaha yake itabaki kituoni kwa muda kwani hali yake kisaikoloji haipo vyema anaweza kuleta madhara kama atakabidhiwa silaha ile kwenda nayo.

    Rama na Faudhia walisimama wakamshukuru yule Mkuu wa kituo, wakashika njia kutoka nje ya kituo kile.

    Faridi aliwatazama kwa jicho baya sana, akiwa amefura kwa hasira, kwani alijuwa pale ndiyo anakwenda kuwakomesha kinyume chake ikawa ni tofauti na fikira zake.

    Faudhia alitembea kwa hatua kadhaa kisha akasita na kurejea hadi mle ndani katika chumba cha upelelezi, akamkabili faridi akamuuliza.

    “Funguo za gari yangu umeziweka wapi?”

    Faridi hakumjibu alikaa kimya huku akiwa hamtazami kabisa kwa namna alivyokasirika, akawa kama hakusikia swali lile.

    Faudhia alimuuliza tena na safari hii Faridi alimjibu kwa hasira;.

    “Kwani ulinikabidhi mie funguo zako mikononi mwangu?”

    Faudhia akamwambia huku akiwa amekunja ndita kwa hasira.

    “Wewe ndiyo uliingiza ndani gari yangu na hukunipa funguo, ndiyo maana nakuuliza umeiweka wapi funguo yangu?”

    “Kama uliiacha ndani ya gari basi nenda kwenye gari utaikuta sikuchukua funguo yako mie”

    Faridi alijibu kwa jeuri akiwa hamuangalii kabisa. Mkuu wa kituo akawaamrisha wale askari waende nao wote hadi huko kwao ili kama funguo zipo itajulikana na kama hazipo, basi itajulikana pia wakienda kule wote itaepusha kusemwa kumechukuliwa kitu, kwani pia pale kwake mtapata uthibitisho wa uhalali wa silaha hiyo atakapowapa vibali vyake.

    Askari wale wakatii agizo la mkuu wa kituo cha Polisi Magomeni wakawachukuwa wote ndani ya gari ya Polisi kasoro Rama aliebakia nje pale Polisi, wakaenda nao hadi Mikocheni nyumbani kwa Faridi, wakaingia ndani, Faudia akaziona funguo za gari yake zikiwa ndani ya gari mahala pake.

    Faudhia akawasha gari yake akatoa nje ya uwa ule akashika njia kwenda Polisi kumpitia Rama aliekuwa amemuacha pale, alipofika akampakia wakashika njia.

    “Tutafute sehemu tule kwanza kwani njaa imenishika sana hadi nadhari imenipotea hapa.”

    Faudhia alimwambia Rama akaendesha gari wakaenda Namanga pale katika mgahawa wa Wapemba.





    3

    Rebeka alikuwa yupo katika chumba cha Vip pale hospitali ya TMJ madaktari wawili waliokuwa wakimshughulikia haraka walimpa dawa za kudhibiti ile hali na hakuchukua muda mrefu akapata nafuu, madaktari wakatoka wakimuacha mgonjwa wao apumzike.

    Rebeka akawa amekaa anatafakari namna matatizo yalivyomtokea. Akiwa katika kuwaza hili na lile, mara alipatwa na taharuki kubwa moyoni mwake nusura isababishe tatizo lingine.

    Katika Luninga iliyokuwa pale chumbani mle alishuhudia habari za papo kwa papo, zilizokuwa zikirushwa na Luninga kutoka katika kituo cha TBC 1, ikimuonesha Mkuu wa kituo cha polisi magomeni akizungumza na waandishi habari, kumuhusu yeye pia ikioneshwa picha yake kuwa anatafutwa na Polisi kwa kosa la kuambukiza virusi vya Ukimwi watu kwa makusudi.

    Rebeka moyo wake ulikwenda mbio sana, kwani katika azma yake ilikuwa imesalia watu wawili ili apate idadi aliyoikusudia ya watu kumi wanaume, kwani siri nzito iliyokuwa kifuani mwake kwa muda mrefu sana alikuwa aiweke wazi akiwa na yeye amesha tekeleza azma yake, sasa akaona kuwa pale hapamfai tena kwani kila atakaekuwa ameiona taarifa ile atatoa taarifa Polisi na yeye atakamatwa, akaona dhamiri yake itakuwa haitimii kabisa, kwani atawekwa ndani na hatimae kufungwa jela. Akaona hapana bora afungwe akiwa ametimiza mambo yake kuliko kuishia njiani. Akizingatia kwamba alipotoka ni mbali alipobakisha ni pachache sana kwani ilikuwa bado watu wawili ili azma yake itimu.

    Aliinuka kutoka kitandani akaingia chooni mlemle chumbani kwake alipokuwa akipata matibabu mle VIP, ambapo gharama yake ilikuwa ni ya juu sana kiasi mtanzania wa kawaida hathubutu kutibiwa huko, hata uangalizi wake upo vizuri matibabu yake ni ya ukweli sana, na hata dawa zake ni zenye uwezo mkubwa sana.

    *******CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Faridi aliwaacha wale askari sebuleni kwake akaingia chumbani kwake, akafungua kabati lake, akatoa vibali vyake vya kumiliki silaha, kisha akawakabidhi wale askari ili wavipitie na kuvithibitisha.

    Askari wale walivitazama wakavithibitisha kuwa ni halali, wakavichukua pamoja na Faridi wakatoka.

    “Twende Hospital hapo TMJ ili kama hali ya mkeo imetengemaa, basi Mkuu kama ulivyomsikia anamuhitaji kwa mahojiano maalum.”

    Faridi akiwa na askari wale walielekea hospital ya TMJ kwa Rebeka ili kama atakuwa yupo vizuri kiafya na dakitari akimruhusu waweze kumchukuwa na kumpeleka kituo cha Polisi Magomeni, kwa Mkuu wa kituo ili akamuhoji kama alivyoelekeza.

    Gari ya Polisi ilitembea hadi pale hospitali ya TMJ ambapo palikuwa ni jirani na pale nyumbani kwa Faridi, wakaiingiza gari yao katika maegesho askari watatu walishuka na Faridi, wakapanda ngazi kwenda katika chumba ambacho Faridi alimuacha Rebeka akipewa matibabu. Walitembea katika ngazi hadi juu katika vyumba vya VIP wakaingia pale katika chumba alichokuwamo rebeka , lakini walikuta kitanda kikiwa kitupu Rebeka hayupo. Wale askari walitazamana kwa haraka macho yao wakayahamishia kwa Faridi na kumuuliza.

    “Vipi humu ndipo alipokuwa mkeo, mbona hayupo au umeamua kutuchezea?!”

    Faridi akawathibitishia askari wale kuwa ndimo alimokuwamo labda atakuwa ameingia chooni, wavute subira, askari wale wakakaa hadi zikatimia dakika ishirini wakamwambia Faridi aingie humo chooni amuhimize ili waondoke, lakini hata faridi alipoufungua mlango wa choo kile cha VIP napo pia palikuwa patupu, hakuwamo Rebeka mtoto wa Makuka.

    Faridi alianza kuchanganyikiwa akawaambia wale askari wawaone madaktari waliokuwa wakimuhudumia labda watakuwa wamemuamisha chumba.

    Faridi na askari wale wakatoka hadi katika chumba cha madaktari wakauliza kuhusu kama Rebeka amehamishwa chumba au kapewa ruhusa ya kutoka, lakini madakitari wale wakatoa jibu lililomfanya Faridi apagawe katika moyo wake.

    “Hapana hakuna mgonjwa kutoka VIP alieruhusiwa kutoka, wagonjwa wote wapo vyumbani mwao wamepumzika”

    Faridi na wale maaskari wote wakawa hawana majibu kuwa amekwenda wapi, ila kitu kilichokuwa kikiwaumiza vichwa vyao ni kwamba, kwanini aondoke ikiwa hajaruhusiwa, na ikiwa ameondoka atakuwa amekwenda wapi.

    Ndipo Faridi alipotoa simu yake akaanza kumpigia simu lakini simu ile iliita bila kupokelewa, alipoipiga kwa mara ya pili hali ikawa ni ile ile, akajaribu kwa mara ya tatu safari hii hali ikawa ni tofauti kabisa kwani simu ile ilikuwa imezimwa.

    Faridi alishusha pumzi nzito macho yakamuwiva lakini hayakuweza kubadilisha ukweli kuwa Rebeka hakuwapo katika chumba chochote cha hospitali ile akaingia mashaka na yale yaliokuwa yakisemwa, moyo wake ukaanza kupiga kwa kasi.

    *******

    Rama na Faudhia walikula chakula kama hawana akili vizuri, kwani njaa iliwafitini na matumbo yao, wakanywa na soda wakapata nguvu, Faudhia alilipa chakula kile wakaondoka wakaingia katika gari ikawa sasa ni zamu ya kwenda nyumbani kwa Rama kisha waende Hospitali kupima tena kama ratiba yao walivyoipanga.

    Rama alikuwa anakaa Tabata Segerea Migombani, ndipo alipojenga nyumba yake ndogo ya kumtosha, walitembea na njia za maraisi wataafu kwani walipitia barabara ya Ally Hassan Mwinyi hadi Mwenge wakapinda kushoto wakashika njia ya barabara ya Sam Nujoma hadi Ubungo, kule wakatembea na Barabara ya Mandela hadi Tabata sheli, wakapinda kulia wakaelekea Segerea, na hatimae wakafika nyumbani kwa Rama, wakaegesha gari nje wakaingia ndani ya nyumba.

    “Karibu Faudhia hapa ndiyo nyumbani kwangu, ingawa siyo pazuri ila naomba ukaribie tu, sina vitu vya thamani kama kwako ulipopazowea hivyo naomba ukae hivyohivyo katika viti vya thamani ndogo, ikiwa vitakuumiza basi nisamehe na univumilie sana.”

    Rama alimwambia Faudhia maneno yale huku akitabasamu, na Faudhia nae akacheka kisha akamjibu.

    “Hongera umejitahidi sana kwani hatua uliyofikia unastahili kumshukuru sana Mungu, kwani kuna kina sie hata kiwanja hatuna sikwambii nyumba yenyewe.”

    Rama alicheka akafarijika kwa majibu yale kwani alishaanza kujishitukia na nyumba yake.

    Rama alivua shati lake palepale sebuleni alipokuwa Faudhia, akavua na fulana mchinjo ya ndani akawa kifua wazi.

    Faudhia alimtazama Rama mara mbili kifuani kwake namna vinyweleo vingi vilivyopamba kifua chake, kisha akamtazama usoni akakuta Rama nae alikuwa akimtazama kwa kumuibia.

    Faudhia alijinyoosha pale kitini kwani mwili wake ulikuwa unamsumbua kutaka kitu ambacho bado kinahitaji uhakiki wa afya, akatazama pembeni huku akimwambia Rama kwa sauti iliyokuwa ikikatikakatika au kuwa na kikohozi hivi;

    “Nenda basi kaoge uvae tuwahi hospital kwani muda unakwenda na ni lazima tupime leo”

    Rama aliingia chumbani kwake akavua suruwali yake iliyokuwa imechafuka akavua na nguo yake ya ndani akatia mswaki dawa akenda bafuni kulipokuwa na choo pamoja, alipomaliza akaingia chumbani kwake kujiremba akanyoosha nguo zake ambazo alikuwa akizivaa zikimkaa vizuri sana, ila katika hali ambayo hakupanga nguo zile alizokuwa akizipenda kuzivaa, zilimfurahisha sana Faudhia. Akasifiwa kuwa amependeza, nae akaitika pongezi ile wakatoka wote wakaingia ndani ya gari na safari ya kwenda Agha Khan Hospital ikaanza.

    Faudhia alishika usukani akaongoza njia, wakacheza na foleni kubwa lakini walikata njia za mkato, wakipitia pale Tabata Matumbi, wakatokea Kigogo, wakashika njia ya Jangwani kutokea pale katika club ya Yanga wakashika njia ile ya mtaa wa twiga hadi Msimbazi, wakapinda kushoto kushika barabara ya Morogoro, wakapinda kulia wakitembea na barabara ile mbele wakapinda kushoto wakashika barabara ya Ally khan, wakanyoosha nayo ile mitaa ikawafikisha hospitali ya Agha Khan wakafanya taratibu ya malipo ya vipimo walivyotaka kutazamwa Faudhia akalipa pesa.

    Wakaingizwa katika chumba maalum cha kupimia wakachukuliwa damu kubwa ya mshipa, wakafanyiwa vipimo vyote kutokana na damu ile kubwa. (FULL BLOOD PICTURE) Dakitari baada ya kuichukuwa damu ile kwa sindano kwa kila mtu na sindano yake akaelekea maabara sindano ya Faudia akiishika katika mkono wa kulia na Sindano yenye damu ya Rama, akaishika katika mkono wake wa kushoto.

    Alipofika maabara akaiingiza damu ile katika mashine maalum ijulikanayo kitaalam kwa jina la BC 2300 MINDRAY, ikaifanyia damu ile, na baada ya muda kipimo kikatoa majibu.

    Daktari akayaandika majibu kama yalivyotoka katika vyeti vya Rama na Faudhia akaenda pale katika chumba kile alipowaacha akawakabili ili kuwapa majibu yao.

    Moyo wa Rama ulikuwa unakwenda mbio kama ngoma ya Lizombe, kwa wahaka na mashaka yaliyomjaa. Mate yalimkauka kinywani mwake matumbo yakawa yanamcheza kifupi hakuwa na amani kabisa alikuwa amekaa duniani hayupo wala akhera hajafika.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Niwape majibu yenu kwa pamoja au kila mtu nimwambie peke yake”

    Dakitari aliekuwa na majibu mkononi mwake aliwauliza Rama na Faudhia kwa pamoja.

    Faudhia akamwambia Dokta.

    “Tuambie tu kwa pamoja dokta haina neno kwani tumekuja kupima pamoja basi tuambie kwa pamoja,”

    Daktari alishika vile vyeti akaanza kuwasomea majibu yao.



    “Tumetazama damu zenu kwa kutumia mashine ya MINDAY BC 2300, ambayo inapima Full Blood Picture hatukuona tatizo sana la damu. Ila kwa kupitia mashine ya ELISA ambayo inauwezo wa kupima VVU, huko ndipo tulipopata majibu yenu halisi mliyokuwa mmeyajia hapa.”



    “Faudhia Baddy Mnyone, kipimo chetu kimeitambua damu yako kuwa ni Negative, kwa maana hiyo bado hujaathirika, hongera sana na endelea kujitunza hivyohivyo, ila nakushauri upime tena baada ya miezi mitatu kwani hiki ni kipindi cha mpito ikiwa umeathirika wiki moja nyuma unaweza usionekane kama una maambukizi, lakini ukipima tena baada ya muda huo ukapata majibu haya haya, basi tembea kifua mbele kuwa ni mzima”

    “Rama kipimo chetu kimeitambua damu yako kuwa ni Positive, kwa maana hiyo umeathirika unaishi na virusi vya Ukimwi, pole sana nakushauri uishi kwa matumaini na epuka mawazo, kwani kuwaza sana hadi kupitiliza ni kitu kibaya sana kwa muathirika kuwa nacho humpelekea kufa haraka. Unatakiwa kuikubali hali yako ulonayo, usipoteze wakati kutazama wapi ulipopata maambukizi haitokusaidia kitu”

    Baada ya kusoma majibu yale Daktari alisimama akaondoka kwenda kuendelea na vipimo vya watu wengine, kwani kulikuwa na watu wengi sana waliokuwa na haja zao za kitabibu katika hospitali ile.

    Yaliposomwa majibu ya Faudhia hakukuwa na tatizo, ila Dokta alipotoa majibu ya Rama hali ikawa mbaya sana. Ilikuwa mbaya kwa Faudhia na Rama mwenyewe kwani kila mmoja alikuwa hayapendi majibu yale kwa upande wake, lakini vipimo ndiyo vilikuwa muamuzi wa mwisho katika jambo lile.

    Faudhia aliweka mikono yake kichwani, huzuni ikamkabili upya hali ya kupata majibu tofauti ikatoweka moyoni mwake.

    Rama hakuwa na nguvu yakusema neno lolote, maumivu yalirejea upya ndani ya moyo wake, akawa amesizi kama zezeta macho yake ameyakodoa huku machozi yakimbubujika bila khiyari yake, hakika alikata tamaa, nafsi yake ilizidi kumlaani Rebeka kwa kutokumkosea lolote lakini akamuambukiza makusudi virusi, kama hiyo haikutosha akamkimbia na kufikia kumkana kuwa hamtambui, na kumwambia kuwa hakuwa na hadhi ya kutembea na yeye dah.

    Pale alipokuwa amekaa Rama alimtazama Faudhia aliekuwa amejiinamia kwa mawazo, Rama akamwambia kwa sauti iliyojaa huzuni na kukata tamaa ya kuishi.

    “Faudhia dada yangu, jitihada hazishindi kudura. Ninakubali kuwa nimeathirika na sina tena ubishi juu ya hilo wala sitapima tena kwa ajili ya kuthibisha kuathirika kwangu. Ila ninakuomba uendelee mbele usirudi nyuma. Hujazaa bado hivyo tafuta mwanaume mwenye moyo wa kupenda kwa dhati akuoe ili uzae, kama Mungu akikujaalia kupata mtoto wa kiume naomba mpe jina langu ili iwe kumbukumbu kwangu katika dunia hii. Mimi siwezi tena kuishi katika dunia hii, wala kuishi na wewe japo nilitamani sana kuishi na wewe kwani maumivu yetu yanafanana, lakini ndiyo hivyo nipo Positive.”

    Rama aliposema maneno yale alilia kwa kwikwi kilio kilichoambatana na kikohozi, donge likimkaba moyoni mwake, pumzi zikampaa kwikwi zikachukua nafasi kwa wingi sana, hali yake ikabadilika ghafla ikawa mbaya tia maji tia maji.

    Faudhia alimkumbatia Rama aliekuwa hajiwezi kwa kulia moyo wake ukiwa unapiga pigo moja moja, ikiwa siyo katika utaratibu wake. Kwikwi nazo zikashamiri sana.

    Faudhia alimuegamisha katika kiti akiwa amemkumbatia akamwambia huku na yeye akiwa anatokwa na machozi machoni mwake.

    “Rama usiseme hivyo bwana kuathirika siyo kufa hebu kuwa kawaida, mie sijaona mwanaume katika miaka hii mwenye moyo wa kupenda kwa dhati, ikiwa wapo basi ni mia kwa mmoja na watakuwa na wake zao hivyo sina sababu ya kuolewa tena. Kwa kuwa wewe umeathirika basi mie sina haja tena ya kuolewa wala kuzaa na mwanaume mwengine. kupitia ndoa na Faridi nimeingia chuo kikuu cha mafunzo sithubutu tena kuingia katika matatizo mengine nikauumiza zaidi moyo wangu.”

    Faudhia aliposema maneno yale alimshuhudia Rama akiishiwa nguvu, mwili wake ukiwa mwepesi uzito ukimtoweka kwa kasi huku jasho jingi likimmiminika mwilini mwake. Akamuegemeza katika kiti akakimbilia kwa madakitari huku akilia akiomba msaada wa kupatiwa huduma kwa haraka kwani hali ya Rama ilikuwa yakukatisha tamaa sana kwa muda mfupi tangu apate majibu yale mabaya kwa upande wake.

    *******

    Faridi akiwa na wale askari alishindwa kuelewa lolote lililomsibu mkewe Rebeka hata akaondoka pale hospitali, akajipa moyo kuwa yawezekana ikawa amekwenda hotelini walipokuwa katika fungate yao. Kwani walikwenda wote kwake kwa sababu kubwa moja tu, ilikuwa Faridi akachukue hati yake ya kusafiria iliyokuwa katika kabati lake ili wasafiri na mkewe. Kwani kazini kwake alikuwa amechukuwa likizo ya mwezi mmoja.

    Alipanga kusafiri kwenda safari ya Africa ya kusini kwa ajili ya kupumzika na mkewe, pesa ya safari, ikiwemo ya matumizi, hoteli, usafiri na kila kilichohitaji pesa alikuwa ameshatoa bank ameziweka pesa zile katika mkoba wake wa safari walioufungia katika kabati la hoteli ile. Funguo hawakukabidhi mapokezi, kama utaratibu ulivyokuwa ukiwaagiza bali walitoka nazo walikuwa nazo Rebeka katika begi yake ndogo ya mkononi, kwani walikuwa na pesa nyingi sana, Milioni hamsini pesa za kitanzania, na pesa za kimarekani zilikuwa ni dola elfu ishirini. Sawa na pesa za kitanzania Tsh Milioni Thalathini na mbili, laki tatu sitini na tatu elfu. 32,363,000/ kwa mujibu wa bei ya maduka ya kubadilishia pesa za kigeni zilizokuwa zinauza dola moja ya kimarekani kwa pesa ya kitanzania 1,618,15/. Kwa hiyo jumla ya pesa zote walikuwa na Tsh, 82363000( MILIONI THAMANINI NA MBILI, LAKI TATU SITINI NA TATU ELFU.) Faridi hakutaka kutembea na pesa nyingi vile kwenye gari, kwa kuhofia kuvamiwa na Majambazi njiani wakazipoteza, ndiyo maana aliufungia mkoba ule katika kabati ya Hoteli kisha funguo hawakuzikabidhi mapokezi, wakihofia watu wa usafi wasije kuona pesa nyingi vile wakapata ushawishi wa kuiba.

    “Inawezekana huyu akawa amekwenda Hoteli kupumzika na simu yake itakuwa imezimika chaji kwani hatukuchaji simu tangu jana tulipoingia Hotel, ngoja nimfatilie kisha nitamleta mimi mwenyewe kituoni”

    Faridi aliwaambia wale maaskari, na wale maaskari wakatabasamu wakamwambia Faridi maneno ambayo hakuyatarajia kuyasikia kwa wakati ule.

    “Faridi mkeo ni mualifu anaesambaza virusi vya Ukimwi makusudi kwa watu, hivyo anahitajika kwa mahojiano na mkuu wa kituo pale Magomeni, ili akahojiwe kwa nini anafanya hivyo kwa kuambukiza watu virusi makusudi, hivyo hata wewe si ajabu ukawa umekwisha ambukizwa virusi, hivyo siyo utuambie kuwa umfate halafu umlete kituoni hatufanyi kazi hivyo, kwani mkuu hatatuelewa kabisa, hapa tunakwenda wote huko hotelini, kisha tutamchukuwa mkeo kama tukimkuta na tutakwenda nae hadi kituoni, kwa mahojiano zaidi”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Faridi alitungua kicheko kikubwa, akawaambia wale maaskari;

    “Hivi na nyie pia mmelishwa uongo na mtalaka wangu na nyie mmeukubali uongo wake? Yule bwana aliekuwa na Mke wangu amedai Rebeka alikuwa mpenzi wake, sasa kinachoshangaza mie nimeoa Bomani, kabla ya kuoa ilitangazwa wiki moja kabla ya ndoa kama kuna mtu ana pingamizi na ndoa ile, ajitokeze kuweka pingamizi lakini hadi wiki imemalizika hakuna mtu hata mmoja aliejitokeza kusema Rebeka ni mchumba wake, sasa mie nimeoa wanaanza kusema maneno mara mchumba wake, mara ameathirika, kama mtu ameathirika wa nini anamtaka? Hayo ni majungu tu hakuna kitu kama hicho, twendeni Hotelini kisha tutakwenda kumpima na mie nikiwepo pamoja na huyo Mkuu wenu, ila Rebeka akiwa mzima mjue mtanilipa pesa nyingi sana kwa kumdhalilisha mke wangu, haya twendeni.”

    Faridi alisema maneno yale huku akianza kuondoka, wale askari wakamfata huku mmoja wao akamwambia.

    “Na vipi ikiwa atakutwa ameathirika?”

    Faridi hakujibu kitu kwani hakuna jambo lililokuwa linamkera moyoni mwake kama kuambiwa mkewe Rebeka ni muathirika, kwani hakutaka kuamini kabisa maneno yale yaani alikuwa hayaamini kama inawezekana kama mbuzi kumpa nyama na chui kumpa majani kula.

    Safari ya kuelekea Hotelini ikaanza, walishuka ngazi wakaifata gari yao pale nje wakaingia katika gari wakaelekea mtaa wa Ohio katika Hotel iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Sheraton, sasa hivi inaitwa Kempisk Hotel. Walipofika Hotelini waliiegesha gari yao pale mkabala na Nyumba ya Sanaa, hawakuiegesha katika maegesho ya kawaida, Faridi akashuka akiwa amefura kwa hasira mkewe kupakaziwa kuwa ni muathirika wa Ukimwi, kwani alikuwa anahisi ni fitina tu za mkewe kutaka kumuharibia mahusiano yake mema na mkewe.

    Ama kweli kupenda ni upofu. Kwani mwenye kupenda Chongo huita Kengeza! Ndivyo ilivyotokea katika moyo wa Faridi, hakutaka mkewe asemwe vibaya, kwani alikuwa amemalizwa na mahaba mazito ya Rebeka, alikuwa haoni wala hasikii, alikisaliti kidole na jiwe liwalo kwake na liwe. Moyo wa kupenda ulikuwa ukimsumbua kifuani mwake.

    Faridi na askari wawili, waliteremka kutoka ndani ya gari ya Polisi, wakapiga hatua kuelekea katika lango la Hotel. Walipofika karibu na lango la Hoteli ile walipishana na gari ya abiria Taxi yenye mstari wa kijani, na wao wakazama ndani ya Hoteli ile.

    “Sie tunakusubiri hapa katika viti, wewe nenda ila tuambie upo chumba gani ili kama tukikuona unakawia tuweze kukufata, kwani tuna kazi nyingine za kufanya”

    Mkuu wa msafara ule, alikuwa akimwambia Faridi maneno yale, huku akimtazama usoni moja kwa moja. Faridi akamtajia chumba alichopanga katika Hotel ile akaondoka hadi kwenye Lifti akabonyeza kitufe pembeni ya Lifti ile, na ile Lifti ikafunguka milango yake akaingia ndani yake, Lifti ile kabla haijafunga milango yake Faridi alishangaa kumuona mmoja wa askari aliekuja nao akiingia nae katika Lift ile, na mara milango ya Lift ikajifunga wakiwa watu wawili ndani ya Lifti ile tu.

    “Vipi mbona umeamua kunifata hamkuniamini kama ninaweza kumleta mke wangu kwenu, haya twende!”

    Faridi alisema maneno yale akabonyeza namba katika Lifti ile, akiiamrisha itakapofika pahala pale iweze kusimama.

    Lifti ile ikapokea maelekezo ikapanda juu hadi pale ilipotakiwa kusimama ikafanya hivyo, ikafungua milango yake wakashuka na kuelekea katika Korido tulivu, lililokuwa na ubaridi wa kiyoyozi, wakapiga hatua kuelekea katika chumba alichopanga Faridi.

    Walipofika pale mlangoni, Faridi aliujaribu mlango wa chumba kile kuufungua, akauona umefungwa kwa funguo. Akatoa simu yake ya kiganjani akaipiga namba ya Rebeka, ili amwambie amfungulie mlango kama yumo mle ndani lakini simu ile bado ilikuwa imezimwa haipatikani. Akapiga tena na tena lakini bado simu ikawa haipatikani. Mashaka yakaanza kumuingia Faridi katika moyo wake kuwa mkewe amepatwa na nini hata simu yake haipatikani.

    Akagonga mlangoni katika chumba kile lakini hakupata majibu, kutoka ndani ya chumba kile. Akakata shauri mbele ya yule askari aliekuwa nae pale.

    “Hebu twende mapokezi nikaulize kama huyu amerudi au laa, kwani hata mtu alietupangisha jana nimemuona pale mapokezi yupo ambae anamjua Rebeka”

    Hakukuwa na ubishi walirudi hadi mapokezi, wakamkuta Yule dada akizungumza na simu, kwa wahaka Faridi akamuuliza mtu wa mapokezi kama amemuona mkewe akirudi pale bila kujali kuongea kwake na simu kwani tayari damu yake ilikuwa inakwenda mbio sana kwa mashaka. Yule dada aliangalia katika droo inayokaa funguo za vyumba akatoa funguo ya chumba cha Faridi akamkabidhi, huku akiendelea kuongea na simu ya mezani kwa lugha ya Kimombo.

    Faridi aliipokea ile funguo akapiga hatua za haraka kuwahi Lifti ili aende chumbani kwake, lakini Yule askari akamzuwia kwa mkono.

    “Hapa tumemfata mkeo, tumetoka katika chumba chako mlango ulikuwa umefungwa, tumekuja hapa mapokezi funguo ya chumba umeikuta, hii ina maana kuwa mkeo hayupo chumbani kwako, sasa unataka kuharakia wapi hapa tunarudi kituoni wewe utatusaidia kumpata mkeo”

    “Afande sijabisha hayo unayosema ila nilikuwa naomba nifike chumbani kwangu, ili nikahakikishe usalama wake kwani hali ishakuwa mbaya hapa, presha naiona inataka kupanda kule kuna pesa zangu nyingi”

    Yule askari akamkubalia kwenda chumbani kwake ila waende wote wawili, ili akatazame hicho chumba chake hivyo vitu vyake pamoja na pesa. Wakaongozana wote kwa kutumia lifti hadi juu wakakiendea chumba kile walichokwenda awali, Faridi akafungua mlango wakaingia ndani ya chumba kile.

    Faridi macho yake moja kwa moja yakapiga katika kabati, akashangaa kuona funguo za kabati zikiwa pale katika kabati, wakati wakitoka na Rebeka kwenda kwake, funguo zile pamoja na za chumba waliondoka nazo akamkabidhi mkewe, inakuwaje funguo ya chumba iwe mapokezi na funguo ya kabati iwe mahala pake?CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Faridi akapiga hatua hadi katika kabati huku Yule askari akiwa nae sambamba, akalifungua kabati lile kwa wahaka mkubwa moyo wake ukapoa alipouona mkoba wake wa safari. Akashusha pumzi ndefu sana huku akitabasamu kinywani kwake, akauchukua mkoba ule akakaa nao kitini, moyo ukamtuma aufunguwe ndani ili ajiridhishe kama upo salama au umepitiwa, akafungua zipu na mkoba ule ukafunguka, alipofika katika sehemu iliyokuwa na pesa, moyo wake ukapiga kwa nguvu sana, macho yalimtoka pima, akatafuta pesa zake lakini hakuziona palikuwa patupu. Faridi hakutaka kuamini akaanza kutoa nguo moja baada ya moja ili kutafuta pesa zilizokuwa sehemu moja ambayo hakuziona.

    Akiwa katika kutoa nguo zile moja baada ya moja ndipo Faridi alipoona kitu kikianguka kutoka katika nguo zile, kitu kilichomfanya apoteze fahamu palepale.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog