Simulizi : Wakili Wa Moyo
Sehemu Ya Tano (5)
Alipomuona anaingia alihamisha macho kwenye runinga na kumtazama mlangoni alikuta ni mama Colin. Alinyanyuka alipokuwa amekaa na kwenda kumpokea. “Karibu dada.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ “Asante,” mama Colin alijibu kwa sauti ya chini huku akificha hasira zake juu ya kitendo cha mzazi mwenzie kwenda kwake na kufanya mwanaye amchukie kwa kumficha kuwemo kwa mpenzi wake nchini. “Karibu, Vipi hujafika nyumbani?” Mama Cecy alimshangaa usiku ule wakati alisema siku ile hawataonana. “Colin yupo wapi?” mama Colin aliuliza kwa sauti kali kidogo. “Dada hata salamu unakimbilia kumuulizia Colin?” “Salamu si muhimu kama kujua hali ya mwanangu.” “Mwanao hajambo.” “Sitaki kusikia hajambo bali kumwona yupo au ameondoka?” “Yupo chumbani na mchumba wake.” “Chumbani? Anafanya nini?” “Mama Colin ni swali gani hilo, ina maana chumbani kwangu kuna mzoga?” mama Cecy alijibu kwa hasira. “Siyo hivyo dada, si unajua Colin bado mgonjwa mpaka sasa sijui yupo wapi.” “Colin na Cecy nani mgonjwa na ugonjwa mwanangu kautoa wapi, mbona tumekwenda vizuri tunataka kuharibu mwisho?” “Basi samahani dada najua Cecy anaumwa, lakini sijui Colin yupo wapi maana nilimwacha nyumbani amesikia amekuja kumwona mchumba wake.” “Nimekujibu nini?” “Sawa ngoja nikamwone.” Mama Colin alielekea chumbani kwa mgonjwa akiamini atamkuta mwanaye pembeni ya kitanda huku akiumizwa na hali ya mpenzi wake aliye katika hali unusu mfu. Alipofika alipigwa na butwaa kumkuta Colin akimlisha Cecy matunda. “Ha!” mama Colin alijikuta akipiga ukelele wa mshtuko. “Aah! Mama karibu, Mungu mkubwa kuja leo mpenzi wangu kanyanyuka kama ningekuja mapema sasa hivi angekuwa hajambo kabisa,” japo yalionekana maneno ya kawaida lakini yalikuwa kama mkuki moyoni mwa mama Colin. “Ha! Kweli Mungu mkubwa Cecy umenyanyuka mama!” mama Colin hakuamini alichokiona mbele yake. “Karibu mama mkwe, sina cha kukulipa ina namuomba Mungu anipe afya niweze kukulea mama yangu katika maisha yangu yote. Umeweza kupigania maisha yangu kwa hali na mali. Naamini kabisa kwa Mungu hakuna kinachoshindikana, karibu mkwe,” Cecy alisema huku akijiweka vizuri. “Asante mkwe wangu, Mungu ni muujiza ninachokiona mbele yangu ni kazi ya Bwana aliyotenda.” Mama Colin alikwenda kumkumbatia Cecy ambaye alikuwa amepururuka na kubaki mifupa mitupu. Mama Cecy naye alikuwa amefika hakutia neno zaidi ya kukaa kimya akimwangalia mzazi mwenzie. “Jamani leo ni katika siku ambazo nimepata furaha ya ajabu, nakuahidi kuipigania afya ya Cecy kwa gharama yoyote ili kuhakikisha anarudi katika hali yake ya zamani,” alisema mama Colin. “Asante mkwe sina cha kukulipa bali kukuonesha mapenzi ya dhati yasiyo na chembe ya unafiki.” “Asante mkwe wangu,” mama Colin alijikuta akitokwa na machozi kwa maneno mazito ya Cecy ambaye alipoteza kauli na viungo vya mwili kufanya kazi kwa zaidi ya miezi sita. “Jamani nina imani Mungu ni mkubwa ameweza kutusimamia kwa hiyo tumshukuru kwa pamoja kwa kuweza kutenda juu yangu,” Cecy alisema huku akitaka kuteremka kitandani. “Baki kitandani tutaomba ukiwa hapahapa kitandani,” Colin alimzuia mpenzi wake. “Naomba niteremke ili nipige magoti pia kwa kauli yangu kufunguka naomba niongoze maombi kumshukuru Mungu.” Baada ya wote kupiga magoti na kufumba macho Cecy alianza kuomba: “Asante baba Mungu kwa wema na utukufu wako, umekuwa nami muda wote wa maradhi na mateso yangu mazito ambayo kila mwanadamu alikata tamaa lakini baba ulikuwa nami muda wote. “Baba sina cha kukulipa zaidi ya kukuabudu kwa kufuata yote unayotaka tuyafanye na kuyaacha yote uliotukataza. Baba rudisha furaha mioyoni mwa wote waliopoteza matumaini na kuwafanyia wasiyo yategemea rudisha furaha kati nyumba yetu iliyopotea kwa muda mrefu tupe afya njema. “Baba kila aliyetokwa na machozi kwa mayeso yetu mfute na umpe furaha kama kuna aliyefurahia matatizo yetu baba msamehe kwa vile hajui atendalo. Umetuumba wanadamu kwa udongo ulio safi basi tupe mioyo yetu upendo tupendani tuoneane huruma na kuombeana mazuri. “Asante Baba kwa kuninyanyua leo, asante kwa kurudisha furaha iliyitoweka kwa muda mrefu katika familia zetu.Walipe mara mia wote waliotoa kwa ajili ya matatizo yetu. Baba yaliyotokea ni majaribu tupe imani ya kusimama upande wako na usimpe nafasi adui shetani kutupotosha. “Baba timiza ndoto yetu ya mimi kuwa mke halali wa Colin, Baba Mungu nashukuru kwa kunichagulia mume mwema mwenye mapenzi ya dhati, nami namwahidi kuwa mke mwema katika siku za pumzi zangu. Simamia ndoa yetu ondoa kila jicho la hasada roho chafu za chuki, uongo na uadui kwa jina la mwanao Yesu Kristo aliye hai, Ameni.” “Ameni,” waliitikia pamoja huku kila mmoja akifuta machozi kutokana na maombi mazito aliyoporomoshwa na Cecy. “Naombeni maji,” Cecy aliomba maji baada ya kuomba kwa muda mrefu na kuvunjwa jasho kama maji, kutokwa na jasho jingi ulikuwa muujiza mwingine kwa mama Cecy baada ya kutotoka jasho jingi kwa zaidi ya miezi sita. Alipatiwa maji na kuomba kupumzika, Colin alimpandisha kitandani na kumfunika shuka. “Colin mpenzi napumzika kidogo ila usiondoke wewe ndiyo furaha yangu.” “Sawa mpenzi.” Walimwacha Cecy amelala na kutoka nje kwa ajili ya mazungumzo. “Jamani kuna nini kimefanyika ambacho mimi sikijui?” mama Colin aliuliza. “Hakuna kilichofanyika na muujiza wa Mungu, wakati narudi nilisikia Cecy ananiita nilipoingia nilishtuka kumwona akiniita. Nilipomsogelea sikiamini kumwona mwanangu katika hali ile kwani niliisha kata tamaa.” “Kweli nimeamini muujiza wa Mungu upo,” alisema mama Colin. “Ni kweli.” “Sasa kwa vile nilikuwa nimekuja ghafla wacha nikapumzike pia tumwache mgonjwa apumzike ili kesho tujue tutafanya nini.” “Dokta Mariam amesema lazima tumpeleke hospitali akafanyiwe vipimo.” “Hakuna tatizo, Colin baba,” alimgeukia mwanaye. “Naam mama” ”Itaidi tuondoke ili ukapumzike kwa vile nawe hali yako haijatengemaa vizuri.” “Mama mimi nimepona kabisa mgonjwa ni Cecy na nipo hapa kwa ajili ya kuhudumia kwa kila kitu.” “Sawa, lakini twende nyumbani tutakuja kesho.” “Mama naomba unisamehe, leo siondoki nitalala na mpenzi wangu.” “Mmh! Sawa.” “Nikutakie usiku mwema.” Mama Colin alimkumbatia mwanaye kisha alimuaga kuelekea alipopaki gari. Alimkuta Mage amesinzia baada ya kumsibiri kwa muda mrefu, alipofika alimwamsha. “Mage pole kwa kukuweka.” “Isijali mama mkwe, vipi mbona umechelewa Colin ameisha ondoka?” “Yupo.” “Mbona umemwacha?” Mama Colin alimweleza Mage yote aliyoyakuta na kumfanya asindwe kuamini na kujikuta akiuliza: “Mama unayosema ni kweli?” Mage hakuamini. “Kweli kabisa, yaani nilichokiona mbele yangu ni muujiza Cecy amenyanyuka tena anaonekana kama mtu aliyepata nafuu wiki nzima.” “Mmh! Nimekwisha!” Mage alisema kwa sauti ya kukata tamaa. “Kwa nini unasema hivyo?” mama Colin alishtuka. “Mama kweli Colin atanioa?” “Sikudanganyi, Colin anampenda sana Cecy, hakuna kiumbe kitakacho mbadili mawazo, yaani nimemkuta kama mwenda wazimu sijui Cecy angekufa mwanangu angekuwaje.” “Mmh! Sawa,” Mage alisema huku nguvu zikimwisha na kujikuta akijilaza kwenye usukani badala ya kuondoa gari. “Vipi mbona hivyo?” “Mama kupona kwa Cecy ni pigo zito moyoni mwangu, hapa nilipo sina hata nguvu za kuendesha gari. Naomba mama yangu uendeshe naweza kugonga.”“Hakuna tatizo.” Mama Colin alizunguka upande wa pili ili kuendesha gari baada ya Mage kupatwa na mshtuko kutokana na Cecy kupona. Mama Colin alishangazwa na hali ya Mage kubadilika ghafla baada ya kupata taarifa ya kupata nafuu kwa Cecy. “Mbona umekuwa hivyo?” “Mama basi tena.” “Lakini Mage hukutakiwa kununua pilipili kwa shughuli ya mwenzio ile ilikuwa pata potea. Nafasi uliichezea mwenyewe huna wa kumlaumu.” “Mmh! Sawa.” Kutokana na kutokuwa kwenye hali nzuri Mage alilala palepale ili kuitafuta siku ya pili, mama Colin naye alikuwa na maswali yasiyo na majibu juu ya hali ya Cecy kubadilika kabisa wakati alikuwa nusu mfu. Lakini upande mwingine alimshukuru Cecy kupona kama angekufa mwanaye angekuwa chzi kwa jinsi alivyopagawa kwa mpenzi wake kupona. ***CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ Siku ya pili Cecy alichukuliwa na kupelekwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa afya yake, majibu yalionesha kila kitu kimo sawa. Majibu yale yalikuwa faraja tele kwa Colin na kwa mama Cecy ambao ndiyo walioteseka kipindi chote cha ugonjwa wa Cecy. Alitakiwa kufanya mazoezi kutokana na viungo kukaa muda mrefu bila kufanya kazi, afya ya Colin ilikuwa imetengemaa aliomba kwenda kupumzika na mchumba wake Afrika ya kusini kwa miezi miwili. Wazazi hawakuwa na jinsi walikubali watoto wao waende Afrika ya kusini kupumzika na kuendelea kupata huduma za kiafya. Baada ya siku mbili Colin na Cecy walielekea Afrika ya kusini katika mji Port Elizabeth katika hotel ya The Beach Hotel kwa ajili ya mapumziko baada ya mateso ya muda mrefu. Colin alichukua muda ule kuhakikisha anafuta machungu yote aliyoyapata mpenzi wake kutokana na ajali mbaya iliyowapata ili kurudisha imani kwake kwa vile Mage alionekana bado yupo karibu na familia yao hasa mama yake hivyo kutia doa upendo wake. Muda mwingi walitumia kukaa wawili chumbani kila asububi na jioni walifanya mazoezi madogo madogo katika Gim iliyowa katika hoteli waliyofika na majira ya saa moja walitembeatembea pembezoni mwa ufukwe. Lilikuwa penzi lililozaliwa upya kwa wapendao baada ya kupoteana kwa kipindi kirefu. Baada ya wiki mbili Cecy naye kimwili kilianza kurudi wakiwa wamejipumzisha chumbani kwao, Cecy alimuuliza mpenzi wake ambaye aliamini alikuwa na ufahamu tofauti na yeye alikuwa nusu mfu. “Colin nina imani wakati naumwa ulikuwa karibu na Mage.” “Si kweli, huwezi kuamini toka ile ajali sina ukaribu na mtu nilikuwa sitoki ndani hata simu kuanzia siku ile situmii. Najua Cecy huniamini lakini nakuhakikishia niliapa mbele ya mama yangu na mama Mage walipokuja kuniona hospitali kuwa sitaoa mwanamke mwingine kama wewe ungekufa. “Niliwaeleza kama utakufa nitatimiza ahadi niliyokuahidi kwa kufunga ndoa na maiti yako na nisingeoa tena mpaka nakufa.” “He! Kwa nini ufanye hivyo, ningekufa mimi si ingekuwa nafasi ya mwingine. Heri tungekuwa tumezaa ulikuwa na sababu ya kufanya hivyo.” “Cecy kuoa mwanamke mwingine wakati ajali nimesababisha mimi ningekuwa nimeshiriki kwenye kifo chako. Wewe ndiye wakili wa moyo wangu umenitetea wakati wote wa matatizo yangu. Bila wewe kitendo alichonifanyia Mage ningeweza kuwa chizi.” “Asante kwa kunipenda kwa kipindi chote cha mateso yangu, Colin nimeamini wewe ni mume wa maisha yangu naomba Mungu adumishe penzi letu ufe nikuzike nife unizike.” “Asante mpenzi wangu nitakupenda siku zote za maisha yangu.” “Hata mimi, Colin,” Cecy alimwita mpenzi wake akimtazama usoni. “Naam.” “Siku ya kuondoka ulikataa kubeba simu sasa tutawasiliana vipi na nyumbani?” “Nimeapa sitatumia tena simu katika maisha yangu kwani ndiyo sababu yakutaka kuyachukua maisha yetu. Pia wazazi nimewajulisha tupo hoteli gani wakitutaka watupata tukiwataka tutawapata kwa njia ya simu ya hotelini.” “Colin, naweza kusema wivu wangu wa kijinga umetufikisha hapa, sikutakiwa kukosa imani kiasi kile cha kutaka kila kitu katika simu yako nikione. Naweza kusema nilijitakia mwenyewe. Nimejifunza kitu sikutakiwa kukubana kiasi kile kwa vile mapenzi ya kweli yako moyoni na wala si kwenye simu. “Colin nilikupenda kupitiliza na kujikuta nakuwa kichaa wa mapenzi kwa ajili yako, lakini umenidhilishia kwa vitendo kuwa unanipenda mapenzi ya dhati kwa vile hukuyumba wakati wa matatizo yangu. Angekuwa mwanaume mwingine angekwisha kuwa na mchumba mwingine au ameisha funga ndoa. “Colin mpenzi wangu nakuomba kuanzia leo hii tumia simu, mimi si limbukeni tena wa simu. Upendo na uaminifu wako ameufanya moyo wangu uwe huru na kukuamini kwa asilimika mia. Colin najivunia kuwa na mwanaume kama wewe nimekutafuta kwa udi na uvumba japo mama yako alifanya utani kuniita mkwe lakini niliamini nami nina haki ya kuwa na mwanaume nimtakaye aliye katika hali yoyote. “Asante Colin kugeuza mazoea ya maskini hana haki ya kupenda, nipende Colin nikupende, Colin unajua wewe ndiye mwanaume wangu wa mwanzo na wa mwisho. Nakupenda Colin zaidi ya kupenda.” “Cecy najua thamani yako moyoni mwangu ni zaidi ya madini yote unayoyajua na usiyo yajua. Niliapa moyoni mwangu sitakupoteza mtetezi wa moyo wangu. Cecy mpenzi wewe ni zaidi ya mwanamke ni malaika wangu.” “Asante mpenzi, ila hujanihakikishia utatumia simu?” “Cecy nilitaka kuacha kutumia simu kwa ajili yako, lakini kwa vile umeniruhusu nitatumia.” “Colin.” “Naam.” “Nina ombi moja naomba ukikubalie kwani toka nimefika hapa kuna kitu kimekuwa kikinisumbua jibu lako ni faraja ya moyo wangu.” “Cecy malkia wangu, sema chochote nitakitekeleza.” “Kuna kitu nimejifunza kwako kila unapotaka kufunga ndoa kuna tokea matatizo umeisha lingudua hilo?” “Dah! Kweli kabisa mpenzi hilo jambo hutokea.” “Sasa nitaka tufanye kitu tofauti katika safari yetu hii.” “Kitu gani?” “Tufunge ndoa kabisa hukuhuku tukurudi tuwe mke na mume.” “Mmh! Lakini ndoa yenye baraka lazima wazazi wawepo.” “Wazazi tutawaita huku tukirudi Tanzania tunafanya sherehe tu.” “Sawa hakuna tatizo.” Walikumbatiana kwa furaha walizima taa ya mwanga mkali na kuwasha ya mwanga hafifu kila mmoja aliyasikia mapigo ya moyo wa mwenzake. *** Mage alionekana kuchanganyikiwa kutokana na taarifa za kupona kwa Cecy mwanamke aliyejua ni wa kufa siku yoyote. Kilichomchanganya zaidi ni kugeuka kwa mama Colin kusimama upande wa Cecy wakati mwanzo alimpa moyo wa kumpata mwanaye. Akiwa bado hajajua atafanya nini alipata taarifa iliyomkata maini ya Colin kwenda Afrika ya Kusini na mchumba wake kwa ajili ya mapumziko ya muda mrefu. Lakini hakutaka kukata tamaa alianini njia ya kumpata Colin ni ni kumuua Cecy au kumtia kilema ambacho kitamfanya asiolewe na Colin. Wazo la kuua aliliweka kando kwa muda kwa kuamini lile lingekuwa la mwisho kabisa baada ya mipango ya awali kuferi. Aliamini anaweza kutumia njia nyingi kuhakikisha Cecy aolewi na Colin. Mpango ulikuwa kumwagia tindi kali au kutuma vijana kubaka na picha zake kusambazwa kitu ambacho aliamini Colin na familia yake wasingekivumilia lazima angempiga chini Cecy. Mpango wake alipanga kuupanga kabla ya Colin na mpenzi wake kurudi kutoka Afrika ya kusini. Alijua ndoa ingechukua muda ili kusubiri afya ya Cecy iimalike naye angetumia nafasi ile kumtia doa Cecy na yeye kuichukua nafasi aliyokuwa akiitafuta usiku na mchana kama wokovu baada ya mwenyewe kuichezea shilingi kwenye tundu la choo. Aliapa kutumia kiasi chochote cha fedha kuhakikisha anampoteza Cecy na kulimiliki penzi la Colin. Walijipanga kutafuta watu ambao angewalipa kiasi cha pesa watakachokubaliana ili wamfanyie kazi yake kwa uhakika bila mtu yeyote kujua kitu. Wakati akiwaza hayo taarifa ya kuitwa Afrika ya kusini iliwafikia wazazi wa Colin na Cecy kuwa wanatakiwa mara moja. Japokuwa hawakujua wanaitiwa nini, walikubaliana kuondoka kwenda kuwasikiliza watoto wao wana lipi. Baada ya siku nne Colin na Cecy waliwapokea uwanja wa ndege wa Port Elizabeth na kuwapeleka katika hoteli ya The Beach waliyofikia wao. Wote walifarijika kukuta afya ya Cecy imeimalika haraka na nuru yake ya awali ikianza kuonekana kwa mbali. Ilikuwa furaha kwa familia kukutana wote wakiwa katika hali ya furaha. Usiku wa siku ile baada ya chakula walikaa pamoja kwa ajili ya mazungumzo. Mzungumzaji mkuu alikuwa Cecy ambaye ndiye aliyemuomba Colin aseme yeye. “Wazazi wetu najua mmeshtuka na wito wetu wa ghafla, lakini wito huu una maana kubwa katika maisha yetu watoto wenu. Wito huu ni kwa ajili ya kuja kusimamia harusi ya watoto wenu.” “Watoto wetu kina nani?” mama Colin aliuliza. “Ya mimi na mume wangu Colin ambayo tumepanga kuifunga wiki ijayo.” “He! Mbona haraka sana kwa nini mnataka kufungia huku?” aliuliza mama Cecy. “Mama kuna kitu kiliniijia haraka akilini mwangu ambacho nilikiamini kabisa na nilipomwambia mwenzangu ambaye alikubaliana na nilichokiona na kukubaliana kufunga ndoa huku.” “Kitu gani?” mama Colin aliendelea kuuliza. “Nilifuatilia hatua zote za harusi za mpenzi wangu ambazo huvurugika mwishoni, mfano wa kwanza muda mfupi kabla ya kumuoa Mage lilitokea tatizo lililomjeruhi moyo mpenzi wangu. Mfano wa pili muda mfupi kabla ya ndoa yetu likatokea la kutokea, hivyo imeonesha kuna tatizo. “Nilichokiwaza mimi ni kuhusiana matukio yote hivyo naamini huku tutafunga ndoa isiyo na starehe ambayo itakuwa na baraka ya wazazi wa pande zote. Kwa hiyo wazazi wetu tunaomba mkubali ombi letu ili tukirudi Tanzani tuwe tayari mke na mume. Kuhusu sherehe tutaifanya tukijipanga.” “Mmh! Colin we ulikuwa unasemaje?” mama Colin alimuuliza mwanaye. “Mi namuunga mkono mpenzi wangu amekuwa na jicho la tatu ambalo wote tulikuwa hatuna.” “Mipango ya harusi mmeisha andikisha kanisani?” “Tumeisha kamilisha kila kitu mlikuwa mkisubiliwa ninyi tu.” “Basi hakuna tatizo kwa vile jambo ni la heri tutakuwa pamoja, sijui dada unasemaje?” mama Colin alimuuliza mama Cecy. “Hata mimi naungana na wewe.” Wazazi hawakuwa na pingamizi lolote walikubaliana kusimamia ndoa ya watoto wao ili wakirudi nyumbani Tanzania wajipange kwa sherehe. ***CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ Baada ya taratibu zote kufuatwa Colin na Cecy alifunga ndoa katika kanisa la Roman Cathotic la Mtakatifu Augustine jijini Port Elizabeth Afrika ya Kusini. Ndoa iliyokuwa na watu wachache lakini ilikuwa ni furaha isiyo kifani moyoni mwa Cecy pale alikupoulizwa kama anakubali kuwa mke halali wa Colin katika shida na raha pia Colin kukubali kuwa Cecy ni mkewe katika shida na raha na kifo ndicho kitakacho watenganisha. Baada ya kufunga ndoa waliondoka na kurudi kwenye hoteli waliyofikia na jioni ya siku ile ilifanyika sherehe ndogo katika ufukwe wa hoteli ya The Beach na baadhi ya jamaa zao walikuwa katika mji wa Port Elizabeth. Japo ilikuwa sherehe ndogo iliyoanzia ufukweni na kuishi kwenye ukumbi wa hoteli ile. Ilikuwa sherehe yenye kufana kila aliyekuwepo alifurahia sherehe ile ambayo watu walikunywa na kusaza. Baada ya shehere maharusi waliingia ndani ya chumba cha VIP ambacho walikichukua mahususi kwa ajili ya fungate. Siku ya tatu mama Colin na Cecy walirudi Tanzania na kuwaacha watoto wao wakila fungate. Wakiwa ndani ya ndege kila mtu alimshukuru Mungu kwa kutenda ambalo lililoonekana kwa akili ya kibinadamu limeshindikana. “Yaani unajua dada mpaka muda huu siamini kama nimeweza kuiona harusi ya Cecy na Colin,” alisema mama Cecy. “Si wewe yaani mpaka sasa naamini Mungu akiamua kitenda hutenda jambo.” “Kwangu naona kama muujiza siamini... siamini kama kuna siku nitamuona mwanangu akitabasamu lazima nimshukuru Mungu asante Mungu kwa kila unitendealo.” “Kweli naamini Colin na Cecy wanapendana mapenzi ya dhati.” “Kwa nini unasema hivyo?” “Mwanzo niliamini labda Cecy anampenda mwanangu kwa ajili ya utajiri wake lakini alinionesha hamuhitaji kwa ajili ya mali zake bali mapenzi ya dhati, Pia Colin alinihakikishia hataoa mwanamke mwingine zaidi ya Cecy na alikuwa radhi kuioa maiti na Cecy kama angekufa.” “Ni jambo la kushukuru watoto wetu kupendana ni mwanzo wa kutengeneza familia yenye upendo.” Wazazi wakiwa wanabadilisha mawazo ndani ya ndege jijini Port Elizabeth ndani ya chumba cha VIP katika hoteli ya The Beach, Cecy alikuwa akimuangalia Colin kwa muda mrefu na kuanza kutokwa na machozi kitu kilichomshtua Colin na kuhoji. “Vipi mpenzi wangu mbona unalia?” Cecy hakujibu machozi yaliendelea kumtoka kama maji na kuzidi kumweka mumewe kwenye wakati mgumu. “Mke wangu kuna nini tena? Leo ni siku ya furaha baada ya kufika nusu ya safari yetu kutokana na mitihani mingi. Badala ya kufurahi mke wangu unalia, kipi kimekusibu mpenzi wangu au kama kuna nilichokukosea nipo radhi kwa adhabu yoyote,” Colin alisema huku akisogeza mbele ya Cecy kumpigia magoti. Kabla hajapiga magoti Cecy alikurupuka alipokuwa amekaa na kumuwahi mpenzi na kumvamia na kuwafanya wote waanguke mweleka. “Colin machozi haya si maumivu bali furaha iliyopitiza nashindwa... nashindwa mume kuvumilia. Siamini kama ndoto niliyoota mchana imekuwa kweli, leo hii mimi ni mke wa Colin, asante Mungu asante kwa kila jambo sitaacha kukushukuru usiku na mchana siku zote za pumzi zangu.” “Cecy mpenzi wangu nilikupenda toka siku ya kwanza nilipokuona lakini nilikuta chaguo lingine la mama yangu. Lakini amini uliingia moyoni mwangu toka siku ya kwanza jicho langu lilipokuona. Naamini kabisa jicho la mwanzo lilikuwa sahihi kuliko mtu niliyechaguliwa. “Umekuwa kiumbe wa ajabu ambaye siwezi kumfananisha na kiumbe wa kawaida, umewaze kunipigania japo katika hali yako ya umaskini, lakini ulikuwa radhi ukose kitu chochote chini ya jua ili unipate mimi. Nakuahidi lile jicho lililokuona mara ya kwanza na kukufungulia mlango moyoni mwangu ndilo hilohilo linalokuona ua zuri lililochanua mbele yangu. “Wewe ni mwanamke niliyepewa zawadi na Mungu, nimeamini bundi hawezi kukaa kundi moja na njiwa.” “Una maanisha nini?” “Mage hakuwa njiwa katika safari ya maisha yangu, naamini mbeleni lazima angenitenda, Mungu alilijua hilo ndiyo maana alikuleta wewe wakili wa moyo wangu bila wewe nina wasiwasi ningekuwa nimeisha kufa kwa vile aliuhukumu moyo wangu kifo, lakini umeweza kuutoa moyo wangu kwenye adhabu nzito niliyopewa na Mage sijui usingekuwepo ingekuwaje?” “Colin niliyafuatilia maisha yako kila hatua ni moyo wa upendo ulinisukuma, niliamini kabisa wewe ndiye mume wangu. Nilikupenda sitachoka kukupenda kwa vile kila siku unakuwa kiumbe kipya moyoni mwangu.” “Hata mimi mke wangu.” Walikumbatiana kwa furaha kuifurahi fungate yao iliyokuwa na raha ya aina yake baada ya safari ndefu yenye misukosuko. **** Nchini Tanzani taarifa za mama Colin kwenda afrika ya kusini zilimshtua sana Mage, alijikuta akiwaza huenda Cecy amezidiwa na hivyo amekwenda kuangalia hali yake inavyoendelea. Aliomba kama ni hivyo basi akute Cecy amediziwa na kufariki dunia, lakini bado alibakia na akiba ya mpango wake wa kumfanyia kitu kibaya Cecy kama atakuwa hai ili kuhakikisha ndoa haifungwi. Aliwaandaa watu kwa ajili ya kufanya utekaji na kumfanyia vitendo vichafu, walikubalia kuifanya kazi baada ya Cecy kurudi nchini kutoka Afrika ya kusini. Vijana walimuahidi kumfanyia kazi vizuri kwa vile walikuwa na uzoefu wa kazi zile. Aliwahidi kuwaongeza mara mbili ya malipo waliyokubaliana kama watafanikisha kazi ile. “Sister mbona utakubali kazi yetu, hata ungetaka kichwa chake tungekuletea,” alijisifia wakora. “Sasa damu yenye virusi tutaipata wapi?” “Hilo dogo mbona kuna mshkaji wetu mmoja ameumia tutachukua damu yake kidogo na kumdunga mtu wako.” “Nawaamini msiniangushe.” “Hatujawahi kuharibu kazi hata siku moja, hata kama kuna kazi nyingine we tupe tukufanyie tena tutakupunguzia kwa vile wewe mtu wetu.” “Picha nimewapa?” “Ndiyo sister, tumemcheki vizuri mbona huyu amekwisha.” Baada ya mipango yake kwenda sawa Mage alijipanga kuhakikisha Colin hamuoi Cecy, alipanga baada ya tukio hilo la kumteka Cecy na kumduga damu yenye virusi atumie laini mpya ya simu na kumtumia picha za Cecy akibakwa na ujumbe kuwa ameathirika. Baada kuwaza yote yale alitabasamu na kuamini kila kitu kipo vizuri anachosubiri utekelezaji tu. Akiwa amejipumzisha alipata taarifa toka kwa mama yake kuwa mama Colin amerudi toka Afrika ya kusini. “He! Mbona hajakaa sana, karudi na Colin?” “Hapana karudi peke yake.” “Mbona karudi peke yake kwani alikwenda kufanya nini?” “Kwa kweli sikumuuza.” Mage hakutaka kuuliza swali lingine alinyanyuka na kutoka kuelekea kwa mama Colin kutaka kujua sababu ya safari yake ya Afrika ya kusini na kwa sababu gani hakurudi na Colin. Alitoka hadi kwenye gari na kuchukua aina ya Toyota Harrie na kuelekea kwa mama Colin, aliendesha kwa kasi ili kuwahi kupata taarifa. Alipofika alipaki gari kwenye maegesho, kwa shauku ya kuyajua ya Afrika ya kusini hakufunga hata mlango wa gari. Alitembea mwendo wa haraka hadi mlangoni wa kuiingia ndani. Alibisha hodi na kukaribishwa na mama Colin aliyekuwa amekaa na mama Cecy wakiangalia mkanda wa video huku wakinywa vinywaji. “Karibu ma mkwe,” mama Colin alisema. “A..a..sa..” Alishindwa kumalizia sentesi ambayo ilikatikia njiani baada ya jicho lake kutua kwenye kioo cha runinga alichokiona mbele yake. Ilikuwa vigumu kuamini kama ni kweli au alikuwa akiangalia ni maigizo. Alimuona Cecy katika vazi la harusi akiwa na Colin katika suti ya gharama, alikaza macho kama yanataka kudondoka. “Maa..a..ma.” “Vipi mkwe?” “Huyu si Colin?” alisema huku akinyoosha kidole. “Ndiyo.” “Na..na..huyu si Cecy?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ “Ndiyo.” “Hii si..si..harusi?” “Ndiyo.” “Wameoana lini?” “Leo ni siku ya nne toka waoane na sisi tumerudi jana usiku kutoka huko.” “Mmh! Si kweli, haya ni maigizo tu ili kuniumiza roho.” “Kukuimiza roho ili iweje? Na picha zao hizi hapa.” Mage alizichukua albam akiwa haamini anachoambiwa, aliifungua na kuanza kuangalia picha mojamoja huku mapigo ya moyo yakimwenda mbio. Kila ukurasa alioufunua uliupasua moyo wake alijikuta machozi yamefunika macho na kushindwa kuona picha. Alihisi mapigo ya moyo yakiongeza kasi pumzi zikamjaa na kutoka kwa shida, kiza kizito kilitanda mbele yake kilichoendelea hakukijua. Mage alianguka kama mzigo akiwa amepoteza fahamu, kitendo kile kiliwashtua sana. Walijikuta wakitaharuki ilibidi wamchukue na kumkimbiza hospitali kisha kumjulisha mama yake. Mama Colin alijua kilichokuwa kikiendelea aliamini Mage alipatwa na mshtuko baada ya kuona Colin amemuoa Cecy. Mama yake alifika mara moja hospitali na kukuta tayari mwanaye kaingizwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi. Baada ya vipimo ilionesha alipatwa na mshtuko na kusababisha mishipa ya damu kupasuka na kusababisha apooze upande mmoja. Kwa vile huduma ile haikuwepo alitakiwa kupelekwa Afrika ya kusini haraka kwani walisema ugonjwa ule ikiwa kupata matibabu ya haraka anaweza kupona. Siku ya pili alipelekwa Afrika ya kusini kwa ajili ya matibabu ya haraka katika hospitali ya Mil park. *** Mage alisafiri na mama yake mpaka Afrika ya kusini katika hospitali ya Milpark iliyopo katika jiji la Johannesburg. Alipokelewa na kuanzishiwa matibabu mara moja, madaktari walifanikiwa kufanya upasuaji uliochukua saa tatu kuondoa damu zilizovuja baada ya mshipa kupasuka. Baada ya upasuaji kwenda vizuri alirudishwa kwenye chumba maalumu chini ya uangalizi ya madaktari bingwa. Taarifa za Mage kuumwa zilimfikia Colin aliyekuwa katika mji wa Port Elizabeth. “Mpenzi nasikia Mage anaumwa ameletwa hospitali ya Milpark, Johannesburg,” Colin alimwambia Cecy aliyekuwa akicheza game kwenye Ipad. “Maskini mke mwenzangu nini kimemsibu?” “Nasikia kapata mshtuko baada ya kuona video na picha zetu za harusi.” “Maskini, Mage alikuwa kama fisi aliyeamini siku moja mwanadamu atadondosha mkono.” “Namshangaa kutaka kufa wakati anajua mimi ni wa nani.” “Wa Cecy.” “Najiuliza bila Cecy, Colin leo ningekuwa wapi?” “Anajua Mungu si sisi wanadamu ambao hupokea matokeo.” “Asante mpenzi wangu kwa kuyaokoa maisha yangu, huwezi kuamini baada ya kuachwa ghafla na Mage nilijaa mawazo mengi na kujiona nina mapungufu.” “Asante niseme mimi uliyoyapa majibu mswali yangu kama kuna siku maji yatapanda mlima.” “Nina imani huu ni muda muafaka wa ku-renew mkataba wako na makapuni yote ya mavazi ya majarida. Waliniuliza afya yako nikawaambia hujambo kabisa hivyo wameomba tupange siku ya wao kuja ili uendelee na kazi yako.” “Mpenzi moyoni mwangu nimepanga kwanza nikae na mume wangu kwa mwaka mzima ndipo nifanye kazi nyingine.” “Cecy si tumeishafinga ndoa wasiwasi wako nini?” “Sijaifaidi raha ya ndoa kazi ipo tu, kama wameweza kunisubiri muda wote waendelee kusubiri.” “Makubaliano ya awali ni kwamba tutakuwa tupo pamoja katika kazi zako zote kwa vile mimi ndiye meneja wako.” “Mmh! Kama hivyo sawa.” “Mmh! Bado tu una wasiwasi wa kuibiwa?” Colin alimtania. “Si umesikia mtu kataka kufa baada ya kusikia umeoa, vipi niwe mbali nawe? Nikisikia upo na Mage ningekufa mimi.” *** Baada ya kuwajulisha siku ya kuonana kampuni ya Ebony walifika katika hoteli ya The Beach na kuingia mkataba mpya wa miaka miwili. Pia kampuni ya maonesho ya mavazi na urembo nayo iliingia mkataba mpya na makubaliano ya kuanza kazi baada ya miezi mitatu. Mage naye alitoka hospitali akiwa na afya njema, mama yake alipotaka kujua sababu ya mshtuko ule, alimweleza ukweli kuwa baada ya kuona harusi ya Colin na Cecy alipata mshtuko wa ajabu kilichoendelea hakujua mpaka alipozindukia Hospitali Muhimbili akiwa amepooza upande mmoja. “Unasema nani kaoa? Sijakuelewa vizuri,” mama Mage alishtuka kusikia Colin kaoa. “Colin, mama.” “Muongo! Hiyo harusi imefanyika lini mbona sina habari?” “Ilikuwa ya siri imefanyikiwa Afrika ya kusini.” “Kama ni kweli basi mwanangu achana na mawazo ya Colin, Mungu atakupa mume wa kweli.” “Mama hata mimi nimejifirikia hivyo lakini Colin nilimpenda sana.” “Si kweli, ulimpenda Hans, Colin anapendwa na Cecy kwa hiyo waache na ndoa yao.” “Ndiyo mama, japo nilikuwa na nia mbaya kwa Cecy, lakini kuanzia sasa sitashughulika na Colin wala Cecy nami nasubiri ndoa yangu.” “Hilo ndilo neno la kujasiri mwanangu.” Baada ya Cecy kumaliza mapumziko alianza kazi rasmi, mwaka mmoja baadaye alishika ujauzito na kusubiri muda wa kujifungua. Mage naye alipata mchumba na mambo yalikwenda kama yalivyopangwa. Siku ya harusi akiwa anajiandaa kwenda kanisani anapata habari zilizo mshtua moyo na kufanya apoteze fahamu kuwa mpenzi wake Hans yupo huru baada ya kushinda rufaa yake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ MWISHO
0 comments:
Post a Comment