Simulizi : Msafiri Safarini
Sehemu Ya Nne (4)
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mchanganyiko wa sauti hizi zilizokuwa na ustadi uliotukuka zilianza kunifanya niwe muoga zaidi. Sauti nyingine ilisikika ikiimba, ilikuwa na sauti nzuri yenye kuvutia ikiimba wimbo uliokuwa na maneno yasemayo:
Leo waishi kama mpotevu,
Mvua na jua vyote vyako. Jipe moyo utashinda, Japo kila ucho ni afadhali ya jana.
Waishi katika mateso, Kwa matabaka yaliyopo. Saa ya ukombozi itafika, Na haya yote yatakwisha. Furaha itakuwa nawe tena, Na huzuni kwako itakoma.
Maneno yale yalipenya ipasavyo kwenye ngoma za masikio yangu, yaliingia ubongoni mwangu na kunichanganya kiasi cha kunifanya nisahau niko wapi.
Nilijaribu kuuvuta mguu wangu wa kushoto ili ukanyage mahali ulipo ule wa kulia, wakati nakanyaga juu ya jiwe ulipo mguu wa kulia nikateleza na kutumbukia kwenye mto ulokuwa ukitiririsha maji kwa kasi. Nilisombwa na yale maji yatiririkayo kuelekea nisikokujua. Kasi ya maji iliongezeka zaidi kadri muda ulivyozidi kusonga mbele.
Nilifanya kila lilowezekana ili kuhakikisha naokoka. Harakati za kujiokoa zilififisha kabisa sauti nilizozisikia hapo awali na hatimaye kutokomea kabisa. Nilitapatapa huku na kule ili kujiokoa lakini jitihada zangu zote zilionekana kugonga mwamba waziwazi. Nilimeza maji mengi na hatimaye nikaishiwa kabisa nguvu.
Matumaini ya wokovu hayakuwa pamoja nami tena kwa wakati ule, nikaanza kuona giza na baadaye sikujua nini kiliendelea.
Watabiri na wanajimu wamedai kuwa mrithi wa zumari hayuko mbali na mahali hapa. Waganga pia hawako mbali na madai ya wanajimu na watabiri.
Lakini cha kushangaza madai yao hayaonekani kutimia. Imepita miongo mingi tangu wayaseme maneno yao, uzee unanielemea na mrithi wa zumari hajaonekana.
Nilifanaya mkutano mkubwa kwa kuwaita wana wa nchi yangu wote wake kwa waume na nikasema yeyote mwenye uwezo wa kupiga zumari aje na aipige zumari hii. Walikuja mamia kwa maelfu na asipatikane hata mmoja aliyefaulu kuipiga zumali kwa ustadi unaotakikana, jambo liloashiria kuwa hakuna msairi katika nchi yangu.
Kauli za watabiri, wanajimu, wachawi na waganga zilinipa matumaini kuwa nchi yangu imo mbioni kupata mshairi atakayeweza kuipiga zumali kwa ustadi unaotakikana. Lakini kwa sababu umepita muda mrefu bila maneno yao kutimia, naaamuru watu hawa wauwawe kwa kuwa ni waongo na wazushi na kama mjuavyo, kwa desturi ya nchi yetu na kwa kuheshimu mila na desturi tulizoachiwa na wazee wetu.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mimi mfalme wa nchi hii naamuru wauwawe kwa sababu uongo na uzushi ni mwiko katika nchi yetu. Na kwa kuanza waganga na wachawi wa nchii hii watauwawa na hii ni pamoja na kupiga marufuku shughuli zozote za kichawi na kiganga katika nchi hii na miaka miwili baadaye kama mrithi wa zumari hatatia mguu wake mahali hapa watabiri na wanajimu watauwawa na shughuli zao zitapigwa marufuku katika ardhi ya baba yangu. Juma moja baada ya mfalme kusema maneno yake wachawi na waganga wote wa nchi ya Pole waliuwawa.
**************
Hofu ilijengeka mioyoni mwa watabiri na wanajimu, walijua wazi kuwa maisha yao chini ya jua hayangezidi miaka miwili kama mrithi wa zumari anayesubiriwa hatafika katika nchi ya Pole kwa muda uliopagwa na mfalme. Walifanya vikao vya siri wakijaribu kubadilishana mawazo juu ya nini cha kufanya.
Na hatimaye walifikia mwafaka kuwa, wateuliwe wawili miongoni mwao ili waende kule walikohisi kuwa mrithi wa zumali angetokea, kwa kudhani kuwa yawezekana amefikwa na matatizo kabla ya kufika katika ardhi ya Pole. Kwa upande wa watabiri aliteuliwa Maneno na upande wa wanajimu aliteuliwa Mnadi.
Lakini kabla ya kuondoka Pole iliwabidi wapate idhini kutoka kwa mfalme, ambaye aliwapa ruhusa lakini pamoja nao waende walinzi watiifu watano kutoka katika safu ya ulinzi wa mfalme, ambao wangeyamaliza maisha yao mara baada ya muda waliopewa na mfalme kutimia kama mrithi wa Zumari hajaingia Pole.
******
Asubuhi na mapema siku iliyofuata, safari ya watu saba kuelekea upande wa magharibi ilianza. Njiani Mnadi na Maneno walikuwa kimya wakitafakari namna maisha yao yatakavyomalizwa kama hawatompata mrithi wa zumari. Walinzi walikuwa wakisimuliana habari za vita na mauaji waliyowahi kuyafanya, hali iliyoongeza hofu kwa Maneno na Mnadi.
Safari iliwachukua mpaka kilele cha mlima Nyamang’uta ambako walipanga kupumzika mpaka usiku utakapokwisha. Nyamang’uta ulikuwa ni mlima pekee wenye kilele chenye tambarare na miti ya kuvutia, pia kwenye kilele cha mlima huo kulikuwa na kisima chenye maji mazuri ambayo watu huyatumia kwa shughuli za matambiko.
Pembeni ya kisima kulikuwa na mitungi mikubwa mitatu ambayo watu hudai kuwa imewekwa kama kumbukumbu ya kuwakumbuka wake watatu wa mfalme wa kwanza wa nchi ya Pole waliopotelea mahali hapo wakati wanafanya tambiko la uzazi.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Miongoni mwa walinzi watano alikuwapo Jahili aliyesifika kwa ukatili na baadhi ya watu hudai kuwa akitoa upanga alani haurudi bila damu. Mlimani Jahili aliupiga teke mtungi uliokuwa mashariki, ukapasuka vipandevipande na maji yalipomrukia akapotea na kisha mtungi ukarudi katika hali ya kawaida kama ulivyokuwa awali. Kila mtu alibaki ameshangaa na woga ukawaingia, mioyo yao iliwadunda kwa kasi hali iliyodhihirisha uoga walionao.
Mpekuzi ambaye ni rafiki wa karibu wa Jahili aliushika mkuki wake barabara na kuanza kuusogelea ule mtungi kwa ujasiri usioelezeka, alipofika aliupiga teke na mara mguu wake ukawa mfupi, Mpekuzi alipiga kelele kwa uchungu kwa maumivu makali aliyoyapata mguuni baada ya kuupiga ule mtungi teke na kilio kiliongezeka zaidi baada ya kujigundua kuwa mguu wake umekuwa mfupi.
Wote walistaajabu huku nafsi zao zikigubikwa na woga zaidi. Askari waliobaki wakaanza kurudi nyuma, Mnadi akamfuata Mpekuzi, akamshika mkono na kuanza kuondoka nae huku akichechemea. Maneno ambaye kwa muda wote alikuwa kimya wakati haya yote yakiendelea, alifungua kinywa na kusema:
Mahali hapa si salama tena kwa sisi kuendelea kukaa. Matendo yetu hayakuwafurahisha wapenda amani wa mahali hapa, yatupasa tuondoke, tena haraka iwezekanavyo.
Wote sita wakaanza safari ya kuteremka mlima kuelekea chini ambako wangeweza kupumzika. Walifika na kujipumzisha chini ya mti mkubwa. Askari wale walikuwa kimya kila mmoja akiwaza kwa namna yake, ni sauti ya Mpekuzi tu ndiyo iliweza kusikika akililia mguu wake ambao kwa sasa ulikuwa mfupi. Mnadi aliuvunja ukimya kwa kusema:
Kweli nimeamini msitari utenganishao kifo na uhai ni mwembamba kuliko unywele! Unaweza ukauvuka ndani ya muda mfupi na ukajikuta upande wapili.
Maneno akauliza:
Unataka kusema kuwa Jahili ameshakufa?
Kama kufa ni kutokuwako, basi nilichokisema kina usahihi. Alijibu Mnadi.
Maneno alionyesha wazi kuwa yumo masikitikoni, kwa unyonge alifungua kinywa na kusema:
“Maisha ya mwanadamu huisha kama mzaha! Mwanadamu huanza kufa tangu ile siku alipoianza safari yake ya maisha, mtu hafi ghafla kama wengi wadhanivyo. Mwanadamu hana tofauti na donge la barafu ambalo limewekwa kwenye jua kali na kuyeyuka polepole mpaka lifikapo hatua ya mwisho.
"Sipingani na kauli yako unaposema kuwa, msitari uliopo baina ya uhai na kifo ni mwembamba kuliko unywele. Hii inatokana na ukweli kuwa, kuna wakati msitari huo ulikuwa mnene lakini kwa sababu ya kulika polepole msitari huwa mwembamba na kufikia hatua ya kuvukwa kwa urahisi.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa mujibu wa wakati, ilionyesha kuwa ni usiku, lakini hakuonekana hata mmoja mwenye dalili ya usingizi. Wote walikaa kwa kuuzunguka moto ambao ulikuwa katikati yao. Waliongea mengi ya kusikitisha na kufurahisha ingawaje hakikusikika kicheko wala kuonekana tabasamu, ila kwa muonekano wa nyuso zao walikuwa ni wenye wasiwasi mwingi. Nadhani hapo utakubaliana na mimi kuwa kuwa kicheko hakitoshi kuashiria furaha na tabasamu pia halifui dafu, huu ni ubatili mwingine katika maisha ya mwanadamu.
Mazungumzo baina yao yaliendelea mpaka mapambazuko yalipofika, baada ya maandalizi walichukua mizigo yao na kuendelea na safari yao.
Walichojua kuhusu safari yao ni lengo pamoja na uelekeo ambao ulikuwa ni magharibi, lakini hakuna hata mmoja aliyejua kuwa safari yao ingeishia wapi.
Jua liliwaka mpaka likazama wakiwa safarini. Milima, mabonde pamoja na misitu minene iliongeza uzito wa safari yao. Hofu miongoni mwao ilizidi kuzivuruga mbongo zao na kuna wakati walijikuta wakitembea kutwa nzima bila kuzungumza neno baina yao. Kila mmoja alikuwa kimya akitafakari juu ya hatma ya maisha yake. Chakula kilichopatikana ndicho kilicholiwa, hata kama hakikuupendeza moyo. Iliwabidi kufanya hivyo ili kupunguza makali ya njaa kali waliyokuwa nayo.
Nilishtuka usingizini na kujikuta nimelala kwenye ngozi ambayo bila shaka ilikuwa ni ya simba. Nilijiuliza ni wapi mahali hapa, lakini jibu halikupatikana kwa urahisi. Kwenye ukuta wa nyumba palitundikwa ngozi za wanyama mbalimbali wa porini. Pembeni yangu kulikuwa na Shaibu amevaa shanga nyingi mabegani na nyingine amezivaa kichwani, na mwilini alikuwa ameivaa ngozi ya chui.
Shaibu alionekana wazi kuwa yumo pirikani akiandaa kitu ambacho baadaye nilibaini kuwa ni dawa. Nilifumbua macho ili niweze kuona kwa umakini zaidi, pembeni ya yule shaibu kulikuwa na makopo na vibuyu vingi ambavyo vilionekana kuanguka kwa sababu ya utupu.
Yule shaibu aliniangalia kisha akatabasamu, akaja karibu yangu na kunipa maji meusi yaliyokuwa ndani ya chombo ambacho bila shaka ni kibuyu kilichokatwa nusu, akaniambia kunywa. Bila pingamizi nikafanya kama alivyoniagiza japo kwa taabu sana kwa sababu ya uchungu wa maji yale. Nilijitahidi kuyanywa na nilipomaliza nikamkabidhi chombo chake, alikipokea kisha akakaa kitako kwenye kigoda na kuanza kuongea maneno yafuatayo:
Nilikukuta pembezoni mwa mto umelala hujitambui, nikakuchukua na kukuleta mahali hapa kwa ajili ya tiba. Kwa kuwa unaendelea vizuri, utapumzika kwa muda zaidi kabla ya kuondoka na kuelekea uendako. Mizimu haina shida na wewe, ndiyo maana matibabu yako yalikuwa rahisi tofauti na wengine.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Niliinuka nikakaa kitako ili kumsikiliza maneno aliyokuwa akiyaongea. Alipomaliza aliondoka mule ndani na aliporudi alikuwa na chombo kama alichonipea dawa ambacho ndani yake mlikuwa na uji. Alinipa kile chombo na kuniambia ninywe ule uji, nilifanya kama alivyosema. Baada ya kumaliza ule uji nikampa chombo chake, alikiweka pembeni kisha akaniuliza:
Unakumbuka unapotoka na unapokwenda unapajua?
Swali hilo lilikuwa gumu sana kwangu, na huwa sipendi kulisikia kwa sababu majibu yake siyajui. Lakini kwa majibu rahisi nikamwambia:
Naelekea mbele nikitokea nyuma.
Huko nyuma ni mahali gani hasa na huko mbele ni mahali gani?
Kwa kusema ukweli sijui nitokako wala niendako, lakini huwa nahisi nalizunguka duara.
Duara gani? Lakini kabla hujajibu hili swali, unakumbuka nini kabla ya kujikuta mahali hapa?
Nakumbuka niliona mwanga ambao nahisi ni wa radi, pia nilisikia sauti nyinginyingi ikiwemo wimbo.
Hiyo ni mizimu yako ilikuwa ikijaribu kukulinda. Aliendelea kusema yule shaibu.
Una maana gani kusema mizimu yangu?
Mizimu yako ni babu zako waliokufa zamani. Alisema Yule Shaibu lakini ni wazi alizidi kinichanganya.
Iweje watu waliokufa zamani wanilinde mimi niliye hai?
Baada ya kumuuliza swali hilo aliniuliza swali jingine,
Nini maana ya kusema roho haifi?
Roho haifi? Inawezekanaje roho isife? Niliuliza.
Watu hufa miili yao, lakini roho zao hutoka na kwenda kuanza maisha mengine mapya ambayo kimsingi ni tofauti na haya tuishiyo.
Kwa hiyo unataka kusema kuwa, mizimu ni roho za watu waliokufa zamani?
Sawa kabisa.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa hiyo inawezekana kabisa kuwa, hata sisi ni mizimu?
Una maana gani?
Mantiki ya hoja yangu ni kuwa, yawezekana kabisa kuwa maisha yetu hayakuanzia katika hali ya ubinadamu kama wengi wajuavyo, hivyo basi, kuna hali tofauti ambayo tulikuwa nayo kabla ya kuwa katika hali ya ubinadamu kama tulivyo leo. Na kama ni hivyo, tulikufa ili kuondokana na hali tuliyokuwa nayo awali ili kua katika hali tuliyo nayo leo. Hivyo basi utakubaliana na mimi kuwa hata sisi ni mizimu tulioondokana na hali yetu ya awali na kuuvaa ubinadamu tulio nao.
“Labda!” Alijibu Shaibu.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment