Search This Blog

Wednesday, 1 June 2022

ONLY YOU ( NI WEWE TU ) - 3

 







    Simulizi : Only You ( Ni wewe Tu )

    Sehemu Ya Tatu (3)

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Bahati nzuri kwake ni kwamba aliwakuta wazazi wote wawili. Kwa jinsi alivyoonekana tu, wote wakahisi kwamba kulikuwa na jambo baya lilikuwa limetokea, akawasalimia na kukaa kwenye kochi.

    Hakutaka kupoteza muda, akawaambia wazazi wa Jackline kila kitu kilichotokea, jinsi msichana huyo alivyoomba muda wa kuonana naye na kumwambia yake aliyokuwa amemwambia kwamba walitakiwa kuachana kwa kuwa alimpata mwanaume mwingine aliyejua kupenda, aliyejua kujali zaidi yake.

    “Yaani Jackline ndiye amesema hivyo?” aliuliza mzee mwamanda.

    “Ndiyo baba! Nimechanganyikiwa. Nyie wenyewe mnajua ni kwa jinsi gani ninampenda binti yenu. Moyo wangu umeumizwa mno, wakati mwingine siamini kile alichokuwa ameniambia!” alisema Peter, machozi hayakuacha kutiririka mashavuni mwake.

    “Au kuna jambo baya ulimfanyia?” aliuliza mama yake Jackline.

    “Hapana mama! Sikumfanyia jambo lolote baya!”

    “Sasa inakuwaje awe ameamua uamuzi mgumu namna hii?”

    “Hata mimi nashangaa!”

    “Basi sawa, tutazungumza naye, tuachie sisi,” alisema mzee Mwamanda.

    Moyo wa Peter kidogo ukaridhika, akasimama, akaaga na kuondoka. Akiwa njiani ndani ya gari, akachukua simu yake na kumpigia Jackline, simu haikuwa ikipokelewa. Moyo wake uliuma kupita kawaida, alichoamua ni kumtumia meseji.

    “Naomba unisamehe kwa kila kitu!” aliandika.

    “Usijali Peter! Nimekusamehe! Najua wewe ni binadamu, wakati mwingine unakosea na unahitaji msamaha pia,” alijibiwa meseji yake.

    “Nashukuru kwa kunisamehe!”

    “Haina shida!”

    “Kwa hiyo?”

    “Kuhusu?”

    “Kurudiana nami?”

    “Hilo ni vigumu Peter. Siwezi kufanya jambo kama hilo!”

    “Lakini si umesema umenisamehe?”

    “Ndiyo! Nimekusamehe lakini si kurudiana nawe tena. Naomba unielewe Peter. Huu ni uamuzi mgumu sana kuufanya katika maisha yangu, kumuacha mtu unayempenda ni jambo gumu sana, ninahuzunika, ninalia lakini naamini kuna siku nitapata furaha kwa huyu niliyekuwanaye. Nakutakia siku njema,” ulisomeka ujumbe aliouandika Jackline.

    Peter aliusoma zaidi ya mara kumi na tano, machozi yaliendelea kutiririka mashavuni mwake, aliumia kupita kawaida, hakuamini kama mtoto wa tajiri kama yeye, mwenye elimu yake alikuwa akipitia maisha yale.

    Aliamini katika pesa na elimu kwamba unapokuwa na pesa, hakuna kitu kigumu mbele yako, unapokuwa na elimu hakuna mwanamke yeyote ambaye anaweza kukubabaisha, muda huo ndipo akagundua kwamba pesa si chochote kile, kulikuwa na uwezekano mkubwa wa tajiri kuachwa na kufuatwa masikini.

    Elimu aliyokuwanayo haikuweza kumsaidia katika suala la mapenzi, alisononeka, alilia lakini hayo yote hayakubadilisha kile kilichokuwa kimetokea.

    Baada ya kufika nyumbani, akaliingiza gari ndani, akalipaki na kuelekea sebuleni. Alihitaji kuzungumza na wazazi wake na kwa sababu hawakuwa wamerudi, akawasubiri mpaka ilipofika majira ya saa mbili usiku ambapo wakarudi na kuanza kuwasimulia kile kilichokuwa kimetokea.

    Wao wenyewe hawakuamini, alimfahamu Jackline, alikuwa msichana mrembo ambaye alimpenda mtoto wao kwa mapenzi ya dhati. Alikuwa tayari kufanya kitu chochote kile lakini si kumuacha Peter.

    Wakahisi kulikuwa na kitu kilichokuwa kimetokea ambacho hakikuwa sawa, walichokifanya ni kumpigia simu msichana huyo, akapokea na alipoulizwa kuhusu jambo hilo, hakutaka kuwaficha, aliwaambia ukweli kwamba aliachana na mwanaume huyo.

    “Kwa nini?” aliuliza baba yake kwa sauti ya chini.

    “Baba! Sitaki kumuumiza Peter,” alisikika Jackline.

    “Unamaanisha nini na wakati tayari ushamuumiza?” aliuliza mzee huyo.

    “Kwa maumivu ambayo atayapata baadaye, ni bora aumue sasa hivi. Baba! Ninatamani Peter awe na furaha, sipendi kumuumiza zaidi ya anavyoumia sasa hivi ndiyo maana ninahitaji awe peke yake, huru kutafuta msichana yeyote yule,” alisema Jackline.

    Mzee huyo akaona kabisa Jackline alikuwa mgumu kuingilika, alichohisi ni kwamba kulikuwa na tatizo kwani kwa mtu kama Jackline ambaye alijielewa asingeweza kuchukua uamuzi wa ghafla kama huo.

    Akamwambia Peter awaambie ukweli wa kila kitu kilichokuwa kikiendelea, yaani waambiwe sababu yote. Hakuwa na jinsi, huo haukuwa muda wa kuficha ugonjwa, alichokifanya ni kuwaambia maneno yaleyale ambayo Jackline alimwambia.

    “Kwamba hukumjali?” aliuliza baba yake.

    “Ndivyo alivyoniambia!”

    “Hukuwa unampa muda?”

    “Hilo nalo aliniambia!”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Na kweli hukuwa ukifanya hayo yote?” aliuliza mzee huyo.

    “Baba! Yaani nashindwa nizungumze nini!” alisema Peter.

    Hilo lilikuwa tatizo kubwa kwenye mahusiano, kumpa mwenza muda wa kuwa naye lilikuwa jambo zuri mno ambalo kila mtu alikuwa akilihitaji.

    Mapenzi hayakutaka ubize, mapenzi hayakutaka kujificha, ili uwe na mpenzi wako kwa kipindi kirefu ilikuwa ni lazima umpe muda wa kuwa naye.

    Peter hakuwa akiyafanya hayo, alimuona Jackline kuwa msichana wa kawaida kwamba hata kama asingemfanyia vile alivyokuwa akitaka bado msichana huyo angeendelea kuwa naye.

    Moyo wa Jackline ulichoka na hatimaye akampata mwanaume aliyempa kila kitu, muda na nafasi ya kumsikiliza japokuwa hakuwa mzuri wa sura kama peter wala pesa alizokuwanazo mwanaume huyo.

    Peter hakulala, usiku mzima ulikuwa ni wa maumivu makali, alikuwa akijifikiria ni kitu gani alitakiwa kufanya. Hakutaka kumpoteza Jackline lakini kwa kile kilichotokea kilionyesha kwamba yeye na msichana huyo wasingeweza kuwa pamoja tena.

    “Ni lazima nipambane! Ni lazima nilirudishe penzi la Jackline kwangu kwa mara nyingine. Kama ni muda, nitampa, nitamjali na kumfanyia kila kitu,” alisema Peter ambaye hakujua kama vile vyote alivyoahidi kumpa msichana huyo, tayari alikuwa akipewa na Daniel.







    Mapenzi yalikuwa motomoto, kila mmoja alimuonyeshea mwenzake jinsi alivyokuwa akimpenda. Japokuwa mara kwa mara Daniel alikuwa akienda nyumbani kwa akina Jackline lakini mzee Mwamanda hakugundua kwamba kijana huyo ndiye aliyemchanganya binti yake na kumuacha Peter.

    Kwake alimchukulia kama daktari ambaye mara nyingi alikuwa akifika nyumbani hapo na kumwangalia mtoto wake. Muda ambao Daniel alikuwa akienda ni ule ambao mzee huyo hakuwa nyumbani hapo.

    Alikuwa akipigiwa simu na Jackline na kuambiwa kwamba mzee hakuwepo hivyo kwenda huko. Hakukuwa na mtu aliyegundua kitu chochote kile mpaka siku moja ambapo mama yake aliwafuma chumbani kwa Christopher wakiwa wamekumbatiana.

    Mwanamke huyo alishtuka, ni kama aliona kitu cha ajabu mbele yake, kile kilichokuwa kimetokea kiliuchanganya kchwa chake na kuhisi kama alikuwa akiota.

    Hakuamini kuwaona wawili hao wakiwa wamekumbatiana, alichokuwa akikijua ni kwamba hawakuwa na mazoea ya karibu sasa iweje wafikie hatua ya kukumbatiana kama ilivyokuwa.

    Hata kabla hajazungumza kitu chochote, haraka sana Jackline akajitoa mikononi mwa Daniel na kumsogelea mama yake, kwanza akamuomba msamaha kwa kile alichokishuhudia lakini pia akamwambia ukweli kwamba huyo ndiye alikuwa mpenzi wake.

    “Unanichanganya! Yaani kujuana juzi tu?” aliuliza mwanamke huyo huku akionekana kuchanganyikiwa.

    “Hatukuanza kuonana juzi!”

    “Kumbe lini?”

    Jackline akaanza kumwadithia mama yake kila kitu kilichokuwa kimetokea nyuma. Wakati huo Daniel alikuwa kimya, aliangalia chini kwa aibu, akahisi kabisa alivuruga kila kitu mahali hapo.

    Jackline alichukua dakika kadhaa kumuhadithia mama yake kilichokuwa kimetokea, mwanamke huyo alikuwa kimya tu. Kwa maelezo ya Jackline yalionyesha ni kwa jinsi gani Daniel alikuwa na mapenzi ya dhati kwa binti yake.

    Hakuamini kama kungekuwa na mwanaume ambaye angeweza kujitoa kama ilivyokuwa kwa Daniel ambaye alikuwa radhi kupoteza kila kitu lakini si kumuacha Jackline.

    “Daniel! Anachokiongea ni kweli?” aliuliza mama yake huku akimwangalia Daniel.

    “Ndiyo mama!”

    “Una uhakika kwamba unampenda binti yangu?” aliuliza tena huku akiwa amemkazia macho.

    “Ndiyo mama! Ninampenda Jackline!” alijibu Daniel kwa kujiamini kabisa.

    Hiyo ilitakiwa kuwa siri, hawakutaka mzee Mwambanda ajue kitu chochote kwa wakati huo kwani miongoni mwa watu ambao walikataa katakata kuona Jackline akiachana na Peter alikuwa yeye.

    Mara nyingi wawili hao walikuwa pamoja, walikuwa wakitoka na kwenda sehemu mbalimbali kuyafurahia maisha. Kwao, hakukuonekana kuwa na watu wengine waliokuwa wakipendana kama walivyokuwa.

    Walibadilishana mawazo na muda mwingi Jackline alimwambia Daniel kwamba angempenda mpaka kufa kwake.

    Uhusiano wao haukuwa siri nyumbani kwa akina Daniel, aliwaambia wazazi wake kwamba Jackline alikuwa mpenzi wa maisha yake na alikuwa tayari kumuoa muda wowote ule ambao msichana huyo angependa.

    “Daniel!” aliita baba yake huku akimwangalia.

    “Naam!”

    “Unanishangaza sana. Unamwamini vipi mtu kama huyo msichana, ni msichana wa maisha mazuri, si ndiyo?” aliuliza baba yake.

    “Ndiyo!”

    “Unadhani hajawaona watoto wa vibosile wote na kukufuata wewe? Hivi Daniel, una akili kweli?” alihoji baba yake.

    “Lakini baba...”

    “Daniel! Unatakiwa kukua na kuufahamu vema ulimwengu wa mapenzi.” Alisema mzee huyo.

    Hakumwamini kabisa Jackline, kwake, wasichana waliotoka katika familia bora walikuwa watu wa tofauti kabisa, wanaoringa na ambao wanaweza kuchukua uamuzi wowote muda wowote ule.

    Hakutaka kumuona kijana wake akipotea, alimwambia wazi kwamba huyo Jackline hakuwa na akili ya kuwaacha watoto wa matajiri na kumfuata yeye wa maisha ya chini.

    Kwa Daniel hakutaka kuelewa lolote lile, kwake, aliamini kwamba Jackline alikuwa msichana wake wa maisha yake yote hata kama kungetokea kitu gani, angekuwa na msichana huyo maisha yake yote.

    Bado Daniel alikuwa akiendelea na masomo yake chuoni, mapenzi yalichukua sehemu kubwa ya maisha yake lakini hakutaka kabisa kuona akimpoteza msichana mrembo kama Jackline.

    Aliwaambia marafiki zake kuhusu msichana huyo na mipango mingi aliyokuwanayo kwake, kila mtu alipomwangalia aliamini kabisa kwamba Daniel alikuwa kwenye penzi la dhati kwani kwa jinsi alivyokuwa akiongea, penzi halikujificha hata kidogo.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku zikaendelea kukatika. Baada ya miezi kadhaa Daniel akaanza kujisikia hovyo mwilini mwake, akaanza kusikia maumivu makali ya mgongo huku wakati mwingine akijisikia kizunguzungu.

    Hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, alichokifanya ni kumwambia mpenzi wake. Jackline aliposikia, moyoni mwake aliumia mno na kumwambia kwamba alitakiwa kwenda kupima.

    Hilo halikuwa tatizo, siku iliyofuata akaelekea huko na kupima kawaida, hakukutwa na ugonjwa wowote ule na kuona kwamba inawezekana kulikuwa na tatizo jingine au kama ni ugonjwa ulikuja na kuondoka.

    “Ulipima nini?” aliuliza Jackline.

    “Maralia, typhord, sina chochote,” alisema Daniel.

    “Hivyo tu?”

    “Ndiyo!”

    “Kingine?”

    “Sikupima!”

    “Na sasa hivi unajisikiaje?”

    “Kidogo afadhali! Nahisi ilikuwa ni ugonjwa wa kupita,” alisema Daniel huku akionekana kudharau alichokuwa akiumwa.

    Akapuuzia, hakutaka tena kwenda hospitalini, akajisikia vizuri kabisa hivyo kuendelea na maisha yake kama kawaida. Penzi likawa penzi, wakati mwingine Jackline alikuwa akitoroka nyumbani kwao na kwenda kwa akina Daniel na kulala huko.

    Hiyo ilikuwa ni siri kubwa, baba yake hakujua ila mama yake ndiye aliyekuwa akifahamu kila kitu. Hakuwa na cha kufanya, alishindwa kabisa kumzuia binti yake kwenda huko.

    Baada ya miezi sita, Jackline akaanza kujisikia tofauti mwilini mwake, akaanza kutapika na mwili kuwa na uchovu mkubwa. Hakutaka kujiuliza hicho kilikuwa kitu gani, jibu lililokuja kichwani mwake ni kwamba alikuwa na mimba.

    Hakutaka kubaki na jibu hilo moyoni mwake, ilikuwa ni lazima kwenda kuthibitisha hospitalini, akaenda huko, akapima na kile alichokuwa akikifikiria ndicho ambacho alikutana nacho, akapewa majibu yake, akayachukua na kuangalia, ni kweli alikuwa na mimba.

    “Ahsante Mungu,” alijikuta akisema huku akitabasamu. Hakumfikiria baba yake, hakujua ni kwa jinsi gani mwanaume huyo angebadilika na kuwa mbogo, alichokuwa amekiangalia ni kuzaa na mwanaume aliyekuwa

    akimpenda, Daniel tu.

    ***

    Moyo wa Peter haukuwa katika hali ya kawaida, bado alikuwa amechanganyikiwa kutokana na kuachwa na msichana Jackline. Alimpenda msichana huyo na kwenye maisha yake hakuona kama angetokea msichana mwingine ambaye angempenda kama ilivyokuwa kwa huyo.

    Alichokihitaji sana ni kuonana na mwanaume aliyekuwa amempokonya Jackline kutoka mikononi mwake, alifikiria namna ambayo alitakiwa kuanzia kwani hata kwenda nyumbani kwao alijisikia aibu, hivyo kitu pekee ambacho alikiona kufaa sana ni kumpigia simu ndugu yake na Jackline, Erick.

    Simu ikaanza kuita, iliita na kuita lakini haikupokelewa mpaka ilipokatika. Hakutaka kuishia hapo, akapiga tena na tena mpaka simu ilipopokelewa na mwanaume huyo.

    Cha kwanza kilikuwa ni kushtaki kwa kile kilichokuwa kimetokea, alimwambia Erick kuwa aliachwa na Jackline kwani aliamua kuwa na mwanaume mwingine kabisa.

    Kwa Erick, hakuamini alichokisikia, alihisi kama Peter alikuwa akimdanganya. Alimfahamu kijana huyo, alimpenda mno ndugu yake na muda mwingine alimwambia kwamba kwenye maisha yake hakukuwa na kitu kilichokuwa na nguvu kama mapenzi waliyokuwa wakipendana watu hao.

    Mbali na hayo akaanza kuyakumbuka maneno ya dada yake, aliyakumbuka vilivyo jinsi alivyokuwa akimwambia kwamba kwake, Peter alikuwa ni mwanaume wa ndoto ambaye alikuwa tayari kuolewa naye, kuishi naye mpaka siku ambayo Mungu angemchukua katika dunia hii.

    Leo, alikuwa akishtakiwa kwamba Jackline alimwacha Peter, haikumuingia akilini mwake na muda mwingi alihisi kama alikuwa akitaniwa.

    “Peter! Hivi unachoniambia ni kweli au?” aliuliza Erick huku akiwa amemsikiliza mwanaume huyo kwa muda mrefu alivyokuwa akijielezea.

    “Erick! Siwezi kukuficha! Jackline ameniacha,” alisema.

    “Hebu tuonane!”

    “Sawa.”

    Ni ndani ya nusu saa wakaonana maeneo ya Mlimani City ambapo wakaingia katika mgahawa wa Marry Brown na kuanza kunywa kahasa. Hapo ndipo Peter alipoanza kumuhadithia mwanaume huyo kila kitu kilichokuwa kimetokea.

    Erick alikuwa kimya, alimsikiliza Peter kwa umakini kabisa. Kwa jinsi alivyokuwa akiongea, ilikuwa ni rahisi kubaini kwamba mwanaume huyo alikuwa na maumivu makali moyoni mwake.

    Aliongea kwa sauti iliyokuwa na uchungu huku macho yake yakimlenga machoni mwake. Alitumia dakika kadhaa, alipomaliza, akanyamaza, akachukua kitambaa chake na kuanza kufuta machozi yaliyoanza kumtiririka.

    “Tatizo hasa ni nini?” aliuliza Erick huku akimwangalia Peter.

    “Sijajua! Ni maamuzi ya ghafla sana,” alijibu Peter.

    “Peter! Dada yangu ana akili sana, hawezi kufanya maamuzi ya kipuuzi ndani ya muda mchache, nahisi kuna kitu, hebu niambie,” alisema Erick.

    “Erick! Kama ningekuwa najua chochote, ningekwambia!”

    “Unanidanganya! Kama hutaki kuniambia sababu, unadhani mimi nitakusaidia vipi? Hata wakili wako ni lazima umwambie kila kitu kilichotokea ili akusaidie,” alisema Erick.

    Peter alipoambiwa hivyo, kwanza akatulia, alichokisema Erick ndiyo ulikuwa ukweli wenyewe, ili ajue ni wapi pa kumsaidia ilikuwa ni lazima amwambie kila kitu kilichotokea.

    Hakuwa na jinsi, akamwambia ukweli sababu ya msichana huyo kumuacha kwamba hakuwa akimjali, akimpa muda wala kumsikiliza.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Erick aliposikia hivyo, kwanza akashusha pumzi ndefu na kumwangalia Peter. Alichokisema kilikuwa sahihi kabisa, alimjua dada yake, alimpenda mtu aliyekuwa akimjali na kumsikiliza, kama peter alishindwa kufanya hivyo basi ilikuwa ni lazima kuachwa kama ilivyokuwa.

    “Nikusaidie nini hapo?” aliuliza Erick.

    “Nahitaji kumfahamu mtu aliyekuwanaye kwa sasa!” alisema Peter.

    “Nitamfahamu vipi?”

    “Erick, yule ni ndugu yako, sidhani kama kuna ugumu wowote ule,” alisema Peter.

    Huo ndiyo msaada pekee aliokuwa akiuhitaji kutoka kwa Erick, alijua kwamba Jackline alikuwa kwenye uhusiano na mwanaume mwingine, alihitaji kumfahamu kwa sura, alihitaji kukutana naye na kuzungumza pamoja ili kama itawezekana basi amwache Jackline ili awe naye.

    Hilo lilikuwa gumu kufanyika kwa Erick, alikataa lakini akabembelezwa sana na mwisho wa siku kukubaliana na Peter na hivyo kuanza kumfuatilia dada yake, hasa kwenye suala la namba ya simu.

    Aliamini baada ya kuipata namba hiyo ingekuwa ni rahisi sana kwake kumsaidia Peter, alimfuatilia na siku ambayo aliisahau simu yake, haraka sana akaichukua, akaenda sehemu ya simu zilizotoka, akaliona jina lililoandikwa Hubby, hakutaka kujiuliza, alijua kuwa huyo ndiye mwanaume aliyekuwa akitoka naye kimapenzi, akaichukua namba ile.

    Haraka sana akawasiliana na Peter na kumpa namba hiyo. Kwa mwanaume huyo ilikuwa ni furaha tele, hakukuwa na kitu alichokuwa akikihitaji zaidi ya namba hiyo.

    Haraka sana akampigia simu na kuanza kuzungumza naye. Aliumia kuongea naye lakini hakuwa na jinsi, alijitambulisha na kumwambia kwamba alihitaji kuonana naye kwani kulikuwa na kitu muhimu alitaka kuzungumza.

    “Kuhusu nini?” aliuliza Daniel.

    “Naomba tuonane!”

    “Sawa, ila ninahitaji kufahamu ni kuhusu ninI!” alisema Daniel.

    “Kuhusu Jackline!”

    “Amefanyaje?”

    “Naomba tuonane na tuzungumze. Cha muhimu ni kwamba hutakiwi kumwambia kama tunaonana,” alisema Peter.

    Kwanza Daniel akahisi kitu, aliona kabisa kama kulikuwa na mchezo uliotaka kuchezwa, alianza kwa kukataa lakini kwa kuwa Peter alikuwa na ushawishi mkubwa, hakuwa na jinsi, akakubaliana kuonana naye.

    Jioni ya siku hiyo wakaonana katika mgahawa wa The Prince uliokuwa Masaki na kuanza kuongea. Hakutaka kumficha, alimwambia kuhusu uhusiano wake na Jackline ulivyokuwa, alivyompenda na mpaka siku ya mwisho alipoachwa na msichana huyo kuwa na Daniel.

    Kwa jinsi alivyokuwa akizungumza ilikuwa ni rahisi kuona ni kwa namna gani Peter alikuwa ameumia moyoni mwake. Daniel alikuwa kimya tu akimsikiliza mwanaume huyo alivyokuwa akiongea kwa hisia kali.

    “Nimekusikiliza sana, unataka nikusaidie nini?” aliuliza Daniel baada ya Peter kumaliza kuzungumza.

    “Ninahitaji uniachie Jackline wangu,” alisema Peter.

    Daniel akashtuka, hakuamini kile alichokisikia kwa mwanaume huyo. Mpaka kufikia hapo akagundua ni kwa jinsi gani mwanaume huyo alivyokuwa amekufa na kuoza kwa Jackline.

    Kwake, kumuacha Jackline lilikuwa suala gumu mno, alimpenda kupita kawaida na kitu ambacho kilimpa furaha ni kwamba msichana huyo alikuwa na ujauzito wake.

    “Peter! Hilo ni jambo gumu sana, unazungumzia kitu kigumu kufanyika,” alisema Daniel huku akimwangalia Peter.

    “Daniel! Nakuomba, najua unampenda sana Jackline, naomba uniachie msichana wangu, ninampenda, bila yeye siwezi kuishi, naomba unionee huruma, Daniel, naomba unionee huruma,” alisema Peter huku akiikutanisha mikono yake juu ya meza kama kumuomba mwanaume huyo.

    “Siwezi kumuacha! Jackline ana mtoto wangu tumboni,” alisema Daniel.

    “Daniel! Si tatizo, nitamlea mtoto wako, ila ninaomba sana uniachie Jackline wangu,” alisema Peter huku akiendelea kumuomba mwanaume huyo.

    Daniel hakukubali, alijua kabisa kwamba Peter alikuwa akimpenda Jackline lakini hakudhani kabisa kama alikuwa akimpenda msichana huyo kama alivyokuwa akimpenda yeye.

    Hawakufikia muafaka japokuwa Peter aliahidi kumgawia kiasi cha shilingi milioni ishirini kama tu angekubaliana naye kuachana na Jackline.

    Baada ya kuongea kwa dakika kadhaa, Daniel akaaga na kuondoka mahali hapo huku akimuacha Peter akiwa kwenye maumivu makali.

    Alipofika kwenye Bajaj tu kitu cha kwanza kilikuwa ni kumpigia simu Jackline na kumsalimia. Alitamani kumwambia kuhusu kile kilichokuwa kimetokea lakini alisita, hakuona kama kulikuwa na umuhimu wa kufanya kitu kama kile.

    “Upo wapi? Kwenye daladala?” alisikika Jackline akiuliza.

    “Nipo kwenye Bajaj! Upo nyumbani?”

    “Ndiyo mpenzi!”

    “Naomba nije nikuone!”

    “Nyumbani?”

    “Ndiyo! Kwani baba yupo?”

    “Hayupo!”

    “Basi nakuja!”

    Hakutaka kuelekea nyumbani kwao, alichokifanya ni kumwambia dereva Bajaj kwamba safari ilibadilika na hivyo walitakiwa kuelekea Mbezi Beach. Hilo halikuwa tatizo, dereva akakata kona na kuanza kuelekea huko.

    Moyo wake ulikuwa na mawazo kuhusu Peter, aliogopa kwa kuona kuwa kama mwanaume yule alikuwa akimpenda Jackline kiasi kile basi kama asingeongeza nguvu ya kumpenda zaidi basi angeweza kupokonywa kitu ambacho hakutaka kabisa kuona kikitokea.

    “Nitapambana! Siwezi kushindwa kulilinda penzi langu, nitapambana mpaka mwisho, yaani mpaka namuoa,” alisema Daniel wakati Bajaj ilipokuwa ikikaribia kwao.





    Daniel akaonana na Jackline, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumsogelea msichana huyo, alipomfikia, akamkumbatia na kumpiga mabusu kadhaa mashavuni mwake.

    Moyo wake ulikuwa katika amani kubwa, kila alipokuwa na msichana huyo alijihisi kabisa kuwa huru, amani na furaha kubwa moyoni mwake. Alimwangalia Jackline, alionekana kuwa msichana mrembo mno, alimpenda kwa mapenzi ya dhati yaliyokuwa moyoni mwake.

    Walikumbatiana kwa dakika nzima na ndipo wakakaa chini na kuanza kuzungumza. Muda mwingi msichana huyo alikuwa akilishika tumbo lake, alifurahi kujiona akiwa mjamzito, kwake, kubeba mimba ya Daniel kilikuwa kitu kikubwa alichokuwa akijivunia nacho.

    Walibaki sebuleni huku wakiongea mambo mengi, mama yake Jackline alikuwa akiwaangalia tu, moyo wake uliridhika kupita kawaida. Katika maisha yake alikuwa akipamba kila siku kuhakikisha watoto wake wanakuwa na furaha, kama kitendo cha Jackline kuwa na furaha kuwa na Daniel, kwake ilikuwa ni furaha tele.

    “Daniel, nadhani ni muda wa kumwambia baba,” alisema Jackline maneno yaliyomshtua Daniel.

    “Kumwambia baba! Kuhusu nini?”

    “Hiki kinachoendelea!”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mmh! Unahisi ni jambo jema?” aliuliza.

    “Ndiyo! Hata kama sitomwambia, jua kwamba kuna siku atajua kuwa mimi ni mjamzito!” alisema Jackline.

    “Mh! Atasemaje? Anaweza kuniua!”

    “Hawezi!”

    “Baba yako si mkorofi?”

    “Ni mkorofi kiasi lakini haimaanishi kwamba atakuua, niachie mimi, nitazungumza naye zaidi,” alisema Jackline huku akimwangalia Daniel.

    Daniel akashusha pumzi ndefu, moyo wake ulikuwa na hofu tele, aliogopa kupita kawaida na muda wote alikuwa akihisi kuwa mzee Mwamanda angemchukia kwa kile kilichokuwa kimetokea.

    Jackline hakuishia hapo, akamwambia pia mama yake kuhusu ule uamuzi aliokuwa amefikia. Mama yake alianza kupinga lakini baada ya kumwambia kwamba ipo siku mzee huyo angejua kwa kuwa mimba hakikuwa kitu cha kujificha, akakubaliana naye na hivyo yeye kutakiwa kumwambia mzee huyo jambo hilo.

    Wakaendelea kuzungumza kuhusu mambo mengi, Daniel hakutakiwa kuondoka mahali hapo, alitakiwa kusubiri mpaka mzee huyo atakapofika na kuzungumza naye huku yeye mwenyewe akiwa hapohapo.

    Alikuwa na hofu kubwa, alikuwa akitetemeka na wakati mwingine kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka. Alihofu kwa kuwa aliheshimiana na mzee huyo na hakujua ni kitu gani kingetokea kama tu angemwambia kile kilichokuwa kimetokea.

    “Unaonekana kuogopa sana,” alisema Jackline huku akimwangalia Daniel.

    “Wewe acha tu! Yaani natamani hata kukimbia,” alisema Daniel huku akililazimisha tabasamu kuonekana usoni mwake.

    “Hutakiwi kuogopa kitu! Hebu piga moyo konde,” alisema Jackline.

    Waliendelea kupiga stori mpaka muda ambao mzee huyo alipofika nyumbani hapo. Hofu ikazidi kuongezeka kwa Daniel, alikuwa akitetemeka, alisalimiana na mzee huyo huku akitamani hata kukimbia.

    “Karibi sana dokta,” alisema mzee Mwamanda huku akionekana kuwa na furaha tele.

    “Nimekwishakaribia,” alijibu huku tabasamu lake bandia likiwa usoni mwake.

    Mzee huyo akaelekea chumbani kwake ambapo akapitiliza mpaka bafuni na kuoga. Muda huo sebuleni hakukuwa na amani, Daniel alikuwa akitetemeka kiasi kwamba alitamani hata kuaga mahali hapo.

    Alimwangalia Jackline kwa macho yaliyoonyesha hofu kubwa, alipokumbuka kwamba aliambiwa mzee huyo alikuwa mkorofi, alitamani hata kuondoka mahali hapo.

    “Jackline, naomba niondoke,” alisema Daniel huku akimwangalia msichana huyo.

    “Hapana! Hili jambo ni lazima tulimalize leo,” alisema msichana huyo.

    “Anaweza kukuua!”

    “Kama akikuua, basi atuue wote, ila hakuna kuondoka mpaka hili jambo tulikamilishe,” alisema Jackline.

    Waliendelea kukaa sebuleni pale mpaka baada ya dakika kadhaa ambapo mzee huyo akarudi sebuleni hapo na kuanza kuongea.

    Alionekana kuhisi kitu, haikuwa kawaida kwa Daniel kuwa nyumbani hapo mpaka muda huo, aliona kabisa kulikuwa na jambo lililokuwa likiendelea hapo nyumbani.

    Mama yake Jackline hakutaka kunyamaza, huo ndiyo ulikuwa muda wa kumwambia mume wake kile kilichokuwa kimetokea.

    Hakutaka kujiuliza mara mbilimbi, akamwambia ukweli wa kila kitu. Mzee mwamanda alikuwa kimya, alimwangalia mke wake alivyokuwa akielezea na muda mwingine alikuwa akiyahamisha macho yake na kumwangalia Daniel ambaye aliuinamisha uso wake chini.

    “Mungu nisaidie,” alijikuta akisema Daniel huku akiwa ameinama.

    Mama yake Jackline alimwambia mume wake kila kitu, mzee huyo akashusha pumzi nzito, ndita zikaanza kuonekana usoni mwake, alionekana kushtushwa na kusasirishwa kwa kile alichokuwa ameambiwa.

    “Dokta...” aliita mzee huyo.

    “Naam baba!”

    “Ni kweli umempa binti yangu mimba?” aliuliza.

    Daniel akanyamaza, swali hilo lilikuwa jepesi kujibika lakini halikutakiwa kujibika kwa pupa. Akanyamaza kwa sekunde kadhaa na kumjibu mzee huyo kwamba kweli alikuwa amempa mimba binti yake.

    “Ndiyo mzee!”

    “Ulikusudia nini hasa?” aliuliza mzee huyo.

    Daniel akanyamaza, hakutakiwa kulijibu swali hilo. Mama yake Jackline alipoona ukimya umetawala akaingilia na kumwambia mume wake kwamba wawili hao walikuwa wakipendana na lingekuwa jambo jema kama wangewaruhusu kuwa wawili na kuishi pamoja.

    Mzee huyo hakuzungumza kitu, akasimama na kumsogelea Daniel pale alipokaa na kumuuliza swali moja tu.

    “Unadhani nimefurahi kumuona binti yangu akipata mimba kabla ya ndoa?”

    Ilikuwa ni rahisi kusikia mapigo ya moyo wa Daniel kwa jinsi yalivyokuwa yakidunda. Kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka huku akizidi kutetemeka.

    “Kama kweli umeamua kuwa na binti yangu, usiuumize moyo wake,” alisema mzee huyo, alipomaliza kusema maneno hayo, akaondoka kuelekea chumbani kwake.

    Daniel akabaki kimya, alikuwa akisikilizia hatua za mzee huyo jinsi zilivyokuwa zikilia wakati akiondoka kuelekea chumbani kwake.

    Mzee huyo alipoondoka kabisa, Daniel akamgeukia Jackline na kumwangalia huku tabasamu likionekana usoni mwake, akajisikia nafuu, mwili ukarudi katika hali ya kawaida.

    “Vipi?” aliuliza Jackline huku naye akitoa tabasamu.

    “Mh! Unaweza kufa!” alisema Daniel na wote kuanza kucheka.

    Waliendelea kukaa mahali hapo huku mama yake Jackline akionekana kuwa na furaha tele, kitendo cha mume wake kukubaliana na Daniel kulimfurahisha kupita kawaida.

    Ilipofika majira ya saa mbili usiku Daniel akaaga, akatoka nje, wakati wakiingia ndani ya gari, akaanza kujiskia kizunguzungu, akashindwa kupanda, akaushikilia mlango, kuunyanyua mguu tu akashindwa, hapohapo akaanguka chini.

    Jackline akashtuka, haraka sana akachomoka upande aliokuwa na kwenda upande ule wa Daniel. Akamuinua pale alipokuwa huku akimuita.

    “Daniel...Daniel...” aliita Jackline, Daniel alikuwa kimya.

    Jackline alichanganyikiwa, akaanza kumuita mama yake kwa sauti kubwa, mwanamke huyo akafika nje, akamuona mlinzi akiwa amemshika Daniel pale chini alipoangukia, akauliza tatizo, akaambiwa alianguka ghafla.

    Hawakujua kilichokuwa kikiendelea, haraka sana wakampakiza ndani ya gari. Kabla hawajaondoka, mzee Mwamanda akatoka ndani, akaanza kuwaangalia huku akionekana kushangaa.

    “Kuna nini?” aliuliza mzee huyo.

    “Ameanguka!” alijibu Jackline huku akianza kulia.

    “Ameanguka?” aliuliza mzee huyo huku akiwasogelea, akamgusa Daniel, haraka sana akawaambia waondoke kuelekea hositalini kwani hali ya Daniel ilionekana si ya kawaida.

    Ndani ya gari Jackline alikuwa akilia huku akiwa amekilaza kichwa cha Daniel mapajani mwake. Hakujua tatizo lilikuwa nini, alishangaa, ilikuwa ni ghafla sana mwanaume huyo kuwa kwenye hali hiyo.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakikuwa kifafa, kama kingekuwa chenyewe basi ilikuwa ni lazima kutokwa na mapovu. Kila alipokuwa akijifikiria tatizo lililokuwa limemsibu mpenzi wake, alikosa jibu.

    “God! Don’t take him, please” (Mungu! Tafadhali naomba usimchukue) alisema Jackline huku machozi yakitiririka mashavuni mwake.

    Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika Hospitali ya St. Marry iliyokuwa hapohapo Mbezi Beach. Haraka sana machela ikaletwa na mwanaume huyo kupakizwa kisha kuanza kusukumwa kuelekea ndani.

    Jackline alikuwa akimsindikiza Daniel huku akilia, kwake, wakati mwingine alihisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa mpenzi wake huyo aliyejitolea kumpenda kwa hali na mali.

    Alipofikishwa kwenye chumba cha matibabu, akalazwa na wao kutakiwa kusubiri kwa nje. Pale walipokuwa, wazazi wake walikuwa na kazi ya kumbembeleza Jackline aache kulia.

    Hakubembelezeka, hakukuwa na kitu kilichokuwa kimemuuma kama kumuona mpenzi wake akiwa kwenye hali hiyo.

    “Don’t cry my queen,” (usilie malkia wangu) alisema mzee Mwamanda huku akimbembeleza Jackline.

    Madaktari walikuwa wakipishana kuingia ndani ya chumba kile. Mgonjwa alionekana kuwa na tatizo lililokuwa kubwa ambalo lilihitaji uchunguzi wa kina.

    Waliendelea kusubiri mahali pale kwa saa mbili, hakukuwa na daktari yeyote ambaye alizungumza nao kwa lolote lile na hata walipokuwa wakiwauliza, hakukuwa na mtu aliyewapa majibu.

    Baada ya saa moja, wazazi wake na Daniel wakafika hospitalini hapo kwani walipewa taarifa juu ya kile kilichokuwa kimetokea kwa mtoto wao.

    Walipofika tu, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuulizia hali yake kama alikuwa mzima au la. Walipoambiwa kwamba alikuwa mzima, kidogo mioyo yao ikapoa.

    Ilipofika majira ya saa sita usiku, daktari mmoja bingwa hospitalini hapo akawachukua na kuwapeleka katika ofisi yake kwani alikuwa na jambo muhimu alilotaka kuzungumza nao.

    “Kuna nini? Amepatwa na nini? Amekufa?” alijikuta akiuliza Jackline huku akiyafuta machozi yake, daktari hakujibu, alibaki kimya huku akisubiri wafike ndani ya ofisi ile na kuwaambia kilichokuwa kikiendelea kwa Daniel.





    Kabla daktari hakujibu kile kilichokuwa kikiendelea kwa Daniel, akabaki kimya, macho yake alikuwa akiwaangalia watu hao kama walikuwa na utayari wa kusikia kile kilichokuwa kimetokea.

    Kichwa chake kilikuwa kikifikiria mengi, hakujua kama huo ungekuwa muda sahihi wa kuwaambia au haukuwa muda sahihi. Alibaki kimya kwa muda na kuanza kuzungumza.

    “Ndugu yenu tumemkuta akiwa na tatizo kubwa,” alisema daktari huyo, huo haukuwa muda wa kuficha, ilikuwa ni lazima aseme ukweli kile kilichokuwa kikiendelea.

    “Tatizo gani?” aliuliza mzee Mwamanda

    “Ndugu yenu ana ugonjwa wa kansa ya damu,” alisema daktari huku akiwaangalia kila mmoja.

    Walishtuka, hawakuamini kile walichokisikia, walimwangalia daktari mara mbilimbili, jibu lake lilionekana kutokuwa sawa na wakati mwingine walihisi kama walikuwa wakitaniwa.

    Waliuliza mara nyingi lakini jibu lake lilikuwa lilelile kwamba Daniel alikuwa na ugonjwa wa kansa ya damu ambao kwa kitaalamu ulijulikana kama Eukemia.

    Jackline akashindwa kuvumilia, hapohapo akaanza kulia, aliumia moyoni mwake, aliya jua magonjwa ya kansa, yalikuwa hatari ambayo yalipoteza maisha ya watu wengi duniani.

    Hakutegemea kabisa kupokea jibu kama hilo. Kansa ya damu haukuwa na dawa, ulikuwa ni ugonjwa wa kutisha zaidi ya Ukimwi na kila mmoja aliyekuwa akiupata, mwisho wake ulikuwa ni kifo tu.

    “Haiwezekani! Dokta, haiwezekani,” alisema alisema Jackline na kuanza kulia.

    Huo ndiyo ukweli ulivyokuwa, majibu hayakubadilika, majibu yalisomeka kwamba Daniel alikuwa na ugonjwa wa kansa ya damu.

    Walizungumza mengi na daktari na kuwaambia maneno ya kuwafariji kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa wa Daniel kupona kama tu wangechukua matibabu ya haraka.

    Haikuwa kansa iliyokuwa imekomaa, ilikuwa imeanza na kama wangewahi tiba kwa haraka hata kabla ya miezi mitatu kukatika basi angeweza kupona kabisa.

    Walizungumza mengi, walipomaliza, wakatoka na kwenda kumuona Daniel katika chumba alichokuwemo. Walipofika humo, Jackline akashindwa kuvumilia, akamsogelea mpenzi wake pale kitandani na kumkumbatia huku akilia.

    Maneno ya daktari yakaanza kujirudia kichwani mwake, aliumia, alikuwa tayari kupoteza kila kitu katika maisha yake lakini si kumpoteza Daniel. Kwake, mwanaume huyo alikuwa kila kitu, furaha yake, tumaini lake na ni mtu ambaye alikaa vilivyo moyoni mwake.

    “Jackline, usilie mpenzi,” alisema Daniel kwa sauti ya chini akbisa.

    “Ninaumia mno! Why Mungu anafanya hivi?” aliuliza huku akilia.

    “Yote ni MungU! Tumshukuru kwa kila jambo,” alisema Daniel kwa maneno ya kishujaa.

    Kilichofuata ni kuanza matibabu. Kwanza akahamishwa katika hospitali hiyo na kupelekwa katika Hospitali ya Living Water iliyokuwa Upanga jijini Dar es Salaam.

    Ilikuwa ni hospitali ya kisasa, ynye gharama kubwa mno. Kwa familia ya Daniel haikuweza kupambana na gharama kubwa bali mtu aliyeahidi kumsaidia alikuwa ni mzee Mwamanda.

    Kila siku Jackline alikuwa akienda hospitalini hapo na wakati mwingine kulala hukohuko. Hakutaka kumuacha Daniel, alikuwa na hofu kwa kuhisi kwamba angeweza kufa hivyo alitakiwa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha anakuwa naye karibu mno kwa kipindi hicho.

    Mzee Mwamanda alitamani kuona Daniel akirudi katika hali yake ya kawaida. Alijua dhahiri kwamba kijana huyo alikuwa akipendwa sana na binti, na kitu kizuri ni kwamba alikuwa na baba wa mjukuu wake, hivyo kumpoteza yeye kilikuwa ni kitu kibaya mno.

    Alichokifanya ni kuanza kuhangaikia matibabu yeye mwenyewe, ilikuwa ni lazima ahakikishe kwamba Daniel anapona kwani ndiyo ingekuwa furaha kwa binti yake, hivyo kaka baba hakutakiwa kulala usingizi.

    Aliwasiliana na madaktari wengine na kuwaelezea kilichokuwa kikiendelea, wao wakamwambia kwamba alitakiwa kumsafirisha na kumpeleka nchini India katika hospitali ya Ganga ambapo kulikuwa na matibabu makubwa na mazuri zaidi.

    Hakutaka kulichukulia jambo hilo kipeke yake, akamuita mkewe na kumwambia, akakubaliana naye, haikutosha, akamuita Jackline, naye akakubaliana naye na kuonyesha furaha aliyokuwanayo moyoni mwake, akamkumbatia baba yake na kumpiga mabusu mfululizo.

    Baada ya hapo akawasiliana na wazazi wa Daniel na kuwaambia. Aliwaweka wazi kwamba hakutaka kuona kijana huyo akifariki kwani tayari alikuwa kama mwanafamilia hivyo ilikuwa ni lazima apambane kuhakikisha anayaokoa maisha yake.

    Kwa wazazi hao ilikuwa ni furaha tele, wakakubaliana naye na wa mwisho kuambiwa alikuwa Daniel mwenyewe ambaye bila kupepesa macho alimwambia mzee huyo alikuwa tayari, si kwa India tu, popote pale alikuwa tayari kwenda kutibiwa.

    Harakati za safari zikaanza kufanyika. Zilifanyika kwa kasi kubwa kwani ilikuwa ni lazima kuyaokoa maisha ya mwanaume huyo aliyekuwa muhimu mno.

    Ndani ya siku mbili tayari walikuwa ndani ya ndege na kuanza kuelekea nchini India. Ndani ya ndege kila mmoja alionekana kuwa na furaha mno, Jackline alikuwa pembeni ya mpenzi wake, muda wote alikuwa akimwangalia, wakati mwingine alikuwa akitabasamu lakini wakati mwingine alionekana kuwa na huzuni kubwa.

    Katika vitu ambavyo hakutaka kabisa kuona vikitokea ni kumpoteza mpenzi wake huyo. Ndege iliendelea kukata mawingu na baada ya saa kumi na sita ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Coimbatore.

    Gari la wagonjwa kutoka katika Hospitali ya Ganga lilikuwa mahali hapo, baada ya abiria kuteremka, na wao wakateremka na kwenda kwenye magari maalumu yaliyofika mahali hapo kwa ajili ya kuwachukua.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Safari ikaanza na kuelekea katika hospitali hiyo. Njiani bado Jackline alikuwa akizungumza na mpenzi wake, alimtia moyo kwa kumwambia kwamba angepona na kuwa kama zamani.

    Hawakutumia muda mwingi wakafika katika hospitali hiyo na hivyo Daniel kuchukuliwa na kuingizwa katika chumba cha mapumziko kabla ya kupewa matibabu.

    Jopo la madaktari wanne wakakutana katika chumba cha mkutano na kuanza kuzungumza kuhusu ugonjwa uliokuwa ukimsumbua Daniel. Mikononi mwao walikuwa na ripoti ya Daniel ambayo ilitoka nchini Tanzania.

    “Ni ugonjwa mbaya lakini kwa sababu ndiyo kwanza upo katika hatua ya kwanza, ninaamini tutafanikiwa,” alisema D. Patesh.

    “Kweli! Ila kabla ya yote ni lazima kwanza tuchukue vipimo vingine kwa sababu ugonjwa mkubwa kama huu huwa unakuja na baadhi ya magonjwa, ni lazima tufanye uchunguzi wa damu yake kwa undani zaidi,” alisema daktari mwingine, wakakubaliana na hivyo kuanza kufanya uchunguzi kuhusu hali ya Daniel.

    “Mungu atakuponya,” yalikuwa ni maneno machache yaliyokuwa yakisikika kichwani mwa Jackline.

    ***



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog