Simulizi : Machungu Ya Usaliti
Sehemu Ya Pili (2)
Yalikuwa ni majira ya saa tatu za usiku, Richard alikuwa nyumbani kwao maeneo ya Mikocheni, muda huo alikuwa chumbani kwake amejilaza kitandani. Akili yake bado iliendelea kumfikiria Monalisa, hakujua ni kwa nini msichana huyo alianza kumuingia kwa kasi katika kichwa chake, kuna kipindi alianza kujilaumu kwa kumkubalia ombi lake lakini alipotaka kuchukua simu yake na kutaka kumuandikia ujumbe wenye lengo la kughairi uamuzi huo alishindwa, alijikuta vidole vyake vikiwa vizito kuandika ujumbe wa aina hiyo mwisho akajikuta akimtumia ujumbe wa salamu na huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuchat na msichana huyo. Alisahau kumjulia hata hali Evelyne msichana ambaye alikuwa katika mahusiano naye, alichokuwa amekiona ni cha umuhimu kwa wakati huo ni kuwasiliana na Monalisa ili aweze kuzikidhi haja za moyo wake, alipanga kushiriki kufanya mapenzi naye halafu huo ndiyo uwe mwisho wa uhusiano wao, hakupanga kumuumiza Evelyne na ndiyo sababu aliomba iwe siri ili msichana wake huyo asiweze kugundua lolote.
Kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika moyo wa Richard aliamini ilikuwa ni siri nzito mno na hakukuwa na mtu mwingine ambaye alikuwa akikifahamu zaidi yake na Monalisa.
Wakati alipokuwa akiendelea kuwasiliana na msichana huyo ndivyo ambavyo Monalisa na yeye alizidi kuwatambia wasichana wenzake mule hostel jinsi ambavyo alikuwa msichana shupavu ambaye hakukubali kushindwa kirahisi kwa kumkosa Richard.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hilo lilizidi kuwaumiza wasichana wenzake mno, walianza kuingiwa na wivu baada ya kusikia kuwa Richard na Monalisa walikuwa ni wapenzi kwa wakati ule, kuna kipindi hawakutaka kukubali kabisa lakini huo ulibaki kuwa ni ukweli. Richard na Monalisa walikuwa katika mapenzi.
“Unafikiri nitakubali kirahisi kuachana naye, nitahakikisha anabaki kuwa wangu tu,” alisema Monalisa huku akiwaambia Penina, Mary na Adela, walionekana kuingiwa na wivu mno, hawakutaka kuamini kabisa.
“Sijui Evelyne atakuwa katika hali gani akisikia kuwa wewe na Richard ni wapenzi?” aliuliza Mary swali la kinafki ambalo jibu lake lilikuwa wazi kabisa, swali hilo likawafanya wote watokwe na kicheko halafu wakagongeana kama ilivyokuwa kawaida yao.
“Evelyne ndiyo mdudu gani?” aliuliza Monalisa huku akiendelea kucheka.
Hakutaka kuona msichana huyo akiendelea kuyafurahia mapenzi na Richard, kitu pekee alichokuwa amepanga kukifanya ni kuhakikisha anafanikiwa kumpokonya Richard mikononi mwake na kisha anakuwa mali yake peke yake tu.
Hakuacha kuendelea kuwasiliana na Richard, walikuwa wakifanya mawasiliano kila siku huku moyoni akizidi kujiapiza kumteka mvulana huyo kimapenzi.
“Nahitaji kukuona Richard.”
“Lini?”
“Leo.”
“Usiku huu?”
“Ndiyo, Kwani kuna tatizo gani mpenzi?”
“Hapana, hakuna tatizo.”
“Sasa kwa nini hutaki?”
“Sio sitaki ila si upo hostel na kesho tunakipindi asubuhi?”
“Ndiyo najua hilo.”
“Sasa huoni hilo ni tatizo?”
“Richard mimi siwezi kusoma ukweli bila kuonana na wewe usiku wa leo, kama ni kipindi kuingia tutaingia tu kwanza kipindi chenyewe hakina umuhimu zaidi yako, tafadhali naomba kukuona japo sekunde moja, nitauridhisha moyo wangu.”
“Sawa nakuja kukufuata muda huu hostel ila tafadhali naomba kila kitu kinachoendelea kibaki kuwa ni siri kati yetu.”
“Nilikuahidi na ninarudia kukuahidi, siwezi kuitoa siri hii, shida yangu kubwa ni kuwa na wewe tu basi.”
“Sawa nakuja.”
“Nilikuahidi na ninarudia kukuahidi, siwezi kuitoa siri hii, shida yangu kubwa ni kuwa na wewe tu basi.”
“Sawa nakuja.”
Yalikuwa ni mazungumzo kati ya Monalisa na Richard waliyokuwa wakizungumza kwenye simu majira ya jioni, baada ya kumaliza kuzungumza Richard alijiandaa, alipomaliza aliwaaga wazazi wake kuwa anakwenda chuoni kwenye kipindi, wazazi wake walimkubalia kisha akaondoka kwa usafiri binafsi kama ilivyokuwa kawaida yake, siku hiyo aliamua kutembelea gari aina ya Toyota prado new model lenye thamani ya shilingi milioni 65.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Safari yake iliishia nje ya chuo cha IFM ambapo ndipo zilipokuwa hostel za chuo hiko, aliposimamisha gari aliamua kumtumia ujumbe mfupi Monalisa wa kumtaarifu kuwa tayari alikuwa eneo lile la chuo na kwa wakati huo alikuwa akimsubiria nje.
Haikuchukua dakika nyingi Monalisa aliweza kutoka nje ya chuo hiko na kuanza kuyaangaza macho yake huku na kule, Richard aliamua kupiga honi baada ya kumuona Monalisa akiwa katika hali hiyo, tabasamu mwanana lilichanua katika uso wa Monalisa ambaye alikuwa amevalia mavazi yaliyompendezesha kupita kawaida, baada ya kumuona Richard akiwa ndani ya gari alilifuata gari lile, alipolifikia Richard alimpa ishara ya kukaa kiti cha mbele, akafungua mlango wa gari hilo na kuingia.
“Umependeza sana,” alisema Richard huku akimtazama Monalisa.
“Asante Mpenzi na uzuri nao unachangia,” alisema Monalisa maneno yaliyowafanya wote wakatokwa na kicheko.
“Kwa hiyo tunaenda wapi?” aliuliza Richard.
“Popote pale mpenzi utakapopapenda wewe,” alijibu Monalisa.
“Sehemu gani itakuwa na utulivu,” alisema Richard huku akionekana kutafakari jambo.
“Pale Serena vipi hapafai kwani?” aliuliza Monalisa swali lililomtoa Richard katika ile hali ya kutafakari.
“Yeah! pako vizuri sana, twende huko,” alijibu Richard kisha akawasha gari na kuondoka eneo hilo.
Walifika katika hoteli hiyo ya kifahari ya Serena kisha wakachukua chumba, Monalisa bado alikuwa haamini kama kweli siku hiyo alifanikiwa kulala na mwanaume huyo kitanda kimoja, alionekana kuwa mwenye furaha mno.
Walipoingia ndani ya chumba cha hoteli hiyo Richard bado aliendelea kuisisitiza siri ambayo ilitakiwa kuendelea kubaki kati yao, moyoni mwake alimpenda sana Evelyne na hakupanga kumsaliti wala kumpa maumivu yoyote ya kimapenzi, aliamini baada ya kumaliza kufanya mapenzi na Monalisa basi huo ndiyo ulikuwa mwanzo na mwisho wa penzi hilo la dharura.
Waliagiza chakula na baada ya kuletewa na muhudumu wa hoteli hiyo walianza kula taratibu huku wakitazamana kwa macho ya kuibiana.
Baada ya kumaliza kula chakula hakukuwa na tukio lingine ambalo lilitakiwa kuendelea kati yao zaidi ya kuanza kushikanashikana huku midomo yao ikiwa imekutana na kuanza kubadilishana mate, walitumia muda kama wa dakika kumi na tano katika kuchezeana miili yao na baada ya hapo kitendo kilichofuata waliamua kuvunja amri ya sita.
****
Evelyne aliendelea kuishi na matumaini ya kumpenda Richard siku zote, aliamini alikuwa ni mwanaume wa maisha yake hivyo hakukuwa na udanganyifu wowote uliyokuwa ukiendelea.
Kipindi hicho ambapo Monalisa alikuwa amefanikiwa kuwa na Richard kimapenzi zilianza kuvuma tetesi za chinichini pale chuoni kuwa wawili hao walikuwa wakitoka kimapenzi, Evelyne baada ya kuzisikia tetesi hizo aliamua kuzipuuzia, alimuamini sana Richard hivyo kila kitu ambacho alikuwa akiambiwa kibaya kilichomuhusu mwanaume wake huyo aliweza kukikanusha, hakutaka kuishi na wasiwasi.
“Why don’t you want to believe everything you’re told about Richard?” (Kwa nini hutaki kuamini kila kitu kibaya unachoambiwa kuhusu Richard?) aliuliza Happy.
“No, one loves him so much, he loves me so much so I know he can’t do any harm to me,” (Hapana, ninampenda sana, ananipenda pia hata hivyo najua hawezi kunifanyia ukatili wowote,) alijibu Evelyne.
Evelyne alizidi kuishi na imani hiyo ya kumpenda sana Richard kuliko mwanaume yoyote chuoni pale, aliwakataa wanaume wengi sana, kila kitu alichokuwa anakifanya alikifanya kwa ajili ya Richard.
Kipindi ambapo zilianza kuvuma tetesi chuoni kuwa Richard na Monalisa walikuwa wakitoka kimapenzi alizikataa, hakutaka kuamini kirahisi bila kujua kuwa huo ndiyo ukweli uliyokuwa ukiendelea nyuma ya pazia.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
***
Katika mapenzi hakuna kitu kibaya kama kumpenda mtu ambaye hakupendi, kumthamini mtu ambaye hakuthamini, Kumjali mtu ambaye hakujali, hatambui thamani yako kwake baada ya kukutumia.
Hakuna maumivu makali ya moyo kama kuwa na mapenzi ya dhati na mtu ambaye nyuma ya pazia anakusaliti. Huo ndiyo huwa mwanzo wa maumivu ya mapenzi, kuna muda unaweza ukafikia mtu usitamani kabisa kupenda, moyo ukajenga chuki ukamuona kila mwanaume au mwanamke ni adui yako.
Waliyosema mapenzi ni upofu hawakukosea na hivi ndivyo ambavyo ilikuwa kwa Evelyne, licha ya kuzisikia tetesi juu ya Richard lakini hakutaka kuziamini, alimuamini mno mwanaume huyo.
Adela, Mary pamoja na Penina hawa ndiyo walikuwa wasichana wa kwanza kumpa taarifika hizo Evelyne, walitumia kila njia ya kumueleza ukweli uliyokuwa ukiendelea kati ya Richard na Monalisa lakini Evelyne hakuwaamini.
“Huo ndiyo ukweli shosti Richard sasa hivi sio wako tena,” alisema Mary, wakati huo walikuwa kwenye kimbweta, ulikuwa ni muda ambao hawakuwa na kipindi darasani.
“Umemaliza?” aliuliza Evelyne huku akionekana kuyapuuzia maneno ya Mary, hakutaka kuyaamini.
“Monalisa sasa hivi ndiyo ameichukua nafasi yako, huna chako tena,” alisema Penina kwa sauti ya juu kidogo.
“Lakini mimi naona tumuache, tusiendelee kumlazimisha auamini ukweli ambao siku si nyingi utakuwa wazi,” alisema Adela huku akionekana kumkomoa Evelyne.
Kila neno alilokuwa akiambiwa Evelyne hakutaka kuliamini, alipuuzia na mwisho wa siku aliendelea kusoma kama ilivyokuwa kawaida yake. Alikuwa ni msichana mwenye mapenzi ya dhati mno kwa mpenzi wake huyo ambaye tayari alikuwa ameshamsaliti.
“Siwezi kuamini kama Richard anaweza akanisaliti, siamini,” alisema Evelyne alipokuwa ndani ya chumba chake, wakati huo Happy alikuwa akimtazama.
“Evelyne hivi unajua kuwa lisemwalo lipo na kama halipo basi jua linakuja,” alisema Happy huku akiendelea kumtazama Evelyne ambaye alionekana kuwa amekufa ameoza kwa Richard.
“Happy nafikiri unamfahamu Richard vizuri, sio mgeni kwako, nadhani unajua ni wapi nilipotoka naye hivi unaweza ukaamini hiki ninachokisikia kuwa ananisaliti?”
“Lakini wanaume sio watu wa kuwaamini kiasi hiko.”
“Sio kwa Richard lakini.”
“Umemuuliza?”
“Kuhusu nini?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kuhusu hizi habari?”
“Hapana.”
“Halafu mbona yeye na Monalisa leo hawajaingia chuo?”
“Aliniambia anajisikia vibaya hivyo ameshindwa kuja.”
“Na Monalisa?”
“Sijui kuhusu habari zake.”
“Mmh!” aliguna Happy.
Alichoamua kukifanya Evelyne ni kuichukua simu yake ya mkononi kisha akampigia Richard, alihitaji kufahamu hali yake kwa wakati huo lakini kitu cha kushangaza simu ya Richard ilikuwa ikiita bila kupokelewa, alianza kuingiwa na hofu kubwa moyoni, hakujua ni nini kilichokuwa kimemkuta mpenzi wake ambaye alimuambia kuwa anaumwa.
“Mungu wangu.”
“Nini?”
“Richard hapokei simu.”
“Umejaribu kupiga namba zake zote?”
“Ndiyo nimepiga lakini hapokei,” alijibu Evelyne huku hofu ikiwa tayari imemuingia, alianza kujiwa na hisia mbaya kwa mpenzi wake huyo kuwa pengine alikuwa amezidiwa kiasi cha kulazwa hospitalini. Kichwani mwake wazo la kuwa pengine Richard alikuwa na mwanamke mwingine na hiyo ndiyo sababu ya yeye kutopokea simu hakutaka kuliwazia.
***
Moyo wa Richard ulikuwa katika hofu kubwa mno, hakutaka kuamini kama kweli alikuwa amemsaliti Evelyne tena katika mazingira ambayo hakuyategemea.
“Nadhani biashara yetu imeishia hapa,” alisema Richard alipoamka asubuhi na kumkuta Monalisa akiwa tayari ameshajiandaa na kwa wakati huo alikuwa ameketi kitandani huku akiiperuzi simu yake.
“Itaisha vipi wakati mimi na wewe tayari ni wapenzi?” aliuliza Monalisa huku akijibebisha.
“Monalisa unajua unanichanganya kwani haya ndiyo yalikuwa makubaliano yetu?”
“Mimi sijui ila fahamu kuwa sisi tumeshakuwa wapenzi.”
“Acha utani Monalisa.”
“Tangu lini nimeanza utani na wewe?”
“Monalisa lakini si unajua kuwa mimi nina mpenzi wangu na ninampenda sana.”
“Hilo silijui kama kweli ulikuwa unampenzi na unampenda kwa nini umekubali kumsaliti, kwa nini umekubali kunikubaliana ombi langu.”
“Unasemaje?”
“Tayari umeshakuwa mpenzi wangu,” alijibu Monalisa huku akitabasamu.
Richard alikurupuka pale kitandani kisha akaanza kuitafuta simu yake, hakuiona ilibidi amuulize Monalisa.
“Simu yangu iko wapi?”
“Ninayo.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Naiomba.”
“Siwezi kukupa,” alijibu Monalisa kisha akaamka pale kitandani akatoka nje huku akiwa anakimbia, Richard alishindwa kumfuata Monalisa kwani kwa wakati huo alikuwa uchi wa mnyama, alibaki pale kitandani huku akilalamika, alijilaumu mno kwa kufanya kosa la kumsaliti mpenzi wake ambaye aliamini kwa vyovyote alikuwa anaenda kumpoteza katika maisha yake huku sababu kubwa ikiwa ni Monalisa msichana ambaye tayari alionekana kuwa sumu ya penzi hilo.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment