Simulizi : Nitakapokufa
Sehemu Ya Pili (2)
WASOMAJI WAPYA KABISAAAA.
Kijana Yusufu amekulia katika maisha ya kimasikini pamoja na rafiki yake, Kelvin. maisha hayo ndio ambayo yanamfanya Yusufu kujiingiza katika uimbaji wa muziki wa kizazi kipya. Anapewa jina la The Ruler, jina ambalo linafanana na la msanii mkongwe, The King.
Baada ya kusota sana kwenye muziki, anampata mfadhili, huyu anaitwa Papaa Pipo, mwanaume mwenye fedha nyingi. Papaa Pipo anampeleka kuzimu, huko Yusufu anasaini mkataba wa damu kwa kumtumikia shetani. Anaambiwa kwamba atapata utajiri mkubwa sana, atapata mvuto mwingi sana. Ameahidiwa mengi na kupewa masharti mawili tu. Asifanye mapenzi siku za Jumapili na Jumatano na hata asipate mtoto. kama akitaka kuoa, aoe tu, ila mtoto hatakiwi kumpata. Yusufu anachukulia kila kitu rahisi.
Je nini kitatokea?
Je Yusufu ataweza kupata kila alichoambiwa kuzimu?
TWENDE PAMOJA SASA.
Jina la mwanamuziki The King likaonekana kuanza kufutika machoni na masikioni mwa watu jambo liliwapelekea wadau wengi wa muziki kuanza kujiuliza juu ya hali hiyo. Nyimbo zake ambazo zilikuwa zikitamba sana, kwa wakati huo wala hazikusikika tena, yaani zilikuwa zimeshushwa chini sana huku nyimbo za The Ruler zikisikika kila kona.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa kipindi kifupi cha miezi mitatu ya Yusufu kuwa juu tayari The King akaonekana kupoteza mvuto kwa wadau wa muziki jambo ambalo lilionekana kumshangaza kupita kawaida. Kitendo cha Yusufu au The Ruler kuwa juu kikaonekana kumpa hasira sana. Hapo ndipo bifu lilipoanza rasmi. Yusufu alikuwa akifanyiwa fujo sana na vijana ambao walikuwa wakijulikana sana kama walikuwa maswahiba wa The King.
Muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania ukaonekana kuanza kuingia doa. Kwa upande fulani tayari kukaanza kuonekana kwamba kuna mambo mengi na matukio ya kutisha yangeweza kutokea hapo baadae kama vyombo vya sheria visipoingilia kati. Hapo ndipo ambapo polisi walipoanza kufanya kazi yao, kila mtu ambaye alikuwa akimletea fujo Yusufu jukwaani alikuwa akikamatwa na kuwekwa ndani kwa muda.
Kadri siku zilivyozidi kwenda na mbele na ndivyo ambavyo Yusufu alivyozidi kujulikana zaidi na zaidi mpaka nchi nyingine za Afrika Mashariki. Jina lake lilizidi kukua zaidi na zaidi, alizidi kuitwa sehemu mbalimbali nje ya Tanzania kwa ajili ya kufanya matamasha ambayo yalikuwa yakimuingizia kiasi kikubwa cha fedha.
Yusufu akawa amepata mafanikio makubwa sana tena ndani ya miezi mitatu tu jambo ambalo wala halikuweza kuaminika mioyoni mwa watu wengi ambao walikuwa wakiyafuatilia mafanikio yake. Baada ya kipindi cha mwezi mmoja zaidi na ndipo hapo ambapo maneno ya chini kwa chini yakaanza kusikika kwamba Yusufu alikuwa akijihusisha na dini ambayo ilimkataa Mungu.
Tetesi zile zilianzia chini kabisa lakini mwisho wa siku zikaanza kuvuma hata zaidi ya upepo jambo ambalo likaonekana kuwa si zuri masikioni mwa watu wengi. Mara kwa mara Yusufu alikuwa akiitwa kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tetesi zile ambazo zilikuwa zikisikika sana lakini alikuwa akipinga vikali.
“Hizi ni tetesi ambazo zimesambazwa na watu wasiopenda maendeleo yangu akiwepo The King. Najua wataongea mengi sana kwa sababu jina langu linazidi kupanda juu zaidi na zaidi” Yusufu alimwambia mwandishi wa habari katika mahojiano maalumu.
“Kwa hiyo tetesi hizi hazina ukweli kabisa?”
“Ndio. Huwa mara nyingi ninashinda ndani nikichukua mazoezi sana kwa kuamini kwamba kama unataka ubaki juu zaidi na zaidi basi yakupasa kufanya sana mazoezi ya muziki. Ila pamoja na hayo yote, ninamtegemea Mungu katika kufanya kila kitu katika maisha yangu. Yeye ndiye ananiongoza, yeye ndiye amenifanya kuwepo mahali hapa” Yusufu alimwambia mwandishi wa habari.
Siku hiyo yalikuwa mahojiano maalumu ambayo yalikuwa yakifanyika katika kituo cha televisheni cha PASUA kilichokuwa na makao makuu jijini Dar es Salaam. Kila swali ambalo alikuwa akiulizwa Yusufu alikuwa akijibu kwa ufasaha sana jambo lililowafanya watu wote kuona kwamba yale yaliyokuwa yakisemwa mitaani zilikuwa ni tetesi tu.
“Kwa kumalizia ungependa kuwaambia nini watu wanaeneza tetesi hizi?” Mtangazaji aliuliza.
“Ningependa kuwaambia kwamba Mungu anapoamua kumuinua mtu fulani katika kazi yake tusitake kuongea maneno mengine. Tunachotakiwa ni kumshukuru Mungu kwa kumuinua mtu fulani. Yakupasa kupigana na kujitoa kwa ajili ya kufanikiwa pia” Yusufu alimalizia.
Mahojiano yale ambayo yalifanyika yakaonekana kubadilisha kila kitu kabisa. Tetesi zile ambazo zilikuwa zikisikika zikaonekana kuzimwa kabisa. Mitaani hakukusikika tetesi zile tena, watu walikuwa wakiendelea na kazi zao huku wakimuona Yusufu kuwa mtu mwenye bahati ambaye Mungu alikuwa amempa nafasi ya upendeleo maishani mwake.
****
“Nataka kumuua. Hili bifu nimechoka kuwa nalo, nataka kumuua tu” The King alikuwa akimwambia mtu fulani simuni.
“Lini?” Sauti ya upande wa pili iliuliza.
“Siku yoyote. Ila nataka kumuua” The King alisema.
“Ok! Nimekusikia, subiri nije ili tupange mipango kabambe” Sauti ya upenda wa pili ilisema.
The King alionekana kukasirika kupita kawaida, tayari akaonekana kupoteza umaarufu wake ambao alikuwa nao kabla. Msanii chipukizi ambaye alikwishawahi kumuomba kumshirikisha nyimbo alikuwa juu hata zaidi yake. The King hakuonekana kukubali, tayari alijiona kufanya jambo moja ambalo lingemfanya Yusufu au The Ruler kunyamaza milele, alitaka kumuua tu.
Mipango tayari alikwishaanza kuisuka, alichokifanya kwa wakati huo ni kuwasiliana na watu ambao aliona kwamba wangeweza kumsaidia sana kwa ajili ya kukamilisha mpango wake ambao alikuwa ameupanga kwa wakati huo. Alipomaliza kuongea na simu, akalifuata kochi na kisha kutulia huku uso wake ukionekana kuwa na hasira sana.
Mawazo yake katika kipindi hicho yalikuwa yakimfikiria Yusufu, tayari mtu huyo alikuwa ameanza kukisumbua kichwa chake zaidi na zaidi. The King alijua fika kwamba thamani yake ilikuwa imeshuka kupita kawaida, alijua fika kwamba umaarufu wake ulikuwa umeshushwa kupita kiasi huku Yusufu akichukua nafasi kubwa katika tasnia ya muziki zaidi yake.
The King hakutaka kujiona akishindwa hivi hivi, tayari alijiona kuwa na uhitaji wa kufanya kitu kimoja tu ambacho kama angekikamilisha basi angeweza kurudi juu tena, kumuua Yusufu. Mpango ambao alikuwa akiupanga kichwani mwake ulikuwa mpango kababe ambao aliamini kwa namna moja au nyingine basi ni lazima angekamilisha kile ambacho alikuwa amekipanga.
Baada ya saa moja, mwanaume mmoja akaingia ndani ya nyumba hiyo huku akiwa ameongozana na vijana watatu ambao alikuwa amekuja nao kwa ajili ya kuutekeleza mpango ambao ulitakiwa kufanyika kwa kumuua Yusufu ambaye alionekana kuwa kama kikwazo katika mafanikio yake ya kimuziki nchini Tanzania.
Waliongea mengi huku wakiwa hawajagusia mpango mzima. Walipoona kwamba wamechukua muda mrefu bila kuliongelea suala hilo hapo ndipo walipoanza kuupanga mpango mzima ambao ulitakiwa kufanyika kwa haraka sana hata kabla mambo hayajawa makubwa.
“Ninachotaka auawe tu” The King alisema.
“Wewe unataka afe kifo gani ili ufurahie?” Sudi alimuuliza.
“Chochote tu ili mladi afe”
“Sawa. Tutakachokifanya sisi ni kumchoma moto garini. Unaonaje hapo?”
“Mmmh! Mna hatari nyie. Ila sawa, kifo hicho kizuri sana” The King alisema na vijana wale kuondoka huku wakiwa wameahidi kwamba siku hiyo ndio ingekuwa siku ya kutekeleza kila kitu ambacho kilitakiwa kufanyika.
****
Mipango tayari ilikuwa imekwishapangwa na Sudi ndiye ambaye alikuwa akisimamia mpango huo ambao ulitakiwa kufanyika kwa haraka sana. Kitu cha kwanza ambacho walikifanya ni kununua dumu la lita ishirini la mafuta ya petroli na kisha kulihifadhi ndani huku wakimsubiri Yusufu ambaye alikuwa mikoani akiendelea kufanya shoo mbalimbali.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Walisubiri kwa kipindi cha wiki moja na ndipo Yusufu akarudi jijini Dar es Salaam tena kwa sababu tu alikuwa akihitajika kusaini mkataba na kampuni ya kutengeneza vyandarua ya Netprotector. Yusufu hakutaka kukaa sana ndani ya jiji la Dar es Salaam, alichokuwa akikitaka kwa wakati huo ni kusaini mkataba na kisha kurudi mikoani kuendelea na shoo kabla ya kwenda Kenya na Uganda ambako alikuwa akihitajika sana.
Mara baada ya kuona kila kitu kimeandaliwa vizuri, Sudi akawachukua vijana wenzake wawili na kisha kuanza kuelekea katika majengo ya kampuni ya Netprotector ambako huko kila kitu kingefanyika kwa haraka sana.
Mara baada ya kufika huko, moja kwa moja wakaanza kumsubiria Yusufu kwa nje huku wakiwa katika gari lao. Wala haukupita muda mrefu sana, Yusufu akatoka katika jengo lile huku akiwa pamoja na meneja wa kampuni ile na baadhi ya waandishi wa habari ambao walikuwa kwa lengo la kupiga picha kila kilichoendelea ndani ya jengo lile.
Walipoongea mambo mbalimbali hapo nje, Yusufu pamoja na rafiki yake, Kelvin wakaingia ndani ya gari ao na kisha kuondoka mahali hapo. Kwa wakati huo walikuwa wakielekea Sinza walipokuwa wakiishi. Njia nzima, wote wawili walionekana kuwa na furaha, walikuwa wakiongea mengi kwa wakati huo.
Maisha yao yalikuwa ya juu, shida mbalimbali ambazo walikuwa wamezipitia katika maisha yao ya nyuma kwa wakati huo zikabaki na kuwa historia tu. Vinywaji mbalimbali vilikuwa ndani ya gari lile, walikuwa wakiendelea kunywa huku stori za hapa na pale zikiendelea.
Walipofika Tandale Kwa Tumbo, wakashtukia gari moja likisimama mbele yao jambo ambalo likamfanya Kelvin kufunga breki ya ghafla. Hata kabla hawajafanya kitu chochote kile, vijana wawili wakatoka ndani ya gari lile huku mikononi wakiwa na bunduki na kisha kuanza kuwafuata. Yusufu na Kelvin walikuwa wakitetemeka, hawakujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kikiendelea mahali hapo.
Tayari watu walikuwa wamekwishakusanyika kuona ni kitu gani kilichokuwa kinaendelea. Alichokifanya Sudi ni kupiga risasi hewani, watu wote wakaanza kukimbia ovyo mahali hapo. Walipolifikia gari lile, wakaufungua mlango na kumtoa Yusufu pamoja na kuchukua ufunguo wa gari lile na kisha kumpandisha ndani ya gari lao na kuondoka nae huku Kelvin akibaki mahali pale akiwa hajui ni kitu gani alitakiwa kukifanya.
Gari lilikuwa likiendeshwa kwa mwendo wa kasi, tayari muda ulikuwa ni saa kumi na mbili jioni. Gari lilipofika Sinza Kijiweni, likakata upande wa kushoto na kuanza kuelekea Shekilango ambako baada ya kufika huko, wakakata kona kulia na kuchukua barabara ya Morogoro huku wakianza kuelekea kwenye mataa ya Ubungo.
Foleni haikuwa kubwa jambo ambalo likawafanya kutokuchukua muda mrefu mpaka kuvuka mahali pale. Muda wote Yusufu alikuwa akitetemeka kwa hofu, kila alipokuwa akijitahidi kuuliza maswali, alikuwa akipigwa vibao tu na kumfanya kunyamaza.
Kila mtu alikuwa bize kwa wakati huo huku bunduki zao zikiwa mikononi mwao. Walikuwa na uwezo wa kumuua hata kwa risasi lakini aina ya kifo cha kuchomwa moto ndicho kilichoonekana kufaa zaidi kwa wakati huo. Safari iliendelea zaidi na zaidi mpaka kufika Mbezi kwa Yusufu na kuendelea mbele zaidi.
“Twendeni wapi ambapo kunaonekana kufaa zaidi?” Ahmad aliuliza.
“Msitu wa Pande” Sudi alijibu.
Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alionekana kupingana nae, msitu ule ulionekana kufaa zaidi kwa kufaya kile ambacho walikuwa wamekikusudia kukifanya kwa wakati huo. Wakazidi kwenda mbele huku mwendo wao ukiwa wa kasi zaidi na zaidi mpaka kufika karibu na Kibamba na kisha kukata kona kushoto na kuingia katika sehemu ambayo wala haikuwa na njia zaidi ya wao kuilazimisha njia kuonekana.
Walikuwa wamekwishaingia porini ambako walikuwa wakiendelea na safari yao zaidi na zaidi. Wakafika katika sehemu ambayo ilikuwa imezungukwa na miti mingi na kisha kulipaki gari lao mahali pale. Sudi na Ahmadi wakateremka na kumuacha Ramadhani na Yusufu garini.
“Tumshushe tumchome moto au tumuache na kumchoma moto humo humo?” Ahmad aliuliza.
“Tumchomeni moto humo humo” Sudi alijibu na kisha kuufungua mlango.
Kitu walichokuwa wakitaka ni kuona kwamba Yusufu alikuwepo au alikuwa amekimbia katika kipindi ambacho walikuwa wametoka nje kuongea. Yusufu alikuwepo ndani ya gari lile lakini katika kipindi hiki alikuwa tofauti sana. Kwanza, hakuwa akionekana kuwa na wasiwasi kama kipindi kilichopita, alionekana kuwa katika hali ya kawaida huku akionekana kufahamu kila kilichokuwa kikienda kutokea mahali hapo.
“Mmmh! Huyu mtu kweli noma. Hata kuogopa haogopi!”Ahmad aliwaambia wenzake huku akimwangalia Yusufu ambaye alikuwa ametulia garini.
Walichokifanya ni kufungua boneti la gari na kisha kutoa dumu la mafuta ya petroli ambalo lilikuwa limejaa mafuta na kisha kuanza kulimwagia gari lile. Yusufu alikuwa kimya garini, hakuongea kitu chochote kile, alikuwa amejiinamia chini tu.
“Hebu mmulikeni tochi usoni. Analia au?” Sudi alisema na Ahmad kummulika Yusufu tochi usoni.
Yusufu alionekana kutokuwa na wasiwasi hata kidogo, hakuwa akilia wala kulalamika hata kidogo. Kitu ambacho kilikuwa kikitaka kutokea kwa wakati huo kilionekana kuwa kama kitu ambacho wala hakikumshtua hata kidogo. Ramadhani bado alikuwa akiendelea kulimwagia petroli gari lile kuanzia nje mpaka ndani na kummwagia Yusufu mafuta yale mwil mzima.
Baada ya kuona kwamba kila kitu kilikuwa kimekamilika, hapo ndipo Sudi alipotoa namba za gari lile na kisha kuliwasha gari kwa kutumia kiberiti ambacho alikuwa nacho mahali hapo. Gari likaanza kuteketea kwa moto. Moto mkubwa ulikuwa ukiendelea kuwaka huku wakiwa wamelizunguka kwa mbali gari lile. Kwa mbali walikuwa wakimuona Yusufu alikuwa akiteketea kwa moto huku akiwa amekaa vile vile kitini huku hata akiwa haangaiki au kupiga kelele zozote zile.
Walichokifanya hasa mara baada ya kuona kwamba Yusufu tayari alikuwa ameteketea kwa moto ni kuanza kuondoka mahali hapo. Wote walikuwa wakipongezana kama kawaida kwa kumaliza kazi ile ambayo wala haikuwa ngumu sana kwa upande wao. Tayari kiasi kikubwa ambacho walikuwa wameahidiwa kilikuwa kimekwishaandaliwa na ilikuwa bado makabidhiano tu.
Walichukua dakika arobaini mpaka kufika barabarani ambapo wakachukua daladala na kisha kuanza kuelekea Mwenge alipokuwa akiishi The King na kisha kumwambia kila kilichokuwa kimeendelea msituni. The King alionekana kutokuamini, kwa furaha aliyokuwa nayo alionekana kuwa kama mtu aliyechanganyikiwa.
“Mungu wangu! Mmefanikiwa bila matatizo yoyote yale?” The King aliuliza huku akionekana kushangaa kwa furaha.
“Kila kitu tayari. Kazi haikuwa kubwa kama tulivyodhani, yaani ilikuwa rahisi kama kumsukuma mlevi mlimani” Sudi alijibu huku akionekana kuwa na uhakika.
Alichokifanya The King kwa wakati huo ni kuandaa bia pamoja na vyakula mbalimbali na kisha kuanza kunywa kama njia mojawapo ya kusherekea. Kila mmoja alionekana kuwa na furaha kwani kifo cha Yusufu kilionekana kuwafurahisha kupita kawaida.
Ilipofika saa mbili usiku, The King akawasha televisheni yake na kuweka kituo cha televisheni cha ITV ambapo hapo akapata uhakika kwamba Yusufu alikuwa ameuawa hasa mara baada ya kutangazwa kwamba alitekwa na watu wasiojulikana ambao walikuwa na bunduki na kisha baada ya saa moja gari hilo ambalo lilikuwa limetumika kwenye utekaji kukutwa limechomwa moto huku garini kukiwa na mwili wa binadamu ambao ulikuwa umeteketezwa vibaya kupita kiasi na ni mifupa tu ndio ambayo ilikuwa ikionekana kwa mbali.
“Mlikumbuka kutoa namba za gari?” The King aliuliza.
“Hatuwezi kusahau hicho. Tulitoa hata kabla hatujalichoma moto. Tena umenikumbusha, ngoja nikupe namba zako” Sudi alisema na kisha kuelekea kule alipouweka mfuko wake na kisha kutoa vibati viwili ambavyo vilikuwa na namba za gari na kisha kumgawia The King ambaye alionekana kuwa na furaha zaidi kwa kuona kwamba kazi kubwa ambayo alikuwa akiitaka kufanyika ilikuwa imekwishafanyika.
“Hakuna kuchelewa. Ngoja niwalipeni haraka sana” The King alisema na kungia ndani, alipotoka, alikuwa na mfuko wa kaki na kisha kumkabidhi Sudi ambaye aliufungua na kuanza kuangalia ndani.
“Kuna milioni kumi kama tulivyokubaliana” The King aliwaambia.
“Poa. Hapa imetulia sasa. Cha msingi jipange kurudi juu tena, mbaya wako kashakufa” Sudi alimwambia The King.
“Hiyo niachieni mimi. Ila kumukeni kwamba kitu hiki kilichotokea itabidi kiwe siri kubwa sana” The King aliwaambia.
“Usijali. Kitaendelea kuwa siri mpaka tutakapokufa” Sudi alimwambia na wote kukubaliana kwamba kila kilichoendelea kilitakiwa kuwa siri.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
‘THE RULER AUAWA KWA KUCHOMWA MOTO GARINI, THE RULER AUAWA KIFO CHA KINYAMA, NI MAUAJI AMBAYO HAYAJAWAHI KUTOKEA, MOTO WAMPELEKA THE RULER KABURINI’ Hivyo vilikuwa baadhi ya vichwa vya habari ambavyo vilikuwa vimeandikwa katika magazeti mbalimbali jijini Dar es Saaam.
Watu walionekana kushtuka, hawakuamini kile ambacho walikuwa wamekiona kwa wakati huo, kila mtu ambaye aliiona habari ile aliamua kulinunua gazeti lile. Japokuwa tukio lile lilitokea usiku wa saa moja lakini waandishi walihakikisha kwamba wanaitoa gazetini habari ile hata kama haikuwa na maelezo mengi.
Watu walionekana kusikitika kupita kawaida huku wengine ambao walikuwa na mapenzi ya dhati kwa Yusufu wakianza kulia. Tukio lile ambalo lilikuwa limetokea lilionekana kuwasikitisha kupita kawaida. Hiyo ndio ilikuwa habari ambayo ilikuwa ikisikika sana katika masikio ya watu wengi ndani ya jiji la Dar es Salaam.
Nyimbo zake zikaanza kupigwa katika vituo mbalimbali vya redio pamoja na televisheni kuwa kama sehemu ya kumuenzi. Katika kila kona ndani ya jiji la Dar es Salaam watu walikuwa wakizungumzia kuhusu tukio lile ambalo katika kipindi hicho lilionekana kuwa kubwa kuliko tukio lolote ambalo lilikuwa limetokea mwaka huo.
Waandishi wengi wa habari walikuwa wakielekea nyumbani kwake, Sinza alipokuwa akiishi, milango ilikuwa imefungwa japokuwa hali ilikuwaikionyesha kwamba kulikuwa na mtu ndani ya nyumba hiyo. Kila walipokuwa wakigonga hakukuwa na mtu aliyekuja kufungua ila walipoendelea zaidi na zaidi, Kelvin akatokea mahali hapo.
“Kuna nini?” Kelvin aliwauliza.
“Tumekuja kufanya mahojiano pamoja nawe Kelvin kwa sababu wewe ndiye mtu wa karibu sana na marehemu Yusufu” Mwandishi mmoja wa habari alimwambia Kelvin.
“Kwa hiyo ninyi mnataka niwaambie nini kuhusu Yusufu?” Kelvin aliwauliza.
“Mambo kadhaa”
“Kama yapi?”
“Turuhusu kwanza tuingie”
“Hapana. Kuna kazi nyingi zinafanyika kwa sasa ndani ya nyumba hii. Njooni kesho” Kelvin aliwaambia.
“Ila umepata taarifa kwamba Yusufu ameuawa garini kwa kuchomwa moto?”
“Yeah! Niliona kwenye magazeti yenu ya leo” Kelvin alijibu.
“Unalizungumziaje tukio hili?”
“La kawaida tu ambalo linaweza kumtokea mtu yeyote. Yaani ni kama mwandishi wa habari Vanessa alivyochomwa moto kule nchini Marekani ndani ya gari lake. Kwa hiyo hakuna cha kushangaa” Kelvin alitoa majibu ambayo yalimshangaza kila mtu.
“Kwa jinsi unav.........” Mwandishi wa habari alisema lakini hata kabla hajamalizia sentensi yake Kelvin akaingilia.
“Nafikiri mmemaliza” Kelvin alisema na kisha kufunga geti.
Kila mwandishi wa habari alionekana kushangaa, hawakuamini kama Kelvin asingewaonyeshea ushirikiano wowote ule juu ya kile ambacho walikuwa wakikitaka kukifahamu zaidi na zaidi. Tayari wasiwasi ukaanza kuwaingia kwamba kulikuwa na uwezekano kwamba Kelvin alikuwa nyuma ya kile ambacho kilikuwa kimetokea.
Bado watu walikuwa wakiendelea kuhuzunika huku taarifa ile ikizidi kuvuma kadri muda ulivyokwenda mbele. Kutokana na kuwa na jina kubwa pamoja na kuwa na mashabiki wengi kuliko msanii yeyote yule nchini Tanzania, baada ya masaa ishirini na nne, Tanzania nzima ilikuwa imefahamu juu ya kile ambacho kilikuwa kimetokea jijini Dar es Salaam.
Kila aliyezipata taarifa zile alikuwa akihuzunika kupita kawaida, nyota ambayo ilikuwa ikiwaka tayari ikaonekana kuzimwa na watu ambao walionekana kutokupendezwa na mafanikio ambayo alikuwa ameyapata. Tetesi nyingi zikaanza kusikika kutoka kwa watu mbalimbali kwamba The King alikuwa amehusika huku wengine wakisema kwamba hata mameneja wa wasanii wengine walikuwa wamehusika katika hilo kwa sababu tu Yusufu alikuwa amepata mafanikio zaidi ya wasanii wote nchini Tanzania.
Tetesi hazikuwa hizo tu bali kadri muda ulivyozidi kuongezeka na ndivyo tetesi zaidi na zaidi zilivyozidi kusikika katika kila kona jijini Dar es Salaam. Watu ambao walikuwa wakipafahamu sehemu alipokuwa akiishi Yusufu, wakaanza kuelekea huko huku wakiamini kwamba wangekuta maturubai ila kitu cha ajabu hakukuwa na maturubai yoyote yale jambo ambalo liliwashangaza sana watu.
“Mbona hali haieleweki sasa?” Jamaa mmoja aliwauliza wenzake.
“Yaani hakuna maturubai wala hakuna kitu chochote kinachoonyesha kwamba kuna msiba umetokea. Au watakuwa wameupeleka msiba Bagamoyo? Hapana bwana, hata kama wameupeleka msiba Bagamoyo, hata hapa inabidi kuwe na maturubai” Jamaa mwingine alisema huku kila mmoja akionekana kushangaa.
Tayari hali ilionekana kuwa tata. Mwili ule wa Yusufu ulikuwa umekwishapelekwa hospitali na kuihifadhiwa mochwari lakini kitu cha ajabu hakukuwa na mtu yeyote ambaye aliufuatilia. Waadishi wa habari ndio ambao walionekana kuwa kwenye wakati mgumu kwa wakati huo, walichokifanya ni kuanza kusafiri kuelekea Bagamoyo nyumbani kwa wazazi wake kwa ajili ya kupata taarifa zote kuhusiana na msiba ule.
“Kuna taarifa kwamba mtoto wako amefariki” Mwandishi wa habari, John alimwambia mzee Kessi ambaye alikuwa pamoja na mke wake, Bi Fatuma.
“Yeah! Tumeziona taarifa hizo magazetini siku ya leo” Mzee Kessi aliwaambia.
“Hizi zimekuwa taarifa za kutuchanganya sana mpaka muda huu. Yaani nyumbani kwa marehemu hakuna hata maturubai, tumekuja hapa napo hakuna maturubai. Hivi msiba huu unaweza kuwa wapi?” John aliuliza.
“Unajua ninachokiamini ni kwamba kila siku waandishi wamekuwa watu wa kuandika hisia zao zaidi ya taarifa inavyoonekana. Mimi kama mimi sidhani kama mtoto wangu ameuawa. Moyo wangu umekuwa mgumu sana kuamini hilo” Mzee Kessi alimwambia John.
“Mmmh! Sasa hapa inakuwaje tena? Tumejaribu kumpigia simu lakini napo haipatikani kabisa. Hivi tuelewe nini tena?” John aliuliza.
“Kwani taarifa zilisemaje?”
“Kwamba Yusufu alitekwa. Baada ya kutekwa, saa moja baadae gari lile likakutwa katika msitu wa pande huku likiwa limechomwa moto na mwili wake kuwa ndani” John alijibu.
“Sasa mnaamini vipi kwamba yule atakuwa ni Yusufu?”
“Vipimo. Mwili ulipimwa urefu, ulikuwa sawasawa na urefu wake ambao uliandikwa kwenye leseni yake ya udereva.
“Mmmh! Sasa mbona Kelvin hakutuambia kama Yusufu ameuawa?”
“Hata sisi hatufahamu kwa nini. Yaani hata tulipokwenda nyumbani kwake anapoishi, hakuna hata turubai” John alijibu.
“Ila na nyie mnaonekana kutuchanganya sana”
“Kwa nini mzee?”
“Mna uhakika kwamba Yusufu ameuawa?”
“Kutokana na mashahidi, vipimo, tuna uhakika huo”
“Kwa hiyo vitu hivyo tu ndivyo ambavyo vinawafanya kuamini hilo?”
“Ndio mzee”
“Gari lilichomwa moto saa ngapi?”
“Saa moja usiku” John alijibu.
“Mmmh! Kwa hiyo aliuawa muda huo?”
“Ndio”
“Sasa mbona jana saa nne usiku alitupigia simu na kutuambia kwamba yupo salama!” Mzee Kessi alimwabia John.
“Unasemaje?”
“Kwani wewe umesikia nimesemaje?”
“Hapana. Alikupigia simu na kukwambia kwamba yupo salama?” John aliuliza huku akionekana kushtuka.
“Ndio” Mzee Kessi alitoa jibu ambalo lilionekana kumchanganya sana John.
****
John alionekana kuchanganyikiwa kupita kawaida, jambo aliloambiwa kwamba Yusufu alikuwa hai lilionekana kumchanganya kupita kawaida. Alichokifanya ni kuanza kurudi jijini Dar es salaam na kuwafikishia taarifa ile waandishi wenzake ambao wote waliamini kwamba Yusufu alikuwa ameuawa kwa kuchomwa moto garini.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakutaka kuwapigia simu na kuwaelezea jambo lile, alichokuwa akikitaka ni kuwaambia ana kwa ana. Garini, John alionekana kuchanganyikiwa, mpaka katika kipindi hicho hakujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kinaendelea. Maswali kibao yalikuwa yakimiminika kichwani mwake juu ya mwili ule ambao ulikutwa ndani ya gari. Katika kila swali ambalo alikuwa akijiuliza, majibu yake yalikuwa yakimchanganya kupita kawaida.
Alipofika jijini Dar es Salaam, akachukua bajaji ambayo ilimpeleka mpaka ofisini kwao na kisha kuwaambia waandishi wenzake kile ambacho kilikuwa kimesemwa na mzee Kessi. Kila mtu aliyezisikia habari zile alionekana kuchanganyikiwa, wakabaki wakimwangalia John mara mbili mbili.
“Unasemaje?” Mhariri mmoja aliuliza kwa mshtuko.
“Hata mimi niliuliza hivyo hivyo” John alijibu.
“Hapana. Ila si vipimo vyote vimepimwa na kujulikana!”
“Ndio”
“Sasa inakuwaje wanaposema kwamba Yusufu alipiga simu usiku?”
“Hata mimi nashangaa sana”
“Hapa kuna kitu bwana. Tayari taarifa hii imeshaonekana kuwa na utata mkubwa”
“Kwa hiyo tuwaambiaje wananchi?”
“Yaani hata cha kuwaambia sikioni. Tukiwaambia kwamba aliuawa, wazazi wanaonekana kukataa hilo. Na kama tukisema yupo hai, Watanzania watatuona wazinguaji kwa sababu tuliandika kwamba ameuawa. Na kama tukisema hivyo hivyo kwamba yupo hai, watatuuliza kwamba yupo wapi?. Yaani kila taarifa tutakayoitoa itaonekana kusababisha maswali mengi” John alisema huku akionekana kuchanganyikiwa.
****
The King alionekana kuchanganyikiwa hasa mara baada ya taarifa kutolewa kwamba Yusufu alikuwa yupo hai, alionekana kutokuamini kabisa juu ya taarifa zile jambo ambalo liimfanya kumuita Sudi na kumuuliza juu ya zile taarifa ambazo alikuwa amezisikia. Akatulia kwenye kochi huku akionekana kutokuwa na furaha.
Mawazo yake kwa wakati huo yalikuwa yakimfikiria Yusufu, hakuamini kama kweli alikuwa hai na wakati alikuwa amelipa kiasi cha shiingi milioni kumi kwa ajili ya kuona kwamba mtu huyo anauawa kwa kuchomwa moto. Maswali mengi yalizidi kuongezeka kichwani mwake hali ambayo ilimfanya kukosa amani.
Akasimama kutoka pale kochini na kisha kuanza kutembeatembea pale sebuleni. Kila wakati alikuwa akiipiga mikono yake kwa hasira, hakuamini kile ambacho alikuwa akikiangali kwenye gazeti. Kila alipokuwa akiliangalia gazeti ambalo lilikuwa na taarifa juu ya Yusufu kwamba alikuwa mzima wa afya na wala hakuwa ameauwa kama ilivyoandikwa ilimfanya kuchukia.
The King alikaa katika hali hiyo kwa muda wa saa moja na ndipo ambapo Sudi akaingia mahali hapo huku akionekana kuwa na mshangao. Wote wakabaki wakiangaliana tu huku kila mmoja akionekana kuwa na dukuduku moyoni.
“Ndio mmefanya nini kutudanganya?” The King aliuliza huku akimwangalia Sudi kwa macho yaliyojaa hasira.
“Wala hatujakudanganya bosi” Sudi alijitetea.
“Kwa hiyo wenye magazeti waongo?” The King alimuuliza huku akichukua gazeti lile na kumpatia Sudi.
“Huu ni uzushi kabisa” Sudi alisema.
“Hapana. Huu si uzushi. Huu ni ukweli kabisa” The King alimwambia Sudi.
“Ni uzushi. Yusufu tulimuua kwa kumchoma moto ndani ya gari. Hatuwezi kukudanganya katika hili” Sudi alijitetea.
“Kwa hiyo waandishi wa habari waongo?”
“Inawezekana. Kama Yusufu yupo hai mbona picha yake hawajaiweka?” Sudi aliuliza.
Swali lile kidogo likaanza kuonekana kuwa na maana kichwani mwa The King. Alijua kabisa kwamba waandihsi wa habari walikuwa wameandika kwamba Yusufu alikuwa ameuawa katika siku iliyopita. Katika siku hiyo, taarifa ilikuwa kinyume chake kwa kusema kwamba Yusufu alikuwa hai, ili kuifanya taarifa yao kuaminika zaidi na zaidi kwa wasomaji, kulikuwa na ulazima wa kuweka picha ya Yusufu.
“Ila inawezekana”
“Umeonaee. Yaani kama yupo hai kama wanavyoamini basi ni lazima picha yake ingeonekana tu” Sudi alimwambia The King.
Kwa wakati huo tayari walikwishaona kwamba waandishi wa habari walikuwa wamefanya makosa ya kuandika kwamba Yusufu alikuwa hai na wakati alikuwa ameuawa ndani ya gari lile ambalo lilichomwa moto na Sudi pamoja na wenzake. Mara baada ya wasomaji kuiona taarifa ile ambayo iliandikwa kwamba Yusufu alikuwa hai, kuna swali moja ambalo liliwajia vichwani mwao, je yule ambaye alikuwa amechomwa moto ndani ya gari alikuwa nani? Hilo lilikuwa swali ambalo lilikosa jibu vichwani mwa watu ambao walikuwa wakijiuliza.
Gari lilikuwa likiendeshwa kwa mwendo wa kasi katika msitu wa Pande ambapo baada ya mwendo fulani likasimamishwa katika eneo ambalo lilikuwa limezungukwa na miti mingi mikubwa na mirefu. Muda wote huo Yusufu alikuwa akiomba aachwe huru huku akiahidi kulipa kiasi kikubwa cha fedha kama vijana wale wangekuwa wanahitaji fedha.
Hakukuwa na mtu ambaye alionekana kujali, kitu ambacho walikuwa wakikitaka kwa wakati huo ni kumuua tu kwa kumchoma moto ndani ya gari lile. Baada ya kulisimamisha gari, Sudi na Ahmad wakateremka na kuanza kuangalia angalia eneo Ramadhani akiwa amebaki na Yusufu garini.
Ghafla katika hali ambayo wala Yusufu hakuitegemea akashangaa mlango wa nyuma katika upande aliokaa ukijitoa loki na kujifungua. Kitu cha kwanza alichokifanya Yusufu ni kumwangalia Ahmadi ambaye alikuwa pembeni yake, Ahmadi alionekana kutokuwa na habari yoyote ile. Yusufu akaanza kutoka nje ya gari lile.
Alipotoka nje, pembeni yake kukaonekana kuwa na gogo ambalo alisikia sauti moyoni ikimwambia kwamba alitakiwa kuliingiza gogo lile ndani ya gari lile tena katika sehemu ambayo alikuwa amekaa. Alichokifanya Yusufu ni kufanya kama ambavyo sauti ile aliyoisikia ilivyomuelekeza.
Jambo ambalo lilionekana kumshangaza Yusufu ni kwamba Ramadhani hakuwa akijua kitu chochote kilichokuwa kikiendelea japokuwa alikuwa kwenye kiti kile kile kule nyuma. Mara baada ya kuliweka gogo lile pembeni ya Ramadhani, hapo hapo akaanza kukimbia kuelekea barabarani. Yusufu hakusimama, alikuwa akiendelea kukimbia mpaka pale ambapo akakutana na barabara na kisha kuingia ndani ya daladala na safari ya kuelekea nyumbani kuanza.
Kutokana na giza kuingia, hakukuwa na mtu yeyote ambaye alijua kwamba mtu ambaye aliingia alikuwa Yusufu au The Ruler kama alivyokuwa akijulikana na wapenzi wa muziki. Safari ile iliendelea zaidi mpaka alipofika Ubungo ambapo akaonganisha na bajaji mpaka kufika nyumbani kwake na kuanza kuugonga lango na Kelvin kuufungua.
“Mungu wangu!” Kelvin alionekana kushangaa.
“Niletee ufunguo wa gari haraka” Yusufu alimwambia Kelvin ambaye akaelekea ndani na kumletea ufunguo wa gari.
“Kuna nini tena? Mbona sikuelewi! Wale watu waliokuchukua ni wakina nani tena?” Kelvin aliuliza maswali mfululizo lakini Yusufu hakujibu kitu.
“Nisikilize Kelvin. Kama kutatangazwa taarifa yoyote ile, kubaliana nao ila usiseme kama umeniona. Umesikia?” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Ndio. Ila nini kiliendelea?”
“Usijali. Nikirudi nitakwambia”
“Hapana Yusufu. Mimi ni rafiki yako, niambie kitu gani kimetokea” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Usijali. Akili yangu haijatulia. Ngoja nikirudi nitakuelezea. Ila jua kwamba wale watu walitaka kuniua” Yusufu alimwambia Kelvin ambaye akaonekana kushtuka.
“Walitaka kukuua?”
“Ndio”
“Sasa unaelekea wapi tena?” Kelvin aliuliza.
“Kuna sehemu naelekea. Nitarudi muda si mrefu” Yusufu alijibu.
“Ngoja twende wote basi”
“Hapana. Acha niende peke yangu. Nitarudi muda si mrefu” Yusufu alisema na hapo hapo kuwasha gari lake na kisha kuondoka mahali hapo.
Japokuwa hakuwa amekimbia lakini kijasho chembamba kikimtoka. Muda wote Yusufu alikuwa na wasiwasi, hakujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kimeendelea. Muda wote alikuwa akijiuliza kuhusu ile sauti ambayo aliisikia ambayo ilimwambia kwamba alitakiwa kuondoka mahali pale huku akitakiwa kuliweka gogo lile katika sehemu aliyokuwa amekaa.
Katika kila swali ambalo alikuwa akijiuliza mahali pale alikosa jibu. Kwa wakati huo safari yake hiyo ilikuwa ni kuelekea nyumbani kwa Papaa Pipo ambapo huko angemuelezea kila kitu ambacho kilitokea. Hakuchukua muda mrefu kufika Kijitonyama, akalipaki gari lake na kuteremka na kuanza kuugonga mlango.
“Karibu” Mlinzi alimkaribisha na kuingia ndani.
Yusufu hakutaka kumsalimia mlinzi, alichokifanya ni kuelekea moja kwa moja ndani ya nyumba ile ambapo akamkuta Papaa Pipo akiwa amejipumzisha kochini akiangalia filamu ya Kitanzania iliyoigizwa na msanii nguri, Vonso Almeida.
“Mbona umekuja bila taarifa? Kuna tatizo?” Papaa Pipo alimuuliza Yusufu hata kabla ya salamu.
“Nimechanganyikiwa” Yusufu alijibu.
“Umechanganyikiwa? Kuna nini tena?” Papaa Pipo alimuuliza huku akionekana kushtuka.
“Nilitekwa”
“Ulitekwa! Na nani?”
“Kuna watu watatu waliniteka maeneo ya Tandale” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.
“Acha utani bwana”
“Kweli tena. Yaani hapa unaponiona ni kwamba nimewatoroka porini ambapo walitaka kuniua” Yusufu alimwambia Papaa pipo ambaye alionekana kupigwa na mshangao.
“Unanitania Yusufu”
“Huo ndio ukweli. Yaani hapa nimechanganyikiwa kabisa” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.
“Yaani ilikuwaje mpaka ukatekwa?”
“Sina muda wa kukuelezea Papaa. Cha msingi naomba twende kwa mzee Onyango kwa sababu kuna vitu bado sijavielewa kabisa” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.
“Kwa mzee Onyango kufanya nini tena?”
“Ili twende kule tulipokwenda”
“Wapi?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nilipoweka agano la damu” Yusufu alijibu.
“Hiyo si lazima mpaka twende kwa mzee Onyango. Hapa hapa kwangu tunaweza kwenda kule” Papaa Pipo alimwambia Yusufu ambaye alionekana kushtuka.
“Sasa mbona siku ile tulikwenda kule kwa mzee Onyango?”
“Ile ni kwa sababu mtu anapotaka kujiunga na imani yetu ni lazima aende kule. Baada ya hapo utaweza kwenda kule kupitia kwa aliyekupeleka. Au haujamuelewa mkuu siku ile ibadani?” Papaa Pipo alimuuliza.
“Nilimuelewa japo si sana”
“Basi hivyo ndivyo ilivyo. Baada ya muda fulani, nawe utapewa kioo chako” Papaa Pipo alimwambia Yusufu na kisha kumtaka kumfuata chumbani.
Wote wakaanza kuelekea chumbani ambapo wakaingia na kisha Yusufu kukaa kitandani huku akionekana kama mtu ambaye alikuwa na shauku ya kutaka kufahamu vitu fulani. Papaa Pipo akalifuata kabati la nguo na kisha kutoa kioo kikubwa na kukiegemeza ukutani na kumtaka Yusufu kuanza kuvua nguo zake kama ilivyokuwa sheria yao. Kwa haraka haraka Yusufu akaanza kuvua nguo na kisha taa kuzimwa huku wote wakiwa watupu.
Wakakisogelea kioo kile na kisha kuanza kuongea maneno yasiyoeleweka. Kama ilivyo kawaida, miale ya radi ikatokea katika kioo kile na kisha Yusufu kuingia huku Papaa Pipo akifuata. Wakafika katika ulimwengu ule mwingine, ulimwengu ambao ulionekana kuwa kama ulimwengu huu ila tofauti ilikuwa pale ambapo watu wa kule walikuwa watupu bila nguo miilini mwao.
Moja kwa moja wakaanza kuelekea katika nyumba ile ambayo mkataba wa damu ulisainiwa na kisha kukalia viti vile ambavyo vilikuwa vimezunguka meza kubwa mahali pale. Wote wakatakiwa kuinamisha vichwa vyao chini katika kipindi ambacho mhusika mkubwa alipokuwa akiingia mahali pale.
Wala haukuchukua muda mrefu, idadi ya viumbe vya ajabu ambavyo vilikuwa na mwili wa binadamu na wanyama wa porini wakatokea mahali pale huku wakiongozwa na mtu ambaye alionekana kuwa kiongozi mkubwa. Huyu hakuwa yule ambaye alimpa mkataba wa damu kuusaini bali alikuwa mwingine kabisa ambaye alikuwa na kichwa cha ng’ombe, miguu ya binadamu na kifuani akiwa na manyoya mengi na videleni akiwa na kucha ndefu.
Mara baada ya kufika katika eneo lile wote wakakaa katika viti huku Papaa Pipo na Yusufu wakiwa wameendelea kuinamisha vichwa vyao chini. Walipotakiwa kuviinua, Yusufu akaonekana kushtuka japokuwa haukuwa mshtuko kama ule wa siku ya kwanza.
Yule kiongozi akaanza kuongea katika lugha ya ajabu ambayo wala haikuwa ikieleweka huku mmoja kati ya vile viumbe ambavyo alikuja navyo vikianza kutafsiri lugha ile kwa lugha ya Kiswahili. Yusufu alikuwa makini kusikiliza.
“Kama tulivyokuahidi ndivyo tutakavyofanya. Tutakulinda kila siku, hakuna atakayenyoosha mkono wake kukuua” Mkalimani alimwambia Yusufu na kuendelea.
“Tulikuwa tumeona kila kinachoendelea. Tulichoamua ni kuendelea kukulinda. Amini kwamba kupitia wewe tumeweza kupa watu wengi sana, tumeweza kupata damu nyingi sana. Kazi yetu unaifanya kwa mafanikio makubwa sana” Mkalimani yule alimwambia Yusufu.
“Sijakielewa kile ambacho kilikuwa kimeendelea kule porini” Yusufu aliwaambia.
“Tulichokifanya ni kumpiga bumbuwazi yule ambaye ulibaki nae gari, hakuelewa kitu chochote kilichoendelea. Tulichokifanya ni kukuwekea gogo na kisha kukutaka kuliingiza garini huku tukilivisha gogo lile taswira yako. Amini kwamba tulichokisema ndicho hicho tutakachokifanya. Kila siku tutaendelea kukulinda na kuwa pamoja nawe” Mkalimani alisema na kuendelea.
“Kuanzia leo hii, kila kitu ambacho tulikupa kitaongezeka mara mbili zaidi. Umaarufu ulioupata utaongezeka mara mbili, fedha ulizozipata zitaongezeka mara mbili. Kila ulicho nacho kitaongezeka mara mbili” Mkalimani alimwambia Yusufu na kutakiwa kupiga magoti na kisha kuanza kumwagiwa damu kama kuwekewa ulinzi zaidi.
Kipindi hicho kila kitu kilikuwa kimefanyika kama kawaida huku akipelekwa katika vyumba vilivyokuwa ndani ya nyumba ile na kisha kupewa begi lililokuwa na nguo mbalimbali ambazo alitakiwa kuzivaa katika kipindi ambacho atakuwa akienda kurekodi au katika kipindi ambacho atakuwa akifaya shoo.
“Na hizi pete ni za nini?” Yusufu aliuliza.
“Hizi nazo utatakiwa kuzivaa muda wote ule. Zinaonekana kuwa pete za kawaida, lakini amini kwamba hizi pete ndizo zitakuwa ulinzi wako na chachu ya mvuto wako kwa wapenzi wa muziki” Yusufu aliambiwa.
“Sawa bwana wangu” Yusufu aliitikia huku akiinamisha kichwa chake kama ishara ya kumuabudu.
Siku hiyo ndiyo ambayo akakabishiwa kioo ambacho angekikuta chumbani kwake katika kipindi ambacho angerudi nyumbani kwake, kioo kile kitakuwa chumbani kwake. Baada ya kukamilisha kila kitu, akaambiwa kwamba hata lile begi la nguo atalikuta chumbani kwake huku likiwa pamoja na manukato yaliyokuwa na mvuto.
Kila kitu kilipomalizika, Yusufu pamoja na Papaa Pipo wakaondoka kule walipokuwa na kutokea ndani ya nyumba ya Papaa Pipo. Yusufu akaonekana kuridhika kwa kila kitu katika kipindi hicho, amani ikarudi moyoni mwake kwa kuona kwamba ulinzi mkali bado ulikuwa ukiendelea kuwekwa katika maisha yake.
“Mbona wamesema kwamba nimewapa sana damu? Hapo walinichanganya sana. Hivi walimaanisha nini pale?” Yusufu alimuuliza Papaa Pipo huku wakielekea nje.
“Unakumbuka kipindi kile ulipokwenda kufanya shoo Mwanza kwenye uwanja wa CCM Kirumba?” Papaa Pipo aliuliza.
“Nakumbuka sana”
“Unakumbuka kwamba kuna watu zaidi ya themanini walipata ajali wakati wanatoka Shinyanga kuja Mwanza kuona shoo yako?” Papaa Pipo alimuuliza.
“Ndio”
“Zile zilikuwa zi zawadi ya damu. Yaani kila kitu ambacho kilitokea siku ile kilikuwa kwenye mipango yetu” Papaa Pipo alimwambia Yusufu ambaye alionekana kushangaa.
“Mmmh! Kweli kila kitu kipo kwenye mipango” Yusufu alisema.
Mara baada ya kuagana, Yusufu akaingia ndani ya gari lake na kisha kuanza safari ya kuelekea nyumbani kwake huku ikiwa imetimia saa nne na robo usiku. Alichokifanya kwa wakati huo ni kuchukua simu yake na kisha kuwapigia wazazi wake na kuwaambia kwamba alikuwa mzima na hivyo hawatakiwi kuamini kitu chochote ambacho wangekisikia juu yake.
Kujiamini kukaonekana kuongezeka zaidi na zaidi moyoni mwa Yusufu.Ulinzi ambao alikuwa akipewa kwa wakati huo ulionekana kuwa mkubwa kupita kawaida. Wala hakuchukua dakika nyingi sana, akawa amekwishafika nyumbani ambako akaanza kuelekea sebuleni na kumkuta Kelvin akiangalia televisheni.
“Vipi tena?” Yusufu alimuuliza Kelvin.
“Wametangaza kwamba umeuawa kwa kuchomwa na moto” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Mungu wangu! Kumbe walikuwa na lengo la kunichoma moto!” Yusufu alisema kwa mshtuko.
“Ndio hivyo. Ila mpaka sasa hivi sijaelewa kipi kilitokea! Kwenye taarifa ya habari wanasema kwamba umeuawa garini na mwili wako kuonekana, hapa inakuwaje kuwaje Yusufu?” Kelvin aliuliza huku akionekana kuwa na maswali mengi kichwani mwake.
“Niliwatoroka porini. Nafikiri wameamua kufanya hivi ili kumzubaisha mtu aliyewatuma” Yusufu alijibu.
“Ila mbona kila nik......” Kelvin alisema lakini hata kabla hajamalizia sentensi yake, Yusufu akaingilia.
“Ngoja nikapumzike kwanza” Yusufu alimwambia Kelvin na kisha kuondoka mahali hapo.
Mpaka katika kipindi hicho Yusufu hakutaka maswali zaidi, hakuona kitu ambacho alitakiwa kukijibu na wakati mpaka anaondoka kule porini, alikuwa haelewi vizuri kile ambacho kilikuwa kimetokea zaidi ya kupewa maelezo na viumbe wale ambao alikutana nao kwenye ulimwengu wa giza.
Yusufu akaufuata mlango wa kuingilia chumbani kwake na kisha kuufungua na kuwasha taa. Kioo kikubwa kilikuwa kikionekana mbele yake huku kikiwa kimeegemeshwa ukutani. Yusufu akaachia tabasamu pana na kisha kuanza kukisogelea. Pembeni mwa kile kioo kulikuwa na begi kubwa la nguo, akainama na kisha kufungua zipu.
Nguo kadhaa zilikuwepo ndani ya begi lile. Yusufu akaanza kuitoa nguo moja baada ya nyingine na kisha kuanza kuziangalia. Kwake, zilionekana kuwa nguo nzuri na zilizokuwa zikivutia sana. Hizo ndizo zilikuwa nguo ambazo alitakiwa kuzivaa kuanzia muda huo. Akaanza kuzitoa na kisha kuanza kuzijaribisha, zilionekana kumtosha sana, zilikuwa zimeendana na mwili wake.
“Nimezipenda” Yusufu alijisemea huku tabasamu pana likionekana kuwa usoni mwake.
****
Hali ilikuwa haieleweki kabisa, waandishi wa habari hawakuwa wakieleweka hata kidogo. Siku mbili ziliyopita walikuwa wameandika kwamba Yusufu alikuwa ameuawa kwa kuchomwa moto ndani ya gari ambalo lilitelekezwa katika msitu wa Pande uliokuwa Mbezi lakini siku hiyo taarifa zilionekana kuwa tofauti kabisa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Watu wakashindwa kuelewa kabisa kwani kila mtu alionekana kuwashangaa waandishi hao ambao waliandika taarifa magazetini bila kufuatilia habari ile kwa kina. Swali likabaki kuwa vichwani mwa mashabiki juu ya mahali alipokuwa Yusufu, msanii ambaye walikuwa wakimpenda kuliko msanii yeyote yule Afrika Mashariki.
Waandishi wa habari walikuwa wakiendelea kumuulizia Yusufu sehemu mbalimbali ikiwemo nyumbani kwake, Sinza lakini wala hawakupata majibu yaliyoridhisha. Uwepo wa Yusufu machoni mwao ndio ambao ungedhihirisha kwamba msanii huyo alikuwa hai na si kama ilivyokuwa imetangazwa na kuandika katika vyombo mbalimbali vya habari.
“Unajua hawa waandishi wa kibongo wanaweza kuua watu aisee” Jamaa mmoja alimwambia mwenzake.
“Umeonaeee. Yaani wanaandika habari bila kuwa na uhakika kabisa” Jamaa mwingine alijibu.
“Yaani niliposoma habari juzi kwamba The Ruler ameuawa, nilijisikia mwili ukifa ganzi kabisa. Yaani kama ningekuwa na moyo mwepesi, ningeweza hata kufa” Jamaa yule aliendelea kumwambia mwenzake.
“Kuna watu kadhaa walikuwa wamekwishaweka maturubai nyumbani kwao, hasa watu wa mikoani”
Siku hiyo mchana ndio ilikuwa siku ambayo Yusufu akajitokeza machoni mwa waandishi wa habari ambao hawakuwa wamemuona kwa muda wa siku mbili tangu gari lile alilokuwa ameingizwa kuchomwa moto na watu wasiojulikana huku mwili wa mtu aliyefanana nae kwa mambo mengi ukikutwa ndani ya gari lile. Waandishi walionekana kushangaa, maswali kibao yakaanza kumiminika juu ya mtu ambaye alikuwa amechomwa moto ndani ya gari lile.
Lawama zote zikashushwa katika jeshi la polisi kwa kutoa taarifa ambazo hazikuwa na uhakika mkubwa na wakati hata uchunguzi haukuwa umefanyika. Yusufu akaanza kuhojiwa mambo mbalimbali na waandishi wale ambao walionekana kuwa na kiu ya kutaka kufahamu ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea mpaka kuwa hai katika kipindi hicho huku kila mtu akijua kwamba alikuwa ameuawa.
“Siwezi kufa kwa matakwa ya mwanadamu. Nitakufa kwa matakwa ya Mungu tu” Yusufu aliwaambia waandishi wa habari.
“Ila taarifa zinasema kwamba ulitekwa. Ni za kweli hizo?” Mwandishi mmoja, Rebecca alimuuliza.
“Yeah! Nilitekwa pale Tandale kwa Tumbo” Yusufu alijibu.
“Nini kiliendelea baada ya hapo?” Rebecca alimuuliza.
“Walinipeleka porini huku wakiwa na lengo moja tu, kuniua” Yusufu alimwambia.
“Sasa ikawaje mpaka mpango wao haukufanikiwa?”
“Nilichokifanya ni kuwahonga tu ili waniachie” Yusufu limwambia Rebecca.
“Uliwahonga?”
“Ndio. Niliwapa kiasi cha shilingi milioni kumi na tano na ndipo wakaniachia” Yusufu alimwambia Rebecca.
“Wakakubali kukipokea kiasi hicho cha fedha?”
“Ndio. Kwa muonekano ambao walikuwa nao walionekana dhahiri kuhitaji fedha. Nilipowapa, wakaniachia na kuondoka zangu” Yusufu alimwambia Rebecca.
“Na vipi kuhusu yule mtu ambaye alichomwa moto?”
“Hapo sifahamu kitu chochote kile. Sijui walifanya kitu gani mpaka kumuua mtu mwingine” Yusufu alimwambia Rebecca.
“Mmmh!”
“Ndio hivyo dada yangu. Fedha ndio kila kitu” Yusufu alimwambia Rebecca.
Yusufu akaonekana kuridhika. Kitu ambacho alikijua ni kwamba watekaji wale walikuwa wametumwa na mtu fulani kwa ajili ya kumuua. Kile alichokisema mahali hapo kilikuwa ni kama uchochezi kati ya watekaji wale na mtu ambaye alikuwa amewatuma kwenda kufanya mauaji.
****
The King akaonekana kuchanganyikiwa, maneno ambayo alikuwa ameongea Yusufu yalionekana kumchanganya. Hakuamini kama vijana wale ambao alikuwa amewatuma walikuwa wamemgeuka kiasi kile kwa kuchukua fedha za Yusufu na kisha kumuacha hai. Kwa haraka sana huku akionekana kukasirika akachukua simu yake na kisha kumpigia Sudi huku akimtaka nyumbani kwake haraka iwezekanavyo.
Ni ndani ya dakika ishirini, Sudi akafika mahali hapo. The King hakuongea kitu chochote kile, alibaki akimwangalia Sudi huku uso wake ukiendelea kuwa katika hali iliyojaa hasira kali. Akachukua chupa yake ya bia ambayo ilikuwa mezani na kupiga fundo moja na kisha kuyapeleka macho yake usoni mwa Sudi.
“Huwa unaangalia taarifa ya habari hasa kipindi cha usiku?” Lilikuwa swali la kwanza ambalo The King alimuuliza Sudi.
“Hapana” Sudi alijibu.
“Kwa nini?”
“Kwa sababu nakuwa na mambo mengi ya kufanya kipindi hicho” Sudi alimjibu The King.
“Sawa. Mara yako ya mwisho kuangalia taarifa ya habari usiku ilikuwa lini?” The King alimuuliza Sudi.
“Mwaka jana. Tena dakika mbili tu” Sudi alijibu
“Ok! Kwa hiyo hata taarifa ya habari ya leo haujaiangalia?” The King alimuuliza.
“Ndio”
“Hivi una uhakika kwamba mlimuua Yusufu?” The King aliuliza huku akianza kubadilika.
“Ndio. Tulimuua kwa kumchoma moto garini” Sudi alijibu huku akionekana kuwa na uhakika.
“Kweli?”
“Ndio”
“Sasa mbona hizi tetesi zinanichanganya sana. Nyie mliniambia mmemuua, ila tetesi zinasema kwamba yupo hai” The King alimwambia.
“Hizo ni tetesi tu na wala hautakiwi kukubaliana nazo. Kila siku tetesi zitazungumzwa sana lakini naomba uniamini kwamba Yusufu aliuawa, tena mbele ya macho yangu. Mimi ndiye niliwasha kiberiti na kulichoma moto gari lile” Sudi alijibu.
“Una uhakika?”
“Asilimia mia tatu”
“Usinidanganye Sudi. Naomba usinidanganye kabisa. Niliwalipa kiasi cha shilingi milioni kumi kwa ajili ya kukamilisha kazi yangu. Kitu mlichokifanya, kazi yangu hamkunifanyia” The King alimwambia.
“Hapana. Kazi tuliifanya”
“Hamkuifanya....” The King alimwambia Sudi kwa sauti ya juu iliyokuwa na ukali na kuendelea.
“Taarifa ya habari ya usiku imemuonyesha Yusufu akiwa hai kabisa. Yaani anaongea huku akiwa hana hata wasiwasi. Amehojiwa leo mchana na taarifa ya habari kuonyeshwa saa mbili. Yaani ni mzima kabisa, hana hata jeraha mwilini mwake” The King alimwambia Sudi ambaye akaonekana kushtuka.
“Unasemaje?”
“Ndio hivyo. Amehojiwa leo hii. Tena mbaya zaidi, amekisema kitu ambacho kimeonekana kuniumiza sana. Yaani mmemuacha hai kwa kuwa tu aliwalipa milioni kumi na tano. Huu ni ujinga. Kama mliona kwamba mna uhitaji wa fedha zaidu kwa nini hamkuniambia niwaongezee ili kazi yangu ifanyike?” The King aliuliza.
“Hapana. Sikubaliani na hilo. Yusufu tulimuua kwa kumchoma moto garini” Sudi aling’ang’ania.
“Nisikilize kwa makini. Yusufu hajafa. Nianachokitaka ni kuona anauawa ndani ya masaa arobaini na nane. Hapo namaanisha kwamba kwa siku mbili kila kitu kiwe kimekamilika. Mkijiona hamuwezi, nipeni fedha zangu niwatafute watu wengine ambao wataifanya kazi yangu. Umesikia?” The King alisema kwa hasira na kuuliza.
“Nimekusikia. Ila ninachoamini ni kwamba Yusufu tulimuua garini”
“Ikifika kesho, nunua magazeti halafu soma na kisha unipigie simu na kuniambia umeona nini. Ninachokitaka ni kwamba mtu huyu awe ameuawa ndani ya masaa arobaini na nane” The King alisema kwa hasira na kumruhusu Sudi kuondoka mahali hapo.
****
Kutokana na umaarufu mkubwa ambao alikuwa nao pamoja na kuingiza fedha kila siku, wasichana wakaonekana kuchanganyikiwa na vitu hivyo. Hapo ndipo fujo za kumtafuta Yusufu zilipoanza rasmi. Wasichana wengi walitamani kuwa na Yusufu ambaye alionekana kuwa bize sana na kazi ya muziki.
Wasichana wakaanza kujaribu bahati zao. Akili ya Yusufu ikafunguka, akakumbuka maisha yake ya nyuma ambayo alikuwa akiishi, alikumbuka vilivyo namna ambavyo alivyokuwa akikataliwa na wasichana kutoka na hali ambayo alikuwa nayo. Kwa kipindi hicho, aliona kwamba muda huo ndio ulikuwa muda wenyewe.
Yusufu hakutaka kuwapuuzia wasichana hao, alichokifanya kwa wakati huo ni kuanza kutembea na wasichana hao. Kwa kila msichana mrembo ambaye alikuwa akipita mbele yake, alikuwa akihakikisha anatembea nae. Yusufu akaonekana kuanza rasmi kazi ya kuwachukua wasichana ambao walionekana kuchanganyikiwa na fedha pamoja na umaarufu ambao alikuwa nao.
Kadri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo alizidi kupendwa zaidi na zaidi. Kulala na wasichana ndio ikawa tabia yake. Kwa kila msichana ambaye alikuwa akionekana katika video zake ilikuwa ni lazima kutembea nae. Mvuto wake kwa watu haukupungua, kila siku alikuwa akizidi kunawiri na kuvutia zaidi.
Leo alikuwa akilala na msichana huyu na kesho alikuwa akilala na msichana mwingine. Kila msichana ambaye alifanikiwa kulala kitanda kimoja na Yusufu alikuwa akijisifia. Vyombo vya habari havikuwa mbali, vikaanza kuandika kuhusu tabia ile ya Yusufu ambayo alikuwa ameanza nayo. Yusufu hakuonekana kujali, alichokuwa akikijali kwa wakati huo ni ngono tu.
Mazoea ya kulala na wasichana mbalimbali kukajenga tabia. Tabia ile ikaonekana kuwa kubwa kiasi ambacho kilionekana kuwa kero hata kwa marafiki zake. Kama kuwapanga, katika kipindi hicho Yusufu aliwapanga kupita kawaida. Leo kulikuwa na habari kwamba alilala na Miss Kinondoni ila kesho analala na Miss Ilala.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mamiss ndio ambao walikuwa wakimvutia kupita kawaida. Yusufu hakutaka wasichana wanene, wasichana wembamba ndio walikuwa na mvuto kwake. Aliwapanga kupita kawaida. Japokuwa alikuwa akitembea na wasichana wengi lakini kila alipofanya ngono, mipira ya Salama kondomu ilikuwa ikitumika kama kujilinda na magonjwa mbalimbali.
“Umezidi sasa” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Nimezidi na nini?” Yusufu aliuliza.
“Nyumba umeigeuza gesti”
“Sasa si wenyewe ndio wanataka. Wanazipenda fedha zangu, umaarufu wangu umewachanganya. Sasa kwa staili hiyo kwa nini nisiwapange?” Yusufu aliuliza huku akicheka.
“Kuwa makini bwana. Si unajua wasichana wenyewe hawaeleweki” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Yeah! Nafahamu sana na ndio maana mara kwa mara nanunua maboksi ya mipira humu ndani” Yusufu alijibu.
Tabia ya Yusufu ikaonekana kuwa kero. Wazazi wakaanza kuja juu. Mabinti zao hawakuwa wakitulia kabisa, mara kwa mara walikuwa wakielekea katika matamasha ambayo Yusufu alikuwa akitumbuiza na mwisho wa siku kuanza kumpapatikia Yusufu ambaye kazi yake ilikuwa ile ile, kulala nao tu.
Kwa kila msichana ambaye aliambiwa kwamba alikuwa akiitwa na Yusufu wala hakugoma, alikuwa akienda na kumsikiliza. Jina lake likaonekana kumbeba, umaarufu wake ulionekana kuwachanganya wasichana, kila alipokuwa, Yusufu alionekana kunukia fedha, wasichana hawakumkataa kabisa, alikuwa akiendelea na kazi yake ya kulala nao kama kawaida.
Miezi ikakatika na ndipo kukawa na tamasha la walemavu ambalo lilikuwa likitarajiwa kufanyika katika uwanja mkubwa wa mpira wa Panama uliokuwa Bagamoyo. Kama kawaida, Yusufu akawa ameitwa huko kutumbuiza pamoja na wasanii wengine akiwepo The King ambaye alikuwa ameanza kusahaulika kabisa.
Siku moja kabla ya kwenda Bagamoyo Yusufu akahitajika kuzimu, sehemu ambayo alikuwa ameweka mkataba wa damu. Alipofika kule ndipo alipoambiwa kwamba sadaka ya damu ilikuwa ikihitajika kama kawaida, na damu hiyo ingetokana na watu ambao wangekwenda kuangalia tamasha lile.
Yusufu hakuonekana kuwa na wasiwasi, kitu ambacho alikuwa akikihitaji kwa wakati huo ni kulinda utajiri, mvuto na umaarufu ambao alikuwa nao. Siku hiyo damu nyingi zilikuwa zikihitajika na kwa sababu Yusufu alikuwa juu, wahudhuriaji wa tamasha lile wangekuwa wengi sana kwa sababu lilikuwa tamasha lisilokuwa na kiingilio chochote kile.
“Watu wengi watavutwa kwa ajili ya kuja kuangalia tamasha hilo” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
“Hakuna tatizo”
“Umeonekana kuwa mtu muhimu sana katika ulimwengu ule. Umekuwa kivutio sana kwa wakubwa wetu kiasi ambacho wamekuwa wakikutumia sana na kukuongezea vitu ulivyovihitaji zaidi na zaidi” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
Matangazo ya tamasha lile ambalo lilitarajiwa kufanyika likaanza kutangazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari. Watu walionekana kama kuchangayikiwa, kitendo cha kutangazwa kwamba kumuona Yusufu akitumbuiza jukwaani ilikuwa bure ilionekana kuwa taarifa nzuri ambayo kila mtu alionekana kuifurahia.
Siku ya tamasha ilipofika, watu zaidi ya elfu kumi kutoka Dar es Salaam walikuwa wakielekea Bagamoyo kwa ajili ya kuhudhuria tamasha hilo. Hali ya hewa ya siku hiyo haikuonekana kuwa nzuri kwani tangu usiku uliopita mvua ya hapa na pale ilikuwa ikinyesha katika ukanda wote wa Pwani, hasa Dar es Salaam na Bagamoyo.
Watu hawakuonekana kujali, mvua ile ikaonekana kuwa si kitu kwao, kitu ambacho walikuwa wakikihitaji ni kumuona Yusufu tu. Magari yalikuwa yamejaza sana siku hiyo huku watu kutoka kwenye camp mbalimbali wakiwa wamekodi magari kwa ajili ya kuwapeleka Bagamoyo kumuona Yusufu ambaye alikuwa akitarajia kusafiri kuelekea nchini Uingereza kwa ajili ya kufanya shoo tatu kali katika jiji la Manchester.
“Hii shoo itakuwa kali sana. Jamaa namkubali hata zaidi ya ninavyomkubali Lil Wayne” Jamaa mmoja alimwambia mwenzake garini.
“Haunishindi mimi. Jamaa anajua sana. Yaani kama nyimbo zake zingekuwa za Kizungu halafu yupo Marekani. Hata uraisi wangempa bila kupenda. Hahahahaha” Jamaa mwingine aliongezea.
The King bado alionekana kuwa na hasira kupita kawaida, bado lengo lake kwa wakati huo lilikuwa ni kumuua Yusufu tu. Siku mbili ambazo alikuwa amewapa Sudi na wenzake zikapita lakini hakukuwa na taarifa zozote ambazo aliletewa zaidi ya kumuona Yusufu akizidi kutangazwa tu kwenye vyombo vya habari.
The King hakuonekana kukubali, akaanza kumpigia simu Sudi lakini simu haikuwa ikipatikana kabisa. Tayari Sudi na wenzake wakaonekana kumgeuka kwa wakati huo kwa kutofanya kile ambacho alitaka wakifanye. The King akaonekana kuwa na hasira kupita kawaida. Kitu ambacho akaamua kujiahidi kwa wakati huo ni kumuua Yusufu kwa mikono yake mwenyewe.
Siku zikakatika na hatimae kupigiwa simu kwamba nae alikuwa miongoni mwa wanamuziki ambao walikuwa wamechaguliwa kutumbuiza katika uwanja wa Panama mjini Bagamoyo katika siku ya walemavu duniani. Taarifa hiyo ikaonekana kuwa nzuri kwake, alichoamua siku hiyo ni kumuua Yusufu huko huko Bagamoyo.
Mara baada ya wasanii wote kulipwa nusu ya malipo yao wakatakiwa kujiandaa kuelekea Bagamoyo huku wakitumia usafiri mmoja kitu ambacho The King hakuonekana kukubaliana nacho.
Kwake, alijiona kuisaliti nafsi yake kama angetumia usafiri mmoja na aliokuwa akiutumia Yusufu. Alipotoa taarifa kwamba angetumia usafiri wake mwenyewe, kila mtu akaonekana kumshangaa ila hawakutaka kuyaingilia maamuzi yake.
Siku hiyo The King alikuwa akiendesha gari kwa kasi huku akionekana kuwa na hasira nyingi. Kichwani mwake, kwa wakati huo kulikuwa kukifikirika kitu kimoja tu, kumuua Yusufu mjini Bagamoyo.
Siku hiyo barabara haikuonekana kuwa nzuri hasa kwa magari ambayo yalikuwa kwenye kasi kubwa. Huku akionekana kutokujali, ghafla matairi ya gari lake yakaanza kuteleza na hatimae gari kupoteza muelekeo wake. Gari likaanza kuingia porini. The King alijitahidi kwa nguvu zake zote kulirudisha gari katika muelekeo sahihi lakini ikaonekana kushindikana kabisa.
Gari likaenda likazidi kwenda pembeni ya barabara zaidi na kuugonga mti mkubwa. Uzembe wake wa kutokufunga mkanda wa kiti ukamfanya The King kurushwa nje kupitia katika kioo cha mbele na kwenda kukibamiza kichwa chake katika mti ule. Kichwa chake kikapasuka, damu zikatapakaa pale mtini na mauti kumkuta hapo hapo.
Kama ilivyokuwa imepangwa ndivyo ambavyo ilivyotokea. Kutokana na mvua kunyesha sana, barabara ikaloa sana na idadi kubwa ya daladala zilizowabeba watu waliokuwa wakielekea kwenye tamasha lile kupata ajali. Zaidi ya watu elfu moja mia tano wakajikuta wakipoteza maisha katika ajali hizo idadi ambayo ilionekana kuwa kubwa sana kuwahi kutokea nchini Tanzania.
Damu nyingi ambazo zilikuwa zimemwagika zilionekana kuwa matunda ya mkataba wa damu ambao Yusufu alikuwa ameusaini. Wasanii walipofika mjini Bagamoyo, tamasha likafanyika kama kawaida. Taarifa za ajali ambazo zilikuwa zimetangazwa ndizo ambazo ziliinua vilio vikubwa mahali hapo.
Hilo likaonekana kuwa janga kubwa la Taifa. Idadi ya watu ambao walikufa kwenye ajali hiyo ilikuwa kubwa. Miili yao ilikuwa imeharibika sana kiasi ambacho hata watu wengine hawakuweza kufahamika kwa ndugu zao na hivyo kuzikwa katika kaburi moja. Katika kila kilichotokea, Yusufu alikuwa akikifahamu zaidi. Kifo cha mbaya wake, The King kikaonekana kumfurahisha.
Baada ya ajali hizo ambazo zilisababisha umwagaji mkubwa wa damu ndipo mafanikio ya Yusufu yakazidi kuongezeka zaidi na zaidi. Ingawa alikuwa amealikwa nchini Uingereza kwa ajili ya kufanya tamasha jijini Manchester hasa kwa watanzania ambao walikuwa wakiishi kule, majiji mengine kama Leicester, London, Birmingham na Liverpool wakahitaji kutaka kuzisikiliza nyimbo zake.
Mafanikio yake yakaonekana kutisha kupita kawaida. Wasichana wakazidi kumpenda na kuvutiwa nae. Kitu ambacho alikuwa akikifanya Yusufu ni kulala nao tu na kufanya nao ngono usiku kucha. Maisha yake yakawa ya kifahari sana. Mara baada ya kurudi kutoka nchini Uingereza, akanunua nyumba kubwa Mbezi Beach ambayo ilimgharimu zaidi ya shilingi milioni mia moja na hamsini na kisha kuibomoa na kutengeneza nyumba ambayo aliitaka yeye.
“Mmmh! Huyu jamaa kwa sasa anatisha. Na kuna tetesi zinasema kwamba anataka kununua ndege” Jamaa mmoja alisikika akiwaambia wenzake.
“Daah! Anaweza bwana. Jamaa anapata kiasi kikubwa cha fedha”
Hayo ndio yalikuwa matunda mazuri ambayo alikuwa akiyapata kutokana na mkataba ambao alikuwa ameuweka. Fedha zilizidi kumiminika katika akaunti yake, umaarufu ukawa mkubwa katika maisha yake, mvuto wa kupendwa ukazidi zaidi na zaidi mpaka pale alipoamua kutangaza kwamba alikuwa akitaka kuoa.
Habari ile ikaonekana kuwa njema. Watu wakawa na hamu ya kusikia ni msichana gani alikuwa akitaka kuolewa na Yusufu. Picha ya msichana ilipotolewa, alikuwa msichana mgeni machoni mwa watu wengi, msichana huyu aliitwa Samiah, msichana mzuri ambaye alikuwa na asili ya Kisomali.
“Anastahili” Watu wengi walisema mitaani na baada ya miezi miwili, harusi kufungwa huku Shekhe Omari Koba ndiye aliyefungisha ndoa hiyo katika nyumba yake iliyokuwa Mbezi Beach.
****CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Maisha ya ndoa yakaanza pamoja na mke wake ambaye alikuwa akimpenda sana, Samiah. Watu walikuwa wakijiuliza maswali mengi juu ya uamuzi ambao alikuwa ameufanya wa kuoa mapema sana lakini jibu lake lilikuwa moja tu, kutengeneza familia yake katika kipindi hicho ambacho alikuwa katika mafanikio makubwa ya kimuziki nchini Tanzania.
Tabia yake ya kutembea na wasichana mbalimbali akawa amekwishaiacha, aliiheshimu sana ndoa yake pamoja na kumheshimu sana mke wake. Akili yake alikuwa ameituliza katika maisha ya ndoa katika kipindi hicho, kila kitu ambacho alikuwa akikifanya alikuwa akimshirikisha mke wake ambaye alikuwa akimpenda sana.
Hakuacha muziki, bado alikuwa akiendelea kuimba muziki kama kawaida yake, mapenzi ya mashabiki wake hayakupungua, kila siku idadi ya mashabiki ilizidi kuongezeka zaidi na zaidi. Mara kwa mara alikuwa akiitwa nje ya nchi kwa ajili ya kutumbuiza katika matamasha mbalimbali ambayo yalikuwa yakifanyika.
Jina lake likawa kubwa, katika kila kona ya Afrika Mashariki, Yusufu au The Ruler alikuwa akijulikana sana. Nyimbo zake zilikuwa katika chati za juu sana jambo ambalo likamfanya kupata mafanikio zaidi. Siku ziliendelea kukatika zaidi mpaka kufika kipindi kile cha ugawaji wa tuzo za muziki zilizojulikana kama Kisima kutarajiwa kufanyika nchini Kenya ndani ya jiji la Nairobi.
Kama kawaida yake, Yusufu alikuwa katika sehemu tano kama mtunzi bora wa muziki, mwanamuziki bora wa kiume, wimbo bora wa mwaka, wimbo bora wa kushirikiana na video bora ya mwaka. Mpaka siku ya ugawaji tuzo unafika, tayari Yusufu alikuwa amepigiwa kura na kuongoza katika vipengele vyote ambavyo alikuwa amechaguliwa.
Hayo yalionekana kuwa mafanikio makubwa katika kazi yake ya muziki, uamuzi ambao aliuchukua wa kuuza roho yake katika ulimwengu wa giza ndio ambao ulikuwa umempa mafanikio hayo yote. Umaarufu wake, utajiri wake ukawa mara nne zaidi ya vile alivyokuwa kabla.
Yusufu hakutaka kuchelewa sana, hapo ndipo alipoamua kufungua biashara mbalimbali, akaanzisha maduka yake makubwa ya nguo ambayo yalikuwa yakichukua nguo na viatu nchini Malaysia na kuvileta nchini Tanzania. Yusufu hakuishia hapo, bado aliendelea kufungua biashara nyingine nyingi kama supermarket na biashara nyingine.
Yusufu akazidi kutangazwa zaidi na zaidi kiasi ambacho mpaka akajiona kuukaribia umaarufu mkubwa kama waliokuwa nao wanamuziki wa Marekani. Kwa sababu alikuwa akijulikana sana katika kipindi hicho, akajikuta akichaguliwa kuwania tuzo kubwa kuliko zote Afrika, tuzo za Kora.
Kama kawaida alikuwa amechaguliwa katika vipengele vichache na akafanikiwa kuwa msanii bora wa kiume barani Afrika katika kipindi hicho. Yusufu akaona kumaliza kila kitu japokuwa kulikuwa na vitu vingi sana mbele yake. Tanzania ikajivunia, Yusufu akaonekana kuwa lulu zaidi ya wanamuziki wote wa Tanzania.
Hapo ndipo maisha ya majigambo yalipoanza rasmi. Yusufu akaanza kubadilika, tayari alijiona kuwa juu zaidi ya wanamuziki wote wa Kitanzania. Akaanza kuhitaji malipo makubwa katika shoo zake mbalimbali ambazo alikuwa akizifanya. Mapromota wengi walikasirika lakini hawakuwa na jinsi, kwa sababu walikuwa wakitaka fedha, walipaswa kumuita Yusufu katika matamasha yao.
“Tupange familia yetu” Samiah alimwambia Yusufu katika kipindi ambacho alikuwa ametulia nyumbani.
“Familia! Mbona kila kitu kipo sawa. Au ulikuwa unamaanisha nini mke wangu?” Yusufu alimuuliza Samiah.
“Kuwa na watoto wetu. Nyumba imekuwa kubwa sana na ukimya umetawala” Samiah alimwambia Yusufu ambaye kwa mbali akaonekana kushtuka.
Tayari kumbukumbu zake zikarudi nyumba kabisa mpaka katika siku ile ambayo alikuwa amesaini mkataba wa damu wa kuiuza roho yake katika ulimwengu wa giza. Alikumbuka vilivyo sharti ambalo alikuwa amepewa katika kipindi ambacho alihitaji utajiri na mvuto. Hakutakiwa kupata mtoto katika maisha yake yote na kama angekwenda kinyume angeweza kuuawa au kupewa adhabu yoyote ile.
“Unasemaje?” Yusufu aliuliza kana kwamba hakusikia vizuri.
“Nahitaji watoto mume wangu” Samiah alimwambia Yusufu kwa sauti ya chini iliyoja upole.
“Haiwezekani kwa sasa” Yusufu alijibu.
“Kwa nini?”
“Fahamu kwamba haiwezekani mpenzi, kuna vitu navirekebisha kwanza” Yusufu alimwambia mke wake, Samiah.
Siku hiyo kukaonekana kutokuwa na maelewano, kila mtu kwa wakati huo alikuwa akitaka kitu chake. Samiah bado alikuwa aking’ang’ania uamuzi ule ule ambao alikuwa amejiwekea kwamba alikuwa akihitaji kuwa na watoto lakini akaonekana kutokuelewa kabisa.
Kutokana na kuonekana kukasirishwa siku hiyo, Yusufu hakutaka kulala nyumbani hapo, alichokifanya ni kwenda katika hoteli ya Serena na kisha kupumzika huko. Kichwa chake kilikuwa na mawazo mengi, hakujua ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya kwa wakati huo.
Si kwamba Yusufu hakutaka kuwa na mtoto, alikuwa akitamani sana jambo hilo kutokea lakini masharti ambayo alikuwa amepewa yalionekana kumkosesha raha, kamwe asingeweza kuwa na mtoto kwani kwa kufanya hivyo aliogopa kupewa adhabu kali na hata kupokonywa vile ambavyo alikuwa navyo katika kipindi hicho.
Siku ziliendelea kukatika kama kawaida. Samiah hakuonekana kukubali kabisa, katika kipindi hicho alikuwa akihitaji kitu kimoja tu katika maisha yake, kuwa na mtoto. Hakujua angeweza vipi kumlaghai mume wake ambaye alionekana kuwa mkali katika kila kipindi ambacho alikuwa akizungumzia kuhusiana na wao kupata mtoto.
Samiah hakutaka kuona hali ile ikiendelea zaidi, kitu ambacho alikuwa akikihitaji kwa wakati huo ni kupata mtoto tu. Alichokifanya ni kuziangalia siku zake na kisha kuanza kupiga hesabu kichwani mwake. Akazijua siku zake vilivyo ila kitu ambacho alitaka kumficha mume wake katika kipindi hicho ni tarehe zake za kuingia mwezini.
Jambo hilo likaonekana kufaulu, katika siku ambayo Samiah alijua fika kwamba angeweza kupata mimba kama angefanya mapenzi na ndio siku hiyo ambayo akafanya mapenzi na mume wake. Kitendo kile kilimpa furaha sana Samiah pasipo kujua kwamba kilikuwa ni kitendo kimoja ambacho kilikuwa ni cha hatari sana katika maisha ya mume wake, Yusufu.
Kuanzia hapo kila siku alikuwa akilishika tumbo lake huku akitabasamu. Tayari katika kipindi hicho Samiah akajiona kuwa mshindi zaidi ya washindi, kitendo alichokifanya cha kufanya mapenzi na mume wake, Yusufu katika tarehe ya hatari ya kupata mimba ikaonekana kumfurahisha kupita kawaida.
Yusufu hakujua kitu chochote kile, hakujua kama kipindi hicho mbegu zake zilikuwa zimekwenda katika yai la uzazi la mke wake, Samiah na kuanza kutengeneza kiumbe. Samiah hakutaka tena kuzungumzia suala la kutaka mtoto kwani katika kipindi hicho alijua fika kwamba ilikuwa ni lazima kupata mtoto wake mwenyewe.
Siku zikaendelea kukatika mpaka kufika siku zile ambazo Samiah akaanza kutapika na kusikia kichefu chefu hali iliyoonyesha kwamba mambo yalikuwa yamekaa sawa. Yusufu alipogundua hali ile akaonekana kuogopa kupita kiasi, alikuwa akimwangalia mke wake kwa wasiwasi mkubwa kwamba tayari alikuwa mjauzito.
“Vipi tena? Mbona unatapika hovyo?” Yusufu alimuuliza Samiah huku akionekana kuwa na wasiwasi.
“Nahisi Homa” Samiaha alidanganya.
Yusufu hakupenda kumuona mke wake akiwa katika hali hiyo, alichokifanya ni kumpeleka hospitali na kisha kupatiwa matibabu. Hali haikubadilika, bado ilikuwa ikiendelea vile vile mpaka pale ambapo tumbo la Samiah lilipoanza kuwa kubwa. Muonekano wa tumbo lake ukaonekana kumuogopesha zaidi Yusufu ambaye alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa.
“Mmmmh! Sio mimba hii?” Yusufu alimuuliza Samiah huku wasiwasi ukiongezeka zaidi.
“Ndio yenyewe” Samiah alijibu huku akitabasamu.
“Mimba ya nani?” Yusufu aliuliza.
“Mimba yako” Samiah alitoa jibu lililoonekana kumchanganya sana Yusufu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Je nini kitaendelea?
Je Yusufu atapewa adhabu au kupokonywa kila alichopewa?
Je Samiah atajifungua mtoto salama?
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment