Search This Blog

Friday, 3 June 2022

NITAKAPOKUFA - 3

 





    Simulizi : Nitakapokufa

    Sehemu Ya Tatu (3)



    Malumbano makali yalikuwa yakisikika kutoka ndani ya nyumba ya Yusufu. Muda wote Yusufu alikuwa akimlalamikia mke wake, Samiah kwa kitendo kile cha kuruhusu kupata ujauzito ule. Yusufu alionekana kukasirika sana huku wakati mwingine akitetemeka mwili mzima na kijasho chembamba kumtoka.

    Tayari alijua kwamba mwisho wa maisha yake ulikuwa umefika kwa sababu alikuwa njiani kuvunja moja ya masharti ambayo alikuwa amepewa katika ulimwengu ule wa giza. Moyoni akakosa raha, kila alipokuwa akimwangalia mke wake, Samiah alionekana kukasirika zaidi. Unyonge ukaanza kuingia katika maisha yake, kichwa chake kilikuwa kikifikiria zaidi kupokonywa umaarufu, utajiri na kila kitu ambacho alikuwa nacho.

    Ndani ya wiki nzima, Yusufu hakutaka kulala nyumbani, alikuwa akishinda hotelini tu akilala. Hakutaka kufanya shoo yoyote ile kwa sababu hakuwa katika hali nzuri hata mara moja. Alijiona kuwa na uhitaji wa kukaa mbali na mke wake, kwa jinsi alivyokuwa na hasira nae katika kipindi hicho, alijiona kama angeweza kumuua muda wowote ule.

    “Huyu mwanamke kwa nini ameamua kunifanyia hivi?” Yusufu alijiuliza huku akiuma meno yake yake kwa hasira.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kulala hotelini akaona kutokusaidia, kitendo cha mke wake kumpigia simu pamoja na kumtumia meseji nyingi mara kwa mara kukaonekana kumuudhi sana kitu ambacho akaamua kuondoka nchini Tanzania na kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya mapumziko ya muda fulani hata kabla hajajua nini kingetokea mbeleni.

    Kwa Samiah mambo yalikuwa hivyo hivyo, hakuonekana kuwa na raha hata kidogo, kitendo cha mume wake kuondoka na kuelekea pasipojulikana kulionekana kumuumiza kupita kawaida. Muda mwingi alikuwa akimpigia simu na hata kumwandikia meseji lakini hali haikuonekana kubadilika.

    Alikuwa akimpigia sana simu lakini haikuwa ikipokelewa, alipiga kwa zaidi ya mara hamsini kwa siku lakini hali ilionekana kuwa ile ile, simu haikupokelewa kabisa na baada ya siku kadhaa, simu haikuwa ikipatikana. Alichokifanya Samiah ni kuanza kumtumia meseji lakini hali napo ilionekana kuwa pale pale, meseji hazikuwa zikijibiwa kabisa.

    Yalikuwa ni maumivu makubwa moyoni mwake, maumivu ambayo wala hayakuelezeka hata kidogo. Kitendo cha mume wake kumfanyia mambo yote yale kilionekana kumuumiza sana. Alichokifanya Samiah ni kuchukua gari lake na kisha kuelekea mpaka Bagammoyo na kisha kuwaeleza wakwe zake juu ya kile ambacho kilikuwa kinaendelea nyumbani kwake.

    Mzee Kessi na mkewe, Bi Fatuma hawakuonekana kumuelewa kabisa Samiah kwamba ingewezekana kwa Yusufu kufanya mambo yale kisa kilikuwa ni ujauzito, walichokifanya ni kuanza kumpigia simu. Kama ilivyotokea kwa Samiah ndivyo ambavyo ilitokea kwa wazazi hao pia, simu haikupatikana kabisa.

    Kila mmoja alionekana kutokuamini kile ambacho kilikuwa kimetokea, hawakujua mahali ambapo Yusufu alipokuwa kwa kipindi hicho, wasiwasi ukaanza kuwashika, hatua waliyoichukua kwa kipindi hicho ni kumpigia simu rafiki mkubwa wa Yusufu, Kelvin. Majibu yaliyotoka kwa Kwelvin yakawachanganya zaidi.

    “Sijamuona kwa siku mbili sasa kitu ambacho si kawaida kabisa” Kelvin aliwaambia.

    “Hebu jaribu kuwapigia marafiki zake wa karibu na kuwauliza kuhusu mahali alipokuwa kwa sasa” Mzee Kessi alimwambia Kelvin ambaye alifanya kama alivyoambiwa.

    Wote wakakaa kwa dakika kadhaa huku wakiisubiria simu ya Kelvin ambayo ingewaambia ni mahali gani alipokuwa Yusufu katika kipindi hicho. Walibaki wakiisubiria simu ile kwa dakika zaidi ya ishirini, simu ikaanza kuingia, alikuwa Kelvin.

    “Yupo wapi?” Mzee Kessi aliuliza.

    “Nimejaribu kuwapigia watu wengi lakini wote wanasema hawajui alipo” Kelvin alijibu.

    Kila mmoja alionekana kuchanganyikiwa zaidi, hawakuamini kama Yusufu angeweza kufanya jambo kama lile la kuondoka nyumbani na kuelekea katika sehemu isiyojulikana. Samiah alikaa Bagamoyo kwa muda wa siku mbili na ndipo alipoamua kurudi jijini Dar es Salaam na kupanga kuelekea Dodoma kwa wazazi wake.

    Katika kipindi hicho hali ikaonekana kuwa vile vile, kila walipokuwa wakijaribu kumpigia simu Yusufu, simu haikuwa ikipatikana kabisa. Hali ilizidi kuwa mbaya kwa Samiah kiasi ambacho muda mwingi alikuwa akijutia uamuzi wake uliompelekea wa kupata ujauzito na wakati mume wake, Yusufu alikuwa amekataa kuhusiana na jambo hilo.

    Mawazo juu ya mume wake ndio ambayo yalimpelekea kutokula kabisa, moyo wake ulikuwa ukimkumbuka sana mume wake, Yusufu. Hakujua ni mahali gani ambako alitakiwa kumtafuta kwa kipindi hicho. Mara kwa mara alikuwa akipigiwa simu na marafiki wa karibu wa Yusufu wakimtaka kumtaarifu ni mahali Yusufu alipokuwa lakini hakuwa na cha kuwajibu.

    Kuondoka kwa Yusufu nyumbani kukaanza kusikika masikioni mwa watu, watu wakaanza kushangaa jambo ambalo liliwapelekea waandishi wa habari kufika nyumbani hapo na kisha kuanza kuongea na Samiah ambaye muda mwingi alionekana kuwa na majonzi mengi usoni.

    “Kwa hiyo hakukuaga?” Mwandishi wa habari, Penina alimuuliza Samiah.

    “Hakuniaga”

    “Kwa nini?”

    “Sijui kwa nini”

    “Au mligombana?”

    “Hapana”

    “Sasa tatizo nini?”

    “Hata mimi sifahamu” Samiaha alificha.

    Magazeti yakaanza kuandika kuhusiana na Yusufu kwamba alikuwa ameondoka nyumbani kwake na kwenda kusipojulikana. Kwa kila mtu ambaye aliiona taarifa ile ilionekana kumshtua, tayari wakaanza kujua kwamba kuna kitu kilikuwa kimetokea nyuma ya pazia ambacho wala hawakutakiwa kukifahamu.

    ****

    Ulikatika mwezi mmoja na ndipo Yusufu aliporudi nchini Tanzania akitokea nchini Afrika Kusini. Mara baada ya kupata taarifa kwamba Yusufu alikuwa amerudi nyumbani, waandishi wa habari wakaanza kufika nyumbani kwake na kisha kuanza kufanya mahojiano pamoja nae. Kwa kila kitu ambacho alikuwa akiongea Yusufu mahali hapo alionekana dhahiri kuficha kitu fulani moyoni mwake.

    Yusufu hakuwa muwazi, kila alipokuwa akiulizwa hili, alijibu lile tena kwa maelezo mengi ambayo yaliwafanya waandishi wa habari kutokumuelewa kabisa. Hakuonekana kama alikuwa radhi kufanyia mahojiano katika kipindi hicho kitu ambacho kiliwafanya waandishi hao kuondoka nyumbani kwake.

    Uamuzi ambao alikuwa ameupanga Yusufu mahali hapo ni kumpa talaka Samiah. Hilo lilionekana kuwa tukio kubwa na baya kutokea katika maisha ya Samiah ila hakuwa na jinsi, akaondoka nyumbani hapo na kuelekea nyumbani kwa wazazi wake waliokuwa wakiishi Dodoma.

    Taarifa ya kuachwa kwa Samiah ndio ambayo ilionekana kutawala sana katika vyombo vya habari, kila mtu alikuwa akijiuliza sababu lakini hakukuwa na mtu aliyeweza kufahamu kitu chochote kile. Katika kipindi hicho Yusufu akaonekana kuwa mkali kwa kila mwandishi wa habari ambaye alikuwa akitaka kufahamu kile ambacho kilitokea katika maisha yake ya ndoa mpaka kuamua kumpa talaka mke wake, Samiah.

    “Ni mambo ya watu wawili kati yangu na Samiah, sidhani kama ninyi mnatakiwa kufahamu” Yusufu aliwaambia waandishi wa habari kwa sauti iliyoonyesha kwamba alikuwa na hasira.

    “Lakini sisi kama waandishi naona kuna umuhimu mkubwa wa kufahamu hilo. Watu wengi wanahoji juu ya hilo” Mwandishi Rebecca alimwambia Yusufu.

    “Mmekosa cha kuandika au mmekosa wa kumhoji?” Yusufu aliwauliza huku hasira zake zikiongezeka zaidi.

    “Punguza hasira Yusufu”

    “Nimewaambieni kwamba jambo hili ni la watu wawili tu kati yangu na mke wangu, ninyi mnang’ang’ania nini sasa? Mlitaka niendelee kuwa nae? Acheni upuuzi wenu huko, kwanza tokeni ndani ya nyumba yangu” Yusufu aliwaambia waandishi wale wa habari.

    Waandishi hawakutaka kuondoka, kitu ambacho walikuwa wakikitaka mahali hapo ni kufahamu ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea katika maisha ya Yusufu mpaka kuamua kumpa talaka Samiah ambaye alionekana kuwa mjauzito. Alichokifanya Yusufu mahali hapo ni kuelekea ndani ya nyumba yake na kutulia.

    Yusufu alikaa katika hali ya mawazo mengi kupita kawaida, kwa wakati huo alijua fika kwamba alikuwa njiani kupoteza kila kitu ambacho alikuwa nacho katika kipindi hicho. Kama Samiah angejifungua salama basi mvuto wake kwa mashabiki wake ungetoweka kabisa, utajiri wake ungetoka kabisa na hivyo kurudi katika hali yake kama zamani.

    Usiku ulipoingia, Yusufu akaamua kumfuata mtu ambaye alikuwa kila sababu zilizomfanya kuingia katika mkataba wa damu na ulimwengu wa giza, Papaa Pipo. Alilipaki gari lake katika uwanja wa nyumba ya Papaa Pipo, akateremka na kuanza kuelekea ndani ya nyumba hiyo na kutulia sebuleni ambapo baada ya muda Papaa Pipo akatokea mahali hapo.

    “Kwa nini ulitoweka ghafla? Ulikwenda wapi rafiki yangu?” Papaa Pipo alimuuliza.

    “Afrika Kusini” Yusufu alijibu.

    “Mbona ghafla sana na wala haukuniaga?”

    “Ilikuwa ni safari ya ghafla sana. Si wewe tu, hata mke wangu na wazazi wangu sikuwaaga” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.

    “Kwa nini sasa uliamua kufanya hivi?”

    “Mawazo. Yaani naona kila kitu kitakwenda kuharibika hapo mbeleni” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.

    “Kwani kuna nini kimetokea?”

    “Nimevunja masharti” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.

    “Unasemaje? Umevunja masharti?”

    “Ndio. Mke wangu kapata ujauzito” Yusufu alitoa jibu lililoonekana kumchanganya Papaa Pipo.

    Papaa Pipo hakuongea kitu chochote kile, alibaki kimya huku akiangalia juu. Kichwa chake kwa wakati huo kikaonekana kuanza kufikiria mambo mengi, baada ya muda wa sekunde kadhaa akayapeleka macho yake usoni mwa Yusufu ambaye alionekana kuwa mwingi wa mawazo.

    “Sasa kwa nini uliamua kuvunja masharti?”

    “Tatizo mke wangu. Mke wangu ndiye aliyenichezea mchezo huu” Yusufu alijibu.

    “Pole sana ndugu yangu”

    “Asante sana. Yaani sijui itakuwaje. Akili yangu imechanganyikiwa kabisa” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Katika kipindi chote Samiah hakuonekana kuwa na furaha kabisa, kitendo cha kupewa talaka na mume wake, Yusufu kilionekana kumuumiza kupita kawaida. Kila siku akawa mtu wa kulia tu, hakujua sababu ambayo ilimfanya mume wake kupinga kwa nguvu zote kupata ujauzito. Wakati mwingine alikuwa akijuta kile ambacho alikuwa amekifanya cha kuruhusu ujauzito.

    Mtoto alionekana kuwa baraka katika familia nyingine lakini kwake akaonekana kuwa kama laana. Muda wote Samiah alikuwa mtu wa kulia tu. Wazazi wake, Bwana Hussein pamoja na mama yake, Bi Warda walikuwa na kazi kubwa ya kumbembeleza kila siku. Moyoni aliumia kupita kawaida, maumivu makali ambayo wala hakuwa akiyategemea kabla.

    Mara zote alikuwa akijifungia chumbani. Kutokana na kuwa na msongo mkubwa wa mawazo huku akiwa na ujauzito, mara kwa mara Samiah alikuwa akiumwa. Kila alipokuwa akipelekwa hospitalini madaktari walikuwa wakimwambia apunguze mawazo na pia awe anakula sana lakini maneno ya madaktari wale hayakubadilisha kitu chochote kile.

    Mwili wake ukanyong’onyea, kila wakati alikuwa akimfikiria mtalaka wake, Yusufu ambaye katika kipindi hicho alikuwa ameamua kuishi maisha ya peke yake. Siku ziliendelea kukatika mpaka katika kipindi kile ambacho akaanza kujisikia uchungu na kupelekwa katika hospitali ya mkoa ya Dodoma na kisha kujifungua salama mtoto wa kiume.

    Kwa kiasi fulani furaha yake ikaonekana kurudi tena moyoni mwake, mtoto wake huyo ambaye aliamua kumpa jina la Nasri ambaye alionekana kumpa furaha katika kipindi hicho. Kila alipokuwa akimwangalia, alifanana nae sana huku baadhi ya maeneo akiwa amefanana na Yusufu. Samiah akapokea zawadi mbalimbali kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki ambao walikuja hospitalini pale.

    Waandishi wa habari hawakutaka kupitwa, mara baada ya kupata taarifa kwamba Samiah alikuwa amejifungua, wakasafiri mpaka Dodoma na kisha kuchukua habari na kuwapiga picha. Taarifa hiyo ndio ambayo ilionekana kuuza sana magazeti hasa pale watu ambapo wangesikia na hatimae kutaka kumuona mtoto huyo, Nasri.

    Kama ilivyotarajiwa na ndivyo ilivyotokea. Magazeti yakanunuliwa sana mitaani kiasi ambacho kiliwashangaza hata wamiliki wa magazeti hayo. Kila mtu alikuwa akitaka kumuona mtoto wa Yusufu au The Ruler kama jinsi ambavyo alivyokuwa akijuliakana katika kipindi hicho.

    Mwezi wa kwanza ukapita, mwezi wa pili ukapita. Yusufu hakuacha mawasiliano pamoja na mtalaka wake, Samiah kwani mara kwa mara alikuwa akipeleka fedha za matumizi kama kuepuka lawama lakini huku moyo wake ukiwa na hasira na Samiah kwani aliona muda si mrefu angeweza kunyang’anywa kila alichokuwa nacho.

    ****

    Yusufu akaamka kutoka usingizi, jasho lilikuwa likimtoka kupita kawaida. Akaanza kuangalia huku na kule, alikuwa akiweweseka sana. Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kupita kawaida. Macho yake akayapeleka katika simu yake, ilikuwa saa tisa usiku. Hofu ikaanza kumjia moyoni, hakuelewa sababu yoyote ambayo ilimpelekea kuwa katika hali ile.

    Huku akiwa anajiuliza, ghafla chumba kikawa na giza kubwa, taa ambayo mara kwa mara alikuwa akiiwasha ikajizima, mwanga mkali ukaanza kumulika kutoka katika kile kioo ambacho kilionekana kuwa kama mlango wake wa kuingilia katika ulimwengu wa giza. Yusufu alizidi kuogopa kupita kawaida, hali ambayo ilikuwa imetokea katika kipindi kile haikuwahi kumtokea hata siku moja.

    Ghafla, sauti kali na nzito ikaanza kusikika kutoka katika kioo kile ambacho hakukuwa na mtu ambaye angeweza kukiona zaidi yake. Sauti ile ilikuwa ikimtaka kuelekea katika ulimwengu ule wa giza. Bila kujiuliza au kuleta mgomo wowote ule, akainuka na moja kwa moja kuanza kukifuata kioo kile.

    Mianga kama ya radi nangurumo za ajabu zikaanza kusikika, kwa sababu ngurumo zile alikuwa amekwishazizoea, hakuogopa, akaelekea katika kioo kile na kisha kutokea katika upande wa pili. Mwendo wa Yusufu ambao alikuwa akitembea siku hiyo ulikuwa ni wa tofauti sana, kichwa chake kilikuwa kikijua wazi kwamba kitendo cha kuvunja moja ya masharti ndicho ambacho kilisababisha yale yote.

    Mara baada ya mwendo fulani akaifikia nyumba ile na kisha kuingia ndani. Muonekano wa nyumba ile siku hiyo ulikuwa ni wa tofauti kabisa. Kwanza nyumba ilionekana kubwa sana kwa ndani siku hiyo, hata idadi ya watu ambao walikuwa ndani ya nyumba ile siku hiyo walikuwa wameongezeka zaidi.

    Watu zaidi ya themanini walikuwa ndani ya nyumba ile, mavazi yao yalikuwa yametofautiana. Wapo ambao walikuwa wamevaa nguo nyeusi na wengine nyekundu. Mavazi yao hazikuwa suruali, zilikuwa kama mashuka makubwa ambayo walikuwa wakiyavaa kuanzia chini mpaka kufunika vichwa vyao.

    Yusufu akabaki akiwa amesimama mlangoni, katikati ya watu wale kulikuwa na chombo ambacho kilikuwa kikiwaka taa huku pembeni kukiwa na kisu ambacho kilionekana kuwa na ncha kali sana. Yusufu hakutaka kupiga hatua zaidi, alichokifanya ni kuanza kuelekea mbele kabisa huku watu wote ambao walikuwa mahali pale wakiwa wameinamisha vichwa vyao huku kwa mbali sauti zao zikisikika mahali pale.

    Mara baada ya kufika mbele kabisa, mtu mmoja ambaye alionekana kutisha sana akaanza kumfuata pale alipokuwa amesimama na kisha kuanza kumwangalia usoni. Macho ya mtu yule hayakuwa ya kawaida kabisa, yalikuwa mekundu kabisa huku meno yake yakiwa na ncha kali kupita kawaida.

    Alichokifanya mtu yule mara baada ya kumwangalia Yusufu kwa muda fulani, akaanza kuelekea kule kulipokuwa na kisu na kisha kukichukua na kumgawia Yusufu. Yusufu hakujua kazi ya kisu kile, alibaki akitetemeka huku akijua kwamba alitakiwa ajichome na kujiua kama adhabu ambayo aliambiwa angepewa.

    “Umevunja moja ya masharti yetu” Mwanaume yule alimwambia Yusufu kwa sauti nzito iliyokuwa na utetemeshi mkubwa.

    Watu wote ambao walikuwa wameinama chini wakainua vichwa vyao na kisha kuanza kumwangalia Yusufu. Yusufu aliwaangalia watu wale, alikuwa akiwatambua sana huku akionekana kushtuka, hakuamini hata viongozi wengine wa nchi pamoja na matajiri wengine nao walikuwa katika ulimwengu ule.

    “Tunakuadhibu” Mtu yule alimwambia Yusufu.

    Mara ghafla mbele ya Yusufu kikatokea kioo kimoja kikubwa, kilikuwa mara mbili zaidi ya kile kioo ambacho kilikuwa chumbani kwake. Yusufu hakuelewa maana ya kioo kile, alibaki akikiangalia tu. Baada ya sekunde kadhaa, sura za wazazi wake, mzee Kessi na Bi Fatuma zikaonekana katika kioo kile kitu ambacho kilimfanya Yusufu kushtuka.

    “Tunakuadhibu. Tunamtaka mtu mmojawapo” Mtu yule alimwambia Yusufu.

    Yusufu akaanza kutetemeka, hakuamini kama adhabu ambayo alikuwa akipewa kwa wakati huo ilikuwa ni kumuua mmoja wa wazazi wake. Ule ukaonekana kuwa mtihani mkubwa sana kwake, hakujua ni mzazi gani ambaye alitakiwa kumuua katika kipindi hicho. Akabaki akiwaangalia wazazi wake kwa muda hata kabla hajaamua ni yupi alitakiwa kumuua kwa mkono wake katika kipindi hicho.

    Mawazo yake yakaanza kurudi nyuma kabisa. Akaanza kukumbuka katika kipindi ambacho wazazi wake hao walivyokuwa wakiangaika sana kila siku kwa ajili yake. Hakuamini kama siku hii ya leo alitakiwa kufanya uamuzi mmoja mgumu, uamuzi wa kumuua mmoja wa wazazi wake ambao walikuwa wamejitoa sana katika maisha yake.

    Alibaki kwa muda wa dakika tano akawa bado hajatoa uamuzi wowote ule. Alikuwa akiendelea kukumbuka mambo mengi ambayo yalikuwa yametokea katika maisha yake ya nyuma ambayo alikuwa amelelewa sana na wazazi wake hao. Japokuwa uamuzi ulikuwa mgumu sana kwake lakini alitakiwa kufanya kitu kimoja tu, kumuua mtu mmojawapo.

    Yusufu hakuwa na jinsi, alitakiwa kufanya kile ambacho alitakiwa kukifanya mahali hapo. Akaunyanyua mkono wake ulioshika kisu. Machozi yalikuwa yakitiririka mashavuni mwake, maumivu makubwa sana yakaukumba moyo wake. Alichokifanya mahali hapo ni kuchoma taswira ya baba yake, mzee Kessi ambayo ilikuwa ikionekana katika kioo kile.

    Mzee Kessi akaonekana akianza kuangaika katika kioo kile, damu nyingi zikaanza kumtoka kwa sekunde kadhaa na kisha kutulia. Yusufu akabaki akilia, hakuamini kama katika kipindi hicho alikuwa amemuua baba yake kwa mikono yake mwenyewe. Adhabu ile ikaonekana kuwa kubwa kwake, hakuamini kama baba yake ambaye alikuwa amemlea katika kipindi chote kile ndiye ambaye alikuwa amemuua kwa mkono wake mwenyewe.

    Hapo hapo akapokonywa kisu kile. Yusufu akapiga magoti chini na kuanza kulia kwa uchungu mkubwa. Japokuwa watu wengine walikuwa wamekwishaanza kuondoka mahali hapo lakini Yusufu hakuondoka, bado alikuwa amepiga magoti chini huku akiendelea kulia. Ghafla akajikuta akisafirishwa kutoka katika ulimwengu ule na kutokea katika kitanda chake huku akiwa amepiga magoti vile vile. Yusufu alibaki akilia tu, hakuonekana kuamini kile ambacho alikuwa amekifanya kipindi kile, kumuua baba yake kwa mkono wake mwenyewe.

    ****CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku hiyo usiku ukaonekana kuwa usiku mgumu kuliko siku zote alizowahi kuishi ndani ya dunia hii. Alijitahidi sana ili aweze kupata usingizi lakini usingizi ukagoma kabisa kuja. Mawazo yake yalikuwa yakimfikiria baba yake tu, mzee Kesy ambaye alikuwa akiishi mjini Bagamoyo. Moyo wake ulikuwa ukimuuma sana, hakuamini kama utajiri, umaarufu na mvuto ambao alikuwa nao ndio ambao ulikuwa umesababisha siku hiyo kumuua baba yake.

    Yusufu alilia sana usiku huo, japokuwa hakuwahi kwenda msikitini lakini kwa kufikia hatua hiyo akaanza kumuomba Mungu aweze kumnusuru baba yake ili kile ambacho alikuwa amekifanya kule kwenye ulimwengu wa giza, kitendo cha kumuua baba yake kisiweze kufanikiwa. Hakujua angeishi vipi baada ya hapo, hakujua ni hali gani ambayo angekuwa nayo mara baada ya kusikika kwamba baba yake, mzee Kessi alikuwa amefariki.

    Masaa yalizidi kwenda mbele mpaka kulipopambazuka, bado Yusufu alikuwa macho na wala hakuwa na nguvu za kutoka kitandani ambako alikuwa amelala tu. Kwa upande wake mmoja wa moyo wake ulionekana kujuta kwa kile ambacho alikuwa amekifanya lakini upande mwingine ulikuwa ukimpongeza kutoka na kitendo kile ambacho kingeufanya utajiri wake, umaarufu na hata mvuto kubaki navyo vile vile.

    Saa 1:07 asubuhi, simu yake ikaanza kuita. Alichokifanya ni kuichukua na kisha kuangalia kioo cha simu ile. Jina lala ‘Dear Mom’ lilikuwa likionekana katika kioo cha simu ile. Hata kabla ya kupokea simu ile Yusufu akajua ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea. Kinyonge akabonyeza kitufe cha kijani na kisha kuipeleka simu sikioni.

    “Baba yako amefariki” Ilisikika sauti ya mama yake simuni hata kabla ya salamu.

    Japokuwa alikuwa akijua kwamba kitu kile kingetokea lakini kwa wakati huo baada ya kupewa taarifa ile moyo wake ukamlipuka, mapigo ya moyo yakaanza kudunda kwa kasi kupita kawaida, mzunguko wa damu yake ulikuwa ukizunguka kwa kasi sana. Yusufu hakuongea kitu, machozi yalikuwa yakitiririka katika mashavu yake, moyo wake ulijisikia uchungu kupita kawaida.

    “Ninakuja huko huko” Yusufu alisema na kisha kukata simu.

    Akabaki akiwa amepigwa na butwa kitandani pale, moyo wake ulikuwa ukifikiria zaidi kuhusiana na baba yake, kosa alilolifanya mke wake ambaye alimpa talaka, Samiah likaonekana kuwa kubwa kwake na ndilo ambalo ilikuwa limesababisha yale yote kutokea. Alichokifanya Yusufu ni kumpigia simu Kelvin na kumtaarifu kile ambacho kilikuwa kimetokea kwamba baba yake alikuwa amefariki.

    Ndani ya dakika ishirini, Kelvin akafika mahali hapo huku akitangulizana na marafiki wengine na kisha kuanza safari ya kuelekea Bagamoyo huku wakiwa pamoja na Yusufu. Kila mmoja ndani ya gari alikuwa akimfariji, hawakujua kwamba huyo huyo Yusufu ndiye ambaye alikuwa amemuua baba yake kwa mikono yake mwenyewe.

    Walichukua dakika arobaini na tano mpaka kufika Bagamoyo ambapo wakaanza kuelekea katika sehemu ilipokuwa na nyumba hiyo. Tayari watu walikwishaanza kufika mahali hapo, vilio vilikuwa vikisikika katika eneo la nyumba hiyo. Yusufu akashindwa kujizuia, akaanza kulia tena jambo ambalo liiwafanya hata marafiki zake kulengwa na machozi.

    Yusufu akaanza kuelekea ndani ya nyumba yao ambapo akakutana na mama yake, Bi Fatuma na kisha kumkumbatia. Wote walikuwa wakilia, walionekana kuumia kupita kawaida. Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo watu walivyozidi kujaa ndani ya eneo la nyumba hiyo. Waandishi wa habari hawakuwa mbali, nao wakafika mahali hapo na kisha kuanza kupiga picha kila kilichokuwa kikiendelea.

    Taarifa zikatangazwa kwenye vituo vya redio pamoja na televisheni. Kila mtu ambaye aliisikia taarifa ile alishtuka. Hawakuamini kama Yusufu yule yule ambaye alikuwa amepata sana umaarufu ndiye ambaye alikuwa akipitia katika mambo magumu namna ile. Wananchi wakaanza kuamini ushirikina kwa kuona kwamba kulikuwa na mtu ambaye alikuwa amesababisha hayo yote.

    “Mmmh! Miezi mitano iliyopita alitalikiana na mke wake, leo hii baba yake amefariki. Nina wasiwasi kuna mkono wa mtu hapa. Kuna mtu ambaye hapendi kumuona akipata mafanikio haya” Mwananchi mmoja alisikika akimwambia mwenzake.

    “Yaani na mimi nilitaka niseme hivyo hivyo. Yaani sjui kwa nini Watanzania tuna roho za kwa nini, yaani hatutaki kuwaona watu wakifanikiwa maishani mwao” Jamaa mwingine alimwambia mwenzake.

    Mapenzi kwa Yusufu yalikuwa makubwa sana, hakukuwa na mtu yeyote ambaye alifahamu kwamba Yusufu huyo huyo ndiye ambaye alikuwa katika kila kilichoendelea mahali pale. Machoni mwa watu alionekana kuwa mtu asiye na hatia yoyote ile. Uso wa majonzi ambao alikuwa akiuonyesha siku hiyo ndio ndio ambao uliwaonyeshea watu kwamba alikuwa hausiki kabisa na kile ambacho kilikuwa kimetokea.

    Vitu vingine viliendelea kama kawaida mhali hapo mpaka pale ambapo Shekhe Oswald alipofika msibani hapo na kisha kuongea maneno machache na mwili kupelekwa msikitini kuswaliwa na kisha kuruudishwa nyumbani ambapo harakati zote za mazishi zikaanza kufanyika mahali hapo.

    Ilipofika saa 10:15 watu zaidi ya mia saba ambao walikuwa wamekusanyika mahali hapo wakaanza kuupeleka mwili wa mzee Kessi makaburini kwa ajili ya kuzikwa. Wakinamama walibaki majumbani wakilia, Bi Fatuma hakuamini kama mume wake ambaye alikuwa akimpenda kwa wakati huo alikuwa amefariki dunia na mwili wake ulikuwa njiani ukipelekwa makaburini.







    Watanzania walikuwa wakimuonea huruma Yusufu kwa msiba mkubwa wa kumpoteza baba yake ambao ulikuwa umemkumta. Muda mwingi Yusufu alionekana kuwa mnyonge kupita kawaida. Marafiki pamoja na mashabiki mbalimbali walikuwa wakimtumia salamu za pole kwa kile ambacho kilikuwa kimemkuta katika maisha yake.

    Kila mmoja alijua fika kwamba Yusufu alikuwa katika kipindi kigumu sana, kipindi ambacho alihitaji faraja kubwa sana kutoka kwa marafiki zake pamoja na mashabiki zake. Japokuwa katika kipindi hicho mazishi yalikuwa yamekwishafanyika lakini Yusufu hakutaka kurudi jijini Dar es Salaam, alihitaji muda mwingi wa kukaa na mama yake kwa ajili ya kufarijiana.

    Bado kila kitu kilibaki kuwa siri, hakukuwa na mtu ambaye alijua kwamba Yusufu huyo huyo ndiye ambaye alikuwa amemuua baba yake tena kwa mkono wake mwenyewe. Moyoni aliumia kupita kawaida lakini lawama zote hizo alikuwa akimpa mke wake, Samiah kwa kufanya kitu ambacho yeye alikiona kuwa cha kijinga, kuruhusu kufanya mapenzi katika siku za hatari za kupata ujauzito. Yusufu hakutaka kuwasiliana na mkewe tena kwani aliamini kwamba kama angeendelea kufanya hivyo, alikuwa akizidi kuumia na kumkasirikia zaidi na zaidi.

    “Mungu amemchukua baba yako” Bi Fatuma alimwambia Yusufu kwa sauti ya chini iliyojaa maumivu makali.

    “Kazi yake haina makosa. Kila mmoja yupo safarini kuelekea huko. Yatupasa kujiandaa kwani hatujua muda wala saa” Yusufu alimwambia mama yake, Bi Fatuma.

    Yusufu alikaa Bagamoyo kwa wiki moja na ndipo ambapo aliamua kurudi jijini Dar es Salaam. Watu walipojua kwamba siku hiyo ndio ilikuwa siku ambayo alikuwa akirudi kutoka Bagamoyo, zaidi ya watu elfu tatu walikuwa wamekusanyika Mwenge jijini Dar es Salaam kumfanyia mapokezi ambayo kwake yangeonekana kuwa ya mshtuko mkubwa.

    “Unasemaje?” Yusufu alimuuliza rafiki yake, Abdul ambaye alikuwa amempigia simu.

    “Ndio hivyo. Watu wamekusanyika hapa Mwenge, wote wanataka kukupokea” Abdul alimwambia Yusufu ambaye bado alikuwa kwenye mshtuko mkubwa.

    “Sasa nifanye nini hapa manake natumia usafiri binafsi?” Yusufu aliuliza.

    “Naomba usiwaangushe. Unajua wanakukubali sana na ndio maana wameamua kufanya hivi. Naomba usiwaangushe” Abdul alimwambia Yusufu.

    Mapenzi ya watu kwa Yusufu yalikuwa makubwa sana kiasi ambacho mpaka yeye mwenyewe alikuwa amechanganyikiwa. Hakuamini kama angeweza kufikia hatua ya kupendwa namna ile kwamba hata kama alikuwa akitoka Bagamoyo watu wangekuwa wamekusanyika wakimsubiria, kwa wakati huo alijiona kuwa mtu mwenye umaarufu mkubwa hata zaidi ya rais wa nchi.

    “Nani huyo?” Kelvin alimuuliza Yusufu huku akiendesha gari.

    “Abdul”

    “Anasemaje?”

    “Mashabiki wangu wamekusanyika Mwenge kwa ajili ya kunipokea”

    “Unasemaje?”

    “Ndio hivyo. Kwa hiyo hapa tunachotakiwa kukifanya tukifika Mwenge ni kuonana na mashabiki hao” Yusufu alimwambia Kelvin.

    “Alisema wapo sehemu gani pale Mwenge?”

    “Hilo sikumuuliza. Ila nafikiri tukifika pale, tutawaona kwani wapo zaidi ya elfu tatu” Yusufu alimwambia Kelvin.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Bado safari ilikuwa ikiendelea kama kawaida, baada ya dakika arobaini, wakaanza kuingia Mwenge. Kwa mbali idadi kubwa ya watu ilikuwa ikionekana huku wakiwa wameshika mabango mengi ambayo yalikuwa yakimtakia pole Yusufu. Yusufu akashindwa kuvumilia, akajikuta akianza kutokwa na machozi, kila kilichokuwa kikionekana kwake kilionekana kuwa kama ndoto fulani ambapo baada ya muda fulani angeamka kutoka katika usingizi mzito.

    Watu walipoliona gari la Yusufu, wakaanza kupiga kelele, waandishi wa habari ambao walikuwa wamekusanyika mahali hapo wakachukua kamera zao na kisha kuanza kupiga picha. Watu walionekana kuchanganyikiwa kupita kawaida, kurudi kwa Yusufu kulionekana kuwapagawisha watu ambao walikuwa mahali hapo.

    Askari wa barabarani wakapata wakati mgumu sana katika kuyaongoza magari yaliyokuwa barabarani, watu ambao walikuwa mahali hapo walikuwa wamefunga barabara zote. Gari la Yusufu lilipokaribia, Yusufu akafungua juu na kisha kutoka nusu mwili na kuanza kuwapungia watu mkono. Watu wakaonekana kuchanganyikiwa zaidi, kwa wale ambao walikuwa na simu zenye kamera wakaanza kumpiga picha, kwao, Yusufu alionekana kuwa mpya.

    Kwa wakati huo Yusufu akaonekana kuwa kama rais, umaarufu wake nchini Tanzania ukaonekana kuwa kama wa Michael Jackson katika kipindi kile ambacho alikuwa akivuma sana miaka ya tisini. Kelvin akalisimamisha gari, Yusufu hakuonekana kuridhika, alichokifanya ni kutoka kabisa garini. Watu wakaanza kumfuata, kila mtu alikuwa akitaka kumshika Yusufu.

    Hata kwa watu ambao walikuwa kwenye daladala nao wakashindwa kuvumilia. Mtu ambaye mara kwa mara alikuwa akiopnekana kwenye televisheni pamoja na kusikika redioni leo hii alikuwa akionekana Mwenge, nao wakajikuta wakishuka na kuanza kumfuata Yusufu. Kila mtu alipokuwa akimshika, alionekana kuridhika kabisa. Mvuto ambao alikuwa nao Yusufu ukaonekana kuwa mkubwa mara kumi ya ule ambao alikuwa nao kabla ya baba yake, mzee kessi kufariki, damu ya baba yake ambayo alikuwa ameimwaga ikaonekana kumzidishia kila alichokuwa nacho.

    “Mimi ni kama mungu wa Tanzania” Yusufu alisema kwa sauti ya chini ambayo hakukuwa na mtu aliyeisikia.

    Yusufu alijiona kuwa juu, juu zaidi ya Mungu. Kupendwa na watu wengi kiasi kile kulionekana kumpa kiburi kikubwa sana, hakuona kama Mungu alipendwa kama alivyokuwa akipendwa yeye. Kiburi chake kikamfanya kujiona kuwa juu, hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akifahamu kwamba miongoni mwa watu waliokuwa wamekusanyika mahali hapo, hata majini yalikuwepo huku wakiwa na kazi ya kuwafanya watu kumuona Yusufu kuvutia na hata kuwa na kiu ya kutaka kumsogelea.

    Uwepo wa Yusufu pale Mwenge ukawa umesimamisha kila kitu, kituo cha daladala cha Mwenge kilikuwa cheupe kabisa, kila mtu alikuwa amekwenda barabarani kwa ajili ya kumuona Yusufu, mtu ambaye alikuwa na umaarufu mkubwa sana katika kipindi hicho. Watu walikuwa wakizidi kuongezeka kiasi ambacho kikawafanya wanajeshi ambao walikuwa karibu na eneo hilo kuanza kusogea kwa ajili ya kuwatuliza watu ambao walionekana kama wamechanganyikiwa kutokana na kumuona Yusufu kwa macho yao katika kipindi hicho.

    “Ingia ndani ya gari” Mwanajeshi mmoja alimwambia Yusufu.

    “Hiyo ngumu mkuu. Watu wanaonekana kuchanganyikiwa sana. Naomba mniruhusu kufanya kitu kimoja” Yusufu alimwambia mwanajeshi yule.

    “Kitu gani?”

    “Nahitaji kutembea kwa miguu mpaka Ubungo kwani naamini hivyo ndivyo watu wataridhika. Ila nitahitaji sana ulinzi wenu” Yusufu alimwambia mwanajeshi yule ambaye alionekana kumshangaa.

    “Haiwezekani kabisa. Ingia ndani ya gari na uondoke katika eneo hili” Mwanajeshi yule alimwambia Yusufu ambaye akatii na kuingia garini.

    Kazi ikabaki katika kuliondoa gari hilo. Watu hawakutaka kutoka barabarani na kuliruhusu gari lile kuondoka barabarani hapo, walikuwa wamesimama mbele huku wakiwa wamelizuia. Japokuwa wanajeshi walikuwa wakiwataka watu hao kuondoka na kuacha barabara nyeupe lakini watu hawakuonekana kuwaelewa, walichokuwa wakikitaka ni kumuona Yusufu akiteremka kutoka garini.

    “Imeshindikana. Watu wengi halafu sisi wachache. Tufanye nini sasa?” Mwanajeshi mmoja alimuuliza mwenzake.

    “Bado sijajua kifanyike nini. Ila nilikuona ukiongea nae mwanzo. Ulikuwa ukiongea nae nini?” Mwanajeshi mmoja alimuuliza yule mwanajeshi ambaye alikuwa ameongea na Yusufu kipindi kichache kilichopita.

    “Alisema kwamba anataka atembee kwa mguu kutoka hapa mpaka Ubungo” Mwanajeshi yule alijibu.

    “Ili iweje?”

    “Kuwaridhisha watu. Ila kama asipofanya hivyo, watu hawa kuondoka mahali hapa itakuwa ngumu sana”

    “Sawa. Inabidi umruhusu. Haina jinsi”

    Mwanajeshi yule akaanza kulifuata gari la Yusufu. Watu waliokuwa mahali hapo bado walikuwa wakiimba huku wakimtaka Yusufu kuteremka kutoka garini vinginevyo wasingeondoka mahali hapo. Mara baada ya mwanajeshi yule kulifikia gari lile, Yusufu akashusha kioo.

    “Vipi?” Yusufu aliuliza.

    “Shuka. Fanya ulichotaka kufanya” Mwanajeshi yule alimwambia Yusufu.

    Yusufu akaufungua mlango na kutoka nje ya gari, watu wakalipuka kwa kelele, Yusufu akanyoosha mikono yake juu na kisha kuwataka watu wanyamaze kwani alikuwa na kitu ambacho alikuwa akitaka kukiongea mahali hapo. Watu wote wakabaki kimya.

    “Nahitaji kufanya kitu kimoja. Kwa sababu wengi mmekuwa mkitamani sana kuwa pamoja nami, naomba nifanye kitu kimoja kama kuwaridhisha na kisha mniache niende nyumbani kupumzika” Yusufu alisema huku akiwaangalia watu hao na kuendelea.

    “Nitataka kuelekea Ubungo kwa miguu pamoja nanyi. Nitaingia garini mara baada ya kufika Ubungo. Mko tayari” Yusufu alisema na kuuliza.

    “Ndiooooooooo” Watu waliitikia kwa sauti kubwa na kuanza kushangilia..

    “Ila naomba mfanye kitu kimoja. Sitopenda fujo zitokee. Kwa anayetaka kunigusa nitampa ruhusa hiyo wakati tunatembea, ila sitaki fujo” Yusufu alisema na watu wote kuanza kushangilia.

    Hapo hapo safari ya kuelekea Ubungo kwa miguu ikaanza. Kila mtu alikuwa akitaka kumgusa Yusufu kwa wakati huo. Watu ambao walikuwa njiani, walipoona kwamba mtu ambaye alikuwa pamoja na watu hao alikuwa Yusufu, nao wakaongezeka katika msafara huo.

    Polisi hawakuwepo katika msafara huo, watu waliojiona kwamba walikuwa na miili mikubwa ndio ambao wakajipa kitengo cha kuzuia fujo mahali hapo. Kila mmoja alionekana kuchanganyikiwa kwa furaha, mbele ya macho yao, Yusufu alionekana kama Malaika ambaye alikuwa ameshushwa duniani kwa kuwaletea Neema.

    Walitembea kutoka Mwenge mpaka Ubungo, kwa mtu ambaye alitaka kumgusa, siku hiyo alimgusa, kwa aliyetaka kumpiga picha, alimpiga picha. Muda wote huo, waandishi wa habari walikuwa bize wakimpiga picha Yusufu kwa ajili ya kuziweka katika magazeti yao siku inayofuata. Watu bado walikuwa wakiendelea na safari ya kwenda Ubungo huku nyimbo mbalimbali za Yusufu zikiimbwa.

    Idadi hiyo kubwa ya watu ikaonekana kuziba barabara yote, kwa yale magari ambayo yalikuwa nyuma ya watu hao, yalisimama huku mengine yakiendeshwa kwa mwendo wa taratibu sana. Mpaka wanafika Ubungo, tayari askari wa barabarani wa Mwenge walikuwa wamekwishawasiliana na askari wa Ubungo, hivyo magari yaliyokuwa yakitumia barabara ile ya Sam Nujoma yalikuwa yamekwisharuhusiwa.

    Mara baada ya kufika Ubungo. Yusufu akawaaga watu na kisha kuingia ndani ya gari na kuondoka mahali hapo. Hayo yakaonekana mapokezi makubwa kupita mapokezi mengine ya msanii yeyote yule, awe wa Tanzania au nje ya Tanzania, Yusufu alionekana kufunika. Baada ya watu kuliona gari la Yusufu likiondoka mahali hapo, wakanza kulipungia mikono na kumtakia safari njema huku wengine wakiwa wameshindwa kujizuia na kujikuta wakilia kutokana na furaha kubwa ya kumuona Yusufu mbele ya macho yao pamoja na kumgusa.

    ****CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unamfahamu yule msichana?” Hilo lilikuwa swali kutoka kwa Yusufu akimuuliza Abdul.

    “Msichana yupi?” Abdul aliuliza.

    “Yule aliyevaa raba nyeupe, kipedo cha blue pamoja na fulani nyeupe.

    “Yeah! Namfahamu”

    “Anaitwa nani?”

    “Christina Tobias. Anaishi Sinza” Abdul alimjibu Yusufu.

    “Naweza kuongea nae?”

    “Ngoja nikakuitie” Abdul alisema na kuanza kumfuata Christina

    Yusufu alikuwa akiangaliana sana na Christina katika kipindi hicho ambacho walikuwa katika sherehe ya kuzaliwa ya msanii Mapac Jnr ambayo ilikuwa ikifanyika Mbalamwezi Beach Resourt. Katika sherehe hiyo, Yusufu alikuwa miongoni mwa watu ambao walikuwa wameitwa kushiriki katika sherehe hiyo.

    Msanii Mapac Jnr alikuwa ametoa tiketi mia moja kwa watu wa nje ambao si ndugu, jamaa na marafiki kushiriki katika sherehe yake hiyo ya kuzaliwa. Watu hawakuwa wakionekana kujali, ila mara baada ya kutangaza kwamba hata Yusufu alikuwa kwenye sherehe hiyo, watu wakaanza kuzitafuta hizo tiketi ambazo ndani ya saa moja tu, tiketi zote zilikuwa zimekwisha na hivyo watu kutaka tiketi nyingine zaidi ziongezwe.

    Mapac hakutaka kuongeza tiketi nyingine, zile ambazo zilikuwa zimetolewa zilionekana kutosha sana. Kwa watu wengi ambao walikuwa wameingia ndani ya sherehe hiyo baada ya kununua tiketi, walikuwa wakimtafuta Yusufu na kisha kutaka kupiga nae picha. Kila mmoja alionekana kuvutiwa na Yusufu, wasichana wengi walikuwa wakimwangalia kwa macho ya mahaba lakini Yusufu hakuonekana kuwajali, mtu ambaye alikuwa akimjali kwa wakati huo alikuwa msichana, Christina ambaye alikuwa akitumia muda mwingi kuangaliana nae.

    Abdul akamfuata Christina na kuongea nae kwamba alikuwa akihitajika na Yusufu, kwanza Christina hakuonekana kuamini kama kweli Yusufu ndiye ambaye alikuwa akimuita kwa wakati huo. Akamwangalia vizuri Abdul na kisha kuyapeleka usoni mwa Yusufu ambaye alikuwa akimwangalia kwa tabasamu pana.

    Kwa mwendo wa mapozi, Christina akaanza kumfuata Yusufu ambaye alionekana kama simba mwenye njaa kali, alipomfikia, akasimama karibu nae. Hata kabla hawajaongea kitu chochote kile, Yusufu akaanza kumwangalia Christina kuanzia chini mpaka juu na kisha kutoa tabasamu pana. Mapigo ya moyo wa Christina kwa wakati huo yalikuwa yakidunda kupita kawaida, hakuamini kwamba mtu ambaye alikuwa amesimama mbele yake alikuwa Yusufu au The Ruler kama alivyojulikana.

    “Umependeza” Yusufu alimwambia Christina.

    “Asante. Nawe umependeza pia” Christina alimwambia Yusufu huku nae akionyesha tabasamu.

    “Ningependa sana usiku wa leo uwe wa kipekee sana kwangu. Ningependa sana kama tutatumia usiku wa leo pamoja” Yusufu alimwambia Christina ambaye alikuwa akijisikisikia aibu.

    “Kwa leo itakuwa ngumu” Christina alijibu huku akionekana kutomaanisha alichokuwa akikiongea.

    “Kwa nini?” Yusufu aliuliza.

    “Nawahi nyumbani”

    “Unaishi wapi?”

    “Naishi Sinza”

    “Sinza kubwa sana”

    “Vatican City” Christina alijibu.

    “Usijali. Nitakurudisha nyumbani. Ninachokitaka ni kuwa nawe usiku wa leo. Hata masaa mawili tu yanatosha” Yusufu alimwambia Christina ambaye alikuwa akiangalia chini huku akionekana kuwa mwingi wa aibu.

    Yusufu hakutaka kuchelewa, alichokifanya kwa wakati huo ni kumchukua Christina na kisha kuanza kuelekea nae nje. Kwa kiasi cha pombe ambacho kilikuwa kimemchukua kwa wakati huo, hakuonekana kujali macho ya watu ambayo yalikuwa yakimwangalia kwa mshangao, alichokijali kwa wakati huo ni kuondoka na Christina tu.

    Mara baada ya kufika nje, akalifuata gari lake na kisha kulifungua. Katika kipindi chote hicho, Christina hakuonekana kuamini kama kweli alikuwa na Yusufu kwa wakati huo. Moyo wake ulikuwa na furaha kupita kawaida, kuwa pamoja na Yusufu kulimfurahisha kupita kawaida.

    “Usiogope” Yusufu alimwambia Christina.

    “Usijali” Christina alisema huku akiufungua mlango na kukaa kitini.

    Hata kabla Yusufu hajaliondoa gari mahali hapo, akamsogelea Christina na kisha kuanza kubadilishana nae mate. Kwa Yusufu, kila kitu kwa wakati huo kilionekana kuwa kama mteremko mkubwa, umaarufu mkubwa ambao alikuwa nao, fedha nyingi ambazo alikuwa nazo katika kipindi hicho zilikuwa zikifanya kila kitu kuwa rahisi kwa upande wake. Walifanya kile kitendo kwa dakika kadhaa huku wakichezeana katika baadhi ya maungo yao na kisha kuondoka mahali hapo.

    Safari hiyo ilikuwa ni kuelekea nyumbani kwake, Kijitonyama ambapo mara baada ya kufika, wakateremka na kisha kuanza kuelekea ndani. Kila alipokuwa akimwangalia Christina, Yusufu alizidi kuvutiwa nae zaidi na zaidi, umbo lake la kimiss, weupe ambao alikuwa nao ulionekana kumdatisha kupita kawaida. Mara baada ya kuufikia mlango wa kuingilia sebuleni, akaufungua huku mlinzi akibaki kumwangalia Christina kwa macho ya mshangao, uzuri wake ulimdatisha hata yeye mwenyewe.

    “Hapa magumashi. Twende chumbani” Yusufu alimwambia Christina na bila ubishi wowote ule, Christina akakubaliana nae.

    Alichokifanya Yusufu ni kumbeba Christina na kisha kuelekea nae chumbani kwake huku akiendelea kubadilishana nae mate. Walipofika chumbani, akamtupa kitandani na kisha kuanza kumvua nguo zote. Kwa kila kitu ambacho kilikuwa kikiendelea mahali hapo, bado Christina hakuwa akiamini kama siku hiyo alikuwa akitaka kufanya mapenzi na Yusufu, mwanaume ambaye alikuwa akipenda sana kusikiliza nyimbo zake pamoja na kutamani hata siku moja kumgusa.

    “Mbona unahema sana?” Yusufu alimuuliza Christina.

    “Siamini” Christina alisema kimahaba.

    “Hauamini nini?”

    “Kuwa na wewe kitanda kimoja. Siamini The Ruler” Christina alimwambia Yusufu huku dhahiri akionekana kutokuamini.

    “Amini kwamba leo upo pamoja nami Christina, amini kwamba leo unakwenda kuuona mwili wangu wote nikiwa mtupu, amini kwamba leo tunafanya mapenzi pamoja” Yusufu alimwambia Christina na kisha kuanza kufanya ngono, tena mbaya zaidi bila kutumia mpira, hakukuwa na aliyejali kwamba wangeweza kuambukiza magonjwa au Christina kupata ujauzito, walichojali kwa wakati huo ni kupeana mapenzi moto moto kitandani.





    Mapenzi yakawa yamewateka wote wawili, tangu siku ya kwanza walipofanya mapenzi wakajikuta wakianza kupendana zaidi na zaidi. Yusufu akazidi kuwa karibu na Christina jambo ambalo lilimfanya kuwa na furaha kupita kawaida. Mara kwa mara walikuwa pamoja, walikuwa wakitoka mitoko ya usiku pamoja huku katika kila safari ambayo Yusufu au The Ruler alipokuwa akienda kwa ajili ya matamasha mbalimbali, Christina alikuwa pamoja nae.

    Wasichana wengine walimuonea wivu Christina, kitendo cha kuwa katika mahusiano ya kimapenzi pamoja na Yusufu kilionekana kuwa kitu cha bahati sana ambacho msichana yeyote yule angefurahi kuwa nacho. Magazeti hayakuchoka kuandika kuhusiana na mahusiano hayo ambayo yalionekana kuwa machanga lakini yenye kasi kubwa, watu hawakuacha kujiuliza kuhusiana na maisha ya Yusufu ambaye alionekana kusahau kabisa kama alikuwa na mtoto ambaye alihitajika kumlea katika kipindi chote.

    Mapenzi ya Christina kwa wakati huo yakaonekana kumchanganya kupita kawaida, kila siku alikuwa akiongea nae simuni lakini hakuwa akichoka, alimthamini sana Christina, alimuona kuwa mwanamke bora hata zaidi ya alivyokuwa Samiah ambaye alikuwa mke wake wa ndoa aliyempa talaka na kumrudisha nyumbani kwao.

    Katika kipindi hiki, maisha ya Yusufu yaliendelea kupata mafanikio makubwa zaidi, watu waliendelea kujiuliza juu ya mafanikio hayo lakini hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akifikiria kuhusiana na maisha ya upande wa pili ambayo alikuwa akiishi kwa wakati huo.

    “Nataka unioe” Christina alimwambia Yusufu.

    “Usijali. Cha msingi kwanza tuendelee kuchunguzana” Yusufu alimwambia Christina ambaye alionekana kushtuka.

    “Tuendelee kuchunguzana tena mpenzi. Kwani hii miezi sita tuliyokuwa pamoja haijatosha kuchunguzana?” Christina alimuuliza huku akionekana dhahiri kushtuka.

    “Mbona muda mchache sana huo mpenzi. Tuendelee tu kuchunguzana” Yusufu alimwambia Christina huku akimbusu busu katika maeneo mengi mwilini mwake.

    “Au bado unampenda mtalaka wako?” Christina aliuliza.

    “Naomba usinikumbushe kuhusu huyo mpumbavu, utanifanya kesho nisafiri niende nikamuue” Yusufu alisema huku akionekana kuanza kukasirika.

    “Pole mpenzi. Sikudhani kama ungeweza kukasirika namna hiyo” Christina alimwambia Yusufu.

    “Usijali”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Maisha hayakuishia hapo, starehe ndio yalikuwa aina ya maisha ambayo walikuwa wakiishi katika kipindi hicho. Wasichana wengi walikuwa wakitamani sana kuwa pamoja na Yusufu lakini wala hakuonekana kuwa radhi kuwa na msichana mwingine, kwake, Christina alionekana kuwa msichana wa ndoto katika maisha yake.

    Mara kwa mara Yusufu alikuwa akisafiri na kuelekea katika nchi mbalimbali kwa ajili ya kufanya shoo mbalimbali. Katika soko zima la Afrika Mashariki, Yusufu alikuwa ameliteka. Tanzania, Kenya, Uganda na nchi nyingine za Afrika Mashariki walikuwa wakipenda sana kumuita Yusufu kwa ajili ya kufanya shoo ambazo zilikuwa zikiendelea kuwaingizia fedha nyingi kupita kawaida. Yusufu akafanikiwa na kuwa mwanamuzi tajiri kuliko wote Afrika mashariki, akanunua magari ya kifahari pamoja na kujenga nyumba tano za kifahari jijini Dar es Salaam.

    Yusufu hakuishia hapo, akaanzisha studio yake ambayo aliipa jina la Nasri Record, huku akiwa amechukua jina la mtoto wake aliyezaa pamoja na mtalaka wake, Samiah. Pamoja na kuanzisha studio hiyo, pia Yusufu akaongeza biashara nyingine nyingi kama maduka mengine ya nguo, maduka ya vipodozi, akafungua sehemu ya kuuzia magari pamoja na biashara nyingine nyingi. Maisha ya kimasikini ya kuishi ndani ya chumba kimoja pamoja na rafiki yake, Kelvin yalionekana kusahaulika katika maisha yake, kwa wakati huo yalikuwa ni maisha ya kula starehe tu.

    “Kuna siku watu hawa wataniabudu tu” Yusufu alimwambia Kelvin mara baada ya kuona watu wamefurika katika uwanja wa taifa kwa ajili ya kuangalia tamasha lake ambalo lilikuwa limetangazwa sana Afrika mashariki, tamasha ambalo lilikuwa ni la kusaidia watoto waliokuwa katika maisha ya kimasikini, hasa ya mitaani.

    “Hiyo inawezekana. Umetokea kupendwa mpaka mimi mwenyewe unanishtua” Kelvin alimwambia Yusufu au The Ruler kama ambavyo alikuwa akijulikana kisanii.

    “Baada ya miaka miwili, nitaanzisha msikiti wangu mwenyewe. Msikitini huo utakuwa maalumu kwa ajili ya watu kuniabudu tu. Nadhani nitapata watu wengi sana” Yusufu alisema huku akionekana kutania.

    “Utawafanya hata mashehe kuja kukuabudu ukianzisha huo msikiti. Jiandae kwani muda wowote utapanda jukwaani” Kelvin alimwambia Yusufu.

    Siku hiyo ilionekana kuwa siku ya kitofauti na ya kuweka historia katika nchi ya Tanzania. Uwanja wa taifa ambao ulikuwa ukifanyikia tamasha hilo kubwa la kusaidia watoto waliokuwa wakiishi katika mazingira magumu ya mitaani ulikuwa umejaa kupita kawaida. Watu zaidi ya elfu sitini walikuwa wamekusanyika ndani ya uwanja huo huku kiingilio cha chini kikiwa ni shilingi elfu kumi na tano.

    Watu walionekana kuchanganyikiwa kwa kumuona Yusufu, kila mtu akaonekana kuwa na ndoto moyoni mwake, ndoto ya kumuona Yusufu akisimama jukwaani na kuanza kuimba. Baada ya wasanii wengine wengine kumaliza kuimba, ikawa zamu ya Yusufu. Uwanja mzima ukaanza kulipuka kwa furaha, vitambaa vikaanza kurushwa hewani katika kipindi ambacho Yusufu alikuwa akipanda jukwaani hapo. Watu wengine wakaonekana kushindwa kuvumilia, wakaanza kutokwa na machozi.

    Yusufu hakuonekana kuwa mtu wa kawaida, upendo ambao alikuwa akipendwa na mashabiki zake uliwafanya watu kuchanganyikiwa kabisa. Katika kipindi hicho, Yusufu alionekana kama msanii Michael Jackson ambaye kila alipokuwa akipanda jukwaani watu walikuwa wakilia na hata wengine kuzimia. Alipopanda jukwaani, Yusufu akaanza kunyoosha mkono juu kama ishara ya kuwasalimia.

    “Piga keleleeeeeeeeeee” Yusufu alisema kwa sauti kubwa kwenye kipaza sauti.

    Uwanja mzima ukapiga kelele kubwa kupita kawaida. Uwepo wa Yusufu au The Ruler katika jukwaa lile uliwafanya watu kuchanganyikiwa kupita kawaida. Wapiga picha hawakuwa mbali, walikuwa wakiendelea kupiga picha kwa kila kitu ambacho kilikuwa kikiendelea jukwaani. Damu ya baba yake ilionekana kumuongezea zaidi mafanikio katika maisha yake, katika kipindi hicho, The Ruler ndiye alikuwa msanii ambaye alikuwa akivuma kupita kawaida.

    Tamasha hilo likaonekana kuwa tamasha la tofauti kuliko matamasha mengine ambayo yaliwahi kufanyika nchini Tanzania. Yusufu alijitoa kwa kuimba kwa nguvu zote kuliko siku nyingine katika matamasha mengine. Watu wakaburudika kupita kawaida, siku hiyo ikaonekana kuwa siku maalumu kwa ajili ya Yusufu ambaye alikuwa akipendwa kuliko hata raisi katika kipindi hicho. Mpaka tamasha linakwisha, watu walikuwa wameburudika vya kutosha.

    “Siku ya leo imebakia kuwa historia katika maisha yangu” Jamaa mmoja alimwambia mwenzake.

    “Hata mimi aisee. Makamuzi aliyoyafanya The Ruler, sijawahi kuyaona kwa msanii yeyote hapa nchini. Halafu naweza kusema ni zaidi ya wasanii wote wa Marekani ambao waliwahi kuja nchini kwa matamasha mbalimbali. The Ruler ametisha ile mbaya” Jamaa mwingine alimwambia mwenzake.

    Siku hiyo ikabaki kuwa siku ya historia kwa watu wote ambao walikuwa wamehudhuria tamasha hilo. Kwa wale watu ambao walikuwa wametoka katika nchi nyingine ndani ya Afrika Mashariki hawakuoneka kujutia nauli zao pamoja gharama nyingine ambazo walikuwa wametumia mpaka kufika nchini Tanzania na kuingia katika uwanja huo kwa ajili ya kuangalia tamasha hilo. Siku hiyo, Yusufu akaonekana kuvunja rekodi, akaweka historia kwa tamasha ambalo alilifanya kuingiza watu wengi kupita kawaida, kwa wakati huo, wasanii wengine ambao walikuwa wametumbuiza katika tamasha hilo hawakuonekana kusikika kabisa midomoni mwa watu, kila mtu alikuwa akimzungumzia The Ruler tu.

    “Umetisha aisee” Papaa Pipo alimwambia Yusufu katika kipindi ambacho walikuwa katika hoteli ya Serena usiku.

    “Kuna wakati mwingine najiona kuwa mungu mtu. Nadhani huu ni wakati ambao watu wanatakiwa kuniabudu sasa” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.

    “Kwa hiyo inatubidi tuanzishe msikiti. Au wewe unaonaje?” Papaa Pipo alimuuliza Yusufu.

    “Poa. Ila unavyoona msikiti huo ujengwe wapi hapa jijini Dar es Salaam?”

    “Kama vipi tuujenge kule Tandale au Tandika, sehemu ambayo ina mkusanyiko mkubwa wa watu” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.

    “Hilo sawa. Kama vipi, ujenzi uanze hata mwaka kesho”

    “Poa poa”

    Siku hiyo ilikuwa ni ya kula na kunywa ndani ya hoteli hiyo. Wote wawili, maisha yao yalikuwa ni ya fedha tu, walikuwa wakimiliki kiasi kikubwa cha fedha mpaka wakati mwingine wakajiona kama watachanganyikiwa. Fedha kwao yalikuwa kama majani kwamba sehemu yoyote ile ungeweza kuyachuma. Maisha yao ya kuuza nafsi zao kwa shetani yakaonekana kuwaletea faida kubwa sana katika maisha yao. Japokuwa Yusufu alikuwa akijitahidi sana kuwa muaminifu kwa mpenzi wake, Christina lakini kuna kipindi kikatokea kuchoka, kujigonga kwa wasichana kulionekana kumpa mshawasha wa kutaka kutembea nao.

    Yusufu akaanza kuvunja amri ya sita na wasichana hao, uhusiano wake na Christina ukaonekana kuwa si kitu katika maisha yake. Alitembea na wasichana ambao alikuwa akitaka kutembea nao katika kipindi hicho, na hata Christina alipokuja kugundua mambo aliyokuwa akiyafanya Yusufu, tayari Yusufu alikuwa ametembea na wasichana wasiopungua ishirini, wote alikuwa akifanya nao mapenzi kama kawaida yake.

    “Kwa nini unautesa moyo wangu? Kwa nini umeamua kunitesa namna hii The Ruler?” Christina alimuuliza Yusufu huku akianza kulia.

    “Wanawake ni vyombo vya starehe tu. Nimetembea na wewe kwa sababu wewe ni miongoni mwa vyombo hivyo vya starehe. Kuna ubaya hapo?” Yusufu alisema kwa dharau na kuuliza.

    “Unanidharirisha Yusufu. Unanidharirisha kwa kuniita mimi ni chombo cha starehe. Leo hii umenichoka na kuamua kuzungumza maneno makali namna hiyo, yaani umesahau kila kitu ambacho tulikuwa tukifanya pamoja? Umesahau kila kitu ambacho tulikuwa tukichangia pamoja? Leo hii unaniita mimi chombo cha starehe!” Christina alisema huku akiendelea kulia.

    “Wewe ulitaka niseme nini sasa? Kwanza jiangalie Christina halafu niangalie na mimi. Una hadhi ya kutembea na mimi?” Yusufu alimuuliza Christina kwa kebehi.

    “Hata kama sina hadhi lakini si kuniambia maneno hayo. Haujui ni kwa jinsi gani ninaumia moyoni mwangu” Christina alimwambia Yusufu.

    “Maumivu yako hayanihusu. Nadhani maumivu yako yangenihusu katika kipindi ambacho tulikuwa pamoja, ila kwa sasa hivi, hayanihusu kabisa” Yusufu alimwambia christina huku akichukua mvinyo na kisha kupiga pafu moja.

    Maneno yale yalionekana kuwa kama msumali wa moto moyoni mwa Christina, alimwangalia Yusufu mara mbili mbili huku akionekana kutokuamini kile ambacho alikuwa akikisikia kutoka mdomoni mwake. Ni kweli maneno yale yalikuwa yamemuumiza sana kuliko kitu chochote kile, machozi ya uchungu ambayo yalikuwa yakimtoka, Yusufu hakuonekana kuyajali kabisa.

    “Leo ninalia Yusufu huku wewe ukifurahia. Ila kumbuka, kuna siku wewe utalia na mimi kufurahia” Christina alimwambia Yusufu.

    “Kama kulia, utalia milele na mimi kama kufurahia, nitafurahia milele na kuna siku utakuja kuniabudu. Upende usipende, utaniabudu tu kwani nimekwishakuwa mungu mtu katika maisha yako” Yusufu alimwambia Christina huku akiendelea kunywa mvinyo.

    “Sawa mungu mtu. Ninaondoka na ninakuahidi kwamba utanitafuta tu” Christina alimwambia Yusufu.

    “Nikutafute? Kwa lipi? Kipi nilichosahau kwako? Nimekwishakupiga alama nyingi sana mapajani kwako, nimeshaona kila kiungo cha mwilini mwako. Nakuhakikishia kuwa sijasahau kitu chochote kile kwako. Kwa hiyo hakuna umuhimu wa kukutafuta katika maisha yangu” Yusufu alimwambia Christina.

    “Sawa. Nimekubaliana na wewe. Ila ningependa kukushauri kitu kimoja tu” Christina alimwambia Yusufu ambaye alitulia akimsikiliza na kuendelea.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Labda unafikiri nilipenda fedha kwako au umaarufu, unaweza kuwa sahihi juu ya hilo. Ila ushauri wangu ambao ningependa kukupa, onana na daktari wako mapema ili aweze kukupa vidonge vya kuishi kwa matumaini. Mwenzako naishi kwa matumaini. Nakukaribisha mungu mtu katika ulimwengu huu wa kuishi kwa matumaini” Christina alimwambia Yusufu huku akianza kuondoka sebuleni hapo. Alipoufikia mlango, akaufungua na kisha kuondoka zake.

    Yusufu akabaki kimya, maneno ambayo aliyaongea Christina mahali hapo yakaonekana kumchanganya. Yusufu akabaki akiwa amesimama tu kama nguzo, ghafla, kijasho chembamba kikaanza kumtoka, akauhisi mwili wake ukianza kutetemeka, alijihisi kama kupigwa sindano ya ganzi. Hapo hapo akajikuta akikaa kochini na kisha kuinamisha kichwa chake chini. Kwa kasi kama mtu aliyekurupushwa kutoka katika lindi la mawazo, akasimama na kisha kutoka nje ya nyumba yake na kulifuata gari lake.

    “Fungua geti....fungua geti” Yusufu alimwambia mlinzi huku akiufungua mlango wa gari lake na huku akionekana kuwa mwenye haraka.

    Kwa haraka haraka mlinzi akalifungua geti. Yusufu akawasha gari na kuondoka mahali hapo kwa kwa kasi. Njiani, ndani ya gari, Yusufu alionekana kuwa na mawazo kupita kawaida, tayari maneno ambayo aliongea Christina yalionekana kumchanganya kupita kawaida. Foleni za barabarani zilionekana kumkasirisha kupita kawaida, kwa wakati huo alikuwa akitaka kufika katika hospitali binafsi ya Dr Lyimo iliyokuwa Mikocheni B.

    Magari yalikuwa yakitembea kwa taratibu sana, mvua ambayo ilikuwa imenyesha siku hiyo ilisababisha foleni kubwa barabarani hapo jambo ambalo lilimfanya Yusufu kushikwa na hasira. Magari yaliporuhusiwa, aliendesha kwa mwendo wa kasi mpaka alipofika Sayansi ambapo akakata kushoto na kuchukua barabara iliyokuwa ikielekea Mikocheni.

    Bado Yusufu alionekana kuchanganyikiwa kupita kawaida, maneno yale ambayo alikuwa ameambiwa na Christina yakamfanya kutaka kujua hali yake ilikuwa vipi. Tayari moyoni mwake alijiona kuanza kujuta kwa uamuzi ambao alikuwa ameuchukua wa kutembea na msichana yule, Christina ambaye alionekana kuwa mrembo kwa kumwangalia, kumbe alikuwa mwanamke hatari sana ambaye alikuwa na mipango kabambe ya kumuangamiza Yusufu.

    Yusufu alichukua dakika ishirini mpaka kufika katika eneo la hospitali hiyo, hospitali ambayo mara kwa mara alikuwa akitibiwa kila alipokuwa akiumwa. Huku akionekana kuchanganyikiwa, akateremka kutoka garini na kuanza kuelekea ndani ya jengo la hospitali hiyo. Siku hiyo hakuonekana kuwa katika hali nzuri, akajikuta akipita moja moja katika sehemu ya mapokezi na safari yake kuishia katika ofisi ya Dokta Lyimo ambaye alikuwa akijiandaa kuwafanyia kazi wagonjwa wengine ambao walikuwa wamekuja katika hospitali hiyo.

    “Nimekuja dokta” Yusufu alimwambia Dokta Lyimo hata kabla ya salamu.

    “Kuna nini tena Yusufu? Umeingia ghafla ghafla bila kugonga hodi. Kuna kitu gani?” Dokta Lyimo alimuuliza Yusufu.

    “Nimekuja unipime” Yusufu alimwambia Dokta Lyimo huku akionekana kuchanganyikiwa.

    “Nikupime. Nikupime nini tena? Hebu tulia kwanza Yusufu. Naona una haraka sana kiasi ambacho hatutoweza kuelewena” Dokta Lyimo alimwambia Yusufu.

    “Tafadhaliiiii. Naomba unipime” Yusufu alimwambia Dokta Lyimo huku akimshika koti.

    “Nikupime nini tena?”

    “Nipime damu yangu. Nataka unipime Dokta nijue afya yangu kama nimeathirika au la. Nipime dokta” Yusufu alimwambia Dokta Lyimo.

    Alichokifanya Dokta Lyimo ni kumwambia asubiri mahali hapo na kisha kuondoka kuelekea katika sehemu ya dawa na kuchukua sindano pamoja na vitu vingine ambavyo vilihitajika kwa mtu ambaye alikuwa akitaka kupimwa damu yake. Yusufu alibaki ndani ya ofisi ile huku akionekana kuchanganyikiwa, hakuonekana kuwa na amani hata kidogo, maneno ambayo aliyaongea Christina yalionekana kumchanganya kupita kawaida.

    Mara baada ya dakika kadhaa, Dokta Lyimo akarudi ofisini hapo huku akiwa na vifaa vyote. Alichokifanya ni kumfunga Yusufu mkanda fulani karibu na mwisho wa mkono kwa kutaka kuona mishipa ya damu na kisha kumchoma sindano kwenye moja ya mishipa ya damu ambayo ilikuwa ikionekana na kisha kuchukua damu.

    “Ngoja nikaiangalie” Dokta Lyimo alimwambia Yusufu na kisha kuondoka ndani ya ofisi hiyo.

    Yusufu alibaki kwenye kiti huku akitetemeka kwa woga, kijasho chembamba kikaanza kumtoka huku akionekana kukosa amani kabisa. Furaha yote ya utajiri, umaarufu ikawa imeondoka moyoni mwake, kwa kipindi hicho alikuwa akifikiria kuhusiana na majibu ambayo angekuja nayo Dokta Lyimo kutoka katika chumba cha uchunguzi.

    “Nikikutwa nao, nitaua mtu” Yusufu alijisemea huku akionekana kuwa na hasira.

    Kwa wakati huo akaanza kujuta, kwanza akaanza kujutia hatua ambayo alikuwa ameichukua ya kumuacha mke wake, alijua kwamba Samiah alikuwa amefanya kosa kubwa la kuruhusu ujauzito lakini hakukuwa na umuhimu wa kumpa talaka kwani tayari kosa lilikuwa limekwishafanyika na hivyo ulikuwa muda wa kuganga mambo yajayo.

    Yusufu alikaa katika chumba kile kwa dakika kadhaa na ndipo Dokta Lyimo kurudi katika ofisi ile. Mapigo ya moyo ya Yusufu yakaongezeka kasi katika udundaji, kijasho chembamba kilichokuwa kikimtoka kikaongezeka zaidi na zaidi. Kitendo cha kumuona daktari akiwa amerudi katika chumba kile huku akiwa na karatasi kadhaa mikononi mwake.

    “Vipi?”

    “Subiri kwanza Yusufu. Hautakiwi kuwa na haraka” Dokta Lyimo alimwambia Yusufu ambaye alionekana kuwa na kiu ya kutaka kujua majibu ya damu yake.

    “Niambie kwanza. Majibu yako vipi?” Yusufu aliuliza.

    “Kwanza tulia kitini” Dokta Lyimo alimwambia Yusufu.

    Akili ya Yusufu kwa wakati huo wala haikutulia, akakaa chini huku akiwa na presha kupita kawaida, kitu ambacho alikuwa akitaka kusikia kwa wakati huo ni majibu ya damu yake tu. Alimwangalia Dokta Lyimo mara kadhaa usoni, alikuwa akiona kama anamchelewesha tu, alichokifanya ni kumnyang’anya ile karatasi ambayo iliandikwa majibu ya damu yake.

    Yusufu akaanza kuiangalia karatasi ile kwa haraka haraka. Japokuwa hakuwa amesoma shule lakini alifahamu fika kwamba mtu ambaye alikuwa ameambukizwa virusi vya UKIMWI majibu yake yalisomeka POSITIVE. Akaangalia karatasi ile na maneno ambayo yaliandikwa, chini kabisa akakutana na neno ambalo alikuwa akitarajia kuliona muda huo, POSITIVE.

    Yusufu akajiona kama mtu aliyepigwa na shoti ya umeme, ghafla, akasimama na kisha kuondoka ndani ya chumba kile huku akiwa kama mtu aliyechanganyikiwa zaidi na huku mkononi akiwa na karatasi ile ya majibu. Kuambukizwa ugonjwa wa UKIMWI na mtu ambaye alikuwa akimpenda na kumuamini, Christina kulionekana kumuumiza kupita kawaida. Tayari machozi yakaanza kutiririka mashavuni mwake.

    Watu wote ambao walikutana nae katika hospitali ile walionekana kumshangaa, Yusufu hakuwa akieleweka kwa wakati huo, alionekana kama mtu aliyechanganyikiwa. Watu wakabaki midomo wazi, ni kweli kwamba walikuwa na hamu ya kumuona Yusufu au The Ruler kama alivyokuwa akijulikana lakini katika hali ambayo alikuwa akionekana kwa wakati huo, hakuonekana kama kuwa katika hali nzuri.

    “The Ruler” Msichana mmoja alimuita lakini Yusufu huku akionekana kutokuamini lakini Yusufu hakuweza kugeuka.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alipofika katika sehemu ambayo alikuwa ameegesha gari lake, akaufungua mlango na kuingia ndani. Hata kabla hajaliwasha, akaulalia usukuni wa gari lile na kisha kuanza kulia. Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno, moyoni alikuwa akijilaumu kutembea na Christina ambaye alionekana kuwa mwanzo wa matatizo yale ambayo alikuwa amekutana nayo kwa wakati huo. Huku akiendelea kulia ndani ya gari lake, Dokta Lyimo akatokea mahali hapo na kuanza kukigongagonga kioo cha gari lake huku akitaka kusikilizwa.

    Yusufu hakutaka kuongea kitu chochote, alijihisi kwamba kama angeongea kitu chochote kile na Dokta Lyimo ndivyo ambavyo angeshikwa na hasira zaidi na kuumia zaidi na zaidi moyoni mwake, alichokifanya ni kuwasha gari lake na kisha kuondoka mahali hapo. Njia nzima alikuwa akilia kama mtoto mdogo, kuugua ugonjwa wa UKIMWI katika umri ambao alikuwa nao kulionekana kumuumiza kupita kawaida.

    Safari yake kwa wakati huo ilikuwa ni kwenda nyumbani kwa Papaa Pipo ambaye alikuwa akiishi Kijitonyama. Alitumia muda wa dakika chache kutoka hapo Mikocheni B mpaka Kijitonyama ambapo baada ya kufika katika geti la nyumba ya Papaa pipo, akaanza kupiga honi na mlinzi kufungua geti na hivyo kuliingiza gari lake. Baada ya kulipaki, Yusufu akateremka na kisha kuanza kuufuata mlango wa kuingilia katika sebule ya nyumba hiyo.

    Kwa jinsi alivyokuwa amechanganyikiwa katika kipindi hicho, Yusufu hakuona kama kulikuwa na mlinzi ambaye alikuwa amemfungulia geti katika nyumba hiyo, alijiona kama kuwa peke yake. Alipoufikia mlango ule, akaufungua na kisha kuingia ndani. Papaa Pipo hakuwepo sebuleni pale kitu kilichomfanya Yusufu kuanza kuita, Papaa Pipo aliyeitikia chumbani kwake, akamwambia kwamba angekuja sebuleni pale

    Papaa Pipo alipofika sebuleni, akashangaa mara baada ya kumuona Yusufu akiwa katika hali aliyokuwa nayo. Hakuonekana kuwa na furaha kama siku nyingine ambazo alikuwa akifika nyumbani hapo, siku hiyo alionekana kuwa tofauti sana na siku nyingine. Macho yake, yalikuwa mekundu sana hali ambayo ilionyesha alikuwa akilia katika kipindi kichache kilichopita.

    “Kuna nini tena Yusufu?” Papaa pipo alimuuliza Yusufu.

    Yusufu hakujibu chochote kile, alichokifanya ni kumpa karatasi ile Papaa Pipo. Papaa Pipo akaanza kuiangalia karatasi ile na kila kitu kilichoandikwa, alipofika chini chini mwa karatasi ile, akaonekana kushtuka. Akayatoa macho yake katika karatasi ile na kisha kumwangalia Yusufu usoni.

    “Immpossible (Haiwezakani)” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.

    “Nimeathirika Papaa” Yusufu alimwambia Papaa Pipo kwa sauti ya chini yenye majonzi.

    “Mungu wangu! Nani amefanya hivi?”

    “Christina. Christina ameamua kuniua. Christina ameniua Papaa” Yusufu alisema huku akianza kulia tena.

    Papaa Pipo akabaki kimya, kwa jinsi Yusufu alivyokuwa akiongea mahali hapo kulionekana kumuumiza kupita kawaida. Akaanza kuiangalia tena karatasi ile huku akirudia zaidi na zaidi, alijiona kama kutokuona vizuri kile ambacho kilikuwa kimeandikwa katika karatasi ile.

    “Vipimo vimekosea. Umekwenda kwenye hospitali gani?” Papaa Pipo alimuuliza Yusufu.

    “Nimekwenda kwa daktari ambaye kila siku amekuwa dokta wangu wa kipindi kirefu, dokta ambaye amekuwa akinitibia kila siku. Hawezi kudanganya, vipimo vyake haviwezi kusema uongo. Ningefikiri kwamba vinasema uongo endapo ningekwenda kupima bila kuambiwa kwamba nimeathirika” Yusufu alimwambia Papaa pipo.

    “Kumbe uliambiwa! Nani alikwambia?”

    “Christina mwenyewe”

    “Huyu mwanamke ni wa kumuua kabisa. Yaani kakuambukiza ugonjwa huu halafu amekupa taarifa kwamba amekuambukiza ugonjwa huu! Huyu ni wa kumuua kabisa” Papaa Pipo alisema huku akionekana kuwa na hasira.

    “Hapana. Kosa si lake” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.

    “Kosa si lake. Sasa unafikiri kosa ni la nani?” Papaa Pipo aliuliza.

    “Kosa ni la wakubwa wetu wa ibadani. Wamenisaliti” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.

    “Wamekusaliti? Kivipi?”

    “Haukumbuki kile ambacho waliniambia?

    “Kipi?”

    “Kwamba wangeilinda afya yangu”

    “Nakumbuka”

    “Sasa kwa nini wameruhusu hili kutokea? Kwa nini wameruhusu mimi kuupata ugonjwa huu wa UKIMWI?” Yusufu aliuliza maswali mfululizo.

    “Bado sijajua”

    “Haiwezekani. Ni lazima niende kule kuuliza. Wamenisalitiiii” Yusufu alisema huku akionekana kuwa na hasira”

    ****

    Usiku wa siku hiyo, Yusufu hakutaka kulala, usiku kucha alikuwa akifikiria jinsi ambavyo majibu ya afya yake yalivyokuwa. Bado karatasi ya majibu alikuwa nayo mkononi, mara kwa mara alikuwa akiiangalia huku akiamini kwamba kuna wakati majibu yale yangeweza kubadilika na kusomeka NEGATIVE. Yusufu alikesha usiku mzima huku akiwa na ile karatasi ya majibu yale lakini hakikubadilika kitu.

    Ilipofika saa saba usiku, kioo kile ambacho kilikuwa kikitumika kama mlango wake wa kuingilia katika ulimwengu wa pili kikaanza kuonekana mianga kadhaa ya radi pamoja na miungurumo ambayo alikuwa akiisikia yeye tu. Hapo hapo Yusufu akasimama na kisha kuanza kukisogelea kioo kile na kisha kuingia ndani ya kioo kile na kutokezea katika ulimwengu wa pili, ulimwengu ambao aliamua kuiuza roho yake ili apate mafanikio makubwa katika maisha yake.

    Mwendo wake siku hiyo ulikuwa ni wa haraka haraka, kichwa chake kilionekana kuwa na maswali mengi ambayo alitaka kuuliza katika usiku huo. Alitembea kwa muda fulani na kisha kuifiki nyumba ile na kuingia ndani. Ndani ya nyumba ile siku hiyo ilionekana kuwa tofauti na siku nyingine, hakukuwa na mtu hata mmoja zaidi ya meza ile ambayo ilikuwa katika sehemu ambayo ilionekana kuwa kama ukumbi.

    Yusufu akainamisha kichwa chini kama kutoa heshima ya kuingia ndani ya nyumba ile na kisha kuanza kuelekea katika moja ya viti ambavyo vilikuwa vimezunguka meza ile na kutulia. Wala hazikupita sekunde nyingi, mwanaume mmoja ambaye hakuwahi kumuona hata siku moja akafika mahali hapo na kuanza kumwangalia Yusufu huku akitabsamu.

    Japokuwa mwanaume huyo alionekana kuwa kama binadamu wa kawaida lakini kwa mbali alikuwa na mabadiliko kiasi. Macho yake yalikuwa makubwa zaidi ya saizi ya macho ya mwanadamu wa kawaida, kichwani hakuwa na nywele, alikuwa na upara huku mdomo wake ukiwa mkubwa mara mbili ya mdomo wa kawaida.

    “Nimekuja kuuliza kitu”Yusufu alimwambia mwanaume yule ambaye alikuwa amesimama wima akimwangalia Yusufu.

    “Kitu gani?” Mwanaume yule aliuliza kwa sauti ya chini lakini iliyojaa utisho mkubwa ambayo kwa kiasi fulani ilimfanya hata Yusufu kusisimka.

    “Kwa nini mmenisaliti?” Yusufu aliuliza huku akimwangalia mwanaume yule usoni.

    “Hatujakusaliti. Bado tunaendelea kukulinda” Mwanaume yule alimwambia Yusufu.

    “Hamjanisaliti! Hamjanisaliti na wakati nimekwishaambukizwa ugonjwa wa UKIMWI! Ulinzi wenu upo wapi sasa juu ya afya yangu? Kama hamjanisaliti, ninapaswa kutumia neno gani hapo?” Yusufu aliuliza. Maswali mfululizo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Tunaendelea kukulinda. Kamwe hautodhoofika. Utakuwa hivyo hivyo na wala hakuna mtu ambaye atajua kama umeathirika kwa kukuangalia. Utaishi maisha yako yote na hakuna atakayegudua kitu chochote kile juu ya afya yako” Mwanaume yule alimwambia Yusufu.

    “Ina maana sitokonda? Ina maana sitoanza kuharisha? Ina maana sitoopatwa na vidonda?” Yusufu aliuliza.

    “Hakuna kitakachokupata. Cha msingi ni kutovunja masharti yetu tu. Ukivunja basi hatuna budi kuuruhusu ugonjwa huu kufanya kazi katika mwili wako” Mwanaume yule alimwambia Yusufu.

    “Nashukuru sana. Naahidi sitoweza kuvunja masharti” Yusufu alimwambia mwanaume yule na kisha kuinuka kitini na kutaka kuondoka.

    “Subiri kwanza” Mwanaume yule alimwambia Yusufu na kisha kuanza kumsogelea.

    “Tunawahitaji watu wengi iwezekanavyo. Utakachotakiwa kukifanya ni kufanya mapenzi na wanawake wengi iwezekanavyo. Kwa kila mwanamke ambaye utafanya nae mapenzi, hatochukua mwezi mmoja, ataanza kuziona dalili za ugonjwa huu katika mwili wake. Fanya mapenzi na wanawake wengi uwezavyo. Tutakachokifanya, tutakupa nguvu ya mvuto wa kimapenzi, hakuna mwanamke ambaye atakukataa. Hakikisha unafanya mapenzi na wanawake wengi uwezavyo” Mwanaume yule alimwambia Yusufu.

    “Ila kwa nini umenihusia sana kufanya hivyo?” Yusufu aliuliza.

    “Tunahitaji sadaka yako zaidi. Mvuto tuliokupa ni mkubwa sana kiasi ambacho hatujawahi kumpa mtu yeyote yule na ndio maana uliupokea ndani ya usiku mmoja tu. Kama malipo ya kila kitu, fanya nilichokwambia” Mwanaume yule alimwambia Yusufu.

    “Nitafanya hivyo”

    “Sawa sawa. Ila kumbuka kutovunja masharti yetu. Endapo utavunja, tutakupokonya pete zetu zinazokuingizia kila kitu” Mwanaume yule alimwambia Yusufu.

    “Nitafanya kila kitu bila kuvunja masharti”

    “Sawa. Unaweza kwenda” Mwanaume yule alimwambia Yusufu ambaye akaondoka mahali hapo.



    Maisha ya Yusufu yakaanza kubadilika, hapo ndipo alipoanza rasmi kutembea na wasichana mbalimbali. Kitu ambacho aliamua kukifanya kwa wakati huo ni kuchukua daftari lake dogo kwa ajili ya kuandika jina la kila msichana ambaye alikuwa akitembea nae na kumuambukiza ugonjwa wa UKIMWI ambao ulikuwa ukizidi kushika kasi nchini Tanzania.

    Kwa sababu alikuwa na fedha nyingi na kwa sababu alikuwa mtu maarufu ambaye alijulikana sana Afrika Mashariki, tena zaidi ya mwanaumuziki yeyote yule, Yusufu akawapata wasichana wengi ambao walikuwa wakipenda kutembea na watu wenye fedha na maarufu. Kadri alivyokuwa akitembea na wasichana hao na ndivyo ambavyo umaarufu wake pamoja na mvuto ulivyozidi kuongezeka zaidi na zaidi.

    Kila kitu ambacho kilikuwa kimepangwa katika ulimwengu wa giza ndicho ambacho kilikuwa kikitokea, kwa kila msichana ambaye alikuwa akitembea nae katika muda huo na kumwambukiza ugonjwa wa UKIMWI, ndani ya mwezi mmoja, msichana huyo alikuwa akibadilika na kuonyesha dalili zote za kuathirika na kuanzia hapo wala hakuchukua muda mrefu, anakufa kwa maumivu makali kitandani.

    Yusufu hakuonekana kuhuzunika kwa kile ambacho alikuwa akikifanya, kazi yake ilikuwa ni kukamilisha kile ambacho alikuwa ameambiwa kukifanya katika ulimwengu ule. Mwili wake haukupungua wala kuonyeha dalili za kuwa na ugonjwa ule, kila siku mwili wake ulikuwa ukinawiri kupita kawaida jambo ambalo ilikuwa ni ngumu sana kugundua kama alikuwa na ugonjwa wa UKIMWI.

    Wanawake walizidi kujigonga kwake, na kama kawaida yake, alikuwa akitembea nao kama kawaida yake. Yusufu alijua kwamba kuna siku maisha yake yangekatishwa na ugonjwa ule japokuwa alijua kwamba alikuwa akilindwa na watu wale, hata kabla hajafa, alitaka kuondoka na wengi, hasa wale wasichana ambao walikuwa wakiwashobokea watu waliokuwa na umaarufu pamoja na fedha nyingi.

    Kulala na wanawake hakukuisha, kila siku alikuwa akilala nao hata zaidi ya watatu na kisha kuachana nao. Hakutaka kurudia kulala na wanawake mara mbili, mara moja ilikuwa inatosha kabisa. Wasichana wengi warembo ndani ya jiji la Dar es Salaam wakaanza kufa kwa ugonjwa wa UKIMWI, mdudu mbaya wa ugonjwa huo akaonekana kulivamia jiji la Dar es Salaam.

    “Unamuona yule mrembo wa Kinondoni?” Yusufu alimuuliza Kelvin.

    “Mzuri sana. Nilibahatika kuongea nae jana pale Blue Pearl. Alisema angefurahi sana kama angeweza japo kuongea nawe” Kelvin alimwambia Yusufu.

    “Alikupa namba yake ya simu?”

    “Yeah! Alisema nikupe kama ungependa kuongea nae” Kelvin alimwambia Yusufu.

    “Anaitwa nani?”

    “Veronica”

    “Poa. Nipe tu. Unajua wananifagilia sana hawa wanawake. Ngoja niwape wanachokihitaji” Yusufu alisema huku akiichukua namba ya simu ya Veronica.

    Yusufu hakutaka kuchelewa, alichokifanya mahali hapo ni kumpigia simu Veronica na kisha kupanga mikakati ya kuonana nae. Kwa wakati huo, wanawake wengi ndani ya jiji la Dar es Salaam walikuwa wakivutiwa na Yusufu, kama ilitokea siku Yusufu akampigia simu msichana na kuomba kuonana nae, msichana huyo alijiona kuwa miongoni mwa wasichana wenye bahati sana nchini Tanzania.

    Hakukuwa na msichana ambaye alikuwa akifahamu kile ambacho Yusufu alikuwa akikifanya kwa wakati huo, hakukuwa na msichana ambaye alikuwa akifahamu kwamba Yusufu alikuwa ameathirika na hivyo alikuwa akifanya hivyo kama njia mojawapo ya kuwaambukiza ugonjwa huo na kuwaua baada ya mwezi mmoja. Wasichana walijiona kuwa na bahati ya kutembea na Yusufu, kwao, kutembea na mtu maarufu ilionekana kuwa sifa kubwa katika maisha yao.

    Mara baada ya kupanga sehemu ya kuonana, Yusufu na Veronica wakaonana katika hoteli ya La Vista Inn Magomeni. Muda mwingi Veronica alikuwa haamini kama kweli kipindi hicho alikuwa akiongea na Yusufu au The Ruler kama ambavyo alikuwa akijulikana na watu wengi nchini Tanzania.

    “Una ndoto gani Vero?” Yusufu alimuuliza Veronica.

    “Nataka kuwa mrembo wa Tanzania” Veronica alijibu huku kwa mbali akionekana kujisikia aibu.

    “Safi sana. Kwa hiyo ndoto yako imeishia hapo?” Yusufu alimuuliza.

    “Hapana. Nataka pia kuwa mrembo wa Dunia au hata Afrika kama alivyokuwa Nancy Sumari” Veronica alijibu.

    “Safi sana. Napenda kuwa na urafiki na msichana ambaye anakuwa na ndoto za mafanikio” Yusufu alimwambia Veronica.

    Bado walikuwa wakiendelea kupiga stori za hapa na pale huku muda ukizidi kusonga mbele. Katika kipindi chote hicho, Veronica bado alikuwa akijihisi kuwa na bahati sana. Waliongea mengi siku hiyo huku wakila na kunywa. Yusufu hakutaka kuchelewa, alichokifanya mahali hapo, akakisogeza kiti chake karibu na kiti alichokalia Veronica na kisha kuanza kumshikashika mapaja.

    Veronica hakuonekana kushtuka, kile ambacho kilikuwa kimetokea mahali hapo alikuwa amekwishakifahamu toka pale alipokuja mahali hapo, kwa hiyo alichokifanya ni kuonyesha ushirikiano. Waliendelea na mchezo ule mahali pale kwa muda mrefu mpaka ilipofika saa saba usiku kuamua kuchukua chumba ndani ya hoteli hiyo.

    “Hii ni ndoto ya kwanza ambayo nilikuwa nayo” Veronica alimwambia Yusufu huku akiwa amemruhusu Yusufu kumvua nguo alizokuwa nazo.

    “Ndoto gani?”

    “Kufanya mapenzi na wewe” Veronica alimwambia Yusufu.

    “Nakukamilishia ndoto yako ya kwanza maishani mwako” Yusufu alimwambia Veronica na kisha kuanza kufanya mapenzi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hiyo ndio ilikuwa siku ambayo Veronica alizifuta ndoto zake zote ambazo alikuwa nazo katika maisha yake. Kwa kuamini kwamba alikuwa akikamilisha moja ya ndoto yake katika maisha yake, alikuwa akipoteza zile ndoto nyingine ambazo alikuwa amezipanga kukamilisha katika maisha yake.

    Usiku huo ulikuwa ni usiku wenye furaha kwa Veronica lakini ni usiku ambao ulikuwa ukisababisha kilio kikubwa katika maisha yake. Hakujua ni kwa namna gani Yusufu alikuwa akitamani sana kumuambukiza ugonjwa ule kwa kuamini kwamba kutokana na urembo wake basi ilikuwa ni lazima hata wanaume wengine ambao walikuwa na tamaa ya kuwa na wanawake warembo wateketee kwa ugonjwa huo.

    ****

    Maisha yalikuwa yakiendelea kama kawaida, Yusufu hakuacha kutembea na wasichana warembo, kila siku alikuwa na kazi kubwa ya kubadilisha wasichana kama ambavyo alikuwa akibadilisha mavazi katika mwili wake. Yusufu hakuishia ndani ya jiji la Dar es Salaam tu, alikuwa akisafiri mpaka mikoani huku akiendelea na kazi yake kama kawaida.

    Yusufu alipoona kwamba kwa Tanzania alikuwa ametembea na wasichana si chini ya mia moja na hamsini ndani ya miezi nane, hapo ndipo alipoamua kusafiri na kwenda Kenya na Uganda pamoja na nchi nyingine za Afrika Mashariki. Yusufu alipokelewa kwa mikono miwili bila kujua kwamba alikuwa amekuja na kitu kingine, ugonjwa ambao ungewafanya watu wengi sana kufa katika maisha yao ya mbeleni.

    Huko napo kazi ilikuwa ile ile. Hakukuwa na msichana ambaye alikuwa na ubavu wa kumkatalia Yusufu. Alitembea na wasichana wengi warembo, alitembea na wasichana ambao wazazi wao walikuwa na fedha nyingi na za kutosha, kitu ambacho walikuwa wakikitaka katika maisha yao ni kutembea na mtu maarufu tu.

    “Unarudi lini Tanzania?” Papaa Pipo alimuuliza Yusufu simuni katika kipindi ambacho alikuwa nchini Uganda

    “Bado kabisa. Ndio kwanza nimetembea na wasichana ishirini hapa Uganda na Kenya nilipotoka wiki iliyopita” Yusufu alimjibu Papaa Pipo.

    “Rudi Tanzania kwanza”

    “Kuna nini tena?”

    “Mambo yameharibika huku” Papaa Pipo alimwambia Yusufu maneno ambayo yalionekana kumshtua.

    “Kivipi tena?”

    “Tetesi zinaenea kwamba unasambaza ugonjwa wa UKIMWI. Magazeti ya udaku yanaandika sana habari yako kuhusu jambo hilo” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.

    “Nakuja. Nakuja leo hii. Nitapanda ndege jioni kuja huko. Jambo hili ni lazima limalizwe haraka iwezekanavyo” Yusufu alimwambia Papaa Pipo na kisha kukata simu.

    Yusufu akaonekana kama mtu aliyechanganyikiwa kwa wakati huo. Alichokifanya ni kwenda katika ofisi za shirika la ndege la Uganda Airways na kisha kukata tiketi ya safari ya kuondoka nchini hapo siku hiyo. Tetesi zile zilionekana kumshtua kupita kawaida, tayari akaona kwamba kulikuwa na watu ambao walikuwa wamevumisha suala lile. Katika kipindi hicho, majina ya watu wawili ndio ambayo yalikuwa yamemjia kichwani.

    Mtu wa kwanza kabisa kumfikiria katika kipindi hicho alikuwa msichana Christina ambaye alikuwa amemuambukiza ugonjwa huo kwa makusudi na wakati alijua fika kwamba alikuwa ameathirika. Mtu wa pili kumfikiria alikuwa Dokta Lyimo ambaye alikuwa amempima miezi kadhaa iliyopita. Hao ndio watu ambao walionekana kueneza habari ile, alichokiona kufaa kukifanya kwa wakati huo, ni kuwatafuta watu hao tu.

    Saa nane mchana Yusufu alikuwa ndani ya ndege akirudi nchini Tanzania huku akionekana kuwa na mawazo kupita kawaida. Ndege ile ilichukua masaa mawili ikaanza kukanyaga katika ardhi ya Tanzania. Yusufu akateremka na kisha kuanza kuelekea katika sehemu ya kuchukua mizigo na kuchukua begi lake ambalo lilikuwa miongoni mwa mabegi ya wasafiri ambayo yalikuwa yakichunguzwa.

    Yusufu akaanza kupiga hatua kuelekea nje ya jengo la uwanja ule, kila mtu ambaye alikuwa akimuona kwa wakati huo alikuwa akimpiga picha huku wengine wakimuita kwa lengo la kutaka kupiga nae picha. Alipotoka nje ya jengo lile, macho yake yakatua usoni mwa Papaa Pipo ambaye alimtaka kuingia ndani ya gari lake.

    “Mambo yameharibika. Hebu soma haya magazeti” Papaa Pipo alimwambia Yusufu huku akimpa magazeti ya udaku ambayo yalikuwa yameandika mengi kuhusiana na habari zake.

    ‘YUSUFU AWAMALIZA WANAWAKE KWA GONJWA LA AJABU, KILA MWANAMKE ANAYETEMBEA NAE NI LAZIMA AONJE MAUTI, WANAWAKE WANAOTEMBEA NA YUSUFU WAZIDI KUTEKETEA’ Hivyo vilikuwa vichwa mbalimbali vya habari ambavyo vilikuwa vikionekana katika magazeti matatu ya udaku ambayo alikuwa ameyashika Yusufu.

    Aliuhisi mwili wake ukitetemeka, kijasho chembamba kikaanza kumtoka, hasira zikaanza kumpanda kwa kuona kwamba watu walewale ambao walikuwa wakifahamu kwamba alikuwa amehusika ndio watu ambao walikuwa wameeneza habari ile ambayo ilionekana kuaminika kwa baadhi ya watu.

    “Nitawaua wote” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.

    “Wakina nani?” Papaa Pipo alimuuliza.

    “Wanaoeneza haya”

    “Unawajua?”

    “Hapana. Ila nawahisi”

    “Wakina nani?”

    “Yule Dokta Lyimo na yule malaya, Christina” Yusufu alijibu.

    “Hata mimi nilihisi hivyo hivyo. Acha tuwafunge midomo milele” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.



    Je nini kitaendelea?

    Je watafanikiwa kuwauawa Dokta Lyimo na Christina?

    Hadithi bado mbichi sana.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog