Search This Blog

Wednesday, 1 June 2022

ONLY YOU ( NI WEWE TU ) - 1

 







    IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI



    *********************************************************************************



    Simulizi : Only You ( Ni wewe Tu )

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Daniel alikuwa chumbani kwake, kichwa chake kilikuwa kikifikiria maisha yake yaliyopita. Moyo wake ulimuuma kwa sababu ya maumivu makali ya mapenzi aliyokuwa ameyapitia.

    Wakati mwingine alimlaumu Mungu kwa kumpitisha katika maisha ya hayo ya mapenzi ambayo yaliwahi kumuumiza na kumliza kila siku. Alitoa machozi yake kwa ajili ya mapenzi, aliwalaumu watu wengine lakini pia wakati mwingine alithubutu kusema kwamba kamwe asingeweza kuingia katika uhusiano wa kimapenzi kwa sababu tu ya maumivu ambayo aliyapitia huko nyuma.

    Hapo chumbani alianza kumkumbuka msichana aliyeitwa kwa jina la Esta Fidel. Huyu alikuwa msichana mweupe, mrembo, mwembamba aliyekuwa na figa matata.

    Siku ya kwanza Daniel kumuona, alishtuka, akahisi kabisa moyo wake ukipata ganzi, mwili ukimtetemeka huku mapigo yake ya moyo yakienda kwa kasi kana kwamba moyo ulitaka kutoka mwilini mwake.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alitokea kumpenda Esta, haikujalisha kama ilikuwa siku ya kwanza kumuona machoni mwake au la. Hakujua tabia yake, hakujua maisha yake lakini akatokea kumpenda kwa moyo wake wa dhati.

    Hakutaka kumuacha msichana huyo, alichokifanya ni kujipanga na kumfuata. Alipomfikia, akaongea naye, walicheka na kuzoeana kwa muda mchache kana kwamba walikutana miaka mingi iliyopita.

    Wakabadilishana namba za simu na kuanza kuwasiliana. Hakutaka kuzificha hisia zake, aliamua kumwambia ukweli msichana huyo kwamba alimpenda na moyoni mwake hakukuwa na msichana yeyote yule zaidi yake.

    “Kweli?” aliuliza Esta.

    “Ndiyo! Ninakupenda sana! Ninakupenda zaidi ya neno lenyewe linavyomaanisha,” alisema huku akitoa tabasamu pana.

    Wakaingia kwenye uhusiano wa kimapenzi, yakawa motomoto kiasi kwamba kila mmoja akahisi kuwa hakukuwa na watu waliokuwa wakipendana kama wao.

    Kipindi hicho alikuwa akitarajia kuingia chuo, kwa jinsi alivyokuwa akiishi na Esta alihisi kama dunia nzima ilikuwa mikononi mwake na yeye ndiye alikuwa mtawala.

    Baada ya kukaa kwa miezi kadhaa, akagundua kwamba Esta hakuwa yule ambaye alikuwa akimfikiria, alikuwa msichana mwingine aliyekuwa na maisha ya kutisha nyuma ya pazia, msichana huyo ambaye alikuwa mzuri wa sura na umbo, hakuwa mwanafunzi kama alivyomwambia bali alikuwa changudoa ambaye kila siku alikuwa akiondoka usiku wa saa mbili na kurudi alfajiri.

    Siku ya kwanza Daniel alipoambiwa kuhusu msichana huyo, hakuamini, alihisi kama alikuwa akipewa habari ya uzushi, hakutaka kusubiri, alihitaji kuhakikisha kwa macho yake, akapanga safari katika hoteli ambayo msichana huyo alikuwa akifanya biashara yake, alipofika huko, akajihakikishia kwa macho yake kitu kilichomuuma sana.

    “Esta!” aliita huku akimwangalia msichana huyo ambaye hakuonekana kuhofia chochote kile.

    Alihisi kwamba angejificha lakini hali ilikuwa ni tofauti kabisa. Esta akatoa tabasamu na kumwambia kwamba amuache kwa muda kwani alikuwa ofisini kwake hivyo hakutaka kuharibu siku yake.

    Kwa Daniel yalikuwa maumivu makali, hakuamini kama yule msichana aliyekuwa akimpenda, akimjali angeweza kuwa mahali hapo. Aliamini kwamba alikuwa mtoto wa geti kali, aliyekuwa akilelewa na wazazi wake katika mazingira ya kidini kumbe haikuwa hivyo, yule Esta alikuwa mtu wa tofauti kabisa.

    Alihuzunika, alilia na kuumia mno moyoni mwake. Wakati mwingine mpaka alitamani kujiua. Alimpenda Esta, kwake, msichana huyo alikuwa kila kitu, alimthamini lakini yote hayo hayakuonekana kuwa kitu kwa Esta, alifanya mambo yake na kuendelea maisha yake.

    Hicho ndicho kipindi ambacho alijiahidi kwamba asingethubutu kuchukua msichana kutoka katika maisha ya juu, akajiahidi kwamba kamwe asingekuja kurudia kosa lake kwa kuwa lilimuumiza mno, alichokifanya ni kumtafuta msichana wa uswahili ambapo aliamini kwamba ingekuwa rahisi kwake kuwa katika uhusiano wenye furaha tele.

    Akampata msichana aliyeitwa Happy Michael aliyekuwa akiishi Mabibo. Kwa kumwangalia, Happy alikuwa msichana wa kipekee, uso wa aibu ambaye hakuweza kuyagandisha macho yake kuangaliana na mwanaume hata kwa sekunde tano.

    Alikutana na Happy katika kipindi alichokwenda kumtembelea rafiki yake katika Chuo cha Usafirishaji cha NIT kilichokuwa Mabibo.

    Alipomuona kwa mara ya kwanza, alimchukulia kuwa msichana wa kawaida lakini baada ya kuzoeana naye na kuzungumza sana, akaona kabisa msichana huyo akiwa wa tofauti na wengine.

    Alikuwa na sura ya aya, mrembo ambaye kila alipokuwa akitabsamu, vishimo viwili vilikuwa vikionekana mashavuni mwake. Wanaume wengi walimpenda lakini kwa jinsi alivyoonekana, hakukuwa na mwanaume yeyote yule aliyebahatika kuwa na msichana huyo.

    Daniel hakutaka kuvumilia, ilikuwa ni lazima kumwambia msichana huyo ukweli juu ya moyo wake kwamba ulikufa, ukaoza na hakuwa akijiweza kabisa.

    Hakutaka kukumbuka kuhusu Esta, hakutaka kuamini kama Happy angeweza kuwa msichana kama Esta, alihitaji kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na hivyo kumwambia ukweli msichana huyo jinsi alivyokuwa akimpenda.

    Happy alishtuka, akaangalia pembeni, aibu ilionekana usoni mwake kiasi kwamba alishindwa kabisa kumwangalia Daniel usoni. Aling’ata kidole chake, akaangalia chini huku akitoa kicheko cha chinichini.

    Daniel hakutaka kumuacha, akamshika na kumvuta pembeni kimahaba na kukaa naye sehemu. Mahali walipokaa ilikuwa ni sehemu ya kusomea, kigiza kilikuwa kimeingia na hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa akiwafuatilia mahali pale, kila mtu alionekana kuwa bize.

    “Ninakupenda sana Happy,” alisema Daniel huku akimwangalia Happy usoni, hakuishia kumwangalia, akaushika mkono wake na kuanza kuuminyaminya.

    Happy akahisi kama wadudu wakitembea mwilini mwake, mwili ukaanza kumsisimka na kujikuta akianza kutokwa na kijasho chembamba, mguso aliokuwa amepewa na Daniel ulikuwa tofauti kabisa.

    “Daniel!” alimuita kijana huyo.

    “Nipo hapa mpenzi! Unasemaje?”

    “Naomba uuachie mkono wangu jamaniiiiii!” alisema Happy huku akimtaka mwanaume huyo auachie mkono wake, ndiyo kwanza Daniel akamsogelea zaidi, akaupeleka mdomo wake shingoni mwa msichana huyo na kumbusu.

    “Mwaaaa...”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Jamaniiiiiiiiii!”

    “Happy! Ninahitaji kuwa nawe, ninahitaji niwe mwanaume pekee katika maisha yako ambaye atakufanya kuyafurahia mapenzi, nakuahidi kutokukuumiza, nitakufurahisha mpaka unaingia kaburini,” alisema Daniel huku akimwangalia msichana huyo.

    Happy hakuwa na jinsi, akajikuta akiingia na kuzama katika penzi la mwanaume huyo na hivyo kuanza uhusiano wa kimapenzi.

    Wakawa wapenzi, waliopenda na kushibana. Kila mmoja alimthamini mwenzake. Wakatambulishana mpaka kwa wazazi, wakawa karibu mno lakini baada ya miezi mitatu, penzi likaanza kuchuja.

    Daniel alianza kuziona dalili hizo mapema kabisa, Happy alibadilika, hakuwa kama yule aliyekuwa kipindi cha nyuma. Alipokuwa akimpigia simu, hakuwa akipokea na hata akimtumia meseji ilichelewa sana kujibiwa.

    Hakutaka kuona akimpoteza Happy, alichokifanya ni kufanya kila liwezekanalo kuliokoa penzi lake. Njia ambazo alizitumia hazikusaidia, msichana huyo hakuweza kubadilisha kitu chochote kile kwani tayari moyo wake ulianza kutekwa na mtu mwingine aliyekuwa akimpa mapenzi motomoto, mwisho wa siku penzi hilo likafa kabisa.

    Daniel aliumia kuliko alivyoumia kwa Esta. Kilio chake kilikuwa cha kuumiza kuliko kile kilichokuwa kwa Esta. Alijuta, alihitaji faraja kutoka kwa Happy baada ya kuachwa na Esta lakini badala ya kupata faraja, akaumia zaidi na zaidi.

    Hakutaka kukubali, alichokifanya ni kwenda katika chuo cha NIT kwa lengo la kumuona Happy na kuzungumza naye ili kama inawezekana penzi lifufuliwe lakini kitu cha kuumiza ni kwamba alizidi kuumia baada ya kufika huko na kumkuta msichana huyo akiwa na mwanaume wake mpya, yaani yale mapenzi yao ya kipindi cha kwanza yalihamishiwa kwa mwanaume huyo.

    “Happy! Why are you hurting me like this?” (Happy! Kwa nini unaniumiza kiasi hiki?) aliuliza kila alipokuwa akimwangalia happy, wakati mwingine machozi ya uchungu yalikuwa yakimtoka.

    Huo haukuwa mwisho wa kupenda, aliendelea kupenda huku akitafuta bahati yake, alihisi kwamba mbele ya safari angeweza kumpata msichana ambaye angeendana naye, msichana ambaye angempenda maisha yake yote na hatimaye kuoana.

    Aliwapata wengine wengi lakini wote hao walikuwa vilevile, walimuumiza mno moyoni mwake mpaka kujutia ni kwa sababu gani aliletwa katika dunia hii iliyokuwa na miba iliyochoma hisia za watu.

    Hayo yote yalikuwa ni mawazo, alikuwa akikumbuka namna alivyokuwa akipitia katika uhusiano wa kimapenzi ambayo yalimuumiza mno. Pale chumbani, kitandani alipokuwa hakuacha kutokwa na machozi, maisha yake ya nyuma yalimchoma kupita kawaida.

    Hakutaka kuendelea kubaki nyumbani, alichokifanya baada ya dakika kadhaa, akainuka na kuondoka hapo kwao, Mwenge na kwenda Mbezi katika Hoteli ya White Paradise.

    Alihitaji kupumzisha akili yake kwani kulikuwa na mambo mengi aliyokuwa akiyafikiria kipindi hicho. Hakuchukua muda mwingi akafika katika hoteli hiyo. Ilikuwa ni moja ya hoteli ya kifahari jijini Dar es Salaam ambapo ndani kulikuwa na bwawa kubwa la kuogelea.

    Kwa nje tu, sehemu ya kuegesha magari hakukuwa na ugumu kugundua kwamba hiyo ilikuwa moja ya hoteli iliyokuwa ikitumiwa na watu waliokuwa na pesa.

    Magari ya thamani yalijazana katika eneo hilo, Daniel alibaki akiyaangalia, hakuamini kama Tanzania hii kungekuwa na watu waliokuwa wakiendesha magari ya thamani kubwa kama aliyoyakuta hapo hotelini.

    “Kijana unakwenda wapi?” alisikia swali kutoka kwa mwanaume mmoja aliyesimama nyuma yake, akageuka, macho yake yakagongana na mlinzi.

    “Kula bata kidogo!”

    “Umechukua chumba humu?”

    “Hapana! Huwa ninakuja kuonana na baba yangu! Kuna lolote mkuu?” alimwambia mlinzi huyo na kumuuliza.

    Akamwangalia kuanzia juu mpaka chini, muonekano wake ukaridhisha kwamba inawezekana kile alichokuwa akikizungumza kilikuwa kweli, akamruhusu na kuingia ndani.

    Humo, kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakila raha, wengine walikuwa wakiogelea katika bwana kubwa, wengine walikuwa wakila na kunywa huku muziki ukiendelea kusikika.

    Asilimia tisini ya watu waliokuwa ndani ya eneo la hoteli hiyo lugha yao ilikuwa ni Kiingereza. Kulikuwa na Wazungu kutoka mataifa mbalimbali na asilimia kubwa ya wasichana waliokuwa humo walikuwa wazuri kiasi kwamba ilikuwa ni rahisi kuamini waliambiana wawe wanakutana ndani ya hoteli hiyo.

    Kwa mwendo wa taratibu, Daniel akaanza kusogea mahali kulipokuwa na kitanda kidogo cha watu waliokuwa wakitoka kuogelea na kukaa mahali hapo.

    Maisha ya watu walivyokuwa wakiishi humo na kula raha yalimpa hasira ya kutafuta pesa. Kila aliyekuwa humo, alionekana kutoka kwenye familia iliyokuwa na uwezo mkubwa. Hakumuona mtu kutoka uswahili, wote waliionekana humo walikuwa na muonekano wa watu waliokuwa wakiishi katika maisha ya raha, kwenye maghorofa makubwa hapo Mbezi Beach.

    “Excuse me,” (samahani) alisikika msichana mmoja aliyekwenda karibu na pale alipokaa Daniel.

    Daniel akayainua macho yake na kutua katika uso wa msichana mmoja mrembo mno. Alizibana nywele zake kwa nyuma, alikuwa na rangi mchanganyiko, mama Mzungu na baba mswahili.

    Alikuwa na figa nzuri, tumbo lake liliingia kwa ndani. Pale aliposimama alikuwa akimwangalia Daniel ambaye kama alihitaji kumuomba kitu fulani.

    “What can I help you miss?” (nikusaidie nini mrembo?) aliuliza Daniel na msichana yule kumwambia kwamba alihitaji kukaa katika kitanda kile ili akauke.

    Hilo halikuwa tatizo, Daniel akasogea na kukaa pembeni kumpisha msichana huyo ambaye akalala chali kwa kuangalia juu, akachukua miwani yake na kuvaa.

    Kwa pembeni Daniel alipokaa alikuwa akitetemeka, kwa jinsi msichana yule alivyokuwa mrembo, hakutamani kumuona akiondoka pasipo kuongea naye.

    Alitamani kuzungumza naye hata kwa dakika kadhaa lakini alishindwa, moyo wake ukaanza kuingiwa na hofu kwamba hakustahili kuongea na msichana mrembo kama huyo kwani walikuwa ni watu wawili wa madaraja tofauti.

    “Nianzaje?” alijiuliza.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati akijiuliza ni kwa jinsi gani angeanza kuzungumza na msichana huyo mrembo, ghafla macho yake yakatua kwa msichana mwingine aliyekuwa amesimama pembeni ya bwawa la kuogelea.

    Alikuwa msichana mwenye rangi ya ngozi ya kawaida lakini alionekana kuwa mzuri mara tano ya yule msichana aliyekuwa pembeni yake.

    Moyo wa Daniel ukapiga paaa. Hakuamini kama katika maisha yake angeweza kukutana na msichana mrembo kama alivyokuwa yule aliyekuwa akimwangalia.

    Kule alipokaa akajiona kama yupo mbali, akasimama na kuanza kusogea kule alipokuwa msichana yule. Alimvutia, umbo lake lilikuwa la kimisi, alivalia mavazi ya kuogelea huku akiwa amezinyoa kidogo nywele zake kwa staili ya panki lililoonekana kwa mbali.

    Alivyokuwa akitembea, ilikuwa ni kama hakuwa akikanyaga ardhi, alitembea kwa madaha akiangalia huku na kule. Mkononi mwake alishika simu huku katika sikio moja akiwa ameweka ‘earphone’.

    Akafika karibu na kule alipokuwa msichana huyo. Alimwangalia kwa karibu na kuona kabisa kwamba macho yake hayakuwa yamemdanganya hata kidogo kwani kwa uzuri ambao alikuwanao alipomuona kwa mbali ulikuwa uleule ambao alimuona nao hata alipokuwa amemsogelea.

    Msichana huyo alisimama karibu na meza moja na kuanza kusikiliza muziki katika simu yake. Hakuwa Daniel peke yake, hata wanaume wengine waliokuwa wakipita karibu yake walikuwa wakimwangalia kwa macho yaliyojaa matamanio, kila aliyemwangalia alitamani kuzungumza naye lakini alishindwa ni kwa jinsi gani angeyaanzisha mazungumzo kwake.

    “Dada habari!” alimsalimia huku akionekana kutetemeka, hakuamini kama alisimama karibu na msichana huyo.

    “What?” (nini?) aliuliza, hakuwa ameisikia sauti ya Daniel vilivyo.

    Daniel hakuzungumza kitu, alibaki akimwangalia tu. Bado uzuri wake ulikuwa umemchanganya, alihisi kama amekutana na malaika aliyeshushwa kutoka Mbinguni na kuambiwa kwamba sasa alitakiwa kuishi duniani.

    Mdomo wake ukawa mzito, msichana yule alipomuona Daniel hazungumzi kitu, akachukua earphone nyingine na kuweka katika sikio jingine na kisha kujifanya kuwa bize akichezea simu yake.

    “Ops! Huyu ni mtu kweli au nimekutana na jini?” alishusha pumzi nzito, alijiuliza huku akiangalia pembeni.

    Japokuwa mahali hapo kulikuwa na wasichana wengi warembo lakini hakuwa na taarifa nao hata kidogo, moyo wake ulikuwa kwa msichana huyo tu, alimpenda, alimchanganya kiasi kwamba katika dunia hii hakutaka kuwa na msichana yeyote zaidi yake.

    Wakati akiwa ametulia huku kichwa chake kikifikiria mengi kuhusu msichana huyo, akamsikia mtoto mmoja akimuita kwa jina la Jackline, haraka sana msichana huyo akatoa earphone moja masikioni na kumsikiliza vizuri mtoto huyo aliyekuwa akiita kwa mbali.

    Daniel akageuza macho yake na kumwangalia mtoto huyo. Kwa sura, hakukuwa na maswali kwamba wawili hao walikuwa ndugu.

    Jackline akaondoka mahali hapo na kumfuata yule mtoto, alipomfikia, akamchukua na kuelekea katika meza moja ambapo kulikuwa na wazazi wake na mwanaume mmoja ambaye naye alifanana sana na Jackline.

    “Anaitwa Jackline! Aisee ni msichana mrembo mno,” alijisemea huku akimwangalia alivyokuwa akitembea, alionekana kuwa simpo sana tofauti na wasichana wa uswahilini.

    Ilikuwa ni kama waliambiwa muda wa kuondoka ulikuwa umefika, wakachukua mabegi yao, wakaweka nguo na nyingine kuzivaa na kisha kuanza kuondoka mahali hapo.

    Kabla ya kuelekea nje ya hoteli ile, Jackline akaelekea sehemu walipokuwa wakiuza chakula na kisha kulipia na kuondoka mahali hapo.

    Daniel hakutaka kubaki ndani, naye akaanza kuwafuatilia, alihitaji kuona mpaka wakipotea mahali hapo. Walipofika nje, wakachukua gari moja la kifahari aina ya Range SV Autobiography toleo jipya yenye rangi ya kijivu, wakaingia na kisha kuondoka mahali hapo.

    “Mmh! Ningemuweza kweli?” alijiuliza wakati gari lile likiondoka mahali hapo. Kichwa chake kilichanganyikiwa kupita kawaida.





    Jackline ndiye aliyemchanganya Daniel kupita kawaida, moyo wake ukafa na kuoza kwa msichana huyo, alichanganyikiwa kiasi kwamba kila wakati alitamani kumuona.

    Alipoona gari lile limepotea usoni mwake, akarudi hotelini na kuendelea kuwaangalia watu walivyokuwa wakila raha. Hakujua kama yule aliyekuwa amemuona alikuwa binadamu kweli au jini kwani uzuri wake ulikuwa tofauti kabisa.

    Wanawake wengine ambao hapo kabla alipoingia ndani ya hoteli hiyo aliwaona wazuri, hawakuwa na thamani tena, hawakuwa wazuri kama msichana Jackline ambaye aliondoka pasipo kuzungumza naye kitu chochote kile.

    Kwa jinsi alivyoonekana yeye na ndugu zake, haikuwa vigumu kugundua kwamba walikuwa wakitoka katika familia bora na kwa sababu Jackline alikwenda katika sehemu ya kuuzia chakula na kulipa pesa, aliamini kwamba muuzaji alikuwa akimfahamu.

    Akaondoka na kuelekea huko, alipofika, kitu cha kwanza alihitaji mazoea na mwanaume huyo aliyekuwa akihusika na kuuza vyakula vya kawaida kama chipsi na mishikaki kisha kumuuliza kuhusu Jackline.

    “Hivi kaka yule mrembo anaishi wapi?” aliuliza Daniel.

    “Yupi?”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Aliyekuja kulipia chakula hapa.”

    “Mmh! Wamekuja wengi sana, wewe unamzungumzia yupi?” aliuliza muuzaji.

    Hakujua ni kwa jinsi gani angemuelezea ili amuelewe. Kama angesema ni msichana mrembo, ndani ya hoteli hiyo kulikuwa na wasichana wengi warembo, kama angesema kuwa alikuja na wazazi wake, kulikuwa na wasichana wengi ambao walikwenda na wazazi wao.

    Akaondoka mahali hapo kwani hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kumuona tena Jackline ambaye alitokea kuuteka moyo wake kupita kawaida.

    Ilipofika majira ya saa moja usiku, akaondoka kurudi nyumbani kwao. Kichwa chake kilikuwa na mawazo mengi, kila alipokuwa akikaa, alimfikiria msichana huyo.

    Alimchanganya, ni kama aliingia kwenye kichwa chake na kukataa kutoka kabisa. Hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kumuona tena kwani kama angelijua hata jina la baba yake ingekuwa rahisi, angekuwa radhi kuzunguka Mbezi Beach nzima kumtafuta msichana huyo tu.

    Usiku wa siku hiyo ulikuwa ni wa mateso makubwa, usingizi haukumjia kirahisi kwani mawazo juu ya Jackline yalimtesa kupita kawaida. Alipoona hapati usingizi, akainuka na kuelekea katika meza yake ya kujisomea, akachukua karatasi na kalamu na kuanza kuandika ujumbe mzuri kwa ajili ya msichana huyo.

    Lengo kubwa la kuuandika ulikuwa ni kumuonyeshea ni kwa jinsi gani alimchanganya tangu siku ya kwanza alipokutana naye, alitaka Jackline afahamu ni kwa namba gani alikichanganya kichwa chake kupita kawaida. Akayaandika maneno haya:

    Jackline!

    Wewe ni msichana mrembo sana ambaye umetokea kukichanganya kichwa changu. Leo ni usiku wa tarehe 15/04, majira ya saa tisa usiku, sijalala, nimekuwa nikikufikiria kupita kawaida.

    Nimetokea kukupenda, najua unaweza kujiuliza ni kwa jinsi gani nimekupenda ghafla, siwezi kuficha hisia zangu kwako, ninakupenda mno, ninakupenda katika mapenzi ambayo hakuna mwanadamu yeyote aliyowahi kumpenda mwingine katika dunia hii.

    Natumaini nitakuona hivi karibuni. Nakupenda sana.

    Daniel Thomasi Kimei.

    Alipomaliza kuandika, akasoma zaidi na zaidi, alihitaji kuonana na Jackline kwa mara nyingine, hata kama ingetokea kutopata nafasi ya kuzungumza naye basi huo ujumbe ungeweza kuzifikisha hisia zake kwake.

    Siku iliyofuata hakutaka kubaki nyumbani, akaondoka na kuelekea kule hotelini kwa lengo la kubahatisha kuonana na msichana huyo.

    Haikujalisha kama ilikuwa wikiendi au siku za kazi, kila siku watu walionekana kuwa wengi mahali hapo. Aliwakuta wasichana warembo lakini moyo wake haukuwa kwao, alifika mahali hapo kwa lengo la kumuona Jackline tu tena huku mfukoni akiwa na ile karatasi yake.

    Akaelekea sehemu iliyokuwa na kiti na kutulia hapo, macho yake yakaanza kuangalia huku na kule, moyoni aliamini kwamba angeweza kumuona msichana huyo kwa mara nyingine na kuzungumza naye.

    Siku hiyo alishinda huko lakini hakuweza kumuona, aliumia lakini akajipa moyo kwamba inawezekana kesho yake angemuona msichana huyo na hivyo kuondoka.

    Hakukoma kufika mahali hapo, kila alipokuwa akifika na kumtafuta Jackline, hakuweza kumuona tena. Hilo halikumsitisha kwenda huko, mwezi mzima alikuwa akienda huko lakini hakufanikiwa kumuona.

    Sura ya Jackline iliendelea kuwa kichwani mwake, alimkumbuka alivyokuwa mzuri, alivyoongea, lipsi nene na hata macho yake ya goroli.

    Kwa kipindi cha miezi miwili alikuwa akifululiza kwenda huko lakini hakufanikiwa kumuona msichana huyo. Moyoni mwake alijipa uhakika kwamba milima haikuwa ikikutana lakini binadamu siku zote walikuwa wakikutana.

    Akaanza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam huku akichukua kozi ya utabibu. Huko chuoni alibahatika kuwakuta wasichana warembo mno lakini bado akili yake, moyo wake uliendelea kuwa kwa msichana mmoja tu, naye ni Jackline.

    Kutokana na upole wake, sura yake ambayo mara nyingi alikuwa akiivisha tabasamu pana, wasichana wengi wakamfuata, walitafuta mazoea naye na hata kumpa zawadi mbalimbali lakini Daniel hakutaka kujali, hakuwa na muda na wanawake wengine, alikuwa tayari kupoteza muda wake kumfuatilia Jackline lakini si kujiona akiingia kwenye uhisiano na msichana mwingine.

    Kila alipoulizwa kama alikuwa na msichana, alisema wazi kwamba alikuwepo, msichana huyo aliitwa Jackline na hakutaka kabisa kuwa na mpenzi mwingine zaidi ya huyo.

    Wasichana wengi wakatamani kumuona huyo Jackline alifananaje, alikuwa na uzuri gani mpaka kuuteka moyo wa Daniel kiasi hicho.

    “Eight months without seeing her, God help me,” (miezi nane pasipo kumuona, Mungu nisaidie) alijisemea chumbani huku akiwa amelala chali.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilikuwa miezi nane tangu siku ambayo alikutana na msichana huyo, hakuweza kumuona tena, moyo wake uliuma mno lakini sura yake haikufutika kichwani mwake.

    Alikuwa tayari kupoteza hata mwaka mzima lakini si kuacha kwenda kwenye hoteli ile, alidhamiria moyoni mwake, wakati mwingine alikuwa akijishangaa, hakuamini kama alikuwa na uvumilivu wa namna hiyo kwani wanaume wengi wangeweza kukata tamaa lakini si kwake.

    Siku ilipotimia mwezi wa tisa kamili tangu siku ya mwisho kumuona Jackline, akaanza kuelekea kule hotelini, siku hiyo alipanga kuogelea kwani mara zote alizokuwa akienda alikuwa akikaa pembeni na kuwaangalia watu waliokuwa wakiogelea.

    Alipofika, kabla ya yote ilikuwa ni kuzunguka kila kona kumtafuta msichana huyo, alihitaji kuona kama alikuwepo au hakuwepo. Alizunguka kote na kumkosa, akatafuta sehemu, akavua nguo zake na kuingia kwenye bwawa la kuogelea.

    Wakati akiwa anaogelea, alisikia uyowe kutoka kwa mtoto mmoja aliyeonekana kuumizwa na kitu fulani, akageuka kule uyowe ulipokuwa umetoka, mtoto mmoja wa kiume alikuwa amechomwa unyayoni na chupa ya bia iliyokuwa imevunjika.

    Watu wakamsogelea, na yeye akatoka kwenye bwawa na kuelekea kule. Alikuwa akisomea utabibu na hivyo kutaka kumpa huduma ya kwanza mtoto huyo.

    Akamchukua na kumpeleka pembeni kisha kuanza kumpa huduma ya kwanza. Alilisafisha jeraha lake kisha kuchukua soksi yake na kumfunga kwa muda katika mguu ule. Alipomaliza, akamwambia kwamba hakutakiwa kukanyaga chini kwani angezidisha maumivu.

    “Wazazi wako wapo wapi?” alimuuliza.

    “Wapo kule,” alisema huku akionyesha kwa kidole kuelekea upande wa pili wa hoteli ile.

    Akamchukua, akambeba na kuelekea huko alipoambiwa. Mbali na kule mbele kabisa, pia kwa upande wa nyuma kulikuwa na sehemu nyingine ya kuogelea, watu ambao hawakuhitaji usumbufu walikuwa huko, palitulia na ukimya wake ulikuwa tofauti na kule walipotoka.

    Daniel mwenyewe akabaki akishangaa, japokuwa ilikuwa hoteli ya matajiri lakini kumbe kulikuwa na sehemu nyingine ambayo waliitumia watu wasiotaka kuchangamana na watu wengine.

    “Unaitwa nani?” alimuuliza mtoto yule huku akiwa mgongoni mwake.

    “Christopher!”

    “Columbus?” aliuliza huku akicheka.

    “No! Mwamanda!”

    Akamuonyeshea mahali wazazi wake walipokuwa na kumpeleka pale. Walipomuona, walishangaa, ilikuwaje mtoto wao apelekwe mahali pale huku akiwa amebebwa, ikawabidi wazazi wake kumuuliza na hivyo Daniel kuwaelezea kila kitu kilichotokea.

    “Alijichoma na chupa, ila nimempa huduma ya kwanza, nimezuia damu, nadhani anaweza kuendelea na matibabu mengine kwa kuwa kidonda kimekuwa kibaya sana,” alisema Daniel huku akionyesha tabasamu pana.

    “Ahsante sana! Ahsante kwa kumsaidia mtoto wetu! Wewe ni daktari?” aliuliza Bi Asteria, mama wa mtoto yule.

    “Naweza kusema ndiyo kwa kuwa nasomea mambo ya utabibu!”

    “Ooh! Sawa. Karibu tule kwanza!”

    “Usijali mama! Nimeshiba!”

    “Mmh! Sawa! Basi karibu hata kwenye sherehe ya kumpongeza binti yetu kwa kumaliza masomo yake hapo kesho,” alisema mzee Mwamanda huku akimwangalia Daniel.

    “Sawa. Natumaini nitaungana nanyi! Nashukuru sana! Naweza kuondoka?”

    “Sawa! Chukua namba yangu! Sherehe itaanza majira ya saa kumi jioni, utasema utakapokuwa, dereva atakufuata,” alisema mzee Mwamanda.

    “Nashukuru sana!”

    Alipomaliza kuongea nao, hakutaka kubaki mahali hapo, akaondoka zake. Mzee Mwamanda na mkewe walimshukuru sana Daniel, alionekana kuwa mtu mwema ambaye aliamua kumsaidia mtoto wao kana kwamba alikuwa ndugu yake.

    Kwa wema wake mkubwa aliomuonyeshea mtoto wao, wakaona kabisa kwamba hata nao walitakiwa kumuonyeshea upendo na kuona kwamba kile kidogo alichokuwa amekifanya kilikuwa muhimu sana kwao.

    Siku iliyofuata, hakutaka kwenda hotelini, akaelekea chuoni ambapo aliendelea na kazi zake kama kawaida. Ilipofika majira ya saa tisa na nusu, akakumbuka kuhusu ile sherehe aliyokuwa ameambiwa.

    Hakutaka kwenda kwa kuwa alikuwa bize lakini ilipofika majira ya saa kumi, hakuona kama ingekuwa busara kuachana na sherehe hiyo kwani watu hao walimthamini kiasi cha mzee huyo kumpa namba yake.

    Akapiga, simu ikapokelewa na mzee Mwamanda ambapo akajitambulisha na kumwambia amuelekeze mahali sherehe ilipokuwa ikifanyika na kuelekea huko.

    “Upo wapi?”

    “Nipo chuo mzee!”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kuna kijana wangu anakuja kukuchukua, ngoja nimpe namba yako,” alisema mzee huyo na kukata simu.

    Baada ya nusu saa, akapigiwa simu na kijana huyo aliyeambiwa, akamuelekeza na kufika hapo na kumchukua. Macho ya Daniel yalipotua usoni mwa kijana huyo, akashtuka, sura yake ilifanana na msichana ambaye alikuwa akimtafuta sana kwa muda wa miezi tisa, Jackline.

    “Mbona umeshtuka?” aliuliza kijana huyo.

    “Nahisi si mara yangu ya kwanza kukuona!” alisema Daniel.

    “Mimi?”

    “Ndiyo!”

    “Ulishawahi kuniona wapi? Mbona mimi sikukumbuki?”

    “Hujawahi kwenda pale White Paradise?”

    “Ni kitambo sana! Huwa sikai sana Tanzania, muda mwingi nipo Nigeria chuoni!”

    “Mara yako ya mwisho?”

    “Nadhani ni miezi kama nane au tisa iliyopita. By the way, naitwa Erick” alisema kijana huyo.

    “Naitwa Daniel,” alijibu na kupeana mikono.

    Akaingia ndani ya gari na kuanza kuzungumza mambo mengi tu kuhusu masomo yao. Kichwani mwa Daniel kulikuwa na kitu kimoja tu, alikuwa na uhakika kwamba huyo alikuwa ndugu yake Jackline kwani mara ya mwisho kumuona, Erick ndiye aliyekuwa akiliendesha lile gari walilokuwa wamelipaki na kuondoka.

    Akahisi moyo wake ukichangamka kupita kawaida na kuona kabisa kwamba huyo binti aliyekuwa akienda kufanyiwa sherehe inawezekana alikuwa Jackline aliyekuwa akimpenda kwa moyo wa dhati.

    Alitamani kumuuliza kuhusu msichana huyo lakini akabaki kimya, alihitaji kuvumilia mpaka pale ambapo angemuona msichana huyo machoni mwake.

    Baada ya dakika kadhaa, wakafika, gari likaingizwa ndani ya jumba moja la kifahari, Daniel alibaki akishangaa kwani katika maisha yake yote hakuwahi kuingia katika jumba kubwa na zuri kama hilo.

    Hapo, kulikuwa na watu wasiopungua thelathini ambao wote walikuja kuhudhuria sherehe hiyo fupi. Daniel akapelekwa walipokuwa wazazi wa Erick na kuwasalimia.

    “Karibu sana! Ulisema unaitwa nani dokta?” aliuliza mzee Mwamanda.

    “Daniel!”

    “Ooh! Karibu sana!”

    “Ahsante! Mgonjwa wangu yupo wapi?”

    “Subiri!” alisema mzee huyo na kumuita msichana mmoja.

    Alikuwa mfanyakazi wa ndani, akaambiwa amchukue Daniel na kumpeleka chumbani kwa Christopher kwa lengo la kumuona. Hilo halikuwa tatizo, akachukuliwa na kupelekwa huko.

    Macho yake yalikuwa yakiangalia huku na kule, alionekana kama mshamba fulani, yaani kila kitu alichokuwa akikiona humo alishangaa. Wakaingia ndani na moja kwa moja kuelekea katika chumba cha Christopher na kuanza kupiga hodi.

    “Who is it?” (nani?) ilisikika sauti ya msichana kwa ndani, haikuwa ngeni, Daniel aliikumbuka, ilikuwa sauti ya Jackline, moyo wake ukapiga paaa.

    “Aisha! Nimeambiwa nimlete dokta wa Christopher aje kumuona!” alisema msichana yule.

    “Mwambie aingie!”

    Mlango ukafunguliwa na Daniel kuingia ndani. Macho yake yakatua kwa Jackline aliyekuwa akimuandaa Christopher. Alipomuona msichana huyo, mapigo yake ya moyo yakazidi kudunda kwa nguvu kubwa, alichanganyikiwa, hakuamini kukutana na msichana huyo mahali hapo.





    Ilipita miezi mingi tangu siku ya mwisho kumuona, alimkumbuka, alimfanya kwenda hotelini kila siku kwa lengo la kuonana naye lakini hakufanikiwa. Baada ya siku zote hizo kupita, hatimaye akaonana naye mahali hapo kitu kilichomfanya kutokuamini kama alikuwa Jackline aliyekuwa akimfahamu.

    Jackline alipomuona Daniel, hakumkumbuka, kwake, mwanaume huyo alionekana kuwa kama watu wengine, alimchukulia kama daktari aliyeambiwa kwamba alikuja kumuona mdogo wake.

    “Jackline...” alijikuta akiita huku akimwangalia, akaanza kumsogelea, msichana huyo akashtuka.

    “Do we know each other?” (tunafahamiana?) aliuliza huku tabasamu pana la mshangao likiwa usoni mwake.

    Daniel hakujibu kitu, alinyamaza huku macho yake yakimwangalia Jackline ambaye naye alianza kuonyesha wasiwasi kwani kila alipojaribu kuvuta picha kama aliwahi kumuona mwanaume huyo sehemu, hakukumbuka.

    “You are a superstar, everybody knows you,” (wewe ni maarufu, kila mtu anakufahamu!)

    “Mimi?”

    “Ndiyo!”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Jackline hakuzungumza kitu, akanyamaza lakini kichwa chake kilikuwa na maswali mengi juu ya mwanaume huyo. Daniel akajifanya kupuuzia na kumjulia hali Christopher huku akimwambia kwamba alihitaji kukiona kidonda chake.

    “Wewe ndiye uliyemsaidia jana?” aliuliza Jackline.

    “Ndiyo! Alijikata na chupa! Unajisikiaje Columbus?” alimuuliza kwa jina lake la utani alilompa.

    “Am fine! Maumivu yamepungua sasa,” alijibu Christopher.

    Daniel alikuwa akifikiria namna ya kuendelea kuzungumza na msichana huyo, alimkumbuka, mara ya mwisho kukutana ilikuwa ni miezi tisa iliyopita, hakujua ni kwa namna gani angeanza kuzungumza naye kwani alitamani kumuona kwa muda mrefu sana.

    Wakati yeye akifikiria hayo, naye Jackline alikuwa akifikiria yake kichwani. Aliendelea kujiuliza kuhusu mwanaume huyo, alionekana kumfahamu vilivyo lakini hakukumbuka kama aliwahi kumuona sehemu fulani.

    Kilichomtisha ni kumwambia kwamba alikuwa supastaa, alijua kwamba alitania kwani hakuwa mtu wa kutoka ndani, sana sana kwenda katika Hoteli ya White Paradise na kuogelea, sasa mwanaume huyo alimjuaje? Kila alipojiuliza, alikosa jibu.

    Pale alipokuwa, Jackline alimwangalia, jinsi alivyokuwa akiongea lakini hakupata jibu kama aliwahi kumuona sehemu fulani. Alipomaliza, Daniel akayarudisha macho yake kwa Jackline.

    “It has been nine months since the last time I saw you!” (ni miezi tisa sasa tangu mara ya mwisho kukuona) alisema huku akimwangalia.

    “Waoo! It is such a long time. Can you remind me where we met?” (Waoo! Ni muda mrefu, unaweza kunikumbusha tulipokutana?) aliuliza msichana huyo.

    Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi yake, akaanza kumwambia Jackline jinsi alivyomuona kwa mara ya kwanza. Alimkumbusha vizuri kabisa na kwa sababu siku ile ilikuwa ya mwisho kwake kwenda hotelini kufurahia maisha na wazazi wake, alikumbuka vizuri.

    “Ooh! Nimekukumbuka! Umekua!” alisema Jackline huku akicheka.

    “Hahah! Hata wewe umekua, uzuri wako umeongezeka!”

    “Ila umejuaje kama naitwa Jackline?”

    “Nakumbuka mdogo wako alikuita siku ile, unakumbuka?”

    “Ooh!! Yeah! Nakumbuka! Halafu nikaondoka!”

    “Yeah! Tena kwa dharau...”

    “Jamaniiiiiii...”

    “Nakutania! Nimekuwa nikikusubiria kwa miaka tisa sasa...”

    “Miaka tisa?”

    “Miezi tisa!”

    “Ooh! My gosh...umenishtua.”

    “Nina zawadi yako nzuri sana!”

    “Zawadi! Ya nini?”

    “Kukukumbusha siku ile. Nimeandika kitu kizuri kwa ajili yako,” alisema Daniel.

    “Hebu nikione!”

    “Nitakuonyeshea!”

    “Lini?”

    “Siku yoyote tu,” alisema Daniel.

    Walibaki wakizungumza kwa pamoja huku wakiangaliana mpaka Daniel kusahau kama alifika mahali pale kwa ajili ya kumjulia hali Christopher ambaye aliamua kuachana naye na kuzungumza na dada yake.

    “Naweza kupata namba yako niwe nakubipubipu wa kishua?” aliuliza Daniel huku akitabsamu.

    “Eti uwe unanibipubipu!”

    “Yeah! Kwani vibaya!”

    “Si vibaya, ila ukinibipu, na mimi nakubipu!” alisema Jackline na kumpa namba ya simu Daniel kwani kwake alionekana kuwa mwanaume mcheshi, mwenye roho nzuri ambaye hakuwahi kukutana naye kabla.

    Daniel akamchukua Christopher na kuondoka naye mahali hapo, wakaelekea nje ambapo sherehe ilianza na watu kuanza kwa kucheza muziki.

    Daniel hakutaka kujionyesha sana, akaelekea sehemu iliyokuwa na makochi na kukaa. Moyo wake ulikuwa na furaha tele, hakuamini kama alifanikiwa kumuona Jackline, kwake, kile kilichokuwa kimetokea kilikuwa kama muujiza mkubwa.

    “Halafu wewe unampenda dada yangu? Si ndiyo?” aliuliza Christopher swali lililomfanya Daniel kushtuka, akamwangalia usoni.

    “Mimi? Hapana! Unajua yule ni rafiki yangu sana!”

    “Kweli?”

    “Ndiyo!”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akili ya Daniel ilikuwa kwa msichana Jackline tu, alimpenda, alihitaji kuwa naye katika maisha yake yote. Alikaa mahali hapo huku akizungumza na Christopher, walitokea kuwa marafiki wakubwa kiasi kwamba mpaka Daniel mwenyewe akawa anashangaa.

    Baada ya dakika kadhaa, Jackline akatoka ndani na kuungana na wageni waliofika kwa ajili ya sherehe yake, kila mtu aliyekuwa mahali hapo akaanza kupiga makofi.

    Haraka sana Daniel akasimama na kuelekea kule watu walipokuwa, alipofika, macho yake yakatua kwa Jackline. Alivalia gauni refu jekundu lililomfika mpaka miguu, nywele zake alizibana huku akiwa amevalia hereni ndoto.

    Miguuni alivalia viatu vya kike vilivyokuwa vimeinuka mpaka juu, kwa kumwangalia tu isingekutia shaka kwamba ulikuwa ukimwangalia mmoja wa wanawake wazuri duniani.

    “Jackline, ninakupenda kwa moyo wangu wote,” alisema Daniel, aliongea kwa sauti ya chini huku akimwangalia msichana huyo.

    Sherehe iliendelea mpaka ilipokwisha majira ya saa tatu. Watu wakaanza kutawanyika, naye Daniel akaaga. Mzee Mwamanda akamshukuru kijana huyo kwa kuja kwake katika sherehe hiyo lakini pia akamsisitiza kwamba huo hautakiwi kuwa mwisho, muda wowote ambao angejisikia kufika mahali hapo, alikuwa akikaribishwa.

    “Haina shida mzee wangu! Nashukuru sana.”

    Akaondoka, ndani ya Bajaj kichwa chake kilikuwa kikimfikiria msichana huyo tu, alimpagawisha kiasi kwamba hakuona kama kulikuwa na mwanamke mzuri katika dunia hii zaidi ya Jackline.

    Akaichukua simu yake, akafungua sehemu ya ujumbe mfupi na kumwandikia ujumbe uliosomeka ‘Nimeondoka bila kukuaga, nahisi ulikuwa bize, namshukuru Mungu kwa kukuona tena, hakika ulipendeza’ alipomaliza, akautuma, wala hazikuchukua sekunde nyingi, ukajibiwa ‘Lol! Nashukuru pia! Safari njema dokta’.

    Alipofika nyumbani, akajilaza kitandani, kichwa chake kilikuwa kwenye mawazo lukuki, bado alikuwa akimfikiria msichana huyo. Aliukumbuka uzuri wake, jinsi alivyokuwa akiongea kwa mapozi, nywele zake alivyokuwa amezinyoa, kwa kifupi kwake alionekana kama malaika.

    Alihitaji kumpigia simu na kuzungumza naye, alihofu kwa kuhisi kwamba angekuwa anamsumbua kwa kuwa ilikuwa ni usiku, ila kwa kuwa alipenda sana, hakutaka kujali. Akampigia na baada ya sekunde kadhaa simu kupokelewa na sauti ya msichana huyo kusikika.

    “Unajua huwezi kujua ni kwa jinsi gani nina furaha siku ya leo,” alisema Daniel.

    “Kivipi?”

    “Kukuona! Miezi tisa ni mingi sana, nilikufikiria mno. Ulikimbilia wapi?” aliuliza Daniel.

    “Nilikuwa chuoni Afrika Kusini!”

    “Ooh! Na umeshamaliza?”

    “Ndiyo! Halafu umenikumbusha, hebu niambie ilikuwaje mpaka ukakutana na familia yangu?” aliuliza.

    “Ni stori ndefu sana!”

    “Ambayo haisimuliki?”

    “No! Ambayo haimaliziki! Ila kwa kifupi, ni Mungu tu. Jack, u msichana mrembo sana, unapendeza kwa kila vazi unalovaa, kukutana na wewe ni kama umeikamilisha ndoto yangu,” alisema Daniel kwa sauti ndogo ya mahaba.

    “Mmh! Nyie wanaume!”

    “Serious! Jack, nikiambiwa nichague kitu kimoja cha kuwa nacho milele yote, hakika ningekuchagua wewe. U msichana mrembo sana, msichana ambaye kila mwanaume angetamani kuwa naye,” alisema.

    “Mmh! Aya nashukuru dokta!”

    “Niite Danny kama utapenda.”

    “Sawa. Nashukuru Dk. Danny!”

    Walizungumza mambo mengi, kuanzia saa tano mpaka saa saba usiku bado walikuwa wakizungumza. Daniel hakutaka kusita, hakutaka kumficha msichana huyo, alimwambia kwamba alikuwa akimpenda mno na ndiyo maana kwa kipindi chote hicho alivumilia, alikuwa akimsubiri kwa kuwa aliamini kuwa kuna siku angekutana naye.

    Kuambiwa hivyo, Jackline alikutegemea, kwa sauti yake ya upole alimwambia Daniel kwamba alikuwa na mpenzi, kulikuwa na mtu ambaye aliuchukua moyo wake.

    “Najua Jackline, msichana mzuri kama wewe hutakiwi kuwa peke yako, tena ungeniambia kwamba hauna mtu, nisingekuamini,” alisema Daniel.

    “Ndiyo hivyo! Ila samahani!”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Usijali! Ila sidhani kama litakuwa jambo baya kama tutaendelea kuwasiliana kwenye simu, kama marafiki,” alisema Daniel kwa sauti ya upole.

    “Haina shida! Wewe tu!”

    “Sawa,” alisema Daniel na kukata simu.

    Ilikuwa ni kama alikuwa akiingia vitani, alijua dhahiri kwamba Jackline alikuwa na mpenzi lakini alihitaji kushinda vita hivyo na kumpata.

    Alijua udhaifu wa wanaume wanapokuwa na wanawake kwa kipindi kirefu, alijua jinsi walivyokuwa wakichoka na hata kule kujali kunavyopungua, kwa kuwa alilifahamu hilo, alitaka kumuonyeshea Jackline kwamba yeye alikuwa mwanaume wa kipekee sana, aliyemsikiliza, aliyemchekesha na hata kumfariji.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog