Simulizi : Only You ( Ni wewe Tu )
Sehemu Ya Tano (5)
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jackson alikuwa akipambana kwa nguvu zote, alionyeshewa mapenzi yote na Felista lakini moyo wake haukutaka kukubali kuwa na msichana huyo.
Walifanya mapenzi lakini mwisho wa siku alikumbuka kabisa kwamba huyo alikuwa kama rafiki yake ambaye alikuwa akifanya kazi fulani kwa ajili ya mtu fulani.
Walikuwa wakitoka na kwenda sehemu mbalimbali, walistarehe huku muda mwingi wakiwa wanapigiana simu. Lengo kubwa la kufanya hivyo lilikuwa ni kumsahaulisha msichana huyo na Daniel kitu ambacho kwa kiasi fulani kilionekana kuanza kufanikiwa.
Huku akiwa bize na Felista, kitu cha kushangaza moyo wake ukaanza kuzama kwa msichana huyo. Hakutaka kuona hilo likitokea, alijikaza mno, alifanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba haangukii kwenye penzi la Felista lakini kikafika kipindi kila kitu kikaonekana kuanza kubadilika.
Kila alipokaa, alimkumbuka msichana huyo, kila alipokuwa akifanya hiki na kile ni picha ya Felista tu ndiyo iliyokuwa ikija kichwani mwake. Alikasirika, alichukia lakini moyo wake ndiyo ulianza kubadilika taratibu kiasi kwamba kila alipokuwa akikaa kimya pasipo kuwasiliana na msichana huyo, moyo wake ulijisikia tofauti kabisa.
Siku zikaendelea kukatika, penzi likaanza kuunyemelea moyo wake na mwisho wa siku kuanza kusikia wivu kila alipokumbuka kwamba Felista alikuwa akitoka kimapenzi na Daniel.
Alitamani kumwambia ukweli kuwa alitakiwa kuachana na mwanaume huyo lakini alishindwa kabisa kwani kama angefanya hivyo ilikuwa ni lazima kuharibu mambo kabisa kitu ambacho hakikutakiwa kutokea hata siku moja.
Alichokifanya ni kuanza kumpa ubize mwingi wa kuwa naye, hakutaka kuona msichana huyo akiwasiliana na Daniel kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma, alimbana na hata wakati mwingine kuichukua simu ile na kukaa nayo.
Hakutaka kuona akichukuliwa msichana huyo, alitokea kumpenda na kila alipokuwa akienda kazini, alihakikisha jioni anakwenda kumchukua hukohuko kazini.
Penzi likanoga, Felista alichanganyikiwa na kuona kabisa kwamba moyo wake ulitekwa na Jackson na kitu pekee alichokuwa akikihitaji ni kuzaa na mwanaume huyo tu.
Wakati akifikiria hilo ndipo akagundua kwamba alikuwa na mimba. Ilikuwa ni ya Jackson, moyo wake uliridhika mno na aliona kabisa hiyo ndiyo ilikuwa nafasi ya kuachana na Daniel hivyo kumwambia kwamba alikuwa na mimba.
Hakutaka kumwambia kama ilikuwa yake au la. Alihitaji kukaa kwa siku kadhaa ndipo amwambia kwamba haikuwa mimba yake, ilikuwa ya mwanaume mwingine hivyo alitakiwa kumuacha na kuendelea na maisha yake.
Wakati hayo yote yakiendelea, hakutaka kujificha, alichokifanya ni kumwambia Jackson kwamba alikuwa na mimba yake hivyo alitakiwa kulifahamu hilo.
Jackson akashtuka, hakuamini alichokisikia, moyo wake ulikuwa na furaha tele, alipenda kuwa na mtoto na ndiyo ilikuwa furaha yake katika maisha yake yote.
Akamsogelea Felista pale alipokuwa, akamsimamisha na kumkumbatia kwani katika vitu ambavyo alitamani sana kuwa navyo, cha kwanza kilikuwa ni mtoto.
“Nimefurahi kuniambia hivyo,” alisema Jackson huku akiwa amemkumbatia.
“Nashukuru kwa kunipa kitu nilichokuwa nakihitaji sana,” alisema msichana huyo na kisha kukumbatiana kwa kung’ang’aniana sana.
Wawili hao walifurahia, mapenzi waliyokuwanayo yakazidi kuongezeka pasipo kujua kwamba upande wa pili Daniel alikuwa akipanga jambo lake. Hakutaka kuona Felista akijifungua kwa kuamini kwamba hiyo ilikuwa mimba yake, kama mwanaume alitakiwa kupambana mpaka kuhakikisha kwamba mimba hiyo inaharibika hata kabla ya kujifungua.
Siku iliyofuata akaamka asubuhi, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumpigia simu mke wake na kumsalimia, alizungumza naye kwa dakika kadhaa kisha kujiandaa kwa ajili ya kwenda kazini.
Kichwa chake kikaanza kumfikiria Felista, moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kama kutembea nje ya ndoa kungemfanya kumpa mimba msichana fulani. Aliona kabisa ndoa yake ilikuwa ikienda kuvunjika kama tu angemucha msichana huyo ajifungue.
Ilikuwa ni lazima kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha mimba hiyo inaharibika. Kabla ya kufika ofisini, akapitia katika duka la dawa ambapo akaulizia dawa iliyokuwa na uwezo wa kutoa mimba ya msichana na kumsafisha kabisa.
“Ipo lakini huwa hatuuzi mpaka uwe na cheti kutoka kwa daktari,” alisema msichana aliyekuwa akiuza dawa.
“Kwa hiyo mpaka niwe na cheti cha daktari?” aliuliza Daniel.
“Ndiyo!”
Daniel akanyamaza, kichwa chake kikaanza kufikiria kitu kingine kabisa. Alijua kwamba hakuruhusiwa kununua dawa hizo kama tu hakuwa na cheki maalumu kutoka kwa daktari lakini aliamini kwamba kwa kutumia pesa angeweza kuzinunua dawa hizo bila tatizo lolote lile.
Hicho ndicho alichokifanya, akachukua noti tano za shilingi elfu kumi na kumgawia msichana huyo na kumwambia kwamba alihitaji sana hizo dawa kwa kuwa hakutaka kupata mtoto na wakati mtoto wake hakuwa ametimiza hata mwaka mmoja.
Msichana huyo hakuwa na jinsi, alizitamani pesa zile na asingeweza kuziacha hata kidogo. Akazichukua dawa hizo na kumpa Daniel dawa zilizoitwa Misoprosol ambazo mhusika alitakiwa kumeza vidonge viwili na baada ya saa sabini na mbili alitakiwa kumeza vidonge vinne.
“Nashukuru sana!” alisema Daniel na kuondoka mahali hapo.
Kidogo moyo wake ukafarijika, akawa na furaha kwamba hatimaye alikuwa akienda kufanikiwa kile alichokuwa akikitaka. Hakuchukua muda mrefu, akafika ofisini ambapo akateremka na kuingia ndani.
Alipofika, akajiachia kwenye kiti na kuendelea kufanya kazi zake kama kawaida. Moyo wake muda wote ulikuwa na mawazo tele, hakujua ni kitu gani kingetokea kama tu asingefanikiwa kwa kile alichokuwa amekikusudia.
Baada ya saa moja, akachukua simu yake na kumpigia Felista na kumwambia kwamba kama alikuwa na muda aende ofisini kwake kwani kulikuwa na vitu kadhaa alitaka kuzungumza naye, hususani mtoto ambaye alitarajiwa kuzwaliwa baada ya miezi tisa.
Hilo halikuwa tatizo, baada ya saa moja, akapigiwa simu na kuambiwa kwamba Felista alikuwa kwa sekretari hivyo kilichohitajika ni ruhusa yake. Kabla ya kuruhusu, haraka sana akaelekea kwenye meza ndogo iliyokuwa na chupa ya chai, akachukua vidonge vinne badala ya viwili, akavisaga na kuviweka katika kikombe ambacho ndicho alichotakiwa kummiminia chai msichana huyo.
Baada ya kuona kila kitu kipo sawa, akaruhusu msichana huyo aelekee ofisini kwake ambapo akaingia na kuelekea kwenye kiti kimoja na kutulia.
Wakaanza kuongea, muda wote Daniel alionekana kuwa na furaha, alimchangamkia Felista kana kwamba hakukuwa na kitu kibaya. Walikuwa wakiongea huku wakati mwingine wakigongesheana mikononi.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Felista alionekana kuwa na furaha tele na hakujua nini kingetokea kama mwanaume huyo angejua siku moja kwamba ile mimba haikuwa yake.
Baada ya kuzungumza kwa dakika kumi huku kiyoyozi kikipiga, Daniel akasimama na kumwambia amuekee chai ili awe anakunywa huku wakiendelea na mazungumzo yao.
“Nitashukuru!” alisema Felista.
Akaenda kwenye kile kimeza na kumimina chai vikombe viwili. Kile ambacho alitakiwa kunywa Felista kilikuwa upande wa kulia na kingine upande wa kushoto na kumpelekea.
Alihakikisha kile alichotakiwa kunywa msichana yule anampa na yeye kuchukua kile kingine na kukaa, wakaendelea na maongezi yao.
Felista alitaka kunywa chai ile lakini alishindwa kwa kuwa ilikuwa ya moto sana, Daniel alilijua hilo hivyo kumwambia kwamba hakutakiwa kuwa na wasi, asubiri kwanza ipoe ndiyo aenze kunywa.
Maongezi yaliendelea, baada ya sekunde kadhaa, Daniel akapigiwa simu na sekretari wake na kuambiwa kwamba kulikuwa na wageni walihitaji kumuona mara moja.
“Niwaambie waingie?”aliuliza sekretari.
“Hapana! Nakuja hapohapo!”
Hakutaka kubaki ndani, akamuaga Felista na kumwambia kwamba angerudi baada ya dakika kadhaa kwani kulikuwa na watu alitaka kuzungumza nao.
Akatoka na kukutana na watu hao. Walikuwa ni watu kutoka katika Kampuni ya Vodacom ambao walihitaji kuzungumza naye. Walikuwa watu muhimu, aliwakalisha hapo kwa sekretari na kuzungumza nao kwa dakika kumi kisha kurudi ofisini kwake ambapo akamkuta Felista akiendelea kunywa chai yake baada ya kupoa.
Moyo wake ukafurahi, alionekana kufanikisha kile alichokihitaji. Wakaendelea kupiga stori kama kawaida huku akimwambia kuwa alikuwa tayari kumlea mtoto wake kwa nguvu zote kwani aliamini kuwa mtoto ni baraka kutoka kwa Mungu.
“Nitamlea kwa nguvu zote. Ninapenda sana watoto, kama ni uwezo wangu, nitahitaji niwe na watoto zaidi ya watano,” alisema Daniel huku akionekana kuwa na furaha mno.
“Kweli mpenzi?”
“Niamini! Ninapenda sana watoto,” alisema Daniel huku akiwa na uhakika kwamba ile mimba ingetoka kwani tayari msichana huyo alikunywa chai iliyokuwa na dawa ile ya kutoa mimba ambayo ingeanza kufanya kazi baada ya saa kadhaa.
***
Daniel alizungumza sana na Felista na alipomaliza, msichana huyo akaondoka kurudi nyumbani kwake. Huku nyuma mwanaume huyo alikuwa na furaha tele, hakuamini kama alifanikisha mpango wake na muda wowote ule mimba aliyokuwanayo Felista ingetoka na hivyo kuachana naye huku msichana huyo akiwa hana cha kujidaia.
Alikaa ofisini na baada ya muda fulani akaondoka kurudi nyumbani. Njiani, alikuwa na furaha tele, moyo wake ulifarijika kwa kile alichokuwa amekifanya, alimpenda Felista lakini moyo wake haukutaka kupata mtoto kwa msichana huyo kwa sababu alikuwa na mke.
Alimchukulia kama msichana wa starehe ambaye alikutana naye pale alipotaka kutimiza haja za mwili wake na ndiyo maana hakuacha kumpenda mke wake ambaye aliamini kwamba ndiye Mungu aliyekuwa amemchagua na kuishi naye.
Kabla ya kufika nyumbani, akapata wazo la kwenda kumsalimia mke wake. Akachukua simu na kumpigia, ilipopokelewa, akamwambia kwamba angefika huko muda si mrefu.
Akaelekea huko na kuonana naye. Alipomuona, moyo wake ukafurahi, tabasamu pana likaonekana usoni mwake na kuona kwamba alikutana na mwanamke mrembo kupita wote katika dunia hii.
Kwa jinsi alivyokuwa akiishi na mke wake, ilikuwa ni vigumu kugundua kwamba aluwa akitembea nje ya ndoa, hakuonyesha mabadiliko yoyote yale kiasi kwamba hata wakati mwingine Jackline alijiona kufanya makosa kuhisi kama mume wake huyo alikuwa akitembea nje ya ndoa.
“Kazi vipi?” aliuliza Jackline huku akimwangalia mume wake.
“Ni nzuri! Nimechoka, nimekukumbuka sana mke wangu, nyumba nayo imekukumbuka, vyombo, mbwa wetu na kila kitu ndani ya nyumba kimekukumbuka,” alisema Daniel huku akimwangalia mke wake huyo.
“Tumewakumbuka pia, natumaini nitarudi baada ya siku kadhaa!” alisema Jackline.
“Kweli?”
“Ndiyo! Wala usijali mume wangu!” alisema Jackline.
Alikaa huko kwa zaidi ya dakika arobaini na tano kisha kuaga na kuondoka mahali hapo. Njiani, kichwa chake kikaanza kumfikiria tena Felista, msichana huyo alimkaa kichwani lakini hakutaka kumuendekeza sana kwani alitarajia kuachana naye wakati mimba hiyo itakapokuwa imetoka kabisa.
Alipofika nyumbani, simu yake ikaanza kuita, alipoangalia kioo, akakuta ni Felista, kwanza akahisi kwamba tayari mambo yalikubali na hivyo msichana huyo alikuwa akitaka kumpa taarifa kuhusu kuchomoka kwa mimba hiyo.
Akaipokea huku uso wake ukiwa na tabasamu pana, alikuwa akifarijika moyoni mwake kwani alikuwa na uhakika simu hiyo ingeufanya moyo wake kufurahia kupita kawaida.
“Niambie bebi!” alisema Daniel.
“Safi tu! Nimekaa na kitumbo changu hapa. Hivi tukipata mtoto wa kiume ungependa tumuite nani?” aliuliza msichana huyo.
Kwanza Daniel akabaki kimya, kile alichokuwa akikitegemea si kile alichokisikia. Alichokitegemea ni kwamba angepewa taarifa mbaya kuhusu kutoka kwa mimba hiyo lakini kitu cha ajabu kabisa alikuwa akipewa taarifa kuhusu jina la mtoto.
“Tumuite Dylan,” alisema Daniel huku akionekana kutokuwa na furaha.
“Kwa hiyo jina lake lianze na D kama baba yake?”
“Ndiyo hivyo! Ninayapenda majina ya D sana, yaani kama langu!” alisema Daniel huku akitamani hata kumuuliza msichana huyo kama alianza kusikia maumivu ya tumbo.
Walizungumza mengi, baada ya dakika kadhaa, akakata simu na kujipa uhakika kwamba kama si siku hiyo basi siku yoyote ile angepigiwa simu na msichana huyo kupewa taarifa kwamba mimba ilikuwa imetokea.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku ziliendelea kukatika, upande wa pili Jackson alikuwa akiendelea kuonyesha mapenzi yake kwa Felista, alimpenda msichana huyo na kila wakati alipokuwa naye alipenda kulishika tumbo la Felista na kujifanya akimsikiliza mtoto wake.
Moyo wake haukumpenda Daniel, alikuwa amepewa kazi kuhakikisha wawili hao wanaachana lakini kilichotokea ni kwamba akajikuta akitumbukia katika penzi na msichana huyo.
Hakutaka kumuacha peke yake, mara kwa mara alikuwa akimchukua na kwenda naye sehemu, walikuwa wakiyafurahia maisha na baada ya saa kadhaa kurudi na kuendelea na mambo mengine.
Kwa kile kilichokuwa kikiendelea, Jackson akashindwa kuvumilia, alihitaji wale watu waliomtuma wajue kila kitu, akachukua simu yake na kumpigia Pendo, msichana huyo alipopokea, akaanza kuzungumza naye.
Hakutaka kumficha, alimwambia ukweli kwamba kutumwa kwake kulimfanya kumpenda msichana huyo na mbaya zaidi alimpa mimba hivyo alitegemea kupata mtoto baada ya miezi tisa.
Pendo alivyosikia hivyo, alishangaa, hawakumtuma kijana huyo kwenda kumpa mimba Felista bali walimtuma kumuachanisha na Daniel. Ila hilo hakulilaumu sana kwani aliamini kwa kuwa alimpa mimba basi ilikuwa kazi nyepesi kuwaachanisha wawili hao kama walivyokuwa wamepanga.
Walizungumza kwa dakika kadhaa, baada ya kukata simu, Pendo akampigia Jackline na kuanza kuzungumza naye. Alimwambia kila kitu alichoambiwa na Jackson, kama alivyoona kwamba hilo lilikuwa jambo jema, naye akaungana naye na kuamua kumpigia simu kijana huyo ili asikie kwa masikio yake kile alichoambiwa.
“Nimesikia umempa mimba!” alisema Jackline.
“Ndiyo! Halafu huwezi kuamini, nimetokea kumpenda sana Felista, tena kwa moyo wangu wote!” alisema Jackson.
“Mmh! Wanaume nyie mmeshindikana!”
“Hahaha! Kweli tena! Yaani sikutaka kabisa hilo litokee lakini imeshindikana, moyo wangu umetekwa na sisikii la mtu yeyote yule,” alisema Jackson na kuanza kucheka.
Wiki ya kwanza ilikatika, wiki ya pili kuingia lakini Daniel hakupigiwa simu na Felista kuambiwa kama mimba ilitoka au la. Moyo wake ulihuzunika, muda wote alikuwa akijiuliza nini kilitokea lakini alishindwa kupata jibu kabisa.
Hakutaka kusubiri, alipoona wiki hizo zimekatika bila kupewa taarifa ya kuharibika kwa mimba, akampigia simu msichana huyo na kutaka kuonana naye.
Kwa felista ilikuwa vigumu kwa sababu muda wote alikuwa na Jackson, na hakutaka kumficha, alimwambia kwamba muda huo alikuwa na mpenzi wake hivyo hakutaka usumbufu kabisa.
“Na mimba?” aliuliza.
“Inaendelea vizuri kabisa. Nilikwenda kuangalia, nikaambiwa ni mtoto wa kike, ungependa tumpe jina gani?” aliuliza Felista huku akitoa tabasamu kana kwamba alikuwa akionana na Daniel.
“Jina? Jina? Daah! Hebu subiri kwanza,” alisema Daniel na kukata simu.
Alichanganyikiwa, moyo wake ulikuwa na presha kupita kawaida. Kwa usalama wa ndoa yake ilikuwa ni lazima mimba hiyo itoke kwa vyovyote vile. Hakutaka kuona msichana huyo akijifungua kwa kuamini kwamba kuna siku angempeleka mtoto huyo nyumbani kwake na hivyo kuzua kizaazaa.
Baada ya kuona hilo halikufanikiwa, moyo wake ukamwambia ni lazima awasiliane na dada wa lile duka alilomuuzia ili apate kujua kama kweli dawa ile aliyoinunua ilikuwa yenyewe au la, na kama ilikuwa yenyewe, kwa nini mpaka kipindi hicho mimba ya Felista haikuwa imetoka?
Hakutaka kubaki ofisini, haraka sana akaondoka mpaka kwenye lile duka, alipofika akaanza kuzungumza na msichana yule. Alimkumbuka vizuri sana, Daniel akamuuliza kuhusu zile dawa alizokuwa amezinunua.
“Kwani zimefanyaje?”aliuliza dada huyo.
“Nilimuwekea mke wangu, lakini mpaka leo naona haumwi tumbo, linazidi kukua tu, yaani tuna wasiwasi,” alisema Daniel huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Ulimuwekea kwenye chai kama nilivyokwambia?”
“Ndiyo!”
“Vidonge viwili?”
“Hapana! Niliweka vinne, yaani niliongeza dozi!” alisema Daniel.
“Na umesema mpaka leo mimba ya mkeo haijatoka?”
“Ndiyo! Yaani nimechanganyikiwa. Na haya maisha kupata mtoto mwingine ambaye hatujapanga, sijui itakuwaje!” alisema Daniel.
“Na chai alikunywa?”
“Ndiyo! Alikunywa! Tena tulikunywa wote,” alisema Daniel.
Kwa jinsi alivyokuwa akionekana tu ilikuwa ni rahisi kugundua kama mwanaume huyo hakuwa sawa, alichanganyikiwa kiasi kwamba kila kitu alichokuwa akikifikiria ni picha ya Felista ndiyo iliyomjia kichwani mwake.
Dada huyo akazungumza naye kwa kumridhisha kwamba hakutakiwa kukata tamaa kwani kuna siku angepewa taarifa kwamba mimba hiyo ilikuwa imeharibika kwani wakati mwingine huchukua hata mwezi lakini majibu ni lazima yapatikane.
***
Felista alikuwa ofisini kwa Daniel, kichwa chake kilikuwa na mawazo tele kuhusu mimba ile. Alijua dhahiri kwamba haikuwa ya mwanaume huyo lakini aliamini kwamba kama angemwambia ukweli ingekuwa vigumu kuja kupata pesa tena.
Alipokorogewa chai na mwanaume huyo kwenda nje, alibaki mule ofisini huku akitaka kunywa chai ile. Alipoonja kidogo sana akagundua kwamba ilikuwa na majani mengi mno kiasi cha kumfanya hata kupata matatizo katika ujauzito aliokuwanao hivyo alichokifanya ni kulifuata sinki la maji, akaimwaga na kuchukua maji mengine, akamimina na kuweka majani kidogo na kurudi kwenye kiti kile.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alitulia hapo na kuisubiria ipoe kwanza, ilipopoa, akaanza kunywa kama alivyotaka. Daniel aliporudi ndani ya ofisi hiyo, akamkuta msichana huyo akinywa chai ile, hakuwa na wasiwasi, aliamini kwamba chai ile aliyokuwa akinywa ilikuwa ileile aliyomuwekea hivyo kuanza kupiga stori huku akiwa na uhakika wa mimba ya msichana huyo kutoka.
Hakujua kama ile chai aliyokuwa amemuwekea aliimwaga na hivyo kuchukua maji mengine na kuweka majani ya chai kidogo kwa ajili ya afya yake.
***
Kile alichokuwa akikiamini Daniel hakikuweza kutokea, mimba ambayo aliamini kwamba ingetoka haikuweza kutoka tena. Alimwambia Felista kwamba anahitaji kumuona, alitaka kuzungumza naye lakini msichana huyo hakutaka kukubali tena kwa sababu alikuwa beneti na mpenzi wake, Jackson hivyo ilikuwa ni vigumu kuonana naye tena.
Walikuwa wakiwasiliana kwenye simu tu na muda mwingi Daniel aliogopa kwani alijua dhahiri kwamba mara baada ya mtoto kuzaliwa ilikuwa ni lazima msichana huyo aende nyumbani kwake na kumbwaga mtoto na kama siyo hivyo basi kitu kingine chochote ambacho kingeiweka ndoa yake katika hali mbaya.
Hakutaka kuona hilo likitokea, alijitahidi kwa nguvu kubwa kuhakikisha analimaliza suala hilo hata kabla mke wake hajagundua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea.
Kwa sababu ilikuwa vigumu kuonana na msichana huyo, alichokipanga kilikuwa ni kuwatafuta watu kwa ajili ya kuifanya kazi yake. Hakutaka kuona akishindwa, kwake, ilikuwa ni afadhali jambo lolote lile limtokee msichana huyo lakini si kuona akipata mtoto kwake.
Wazo moja ambalo lilimjia kichwani mwake ilikuwa ni kumteka Felista. Alijua kwamba alikuwa akienda kufanya jambo la hatari mno lakini hakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima kupambana kwa ajili ya familia yake.
Hakujua ni kwa namna gani angeweza kuwapata watu wa kumfanyia kazi yake. Hakuwa akiwafahamu, hakujua walikuwa wakiishi wapi lakini aliamini kwamba kama kweli alidhamiria kuwatafuta, asingeshindwa kwa lolote lile.
Akawaulizia matajiri wenzake ambao hao ndiyo waliomwambia kwamba kulikuwa na kundi moja lililokuwa likiishi Manzese Darajani lililoitwa Cobra ambalo lilikuwa likifanya kazi hiyo bila tatizo lolote lile.
Kidogo akafurahia na kuona kabisa kwamba alikuwa akienda kufanikisha kile alichokitaka. Akatafuta mawasiliano yao, alipoyapata, haraka sana akawasiliana nao na kuwaambia kile alichohitaji kuona kikifanyika.
“Hilo si tatizo,” ilisikika sauti kutoka kwa mwanaume aliyekuwa upande wa pili.
Akawapa maelekezo yote kuhusu mahali alipokuwa akiishi msichana huyo, muonekano wake na kila kitu kilichokuwa kikihitajika. Alipomaliza, akawatumia kiasi cha pesa walichokuwa wakikihitaji na kuwatakia kazi njema.
Kundi hilo likaanza kupanga mipango kuhakikisha kazi hiyo inafanyika haraka sana. Hawakutaka kupoteza muda, walijua kabisa kwamba walilipwa vizuri hivyo ilikuwa ni lazima kuhakikisha wanaifanya kazi hiyo.
Baada ya siku moja, vijana wa kundi hilo la Cobra wakaanza kufanya kazi yao. Ilikuwa ni lazima waifanikishe ndani ya muda hivyo walichokifanya ni kwenda katika nyumba aliyokuwa akiishi Felista kwa lengo la kumteka.
Walihitaji kumteka katika kipindi ambacho alichokuwa akitoka nyumbani kwa na kuelekea kliniki. Waliamini kwamba wangefanikiwa katika hilo kwani kama mwanamke mjauzito ilikuwa ni lazima kwenda huko.
Ilipofika majira ya saa 5:10, Bajaj moja ikaanza kusogea katika geti la nyumba hiyo na kusimama, walijua dhahiri kwamba ilikuja kumchukua msichana huyo na kwenda naye kliniki.
Wala hazikupita dakika nyingi, wakamuona Felista akitoka ndani ya nyumba ile na kuingia ndani ya Bajaj na kuondoka mahali hapo. Hawakutaka kubaki, walichokifanya ni kuanza kuifuatilia kwa gari lao.
Kwa kuwa mitaa hiyo ilikuwa kimya kabisa, hawakutaka kuwafikisha barabarani bali ni kuwawahi na kwenda kwa mbele na kulisimamisha gari lao.
Hilo ndilo walilolifanya, wakalisimamisha gari hilo mbele ya Bajaj ile na wanaume wawili waliokuwa na bastola kuteremka.
Kila mmoja aliyekuwa ndani ya Bajaj ile akaogopa, bastola zile ziliwatisha na kuona kwamba walikuwa wakienda kuuawa kinyama mahali pale.
Wakawasogelea, hawakutaka kumjeruhi mtu yeyote, wakamwambia Felista ateremke ili waondoke naye. Huku akiwa na kitumbo chake, Felista akatereka, alikuwa akitetemeka kwa hofu, hakuamini kama watu wale walimfuata yeye kwa lengo la kumteka.
“Jamani msiniue...jamani msiniue,” alisema Felista huku akitetemeka, na kilio juu.
Akachukuliwa na kuingizwa ndani ya gari lile na kuondoka mahali hapo. Humo garini alikuwa akilia, aliomba msamaha pasipo kujua kosa alilokuwa amelifanya.
Hakuwa na ugomvi na mtu, hakuwahi kulumbana na mtu yeyote yule, alimheshimu kila mmoja, kila alipojiuliza kuhusu utekaji ule alishindwa kupata jibu na wakati mwingine alihisi kwamba watu hao walikosea na kumteka mtu ambaye hakuwa tageti yao.
“Jamani naomba msiniue, naomba msiniue,” alisema Felista huku akilia.
“Usijali Felista! Hutokufa, ila ukiongea sana, kulia sana, tutakuua,” alisema mwanaume mmoja.
Kitendo cha kutajwa jina lake kikamfanya kugundua kwamba watu wale hawakukosea kumteka mhusika, alihitajika yeye na ndiyo maana walimfuata na kumteka.
Hakujua kosa alilokuwa amelifanya, aliomba msamaha lakini hakukuwa na mtu aliyekuwa akijali. Akafungwa kitambaa usoni huku gari kuendelea na safari.
Alibaki akimuomba Mungu tu, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikienda kutokea huko. Moyo wake ulimuuma na muda wote alikuwa akiomba sala yake ya mwisho kwani muda wowote ule angeweza kuuawa kinyama.
Safai iliendelea kwa dakika kumi na tano ndipo gari likasimama ndani ya jumba moja kubwa lililokuwa uswahilini. Akateremshwa na kuingizwa ndani huku akiwa amefungwa kitambaa machoni mwake.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akapelekwa mpaka katika chumba kimoja na kutolewa kitambaa kile. Mandhari ya chumba kile ilimtisha kupita kawaida. Kulikuwa na michirizi ya damu, kiti kilichokuwa na uwazi mkubwa sehemu ya kukalia.
Kulikuwa na nyaya za umeme, pasi ya umeme na vitu vingine ambavyo vyote hivyo vilikuwa na kazi ya kuwatesa watu waliokuwa wakiingizwa humo.
Moyo wake ukaogopa, hofu kubwa ikautawala moyo wake na kujipa uhakika kwamba hakutakiwa kutoka salama ndani ya chumba hicho. Kilio chake kikaanza upya, akaanza kulia kwa maumivu makali, alimlilia Jackson, alikililia kiumbe chake kilichokuwa tumboni, kwa kifupi, hakuwa na uhakika wa kutoka salama.
“Mpigie simu bosi,” alisema mwanaume mmoja maneno ambayo yalisikika vema masikioni mwa Felitsa.
Haraka sana simu ikapigwa na baada ya sekunde kadhaa kijana huyo akawa anazungumza na mwanaume kutoka upande wa pili, alikuwa ni Daniel.
Alichokihitaji yeye si kuuawa kwa Felista bali kitu alichokihitaji ni kingine kabisa. Alimwambia kijana huyo kwamba lengo lake lilikuwa ni kuhakikisha mimba hiyo inatoka kwani hakuwa na mpango wa kuwa na mtoto wa nje hata kidogo.
Aliwaambia waende kwenye duka la dawa ambapo huko wangenunua vidonge viitwavyo Misoprosol na kwenda kumnywesha msichana huyo.
“Hakuna shida bosi.”
“Ila hakikisheni mnapewa Misoprosol, tena vidonge vyote inabidi anyweshwe kwa mkupuo!”
“Sawa bosi!”
Baada ya kuzungumza na Daniel, kilichofuata kilikuwa ni kuwaambia wenzake kile alichoambiwa. Hakuongea kwa sauti ya chini kama siri, aliongea kwa sauti ya kawaida ambayo iliweza kusikika mpaka kwa Felista aliyekuwa chumbani.
“Kwa hiyo lengo lake ni kuitoa mimba hiyo?” aliuliza mwanaume mmoja.
“Ndiyo! Yaani kwa kifupi ni kwamba hataki mtoto wa nje ya ndoa,” alisema jamaa aliyeongea kwenye simu.
“Basi sawa! Hilo si tatizo, ila kwa tumbo lake lile, tukimpa hivyo vidonge si atakufa?”
“Nahisi itakuwa hivyo! Ila hatuna jinsi, jamaa katupa hela nyingi hivyo tufanyeni kama anavyotaka, ngoja nifuate vidonge,” alisema kijana huyo aliyeitwa Ramadhani na kwenda kununua vidonge hivyo.
Mule ndani alipokuwa Felista hakuamini alichokisikia, moyo wake ulimuuma baada ya kugundua kwamba mtu aliyekuwa nyuma ya kila kitu ni Daniel.
Alilia mno, alijuta kuwa na mwanaume huyo, alijuta kumdanganya kwamba mimba ilikuwa yake. Hakuona kama angefanikiwa kutoka salama humo kama tu angenyweshwa dawa hizo za kutoa mimba.
Mimba yake ilitimiza miezi saba kwa maana hiyo ilikuwa ni lazima afe tu kama tu angekunywa dawa alizokuwa akitakiwa kupewa.
Alibaki akimuomba Mungu, hakuona tumaini kama angeweza kupona kutoka katika mikono ya watu hao salama. Alisali kila sala aliyokuwa akiifahamu kwani alijua baada ya muda fulani tu angenyweshwa dawa za kuondoa mimba ambazo ilikuwa ni lazima zimuue.
Ndani ya dakika ishirini, kijana aliyekuwa ametumwa kununua dawa hizo, Ramadhani akarudi huku akiwa na dawa hizo mikononi mwake. Mwenzake akazichukua na kusoma kiboksi chake, ziliandikwa Misoprosol.
“Safi sana!” alisema mwanaume huyo.
Hakukuwa na sababu ya kupoteza muda, haraka sana maji yakaletwa yakiwa kwenye glasi, akafumbuliwa mdomo na kuanza kunyweshwa vidonge hivyo.
Felista alikuwa akinywa huku akilia, alijua kabisa kilichokuwa kikifuata baada ya dakika chache ni kufariki dunia. Wanaume hao wakahakikisha mpaka dawa hizo amezinywa zote na kumtoa nje ambapo wakamwambia aondoke kwani hawakutaka msichana huyo afie mikononi mwao ndani ya chumba hicho.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Felista akaondoka, alikuwa analia, aliamini kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wake. Hakujua alikuwa wapi, alitembea kwa dakika kama tano, akahisi mwili wake ukiishiwa nguvu, hakuweza kupiga hatua zaidi, akaanza kuona giza, hapohapo akaanguka chini na kutulia.
***
Fred ndiye ambaye alitumwa kwenda kununua dawa ya Misoprosol kwa ajili ya kutoa mimba ya Felista. Aliondoka mahali hapo huku akiwa na mawazo tele.
Hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea, kila siku alikuwa akifanya kazi na kundi lake hilo, alikuwa muuaji ambaye alikuwa tayari kufanya kitu chochote kile. Siku hiyo ambayo walikwenda kumteka Felista, moyo wake ulimuuma mno.
Hakuamini kama walitakiwa kumuua mwanamke aliyekuwa na ujauzito, kila alipokuwa akimwangalia msichana yule jinsi alivyokuwa akilia, tumbo lake moyo wake ulimuuma kupita kawaida.
Hakutaka kumuua, hakutaka kuona msichana huyo akifa, kwake, hakumfikiria zaidi yeye bali alifikiria kile kiumbe kilichokuwa tumboni. Alijua kabisa watoto wengi wanaozaliwa katika mazingira hayo, nje ya ndoa ndiyo wanakuwa maisha mazuri hapo baadaye, alikumbuka kuhusu mfalme Daudi, jinsi alivyomtamani mke wa askari wake na kuamua kumuua vitani ili amchukue mkewe.
Mtoto aliyezaliwa kwenye dhambi hiyo ndiye alikuja kuwa mfalme Suleimani ambaye alibarikiwa kuliko wafalme wote katika dunia hii. Alijua kabisa kwamba Mungu alikuwa na mipango na mtoto huyo na ndiyo maana hakutaka kabisa kushiriki dhambi kubwa namna hiyo.
Alielekezwa mpaka kwenye duka la dawa na kwenda huko, alipofika, akamuuliza muuzaji vidonge ambavyo isingekuwa hatari kwa mwanamke mjauzito kunywa, yaani hata akinywa, asife.
“Ninahitaji vidonge vya malaria kwa ajili ya mjauzito,” alisema Fred huku akimwangalia dada aliyekuwa akiuza.
“Vipi?”
“Wewe una vipi?”
“Vipo vya aina nyingi.”
“Naomba ambavyo ni vizuri,” alisema Fred na msichana huyo kumpa vidonge vilivyoitwa Clindamycin.
Akamuelekeza jinsi ilivyotakiwa kutumika, ilikuwa kwenye kiboksi kilichokuwa na dawa sita. Fred aliyasikiliza maelezo vizuri na kisha kuondoka mahali hapo huku akiomba kikaratasi kingine cha akiba kwa ajili ya kuwekewa dawa.
Alipofika njiani, akapitia dukani na kuandika kwenye kikaratasi kile Misoprosol na kuondoka kurudi katika jumba lile walilomuhifadhi Felista.
Alipofika, akawaonyeshea wenzake dawa zile ambapo wakachukua na kumnywesha Felista vidonge vitatu kwa kuamini kwamba vingefanya kazi na kumuondoa mahali hapo.
Moyo wa Fred ukaridhika japokuwa alijua kabisa alitakiwa kumfuatilia msichana huyo ili hata kama angepata tatizo njiani basi amsaidie. Alipowaambia wenzake kwamba alitakiwa kuondoka, walimkatalia kwani bado walikuwa na mambo mengine waliyotakiwa kufanya, hivyo akabaki na kumuomba Mungu amlinde Felista kule alipokuwa.
Felista alishtuka na kujikuta akiwa kitandani. Mkononi mwake kulichomwa sindano ambayo ilikwenda moja kwa moja mpaka kwenye dripu ya maji iliyokuwa imening’inizwa kwa juu.
Hakutaka kujiuliza mahali hapo palikuwa wapi, alijua kabisa kwamba palikuwa ni hospitalini, swali ambalo lilikuja kichwani mwake ni jinsi alivyofika hospitalini humo.
Akajiinua na kuangalia huku na kule, ndani ya chumba kile alikuwa peke yake. Kumbukumbu za kile kilichotokea zikaanza kumjia kichwani mwake, alikumbuka jinsi alivyotekwa na watu wale kisha kupelekwa ndani ya nyumba moja na kunyweshwa dawa.
Hapo, pia akakumbuka kuhusu maneno yao, moyo wake ulimuuma baada ya kugundua kwamba mtu aliyekuwa amefanya hayo hakuwa mwingine bali Daniel ambaye kila siku alimwamini na kumdanganya kwamba alikuwa na mimba yake, ili mwanaume huyo kuhakikisha hapati mtoto nje ya ndoa, akaamua kuwatuma watu wamteke na kumnywesha dawa ili mimba itoke.
Akabaki akilia kwa uchungu, moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kama mwanaume huyo ndiye aliyefanya hilo huku akiwa na lengo la kumuua yeye na mtoto wake wa tumboni.
Alilia sana lakini hakuwa na jinsi, baada ya dakika kadhaa nesi akaingia ndani ya chumba hicho na kumjulia hali, alimwambia kwamba alipelekwa mahali hapo na wasamaria wema ambao walimuokota alipokuwa ameanguka barabarani na alifanyiwa vipi kukaonekana hakuwa na tatizo lolote lile.
Alimshukuru Mungu, akaomba simu na kumpigia Jackson ambaye baada ya dakika kadhaa akafika hospitalini hapo. Alishangaa kumkuta mpenzi wake hospitalini huku akionekana kuwa na tatizo fulani, akauliza kilichotokea, akaambiwa jambo lililomshtua yeye mwenyewe.
“Hebu niambie kuna nini?” aliuliza Jackson aliyeonekana kujiuliza sana juu ya kile kilichokuwa kimetokea.
“Nilitekwa!”
“Na nani?”
“Sijajua! Ila lengo lao lilikuwa ni kutoa mimba yangu, kwa maana hiyo ningeweza kufa,” alijibu Felista.
Alipoambiwa hivyo tu, Jackson akahisi kwamba aliyefanya jambo hilo alikuwa Daniel hivyo kutoka ndani ya chumba hicho na kumpigia simu Jackline na kuanza kuzungumza naye.
Mwanamke huyo alishtuka, hakuamini kama mume wake angeweza kufanya jambo kama hilo hivyo kumwambia waonane.
“Mumeo awe makini, nitaweza kumuua,” alisema Jackson huku akionekana kumaanisha alichokisema.
“Hebu tuonane kwanza!”
“Sawa.”
Jackson akamuaga Felista na kuondoka mahali hapo huku lengo likiwa ni kuonana na Jackline, baada ya dakika kadhaa, akaonana na mwanamke huyo katika Hoteli ya Wanyama na kuanza kuongea.
Alimwambia kilichotokea na alikuwa na uhakika kwamba Daniel ndiye aliyekuwa amesababisha hayo yote kwa kuhisi kwamba mimba ilikuwa yake kitu ambacho hakikuwa kweli kabisa.
“Kwa hiyo!”
“Tumtumie huyuhuyu Felista! Nataka tuchukue chumba, Felista amuite kuzungumza naye, wakati huo wewe na mimi tunakuwa chooni, akija, tunatokea na kuzungumza naye,” alisema Jackson.
Wakakubaliana na kuwasiliana na Pendo, siku hiyo naye alitakiwa kuwepo kwani walihitaji kufanya kitu ambacho Daniel asingejua kama nyuma ya hicho walikuwepo wao.
Hilo halikuwa tatizo, Jackson akaondoka na kurudi hospitali ambapo akaanza kuzungumza na Felista na kumwambia kuhusu mpango waliokuwanao.
Felista alishtuka, hakuamini kama Jackson alikuwa akifahamu kila kitu kilichotokea. Hakuwa na jinsi, akakubaliana naye na hivyo baada ya kutoka hospitali, siku iliyofuata akachukua simu na kumpigia Daniel huku nyuma tayari watu watatu, Jackson, Jackline na Pendo walikuwa ndani ya chumba namba 27 katika Hoteli ya Pacifician Royal iliyokuwa Mikocheni B.
*** CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Daniel alikuwa na uhakika kwamba vijana wale walifanya kazi kama alivyotaka ifanyike, moyo wake ulikuwa na furaha baada ya kupigiwa simu na kuambiwa kwamba kila kitu kilifanyika kwa mafanikio makubwa na hivyo ajiandae kusikia taarifa za kifo chake kwani kwa jinsi mimba ile ilivyokuwa kubwa, lisingekuwa jambo la kawaida kufa mtoto na mama kupona.
Alikaa na presha nzito, kwake, kuua halikuwa tatizo tena, alifanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba Felista anakufa hivyo alichokuwa akisubiri ni taarifa kuhusu kifo cha msichana huyo.
Siku iliyofuata, majira ya saa 4 asubuhi, huku akiwa ofisini kwake akapigiwa simu na Felista ambaye aliomba kuonana naye. Kwanza hakuamini kuisikia sauti ya msichana huyo, alichoamini ni kwamba alikufa baada ya kunywa vidonge, sasa ilikuwaje ampigie simu na kumwambia kwamba alitaka kuonana naye.
Kwa jinsi alivyokuwa akizungumza kwa kilio, akahisi kwamba alitaka kumpa taarifa ya kutoka kwa mimba yake hivyo alivyoambiwa kuonana naye, hakutaka kuchelewa, akaelekea katika hoteli hiyo kwa lengo la kumuona msichana huyo.
Alipofika, haraka sana akateremka na kwenda mpaka mapokezini ambapo akaomba kuonana na msichana aliyekuwa katika chumba namba 27. Simu ikapigwa mpaka huko, Felista akathibitisha kumfahamu mwanaume huyo na hivyo kuruhusiwa kwenda huko.
Alipofika, akaingia kwa kujiamini, alimuona Felista amekaa kwenye kiti huku akionekana kuwa na huzuni tele, kitendo cha kumuona vile tu, Daniel akawa na uhakika kwamba kila kitu kilikuwa poa.
“Kuna nini mpenzi? Mbona unalia?” aliuliza Daniel huku akimsogelea msichana huyo.
Akamshika na kumvutia kwake, alitaka kuona kama mimba ilikuwepo, alipoliangalia tumbo, lilikuwa vilevile kiasi kwamba ilionekana kumshangaza kupita kawaida, alitamani kuuliza lakini alikosa jibu kabisa.
“Umefurahi mimi kubeba mimba yako?” aliuliza Felista huku akimwangalia mwanaume huyo.
“Nani? Mimi? Kwa nini nichukie sasa?” aliuliza Daniel huku akimwangalia msichana huyo.
“Sasa kwa nini ulituma watu waniteke na kutaka kuniua kwa kuninywesha vidonge?” aliuliza felista.
Swali hilo lilimshtua Daniel, alimwangalia msichana huyo huku akionyesha mshtuko aliokuwa ameupata. Hakutegemea swali kama hilo, hakutegemea kuona msichana huyo akifahamu kile kilichotokea, sasa nani alimwambia?
“Eti! Kwa nini ulitaka kuniua na mtoto wangu?” aliuliza Felista huku akianza kulia.
“Felista! Ulichokisikia si kweli, naanzaje kumuua mtoto wangu?” aliuliza Daniel huku akionekana kutokujiamini.
“Ulitaka kuniua, kwa nini?”
“Mpenzi...”
“Nijibu kwanza!”
Daniel akabaki kimya kama mtu aliyekuwa akijifikiria kitu fulani. Wakati akiwa kwenye hali hiyo, mara mlango wa chooni ukafunguliwa na Jackson kutoka.
Daniel alipigwa na mshangao, hakumfahamu mwanaume huyo alikuwa nani na kwa nini alikuwa ndani ya chumba hicho. Akasimama na kuanza kumfuata.
“Kwa hiyo ulitaka kumuua mtoto wangu?” aliuliza Jackson swali lililomfanya Daniel kusimama kwanza, akayarudisha macho yake kwa Felista.
“Daniel! Kwa nini ulitaka kumuua mtoto wa mwanaume mwenzako?” aliuliza Felista huku naye akisimama na kumwangalia mwanaume huyo.
“Felista! Yaani ulikuwa ukinisaliti?” aliuliza Daniel.
“Nilikwambia kwamba nina mpenzi!”
“Sasa ndiyo unisaliti! Wewe wa kunifanyia hivi kweli?”
“Mbona hata wewe ulimsaliti mkeo, au umesahau?”
Daniel akabaki kimya, alionekana kuwa na hasira kupita kawaida, alitamani amfuate Jackson na kupigana naye kwani hakutamani kabisa kuona Felista akichukuliwa na mwanaume mwingine.
Wakati akijifikiria kumvamia Jackson, mara mlango wa chooni ukafunguliwa na mkewe kutoka. Moyo wa Daniel ukapiga paa! Hakuamini alichokuwa akikiona, macho yake yakatua kwa Jackline ambaye alikuwa akilia tu.
Akaishiwa nguvu za miguu na kujikuta akikaa kitandani, machozi yakaanza kumlenga kwani hakuamini kama Jackline alikiona kile kilichokuwa kimetokea.
Alihuzunika, moyo wake ukaanza kujutia kile alichokuwa amekifanya. Kukaa kimya haikusaidia, kama mwanaume alitakiwa kuzungumza neno lolote lile hata kumuomba msamaha mke wake kwa kile kilichotokea.
Akasimama na kumsogelea Jackline, alipofika karibu naye, akapiga magoti na kumshika miguu yake. Alishindwa kuzungumza kitu chochote kile, alibaki akilia tu, moyo wake ulimuuma, mwanamke mzuri kabisa ambaye alimwambia kuwa alimpenda kwa mapenzi ya dhati leo hii alikuwa akimsaliti kwa msichana mwingine.
“Mke wangu! Naomba unisamehe!” alisema Daniel huku akimwangalia mke wake, tena huku akiwa amepiga magoti.
“Daniel! Ulikosa kitu gani kwangu?” aliuliza Jackline huku akilia.
“Sikukosa kitu chochote kile!”
“Kwa nini ulikuwa unanisaliti? Kwa nini umeamua kuniumiza kwa namna hii?” aliuliza Jackline huku akimwangalia mume wake huyo.
Alishindwa kuzungumza lolote lile, kila swali alilokuwa akiulizwa lilikuwa gumu kujibika, hakujitetea zaidi ya kuomba msamaha tu kwani kwa kile alichokifanya kilikuwa ni cha aibu mno.
Alilia kupita kawaida, hakuangalia kama alikuwa mbele ya mwanamke mwingine, hiyo ilikuwa nafasi yake ya kuinusuru ndoa yake. Hakuangalia suti yake, alikuwa akilia huku akiwa amepiga magoti.
Jackline hakuwa na kinyongo, alijua kwamba mume wake alianguka na kamwe hakutaka kuzaa nje ya ndoa na ndiyo maana aliamua kuchukua uamuzi mgumu wa kutaka kuua mtoto.
Alimpenda, pamoja na kugundua kwamba mume wake alikuwa akisaliti, hakutaka kuonyesha kinyongo chochote kile, kama alivyokosewa alijua kabisa kwamba kuna siku naye angeweza kumkosea mwanaume huyo kwa kuwa moyo wa binadamu haukukamilika hata kidogo.
Akaamua kumsamehe kwa kuamini kwamba hilo lilikuwa onyo kubwa na tishio kuliko hata kama angeamua kuondoka na kurudi nyumbani kwao na kuwa mwisho wake kuwa naye.
Akamnyanyua na kumkumbatia. Wote hawakuamini, waliamini kwamba Jackline angechukua uamuzi mgumu lakini matokeo yake aliwaonyeshea kwamba kwenye mahusiano ya ndoa, kuna msamaha, kitu ambacho kila mwanandoa alitakiwa kukifanya kwa mtu wake.
“Nimekusamehe!” alisema Jackline, kila mmoja mahali pale akashusha pumzi ndefu.
Hilo likawa kama fundisho kwa Daniel, hakutaka kumsaliti tena mke wake, hakujiamini, kila msichana mzuri ambaye alipita mbele yake kumbukumbu zake zilirudi kwa Felista aliyesababisha kuonekana kuwa msaliti.
Penzi lake kwa mke wake likaongezeka, kwa kile kilichokuwa kimetokea, kilimpa fundisho. Kwa kuwa alifumaniwa pasipo kufanywa kitu chochote kile, hilo likamfanya kutokuthubutu kufanya kitu chochote nje ya ndoa.
Kwa upande wa Felista, msichana huyo akafanikiwa kujifungua mtoto wa kike na kumuita jina la Love yaani likimaanisha upendo mkubwa aliokuwanao kwa mpenzi wake huyo ambaye baadaye wote kwa pamoja wakaamua kuoana na kuishi pamoja.
MWISHO.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
0 comments:
Post a Comment