Simulizi : Dunia Haina Usawa
Sehemu Ya Pili (2)
Mawasiliano yalikuwa yamefanyika kwamba Madam Angelina alitakiwa kuuawa haraka iwezekanavyo. Hakutakiwa kuachwa hai, kitendo cha kutaka kumsaidia Rosemary na familia yake tayari alijiwekea uadui kati yake na watu waliokuwa wamesababisha mwanamke huyo kuwa kwenye hali hiyo.
Vijana waliowatuma walifanya kazi, walifanikisha mpango wa kumteka na muda huo walikuwa safarini kuelekea msituni ambapo ndipo wangefanya mauaji hayo.
Baada ya dakika kadhaa, mwanaume mmoja akapiga simu na kuanza kuzungumza na mtu aliyekuwa Masaki ambaye kazi yake ilikuwa ni kuchukua maelekezo na kuwapa vijana wale.
“Wamefikia wapi?” aliuliza mwanaume huyo kwa sauti nzito.
“Ndiyo wapo njiani kwenda kummaliza,” alijibu huku siku ikiwa sikioni.
“Nimebadili mawazo!”
“Yapi hayo!”
“Asiuawe kama ilivyotakiwa bali anatakiwa kupewa onyo kali!” alisema mwanaume huyo.
“Lakini tutakuwa tumechelewa, nahisi tayari watakuwa wamemuua!” alisema mwanaume huyo.
“Wasiliana nao! Kama bado, waambie waache kufanya hivyo, ila wamwambie akae mbali na familia hiyo, kama ataonekana tena, tutammaliza,” aliikika mwanaume huyo.
Baada ya kukata simu, haraka sana simu nyingine ikapigwa kwenda kwa wale vijana kwa ajili ya kuwapa maagizo aliyokuwa amepewa na mtu aliyemzidi cheo.
Wakati huo ambao simu ilikuwa ikiita ndiyo kipindi ambacho wanaume hao walikuwa msituni na mmoja alishikilia bastola kwa ajili ya kumuua Madam Angelina.
Mwanamke huyo alilia, alisali sala yake ya mwisho, hakuona dalili za kunusurika kifo mahali hapo. Wakati akiwa anamalizia sala ya Baba Yetu, mara simu ya mwanaume aliyeshika bastola ikaanza kulia.
“Halo mkuu!” aliita.
“Umekwishafanya nilichokuagiza?”
“Ndiyo nataka nimuue hapa!”
“Ila bado?”
“Ndiyo!”
“Sasa kuna maagizo mapya!”
“Yapi? Tumchinje kama mbuzi chang’ombe?” aliuliza.
“Hapana! Muacheni ila mumpe masharti kwamba hatakiwi kuisogelea familia ile, vinginevyo, atauawa,” alisema mwanaume huyo na simu kukatwa.
Yule jamaa akabaki akimwangalia Madam Angelina, hakuamini kama alinusurika kuuawa na wakati tayari kila kitu kiliandaliwa na kilichobaki kilikuwa ni kubonyeza kitufe cha kuruhusu risasi itoke.
Akamshika mkono na kumuinua, akamwambia aingie ndani ya gari kitendo ambacho wenzake wote walibaki wakishangaa kwani hayo hayakuwa maagizo waliyokuwa wamepewa, hawakusikia maagizo hayo mapya.
“Vipi tena?” aliuliza jamaa mwingine huku akionekana kushangaa.
“Huyu mwanamke inabidi aende kusali! Tena akasali mpaka ibada za katikati ya wiki. Amepona! Kweli ana Mungu,” alisema jamaa huyo.
“Kwani imekuwaje?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nimepigiwa simu na kuambiwa tumuache huru, aondoke, ila kuna mambo nataka nimwambie,” alisema yule jamaa na kumwangalia Madam Angelina aliyekuwa akilia, hakuamini kama alinusurika.
Alimwambia kama aliyoambiwa kwamba hakutakiwa kujihusisha na familia hiyo, hakutakiwa kujifanya kuwa msamaria mwema kwa familia hiyo, hilo lilikuwa onyo kali na kama angeendelea kuwasaidia basi mwisho wake ungekuwa mbaya, ni lazima angerudishwa tena msituni pale kuuawa.
“Ahsanteni! Ahsanteni!” alisema Madam Angelina.
“Na kilichotokea huku hutakiwi kumwambia mtu yeyote, hata ukimwambia mumeo na tukajua, bado tutakutafuta na kukuua! Umesikia?” alisema mwanaume huyo.
“Ndiyo!”
“Sawa. Ila una Mungu sana! Hudhuria kanisani kila siku! Kupona kwako ni mpango wa Mungu tu,” alisema jamaa huyo na safari ya kurudi mjini kuanza huku Madam Angelina akiwa haamini kama kweli alinusurika kuuawa msituni.
***
Madam Angelina aliogopa, hakuamini kama alinusurika kufa kutoka katika mikono ya watu asiowafahamu ambao walitumwa kwa ajili ya kummaliza. Kila wakati aliikutanisha mikono yake na kuanza kumshuruku Mungu kwa muujiza aliomtendea.
Gari lilirudi mpaka Sayansi, Kijitonyama na kuambiwa kwamba gari lake lilikuwa katika Kituo cha Polisi cha Mabatini. Akateremka, akachukua bodaboda huku akionekana kuhofia mno, hakujiona kama alikuwa salama, hakuona kama alitakiwa kumwambia mumewe kwani aliamini kuwa watu wale wangeweza kumfuata muda wowote ule.
Wakati safari ya kwenda kituoni ikiendelea kichwa chake kilikuwa na mawazo mengi, alikuwa akijiuliza kuhusu wale watu, walitoka wapi na kwa nini hawakutaka kuona akimsaidia Rosemary na watoto wake.
Moyo wake ukauma, ukachoma kupita kawaida. Aliikumbuka familia ile, ilikuwa moja ya familia masikini kuliko za watu wote aliokuwa akiwafahamu. Walishuka kwa kasi kubwa kwenda chini, yeye na mumewe walipanga kuwasaidia lakini mwisho wa siku akatekwa na kupelekwa polisi mpaka simu ilipopigwa na vijana wale kupewa maagizo kwamba hawakutakiwa kumuua.
“Ni nani yupo nyuma ya mpango huu? Na kwa nini hawataki nimsaidie Rosemary na familia yake?” alijiuliza Madam Angelina.
Safari haikuwa ndefu sana wakafika katika Kituo cha Polisi cha Mabatini. Kwa mbali, akaliona gari lake, akamshukuru Mungu, akateremka na kuanza kuelekea ndani ya kituo hicho mpaka kaunta ambapo akawahadithia polisi aliowakuta kila kitu kilichotokea.
Polisi walikuwa kimya wakimwangalia na kumsikiliza. Madam Angelina alisimulia huku akionekana kuumia moyoni, machozi yalikuwa yakimtiririka mashavuni mwake kiasi kwamba polisi wote waliokuwa kituoni hapo wakamuonea huruma.
“Pole sana mama! Ila watu wanapotea sana sasa hivi, nafikiri kuna kitu,” alisema polisi mmoja aliyekuwa na muonekano wa kikakamavu, hata mwili wake ulikuwa na misuli mingi.
“Sisi kama jeshi la polisi ni lazima tupambane kwa ajili ya wananchi wetu, hatutaruhusu kuona jina la nchi yetu likichafuliwa,” alisema polisi mwingine maneno yaliyoungwa mkono na kila mmoja.
Akaandikisha maelezo yote yaliyotakiwa kituoni hapo na polisi walipojiridhisha, wakamruhusu kuondoka na gari lake ambapo breki yake ya kwanza ilikuwa nyumbani kwake.
Alimkuta mumewe akiwa na wasiwasi tele, muda mwingi alijaribu kumpigia simu, haikuwa ikipokelewa mpaka kikafika kipindi simu ikazima chaji na kutokupatikana kabisa.
Alikuwa na hofu, alihisi kwamba kulikuwa na jambo baya lilikuwa limetokea, aliwasiliana na ndugu zake wengine kumuulizia, hakumpata, akawasiliana na marafiki zake lakini kote huko aliambulia patupu mpaka pale ambapo alimuona akiingia ndani ya nyumba hiyo.
Muonekano wake tu ulionyesha kulikuwa na kitu kibaya kimetokea, alizoea kumuona mkewe akiwa kwenye hali ya furaha hata kama kulikuwa na jambo baya, hakuonekana kuwa mwanamke mwenye kuonyesha huzuni zake lakini kwa siku hiyo, Madam Angelina alishindwa kabisa, mumewe aliposimama na kumsogelea tu, akaanza kulia.
“Kuna nini? Kuna nini mke wangu?” aliuliza mumewe, Mzee Paul Semenya.
“Nilitekwa!”
“Ulitekwa? Kivipi? Ilikuwaje?” aliuliza mumewe maswali mawili mfululizo.
Madam Angelina akaanza kumuhadithia kila kitu kilichotokea. Mzee Semenya alikuwa kimya akimsikiliza mkewe, moyo wake ulimuuma kwani suala la kutekwa aliwahi kulisikia sehemu nyingi na hakuamini kama kuna siku hata mke wake angetekwa kama watu wengine.
Huo ndiyo ukawa mwisho wa kuisaidia familia hiyo. Kwa tukio lililotokea waliamini kwamba kulikuwa na watu wabaya ambao walikuwa wakiwafuatilia kwa kila kitu kilichokuwa kikitokea.
Madam Angelina hakutaka kuzungumza na watoto wa Rosemary, kila alipokuwa akielekea kazini, barabarani alikuwa akiwaona, aliumia, maisha yao yalimuumiza moyo wake lakini hakuwa na jinsi, alikuwa akiwapita kama hawaoni kwani alijua kuwa endapo angethubutu kutoa kiasi chochote na kuwasaida, angeweza kutekwa kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.
***
Maisha hayakuwa na afadhali hata siku moja, waliendelea kuteseka mitaani, pale walipokuwa wakiishi hapakuwa salama hata mara moja, hawakuwa na nyumba, kilikuwa ni kibanda kidogo sana ambacho kila walipokuwa wakilala kipindi cha mvua na kunyesha, walilowa na hivyo kukesha macho usiku mzima.
Hawakuyapenda maisha hayo ila hawakuwa na jinsi kwani mtu ambaye waliamini kwamba angewasaidia alikuwa Madam Angelina ambaye mpaka kipindi hicho hakujua alikuwa wapi kwani aliwaahidi kwamba angewarudia tena na kuwasaidia lakini, hakuonekana.
“Mama! Mbona Madam Angelina harudi?” aliuliza Godwin huku akimwangalia mama yake.
“Atarudi tu! Labda amepata matatizo! Ila atarudi tu,” alijibu Rosemary huku akimwangalia Godwin, japokuwa alimtia moyo lakini alijua kabisa kwamba ilikuwa ni vigumu kwa mwanamke huyo kurudi tena mahali hapo.
“Kwa hiyo tumsubiri tu?” aliuliza Irene.
“Ndiyo! Tuendelee kumsubiri! Atarudi na nyie mtakwenda shuleni tena,” alisema Rosemary.
“Sawa mama!”
Mama yao aliwaambia kwamba Madam Angelina angerudi tena, walimwamini mama yao, hawakuwahi kumsikia akiwadanganya na kila siku alikuwa mkweli na kila kitu ambacho aliwaambia, haikuchukua muda mwingi, kilitokea.
Walikuwa wavumilivu, waliendelea kusubiri, maisha yaliwapiga lakini mioyo yao iliendelea kuwaambia kwamba Madam Angelina angerudi tena na kuwasaidia kama alivyowaahidi kipindi cha nyuma.
Mwezi wa pili ulipoingia na kukatika tangu mara ya mwisho kuonana nao, wakajua kabisa mwanamke huyo asingeweza kurudi tena nyumbani hapo. Hawakujua ni kitu gani kilitokea, kwa jinsi alivyokuwa akizungumza nao kipindi cha nyuma, aliwaonyeshea kila dalili kwamba angerudi tena na kuwasaidia kama alivyokuwa amewaambia.
“Mama! Ndiyo basi tena! Madam hatoweza kurudi tena,” alisema Godwin huku akionekana kuumia mno. Alitamani sana kurudi shuleni, mwanamke huyo aliwaahidi mambo mengi likiwemo suala la kurudi shuleni na kusoma lakini mwisho wa siku, hakurudi, hata kuonekana mbele ya macho yao hakuweza kuonekana tena.
“Tuendelee kusubiri! Naamini kwamba kuna siku atarudi tena. Godwin! Mchungaji huwa anasemaje kuhusu maisha yetu?” aliuliza Roseemary.
“Kuwa na imani!”
“Unaamini kama atarudi tena?”
“Mama! Lakini….”
“Amini mwanangu. Atarudi tena na mtakwenda shuleni kwa mara nyingine. Hili ni jaribu na lazima mkumbuke kwamba kwenye kila jaribu, Mungu ameweka mlango wa kutokea,” alisema Rosemary maneno ambayo kidogo yakawatia nguvu watoto wake na kukubaliana naye kwamba ipo siku Madam Angelina angerudi tena, hawakujua kile kilichokuwa kimemtokea mwanamke huyo.
****
“Mkuu! Kuna simu imepigwa,” alisikika mwanaume mmoja akimwambia kiongozi wake.
“Kutoka wapi?”
“Makao makuu!”
“Inasemaje?”
“Nimepewa maelezo kwamba yule mwanamke anatakiwa kuuawa,” alisema mwanaume huyo.
“Mwanamke gani?”
“Rosemary!”
“Kwa nini umekuwa ni uamuzi wa ghafla namna hiyo?” aliuliza mwanaume aliyepewa ujumbe huo.
“Sijajua! Ila hilo ni agizo!”
“Sawa.”
Hakukuwa na mtu aliyebisha, hayo yalikuwa maagizo kutoka makao makuu kwamba Rosemary alitakiwa kuuawa wakati wowote ule. Watu ambao walisababisha kuwa mahali hapo hawakutaka kumuona akiendelea kuishi, walitaka kummaliza kwani uwepo wake ungeweza kuwasababishia gharama kubwa kwa ajili ya kuwalipa watu ambao kila siku walitakiwa kumfuatilia alikula nini na alifanya nini.
Mikakati kabambe ikaanza kupangwa, kila mmoja alitakiwa kumwambia mwenzake hatua ambayo walitakiwa kuichukua haraka iwezekanavyo. Kikao cha siri cha watu watatu kikawekwa ndani ya chumba kimoja kikubwa kilichokuwa na meza ndogo na viti vitatu.
Wanaume hao waliovalia suti walikaa huku wakiwa na karatasi zao, walikuwa na kalamu kwa ajili ya kuchora ramani ya mauaji ambapo kusingekuwa na mtu yeyote ambaye angegundua kitu chochote kile.
Walikubaliana kwamba wamuue kwa kumuwekea sumu kwenye chakula ila baada ya kufikiria kama kungekuwa na urahisi wa kumpa chakula, wakaona lingekuwa jambo gumu sana hivyo wakakubaliana kumuua kwa kumpiga risasi.
“Lakini ni lazima isionekane kama ameuawa,” alisema mwanaume mmoja.
“Ndiyo!”
“Sasa hamuoni kama tukimuua kwa kumpiga risasi itagundulika kama ameuawa?” aliuliza jamaa mmoja.
“Hilo nalo neno! Kweli kabisa. Sasa kifo gani?”
“Tumgonge na gari! Tuna sababu ya kusingizia kwamba gari lilikatika breki! Halafu hata kama tukiomgonga na kusepa, nani atagundua kama ameuawa? Mbona kuna madereva wengi wanaua na kusepa! Nadhani hakuna tatizo,” alisema mwanaume mwingine.
Wakakubaliana kwamba Rosemary alitakiwa kuuawa kwa kugongwa kwa gari hivyo walitakiwa kupanga vijana kwa ajili ya kuifanya kazi hiyo haraka iwezekanavyo.
“Sawa. Wapigie simu vijana. Mpaka kesho mchana tupewe taarifa ya kifo chake,” alisema mwanaume mmoja.
“Hakuna tatizo!”
Wakakubaliana na kikao kufungwa, kilichobaki kilikuwa ni utekelezaji tu.
Rosemary aliishi kwa kujificha, kila alipokuwa akitoka nje ya kibanda chake alikuwa akijifunga kilemba na uso wake, asilimia kubwa ulikuwa umefunikwa kwa kitambaa kikubwa.
Hakutaka kujulikana, hakutaka kuona akigundulika na watu wengine kwani ingekuwa aibu kubwa kwa taifa, aibu kubwa kwa viongozi wa Chama cha Tanzania National Party ambao mpaka wakati alipoanza kupata matatizo hakukuwa na mtu aliyejali, kila mmoja alimpuuzia kana kwamba hakukuwa na mtu aliyeyaona matatizo aliyokuwa akipitia.
Aliamua kuishi maisha yake na familia yake, hakutaka kumbughudhi mtu yeyote yule. Japokuwa alikuwa akiumia moyoni mwake lakini hakuwa na jinsi, hakutaka kuona watoto wake wakiyaona maumivu makubwa yaliyokuwa moyoni mwake, alitaka watoto wake waamini kwamba katika kila hatua waliyokuwa wakipitia, hakuumia kama alivyotakiwa kuumia.
Wakati Godwin na Irene wakiwa barabarani kuombaomba pesa, yeye alikuwa akibaki nyumbani, aliandaa chakula cha mchana ambapo walirudi kula na baadaye kurudi tena barabarani kama kawaida yao.
Siku ya Jumamosi, katika tarehe 1 mwezi wa 5, siku ambayo wafanyakazi huadhimisha siku yao ndiyo siku ambayo mauaji ya mwanamke huyo yalitakiwa kufanyika kama ilivyopangwa.
Alikuwa ndani ya kibanda chake akiandaa chakula kama kawaida. Ilipofika majira ya saa nne asubuhi, huku akiwa amejipumzisha katika maboksi yaliyokuwepo ndani ya kibanda hicho ambayo waliyafanya kama kitanda, ghafla gari moja, Land Cruiser nyeusi ikasikika ikija kwa kasi kule alipokuwa.
Hakuogopa, ilikuwa ni kawaida kwa kuwa kibanda chake hakikuwa mbali sana na barabara ya vumbi ambapo magari machache yalikuwa yakipita mara mojamoja. Ghafla, akiwa ndani ya kibanda hicho huku hajui hili wala lile, gari hilo likakigonga kibanda kile, akaanguka, matairi ya gari hilo yakapita tumboni mwake.
Watu wote waliolishuhidia tukio hilo wakashika vichwa, hawakuamini kile walichokiona, hata kabla hawajashika namba za gari lile vizuri, likaondoka mahali hapo kwa kasi kubwa.
“Mungu wangu! Kuna mtu mule?” aliuliza jamaa mmoja, hata kabla jibu halijatolewa, sauti ya mwanamke ikaanza kusikika kwa shida.
Sauti hiyo ndiyo iliwashtua watu kusogea kule kilipokuwa kibanda kile, kila mtu alishika kichwa kwa majonzi, hawakuamini kile walichokuwa wakikiona. Rosemary alikuwa chini, alishika tumbo lake huku akilia kwa maumivu makali.
Kabla ya kumsogelea, watu wale wakaanza kumwangalia, aliumia vibaya, ubavuni mwake kulibonyea kuonyesha kwamba mbavu zake zilikuwa zimevunjika na damu kuvilia kwa ndani pasipo kuonekana kwa nje.
“Jamani tumpelekeni hospitali,” alisema mwanaume mmoja.
Huo ndiyo uamuzi walioufanya, hawakutaka kumuacha, wakambeba na kumpeleka katika barabara ya lami ambapo hapo wakapata msaada wa gari moja na kuanza kumpeka katika Hospitali ya Palestina iliyokuwa Sinza.
Ndani ya gari kila mtu alimuonea huruma Rosemary, pale alipokuwa alikuwa akilia kwa maumivu makali, hakutoka damu hali iliyoonekana kuwa mbaya zaidi kwani ilionyesha kwamba damu ilivilia kwa ndani na hivyo kusababisha hatari kubwa kwa maisha yake.
Kila mmoja alikuwa akilizungumzia gari lililomgonga mwanamke huyo, hakukuwa na mtu ambaye aliziona vizuri namba za gari lakini kijana mmoja aliwaambia wenzake kwamba gari ambalo lilimgonga mwanamke huyo lilikuwa na namba za serikali.
“Unasemaje?” aliuliza jamaa mwingine kwa mshtuko.
“Lile gari lina namba za serikali!”
“Namba za serikali?”
“Ndiyo!”
“Una uhakika?”
“Ndiyo kwa sababu niliziona herufi zake,” alisema kijana huyo.
Kila mmoja aliongea lake, hawakuamini kama dereva wa serikali angeweza kufanya unyama kama huo kwani hata kama alimgonga kwa bahati mbaya basi ilikuwa ni lazima ateremke na kumsaidia na si kukimbia kama alivyofanya.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika hospitali hiyo ambapo moja kwa moja machela ikasogezwa na mwanamke huyo kupakizwa kisha kuanza kusukumwa kuelekea ndani.
Kila mtu alishangaa, walimuona Rosemary akilia lakini hawakujua tatizo lilikuwa nini. Hakutoka damu hivyo kila mtu aliyekuwa akimwangalia aliona kuwa mwanamke huyo alikuwa na tatizo la kawaida, kuumwa na tumbo au maumivu mengine.
“Kuna nini?” aliuliza daktari mmoja, mwanaume aliyekuwa na ndevu nyingi nyeupe huku akiwa na mashine ya kusikilizia mapigo ya moyo.
“Amegongwa na gari!”
“Amegongwa na gari?” aliuliza daktari huyo huku akionekana kushangaa.
“Ndiyo!”
“Mleteni huku.”
Manesi wawili wakaisukuma machela ile mpaka katika chumba cha upasuaji ambapo huko madaktari walitakiwa kuangalia tatizo kubwa alilokuwa nalo mwanamke huyo.
Baada ya kusikia kwamba mwanamke huyo aligongwa na gari, walishangaa, hakukuwa na mtu aliyekuwa na uhakika wa mwanamke huyo kupona kwani kitendo cha kugongwa na damu kuvilia ndani kwa ndani kilikuwa kitu kibaya mno kutokea kwa mtu yeyote yule.
“Sidhani kama atapona,” alisema dokta huyo kimoyomoyo, pamoja na ubingwa wake katika mambo ya matibabu lakini yeye mwenyewe hakuwa na uhakika kama mwanamke huyo angeweza kupona.
***
Godwin na Irene walikuwa barabarani kama kawaida, waliendelea kuomba huku wakitembea huku na kule. Kila gari ambalo lilisimama katika foleni walilifuata na kuanza kuomba kwa kugonga kioo, wengine walioguswa na maisha yao waliwasaidia lakini wengine hata kufungua vioo hawakufanya hivyo.
Waliendelea kama kawaida, hawakutaka kuacha, ili mama yao nyumbani apike ilikuwa ni lazima kuomba pesa mitaani na kumpelekea. Walizunguka mpaka ilipofika majira ya saa kumi na moja jioni ndipo wakaanza kurudi katika kibanda walichokuwa wakiishi.
Walichokikuta, hawakuamini macho yao, kibanda kile ambacho ndicho walichokuwa wakikitumia kama nyumba yao kilikuwa kimevunjwa, hakukuwa na mtu aliyejua kilichotokea, wakahisi kulikuwa na jambo la hatari lilikuwa limetokea.
Wakaanza kukimbia kuelekea kule huku wakimuita mama yao. Walipofika, wakaanza kulia, mama yao hakuwepo, wakajaribu kutoa mbao kwa kuhisi kwamba inawezekana alikuwa amefunikwa na mbao hizo pamoja na mabati lakini hawakuambulia kitu.
Hawakujua ni kitu gani kilitokea. Walibaki wakilia, majirani zao waliokuwa pembeni kabisa na mahali pale ndipo wakawafuata na kuwaambia kile kilichokuwa kimetokea.
“Wamemuua mama!” alisema Godwin huku akionekana kushtuka.
Hawakutaka kubaki mahali hapo, wakaambiwa mahali mama yao alipokuwa, wakaanza kukimbia kuelekea huko. Kila mmoja alikuwa akilia kwa maumivu makali, hawakuamini kile kilichokuwa kimetokea.
Hawakuwa radhi kuona mama yao akifariki, walimpenda, alikuwa kila kitu katika maisha yao, kitendo cha kumuua mama yao kilimaanisha kwamba wangebaki yatima maisha yao yote.
Njiani, watu walikuwa wakiwashangaa, walikuwa watoto wa mitaani, wengine walihisi kwamba walikuwa wezi na kuangalia kama kulikuwa na watu waliokuwa wakiwakimbiza.
Walichukua dakika thelathini mpaka kufika katika hospitali hiyo ambapo wakamsimamisha nesi mmoja na kumwambia kuhusu mama yao aliyepelekwa mahali hapo saa kadhaa zilizopita.
“Yule aliyeletwa mchana wa leo?” aliuliza nesi.
“Ndiyo!” alijibu Godwin, muda wote Irene aliyekuwa pembeni yake alikuwa akilia tu.
“Twendeni!”
Wakaanza kumfuata nesi yule, wakaongozana naye mpaka katika ofisi ya daktari na kuugonga mlango ambapo wakakaribishwa. Kitendo cha kumuona daktari huyo tu, Godwin akashindwa kuvumilia, naye akaanza kulia mfululizo kama ilivyokuwa kwa ndugu yake.
“Kuna nini tena?” aliuliza daktari huku akishangaa.
“Hawa ni watoto wa yule mama!” alijibu nesi.
“Mama yupi?”
“Yule aliyeku…” alijibu nesi lakini hata kabla ya kumalizia jibu lake akanyamaza na harakaharaka kutoka ndani ya chumba hicho.
“Mama amekufa? Mama yetu amekufa?” aliuliza Godwin huku akiisogelea meza ya daktari ambaye alibaki kimya, hakujua ni kitu gani angewaambia watoto hao, hakujua kama alitaka kuwaambia ukweli juu ya kilichotokea au kuwadanganya.
“Mama yetu amekufa?” aliuliza Godwin, tayari alianza kulishika koti la daktari huyo. Maumivu makali aliyokuwa nayo moyoni mwake, hayakuweza kusimulika.
***
Hawakuambiwa kuhusu mama yao lakini muonekano aliokuwa nao daktari ulionyesha kabisa kwamba mama yao alikuwa amefariki dunia. Waliumia, walilia mno humo ndani, Godwin hakutaka kuliachia koti la daktari, alilishikilia huku akiendelea kumsisitiza amwambie ukweli kuhusu mama yao kwamba alikuwa amekufa au la.
Daktari alinyamaza, alimlaumu nesi kwa kuongea sentensi ambayo haikumalizika, ambayo kwa mtu yeyote yule angegundua kwamba mwanamke huyo alikuwa amekufa.
Huo ndiyo ulikuwa ukweli, Rosemary, mwanamke shupavu alikuwa amefariki dunia. Alivunjika mbavu, mapafu yake yalipasuka hali iliyopelekea kifo chake.
Manesi na madaktari waliumia kwani walijitahidi sana kuyaokoa maisha ya mwanamke huyo lakini ilishindikana kabisa. Hawakumjua ndugu yeyote yule, hawakujua kama mwanamke huyo alikuwa wa mitaani tu, hakujua kama yule aliyekuwa akimtibu alikuwa Rosemary, mke wa Mapoto, mwanaume aliyekuwa na kiu kubwa ya kuibadilisha Tanzania.
“Nyamazeni! Huu si mwisho wa maisha yenu. Kama Mungu alivyokuwa akiwalinda, ataendelea kuwalinda,” alisema daktari huku akiwaangalia watoto hao waliokuwa wakiendelea kulia.
“We want her back! Lord! Why? Why us?” (Tunamtaka arudi! Bwana! Kwa nini? Kwa nini sisi?) aliuliza Godwin huku akilia.
Daktari alishtuka, hakuamini kama watoto hao walikuwa wakijua kuzungumza Kiingereza, walionekana kuwa watoto wa mitaani kama wengine, hakuamini kama watoto hao walikuwa wamepitia maisha ya kifahari kwani muonekano wake ulifanana na watoto wengine.
Alibaki akiwashangaa, alitamani kuwauliza ni kwa namna gani waliifahamu lugha hiyo lakini alishindwa kabisa kutokana na hali waliyokuwa nayo mahali hapo.
Akawachukua na kuwapeleka nje, akawaweka kwenye benchi na kuwataka wapumzike mahali hapo. Hawakunyamaza, bado waliendelea kulia kwa uchungu mkubwa, mioyo yao iliumia na hawakujua wangeweza kuishi vipi pasipo mama yao ambaye alikuwa kila kitu katika maisha yao.
Watu waliokuwa mahali hapo walikuwa wakiwaangalia, hawakuwafahamu, walionekana kutoka katika familia ya kimasikini, muonekano wao uliwafanya kuona kwamba walikuwa watoto wa mitaani tu.
“Kuna nini? Wamepatwa na nini tena?” aliuliza jamaa mmoja huku akiwaangalia.
“Mmh! Sijui! Labda wamefiwa!”
“Haiwezekani! Nahisi kuna kitu kingine zaidi,” alisema jamaa huyo.
Walilia, walihuzunika sana lakini machozi na huzuni zao zilishindwa kubadilisha kitu chochote kile, walishindwa kuubadilisha ukweli, mama yao hakurudi, alikuwa amefariki dunia na hivyo kuiomba hospitali hiyo kusimamia mazishi kwani hawakuwa na kitu chochote kile.
Baada ya siku mbili, Rosemary akazikwa katika makaburi ya Sinza na hivyo Godwin na Irene kuanza maisha mapya, maisha bila mama. Maisha hayakuwa kama walivyozoea, yalibadilika, muda mwingi walitawaliwa na majonzi mazito, walilia kila siku.
“Mama aliuawa!” alisema Godwin huku akimwangalia Irene.
“Unasemaje?”
“She was murdered,” (aliuawa!)
“How do you know?” (umeajuaje?) aliuliza Irene huku akimshangaa kaka yake ambaye hakujibu kitu, akanyamaza huku akionekana kuwa na hasira kali moyoni mwake.
***
Kila kitu kilichokuwa kimepangwa kilifanyika kama kilivyotakiwa kufanywa. Mwanaume mwenye mwili mkubwa ambaye alitumwa kwa kazi ya kumuua Rosemary akarudi ofisini na kupeleka taarifa kwamba kila kitu kilikuwa kimefanyika kwa mafanikio makubwa ya asilimia mia moja.
Taarifa hiyo ilimfurahisha kila mmoja, wakapongezana kwamba hatimaye walikuwa wakienda kukamilisha lengo lao walilokuwa wamejiwekea. Hakukuwa na mtu aliyekuwa na huruma, hakukuwa na mtu aliyehuzunika juu ya kifo cha Rosemary, kila mmoja alionekana kuwa na furaha na kubwa zaidi wakaweka pombe kwenye glasi zao na kuanza kunywa.
“Na watoto wake?” aliuliza mwanaume mmoja.
“Nao wafe. Kwa kifupi ni kwamba familia nzima ipotee katika uso wa dunia,” alisema jamaa mwingine.
“Kwa hiyo nitume watu wakawaue?”
“Hapana! Subiri kwanza waishi maisha yenye majonzi, mioyo yao iume kila siku, baada ya hapo, tutawaua,” alisema mwanaume huyo maneno ambayo yaliungwa mkono na kila mmoja mahali hapo.
****
Mwezi mmoja ulikuwa umepita, maisha yao yaliendelea kuwa ya mitaani. Hawakuwa wamehama pale walipokuwa, kibanda kile ambacho kilikuwa kimebomolewa ndicho hichohicho wakakisimamisha na kuendelea na maisha yao kama kawaida.
Baada ya siku kadhaa, Godwin akakutana na kijana mmoja, masikini kama alivyokuwa na kumpa kazi ambayo kama angeifanya, hakika wangeingiza kiasi kikubwa cha fedha.
“Una uhakika tutapata pesa?” aliuliza Godwin huku akimwangalia mwanaume huyo.
“Ndiyo! Watu wengi wanajenga, tena majumba makubwa. Tukafanye hivyo huko,” alisema jamaa huyo.
Hicho ndicho walichokipanga kufanya. Godwin akamwambia Irene kwamba alipata kazi ya ujenzi, kuwa mmoja wa wasaidizi wa mafundi waliokuwa wakijenga nyumba mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Irene alifurahi lakini moyo wake ulikuwa mzito kukubaliana na Godwin, alikuwa na hofu kubwa moyoni mwake na alihisi kama kulikuwa na jambo baya lililokuwa likienda kutokea.
Hakutaka kumficha Godwin, alimwambia ukweli jinsi alivyokuwa akijisikia moyoni mwake. Alijua fika kwamba angemtia hofu kaka yake lakini hakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima amwambie jinsi alivyokuwa akijisikia.
Godwin alipoambiwa, kwanza akacheka, akamwambia Irene kwamba hakutakiwa kuwa na hofu yoyote ile kwani kila kitu kingekuwa salama kama inavyotakiwa kuwa.
“Una uhakika?”
“Niamini Irene! Hakuna baya lolote lile,” alisema Godwin.
Baada ya siku tatu, kijana yule aliyeongea naye, Albert Mazongozongo akafika katika kibanda hicho na kumchukua kwenda katika moja ya ghorofa kubwa lililokuwa likijengwa Masaki jijini dar es Salaam.
Kabla ya kuanza kazi hiyo, aliyaona maisha yake yakibadilika, aliamini kwamba kama angefanya kazi hizo za ujenzi basi maisha yake na Irene yangebadilika milele.
Kazi ikaanza, huko akakutana na mafundi wengi, wakaanza kulijenga jengo hilo huku wakilipwa kiasi cha shilingi elfu saba kwa siku. Ilikuwa ni kazi kubwa na ngumu lakini alihakikisha anapambana nao kila siku.
Alipokuwa akirudi, alikuwa akichoka sana, alifikia kulala mpaka siku nyingine aliporudi tena. Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake kila siku. Kutokana na ucheshi wake, akajikuta akipata marafiki wengi, akapendwa na hata wakati mwingine kupewa michongo mingine ya kazi nyingine nyingi.
“Utakuwa unapeleka hizi nondo kwenda kule juu. Kuwa makini na ngazi,” alisema jamaa mmoja, fundi mkuu, alikuwa akimwambia Godwin.
“Haina tatizo!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Chukua kofia ngumu uvae!”
“Mkuu! Kofia ngumu na hili joto! Kichwa kitawaka, wala usijali,” alisema Godwin.
“Basi sawa.”
Siku hiyo kazi yake kubwa ilikuwa ni kupandisha vifusi kwenda ghorofa ya saba. Ilikuwa kazi kubwa na ngumu kwani nondo zenyewe zilikuwa nzito mno. Alizipandisha kwa mahesabu makubwa, kazi hiyo ilichukua saa mbili, akamaliza na kwenda kupumzika chini.
Sehemu aliyokaa haikuwa sehemu salama, kwa juu kulikuwa na vifusi vya kokoto na mchanga vilivyokuwa vimewekwa katika chombo kimoja kwa kilichokuwa kikivutwa na kamba ngumu kupelekwa juu.
Wakati kila mmoja akiwa hana habari, huku Godwin akiwa chini amepumzika, ghafla kamba ngumu iliyokuwa imeshikilia chombo kilichobeba vifusi vile ikakatika na vifusi hivyo kuanza kuanguka chini.
Walioliona tukio hilo wakaanza kupiga kelele, vifusi hivyo vilianza kuangukia kule alipolala Godwin. Wakati akishtuka kutokana na kelele za mafundi wengine, hata kabla hajachukua uamuzi wowote mahali hapo, vifusi zaidi ya kumi na tano vikamuangukia pale alipokuwa na kumfunika.
“Mungu wangu!” alisema jamaa mmoja huku wakishuka kwa kasi kuelekea kule alipokuwa Godwin ambaye alifunikwa na vifusi zaidi ya kumi na tano.
“Toa vifusi….toa vifusi,” alisema fundi mmoja akiwaambia wenzake, kila mtu alichanganyikiwa na walichokijua ni kwamba Godwin alikuwa amekufa mahali pale kwani vifusi vilivyokuwa vimemwangukia vilikuwa vyenye mchanga na kokoto nyingi.
***
Kila mmoja alichanganyikiwa, hawakujua kama Godwin aliyekuwa chini ya kifusi alikuwa hai au alikufa. Waliogopa, vifusi vile vya mchanga na kokoto vilikuwa vizito mno na hata walipokuwa wakivitoa, walipata wakati mgumu mno.
Walisaidiana, walivitoa vyote juu yake na kisha kumfikia yeye. Alikuwa kimya, damu zilikuwa zikimtoka kichwani, alitulia, kwa kumwangalia harakaharaka alionekana kama mfu mahali pale.
“Mungu wangu!” alisema jamaa mmoja huku akishika kichwa kwa mshtuko.
Wakamtoa mahali pale, kwa haraka sana wakamkimbizia kwenye gari na kuanza kuelekea naye hospitalini. Kila mmoja alikuwa na hofu juu ya hali aliyokuwa nayo Godwin, mapigo yakeya moyo yalikuwa yakidunda kwa mbali sana kiasi kwamba kila mmoja akahisi kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wake.
Rafiki yake, Albert alikuwa kimya, aliogopa, hakuona kama kulikuwa na dalili za Godwin kupona. Kichwani mwake akaanza kumfikiria Irene, hakujua ni kwa kiasi gani angeumia kama angemwambia kwamba kaka yake mpendwa, alikuwa katika hali mbaya na muda huo walikuwa njiani kuelekea hospitalini.
Hawakuchukua muda mwingi wakafika katika Hospitali ya Mwananyamala ambapo gari lilipoingia, kwa haraka sana machela ikaletwa, akapakizwa juu na kuanza kusukumwa kuelekea ndani.
Kila mtu aliyekuwa akimwangalia Godwin, alishika kichwa, hakukuwa na aliyeamini kama kijana huyo angepona kwani kwa muonekano aliokuwa nao, damu zilizokuwa zikiendelea kumtoka, kila mmoja aliamini kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wake.
“Nini jamani? Ajali?” aliuliza nesi mmoja huku akimshangaa Godwin kana kwamba hakuwahi kupokea mgonjwa aliyekuwa kwenye hali mbaya kama aliyokuwa nayo Godwin.
“Yeah! Ameangukiwa na vifusi saiti! Tunaomba mumsaidie jamani, jembe letu hili!” alijibu jamaa mmoja.
Mtihani mkubwa ukabaki kwa Albert, bado kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, mtu aliyekuwa akimfikiria alikuwa Irene ambaye hakujua angezipokeaje taarifa za kaka yake kupata ajali mbaya ya kuangukiwa na vifusi saiti.
Hakutaka kuondoka hospitalini hapo, alitaka kujua ni kitu gani ambacho kingeendelea. Alibaki kwenye mabenchi pamoja na wenzake, kwa zaidi ya saa moja walikuwa hapo mpaka hao wenzake walipoamua kuondoka na yeye kubaki.
Hakutaka kumuacha Godwin mahali hapo, alikuwa rafiki yake mkubwa, alimzoea na kwa kipindi hicho alikuwa akiishi naye kama ndugu yake wa damu. Pale kwenye benchi, alikuwa akimuomba Mungu, hakutaka kuona Godwin akifa, hakutaka kuona Mungu akiichukua roho yake.
Baada ya saa mbili, Godwin akapelekwa katika wodi ya wagonjwa wengine na kulazwa humo. Japokuwa kulikuwa na wagonjwa wengi lakini hawakuacha kumwangalia Godwin aliyekuwa kwenye hali mbaya kuliko hata wagonjwa wengine waliokuwa katika wodi hiyo.
Muda wa kuona wagonjwa ulipofika, Albert akaelekea katika wodi ile na kusimama pembeni ya kitanda alicholazwa Godwin, alikuwa akimwangalia, moyo wake ulikuwa kwenye majonzi tele, hakuamini kama rafiki yake huyo alikuwa kwenye hali hiyo, alimwangalia kwa masikitiko makubwa, akashindwa kuyazuia machozi yake ambayo yalianza kumtiririka.
Moyo wake ulimuuma mno, alimchukulia Godwin kama ndugu yake ambaye alimpa nafasi kubwa katika maisha yake, kitu kilichomuhuzunisha ni ajali mbaya aliyokuwa ameipata, aliumia kwa kuwa yeye ndiye aliyemtafutia kazi hiyo ambayo ilionekana kuyabadilisha maisha yake na kumlaza kitandani.
Hakukaa sana hospitalini hapo, muda ulipokwisha, akaondoka kurudi nyumbani. Bado alikuwa akijifikiria namna ya kumfikishia Irene ujumbe kwamba kaka yake alikuwa hoi hospitalini, hakujua binti huyo angezipokeaje taarifa hizo.
Wakati mwingine alisita kwenda huko lakini wakati mwingine aliona kwamba kulikuwa na umuhimu mkubwa wa kwenda nyumbani hapo kwani iwe isiwe ilikuwa ni lazima ajue kuhusu kile kilichoendelea kwa kaka yake.
Hakuwa na jinsi, akaondoka na kuelekea huko. Hakuchukua muda mrefu akafika katika kibanda hicho, akapiga hodi na kuingia ndani. Hakuonekana kuwa na furaha, alitamani kutoa tabasamu kumdanganya Irene lakini ilishindikana kabisa, uso wake ukavaa sura ya kile kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake.
“Kuna nini? Godwin yupo wapi?”aliuliza Irene huku akimwangalia Albert aliyeonekana kuwa na huzuni tele machoni mwake.
Albert hakujibu kitu, akabaki kimya akimwangalia msichana huyo, hakujua ni kitu gani alitakiwa kumwambia, hakujua ni kwa jinsi gani msichana huyo angeumia moyoni mwake.
Irene akahisi kulikuwa na jambo baya lililokuwa limetokea kwani kama kusingekuwa na jambo baya, Albert angemjibu swali lake au angekuja kibandani hapo akiwa na kaka yake. Akamlazimisha mno kumwambia, hata kama alikuwa amekufa, amwambie kwani hata kama angemficha ilikuwa ni lazima aujue ukweli.
Albert hakuwa na jinsi, akaanza kumuhadithia Irene kilichokuwa kimetokea. Moyoni mwake aliumia lakini hakuwa na jinsi. Irene alikuwa kimya akimsikiliza Albert, alionekana kuwa katika hali ya kawaida lakini wakati ambao Albert alimaliza kumuhadithia, hapohapo akaanza kulia kwa sauti kubwa.
Aliumia moyoni mwake, hakuamini kilichokuwa kimetokea, moyo wake ulichoma kupita kawaida, kitendo cha kuambiwa kwamba kaka yake alikuwa kwenye hali mbaya ilimuuma mno.
Wazazi wao walikufa, walibaki wawili tu lakini jambo la kuumiza kabisa, kaka yake alikuwa njiani kufa kitu ambacho kingemfanya kubaki peke yake. Aliumia, hakutaka kuona hilo likitokea maishani mwake.
Alitaka kumuona kaka yake, hata kama alikuwa kwenye hali mbaya, hata kama alikuwa amekufa, alitaka kuiona maiti yake. Alikuwa akipika, akaacha kupika na kutoka ndani ya kibanda hicho.
Alijua mahali Hospitali ya Mwananyamala ilipokuwa hivyo kuanza kukimbia kuelekea huko. Moyo wake ulihuzunika, njiani alionekana kuwa kama kichaa, kila mtu alimwangalia, khanga yake aliyoivaa ilianza kumvuka na kubaki na sketi lakini hakujali, kubaki mtupu kwake halikuwa jambo baya, kitu cha muhimu alichokuwa akikihitaji wakati huo ni kujua hali ya kaka yake tu.
Wakati akikimbia kuelekea hospitalini, naye Albert alikuwa nyuma yake akimkimbiza huku akimtaka asimame na wazungumze kwanza. Si kwamba Irene hakusikia, alisikia lakini hakuwa radhi kusimama.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika hospitalini hapo. Kama kulia, Irene alikuwa amelia vya kutosha, aliumia pasipo kawaida. Akaingia ndani ya eneo la hospitalini hapo, haukuwa muda wa kuona wagonjwa hivyo akazuiliwa.
“Irene! Ungenisubiri kwanza,” alisema Albert huku akihema kwa nguvu.
“Nimeumia. Ninataka kumuona kaka yangu, ninataka kumuona Godwin,” alisema Irene huku akilia, akamsogelea Albert, akamkumbatia na kuendelea kulia kifuani mwake.
Kila mtu aliyemuona Irene alimuonea huruma, alikuwa akilia sana kana kwamba alikuwa amefiwa na kaka yake. Wakaondoka karibu na sehemu ya kuingilia ndani ya jengo la hospitali na kuelekea sehemu ya kupumzikia watu wanaofika mahali hapo kwa ajli ya kuwaona wagonjwa wao.
Irene hakuwa na raha, alikuwa na huzuni kubwa moyoni mwake. Muda mwingi alikuwa akilia kwa uchungu, kilichomuumiza kichwa na kumchoma moyo ni kwamba walibaki wawili tu na kaka yake huyo ndiye alikuwa kila kitu.
Alimuomba Mungu, alimkumbusha kwamba Godwin ndiye alikuwa kaka yake pekee, hakuwa na ndugu yeyote yule, kumchukua kutoka mikononi mwake ilikuwa ni sawa na kuchukua kila kitu alichokuwa nacho mikononi mwake.
“Mungu! Sina mwingine, Godwin ndiye kaka yangu, mama yangu na baba yangu. Kumchukua kutoka mikononi mwangu ni sawa na kuchukua kila kitu kutoka kwangu! Nakuomba usimchukue kaka yangu, nakuomba uniachie kaka yangu! Mungu! Bado tuna safari ndefu pamoja, naomba tuimalize lakini si kumchukua kaka yangu huyu,” alisema Irene huku akilia kama mtoto pale alipokuwa amekaa.
Walikaa hapo kwa dakika kadhaa. Muda wa kuona wagonjwa ulipofika, wakaondoka na kuelekea ndani ya wodi ile. Irene akapiga hatua mpaka katika kitanda alicholazwa Godwin. Alimwangalia, alionekana kuwa mfu, ni mashine ya oksijeni ndiyo ilimfanya kugundua kwamba kaka yake huyo alikuwa hai.
“Godwin kaka yangu! Nakuomba usiniache peke yangu, naomba ubaki nami, naomba ufumbue macho yako na kuniangalia. Naomba usiondoke, Mungu alitupokonya wazazi wetu, nakuomba usiondoke, sitotaka kumuona Mungu akinipokonya wewe kutoka maishani mwangu. Godwin, naomba usife, naomba ufumbue macho na kuniangalia tena,” alisema Irene huku akiwa pembeni ya kitanda cha Godwin, alikuwa akibubujikwa na machozi tu mashavuni mwake.
***
Godwin alikuwa kimya kitandani pale, hakujua kitu chochote kilichokuwa kikiendelea. Dripu ilikuwa ikining’inia pembeni ya kitanda chake huku huku mashine ya oksijeni ikiwa mdomoni mwake huku ikimsaidia kupumua pale kitandani alipokuwa.
Irene hakuondoka, alibaki pembeni ya kitanda kile huku akilia. Moyo wake uliendelea kuchoma mno, maumivu aliyoyasikia kipindi hicho hayakuelezeka, aliongea peke yake pembeni ya kitanda kile akimtaka Godwin ayafumbue macho yake lakini hilo halikuweza kutokea.
Moyo wake ukakata tamaa, kwa mbali aliisikia sauti ikimwambia kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa ndugu yake huyo, kama wazazi wao wote walifariki, huo ndiyo ulikuwa muda wa kaka yake, naye alitakiwa kufariki kama hao wengine.
Albert alisimama pembeni, alikuwa akimwangalia rafiki yake jinsi alivyokuwa akiteseka kitandani pale. Alihuzunika mno na muda wote alikuwa akimuomba Mungu afanye muujiza, rafiki yake huyo afumbue macho na kuangalia tena lakini jambo hilo halikutokea.
Madaktari walikuwa wakiingia ndani ya wodi hiyo kuwaangalia wagonjwa lakini kila aliyeingia ilikuwa ni lazima kusogea katika kitanda alicholala Godwin na kumjulia hali.
Waliguswa na hali yake, mioyo yao ilitokea kumpenda tofauti na wagonjwa wengine na kwa kuwa Irene alikataa kuondoka hospitalini hapo, iliwabidi madaktari wampe chakula cha wagonjwa kwani muonekano aliokuwa nao uliwaonyesha ni kwa jinsi gani msichana huyo alikuwa masikini.
“Kula kwanza…” alisema Dk. Mende, mmoja wa madaktari maarufu hospitalini hapo.
“Hapana! Siwezi kula!” alijibu Irene.
“Kwa nini?”
“Sina hamu ya kula.”
“Jaribu kujilazimisha. Utakaaje bila kula hata kidogo?” aliuliza daktari huyo.
“Siwezi kula na wakati kaka yangu hana hata uwezo wa kufumbua mdomo. Siwezi kula,” alisema Irene huku akimwangalia daktari huyo.
Hakuwa radhi kula, hakuona kama kulikuwa na umuhimu wa kufanya hivyo na wakati kaka yake alikuwa hoi kitandani na hakujua ni muda gani angeweza kufumbua tena macho yake.
Muda ulizidi kwenda mbele, wakati mwingine alitakiwa kutoka ndani ya wodi hiyo, aliondoka na kwenda nje ambapo akakimbilia chini ya mti kulipokuwa na viti vingi na kutulia hapo pamoja na wenzake waliokuja kuwaona ndugu zao.
Irene hakutaka kurudi nyumbani, alikuwa akishinda hospitalini hapohapo. Hakutaka kumuacha kaka yake akiendelea kuteseka, alitaka kumuona kuanzia hatua moja mpaka nyingine.
Mara nyingi Dk. Mende alikuwa akimuita na kuzungumza naye. Alitaka kufahamu zaidi kilichokuwa kimetokea maishani mwao kwani tangu Godwin apelekwe hospitalini hapo, mbali na mafundi wa ujenzi, hakukuwa na watu wengine waliofika mahali hapo kumjulia hali.
Alimdadisi Irene lakini msichana huyo hakumwambia kitu chochote kile. Hakutaka ajue walipotoka, hakutaka ajue historia ya maisha yao, kuhusu wazazi wake kwani alihisi kwamba endapo angejua basi angeweza kuwasiliana na waandishi wa habari na kuwaambia kuhusu wao.
“Sisi ni watoto wa mitaani tu,” alijibu Irene huku akimwangalia Dk. Mende.
“Sawa. Najua ni watoto wa mitaani! Ila ilikuwaje mpaka mkawa hapo?” aliuliza daktari huyo.
“Wazazi wetu walifariki. Baada ya hapo ndipo tukaanza kuishi maisha ya mitaani bila ndugu,” alijibu Irene.
Kila swali alilouliza daktari huyo, jibu alilokuwa akipewa halikuwa la ukweli. Irene alificha mengi kuhusu maisha yao ya nyuma, alimficha mengi tu kuhusu wazazi wake. Dk. Mende hakujali, aliuamini uongo alioambiwa hivyo kumruhusu msichana huyo kwenda kumuona kaka yake.
Kila alipoingia ndani ya wodi hiyo Irene alikuwa akilia tu hata kabla hajamfikia kaka yake. Moyo wake ulichoma mno na alipokifikia kitanda, kitu cha kwanza kilikuwa ni kupiga magoti na kuanza kumuomba Mungu huku machozi yakimtoka.
“Mungu! Naomba usimchukue kaka yangu. Tazama ninavyoumia moyoni, nimekosa furaha kwa kipindi chote hiki. Uliwachukua wazazi wetu kutoka mikononi mwetu, bado hujaridhika, unataka kumchukua Godwin kutoka mikononi mwangu. Nitaishi vipi Mungu! Ni nani atanifuta mchozi? Nitakimbilia wapi? Mungu! Ni mapema mno, naomba unipokonye kila kitu kutoka mikononi mwangu lakini si kunipokonya Godwin!” alisema Irene huku akilia.
Hali ya Godwin haikubadilika, aliendelea kuwa vilevile, kila siku ilikuwa ni afadhali ya jana. Kila mtu aliogopa, madaktari walikata tamaa kwani tayari wiki moja ilipita na hakukuwa na mategemeo yoyote yale, jinsi alivyokuwa amefikishwa hospitalini hapo ndivyo alivyokuwa siku hiyo.
Siku ziliendelea kukatika huku Irene akiendelea kubaki hapohapo hospitalini. Hakujua kibanda chao kiliendeleaje, hakujua kama kilikuwa palepale au kilitolewa, kwa wakati huo kitu alichokuwa akikijali kilikuwa ni hali ya kaka yake tu.
***
“Kuna taarifa mpya mkuu!” alisikika mwanaume mmoja kwenye simu.
“Taarifa gani?”
“Kuhusu wale watoto!”
“Imekuwaje?”
“Ni kwamba yule wa kiume amepata ajali. Aliangukiwa na kifusi alipokuwa akifanya kazi ya ujenzi!” alisema mwanaume huyo.
“Unasemaje?”
“Ndiyo hivyo mkuu! Kwa sasa amelazwa hospitalini. Taarifa zinasema zaidi kwamba hali yake mbaya, alivyoingia ndivyo alivyo mpaka sasa hivi,” alisema mwanaume huyo.
“Ni habari mpya kwangu! Ni lazima lifanyike jambo fulani!”
“Ndiyo nakusikiliza mkuu!” alisema kijana aliyekuwa amepiga simu.
“Hii ndiyo nafasi! Mnachotakiwa kufanya ni kimoja tu. Muueni hapohapo kitandani kwa kuwa sababu ipo wazi kwamba ni mgonjwa. Jipangeni na hakikisheni mauaji yanafanyika kidigitali,” alisema mwanaume huyo.
“Sawa mkuu! Na msichana?”
“Huyo zamu yake itafika!”
“Haina shida.”
Yalikuwa ni mazungumzo ya simu baina ya pande mbili. Kilichokuwa kikitakiwa kufanyika kwa haraka sana kilikuwa ni kumuua Godwin kitandani alipokuwa. Alikuwa hoi, hakujitambua na wao waliona kwamba kama wangemuua kitandani hapohapo ingekuwa rahisi sana kuwaaminisha watu wengine kwamba mtu huyo alikufa baada ya kupata ajali hiyo na hakuweza kupata nafuu.
Hawakutaka kukurupuka kufanya kazi hiyo, walitaka kumuua kwa staili ambayo hata madaktari wasingeweza kufahamu. Vijana watatu wakajipanga kwa ajili ya kufanya kazi hiyo. Kwa kuwa Godwin alilazwa katika wodi iliyokuwa na wagonjwa wengi, hivyo walitakiwa kujifanya watu wa dini ambao walikuwa na lengo la kutembelea hospitalini humo na kujifanya kuwaombea wagonjwa Mungu aweze kuwalinda na kuwaponya.
Ulikuwa mpango kabambe na hata wakubwa walipopewa mpango huo, wakaridhika nao na hivyo kuwaongezea kwamba katika vijana hao watatu, mmoja alitakiwa kutolewa na kuingizwa msichana ambaye ndiye angekuwa na nguvu kubwa ya kuwashawishi madaktari kwamba kweli wao walikuwa watu wa msaada.
“Ni wazo zuri!”
Msichana aliyetakiwa kuifanya kazi hiyo aliitwa Magdalena Urassa, msichana mwembamba, mrefu aliyekuwa na mwanya uliomfanya kuvutia kila alipokuwa akitabasamu au kucheka.
Kabla ya kwenda huko walitaka kuona wakiwa na muonekano wa kikanisa ili iwe rahisi kwao kufanya kile walichotaka kukifanya. Haikuwa hivyo tu bali walitaka kuhakikisha wanatumia kiasi cha fedha kwa ajili ya matunda na maji kwa ajili ya wagonjwa hospitalini hapo.
Mipango yote hiyo, gharama zote hizo zilikuwa ni kwa ajili ya kumuua mgonjwa mmoja ambaye alikuwa akiteseka kitandani akipumulia mashine ya gesi.
Hawakujali gharama, kitu pekee walichokijali ambacho walitaka kukiona kikitokea ni kumuua Godwin kitandani pale ili baadaye wamalizane na Irene kisha kufunga daftari lao la mauaji kwa familia hiyo.
“Tunakwenda Alhamisi, tutarudi Ijumaa na Jumamosi, wakati wametuzoea, Jumapili tunafanya kazi yetu,” alisema Majura, mmoja wa vijana waliokuwa wametumwa.
“Haina shida. Kitu cha kwanza tuandae mavazi. Nitakuwa padri wa Kanisa Katoliki,” alisema mwanaume mwingine aliyeitwa Yusufu, alizungumza kwa utani huku akicheka.
“Na mimi nitakuwa sista. Nitaitwa Sista Theopista. Mkiona jina mnalisahau sana, mtaniita Sista T, nitawaelewa,” alisema Magdalena na wote kuanza kucheka. Mipango ikaanza kusukwa.
Vijana watatu, Yusufu, Majura na msichana Magdalena walikuwa wamejiandaa kwa ajili ya kufanya mauaji. Walidhamiria kumuua Godwin ambaye bado aliendelea kuwa kitandani akiteseka. Maagizo waliyokuwa wamepewa na viongozi wao yalimaanisha kwamba mtu huyo alitakiwa kuuawa kitandani hapo haraka iwezekanavyo.
Hawakuwa na njia nyingine ya kufanya zaidi ya kujifanya mapadri huku msichana Magdalena akijifanya sista. Ndani ya siku moja, tayari walipata kila kitu walichokuwa wakikihitaji, hasa mavazi ambayo yangewafanya kuonekana kama viongozi hao wa dini.
Siku ya Jumatatu wakaandika barua katika uongozi wa Hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya kwenda huko kuwatembelea wagonjwa na kuwafundisha neno la Mungu kwa ufupi.
Hilo halikuwa tatizo na kwa sababu walisema kwamba walitaka kuanza Siku ya Alhamisi mpaka Jumapili, walipoandika barua hiyo, Jumatano wakajibiwa na hivyo kutakiwa kwenda huko siku inayofuata.
Asubuhi na mapema walikuwa ndani ya hospitali hiyo. Kwa muonekano wao ilikuwa vigumu mno kugundua kwamba watu hao hawakuwa kama vile walivyokuwa wakionekana. Walikuwa wanyenyekevu na hata walipokwenda kuzungumza na dokta mkuu, walizungumza kwa upole huku shingoni mwao waliwa wamevaa rozali kubwa, zilizong’aa ambazo zilikuwa na sanamu ya Yesu akiwa msalabani.
“Mungu ni mwema,” alisema Yusufu huku akimwangalia Dokta Cassim ambaye ndiye alikuwa dokta mkuu katika hospitali hiyo.
“Kwa hiyo mtafanya nini na nini?” aliuliza Dk. Cassim huku akiwaangalia watu hao.
“Kuwatembelea wagonjwa na kuwasaidia matunda. Tumekuwa tukifanya hivyo kwa kipindi kirefu, hasa katika kipindi hiki cha Kwaresma. Tumejitoa kwa ajili ya wagonjwa, kuwaombea na kuwasaidia,” alisema Majura huku akimwangalia daktari huyo, tena kwa kumzuga zaidi, mara nyingi alikuwa akifanya ishara ya msalaba.
Daktari huyo hakuwa na hofu nao, aliamini kwa asilimia mia moja kwamba watu hao walikuwa watumishi wa Mungu na hivyo kuwaruhusu kuingia ndani ya hospitali hiyo.
Walitembea kwa mwendo wa taratibu, katika kila kitanda walichokuwa wakifika, walizungumza na mgonjwa, walimfanyia maombezi kisha kumgawia matunda ambayo yalifanyiwa uchunguzi na madaktari wa hospitali hiyo.
Hawakuanzia kwenda katika wodi aliyolazwa Godwin, walipita katika wodi nyingine kabisa huku kwa kila kitu kilichokuwa kikifanyika, msichana Magdalena alikuwa akirekodi kwa kutumia miwani yake aliyokuwa ameivaa ambayo ilikuwa na kamera ndogo isiyoonekana.
“Tumsifu Yesu Kristo,” alisema Majura.
“Milele amen!”
Siku hiyo hawakuwa na presha, walitaka kufanya kila kitu taratibu kwani kumuua mtu katika hospitali kubwa kama hiyo halikuwa jambo dogo hata kidogo.
Waligawa matunda kwa wagonjwa wengi, kwa jinsi walivyokuwa wakizungumza, upendo waliokuwa wakiwaonyesha wagonjwa wengine na hata kwa jinsi walivyokuwa wakijitolea kwa kufanya kazi ndogondogo katika wodi za humo, watu wengi waliwapenda na wengine kuhisi kwamba watu hao walikuwa malaika waliotumwa kwa ajili yao.
“Mungu awabariki,” alisema Yusufu wakati wakiwaaga madaktari na wao kuondoka kwa miadi ya kurudi tena siku inayofuata.
Wakaondoka huku wakiwa na matumaini makubwa kwamba ilikuwa ni lazima wafanikiwe kwa kile walichokuwa wakitaka kukifanya. Walipongezana kwa hatua waliyokuwa wamefikia na walipofika hotelini walipokuwa wamepanga kwa ajili ya kazi wakaanza kuangalia video ya kile kitu walichokuwa wamerekodi kwa kutumia miwani ya Magdalena.
“Ni kazi nzuri sana. Hebu watumie video hiyo wakuu waitazame,” alisema Majura na Magdalena kufanya hivyo.
Wakapongezwa kwa kazi nzuri waliyokuwa wameifanya na hivyo kutakiwa kuifanya zaidi na zaidi mpaka kuhakikisha wanafanikisha kile walichokuwa wamekipanga.
Siku iliyofuata asubuhi na mapema wakaondoka kuelekea hospitalini huko na walipofika, wakapokelewa kama kawaida. Siku hiyo walitaka kumuona mtu aliyetakiwa kufa. Hawakuona kama kulikuwa na ugumu wa kufanikisha jambo hilo kwa sababu tu Godwin alikuwa mgonjwa kitandani, alizidiwa na hakukuwa na dalili zozote za kuinuka pale alipokuwa amelala.
Wakaelekea mpaka katika wodi ile. Kwa kile walichokifanya jana yake, kila kona stori zao zilikuwa zikisikika kwamba walikuwa watu wema, waliokuwa na upendo wa dhati na walimsaidia kila mtu pasipo kujali dini, kabila au jinsia.
Wakati wanaingia ndani ya wodi hiyo, kila mmoja aliwaona, kwa muonekano wao ilikuwa ni vigumu kuamini kama watu hao walikuwa wauaji wakubwa waliokuwa nyuma ya watu fulani wenye nguvu nchini Tanzania.
Walitembea kwa mwendo wa taratibu kama kawaida yao, Irene aliwaona, moyo wake ukajawa na furaha kwani tangu awe ndani ya hospitali hiyo akimuuguza kaka yake, hakukuwa hata na siku moja ambayo alifarijiwa vya kutosha na watu wengine, madaktari waliishia kumpa pole ila si kumfariji kama ilivyotakiwa iwe.
Waliwafahamu wote wawili, walipowaona, walikuwa na uhakika kwamba walikuwa wao. Wakawasogelea, wakamwangalia Godwin aliyekuwa kimya kitandani huku ndugu yake, Irene akiwa pembeni yake.
Wakajifanya kuingiwa na huruma nyingi mioyoni mwao, wakamuuliza Irene juu ya mgonjwa huyo kwani hakuonekana kuwa na nafuu kama walivyokuwa wengine.
Irene akaanza kuwahadithia jinsi kaka yake alivyoangukiwa na vifusi kazini mpaka kufikishwa hospitalini hapo akiwa hajitambui. Wakati anasimulia, macho yake yalikuwa mekundu, machozi yalimlenga na baada ya dakika chache, akaanza kulia.
“Pole sana,” alisema Magdalena huku akimkumbatia.
“Inaniuma. Moyo wangu unauma sana sista,” alisema Magdalena huku akilia kifuani mwa Magdalena.
Wakajifanya kuguswa zaidi ya marafiki wa Godwin, walikaa katika kitanda kile huku wakimwangalia Godwin aliyekuwa akiendelea kupumulia mashine ya oksijeni.
Wakashikana mikono na Irene na kisha kuanza kumuombea Godwin aliyekuwa kitandani pale. Msichana huyo akajisikia amani moyoni mwake, akafarijika kwa kuamini kwamba maombi hayo yangebadilisha kila kitu kwa kaka yake.
Walipomaliza, wakaondoka kwenda kwa wengine huku wakimuahidi Irene kwamba ilikuwa ni lazima kumrudia kitandani pale na kuzungumza naye tena ili kama ingewezekana basi wangemuhamisha na kumpeleka katika hospitali nyingine kubwa, yenye matibabu makubwa ambayo yangemfanya Godwin kurudiwa na fahamu haraka sana.
“Nitashukuru,” alisema Irene lakini wakati ameshikana mkono na Yusufu, akashtuka hali iliyomfanya naye mwanaume huyo kushtuka.
“Kuna nini?” aliuliza Yusufu.
“Hakuna kitu baba padri!”
“Umenitisha ulivyoshtuka! Niambie tu wala usiogope!” alisema Yusufu huku akiachia tabasamu pana.
“Una mikono laini sana!”
“Hahah! Huwa ninatumia mafuta mengi! Hilo ndilo lililokufanya ushtuke?”
“Ndiyo baba! Sijawahi kugusa mkono laini wa mwanaume kama wako,” alisema Irene huku akililazimisha tabasamu pana kuonekana usoni mwake.
“Ni kazi ya Mungu pia!”
Wakaondoka kuelekea kwa wagonjwa wengine, walikwishampata mtu ambaye walitakiwa kumuua haraka iwezekanavyo siku hiyo. Ilikuwa ni lazima kutekeleza hilo haraka iwezekanavyo.
Siku hiyo ilikuwa ni Ijumaa, hiyo ilikuwa na maana kwamba Siku ya Jumapili Godwin alitakiwa kuuawa palepale kitandani, kama kwa kuwekewa sumu kwenye maji ya dripu yaliyokuwa yakiingia kwenye mshipa wake au kwa kuzibwa mdomo pasipo mtu yeyote kugundua.
“Jumapili ndiyo kazi yenyewe. Kesho tunakwenda kuchunguza vitu vichache, baada ya hapo, tunamaliza kazi,” alisema Majura.
“Sawa. Ila kuna kitu!” alisema Yusufu.
“Kitu gani?”
“Yule msichana aliposalimiana nami kwa kushikana mkono, alishtuka sana,” alisema Yusufu huku akiwaangalia wenzake.
“Alishtuka?”
“Ndiyo!”
“Kilichomshtua?”
“Eti nina mikono laini sana. Hilo limenitia shaka kwani macho yake hayakuendana kabisa na kile alichoniambia!” alisema Yusufu.
“Wewe umehisi nini?”
“Sijajua! Sijagundua chochote ila kuna kitu!”
“Wasiwasi wako tu! Inawezekana ikawa kweli ni mikono laini, hutakiwi kufikiria sana kuhusu hilo,” alisema Magdalena.
“Mmh! Sawa! Ila tufanyeni haraka tummalize manake kwa ule mshtuko alioshtuka yule binti, hakika si mshtuko wa nchi hii! Lazima tufanye haraka iwezekanavyo!” alisema Yusufu.
“Haina shida. Kesho ni kufanya maombi wodi nzima, Jumapili ni kufanya mauaji! Tena siku hiyo tutakwenda saa moja usiku, halafu tuwasiliane na mtu akate umeme hospitalini hapo, ndani ya dakika tano tu, kukiwa na giza pasipo jenereta kuwashwa tutakuwa tumekamilisha kila kitu,” alisema Majura.
“Haina shida,” wakakubaliana na hivyo kuhitaji mtu mwingine kwa ajili ya kuzima umeme kwenye transifoma na kulegeza nyaya za jenereta hospitalini hapo. Hilo halikuwa na tatizo lolote lile. Ilikuwa ni lazima kazi ifanyike kwa haraka na kwa mafanikio makubwa.
***
Ilikuwa ni lazima mtu wa kuzima umeme apatikane katika siku ambayo walitakiwa kumuua Godwin kitandani pale pasipo kugundulika. Kazi hiyo haikuwa ngumu sana, waliiona kuwa miongoni mwa kazi nyingi nyepesi ambazo waliwahi kuzifanya kila walipokuwa wakiagizwa.
Wakawasiliana na wakuu wao, wakawaambia kila kitu kilichotokea. Kwanza wakapongezwa kwa kila kitu walichofanya, walionekana kuwa watu shupavu, makini ambao wangeweza kufanya kitu chochote kile kwa mafanikio makubwa.
Waliwaambia hitaji lao kwamba ilikuwa ni lazima wapatikane watu wawili ambao walikuwa wataalamu wa umeme kwa ajili ya kuzima umeme katika transifoma ya hospitali ile na mwingine kwenda kuzikata nyaya za jenereta ambalo lilikuwa likijiwasha baada ya umeme kukatika.
Hilo halikuwa hata tatizo, vijana wawili wakatafutwa, wakapewa makoti makubwa yaliyosomeka Danesko kwa nyuma ambalo lilikuwa moja ya mashirika mengi ya umeme Tanzania kipindi hicho.
Vijana hao wakajipanga, walitakiwa kufika katika hospitali hiyo siku ya Jumapili kuanzia majira ya saa moja usiku kwa ajili ya kufanya kazi waliyotakiwa kuifanya. Majura na wenzake wakapewa taarifa kwamba kila kitu walichokuwa wamekihitaji kilikuwa tayari, vijana ambao walitakiwa kushughulika na umeme waliwekwa na kilichobaki kilikuwa ni utekelezaji tu.
“Ni vizuri sana, tutahakikisha tunamuua hiyo Jumapili,” alisema Majura kwenye simu wakati akipewa taarifa juu ya vijana hao.
****
Irene alishtuka, hakuamini kile alichokuwa amekiona baada ya kumpa mkono Yusufu na kugundua kwamba mwanaume huyo alikuwa na tatuu kubwa aliyokuwa amejichora mkononi mwake.
Alishangaa, hakuwahi kumuona padri aliyekuwa na tatuu mwilini mwake, mwanaume huyo alikuwa wa kwanza duniani kitu kilichomfanya kuhisi kwamba hao hawakuwa mapadri kama alivyokuwa akifikiria bali walikuwa watu wengine kabisa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akaanza kuwachunguza, ilikuwa ni lazima apate ukweli juu ya watu hao, akayapeleka macho yake katika viatu walivyokuwa wamevaa, havikuwa viatu vya heshima ambavyo vilitakiwa kuvaliwa na mapadri.
Akawa na hofu, moyo wake ukaogopa kwa kuhisi kwamba watu wale walikuwa watu wengine waliokuwa na kusudio jingine kabisa. Alipozungumza nao, walimwambia kwamba kesho wangerudi tena asubuhi na wangekaa mpaka mchana ila kwa siku ya Jumapili, kwa kuwa kulikuwa na ibada wangechelewa kufika hapo, wangefika majira ya saa kumi na mbili au saa moja usiku.
Hizo kauli ndizo zilizomtia hofu zaidi Irene na kujipa uhakika kwamba wanaume hao hawakuwa watu wazuri hata kidogo. Hakutaka kubaki na jambo hilo moyoni mwake, alichokifanya ni kumfuata Dk. Cassim na kumwambia kile alichokuwa amekiona.
“Unasema mmoja ana tatuu?” aliuliza daktari huyo, hakuamini alichoambiwa.
“Ndiyo!”
“Haiwezekani! Utakuwa unatania,” alisema Dk. Cassim.
“Niamini dokta. Nahisi kuna kitu! Nahisi wanataka kumuua kaka yangu,” alisema Irene maneno yaliyomshtua daktari huyo.
Hakutaka kukaa naye pale wodini, alichokifanya ni kumchukua na kuelekea katika ofisi yake kwa ajili ya kuzungumza naye. Alitaka kusikia mambo zaidi kutoka kwa msichana huyo, ilikuwaje awe na uhakika kwamba watu hao, mapadri ambao walionekana kupendwa na kila mtu hospitalini hapo wawe kama vile alivyosema msichana huyo.
Ndani ya ofisi, Irene hakutaka kuficha kitu, alijaribu kumwambia daktari yule kila kitu kilichokuwa kimetokea katika maisha yao kama familia. Alimwambia ukweli kwamba wao walikuwa watoto wa Balozi Mapoto ambaye alikufa kwenye ajali ya gari nchini Marekani, ajali ambayo watu wengi walijua kwamba ilipangwa na watu fulani.
Dk. Cassim alibaki kimya akimsikiliza msichana huyo, kila kitu alichokisimulia, jinsi baba yake na mama yake walivyokufa, akakubaliana naye kabisa kwamba watu hao, mapadri nao walikuwa katika mipango ya kuwaua watoto hao.
“Tusaidie, sitaki kuona kaka yangu akifa,” alisema Irene huku akimwangalia daktari huyo, machozi ya uchungu yalikuwa yakimtoka.
“Hatokufa. Hakuna mtu atakayeweza kumuua Godwin,” alisema daktari huyo.
Dokta Cassim akawaita madaktari wenzake wawili na kuwaambia kila kitu kilichokuwa kikiendelea kuhusu wale mapadri na yule sista waliokuwa wakifika hospitalini hapo kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa.
Nao,kama alivyokuwa yeye wakati anaambiwa, madaktari hao hawakukubaliana naye kwani watu aliokuwa akiwazungumzia walikuwa watu wa dini hasa, watu waliokuwa kufanya jambo lolote jema kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wengine.
“Wale mapadri na yule sista?” aliuliza Dk. Felix.
“Ndiyo!”
“Hapana! Huyo binti atakuwa anadanganya. Kwanza tangu lini padri akawa na tatuu? Halafu anasema kwamba wale watu ni wauaji! Hivi kweli padri anaweza kuwa muuaji? Hapana! Huyu mtoto atakuwa na yake,” alisema Dk. Jema.
“Jamani! Cha msingi ni kufuatilia tu, sidhani kama tunaweza kumuhukumu moja kwa moja huyu mtoto, cha msingi ni kufuatilia tu,” alisema Dk. Cassim.
Wakakubaliana kuanza kufuatilia japokuwa madaktari wenzake waliona kama wakijisumbua kutokana na wema wa wanaume wale. Siku iliyofuata, Jumamosi ndiyo siku ambayo kwa mara ya kwanza tangu afikishwe hospitalini hapo Godwin akayafumbua macho yake.
Akaanza kuangalia huku na kule, macho yake yalikuwa mazito na muda wote alikuwa akishangaa kwamba ni kwa namna gani alikuwa ndani ya hospitali hiyo na wakati mara ya mwisho alikumbuka kwamba alikuwa kazini kwake akijenga nyumba pamoja na mafundi wengine.
“Irene…Irene….” Hilo ndilo lilikuwa jina la kwanza kumjia kichwani mwake, akaanza kuangalia huku na kule kwa matumaini ya kumuona ndugu yake huyo lakini hakufanikiwa kumuona.
Akataka kuinuka kutoka kitandani hapo, akashindwa. Wagonjwa wengine waliokuwa pembeni baada ya kumuona amefumbua macho na kutaka kuinuka kutoka kitandani pale, wakamuita nesi ambaye baada ya kufika mahali hapo, akashangaa, kwake ulikuwa ni kama muujiza.
“Hatimaye umefumbua macho!” alisema nesi huku akimwangalia Godwin.
“Nipo wapi?” aliuliza Godwin kwa sauti ndogo.
“Unasemaje?”
“Nipo wapi?” alirudia swali lake.
“Hospitali!”
“Imekuwaje mpaka nimefika hapa? Irene yupo wapi? Kwa nini niwe hapa na Irene hayupo? Wamemuua?” aliuliza Godwin huku akiangalia huku na kule, alionekana kuchoka mno.
Nesi huyo akaondoka mahali hapo na kwenda kumuita Dk. Cassim ambaye alionekana kuwa karibu sana na mgonjwa huyo tangu siku aliyoletwa mahali hapo. Daktari huyo alipofika hapo, hakuamini, moyo wake ulijawa na furaha tele kwani hali aliyokuwa nayo Irene, kuwa na majonzi kupita kawaida ilimuumiza moyo wake, aliamini kwamba msichana huyo atakapomuona kaka yake amerudiwa na fahamu basi furaha iliyokuwa imepotea moyoni mwake ingerudi tena.
“Pumzika kawanza Godwin!” alisema Dk. Cassim.
“Nataka nimuone Irene! Irene yupo wapi? Dokta naomba umsaidie Irene wasimuue kama walivyomuua mama,” alisema Godwin maneno yaliyomfanya daktari huyo kuamini kwamba alichokuwa ameambiwa na Irene kilikuwa kweli kabisa.
“Sawa. Pumzika kwanza!”
Akampa nafasi ya kupumzika kwani hali yake haikuwa imetengemaa na muda wa kuona wagonjwa ulipofika, Irene hakuamini alipomuona kama yake ameyafumbua macho na kumwangalia. Akashindwa kujizuia, palepale kitandani akamkumbatia kwa furaha kiasi kwamba mpaka machozi yakaanza kutiririka mashavuni mwake.
“Hatimaye umerudiwa na fahamu. Godwin! We have to go, they are coming,” (Godwin! Inatupasa kuondoka, wanakuja) alisema Irene huku akimwangalia kaka yake na machozi yakimtoka.
“Wakina nani wanakuja?”
“Waliomuua mama!” alijibu Irene lakini hata kabla Godwin hajasema kitu chochote wakaanza kusikia watu wakishangilia, alipoyageuza macho yake na kuangalia kule watu walipokuwa wakiangalia mlangoni, macho yake yakatua kwa watu watatu, Majura, Yusufu na Magdalena ambao walifika mahali hapo kwa gia ileile ya kujifanya watumishi wa Mungu.
“Tumsifu Yesu Kristo!” alisema Majura kwa sauti kubwa.
“Milele amina!” watu wote waliokuwa kwenye wodi hiyo waliitikia kwa shangwe.
Pale alipokuwa, Irene alionekana kuwa na hofu tele moyoni mwake, hakuamini kama watu hao walirudi tena ndani ya wodi hiyo kwa kutekeleza kazi waliyokuwa wamepangiwa. Aliamini kwamba watu hao waliojifanya mapadri walitaka kummaliza kaka yake aliyekuwa akiteseka kitandani.
Aliwaangalia kwa hasira, aliamini kwamba watu hao ndiyo walioimaliza familia yake, ndiyo watu waliopanga mauaji ya baba yao na kumuua mama yao kwa kumgonga kwa gari na kumpasua mapafu. Hakuona kama kulikuwa na ulazima wa kuendelea kubaki ndani ya hospitali hiyo kwani aliamini kwamba ilikuwa ni lazima watu hao wamuue kaka yake, Godwin kama tu asingemtoa ndani ya wodi hiyo.
Kama kawaida, Majura na wenzake wakaanza kutembea huku na kule ndani ya wodi ile, kama ilivyokuwa siku nyingine, walionekana kuwa watakatifu, wenye furaha tele ambao walitaka kuona wagonjwa wote ndani ya hospitali hiyo wakipona magonjwa yao.
Waliendelea kugawa vinywaji na chakula kwa wagonjwa walioonekana kuwa hoi vitandani. Walitembea kwa mwendo wa kipadri huku nyuso zao zikionyesha huruma kubwa juu ya kila mtu aliyelala kitandani.
Walipomfikia Irene pale alipokuwa na kaka yake, msichana huyo akasimama, hakutaka kuwaonyeshea tofauti yoyote ile kwa kuamini kwamba kama angejulikana kuwa amegundua watu hao walikuwa wauaji basi ingekuwa ngumu kufanikisha mpango wake wa kutoroka na kaka yake hospitalini hapo.
Akazungumza nao huku akiwa na tabasamu la kinafiki. Ilikuwa ngumu kwa wengine kugundua kama kama watu hao hawakuwa mapadri na wala Magdalena aliyejiita Sista Theopista hakuwa sista kama walivyokuwa wakijiweka.
Dk. Cassim ambaye alikuwa nao macho yake yalikuwa kwenye mkono wa Yusufu, alitaka kuona tatuu ambayo msichana Irene alisema kwamba mwanaume huyo alikuwa nayo. Ilikuwa vigumu kuiona kwani kila alipojitahidi kufanya hivyo, joho kubwa la kipadri lenye mikono mirefu la mwanaume huyo lilikuwa likiziiba mikono yake.
Hakujali sana, akamwangalia mwanaume huyo miguuni, hakuwa amevaa viatu kama padri, alivaa viatu ambavyo kwa mitaani huitwa mabuti makubwa yaliyofanana na yale wanayovaa wanajeshi.
Alishangaa, haikuwa kawaida kwa mapadri, watu wa dini kuvaa viatu kama hivyo, naye mwenyewe akaanza kuona kasoro, moyo wake ukakubaliana na Irene kwamba watu hao hawakuwa watu wema kama alivyohisi, akagundua kwamba walikuwa na mambo yao binafsi.
Majura akamsogelea Godwin pale alipolala, akamwangalia, akatoa tabasamu na kumsalimia huku akijifanya kuwa na huzuni kubwa. Godwin hakujua kitu chochote kile, aliambiwa kwamba kulikuwa na watu walikuwa wakija, hakuambiwa walikuwa ni watu gani, alipowaona wanaume hao na msichana Magdalena, yeye mwenyewe akahisi kwamba walikuwa watu wa dini.
“Mungu atakupigania, utapona mtoto wa Mungu,” alisema Majura kwa sauti ya kipole kabisa iliyomfanya Godwin kuamini kama watu hao walikuwa watumishi wa Mungu.
“Nashukuru baba padri,” alisema Godwin.
Wakaondoka na kwenda sehemu nyingine. Moyo wa Godwin ukaridhika, alijihisi kuwa mtu mwenye furaha tele, kitendo cha kutembelewa na watu hao kikampa uhakika kwamba alikuwa na bahati kuliko hata watu wengine. Akamwangalia Irene huku akitabasamu, alitaka kusikia ndugu yake huyo angesema nini.
“Mbona unawaangalia watumishi wa Mungu kwa macho ya chuki?” aliuliza Godwin huku akimwangalia Irene.
“They are here to kill you!” (wapo hapa kukuua)
“What? To kill me? How? They are servants of God!” (Nini? Kuniua? Wao ni watumishi wa Mungu!) alisema Godwin.
“They are not!” (wala siyo!)
“What are you talking about?” (unazungumza kuhusu nini?) aliuliza Godwin.
Godwin alishangaa, hakumuelewa ndugu yake hata kidogo, aliwaangalia watu hao, muonekano wao na hata jinsi walivyokuwa wakizungumza walionekana kuwa watumishi wa Mungu.
Irene hakutaka kumficha Godwin, akaanza kumuhadithia kila kitu kilichokuwa kimetokea. Godwin alibaki kimya akimsikiliza, kila kitu alichokuwa akiambiwa, aliwaangalia kuona kama walikuwa navyo, vitu vyote alivyosema Irene ndivyo walivyokuwa navyo.
“Na tatuu?”
“Ndiyo!”
“Ngoja, nitamwangalia kesho!”
“Kesho? Kesho ni siku ya mwisho kuja hapa. Nafikiri ndiyo siku yako ya mwisho wewe kuvuta pumzi ya dunia hii! Ni lazima tutoroke,” alisema Irene huku akimwangalia kaka yake.
“Siwezi kuinuka, bado naumwa sana,” alisema Godwin.
Majura na wenzake walivyoondoka, haraka sana Dk. Cassim akarudi mahali hapo, akamwangalia Irene huku akionyesha kukubaliana naye kwamba kweli kile alichokuwa amekisema ndicho kilichokuwa kimetokea na aliamini kwamba watu wale hawakuwa watumishi wa Mungu kama alivyohisi bali walikuwa wauaji.
“Naomba mumsaidie kaka yangu!” alisema Irene.
“Usijali! Kesho asubuhi tutambadilishia kitanda,” alisema Dk. Cassim.
Usiku huo Godwin hakulala, alikuwa akizungumza na dada yake, aliogopa kwa kuhisi kwamba watu wale wangeweza kurudi hata usiku huo na kummaliza kitandani hapo.
Aliumia sana, hakutaka kufa, alijua kwamba wazazi wake walikuwa wameuawa na hivyo alitaka kulipiza kisasi hapo baadaye. Walizungumza kwa kipindi kirefu, ilipofika saa tisa usiku, wakalala na kushtuka asubuhi.
Dk. Cassim akawasiliana na wenzake na kuwaambia ukweli kwamba hata naye tayari aliingiwa na hofu kwamba watu wale hawakuwa watumishi wa Mungu kama alivyokuwa amehisi bali walikuwa wauaji ambao walifika hospitali hapo kwa kazi maalumu ya kuua.
“Ila wamesema leo ndiyo mwisho wao kuja hapa. Inawezekana kweli leo ndiyo siku yao ya kuja kuua?” aliuliza Dk. Felix
“Hatujui! Ila swali la msingi je, ni kweli wanataka kumuua yule kijana?” aliuliza Dk. Cassim.
Walikaa na kuzungumza kwa muda fulani, walipomaliza, wakajipanga kwa ajili ya kuokoa maisha ya Godwin ambaye alikuwa kwenye hali mbaya kitandani.
Ilipofika saa moja kasoro usiku, watu hao wakafika hospitalini hapo, kama kawaida yao walipoanza kuingia, wagonjwa walifurahi mno kwani kitendo cha kuwaona watu hao kilionyesha kwamba neema ilikuwa imeingia.
Siku hiyo hawakuanza katika wodi ile aliyolazwa Godwin, walianza katika wodi nyingine kabisa ili giza liingie. Baada ya kutembelea katika wodi hizo, hatimaye wakabakiza wodi aliyolazwa kijana huyo ambapo wakaanza kuelekea huko huku tayari ikiwa ni saa mbili kasoro usiku.
Walipofika katika wodi hiyo, muda mwingi Yusufu alionekana kuwa bize na simu. Hilo liliwashangaza, alijifanya kuwasiliana na mtu fulani na muda mwingi aliwaambia wenzake kwa sauti iliyosikiwa na wengine kwamba alikuwa akiwasiliana na Kardinari Kajuma kwani baada ya hapo walikuwa na safari ya kwenda kwake kula chakula cha usiku.
Madaktari hao wakajua kwamba huo haukuwa ukweli, wakahisi kwamba mwanaume huyo alikuwa akiwasiliana na mtu mwingine mbaya. Waliendelea kwenda kwenye kitanda kimoja baada ya kingine. Muda wote huo, Irene alikuwa pembeni mwa kitanda alichokuwa akikitumia Godwin, moyo wake ulikuwa na hofu kupita kawaida.
Watu hao walipofika kwenye kitanda kile, Majura akaelekea upande mwingine, ambao Godwin alikuwa amewekea kichwa, alisimama hapo huku akijifanya kuwa bize na simu yake.
Huku hata kabla mambo mengine hayajaendelea, ghafla, umeme ukakatika na mahali hapo kuwa na giza nene.
“Yesu wangu! Danesko nao vipi tena?” alijifanya kuuliza Majura! Huo ndiyo ulikuwa muda wa kazi ambao walitakiwa kuutumia haraka sana. Hapohapo Yusufu ambaye alikuwa pembeni ya Godwin akamziba mdomo na kuanza kumchoma visu kadhaa ubavuni.
Alimchoma visu vitano harakaharaka, alipomaliza, huku kukiwa na giza akawagusa wenzake kuonyesha kwamba kazi ilikuwa imefanyika, hapohapo, kwa haraka wakaanza kuondoka wodini humo na kwa kuwa kulikuwa na giza, na jinsi walivyokuwa wakiondoka, hakukuwa na mtu yeyote aliyewaona, umeme uliporudi baada ya dakika kumi, cha ajabu, watumishi wa Mungu hao hawakuwa wodini.
“Godwin…Godwin…” alipiga kelele Irene huku akimwamsha Godwin kitandani pale. Alama tano za visu zilikuwa ubavuni mwake.
***
Kazi ilikuwa imekamilika, kila mmoja alikuwa na furaha, hawakuamini kama kweli kazi ile ilifanyika pasipo kugundulika lengo lao la kuwepo ndani ya hospitali ile.
Wakaingia ndani ya gari lao na kuondoka mahali hapo huku kukiwa na giza totoro, umeme ulikatika na jenereta halikuwaka kwani vijana ambao waliwaweka kwa ajili ya kufanya kazi hiyo waliifanya kikamilifu kabisa.
Ndani ya gari kila mmoja alikuwa akifurahia, walipongezana kwani waliamini kwamba kama wangewaambia wakuu wao wangefurahia na kuonekana kwamba walikuwa makini na kazi zao.
Walikuwa wakizungumza kwa furaha, waliwatoroka madaktari hospitalini pale, hawakutaka kugundulika baada ya Godwin kufa na ndiyo maana wakamua kuondoka ili hata kama umeme ungerudi, wasiwepo eneo lile la tukio.
“Ilikuwaje?” aliuliza Magdalena.
“Nilimchoma visu vitano mbavuni, tena vilipokuwa vikiingia, ndani nilivinyonganyonga ili vimuue kwa urahisi,” alisema Yusufu huku akikenua.
“Safi sana. Kwa visu vitano hawezi kupona. Tena na hivi umeme umekatika, wanachotakiwa kusubiri ni kwenda kuuzika mwili wake,” alisema Majura na kugongesheana mikono na wenzake.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika hoteli waliyokuwa wamepanga, wakaelekea chumbani ambapo huko wakachukua mvinyo na kuanza kujipongeza kwa kazi kubwa waliyokuwa wameifanya kwani kitendo cha kujifanya kwamba walikuwa mapadri na sista hakika haikuwa kazi nyepesi.
Baada ya nusu saa, wakawapigia simu wakubwa wao na kuwaambia kwamba kazi ilikamilika, mtu ambaye alitakiwa kuuawa alikuwa ameuawa na hivyo walichokuwa wakisubiri ni kazi nyingine kabisa.
“Ni kweli kazi imefanyika?”
“Ndiyo mkuu! Tumemchoma visu vitano hapohapo kitandani,” alisema Majura alipokuwa akiongea kwa simu na mwanaume wa upande wa pili.
“Safi sana! Ngoja niwasiliane na mkuu! Nadhani baada ya nusu saa miamala ya simu yenu itakuwa ikizungumza lugha ya pesa,” alisema mwanaume huyo na kukata simu.
Hawakuacha kunywa, bado walikuwa wakiendelea kupongezana na baada ya nusu saa, kama walivyoambiwa simu zao zikapokea ujumbe uliosema kwamba walikuwa wamepokea kiasi cha shilingi milioni tatu kila mmoja.
Wakafurahia! Mbali na kiasi hicho cha fedha, wakaahidiwa kwamba wangepelekwa visiwani Zanzibar kwa ajili ya kula bata kwani ile misheni nzito waliyokuwa wamepewa ilikuwa imefanyika bila wasiwasi.
“Mtachagua hoteli. Mtakwenda kukaa huko kwa wiki moja kisha tutawapangia kazi nyingine,” alisikika mwanaume upande wa pili.
“Sawa mkuu!”
****
Emmanuel Kihampa ndiye aliyekuwa akiwasiliana na vijana hao na kuwapa mipango kabambe ambayo walitakiwa kufanya. Yeye ndiye aliyekuwa akipokea simu kutoka kwa mwanaume mwingine na kumpa maagizo ambayo walitakiwa kuyafanya pasipo kuuliza swali.
Aliwapa kazi ya kumuua Rosemary, waliifanya kwa mafanikio makubwa, baada ya hapo akawapa kazi nyingine ya kumuua Godwin ambayo pia waliifanya kwa mafanikio makubwa.
Baada ya kupewa taarifa hiyo, kitu cha kwanza kabisa alichokifanya Kihampa ni kuanza kusikilizia taarifa ambayo ingetangazwa kutoka katika hospitali hiyo kuhusu mapadri ambao walikwenda na kufanya mauaji.
Alitegemea habari kuhusu tukio hilo angeisikia asubuhi kabisa kwenye taarifa ya habari lakini hakukuwa na taarifa yoyote kutoka katika Hospitali ya Mwananyamala.
Alishangaa, hilo lilikuwa tukio kubwa ambalo aliamini kwamba lingeshika sana hisia za watu kwamba iweje watu waliojifanya mapadri waingie hospitalini hapo na kufanya mauaji. Hakuacha kusikiliza kituo cha redio cha taifa, akahamia katika vituo vingine napo hakukuwa na habari kama hiyo.
“Au mitandaoni! Ngoja niingie kwenye Mtandao wa Global Publishers,” alisema, akachukua simu yake na kuingia huko.
Hakukuwa na kitu kama hicho, alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, alitamani aondoke nyumbani na kwenda hospitalini hapo na kuuliza lakini hakuwa na sababu ya kufanya hivyo.
Akavumilia, akahisi kwamba habari hiyo ingetangazwa mchana, napo kukawa kimya. Akavumilia na kusubiri usiku, napo hakukuwa na habari kama hiyo jambo lililomfanya kuwa na wasiwasi, akawapigia simu vijana wake.
“Majura! Mmekwishakwenda Zanzibar?” aliuliza Kihampa hata kabla ya salamu.
“Bado mkuu!”
“Sawa. Hivi ile kazi mliifanya kweli?” aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Ndiyo mkuu!”
“Hapana! Kama mngekuwa mmeifanya, ingetangazwa kwenye taarifa ya habari. Na hata kama taarifa za habari za redio hazikutangaza, kweli Global Publishers washindwe kuiweka kwenye mtandao wao! Kweli inawezekana hii?” aliuliza Kihampa huku akionekana kutokuamini.
“Mkuu! Sijajua kwa nini! Inawezekana hawakusema ili hospitali isiumbuke na watu kutumbuliwa,” alisema Majura.
“Hapana! Hebu subirini kwanza. Nina hofu kazi haikufanyika. Msiondoke kwenda Zanzibar mpaka nitakapojiridhisha, kesho nitatuma watu huko,” alisema Majura na kukata simu.
Alichanganyikiwa, hakujua angeuficha wapi uso wake. Alimwambia mkuu wake kwamba kazi ilifanyika na fedha za pongezi zikatumwa na wakati inawezekana kazi haikuwa imefanyika.
Hakutaka kuona akipata aibu, hakutaka kuona bosi wake akitoa uaminifu kutoka kwake, alichokifanya kilikuwa ni kuwatuma watu wawili, mmoja alikuwa msichana aliyekuwa akiumwa, huyu aliitwa kwa jina la Aisha na mwanaume ambaye alijifanya mume wake, huyo aliitwa Hamisi.
Wakaelekea katika hospitali hiyo, Aisha alilalamika maumivu makali tumboni mwake na hivyo kulazwa hospitalini hapo. Kazi kubwa ilikuwa ni kufuatilia ili wajue kama kulikuwa na tukio kama hilo limetokea hospitalini hapo au la.
Siku ya kwanza wakawa hospitalini hapo, hakukuwa na taarifa yoyote ile, hawakusikia hata tetesi kama kulikuwa na mtu alikuwa ameuawa na mapadri hospitalini hapo. Hawakutaka kukata tamaa, waliendelea kusikilizia lakini hakuwa na taarifa zozote zile.
Hamisi hakutaka kubaki kwenye wodi hiyo aliyolazwa Aisha, akaelekea katika wodi nyingine ile ambayo tukio lilipokuwa limefanyika, katika kitanda kilekile alichoambiwa kwamba ndipo alipouawa Godwin, macho yake yakatua kwa mgonjwa mwingine kabisa, mwanamke mtu mzima aliyeonekana kuugua hasa.
“Mh! Mbona hata tetesi sisikii chochote kile?” alijiuliza Hamisi huku akiangalia huku na kule.
Alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya. Hakuwa na jinsi, alitaka kufahamu kila kitu kilichokuwa kimetokea, hata kama ni kuuliza, aulize lakini aujue ukweli juu ya tukio hilo.
Akamfuata mwanaume mmoja aliyekuwa amekaa kitandani, alionekana ni muda mrefu kuwa mahali hapo. Alipomfikia, akaanza kuzungumza naye kirafiki, akampa pole na kumuulizia kuhusu afya yake kwani alijitambulisha kama mtu ambaye alikuwa na lengo la kuwasaidia baadhi ya wagonjwa humo.
“Shika hii kwanza,” alitoa kiasi cha shilingi elfu kumi na kumpa mzee huyo ambaye alimshukuru sana.
“Nashukuru sana,” alisema mzee huyo.
“Usijali! Halafu hivi kuna lile tukio lililotokea juzi ilikuwaje?” aliuliza Hamisi.
“Tukio gani?”
“Yule mgonjwa aliyechomwa visu katika kitanda kile,” alisema Hamisi huku akimuonyeshea kitanda hicho.
“Mmh! Mgonjwa aliyechomwa visu?”
“Ndiyo!”
“Lilitokea wapi?”
“Humuhumu!”
“Sijawahi kulisikia kabisa.”
“Kwani wewe upo humu kwa muda gani?”
“Mwezi mzima, ila sijawahi kulisikia tukio hilo kabisa,” alisema mzee huyo.
“Basi umbeya wa mjini tu,” alisema Hamisi, akazuga na kuondoka mahali hapo.
Akampeleka taarifa Aisha kwamba hakukuwa na tukio kama hilo lililotokea, siku hiyohiyo Aisha akaruhusiwa kutoka na kumpigia simu Kihampa na kumwambia kwamba hakukuwa na tukio kama hilo lililotokea.
“Unasemaje?” aliuliza Kihampa huku akiwa amechanganyikiwa.
“Hakuna mtu aliyechomwa kisu. Si kisu tu. Wiki nzima kwenye hii wodi hakuna hata mgonjwa aliyekufa,” alisema Hamisi maneno yaliyomfanya Kihampa kuvimba kwa hasira.
***
Dokta Cassim alikuwa kimya, alibaki akiwa amesimama pembeni mwa kitanda alicholala Godwin, alikuwa akimwangalia, alimuonea huruma, hakuamini kama kulikuwa na watu walitaka kumuua kijana huyo japokuwa waliitenda vibaya familia yake.
Kumuacha kitandani ilimaanisha kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wake, hakutaka kuona hilo likitokea, ilikuwa ni lazima wamuokoe kwa staili yoyote ile lakini si kuona kijana huyo akiuawa kitandani hapo.
Madaktari wenzake wawili ambao aliwashirikisha suala hilo, Jema na Felix walimwambia kwamba hata kama watu hao hawakuwa wabaya lakini ilikuwa ni lazima kumuondoa Godwin katika kitanda kile na ikiwezekana iwekwe maiti katika siku ambayo watu hao wangefika kwa ajili ya kufanya mauaji.
Huo ndiyo mchakato walioupanga. Siku hiyo usiku Godwin akaambiwa kila kitu kwamba jioni ya siku inayofuata hakutakiwa kuwa kitandani hapo, angeondolewa na maiti kuletwa ili kama watu hao walikuwa wabaya basi waitendee ubaya maiti na si yeye.
Akakubali na kuwashukuru na Jumapili ilipofika, jioni majira ya saa kumi na moja akatolewa kitandani pale na maiti kuletwa huku ukiwa imening’iniziwa dripu kwa juu na kwa jinsi ilivyokuwa, watu wengi wakahisi kwamba alikuwa mgonjwa mwenye hali mbaya.
Godwin akapelekwa katika chumba kingine kabisa na kutulia humo. Madaktari wale walikuwa wakifuatilia kila kitu, Majura na wenzake walipofika hospitalini hapo, wakajifanya kuwachangamkia, hawakutaka kuwaonyeshea tofauti yoyote ile.
Walikuwa makini, tangu Yusufu alivyokuwa akijifanya kuzungumza kwa simu na kusimama pembeni ya kitanda alicholala Godwin walikuwa wakifuatilia, na mpaka umeme ulipokatika, wakajua kwamba hiyo yote ilikuwa mipango ya watu hao hivyo wakaacha.
Yusufu akafanya kazi yake, hakujua kama kisu kile aliichoma maiti, hakujua kwani hata shuka iliyokuwa imefunikwa, ilifunikwa kuanzia miguuni mpaka karibu na macho yake hivyo kutambua kwamba mtu huyo hakuwa Godwin lilikuwa jambo gumu.
Baada ya dakika kumi na tano umeme uliporudi, watu hao hawakuwepo mahali hapo na madaktari walipofunua shuka lililoifunika maiti ile, wakaona ikiwa imechomwa visu mara tano na kuwa na uhakika kwamba watu hao kweli walikuwa wauaji kama walivyokuwa wameambiwa na Irene.
“Mungu wangu! Kweli walikuwa wauaji,” alisema Dk. Cassim huku akiwaangalia wenzake.
Waliuangalia mwili ule, wakaamini maneno ya Irene kwamba watu wale hawakuwa mapadri kama walivyohisi bali walikuwa wauaji ambao walifika mahali hapo kwa ajili ya kufanya mauaji tu.
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa uongozi wa hospitali hiyo kukataa misaada kutoka kwa watu wa nje ambao walijifanya kuwa watu wa dini au mtu mmoja mmoja kwani kama wasingekuwa makini, tayari hospitali hiyo ingekwaa kashfa nzito ya kuwaruhusu watu kuingia humo na kufanya mauaji.
Kule alipokuwa amelala, Godwin alikuwa na hasira kali, aliamini kwamba kulikuwa na mtu aliyekuwa nyuma ambaye alitaka kumuangamiza yeye na ndugu yake. Hakutaka kuona akiuawa, alikuwa hoi hospitalini lakini kitu alichokitaka ni kulipa kisasi kwa mtu yeyote ambaye alishiriki katika mauaji ya wazazi wake.
Hakukuwa na watu wengine waliojua kile kilichokuwa kimetokea, madaktari hawakutaka stori hizo zisambae kwani kama zingesambaa wagonjwa wengi wangeshikwa na hofu na hata kutamani kuondoka mahali hapo.
Godwin aliendelea kuwa hospitalini hapo, kwa kuwa hata Irene alikuwa akijulikana, hawakumruhusu kuwa huru kama kipindi cha nyuma kwa kuhofia kwamba kama angeonekana basi watu hao wangeweza kumuua hata yeye.
Godwin alikaa hospitalini kwa wiki nyingine mbili na ndipo akaruhusiwa. Kila mmoja aliwaonea huruma, walijua kwamba endapo wangekwenda mitaani basi watu hao wangeweza kuwaua kama walivyotaka kuwaua hospitalini hapo lakini hawakuwa na jinsi, ilitakiwa kuondoka.
Wakawagawia kiasi cha fedha kwa ajili ya kuwalinda huko watakapokwenda. Kila mmoja alisikitika kwani walijua kwamba watu wale waliotoka mahali hapo wangegundua kwamba Godwin hakufa hivyo kuanza kuwatafuta hukohuko kuwaua.
Hawakutaka kuona hilo likitokea lakini hawakuwa na jinsi. Godwin na Irene wakaingia mitaani kama kawaida. Hawakujua ni mahali gani walitakiwa kwenda, kurudi katika kibanda chao lilikuwa jambo lisilowezekana kwani walijua fika kwamba watu wale wangerudi na kuwaangalia kama walikuwa hivyo.
Ilikuwa ni lazima kujificha. Wakaondoka na kuelekea katika Ufukwe wa Coco, ule upande uliokuwa na vichaka, walitaka kuanza maisha yao huko na kwa kuwa upande waliokwenda hakukuwa na watu wengi, waliamini kwamba wangejificha na sehemu hiyo kuwa salama kwa maisha yao.
“Haya maisha mpaka lini Godwin?” aliuliza Irene huku akimwangalia kaka yake.
“Bado sijajua! Ni maisha yanayochosha sana, ni lazima tupambane kuhakikisha tunafanikiwa. Irene, acha maisha yetu yawe hukuhuku ufukweni, tukitoka tu, tutatekwa na kuuawa,” alisema Godwin huku akimwangalia ndugu yake huyo.
Hawakutoka huko, waliishi hukohuko na usiku walikuwa wakilala kwenye miamba iliyokuwa huko. Walipigwa na baridi lakini hawakutoka, waliteseka, wakati mwingine usiku mzima walikuwa wakikesha kutokana na upepo mkali lakini hawakujali, ilikuwa ni lazima wavumilie ili maisha yasonge mbele.
Hawakuondoka huko, waliendelea kuishi ufukweni. Kwa kuwa hapo ndipo kulipoonekana kuwa kama nyumbani kwao, Godwin akaanza kuzoeana na watu wengine wakiwemo vijana wa baharini (Beach boys) ambao wao miaka yote walikuwa wakifikiria kuhusu kuzamia kuelekea barani Ulaya.
Mbali na watu hao pia Godwin akaanzisha urafiki na wahudumu wa Baa ya Malaika ambayo haikuwa mbali kutoka hapo walipokuwa. Lengo si kuhitaji marafiki ila ni kuhitaji masalia ya vyakula walivyokuwa wakila wateja mbalimbali.
Kila siku ilikuwa ni lazima Godwin kuelekea katika baa hiyo, alipokuwa akifika, alipewa masalia ya chakula na kurudi nayo mpaka kule alipokuwa akiishi na ndugu yake. Walikuwa na maisha magumu, yenye kutesa lakini hawakuwa na jinsi. Waliyazoea, hawakuwa na maisha mengine zaidi ya hayo.
“Unaitwa nani?”
“William Massawe.”
“Ooh! Sawa mshikaji wangu. Nimekuwa nikikuona kila siku hapa, maisha yako yamenigusa sana,” alisema mwanamke mmoja alipokuwa akizungumza na Godwin.
“Usijali mama! Ndiyo maisha ila namshukuru Mungu kwa sababu ninapumua bila ushuru,” alisema Godwin na kutoa tabasamu pana.
Hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kwanza kukutana na mwanamke huyo, mama mtu mzima aliyejitambulisha kwa jina la Rachel. Alikuwa mwanamke mtu mzima, mweupe, mnene kidogo ambaye kwa kumwangalia tu isingekuwa vigumu kugundua kwamba pamoja na umri wake mkubwa alipenda maisha ya ujana.
Alivalia wigi la Peruvian na kila alipotembea, alitembea kwa mwendo wa mikogo huku akijitingisha kwa nyuma. Katika maisha yake hakupenda wazee, alikuwa na mume wake nyumbani lakini hakutaka hata kulala naye, alipenda vijana, walimsisimua na kila alipokuwa akiwaona, moyo wake uliweweseka kupita kawaida.
Alipomuona Godwin kipindi alichokwenda kununua chakula katika baa hiyo, moyo wake ukashtuka, hakuamini kama angemuona mvulana aliyekuwa na sura nzuri kama alivyokuwa Godwin. Hakutaka kuvumilia, alichokifanya ni kumuita na kuzungumza naye.
Moyo wake ukafarijika, alitaka kufahamu mengi kuhusu kijana huyo, alipouliza, akaambiwa kwamba mara kwa mara alikuwa akifika mahali hapo na ilikuwa ni rahisi kuzungumza naye kwani alionekana kuwa kijana aliyehitaji sana msaada wa kifedha.
“Kwa hiyo hakuna shida kumpata?” aliuliza Bi Rachel.
“Hakuna shida hata kidogo! Kama unataka niambie nikuwekee sawa,” alisema mpika chipsi katika baa hiyo.
“Haina noma! Utanifanyia mipango. Shika hii kwanza,” alisema Bi Rachel kisha kumpa kijana huyo kiasi cha shilingi elfu ishirini kisha kuondoka.
Ndani ya gari Bi Rachel alikuwa na mawazo tele, moyo wake ulikuwa juu ya kijana ambaye alikuwa amemuona, alichanganyikiwa, japokuwa Godwin alikuwa amechoka, maisha yamempiga lakini uzuri wa sura yake ulionekana dhahiri.
“Ni lazima nimpate, nitatumia hata kiasi kikubwa cha pesa ilimradi nimpate huyu kijana,” alisema Bi Rachel pasipo kujua kwamba kuwa na kijana huyo ilikuwa ni sawa na kulikumbatia bomu, muda wowote ule lingemlipukia.
***
Godwin hakujua kilichokuwa kikiendelea, kila siku, kama kawaida yake aliendelea kwenda katika baa ile kwa ajili ya kuchukua masalia ya chakula na kumpeleka ndugu yake, Irene ambaye alikuwa kule ufukweni.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yao, kila siku waliishi hivyo na hakukuwa na mtu aliyewashangaa kwani kule walipokuwa wakiishi, si wao peke yao bali kulikuwa na watu wengi ambao maisha yao yalikuwa kama wao.
Hakujua kama kulikuwa na mwanamke aliyekuwa akimpenda, kama kawaida alikuwa akifanya mambo yake, hakutaka kuzoeana na watu wengi kwani mpaka muda huo bado maisha yake yalikuwa na hatari kubwa. Hakutakiwa kumwamini mtu yeyote yule zaidi ya Irene ambaye alikuwa akijificha naye kila kona.
Siku ambayo Bi Rachel alimuona na kumpenda, kesho yake Godwin akafika katika baa hiyo. Mtu wa kwanza kabisa kuongea naye alikuwa yule mpika chipsi aliyeitwa Omari ambaye akamuita pembeni kwa ajili ya kumwambia kile kilichokuwa kimetokea jana yake.
Hakuficha kitu, alimwambia kila kitu alichoambiwa na Bi Rachel kitu kilichomfanya Godwin kushangaa kwani tangu azaliwe, hakuwahi kusikia kulikuwa na mwanamke aliyekuwa akimpenda, na cha zaidi, jinsi alivyokuwa, alikuwa mchafu mchafu asiyekuwa na fedha, sasa ilikuwaje mpaka mwanamke huyo ampende tena kwa moyo wa dhati.
“Haiwezekani!” alisema Godwin huku akimwangalia Omari.
“Kweli tena! Nimezungumza naye yule mama. Aisee amekuelewa ile kinyama,” alisema Omari huku akiendelea kumwambia Godwin ni jinsi gani mwanamke yule alitamani sana kuwa naye.
Hakutaka kujali, akachukua masalia aliyoyafuata na kuyaweka kwenye mfuko na kuondoka zake. Njiani, mawazo yake yalikuwa kwa mwanamke huyo, moyoni alipinga, hakukubaliana na Omari kwamba kulikuwa na mtu aliyemuulizia tena kwa kumpenda kimapenzi, wakati mwingine alihisi kama Omari alitumia njia hiyo kumfariji kutokana na matatizo aliyokuwa nayo, yaani na yeye ajione kwamba alikuwa akipendwa.
Hakukubaliana na Omari, alihisi kabisa hakukuwa na kitu kama hicho. Hakumbia Irene alichoambiwa bali alichokitaka ni kusikia kutoka kwa mwanamke yule kila kitu alichokuwa ameambiwa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hilo halikuwa tatizo kwani baada ya siku mbili, Bi Rachel akafika hapo baa na kitu cha kwanza kabisa alitaka kumuona Godwin. Hakukuwa na mtu aliyejua mahali alipokuwa akiishi bali walikuwa wakimuona mahali hapo nyakati za jioni na usiku na hivyo mwanamke huyo kusubiri.
Ilipofika saa kumi na mbili, Godwin akatokea mahali hapo na kuunganishwa na Bi Rachel. Alipomuona, mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kwa nguvu, hakuamini kama mwanamke aliyekuwa ameambiwa alikuwa huyo, alikuwa mtu mzima na kwa jinsi alivyoonekana, hakuonekana kuwa mwanamke aliyetulia hata kidogo.
“Karibu,” alisema Bi Rachel.
Godwin akatulia kwenye kiti, alionekana kuwa na hofu moyoni mwake, alimwangalia mwanamke huyo kwa macho yaliyojaa shaka tele, hakumwamini, alihisi kwamba inawezekana mwanamke huyo alikuwa mmoja wa watu waliotumwa kwa ajili ya kumuua kama alivyotakiwa kufa katika Hospitali ya Mwananyamala.
“Wewe ni kijana mzuri sana,” alisema Bi Rachel.
Mazungumzo yao yalianzia hapo, mwanamke huyo alianza kumwambia Godwin maneno mengi ya kimapenzi, hakutaka kumficha kitu chochote kile, alimuelezea hisia zake za ndani kabisa jinsi alivyokuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati na kukichanganya kichwa chake.
Godwin alibaki kimya, kichwa chake kilikuwa kikifikiria mambo mengi. Hakufikiria mapenzi, aliyafikiria zaidi maisha yake ambayo yalijaa msukosuko wa kila aina. Hakutakiwa kumwamini mtu yeyote lakini kwa jinsi Bi Rachel alivyokuwa akijielezea, ilionyesha kabisa kwamba alikuwa na penzi la dhati moyoni mwake.
“Kwa hiyo?” aliuliza Bi Rachel baada ya kuzungumza sana maneno mengi ya kimapenzi.
“Bado unanichanganya!” alisema Godwin huku akimwangalia mwanamke huyo.
“Kipi kinakuchanganya?”
“Unanipenda mimi?”
“Ndiyo! Nakupenda wewe hapo!”
“Hapana! Labda utakuwa umekosea! Una uhakika kijana uliyemuona siku ya kwanza nilikuwa mimi?” aliuliza Godwin huku akiangalia huku na kule.
“Ndiyo! Nisikilize. Ninakupenda, mimi si kipofu, nilikuona wewe na ndiyo maana nimeamua kukufuata na kukwambia ukweli! Ninakupenda mno! Ninahitaji uwe mpenzi wangu,” alisema Bi Rachel.
Godwin hakujibu kitu, akabaki kimya na kukiinamisha kichwa chake. Alikuwa kwenye wakati mgumu sana, hakutaka kuwa na mwanamke yeyote katika kipindi hicho lakini kwa jinsi Bi Rachel alivyoonekana, alionekana kuwa mwanamke mwenye pesa ambaye hakuyumbishwa na umasikini hata mara moja.
Aliona neema ikiwa imemsogelea, kumkataa mwanamke huyo ilikuwa ni sawa na kulipiga teke brifukesi la pesa, ili asionekane kama alikuwa na tamaa, akamwambia mwanamke huyo kwamba alihitaji muda wa kujifikiria kuhusu hilo.
“Mpaka lini mpenzi?” aliuliza.
“Keshokutwa. Naomba niwe na muda wa kujifikiria!” alisema Godwin.
“Sawa. Nakupenda! Naomba usiniangushe!” alisema Bi Rachel.
Mwanamke huyo akasimama, akafungua pochi yake mkobani na kutoa kiasi cha shilingi elfu hamsini na kumgawia Godwin. Kijana huyo hakuamini, kiasi cha pesa alichopewa kilikuwa kikubwa mno, hakuwahi kukishika kwa kipindi kirefu sana na hata alipokuwa akikipokea, mikono yake ilikuwa ikitetemeka mno.
“Asante sana!”
“Wala usijali bebi! Ilimradi upo na mimi hakuna shida!” alisema Bi Rachel.
Godwin hakutaka kubaki mahali hapo, harakaharaka akaondoka mahali hapo huku moyo wake ukiwa na furaha mno. Hakuamini kama yeye ndiye aliyepewa kiasi kile cha fedha, alikuwa akikimbia kuelekea alipokuwa ndugu yake, Irene.
Hakuziweka mfukoni, aliona kama zingedondoka, alizishikilia vilivyo mkononi mwake. Kila mtu alikuwa akimshangaa, wengi walihisi kwamba alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakifanya mazoezi ya kukimbia ufukweni hapo kumbe mwenzao alichanganywa na pesa na alikuwa akikimbia kwenda kumuonyeshea ndugu yake.
Alipofika huko, alikuwa akihema kwa nguvu, Rachel ambaye alikuwa amejilaza kwenye kipande cha boksi akashtuka na kumwangalia kaka yake. Siku hiyo alionekana kuwa tofauti kabisa, alionekana kama mtu aliyechanganyikiwa na jambo fulani kiasi kwamba akaanza kuogopa kwa kuhisi kwamba alionekana na watu waliokuwa wakimtafuta.
“Kuna nini?” aliuliza Rachel.
“Subiri kwanza!”
“Nisubiri! Kuna nini? Wamekuona? Tuondoke kuyanusuru maisha yetu,” alisema Irene huku akimwangalia kaka yake huyo.
“Hapana! Hakuna aliyeniona! Chukua hizi,” alisema Godwin huku akimgawia pesa zile ndugu yake huyo.
Rachel alishangaa, hakuwahi kumuona kaka yake akiwa na kiasi kikubwa cha pesa kama hicho. Hakuzichukua, alibaki akiziangalia huku zikiwa mkononi mwa ndugu yake huyo. Alikuwa na maswali mengi aliyokuwa akijiuliza juu ya pesa hizo, alizitoa wapi? Kuna mtu alimuibia au?
“Umezitoa wapi?” aliuliza Rachel.
“Ni stori ndefu!”
“Umeiba?”
“Ushawahi kuniona nikiiba? Ni stori ndefu. Kaa chini kwanza,” alisema Godwin na Rachel kukaa chini, akayategesha masikio yake kumsikiliza ndugu yake huyo angezungumza nini.
Hakutaka kumficha, alimwambia ukweli kila kitu kilichotokea kati yake na Bi Rachel. Irene alibaki akishangaa, alimsikiliza kaka yake, simulizi yake ilionekana kama filamu fulani ya Bongo Muvi. Alisikia tu watu wakipata mazali lakini siku hiyo, kaka yake naye alionekana kupata zali la mentali.
“Huyo mwanamke ni nani?” aliuliza Irene.
“Simjui! Alikuja, akaniambia ananipenda, akanipa hela,” alisema Godwin.
“Alipokwambia anakupenda, ukamwambiaje?”
“Kwamba nataka kujifikiria! Nisingeweza kukubali harakaharaka!” alijibu Godwin.
“Umejifikiriaje?”
“Mimi sifikirii mapenzi! Nafikiria pesa tu! Nadhani kupitia huyu mwanamke, tunaweza kupata pesa na hata sehemu nzuri ya kulala,” alisema Godwin.
“Ila nina wasiwasi naye! Isijekuwa ni mmoja wa watu wale!”
“Sidhani! Nilidhani hivyo lakini kwa jinsi anavyozungumza, anaonekana kabisa kumaanisha, au aje kubadilika baadaye,” alisema Godwin.
****
“Mmefikia wapi?” aliuliza mwanaume kwenye simu kutoka upande wa pili.
“Tumewatafuta sana! Tumewakosa!”
“Haiwezekani! Mtawakosaje watu kama wao. Mtandao wetu ni mkubwa. Mmewakosaje sasa?” aliuliza mwanaume huyo.
“Mkuu! Nadhani utupe muda zaidi!”
“Na vipi kuhusu hao madaktari?”
“Wote tuliwateka, tukawatesa sana kama ulivyoona kwenye hizo video lakini hawakutuambia mahali walipokuwa. Walisema kwamba waliwaruhusu, ila kujua walipo, nao hawajui,” alijibu Majura.
“Majura. Kuweni siriazi, ninataka kujua mahali walipo ndani ya wiki hii! Mmenielewa? Nendeni kila kona, ufukweni, mitaani, kwenye majumba mabovu lakini mwisho wa siku nataka kujua wapo wapi ili tuwamalize wote. Mmenielewa?” aliuliza mwanaume huyo.
“Ndiyo mkuu! Tutahakikisha wanapatikana ndani ya wiki hii!”
“Safi sana! Nawatakieni kazi njema,” alimalizia na kukata simu. Kilichobaki kilikuwa ni kuwatafuta Godwin na Irene ambao mpaka muda huo hawakujua walikuwa mahali gani.
Bi Rachel alikuwa na presha kubwa, moyo wake ulichanganyikiwa, kitendo cha kuzungumza na Godwin kiliuchanganya mtima wa moyo wake. Usiku, mawazo yake yalikuwa kwa Godwin, hakujiamini, wakati mwingine aliona kama kijana huyo angekataa kuwa naye na hivyo kufikiria zaidi kutumia pesa, kitu ambacho kwa kijana wa kileo ingekuwa ngumu sana kukataa kuwa naye.
Katika maisha yake alitembea na vijana wengi wadogo, walimpenda kwa kuwa hakuangalia mfuko wake, pale kulipokuwa na ulazima wa kutumia pesa, alitumia pasipo kuangalia kitu chochote kile.
Mumewe alikuwa mfanyabiashara mkubwa, alikuwa na vituo vitatu vya mafuta vya Seven Oilcom ambavyo kwa siku viliwaingizia mamilioni ya pesa. Ukiachana na vituo hivyo, pia alikuwa na kampuni mbalimbali ambazo pia zilizifanya akaunti zao kusoma mabilioni ya shilingi kila kukicha.
Bi Rachel alikuwa na pesa, alizitumbua kupita kawaida na ndiyo maana hakuona kama kungekuwa na ugumu wa kumhonga Godwin kiasi chochote cha pesa alichokuwa akikihitaji.
Hakupenda vijana kwa sababu alihitaji mapenzi ya kweli, aliwapenda vijana kwa sababu tu aliamini kitandani walikuwa na nguvu ya kumfanya vyovyote vile. Mume wake alizeeka, hakuwa na nguvu, japokuwa mwanamke huyo alikuwa na umri mkubwa lakini cha kushangaza damu yake bado iliendelea kuchemka kwa nguvu kubwa hivyo kuhitaji mtu ambaye naye alichemkwa na damu na si mtu kama mumewe ambaye damu yake ilipoa.
Kwa kumfikiria Godwin, alidata, usiku wa siku hiyo ambao alizungumza naye hakulala vizuri kama siku nyingine, alilala huku akiwa na mawazo tele juu ya kijana huyo wa mitaani ambaye kwa kumwangalia tu usingepata wakati mgumu kugundua kwamba alikuwa fukara wa kutupwa aliyekuwa akiishi mitaani.
Siku iliyofuata, hakutaka kubaki nyumbani, moja kwa moja akaelekea mpaka katika baa ile kwa kuamini kwamba angebahatika kumuona Godwin lakini bahati mbaya kwake, baada ya kwenda huko, aliambiwa kwamba siku hiyo, mpaka muda huo kijana huyo hakuwa ameonekana hivyo alipaswa kusubiri.
Alikuwa na presha kubwa moyoni mwake, kwa wakati huo moyo wake ulibadilika, haukutaka kusikia jambo lolote lile, alichokuwa akikihitaji ni penzi kutoka kwa Godwin tu.
Alisubiri na kusubiri lakini hakufanikiwa kumuona hivyo kuaga na kumpa simu muuza chipsi na shilingi laki moja, vyote hivyo vilikuwa kwa ajili ya kuwasiliana naye na fedha kwa ajili ya matumizi madogomadogo.
“Nitamfikishia!” alisema muuza chipsi.
“Sawa. Na wewe shika hii,” alisema Bi Rachel na kumpa kiasi cha shilingi elfu thelathini kama shukrani yake.
Muuza chipsi akabaki mahali hapo huku akiwa amepigwa na butwaa, maishani mwake aliwahi kuwaona watu wengi wakiwa na bahati lakini kwa Godwin, alimuona akiwa na bahati zaidi.
Vijana wengi waliwataka wanawake kama hao, wanawake ambao hawakufikiria mifuko yao, wanawake ambao walikuwa radhi kutoa kiasi chochote kile cha fedha lakini mwisho wa siku wapate penzi kutoka kwa watoto wadogo ambao kwa mjini hujulikana kama marioo.
Siku hiyo Godwin hakufika mahali hapo, alikuwa akifanya mambo yake mengine, asingeweza kwenda kuchukua masalia ya chakula na wakati alipewa fedha. Kama ilivyo kwa Bi Rachel, naye kichwa chake kilikuwa kikimfikiria mwanamke huyo, hakuwa na uhakika kama kweli alimpenda au alitaka kumuua baada ya kutumwa na wabaya wao kutaka kummaliza kama ilivyokuwa kwa wale mapadri.
Hakuwa na amani, maisha yake akayaacha kwa Mungu kwamba kama kweli watu hao walitaka kumuua, basi angeuawa sehemu yoyote ile kama kama Mungu aliamua kumlinda, basi angemlinda maisha yake yote.
Baada ya siku tatu, akaelekea tena katika baa ile. Alipofika tu, kitu cha kwanza alichokifanya muuza chipsi ni kumpa simu na kiasi cha fedha alichokuwa ameachiwa, Godwin akachukua na kuelekea kule kichakani, kwenye majabari alipokuwa akiishi na ndugu yake, Irene.
“Amekupa simu?” aliuliza Irene huku akionekana kushangaa.
“Ndiyo! Daah! Sasa sijui iweje,” alisema Godwin.
“Nina hofu sana! Hivi kweli anachokihitaji ni mapenzi au roho yako? Ananitia hofu sana,” alisema Irene, hata uso wake ulionyesha hofu kubwa aliyokuwa nayo moyoni mwake.
“Sijajua! Tulikabidhi jambo hili kwa Mungu! Kama kweli si mtu mbaya, basi huu ndiyo utakuwa mwisho wa shida zetu ila kama ni mtu mbaya, basi Mungu azilaze roho zetu mahali pema peponi,” alisema Godwin huku akimwangalia dada yake.
Usiku huohuo akachukua simu hiyo iliyokuwa na laini, namba moja tu ya mwanamke huyo iliyokuwa imeseviwa na kumpigia simu. Simu haikuita sana Bi Rachel akaipokea na kuanza kuzungumza naye.
Mwanamke huyo hakuamini kama kweli aliyekuwa akizungumza naye alikuwa Godwin, alimkumbuka mno, muda wote aliongea huku sauti yake tu ikisikika kama mtu aliyekuwa na furaha kubwa mno.
Wakapanga kuonana, mwanamke huyo akamwambia Godwin kwamba hakutakiwa kuwa na hofu yoyote ile kwani alimfuata kwa kuwa alimpenda sana, alitaka kumpa maisha ya furaha ambayo hakutegemea kama yangekuja kupatikana katika maisha yake yote.
****
Vijana zaidi ya ishirini wakapewa kazi ya kuwatafuta Godwin na Irene ambao mpaka muda huo hawakujua walikuwa mahali gani. Ilikuwa kazi kubwa sana, walianzia kupata taarifa kutoka kwa madaktari katika Hospitali ya Mwananyamala ambao pamoja na kuwateka huku wakiwalazimisha kuambiwa walichokuwa wakikitaka, watu hao hawakuwapa chochote cha maana kwani nao hawakuwa wakijua.
Walichanganyikiwa, walijua kwamba wawili hao walikuwa sehemu wakiendelea na maisha yao, wakaelekea katika kibanda chao walichokuwa wakiishi, hawakufanikiwa kuwapata, wakaelekea katika nyumba zote zilizokuwa zikiendelea kujengwa kwa kuhisi labda walikuwa huko napo hawakufanikiwa kuwapata.
Vichwa vyao viliumwa, watu wote ishirini walishindwa kujua mahali vijana wawili walipokuwa. Wiki ya kwanza ya kutafutwa ikapita, hakukuwa na kitu chochote walichokipata, wiki ya pili nayo ikaingia na kupita lakini bado hali ilikuwa ileile.
Walijaribu kutembea mitaani, kwa watoto ombaomba waliokuwa barabarani lakini napo hawakukuta kitu, hawakuweza kuwaona vijana hao na hata walipoulizia kwa watoto wengine hawakuwa wakiwafahamu kitu kilichowafanya kuchanganyikiwa zaidi.
Kutafuta kwao hakukuishia huko, walikwenda mpaka mitaani, mitaa ya uswahilini kama Tandale, Temeke, Manzese, Mwananyamala na sehemu nyingine zote lakini kote huko hawakuweza kuwaona watu hao.
“Watakuwa wapi?” aliuliza jamaa mmoja.
“Twendeni ufukweni!”
Hilo ndilo lililofanyika, walijigawa kimakundi na kuanza kwenda katika fukwe mbalimbali. Wengine walianzia Msasani Beach, Kigodeko na katika fukwe nyingine lakini huko hawakuambulia kitu na mwisho wa siku kabisa wakaamua kwenda katika Ufukwe wa Coco ambao walihisi kwamba kwenda huko ingekuwa ni sawa na kujisumbua tu kwani watu hao hawakuwa huko kwa sababu tu kulikuwa na idadi kubwa ya watu.
Walipofika, wakaanza kuzunguka kwa kujigawa, welikwenda kula kona, hawakuweza kumuona Godwin wala Irene. Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa msako wao, kitu kilichowajia akilini ni kwamba watu hao walikuwa wametorokea katika mikoa ya mbali ili wasiweze kuonekana.
“Siamini hilo! Yaani wawe wamekwenda mikoani! Wanakwendaje na wakati wote tunaamini hawana pesa?” aliuliza jamaa mmoja, wakati huo walikuwa katika baa iliyokuwa hapo Coco.
“Inawezekana lakini! Ila sisi wote tumewakosa hawa watoto! Yaani ni uzembe mkubwa sana,” alisema jamaa mwingine, katika meza hiyo walikuwa watu wawili ambao waliagiza pombe na kunywa taratibu.
Wakati mazungumzo yakiendelea, Godwin akafika hapo baa na moja kwa moja kwenda kukaa na Bi Rachel. Kwa kuwa ilikuwa ni usiku na kulikuwa na mwanga hafifu, vijana wale hawakumgundua japokuwa walimuona alipokuwa akitembea mpaka kukaa katika kiti alichokuwepo mwanamke huyo na kuanza kuzungumza.
Muda ulizidi kwenda, Godwin hakutoka pale alipokuwa, aliendelea kuzungumza na Bi Rachel mpaka alipomaliza na kuondoka mahali hapo. Vijana wale walibaki wakimwangalia tu, alionekana kuwa kijana mdogo kulinganisha na muonekano wa mwanamke huyo. Walibaki wakiulizana kwamba ilikuwaje mwanamke kama huyo kuwa na mpenzi mdogo kama kijana huyo?
Wakati wakiulizana hivyo, Bi Rachel akasimama, akatoa simu yake na kumpigia Godwin, wakati simu imepokelewa ndiyo muda aliokuwa akiwakaribia vijana wale ambao nao walitega masikio kumsikiliza kwani kwa jinsi alivyokuwa amenona, ilikuwa vigumu kwa wanaume marijali kuyatoa macho yao katika mwili wake.
“Nitakuja kukuona kesho mpenzi wangu,” alisema mwanamke huyo huku akiachia tabasamu.
“Naomba kesho usiniangushe. Nitakuja kukuchukua! Msalimie dada yako Irene, hata kama sijamuona, mpe salamu zangu shemeji yangu. Nakupenda Godwin! Nakupenda mpenzi wangu! Mwaaaa!” alisema Bi Rachel maneno ambayo yaliwafanya vijana wale kushtuka, wakaangaliana.
“Godwin!” alisema mmoja.
“Irene!” mwingine akaitikia, wote wakashtuka, jinsi majina yalivyotaja, wakawa na uhakika kwamba watu waliotajwa ndiyo wale waliokuwa wakiwatafuta.
***
Walijua fika kwamba yale majina waliyoyasikia kutoka kwa Bi Rachel ndiyo watu ambao walikuwa wakiwatafuta kwa kipindi chote hicho. Hawakutaka kuishia hapo, walijua kwamba mwanamke huyo alikuwa akiwafahamu zaidi watu hao hivyo walichokitaka ni kujua mahali mwanamke huyo alipokuwa akiishi na sababu za kuwafahamu watu hao ambao kwao walikuwa muhimu kuliko hata mishahara yao.
Wakainuka kutoka pale walipokuwa na kuanza kumfuatilia Bi Rachel ambaye kwa mwendo wa mikogo akaanza kuelekea kule alipopaki gari lake, akaingia na kuondoka mahali hapo huku akiwa na uhakika wa kufanikiwa kwa kile alichokuwa akikihitaji wakati huo.
Wanaume hao wawili hawakutaka kumuacha Bi Rachel, nao wakaingia ndani ya gari lao na kuanza kumfuatilia. Ilikuwa ni lazima wajua mahali alipokuwa akiishi ili hata kama kungekuwa na ugumu wa kuwapata Godwin na Irene basi wamtumie yeye mwenyewe mpaka kuwapata na kuwaua kama walivyokuwa wakitaka kufanya.
“Tukimtumia huyu, tutafanikiwa, ni lazima tujue mahali anapoishi,” alisema jamaa mmoja, huyo aliitwa Abdallah, ila kutokana na ukatili wake, alipenda kuitwa kwa jina la Mafia.
“Haina shida. Ninaona mafanikio makubwa sana mbele yetu, huyu ndiye ambaye atatuwezesha kuwapata watu wetu,” alisema mwenzake aliyeitwa Fred, ila alipenda kujiita Saint kwa maana ya utakatifu katika kufanya mauaji.
Waliendelea kumfuatilia Bi Rachel ambaye aliendesha gari kutoka katika Ufukwe wa Coco, akaelekea mpaka kule ilipokuwa Maisha Club ya zamani, akachukua kona ya kulia na mbele kidogo akakata kushoto na kuanza kuelekea ilipokuwa Hospitali ya CCBRT.
Walikuwa makini njiani, hawakutaka kugundulika kama walikuwa wakimfuatilia na hata umbali ambao walikuwa wamemuacha ulikuwa ni wa mita hamsini, yote hiyo ikiwa ni kutotaka kugundulika.
Waliendelea kumfuatilia mpaka alipofika Msasani ambapo gari lake likasimama nje ya jumba moja la kifahari, walibaki garini, waliliangalia gari lile mpaka geti lilipofunguliwa na mwanamke huyo kuliingiza gari lile ndani ya jumba hilo la kifahari.
Wakaona mafanikio makubwa, wakawa na uhakika kwamba huo ndiyo ungekuwa mwanzo wa kupata kila kitu walichokitaka. Kesho yake, mapema kabisa wakawa katika ufukwe wa Coco, walitaka kuona kama kijana yule wa jana, ambaye alizungumza na mwanamke yule angekuja mahali pale kwani walikuwa na uhakika kwamba inawezekana alikuwa ni Godwin waliyekuwa wakimtafuta kwa udi na uvumba.
Walikaa katika ufukwe huo ndani ya baa ileile ambayo Godwin alikuwa akifika sana kwa ajili ya kuchukua masalia ya chakula na kuonana na mwanamke huyo. Walitumia muda wa saa kumi hapo lakini hawakuweza kuona uwepo wa mwanamke huyo wala Godwin kitu kilichowapa hofu kwamba walikuwa wamewashtukia na hivyo kubadilisha sehemu ya kuonania.
“Sidhani kama inawezekana! Kwa nini tusiendelee kusubiri?” aliuliza Saint.
“Unahisi wataweza kuja mahali hapa? Kuna uhakika kwamba inawezekana wakawa wametushtukia,” alisema Mafia huku akionekana kuwa na wasiwasi.
“Hakuna kitu kama hicho, tuendelee kusubiri!”
Waliendelea kusubiri lakini hakukuwa na dalili za watu hao kuonekana mahali hapo, waliendelea kushikwa na wasiwasi kwamba inawezekana wakawa wamewashtukia kwamba walikuwa mahali hapo.
Saa moja usiku ikaingia, hakukuwa na dalili zozote za watu hao kuonekana mahali hapo kitu kilichowapa uhakika zaidi kwamba inawezekana kabisa watu hao waliwaona na hivyo kubadilisha mahali pa kuonania.
Wakaondoka lakini hawakutaka siku hiyo iwe mwisho wa wao kufika mahali hapo, waliamini kwamba kama mwanamke yule alikuwa amewasiliana na Godwin, tena dakika chache zilizopita walionana, waliamini kwamba kuna siku watu hao wangeonana tena mahali hapo na hivyo kufanya kile walichotakiwa kufanya.
****
Bado Godwin na Irene walikuwa na hofu kubwa, hawakumwamini Bi Rachel hata kidogo, wakati mwingine walihisi kabisa kwamba mwanamke huyo alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakiwatafuta usiku na mchana kwa ajili ya kuwamaliza.
Walikaa na kuzungumza sana na uamuzi waliofikia ni kwamba wamuamini mwanamke huyo endapo angekuwa mwanamke aliyekuwa na lengo la kuwaua, angefanya hivyo zamani kwani kama kuonana na Godwin, alionana naye kabla na kupata nafasi ya kufanya hivyo.
Walizungumza kwa njia ya simu, wakapanga kuonana lakini isingekuwa mahali hapo walipotumia kuonana, wakapanga sehemu nyingine, sehemu ambayo Bi Rachel aliona kwamba ilikuwa na hadhi ya kukaa mtu kama yeye.
Bi Rachel akapanga mahali pa kuonana, ilikuwa katika Hotel ya Jumanj iliyokuwa Kijitonyama jijini Dar es Salaam. Hilo halikuwa tatizo kwa Godwin, kwa kuwa alikuwa na pesa za kutosa, akanunua nguo nzuri na kuzivaa katika siku ambayo alipanga kuonana na mwanamke huyo.
Siku yenyewe ilipofika, akaondoka na kuelekea katika hoteli hiyo. Njiani alikuwa na hofu kubwa moyoni mwake, alimuomba Mungu kwamba amlinde kwani kama ni kuuawa, alikuwa akijipeleka huko kuuawa na maadui zake ambao walimtumia mwanamke huyo ili kumnasa kiulaini.
Hakuchukua muda mrefu akafika mahali hapo. Akateremka kutoka katika bodaboda aliyokuwa amekodi na kumlipa dereva kisha kuelekea katika sehemu ya mgahawa wa hoteli hiyo.
Akaelekea katika mgahawa wa hoteli hiyo na kumpigia simu Bi Rachel na kumwambia kwamba tayari alikuwa amefika katika hoteli hiyo ambapo mwanamke huyo akamwambia kwamba lingekuwa jambo jema kama angekwenda katika chumba alichokuwa amechukua kwa ajili ya kuongea.
“Hapana!” alisema Godwin.
“Kwani tatizo nini mpenzi? Huniamini?” aliuliza mwanamke huyo kwenye simu.
“Nadhani hapa panafaa zaidi kwa leo,” alisema Godwin na kisha kukata simu.
Alijua kile ambacho kingekwenda kutokea chumbani, hakutaka kitokee, alijua kwamba mwanamke huyo alikuwa akimpenda kupita kawaida hivyo angetumia ushawishi wowote ule kulala naye kitu ambacho hakutaka kuona kikitokea.
Alimwambiawazi kwamba sehemu nzuri ya kukaa na kuzungumza ilikuwa katika mgahawa ule ambapo mwanamke huyo hakupinga, akakubaliana naye na hivyo kwenda hapo na kuonana naye huko.
Kitendo cha kumuona Godwin kwa mara nyingine, moyo wake ukawa na furaha mno, mapenzi mazito aliyokuwa nayo moyoni mwake yakaongezeka zaidi. Hakukukuwa na mwanaume yeyote aliyeuchanganya moyo wake zaidi ya kijana huyo ambaye kwa kumwangalia tu, alionekana kuwa mwanaume mzuri kuliko wote ambao aliwahi kuonana nao.
“Kwa nini huniamini?” aliuliza mwanamke huyo baada ya kukaa na kuanza kuzungumza naye.
“Inategemea uliniambiaje kwenye simu! Ulisema kwamba unataka kuzungumza nami, si ndiyo?” aliuliza Godwin huku akimwangalia Bi Rachel.
“Ndiyo!”
“Tuongee halafu hayo mengine tutafanya siku nyingine,” alisema Godwin huku akichukua glasi ya juisi na kuanza kunywa.
****
Saint na Mafia waliamini kwamba kama wangetumia nafasi waliyokuwa wameipata basi ingekuwa kazi nyepesi kabisa kumpata Godwin na kumuua kama walivyokuwa wameambiwa.
Walihakikisha wanakuwa karibu na Bi Rachel kwa kuamini kwamba ilikuwa ni lazima kwa mwanamke huyo kuwasiliana na kijana huyo na hatimaye kuonana. Hawakukauka nyumbani kwake, mara kwa mara walikuwa wakifika mahali hapo kuhakikisha wanamfuatilia mwanamke huyo.
Wakafanikia kupafahamu mahali alipokuwa akifanya kazi na mwisho wa siku kabisa walipomfuatilia, wakagundua kwamba muda huo alikuwa akienda kuonana na mtu mahali fulani, hawakujua alikuwa nani lakini wakawa na uhakika kwamba inawezekana mtu huyo akawa Godwin.
Wakamfuatilia mpaka alipoingia katika Hoteli ya Jumanj, mmoja akaelekea ndani kuona kama Godwin alikuwa mule ndani huku mwingine akibaki nje kuona kama Godwin angefika mahali hapo kwa lengo la kuonana na mwanamke huyo.
“Vipi ndani huko?” aliuliza Mafia.
“Kaenda chumbani! Sijajua kama huyo mtu yupo huko au siyo. Vipi huko nje?” aliuliza Saint.
“Huku hakuna kitu! Ila tuendelee kusubiri,” alisema Mafia.
Hawakutaka kuwa na haraka, wakaendelea kusubiri kwa kuamini kwamba kulikuwa na mtu aliyekuwa akienda kuonana naye na walikuwa na uhakika kwamba inawezekana mtu huyo alikuwa Godwin.
Waliendelea kusubiri, mmoja akiwa nje na mwingine ndani. Baada ya saa moja, Saint aliyekuwa nje akaona bodaboda ikija ndani ya hoteli ile na kusimama, akaiangalia kwa makini, abiria aliyeteremka alimfahamu kwa kumuona, alikuwa Godwin ambaye ndiye waliyekuwa wakimtafuta kipindi chote.
“He is here,” (amefika) alimtumia Mafia ujumbe mfupi.
“Just roll with him,” (tembea naye) aliandika Saint.
Haraka sana Saint akatoka ndani ya gari alilokuwemo na kuanza kumfuata Godwin ambaye alipiga hatua mpaka katika mgahawa wa hoteli hiyo, pale alipokwenda kukaa, naye akaenda katika meza nyingine kabisa, akatulia, ndani ya dakika chache, Mafia akatokea mahali hapo, akaungana naye na kuanza kumsubiria Bi Rachel ambaye baada ya dakika kumi, akafika mahali hapo na kwenda kukaa na Godwin.
“Tukimkosa leo, kumpata tena mwakani,” alisema Mafia huku akijigusa kiunoni kuhakikisha kama bastola yake ilikuwepo.
***
Mtu waliyekuwa wakimuhitaji ambaye walimtafuta kila kona, hatimaye alikuwa mbele yao, walimwangalia jinsi alivyokuwa akizungumza na Bi Rachel, alionekana kuwa kijana mwerevu, mjanja ambaye hata alivyokuwa akiongea, macho yake alikuwa akiyapeleka huku na kule kuona kama alikuwa akifuatilia.
Walijua kwamba hiyo ndiyo ilikuwa nafasi yao pekee, na kama ingetokea wangemkosa mahali hapo basi wasingeweza kumpata tena. Hawakuyatuliza macho yao, mara kwa mara walikuwa wakimwangalia kwa kuibia na alipokuwa bize kuzungumza na Bi Rachel, waliyatuliza macho yao kumwangalia vizuri.
Mpaka wanafikia hatua hiyo, hawakuwaambia wakuu wao kwamba mtu waliyemtaka kwa kipindi kirefu alikuwa mbele yao, walitaka kufanya mambo kimyakimya, hawakutaka mtu yeyote afahamu kile kilichokuwa kikiendelea kwani kuna wakati walihisi kwamba kulikuwa na ugumu wa kumpata Godwin na Irene kwa sababu kulikuwa na watu waliokuwa wakitoa siri kwa vijana hao.
Waliendelea kusikilizia, walijifanya kuwa bize. Walikuwa na uwezo wa kumvamia mahali pale, kumteka na kuondoka naye lakini kitu kilichokuwa kikiwatia hofu ni kwamba kulikuwa na idadi kubwa ya wateja katika mgahawa huo. Walijua kwamba endapo wangefanya kitu kama hicho ingekuwa rahisi sana kwa watu wengine kujua kwamba walikuwa watekaji na hivyo kupambana nao.
Walitaka kufanya mambo yao kiakili, walikuwa watu wa kawaida lakini walihitaji kufanya mambo kama majasusi wa Kimarekani nje ya nchi, CIA. Baada ya dakika arobaini na tano, Godwin akasimama pale alipokuwa amekaa, alimuaga Bi Rachel kwamba alikuwa akienda chooni kujisaidia.
Wakati kijana huyo akiwa amepiga hatua kuelekea katika choo kile ambacho hakikuwa mbali kutoka katika mgahawa ule, naye Mafia akasimama na kuanza kuelekea kulekule. Hakwenda kwa lengo la kumteka huko, alitaka kufuatilia, alichohisi ni kwamba Godwin alitaka kutoroka hivyo ilikuwa ni lazima kufuatilia kwa makini.
Godwin alipoingia chooni, baada ya sekunde kadhaa, naye Mafia akaingia na wote wawili kujisaidia huku wakiwa kimya, hata kusalimiana, hawakusalimiana. Godwin hakuonekana kuwa na hofu, alipomaliza kufanya mambo yake, akarudi pale alipokuwa Bi Rachel na kutulia, mazungumzo yakaendelea.
“Vipi huko?” aliuliza Saint mara baada ya mwenzake kurudi.
“Poa! Dogo anaonekana yupoyupo sana. Ila kuna kitu nimefikiria,” alisema Mafia.
“Kitu gani?”
“Nahisi watakwenda chumbani, kwa jinsi hili jimama linavyozungumza, jinsi linavyorembua na kuongea kwa mhemko, lazima wataelekea chumbani. Sasa wakienda huko, tuhakikishe tunakwenda na kufanya kile tunachotakiwa kufanya,” alisema Mafia huku akimwangalia mwenzake.
“Hakuna shida. Ni wazo zuri. Kwanza tunaweza kufika chumbani, tukawateka halafu tukawapigia simu wakuu, wakatoa amri hotelini dogo atolewe bila tatizo halafu tunakwenda kummaliza,” alisema Saint.
“Sawasawa.”
Wakati wakiendelea kuzungumza, Godwin akamuita mwanaume aliyekuwa akihusika na chakula na kuzungumza naye kuhusu chakula alichokuwa akihitaji. Baada ya kuzungumza kwa sekunde kadhaa na mhudumu huyo kuanza kuondoka, wakasimama, kwa haraka sana Godwin akamuita mhudumu huyohuyo, alipogeuka tu, kwa kuwa alikuwa mbali kidogo akaamua kumpa maagizo hapohapo.
“Weka pilipili kidogo. Utaomba mapokezi utuletee chumba namba sitini,” alisema Godwin kwa sauti huku watu wote wakisikia, hakujali, yeye na Bi Rachel wakaanza kuondoka kuelekea ndani kwani kwa jinsi mazungumzo yalivyokuwa yamenoga, hakukuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima hatua inayofuata wazungumze wakiwa kitandani.
Wakaondoka, watu wote wakabaki wakiwashangaa watu hao, walikuwa wakitembea kama wapenzi, Bi Rachel alionekana kuwa mkubwa kiumri, kitendo cha kumchukua kijana mdogo kama Godwin kiliwafanya watu wote pale mgahawani kumshangaa.
Wakafika katika sehemu ya kuchukua lifti kwenda kwenye chumba hicho kilichokuwa katika ghorofa ya tisa, lifti ilipofika, wakaingia na kuondoka. Kwa haraka sana Mafia na Saint waliokuwa mgahawani, wakaondoka na kuelekea katika sehemu ile ya kusubiria lifti, wakasimama huku wakiwa na presha, walitaka kwenda kule walipokuwa watu hao katika chumba namba sitini ambapo ndipo wangehakikisha mwisho wa Godwin unaanzia huko.
Walisubiri lifti huku wakiwa na presha kubwa, waliamini kwamba kama wangefanikiwa kupatikana kwa Godwin basi ingekuwa sifa kubwa kwao kwani kwa kipindi kirefu, vijana zaidi ya ishirini walitumwa kumtafuta lakini hawakufanikiwa.
Hawakusimama sana, lifti ikafika na kujifungua, wakaingia ndani na kuanza kupanda juu. Kila mmoja alihakikisha bastola yake ipo kiunoni ili watakapofika ndani ya chumba hicho, kusiwe na kitu chochote cha kufanya zaidi ya kumuweka chini ya ulinzi Godwin na kuwapigia simu wakuu wao ili wawasiliane na uongozi wa hoteli kwa ajili ya kutoka na mtu huyo salama.
Hawakuchukua sekunde nyingi lifti ikafika katika ghorofa ya tisa, haraka sana wakateremka na kuanza kukitafuta chumba namba sitini ambacho waliamini kuwa Godwin alikuwa humo na huyo mwanamke.
“Hamsini na nane,” alihesabu Sainti.
“Hamsini na tisa. Nadhani kile kule,” alisema Mafia na kuanza kuusogelea mlango wa chumba hicho.
Walipoufikia, wakasimama kwa lengo la kuvamia ndani ya chumba hicho. Mafia akashika kitasa na kuanza kukitekenya huku akijaribu kuufungua mlango huo, haukufunguka, ulionyesha kufungwa kwa ndani.
“Ngo ngo ngo,” alipiga hodi.
Waliendelea kusimama pale mlangoni, mlango haukufunguliwa, walikuwa na hofu kwamba inawezekana wawili hao waligundua kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wakiwafuatilia. Walisimama huku wakiendelea kupiga hodi na kamera ndogo za CCTV zikichukua kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.
“Nani?” aliuliza Bi Rachel huku akiwa ndani.
“Kaka wa chakula. Nimekuleteeni chakula,” alisema Mafia, hapohapo mlango ukafunguliwa na mwanamke huyo.
Bi Rachel akashtuka, watu waliosimama mbele yake hawakuwa wahudumu, walionekana kuwa tofauti kabisa, sura zao hazikuwa za kipole na hapohapo mlangoni walipokuwa wamesimama, wakatoa bastola zao, wakamsukumia ndani.
“Rudi ndani!” alisema Mafia huku akiwa amemsukuma kwa ndani.
Walitegemea kumkuta Godwin ndani ya chumba hicho, wakapeleka macho yao kila kona humo ndani, Godwin hakuwepo, wakaangalia chini ya kitanda, Godwin hakuwepo kitu kilichowafanya kuhisi kwamba kijana yule alikuwa mahali amejificha, mahali ambapo Bi Rachel alipafahamu vilivyo.
“Yupo wapi?” aliuliza Mafia kwa sauti ya juu na ya kikatili.
“Nani?” aliuliza Bi Rachel.
“Paaaaaa…” alizabwa kibao kimoja cha haja mpaka damu kumtoka mdomoni.
“Yupo wapi?”
“Jamani! Mtaniua! Sijui mnamtafuta nani!” alisema Bi Rachel.
“Paaaa…” akazabwa kibao kingine. Hapohapo Mafia akakoki bastola yake.
“Unatuficha! Unataka kufa? Unataka kujitoa sadaka?” aliuliza Mafia huku akimuelekezea mwanamke huyo bastola.
“Jamani! Mimi sijaingia na mtu humu ndani!”
“Yule kijana yupo wapi?” aliuliza Mafia kwa sauti ya juu.
“Jamani! Sijui! Sijui kaenda wapi,” alijitetea Bi Rachel.
“Una masihara sana!”
“Jamani! Sijui chochote!” alisema mwanamke huyo, alikuwa akilia kwa sauti, aliumia, damu ziliendelea kumtoka mdomoni.
Saint akatoka chumbani hapo na kwenda bafuni, alipofika, akaanza kuangalia huku na kule kwa kuamini kwamba kijana huyo alikuwa humo, Godwin hakuwepo. Walichanganyikiwa, hawakujua kijana huyo alikwenda wapi. Walimuona akiondoka na mwanamke huyo na kuingia ndani ya lifti na kuja ndani ya chumba kile, kitu cha ajabu kabisa, kila kona ndani ya chumba hicho hakuonekana hali iliyoonyesha kwamba walitorokwa.
“Haiwezekani! Hawezi kutoroka. Huyu mwanamke anajua. Nakuhesabia mpaka tatu, nikimaliza bila kutuambia mahali alipo, tunakuuua,” alisema Mafia, uso wake tu ulionyesha kumaanisha alichokuwa akikisema.
“Jamani sijui chochote!”
“Moja….”
“Kweli sijui chochote, sijui amekwenda wapi!”
“Mbili…”
“Haki ya Mungu sijui alipo. Jamani nisameheni, sijui alipo.”
“Tat….” alihesabu Mafia huku akijiandaa kubonyeza kitufe cha kuruhusu risasi itoke.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Moyo wa Godwin haukuwa na amani hata kidogo, kila alipokuwa akiangalia huku na kule, aliamini kwamba sehemu hiyo haikuwa na salama hata kidogo. Macho yake hayakutulia, yalikuwa yakiangalia huku na kule kila wakati.
Katika mgahawa huo, kulikuwa na wateja wengi, kila mtu alikuwa na mambo yake na hakukuwa na mtu aliyeonekana kuwa na taarifa naye. Aliongea na Bi Rachel huku mwanamke huyo akimwambia maneno mengi ya kimapenzi, jinsi alivyokuwa akimpenda na ambavyo angeweza kutumia kiasi chochote cha pesa kumfurahisha.
Wakati akiwa anazungumza na mwanamke huyo, macho yake yakatua kwa wanaume wawili waliokuwa wamekaa mbali kidogo kutoka pale alipokuwa. Wanaume hao walikuwa wakizungumza mambo yao lakini mara chache walikuwa wakimwangalia sana tofauti na watu wengine.
Godwin akahisi kitu, akajua kabisa kwamba hao hawakuwa watu wazuri kwani hata alipoyaweka macho yake kwa Bi Rachel na kuwaangalia wanaume hao kwa macho ya kuibia, walikuwa wakimwangalia vilevile.
Akahisi kulikuwa na tatizo, alitaka kupata uhakika kama watu hao walikuwa wabaya kwake au alikuwa na hofu tu. Akamuaga Bi Rachel kwamba alikuwa akienda chooni, aliposimama na kuelekea huko, umbali kama hatua ishirini, mwanaume mmoja akasimama na kuelekea kulekule alipoelekea.
Akaingia chooni na baada ya sekunde chache, mwanaume huyo naye akaingia. Mpaka hapo akawa na uhakika kwamba watu hao walikuwa ni wabaya hivyo alitakiwa kuwatoroka haraka sana.
Hakujua ni kwa namna gani angeweza kuwakimbia, ila alipokumbuka kwamba Bi Rachel alimlazimisha sana kwenda chumbani, akakubaliana naye kwani hiyo ndiyo ingekuwa njia ya kuwakimbia wanaume hao.
“Sawa nimekubaliana na wewe,” alisema Godwin.
“Kuwa mpenzi wangu?”
“Hapana! Kwenda chumbani kuzungumza
“Nashukuru sana!”
“Ila chakula kije! Muite mtu wa chakula,” alisema Godwin.
Mtu wa chakula akaitwa na kuagizwa, alipokuwa akiondoka, ili mchezo aucheze vizuri, Godwin akamuita na kumuagiza kwa sauti ya juu kwamba chakula kiwekwe pilipili kisha kupelekewa katika chumba namba sitini, ghorofa ya tisa, alifanya hivyo kama kuwaaminisha watu wale kwamba angekuwa huko.
Akaondoka na Bi Rachel, wakaingia kwenye lifti. Alichokijua ni kwamba wanaume wale wangemfuatilia hivyo baada ya kuteremka tu, Godwin akamwambia Bi Rachel kwamba alisahau kununua kinga, hivyo aende kununua kwani ilikuwa ni lazima amalize mchezo siku hiyohiyo.
“Jamani mpenzi umebadilika tena! Umenisapraizi! Nimefurahi kusikia hivyo! Basi nenda mimi nakusubiri bebi’ ake alisema Bi Rachel na kumbusu Godwin shavuni.
Kwa haraka sana Godwin akaanza kuteremka chini kwa kutumia ngazi, alikuwa na haraka, aliamini kwamba wanaume wale ilikuwa ni lazima kuchukua lifti kwenda kule juu. Alitembea kwa machale, alikuwa akishuka huku akiangalia.
Hakuchukua muda mrefu akafika chini na uzuri wake hakuwakuta watu hao hivyo kutoka ndani ya hoteli ile na kuondoka zake. Moyo wake ukabaki ukimshukuru Mungu kwani alimuokoa kutoka katika mikono ya watu hao.
Akakimbia kuelekea barabarani. Wakati huo moyo wake ukamwambia kwamba hata Bi Rachel alikuwa miongoni mwa wale watu waliokuwa wakimtafuta na alikuwa akitumika kwa ajili ya kumteka lakini baada ya kufikiria kwa kina, akahisi kwamba mwanamke huyo hakujua kitu chochote kwani kama kweli lengo lake lilikuwa ni kumteka, angemng’ang’ania asiondoke kwenda kununua kinga.
“Ngoja nimpigie simu!” alisema Godwin na kuchukua simu kisha kumpigia mwanamke huyo.
Wakati huo ndiyo Mafia alikuwa amekwishamaliza kuhesabu, alijiandaa kubonyeza kitufe cha bastola lakini ghafla simu ya mwanamke huyo iliyokuwa kitandani ikaanza kuita. Haraka sana Saint akaichukua, alipoangalia jina, akagundua kwamba mpigaji alikuwa Godwin.
“Ni Godwin!”
“Mpe azungumze naye. Mwambie ajitokeze vinginevyo tunakuua,” alisema Mafia na Bi Rachel kukabidhiwa simu ile.
Mwanamke huyo akaichukua simu huku akitetemeka, akaanza kuzungumza na Godwin. Alichokuwa akikitaka kijana huyo ni jinsi sauti ya mwanamke huyo ilivyokuwa ikisikika. Japokuwa alijikaza kuzungumza kawaida lakini Godwin alipoisikia akahisi kulikuwa na kitu nyuma ya pazia.
“Upo salama?” aliuliza Godwin.
“Ndiyo! Mbona unachukua muda mrefu?” aliuliza mwanamke huyo kwa sauti ambayo haikuonyesha kama mahali hapo palikuwa salama.
“Nataka kuja ila ungewaambia hao majamaa waje huku chini na siyo wanakuonea wewe ambaye hujui lolote lile. Kwanza wanaume watamuoneaje mwanamke bwana?” alisema Godwin kwa sauti ya kutamba, hapohapo Mafia akachukua simu.
“Halo!” akaita kibabe.
“Oya! Mnamuonea bure huyo mwanamke, halafu mwanamke havamiwi kwa bastola. Nyie kama vidume si mshuke huku chini mpambane na mimi! Kama mtaweza, niueni ila kama hamtoweza, nitawaua nyie na hao waliowatuma,” alisema Godwin kana kwamba alikuwa na nguvu za kupambana na hao watu.
“Upo wapi?”
“Wewe unataka niwe wapi?”
“Si umesema unataka kupambana!”
“Sasa mbona mnakimbilia bastola? Hamjiamini? Huo uboya wewe,” alisema na kumalizia neno ambalo lilionyesha kama dharau kwa Mafia.
Kwa hasira, Mafia akaipiga simu chini simu hiyo, maneno aliyokuwa ameongea Godwin yalimuumiza mno, akamzaba kibao cha haja Bi Rachel, akaanguka chini na kupoteza fahamu. Hawakutaka kubaki ndani ya chumba hicho, haraka sana wakaondoka huku wakiwa na bastola mikononi mwao, hata kuziweka kiunoni wakashindwa.
Walipofika chini, wakaanza kukimbia kuelekea nje, hawakumuona Godwin, hawakujua mahali alipokuwa ila kwa kuwa mara ya kwanza walimuona Bi Rachel akizungumza na Godwin kule Coco akajua kwamba kijana huyo alikuwa huko, hivyo wakaanza kuelekea pande hizo.
Upande wa pili Godwin alikuwa akikimbia kuelekea barabarani ambapo akasimamisha bodaboda, akapanda na kuondoka zake. Macho yake hayakutulia, yalikuwa yakiangalia huku na kule kuhakikisha kwamba kila kitu kilikuwa salama.
Hakujua Bi Rachel alikuwa kwenye hali gani ila alichokuwa akikitaka ni kufika salama Coco ambapo angemwambia Irene kwamba sehemu hiyo haikuwa salama hivyo walitakiwa kuondoka haraka iwezekanavyo.
Hawakuchukua muda mrefu wakawa wamekwishafika mahali hapo, akamlipa dereva kisha kuondoka harakaharaka kuelekea kulipokuwa na mahali alipokuwa akiishi na dada yake.
“Kuna nini?” aliuliza Irene huku akimwangalia kaka yake aliyekuwa akihema kwa nguvu.
“Tuondoke!”
“Tuondoke! Kwenda wapi?”
“Popote ila tuondoke hapa,” alisema Godwin.
Irene hakutaka kubisha, alipoambiwa hivyo, haraka sana akachukua kila kilichokuwa chake na kuondoka mahali hapo. Alitaka kufahamu ni kitu gani kilikuwa kimetokea kule alipokwenda kuonana na Bi Rachel.
Kila alipokuwa akimuuliza kaka yake, hakujibu zaidi ya kuangalia huku na kule kana kwamba kulikuwa na mtu fulani alikuwa akimtafuta. Safari yao ikaishia barabarani ambapo wakasimamisha Bajaj iliyokuwa ikipita na kisha kuingia ndani.
“Wapi?”
“Manzese Midizini!”
“Elfu kumi na tano!”
“Wewe twende,” alisema Godwin.
Wakaondoka, hakuzungumza kitu, moyo wake ulikuwa na hofu tele, kila wakati alikuwa akiangalia nyuma kuona kama kulikuwa na mtu aliyekuwa akimfuatilia. Irene alibaki kimya, hakumuelewa Godwin, alitaka kujua kilichokuwa kikiendelea lakini kila alipotaka kufanya hivyo, hali aliyokuwa akiionyesha Godwin, haikumruhusu kabisa kuuliza swali.
“Dereva unaweza kuongeza kasi kidogo tuwahi?” alimuuliza dereva.
“Hakuna shida!”
“Godwin! Kuna nini?” aliuliza Irene huku akimwangalia kaka yake usoni.
“Ni hatari!”
“Imekuwaje?”
“Tutaongea mbele ya safari!”
“Yule mwanamke amekuchoma?”
“Hapana!”
“Ila?”
“Tutaongea tu Irene, usiwe na presha!”
Wakaendelea na safari, walipofika Macho, Bajaj ikachukua barabara ya lami kushoto kuelekea Namanga lakini wakati wakiichukua barabara hiyo, ghafla wakaona gari nyuma yao likianza kuwafuata.
Godwin akashtuka, moyo wake ulimwambia kwamba gari hilo lilikuwa la wale wanaume aliokuwa amewaacha hotelini. Alimwambia dereva kuongeza kasi zaidi na zaidi kwani hakutaka kukamatwa, kwa jinsi alivyokuwa amewatambia kwenye simu, aliamini kwamba kama wangemkamata ilikuwa ni lazima kumuua.
“Dereva ongeza kasi!”
“Kaka hii siyo gari! Tutapata ajali! Halafu magari yapo mengi sana, au unataka trafki anipige bao? Tulia kwanza,” alisema dereva yule, na kila wakati Godwin alipokuwa akiangalia nyuma, gari lile liliendelea kuwafuata kitu kilichomtia hofu kubwa moyoni mwake.
“Irene! Tunafuatiliwa!” alisema Godwin.
“Tunafuatiliwa! Na nani?”
“Wale wanaume wa hotelini!”
“Wanaume gani?”
“Irene! Leo ndiyo leo! Unaiona hiyo gari hapo nyuma, tunafuatiliwa!”
“Na wakina nani?”
“Tuombe tufike salama halafu nitakwambia kila kitu,” alisema Godwin huku kila alipokuwa akiangalia nyuma, gari ile iliendelea kuwafuatilia.
***
Kila mmoja alikuwa na hofu, wakajua kwamba gari lile lililokuwa nyuma yao lilikuwa la wale jamaa waliokuwa wakiwataka kwa lengo la kuwamaliza. Ndani ya Bajaj, kila wakati Godwin alikuwa akigeukageuka nyuma na kuliangalia gari lile.
Aliendelea kumwambia ndugu yake kwamba gari lile lililokuwa nyuma yao lilikuwa la watu hao hivyo ilikuwa ni lazima dereva wa Bajaj aongeze kasi ili waweze kupotea katika uwepo wao.
Hawakumwambia dereva kwamba walikuwa wakifuatiliwa na gari hilo ila kitu pekee ambacho Godwin alimwambia dereva huyo ni kuongeza kasi ya Bajaj ili wawapotee kabisa. Bajaj ilipofika Namanga, dereva akakata kona upande wa kulia na kuchukua barabara iliyokuwa ikienda katika ubalozi wa Marekani na kitu kilichomfurahisha Godwin na kumpa amani moyoni mwake, gari lile likanyooka mbele kabisa kuelekea katika makutano ya barabara hiyo na Ally Hassani Mwinyi.
“Ooppss!” Godwin alishusha pumzi nzito.
Kidogo moyo wake ukatulia, furaha iliyokuwa imepotea dakika chache zilizopita ikarudi upya moyoni mwake. Akafurahi kugundua kwamba gari lile ambalo liliwafanya kuwa na hofu nalo halikuwa na hatari yoyote ile.
Hakutaka kuficha, akamwambia Irene kwamba alikuwa na hofu kubwa kwani kule alipokuwa ametoka kulikuwa na jambo kubwa lililokuwa limetokea lakini stori yote kuhusu kile kilichokuwa kimetokea angemwambia baada ya kufika MAnzese Midizini.
Walichukua dakika arobaini mpaka kufika Manzese ambapo wakateremka na kuanza kuulizia sehemu kulipokuwa na madalali wa chapchap. Hilo wala halikuwa tatizo kwani ndani ya dakika chache wakaonana na dalali mmoja ambaye akawatoa hofu kwa kuwaambia kwamba chumba kilikuwepo, tena ilikuwa vizuri kabisa kwa kuwa waliwahi.
“Kiasi gani?”
“Elfu ishirini kwa mwezi. Kina umeme, kwa ujumla ni kizuri,” alisema dalali huku akiwaangalia vijana hao.
Hawakutaka kupoteza dakika yoyote ile, walikuwa na hela ya kutosha kulipa kodi ya mwaka mzima hivyo wakataka kupelekwa, wakaenda na kuonana na mwenye nyumba ambaye aliwaambia kuwa ishu ya kuhamia humo siku hiyo haikuwa na tatizo lolote lile, hivyo wakahamia.
“Ila kuna jambo moja la msingi naomba unisaidie,” alisema Godwin, alikuwa akizungumza na mwenye nyumba.
“Jambo gani?”
“Sisi tupo wawili, mimi na dada yangu, hatuwezi kulala chumba kimoja, hakuna chumba cha ziada utusaidie hata kwa kipindi hiki?” aliuliza Godwin.
“Chumba cha ziada?”
“Ndiyo!”
“Nacho utalipia?”
“Kwa kweli sitoweza kulipia hasa kwa kipindi hiki. Hatuna pesa ya kutosha lakini pia sipo tayari kulala na dada yangu chumba kimoja. Kama itawezekana, naomba unisaidie ila kama haitowezekana, haina shida, mimi mwanaume nitapambana,” alisema Godwin huku akimwangalia baba mwenye nyumba huyo.
Kwa jinsi alivyoonekana, Godwin alihitaji msaada wa chumba, baba mwenye nyumba hakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima kumsaidia kijana huyo hivyo kumchukua na kumpeleka uani na kumpa chumba ambacho kilikuwa kikitumika kama stoo.
Kulikuwa na vitu vingi ambavyo havikuwa vikitumika, chumba kilitelekezwa, hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akiishi ndani ya chumba hicho, kilitumika kwa ajili ya kuhifadhia vitu ambavyo havikuwa vikitumika humo.
Akapewa kazi ya kukisafisha, hilo halikuwa tatizo hata kidogo, akaanza kupasafisha huku akisaidiana na Irene. Muda wote walikuwa wakikutana na vumbi kali lililowasababishia mafua lakini hawakutaka kuacha, ni ndani ya saa mbili, tayari chumba kilikuwa kisafi, kila kitu kilitolewa, kilipigwa deki na kidogo kuonekana kuwa na unafuu fulani.
Hakuwa na kitanda, akachukua kiasi cha pesa na kwenda kununua mikeka miwili Manzese Sokoni na mmoja kumpa Irene huku mwingine akibaki nao chumbani. Hapo ndipo walipotakiwa kuanza maisha mapya, hakujua kuhusu Bi Rachel, hali yake iliendeleaje, alichokuwa akikiangalia kipindi hicho ni maisha yake tu.
Siku ya kwanza ikapita, ya pili ikapita na mpaka siku ya tatu inaingia, bado maisha yalikuwa hivyohivyo. Godwin hakutaka kumpigia simu Bi Rachel, alitaka kuona siku ambayo mwanamke huyo angempigia na kuzungumza naye ili amwambie ni kitu gani kiliendelea ndani ya chumba kile.
“Mmh! Hawakumuua kweli?’ alijiuliza huku akionekana kuwa na hofu tele.
Wakati akiendelea na maisha kama kawaida, akaanza kupokea simu kutoka kwa namna ngeni, mtu huyo aliyekuwa akimpigia alijitambulisha kwa jina la Edward Albert. Mtu huyo alimwambia kwamba alikuwa mfanyabiashara mkubwa ambaye lengo lake kubwa lilikuwa ni kushirikiana naye katika biashara hiyo.
Godwin alishangaa, alimwambia mwanaume huyo kwamba hakuwa mfanyabiashara lakini hakutaka kusikia, kila siku alikuwa akimpigia na kuzungumza naye, alimwambia wazi kwamba aliwahi kumpa namba yake na kuwa alimuahidi kwamba angemuunganishia na wauza mchele wa soko la Kariakoo.
“Umekosea namba kaka! Mimi siyo mfanyabiashara!” alisema Godwin.
“Hapana! Kuna siku ulinipa namba yako! Umesahau?”
“Mimi?”
“Ndiyo! Na ukasema unaitwa Hemedi!”
“Mimi?”
“Ndiyo!”
“Kwanza mimi siitwi Hemedi!”
“Wewe unaitwa nani?”
“Si lazima ujue. Ila umekosea namba. Mimi siishi Dar, naishi Lindi!” alisema Godwin.
“Duuh!”
“Ndiyo hivyo!” alijibu Godwin na kukata simu.
****
Mafia na Saint wakaondoka hotelini, safari ya kuelekea katika Ufukwe wa Coco ikaanza. Kila mmoja alitaka kumpata Godwin, aliwasumbua mno, wakati mwingine walijuta sababu iliyowafanya kutokumvamia palepale hotelini na kumteka kuliko kumpa nafasi ya kuondoka mgahawani.
Waligundua kwamba walifanya makosa lakini hawakutaka kujutia makosa hayo, walijua kwamba kulikuwa na nafasi kubwa ya kujirekebisha kwa kufanya mambo yaliyokuwa sahihi.
Hawakuchukua dakika nyingi wakafika katika ufukwe huo, walijaribu kuzunguka kila kona lakini hawakufanikiwa hata kidogo. Iliwauma, walikuwa na asilimia zaidi ya tisini kumpata Godwin lakini kwa uzembe wao, kijana huyo akawatoroka kirahisi kabisa.
Hawakujua mahali kijana huyo alipokuwa lakini walikuwa na uhakika kwamba hiyo ndiyo ilikuwa sehemu yake, makazi yake ambayo kila siku ilikuwa ni lazima kuwa mahali hapo.
Hawakuishia siku hiyo, waliendelea kufika mahali hapo kumtafuta lakini bado hawakumpata. Baada ya siku tatu bila mafanikio wakawasiliana na kiongozi wao na kumwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea.
Yeye mwenyewe alishangaa, ilikuwaje wawe karibu na mtu huyo halafu washindwe kumpata? Akawalaumu lakini wanaume hao wakaja na njia nyingine, kwa kuwa walikuwa na namba yake ya simu, walitaka kuitraki simu hiyo kujua mahali ilipokuwa.
Hilo halikuwa tatizo, wakapewa vijana wawili waliokuwa wataalamu wa kompyuta na hao ndiyo waliotaka kufanya nao kazi. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuwakabidhi namba hiyo, ilikuwa ni lazima kujua mahali alipokuwa,
Hiyo haikuwa kazi kubwa, ilikuwa ni lazima kumpigia simu mtu huyo ili kuweza kuidaka vizuri na kujua mahali ilipokuwa. Mafia ndiye aliyekuwa akiipiga mara kwa mara kwa kujifanya mfanyabiashara ambaye aliwahi kuzungumza naye kipindi cha nyuma.
Kila Godwin alipokuwa akipokea simu ile, kifaa kidogo cha GPS Trackers kilikuwa kikionyesha alama nyekundu na mahali alipokuwa, ila alipokuwa akikata simu, kilikuwa kikitokea.
“Ni lazima uongee naye mfululizo, hata mambo yasiyokuwa na maana, wewe zungumza tu ilimradi simu iwe hewani,” alisema kijana mmoja wa IT.
“Haina shida.”
Hicho ndicho alichokifanya Mafia, akampigia simu Godwin na kuanza kuzungumza naye mambo mengi, kijana huyo hakujua kwamba kila kitu alichokuwa akielezwa, ilikuwa ni kwa sababu ya simu yake kuwa hewani na watu hao kuanza kuifuatilia.
Kifaa kile ambacho kilikuwa na sehemu ndogo ya skrini ikaanza kuonyesha dunia, baada ya hapo, kile kialama chekundu kikaanza kushuka na kutafuta mahali simu ile ilipokuwa. Ikatokea Afrika, kialama kile kikaenda mpaka nchini Tanzania, ikaendelea kutafuta mpaka jijini Dar es Salaam, kote huko ilikuwa ikiitafuta simu ile ilipokuwa.
Baada ya sekunde chache ikaanza kuelekea Manzese Midizini kitu kilichowafanya watu hao kugundua kwamba mtu waliyekuwa wakimtafuta alikuwa huko.
“Manzese Midzini,” alisema kijana huyo lakini hapohapo Godwin akakata simu na kialama kile kilichoonyesha mahali simu ile ilipo kupotea.
“Twendeni Manzese haraka sana,” alisema Mafia, hawakutaka kuchelewa, wakaanza kuelekea huko kwa lengo la kumpigia huko na kujua alikuwa nyumba gani.
***
Godwin hakuwa akijali kabisa, alijua kwamba mtu aliyekuwa amempigia simu alikosea namba na hivyo kufanya mambo yake. Akili yake haikutulia, muda mwingi alikuwa akimfikiria Bi Rachel ambaye mpaka kipindi hicho hakujua alikuwa wapi, alikuwa akifanya nini na hakujua kama siku ile ambayo aliachana naye hotelini alinusurika kuuawa au la.
Alibaki akiiangalia simu yake, alitamani sana kumpigia na kusikia sauti yake. Kuwa karibu na mwanamke huyo kulimpa uhakika wa kupata pesa kwani alihongwa na mwanamke huyo ambaye alimuonyeshea dhahiri kwamba alikuwa akimpenda kwa moyo wa dhati.
Huku akiwa amekata simu ya Mafia, akaamua kumpigia simu Bi Rachel. Alishindwa kuvumilia, alisema kwamba kamwe asingempigia simu lakini alishangaa kuona moyo wake ukiwa na hamu kubwa ya kumpigia mwanamke huyo.
Hakujua sababu ya kuwa hivyo, baada ya muda simu ikapokelewa na sauti ya mwanaume mmoja kusikika kutoka upande wa pili ambayo ilimfanya Godwin kuhisi kwamba mwanaume huyo alikuwa mume wa Bi rachel.
“Halo!” ilisikika sauti ikiita.
“Halo! Shikamoo!” alianza kwa kusalimia, aliamini kabisa kwa kumuamkia mwanaume huyo asingeweza kuhisi chochote kile.
“Marahaba!”
“Samahani! Anti yupo?” aliuliza Godwin.
Hapo ndipo akapewa taarifa kuhusu mwanamke huyo. Tangu siku ambayo aliachana naye hotelini, alikuwa ameumizwa vibaya na hivyo kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Godwin alishtuka, hakutaka tena kubaki nyumbani, ilikuwa ni lazima aondoke kuelekea huko kwa ajili ya kumuona Bi Rachel. Alijua kwamba kwa kitendo chake cha kufika mahali hapo kwanza mwanamke huyo kingemfariji na hata kumwambia kuhusu wanaume wale waliokuwa wameingia hotelini.
Hakutaka kujifikiria mara mbili, akaondoka na kuelekea huko. Hakumwambia Irene alipokuwa akienda, alipotembea na kwenda mpaka katika kituo cha daladala cha Bakhresa ambapo kabla ya kupanda daladala, akanunua kofia na kuvaa kisha kuchukua gari na kwenda huko.
Njia nzima mawazo yake yalikuwa kwa mwanamke huyo, wakati mwingine alijihisi kuwa mkosaji kwani bila yeye, hakika mwanamke huyo asingeweza kuumizwa namna hiyo. Moyo wake uliumia, aliyafikiria maisha yake, alijua kwamba watu waliokuwa wakimtafuta kwa ajili ya kumuua walikuwa watu walewale waliomuua mama yake, hakujua ni wakina nani lakini katika maisha yake, alijiapiza kwamba ni lazima awatafute watu hao na kuwaua kwa mkono wake mwenyewe.
Wakati akiwa njiani, simu yake ikaanza kuita, akaangalia kioo cha simu yake, namba aliyoiona ilikuwa ya mwanaume yuleyule, aliyedai kwamba alikuwa mfanyabiashara. Hakuwa akijua alihitaji nini na wakati alikwishamwambia kwamba yeye hakuwa mfanyabiashara. Akaipokea.
“Unasemaje?” aliuliza Godwin kishari.
“Sasa nimekumbuka. Kumbe muda wote huo nilikuwa nazungumza na mtu ambaye siye mwenyewe. Hahahah!” alisikika mwanaume huyo na kisha kucheka.
“Ooh! Usijali! Kukosea namba ni kitu cha kawaida,” alisema Godwin.
“Sasa kaka! Hivi huko ulipo kweli hakuna soko la nafaka nikayaleta mahindi yangu?” aliuliza mwanaume huyo, wakati huo daladala ilikuwa imefika Jangwani.
“Soko la Mahindi?”
“Ndiyo! Naomba unitafutie wateja, nitakupa asilimia kumi na mauzo yangu. Nakuahidi na kama huamini tuandikishiane,” alisema Mafia.
“Sawa, Nitakutafutia. Tutawasiliana mkuu!”
“Sawa. Ulisema unaishi Lindi, si ndiyo?”
“Hapana! Dar es Salaam! Kwa kuwa umekuja kibiashara, naishi Dar es Salaam. Nitakupigia baadaye, naingia hospitalini mara moja,” alisema Godwin na kukata simu.
Hakuchukua muda mrefu akafika katika hospitali hiyo, haraka sana akateremka, kwa kuwa ulikuwa ni muda wa kuona wagonjwa, hakutakiwa kusubiri, akaanza kwenda katika wodi ya Mwaisela alipoelekezwa na mwanaume yule kwamba ndipo Bi Rachel alipokuwa amelazwa.
Akafika ndani ya wodi hiyo, akaanza kuangalia huku na kule, lengo lake lilikuwa ni kutaka kumuona mwanamke huyo, alipoona kuna idadi kubwa ya wagonjwa akaanza kuzunguka huku na kule, macho yake hayakutoka kwa wagonjwa waliokuwa wamelalia vitanda vyao.
“Yule pale,” alijikuta akisema mara baada ya macho yake kutua kwa mwanamke huyo aliyekuwa kitandani.
Godwin akaumia zaidi, Bi Rachel alikuwa kitandani, kichwa chake kilifungwa bandeji, alikuwa akipumua kwa msaada wa mashine ya oksijeni. Alikuwa amelala, hakuonekana kujua kitu chochote kilichokuwa kikiendelea ndani ya wodi hiyo. Alikuwa kimya na ilikuwa ni rahisi sana kujua kwamba mwanamke huyo alikuwa amekufa kitandani pale.
Kwa mwendo wa tarartibu Godwin akaanza kusogea kule alipokuwa mwanamke huyo na mumewe, alipomfikia, akamsalimia mumewe Bi Rachel na kujitambulisha kwamba yeye ndiye aliyempigia simu kumjulia hali shangazi yake.
“Ulimfahamu vipi?” aliuliza mume wa Bi Rachel aliyeitwa Shedrack.
“Alikuwa akija sana kuosha magari katika kituo changu! Sasa zimepita siku kadhaa sijamuona ndiyo maana nimeamua nimpigie simu. Si unajua ndiyo anatuweka mjini! Akifika pale, angalau ananilipa vizuri,” alisema Godwin huku akionekana kuwa kwenye uso wa majonzi.
“Ooh! Sawa.”
“Ilikuwaje?”
“Watu wanasema alipigwa! Sijajua na nani ila taarifa zinasema hivyo! Ninachokihitaji si taarifa bali ninahitaji mke wangu arudi katika afya yake. Ameumia kichwa vibaya sana, mishipa yake ilishtuliwa kitu kilichomfanya apoteze fahamu!” alisema Mzee Shedrack huku akimwangalia mke wake kwa majonzi mazito.
“Pole sana! Nadhani anti atapona tu,” alisema Godwin huku macho yake akiyapeleka huku na kule, ghafla, yakatua nyusoni mwa watu wawili, aliwafahamu kwa kuwaona, hawakuwa wageni, hiyo ilikuwa mara ya pili kuwatia machoni mwake, wanaume hao walikuwa ni Mafia na Saint ambao waliingia hapo wakiwa na kijana mmoja aliyeshika kifaa fulani mkononi, kwa kumwangalia, hakuwa akimfahamu alikuwa nani.
Walikuwa wakiendelea safari ya kuelekea Manzese Midizini ambapo ndipo walipokuwa wamekwishafika. Hawakujua Godwin alikuwa katika nyumba ipi, kulikuwa na nyumba nyingi, kujua kwa mara moja kwamba nyumba aliyokuwa mtu wao ilikuwa ipi, ilikuwa vigumu kutambua.
“Ngoja nimpigie simu tujua ni magali gani,” alisema Mafia na hivyo kupiga simu.
Bahati mbaya ni kama ilikuwa upande wao, simu haikuwa ikipatikana. Kila mmoja alishangaa, walikuwa na uhakika kwamba namba yake ilikuwa hewani, sasa kwa nini simu isiwe inapatikana?
Mafia hakuwa na haraka, alikuwa na uhakika kwamba Godwin angewasha simu na kuanza kuidaka simu yake na kujua nyumba aliyokuwepo. Baada ya dakika kadhaa, akampigia tena simu na muda huo simu ilikuwa ikiita.
Alifurahi na kuwaambia wenzake kwamba Godwin alikuwa hewani na hivyo kuanza kuzungumza naye. Alijifanya kama mfanyabisahara yule aliyekuwa amepigia simu. Wakati huo, yule kijana wa kunasa mawasiliano kwa kutumia GPS Tracker alikuwa akikiangalia kifaa kile kwa umakini kabisa.
“Hayupo Manzese!” alisema kijana yule.
“Unasemaje? Yupo wapi?”
“Anaelekea sehemu! Nahisi Kariakoo! Hapa kifaa kinanionyesha yupo njiani anatembea!” alisema kijana huyo.
Saint hakutaka kuchelewa, akawasha gari na kuligeuza, safari ya kuelekea huko Kariakoo ikaanza huku Mafia akiendelea kuzungumza na Godwin, alipomaliza akawageukia wenzake.
“Anakwenda Muhimbili! Ongeza kasi. Tunaua hukohuko hakuna kuremba,” alisema Mafia na hivyo Saint kuongeza mwendo.
Kutokana na kutokuwa na foleni, hawakuchukua muda mrefu kufika katika hospitali hiyo ambapo hapo wakaanza kuelekea kwenye wodi kubwa kwa kuamini kwamba Godwin ilikuwa ni lazima wepo ndani ya hizo wodi.
Wakaanzia katika wodi ya Sewa Haji. Wakaingia humo na kwa haraka sana wakaanza kumtafuta Godwin. Ilikuwa wodi yenye wagonjwa wengi lakini hawakuweza kumpata. Wakaondoka haraka sana na kwenda katika wodi ya Kibasila ambapo napo kama kawaida wakaanza kumrafuta Godwin.
Matumaini yao yakaanza kufifia, walijua kwamba kama wangemkosa humo ilikuwa ni lazima waende katika wodi ya Mwaisela ambapo kama wangemkosa humo, ingekuwa kazi nyingine kumpata kwani napo muda haukuwa ukiwasubiri.
Wakamkosa katika wodi ya Kibasila na hivyo kwenda kwenye wodi ya Mwaisela. Macho yao yalikuwa makini kuangalia huku na kule. Katika hali iliyowafurahisha kabisa, macho yao yakatua kwa mtu waliyekuwa wakimtafuta, alikuwa Godwin ambaye alisimama pembeni ya kitanda cha mgonjwa mmoja ambaye hawakumfahamu. Ila jambo lililowatia shaka ni kwamba kijana huyo naye aliwaona, wakajua kwamba angeweza kukimbia.
“Yule pale!” alisema Mafia huku akishika kiunoni kuona kama alikuwa na bastola yake.
“Tukamtekeni! Watu wakituuliza tunawaambia ni ndugu yetu mwenye matatizo ya akili,” alisema Saint na kuanza kumfuata Godwin ambaye alikuwa akitetemeka, hata pa kukimbilia hakupajua.
***
Godwin akabaki akitetemeka, hakuamini kuwaona watu wale wakiwa wamemfuatilia mpaka kule alipokuwa. Alibaki akiangaliana na wanaume wale, alijua kwamba watu hao walifika hospitalini hapo kwa sababu moja tu, kumteka na kumuua kama walivyotaka kufanya kipindi kilichopita hotelini.
Sehemu hiyo haikuwa salama kwa maisha yake na ilikuwa ni lazima aondoke haraka iwezekanavyo. Humo wodini kulikuwa na watu wengi, hakujua ni kwa namna gani angeondoka kwani pale alipokuwa, hasa katika mlango mwingine wa kutokea hakukuwa na nafasi ya kupita kutokana na muda huo kujaa watu wengi mahali hapo.
“Vipi mbona unaonekana kuogopa?” aliuliza Mzee Shedrack huku akimwangalia Godwin, kwa kipindi kichache tu alionekana tofauti.
“Kuna kitu nimekumbuka! Kuna mshua mmoja anakuja kuliosha BMW lake, halafu naye huwa anatoa mpunga mrefu kama anti,” alisema Godwin, alijitahidi kudanganya.
“Sasa ndiyo uogope?”
“Siogopi! Ila nilivyokumbuka nimeona naweza kukosa huo mpunga,” alisema Godwin.
“Kwa hiyo?”
“Acha niondoke, nitarudi baadaye,” alisema Godwin, hakutaka kuchelewa, hapohapo akaondoka huku akimuacha Mzee Shedrack akiwa haelewi ni kitu gani kinaendelea.
Akaanza kukimbia kuelekea getini, alitaka kuwatoroka wanaume hao ambao alijua kabisa kwamba walikuja mahali hapo kwa lengo moja la kumuua tu. Mafia na Saint walipoona Godwin anakimbia wakatoka ndani ya wodi ile na kuanza kumkimbiza.
Walikuwa na mbio, walijua kuwakimbiza watu waliokuwa wakiwataka hivyo hata kabla ya Godwin kufika getini walimdaka na kumbeba juujuu. Akaanza kulia huku akiomba msaada, kila mtu aliyewaona aliwashangaa, hawakujua sababu za wanaume hao kumkamata kijana huyo.
“Niacheni! Niacheni!” alipiga kelele Godwin huku akijaribu kujitoa mikononi mwa watu hao.
“Nyie! Kuna nini?” aliuliza mlinzi mmoja, aliwasogelea huku akiwa na bunduki yake.
“Ndugu yetu huyu! Anaumwa akili! Tutafutie kamba tumfunge,” alisema Mafia huku akimshika vilivyo Godwin.
“Mimi siyo chizi! Nisaidieni! Nisaidieni!” aliendelea kupiga kelele Godwin kiasi kwamba watu wakaendelea kukusanyika huku wakiendelea kuwashangaa.
Haraka sana mlinzi yule akarudi mahali pale huku akiwa na kamba mkononi, akaanza kumfunga kamba Godwin aliyekuwa akiendelea kulia tu. Alipomaliza, Mafia na Saint wakamchukua kwa kumbeba juu juu na kuondoka naye mpaka kulipokuwa na gari lao ambapo wakamuingiza.
Kila mtu aliyeliona tukio hilo akajua dhahiri kwamba Godwin alikuwa kichaa kwani kwa jinsi alivyokuwa akipiga kelele na kufungwa kamba zile, hizo zilikuwa sababu tosha zilizowafanya watu hao kujua kwamba hakuwa mzima kiakili.
Gari likawashwa, hakukuwa na muda wa kupoteza, mtu waliyekuwa wakimtaka tayari walimpata na hivyo haraka sana ilibidi apelekwe katika jumba moja lililokuwa Tegeta Kibaoni, jumba ambalo lilitumika kuhifadhia watu waliotekwa, jumba hilo lilijulikana kama Sodoma.
Kabla ya kuelekea huko, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumpigia simu bosi wao, Kihampa na kumwambia kwamba tayari zoezi lilikamilika na muda huo walikuwa na Godwin hivyo walichokuwa wakisubiri ni neno kutoka kwake.
“Hakuna neno zaidi ya kumuua,” alisikika Kihampa.
“Sawa mkuu! Tunampeleka Sodoma kumuulia huko kama wengine,” alisema Mafia.
“Sawa!”
Mazungumzo yote hayo Godwin alikuwa akiyasikia, akagundua kwamba alikuwa sahihi kuwa watu hao walikuwa na lengo moja la kumuua. Moyo wake ukajawa na hofu, muda wote alikuwa akiwaomba msamaha watu hao, hakutaka kuona akifa kwani kulikuwa na mambo mengi ambayo alitakiwa kuyafanya.
Alilia lakini hakukuwa na mtu aliyejali, kila mmoja alikuwa na lengo moja tu kichwani mwake, kumuua na kuondoka zao kwani aliwasumbua kwa kipindi kirefu na hatimaye walimdaka.
“Unaomba msamaha wa nini na wakati ulisema unataka kupambana kiume,” alisema Mafia huku akimwangalia Godwin.
“Naomba mnisamehe!”
“Tukusamehe wewe! Siku ile hotelini ulitubabaisha sana! Ukasema kwamba huogopi, halafu ukatusumbua kushuka chini kwa lengo la kupambana! Sasa leo tumekudaka unaanza kulialia. Kama ulipanga tupambane, basi leo tutapambana,” alisema Mafia huku akimwangalia Godwin aliyekuwa akitia huruma pale chini alipokuwa.
Safari iliendelea, wakaingia katika Barabara ya Ally Hassani Mwinyi! Waliendelea kusonga mbele, hawakuwa wakienda kwa mwendo wa kasi kwani kulikuwa na msongamano wa foleni njiani.
Walipofika Morocco, wakakutana na foleni kubwa, wakatakiwa kusimama hapo kwa dakika kadhaa kwani kulikuwa na msafara wa rais uliokuwa ukipita. Kila mmoja alikasirika, hawakutaka kuona wakicheleweshwa, walikwishatoa taarifa kwamba kijana huyo walikuwa naye na kilichotakiwa ni kumuua haraka sana.
“Msafara umepita! Tembeatembea,” alisema Mafia akimwambia Saint ambaye hapohapo akapiga gia na kuanza kuondoka na magari mengine yaliyokuwa yakielekea Makumbusho, Mwenge na sehemu nyingine.
“Dogo sali sala yako ya mwisho kabisa. Kule hakuna kupeana nafasi za kusali, kutakuwa na kazi moja tu, kuchinjana,” alisema Mafia maneno yaliyomfanya Godwin kuona kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa maisha yao.
****
Irene hakuwa na amani, moyo wake ulikuwa mzito, ulikuwa ni kama umefunikwa na wingu zito na kushindwa kuona mbele. Hakujua sababu hasa ya kuwa hivyo, wakati mwingine alihisi kama alikuwa mgonjwa, ila alipojaribu kurukaruka, mwili ulikuwa sawa ingawa moyo wake haukuwa na amani kabisa.
Akahisi kulikuwa na jambo zito mbele yake, hakujua ni jambo gani ila kwa harakaharaka alihisi kabisa kwamba kulikuwa na watu waliokuwa njiani kwa ajili ya kufanya jambo la kuumiza moyo wake, hakutaka kuona hali hiyo ikiendelea, kitu cha kwanza kabisa ambacho alikifikiria ni kumwambia kaka yake.
Akamuita, Godwin hakuwepo, akaanza kumtafuta huku na kule, alitaka kumshirikisha hali aliyokuwa nayo moyoni ili hata kama kulikuwa na ubaya mbele yao basi wawe makini na kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha hawapatwi na ubaya huo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alimtafuta kila kona ndani ya nyumba hiyo, hakuonekana, hata katika chumba alichokuwa akikaa, napo hakuwepo. Mpaka hapo akawa na hofu, akahisi kabisa kwamba Godwin ndiye aliyesababisha ile hali aliyokuwa nayo moyoni mwake.
Akatoka nje na kwenda kumtafuta huko, tena kwa kuwauliza watu wengine lakini majibu yalikuwa yaleyale kwamba kaka yake huyo hakuonekana. Akahisi kabisa moyo wake ukianza kufa ganzi, akaona kifo mbele yake, akaona kaka yake akiwa njiani kuelekea kaburini.
Haraka sana akarudi chumbani, kitu cha kwanza, akapiga magoti chini na kuanza kumuomba Mungu. Mbele yake aliona giza totoro, pale chini alipokuwa, alikuwa akisali huku akilia, mashavu yake yalilowanishwa machozi kwa ajili ya kulilia ulinzi kwa kaka yake.
“Godwin anakufa! Anauawa kifo kibaya sana, hutoweza kumuona tena, hata mwili wake hautouona, utatumbukizwa kwenye tindikali na kuyeyuka,” aliisikia sauti ikimwambia moyoni mwake, hakujua kama sauti hiyo ilikuwa yake, ya shetani au ya Mungu.
“Godwin hawezi kufa! Mungu atamlinda na watesi! Ndugu yangu Godwin hawezi kufa,” alisema maneno hayo kwa ujasiri mkubwa kabisa, sauti ile aliyoisikia ikaanza kwa dharau.
Moyo wake ulimuuma mno lakini hakuacha kusali, aliamini kwamba kama Mungu alimuokoa kutoka kwenye mdomo wa kifo alipoangukiwa na kifusi, basi angeweza kumuokoa tena hata huko alipokuwa.
Sala yake ilichukua dakika zaidi ya arobaini, alipomaliza hapohapo akajikuta akilala kwenye mkeka, machozi yaliendelea kumtitika mashavuni mwake. Aliamini kwamba Mungu angemuokoa lakini wakati mwingine imani yake ilitingishika na kusikia sauti ile ikimwambia kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa kaka yake.
***
Ilikuwa ni milio ya risasi tu ndiyo iliyokuwa ikisikika mahali hapo. Watu walikimbia, kila mtu alikuwa akihofia na kuona kwamba suluhisho zuri la kuyaokoa maisha yake ilikuwa ni kukimbia tu kutoka mahali hapo.
Mafia alikuwa makini, alikuwa mzoefu aliyekuwa na shabaha kubwa katika kutumia bunduki yake. Gari lile aina ya Noah lilikuwa mbele yao, lilisimama kiupandeupande kitu kilichomfanya kumlenga dereva na mtu aliyekuwa naye mbele.
Polisi walidhani kwamba walikuwa wakipambana na mtu wa kawaida, hawakujua kwamba mtu huyo alikuwa hatari, aliyepewa mafunzo makali. Hawakutaka kukamatwa, japokuwa walikuwa wametumwa kazi hiyo na ngazi ya juu lakini hawakutaka kuonyesha kitu chochote kile kwa kuamini kwamba wasingeweza kuaminika hata mara moja.
“Paaa….paaa…paaa…” milio ya risasi iliendelea kusikika mahali hapo.
Godwin na yule kijana wa IT walikuwa kimya ndani ya gari, waliogopa, mioyo yao ilikuwa na hofu tele, milio ya risasi iliyokuwa ikisikika iliwaogopesha, walilala chini kifudifudi huku wakiziba masikio yao.
Godwin alijiona kuwa kwenye hatari, hakuona kama angepona, alichokiona ni kifo mahali hapo kwani nje ambapo ndipo alipotakiwa kukimbilia, napo kulikuwa na milio ya risasi kila kona.
Saint hakutaka kubaki kwenye usukani, huo ulikuwa muda wa mapambano hivyo alichokifanya ni kuungana na mwenzake na kuanza kupambana na polisi hao.
Shabaha ziliwasaidia, waliweza kutumia bastola zao, polisi wale waliokuwa kwenye Noah wakaanza kumiminiwa risasi hovyo huku Mafia akiwa ametokeza kwenye rufu juu ya gari na kuendelea kuwamiminia risasi mfululizo.
Hawakujua kama kulikuwa na gari nyingine ya polisi nyuma yao, walikuwa bize kuishambulia Noah ile iliyokuwa mbele yao ambayo ilibloki njia na kuwazuia kupita.
“Tuwapige risasi?” aliuliza polisi mmoja ambaye alikuwa kwenye difenda kwa nyuma kama umbali wa mita hamsini.
“Hapa inahitajika shabaha kubwa. Sniper John yupo?” aliuliza kamanda aliyekuwa kwenye gari hilo.
“Nipo mkuu!”
“Uwanja wako huo. Nitungulie yule mtu aliyetokeza kwenye rufu,” alisema kamanda huyo.
Aliitwa John J, alikuwa mmoja wa vijana waliokuwa na shabaha kubwa katika Kituo cha Polisi cha Salenda. Alifundishwa shabaha, alijua kulenga na miongoni mwa vijana ishirini Tanzania waliokuwa na shabaha alikuwa yeye.
Alichukua bunduki yake, akaiweka juu ya gari na kuanza kuangalia kule ilipokuwa ile Noah ya kina Mafia. Kila polisi aliyekuwa ndani ya gari lile alikuwa kimya. Alitaka kumtungua Mafia ambaye kama kawaida yake alikuwa amecharuka, alipambana na polisi kwa kasi kubwa, bastola yake ilipoishiwa risasi, aliingiza risasi nyingine kwa kasi kubwa kiasi kwamba hata polisi wenyewe walikuwa wakishangaa.
“Kachukueni maiti yenu kule,” alisema John huku akimuweka Mafia katika saiti yake.
John hakupiga risasi nyingi, alipiga moja tu ambayo ilikwenda na kupenya katika kisogo cha Mafia, damu zikaruka, hapohapo akaanguka na kuangukia garini.
“Mafia!” aliita Saint baada ya kusikia kishindo cha mtu akiwa amedondoka kwa nyuma.
Alichanganyikiwa, akaanza kurusha risasi hovyo. Alizidiwa nguvu, asingeweza kupambana na polisi waliokuwa wamemzunguka nyuma na mbele.
“Ni lazima nipambane kiume,” alisema Saint.
Hakutaka kuacha, aliendelea kushambuliana nao mpaka risasi zake zilipokwisha. Huo ndiyo ulikuwa mwisho wake, akatulia kitini, akalala huku akiona kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wake.
Alikuwa na mawazo mawili, kulisogelea gari lile la polisi lililokuwa mbele na kuligonga au kutoka na kukimbia. Wazo ambalo lilipata nafasi moyoni mwake ni kuliwasha gari lile na kuligonga gari la polisi.
“Kama kufa! Bora tufe wote,” alisema Saint.
Akaliwasha, akakoleza moto na kuliachia. Kwa kasi ya ajabu gari hilo likaanza kusogea na kuligonga gari lile la polisi lilolokuwa limebloku njia nzima, likasogezwa pembeni na kupinduka, alichokifanya ni kusogea mbele kwa kasi kubwa.
Polisi waliokuwa kwenye difenda wakaanza kulikimbiza. Walijua kwamba aliishiwa risasi, hivyo ilikuwa ni lazima wamkamate kwa kulizingira gari lile.
Hakutaka kuona akikamatwa kirahisi, alichokifanya ni kuongeza kasi zaidi, gari likawa kwenye mwendo mkali, ilikuwa ni lazima kujiua kama tu kusingekuwa na njia nyingine ya kusalimika.
Hivyo akaliendesha mpaka Kijitonyama Sayansi ambapo kwa pembeni aliyaona magari ya maji safi yakiwa yamepaki, alichokifanya ni kwenda kwa kasi upande uleule uliokuwa na magari yale na kuligonga moja.
Kwa ugongaji ule, na kwa kuwa hakufunga mlango, akatolewa kwenye kioo cha mbele kwa kasi kubwa na kwenda kukibamiza kichwa chake katika gari lile, kichwa kikapasuka, ubongo ukatoka na mwili wake kutulia chini.
“Mungu wangu! Ajali!” alisema jamaa mmoja huku akiwa ameshika kichwa chake.
Hazikupita sekunde nyingi polisi wakafika mahali hapo, wakateremka huku wakiwa na bunduki zao mikononi, wakaanza kusogea kule lilipokuwa gari lile, mwili wa Saint ulikuwa chini, wakafungua milango kwa tahadhali kubwa, wakawakuta Godwin akiwa na kijana yule wa IT, wote walikuwa wamepoteza fahamu.
“Hebu watoeni hawa watu,” alisema polisi mmoja na kufanya hivyo haraka sana.
Godwin na kijana yule wakatolewa na kupakizwa ndani ya gari na kuanza kupelekwa katika Hospitali ya Mwananyamala ambayo haikuwa mbali kutoka mahali hapo.
Njiani, polisi walikuwa wakijiuliza maswali mengi kuhusu watu wale waliokuwa nao kwenye gari. Walipigiwa simu na kuambiwa kwamba gari lile la watekaji lilikuwa na kijana mmoja waliyekuwa wamemteka, hawakujua alikuwa kijana gani, na mbaya zaidi hawakujua sababu ya kijana huyo kutekwa.
Kilichowashangaza ni kwamba ndani walikuwa vijana wawili. Kama mmoja alitekwa, yule mwingine alikuwa nani? Na kati ya vijana hao wawili, yupi alikuwa mateka na yupi alishirikiana na polisi.
Hawakuwa na majibu ya maswali hayo, wakatulia, walipowafikisha hospitalini, wakawapeleka mpaka ndani na kulazwa, hawakutosheka, wakawafunga pingu.
“Ni watuhumiwa?” aliuliza daktari mmoja.
“Ndiyo! Hebu walazeni kwanza na ulinzi uongezwe mahali hapa,” alisema kamanda Kipate aliyekuwa amekiongoza kikosi cha polisi waliokwenda kupambana na kina Mafia.
Godwin alikuwa kimya kitandani, hakujua kitu kilichokuwa kikiendelea, alipoteza fahamu baada ya kujigonga ndani ya gari mara baada ya gari lile kugonga gari la maji ambalo lilikuwa limepakiwa.
Yeye na kijana yule walikaa hospitalini hapo kwa saa moja ndipo wakarudiwa na fahamu. Hakujua alikuwa wapi lakini baada ya kuwaona wanaume waliovalia makoti meupe na dripu zilizokuwa zikining’inia, akagundua kwamba mahali hapo palikuwa ni hospitali.
Kumbukumbu zake zikaanza kurudi nyuma mpaka kipindi kile alipopata ajali ile. Hakujua dereva alikuwa wapi lakini alipotaka kuinuka, akagundua kwamba alikuwa na pingu mkononi.
“Daktari nini kinaendelea?” alimuuliza daktari aliyekuwa mbele yake.
“Umekamatwa!”
“Kisa nini? Nilitakiwa kuuawa. Wale watu walikuwa wakienda kuniua daktari,” alisema Godwin huku akiwa hajui kilichokuwa kimetokea mpaka kufungwa pingu na wakati hakuwa mhalifu.
Hakutoka, kulikuwa na polisi wawili waliokuwa wakiwalinda mahali hapo. Saa ziliendelea kukatika mpaka ilipofika majira ya saa kumi na moja na nusu ndipo wanaume wawili wakafika hospitalini hapo na kuwaonyeshea polisi wale kibali cha kuwaruhusu kuondoka na Godwin mahali hapo.
Kwanza walishtuka, hawakuwaamini watu hao, walianza kuwauliza maswali kadhaa, watu hao wakawaonyeshea vitambulisho vyao, vilikuwa na muhuli ambao waliujua kabisa ulitoka ngazi ya juu. Kabla ya yote, polisi hao wakaanza kupiga saluti nyinginyingi kuonyesha heshima.
“Tumemfuata huyu kijana,” alisema mwanaume mmoja, alikuwa na ndevu nyingi.
“Hakuna shida!” aliitikia polisi mmoja.
Godwin hakuwafahamu watu hao, kwa jinsi walivyoonekana, hawakuwa watu wazuri hata kidogo, aliwaambia polisi wale kwamba hakuwa akiwafahamu wanaume wale na inawezekana kwamba walikuwa watu wabaya lakini polisi hao hawakumuelewa, wakamwambia anyamaze na asiwapangie polisi nini cha kufanya.
“They are going to kill me,” (wanakwenda kuniua) alisema Godwin, hakukuwa na aliyejali, akachukuliwa peke yake na kupelekwa ndani ya gari walilokuja nalo hao wanaume kisha kuondoka mahali hapo.
***
Dar es Salaam nzima ilizizima kwa kile kilichokuwa kimetokea Victoria baada ya milio ya risasi, kila mtu alizungumza lake, wengine walisema kwamba walikuwa majambazi, wengine walisema kwamba walikuwa polisi waliokuwa wakifanya mazoezi, kila kona, watu walizungumza yao kitu kilicholeta manenomaneno mengi ndani ya jiji hilo.
Taarifa hizo zilivyokuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ndipo zinamfikia Kihampa. Kwanza akashtuka baada ya kuliona gari lililopata ajali, lilikuwa gari lilelile alilowapa vijana wake kwa ajili ya kuifanya kazi ambayo yeye mwenyewe aliagizwa kutoka ngazi ya juu.
Akahisi kulikuwa na kitu, hapohapo akachukua simu yake na kuanza kumpigia Mafia. Simu haikuwa ikipatikana, hakutaka kujali sana, akampigia simu Saint, kidogo simu yake ikaanza kuita na kuamini kwamba ingepokelewa.
Haikupokelewa, akazidi kuwa ha hofu. Moyo wake ulimwambia kwamba inawezekana watu waliokuwa ndani ya gari hilo walitoroka, alitaka kujua ukweli na asingeweza kuupata kama tu asingewasiliana na polisi waliofanya oparesheni ile.
Akapiga simu makao makuu ambapo akaambiwa kwamba oparesheni ile ilifanywa na polisi wa Kituo cha Polisi cha Osterbay, hapohapo akapiga simu huko kujua nini kiliendelea.
Akaambiwa kila kitu kilichokuwa kimetokea katika tukio lile ambalo kwa polisi walilifananisha na tukio la kiujambazi na utekaji. Kihampa alivyoambiwa, alikuwa na uhakika kwamba kile alichokuwa amehisi ndicho kilichokuwa kimetokea, vijana aliokuwa akiwategemea kufanya kazi ile aliyoambiwa ndiyo walewale waliokuwa wameuawa.
“Mnasema walikuwa watekaji?” aliuliza Kihampa.
“Ndiyo! Walikuwa wamemteka kijana mmoja. Walikuwa na mtu wao mwingine ambaye yupo chini ya ulinzi,” alisema kamanda kutoka katika kituo hicho.
“Mmefanya makosa makubwa sana!”
“Kwa nini?”
“Subiri kwanza. Huyo kijana yupo wapi?”
“Yupi mkuu? Aliyekuwa na watekaji?”
“Hapana! Huyo aliyetekwa!”
Mkuu huyo akamwambia kila kitu alichokuwa akikihitaji Kihampa na baada ya hapo, simu ikakatwa huku mkuu huyo akiambiwa kuwa kulikuwa na watu ambao wangefika hospitalini hapo kwa ajili ya kumchukua kijana huyo kwani kulikuwa na kitu alichotakiwa kukitolea ufafanuzi.
Hilo halikuwa tatizo hata kidogo na kwa sababu alitumia jina la viongozi wa juu, akaambiwa kwamba kila kitu kingekuwa kama alivyosema hivyo kuwatuma vijana hao huko kwa ajili ya kumchukua Godwin.
“They are going to kill me,” (wanakwenda kuniua) alipiga kelele Godwin huku akiwa ameshikwa na wanaume wawili ambao walimpeleka mpaka kwenye gari lao na kuondoka mahali hapo.
Kila mmoja alibaki akishangaa, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mahali hapo. Walishangaa, walimjua Godwin kuwa ni mgonjwa aliyekuwa ameletwa mahali hapo ila kitu cha kushangaza kabisa, alichukuliwa na watu kinguvu na kuondoka naye mahali hapo huku wale polisi waliokuwa mahali pale wakiwa kimya, hawakujisumbua hata kuuliza hali iliyoonekana tayari walikwishapewa maagizo juu ya kile kilichokuwa kikienda kutokea.
Godwin alikuwa akilia. Mwili wake ulikuwa kwenye maumivu makali, aliwaambia wale wanaume kwamba alikuwa akiumwa na alitaka kupata matibabu lakini hakukuwa na yeyote aliyemuelewa.
Alijua fika kwamba wanaume hao walikuwa watu wabaya ambao walitumwa na watu walewale waliokuwa wakiwatafuta kwa lengo la kuwamaliza. Moyo wake ulimuuma, alikuwa tayari kufa lakini si kwa namna ambavyo watu hao walivyokuwa na kiu ya kumuua.
Alitaka kumuaga ndugu yake, Irene kwani huyo ndiye alikuwa ndugu pekee aliyebaki naye, hakukuwa na mtu yeyote yule aliyemfahamu zaidi ya msichana huyo tu.
Gari liliendeshwa mpaka Ubungo Maziwa, likaingizwa ndani ya jumba moja. Lilikuwa limezungushiwa ukuta mkubwa huku kwa juu kukiwa nyaya za umeme. Hakujua sababu ya kuletwa ndani ya jumba lile lakini kitu alichohisi ni kwamba alipelekwa mule kwa kuwa alitakiwa kuuawa haraka sana.
“Why have you brought me here?” (kwa nini mmenileta hapa?) aliuliza Godwin huku akimwangalia mwanaume mmoja ambaye hakuzungumza kitu chochote, alikuwa mtu wa kufuata amri tu.
Akapelekwa ndani ya chumba kimoja na kuachwa humo. Alikuwa akitetemeka, hakujiamini, kadiri alivyokuwa akikiangalia chumba kile huku akiwa na hofu kubwa moyoni mwake kwani kwa muonekano wake tu kilionyesha kuwa chumba cha matukio kwani michirizi ya damu ilionekana kwenye kila kuta.
“Helo! Nisaidieni! Nisaidieni!” alipiga kelele Godwin huku akipigapiga mlango.
Nyumba ilikuwa kimya, kila alipopiga kelele, sauti yake ilirudi kwa mtindo wa mwangwi. Hakukuwa na mtu aliyetokea mahali hapo, mlango haukufunguliwa, alilia kwa kuamini kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa maisha yake.
Alipoona amepiga sana kelele na hakukuwa na msaada wowote ule, akaanza kuangalia huku na kule. Kama mwanaume alitakiwa kutumia kila njia kuondoka ndani ya chumba hicho.
Mawazo yake yakamwambia kwamba alitakiwa kutoroka ndani ya chumba hicho kupitia dari ambapo ndani ya chumba hicho kulikuwa na mlango wa kuingia darini. Ilikuwa njia nzuri ya kuwatoroka watu hao lakini tatizo kubwa lililompata ni kwamba hakukuwa na ngazi ya kumuwezesha kupanda mpaka katika mlango ule.
“Nifanye nini?” alijiuliza.
Alijitahidi kufikiria kila njia kutoka ndani ya chumba kile lakini hakufanikiwa. Mlango ulifungwa kwa nje na madirisha yalikuwa ya nondo ambayo yangempa kazi kubwa mpaka kuyavunja. Akaelekea pembeni ya chumba kile na kuanza kulia kwa uchungu.
“Mungu nisaidie nitoke salama! Mungu naomba usiniache,” alisema Godwin huku akiwa katika pembe ya chumba hicho akilia.
Muda ulizidi kwenda mbele, ilipofika saa moja usiku, mlango ukafunguliwa, mwanaume mmoja aliyekuwa na mwili uliojazia akaingia ndani ya chumba kile. Hakutaka kuzungumza kitu, akamsogelea Godwin na kumshika mkono kisha kumvuta kuelekea nje ya chumba kile.
Alipiga kelele lakini mwanaume yule hakumuelewa, ni kama alikuwa bubu kwani pamoja na Godwin kupiga kelele zote hizo, mwanaume huyo hakuzungumza kitu chochote kile zaidi ya kumpa ishara kwamba alitakiwa kunyamaza vinginevyo angeuawa.
Akapelekwa mpaka nje ya chumba kile, akaingizwa ndani ya gari, wanaume wawili wakatokea, walikuwa na bastola mikononi mwao. Kama alivyokuwa yule mwanaume, hata nao hawakuongea kitu chochote kile. Wakachungua gunia moja na kuliingiza ndani ya gari lile.
Godwin alikiona kila kitu, kitendo cha kuona gunia lile likiwa limeingizwa ndani ya gari lile, akajua kwamba baada ya kuuawa angeingizwa ndani ya hilo gunia kisha kutupwa sehemu fulani.
“Jamani! Naomba msiniue,” alisema Godwin huku akilia kama mtoto.
Gari likawashwa na kuondoka mahali hapo. Godwin aliendelea kulia, tangu alipochukuliwa kutoka hospitalini na wanaume hao, hawakuzungumza kitu chochote, hakusikia sauti zao hata kidogo.
Hakujua walikuwa wakienda wapi, safari ile iliendelea, hakuona vizuri kwa nje, ila gari lilipokuwa kwenye barabara ya lami, alijua na hata lilipohamia katika barabara ya vumbi alilifahamu hilo.
Safari ikaendelea mpaka walipofika sehemu ambapo hakukusikika sauti ya mtu yeyote yule. Mlango wa gari ukafunguliwa na kutolewa ndani. Sehemu hiyo kulikuwa na upepo mkali, baridi lilimpiga, aliikunja mikono yake huku akiangalia huku na kule, hakuona nyumba yoyote, taa au gari lolote lile na alipoangalia vizuri akaona pori kubwa likiwa karibu nao, pembeni kidogo ya barabara hiyo.
“Mnataka kuniua hapa? Jamani! Naomba mnisamehe! Jamani naomba msiniue. Najua nyie ndiyo mlimuua mama yangu, naomba msiniue, naomba mnionee huruma,” alisema Godwin huku akianza kulia tena kama mtoto.
Wakati akiendelea kuomba msamaha, mara akashtushwa na mlio wa simu kutoka kwa mwanaume mmoja aliyekuwa mahali hapo. Haraka sana akaipokea na kuipeleka sikioni na sauti ya mwanaume mmoja kusikika kutoka upande wa pili.
“Mmekwishamuua?” alisikika mwanaume huyo.
“Bado ila ndiyo tunataka kumuua hapa!” alijibu mwanaume huyo.
“Basi muueni haraka halafu mwili wake uwekeni kwenye gunia kama tulivyokubaliana,” alisikika mwanaume huyo.
“Haina shida mkuu! Tupe dakika tano!” alisema mwanaume huyo na kukata simu. Kila mtu akakoki bastola yake na kumwangalia Godwin kwa macho yaliyoashiria kwamba walitaka kusikia sala yake ya mwisho kabla ya kumuua.
***
Usiku mzima Irene hakulala, kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, alimfikiria kaka yake, Godwin. Hakujua mahali alipokuwa, wakati mwingine alihisi kwamba Mungu hakuwa akijibu maombi kwani kama kumuomba kwa ajili ya kaka yake, alifanya hivyo lakini bado hakurudi nyumbani.
Hakuingia ndani, alishinda nje huku akiwa na mawazo tele. Moyo wake ulikuwa na hofu kupita kawaida na muda wote kulikuwa na sauti iliyokuwa ikimwambia kwamba kaka yake aliyekuwa akimtegemea, ndugu pekee aliyembakiza alikuwa ameuawa na watu ambao kila siku walikuwa wakimtafuta kumuua.
Alikuwa akilia, usiku kucha kichwa chake kilikuwa na mawazo juu ya Godwin tu. Watu walimshangaa, siku hiyo alionekana kuwa tofauti, walizoea kumuona akiwa na furaha tele, kitendo cha kuwa katika hali ile kilizuia maswali mengi.
Baba mwenye nyumba hakutaka kuvumilia, akamsogelea Irene na kumuuliza kilichokuwa kikiendelea, hakumficha, alimwambia kweli kwamba kaka yake hakuwa ameonekana mpaka kipindi hicho.
“Alikuwa wapi?” aliuliza baba mwenye nyumba.
“Sijui! Aliondoka, mpaka sasa hivi hajarudi,” alijibu Irene huku akimwangalia mzee huyo.
Baba mwenye nyumba hakuona kama kulikuwa na tatizo, hapo Manzese kulikuwa na vijana wengi waliokuwa wakiondoka nyumbani kwao na kurudi usiku sana na wakati mwingine kulala hukohuko.
Hakujua kwamba kwa Irene na Godwin, siku zote maisha yao yalikuwa ni kutafutwa kila kona, walinusurika kuuawa mara kadhaa kitu kilichowafanya kila siku kuishi kwa hofu kuliko watu wengine.
“Ila atarudi tu! Wala hutakiwi kuhofu chochote kile,” alisema baba mwenye nyumba na kuingia ndani.
Mpaka inafika asubuhi Godwin hakuwa amerudi nyumbani, Irene alizidi kuwa na hofu zaidi na mbaya zaidi alipoazima simu kwa ajili ya kumpigia kaka yake, hakufanikiwa kumpata kwani simu haikuita hali iliyoonyesha kwamba ilikuwa imezimwa.
Irene aliendelea kusubiri mpaka saa moja usiku alipopata taarifa za majambazi waliokuwa katika Mtaa wa Victoria, Mikocheni. Aliisikia taarifa nzima jinsi polisi walivyokuwa wakishambuliana na watu hao, hakujua undani wa habari hiyo lakini alihisi moyo wake kuwa mzito sana kuondoka pasipo kuendelea kuisikiliza taarifa hiyo ambayo ilielezea mapigano makali kati ya polisi na majambazi hao yaliyodumu kwa dakika kadhaa.
“Halafu ikawaje?” alijiuliza lakini hata kabla hajapata jibu la swali lake, akamsikia Kamanda Mkuu Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Shamsia Ikunde akilizungumzia tukio hilo na utekaji ambao ulikuwa umefanyika.
Moyo wa Irene ukamlipuka, kile alichokisikia kikamfanya kuhisi kwamba Godwin alihusika katika tukio hilo kwani kama hakurudi nyumbani na kila simu yake ilipokuwa ikipigwa haikupatikana, ilionyesha kabisa kwamba alikuwa amepata tatizo fulani au kutekwa na watu hao waliokisiwa kuwa majambazi.
“Amesemaje? Kuna kijana alitekwa?” aliuliza Irene huku akimwangalia muuza duka aliyekuwa amefungulia redio kusikiliza taarifa ya habari ya saa moja usiku.
“Ndiyo! Kuna kijana alitekwa! Ila hizo ni taarifa za kamanda, unaweza kukuta hakuna kitu!” alijibu muuza duka.
“Na alisema kwamba amepelekwa Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu?” aliendelea kuuliza.
“Ndiyo! Tangu saa kumi na moja jioni!”
Irene hakutaka kubaki mahali hapo, ilikuwa ni lazima ayaokoe maisha ya kaka yake. Kitendo cha kupelekwa hospitali bado hakikuonekana kuwa salama kwa maisha yake, alijua fika kwamba kama watu wale waliokuwa wamemteka mara ya kwanza wameuawa basi ilikuwa ni lazima watumwe wengine kwa kuwa wale waliokuwa wakiwatafuta walikuwa na mkono mrefu.
Hakutaka kupanda daladala. Alikujua kama angechukua daladala ilikuwa ni lazima kuchelewa kutokana na foleni kubwa iliyokuwa katika Barabara ya Morogoro, hivyo akaanza kukimbia.
Alipitia njia ya Bakhresa ambayo ilimpeleka mpaka katika Kituo cha Polisi cha Tandale, hapo akachukua barabara ya lami na kukimbia mpaka katika Hospitali ya Tandale, akakata kona kushoto na kuchukua barabara iliyokuwa ikielekea Tandale Kwa Mtogole.
Muda wote alikuwa akikimbia, watu aliokuwa akipishana nao walimshangaa, walihisi kulikuwa na tatizo kwani kwa jinsi alivyoonekana, hakuonekana kuwa na amani, wengi wakahisi kwamba nyuma ya mbio zile kulikuwa na tukio moja kubwa.
Alichukua dakika thelathini mpaka kufika katika hospitali hiyo ambapo alipokwenda mapokezini na kuulizia, akaelekezwa wodi aliyokuwa amelazwa Godwin na kuanza kwenda huko.
Hakutuliza macho yake, alionekana kuwa na hofu kubwa, aliangalia huku na kule kama mtu aliyekuwa akimtafuta mtu fulani. Wakati akiwa amekaribia katika wodi aliyoambiwa kwamba kaka yake alikuwemo, akawaona wanaume wawili wakitoka huku wakiwa wamemshika Godwin na kuanza kuondoka naye.
Haraka sana akajificha, alijua kwamba kama angetokeza basi watu hao wangemteka na yeye na kuondoka naye. Godwin alikuwa akipiga kelele akisema kwamba watu hao walikuwa wakienda kumuua kitu kilichowafanya watu wengine kumshangaa na kuona kama alikuwa amechanganyikiwa.
Irene hakutaka kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kuanza kufuatilia kwa nyuma, alitaka kuona ni mahali gani watu hao walikuwa wakimpeleka kaka yake.
Gari lilipowashwa, akamwambia dereva wa bodaboda aifuate gari hiyo mpaka ilipokuwa ikienda, alitaka kuwa na uhakika juu ya mahali ambapo kaka yake angepelekwa ili aweze kuwaita polisi na kumuokoa katika mikono yao.
Walilifuatilia gari lile kwa nyuma mpaka lilipofika Ubungo Maziwa ambapo likaingia ndani ya jumba moja kubwa, akawa na uhakika kwamba humo ndipo mahali atakapowekwa hivyo kufanya harakati za kwenda kuwaita polisi.
Akaondoka na bodaboda ile mpaka katika Kituo cha Polisi Ubungo kilichokuwa ndani ya kituo cha mabasi, alipofika, akawaambia kile kilichokuwa kimetokea kwamba kaka yake, Godwin alikuwa ametekwa na wanaume waliokuwa na lengo la kumuua.
“Wapo wapi?’ aliuliza polisi mmoja huku akiichukua bunduki yake.
“Ubungo Maziwa!”
“Twendeni!”
Akamlipa pesa yake dereva wa bodaboda na kuondoka kituoni hapo huku akiwa na polisi sita waliokuwa na bunduki mikononi mwao. Gari liliendeshwa kijeshi mpaka lilipofika karibu na nyumba hiyo ambapo wakaambiwa wasubiri kwanza kwani kwa muonekano wa nyumba hiyo uliwatia hofu na kuona haikuwa nyumba ya kawaida, na kama wangevamia kichwakichwa wangeweza kuuawa.
Walisubiri hapo kwa saa kadhaa ndipo wakaliona gari moja likirudi mahali hapo ambapo geti likafunguliwa, likaingizwa na ndani ya dakika tano tu, gari lile likatoka, geti likafungwa na kuanza kuondoka mahali hapo.
Kila mmoja akahisi kwamba mtu aliyekuwa ametekwa alikuwa ndani ya gari lile, walichokifanya ni kuanza kulifuatilia. Gari lile likaenda mpaka Ubungo Maraa ambapo likachukua Barabara ya Morogoro na kuanza kuelekea upande wa Kimara huku likiwa kwenye mwendo wa kawaida.
“Nafikiri watakuwa wanakwenda Msitu wa Pande,” alisema polisi mmoja.
“Bila shaka! Kama ni kweli, tukifika Kibamba, hebu mtazima taa tumfukuze mwizi kimyakimya,” alisema mkuu wa kikosi hicho.
Waliendelea kulifuatilia na walipofika Kibamba wakafanya kama walivyoagizwa, taa za gari zikazimwa na kuanza kulifuatilia gari hilo. Safari hiyo ilichukua dakika kadhaa, gari lile likasimamishwa pembezoni mwa barabara. Kwa haraka sana wanaume wale wakateremka na kumteremsha Godwin ambaye wakamchukua na kuingia naye kidogo msituni.
Huko, wakamuweka chini kwa lengo la kumuua. Kila kitu kilichokuwa kikiendelea, polisi wale walikuwa wakifuatilia kwani walitembea kwa mwendo wa harakaharaka, tena wa kujificha mpaka kufika karibu na msitu huo na kuangalia kilichokuwa kikiendelea.
“Haina shida mkuu! Tupe dakika tano!” ilisikika sauti ya mwanaume mmoja hapohapo akaikoki bastola yake.
“Mfyatue risasi…” alisema mkuu wa kituo, polisi mmoja akachukua bunduki yake lakini hata kabla hajamnyooshea mwanaume yule kwa lengo la kumpiga risasi, mlio wa risasi ukasikika, kila mmoja akashtuka kwa kuhisi kwamba walikuwa wamechelewa na mwanaume yule kumpiga risasi Godwin pale alipokuwa.
“Oooh! Umechelewa Husseni! Amekwishampiga risasi kijana wa watu,” alisema mkuu wa kikosi kile huku akishika kichwa kuonyesha masikitiko makubwa aliyokuwa nayo.
Milio ya risasi ilisikika mahali hapo, kila mmoja alihisi kwamba mwanaume yule aliyekuwa ameishika bastola alimpiga Godwin kutokana na jinsi alivyokuwa amejiandaa kwa ajili ya kumuua mahali pale.
Kilichowashtua ni kwamba wanaume wale ndiyo walioanguka chini na damu kuanza kutoka miilini mwao. Mkuu wa kikosi kile alishangaa kwani kijana aliyemwambia apige risasi hakuwa amefanya hivyo, sasa ni nani alikuwa amewapiga risasi watu hao?
“Eeh!” alishangaa mkuu wa kikosi hicho na kuanza kuangalia kama kulikuwa na polisi aliyekuwa amewapiga watu hao risasi.
Macho yake yakatua kwa Mustapha, kijana machachari, polisi aliyekuwa shapu katika matukio mengi, yeye ndiye aliyewapiga risasi watu hao kutoka pale aliposimama. Kila mmoja alishangaa, kwa uharaka aliokuwa nao wa kuwafyatulia risasi watu wale ulionekana ni wa kasi kuliko kawaida.
“Mnachelewa sana! Dogo angekufa pale,” alisema Mustapha huku akitoka kule alipokuwa amesimama.
Godwin alikuwa chini, milio ya risasi ilimuogopesha na kudhani kwamba yeye ndiye aliyekuwa amepigwa risasi mahali hapo. Akaanza kujipapasa mwilini mwake, hakuwa amejeruhiwa na alipowaangalia watu waliokuwa wamesimama mbele yake, wote walikuwa chini huku damu zikiwatoka miilini mwao.
“Nini kimetokea?” wakati akijiuliza hivyo, mara polisi waliokuwa wamejificha hatua kadhaa kutoka mahali hapo wakatokea na kuelekea kule alipokuwa.
Alishtuka, hakuamini kama kungekuwa na watu wengine mahali hapo. Alibaki akitetemeka na kuhisi kwamba watu hao walikuwa hatari kama wale waliokuwa wamepigwa risasi kwani kule walipokuwa wakitoka, ilikuwa vigumu kugundua kama walikuwa polisi kutokana na giza lililokuwa mahali hapo.
“Naomba msiniue! Naomba msiniue,” alisema Godwin huku akilia kuwaomba polisi hao wasimuue.
Hawakuzungumza kitu, wakamchukua na kuondoka nao. Alipowagundua kwamba watu hao walikuwa polisi kidogo moyo wake ukawa na amani, akaona Mungu amemuokoa kutoka kwenye mdomo wa kifo kwa mara nyingine tena.
Akapelekwa ndani ya gari ambapo huko akakutana na dada yake, Irene. Kabla ya kuongea chochote kile, wakakumbatiana. Godwin alishangaa, hakujua ni kwa namna gani ndugu yake huyo alikuwa mahali hapo kwani alipokuwa ametekwa, hakuwepo na hata alipoondoka kuelekea hospitalini msichana huyo hakuwa akifahamu lolote lile.
“Godwin! Godwin! Godw…” aliita Irene huku akiwa amemkumbatia ndugu yake huyo, alishindwa kumaalizia, sauti ya kilio ikaanza kusikika.
Polisi wakaichukua miili ya wanaume wale na kisha kuipeleka ndani ya gari na kuanza kuondoka mahali hapo huku wakizungumza mambo mengi ya utekaji ambayo yalikuwa yakifanyika sana kipindi hicho.
Godwin na Irene nao walikuwa nyuma ya gari lile, muda wote walikuwa wamekumbatiana huku wakiendelea kulia kwa furaha kwani kitendo cha kuokolewa namna ile kilionekana kuwa kama muujiza mkubwa kwa Godwin.
Kwa kuwa hakukuwa na magari mengi barabarani kutokana na muda kwenda sana, hawakuchukua muda mrefu wakafika kituoni ambapo moja kwa moja wakapumzishwa mapokezi, Godwin akatakiwa kuandika maelezo juu ya kile kilichokuwa kimetokea na kisha kuruhusiwa kuondoka kituoni hapo kwa kuambiwa kwamba walitakiwa kuripoti siku inayofuata.
****
Kihampa alikuwa nyumbani kwake, simu yake ilikuwa mezani, alikuwa na shauku kutaka kujua kile kilichokuwa kimetokea katika msitu ule. Kila wakati alipokuwa akipigiwa simu, harakaharaka alichukua na kuangalia kwenye kioo kuona kama mpigaji alikuwa mmoja wa vijana wale aliokuwa amewatuma kufanya mauaji msituni au mtu mwingine.
Alikuwa na presha kubwa, muda mwingi mkuu wake ambaye ndiye alikuwa akisimamia kazi yote alikuwa akimpigia simu na kumuuliza kilichokuwa kimetokea. Godwin alikuwa mtu wa kawaida, hakuwa komando au mtu yeyote mwenye mafunzo makubwa ya kijeshi lakini kitu cha ajabu kabisa walishindwa kumuua tena kilichokera zaidi ni kwamba wakati mwingine walikuwa wakimteka na kuondoka naye.
“Nini kinaendelea?” alijiuliza.
Baada ya dakika kadhaa akawapigia simu kwa lengo la kuwauliza kama kazi ilifanyika kwani walimwambia kuwa kila kitu kilikuwa tayari na kilichokuwa kikisubiriwa ni bonyeza kitufe cha bastola na kumuua Godwin.
Simu ilikuwa ikiita, iliita na kuita lakini haikupokelewa. Alijua kabisa kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kimetokea, haikuwa kawaida ya watu hao kutokupokea simu na wakati alikuwa amewapa kazi nzito ya kufanya. Machale yakamcheza, akahisi kabisa kulikuwa na kitu kimetokea, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kupiga simu katika vituo kadhaa vya polisi kuuliza kama kulikuwa na tukio limetokea usiku huo.
Alijulikana na kuheshimika na polisi wengi, kila kituo alichopiga simu aliambiwa kuhusu wavuta bangi na watu waliokuwa wakizurura tu lakini hakupewa tukio jingine lolote lile.
“Hapa tuna tukio la mwanaume kumpiga mkewe,” alisikika polisi kutoka upande wa pili.
“Basi! Achana nalo!”
Aliendelea kupiga simu zaidi na zaidi na baada ya kumaliza vituo kadhaa ndipo akakumbuka kwamba pale Ubungo, ndani ya kituo cha mabasi kulikuwa na kituo kidogo cha polisi hivyo kupiga simu hapo. Ilipopokelewa na kuuliza, akapewa taarifa kwamba kuna tukio la utekaji lililokuwa limetokea Ubungo Maziwa na mateka kutakiwa kuuawa msituni.
“Ikawaje?”
“Tulifanikiwa kupambana na watekaji! Walikuwa wanne na walitaka kumuua kijana mmoja hivi!” alisikika polisi.
“Yupoje?”
“Nani? Huyo kijana?”
“Ndiyo!”
“Mweusi, mwembamba, ana nywele nyingi. Pia alikuwa na dada yake ambaye ndiye aliyesaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa maisha yake,” alisikika polisi kutoka upande wa pili.
“Huyo kijana yupo hapo?”
“Hapana! Ameondoka sasa hivi na dada yake, yaani hata daladala inawezekana bado hawajapanda!” alisikika polisi huyo.
“Nasema hivi! Fanyeni kila linalowezekana huyo kijana arudishwe hapo kituoni! Yaani hakikisheni aondoki kwenda sehemu yoyote mimi nakuja,” alisema Kihampa kama mtu aliyechanganyikiwa.
“Sawa mkuu!”
Hakutaka kubaki chumbani kwake, ilikuwa ni lazima aondoke. Maneno aliyoambiwa na polisi yule kwamba kijana yule alipatikana na vijana wake kuuawa zilimchanganya. Hakujua sababu iliyolifanya tukio la kumuua Godwin kuwa gumu namna ile.
Aliwatuma vijana wengi kwa ajili ya kukamilisha mchakato huo, matukio yote, wakati wapo katika hatua za mwisho, polisi walikuwa wakiwaua watekaji pasipo kugundua kwamba watu hao walitumwa kwa ajili ya kukamilisha mauaji hayo.
Hakuchukua muda mrefu akafika katika kituo hicho, alimwangalia polisi mmoja baada ya mwingine, uso wake ulikuwa na hasira kali. Kuitoa roho ya mtu mmoja ilionekana kuwa ngumu na hivyo kusababisha roho za watu wengi kutoka.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akawauliza polisi kama kijana huyo alirudishwa lakini polisi mmoja akamwambia kwamba haikuwezekana kwa sababu tayari walipanda daladala na kurudi nyumbani kwao.
“Na mlisema kwamba aliacha namba ya simu! Si ndiyo?” aliuliza Kihampa.
“Ndiyo!”
“Mpigieni simu! Mwambieni arudi haraka sana,” alisema Kihampa.
“Hakuna tatizo!”
Hilo ndilo lililofanyika. Haraka sana simu ikapigwa, ilianza kuita, iliita kwa muda mrefu sana lakini haikupokelewa. Kila mmoja alikuwa na presha, jinsi Kihampa alivyokuwa akiwaangalia kwa jicho la ghadhabu ilionyesha kabisa kwamba kama wasingefanikisha kupatikana kwa kijana huyo basi ingekuwa hatari hapo kituoni.
Wakajaribu tena na tena lakini majibu yaliendelea kuwa vilevile. Baada ya kupiga zaidi ya mara kumi, hatimaye simu ikapokelewa, kwanza kukaanza kusikika sauti ya muziki kwa mbali na baada ya sekunde chache mwanaume mmoja kuanza kuongea.
“Unasumbua sana na namba yako ngeni! Wewe nani?” aliuliza jamaa huyo kwenye simu mara baada ya kuipokea.
“Kituo cha polisi hapa!”
“Nikusaidie nini jamaa! Nimeua au?” aliuliza jamaa huyo kijeuri.
“Naongea na nani?”
“Wewe chizi kweli! Sasa unawezaje kumpigia simu mtu usiyemjua? Wewe ulikuwa unampigia nani?” aliuliza mwanaume huyo.
“Godwin! Ni Godwin hapo?”
“Ndiye nani?”
“Kwani hii namba ya nani?”
“Yangu!”
“Siyo ya Godwin?”
“Mwana unarusha stimu sana! Kama vipi nikaushie!” alisema jamaa huyo na kukata simu.
“Atakuwa ametupa namba ya uongo,” alisema polisi huyo huku akiwaangalia wenzake kwani kwa jinsi mwanaume huyo alivyokuwa akisikika, hakuwa Godwin.
“Hebu angalia usajili wa namba!” alisema polisi mmoja na hivyo kufanyika hilo.
“Hapa naona jina limekufa Timotheo Mkunjuli!”
“Mmh! Tumeingizwa cha kike! Dogo katupa namba ya gari,” alisema polisi mmoja, Kihampa akaishiwa nguvu, miguu ikamlegea, akakaa kwenye benchi na kama lisingekuwa mahali hapo, angeanguka chini.
***
Bado moyo wa Godwin ulikuwa na hofu tele, hakutaka kumwamini mtu yeyote, si raia wa kawaida wala polisi, kwake, kila mtu alionekana kuwa adui wake.
Aliandikisha maelezo kituoni, hakuandika ukweli, alidanganya kila kitu kuanzia mahali alipokuwa akiishi mpaka namba yake ya simu. Hakutaka kutafutwa na polisi, alijua kwamba kama polisi haohao walihusika yeye kutekwa hospitalini basi ndiyo haohao ambao wangehusika kutoa mawasiliano yake, anuani na mpaka kutekwa tena.
Akaondoka na Irene, njiani walikuwa wakizungumza mambo mengi, alimwambia kwamba katika maisha waliyokuwa wakiishi, katika kila hatua walizokuwa wakipitia hawakutakiwa kumwamini mtu yeyote yule kwani waliona dunia nzima ikiwa imewageuka.
“We don’t have to trust anybody,” (hatutakiwi kumwamini mtu yeyote yule) alisema Godwin huku akimshika mkono Irene.
“Who is behind all of this?” (nani yupo nyuma ya haya yote?) aliuliza Irene.
“I don’t know! We got to hide,” (Sijui! Tutatakiwa tujifiche tu) alisema Godwin, wakati huyo tayari walifika kituoni na kusubiri daladala, baada ya dakika chache, ikafika na kuingia kisha kuelekea Manzese walipokuwa wakiishi.
Muda wote walionekana kuwa na hofu, maisha yalibadilika na kila waliyekuwa wakimuona walimuona kama adui. Hawakujua ni nani alikuwa nyuma ya mambo yote hayo, roho zao zilikuwa zikisakwa kila kona, waliogopa na kuona kwamba kama wasingejificha kila siku basi ingekuwa rahisi kutekwa na kuuawa kama ambavyo watu hao walitaka kuwaua.
****
Kihampa alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya ili kuwakamata vijana wale na kuwaua, kichwa chake kilimuuma, alikuwa na presha kubwa kwani hata mtu ambaye alikuwa nyuma yake alikuwa akimsisitiza sana kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima vijana hao wauawe kwani kama wasingefanya hivyo, kuna siku dunia ingefahamu kila kitu kilichokuwa kimetokea.
Yeye mwenyewe hakujua ni jambo gani ambalo liliwafanya vijana hao kutafutwa kwa udi na uvumba, hakujua sababu iliyowafanya watu waliokuwa juu yake kutamani kufanya mauaji hayo, kwa kuwa yalikuwa ni maelekezo, tena kutoka kwa watu wa juu yake alitaka kufanya kama ambavyo watu hao walivyomtaka yeye kufanya.
“Hakikisheni wale vijana wanapatikana!” alisema Kihampa huku akiwaangalia polisi wa pale.
“Sawa mkuu! Haina shida!”
“Tena haraka iwezekanavyo!”
“Sawa bosi!”
Kwa hasira akaondoka kituoni hapo, moyo wake ulikuwa na hasira kali kwani hakuamini kama polisi wale wangemruhusu Godwin kuondoka na wakati alikuwa na hamu naye.
Polisi hawakuwa wa kulaumiwa, wao kama watu waliohakikisha raia wanakuwa salama walifanya kazi yao kama walivyotakiwa kufanya ila kwa Kihampa lilionekana kuwa kosa kubwa mno.
Njiani alikuwa na mawazo tele, kila wakati alipiga usukani wa gari lake, alikuwa na hasira kupita kawaida. Aliwaona vijana waliofanya kazi yake kuwa ni wazembe kupita kawaida kwani aliwapa kila kitu, tena wakati mwingine aliwaahidi mambo mengi, walipokuwa wanafanikiwa kumteka Godwin, walizembea na mwisho wa siku kuuawa wao kitu kilichompa hasira nyingi.
Alipofika nyumbani, akachukua simu yake na kumpigia mkubwa wake, alitaka kumweleza ukweli kwamba kazi aliyokuwa amepewa, ilifanikiwa kwa asilimia mia moja lakini kwenye utekelezaji wake ikashuka mpaka asilimia sifuri kabisa.
Simu ilipopokelewa, akamwambia mwanaume huyo kila kitu kilichotokea, kuanzia Godwin alipotekwa mpaka vijana hao walipouawa kwa kuhisiwa kwamba walikuwa watekaji kutoka upande mbaya.
Akalaumiwa vya kutosha kwani alitakiwa kupigiwa simu wakati utekaji umefanyika na kisha kuelekea hukohuko kuona jinsi kijana huyo alivyokuwa akiuawa na si kukaa nyumbani na kuangalia televisheni huku akisubiri kazi ifanyike.
“Kwa hiyo wakati kijana ametekwa wewe ulikuwa nyumbani ukiangalia televisheni?” aliuliza mwanaume wa upande wa pili.
“Nilikuwa nasubiri simu yao!”
“Ila si ulikuwa nyumbani?”
“Ndiyo!”
“Huo ni uzembe mkubwa mno! Kazi haiwezi kufanikiwa wakati wewe upo nyumbani tu! Kihampa! Kama umechoka kazi sema,” alisema mwanaume huyo, kwa jinsi sauti yake ilivyosikika, alionekana kukasirika kupita kawaida.
“Nisamehe bosi! Nitahakikisha awamu inayofuata kazi inafanyika kikamilifu,” alisema Kihampa.
“Sawa!”
Simu ikakatwa! Kihampa akabaki ndani ya nyumba yake akiwa na mawazo tele, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya mpaka kuwapata vijana hao waliokuwa wakimsumbua na kuonekana hakukuwa na kazi aliyokuwa akiifanya.
Hakujua walikuwa mahali gani lakini baada ya kujifikiria sana, akakumbuka kwamba wakati Mafia na Saint wanauawa walikuwa na kijana wa IT ambaye ndiye aliyekuwa akifuatilia mawasiliano ya Godwin na mahali alipokuwa.
Kijana huyo alikuwa muhimu kwa wakati huo, alichokifanya usiku huohuo pasipo kujali kwamba alichelewa akaondoka nyumbani na kuelekea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Alipofika huko, kwa kutumia kitambulisho chake kilichomuonyesha kuwa na cheo kikubwa serikalini, akaruhusiwa na moja kwa moja kupelekwa katika wodi aliyolazwa kijana huyo.
Alimkuta akiwa amelala, akamuamsha. Kijana yule alipoamka na kumuona Kihampa, aliogopa kwani mtu aliyekuwa mbele yake alionekana kuwa mtu hatari kwa kumwangalia tu.
Akaulizwa maswali kadhaa, akatakiwa kusema mahali Godwin alipokuwa, yaani walipokuwa wamempigia simu na kubaini mahali alipokuwa, alikuwa wapi?
“Manzese Midizini!”
“Una uhakika?”
“Ndiyo!”
Hakutaka maswali zaidi, akaondoka na kuwasiliana na vijana wengine kwamba siku inayofuata ilikuwa ni ya kumtafuta kijana huyo na dada yake huko Mizidini, ilikuwa ni lazima wawapate kwani walikuwa watu muhimu waliokuwa wakitafutwa kila kona.
“Haina shida!”
Asubuhi vijana wawili, Michael na Selemani walioonekana kuwa kwenye mavazi ya kawaida wakaelekea huko. Kwa kuwaangalia walionekana kuwa vijana wa mitaani tu, waliambiwa kuhusu vijana hao, na kwa kuwa walipewa mpaka picha zao za nyuma walizopigwa wakiwa mitaani hakukuwa na tatizo lolote lile.
Walipofika huko, wakaanza kuzunguka huku na kule, walitengeneza urafiki na vijana wa huko, tena mbaya zaidi wakajifanya kuwa wauza bangi wakubwa na kuwauzia vijana waliokuwa humo.
Ndani ya wiki moja bado walikuwa wakihangaika, hawakujua vijana hao walikuwa wapi, hawakutaka kuwauliza watu wengine kwani kila kitu kilichokuwa kikifanyika wakati huo kilikuwa ni kwa siri kubwa.
Wakati vijana hao wakiwa hapo mtaani, Godwin na Irene hawakuwa wakifahamu chochote kile, waliogopa hata kutoka nje na kila siku walikuwa watu wa kukaa ndani tu.
Hawakujua kama kulikuwa na watu waliotumwa kwa ajili ya kuwateka, walikuwa ndani huku maisha yakiendelea kama kawaida na kila siku walipotaka kutoka, walitoka usiku tena huku wakiwa na mavazi ambayo kuwagundua ilikuwa vigumu sana.
Baada ya wiki mbili kupita pasipo kupata tatizo lolote lile, wakajisahau na kuhisi kwamba kwa wakati huo kila kitu kilikuwa shwari, kwamba kulikuwa na hali ya hatari kiasi kwamba hata kama wangetoka, wasingeweza kugundulika kwani hakukuwa na mtu aliyekuwa akiwafahamu.
“Nadhani kila kitu kipo salama! Sidhani kama watu hao wataweza kufika huku,” alisema Irene huku akimwangalia ndugu yake.
“Nilikwishawahi kukwambia kwamba hutakiwi kumwamini mtu yeyote yule,” alisema Godwin, yeye ndie ambaye alipitia misukosuko mingi, moyoni mwake alikuwa mtu mwenye hofu kuliko hata Irene.
“Najua! Lakini unahisi wanaweza kujua kama tupo huku?” aliuliza Irene.
“Sijajua! Lakini hilo neno la uaminifu naomba liendelee kudumu moyoni mwako Irene,” alisema Godwin.
“Haina shida!”
Hakuona kama kulikuwa na sababu ya kuendelea kuwa na hofu zaidi, alichokifanya ni kuanza kutoka ndani na kukaa nje na wanawake wengine na kuanza kupiga stori.
Akajisahau kabisa, akasahau kama kulikuwa na watu waliokuwa wakiwatafuta. Kitendo cha kuendelea kukaa kibarazani kila siku ndipo vijana wale wakamuona, hawakujua kama alikuwa ndiye mtu waliyekuwa wakimtafuta au mwingine, walichokifanya ni kuangalia picha, japokuwa ilikuwa imepigwa kitambo hicho lakini wakagundua kwamba alikuwa ndiye yeye.
“Ndiye yeye!” alisema jamaa mmoja.
“Kumbe anaishi pale!”
“Inawezekana! Wasiliana na bosi haraka tujue ni kitu gani tunatakiwa kufanya!”
Simu ikapigwa mpaka kwa Kihampa, akaambiwa kile kilichokuwa kimetokea, kwamba walifanikiwa kumuona msichana lakini hawakujua mvulana alikuwa wapi.
“Mna uhakika ni yeye?” aliuliza Kihampa.
“Macho huwa hayadanganyi mkuu! She is the one,” (ndiye yeye) alisema Michael.
“Kazi nzuri sana! Pangeni mipango ya kuhakikisha anatekwa haraka iwezekanavyo! Mtakapofanikiwa, msimuue mpaka mimi nije! Mmenielewa?” aliuliza Kihampa.
“Ndiyo mkuu!”
“Sawa! Kazi njema!” alisema Kihampa na kushusha pumzi! Kidogo moyo wake ukaingiwa na furaha kwa mara nyingine na kuona kwamba kwa wakati huo kazi hiyo ingefanyika hata kama kungekuwa na kizuizi cha aina gani. Kabla ya kumuua Godwin, kwanza walitakiwa kuanza na Irene, hivyo mipango ikaanza kusukwa.
***
Kumpata Irene hakukuwa na tatizo tena, walijua mahali alipokuwa akiishi, hawakuwa na wasiwasi naye, walichotaka kukikamilisha kwa wakati huo ni kumteka na kwenda kumuua tu.
Hawakutaka kuchelewa, walihisi kwamba kama wangemuacha siku hiyo basi kungekuwa na ugumu wa kumpata siku nyingine, kwa kuwa walikuwa wamekwishamuona, hivyo walichotakiwa kufanya ni kumteka hapohapo alipokuwa.
Bastola walikuwa nazo viunoni mwao, wakaondoka na kuelekea katika gari lao ambalo walikuwa na kawaida ya kulipaki katika Kituo cha Mafuta cha Ericom kilichokuwa Manzese Bakhresa.
Walipofika, wakalichukua na kuanza kurudi Midizini, walikuwa na mipago kabambe, ilikuwa ni lazima msichana huyo atekwe, auawe kama walivyokuwa wameambiwa. Wakiwa njiani, wakampigia simu Kihampa na kumwambia mpango ulivyokuwa ukienda kwamba ndani ya dakika kadhaa msichana huyo angetekwa hivyo kama kuondoka nyumbani alitakiwa kuondoka haraka sana na kuonana katika jumba moja lililokuwepo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
“Kwani mmekwishampata?” aliuliza Kihampa kwenye simu.
“Hilo si tatizo! Wewe njoo tu, kuhusu kumteka hakuna tatizo lolote lile,” alisema Michael kwenye simu.
Walikuwa na uhakika kwamba kumteka Irene hakukuwa na kazi yoyote ile, ilikuwa ni kazi nyepesi kama kumsukuma mlevi katika mteremko wa mlima. Kutoka hapo katika kituo cha mafuta mpaka Mizidizini hakukuwa mbali, walitumia dakika chache tu wakafika na kuanza kujipanga upya.
“Twende pale, tukifika ni kuzungumza nao kikawaida ila wakiwa wabishi ni kupiga risasi hewani!” alisema Michael na kuelewana na Selemani kwamba kile walichokizungumza ndicho walichotakiwa kufanya.
Gari likazidi kusogea kule walipokuwa wanawake wale, hakukuwa na mtu aliyekuwa na hofu nalo, kila mtu aliyeliona alihisi ni gari la kawaida miongoni mwa magari yaliyokuwa yakipita katika barabara hiyo.
Gari lile lilipofika usawa wa wanawake wale, Michael na Selemani wakateremka, wakajifanya kama wanaliangalia gari lile. Wanawake wale hawakuzungumza kitu, waliendelea kusukana huku wakipiga stori.
Michael hakutaka kupoteza muda, alipoona kwamba amani imetulia mahali hapo, akawasogelea wanawake wale, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kutoa bastola, akawaambia kwamba wanyamaze na kama wangekaidi basi angewaua wote.
“Yeyote atakayepiga kelele, naumwaga ubongo wake,” alisema Michael, kwa jinsi sauti yake ilivyotoka na uso wake ulivyokuwa wakajua kwamba jamaa hakuwa akitania.
Wanawake wote wakaogopa, wakabaki kimya huku wakitetemeka. Bastola ilitisha, walizoea kuiona katika filamu mbalimbali za mapigano lakini siku hiyo ilikuwa mbele ya macho yao. Muda wote huo, kama walivyokuwa wanawake wengine hata naye Irene alikuwa kimya, alimwangalia mwanaume huyo, hata kabla hajazungumza maneno mengi akajua tu kwamba alikuwa mahali hapo kwa ajili yake.
“Wewe! Simama uje huku,” alisema Michael huku akimwangalia Irene ambaye bila ubishi wowote ule akasimama na kumsogelea Michael.
Akashikwa mkono na kuambiwa aingie ndani ya gari mwenyewe. Hakuwa mbishi, akafanya kama watu hao walivyotaka na hivyo kuingia ndani.
“Yeyote atakayepiga kelele, namuua,” alisema Michael, akaingia ndani ya gari na kuondoka mahali hapo.
Gari lilipopotea machoni mwao, wanawake wale wakaanza kupiga kelele za kuomba msaada. Wanaume waliokuwa pembeni wakasogea kule walipokuwa na kuwauliza kilichokuwa kikiendelea.
“Majambazi!” alisema mwanamke mmoja huku akitetemeka.
“Majambazi?” aliuliza jamaa mmoja.
“Ndiyo! Walikuwa na bunduki!”
“Bunduki? Mbona sisi hatukusikia hata mlio wa risasi?” aliuliza jamaa huyo.
Mwanamke huyo akasimulia kila kitu kilichokuwa kimetokea, kila mmoja alishangaa, hawakujua ni sababu gani iliyowafanya watu hao kumteka Irene na kuondoka naye na wakati walijua kwamba hakuwa na tatizo lolote lile.
Mwanamke mmoja akaingia ndani na kumwambia Godwin kilichotokea. Kijana huyo akatoka ndani, alichanganyikiwa, alipoambiwa kwamba kulikuwa na wanaume walifika mahali hapo na kumteka ndugu yake, Irene, alichanganyikiwa, akawauliza upande waliokuwa wamekwenda, alipoambiwa akaanza kukimbia kuelekea huko.
Alikuwa akilia kwa uchungu, aliumia moyoni, alijua kabisa kwamba watu hao waliokuwa wamemteka hawakuwa watu wazuri, walikuwa watu walewale waliokuwa wakiwatafuta usiku na mchana kwa lengo la kumuua.
Alikimbia na kukimbia mpaka akatokea katika barabara ya pili lakini hakuweza kuliona gari hilo lililombeba ndugu yake. Alilia sana, aliumia na kuona kwamba inawezekana huo ndiyo ukawa mwisho wa ndugu yake huyo.
Hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kumpata na hata kwenda kituo cha polisi aliogopa kwani alijua kwamba kote huko alikuwa akitafutwa kwa udi na uvumba. Kila mtu aliyekuwa akipita njiani alimshangaa, alilia peke yake huku akiliita jina la Irene kiasi kwamba watu wengine walihisi kwamba alikuwa mwendawazimu.
Akarudi nyumbani, hakujua ni kitu gani ambacho kingemtokea ndugu yake lakini kwa jinsi alivyowafahamu watu wale, jinsi walivyokuwa na roho mbaya, walivyotaka kumuua aliamini kwamba hata ndugu yake huyo angeweza kuuawa.
“Mungu naomba umlinde Irene! Mungu naomba umpiganie,” alisema Godwin na kuanza kumuomba Mungu.
Siku hiyo hakulala, hakula, muda wote alikuwa akimuwaza ndugu yake, aliteseka moyoni mwake, hakujua mahali alipopelekwa, hakujua ni mateso ya namna gani ndugu yake huyo alikuwa akiyapata huko alipokuwa.
Ndani pia hakukukalika, usiku alikesha nje kwa kuamini labda angeweza kumuona Irene akirudi nyumbani hapo lakini usiku mzima ulikuwa kimya, Irene hakuwa amerudi mahali hapo.
Siku hiyo hakutaka kubaki nyumbani, alikumbuka mahali alipokuwa ametekwa na kupelekwa, alilikumbuka lile jumba lililopo Ubungo Maziwa na kuanza kwenda huko, alipofika, hakukuta mtu, lilionekana kama limetelekezwa, kwa kutumia ujanja wake, akaruka ukuta kwa nyuma na kuingia ndani, akapitia katika mlango wa jikoni ambao haukuwa umefungwa.
Akaingia mpaka ndani, hakukuta mtu. Siku hiyo alijiamini, alijiona kuwa na nguvu kubwa na ndiyo maana hata kuingia humo hakuwa amejishauri mara nyingi. Akaingia katika kila chumba, Irene hakuwepo, hakutaka kuishia hapo, akaanza kuita pia lakini hakusikia sauti ya mtu yeyote yule.
Akaondoka na wazo lililomjia kichwani lilikuwa ni kwenda katika Msitu wa Pande, alitaka kwenda kuona kama angemkuta huko, hata kama asingemkuta akiwa hai basi aikute hata maiti yake. Akafika huko, ulikuwa msitu uliotisha lakini hakuogopa kuingia, alimtafuta kila kona lakini hakuweza kumpata Irene wala mzoga wake.
Akarudi nyumbani majira ya saa kumi jioni. Alichoka lakini hakukata tamaa, aliposimama katika duka lililokuwa nyumbani hapo ndipo akasikia taarifa ya habari iliyosema kwamba kulikuwa na mwili wa msichana uliokuwa umeokotwa ufukweni huku ukiwa umenyongwa.
Godwin akashtuka, akasikiliza vizuri taarifa ile ya habari ambayo ilisema zaidi kwamba msichana huyo alikuwa akikisiwa kuwa na miaka kumi na tisa, alivalia gauni jekundu na nywele zake alikuwa amezibana kwa nyuma, kila kitu alichokisema kilikuwa sawasawa na muonekano wa Irene kipindi alichotekwa.
“Wamemuua Irene,” alisema Godwin huku akianza kutiririkwa na machozi mashavuni mwake.
Taarifa ile ilizidi kusema kwamba mwili wa marehemu ulikuwa katika Hospitali ya Mwananyamala hivyo kwa yeyote aliyehisi kwamba huyo anaweza kuwa ndugu yake basi aende huko.
Godwin akawapa taarifa watu wengine juu ya kile alichokuwa amekisikia, yeye na vijana wengine saba wakaanza kuelekea katika hospitali hiyo kwa ajili ya kuutambua mwili huo.
Njiani, moyo wake ulimwambia kwamba hakutakiwa kujisumbua kwani ndugu yake, Irene aliuawa na hivyo alitakiwa kuishi maisha mapya, maisha bila ya kuwa na ndugu yake huyo.
“Haiwezekani! Irene hawezi kufa!” alisema Godwin huku akiwa njiani na vijana hao kuelekea katika hospitali hiyo. Wakati mwingine alitamani kila kitu kilichokuwa kikiendelea kiwe ndoto moja ya kusisimua kwani maisha aliyokuwa akipitia na dada yake, yalitisha mno.
***
Michael na Selemani waliondoka na Irene kuelekea Kinondoni ambapo walipanga kuonana na Kihampa aliyewaambia kuwa awakute mahali hapo kwa lengo la kumuua msichana huyo.
Hapo kabla waliambiwa kwamba kulikuwa na ugumu mno kuwapata watu hao kwa kuwa kulikuwa na watu wengi waliojaribu lakini mwisho wa siku hawakufanikiwa na ndiyo kwanza waliuawa wao.
Walimpata Irene kiwepesi sana, ndani ya gari walikuwa wakizungumza mambo mengi huku Irene akiwa amefungwa kamba kwani walihisi kwamba kama wasingefanya hivyo basi msichana huyo angeweza hata kuruka kutoka garini na kuwakimbia.
Wakati wakiwa njiani, Kihampa akawapigia simu na kuwauliza kama walikuwa na msichana huyo. Wakamwambia kwamba kama walivyomuahidi ndivyo walivyofanya kwani msichana huyo alikuwa ndani ya gari lao na wakati huo walikuwa wakielekea Kinondoni tayari kwa kufanya kazi waliyotakiwa kuifanya.
“Nakuja! Asikimbie bwana!” alisema Kihampa, hakujiamini hata kidogo, kwa jinsi alivyokuwa amehangaika na vijana hao, aliona muda wowote ule msichana huyo angetoroka kama ilivyokuwa kwa kaka yake.
“Hilo wala usijali! Na hata kama akijaribu, tutampiga risasi za mgongoni,” alisema Michael.
Muda wote huo Irene alikuwa akilia, moyoni mwake alijua kabisa kwamba watu hao walikuwa hatari na walikuwa wakimpeleka sehemu kwenda kumuua tu.
Alimuomba Mungu amnusuru, hakutaka kufa, hakutaka kumuacha kaka yake, alijua kwamba walikuwa wakiishi katika maisha magumu, alimwambia Mungu kwamba alikuwa tayari kuendelea kuteseka na kaka yake lakini si kuuawa kama watu hao walivyotaka iwe.
Gari lilikwenda mpaka lilipofika Kinondoni, likasimama nje ya jumba moja, halikuwa la kifahari sana, lilikuwa la kawaida ambalo lilikuwa na geti lililofunguliwa na gari kuingizwa ndani. Baada ya hapo, likasimamishwa, mlango ukafunguliwa na kuteremshwa.
Hakukuwa na mtu zaidi yao, bado Irene alikuwa akilia na kutaka kuachwa lakini hakukuwa na mtu aliyemuelewa, wakamchukua mpaka katika chumba kimoja kilichokuwa ndani ya jumba hilo. Chumba hicho hakikuwa kama vyumba vingine, kwanza hakikuwa na dirisha, kilikuwa na mlango, feni kwa juu lililoonekana kuwa bovu kabisa, ukuta wake ulichakaa na ulikuwa na michirizi mingi ya damu zilizoganda.
Mbali na vitu hivyo pia kulikuwa na kistuli kikuukuu huku kwa pembeni kabisa kukiwa na beseni lililokuwa na maji na taulo moja jekundu. Kwa kukiangalia tu chumba kile ilionyesha kabisa kilikuwa ni chumba kilichokuwa na mateso mengi, Irene alikuwa akitetemeka, aliogopa na kuona kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wake.
Watu wale walipomfikisha ndani ya chumba hicho, wakaufunga mlango na kutoka. Irene akabaki ndani ya chumba hicho na kuendelea kulia. Chumba kilitisha, alipokuwa humo alihisi akizungukwa na malaika wa kifo kitu kilichomfanya kuwa na hofu kupita kawaida.
Alipiga kelele za kutaka msaada lakini hakukuwa na mtu aliyefika kumsaidia. Kichwa chake kilimkumbuka kaka yake, hakuwa tayari kufikiwa na ubaya wowote ule mpaka pale atakapomuona na kumuaga.
Alikaa kwa dakika kadhaa, mlango ukafunguliwa na wanaume wawili kuingia ndani ya chumba hicho, mmoja alikuwa Michael na mwingine alikuwa Kihampa ambaye hakuwa akimfahamu kabisa.
“Kazi nzuri sana,” alisema Kihampa huku akimwangalia Irene, uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana, hakuamini kama msichana huyo alikuwa mikononi mwao.
“Tumfanye nini?” aliuliza Michael.
“Hilo tutazungumza nje ya chumba hiki,” alijibu Michael.
Irene alihisi kwamba Kihampa angeweza kumsaidia kwani ndiye aliyeonekana kuwa kiongozi wa watu hao. Akaanza kumuomba msamaha kwamba kama kulikuwa na kitu kibaya aliwafanyia basi wamsamehe lakini maneno hayo hayakumuingia Kihampa, moyo wake ukakosa huruma na kila alipomwangalia Irene kulikuwa na kitu kimoja tu moyoni mwake, ni lazima wamuue msichana huyo.
Wakatoka ndani ya chumba hicho, wakaelekea sebuleni na kuanza kujadili ni kitu gani kilitakiwa kufanyika, na kama walikubaliana kumuua, je, ilikuwa vizuri kuuliwa ndani ya chumba kile au sehemu nyingine.
“Nitamuua ndani ya gari halafu tutakwenda kuutupa mwili wake ufukweni,” alisema Kihampa.
“Sasa hivi?”
“Hapana! Usiku, kama saa nne hivi!”
“Sawa bosi!”
Kihampa hakutaka kuondoka, bado moyo wake haukuwa na amani hata kidogo, alihisi kwamba kama angeondoka pasipo msichana huyo kuuawa basi huku nyuma kungetokea la kutokea na kuambiwa kwamba msichana huyo hakufa kama ilivyotokea kwa kaka yake.
Alitaka kufuatilia kila kitu. Muda ulisogea, ilipofika saa nne kamili usiku, mlango ukafunguliwa na kumbeba Irene juujuu na kuondoka naye mahali hapo.
Msichana huyo alikuwa akilia, tumbo liliuma, njaa ilimkamata kwani tangu alipolekwa mchana hakuwa ameingiza chochote tumboni mwake. Hakukuwa na mtu aliyemsikiliza, walikuwa na kazi moja ya kumuua, hata kama wangempa chakula ingekuwa kazi bure kwani ilikuwa ni lazima kumuua.
“Nasikia njaa…naomba msiniue, naombeni chakula,” alisema Irene huku akilia.
“Paaa!” kilisikika kibao kizito kilichoshuka shavuni mwake, alama za kiganja cha Kihampa zilibaki shavuni mwake, alichukia kumsikia msichana huyo akipiga kelele.
“Nyamazaaaaa!” alisema mwanaume huyo kwa sauti kubwa.
Irene akanyamaza, akaingizwa ndani ya gari huku akilia. Alikuwa akitetemeka, alihisi kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wake. Mule ndani ya gari Kihampa akamsogelea Irene aliyekuwa akiendelea kulia, hata kabla hajazungumza chochote akamvutia kwake, akamgeuza, akakaa nyuma yake na kuanza kumkaba msichana huyo.
Alimkaba kwa nguvu, Irene alikuwa akikukuruka kuiondoa shingo yake mikononi mwa Kihampa lakini ilishindikana kwani mikono ya mwanaume huyo ilikuwa na nguvu na alimkaba vilivyo.
Ndani ya sekunde kadhaa, mishipa yake ikasimama, damu ikaacha kuzunguka na kujaa katika mishipa ya kichwani mwake, pumzi zikaanza kukata, kila alipojitahidi kujinasua mikononi mwa mwanaume huyo alishindwa kabisa.
Alikabwa kwa dakika nne nzima, hata alipokuwa amekufa kwa kukabwa lakini Kihampa hakutaka kumuacha, aliendelea kumkaba hivyohivyo mpaka dakika hizo zilipotimia.
Mwili wa Irene ukaanguka chini, roho ikaacha mwili. Kihampa akatoa tabasamu, hiyo ndiyo kazi kubwa aliyotaka kuifanya, aliamini kwamba baada ya kumuua kazi yake ingekamilika kwa Godwin ambaye vijana wake walikuwa na uhakika kwamba alikuwa akiishi katika nyumba ile waliyomkuta msichana huyo.
“Kwisha habari yake,” alisema Kihampa huku akijifuta mapovu ya msichana huyo yaliyokuwa yamemwagikia katika mikono yake baada ya kumkaba shingoni.
Hawakuchukua muda mrefu wakaingia katika Ufukwe wa Coco, hawakutaka kufika mpaka baharini kabisa, wakautupa mwili wake pembezoni mwa barabara huku kukiwa hakuna watu eneo hilo kisha kuondoka kwa kuamini kwamba polisi wangepigiwa simu na kwenda kuichukua maiti ile.
Godwin alikuwa akilia, hakuwa na uhakika kama msichana aliyekutwa ufukweni akiwa amekufa alikuwa Irene au mtu mwingine aliyekuwa amefananishwa naye. Alipofika na wenzake sehemu kilipokuwa chumba cha mochwari, akaelezea shida yake, tena kwa kuwa alitangulizana na vijana wenzake na daktari waliyemuomba sana, wakaruhusiwa watatu kuingia humo.
Wakaanza kuzunguka huku na kule wakionyeshewa maiti zilizokuwa zimeletwa usiku uliopita. Godwin aliziangalia, kila maiti aliyoiangalia haikuwa ya Irene, alijipa uhakika kwamba inawezekana maiti iliyokuwa ikizungumziwa ilifananishwa na msichana huyo.
Baada ya kuzunguka kwenye masanduku ya maiti zilizoingizwa usiku uliopita ndipo wakafika katika sanduku moja ambalo lilivutwa na kufunguliwa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Macho ya Godwin yakatua usoni mwa maiti ile, hakuamini alichokiona, maiti iliyokuwa kwenye sanduku mbele yake ilikuwa ni maiti ya dada yake, Irene.
Ilikuwa imefumba macho, picha hiyo iliyokuwa ikionekana mbele yake ilimtisha, ilimuogopesha na kubwa zaidi ilimuumiza kupita kawaida.
Moyo wake ukajawa na majonzi makubwa, hasira kali ikamkamata, hakumjua mtu aliyefanya vile, hakujua sababu ya iliyowapelekea kumuua dada yake, ila popote pale alipokuwa, ilikuwa ni lazima kumtafuta kwa ajili ya kumlipizia kisasi.
“Why? Why have they done this? Why have they killed her? I will look for them, and when I find them, I will kill them all,” (Kwa nini? Kwa nini wamefanya hivi? Kwa nini wamemuua? Nitawatafuta, na nitakapowapata wao wote) alisema Godwin huku pale alipokuwa machozi yakiwa yakimtiririka mashavuni mwake.
***
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment