Search This Blog

Wednesday, 1 June 2022

MSAFIRI SAFARINI - 5

 







    Simulizi : Msafiri Safarini

    Sehemu Ya Tano (5)







    Wakati tunaendelela na mzungumzo, kuna watu walikuja na kubisha hodi wakakaribishwa na kuingia ndani. Baada ya salamu walijitambulisha kwa kusema kuwa wao ni wasafiri na wanaomba hifadhi ya muda kabla ya kuendelea na safari yao siku inayofuata.

    Walipewa viti na kukaa sebuleni, kasha yule shaibu akaja chumbani na kuniambia nijumike nao pale



    sebuleni, nilifanya kama nilivyoagizwa. Nilipofika sebuleni tulisalimiana na wale wageni nilioelekezwa kujumuika nao pale sebuleni.



    Walikuwa ni wanaume watatu wa makamo ya kuitwa watu wazima. Watu hawa walisema wanapita kutoa taarifa ya msiba ukiotokea katika nchi ya Mlima, sanjari na utoaji wa taarifa ya msiba pia walidai wanaelekea nchi ya Pole kushughulikia uchapishwaji wa miswada ya vitbu iliyoandikwa na mwalimu ambaye amefariki katika nchi ya Mlima.



    Watu hawa walidai wananifahamu mimi, na walishawahi kuniona katika nchi ya Mlima miaka kadhaa iliyopita. Pia wakadai kuwa mafundisho ya mwalimu ambaye kwa sasa ni marehemu, yameleta mapinduzi makubwa katika uwanda wa elimu nchini Mlima. Mafundisho haya ya mwalimu pia yamesababisha nchi ya Mlima kuwa na idadi kubwa ya wasomi ukilinganisha na majirani zake, wasomi ambao hujadili mambo tele ikiwemo safari yangu ambayo imezua maswali mengi ambayo majibu yake bado yana wingi wa mashaka.



    Mmoja kati yao aliyejitambulisha kwa jina la Kasimu alisema kuwa:

    Safari yako imeipamba mijadala na mihadhara ya wasomi ndani ya MLIMA. Mwanzo na mwisho wa safari yako ndiyo unaonekana zaidi kuchanganya akili zao. Safari yako imewagawa watu katika makundi kwa majibu wanayoyatoa kuhusu safari yako.



    Kwa muda wote huo nilikuwa nimekaa kimya nikijaribu kuruhusu kila neno kupenya kwenye ngoma za masikio yangu ili niweze kujua wanamaanisha nini.



    Kasimu aliendelea kusema kuwa;

    Kuna kundi la wanasayansi ambao pia hujiita wanauhalisia, wao hudai kuwa wewe ni tone la manii na safari yako ilianzia kwenye chembe hai, ambayo iliungana na chembe hai zingine na kukufanya uwe kama ulivyo leo. Na huendelea kudai kuwa, mwisho wa safari yako ni kushindwa kwa chembe hai amabazo zimekufanya uwe kama ulivyo. Na safari yako haitakuwa na la ziada, baada ya kushindwa kwa chembe hai hizo zaidi ya kuoza na kutumika kama rutuba kwa viumbe wengine ambao bado wamo safarini.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alimeza funda la mate na kuendelea kusema;

    Kundi jingine la wasomi ambao huijadili safari yako ni wana dini, hawa huifasiri safari yako tofauti na wanasayansi kwa kusema kuwa, safari yako ilianzia kwenye udongo uliofinyangwa katika sura na umbo ulilo nalo, baada ya ufinyanzi, ule udongo ulipuliziwa pumzi ya uhai na huo ndiyo ukawa mwanzo wa safari yako.



    Wanaoamini katika mkondo huu wa fikra, wakaendelea kusema kuwa, mwisho wa safari yako ni kuondokewa na pumzi ya uhai uliyopuliziwa, pumzi hiyo itaondoka na kurudi mahali Fulani ambapo ni maalumu kwa ajili ya kuisubiria safari nyingine ambayo msingi wake ni safari yako ya mwanzo. Baada ya pumzi kuondoka udongo nao utarudi katika hali yake ya mwanzo kabla ya kufinyangwa katika umbo na sura uliyonayo!





    Kila neno lililosemwa lilipenya vyema katika masikio yangu na kufasiliwa ubongoni kwa kadiri ya uwezo. Nilijiuliza kwa nini safari yangu iwafikirishe sana watu kiasi cha kuwafanya wagawanyike katika makundi ambayo msingi wake ni kutokufanana kwa mawazo! Nilijiuliza maswali mengi sana lakini majibu yake ya kinadharia hayakunipa suluhisho zaidi ya kuongeza maswali zaidi. Nikajikuta nina msululu wa maswali ambao ulizaa maswali juu ya maswali zaidi.

    Nikiwa katika lindi hili la mawazo nilijitenga kabisa na wenzangu kwa kuwanyima usikivu bila kujua. Mara ghafla nikashtuliwa na Sauti ya Kasimu ikiniashiria kuwa mazungumzo bado yanaendelea.

    Nilijiweka sawa kisha nikampa tena usikivu kwa yale aliyokuwa Anayasema. Katika maongezi yake nilimsikia akisema;

    “Pamoja na maendeleo makubwa ya kimaisha yaliyoletwa kutokana na tafititi za kisayansi, ugunduzi kuhusu mwili wako bado haujafanyika vya kutosha! Na ndiyo maana safari yako ina ukomo. Yawezekana kuwa ugunduzi utakapokamilika, ukomo wa safari yako utabaki kuwa simulizi kwa vizazi vijavyo!

    Nilikuwa nikimfuatilia kwa makini kwa kila neno lililokuwa likimtoka kinywani mwake, ni wazi kuwa alikuwa akiongea vitu ambavyo vilinigusa moja kwa moja! Kwa uzamivu na nia ya dhati, Kasimu aliendelea kusherehesha:

    “ Lakini pamoja na hayo yote, ni lazima tukumbuke kuwa chembe hai ambayo ndiyo kiini cha safari yako haikutokea katika ombwe! Ni lazima kutakuwa na chanzo kilichoitangulia chembe hai, na kitu hicho chaweza kuwa ndiyo mwanzo wa yote na chembe hai ikiwemo. Lakini je, chanzo hicho hakina mwanzo?

    Na kama kina mwanzo basi hapana shaka kuwa mwanzo huo pia una chanzo! Ni wazi kuwa mtiririko huu unatupeleka katika mlolongo wa maswali usiokuwa na mwisho!”

    Hali hii inanifanya kukubali kuwa maisha ni msitari usio na mwisho katika umbo la duara! Swali tunaloweza kujiuliza ni je, tutajiuliza maswali kuhusu mwanzo na chanzo cha huo mwanzo mpaka lini? CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wanaoamini katika dini hudai kuwa, Mungu ndiye chanzo cha yote na yeye hakuanza wala hatakwisha kwa sababu yuko tangu milele yote! Kama njia ya kwanza haitupeleki kwenye jibu, basi hatuna budi kuifuata njia hii ya pili kwa sababu ndiyo yenye ushawishi zaidi ingawaje inahitaji moyo wenye imani na uliojaa woga katika mambo ya kiungu! Kama nayo haitatupeleka kwenye jibu basi milango ya fikra iachwe wazi kwa ajili ya njia nyingine zitakazotupa ukweli kuhusu safari.

    Kasimu alionekana wazi kuwa ni mweledi katika taaluma ambayo sikuweza kuitambua! Hii yote ianatokana na ujuzi mkubwa alio nao katika kueleza na kufafanua mambo. Kwa kubashiri nilijiaminisha kuwa yawezekana kuwa Kasimu ni mwalimu! Wakati naendelea kuwaza yote haya yeye alikuwa anaendelea kuongea, na maneno yalikuwa hivi:

    Katika miswada tunayokwenda kuichapisha, mwalimu ameandika kuwa;

    Lugha kama sehemu ya utamaduni wa watu haina budi kuheshimiwa, kwa sababu hakuna lugha iliyo bora kuliko nyingine na pia si busara kuipuuza lugha kwa uzembe au kwa kukusudia. Wasemaji wa lugha Fulani wanapaswa kujivunia lugha yao kama sehemu ya utamaduni wao kwa kuipa kipaumbele shughuli za kielimu na kiutawala. Lugha yoyote inafaa kwa matumizi yote, na kama kuna mapungufu katika misamiati kwa ajili kukidhi matakwa ya wasema lugha, wasemaji wa lugha husika hawana budi kubuni misamiati mipya au kukopa katika lugha nyingine kwa maana ndiyo tabia ya lugha.

    ***************

    Masaa yalienda kwa kasi huku yakisindikizwa na maongezi ya hapa na pale. Haikuwa rahisi kuamini kuwa jiono ilikuwa imeshafika na haukuwepo ukweli zaidi ya huo.

    Shaibu alikoka moto nje kasha akatuita tujumuike nae! Tulikaa kwa kuuzunguka moto ambao ulikuwa katikati yetu.

    “Nafikiri sasa ni wakati wa kuupa jina mkutano huu! Alisema shaibu akiwa katika sura iliyojaa furaha.

    “Mi nafikiri tuuite mkutano huu kikao cha jioni” niilitoa kauli hii nikwa katika hali ya kujiamini ingawa ilipingwa na Kasimu ambaye alipendekeza tuuite mkutano ule “KILINGE CHA HEKIMA” hakuna aliyebisha kwani wote tuliyaunga mkono mawazo yale na mkutano ule ukaitwa kilinge cha hekima kama ailivyopendekeza Kasimu

    Enhe! Ndugu Kasimu, uliniambia kuwa mnakwenda POLE kutoa taarifa za msiba pamoja na kuchapisha miswada ya vitabu. Alisema Shaibu katika sura iliyoonesha wazi kuwa ilikuwa ameshaanza kuzama katika kina kirefu cha fikra.

    “Ndiyo mkuu!

    “Unaweza kutueleza kuwa mliwezaje kufika hapa tulipo?

    “Tulikuja kwa kufuta njia. Njia iliyotupitisha katika milima, mabande, misitu na nyika! Kuna wakati njia ilitupotea mara tulipoufikia mkondo wa maji na hapo tukaendelea na safari kwa kufuata harufu ya utu kwa maana hatukuiona njia! Mara kadhaa baada ya kuumaliza mkondo wa maji tulikutana tena na njia na safari ikaendelea kwa kufuata njia na harufu ya utu.

    “Harufu ya utu?

    Ndiyo! Mbali na harufu hiyo ya utu pia tuliibaini harufu ya roho yenye utakatifu ndani yake! Alidakia Karimu ambaye alikuwa katika msafara wa Kasimu

    Pamoja na harufu hizo pia tuna kaitabu cha jiografia ambacho hutuongoza katika safari yetu! Alisema Kasimu

    “Hapana! Hicho hakiitwi kitabu cha jiografia, ni Insaiklopidia kwa sababu kina maarifa yote na jiografia ikiwemo! Alidakia Kumbuka ambaye pia ailikuwa ameongozana pamoja na kina Kassimu na KarimuCHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati hayo yakiendelea, mimi nilikuwa kimya nikifuatilia kwa makini mazungumzo yote,

    “Hicho kitabu kiko wapi? Aliuliza Shaibu na mara Kasimu akakitoa kitabu na kumkabidhi Shaibu.

    “Mbona kikubwa hivi, kimeandikwa na nani?

    “Uandishi wa kitabu hiki ulichukua mamilioni ya miaka mpaka kukamilika! Kimeandikwa na watu tofauti katika nyakati tofauti, baada ya kufunuliwa na mamlaka iliyo juu ya mamlaka zote. Ndani yake mna hadithi amabzo ndiyo msingi wa hadithi zinazosimuliwa na kuandikwa leo, mbali ya hadithi pia mna mashairi ambayo ndiyo msingi wa mashairi ya leo!

    Niliendelea kusikiliza kwa makini kila neno lililosemwa huku macho yangu yakiwa yamekodoka kwa kukiangalia kile kitabu. Wakati bado nakiangalia mara nikajikuta naongea,

    “Hata mimi pia ninacho kitabu kama hicho!

    “Kiko wapi? Kwa pamoja wote wane wakauliza

    Niliinuka na kwenda ndani, na haikupita muda mrefu nikawa nimerejea na vitabu mkononi na kuwakabidhi kimoja kati ya vitabu vile.

    “Ulikitowa wapi kitabu hiki? Shaibu aliuliza

    “Siku moja safarini nalikutana na watu wawili wenye matendo ya kustahili kuigwa. Kwa kuwa na wao walikuwa safarini nilijumika nao mahali pamoja katika mapumziko ya usiku. Kabla ya kulala tulizungumza mengi na wakanieleza adhma ya sfari yao, na asubuhi wakati tunaagana wakanipatia vitabu viwili na hicho kikiwemo. Na walinaimbia kuwa kinaitwa biblia!

    “Kingine kiko wapi? Kasimu aliuliza

    “Hiki hapa, na walisema kinaitwa kuruani.” Niliongea wakati namkabidhi kile kitabu kingine.

    “Kabla sijasahau, waliniambia kuwa mmoja kati yao ni sheikh na mwingine ni Kasisi”

    “Vitabu hivi vimeenea sana nchini MLIMA, watu huvisoma kwa bidii, hadithi na mashairi yake yamekuwa ni msingi wa maisha ya watu wa MLIMA. Na mitaala kumi iliyomo ndiyo mwongozo wa kila kitu” alisema kumbuka

    “kesho itakapofika tutaendelea na safari yetu kuelekea nchini POLE, ni muhimu kufika huko mapema, kwa sababu ni muhimu kuwafikishia taarifa za msiba wa Mwalimu mapema na machapisho ya vitabu hayana budi kufika MLIMA mapema ili kulisukuma mbele gurudumu la fikra zenye mantiki” aliongezea Karimu

    Mimi pia si mkaaji, itanibidi kesho kuendelea na safari yangu! Niliyasema maneno haya huku nikimuangalia Shaibu. Wakati namalizia kuongea, mara Kasimu akanitandika swali:

    “Kwani unaelekea wapi?

    Kwa jibu rahisi nikasema, “Magharibi”

    “ Huko Magharibi waenda kufanya nini?

    “nahisi huko ndiyo kuna ukweli! Kwa sababu mara zote wakati hunisukuma kuelekea huko! jua huchomoza kutoka Mashariki na kuzama Magharibi, sijui kama umewahi kujiuliza kwa nini mawio hufanyika huko?

    Wakati namalizia kuongea haya, wote walicheka sana! Tukafunga kile kilinge cha hekima na kwenda kulala.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    **********

    Asubuhi ilipofika, tulitoa shukrani zetu kwa Shaibu kutokana na wema na ukarimu wake, kisha tukamuga.

    “Nitakukumbuka sana kwa wema na ukaribu wako” Nilijikuta natamka maneno haya huku machozi yakinilengalenga.

    “msafirie ndani ya tumbo la tembo!” alisema Shaibu akimaanisha kututakia heri katika safari yetu.





    MWISHO





0 comments:

Post a Comment

Blog