Simulizi : Msafiri Safarini
Sehemu Ya Tatu (3)
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilikuwa niketembea kwenye njia ambayo upana wake haukunipa matumaini ya kupiga hata hatua moja mbele, ulikuwa ni upana wa nywele mbili zilizounganishwa kwa pamoja na kila mara nilihisi kama inaelekea kukatika. Sikuweza kuona mbele kwa
sababu ya ukungu ambao ulitanda muda wote. Niliona vivuli ambavyo vilinifanya nihisi kuwa mbele kuna uzuri ambao punde tu nitaufikia. Safari kwenye njia ile nyembamba iliendelea bila kuufika uzuri ambao uliwakilishwa kwa vile vivuli. Matumaini kuwa ipo siku nitaufikia uzuri ule yalinikaa vema. Japokuwa niliamini kuwa mbele kuna uzuri kuliko mahali nilipo, hofu yangu kubwa ilikuwa ni uimara wa njia ambayo ilionekana kuyumba na kuashiria kuwa muda wowote inaweza kukatika.
Niliambiwa kuwa njia hii imepitwa na wengi na wote wameishuhudia hali hii kwa kipindi chote cha safari yao. Njia haijawahi kukatika bali ni watu wadondokao. Wamedondoka mamilioni na bado mamilioni wako safarini. Wakati wengine wanadondoka wengine huibuka na kujiunga na safari. Kila mmoja alitembea kwa mtindo anaoujua ama baada ya kuiga toka kwa wengine au baada ya kubuni mtindo wake ambao nao uliigwa na wachache waliovutiwa.
Njiani tulikuwa wengi kila mmoja akijaribu kupiga hatua kuelekea mbele. Wazee, vijana na watoto wake kwa waume walikuwapo njiani. Njia ilichukuwa sura tofauti karibu kila siku, lakini haikuonyesha tumaini la kuwepo uimara wa njia. Kuna wakati niliyumba kiasi cha kukaribia kudondoka shimoni na baadhi ya watu wakasema kuwa yawezekana nilikosea kukanyaga wakati naanza kupiga hatua, na wakadai kuwa inaweza kunifanya nidondoke kwa kosa nililolifanya siku za nyuma.
Roho iliniuma sana na huzuni ikanitawala, nilitamani kurudi nyuma ili nianze upya safari yangu lakini haikuwezekana hata kidogo. Nyuma yangu kulikuwa na kitu ambacho kilikuwa kinanizuia kurudi nyuma na kunisukuma kuendelea mbele. Haikuwezekana kurudi tena nyuma isipokuwa kuyakumbuka tu baadhi ya mambo yaliyowahi kutokea hapo awali.
Njiani nilishuhudia mambo mengi ya kustajaabisha, watu walidondoka kuelekea kule ambako nilipaogopa zaidi; vijana, wazee na watoto, wote wake kwa waume walidondoka. Kuna wakati alidondoka mtoto na kumuacha mzee ambaye alijikongoja kwa taabu
kuelekea mbele. Kuna wakati alidondoka mzee na kuwaacha watoto ambao walijiegemeza kwake, hali iliyowafanya watoto wapepesuke kwa muda kabla ya kukaa tena sawa na kuna wakati ilishindikana wakadondoka. Wengine walidondoka ghafla wakiwa wenye nguvu na afya, wengine walisukumwa na wenzao kwa sababu mbalimbali, hii ilinifanya nitambue ukatili wa binadamu kwa binadamu wenzao. CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wapo pia waliojidondosha kwa madhira ya safari. Watu walidondoka usiku na mchana bila kujua ni nani atakayefuata hali iliyowafanya watu wote safarini kuwa na hofu.
Niliambiwa kuwa njia hii imepitwa na wengi na wote wameishuhudia hali hii kwa kipindi chote cha safari yao. Njia haijawahi kukatika bali ni watu wadondokao. Wamedondoka mamilioni na bado mamilioni wako safarini. Wakati wengine wanadondoka wengine huibuka na kujiunga na safari. Kila mmoja alitembea kwa mtindo anaoujua ama baada ya kuiga toka kwa wengine au baada ya kubuni mtindo wake ambao nao uliigwa na wachache waliovutiwa.
Safari hii ilianzia wapi hilo silijui na ilianza anzaje hilo pia sijui. Kwa uchache wa hatua nilizopiga safarini nimeshuhudia mengi ya kufurahisha na kuhuzunisha. Nimekuwa na marafiki lakini maadui pia hawakukosa. Wapo walionifanya niifurahie safari na wapo pia walionifanya niichukie, wote na waombea mema na wepesi katika hatua za miguu yao.
Ukiniuliza nimetembea umbali gani na nimebakiza umbali gani sitoweza kukujibu. Nahisi nimechoka kwa umbali niliotembea, nimeshuhudia misiba na furaha ya safari lakini kiu yangu bado haijakatika. Macho hayaoni tena mbele, mikono haina nguvu ya kushikilia na miguu nayo inatetemeka kwa machovu ya safari. Mapigo ya moyo yalipungua kasi kadri muda ulivyozidi kwenda na midomo ilikosa uwezo wa kulumba wakati nina mengi ya kuongea. Watu wa karibu yangu walionekana kuwa na huzuni walioshindwa kujizuia walibubujikwa na machozi. Walijitahidi kunilisha lakini chakula hakikupata kuzigusa nyama laini za koo langu. Walinisemesha lakini sikuweza kuwajibu. Dalili zilikuwa wazi kuwa naelekea kudondoka, taratiibu nilidondoka na kuwaacha mbali pamoja na jitihada zao za kunishikilia ili nisidondoke.
Hali ya kuwashuhudia watu wakidondoka imekuwapo kwa miaka mingi lakini imeshindwa kuzoeleka kabisa, ndiyo maana hata nilipodondoka hawakuweza kujizuia kwa machozi ya huzuni na simanzi.
Nilidondoka na hakuna kilichoweza kuubadili ukweli kuwa nilikuwa nimedondoka kutoka kwenye ile njia nyembamba yenye upana wa nywele mbili zilizounganishwa kwa pamoja na urefu usiojulikana. Nilikuwa nikipiga ukelele kwa woga lakini sikuwa na hakika kama kuna yeyote aliyeweza kunisikia kwa kelele zile, ambazo zilifuatiwa na mwangwi uliojirudia mara nyinginyingi na kuufanya uwoga wangu uongezeke maradufu, katika utupu wenye giza ambalo siwezi kulifananisha na chochote nilichowahi kukiona.
Ilinichukuwa muda mrefu bila kufika kwenye kitako cha shimo lile, nilihisi labda nitadondoka kwenye jiwe kubwa na kupasuka vipandevipande na kuna wakati nilihisi nitadondoka kwenye kitu chenye ncha kali na kunichoma vibaya au kwenye moto mkali na kuungua mpaka hatua ya mwisho. Nilipoyafikiria yote haya nilikata tamaa nikanyamaza na kuacha lolote litokee kwa sababu sikuwa na jinsi. Niliendelea kushuka kuelekea chini kwa muda mrefu na mara ghafla nilishangaa kwa yale niliyoyashuhudia.
Nilijikuta nimesimama mahali ambapo sikupafahamu. Mahali pale palikuwa na uzuri wa kustajaabia, maua mazuri yenye rangi za kupendeza, majani yenye rangi ya kijani kibichi yaliweza kuvutia kila jicho lililo na uono. Miti iliyo na matunda ambayo kwa macho tu yalionekana ni matamu ajabu.
Wanyama wa kila aina walionekana wenye furaha. Niliwaona simba wakicheza na swala, chui akinywa maji na watoto wa pundamilia.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Duma, nyati na nyumbu walikuwa karibu na mtu aliyeonekana akiwarushia maji kwa furaha. Nilipogeuka upande mwingine nilimuona mtu akiwa amejiegemeza kwenye mgongo wa kiboko akiwashuhudia nyoka watatu waliokuwa wakicheza na vinyonga na vyura kwenye uvungu wa tembo ambaye alionekana hana wasiwasi. Kila nilichokiona kilikuwa ni cha kustajaabisha.
Wakati bado naendelea kushangaa nilihisi kuguswa na kitu mwilini mwangu, nilipogeuka nilikutana uso kwa uso na simba dume aliyenawiri barabara, mwenye misuri iliyoshiba, cha kushangaza ni kwamba sikupatwa na woga hata kidogo, simba Yule aliondoka na kuniacha nikiwa nimeduwaa.
Nilipata shauku ya kutembeatembea ili nipate kuyafaidi mandhari yale ya kuvutia, nilizungukia maeneo yale huku nikiyaruhusu macho yangu kuvinjari kila yalipotaka. Kwa mbali nilimuona mtu aliyevalia mavazi ya kupendeza, nilitamani kuwa karibu yake japo nimsemeshe, ghafla nikajikuta niko mbele yake.
Mavazi yake yalikuwa ni meupe yasiyo na hata chembe ya doa, uso wake ulikuwa na mvuto japo ilionyesha wazi kuwa aliachana na ujana miaka mingi iliyopita.
Wakati bado naendelea kumshangaa mara ghafla akatabasamu na kuongeza tabasamu zaidi usoni mwake, hali iliyonifanya nimtazame zaidi. Kwa upole na unyenyekevu alifungua mdomo wake na kuanza kusema:
“Hapa ndipo watu waishipo milele, popote tofauti na hapa huwa ni pa mapito tu. Makazi ya milele yako hapa. Wewe ni mmoja kati ya mazao ya nyonga zangu, tangu mimi mpaka wewe ni vizazi kumi na nne. Nilikuwako utokako miaka mingi iliyopita, wakati ambao watu walizikwa kwa sanda nyeusi. Riziki yetu ya siku ilipatikana mawindoni na hatukuwinda tena mpaka machweo mengine.
Baadaye kidogo harakati zetu zilitupeleka mpaka kwenye uhifadhi wa akiba, na mapumziko yetu yakaanzia pale.
Mgawanyo wa majukumu ukaibua taaluma mbalimbali, waliibuka wafugaji, wakulima wa zana duni ambao waliwezesha kuwepo chochote ghalani, wafinyanzi, wasusi, wahunzi na washairi kwa ajili kuhimiza uchapaji kazi na kuburudisha wenye machovu ya kazi tangu machweo mpaka mawio.
Nikawa mpiga zumali stadi kuunogesha ushairi wa wakati ule. Kaka yangu alipiga marimba na mdogo wetu wa mwisho alipuliza pembe iliyotoa mlio wa kuvutia.
Familia nzima ilifaa kwa ushairi. Baadye baba akagundua zeze ambalo lilipigwa sambamba na vyombo vingine. Sauti nzuri ya mama ilipenya katikati ya sauti za vyombo na kuyafanya mashairi yake yenye kuadibu yapenye kwenye ngoma za masikio ya kila aliye karibu. Watu walizoea kusema sauti yake yafaa hata bila vyombo na wengine wakasema wanapenda kumsikia akiimba bila vyombo.
Baada ya mavuno burudani ilitawala kijiji kizima watu wakila na kunywa kwa pamoja. Maisha yalifurahiwa na kila mtu, kila kilichopatikana kilikuwa ni cha wote. Maisha yaliendelea hivyo mpaka pale misamiati mipya ilipoingizwa kwenye lugha yetu, miasmiati ambayo haikuwapo hapo awali.
Neno ubinafsi liliibua tabu inayowakumba walimwengu mpaka leo hii. Neno hili pia lilileta misamiati ambayo ni muendelezo wa chungu ya maisha.
Maisha katika mfumo wa uchumi wenye masoko na bei ya bidhaa ni magumu sana kama huna pesa ambayo ndiyo njia kuu ya mabadilishano. Hali hii imesababisha utengano kwa wanajamii wa jamii moja. Yote haya ni matokeo ya ubinafsi wa wasaliti wachache, walioaminiwa na kupewa dhamana kama viongozi wa jamii.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa muda wote huo nilikuwa kimya nikimsikiliza. Alimeza funda la mate kisha akaendelea:
Kuna siku yalitokea mafuriko yaliyoleta maafa makubwa ambayo mpaka leo husimuliwa ulimwenguni.
Niliponea chupuchupu kwenye gogo lililokuwa likielea juu ya vilindi vya maji, ndugu zangu walikufa wote na nikawa nimebaki peke yangu kwenye familia yetu. Hakuna kilichosalia zaidi ya zumari niliyokuwa nimeining’iniza kifuani baada ya kuifunga kwa kamba. Niliikung’uta maji na kuanza kuipiga, niliipiga kwa muda mrefu, niliipiga tena na tena kila nilipowakumbuka ndugu zangu. Niliipiga kwa huzuni kubwa na kwa sababu ya utupu na ukimya uliokuwepo mlio wa zumari ulifuatiwa na mwangwi ambao husikika mpaka leo duniani kwa wajukuu zangu walio katika upweke na woga. Wewe pia uliusikia ulipokuwa katika hali niliyoisema.
Gogo lilielea, lilielea, likaelea kwa muda mrefu mpaka nikapoteza matumaini ya wokovu, Niliipigaa tena zumari yangu nikijua kua ndiyo naipiga kwa mara ya mwisho. Kwa bahati nzuri niliokolewa na wavuvi ambo walinichukuwa mpaka maskani yao, nikawa nachunga mifugo yao hadi waliponiozesha nami nikaanzisha familia yangu, ambayo imepokezana nyakati mpaka kufikia wewe. Alisema yule mtu.
Niliendelea kumsikiliza kwa makini kwa kila neno aliloongea. Nilitaka kuzungumza kitu lakini aliniwahi kwa kusema, siruhusiwi kuzungumza chochote mpaka nikae mahali hapa kwa karne nne, nilikaa kimya na yeye akaendelea kesema:
Hapa wapo watu wote mashuhuri waliokuwako ulimwenguni kabla yako. Wapo pia waliokuwako huko katika wakati wako. Hata wale ambao mambo yao hayakutosha kuwafanya mashuhuri ulimwenguni wapo mahali hapa wakiyafurahia maisha kama walivyo wengine. Wapo viongozi wa nchi mbalimbali za ulimwengu, waliowahi kutawala katika wakati wao. Wapo washairi maarufu na mashujaa waliovuma enzi zao. Wasomi na wanafalsafa nao wapo.
Wapo ambao wanaonjeshwa furaha ya maisha ambayo walistahili kuipata milele yote. Lakini kwa uovu wa matendo yao watahamishiwa wanakostahili kuwa baada ya muda kuwa umefika.
Wakati anaendelea kuongea ghafla tulijikuta tunaelea angani tukielekea mahali Fulani, wakati tukiwa angani alionesha sehemu iliyokuwa na uji wa moto uliokuwa ukitokota kwa joto kali. Yule mtu aliyedai kuwa ni babu yangu wa zamani aliendelea kunieleza kuwa:
Chochote kinachoukaribia moto ule huyeyuka kwa sababu ya joto kali lililoko mahali pale. Vyote huyeyuka na kuchanganyikana na moto isipokuwa binadamu ambao huungua bila kuisha ili kufidia maouvu yao walipokuwa ulimwenguni.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mara ghafla nilijikuta tuko mahali tulipokuwa awali na mtu Yule. Alinitembeza sehemu zote zenye kuvutia na nikatamani niwe pale maisha yangu yote. Lakini alinigundua toka mawazoni kwa kusema
Imebaki muda kidogo sana kutimia karne nne, ambazo zingetosha kukufanya unyanyue midomo yako na kuanza kulumba, mafunzo yako ya hekima na utii uliyoyapata kwa kuona, kusikia na kuiga yamekukaa vema lakini huna budi kurudi duniani kwa maana unasubiriwa.
Mwanadamu ni mwepesi sana wa kukata tamaa na hapo alipo ameanza kupoteza imani juu ya kile alichokiamini. Wakumbushe na uwahimize kufuata mitaala kumi ya maisha ambayo kwa kiasi kikubwa wameipuuza. Waambie kuwa mitaala hiyo ndiyo njia pekee itakayowafanya kuhitimu vema safari ya maisha ya ulimwenguni.
Nilishtuka ghafla kutoka usingizini nikajikuta niko chini ya mti mkubwa uliokuwa katikati ya miti miwili na kufanya idadi ya miti ile kuwa mitatu. Hapo ndiyo nikabaini nilikuwa ndotoni.
Niliinuka na kusimama nikanyoosha viungo vya mwili wangu kisha nikatembea umbali wa kilomita zipatazo tano hivi, nikayakuta maji kisimani. Nilishusha begi langu na kuliweka pembeni kisha kwa viganja vyangu nikachota maji na kusafisha uso wangu. Maji mengine niliyatia kinywani nikasukutua na kuyatema pembeni. Niliruhusu kiasi Fulani cha maji kiingie tumboni mwangu.
Baada ya kufanya yote hayo nilichukua begi langu na kuliweka vema mgongoni kama ilivyokuwa awali, halafu nikaendelea na safari yangu.
Nilitembea kwa umbali mrefu nikiyapita mabonde na nyika, misitu ya kutisha pamoja na vikwazo vingi nilivyovivuka kwa taabu kubwa.
Wakati jua lianaelekea kuzama nilikata shauri ya kujipumzisha kwenye mwamba mkubwa ili nisubiri asubuhi ifike niendelee na safari na mara kwa mbali niliwaona watu wakija mahali nilipokuwa. Walipofika mahali nilipo walinisabahi na kujitambulisha kuwa mmoja kati yao ni shehe na mwingine ni kasisi.
Walisema kuwa wamo kazini wakiwaandaa wana na binti za binti za Mungu kwa maisha ya uzima wa milele. Kuwarudisha waliopotea na kuimarisha imani ya wale ambao bado wamo kundini. Wakati kasisi akiniambia nibatizwe, Shehe aliniambia nisilimu.
Nikawauliza:“Mbona mwanichanganya?
Mmeniambia kuwa mmo kazini kuwaandaa wana na binti za Mungu kwa maisha ya uzima wa milele. Sasa tena mwaniambia kubatizwa na kusilimu mna maana gani?
Kasisi alianza kwa kusema:
“Biblia niliyo nayo inaniambia kuwa, aaminiye na kubatizwa ataokoka.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Halafu Shehe akafuatia kwa kusema:
“Kuruani inaniambia kuwa, ukimkiri mwenyezi Mungu Kwa kusema; hakuna Mola apasaye kuabudiwa na kutukuzwa isipokuwa Allah.
Akili yangu ilizidi kuchanganyikiwa zaidi baada ya kusikia maneno hayo, nilihisi kama ubongo wangu umegeuka chini- juu na kunifanya nisielewe chochote, hali iliyonilazimu kutaka kuhoji zaidi juu ya yale niliyoyasikia. Ili kupata mwanga niliuliza maswali ya mjumuisho kama ifuatavyo;
Wote mnakubaliana kuwa kuna uzima wa milele?
Kwa pamoja walijibu ndiyo.
Mungu mnayemzungumzia ndiye huyo huyo mmoja?
Jibu la safari hii halikupishana na lile lililotolewa awali. Akilini mwangu niliwaza kuwa watu hawa mbona ni wamoja, na kama hali iko hivyo tofauti yao iko wapi?
Nilikumbuka kuna mtu aliwahi kuniambia kuwa:
Dini ni mfumo wa maisha ya kiroho yanayomuunganisha mwanadamu na mamlaka iliyo juu ya mamlaka zote, kwa imani.
Baada ya kumbukumbu hizo nikarejea kwenye majibu yaliyotolewa na Kasisi pamoja na Shehe. Nilibaini kuwa, wote wanatambua uwepo wa mamlaka hiyo kwa imani.
Ila tofauti baina yao ipo katika mifumo ya maisha waliyonayo. Kwa kawaida mazingira huathiri maisha ya mwanadamu kwa kiasi kikubwa, hivyo hapana shaka kuwa, tofauti iliyopo baina ya watu hawa imetokana na dini zao kuibukia katika maeneo tofauti na hivyo kufanya tofauti kubwa katika mifumo yao ya maisha na njia za uendeshaji wa ibada.
Tulizungumza mengi na usiku ulipozidi kuwa mkubwa, walifanya ibada kwa namna tofauti kila mmoja kabla ya kulala. Mimi nikasema tu Mungu nakuomba unilinde, nakuomba uniongoze kisha nikalala pembeni yao.
Asubuhi ilipofika walifanya tena ibada, mara tu baada ya kuamka. Baada ya ibada shehe alinipa kitabu cha kuruani chenye maandishi ya kiarabu na tafsiri ya Kiswahili, na kasisi alinipa biblia iliyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili. Tuliagana kwa kutakiana kheri kisha nikaondoka, nikawaacha nao wakijiandaa kuondoka.
Safari yangu ilinipitisha katika misitu na nyika, nikiwa peke yangu katika upweke mwingi. Mawazo na fikra juu ya yote niliyokutana nayo yaliniganda kama luba. Jua lilichoma na kupoa, liliwaka na kupoa tena nikiwa bado safarini na hatimaye lilizama nikiwa katika msitu mnene. Sauti za kutisha zilisikika kila upande na kwa sababu ya giza totoro sikuweza kuona chochote, iliogofya sana. Kwa ghafla ulitokea mwanga mkali kama wa mwanga wa radi, uliofanya kila kitu msituni kionekane bayana. CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mbele yangu kulikuwa na mto uliokuwa ukitiririsha maji, nikayaona na mawe yaliyokuwa mtoni mule, ghafla mwanga ulitoweka na giza likatawala tena kama ilivyokuwa awali. Kumbukumbu za mikao ya mawe kwenye mto ule zilinipa moyo kuwa nitafika ng’ambo ya mto kwa kukanyaga juu ya mawe yale.
Wakati nanyoosha mguu kukanyaga juu ya jiwe kwa mbali nikausikia mlio wa zumari, nikaurudisha mguu wangu, kwa muda wote huo sauti ya ule mlio wa zumari ikaongezeka na kusikika kwa karibu zaidi, nikanyoosha tena mguu ambao ulitua sawia kwenye jiwe mtoni, nikavuta na mguu wa pili na yote ikawa
imesimama juu ya jiwe. Nikanyoosha tena mguu ili kukanyaga jiwe nililoliona wakati ule mwanga ukimulika, mguu wa kwanza ulikanyaga barabara juu ya jiwe na ule mwingine ukiwa bado umekanyaga kwenye jiwe nililo kanyaga kwa mara ya kwanza.
Wakati miguu yangu yote miwili ikiwa imekanyaga juu ya mawe mawili tofauti, zumari iliendelesa kusikika na wakati huu zilianza kusikika na sauti nyingine ambazo nilipata kuzitambua kuwa ni sauti ya zeze, marimba, na pembe ilipulizwa ikitoa sauti nzuri kuliko tarumbeta.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment