Karibu Katika Maktaba ya Simulizi, Riwaya, Chombezo na Hadithi Afrika Mashariki. %% Welcome to the Library of Stories, Novels, Comedy and Stories in East Africa.
BURE SERIES: https://bure0.blogspot.com/
IMEANDIKWA NA : ALLY MBETU 'DR AMBE'*********************************************************************************Simulizi : Wakili Wa MoyoSehemu Ya Kwanza (1) CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Maumivu ya moyo hayana msaidizi na moyo wa kupenda hauna subira, kilichojificha moyoni huwa sawa na mfungwa asiye na kosa lakini hajui kujitetea. Siku zote anayependa kama mhusika hajui kama anapendwa huwa mateso ya kujitakia. Cecilia msichana alinayetoka katika familia ya maskini anampenda Colin mvulana aliye katika familia ya kitajiri mwenye mchumba anayetaka kufunga naye ndoa. Anajikuta akiumia kila akimuona, pamoja na kuonekana jambo hilo kama maji kupanda mlima lakini msichana Cecy anauapia moyo wake kuwa atauwekea wakili na kuweza kushinda kesi ya maumivu ya mapenzi. Je, atafanikiwa? Kuyajua yote ungana tena na mtunzi mahiri katika hadithi tamu ya mapenzi ili upate uhondo mwanzo mwisho.TWENDE KAZI..... Mama Cecy alishangaa kumuona mwanaye amerudi mapema huku sinia likiwa limejaa ndizi, alimalizia kupuliza moto wa kuni kisha alitoka jikoni huku akifuta machozi kwa upande wa khanga kutokana na moshi wa kuni kumuingia machoni. Alimtazama binti yake aliyekuwa amekaa chini huku ameshika tamaa na machozi kumtoka.“Cecy nini tena mama?” alimuuliza huku akimsogelea.“Mama hata nashindwa kujielewa sijui ni kwa nini inakuwa hivi?” alisema huku akiondoka mkono shavuni bila kufuta machozi. “Una lingine au ni lilelile za siku zote?”“Kuna lingine lipi mama yangu! Hata sijui kwa nini nimejiingiza kwenye mateso ya kumpenda Colin mtu ambaye hayajui mapenzi yangu kwake.”“Lakini kwa nini mwanangu unapenda kuota ndoto za mchana, wewe na Colin wapi na wapi kama mbigu na ardhi.”“Najua mama utasema hivyo lakini katika mapenzi hakuna kitu kama hivyo, nakuapia kwa Mungu Colin atakuwa mume wangu wa ndoa.”“Cecy mwanangu hebu achana na kujishugulisha na masuala ya mapenzi, hebu jiangalie ulivyo na alivyo Colin. Kwanza mwenzako hand same.”“Hata mimi beutiful girl,” Cecy alijibu kwa kujiamini huku akinyanyuka na kujishika mkono kiunoni kujionesha kuwa ni mrembo.“Mwenzio ana elimu ya chuo kikuu wewe darasa la saba la kufeli, mwenzako anatoka kwenye familia ya kitajiri wewe pangu pakavu tia mchuzi. Kingine ambacho kinafanya usiweze kabisa kumpa ni kuwa Colin ana mchumba na mipango ya harusi ipo karibuni sasa huyo Colin yupi wa kukuona?”“Mama nina uhakika kwa asilimia mia Colin kunioa,” Cecy alisema kwa kujiamini.“Wee mtoto una wazimu? Au kuna mganga kakudanganya, maana siku hizi ushirikina hauna mtoto wala mzee.”“Mama katu mapenzi sitayaendelea kwa mganga, ila nitayapigania kwa nguvu zote.”“Kipi hasa kinakupa jeuri ya kusema hivyo?”“Ipo siku nitakwambia lakini amini ndoa ya Colin na Mage haipo ila mimi ndiye mke wake.”“He he he heee, usinichekeshe miye, kwa nini unasema hivyo?” mama Cecy alicheka mpaka machozi yakamtoka.“Mage hampenzi Colin.”“We umejuaje?”“Ni historia ndefu mama.”Cecy alianza kumhadithia mama yake sababu ya kuamini siku moja Colin atakuwa mpenzi japokuwa hajawahi kumtamkia kitu kama hicho hata siku moja.Alianza toka siku ya kwanza kumuona Colin, Mage msichana aliyetoka katika familia ya kimaskini elimu yake ya darasa la saba shuleni alikuwa mmoja wa wasichana waburuza mkia.Baada ya kufeli kwenye mtihani wa mwisho aliamua kufanya biashara ya ndizi kwa kupita mtaani kuuza. Japokuwa alikuwa maskini lakini alijipenda sana.Baada ya kuuza ndizi siku za mwanzo alinunua nguo nzuri ambazo alizivaa kila alipozunguka mkaani kuuza ndizi zake.Kitu kilichopelekea apendwe na wateja wengi kutokana na umaridadi wake na heshima kwa wote akiwemo mama Colin ambaye alikuwa mnunuzi wake mkubwa.Nyumba ya mama Colin ilikuwa ndiyo iliyokuwa ikinunua ndizi nyingi kitu kilichomfanya Cecy aongeze mtaji. Mama Colin alitokea kumpenda sana na kumwita mkwe.Siku moja alipitisha ndizi kama kawaida bila kujua kama nyumba ile ina kijana mzuri aliyekuwa nje amerudi baada ya kumaliza masomo yake. Baada ya kufika nje ya geti alibonyeza kengele na mlinzi alimfungulia mlango na kuingia ndani. “Mwambie mama mkwe leo nimeleta ndizi za ukweli,” alimwambia mlinzi aliyekuwa amemzoea sana.“Mamkweee,” Cecy alipaza sauti kama kawaida yake kila alipofika.Mara alitoka mama Colin akiwa katika muonekano wa mtoko.“Ha! Ma mkwe safari ya wapi tena?”“Nampeleka mchumba wako mjini.”“Muongo, yupo wapi?”“Yupo ndani anakuja.”“Amekuja lini?”Siku zote Cecy alipokuwa akipeleka ndizi alitaniwa na mama Colin kwa kuitwa mkwe japokuwa hakuwahi kumuona huyo mwanaume. Kila siku alikuwa na hamu ya kumuona japokuwa alikuwa akitaniwa.“Jana usiku na ndege.”“Waawooo,” Cecy aliruka juu kama anamfahamu.Ghafla alinyamaza baada ya kumuona mvulana mzuri tena mtanashati akitoka ndani. Alibakia kama kapigwa shoti ya umeme kwa jinsi alivyosimama kwa mshangao kidole mdomoni.“Colin umemuona mchumba wako niliyekuandalia?” mama Colin alitania.“Nimemuona mzuri tena mrembo,” Colin alisema huku akimtazama Cecy aliyekuwa bado amesimama.“Cecy umemuona Colin?”“Ndi..ndi..yo,” Cecy alipatwa na aibu na kushindwa kuzungumza.“Sasa mkwe, msichana wa kazi atachukua ndizi sisi tuna safari ya mjini.”“Sawa mkwe.”Mama Colin alifungua pochi na kutoa noti ya elfu tano na kumpatia Cecy, wakati huo Colin alikuwa akilisimamisha gari pembeni ya mama yake. Mama Colin alifungua mlango wa gari wa nyuma na kuingia. “Bai mchumba,” Colin alimuaga Cecy aliyekuwa ameingiwa aibu.“Bai,” Cecy alisema huku akiangalia pembeni kwa aibu.Geti lilifunguliwa na gari lilitoka nje kuelekea mjini na kumuacha Cecy akitoa ndizi kwa msichana wa kazi kisha alitoka na kuendelea kufanya biashara kama kawaida.****Safari ya mama Colin na mwanaye ilikuwa kwenda nyumbani kwao Mage msichana aliyemchagua kuwa mke wa mwanaye. Alimuona siku moja alipokuwa na mama yake walipokutana na shoga yake Super Market, wakati akiwa katika manunuzi ya bidhaa muhimu.“Ha! Shoga za siku?” Mama Colin alimsemesha mama Mage.“Nzuri shoga, za kupotezana?”“Mmh! Nzuri, vipi Colin bado hajarudi?”“Anarudi mwezi kesho mwishoni.”“Shikamoo,” Mage alimwamkia mama Colin.“Marahaba, hujambo mama?”“Sijambo.”“Monika, binti yako?” mama Colin alimuuliza shoga yake.“Ndiyo amemaliza chuo kikuu Mlimani anasubiri ajira.”“Nimempenda sana, unafaa kuwa mke wa Colin.”“Tena wataendana wasomi kwa wasomi,” mama Mage aliunga mkono.“Anaitwa nani?”“Mage,” Mage alijibu mwenyewe.Tokea siku ile wakawa wakiwasiliana hata kutembelea huku wakisubiri muda wa Colin kurudi toka masomoni ili wapange mipango ya ndoa. Mama Colin alimpenda sana Mage kwa umbile lake nzuri na heshima aliyoionesha siku zote kwake. Naye mama Mage alifurahi mwanaye kuolewa na Colin kutokana na kumfahamu vizuri.Siku Colin aliyofika hakutaka kuwajulisha, kesho yake alimpeleka nyumbani kwao Mage bila taarifa ili wafanye surprise. Familia ya kina Mage ilikuwa ikikaa Kigamboni walikwenda hadi kwao na kupiga honi nje ya geti. Wakati wote huo Colin alikuwa hajui anakwenda wapi.Baada ya geti kufunguliwa Colin aliliingiza gari ndani na kwenda kulipaki kwenye maegesho. Mama Mage alitoka nje baada ya kusikia gari likingia ndani na kujiuliza nani amekwenda kwake bila taarifa. Alishtuka kumuona mama Colin akiteremka kwenye gari.“Waawooo jamani, ha! Colin siamini jamani karibu mwanangu,” alikuwa akimfuata mama Colin kumkumbatia lakini aligeuza baada ya kumuona Colin na kwenda kumkumbatia.Colin alijikuta akishangaa baada ya kuteremka kwenye gari na kujiuliza pale ni wapi na yule aliye mfurahia na kumkumatia ni nani.“Asante, shikamoo.”“ Marahaba karibu sana mwanangu,” mama Mage alisema kwa furaha huku amemshika mabegani Colin na kumtazama.Aliwapokea wageni na kuingia nao ndani kwenye sebuleni, baada ya kukaa alimwita Mage kwa sauti kubwa.“Mageee.”“Abee mama,” sauti ya Mage ilitoka chumbani.“ Njoo mara moja.”“Nakuja.”Mage alikuja mbio bila kujua anaitiwa nini, alipofika alishtuka kumuona mama Colin.“Ha! Mama mkwe.”“Nimejaa tele,” mama Colin alijibu kwa tabasamu pana.“Shikamoo.”“Marahaba.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/“Mambo?” Mage alimsabahi Colin bila kumjua.“Poa za hapa?”“Nzuri,” Mage alijibu huku akishtuka na kujiuliza yule kama ndiye Colin, ili kupata uhakika aliomba msamaha na kutoka mara moja.“Jamani samahanini nakuja mara moja.”“Bila samahani,” alijibu mama Colin.Alichepua mwendo na kwenda upande wa vyumba huku akimwambia mama yake.“Mama njoo mara moja.”“Jamani samahanini nakuja mara moja.”“Hakuna tatizo,” mama Colin alijibu.Baada ya mama Mage kuondoka kumufuata mwanaye, mama Colin alimsemesha mwanaye kwa sauti ya chini.“Mchumba unamuonaje?”“Yupo vizuri.”“Umempenda?”“Sana.”“Nimefurahi kuona chaguo langu amelikubali.”“Mama wee kiboko unajua kuchagua.”Mama Mage baada ya kufika kwa mwanaye aliyekuwa amesimama upande wa vyumba.“Vipi?” alimuuliza mwanaye.“Safi, eti mama yule si Colin?”“Ndiyo.”“Mamaaa! Kwa nini hukuniambia mapema nijiandae anaweza kuniona sijipendi.”“Walaa mbona umependeza, vipi umempenda?”“Ndiyo,” Mage alikubali huku akinyanyua kichwa.“Basi turudi.”“Naona aibu ngoja nikaoge na kubadili nguo.”Mama Mage aliwarudia wageni wake ili kuwapatia kinywaji kabla ya kuanza mazungumzo.Mage msichana mwenye elimu ya chuo aliyekuwa na shahada ya Uhusiano, baada ya kuachana na mama yake alikwenda chumbani kwake ili kujiandaa kuonana na wageni. Kwanza alikwenda kuoga kisha alibadili nguo ambayo aliamini ni sahihi kwa ajili ya kumpokea mgeni wake.Alijipulizia manukato ya bei mbaya aliyonunuliwa na baba yake alipokwenda Ufaransa kikazi. Alisimama mbele ya kioo kikubwa cha ndani na kujitazama kisha kujigeuza kila pembe. Baada ya kuridhika na gauni alilovaa alikisogelea kioo na kujitazama jinsi Mungu alivyomuumba kwa uzani unaolingana, alijikuta akitokwa machozi ( siri ya machozi yake soma katika muendelezo wa hadithi hii.)Aligundua kuna mapungufu kichwani mwake, alikwenda mpaka kwenye dresing table na kukaa kwenye kiti kidogo kisha alivuta droo na kutoa wanja. Alipaka wanja mwembamba ulioongeza uzuri wa sura yake.Alichukua heleni ndogo na kuvaa kisha alichukua cheni yake ndogo ya dhahabu na kuivaa, kidani chenye jila lake kilikaa kwenye mfereji ya matiti yaliyojaa na kumfanya apendeze zaidi. Mage aliamini mpaka pale alikuwa amekamilika kwenda mbele ya wageni wake ambao walikuja mahususi kwa ajili yake. Alikwenda kwenye kabati na kutoa kiatu cha kisigino kifupi cha rangi ya machungwa kilichoendana na linda la chini la gauni lake alilovaa lenye mchanganyiko wa rangi nyeusi na weupe kwa mbali.Hakika Mage alikuwa amependeza kama malkia aliyekuwa tayari kuonana na mfalme. Alitembea kwa madaha toka chumbani kwake kuelekea sebuleni palipokuwa na wageni.Harufu ya manukato yake yalitangulia kabla yake. Colin na mama yake waligeuza macho kuangalia upande wa chumba na kukutana na Mage aliyetokeza akiwa amependeza mara dufu na awali alivyokuwa.Moyo wa Colin alipasuka vipande na kuwa hoi taabani kwa uzuri wa Mage msichana chaguo la mama yake. Alijikuta akijiuliza hali ile mama yake ni mwanamke amejua kuchagua binti mrembo kama yule, je, angekuwa mwanaume angekuwa na uwezo gani wa kuchangua wanawake warembo.Mama Colin alitulia kama mtu aliyepigwa na shoti ya umeme hata kukapua macho alishindwa kutokana na uzuri wa Mage mkwewe mtalajiwa.“Wageni karibu sana huyu mnayemuona ndiye Magreth halisi.”“Asante, tunashukuru kukutambua,” Colin alijitahidi kuitikia japo mwili ulipoteza ujasiri wa kiume baada ya kuingiwa baridi la mshtuko.“Mama zangu samahanini namuomba mgeni wangu,” Mage alisema huku akisogea kwa Colin na kumshika mkono.Colin alinyanyuka na kukiacha kinywaji chake juu ya meza ndogo, lakini Mage alikichukua na kukishika mkono wa kushoto huku wa kulia akimshika mkono Colin na kuondoka naye kuelekea nyuma ya nyumba kwenye bustani.Walivyokuwa wakitembea wazazi wao waliwasindikiza kwa macho mpaka walivyopotea kwenye macho yao. Waligeuka na kutazamana kisha walitabasamu.“Yaani walivyopendeza nilitamani leo ndiyo iwe siku ya sendoff ya mwanangu,” mama Mage alisema kwa hisia kali.“Kila kitu kina wakati wake, kilichonifurahisha mimi jinsi walivyoonekana kupenda. Wasiwasi wangu huenda Mage asingempenda Colin.”“Isingekuwa rahisi, Colin ni mmoja wa vijana wazuri ambao Mungu kawajalia. Nitajivunia kuwa na mkwe kama yeye, nitatembea kifua mbele.”Upande wa pili Mage alimpeleka Colin mpaka kwenye bustani.“Karibu kwenye kiti mgeni wangu,” Mage alimkaribisha kwenye kiti cha uvivu na meza ndogo katikati ya kuwekea vinywaji. Mage kabla ya kukaa alikumbuka amesahau kinywaji chake.“Sorry Colin nakuja nimesahau kinywaji changu,” Mage alisema huku akigeuka ili arudi ndani.“Mage,” Colin alimwita Mage aliyeanza kwenda ndani.“Abee,” Mage alitikia huku akigeuka kumsikiliza Colin.“Kinywaji hiki kinatutosha.”“Mbona kidogo hakitutoshi.”“Kinatutosha, kwangu wewe ni zaidi ya kinywaji.”“Colin nimefurahi kufahamu hilo.”Mage alirudi na kukaa pembeni ya Colin, baada ya kukaa Colin alibeba glasi iliyokuwa na kinywaji na kumnywesha Mage ambaye alisogeza mdomo kuipokea.Baada ya kumeza funda ya juisi alimumunya midomo yake mipana na kusema:“Colin, leo ni siku yetu ya kwanza kuonana lakini umenifanya nikuone mwenyeji katika moyo wangu. Nasikia fahari kuwa mkeo,” Mage huku akimtazama kwa macho yake makubwa kidogo yaliongezwa uzuri na wanja aliojipaka.“Nashukuru kwa hilo,” Colin alijibu huku akiachia tabasamu pana.“Lakini nina wasiwasi mmoja ambao umekuwa ikisumbua mawazo yangu na kuukosesha amani moyo wangu,” Mage alisema huku uso wake ukionesha uzuni.“Wasiwasi wa nini Mage?” Colin aliuliza huku akijiweka vizuri kitini na kuiweka glasi ya juisi juu meza kisha alipeleka mkono kwenye nywele fupi za kipilipili na kuzichezea kitu kilichofanya Mage mwili umsisimke.“Najua ndiyo siku yako ya kwanza kuniona, siamini kama Colin unanipenda kama ninavyokupenda?”“Mage toka nilipoelezwa nimepatiwa mchumba moyo wangu ulikuwa taabuni kutaka kukuona. Nilikuumba akilini kwa kila umbile na kukupamba kwa rangi nyingi.“Amini Mage kila nilichokiwaza moyoni mwangu kilikuwa uongo. Nilichokiona ni zaidi ya vyote nilivyoviwaza,” Colin alisema huku amemshika mabegani Mage na kumtazama usoni kwa jicho la huruma. “Vitu gani hivyo Colin?” Mage aliuliza huku akijitahidi kuyatoa macho nje kama anaweza kuyaona maneno kwa macho.“Kila umbile na sura niliyoiwaza ambayo niliamini huenda moja wapo litakuwa yako imekuwa kinyume kabisa.”“Mmh! Colin, kwa nini?”“ Mage we ni mzuri wa wazuri mrembo wa warembo. Najiona kiumbe mwenye bahati kama nitakuwa mume wako,” Colin alisema akiwa ameyakaza macho kuonesha anachokizungumza hatanii. “Siamini, Colin siamini,” Mage alisema mikono ameshika kifuani huku machozi yalinitoka.“Mage huamini nini?”“Inawezekana Colin unalitamani umbile langu lakini si mapenzi ya dhati toka moyoni mwako,” Mage alisema huku machozi yakimtoka na kuweka michirizi kwenye mashavu.“Mage amini nakupenda kama ugonjwa wa shinikizo la damu linavyochukuwa uhai wa mtu ghafla.”“Colin sijui wewe ni mwanaume wa aina gani,” Mage alijisema huku akijitahidi kutengeneza tabasamu ndani ya machozi.“Kwa nini mpenzi?”“Maneno yako yamekuwa na sumaku yenye nguvu ya ajabu kuweza kunasa chuma kilichomo moyoni mwangu.”“Sijakuelewa mpenzi.”“Ameweza kuuteka moyo wangu na kukubali kuwa mateka wako. Colin nakuamini, usiniache katikati ya bahari nitakufa maji boya langu ni wewe. Maumivu ya mapenzi ni zaidi ya kung’olewa jino bila ganzi.”“Amini Mage nakuahidi kuwa mume mwema.”“Nami nakuahidi kuwa mke mwema.”Baada ya hapo mazungumzo yaliendelea kila mmoja kuitaka kumjua mwenzake kiundani mpaka muda ulipofika wa kuondoka.Colin akiwa mtu mwenye furaha na mama yake waliondoka na kuwaacha Mage na mama yake nje baada ya kuwasindikiza wageni. Walirudi ndani mtu na mama yake wakishikana mikono.Walipoingia ndani Mage alimuuza swali mama yake.“Mama, kweli Colin atanioa?” alimuuliza huku akimkazia macho.“Mbona umeniuliza hivyo, kwani mmezungumza nini?”“Amenihakikishia atanioa.”“Sasa wasiwasi wako nini?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/“Mama anaweza kuwa na mwanamke mwingine na kuniacha njia panda kama alivyofanya Hans. Najiona nimefanya haraka sana kumkubali Colin bila kujua historia yake. Safari hii sitakubali kuumizwa mara mbili lazima nitanyongwa tu,” Mage alisema kwa hisia kali.“Kwa hiyo ukigundua Colin ana mwanamke mwingine utamuua?”“Siwezi kumuua Colin bali mwanamke wake.”“Lakini Hans alikuwa akikupenda tatizo wazazi wake ndiyo waliomchagulia mwanamke mwingine.”“Mama, Hans hakuwa ananipenda ni muongo mkubwa.”“Kwa nini?”“Alisema anamuoa yule mwanamke hatakaanaye atamuacha, mwezi jana nilimekutana na yule mwanamke akiwa mjamzito.”“Ndiyo basi tena, nawe umepata wako tena kijana mzuri msomi mwenzako.”“Mama bado inaniuma sana, niliutoa mwili wangu kwa Hans kwa kujua ndiye atakaye kuwa mume wangu. Mama sijui mwanaume yeyote zaidi ya Hans, nilijitunza kwa ajili yake matokeo yake alinidanganya ataachana na yule mwanamke aliyelazimishwa kuoa.“Nilimuamini lakini mwezi ulioisha nilijikuta nikimchukia Hans baada ya kumuona yule mwanamke mjamzito. Imeniuma sana mama nakuahidi sitamsamehe Hans na sitakubali kuchezewa tena na Colin nitakufa mimi au yeye,” Mage alibadili uzuri wake wote ulipotea alikuwa kama akipigana na mtu.“Mage mwanangu, ya Hans tuliyazungumza tukayamaliza.”“Mama hujui kiasi gani nilivyoumizwa na Hans kuoa, lakini alinituliza na kusema kuwa ataachana na mpenzi wake ili anioe. Lakini nilichokiona niliwaza mbali sana mama.“Leo nakupa siri niliyoificha moyoni, siku niliyokutana na mke wa Hans mjamzito, nilinunua vidonge na pombe kali ambavyo nilipanga kunywa usiku ili asubuhi ukiamka ukute mzoga.“Usiku ulipoingia niliandaa vitu vyote kwa ajili ya kuutoa uhai wangu, kabla ya kufanya tendo lile nilikumbuka kauli ya profesa mmoja wakati tupo chuoni, kuwa thamani yangu haipo kwa mtu mmoja bali ya ulimwengu mzima kwa hiyo nisipoteze uhai wangu kwa kosa la makusudi bali niitazame thamani yangu mbele ya jamii.“Mama nililia sana na kuchukua vitu vyote na kwenda kuvitupa. Huwezi kuamini nimchukia Hans kama kifo. Ujio wa Colin umenishtua na kuona kama maumivu mengine yanakuja.”“Mage mwanangu naiamini familia ya kina Colin, uzuri mama yake kakuchagua.”“Mamaa! Ngoja tuone.”Mage alisema huku akielekea chumbani kwake. ***Cecy baada ya kufanya biashara yake ambayo iliisha mapema na kurudi nyumbani akiwa mwenye furaha. Mama yake alijua furaha ile ni kwa ajili kumaliza bishara mapema kumbe sivyo. Usiku ulipoingia aliwahi kula, baada ya kuoga alipanda kitandani mapema. Kitendo kile kilimshtua mama yake na kuamini mwanaye labda anaumwa. Mama Cecy baada ya kumaliza kazi zake alimfuata mwanaye chumbani aliyekuwa amejilaza chali mikono ameilalia kwa nyuma.Mpaka anaingia chumbani Cecy alikuwa ametulia macho kayaelekeza juu. Mama yake alitulia akimuangalia na kumuona mwanaye yupo katika lindi la mawazo jambo ambalo halikuwa kawaida kuliona kwa mwanaye. Baada ya muda alimuona akitabasamu na kujikuta akitazama juu labda kuna kitu mwanaye anakitazama na kumfurahisha, lakini hakuona kitu. Alijiuliza kipi kilichomfanya mwanaye awahi kitandani kisha kutulia akitazama juu na kutabasamu.Baada ya kutabasamu alimuona alishika mikono kifuani na kusema kwa sauti ya chini ambayo mama yake aliisikia.“Cecy mimi,mmh! Sijui?”Baada ya kusema vile aligeukia ukutani na kumpa mgongo mama yake aliyekuwa amesimama mlangoni bila kumuona. “Cecy..Cecy,” mama yake alimwita.“A..a..bee,” Cecy aliitikia huku akigeuka kumtazama mama yake na kumshangaa kumuona amesimama mlangoni.“Vipi mama?” alimuuliza bila kunyanyuka zaidi ya kujigeuza.“Unajua leo sikuelewi kabisa.”“Kivipi?” Cecy alijibu huku akikaa kitako.“Umewahi kupanda kitandani si kawaida yako, nimefika muda nimekuona akitazama juu na kutabasamu peke yako. Kisha unazungumza peke yako una nini leo mwanangu?”“Mama nipo kawaida, siku azilingani.”“Kipi kilichokupa furaha leo.”“Mama nawaza kama siku moja nitaolewa na mwanaume mzuuuri mwenye uwezo tena mwenye mapenzi ya dhati nitafurahi sana.”“Utapata tu mwanangu, Mungu nawezi kutunyima vyote.” “Asante mama yangu kunipa moyo.”“Lakini huna tatizo lolote?”“Sina mama yangu.”“Haya mwanangu usiku mwema.”“Na wewe pia mama yangu.”Mama Cecy aliondoka na kurudi chumbani kwake kulala na kumuacha mwanaye akirudi kujilaza kama mwanzo macho yake yakiangalia juu.Alijikuta akikumbuka kauli ya mama Colin baada ya kutoka ndani, mwanaume mzuri ambaye alikuwa na kila sababu ya kujivunia kama akiwa mumewe au mpenzi wake.Alikumbuka jinsi alivyoshtuka baada ya kumuona Colin. Kauli ya mama Colin ilijirudia kichwani mwake. “Colin umemuona mchumba wako niliyekuandalia?” “Nimemuona mzuri.”“Cecy umemuona Colin?”“Ndi..ndi..yo,” Cecy alikumbuka alipipata kigugumizi na kuugua ugonjwa wa mapenzi ghafla.“Sasa mkwe, msichana wa kazi atachukua ndizi sisi tuna safari ya mjini.”“Sawa mkwe.”Cecy alijiuliza kauli ile ya mama Colin ilikuwa na ukweli gani kutokana na kuona kuolewa na Colin sawa na ngamia kupita kwenye tundu la sindano.“Mbona sielewi, kweli Colin atanioa au ananitania, mbona hakukataa mbele ya mama yake, na kwa nini mama yake aendelee kuniita mkwe?”Cecy alijiuliza bila kupata jibu la moja kwa moja. Lakini wasiwasi wake ikawa kwenye hali zao yeye muuza ndizi anazurura mitaani na mwenzake mtoto wa kitajiri.“Watakuwa wananitania,” alisema kwa sauti ya kakata tamaa na kugeukia ukutani kuutafuta usingizi.Usiku ulikuwa mrefu kwake baada ya kushtuka katikati ya usiku kutokana na ndoto aliyoota akiwa na Colin ndani ya gari yeye akiwa anafundishwa na baada ya hapo walikwenda ufukweni kupumzika. Wakiwa wamejilaza ufukweni Cecy alitembeza mikono yake kwenye kifua cha Colin kilichojaa kimazoezi na vinyweleo vingi ‘garden love.’ Upepo mwanana wa bahari uliwapepea.Aliposhtuka alijikuta yupo kitandani peke yake, mapigo ya moyo yalimwenda mbio na kijacho chembamba kilimtoka. Alikaa kitandani na kujiuliza ndoto ile ina maana gani. Aliwasha taa na kukaa kitandani mkono shavuni akijitahidi kujua ndoto ile ilikuwa na maana gani. Mama yake aliyeshtuka usingizi alishtuka kuona taa inawaka, alijiuliza usiku ule Cecy alikuwa akifanya nini.Alinyanyuka taratibu na kwenda chumbani kwa mwanaye. Kwa vile chumbani hakikuwa na mlango zaidi ya pazia la kitenge kichakavu. Alipofika alifunua taratibu na kuangalia ndani.Alimkuta mwanaye amekaa kitandani mkono shavuni. Alitulia kwa muda bila kumsemesha na kutaka kujua mwisho wake nini. Baada ya muda kidogo Cecy alizima taa na kujilaza kitandani.Mama yake aliendelea kusimama mlangoni kwa muda huku akiwa na maswahi na hali ya mwanaye toka jana yake. Aliamua kurudi chumbani kwake na kupanga kumuuliza siku ya pili kwa kumbana sana ili ajue sababu ya mwanaye kuwa katika hali ile ambayo kwake ilikuwa ngeni. ***Colin akiwa chumbani kwake amejilaza kitandani aliukumbuka uzuri wa Mage msichana aliyeonekana mwelewa lakini mwenye jeraha la mapenzi. Sifa zake za elimu ya juu pia urembo na ucheshi ni vitu vilivyomteka kimwili na kiamili.Moyoni alijiapiza kumpenda Mage kwa moyo wake wote, aliiona familia bora mbele yake yeye akiwa baba, Mage mama na watoto wao wawili wa kike na kiume.Siku zote alipanga kuzaa watoto wachache ambao angewamudu kuwahudumia kimalazi na elimu. Hakupenda kuwa na familia kubwa japokuwa wao walizaliwa sita, lakini yeye alitaka watoto wawili wakizidi basi wanne.Alitaka ndoa yake ifanyike haraka ili kujipanga kwa maisha mapya. Wazo lake la kuanzisha kampuni aliliona litakwenda zuri kama Mage mwanamke mwenye Shahada ya uhusiano akiwa mkewe ambaye ingesaidia kampuni yao kukua na kutanuka.Moyoni alimshukuru mama yake kuwa na jicho la tatu kumtafutia mwanamke ambaye hakuwa tofauti na samaki anayekaa kwenye maji marefu bila kuwa na chombo madhubuti huwezi kumpata.Alijikuta akiyakumbuka maneno mawili ya Mage ambayo yaliuumiza moyo wake na kuamini ana deni kubwa kwa msichana yule: “Inawezekana Colin unalitamani umbile langu lakini si mapenzi ya dhati toka moyoni mwako,” Mage alisema huku machozi yakimtoka na kuweka michirizi kwenye mashavu.Baada ya kumuhakikishia anampenda mapenzi ya dhati alimpa mtihani ambao Colin aliamini anauweza kwa vile hakuwa mwanaume kigeugeu.“ Colin umeweza kuuteka moyo wangu na kukubali kuwa mateka wako. Colin nakuamini, usiniache katikati ya bahari nitakufa maji boya langu ni wewe. Maumivu ya mapenzi ni zaidi ya kung’olewa jino bila ganzi.”Baada ya kuyakumbuka maneno ya Mage, Colin alijiapiza kuwa tiba ya maumivu aliyoyapata siku za nyuma. Aliamini maumivu yale yalikuwa na sababu ya kuwakutanisha ili wajenge familia bora. Usingizi mororo ulimpitia Colin huku akitabasamu. *** Asubuhi Cecy aliamka kama kawaida na kwenda kwenye gulio kununua ndizi za kuuza. Mama yake aliposhtuka alikuta ameishatoka muda. Baada ya kupata alirudi nyumbani na kuzipanga kwenye beseni kisha alikwenda kuoga na kutafuta nguo nzuri ambayo aliiteua kwa ajili ya kanisani tu.Hakutoka kama siku nyingine anazokwenda kwenye biashara, alitumia muda mwingi kujipamba zaidi ya siku ya jumapili akienda kanisani. Baada ya kuhakikisha amependeza sana alitoka kwa ajili ya kwenda kuuza ndizi. Mama yake alishtuka kumuona mwanaye kwenye hali ile aliingiwa wasiwasi labda mwanaye ana safari nyingine si kwenda kufanya biashara.“Cecy safari ya wapi?”“Kwenye biashara mama.”“Kwenye biashara! Ndiyo uvae vizuri hivi?”“Basi tu leo nimeamua.”“Si kweli toka jana sikuelewi kabisa, sasa nimeanza kupata mwanga.”“Mwanga gani mama?” Cecy alishtuka.“Si bure lazima utakuwa umepata mwanaume, Cecy angalia mwanangu, we bado mdogo usijishughulishe na wanaume mwisho wake mbaya.”“Mamaaa!” Cecy alimshangaa mama yake.“Unashangaa nini, ndiyo maana eti unatamani kuolewa kumbe una mwanaume,” mama Cecy alizungumza ameshika pua.“Maama...mama kwa nini unanihukumu bila kosa?” Cecy alimlalamikia mama yake.“Huna kosa, haya endelea ukiniletea tumbo hapa utatafuta mbereko ya kunibebea.”“Mama yangu sijawaza kufanya hivyo, japokuwa nami napenda siku moja niolewe na mwanaume mwenye mapenzi ya dhati si kuanza mapenzi kihuni.”“Haya kipi kilichokufanya nguo ya kanisani kwenda kuuzia ndizi na kujipamba kupita kiasi?”“Mama nikueleze mara ngapi siku hazilingani.”“Mmh! Haya biashara njema.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/“Asante mama.”Cecy alibeba ndizi zake na kuelekea kwenye bishara zake, hakutaka kupita popote mpaka kwa mama Colin ndipo alipopanga kuanzia biashara yake kwa siku ile. Alipofika kama kawaida alibofya kengele na mlinzi alimfungulia.“Ha! Cecy mbona umependeza hivyo?” mlinzi alimshangaa Cecy.“Mbona kawaida yangu,” Cecy alisema huku akiingia ndani ya geti, aliweka ndizi chini na kumwita mama Colin kwa sauti ya juu.“Mamkweee nimeisha fika.”Colin ndiye aliyetoka kufuata ndizi kutokana na wasichana wa kazi kuwa na majukumu mengine. Macho yake yalishtuka kumuona Cecy.“Ha! Mchumba ni wewe?”“Ndiyo mpe...,” Cecy hakumalizia aliingia kigugumizi.“Karibu sana.”“Asante.”Colin alinunua ndizi na kumlipa fedha yake.“Mama mkwe yupo wapi?”“Anatoka sasa hivi.”Mara alitoka mama Colin, Cecy baada ya kumuona alimsalimia kwa kuchuchumaa chini kuonesha heshima.“Shikamoo mkwe.”“Marahaba mkwe wangu hujambo?”“Sijambo.”“Nyumbani?”“Wanakusalimia.”“Mkwe una safari nyingine?” mama Colin aliuliza Cecy.“Kwa nini mama mkwe?”“Umependeza sana.”“Hapana nipo kwenye biashara, mwanamke kujipenda bwana,” Cecy alisema kwa pozi.“Hongera, nina wasiwasi mwanangu anaweza kuibiwa.”“Walaa,Colin mpenzi nipo kwa ajili yako na wewe ndiye itakuwa mwanaume wangu wa kwanza.”“Muongo! Usimdanganye mwanangu,” mama Colin alisema.“Kweli mamkwe.”“Mchumba umenifuhisha sana, kesho ukija nitakupa zawadi,”Colin alisema.“Zawadi gani?”“Utaiona hiyo kesho.”“Mmh! Asante.”“Unakubali tu, hujui zawadi gani?” mama Colin alitania.“Yoyote atakayonipa, zawadi haipangwi.”Baada ya manunuzi Cecy aliondoka kuendelea na biashara zake. Colin na mama yake walirudi ndani, baada ya kuweka ndizi jikoni alirudi sebuleni alipokuwa amekaa mama yake.Alipofika alikaa pembeni ya mama yake aliyekuwa yupo bize na simu. Baada ya kuachana na simu Colin alimuuliza mama yake.“Mama unajua Cecy ni mzuri?”“Ni kweli mwanangu, Cecy ni binti yule mzuri sana,” mama yake alimuunga mkono.“Tena anajipenda, ana tofauti na wasichana wengi wanaofanya biashara kama yake. Hali hii anauza ndizi yupo vile akifanya kazi za ofisini itakuwaje?” Colin alisema huku akitazama mama yake aliyejenga tabasamu kutokana na maneno ya mwanaye.“Ni kweli, ndicho kitu kilichonifanya nipende kununua biashara yake. Toka nimfahamu sijawahi kumuona mchafu.”“Sasa kipi kilicho kufanya umwite mkwe?” Colin alimuuliza mama yake akiwa amemkazia macho.“Nilitokea kumpenda sana binti yule na kutamani awe mkwe wangu lakini alikosa sifa muhimu.” “Zipi mama?”“Kwanza elimu yake darasa la saba tena la kuferi, pia anatoka katika familia ya kimaskini.”“Tabia yake?”“Kwa kweli binti yule ana tabia nzuri sana, ila tatizo ni hilo. Kama angekuwa na sifa angalau ya elimu ya kidato cha sita au chuo kama Mage basi yeye ndiye alikuwa chaguo langu la kwanza.”“Kweli mama Cecy ni mzuri, lazima nikusifie unajua kuchagua wasichana wazuri.”“Nataka mwanangu mwanamke utakaye muoa basi moyo utabasamu kila ukimuona.”“Nashukuru kwa hilo mzazi wangu.”*** Kama kawaida Cecy baada ya biashara zake, usiku aliwahi kuoga na kula kisha kuwahi kitandani. Alitaka kupata muda wa kuyatafari yote aliyokutanana nayo mchana. Mama yake hakutaka kupoteza wakati alimfuata na kumwita ili ajibiwe maswali yanayomsumbua mwanaye.“Cecy.”“Abee mama.”“Tabia gani uliyoanzisha akimaliza kula inawahi kitandani?”“Mama kazi ya kuzurura na ndizi inachosha.”“Umeanza leo?”“Mama siku azilingani.”“Hebu njoo.”Cecy kwa mara ya kwanza alimuona mama yake anamsumbua kwa kumnyanyua kitandani wakati yeye alitaka kuzama kwenye dunia nyingine ya kufikilika yenye raha zisizo na kikomo.Alitoka ndani akiwa amekunja uso kitu alichokigundua mama yake na kumuonya:“ Tabia ya kukasirika nikikuita imeanza lini?”“Mama nimechoka.”“Hata ukichoka hujawahi kunikunjia uso, hebu njoo hapa.”Cecy alikaa kwenye kigoda pembeni ya mama yake huku ajitahidi kuficha hasira alizokuwa nazo.“Umepata mwanaume?” mama yake alimuuliza kwa sauti kavu.“Hapana mama.”“Cecy, mi mtu mzima nimeona jua kabla yako, wasichana wakipata wanaume hujenga kiburi na kujiona wapo sawa hata na wakubwa zao.”“Haki ya Mungu mama sijapata mwanaume,” Cecy alijiapiza.Mama yake alimweleza yote aliyoyaona kwa mwanaye usiku wa kuamkia siku ile.“Haya bisha ninakusingizia?”“Najua utasema hivyo, lakini mama sina mwanaume ila kuna mtihani moyoni mwangu wenye majibu tata.”“Mtihani gani?”Cecy alimwelezea ukaribu wake na mama Colin wa kuwa mteja mzuri wa ndizi zake na tabia ya kumwita mkwe mpaka siku aliporudi Colin kutoka Ulaya na kutambulishwa kama mchumba wake. “Sasa hapo kipi kinakitatiza?” mama yake alimuuliza baada ya kumsikiliza.“Mama sielewi kama kweli mama Colin amenichagua niwe mchumba wa mwanaye.”“Mwanangu kumbe ndicho kinachokuchanganya?”“Ndiyo mama yangu hakuna kingine, sijawahi kupenda wala simjui mwanaume. Lakini nimetokea kumpenda sana Colin na kutamani awe mume wangu.”“Umesema ametoka Ulaya kusoma, sasa akuoe wewe mbumbumbu ambaye hata darasa la saba limekushinda?”“Mama elimu haina mwisho, naweza kujiendeleza najua tatizo labda kuzungumza kingereza.”“Sasa hicho kingereza utakijualia wapi?”“Zipo shule nitajifunza nitajua.”“Nataka nikuambie mwanangu, mama Colin kukuita mkwe ni kukutania tu, siku zote matajiri huwapeleka watoto wao kusoma Ulaya ili wawaoe watoto wa matajiri wenzao tena wasomi. Sasa wewe pangu pakavu wapi na wapi?”“Sawa mama, lakini naamini ipo siku maji yatapanda mlima.”“Hizo ni ndoto za mchana.”“Sawa mama, ipo siku utakubali ndoto za mchana huwa zina ukweli.”“Mwanangu naomba uachane na mawazo hayo muda ukifika Mungu atakupa mume mzuri mwenye mapezi na wewe.”“Asante mama yangu.”“Haya kalale mwanangu.”“Haya mama usiku mwema.”“Na kwako pia.”Cecy aliagana na mama yake na kurudi chumbani kwake kulala, alipofika chumbani alizima taa na kujilaza kitandani. Hakukubaliana na mama yake, akili yake kubwa ilikuwa kwenye zawadi aliyoahidiwa na Colin.Alijiuliza ni zawadi gani anayotaka kumpa ambayo hakuweza kumpa siku ile mpaka asubiri siku ya pili. Alijikuta akiuona usiku ukienda taratibu sana, hamu yake kukuche upesi ili akaione zawadi aliyoahidiwa na Colin.Mage pamoja na kukubali kuolewa na Colin bado alikuwa na kovu moyoni mwake la kutendwa na mtu aliyempenda kuliko kitu chochote chini ya jua Hans, mwanaume aliyemuingia kwenye ulimwengu wa mapenzi. Wasiwasi wake mkubwa kwa Colin kuwa na mpenzi mwingine ambaye ametoka naye mbali na mwisho kuwa kama Hans na kuumizwa kwa mara ya pili kitu ambacho hakutaka kijirudie. Japokuwa hakuwa tayari kuliona lile na alikuwa tayari kulipigania penzi lake kwa nguvu zake zote.Wazo la peke yake liliisumbua akili yake alihitaji msaada wa mtu wa karibu. Mtu muhimu katika maisha yake alikuwa shoga yake Brenda ambaye aliamini anaweza kumsaidia juu ya uamuzi wake wa ghafla wa kumkabidhi moyo wake Colin bila kumchunguza.Akiwa amejilaza kitandani alichukua simu yake na kumpigia Brenda, baada ya kuita kwa muda ilipokelewa upande wa pili.“Vipi shoga kulikoni mpaka leo kupiga simu, badala ya kutumia njia ya whats up au twiter?”“Shoga si la kulizungumzia kwenye mtandao, hili ni la uso kwa macho.”“Mmh! Una nini tena shoga?” Brenda alishtuka.“Kwanza upo wapi?”“Nimerudi muda si mrefu natoka kufuatilia ile ishu.”“Sasa naomba basi nikupitie tukakae ufukweni tuzungumze vizuri.”“Hakuna tatizo.”“Basi nakuja sasa hivi.”“Poa.”Mage alikata simu na kwenda kubadili nguo, kwa vile alikuwa ametoka kuoga muda si mrefu hakuwa na haja ya kwenda kuoga tena. Baada ya kuchagua nguo nzuri iliyompendeza alitoka kuelekea nje. Mama yake aliyekuwa sebuleni alishangazwa na mwanaye kutoka bila taarifa.“Mage safari ya wapi?”“Ufukweni mama.”“Kufanya nini?”“Mama akili yangu bado haipo vizuri ngoja nikaipoze kwa kuangalia maji.”“Brenda mwanangu kumbuka sasa hivi wewe ni mchumba wa mtu, japokuwa hujavalishwa pete. Hiki huwa kipindi kibaya sana kwa msichana kwani anatakiwa kutulia. Unaweza kuharibu kila kitu na matokeo yake useme umerogwa.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/“Mama hujui kiasi gani nilivyo na msogo wa mawazo juu ya uamuzi wangu wa haraka wa kumkubali Colin. Katika mapenzi yangu na Hans sikuwaza kama kuna siku tutakuwa mbalimbali. Hivyo nimekuwa muoga sana mama naona kama nimefanya uamuzi wa ghafla sana.” “Katika penzi lenu na Hans kuna kosa mlifanya ambalo nina imani kwa Colin limekuwa wazi sana.”“Kosa gani mama?”“Penzi lenu lilitawaliwa na usiri na mambo mengi mlifanya kwa siri bila wazazi wa mwenzako kujua.”“Mamaa! Wadogo zake wote wananitambua.”“Wazazi wake?”“Ndiyo tulikuwa katika harakati za kutambulishana likatokea la kupatiwa mchumba,” Mage alisema kwa sauti ya masikitiko.“Umeona! Pengine kama mngekuwa wawazi yote yasingetokea, sasa hivi ungekuwa mke wa Hans.”“Mamaa! Usinikumbushe, kutaja ndoa yangu na Hans moyo unaniuma. Nampenda Colin lakini hawezi kumfikia Hans, kwake nilikuwa kama kipofu niliyebahatika kufumbua macho mara moja na kitu cha kwanza na mwisho kukiona kilikuwa ni yeye.”“Ndiyo hivyo ukificha moto kwa kuufunika na shuka moshi utakuumbueni. Penzi mlilifanya la siri ndoa ya mwanamke mwingine imekuumiza.”“Basi mama inatosha, niache nikapunguze mawazo ufukweni.”“Kwa nini usimfuate mwenzio ili mwende pamoja, kufanya hivyo unaonesha jinsi gani unavyo muhitaji kama mumeo.”“Mama siku za kutoka na Colin zipo, leo nina mazungumzo na Brenda.”“Haya ila punguza mawazo, Mungu kasikia kilio chako umempata mwanaume wa haja anamzidi kila kitu Hans.”“Kwa macho ni rahisi kusema hivyo, macho huwa yanaona lakini moyo ndiyo wenye jukumu la kuchagua ulichokipenda. Colin anaweza kuwa na umbile na sura nzuri lakini hakawa hana mapenzi kama Hans.”“Mmh! Huyu Hans kakuchanganya sana mwanangu, ina maana akiachana na mkewe upo tayari kuolewa?”“Mkewe angekuwa hajazaa ningekubali, lakini alichonifanyia Mungu anajua. Sasa hivi namchukia Hans kuliko kifo.”“Basi mwanangu muwahi Brenda.”“Sawa mama.”Mage alitoka hadi nje na kuchukua gari aina ya Harrier Lexus na kuelekea Osterbay kwa shoga yake Brenda. Alimkuta akiwa tayari amejiandaa, hakuwa na haja ya kuingiza gari ndani kwani alikuta tayari ameishatoka nje ya geti.Baada ya Brenda kuingia ndani ya gari Mage aliliondoa bila kusema kitu. Shogaye aligundua mabadiliko kwenye uso wa rafiki yake.“Shoga kuna usalama?”“Kiasi.”Mage alijibu kwa mkato bila kumtazama shoga yake huku akifunga bleki katika foleni ndogo kwenye taa za daraja la Salenda. Baada ya taa kuruhusu aliondoa gari, Brenda hakubandua uso wake kwenye uso wa Mage na kugundua michirizi ya machozi kitu kilichomshtua sana.“Shoga kulikoni?”Mage alijikuta akipaki gari pembeni na kuanza kulia kilio cha chinichini. Brenda alishtuka sana na kumsogelea shoga yake aliyekuwa amelalia usukani huku akilia.“Mage nini tena shoga si umesema tukazungumzie ufukweni?”“Ni kweli, lakini inauma sana.”“Sawa, hebu twende huko tutayaongea yote.”“Papara ya mapenzi itaendelea kunitesa, hata sijui kwa nini nimeshindwa kujikontroo,” Cecy alisema akiwa bado ameinama kwenye usukani.“Jamani Cecy, nani kakutenda tena?”“Shoga hebu njoo uendeshe gari naweza kugonga maana kichwa changu hakipo sawa.” Brenda alizunguka upande wa pili na kuingia kwenye gari na kuliondoa kuelekea Kigamboni. Baada ya kusubiri pantoni Kivukoni kwa robo saa, walivuka upande wa pili.“Twende ufukwe gani?” Brenda alimuuliza baada ya kutoka nje ya geti.“Yoyote ile,” Cecy alijibu akiwa amejilaza kwenye kiti ilichokilaza kwa nyuma.“Mikadi panafaa?” Brenda alimuuliza huku akimtazama.“Popote utapopaona panafaa.”Brenda alipaki kwenye maduka na kununua vitu vya kutafuna wakiwa ufukweni kisha aliendesha gari hadi ufukwe wa Mikadi. Waliteremka na kuelekea upande wa bahari.Hali ya hewa ilikuwa ya kawaida jua lilikuwa limefichwa kwenye mawingu huku upepo wa bahari ukipepea bila kuwa kero kwa mtu aliyekuwa ufukweni.Kwa vile ilikuwa katikati ya wiki watu walikuwa wa kuhesabu ufukweni. Walitafuta sehemu nzuri na kutandika khanga na kukaa juu yake, kila mmoja kulinyoosha miguu kuelekea baharini.Baada ya utulivu wa muda huku kimya kikitawala, Brenda alikuwa wa kwanza kuuvunja ukimya ule kwa kumsemesha shoga yake aliyekuwa ametuliza macho akitazama baharini.“Mage.”“Abee.”“Hebu nitoe tongotongo, najiona kama nipo kizani na sauti ya upande wa pili ikiomba msaada bila kumuona mwenye tatizo. Siku zote tumekuwa watu tunaotegemeana kwenye matatizo yetu. Najua umeniita ili tusaidiane mawazo.“Naomba unieleze tatizo lako, siku zote tunajua machozi si ufumbuzi wa tatizo zaidi ya kupambana nalo na kulitatua. Basi naomba unieleze kinachokusibu,” Brenda alisema kwa sauti ya kubembeleza.“Brenda, nimekuwa nikikurupuka mara nyingi katika suala la mapenzi kitu ambacho kimekuwa kikinihukumu,” Mage alisema huku akimtazama Brenda.“Mage mara ngapi umekurupuka? Suala la Hans pale ulikurupuka nini, ikiwa wote mlikuwa mkipendana tatizo wazazi wake.”“Alichonitenda Hans hukijui?” Mage alimuuliza Brenda huku akimkazia macho.“Mage nilikueleza toka siku ya kwanza, kitu kama kile hakiwezekanani. Hawawezi kulala pamoja kufanya mapenzi bila kinga ujauzito usipatikane.”“Hans alinihakikishia hawezi kuzaa na yule mwanamke, kitu ambacho tungekifanya tukioana ili tuanze kutafuta mtoto pamoja.”“Inawezekana alipanga vile, lakini imetokea bahati mbaya. Lakini nilikueleza mapema kuhusu mategemeo yako kwa Hans baada ya kuoa kuwa usimtegemee kabisa, lakini ulinibishia.”“Brenda, unajua kiasi gani nilivyokuwa nampenda Hans?”“Hilo lipo wazi, lakini ndiyo hivyo tena, kitu gani kingine kilichokufanya mpaka ukawa kwenye hali hii tofauti na la Hans?” Brenda alimuuliza Mage huku akimkazia macho.Mage alimweleza kila kitu toka walipokutana kwa mara ya kwanza na mama Colin na kumwita mkwe kwa kujua anamtania mpaka siku alipomfanyia surprise ya kuletewa mwanaume nyumbani kwao.“He! Makubwa, mbona kama umegeuzwa mbuzi hata bila ridhaa yako?” Brenda alihoji huku akigeuka kumtazama Mage usoni.“Si kwamba sikutaarifiwa bali niliona kama utani, lakini kumbe yule mama alikuwa hatanii.”“Ehe, baada ya kuletwa ikawaje?”“Yaani hata sijielewi, baada ya kumuona nikawa nimevurugwa mtoto wa kike.”“Mtume!” Brenda alisema huku akimtazama shoga yake kwa jicho la huruma.Mage alimweleza chote kilichoendelea baada ya kumuona Colin. “Mmh! Basi inaonekana Colin ni kitu cha haja?”“Kwa kitu? Kitu hasa! Colin Mungu kajua kumtengeneza mwanaume yule. Yaani mpole na mstaarabu hadi raha,” Mage alisema huku akijishika kifuani na kufumba macho.“Sasa tatizo nini?”“Najiona nimejirahisi mapema sana bila kuijua historia yake.”“Lakini si amekuhakikishia kuwa yupo tayari kukuoa?”“Ndiyo, lakini mvulana mzuri kama yule lazima atakuwa na mpenzi tu. Mimi kumkubali nitakuwa naingilia penzi la mtu. Huoni kumkubali Colin ni sawa na kuyatafuta maumivu mengine?”“Lakini bado hamjavishana pete ya uchumba una nafasi ya kumchunguza, kwani mmeisha du?”“Bado.”“Kumbe! Sasa tatizo nini?”“Hata kama bado, najua nimechelewa kwa vile Colin, maisha ya Tanzania hajaishi sana. Kuna vitu aliniambia vimenichanganya sana.”“Vitu gani?”“Nilimweleza jinsi nilivyoumizwa na mapenzi na kumweleza najitupa tena ndani ya dimwi la huba bila kujua kina chake. Kuwa yeye ni boya la kuniokoa bila hivyo nitakufa maji.”“Ukasemaje?”“Alinieleza ananipenda zaidi ya kupenda huku akinithibitishia kuwa yeye ndiye tiba sahihi ya maumivu ya moyo wangu. Nilimweleza huenda hanipendi bali ananitamani na baada ya kuufaidi mwili wangu akinimbie.”“Akajibu nini?”“Brenda, Colin alizungumza kwa taratibu na kunihakikishia ananipenda sana nakumbuka baadhi ya mazungumzo yetu baada ya kumbana na maswali, nilimwambia: “Najua ndiyo siku yako ya kwanza kuniona, siamini kama Colin unanipenda kama ninavyokupenda?”Colin alinijibu: Mage toka nilipoelezwa nimepatiwa mchumba moyo wangu ulikuwa taabuni kutaka kukuona. Nilikuumba akilini kwa kila umbile na kukupamba kwa rangi nyingi.“Amini Mage kila nilichokiwaza moyoni mwangu kilikuwa uongo. Nilichokiona ni zaidi ya vyote nilivyoviwaza,” Colin alisema huku amemshika mabegani na kunitazama usoni kwa jicho la huruma. Nilimuuliza: Vitu gani hivyo Colin?” niliuliza huku nikijitahidi kuyatoa macho nje kama naweza kuyaona maneno atakayo niambia kwa macho.Colin alinijibu: Kila mtu anapenda kuwa na mwenza mwenye sura anayoiwaza ambayo huamini huenda moja wapo, nami niliitengeneza yako niwezavyo. Lakini imekuwa kinyume kabisa,” Colin aliniambia huku akiachia tabasamu ambalo lilivunja nguzo za moyo wangu.Nilijitahidi kumuuliza: Mmh! Colin, kwa nini?” nilimuuliza nami niliilazimisha tabasamu.Alinijibu: Mage we ni mzuri wa wazuri mrembo wa warembo. Najiona kiumbe mwenye bahati kama nitakuwa mume wako,” Colin alisema huku akiwa ameyakaza macho kuonesha anachokizungumza hatanii. Huku moyo wangu akiwa umetawaliwa na tabasamu nilimwambia: Siamini, Colin siamini,” nilisema mikono yangu nikishika kifuani huku machozi yakinitoka.“Mage huamini nini?” Colin aliniuliza kwa uso wa huruma.“Inawezekana Colin unalitamani umbile langu lakini si mapenzi ya dhati toka moyoni mwako,” nilisema huku machozi yakinitoka na kuweka michirizi kwenye mashavu yangu.“Mage amini nakupenda kama ugonjwa wa shinikizo la damu linavyochukuwa uhai wa mtu ghafla,” kila kauli ya Colin ilizidi kuusambalatisha moyo wangu.“Colin sijui wewe ni mwanaume wa aina gani?” nilijisema huku akijitahidi kutengeneza tabasamu ndani ya machozi.“Kwa nini mpenzi?” aliniuliza huku akinitazama kwa huruma kitu ambacho sikuwahi kukiona kwa Hans pamoja na kumpenda kote.“Maneno yako yamekuwa na sumaku yenye nguvu ya ajabu kuweza kunasa chuma kilichomo moyoni mwangu,” nilimweleza nilivyo kuwa radhi kuwa mateka wa penzi lake.“Sijakuelewa mpenzi?” Colin aliniuliza.“Ameweza kuuteka moyo wangu na kukubali kuwa mateka wako. Colin nakuamini, usiniache katikati ya bahari nitakufa maji boya langu ni wewe. Maumivu ya mapenzi ni zaidi ya kung’olewa jino bila ganzi,” nilimtaadhalisha Colin.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/“Amini Mage nakuahidi kuwa mume mwema,” Colini aliniahidi japokuwa sikujua aliyosema yanatoka moyoni au mdomoni.“Nami nakuahidi kuwa mke mwema,” nami nilimuahidi ahadi toka moyoni wangu.Baada ya Brenda kumsikiliza kwa muda shogaye alisema:“Mmh! Mbona kina kitu kipo wazi tatizo nini?”“Wasiwasi wangu anaweza kuwa na mtu wake.”“Anaweza kuwa naye lakini si wa malengo ya kuwa mke na mume, kwani picha yake unayo?”“Ndiyo, tulipiga siku ile tena alilazimisha yeye.”Mage alisema huku akifungua simu yake upande wa picha. Baada ya kuijaza kwenye kioo cha simu alimuonesha Brenda. Shoga yake alishtuka kumuona mwanaume mzuri akiwa na Mage katika pozi tofauti za mahaba.“Mage! Colin ni mwanaume mzuri sana, mlivyokaa kama mke na mume sijui picha za ndoa yenu zitakuwaje?”“Nina wasiwasi nimekurupuka sana katika kumkubali.”“Walaa, mapenzi shoga yangu hayana fomula, mnaweza kukutana hivi na penzi lenu likadumu milele, lakini mnaweza kuandaana mwisho mkawa maadui wakubwa kama unavyomuona Hans.”“Umeona! Yaani sasa hivi sitakiwa kumuona wala kusikia jina lake.”“Nina imani hili litakwenda vizuri kwa vile hata mzazi wake amekupenda pia familia zenu zinafahamiana na zinapendana.”Wakiwa katikati ya mazungumzo simu ya Mage iliita, namba ilikuwa mgeni. Aliiangalia kwa muda bila kuipokea.“Mbona hupokei?” Brenda alihoji.“Hata sijui nani, inawezekana ni Hans, niliapa sipokei simu yake.”“Hebu pokea hujui anataka kukuambia nini?”“Hana chakuniambia.”Wakati huo simu ilikuwa imekatika, baada ya muda uliingia ujumbe mfupi wa maneno. Mage aliufungua na kuusoma:Najue upo bize na mambo ya mchana, ushikapo simu naomba unipigie, Moyo wangu u taabuni mpaka sikie sauti yako.It ‘s me Colin.Mage baada ya kusoma ujumbe ule alipiga kelele huku akishika kifua.“Mungu wangu!”“Nini tena mbona unanitisha?” Brenda alishtuka.“Mungu wangu! Kumbe alikuwa Colin,” Mage alisema huku akishika kifua.“Mmh! Ina maana huna namba yake?”“Sina.” “Ina maana mlipokutana hamkupeana namba za simu?”“Hatukupena, wote tulichanganyikiwa.”“Basi mpigie.” “Duh! Sijui anielewaje?” Mage aliingia wasiwasi.“Mage akuelewe kivipi? Brenda alimshangaa rafiki yake.”“Ataona kama ninalinga au siyo muaminifu!”“Hawezi kwa vile leo ndiyo siku yake ya kwanza kukupigia.”“Mmh! Ngoja nijaribu.”Mage alichukua simu na kumpigia Colin, iliita kwa muda bila kupokelewa. Alirudia zaidi ya mara nne lakini haikupokelewa kitu kilichomnyima raha Mage.“Brenda lazima Colin atakuwa amekasirika, siwezi kupiga mara nne bila kupokelewa.”Usiku ulikuwa mrefu kwa Cecy, alitamani siku ya pili ifike haraka ili akaijue hiyo zawadi aliyoahidiwa na Colin. Alijikuta akipindua kitandani usingizi ulikimbia kabisa. Kutokana na kukosa usingizi akiwazia zawadi alijikuta akichelewa kuamka, kitu kilichofanya akose ndizi nzuri.Kwa vile shida yake ilikuwa kufika kwa kila Colin akachukue zawadi, ilibidi anunue ndizi nzuri kwa wenzake ambazo kwake hazikuwa na faida kwa vile angekwenda kuuuza kwa bei ileile.Hakuchukua ndizi nyingi, alirudi hadi nyumbani. Baada ya kuoga na kujipamba na kuhakikisha amependeza alibeba ndizi zake na kuelekea kwa mama Colin huku akijiuliza Colin anataka kumpa zawadi gani.Kama kawaida alipofika kwenye mlango wa geti alibonyeza kengele, mlinzi alimfungulia na kuingia ndani.“Mmh! Cecy muuza ndizi unapendeza kuliko mfanyakazi ofisini!” Mlinzi alimshangaa Cecy kila siku kupendeza na kuonesha uzuri wake.“John acha ushamba nani alikuambia muuza ndizi anatakiwa kuwa mchafu?”“Pamoja na hayo, wee umezidi.”“Kwa hiyo ulitakaje?”“Walaa, nakupongeza tu.”“Asante.”“Ila mama ametoka sasa hivi umechelewa kama dakika mbili.”“Na..na Colin?” Cecy alishtuka.“Ye yupo.”“Ooh! Afadhali!” Cecy alisema huku akishusha pumzi ndefu kitu kilichomshangaza mlinzi.“Mbona umeshusha pumzi?”“John, mbona una maswali mengi kama polisi?” Cecy alimjia juu mlinzi.“Basi Cecy nisamehe.”Cecy alisogea mlangoni wa kuingilia nyumba kubwa, aliweka beseni la ndizi chini na kuita kwa sauti.“Ndiziii.”Colin alitoka mlangoni akiwa amebeba mfuko mkubwa kidogo mkononi, Cecy alipomuona alijikuta akipoteza kujiamini na mapigo ya moyo kwenda mbio.“Karibu mchumba,” Colin alimkaribisha huku akitabasamu.“Asante.”Colin alisogea hadi beseni na kuchagua ndizi.“Mbona leo ndizi kidogo?”“Chukua zote, nilichelewa kuamka.”“Ooh!Pole.”Baada ya kuchukua ndizi aliingia nazo ndani huku akiacha mfuko wake pembeni ya Cecy. Cecy alimsindikiza kwa macho huku moyo wake ukiendelea kuteseka juu ya Colin.Aliutazama mfuko ulioonekana una vitu ndani, alijiuliza ni wake na kama wake kuna zawadi gani? Lakini hakujua kama ndiyo wake. Baada ya muda alitokeza tena Colin akiwa kwenye tabasamu. “Mmh! Mchumba samahani nilisahau kukusifia umependeza sana.”“Asante,” Cecy alijibu huku akiwa ametawaliwa na aibu.“Jana nilikuahidi nini?” Colin alimuuliza Cecy.“Zawadi.”Colin alichukua mfuko na kumpa, Cecy aliupokea kwa kupiga magoti kwa heshima mpaka chini.“Asante mpe...M..chumba,” Cecy aliingia kigugumizi.“Usijali, sasa ni hivi...leo jioni nitakuwa na sherehe ndogo ya kuzaliwa kwangu.”“Waaaooo, hongera mchumba.”“Asante, naomba kila kilichomo ndani ya mfuko huu, uvae leo kwenye sherehe yangu sawa mchumba?”“Sawa.”Colin alimpa elfu ishirini, Cecy alishtuka kwa vile ilikuwa nyingi tofauti na malipo ya siku zote ya shilingi elfu tano.“Colin mbona nyingi?”“Usiwe na wasi chukua zote.” “Asante, kwa hiyo sherehe inaanza saa ngapi?”“Saa moja usiku, ukikosa utaniudhi.”“Jamani si usiku?”“Kodi gari.”“Basi nitakuja.”Cecy aliondoka na kumuacha Colin akimsindikiza kwa macho. Wakati Cecy akiingia getini Colin alikuwa ghorofani akimtazama. Aligundua Cecy ni mzuri kuliko Mage, lakini alikosa vigezo kutokana na hali ya maisha kuwa ya sayansi na tekinolojia inayomtaka kila mtu kuwa na elimu ili kukabiliana na kasi yake bila hivyo lazima ikuache.Wakati Cecy anatoka alipishana getini na Mage aliyekuwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser V8. Colin aliyekuwa ghorofani alishtuka kuona gari la kifahari likiingia nyumbani kwao. Hakuteremka chini haraka, alisubiri kumuona nani anaingia. Baada ya gari kusimama kwenye maegesho alishtuka kumuona Mage akiteremka.Alijikuta akimsahau Cecy ghafla kutokana na jinsi Mage alivyokuwa amependeza kwa vazi la gauni fupi la rangi nyeusi na weupe lililoishia chini kidogo ya makalio.Alijikuta akijisemea mwenyewe moyoni.“Mage ni msichana mrembo sana.”Aliteremka chini kwenda kumpokea, Mage alipomuona alimkimbilia na kumrukia kwa furaha.“Waaaoo my husband to be.”“Waaaooo my wife.”Walishikana mikono na kuelekea ndani kila mmoja akiwa na furaha tele moyoni. Wakiwa wanaelekea ndani Mage alimwambia Colin.“Baby, naomba ujitayalishe tuna mtoko mdogo.”“Wapi baby?”“Surprise.”“Mmh! Haya.”Walikwenda wote chumbani kwa Colin, ili kuokoa muda aliingia bafuni kuoga ili watoke. Akiwa bafuni Mage alimfuata.“Vipi Mage,” Colin alishtuka huku akigeuka nyuma.“Nimekuja kukuosha mpenzi wangu, au kuna ubaya?”Colin hakuwa na jinsi alikubali kuoga na Mage, baada ya kuoga waliondoka kuelekea mjini. Mage alimpeleka kwenye duka la nguo na kumtaka mpenzi wake achague itakayo mpendeza kwenye sherehe yake ya kuzaliwa.“Colin mpenzi nataka uchague suti nzuuuri, itakayokupendeza jioni ya leo. Nami unichagulie nguo nzuri ambayo tukisimama wakati wa kulishana keki kila mtu moyo umchome.”“Suti nichagulie wewe, nguo yako nitakuchagulia mimi,” Colin alijibu huku akitabasamu na kufanya Mage auone vizuri uzuri wa mpenzi wake.“Sawa.”Walikubaliana kila mmoja kumchagulia mpenzi wake nguo nzuri.***Cecy baada ya kutoka kwa kina Colin hakuwa na biashara yoyote alirudi moja kwa moja nyumbani kwao akiwa na shauku ya kuiona zawadi aliyopewa. Alijikuta akianza kuiamini ndoto yake kuwa Colin naye anampenda kama yeye bila kujali elimu yake ya kata.Kutokana na kuchanganywa na zawadi, alipofika kwao alisahau kumsalimia hata mama yake aliingia moja kwa moja chumbani kwake na kutoa vilivyokuwemo kwenye mfuko na kuviweka kitandani.Alikuta gauni zuri la rangi ya zambarau lenye mchanganyiko mweusi kwa mbali. Alishtuka kukuta nguo za ndani mbili moja nyekundu na nyingine nyeupe.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Viatu vilikuwa vya kisigino kirefu kidogo chenye mikanda. Alivaa na kuzunguka chumbani kama miss aliyekuwa akitafuta pointi. Aliufungua mkebe kidogo na kukuta mkufu mdogo ya fedha.Aliivaa na kuchukua kioo na kujikuta akitabasamu huku akiwa na hamu ya kutoka nje ili walimwengu wamuone alivyopendeza.“Kumbe na mimi mzuri namna hii, kwa nini Mungu umeninyima elimu?” Cecy alijikuta akianza kulia.Mama yake alikuwa amesimama mlangoni baada ya kupitwa na mwanaye bila kusemesha na kuacha kazi zake kumfuata ili kujua mwanaye amepatwa na kitu gani.Alipofika alimuona akitoa vitu kwenye mfuko alitulia mpaka aone mwisho wake. Alishtuka kumuona akitoa nguo za gharama na kuvaa. Alijiuliza amezitoa wapi, lakini hakutaka kumuuliza haraka alisubiri aone mwisho wake.Kauli ya mwanaye ya kujisifia ilimfanya atabasamu, lakini alipoanza kulia huku akimlaumu Mungu kukosa elimu alimshtua.“Cecy.”Cecy alishtuka na kugeuka bila kuitikia huku akifuta machozi, alipomuona mama yake aliitikia.“Abee mama.”“Unalia nini?”“Roho inaniuma kukosa elimu pia nipo njia panda kwa Colin.”“Kwanza nguo hizi umetoa wapi?” mama yake alikaza sauti.“Kanipa Colin.”“Ili?”“Mama alisema atanipa zawadi, nilipofika kwao leo alinipa na ameniomba leo nihudhulie kwenye sherehe yake ya kuzaliwa.”“Saa ngapi?”“Saa moja usiku.”“Utakwendaje usiku na utarudije?”“Amenipa hela ya gari.”“Mmh! Haya, mwisho wako na Colin tutauona.”“Mama unavyonifikiria sivyo,” Cecy alijitetea.Mama yake aliachana na mwanaye na kurudi nje kuendelea na kazi zake na kumuacha Cecy akibadili nguo. Aliziweka vizuri nguo zake ambazo alitakiwa kuzivaa jioni ya siku ile.***Cecy alitumia zaidi ya nusu saa bafuni kuoga na saa nzima kujipamba kuhakikisha ile inakuwa kete ya kumfanya Colin aamini yeye ni msichana mrembo. Kabla ya kutoka alimwita mama yake aongeze kumremba.“Mmh! Mwanangu inatosha.”“Mamaa! Sitaki nionekane tofauti na nitakaowakuta si unajua lazima kutakuwa na wageni wengi.”Mama yake alimtengeneza mwanaye kwa kumpaka vizuri poda lipsitiki na wanja mwembamba na kumfanya Cecy kuwa kama malkia. Baada ya kujiamini amependeza alitembea taratibu kuelekea barabarani na kukodi gari kuelekea kwa kina Colin.***Sherehe ilifanyika kwenye ua wa jengo la nyumba ya kila Colin kwa kupambwa vizuri kuwafanya wageni wafurahie mandhali ile. Wageni walifika kwa wakati kila mmoja alionekana ana maisha mazuri kutokana na magari ya kifahari kupaki kwenye maegesho.Asilimia kubwa ya wageni walikuwa wamefika na kukaa kwenye nafasi zao huku wakiendelea kutumbuizwa na muziki laini. Kutokana na foleni Cecy alikuwa wa mwisho kuingia, ilikuwa dakika chache kabla ya sherehe haijaanza.Baada ya kuteremka kwenye teksi, alishika gauni lake kwa kulipandisha juu na kusogea mlangoni. Mlinzi alimfungulia bila kumfahamu kama ni Cecy muuza ndizi kwa jinsi alivyokuwa amependeza kupita kiasi.Aliingia kwa mwendo wa taratibu kuelekea kwenye kiti kilichokuwa wazi, kila mmoja aligeuka kumuangalia Cecy msichana maskini mwenye elimu duni lakini mwenye urembo wa asili.Mama Colin aliyekuwa amekaa na mama Mage alishtuka kumuona msichana mrembo lakini mgeni machoni mwake. Alimsindikiza kwa macho mpaka alipokwenda kukaa.Baada ya Mage kukaa na kupatiwa kinywaji, zilipita dakika tano sherehe ya kuzaliwa Colin ilianza kwa Colin kutokeza akiwa ameongozana na Mage.Moyo ulimshtuka Cecy lakini hakujua yule msichana aliyetoka naye ndani ni nani yake. Lakini hakutaka kuumiza moyo wake kwa kuamini kabisa huenda yule ni mpambe aliyechaguliwa kwa ajili ya kumsindikiza. Alijikuta akiingia wivu kwa kujiuliza kwa nini hakuchaguliwa yeye ndiye awe mpambe wake.Lakini kwa upande mwingine aliamini huenda kutojua kingereza kulichangia, kwa vile mambo mengine yanayohitaji kuzungumza kingereza yangemshinda. Wazo lile aliliafiki na kujiona ana deni la kwenda twisheni kujifunza maneno mawili matatu ya Kingereza ili aendane sawa na Colin.Kila alivyomuangalia Colin alivyokuwa amependeza katika vazi la suti, moyo wake ilizidi kuteketea na kutamani siku ile ndiyo ingekuwa siku ya kuvishwa pete ya uchumba na kila mtu kujua yeye ni mchumba wa Colin angekuwa juu zaidi ya mawingu.Wakati sherehe ikiendelea Colin alishtuka kutomuona Cecy kwenye sherehe ile, pamoja hakuwa mpenzi wake lakini alitokea kumpenda kumuona kutokana na jinsi alivyojiweka na kuwa tofauti na wasichana wengi wanaotoka familia duni.Alijikuta akiwa na wasiwasi wa kutomuona kwenye sherehe yake wakati alimualika. Aliondoka kwenye kiti chake na kumfuata mama yake kumuuliza kama amemuona Cecy.“Vipi Colin?” mama yake aliinama kumsikiliza.“Eti, hujamuona Cecy?”“Cecy! Yupi?”“Mkweo.”“Mmh! Sikumualika si unajua watu waliokuja hapa mwenye hadhi zao, hivyo angekuwa tofauti na wengine.”“Mimi nilimualika.”“Sasa Colin... yule msichana atavaa nini ili alingane na hadhi ya sherehe hii. Inawezekana kabisa John kamzuia getini kutokana na hadhi ya sherehe yako.”“Kama atakuwa amefanya hivyo atakuwa hakutenda haki kwa vile mimi ndiye niliyemualika.”“Achana naye, si muhimu kama sherehe yako,” mama Colin alijibu kwa mkato huku akichukua glasi ya kinywaji na kupeleka mdomoni.“Hapana,” Colin alisema huku akielekea getini.Mama yake hakushughulika naye alimuacha aende, alipofika getini alimuuliza John kama amemuona Cecy.“Sijamuona, sizani kama anaweza kuja kwenye sherehe ya watu wazito kama hii. Kila mmoja kaja na gari la kifahari, msichana mmoja ndiyo kaja na gari la kukodi, muuza ndizi kama Cecy atakaa wapi?” John alisema kwa dharau.“John au umemkatalia?” Colin alimuuliza huku akimkazia sauti na macho.“Hapana bosi,”John aliingiwa hofu.“Sasa kesho aje aseme umemzuia jihesabu huna kazi.”“Sijamuona kwa kweli, kama akifika nitamruhusu aingie.”Wakati Colin akirudi ndani, Cecy alikuwa akitoka msalani na kukutana uso kwa uso. Kwa vile Colin alikuwa na hasira alimuona msichana mrembo lakini akili yake haikumtambua. Baada ya kusalimiana alimchangamkia kama wageni wengine na kutaka kuelekea ukumbini.“Colin jamani ndiyo nini?” Cecy alimsemesha. Sauti ya Cecy ilimshtua Colin na kugeuka na kujikuta akitazamana na msichana mrembo.“Mungu wangu, nini wewe Cecy?” Colin alishtuka.“Naam, ni mimi,” Cecy alisema kwa sauti ya kike huku akishika mkono mmoja kiunoni na kunesa kwa madaha na macho kuyarembua.“Yaani huwezi kuamini, natoka nje kukuuliza.”“John kasemaje?”“Cecy ulivyopendeza umetuchanganya wengi, kuanzia mama mpaka John getini amekusahau, anasema hajakuona.”“Jamani! Ndizi ni kazi lakini umbile kazi ya Muumba, ninyimwe kila kitu? Nimemkosea nini Mungu?” Cecy alisema kwa sauti ya kinanda na kumfanya Colin aamini kama si kutangaza uchumba basi yeye angekuwa chaguo lake.“Basi nimefurahi kukuona pia hongera umependeza sana na karibu sana.”“Asante.”“Wacha niwahi sherehe inanisubiri mimi.”“Hakuna tatizo tupo pamoja.”“Nilisahau kamsalimie mama ajue upo.”“Sawa.”Cecy baada ya kuagana na Colin alikwenda mpaka alipokuwa amekaa mama Colin na kumsemesha.“Shikamoo ma’ mkwe,” alimsalimia huku akipiga magoti kwa heshima.“Ha! Cecy mkwe wangu jamani, nisamehe sana nilikusahau nawe umependeza sana.”“Ni kawaida yangu.”“Karibu mkwe.”“Asante, nipo mbele.”“Hakuna tatizo.” Mama Colin alimsindikiza mpaka anakaa na kutikisa kichwa na kujisemea moyoni: “Cecy msichana mzuri sana.”Sherehe iliendelea kila mmoja akiifurahia huku Mc akieleza kila hatua iliyokuwa ikiendelea. Ilifika wakati wa kukata keti, kama kawaida Mage ndiye aliyekata keki na kumlisha kisha Colin kumlisha Mage. Kisha keki ilikatwa vipande kisha Colin alipita kila meza ya wageni na kumlisha mojamoja huku akipiga naye picha. Baada ya zioezi lile alimwambia mpigapicha ahakikishe anampiga Cecy picha zaidi ya ishirini za mikao tofauti na kumpelekea.Mpiga picha alifanya kama alivyoelekezwa kwa kumfuata Cecy na kwenda naye kumpiga picha tofauti.Baada ya zoezi la kulishana keki kumalizika, Colin aliomba kipaza sauti na kuzungumza machache kuhusiana na sherehe yake kwa kuwashukuru wageni waalikwa.“Kwanza namshukuru wazazi wangu kunizaa kwa mama yangu mzazi kunilea na baba yangu aliyetangulia mbele ya haki. Pia nawashukuru wageni waalikwa kwa kufika katika sherehe ya kuzaliwa kwangu.“Leo ni siku muhimu na maalumu katika historia ya maisha yangu, kitakacho kifanya ni hatua moja kuelekea katika maisha yangu ya kujitegemea. Wazazi wangu na wageni waalikwa natumia siku ya yangu ya kuzaliwa ili kumtambulisha mchumba wangu kwa kumvisha pete.”Kauli ile ilifanya moyo wa Cecy ilipuke pa! Na kufanya mapigo ya moyo kwenda kwa kasi. Alijiuliza kauli ile anayoisikia ni ya kweli au anaota ndotoni. Akili yake ilipata jibu la kupewa nguo nzuri na kualikwa kwenye sherehe ile. Aliiona ndoto yake ya mchana kuwa mke wa Colin ilikuwa ikitimia muda si mrefu. Alitulia akijipa ujasiri ili kunyanyuka kwenda kuvishwa pete mbele ya umati ule akiitwa. Colin aliendelea kuzungumza huku akiingiza mkono mfukoni na kutoa mkebe wenye pete ya uchumba. “Jamani naomba mpenzi wangu wa moyo ambaye anatarajiwa kuwa mama wa watoto wangu asogee mbele.”Kauli ilimfanya Cecy atake kunyanyuka akiamini kabisa yeye ndiye mchumba wa Colin. Kabla hajanyanyuka kwenda mbele alishangaa kumuona Mage msichana aliyetoka naye ndani akisogea mbele akiwa ameshika kifuani asiamini kilichosemwa.Baada ya kufika hapo Mc alichukua kipaza sauti na kuongoza zoezi lile. Wakati huo Cecy alikuwa ameingiwa ganzi mwilini na kuona kama Colin kumuita kwenye sherehe ile ilikuwa amemtendea unyama. Alijiuliza kitu gani alichomtendea Colin mpaka kumfanyia ukatiri kama ule. Alijitahidi kuzuia hali ile kwa kushika mkono kifuani kuzuia mapigo yaliyokuwa yakienda kasi huku kijasho chembamba kikimtoka.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Wakati wa kuvishwa Mage pete kilikuwa kipindi kigumu kwa Cecy, ilikuwa sawa na kupasuliwa moyo wake kwa kisu butu bila ganzi. Bila kujielewa presha ilimpanda alishindwa kuizuia na kujikuta akiona kiza kizito mbele yake , alipiga kelele. “Mungu wangu.” alijikuta akinguka chini kama mzigo na kuwashtua waliokuwa wamekaa naye karibu. Tukio lile lilizua taharuki na kusababisha sherehe kusimama, wakati huo zoezi la pete lilikuwa limeisha. Colin na mama yake walishtuka kusikia aliyeanguka ni Cecy.Walikimbia eneo la tukio na kumkuta amezungukwa na watu.“Vipi?” waliuliza kwa sauti ya mshtuko.“Hata sijui, nilimuona akishika kifuani na kuhema kwa kasi kisha kufumba macho. Nilipotaka kumuuliza nilimsikia akisema Mungu wangu na kushangaa kumuona akianguka chini. Nilijitahidi kumuwahi nilichelewa tayari alikuwa ameanguka chini,” alisema dada mmoja aliyekuwa amekaa meza moja na Cecy.“Labda ana kifafa?” mmoja alichangia.“Hapana kile si kifafa, kwa jinsi nilivyomuona si kifafa,” alijibu aliyekaa naye meza moja.“Kifafa gani kisicho na povu,” mwingine aliongezea.“Jamani tumuwahishe hospitali,” mama Colin alisema.“Mama we’ baki na wageni acha mimi nimpeleke,” Colin alisema huku akipiga magoti na kushika kichwa cha Cecy aliyekuwa ametulia kama amelala.“Hapana Colin wewe baki na wageni kumbuka sherehe ni ya kwako pia umemaliza kumvisha mchumba wako pete muda mfupi, hivyo unatakiwa kuwa naye karibu. Endeleeni na sherehe mimi ninatosha.”Colin alikubaliana na mama yake, yeye alibaki na kuendelea na sherehe na mama aliyemchukua Cecy na kumuwahisha hospitali.***Cecy baada ya kufikishwaa hospitali alichukuliwa vipimo na kuoneka hana tatizo kubwa ila presha ilikuwa juu. Lilifanyika zoezi kuishusha mara moja na kurudi katika hali ya kawaida.“Nafikiri tatizo siyo kubwa sana, baada ya kumaliza drip nitamruhusu,” daktari alisema.“Itachukua muda gani?”“Si muda mrefu mtaondoka naye.”Mama Colin alitoka na kukaa kwenye makochi huku amekasirika na kulaumu kitendo cha mwanaye kumualika msichana yule ambaye hakuwa na hadhi ya sherehe ile na kufikia kuharibu starehe yake kwa kuacha shughuli ya mwanaye kwa ajili ya msichana dhalili kama yule.Alipanga kupiga marufuku ukaribu wa Cecy na Colin kwa vile aliuona unataka kwenda ndivyo sivyo. Yeye alitengeneza utani ambao ulimtia wasiwasi kwa mwanaye kuamini ni kweli, akiwa katikati ya mawazo daktari alimshtua:“Mama mgonjwa wapo yupo tayari unaweza kumchukua.”Alinyanyuka na kwenda wadini alipomkuta Cecy amekaa kitandani.“Vipi mkwe?”“Nashukuru sijambo.”“Tatizo nini?”“Hata najua! Nimejikuta nikiona kiza ghafla,” Cecy alipindisha ukweli.“Imeisha wahi kukutokea?”“Hata siku moja, hata mimi najishangaa, ila samahani mkwe kwa kuharibu sherehe ya mwanao.”“Ujaharibu kitu sherehe inaendelea kama kawaida.”“Naomba uniende nyumbani.”“Hapana nitakupeleka.”Alimchukua na kumuwahisha kwao ili yeye ageuke awahi sherehe. Alipomfikisha alimpa elfu hamsini kwa ajili ya kujiangalizia hali yake.“Mkwe ugua pole.”“Asante ma’ mkwe.”Cecy aliagana na mama Colin na kwenda kugonga mlango, mama yake aliyekuwa hana amani na moyo wake toka aondoke mwanaye kwenda kwenye sherehe za usiku. Muda wote alikuwa macho, mwanaye alipogonga aliwahi kufungua.“Umerudi mwanangu?” “Ndi..ndi..ndiyo mama.” Kauli ya Cecy iliyochanganyikana kigugumizi na kilio ilimshtua.“Cecy nini mama?”“Ningejua nisingeenda,” alisema sauti ya kilio. “Kwa nini?”“Yaani wameniita kuniumiza! Nimewakosea nini?”“Kukuumiza! Kivipi?”“Mama yaani sijawahi kuumizwa moyo wangu kama leo, najua unaniona mtoto mdogo lakini nina hisia kama mtu mwingine, mama inaumaa,” Cecy alisema kwa uchungu huku akishika mkono kifuani.“Kuna nini mbona uniweki wazi?” mama yake alishtuka.“Mama Colin wa kuniita kunionesha mchumba wake?”“Kukuonesha kivipi?”Cecy alimweleza kila kitu kilivyokuwa katika sherehe, mama yake alishtuka na kusema:“Mwanangu unataka kujiua bure, nilikueleza na mapema tajiri na sisi kina pangu pakavu wapi na wapi?”“Kwa nini mama yake ananiita mkwe wakati mwanaye ana mwanamke mwingine?” Cecy aliuliza macho yakijaa machozi.“Kuna siku alikutamkia suala la uhusiano kati yake na wewe?”“Hapana.”“Sasa kuumia huko kumetoka wapi?”“Mama! Nampenda sana Colin.”“Ulimwambia unampenda?”“Nilikuwa naona aibu.”“Siku zote moyo ni mfungwa wa mapenzi hasa kumpenda asiyejua anapendwa mdomo wako ndiyo wakili wa kuutetea moyo wako. Bila hivyo upendo wako utateketea kama mwanga wa mshumaa mchana wa jua kali, hakuna atakayeuona mwanga wake.” “Mama, Colin alionesha ananipenda.”“Nilikueleza toka zamani ule ni utani tu wala hakuna ukweli wowote.”“Kwa kitendo walichonifanyia siendi tena kwao kuuza ndizi.”“Mwanangu nikueleze mara ngapi kila kitu kinatokana na baraka za Mungu. Muombe yeye ndiye atakayekuchagulia mwanaume wa maisha yako.”“Asante mama kwa kunitia moyo.”“Basi badili nguo kisha uoge ule ulale.”“Mama hata hamu ya kula ninayo, wacha tu nikalale.”Cecy aliingia chumbani kwake kulala na kumwacha mama yake akiwa amesimama na kuyafikiria yote aliyoelezwa na mwanaye. Alimuonea huruma kwa kujiingiza kwenye mapenzi ya kumpenda mtu mwenye mpenzi mwingine anayempenda.Kingine kibaya ilikuwa hali yao duni ambayo ilikuwa tofauti na matazamo ya familia yenye fedha kuwaangalia matajiri na wasomi wenzao. Alijiuliza kwa hali iliyomtokea mwanaye iliyopelekea kupatwa na presha kupelekea kukimbizwa hospitali itachukua muda gani kumtoa.Aliamini ingemtesa mwanaye kwa kipindi kirefu na kumfanya akose amani ya moyo wake. Lakini aliamini atampatia ushauri nasaha utakaomrudisha katika hali ya kawaida. Aliachana na mawazo yale na kwenda chumbani kwake kulala.Cecy siku ile ilikuwa mbaya katika siku alizowahi kuishi, aliyakumbuka maneno ya mama yake kuhusu Colin kumtamkia mpenzi wake zaidi ya utani wa uchumba.Kwa vile kichwa kilikuwa kikimuuma, alimeza dawa za usingizi na kupanda kitandani kuitafuta siku ya pili.***Wakati hayo yakiendelea, Colin na Mage walikuwa kwenye furaha ya ajabu. Mage hakuamini tukio lililotokea usiku ule la kuvalishwa pete ya uchumba mbele ya watu.Kilikuwa kitu kikubwa sana katika maisha yake, pamoja na kupendana sana na Hans kwa muda mrefu lakini hakikufanyika kitu kama kile. Aliamini Colin alikuwa mwamaume aliyeletwa kwake na Mungu kwa kuonesha ana mapenzi ya dhati na yeye.“Colin asante sana mpenzi wangu,” Mage alisema huku akiitazama pete yake ya kito cha Tanzanite kidoleni kwake.“Kawaida tu, nina vitu vingi vya kukufanyia mpenzi wangu,” Colin alijibu huku akichezea vidole vya mikono ya Mage.“Colin nakuahidi kuwa mke mwema.”“Nashukuru, nataka harusi yetu isichukue muda mrefu.”“Hujui tu, ukitaka sasa hivi nipo tayari hata unioe bure kwa vile upendo wa kweli ni ghari kuliko kuitafuta fedha. Nakuhitaji kuliko kitu chochote chini ya jua.”Mage alisema huku machozi yakimtoka akikumbuka alichofanyiwa na mpenzi wake Hans, mwanaume aliyeamini ndiye wake wa kufa na kuzikana. Lakini kilichotokea kilikuwa kinyume na matarajio yake, kiliufanya moyo wake kuingia wasiwasi wa kumkosa hata yule.“Mage usilie nataka ulie kwa furaha ukiwa nami si kwa huzuni,” Colin alimwambia Mage huku akichezea vidole vyake na macho yake kutazama usoni kwake.“Nina wasiwasi naweza kutendwa tena, Colin ukinitenda nitakufa mwenzio nakuona wewe ndiye uliyeshika uhai wangu,” Mage alisema kwa sauti iliyohitaji huruma.“Nakuhakikishia furaha yako itapitia mikononi mwangu.”“Kweli Colin?” Mage aliuliza huku ametoa macho.“Amini nakupenda sana Mage, wewe ni ua la moyo wangu sitachoka kulitunza na kulimwagilizia ili liendelee kustawi na kuchanua.”“Asante Colin, nami nitahakikisha chaguo la mama yako hutajutia maishani mwako. Hazina yote ya mapenzi nahamishia kwako.”“Asante mpenzi wangu nami nitakuwa benki yenye usalama kwa ulichokiweka kila sekunde kinaongezeka faida ya upendo.”“Nimefurahi kusikia hivyo, nina imani kovu la kutendwa litaondoka.”“Niamini nikisemacho, kwa vile nami nahitaji furaha yangu itoke kwako.”“Asante mume wangu mtarajiwa,” Mage alisema huku akimkumbatia Colin kwa mahaba mazito.Baada ya sherehe, Mage alikataa kuondoka na mama yake na kulazimisha kubaki na Colin.“Mage mwanangu muda wa kuwa karibu na Colin bado.”“Hapana mama, alichokifanya leo ni zaidi ya ndoa. Naomba uniache nina mengi ya kuzungumza naye usiku wa leo.”“Mama Mage mwache mtoto abakie na mwenziye, bado wana mengi ya kuongea wakiwa karibu,” mama Colin aliingilia kati na kufanya mama Mage kukubaliana na mzazi mwenzie kumuacha Mage alale na Colin siku ile.**** Cecy alishindwa kutoka kwao kwa siku mbili, muda mwingi aliitumia kuwaza na kujiona ni kiumbe kwenye mkosi ambaye hakufaa kuishi katika dunia ile. Alijiona hana thamani yoyote kutokana na kukosa kila kitu ambacho mwanadamu alitakiwa kuwa nacho.Maisha yao yalitawaliwa na umaskini wa kutupa, elimu nayo ilikuwa duni ya shule za kata, kwake alichombulia ni kujua kusoma na kuhesabu zaidi ya hapo hakuna alichokijua.Kingine kibaya ambacho ndicho kilichomuuliza sana kukosa haki ya kupenda kwa vile tu hana elimu pia anatoka katika familia duni. Japokuwa hakuwa msomaji wa vitabu lakini alikuwa akipenda kusikiliza vipindi vya usiku hasa vinavyohusu mapenzi na uhusiano.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Alikuwa muumini mzuri wa vipindi hivyo kwa kujifunza vitu vingi, aliweza kujua thamani ya kuwa mwanamke pia mapenzi hayahitaji mtaji wa fedha wala elimu bali hisia za mtu ambazo hupokelewa na mtu mwingine na kuwa kama ncha mbili zinasababisha umeme zikiungana ndipo umeme hupatikana.Siku zote mada zile zilimfanya ajiamini na kuamini anaweza kuwa na mpenzi wa aina yoyote mwenye hadhi yoyote kwa hali yake duni na elimu yake ileile. Alichojifunza kingine msichana kuwa msafi wakati wote hata kama anauza karanga hakutakiwa kijifuja na kutembea na nguo chafu au kutojijali.Cecy aliamini kupendwa na watu wengi huku biashara yake ukiuzika sana ilikuwa ni kutokana na kujipenda kwa kununua nguo nzuri na muda wote kuwa msafi. Lakini kitendo alichofanyiwa na Colin kilimvunja nguvu na kuona hakuwa na sababu ya kupoteza fedha zake kununua nguo na vipodozi, kwa vile hakuona umuhimu wake zaidi kurudia maisha ya zamani ya kuvaa nguo nzuri siku jumapili atakapokwenda kanisani tu lakini siku nyingine alivaa hovyo. Kitendo cha kutokwenda kwenye biashara kilimshtua sana mama yake na kutaka kujua kulikoni.“Mwanangu kwa nini huendi kwenye biashara?”“Mama yaani sijui nitatembeaje najisikia aibu naona kama kila mtu anajua kilichonitokea siku ile.”“Mwanangu, kilichotokea ni siri yako kwa vile hakuna aliyejua moyoni unawaza nini.”“Ni kweli, lakini moyo unaniuma sana mama.”“Kuumwa moyo ni kujitakia kwa vile Colin hakukutamkia wala wewe hukumtamkia kipi kikuumize.”“Kwa nini aliniita kwenye sherehe yake?”“Kama walivyoitwa wengine.”“Mmh! Sawa, lakini nimeapa sitapeleka tena ndizi kwa mama Colin.”“Hiyo ni juu yako, lakini kumbuka katika sehemu uliyokuwa na uhakika wa fedha ni katika nyumba ile. Siku zote usiingize mapenzi kwenye biashara.”“Siwezi..siwezi mama watanionaje?”“Wakuoneje, kwani wao wanajua nini juu ya kuanguka kwako?”“Hata kama hawajui siendi,” Cecy alishikilia msimamo wake.“Siwezi kukulazimisha kwa vile wateja wale sikukutafutia uliwatafuta mwenyewe.”Cecy alipanga kuendelea na biashara yake mwisho wa wiki huku akisimamia msimamo wake wa kutopeleka ndizi kwa mama Colin.***Upande wa Colin alishtushwa na ukimya wa Cecy kutoonekana kwa siku tatu nyumbani kwao kupeleka ndizi. Akiwa chumbani kwake alichukua picha alizopigwa Cecy na kuzitazama.Aliusifia uwezo wa mpiga picha kwa kumpiga picha nzuri za tofauti, alituza macho na kuangalia uzuri wa asili wa Cecy.“Hakika binti huyu ni mrembo,” alisema kwa sauti ya chini na kurudia tena picha moja baada ya nyingine.Alitabasamu na kuamini wazo lake la kuanzisha kampuni ya mitindo litafanikiwa kwa kukusanya mabinti wenye uzuri wa asili wasiotumia madawa ya ngozi kama Cecy ambao angewatumia katika maonesho ya mitindo mbalimbali huku akiuza nguo.Japokuwa elimu ya Cecy ilikuwa darasa la saba, kwa umri wake aliamini akisoma twisheni ya Kingereza kwa kipindi anajiandaa kufungua kampuni angekuwa amepiga hatua katika kuzungumza na kusoma Kingereza vizuri.Alijikuta akitoka sebuleni na picha ya Cecy mkononi hadi alipokuwa amekaa mama yake.“Mama mbona mchumba haonekani siku hizi?”“Colin, wa nini kwani siku ambazo hakuja tumekosa ndizi?” mama yake alimuuliza huku akiondoa macho kwenye gazeti na kumtazama mwanaye.“Hapana mama kumbuka alipata matatizo siku ya sherehe yangu huenda amezidiwa.”“Daktari alisema hakuwa na ugonjwa wowote alichopata ni mshtuko tu.”“Lakini kumbuka toka apate tatizo lile hatujamuona kuleta ndizi.”“Hata tukimuona atatusaidia nini?”“Mamaaa! Mbona majibu yako kama yanaonesha chuki.”“Colin, mimi na wewe nani anamjua sana Cecy?”“Wewe.”“Sasa kipi kinakufanya kutaka kuyajua mambo yake?”“Kwa kawaida mtu ambaye alikuwa akituletea biashara atoweke ghafla lazima nihoji.”“Hiyo picha ya nani?”“Ya Cecy.”“Ya Cecy! Imefikaje kwako..hebu.” Mama Colin alisema huku akinyanyuka na kumfuata alipokuwa amesimama mwanaye na kuichukua picha ya Cecy aliyokuwa amekaa pozi tata. Aliitazama kwa muda kisha alimuangalia mwanaye na kumuuliza.“Hii picha umeitoa wapi?”“Kwa nini unaniuliza hivyo?”“Colin mwanangu sasa nimejua sababu ya Cecy kuja kwenye sherehe yako, yaani unajifanya unampenda Mage kumbe upo na Cecy.”“Mamaa!” Colin alimshangaa mama yake kusema kauli ile.“Nasema hivi sitaki kukuona na uchafu huu na tena nitakwenda kumkomesha.”“Mama mbona unanihukumu bila kuniuliza?” Colin alizidi kumshangaa mama yake.“Nikuulize nini, yaani uchafu huu sitaki kuuona,” alisema huku akiichana picha ya Cecy na kuvitupa vipande chini na kumwita msichana wa kazi kuja kuvizoa.“Mama unafanya nini, nilikueleza nini kuhusu production yangu?”“Production na mapenzi yako na msichana mchafu maskini tena mbumbumbu hainiingia akilini,” mama yake alisema huku akibinua midomo.“Mama Cecy si mpenzi wangu bali niliamini kwa muonekano wake pamoja na wasichana wengine wa muonekano kama wake angenisaidia katika kampuni yangu kufanya vizuri.”“Sitaki mazungumzo mengi nataka uvunje uhusiano wako na Cecy au nitamfanyia kitu kibaya ili nikanyogwe hawezi kuharibu mipango ya maisha yangu.”“Mama sina mpango wowote na Cecy ulipoelekea sipo,” Colin alimshangaa mama yake.“Naomba uondoke mbele yangu.”Colin hakusema kitu aliondoka na kurudi chumbani kwake, alipofika alizichukua picha zote za Cecy na kuzificha kwa kuamini kwa jinsi alivyopendeza hata Mage angeziona angejua lazima ana uhusiano naye.Kitendo cha Colin kuwa na picha ya Cecy pia kumkaribisha kwenye sherehe ya kuzaliwa kwake, kiliamsha hasira za mama yake na kujikuta akimchukia Cecy ambaye aliamini kabisa mwanaye anampenda kuliko Mage. Alinyanyuka na kutoka nje akiwa mwenye hasira hadi kwenye gari. Aliingia na kuondoka nalo kuelekea nyumbani kwao na Cecy ili kwenda kumkomesha aachane na mwanaye.Aliendesha gari kwa kasi mpaka nyumbani kwao na Cecy. Alipofika aliteremka bila kufunga mlango na kwenye anapoishi Cecy na mama yake. Alimkuta mama yake akitengeneza samaki wa biashara.“Cecy yupo wapi?” aliuliza kwa hasira hata bila salamu.“Dada yangu hata bila salamu?” mama Cecy alisema kwa sauti ya upole.“Haikusaidii kitu, huyo kiinyago wako yupo wapi?” “Tatizo nini mzazi mwenzangu?”“Sina shida ya maswali namtaka Cecy.”“Amekwenda kwenye biashara zake.”“Ooh! Kumbe ndiyo janja yake mwambie nimeisha mbaini. Akija mwambie sitaki kuvuruga maisha ya mwanangu nasema amkome.”“Kwani kafanya ni...” alikatwa kauli.“Ee..ee, nimesema amkome kama ana tabia ya kenge basi damu itamtoka maskioni.”“Mbo..mbona ..si..si.”“Nimesema nikisikia tena usije kunilaumu, mwambie mwanao amkome mwanangu kama alivyokoma kunyonya ziwa lako.”Baada ya kusema vile aligeuka na kuondoka na kumuacha mama Cecy ameganda kama sanamu asielewe chochote zaidi ya kashfa walizomiminiwa na mama Colin.Alilitizama gari liliondoka kwa kutimua vumbi mpaka lilipopotea kwenye macho yake.“Maama, ” alishtuliwa na kauli ya Cecy aliyetokea nyuma ya nyumba akiwa na beseni tupu baada ya kumaliza ndizi.Mama yake aligeuka na kumtazama mwanaye aliyegundua kulegwa kwa machozi kwa mama yake ambaye uso wake ulipoteza furaha.“Mamaa! Kuna nini?” Cecy alishtuka.“Mwanangu umaskini mbaya,” mama yake alisema huku akielekea kukaa kwenye kizingiti cha nyumba.“Kwa nini mama?”“Umemfanya nini mama Colin?”“Kivipi?”Mama yake alimweleza yaliyotokea muda mfupi, Cecy alishtuka sana kusikia habari zile.“Mama yaani ndiyo kasema hivyo! Hayo mapenzi na mwanaye yameanza lini?”“Sijui.”“Mama namfuata sasa hivi anieleze kuja kututukana bila sababu, kama umaskini wetu tumeridhika nao.”“Hapana mwanangu mwenye nguvu mwache apite.”“Si kwa hilo, wameniumiza bado wananifuatafuata,” Cecy alisema kwa sauti ya kilio.“Wee waache.”“Mama tukiwaacha watatuzoea, nimeacha kwenda kwao bado tu hawajaridhika mama niache akanithibitishie alichokisema. Ni kweli nampenda Colin lakini hatujatamkiana mambo ya mapenzi yeye kayatoa wapi?” Cecy alisema kwa jazba.“Mwanangu jasho la mnyonge haliendi joshi.”“Sawa, lakini Mungu yupo.”Cecy aliweka beseni lake na kwenda chumbani kwake akiwa amefura kwa hasira. Moyoni alijiapia siku akikutana na mama Colin siku hiyo atamkosea adabu kwa dharau aliyoifanya nyumbani kwao.Familia mbili zilikutana kupanga tarehe ya harusi ya watoto wao. Kila mmoja alitaka kufanyika harusi ya kifahari kutokana na watoto wao kuwa wa kwanza kuoa na kuolewa katika familia zao. Baada ya makubaliano ya tarehe ya ndoa, waliwataarifu watoto wao kilichokuwa kikiendelea juu ya ndoa yao. Mara moja zilisambazwa taarifa kwa ndugu na jamaa kwa kupewa kadi na wengine kuhudhulia vikao vya maandalizi ya harusi vilivyoanza mara moja. Mage alipanga picha zake za harusi kuzisambaza katika mitandao yote ili kumuonesha Hans naye ana watu wanaompenda kwa dhati kuliko yeye aliye upasua moyo wake kwa kisu butu bila ganzi. Wakiwa katika Mgahawa wa Samakisaki Mlimani City walipokutana Mage na shoga yake kipenzi Brenda kwa ajili ya kula raha. Wakiwa wanakula piza na juisi, baada ya kutafuna kipande cha piza na kusukumia na juisi ya embe, alisema: “Brenda yaani sijui siku ya harusi yangu itakuwaje?” “Mage, litakuwa bonge la harusi ambalo halijawahi kutokea jijini. Mama yako alivyopania, sijui!” “Yaani, baada ya ndoa wakati tupo honey moon nitazisambaza picha za harusi mitandao yote ili kuwakonga wavimba macho walionicheka baada ya Hans kuoa.” “Najua Hans ataumia sana,”Brenda alisema huku akikata kipande cha piza. “Aumie nini wakati amefurahia, lakini Mungu yupo, kisasi changu kwake hakijaisha ningekuwa na uwezo ningemmwagia tindi kali,” Mage alisema huku akikunja uso kwa hasira. “Magee! Tindi kali ya nini ikiwa tayari umepata mtu mwenye mapezi ya kweli?” “Brenda hujui tu jinsi nilivyoumia kwa kitendo cha Hans kunihalibia ndoto zangu za maisha.” “Mage bado unampenda Hans!” “Aah, wapi!”Mage aliruka kimanga. “Muongo unampenda na akitokea leo haki ya nani ndoa hakuna,” Brenda alimwambia shoga yake akiwa amemkazia macho.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ “Haitatokea hata siku moja, labda jua litoke Magharibi kwenda Mashariki.” “Unajikomba tu, lakini upo na Colin kama bodi lakini injini ni Hans.” “Mawazo yako, kwanza tuachane na mambo ya Hans tuzungumzia harusi yangu.” “Kama kweli umedhamilia kuolewa na Colin basi litakuwa bonge la harusi.” Wakiwa katika ya mazungumzo simu Brenda iliita, alipoangalia alikuta namba ngeni alipokea. “Haloo.” “Haloo Brenda.” “Abee, nani mwenzangu?” “Yaani nawe umenichukia kama shoga yako, Brenda nimekukosea nini?” Sauti ile ilimshtua na kugundua anazungumza na Hans. “Jamani shemu mambo mengi si unajua mitihani ilitukamata.” “Pamoja na mitihani, lakini umenitenga shemeji yangu!” “Siwezi kukutenga.” “Naomba msaada wa kunikutanisha na Mage, kuna tetesi zimeniumiza moyo wangu. Usishangae wakati wowote ukisikia kifo changu.” “Brenda unazungumza na nani?” Mage aliingilia kati mazungumzo kwa kusimama na kusogea kwa Brenda. “Mage hebu subiri,”Brenda alimtuliza Mage na kuendelea kuzungumza. “ Kipi tena kitasababisha kifo chako, unaumwa?” “Heri ningeumwa kuliko ukatili anaonifanyia shoga yako. Anajua mimi na yeye tumetoka wapi na tuliahidiana nini. Kweli Mage unakubali kuolewa na mwanaume mwingine tofauti na mimi?” Hans alisema kwa sauti ya huzuni. “Hans utakuwa unakosea kusema hivyo, wewe ndiye uliyesababisha yote. Ulikuwa ukifahamu Mage alikuwa akikupenda kiasi gani na unajua nini kilimpata baada ya wewe kufunga ndoa.” “Najua, lakini nilimweleza kila kitu.” “Mbona ulikwenda kinyume?” “Nilikuwa na sababu yangu ambayo Mage alitakiwa kunisikiliza na kuelewa sababu ya mimi kufanya vile wala asingefikia huko.” “Hans usimlaumu Mage kwa vile naye kafanya kama wewe.” “Kivipi?” “Mume katafutiwa na mama yake.” “Duh! Haijawahi kutokea.” “Basi imetokea.” “Basi naomba anipe nafasi ya kuzungumza naye kwa dakika chache.” “Sidhani kama anaweza kupata nafasi kwa muda huu wa maandalizi ya harusi.” “Najua, ila nilikuwa nataka kuzungumza naye hata dakika kumi kabla ya ndoa yake.” “Hans, hiki si kipindi cha kuzungumza chochote na Mage, unaweza kuivuruga ndoa yake.” “Siwezi, nataka tu nizungumze naye ili akiolewa ajue mimi si adui yake.” “Mmh! Nitafikisha ujumbe.” “Naomba shemeji yangu unikutanishe na Mage nitakupa zawadi yoyote unayotaka.” “Sawa shemu.” “Nashukuru kwa kunisikiliza pia wewe ni daraja muhimu kati yangu na Mage.” “Nimekuelewa.” Brenda alikata simu na kumgeukia shoga yake aliyekuwa na kumuhemuhe cha kutaka kujua Hans alikuwa akisemaje. “Vipi mzushi alikuwa akisemaje?” Brenda alimweleza mazungumzo yote waliyozungumza na Hans. “Mmh! Anataka kuniambia nini?” “Sijui, ninyi ndiyo unajua mlizungumza nini katika ahadi ya penzi lenu.” “Uhuu!” Mage alishusha pumzi na kusema: “Brenda unanishauri nini?”Mage alionekana kama ametahayari kusikia taarifa za Hans. “Kwa vile upo katika hatua nzuri ya harusi, huu si muda wa kuzungumza na Hans unaweza kuharibu kila kitu ukakosa bara na pwani,” Brenda alimtaadhalisha rafiki yake. “Eti eeh, sijui Hans anataka kuniambia nini?” “Achana naye.” “Mmh! Sawa.” Kwa vile muda uliokuwa umekwenda sana, kila mmoja aliingia kwenye gari lake kurudi nyumbani. *** Brenda alipofika nyumbani kwao alikwenda kuoga na kupata chakula kisha alijifungia chumbani kwake na kuwasha Ipad yake na kuanza kuchati na marafiki zake kwenye Twiter na Skype. Akiwa anaendelea kuchati simu yake iliita, namba ilikuwa ngeni aliipokea. “Haloo.” “Haloo Brenda.” “Abee, nani?” “Brenda unaniuliza nani wakati tumetoka kuzungumza muda si mrefu.” “Hans?” Brenda aliuliza. “Ndiyo.” “Unasemaje?” “Brenda samahani sana.” “Bila samahani.” “Naomba unikutanishe leo na Mage.” “Hans, si tumeisha ongea?” “Hapana Brenda, kuna kitu cha muhimu sana nataka nizungumza naye kabla siku ya kesho.” “Samahani Hans, nipo Bagamoyo sitarudi leo.” “Naomba hata umpigie simu ili anisikilize hata kwa sekunde tano tu.” “Hans kwanza samahani, hapa nipo na boy friend yangu, ana wivu sana naomba tuzungumze kesho,” Brenda alidanganya. “Samahani, ila utakacho kisikia kesho usishangae najua Mage atafurahi.” “Unataka kufanya nini Hans?” “Nilitakiwa kumweleza Mage mwenyewe, kwa heri.” Hans alikata simu na kumfanya Brenda abakie na simu mkononi kama anatazama kitu cha kumshangaza, alijikuta akijuliza. “Hans anataka kufanya nini? Au anataka kujiua? Mmh! Ngoja nimweleze Mage maana sasa imekuwa kazi. Lakini kipi cha ajabu Mage akiolewa? Kwani alitaka akae vile mpaka lini? Hivi Hans anashida na Mage au anataka kumvuruga maisha tu?” Brenda alijikuta akiwaza peke yake, wakati huo simu aliyopiga ilikuwa ikiita. Ilipokelewa upande wa pili. “Haloo shoga lete stori,” Mage alipokea. “Mmh! Mtu wako ananisumbua sana.” “Nani?” “Hans.” “Kakupigia tena?” Mage alishtuka. “Ndiyo.” “Brenda achana naye, kwa nini unamsikiliza?” “Mage siwezi kumkatia simu kwa vile sina ugomvi naye.” “Yaani hivi najiandaa kwenda kwa Colin, tulikuwa tunachati tukaona haitoshi, tukaongea vilevile tukaona haitoshi, nimeamua kwenda kabisa kuonana uso kwa macho.” “Duh!” “Brenda, nimeamini Colin ananipenda sana.” “Sasa ndiyo utulie.” “Brenda, lazima nitulie Colin kaniahidi vitu vingi sana baada ya ndoa nina imani ndoto zangu nilizoziota kwa Hans zitakuwa mara kumi.” “Basi ndiyo hiyo mtu wako wa roho ya Mungu anatapatapa kama mfa maji.” “Kwani alikuwa akisemaje?” Brenda alimweleza yote aliyoelezwa na Hans na alivyomdanganya, Mage baada ya kumsikiliza alishusha pumzi na kusema: “Kwani Hans anataka kuniambia nini?” Mage aliuliza. “Akwambie nini! Yule muharibifu, huu si muda wa kumsikiliza, ukirogwa kumsikiliza tu ndoa huna.” “Mmh! Nimekuelewa japo moyo unatamani kumsikiliza ili nijue anataka kusema nini?” “La kusema hakosi, anaweza kukuvuruga akili na ndoa yako ukaiona chungu. Najua bado unampenda sana Hans, kama utampa nafasi narudia tena ndoa hakuna,” Brenda alimtaadhalisha Mage. “Hata siku moja, labda siyo Mage mimi, siwezi kuumizwa mara ya tatu mbili zinatosha.” “Basi ndiyo hivyo kuwa makini na Hans, kwa nini muda wote akae kimya, kusikia unataka kuolewa ndiyo ajifanye anakupenda sana.” “Nimekuelewa basi wacha niwahi kwa mahabuba wangu.” “Mambo si hayo.” Brenda alikata simu na kuendelea kuchati na mashoga zake. *** Sauti ya simu kuita ilimshtua Brenda aliyekuwa bado amelala, alipoangalia ilikuwa namba ngeni, aliipokea. “Haloo.” “Haloo, nazungumza na Brenda?” “Ndiyo, nani mwenzangu?” “Naitwa Ndubi rafiki mkubwa wa Hans.” “Ndiyo Ndubi.” “Kuna habari siyo nzuri.” “Habari gani?” “Hans amepata matatizo makubwa sana, nilijaribu kumpigia Mage simu yake haipatikani nikaona nikupigie wewe ili umjulishe.” “Mmh! Matatizo gani?” “Jana usiku wamevamiwa nyumbani kwake na majambazi, mkewe na mwanaye wameuawa na yeye hatujui kama yupo hai.” “Mungu wangu! Yupo wapi kwa sasa?” “Yupo hospitali ya muhimbili chumba cha wagonjwa mahututi.” “Mungu wangu! Ngoja nimjulishe Mage.” “Itakuwa vizuri.” Baada ya simu kukatwa Brenda alimpigia simu Mage aliyekuwa bado yupo kwa mchumba wake Colin. Baada ya simu kuita kwa muda ilipokelewa upande wa pili. “Haloo Brenda mbona unaharibu pozi za watu,” Mage alisema kwa utani. Brenda hakupoteza muda alimweleza taarifa aliyopokea asubuhi ile, taarifa ile ilimshtua sana Mage. “Mungu wangu! Yupo wapi?” “Mihimbili.” “Nakuja sasa hivi twende.” “Noo, tutakutana hospitali.” Mage alinyanyuka kitandani na kupitia nguo zake na kuvaa bila kuoga, hakutaka kumwamsha Colin aliyekuwa bado amepitiwa usingizi. Alitoka hadi kwenye gari lake na kuondoka kuelekea muhimbili kumuona Hans. Njia nzima alijilaumu kukataa kusikiliza wito wa Hans kwa kuamini kuna kitu cha muhimu alitaka kumweleza. Alijiuliza Hans alitaka kumweleza nini na kwa nini alilazimisha waonane usiku wa jana yake kisha asubuhi asikie habari kama zile za kushtusha. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ “Mungu wangu kama Hans atakuwa amekufa atakufa na kinyongo, sikutakiwa kuwa katili kiasi kile. Japokuwa sikuwa tayari kurudiana naye lakini nilitakiwa kumsikiliza.” Mage alikuwa kwenye lindi la mawazo juu ya Hans kuwa katika hali ile. Alijikuta akitokwa na machozi kumlilia. Alijiuliza kama ndiye yeye angekuwa mke wa Hans na tukio lile likatokea ina maana angekufa yeye. Kutokana na mawazo mengi alijikuta akiendesha gari pasipo umakini, alifunga breki mbele ya gari lililosimama baada taa nyekundu kuwaka za makutano ya barabara ya Oceon na Upanga. Alikanyaka breki kwa nguvu zote huku akifumba macho na kuuma meno. Gari lilisota na kwenda kujigonga kidogo kwenye Land Cruser la Mwarabu. Kelele za breki zilifanya watu wote kugeuka kuangalia, askari wa barabarani alifika lakini Mwarabu hakutaka kesi kwa vile gari lake halikuharibika sehemu yoyote. Aliliruhusu na kumfuata Mage kumuuliza: “Vipi mbona hivyo?” Mage alishindwa kumjibu kwa vile presha ilikuwa juu na uso ulikuwa umejaa machozi. Askari hakutaka kumuhoji kitu alimruhusu kuondoka. Mage aliondoa gari kuingia barabara ya Upanga kuelekea Muhimbili kumuona Hans. Njia nzima Mage alikuwa akilia, alikumbuka maisha aliyoishi na Hans, mwanaume akiyempenda kuliko kitu chochote chini ya jua. Waliishi maisha ya mapenzi kama njiwa, kila mmoja alimpenda mwenzake penzi la glasi halikuwa na kificho kila mmoja aliamini anapendwa na mwenzake. Alikumbuka ahadi ya Hans alipomwambia kumuacha yeye ni sawa na roho kuachana na mwili. Alimuhakikisha yeye ndiye mwanamke wa maisha yake. Baada ya Hans kuozwa kwa shinikizo la wazazi, walikubaliana avumilie ili baadaye amuache mwanamke wa kulazimishwa ikiwa pamoja na kuitozaa naye. Lakini Hans alionekana kugeuka pale alipopata mtoto ndani ya ndoa yake tofauti na walivyokubaliana kutozaa na yule mwanamke na kwenda kinyume na kumfanya naye akubali kuolewa na Colin. Alijiuliza nani aliyefanya kitendo kile, alijikuta akitengeneza mawazo ya kijiunga kuwaza labda mpango ule kaufanya Colin kutokana na wasiwasi wa kurudiana na Hans. “Nikigundua Colin kama ndiye aliyemuua mpenzi wangu, nitamchukia mpaka kufa na nitakuwa shahidi namba moja kuhakikisha na yeye ananyongwa,” Mage aliwaza. Alipofika Muhumbili alisimamisha gari na kuelekea kwenye wadi ya wagonjwa mahututi. Nje ya wadi aliikuta familia ya Hans, hakuna aliyemjali japokuwa alionekana amevimba macho kutokana kumlilia Hans. Alipojaribu kuingia wadini alikatazwa na kuamua kusimama pembeni peke yake, baada ya muda shoga yake Brenda alifika na kwenda aliposimama. “Vipi shoga?” “Yaani mama Hans kanifukuza kama mbwa!” “Kwa nini?” “Hata sijui wakati anafahamu mimi na mwanaye tulikuwa vipi.” “Kwa hiyo hujui hali ya Hans?” “Sijui chochote.” Mara simu ya Mage iliita alipoangalia ilikuwa ikitoka kwa Colin, aliitazama na kukunja uso bila kuipokea. Brenda aliyekuwa akimtazama usoni alimuuliza. “Simu ya nani?” “Achana nayo,” alijibu kwa mkato. “Mmh!” Baada ya muda simu iliita tena, Brenda alishtuka kuona jina la Colin bila kupokelewa. “Shoga mbona hupokei?” “Achana naye.” “Ha! Wewe si ulikuwa kwa Colin na umeondokaje?” “Sijamuaga nimemuchana bado amelala.” “Unajua unacho kifanya unaiweka ndoa yako njia panda.” “Kwani asiponioa nitapungukiwa nini?” Mage alijibu huku akibinua midomo. “Mage, usipoteze muda wa Colin, kuamini unampenda kumbe upo naye kivuli tu.” “Brenda mwenye uamuzi wa kumpenda nani ninao mimi.” “Kwa hiyo Colin si chaguo lako?” “Brenda huu si wakati wa kuzungumzia Colin zaidi ya kujua hali ya Hans ndiye aliyetuleta hapa.” “Mmh! Sawa.”ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment