Search This Blog

Friday, 3 June 2022

NITAKAPOKUFA - 5

 





    Simulizi : Nitakapokufa

    Sehemu Ya Tano (5)



    Bara baada ya kumaliza kazi zake za siku mbili, Yusufu akaanza kuwasiliana na Manka na kisha kuanza kuongea nae. Muda huo, Yusufu alionekana kuwa mwingi wa furaha, hakuamini kama msichana ambaye alikuwa amemvutia kupita kawaida, Manka alikuwa akiongea nae katika kipindi hicho. Waliongea kwa muda mwingi sana huku kila mmoja akisikika kuwa na furaha na kisha kupanga kuonana.

    Kwa Manka ikaonekana kuwa kama tukio moja la ajabu na lenye furaha ambalo hakuwa amelitegemea katika maisha yake, hakuamini kabisa kama siku hiyo alikuwa akitakiwa kuwa meza moja pamoja na Yusufu, msanii mkubwa mwenye fedha ambaye alikuwa akiheshimika sana barani Afrika. Manka hakutaka kulaza damu, siku ambayo walipanga kuonana, alijitahidi kujipendezesha kuliko siku nyingine.

    Siku ya kuonana ikatimia, Manka akavaa mavazi yake mapya ambayo alikuwa ameyanunua kwa ajili ya siku hiyo ambayo kwake ikaonekana kuwa muhimu sana. Japokuwa katika kipindi cha nyuma alikuwa amejiapiza kutokutembea na supastaa yeyote yule lakini siku hiyo kiapo chake kikaonekana kuvunjwa, Yusufu akaonekana kuwa mwanaume wa ajabu ambaye alikuwa amejaa mvuto mkubwa kupita kiasi.

    Manka akalifuata gari lake ambalo alikuwa amenunuliwa na Anko na kisha kupanda na kuondoka mahali hapo. Muda wote ndani ya gari Manka alikuwa akionekana kuwa na furaha, hakuamini kama siku hiyo alikuwa njiani kwenda kumuona Yusufu, mwanaume ambaye alikuwa amevutiwa nae kupita kawaida. Baada ya dakika thelathini, Manka akalisimamisha gari lake katika hoteli ya La Vista Inn iliyokuwa Magomeni, hoteli ambayo Yusufu alikuwa akipenda sana kuitumia kwa ajili ya kulala na wasichana mbalimbali aliokuwa akitembea nao.

    Mara baada ya macho ya Manka kutua kwa Yusufu, mvuto wa Yusufu ukaongezeka zaidi machoni mwake, akamuona Yusufu kuwa mwanaume mzuri kuliko wanaume wote ambao aliwahi kukutana nao katika dunia hii. Wote wakaanza kusogeleana na kisha kukumbatiana kwa nguvu kiasi ambacho kilimshangaza hata Yusufu mwenyewe.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unanukia vizuri” Manka alimwambia Yusufu.

    “Hata wewe pia” Yusufu alimwambia Manka.

    Mwili wa Yusufu kwa wakati huo ulikuwa umekwishabadilika kabisa, kitendo cha kukumbatiana na Manka kiliufanya mwili wake kusisimka kimapenzi kupita kawaida. Akashindwa kujizuia, japokuwa alikuwa akihitaji kukaa na Manka tu mahali hapo na kunywa pamoja na kula lakini kwa hali ya mwili wake ilivyobadilika, akaamua kuchukua chumba kitendo ambacho wala hakikupingwa na Manka.

    Walipofika chumbani, Manka akajilaza kitandani. Yusufu akabaki akimwangalia Manka tu pale kitandani. Ni kweli kwamba mpaka katika kipindi hicho alikuwa amefanya ngono na wasichana wengi katika maisha yake lakini kwa Manka, alionekana kuwa msichana wa tofauti sana. Mvuto wa Manka ulikuwa mkubwa sana katika macho yake.

    Yusufu hakutaka kusubiri, alichokifanya ni kuanza kuzivua nguo zake huku Manka akiwa amebaki kitandani pale akitabasamu tu. Alipoona amemaliza kuzivua nguo zake, akamsogelea Manka na kisha kuanza kumvua nguo zile alizokuwa amezivaa. Kwa mara ya pili toka waonane, hawakuwa wameongea neno lolote la kuonyesha kwamba walikuwa wakitakana, wakajikuta wakifanya mapenzi kwa mara ya kwanza.

    Kwa kipindi hicho, Manka hakuwa akimfikiria Anko, Yusufu ambaye alikuwa juu ya kifua chake kwa wakati huo ndiye ambaye alionekana kuwa mwanaume sahihi. Kitanda kilikuwa kikilia tu huku kila mtu akitoa miguno yake. Kwa Manka wala hakuwa akifahamu kwamba mtu ambaye alikuwa akifanya nae mapenzi kwa wakati huo alikuwa ameathirika, mbaya zaidi walikuwa wakifanya ngono zembe, ngono ambayo wala mpira haukuwa ukitumika.

    ****



    Mapenzi kati ya Manka na Yusufu yakaonekana kuanza kuchanganya, kila wakati walikuwa pamoja huku muda mwingi Manka akiwa na hamu ya kuwa na Yusufu ambaye alionekana kuwa kwenye mapenzi nae ya dhati. Yusufu hakutaka kuzificha hisia zake, alikuwa wazi kumwambia kila mtu kwamba kwa wakati huo alikuwa pamoja na Manka ambaye nae alikuwa akimpenda kwa dhati.

    Watu ambao walikuwa wakipewa taarifa juu ya uhusiano ule wakaonekana kufurahia huku wengine wakionekana kukasirika. Uzuri wa Manka haukuonekana kama alistahili kuwa na Yusufu japokuwa walijua kwamba kijana huyo alikuwa mtu maarufu na mwenye fedha nyingi. Manka alionekana kustahili kuwa na mtu mwenye fedha lakini asiyekuwa maarufu kwani watu wengi ambao walikuwa maarufu hawakuonekana kuwa na mapenzi ya dhati.

    Tetesi zile ambazo zilikuwa zikiendelea kusikika ndizo ambazo zilimfikia Anko ambaye alionekana kuchanganyikiwa kupita kawaida. Katika kipindi cha kwanza, Anko hakutaka kutilia maanani sana kile ambacho alikuwa amekisikia kutokana na kujua kwamba zile zilikuwa tetesi tu ambazo zilikuwa zikivuma, ila mara baada ya kuusikia wimbo ambao Yusufu alikuwa ameutunga kwa ajili ya mpenzi wake mpya, Manka, hapo ndipo alipopata uhakika kwamba tetesi zile hazikuwa tetesi tu bali lilikuwa jambo la kweli ambalo lilikuwa likiendelea.

    Moyo wake ukaumia kupita kawaida, aliuhisi ukiwa umepigwa na msumali mkubwa wa moto, tena ukiwa msumali ambao ulikuwa na ncha kali. Mawazo yakaanza kujaa kichwani mwake, hakuonekana kuamini kile ambacho alikuwa akikisikia katika wimbo ule ambao alikuwa ameutunga Yusufu kwa ajili ya mpenzi wake, Manka.

    Anko hakutaka kukubali, alichokifanya ni kuanza kumtafuta Manka ili apate kujua ukweli juu ya kile ambacho kilikuwa kikiendelea. Simu ya Manka ilikuwa ikiita kila siku lakini wala haikuwa ikipokelewa. Anko akaanza kujuta moyoni, hakujuta juu ya fedha ambazo alikuwa amezitumia kwa ajili ya Manka au vitu mbalimbali ambavyo alikuwa amempa, alikuwa akijuta kutokana na muda wake ambao alikuwa ameupoteza, muda ambao alikuwa ameutumia kumpenda Manka na kumthamini.

    Anko hakuonekana kukubali kwa wakati huo, alijiona kwamba kila kitu kilikuwa kimekwenda tofauti na jinsi alivyopanga, aliona kulikuwa na kila sababu ya kuirudisha furaha ambayo ilikuwa imepotea moyoni mwake katika kipindi hicho. Hakukuwa na njia nyingine ya kufanya ili furaha yake irudi tena moyoni mwake, alijiona kutakiwa kufanya kitu kimoja kwa wakati huo, kumuua Manka pamoja na Yusufu tu.

    Kadri siku zilivyozidi kwenda na ndivyo ambavyo Anko alivyozidi kuumia zaidi na zaidi, kila alipokuwa akiziona picha ambazo Yusufu alikuwa akipiga pamoja na Manka ambazo zilikuwa zikitolewa katika magazeti mbalimbali, Anko alikuwa akikasirika kupita kiasi. Japokuwa alikuwa amepanga kuanza kuwatafuta na kuwaua baada ya mwezi mmoja, lakini picha zile zikamfanya kusitisha mpango wake mrefu, akaweka mpango wa muda mfupi.

    Alichokifanya ni kuwaandaa vijana wake ambao alitaka kufanya nao kazi ya kutekeleza kile ambacho alikuwa amekipanga kwa wakati huo. Vijana ambao walikuwa wakimfanyia kazi ya kuwaua wanachuo wa chuo cha IFM ndio ambao walitakiwa kuifanya kazi ambayo alikuwa ameipanga kufanyika kwa wakati huo. Alichokifanya ni kuwapigia simu na kutaka kuonana nao, tena nyumbani kwake, sehemu ambayo aliiona kuwa salama katika mipango yake yote.

    “Kwa hiyo wewe unatakaje bosi?” Sudi aliuliza.

    “Unamaanisha nini sasa kwa swali lako?” Anko aliuliza huku akionekana kuwa na hasira.

    “Yaani tuwaue na kukuletea japo damu zao kwenye vidumu au tuwateke na kisha uje kuwaua wewe mwenyewe?” Sudi alimuuliza.

    “Nyie mnaona zuri lipi hapo?”

    “Chagua wewe”

    “Nisaidie lipi zuri hapo”

    “Labda tuwateke halafu uje kuwauwa wewe mwenyewe”

    “Kwa nini msimalize kazi ninyi wenyewe na kuniletea damu kwenye vidumu kama ulivyosema?” Anko aliuliza.

    “Tunahofia lawama?”

    “Lawama zipi?”

    “Kama tukikuletea damu kwenye vidumu unaweza kusema kwamba ni damu ya ng’ombe” Sudi alimwambia Anko.

    “Hilo nalo neno. Watekeni halafu nije kufanya yangu”

    “Poa bosi”

    Sudi pamoja na wenzake, Kemo na Yati hawakutaka kupoteza muda, kwa kuwa kiasi cha shilingi milioni nne walikuwa wamekwishakabidhiwa kama nusu ya malipo ya kufanya kazi ile, wakaanza kuondoka kuelekea katika maskani yao kwa ajili ya kupanga juu ya namna ambavyo mchakato ule ulivyotakiwa kufanyika katika siku ya tukio ambalo walitakiwa kulifanya.

    Usiku mzima walikuwa wakipanga ni kwa namna gani ambayo walitakiwa kukamilisha kile ambacho walikuwa wameambiwa kukamilisha, kuwateka Yusufu na Manka na kisha kuwasiliana na Anko ambaye angefika sehemu ambayo watakuwa wamewahifadhi kwa ajili ya kufanya kile ambacho alikuwa akitaka kuwafanyia.

    Mipango kabambe ikapangwa usiku huo na ilitakiwa kufanyika katika siku ambazo watu hao wangekuwa pamoja hivyo kuwateka na kisha kufanya kile ambacho wangetakiwa kukifanya katika siku hiyo. Walipoona kwamba kila kitu kilikuwa tayari na ni ufanyaji wa kazi tu ndio ambao ungebakia, wakalala huku wakiwa wamepanga kila kitu.

    ****

    “Sijui ni kitu gani ambacho kinaendelea chuoni kwetu” Manka alimwambia Yusufu.

    “Kwa nini unasema hivyo?”

    “Wanaume wanauawa sana na watu wasiojulikana” Manka alimwambia Yusufu huku wakiwa mezani wakipata chakula cha usiku.

    “Nazisikia sana habari hizo. Kwa nini wanauawa?”

    “Hata mimi sifahamu mpenzi. Halafu mbaya zaidi, kila aliyeuawa basi alikuwa akinitaka” Manka alimwambia Yusufu.

    “Au wewe jini?” Yusufu alitania,

    “Hapana bwana”

    “Sasa ni nani anawaua?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Labda........” Manka alisema na ghafla kukaa kimya.

    Hapo hapo kumbukumbu zake zikaanza kurudi nyuma kama mkanda wa video na kuanza kukumbuka baadhi ya matukio ambayo yalikuwa yametokea. Ni kweli wanaume wengi ambao walikuwa wakisoma katika chuo cha IFM walikuwa wakiuawa, swali lilikuja, kwa nini wanaume ambao walikuwa wakiuawa ni wale ambao walikuwa wakimtaka kimapezi?

    Mtu wa kwanza kuuawa alikuwa Joseph na maiti yake kisha kutupwa katika ufukwe wa Coco, mtu wa pili kuuawa alikuwa Steve ambaye maiti yake pia ilitupwa katika ufukwe wa Coco. Ukiachana na hao, watu waliofuatia kuuawa walikuwa zaidi ya kumi na tano na mtu wa mwisho kabisa kuuawa alikuwa Emmanuel, kijana ambaye alikuwa na akili nyingi sana darasani. Wanaume wote hao ambao walikuwa wameuawa walikuwa wakimtaka kimapenzi, ni ndani ya wiki moja ya mishemishe zao za kumpata zilipokuwa zikiendelea, walikuwa wakiuawa.

    Mpaka kufikia hatua hiyo, tayari Manka akahisi kwamba kulikuwa na kitu kinaendelea nyuma ya pazia. Haikuwezekana kwamba kila mwanaume ambaye alikuwa akiuawa ni yule ambaye alikuwa akimtaka kimapenzi. Hapo akaonekana kugundua kitu, hapo ndipo hisia zake zilipokwenda moja kwa moja kwa mpenzi wake wa nyuma, Anko ambaye alikuwa na fedha nyingi.

    “Anko” Manka alijikuta akisema.

    “Ndiye nani huyo?” Yusufu aliuliza.

    “Ndiye aliyeuwa watu wanaume wa pale chuoni” Manka alimwambia Yusufu.

    “Ndiye nani huyo?”

    “Alikuwa mpenzi wangu kabla ya kuwa na wewe. Nadhani alikuwa akimuua kila mvulana ambaye alikuwa akitamani kuwa na mimi” Manka alimwambia Yusufu.

    “Kwa hiyo kila aliyetaka kuwa na wewe alimuua?”

    “Ndio”

    “Kwa hiyo ina maana hata mimi ataweza kuniua?”

    “Inawezekana” Manka alijibu na kumfanya Yusufu kuanza kucheka.

    “Usicheke mpenzi. Unahitaji kuwa makini kwa sasa” manka alimwambia Yusufu.

    “Hawezi kuniua. Kila aliyetaka kuniua, aliuawa yeye” Yusufu alimwambia Manka huku akiendelea kucheka.

    “Inakupasa kuwa makini mpenzi, hili si jambo la kulipuuzia” Manka alimwambia Yusufu ambaye bado alikuwa akiendelea kucheka.

    “Kuna watu wapo makini kwa ajili ya maisha yangu. Usiogope” Yusufu alimwambia manka.

    Bado waliendelea kula chakula kama kawaida. Walipomaliza kula, bia zikaletwa mezani hapo na kisha kuanza kuzinywa kwa fujo. Kila walipokuwa wakimaliza chupa tatu, mfanyakazi alikuwa akiwaletea chupa nne. Usiku huo ulikuwa ni usiku wa kunywa pombe tu kiasi ambacho kiliwafanya kuwa hoi.

    Wote wakainuka na kisha kushikana, kilichofuata baada ya hapo ni kuanza kupelekana chumbani huku wakiyumba yumba kupita kawaida. Walipoufikia mlango, wakaufungua na kisha kuingia na kujilaza kitandani. Wote wakabaki wakiangaliana kwa macho ya mahaba kitandani hapo, Manka hakutaka kukubali, alichokifanya ni kuanza kumsogelea Yusufu na kisha kuanza kumshikashika kifuani jambo ambalo likaanza kuziamsha hisia za Yusufu.

    “Unataka tufanye nini mpenzi?” Yusufu aliuliza kwa sauti iliyojaa ulevi.

    “Nataka tufanye mapenzi” Manka alimjibu huku akiendelea kukichezea kifua cha Yusufu.

    “Hapana baby. Leo Jumapili” Yusufu alimjibu Manka kwa sauti ya chini iliyojaa kilevi.

    “Nafahamu baby. Leo jumapili, walokole walikwenda kanisani asubuhi” Manka alimwambia Yusufu.

    “Kama unajua leo Jumapili, sasa kwa nini unataka tufanye mapenzi?” Yusufu aliuliza huku akionekana kuzidiwa.

    “Kwa sababu leo ni siku ya mapumziko”Manka alijibu.

    Katika kila jibu ambalo alikuwa akilitoa Manka na ndivyo ambavyo alikuwa akizidi kumvua Yusufu nguo moja baada ya nyingine na kisha kuanza kuzivua nguo zake. Baada ya dakika mbili, wote wakabaki watupu. Japokuwa Yusufu alijua fika kwamba siku hiyo ilikuwa ni Jumapili, siku ambayo hakutakiwa kufanya mapenzi lakini akaonekana kushindwa kumzuia Manka kwani mwili wake haukuwa na nguvu kabisa kutokana na kulewa kupita kiasi pamoja na kuzidiwa katika suala zima la msisimko wa mwili wake.

    Manka akamlalia Yusufu kifuani na kisha kuanza kufanya mapenzi kama kawaida yao. Kitendo kile kilipoanza, Yusufu hakutaka kukumbuka tena, hakutaka kukumbuka kwamba siku hiyo ilikuwa ni siku ya Jumapili, siku ambayo ilionekana kuwa mbaya kwake kama ambapo angefanya kile ambacho alikatazwa kukifanya siku hiyo. Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo waliendelea kufanya zaidi na zaidi mpaka pale ambapo wote wakahisi kuchoka na kisha kulala.



    Yusufu amevunjwa moja ya masharti aliyopewa kwenye ulimwengu wa kuzimu kwa kufanya mapenzi na manka katika siku ya Jumapili.





    Yusufu akaamka asubuhi na kisha kuanza kujiangalia kitandani pale. Alipojiona kwamba yupo mtupu na Manka nae alikuwa kama alivyokuwa, Yusufu akaonekana kuwa na wasiwasi. Kitu cha kwanza ambacho alikuwa amekifikiria kwa wakati huo ni siku hiyo ya siku hiyo. Ilikuwa ni siku ya Jumatatu, kwa maana hiyo ilimaanisha kwamba siku iliyopita ilikuwa ni siku ya Jumapili.

    Kama mtu aliyechanganyikiwa, Yusufu akainuka kutoka kitandani, akaanza kumwangalia Manka mara mbili mbili huku akionekana kutokuamini kile ambacho kilikuwa kimetokea usiku uliopita. Japokuwa katika usiku uliopita alikuwa amelewa lakini alikumbuka dhahiri kwamba walikuwa wamefanya mapenzi, Yusufu akachanganyikiwa kupita kawaida.

    “Manka....Manka...” Yusufu akaanza kumwamsha Manka.

    Manka alikuwa mzito kuamka. Yusufu aliendelea kumwamsha zaidi na zaidi mpaka pale ambapo manka akaamka na kisha kuanza kumwangalia Yusufu usoni ambaye alionekana kuwa kama mtu aliyechanganyikiwa. Yusufu hakuongea kitu, kwanza akaanza kumwangalia Manka kwa makini huko uso wake ukionekana kuwa na wasiwasi mwingi.

    “Hivi tulifanya mapenzi usiku uliopita?” Lilikuwa swali la kwanza lililotoka mdomoni mwa Yusufu.

    “Ndio tulifanya” Manka alijibu na kisha kujilaza tena.

    “Kwa nini tulifanya?” Yusufu alimuuliza Manka ambaye wala hakuonekana kujali zaidi ya kuendelea kulala.

    Akili ya Yusufu kwa wakati huo ilikuwa imekwishachanganyikiwa. Hakuamini kama hiyo ilikuwa ni mara yake ya pili kuvunja masharti ambayo alikuwa amewekewa katika ulimwengu wa giza. Akaanza kuikumbuka siku ambayo alivunja sharti la kwanza na hivyo kupewa adhabu ya kumuua baba yake jambo ambalo lilikuwa limemuuma kupita kawaida.

    Siku hiyo, kwa mara ya pili akawa amevunja sharti la pili ambalo alikuwa amepewa la kutofanya mapenzi katika siku ya Jumapili. Tukio lile likamuuma sana Yusufu kwa kuona kwamba ilikuwa ni lazima viumbe wa ulimwengu ule wa giza wampe adhabu, adhabu ambayo aliamini ingekuwa kali sana katika maisha yake.

    Yusufu hakutaka kuendelea kubaki ndani ya chumba kile, alichokifanya ni kutoka na kuanza kuelekea nje huku akiwa ameuchukua ufunguo wa gari lake. Machozi yakaanza kutoka machoni mwake, moyoni mwake alikuwa ameumia kupita kawaida. Tayari akajiona kuwa mtu ambaye hakuuonea raha utajiri na umaarufu wake ambao alikuwa amepewa. Kwake, tayari vitu vile ambavyo alikuwa amepewa aliviona kumnyima uhuru kabisa kwa kumuwekea masharti ambayo yalikuwa mazito sana kuyaepuka.

    Yusufu akaingia ndani ya gari lake na kisha kuanza kuelekea nyumbani kwa Papaa Pipo, Kijitonyama. Kichwa chake kwa wakati huo kilikuwa kimechanganyikiwa kupita kawaida. Hakuamini kama tayari alikuwa amevunja sharti jingine, sharti ambalo halikumtaka kufanya mapenzi katika siku ya Jumapili. Yusufu aliendelea kuendesha gari huku akiwa na mawazo mengi, mpaka katika kipindi hicho, hakujua ni adhabu gani ambayo angepewa.

    Baada ya dakika kadhaa akawa amekwishafika nje ya nyumba ya Papaa Pipo ambapo akateremka na kisha kuanza kulifuata geti lile. Hakutaka kuliingiza gari lake ndani ya eneo la Papaa Pipo, kwa wakati huo akili yake ilikuwa imechanganyikiwa kupita kiasi. Alipolifikia geti akaanza kugonga kifujo fujo na mlinzi kutokea na kufungua.

    “Karibu The Ruler” Mlinzi alimkaribsha.

    Yusufu hakuongea kitu chochote kile, alichokifanya ni kuingia ndani ya nyumba ile huku akili yake ikiwa bado haijakaa sawa kabisa. Alipoufikia mlango wa kuingilia sebuleni akaugonga na mfanyakazi wa ndani kuja kuufungua. Mfanyakazi wa ndani alionekana kushangaa sana, katika maisha yake yote hakuwahi kumuona Yusufu akifika nyumbani hapo asubuhi sana tena huku akionekana kuwa ovyo ovyo kama ambavyo alivyokuwa kwa wakati huo, hakuwa amenawa, na alikuwa amevaa bukta tu pamoja na kaoshi.

    “Karibu” Yule mfanyakazi wa ndani alimkaribisha huku akionekana kushangaa.

    “Asante” Yusufu aliitikia na kisha kuingia ndani.

    Hakutaka kukaa sebuleni hapo, alichokifanya ni kuanza kupiga hatua kuelekea katika chumba alichokuwa akilala Papaa Pipo. Alipoufikia mlango wa chumba kile, akaanza kuugonga na baada ya muda Papaa Pipo kutokea na kisha kumfungulia huku akionekana kumshangaa Yusufu. Yusufu akaingia na kisha kukifuata kitanda na kutulia.

    “Vipi tena? Mbona asubuhi asubuhi kama mtu aliyeitwa kwenye usaili?” Papaa Pipo alimuuliza Yusufu huku akionekana kushangaa.

    “Nimevunja sharti la pili” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.

    “Unasemaje?” Papaa Pipo aliuliza huku akionekana kushtuka.

    “Nimevunja sharti la pili” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.

    “Samiah amepata mtoto wa pili?” Papaa Pipo aliuliza

    “Hapana. Nimefanya mapenzi jana na Manka” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.

    “Acha kunitania Yusufu”

    “Huo ndio ukweli Papaa Pipo. Nimefanya mapenzi na Manka usiku uliopita” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sasa kwa nini ulikubali kufanya mapenzi?”

    “Nilikuwa nimelewa”

    “Kwa nini ulewe siku kama ile, siku ambayo unajua fika kwamba ni siku ya majanga?”

    “Hata sijui kwa sababu gani. Yaani hapa nilipo nimechanganyikiwa” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.

    “Kwa hiyo tufanye nini?”

    “Hata sijui. Labda niwaombe msamaha wakiniita” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.

    “Kukusamehe ni jambo gumu sana. Ni lazima uitumikie adhabu” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.

    Yusufu akabaki kimya, hakuwa akiamini kile ambacho kilikuwa kimemtokea kwa mara ya pili katika kipindi hicho. Masharti yote ambayo alikuwa amepewa tayari alikuwa amekwishayavunja ndani ya miaka mitatu tu ya mafanikio yake. Aliikumbuka siku ile ambayo alivunja sharti la kwanza mara baada ya kupata mtoto kitu ambacho hakutakiwa kukipata katika maisha yake yote. Kuvunjika kwa sharti lile, lawama zote alikuwa akimpa mtalaka wake, Samiah ambaye alifanya kitendo kile kwa makusudi bila kumpa taarifa.

    Yusufu aliumia sana mara baada ya kupewa adhabu ya kumuua baba yake tena kwa mkono wake mwenyewe. Leo hii, tayari alikuwa amevunja sharti jingine. Hakutaka kumlaumu sana Manka katika kuvunja sharti lile bali lawama zote alikuwa akijipa yeye mwenyewe kwa kuruhusu kunywa pombe na hatimae kuvunja sharti la kufanya mapenzi katika siku ambayo hakutakiwa kufanya mapenzi. Jambo hilo ndilo ambalo lilikuwa likimuumiza sana kichwa kwa wakati huo, hakujua ni kitu gani alitakiwa kukifanya.

    “Siadhibiwi” Yusufu alisema kwa sauti kubwa huku akionekana kuwa na hasira.

    “Unasemaje?” Papaa Pipo aliuliza kana kwamba hakuwa amesikia.

    “Siadhibiwi. Sipo tayari kupokea adhabu yoyote kwa sasa” Yusufu alimwambia Papaa Pipo na kisha kuondoka mahali hapo.

    Njia nzima Yusufu alikuwa na mawazo, hakuamini kama kitendo chake cha kukubali kupata mvuto pamoja na utajiri vingemfanya kufikia hatua ile. Japokuwa utajiri na mvuto ule vilikuwa vitu vizuri sana katika maisha yake lakini muda wingi vilikuwa vikimkosesha sana amani jambo ambalo wakati mwingine lilimfanya kujuta kupita kawaida kwa uamuzi ambao alikuwa ameuchukua. Kwa wakati huo, aliiona dunia ikiwa imemuinamia, hakuamini kama matokeo ya kuchukua uamuzi ule yangekuwa namna ile.

    “Ulikwenda wapi mpenzi?” Ilikuwa ni sauti ya Manka ambayo ilisikika masikioni mwake mara baada ya kufika nyumbani.

    “Nilikwenda sehemu fulani”

    “Mbona haukuniaga jamani baby wangu?”

    “Nilikuamsha ili nikuage lakini ukalala tena” Yusufu alimwambia Manka ambaye alikuwa akimwangalia kwa mshangao.

    “Ila unaonekana haupo sawa. Kuna nini?” Manka alimuuliza Yusufu.

    “Hakuna kitu. Mbona nipo sawa tu”

    “Hapana. Haupo sawa kabisa. Nieleze kitu gani kimetokea”

    “Nipo sawa mpenzi. Ni uchovu wa asubuhi tu” Yusufu alimwambia Manka.

    Bado kichwa cha Yusufu hakikukaa sawa kabisa kwa wakati huo, mawazo yake yalikuwa yakifikiria juu ya adhabu ambayo angepewa mara tu baada ya kuitwa katika ulimwengu wa giza. Hakujua ni kitu gani ambacho angetakiwa kukifanya kama ni kukubali adhabu ambayo angepewa au kukataa kuipokea. Yusufu alikaa katika hali ya mawazo mpaka pale ambapo Manka akahitaji kuondoka, akaamua kumsindikiza.

    “Ila bado unaonekana kutokuwa sawa kabisa. Naomba uniambie ni kitu gani kinaendelea” manka alimwambia Yusufu.

    “Mbona nipo kawaida tu”

    “Hapana. Haupo kawaida. Asubuhi ulisema kwamba ulikuwa na uchovu, sidhani kama uchovu wa asubuhi unaweza kuendelea mpaka sasa hivi, jioni hii” Manka alimwambia Yusufu.

    “Siko sawa mpenzi”

    “Kwa nini tena?”

    “Sipo sawa” Yusufu alimwambia Manka kwa sauti yenye ukali.

    Manka akaonekana kuogopa, siku hiyo Yusufu alionekana kuwa mtu wa tofauti kabisa. Toka alipoanza kumfahamu, hakuwahi kumuona Yusufu akiwa katika hali hiyo, alikuwa akimuona kuwa katika hali ya furaha na utulivu mkubwa sana. Siku hiyo, Yusufu hakuonekana kuwa sawa, alijua fika kwamba kulikuwa na kitu ambacho kilitokea lakini kila alipokuwa akijaribu, Yusufu hakuonekana kuwa radhi kumwambia.

    Hali ile bado ilikuwa ikimtia Manka wasiwasi, hakupenda kumuona mpenzi wake akiwa katika hali ile, alitamani amwambie ni kitu gani ambacho kilikuwa kimeendelea ili hata kama alikuwa na uwezo wa kumsaidia basi afanye hivyo. Yusufu alionekana kuwa mgumu kujiweka wazi kwa Manka, kumwambia ukweli kwamba alikuwa amevunja masharti aliyokuwa amepewa lisingeonekana kuwa jambo sahihi kwake kwani hakutaka Manka afahamu jambo lolote lile.

    “Nataka kwenda chuo” Manka alimwambia Yusufu ambaye akainuka kutoka kitandani na kuchukua ufunguo wa gari.

    Garini, bado Yusufu hakuonekana kuwa sawa kabisa, alionekana kuwa mwingi wa mawazo, akili yake ilikuwa ikiwafikiria wale viumbe wa ajabu ambao walikuwa wakipatikana katika ulimwengu wa ajabu pamoja na adhabu ambayo wangempa mara baada ya kumuita katika moja ya vikao vyao.

    Manka alionekana kuwa na wasiwasi mwingi, hali ambayo alikuwa nayo mpenzi wake ilionekana kumhuzunisha kupita kawaida. Hakuzoea kumuona Yusufu akiwa katika hali hiyo, alikuwa amezoea kumuona Yusufu akiwa katika hali ya furaha huku wakiyafurahia mapenzi yao ambayo yalionekana kuzidi kukua kadri siku zilivyozidi kwenda mbele.

    Walichukua dakika thelathini na ndipo walipofika Mabibo ambapo Yusufu akalisimamisha gari lile na kisha kuanza kumwangalia Manka usoni huku ikiwa imetimia saa kumi na mbili na robo jioni. Hata kabla manka hajateremka kutoka katika gari lile, akayapeleka macho yake usoni mwa Yusufu ambaye bado alionekana kuwa mwingi wa mawazo.

    “Nakuomba uniambie simuni baadae kile kinachokusumbua” Manka alimwambia Yusufu.

    “Hakuna kinachonisumbua mpenzi. Nipo sawa tu” Yusufu alimwambia manka.

    “Hapana. Sijazoea kukuona katika hali hiyo. Naomba uniambie mpenzi” Manka alimwambia Yusufu ambaye akashusha pumzi ndefu na kumwangalia usoni.

    “Usijali. Nitakwambia” Yusufu alimwambia Manka ambaye akaanza kuteremka garini.

    Yusufu hakutaka kuendelea kubaki, alichokifanya ni kuondoka mahali hapo na kurudi nyumbani kwake. Mwendo wa gari ulikuwa ni wa taratibu sana, bado hali ya mawazo hayakuweza kumtoka, adhabu ambayo alikuwa akitarajia kuipata ndio ambayo ilimfanya kuwa kwenye hali hiyo ambayo haikuonekana kuwa ya kawaida kabisa.

    Kutokana na foleni kubwa ya Ubungo, magari yalikuwa yakitembea tembea taratibu huku yakisimama kila baada ya hatua kadhaa. Huku akiwa amelisimamisha gari katika foleni ile, mara mwanaume mmoja ambaye alionekana kuwa kama kijana wa mitaani akatokea mbele ya gari lake na kisha kujifanya kuosha kioo cha gari lake. Yusufu alitamani kumwambia aache kufanya hivyo lakini hata nguvu ya kumwambia akaiona kupotea kabisa.

    Huku macho yake yakimwangalia kijana yule ambaye alikuwa akiendelea kuosha kioo cha gari lake, mara akasikia kioo cha gari lake cha mlangoni kikigongwa, alipoangalia, alikuwa muuza magazeti. Yusufu akakifungua kioo kile na kisha kuanza kumwangalia kijana yule ambaye alikuwa ameshika magazeti mengi.

    “Utataka gazeti moja kaka?” Kijana yule alimuuliza Yusufu.

    “Hapana” Yusufu alijibu huku akijiandaa kupandisha kioo cha mlango ule.

    Huku hata kabla hajaanza kukipandisha kioo kile, macho yake yakatua katika mkono wa muuza magazeti yale, mkono ambao ulikuwa umeshika magazeti yale, ulikuwa umeshika bunduki kwa chini, sehemu ambayo hakukuwa na mtu mwingine yeyote ambaye angefanikiwa kuiona kutokana na kufunikwa na magazeti yale.

    “Ukileta ubishi wowote hapa, nakifumua kichwa chako” Kijana yule alimwambia Yusufu huku mdomo wa bunduki ukiwa umemlenga usoni mwake.

    “Fungua mlango huo huko” Kijana yule alimwambia Yusufu ambaye bila ubishi akaufungua mlango wa upande wa pili na kisha huku akionekana kushangaa, kijana yule ambaye alikuwa akikiosha kioo cha gari lake akiufuata mlango, akaifungua na kisha kuingia ndani.

    Yusufu akatakiwa kutulia katika usukuni ule huku kijana yule ambaye alikuwa na bunduki akiufungua mlango wa nyuma na kuingia ndani. Yusufu akaonekana kuwa na wasiwasi, hakuamini kama kwa mara ya pili tena alikuwa amewekwa chini ya ulinzi wa watu asiowajua, alichokifanya mahali hapo, ni kufanya kile ambacho watu wale walitaka akifanye.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unatakiwa uendeshe gari mpaka katika barabara ya Sam Nujoma, pembezoni mwa jengo la Mawasiliano” Sudi alimwambia Yusufu.

    Yusufu akatulia, mdomo wa risasi ambao alikuwa ameelekezewa na Sudi ambaye alikuwa katika viti vya nyuma ulionekana kumtia wasiwasi, alikuwa akitetemeka huku kijasho chembamba kikianza kumtoka. Foleni ile ilichukua muda wa dakika ishirini na ndipo wakafanikiwa kuvuka katika maunganisho ya barabara ya Morogoro na kisha kuingia katika barabara ya Sam Nujoma.

    Safari iliendelea zaidi na zaidi mpaka pale ambapo walifika karibu na jengo la Mawasiliano na kisha kutakiwa kulisimamisha gari lake pembeni ya barabara karibu kabisa na mahali ambapo Yati alipokuwa amesimama. Gari liliposimamishwa, Yati akaufungua mlango na kisha kuingia ndani huku nae akionekana kuwa na bunduki.

    “Wapi sasa” Kemo, ambaye alikuwa pembeni ya Yusufu katika viti vya mbele aliwauliza.

    “Kwanza shikilia usukani na huyo mjinga aje huku nyuma” Sudi alimwambia Kemo ambaye alimwambia Yusufu ampishe katika kiti kile na kisha kukaa yeye huku Yusufu akielekea katika kiti cha nyuma na kuwekwa katikati.

    “Tanganyika Pakers” Sudi alimwambia Kemo ambaye akawasha gari na kisha kuondoka mahali hapo na safari ya kuelekea katika uwanja wa Tanganyika Pakers uliokuwa Kawe kuanza.

    Katika muda wote wa safari ile Yusufu alionekana kuwa na wasiwasi, hakuamini kama kweli katika siku hiyo angeweza kuwa mikononi mwa watu ambao wala hakuwa akiwajua kabisa. Wasiwasi wake ulizidi kuongezeka mara baada ya kugundua kwamba tayari alikuwa amevunja sharti hivyo aliona kama ulinzi kwake usingekuwepo kabisa kutoka katika ulimwengu wa giza.

    Kutokana na foleni za hapa na pale, walichukua saa moja na dakika kumi na tano na ndipo walipofika katika viwanja hivyo na kisha kulipaki gari huku tayari ikiwa imetimia saa mbili kasoro kumi usiku. Hapo hapo wakamtaka Yusufu kuteremka pamoja nao huku wakiwa pamoja nae na kisha kumtanguliza mbele katika jumba moja bovu ambalo lilionekana kutelekezwa ambalo lilikuwepo katika uwanja huo.

    “Mpigie simu bosi” Sudi alimwambia Kemo huku wakiingia ndani ya jumba lile bovu.

    “Ila si bado msichana?”

    “Wewe mpigie tu. Hatuna muda. Ni bora tuanze na huyu halafu huyo demu atafuata” Sudi alimwambia Kemo.

    Kemo akachukua simu yake na kisha kuanza kumpigia Anko na kisha kuanza kumpa taarifa ile kwamba kile kitu ambacho aliwataka wakifanye tayari kilikuwa kimekwishafanyika na katika kipindi hicho walikuwa pamoja na Yusufu katika uwanja wa Tanganyika Pakers uliokuwa Kawe.

    “Nakuja. Na vipi kuhusu yule malaya?”Ilisikika sauti ya Anko.

    “Yule bado ila tu.....” Kemo alisema lakini hata kabla hajamalizia, Anko akaingilia.

    “Msijali. Huyo mjinga ndio wa muhimu zaidi ya yule malaya. Yule malaya hasumbui, nitamtafuta hata kesho. Nisubirini nakuja hapo hapo ndani ya dakika ishirini kwani nipo hapa Leaders Club” Sauti ya Anko ilisikika na kisha kukata simu.

    “Amesemaje?” Sudi alimuuliza Kemo.

    “Anakuja ndani ya dakika ishirini kwani yupo hapo Leadres Club” Kemo alijibu.

    Yusufu akaamriwa kukaa chini, bado alikuwa na wasiwasi tele, hakuamini kama katika kipindi hicho alikuwa mateka na muda wowote ule kuanzia hapo angeweza kuuawa. Tayari akaonekana kufahamu kwamba inawezekana kwamba mtu ambaye alikuwa amemzungumzia Manka ndiye ambaye alikuwa nyuma ya mipango yote ya kutekwa kwake.

    Japokuwa toka aishi maisha yake ndani ya jiji la Dar es Salaam hakuwahi hata kwenda msikitini, kwa wakati huo akaanza kumuomba Mungu amuepushe na hatari ambayo ilikuwa mbele yake. Yusufu hakuishia hapo, alichokuwa akikijua yeye ni kwamba alikuwa akienda kufa na hivyo alihitaji Mungu amsamehe kwa kila kitu ambacho alikuwa amekifanya.

    “Hata ukimuomba Mungu! Ni lazima tukuue tu” Sudi alimwambia Yusufu huku akimgonga gonga na bunduki yake kichwani.





    Anko akabadilika, uso wake ukaonekana kuwa kwenye furaha kubwa, hakuamini kile ambacho alikisikia kutoka simuni mwake, alichoambiwa na Kemo. Japokuwa alikuwa katika uwanja wa Leaders akiiangalia bendi ya Twanga Pepeta ambayo ilikuwa ikitumbuiza mahali pale, hakujali, akasimama na kisha kuanza kuondoka mahali hapo.

    Moja kwa moja akalifuata gari lake ambalo alikuwa amelipaki katika uwanja wa mpira uliokuwa mahali hapop, akaufungua mlango wa gari na kuanza kuondoka mahali hapo. Moyo wake ulikuwa kwenye furaha tele, hakuamini kama wakati huo vijana ambao aliwaambia wamkamate Yusufu pamoja na Manka walikuwa wamekwishafanikisha kile alichowaambia. Hakuwa na wasiwasi na Manka, alijua kwamba kazi kubwa ilikuwa kwa huyu Yusufu, mtu ambaye alikuwa akionekana kuwa makini katika kipindi chote.

    Mwendo wake haukuwa mdogo, alikuwa akiendesha gari lake kwa kasi kuelekea Kawe katika viwanja vya Tanganyika Pakers huku lengo lake likiwa ni kuonana na vijana wale ambao alikuwa amewatuma pamoja na kufanya kile ambacho alikuwa akikitaka, kumuua Yusufu na kuondoka zake huku moyo wake ukianza kuwa na amani.

    Akajipapasa kiunoni mwake, bunduki yake ilikuwa vizuri mahali hapo, hakuridhika, akaitoa na kuanza kuiangalia vizuri huku mkono mmoja ukiwa umeshika usukani wa gari lake. Risasi za kutosha bado zilikuwepo ndani ya bunduki ile ambayo wala haukuwa umepita muda mrefu tangu ainunue nchini Uganda, na alikuwa akiimiliki kinyume na sheria.

    Mwendo wake bado haukuwa wa taratibu, alikuwa akiendesha gari kwa kasi kwa kuona kwamba kama angechelewa basi Yusufu angeweza kuwatoroka watu hao kitu ambacho hakutaka kitokee mahali hapo. Mara baada ya kufika Mikocheni B karibu kabisa na mtaa wa Mbuni, mbele yake kukaonekana umati mkubwa wa watu ambao walikuwa wamevaa nguo nyeupe tupu huku watu hao wakiwa wameshika majeneza mengi wakielekea upande wa baharini kuzika.

    Anko akapigwa na mshtuko kupita kawaida, hakuamini kile ambacho alikuwa akikiona machoni mwake kwa wakati huo, ilikuwaje watu waelekee kuzika muda kama huo, usiku tena mbaya zaidi wakielekea baharini, sehemu ambayo wala haikuwa na makaburi yoyote yale. Hayo yakaonekana kuwa mauza uza kwake, akawaangalia watu wale vizuri, hawakuwa watu weusi, walikuwa waarabu tupu huku idadi yao ikiwa kubwa kupita kawaida.

    Wale watu ambao walikuwa wakivuka barabara kwenda baharini kuzika huku wakiwa na majeneza hawakuweza kuisha, bado walikuwa wakiendelea kuvuka barabara ile huku wakiimba nyimbo ambazo wala hakuwa akizielewa kabisa. Alikaa kwa zaidi ya nusu saa, idadi ile bado haikuonekana kuisha mahali pale, bado watu wale walikuwa wakiendelea kuvuka barabara kuelekea kuzika.

    Mpaka kufikia hatua hiyo, Anko akaonekana kuchanganyikiwa kupita kawaida, hakujua ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya zaidi ya kuteremka kutoka garini na kisha kuanza kuangalia huku na kule. Barabarani, hakukuwa na gari lolote lile zaidi ya gari lake. Hilo nalo kwake likaonekana kuwa la mauza uza, hakutegemea muda kama huo wa saa tatu kusiwe na gari lolote mahali hapo, Anko alionekana kuchanganyikiwa.

    Muda bado ulikuwa ukizidi kwenda mbele, watu wale ambao walikuwa wakielekea kuzika hawakuisha, bado walikuwa wakiendelea kuvuka barabara ile huku majeneza yakiwa mikononi mwao. Anko akaonekana kuchoka, alichokifanya ni kurudi garini mwake na kisha kuanza kupiga honi kadhaa lakini watu wale wala hawakuonekana kusikia, na kama walisikia basi hawakuonekana kujali.

    Anko hakuwa na jinsi, kwa wakati huo alikuwa amevumilia kupita kawaida, alichokifanya ni kurudisha gari nyuma na kuchukua uamuzi mmoja tu, kuwagonga watu hao ambao walikuwa hawaishi kuvuka barabara ile kuelekea makaburini baharini. Alipoona amerudisha gari lake umbali wa kutosha, hapo ndipo alipopiga gia na kisha kuanza kuliondoa gari lile kwa kasi ya ajabu na kuwagonga watu wale ambao walikuwa mbele yake ambao ghafla wakapotea. Gari lake likakosa muelekeo, likatoka nje ya barabara na kuuvamia mtaro uliokuwa pembeni mwa barabara ambapo kulikuwa na mtaro na gari lile kujibamiza kwa nguvu hivyo yeye mwenyewe kutolewa nje ya gari lile.

    Kichwa chake kilikuwa kimepiga kioo cha mbele cha gari lile na hivyo kutolewa nje ambapo akakibamiza kichwa chake katika ukuta wa mtaro huo, kichwa kikapasuka, ubongo ukatoka, damu zikatapakaa mahali hapo. Hiyo ikaonekana kuwa ajali moja kubwa ambayo ilionekana kuwa ya kizembe kupita kawaida.

    Ndani ya sekunde ishirini tu, watu wakafika mahali hapo na kisha kuanza kuuangalia mwili wake ambao ulikuwa mtaroni. Ile ikaonekana kuwa ajali mbaya sana, kichwa kilikuwa kimepasuka kabisa huku ubongo ukiwa mtaroni katika maji machafu. Waliokuwa na simu zenye mwanga wakaanza kupiga picha mwili huo bila mtu yeyote kujua kwamba mtu yule alikuwa Anko.

    “Mmmh! Inatisha” Jamaa mmoja aliwaambia wenzake.

    “Hivi ilikuwaje? Unajua sijaiona hii ajali” Jamaa mmoja aliuliza.

    “Huyu dereva sijui alikuwa amelewa. Yaani hadi nashangaa” Jamaa mwingine alisema.

    “Kwani ilikuwaje?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Huyu dereva alikuwa amelisimamisha gari barabarani bila sababu yoyote ile kwa zaidi ya nusu saa” Jamaa yule alielezea.

    “Alisimamisha gari barabarani?”

    “Ndio. Kila akipigiwa honi alikuwa hatoi gari. Bado alikuwa amelisimamisha tu”

    “Au lilikuwa limeharibika?” Jamaa mwingine aliuliza.

    “Hakuna. Yaani nilishangaa nini kimetokea. Madereva wa magari mengine hawakuonekana kujali, wakawa wakimpita na kuendelea na safari zao”

    “Sasa kwa nini hukwenda kumshtua?”

    “Nilitaka kufanya hivyo ila kila nilipotaka kwenda, nilikuwa mzito kweli”

    “Sasa ikawaje? Mbona yupo mtaroni?”

    “Baada ya kusimama kwa muda mrefu, nikaona anarudisha gari kwa nyuma na kisha kuliendesha kwa mwendo wa kasi. Cha kushangaza sasa, akaanza kuufuata mtaro kwa mwendo huo huo wa kasi. Kilichotokea ndicho hiki mnachokiona” Jamaa huyo alielezea.

    “Kwa hiyo hii ni ajali ya kujitakia?”

    “Asilimia mia moja. Ila inawezekana alikuwa amelewa” Jamaa yule alimalizia.

    ****

    Muda ulikuwa ukizidi kwenda mbele lakini wala Anko hakuonekana kufika mahali hapo. Sekunde zilikuwa zikisogea huku dakika zikizidi kusonga mbele lakini bado Anko hakuweza kufika mahali hapo. Mara kwa mara walikuwa wakimpigia simu yake, simu ilikuwa ikiita tu lakini wala haikuwa ikipokelewa jambo ambalo lilikuwa likimkasirisha kila mtu mahali pale.

    Tayari mtu ambaye alikuwa akimhitaji kwa udi na uvumba alikuwa mikononi mwao, yeye ndiye ambaye alikuwa akisubiriwa tu mahali hapo na kisha kumkabidhi mtu wake ambaye angemfanya kitu chochote kile ambacho angetaka kumfanya mahali hapo. Muda mwingi walikuwa wakiangalia saa zao lakini wala Anko hakuweza kutokea mahali hapo.

    Mpaka inatimia saa tano usiku, bado Anko hakuwa mahali hapo. Kila walipokuwa wakipiga simu masaa ya nyuma ilikuwa ikiita tu, kwa sasa hata kuita haikuwa ikiita, ilikuwa haipatikani kabisa jambo ambalo lilimshangaza kila mmoja mahali hapo. Wakaanza kujadiliana ni kitu gani ambacho walitakiwa kukifanya mahali hapo, hapo ndipo ambapo simu ile ambayo walikuwa wameitumia kumpigia Anko ilipoanza kuita, Kemo akaipokea na kuipeleka sikioni.

    “Unasemaje?....Amepata ajali?...... Wapi?.... Muhimbili?... Hapana, mimi ni rafiki yake tu. Sawa nakuja........” Kemo aliongea na mtu simuni na kisha kukata simu ile.

    “Vipi?” Yati alimuuliza.

    “Anko amepata ajali na mwili wake kupelekwa hospitalini?” Kemo alijibu huku akionekana kuchoka.

    “Kwa hiyo amekufa ajalini?” Sudi aliuliza.

    “Sijui”

    “Sasa inakuwaje amesema mwili wake umepelekwa hospitalini? Hivi angekuwa hai angesema mwili umepelekwa hospitalini? Atakuwa amekufa tu” Sudi aliwaambia.

    “Sasa inakuwaje?” Kemo aliuliza

    “Kuhusu nini? Kuelekea hospitalini?”

    “Hapana. Hospitalini siendi. Sio ndugu yangu yule. Nauliza kuhusu huyu mpumbavu” Kemo alijibu huku akimwangalia Yusufu.

    “Huyu tumuacheni tu. Amesalimika. Au nyie mnaonaje?” Sudi aliwaambia na kuwauliza.

    “Hiyo sawa sawa. Tuondokeni tu” Yati aliwambia.

    Hawakutaka kubaki mahali hapo, walichokifanya ni kuondoka mahali hapo na kuanza kushuka chini ya jengo lile kuu kuu. Walipolifikia gari lile la Yusufu, Kemo akashikilia usukani na kisha kuanza kuondoka mahali hapo. Wala hawakufika mbali, Kemo akasimamisha gari huku akionekana kushtuka.

    “Vipi?” Sudi alimuuliza kemo.

    “Hivi tumemuacha Yusufu hai?”

    “Kwani hatukumuua?” Sudi aliuliza.

    “Hapana. Nafikiri tumemuacha hai. Kwa nini tumemuacha hai?” Kemo aliuliza huku akiteremka kutoka garini huku akiwa na bunduki.

    “Tulimuacha hai? Kivipi?” Sudi aliuliza huku akiteremka garini pamoja na Yati.

    “Tulimuacha hai. Haiwezekani. Kwa nini hatukumuua?” Kemo aliuliza.

    “Mmmh! Kweli tulimuacha hai!” Sudi alisema kwa mshangao.

    Hapo hapo wakaanza kukimbia kuelekea katika jengo lile. Wote wakaonekana kuchanganyikiwa kupita kawaida, hawakuamini kama kweli walikuwa wamemuacha Yusufu hai katika jengo lile pasipo kumuua. Ni kweli kwamba mtu wao ambaye alikuwa amewatuma kumuua Yusufu alikuwa amekufa lakini hiyo haikuwa sababu ya kumuacha Yusufu hai, ilibidi wamuue tu.

    Mara baada ya kufika katika jengo lile kule juu, Yusufu hakuwepo jambo ambalo lilionekana kuwashangaza kupita kawaida. Wakabaki wakiangaliana, hapo ndipo wakakumbuka kwamba walikuwa wameshauriana kwamba wamuache Yusufu hai. Kila mmoja alionekana kujishangaa kwa kupanga uamuzi ule, hakukuwa na mtu ambaye alitambua kwamba kulikuwa na nguvu ya ziada, nguvu ambayo iliwaingia na kuanza kumuonea huruma Yusufu.

    Huku wakiwa wamepigwa na butwaa katika jengo lile, kwa mbali wakaliona gari lile la Yusufu ambalo walikuwa wamekuja nalo mahali pale likiwa linaanza kuondoka katika viwanja vile vya Tanganyika Pakers. Kila mmoja akashtuka na kujua kwamba yule mtu ambaye alikuwa ameingia ndani ya gari lile alikuwa Yusufu.

    Hapo ndipo walipoanza kuteremka ngazi kwa kasi ya ajabu kuelekea chini huku wakiwa na lengo la kulifuata gari lile. Mpaka wanafika chini ya jengo lile, gari lile likawa limekwishaingia katika barabara ya lami na kisha kuendeshwa kwa mwendo wa kasi kuondoka katika maeneo hayo.

    “Tumemkosa...!” Sudi alisema huku akijishika kichwa chake kwa hali ya kusikitika.





    Yusufu alikuwa akitetemeka kwa woga kwani alijua muda wowote ule kuanzia kipindi hicho mtu ambaye alikuwa akisubiriwa kwa ajili ya kazi moja ya kumuua basi angefika mahali hapo na kumuua. Bado sala ya kimoyo moyo ilikuwa ikiendelea moyoni mwake huku akimtaka Mungu amuepushe na kile ambacho kilitaka kutokea mahali pale.

    Alijua fika kwamba toka aingie ndani ya jiji la dar es Salaam hakuwahi kuingia msikitini, alijua fika kwamba ulimwengu wa giza ndio ambao alikuwa akiuabudu katika maisha yake yote ila katika siku hiyo, moyo wake ulikuwa ukimuomba Mungu aweze kumuokoa katika hali ambayo alikuwa nayo mahali pale.

    Yusufu hakuonekana kuamini mara baada ya kusikika kwamba mtu ambaye alikuwa akitarajiwa kufika mahali hapo alikuwa amepata ajali. Hiyo ikaonekana kuwa furaha kwake, alijua kwamba ule ulimwengu wa giza bado ulikuwa katika upande wake, haukutaka kuacha auawe katika kipindi hicho kwa sababu bado walikuwa wakiendelea kumhitaji.

    Alipowasikia Sudi na wenzake wakipanga shauri la kumuacha hai mahali pale, moyo wake ukafurahi zaidi kwa kuona kwamba kila kitu ambacho alikuwa akitaka kifanyike kilikuwa kinafanyika kama alivyokuwa akitaka. Sudi na wenzake hawakuendelea kubaki ndani ya jumba lile, walichokifanya ni kuondoka mahali hapo.

    Yusufu hakutaka kubaki, alichokifanya nae ni kuanza kushuka ngazi katika jumba lile bovu na kuanza kukimbia kuelekea upande wa kaskazini. Yusufu alikimbia kwa muda fulani na kisha kusimama. Moyo wake akauhisi kuanza kujawa na uzito fulani hali iliyomuonyesha kwamba hakutakiwa kukimbilia kule alipokuwa akikimbilia bali alitakiwa kwenda kule kulipokuwa na gari lake.

    Yusufu hakutaka kujiuliza mara mbili mbili, japokuwa aliliona gari lake likiwa linaanza kuondoka mahali pale, akaanza kuelekea kule lilipokuwa. Alipolifikia, akaingia huku likiwa limeendeshwa kwa umbali fulani. Bahati ilikuwa upande wake, ufunguo wa gari ulikuwa mule garini, alichokifanya ni kuutekenya ufunguo ule na kisha kuliondoa gari mahali pale huku akiwa hajui sababu ambayo iliwafanya vijana wale kuliacha gari lake huku wakiwa wameliendesha kwa umbali fulani.

    “Asante Mungu kwa kusikia maombi yangu” Yusufu alisema huku akiwa amekwishaingia barabara ya lami na kuanza kuelekea nyumbani kwake.

    ****CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Yusufu hakutaka kukaa kimya, siku iliyofuata akaamua kuwafuata waandishi wa habari na kisha kuwaambia kwamba alikuwa ametekwa na watu wasiojulikana kwa lengo la kuuawa ila Mungu alikuwa upande wake na hivyo kumsaidia. Maneno yale yakaonekana kumshtua kila mtu aliyeyasikia, roho ya Yusufu ikaonekana kuwa dili kwa watu ambao walikuwa wakimtafuta katika kipindi hicho.

    Yusufu hakumpa taarifa Manka kwamba mtu ambaye alikuwa mwanaume wake ndiye ambaye alikuwa amewatuma vijana ambao walikuwa wamemteka na hatimae kutaka kumuua katika jumba bovu lililokuwa katika viwanja vya Tanganyika Pakers. Magazeti pamoja na vyombo mbalimbali vya habari vikaandika jambo lile ambalo lilizidi kumpaisha Yusufu zaidi na zaidi. Japokuwa kila siku maisha yake alikuwa akijulikana sana lakini bado katika kipindi hicho alizidi kusikika zaidi na zaidi.

    Yusufu akazidi kuitwa katika matamasha mbalimbali ambayo yalikuwa yakimuingizia kiasi kikubwa cha fedha. Katika kipindi cha miaka mitatu tu, Yusufu alikuwa amepata kiasi kikubwa cha fedha ambacho kilimfanya hata wakati mwingine kufikiria kuchana na muziki na kujiingiza katika mambo ya biashara.

    Japokuwa alikuwa akitanua kila siku lakini bado kichwa chake kilikuwa kikifikiria kitu kimoja tu, kuitwa katika ulimwengu wa giza na kisha kupewa adhabu juu ya kile ambacho kilikuwa kimetokea, kuvunja moja ya masharti ambayo walikuwa wamempa, kufanya mapenzi na Manka katika siku ya Jumapili, siku ambayo ilionekana kuwa mbaya kwake.

    Alikunywa na kula lakini wakati mwingine alijiona kuwa kama kwenye kifungo kikubwa moyoni mwake, alijua kwamba ulimwengu ule wa giza ulikuwa umempa kila kitu lakini ulikuwa umemnyima uhuru wa kufanya kila kitu vikiwepo kupata mtoto na hata kufanya mapenzi katika siku ya Jumapili na Jumatano, siku ambazo alikuwa akishinda klabu za usiku pamoja na wanawake wazuri na kuondoka bila ya kufanya kitu chochote kwao.

    Moyoni alijihisi upweke sana hali ambayo ikamfanya kuwa na mawazo kila wakati. Kuna wakati alijipa moyo kwamba inawezekana kwamba watu hao wa ulimwengu wa giza walikuwa wamesahau kumpa adhabu lakini katika kipindi kingine aliisikia sauti ikimwambia kwamba hawakuwa wamesahau ila kuna siku moja angeitwa na kuambiwa adhabu yake ingekuwa nini.

    Alipata kila kitu katika maisha yake lakini uhuru ndicho kitu ambacho kilimfanya kujiona kuwa kwenye kifungo kikubwa sana. Kwa wakati mwingine alikuwa akitamani sana kuachana na vitu vile lakini alijua fika kwamba kama angeamua kufanya hivyo basi wangechukua kila kitu kilicho chao ambacho walikuwa wamempatia katika maisha yake.

    Asingekuwa tena na utajiri, mvuto ungeondoka machoni mwa watu, wasichana wasingempenda tena na hivyo kurudi katika maisha ya kimasikini ambayo alikuwa akiishi katika kipindi cha nyuma. Kila alipokuwa akifikiria kuhusu wazo lake la kurudisha kila kitu ambacho alipewa, moyo wake ulikataa katakata kumruhusu kufanya hivyo.

    “Ila inawezekana wakawa wameamua kuniacha kwa sababu nimewatumikia sana” Yusufu alijisemea.

    “Mmmh! Inawezekana kweli wakawa na mioyo ya msamaha kirahisi namna hiyo? Lakini mbona hawaniiti na huu ni mwezi unakatika? Inawezekana wakawa wamenisamehe” Yusufu alikuwa akijiuliza maswali mengi na kujijibu.

    Kwa wakati huo hakuwa na uhakika kama alikuwa amesamehewa au watu wa ulimwengu ule walikuwa wakisubiri siku maalumu ifike na hatimae kumuita tena katika sehemu yao ya makutanio na hatimae kumpa adhabu juu ya kile ambacho alikuwa amekifanya. Kama alivyokuwa akiwaza na ndicho kitu ambacho kilitokea.

    Baada ya siku kadhaa huku akiwa chumbani kwake usiku, kioo kile ambacho kilikuwa mlango wake mkuu wa kuingilia katika ulimwengu wa giza kikaanza kuonyesha miale kadhaa ya radi huku kwa mbali ngurumo zikiwa zinasikika. Yusufu akashtuka kutoka usingizini, alipoiona miale ile ya radi, mapigo yake ya moyo yakaanza kudunda kwa kuona kwamba siku hiyo ilikuwa ni siku ya balaa.

    Akaamka kutoka kitandani mwake na kisha kuvua nguo zote na kubaki mtupu. Akaanza kukifuata kioo kile na kisha kuingia katika ulimwengu huo. Siku hiyo kwake ikaonekana kuwa siku tofauti, mwili wake ulikuwa ukitetemeka kupita kiasi, woga ulikuwa umemtawala sana kwa kuona kwamba siku hiyo ilikuwa ni siku ya hatari sana kwake.

    Alipofika katika mlango wa nyumba kubwa ambayo ilikuwa ikifanyika kama makutano yao, nje ya nyumba ile kulikuwa na mavazi ya aina mbili, mavazi yalikuwa na rangi nyeusi na rangi nyekundu. Akainamana na kutaka kuchukua mavazi meusi ambayo mara kwa mara alikuwa akiyavaa, akakatazwa na kutakiwa kuchukua mavazi mekundu, mavazi ambayo yalikuwa kama shuka kubwa.

    Hapo ndipo Yusufu alipojua kwamba siku hiyo ilikuwa ni siku ya balaa ndani ya jengo lile kutokana na kutakiwa kuchukua mavazi mekundu, mavazi ambayo yalimaanisha umwagaji wa damu katika siku hiyo. Yusufu akaanza kupiga hatua kuelekea ndani ya jengo lile. Alipoingia ndani, wenzake walikuwa wamekwishafika kitambo na hali ilionyesha kwamba ni yeye tu ndiye ambaye alikuwa akisubiriwa mahali hapo.

    Yusufu akawa anatembea taratibu huku akionekana kuwa mwenye wasiwasi mwingi. Kiumbe cha ajabu, kiumbe ambacho kilikuwa na mwili wa kibinadamu ila baadhi ya viungo vilikuwa kama vya paka akatokea mahali hapo na kisha kumtaka yusufu kusimama. Yusufu akatii, akasimama na kisha kuanza kukiangalia kiumbe kile.

    Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakiongezeka kudunda kupita kawaida, siku hiyo ikaonekana kuwa siku ya hatari tupu. Viumbe wengine wawili wakatokea mahali pale na kisha kuanza kumwangalia, bado Yusufu alikuwa akitetemeka tu.

    “Umevunja moja ya masharti yetu” Kiumbe kile alimwambia Yusufu ambaye alibaki kimya huku akiwa ameuinamisha uso wake chini.

    “Kwa sababu umevunja moja ya masharti yetu, tutakuadhibu” Kiumbe yule alimwambia Yusufu ambaye alikuwa kimya.

    Yusufu akatakiwa kupiga hatua mbele mpaka karibu na kioo kile kilichokuwa mbele ya chumba kile. Kila mtu mahali hapo alikuwa kimya, watu ambao walikuwa wamezunguka katika kila sehemu ya chumba kile, nao walikuwa kimya huku wakiwa wameviinamisha vichwa vyao chini.

    Yusufu akapiga hatua mpaka mahali pale. Chini ya kioo atika meza kulikuwa na kisu ambacho akaamriwa kukichukua, akakichukua huku mikono yake ikitetemeka kupita kawaida. Kioo kile ambacho hakikuwa kikionyesha kitu chochote kile, kikaanza kuonyesha mianga ya radi, sehemu ile ikajaa moshi mwekundu ambao kwa mtu wa kawaida ungemfanya kuogopa sana. Ghafla katika kioo kile ikatokea taswira ya mama yake, Bi Fatuma ambaye alikuwa amelala.

    “Tunataka utoe kafala kwa kile ulichokifanya cha kuvunja moja ya masharti yetu” Kiumbe yule alimwambia Yusufu ambaye alikuwa akitetemeka kwa woga.

    “Nimuue mama yangu?” Yusufu aliuliza huku akionekana kutokuamini.

    “Ndicho unachotakiwa kukifanya” Kiumbe yule alimwambia Yusufu.

    Yusufu akabaki kimya kwa muda, akaanza kuwaangalia watu wale ambao walikuwa wamekusanyika ndani ya ukumbi wa nyumba ile na kisha kuyapeleka macho yake kwenye taswira ya mama yake katika kioo kile, bado Yusufu alikuwa akitetemeka tu. Mawazo yake yakaanza kurudi nyuma toka katika kipindi ambacho alikuwa mtoto, kipindi ambacho mama yake alikuwa ameangaika sana kwa ajili yake.

    Mambo mengi ambayo yalitokea katika miaka ya nyuma yakaonekana kuugusa moyo wake, kwa jinsi ambavyo mama yake alivyokuwa ameangaika kwa ajili ya maisha yake na leo hii amuue kwa kumtoa kafala, lilionekana kuwa jambo moja ambalo wala hakutaka litokee. Mama yake ndiye mtu pekee ambaye alikuwa amembakisha katika dunia hii, kumuua mama yake kulimaanisha kwamba alikuwa akimpoteza mtu muhimu sana maishani mwake.

    “HAIWEZEKANI. SIWEZI KUMUUA MAMA YANGU” Yusufu alisema kijasiri huku akikitupa kisu kile chini.

    Watu wote ambao walikuwa wamekusanyika ndani ya ukumbi ule wakaonekana kushtuka, maneno ambayo aliyaongea Yusufu kwa wakati huo yalimshtusha kila mmoja mahali pale. Hilo lilikuwa tukio la kwanza kutokea kwa mtu kukataa kumtoa kafala mtu ambaye aliambiwa amtoe kafala katika kipindi ambacho alivunja moja ya masharti aliyopewa.

    “Siwezi kumuua mama yangu. Ametoka mbali sana pamoja nami. Amenilea katika mazingira ya shida sana. Yeye ndiye mtu pekee ambaye amebaki katika maisha yangu. Kumuua mama yangu, hicho ni kitu kisichowezekana kabisa. Mliniambia nimuue baba yangu, nilifanya hivyo, bado hamjaridhika, mnaitaka roho ya mama yangu, hakika sitoweza kuunyanyua mkono wangu kumuua mama yangu” Yusufu aliwaambia huku akianza kulia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kama hautaki kufanya hivyo, tunavunja mkataba na wewe. Utatakiwa kurudisha pete zetu, nguo zetu., mali zetu, utajiri wetu na kila kitu ulichochukua kutoka kwetu” Kiumbe yule alimwambia Yusufu.

    “Sirudishi kitu chochote kile. Pete siwapi, utajiri siwarudishii, yaani kwa kifupi ni kwamba siwapi kitu chochote kile. Kama mtaweza, mtavichukua kinguvu, ila kiukweli siwezi kuwakabidhi vitu hivi” Yusufu aliongea kwa sauti ya juu iliyojaa hasira.

    Muda huo alionekana kama mtu aliyechanganyikiwa, Yusufu alionekana kuwa radhi kwa kila kitu katika kipindi hicho, hakuwa radhi kurudisha kitu chochote kile ambacho alikuwa amepewa katika kipindi cha nyuma. Alikuwa radhi kupokonywa kinguvu lakini si kurudisha kwa mkono wake.

    “Tunachukua kila kitu tulichokupa. Ulinzi wetu juu ya afya yako tunauchukua kuanzia sasa na kuuacha ugonjwa wa UKIMWI ukutafune mpaka kifo chako. Ndani ya mwezi mmoja tu, usiporudisha kitu chochote kile tunakuua kwa ugonjwa huo. Tarehe 2 mwezi ujao ndio utakuwa mwisho wako wa kuvuta pumzi ya dunia hii. Tutakumaliza kwa ugonjwa huu. Tutakifanya kifo chako kuwa kifo cha aibu kwa kila mtu atakayekisikia” Kiumbe yule alimwambia Yusufu huku siku hiyo ikiwa ni tarehe 2 mwezi wa tano.

    “Fanyeni chochote kile lakini siwezi kurudisha chochote mikononi mwenu. Binadamu ni mavumbi na mavumbini atarudi” Yusufu alisema na hapo hapo kuanza kuondoka. Yusufu hakutaka kutembea, akaanza kukimbia kutoka ndani ya nyumba ile. Kila kitu ambacho alikuwa amewaambia ndicho alichokifanya, hakurudisha kitu chochote kile ambacho alikuwa amepewa kutoka katika ulimwengu wa giza. Alikuwa tayari kufanya kitu chochote lakini si kumuua mama yake wala kurudisha vitu ambavyo alikuwa amepewa awe navyo.





    Yusufu hakuonekana kuwa na raha hata mara moja, muda mwingi alionekana kuwa mtu wa mawazo kupita kawaida. Adhabu ambayo alikuwa amepewa ya kuweza kumuua mama yake kwake ilionekana kuwa kubwa kubebeka kwa mkono wake mwenyewe. Njia nzima alikuwa akifikiria, hakutaka kujiona akimpoteza mama yake ambaye kwake alionekana kuwa mtu muhimu kuliko mtu yeyote ambaye alikuwa amebaki katika dunia hii katika kipindi hicho.

    Alipofika nyumbani, kitu cha kwanza alichokifanya ni kulala usingizi mzito. Asubuhi ilipoingia, moja kwa moja akaanza safari ya kuelekea Bagamoyo. Huko, akaenda kuonana na mama yake. Kitendo cha kumtia mama yake machoni mwake, machozi ya uchungu yakaanza kumlenga na hatimae kumtoka.

    Moyoni alijisikia uchungu, alikuwa akimpenda mama yake kupita kawaida katika maisha yake. Alichokifanya ni kumsogelea mama yake na kisha kumkumbatia. Bi Fatuma hakuelewa ni kitu gani ambacho kilikuwa kikiendelea katika kipindi hicho, yeye mwenyewe alikuwa akijisikia uchungu sana kila alipokuwa akimwangalia mtoto wake wa pekee, Yusufu akiwa analia.

    “Nakupenda mama” Yusufu alimwambia mama yake.

    “Nakupenda pia” Bi Fatuma alimwambia Yusufu.

    Siku hiyo walikaa na kuongea mengi, muda mwingi Yusufu alionekana kuwa mtu wa huzuni, alijua fika kwamba hakuwa na siku nyingi za kuishi ndani ya dunia hii. Alifahamu fika kwamba alikuwa njiani kuelekea kaburini jambo ambalo lilikuwa likimhuzunisha kupita kawaida.

    “Mbona leo unaonekana kuwa hivyo Yusufu?” Bi Fatuma alimuuliza Yusufu ambaye alionekana kuwa na huzuni kipindi chote.

    “Ninataka kumrudia mke wangu mama” yusufu alimjibu mama yake.

    “Unataka kumrudia Samiah?”

    “Ndio mama. Ninataka kumrudia mke wangu. Ninataka kuishi na familia yangu” Yusufu alimwambia mama yake.

    “Hilo ndilo linalokufanya kuwa hivyo mwanangu? Au kuna kitu kingine?” Bi Fatuma alimuuliza.

    “Hapana mama. Ni hilo tu”

    “Hakuna tatizo. Umekwishaongea nae juu ya hilo?”

    “Hapana”

    “Hata haujaongea nae simuni?”

    “Sijaongea nae”

    “Ongea nae kwanza”

    “Hapana mama. Nataka twende Dodoma pamoja” Yusufu alimwambia mama yake.

    Haikuwa na jinsi, walichokifanya ni kuelekea jijini Dar es Salaam ambapo huko wakakata tiketi ya ndege na kisha kuanza kuelekea Dodoma. Bado Yusufu hakuonekana kuwa na furaha kabisa, tofauti na kuihitaji familia yake lakini alionekana kwamba kulikuwa na kitu kingine ambacho kilikuwa kimemsibu moyoni mwake.

    Ndege ilichukua dakika sitini na ndipo ilipoingia katika uwanja wa ndege wa Dodoma ambapo wakateremka na kisha kukodi teksi ambayo iliwapeleka mpaka katika mtaa wa Area C ambapo alikuwa akiishi Samiah.

    Kitendo cha Yusufu kuonekana ndani ya eneo la nyumba hiyo lilionekana kumshtua kila mtu ambaye alikuwa akimwangalia. Yusufu hakutaka kujali sana, alichokifanya ni kuanza kuelekea katika nyumba hiyo pamoja na mama yake na kisha kukaribishwa.

    Siku hiyo hakukuwa na sababu ya kupoteza muda, Bi fatuma akaanza kuongea kile ambacho kilikuwa kimewaleta mahali pale kwamba Yusufu alikuwa akitaka kurudiana na mke wake, Samiah. Jambo hilo lilionekana kuwa gumu kukubalika moyoni mwa Samiah kwani alijua fika kwamba kulikuwa na uwezekano wa mwanaume huyo kuwa katika matatizo makubwa na ndio maana alikuwa akiwahitaji.

    “Ila aliniacha kwa dharau sana” Samiah alimwambia mama yake, Bi Warda.

    “Hata kama Samiah. Kumbuka kwamba alikupa talaka moja” Bi Warda alimwambia Samiah.

    Bi Warda alichukua muda wa dakika arobaini na tano kumbembeleza Samiah. Samiah akaonekana kuelewa kitu ambacho kilimfanya kuelekea sebuleni pale huku akionekana kuwa mwingi wa huzuni. Alichokifanya Yusufu mara baada ya kumtia machoni Samiah, akasimama, akamsogelea na kisha kumkumbatia.

    Yusufu akaanza kulia, hakuamini kama kweli Samiah alikuwa amemsamehe kwa kila kitu na kwa kipindi hicho alikuwa akirudi nae kuishi maisha kama zamani. Baada ya kukumbatiana kwa muda mrefu huku wote wakilia, mtoto Nasri akaletwa mahali hapo, Yusufu akamchukua na kisha kumbeba huku akionekana kuwa mwingi wa furaha.

    “Huyu ndiye atakuwa mrithi wangu wa kila kitu” Yusufu alisema huku akiwa amembeba nasri mikononi mwake.

    Kilichoendelea ni kulala Dodoma na kisha kesho asubuhi kurudi jijini Dar es Salaam huku Yusufu akiwa amekwishawaambia marafiki zake wote kwamba alikuwa akirudi jijini huku akiwa pamoja na familia yake. Hiyo ikaonekana kuwa furaha kwa marafiki zake ambao wakawapelekea taarifa ile waandishi wa habari.

    Asubuhi ya saa nne waandishi wa habari tayari walikuwa wamekwishafika katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa ajili ya kumpiga picha Yusufu huku akiwa pamoja na familia yake.

    Ndege ya precision Air ilipoanza kuingia, waandishi wa habari wakajiandaa vilivyo. Yusufu alipotoka katika jengo la uwanja wa ndege, waandishi wakaanza kumpiga picha na huku wengine wakianza kumfuata kwa ajili ya kumhoji maswali machache.

    “Ndugu mwandishi. Mke ni mke na familia ni familia. Ninampenda sana mke wangu na ninampenda sana mtoto wangu” Yusufu alimwambia mwandishi wa habari.

    “Na vipi kuhusu Manka?”

    “Sijali chochote kile. Yeye alikuwa msichana wa mpito kama walivyokuwa wengine, sitotaka kujali chochote kuhusu yeye. Ninachokijali ni familia yangu tu” Yusufu alimjibu mwandishi.

    “Kwa hiyo tutegemee nini kutoka kwako?”

    “Mengi. Ila mnatakiwa kutegemea albamu yangu iitwayo NITAKAPOKUFA pamoja na kitabu cha maisha yangu cha NITAKAPOKUFA ambacho ningependa vianze kuuzwa tarehe 2 mwezi ujao” Yusufu alimwambia mwandishi wa habari.

    “Mbona albmu yako hiyo pamoja na kitabu cha maisha yako umevipa jina linalofanana tena likiwa na msismko mkubwa?” Mwandishi alimuuliza.

    “Duniani tunapita tu, bado tupo safarini kwa sasa. Ni lazima tujue kwamba kuna siku tutakufa, sisi tutaendelea kuwa mavumbi na mavumbini tutarudi” Yusufu alimwambia mwandishi wa habari.

    Hawakutaka kukaa sana mahali hapo, moja kwa moja wakaanza kuelekea garini ambapo Kelvin alikuwa amekuja kuwachukua mahali hapo. Njiani, kidogo japo si sana Yusufu alikuwa akionekana kuwa na furaha, uwepo wa familia yake ulionekana kumfurahisha kupita kawaida.

    Walipofika nyumbani, moja kwa moja wakaelekea ndani ambapo wakakaa kochini huku Yusufu akionekana kuwa katika hali ambayo ilionyesha kwamba hakuwa na furaha kabisa japo tabasamu la kinafiki lilikuwa likionekana usoni mwake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nataka kuandika kitabu cha maisha yangu” Yusufu aliwaambia.

    “Mbona mapema sana?” Kelvin alihoji.

    “Yeah! Hiyo ni kwa sababu sina muda mrefu wa kuishi” Yusufu alijibu.

    “Mmmh! Kuna nini tena?” Bi Fatuma aliuliza huku akionekana kushtuka.

    “Nitakufa, tena si muda mrefu kuanzia sasa” Yusufu aliwaambia.

    “Mbona unaonekana kutokuwa sawa Yusufu. Kuna nini mpenzi?” Samiah alimuuliza Yusufu mbaye akaanza kutoka na machozi.

    “Naombeni mnisamehe kwa kila kitu. Sina muda mrefu wa kuishi kuanzia sasa. Naomba unisamehe mama” Yusufu alisema huku akiinuka kutoka katika kochi na kupiga magoti mbele ya mama yake.

    “Nimekwishakusamehe. Ila kuna nini Yusufu? Mbona unatuchanganya?” Bi Fatuma alimuuliza Yusufu.

    “Ninahitaji kuishi na familia yangu katika hizi siku za mwisho mama. Nimekuwa mtu muovu sana katika maisha yangu” Yusufu alimwambia mama yake.

    “Yusufu, mbona unaonekana kutokueleweka rafiki yangu?” Kelvin aliuliza.

    “Ninakwenda kufa Kelvin. Ninakwenda kuacha kila kitu nilichokuwa nacho. Ila kabla sijafa nahitaji mnisamehe sana” Yusufu aliwaambia.

    “Tatizo nini Yusufu?” Samiah aliuliza huku akiinuka.

    “Nilimuua baba” Yusufu alisema na kisha kuanza kulia.

    Kila mmoja mahali hapo akaonekana kushtuka, hawakuamini kile ambacho kilikuwa kimesemwa mdomoni mwa Yusufu ambaye alikuwa akilia kupita kawaida kama ishara ya kuwaonyeshea kwamba alikuwa akihuzunika sana kwa kile ambacho alikuwa amekifanya katika maisha yake.

    Katika hali isiyotarajiwa, Bi fatuma akaanza kulia, akaonekana kushtuka kupita kawaida. Hakukuwa na mtu ambaye alionekana kuyaamini maneno yale ya Yusufu moja kwa moja, kwao waliyaona maneno yale kuwa ya uongo.

    “Nimemuua baba kwa tamaa zangu za fedha na umaarufu. Nimekuwa nikimtumikia shetani katika kipindi chote hiki” Yusufu aliwaambia maneno ambayo yalionekana kuwashtua zaidi.

    “Imekuaje Yusufu? Usimlize Bi Mkubwa, hebu tueleze kipi kimetokea” Kelvin alimwambia Yusufu.

    Hapo ndipo ambapo Yusufu akaanza kuelezea kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea katika maisha yake toka siku ya kwanza ambayo alikuwa ameamua kuiuza nafsi yake katika ulimwengu wa giza. Ilikuwa ni stori ndefu na ya kusisismua ambayo ilionekana kumshtua kila mtu mahali pale. Stori hiyo ndefu ikasababisha kilio kikubwa kutoka kwa Bi fatuma na Samiah.

    “Nimesababisha mauaji ya watu wengi maishani mwangu” Yusufu aliwaambia huku akiendelea kulia.

    Kila mmoja mahali pale alionekana kuwa na huzuni kupita kawaida, historia ambayo Yusufu aliizungumza mahali pale ilikuwa imewagusa kupita kawaida. Hawakuamini kwamba Yusufu angeweza kufanya yale ambayo alikuwa ameyafanya. Umaarufu wote ambao alikuwa ameupata, mvuto wote ambao alikuwa ameupata vyote hivyo vilitokana na mkataba wa damu ambao alikuwa ameusaini katika ulimwengu wa giza.

    Maneno yake yalimuuma kila mmoja mahali pale, Yusufu yule ambaye alikuwa amefanya mambo mengi katika maisha yake, mtu ambaye alikuwa amependwa na watu wengi katika maisha yake leo hii kila kitu kilikuwa kimejulikana katika familia yake.

    “Kwa nini ulifanya haya Yusufu?” Mama yake, Bi Fatuma aliuliza huku akilia.

    “Umasikini mama. Sikuwa nikiupenda umasikini, nilitaka kujiondoa katika maisha haya ambayo yalikuwa yakinikasirisha kila siku. Pamoja na hayo, nikatamani fedha, nikatamani kutembea na wanawake wazuri, nikatamani kuendesha magari ya kifahari pamoja na kumiliki nyumba nyingi za gharama. Hizo ndizo sababu ambazo zilinifanya kumtumikia shetani mpaka siku ambayo waliniambia nikuue na kukataa” Yusufu alimwambia mama yake.

    Japokuwa moyoni alikuwa ameumia sana lakini hakukuwa na jinsi, Bi Fatuma akasimama kutoka pale alipokuwa amekaa na kisha kumsimamisha Yusufu na kukumbatia. Katika kipindi hicho, hakikuwa kipindi cha kupeana lawama kwa kile ambacho kilikuwa kimetokea, walitakiwa kusahau kile kilichopita na kupanga mambo mengine.

    “Ninakufa mama. Ninakufa nikiwa mdogo sana, ninakufa nikiwa katika mafanikio makubwa sana” Yusufu alimwambia mama yake huku akiendelea kulia.

    “Mungu atakuwa pamoja nawe kijana wangu”

    “Hapana mama. Mimi ni muovu, moyo wangu umejaa dhambi, mikono yangu imejaa damu. Nimesababisha vifo vya watu wengi katika nchi hii, watu ambao walinionyeshea mapenzi, watu ambao hawakuwa na hatia” Yusufu alimwambia mama yake na kuendelea.

    “Naombeni mnisamehe. Naombeni msamaha wenu kwa kila nilichokifanya” Yusufu alisema huku akiendelea kulia.

    Siku hiyo ikaonekana kuwa ya huzini katika maisha ya kila mmoja aliyekuwa mahali hapo. Alichokifanya Yusufu ni kuingia ndani na kisha kuleta hati za nyumba zake pamoja na biashara zake na kisha kuliandika jina la mtoto wake, Nasri pamoja na mke wake, Samiah.

    Yusufu hakuishia hapo, alichokipanga kukifanya ni kuzigawa fedha zake zote zilizokuwa benki ambazo zilikuwa ni zaidi ya bilioni mbili na kisha na kumgawia mama yake, mke na mtoto wake pamoja na mama yake.

    “Sitakiwi kumiliki kitu kwa sasa. Ninakwenda kufa, haina jinsi, naomba mkubali kwamba ninakufa katika kifo kibaya sana” Yusufu aliwaambia.

    ****

    Siku iliyofuata asubuhi na mapema, Kelvin akatumwa kwenda kumtafuta mwandishi bora wa vitabu katika kipindi hicho, George Iron Mosenya kwa ajili ya kumwandalia kitabu chake cha maisha yake kwa malipo makubwa. Mara baada ya Mosenya kufika katika nyumba ile, moja kwa moja akaanza kuongea na Yusufu.

    “Ninataka uandike kitabu cha maisha yangu” Yusufu alimwambia Mosenya.

    “Hakuna tatizo” Mosenya alijibu kwa haraka kwani nae aliona kama zali kuambiwa aandike kitabu cha mtu maarufu kama Yusufu.

    “Ila ninataka kiuzwe kuanzia tarehe 2 mwezi ujao” Yusufu alimwambia Mosenya.

    “Mmmh! Mbona haraka sana?”

    “Ni kwa sababu sina muda mrefu wa kuishi katika dunia hii” Yusufu alimwambia Mosenya.

    “Sawa. Hakuna tatizo ila itabidi hata malipo yake yawe makubwa kidogo” Mosenya alimwambia Yusufu.

    “Hakuna tatizo. Unataka nikulipe kiasi gani?”

    “Milioni nne”

    “Hilo si tatizo. Nitakupa milioni tano” Yusufu alimwambia Mosenya.

    Hapo ndipo Yusufu akamtahadhalisha Mosenya kwamba kila kitu ambacho angekwenda kumwambia muda huo kibaki siri yake na si kwenda kumwambia mtu yeyote yule mpaka kitabu kitakapotoka. Mwandishi Mosenya akakubali kwamba angekwenda kuitunza siri hiyo, hapo ndipo Yusufu alipoanza kumhadithia kila kitu.

    Muda wote Mosenya alikuwa akimya huku akisikiliza kwa makini, kila kitu ambacho alikuwa akiambiwa alikisikiliza kwa makini kabisa huku akikataa kupitwa na kitu chochote kile hali iliyompelekea kuchukua simu yake na kisha kuanza kurekodi kila kitu ambacho aliongea Yusufu.

    Ilikuwa ni stori ambayo ilimgusa sana Mosenya kiasi ambacho hakuonekana kuamini kwamba vile vitu ambavyo alikuwa akivisikia vilikuwa vikitokea na wala havikuwa simulizi kama ambavyo alivyokuwa akihisi katika kipindi cha nyuma.

    Kila siku Mosenya alikuwa akifika nyumbani hapo na kuendelezewa stori ile mpaka wiki ya kwanza ilipokatika, katika kipindi ambacho Yusufu akaanza kuumwa. Kwanza akaanza kukonda, mwili wake ukaanza kukosa nguvu jambo ambalo lilimfanya kupelekwa hospitalini.

    Kila mtu ambaye alikuwa amesikia hali ambayo alikuwa nayo Yusufu, alionekana kuumia kupita kawaida. Waandishi wa habari walipompiga picha na kutoa kwenye magazeti, watu walibaki wakishangaa kupita kawaida, hawakuamini kama yule ambaye alikuwa akionekana alikuwa Yusufu au mtu mwingine ambaye alionekana kuwa mfano wa Yusufu.

    Kila mtu akaanza kuhoji ni kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka ugonjwa wa ghafla vile kumpata lakini hakukuwa na mtu ambaye alipata jibu lolote lile.Yusufu aliendelea kuugua kitandani pale huku akiendelea kumwadithia mwandishi Mosenya kile ambacho kilikuwa kimeendelea katika maisha yake. Kadri siku zilivyokuwa kwenda mbele na ndivyo ambavyo alizidi kuugua zaidi na zaidi. Mara kwa mara watu walikuwa wakifika mahali hapo na kumpa pole.

    “Hii ngoma aiseee” Jamaa mmoja alimwambia mwenzake.

    “Ndio yenyewe. Daah! Jamaa kakonda mshikaji”

    “Ndio hivyo. Kila siku tunaambiwa ugonjwa unaua lakini hatusikii. Sisi tunaendekeza kuwavua wanawake sketi bila kutumia kinga, tunaendelea kutumia vitu vyenye ncha kali tena kwa kuchangia pamoja. Majanga yake ndio huwa namna hii sasa” Jamaa mwingine alimwambia mwenzake.

    “Albamu yangu ipo tayari na itaanza kuuzwa tarehe 2. Kitabu changu pia kinakamilika na kitaanza kuuzwa tarehe 2 pia. Fedha ambazo zitapatikana naomba ziwasaidie watoto yatima, zikiwezekana zijenge hospitali moja kubwa ya watoto mtaa wa Tandale. Kiasi kingine kitakachobaki naomba ipewe familia yangu pamoja na Kelvin ambaye ni rafiki wangu wa siku nyingi” Yusufu alimwambia mwanasheria wake.

    “Hakuna tatizo. Sasa tugawe asilimia ngapi hapo?”

    “Asilimia arobaini zitengeneze hospitali, asilimia kumi na tano apewe Kelvin, asilimia ishirini na tano ipewe familia yangu na asilimia ishirini apewe mama yangu” Yusufu alimwambia mwanasheria wake ambaye akaandika kila kitu.

    Yusufu aliendelea kubaki kitandani pale zaidi na zaidi. Kutokana na jina lake kuwa kubwa sana, wanamuziki wengi kutoka barani Afrika wakafika nchini Tanzania kwa ajili ya kumuona Yusufu ambaye alikuwa amekonda sana kitandani. Viongozi mbalimbali wa nchi wakiwepo maraisi wa nchi mbalimbali nao hawakuachwa nyuma, walikuwa wakifika hospitalini hapo na kumuona Yusufu.

    Yusufu akaonekana kuwa mfano mzuri kwa vijana wote ambao walikuwa wakiendekeza matendo ya ngono huku wakijifanya kutokujua ni kwa namna gani ugonjwa ule ulivyokuwa ukiua. Picha ya Yusufu kitandani pale ilikuwa ni fundisho tosha kwa kila mtu ambaye alikuwa akimwangalia.

    Muda mwingi Yusufu alikuwa akilia. Hakuwa akilia kwa sababu alikuwa akifa, hapana, alikuwa akilia kwa sababu alikuwa amefanya mambo mengi sana ya kusikitisha katika ulimwengu huu hasa likiwa hili la kumtumikia shetani katika maisha yake.

    “Ninakufa ila nitataka watanzania wajue kila kitu kuhusiana na maisha yangu ya nyuma” Yusufu aliwaambia waandishi wa habari katika kipindi ambacho walikuwa wamekusanyika hospitalini hapo.

    “Hii ndio sababu ya kukufanya kuandaa kitabu na albamu yako ya mwisho ya NITAKAPOKUFA?”Mwandishi alimuuliza.

    “Ndio”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwa hiyo ulikuwa ukijua kwamba unakwenda kufa karibuni?”

    “Ndio”

    “Ulijuaje?”

    “Majibu yote yatapatikana katika kitabu hicho” yusufu alijibu.

    Taarifa ile ikatolewa katika magazeti mengi nchini kwamba siri ya kifo cha Yusufu ilikuwa ikipatikana katika kitabu cha stori ya maisha yake cha NITAKAPOKUFA ambacho kilitarajiwa kutoka tarehe 2 mwezi ujao, siku ambayo alisema kwamba ilikuwa siku ambayo atayafumba macho yake milele.

    Kila mtu akawa na hamu ya kutaka kukisoma kitabu hicho, walitaka kufahamu mambo mengi katika kitabu hicho huku wakitaka kufahamu zaidi majina ya wasichana wengi ambao alikuwa amewaandika mule ambao alikuwa ametembea nao huku asilimia tisini na nane wakiwa wamekwishakufa kwa ugonjwa wa UKIMWI.

    “Ninakupenda mke wangu. Ninaacha kila kitu katika maisha yako, sikutaka kumuachia hawala yeyote mali yangu yoyote, nimekuachia wewe mpenzi. Naomba uishi maisha mema, naomba umlee Nasri katika maisha bora mke wangu” Yusufu alimwambia Samiah ambaye muda mwingi alikuwa akilia.

    “Nitafanya hivyo mume wangu” Samiah alimwambia Yusufu huku akiendelea kulia.

    “Naomba uniahidi”

    “Nakuahidi kufanya hivyo”

    “Nashukuru. Nakuacha na maisha yako. Kufa kwangu haimaanishi kwamba nawe umeathirika, hapana. Katika kitabu changu nimejaribu kuelezea kwa kina kwamba niliporudiana nawe sikulala nawe kabisa. Ila katika yote kumbuka kwamba kuna wanaume wengi watataka kuja kukuoa, si kwamba wewe ni mzuri, bali wengi wao watakuja wakiwa na tamaa ya kumiliki kila ulicho nacho. Sikuzuii usiolewe, hapana. Kama ukitaka kuolewa, olewa ila yakupasa kuwa makini mke wangu” Yusufu alimwambia Samiah.

    “Nimekuelewa mume wangu” Samiah alimwambia Yusufu ambaye macho yake akayageuza kwa Kelvin.

    “Wewe ni rafiki yangu Kelvin” Yusufu alimwambia kelvin.

    “Najua sana Yusufu. Wewe ni rafiki yangu ambaye kwangu nakuona ni ndugu yangu pia” kelvin alimwambia yusufu.

    “Unaniona ninavyoteseka?”

    “Ndio. Nakuona Yusufu”

    “UKIMWI mbaya rafiki yangu. UKIMWI unatisha. Huu si ugonjwa wa kuchezea. Watu niliokuwa nawatumikia wameuacha huu ugonjwa unitese. Na kweli unanitesa sana hapa kitandani” Yusufu alimwambia Kelvin.

    “Pole sana”

    “Fedha nilizokuachia ni nyingi mno. Nakuomba usifanye mambo ya anasa, jaribu kuzifanyia mambo ya maana fedha hizo” Yusufu alimwambia Kelvin.

    “Usijali”

    “Ninakufa lakini nikiwa na uchungu sana. Nakufa nikiwa kijana mdogo sana. Nakuomba sana kelvin usifanye anasa. Nakusisitiza kwa mara nyingine, usifanye anasa” Yusufu alimwambia Kelvin.

    “Usijali Yusufu” Kelvin alimwambia Yusufu ambaye akamgeukia mama yake.

    “Umekuwa kila kitu kwangu mama. Wewe ndiye mtu ambaye nilikubakiza kwenye dunia hii, sikutaka kukuona unakufa ili niendelee kuishi katika maisha ya kitajiri, nilitamani kukuona ukiishi kila siku katika maisha yangu. Ninakufa sasa mama, ninahitaji umlee mtoto wangu ambaye ni mjukuu wako, Nasri katika malezi bora kama ambavyo ulivyokuwa ukinilea mimi” Yusufu alimwambia mama yake.

    “Nitafanya hivyo Yusufu”

    “Nakuomba usahau kila kilichopita mama”

    “Usijali mwanangu. Siwezi kuvikumbuka tena” Bi Fatuma alimwambia Yusufu huku akilia.

    Siku hiyo ndio ikawa siku ya mwisho kwa Yusufu kuongea nae, siku iliyofuata, siku ya tarehe 2 mwezi wa sita ikawa mwisho wa Yusufu kuvuta pumzi ya dunia hii. Alikufa huku pete zile ambazo alikuwa amepewa katika ulimwengu ule wa giza zikiwa vidoleni mwake ambapo baada ya dakika kadhaa, zikapotea.

    Kioo pamoja na nguo ambazo alikuwa amekabidhiwa na kuviweka chumbani kwake navyo vikawa vimepotea. Hivyo ndivyo vitu ambavyo vilichukuliwa kutoka kwake. Fedha na mali nyingine vikaachwa kama vilivyo.

    Huyo ndiye alikuwa msanii maarufu wa muziki barani Afrika, Yusufu au The Ruler kama alivyokuwa akijulikana na wengi. Maisha ya tamaa yalionekana kumkaribisha katika ulimwengu wa giza, ulimwengu ambao alikuwa ameamua kuutumikia kwa nguvu zote.

    Siku hiyo ambayo alifariki ndio siku ambayo albamu yake aliyoiita NITAKAPOKUFA pamoja na kitabu cha stori ya maisha yake cha NITAKAPOKUFA vilipoanza kuuzwa. Vitabu na albamu ile vikagombaniwa sana mitaani. Kopi za vitabu zaidi ya milioni saba zikauzika, albamu yake ikauza zaidi ya kopi milioni tatu na nusu. Kiasi kikubwa sana cha fedha kikaingia, kiasi ambacho hakupata nafasi hata ya kutumia shilingi mia moja.

    Japokuwa alikuwa amekufa, familia yake ikabaki kwenye utajiri mkubwa sana, rafiki yake, Kelvin nae akawa kwenye utajiri mkubwa sana. Yusufu akazikwa Bagamoyo, mazishi ambayo yalihudhuriwa na watu wengi zaidi ya mazishi ya mwalimu Nyerere au mwigizaji Steven Kanumba.

    Maisha yake ya muziki pamoja na kazi zake zilionekana kuwa kumbukumbu vichwani mwa Watanzania ambao mpaka leo hii bado wanaendelea kumkumbuka kwa vile alivyokuwa amefanya hapa nchini. Japokuwa watu walijua fika kwamba alikuwa ametumia nguvu za giza lakini bado mapenzi yao yalikuwa makubwa kwa Yusufu, mvuto wake bado uliendelea kubaki mioyoni mwao.

    “PUMZIKA KWA AMANI” Yalikuwa maneno ya kila mtu ambaye alikuwa akielekea Bagamoyo na kuliona kaburi lake.



    MWISHO.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Maisha anapanga Mungu, Yeye ndiye anajua kwamba fulani aishi maisha ya kuwa hivi na fulani aishi maisha ya kuwa vile. Hatutakiwi kulazimisha vitu vile ambavyo Mungu hakupanga tuwe navyo katika kipindi fulani kama ilivyokuwa kwa Yusufu. Mungu anapoamua kukupa utajiri, hauna masharti, Mungu anapoamua kukupa usupastaa, pia hauna masharti hata kidogo.

    Shetani ni mjanja sana, kila kitu unachotaka akugawie, atakupa kwa sababu amekwishapewa mamlaka kuitawala dunia hii na mambo yake ya anasa. Ukitaka fedha, shtani atakupa, ukitaka utajiri, shetani atakupa ila kumbuka kwamba hawezi kukupa vitu hivyo bila masharti. Atakupa pamoja na masharti ambayo ana uhakika ni lazima utayavunja na hivyo kukudai damu.

    Katika maisha yako, usikubali kutafuta vitu kwa kutumia nguvu za giza kwani kamwe hautouonea raha utajiri utakaokuwa nao.

    Mpe Mungu nafasi nae atakwenda kufanya kile uombacho kwa muda wake ambao anasema hachelewi wala hawahi, huja kwa muda muafaka.

0 comments:

Post a Comment

Blog