Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

NIACHE NA MOYO WANGU - 4

 





    Simulizi : Niache Na Moyo Wangu

    Sehemu Ya Nne (4)



    Ilipoishia jana…



    Wakaingia hadi meza kuu ya polisi. Stan akaenda kuitwa na polisi mmoja akiwa ameshika tochi kubwa mkononi mwake.



    Songa nayo sasa…



    Punde Stan aliletwa na yule polisi alioingia selo akiwa na tochi kubwa mkononi.

    Macho ya Stan yakatizamana na ya mchungaji John pamoja na yule mzee. Stan alishamsahau mchungaji John akilini mwake, japokuwa alikuwa amevaa mavazi ambayo shingoni kuna kitambaa cheupe kilichokatiza kwenye mbele ya kola kuonesha kuwa ni mzee wa kanisa au mchungaji haswa. Picha ya karibu iliyokuwa ikimjia ni ya yule mzee kutokana na kuonana naye siku mbili zilizopita. Mzee ambaye hawezi kumsahau kwa msaada aliokuwa amaeutoa wa kumuhifadhi yeye na Sara wake. Mzee ambaye alimwambia ukweli kuhusu wazazi wake halisi walipo na kuwa ni vichaa wa kutupwa.

    “Shimkamoo mzee!! Shikamoo mchungaji” Alisalimia Stan.

    “Stan?” Aliita mchungaji.

    “Naam!!”

    “Unanikumbuka mwanangu?” Aliongea mchungaji akimkazia macho Stan

    “Hapana sikumbuki nikumbushe mzee wangu?” Aliongea Stan.

    Yule mchungaji aliangalia uku na kule, mapolisi walikuwa bado wakimtolea macho yule mchungaji na Stan. Bado Stan alikuwa katika ulinzi mkali akiwa na pingu mikononi. Mchungaji alimvuta mpaka karibia na masikio yake kisha akamnong’oneza kitu Stan.

    “Stan mwanangu mimi ndio niliokubatiza toka ukiwa mdogo naitwa mchungaji John”

    Stan akaitikia kwa kichwa. Yule mchungaji akaichukuwa mikono yake nakutoa ile biblia ndogo aliokuwa ameichukuwa. Akamuekea kichwani Stan nakuanza kumfanyia maombi ya muda mfupi kwa sauti ya chini. Maombi juu ya Stan aweze kuyashinda majaribu aliokuwa nayo. Majaribu yaliompelekea mpaka kuwekwa ndani. Mapolisi hawakuwa na kipingamizi chochote juu ya yale maombezi kutokana na kupokea kiasi kidogo cha pesa kutoka kwa mzee wa pembeni na mchungaji. Kiasi kile kiliwazubaisha nakumuacha Stan na wale wazee wajitanue naye kwa muda. Baada ya maombezi ambayo hayakuwa maombezi ya sauti ya juu sana. Yule mchungaji alimtoa ile biblia kichwani mwa Stan.

    “Stan mwanangu?” Aliita mchungaji.

    “Naam”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mchungaji John akamfanyia Stan kama alivyofanya awali. Alimvuta Stan sikio na kunong’ona kitu kwa mara nyingine tena.

    “Hii biblia chukua, itakukinga na mabalaa yote pia itakusaidia. Muombe sana Mungu, Mtangulize kwa kila jambo utafanikiwa mwanangu Stan, sawa?..

    Kabla hajamalizia kuongea polisi akahisi kitu.

    “Hiko nini unampa? wee mzee? Wee wewe si naongea na wewe nini hiko?”

    “Ammhhh hii ni biblia mkuu na hii haina tatizo kwani ni maandishi tu yaliomo ndani.”

    “Haturushu kitu chochote achukuwe na hakuna makubaliano ya aina hiyo. unataka tufukuzwe kazi kwa ajili yako? Hivi kwanini watanzania mkipata nafasi kidogo mnataka kuitumia tofauti? haya kijana?” Aliongea polisi yule wa zamu.

    “Naam afande!!”

    “Mguu mmoja nataka ugeuze nyuma mwenyewe, kamanda Jose, mchukue mrudishe ndani kama kuombea umeshamuombea inatosha!!” Alimaliza kuongea yule polisi kwa ukali.

    “Lakini mkuu…

    Kabla hajamalizia kuongea yule mzee polisi yule alimdakia.

    “Lakini nini? sihitaji mjadala afande mrudishe huyo ndani!!”

    Hasira kali zilikuwa zimeshazunguka kichwa cha Stan. Mishipa ya hasira pembezoni mwa uso ilikuwa imemtuna vilivyo. Hakuwa Stan wa kawaida kwani na macho pia yalikuwa yamemtoka sana. Ule unyenyekevu aliokuwa ameonesha kwa maaskari akaona ni bora upotee kuliko kukataliwa kuchukuwa biblia ambayo haina kitu chochote ndani yake. Alichokifanya alikaa kimya kwa muda.

    “Wee mchungaji? Wa kanisa gani? na nitaamini vipi kama wewe mchungaji mpaka umkabidhi huyu kijana biblia?”

    Haraka haraka mchungaji alikuwa na vibali vyake katika gari. Aliomba kwenda kuchukua. Haraka haraka akaenda alipopaki gari lake na kurudi pale kituoni. Stan na yule polisi walikuwa wameganda. Hakuweza kupelekwa tena ndani kama alivyotumwa yule afande na mwenzake. Walibaki wakishangaa tukio linaloendelea.

    “Hivi hapa afande?” aliongea mchungaji John baada ya kuleta vielelezo vyote vilivyokuwa vikithibitisha kuwa yeye ni mchungaji halali na tena ni mmiliki wa kanisa kubwa maeneo ya Tumbi,kibaha.

    Yule afandea lichukua vile vielelezo vyote kutoka kwa mchungaji John nakuanza kuvipitia kimoja baada ya kingine uku akitikisa kichwa.

    “Mchungaji John” aliita afande baada ya kulisoma jina la mchungaji katika moja ya vile vitambulisho vyake vya uthibitisho.

    “Naam!!”

    “Nipe hiyo biblia hapa na wewe kijana hakikisha hii bibilia unaificha asije kuona mkuu wetu ama kamanda mwingine yoyote tofauti na hapa siye unaotuona. Narudia tena ole wako ionekane ujue kesi yako itaongezeka sa

    wa!! Utakuwa ukiificha wakati wa kuomba naheshimu sana dini yako na ndio maana nilitaka kuthibitisha kama huyu anayekupa hii biblia ni mchungaji halali. Pengine ni madawa ya kulevya yamechanganywa au kuna sumu za kuwadhuru wenzako humo ndani. Vichukue.” Aliongea yule polsi na kumpatia Stan ile biblia ndogo.

    Stan alikabidhiwa na kilichofuata baada ya hapo ni Stan kurudishwa Selo kisha mchungaji na yule mzee kuondoka zao nakuwaacha mapolisi kuendelea na lindo lao la usiku kama kawaida.





    *********



    Jiji la Dar es salaam lilikuwa likizidi kunga’ra kila kona kwa taa taa zilizokuwa zimewekwa pembezoni mwa barabara kuashiria usiku umewadia. Pilika pilika za watu kwa usiku zilikuwa zimeshapungua kutokana na muda kwenda sana. Kwa kukadiria huenda ilikuwa imetimu saa sita au saba za usiku. Barabara nyingi hazikuwa na foleni kabisa kutokana na muda kwenda sana.

    Katika barabara ya Mandela itokayo Buguruni kuelekea Ubungo alionekana Sara akishindwa kukatiza barabara ya lami japokuwa kulikuwa na magari machache. Honi za hapa na pale za kila gari lililopita ndio zilimtia woga sana. Alionekana kupapasa mikono hewani kwa kila alivyokuwa akipiga hatua. Hakukuwa na msamaria mwema wa karibu kumuwezesha kuvuka ile barabara na hata kama angevuka haikueleweka mara moja Sara anapotoka wala anapolekea. Eneo la pembeni yake alikuwepo Devotha. Alionekana akiwa amelala pembezoni mwa barabara ile ya lami uku akitokwa na damu nyingi zikitambaa chini yake.

    Baada ya kukatiza magari mengi pasipokusimama,hatimaye gari ndogo aina ya ‘Vitz’ ilisimama kando kando ya ile barabara karibu na Sara.Ile gari baada ya kusimama ikapiga sana honi kumuita Sara. Sara ambaye hakujua hata mlio wa honi unapotokea. Ganzi!! kimya kikatawala kwa muda kutoka kwa Sara.

    Ndani ya ile gari alishuka mdada mmoja nakumfuata Sara eneo alipo nakumshika mikono akimuangalia usoni kwa kutumia mwanga wa zile taa za pembezoni mwa barabara.

    “Binti nini kimekusibu jamani? unaenda wapi na umetoka wapi usiku huu?” Aliongea yule mama.

    “Niache, niache nimeteswa sana nilipotoka sipajui na hata ninapoelekea sipajui nateseka tu nateswa kila kukichwa najua na wewe unataka kunitesa haya fanya ufanyavyo? fanya ni bora mniue tu nimeshachoka na maisha mie. Niueni tu si ndio mnavyotaka?” Aliongea Sara kwa kulalamika.

    Yule mama alioonesha huenda ni msamaria mwema alikuwa akitaka kumuokoa kwanza Sara asiije kujiingiza katika barabara ya lami akagongwa na magari. Alimshika na kumpeleka pembeni kiubishi bishi japokuwa Sara aliendelea kuwa mkali kwa yule mama.

    “Kwani unaitwa nani? binti mimi nipo hapa kukusaidia na si kingine. Mimi si mtu mbaya kama unavyofikiria, nakusaidia niambie kwenu wapi?“ Aliendelea kumhoji yule mama msamaria mwema.

    “Naitwa Sara!” aliongea.

    “Huyu mwenzako hapa chini anaitwa nani na mmetoka wapi na amefanyaje mpaka anatokwa damu”

    “Hapana simjui na sijamuona. Nilipotoka sipajui tizama macho yangu? sina macho nitawezaje kutambua nilipotoka? ila nachokumbuka nimeteswa sana mwili wote nakuparauliwa kama ‘Tai’.” Aliongea Sara.

    “Pole sana binti twende ndani ya gari langu, twende!!” Aliongea yule mama uku akimshika mkono Sara nakumuongoza mpaka alipokuwa amelipakai gari lake. alimpakaiza Sara garini kisha akamrudia Devotha nakumpakiza hivyo hivyo bila kujali damu damu alizokuwa nazo.

    “Hapa niwapelekeni kwanza mkapatiwe matibabu hospitalini kisha nitajua jinsi ya kuwapata ndugu zenu sawa?” Aliongea yule mama baada ya kumpakiza Devotha. Alikuwa tayari ameshakaa siti ya mbele na pembeni yake akiwa Sara na upande wa siti ya nyuma alimlaza Devotha.

    Safari kutoka katika lile eneo ambalo alipatikana Sara na Devotha ilianza. Safari ya kuelekea hospitali uku Sara akiwa mzima lakini Devotha akionesha kutokuwa na matumaini ya kupona. Baada ya mwendo mrefu kidogo kimya kikiwa kimetawala ndani ya gari yule mama alifungulia redio ya gari ake. Alikuwa akipenda sana miziki aina ya ‘country’ redio ya gari ilianza kwa kupiga nyimbo ya Dolly Parton. Nyimbio ya ‘Coat of Many Colours’ ndio ilikuwa ikimliwaza. Kimya kiliendelea kutawala na sasa baada ya kuisha nyimbo ya mkongwe wa muziki wa ‘Country’ Dolly Parton ilifuatia nyimbo ya mkongwe mwingine wa muziki huo Don Williams. Nyimbo ya ‘This world is not my home’ ndio ilikuwa ikichukua nafasi yake katika gari la yule mama msamaria mwema. Nyimbo ilizidi kumkosha yule mama msamaria mwema pemebi akiwa na Sara na kwa upande wa nyuma akiwepo Devotha. Maruani!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Taratibu nyimbo ile ikaingia katika ngome ya masikio ya Devotha. Devotha ambaye tayari alikuwa ni mmoja wapo kati ya kina Kakamega waishio mjini. Devotha ambaye mikoba ya kinakakamega alirithishwa kutoka kwa baba yake na ndio kazi wanayofanyaga maishani mwao ifikapo usiku kila siku. Nyimbo ya ‘This world is not my home’ ndio ilichukuwa sura mpya katika gari la yule mama msamaria mwema. Maskini kutokujua!! Nyimbo ile aliyeipenda yeye ndio nyimbo ambayo ilikuwa ikipendwapia na kina Kakamega wote, popote inapopigwa nguvu ya mwanakakamega yoyote aliokuwa amezidiwa hurejewa na ufahamu upya. Nyimbo hiyo sasa ikawa ikiutekenya mwili wa Devotha. Devotha akatekenyeka!! akajigalagaza taratibu mithili ya nyoka akinyemelea kitoweo cha alfajiri sana. Devotha akajipenyeza kiupande upande akitaka kuelekea siti ya mbele ya dereva. Alitaka kwenda kumdhuru yule mama na afanye njia zozote afike naye Kakamega yeye na Devotha baada ya kuishiwa nguvu nakudondoka barabarani akiwa na Sara kwa nguvu za kishirikina. Devotha aliutoa ulimi mrefu kinywani mwake. Ulimi uliokuwa ukinona damu damu nyingi alizokuwa nazo pindi alipokuwa amelala eneo alilookolewa. Eneo la pembezoni mwa barabara ya lami iendayo Ubungo. Ule ulimi ukazidi kasi na utelezo mpaka ukagonga hodi shingoni mwa yule mama msamaria mwema aliokuwa akiburudika kwa nyimboi ile ya utaratibu.

    Muda wote Sara hakuweza kujua kinachoendelea pembeni yake kutokana na kuwa mpofu wa macho yote mawili.



    ********







    Ulimi wa Devotha ulizidi kupenyeza pembezoni mwa siti ya pembeni ya yule mama msamaria mwema. Hakuweza kuuona ulimi kutokana kwanza na ule ulimi kuwa mrefu sana na mweusi kupitiliza. Pili mawazo ya yule mama msamaria mwema yalikuwa mbali sana yakiliwazwa na nyimbo laini kutoka kwa Don Williams. Yule mama akiwa bado katika mawazo ya hapa na pale mara simu ya yake ikaita. Akainama mpaka karibia na redio yake ya gari ilipokuwa nakuipunguza sauti ile nyimbo iliokuwa ikiendelea kuimba. Nyimbo ambayo kwa upande wa Devotha ilikuwa ikimletea msisimko wa hali ya juu wa kutaka kumdhuru yule mama kutokana na kuwa nguvu za ziada mara mbili yake.

    “Halloo!! halloo!!” aliongea yule mama na simu.

    “Nakusikia, haloo nani mwenzangu sikusikii vizuri, sikusikii nani??”

    Kitendo cha yule mama kushindwa kuelewa simu yake iliokuwa ikizungumza pale pale alishangaa shingoni mwake kupita kitu kilaini sana. Kitu kilichomlowesha shingo yake mara moja nakuwa laini.

    “Mamaaaaa maaaaaa” Alilalama yule mama kwa sauti ya juu.

    Hali iliyomsababishia kupoteza uelekeo wa ile gari yake. Gari ikahama njia. Ikaweweseka!!

    Devotha akapata ukakamavu.. Akaunyosha ule ulimi wa miujiza kwa nguvu zote. Ulimi ukamtoka vilivyo. Ukahama kutoka shingoni mwa yule mama nakuhamia maeneo ya kiunoni. Haukuwa ulimi kama wa binadamu wa kawaida kwa jinsi ulivyokuwa mrefu kupitiliza na hata rangi yake kuwa tofauti kabisa. Yule mama msamaria mwema akaweweseka mithili ya binadamu anapotaka kukata roho. Akapoteza fahamu ghafla!

    Devotha alichokifanya baada ya hapo aliurudishia ulimi ndani ya mdomo wake. Ulimi ule wa maajabu ukarudi. Akafungua mlango bila kujali uelekeo wa gari lililokuwa limehama njia kutokana na yule mama kutokuendesha tena. Akamtupa yule mama msamaria mwema mpaka nje kabisa ya ile gari. Puuu!! akadondoka nakugalagala!!

    Devotha akahamia rasmi siti ya mbele yake. Siti ambayo ilikuwa imebakiwa na mtu mmoja tu kwa upande wa pembeni yake. Sara. Ndio Sara ndio alikuwepo upande wa pembeni akiwa hajui kinachoendelea kutokana na kuwa kipofu. Hata ule mtingishiko wa gari kuhama njia kwake aliuhisi tu. Hakujua kama yule mama msamaria mwema alishafunguliwa mlango muda mrefu na Devotha kumtoa nje.

    “Umetulia tu mwangalie kwanza!!” Aliongea Devotha baada ya kuhamia siti ya mbele pembeni ya Sara.

    “Ndio” Alijibu Sara. Akili yake yote alikuwa akijua kuwa anayemwongelesha ni yule mama msamaria mwema.

    “Na ole wako unisumbue tena kama ulivyonisumbua wakati nimekutoa kule hospitali” Alilalama Devotha.

    “Nikusumbue kwa kipi? Kwanini mimi tu? Nimewakosea nini jamani?” Aliongea Sara kwa kulalamika.

    Alishajua wazi hakuwa na mtu sahihi. Alionesha kukata tamaa kabisa kutokana na kukaripiwa na Devotha.

    Devotha hakujua kuendesha gari zaidi ya kukaa ile siti ya mbele nakusubiri gari ligote. Gari likaenda mwendo wa kawaida likidunda dunda kutokana na kuwa katika kimlima. Likagota kwa kugonga mtaro kwa pembeni yake. Likasimama!!

    Hakukuwa hata na mmoja alioumia. Si Devotha wala Sara waliokuwa hawajajerehuliwa kutokana kwanza na lile gari kuwa na mwendo wa kawaida sana. Haraka haraka Devotha alishuka na kuelekea upande wa pili wa lile gari. Upande wa pili wa siti alipokuwamo Sara amezubaa mwenyewe kwa kutokuwelewa anapoelekea kutokana na upofu wake.

    “Twende umezubaa tu kama ng’ombe jike. Haya twende nikupeleke kwa wazee huko” Aliongea Devotha kwa kejeli.

    “Siendi!!, wewe nani unayenifuatilia hivi. Wewe ni nani unanitesa muda wote huo na kunifanya hivi. Eee mwenyezi Mungu nifungue japo macho kwa sekunde tu nimuone huyu anayetaka kuniharibu. Anayenitesa kutwa!!” Aliongea Sara uku akilalamika kwa kwikwi ikiwa imembana vilivyo.

    Devotha hakutaka kusikio hata neno moja linalotoka mdomoni mwa Sara kuliweka kichwani mwake. Hakutaka kusikia la mkuu. Mawazo Mgando!!

    Mawazo yake yote yalikuwa yamekaa kikakamega. Aliona ni wazi wana Kakamega watafurahi endapo akimpeleka Sara. Aliona ni moja ya kafara kubwa sana maishani mwake kutokana na kutokuwahi kupeleka kafara ya mtu akiwa mzima zaidi ya wote kuwafikisha wakiwa wameshapoteza ufahamu au maisha. Akili yake yote ikawa ni kulekea nyumbani kwao tena katika kile chumba chao cha siri. Chumba cha siri cha yeye na baba yake. Chumba ambacho kuna mlango mmmoja tu chumbani tena nyuma ya kabati. Kabati ambalo ukilisogeza tu unaingia moja kwa moja mpaka kwenye giza ambapo unachukuwa hirizi kwa chini nakuzimeza kisha unajikuta upo katika himaya yakina Kakamega.

    Devotha alimbeba Sara begani nakujikongoja kama awali. Safari hii hakuona pembe yoyote ya chumba kutokana na maeneno ambayo alikuwepo. Maeneno aliokuwepo yalikuwa ni maeneo ya nje. Tena nje kabisa ambapo kulikuwa na miti pekee iliofunikwa na giza la usiku.

    Hatua moja baada ya nyingine uku Sara akiwa begani, Devotha alianza kuchanja mitaa pasipo kumuogopa mtu yoyote atakayekutana naye. Mwanzoni Sara alionesha kuwa mbishi lakini kadri muda ulivyokuwa ukienda ndivyo alivyozidi kulegea kabisa viungo vyake vyote. Alishakata tamaa nakumuachia mwenyezi Mungu atende miujiza kwake.





    *********



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Stan alirudishwa na polisi yule yule aliyekuja kumchukuwa akiwa na tochi kubwa mkononi mwake. Alimrudisha Selo Stan alipokuwepo lakini safari hii hakurudi Stan mtupu bali alikuwa amerudi akiwa na muonekano tofauti mikononi mwake. Alikuwa ameshikilia biblia ndogo mkononi mwake. Si baba Devotha wala wale watuhumiwa wengine walioweza kuiona ile biblia zaidi ya yule poilisi na Stan kujua. Giza lililokuwa limetawala katika eneo la ndani ya ile Selo lilisababisha wote kutokuoelewa chochote kinachoendelea kutoka kwa Stan japokuwa walisikia sauti tena kwa mbali Stan akiombewa na wakibishana kuhusu biblia.

    “Haya kakae na wenzio kulee” aliongea yule polisi baada ya kumfungulia Stan mlango wa Selo.

    Stan aliingia na kukaa na wenzake kisha yule polisi akafunga kwa kufuli nakurudi zake kaunta kuu.

    “Stan mwanangu?” Aliita baba Devotha baada ya Stan kuingia na kukaa eneo la peke yake mule ndani.

    “Usiniongeleshe wee mzee na mimi sio mtoto wako” Stan aliongea.

    “Nilishakwambia mimi nitaendelea kuwa baba yako milele hata kama nikikurudisha kwa wazazi wako walipo.”

    Stan alikuwa na hasira zaidi. Alijitahidi kuishinda ile hasira yake kwa kuishikilia ile biblia wa nguvu zote mikononi mwake.

    “Stan mwanangu nilikuwa nikiyasikia japo kwa mbali yote ambayo ulikuwa ukiambiwa na watu waliokuja kukuona. Na nimeshawajua tayari ni kina nani na wao nafikiri wanahitajika Kakamega..

    Kabla baba Devotha hajamalizia kuongea chochote, Stan alishtuka baada ya kusikia jina Kakamega. Moyo wake ukamlipuka. Paa!!

    “Kakamega? ndio wapi huko?” Alihoji Stan

    “Mwanangu Stan!! Kakamega ndio nyumbani kwenu nilishawahi kukwambia. Na ndio wazazi wako walipo nakuishi huko. Nitahakikisha unarudi Kakamega tena usiku huu huu” Aliongea baba Devotha kwa msisitizo.

    Stan ilimbidi kumtolea macho sana baba Devotha kwa hasira ya hali ya juu. Alijijaza ujasiri kwa kuwa na ile biblia na maneno ya yule mchungaji baada ya kumkabidhi ile biblia na kumuombea ndio yalijaza kichwa cha ujeuri kwake. Alijiona nusu Mungu nusu binadamu.

    “Huko utaenda wewe!!” Aliongea Stan kwa hasira.

    Safari hii baba Devotha hakutaka kuongea zaidi ya kuendeleza kwa vitendo. Ile hirizi yake ambayo aliitoa mwanzo ilionekana kama kuisha nguvu. Alisogelea kamwanga kadogo kalikokuwa kakipenyeza kutoka katika kidirisha kidogo sana ndani ya ile selo. Kamwanga kalichokuwa kamejichora kama mstari mmoja mrefu mpaka chini ya sakafu.

    Baba Devotha aliusogelea ule mwanga mpaka karibu na alipoufikia alivuta suruali yake mpaka karibia na pindo nakuchomoa kikaratasi cha nailoni kilichokuwa kimefungwa vilivyo mithili ya ugoro ule unaopendwa na kabila la wamasai kutoka Arusha,Tanzania. Akakichomoa kile kikaratasi nakufungua ndani yake. Muda wote macho ya Stan yalikuwa hayakwepeshi kitu kwa kuendelea kuangalia anachokifanya baba Devotha kwa kupitia kale kamwanga.

    Punde baba Devotha akafakamia kile kitu alichokuwa amekitoa katika kile kimfuko cha nailoni. Akakimumusa!!

    Wale watuhumiwa wengine waliokuwa ndani ya selo wakafanya kama mwanzo. Walikuwa ni waoga kupitiliza. Walijisogeza wote pembeni uku wengine wakiguna kwa kutokutoa makelele nakutoa machozi kwa uwoga wa hali ya juu.

    “Stan mwanangu sogea mwenyewe nikwambie kitu!!” Aliita baba Devotha.

    “Siji na hunifanyi lolote!!” aliongea Stan.

    Stan aliinua mkono wake mmoja. Mkono ule ambao ulikua umeing’ang’ania biblia yake vilivyo. Akaifungua lakini hakuweza kuona hata neno moja kutokana na lile giza lililokuwa limetawala mule ndani. Alichokifanya nayeye kwa ujasiri alisogelea mpaka eneo lililokuwa na mwanga mdogo. Mwanga ule ule uliokuwa ukitokea kupitia kale kale kadirisha kisha akafunua maeneo ya kati kati ya ile biblia nakutafuta neno la kusoma na kuomba ili aepushwe na yale majaribu.

    Kitendo cha Stan kujisogeza tu pembeni kabla hajafikia lile eneo la ule mwanga mara alishangaa baba Devotha akimfuata. Hakuwa baba Devotha yule aliyozoeleka machoni kwake. Alimsukuma Stan pembeni. Stan akadondoka nakujikuta ile biblia ikimponyoka nakutambaa mpaka ukutani. Ikamteleza nakugonga ukuta!

    “Stan twende muda umewadia mwanangu sasa wazazi wako wataenda kukuona baada ya muda mrefu kuniachia!!” aliongea baba Devotha.

    “Kama kuniua niue tu sasa hivi siendi popote na wazazi wangu ninavyojua wapo sokoni. Wazazi wangu ni vichaa lakini naimani ipo siku watakuwa na akili zao za kawaida na watasema yote kwakuwa naamini yupo mmoja tu juu mbinguni awezaye kuyabadilisha yote haya!!” Aliendelea kuongea Stan kwa kulalamika.

    Baba Devotha aliuchukuwa mkono wa Stan kwa kutumia zile nguvu zake za kichawi alizokuwa amezipata ndani ya muda mfupi. Alimburuta lakini Stan alikuwa mbishi. alikuwa yupo tayari kuifuata ile biblia eneo iliposelelekea. Aliburuzana na baba Devotha. Stan akafanikiwa kuporochoka!!

    Akakimbia mpaka eneo alilohisi huenda ile biblia imetelezea. Akaanza kupapasa mithili ya mtu mwenye upofu wa macho. Akaipata!!

    Kugeuka upande wa nyuma yake akashangaa kushikwa na kitu kama binadamu. Akajua huenda baba Devotha amemfikia na ndio aliyemshika. Alikuwa ameshikwa kwa nguvu zote na usoni yule mtu alionekana kung’aa sana maeneo ya machoni mwake na mdomoni mwake akiwa na meno meno makali kama filamu zile za mazombi.

    “Niache uko!!” Aliongea Stan kwa sauti ya ukali.,





    ********



    “Stan mwanangu siwezi kukuacha kamwe. Bado nitaendelea kuwa na wewe mwanangu haya sasa twende Kakamega!” Ile sauti iliongea nakumfanya Stan asielewe mtu anayeongea naye.

    Stan aliinyanyua ile biblia yake juu kama ishara ya ushindi na kuomba kwa sauti ya chini chini.

    “Ehhh Mungu baba tazama kiumbe chako nipo tena katika majaribu haya mengine. Baba weza kuniponya katika mikono ya huyu ibilisi. Niongoze Baba na weza kunilinda niepukane na haya majaribu yanayoendelea kuniandama .Amen!!” Stan alipomaliza kuomba aliishusha ile biblia yake chini. Chini kabisa akaiweka.

    Yule mtu mbele yake aliokuwa akionesha kutisha sana ndani ya ile selo alibadilika kabisa. Alinywea na hata yale macho ya kung’aa pamoja na meno meno yake ya ukali yalipotea ghafla. Giza likafunika likiachia kale kale kamwanga kembamba ka mbalamwezi kutoka nje kakichukua mkondo wake. Wote wa mule ndani wakapitiwa na usingizi. Wakadozi!!





    **********







    Baridi kali la asubuhi liliendelea kutawala kila kona ya msitu. Baridi lililofanya sauti za upepo kutoka kwenye miti mirefu zizidi kuvuma,majani kudondoka na hata miti yenye matunda na mbegu zilizokomaa kuanza kudondoka ovyo pia. Baridi hilo halikuogopwa hata kidogo katika msitu wa maajabu ya kila aina. Msitu wa Kakamega!!

    Ndio kwanza watu walikuwa wamevaa nguo nusu uchi. Juu wakiwa vifua wazi na chini wakiwa na majani mapana makavu yalioweza kuzuia sehemu zao za siri kwa upande wa mbele na nyuma kuacha makalio wazi. Ni wakina mama tu ndio walioonekana kujishughulisha asubuhi sana katika kukusanya maji kutoka katika majani mapana ya miti ya chinichini. Maji ambayo huwa yakiwasaidia katika kupika na hata kunywa. Wakiwa bado bize kila mmmoja mara kwa upande wa mbele yao alitokea mwenzao na kwa kipindi hiki alionekana kuwa tofauti na waliovyokuwa wamemzoea. Alionekana kubadilika kwa kiasi kikubwa sana kisura pili alikuwa ambembelea mwenzake mgongoni wakiwa wote hoi kwa kuchoka sana. Alikuwa ni Devotha. Devotha yule mtesaji wa chinichini. Devotha aliokuwa akiishi nyumba moja na baba yake pamoja na Stan.

    “Devo? Devo nini umefanya tena?” Alioongea mmoja wa wanakakamega. Mwanamke ambaye alionesha ni mmoja kati ya wanawake viongozi kutokana na wale wanzake wote kuwa nyuma yake.

    “Anaitwa Sara, Nimemleta hapa kwetu kama zawadi katika jiwe letu la kafara. Baba yangu amefika huku?” Aliongea Sara uku akihema hoi.

    “Hapana hajaja ila alikuwa aje kwani ishara zote alionesha kuwa anakuja lakini mpaka sasa zile ishara zikapotea ghafla na hatujamuona tena akitokelezea, sasa nyie wengine embu msaidieni dada yenu kumchukuwa huyu” Aliongea yule mwanamke akiwaamrisha wenzake.

    Walimpokea Devotha yule dada aliokuwa naye,Sara. Kisha Devotha alivua yale mavazi yake ya mjini na kuokotewa majani makavu chini nakuyakusanya kwa kuyafunga funga yakawa kama nguo ya ndani. Devotha akajisitiri!! Akawa mwanakakamega halisi.Akaunga ule msururu mpaka katika himaya yao kuu ya wanakakamega.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Muda wote huo Sara alikuwa ameshapoteza fahamu. Hakuwa Sara wa kawaida kutokana na mateso makali ambayo alipitia kutoka kawa Devotha. Ni mateso makali alipitia pale alipokuwa mbishi kwa Devotha. Kuna wakati aliweza kuchomwa na makuchwa yale marefu ambayo yalikuwa yakimtoka Devotha mara kwa mara katika mikono yake. Alimchoma karibia kila sehemu. Maumivu makali ya ndani kwa ndani sana sana maeneo ya usoni mwa Sara ndio yaliomfanya apoteze fahamu. Mpaka walivyoingia katika msitu wa Kakamega bado Sara hakuweza kujitambua kwa lolote.

    Ndani ya muda mfupi wakutembea ndani kwa ndani katika msitu wa Kakamega walikuwa wameshafika katika himaya yao kuu. Devotha, Sara pamoja na wale wakina mama waliokuwa wakitafuta maji walikuwa tayari wameshamfikisha Sara katika himaya yao mpya. Zoezi la kwanza walimfunga kamba katika eneo lao la kutolea adhabu endapo mwana Kakamega atakosea masharti yao. Wakachukuwa mikono yote miwili ya Sara na kufunga kamba zile za miti pande zote mbili. Wamkamning’iniza Sara!

    “Mamaaaaa, Nakufaaaaaa!!” Sara alitoa sauti ya juu.

    Ilikuwa baada tu ya kumalizwa kuning’nizwa kwa juu. Alizinduka kutoka katika ufahamu asielewe yupo maeneno gani na anafanywa nini kutokana na kuwa kipofu. Alihisi mikono yake kufungwa kwa kamba ngumu nakuvutwa.

    “Nimewakosea nini jamani? Kwanini kila siku mimi tu jamani? Haya niuneni si ndivyo mnavyotaka kunichinja nichinjeni sasa hivi?” Sara aliongea pasipo kujielewa wala kushuhudia. Ndio kwanza yale maneno yalikuwa kama furaha kwa wana Kakamega. Walijikusanya karibia wote katika kijiji chao na kumshangaa Sara. Kamwe katika mawindo yao hawajawahi kumpata binadamu kipofu. Ilikuwa ni maajabu sana ya kushangaza kwao. Walichukua mikuki nakuanza kugusa gusa meaeneo ya usoni mwa Sara. Maeneo yaliokuwa yameshonwa nyuzi kwa kutolewa macho. Kina Kakamega walikuwa wakimchoma Sara wakiwa na imani huenda macho yake kayaficha yatageuka na watayaona. Walishangazwa sana na nyuzi nyuzi zilizokuwa zimepita maeneo ya machoni mwa Sara. Nyuzi zilizofunika mboni za macho.

    “Fumbua, fumbua tuone!!” Aliongea mmoja kati ya wanaume wa kakamega ambaye alikuwa akimchokonoa Sara maeneo ya uso wake kwa kutumia mkuki akitaka Sara afumbue macho.

    “Weeeeee tuliaaaaaa!! acha kufanya michezo hiyo!!?” Sauti kali ilisikika. Ilikuwa ni Sauti ya kiongozi wao mkuu. Hakuwa Aguati wa msimu ule kutokana nakufa katika shimo la kutolea kafara bali alikuwa ni kiongozi wao mpya. Kiongozi mwenye sifa kama zilizokuwa za Aguati mwana wa thorong’ong’o. Alikuwa akiitwa Thiwa! Alikuwa kajaza sana mwili wake. Pande la jitu lililojawa na alama mbalimbali mwilini mwake. Walipenda sana kumuita Thiwa mwana wa Thiring’ong’o. Kutokana na jina la Thorong’ong’o kwa watu wa Kenya au uko msitu wa Kakamega mpakani mwa Kenya na Tanzania kumaanisha ‘Shupavu’.

    Wakina kakamega wote walimpisha Thiwa nakuacha mstari mmmoja. Thiwa alimsogelea Sara mpaka karibu nakuanza kumfungua kamba zile za miti alizokuwa amefungwa na kina Kakamega wenye hasira kali. Alipomaliza kumfungua akambeba Sara mgongoni. Kisha akasikitika sana kwa kutoa machozi. Wote wakajikusanya nakumsogelea mpaka karibu kumshangaa mkuu wao anacholilia. Thiwa alitetemeka sana mikono yake na machozi yalikuwa yakifuata mkondo wa mashavu katika kuomba njia. Yakamtiririka kama mtoto mdogo aliyejisaidia haja kubwa na ndogo akishindwa kuomba msaada wa kusafishwa. Thiwa akanyong’onyea!



    Mshindo mithili ya tetemeko la ardhi ukaanza kutikisa. Wakinamama wachache kwa uwoga wakaanza kukimbia kwenye vibanda vyao nakuwaacha wanaume wakiwa bado na mikuki yao mikononi mwao wakisikilizia ni kitu gani. Thiwa,kiongozi mkuu akasimama pale nakumuacha Sara akiwa chini. Akawaoneshea ishara ya kusikia kitu. kisha kidole chake akakiweka mdomi kama ishara ya kunyamazisha wenzake. Wote wakakaa kimya!! Kimya cha ghafla!! hali hiyo ikasababisha hata ule mlio wa kile kishindo kusimama kwa muda. Thiwa akaachana kuangalia lile eneo waliokuwa wakiihisi mlio ukitokeaa nakuwageukia wenzake.

    “Kakamega wenzangu?” aliita Thiwa.

    “Ndio, ndio kiongozi!!” Waliitikia kwa kushangaa.

    “Ishara kama hii ni kubwa sana na inanihusu mimi kiongozi wenu. Ishara kama hii katika msitu huu huwa ikitokea kipindi cha adhabu kwa mtu mgeni hapa kwetu. Ishara hii ni kuwa huyu binti hana makosa na hatakiwi kufanywa vyovyote vile wala kutolewa kafara yoyote ni dhambi kubwa kwa mungu wetu katika lile shimo la kule.” Aliongea Thiwa nakufanya kina Kakamega wote kuangaliana wenyewe kwa wenyewe.

    “Nani aliyemleta huyu binti niliombeba?” Aliuliza Thiwa.

    Wote wakaendelea kutazamana kwa kusakiziana. Wakayaelekeza macho yote kwa Devotha wakamsukuma aende mbele. Devotha akasogea mpaka eneo la mbele alipokuwa yule kiongozi,Thiwa.

    “Wewe ndio uliomleta humu kakamega?” Aliuliza Thiwa.

    “Ndio nimemtoa Dar es Salaam tulipokuwa tukiishi na baba siku zote!” Alijibu Devotha kwa kujiamini.

    Muda wote Sara alikuwa akiwasikiliza kwa utulivu akiwa begani mwa kiongozi mkuu wa Kakamega,Thiwa. Sara hakutaka kufanya vurugu yoyote kwani hakujua wala kuona chochote kinachoendelea zaidi ya kusikia tena kwa mbali kutokana na mwili wake kuchoshwa kwa mateso.

    “Sheria za hapa kakamega unazijua na kama bado hujazijua nitakushangaa sana wakati baba yako anacheo kikubwa sana hapa kwetu. Kwanini unatuletea mtu asie na hatia? umesikia ule muungurumo? Ule muungurumo umetoka kwa mungu wetu kule kwenye jiwe la kutolea kafara. Hatuwezi kumpeleka huyu binti ni dhambi kubwa sana na mungu wetu hapendi kuchukuwa walemavu. Huyu binti hana jicho hata moja ameshonwa na hata uko alipotoka inaonekana katoka kwa matatizo!! Sasa basi mungu wetu hawezi kufurahi mpaka sasa kachukia na ukitaka awe na furaha ni lazima wewe uliyemleta huku kakamega utolewe kafara kwa mungu wetu haraka iwezekanavyo. Huyu binti atachukua cheo na nafasi yako sawa!” Aliongea Thiwa.

    Safari hii aliongea kwa ukali sana uku akimkazia macho Devotha.

    “Hapana mimi siwezi kabisa kwenda kwenye jiwe la Kafara. Sina makosa!” Devotha alianza ubishi.

    Thiwa aliwaamrisha kina Kakamega. hawakuwa na masihara hata kidogo kutokana na kuchukia kwa mungu wao wanaompelekeaga kafara. Ilikuwa ni lazima wafuate sheria walizozikuta toka miaka ya nyuma. Sheria za kumtupa mwenzao endapo atakiuka masharti tena makubwa ama kujisahu hata kukosea kwa namna yoyote ile.

    Devotha alizidi kuwa mbishi. Kina kakamega walimvua Hirizi zote Devotha kila kona. Walimtapisha akatema na zile ambazo alikuwa amezimeza. Devotha akalegea sana. Hakuwa Devotha wa nguvu za kina Kakamega tena. Walimbeba Mzegamzega!! Mputamputa!! Kenekene!! Hoihoi!! Winjiwinji!! juu kwa juu!! mpaka katika eneo lililokuwa na jiwe la kutokea kafara. Wakapanda mpaka juu kabisa kisha wakamtupa Devotha bila ya huruma wala kujali mchango wake wa siku za nyuma alizokuwa akileta watu waliokuwa majeruhi nakutupwa katika shimo hilo. Devotha akamezwa rasmi na jiwe la kafara.mungu wao akampokea. msitu ukatetemeka kwa ubaridi kuashiria mungu wao kafurahia ile zawadi ya kafara. Kina kakamega wote wakanyoosha mikono na mikuki yao juu ishara ya kufurahia ushindi. Wakarudi uku yule kiongozi, Thiwa akiwa na Sara begani mwake akimning’iniza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    **********



    Si yule mzee wala Mchungaji John wote hakuna kati ya hao aliyeweza kupata hata tone la usingizi. Hata yule mzee hakuenda kulala kwake. Aliongozana moja kwa moja mpaka kwa mchungaji John. Kitendo cha Stan kuwekwa selo kiliwasononesha sana mchungaji na yule Mzee, mbaya zaidi walipoambiwa kuwa Stan anahusika na kesi ya kuua. Walivyofika Kibaha waliamua kupitiliza katika kanisa la Mchungaji John. Waliamua kukesha katika madhabahu wakiomba. Hawakutaka hata kupata maji wala chakula chochote kipite katika makoo yao zaidi ya kukesha kwa maombi usiku wote.

    Hata asubuhi napo ilipowadia hawakutaka kupata kifungua kinywa zaidi ya kunawa nyuso zao zilizokuwa zimeonesha kunyauka kwa kukesha macho. Hawakujali uchovu uliosababishwa na jasho kali wakati wa maombi.

    “Sasa hapa twaweza kwenda!” Aliongea mchungaji John akimwambia yule mzee.

    Chai na vitafunwa ambavyo vilikuwa vimeandaliwa na mkewe ili wanywe na yule mzee, waliomba viwekwe kwenye chupa na vitafuno kwenye mfuko kwa kusudi la kumpelekea Stan.

    Moja kwa moja mchungaji John alimwaga mkewe kisha wakaingia ndani ya gari na safari ya kutokea Kibaha mpaka kituo kikubwa cha Polisi,Kimara ikaanza.

    Njia nzima walikuwa ni kumpokea Mwenyezi Mungu kimoyo moyo aweze kutenda miujiza yoyote ili tu Stan aweze kuwa huru. Ile minyororo ya dhambi aliyofungwa ifunguke. Walipofika tu pale kituoni walikuta ndio kwanza mapolisi wakibadilishana zamu na wengine ku ‘double’ kazi. Haraka haraka mchungaji John pamoja na yule mzee walishuka katika gari lao nakuelekea mpaka kaunta kuu ya polisi.

    “Samahani sisi ni wale tuliokuja jana kwa ajili ya mtoto wetu. Tunaweza japo kumuona tumpatie hata chai hii hapa?” Aliongea mchungaji John kwa kutetemeka.

    “Hapana!! hapa haturuhusu kupokea kitu chochote na tena asubuhi hii mkubwa wetu hachelewi kuja hapa kama ni hiyo chai yako utampelekea Segerea. Hapa tulipo tunaelekea huko huko Segerea labda utufuate!” Aliongea polisi mmoja.

    Mchungaji John na yule mzee hawakuwa na ujanja tena. Walibaki wakishikilia chupa yao ya chai na mfuko pembeni uliokuwa umewekwa vitafunio.





    **********





    Mpaka asubuhi kunakucha Stan alikuwa amejikunyata na ile biblia akiwa ameikumbatia kwa nguvu zote mithili ya blanketi katika eneo lenye ubaridi mkali. Kila mmoja kati ya wale watuhumiwa alikuwa ameshaamka na kujitenga pembeni wakisubiri kuitwa ama kuja kupelekwa Selo kubwa,Segerea.

    “Stan mwanangu umeshaamka?” Aliongea baba Devotha kwa sauti tulivu.

    Alionesha kama kubadilika kidogo. Hakuwa baba Devotha wakawaida. Usoni

    mwake dhahiri alionesha kuwa na majonzi makubwa. Majonzi mithili ya binadamu aliyefiwa na mzazi wake. Stan alishtuka uku akiwa na biblia yake kifuani. Alimtolea macho baba Devotha ya ukali na hasira. Macho ya asubuhi ya mtu aliotoka kuamka na hasira.

    “Mie sio mtoto wako nilishakwambia!!” Stan alijibu uku akiutunisha mdomo wake akikaa vizuri na biblia yake. Baba Devotha uvumilivu uliendelea kumshinda. Alijisogeza taratibu mpaka alipoketi Stan chini nakutaka kumshika mikono. Stan alishtuka nakujisogeza akitaka kumyanyapaa!

    “Stan? Stan mwanangu nahitaji twende wote Kakamega, Najuta hata kwanini sikukupeleka mapema? Haya yote mpaka unawekwa ndani yasingetokea. Kakamega wangekulinda Stan. Hata hivyo nakuhakikishia kwamba kwa nguvu ya Kakamega hapa hakuna kesi yoyote” Aliongea baba Devotha kwa msisitizo.

    Safari hii alijikuta akiongea kwa sauti ya kupayuka. Sauti iliowafanya wale watuhumiwa wengine kujivuta karibu na baba Devotha baada ya kusikia maneno yale. Baada ya kusikia kuwa nguvu ya Kakamega inaweza kufuta kesi.

    “Tushirikishe na sisi mzee basi tuonane na hao Kakamega” Alihoji kijana wa makamo uku nayeye akijivuta mpaka karibia na eneo alipokuwapo baba Devotha.

    “Mnataka kwenda na nyinyi Kakamega?” aliuliza baba Devotha.

    “Ndio” Wote waliitika kwa furaha.

    Hakukuwa hata na mmoja aliyependa kubaki mule ndani. Ukubwa wa baadhi ya kesi zao ulionesha kukata kabisa tamaa ya kurudi uraiani. Waliona ni bora wapelekwe uko Kakamega huenda mambo kwao yakawa nafuu kuliko kwenda kuozea Segerea.

    “Subirini!! Wee Satan hiyo biblia weka pale pembeni kwanza!!” Aliongea baba Devotha akimwambia Stan.

    Stan alitikisa kichwa akimaanisha hataki kabisa kuiacha ile biblia peke yake. Wenzake waliokuwa wakihitaji kupelekwa uko Kakamega wakamgeuka Stan. Wakamjia juu. Wakamlazimisha Stan aiweke ile biblia kando ili baba Devotha aoneshe miujiza wapelekwe Kakamega. Moyo wa Stan ulikuwa mzito sana. Ulikuwa kama umegongwa na treni nakuganda. Kamwe hakukubaliana na hilo tukio lakuweka biblia kando. Tayari moyo wake ulishaingiwa na chembechembe za Yesu. Alikuwa ameupokea uzima wa bwana Yesu kwa mara nyingine.

    “Sitaki mnielewe kama huko sijui Kakamega nendeni wenyewe mimi niacheni. Biblia yangu ndio uzima wangu nyie nendeni mie niacheni!!” Aliongea Stan.

    Hasira zilizidi kumtawala mara mbili yake. Akajisogeza tena kwa pembeni karibia na kona ya ukuta akiwatenga. Akaendelea kujikunyata na ile biblia yake akiikumbatia kifuani mwake. Kiroho Papi!!

    Wale watuhumiwa wengine wote waliokuwa ndani ya ile selo waliamua kuachana na Stan. Walimtenga!! Walimnyanyapaa!! Walimuhaso!! na kuwa kitu kimoja na Baba Devotha. Walimzunguka baba Devotha ili washuhudie maajabu ya Kakamega. Washuhudie ni jinsi gani watapelekwa Kakamega. Jina la Kakamega tayari lilikuwa limeshawaingia vichwani mwao nakuwapumbaza!! kuwaduwaza!!.



    Wakawehuka!! Wakatamani sana kuujua mji wa Kakamega ulivyoumbwa.

    Baba Devotha akaonekana mtukufu wao kwa muda. Akaonekana kama Mungu mtu kwa muda mchache ndani ya ile selo. Aibu ya uzee aliokuwa nao akaiweka pembeni. Kichwa chake kikaulizana na moyo kisha kikakenua nakucheka kwa vikwifukwifu!! Kikaupigia moyo makofi ya shangwe. Shangwe za kupeleka baadhi ya watu Kakamega.Moyo wake ukatoa bonge la tabasamu!! Mawazo yake yote akayaelekeza mpaka katika shimo la kutolea Kafara. Shimo maarufu katika msitu wao wa Kakamega na wana Kakamega.

    “Wewe njoo upande huu ziba huu mwanga usitupate na nyinyi zingireni upande wa uku ninachotaka tupate kagiza kidogo kwani kuingia Kakamega hakuhitaji mwanga sana!!” Aliongea baba Devotha uku akiwapanga.

    Wale watuhumiwa walikuwa wameshajitoa kwa vyote. Walishamkabidhi baba Devotha mioyo na miili yao hata na akili pia. Baba Devotha aliuchukuwa mkono wake moja kwa moja mpaka katika pindo la suruali yake. Akachomoa hirizi kubwa kiasi. Wote wakashtuka!! wakaruka na kutaka kutawanyika.

    “No, no Kakamega hawapendi hivyo. Kama tayari mmeshasogea hapa uruhusiwi kujitenga!!” Aliongea baba Devotha.

    Wale watuhumiwa wakajkusanya tena upya wote. Wakakumbatiana kwa kuweka mduara. Ile hirizi aliokuwa ameitoa baba Devotha akaanza kuichezesha kwa kuizungurusha kichwani mwake. Kuna baadhi ya watuhumiwa walikuwa wakitetemeka mikono yao kwa woga. Mwanga mkali wa rangi nyekundu iliokuwa imechanganyikana na njano ikatoka. Uso wa baba Devotha ukaonesha furaha ya kufanikiwa kwa kitu. Taratibu akakenua mdomo wake.

    “Safari sasa inakaribia muda na sekunde yoyote tutakuwa njia moja ya kuelekea Kakamega wote kasoro yule mpumbavu aliyeng’ang’ania biblia” Aliongea baba Devotha.

    Muda wote Stan alikuwa ameifungua ile biblia yake katika kujisomea neno la Mungu. Hakutaka kuangalia wala kujua kinachoendelea katika mikono ya baba Devotha. Tayari alishajua kuwa baba Devotha ni mchawi na siyo mtu wa kawaida hivyo jambo kubwa alilokuwa akilifanya Stan ni katika kumuomba mwenyezi Mungu ajiepushe na baba Devotha. Asishirikiane naye hata kwa kitu chochote.

    Baba Devotha akiwa bado katika kufanya ujanja ujanja wake wa kupotea na wale watuhumiwa ndani ya ile selo mara wakasikia geti lao likigongwa. Alikuwa ni polisi akitaka watoke tayari kwa kupelekwa Selo kubwa,Segerea.

    “Haya haya kunanini kinaendelea hapo? Mbona mmejikusanya?” Aliongea polisi.

    Wote walikuwa bado katika midadi. Hakukuwa hata na mmoja aliokuwa ameisikia ile sauti ya polisi kuanzia anafungua lile geti na mpaka anawasogelea. Akili na pua za wote zilikuwa zimeshanusa nusa hewa ya Kakamega. Ni Stan pekee akili zake zilikuwa sawa. Aliinuka nakumsogelea polisi.

    “Hawa wanamatatizo gani?” Aliongea polisi kwa sauti akimuuliza Stan.

    Stan hakuwa na jibu kamili lolote. Alionesha ishara ya mabega kuwa hafahamu kinachoendelea. Kwa hasira polisi aliingia katikati yao.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Narudia tena mnafanyaje hapa?” Alihoji polisi kwa mara nyingine.

    Hakukuwa bado na jibu rasmi zaidi ya wale watuhumiwa kukohoa kila mmoja. Chafya mbali mbali zilitawala. Baba Devotha kwa ujanja wake alikuwa tayari ameshamuona Polisi kwa jicho la tatu. Alikuwa ameshaichukuwa hirizi yake iliokuwa ikianza kuleta mabadiliko miongoni mwa watuhumiwa. Aliibana mkononi kisha akaipitilizisha mpaka kwapani mwake. Akaifumbata!!

    Polisi hakuweza kuiona ile hirizi. Wale watuhumia kila mmoja alionekana kurudi katika hali yake. Polisi yule akawaita wenzake wakaja wameshikilia pingu mikononi mwao. Kila mtuhumiwa akafungwa pingu nyuma. Si baba Devotha wala Stan wote walifungwa pingu mikononi kwa nyuma. Stan aliomba kuificha biblia yake yake upande wa mbele. Polisi yule alikuwa akijua ile biblia Stan alipoipata hakuwa na kinyongo naye. Alimkubalia na Stan aliiweka na kisha kuruhusu mikono yake igusane na pingu nakutolewa nje tayari kuelekea katika gari tayari kwa kuelekea Selo kubwa,Segerea.

    Walipofika nje tu si yule mzee wala Mchungaji John wote waligubikwa na majonzi ya ghafla baada ya kuiona sura ya Stan kwa jinsi ilivyochooka na kukata tamaa. Stan na yeye akasimama kwa muda baada ya kumuona mchungaji John na yule mzee. Hasira na macho ya ukali akawaangalia akitamani kuporochoka pale. Askari nyuma yake akamshtua kwa kumsukuma. Stan akaendelea na safari ya kupandisha gari kwa kuelekea Segerea. Uzalendo ulimshinda mchungaji John nakujikuta akiropokwa maneno ovyo. Mpumbati!!

    “Stan mkumbuke sana Mwenyezi Mungu kumbuka kuomba kila muda. Tupo nyuma yako kwa sala na maombi. Hatutakuacha kamwe!!”



    ***********



    Kigugumizi!! Machozi ya huruma yaliochanganyikana na hasira yakamtoka Stan. Hakuwa na jinsi zaidi ya kuingia katika basi lile la kuchukulia watuhumiwa wa makosa mbali mbali na kisha safari ya kuelekea selo kuu,Segerea ikaanza rasmi.

    Mchungaji John pamoja na yule mzee walibaki wameduwaa. Macho Kodo!! Yule mzee alikuwa ameshikilia chupa kubwa ya chai na mkono mwingine akiwa na mfuko uliokuwa na vitafunwa. Vyote hivyo walipanga kuja kumletea Stan. Stan alioonesha kutokuwa na msaidizi katika maisha kwa muda huu.

    “Hapana hapa tuwafuatilie tu mpaka huko Segerea lazima wataturuhusu kumpatia hii chai na vitafunwa, twende!” Aliongea yule mzee akimwambia mchugaji John. Mchungaji ambaye bado alikuwa akiduwaa kwa kuliangalia basi la polisi likikunja kona na kuondoka.

    “Twende, Twende mpaka Segerea!” Aliropoka mchungaji John.

    Walielekea ndani ya gari lao. Safari ya kutokea kituo kikubwa cha polisi Kimara ikaanza. Lengo lao kuu likiwa ni kutangulia Segerea kwa sjili ya kumsubiri Stan. Si mchungaji John wala yule mzee wote walikuwa hawajielewi. Akili zao zilionesha kuchoka kabisa kwanza kwa kukesha kwa maombi pili kukataliwa kumpatia Stan vile vitu walivyokuwa wamemletea. Kamwe hawakutaka kukata tamaa. Hata walivyoingia ndani ya lile gari lao, mchungaji John akiwa dereva hawakusita kufanya maombi ya kimya kimya njiani. Maombi ya kufanikisha uko waendako. Maombi juu ya kupokelewa vile vitu walivyokuwa navyo. Walitamani washuhudie Stan akinywa japo chai kavu kwani waliamini kabisa mawazo makubwa aliokuwanayo kwa umri wake juu ya kesi yake ya kuua yatamnyima kabisa hamu hata ya kula. Mawazo yao yote yakawa ni kufika tu kwanza huko Segerea.



    **********



    Hospitali ilionekana kupwaya kutokana na madaktari bingwa wa kufanya uchunguzi kutoonekana kirahisi. Walikuwa katika kazi moja ya kuweza kushirikiana na mapolisi katika kuhakikisha kimejulikana chanzo haswa kilichopelekea kufariki kwa mfanyabiashara maarufu maeneo ya mbezi Luis. Ndani ya masaa kadhaa madaktari wawili bingwa wakiwa na mwili ule tayari walikuwa wameshafanya uchunguzi wa kina. Mapolisi kwa kusaidiana na madaktari waliweza kugundua kuwa marehemu alikuwa amejerehuliwa kwa kupigwa risasi mbili maeneo ya tumboni. Madaktari kwa asilimia mia walifanikiwa kufanya upasuaji mdogo na kutoa risasi mbili zenye nambari SS12H na nyingine yenye nambari SS13H zote zikisadikiwa kutoka katika bastola ndogo walioikamata. Bastola ambayo mmiliki halali alikuwa ni Laurent Kimaro, mfanyabiashara maarufu Jijini na haswa maeneo ya mbezi Luis.

    Kamanda mkuu wa kikosi Rafaeli akisaidiana na madaktari walipokea majibu hayo nakuomba uchunguzi wa kina uendelee kufanyika na wao kufuatilia mpaka kumjua muuuaji wa mfanyabiashara maarufu. Mapolisi walikuwa njia panda kwa kutokumjua haswa aliyehusika na tukio la mauaji. Kuna wakati walikaa kikao nakukusanya maelezo yao wakidhania moja kwa moja Stan na Sara yule binti kipofu wanahusika kutokana na kupatikana mikononi mwao usiku.

    Akili nyingi ya mapolisi iligota katika tukio la kupatikana kwa mwili wa mwanamke. Yule mama msamaria mwema ambaye alihusika katika kumtoa Stan lokapu kwa rushwa kidogo hapo awali. Mama aliyepatikana akiwa ameshafariki na yeye kupigwa kwa kutumia bastola hiyo hiyo ya mfanyabiashara maarufu. Risasi walizomtoa yule mama ndizo walizomtoa mfanyabiashara maarufu. Hazikuwa na tofauti hata chembe. Zote zilikuwa zimefanana kwa namba. Vikao vya mara kwa mara vya mapolisi wakipelelezi juu ya tukio havikuisha toka usiku wa tukio mpaka hospitalini ndani ya chumba cha uchunguzi. Walijitahidi ndani ya siku moja hiyo hiyo wawe wameshaujua ukweli wote na kesi iende haraka mahakamani kutokana na yule mfanyabiashara kujulikana sana.

    “Mkuu hapa cha kufanya apelekwe kuzikwa tu. Madam tumeshajua kuwa marehemu alipigwa kwa risasi mwilini mwake hali iliyompelekea kufa kwake basi akazikwe halafu taratibu za kumpata mtuhumiwa zitafuata.” Aliongea kamanda mwingine wa kipelelezi. Alikuwa akimwambia kamanda wa kikosi,Rafaeli.

    “Sawa nakubaliana na nyie pamoja na madaktari. Ni sawa tutoe kibali akazikwe na kwa sababu tayari tunao wahusika waliohusika katika tukio lazima kesi itakwenda sawa hapa!” Alimaliza kuongea Rafaeli.

    Wale wapelelezi walisaidina na madaktari katika kuufunga ule mwili wa marehemu Laurent Kimaro. Kibali cha kuruhusu kuzikwa kikaandikwa na kupigwa sahihi na kamanda mkuu wa kikosi,Rafaeli.





    *********



    Msitu wa Kakamega ulikuwa umelipukwa kwa sherehe kubwa. Sherehe ya kumtoa mwenzao kafara kwa kitendo cha kukiuka masharti ya msitu. Devotha! Devotha ambaye tayari alikuwa ameshasahaulika baada ya kumezwa katika shimo la kafara. Kakamega akili yao waliielekeza sasa kwa Sara mwanachama mpya kwao. Thiwa kiongozi wao alionekana shujaa mara mbili kwa uamuzi aliokuwa ameufanya wa kuamuru Devotha atupiwe kwenye shimo la kafara.

    Njia nzima wakiwa wanarudi katika himaya yao baadhi ya kina Kakamega walikuwa kama ni washamba kwa kumtolea macho Sara. Walimchukulia kama kiumbe cha ajabu sana usoni mwao.

    Walipofika katika himaya yao walimuweka Sara katika chumba chao kimojawapo na ilikuwa ni ruhusa kwa kila mwana Kakamgea aliokuwa akitaka kushangaa kuona maajabu aingie. Walijazana wote ndani ya chumba kimoja kwa kumshangaa Sara machoni mwake.

    Si wanaume kwa wanawake walishindwa hata kuendelea kufanya kazi zao siku nzima. Ilikuwa ni kama wakishuhudia kuangalia televisheni ya bure machoni mwao. Ni Sara ambaye aligeuka kuwa kivutio miongoni mwao kutokana na ule upofu wake aliokuwa nao. Upofu wa kutolewa macho yote mawili na kisha kushonwa maeneo ya usoni ambapo hakuwa na jicho hata moja. Kuna waliokuwa wakimchokonoa maeneo ya usoni na hata wengine kupapasa maeneo ya usoni mwa Sara uku wakimcheka. Sara hakuweza kuwaona wala kujua mazingira ya hicho kijiji cha Kakamega kilivyokuwa kimekaa.

    Wale kina Kakamega walichukuwa kibuyu kilichokuwa kimechemshwa damu damu za mnyama. Wakamsogezea Sara mpaka maeneo ya mkononi mwake. Sara akapokea, hakujua kuna nini ndani yake zaidi ya kushika. Njaa na kiu vilivyokuwa vimemzidia kichwani mwake alijua wazi huenda ameletewa maji anywe. Upofu ukamjaza mawazo chanya. Sara akajua ni maji akapokewa kile kibuyu nakuanza kufakamia kwa kuyanywa. Kichefuchefu!!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akatapika nakutema kilichofuata alijikuta akipiga chafya mfululizo.

    “Kunywa acha kutema!” Aliongea Thiwa yule kiongozi mkuu wa Kakamega.

    “Hapana siwezi na sijui nini?” Sara alilalama!!”

    “Kunywa wewe. Najua unanjaa sana kunywa ni muzuri”

    “Chungu, hainifai kunywa mnataka kuniua. Niueni kawaida na sio kunipa masumu yenu” Sara aliendelea kucharuka akikitupa kile kibuyu mpaka chini kikamwagika.

    Ilibidi wale wakina Kakamega wafanye kukiokota na kumlazimisha Sara kunywa zile damu zilizokuwa katika kile kibuyu kwa mara nyingine. Mwanzoni Sara alikuwa mbishi sana. Alibishana nao lakini mwishoni hakuweza kuzishinda nguvu za kina Kakamega. Wakamkaba na kumnyeshwa zile damu kwa nguvu. Sara akatapatapa kwa kunywa.Akaishiwa nguvu kabisa. Akazimeza zile damu akatulia. Tuli!!

    Kakamega wote wakalipukwa kwa furaha ya ajabu. Thiwa akaomba kiletwe kisu cha kwao. Kisu ambacho si kisu kinachotumiwa na binadamu wa kawaida. NI mfupa wa mnyama mkubwa uliokuwa umechongwa mithili ya kisu atumiacho binadamu wa kawaida. Kisu cha kikakamega kikaletwa. Thiwa akakichukuwa kile kisu na kukitoweza katika damu damu alizozibakiza Sara katika kile kibuyu. Akaanza kumuweka alama maeneo ya mapajani mwake na mwishoni akamalizia maeneo ya kwenye kifua chake. Muda wote kile kisu kilivyokuwa kikipita katika mapaja ya sara aliweza kuhisi. Alihisi ni kitu cha kawaida lakini hakuwa na jinsi kutokana na kukabwa na kinakakamega hali iliyomfanya Sara kuishiwa nguvu kabisa. Alikuwa ameshajitolea kufa. Hakuweza kutoa neno hata moja zaidi ya kuhema juu juu.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    *******



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog