IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI
*********************************************************************************
Simulizi : Nitakapokufa
Sehemu Ya Kwanza (1)
Mlango ulisikika ukigongwa kifujo fujo na mzee Kessi ambaye alikuwa ametoka kunywa pombe za kienyeji katika mtaa wa pili kutoka katika mtaa huo aliokuwa akiishi wa Kilingira uliopo Bagamoyo. Sauti yake kali iliyojaa ulevi ilikuwa ikisikika kwa juu sana huku akimtaka mke wake aufungue mlango huo.
Mzee Kessi hakuwa na uwezo wa kusimama wima na kutulia, muda wote alikuwa akiyumbayumba tu kutokana na kunywa kiasi kikubwa cha pombe za kienyeji. Miguuni, mzee Kessi alikuwa na kiatu kimoja tu, chupa moja ya maji ya uhai ambayo ilikuwa na pombe hiyo ya gongo ilikuwa mkononi mwake. Shati lake lilikuwa limeloa jasho, kwa kifupi, hakuonekana kuwa na utanashati wowote ule.
Bi Fatuma alikuwa chumbani kwake, usingizi kwake ukaonekana kuwa mzito kupatikana. Muda wote alikuwa akijigalagaza tu kitandani lakini bado usingizi haukupatikana. Mawazo yake kwa wakati huo yalikuwa yakimfikiria mume wake, mzee Kessi ambaye alikuwa kilabuni akinywa gongo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tayari ilikuwa imetimia saa saba usiku lakini bado mzee Kessi hakuwa amerudi nyumbani kitu ambacho kilionekana kumnyima raha Bi Fatuma. Ilipofika saa nane na robo usiku, akasikia mlango ukigongwa kifujo fujo huku sauti ya mumewe ikisikika ikimtaka kuufungua mlango hata kabla hajauvunja.
Huku akionekana kuwa na uchovu mwingi, Bi Fatuma akainuka na kuanza kuelekea ulipokuwa mlango na kisha kuuufungua. Kwanza akakutana na harufu mbaya na kali ya pombe, akaziba pua yake huku mume wake akiingia ndani. Mzee Kessi alikuwa akitembea huku akiyumbayumba kama kawaida yake.
Breki yake ya kwanza ilikuwa katika makochi yaliyokuwa sebuleni hapo, makochi ambayo yalikuwa yamechakaa kupita kawaida. Akajilaza mahali hapo huku pombe yake iliyokuwa katika chupa ya uhai akiwa ameikumbatia kana kwamba hakutaka mtu yeyote aichukue kutoka katika mkono wake.
“Twende ndani ukalale mume wangu” Bi Fatuma alimwambia mume wake, mzee Kessi ambaye hakuonyesha hata dalili kwamba angekwenda kulala chumbani.
“Niache nilale hapa hapa” Mzee Kessi alisema kwa sauti iliyojaa ulevi.
Kila kitu kilikuwa kikionekana kuwa kama zamani. Mzee Kessi alikuwa akilewa kila siku jambo ambalo lilionekana kumkasirisha sana mke wake, Bi Fatuma. Mara kwa mara mzee Kessi alikuwa akirudi nyumbani hapo usiku mkali huku akiwa amelewa kupita kawaida.
Maisha ya ulevi yakaonekana kuwa sehemu ya maisha yake, hakupenda wanawake hata kidogo, starehe yake kubwa wala haikuwa ngono kama walevi wengine, pombe ndio ilionekana kuwa starehe yake kubwa ambayo alikuwa akiipenda kupita kawaida.
Miaka mingi ya nyuma, mzee Kessi hakuwa mlevi kabisa, alikuwa mtu safi, Muislamu ambaye alikuwa akiswali swala tano kila siku. Kila kitu kikaanza kubadilika pale ambapo alipokuja kuchujwa kazini kutokana na kampuni kuwa na wafanyakazi wengi ambao wengine hawakuonekana kuwa na kazi yoyote kazini.
Tukio lile likaonekana kumhuzunisha sana mzee Kessi, kila siku akawa mtu wa mawazo, japokuwa mke wake alikuwa akimfariji sana lakini faraja ile wala haikuonekana kubadilisha kitu chochote kile. Hapo ndipo alipoamua kuanza kunywa pombe kwa kisingizo cha kupunguza mawazo aliyokuwa nayo.
Kila alipokuwa akilewa, mawazo yalikuwa yakimtoka kichwani mwake lakini pombe zilipokuwa zikiisha kichwani mwake, mawazo yalikuwa yakirudi kama kawaida. Mzee Kessi hakufikiria kuanzisha biashara yoyote ile japokuwa alikuwa amelipwa kiasi kikubwa cha fedha. Fedha ambazo alikuwa ameliwa akaziingiza kwenye ulevi.
Baada ya mwaka mmoja kupita, hali ya umasikini ambayo ilikuwa ikiwanyemelea ikawaingia. Fedha zikakatika, hapo ndipo akili ya mzee Kessi ilipoanza kukaa sawa. Akaanza kufanya kazi mbalimbali kama ujenzi na kazi nyingine ndogondogo.
Hawakuweza kugharamia gharama za chumba kikubwa ambacho walikuwa wakikaa maeneo ya Block P jambo ambalo likawafanya kuhamia Kisutu tena katika nyumba mbovu isiyokuwa na thamani yoyote ile.
“Mtakaa kwa muda kabla ya nyumba hii kubomolewa. Nimeamua kukusaidi kwa sababu sisi ni marafiki wa kitambo sana” Mzee Shomari alimwambia mzee Kessi.
Hapo ndipo maisha yao yalipoanzia. Maisha ya ndoa hayakuwa ya amani hata mara moja, kila siku mzee Kessi alikuwa akimpiga mke wake hasa katika kipindi ambacho alikuwa akilewa na kurudi nyumbani. Bi Fatuma alionekana kuwa mvumilivu kwa kila kitu, japokuwa alikuwa akipigwa lakini alikuwa akimpenda sana mume wake.
Siku zikaendelea kukatika, maisha ya Kisutu yakaonekana kuwazoea. Mara kwa mara mzee Kessi alikuwa akigombana na majirani zake kwa tabia zake za kurudi usiku na kupiga kelele ovyo. Japokuwa alikuwa akigombana sana na majirani zake lakini kamwe mzee Kessi hakutaka kubadilika, ndio kwanza alikuwa akipiga kelele zaidi na zaidi kila siku.
Katika maisha yao ya miaka ishirini na tano ya ndoa ambayo waliishi pamoja kama mume na mke, wawili hao walifanikiwa kupata mtoto mmoja tu wa kiume aliyeitwa Yusufu. Kipindi cha nyuma Yusufu ndiye ambaye alionekana kuwaunganisha wote wawili na kuwapa amani kubwa katika maisha yao ya ndoa, walimthamini sana Yusufu na kumpa kila kitu ambacho alikuwa akikihitaji kama mtoto wao, hasa katika kipindi kile ambacho walikuwa na fedha za kutosha.
Kwa sasa Yusufu hakuwa pamoja nao, alikuwa amekwishaanza maisha yake ndani ya jiji la Dar es Salaam huku muda mwingi akiwa anaelekea Bagamoyo kwa ajili ya kuwaona wazazi wake. Hali ambayo walikuwa nayo wazazi wake ikaonekana kumuumiza sana jambo ambalo likamfanya kutafuta sana fedha ndani ya jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kuwatunza wazazi wake ambao walikuwa wakiishi maisha mabovu ambayo hakuyapenda kabisa.
“Nitapata fedha tu na ninyi mtaishi kwenye nyumba nzuri kama ile ya mtaa wa Block P” Yusufu alikuwa akipenda kuwaambia wazazi wake maneno hayo katika kila kipindi alichokuwa akienda kuwasalimia.
*****
Maisha ndani ya jiji la Dar es Salaam hayakuwa rahisi hata mara moja. Kila siku Yusufu alikuwa akifanya kazi mbalimbali lakini wala hazikuweza kubadilisha maisha yake. Kazi zake zilianzia katika kubeba mizigo katika soko la Tandale, huko, maisha yaliendelea kuwa vile vile jambo ambalo likamfanya kuamua kufanya kazi ya ukonda, kwa mbali maisha yake yakaonekana kupata mwanga.
Japokuwa kila siku Yusufu alikuwa na uhakika wa kupata fedha zaidi ya shilingi elfu kumi lakini gharama mbalimbali za maisha ya Dar es Salaam zikamfanya kutumia kiasi kikubwa cha fedha kila siku ambacho hadi inafika usiku, hakuwa na fedha za kutosha mifukoni mwake.
Maisha yale yalikuwa yakimuumiza sana, hakuyapenda maisha yale ya umasikini ambayo alikuwa akiishi katika kipindi kile, nafsi yake ilikuwa ikitamani kuishi maisha ya kifahari, maisha ya kutanua mitaani na gari, maisha ya kuchukua kila aina ya msichana ambaye alikuwa akimtaka.
Maisha yaliendelea zaidi na zaidi, urafiki wake na Kelvin ukaonekana kuwa mkubwa, wakapanga chumba kimoja na kuishi pamoja. Gharama za kulipia chumba ilikuwa jukumu lao wote. Kila siku asubuhi wote walikuwa wakitoka pamoja na kwenda kutafuta fedha kwa kufanya kazi mbalimbali na usiku kurudi wote.
Maisha hayakuonekana kubadilika, kila walipokuwa wakipata fedha ambazo wala hazikumaliza shida ambazo walikuwa nazo. Fedha ambazo walikuwa wakizipata ziliwatosha katika chakula na kubadilisha mavazi tu.
“Maisha magumu sana” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Yaani ni magumu kiasi ambacho wakati mwingine nafikiri ni bora ningekuwa mwizi tu” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Hivi hali hii tutakuwa nayo milele au kuna siku itakuja kubadilika?” Kelvin aliuliza.
“Mmmh! Nafikiri itakuwa hivi milele. Kama unaona kuna siku itakuja kubadilika, itabadilika vipi? Tutapata vipi fedha za kufanyia mambo mengine ambayo hatujayafanya?” Yusufu aliuliza.
“Kufanya mambo gani zaidi?”
“Kumiliki magari, kuwa na mademu wakali, fedha za kutosha na kufanya mambo mengine pia” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Yaani bado unafikiria wanawake tu?” Kelvin aliuliza huku akitabasamu.
“Wewe unafikiri nitafikiria nini zaidi? Ili ujione umefanikiwa katika kila kitu basi ni lazima utembee na msichana yeyote unayemtaka kwa kipindi hicho. Hivi unafikiri kama ningekuwa na fedha yule Agness angenikataa?” Yusufu alisema na kuuliza.
“Ndio. Angekukataa” Kelvin alijibu.
“Thubutuuuuu. Niwe nimemfungia breki miguuni mwake na Range, nashusha kioo na kisha kuongea naye, unafikiri angenikataa. Acha masihala Kelvin, fedha ndio kila kitu katika maisha haya” Yusufu alimwambia Kelvin.
Siku hiyo ilikuwa kama siku nyingine tu, muda wote walikuwa wakiongea kuhusu fedha, walikuwa wakihitaji fedha kuliko kitu chochote kile katika maisha yao. Maisha ya kifahari ambayo walikuwa wakiishi watu wengine yalikuwa yakiwatamanisha kupita kawaida.
“Hivi inakuwaje kuhusu kipaji chako cha muziki? Hakitaweza kukutoa kwenye maisha haya kweli?” Kelvin alimuuliza Yusufu.
“Mmmh! Nafikiri hakiwezi” Yusufu alijibu.
“Hakuna bwana. Inakupasa kujaribu, huwezi jua, unaweza kuwa kama The King” Kelvin alimwambia Yusufu huku akimtaja msanii wa muziki ambaye alikuwa juu sana katika kipindi hicho nchini Tanzania.
“Kitu cha kwanza ni lazima tukumbuke kwamba kurekodi muziki si chini ya shilingi laki tano. Unaweza ukagharamia muziki kwa kiasi hicho halafu mwisho wa siku Madj wa vituo mbalimbali wakaanza kukubania tena” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Ila ngoja tujaribu” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Poa. Ila fedha tutazipata wapi? Kutunga nyimbo si jambo gumu kwangu, tatizo upatikanaji wa fedha za kurekodia tu” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Hakuna jinsi Yusufu. Kila kitu kinaonekana kuwa kigumu kwetu. Nitafanya kitu kimoja kwa ajili ya kuhakikisha kwamba unapata fedha za kurekodia” Kelvin alimwambia Yususfu.
“Kitu gani?”
“Kuiba”
“Acha masihala Kelvin”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hakuna jinsi Yusufu. Acha nijaribu kwa ajili yako ila nakuomba nawe fanya kitu kimoja tu” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Kitu gani?”
“Tunga wimbo mkali, wimbo ambao kila atakayeusikia ataupenda na kuanza kukuita sehemu mbalimbali kwa ajili ya kutumbuiza kwenye matamasha mbalimbali” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Hilo si tatizo. Ila na wewe itakubidi kuwa makini kwenye kufanya huo wizi wako. Si unajua sitaki kukupoteza” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Najua. Usijali, kila kitu kitakuwa sawa” Kelvin alimwambia Yusufu na kisha kulala huku kila mtu kichwa chake kikifikiria fedha tu.
*****
Muda ulikuwa ni saa 2.14 asubuhi, Kelvin alikuwa akilandalanda katika barabara za Posta Mpya huku macho yake yakiangalia katika kila gari ambalo lilikuwa limepakiwa. Kichwa chake kwa wakati huo kilikuwa kikifikiria kitu kimoja tu, kufanya wizi wa kitu chochote kile ambacho atakiuza na mwisho wa siku kupata fedha ambazo zitamfanya Yusufu kuingia studio na kurekodi muziki.
Idadi kubwa ya watu ambao walikuwa wakitembea huku na kule ilimfanya kuhofia sana kufanya kile ambacho alikuwa akitaka kukifanya. Mara nyingi alikuwa akiyaona magari ambayo ndani kulikuwa na laptop pamoja na simu za gharama kubwa lakini kukishusha kioo kwa kutumia waya mgumu aliokuwa nao lilikuwa jambo gumu kufanyika.
Alipoona kwamba kila kitu kimeshindikana, hapo ndipo akaamua kwenda katika ghorofa la Macafee lililokuwa Posta mtaa wa Samora View na kisha kupanda kule ambako magari yalikuwa yakiegeshwa. Kelvin akaanza kutembea huku na kule huku akiyaangalia magari yale ambayo yalikuwa yamepakiwa.
Tayari hali ikaonekana kuwa rahisi kwake, kutokana na kuwa na idadi ndogo ya watu ikaonekana kuwa kama nafasi kubwa kwake ya kuanza kufanya kile ambacho alikuwa amepanga kukifanya. Alichokifanya kwa wakati huo ni kuanza kulifuata gari moja la kifahari, Range ambalo lilikuwa limepakiwa pembezoni kabisa mwa sehemu ile ya kuegesha magari.
Alipolifikia, akaanza kuangalia huku na kule kuona kwamba hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa akimwangalia, alipoona kwamba kila kitu kipo salama, akaanza kuchungulia ndani ya gari lile huku akiuandaa waya wake.
Macho yake yakatua kwenye laptop moja aina ya Apple pamoja na simu mbili za aina ya iPhone 5. Kelvin hakutaka kuchelewa, kwa hali jinsi ilivyoonekana, ilionyesha kwamba mwenye gari angerudi muda wowote ule kutokana na vitu vyake vyote kuwa ndani ya gari.
Akauchukua waya wake na kisha kuupitisha kwenye uwazi wa kioo ambao ulikuwa umeachwa kwa ajili ya hewa na kisha kuangaika kuitoa loki kwa kutumia waya ule. Kazi haikuwa ndogo hata kidogo, kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka huku akihakikisha kwamba haligusi gari hilo hata kidogo kwa kuona kwamba lingepiga kelele ya kumshtua mmiliki wa gari lile.
Alijitahidi sana huku kijasho kikiendelea kumtoka, kila alipokuwa akiikamata loki ya mlango wa gari ile na kujaribu kuivuta kwa kutumia waya ule, loki ilionekana kuwa ngumu kuvutika. Kelvin hakutaka kukata tamaa, kila alipokuwa akiziangalia mali zilizokuwa ndani ya gari lile aliendelea kuvuta zaidi na zaidi.
Huku akiwa anaendelea na kazi yake, mara sauti za watu zikaanza kusikika kutoka katika upande mwingine jambo lililomfanya kuinama na kuanza kusikilizia kwa makini kama watu wale walikuwa wakija upande aliokuwepo. Akasikia mlango wa gari moja ukifunguliwa, watu wale kuingia na kisha gari kuwashwa na kuondoka mahali hapo.
Kelvin akaendelea kufanya kazi yake kama kawaida. Hakujua alijisahau vipi mpaka kuligusa gari lile, ghafla likaanza kupiga kelele. Kadri sekunde zilivyokuwa zikizidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo kelele zile zilivyozidi kuwa za juu zaidi na zaidi jambo ambalo liliwashtua walinzi ambao walikuwa wamewekwa kuhakikisha ulinzi wa magari yale yaliyokuwa yamepakiwa kwenye ghorofa ile kwa juu.
Vishindo vya watu vilikuwa vikisikika vikija kule ambako alipokuwepo, sehemu ambayo gari ile ilikuwa ikiendelea kupiga kelele. Kelvin alikuwa akiendelea zaidi na zaidi kuhakikisha kwamba mlango unafunguka na kisha kuchukua mali zile ambazo zilikuwa kwa juu kabisa.
Kila alipokuwa akijitahidi kutoa loki ile, loki ilionekana kuwa ngumu kufunguka jambo ambalo lilionekana kumtia wasiwasi zaidi. Kuondoka mahali hapo hakutaka kabisa, hakutaka kuondoka na kuziacha mali zile ambazo kwa haraka haraka zilikuwa na thamani isiyopungua milioni sita.
“Funguka. Loki funguka” Kelvin alisema huku akiendelea kufungua loki ile kwa kutumia waya mgumu huku walinzi wale wakizidi kusogea kule kulipokuwa na gari lile ambalo lilikuwa likizidi kupiga kelele.
*****
Walinzi ambao walikuwa na bunduki walikuwa wakizidi kusogea kule ambako kulikuwa na gari lile lililokuwa likipiga kelele, tayari walikwishajua kwamba kuna mtu ambaye alikuwa ameligusa gari lile na hivyo kuanza kupiga kelele. Tayari wasiwasi kwamba mtu aliyeligusa gari lile alikuwa mwizi ukaanza kuwaingia akilini.
Wakaziandaa silaha zao tayari kwa ajili ya kumfyatulia risasi mtu huyo ambaye alikuwa ameligusa gari lile kwa lengo la kuliiba au kuiba kitu chochote kile ambacho kilikuwa ndani ya gari lile. Wakaongeza kasi zao zaidi na zaidi mpaka kulifikia gari hilo ambali lilikuwa likiendelea kupiga kelele kama kawaida.
Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa akionekana mahali hapo, milango yote ilikuwa imefungwa kama kawaida japokuwa gari lile lilikuwa likiendelea kupiga kelele. Walichokifanya kwa wakati huo ni kuanza kuangalia huku na kule kuona kama wangeweza kumuona mtu yeyote ambaye alikuwa ameligusa gari lile lakini hawakumuona mtu yeyote.
“Mbona patupu?” Mlinzi mmoja alimuuliza mwenzake.
“Inawezekana kuna ndege aliingia na kuligusa” Mlinzi mwingine alimwambia mwenzake.
“Labda inaweza kuwa hivyo”
Mara mmiliki wagari lile ambaye alikuwa mwanamke wa makamo akatokea mahali hapo huku akiwa na ufunguo wa gari lake na kisha kuanza kuwaangalia walinzi wale ambao walikuwa wamesimama pembeni ya gari lake.
“Kuna nini? Alamu imenishtua kwamba kuna kitu kimetokea garini mwangu?” Mwanamke yule aliuliza.
“Hata sisi tulisikia alamu na ndio maana tukafika haraka sana ila hatukuona mtu. Inawezekana kuna ndege alikuja na kutua kwenye gari lako” Mlinzi mmoja alimwambia mwanamke yule.
Alichokifanya mwanamke yule ni kuufuata mlango wa gari lake na kisha kuufungua. Macho yake hayakuamini kile ambacho alikuwa akikiona mahali pale, laptop yake pamoja na simu zake mbili hazikuwa zikionekana. Hapo hapo akawageukia walinzi huku macho yake yakionekana kubadilika.
“Nani kachukua simu zangu na laptop yangu?” Mwanamke yule aliuliza swali ambalo liliwafanya walinzi wote kushangaa.
“Unasemaje?” Mlinzi mmoja aliuliza.
“Nani ameniibia simu zangu na laptop yangu?” Mwanamke yule aliuliza kwa sauti ya juu.
Walinzi wote wakapigwa na mshangao, maneno aliyoongea mwanamke yule yakaonekana kuwashangaza kupita kawaida. Hawakujua kwamba kuna vitu vilikuwa vimeibiwa ndani ya lile gari, wakausogelea mlango ule na kuchungulia ndani.
“Nimeibiwa” Mwanamke yule alisema huku akionekana kukasirika.
“Mbona tulipokuja hapa hatukuona mtu yeyote?”
“Ila nimeibiwa. Nimeibiwa kila kitu nilichokiacha ndani ya gari langu. Hadi pochi yangu imeibwa ambayo ilikuwa na fedha nyingi pamoja na kadi yangu ya ATM” Mwanamke yule alisema maneno yaliyowafanya walinzi wale kuondoka mahali hapo na kuanza kuzunguka huku na kule kwa lengo la kumtafuta mtu aliyeiba simu, laptop na pochi ya yule mwanamke.
Kelvin alikuwa akiendelea kujitahidi kuufungua mlango ule, sauti za walinzi ambao walikuwa wakija kwa kasi zilikuwa zikizidi kusikika masikioni mwake. Tayari kijasho chembamba kilichokuwa kikimtoka kilizidi kuongezeka zaidi na zaidi na kuliloanisha shati alilokuwa amelivaa.
Loki ilionekana kuwa ngumu kuvutika kwa juu, alijitahidi zaidi na zaidi, bahati ikaonekana kuwa upande wake, loki ile ikafanikiwa kupanda kwa juu. Hiyo ikaonekana kuwa nafuu kwake, alichokifanya mahali hapo tena kwa haraka sana ni kuufungua mlango.
Hakutaka kuchelewa hata mara moja, kila kitu ambacho alikuwa akikifanya mahali hapo alikuwa akikifanya kwa haraka haraka. Kitu cha kwanza akachukua laptop ile aina ya Apple pamoja na simu zile mbili zilizoonekana kuwa za gharama na kisha kutaka kutoka nje.
Huku akionekana kutokuamini, macho yake yakatua katika pochi kubwa iliyokuwa mule ndani ya gari. Hakutaka kuifungua na kujiuliza kwamba ndani ya pochi ile kulikuwa na nini, alichokifanya mahali hapo ni kuichukua na kutoka nayo.
Akaufunga mlango kama ulivyokuwa na kisha kuondoka mahali hapo kwa mwendo wa kuinamainama. Kasi yake ya kutembea ilikuwa kubwa sana jambo lilimfanya kufika sehemu ya kushukia chini na kisha kuanza kukimbia.
Tayari moyo wake ukaonekana kuwa na furaha, alipofika chini, akajibanza sehemu ambayo ilikuwa na ukuta na kisha kuifungua pochi ile. Fedha ambazo alikutana nazo ndani ya ile pochi zikaonekana kumchanganya kupita kawaida.
“Zaidi ya milioni tatu hizi” Kelvin alijisemea huku akikenua kwa furaha.
“Kuna kadi ya benki pia. Huu sasa utajiri” Kelvin aliendelea kujisemea huku akiwa ameipekua ile pochi kwa haraka sana.
Hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kuondoka kwa mwendo wa kasi na kuanza kuifuata bajaji ambayo ilikuwa imepakiwa karibu na benki ya Kihindi iliyokuwa posta karibu kabisa na Maktaba ya Taifa.
“Nipeleke Tandale” Kelvin alimwambia dereva wa bajaji.
“Elfu kumi”
“Wewe nipeleke tu”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Safari ya kuelekea Tandale ikaanza mahali hapo kwa kupitia njia ya Salander Bridge. Muda wote Kelvin alikuwa akiangalia nyuma huku akionekana kuwa na wasiwasi wa kufuatiliwa. Alipoona kwamba kila kitu kipo salama, akaitoa ile kadi ya benki ya ATM ya CRDB na kisha kuanza kuiangalia.
Namba zote za akaunti ile, jina zilikuwa zikionekana lakini hakuwa akifahamu namba za siri. Kelvin akatulia kwa muda huku kichwa chake kikifikiria kitu. Alikaa katika hali ile na ndipo hapo alipoamua kuchukua simu moja kati ya zile mbili na kuanza kupekua.
Kwanza akaenda katika sehemu ya majina na kuanza kuangalia majina mbalimbali. Tayari kichwa chake kilikuwa na uhakika kwamba namba za siri za kadi ile zingekuwa kwenye simu ile. Aliangalia jina moja hadi jingine mpaka pale alipofikia jina lililosomeka CRDB.
Hakutaka kujiuliza, alichokifanya mahali hapo ni kuangalia namba zile na macho yake kutua kwenye namba zilizosomeka 2389. Kuanzia hapo akawa na uhakika kwamba namba zile ndizo zilikuwa namba za siri za kadi ile ya ATM.
“Unaweza kupitia Magomeni pale kituo cha mafuta?” Kelvin alimuuliza dereva wa bajaji.
“Yeah! Ila itabidi tupitie huku Kinondoni”
“Hakuna noma”
Safari iliendelea zaidi na zaidi. Walipofika Kinondoni Manyanya, wakaonganisha kuelekea Magomeni. Muda wote kichwa cha Kelvin kilikuwa kikiendelea kufikiria kiasi cha fedha ambacho angeweza kukutana nacho katika akauti ya yule mwanamke.
“Hivi leo lini?” Kelvin alimuuliza dereva wa bajaji.
“Jumamosi”
“Safi sana. Saa yako inaonyesha saa ngapi?”
“Saa nane na robo”
“Hapo imetulia zaidi” Kelvin alimwambia dereva.
Tayari kichwa chake kilikuwa kikifikiria mbali zaidi. Kwanza alikuwa akifikiria namna ya kukitoa kiasi kile cha fedha ambacho kilikuwa kwenye akaunti ile. Alijua fika kwamba kiasi cha mwisho kutoa fedha kwenye mashine za ATM za CRDB kilikuwa mwisho shilingi milioni tatu kwa siku.
Alichokuwa akitaka kukifahamu kwa wakati huo ni mara ngapi angeweza kutoa kiasi hicho hata kabla ya mwanamke yule kufunga akaunti yake. Tayari alikwishaona kwamba kama kiasi kingekuwa kikubwa zaidi basi angeweza kutoa kiasi cha shilingi milioni sita, yaani akiwa na maana kwamba shilingi milioni tatu angezitoa siku hiyo na milioni tatu angezitoa siku inayofuatia, siku ambayo mwanamke yule angekuwa hajaifunga akaunti ile kwa kuwa huduma za kibenki zisingekuwa zinatolewa siku hiyo.
“Tumekwishafika” Dereva alimwambia Kelvin huku akiwa amesimamisha gari katika kituo cha mafuta cha Magomeni.
Kwa haraka haraka Kelvin akateremka na kuingia katika chumba cha mashine ya ATM ya CRDB na kisha kuchukua ile kadi na kuichomeka. Alipotakiwa kuingiza namba za siri, akaingiza namba zile ambazo alikuwa ameziona kwenye simu ile. Namba zikakubali na kisha kuangalia salio. Salio la shilingi milioni thelathini na tano lilikuwa likionekana katika akaunti ile.
“Mungu wangu! Huu utajiri sasa” Kelvin alisema na kisha kutoa kiwango cha mwisho kabisa cha shilingi milioni moja na nusu na kisha baada ya saa moja kutoa kiasi kama hicho na kuondoka mahali hapo.
Tayari akayaona maisha yakiwa yamebadilika sana, umasikini ambao alikuwa akiishi pamoja na Yusufu ukaonekana kuanza kupotea taratibu. Bajaji ikaendedelea na safari mpaka Tandale ambako akateremka na kumlipa dereva wa bajaji kiasi kilichohitajika na kuelekea ilipokuwa nyumba ambayo walikuwa wamepanga.
“Vipi tena? Mbona unaonekana kuwa na furaha?” Yusufu alimuuliza Kelvin.
“Umekwishatunga wimbo wenyewe kesho twende studio?” Kelvin alimuuliza Yusufu.
“Ndio naendelea nao, upo katika hatua za mwisho kumalizika” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Poa. Wewe jitahidi, yaani nataka wiki hii hii twende studio” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Sawa. Ila mbona unaonekana kunificha kitu fulani. Kumetokea nini uko ulipokwenda?” Yusufu aliuliza.
Hapo ndipo Kelvin alipoanza kumhadithia Yusufu kila kitu ambacho kilitokea toka katika sehemu ya kuegesha magari iliyokuwa ghorofani na mpaka alipoufungua mlango ule na kuchukua kila kitu alichokiona kufaa kuchukuliwa.
“Una hatari sana Kelvin” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Nimefanya hivi kwa ajili yako tu. Nataka kuwekeza fedha zangu katika kipaji chako cha muziki” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Daah! Shukrani sana. Ninaahidi kujitolea zaidi na zaidi” Yusufu alimwambia Kelvin.
Hapo ndipo maisha ya usanii yalipoanzia. Mpaka akaunti ya mwanamke yule inafungwa, tayari Kelvin alikuwa amekwishachukua kiasi cha shilini milioni tisa katika mashine mbalimbali za ATM zilizokuwa ndani ya jiji la Dar es Salaam huku kiasi kingine cha shilingi milioni tatu akiwa amekitoa asubuhi ya Jumatatu.
Yusufu akaanza kurekodi muziki katika studio ya Metropolian iliyokuwa Kijitonyama jijini Dar es Salaam. Wimbo wake ulikuwa mzuri sana ambao aliamini kwamba ungeweza kumtambulisha katika jamii kwamba alikuwa mmoja wa wanamuziki wanaochipukia.
Japokuwa wimbo ulikuwa mzuri lakini bado fedha zilikuwa zikihitajika kutumika kuwahonga madj mbalimbali wa vituo vya redio kwa ajili ya kuupiga wimbo wake. Kila siku Kelvin alikuwa akionekana kuwa karibu nae zaidi. Japokuwa walikuwa wakitumia kiasi kikubwa cha fedha lakini Kelvin hakuonekana kujali kabisa, bado alikuwa akiendelea kutumia fedha zile.
“Haujaanza kuitwa hata kwenye matamasha mbalimbali?” Kelvin aliuliza huku akionekana kutokuamini.
“Bado”
“Daah! Kwa hiyo tufanye nini sasa?”
“Kwani umebakiwa na kiasi gani hapo?”
“Milioni sita na nusu tu”
“Ngoja nirekodi wimbo wa pili halafu tuangalie upepo” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Sawa”
Hakukuwa na cha kusubiri, kwa sababu nyimbo zilikuwa nyingi, Yusufu akautoa wimbo wa pili. Hali haikubadilika, bado ilionekana kuwa vile vile, watu walikuwa wakiuona kuwa wimbo wa kawaida sana. Jambo hilo likaonekana kumuumiza sana Yusufu, kila siku alikuwa akitumia kiasi kikubwa cha fedha lakini hali haikuonekana kubadilika.
“Kwa hiyo tufanye nini sasa?” Yusufu aliuliza huku akionekana kukata tamaa.
“Tutoe video, inawezekana ikaleta hamasa kwa watu. Si unajua watu siku hizi hawapendi kusikiliza redio kwa sana” Kelvin alimwambia Yusufu.
Uamuzi huo ndio ambao ulikuwa umefikiwa kwa kipindi hicho, wakakubaliana na kampuni ya kurekodi video ya Metro iliyokuwa Sinza na kisha kurekodi video hiyo ambayo iliwagharamu kiasi cha shilingi laki tisa.
Kidogo, wimbo huo ukaonekana kuanza kusikika katika masikio ya watu kiasi ambacho kikamfanya Yusufu kuanza kutambulika kama msanii. Hapo ndipo alipoanza kuitwa kwenye matamasha madogo na kisha kuanza kutumbuiza.
Japokuwa alikuwa msanii mdogo ambaye alikuwa akichipukia lakini alionekana kuwa mkali katika siku za usoni. Matamasha mbalimbali ambayo alikuwa akiitwa kwa ajili ya kutumbuiza ndio ambayo kwa kiasi fulani yakaonekana kuanza kumuingizia fedha huku akizitumia pamoja na Kelvin ambaye alionekana kuwa kama familia yake pia.
Yusufu hakutaka kuwasahau wazazi wake, alichokuwa akikifanya ni kuwatumia fedha hata wazazi wake ambao walionekana kufurahia kipaji cha muziki ambacho alikuwa nacho Kelvin. Kila siku Kelvin alikuwa akijitahidi kutunga nyimbo mbalimbali, kitu ambacho alikuwa akikihitaji kwa wakati huo ni fedha za kutosha pamoja na umaarufu tu kwa kuona kwamba kama angekuwa maarufu basi angeweza kuingiza fedha zaidi.
“Fedha na umaarufu” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Vimefanya nini sasa?” Kelvin aliuliza.
“Ndio ninavyovitaka. Ili uweze kuuza basi ni lazima uwe maarufu” Yususfu alimwambia Kelvin.
“Na ili uwe maarufu basi ni lazima uwe na fedha” Kelvin alimwambia Yusufu.
Kila siku Yusufu alikuwa akitamani kuwa na umaarufu mkubwa pamoja na kupata fedha za kutosha, tayari alikwishaona kwamba alikuwa akikaribia kuupata umaarufu na kupata fedha kama ambavyo alivyotaka. Alitamani kuona nyimbo zake zikisikilizwa na watu wengi, kupata mashabiki wengi kwa kuamini kwamba ndio angeuza kupita kawaida.
“Inabidi utoe wimbo mmoja wa mwisho na tuangalie upepo” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Sawa”
“Ila wimbo huu itakubidi ufanye kitu kimoja” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Kitu gani?”
“Itakubidi umshirikishe The King” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Itawezekana kumlipa fedha atakazozihitaji? Naona kama atahitaji kiasi kikubwa cha fedha” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Nafikiri hilo halitakuwa tatizo. Una kiasi gani kwa sasa?” Kelvin alimuuliza Yusufu.
“Milioni tatu na nusu”
“Inatosha sana. Hapa nina milioni mbili. Cha msingi tunamuita, unarekodi nae wimbo na kisha tunarekodi na video tuone itakuwaje” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Sawa. Haina noma”
*****
Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Jumanne Rajabu ndiye alikuwa msanii ambaye alikuwa akisifika na kusikika sana nchini Tanzania kwa wakati huo. Msanii huyo alikuwa na mashabiki wengi nchini Tanzania na hata nje ya nchi ya Tanzania kiasi ambacho alikuwa akiingiza kiasi kikubwa cha fedha katika kila shoo moja ambayo alikuwa akifanya.
Watanzania wakamkubali kupita kawaida, kila alipokuwa akipita Jumanne ambaye alikuwa akijulikana kwa jina la kisanii kama The King, watu walikuwa wakimpiga picha huku wengine wakitaka hata kupiga nae picha.
Jina lake lilikuwa likizidi kuvuma kupita kawaida, kwa kila wimbo ambayo alikuwa akiimba, ulikuwa ukipendwa sana hata kama ilikuwa mbaya kiasi gani. Nyota ya kupendwa ambayo alikuwa nayo ikaonekana kuwa na mvuto mkubwa sana kwa mashabiki mbalimbali wa muziki Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
The King hakuwa mtu wa kutulia, mara kwa mara alikuwa akiitwa sana nje ya nchi kwa ajili ya kufanya shoo ambazo zlikuwa zikimuingizia sana fedha, fedha ambazo zilikuwa zimebadilisha maisha yake kwa kiasi kikubwa sana. Katika kila wimbo ambayo The King alikuwa akishirikishwa, watu walikuwa wakiupenda hata kama huyo aliyemshirikisha alikuwa akiimba vibaya.
Nembo ya jina lake ilikuwa ya kibiashara sana, mvuto ambao alikuwa nao ulionekana kuwa mkubwa sana jambo ambalo kila wakati alikuwa akinukia fedha tu. The King akanunua magari ya kifahari pamoja na kumiliki nyumba mbili za kifahari sana. Maisha yake yote alikuwa akitegemea muziki ambao ulikuwa ukimuuingizia kiasi cha shilingi milioni ishirini kwa shoo mbili tu ambazo alikuwa akizifanya kwa mwezi.
The King hakuwa mchoyo, kwa kila msanii ambaye alikuwa akitaka kushirikiana nae, alikuwa akishirikiana nae kama kawaida tena kwa malipo ya chini kwa kugundua kwamba kiasi ambacho angekihitaji chenye hadhi ya jina lake, wasanii wasingeweza kumlipa.
Wasanii wengi walikuwa wakipanga foleni katika kutaka kushirikiana na msanii huyo katika nyimbo zao mbalimbali. Zaidi ya wasanii kumi ambao alikuwa amewahi kushirikiana nao tayari majina yao yalikuwa yakijulikana sana nchini Tanzania.
“Mnataka kunishirikisha kwenye wimbo wenu?” The King alimuuliza Kelvin simuni.
“Ndio” Kelvin alijibu.
“Sawa. Mna kiasi gani?”
“Tunakusikiliza wewe mkuu”
“Mna milioni mbili?” The King aliuliza.
“Hizo nyingi sana kwetu mkuu”
“Sawa. Ninyi mna kiasi gani?”
“Milioni moja tu”
“Ongezeni nusu”
“Sawa. Hakuna tatizo”
“Sawasawa. Ila kutokana na ratiba niliyokuwa nayo pamoja na kiasi mnachotoa, hakuna budi mkasubiri mpaka mwezi wa tisa” The King alimwambia Kelvin ambaye alionekana kushtuka.
“Mwezi wa tisa?” Kelvin aliuliza huku akionekana kushtuka kwani muda huo ndio kwanza ilikuwa mwezi wa pili.
“Ndio. Mkipanda dau zaidi napo miezi inapungua zaidi” The King aliwaambia.
“Sisi tunataka tufanye kazi hata wiki ijayo mkuu”
“Kama wiki ijayo, fanyeni tu milioni mbili” The King aliwaambia.
Hakukuwa na kukataa tena, kwa wakati huo tayari walikwishaona kwamba wanahitaji sana kupata fedha nyingi zaidi na zaidi, hivyo kiasi kile cha fedha ambacho walikuwa wakihitajika kukitoa wala hakikuwa na tatizo lolote lile kwani waliamini kwamba wangeweza kupata kiasi kikubwa cha fedha endapo wangefanya kazi na The King.
*****
Kila siku Yusufu na Kelvin walikuwa wakielekea katika nyumba ya The King kwa ajili ya kuuchukulia mazoezi wimbo ambao tayari walikuwa wamekwishautunga. Mara kwa mara The King hakuwa mtu wa kushinda nyumbani jambo ambalo liliwafanya Yusufu na Kelvin kurudi ndani ya nyumba hiyo bila ya mafanikio yoyote.
Ubize wa The King, kusafiri nchi mbalimbali kwa ajili ya kufanya shoo mbalimbali kulimfanya kuwa na wakati finyu sana wa kukutana na Yusufu na kufanya kazi kama ambavyo alikuwa amemuahidi kabla.
Yusufu hakuonekana kukata tamaa kumfuata The King, kwake, mtu huyo alionekana kuwa muhimu sana ambaye angemfanya kusikika katika masikio ya Watanzania na kumjua kwamba alikuwa nani katika anga nzima ya muziki Tanzania. Kila siku alikuwa mtu wa kwenda nyumbani kwa The King bila kufanikiwa kitu chochote kile.
Simuni hakuwa akipatikana kwa wakati huo jambo ambalo lilikuwa likimtia sana wasiwasi Yusufu kiasi ambacho akaonekana kukata tamaa ya kufanya nae kazi. Hapo ndipo Yusufu alipoona kwamba alitakiwa kufanya kitu kingine zaidi, kumuita msanii mwingine na kufanya nae kazi kama kawaida.
“Gorila vipi?” Kelvin alimuuliza Yusufu.
“Anafaa. Kama vipi tutafute namba yake ya simu” Yusufu alimwambia Kelvin.
Hapo ndipo walipoanza harakati za kutafuta namba ya simu ya Gorila, msanii ambaye kwa kipindi hicho alikuwa akisikika sana japokuwa umaarufu wake haukuwa ukilingana na umaarufu wa The King. Kumpata Gorila wala hakukuwa na kazi kubwa, mara baada ya kumpata, wakaanza kufanya mazoezi na kisha kuurekodi wimbo huo ambao aliupa jina la MACHOZI YANGU.
“Unatumia jina gani la kisanii?” Gorila alimuuliza Yusufu.
“Jina langu halisi la Yusufu” Yusufu alijibu.
“Haitakiwi kuwa hivyo, unachotakiwa ni kutafuta jina jingine ambalo litakuwa tofauti zaidi. Jina ambalo litawafanya hata watu kuvutiwa na kutaka kusikiliza nyimbo zako” Gorila alimwambia Yusufu.
“Sawa. Itabidi nianze kutumia jina jingine” Yusufu alimwambia Gorila.
“The Ruler” Gorila alimwambia Yusufu.
“Ndiye nani huyo?”
“Hilo ndilo jina jipya ambalo unatakiwa kulitumia kwa sasa” Gorila alimwambia Yusufu.
“Maana yake nini sasa. Si unajua sisi wengine kingereza kimetupiga chenga”
“Maana yake ni Mtawala” Gorila alimwambia Yusufu.
“Sasa hilo si litafanana na The king”
“Hapana. Yeye atakuwa ni mfalme tu, ila wewe utakuwa ni mtawala. Au unaliogopa jina hilo?” Gorila alimwambia Yusufu.
“Jina hilo haliwezi kuleta bifu kati yangu na The King?” Yusufu aliuliza huku akionekana kuwa na wasiwasi.
“Litaleta bifu. Ila bifu si ndio zuri?”
“Bifu ndio zuri? Uzuri wake nini hapo?”
“Litakufanya kujulikana, litawafanya watu kutaka kufahamu huyu The Ruler ni nani hasa na anaimba nyimbo gani. Watakapoanza kukutafuta kwa lengo la kukufahamu, utakuwa umekwishakuwa maarufu” Gorila alimwambia Yusufu ambaye kwa kiasi fulani maneno yale yakaonekana kumuingia.
“Nimekubaliana nalo. Unalionaje jina hilo Kelvin?” Yusufu alimuuliza Kelvin.
“Limetulia. Limetulia sana” Kelvin alijibu.
Kuanzia siku hiyo jina la kisanii la Yusufu likawa The Ruler. Maswali mfululizo yalikuwa yakimiminika kichwani mwa wafuatiliaji wengi wa muziki ambao walikuwa wakilisikia jina hilo. Tayari matatizo na ugomvi ukaonekana kuanza kunukia kati ya msanii nguri wa muziki wa kizazi kipya, The King pamoja na msanii ambaye alikuwa akichipukia, Yusufu au The Ruler kama alivyoanza kujulikana.
Jina lile na ugomvi ambao ulikuwa ukianza kufurukuta chini kwa chini ndio ambao uliwafanya watu wengi kuvutiwa kutaka kumsikiliza msanii The Ruler kwa kutaka kuona kwamba alikuwa na kitu gani kipya na kama alikuwa na uwezo wa kumfunika The King ambaye alikuwa amekaa katika fani ya muziki kwa muda mrefu sana.
Kadri ambavyo watu walivyozidi kumsikiliza The Ruler na ndivyo ambavyo akaanza kujulikana miongoni mwa watu wengi mpaka kufikia hatua ambayo alizidi kuitwa katika matamasha mbalimbali kwa ajili ya kupiga shoo ambazo zilikuwa zikimuingizia kiasi kikubwa cha fedha ambacho alikuwa akikitumia pamoja Kelvin ambaye kwake tayari alikuwa meneja wake.
“Huu ugomvi hautokwisha, huu ugomvi tutapigana sehemu yoyote ile, kuanzia mitaani mpaka stejini” Yalikuwa maneno ambayo alikuwa akiyaongea The King kila alipokuwa akikaa na watu wake.
Tayari ugomvi wa chini kwa chini ukaonekana kuwa mkubwa sana kiasi ambacho kiliwafanya waandishi wa habari kufanya jitihada nyingi za kuwaita pamoja na kuwapatanisha lakini hakukuwa na mapatano yoyote ambayo yaliafikiwa. Kila siku magazeti mbalimbali yalikuwa yakitangaza juu ya ugomvi huo ambao ulikuwa ukizidi kushika kasi kadri siku zilivyozidi kwenda mbele.
“Dogo haniwezi. Yaani haniwezi hata chembe japokuwa ameliiba jina langu” The King aliwaambia waandishi wa habari.
Ugomvi huo ukahama kabisa. Haukuwa ugomvi wa kutafutana na mapanga mitaani, sasa ukaingia ugomvi mpya ambao ukaonekana kuwavutia wapenzi mbalimbali wa muziki nchini Tanzania. Waandaaji wa matamasha mbalimbali wakafanya ugomvi huo kuwa sehemu ya kuingizia fedha, mara kwa mara walikuwa wakiandaa matamasha huku majina ya wasanii hao yakionekana kuwa kivutio zaidi.
Wapenzi wa muziki walikuwa wakiingia kwa wingi kwenye matamasha kwa sababu tu walikuwa wakitaka kuwaona wawili hao juu ya steji moja wakiimba huku wakijitahidi kufunikana. Kwa uwezo, The Ruler alionekana kuwa mdogo sana mbele ya The King kiasi ambacho wakati mwingine mashabiki walikuwa wakimzomea kila alipokuwa akipanda jukwaani kutumbuiza.
Hali ile ilionekana kumuumiza sana Yusufu kupita kawaida, hakuamini kama mwisho wa kulichagua jina lile lingekuwa namna ile. Japokuwa alikuwa akijulikana kama alivyokuwa akitaka lakini mvuto wote ukaonekana kupotea kabisa jambo ambalo likamfanya kutamani kutoka katika anga ya muziki wa kizazi kipya.
“Lakini fedha si tunapata kama tulivyokusudia!” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Tunapata lakini unafikiri kila siku kuzomewa najisikia furaha! Natamani kila nitakapokuwa jukwaani watu wawe wanashangilia kwa furaha na si kunizomea” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Kwa hiyo unaona kipi kifanyike?” Yusufu aliuliza.
“Nibadili jina” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Hapana. Hilo ni jambo lisilowezekana kabisa. Usibadili jina, acha liwe hili hili” Kelvin alimwambia Yusufu,
Kazi ya muziki bado ilikuwa ikiendelea kama kawaida, Yusufu hakutakiwa kukata tamaa au kurudisha nyuma matumaini yake, alitakiwa kuendelea kupigana mpaka pale ambapo kila kitu kingeeleweka. Bado alikuwa akizidi kuzomewa jukwaani lakini wala hakukata tamaa, bado alikuwa akiendelea kuingiza fedha kama kawaida.
Kamwe hakuwasahau wazazi wake, mara kwa mara alikuwa akiwatumia fedha nyingi ambazo zilikuwa zikibadilisha maisha yao kila siku. Jina la The Ruler likaonekana kuwagawa mashabiki, kuna wengine ambao walikuwa wakimuona The King kuwa mkali zaidi yake lakini kuna wengine walikuwa wakimuona The Ruler kujitahidi kutafuta ugomvi na The King kama namna moja wapo ya kujitangaza.
“Kwa hiyo kipi kifanyike? Ninatamani kuwa juu zaidi ya The King, watu wanipende kila ninapopanda jukwaani. Ikiwezekana niwachukue hata mashabiki wake na umaarufu wangu uwe mkubwa” Yusufu alimuuliza Kelvin.
“Hapa ni kuongeza juhudi tu. Kama ukiongeza juhudi, kila kitu kitakuwa safi” Kelvin alimwambia Yusufu.
Yusufu hakutaka kupuuzia ushauri ule, alichokifanya kwa wakati huo ni kutuliza zaidi kichwa chake na kutunga nyimbo ambazo aliziamini kuwa kali sana zaidi ya nyimbo alizokuwa akiimba The King. Kila alipokuwa akizirekodi nyimbo zile, bado alikuwa pale pale alipokuwa hali ambayo kwa kiasi kikubwa ikamkatisha sana tamaa.
Baada ya siku kadhaa mambo yakaonekana kuwa mabaya kwa Yusufu, kitu cha redio cha Peackok Fm ambacho kilikuwa kinapiga sana miziki ya wasanii wengi na kuwatangaza kikatangaza hadharani kwamba kisingeweza kupiga tena nyimbo za The Ruler ambaye alikuwa kwenye ugomvi mkali na msanii nguri, The King.
Hilo lilionekana kuwa kama pigo kwa Yusufu, hakujua angeendelea vipi katika anga ya muziki kama kituo hicho kilikuwa kimekataa kupiga nyimbo zake. Tayari akajihesabia kushindwa, ndoto za kuwa msanii mkubwa hapo baadae zikaanza kufutika kichwani mwake.
Watanzania wengi walikuwa wakikipenda kituo hicho cha redio cha Peackok Fm kwa sababu kilikuwa kikiwatangaza sana wasanii wa Tanzania kitaifa na Kimataifa. Uamuzi huo ambao ulikuwa umechukuliwa na kituo hicho cha redio kilimaanisha kwamba ule umaarufu mchache ambao alikuwa nao Yusufu ungepungua zaidi na kupotea kabisa. Hiyo ilimaanisha kwamba asingekuwa akialikwa kwenye matamasha mengine mfululizo kama ambavyo ilikuwa hapo kabla.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hilo lilikuwa pigo kubwa kwa Yusufu, hakuamini kama ugomvi wake na The King ungeweza kufikia hatua mbaya kama ile. Moyoni alitamani sana amtafute The King na kisha kumuomba msamaha ili mladi tu nyimbo zake ziweze kupigwa tena katika kituo hicho cha redio.
“Kwa hiyo tufanye nini sasa ili niwe juu?” Yusufu alimuuliza Kelvin.
“Au tutafute mfadhili”
“Tutampatia wapi na wakati watu fedha zao wanazichungulia?”
“Usihofu. Najua kuna wengi ambao wanatamani sana kukufadhili. Cha msingi twende tukamuone Papaa Pipo” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Itawezekana kweli kunifadhili?”
“Ondoa hofu, itawezekana tu” Kelvin alimwambia Yusufu.
Hakukuwa na cha kusubiri, kwa hatua ambayo walikuwa wameifikia waliona kwamba bila kupata mfadhili basi kumfanya Yusufu kuwa juu lingekuwa jambo gumu sana. Mtu ambaye walimfikiria kwa wakati huo alikuwa Papaa Pipo tu ambaye alikuwa akitisha kwa utajiri mkubwa ambao alikuwa nao.
Papaa Pipo ndiye ambaye alikuwa akimiliki kumbi kubwa za starehe ambazo ziliitwa Veteran Club ambazo zilikuwa Dar es Salaam, Arusha na Mwanza. Papaa Pipo ndiye ambaye alikuwa akiwadhamini wasanii wengi sana akiwepo The King ambaye alikuwa akinunuliwa magari ya kifahari na kutanuliwa nayo mitaani.
Kitu ambacho alikuwa akikihitaji Papaa Pipo ni kutajwa tajwa tu katika nyimbo zote za watu ambao alikuwa akiwafadhili. Alichokuwa akikitaka yeye ni umaarufu tu, alijijua kwamba alikuwa na fedha nyingi ambazo zilikuwa zimebadilisha maisha yake lakini alikuwa akihitaji kitu kingine zaidi, umaarufu.
Kutajwa mara kwa mara na wasanii mbalimbali kukamfanya kujulikana na watu mbalimbali kitu ambacho alikuwa akikihitaji sana kukipata katika maisha yake. Ujio wa Yusufu pamoja na Kelvin tayari ukamfanya kuona kwamba kile ambacho alikuwa akikitaka kilikuwa kinakwenda kukamilika, kwani kwa wakati huo alikuwa na uhitaji mkubwa wa kumfadhili Yusufu pamoja na kuongea nae kitu kingine ambacho kilikuwa nje ya muziki.
“Karibuni” Papaa Pipo aliwakaribisha nyumbani kwake.
Kelvin ndiye ambaye alikuwa akiongea huku Yusufu akiwa kimya kusikiliza. Papaa Pipo alikuwa kimya akimsikiliza Kelvin ambaye alizungumzia hatua nyingi walizozipitia mpaka Yusufu au The Ruler kufikia hatua hiyo.
“Mmejitahidi sana” Pipo aliwaambia huku akipiga makofi ya chini.
“Asante sana” Wote walijibu kwa pamoja.
“Kwa hiyo unataka kuwa maarufu zaidi ya hapo?” Pipo alimuuliza Yusufu huku akimwangalia usoni.
“Ndio bosi”
“Na unataka kuwa tajiri mkubwa kupitia muziki?” Papaa Pipo alimuuliza.
“Ndio bosi”
“Hakuna shida. Nakuahidi utakuwa na umaarufu mkubwa sana hapa Tanzania, au labda tuseme Afrika nzima. Kila mtu atakutambua wewe ni nani, muziki wako utapendwa na kila mtu. Utapata mashabiki wengi na hata wale wengine ambao haukuwa ukiwatarajia” Papaa Pipo alimwambia Yusufu maneno ambayo yalionekana kuwafurahisha kupita kawaida.
“Unasema kweli bosi?” Yusufu aliuliza huku akionekana kutokuamini.
“Niamini. Wewe nitakufadhili zaidi ya ninavyowafadhili wasanii wengine. Umenifurahisha sana kuanzisha uhasama na The King” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
“Nimekufurahisha! Kivipi tena?”
“Yule mtoto anajidai sana, yaani kupata vijisenti vinamfanya hadi kunisahau kabisa. Anatoa nyimbo nyingine wala jina langu silisikii. Bora umekuja ili tumpindue” Papaa Pipo alimwambia Yusufu ambaye alionekana kufurahia kupita kawaida.
Huo ndio ukawa mwanzo wa urafiki kati ya Yusufu na Papaa Pipo, katika kila wimbo ambao alikuwa akiutoa Yusufu, jina la Papaa Pipo lilikuwa likisikika hali ambayo ilikuwa ikimfurahisha sana bosi huyo. Wala haukupita muda mrefu, Papaa Pipo akamnunulia Yusufu gari aina ya X Trail kwa ajili ya kufanyia mizunguko yake huku akimjazia mafuta kila wiki.
Maisha yakaonekana kubadilika kwa Yusufu, hapo ndipo alipoamua kuhamia Sinza, katika nyumba kubwa na nzuri huku gharama za upangaji wa nyumba ile ukiwa chini ya Papaa Pipo. Jina la Papaa Pipo likazidi kujulikana zaidi na zaidi, Yusufu alijitahidi kwa nguvu zote kulipaisha jina hilo kiasi ambacho hata wale ambao hawakuwa wakimfahamu mtu huyo wakawa na kiu ya kutaka kumfahamu.
“Hivi ndivyo ninavyotaka iwe. Hapo ndipo tunakwenda sawa” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
Siku zikaendelea kwenda mbele zaidi, jina la The King bado lilikuwa likiendelea kuwa juu zaidi ya Yusufu ambaye alikuwa akitumia jina la kisanii la The Ruler. Mashabiki wengi walikuwa wakitamani sana kumsikiliza The King zaidi ya The Ruler ambaye kwao alionekana kuwa kama mtu ambaye alikuwa akitamani sana sifa za kutaka kujulikana zaidi ya msanii nguri, The King.
Kila siku Papaa Pipo alionekana kuwa na kiu ya kumwambia Yusufu afanye kitu kimoja, kitu ambacho aliamini kwamba kingemfanya kuwa juu zaidi ya pale alipokuwa kwa kipindi kile. Papaa Pipo hakuonekana kuwa muwazi kumwambia Yusufu kitu kile japokuwa moyo wake ulitamani sana kumwambia akifanye kitu kile haraka iwezekanavyo.
“Kuna kitu nitataka uje nyumbani tuongee” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
“Kitu gani Bosi?” Yusufu aliuliza.
“Wewe njoo tu. Tutaongea kuanzia mwanzo hadi mwisho. Tutakapomaliza, nadhani utakuwa umenielewa zaidi” Papaa Pipo alimwambia Yusufu kwa kutumia njia ya simu.
“Sawa. Nitakuja mchana”
“Hapana. Mchana sitokuwepo nyumbani, njoo usiku kama saa mbili hivi” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
“Sawa. Nitakuja tu”
“Ok! Ila naomba uje peke yako. Hapa ninamaanisha kwamba hata Kelvin asijue kitu chochote kile” Papaa Pipo alimwambia Yusufu maneno ambayo kwa kiasi fulani yalionekana kumshtua.
“Kwa nini tena nisije nae bosi?”
“Hii ni kwa ajili yako tu. Kama nae angekuwa mwanamuziki ningekwambia uje nae” Papaa Pipo alimwambia Yusufu ambaye alionekana kuelewa.
Saa 2: 20 usiku gari aina ya X Trail alilokuwa akilimiliki Yusufu lilikuwa likiingia katika jumba la kifahari la Papaa Pipo. Gari liliposimama, Yusufu akateremka na kisha kuufunga mlango wa gari lile. Akaanza kupiga hatua kuelekea ndani ya jumba hilo na kisha kukaribishwa na Papaa Pipo ambaye alikuwa akiishi peke yake bila mtu yeyote zaidi ya mfanyakazi wake wa getini.
Ujio ule ukaonekana kumfurahisha sana Papaa Pipo, muda wa wote walikuwa wakiongea kwa furaha kana kwamba walikuwa wameahidiwa kupewa kitu kimoja kikubwa ambacho kingewafanya kuwa matajiri milele. Muda mwingi Papaa Pipo alikuwa akimsifia Yusufu kwa kile ambacho alikuwa amekifanya cha kuwa na ugomvi na The King ambaye alikuwa akijiona kuwa juu zaidi yake.
Walitumia masaa mawili kula na kunywa na ndipo hapo ambapo Papaa Pipo akamtaka Yusufu kumsindikiza sehemu fulani ambako Yusufu wala hakupafahamu. Usafiri ambao ulikuwa ukitumika lilikuwa ni gari la Papaa Pipo ambaye aliushikiria usukani na kuanza kuelekea huko ambako alitaka waelekee kwa wakati huo.
Safari hiyo ilitumia zaidi ya dakika ishirini, wakawa wamekwishafika katika eneo ambalo Yusufu alikuwa akilifahamu sana, lilikuwa eneo la Msasani. Katika kipindi hicho Yusufu alikuwa akishangaa sana. Kwa nyakati za mchana ambazo alikuwa akipita sana mahali hapo, sehemu ile ambayo ilikuwa na nyumba wala hakukuwa na nyumba yoyote ile, ila kwa wakati ule kulikuwa na jumba kubwa na la kifahari jambo ambalo lilioekana kumtia wasiwasi moyoni.
Baada ya kuliegesha gari wote wakateremka na kuanza kuelekea ndani huku Yusufu akionekana kuwa na wasiwasi mwingi. Kitu ambacho alikuwa akikiona mahali hapo hakuwa akikiamini kabisa. Maswali mfululizo yalikuwa yakimiminika kichwani mwake kwamba ni muda gani ulitumika kuijenga nyumba ile na wakati si muda mrefu sana eneo lile lilikuwa na kiwanja tu
“Mbona una wasiwasi?” Papaa Pipo alimuuliza Yusufu.
“Hili jumba. Linaonekana kuwa la kifahari sana, inaelekea linamilikiwa na mtu mwenye fedha nyingi sana” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.
“Yeah! Mmiliki wa jumba hili ana fedha sana hata zaidi yangu” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
“Hivi amelitengeneza jumba hili kwa siku ngapi?” Yusufu aliendelea kuuliza.
“Kwa nini unauliza hivyo?”
“Wiki iliyopita nilipita hapa wakati naelekea kwenye ukumbi wa Bosnia ila mahali hapa hakukuwa na nyumba zaidi ya kiwanja. Nashangaa leo tunakuja tunakuta nyumba. Ujenzi wake unaonekana kwenda haraka haraka sana” Yusufu alimwambia Papaa Pipo ambaye alikuwa kimya tu.
“Utafahamu kila kitu. Subiri kwanza” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
Mara baada ya kuingia ndani ya jumba lile, wakakaa kwenye makochi ya kifahari. Wala hazikupita dakika nyingi, mwanaume mmoja ambaye alikuwa na ndevu nyingi akatokea mahali hapo. Huku akionekana kuwa na furaha. Papaa Pipo akasimama na kuanza kumsalimia mwanaume yule kwa kutumia salamu ambazo wala hazikuwa zikieleweka kabisa machoni mwa Yusufu.
“Naona umekuja na kijana mtumishi mpya. Hongera sana” Mwanaume yule ambaye alitambulishwa kwa jina la Onyango alimwambia Papaa Pipo.
“Ndio. Nadhani huyu atakuwa mwenzetu bila shaka” Papaa Pipo alimwambia mzee Onyango.
Yusufu alikuwa kimya akiwasikiliza huku muda mwingi akimwangalia mzee Onyango ambaye alikuwa akionekana kuwa na uso uliojaa tabasamu pana. Kwa wakati huo, Yusufu akaanza kujiona kuwa katika hali ya tofauti sana, hamu ya kutaka kupata umaarufu pamoja na utajiri ikaanza kumshika kwa nguvu moyoni mwake. Kiu ya kuvitamani vitu vile ikaanza kumkaba zaidi na zaidi jambo ambalo lilionekana kumshangaza hata yeye mwenyewe.
“Mwambie mzee Onyango vitu unavyovitaka nae atakupa” Papaa Pipo alimwambia Yusufu ambaye alionekana kutokuielewa kauli ile.
“Vitu gani?”
“Wewe uliniambia unataka nini?”
“Sikumbuki”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nakumbuka uliniambia unataka kuwa maarufu zaidi” Papaa Pipo alimwambia Yusufu maneno yaliyomfanya Yusufu kukumbuka zaidi.
“Ndio”
“Aya sasa mwambie mzee Onyango kila kitu unachokitaka” Papaa Pipo alimwambia Yusufu ambaye akayapeleka macho yake usoni mwa mzee Onyango.
“Nataka kuwa na mvuto wa kupendwa kwa mashabiki wote wa muziki ambao watazisikiliza nyimbo zangu. Ninataka kuwa na utajiri mkubwa katika maisha yangu. Ninataka niwe na hofu kubwa sana kiasi ambacho kwa mtu yeyote ambaye atataka kunifanyia ubaya wowote basi aniogope” Yusufu alimwambia mzee Onyango.
“Ni hayo tu?” Mzee Onyango aliuliza.
“Ndio” Yusufu alijibu.
“Kuna moja umelisahau Yusufu” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
“Lipi?”
“Vipi kuhusu mambo yetu yale?”
“Ok! Umenikumbusha. Pia ninataka kupendwa na kila msichana ambaye ananifahamu. Yaani nisipate shida sana kwa msichana yeyote. Niwe na mvuto kwa kila msichana” Yusufu alimwambia mzee Onyango.
“Ni hayo tu?”
“Ndio”
Mzee Onyango akasimama na kisha kuelekea chumbani kwake, aliporudi, alirudi na kioo kikubwa mahali hapo na kisha kukiegemeza ukutani. Akaondoka tena sebuleni hapo na kisha kurudi chumbani tena, aliporudi alirudi na nguo kubwa kama shuka tatu zilizokuwa na rangi nyekundu.
Nguo moja akampatia Yusufu, akaivaa na kisha nguo nyingine kupewa Papaa Pipo ambaye nae akaivaa na nyingine kuivaa yeye mwenyewe. Kitu ambacho kilitakiwa kufanyika mahali hapo kilikuwa ni kimoja tu, kuingia katika kile kioo kikubwa na kutokea katika upande mwingine huku taa zikiwa zimezimwa.
“Itawezekana kweli?” Yusufu alijiuliza moyoni.
Papaa Pipo akaanza kupiga hatua na kukisogelea kioo kile, alipokifikia, akaingia. Mianga kama ya radi ikaanza kumulika katika kioo kile, hofu ikamjaa Yusufu, akaanza kutetemeka kupita kawaida.
Mtu wa pili kuingia ilikuwa zamu yake. Akaanza kupiga hatua kukisogelea kioo kile na kisha kuhisi akivutwa na kuingia ndani ya kioo kile. Upande wa pili ambao alitokea ulikuwa upande mwingine kabisa ambao ulionekana kuwa tofauti na ulimwengu wa kawaida. Macho yake yakatua kwa watu wengi na wa aina mbalimbali ambao walikuwa wakionekana kuwa katika maumbo mengi ya ajabu ajabu.
Yusufu alionekana kuhofia, mwili ulikuwa ukimtetemeka kupita kawaida. Mzee Onyango akatokea mahali hapo na kisha wote watatu kuanza kuelekea sehemu fulani ambayo ilikuwa na giza nene na kisha kuingia ndani ya lile giza.
Kitu cha ajabu ambacho kilionekana kumshangaza Yusufu mara baada ya kuingia ndani ya giza lile ni uwepo wa mwanga mkali ambao wala hakuuelewa ulitoka wapi. Mbele yao kulionekana kuwa na nyumba ambayo wakaanza kuisogelea na kisha kuingia. Kama zilivyokuwa nyumba nyingine nyingi ndivyo ilivyokuwa nyumba ile. Kulikuwa na makochi, televisheni pamoja na meza moja kubwa ambayo ilikuwa imezungukwa na viti vingi.
Mzee Onyango na Papaa Pipo wakaanza kuisogelea meza ile, walipoifikia, wakakaa katika viti vile. Wala hazikupita sekunde nyingi mzee mmoja ambaye alikuwa na kwato za ng’ombe pamoja na mapembe akatokea mahali hapo. Yusufu alikuwa akitetemeka kwa hofu, hapo hapo akatakiwa kusogea katika meza ile na kukaa.
Mzee yule ambaye alikuwa na umbo la kutisha akaondoka mahali hapo na kuelekea ndani, aliporudi, alikuwa na karatasi nyeupe mkononi mwake pamoja na kalamu ambayo ilikuwa na mrija ambao wala haukuwa na wino na kisha kuviweka mezani pale. Kila kitu ambacho kilikuwa kiiendelea mahali pale kilikuwa kikimtisha Yusufu kiasi ambacho wakati mwingine alifikiri kwamba alikuwa katika ndoto moja ya mbaya na ya kutisha sana.
Alichokifanya yule mzee wa kutisha ni kutoa sindano na kisha kumtaka Yusufu kuuweka mkono wake juu ya meza na kisha yule mzee kumchoma mkononi kwenye moja ya mshipa wa damu na kisha kutoa damu ambayo akaiweka katika mrija ule wa kalamu ambayo alikuwa ameishika na kisha kumgawia Yusufu.
“Kila ulichoomba utakipata tu endapo utaandika maagano yetu pamoja nawe katika karatasi hiyo” Mzee Onyango alimwambia Yusufu ambaye alikuwa akitetemeka.
“Andika mahitaji yako huku ukiwa umekubali kuutumikia ulimwengu huu” Mzee Onyango alimwambia Yusufu ambaye bila tatizo lolote akaanza kuandika mahitaji yake kwa kutumia kalamu ile iliyokuwa na wino ambayo ilikuwa ni damu yake. Alipomaliza, akamgawia karatasi ile mzee yule wa kutisha.
“Umeiuza nafsi yako katika ulimwengu huu. Na kama umeiuza, kamwe hautoweza kuipata mpaka pale utakapokufa. Sisi tutakuwa pamoja nawe, tutakulinda kila uendapo, ulinzi wetu utakuwa pamoja nawe. Afya ya mwili wako itakuwa bora, hakutokuwa na ugonjwa wowote ambao utakuwa ukikusumbua katika maisha yako yote. Sadaka ya kafara itakapotakiwa, utatakiwa kuitoa muda muafaka, kamwe hakutokuwa na mtu yeyote ambaye atakuyumbisha, utakuwa imara kadri siku zitakavyokuwa zinakwenda mbele na ndivyo ambavyo umaarufu wako utazidi kuongezeka zaidi na zaidi, utakuwa na fedha nyingi katika maisha yako kuliko msanii yeyote yule hapa Afrika” Mzee yule wa kutisha alimwambia Yusufu na kuendelea.
“Kwa sasa tutakupa masharti mawili tu. Utatakiwa kuoa muda wowote ule upendao ila kamwe hautotakiwa kuwa na mtoto. Siku yoyote ambayo msichana wako au mke wako atakuwa katika siku za kupata mtoto, hautotakiwa kufanya nae mapenzi. Sharti la pili, hautakiwi kufanya mapenzi katika siku ya Jumapili na Jumatano. Kama kufanya mapenzi basi utatakiwa kufanya mapenzi katika siku nyingine lakini si ndani ya siku hizo mbili ambazo tumezitenga. Kama itatokea siku kuvunja masharti yetu, tutakuadhibu ila kama hautoikubali adhabu yetu, basi hatutokuwa na kizuizi cha kukuua” Mzee yule alimwambia Yusufu.
“Nimekubaliana nawe” Yusufu alimwambia mzee yule huku ile hofu ambayo alikuwa nayo katika kipindi cha nyuma ikionekana kuanza kupotea.
“Mnaweza kwenda. Siku za ibada zitakapofika, mnatakiwa kuja nae katika nyumba ya ibada mpaka pale atakapozoea” Mzee yule aliwaambia mzee Onyango na Papaa Pipo.
“Sawa” Wote waliitikia na kisha kuondoka mahali hapo huku Yusufu akiwa amejiunga na kundi hilo ambalo lilionekana kuwa na nguvu za kumpatia utajiri pamoja na umaarufu mkubwa ambao alikuwa akiutaka.
****
Usiku ulionekana kuwa mrefu kwa Kelvin, muda wote alikuwa akimsubiria Yusufu lakini hakuweza kurudi nyumbani. Dakika ziliendelea kusogea huku masaa yakizidi kukatika zaidi na zaidi lakini hali bado ilikuwa ile ile, Yusufu hakurudi nyumbani. Kelvin akashindwa kuvumilia, mara kwa mara alikuwa akimpigia simu lakini simu haikuwa ikipokelewa, ilikuwa ikiita mpaka kukata.
Hali ile ilionekana kumshangaza Kelvin, tayari wasiwasi ukaanza kumuingia kwa kuona labda Yusufu alikuwa amepata tatizo huko alipokuwa. Alichokifanya ni kuanza kuwapigia simu marafiki zao wa karibu lakini napo huko Yusufu hakuonekana. Alichokifanya Kelvin baada ya kuona sehemu zote muhimu alikuwa amemkosa Yusufu, hapo ndipo akaamua kumpigia simu Papaa Pipo.
Hakukuwa na utofauti na simu ya Yusufu, simu ya Papaa Pipo ilikuwa ikiita bila kupokelewa. Kelvin hakutaka kujiuliza zaidi, tayari akahisi kwamba Yusufu alikuwa pamoja na Papaa Pipo ambaye alikuwa mfadhili wake. Alichokifanya Kelvin ni kutoka nje na kisha kuelekea barabarani ambako akakodisha bajaji na kuelekea nyumbani kwa Papaa Pipo.
“Unataka nikupeleke wapi?” Dereva wa bajaji alimuuliza Kelvin huku tayari imekwishatimia saa nne usiku.
“Unasemaje?” Kelvin alimuuliza kana kwamba hakusikia swali lile aliloulizwa.
“Unataka nikupeleke wapi bosi wangu?” Dereva yule alimuuliza kwa mara ya pili.
“Naomba unipeleke Kijitonyama” Kelvin alimwambia dereva wa bajaji ambaye akawasha gari na kuanza kuelekea Kijitonyama alipokuwa akiishi Papaa Pipo.
Ndani ya gari, Kelvin hakutaka kukata tamaa, bado alikuwa akiendelea kumtafuta Yusufu simuni lakini bado majibu yalikuwa yale yale. Wasiwasi haukupungua kwa Kelvin, muda wote alikuwa akionekana kuwa na mashaka. Hakujua ni kwa sababu gani Yusufu alikuwa ameondoka nyumbani bila kumtaarifu ni sehemu gani alipokuwa amekwenda.
Hiyo ilikuwa imetokea kwa mara ya kwanza tangu walipoanza kuwa marafiki. Ukaribu wao ulikuwa mkubwa sana na ndio maana mpaka katika kipindi hicho Kelvin alikuwa akiendelea kushangaa. Huku akiwa kwenye lindi la mawazo kwa muda mrefu, dereva wa bajaji akamshtua.
“Tumefika Sayansi broo. Tuelekee wapi hapa?” Dereva wa bajaji alimuuliza.
“Twende kule kulipokuwa mtaa wa Hollwoody” Kelvin alimwambia dereva bajaji.
“Upo wapi huo mtaa?”
“Twende na barabara ile ya kwenda Tandale kwa Mtogole. Ukifika kule kulipokuwa na kanisa la Kilokole, kata kona kulia. Nyumba ya pili upande wa kulia” Kelvin alitoa maelekezo na dereva waa bajaji kufuata.
Kutoka Sayansi hadi katika mtaa wa Hollwoody wala hakukuwa mbali sana, ni ndani ya dakika moja wakawa wamekwishafika katika nyumba ya Papaa Pipo na kisha Kelvin kuteremkana kuanza kugonga geti. Mara baada ya kujitambulisha kwa mlinzi, geti likafunguliwa na Kelvin kuingia ndani huku dereva wa bajaji akiwa nje akimsubiria.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nimejua tu kama atakuwa hapa” Kelvin alijisemea mara baada ya kuliona gari la Kelvin sehemu ya maegesho.
“Karibu Kelvin” Mlinzi alimkaribisha.
“Asante sana. Wapo ndani?” Kelvin aliuliza.
“Wametoka”
“Wametoka? Mbona ameacha gari lake hapa?”
“Bado sijajua. Ila wametumia gari ya bosi mwenyewe” Mlinzi alimwambia Kelvin.
“Ameondoka na Papaa mwenyewe au?”
“Ndio. Ila wamesema hawatokawia kurudi. Ingia ndani uwasubirie” Mlinzi alimwambia Kelvin ambaye kabla ya kuingia ndani, akamtoka nje ya eneo la nyumba ile na kisha kumlipa dereva wa bajaji kiasi cha fedha ambacho alikuwa akikihitaji.
Kelvin akaelekea ndani na kutulia sebuleni huku akiangalia televisheni. Muda ulikuwa ukizidi kwenda zaidi na zaidi lakini si Yusufu wala Papaa Pipo ambaye alitokea mahali hapo. Ilipoingia saa sita usiku, mlio wa gari ukasikika nje na honi kupigwa. Kelevin akainuka na kuelekea dirishani na kisha kuchungulia, gari la Papaa Pipo aina ya Prado lilikuwa likiingia ndani ya geti lile na Kelvin kurudi kitini na kutulia.
Haikuchukua muda mrefu, Papaa Pipo na Yusufu wakaingia ndani, macho yao yakagongana na macho ya Kelvin ambaye alikuwa sebuleni pale. Kila mmoja alionekana kushangaa lakini hawakutaka kuonyesha waziwazi mishangao yao, walichokifanya wakaanza kusalimiana na Kelvin. Hawakutaka kukaa sana, kilichofuata ni kuaga na kuondoka huku Yusufu akionekana kuwa mwenye furaha tele.
“Vipi tena Yusufu? Mlikuwa wapi?” Kelvin alimuuliza katika kipindi ambacho walikuwa garini wakirudi nyumbani.
“Si unajua Papaa alivyokuwa mtu wa wanawake. Alinipeleka kwa mademu zake kupata nao kinywaji na kunitambulisha kwa watu wake” Yusufu alimdanganya Kelvin.
“Sasa mbona uliniacha? Au haukutaka nami niende kuwaona hao mademu?” Kelvin aliuliza.
“Aliniambia niende mimi tu na ndio maana alitaka hata gari langu niliache kwake” Yusufu alidanganya.
Hawakutumia muda mrefu wakawa wamekwishafika nyumbani huku ikiwa ni saa saba na na robo usiku. Hawakuwa na kitu kingine zaidi ya kujitupa kitandani tayari kwa kulala. Usiku huo ulionekana kuwa mrefu kwa Yusufu, kichwa kwa wakati huo alikuwa akifikiria fedha tu. Tayari alikuwa na uhakika kwamba hata umaarufu mkubwa ambao alikuwa akiutamani sana ungeweza kuwa kwake.
Akajaribu kuvuta picha kama tu angefanikiwa kuwa kama vile alivyoandika katika karatasi ya mkataba wa damu. Akashindwa kuelewa angepata umaarufu na mvuto wa aina gani. Kiasi fulani alitamani kumwambia Kelvin lakini akaamua kunyamaza kwani aliona kama angemwambia basi lingeweza kuwa kosa kubwa ambalo angeweza kulijutia hata baadae.
Ingawa katika kipindi hicho alikuwa ametumia kiasi kikubwa kupanga nyumba nzima ambayo ilikuwa hapo Sinza ndani ya jiji la Dar es Salaam lakini kwa wakati huo tayari alikuwa amekwishaona kwamba kulikuwa na uhitaji mkubwa wa kununua nyumba tena katika maeneo mazuri ambayo yangemfanya kutuliza akili yake kutokana na maisha ya dhiki ambayo alikuwa amekulia.
Mpaka muda huo tayari alikuwa akijiona kuwa tajiri japokuwa hakukuwa na dalili zozote ambazo zilikuwa zimekwishajionyesha katika maisha yake. Alikuwa akijiona kwamba tayari amekwishakuwa na umaarufu mkubwa ambao ulimfanya kumuingizia fedha nyingi na kupiga shoo kwa kiasi kikubwa cha fedha.
Kwa wakati huo hakuacha kumfikiria The King ambaye alionekana kuwa adui yake namba moja duniani. Alijua fika kwamba katika kipindi hicho msanii huyo ndiye ambaye alikuwa akivuma sana Tanzania na ndiye ambaye alikuwa na mashabiki wengi sana. Kwa wakati huo, tayari Yusufu akajiona kuvaa magwanda kwa ajili ya kuingia vitani kupigana na The King ambaye kila siku alikuwa akitamba kwamba uwezo wake haukuweza kulinganishwa na msanii yeyote Tanzania.
“Ngoja kila kitu kikamilike. Nitahakikisha namuacha mbali kimafanikio” Yusufu aliwaza na muda mfupi baadae akapitiwa na usingizi huku ikiwa imetimia saa tisa usiku.
Simu ilikuwa ikipiga kelele kuashiria kwamba kuna mtu ambaye alikuwa akimpigia kwa wakati huo. Simu ile ilikuwa ikiendelea kuita zaidi na zaidi hali ambayo ilimshtua Yusufu kutoka usingizini na kisha kuupeleka mkono wake pembeni mwa kitanda na kisha kuichukua simu ile. Huku macho yake yakiwa mazito na huku akiwa amefumbua jicho moja, akaanza kuangalia namba ya mpigaji ambaye alikuwa amempigia simu asubuhi hiyo ya saa kumi na mbili.
Namba ilikuwa ngeni machoni mwake, kichwa chake kikaanza kujiuliza maswali mengi kuhusiana na namba ile ambayo ilikuwa ikiingia kwa wakati ule kama alikuwa amekwishawahi kuiona sehemu yoyote ile lakini hakuweza kukumbuka kitu chochote kile. Akabonyeza kitufe cha kijani na kisha kuipeleka simu ile sikioni.
“Halllooow” Yusufu aliita kwa sauti nzito iliyojaa uchovu.
“Mambo vipi The Ruler!” Sauti ya upande wa pili ilisikika.
“Poa. Naongea na nani?” Yusufu aliuliza.
“Unaongea na Dj Mimi hapa wa Peackok Fm” Sauti ya upande wa pili ilijibu.
Yusufu akaonekana kushtuka, hakuamini kile ambacho alikuwa amekisikia. Maswali kibao yakaanza kumiminika kichwani mwake, hakutaka kuamini kama kile ambacho kilikuwa kikiendelea kilikuwa uhalisia au ndoto moja ambayo ilikuwa imemjia kwa lengo la kumletea furaha ya muda mchache.
“Wewe nani na kutoka wapi?” Yusufu aliuliza maswali mawili mfululizo huku akionekana kutokuamini masikio yake.
“Dj Mimi hapa wa Peackok Fm” Sauti ile ilijibu.
“Nikusaidie nini tena? Mbona asubuhi asubuhi sana?” Yusufu aliuliza huku bado macho yake yakiwa mazito kutokana na usingizi ambao bado alikuwa nao.
“Tunataka uje tufanye interview na wewe leo asubuhi ya saa nne” Sauti ya Dj Mimi ilisikika.
“Nije kufanya interview na wewe. Dj wa Peackok Fm?” Kelvin aliuliza huku akionekana kutokuamini.
“Ndio”
“Hicho ni kitu kisichowezekana” Yusufu alisema na kisha kukata simu na kuizima kabisa.
Yusufu akabaki kimya kwa muda, hakuamini kile ambacho kilikuwa kimetokea, tayari mafanikio yakaanza kuonekana. Mkataba wa damu ambao alikuwa ameuandika kuzimu ukaonekana kuanza kufanya kazi yake. Yusufu akatamani kuruka ruka kwa furaha, tayari mafanikio makubwa yakaanza kuonekana kwake.
Hakutaka kupoteza muda wake kujiuliza zaidi juu ya nini kilichokuwa kinaendelea, tayari alikwishaona mkataba wa damu tayari ulikuwa umeanza kufanya kazi yake. Alichokifanya ni kulala tu huku kila wakati uso wake ukionekana kuwa na furaha.
Saa tano na nusu asubuhi Yusufu akaamka kutoka usingizini. Kitu cha kwanza alichokifanya ni kuwasha simu yake. Meseji zaidi ya nane zilikuwa zimetumwa kutoka kwa madj tofauti tofauti wa redio ya Peackok Fmambao walikuwa wakimtaka awasamehe, wakae mezani na kisha kuelewana. Yusufu alibaki akiziangalia meseji zile, akaanza kucheka kwa sauti kitu ambacho kilimfanya Kelvin aliyekuwa sebuleni kumfuata chumbani.
“Kuna nini tena?” Kelvin aliuliza huku akimwangalia Yusufu.
“Hebu soma meseji za hawa wapumbavu” Yusufu alimwambia Kelvin huku akimpa simu.
“Wapumbavu gani?”
“Peackok Fm”
Kelvin akaichukua simu ile na kisha kuanza kuzisoma meseji zile. Kelvin akabaki akishangaa, hakuamini kile ambacho alikuwa anakiona kwa wakati ule. Kituo cha redio kile kile ambacho kilikuwa kimetangaza kutokupiga nyimbo za Yusufu au The Ruler ndicho ambacho leo hii walikuwa wametuma meseji mbalimbali za kumuomba Yusufu msamaha. Kelvin akashindwa kusimama, akaamua kukaa kitandani.
“Hili shavu Yusufu. Kubali yaishe” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Si kirahisi kama unavyolichukulia jambo hili. Kama walitangaza kwamba hawatopiga wimbo wangu wowote basi watangaze wao wenyewe kwamba walinikosea” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Hii ndio nafasi Yusufu. Usiidharau. Hapa ndipo pa kujitangaza” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Usitake nionyeshe udhaifu. Unajua mimi ni msanii mkubwa sana ambaye siwezi kubabaishwa na wao hata mara moja” Yusufu alimwambia Kelvin ambaye alibaki akimshangaa tu.
“Huo usanii ukubwa bado haujafika Yusufu. Nenda kawasikilize bwana”
“Hapana siendi mpaka watangaze kwamba walinikosea”
“Unafikiri wataweza kufanya hivyo?”
“Kwa nini wasiweze? Kama wameweza kuniomba msamaha unafikiri watashindwa kufanya hivyo? Lazima wafanye. Jina langu linakwenda kuwa kubwa sana” Yusufu alimwambia Kelvin.
Yusufu hakutaka kuonyesha udhaifu, tayari alikwishajua kwamba kila kitu kilikuwa kimeanza kukaa sawa. Tayari alikwishaanza kuyaona mambo yake yakianza kukaa sawa. Hapo aliposimamia ndipo alipotaka kusimamia zaidi, asingeweza kufanya kitu chochote mpaka pale kituo kile cha redio cha Peackok kimuombe msamaha kwa kile walichokifanya.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Yusufu hakutaka kukaa kimya, alichokifanya ni kumpigia simu Papaa Pipo na kuanza kumuelezea kile ambacho kilikuwa kimetokea. Papaa Pipo hakuonekana kushangaa kwani tayari alikuwa amekwishaona kwamba kitu kama kile ni lazima kitatokea tu kutokana na ule mkataba ambao alikuwa ameuandika kuzimu.
“Mbona kuna wengi watakuja tu. Huo ni mwanzo tu. Karibu katika ulimwengu huu mpya. Ulimwengu wa umaarufu uliojaa mvuto na utajiri” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
“Nimekwishakaribia” Yusufu aliitikia huku akionekana kuwa na furaha.
Saa sita na nusu mchana simu yake ilikuwa ikiita. Akaichukua kutoka mfukoni na kisha kuanza kuangalia namba ya mpigaji, namba ilikuwa ngeni. Tayari alikuwa na uhakika kwamba mpigaji wa simu ile alikuwa mmoja wa madj waliokuwa wakifanya kazi katika kituo cha redio cha Peackok Fm. Bila kuchelewa, Yusufu akabonyeza kitufe cha kijani na kisha kuipeleka simu sikioni.
“Mambo vipi Yusufu!” Sauti ya upande wa pili ilimsalimia.
“Poa. Naongea na nani?” Yusufu aliuliza.
“Mkurugenzi wa Peackok Fm hapa, Bwana Stambuli” Sauti ya upande wa pili iliskika.
“Nikusaidie nini?” Yusufu aliuliza.
“Unaweza kuja ofisini mara moja?”
“Hapana. Siwezi. Niko bize sana” Yusufu alimwambia.
“Muda gani ubize wako utakwisha?”
“Labda mwezi ujao” Yusufu alijibu kijeuri.
“Mwezi ujao?”
“Ndio”
“Tunakuomba mara moja. Kuna kitu tunataka tukiweke sawa mara moja” Bwana Stambuli alimwambia Yusufu.
“Kuna fedha nije?” Yusufu aliuliza.
“Kama unahitaji fedha. Tutakupatia. Unahitaji kiasi gani mpaka wewe kufika hapa ofisini?” Bwana Stambuli alimuuliza.
“Milioni moja na nusu”
“Hapana bwana. Ni kiasi kikubwa cha fedha hicho Yusufu”
“Kama hakipo, pangeni foleni. Kuna watu waliotoa fedha zao ambao nahitaji kuonana nao sasa hivi” Yusufu alimwambia Bwana Stambuli huku sauti yake ikisikika kuwa na jeuri.
“Sawa. Tutakulipa, wewe njoo tu” Bwana Stambuli alimwambia Yusufu.
“Sawa. Nitakuja”
“Saa ngapi?”
“Nitakapojisikia” Yusufu alijibu na kukata simu huku akiizima.
****
Mkurugenzi wa Peackok Fm, Bwana Stambuli alionekana kukasirika kupita kawaida kutokana na mambo ambayo yalikuwa yameendelea katika kipindi cha nyuma. Kitendo cha Yusufu au The Ruler kutokupigiwa nyimbo zake katika kituo hicho redio kilionekana kumkasirisha kupita kawaida. Madj walikuwa wakiingia kwa zamu ndani ya ofisi yake na kisha baada ya masaa kadhaa kuhitisha kikao cha dharura cha wafanyakazi wa kituo hicho cha redio.
Bwana Stambuli alionekana kuwa mwenye hasira sana, siku hiyo alionekana kuwa tofauti kabisa na siku nyingine. Alimwangalia kila mtu katika kikao kile, hasira kali ilikuwa imemkaba kooni. Kila mfanyakazi alionekana kutetemeka kwa hofu, haikuwahi kutokea siku ambayo mkurugenzi wao alikuwa na hasira kali kama alivyokuwa siku hiyo.
“Kuna watu nawafukuza kazi leo” Bwana Stambuli aliwaambia na kisha kuinuka kitini.
Akaanza kuzunguka zunguka ndani ya chumba kile kidogo cha mkutano. Tayari alionekana kuwa kama mtu ambaye alikuwa amechanganyikiwa. Kila alipokuwa akiwaangalia wafanyakazi wake ndivyo ambavyo hasira yake ilivyozidi kuongezeka zaidi na zaidi. Alipoona kwamba ameridhika kuzungukazunguka ndani ya chumbani kile cha mkutano, akarudi kitini na kuanza kuwaangalia wafanyakazi kwa zamu.
“Ni nani alitangaza kwamba kituo hiki kisingepiga wimbo wowote wa msanii The Ruler?” Hilo lilikuwa swali la kwanza ambalo liliulizwa na Bwana Stambuli huku akionekana kuwa na hasira kali. Hata kabla jibu halijatolewa, wafanyakazi wote wakaanza kuangaliana kwa zamu.
Kila mmoja alionekana kuwa na wasiwasi katika kipindi hicho, uso wa Bwana Stambuli haukuonyesha masihala hata mara moja, alionekana kukasirika sana. Hakukuwa na mtu ambaye alijibu chochote kile, wote walibaki kimya huku wakiangaliana tu. Bwana Stambuli alibaki kimya huku akiwaangalia katika staili ambayo ilimuonyesha kwamba alikuwa akitaka kusikia jibu.
“Kwa hiyo alijikataza yeye mwenyewe kupigiwa nyimbo zake?” Bwana Stambuli aliuliza mara baada ya kuona ukimya ukiwa umetawala.
“Hapana” Michael alijibu.
“Kumbe nani alifanya hivi?”
“Dj Thumb” Michael alijibu hali iliyomfanya Bwana Stambuli kumgeukia Dj Thumb ambaye alionekana kuwa na wasiwasi.
“Kwa nini uliamua kufanya uamuzi huu? Hii ni kwa sababu wewe ni mmiliki wa kituo hiki cha redio au kwa sababu unajiona kuwa na mamlaka zaidi yangu?” Bwana Stambuli alimuuliza Dj Thumb.
“Naomba unisamehe bosi”
“Ishu iliyokuwepo hapa sio kusameheana tena, yaani ninachotaka ni kusikia mengi kutoka kwako. Kipi kilichokufanya kutokutaka kupiga nyimbo za The Ruler? Chuki binafsi au?” Bwana Stambuli alimuuliza Dj Thumb ambaye alibaki kimya.
Siku hiyo haikuonekana kuwa siku ya amani kabisa, watu hawakutulia hata kidogo, hasira za Bwana Stambuli ziliwafanya wafanyakazi wote kuanza kuoneana aibu. Dj Thumb ndiye ambaye kwa wakati huo alitakiwa kumuita Yusufu au The Ruler kwa ajili ya kumuomba msamaha kwa kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea.
Kila alipokuwa akipigiwa simu, Yusufu alikuwa akileta mapozi, tayari alijiona kuanza kuwa na jina kubwa nchini Tanzania, kitendo alichokifanya cha kuiuza nafsi yake kuzimu ilionekana kumpa kiburi kupita kawaida.
*****
Yusufu hakutaka kuwa na haraka kwa kila kitu ambacho alitakiwa kukifanya kwa kipindi hicho, siku hiyo alikuwa amekaa chumbani kwake huku akisikiliza redio tu. Nyimbo zake ndizo ambazo zilikuwa zikipigwa mara nyingi kutoka katika redio tofauti tofauti ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam.
Muda wote Yusufu alionekana kuwa na furaha, hakutaka kujuta kwa kitendo chake cha kuiuza nafsi yake kuzimu bali kwa wakati huo alionekana kufurahi huku akiona kitendo alichokifanya kuwa sahihi kwa sababu alikuwa akitafuta sana utajiri pamoja na mvuto kwa mashabiki wa muziki wa kizazi kipya.
Kitu ambacho aliamua kukifanya Yusufu kwa wakati huo ni kuanza kutunga wimbo mwingine, wimbo ambao aliamini kwamba ungempa sana umaarufu na fedha za kutosha. Jambo la kutunga wimbo halikuwa jambo dogo kwa upande wake, ilimchukua zaidi ya wiki nzima na ndipo alipokuja kuukamilisha.
Baada ya kumaliza kila kitu, akaanza kuuchukulia mazoezi na kisha kuurekodi rasmi na kuuachia katika vituo vya redio. Hapo ndipo ambapo Yusufu alipokuja kuona kitu ambacho kilionekana kuwa kama muujiza. Wimbo wake ukaonekana kuwa lulu katika masikio ya watu, kila wakati watu mbalimbali walikuwa wakiuimba wimbo ule ambao ulionekana kuwavutia kupita kawaida.
Kila kona jina lake lilikuwa likisikika kitu ambacho kiliwafanya watu kuuchagua kuwa wimbo bora katika kipindi hicho. Yusufu akaanza kuitwa katika matamasha mbalimbali kufanya shoo jambo ambalo lilimfanya kujulikana zaidi na zaidi. Mashabiki wengi wakaonekana kuwa na mvuto kwa Yusufu, kuitwa kwake katika matamasha mbalimbali kukamuongezea umaarufu kupita kawaida.
Hiyo ikaonekana kuwa njia moja ya mafanikio ambayo alikuwa akiyataka. Vyombo vingi vya habari vikaanza kumtangaza jambo ambalo akaanza kuonekana kuwa msanii mkubwa ambaye hakuwahi kutokea nchini Tanzania. Katika kila shoo ambayo alikuwa akiifanya, watu wengi walikuwa wakihudhuria huku wakitaka kumuona msanii huyo ambaye alikuwa amekuja kwa kasi katika anga ya muziki wa kizazi kipya.
Hapo ndipo maisha ya starehe yalipoanza rasmi, kwa sababu jina lake lilikuwa kubwa, wasichana wengi wakatokea kumpenda, mara kwa mara alikuwa akipigiwa simu na wasichana wengi huku wakimtaka kimapenzi lakini Yusufu hakutaka kuwaelewa. Kwa wakati huo, utulivu wake ulikuwa katika muziki, hakutaka kabisa kuyapa mapenzi nafasi maishani mwake.
Ndani ya miezi miwili tu, Yusufu alikuwa akiingiza kiasi kikubwa cha fedha cha zaidi ya milioni kumi kwa kila shoo ambayo alikuwa akiifanya kwenye matamasha mbalimbali. Mafanikio yae yakaonekana kuwa makubwa kwa msanii kama yeye, kitu alichokifanya kwa wakati huo ni kununua gari la kifahari, Range na kisha kuanza kujenga nyumba maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Makampuni mengi nchini Tanzania yakaanza kufanya kazi pamoja nae kwa malipo makubwa ya fedha, matangazo ya bia, matangazo ya sigara, simu za mkononi pamoja na makampuni mengi yalikuwa yakifanya matangazo mengi ya kibiashara pamoja nae. Sura yake ikaonekana kuwa biashara kubwa, katika kila tangazo ambalo sura yake ilionekana, bidhaa hizo zilikuwa zikinunulika au kutumika sana.
Yusufu akafanikiwa kuliteka soko la muziki Tanzania, akaonekana kuwa mfano wa kuigwa kwa wasanii wengine. Kwa wakati huo Yusufu hakuwa akilala nyumbani kwake, muda mwingi alikuwa akishinda katika matamasha mbalimbali mikoani jambo ambalo lilimfanya kuwa bize kupita kawaida. Katika kila shoo ambayo alikuwa akienda, Kelvin alikuwa pamoja nae huku akisimama kuwa kama meneja wake.
Tayari maisha yao ambayo walikuwa wamepitia yakawa yamebadilika kabisa ndani ya miezi mitatu tu. Yusufu hakutaka kusubiri zaidi, alichokifanya ni kuwanunulia wazazi wake nyumba kubwa na ya kifahari mjini Bagamoyo pamoja na usafiri ambao wangekuwa wanautumia katika kufanya mizunguko yao ya hapa na pale.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mafanikio yale yalikuwa yamekuja kwa haraka sana katika hali ambayo ilimfanya hata yeye mwenyewe kushangaa kwani haikuwa kawaida sana hata kwa watu wengine ambao walikuwa wameuza nafsi zao kuzimu.
“Mbona mafanikio yamekuja haraka sana?” Yusufu alimuuliza Papaa Pipo simuni.
“Hata mimi mwenyewe nashangaa. Sikutarajia kama yangeanza kuonekana kwa haraka namna hii” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
“Mmmh! Unajua mpaka nimeshangaa”
“Yeah! Ia ninachohisi ni kwamba wakubwa wanataka uwatangaze. Unajua hapo bado hawajiaanza kufanya kazi pamoja nawe” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
“Bado hawajaanza kufanya kazi na mimi! Mbona nimeanza kufanikiwa sasa?” Yusufu aliuliza.
“Mafanikio wanakupa. Kitu ambacho utatakiwa kukifanya ni kuanza kuwatangaza kupitia mambo mbalimbali” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
“Kivipi?”
“Mambo mengi tu. Kwa sababu ushaanza kuhudhuria ibada, utaambiwa mambo mengi ya kufanya” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
“Sawa. Ngoja niendelee kula maisha”
“Kula kwa raha zako. Ila usivunje masharti. Si unakumbuka hilo?”
“Nakumbuka sana. Si wameniambia nisiwe na mtoto na nisifanye mapenzi katika siku ya Jumapili na Jumatano, nakumbuka sana”
“Kama unakumbuka, vizuri sana” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
Kadri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo jina la Yusufu kama The Ruler ndivyo lilivyozidi kuvuma zaidi na zaidi. Kila siku alikuwa alikuwa akikusanya fedha kupita kawaida, mafanikio makubwa ambayo alikuwa akiyapata katika kipindi hicho yalionekana kumshangaza kupita kawaida. Hakutaka kujiambia kuhusu madhara ambayo angeyapata baadae, kitu ambacho alikuwa akikifikiria kwa wakati huo ni kuendelea kuingiza fedha na kutumia alivyotaka.
Je nini kitaendelea?
Je nini kitaendelea katika maisha ya Yusufu?
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment