Search This Blog

Wednesday, 1 June 2022

MSAFIRI SAFARINI - 1

 







    IMEANDIKWA NA : CHANGAS MWANGALELA



    *********************************************************************************



    Simulizi : Msafiri Safarini

    Sehemu Ya Kwanza (1)

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    MAJIRA yalizidi kujongea mbele pasipo na kurudi nyuma. Upepo mwanana nao uliendelea kuvuma kwa kasi ya kupendeza ili kuyasindikiza majira. Ndege pia hawakubaki nyuma, kwani walitoa nao milio ya kupendeza. Sauti tofauti tofauti zilisikika na kuashiria kuwa mahali hapo hapakuwa na ndege wa aina moja. Sambamba na yote hayo, mirindimo ya maji yatiririkayo mtoni iliendelea kusikika na kwa pamoja sauti hizi ziliunda muziki maridhawa ambao ungeweza kuukonga moyo wa kiumbe yeyote apendaye burudani. Mchanganyiko wa sauti hizi ulianza kunifanya nipoteze kumbukumbu juu ya uchovu wa safari niliyosafiri kwa muda mrefu

    usiojulikana bila kufika nielekeako.



    Mawe makubwa pamoja na miti ya aina mbalimbali yenye maua ya kuvutia na majani yenye rangi ya kijani kibichi, sambamba na ndege waliokuwa wakiruka kutoka mti mmoja na kuelekea mwingine, na walioruka kutoka kwenye miti na kutua kwenye mawe na kisha kurudi tena kwenye miti walipafanya mahali hapa paweze kunivutia sana. Uzuri wa mahali hapa uliyapendeza macho yangu kwa kiwango cha kuusuza moyo.



    Haikuwa dhamira yangu kupumzika mahali hapa, bila kutegemea nilijikuta naketi chini ya mti mkubwa uliokuwa pembezoni mwa mto na kujiegemeza bila matata yoyote huku akili yangu ikitafakari kwa kina juu ya mkusanyiko wa sauti nilizokuwa nikizisikia mahali hapa. Na mara mawazo juu ya dhana na asili ya ushairi yakazivamia fikra zangu. Baada ya tafakuri ya kina nikajikuta nashawishika na kuyakubali mawazo niliyowahi kuyasikia hapo awali kuwa, fasihi ni mwigo.



    Yaelekea mwanadamu alijikuta katika bahari ya ushairi baada ya kuwa ameigiza sauti mbalimbali alizowahi kukutana nazo katika mazingira yake kwa kipindi fulani cha muda. Na kwa kuwa hata mimi nimeshawishika baada ya kuzisikia sauti hizi, basi sina budi kuuthibitishia ulimwengu juu ya madai kuwa fasihi ni mwigo.

    Kwa uzuri wa hali ya hewa ya mahali hapa, nilijikuta narubunika na hatimaye nikawa mateka wa usingizi mzito bila hata ya kujitambua! Yawezekana nisingeamka mapema kama nisingezisikia kelele ambazo zilinikurupua kutoka usingizini.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Zilikuwa ni sauti za vigeregere sambamba na midundo ya ngoma zilizopigwa kwa ustadi wa kipekee. Sauti hizo zilizidi kuwa kali kadri muda ulivyokuwa ukienda, na ilionyesha wazi kuwa zilikuwa zikijongea mahali nilipokuwa.



    Kama ilivyo kwa kiumbe yeyote, asiyekubali kupitwa na mambo nilijikuta napata shauku ya kutaka kushuhudia kilichokuwa kinaendelea. Lakini kabla ya yote niliona ni vema kama nitabeba begi langu mgongoni na nikafanya hivyo. Wakati namalizia kuweka begi langu mgongoni hali niliyoishuhudia mbele yangu ilinifanya nipigwe na butwaa, wakati bado naendelea kushangaa tayari haja ndogo ilikwisha kuifanya suruali yangu iwe mbichi kama imefuliwa au kulowekwa kwenye maji! Kwa umbali wa mita zipatazo tano kutoka mahali niliposimama kulikuwa na joka mkubwa sana! Licha ya ukubwa wa kutisha joka lile pia lilikuwa na majani mgongoni likishuka taratibu kuelekea mtoni. Joka lile liliteleza kwa madaha ya aina yake, huku likitoa ulimi nje na kuurudisha ndani. Nilijituliza kimya nikimshuhudia nyoka yule mwenye ukubwa wa ajabu, rangi nyeusi na majani mgongoni, alivyokuwa akizama polepole katika maji ya mto ule! na mara baaada ya kumalizika mkia sauti za ngoma na vigeregere nazo zikakoma.



    Nilitoka mbiombio maeneo yale kwa kasi ya duma awapo mawindoni, nilikimbia sana kwa kipindi fulani cha muda huku nikihema na kutweta kwa woga. Pamoja na woga niliokuwa nao niligeuka nyuma ili kuona kama nafuatwa na kitu chochote! hakukuwa na kitu zaidi ya msitu mnene niliokuwa nikiuacha kwa kasi. Nilizidi kukimbia kwa jitihada zisizo na kifani huku nguvu zangu nazo zikinisaliti. Nilianza kuchoka zaidi kwa kila hatua niliyokuwa nikipiga, na sasa nilianza kutembea kama mlevi kwa uchovu wa mbio,



    nilisimama kidogo kuvuta pumzi, halafu nikaendelea na safari yangu. Nilipogeuka tena nyuma niliuona ule msitu ukiwa bondeni na hapo ndiyo nikagundua kuwa nilikuwa napandisha mlimani.

    Niliendelea kusonga mbele, na sasa jua lilielekea kuzama, giza nalo likaanza kujitokeza polepole. Hakukuwa tena na miti mbele yangu na badala yake niliyaona majani mafupi yaliyofubaa kwa ukosefu wa mvua, pamoja na suluba kutoka kwa jua kali. Kadri nilivyokuwa nikipiga hatua mbele giza lilizidi kutanda na hatimaye pote pakawa peusi kwa giza totoro, hali iliyonifanya nitawaliwe na woga usiomithirika nafsini mwangu.



    Na mara kwa mbali nikasikia mlio wa kitu, mlio huo haukuwa mgeni masikioni mwangu ingawaje kuutambua bado ilinipa shida. Kadiri muda ulivyozidi kwenda, ule mlio ulizidi kusikika kwa ukaribu zaidi, hatimaye nikapata nafasi ya kuutambua kuwa, ulikuwa ni mlio wa zumari iliyokuwa ikipigwa kwa ustadi wa hali ya juu na mtu ambaye ni mbobezi katika burudani ya zumari.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilihisi yawezekana niko karibu na makazi ya watu, niliongeza kasi ya miguu yangu ili niweze kupafikia mahali ulipokuwa ukitokea mlio huu lakini bado jitihada zangu hazikufaa kitu. Nilitembea kwa umbali mrefu bila kuona hata dalili ya nyumba wala makazi, wakati huo wote mlio wa zumari uliendelea kusikika, kuna wakati nilihisi labda mpiga zumari alikuwa akinikimbia, na matumaini ya kuufikia mlio wa zumari yakaanza kupungua.kadri mud ulivyozidi kwenda mbele.



    Giza lilianza kupungua na upepo wa wastani ukaanza kupuliza, kwa uzoefu wa muda niliokuwa nao niliweza kutambua kuwa ilikuwa ikielekea asubuhi. Ule mlio wa zumali ulianza kupungua polepole na hatimaye ukatoweka kabisa na bado nisione dalili ya nyumba wala makazi.

    ***********



    Safari ilinichukua mpaka mahali nilipoanza kuona nyumba zilizoniashiria kuwa mahali hapa ni makazi ya watu. Na baada ya kutembea kwa masaa mawili zaidi, sasa nilikuwa kijijini. Nilikutana na watu wa aina mbalimbali, wafupi kwa warefu, wanene kwa wembamba na weusi kwa weupe. Jambo la ajabu ni jinsi watu hawa walivyoonekana kunishangaa kwa muda mrefu, na hata nilipowasalimia hawakuonekana kunijibu, hali iliyonifanya nihisi kuwa labda hawakuielewa lugha yangu, nilijaribu kuwasalimia kwa ishara lakini hakuna hata mmoja aliyejishughulisha na salamu yangu.



    Mbele yangu akatokea mzee aliyekuwa amejifunika mashuka yenye rangi ambayo sikuweza kuitambua kwa haraka, yalionekana kama meusi na mara yalionekana kuwa na rangi ya ugoro na kuna wakati yalionekana kuwa na rangi ya bluu iliyokolea. Mkono wa kulia alishikilia fimbo iliyosimikwa vema chini kwa kila hatua aliyopiga. Mkono wa kushoto alibeba birika la chuma ambalo sikuweza kujua mara moja kuna nini ndani yake.



    Yule mzee alikuja na kusimama mbele yangu kwa kujiegemeza kwenye fimbo yake kisha akasema:Nimekusubiri kwa masaa, siku, majuma, miezi, miaka na hatimaye sasa ni miongo kadhaa. Nilikuwa nimekaribia kukata tamaa. Watu walishaanza kuniita muongo, mzushi na majina yote yenye kufanana na hayo. Namshukuru Nyamukwararyohoka amekuleta katika muda muafaka.”



    Baada ya kusema hayo akasema:



    “Nifuate.”

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Tuliongozana na yule mzee bila kujua tunapoelekea kwa takribani muda wa masaa mawili njiani. Kote tulikokuwa tukipita palitapakaa makaratasi yaliyoonekana kunyofolewa kutoka kwenye vitabu na magazeti, karatasi zilirushwa huku na kule kwa upepo. Kuna karatasi iliyopeperushwa kwa upepo na kuja kunata kifuani kwangu, nikaichukua na mara baada ya kuitazama vema nikagundua ni gamba la kitabu, na nilipoitazama barabara picha ya mtu aliyekuwa kwenye karatasi ile, nikagundua kuwa alikua ni ‘Albert Camus’ ambaye nilipata kumfahamu kupitia maandishi yake ya “The Myth of Cysiphus.”

    Sasa tulikuwa tukiingia katika mji fulani ambao kwa hesabu ya haraka haraka nilibaini kulikuwa na nyumba zipatazo tano, zilizoezekwa kwa nyasi, kusimamishwa kwa miti, na kunakshiwa kwa udongo sanjari na mbolea ya ng’ombe. Kwa muda wote huo hatukuwa tumezungumza tena na mzee na mara akaanza kwa kusema:

    “Hapa ndiyo nyumbani kwangu, eneo lote unaloliona tangu kwenye mlima uleee! Mpaka kwenye muembe



    huo, lote ni eneo la ukoo wetu, alianza kuishi babu yake baba yangu na mpaka wajukuu wangu wote wako hapa. Magovi na vitovu vyetu wote vimefukiwa hapa na patabaki kuwa mali yetu daima.”

    Alinionesha huku akigongagonga fimbo yake chini.

    Aliniamuru niingie ndani nami nikafanya hivyo, kisha naye akaingia. Aliketi kwenye kigoda nami nikaelekezwa kukaa kwenye kitanda cha kamba kilichokua ndani mule.



    ************

    Baada ya kunawa mikono, Mzee alianza kwa kuniuliza, “habari za safari?”

    Wakati bado nafikiria namna ya kujibu, ghafla akaanza kusema:

    “Najua fika kuwa, kwa mujibu wa mawazo yako, mwanzoni safari ilikuwa shwari. Lakini ushwari ulianza kutoweka polepole baada ya kuanza kujifikirisha. Na tangu ulipoanza kufikiri, matumaini ya kuipata tena shwari yamekuwa yakipungua siku hadi siku, na hii ni kwa sababu uwezo wako wa kufikiri nao hauko nyuma katika kujengeka. Sikushangai kwa sababu; kwa muda wote wa maisha yake mwanadamu amekuwa mtumwa wa furaha, na yote ayafanyayo au akusudiayo kuyafanya ni kwa ajili ya kujiridhisha nafsi. Na kwa vile nionavyo, sijui kama ipo siku mwanadamu atakombolewa au kujikomboa kutoka kwenye utumwa wa furaha. Na yote ni kwa sababu ya matumaini yaliyojengeka mawazoni mwake. Na katika harakati hizo za kuisaka

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    furaha ndiyo mwanadamu hupata nafasi ya kutambua kuwa anakabiliwa na vikwazo au matatizo kwa lugha nyingine katika kuifanikisha adhma yake ya kujiridhisha nafsi.”

    “Kwani tofauti kati ya kujiridhisha nafsi na furaha inaweza kubainikaje?” Niliuliza.

    “Furaha na Kujiridhisha nafsi, ni ishara mbili tofauti ambazo tofauti zake zinajibainisha kimsamiati tu. Lakini kimantiki zote huwa zimebeba dhana moja, au kwa namna nyingine naweza kusema furaha ni maridhio ya nafsi juu ya jambo Fulani.” Alisema

    Wakati tunaendelea na mazungumzo, mara chakula kikaletwa na binti aliyepiga magoti chini wakati akitukaribisha chakula. Baada ya chakula Mzee alitoa chupa ya mvinyo, akamimina kwenye kikombe chake na baadaye kwenye kikombe changu, taratiibu tukaanza kunywa. Kimya kilitawala na baadaye nikavunja ukimya kwa kuuliza:

    “hivi kwa nini mwanadamu anaishi jinsi aishivyo?”

    “Mwanadamu anaishi kwa kufuata mazingira yake yanamtaka afanye nini, na kwa sababu ya kufuata matakwa ya mazingira mwanadamu amejikuta akifanya mambo ambayo hakuwahi kuyafikiria kuwa ipo siku atayafanya. Mazingira yamemfanya binadamu atawaliwe na mihemko katika kuamua na kutenda, bila kufungamanisha utashi katika maamuzi na matendo yake”.Alisema Mzee

    Wakati najiandaa kuuliza swali jingine mara, watu wawili wa makamo wakaingia ndani na kuketi kwenye viti vya mkunjo vilivyokuwa viko wazi kwa muda wote. Na baada ya salamu Mzee alifanya utambulisho, ni katika utambulisho huo ndio nikajua Mzee alinifahamu mimi pamoja na chimbuko langu. Baada ya utambulisho Mzee aliongeza chupa nyingine ya mvinyo na wote mimi, Mzee, Kasimu na Tamimu, kila mmoja na kikombe chake, tuliendelea kunywa mvinyo huku tukibadilishana mawazo, kwa kuibua mijadala iliyojibiwa kwa hoja nzito na zenye nguvu. Tulizungumza mengi ila jambo moja lilionekana kutuchukulia muda mwingi zaidi. Ilikuwa ni baada ya mimi kuuliza swali kuhusiana na nini maana ya maisha. Tamimu alifungua dimba kwa kusema:

    “Maisha ni kuishi”

    Kisha Kasimu akasema:

    “maisha ni kile unachopata”

    Mzee alionekana wazi kuwa hakuridhishwa na majibu yaliyotolewa, nae akaendelea kwa kusema:

    “ maisha ni leo na kesho”

    Niliyatafakari kwa kina majibu yote yaliyotolewa, niliona kuwa yote yalikuwa sahihi, ingawaje usahihi wake usingetosha kuondosha lakini nilizokuwa nazo juu ya majibu yao.

    Mvinyo ulitushika, na baadaye Kasimu na Tamimu waliaga na kuondoka, kwani ilikuwa imekwishakuwa usiku. Mzee alinionyesha pa kulala kisha akaniambia: Alamsiki!

    *************CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Asubuhi ilipofika Yule Mzee alikuja kuniamsha, kwa bahati nzuri alikuta usingizi umeshanitoka. Baada ya salamu akaniagiza nimfuate, tulifuatana bila kuzungumza lolote kwa kipindi Fulani cha muda. Tulipofika kwenye eneo ambalo lilionekana kuwa na makaburi mengi, Mzee akaanza kwa kusema:

    “Nimekuleta hapa ili uone maajabu ya ulimwengu huu. Haya unayoyaona ni matokeo ya kile mwanadamu anachokiita maendeleo ya sayansi na teknolojia. Watu wote waliolala hapa ni kwa sababu ya vita mbalimbali vilivyowahi kupiganwa ulimwenguni. Walipigana Kaburu na mwafrika, watu wengi wakauawa na kuja kuhifadhiwa hapa. Mapigano haya yaliwaacha maelfu wakiwa maiti na wengine wakaachwa na ulemavu wa kudumu”

    Nilimsikiliza kwa makini sana wakati akinieleza juu ya habari hizi. Alishusha pumzi ndefu kisha akaendelea tena:

    “Tangu vita vya kaburu mpaka vita ya Kagera ni mamilioni ya watu wameuawa.”

    Tuliendelea kuzungukia maeneo yale akinionyesha makaburi ya wale walioitwa mashujaa. Katika kuzunguka huko nilibaini kuwa makaburi mengi hayakuwa na misalaba, nikaona si vema kukaa kimya nikamuuliza:

    “Mbona naona makaburi mengine hayana misalaba, kulikoni?”

    “Kuna vichaa wachache ambao hujiona ni bora kuliko wengine, wao huona kuwa maisha ni ya kwao na wengine hawana maana. Wameng’oa misalaba kwenye makaburi na kwenda kuiuza kama chuma chakavu” alisema Mzee

    Nilitikisa kichwa kwa huzuni, na wakati bado natafakari jambo, mara akasema:

    “Hebu tazama hapa tulipo palishawahi kuwa na ziwa. Watu wa maeneo ya karibu walitegemea maji yaliyokuwa hapa, samaki chungunzima waliwafaidisha watu kwa minofu. Kilimo kilistawi na watu wakajitwalia mavuno tele kwa msaada wa unyevu uliopatikana katika ziwa hili. Tangu likauke ni zaidi ya miongo miwili na maelfu ya watu wamekufa kwa sababu ya njaa kali”

    Jua lilikwisha anza kuzama, na hiyo ilikua ni ishara kuwa siku inaelekea ukingoni. Mzee aliniamuru tuondoke, nikafanya kama alivyosema na tukaanza safari kuelekea nyumbani, ilituchukua muda wa masaa mawili na nusu na sasa tulikuwa nyumbani kwa Mzee. Tuliingia nyumba tulimo kuwa jana, na mara baada ya chakula Mzee alitoa chupa ya mvinyo akamimina kwenye vikombe na kisha tukaanza kunywa. Ukimya ulitawala kati yetu kwa muda mrefu, na mara Mzee akavunja ukimya kwa kusema:

    “Kwa zaidi ya miongo miwili, mwanadamu popote alipo amekuwa akikabiliwa na hofu juu ya gonjwa hatari la ukimwi. Wakati wengine wakitawaliwa na hofu mamilioni ya watu wanaishi na virusi vya ukimwi, na mamilioni wengine hawapo duniani baada ya kuwa wameathirika na ugonjwa huu. Cha kushangaza ni kwamba, kwa miaka nenda rudi idadi ya waathirika inaongezeka badala ya kupungua. Wengine hudai kuwa gonjwa hili limekaa pabaya hivyo litaendelea kutuua kwa kila uchao



    Mzee alivuta pumzi kidogo kisha akageukia kikombe cha mvinyo, na baada ya kubaini kuwa kikombe kilikuwa tupu, aliielekea chupa na kuanza kumimina mvinyo kwenye vikombe kwa mara nyingine. Baada ya kunywa mafundo yapatayo matatu Mzee aliweka kikombe chini na kuendelea kusema:CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mwanadamu ana maadui wengi ambao anapaswa kukabiliana nao ili kuyafanya maisha ya sayari hii yawe mepesi. Licha ya kuwa na maadui hao mwanadamu bado anaendelea kupandikiza na kuendeleza uadui baina yake na mwenzi wake, badala ya kushirikiana ili kudhoofisha nguvu za maadui wengine ambao ni tofauti na mwanadamu. Mwanadamu analala mwenye maabara akitengeneza silaha kali za nyuklia ili kuweza kumpiga mwenzi wake.

    Mwanadamu huyo huyo mwenye maabara yake anajinyima usingizi ili kutengeneza virusi kwa lengo la kumuangamiza mwanadamu mwenzie. Wakati akijitahidi kufanya yote haya, adui aitwaye maradhi humfyonza polepole mpaka ahakikishe amemmaliza uhai.

    Kama mwandamu angelala mwenye maabara yake kwa ushirikiano na binadamu mwenzake kutengeneza chochote cha kumuepusha na maadui kama; njaa na maradhi maisha ndani ya sayari hii yangevutia hata viumbe wa sayari nyingine kuishi mahali hapa.”

    Kwa wakati huo wote nilikuwa kimya nikimsikiliza Mzee kwa umakini usiomithirika. Mzee alizungumza mengi yaliyonifanya nimshangae mwanadamu kwa yale ayafanyayo. Masaa hayakutaka kutungoja, yaliendelea kusonga mbele. Wakati nikitafakari jambo nilishtushwa na mlio ambao ulinishangaza sana. Sikushangazwa peke yangu, kwani hata Mzee naye alikuwa kwenye mshangao na mara Mzee akaongea tena:

    “Kesho ataongea tena!”

    Nilijiuliza kuwa ni nani atakayeongea kwa mara kadhaa lakini bado sikuwa na jibu mwafaka. Wakati bado nawaza, Mzee alionekana kuwa na furaha, aliinuka alipokuwa amekaa kwa kasi na kutoka nje. Baada ya muda mfupi alirudi akiwa na chupa mbili za mvinyo, akaketi kwenye kile kiti chake cha mkunjo kisha akaanza kusema:

    “Kesho ataongea tena.”

    Baada ya kuwa nimetaharuki kwa muda huku nisijue cha kufanya nikajikuta nauliza:

    “Ni nani huyo atakayeongea tena?

    Bila ubishi Mzee alianza kwa kuniambia kuwa:

    “Watu humwita kichaa, lakini kwa vile ninavyoifahamu fasili ya neno kichaa, yeye hafanani na ukichaa.” Alisema Mzee

    Mpaka wakati huo majibu ya swali langu yalikuwa hayajapatikana kwa namna niliyoitaka. Hivyo nikaendeleza mfululizo wa maswali ambayo yalijibiwa na Mzee bila pingamizi. Ni hapo ndiyo nilipata nafasi ya kujua kuwa mwalimu huitwa kichaa na wakazi wa maeneo haya, ambao huiona elimu katika mfumo rasmi haina maana zaidi ya kupotosha na kupoteza wakati.

    Kila awapo tayari kutoa muhadhara, hupulizwa pembe ya Nyati ambayo hutoa mlio usikikao katika eneo kubwa, na kwa sababu siyo wote humwona kuwa kichaa, baadhi ya watu huja kumsikiliza anachohudhurisha katika wakati ambao huanza kesho.

    Wakati wenye majira yaliyochanganyikana kwa joto na baridi. Haikutuchukua muda mrefu sana tukawa tumeshalewa. Mzee aliniaga na kusema tuonane asubuhi ili tukamsikilize huyo wanayemwita kichaa.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    **********

    Midundo ya ngoma ilisikika na baadhi ya watu, walionekana wakielekea mahali tulipokuwa tukielekea, ambako ndiko sauti za ngoma zilikua zinatokea. Sauti hizi zilizidi kukita ngoma za masikio yetu kadri tulivyokuwa tukisogea mbele. Na sauti za nyimbo pia zilianza kusikika. Mwanzoni zilikuwa zikisikika kama kelele lakini kadri tulivyosogea karibu, nyimbo ziliweza kusikika bara bara na hata tukaanza kuyasikia maneno yaliyokuwa yakiimbwa kwenye nyimbo. Nayakumbuka mashairi mengi yaliyoimbwa siku hiyo lakini mashairi yaliyoiteka akili yangu yalikuwa ni haya:



    Ntale mwuuzi wa hano…

    Kwibhulwa kwandetile..

    Kwibhulwa kwandetileeee….x3



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog