Simulizi : Machungu Ya Usaliti
Sehemu Ya Tano (5)
Moyo wa Evelyne ulihamisha mapenzi kutoka kwa Richard kwenda kwa mwanaume mwingine ambaye alikuwa ni Fredrick, hakutaka kusikia lolote kutoka kwa mwanaume huyo ambaye alizidi kuiteka akili yake, alimuona kuwa kama Malaika ambaye alishusha kwa ajili ya kumfariji kwa maumivu aliyokuwa ameyapata.
Mpaka kufikia kipindi hicho alikuwa bado hajaonana na Fredrick, aliishia kumuona kwenye mtandao wa Intagram na kuwasiliana naye kwenye simu, muda mwingine walikuwa wakitumiana picha WhatsApp.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Fredrick alikuwa akiishi Daresalaam maeneo ya Tabata Segerea lakini pia alikuwa ni mfanyakazi katika kampuni moja binafsi iliyokuwa ikijihusisha na mambo ya Bima.
Alizidi kuiteka akili ya Evelyne bila kujijua na kila siku penzi lao lilizidi kuota mizizi. Katika moyo wa Evelyne hakukuwa na nafasi ya mwanaume mwingine zaidi ya Fredrick mwanaume ambaye alitokea kumpenda bila kujua sababu.
“Nitakuona lini mpenzi?”
“Usijali utaniona tu.”
“Lini?”
“Wikiendi hii.”
“Kweli?”
“Ndiyo uhakika.”
“Nitafurahi bebi.”
“Hata mimi nitafurahi pia.”
“Kwa nini?”
“Kwa sababu nitakuona kiuhalisia, nitaushuhudia uzuri wako kwa macho lakini pia nitapata nafasi ya kukushika.”
“Nakupenda Fredick natamani hata kesho nikuone jamani.”
“Usijali tumuombe Mungu atufikishe salama Jumamosi hii tuonane.”
“Ameen.”
Walimaliza kuzungumza kwenye simu huku kila mmoja wao akionekana kutawaliwa na furaha kwa kuzungumza na mwenzake. Walipanga wikiendi ya wiki hiyo wakutane na ndiyo ilikuwa siku yao ya kwanza ambayo walikuwa wanaenda kuonana tangu walipoanzisha mahusiano yao ya kimapenzi mtandaoni.
Japo hawakuwahi kuonana lakini walipendana sana, walifarijiana, walishauriana, waliahidiana mambo mengi sana kama wapenzi. Picha za Fredrick alizomtumia Evelyne pamoja na sauti yake ya upole iliyosanjari na maneno yake ya faraja yalitosha kabisa kumteka Evelyne, kila alipokuwa akizitazama picha za mwanaume huyo aliona alikuwa na kila sababu ya kumpenda.
“Kwa hiyo Richard hana lake tena?” aliuliza Happy.
“Ndiyo naweza kusema hivyo,” alijibu Evelyne.
“Lakini kwa nini umeshindwa kumsamehe huoni kama utakuwa umemuhukumu bure?” aliuliza Happy.
“Nimeshamsamehe lakini siwezi kurudiana naye,” alijibu Evelyne.
“Huyo Fredrick atakusaidia nini, kwa nini usirudiane na Richard ambaye umetoka naye mbali na amekiri makosa yake?”
“Siwezi Happy.”
“Mapenzi ya mtandaoni hayadumu, huyo Fredrick atakuchezea mwisho wa siku akuache.”
“Siamini kama anaweza kunifanyia hivyo.”
“Kwani umeshaonana naye?”
“Hapana ila wikiendi hii nakwenda kuonana naye.”
“Unamjua?”
“Ndiyo amenitumia picha zake.”
“Unaamini vipi kuwa ndiyo yeye je, kama amekudanganya?”
“Ndiyo yeye nina uhakika.”
“Kuwa makini,” alisema Happy.
Licha ya mambo yote yaliyokuwa yametokea lakini bado Happy alitamani Evelyne arudiane na Richard, hakutaka kuona wawili hao wakitengana, mwanzoni alihisi labda zilikuwa ni hasira za Evelyne na mwisho wa siku zingeisha na kuweza kurudiana na mpenzi wake lakini hilo halikuweza kutokea. Evelyne alikuwa tayari ameanzisha mahusiano na mwanaume mwingine.
Hatimaye siku ya Jumamosi iliweza kufika, Fredrick alimpigia simu Evelyne na kumwambia kuwa siku hiyo walitakiwa kuonana nyumbani kwake, Evelyne hakutaka kuamini siku hiyo alikuwa anaenda kuonana na mwanaume aliyekuwa anampenda.
Hakutaka kupoteza muda alijiandaa haraka, alipomaliza kujiandaa safari ya kuelekea Tabata Segerea akaianza. Moyo wake ulikuwa na furaha muda wote kila alipomkumbuka Fredrick, katika mawazo yake aliunda taswira ya Fredrick ambaye alikuwa akizungumza. Mapigo ya moyo wake yalikuwa yanamuenda mbio, hakutaka kuamini hata kidogo kama alikuwa anaenda kukutana na mwanaume huyo.
Baada ya kupita dakika arobaini alikuwa tayari ameshafika Tabata Segerea, alimpigia simu Fredrick kumjulisha kuwa tayari alikuwa ameshafika, haikuchukua dakika chache Fredrick aliweza kufika, walipoonana kwa mara ya kwanza walikumbatiana, Evelyne hakuamini macho yake kama aliweza kumuona Fredrick mwanaume ambaye aliishia kumuona Instagram na kuzungumza naye kwenye simu. Ilikuwa ni zaidi ya furaha kwa wawili hao kuweza kukutana.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Fredrick alimpeleka Evelyne nyumbani kwake alipokuwa anaishi, siku hiyo Evelyne kila kitu alichokuwa akikiona kwa Fredrick kiliweza kumshangaza, licha ya umri mdogo aliyokuwa nao mwanaume huyo lakini alikuwa tayari ameshajipanga kimaisha.
“Hapa ni kwako?” aliuliza Evelyne alipoingia nyumbani kwa Fredrick.
“Hapana ni kwako pia,” alijibu Fredrick huku akimtazama Evelyne ambaye kwa muda huo alikuwa akitazama samani zilizokuwa ndani ya nyumba hiyo.
Fredrick hakutaka kumuacha Evelyne aendelee kumuuliza maswali mengi kwa wakati huo, alichoamua kukifanya ni kumuuliza aina ya kinywaji ambacho alikuwa anatumia baada ya kuketi katika sofa.
“Unatumia Juisi, maziwa au soda?” aliuliza Fredrick huku akimtazama Evelyne.
“Niletee chochote,” alijibu Evelyne kwa sauti ya aibu.
“Ndiyo maana nikakutajia inabidi uchague kimoja wapo hapo,” alisema Fredrick.
“Ok basi niletee juisi.”
“Unapenda ya tunda gani?”
“Lolote lile mimi natumia,” alijibu Evelyne kisha Fredrick akaenda kumletea.
Evelyne hakutaka kuamini kama kweli mwanaume huyo alikuwa peke yake siku zote hizo, huo ulikuwa ni wasiwasi uliyoanza kumuingia mara baada ya kuyaona mazingira ya nyumba hiyo jinsi yalivyokuwa mazuri.
“Karibu,” alisema Fredrick baada ya kurudi, mikononi alikuwa amebeba glass mbili, moja ilikuwa ni ya juisi na nyingine ilikuwa ni ya maziwa. Alipomkaribia Evelyne alimpatia ile glass ya juisi halafu na yeye akaketi pembeni yake, mkononi alikuwa amebakiwa na glass ya maziwa. Wakaanza kunywa taratibu huku wakitazamana kwa macho ya kuibianaibiana.
“Nikuulize kitu?” aliuliza Evelyne.
“Ndiyo niulize,” alijibu Fredrick.
“Kwani unaishi na nani hapa?”
“Mwenyewe.”
“Una uhakika?”
“Ndiyo.”
“Hauna mwanamke mwingine kweli?”
“Atokee wapi wakati tayari nipo na wewe.”
“Fredrick niambie ukweli usinidanganye.”
“Niamini upo peke yako katika moyo wangu,” alisema Fredrick.
Kila maneno aliyokuwa akiyasema Fredrick yalizidi kumteka Evelyne, alijikuta akikosa la kusema, alibaki akimtazama mwanaume huyo ambaye alitofautiana mambo mengi sana na Richard.
***
Monalisa hakuishia kumpenda Richard pale chuoni, kila mwanaume mwenye pesa na muonekano mzuri ambaye alijitokeza mbele yake alikuwa akianzisha mahusiano naye na hiyo ndiyo ilikuwa tabia yake. Hakukuwa na watu waliyokuwa wakifahamu hilo zaidi ya marafiki zake Penina, Adela pamoja na Mary.
Tabia yake hiyo ya kuwachanganya wanaume ndiyo iliyosababisha mpaka akapata mimba ambayo hakuwa anamfahamu baba halisi, hakuwa na njia nyingine ya kufanya zaidi ya msingizia mimba hiyo Richard mwanaume ambaye tayari alikuwa ameshafanya naye mapenzi.
Richard baada ya kupewa taarifa hizo za ujauzito hakutaka kukataa, alikubali huku akiamini ulikuwa ni ujauzito wake.
Hakutaka kuamini kama kweli alikuwa amempa ujauzito msichana huyo ambaye moyo wake haukumpenda, alizidi kujilaumu mno baada ya kukumbuka kuwa msichana huyo ndiye alikuwa sababu ya kumgombanisha na mpenzi wake na kwa wakati huo tayari alikuwa ameanzisha mahusiano na mwanaume mwingine.
Tukio hilo bado liliendelea kumuumiza sana moyo wake, hakutaka kuamini kile kilichokuwa kimetokea, alihisi alikuwa katika ndoto lakini haikuwa hivyo, kila kitu kilichokuwa kimetokea ndiyo ulikuwa ukweli halisi.
Alitamani kuwaeleza ukweli wazazi wake kwa kile kilichokuwa kimetokea kuhusu Monalisa mpaka kufikia hatua ya kumpa ujauzito lakini alipokumbuka maswali ambayo angeweza kuulizwa na Mama yake kuhusu Evelyne alighairi kufanya hivyo.
Alipokuwa akimuona Monalisa chuoni moyo wake ulizidi kumchukia, alimuona kuwa msichana aliyeyaharibu mahusiano yake na mpenzi wake, kitu kibaya zaidi alikuwa ameubeba ujauzito wake na hilo ndilo lilizidi kumchanganya akili yake bila kujua kuwa alisingiziwa ujauzito huo haukuwa ni wake.
****
Penzi kati ya Fredrick na Evelyne lilizidi kupamba moto, hakukuwa na tatizo lolote kati yao, tangu walipoweza kukutana siku ya kwanza mapenzi yao yalizidi kuongezeka.
Fredrick alikuwa ni mwanaume wa tofauti sana, alifanya kila awezalo ilimradi ahakikishe msichana huyo anapata furaha, hakutaka kuona anakuwa sababu ya kumuumiza bila sababu, hakutaka kuona tukio hilo linatokea hata mara moja, alihakikisha anamtimizia kila kitu alichokuwa akikihitaji katika mapenzi, hata hivyo mbali na yote hayo ndoto yake kubwa ilikuwa ni siku moja kuja kufunga pingu za maisha na msichana huyo pale pindi ambapo angeweza kumaliza chuo na kufanikiwa kupata kazi.
Sehemu ya 11.
Evelyne alizidi kutekwa na mapenzi ya Fredrick, muda wote furaha ndiyo ilikuwa imemtawala, hakuona sababu ya kuyachukia tena mapenzi, aliyapenda na moyo wake ulikuwa ukimpenda Fredrick tu.
“Una nini wewe mbona unacheka mwenyewe?” aliuliza Happy.
“Hakuna kitu,” alijibu Evelyne.
“Umeanza kuchanganyikiwa?”
“Hapana kuna kitu nimekikumbuka ndiyo kimefanya nimecheka.”
“Kitu gani?”
“Ni kuhusu Fredrick.”
“Mwenzetu ndiyo tayari umeshakolea kiasi hicho?”
“Yeah! nampenda sana na ninaimani hata yeye pia ananipenda.”
“Unajua siku hizi umebadilika sana tofauti na siku zote.”
“Nimekuwaje?”
“Umekuwa ni mtu wa kufurahi tu kila wakati.”
“Nimeipata furaha, nimeipata amani sasa kwa nini nisifurahie?”
“Kweli huyo mwanaume amekuteka,” aliniambia Happy.
****
Adela alifahamu kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika maisha ya Monalisa, hakuipenda tabia ya rafiki yake huyo ambaye kila mwanaume mwenye pesa na muonekano mzuri aliyejitokeza mbele yake alikuwa akianzisha mahusiano naye. Alikuwa ametembea na wanaume wengi sana na mpaka kufikia wakati huo alikuwa amepata ujauzito na hakujua ulikuwa ni wa nani zaidi alichoamua kukifanya nikumsingizia Richard kwa kuwa tayari alikuwa ameshalala naye, alihitaji kutumia pesa zake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alichoamua kukifanya Adela ni kutafuta muda wa kukutana na Richard kisha akahitaji kumueleza kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
“Kuna nini?” aliuliza Richard.
“Nahitaji kuzungumza na wewe,” alijibu Adela.
“Ni mazungumzo ya umuhimu?” aliuliza Richard.
“Ndiyo ni muhimu sana,” alijibu Adela.
Baada ya kujibiwa hivyo Richard hakutaka kupoteza muda alichoamua kukifanya ni kumpa nafasi msichana huyo ya kumsikiliza kile alichokuwa amedhamiria kumwambia kwa wakati huo.
“Ok, nakusikiliza niambie,” alisema Richard.
“Richard najua unatembea na rafiki yangu, hilo sio jambo la siri tena ila kuna kitu kimoja nahisi haukifahamu na kinaniumiza sana,” alisema Adela.
“Kitu gani?” aliuliza Richard.
“Monalisa hakupendi isipokuwa amekutamani, tamaa zake za kimwili ndiyo zimempelekea mpaka akakuharibia mahusiano yako,” alijibu Adela huku akionyesha msisitizo wa maneno yake.
“Mbona sijakuelewa ni nini unachokimaanisha?” aliuliza Richard.
“Monalisa sio msichana sahihi kwako, hastahili kuwa mpenzi wako ni muuaji yule,” alijibu Adela.
“Bado sijakuelewa.”
“Ninachotaka kukuambia ni kwamba ule ujauzito wa Monalisa sio wako,” alisema Adela.
Maneno hayo yalimchanganya sana Richard, alishindwa kuelewa ukweli wa maneno yale, kama ule haukuwa ujauzito wake ulikuwa ni wa nani. Hili ndilo lilikuwa swali pekee lililokuwa linamuumiza kichwa chake, hakujua nyuma ya pazia kama alishiriki mapenzi na msichana ambaye kwake kitendo cha kuwabadilisha wanaume kama nguo kilikuwa ni cha kawaida.
“Unasemaje?” aliuliza kwa mshangao.
“Huo ndiyo ukweli,” alijibu Adela lakini kama haitoshi aliamua kumsimulia kila kitu kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia.
****
Taarifa za ujauzito wa Monalisa zilisambaa chuo kizima, hakukuwa na siri juu ya uhusiano wake na Richard, kila mtu alifahamu kuhusu habari za wawili hao. Waliyomfahamu Richard walimlaumu sana kwa kitendo alichokuwa amekifanya cha kumsaliti mpenzi wake kisha akaanzisha mahusiano na msichana mwingine ambaye tayari alikuwa amembebesha ujauzito. Jambo hilo lilizidi kumfanya achukiwe na baadhi ya watu.
“Jamaa karuka mkoja kakanyaga mavi,” alisema mwanachuo mmoja.
“Hili ndilo tatizo letu sisi wanaume hatuwezi kutulia na mwanaume mmoja,” alisema mwanachuo mwingine.
Hakukuwa na kitu kilichokuwa kikiwakasirisha watu kama kusikia kuwa msichana huyo aliyelisambaratisha penzi la Evelyne alikuwa amebeba ujauzito.
Baada ya kuzisikia taarifa hizo Happy na yeye alianza kumchukia Richard, hakutaka kuzungumza naye, aliamua kuwa upande wa rafiki yake na kuanzia siku hiyo alimuunga mkono kwa uamuzi aliyokuwa ameuchukua wa kuanzisha mahusiano na Fredrick.
Alifahamu ni maumivu kiasi gani aliyokuwa ameyapata hivyo kwa uamuzi aliyokuwa ameuchukua aliamini uliweza kumpunguzia maumivu hayo.
“Yaani pamoja na uchafu aliyoufanya ameona haitoshi ameamua bora ampe ujauzito kabisa,” alisema Happy.
“Wanaume ndivyo walivyo hawaridhiki,” alisema Evelyne.
“Nimemchukia sana.”
“Sio wewe tu hata mimi sitaki kuzungumza naye,” alisema Evelyne.
Mpaka kufikia hapo hakukuwa na mtu aliyefahamu ni nini kilichokuwa kikiendelea, wanachuo walimchukia sana Richard kwa ujinga aliyokuwa ameufanya wa kumsaliti mpenzi wake.
Ilikuwa imebakia miezi miwili ili waweze kufanya mitihani ya kumaliza degree yao, kila mwanachuo alionekana kuwa bize na kusoma kwa ajili ya kujiandaa na mitihani hiyo.
Kwa upande wa Richard hali ilikuwa tofauti, alijitahidi kujisomea lakini badala ya kuelewa alichokuwa akikisoma ndiyo kwanza mawazo yake yalikuwa yakitafakari ukweli aliyoelezwa na Adela kuhusu ujauzito wa Monalisa.
Alihisi kuchanganyikiwa kila alipokuwa akiyakumbuka maneno ya Adela, alitumia pesa nyingi mno kwa ajili ya Monalisa, hakutaka kuamini kama msichana huyo aliyedai kuwa anaujauzito wake hakuwa muaminifu, alishiriki mapenzi na wanaume wengi na mpaka kufikia wakati huo ujauzito haukuwa ni wake. Hilo liliendelea kumuumiza sana moyo wake, alijiona kuwa mwanaume mwenye mikosi kila kukicha.
***
Mwezi wa kwanza ulikatika huku wanachuo wakiendelea kujiandaa na mitihani yao, mwezi wa pili nao ukakatika, hatimaye wiki ya kwanza ya mitihani ikaanza. Wanachuo wakaanza kuifanya mitihani yao ambayo iliwachukua takribani mwezi mzima kuweza kuimaliza.
Ilikuwa ni furaha kwa kila mwanachuo kuweza kumaliza salama mitihani hiyo, kila mwanachuo alimshukuru Mwenyezi Mungu kutokana na hatua waliyokuwa wameifikia. Kama kawaida pia hawakuacha kupongezana, sherehe mbalimbali ziliandaliwa kama ishara ya kupongezana kwa kufanikiwa kumaliza masomo yao salama.
Wiki moja baadaye Richard aliamua kumueleza ukweli Monalisa juu ya taarifa alizozisikia kuhusu ujauzito huo kuwa haukuwa ni wake, alipokuwa akimueleza hayo macho yake yalikuwa yakitoa machozi. Alishindwa kuyavumilia maumivu ambayo moyo wake ulikuwa ukipitia.
Monalisa alibaki kinywa wazi baada ya kusikia maneno hayo kutoka kwa Richard, hakutaka kuamini kama alifahamu kila kitu kilichokuwa kikiendelea, siri ambayo aliamini ilikuwa ni vigumu kufichuka kwa wakati huo ilikuwa tayari imeshafichuka.
Swali ambalo alianza kujiuliza ni rafiki yake gani ambaye alimgeuka na kumueleza Richard kila kitu, hakupata jibu hata alipoamua kumuuliza Richard hakuwa tayari kumuweka wazi. Hilo lilizidi kumshangaza sana, alichanganyikiwa, hakutaka kuamini kama alikuwa ameshagundulika.
“Sidhani kama nitakuwa ninanafasi ya kuendelea kuwa na wewe, naomba huu ndiyo uwe mwisho wetu, umeniharibia mahusiano yangu vya kutosha, please naomba uniache, niache Mona na maisha yangu,” alisema Richard kwa sauti ya uchungu, machozi yalikuwa yakimbubujika.
“Hapana Richard usiseme hivyo, nakupenda, nakupenda tena sana na ndiyo maana nimefanya yote haya kwa sababu yako, sikutaka nikupoteze kirahisi kiasi hiki. Richard ni kweli huu ujauzito sio wako lakini naomba unisamehe bado naamini nina nafasi ya kufanya kitu kwa ajili yako,” alisema Monalisa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kila alipokuwa akimtazama Richard alivyokuwa akilia mbele yake alijisikia vibaya mno, alimkosea sana, alimfanyia kila aina ya uhuni, alimchanganya na wanaume wengi sana ambao alikuwa akitembea nao kwa ajili ya kuwachuna, hakuwa na mapenzi ya dhati, huo ndiyo ulikuwa ukweli lakini alipogundua kuwa siri hiyo ilifichuka alizidi kujisikia vibaya.
Hakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kumuomba msamaha na kumuahidi kufanya kitu kwa ajili yake, licha ya mambo yote ambayo alikuwa amemfanyia lakini hakutaka kuona akimpoteza mwanaume huyo, aliendelea kuushikilia msimamo wa kumpenda zaidi kila kitu katika dunia hii.
Richard alipomuona Monalisa mbele yake pamoja na maneno ambayo alikuwa akiyazungumza yalizidi kuweka katika wakati wa hasira, alimuona kuwa adui mkubwa sana wa maisha yake, alimchukia mno.
“Sijui nikuambie nini mpenzi?”
“Usiniambie kitu, sitaki kusikia lolote kutoka kwako ni bora uendelee kukaa kimya.”
“Hapana Richard usiseme hivyo utazidi kuumiza moyo wangu.”
“Mona kwa uliyonifanyia inatosha, nashindwa kuvumilia, moyo wangu haukuhitaji.”
“Richard hunipendi?”
“Ndiyo sikupendi Mona,” alijibu Richard.
Monalisa alizidi kuchanganyikiwa baada ya kuyasikia majibu hayo, hakutaka kukubaliana na ukweli wa kile kilichokuwa kimetokea. Alijitahidi sana kumbembeleza, muda mwingine alikuwa akimlilia lakini yote hayo bado hayakuweza kuwa sababu iliyomfanya Richard akubali kuendelea kuwa naye.
Alimpenda sana mwanaume huyo, alitamani kumuona kila wakati akiwa naye. Baada ya kuona Richard ameshindwa kumsamehe uamuzi aliyoamua kuuchukua ni kuutoa, aliamini ujauzito huo ndiyo ulikuwa sababu ya yeye kuchukiwa na Richard. Hakutaka kupoteza muda haraka alipanga mipango ya kuutoa ujauzito huo na hatimaye aliweza kufanikiwa kuutoa salama.
Furaha ilizidi kumtawala, aliamini huo ndiyo ulikuwa muda wake muafaka wa kuweza kumuomba msamaha Richard kisha akaweza kumsamehe, hilo lilikuwa ni jambo gumu mno kwa Richard kuweza kutokea licha ya msichana huyo kuwa ni mzuri.
***
Baada ya kupita miezi kadhaa hatimaye Evelyne pamoja na Happy walifanikiwa kupata kazi katika moja ya kampuni iliyokuwa ikiwalipa wazuri. Richard na yeye kutokana na utajiri aliyokuwanao baba yake aliweza kuachiwa kampuni aweze kuiongoza. Kwa upande wa Monalisa pamoja na marafiki zake na wao pia walifanikiwa kupata kazi katika moja ya kampuni hapa mjini.
***
Fredrick aliamua kujitambulisha kwa wazazi wake Evelyne pamoja na kumtambulisha mpenzi wake, hakutaka kufanya utani hata mara moja, baada ya kufuata taratibu zote aliamua kumvalisha pete ya uchumba na baadae kufunga naye ndoa kabisa.
Evelyne hakuamini kama aliweza kupata mwanaume ambaye alimpenda na kumthamini kiasi kile, alizidi kumpenda sana mwanaume huyo ambaye kila kitu alichokuwa akikifanya hapa duniani alikifanya kwa sababu ya mapenzi yake.
Taarifa hizo za Evelyne kuolewa na Fredrick ziliweza kumfikia Richard, alipoambiwa kwa mara ya kwanza mapigo ya moyo wake yalimuenda mbio, hakutaka kuamini, alihisi kutaniwa.
Alibaki katika simanzi baada ya kuthibitisha ukweli wa taarifa hizo, zilizidi kumuumiza mno moyo wake. Kila alipomkumbuka Evelyne wakati alipokuwa ofisini machozi yalikuwa yakimbubujika muda wote, taswira ya msichana huyo ikajijenga upya akilini mwake, alishindwa kufanya kazi kabisa siku hiyo.
Hisia za mapenzi bado ziliendelea kumuumiza, kichwa chake kilikataa kabisa kumsahau Evelyne.
Muonekano wake mzuri uliendelea kuwatesa wasichana waliyokuwa katika kampuni yake hiyo, wote walimtetemekea. Kama kulikuwa kuna uwezekano wa kutokea walau siku moja kila moyo wa msichana katika kampuni hiyo kusema chochote, hakika sauti za maombi ya kumuhitaji Richard ndiyo zingesikika ndani ya ofisi nzima, hakukuwa na msichana ambaye alipomuona Richard moyo wake haukuacha kushtuka, ulimuhitaji mno mwanaume huyo.
Kama kawaida maneno na mabifu ya chinichini hayakuacha kuwepo kwa wasichana hao, walijikuta wakiingia katika ugomvi na chuki kila wakati, sababu ikiwa ni Richard. Msichana aliyepata bahati ya kutolewa lunch na Richard aliitumia nafasi hiyo katika kuwaumiza roho wafanyakazi wenzake, hilo lilizidi kutengeneza chuki kati yao.
Licha ya kuwepo na mambo yote hayo ofisini lakini hakukuwa na msichana aliyebahatika kuumiliki moyo wa Richard, kila siku waliishia kumpelekea zawadi na mialiko mingi ambayo haikuweza kuzaa matunda yoyote.
"Ni Mzuri ndiyo tena anavutia mno ila sijakuelewa kwani nini unachokitaka hasa kwa Boss?" Aliuliza msichana mmoja.
"Sijui niseme nini, sijui nianzie wapi kukuelezea ila kwa kifupi nampenda sana, natamani siku moja ajue ni jinsi gani moyo wangu unavyomuhitaji," alijibu msichana mwingine ambaye alizungumza kwa hisia.
Kitendo cha wasichana kuamini siku moja kufanikiwa kulimiliki penzi la Richard kilibaki kuwa ndoto, ulikuwa ni ukweli uliyowaumiza mno.
Maisha ya Richard yalikuwa mazuri kwa upande wake lakini upande mwingine alijiona kukosa bahati, licha ya kuwa alifanikiwa kununua nyumba maeneo ya Mbezi, kumiliki pesa, kutembelea gari la kifahari lakini tukio la kumpoteza Evelyne kilimuacha na pigo kubwa mno.
Alifahamu kwa wakati huo msichana huyo alikuwa ni mke wa mtu lakini bado alijipa matumaini ya kuwa naye siku moja, moyoni hakutaka kukubaliana na ukweli, alijiapiza kufanya lolote ili aweze kulirudisha penzi lake.
"Nitatumia kila nilichonacho, kama ni pesa, nguvu hata kwa kumwaga damu ilimradi urudi kwangu, sikubali na siwezi kuvumilia maumivu na mateso haya ninayoyapata katika moyo wangu," alijisemea Richard alipokuwa nyumbani kwake, wakati huo alikuwa akiitazama picha ya Evelyne kwenye simu. Ilizidi kumuumiza mno.
Alijitahidi kuvumilia, kuficha kwa kipindi kirefu lakini kuna muda uzalendo ulimshinda. Akatamani kuwaeleza wazazi wake ukweli kwani katika kipindi hicho tayari walishaanza kumuuliza kuhusu mipango yake ya kufunga ndoa na Evelyne.
Alihisi kuchanganyikiwa kila alipokuwa akiulizwa kuhusu Evelyne, wazazi wake hawakufahamu kilichokuwa kimetokea hivyo walionekana kumuhitaji sana msichana huyo.
Baada ya kuona wazazi wake wamezidi kumsumbua sana kuhusu suala hilo la kumuoa Evelyne ilibidi awaeleze ukweli wa kilichotokea kati yake na msichana huyo ambaye kwa wakati huo alikuwa ni mke wa mtu, zilikuwa ni taarifa zilizowashtua wazazi wake, hawakutaka kuamini walichokuwa wakiambiwa.
"Umefanya ujinga gani mwanangu?" Aliuliza Mama yake, hakuishia kuuliza swali tu isipokuwa alianza kumlaumu kwa kosa alilokuwa amelifanya hata kwa upande wa baba yake Mzee Gombanila na yeye alimlaumu pia.
Richard alipoona lawama zimezidi kuwa nyingi aliamua kuondoka nyumbani kwao, alipokuwa barabarani kichwa chake bado kilitawaliwa na mawazo mengi sana, hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kuyatatua. Kuna kipindi alijikuta akilipa faini kwa kosa la uzembe wake mwenyewe barabarani.
Licha ya kuwa na maisha mazuri, kutamaniwa na wasichana lukuki lakini alipokumbuka yaliyomtokea katika maisha ya kimahusiano hakutaka kumkabidhi msichana mwingine moyo wake, aliogopa mno.
**
Fredrick na Evelyne walizidi kuyafurahia maisha ya ndoa yao, kila wakati furaha iliendelea kushika hatamu.
Baada ya kupita miezi miwili, siku moja majira ya jioni Fredrick alipokuwa akirudi nyumbani kwake Tabata, alipata ajali mbaya sana maeneo ya Ubungo mataa, gari yake ndogo aina ya Toyota Harrier lenye rangi nyeusi liligongana uso kwa uso na lori.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa ni ajali mbaya sana ambayo kila mtu aliyeishuhudia hakutaka kuamini kama angeweza kupona mtu.
Mwili wa Fredrick haukuweza kutambuliwa kwa haraka kutokana na damu zilizokuwa zimetapakaa kila sehemu, wasamaria waliyojitokeza wakamsaidia kumtoa ndani ya gari hiyo iliyokuwa imebondekabondeka na kupoteza umbo lake la kawaida, walijitahidi kadri ya uwezo wao na hatimaye walifanikiwa kumtoa lakini alikuwa amepoteza fahamu.
Baada ya kupita dakika kadhaa polisi waliweza kufika eneo la tukio, kama ilivyokuwa kawaida yao walianza kuwatawanyisha watu, walihitaji kuona usalama wa eneo hilo ukiendelea kuwepo. Wakati polisi wakiendelea kufanya kazi yao ghafla! Ving'ora vya gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) viliweza kusikika na ndani ya dakika chache liliweza kufika eneo la ajali kisha wakamchukua Fredrick ambaye alikuwa katika hali mbaya sana.
Walipomfikisha hospitali taratibu za kuyaokoa maisha yake zilianza kufanyika, wakati huo Evelyne alishapigiwa simu na kwa wakati huo alikuwa njiani akielekea katika hospitali ya Muhimbili, alipofika alionekana kuchanganyikiwa, hakuamini kama Fredrick alikuwa amepata ajali na kwa wakati huo alikuwa katika chumba cha upasuaji akiendelea kupatiwa matibabu.
Baada ya masaa kadhaa kupita, hatimaye majibu yaliweza kutolewa na daktari, kutokana na ajali aliyoipata Fredrick ilimsababishia matatizo katika kizazi chake pamoja na mshtuko aliyoupata ulimpelekea kupooza hivyo katika maisha yake angeshindwa kuamka na kufanya shughuli zake kama ilivyokuwa kawaida na badala yake maisha yake yalibadilika na kuwa ni ya kitandani.
Fredrick alikuwa amelala kitandani, uso wake ulikuwa umetawaliwa na furaha, alizidi kuonekana kuyafurahia maisha yake.
Alimtazama mke wake ambaye machozi yalikuwa yakimdondoka kwa muda huo, Evelyne kila alipokuwa akimtazama mume wake jinsi alivyokuwa amelala kitandani alihisi maumivu makali mno ndani ya moyo wake. Alimpenda sana mume wake, hakutaka kumuona akiendelea kuteseka, alipanga kufanya kila awezalo ili aweze kuyaokoa maisha yake lakini alipoyakumbuka majibu ya daktari kuwa asingeweza kupona, alizidi kuumia mno.
Hakuna maumivu makali kama kumuona yule umpendae akiteseka kwa ugonjwa katika dunia hii, ni zaidi ya maumivu makali mno.
Machozi yaliendelea kumbubujika Evelyne pale hospitalini, hakutaka kuamini kama mume wake alikuwa amepooza na kibaya zaidi alipoteza uwezo wa kupata mtoto. Hilo liliendelea kumuumiza sana moyo wake.
Ilikuwa imepita miezi kadhaa tangu walipofunga ndoa yao, kabla ya kufika hata mwaka tayari ndoa hiyo ilikuwa imeingiwa na tatizo.
Ndugu wa mume wake walipozipata taarifa za ajali hiyo hawakutaka kuelewa chochote, waliamini ilikuwa ni ajali ya kupangwa na ilisababishwa na Evelyne ambaye walidai alizitamani mali za ndugu yao.
Mwanzo wa maneno na vitisho vikaanzia hapo, hakukuwa kuna ndugu upande wa mume aliyekuwa upande wa Evelyne, wote walimchukia.
Kuna muda Evelyne alikuwa akikufuru Mungu, alihisi kuonewa, hakutaka kuamini kama yeye ndiye alikuwa binadamu mwenye makosa mengi zaidi hapa duniani mpaka akafikia hatua ya kupewa matatizo hayo.
"Usilie mke wangu, usilie futa machozi yako," alisema Fredrick.
"Nashindwa kufanya hivyo mume wangu," alijibu Evelyne huku machozi yakiendelea kumdondoka.
Alipokuwa akiendelea kumtazama mume wake pale kitandani machozi yalizidi kumbubujika tu, kila kitu kilibadilika katika maisha yake, alipowakumbuka ndugu wa mume wake alizidi kujisikia vibaya mno, alijua fika hawakumpenda, walimtenga hivyo kila kitu alichokuwa akikifanya kilionekana kuwa kibaya.
Aliamua kuwapigia simu wazazi wake na kuwaeleza kila kitu kilichokuwa kikiendelea, alihitaji msaada wao lakini walionekana kuchukizwa na taarifa hizo, hawakutaka kuona akiendelea kuteseka wakati bado walikuwa hai. Maamuzi ambayo waliamua kuyachukua ni kumuhitaji binti yao arudi nyumbani haraka iwezekanavyo.
"Naomba upande basi kesho uwe umeshafika hapa nyumbani," alisema baba yake kwa sauti ya ukali.
"Nitaondokaje baba halafu nitamuacha Mume wangu na nani?" Aliuliza Evelyne.
"Muache na ndugu zake wewe rudi zako nyumbani," alijibu baba yake kwa msisitizo.
"Hapana baba bado itakuwa ni vigumu kwani nitahitajika pia kazini," alisema Evelyne.
Yalikuwa ni mazungumzo mafupi ambayo yalihitajika utekelezaji wa haraka sana lakini Evelyne hakutaka kukubaliana nayo. Hakutaka kuona akiondoka na kumuacha mume wake akiendelea kuteseka kitandani. Alikumbuka siku yao ya harusi jinsi alivyokula kiapo mbele za watu na kuahidi kuishi naye katika shida na raha, aliamini katika kipindi hicho kilikuwa ni cha shida hivyo hakuwa na jinsi ya kufanya ilibidi amvumilie mume wake.
Rafiki yake Happy hakumtupa mkono katika kipindi hicho, alikuwa na yeye bega kwa bega katika kila hali, alionyesha msaada mkubwa sana. Alipokuwa akimuona Evelyne akiteseka na mume wake hospitalini alimuonea huruma sana, alizidi kumfariji kwa maneno ya matumaini ambayo yalizidi kumpa nguvu. Ndoto yake kubwa aliamini siku moja mume wake angeweza kuinuka kitandani na maisha yakaendelea lakini hilo lilikuwa ni jambo lisilowezekana.
Siku ziliendelea kukatika huku Fredrick na yeye akizidi kuteseka hospitalini, alianza kupoteza matumaini ya kuishi baada ya afya yake kuanza kudhoofika, aliamini ule ndiyo ulikuwa mwisho wa maisha yake, mwisho wenye mateso makali mno.
"Hapana usijiwazie kifo, huwezi kufa mume wangu," alisema Evelyne.
"Angalia ninavyoteseka hapa kitandani mke wangu, madaktari wameshindwa kunitibu hivi unafikiri nitapona kweli?"aliuliza Fredrick huku machozi yakimbubujika.
"Hapana huwezi kufa," alisema Evelyne.
Yalikuwa ni maneno machache lakini aliamua kuishi ndani yake, hakutaka kumpoteza Fredrick, alichoamua kukifanya ni kuanza kuhangaikia matibabu yake.
Madaktari walimshauri ampeleke mume wake nchini India katika hospitali ya Apollo iliyokuwepo nchini humo kwani huko ndipo palipokuwa na uwezekano mkubwa wa mume wake kutibiwa na kupona kabisa.
Alipoambiwa hivyo hakutaka kupoteza muda, alianza kupanga mipango wa kumsafirisha mume wake nchini humo na baada ya kufanyiwa matibabu iligundulika kuwa Fredrick asingeweza kupona.
Hilo lilizidi kumuumiza sana, hakutaka kuamini maneno hayo hata kidogo. Aliporudi nchini Tanzania bado aliendelea kuhangaika na mume wake.
Ilifikia wakati akaanza kuwaamini wachungaji, alipokuwa akisikia palikuwa na mchungaji ambaye aliweza kumuombea kilema kisha akapona aliamua kwenda, kila kanisa alilokuwa akienda kwa ajili ya maombi ya mume wake hakuna miujiza iliyoweza kutendeka.
***
Richard alifahamu kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika maisha ya Evelyne, alimpenda mno msichana huyo, kutokana na hali aliyokuwa nayo aliamini ulikuwa ndiyo muda wake muafaka wa yeye kujitokeza kwa mara nyingine, hakutaka kumuomba msamaha ila alichoamua kukifanya ni kurudi kama rafiki ambaye aliguswa na matatizo yaliyompata Evelyne katika ndoa yake.
Alijitoa katika kila hali na mali, hakutaka kuonekana adui kwa msichana huyo, kila alilokuwa akilifanya alilifanya kwa kuonyesha moyo wa msaada.
Baada ya kupita miezi miwili Fredrick alipoteza maisha, kilikuwa ni kifo ambacho kilimuacha Evelyne na maumivu makali mno, ndugu zake Fredrick waliamua kumshtaki Evelyne polisi na kisha wakamfungulia kesi ya mauaji, ilikuwa ni kesi nzito ambayo ilimuweka Evelyne na hatia ya mauaji lakini kutokana na uwezo wa kifedha aliyokuwa nao Richard alihakikisha anapigana mpaka anafanikiwa kumuweka huru Evelyne.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Richard alimuomba msamaha Evelyne na kumuahidi kuwa muaminifu katika maisha yake yote. Evelyne hakuwa na kipingamizi chochote, aliamua kumsamehe Richard kisha mapenzi yao yakarudi kuwa kama zamani.
Walifanikiwa kufunga ndoa na baada ya mwaka mmoja kupita walifanikiwa kupata mtoto wa kiume, alikuwa ni mtoto mzuri sana, aliyekuwa na afya njema. Evelyne aliamua kumpa jina la Fredrick ikiwa ni kama kumbukumbu ya kumuenzi mwanaume huyo huko alipo.
Kila siku maisha yao yalizidi kutawaliwa na furaha huku mtoto wao akiendelea kukua vizuri bila matatizo yoyote.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment