CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Simulizi : Niliua Kumlinda Mama Yangu
Sehemu Ya Nne (4)
“Si bwana Nkone huyu?” aliuliza nesi mmoja huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Ndiyo! Mpelekeni ndani!”
Mwili ule ambao tayari uliwekwa kwenye machela ukaanza kusukumwa kuelekea ndani ya hospitali hiyo. Waandishi wa habari ambao tayari walipewa taarifa kitambo, walikuwa mahali hapo huku wakipiga picha kila hatua iliyokuwa ikiendelea.
Shati lake jeupe alilokuwa amelivaa ilikuwa vigumu kujua kama shati hilo lilikuwa jeupe kutokana na damu zilizokuwa zimetapakaa baada ya kuchomwa visu mfululizo vya tumbo kiasi kwamba mpaka utumbo wake kutoka nje.
Mwili wake ulitisha mno. Ukapelekwa mpaka katika chumba cha kuhifadhiwa maiti na kuachwa humo. Kifo chake kikazua gumzo kubwa kwa watu, maswali mbalimbali yaliulizwa juu ya kile kilichokuwa kikiendelea, kilikuwa ni kisasi au kilikuwa nini.
“Jamani! Watu wema wanakufa, wabaya wanabaki, hii kweli kasheshe,” alisikika mtu mmoja akimwambia mwenzake.
Siku hiyo, taarifa zilizoigubika Tanzania ilikuwa ni kifo cha bwana Nkone, ilikuwa ngumu kuamini lakini huo ndiyo ulikuwa ukweli wenyewe kwamba mtu huyo alikuwa ameuawa kikatili huku maneno yaliyoonekana kufanana na yale yaliyoonekana wakati mzee Kambani alipouawa yalionekana katika miamba hapo ufukweni, tena pembeni na pale alipouawa.
“Polisi wahakikishe muuaji anapatikana, vinginevyo, kuna siku utasikia hata rais kauawa” alisema jamaa mmoja.
“Hiyo kweli bwana! Polisi wanatakiwa kufanya jambo!”
*****
Kundi la watu wanne, walibaki wawili, bwana James Marimba na mchungaji Yekonia ambao wote walikuwa na hofu kwamba walikuwa wakilindwa na mtu wasiyemfahamu ambaye alitaka kuwamaliza.
Mauaji hayo ndiyo yaliyowafanya kuongeza ulinzi katika maisha yao kwa kuamini kwamba kwa namna moja au nyingine ni lazima muuaji huyo angewatafuta na kuwaua. Hawakuwa na maisha ya furaha tena, waliishi kwa wasiwasi kama digidigi.
Polisi nao walichanganyikiwa kama wao, kitendo cha mabilionea wawili waliokuwa wakipendwa kuuawa, kuliwafanya kutokukaa ofisini kabisa. Kila siku watu waliyazungumzia mauaji hayo na kuwaona polisi hawafanyi kazi zozote zile na ndiyo maana wauaji walitumia siku thelathini tu kuwaua mabilionea wawili, tena waliokuwa wakipendwa mno.
Kila kona, stori ikawa ni juu ya mauaji ya bilionea Nkone ambaye mwili wake ulikutwa katika miamba ya ufukwe wa Coco. Tetesi zikaanza kuenea kwamba wauaji wa mabilionea hao walikuwa Wakenya ambao walishindwana na wafanyabiashara hao katika biashara zao.
Tetesi hizo hazikuishia hapo, waliibuka wengine na kusema kwamba wauaji walikuja kutoka nchini Rwanda ambapo nao pia walikuwa wametapeliwa na wafanyabiashara hao na kuamua kuwaua, yaani kila kona, tetesi za uongo ndizo zilizokuwa zikisikika.
Polisi walijitahidi kuwatafuta wauaji lakini hawakufanikiwa, kitengo cha upelelezi kila siku kilifanya kazi yake tangu kuuawa kwa bwana Kambani lakini hawakufanikiwa kumpata muuaji.
Hapo ndipo walipoamua kuwasiliana na mtu aitwaye Dismas Komu, mpelelezi wa kimataifa ambaye aliifanya kazi hiyo kwa miaka ishirini na tano kabla ya kuamua kustaafu.
Kipindi hicho alikuwa nchini Marekani na familia yake wakila bata. Alipopigiwa simu na kuambiwa kwamba bwana Nkone naye aliuawa, alishangaa kwani ndiyo kwanza polisi walikuwa wakifanya upelelezi wa wauaji wa bwana Kambani, tena mwingine akawa ameuawa.
“Kwa hiyo hamkufanikiwa kuwapata?” aliuliza Dismas.
“Bado, tumejitahidi, ila kuna vitu tunavikosa na ndiyo maana tunahitaji uje,” alisikika kamanda mkuu wa kitendo cha upelelezi, bwana Nzobia.
“Vitu gani?”
“Huwa wauaji wana akili sana.”
“Kivipi?”
“Kila walipopashika, walifuta alama za vidole vyao, kwa hiyo inakuwa ngumu sana kuwapata,” alisikika bwana Nzobia.
“Sawa, ninakatisha kila kitu changu kwa ajili yao, ninakuja,” alisema Dismas.
Ni kweli alikuwa na familia yake nchini Marekani lakini hiyo haikuwa sababu ya kutokuifanya kazi aliyokuwa amepewa. Kwa haraka sana, akaiacha familia yake na kurudi nchini Tanzania tayari kwa kuwatafuta wauaji ambao waliamini kwamba walikuwa wengi.
Ndani ya ndege, alikuwa na mawazo lukuki, alijiuliza ni kwa nini nchi kama Tanzania ilikuwa na wapelelezi wengi lakini wote hao walikuwa wameshindwa kuwapata wauaji hao. Mbele yake aliona kukiwa na kazi kubwa lakini alitakiwa kuhakikisha kwamba wauaji wanapatikana kwa gharama zozote zile.
Humo ndani ya ndege alikumbuka namna alivyoweza kuwatafuta wauaji wakubwa na hata majambazi ambao walivamia benki, walitoweka lakini kutokana na upelelezi wake wa kina, alifanikiwa kuwapata kirahisi kabisa.
Ukiachana na kazi hiyo, pia alikumbuka namna alivyopelekwa nchini Urusi kwa ajili ya kuwatafuta Wamarekani waliokuwa wameiba fedha kiasi cha dola bilioni moja katika benki ya People, alifanikiwa kuwapata japokuwa walikimbilia katika sehemu ambayo haiufikiwa na watu kutokana na baridi kali lilokuwepo huko.
Kazi zote alizozifanya, zilimpa uhakika kwamba hata kazi iliyokuwa mbele yake ilikuwa nyepesi sana, hivyo hakutaka kuhofia kitu chochote kile. Ndege ilichukua zaidi ya saa ishirini ndipo alipofika nchini Tanzania. Alipokelewa na wakuu wa kazi na kuelekea katika hoteli aliyopangiwa na kesho yake kuonana na wakuu wake ambao walimwambia pa kuanzia.
“Kwanza nyumbani kwao,” alisema kamana Nzobia.
“Kwa nini kwao?”
“Ndipo tutapata uhalisia juu ya wapi pa kuwapatia.”
“Sidhani! Kitu cha kwanza tuanze kwa marafiki zao,” alisema Dismas.
“Hakuna tatizo...wewe tu.”
Hicho ndicho alichotaka kufanya, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuonana na marafiki zao wakubwa, wakawapata mabilionea wengine, mchungaji Yekonia na bwana Marimba ambao akawachukua na kuanza kuongea nao. Alitaka kusikia mengi kutoka kwao kwamba ilikuwaje watu hao waliuawa na ni nani alikuwa karibu nao.
“Kwa bwana Kambani, sidhani kama alikuwa karibu zaidi ya hawara wake,” alisema bwana Marimba.
“Alikuwa na hawara?”
“Ndiyo!”
“Ni nani?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Msichana mmoja hivi, mzurimzuri...”
“Anaitwa nani?”
“Alimtambulisha kwa jina la Mage...”
“Ninaweza kumpata msichana huyo?”
“Mmh! Sijajua, hebu tujaribu kutafuta namba yake...” alisema mchungaji yekonia.
Kilichofuata ni kutafuta namba ya msichana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Mage. Haikuwa kazi nyepesi kwani hawakuwa na namba yake hivyo hawakujua ni kwa jinsi gani wangeweza kuipata namba yake. Alipowaambia hivyo, Dismas akaondoka huku akitarajia ndani ya siku chache angeweza kupata namba ya msichana huyo.
Mpaka hapo, tayari kazi hiyo ikaonekana kuanza kuwa ngumu kutokana na watu ambao aliwaamini kwamba wangempa ushirikiano wa kutosha, kutokuwa na kitu alichokihitaji. Alielekea hotelini ambapo huko alikaa kwa saa kadhaa kisha kuwarudia mabilionea wale ambao walikuwa na simu ya marehemu Kambani na kumkabidhi.
Wakaanza kupitia namba moja baada ya nyingine, zile namba ambazo waliamini kwamba zilikuwa ni za mahawala wake wakazichukua na kuanza kuwapigia mmoja baada ya mwingine. Simu zote zilipokelewa isipokuwa simu moja ambayo kwa wakati huo haikuwa ikipatikana.
“Naitaka hii namba...” alisema Dismas na kuichukua namba ile.
Kitu cha kwanza kilikuwa ni kwenda katika Makao Makuu ya Simu ya Alcatel na kuhitaji kuangalia usajili wa namba ile. Alipoletewa taarifa, namba ilionyesha ikiwa imesajiliwa kwa jina la Fatuma Abdallah.
Hakutaka kupoteza muda huko, alichokifanya ni kuanza safari ya kurudi hotelini. Alipofika njiani, mawazo yakamjia kwamba kama bwana Nkone aliuawa na wauaji haohao basi ilikuwa ni lazima kuwe na mawasiliano kwani isingetokea kwa bilionea kama huyo kuuawa kizembe kama ilivyokuwa, dalili zote zilionyesha kwamba muuaji alikuwa ndani ya hiyo gari yake.
Alichokifanya ni kwenda mpaka nyumbani kwa bwana Nkone. Watu walikuwa wamejaa huku vilio vikiendelea kusikika kila kona. Hakutaka kujali sana zaidi ya kuifuata familia yake na kuanza kuzungumza nayo.
“Naitwa Dismas Komu, ni mpelelezi kutoka TISS...” alijitambulisha Dismas.
Alichokuwa akikihitaji ni simu ya bwana Dismas. Alipoletewa, akaichukua na kuuliza siku ambayo mzee huyo aliuawa, alipoambiwa na muda, akaanza kuiangalia simu ile hasa kwa upande wa simu zilizotoka, simu ya mwisho kupiga marehemu ilikuwa ipi.
“Ni yeye...ni mtu mmoja,” alisema Dismas
Namba ya mwisho ambayo alipiga bwana Nkone ilikuwa namba hiyohiyo iliyotumika kwa bwana Kambani, hapo akapata picha kwamba muuaji huyo ndiye aliyefanya mauaji kwa watu hao wawili. Kazi aliyokuwa akiiona kuwa na ugumu, kidogo ikaonekana kuwa nyepesi kwani kitendo cha kuipata namba ile, kilimpa uhakika kwamba ni lazima ampate muuaji.
“Ni lazima atapatikana.”
Hakutaka kuishia hapo, alichokifanya ni kuondoka na kurudi hotelini, huko, akaichukua namba ile na kuanza kuipiga. Simu haikuwa ikipatikana. Hakukaa sana hotelini, alichokifanya ni kwenda makao makuu ya TISS ambapo huko akakutana na mkuu wake wa kazi na kuanza kuzungumza naye na kumwambia kila kitu kilichokuwa kimeendelea.
“Ni lazima apatikane,” alisema mkuu wake.
Alichokifanya ni kuondoka na kurudi katika makao makuu ya mtandao wa simu wa Alcatel ambapo baada ya kufika huko, akaanza kuitraki simu ile ili kujua mahali alipokuwa huyo muuaji. Simu ilizimwa ila betri halikuwa limetolewa, hivyo mnara uliosoma ni wa Tandale Kwa tumbo.
Akawachukua wafanyakazi wawili wa kitengo cha IT na kuelekea huko ambapo aliamini kwamba muuaji huyo alikuwepo. Hawakuchukua muda mrefu wakafika Tandale, jamaa mmoja wa IT akachukua GPS Detector, kifaa maalumu cha kuangalia mahali simu ilipokuwa na kuanza kukiangalia.
GPS ilikuwa ikiwaka kitaa chekundu kadiri walivyokuwa wakiisogelea simu ile ya muuaji ambayo ilionyesha mpaka ramani ya sehemu ilipokuwa. Walizidi kusogea mbele mpaka walipofika katika gesti moja iliyoandikwa Mama Mau na kusimama nje.
“Simu ipo humu mkuu...” alisema kijana mmoja.
“Safi sana!” alisema Dismas, akateremka kutoka garini tayari kwa kuingia humo.
****
Hakuwa mgeni kwenye mambo ya mitandao, alikuwa mpelelezi hivyo alifahamu mambo mengi mno. Alijua kwamba mtu anapoua, ilikuwa ni lazima uufute mwili kwa kitambaa sehemu zote ulizokuwa umeushika mwili huo na kama ilikuwa vigumu kufanya hivyo, basi ilikuwa ni lazima uvae glavu ili usigundulike.
Aliyafahamu hayo yote na la mwisho kabisa ambalo halikutoka moyoni mwake ni kuhusu matumizi ya simu. Aliwafahamu magaidi wengi wakiwemo Osama bin Laden. Mullah na magaidi wengine ambao hawakuwa wakitumia simu katika kipindi chote hasa baada ya kuanza kutafutwa, utumiaji wa simu ulikuwa unawawezesha wapelelezi kufahamu muuaji alikuwa wapi hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kumkamata.
Kitu ambacho kwake aliona kwamba alifanya kosa kubwa baada ya kufanya mauaji ni kutokuchukua simu ya bwana Nkone mara baada ya kumuua. Alijua fika kwamba kama polisi walikuwa na akili, kitu cha kwanza kabisa ambacho wangekitumia kumtafuta muuaji basi wangechukua simu.
Alilijua hilo na ndiyo maana muda wote alitulia chumbani akiwaza, kosa alilolifanya la kusahau kuchukua simu ile lilikuwa kubwa na la kizembe sana. Alijiandaa kutoroka kwani pasipo kufanya hivyo ilikuwa ni lazima kukamatwa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati wazo la kutoroka likiwa limekubalika kichwani mwake, kitu kingine ambacho alikifikiria akilini mwake ni kuizima simu tu, kweli akafanya hivyo. Siku ya kwanza ikapita, siku ya pili, ya tatu na hatimaye wiki nzima.
Baada ya kufanya uchunguzi wake, akagundua kwamba mara simu inapozimwa, huwa haizimiki kama watu wanavyofikiria bali huwa ipo ON na ndiyo maana ukitegesha alamu ni lazima muda unapofika ikuamshe ingawa ulikuwa na uhakika kwamba uliizima.
Alipofikiria hilndiyo akakumbuka kwamba kwa namna moja au nyingine ilikuwa ni lazima kupatikana kama tu asingefanya jambo la ziada. Siku ambayo alikuwa akifikiria kutoa betri la simu yake ndiyo siku ambayo polisi walikwenda na Dismas katika nyumba ya wageni na kusimama nje huku GPS Detoctor ikiwaka kuashiria kwamba simu ile iliyokuwa ikitafutwa ilikuwa ndani ya nyumba hiyo ya wageni.
“Mbona kuna kelele za watu nje? Kuna nini?” alijiuliza.
Hakutaka kubaki ndani, alichokifanya ni kuchungulia dirishani. Aliiona idadi kubwa ya watu, hakujua walikuwa wamekusanyika kutafuta nini lakini katika mazungumzo ya watu wachache, aliwasikia wakisema kwamba muuaji alikuwa ndani ya nyumba hiyo.
“Mmmh!” alijikuta akiguna.
Alijua kwamba watu waliokuwa nje ya nyumba hiyo walikuwa polisi na kama asingefanya juhudi za kutoroka ndani ya nyumba hiyo basi ilikuwa ni lazima kudakwa. Kutoka ndani ya chumba kile kupitia mlango, alichelewa, hivyo njia pekee aliyoiona kufaa kupita ilikuwa ni mlango wa darini.
Hakutaka kuchelewa, alichokifanya ni kuchukua meza iliyokuwa mule ndani, akaisimamisha, akaipanda na kisha kuufungua mlango wa dari na kuingia ndani kisha meza ile kuisukumia pembeni na kuufunga mlango ule wa dari.
Hakuchukua dakika nyingi akasikia watu wakiugonga mlango wa chumba kile, hakutaka kuitikia, aliganda huku masikio yake yakisikiliza kwa makini kilichokuwa kikiendelea kule chini. Akashtukia mlango ukivunjwa na watu kuingia ndani. Hakuwaona, hakujua ni wakina nani ila alichokijua ni kwamba walikuwa wakimtafuta yeye.
“Yupo wapi?” alisikia sauti ya mwanaume mmoja.
“Sijui! Ila alikuwa humu ndani.”
“Una uhakika dada?”
“Ndiyo! Si unaona hata nguo zake hizo hapo!” aliisikia sauti ya dada wa mapokezi.
“Mkuu! Na simu yake hiyo hapo!” alisema kijana mmoja wa IT.
“Sasa yupo wapi?” alisikika mwanaume huyo, hapohapo akasikia vishindo vikielekea chooni.
Cynthia alikuwa kimya, kwa mara ya kwanza akajikuta akimuomba Mungu amsaidie asionekane na aondoke salama ndani ya dari lile alilokuwemo. Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda mno, kadiri dakika zilivyokuwa zikizidi kwenda mbele, alijua kwamba angeweza kuonekana na hivyo kukamatwa.
“Umesema hizi ni nguo zake?” aliuliza Dismas.
“Ndiyo!”
“NA hili begi pia?”
“Ndiyo!”
Dismas akalichukua begi lile na kuanza kuliangalia kwa ndani. Kitu alichokutana nacho ni pasipoti zaidi ya nne na hati nyingine za kusafiria ambazo zilionyesha kwamba mtu huyo alikwenda sehemu nyingi duniani. Hilo likamtia shaka kwa kuona kwamba mtu aliyekuwa akimtafuata alikuwa mpelelezi mwenzake au muuza madawa ya kulevya.
Unasema kwamba alikuwa msichana?” aliuliza Dismas huku kwa mbali akionekana kuchanganyikiwa.
“Ndiyo!”
“Hajaja na mizigo mingine?”
“Hajaja nayo! Alikuwa na hiki kibegi tu.”
“Mhh!”
“Ndiyo hivyo!”
Hakutaka kukaa ndani ya chumba hicho, akili yake ilimwambia kwamba piga ua ilikuwa ni lazima mwanamke huyo apatikane. Wakatoka ndani ya chumba hicho na kuelekea katika choo cha nje kwa kuamini kwamba inawezekana alikuwa huko, walipofika, hakukuwa na mtu.
Wakarudi chumbani mule harakaharaka. Dismas akaanza kukiangalia kile chumba kwa umakini mkubwa, alijichukulia yeye kuwa mtuhumiwa halafu polisi walikuja kwa lengo la kumkamata, je angejificha wapi? Jibu lililokuja harakaharaka kichwani mwake ni juu ya dari tu.
“Atakuwa juu ya dari...kalete ngazi...” alisema Dismas na kuwafanya watu wote washangae.
“Juu ya dari?”
“Ndiyo! Kaleteni ngazi...” alisema Dismas, hapohapo dada wa mapokezi akatoka na kuelekea uani na baada ya dakika moja, akaingia huku akiwa na ngazi mkononi. Dismas akaichukua, akaiweka sawa, akaanza kupanda na kuufungua mfuniko wa dari kwa lengo la kuchungulia ndani.
“Nishaanza kusikia harufu ya pafyumu, nilijua yupo humu ndani,” alisema Dismas, akachukua simu yake, akawasha tochi, mkono wa kulia, akaupeleka kiunoni na kuchukua bastola yake tayari kwa mapambano.
*****
Cynthia alibaki akitetemeka, hakuwa na amani kule juu na alijua piga ua ilikuwa ni lazima kwa Cosmas au mtu yeyote kupanda kule juu na kuchungulia kilichokuwa kikiendelea. Hakutaka kujiuliza sana, alichokifanya ni kuanza kutambaa kwa umakini pasipo kusikika sauti yoyote ile, lengo lake likiwa ni kwenda kwenye chumba kingine kabisa kilichokuwa na mlango wa kutokea.
Kulikuwa na mabomba mengi yaliyopitishwa nyaya nyingi za umeme, hakujali, kulikuwa na panya lakini hakuwaogopa, kitu pekee alichokuwa akikihofia ni kukamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
“Hawawezi kunikamata...” alisema Cynthia na hapohapo akamsikia Cosmas akisema kwamba apande juu ya dari kuangalia kama kulikuwa na mtu.
Hapo ndipo akapata nguvu ya kutambaa zaidi, alitambaa kwa harakaharaka, mpaka mhudumu kwenda kuchukua ngazi na kuisimamisha, tayari aliufikia mlango wa dari, akaufungua, akatumbukia chumbani na harakahataka kuufunga.
Alichokifanya ni kuufuata mlango wa kutokea ndani ya chumba hicho, kilichomshtua zaidi, mlango ule haukuwa na mteja yeyote hivyo bado ulikuwa umefungwa kwa ufunguo. Hapo ndipo akili yake ilipoanza kucheza ni kitu gani alitakiwa kukifanya.
Hakutaka kuchelewa, harakaharaka akakimbilia chooni ambapo huko akakutana na kidirisha kidogo, kilikuwa na mbao zilizoonekana kuchoka, hakikuwa na nondo kama vilivyokuwa vidirisha vingine vya gesti nyingine, alichokifanya ni kusimamisha ndoo kisha kuanza kupanda.
Kutokana na kuwa mtu wa mazoezi, hilo wala halikuonekana kuwa tatizo kwake, aliweza kupanda harakaharaka kisha kuzipiga zile mbao ambazo zikavunjika na kudondokea nje, kilichofuata ni kupanda na kujipenyeza katika kidirisha kile, alipofanikiwa, akatua upande wa pili ambao ulikuwa na uchochoro na kisha kutokomea zake huku akiacha pasipoti ndani ya chumba kile.
*****CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Vipi mkuu! Yupo?”
“Hakuna mtu aiseee...”
“Ila si umesema umekutana na harufu ya pafyumu?”
“Harufu ipo ila mwenyewe hayupo,” alijibu Cosmas huku akichungulia ndani ya dari lile.
Cosmas akatoka harakaharaka, alikuwa na wasiwasi kwamba inawezekana mtu aliyekuwa akimtafuta alishukia upande wa pili. Akamuuliza dada wa mapokezi kama kulikuwa na mlango mwingine wa dari, dada yule akamwambia kwamba kulikuwa na mlango mwingine chumba cha jirani, wakaelekea huko, hakukuwa na mtu yeyote yule na walipokwenda chooni kuhakiki, wakakuta kidirisha kikiwa kimevunjwa.
“Daah! Tushamkosa...” alisema Cosmas huku akionekana kukata tamaa.
*****
*************************************************
Ilikuwa ni Jumapili ambayo idadi kubwa ya watu walikusanyika katika Kanisa la Praise And Worship kwa ajili ya kumuabudu Mungu kama zilivyokuwa Jumapili nyingine. Idadi ya watu siku hiyo ilikuwa kubwa mno kwani ndiyo siku iliyokuwa ikitangazwa kwamba Mungu angefanya miujiza mikubwa, viwete wangetembea, vipofu wangeona na hata wale ambao walikuwa kwenye vifungo vya shetani kufunguliwa na kuwa watu wapya.
Watu kutoka katika mikoa mbalimbali walifika kanisani hapo, walitaka kumsikia mtumishi wa Mungu, mpakwa mafuta wa Bwana, mchungaji Yekonia ambaye alijulikana kuwa na upako mkubwa kutoka kwa Mungu. Kila alipokuwa akihubiri, alichukua kitambaa chake, akawapuliza watu, wakaanguka huku wakipiga kelele, watu wakashangilia pasipo kujua kama watu wote hao walikuwa wamepangwa.
“Leo ni siku ya kufunguliwa...” alisema mchungaji Yekonia, aliongea mpaka jasho likamtoka, aliwaangalia watu huku akionekana kuwa na hamu ya kuongea maneno mengi zaidi, tena yenye tumaini ambayo yangewafanya watu kumuamini zaidi.
Kila aliyekuwa akiyasikia maneno hayo, alipiga kelele za shangwe, kwao, mchungaji Yekonia alionekana kuwa na nguvu za Mungu, uchafu wake aliokuwa akiufanya ulikuwa siri kubwa, hakutaka mtu yeyote yule afahamu kilichokuwa kikiendelea.
Alihubiri kwa nguvu zote, ibada ilichukua saa sita mpaka kumaliza ndipo alipohitaji watu wenye matatizo mbalimbali kuombewa wafike mbele, kama kawaida ya watu waliopangwa ambao walijifanya vipofu, viziwi wakasogea mbele na kuanza kuombewa.
“Mungu atawaponya, leo ni siku yenu...” alisema mchungaji Yekonia.
“Amen....”
Alianza kuomba, alikemea sana na baada ya dakika kumi, kila mtu aliyejifanya kuwa na matatizo, akajifanya kufunguliwa na hivyo kuibua shangwe ndani ya kanisa hilo.
“Mungu wangu si muongo...” alisema kwa sauti kubwa.
Baada ya watu hao kufanyiwa maombezi, akahitaji watu waliotaka kuokoka wasogee mbele, watu kumi na sita wakasogea akiwemo Cynthia ambaye alijifanya kuwa changudoa ambaye alitaka kukombolewa kutoka katika kifungo cha shetani kilichomtesa miaka mingi.
“Unaitwa nani dada?” alimuuliza Cynthia.
“Naitwa Marry John...”
“Unataka nini binti yangu?”
“Nataka kuokoka...nimechoka kuishi maisha ya kidunia...”
“Leo Mungu atakuokoa, nuru yake itaangaza katika maisha yako....” alisema na kanisa zima kuitikia kwa kusema ‘Amen’.
Akaanza kuwaongoza watu hao sara ya toba. Alipomaliza akaanza kuwaombea kisha kuwaambia waende kukaa. Muda wote huo, Cynthia alikuwa akimwangalia mchungaji Yekonia, lengo lake kubwa lilikuwa ni kumuua na hapo alipokuwa alikuwa akiangalia ni kwa jinsi gani angeweza kumshawishi amuombee maombi binafsi.
“Mchungaji...” aliita Cynthia mara baada ya ibada kuisha.
“Ndiyo binti yangu!”
“Nahitaji maombi binafsi...”
“Hakuna tatizo....”
“Nataka nije ofisini kwako, Shetani amenitesa sana maishani mwangu, ninataka kuishi maisha mapya, maisha ya kumtumikia Mungu milele...” alisema Cynthia huku akijifanya kulia.
“Nyamaza binti! Mungu atakufungua...” alisema mchungaji Yekonia.
Akamwambia Cynthia kuonana naye jioni ya siku hiyo! Msichana huyo akakubaliana naye.
****
Watu waliendelea kusubiri nje ya ofisi ya mchungaji kwa ajili ya kufanyiwa maombezi binafsi. Muda ulizidi kwenda mbele, japokuwa msichana aliyetoka ndani ya chumba kile alisema kwamba mchungaji Yekonia alihitaji dakika thelathini kwa ajili ya kufanya maombezi yake binafsi, kitu cha kushangaza ni kwamba muda huo ulikuwa umepita kitu kilichowafanya kuchoka kusubiri.
Kila mmoja akaanza kuangalia saa yake, walichoka kusubiri hivyo mmojawapo kusimama na kujaribu kutegesha sikio mlangoni kwa ajili ya kusikiliza kile kilichokuwa kikiendelea ndani, ukimya mkubwa ulikuwa umetawala.
Hilo likawatia wasiwasi mno na kudhani kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea, ila kupiga hodi, walishindwa kwa kuwa hawakuona kama ingekuwa heshima kutokana na mchungaji huyo kuagiza kwamba angechukua dakika thelathini tu kwa kufanya maombi binafsi.
“Saa moja limekata...” alisema mwanamke mmoja.
“Mmh! Ila hii si kawaida yake....mara nyingi hutembea na wakati...” alisema mwanaume mmoja.
“Au kuna tatizo?”
“Sidhani kwa kweli...”
Waliendelea kusubiri kwa nusu saa nyingine ndipo walipoamua mmojawapo agonge mlango kwani tayari watu walizidi kuongezeka. Mlango ukagongwa lakini hakukuwa na sauti yoyote kutoka ndani kitu kilichoibua maswali mengi, kwa nini iwe hivyo?
Wakapiga mioyo konda, liwalo na liwe lakini ilikuwa ni lazima kuufungua mlango, wakafanya hivyo. Walichokutana nacho, wanawake wakabaki wakipiga kelele, mwili wa mchungaji Yekonia ulikuwa juu ya meza, damu zilizoonekana kuganda zilitapakaa kwenye meza hiyo na nyingine sakafuni.
Picha iliyokuwa ikionekana, ilimtisha kila mtu, wakabaki wakiiangalia maiti ile huku wakionekana kutokuamini kile walichokuwa wakikiangalia. Harakaharaka simu zikapigwa polisi na ndani ya dakika mbili, tayari watu wakaanza kujazana katika eneo la ofisi hiyo.
“Unasemaje?”
“Nasikia mchungaji amejiua kwa kujichoma kisu...”
“Acha utani, mchungaji ajiue?”
“Ndiyo! Huamini sasa?”
“Siwezi kuamini bwana...mchungaji kujiua, sidhani...”
Kutokana na tukio hilo kutokea, kila mtu alikuwa akiongea lake. Wapo waliosema kwamba mchungaji alikuwa amejiua kwa kujichoma kisu lakini pia walikuwepo wale waliosema kwamba mchungaji huyo alikuwa ameuliwa na mtu fulani.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Atakuwa nani sasa?” aliuliza jamaa mmoja.
“Mmh! Hapa inawezekana akawa yule msichana...”
“Kuna msichana alikuwa humu?”
“Ndiyo! Tena alituambia kwamba mchungaji alihitaji nusu saa za kufanya maombi binafsi...”
Hapo ndipo wakapata jibu kwamba inawezekana yule msichana aliyekuwa ametoka ndani ndiye ambaye alimuua mchungaji ndani ya ofisi yake. Walichanganyikiwa, hata polisi walipofika, waliwaambia kwamba kabla ya kugundua kwamba mchungaji alikuwa ameuawa, ndani kulikuwa na msichana ambaye aliyafanyiwa maombezi binafsi kabla ya kutoka na kusema kwamba mchungaji alihitaji dakika thelathini za kufanya maombi binafsi.
“Huyo msichana mnamfahamu?”
“Hapana afande...”
“Ila mkimuona?”
“Tutamfahamu...”
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment