Simulizi : Wakili Wa Moyo
Sehemu Ya Pili (2)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Colin baada ya kushtuka usingizini alijua mpenzi wake yupo msalani au bafuni, lakini muda ulikatika bila kuonekana. Alikwenda msalani kumtafuta huku akimwita bila kupata jibu. Alitoka hadi nje na kumuuliza mlinzi. “John umemuona shemeji yako?” “Ametoka asubuhi sana, hakukuaga?” “Ameniacha nimelala.” “Tena alionekana kama analia nilijua mmegombana.” “Hata sielewi kitu.” Colin alimpigia simu mchumba wake, lakini iliita bila kupokelewa. Alirudia zaidi ya mara tatu vilevile haikupokelewa. Alijiuliza Mage amepatwa na nini, wasiwasi wake labda kwao kumetokea tatizo. Aliingia ndani na kuvaa pensi na fulana chini alivaa ndala na kuingia kwenye gari kuelekea Kigamboni kwa kina Mage ili ajue amepatwa na nini. Alikimbiliza gari, kutokana na foleni aliamua gari lake kulipaki Posta ya zamani na kuchukua bodaboda ili awahi kuifika. Baada ya kuvuka alichukua nyingine iliyo mpeleka nyumbani kwao Mage. Alimlipa dereva na kuingia ndani ya geti, alipofika sebuleni alimkuta msichana wa kazi akifanya usafi. “Habari Sofi?” “Nzuri shemu, shikamoo.” “Marahaba, vipi Mage yupo?” “Sijamuona toka asubuhi.” “Mama.” “Yupo chumbani kwake.” “Kaniitie.” Colin alibakia sebuleni kumsubiri mama Mage, baada ya muda alitokea na kushangaa kumuona Colin katika hali ile. “Vipi baba, kwema?” “Kwema, sijui hapa.” “Hapa hatujambo, mwenzio yupo wapi?”mama Mage alimuulizia mwanaye baada ya kumuona Colin peke yake. “Nimeshtuka kitandani sikumkuta, nimempigia simu haipokelewi, nikawa na wasiwasi na kuamua kuja huku.” “Hapa sijamuona, atakuwa amekwenda wapi? Mmh! Basi atakuwa kwa Brenda tu.” Colin alipiga simu kwa mara nyingine lakini haikupokelewa, alirudia mara mbili vilevile haikupokelewa baadaye ikazimwa kabisa. “Mama simu haipokelewi niliporudia imezimwa kabisa.” “Mmh! Atakuwa wapi mtoto huyu la..” Mama yake alinyamaza baada ya kumuona mwanaye akiingia, wote walipeleka macho kwake. Walishtuka kumuona macho yake yamevimba kuonesha alikuwa akilia. Aliwapita bila kuwasemesha na kuelekea chumbani kwake kitu kilichomshtua mama Mage na kumuuliza Colin. “Colin umemfanya nini mwanangu?” “Mama sijamfanya kitu, si umuulize mbele yangu.” Mama Mage alimfuata mwanaye chumbani na kumkuta amejilaza kwa kulilia tumbo. “Mage.” “Abee.” “Kuna nini?” “Hans ana hali mbaya asishangae kusikia amefariki.” “Amefanya nini?” “Amevamiwa na majambazi, mke wake na mwanaye wameuawa.” “Mungu wangu! Ndipo unapotoka?” “Ndiyo, mama.” “Mbona hukumuaga mwenzio?” “Ningemuaga nakwenda wapi?” “Na mbona umempita bila kumsalimia.” “Nitamweleza nini?” “Kwa hiyo itakuwaje?” “Mwambie aondoke siwezi kuzungumza naye chochote kwa sasa.” “Magee, unajua Colin ni nani yako?” “Mchumba wangu na mume wangu mtalajiwa, lakini kwa leo naomba aniache nitamtafuta mwenyewe.” “Mage, unajua unanitafutia lawama, Colin atatuelewa kweli?” “Mama tumia kila uwezavyo ili Colin aondoke nitamtafuta.” “Unanitia kwenye ubaya, Mage unaibomoa ndoa yako kwa mikono yako, unapoteza uaminifu kabla ya ndoa.” “Mama ndoa ni zawadi toka kwa Mungu, kama si riziki yangu siwezi kuilazimisha.” “Mmh! Sawa wacha nikajaribu,” mama Mage alitoka chumbani na kumwacha mwanaye amejilaza huku akiwa na mtihani wa kumweleza Colin ili aondoke bila kuhoji kitu. Colin alibakia sebuleni akiwaza kipi kimempata mchumba, alijiuliza alikwenda wapi asubuhi ile mchumba wake kama hakurudi nyumbani na kwa nini ameonekana analia kipi kimemsibu. Alibakia kusubiri kwa hamu kujua kipi kimemsibu mchumba wake, ambaye aliamini ndiye moyo wake yeye alibakia na mwili tu. Mama Mage alirudi hadi sebuleni, Colin aliyekuwa ametazama juu akiwa mwingi wa mawazo kutokana na kilichotokea asubuhi ile. Aliposikia sauti ya miguu ikisogea alipokuwa amekaa aliyahamisha macho yake na kumuona mama Mage, alijikuta akinyanyuka kama anampokea mheshimiwa. “ Vipi mama?” “Mmh! Safi tu,” Mama Mage alijibu huku akijitahidi kutengeneza uso wa mbuzi ili aweze kutengeneza mambo hasa kutokana kuwa mzazi. “Vipi Mage alikuwa wapi na amepatwa na nini?” Colin aliuliza akiwa amemkazia macho. “Mmh! Si..si..au fanya hivi, baba wewe nenda nyumbani mpenzi wako kuna mambo yao ya kitoto si unajua baba mwenzio bado mdogo?” “Ndiyo najua, lakini amepatwa na nini na alikwenda wapi bila kuniaga ikiwa hawa wewe hujui?” “Mwanangu, wala hakuna jambo la kutisha, u..u..najua mwenzio, baba eeh, hebu kwanza hili tuliache jioni mwenyewe atakueleza kila kitu,” mama Mage alijitahidi kubadili mazungumzo. “Sawa mama, lakini Mage ni mchumba wangu ninatakiwa kujua kila kitu chake, sasa hivi ni mke wangu, tumetenganishwa na ndoa tu ambayo haipo mbali. Hivi nirudi nyumbani namweleza mama nilichokikuta hapa kisha naulizwa kimetokana na nini nitajibu nini?” Colin alitetea hoja yake. “Mwanangu ngoja nikutoe wasiwasi, mwenzio alikwenda kwa shoga yake sijui nini anamdai, basi wametibuana ndiyo maana yupo vile,” mama alitengeneza uongo. “Sasa mama kama ni hivyo kwa nini hataki kuzungumza na mimi?” “Colin mwanangu, mi mkubwa naomba uondoke ili jioni uzungumze vizuri na mwenzako. Atakachokuambia hata wewe utacheka.” “Mmh! Sawa, basi mi’ naondoka.” Colin alisema huku akinyanyuka kuelekea nje, alipofika nje alikodi bodaboda hadi Kivukoni ambako alivuka upande wa pili na kukodi bodaboda nyingine hadi kwenye gari lake na kuingia ndani. Kabla ya kuondoka alitulia mikono aliweka juu usukani na macho aliangalia mbele, alikuwa kama anaona lakini alizama kwenye mawazo na kujiuliza Mage alikwenda wapi bila kuaga na kwa nini amerudi akilia kipi kimempata alipokwenda na mwisho alijiuliza kwa nini amekataa kuzungumza naye. Baada ya kukosa majibu ya maswali yake aliondoa gari kuelekea nyumbani, alitembea mwendo wa kawaida huku akili yake ikiwa haijakaa sawa. Alipofika katika makutano ya barabara ya Kawawa na Morogoro macho yake yalishtuka kumuona msichana mmoja akiuza ndizi. Sura yake haikuwa ngeni machoni mwake lakini mavazi yalifanya macho yapingane na akili yake. Sura ilikuwa ya Cecy lakini mavazi yake yalikuwa machakavu na mwili ulimvaa vumbi kwa ajili ya kutembea barabarani kwa miguu kuuza ndizi. Kwa vile alikuwa kwenye foleni alituliza macho yake kwa binti yule ambayo yalimwambia ni Cecy. Wakati anataka kuondoa gari alisikia mtu akimwita. “Cecy leta ndizi mbili.” Kwa vile taa ziliruhusu aliliondoa gari na kwenda kulipaki kituo cha mafuta cha Magomeni, alilizima na kutoka nje, kwa vile Cecy alikuwa amevuka barabara kwenda kuuza ndizi maeneo ya Hospitali. Alimtuma kijana mmoja aliyekuwa akiuza miwa. “Samahani mkubwa, naomba kwamwambia yule msichana alete ndizi kumi.” Yule kijana alimfuata Cecy aliyekuwa ametua beseni lake chini akiuza ndizi, alipofika alimwambia. “Dada peleka ndizi kumi kwenye lile gari.” “Kumi hazitafika zitabaki sita.” “Mpelekee zote.” “Sawa, ngoja nichukue hela.” Baada ya kuuza alibeba beseni lake na kuvuka barabara mpaka kwenye gari, kioo cha gari kilikuwa kimepandishwa kidogo hivyo hakumuona aliyekuwa kwenye gari. Aligonga kioo kidogo ili auze ndizi. “Kaka.” Colin aliteremsha kioo na kufanya Cecy amuone vizuri kitu kilichomfanya ashtuke. “Ha! Colin?” mshtuko alioupata ulifanya adondoshe beseni la ndizi. Hakuliokota alibakia amesimama mpaka Colin alipoteremka kwenye gari na kuokota ndizi zote kisha alimshika mkono Cecy. “Cecy.” “Abee,” Cecy aliitikia huku machozi yakimtoka na mwili kumtetemeka. “Unalia nini mchumba?” “Colin mimi si mchumba wako, mchumba wako Mage,” Cecy alijibu kwa ukali kidogo. “Kwa nini unasema hivyo?” “Mama yako amechotufanya kwa ajili yako, Colin lini nilikutamkia nakupenda?” “Hujawahi hata siku moja.” “Kwa nini mama yako amefunga safari ya kuja kunituka kuwa naingilia ndoa yako na kutudhalilisha kwa ajili ya umaskini wetu. Colin maskini hapendi?” “Anapenda.” “Ni kweli Colin nakupenda zaidi ya kukupenda, nailaumu nafsi yangu kuchelewa kukueleza ukweli kuwa nakupenda. Najua haikuwa bahati yangu unayetaka kumuoa ndiye chaguo la moyo wako. Kipi kilichomtuma mama yako kuja kunitukana na kutudhalilisha bahati yake sikumkuta najua ningemfanya nini!” Cecy alisema kwa sauti ya hasira.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ “Lini?” Cecy alimtajia siku na kukumbuka siku ambayo Colin alikumbuka ndiyo siku aliyokamata picha kumbe alikwenda kumtukana Cecy bila kutaka kuujua ukweli. “Cecy samahani sana, pia pole kwa kushindwa kuujua upendo wako.” Alimweleza ukweli juu ya uchumba wake na Mage alivyotengenezwa na mama yake. “Kwa hiyo Mage si chaguo lako ni la mama yako?” “Hapana, mwanzo lilikuwa chaguo la mama baada ya kumuona nilikubaliana naye na ndiyo tulipanga kuoana.” “Kwa hiyo siku ile uliniita kuja kunidhalilisha na kuumiza moyo wangu?” “Hapana nilikualika kama wageni wengine, pia nina mpango mkubwa sana kwako ambao utakusaidia kimaisha.” “Colin mpango ambao naukubali kwako labda niwe mkeo lakini zaidi ya hapo usijisumbue,” Cecy alisema kwa sauti ya kike kwa kujiamini. Colin alijitahidi kumwelewesha sababu ya picha zake na kipi alichokipanga juu yake. “Hivi leo hii nifanye kazi kwenye kampuni yetu mama yako atakubali anajua sisi ni wapenzi, kuna kazi?” “Kwanza hebu nieleze sababu ya wewe kuwa kwenye hali hii?” Colin alimuuliza huku akiangalia mavazi na hali aliyokuwa nayo Cecy. “Sina thamani haya ndiyo maisha niliyoyachagua ili mama yako akiniona asiwe na wasiwasi na ndoa yako.” “Cecy nitakutafuta tuzungumze akili yako ikitulia.” “Usijisumbue.” “Lazima nijisumbue kwako kwa vile kuna kitu ndani yako nilichokiona.” “Colin niache nirudi nyumbani.” “Unakaa wapi nikupeleke.” “Colin unataka mama yako aje kuchoka pagala letu, aliona picha ikawa vile vipi anione kwenye gari lako?” “Hawezi, na ungeniambia alichokifanya ningempa ukweli, tabu ya kina mama wa kiswahili wazungu hawajali vitu vya kijingakijinga.” “We nenda tu.”Colin alimbembeleza sana Cecy, kwa vile naye alikuwa akimpenda akiingia kwenye gari na kurudishwa nyumbani kwao. Walipomfikisha Colin naye aliteremka na kuongozana hadi kwa kina Cecy ambako kulikuwa na nyumba ya vyumba viwili na sebule. Lakini nyumba ilikuwa ya hali ya chini bati zake zilikuwa na kutu na juu waliweka mawe ili kuzuia bati lisiezuliwe na upepo. Cecy baada ya kufika eneo la kwao alishukuru na kuanza kuelekea nyumbani, lakini Colin alimsemesha. “Cecy mbona unaniacha mgeni?” “Colin nashukuru umenileta, lakini naomba usifike nyumbani.” “Kwa nini unasema hivyo?” “Nimekueleza mara ngapi kuhusu mama yangu, unataka mama yako aje akitie moto kibanda chetu.” “Cecy suala la kuhusu mama yangu niachenie mimi, naomba nimsalimie mama mara moja.” “Mmh! Sawa.” Waliongozana Cecy na Colin hadi nyumbani kwao ambako alitambulishwa kwa mama yake na kumfanya mama Cecy ashtuke. “Ha! Wewe ndiye unayenyanyasa mwanangu?” “Kumnyanyasa kivipi mama?” Mama Cecy alimweleza mateso yote ya mwanaye juu yake na jinsi mama yake alivyokwenda kuwatukana huku akitishia maisha ya Cecy kama ataharibu ndoa yake na Mage. Colin baada ya kusikilia maneno yale aliyarudia maneno ya Cecy juu ya mapenzi yake kwake. Ashangaa kuona penzi la Cecy kwake lilikuwa wazi kwa mama yake lakini mhusika mkuu alikuwa hajui kitu zaidi ya kumuona Cecy kama msichana mzuri lakini hakuwa na uwezo wa kumtamkia chochote kutokana na mama yake kumtafutia mwanamke aoe ambaye kwa upande wake aliungana na uchaguzi wa mama yake. “Mzazi wangu, kwanza niwaombeni radhi kwa yote yaliyotokea kwa mama yangu kuja kuwatukana bila sababu. Naweza kusema labda makosa nimefanya mimi kwa kutomjulisha nini nilichotaka kukifanya na Cecy. “Najua mama yangu alimpenda Cecy lakini si kuwa mke wa mwanaye bali msichana mzuri anayejiheshimu. Inawezekana kigezo cha elimu ndicho kilichomfanya mama yangu amtafute Mage, nina imani kama Cecy angekuwa na elimu kama ya Mage basi angekuwa chaguo la kwanza la mama. “ Wasiwasi mkubwa wa mama ilianzia siku alipomuona Cecy kapendeza naweza kusema aliwashinda wote waliokuwa kwenye sherehe yangu. Kilichomshtua mama yangu kunikuta na picha ya Cecy aliyokuwa amependeza sana. Aliamini kabisa ni mpenzi wangu hivyo kujihami kabla mambo hayajaharibika kutokana na harusi yetu kuandaliwa kwa fedha nyingi sana. “Lakini hakutakiwa kuchukua uamuzi aliochukua bila kuniuliza mimi japokuwa nilimweleza sababu ya kuwa na picha ile. Ila napenda kuwaeleza kitu kimoja kuwa sitauacha upendo wa Cecy upitee hivihivi najitolea kumsomesha ili aongeze elimu na ujuzi. Baada ya elimu hiyo nitafanya naye kazi ndani na nje ya nchi ambayo naamini itamweka katika maisha mazuri na ramani ya dunia. Pia nitahakikisha naijenga nyumba yenu katika hadhi ya kisasa pia mama nitakufungulia mradi ili muendeshe maisha yenu,” Colin alieleza nia yake nzuri kwa Cecy na mama yake. “Asante bab..” “Mama nani kamwambia sisi tuna shida ya vitu hivyo? Kama kilichonitesa nimekikosa, sihitaji kitu kingine toka kwako,” Cecy alimkatisha mama yake na kumjia juu Colin kwa kauli yake. “Cecy mimi na wewe nani mwenye kosa, ulilolisema leo ungelisema mapema situngefika huku,” Colin alijitetea. “Muongo! Colin hata ningesema ingekuwa sawa na kazi bure kwa vile tayari mama yako aliisha kuchagulia mwanamke,” Cecy alisema kwa hisia kali. “Kabla ya kutoa uamuzi ningechagua.” “Mimi na Mage unampenda nani?” “Nawapenda wote, ila kwa sasa Mage kwa vile ndiye tupo katika mipango ya ndoa.” “Kwa kauli hiyo naomba tukomane kila mtu ashike hamsini zake ukinikuta njiani nipite kama nguzo ya umeme,” Cecy alisema kwa hasira. “Cecy kuwa na adabu, heshimu anachokisema mwenzako...Baba kama una nia hiyo ifanye faida hataiona leo, lakini baadaye atakushukuru.” “Sawa mama nimekuelewa, Cecy punguza hasira nina nia nzuri na wewe, uzuri wako nitaulinda na baadaye utakuingia fedha nyingi na kumsaidia mama. Utauza ndizi mpaka lini?” Cecy hakujibu kitu aliinama chini, Colin alimsogelea na kumbembeleza kitu kilichomfanya Cecy aangue kilio na kusema: “Colin nisamehe kwa yote, hujui kiasi gani penzi lako lilivyouathiri moyo wangu, najua nilikupenda bila kushauriana na moyo wangu. Mnaweza kuniona mdogo lakini nami nina hisia za mapenzi kama wengine,” Cecy alisema huku akimtazama Colin kwa macho yaliyojaa machozi. “Najua Cecy, isingekuwa mipango ya harusi ningeza kufanya chochote ili ujue nauthamini upendo wako.” “Sawa Colin nimekuelewa.” Kwa vile muda ulikuwa umekwenda Colin aliaga kuwahi nyumbani baada ya kuondoka bila kuaga. Alikwenda kwenye gari na kuwaletea laki moja, walimshukuru naye aliondoka kuelekea nyumbani. Njiani alijikuta akimuwaza Cecy msichana mdogo lakini alikuwa jasiri kuzielezea hisia zake japo aliamini mama yake asingemkubali kutokana na uduni wa maisha na kukosa elimu. Kwa upande mwingine aliamini kabisa kutokana na kasi ya mabadiliko duniani Mage ndiye mwanamke sahihi kwake. Kwani aliamini maisha ni zaidi ya mapenzi kwa vile maisha yakiwa vizuri kila kitu kinakwenda. Aliamini kwa umbile adimu la Cecy angeweza kuifanya kazi yake vizuri ya maonesho ya mavazi. Kitu kikubwa aliamini Cecy kama atapata twisheni ya kingereza ataweza kuongeza uwezo wake hata kusafiri nchi za nje kufanya kazi ya maonesho ya mavazi pia kupata tenda ya kupamba majarida. Aliamini akimtumia vizuri Cecy kampuni yake itafika mbali na yeye kujitengezea kipato kikubwa. Alipanga kuwekeza fedha nyingi kwa Cecy baadaye angevuna fedha nyingi kwa kuamini alikuwa na kitu cha ziada ambacho wasichana wengi hawakuwa nacho. Japokuwa alikuwa na wasiwasi na kikwazo cha mama yake, lakini kwa vile yupo kikazi alijua mama yake angemuelewa tu. Alipanga ndani ya wiki mbili nyumba ya kisasa ya kina Cecy iwe imesimama huku akimtafutia twisheni nzuri ili kuijua lugha haraka. Alipanga kufungua duka mbele ya nyumba yao ambalo litawafanya waingize kipato kila siku. Kutokana na kuzama kwenye mawazo ya kumuwaza Cecy alijikuta akimsahau Mage mpaka alipofika kwao. *** Alipoingia ndani alikutana na mama yake ambaye alishangaa kumuona mwanaye akiteremka kwenye gari. “Colin unatoka wapi?” Colin ilibidi amweleze mama yake kilichotokea, baada ya kumsikiliza alimuuliza: “Colin mwanangu umemfanya nini mtoto wa watu?” “Mama sijamfanya kitu chochote kama nilivyokueleza.” “Mage si mjinga kulia tu na kukataa kuzungumza na wewe wakati mlikuwa pamoja?” “Yaani sijui kitu labda uulize wewe utapata jibu.” “Nitauliza, lakini Colin kuna kitu unanificha haiwezekani Mage aondoke bila kukuaga kisha akatae kuzungumza na wewe wakati usiku mmelala pamoja?” “Mama piga simu uulize labda utagundua kitu.” “Mmh! Sasa nimepata jibu,” mama Colin alisema huku akitikisa kichwa kama kakumbuka kitu. “Jibu gani?” “Colin lazima kuna kitu Mage amegundua kuhusu wewe na Cecy, nasema hivi ndoa ikivunjika Cecy atanitambua.” “Mama unamuonea bure mtoto wa watu, toka siku ile ya sherehe sijaonana na Cecy,” Colin alidanganya. “Muongo umemkataza asilete ndizi ili mkutane sehemu nyingine. Colin Mage akinieleza kuwa amegundua una uhusiano na msichana mwingine pagala lao nakwenda kulitia moto sasa hivi.” “Mama kwa nini unanihukumu kwa kosa nisilofanya, nimekueleza piga simu uulize unaanza kutengeneza mawazo yako. Cecy amekukosea nini mpaka kumchukuia hivyo, ni wewe ndiye uliyekuwa naye karibu?” Mama Colin hakusema kitu aliingia ndani kuchukua simu ili ampigie Mage kujua amepatwa na nini. *** Baada ya Colin kuondoka mama Mage alimfuata mwanaye chumbani aliyekuwa amezama kwenye dimbwi la mawazo juu ya hali ya Hans na familia yake ilivyomtenga na kumuona kama kinyesi. Moyo ulimuuma na kujua hakukuwa na haja ya yeye kwenda hospitali pia kumuacha mchumba wake mumewe mtarajiwa akiwa amelala na kuondoka bila kumuaga. Alijilaumu kwa kitendo chake cha kumpita Colin bila kumsemesha, alijiuliza atamfikiliaje. Alijiuliza ndoa yake ikivunjia na ijulikane sababu ya Hans mwanaume asiye na mapenzi naye ataiweka wapi sura yake. Lakini alijiuliza angesimama na kuzungumza na Colin angemwambia anatoka wapi na kwa nini hakumuaga? Akiwa katika dimbwi la mawazo mama yake aliingia na kumkuta amezilaza chali huku ameukumbatia mto wake na wacho yake alikuwa akiangalia darini. “Mage..Mage.” “A..a..bee.” “Mbona sikuelewi mwanangu?” “Mama nahitaji msaada wako najua nimechanganya madawa.” “Nikusaidie nini?” “Sijui Colin atanielewaje maana nilichomfanyia si kitu kizuri.” “Kwa kweli hatua tuliyofikia huku vikao vikienda vizuri halafu mwenzako abadili uamuzi sijui sura zetu tutaziweka wapi?” “Hapo ndipo ninapochanganyikiwa, mama kitendo walionifanyia familia ya kina Hans sitawasahau.” “Umeona eeh, nilikueleza toka zamani familia ile ilikuwa haikupendi kama ungeolewa na Hans ndoa yako isingedumu. Mungu amekuletea mwanaume wa maisha yako unamchanganya.” “Mama nimeisha fanya kosa naomba msaada wako, nitamweleza nini Colin anielewe.” “Wala usiwe na wasi kamwambie kuwa ulimtuma Brenda cheni ambayo ulipanga kumpatia kama surprise umekuta hajaitengeneza na kujikuta umekasirika na kuanza kulia.” “Mmh! Atanielewa? Naona kama utetezi mwepesi.” “Walaa, ye anajua ulikuwa kwa Brenda, nilimwambia kuna kitu mmeshindwa kuelewana ndiyo maana ulirudi katika hali ile.” “Mmh! Basi ngoja nifanye hivyo.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ Wakiwa katikati ya mazungumzo simu ya iliita ilikuwa ikitoka kwa mama Colin. “Mkweo,” mama Mage alisema. “Mmh! Lazima ataulizia kilichotokea.” “Ngoja nimsikilize,” alisema huku akibofya cha kupolelea na kuweka simu sauti ya nje. “Haloo mama Colin.” “Eeh! Dada kuna nini huko?” “Kwani vipi?” “Naona Colin ananichanyanyia maneno wala simuelewi.” “Wala hakuna kitu cha kutisha bali mkweo aliudhiwa na shoga yake, lakini kwa sasa yupo sawa na wakati wowote atakuja huko.” “Mmh! Afadhali maana nilikuwa na wasiwasi.” “Wa nini?” “Nilijua Colin kisha mtibua mkwe wangu.” “Walaa, sema mkweo ana hasira za kitoto kitu kidogo analia kama kafiwa.” “Basi nikuacheni muendelee na mambo mengine.” Baada ya simu kukatwa mama Mage alimgeukia mwanaye na kumwambia. “Unaona ulivyotaka kumsababishia matatizo mwenzako?” “Mama lazima niende sasa hivi najua mpenzi wangu hayupo kwenye hali nzuri.” “Fanya hivyo na...” mama Mage alinyamaza baada ya mlango kugongwa. “Unasemaje?” aliuliza kwa sauti. “Kuna wageni.” “Nakuja,” mama Mage alitoka nje kwenda kumsikiliza mgeni. Alitoka hadi getini na kukutana wa wanaume wawili na mwanamke mmoja, aliwatazama walikuwa wageni kwake. “Karibuni.” “Asante.” Aliwakaribisha hadi sebuleni, baada ya kuketi mama Mage alitaka kujua wana shida gani. “Ndiyo jamani mna shida gani?” “Sisi ni maafisa wa polisi,” walitoa vitambulisho vyao. “Ndiyo, mna shida gani?” “Tuna imani hapa ndipo anaishi Magreth Chogo.” “Ndiyo.” “Yupo?” “Mna shida gani?” Kabla hajajibu Mage alitoka chumbani ili awaone wageni ni kina nani, askari mmoja baada ya kumuona alijua ni Mage alibahatisha kwa kumwita jina. “Mage.” “Abee.” “Upo chini ya ulinzi,” alisema askari wa kike. “He! Kwa kosa gani?” Mage alishtuka. “Kutokana na tukio lililomtokea mpenzi wako wa zamani.” “Sasa mimi nahusika kivipi?” “Utajua yote kituoni.” “Mi siendi,” Mage alitaka kugoma kwenda. “We nenda wala usihofu, ila jamani chondechonde mwanangu asiguswe wala kulazimisha kusema uongo tutaelewana vibaya.” “Hakuna tatizo, atakuwa salama baada ya mahojiano atarudi.” Ilibidi Mage achukuliwe kupelekwa kituo cha kati cha polisi, mama yake alichukua simu na kumpigia mkuu wa polisi ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa mzee Chogo baba yake Mage. “Vipi shemeji?” ulipokewa upande wa pili. “Mwanao Mage amekamatwa na vijana wako sasa hivi.” “Kwa kosa gani?” Alimwelezea kila kitu, baada ya kumsikiliza alimjibu. “Basi hakuna tatizo shemeji nitalishughulikia mwenyewe, yupo kituo gani?” “Cha kati.” “Usiwe na wasi waache wamuhoji watamwachia tu.” “Sawa shemeji kwa hiyo niende.” “Hapana nitamfuta mwenyewe.” “Asante shemeji.” Mama Mage baada ya kukata simu alijikuta njia panda, alijifikiria kumpigia simu Colin lakini alijiuliza akimpigia atamwambia nini. Aliamua kukaa kimya ili kusubiri hatima yake ndipo ajue afanye nini. *** Mage alipelekwa hadi kituoni na kuingizwa chumba cha mahojiano, Inspekta Koleta alikaa mbele ya meza aliyokuwa amekaa Mage na kalatasi ili kuandika mahojiano yale. “Unaitwa nani?” “Mage.” “Nataka jina kamili.” “Magreth Chogo,” Mage alijibu kwa sauti ya chini kidogo. “Una umri gani?” “Miaka 24.” “Unamfahamu vipi Hans?” “Namfahamu kama mpenzi wangu wa zamani.” “Ulijuaje amepata matatizo?” Mage alielezea jinsi alivyopigiwa simu na shoga yake Brenda ambaye alipigiwa simu rafiki yake Hans, Ndubukile. “Wewe ulikuwa wapi?” “Kwa mchumba wangu.” “Anaitwa nani?” “Colin.” “Inasemekana mlikuwa ikipendana sana na Hans kwa nini hakukuoa akamuoa msichana mwingine?” “Alichaguliwa na wazazi wake.” “Unafikiri kwa sababu gani alichaguliwa msichana mwingine wakati wewe ndiye uliyekuwa mpenzi wake kila mtu alijua.” “Kwa kweli kwa hiyo siwezi kujua.” “Hans alipoona mwanamke mwingine wewe ulichukuliaje?” “Sikuwa na jinsi ila roho ilinikuma sana.” “Ulifikiria kufanya nini baada ya kuachwa na Hans?” “Nilipanga kutojishughulisha na mapenzi tena.” “Hukupanga kulipa kisasi?” “Kisasi cha nini?” “Kwa vile ndoto zako zilikuwa kuolewa na Hans.” “Ni kweli ndoto zangu zilikuwa kuolewa na Hans lakini sikuwa chaguo la wazazi wake.” “Unafikiria kwa nini unahusishwa na matukio ya mauaji na shambulizi la Hans?” “Hata mimi nashangaa.” “Kuna ukweli gani umelipa kisasi cha kuachwa kuolewa?” “Hakuna ukweli wowote kwa vile sasa hivi nami nipo katika maandalizi ya ndoa yangu, kwanza nifanye vile kwa ajili gani kwa vile Hans sijagombana naye ameoa tukiwa tunapendana. Pia sikuwa na kinyongo na familia yake.” “Unaweza kufikiria nani aliyefanya vile?” “Mmh! Kwa kweli sijui kwa vile niliisha kata mawasiliano na Hans toka alipooa.” “Kuna taarifa mlikuwa na penzi la siri na Hans?” “Si kweli, mara nyingi Hans alinitafuta kuniomba msamaha nilimkatalia kwa vile yeye ni mume wa mtu sikutaka kuonekana naingilia ndoa yake hasa baada ya familia yake kutonihitaji.” Wakiwa katika ya mazungumzo mkuu wa polisi aliingilia Mr Clarence, Inspekta Koleta alinyanyuka na kupiga saluti. Mage alipomuona alifurahi kwani siku zote alikuwa mtu wa karibu katika familia yao. “Shikamoo baba.” “Marahaba, kuna nini?” “Mkuu kuna tukio la mauaji na mashambulizi ambayo inaonekana mshukiwa wa kwanza ni huyu binti,” alijibu Inspekta Koleta. “Hebu nipe hiyo kalatasi ya maelezo.” Mkuu wa Polisi Mr Clarence aliichukua na kuisoma kisha aliomba kuzungumza na Mage kidogo. Baada ya kupishwa alimuuliza mswali kuhusiana na tukio lile. “Mage.” “Abee baba.” “Naomba uniambie ukweli ili nikusaidie hata kama umehusika niambie ili nijue jinsi ya kukusaidia,” Mr Clarence alimwambia kwa upole. “Baba haki ya Mungu sijui chochote zaidi ya kupigiwa simu asubuhi nikiwa kwa mkweo, kwa vile Hans ndiye aliyekuwa chaguo la moyo wangu pia sikukosana naye bali penzi letu lilivunjwa kwa nguvu ya wazazi wake nilishtuka sana kupata habari ile. Huwezi kuamini taarifa ile ilisababisha nitoke hata bila kumuaga mkweo hivi ndiyo nilikuwa najiandaa kwenda kuzungumza na mkweo japo sikutaka ajue nimekuja kumuona mpenzi wangu wa zamani.” “Una muda gani ujaonana na Hans?” “Mmh! Sasa ni mwaka na nusu.” “Kwa nini?” “Baba, yeye kaoa na mimi Mungu kanipa wangu kuna umuhimu gani kuendeleza ukaribu?” “Nimekuelewa, sasa nitawaambia utoke kazi yote niachie mimi.” “Asante baba.” Mkuu wa polisi alimwita Inspekta Koleta na kumweleza amwachie Mage na kumweleza waendelee na upelelezi kwa vile Mage ahusiki na matukio yake. Walikubaliana na Mage aliruhusiwa kutoka. Mkuu wa Polisi Mr Clarence alimchukua Mage na kumrudisha nyumbani. Mama yake alifurahi kumuona mwanaye na Mr Mulisa. “Asante shemeji.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ “Kawaida, nina imani Hans akipata nafuu kila kitu kitakuwa wazi.” “Tena Mungu ampe afya ili kuwaumbua wenye roho mbaya wanataka kuiharibu harusi na mwanangu.” “Usiwe na wasi kila kitu kitakwenda kilivyopangwa na aliyetenda unyama ule atajulikana mkono wa dola ni mrefu.” Mkuu wa polisi aliaga na kumuacha Mage na mama yake, baada ya kuondoka Mage aliagungua kilio. “Mama kosa langu nini? Mbona familia ya kina Hans wameniandama hivyo, jamani mimi nimuue mke wa Hans na mwanaye na kutaka kumuua Hans ili iweje?” “Ndiyo dunia mwanangu, kwa vile baba yako yupo atakusimamia.” “Unajua mama mi’ nilikuwa na wasiwasi labda aliyefanya vile ni Colin.” “Wee! Temea chini tena usirudie kusema kitu kama hicho, Hans na Colin wapi na wapi?” Mama yake alikuwa mkali. “Basi mama nisamehe ni mawazo tu.” “Tena umeniudhi sana, wee kidogo ufe kwa presha kwa kusingiziwa unataka kumpaka shombo mtoto wa watu.” “Basi mama nisamehe ulikuwa wasiwasi wangu.” “Nataka uoge ubadili nguo uende kwa mwenzio ukamtoe hofu usimweleze ya kupelekwa polisi.” “Sawa mama.” Mage alikwenda kuoga na kubadili nguo alichukua gari na kwenda kwa Colin, akiwa njiani alijawa na mawazo juu ya familia ya Hans kumshukia yeye katika tukio lile. Alijiuliza kipi hasa kilichofanya wamfikirie yeye kwanza. Aliona jinsi gani familia ile jinsi ilivyokuwa ikimchukia na kuamini kauli ya mama yake kuwa hata kama angeolewa asingedumu kwenye ndoa yake kwa vile hakuwa chaguo lao. Alijikuta taratibu mapenzi yake yote akiyahamishia kwa Colin na kuuapia moyo wake kumpenda kwa nguvu zake zote na kwa akili zake zote. Alipofika nyumbani kwao Colin baada ya kuteremka kwenye gari aliingia ndani huku akikimbia kama mtu aliyepagawa. Sebuleni alimkuta mama Colin, alishtuka kumuona katika hali ile. “Vipi Mage?” “Mama, mume wangu yupo wapi?” aliuliza akionesha kuchanganyiwa. Wakati huo Colin alikuwa akitokea chumbani kwake kuja sebuleni, alipomuona alikimbilia na kumkumbatia. “Jamani mume wanguu!” “Vipi mbona hivyo?” Colin alishtuka uchangamfu wa Mage uliopitiliza. “Najua nimekuudhi nisamehe sana, mama nimemuudhi sana mume wangu,” Mage alisema huku akilia. “Hujamuudhi chochote,” mama Colin alisema. “Najua nimemuudhi, Colin naomba twende chumbani.” Walishikana mikono na kuelekea chumbani na kumuacha mama Colin akiwatazama na kuchekelea moyoni na kusema kwa sauti ya chini. “Kweli wanapendana.” Aliwatazama mpaka walipopotea machoni kwake. Colin na Mage alikwenda hadi chumbani, alipofika ndani Mage alijifupa kifuani kwa mpenzi wake na kuanza kulia kitu kilichomshtua Colin na kuhoji. “Vipi mpenzi?” “Colin nisamehe sana mpenzi wangu.” “Kwa lipi?” “Najua leo nimekukosea kwa kuondoka bila kukuaga kitu kilichokufanya usumbuke kunitafuta, kibaya zaidi zijapokea simu zako na kukataa kuzungumza na wewe uliponifuata nyumbani.” “Kumbe ni hayo? Achana nayo.” “Hapana najua umenikubalia ili yaishe lakini umejenga picha mbaya juu yangu.” “Walaa.” “Colin nihukumu hukumu yoyote lakini elewa nakupenda sana mpenzi wangu, nilitaka kufanya surprise lakini ikaenda ndivyo sivyo. Nilishindwa nikueleze nini kwa vile sikuwa na lakukueleza kwa wakati ule hasa baada ya Brenda kunichanganya.” “Yote mama alinieleza ndiyo maana nilikuelewa toka asubuhi.” “Colin lakini si unajua nakupenda?” Mage alimuuliza kwa sauti ya kudeka. “Najua, ndiyo maana upo hapa.” “Nashukuru kulifahamu hilo.” Siku ile Mage alishinda pale na kufanya kazi zote za nyumbani ikiwa pamoja na kupika chakula cha jioni. Colin aljikuta akisahau yote na kujiona kama tayari kaisha muoa Mage. Siku ile muda wote walikuwa pamoja kama kumbikumbi kwa kufanya kazi kwa kusaidizana. Mama Colin muda wote alikuwa mtu wa tabasamu na kuona ndoa ya mwanaye jinsi itakavyojaa furaha na upendo. Aliwaangalia walivyopendeza kwa kusaidizana kazi zote za jikoni mtu na mchumba wake. Alifumbata mikono yake na kuomba kwa sauti ya chini. “Eeh! Mwenyezi Mungu baba nijalie ndoa ya wenetu iwe yenye matunda,” baada ya dua alipiga njia ya msalaba kumshukuru Mungu. Siku ile ilikuwa ya furaha kwa wapenzi wawili kwa Mage ambaye alihamishia mapenzi yake yote kwa Colin baada ya kujua hata kama angempenda vipi Hans asingekuwa na nafasi ndani ya familia yake. Aliona jinsi gani sivyo mpenda mpaka kumzushia shutuma nzito za mauaji ya shambulio la kuua. Kingine kilichomuweka njia panda kama Mungu atamsaidia Hans kupona atamchukuliaje, lazima naye atangeamini mhusika ni yeye. Lakini kwa upande wa Hans alijua ni vigumu kumshuku yeye kutokana na ukaribu wao ulivyokuwa. Angekuwa na wasiwasi kama angekuwa akilipigania penzi la Hans. Kama tatizo lile lingemtokea baada ya kuoa lazima Hans angejua ni yeye, lakini baada ya mkewe kupata ujauzito na kujifungua penzi lake alilizika rasmi. Aliamini ule ndiyo muda wa kulionesha penzi lake halisi kwa Colin, siku ile alilala tena na kuondoka siku ya pili huku kila mmoja akifurahia penzi la mwenzake. **** Ukaribu wa Mage na Colin kwa kufuatana muda wote kama kumbikumbi, Ulifanya Colin ashindwe kutekeleza ahadi yake kwa kina Cecy. Baada ya kusubiri kwa wiki bila kuonekana dalili zozote za kutekelezwa ahadi. Cecy aliyekuwa amejilaza kitandani na kukosa usingizi. Alijikuta akinyanyuka kitandani na kumfuata mama yake aliyeamini ameisha pitiwa usingizi ambaye alikuwa na matumaini ya kuyakimbia maisha ya kulala nyumba ya kuvuja na taa ya kibatari. Alitoka chumbani kwake na kwenda hadi kwenye mlango wa mama yake na kugonga. “Mama..mama.” “Unasemaje Cecy,” alimuuliza bila kuamka kwa vile tayari alikuwa amepitiwa usingizi. “Kuna jambo nataka tushauliane.” “Jambo gani, kwani lazima tuzungumze usiku?” “Ndiyo, asubuhi nikiamka nijue cha kufanya.” “Mmh! Nakuja.” Mama yake aliamka na kutoka sebuleni, alimkuta Cecy amesimama, mama yake aliketi kwenye kigoda na kumtazama mwanaye aliyekuwa bado amesimama. “Unasemaje mama?” “Mama siku zote japo mdogo lakini huwa nayaamini mawazo yangu japokuwa sina elimu kubwa, lakini busara haina elimu bali kipawa toka kwa Mungu.” “Ni kweli.” “Hivi mama tulipokuwa tukifanya biashara zetu tulipungukiwa nini?” “Hatukupungukiwa kitu, kwani maisha ya mwanadamu Mungu ndiye anayetuongoza.” “Kwa hiyo hatuwezi kumtegemea mtu?” “Ndiyo, kwani amelaaniwa kila amtegemea mwanadamu.” “Nimefurahi sana kulifahamu hilo.” “Ulikuwa una maanisha nini?” “Huoni kama tunamkosea Mungu kumtegemea mtu.” “Tunamtegemea nani?” “Tumeacha kufanya biashara zetu kwa ajili ya Colin aliyetugeuza watoto kutuahidi pipi, leo ni siku ya ngapi hatufanyi biashara kwa ajili ya kusubiri ahadi yake. Wiki inakatika hakuna cha tofari wala mchanga.” “Cecy mwanangu Colin, naye binadamu huenda amepatwa na matatizo. Hivyo tulitakiwa kuvuta subira.” “Mama niliyajua haya mapema, sikutaka kukukata kauli kwa vile wewe ni mtu mzima. Lakini nilijua hakuna kitu, Colin atujengee nyumba kwa kipi cha maana tulichompa?” “Kwa hiyo ulikuwa unasemaje?” “Kesho asubuhi nakwenda Mabibo kununua ndizi na kuendelea na kazi yangu inayoniweka mjini.” “Mmh! Si wazo baya.” Walikubaliana siku ya pili Cecy aendelee na biashara yake ya ndizi kama kawaida. Kila mmoja alirudi chumbani kwake na kupanda kitandani. Cecy alichelewa kulala huku moyo ukimuuma kwa kitendo cha Colin kuwadhalilisha kwa kuwaahidi kitu kisichowezekana. Alijikuta akimchukia Colin na kuapa hata zungumza naye siku zote za maisha yake. Kutokana na hasira alijikuta akichelewa kulala. Siku ya pili Cecy aliamka na mapema na kuwahi kununua ndizi, baadaye alirudi nyumbani na kuoga kisha aliingia chumbani na kuchagua nguo za kuiingia nazo mtaani. Alitafuta gauni lililochoka na upande wa khanga uliopauka na kuvaa. Alitoka kuelekea nje, alipofika mlangoni alisita kidogo na kujiuliza swali. “Hivi maisha yangu namtegemea nani? Jibu Mungu, kwa nini niishi maisha kwa ajili ya mtu fulani? Ina maana bila Colin sina maisha? Hapana..hapana,” Cecy alisema huku akirudi chumbani na kuvua nguo chakavu na kufungua sanduku lake na kutoa nguo nzuri na kuzivaa kisha alitoka na kuchukua beseni lake la ndizi na kumuaga mama yake aliingia mtaani kuuza ndizi.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ Alishangaa siku ile alimaliza ndizi mapema tofauti na alivyobadili mfumo wa maisha baada ya kuumizwa na penzi la Colin na kuamua kuishi kwa kutojijali. Toka alipoamua kuishi maisha yale biashara yake haikuwa kama awali alijikuta akimaliza biashara zake kwa kutembea umbali mrefu pia kutumia muda mwingi. Alijikuta akijilaumu kwa kupoteza muda wake mwingi kumuwaza Colin mwanaume asiye na mapenzi naye ambaye tayari alikuwa na mpenzi wake. Moyo wake aliutoa kifungoni na kuwa tayari kupokea penzi jipya ila la mtu atakaye mpenda naye ampende ambaye atakuwa sahihi kwa moyo wake. Hakuwa tayari kumkubali mwanaume anayetumia umaskini wake kufanya naye ngono. Siku zote aliamini mwenye mapenzi ya kweli hawezi kutanguliza ngono mbele zaidi ya upendo kwanza. Lakini kwa Colin alikuwa radhi kuupoteza usichana wake hata bila ndoa kwani aliamini penzi la Colin lilizidi furaha ya maisha yake. Baada ya matukio yote aliamini muda wa uvumilivu ulikuwa umepita hivyo alitakiwa kitengeneza mawazo mapya na kuwaza kitu kingine kabisa kigeni katika ubongo wake. Kila usiku ulipoingia alitumia muda mwingi kuwaza maisha wanayoishi ya kuuza ndizi mwisho wake nini. Aliamini muda ule bado ana nguvu alitakiwa atafute njia mbadala itakayomsaidia kukabiliana na ukali wa maisha aweze kumsaidia mama yake. Wazo lilikuwa kila jioni baada ya kutoka kwenye biashara zake ambazo zilikuwa zikifanya vizuri japokuwa changamoto za wanaume zilikuwa kubwa ambazo alikabiliana nayo. Wazo kubwa lilikuwa aanze kusoma masomo ya jioni kujifunza kingereza ambacho kingemsaidia kufafuta kazi ya kuajiliwa na kuachana na kazi ya kuzurula huku akila vumbi la barabarani. Wazo lile alimwambia mama yake ambaye naye aliliafiki, jioni ilipofika alikwenda sehemu moja iliyokuwa ikifundisha twisheni na kuomba kusoma kingereza ambacho aliahidiwa kukijua baada ya miezi mitatu. Alilipa ada na kuanza kusoma siku ileile huku akiwa na ndoto za siku moja naye kuzungumza kingereza. Mipango ya harusi ya Colin na Mage ilizidi kupamba moto huku kila familia ikijipanga kufanya sherehe ya kufuru. Nayo Hali ya Hans iliendelea vizuri iliyofanya atolewe hospitali na kurudishwa nyumbani. Baada ya kutulia kwa wiki moja aliitwa polisi kutoa maelezo kutokana na tukio lililomtokea lililopeleka kupoteza mke na mtoto. “Pole sana,” Inspekta Koleta alianza kwa kumpa pole. “Asante.” “Unajisikiaje kwa sasa?” “Namshukuru Mungu sijambo kabisa.” “Unakumbuka tukio lilivyotokea?” “Ndiyo, nilikuwa chumbani mke na mwanangu wakiwa sebuleni ghafla nikasikia sauti kama ya amri, mwanzo nilifikiri labda sauti inatoka kwenye tivii kwa vile alikuwa akiangalia tamthilia. Lakini sauti ya maumivu ya mke wangu ilinishtua na kunifanya nitoke chumbani. Nilishtuka kuona mke na mwanangu wamelala chini. “Nilipotaka kwenda kuwasaidia nilipigwa na kitu kizito kichwani kilichonifanya nipoteze fahamu. Nilipozinduka nilijikuta nipo hospitali na kupewa taarifa za kushtusha za kifo cha mke wangu na mwanangu,” Hans alipofika hapo alianza kulia na kumfanya Inspekta Koleta kumbembeleza. “Pole sana.” “Asante, lakini inauma sana heri wangeniua mimi kuliko mke na mwanangu!” “Najua inauma, unawafahamu waliofanya unyama ule?” “Kwa kweli siwafahamu kutokana na kuziba nyuso zao na kofia za kuziba kichwa.” “Unamjua Mage?” “Mage yupi?” “Wewe unamjua Mage yupi?” “Mmh! Mmoja.” “Yupi?” “Aliyewahi kuwa mpenzi wangu.” “Unamfahamu vipi?” “Alikuwa mpenzi wangu, lakini bahati mbaya nilioa mwanamke mwingine badala yake.” ”Kwa sasabu gani ulioa mwingine na kumuacha mpenzi wako wa muda mrefu?” “Wazazi wangu walikuwa hawamtaki.” “Unafikiri kitendo cha wazazi wako kumkataa Mage na kumchukua mwanamke mwingine kilimpandisha Mage hasira na kuamua kukukomoa?” “Walaa, yule msichana hausiki kabisa.” “Kwa nini unasema hivyo?” “Sasa hivi yupo katika mipango ya harusi anategemewa kuwa mke wa mtu afanye vile ili iweje?” “Kwa hiyo huna mtu yeyote unayemshuku?” “Mmh! Hakuna,” Hans alikataa. “Basi tukikuhitahi tutakuita.” “Hakuna tatizo.” Baada ya mahojiano yale Hans aliruhusiwa kuondoka, alirudi kupumzika nyumbani. Kila alipokaa peke yake moyo aliendelea kuumia bila kuonana na Mage na kumweleza neno lililo moyoni mwake kabla ya kuolewa. Aliamini kwa vile ulikuwa umebakia mwezi mmoja na nusu harusi ifungwe ingekuwa vigumu kuonana ana kwa ana. Wasiwasi wake ulikuwa kutopata nafasi baada ya kupata taarifa kwenda kumuona hospitali na kufukuzwa kisha kufunguliwa shtaki la kuishambulia familia yake. Aliamini Mage hatakuwa tayari kumsikiliza. Alijaribu kumpigia shoga yake Brenda ili amsaidie aweze kuzungumza naye hata kwa dakika mbili kisha moyo wake uwe radhi Mage kuolewa. Alichukua simu yake na kumpigia Brenda ambaye aliipokea upande wa pili. “Haloo.” “Haloo Brenda.” “Abee, nani mwenzangu?” “Hans.” “Hans yupi?” “Shemu kweli umenichoka yaani leo unaniuliza hivyo?” “Ha! Kumbe wewe? Vipi unaendeleaje?” “Nipo fiti kama chuma.” “Wewee! Utani huo upo wapi?” “Nyumbani, kwanza niwapeni pole kwa kitendo cha familia yangu kuwazuia kuniona kimeniuma sana kwa hiyo nakuombeni radhi sana.” “Hans wewe siku zote huna kosa, familia yako ndiyo kikwazo katika maisha yako.” “Hilo nalijua.” “Hans mtoto bado ana mapenzi na wewe baada ya taarifa zile kachanganyikiwa mbio hospitali lakini walichomfanya familia yako hawezi kusahau kibaya zaidi wamempakazia tatizo lako.” “Yaani wamenichanganya ile mbaya, Brenda naomba unikutanishe na Mage ili nimuombe msamaha.” “Mmh! Sijui kama utampa kwa vile sasa hivi yupo katika maandalizi ya ndoa yake.” “Sikiliza Brenda naomba nikupitie kwenu twende hadi nje ya nyumba yao Mage kisha uje naye nizungumze naye kwa dakika tano kisha nikurudishe nyumbani kwenu. Nakuahidi zawadi nzuri ukiniwezesha kumuona Mage kwa dakika hata mbili tu.” “Mmh! Kwani sasa hivi upo wapi?” “We nieleze nikufuate wapi?” “Njoo home basi.” “Fanya hivi chukua gari la kwenu tukutane Kivukoni.” “Haina tatizo.” Hans baada ya kuelezwa vile alitoka na kuingia kwenye gari aina ya Toyota Verosa na kuelekea Kigamboni kwa kina Mage. Alipofika Kivukoni hakukaa sana simu yake iliita ilikuwa ya Brenda, aliipokea. “Haloo Brenda.” “Hans nimefika, upo wapi?” “Nami nimefika umekuja na gari gani?” “Nissan Patrol nyeupe.” “Basi tuvuke.” Walikubaliana kuvuka upande wa pili, baada ya watu na baadhi ya magari kujaa ndani ya kivuko safari ya kuelekea Kigamboni ilianza. Kivuko kiliposimama upande wa Magogoni, watu waliteremka na kuelekea maeneo ya Kigamboni, Mji mwema mpaka Geza ulole na kwingineko. Brenda alitangulia baadaye aliliona gari la Hans likija nyuma, hakusimama aliendelea na safari mpaka karibia na kwa kina Mage alisimamisha gari pembeni Hans naye alisimamisha pembeni yake na kuteremka. Hans na Brenda walikumbatiana na kupeana pole upya huku Brenda akiwa haamini kama Hans amepona. “Dah! Pole sana.” “Asante.” “Sasa inakuwaje?” “Fanya hivi hili gari langu tuliache sehemu salama ili twende na lako tukifika utaingia ndani kwenda kumuita akija utamuingia kwenye gari lako najua atashangaa kuniona lakini nitatumia muda huo kuzungumza naye kisha atarudi ndani mwao na sisi tuondoke.” “Hakuna tatizo.” Hans alilipaki gari lake sehemu ya usalama na kuingia kwenye gari la Brenda hadi nyumbani kwao na Mage. Alipofika alilisimamisha gari pembeni ya geti hakutaka kuliingiza ndani na kuteremka. Mlinzi alishangaa kuliacha gari nje na kumuuliza. “Da’ Brenda mbona huingizi gari ndani?” “Hapana sikai sana,” Brenda alijibu huku akiingia ndani ya geti. Alitembea kwa mwendo wa kukimbia hadi ndani, alimkuta msichana wa kazi akiondoa vyombo mezani na kumuuliza. “Mage yupo wapi?” “Chumbani kwake.” Alikwenda hadi chumbani na kugonga. “Ingia,” sauti ya Mage toka ndani ulisema. Brenda alisukuma mlango na kuingia ndani Mage alishtuka kumuona shoga yake muda ule, kwa vile hawakuwa na miadi ya kukutana muda ule wakati mchana wa siku ile walikuwa pamoja na kuachana jioni. “He! Vipi mbona huku muda huu?” Mage alimshangaa Brenda. “Shoga hebu twende nje mara moja.” “Kuna nini?” “Utajua huko, we twende mara moja.” Mage bila kuongeza neno alinyanyuka kitandani na kuongozana na Brenda hadi nje, alishangaa kuona wanatoka nje ya geti. Lakini hakuhoji alisubiri kuona Brenda kamuitia nini. Alipotoka nje ya geti aliliona gari la Brenda, kwa vile alikuwa akisubiri muda wa kwenda kwa Colin na alichelewa kwenda kutokana na mama yake kutoka alimwambia shoga yake. “Brenda siwezi kufika mbali namsubiri mama ili niende kwa mume wangu.” “Hata huendi popote twende ndani ya gari.” “Kuna nini?” “Hebu punguza maswali.” Waliongozana wote hadi kwenye gari.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ “Ingia mlango wa nyuma,” Brenda alimwambia Mage, naye hakubisha aliingia. Ndani ya gari palikuwa giza, Brenda baada ya kuingia mbele aliwasha taa na kumfanya Mage ashtuke kumuona Hans. “Ha! Hans?” “Ndiyo mimi Mage samahani kwa kukushtukiza.” “Bila samahani, kwanza unaendeleaje?” “Namshukuru Mungu sijambo kabisa.” “Pole na kufiwa mke na mtoto.” “Asante, pole na wewe kutokana na ulichotendewa na familia yangu.” “Hans achana na hayo yameisha pita, nina imani kuna kitu kimekuleta naomba tuzungumze kwa haraka nataka kwenda kwa mume wangu muda si mrefu.” Hans alijikuta akitulia huku maneno yakigoma kutoka mdomoni, Mage alishangaa kuona mpenzi wa zamani akitokwa na machozi. Brenda alitoka nje ya gari na kuwaacha wapenzi ndani ya gari wazungumze yao. “Jamani nipo nje.” “Hakuna tatizo, usikae mbali natoka sasa hivi,” Mage alisema. Baada ya kutoka Mage alimuuliza Hans aliyekuwa akitokwa machozi. “Hans ameniita kuona machozi yako au kuna kitu kingine kama ni machozi nimeisha yaona, naomba niende zangu,” Mage alizungumza kwa sauti ya upole huku akimtazama usoni Hans. “Ma..ma..ge,” Hans alisema kwa kigugumizi. “Jina langu.” “Kilichonileta si kuja kukuonesha machozi bali moyo wangu umejaa maumivu makali.” “Najua inauma kupoteza mke na mtoto si kitu cha kawaida yataka moyo wa chuma kuyashinda maumivu yake lakini Mungu siku zote ni mfariji na kukufanya utayasahau yote kisha atakuletea mke mwingine.” “Mage mimi na wewe tuliahidiana nini?” “Kuoana kuwa mke na mume.” “Baada ya matatizo ya familia yangu nilikueleza nini?” “Ulisema huwezi kuzaa na yule mwanamke, baadaye utamuacha na kunioa mimi.” “Kwa nini umekubali kuolewa na mwanaume mwingine?” “Kwa sababu umevunja ahadi yetu.” “Mage nina imani unajua jinsi gani ninavyokupenda?” “Siyo unavyonipenda bali ulivyokuwa ukinipenda.” “Mage moyo wangu hautachoka kukupenda, nilikueleza nini baada ya kulazimishwa kuoa mwanamke mwingine?” “Ulisema wakikulazimisha kuoa utajiua.” “Ulinishauri nini?” “Nilikuwa radhi uoe lakini si kukupoteza maishani, ulichoniahidi ndicho kilinipa moyo na kuwa radhi kukusubiri hata miaka mia. Lakini wewe ndiye ulivunja mkataba na kuamini sina changu na kuamua nami kutafuta wangu japokuwa ilikuwa sawa na kunimezesha mfupa.” “Ndiyo sababu ya mimi kuja kuzungumza na wewe, baada ya kunisikiliza uamuzi utakaoutoa hapa sitapingana nao hata kama utaniumiza.” “Haya niambie hicho kilichokuleta.” Hans alianza kuzungumza kwa sauti ya chini yenye kusikika huku machozi yakiweka michirizi kwenye mashavu. Mazungumzo yalikuwa (Of air) ambayo hayakutakiwa mtu yeyote kusikia zaidi ya watu wawili tu. Hans alimaliza kuzungumza huku machozi na kamasi zikimtoka chapachapa. Muda wote Mage alijitahidi kumbembeleza Hans japokuwa naye alikuwa akilia. “Hans nimekuelewa lakini hukutakiwa kufanya hivyo.” “Sikuwa na jinsi, hukutaka kunisikiliza nilikuwa na wakati mgumu wa kuweza kunisikiliza. Kama ningekufa bila wewe kuujua ukweli wa moyo wangu ningekuwa nimekufa kibudu. Kama ningeshindwa kabisa ningekuja kujiua kwenye harusi yako ili ujue nilichokuahidi hakitabadilika moyoni mwangu kuwa kifo pekee ndicho kitanitenganisha na wewe.” “Mmh! Mbona Hans unanipa mtihani mkubwa, japokuwa uamuzi ni wangu lakini dunia itanitenga.” “Lakini Mage nilikueleza kila kitu juu yetu, wewe ndiye uliyeshikilia uhai wangu kwa mara nyingine wa kuniua au kuniacha hai ni wewe.” “Hans hata siku moja kifo chako hakitatoka mikononi mwangu, naombani uniache kwa leo mengine tutazungumza kesho kichwa changu kimevurugika hata sielewi jifanye nini.” “Ila kumbuka uhai wangu umeubeba wewe.” “Naelewa Hans.” “Kwa hiyo niondoke na jibu gani?’ “Niache kwa leo, nimekuelewa Hans.” “Sawa lakini bado nipo njia panda.” “Hans kuwa muelewa nimekueleza nimekuelewa unataka nini tena?” “Basi nashukuru.” “Nikutakie usiku mwema.” “Na kwako pia.” Mage aliteremka kwenye gari na kumuaga shoga yake huku akifuta machozi yaliyokosa kizuizi kisha alielekea ndani mwao. Brenda aliingia ndani ya gari na kushangaa kumkuta Hans akifuta machozi wakati Mage naye alitoka akifuta machozi. “Vipi kuna usalama?” “Kiasi.” “Umeelewana?” “Ndiyo.” “Kwa hiyo tunaweza kwenda.” “Ndiyo.” Brenda aliwasha gari na kuliondoka kuelekea walipokuwa wameliacha gari la Hans, njiani alijaribu kudodosa kwani kila mmoja alionekana kulia.“Vipi kuna usalama?” “Kiasi.” “Umeelewana?” “Ndiyo.” “Kwa hiyo tunaweza kwenda.” “Ndiyo.” Brenda aliwasha gari na kuliondoka kuelekea walipokuwa wameliacha gari la Hans, njiani alijaribu kudodosa kwani kila mmoja alionekana kulia. “Hans, Mage anasemaje?” “Hana la kusema bali nilitaka tu kumfikishia ujumbe, nashukuru amenisikiliza.” “Kwa hiyo roho yako umetulia?” “Nashukuru, tukifika kwenye gari nitakupa zawadi yako niliyokuahidi.” “Nitashukuru.” *** Muda ulizidi kukatika bila Mage kuonesha dalili zozote za kutoka kwenda kwa Colin, kitu kiliochomshtua mama yake ambaye aliwahi kurudi kwa ajili ya mwanaye kwenda kwa mchumba wake. Aliangalia saa ya ukutani ilimuonesha inakaribia saa nne usiku, alijiuliza labda mwanaye ametoka bila yeye kujua. Ilibidi amuulize msichana wa kazi kama Mage ametoka yeye akiwa chumbani. “Sofi Mage ametoka saa ngapi bila kuniaga?” “Mmh! Mama sijamuona kutoka.” “Una maanisha yupo chumbani kwake?” “Sijajua ila sijamuona.” Mama Mage alinyanyuka na kwenda chumbani kwa mwanaye, alikuta mlango umerudishwa alisukuma na kuingia bila hodi na kumkuta Mage amejilaza akiwa amekumbatia mtu huku machozi yakimwagika kama maji. Mama yake alishtuka na kutaka kujua kuliko mwanaye kuwa katika hali ile. “Mage! Nini mwanangu?” “Mamaa..maamaa,” Mage alishindwa kuzungumza aliangua kilio. “Mage una nini?” mama yake alizidi kumshangaa. “M..m..maa..ma,” Mage kila alipotaka kusema maneno yaligoma kutoka mdomoni. “Mage mwanangu umepatwa na nini, hebu nieleze mimi ndiye mama yako nipo tayari kukusikiliza na kukusaidia.” “Mama nipo kwenye wakati mgumu sana maishani mwangu.” “Kwa nini unasema hivyo?” “Najua nitakuudhi wewe mama yangu lakini nina imani ndiyo tiba sahihi ya moyo wangu ambao umekuwa matesoni kwa muda mrefu.” “Una maanisha nini?” mama yake alishtuka mpaka mapigo ya moyo yalianza kumwenda kasi. “Mama nitakacho kisema najua kitakuwa sawa na kumng’oa mtu jino bila ganzi.” “Una maanisha nini?” “Mama sitaki kuolewa tena.” “Niniii?” mama alishtuka. “Mama sitaki kuolewa na Colin.” “Kwa nini?” “Si chaguo la moyo wangu.” “Mwanangu unasema ukweli au unatania?” “Nasema kweli kabisa.” “Mmh! Na mipango ya ndoa?” “Tunasitisha kwa vile muda bado.” “Na watu tuliowachangisha fedha za send of.” “Tutawarudishia fedha zao.” “Wee mwana tutazupata wapi?” “Mi najua pa kuzipata.” “Hebu mwanangu nieleza tatizo nini, kama Colin amekukosea bado tuna nafasi ya kuzungumza tukalimaliza.” “Mama, Colin hajawahi kunikosea toka tujuane, ila mimi ndiye nimekuwa nikimkosea muda wote. Najua ananipenda sana na uamuzi wangu utamchanganya, lakini ukweli utabakia palepale si chaguo la moyo wangu. Nimejilazimisha kumpenda lakini moyo umekataa hivyo sina budi kuusikiliza moyo wangu unachotaka. “Siku zote moyo wa mtu huwa ndiyo muamuzi kwa jambo lolote kwa vile wenyewe ndiyo unaopokea furaha kwa jambo zuri au huzuri kwa jambo baya.” “Kwa hiyo unasema hujakosana na Colin?” “Walaa, najua Colin ananipenda sana na ataumizwa na uamuzi wangu lakini sina jinsi kila ndege hutua mtu aupendao.” “Mage upo sawa mwanangu?” “Nipo sawa mama.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ Kauli ile ilimfanya mama yake akae kwenye kitanda baada ya miguu kukosa nguvu. “Mage mwanangu mbona sikuelewi, kipi kimekusibu mama?” “Mama najua itakuwa vigumu kunielewa lakini utanielewa tu.” Mara simu ya Mage iliita, aliichukua na kuitazama na kuirudisha bila kuipokea kitu kilichomfanya mama yake kuuliza. “Mbona upokei kwani inatoka wapi?” “Kwa Colin.” “Sasa kwa nini hupokei?” “Sasa nitazungumza naye nini?” “Pokea mwambie leo huwezi kwenda hujisikii vizuri.” “Siwezi kuzungumza naye kwa leo, nitajisikia vibaya.” Simu iliita tena lakini haikupokelewa mpaka inakatika, baada ya muda msichana wa kazi alimwita mama Mage kuwa kuna simu yake inaita. Alitoka na kuichukua ilikuwa inatoka kwa mama Colin, aliipokea mara moja. “Haloo dada.” “Eeh! Kuna usalama huko?” “Kiasi.” “Kulikoni?” “Mage kichwa kilimshika ghafla.” “Jamani mkwe wangu! Vipi hali yake?” “Kidogo hajambo amelala kwa sasa.” “Basi tunakuja kumuona.” “Usisumbuke, alitaka kuja nikamzuia hayupo serious sana.” “Basi augue pole maana mwenzake alikuwa na wasiwasi baada ya kupiga simu isipokelewe.” “Mwambie asiwe na wasiwasi ni kichwa tu lakini anaendelea vizuri kesho atakuwa hajambo.” “Basi niwatakie usiku mwema.” “Na ninyi pia.” Mama Colin baada ya kumaliza kuzungumza alimgekia mwanaye aliyekuwa pembeni ya mama yake akifuatilia mazungumzo yale. “Vipi mama?” “Kumbe kichwa kilimshika ghafla amekunywa dawa kimetulia, alitaka kuja lakini mama yake kamwambia alale kwa leo atakuja kesho.” “Duh! Afadhali, nilikuwa na wasiwasi sana.” “Kapumzike, kesho mchumba wako atakuja.” “Sawa mama.” Colin alikwenda chumbani kwake, kabla ya kulala alichukua simu yake na kuangalia picha zote alizopiga na Mage na nyingine iliyopigwa siku ile mchana aliyotumiwa na Mage alipokuwa na shoga yake Brenda Mlimani City Samakisamaki. Aliibusu picha picha kubwa ya mpenzi wake aliyokuwa katika tabasamu la kufa mtu na kusema kwa sauti ya chini. “Mage wewe ndiye mke wa maisha yangu,” aliikumbatia na kujilaza. *** Mama Mage usingizi uligoma kabisa na kukiona kichwa kikitaka kupasuka kutokana na kuchanganywa na kauli ya mwanaye, alijiuliza kama mwanaye atasimamia uamuzi ule angeuweka wapi uso wake. Wasiwasi wake huenda amemfumania Colin na mwanamke mwingine na kuamua kuvunja uchumba. Bado aliona kama ni hivyo linazungumzika kwa vile wote wamejuana wakiwa tayari wanayajua mapenzi. Alinyanyuka kitandani na kutoka kwenda kwa mwananaye kupata ukweli kwani alikuwa amechanganyikiwa sana. Alitoka taratibu taa ya sebuleni zilikuwa zimezimwa kulikuwa na hali ya ukimya kutokana na watu wote kuwa wamelala. Hakutaka kuwasha taa ya sebuleni alitembea taratibu hadi chumba cha Mage alipotaka kuushika mlango alimsikia mwanaye akizungumza na simu alitulia ili asikilize anazungumza nini na nani. Alimsikia mwanaye akisema: “Kama hivyo nimeisha litibua yote kwa ajili ya mapenzi yangu mazito kwako, kama umemejitoa muhanga kwa ajili yangu nami sina budi kujitoa kwa ajili yako. Najua uamuzi wangu utamchanganya mama na yule mchovu lakini wewe ni zaidi yao wote nakupenda sana zaidi ya kukupenda. “ Nipo radhi vyote duniani viondoke ubakie peke yako, please mpenzi usinitende kosa lako ni mauti yangu, nashukuru kwa kujali mapenzi yangu kwako. Asante mpenzi wangu naomba ulale usingizi mororo huku ukiniota. I love you and i need you in all my life, mmmmwa.” Mama Mage alijiuliza mwanaye anazungumza na nani, wazo lake lilipelekea labda ni Hans, lakini hakukubaliana nalo kutokana na maumivu aliyoyapata mwanaye kutoka kwa Hans na familia yake. Wazo lilielekea huenda kapata mpenzi mwingine ambaye kamzidi kete Colin. Alishangaa mabadiliko yake ya ghafla kwani mpaka saa tatu kasoro usiku mwanaye alikuwa na kimuhemuhe cha kwenda kwa mchumba wake Colin na kumuhimiza kuwahi. Lakini aliporudi alikuwa mambo yamebadilika ghafla kama saa sita mchana ugeuke kiza totoro na watu wasionane. Alipata wazo la kwenda chumbani kwa Sofia msichana wa kazi kumuuliza kuna kitu gani kilitokea kabla ya kurudi na kusababisha hali ile. Alikwenda kugonga chumba cha msichana wa kazi aliyeamka. “Abee mama.” Mama Mage aliingia chumbani bila kusema kitu kisha alirudisha mlango na kumuuliza kwa sauti ya chini. “Sofi.” “Abee mama.” “Eti nilipotoka, Mage alitoka?” “Hapana hajatoka,” Sofi alikataa huku akitikisa kichwa. “Colin alikuja?” “Hapana.” “Nani alikuja.” “Mmh! Da’ Brenda.” “Brenda si alikuja mchana na kuondoka na Mage?” “Hata usiku alikuja na kwenda chumbani kwa dada Mage kisha walitoka nje baadaye nilimuona dada Mage akirudi peke yake huku ameshikilia kitambaa mkononi kama anafuta machozi lakini sikumtilia maanani.” “Mmh! Sasa nimeelewa,” mama Mage alisema huku akishika mikono kiunoni. “Kuna nini mama?” Sofi alishtushwa na kauli ya mama Colin. “Kawaida, ila nimeelewa,” alisema huku akitoka chumbani kwa Sofi na kurudi chumbani kwake. Alipoingia chumbani alichukua simu na kumpigia Brenda ili amwambie alimpeleka wapi mwanaye mpaka kugeuka ghafla na kumtia gharama na fedheha kubwa. Baada ya kupiga simu ya Brenda ulipokelewa upande wa pili. “Haloo mama.” “Brenda za saizi?” “Nzuri mama.” “Eti Brenda kumetokea nini mama?” “Kuhusu nini?” “Ulimpekeka wapi Mage?” “Sijampeleka popote nilitoka naye nje mara moja akarudi ndani kujiandaa kwenda kwa shemeji Colin.” “Unajua wewe ndiye umevunja ndoa ya Mage?” “Kivipi mama?” Brenda alishtuka. “Umemwambia nini Mage mpaka akakataa kuolewa, gharama za harusi utazilipa wewe?” “Mama kwa nini unasema hivyo?” Brenda alishtuka. “Haiwezekani kuja wewe ghafla na Mage kubadili uamuzi wa kuolewa.” “Mamaa! Hebu subiri,” Brenda alikata simu na kumpigia Mage. Baada ya kuita kwa muda simu ilipokelewa. “Haloo Brenda afadhali umenipigia.” “Mage kuna nini?” “Nimevunja uchumba na Colin.” “Mungu wangu! Kwa nini tena?” “Nimepata tiba ya moyo wangu.” “Mage unajua lawama zote nabebeshwa mimi?” “Brenda walaa hilo halikuhusu, kila kitu kitaeleweka, nitazungumza na mama muda si mrefu.” “Mage ndugu yangu naomba usivunje ndoa yako utaniweka mahari pabaya,” Brenda alimbembeleza Mage. “Nitaolewaje na mtu nisiyempenda?” “Mage leo yamekuwa hayo? Si ni wewe ndiye ulinihakikishia Colin ndiye tiba ya moyo wako?” “Hakuwa tiba bali dawa ya kupunguza maumivu lakini Hans ndiye tiba kamili, kama alijitoa kwa ajili yangu nami sina budi kujitoa kwa ajili yake.” “Colin anajua?” “Hajajua ila sitaki mtu yeyote amwambie nitamwambia mimi mwenyewe nina imani tutaelewana tu.” “Mmh! Mbona najuta kiherehere cha kumleta Hans!” Brenda alijua yeye ndiye chanzo cha yote yaliyotokea. Alijiuliza Hans alimweleza Mage kitu gani kilichomfanya abadili ghafla uamuzi wa kuolewa. Aliamua kumpigia simu Hans kutaka kujua aliwambia nini Mage mpaka kuamua kuvunja uchumba wakati kila kitu kilikuwa kipo katika hatia za mwisho. Lakini simu ya Hans haikuwa hewani, alijikuta akijiuliza atamwambia nini mama Mage mpaka amwelewe. Usiku ulikuwa mrefu kwa Brenda na kujuta kwa nini alimkubalia Hans kwenda kuonana na Mage. *** Siku ya pili Mage aliamka asubuhi na kuoga na kujipamba kisha alitoka, alimkuta mama yake amekaa sebuleni ameshika tama. “Mama vipi mbona hivyo?” alimuuliza huku akijilazimisha kujenga tabasamu. “He! Safari ya wapi?” “Naenda kwa Colin mama.” “Kweli?” mama yake alishtuka. “Ndiyo mama.” “Haya wasalimie.” “Sawa mama, ila sitakuwa hewani kwa siku mbili.” “Kwa nini?” “Utajua nikirudi.” “Kwani mnakwenda wapi?” “Itajua tu mama.” “Haya mwanangu safari njema.” “Asante mama.” Mage kabla ya kutoka alimbusu mama yake na kuelekea nje na kumfanya mama yake kumsindikize kwa macho kisha alinyanyua mikono juu kumshukuru Mungu kwa kuweza kumbadili msimamo wake. Alijiuliza kama angesimamia msimamo wake kwake ingekuwa aibu na fedhea ya kuvunjika harusi aliyoiandaa kwa nguvu kubwa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ Ilikuwa toka aamke alikuwa hajaoga zaidi ya kukaa sebuleni kutafuta njia ya kuinusuru ndoa ya mwanaye ambayo aliamini ni muujiza pekee ndiyo wenye kuiponya kwa kuamini nguvu za kibinaadamu zisikingeweza. Alinyanyuka na kwenda kuoga ili apate kifungua kinywa. Mage alikwenda kuchukua gari aina ya Prado nyeupe na kutoka kuelekea nyumbani kwa kina Colin. Aliendesha gari taratibu tofauti na siku zote aliendesha kwa fujo. Alirudisha kukumbuka ya muda mfupi ya picha ya mama yake aliyokuwa amekaa ameshika tama kuonesha kabisa uamuzi aliochukua umemchanganya sana na kumnyima raha. Alipeleka macho yake kwenye simu yake iliyokuwa pembeni yake na kuichukua alitafuta namba ya Hans na kumpigia. Iliita kidogo na kupokelewa. “Haloo ma adorable.” “Vipi umeamka salama?” alimuuliza kwa sauti iliyopooza. “Mmh! Naweza kusema nimezaliwa upya nimelala usingizi mtamu nilioukosa muda mrefu.” “Nashukuru kama ni hivyo.” “Mmh! Niambie moyo wangu?” “Hans nilitaka kukujulisha kuwa sitakuwa hewani kwa siku mbili ila ya tatu nitarudi kama kawaida.” “Kuna nini?” “Utajua baadaye.” “Upo wapi?” “Nimetoka mara moja.” “Sawa nimekuelewa mpenzi.” “Basi nikutakie siku njema yenye furaha.” “Na kwako pia.” Mage alikata simu na kumpigia shoga yake Brenda, haikuchukua muda ilipokelewa upande wa pili. “Vipi shoga?” “Poa, za asubuhi?” “Nzuri tu.” “Nilitaka kukujulisha sitakuwa hewani kwa siku mbili.” “Kwa nini shoga halafu mbona leo kama hujachangamka?” “Aah! Nipo katika kipindi kigumu lakini nitakivuka tu japokuwa najua jasho la damu lazima litoke.” “Bado unamsimamo uleule?” “Utajua baada ya siku mbili.” “Sasa upo wapi?” “Nakwenda kwa Colin.” “Loh! Afadhali shoga maana mimi mwenyewe nilikuwa sina amani moyoni mwangu.” “Basi ndiyo hivyo tutawasiliana kesho kutwa.” “Na kesho?” “Sitakuwa hewani kwa siku mbili.” “Mmh! Umeamua, safari njema msalimie sana shemu Colin mwambie nimemmisi.” “Salamu zimefika.” Baada ya Mage kukata simu shoga yake Brenda alitipa simu kwenye kochi na kushika kifua na kusema: “Ooh! Afadhali Mage kabadili uamuzi sijui kama mama yake angenielewa.” Mage baada ya kumaliza kuzungumza na Brenda aliweka simu pembeni na kuiweka mikono yote juu ya usukani na kukanyaka mafuta kuelekea nyumbani kwao Colin. Macho yake yalitulia kutazama mbele huku machozi yakijaa taratibu katika macho yake. Alijikuta akisema kwa sauti kama anazungumza na mtu. “Mapenzi haya! Kwa nini Mungu uliumba mapenzi kwa nini yakuwa kila siku yanachukua furaha yangu badala ya kunifariji?” Alichukua kitambaa pembeni yake alifuta machozi na kuendelea na safari. Alisimamisha gari mbele ya geti la nyumba ya kina Colin, geti lilifunguliwa na kuingia ndani. Aliliweka kwenye maegesho kabla ya kuteremka alivaa miwani ya jua ili kuficha macho yake na kuteremkaWa kwanza kuonana naye alikuwa mama Colin ambaye alimkimbilia na kumpokea Mage. “Wawaooo mkwe wangu.” “Waawoo mama, Shikamoo.” “Marahaba.” “ Colin yupo wapi?” “Yupo chumbani kwake, aliniambia utakuja.” “Ndiyo mama.” “Vipi unaendeleaje?” “Namshukuru Mungu nipo sawa.” “Haya mwanangu kamuone mwenzio maana alikuwa na kimuhemuhe hasa baada ya kusikia unaumwa.” “Sawa mama.” Mage alielekea chumbani kwa Colin, mlango ulikuwa umerudishwa aliusukuma bila hodi na kuingia ndani alimkuta Colin akibadika picha kubwa ya rangi ukutani wakiwa ufukweni wamelaliana chini ya picha ule kulikuwa na maneno ya rangi nyekundu yaliyokuwa yanasomeka, kwa juu yaliandikwa: ASANTE MUNGU KWA KUNIPA MKE MWEMA na chini kuliandikwa MAGRETH NAKUPENDA ZAIDI YA KUPENDA . Mage aliposoma yale maneno na kuiona ile picha moyo ulimuuma na kuangua kilio cha sauti, Colin alishtuka kusikia sauti ya mchumba wake, alipogeuka alimuona Mage amesimama akiwa ameshika kifua chake. Aliteremka haraka kitandani alipokuwa amepanda kubandika picha ile kubwa na kumfuata alipokuwa amesimama na kumkumbatia kwa kumlazia kifuani. “Vipi mpenzi kipi kinakuliza?” “Najua nina mtihani mzito moyoni mwangu lakini Mungu atanipa nguvu na nitashinda.” “Kuna nini mbona unanitisha?” “Kawaida tu, Colin naomba ujiandae tuna safari.” “Ya wapi?” “Surprise.” “Waawoo!” Colin alisema huku akimkumbatia Mage. Kwa vile alikuwa ametoka kuoga alibadili nguo na kumweleza Mage. “Nipo kamili mpenzi.” “Chukua na nguo nyepesi za kupumzikia.” “Tunaenda wapi?” “Utajua tu.” Walichukua begi dogo na kuongozana hadi sebuleni, walimkuta mama Colin akimuelekeza jambo msichana wa kazi alipowaona aliacha na kuwageukia. “Jamani wapendanao safari ya wapi?” “Tunatoka kidogo,” alijibu Mage. “Haya mwende salama.” “Asante mama, ila hatutakuwa hewani kwa siku mbili.” “Kwa nini?” “Utajua tu,” Mage alijibu “Kwa hiyo leo hamrudi?” “Ndiyo mama tutarudi kesho kutwa.” “Mmh! Haya wanangu nawatakieni safari njema,” mama Colin aliwakumbatia wote na kuwabusu kisha aliwasindikiza nje hakuondoka mpaka walipotoka nje ya geti ndipo aliporudi ndani. *** Baada ya gari kuingia barabarani Mage alimgeukia Colin aliyekuwa ametulia na kumwambia. “Colin zima simu yako.” “Kwa nini?” “Sitaki uwasiliane na mtu yeyote zaidi yangu.” “Sawa mpenzi,” Colin alizima simu yake. “Zima na yangu.” Colin alichukua simu ya Mage ni kuizima, safari iliendelea, gari lilielekea barabara ya Kawawa mpaka Mwenge na kukata mtaa wa viwanda mpaka njia panda ya Kawe. Mage hakukunja alinyoosha na kutokea Afrikana alikata kulia kuelekea Tegeta. Colin hakuhoji gari lilivuka Tegeta likaingia Boko likavuka Bunju na kuitafuta Bagamoyo Ndani ya gari muziki laini uliendelea kuunguruma kila mtu akiwa kimya kutokana na mwendo wa kasi aliokuwa akienda nao Mage. Alisimamisha gari mbele ya hoteli ya Oceanic Bay, baada ya kusimamisha gari alimgeukia Colin aliyekuwa ametulia akiuangalia umahiri wake kuendesha gari. “Nina imani tuna siku mbili ya kila mmoja kumaliza hamu zake kwa mwenzie.” “Mage mpenzi siku zote kitamu hakiishi hamu, penzi lako kwangu siwezi kulikinai.” Mage hakuongeza neno alimshika mkono na kuongozana naye mpaka mapokezi na kukodi chumba kizuri kwa siku tatu. “Mage si umesema tunarudi kesho kutwa.” “Tatizo nini hata tukikaa mwaka kuna mtu anatudai?” “Hakuna.” Baada ya kupata chumba walikwenda chumbani kwao, chumba kilikuwa kizuri sana. “Colin unakionaje chumba hiki?” “Kizuri sana, unaonaje fungate yetu tuje tuifanye huku.” “Tutaangalia muda ukifika.” Baada ya kuoga kwa vile muda ulikuwa umekwenda walivaa nguo nyepesi na kwenda hotelini kupata chakula cha mchana. Kisha walihamia ufukweni kupata upepo wa bahari, muda mwingi Colin alikuwa mtu mwenye furaha kuwa karibu na mpenzi wake mchumba wake mkewe mtalajiwa. Lakini Mage alionekana kulazimisha furaha kutokana na siri nzito iliyokuwemo moyoni mwake. Baada ya kutosheka na upepo wa bahari walirudi ndani na kujilaza kitandani mkao wa mahaba huku wakiangalia video. Colin muda mwingi alijiuliza kwa nini wamezima simu ilibidi amuulize Mage. “Mpenzi kwa nini tusiwashe simu hata kwa muda?” “Colin hizi ni siku zetu ambazo ni muhimu kwetu sitaki kusikia chochote masikioni kwangu zaidi ya sauti yako.” “Nimekuelewa mpenzi wangu.” “Colin,” Mage alimwita. “Naam mpenzi.” “Hivi mfano uwe nyumbani kwenu mara mama yangu anakupigia siku kukueleza nimefariki utafanyaje?” “Mage hayo ni maneno gani, umesema tupo kwenye furaha sasa maneno ya kifo yanafuata nini?” “Najua hapa siyo sehemu yake lakini naomba unijibu.” “Kwa kweli nitachanganyikiwa naweza hata kufa.” “Hivi umpendaye akifa kuna sababu ya kuchanganyikiwa ikiwa baada ya mazishi yake kuna wengine wapo pengine zaidi ya yule aliyeondoka?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ “Ni kweli, lakini kinachomtesa mtu ni mazoea si uzuri wa sura wala umbile la mtu.” “Kwa mfano mi nikisema sikupendi utafanyaje?” “Nitafanyaje nawe umeamua.” “Hutaumia?” “Nitaumia lakini nitafanya nini, lakini naamini mimi na wewe tunapendana hakiwezi kutokea kitu kama hicho.” Mage alibadili mazungumzo kwa kumshika mkono Colin na kuelekea naye bafu kuoga, waliingia kwenye jakuzi na kuoshana kisha walirudi kitandani kuburudisha mioyo yao. Mage alimpa penzi Colin penzi shatashata ambalo lilimrusha akili naye alijibu mashambulizi kitu kilichomfanya Mage aangue kilio na kumshtua mpenzi wake. “Vipi mpenzi mbona unalia?” “Colin sina jinsi lazima iwe.” “Iwe nini?” “Utajua tu.” Mage alimvamia Colin na kuendelea kustarehe bila kuliweka wazi lililikuwa likimliza, alijitahidi kurudi katika hali yake ya kawaida ya uchangamfu na kumfanya Colin asahau kitendawili chake. Walikaa kwenye hoteli ile kwa siku mbili huku wakiongozana kama kumbikumbi huku kila mmoja alijua watu wale wanapenda mapenzi ya dhati. Siku iliyofuata majira ya mchana baada ya kupata chakula walipumzika kwa muda kabla ya kurudi mjini. Mage akiwa amejilaza pembeni ya Colin alijinyanyua na kumgeukia mpenzi wake na kumwita. “Colin.” “Naam mpenzi.” “Hivi unajua kwa nini toka juzi sijakuita mpenzi?” “Sijajua.” Mage alitulia kwa muda akimtazama Colin usoni mara machozi yalianza kumtoka, Colin alizidi kumshangaa mpenzi wake kwani toka wamefika Bagamoyo ameshindwa kumwelewa. “Colin, “ alimwita tena.” “Naam.” “Najua unanipenda.” “Sana.” “Najua kabisa nitakachokueleza kitakushtua na kukumiza moyo wako sawa na kuupasua bila ganzi kwa kisu butu. Lakini ukweli utabakia palepale sina jinsi, nina imani penzi la kweli huwa alitengenezwi na mtu bali mhusika mwenyewe.” “Ni kweli kabisa.” “Unajua penzi letu halikuwa la sisi kupendana bali kutengenezwa na wazazi wetu?” “Najua lakini tulipoonana kila mtu alimpenda mwenzake.” “Unajua hiyari yashinda utumwa?” “Najua.” “Nina imani nilikueleza jinsi mapenzi yalivyoniumiza.” “Ndiyo.” “Na aliyesababisha nilikueleza.” “Ndiyo.” “Basi napenda kukueleza hili ambalo moyo wangu unavuja damu kwa maumivu kwa vile sikupenda liwe kwa vile hiyari yashindwa utumwa, lazima niseme ukweli wa moyo wangu kuwa Colin nilikupenda lakini Hans nilimpenda zaidi. Hans baada ya kufiwa na mkewe amerudi kwangu na yupo tayari kutimiza ndoto yetu tuliiweka muda mrefu,” Mage alimeza mate huku akiendelea kutokwa machozi kisha aliendelea kuzungumza kwa sauti ya chini yenye mchanganyiko na kilio. “Najua kauli yangu itakumiza lakini ndiyo ukweli wenyewe, Colin nimeamua kwa hiyari na mapenzi yangu nikiwa na akili timamu kuuvunja uchumba wetu kwa hiyo harusi yetu haitakuwepo tena, Penzi tamu tulilopeana ndilo la mwisho tukitoka hapa kila mtu ashike hamsini zake.” “Mage,” Colin alimwita kwa sauti ya chini. “Abee.” “Unasema kweli au unatania?” “Nasema kweli,” Mage alijibu huku akikaza macho. “Hapana acha utani Mage unaweza kuniua kwa presha.” “Huwezi Colin, wewe ni mwanaume umeubwa kukabiliana na matatizo, kumbuka amenikuta tayari nimeishaanza uhusiano na mtu ambaye ndiye aliyenionjesha dunia ya mapenzi na aliniahidi kunioa. Toka niachane naye sikuwahi kuwa na mwanaume mwingine zaidi yako kilichotokea ni kutoelewana lakini sasa hivi tumeelewana na mipango yetu lazima itimie.” “Mage japo Hans ndiye alikuonjesha dunia ya mahaba lakini alikutenda, Mage nimekukosea nini mpaka uchukue uamuzi mzito na wa kikatili kama huo?” Colin aliuliza huku machozi yakimtoka. “Hujanikosea kitu, hata mimi nilikupenda sana, lakini siwezi kuishi na wewe kwa kujilazimisha au kukufanya kama bodi lakini injini awe Hans. Colin, Hans nampenda sana aliniudhi na kuumiza moyo wangu lakini siku aliponiomba msamaha moyo wangu aliyeyuka kama bonge la mafuta kwenye kikaango cha moto. Siwezi kuwa nawe kimwili wakati mawazo yangu yote yapo kwa mwanaume mwingine. “Narudia naomba ukubaliane na uamuzi wangu wa kuvunja uchumba tukiwa na mioyo safi, kuachana kwetu kusijenge uadui tuendelee kuwa marafiki kwenye harusi yangu uje ya kwako nije.” “Mage uamuzi uliochukua ni kuupasua moyo wangu bila ganzi, naomba urudishe moyo nyuma mpenzi wangu, bora ungeninyang'anya kila kitu katika mwili wangu na kuniachia moyo wako ni muhimu kuliko chochote duniani japo nipo nawe kwa muda mfupi lakini nimekuzoea sana.” “Siwezi kuishi mapenzi ya kuigiza niache nimpende aliyechaguliwa na moyo wangu.” "Mage siwezi kukubali kirahisi namna hiyo nasema sikubali, lolote na liwe nasema huondoki kama sio nitamwaga damu ya mtu," Colin alisema huku akisimama. "Colin mapenzi si lazima usisababishe nikakasilika na kutoa maamuzi yatakayokuumiza mara mbili." "Nasema sikubali...toa uamuzi wowote kumbuka nimekutoa kwenye mateso ya kutendwa , leo nikuache uondoke hivihivi sikubali," Colin alikuwa mkali. "Colin nasema hivi kila usemalo ni kweli tupu na una haki yoyote ya kufanya lakini kumbuka penzi alilazimishwi nina imani umenielewa kuwa mstaarabu tuachane kwa usalama." Mage alinyanyuka na kumsogelea Colin aliyekuwa ameinama akilia na kumpigapiga mgongoni. "Sweet naomba usilie mwanaume kaumbwa kukabiliana na matatizo hili ni moja wapo.” Colin alinyanyuka kama mbogo na kumsukuma Mage aliyeanguka chini huku akibwata. "Muongo mkubwa mnafiki wewe unanipaka mafuta kwa mgongo wa chupa eti sweet!" "Huwezi amini Colin nakupenda sana japo Hans nampenda zaidi, nipo yatari kulipa gharama zote za maandalizi ya harusi yetu, pia hata kulipa gharama zozote ili kuhakikisha nawe unakuwa na mke atakayeziba pengo langu." Mage pamoja na kusukumwa hakukasirika akiamka pale chini alipoanguka Colin hakumjibu neno lolote zaidi ya kuinama huku akilia. Mage alimshika mkono na kunyanyua, alimtazama kwa macho yaliyojaa machozi na kusema kwa sauti ya chini. “Colin nisamehe sana siwezi kuwa mnafiki mapenzi nayajua, nipe ruksa mpenzi wangu. Nilikuja huku ili tupate muda wa kulizumgumza hili, sikutaka tulizungumze juujuu. Nakupenda lakini sitaki nikutese kwa kukunyanyasa kimapenzi kwa vile mapenzi nayajua yanavyoumiza.” Colin alitulia huku akimtazama Mage aliyekuwa akitia huruma, alijiona mjinga kulazimisha mapenzi. Alikohoa kidogo na kusema: “Sawa nimekuelewa.” “Nashukuru.” “Kuna la zaidi?” Colin alimuuliza Mage. “Hakuna.” “Tunaweza kuondoka.” Walichukua vitu vyao na kuelekea nje kwenye gari ili warudi mjini. *** Cecy baada ya kutoka twisheni alisimama chini ya mti kuagana na shoga yake huku wakijikumbusha baadhi ya mada walizopewa wakasome nyumbani. Alikuwa amepiga hatua kubwa katika kusoma na kundika hata kuzungumza lugha ya kingereza baada ya kusoma kwa uchungu mkubwa. Siku zote aliamini kumkosa Colin kulitokana na kukosa elimu, kwake umaskini hakuuona sababu kama ungekuwa na elimu yake ambayo hata mama Colin angeiheshimu. Toka aanze kusoma alionekana ndiye mwanafunzi aliyetaka kujua lugha kuisoma kuiandika na kuizungumza. Japokuwa hakukijua sana lakini aliweza kumsikia mtu na kumwelewa hata kumjibu mawili matatu. Ile ilimpa kiburi cha kuzungumza muda wote hata alipokosea hakujisikia vibaya kwa vile alielekezwa. Baada ya kujadiliana na shoga yake alisogea mbele kuelekea njia ya kwao japo palikuwa mbali kidogo lakini hakujali umbali ule kutembea kwa miguu kwa vile alikuwa akitafuta kitu. Siku zote aliingia darasa la mchana kwa vile asubuhi alikuwa akienda kwenye biashara zake. Ada ya mwanzo alitumia fedha aliyoachiwa na Colin siku aliyompeleka kwao na kuwaacha kwenye mataa kwa ahadi tamu ya kuyabadili maisha yao. Alikumbatia daftari lake na kutembea taratibu kukifuata kichochoro cha kuingilia njia ya mkato. Aliangalia saa yake ilimuonesha ni saa kumi na moja na nusu jioni. Alishtushwa na sauti ya gari aina ya Prado jeupe new model lililosimama nyuma yake. Alipogeuka aliona msichana akiteremka kwenye gari huku akibwata kwa sauti kuonesha anazozana na mtu ndani ya gari. Alipomwangalia aligundua ni Mage mwanamke aliyezima ndoto zake za kuwa mke wa Colin. Alisimama nyuma ya mti kumwangalia, alimuona akisema kwa sauti: “Wewe mtu gani unayelazimisha mapenzi nimekueleza ninaye ninayempenda hutaki kunielewa. Naomba uteremke kwenye gari langu, siwezi kutembea na mtu asiyeelewa. Sasa hiyo elimu uliyosoma inakusaidia nini ikiwa hutambui nini maana ya upendo? Nasema teremka la sivyo nitakuachia gari niondoke zangu.” Baada ya muda Cecy alishtuka umuona mwanaume aliyekuwa akiambiwa vile ni Colin, baada ya kuteremka kwenye gari kinyonge na alisogea pembeni na kusimama bila kujua nyuma yake yupo Cecy. Cecy roho ilimuuma kuona mtu ampendaye akidhalilishwa vile, Colin alionekana machozi yakimtoka kitu kilichozidi kuumiza moyo wake na kushangaa watu ambao muda si mrefu walitegemea kufunga ndoa lakini ajabu mwanamke kutoa maneno makali kama yale ya kumdhalilisha mumewe mtalajiwa. Alitulia aione sinema ile inaishaje kwa kujificha nyuma ya mti ili wasimjue, baada ya muda alisikia sauti ya Colin. “Mage pamoja na hayo lakini kumbuka tumepanga nini mimi na wewe katika maisha yetu?” “Hainihusu! Nimekwambia mapenzi siyo lazima, ninaye nimpendaye wewe nikuweke wapi?” “Mage...Mage.” “Jina langu, kwa heri.” Mage alisema huku akielekea kwenye gari ili aondoke na kumuacha Colin aliyekuwa bado amesimama akilia. Kitendo kile kilimuumiza sana Cecy bila kujitambua alitoka nyuma ya mti na kwenda kumvamia Mage kwa nyuma na kuzivuta nywele zake na kuanza kumshushia kipigo. Colin alishtuka kumuona Cecy eneo lile na kujiuliza ametokea wapi, ilibidi amuwahi kumtoa juu ya Mage aliyekuwa akipiga kelele za maumivu. “Cecy muache.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ “Hawezi kukudhalilisha kiasi hicho kama umalaya wake apeleke mbele,” Cecy alisema huku akitweta kwa hasira akitaka kujitoa mikononi mwa Colin ili akamfunze adabu Mage. “Colin have you sent this bastard to come and attack me?“ (Colin umemtuma chokoraa huyu aje anipige?) Mage alibadili lugha na kusema huku akisikilizia maumivu. “No, baby, I’m also suprised as to where she came from.” (Hapana mpenzi hata mimi nashangaa sijui katokea wapi.) Colin alijitetea. “Colin, what type of a man who forces to be loved, what’s wrong with you? Let her go!” (Colin wewe ni mwanaume gani unang’ang’aniza mapenzi una kasoro gani mwacha aende) Cecy safari hii naye alivunja yai na kufanya Colin abakie mdomo wazi. “Colin thank you, stay with that bastard whom you sent to beat me.” (Colin asante, baki na huyo chokoraa uliyemtuma kunipiga) Mage alisema huku akielekea kwenye gari. Colin aliyekuwa amemshika Cecy ili asiendelee kumuadhibu Mage, alimuachia na kumfuata Mage kumuomba msamaha. “Please Maggie excuse me, do not be so cruel to me.” (Tafadhali Mage rudisha moyo nyuma usinifanyie ukatiri huo.) Alipopiga hatua ili amfuate Mage kwenye gari, Cecy alimfuata na kumzuia kwenda kuomba msamaha. “Colin...Colin... why do you cling to her, how good is her; do you love her for her riches or behaviour? (Colin... Colin... unamng’ang’ania ana sifa gani, unampendea utajiri au tabia?) Colin alijitahidi kujitoa mikononi mwa Cecy lakini alikamatwa madhubuti, wakati huo Mage alikuwa ameingia kwenye gari na kutupa nje begi la Colin na kuondoa gari kwa kasi na kumuacha Colin akilisindikiza kwa macho. Baada ya gari kupotea machoni alitulia huku machozi yakiziba macho. Cecy roho ilimuuma kuona mtu ampendaye akitokwa machozi kwa ajili ya kulilia penzi lisilokuwepo. “Colin, mbegu ya penzi humea kwenye moyo wenye rutuba ya mapenzi, kwa nini unalazimisha kupanda mbegu yako kwenye mawe? Kwani nini unakuwa kenge asiyetaka kuelewa. Mshukuru Mungu msichana wa watu amekuwa mkweli mapema,” Cecy alisema kwa sauti ya kilio iliyomshtua Colin na kurudisha macho kwake. Pamoja na yote yaliyomtokea alishangazwa na ujasiri wa Cecy msichana aliyeonesha kuumizwa na kitendo cha kudhalilishwa na Mage. Kingine na uwezo wa kuzungumza kingereza kwa ufasaha mkubwa pia kuonekana binti mwenye mvuto kutokana na mavazi na muonekano. “Cecy,” alimwita kwa sauti ya upole. “Abee.” “Kwanza samahani.” “Ya nini Colin?”“Najua nimekudhalilisha kwa kitendo changu cha kumlilia Mage.”“Colin siwezi kukulaumu kwa vile ile ni haki yako japo sijui sababu ya yeye kukudhalilisha kiasi kile ikiwa kila kitu kipo katika hatua za mwisho kilichobaki ni ndoa.”“Mage amerudiana na bwana yake wa zamani na kuamua kuvunja uchumba wetu.”“Kama amekueleza ukweli sasa unamng’anganiza wa nini?”“Cecy ni ghafla sana heri kungekuwa na tatizo, kanifuata nyumbani juzi na kunipeleka Bagamoyo, niliamini ana mapenzi yake ya dhati kwangu lakini baada ya kukaa siku mbili za furaha siku ya tatu alinieleza kitu ambacho kimenichanganya sana.”“Colin ulikuwa unampenda Mage mapenzi ya dhati au tamaa ya macho?” Cecy alimuuliza akiwa amemkazia macho.“Mapenzi ya dhati.”“Muongo! Umempenda kwa shinikizo la mama yako, kama amejitoa kwa hiyari yake huoni hii ni nafasi ya kuipanda mbegu yako sehemu sahihi ambayo utaotesha mti mwenye kivuli na matunda matamu?”“Cecy kwanza unatoka wapi muda huu?” “Shule.”“Hongera.”“Siwezi kusema asante.”“Kwa nini?”“Mpaka ufute machozi yangu.”Colin alitoa kitambaa mfukoni ili amfute Cecy machozi, lakini alishikwa mkono na kumfanya aulize:“Vipi Cecy mbona unanishika mkono?”“Si machozi haya Colin.”“Machozi gani Cecy?” Colin alishtuka.“Ya moyoni, nimeumizwa sana pia nimedhalilishwa sana juu ya penzi lako, lakini Mungu si mnafiki leo amekudhihilishia mbele ya macho yangu kuwa mke uliyechaguliwa mara ya pili hakuwa mke sahihi bali lilikuwa penzi la kuingiza. Colin mimi ndiye mkeo uliyechaguliwa na Mungu. Nifute machozi yangu kwa kufunga ndoa na mimi si kwa kitambaa cha mkononi bali cha moyoni,” Cecy alisema kwa sauti iliyojaa hisia kali za mapenzi.“Cecy nimekuelewa naomba unipe muda.”“Muda wa nini wakati nafasi yangu imerudi tena nikiishuhudia si kwa kuhadithiwa na mtu.” “Nimekuelewa, niache kwanza nifike nyumbani kwanza kumbuka toka juzi sipo nyumbani na ninarudi na taarifa hizo sijajua mama atazipokeaje?”“Mmh! Sawa, ila pole kwa yote yaliyokukuta.”“Nashukuru.”“Colin naomba nikusindikize mpaka kwenu,” Cecy aimwambia Colin huku akiuchezea mkono wake.“Hapana si unamjua mama atapata la kusema.””Nimekuelewa mpenzi.”Colin alitoa hela mfukoni bila kuzihesabu na kumpatia Cecy, alizipokea na kushukuru kwa kupiga magoti kitu kilichomshtua Colin na kuona tofauti yake na Mage. Siku zote Cecy alikuwa msichana mtiifu ambaye mwanzo alikuwa chaguo la mama yake baadaye alimgeuka baada ya kumuona Mage. Waliagana kila mmoja kukodi gari mpaka kwao.**** Mage baada ya kuachana Colin alijiendesha gari kwa kasi huku moyo ukimuuma kwa kitendo chake cha kikatili alichomfanyia mtu aliyeonesha mapenzi mazito kwake na aliyemkabidhi moyo wake mzimamzima kutokana na kumuamini. Aliyakumbuka maneno yaliyokuwa kwenye picha kubwa chumbani kwa Colin yaliyosema, moja lilisema: ASANTE MUNGU KWA KUNIPA MKE MWEMA na lingine MAGE NAKUPENZA ZAIDI YA KUPENDA.Mage alijikuta akilia na kufanya machozi kuziba macho, alisimamisha gari pembeni ya kuendelea kulia kilio cha kwikwi. Aliisikia sauti ya Colin ikisema: ““Mage uamuzi uliochukua ni kuupasua moyo wangu bila ganzi, naomba urudishe moyo nyuma, mpenzi wangu bora ungeninyang'anya kila kitu katika mwili wangu na kuniachia moyo wako ni muhimu kuliko chochote duniani japo nipo nawe kwa muda mfupi lakini nimekuzoea sana.”Sauti ile ilimfanya apaze sauti na kusema:“Colin nisamehe sana, najua jinsi gani nilivyokuumiza najuayajua mapenzi yanavyo jeruhi moyo wa mtu. Colin nisamehe sina jinsi nilikupenda lakini Hans ni pumzi zangu siwezi kuiacha nafasi adimu aliyonirudishia.”Mage aliongea kwa sauti kama anazungumza na Colin, alinamia usukani na kuendelea kulia. Uchungu ulimjaa moyoni kila alivyomfikilia Colin jinsi alivyokuwa akimbembeleza na kutokata tamaa ya kukubaliana na ukweli kwamba penzi limekwisha.Aliamini asingeweza kuendesha gari kwa hali aliyokuwa nayo kwani hata nguvu zilikuwa zimemuisha kwa ajili ya uchungu uliomjaa moyoni. Aliwaza kumpigia Brenda ili aje amchukue. Wazo lile hakukubaliana nalo kwa vile siku ile alitaka kwanza kuonana na Hans ili amweleze kilichojili ndipo aende nyumbani.Aliamua kumpigia Hans, alichukua simu ili ampigie ilibidi afute machozi kwanza kuziona ‘kiipadi’ .Alitafuta jina la Hans na kupiga, hakuita mara mbili ilipokewa upande wa pili.“Haloo.”“Hans,” Mage aliita.“Naam Mage vipi mpenzi?”“Upo wapi?”“Nipo Masaki.”“Naomba uje haraka.”“Nyumbani kwenu?”“Hapana nipo njiani karibia na njia panda ya Masaki.”“Mbona kama unalia?”“Hans njoo kwanza.”“Haya nakuja.”“Kodi bodaboda.”“Sawa.”Baada ya kukata simu aliitupia kwenye kiti cha pili na kujilaza kwenye kiti baada ya kukiteremsha kwa nyuma ili kumsubiri Hans.****Cecy baada ya kuachana na alikwenda hadi nyumbani kwao, baada ya kusalimiana na mama yake aliingia chumbani kwake na kujifungia chumbani kwake. Baada ya kuvua nguo zote alijifunga upande wa kanga na kujilaza chali kitandani na kuweka mikono nyuma ya kichwa na kutazama kwenye dali. Alitulia kwa muda na kuanza kuyakumbuka matukio yalitokea muda mfupi.Alijikuta akijilaumu kuingilia mambo yasiyo muhusu, kwani ule ulikuwa ugomvi wa wapendao, lakini kwa upande mwingine aliona kufanya vile ni kulipigania penzi lake. Aliamini ndoa ya Mage na Colin haitakupo na ile ndiyo ilikuwa nafasi yake kukipata alichokipoteza.Alijiuliza kama ndoa ile itavunjika nani atakuwa mke wa Colin, kwake aliona ana nafasi ndogo hasa baada ya mama Colin kumdharau kutokana na umaskini wake lazima angemtafuta mwanamke mwingine kutoka familia yenye uwezo. Bado alitaka kujua sababu ya Mage kuuvunja uchumba ambao ulibakia siku chache kufunga ndoa kanisani Moyoni alijiapiza kama ndoa ya Colin na Mage itavunjika basi ataipigania nafasi yake kwa nguvu zake zote. Mama yake alishangaa kumuona mwanaye yumo ndani muda mrefu, alipomfuata alikuta umefungwa. Aligonga mlango huku akiita.“Cecy mbona umeingia ndani mwaka mzima kuna usalama?”“Ndiyo mama.”“Hebu toka basi.”Cecy alitoka nje, mama yake macho yake hakucheza mbali na uso wa mwanaye na kugundua mabadiliko.“Cecy upo sawa?”“Ndiyo.”“Hapana kuna kitu kimekutokea, si kawaida yako kuingia ndani moja kwa moja bila kunitania na kizungu chako cha kuombea maji.”“Ni kweli mama kuna kitu kimenitoka kumenichanganya sana.”“Kitu gani?”Cecy alimweleza mama yake yote yaliyotokea wakati akitoka twisheni, mama yake alishtuka kusikia kampiga mchumba wa Colin.“Cecy kwa nini unatafuta balaa, unakumbuka mama Colin alituambia nini?”“Mama mimi sijavunja ndoa yao bali wenyewe mimi kiichoniudhi ni kashfa aliyokuwa akiitoa yule mwanamke.”“Colin kasemaje?”“Amesema amechanganyikiwa kwani maamuzi yalikuwa ya ghafla ila alisema atanitafuta.”“Mmh! Sawa, basi kaoge ule.”“Sawa mama.”Cecy alipitia ndoo ya maji na kuelekea bafuni kuoga na kumuacha mama yake akimtazama mwanaye na kutikisa kichwa aliamini vita ya mapenzi ni nzito kuliko ya kumsaka gaidi mapangoni.***Colin baada ya kuachana na Cecy na kukodi gari lililompeleka hadi kwao, aliteremkia nje ya geti na kuingia ndani kwa miguu. Mama yake alikuwa wa kwanza kumuona akiingia sebuleni, lakini uso wa mwanaye haukuonesha furaha kitu kilichomshtua na kuhoji.“Colin, baba vipi kwema utokapo?”“Kwema si kwema.”“Una maanisha nini?”“Nitakwambia naomba kwa sasa niache nikapumzike kwanza.”“Kuna nini? Mbona unanitisha?”“Mama naomba uniache kwanza.”“Mage yupo wapi?”“Sijui.”“Colin ni majibu gani hayo?” mama alishtuka majibu ya mwanaye.“Mama yangu nipo chini ya miguu yako naomba uniache kwanza.”“Mmh! Sawa.”Mama Colin aliachana na mwanaye aliyeelekea chumbani kwake, moyo wake ulimsukasuka alichukua simu kumpigia mama Mage kutaka kujua kuna nini kimetokea. Baadaya simu kuita kwa muda ilipokelewa upande wa pili.“Haloo dada.”“Za saa hizi?”“Nzuri, lete habari.”“Mage yupo hapo?”“Mmh! Toka atoke juzi sijamuona kwani vipi?”“Nimemuona Colin akirudi peke yake huku uso wake ukionesha kuna kitu si cha kawaida, nimemuuliza kuhusu Mage amesema hajui.”“Mmh! Lazima watakuwa wametibuana, sasa Mage yupo wapi?”“Hapo ndipo pananichanganya, nilipotaka kumchimba sana Colin ameniomba nimuache kwanza apumzike.”“Mmh! Lazima watakuwa wametibuana tu.”“Kwa hiyo hajafika?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/“Bado, akifika atanieleza tatizo, nitakujuza kila kitu.”“Sawa dada.”Mama Colin alikata simu, alipogeuka alimuona mwanaye amebeba vitu akitoka navyo nje, hakujua amebeba nini. Alisubiri muda ili akaone mwanaye amechukua nini na anapeleka wapi. Colin baada ya kuachana na mama yake alikwenda chumbani kwake, baada ya kufungua mlango wa chumba chake macho yake yalikutana na picha kubwa aliyoibandika muda mfupi kabla ya kuelekea Bagamoyo akiwa na Mage katika pozi zito la mahaba.Picha kubwa aliyoibandika ukutani ambayo mwanzo aliiona ni sehemu ya kuongeza furaha ya moyo wake. Lakini siku ile ilikuwa chukizo la moyo wake, alipanda kitandani bila kuvua viatu na kuibandua na kuitupa chini huku akiitemea mate. Alifungua kabati na kutoka picha zote alizopiga na baadhi ya nguo za Mage alizikusanya na kutoka nazo nje kwenda kujichoma moto.Alipofika nje alizikusanya sehemu moja na kuzimwagia mafuta ya taa na kuzitia moto, mama yake alitokea kwa nyuma yake. Alipotupa jicho aliona moja ya picha ya Mage ikiteketea na moto pia nguo za mkwewe mtarajiwa.“Colin! Unafanya nini?” alimuuliza kwa sauti mwanaye.Colin hakujibu kitu aligeuka kumtazama mama yake aliyekuwa ameshangaa mkono kiunoni.“Colin mwanangu una nini mbona unachoma picha na nguo za mchumba wako?” “Mama uliponichagulia mchumba ulifanya uchunguzi kwanza.”“Wa nini?”“Kama ana mpenzi anayempenda kuliko mimi.”“Mage hakuna na mpenzi, kwani nini unaniuliza hivyo?”“Ndiyo maana nikakuuliza ulifanya uchunguzi kabla ya kumchagua kuwa mkweo?”“Ndiyo, kwani vipi?”“Tulitaka kujenga nyumba kwenye kiwanja cha watu.”“Una maana gani?”“Mage ni mchumba wa mtu.”“Una maanisha nini kusema hivyo?” mama Colin alishtuka kusikia habari ile.Colin alimweleza yote yaliyojili Bagamoyo walipokaa siku tatu mpaka kumteremsha njiani na kumtupia mfuko wake. Lakini hakumweleza jinsi Cecy alivyo ingilia ugomvi ule na kipondo alichompa Mage. Mama yake alibakia macho yamemtoka kama kaona meli ikitembea barabarani. Alishusha pumzi nzito na kubakia akimuangalia mwanaye asipate la kusema.***Hans alifika na bodaboda sehemu aliloelekezwa na Mage, aliliona gari limepaki pembeni. Alimuomba dereva wa bodaboda amshushe, aliteremka na kumlipa hela yake na kuchepua mwendo hadi kwenye gari alilolikuta limefungwa vioo vyote. Aligonga kwenye kioo na kumfanya Mage anyanyue kichwa kuangalia, alimuona Hans alifungua mlango.Hans alishangaa kumkuta Mage macho yamemuiva kwa kulia.“Vipi mpenzi?” alishtuka kuiona hali ile.“Hans mpenzi umekuja?”“Ndiyo mpenzi wangu mbona unalia?”“Hans nimekaza moyo ili niumeze mfupa nisikupoteze mpenzi wangu.”“Una maanisha nini?”“Hii si sehemu sahihi ya mazungumzo, endesha gari tuondoke,” Mage alisema huku akihama kwenye usukani kumpisha Hans.“Mmh! Safari ya wapi, nyumbani?” alimuuliza huku akimtazama usoni.“Nyumbani siendi sasa hivi mpaka tumalizane na wewe.”“Sasa twende wapi?”“Sea Cliff hoteli.”“Hakuna tatizo.”Hans aligeuza gari na kuelekea Masaki, muda wote Mage alikuwa amejilaza kwenye siti baada ya kuilaza kwa nyuma. Hans alisimamisha gari kwenye maegesho ya Sea Cliff hoteli. “Bebi tumefika,” alimshtua Mage aliyekuwa amefumba macho. “Kachukua chumba kabisa,” Mage alijibu bila kufumbua macho. “Sawa.” Hans aliteremka na kwenda kulipia chumba kisha alirudi kumweleza Mage. “Tayari.” Aliteremka na kufunga gari lao kisha waliongozana hadi ndani ya chumba walichokikodi. Mage alipofika alijilaza kitandani macho alitazama juu mikono alilalia kwa nyuma. Pembeni ya macho yake michirizi ya machozi iliendelea kuteremka na kulowesha shuka. “Vipi bebi?” Hans alizidi alishtuka. “Hans sijui nikueleze nini uelewe najua jamii itanitenga kwa ajili ya uamuzi wangu wa kuvunja uchumba, wapo watakao niona sina akili lakini anayejua mapenzi ataniunga mkono. Nimekubali kubeba lawama zote za wanadamu lakini niufurahishe moyo wako. Sijui nitakaporudi nyumbani mama atanipokeaje naweza kutengwa na familia kwa uamuzi wangu huu.” “Kwani huyo jamaa umeisha mwambia ukweli?” “Siku tatu zilizokuwa naye Bagamoyo nilizitenga mahususi kwa ajili ya kumweleza taratibu kuuvunja uchumba wetu rasmi. Ningeweza kumwambia tu, lakini naheshimu mapenzi yake kwangu.” “Amepokeaje?” “Ilikuwa kazi kwelikweli jamaa alichachamaa mpaka kutishia kutoa mtu roho, siyo siri alikuwa amekufa kaoza nina wasiwasi akawa mwendawazimu au kuchukua uamuzi wa kujinyonga.” “Mi nafikiri mshale umerudi porini haujapotea, Mage nakuapia kwa Mungu kutoujutia uamuzi wako. Kama ulivyojitoa kwangu nami nitazishia mapenzi mara mia ya mwanzo. Nina amani ulikubali kuolewa kwa shinikizo, lakini moyo wako bado ulikuwa kwangu nami unaamini hivyo. “Hii ni nafasi nyingine ya kuidhihilishia dunia kuwa mimi na wewe tulizaliwa ili tuwe mwili mmoja. Mage nashukuru kuuponya moyo wangu uliokuwa na maumivu ya muda mrefu kulishwa nisicho kitaka, lakini kwa sasa nakula ninachokitaka.” “Hans naamini unanipenda zaidi ya kunipenda ndiyo sababu ya mimi kukubali kurudi kwako, wasiwasi wangu mkubwa ni familia yako. Hans nitakufa na mtu kila atakayetia mkono katika penzi letu sijali ni nani,” Mage alitoa mkwala mzito. “Mage nitalipigania penzi letu nakuahidi hakuna atakayeingilia penzi letu, nakuahidi mapenzi ya peponi. Nitayafuta machozi yako kwa kitambaa cha upendo,” Hans alisema huku akimfuta machozi kwa kiganja cha mkono. “Hans nimejilipua ukinitenda umenimaliza,” Mage alisema kwa sauti ya kilio huku akijitupia kifuani kwa Hans. “Nakuhakikishi na harusi yetu haitachukua muda mrefu.” “Kweli Hans?” alimuuliza huku akiyatoa macho yake yaliyojaa machozi kumtazama Hans. “Toka uliponitamkia matumaini ya kurudi kwangu nilikwenda mbali zaidi ya maandalizi ya ndoa yetu. Nilikuwa nasubiri kauli yako ili nikueleze hili.” “Wazazi wako je?” “Niliwaeleza wakasema hawawezi kunichagulia tena.” “Huoni kama ule wasiwasi wao juu ya kifo cha mkeo utazidi na mimi kuonekana ndiye muhusika?” Mage aliingiwa wasiwasi. “Nilijua hilo litatokea lakini nimewaeleza mimi ndiye niliyekufuata japokuwa wewe haukuwa tayari kurudiana na mimi hasa baada ya kukutosa kukuoa pia familia yangu kukuingiza kwenye matatizo. Nashukuru walinielewa.” “Mmh! Sawa, kwako umemaliza sijui kwangu mama atapokeaje.” “Atakuelewa kwa vile anajua penzi letu lilivyokuwa naamini moyo wake utafurahi kumpata mkwe sahihi.” “Mmh! Tutaona.” Walikwenda kuoga kisha walipata vinywaji na kufurahisha nafsi zao walipanga kuondoka pale saa sita usiku. **** Muda ulizidi kukatika bila Mage kuonekana kitu kilichozidi kumtia wasiwasi mama yake na kujiuliza atakuwa amepitia wapi. Mawazo yake yalimpeleka labda yupo kwa shoga yake Brenda. Lakini aliamini kama aliondoka nyumbani siku tatu zilizopita alitakiwa afike nyumbani kwanza ndipo aende kwa shoga yake. Alipiga simu ya Mage haikuwa hewani kitu kilichofanya azidi kuingiwa wasiwasi, aliamua kumpigia simu Brenda. Simu iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa na kushindwa kuelewa kuna nini ikiwa simu ya Mage haipatikani na simu ya shoga yake haipokelewi. Akiwa katika ya mawazo simu iliita aliichukua haraka na kupokea ilikuwa inatoka kwa Brenda. “Haloo mama.” “Brenda, kwema?’ “Kwema mama, samahani simu ilikuwa mbali kidogo nimekuta umepiga, unasemaje mama?” “Mage amefika huko?” “Sijamuona, kwani amerudi?” “Nasikia amerudi toka saa kumi na moja lakini mpaka sasa sijamuona na simu yake haipatikani.” “Umemuulizia shemeji Colin si ndiye aliyekuwa naye?” “Mmh! Ipo kazi.” “Kwa nini unasema hivyo?” “Basi ngoja nimpigie Colin alinieleze Mage kaenda wapi.” “Itakuwa vizuri.” Baada ya kukata simu, alimpigia Colin nayo haikuwa hewani kitu kilichozidi kumweka njia panda asijue nini kinaendelea aliamua kumpigia mama Colin simu iliyopokelewa. “Haloo shoga kuna habari gani maana mimi mwenyewe moyo hauna raha, toka Colin kafika kajifungua ndani kuna habari gani huko?” mama Colin alipokea na kuanza kumwaga maneno. “Dada mbona umezungumza mengi, huku mpaka muda huu Mage sijamuona wala simu yake haipatikani. Nimemuulizia kwa shoga yake hajafika, simu ya Colin haipatikani kuna nini katikati mbona sielewi, Colin yupo?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ “Ndiyo.” “Naomba kuzungumza naye.” “Sawa.” Mama Colin alimpelekea simu Colin aliyekuwa amejilaza akitafakari kilichotokea. Mpaka muda ule alikuwa akiona kama ndoto yenye ukweli. Alijiuliza maandalizi yote na matangazo ya sherehe ya kukata na shoka atafanya nini atawaeleza nini jamaa zake aliojitolea kusimamia sherehe ya harusi yao kwa gharama zao. Rafiki zake wa nje ya nchi aliosoma nao Ulaya nao alijiuliza atawaambia nini ikiwa tayari walikuwa wameshona suti kwa ajili ya sherehe ile na walikuwa tayari kuja nchini ikiwa pamoja na kukodi vyumba kwenye hoteli za nyota tano na malipo yalikuwa tayari. Kila alivyofikiria alikosa jibu, alitamani hata kumshawishi Mage akubali amuoe hata kwa mkataba wa mwezi mmoja ili jamaa zake wakiondoka waachane lakini wakiwa wamedhudhulia sherehe yake iliyopangwa kutekekeza mamilioni ya fedha. Pamoja na kuujua msimamo wa Mage bado aliamini kupitia wazazi wao anaweza kukubaliana nao. Lakini wazo la kuendelea kumbembeleza aliona kama kujidhalilisha, alikumbuka kitu. Alinyanyuka kitandani na kwenda kwenye kabati, kabla hajashika mlango uligongwa alipaza sauti ukuuliza. “Nani?” “Mimi,” ilikuwa sauti ya mama yake. “Naam mama, unasemaje?” ”Hebu fungua mlango.” Alirudi hadi mlangoni na kufungua mlango, alionekana amechoka sana kitu kilichozidi kumuumiza mama yake. “Mama Mage anataka kuzungumza na wewe.” “Kuhusu nini?” “Inasemekana toka ulipoachana naye hajarudi nyumbani na simu yake haipatikani, Colin mwanangu usiwe umemuacha wewe mtoto wa watu akaenda kujinyonga?” “Mama mimi na wewe tunataniana hasa katika jambo zito kama hili? Inaonekana tukiwa ndani ya uchumba Mage alikuwa na mpenzi wake. Ni wazi lilikuwa shinikizo toka kwa mama yake ili nimuoe lakini ukweli umejidhihili maji hayachanganyikani na mafuta.” “Hebu kwanza zungumza na mama Mage.” “Mama nitaongea naye nini?” “Ulichonieleza.” Colin alichukua simu ya mama yake ambayo ilikuwa wakati huo imekata na kupiga, baada ya muda ilipokelewa upande wa pili. “Haloo dada.” “Hapana ni mimi Colin.” “Ooh! Baba za siku mbili?” “Nzuri, shikamoo.” “Marahaba.” “Naam mama.” “Eti baba, mwenzio yupo wapi?” “Sijui,” alijibu kwa mkato. “Kwa nini unasema hujui wakati mlikuwa wote siku tatu.” “Mama, nimeachana na Mage baada ya kunifukuza ndani ya gari lake kama mbwa.” “Wee! Kwa sababu gani?” mama Mage alishtuka. “Ana mtu ambaye ndiye aliyemuingiza dunia ya mapenzi na kwa kunitamkia kuwa amevunja uchumba wetu. Kumbembeleza kwangu kumekuwa kero kwake na kuamua kuniteremsha njiani kisha kunitupia mzigo wangu huku akinitolea maneno ya dharau kuwa yupo mwanaume wa ndoto yake.” “Yupo wapi baba, yule mwanaume alimtenda.” “Basi ameamua kurudi huko.” “Sasa atakuwa amekwenda wapi?” “Si kwa mpenzi wake,”Colin alijibu kwa kifupi. “Lakini baba linazungumzika, mimi ndiye mzazi wake.” “Ni kweli wewe ndiye mzazi wake lakini moyo wa uamuzi ampende nani unabakia kwa Mage.” “Basi baba, niachie kazi hiyo.” “Wala usisumbuke mwachie uamuzi wake, mapenzi hayalazimishwi japo kaniweka katika wakati mgumu maishani mwangu.” “Baba…baba..naomba usifike huko nimekueleza niachie mimi naomba kuzungumza na mama yako.” Colin alimpa simu mama yake aliyekuwa amesimama pembeni yake akiwa amepigwa na bumbuwazi kutokana na kauli za mwanaye. “Haloo dada.” “Dada kwanza nisamehe sana kama kweli asemayo Colin ni kweli, yaani nilidhania utani kumbe kweli. Dada naomba uniachie suala hilo.” “Sawa, nikutakie usiku mwema.” *** Majira ya saa sita usiku Mage aliingia ndani ya sebule ya nyumbani kwao, alishangaa kumkuta mama yake yupo kwenye sofa akiwa amepitiwa usingizi. Alimsogelea na kumbusu shavuni kitu kilichomfanya mama yake ashtuke. Mbele yake alikuwa amesimama mwanaye Mage. Kabla ya kusema lolote aliangalia saa kubwa ya ukutani iliyomuonesha ni saa saba kasoro usiku. Hakuiamini aliangalia ya mkononi iliyokuwa sawa na ya ukutani, alimwangalia mwanaye kuanzia juu mpaka chini kama ndiyo siku yake ya kwanza kumuona kitu kilichomshtua Mage. “Vipi mama?” “Unatoka wapi?” mama yake alimuuliza kwa sauti kali huku akinyanyuka kwenye kochi. “Kwani vipi?” Mage alijifanya kushangaa. “Nijibu unatoka wapi muda huu?” “Niliporudi nilipita kwa shoga yangu.” “Nani?’ “Debora, humjui.” “Kufanya nini?” “Mama mbona maswali mengi?” “Kwa nini unanitia aibu, Colin umemfanya nini?” “Kama alivyokuambia kwa vile alichokueleza niliisha kueleza muda mrefu si kigeni kwako.” “Kwa hiyo umerudiana na Hans?” “Ndiyo mama ndiye chaguo la moyo wangu.” “Wewe si ulikuwa unasema humpendi tena na mapenzi yako yote kwa Colin?” “Mama ningempenda Colin kama Hans asingekuwepo, kama matatizo yangemtokea nimo ndani ya ndoa nisingeweza kutoka. Lakini amerudi kabla ya ndoa sina budi kumpokea, mama Hans nampenda zaidi ya kupenda nipo tayari kunioa bila mahari.” “Mage mwanangu nitaweka wapi sura yangu?” “Ukiwaogopa walimwengu huwezi kufanya jambo la kimaendeleo, watasema mwanzo lakini watanyamaza na kusahau.” “Mage mwanangu naomba ukalale ili kesho tuzungumze vizuri.” “Sawa mama.” Mage alikwenda kulala na kumuacha mama yake akiwa bado yupo sebuleni. *** Mama Colin usiku ulikuwa mkubwa kwake kila alivyojitahidi kulala usingizi ulikataa, aliamini kabisa Mage hana tatizo bali mwanaye ndiye aliyevunja uchumba na kusingizia Mage ana mwanaume mwingine anayempenda. Akili yake ilimpeleka kwa Cecy tu msichana aliyemuona ndiye tatizo kwa vile tokea awali aliona dalili mbaya. Alipanga kesho asubuhi kwenda kwa kina Mage ili aweze kuzungumza naye na akimwambia Colin ndiye aliyevunja uchumba basi bleki yake ya kwanza kwa Cecy na kukitia moto kibanda chao na kumfanyia kitu kibaya ambacho hata kisahau mpaka kufa kwake. Asubuhi alikuwa wa kwanza kufika mbele ya nyumba ya kina Mage na kipiga honi mbele ya geti. Baada ya kufunguliwa geti aliliingiza gari ndani na kwenda kupaki kwenye maegesho. Aliteremka na kuelekea ndani ambako ilionesha bado wamelala baada ya kumkuta msichana wa kazi akifanya usafi, alipomuona alimkaribisha: “Karibu mama.” “Asante, mama yupo wapi?” “Bado yupo chumbani kwake.” “Kamwite.” Msichana wa kazi alikwenda kumuamsha mama Mage, baada ya muda alitokea na kushtuka kumuona mzazi mwenzie asubuhi ile. “Karibu dada.” “Asante, mmeamkaje?” “Mmh! Tunamshukuru Mungu.” “Mage yupo?” “Yupo chumbani kwake.” “Ndiye kanileta asubuhi yote hii.” “Ngoja nikamwamshe.” “Sawa.” Mama Mage alikwenda chumbani kwa mwanaye na kumuamsha. “Vipi mama mbona asubuhi sana?” “Mama Colin anataka kuzungumza na wewe.” “Ha! Mbona asubuhi sana?” Mage alishtuka. “Kwani uliyofanya madogo?” “Mmh! Haya twende nikamuone.” Walitoka pamoja hadi sebuleni alipokuwa amekaa mama Colin. “Shikamoo mama,” Mage alimsalimia mama Colin. “Marahaba mwanangu, samahani kwa kukurupusha asubuhi.” “Bila samahani mama.” “Naomba tuzungumze kidogo.” “Hakuna tatizo.” “Na mimi niwepo?” mama Mage aliuliza. “Kwanza naomba tuzungumze wawili kisha tutazungumza wote.” Mama Mage aliondoka na kuwaacha mtu na mkwewe, baada ya kubaki wawili mama Colin alimuuliza Mage. “Mage mwanangu, kuna tatizo gani kati yako na mwenzako?” “Hakuna tatizo lolote.” “Mbona anasema kuwa eti wewe umevunja ndoa yenu, ni kweli?” “Ni kweli.” “Kama ni hivyo sasa mbona unasema hakuna tatizo?” “Ndiyo mama hakuna tatizo, ila ni kweli alichokisema Colin.” “Wewe na yeye nani kavunja uchumba wenu?” “Mimi.” “Kwa nini?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ “Mama kabla ya kuwa na Colin nilikuwa na mchumba wangu ambaye kipindi hicho akuwa ameoa. Lakini kabla ya ndoa, alipata matatizo ya kufiwa na mkewe na kurudi kwangu. Kwa vile ndiye aliyekuwa chaguo la moyo wangu aliporudi kuniomba niwe naye wala sikuhitaji ushauri nilimkubalia na ndiye nategemea ufunga naye ndoa na si Colin,” Mage alisema kwa kujiamini. “Mage, hebu kuwa mkweli naomba usinifiche, Colin amekufanya nini kilichopelekea kuchukua uamuzi huo?” “Kwa haki ya Mungu hajanifanya lolote baya.” “Hujamfumania na mwanamke?” “Walaa.” “Kwa nini unavunja ndoa yako? Mage nakuahidi kukupa chochote ukitakacho ili tu ukubali kufunga ndoa na Colin.” “Mama naomba kuwa mkweli wa moyo wangu, japokuwa bado mdogo mapenzi nayajua kwa vile yalinijeruhi. Ningeweza kuolewa na Colin jina lakini mapenzi yangu yangekuwa kwa Hans. Lakini siwezi kufanya kitu kama hicho sitaki kumtesa Colin bila sababu.” “Hans ndiye nani?” “Mwanaume wa ndoto yangu.” “Mmh! Nimekuelewa, basi Mage naomba ubadili uamuzi ili uolewe na Colin.” “Siwezi kuulazimisha moyo wangu, najua nawavunjia heshima, lakini nayaogopa maumivu ya moyo, niliumia sana wakati Hans ameoa. Kurudi kwake kwangu ni kutibu majeraha ya moyo wangu siwezi…siwezi kubadilika kwa vile nampenda sana Hans,” Mage alisema kwa sauti ya hisia kali. “Mmh!” mama Colin alishusha pumzi ndefu na kusema: “Nimekuelewa.” “Una la ziada?” Mage alimuuliza. “Mpaka hapo sina, nikuache upumzike.”ITAENDELEA.
0 comments:
Post a Comment