IMEANDIKWA NA : FRANK MASAI
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
SIKU hiyo ilikuwa ni Jumamosi tulivu sana katika Mji ule wa Dodoma, ndege walirembesha anga huku miti ikilalamika kwa mvuto wa sauti yake kutokana na upepo mwanana uliokuwa unavuma kwa wakati huo. Watu walikuwa katika harakati mbalimbali za kufanya maisha yao yapendeze kama si kuvutia kabisa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hatukuwa nyuma katika harakati hizo. Kama kawaida ya Jumamosi nyingine, nilipenda sana kutoka na familia yangu kwenda mahala tulivu na kujadiri mambo mbalimbali ya kimaisha. Siku hiyo nilipanga kuipeleka familia yangu ya watoto wanne na mke wangu kwenye moja ya sehemu nilizokuwa nazimiliki. Sehemu hiyo ilikuwa na michezo ya kila aina kwa ajili ya watoto na kuwa na sehemu maalum kwa ajili ya wazazi kupumzika na kufanya mambo mengine.
Tulienda huko siku hiyo mimi pamoja na familia yangu . Tuliwaacha wana wetu wale wanne,huku wawili tulikuwa tumeachiwa na marehemu Solomon na mkewe Silvia na wawili wakiwa wa kwetu na wote wanne walikuwa ni mapacha.Tulijitenga pembeni wanapokaa wazazi au walezi na tuliagiza vinywaji ili tuburudike. Tulikuwa hatuna cha maana kilichotupeleka pale zaidi ya kuwaleta watoto wafurahi.
“Mme wangu,nilikuwa nimekumbuka sana hali hii ya kukaa pamoja na wewe, sikudhani kama ipo siku tutakuja kukaa hivi tena”. Alianza mke wangu Miriam kuniongelesha maneno yale aliyatoa kwa huzuni lakini ni kwa faraja pia.
“Yashapita hayo mke wangu. Yalikuwa ni Mawio na Machweo tu!. Katika maisha watakiwa kujua kuwa unavoishi ni sawa na jua, yaani lina mawio (kuchomoza kwa jua) lakini hapa katikati kuna mengi sana hadi kufikia machweo (kuzama kwa jua), na ndiyo yale tuliyopitia”
“Ha ha haaa, yaani baby wangu hapo ndipo nakupendeaga, una vimisemo vizuri halafu unajua kuvielezea kabla hata hujaulizwa, nakupenda sana Frank wangu AKA Jay Z”. Aliongea Miriam baada ya mimi kumpa faraja ya maneno yangu yale machache lakini yamejitosheleza kihisia.
“Mh! Na wewe bado umeling’ang’ania hilo Jay Z. Haya bwana my wife AKA Beyonce”. Na mimi nilimjibu kiutani na kusababisha wote tucheke na kuendelea kuwaangalia watoto wetu wakiendelea kufurahi pale kwenye bembea na wengine wakitereza na kutumbukia kwenye maji nakuanza kuogelea.
“Baby samahani”
“Bila samahani wife wangu”. Alianza tena Miriam kuniongelesha na mimi nikaitikia.
“Sijui kama nitakukera,lakini kuna jambo ambalo nilikuwa na hamu sana nilijue kuhusu wewe”.
“Mh! Wife na wewe, hivi mimi naweza kukerwa na harufu ya chokoleti au ua waridi wakati ndiyo vitu vinavyonipa raha?. Wewe ndiye kila kitu, sema tu! Mama yangu”. Nilimpa uhuru Miriam wa kuongea jambo linaliomtatiza.
“Asante mme wangu, na wewe ndiye kila kitu kwenye pumzi yangu. Kitu chenyewe niiiii …….”. Akawa kama ana sita kuendelea huku anatafuna kucha zake. Niligundua ni kitu cha siri au cha aibu ndiyo maana anashindwa kukitamka.
“Wee Miriam wewe, hizo aibu umetoa wapi? Ha ha haaa,embu usinifurahishe. Ongea tu! Usiogope bwana. Si wajua kiasi gani navochukia ukiniogopa?”.Nilimtania kidogo Miriam na kumpa hamasa ya kuongea jambo lake.
“Hivi na wewe mme wangu bado ujaachaga tu utani? Mimi sioni hata aibu, nilikuwa nakula kucha ili nikumbuke na niwaze wapi kwa kuanzia. Sasa hivi nimepata pa kuanzia. Baby, una kumbuka siku ile nilipokuulizia kuhusu mpenzi wako wa nyuma? Ulipoaga na kuniambia ni hadithi ndefu,unakumbuka siku ille?”.Alianza Miriam kuongea suala linalomsibu baada ya kujitetea kuwa haoni aibu.
“Yes, naikukumbuka sana siku ile na hadithi ile haiwezi kunitoka kichwani hata kidogo. Ni sawa na hii iliyonitokea hapa majuzi”.
“Ehee,basi leo naomba unihadithie kilichokutokea hadi kikakufanya siku ile kupoa vile”.Alingeoa Miriam baada ya mimi kumjibu kuwa naikumbuka siku ile.Tukaendelea na maongezi.
“Mh!We nawe, hujachoka kupata mahuzuni? Ujue ile inahuzunisha sana, na ndio maana siku ile nilipoa sana”.
“Baby bwana,mi sitaki. Nataka unihadithie hivyo hivyo hata kama ina huzuni hadi iishe. Isipoisha tutaendelea nyumbani”.
“Ok mama yangu, ngoja nikuhadithie ulizike si wajua sipendi ukae na kisununu kwa ajili yangu?Sasa ngoja nikupe mkasa uliyonisibu mie”.
“Ehee, we ndiye Baba Hailley sasa. Haya nipe hadithi hiyo”. Aliongea Miriam kwa furaha baada ya kumuambia kuwa nitamuhadithia mkasa mzima. Nilivuta pumzi ndefu na kuishushia na funda moja la ukweli la juisi ile ya ukwaju na kuanza kumpa hadithi ile Miriam.
MY ROSE NDIYO INAANZIA HAPA. NI KAMA NAMUHADITHIA MIRIAM LAKINI NITAENDA MOJA KWA MOJA BILA KUONESHA KAMA NIMERUDI NYUMBANI AU NIMEPUMZIKA MAHALA.
Ilikuwa ni mwaka 2004 nikiwa kidato cha tano katika shule moja maarufu pale Dodoma kwa jina Jamhuri. Shule ile ilisifika sana kwa kufaurisha hasa wanafunzi wa kidato cha sita. Sifa zile zilimpelekea baba yangu kunipeleka pale na moja kwa moja nikaanza kidato cha tano huku nikichukua mchepuo wa masomo ya HGL.
Sikuwa na mpenzi wa kudumu kipindi hicho japo nilikuwa najijua kabisa mimi ni mvulana mzuri kisura yaani kwa kiingereza ungeniita Handsome boy. Maisha yangu yalikuwa ni kuwachukua wasichana na kujiridhisha nao na kisha kuachana nao.Hayo ndiyo yakawa maisha yangu tangu kidato cha tatu nilipotendwa na mpenzi wangu mwingine ambaye nilimpenda kupita kiasi na ndiye alikuwa ni mtu wa kwanza kuingia moyoni na kuteka vizuri hisia zangu. Nadhani alitambua hilo na ndiyo maana akaamua kunitenda na mwisho wa siku alifanya hata mitihani yangu ya kidato cha nne nisifanye vizuri..
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tuyaache hayo maana hayahusiani na hadithi hii.
Nilipokuwa namaliza masomo yangu na kazi mbalimbali, nilikuwa napenda sana kwenda kuwatembelea marafiki zangu.Na siku hiyo nilikuwa na mihadi na rafiki yangu mmoja kwa ajili ya kwenda kumuelekeza somo la Jografia. Baada ya kutoka shule na kupata chakula cha mchana, nilifua sare zangu za shule na kwenda kupumzisha kwanza ubongo kabla sijaenda kwa rafiki yangu yule.
Mida ya saa moja na dakika kadhaa nilishitushwa na mlio wa simu yangu, nilipo iangalia ilisomeka ni Wa Kitaa ndiye anapiga.
“Oya mwanangu vipi? Njoo basi tunakusubiri”. Yalikuwa ni maneno ya haraka haraka aliyoyatoa Wa Kitaa kuniomba niende kwao,nadhani aliongea haraka vile sababu ya salio kwenye simu, si mwajua 2004? Hata X.Trim ilikuwa bado.
Wa Kitaa ni jina nililompa mimi kutoka kwa yule masanii wa Bongo Flava,lakini jina lake halisi aliitwa Babuu na ndiye nilikuwa na mihadi ya kumfundisha siku ile.
Baada ya simu ile ya Babuu AKA Wa Kitaa, nilinyanyuka pale kitandani kwangu na kwenda bafuni kwa ajili ya kuutoa uchovu nilio nao kwa kuoga maji ya baridi na kisha nikarudi chumbani mwangu na kuvaa kadeti fulani ya kaptula,nikabeba dhana zangu kwa ajili ya kufundishia na kutoka nje. Nilimuaga mama na kumwambia asini hesabu kwenye chakula cha usiku kwani nitachelewa kurudi na huko niendapo ni lazima nitapa chakula. Baada ya maagano hayo na mama yangu, nikafungua geti na safari ya kwenda kwa akina Babuu ikashika hatamu..
Nilipofika tu! Pale nje ya mlango wa kuingilia kwa akina Babuu, nilisika kelele zikiendele mle ndani kama pana vurugu au kama mjadala wa kisiasa vile. Nilishazoea hali ile kuikuta pale kwa akina Babuu lakini ule ulipitiliza. Nilifungua mlango na kuingia chumbani kwa Babuu na hapo nilimuona Babuu kama kafarijika na ujio wangu.
"Eheee,afadhari umekuja Man'Sai maana hapa leo....".
"Aaah!, mi leo hata sitaki kuingilia mabishano yenu,nisije kupasuka koo bure". Aliniwahi Babuu kwa maneno yake ya afadhari lakini nilimkatisha kauli yake kwa kutotaka kuingilia mjadala wao.
Wakati huo nilikuwa naona jamaa watatu wakiwa wametulia tuli na midomo yao kuwakauka,nadhani ni sababu ya kuongea kwa muda mrefu sana.
"Sikiliza Yeroo, ni kitu kidogo tu! We ndo wa kukimaliza kwa kusema neno lako na kutoa ushauri vilevile". Hakukata tamaa Babuu, huku akiingiza utani wa jina la Yeroo akimaanisha ile salamu ya Wamasai, hiyo ni sababu ya jina langu ndio maana aliniita vile.
"Okey, kama ni neno dogo tu! basi we toboa Wa Kitaa". Nilimpa nafasi ya kusema kinacho wasibu.
"Ehee,hapo mwake. Eti mwanangu, hivi wewe kweli eti unaweza kuja kumpenda demu ambaye ujawahi kumuona hapo kabla, yaani eti umemsikia tu mahala kama kwenye radio hivi, eti ukampenda kweli kweli na ukawa unashindwa hata kula usipomuona. Eti hiyo inawezekana kweli?". Kwanza niliposikia ile mada ambayo ilikuja kwangu kama swali. Nikakumbuka mbali kidogo, kama miaka miwili nyuma.Wakati huo nilikuwa kidato cha tatu, kwenye ile mada ya Reproduction.
Mwalimu wangu wa Bailojia alikuwa anajua sana hisia za watu,na aliwahi kutoa kamsemo fulani ambako hadi leo ninako kichwani, alisema hivi,
"Popote penye mkusanyiko wa kundi la jinsia moja, basi hadithi zao huwa mapenzi na wakichoka sana huanza kujadiri watu na vyakula". Na mimi nikatabasamu tena baada ya ule msemo kupita kwenye medula wangu.
"Ha haaa,nyie madogo bwana. Yaani ndio kelele zote zile hadi barabarani wanasimama kusikiliza kama kuna ugomvi?". Kiukweli nilishangaa sana ile mada na kuona ni ujinga sana wanachobishania.
Lakini endapo ningejua ni nini kipo ndani ya swali lile, wala nisingeleta dharau na zaidi ningesipoenda pale kabisa.Lakini sikujua hilo, na kama Wahenga hawakukosea waliposema kuwa
"Majuto ni Mjukuu".Na mimi leo hii nimekuwa Majuto.
"Sasa mwanangu si ujibu tu! Mbona mashau mengi hivyo? Kama unajisaidiaga keki bwana". Aliongea dogo mmoja anaitwa Paul,ambaye alikuwa anasoma kidato cha tatu pale pale Dodoma.
Katika marafiki wote wa Babuu,huyo Paul tulikuwa hatupatani sana na tulikuwa tunajibishana majibu ya hovyo pale tukikutana.Na mara nyingi nikiona ananizidi huwa nampiga mkwara ambao saa nyingine unageuka mangumi na kilio kwake.
"Tulia wewe makalio, mtu mzima akiwa anafikilia cha kujibu we yapaswa ufyate mkia kama jike la mbwa ambalo alitaki kupandwa". Nilimjibu hivyo Paul na kusababisha kicheko kwa watu wengine, wakati huo yeye kishajaa sura yake sababu ya hasira.
"Oya, Paul tulia bwana kaka ajibu swali letu kwanza. Ehee tupe jibu lako mkubwa". Hapo aliongea dogo mwingine aitwaye Seth.
Seth yeye alikuwa anasoma pamoja na Babuu kidato cha tatu kwenye shule moja inaitwa City pale pale Dodoma.
"Poa vijana.Ngoja na mimi niwaulize swali dogo kabla sijawajibu lenu". Wote wakakubali niulize, nikaendelea.
"Hivi ninyi nyote, mnaweza kupenda harufu ya pafyumu ambayo ujawahi kuinusa wala kuiona? Yaani hujawahi ata kuigusa lakini ukaipenda, yawezekana hiyo?". Wote wakajibu hapana. Nikazidi kuwachimba.
"Lakini vipi ile pafyumu uliyozoea kujipulizia au unaonaga ndugu au wazazi wako au saa nyingine rafiki zako. Hiyo nayo waweza kuipenda?". Wakajibu kuwa hilo linawezekana. Na mimi sasa nikaingia kwenye mada yao rasmi.
"Basi mapenzi yapo hivyo. Mapenzi ni kama pafyumu, jinsi unavyoitumia na jinsi unavyo endelea kuiona,ndivyo unavyoipenda. Kwani ujawahi kusikia ule usemi usemao kuwa, 'Ukiwa karibu na Ua Waridi basi na wewe utanukia?'. Mjawahi kusikia hilo?".
"Tumewahi, lakini Yeroo, ujajibu swali langu bado". Alijibu Babu huku akinikumbusha kujibu swali lake.
"Ndio nakuja huko Wa Kitaa. Kama hayawezekani niliyo wauliza pale mwanzo,basi vilevile haiwezekani nikampenda mtu ambaye simjui.Sijawahi kumuona wala.....". Kabla hata sijamaliza kauli yangu niliyokuwa nakusudia kuitamka,likalipuka shangwe na kelele la wale jamaa watatu likiongozwa na Paul. Wote walimzonga Babuu na saa nyingine walimpiga hadi masingi.
"Si tulikwambia wewe Ajuza Babuu, bishi kinoma noma. Haya sasa hadi Masai kukuambia ndo umefurahi eeh". Hapo aliongea jamaa mwingine ambaye tangu nimekuja pale alikuwa hajaongea neno zaidi ya kukubali kwa kichwa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilikuwa sijazoeana naye kama wale wengine. Yeye tulipenda kumuita Willy na alikuwa ana undugu na Paul.
Ni kama tayari niliruhusu vurugu ziendelee kwani Babuu na yeye hakukata tamaa ya kuendelea kubisha. Hapo ndipo niliamini kuna watu wabishi duniani, nilidhani kwa sifa zangu za ubishi pale mtaani hakuna awezaye kupambana na mimi kwa suala kama hilo. Lakini kwa kitendo cha Babuu kubishana na watu wanne bila sapoti ya mtu mwingine, ndiyo nikaamini mimi si kitu,kuna zaidi yangu pale mtaani.
Kelele zikawa kelele mle ndani, mimi sitaki kushindwa na Babuu kapamba moto tena anabisha kwa pointi. Kelele zikasimamishwa na mama yake Babuu huku akinishangaa na mimi nikipiga zile kelele.
Mama yake Babuu alikuwa ananiamini sana kati ya rafiki wote wa Babuu,hivyo alihamaki sana kusikia na mimi napiga kelele.
"Haaa, yaani na wewe mtoto wa Masai unabishana na haya mapunguwani? Haya hayana akili mwanangu,tangu saa kumi na moja jioni nimeyaacha yanapiga kelele hadi sasa hivi saa mbili yanaendelea tu! Tena yame kuingiza na wewe,sijui kama yamesoma haya leo". Aliongea mama yake Babuu kwa rafudhi ya Kichaga huku akiwa ana hamaki kwa kinachoendelea.
"Hamna mama, hawa vijana wangu,ni lazima niwape ya darasani na ya duniani pia ili waelewe inavyopaswa kuwa. Sasa ikitokea yule unayemuelimisha na yeye anayajua kinyume na wewe, basi ni lazima litokee zogo kama hili". Nilijitetea kwa mama yake Babuu na alinielewa lakini aliomba tupunguze kelele.
Baada ya kubishana kwa muda mrefu ikabidi tukubaliane kuumaliza ubishani ule kwa kufanya vitendo na kwa kuwa mimi ndiye nilikuwa sina msichana wa kudumu, ikabidi wanikabidhi jukumu hilo.
"Sasa we Masai si ndiyo unajidaigi hutoswi? Basi tutafute demu ambaye ujawahi kumuona wala kumsikia,halafu mtokee na umfanye mpenzi wako kwa miezi mitatu tu! Halafu tuone kama utapenda au vipi". Aliongea Babuu hoja hiyo na kuungwa na watu wote mle ndani.
"Hilo si tatizo kabisa.Nadhani mwanijua kwa sound zangu za mtaani. Tatizo ni demu gani ambaye natakiwa nimpate. Mademu wa siku hizi hawana hata sumu, yaani ukimpa Big Bom mbili na nauli,unajipigia bila wasiwasi. Mi nataka mnitafutie nyie wenyewe,mtoto mwenye msimamo na nitakayechukua muda kumfukuzia. Siyo kidogo tu! Linakubari na unalila mate hapo hapo". Niliongea hayo huku nikiwaonesha kuwa na uzoefu na mabinti wengi wa kipindi hicho.
"Hilo halina tatizo. Eti Seth, huyu tumpe demu gani pale class". Aliongea Babuu huku akimuulizia Seth msichana wa kunitafutia.
"Huyuuu….. labda yule demu yule,rafiki yako. Aliyewatosaga wakina Ally na Jonas".Alijibu Seth.
"Ehee, Rose eeh. Yule yule ndiyo mwenyewe". Akaongeza Babuu.
"Huyo huyo Generose, alafu tuone kama ataweza hata kumpata huyu". Seth akazidi kuchombeza wakati huo mimi na wakina Paul tunawasikiliza mikakati yao.
"Na awe mzuri siyo mnaniletea maprideta mara nyamaume,sijakaa vizuri kumbe Likasa mende au lizombi, mi hayo sipatani nayo hata kidogo". Nikawapa onyo la mapema kabla awajafanya vitu vyao.
"We utamuona tu kaka,utakubali mwenyewe". Akaongea Seth na wote tukakubaliana kwa kumpitisha Generose au kwa kifupi Rose.
Baada ya hapo nikawaelekeza kidogo Jografia na kisha nilikula pale pale na kurudi zangu nyumbani wakati huo ilikuwa ni saa nne za usiku.
NILIPOFIKA nyumbani nilikuta tayari mama amekwisha lala,hivyo sikumsumbua kumpa taarifa kuwa nimerudi wakati huo baba yeye alikuwa safarini katika mihangaiko mingine ya maisha.
Nilifungua mlango wa chumba changu na kuingia ndani lakini nilikumbwa na roho ya kukereka pale nilipokutana na hot pot kwenye meza yangu ya kusomea kwani nilishamuaga mama na kumuambia asiniwekee chakula usiku ule.
"Aaah, mama na yeye, ata kama kunidekeza siyo hivi, huku ni kujiumiza tu! Mimi nilishamwambia sitokula leo,lakini yeye anajidai ana nguvu nyingi sana za kupika mara tatu kwa siku.Baada ya wiki anaanza kulalamika mabega yanamuuma, mara mgongo sijui viganja vya mkono,kumbe sababu ni kupika mara nyingi". Nilikuwa najiongelea peke yangu huku nikiliendea lile hot pot na kulifunua.
"Eheee! Dah! Kwanza mama samahani kwa kukupatia hasira, kumbe leo umenipikia kitu kitamu tamu.Yaani hadi utumbo umeruka kwa furaha baada ya kuona mfumo mzima wa msosi ulivojipanga kwenye hot pot.
Sasa hapa kwa kuwa menyu ipo ya kutosha basi leo ni kutakesha naitafuta njaa kwa kusoma". Nilijikuta natokwa na ile roho ya kukerwa na kuivaa roho ya furaha baada ya kuona hot pot limesheheni tambi pamoja na maini vilivokifanya chumba changu kibadilike ghafla na kuwa na harufu ya kuvutia.
Kiukweli nampenda sana mama yangu, sipendi kumuona akipika pika hovyo katika umri wake uliokwisha enda sana, na ndiyo maana nilishikwa na kero nilipokuta kaniwekea chakula wakati nilimuambia asiweke.Ndipo nikiwa nadhani ni wali au ugali,nikakutana na tambi ambazo hutumii nguvu kwenye upishi wake.
Nilishika daftari la Jografia na kuanza kulipitia wakati huo nilishayatoa yale mawazo tuliyokuwa tunabishania kwa akina Babuu. Kwa kifupi mimi nilikuwa na tabia za kuwa na wanawake wengi sana hasa pale mtaani.Sikujua kupenda bali kuwachezea, hivyo hata ile taarifa ya kutafutiwa msichana kwangu ilikuwa changamsha bongo tu! Sikuitilia maanani.
Hadi mida ya saa tisa usiku ndipo nilipomaliza kusoma,kisha nikala zile tambi na kulala ambapo saa kumi na mbili nilikuwa macho nikijiandaa kwa ajili ya kwenda shule. Ilikuwa kawaida yangu kuwahi kuamka na kwenda shule kwa sababu shule ilikuwa na wanafunzi wengi sana,hivyo ukichelewa unaweza kusoma huku umekalia meza au ukasoma kwa kuchungulia dirishani,hiyo ndiyo Jamhuri Sekondari ilivyokuwa.
Mida ya saa nane za mchana, wanafunzi waliruhusiwa kurudi majumbani mwao lakini mimi na wanafunzi wengine tulibaki kwa ajili ya kujadili masomo hadi pale ilipotimu saa kumi na moja jioni ambapo ndipo nilipoamua kuanza kurudi nyumbani. Lakini kabla sijarudi nyumbani nilipitia kwanza kwa akina Babuu ili nijue mchakato wao umefikia wapi.
Kama kawaida yao,kelele huwa haziishi kwao. Wakati nipo njiani kwenda kwao nilikuwa nasikia kelele za kucheka kwa fujo na huku nikisikia na maneno mengine ya kejeli yakimtoka Babuu. Nilitulia kwanza mlangoni nikisikiliza nini kinaendelea mle ndani, ili kama kuna ubishi nisiingie maana nilikuwa na njaa ambayo ingeleta hasira mwilini mwangu na kumpiga mtu kwa sababu ya ubishi wake.
Baada ya kuhakikisha hakuna mabishano ndipo nikaingia na kulakiwa kama kawaida na Babuu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Oyooo, Masai beibe. Yaani kama mbunge, huo mtai ulivounyonga shingoni, hicho kishati kilivokushika body kama Justine Timberlake,na hicho kiatu kwa chini aisee, Generose akikuona lazima apige saluti. Vipi lakini skuli? Dah! Na mimi natamani niwe navaa tai na shati la mikono mirefu skonga". Ni maneno ya Babuu yaliyokuwa yanamtoka bila kipimo maalumu cha kukadilia maneno.
"Soma dogo,hivi vitu vipo tu! Vipi Seth, mbona umepoa mkubwa". Nilimjibu Babuu kifupi na kisha nikamgeukia Seth ambaye alikuwa amepoa kwa muda mrefu sana. Alikuwa yeye na Babuu mle ndani na kitendo cha mimi kumsalimia kiliangusha cheko kwa Babuu na kumfungulia tena maneno yake.
"Ha ha haaa,leo ungekuwepo ungecheka hadi ukae. Jamaa si kajidai ana madini bwana. Kamfata demu eti akaanza kukupigia saundi. Niulize nini kilitokea". Babuu alianza hivyo na mimi kwa kuwa na usongo wa kujua nini kilijiri,nikamuuliza nini kilitokea. Akaendelea
"Jamaa kapigwa za mbavu na kuaibishwa mbele za watu. Demu akamshikia kiuno kwanza,halafu midomo ikabetuliwa ikawa kama ya mbwa aliyepigwa tofari la kichwani. Jamaa hadi anamaliza kuongea tayari demu kishafura kama parachuti. Hapo sasa ndiyo kimbembe kikaanza. Demu akaita na rafiki zake, wakaanza kusuta njemba hii. Haha haaaa,jamaa akanywea kama mchicha uliopikwa". Babuu akawa anahadithia huku anamcheka Seth, mimi mwenyewe nilitamani kucheka lakini nilijikaza ili Seth asijisikie vibaya.
"Sasa dogo hilo la kumcheka mwenzako?".
"Mwambie huyo braza,yaani njia nzima tumekuja ananicheka". Seth naye akaongea baada ya mimi kumshangaa Babuu.
"Mi namcheka huyu kwa sababu nilimuonya mapema kuwa yule siyo maharage ya Mbeya, maji mara moja, halafu mkaa ni makaratasi. Sasa hapo ana adhabu ya kumwagilia maua wiki nzima pale skuli,halafu akimaliza adhabu, anatakiwa aende na mzazi.
Unajua nini,ule ugomvi na yule demu ukafika hadi kwa mwalimu wa nidhamu. Kengele ikagongwa mzee, tukajipanga mstarini halafu ikatolewa njemba hapo. Ikatangazwa kesi yake halafu zikafata stiki nyingi kinoma. Jamaa kapigwa fimbo huyu leo". Babuu aliendelea kutoa hadithi iliyomkuta rafiki yake Seth wakati huo mimi huruma ilishaniingia baada ya kumuona Seth anafuta machozi.
"Sikiliza Wa Kitaa,huyu ni jamaa yetu bwana,ni ujinga wetu ndiyo umesababisha haya yote. Kama vipi tuachane na mitikasi za huyo demu maana kishajiona keki. Cha msingi wewe Babuu nenda kamsaidie jamaa kwa kumuombea msamaha kwa ticha na demu maana haya ya kuita wazazi tena ni mengine."
"Poa,mi nitajaribu hilo,lakini yule demu lazima nikuletee na wewe upigwe za mbavu kama Seth, hahaaa". Babuu alikuwa anapatana na walimu wengi sana pale shuleni kwao,kwa hiyo lile suala la Seth lingeisha tu kisela.
"We dogo mimi siyo wa kupigwa za mbavu kama nyie. Kwanza sinaga historia hiyo, mama kanizaa handsome ili niwape tabu watoto wenye viburi kama hao. Sasa na wewe peleka fuvu lako wakalipasue. Kama ukifanikiwa kumleta ndiyo utaona jinsi navyoruka majoka kwa mtoto aliyemzingua kamanda Seth". Niliongea hayo kwa kujiamini wakati huo nilikuwa sijui kitakachojiri katika maisha yangu ya baadaye endapo nitampata huyo msichana aitwaye Generose. Laiti ningelijua,kamwe nisingeli thubutu kumtafuta, lakini bado nasema kuwa majuto ni mjukuu lakini upande mwingine naweza nikamshukuru sana Wa Kitaa.
"Poa mwanangu,we jisifie tu! Lakini sisi tunayemjua, nadhani ni lazima utasafa. Kumbuka lengo letu ni moja tu! Unaweza kumpenda ndani ya miezi mitatu!!?". Aliongezea Babuu na mimi nikamjibu kiufasaha jambo ambalo kaliongelea,na kisha nikawaaga na kuanza
Safari ya kurudi kwetu huku nikiwaahidi kuwaôna kesho yake.
Nilirudi nyumbani na kumkuta mama akiwa anapeta mchele na hapo nikamsalimia huku nainamana kudokoa mchele ule, kitendo kilichofanya mama anifinye mkono na kunionya kuwa wanaume hawaingizi mikono kwenye nyungo eti nitakosa mke. Nikacheka na kumuuliza je! nikiwa peke yangu ina maana sitopeta mchele? Alichofanya mama ni kunifukuza huku anacheka kwa jinsi nilivyokuwa na maswali ya kijinga lakini yenye mitego.
“Halafu wee Frank”. Mama aliniita wakati naelekea chumbani kwangu.
“Naam Miss Mama yangu”. Nilimuitikia mama kwa utani huku naenda pale alipo.
“Wee mwana wee, mimi miss tangu lini?”.
“Aaah! Mama we Miss bwana”.
“Kwa hiyo na mimi ni vile vinavyotembea kama vitumbwili vimeona maindi?”.
“Ha ha haaa,mama bwana, wewe ni kama wale wanotembea kwa maringo kama twiga”.
“Embu nitokee hapa, matoto ya mwisho sijui yakoje, yameshaniona mimi bibi yao. Lione kwanza kichwa”.
“Malizia sentensi yako tu! Kichwa kama nini mama, au kama cha Mzee Masai”.
“Halafu ndicho hicho nilichokurudisha hapa, Baba yako yupo humo ndani kakaa”.
“Acha mama, usiniambie,kumbe Dr.Dre yupo ndani?”
“Yupo eee,kaja tangu saa nane”.
“Ngoja nikaze kwanza tai na kuchomekea vizuri, anaweza akanipeleka nikaongee na Sumaye”.
“Na ukichomekea unavyokuwa mbaya, kama umechomekwa au kama Muhogo Mchungu”.
“Mama nitakubutua teke, wewe nitanie tu”. Yalimalizika maongezi yangu na mama yakiwa na utani mwingi ndani yake. Na mimi nikaelekea sebuleni kwa ajili ya kumsalimia baba ambaye alikuwa safarini kwa muda mrefu huku nikimuacha mama akiendelea kutabasamu kwa furaha kwa sababu ya maongezi yale.
“Shikamoo baba”.Nilianza kwa kumsalimia baba baada ya kumkuta sebuleni akiangalia kipindi cha Matukio Ya Wiki kwenye TV.
“Marahaba, hujambo?”. Aliitika Baba.
“Mimi sijambo,pole na safari”.
“Aaah, namshukuru Mungu nimefika salama. Vipi wewe na shule yako”.
“Shule naendelea vizuri,hapa wiki ijayo ndiyo naanza mitihani ya muhula wa kwanza”.
“Ahaa,basi vizuri. Ujitahidi sana si unatuona wazazi wako tunavyo angaika ili msome? Kwa hiyo lipeni hizi fadhira zetu kwa kuleta matokeo mazuri”.
“Hilo halina tatizo mzee, ndicho nachofanya hapa”.
“Basi vizuri, wewe nenda kabadili hizo uniform halafu uje tuongee mengine”. Alimaliza baba kuongea na mimi, na mimi nikajibu sawa na kutoka nje ambapo nilimkuta mama ndiyo anaosha mchele.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mama na wewe, huo mchele una ufua nini?”.
“Nitakupiga na mwiko wewe, embu lione kwanza tumbo lake”.
“Hahaa, wewe mama matani yako unataniaga viungo vya mwili tu”
“Embu ondoka hapa,nisije nikagonga hilo likisogo lako na mwiko bure”.
“Haya mama wewe si haunijali, mimi tangu nile tambi jana…………. Ehee, halafu nimekumbuka, jana zile tambi mama sijui ulipika na vidubuwasha gani, tambi tamu kama nyimbo za dini”.
“Lione kwanza.Wewe si ulisema hauli? Yamekukuta yapi tena”.
“Hahahaaa, ungeniwekea ugali uone kama ungelika”. Bado nilikuwa naongea na mama ambapo wakati huo alikuwa anaeleke jikoni na kuanza kupika ule mchele huku mimi nikiondoka na kuachia kicheko kwa kamkwara kangu kadogo.
Nilivua sare zangu za shule na kuzitoa nje kwa ajili ya kuzifua na baada ya kuzifua niliingia sebuleni kujumuika na baba kwa chakula cha usiku na baada ya kula tuliongea kidogo kisha nikamuaga kwa ajili ya kwenda chumbani kwangu kujisomea.
Nilikaa wiki nzima sijaenda kwa akina Babuu kwa sababu nilikuwa katika harakati za kujisomea kwa ajili ya mitihani ya muhula, hivyo mara nyingi nilikuwa nachelewa kurudi nyumbani na huwa nimechoka jambo lililokuwa linasababisha nikifika nile na kulala.Baadaye kidogo naamka na kupitia maswali halafu nalala tena hadi asubuhi. Hiyo ndiyo ikawa ratiba yangu.
Ilikuwa ni Jumapili moja nikiwa natokea kanisani, ndipo nikaamua kupitia kwa akina Babuu ili kumjulia hali. Siku hiyo kulikuwa kimya sana hivyo nikafarijika kwa hilo.Moja kwa moja nikaenda hadi ndani kwao.
“Hilooo,limeogopa ndiyo maana lilikuwa halitaki kuja kupata taarifa”. Yalikuwa ni maneno ya kunilaki kutoka kwa Babuu.
“Tulia dogo “advance” siyo kirundo cha mchanga bali ni mlima mrefu ambao hujui mwisho wake.Ukilegea,unalegea na maisha yako. Shikamoo mama”. Nilimpaka Babuu na kumaliza kwa kumsalimia Mama yake ambaye siku hiyo alikuwa nyumbani na siku zote kama hizo.
Baada ya kuitikia salaam yangu aliniomba nimfundishe Babuu masomo ya ziada jambo ambalo sikukana hata kidogo.
Baada ya kukubaliana na mama yake Babuu, Babuu alinishika mkono na kunivutia chumbani kwake na kuanza kuniraumu kwa nini sikuonekana muda wote huo.
“Yaani wewe jamaa sijui vipi,au na wewe unadevela kupigwa masingi na kushikiwa mauno kama Seth.Mimi nimeshachonga na mtoto yaani kitu mwake kabisa,ilibaki wewe tu! Kuja kutema madini halafu ukazingua”. Yalikuwa ni maneno ya Babuu kuonesha kuwa mambo yamewiva.
“Dogo si nimekuambia kitabu kinabana? Embu nipe mchakato uliendaje”.Yalikuwa maneno yangu ya kujitetea huku nikitaka anipe habari kamili.
“Mtoto si ndo nikamfata bwana,mashau kibao. Anataka kuleta habari za kunifanya mimi Seth. Nikamtuliza kwa samahani na kumsihi asilete filamu kama ile”. Kwa manjonjo mengi ya Babuu alikatulia kidogo halafu akatoka nje.
Baada ya dakika kama tatu alirudi chumbani akiwa na sahani ya wali pamoja na chupa ya chai. Akatoka tena kisha akarudi na vikombe viwili halafu akanikaribisha lakini nilikataa kwa kuwa huwa sipendi kunywa chai nyakati za asubuhi.Huku anaendelea kula akaendelea kunipa habari
“Mtoto akawa mpole kama moto umeona maji sababu mimi ndiyo kichwa chake, huwa namsaidia kwenye masomo yake.Kwanza nikamuambia kuhusu Seth na kumuombea msamaha halafu nikamuingizia ile taarifa kama tulivyopanga. Alianza kuleta ugumu wake lakini mwisho wa siku alinipa namba yake ya simu na kusema anataka akujue vizuri kwa maelezo yako wewe binafsi”. Hapo nikatabasamu baada ya Babuu kunipa namba ya mtu ambaye sijawahi kumuona wala yeye hajawahi kuniona, simjui wala hanijui.
Nikapokea namba ile na kumuahidi Babuu kuwa niataongea naye siku ile ile kisha nikamuaga Babuu na mguu kuelekea nyumbani ukaanza huku nikiwa na shauku ya kufika mapema ilinimpigie simu mtoto huyo nisiyemjua. Nilipofika nilifungua mlango wa chumba changu na kuchukua simu yangu halafu nikaifungua kisha nikaanza kubofya namba ambazo kanipa Babuu.
“Haloo”.Ilikuwa ni sauti ya kike ikipokea simu yangu baada ya kuita kama mara tatu.
“Haloo, mambo vipi Rose?” Nami nikajibu kama namjua.
“Poa, nani mwenzangu”.Alijibu salamu yangu na kisha akachimbia msalaba wa swali masikioni mwangu.
“Mimi ndiyo yule rafiki yake Babuu ambaye nilimtuma aje kuchukua namba yako aniletee”.
“Ehee afadhari, ulikuwa unataka nini?”
“Ngoja kwanza, taratibu tutaelewana tu!”.
“Wewe kama huongei bora ukate simu, mimi sina muda wa kipumbavu hivyo”.
“Basi naomba kuonana na wewe”.
“Sina muda, kwa heri eeh”.
Yalikuwa maongezi yetu na mwisho wa siku alikata simu na hata nilipompigia hakupatikana tena na nahisi alibadilisha na namba ya simu kabisa. Nilikuwa sipendi kabisa wasichana wasumbufu kama wale hivyo nikaona kama ananizingua tu! Isitoshe mtu mwenyewe simjui, hivyo nikapuuzia na kuendelea na mambo yangu hasa kimasomo.
*****************
Kama kawaida yangu, nilikuwa mtu wa wanawake sana lakini naporudi kwenye suala la masomo nakuwa mtu mwingine kabisa, na ndiyo maana hata wakina Babuu waliniamini sana na kunipa nafasi ya kuwafundisha masomo ya ziada baada ya kutoka shule.
Nilikuwa najiandaa na mitihani yangu ya muhula wa kwanza hivyo sikuonekana mtaani kwa muda mrefu sana jambo lililomfanya siku moja Babuu aje nyumbani kunitembelea. Kiukweli dogo alikuwa anajipenda na anaelewa cha kuufanya mwili wake upendeze, lakini alikuwa anishindi hata kidogo kwani alivyoingia chumbani kwangu aligundua kuna tofauti kubwa sana kati yangu na yake, kuanzia chumba changu,mavazi, hadi mpangilio wa vitu vyangu. Labda yeye alinizidi weupe na ujanja wa mdomo. Mimi ni mweusi lakini siyo mweusi tii na mwili wangu mrefu niliyoujenga kwa mazoezi hasa ya kukimbia na kucheza mpira wa miguu,nikichanganya na sura yangu ya upole lakini haishi tabasamu, nimtake nani kwenye kile kimtaa chetu anikatae? Kwanza wakisikia wanaitwa na mtoto wa Masai wanaona kama wameitwa na Malaika au wanaona kama maisha mazuri yamewakaribia, kumbe nilishawawekea rehani kuwa sitokuja kuwapenda hata mara moja.
Kwangu ilikuwa ni kuwajulia hali kwenye miili yao halafu baada ya hapo kila mtu anafata njia yake. Huyo ndiye Frank Masai au Man’Sai kama mwenyewe nilivyopenda kujiita.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Dah! Mwanangu ghetto lako linang’aa halafu linanukia vizuri”. Alianza kusifia Babuu baada ya kuingia chumbani mwangu na kukutana na mambo mazuri.
“Hahaaa, dogo uadhani kuna kizuri cha bure? Usione vinaelea,vimeundwa”.Nikamjibu Babuu kwa mafumbo huku nikicheka kwa furaha baada ya kuona hata mwanaume kakubari chumba changu.
“Sasa hapo umeanza majungu, au na wewe ni Nasma Khamis? Watu tunakusifia we unaanza kuleta mambo ya kuelea hapa”. Babuu alikuja juu baada ya maneno yangu yale.
“Sasa sikia dogo,si una mmanya yule demu dingi yake mwanajeshi?”.
“Yupi huyo? Na baba yake anaitwa nani?”
“Dogo na wewe. Yule dingi yake siku ile alikuwa anatoka kazini halafu kwa bahati mbaya mdogo wake Isaya akamkosa kosa na baiskeli, dogo hadi alipigwa banzi la kisogoni”.
“Ahaaa, hahahaaaa. Lile dingi wanaliita Mbogombogo?”.
“Eheee,yule yule. Sasa si uamfahamu yule mtoto wake wa mwisho wa kike?”.
“Yeah, si kale kazuriii”
“Mimi sijui kama kazuri au kabaya, anaitwa Ritah yule demu”.
“Eee, ndiyo ndiyo, anaitwa Ritah. Sasa kafanyaje”.
“Ndiyo siri ya geto kuwa safi hivi.Wewe unadhani mimi naweza kuinama na kupiga deki humu? Nampigia deki nani? Ma broo wapo huko far ya mbali”.
“Acha bwana, ina maana na kale ni kademu kako”.
“Siyo kale,sema yule. Tayari kishakuwa mkubwa mwenzako, tena nimekata utepe mwenyewe,hapoo kwenye bed. Siku hiyo ilikuwa jasho na vidamu”.
“Dah! Mwanangu namzimia kichizi yule mtoto ila kila nikitema madini naambulia nazi za mbavu”.
“Tatizo mnatema makaa ya mawe wakati mwenzenu natema Diamond mixer Tanzanight, unadhani mimi na wewe tutakuwa sawa?.”
“Hahaaa,kwa kujisifia boya wewe. Sasa mbona Generose kakushinda?”.
“Siyo kanishinda, kimtu kinajidai matawi ya juu kichizi, wewe unadhani mimi nitapigania utumbo huo?”.
“Lakini mwanangu wewe si ulisema unataka mgumu kumpata? Vipi tena umegairisha?”.
“Sijasema awe mgumu hata kwenye kuongea, ila aoneshe msimamo wa kuwa yeye siyo ndondo la Mbeya”.
“Sasa si ndiyo kama hivyo? Kwani wewe ulipompigia simu alisemaje?”
“Kama kawaida yao, kanishushua pale halafu kakataa kuonana na mimi”.
“Hahaa, nilidhani utanidanganya. Kaniambia hivyo hivyo,halafu akaniambia kaitupa na ile line”.
“Ndiyo hivyo,maana tangu siku ile,hakupatikana tena”. Nilikuwa naongea na Babuu huku napanga nguo zangu nilizozifua na baada ya hapo nikatoka nje mara moja na niliporudi, nilirudi na soda mbili za fanta na moja nikampa Babuu,kisha tukaendelea kuongea.
“Dah! Mwanangu unajipenda kichizi,kitu cha Fanta nini pale kati”. Alianza Babuu baada ya kupokea ile soda.
“Dogo mbona kawaida tu! Lakini angalia usije ukatapika maana najua hujawahi kupiga hicho kitu mida kama hii”.Nikamzingua kidogo Babuu halafu tukaendelea.
“Aaah wewe, uandhani mimi wa hivyo?Ehee kwanza nipe taarifa za mtoto Ritah”.
“Aaah, mi kile napita tu! Kwanza nilikuwa sina hata mpango nacho. Ila mama anampenda kichizi. Unakuta nipo skuli Bi Mkubwa anakileta geto, kinapiga deki halafu ndo kinasepa”.
“Haa, ina maana hata maza wako anamfahamu? Dah!kweli una bahati”.
“Mama ndiyo alikuwa anamtaniaga hapa akija kuchota maji. Ile mama mkwe nini, katoto kakawa kanapenda kinoma.Siku moja nini,ndo nikapiga saundi,mtoto akasahisha kwa kuweka pata. Ndo basi”.
“Dah! Kweli. Haya bwana wewe endelea kujilia katoto hako. Kwa hiyo vipi Generose?”.
“Sasa yule ngoja nimpangie mkakati wa kumpata. Kesho kwa kuwa ndiyo namaliza pepa,basi kuanzia keshokutwa nitaanza kuja kwenu nikupe mkakati wangu”.
“Poa, mimi nikusubiri kamanda mwenyewe”.
“Vipi Seth? Kesi yake iliendaje?”
“Yule tuliyamaliza kibingwa na ticha. Halafu Paul na Willy wanaulizia kichizi kuhusu huu mpango”.
“Waambie wasijali,nipo kwenye mkakati kabambe, nitauita ‘Generose Time’, yaani huo ni muda kwa ajili yake tu! Ila itabidi tuufanye mimi na wewe hadi tufanikishe”.
“Poa,wewe maliza pepa halafu unipe huo mkakati wako”. Tulimaliza kuongea kuhusu mambo yale ya kishetani na kisha tukaanza kuongea mambo mengine huku tunashushia na soda zetu.Hadi saa tano za usiku Babuu alikuwa pale na kwa kuwa alishaaga kwao wala alikuwa hana wasiwasi. Baada ya kumaliza maongezi yetu na kusoma kidogo ndipo nikamsindikiza kurudi kwao.
Kesho yake mapema ikiwa ni Ijumaa, tulimaliza mitihani ile ya muhula wa kwanza hivyo na mimi niliamua kuwahi kurudi nyumbani mapema kwa ajili ya kupumzisha ubongo wangu. Wakati narudi nilikutana na kundi kubwa la wasichana waliokuwa wanasoma ile shule anayosoma Babuu na wengi wao walikuwa wanasoma kidato cha tatu kutokana na rebo zao walizoweka mabegani kujielezea.Sikuwa na wasiwasi katika maswala ya kuongea na watoto wa kike, hivyo kwa ujasiri mkubwa nikalisimamisha kundi lile la wanawake na bila kuwachelewesha nikaanza kuwaongelesha.
“Samahanini wanafunzi, namuulizia dada mmoja anaitwa Generose”.Nikawatupia hilo swali.
“Aaah, huyo mbona hatumjui, kwanza ndiyo kwanza hilo jina tunalisikia kwako”. Aliongea mwanafunzi mmoja kwa kudakia huku akionekana yeye ndiye kiongozi wa kundi lile.
“Mh! Jamani haiwezekani, mimi nina taarifa za…..”. Kabla sijamaliza kauli yangu nilimuona Babuu anakuja huku anatabasamu kwa mbali.
“Eheee, yule pale anakuja ngoja afike”.Niliongea hayo huku nawaoneshea wale wanafunzi barabara anayokujia Babuu.
“Hichi kitoto kimbea, embu twendeni jamani. Kaka sisi hatumsubiri mtu halafu huyo Generose sisi hatumfahamu”. Aliongea yule kiongozi wa kikundi kile na kuanza kuondoka, na mimi hapo hapo nikaanza kwenda kule anapotokea Babuu na nikakutana naye.
“Naona ulikuwa unaongea na mtoto”. Alianza Babuu baada ya kunipa tano kama salamu
“Mtoto yupi dogo?”
“Si Generose!!”
“Ishi!,kwani pale yupo wapi?”. Huku nageuka nyuma kuangalia lile kundi.
“Si yule pale mrefu mrefu aliyesuka!!”
“Alaa, sasa mbona nimewauliza kama wanamjua Generose,tena yeye ndiyo akajibu kuwa hawamjui!!”
“Hahahaaa,kakuzingua tu! Ndiye yeye yule”.
“Ahaaa,basi poa. Kumbe ndo mtoto mzuri vile? Nisubiri, baadaye nakuja na mkakati wangu, lazima nimpate”. Niliongea kwa hamasa huku nikiahidi kumuona Babuu baadaye kwa ajili ya kumpa mkakati wangu. Kiukweli Generose alikuwa mzuri sana tu! Hivyo niliahidi kumpata baada ya kumuona kwa mara ya kwanza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilimpa mgongo Babuu na yeye akanipa wake, na hapo safari ya kila mtu kuelekea anapoishi ikaanza.Njiani mawazo mengi yakawa yanapita huku nikijiuliza kama mkakati wangu utafanikiwa. Japo niliahidi kukutana na Babuu baadaye lakini roho ilikuwa inatamani sana nionane naye muda ule ule kwa maana ule uzuri wa Generose, ni kama ulichafua nafsi yangu kwa udongo ambao MUNGU alimuumbia. Acheni nimsifie tu jamani, japo alikuwa kavaa nguo za shule lakini kile kibiongo kilichokaa chini ya mgongo wake, kilionekana vyema na kupelekea huku nyuma kuacha lawama kila atembeapo. Nilijiwazia peke yangu hadi nikajikuta nikiwa na tabasamu huku natembea jambo lililofanya baadhi ya watu kunioneshea vidole kwa kuhisi labda nimeanza kuwehuka, kumbe mwenzao macho yangu yaliona lulu ya ajabu wakati natoka huko napotoka.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment