Search This Blog

Wednesday, 1 June 2022

ONLY YOU ( NI WEWE TU ) - 4

 







    Simulizi : Only You ( Ni wewe Tu )

    Sehemu Ya Nne (4)



    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Matibabu yalikuwa makubwa, yaliendelea kufanyika nchini India. Kila siku walikuwa ni watu wa kumuomba Mungu kuhakikisha kwamba Daniel anapona na kurudi katika hali yake kama kawaida.

    Siku ziliendelea kukatika, madaktari hawakuchoka, kila siku kulikuwa na kazi ya kuhakikisha mwanaume huyo anarudiwa na afya yake kama ilivyokuwa zamani. Walibadilishana zamu, waliingia kwa zamu ndani ya chumba hicho na kuendelea kumtibu.

    Walimpa dawa zenye nguvu, ilikuwa ni lazima kuiteketeza kansa hiyo hata kabla haijaanza kusambaa mwilini mwake. Hilo lilifanyika kwa nguvu kubwa na hatimaye baada ya mwezi akaruhusiwa kurudi nyumbani huku akipewa dawa ambazo alitakiwa kuzitumia kwa miezi sita.

    “Baada ya hapo?” aliuliza mzee Mwamanda.

    “Atakuwa mzima wa afya, cha kumshukuru Mungu ni kwamba tumeiwahi, vinginevyo mambo yangekuwa mabaya zaidi,” alijibu daktari.

    Daniel akawa na furaha, alimshukuru mzee Mwamanda, alimuona mwanaume huyo kuwa na moyo wa kipekee, si kwa sababu alikuwa na uhusiano na mtoto wake na kumpa mimba, ila kujitoa kwa kiasi kikubwa namna ile ilikuwa ni upendo wa dhati.

    Alikuwa na biashara zake, aliacha kila kitu kwa ajili yake, kila alipokuwa akifikiria hilo, aliona kabisa kwamba mzee huyo alistahili kumshukuru kwa yote aliyokuwa amemfanyia.

    Siku moja kabla ya safari alikesha na Jackline katika chumba alichokuwa amelazwa, kila alipomwangalia msichana huyo, alikuwa mrembo mno, alimpenda kuliko kitu chochote kile katika dunia hii.

    Hakuacha kumbusu, hakuacha kumshukuru kwa kuuruhusu moyo wake kumpenda. Alimtafuta mno, alilitafuta penzi la msichana huyo na hatimaye alifanikiwa kulipata, kubwa zaidi ni kwamba alimchukua kutoka kwa mwanaume mwingine kabisa.

    Siku ya safari ilipowadia, wakapanda ndege na kurudi nchini Tanzania. Huko, waliendelea kupendana na hatimaye kuanza mipango mipya ya kuishi pamoja, hakukuwa na kitu walichokitamani kama hicho.

    Wazazi waliposhirikishwa, hakukuwa na tatizo, wakakubaliana nao na hatimaye watu hao wawili kufunga ndoa takatifu kanisani. Wakawa mume na mke na baada ya miezi ya kujifungua ilipokamilika, Jackline akajifungua mtoto wa kike hospitali.

    “Mke wangu!” aliita Daniel huku akionekana kuwa na furaha kupita kawaida.

    “Ndiyo mpenzi!”

    “Ninashukuru kwa zawadi hii, hakika ni zawadi kubwa ambayo nisingeweza kuipata sehemu yoyote ile,” alisema Daniel huku uso wake ukionyesha ni kwa jinsi gani moyoni mwake alikuwa na furaha kupita kawaida.

    Maisha yakawa matamu, ya furaha, walionyesheana mapenzi kemkem, mtoto yule akawaunganisha na kuifanya mioyo yao kupendana kupita kawaida.

    Daniel akawekwa katika kampuni moja ya mzee Mwamanda ambayo ilikuwa ikihusika na uchukuaji mizigo kutoka bandarini na kuisambaza sehemu nyingi jijini Dar es Salaam na nje ya nchi.

    Alikuwa bosi, aliheshimika japokuwa alikuwa na umri mdogo. Alinyenyekewa, alipendwa na kuheshimiwa kila alipokuwa akipita.

    Ofisi yake haikuwa bandarini, ilikuwa Posta Mpya katika Jengo la Mkapa. Ilikuwa moja ya ofisi nzuri ambapo ndani yake ilikuwa imezungukwa na vioo huku kiyoyozi kikipiga muda wote aliokuwa ofisini humo.

    Mezani kulikuwa na kompyuta yake na pembeni kulikuwa na picha kadhaa za familia yake, kila alipokuwa akiziangalia, moyo wake ulikuwa na hamu ya kufanya kazi zaidi kwani aliamini kuwa kitu pekee kitakachoifanya familia yake kuishi maisha mazuri ni kufanya kazi kwa bidii tu.

    “Samahani bosi,” alisema sekretari kupitia simu yake ya mezani.

    “Ndiyo!”

    “Kuna mgeni anakuulizia!”

    “Nani? Adul?”

    “Hapana! Amejitambulisha kwa jina la Felista!”

    “Oh! Mwambie aingie!” alisema.

    Ni ndani ya sekunde kadhaa mlango wa ofisi yake ukafunguliwa na msichana huyo kuingia. Alikuwa mweupe, mrefu kidogo, kifua saa sita, alipendeza kwa kuvaa sketi fupi ambayo iliiacha miguu yake wazi kwa kiasi kikubwa.

    Alikuwa mzuri wa sura, hata kama hakuwa akiongea lolote, kwa mbali tabasamu lake lilikuwa likionekana. Alipoingia, Daniel alipomuona, kwanza akashtuka lakini akapiga moyo konde baada ya macho yake kuziona picha akiwa na familia yake.

    “Karibu!” alimkaribisha huku akisimama, wakapeana mikono.

    “Ahsante!” aliitikia msichana huyo na kukaa kwenye kochi.

    Harufu yote ndani ya ofisi ikabadilika, harufu ya manukato ikatawala kila kona humo ndani. Pale alipokaa, Felista aliikunja miguu yake kwa staili ya nne, mapaja yakawa wazi lakini Daniel hakuonekana kushtuka kabisa.

    Felista akaanza kumwambia kuhusu jambo lililomfanya kufika mahali hapo, alimwambia kwamba alikuwa na shida, alikuwa mfanyabiashara, alihitaji kupokea mizigo kutoka nchini Marekani lakini kwa bahati mbaya hakuwa na kampuni ambayo ingemuwezesha kusafirisha mizigo hiyo mpaka kulipokuwa na ofisi yake.

    Hilo halikuwa tatizo kwa Daniel, hiyo ilikuwa kazi yake, ilikuwa ni pesa ambayo ilijileta. Akamwambia kwamba hakukuwa na shida, kama alihitaji msaada, kampuni yake ilijitolea kumsaidia kwa malipo ya kawaida kabisa.

    Felista akafurahi, wakakubaliana kuhusu malipo, na baada ya hapo, akampa business namba yake na msichana huyo kusimama kwa lengo la kuondoka.

    “Tutawasiliana bosi!” alisema Felista.

    “Usijali!”

    Akageuka na kuanza kuelekea mlangoni. Hapo ndipo kidogo Daniel akashtuka, alipomwangalia msichana huyo kwa nyuma, alijazia kidogo, umbo lake lilijigawa vilivyo, yaani ilikuwa ni sawa na kumuona mrembo wa Tanzania.

    Hipsi zilipangwa na kupangika, kiwowo kidogo, miguu yake ilikuwa imejaa kidogo. Daniel akashindwa kuvumilia, akamfuata na kumfungulia mlango, kwa tabasamu pana, Felista akashukuru, akatoka, akamsindikiza kidogo na kisha kuondoka.

    “Mmh! Mungu unajua kuumba,” alijisemea wakati msichana huyo akiifuata lifti kwa lengo la kuingia na kuondoka. Akashusha pumzi nzito na kurudi ofisini kwake.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Kichwa cha Daniel kilichanganyikiwa, hakuamini kama angeweza kumuona msichana mrembo kama alivyokuwa Felista. Alitokea kumpenda, kwa jinsi alivyovaa, alivyokuwa ameumbika kwake alionekana kuwa msichana wa ajabu kabisa.

    Wakati mwingine alihisi kama Felista alikuwa ameshushwa, alipendeza machoni mwake na kila alipokumbuka jinsi alivyokuwa, ni kitu kimoja tu ndicho kilichokuja kichwani mwake, ngono.

    Alikuwa na namba ya msichana huyo, alikumbuka kwamba alipewa business card hivyo haraka sana akaingiza mkono wake katika mfuko wa suruali na kuitoa kadi ile na kuanza kuiangalia, kadiri alivyokuwa akiitazama ndivyo alivyozidi kumuwaza msichana huyo.

    “I must take her,” (ni lazima nimchukue) alijisemea.

    “How can I win her? Should I make a call and ask her to meet me or?” (nitampataje? Nimpigie simu na kumbuomba aonane na mimi au?) alijiuliza.

    Kichwani mwake hakumfikiria mke wake tena, mtu aliyekuwa ndani ya moyo wake alikuwa msichana huyo tu. Alijua dhahiri kwamba Jackline alikuwa na mtoto mdogo, alihitaji kuonyeshewa mapenzi motomoto lakini kwake akili yake ilibadilika kabisa na kitu pekee alichokihitaji alikuwa Felista tu.

    Alijitahidi kukaa kimya siku hiyo, alijifanya kama kutotilia mkazo kuhusu kumpigia simu msichana yule lakini siku iliyofuata, akashindwa kuvumilia, haraka sana akampigia msichana huyo.

    “Nimekumbumbuka Felista,” alisema Daniel huku akiangalia nje kupitia katika dirisha la kioo lililokuwa ofisini kwake.

    “Naongea na nani?”

    “Daniel!”

    “Ooh! The big Boss!”

    “Hahah! Hakuna buana! Mimi wa kawaida sana!” alijitetea.

    “Sawa! Nimefurahi kuiona simu yako,” alisema Felista.

    Daniel akatoa tabasamu pana kana kwamba msichana huyo alikuwa mahali hapo. Akabaki akizungumza naye, moyo wake ulikuwa na furaha kubwa kupita kawaida.

    Alitokea kumpenda, alitamani kuwa naye, alimfikiria sana na muda huo ulikuwa ni wa kumwambia kwamba alitaka kuonana na kuzungumza naye kwani hakuona kama kungekuwa na msichana mwingine ambaye alitakiwa kuonana naye zaidi ya huyo.

    Alizungumza naye kwa kujiamini, alichombeza kwa maneno matatu, alimsifia kwa kumwambia kwamba alikuwa mzuri wa sura, mpole, aliyependeza kwa kila mwanaume aliyekuwa akimwangalia.

    Felista alifurahi, alipenda kusifiwa, alijiona mzuri hivyo alivyoambiwa maneno hayo moyo wake ukaridhika na kuona kabisa kwamba alistahili kwa kile alichokuwa akiambiwa.

    “Ningependa kuonana nawe,” alisema Daniel.

    “Leo?”

    “Ndiyo! Kuna ugumu?”

    “Wala hakuna!”

    “Basi ningependa nikuone!” alisema.

    Hilo halikuwa tatizo hata kidogo, msichana huyo akakubaliana naye na hivyo kuahidi kuonana sehemu moja maalumu ambayo ilizoelewa kutembelewa na watu waliokuwa kwenye uhusiani wa kimapenzi.

    Ilikuwa ni katika bustani ya Las Vegas iliyokuwa Masaki jijini Dar es Salaam. Walikutana mahali hapo na kuanza kuongea. Hawakuwa peke yao, walikuwepo watu wengine ambapo kila mmoja alionekana kuwa bize na mpenzi wake.

    Daniel alipomwangalia Felista, msichana huyo alionekana kuwa mzuri zaidi ya jinsi alivyokuwa siku ile aliyokutana nayo. Alimwambia jinsi alivyopendeza, jinsi alivyouteka moyo wake kiasi kwamba hakuwa akijiweza kwa ajili yake.

    “Kweli?”

    “Ndiyo! Ninakupenda sana Felista! Wewe ni msichana wa kipekee sana moyoni mwangu, ninatamani kuwa nawe,” alisema Daniel huku akimwangalia msichana huyo.

    Felista akanyamaza, hakuzungumza kitu, aliuinamisha uso wake chini, akashikwa na aibu za kike. Daniel akamsogelea na kumbusu shavuni mwake.

    Kitendo hicho kikausisimua mwili wa msichana huyo, hakuamini kama mtu mwenye pesa kama Daniel angempenda msichana kama yeye ambaye alikuwa ameajiriwa sehemu akifanya kazi zake, tena za kutumwa kila siku.

    “Sipendi kutembea na mume wa mtu!” alisema Felista huku akiangalia chini.

    “Kwa nini? Tunauma?” aliuliza.

    “Kwa sababu hamna malengo!”

    “Felista! Nina malengo kwako!”

    “Malengo gani? Kunioa? Hivi utaweza kumuacha mkeo kwa ajili yangu?” aliuliza Felista huku akimwangalia mwanaume huyo.

    Daniel akabaki kimya, alichokizungumza msichana huyo kilikuwa kweli kabisa lakini hakutaka kuonekana kwamba hakuwa na malengo kwa Felista. Akamwambia mambo mengi lakini kusudi kubwa lilikuwa ni kukubaliwa ombi lake tu.

    Kwa jinsi alivyokuwa akizungumza, alivyoonekana, alitia huruma kiasi kwamba ilikuwa vigumu kwa felista kuendeleza msimamo wake wa kumaktaa. Akakubaliana naye na hivyo kumbusu shavuni.

    Moyo wake haukutaka kukumbuka kwamba alikuwa na mke nyumbani, tena aliyekuwa na mtoto mdogo kabisa, alikuwa bize na msichana huyo na kwa muda alitakiwa kumsahau mke wake.

    Walikaa na kuzungumza mengi kisha kuingia ndani ya gari na kumpeleka msichana huyo nyumbani kwake maeneo ya Kijitonyama. Siku hiyo hawakufanya kitu chochote zaidi ya kubadilishana mate na kuondoka.

    Njiani, kichwa chake kilivurugika, alijiahidi kwamba mara baada ya kumuoa Jackline asingeweza kutembea na mwanamke yeyote yule lakini kwa jinsi Felista alivyoonekana, hakuweza kuvumilia hata kidogo.

    Ujanja aliokuwa akiutumia ni kwamba alihitaji kumuonyeshea Jackline mapenzi yakeyale, hakutakiwa kumuonyeshea utofauti wowote ule, kama alikuwa akimbusu kila siku alipokuwa akirudi, hata kipindi hicho ambacho moyo wake ulikuwa umechukuliwa na mwanamke mwingine, alitakiwa kufanya vilevile.

    Alichangamka, Jackline hakugundua kitu chochote kile, hakubadilika, kama alivyokuwa siku nyingine ndivhyo alivyokuwa hata siku hiyo. Walizungumza mambo mengi lakini kichwa cha Jackline kilikuwa kikimfikiria Felista tu.

    Waliachana kwa kipindi kifupi kilichopita lakini tayari mwanaume huyo alionekana kumkumbuka msichana huyo kupita kawaida, akatamani kumpigia simu na kuzungumza naye, alihitaji hata kuisikia sauti yake tu.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akatafuta njia ya kumkimbia mke wake, apate nafasi ya kukaa peke yake na kumpigia simu ili hata amtakie usiku mwema.

    Alichokifanya ni kumwambia mke wake kwamba alitaka kwenda kumfungulia mbwa kutoka kwenye banda lake. Hiyo haikuwa kazi yake, ilikuwa ni ya mlinzi lakini kwa kuwa alimwamini sana mume wake, hakutaka kumuuliza.

    Akaelekea huko huku akiwa na simu yake, alipofika, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumpigia simu Felista na kuanza kuongea naye.

    “Wewe! Humuogopi mke wako?” aliuliza msichana huyo.

    “Hapana! Yupo chumbani!”

    “Na wewe upo wapi?”

    “Nimekuja kumfungulia mbwa!”

    “Ehh! Huna mlinzi!”

    “Nimezuga kufanya hivyo ili nije kuongea nawe, japo nikutakie usiku mwema,” alisema Daniel.

    “Nashukuru kwa kunijali!”

    “Usijali! Nakutakia usiku mwema mpenzi!”

    “Na wewe pia!”

    “Nakupenda!”

    “Nakupenda pia!”

    Moyo wake ukaridhika, akajisikia faraja kupita kawaida. Alipomaliza, akamfungulia mbwa na kurudi chumbani. Alipofika, akamsogelea mke wake pale alipokuwa na kumwambia alale kifuani mwake.

    “Nakupenda mke wangu!” alisema huku mwanamke huyo akiwa kifuani.

    “Nakupenda pia mume wangu,” alisema Jackline huku akifarijika, kwa jinsi walivyokuwa wakiishi na mapenzi aliyokuwa akionyeshewa, ilikuwa ni vigumu kuamini kama mume wake huyo alikuwa akimsaliti.

    ***

    Japokuwa alikuwa na mwanamke mzuri lakini bado macho ya Daniel yalikuwa nje yakimwangalia mwanamke ambaye hakumfikia hata mke wake kwa uzuri. Alichanganyikiwa na kila wakati alipokuwa akimfikiria msichana Felista moyo wake ulikuwa kwenye presha kubwa.

    Hakutaka kumuacha msichana huyo, alimpenda na kila wakati alikuwa akimfikiria. Kazi hazikufanyika kama ilivyotakiwa na hivyo kwa sababu ya msichana huyo.

    Siku ziliendelea kwenda mbele huku mawasiliano yao yakiendelea kukua. Walikaa kwa wiki moja Daniel akamwambia Felista kwamba alimkumbuka na hivyo walitakiwa kuonana katika Hoteli ya Livingstone iliyokuwa Upanga kwa ajili ya kuzungumza.

    Hilo halikuwa tatizo, wakaonana huko, wakazungumza sana katika mgahawa mmoja na baada ya hapo kwenda chumbani kutulia. Wakaanza kushikana huku na kule, baada ya hapo wakajifunika shuka na sauti ya kitanda kuanza kusikika.

    Siku hiyo moyo wake ukaridhika, hakufikiria ni kwa kiasi gani moyo wa Jackline ungeumia kama tu angesikia kile kilichokuwa kimetokea.

    Baada ya kumaliza, wakarudi tena kwenye mgahawa na kuanza kunywa kahawa kama kawaida. Hapo akakumbuka kwamba hakuwa amempigia simu mke wake kwa zaidi ya saa tatu, akaichukua na kumpigia na kuanza kuongea naye.

    Walizungumza huku akimtania kama alivyozoea na kumwambia kwamba angerudi nyumbani mapema kabisa. Mkewe akaridhika na kukata simu.

    Baada ya kuzungumza na msichana huyo, akaondoka kurudi nyumbani. Alipofika huko, akapokelewa kama kawaida, akakumbatiwa na kumwagiwa mabusu mfululizo shavuni na mdomoni na kuingia ndani.

    Kitu cha kwanza kilikuwa ni kumuona mtoto wake, akacheza naye na baadaye kwenda kuoga. Muda wote Jackline alionekana kuwa na furaha tele, kila alipokuwa akimwangalia mume wake, uso wake ulikuwa na tabasamu pana kama mtu aliyeshinda mamilioni.

    “Una furaha sana leo,” alisema Daniel huku akimwangalia mke wake.

    “Nahisi baada ya mwaka nitakwenda kupata mtoto wa pili,” alisema Jackline.

    “Hicho ndicho kinachokupa furaha?”

    “Ndiyo! Napenda sana watoto. Nilishawahi kumwambia Mungu kwamba nitakapoanza kuzaa, nitazaa kama kuku,” alisema Jackline na kuanza kucheka.

    Kitandani, walikuwa wakiongea mambo mengi, kila mmoja alionekana kuwa na furaha kupita kawaida jambo lililoashiria kwamba mapenzi yao yalikuwa makubwa kuliko mtu mwingine yeyote yule japokuwa katika upande wa pili, Daniel alichukua uamuzi mbaya wa kumsaliti mke wake huyo.

    ***

    “Shoga upo wapi?” ulikuwa ni ujumbe uliosomeka katika simu ya Jackline.

    “Nyumbani! Kuna nini kwani?”

    “Mume wako yupo wapi?”

    “Kazini!”

    “Eeh! Basi inawezekana huyu ninayemuona siyo yeye,” aliandika mwanamke huyo kutoka upande wa pili.

    Moyo wa Jackline ukashtuka, hakuwa radhi mawasiliano hayo yaishie hapo, haraka sana akampigia simu mtu huyo na kuanza kuzungumza naye.

    Alikuwa mwanamke aliyejulikana kwa jina la Pendo, alikuwa mwanamke mrembo ambaye alikuwa na urafiki wa dhati na Jackline. Walisoma wote kwa kipindi kirefu na kushirikiana kwenye mambo mengi mno.

    Wakaanza kuongea. Pendo akamwambia Jackline kile kilichokuwa kikiendelea, alimwambia kuwa alimuona mume wake akiwa na mwanamke mwingine katika Hoteli ya Livingstone iliyokuwa Upanga.

    Hilo lilimshtua mno Jackline na kuhisi kwamba inawezekana Upendo alikuwa amechanganya. Mwanamke huyo alimwambia kwamba hakuwa amechanganya ila alikuwa na uhakika kwamba mtu aliyekuwa akimuona mbele yake alikuwa Daniel.

    “Hebu mpige picha.”

    “Hakuna tatizo!”

    Picha zikapigwa na kutumiwa Jackline, alipoziona, moyo wake ukawa kwenye maumivu makali, alikuwa mume wake. Alihisi kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake kupita kawaida lakini upande mwingine wa moyo wake ukamtoa hofu na kuhisi kwamba inawezekana msichana yule alikuwa wa kawaida tu.

    “Wanaondoka, nadhani wanakwenda chumbani!” alisema Pendo.

    “Nakuja!”

    Haraka sana Jackline akaondoka nyumbani, alichanganyikiwa, hakuamini alichokuwa amekisikia, aliondoka kwa mwendo wa kasi mpaka katika hoteli hiyo, alilipaki gari lake mbali kabisa na hoteli hiyo, akateremka na kuelekea katika hoteli ile na kuonana na Pendo.

    Mwanamke huyo alimwambia kwamba wawili hao waliondoka na kuelekea chumbani kupumzika. Hilo lilimuumiza mno Jackline, alitamani kutoka na kwenda kufumania lakini hakutaka iwe hivyo, hakutaka kugombana na mume wake kisa mwanamke mwingine, akavumilia.

    Baada ya saa moja na nusu wawili hao wakatoka. Kila mmoja alionekana kuwa na furaha. Picha aliyokuwa akiiona Jackline ilimuumiza mno, kwa jinsi walivyoonekana, ilionyesha kabisa kwamba walikuwa wapenzi walioshibana na walitoka kufanya mapenzi.

    Huku alipokaa kwa kujificha, alikuwa akilia, moyo wake ulikuwa na maumivu makali kupita kawaida. Baada ya dakika kadhaa, akashtukia simu yake ikianza kuita, alipoangalia kioo, alikuwa mume wake.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwanza akasita kuipokea, alichukia, moyo wake ulikuwa ukiwaka kwa hasira lakini mwisho wa siku akaona bora apokee na kuzungumza na mume wake huyo.

    Hakutaka kuonyesha tofauti yoyote ile, alimuonyeshea furaha kama kawaida, walizungumza kwa dakika kama tano huku kila mmoja akionekana kumfurahia mwenzake.

    “Upo wapi my prince?” aliuliza Jackline.

    “Ofisini! Ila ndiyo nataka nijiandae nirudi nyumbani! Nimewakumbuka sana,” alisema Daniel bila kujua alikuwa akitazamwa.

    “Tumekukumbuka pia! Nakusubiria mume wangu kipenzi,” alisema Jackline na kukata simu.

    Alilia mno, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea, wakati mwingine alihisi kama alikuwa akiota, hakuamini kama Daniel angeweza kufanya kitu kama kile. Alimwamini mno, alimuonyeshea mapenzi ya kila aina lakini mwisho wa siku akaanza kusalitiwa.

    Alihisi kuwa na tatizo sehemu fulani, mtu kama Daniel asingeweza kumsaliti kama kungekuwa na tatizo sehemu fulani, na hili kufahamu tatizo lilipokuwa alitakiwa kuonyesha mapenzi kama ilivyokuwa siku za nyuma.

    Hakutaka kukaa sana mahali hapo, akaondoka huku moyo wake ukiwa umejeruhiwa kupita kawaida. Katika muda ambao Daniela lirudi nyumbani, hakutaka kumuonyeshea tofauti yoyote ile, alimuonyeshea furaha ya ajabu ambayo hakuwahi kumuonyeshea katika kipindi chote.

    Furaha ile ilificha maumivu makali yaliyokuwa moyoni mwake, uso ulitabasamu lakini moyo wake ulikuwa ukilia kwa ndani. Alijikaza, alijipa ujasiri wa kutokuyaonyesha maumivu yake mbele ya mume wake.

    Usiku walikuwa wakizungumza, wakicheza lakini moyoni mwake hakuwa na furaha hata kidogo. Walifanya kila kitu na hata siku iliyofuatia, akamuaga na kwenda kazini.

    Jackline akashindwa kuvumilia, mume wake alipoondoka, akajifungia chumbani na kuanza kulia kwa maumivu makali moyoni mwake. Alijiuliza juu ya kile kilichokuwa kikiendelea, kwa nini mume wake kipenzi aliamua kumsaliti kwa msichana ambaye aliamini kwamba hakuwa mzuri kama yeye zaidi ya makalio makubwa kidogo aliyokuwanayo?

    Kila alichokuwa akijiuliza akakosa jibu lakini bado moyo wake ulikuwa na uhakika kwamba kulikuwa na tatizo mahali fulani kwani kwa jinsi alivyokuwa akimfahamu Daniel, namna alivyomuonyeshea mapenzi ya dhati, akilini mwake hakukuingia suala la usaliti hata kidogo.

    “Kwa nini lakini? Nahisi kuna kitu, nitafuatilia nijue nini kinaaendelea,” alisema Jackline huku macho yake yakiwa mekundu mno kwa sababu ya kulia sana.

    ***

    Jackline hakutaka kukurupuka, alitakiwa kuwa na ufundi mkubwa katika kumfuatilia mume wake. Alijua kabisa kwamba kama angefanya hayo kwa pupa asingeweza kufanikiwa kwani angeharibu kila kitu na kuonekana mbabaishaji.

    Aliwajua wanaume, hawakuwa watu wa kuambiwa tu, walikuwa watu wa kushikwa huku wakiwa na mali mkononi, lakini pia pamoja na hilo alitakiwa kuhakikisha anamdaka huku akiwa na uhakika kwamba huyo alikuwa mpenzi wake vinginevyo angeambiwa kwamba ni rafiki yake tu.

    Ili aucheze mchezo huo hakutakiwa kubaki nyumbani hapo, wazo lililokuja ni kwamba aondoke kurudi nyumbani kwa wazazi wake huku akiwa huko ndiyo aanze kucheza mchezo huo kwa lengo la kumtuliza mume wake.

    Kumuaga halikuwa tatizo, aliamini kwamba atakapomwambia kuwa anataka kurudi nyumbani kwanza ampeleke mtoto kwa bibi na babu kusingekuwa na maswali mengi.

    Usiku mume wake alivyorudi, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumwambia kile alichokuwa amekifikiria. Hilo halikuwa tatizo kwa Daniel, alimruhusu mke wake kumpeleka mtoto kwa babu na bibi yake.

    Siku ya kuondoka, alimsindikiza hadi huko ambapo alimwambia kwamba angekaa kwa muda wa mwezi mmoja na kurudi nyumbani.

    Kwa jinsi alivyokuwa akizungumza, Daniel hakuweza kugundua maumivu aliyokuwanayo mke wake moyoni mwake. Alitabasamu, walicheka pamoja huku wakitaniana lakini ndani kabisa ya moyo wake kulikuwa na mpasuko mkubwa mno.

    Wakati akifikiria kuhusu mpango wake ndipo wazo jingine likamjia kichwani mwake, ilikuwa ni lazima amshirikishe rafiki yake aliyeitwa Pendo kwa lengo la kumpa ushauri juu ya kile alichotakiwa kufanya.

    Haraka sana akampigia simu na kuanza kuzungumza. Akaomba kuonana naye na ndani ya dakika kadhaa msichana huyo alikuwa mahali hapo na kuanza kuzungumza.

    Alichomwambia Pendo ni kwamba wao wawili walitakiwa kuhakikisha Daniel na Felista wanaachana kwa kuwachezea michezo mingi ambayo ingewafanya wasiwe na amani katika mapenzi yaliyokuwa yakiendelea.

    “Ishu si kumuua yeyote, hapa ni lazima tuhakikishe kwamba wanaachana,” alisema Pendo huku akimwangalia Jackline.

    “Sawa kabisa. Ni wazo zuri mno! Tunafanyaje sasa?”

    “Ni rahisi! Una pesa?”

    “Ninazo!”

    “Basi tumkodi mwanaume mmoja, awe mzuri wa haja, halafu huyo ndiye ambaye atatumika, lakini pia tumuandae msichana mzuri wa haja, yaani hao ni kwa ajili ya kuwaachanisha wawili hao. Unaonaje?” alisema Pendo na kumalizia kwa swali.

    “Wataweza?”

    “Kwa nini washindwe! Yaani tujenge chuki kati yao, basi.”

    “Sawa.”

    Pendo ndiye alikuwa kila kitu, alijua kucheza na mambo kama hayo, katika kipindi ambacho mume wake alikuwa akichepuka na mwanamke mwingine alitumia njia ileile ambayo ndiyo alihitaji hata Jackline aitumie pasipo kushtukiwa.

    Haraka sana akampigia simu mwanaume mmoja aliyeitwa kwa jina la Jackson na kumwambia kuhusu dili lililokuwa limewekwa mezani. Mwanaume huyo aliposikia, akafurahia kwani mbali na kupewa pesa, pia alikuwa na uhakika wa kufanya mapenzi na msichana mwingine mrembo.

    “Naona unaniletea mpenzi mwingine! Safi sana,” alisema Jackson kwenye simu.

    “Hebu tuonane kwanza na mhusika,” alisema Pendo.

    Ndani ya saa moja, watatu hao wakakutana katika mgahawa wa Armando uliokuwa Kijitonyama. Jackline mwenyewe alipomuona Jackson akakiri kwamba kweli ingekuwa kazi nyepesi kwa msichana yeyote kudanganyika kutokana na uzuri wa sura aliokuwanao mwanaume huyo.

    “Naitwa Jackson, mzee wa kazi,” alisema Jackson huku akimsalimia Jackline, kwa jinsi alivyokuwa akitabasamu, hata uzuri wake ukaongezeka.

    “Naitwa Jackline!”

    “Ooh! Kwa hiyo sisi ni JJ, safi sana,” alisema Jackson ambaye muda wote alikuwa mtu mwenye uchangamfu mkubwa.

    Wakakaa na kuanza kuzungumza. Pendo akaanza kumwambia Jackson kila kitu kilichokuwa kikiendelea kwamba alitakiwa kumshawishi msichana fulani kimapenzi lakini pia angelipwa kiasi kikubwa cha pesa kama tu angekamilisha kile kilichotakiwa.

    “Namba yake?”

    “Hiyo si tatizo! Nilifanikiwa kuiiba,” alisema Jackline na kumpa namba ya simu.

    “Sawa. Nyie niachieni! Si mnataka aachane na mumeo? Hiyo niachie mimi,” alisema Jackson na kuondoka mahali hapo.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Halo! Mambo vipi!”

    “Safi! Naongea na nani?”

    “Jackson Edward!”

    “Nikusaidie nini?”

    “Nilikuwa nahitaji kuonana nawe, sijui una muda?”

    “Mimi? Kwanza namba yangu uliipata wapi?”

    “Eeh! Yaani hukumbuki mtu unayempa namba yako?”

    “Nilikupa namba yangu?”

    “Ndiyo! Niliagiza gari, ukanipa business yako.”

    “Mmh! Sikumbuki!”

    “Nahisi tukionana utanikumbuka! Upo ofisini kesho?”

    “Yeah!”

    “Nitakuja!”

    “Sawa.”

    Yalikuwa ni mazungumzo mafupi baina ya Jackson na msichana Felista. Walizungumza kwa kidogo sana na mwanaume huyo kutaka kuonana na msichana huyo mrembo.

    Hakutaka kuwapa taarifa akina Jackline mpaka pale mambo ambapo yangekuwa motomoto. Siku iliyofuata, akaondoka na kuelekea mahali ilipokuwa ofisi ya akina Felista na kuonana naye huko.

    Felista alipomuona mwanaume huyo na kujitambulisha kwake alionekana kuwa mgeni, hakuwa amemuona kabla na hata aliposisitiza kwamba alikuwa akifahamiana naye moyo wake ulikataa vilivyo.

    Alipenda kuwa na wanaume wazuri, kwa jinsi Jackson alivyokuwa, kwake ingekuwa vigumu sana kutokumkariri kwani kila siku katika maisha yake alipenda kutembea na wanaume wa aina hiyo.

    Pale ofisini, si yeye tu, kila mtu alikuwa akimwangalia Jackson kwa macho ya mshangao. Ni kweli waliwahi kukutana na wanaume wazuri lakini kwa kijana huyo, alikuwa mzuri kupita kawaida.

    Muda wote tabasamu lilikuwa usoni mwake, alipenda kufurahia na hata alipokuwa akiongea alichanganya na Kingereza cha Mmarekani mweusi kitu kilichowapagawisha wasichana wengi.

    “You look so stunning,” (umependeza sana) alisema Jackson huku akimsalimia Felista, tena alikuwa akimwangalia kuanzia chini hadi juu.

    Walikaa na kuzungumza kidogo na kumwambia kwamba alitaka kuagiza gari lake hivyo alihitaji kufahamu gharama zenyewe. Kwa Felista halikuwa tatizo, akampa gharama hizo na baada kumwambia kwamba lingekuwa jambo zuri kama wangeonana baadaye.

    “Hakuna shida! Nitakushtua,” alisema Felista huku akionekana kuingia kwenye penzi la mtu ambaye ndiyo kwanza alimuona siku hiyo.

    “Nashukuru sana malkia!” alisema Jackson, akaachia tabasamu pana, kali lililokuwa la kumuulia adui wake, tabasamu hilo likazidi kumchanganya Felista, akaukuta moyo wake ukianza kuburuzwa vilivyo.

    ***

    Felista alidata na wanaume wenye pesa lakini kwa Jackson hakuweza kupindua kwa sababu mwanaume huyo alikuwa mzuri wa sura. Waliagana na kuondoka.

    Picha ya Jackson ikaganda kichwani mwake, hakuelewa kama alikutana na jini au binadamu wa kawaida kama alivyokuwa yeye. Alilikumbuka tabasamu lake, aliikumbuka sauti yake, alikumbuka namna alivyokuwa akizichezesha lipsi zake kila alipoongea, moyo wake ulichanganyikiwa mno.

    Hakutaka kusikia kitu chochote kipindi hicho zaidi ya kuwa mpenzi wa mwanaume huyo. Kila alipokuwa akimfikiria mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kupita kawaida.

    Aliporudi nyumbani, akatulia kitandani na kuanza kumfikiria mwanaume huyo, alihitaji kuwa naye lakini wakati mwingine alikuwa na hofu kwamba inawezekana Daniel akagundua na hivyo kumuacha.

    Moyo wake ukagawanyika, upande mmoja ulikuwa ukifikiria mapenzi lakini upande mwingine ulikuwa ukifikiria pesa. Vilikuwa vitu viwili vilivyokuwa vikishindana, hakujua ni upande gani ungeibuka na ushindi mkubwa.

    Nyumbani hapo, tena akiwa kitandani akachukua simu yake na kumpigia Jackson na kuanza kuongea naye. Sauti yake alipoisikia, mapigo yake ya moyo yakaongezeka kiasi kwamba akahisi kabisa moyo wake ungeweza hata kuchoma.

    “Jackson!” aliita kwa sauti ndogo, nyororo iliyofanana na ile ya kumtoa nyoka pangoni.

    “Niambie malkia,” alisema Jackson, Felista akazidi kuchanganyikiwa.

    “Ulifika salama?”

    “Ndiyo! Nimekukumbuka, ninatamani hata niwe na wewe au nije kwenu,” alisema Jackson na kutoa kicheko cha chini kilichompagawisha Felista kishenzi.

    “Nimekukumbuka pia! Gari lako linafika lini?” aliuliza felista.

    Jackson hakutaka kujivunga, alimwambia ukweli kwamba hakuwa na gari lakini kitu alichokihitaji kutoka moyoni mwake ni kuweka ukaribu naye kwani siku ya kwanza kumuona, alijisikia tofauti moyoni mwake na ndiyo maana aliamua kumfuatilia.

    Felista alivyosikia hivyo, kama kawaida ya msichana yeyote yule wa Kitanzania, akaanza kuringa na kunata lakini moyo wake ulikuwa ukimuomba Mungu mwanaume huyo asibadilishe mawazo na kuachana naye.

    Aliringa lakini hakutaka kukaza, kila alichoambiwa alikubali kwa kuwa moyo wake ulitokea kumpenda Jackson kupita kawaida. Wakazungumza mambo mengi mno usiku huo, Jackson alijitahidi kutokumpenda msichana huyo lakini mwenyewe akawa amefika, haambiwa wala hasikii lolote lile.

    Baada ya kumaliza, Daniel akapiga simu na kumwambia kwamba sasa alikuwa huru kwani mke wake, Jackline hakuwa nyumbani, aliondoka kuelekea kwa wazazi wake kwa kuwa walihitaji kumuona mjukuu wao.

    Kwa jinsi alivyoongea Daniel, alionekana kuwa na furaha tele, alimpenda felista, kwake, msichana huyo alionekana kuwa kila kitu, yaani pumzi yake, kituo chake na mwisho wa moyo wake.

    “Ni kweli kaenda nyumbani au kakuzuga?” aliuliza Felista.

    “Amekwenda. Mke wangu hajui chochote kile, usiogope,” alisema Daniel huku akionekana kuwa na furaha tena.

    Wakati hayo yakiendelea, ili kumpa urahisi wa kumkamata mume wake, Pendo alimkutanisha Jackline na msichana aliyekuwa katika kitengo cha huduma kwa wateja cha mtandao aliokuwa akiutumia mume wake na kumuunganishia namba yake ili kila meseji aliyokuwa akitumiwa, ilipitia kwake na kila siku iliyokuwa ikipigwa, na kwake ilifika.

    Daniel aliwasiliana na Felista huku mke wake akifuatilia kila kitu. Aliumia mno, alilia kupita kawaida, bado hakuamini kama mume wake yule aliyekuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati angeweza kubadilika kiasi hicho.

    Pamoja na kufanya ujinga wote huo lakini bado Daniel hakutaka kumuonyeshea mke wake tofauti yoyote ile, kila siku aliwasiliana naye na kwenda nyumbani kwake na kuzungumza naye.

    Alimwambia kwamba alimkumbuka na alitamani sana muda ufike ili arudi nyumbani kwani upweke ulitawala nyumbani hapo na alihitaji sana kumuona akirudi.

    Alijua kwamba mume wake alikuwa akimsaliti lakini kwa mapenzi ambayo aliendelea kumuonyeshea bila kubadilika yalimuonyeshea kabisa kwamba hakuwa mwanaume wa kawaida na inawezekana kabisa kwamba alitembea na felista kwa tamaa ya mwili lakini si kwa mapenzi.

    “Nakupenda mke wangu!” alisema Daniel huku akimwangalia mwanamke huyo.

    “Nakupenda pia!”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nataka niende nawe nikale chakula cha usiku na wewe halafu nitakurudisha, upo tayari?” aliuliza Daniel.

    Hilo halikuwa na tatizo hata kidogo, Jackline akakubaliana naye na kwenda naye kula chakula cha usiku pamoja. Njiani kama kawaida yao waliendelea kutaniana, walicheka pamoja kiasi kwamba mpaka wakati mwingine Jackline alihisi kwamba zile meseji alizokuwa akizisoma hazikuwa za mume wake, inawezekana hata ile sauti aliyokuwa akiisikia ikizungumza na Felista ilikuwa ni ya mtu mwingine kabisa.

    Walikwenda huko na kula pamoja, walipomaliza, Daniel akamrudisha nyumbani na yeye kurudi kulala. Alipofika nyumbani, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumpigia simu Felista na kuanza kuzungumza naye, alimpenda msichana huyo kwa sura lakini kila alipokuwa akilikumbuka umbo lake matata la nyuma, tamaa ilimuingia.

    “Naomba nije nikuone, mke wangu hayupo hivyo hata nikilala nje hakuna atakayeniuliza,” alisema Daniel huku akionekana kuwa na mhemko kupita kawaida.

    “Sasa hivi?”

    “Ndiyo! Mbona saa nne mapema sana!”

    “Hapana! Nimepumzika bebi!”

    “Jamaniii! Halafu unaongea kwa sauti ndogo, upo nyumbani kweli?” aliuliza Daniel alionekana kuwa na wasiwasi kwani kwa sauti aliyokuwa akiitumia Felista kuzungumza ilikuwa tofauti kabisa na siku hiyo.

    “Ndiyo! Mama amekuja kunitembelea, yaani ulipopiga simu, nikatoka chumbani,” alisema Felista.

    “Kumbe mama yupo?”

    “Ndiyo!”

    “Basi nitakucheki kesho. Nakupenda bebi!”

    “Nakupenda pia!”

    Upande wa pili felista alikuwa nyumbani kwake. Alimwambia Daniel kwamba mama yake alikuwa nyumbani lakini ukweli ni kwamba mtu huyo hakuwepo bali alikuwa Jackson ambaye alikwenda kumtembelea na kulala naye usiku mzima.

    Wakati msichana huyo alipotoka kwenda nje kuzungumza kwa simu, Jackson alikuwa akifuatilia, alijua ni mtu gani alikuwa akienda kuongea naye hivyo hakuonekana kujali kwani hakuwa kwenye mapenzi ya dhati na msichana huyo bali alichokihitaji ni kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba msichana huyo anaachana na Daniel.

    “Ulikwenda wapi bebi?” aliuliza Jackson mara baada ya Felista kurudi chumbani.

    “Nilikwenda kuongea na shoga yangu! Ananidai nikawa nakwenda kumpiga maneno kidogo,” alisema Felista huku akitoa tabasamu ambalo aliamini lingemfanya Jackson kumwamini.

    “Ooh! Kumbe nimepata mchumba mjanja sana, hivyo ndivyo unavyotakiwa kufanya,” alisema Jackson pasipo kuonyesha wivu wowote ule, akamvuta msichana huyo, akampiga mabusu mfululizo na kisha kulala naye kwa kujifunika kwenye shuka, kilichosikika baada ya hapo ni sauti ya kitanda hicho tu.

    “Kwichiiii...kwichiii...kwichiiii...”



    Maisha ya mapenzi yakamteka Felista, moyo wake ulichanganyikiwa kwa Jackson, ni kweli aliwahi kukutana na wanaume wengi waliokuwa na uwezo mkubwa kitandani lakini kwa mwanaume ambaye alikutana naye kipindi hicho alikuwa na uwezo mkubwa kupita kawaida.

    Akachanganyikiwa, moyo wake ukatokea kumpenda kuliko mwanaume yeyote yule, kila siku alikuwa akimpigia simu na kumsisitizia kwamba alikuwa akimpenda kupita kawaida.

    Kwa Jackson, hakutaka kuuruhusu moyo wake uwe kwa msichana huyo, hakumpenda kutoka moyoni mwake bali kila kitu alichokuwa akikifanya, alifanya kwa kuwa alitumwa, yaani alifanya kwa sababu kulikuwa na kazi aliyokuwa akiifanya.

    Aliendelea na maisha ya maigizo, kila siku alikuwa akikutana na msichana huyo na kumuigizia kwamba alikuwa akimpenda kupita kawaida.

    Kwa upande wa pili, Daniel hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea. Moyo wake ulimpenda sana Felista na hakuona kama kungekuwa na mwanamke ambaye angeweza kuutoa moyo wake kutoka kwa msichana huyo.

    Alimpa kila kitu alichokitaka na hakuhisi kabisa kama Felista angeweza kumsaliti kwani hata walipokuwa wakikutana na kuzungumza, msichana huyo alizungumza naye kwa mapenzi ya dhati kiasi kwamba Daniel alichanganyikiwa zaidi.

    Siku zikaendelea kukatika kama kawaida. Mara kwa mara wawili hao walikuwa wakikutana lakini kwa kipindi hiki hali ilionekana kuwa tofauti na si kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

    Yule Felista hakuwa na furaha kama kipindi cha nyuma, kila alipokuwa akikutana na Daniel alionyesha mabadiliko fulani ambayo yalionekana kuanza kumtia hofu Daniel.

    Hakujua kulikuwa na kitu gani kilichokuwa kikiendelea, alijaribu kumuuliza kulikuwa na nini lakini msichana huyo alikuwa akimdanganya kwamba hakukuwa na kitu chochote kile, mambo yote yalikuwa supa kabisa.

    Hilo halikuaminika kwa Daniel lakini hakuwa na jinsi, alijifanya kumwamini lakini upande wa pili moyo wake ulikata katakata kukubaliana na kile alichokuwa akimjibu kila alipokuwa akimuuliza.

    Felista alibadilika kwa kiasi kikubwa, kilichombadilisha si kitu kingine zaidi ya Jackson ambaye aliingia kwa kasi moyoni mwake. Mabadiliko hayo makubwa yakampelekea kumuona sana Daniel kwamba kila watakapokuwa wakifanya mapenzi ilikuwa ni lazima kutumia mpira.

    “Kwa nini?” aliuliza Daniel huku akionekana kushtuka.

    “Ni maamuzi!”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Yaani imekuwaje? Mbona yamekuja ghafla sana?” aliuliza Daniel, kuambiwa vile kulimchanganya kwani hakutegemea kama Felista angemwambia jambo hilo.

    Akawa na hofu kwamba inawekana msichana huyo alikuwa ameathirika na hivyo kwenda kupima. Alipofika huko, afya yake ilionekana kuwa safi kabisa.

    Alijiuliza zaidi kuhusu uamuzi wa msichana huyo lakini hakupata majibu yoyote yale. Hakutaka kuwa na hofu, hakutaka kujipa presha hivyo akakubaliana naye kwa kila kitu na maisha kusonga mbele.

    Kadiri siku zilivyosonga ndivyo msichana huyo akaanza kuonekana kupunguza mapenzi kwake. Alitumia kiasi kikubwa cha pesa kuyarudisha mapenzi ya msichana huyo lakini alishindwa kabisa.

    Katika kipindi hicho akahisi kabisa kwamba Felista alikuwa na mwanaume mwingine. Alihisi hicho, zikawa hisia zilizokuwa zikimuumiza kupita kawaida. Alikaa chumbani kwake huku akihuzunika, kila alipokuwa akimpigia simu msichana huyo, aliipokea na jibu moja tu ndilo alilokuwa akimpa “Nipo bize sana”.

    Neno hilo liligeuka kama msumali wa moto moyoni mwake, hakutaka kuamini kama msichana yule ambaye alitumia muda wake mwingi, pesa zake mwisho wa siku angemwambia maneno kama hayo.

    Alijiamini kwa sababu alikuwa na pesa hivyo kuanza kumpeleleza mpenzi wake huyo. Siku alipokutana naye, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuchukua simu yake, akaifungua na kukutana na meseji za kimapenzi alizokuwa amewasiliana na Jackson.

    Moyo wa Daniel ukawaka kwa hasira, wivu mkali ukamkamata na kumuumiza kupita kawaida. Alimwangalia msichana huyo huku macho yake yakionyesha kuwa na hasira kupita kawaida. Alitamani kumpiga lakini mapenzi aliyokuwanayo yalikuwa makubwa na mbaya zaidi hakutamani kabisa kumkasirisha msichana huyo.

    “Kwa nini Felista?” aliuliza Daniel huku machozi yakitiririka mashavuni mwake, alijishangaa kwani hata kwa mke wake hakuwahi kulia kiasi hicho.

    “Daniel! Una mke, si ndiyo?” aliuliza Felista swali ambalo lilimshtua mno Daniel.

    “Unasemaje?”

    “Wewe si una mke?”

    “Ndiyo!”

    “Kwa hiyo hutaki mimi niolewe?” aliuliza Felista.

    Swali hilo likamfanya Daniel kubaki kimya. Hakutegemea kusikia swali kama hilo akiulizwa na msichana huyo. Alimwangalia mara mbilimbili, swali lake lilikuwa la msingi sana lakini hakutaka kulijibu kwa haraka, ilihitajika hekima ya zaidi kulijibu swali hilo.

    “Hutaki niolewe?” aliuliza Felista huku akimwangalia Daniel machoni.

    “Si kwamba sitaki!”

    “Kumbe?”

    “Ninaumia moyoni!” alijibu.

    “Kwa hiyo mimi siumii kila siku unavyolala na mkeo?” aliuliza Felista.

    Daniel akanyamaza, akayatuliza macho usoni mwa Felista. Aliona jinsi msichana huyo alivyokuwa na maumivu moyoni mwake lakini pia alimuona jinsi alivyokuwa na wivu mkali uliokuwa ukiutesa moyo wake.

    “Daniel!” aliita Felista.

    “Naam!”

    “I am pregnant?”(nina mimba) alisema Felista, moyo wa Daniel ukapiga paa.

    “Unasemaje?” aliuliza.

    “Nina mimba!” alirudia jibu lake.

    Daniel akanyamaza, akaelekea pembeni, akatulia na kumwangalia Felista. Moyo wake ulishtuka, hakuamini kile alichokisikia kutoka kwa msichana huyo.

    Picha ya mke wake ikamjia kichwani mwake, hakuona kama lilikuwa jambo jema kumfanyia mkewe, moyo wake ulimuuma mno na kitu ambacho kilikuja moyoni mwake ni kumshawishi msichana huyo aitoe mimba yake.

    “Felista! Hapana! Ni mapema mno mimi kuzaa na wewe!” alisema Daniel huku kijasho kikimtoka.

    “Kwa hiyo nisizae!”

    “Ikiwezekana hata kutoa mimba mpenzi!” alisema Daniel bila hofu yoyote ile.

    “Yaani nitoe damu yako?”

    “Kwani kuna tatizo?”

    “Mbona hukumwambia mkeo atoe mimba ya mtoto wako?” aliuliza felista swali lililomuumiza Daniel lakini hakuwa na jinsi kwani kile alichoulizwa, kilikuwa ni ukweli mtupu.

    Hakujua ni lipi alitakiwa kujibu, alitulia na kuamua kuondoka huku akiwa amechanganyikiwa. Felista alibaki akicheka tu, aliamini kwamba mimba haikuwa ya Daniel, alipewa mimba hiyo na Jackson ambaye alifika kwake huku akiwa hana hata mapenzi.

    Lakini mbali na hilo akagundua kwamba Daniel hakuwa na mapenzi ya dhati kwake kwani kama kweli alikuwa na mapenzi ya dhati asingeweza kumwambia aitoe mimba hiyo na wakati alijua kwamba ilikuwa yake.

    Nyumbani Daniel alikuwa na mawazo tele, moyo wake ulimuuma, alichanganyikiwa. Alimpenda felista lakini kitendo cha kubeba mimba aliyohisi kwamba ni yake kilimuumiza mno.

    Kitu pekee kilichokuja kichwani mwake kilikuwa ni kuitoa mimba hiyo kinguvu. Yaani amuite ofisini mwake kwa lengo la kuzungumza naye na kumpa kahawa ambayo ndani ingekuwa na dawa ya kutoa mimba na kusafisha kabisa.

    Hilo wazo likapita kichwani mwake, hakutaka kujiuliza, kilichotakiwa kufuata ni utekelezaji wa kile alichotakiwa kufanya. Kwa hali aliyokutana nayo, hakutakiwa kuwa na huruma tena, iwe isiwe ilikuwa ni lazima mimba ya Felista itoke.

    ***

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog