Search This Blog

Wednesday, 1 June 2022

MOYO WA KUPENDA - 4

 







    Simulizi : Moyo Wa Kupenda

    Sehemu Ya Nne (4)





    Akiwa katika kutoa nguo zile moja baada ya moja ndipo Faridi alipoona kitu kikianguka kutoka katika nguo zile, kitu kilichomfanya apoteze fahamu palepale.

    *******CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ile Taxi yenye mstari wa Kijani iliongoza njia, ikaingia ile Barabara ya Ohio hadi katika makutano ya Barabara ya Ally Hassan Mwinyi, ikapinda kushoto kushika Barabara ile ya Ally Hassan Mwinyi, wakaongoza hadi katika Barabara ya Uhuru, wakapinda Kulia kukamata ile Barabara ya Uhuru, walipofika makutano ya Barabara ya Uhuru na Nyamwezi, abiria aliekuwa kiti cha nyuma akamwambia dereva wake kuwa amefika, akatoa noti nyekundu ya shilingi Elfu kumi akampa dereva wa Taxi ile ikiwa ni malipo ya kumfikisha pale kutoka mtaa wa Ohio.

    Yule abiria baada ya kuona ile Taxi imeondoka aliingia katika duka la nguo la Baniani akanunua nguo na miwani pambe nyeusi. Akamuuliza muuza duka kama anaweza kubadilisha nguo pale dukani.

    Muuza duka akamjibu kuwa anaweza. Akaoneshwa sehemu maalum ya kujaribia nguo za duka lile na kubadilishia pia. Alibadilisha zile nguo zake alizokuja nazo, akavaa viwalo vipya akapendeza mara dufu ya mwanzoni, usoni mwake alivaa ile miwani pambe iliyokuwa pana ya vioo vya kiza iliyomkaa vyema. Alipotoka pale kwa muuzaji akiwa amebadilika, Baniani akamsifia sana kuwa amependeza. Akamtajia bei ya nguo ile, na Yule mteja wake akalipa pesa akatoka dukani mle akaelekea mtaa wa Nyamwezi na Kipata, pale akapinda kulia akatembea kwa haraka hadi mtaa wa Congo akazikuta Taxi nyingi zimejipanga akatafuta taxi moja iliyokuwa na kioo cha kiza, akapanda nyuma ya gari ile.

    Dereva mmoja mtanashati mwenye maneno mengi, aliingia katika gari ile kwa mbwembwe nyingi akiwaringishia wenzake kwa kupata abiria, aliingia garini akawasha gari na kufungulia mziki wake mkubwa wa Rusha roho, huku akimuuliza abiria wake sehemu anayokwenda akiwa amemgeukia akatazamana nae.

    “ Niambie Mrembo unaelekea wapi?”

    Yule abiria alicheka kicheko cha kishangingi, akamjibu yule dereva Taxi kwa pozi sana.

    “Mrembo nitakuwa mie, kwenye warembo wakihitajika mie nitakuwamo? Acha masihara wewe kaka hebu nitafutie Lodge nzuri, nikapumzike mie nimetoka safari nimechoka sana!”

    Dereva Taxi alitabasamu akamwambia Yule dada kwa dhihaka lakini moyoni mwake akimuingizia maneno ya kumtaka.

    “Dada usimkufuru Mungu, umeumbika mashaallah yaani mimi ningekuwa na mke kama wewe ningeringaje? Ningetembea kifua mbele. Siyo mtu unakuwa na mwanamke hata marafiki zako huwezi kuwaonesha alivyokuwa kituko”

    Yule abiria aliangua kicheko kikubwa sana mle ndani ya gari ile, kisha akamwambia dereva wake aliekuwa ameshaanza kuiondosha ile gari, akishika barabara ya Uhuru kuelekea Ilala.

    “Kaka wewe mchangamfu sana unapata kilevi nini? Huyo mkeo nyumbani naona hakuna kununa ni mwendo wa vicheko tu hadi raha eee?”

    Dereva Taxi aliendesha gari taratibu huku akimchombeza abiria wake.

    “Mie dada yangu Napata kilevi siku moja moja, siyo kila siku nikipata bia zangu nne au tano nakuwa hapo tena mzuka umeshapanda. Kwani nikinywa pombe huamia chini huniamsha hisia sana ndiyo maana sipendi kunywa mara kwa mara, vipi kwani mrembo unataka kunipa ofa nini? Niambie kama unataka kunipa ofa nipaki gari mie nimpe shanta atafute hesabu mie niburudike kwa ofa zako mrembo”

    Yule abiria alijiona ana bahati ya Mtende kuotea Jangwani. Kwani alikuwa anahitaji sana mtu wa kumaliza nae siku ile hata na zaidi, kwani kwa macho yake aliwaona askari wakiwa na Faridi wakati alipokuwa akiondoka pale Hotelini, alitambua kuwa baada ya kupanda juu chumbani nakumkosa, atapokwenda pale mapokezi akakabidhiwa funguo za chumba, basi Majanga atakayokutana nayo chumbani ndani ya kabati katika mkoba wake, lazima atatafutwa kwa Udi na uvumba. Hivyo isingekuwa busara kuondoka mikoani kwa siku ile kwani askari wanaweza kumkamata ikiwa watajipanga njiani na katika kituo cha mabasi ya kwenda mikoani kabla hajamaliza azma yake, kwani picha yake ameiona yeye mwenyewe katika luninga akitafutwa na Polisi. Hivyo kwa kumpata huyu dereva Mkwale akaona atapitisha usiku wake kwa amani kwani atakuwa anaongeza hesabu yake, lakini pia hatatiliwa mashaka sana katika nyumba za kulala wageni kwa kuwa atakuwa na mwanamme hivyo itaonekana kama mtu na mpenzi wake kuliko kuingia Lodge akiwa yupo peke yake.

    “Kumbe basi wewe kama mimi kwani hata mie pia nikinywa pombe yote hushuka chini, ila bahati mbaya niliyonayo mwanamke mimi, mume wangu anamatatizo ya presha hivyo hawezi kushughulika sawasawa, ndiyo maana huwa ninapata shida sana kunywa, kwani nikinywa pombe itanisumbua sana na mtu wa kunipunga sina ndiyo maana hupenda kuutumia muda mwingi sana kulala tu kwani sina mtu, wanaume wananiogopa sijui kwa nini?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Dada yangu siyo siri wewe ni mrembo sana unadhani nilikuwa nakutania. Ndiyo maana wanaume wanakuogopa kwani wanajua wewe ni matawi ya juu hivyo hata kujaribu kukuingia tu, hawathubutu, ila kina sie ambao tunajuwa baadhi ya wanawake wa watu wenye pesa au wa wakubwa, wengi hawapati burudani ya miili yao, kwani muda mrefu waume zao wanakuwa bize na semina mara mikutano mara safari, lakini cha kushangaza huko wanakuwa na wanawake wa nje, wake zao ndani wamewavundika tu!”

    “Kaka yangu umeuchoma moyo wangu kweli tena kwani hapa unavyoniona, natoka safari kama nilivyokwambia mume wangu nilikuwa nalala nae kwa ajili ya kumkanda tu, kwani muda mrefu yupo katika vikao weee, akirudi huko amechoka hoi, basi tangu nimekwenda hadi nimerudi, sijakutana na mume kimwili na mie nina moyo pia sina chuma natamani kupata raha katika mwili wangu”

    Dereva Taxi alijiona ni mtu alieamka na kismati, aliona zali la mentari limemuangukia kwani alimuingizia Yule abiria wake hadi mwisho wa safari yao, ikawafikisha Ilala Bungoni katika Guest iitwayo Mapoloni. Dereva alipewa pesa ya hesabu ya gari ya siku tatu, ili awe na bibie tu wanaburudika akapewa na pesa za kuacha nyumbani kwa siku tatu kwa mkewe, ili tu aweze kutulia na kutoa burudani ya kuridhisha kwa mrembo, asiwe na mawazo akashindwa kufanya kazi ipasavyo.

    Dereva Yule alimrushia mkewe pesa ya matumizi katika simu yake, akamdanganya amepata abiria atakaekuwa nae kwa muda wa siku tatu mfululizo, akidanganya kuwa ametoka nje ya mkoa wa Dar es saam.

    Mkewe kwa shingo upande alikubali uongo ule akijua mumewe anatafuta riziki kumbe alikuwa anatafuta matatizo makubwa sana.

    Baada ya kupitishwa uzushi wake dereva yule akaingia katika kula bata na mwanamke asiemjua, mwanamke aliekuwa akiongeza mtandao wa waathirika wa VVU, sasa akiwa ametimiza idadi ya watu tisa aliowaambukiza virusi vya Ukimwi akibakisha mtu mmoja katika hesabu yake ya watu kumi.

    Rebeka John makuka alikuwa na pesa ya wizi, hivyo alikuwa anaitumia kwa dhamiri maalum pesa ile, alikuwa akitimiza malengo aliyojiwekea ya kutimiza kuwapa virusi wanaume kumi. Katika wakati huu akiwa na mtu wa tisa pamoja na pesa nyingi katika pochi yake kubwa, aliamini angeweza kutimiza malengo yake, kisha angetafuta mawakili bingwa wa kumtetea katika kesi inayomkabili. Kwani siku zote Papa hujikaanga kwa mafuta yake mwenyewe!

    4

    Faridi alikiona kitu kile katika zulia kikimuangukia miguuni mwake, akaweka mkoba ule pembeni. Akatazama kitu kile kwa makini sana ndipo alipokiona kifuko cha plastiki na karatasi ndani yake yenye rangi ya Blue Bahari iliyokoza, alipokifungua kikaratasi kile, aliliona jina la Rebeka John Makuka, pamoja na namba yake ya usajili ya kituo kilichokuwa kinasomeka Tanga, tarehe, mwezi, na mwaka aliopima, ambao ulikuwa ni miezi miwili tu nyuma iliyopita. Pia kuliandikwa majibu ya kupima VVU na kusomeka POSITIVE CARRIER. Na katika kile kiplastiki kulikuwa na vidonge vipana vya ARV.

    Faridi alipata mshituko katika moyo wake, kichwa kikawa kizito, macho yake yakapoteza nuru ya kuona sawasawa, nguvu zikamwishia mwilini mwake, akatamka maneno kivivu;

    “Rebekaaa, kumbe Fau amesema kweli, umeathirika aaaah”

    Kutokana na mawazo ya pesa zake nyingi kuibiwa na mkewe ambae hakumtarajia kumfanyia kitendo kama kile, lakini pia kutambua kuwa Rebeka ni muathirika Carrier, moyo wake ulishindwa kuhimili maumivu yale ukapata athari kubwa sana. Akapiga mweleka chini kama mzigo, akawa hana fahamu, hayaelewi ya dunia yanavyokwenda.

    Yule askari aliekuwa nae pale, alishuhudia kila kitu kwa ufasaha. Alipomuona Faridi anaanguka chini, akajaribu kumdaka lakini alichelewa kwani Faridi alianguka vibaya, aliangukia kichogo akapigiza kichwa chake chini kwa nguvu akatulia kama ubao macho yake yakiwa yanatazama lakini hayaoni kitu chochote.

    Yule askari alitoa simu yake ya mkononi, akawapigia wenzake waliokuwa chini wamebarizi kuwasubiri, waliipokea simu yake wakapokea taarifa ile na mara moja wakapanda juu ya Hotel ile, katika chumba walichoelekezwa kuwa tukio limetokea, walipofika juu wakaingia katika chumba kile kwani mlango wake ulikuwa haukufungwa na funguo, mkuu wa msafara ule akataka kujua kilichojiri, akapewa taarifa na askari aliekuwa na Faridi, na askari yule akatikisa kichwa chake juu chini kukubali taarifa ile lakini pia akithibitisha kwa macho yake vidonde vya ARV pale chini pamoja na cheti cha Rebeka, vikiwa mita chache kutoka ulipokuwa umelala mwili wa Faridi.

    Wakiwa katika kujishauri cha kufanya mara mlango wa chumba kile ulifunguliwa, akaingia meneja wa hoteli ile pamoja na walinzi watatu wenye silaha. Kwa kuwa askari wale walikuwa hawana sare isingekuwa rahisi kuwatambua. Kwani askari wawili wenye silaha walikuwa nje katika gari wakisubiri, pamoja na dereva.

    Askari mkuu wa msafara ule alijitambulisha kwa kitambulisho, na kujieleza kwa nini walikuwa pale wakati ule. Meneja wa hoteli akawaamuru walinzi wa kampuni binafsi aliokuwa nao pale washushe silaha zao chini, baada ya kutambulishwa kuwa wale ni askari Polisi.

    “Kamanda mmekosea lakini, hii ni hoteli kwa ajili ya biashara ina uongozi wake. Kama mlimfata mtu mkamuhitaji ilipaswa mtoe taarifa kwa uongozi ili kupata ushirikiano, kwani walinzi wetu kupitia cctv camera, wameweza kuwaona nyie mkiingia katika chumba hiki kwa mwendo wa haraka, ndiyo maana mkatiliwa mashaka labda ni waalifu. Hivyo tafadhalini wakati mwengine kama linatokea jambo kama hili, tafadhali fateni taratibu.”

    Yule Meneja aliwaeleza wale askari ambao walivunja sheria, na wale askari wakatahayari kwa maneno yale, wakamtaka radhi meneja, mambo yakatengenezwa, yakawa funika kombe mwanaharamu apite.

    Mwili wa Faridi ulitolewa mle ndani ya chumba kile chini ya usimamizi wa meneja wa hoteli, askari waliubeba mwili wake pia walichukuwa na vielelezo vilivyomfanya aanguke na kupoteza fahamu, wakamuwahisha katika Hospitali ya taifa ya muhimbili kwa matibabu zaidi.

    Pale Muhimbili alipokelewa akawekwa katika wadi namba moja ya wagonjwa mahututi, Mwaisela akalazwa katika kitanda namba nane, kitanda ambacho aliwahi kukilalia mtalaka wake Faudhia. Kitanda ambacho hakitamtoka Faudhia katika historia ya maisha yake kwani hata alipopewa talaka katika simu alikuwa amekilalia kitanda kile, ambacho leo hii Faridi amefikishiwa katika kitanda kile kile, nae akionja uchungu wa maumivu aliyoyapitia mwenzake.

    *******CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Faudhia alifanikiwa kumpata dakitari mmoja akaenda nae hadi pale alipokuwa amemuacha Rama juu ya kiti, lakini hakutambua kuwa pale alipomuegesha hakuwa na uwezo wa kukaa yeye mwenyewe bila kushikiliwa na mtu, hivyo walipofika pale walimkuta Rama ameanguka chini, sakafuni jasho jingi likiwa linamtoka, Inzi wengi walikuwa wamemjalia wakimdandia huku na kule, lakini hakuwa na uwezo wa kuwaondosha, kwani alikuwa hajijuwi, hajitambui amepoteza fahamu zake.

    Dokta haraka akampima mapigo yake ya moyo, pamoja na mapafu kuangalia upumuaji wa mgonjwa akiwa pale pale sakafuni alipoanguka kwa chali. Kisha akatoa vile vifaa vyake, akamwambia Faudhia kwa upole.

    “Hali ya mgonjwa wako siyo nzuri, nakushauri apelekwe katika hospitali ya rufaa Muhimbili kwani pale ataweza kumudu gharama, hapa kwa maradhi haya utatumia pesa nyingi sana, kwa kuwa hospitali hii siyo ya Serikali, hivyo lipia gari ya kubebea wagonjwa pale dirishani ili awahishwe hospitali, kwani moyo wake unapiga pigo moja baada ya sekunde ishirini, hiyo siyo hali nzuri kwa mgonjwa unaweza kumpoteza.”

    Faudhia hakutaka kumpoteza Rama, alikuwa yupo tayari kwa gharama zozote zile ayaokoe maisha ya Rama, hivyo hakufanya ajizi alikimbilia katika dirisha la kulipia akaeleza haja yake akatajiwa pesa zilizohitajika akalipia, ndani ya dakika ishirini tangu kulipia huduma ile, daktari mmoja pamoja na wauguzi wawili akiwemo na Faudhia walikuwa ndani ya gari ya wagonjwa iliyokuwa imewasha taa kubwa za gari ile, ikiliza king’ora kwa sauti ya juu, ikawa inatanua barabara kuwahi Hospitali ya taifa ya Muhimbili.

    Rama ndani ya gari ile alikuwa bado yupo kwenye koma, hana habari na juhudi anazozifanya Faudhia juu yake. Alikuwa yupo katika dunia nyingine kabisa.

    Drip ilikuwa imewekwa ikitembea kwa kasi ili kuokoa maisha yake kwa kuitafuta fahamu yake, iliyokuwa imemtupa mkono kwa muda. Hakika naweza kusema Rama alikuwa katika Sakalatilmauti

    Dereva wa gari ile ya wagongjwa aina ya Toyota Hiace alikuwa akijitahidi sana, kuendesha gari ile ya kubebea wagonjwa, na hatimae wakafika hospitali ya Rufaa Muhimbili. Taratibu za kukabidhiana mgonjwa zikafanywa, Rama akakimbizwa katika wodi namba moja ya wagonjwa mahututi Mwaisela, akapewa kitanda namba saba.

    Wakiwa katika pilikapilika za kumlaza mgonjwa pale kitandani ndipo Faudhia katika kitanda cha pili toka pale alipolazwa Rama akamuona Faridi akiwa amelazwa. Drip mbili kwa pamoja zikiingia katika mwili wake, Faudhia akafanya kitu!



    Faudhia aliwatazama wale wahudumu walivyokuwa wamezama katika kumshughulikia Rama, alisogea hadi pale kwa Faridi akanyoosha mkono wake akaisimamisha ile Drip kuingia katika mwili ule, kisha akageuka akatoka nje kuungana na watu wengine waliokuwa nje ya hospitali ile, katika jengo la Mwaisela.

    Madaktari walijitahidi kuyaokoa maisha ya Rama kadiri walivyoweza, kwa kumpa matibabu na huduma zote alizostahili, hata daktari aliekuwa zamu alipompima mapigo ya moyo akamuona anapumua katika hali ya kawaida, ingawa bado alikuwa hajaamka. Kitendo kile kiliwapa imani madaktari wale, na hakika hali ya Rama ilibadilika kadiri muda ulivyokuwa unasogea mbele ikawa inatengemaa taratibu.

    Daktari alipomaliza kumuhudumia Rama alifika kitanda cha pili kwa Faridi ili kukagua maendeleo yake, akaiona Drip ikiwa imesimama haitembei kwa haraka haraka alidhani mgonjwa wake amefariki Dunia, kwani mtu anapofariki Drip huzuiliwa na mwili wa mwanaadamu kuingia ndani ya mwili.

    Ila alipompima aliusikia moyo wa mgonjwa ukifanya kazi japo ilikuwa mapigo yake yanakwenda polepole sana, alipoitazama kwa makini katika INFUSION GIVING SET ya Drip ile akagundua kuwa imezuiliwa kutembea Drip ile. Dakitari akawaita manesi akawauliza kwa nini wameisimamisha drip ile kuingia kwa mgonjwa, kila mmoja katika manesi wale watatu waliokuwa zamu walikuwa hawajui nani aliesimamisha Drip ile, wala wao wasingethubutu kufanya yale kutokana na uelewa wao katika tiba.

    Dokta akairuhusu ile Drip kuingia kwa kasi ile ile ya awali na baada ya saa moja hivi, Faridi aliweza kupata nafuu ya kufumbua macho yake, lakini hakuwa na nguvu ya kutamka kitu chochote kwani alisikia maumivu makali katika kichwa chake, kutokana na ule muanguko alioufikia pale katika zulia la hotel, lau kama kichwa chake kingeangukia katika sakafu pengine tungeweza kusema mengine. Ila Mungu bariki ameangukia katika zulia hivyo kumepelekea kupoza ugumu wa sakafu pale chini.

    Faudhia akiwa nje amekaa na watu wengine huku akiombea akiingia ndani akute pazia za kijani zimezungushiwa katika kitanda cha Faridi, mara aliwaona askari wawili wakiwa wanatoka nje ya wadi ile mmoja wapo akimaliza kuzungumza na simu. Akawakumbuka kuwa alikuwa nao wakati wanakwenda kwa Faridi kufata funguo za gari yake, akawafata na kuwauliza kilichojiri hadi Yule bwana Faridi kuwa yupo pale akiwa hajitambui. Yule askari aliekuwa amemaliza kuzungumza na simu, alimuhadithia kilichompata mtalaka wake hadi wao kumpeleka pale.

    Faudhia hakufurahi, hakuudhika, ila alibaki kimya akitafakari kwa makini kisha kama mtu aliekurupuka hivi akasema.

    “Ina maana Rebeka amemuibia pesa zote hizo huyu bwana kisha amemkimbia na amemuachia ARV pamoja na cheti alichopima virusi ndiyo Faridi amepoteza fahamu. Sie tulipokuwa tukimueleza alituona tuna wivu. Ama kweli ujinga donga la kichwa, mkaguzi mkono! Je? Hamuoni huyo Rebeka baada ya kuwa na pesa ataendelea kuwaambukiza watu wengine zaidi kwa pesa zake? Kwani wakati hana pesa kafanikiwa kumbukiza watu wanane, je hivi ana pesa si itakuwa hatari zaidi?!”

    “Ni kweli maneno yako usemayo, ila tumejipanga na hivi nikwambivyo dereva Taxi aliemkodi Rebeka kutoka pale hotel, tupo nae tunamuhoji ili atuambie alipomfikisha Rebeka pamoja na nguo alizovaa, tumeshatangaza katika vyombo vyetu, hivi anatafutwa muda wowote atakuwa mikononi mwetu.”

    Faudhia alimsikiliza Yule askari aliekuwa nae pale, akashangaa taarifa ile sana akamuuliza ili kuondosha wasiwasi wake.

    “Sasa mlijuwaje kama yeye ndiye aliemkodi Rebeka wakati hamkumuona wakati anampakia?!”

    Yule askari alicheka kisha akasema.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hiyo ndiyo kazi yetu askari, kuchunguza na kukamata, na kufikisha katika vyombo vya sheria. Pale hoteli wanautaratibu ambao tuliufata ukatupa majibu. Kila gari inayopakia abiria au kuegeshwa katika maegesho ya hoteli ile, huwa inaandikwa katika kitabu cha walinzi kwa kumbukumbu. Hivyo tulipofika kwa ajili ya hilo, tukapata faida hiyo tukajua namba ya gari iliyombeba Rebeka, kwani pale hadi tunafika kwa ajili ya jambo hili, haikukuwapo taxi nyingine iliyokuwa imebeba abiria pale zaidi ya ile, hivyo tulitangaza katika redio za upepo kukamatwa kwa gari namba ile, na mara moja ikatiwa mkononi. Uzuri dereva wake hakukana kupakia abiria pale hotelini, ila alisema kwamba yeye amemuacha pale mtaa wa Nyamwezi na Barabara ya Uhuru. Akamshusha kisha akageuza hakuweza kumtilia mashaka. Ila bado kwa hatua tuliyopiga muda wowote kutoka sasa Rebeka atakuwa mikononi mwetu amin hivyo.”

    Faudhia alitikisa kichwa akashukuru sana kwa hatua walizopiga askari wale.

    Yule askari akaagana na Faudhia kuelekea katika majukumu yake mengine ya kikazi.

    Katika kituo cha Polisi Ostabey, dereva wa taxi aliembeba Rebeka alikuwa ameeleza aina ya nguo, pamoja na rangi zake alizokuwa amevaa Rebeka, pia kituo alichomshusha akiambiwa kuwa amefika, na yeye akageuza na kuondoka zake. Askari wale walikwenda na dereva Yule hadi katika kituo cha Polisi Magomeni, wakaingia kwa mkuu wa kituo wakampa taarifa yote ya tukio zima la Rebeka kutoweka pale Hospitali bila ruhusa ya Dakitari, uhalifu alioufanya na mwenye mali Faridi madhara aliyoyapata, na mahali alipo.

    Yule mkuu wa kituo alifikiri kwa kina, kisha akawaambia askari wale mawazo yake yanavyomtuma ili kufanikisha kumtia mikononi Rebeka.

    “Fikra zangu zinanituma kwamba, Rebeka ametambua kwamba kwenda na gari ya huyo kijana hadi mwisho wa safari yake ni jambo la hatari kwake, na akizingatia kwamba gari ile ameipandia pale pale hoteli, hivyo inaweza kumpa madhara kama tukiifatilia. Ndiyo maana ameamua kushukia njiani, na sina shaka anaweza kubadilisha gari hivyo nawashauri chukueni picha ya Rebeka nitakayowapa, kisha huyu dereva wa taxi kuanzia pale mtaa wa nyamwezi alipomshushia, awaoneshe madereva wa taxi wa pale labda inawezekana akachukulia gari nyingine pale na kuendelea na safari yake. Ikiwa pale hamkupata mtu aliempandisha basi ulizeni vituo vya jirani na mtaa ule, tunaweza kufanikiwa kumtia mikononi mwetu.”

    Askari wale waliichukua picha ya Rebeka kwa mkuu wa kituo, wakamuonesha dereva taxi kama mtu aliempakia ndiyo huyo anaeonekana katika picha ile? Dereva Yule baada ya kuitazama tu picha ile akakubali kuwa ndiye abiria aliempakia kutoka pale Hoteli.

    Askari wale walipanga mikakati yao kwa kina, hesabu zao zikawaruhusu wakaingia kazini. Dereva taxi alipewa simu aina ya Blackbery mpya kabisa pamoja na picha ya Rebeka, akapewa maelekezo kuwa ndani ya gari yake atakuwa yupo peke yake, watakwenda hadi pale Mtaa wa Nyamwezi alipomshusha, kisha atawauliza wale madereva wa taxi mmoja baada ya mmoja kuwa kuna abiria alimuacha pale, akampa risiti ya gari ya gari yake yenye namba ya gari, ila abiria wake amesahau bahasha yake katika gari, ambapo bahasha ile ilikuwa na picha ambayo atawaonesha pamoja na simu yake, hivyo kama kuna dereva aliempakia amuelekeze alipomshushia ili aende akamkabidhi vitu vyake, wakati huo wote dereva Taxi atakuwa peke yake ndani ya gari yake, na askari watakuwa katika gari yao yenye namba za kiraia, wakiwa wanafatilia kwa karibu jambo lile. Dereva alielewa mbinu ile mara moja wakaingia barabarani kuelekea mtaa wa Uhuru na nyamwezi.

    Walipofika pale mtaa wa Nyamwezi na Uhuru, dereva taxi kama alivyoelekezwa na askari wale akafanya kuwauliza madereva wa taxi wa mtaa ule kama wamemuona au kumpakia abiria aliyopo katika picha ile, huku akieleza kuwa amesahau simu yake mpya ndani ya gari yake. Madereva wale kila mmoja alipoitazama picha ile, hawakuweza kuielewa, wakamwambia hawajamuona labda aende kituo cha jirani pale mtaa wa Congo na Uhuru, au Kipata na Congo akaulizie huko. Yule dereva aliingia ndani ya gari yake akaelekea mtaa wa Kipata na Uhuru, kwenye makutano ya mitaa ile, dereva taxi alishuka akatoa picha ya Rebeka akaulizia mara moja akapata jibu.

    “Huyo dada bomba kweli mwanangu amempandisha Luka misifa hapa ameondoka nae hadi sasa hajarudi, naona kala kichwa cha mzunguko akija hapa keshafunga hesabu na pesa ya kula ishapatikana.”

    Wale askari waliokuwa makini kabisa na tukio lile wakiwa mita chache ndani ya gari yao, mmoja wao akashuka hadi pale akajichanganya kwa wale madereva waTaxi waliokuwa mawemzunguka dereva mwenzao, wakiitazama ile picha.

    Wapo madereva wengine waliokuwa wanaibusu picha ile huku wakiigiza kufanya mapenzi na picha ile, wapo pia madereva taxi waliomshauri yule dereva taxi aichukue ile simu aiuze au kuitumia eti wakidai kuwa Riziki ya mtu ipo mikononi mwa mtu. Ilimradi kila mmoja alikuwa anasema lake alilojisikia, ama kweli usilolijua litakusumbua, laiti kama wangelijua pale kati yao kuna askari wala wasingelisema yale, ila ndiyo hivyo dunia uwanja wa fujo, kila mmoja hufanya lake.

    “Sikiliza kijana, waambie madereva wa Taxi wenzako wakusaidie wakupe namba za simu za huyo dereva aliempakia huyo dada aliesahau bahasha yake yenye simu, ili umpigie akuelekeze alipo na huyo abiria wake. Ikiwa kama ameshamshusha kala kichwa kingine, akwambie alipomshushia ili uende umfate kwani ukisema hapa umsubiri utakaa hadi saa ngapi, na hiyo gari inataka hesabu?”

    Yule askari aliekuwa katikati ya madereva wa taxi, alikuwa akimueleza Yule dereva wa Taxi akijifanya yeye kama msamalia mwema tu, ila ndiyo alikuwa akimpa maagizo afanye hivyo, mara madereva wale walipoambiwa na dereva mwenzao aliekuwa ameiegesha gari yake mbele yao kuhusu kuomba namba ya simu ya Luka, walitoa simu zao wakampa yule dereva taxi, kisha Yule dereva taxi akawashukuru, akaondoka akidai anakwenda kutia salio ili ampigie kumfahamisha suala lile.

    Wakaagana na Yule dereva mwenzao, nae akaondoka pale akishika njia ya kushoto kuufata ule Mtaa wa Congo, alipofika makutano ya mtaa wa Congo na Lindi, akapinda kulia kushika mtaa wa Lindi, akatembea hadi katika makutano ya mtaa wa Lindi na Msimbazi akaendelea mbele hadi pale SUWATA, akaegesha gari yake pembeni, na gari aina ya Toyota Mack 11 Balon ikaegesha nyuma yake, kisha askari yule aliekuwa amejichanganya na wale madereva wa taxi akashuka na kumfata Yule dereva wa taxi, huku wakijipongeza kwa hatua waliyoipiga.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Yule dereva taxi alimpa ile namba yule askari, Yule askari aliichuua namba ile akaiingiza katika simu yake, akarudi katika gari yao ya Balon wakajishauri kwa pamoja, wakabawabu kwa muda hatimae wakapata wazo.

    Askari mmoja aliitazama ile namba ya yule dereva ya voda katika Mpesa, akapata jina lake kamili alilojisajili Yule dereva taxi misifa, ambalo ni Lukas Ladebe. Kitendo bila kuchelewa askari yule akampigia simu bwana misifa, na simu yake ikawa inaita.

    “Halow nani mwenzangu?”

    Yule dereva taxi alipokea simu ile kwa sauti ambayo dhahiri ilionesha aidha alikuwa ametoka usingizini, au ametoka kufanya tendo la ndoa, kwani ilikuwa ni sauti ya kivivu isiyochangamka, na ndani yake ilisikika kama ina kilevi hivi.

    “Mie bwana abiria wako wa siku ilee, nataka gari yako nina harusi ya mshikaji wangu bwana, sasa gari yako nilitaka kwa ajili ya kumbebea bwana harusi, upo wapi ndugu yangu?”

    “Duh ebwana eee mie nipo na shemeji yako wangu, yaani ninatawishwa hapa hata hii simu nimepokea basi tu, kwani shemeji yako ana wivu hatari hataki hata niongee na simu. Lini hiyo shughuli kwani mie siku tatu sipo kazini napumzika kidogo na shemeji yako namliwaza liwaza.”

    Wale askari walitazamana kwa haraka kwa majibu ya dereva luka, wakatikisa kichwa kwa masikitiko kumuhurumia kwani walihisi lazima atakuwa yupo na Rebeka tu, kwa kuwa ndiye anaewaambukiza wanaume virusi vya VVU.

    “Ok basi kama unapumzika naomba unielekeze ulipo tu ili nikuletee pesa yako kabisa kwani shughuli yenyewe ni siku nne kutoka leo, kwa hiyo utakuwa umeshapumzika vya kutosha.”

    ‘Ahaa kama ni siku nne kutoka leo basi hiyo itawezekana, huwezi kunitumia huo mpunga kwenye M pesa? Kwani mie siwezi kutoka ninatawa kama nilivyokwambia na shemeji yako wa ukweli hapa.”

    “Hahahahaha hongera bwana mie nakuamini mzee kwa mambo hayo unatisha sana wewe, sema nini sina pesa kwenye simu yangu pesa ninazo mkononi lakini pia inabidi tuzungumze kama shughuli itakuwa wapi, gari itapambwa wapi na vitu kama hivyo kwa hiyo sidhani kama itakuwa busara kuongoea ndani ya simu pekee, muombe shem wangu wa ukweli akuwachie japo kwa dakika mbili tu tuongee biashara, kisha utakwenda kuendelea kutawa, wani umenambia upo nae kwa siku tatu sasa mchecheto wa nini bwana Luka mzee wa totoz?”

    Kama kuna kitu kilimfurahisha sana mzee wa misifa basi ilikuwa ni kusifiwa. Alikubali kumuelekeza yule mtu aliekuwa akiongea nae ndani ya simu mahali alipo bila kumtambua kama alikuwa akiongea na mtu wa aina gani.

    “Poa mwana njoo Mapoloni Lodge chumba namba mbili hapa Ilala Bungoni, nipo Napata mambo yangu wewe si unanijuwa mie tena, nina shemeji yako hapa anakusikia ni Bomba ile mbaya, mambo ya Masaki kwa mashefa mwana, mambo ya mboga saba, siyo videm vyenu vya uswahilini, videmu vya mizinga kila siku vinaomba vocha halafu wewe uliovipa hiyo vocha vinakubeep havikupigii, hahahahaha njoo mwana ukifika nigongee tu chumba namba mbili.”

    Askari Yule alimaliza mazungumzo na bwana misifa, akakata simu kisha akawageukia wenzake wakampa tano, safari ya Ilala Bungoni katika Lodge ya Mapoloni ikawiva.

    Askari mmoja alishuka ndani ya gari ile akaenda kupanda gari ya mbele taxi ya Yule dereva aliewafikisha pale, akaingia kisha msafara wa kuelekea Ilala bungoni ukaendelea huku wakijipongea kuwa hawana muda mrefu watamtia mikononi Rebeka. Yule askari aliekuwa ndani ya taxi alitoa simu yake, akawapigia simu wenzake waliokuwa muhimbili waliompeleka Faridi kwa hatua walizozichukuwa na muda wowote wataweza kumtia mikononi Rebeka.

    Gari zile kwa kutumia Barabara ile ya mtaa wa Lindi, walitembea hadi Ilala Bungoni, wakaiacha ile barabara ya lami, wakaingia katika njia ya vumbi, hatimae wakafika katika Lodge ya Mapoloni, askari waliokuwa ndani ya Toyota Mack 11 Balon wawili waliteremka wakiwa na bastola viunoni mwao, wakaingia mle Lodge wakamwambia Yule muhudumu wa Lodge ile aliekuwa anataka kufahamu kama wanataka vyumba ama laa, walimueleza kuwa wana jamaa yao aliyopo chumba namba mbili wamekwenda kumtembelea kumpa pesa yake. Yule muhudumu akawaruhu kupita wakaenda hadi chumba namba mbili wakagonga mlango wa chumba kile, na mzee wa misifa akafungua mlango wa chumba kile, wale askari wakajichoma ndani ya chumba kile kwa haraka.



    Askari wale walimkuta mtarajiwa wao akiwa amejiachia juu ya kitanda amejistiri kwa shuka tu huku chini, lakini vitu vingine vyote vilikuwa wazi vikipata upepo.

    Rebeka alistuka sana, baada ya kuona ananyooshewa mtutu wa Bastola, na kuwekwa chini ya ulinzi.

    Kama kuna kitu kinachomtia hofu zaidi Rebeka ilikuwa ni kuoneshewa mtutu wa bunduki, tena haijalishi iwe bunduki kubwa au ndogo. Kwani anakijua kifaa kile kama hakina mzaha kabisa.

    “Rebeka John Makuka, umekimbia ila leo ndiyo khatma yako imefika upo chini ya ulinzi kwa makosa makubwa mawili. Kwanza kuambukiza watu virusi vya Ukimwi makusudi ukijuwa kabisa wewe ni muathirika, lakini pili ni kosa la wizi wa kuaminiwa kwa mumeo Faridi Kacheche. Hivyo hapa tunakwenda kituoni magomeni vaa nguo zako vizuri ili tuondoke.”

    “Oyaa sema nini mnaniharibia washikaji huyo haitwi Rebeka, nyie mmekosea mtu mnaemtafuta huyu ni mke wangu anaitwa Qeen, labda nendeni chumba cha pili hapo.”

    Dereva Taxi Luka misifa alikuwa anamtetea mtu asiemjua akijinasibu kuwa ni mkewe wa ndoa. Wale askari walimtazama kwa dharau kisha wakamjibu na kumkomesha kabisa asirudie maneno yake yakipumbavu, yasiyokuwa na kichwa wala miguu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Wewe nyamaza marehemu mtarajiwa! Unaambukizwa virusi na Malaya huyu unasema ni mkeo, mjinga sana wewe yaani sie tumeacha nyumba ngapi hadi kuja hapa Mapoloni, hatufanyi kazi kwa kubahatisha, tunafanya kazi zetu kwa uhakika. Huyu mwanamke ameshawaambukiza virusi watu tisa ukiwamo wewe kama utakuwa umeshaingia katika kufanya mapenzi nae kwa ujinga wako. Kwani hivi na Taulo hilo najua ushayakanyaga tayari mawaya, sasa subiri yakulipukie ufe bwege mkubwa kabisa wewe na misifa yako ya kijinga hiyo!”

    Lukas Ladebe au mzee wa misifa, aliposikia maneno yale, bado akaoneshwa na picha ya Rebeka waliokuwa nayo mkononi mwao, akaishiwa pozi kabisa akakaa kitako akawa mdogo kama nukta.

    Rebeka pale alipokuwa amekaa, alikuwa ameubebedua mdomo wake amefura kwa hasira, na woga tele ukiwa umemjaa pia akasema kuwaambia wale askari.

    “Naomba tuyamalize jamani niwape pesa ili mniachie ili nitimize azma yangu, kwani ningefanikisha azma yangu nisingekuwa na shida tena wala nisingeendelea kufanya tena jambo hili nambieni mnataka kiasi gani ili tumalizane?”

    Wale askari wakatabasamu kwa kebehi kisha askari nmmoja akatoa kauli ya kuudhi kumjibu Rebeka.

    “Rebeka unaongeza kosa tu hapa, kutoa rushwa nalo ni kosa, lakini pia hizo pesa umemuibia mumeo Faridi, kwa hiyo kutugawia sie wakati tunafahamu ni pesa za wizi tutakuwa nasi tumeshiriki jambo hilo, kwa hivyo hatuwezi kufanya tendo hilo kwa kuwa lipo kinyume na kiapo chetu.”

    Rebeka aliinuka akiiachia ile shuka ikianguka kitandani, akatembea kuliendea kabati kwenda kuchukua nguo zake ili avae, lakini alipofika usawa wa kati ya chumba kile kabla hajalifikia lile kabati, akasimama kisha akageuka kuwatazama wale askari waliokuwa wanamfatisha kwa macho yao akiwa yupo mtupu kama alivyozaliwa.

    Rebeka akatanua miguu yake kama mtu aliekuwa anaonesha maonesho ya mavazi,ila yeye alionesha mwili wake akawatazama wale askari akawaambia.

    “Hamjui kilichonisibu katika mwili wangu huu, ndiyo maana nyie na jamii yote inanilaani sana lakini watu wanaangalia ubaya wa mwisho hawatazami ubaya wa mwanzo! Kifupi Ubaya wa mwanzo hauvumi ila Ubaya wa mwisho ndiyo unaovuma, haya niambieni mwanamme gani aliefungua kesi kwenu kwamba mimi Rebeka mtoto wa Makuka kuwa nimembaka kwa nguvu, kwa kumtolea silaha ili afanye mapenzi na mimi?! Yupo hata mmoja nikasimame nae Mahakamani, ambae ataweza kuongea mbele ya mahakama kuwa nimembaka kwa nguvu?! Hivi mtu anapokuwa ni muathirika anakatazwa kutongozwa?! Nyie askari mnaosema mnafanya kazi kwa mujibu wa viapo je mmeruhusiwa kumkamata mwanamke chumbani akiwa uchi kama nilivyo mimi, mlishindwa nini kuja na askari wa kike, hamuoni kuwa mnanidhalilisha kijinsia?! Haya sasa mie nakwenda huko mtakapo kisha huko ndiko kutakapojulikana mbichi na mbivu kwa nini mimi nafanya haya! Siyo mnawalaumu watu wanapokuwa mitaani tu wakiomba au kuuza miili yao, ulizeni sababu zao kwa nini wamekuwa wapo mitaani wanafanya hayo!”

    Rebeka baada ya kusema maneno yale aligeuaka nyuma akaliendea kabati akavaa nguo zake akawaambia wale askari kwa maringo.

    “Haya nyie mliokataa pesa hapa, nipelekeni huko mtakako nikawape pesa wakubwa zenu kwani nyie inaonekana shetani wenu hapendi pesa!”

    Wale askari wakati Rebeka alipokuwa akiwatazama huku akiwa ametanuwa miguu yake, hata pale alipogeuka kulielekea kabati kwenda kuvaa, nguo za askari wale katika sehemu zao za kati zilikuwa zikiwapa shida sana kwa muda.

    Lakini walifanikiwa kuituliza hali ya tamaa ya kimwili, wakarejea katika amani ya nafsi yao, hakika Rebeka alikuwa kama mfano wa mchicha uliomea chooni, mchicha unavutia kuula kwa namna ya uzuri wake lakini kwa kuwa umemea chooni, unashindwa kuula kwa mtu uujuwae. Yaani Rebeka kila mwanaume rijali angetaka kufanya nae mapenzi ila kwa Yule amjuae kuwa ni muathirika angeishia kula kwa macho tu, asingethubutu kulishika Transfoma lenye umeme ilihali akijua kwamba litamlipukia.

    Rebeka baada ya kuvaa, alichukuliwa yeye pamoja na bwana misifa hadi kituo cha Polisi Magomeni, ili kwenda kuandika maelezo yake, na hatua zaidi za kisheria ziweze kuchukulia dhidi yake.

    Mkuu wa kituo cha Polisi Magomeni, baada ya kufikishiwa Rebeka kituoni kwake, na askari wale wakamcharazia maneno aliyopsema rebeka kuwa atawapa pesa wakubwa zao, hivyo walikuwa wanamjengea mazingira magumu ili asiweze kupata hata dhamana.

    Mkuu wa kituo alimtazama Rebeka aliekuwa amekaa kitako chini, akiwa na mzee wa misifaaliekuwa amekaa pembeni yake akamuuliza Rebeka kwa utulivu.

    “Wewe mtoto kwa nini unafanya maambukizi makusudi kwa watu?! Wakati wewe unatambua kwamba umeathirika?!”

    Rebeka alimtazama mkuu wa kituo kile, kisha akamwambia kwa kauli ya upole na utulivu.

    “Huyu naomba atolewe hapa ili nikueleze kwa kina kwa nini ninafanya yote haya, kwani ni habari ndefu sana mzazi wangu.”

    Mkuu wa kituo umri wake, ulimfanya Rebeka awe na kila sababu ya kumwita mzazi wake.

    Rebeka alisema maneno yale huku akiviliwa na machozi machoni mwake, mkuu wa kituo aliinua simu yake iliyokuwa mezani akaipiga simu ya Sajenti Mbago Kizega, ilipopokelewa simu yake upande wapili akamwita aende ofisini kwake .

    Sajenti Mbago Kizega aliingia pale kituoni na kupiga saluti kwa mkuu wake, akapokea maagizo kutoka kwa mkuu wake, akamchukua Bwana misifa akatoka nae nje. Mkuu wa kituo alitoa Tape Recoder kutoka katika mtoto wa meza, akaiweka juu ya meza akabonyeza kitufe cha kukifanya chombo kile kinase sauti, kifaa kile kikawa kipo tayari kufanya kazi yake. Naam Rebeka Binti John Makuka, akaanza kueleza kwa hisia ya hali ya juu sana, kwa nini yeye anafanya hayo aliyokuwa akiyafanya, hakika maelezo yake yalimfanya mkuu wa kituo kuacha mdomo wazi akaviliwa na machozi. Ukimuona mtu mzima analia ujue kuna jambo ni kweli.

    *******CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Katika hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Muhimbili, ilikuwa wakibadilishana zamu watendaji wake kutoka madaktari walioingia asubuhi na waliokuwa wakiingia mchana. Dokta Neema Mnyampala alikuwa akichukuwa zamu yake ya kuingia mchana, wakati ameshasaini katika kitabu akiingia wodini pale Mwaisela, katika mlango akakutana na Faudhia ana kwa ana, akamsalimia na kumuuliza kulikoni na Faudhia akamwambia kwa ufupi kuwa mtu aliepelekea wao kulazwa katika hospitali ile siku moja nyuma, na yeye ameletwa yupo amelazwa tena akiwa katika kitanda kilekile, alichokuwa amelazwa yeye siku ya jana.

    Dokta Neema Mnyampala alimshika mkono Faudhia akaingia nae wodini, akaenda nae hadi katika kitanda cha Faridi katika kitanda namba nane, wakamuona Faridi amefumbua macho yake akili zake zikiwa zimerudi.

    Faridi alipomuona Faudhia akamwambia taratibu kwa unyenyekevu.

    “Faudhia mke wangu nilikukosea sana hadi nikakuwacha, hivyo naomba unisamehe ili tuishi tena kama zamani, kwani nimejifunza tayari nimeona ndani ya nafsi yangu kuwa nimekukosea naomba urudishe nyuma msimamo wako unisamehe wangu, nimekoma Faudhia sitokutenda tena,”

    Maneno yale badala yakumpa faraja faudhia badala yake yalimpa huzuni kubwa sana yakamtoa machozi, akaweka mikono yake usoni mwake akaanza kulia kwa uchungu, huku akitikisa kichwa chake kulia na kushoto akiashiria kutokukubaliana na jambo lile kwa wakati ule.

    “Faridi umeniumiza sana, umeharibu furaha yangu ya maisha umenitesa sana, nimekuwa na kinyongo na wewe fil Dunia wal akhera. Kosa langu lilikuwa lipi kwako au ni kule kukutunzia ndoa yako, au ule ujinga wangu ambao nilikuwa nawakataa wanaume waliokuwa wananitongoza kwa kukuheshimu wewe? Leo wakati unanitaka msamaha kuna vitu viwili ambavyo huwezi kuvizuwia kwani havizuiliki tena. Kwanza naamini tayari hapo ulipo umeshaambukizwa VVU na Rebeka, lakini pili umeniacha Talaka tatu ukimuhusisha mwenyezi Mungu katika ushahidi wa ujinga wako, nani kakwambia mke alieachwa Talaka tatu, anarejewa na mumewe aliemuacha? Faridi nimekaa na wewe kwa muda wa miaka mitatu hujawahi kunipa hata talaka moja, imekuwaje ukanipa Talaka zote tatu kwa pamoja?Ulipatwa na nini, Uliniona sikufai tena ndiyo maana ukaamua kukata kabisa uwezekano wa kunirejea si ndiyo? Sasa leo unataka kunirejea kwa misingi ya dini ipi?!”

    Rebeka aliposema maneno hayo alisogea pembeni katika kitanda cha mgonjwa aliekuwa amelala hana fahamu akaanza kulia kwa uchungu mkubwa. Machozi yake bila kutarajia yakadondoka na kumdondokea usoni mgonjwa aliekuwa amelala hana habari pembeni ya kitanda cha faridi. Mgonjwa Yule kwa machozi yale yaliokuwa yakimdondokea usoni mwake, akaweza kufumbua macho yake kwa machozi yale.

    Baada ya kufumbua macho yake mgonjwa yule, uso wake ukamuona mtu aliekuwa amefunika mikono yake usoni akiwa analia, mgonjwa yule alimtazama kwa kukaza macho yake mtu anaelia hatimae akafanikiwa kutamka;

    “Faudhia nini kinakuliza, kwa nini unalia mie nipo salama usilie, futa machozi yako!”

    Faudhia aliondosha mikono yake usoni mwake, akamtazama Rama pale alipokuwa amelala kitandani, akamuinamia akamkumbatia huku akiwa analia kwa kwikwi kwa furaha ya kuamka kwa Rama, lakini pia kwa uchungu wa maneno ya Faridi, akawa nusu ana furaha na nusu ana hasira.

    Dokta Neema Mnyampala aliekuwa amesimama akifatilia mwenendo ule, alimfata faudhia akamuinua akamwambia;

    “Bado Rama ameletwa hapa na yaleyale, au mengine tena?!”

    Baada yakusema maneno yale, Dokta Neema mnyampala akachukua faili la Rama lililokuwa pembeni ya kitanda chake akaanza kulipitia kwa kulisoma faili lile.

    Faudhia alikaa pembeni ya kitanda alipolala Rama upande wa kichwani, akawa kwa mkono wake, anampetipeti kichwani huku akimpa pole nyingi sana.

    Rama aliitikia pole ile kwa moyo mkunjufu, akajitahidi kukaa kitako lakini akashindwa kwani hakuwa na nguvu za kutosha, Faudhia alimwambia Dokta Neema Mnyampala kuwa mgonjwa wake anataka kukaa kitako je Drip inayoingia haiwezi kumletea tabu kwa kukaa kitako?

    Dokta Neema Mnyampala akwambia kuwa haiwezi kumletea tabu hasa kwa aina ya drip aliyokuwa amewekewa akamsaidia kumuinua akamuweka kwa kuegeme,kwa kukiinua zaidi kitanda kichwani kwake

    Rama akawa amekaa kitako, kwa namna alivyokuwa amekaa, macho yake yakamuona Faridi akiwa amekaa na drip yake mkao uleule aliokuwa amekaa yeye. Walikuwa wakitazamana kwa namna vitanda vile vilivyokuwa vimewekwa waliweza kuonana ana kwa ana.

    Faudhia alivyokuwa akimpetipeti Rama, alikuwa akifanya makusudi hajali lolote, akimsugua Roho Mtalaka wake, ambae alikuwa hakika anaumia vibaya sana, kwani Faridi alikuwa kama nyani aliekuwa akitaka kushika mtawi, na mtawi huo ukawa na miba. Lakini isitoshe umeanguka mweleka wa chali kwa kumuacha Faudhia. hivyo faridi akawa ananing’inia asijuwe pa kushika.

    Dokta Neema alimtembelea Faridi, kwani Drip yake ilikuwa inakwisha na ile ndiyo iliyokuwa ya mwisho, hivyo akiwa pale akiisubiria ile Drip ili aitowe, Faridi akamwambi Dokta kwa sauti yakuomba na iliyojaa huzuni kubwa.

    “Dokta naomba ukaniitie Faudhia, niongee nae kwani moyo wamgu unauma kumkosa kwa kosa nililomfanyia, hakika nilitupa Mbachao kwa Msala upitao, nilitupa jongoo na mtiwe, nimejifunza sasa nimeshaona naomba Dokta uniombee, japo aje niongee nae kwani anayomfanyia mchumba wa Rebeka mie naumia sana moyoni mwangu, kwani Faudhia bado ninamtaka bado ninahitaji kuishi nae, hakika amenivumilia sana, kwa hilo nakili na anastahili pongezi.”

    Dokta Neema Mnyampala akamjibu asubiri kwanza amalize kuiondosha ile Drip iliyokuwa imebakisha matone kadhaa kwisha.

    Ilipokwisha Drip ile Dokta Neema Mnyampala, aliiondosha sindano yake pale katika mwili wa Faridi, akamuweka pamba iliyokuwa na Spiriti akaizuilia pamba ile kwa Plasta katika sehemu ile iliyokuwa na sindano ili isikae wazi wadudu wakapaghasi.

    Dokta Neema Mnyampala akaondoka hadi katika kitanda alichokuwa amelala Rama, ambapo pia Drip yake ilikuwa inafika mwisho akaiondosha ile Drip tupu iliyobaki, akamkabili faudhia akampa ujumbe kutoka kwa Mtalaka wake wa wito.

    Rama alisikia maneno yale kutoka kwa Dokta Neema mnyampala, akamwambia Faudhia aliekuwa anakataa kwenda, kuwa aende akamsikilize Faridi asikatae wito, bora akakatae neno kama likiwa baya.

    “Kwa ruhusa yako nitakwenda, ila usingeniruhusu kamwe nisingekwenda kwani sina hata punje ya mahaba kwa mtu niliempa moyo wangu wote wa kupenda, hatimae akanitenda mimi ni binaadam pia sijatolewa nyongo. Alikuwa hajui Faridi kama mwisho wa ubaya ni aibu?.”

    Faudhia baada ya kusema maneno yale, akambusu katika paji la uso Rama, akaondoka kuelekea kumsikiliza faridi.

    Faridi kitendo kile cha Faudhia kumbusu Rama, alikiona akafumba macho yake ili asione tendo lile, lakini alikuwa amechelewa kwani tayari alikuwa ameshaona. Ama kweli jicho halina pazia.

    Faudhia alifika pale kitandani kwa faridi aliekuwa amekaa kinyonge, akasimama wima mikono yake akaifunganisha kifuani kwake, akawa anamtazama kwa macho makali, yakiashiria aambiwe wito alioitiwa.

    Faridi alimtazama Faudhia juu hadi chini, kisha akatingisha kichwa chake, kwa kumpoteza mrembo yule, ndipo alipomwambia neno ambalo Faudhia akashangaa sana!



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Faudhia mpenzi, najua nimekukosea sana. Nipo chini ya miguu yako nakuomba msamaha, kumbuka binaadamu hatujakamilika sie sote ni wakosefu, aliekamilika ni mmoja Mungu peke yake, mie siyo malaika kama sikosei mimi ni binaadam, kama suala ni kuambukizwa mbona huyo aliekuwa mchumba wa Rebeka nae atakuwa ni muathirika pia. Ikiwa tatizo ni talaka tatu ndiyo sitoweza kukurejea, basi naomba uolewe na mtu mwingine yoyote. Ila akuoe Alhamisi akuache Ijumaa ili niweze kukuoa upya, ila naomba usiolewe na Huyo Rama kwani hatokubali kukuacha huyo baada ya kukuoa na pia atanilipizia kisasi kumuachanisha na mchumba wake, nakuomba sana Faudhia hata kukulipa fidia mie nipo tayari utachotaka, ili nikuangukie kwa hili nilokutenda.”

    Faudhia alishangaa sana maneno yale, kwani busara na upole aliouonesha Faridi kama angefanya hivyo tangu awali, hakika wasingefika hapo walipo. Sasa afanyeje ndiyo ukawa mtihani mwengine kwake, kwamba je amsamehe Faridi ili katika kuangukiwa atake nyumba anunuliwe? Kwani uwezo huo Faridi anao, au aachane nae akae na Rama?! Kichwa kilimzunguka akapanga na kupangua lakini hakupata majibu stahiki juu ya suala lile.

    Alimtazama Faridi usoni mwake, na Faridi bila soni alishuka kitandani akapiga magoti chini yake akamshika miguu, akimuomba msamaha huku uso wake ukiwa umemuwiva kwa simanzi na majonzi.

    Faudhia aligeuka kutazama kitandani kwa Rama, akamuona Rama ameinuka amekaa kitako miguu ikiwa chini ya sakafu akiwaangalia wao.

    Uso wa Rama pale alipokuwa alikuwa akilaani toba zote za Faridi dhidi ya Faudhia, kwani ndani ya moyo wa Rama faudhia alikuwa ameshaingizwa mzimamzima, alipewa asilimia mia hakunyimwa hata punje ya kupendwa, ama kweli moyo wa kupenda ni mbaya sana. Rama alikuwa akiumia kwa mtu na mpenzi wake waliokuwa wametalikiana!

    Faudhia alipouona uso wa Rama umejaa huzuni akamuacha Faridi pale alipokuwa akamfata Rama lakini kabla hajafika kitandani kwa Rama, Faridi akaangua kilio cha kukata tamaa, alikuwa akilia kilio cha kusaga meno, pamoja na kuomboleza.

    “Faudhia fikiria mpenzi, haiwi baya moja lifute mema elfu moja. Kumbuka mema niliyokufanyia kisha linganisha na ubaya niliokufanyia wapi mizani yake inakuwa mizito? Nimekununulia gari mbili zote nikaandika jina lako, nimekufungulia duka la thamani kariakoo, ili pesa yako yakujikimu wewe mwenyewe uipate hapo, nimefanya mengi sana kwenu kwa wazazi wako, sio kama nakusimanga nayo laa, hivi yote yale huwezi kuona kwamba mimi ni mtu mwema kwako ila shetani alinipitia kati yangu tu? Huba huna basi hata hisani hukumbuki?! Huyo bwana anaekuzuzua anaweza kukufanyia hayo yote? Kumbuka Zimwi likujualo halikuli likakwisha, huwezi jua hapo unapotaka kwenda unaweza ukastaajabu ya Mussa ukayaona ya Firauni! ”

    Maneno yale Faridi alikuwa akiyaongea kwa sauti ya wastani, hivyo yalimfikia Rama kwa ufasaha ndani ya masikio yake, nafsi yake ikahama ikarudi katika maisha aliyoyaona kwa Faridi akajilinganisha na yeye. Kwa Faridi kuna maisha ya juu kabisa ya kifahari, kwake yeye kuna maisha ya mtanzania wa kawaida. Uwezo wa kumnunulia hata Bodaboda Faudhia hana, sembuse gari tena mbili, sikwambii duka kubwa la urembo tena Kariakoo, kodi yake ya pango ilivyokuwa kubwa, alipoyafikiri hayo Rama akakata tamaa kuwa na Faudhia, kwani sera za Faridi zilikuwa zimempiga vibaya, zimeharibu ngome yake ya kujimini kama kwa ubwete tu atamchukua Faudhia, kwani imemthibitikia kuwa ana upinzani mkali sana umemuandama, ili afanikiwe alihitaji nguvu ya ziada. Pahala pale palihitaji nguvu ya shoka siyo ya panga.

    Faudhia yeye alikuwa amepagawa, kwani kwake alikuwa kama yupo njia panda kulia anataka, na kushoto anataka kwa namna pale alipokuwa, ila maisha ya Rama ameyaona, ni maisha duni sana akilinganisha na maisha ya Faridi, ila Faridi amemtenda japokuwa sasa hivi anamuomba radhi akajiuliza katika nafsi yake je amkubalie? Lakini akiwa amemkubalia ana uhakika gani kuwa hatamtenda tena? Faudhia akafikiri pale alipokuwa hatimae akageuka kwa Faridi akamwambia kwa utuo.

    “Kama unataka urejeane na mimi basi sharti langu, ni mimi kuolewa na Rama kwanza na siyo mtu wako mwengine yoyote Yule awae, kwani kuolewa kwa mipango haitokuwa ndoa hata kidogo, kwani ndoa ni kitendo ambacho Mungu amekiridhia, kama wakubaliana na hilo Rama anioe kisha ikitokea kuachana ndiyo wewe uje unioe, kwa kuwa haya umeyataka mwenyewe kwa kunipa Talaka tatu kwa dafaa! Hivi ungekuwa umenipa Talaka moja au mbili hivi siingekuwa eda haijesha si ingekuwa rahisi kunirejea, lakini ulipanga kunikomoa, ulitaka kunikomesha ndiyo maana uliamua kunipa Talaka zote tatu. Kwa hiyo lazima vigezo na masharti yazingatiwe kama bado unataka kuwa na mie , kwani hakuna njia nyingine ya mimi kuolewa na wewe, ila niolewe pengine kwanza!”

    Maneno yale ya Faudhia yalisikika vyema kwa Rama na Faridi, ila yalikuwa ni Shubiri kwa Faridi, na yalikuwa Asali kwa Rama. Moyo wa kupenda ulikuwa ukiwasumbua watu wale.

    “Basi naomba tusafiri pamoja nchi utakayo huko tukiwa pamoja unaweza kupata mawazo bora zaidi, kwani sasa hivi naamini umechanganyikawa kwa hivyo hutoweza kupata maamuzi ya busara”

    Faridi alikuwa akivutia kwake kwani alitaka akiwa na Faudhia nje ya nchi atakuwa amemuweka mbali sana na Rama, hivyo atakuwa hamuoni lakini pia huko nje atatafuta mtu wakumuoa, kisha yeye atatowa kila kitu, na baada ya kuolewa atafanya mipango aachwe ili aje kumuoa yeye. Lakini pia aliona kama Faudhia ataolewa hapa nchini itakuwa kila akimuona huyo mwanaume atakuwa hana amani, ila ikiwa ameolewa nje ya nchi moyo wake utatulia kwani huyo bwana hataweza kuja Tanzania kumfata Faudhia.

    Faudhia maneno yale yalimuingia sana ya kwenda nje ya nchi kupumzika, ila aliamini mume pekee anaeweza kumuoa ili amfute machozi ni Rama, akamwambia Faridi ampe muda hadi kesho atampa jibu juu ya jambo lile. Faridi akakubali kwa shingo upande. Lakini ndani ya moyo wake aliazimia lazima amuangamize Rama amuondoshe Duniani ili asiwe na mpinzani.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Rama kwa upande wake, fikra zake zilikuwa zinamtuma kama zali lile litamdondokea basi yeye atajuwa kuoa tu ila si kuacha, kama ni kuondoka Faudhia ataondoka yeye ila kamwe hatotowa Talaka hata moja sikwambii Talaka tatu. Na hiyo ndiyo itakuwa pingamizi kubwa sana kwa Faridi kumuoa faudhia, alijipanga kuwa Faridi ana pesa nyingi sana, ila yeye amejaaliwa mapenzi mengi sana hivyo kama Rebeka alivyomwambia katika ujumbe wake kuwa, aliowauwa sita, kwa Ukimwi hatotoka, mtu aliemkubali katika majambo kama yeye, basi akaona hiyo itakuwa ndiyo silaha yake kubwa itakayomfanya Faudhia asifikirie kudai Talaka kabisa kwa mahaba na raha atakazompa.

    Faudhia baada ya kukubaliwa wazo lake, akamfata Rama pale alipokuwa akakaa nae kitandani, akamuuliza Rama hali yake anavyoendelea, nae akamjibu kwa masikitiko.

    “Faudhia naomba ufahamu kwamba Masikini nae mtu japokuwa hana kitu, mie sina mali lakini nina mahaba ya dhati kwako, zingatia kwamba mali inatafutwa lakini mapenzi bora wachache sana waliojaaliwa kuwa nayo, naomba usiniache tafadhali, sikupenda mie niwe lofa, ni mipango ya Mungu, kumbuka kama ungekuwa umeshajiuwa hivi huyo Faridi angemuoa Faudhia yupi? Kumbuka mtalaka wako anajifanya kukuhitaji sasa kwa sababu ameona unae mtu, ndiyo maana anafanya hivyo, akishafanikisha kukuoa tena ukawa ndani ya himaya yake, huyo atakutenda zaidi utakuja kuyakumbuka maneno yangu kama bado nitakuwa nipo hai, na ikiwa nimekufa basi nitasikia na wachunga mbuzi wanaopita makaburini. Usirudi nyuma Faudhia angalia changamoto mpya, kumbuka kila likuepukalo lina kheri na wewe.”

    Maneno ya Rama na maneno ya Faridi, yalimfanya Faudhia awe hana maamuzi sahihi, kwani wote walikuwa kila mtu kama muwamba ngoma ngozi huvutia kwake, akapata wakati mgumu wapi pa kuelekea, akaamua atoke nje atafute pahala akapumzike ili kuyatafakari maneno ya wale wanaume wawili wanaomchanganya akili zake. Faudhia alisimama akatoka nje bila ya kumuaga mtu siyo Rama wala Faridi, alitoka nje akaitazama gari yake pale nje hakuiona, ndipo mawazo yalipomjia kuwa ameiwacha Agha Khan Hospital, akajihisi ni mtu ambae anaweza kusizi muda wowote kwa mawazo kwani alikuwa ameshachanganyikiwa. Alichukuwa Taxi akaelekea hospitali ya Agha Khan, kufata gari yake.

    *******

    “Mimi Rebeka Binti John Makuka, mzaliwa wa Tanga katika eneo la Ngamiani pale Tanga mjini. Nililelewa na familia yangu katika mazingira mazuri kiasi kwamba ilikuwa nikitoka shule ya Msingi Mkwakwani, niliku nikirudi nyumbani ni kula na kujisomea, sikupata nafasi hata ya kwenda Sokoni pale Ngamiani ambapo soko lile lilikuwa jirani na nyumbani kwetu. Hali ilikuwa ni hiyo hadi nilipomaliza shule ya Msingi nikachaguliwa kwenda secondary. Nilikuwa ni msichana ambae sikuwa kabisa na habari na wanaume, kwani nilifata masomo sikuwa kabisa na mawazo na wanaume. Shuleni kwetu wasichana wenzangu walikuwa na mabwana zao, waliokuwa wakiwapa pesa na kufanya nao mapenzi, lakini mie nilikuwa na misimamo yangu kuwa elimu ndiyo msingi wa maisha ya mwanaadamu. Kwa kitendo kile cha mimi kushikamana na masomo kuachana na mambo ya wanaume, marafiki zangu wengi wa kike walinikacha wakiniona labda ni mwanamke niliekuwa tofauti kwa kuwa tu, sifati tabia zao mbaya walizokuwa nazo. Wakanipachika majina mengi tu. Nikachukiwa na wanafunzi wa kike na wakiume pia. Kama hiyo haitoshi wavulana walikuwa wakinikamia kwamba ninajifanya mjanja basi ipo siku watanikomesha, nijute maisha katika maisha yangu.”

    Alipofika hapo Rebeka alifuta machozi kwa mgongo wa kiganja chake cha mkono. Kisha akaendelea kueleza kwa nini amekuwa mbaya vile kwa wanaume?!

    “Basi walipokuwa wakiniambia vile nilikuwa naripoti kwa mwalimu wangu wa Darasa ambae nae alikuwa ni mwanaume, lakini katika hali ya ajabu mwalimu Yule aliwaadhibu wale vijana wanafunzi wenzangu lakini pia na yeye akiwa ananitaka kimapenzi! Kwa kweli hali ile ilinisumbua sana, ilibidi niipeleke ripoti ile kwa mwalimu mkuu kumshitaki mwalimu wa darasa kunitongoza, lakini kwa mwalimu mkuu kwa kuwa nae alikuwa ni mwanaume, hakika sikupata ushirikiano wa kutosha, kwani mwalimu wangu wa darasa alinikana mbele ya mwalimu mkuu, akisema kuwa mie nampelekea yeye kesi kila leo ya kusumbuliwa na wanafunzi wenzangu, nay eye alikuwa akiwaadhibu, tena bila ya ushahidi wowote, kiasi malalamiko yangu yakawa ni ya kudumu ndipo alipokataa kuwaadhibu watoto wa watu kila siku tena akidai kuwa kama hao wavulana ile ingelikuwa ndiyo tabia yao, basi angepelekewa pia kesi za wasichana wengine, kwa nini kila siku niwe natakiwa mie tu, kwani mie nina nini?! Mwalimu mkuu aliniambia nikawaite wazazi wangu ili kufahamishwa tabia yangu mbaya ya uongo shuleni, kwa wanafunzi wenzangu hadi kwa walimu. Wazazi nilipowaita walipokwenda shuleni, mwalimu mkuu akawaambia kuwa wanikanye sana kwani nina tabia mbaya ya uongo ambayo hata wanafunzi wenzangu wameithibitisha, mwalimu mkuu akenda mbali sana hadi kufikia kuwa kama nitaendelea na tabia ile ya kusema uongo basi atanifukuza shule. Wazazi wangu walinishambulia sana kwa maneno bila kujali kuwa sikuwa muongo bali nilikuwa natakiwa kweli kabisa na wanafunzi pamoja na mwalimu, ila sikupata haki kabisa nikasusuikwa kama Paka aliekunya!”

    Rebeka alipofika hapo macho yake yalijaa machozi sana, akayafuta machozi yale safari hii akitumia nguo yake.

    “Ehee nini kikaendelea hata kikakufanya uwe adui kwa wanaume ni huko kukutaka tu au nini kilijiri kwani bado hujapata sababu za wewe kuambukiza virusi watu, na hivyo virusi ukavipataje wakati wewe inaonesha hapo ulikuwa bikira kwani usitake kupoteza muda hapa kwa mambo ambayo ya miaka na miaka, eleza sababu gani hadi unasambaza virusi makusudi?!”

    Mkuu wa kituo cha Polisi Magomeni alimsaili Rebeka kwa sauti ya ukali lakini Rebeka hakutetereka. Akamjibu.

    “Huko ndipo ninapoendea huko, kwani mimi siyo mwendawazimu wala mie sikupata Virusi kwa kupenda laa hasha. Ila nisikilize kwa makini ili ufahamu kilichotokea.”

    Rebeka alimwambia mkuu wa kituo ambae nae akamruhusu kuongea hiyo historia yake, huku akitazama ile Tape Recoder kama inafanya kazi yake sawasawa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Wakati huo nilikuwa nipo kidato cha tatu, nakumbuka tulipofunga shule mwezi wa kumi na mbili, nilipokuwa naondoka shule nikiwa natembea kwa miguu, ilitokea Pikipiki aina ya Watco ikanigonga kwa nyuma nikaanguka chini huku nikisikia maumivu makali sana. Yule dereva wa pikipiki alikimbia hakusimama kabisa. Mara wakatokea wanafunzi wenzangu wengi lakini walikuwa wakinipita tu bila kunipa msaada wowote huku wakinikebehi kuwa najisikia sana hivyo na wao hawana msaada na mie. Mara wakatokea wale wavulana niliokuwa nawachongea shuleni walivyokuwa wakinitongoza. Mvulana mmoja aliekuwa anaitwa Jackson Mwapachu alikuwa akiletwa na kuchukuliwa na gari kila siku na dereva wao, ila sijui siku ile ilikuwaje hata akaja na gari shuleni yeye mwenyewe. Nikiwa pale chini nimekaa naugulia maumivu ya mguu, akatokea Jackson Mwapachu, akasimamisha gari kisha wale wavulana wengine wakanibeba na kunipakia nyuma ya gari ile Pick up Toyota Hilux, kisha na wale wanafunzi wakapanda ndani ya gari ile, mie nikawa nimelala nyuma ya gari ile Pick up, sikuwa najua napelekwa wapi, japo nilikuwa nadhani labda napelekwa nyumbani au labda Hospitali ya Bombo lakini badala yake ilikuwa ni tofauti na mawazo yangu!”



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog