Search This Blog

Tuesday 1 November 2022

NIKUITE NANI? - 4

 






Simulizi : Nikuite Nani? 
Sehemu Ya Nne (4)




Kitendo hicho kikawa cha mshangazo kwa wamulikwa. Wakatawanyika pasipo mapendo yao kama wezi wafumwapo tukioni. Yule mdada alitoka mbio za riadha, akiwa kausitiri mwili wake kwa vi—nguo vifupi vilivyoacha sehemu kubwa wazi, na kuchangia utamanishaji kwa mwanaume rijali. Askari naye, alirejea bandani haraka. Na kuikumbuka bunduki yake alikoitupia na kujaza akili kuikamata katika mitindo ya kimapigano kama kuna lolote linaloweza kujiri.



Baada ya kuona hivyo, afande Mzee hakuona haja ya uwepo wake mahali hapo. Alitokomea kama kimbunga kwa kukatiza vichochoro tofauti hadi akatokeza anakoishi. Ambako alifikia kuvua nguo na kwenda kuoga kisha kujipumzisha kwa ajili ya mipango mingine siku inayofuata.



Asubuhi kulivyopambazuka, kitu cha kwanza baada ya kupata stafutahi alienda kwenye moja ya studio ya usafishaji picha, akaisafisha, kisha akaendelea na safari hadi maeneo ya Nzovywe kwenye nyumba moja yenye hadhi ya kati. Alibisha hodi, ikaitikiwa. Na sauti ya kike iliyomtanabaisha katoka usingizini dakika chache zilizopita.



Zilichukua dakika mbili, toka abishe hodi hadi alivyokuja kufunguliwa aingie ndani. Akakaribishwa aketi sofani sebuleni, huku mandhari yakimfurahisha vyema, kwamba kaingia sehemu yenye sifa inayostahili kukaliwa na mtu mwenye wadhifa wa aina yoyote.

“Karibu sana afande,” alisema mwenyeji wake aliyemkaribisha. Chitoko Chindume!

“Nishakaribia.”

“Sina hakika kama nishawahi kukutambulisha nyumbani kwangu...”

“Sahihi! Ila kuna watu walinitambulisha siku kadhaa zilizopita. Hivyo ramani yake haikupotea akilini.”

“Mmmmh!...haya, naweza kukusaidia afande wangu,” alisema Chitoko, mara baada ya kuvuta pumzi kwa muda na kuziachia.

“Nina shida ndogo sana kama utanipatia ushirikisho wako.”

“Wala usihofu, nipo huru kukusaidia.”



Kikapita kimya cha sekunde chache, kisha afande Mzee akaufukuza mara baada ya kusafisha koo kwa kutoa kikohozi kidogo.

“Chitoko, unachafua picha ya jeshi letu kwa yale uyatendayo. Wewe ni afisa mwenye hadhi yako. Ila una matendo yasiyolandana na wadhifa huo.”

“Kivipi afande?”

“Biashara unayojihusisha nayo naifahamu.”

“Biashara?”

“Ndiyo! Biashara ya kugeuza mwili wako kuwa kitega uchumi.”

“Hee! Wewe mzee wewe? Ushakuwa mwanga siku hizi? Nawezaje kujiuza? Kwa hili umbo nililonalo unahisi nakosa mwanaume hadi niende viwanja nikajinadishe?”

“Leo nimekuja kukupa onyo, ili utambue mchezo wenu unaenda kufungwa kwa sababu ushabainika. Acha kushirikiana na wale watu, la sivyo utaenda kuishia kubaya. Kwani Abdul ataenda kutoka gerezani,” alisema afande Mzee na kunyanyuka pale alipoketi kuianza safari ya kuondoka. Alipoufikia mlango akakatishwa mwendo na kauli ya Chitoko.

“Kumbe wewe ndiye askari uliyejitosa kumsaidia Abdul? Nikupe pole, kwa sababu hufahamu mchezo huu unahusu nini. Pia, nikupe pole kwa kukawia kutoa msaada. Umechelewa sana. Hata Abdul akitoka, haitosaidia, na ni heri abaki hukohuko kwa sababu atapata machungu atayoshindwa kuyaelezea. Huu ni mchezo, usiohitaji kuaminiana. Endapo utaenda kuonana naye, kamuulize, bado anawakumbuka watu wake wa karibu? Hasa shangazi na baba yake? Akisema ndiyo, basi mwambie, ana saa arobaini na nane tu, za kuwafanya watu hawa wawe huru kuanzia sasa.”



Awali, afande Mzee hakuitilia maanani hii kauli. Akaondoka, ila alivyouacha uga wa nyumba aishiyo Chitoko, kauli ya mwisho kuambiwa ikaanza kujirudia rudia mfululizo akilini. Na kumpatia wakati mgumu wa utambuzi wa nini kimaanichwasho.

__________



Asubuhi ya saa nne, afande Mzee alizuru gerezani. Kwa ombi lake, nami nikapata wasaa wa kutolewa chumba nihifadhiwacho, nikapelekwa chumba kilekile tukutaniacho siku zote tuwapo na jambo la kuzungumza. Kitendo hicho hufanywa kwa usiri mkubwa ijapokuwa afande Mzee alikuwa mwingi wa wadhifa kwa kiasi fulani ndani ya jeshi la polisi kwa jiji la Mbeya.



Ujio wake wa siku hii ukawa tofauti na siku nyingine. Zilizokwisha pita! Wajihi ulimtanabaisha namna alivyo na mengi yenye kumletea udhia moyoni. Ambayo hata kama yatapatiwa maelezo, yatakosa ufumbuzi wa kumfanya fuadi ubaki na amani.

“Ngoma bado nzito kijana wangu,” alinena. Sauti ikikosa ukaramkaji, ulionisukuma kumtia moyo, ili nami niliyoko nyuma ya nondo nipate ahueni kwa kiasi.

“Usikate tamaa mapema hivyo. Tuna nafasi kubwa sana ya ushindi,” nilimsihi.

“Kwa sababu hufahamu ukweli wa kile...” hakumalizia, nikamkatisha.

“Kuna nini? Mbona leo umekuwa wa tofauti hivyo?”

“Baba na shangazi yako ndiyo wamenifanya niwe hivi,” alisema afande Mzee. Kauli iliyosikika kwa utata ndani ya viwambo vyangu vya sikio. Kiasi kwamba nikaipeleka akili yangu sehemu aliyoko shangazi, na kupata ukumbusho wa mazingira niliyotoroka nyumbani.



Nilichukua muda mrefu kufanya kumbukizi. Takribani dakika nne, afande Mzee macho yake yakiwa pima kwangu kunisaili nihangaikavyo na ubadilishaji wa fikra.



Hakika! Siku hii nikapakumbuka nyumbani. Namna nilivyotoroka na mzigo mzito niliowaachia wale waliosalia. Hasa baba, wa kunitafuta sehemu nilipoelekea, mwishowe, nilihisi washapitisha hitma wakiamini nishatoweka duniani. Niliamini hivyo, kwa sababu ya muda mrefu uliopita. Angali nipo mdogo hadi hatua niliyofikia. Chozi likanidondoka!



Katikati ya chozi langu nikapatwa na kumbukizi imhusuyo shangazi. Naye nilimfikiria mazingira aliyonayo kwa wakati huo gerezani ukizingatia umri unazidi kumtupa mkono. Niliumia sana, kiasi kwamba nikajiona mkosefu pekee niliyopo ulimwenguni. Ambaye sistahili tunuku yoyote ya motisha katika uendelezaji wa maisha yangu.



Fikra zikanipeleka mbali kwa kuniaminisha gerezani ndiyo sehemu pekee nayostahili kubaki. Ule mpango wa rufaa niachane nao, kwa sababu nikirudi uraiani hamna cha maana nitachofanya, ukizingatia walioniweka ndani, ni watu waliokuwa sehemu ya uaminifu kwangu. Nipambane na tabu za gerezani, kama mabadiliko, niwabadilishe wafungwa wenzangu ambao hukumu zao zina ukomo, wakirejea uraiani wasiwe na roho ya kisasi.



Milango ya nuru niliiona kwa mbali ikififia. Kiza kikiingia, ishara tosha ya ufahamu mzigo uliopo mbele yangu ni mzito sitoumudu.

“Dawa ya hawa wajinga, wakikamatwa ni kupigwa ki—sawa sawa,” nilijisemeza. Ila ghafla nikatoa kauli nyingine ya utenguzi wa kauli ya awali. Nilikumbuka moja ya kauli ya shangazi.

“Hamnaga suluhu ipatikanayo kwa mapigano,” nilikumbuka. Moja ya kauli pana yenye msukumo wa kuleta amani.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Sauti ya afande Mzee ndiyo ilinishtuza toka kwenye lindi la fikra. Tena sauti iliyojaa maneno makali yaliyotoboa moyo wangu na kujaza ulizo lililoniacha hayawani.

“Uwapendao wamebakiza saa arobaini na nane wahitimishe maisha yao hapa duniani.”

Nikabaki kumtumbulia macho, kana kwamba kaokota shilingi yangu niliyopaswa kwenda kulipa deni. Wajihi wangu ukajaa ulizo lililomtanabaisha pia, kuwa niko kwenye wakati mgumu wa utambuzi.

“Hawa ni watu wa aina gani?” nilijiuliza, chozi likiambaa ambaa kunitoka. Kwa sababu nilikuwa kwenye fumbo pana nililoshindwa litambua awali.

“Saa zilizotajwa na mazingira uliyopo yanatoa jibu la wazi kwamba hauna msaada utaofanya kuwaokoa hao watu.”

“Sahihi. Ila kinachonishangaza, wanauwawa vipi? Ilhali maisha yangu yote ya ufahamu simtambui baba yangu na shangazi yuko gerezani?”

“Nami napata ulizo hapo.”







“Dah! Kwa sasa haina haja ya wewe kunisumbukia, nenda kaendelee na mipango yako, wacha mimi nibaki humuhumu ndani,” nilisema kwa sauti iliyojaa unyonge wa hali ya juu. Huku, akili ikishindwa kutulizana kwa fikra, toa hii weka ile, mithili ya mtu aliyezingirwa na mbwa wakimkoromea kwa bweko zao.

“Kuna jambo limejificha katika hili. Hivyo unapaswa kulifahamu, usikate tamaa, muda bado upo naamini tukithubutu tunaweza kuwakomboa.”

“Tunawakomboaje wakati hatujui mazingira waliyonayo kwa sasa?”

“Niachie kazi. Nakuhakikishia, kwa muda huo uliosalia nitapata ukweli wa kisa kilichopo na nini kiendeleacho,” alisema afande Mzee. Maneno machache yaliyofuta hali iliyonifunga.

__________



Hatimaye tukaagana. Mimi, nikarudishwa chumbani, na afande Mzee naye alirejea makwao huku nikimpa ombi la kuniletea shajara, ile aliyoniachia shangazi kwa lengo la kuendelea kuangalia aliyoyaandika na tafsiri yake. Kwani niliamini kuna kitu kipo tofauti na zile kauli.



Maagano yetu hayakuwa mwisho wa usahaulifu kuhusu yaendeleayo. Picha za Jamila na mzee Namahala hazikubanduka kuwafikiria wanacheza filamu ya aina gani hadi nihusishwe nami moja kwa moja, mtu niliyoko mbali na familia yao. Hata kama hawakuhitaji niwaingilie si wangeliniambia tu, na sio kunileta sehemu iliyohalalishwa kwa ajili ya wahalifu.

Muda mwingine nilijiambiza kuwa kimbelembele ndicho kimeniponza. Ila kimbelembele kinatokeaje sehemu ya uhitaji wa amani na maadili mema? Sikuishia kujiuliza, ulizo lililokosa jibu binafsi, kwa sababu sikutaka kuwashirikisha watu wengine. Ukimya wa nafsi ulienda kunidhuru, kama sio kuniangamiza kabisa duniani.



Jioni, ya saa kumi afande Mzee alirejea kwa mara nyingine. Akiwa na aalimu iliyotokana na agizo nililompatia mwanzo. Hakutaka kukawia, alinikabidhi chap kisha akaendelea na ratiba zake kulingana na namna alivyojipangia.

“Humu kuna kitu chenye kunisaidia,” nilijisemeza, wakati huo nikikung’uta vumbi jalada la shajara ili kuleta mng’aro wenye utazamikaji machoni mwa wengi.



Sikukawiza! Punde, nilianza pitisha macho kurasa moja baada ya nyingine kupangusa ubongo wangu juu ya mambo ya gerezani na kesi ziniandamazo na kuingiza kitu kipya chenye utofauti wa mazingira niliyopo. Nilivyoifikia kurasa niliyoishia kusoma hapo awali nikapiga tuo. Nikajirudishia yale maneno kwa sekunde kadhaa kisha nikasonga mbele hadi kurasa iliyofuata. Ambayo, mwanzo tu wa kurasa nilikaribishwa na andiko lenye uvuto. ‘usiache kusoma sehemu hii' kilisomeka kichwa cha habari. Nami kwa pupa ya ubongo, nikaweka tuo la kudumu nipate kilichowekewa msisitizo wa usomaji.



Kwako Abdul mpendwa,

Awali nikupe pole na mihangaiko mingi unayoendelea nayo. Pole sana! Hiyo ndiyo dunia, inahitaji uvumilivu wa hali ya juu na uthubutu mahiri wa maamuzi. Mambo mengi ya duniani hayatulizi kichwa, bali hukiangaisha kwa sababu ya ukosefu wa mbadala wa tulizo. Naamini, hadi kufikia sasa hakuna tulizo la changamoto. Lililopo bado halijajitosheleza, ndiyo maana ukiitatua hii kwa uchache, siku zijazo unazongwa na nyingine inayohitaji utatuzi wa kina zaidi ya ile ya awali. Itachukua muda kumalizika!



Leo, nimediriki kutumia kurasa hii kukuweka wazi. Ili angalau upate cha kuanzia kwenye yale yanayokukabiri. Abdul! Shangazi yangu, kwanza; naomba uniwie radhi kwa mahusiano baina yetu. Najua utajiuliza, mahusiano gani hayo? Jibu langu ni kwamba, mimi nawe ni ndugu wa damu. Ewe ni mtoto wa kaka yangu, Bw. Vumilia Matatizo. Nilidiriki kukuficha muda wote kwa sababu ya kuhofia usumbufu wa kumtaka baba yako, ilhali baba yako hakuhitaji uishi naye kutokana na matatizo aliyonayo.



Baba yako yupo matatizoni, kwa muda mrefu tu. Tena naweza sema vitani, vita ya kibiashara, ndiyo maana akadiriki kuisambaratisha familia yake ili asalie pekee kwenye vita hiyo. Maadui wasitumie mwanya wa familia yake kumuangamiza. Ijapokuwa njia alizotumia kuisambaratisha familia si nzuri, alitumia nguvu za giza kukutanisha na jamaa, jamii wasitambue sehemu mulipo.



Hivyo makutano yetu kwa siku ya kwanza, yalikuwa makutano yaliyopangwa. Tofauti kabisa nami nilivyokuhadithia mwanzo. Naomba kwa mara ya pili, niwie radhi kwa hili.

Nikiachana na mkasa huo, sasa nataka nikupe dondoo chache zimuhusuzo baba yako. Na ukipata mwanya kwa hili, usisite kwenda kumsaidia. Ili jamii pana iweze kunufaika na maamuzi yenu.



Abdul! Baba yako ana maadui wakubwa wawili. Wa kwanza, mzee Namahala; na afuataye ni Jamila, pasi na msahau mshirika wa Jamila, Chitoko Chindume. Vita iliyopo baina yao, sababu ni moja tu. Baba yako, anaenda kuanzisha kliniki kubwa nchini ya matibabu ya ugonjwa wa ukimwi. Ikiwa na maana kwamba, anaenda kutoa msaada wa kugawa dawa kwa waathirika bure, dawa ziaminikazo zina nguvu kubwa ya kupunguza makali ya virusi kama sio kuua kabisa tofauti na hizi za sasa zitumiwazo kwa wingi.



Hatua hii, maadui zake hawajaipenda. Sasa wanataka kufanya kila hila kuhakikisha wanavunja mpango wake ili wao waendelee na kile walichodhamiria. Cha kwanza; kutoa maambukizi kwa vijana wengi zaidi kutokana na kisasi walichonacho. Kama unavyofahamu, Jamila ana kisasi kikubwa na wanaume kwa sababu ya kitendo alichotendewa angali mdogo. Cha pili; mzee Namahala ndiyo wakala mkubwa wa madawa yatumikayo sasa. Mzee wako akianzisha kliniki atakosa ulaji. Cha tatu; kupitia visasi hivyo, wanataka kwenda kutengeneza taifa legelege, ndiyo maana wanadiriki kwa kiasi kikubwa kumwinda. Hivi, unahisi nini kitajiri endapo vijana wengi watakuwa waathirika?



Nimeamua kukufumbua, kwa sababu naamini kwa sasa una nguvu nyingi za kuamua. Nenda kamsaidie kwanza baba yako, kisha fanya kile ulichoniahidi. Ila nakukumbusha, ‘hakuna picha kamili ya binadamu ionekanayo hadharani.’

“Mmmmh!” nilihema kwa nguvu mara baada ya kuhitimisha usomaji. Huku nikifunika na kukielekezea kichwa ukutani kufikiria yale niliyosoma.



Kichwa kikazama kwenye fikra nzito. Chozi nalo taratibu likaanza kunitiririka, simanzi ikachanua mbele ya wajihi wangu, mkosefu nisiye na hatia.

“Ina maana, wamegundua kuwa mimi ni mtoto wa Vumilia?” nilijiuliza, wakati huo nikijenga taswira za watu mbalimbali na matendo yao.



Ilivyokuja ya Jamila, nikaigandisha kwa muda mrefu. Nikaanza kumfikiria, hatua moja baada ya nyingine. Kuanzia umri, umbo na matendo yake. Hayakulingana hata chembe!

“Jamila, ushakuwa muathirika?” nilijiuliza kwa mara nyingine, taswira ya Jamila ilivyoanza niondoka.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Baadaye akafuatia Chitoko. Nikajiuliza huyu naye ana kisasi gani hadi awe mshirika wa Jamila, ila sikupata jibu kwa sababu sikuwa na historia naye. Lakini niliendelea kumchambua kwa uchache niliomfahamu. Nikiamini nitapata uhalisia wake japo sijawahi pata somo la saikolojia.



Kabla sijahitimisha naye, ghafla umeme ukakata. Sauti za manung’uniko zikatawala utadhani wengi wetu tulikuwa na jambo la maana tufanyalo. Kitendo hicho, kikapelekea nami kuzinduka. Toka kwenye lindi la tafakuri lililonijaza simanzi na ushindwa wa mambo ya ulimwenguni.

“Nini tena hawa jamaa? Mbona wanakata kata umeme ovyo?” niliuliza. Nikiwa na maana ya kujiuliza mwenyewe, ila mmoja miongoni mwa watu tuliomo mule chumbani akadakia kujibu.

“Wanaboa vibaya mno. Yafaa ukikutana nao unawapa vibao hadi washike adabu,” alisema. Tena kwa mkazo kuashiria kamaanisha na kachukizwa kwa kitendo hicho.



Sekunde chache baadaye taharuki zaidi ikazizima. Kufuatia mlio wa king’ola ulioashiria kuna hatari. Vishindo vya askari wakikatiza kwenda huku na kule vikatamalaki, na kujenga ulizo pana kwa kila mtu aliyopo ndani. Upande wa wafungwa tuliishia kuwa na dhanio tu, kwamba yumkini kuna hitilafu ya umeme, baadaye dhanio likazaa hitajio, tutakuja tolewa tuwekwe mahali salama zaidi kutukinga na adha hiyo.



Ajabu! Sekunde zilizidi yoyoma kile tutarajiacho hakikutokea. Ikatubidi tuanze kugonga gonga nondo kuwashinikiza askari waliopo watukumbuke nasi na sio kuangalia kwanza usalama wao. Sio ugongaji wa nondo tu, wengine walipaza sauti kutoa manung’uniko.



Dakika saba baadaye, toka tatizo hilo litokee tukaanza kusikia vishindo vya nguvu vya viatu vilivyotokana na utembeaji. Vishindo vilivyonipa picha kuwa idadi ya askari inazidi kuongezeka, huku wakionekana wenye uharaka wawahi waelekeako. Tembea yao iliambatana na kitendo kingine. Cha ukokiji wa bunduki. Sio zile walizozoeleka nazo kutumia muda mwingi wakiwa kazini SAR (semi—automatic rifle). Walikuwa wamebeba zile za kazi, zenye uwezo mkubwa wa kiupigaji tofauti na SAR. Walibeba SMG (sub—machine gun) al—maarufu AK 47 (alexandra Kalashnikov).



Hatua hiyo ikapeleka fikra zetu mbali zaidi. Baada ya hisio kuwa kuna tatizo la moto kutoendana na tukio liendelealo. Baadhi tukaanza kuhisi, yumkini, kuna mmoja miongoni mwa wafungwa kagoma huko chumba kingine ama kahatarisha maisha. Hivyo anaenda kuzibitiwa kwa njia hiyo.



Fikirio hili nalo halikudumu sana akilini. Ilikuwa kama njozi ya mchana majini, daima haina ushindo, na wala haifiki mwisho. Ndivyo ilivyokuwa na fikra za wakati huo. Kwani milio iliyokuwa inatema kwa kasi toka kwenye mitutu ya bunduki walizobeba ilitupa majibu tosha, japo hayakuacha dhanio. Hali iliyochangia kuleta ukimya. Ile gonga gonga haikuwepo tena, wengi wetu tulitulia tuli, huku tukiipa akili kazi ya subirio la matokeo.



Tukio hilo halikuwa la muda mfupi. Lilichukua muda mrefu kiasi kwamba, halikuacha kujenga hofu ndani ya mioyo yetu. Tena hofu iliongezeka maradufu punde tulivyosikia baadhi ya maongezi ya askari.

“Afande, hali inazidi kuwa tete, kwani wapiganaji wengi wameuwawa na bado hatujafahamu nguvu ya adui ikoje,” yalisikika maongezi ya askari huyo, pindi akizungumza kupitia redio na mtu wa upande wa pili, hofu ikimtweta muda wote.



Kauli hii ikatuvumbua wachache tuliosikia. Kuwa kuna hali ya hatari iendeleayo ndani ya gereza. Tena si hatari ya kawaida, hatari haswa isiyoweza kuelezewa.

“Kuna uvamizi unaoendelea humu ndani,” alisema mzee mmoja miongoni mwa wafungwa tuliopo mule chumbani. Akiwa kaketi jirani nami, na kunifanya ile kauli yake niisikie vyema zaidi ya watu wengine. Na kunipa mwanya wa kufikiria, uvamizi huo unatokea vipi ilhali jengo tulilomo limezungushwa kwa kuta nene ya mawe?

Sikupata jibu!



Sekunde chache baadaye vishindo vingine vya viatu vikaanza kusikika. Wakitembea kwa mnyato, wamepindisha mgongo kiasi kwa mwendo wa kimapigano mithili ya wapiganaji wa CQB (close quarter battle).

“we are going into two, four men team. We are going into two, four men team,” ilisikika sauti toka kwenye redio iliyopachikwa kwenye suruali usawa wa kiuno kwa kila askari. Ikiwasisitiza wanapaswa kwenda katika mpangilio wa timu mbili yenye wapiganaji wanne wanne.

“Nani hao waliojileta kufuata vifo vyao?” nilijiuliza, baada ya hisio lililoniaminisha waliokuja kuvamia hawatochukua muda mrefu kutokana na mafunzo na uzoefu wa mazingira wa askari.



Ila baadaye nikapata hisio lingine. Kwamba, wavamiaji itakuwa wamejipanga vya kutosha ndiyo maana wamethubutu kuja. Si wazembe. Nao ni mafundi wenye ufundi wao wa kutumia silaha. Ijapokuwa sikuwahi pata dondoo kama kuna uvamizi utokeao gerezani ukafanikiwa, zaidi ya kuona kwenye filamu za nje ya nchi.

__________



Dakika tano baadaye ukimya ukatamalaki. Si nong’onong’o wala chembe ya nong’onong’o iliyoweza kusikika. Hofu ikachipua ndani ya mioyo ya wengi, huku kiza nacho kikimeza zaidi uono wa mboni zetu.

“Hicho chumba kinachofuata,” ilisikika sauti, iliyojaa ngurumo ikipasua kwenye ule ukimya.



Mara baada ya sekunde nne tukasikia mchakacho wa ufunguzi wa kufuli kwenye mlango wa chumba tulichopo. Haukuchukua muda mrefu, ukamalizika kisha kufuli ikafunguka na kumpa utambuzi mfunguaji afanye hatua inayofuata. Aliingia ndani! Akiwa kakamatia bunduki mkono mmoja, mkono wa kuume, mtutu akielekezea chini.

“Abdul!” akaita, wakati huo tuliomo tukihangaika kukaza macho yetu yapasue kiza yamuone. Ila hatukufanikiwa, kwani kiza kilikuwa kikali mno.









Kikapita kimya kifupi. Takribani sekunde kumi na tano, huku yule mtu akizunguka kwa mmoja baada ya mwingine. Sikujua alikuwa na ufahamu upi, kwani alivyonifikia nilipo alisimama na kuelekeza mdomo wake kwenye moja ya sikio langu.

“Hatuna muda wa kupoteza, nipo hapa kwa ajili yako. Huu ndiyo muda wa kuwasaidia wale uwapendao uliotahadharishwa nao,” alinong’ona hadi nikashtuka.

“Hapana. Nitajiweka mahali pabaya, ni heri niendelee kubaki humu ndani.”

“Shwaiiin!!” alisema, akiambatanisha na ngumi nzito, akaielekeza kwenye moja ya kiungo changu. Nikazima!

__________



Nilivyorejewa na fahamu, nilijikuta nipo mazingira tofauti na yale ya gerezani. Nikashangaa, nimefikaje hapo? Nilivyopiga jicho huku na kule, nikaona nimezingirwa na watu wawili wakinitumbulia macho, utadhani kama mfugo wa sherehe niliyepatwa na homa ghafla, huku zikisalia saa chache kuelekea kwenye shughuli. Ikanilazimu nami kuwatumbulia macho, lengo niwabaini. Kwa sababu wakati huo kulikuwa na mwanga hafifu, sikuchukua muda mrefu kuwafahamu. Walikuwa afande Mzee na yule bwana jela wa gereza la Karanga mjini Moshi.



Juu ya uhafifu wa mwanga, uliojengwa na majira tuliyopo, alfajiri, nikashuhudia vingine pia, ambavyo vilionekana wametumia kazi kubwa kuviondoa vikashindikana. Madoa ya damu kwenye nguo walizovaa.

“Ina maana hawa ndiye waliokuwa wanapambana na wale askari magereza?” nilijiuliza, huku nikijitahidi kuinuka lengo niwasogelee walipo. Kabla sijasimama sawa kuwafuata wakanisitisha nisifanye kile nitakacho.

“Sasa ni saa 12:06 asubuhi. Zimesalia saa ishirini na saba ili tuwakomboe uwapendao. Hivyo toa pendekezo, tunaanzia wapi?” alisema afande Mzee.



Sikujibu kwa uharaka, nilitulia kwa muda mchache huku nikifanya fikirio, nilipo lihitimisha ndipo nikajibu.

“Mbona mumekwenda kinyume na jibu langu? Hamuoni kuwa mnanitengenezea kesi nyingine dhidi ya jamhuri? Huko mtaani nitakuwa katika hali gani nionekanapo wakati huo kukiwa na mabango mengi yaliyobeba ujumbe wa kutafutwa na utangazwaji wa donge nono kwa mtu atayefanikisha upatikanaji wangu,” nilinena kwa lugha, lugha madhubuti iliyowafumbua na kuwapa hofu ya utendaji.



Ajabu! Hofu hiyo haikuwachukua muda mrefu wakarudi kwenye hali yao ya kawaida.

“Ndugu wakati ni huu. Umediriki kuvaa huruma kwa kuingia kwenye matatizo ya nduguyo, huna budi, kuendelea na mvao uliouanza. Hupaswi kuuvulia kati,” alisema yule bwana jela. Ambaye mpaka kufikia muda huo sikufahamu jina lake. Na imekuaje hadi akaamua kushiriki kutoa msaada kwangu wakunitorosha gerezani.



Baadaye bwana jela akaondoka na kutuacha wawili tukianza kupambanua mbinu za uokoaji kwa wapendwa wangu. Ijapokuwa nilionesha ushirikiano kwa shingo upande, kwa sababu ya kutofurahishwa na kitendo walichofanya gerezani. Kunitorosha, na kukatisha maisha ya watu wasio na hatia, pasipo kusahau utafutwa utaonikosesha amani.

“Abdul, piga moyo konde. Angalia wapendwa wako, hayo mengine kwa sasa yasahau, mimi nipo nitakuhakikishia msaada wa hali na mali. Niamini, hamna baya litakunyemelea kwa hili lililotokea,” alisema afande Mzee, maneno aliyoyatamka kwa sauti ya upole na yenye kuleta ushawishi kwa msikilizaji. Wakati huo akipiga piga moja ya bega langu kwa kiganja chake cha mkono kuonyesha msisitizo.



Sikuwa na budi. Mwishowe niliridhia. Baada ya kupewa maneno ya busara kwa kina yaliyofukuza unyonge na kuingiza nuru iliyojaa matumaini. Baadaye, nikapewa nguo za kuvaa. Niachane na zile nilizotokanazo gerezani. Ambazo zilinitambulisha kuwa ni mtu wa aina gani kwa yeyote ambaye angeniona. Kitendo ambacho ningediriki kung’ang’ana nazo, nisingelichukua muda mrefu uraiani. Hata dakika tatu, zisingelifika, taarifa zingewafikia wahusika.



Hayakuwa mavazi sahihi kwa mtu aishiye uraiani. Ni mavazi ya kihayawani, yaliyojaa neno lenye hekima sana, litambulishalo jamii kazi yao ni ipi, lakini kitendekacho ndani tofauti na ujinasibu wa kwenye vazi.



Urekebishaji! Ndilo neno lililojaa katika vazi hili. Likiielezea jamii, kwamba kazi ifanyikayo kule ni kurekebisha tabia ya mtu. Ila mbona wanapokea watu wasio na hatia? Wanarekebisha nini kwa watu wa namna hii kama si kuwazalishia chuki?

__________



Chitoko Chindume! Ndiyo tulianza naye. Tena kwa uharaka mno, kwa sababu muda ulikuwa hautusubiri. Ulizidi kuyoyoma! Hadi ukatukosesha uhakika wa makadirio, kama kazi iliyopo mbele yetu itakamilika. Lakini hofu haikunipotea. Kutokana na kukosa imani na afande Mzee, hana ubavu wa ushawishi kwa waandamizi waliomzidi vyeo. Niliamini hivyo! Na kujiambiza, gerezani nitarejea kwa mara ya pili, tena awamu hii nitakuwa na wakati mgumu zaidi. Kwa sababu ya kutoroshwa.



Hivyo, tulivyokuwa tunapita pita mtaani, nilikuwa na hadhari kubwa mno. Muda wote nimeinamisha sura chini, ijapokuwa nilipambwa na kofia ya koti kubwa nililovaa. Woga, ulinisumbua, ushujaa ulinichoropoka, mambo ya jamhuri huwaga mazito. Ndicho kilichochangia. Niliteseka na nafsi yangu.



Nilikuja kuinua uso pale tu, tulivyokuta sehemu ina bango kubwa lililosheheni matangazo. Hapo niliinua kichwa kuyaangaza matangazo yaliyobandikwa, nikihisi, labda lipo linihusulo. Ama nilitega sikio vyema, sehemu ziungurumazo sauti redioni, nilivyosikia wakizungumza kuhusu mambo ya jeshi.

“Ushafahamu chanzo kwa nini wapendwa wangu wanaenda kufa?” nilimchombeza afande Mzee. Lengo anifahamishe chochote akifahamucho.

“Hapana! Bado sijafahamu. Hivyo nimeamua tuje hapa, ili Chitoko atueleze yote anayoyafahamu,” alinijibu. Tukiwa tushafikia lango la kuingilia la nyumba ya Chitoko.

“Una uhakika atatueleza?”

“Ndiyo, kwa sababu nina vielelezo vitavyompa shinikizo la kutuambia ukweli, ili nisiviachie hadharani. Kwani endapo vitakuwa wazi, atakuwa na wakati mgumu sana kuhusu ajira yake.”

“Mmmh!...ila,” nilisema na kuweka tuo kwa muda.

“Nini tena?”

“Sina hakika na ukinenacho. Kwa sababu, biashara, ndiyo chanzo cha mihangaiko hii itokeayo.”

“Biashara? Inahusiana vipi?” aliuliza afande Mzee akiwa mwenye hamaniko tele.

“Twende ndani. Utafahamu namna inavyohusiana.”



Kabla hatujapiga hatua kusonga mbele, tukajionea mlango wa mbele, usawa tuliopo wa nyumba ya Chitoko ukifunguliwa. Ikatupa hamasa ya kupiga jicho kumuona atokaye ni nani. Alikuwa Chitoko! Kweli, ni yeye, tulimshuhudia pasi na chembe ya shaka.

“Twende tumuwahi,” alisema afande Mzee, huku akipiga hatua za haraka kusonga mbele. Ila hatukufanikiwa, kwani, punde tu alivyotuona alirudi ndani haraka, akafunga mlango na kutuacha tukihangaika kumuomba atufungulie.



Kwa nini?



Tulijiuliza. Kabla hatujijibu, tukapata wazo la kuzunguka nyumba nzima kujionea kama kuna nafasi nyepesi ya kutuwezesha kufika ndani. Tulikuwa na ulazima wa kuingia, ili mpango ukamilike, kutofanikisha, ilikuwa sawa na kuruhusu mauaji ya wapendwa.



Tulivyozunguka upande wa pili, nikiwa na maana ya nyuma ya nyumba, tukakuta mlango uko wazi, uliotupa mashaka yumkini Chitoko katumia sehemu hiyo kutukimbia. Tukajaribu kuangaza angaza pembeni, maeneo jirani, lakini hatukumuona. Ikatubidi tuingie. Kwa hadhari kubwa mno ili tusiingie mtegoni utaotufifisha akili kuhusu mipango na kutuingizia kitu kipya. Kufikiria namna ya kujikomboa! Jambo ambalo lingeturudisha nyuma kimkakati.



Mule ndani tukazunguka kila chumba kilicho wazi. Tulivyokuta vimefungwa hatukuweza kuingia japokuwa hatukuacha kujaribu kugonga gonga kwa lengo la kujiaminisha.

“Ashatukimbia huyu mjinga,” alisema afande Mzee pindi tukiuaga ule mlango tulioingilia kwenda nje.

“Na sioni dalili zozote za kufanikiwa. Ndiyo maana nikawaambia heri nibaki gerezani,” nikachangia hoja, huku tukitumbua macho kuangaza viwanja mbalimbali yumkini tungelimuona.



Baadaye, takribani dakika nane toka tutoke mule ndani, afande Mzee akatoa wazo. Tumgeukie, afande Tumainiel Madevu, ambaye ndiye kigogo kisaidizi wa mchezo huo kwa upande wa pili.

“Tukimdhibiti huyu, itakuwa jambo rahisi kumdhibiti Chitoko,” alitoa hoja. Niliyokubaliana nayo moja kwa moja pasipo pingamizi.



Tukainza safari sekunde chache baadaye. Kwa kutumia usafiri wa bajaji tuliyobahatika kukutana nayo ikishusha mteja njia panda ya kwenda Iyunga.

“Tufikishe kituo cha kati,” aliamuru afande Mzee, kauli iliyompa shinikizo dereva kutafuta uelekeo sahihi wa kupita awahi kufika tutakako.



Tulivyofika maeneo ya kambi ya Itende JKT afande Mzee akaghairisha uamuzi. Akapanga, kituoni aende peke yake, halafu, mimi anikute kwenye kile chumba walichonipeleka mara baada ya kunitorosha gerezani. Sikupingana naye, nilitii. Akanipa kiasi kidogo cha pesa kwa ajili ya nauli kisha akaendelea na safari, mimi nikapunga mkono bodaboda, ilivyosimama nikamueleza dereva mahali nakohitaji nifike.

Baada ya mwendo wa dakika chache nikawasili sehemu husika. Nikabaki na kazi moja tu, ya kumsubiri afande Mzee awasili akiambatana na yule mhitajika. Hatimaye dakika zikakatika, nikiendekeza zoezi la subira, lililozalisha shauku, yote sababu ya afande Madevu. Mmoja miongoni mwa watu walionikandamiza pasi na kosa.



Lakini, kuna wakati nikajawa na hisia. Nilipo si sehemu sahihi kuwepo. Naweza rudi matatizoni punde, kwa imani niliyoingiwa. Kwamba, ujio wa afande Madevu, unaweza ambatana na askari mwingine, ukizingatia na wadhifa alionao. Hivyo kutasababisha kutokea varangati litalowashtua wengi, raia, waishio jirani, mwishowe, afande Mzee akose nguvu ya kunipambania. Kwa kuhofia, watu wa vyombo vya ulinzi na usalama washapatiwa taarifa juu ya kutoroshwa kwangu.



Hatimaye nikaingiwa na wazo la kuondoka! Ila halikuwa na nguvu, baada ya kuingiwa na wazo lingine sekunde chache baadaye la kuendeleza subira.



Subira, ikanichukua takribani dakika arobaini na tano, ndipo ujio wa wale niliokuwa nawasubiri ukajitokeza. Alianza kutangulia afande Mzee, akafuatia afande Madevu, wajihi wake ukimtambulisha kuwa na chukizo na uharaka, kana kwamba kalazimishwa huko watokako.

“Eh! Bhana eh! Tufanye hiyo shughuli chap,” alisema afande Madevu, wakati huo afande Mzee akifunga mlango.

“Usiwe na shaka. Ni zoezi la haraka tu,” afande Mzee akasema. Huku moja ya mkono wake akibonyeza kitufe cha swichi kiruhusicho mwanga wa taa iliyotegwa juu ya mbao ya upauo kuwaka.



Afande Madevu akaduwaa!



Alivyotupa mboni zake mbele, na kung’amua uwepo wangu.

“Nini hii?” akauliza. Macho yakimjaa kila ishara ya mshangao, na ukosefu wa kuamini.

“Hii ndiyo shughuli iliyonihimiza nikuite tushughulikie,” alijibu afande Mzee.



Wakabaki kukodoleana macho!



Wakabaki kukodoleana macho!



Kikapita kimya cha muda. Chenye mshangao na fikirio kwa kila mmoja. Kwa upande wangu nilihisi, alichofanya afande Mzee si kitu chema. Kwa sababu, afande Madevu ni mtu mwenye cheo cha juu dhidi yake, hivyo akiamua kumpa amri ya kunikamata, afande Mzee anaweza kunywea na kufanya utekelezaji. Ama atajitengenezea mazingira magumu kazini.



Lakini, kuna hisia zingine zikawa zinanijia. Kwamba akifanyacho afande Mzee ndiyo msaada pekee. La sivyo, huko mtaani mambo yataharibika. Kisasi cha Jamila na Chitoko kitaenda angamiza taifa letu hali itayojenga ugumu wa kujikwamua kiuchumi, hasa binafsi na taifa nzima.

“Kwa nini wanapinga upatikanaji wa tiba ya hili tatizo sugu?” nilijiuliza. Baada ya kutafakari dhamira ya baba yangu na mahasimu wake.

Baada ya wawili hao kukodoleana macho kwa muda mrefu, zoezi hilo likaamia kwa wote. Hakika, hakuna aliyekuwa na mwenye jambo la kuzungumza kwa mwenzake kwa wakati huo. Si, afande Madevu aliyeonekana mwenye haraka, wala afande Mzee naye, aliyejawa na shauku awali ya makutano baina yetu sote.



Laiti angelikuwepo mtunza muda, kwa ukimya tulio uzalisha angelitupatia muda sahihi tulioutumia. Ila hakuwepo. Bali kwa ubashiri wa haraka nilioufanya tulitumia takribani dakika tano, ndipo akajitokeza mmoja wetu kuufukuza. Afande Mzee! Wajihi ukitahadharisha kiwango cha shari alichonacho kwa amtazamaye. Ila kwangu hakikujenga uogofyaji, labda, afande Madevu. Maana angaza yake, ilikuwa kipimo tosha cha kiasi cha woga alionao.

“Tunamuhitaji Chitoko hapa. Haraka iwezekanavyo,” alisema afande Mzee. Moja ya kiganja chake cha mkono akipiga kwenye ubao wa meza iliyopo ndani kuonyesha msisitizo. Hadi afande Madevu akashtuka kwa hofu. Kana kwamba hajasikia vyema ile kauli.

“Naamini umenielewa. Fanya hima aje hapa, ili tufanye kwa umoja kile nilichokuitia,” alikazia afande Mzee, huku akitoa bahasha iliyo na picha za mnato ndani, alizompiga Chitoko usiku ule wa siku kadhaa zilizopita. Akamkabidhi!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Endapo ataleta ukaidi, basi hiyo itakuwa halali ya macho ya umma mtandaoni.”



Kazi ikawa kwa afande Madevu. Afanyaje? Atumie wadhifa wake? Ama atii, kile tutakacho. Aache harakati za kuhalalisha haramu kuwa takwa huru.

“Abdul, hamna namna nyingine ya kufanya, zaidi ya kupingana na matakwa ya kisheria, ili watu wako wawe hai,” alinidokezea afande Mzee, wakati huo afande Madevu akisaili picha alizokabidhiwa. Zikimuonyesha Chitoko katika mazingira tofauti ya ukahaba.



Ukimya ukaja jirudua upya. Wakati tukimsubiri afande Madevu afanye uamuzi. Kupitia picha hizo, zilizomuacha mdomo wazi kwa mshangao wa kutoamini.

“Huyo ndiyo askari wako unayemlea pale kituoni. Hivyo, fanya nilivyokuambia, ili mupate nafuu yenu ya matatizo,” alisema afande Mzee. Pindi akiwa karibu na meza nyingine iliyobeba televisheni. Akaiwasha! Kisha moja ya kituo cha runinga kikajibainisha kurusha taarifa ya habari. Iliyokuwa inasomwa na mtangazaji wa kike afahamikaye Samira.



Baadaye, afande Madevu akaonekana kuzungumza na mtu wa upande wa pili wa simu. Tena alizungumza kwa uchache tu, na maneno mafupi yaliyoashiria kumpa amri mzungumzaji mwenza. Kidogo kitendo hicho kikanipa hofu. Nilihisi! Yumkini, anawapigia askari polisi waje pale tulipo kutuvamia na kutukamata. Kiasi kwamba, nikaingiwa na ushawishi wa kumwambia afande Mzee, kwani hakushuhudia.



Nikapiga hatua hadi alipo. Nikasogea usawa mmoja alikoelekezea sikio, nikafungua kingo za mdomo wangu kuzungumza. Ila kabla ya kutekeleza hilo, nikakatishwa na sauti ya mtangazaji runingani.

“Kamishna wa jeshi la polisi, wa oparesheni na mafunzo, asubuhi ya leo kafanya mkutano na waandishi wa habari kuwaelezea hali ilivyofikia kuhusu tukio la mfanyabiashara Vumilia Matatizo aliyevamiwa nyumbani kwake usiku wa wiki iliyopita na kupelekwa mahali kusikojulina…



Pia, mkuu wa jeshi la magereza nchini, anautaarifu umma wa watanzania, kuhusu uvamizi wa gereza la Luanda mkoani Mbeya lililopelekea kutoroshwa kwa mfungwa mmoja aliyehukumiwa kwa kosa la mauaji…kwa habari zaidi, tujiunge na wanahabari wetu toka maeneo ya tukio.”



Si kwangu tu, wote tuliomo tukabaki kuduwaa. Na kuanza kutoleana macho, mmoja baada ya mwingine. Huku ile sauti ikizidi kurindima vilivyo ndani ya viwambo vya masikio yetu.

“Itakuwa kuna msako mkali sana huko mtaani,” nilijisemeza. Huku afande Mzee akinisukumizia kidogo pembeni apate nafasi nzuri ya kutembea. Akapiga hatua hadi alipo afande Madevu.

“Hiyo habari, haiwezi kukupa nafuu ya shughuli yetu. Ngoma lazima ilie na kuchezwa,” alisema afande Mzee. Akiwa kamkazia macho yenye ishara tosha hatanii kile anenacho.

__________



Simu iliyopigwa na afande Madevu ilitua kwa Chitoko. Akiwa pembezoni mwa barabara akitembea kwa miguu maeneo ya Kabwe. Kituo cha daladala! Jasho tele likimtiririka, muonekano wake ukimya wa ovyo mithili ya mtu aliyechoshwa na hali ngumu ya kimaisha. Alijiweka ovyo, kana kwamba si mtumishi ndani ya moja ya majeshi nchini.



Nywele, alikuwa kaziacha shaghala baghala, pasipo kuchanwa, huku zikikithiri vumbi na harufu chafu ya kuchachafya. Mavazi ndiyo zaidi. Dhahiri! Kwa wakati huo hakuhitaji heshima kama awapo majukumuni. Juu alikuwa kavaa blauzi, nyepesi ionyeshayo ndani, na kufanya umbo la tumbo na kanchiri aliyovaa yenye rangi nyeusi kuonekana. Utata wa vunjo la heshima yake haukuishia hapo. Uliendelea!... Kwa mtindo wa blauzi ilivyotengenezwa. Iliacha sehemu kubwa ya kifua wazi, kiasi kwamba kanchiri ikawa nje tu, ikinadisha ukubwa wa matiti aliyobeba. Ukizingatia kanchiri yenyewe, haikuzuia matiti sehemu kubwa. Yumkini, matiti yake yalikuwa makubwa.



Chini, alivaa ki—sketi kidogo kilichoishia juu ya magoti. Urefu takribani sentimita kumi na tano toka magotini ndipo sketi iliishia. Kwa nyuma ikiwa na mpasuo, ulioacha unono wa paja nje. Vidume wakawa na kazi ya kukodolea macho huku wakipiga funda la mate kusindikizia. Hakuacha kutamanisha na kuinua misuli ya watu nguoni.



Alivyoangaza namba ya mtu aliyempigia, ilikuwa ngeni. Ila haikumpatia wakati mgumu wa kuamua afanye nini. Aliipokea!

“Fungua whatsapp, kuna ujumbe nimekutumia,” ilisikika sauti ya mpigaji. Ambaye aliifahamu pasi na hangaiko la kutafakari ni nani.



Hakupuuzia! Chap, aliwasha data, akaingia mtandao husika. Kweli! Alikutana na orodha ya watu wengi waliomtumia jumbe. Akiwemo afande Madevu. Hivyo hakuhangaika na wengine, alienda moja kwa moja hadi kwenye namba ya afande Madevu. Akafungua, akakuta katumiwa picha mbili za mnato. Pasi na kukawia, akazipakua. Zilipokamilika, akijionea dhahiri shahiri, ni picha za namna gani. Akaduwaa! Pozi likamuishia. Akili ikayumba, hasira ikachipua, morali ya mwendo ikampwaya.

“Anataka nini huyu mzee? Kapiga lini hizi picha?” alijiuliza. Huku akizitumbulia macho kuzisaili.



Kabla hajajijibu, simu ikaanza kuita. Alivyoangaza mpigaji, alikuwa afande Madevu. Akapokea! Huku kingo za mdomo zikiwa zimefura kuonyesha hajafurahishwa na tukio liendelealo upande wake.



Maongezi yakawa mafupi. Hata dakika moja haikumalizika, simu ikakatwa na kumfanya azidishishe kingo za mdomo wake kuzirefusha kama kasuku. Alichoambiwa hakikuwa chema!

__________



Ujasiri, ukawa nguzo kwa afande Mzee. Nami ikanibidi nipite kwenye nyayo zake, ili kumuadabisha afande Madevu. Huo ndiyo ulikuwa wakati, zaidi ya hapo, mambo yangelikuwa makubwa zaidi.

“Muda si mrefu mumtakaye atakuwa hapa. Hivyo naamini uwepo wangu mahali hapa utakuwa mwisho,” alisema afande Madevu. Akiwa katukodolea macho, utadhani ndiyo watu wa mwisho tushikiliao uhai wake.

“Wala usihofu,” tulimjibu kwa pamoja.



Kweli! Baada ya dakika kumi, afande Mzee alikabidhiwa simu na afande Madevu wazungumze na Chitoko amuelekeze mahali tulipo. Afande Mzee akafanya hivyo. Akaongea naye kwa uchache kisha akamrejeshea afande Madevu simu yake.



Zikapita dakika nne, tukasikia kishindo cha mlango ukigongwa. Afande Mzee akaenda kuchungulia kwanza sehemu fulani, usawa wa dirishani amuone agongaye, alivyomuona, akaenda kufungua mlango. Alikuwa Chitoko, aliingia ndani kisha afande Mzee akafunga mlango kwa mara nyingine.

“Una uhakika na usalama wa eneo tulilopo juu ya uwepo wa hawa watu?” nilimnong’oneza afande Mzee, kiasi kwamba akashtuka na kuchukua uamuzi wa haraka wa kutuweka salama. Aliwanyang’anya simu zao.



Chitoko naye hakusita kushikwa na mshangao, kama sio bumbuwazi. Hakuamini akionacho. Hakuamini kama naweza kuwa uraiani muda ule. Muda ambao ulikuwa ndani ya tekelezo la mpango waliotuhadhari. Akapoa!

“Hatuna cha kupoteza. Uwepo wenu utatufanya tupate tukitakacho,” alisema afande Mzee. Mtu ambaye nilianza muhusi yuko mahiri kwenye suala la ukachero.



Kwa namna moja, tulifanikiwa kwa hatua kadhaa. Sasa, nyota niliyohisi imefukiwa na vumbi jingi, niliiona ikianza kung’ara. Tena kwa mng’aro wa nguvu umtamanishao na kuvutia kila aonaye.



Baada ya muda tukauanza mjadala. Kwa kuwashinikiza wote wawili watueleze walipowaficha wapendwa wangu. Tena, afande Mzee hakuonesha mzaha katika hili. Alifanya mambo, mambo makubwa kana kwamba hawafahamu.



Penye kuwapiga hakusita kutoa kipigo, cha kimyakimya kisisikike nje. Hadi wakatoa machozi yaliyowasukuma kuangua kilio kidogo. Walishindwa kuvumilia maumivu. Ambayo naamini yalikuwa makali mno, kutokana na kipigo atoacho afande Mzee. Aliyediriki kuvaa huruma na matatizo yangu.

“Okoka yenu, hadi mueleze mahali walipo,” alisema afande Mzee. Wakati huo akiwachoma choma sindano ya kushonea nguo baadhi ya sehemu ya mwili. Kama wako kwa mganga wa jadi.

“Sasa sisi tunahusikaje?” alipayuka Chitoko. Sauti niliyoihisi inaweza wavuta watu wasogee eneo tulilopo.

“Tena nyamaza kabisa. Kahaba mkubwa wee…!” afande Mzee naye alikoroma. Kauli ambayo ilinipa udhoofu kidogo. Sikufurahishwa na neno lililotamkwa kumpa utambulisho Chitoko. Kahaba! Neno lenye udhalilisho sana.



Naamini hata naye alifadhaika kwa kiasi fulani. Kwani, sekunde chache baadaye nilimshuhudia akizidiwa kutokwa na machozi, huku wajihi ukioneshwa katisho la tamaa. Ikanipa picha, yumkini kuna la ziada alilonalo. Huruma dhidi yake ikanivaa! Japokuwa, dhana kama hizi, wakati mwingine hutumiwa maalumu kwa ulaghai. Ila muonekano wake ukanipa utambuzi wa jambo alilonalo moyoni. Nikaweka nadhiri, kulifahamu. Sikuangalia, nguvu ya uadui tulionao. Nilichoangalia, namna atavyoondoka na fadhaa hiyo, kisha iwe kinga kwangu ya ushindi







Ukimya ulitamalaki ndani ya chumba tulichopo. Afande Madevu na Chitoko walitulia, baada ya kutoa machozi hadi kuchoka. Mara walivyoamua kuwa wawazi kwa kutuahidi watatuambia walipo wapendwa wangu, ili tusiendelee kuwaadhibu.

Ukimya huo ulifukuzwa na Chitoko. Kwa kutuambia, anahitaji kutueleza historia yake kwa uchache kabla hajaenda kwenye hoja husika tuitakayo.



Tukampatia muda. Naye, pasi na hiyana, akaanza kutiririka. Sauti ikiwa na dalili za kutosha kwamba katoka kuangulia kilio sekunde chache zilizopita.



“Mimi Chitoko Chindume. Hili si jina langu halisi. Jina langu halisi ni Zaubia Arafat. Ni mtoto pekee katika familia yetu. Ijapokuwa kwa sasa niko pekee, nikiwa na maana wazazi wangu wote hawako hai. Nafahamu, mtajiuliza kwa nini Chitoko ndilo maarufu. Jibu lake ni kwamba; hili ni jina lililotokana na nadhiri yangu. Niliyopata kujiapiza miaka ya nyuma, kupitia mkasa uliomkumba mama yangu. Kiapo nilichokula katikati ya watu wengi mjini Mtwara. Na kufanya walioshuhudia kiapo kile waangue kicheko…



“Kupitia mkasa wa mama yangu nilijiapiza, mimi Zaubia Arafat, endapo nikija kuolewa, nipatwe na tatizo la jina nijiitalo sasa. Chitoko Chindume!” alisema Chitoko na kuweka tuo kwa muda. Akajikohoza kufukuza vikwazo vyenye kufanya sauti isitoke vyema kisha akaendelea.



“…historia yangu, inaanzia, punde mama yangu alivyobakwa enzi za uhai wake. Akiwa msichana mbichi ang’aaye muda wote na mwanaume afahamikaye Arafat. Ambaye ndiye baba yangu. Arafat alimbaka mama, Arafat nimzungumziaye hapa. Ni Arafat, kijana aliyekuwa anashinda muda mwingi kijiweni, anatumia madawa ya kulevya, kazi yake kubwa ni udokoaji na wizi. Japo alijiibia kidogo utanashati, na kumfanya asipotumia aina ya vitu nilivyozungumza awali, huonekana maridadi, atamaniwaye na mwanamke yeyote.



“Ila haikuwa hivyo kwa mama yangu. Ndiyo maana alidiriki kumbaka. Ubakaji, uliopelekea mama aukwae ujauzito na ugonjwa sugu utetemeshao ulimwengu. Ukimwi!



“Hii ikawa zawadi ya milele kwa mama yangu toka kwa Arafat. Ambaye baadaye alitoroka mjini kwetu, kuelekea kusikojulikana baada ya kuvujishiwa siri na watu wake wa karibu anatafutwa na polisi. Zawadi hii ilikerehesha maisha ya mama, nami pia baada ya kupata ufahamu. Hakika! Umivu lilituvaa.



“Miaka ya mbeleni mama akapata ajira ya upishi katika moja ya kampuni waliyopewa tenda ya kuwapikia askari wa jeshi la kujenga Taifa. Kambi ya Mlale, mkoani Ruvuma. Ajira iliyotuaminisha, itakuwa mkombozi wa maisha yetu. Ila haikuwa hivyo; ajira ile ilileta shida tu, na kupelekea katisho la uhai wa mama yangu.



“Ajira ile, ilikuwa chungu, tena kwa uchungu usiosimulika. Kwani, mama aligeuzwa kuwa mtumwa wa ngono, kwa askari waajiriwa na vijana wa kujitolea. Iliniumiza mno, ila sikuwa na uwezo wa kuzuia, kwa sababu hali ya uchumi wetu haikuwa nzuri. Ikizingatiwa jamaa walitutenga,” alisema na kutulia tena. Akafanya tafakuri kwa muda kisha akaanza kukenua kingo za mdomo wake tayari kwa kuendelea. Lakini hakufanikiwa. Alikatishwa na afande Mzee.

“Hadithi yako ni ndefu sana. Tueleze kwa kifupi kwa nini umeshiriki kuwakamata watu wasio na hatia wenye nia ya kutengeneza jamii huru?”

“Mama yangu, alipata pigo la ubakaji mara mbili. La kwanza, lilifanywa na Arafat, la pili, likatekelezwa na askari wa JKT waliojaa uchu usiovumilika. Kisa, aliwaeleza ukweli, kwamba yeye ni muathirika hivyo si vyema kushiriki nao katika tendo. Ila hawakumuamini, sababu tu, alikuwa na unoofu ulioficha maradhi yake. Na siku hii, ndiyo aliaga dunia punde alivyobakwa na askari hao. Wapatao watatu.”

“Hii haiwezi kukufanya uonewe huruma. Kisa cha mama yako kinatuhusu nini?”

“Lengo mufahamu binadamu tulivyo. Asili yetu ni ubinafsi wenye maslahi pekee. Sasa hao ni nani wanaotaka maslahi ya wengi? Waache, watu wahangaike kivyao.”

“Nimeambiwa una kisasi…” nilisema.

“Sahihi. Tena kikali mno, cha kuhakikisha, waume, pasi na kujali umri mnaangamia.”

“Ina maana nawe ni muathirika?”

“Ilinibidi niutafute huo ugonjwa kwa udi na uvumba, kisasi changu kipate kutimia. Na ndiyo maana nimeanza na wale wa majeshini. Watu waliochangia katizo la uhai wa mama yangu.”

“Oohoooo!”

“Haina haja ya kushangaa. Ninyi ni watu waovu sana. Hampaswi kusamehewa. Na adhabu yenu pekee ni hiyo. Ili mustahimili hisia zenu.”



Maongezi yakawa mengi. Kwani kila mmoja alielezea historia iliyomfanya aingie katika mpango huo, baadaye, ndipo wakawa radhi kutuelezea wapi walipo wapendwa wangu, na mahasimu wakubwa wa waratibu wa mipango hiyo. Jamila na mzee Namahala. Lakini, haikuwa bahati upande wetu. Kwani punde tu, mmoja wao alivyoanza kuingia na nuio la kuzungumza, mlio wa ving’ora ulisikika. Tena kwa kasi ya ajabu kuzunguka jengo tulilopo. Kitendo kilichotufahamisha sote, mlio huo unasikika kwenye gari za jeshi la polisi.

“Tumevamiwa!” nilijisemeza. Hofu ikichipua kwa kasi na kupoteza kiasi cha amani nilichonacho.



Tukaduwaa!



Hasa mimi na afande Mzee. Hatukutaraji tukio hilo lingelitokea. Lililotokana na uzembe wetu, wa kumpa nafasi awali, afande Madevu achezee simu atakavyo.

“Tushapoteza,” nilisema. Macho yangu yakiwa pima kwa afande Madevu na Chitoko, wakionekana wenye nyuso za furaha, kufurahia tukio lililojiri.

“Hapana! Bado tuna nafasi, usihangaike na hayo makelele ya nje,” alisema afande Mzee. Kauli aliyoitamka pasi na chembe ya hofu. Huku, akielekea eneo lile lile la mwanzo kuchungulia nje ajionee kiendeleacho.



Kweli! Walikuwa askari. Askari wa jeshi la polisi. Wengi tu, wakiwa wamebeba bunduki vyema. Kwa mtindo ufahamikao ki—komando. Na wamevaa mavazi yazuiayo risasi kuingia mwilini baadhi ya sehemu. Hasa, kuanzia kifuani hadi kiunoni walivaa ballistic vest, na kofia ngumu pia kichwani. Nilishuhudia hili, baada ya nami kufanya chungulio mara afande Mzee alivyomaliza kuchungulia.



Baadaye aliwarudia wale watu. Tena akiwa na ukakamavu wa hali ya juu, wajihi umefunga utisho, cheko limezibwa na kingo za mdomo, si wakati wa mzaha. Kiasi kwamba afande Madevu na Chitoko wakaishiwa pozi kitu gani kimpacho ujasiri.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Afande Madevu. Ewe ni mkubwa wangu, kuanzia umri, kikazi, ila sina budi kukuonesha ukubwa wa busara nilionao, ambao Mwenyezi Mungu kakupunguzia. Nahitaji jamii yetu iwe huru, iwe na amani, na kitu kiitwacho fedheha, baina ya mtu na mtu kitoweke. Ndiyo maana nafanya haya yote kwa sasa. Nikihitimisha, sina mbadala wa kuendelea. Nitaachana nayo. Jamii ibaki kusherehekea ushujaa na busara zangu, kwa sababu wazee, tuwategemeao kwenye kazi, munashindwa kusimama kwenye misingi hitajika.



Inaumiza sana. Kuona mtu uliyebarikiwa wajihi wenye kuaminisha uaminifu machoni mwa wengi, unakuwa baradhuli, usiyepaswa kupewa nobe! Ya chembe ya msamaha. Ama nini imani kuhusu malipo ya ubaya kwa baadaye?



Sasa, nakupa ombi, kama sio onyo. Nafahamu, wewe ndiye uliyewaleta hao waliopo nje. Lengo waje watuweke chini ya ulinzi. Sikatai, ni uamuzi sahihi, ila nina jambo nalohitaji ulifanye. Fanya, kama ulivyofanya mwanzo, kuwaondoa watu hao mahali hapa, la sivyo familia yako, itaenda kukukosa hivi punde, kabla nasi hatujaingia kwenye mikono ya sheria. Sio hivyo tu, utaenda kudhalilika muda si mrefu, na kupoteza imani yote ndani ya jeshi na jamii ituzungukayo,” alisema afande Mzee. Kauli ambazo, ziliishiwa kupotezewa tu kwa muambiwa.



Aliziona hazina nguvu yoyote ya kuleta mabadiliko kwa upande wake. Aliziona kama kelele, za paka aombapo chakula. Na kuonesha kwamba hajatishika. Alibinua mdomo kumkebehi, kisha akatema mate pembeni. Wakati huo macho yangu yakiwa pima, kuchungulia kule nje, muda mwingine kuangalia kiendeleacho ndani. Hofu! Haikuniacha.



Baadaye nilimuona afande Mzee akitoa picha ya mnato katika moja ya mfuko wake wa suruali akakamkabidhi afande Madevu.

“Fanya chaguzi hapo, kabla sijaamua cha kuamua,” alisema afande Mzee. Afande Madevu akiwa katumbulia picha aliyokabidhiwa. Huku dhihaka na kebehi alizozijaza awali zikipotea taratibu. Mshangao ukichukua nafasi, pasi na sahau hofu.



Picha ilimuonyesha akipokea burungutu la pesa toka kwa mzee Namahala!

“Amua mapema. Kabla ya hao wa nje hawajapandwa na morali ya…” alisema afande Mzee, ila hakuhitimisha kauli yake. Alisitishwa na sauti ya kipaza sauti toka nje iliyokuwa inatuhadhari.

“Ilani!... Ilani!... Ilani! Enyi watu wote waliomo ndani, mnaamriwa na serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania, kujisalimisha mbele yetu haraka na kwa amani, la sivyo tutatumia nguvu,” ilisikika sauti hiyo mara tatu. Toka kwa kamanda aongozaye kundi la askari waliopo.



Wote tukabaki kumkodolea macho afande Madevu. Kushuhudia uamuzi ataoufanya nusura ipatikane.









Jioni! Ya saa kumi na moja. Vijiwe vingi vilipambwa kwa habari za upatikanaji wa tiba ya ugonjwa sugu duniani. Ukimwi! Si vijiwe vya kina mama wala waume, kwa pamoja hawakusita kuzungumzia mbadala wa gonjwa hilo, lililosumbua mamia ya wengi, miaka nenda rudi.



Wengi wao, walijawa na furaha. Tena iliyopitiliza, ishara kuwa wako huru kucheza watakavyo. Kile kiwapacho hofu, kiwakosechasho amani kinaenda kutokomezwa. Ama kuwa sawa na magonjwa mengine yachukuliwayo kawaida.



Dhahiri! Taarifa hiyo kwao, ilikuwa sawa na zuio la kina mchezoni. Waliona wamehalalishiwa kucheza pasipo kinga zozote, kwa sababu baadaye wakijikwaa, watapata tiba pasi na shaka ya aina yoyote.



Shaka yao iliondolewa, kwa ongezeko la taarifa nyingine, iliyowafikia mara baada ya ile ya mwanzo. Kwamba, nchi yetu inakuwa ya kwanza kwa ajili ya matumizi ya dawa hizo.

“Watoa taarifa wanasema, miongoni mwa watu waliochangia upatikanaji wa dawa kwa kiasi kikubwa yumo pia mtanzania, ndiyo maana wanaanza kuleta huku ndipo yanafuata mataifa mengine,” alisikika mmoja wa vijana walioketi kituo cha daladala Mwanjelwa.

“Acha utani ndugu. Ina maana siye ndiye wa mwanzo?” aliuliza kijana mwingine miongoni mwao. Akionekana mwingi wa furaha.

“Huamini?”

“Eeh!...naona kama njozi hiki nisikiacho.”

“Basi huo ndiyo ukweli. Hospitali yenyewe inaenda kujengwa wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma. Huko ndiko kutakuwa na kliniki kubwa ya tiba ya huu ugonjwa.”

“Aaaah! Ewe baba wa mbinguni, tuangazie nuru waja wako,” aliendelea kusema yule kijana. Afahamikaye kwa jina la Mwaipopo, na kuvuta macho ya wengi huku akiwatengenezea ulizo na dhanio akilini mwao.

“Yumkini naye ni mmoja miongoni mwa waathirika,” walijisemeza wengi wao. Waliopoteza muda kumtumbulia macho pasi na kitu cha msingi chenye manufaa kwao.



Pindi mamia ya watu wakifurahishwa na upatikanaji wa tiba ya ugonjwa wa ukimwi, hali ilikuwa tofauti kwa Jamila. Taarifa hizo zilikuwa kero kwake. Zilimletea ukerehekaji, ambao siwezi utambua ni kwa kiwango gani.



Kilichomkerehesha, watu aliowapatia maradhi wanaenda kusimama siku si nyingi. Hivyo kufanya kazi yake kuwa sawa na bure. Akajiona kajisumbua, jambo ambalo kwake aliliweka mwiko.

“Huyu mfanyabiashara kamwe sitompa nafasi ya kukamilisha hili. Lazima taifa liangamie, ili iwe fundisho kwa vizazi vijavyo, viwe makini na kitu kiitwacho hisia,” alijisemeza. Akiwa, kaketi mbele ya jengo moja kuukuu. Maeneo ya Sai.

Hakuwa radhi, kujionea kisasi chake kinateketea motoni, ilhali ana uwezo thabiti wa kuudhihirishia umma yeye ni mtu wa aina gani. Pia anaichukuliaje jamii kwa ujumla.



Upande wa pili, mzee Namahala alikuwa sawa na Jamila. Ukizingatia wote ni waathirika. Wao hawakuhitaji tiba. Shida yao kubwa ni ubinafsi wa matatizo yaliyowakumba. Naye hakuwa radhi kumuacha Vumilia anatamba katika ulimwengu wa biashara aushikiliao kwa muda mrefu.



Tiba ya ugonjwa wa ukimwi aliipiga marufuku kuingizwa nchini. Ulaji wake, uendelee kuneemeka.

“Kumruhusu afanye hiki kitu ni sawa na kukubali angamizo langu. Mbona kwa kutumia hizi dawa watu wanaendelea kuishi?” alijiuliza mzee Namahala. Akiwa nyumbani kwake akifanya maandalizi ya hapa na pale tayari kwa kuondoka.

__________



“Naomba usifanye chochote, nitawaondoa hao watu,” alisema afande Madevu. Baada ya tafakuri ya muda mrefu.



Kweli!



Kuthibitisha. Aliomba simu, akaandika ujumbe kwa mtu kusudiwa, alivyomaliza aliirejesha kwa afande Mzee.



Haikuchukua muda. Askari wakaanza kuingia ndani ya gari zao na kuondoka. Tena kwa kasi mno, ijapokuwa kuna baadhi wakawa wanatolea sana macho jengo tulilopo kwa matamanio warejee wafanye yao. Kama mjuavyo, pasi na kugusa gusa mwili wa mhalifu hawajisikii vizuri. Kama mgonjwa aliyoko chumba cha uangalizi maalumu.

Hakika walijaa uchu. Kwangu, niliuona wa waziwazi kutokana na angaza yao pindi nachungulia.

“Mmmh! Hapana, hawa jamaa wanaweza kurudi muda si mrefu,” nilijisemeza.



Kwa sababu ya hofu na mambo ya intellijensia. Niliyahofia sana. Japo sikuwa mwanataaluma kindaki ndaki. Niliyafahamu kwa uchache, ambayo asilimia kubwa huficha uhalisia machoni mwa wengi. Huonesha na hualalisha porojo za kinafiki kuwa ukweli. Hivyo niliamini, lazima warejee kwa mara nyingine na kwa namna tofauti na ile ya mwanzo.

“Sina imani napo tena hapa,” nilimnong’oneza afande Mzee.

“Hata nami. Ila hatupaswi kuonesha hali hiyo, tutawapa nguvu hawa mabaradhuli. Tuendelee na huu ukomavu, huku nikitafuta suluhisho kabla hapajaharibika zaidi.”

“Sawa. Naendelea kuangaza angaza hapa nje, kama kutakuwa na jipya, nitakushtua.”



Kazi ikasalia moja tu. Kufahamu eneo. Wapendwa wangu walikohifadhiwa. Japo, kuna ulizo halikuacha kujichimbua na baadaye kufifia. Shangazi alitoka gerezani? Kama alitoka, maisha yake yalikuwa wapi baada ya hapo?



Maswali haya yaliniumiza vilivyo. Kama sio kunipotezea amani wakati mwingine. Abdul nilipatikana. Kila kona ilinipamba kwa matatizo. Yaliyojitengeneza kisa tu, nimeonesha wema wa manufaa ya wengi. Hapa ndipo nikaamini, duniani hamna mtu mwenye huruma, kama tunaiamini ile kauli aliyoitamka shangazi siku za nyuma. ‘Kila mnyonge, na mnyonge wake.’



Nikaenda mbali pia, kwa kuiamini kauli ya Chitoko. Kwamba, sisi ‘binadamu asili yetu ni ubinafsi.’ Hii kauli ilinipeleka kwa kutazama muda wa maongezi yetu. Asilimia kubwa, hupenda kusikia mazuri yatuhusuyo na sio mabaya. Na tumekuwa waumini wa kufurahia mabaya ya wenzetu kana kwamba tuna chembe ya utakatifu wa milele.

Kamwe! Amani haitokuja patikana ulimwenguni.



Kwa kuwa wengi wetu hatuna huruma. Vigogo wengi huamini katika mapigano kuleta amani, jambo ambalo si sahihi. Suluhu haipatikani kwa mapigano. Suluhu hupatikana kwa maongezi. Tena mema yaliyotakasiwa toka yatamkwapo. Hayatamkwi, huku mtamkaji akiwa mwenye uficho wa chuki nafsini.



Mnamo saa 1:45 usiku nikapatiwa kikaratasi kidogo kilichokunjwa na afande Mzee. Alinikabidhi, akiwa ameniambatanishia maneno machache ya kunihadhari.

“Kakifungue huko nje. Tumia huu mlango wa nyuma kutokea.”



Wakati huo kiza kilitapakaa vyema, na kuficha mwanga, utupao nuru ya uangavu wa mboni zetu. Nikawa naona kwa shida, hadi nikaze macho, labda kwenye majengo yaliyopambwa kwa taa kubwa ziwezeshwazo na umeme zilizofungwa kwenye ukigo uzungukao boma. Ama boma lenyewe. Hapo ndipo mboni zangu zilikuwa na nguvu ya kuangaza.



Nilivyoufikia umbali wa kilomita takribani mbili toka mjengoni nilikokuwa, nikakikumbuka kile kikaratasi. Nilikihifadhi katika moja ya mfuko wa suruali niliyovaa. Nikaingiza mkono, nikakitoa. Sikukawia. Nilifanya nililodhamiria. Nilikikunjua na kukisoma. Hii ilikuwa mara ya pili. Mwanzo, nilikisoma mara tu, nilivyouaga mlango wa jengo nililokuwa.



Nikajikumbusha yaliyoaandikwa! Maneno yaliyonitaarifu mahali panapo paswa kuwa mwisho wa safari.

“Mbalizi NMB!”



Sikushangaa kufika hapo. Kilichonitatiza, naenda kukutana na nani, na kwa minajili ipi? Ukizingatia sehemu niendayo ni sehemu ya ulinzi wa askari polisi. Itakuaje endapo nitabainika na mmoja wa askari walindao kabla sijakutana na mlengwa? Iliniumiza kichwa. Ila sikuwa na budi kufuata maelekezo niyavae mafanikio. Ya kujenga heshima kwa wanawake waponzwao na sifa za kile wakifanyacho kwa starehe ya wote wafanyaji. Wake kwa waume!

Mbona wanaume hatupati sifa mbaya kama wao? Kwani, sisi ndiyo tumehalashiwa umiliki wa kutembea ovyo zaidi yao?



Baada ya kutembea umbali mrefu kwa miguu, hatimaye uchovu ukanikamata. Miguu iligoma kusukuma hatua, iling’ang’ana sehemu moja, kuthibitisha haiwezi kuendelea. Nilivyojitia ukaidi, kwa kujaribu kusogeza hatua mbele, nikawa nazalisha maumivu magotini. Maumivu makali, yaliyonishinikiza niichukie safari.



Uzuri!



Tembea yangu ilikuwa ng’ambo ya barabara kuu. Ielekeayo Mbalizi na miji mingine ya mbele. Vwawa, Tunduma mpaka Ndola nchini Zamibia. Hivyo kulikuwa na urahisi wa kupata usafiri wa kunifikisha sehemu nayohitaji na kupooza miguu kwa uchache. Ipate nguvu ya kutembea kwa mara nyingine.



Shauku ya kuwa ndani ya usafiri ikanivaa. Hasa wa gari. Kutokana na kiasi cha pesa nilichonacho. Nilikuwa na shilingi elfu moja tu. Gharama ambayo inajitosheleza kwa usafiri wa daladala ama kosta. Hivyo nikazalisha jukumu, la kuanza kupungia mkono daladala zipate kusimama, ama usafiri wowote wenye nafasi ya kuketi kwa kujinafasi. Sikuhitaji nisimame!



Zoezi hilo likanichukua dakika sita, ndipo nikafanikiwa kupata gari. Mwendo ukawa wa wastani. Mwendo wa hadhari, tusipatwe na madhara. Ijapokuwa sina taaluma ya mambo ya gari, ila sikusita kufanya ukadirio wa mwendo tuliokuwa tunatembea. Spidi hamsini! Hisia zilinituma, dereva hajavusha mshale uonyeshao spidi sehemu hiyo.



Saa 2:09 usiku ndipo niliwasili sehemu nayohitajika. Nikasimama umbali mchache toka jengo la benki lilipo. Hofu ikinikamata vibaya mno kwa sababu ya ufahamu mchache nilionao kuhusu mambo ya ki—benki. Kama sio mteja wa huduma za benki, iwe usiku iwe mchana, huruhusiwi kukaa mahali hapo kutokana na sababu za kiusalama. Lakini nililazimika, kufuata maelezo niliyopatiwa. Sikuwa na jinsi.



Pasi na kufahamu kama najitengenezea hatari!



Kwani! Mwanga mkali wa taa zilizofungwa ukutani mwa jengo zilinimulika haswa na kutoa utambulisho wa wazi mimi ni nani. Nikaanza kata sekunde nikisubiri kifuatacho. Huku nikihangaisha mboni zangu huku na kule, kama kidokozi. Kuona mtu anayekuja pale nilipo, ama kitu chochote.



Zikapita dakika nne. Nikiwa nimesisimama palepale pasipo mafanikio. Hofu ikizidi kupanda kasi, chanuo la kuondoka nalo likashika nafasi. Nilivyoanza kupiga hatua, tayari kwa kuondoka, nikashtushwa na sauti kali nyuma yangu. Iliyosheheni ngurumo na kunipa ubainisho aitaye ni mtu mzima. M—baba mwenye miaka yake. Aliyeumbwa na umbo nene, refu na rangi tuliyoasiliwa nayo. Nyeusi!



Kweli!

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Nilivyogeuka nyuma kumuangalia aniitaye, hakutofautiana na ubashiri wangu. Alikuwa vilevile namna nilivyodhania. Mweusi, mnene na kabahatika kurefuka. Sifa iliyowapiga chenga wanene wengi.

“Ewe kijana njoo hapa,” alisema. Kauli iliyokaribia kunitolesha uharo pasipo matarajio. Ila nikaishia, kutokwa na jasho jingi la woga. Kutetema na hisio la haja kunikaribia.

“Nilijua tu. Kukaa hapa muda mrefu yangelitokea haya,” nilijisemeza. Huku nikipiga hatua kumfuata yule aliyeniita. Ni askari. Askari wa jeshi la polisi kitengo cha kutuliza ghasia. Al—maarufu FFU (field force unit).









Nikawa natembea kwa unyonge. Akili ikiwazua nitachoenda kukutana nacho. Maana, sifa za kitengo hiki nilikwisha zisikia mtaani. Muda mwingine, nikawa na wazo la kutoka mbio. Nimkimbie, ili nipate salama yangu. Ila halikudumu muda mrefu nilivyofikwa na lingine.

“Nenda. Atakuhoji tu, baada ya hapo atakuruhusu uondoke,” kuna sauti niliisikia ikinihasa. Na kunifanya nikubaliane naye. Ikanipa hamasa ya kuzidisha mwendo, nilivyomkaribia, akanisimamisha. Umbali mdogo toka aliposimama. Kwa ajili ya usalama wake.

“Umekaa muda mrefu pale, shida yako nini?” alisema, pasi na salamu. Huku akinitumbulia macho kusaili umbo langu kuanzia unyayoni hadi utosini.

“Aaah!...namsu…” nilisema. Kabla sijahitimisha, nikakatishwa na sauti toka nyuma ya yule askari.

“Huyo ndiye mtu wangu niliyekuwa namsubiri.”



Kauli iliyonishinikiza kupindisha kichwa kumchungulia nipate kumfahamu ni nani.

Bwana jela! Gereza la Karanga. Aliyesaidiana na afande Mzee kunitorosha gerezani.



Ndiyo. Ni yeye. Ila muonekano wake ulizuiwa na mavazi aliyovaa. Mavazi makubwa na mazito kiasi, yaliyompa ugumu wa kutambulika kwa urahisi na wamuonaye. Alivyotufikia, aligongeshana kiwiko na yule askari niliyekuwa nazungumza naye. Ishara ya amani na kumuachia nafasi bwana jela.



Akaondoka. Lakini kwa mtembeo uliojaa wasiwasi sana dhidi yangu. Aliiruhusu akili yake iwe na mashaka kunihusu. Jambo ambalo lilianza kunipa hofu.

“Tuondoke,” alisema bwana jela. Taratibu tukaanza piga hatua kuelekea mahali nisikokufahamu. Macho yangu yakijiibia kumuangalia yule askari. Atafanya nini baada ya kuhisi kitu dhidi yangu.



Sikuamini! Nilimuona kamtoa askari mwenziye kwenye banda na kuanza kuteta jambo, huku akielekeza vidole kule tulikoelekea.

Hofu ikazidi kunipanda!

“Nishashtukiwa,” nilijisemeza.

__________



Mwisho wa safari yetu baina yangu na bwana jela ulikuwa nyumbani kwake. Jambo la kwanza, nilimueleza kuhusu hofu yangu juu ya wale askari. Nilimuhadithia, kuanzia mwanzo hadi ukomo. Mwisho nikampa na ushauri, tunapaswa kufanya nini ili tuwe katika mazingira salama zaidi. Kwani nilivyokumbuka matukio ya mchana, niliona kila dalili ya nyemeleo la ubaya.

“Nimepoteza amani kabisa. Naona naenda kupoteza kila kitu.”

“Ondoa shaka. Hamna baya litalokusogelea,” alisema bwana jela. Kauli iliyonisukuma kupata ulizo. Kama hamna baya litalonikuta, wale askari wa mchana walikuja kwa lengo lipi?



Nikakosa jibu!



Baadaye, simu ya bwana jela ikaita. Chap, aliipokea na kuweka sikioni.

“Tunaanza,” ilisikika sauti ya upande wa pili.

“Nasi tupo tayari,” alijibu. Kisha akaitoa simu sikioni na kuweka juu ya meza. Hakukata!



Kilichofuata toka simuni ni sauti ya kilio. Sauti ya mwanamke na mwanaume. Wakilia, huku wakiambatanisha na kauli za kuomba msamaha, lakini hazikuonekana zina thamani kwa muambiwa.

“Haya nielezeni, mzee Namahala na Jamila wanapatikana wapi?” ilisikika sauti ya mtu aliyekuwa anaombwa msahama na waangua kilio. Afande Mzee. Niliitambua sauti yake!

“Sisi hatufahamu wanaishi wapi, maana makazi yao ni ya kuhama hama.”

“Vumilia na dada yake nao mumewahifadhi wapi?” aliuliza afande Mzee. Swali lililosindikizwa na mbata mgongoni. Nadhani walipigwa kwa bapa ya panga.

“Hao,…hao…wamehifadhiwa. Wamehifadhiwa Chimala. Na usiku huu, wanahitaji wasafarishwe kuelekea jijini Dar es salaam, hapo watapakizwa kwenye usafiri wa basi, hadi mjini Mtwara. Huko ndiko wanakoendwa kuangamizwa.”

“Huo ni mpango wa nani?”

“Mzee Namahala!”

“Nawe vipi kuhusu Jamila?” aliuliza afande Mzee. Swali kwenda kwa Chitoko.

“Mhasimu mkubwa na wa kwanza wa Jamila ni mzee Namahala. Hivyo azma yake ya awali ni kupambana na huyu ndipo afuate Vumilia. Ila nguvu ya Vumilia ikiwa kubwa kwa wakati huu wa mwanzo, ataanza na Vumilia atamalizana na mzee Namahala.”

“Kwa hiyo, muda ulioniambia awali, uliniongopea?”

“Labda wamebadili tu ratiba. Lakini dhumuni liko palepale. Watu hawa lazima wauwawe. Kwa sababu ya umbelembele wao wa kuwapigania wengine, kana kwamba, wawapiganiao hawana macho, mdomo, sikio na ufahamu wa kufanya jambo. Ndiyo maana kwenye majeshi waliepusha dhana hii. Ya kusemeana. Kila mmoja anabeba msalaba wake.”

“Mmmmmmh!” afande Mzee alitoka na mtweto. Ulionitanabaisha kakata tamaa. Ngoma inazidi kuwa ngumu. Ile hali ya kulia haikuwepo tena. Zaidi ya kuhitaji moto kwa ajili ya kubanika, angalabu sauti inaweza sikika baada ya hapo.

__________



Mtweto wa afande Mzee, nami ukaniingizia unyong’onyo. Hata bwana jela naye. Kwani mzunguko alioutamka Chitoko ulikuwa mkubwa, na ulihitaji gharama za haraka ili tuendane sawa.



Hata bwana jela naye hili lilimtatiza. Na kumpandisha hasira maradufu. Tuligwaya, mithili ya mashabiki wa soka tuliokuwa na matumaini ya klabu yetu kuvuka hatua mwishowe tumaini likafifia. Kwa kupata kipigo toka timu pinzani.



Tena simu ilivyokata ndiyo kabisa. Tumaini likazikwa. Kwa kina kirefu, chenye utata wa kukadiria umbali.



Sekunde kadhaa baadaye muito wa ujumbe simuni ukasikika. Kwa pupa, tukaisogelea kuangalia kilichotumwa, kwani nilishahisi mtumaji atakuwa afande Mzee. Kweli! Ni yeye. Alituma ujumbe wenye maneno machache tu. Yaliyosomeka ‘anzeni safari.’

“Tunatolea wapi nauli ya kufika huko?” nikajikuta nimepayuka. Na kumfanya bwana jela anitumbulie macho, niliyohisi anasaili mimi ni mtu wa jinsia gani. Maana malalamiko na hofu yangu haikuendana na jinsia niliyonayo.



Saa 6 usiku safari ikaanza. Baada ya taratibu zote za maandalizi kukamilika. Hasa maandalizi ya kipesa, zitazotusaidia kule tuendako. Tukasafiri na lori, miongoni mwa zile za masafa marefu zitumiazo mpaka wa Tunduma.

“Tumetoka Congo wiki iliyopita. Hapa tunaelekea Dar es salaam kuchukua mzigo,” ilisikika kauli ya dereva katika maongezi yetu, yaliyofanya safari ichangamke.



Mwendo ukawa wa kawaida. Ni maeneo machache sana dereva alijivika ushujaa wa kuongeza kasi kupunguza muda wa kuwasili. Lengo tuwahi! Usingizi ulivyotunyemelea haukuacha kutuathiri. Ulitulevya, na hatimaye tukapiga miangusho. Tena ya muda mrefu sana, kwa sababu ya uchovu.



Tulivyokuja kuzinduka, mapambazuko yalikwishaingia. Huku tukiwa tumevuka miji mingi, na kuukaribia ule tunaopaswa kuwasili. Kisha tuunge safari hadi mkoani Mtwara.



Mchana! Wa saa saba ndipo tuliwasili jijini Dar es salaam. Tukafanya malipo machache kwa dereva wa lile lori na kuondoka kuelekea kituo cha mabasi yaendayo mikoa ya kusini Temeke.

“Wahini Temeke, mutapata basi ya kwenda Mtwara muda huu,” alituasa mmoja wa wasamaria wema miongoni mwa wale tuliowauliza.



Kweli! Kwa kutumia usafiri wa bodaboda tulifanikiwa kuwasili Temeke na kusadiki maelezo ya yule msamaria mwema. Tulikuta basi kituoni, kampuni ya Buti la zungu, tena ikipashwa pashwa tayari kwa kuondoka. Pasi na kukawia tukafanya maongezi na mmoja wa wahudumu kuhusu hitajio letu. Kupata siti!



Muhudumu akatutekelezea, na baada ya sekunde chache tukawa ndani ya gari kwenye siti husika tulizoandikiwa katika tiketi tulizokabidhiwa.

“Uzuri, safari za jioni hamnaga mambo ya trafiki,” alisema bwana jela. Wakati huo macho yangu yakiangaza mazingira ya mule garini na abiria wenzangu. Sauti ya redio ikipasua viwambo vyetu kutuhabarisha yaendeleayo ulimwenguni.



Saa 8:00 mchana safari ikaanza. Taratibu, huku wengi wao tukipata sauti kubashiri muda tutaowasili mjini Mtwara.

“Nahisi hadi kufikia saa nne usiku tutakuwa tushafika,” alisikika mmoja wa abiria aliyeketi siti jirani. Mbele yetu!

“Yeah! Tukishavuka foleni ya hapa mjini, huko mbele hamna shida,” mwenziye alichangia hoja.



Taratibu tuliliacha jiji, na kuanza kuingia miji midogo ya mkoani Pwani. Tulivyofika Mkuranga, sauti ya redio ikatushtua wengi. Kuhusu tukio langu. La kutoroshwa kule gerezani. Wengi wakatega sikio kwa umakini kusikiliza sauti ya mtangazaji, ilivyomalizika, ndipo walibinua kingo za mdomo kutoa maoni.

“Kwa nini hawasemi walichofanya kuwa ni mchezo? Wamemtorosha ili wawasaidie kwenye majukumu yao?” sauti ya wengi ilisikika. Na kunifanya nipatwe na mshtuko. Hizo habari wamezipatia wapi ilhali muhusika sina taarifa.

“Wanataka kunitumia? Kwenye kazi ipi? Na kwa nini hawajaniambia toka mwanzo?” nilijiuliza. Huku nikitumbua macho yangu kumwendea bwana jela. Ambaye alionekana kutojali chochote kuhusu kiongelewacho.

“Hulali?” aliuliza bwana jela. Lengo apotezee angaza yangu iliyojaa shauku na ulizo la ufahamu wa kina.

“Inabidi ulale. Ili ukiamka uwe na nguvu ya kutosha ya utendaji,” aliendelea kusema bwana jela.

“Sawa. Lakini nikiamka, yakupasa uwe na jibu kuhusu nia yenu.”

“Sio ya kwetu. Sema ya serikali,” alisema bwana jela. Kauli tata, iliyoniacha njia panda na kunipa mshangao nilioshindwa kuuzuia.

“Serikali wanahitaji nini kwangu?”









Saa nne usiku tuliwasili mjini Mtwara kama wale abiria walivyobashiri. Kitu cha kwanza bwana jela alitoa taarifa kwa njia ya simu kwa afande Mzee kuomba muongozo unaofuata.

“Fikeni Mangaka! Safari ya saa sita toka hapo,” ilisikika sauti ya afande Mzee.



Sababu ulikuwa ni usiku. Na uchovu ulitukamata, kauli ya afande Mzee tuliifanyia kazi siku iliyofuata. Tulifunga safari hadi Mangaka. Kisha tukaomba muongozo mwingine, tunaopaswa kuutekeleza kuleta amani ya wengi.



Niliamini, ukombozi wa shangazi na baba yangu ungeleta manufaa makubwa kwa wengi. Hivyo walipaswa kukombolewa jamii inufaike nao. Tena kwa ushirikiano madhubuti wa jamii nzima.

“Mchangani, stendi, mkabala na kituo cha mafuta kifahamikacho Kinje,” ulikuwa ujumbe toka kwa afande Mzee kumtaarifu bwana jela. Tunakopaswa kumalizia misheni yetu. Ili ikiwezekana, tufanye ukombozi.

“Watu wenye maono na manufaa ya wengi. Wanapaswa kupiganiwa na wengi!” nilijisemeza. Baada ya tafakuri kwa kina, kuhusu ushiriki wa jamii kufanikisha ukombozi wa wapendwa wangu, ambao kila uchao taarifa zao hazikuacha kurushwa. Kupitia vyombo mbalimbali vya habari.



Saa kumi jioni tukaenda kuchunguza mazingira tuliyoambiwa. Tulifunga safari hadi stendi. Iliyojengwa nje ya mji barabara kuu ielekeayo Masasi. Stendi na hicho kituo cha mafuta tulivyoelezwa ndiyo yalikuwa majengo ya mwisho kama unaelekea Masasi. Na ndiyo ya mwanzo kama unaingia mji wa Mangaka. Baada ya hapo unakutana na kichaka kabla hujakutana na kijiji kiitwacho Ndwika.



Mazingira tuliyokutana nayo, dhahiri yakatuhaminisha kuna uwezokano mkubwa wa mtu kufanya uhalifu kisha unatokomea. Kwani pande zote kulitawaliwa na kichaka kikubwa kilichobeba baadhi ya mashamba ya wakazi wa Mangaka.



Tukaanzia stendi. Baada ya hapo tukavuka upande wa pili ilikojengwa sheli. Kilikuwa kituo kidogo tu. Huku huduma yake ikiwa haba. Nadhani hakikuwa kituo cha uhakika sana kwa huduma.

“Kwa hiyo hapa ndipo watafanyia tukio?”

“Mmmh! Si unaona mazingira yanaruhusu. Wanafanya chap, kisha wanaenda kuwatupia porini huko.

“Kitendo cha kikatili sana waendacho kufanya hawa watu. Kwa nini wanashindwa kutambua umuhimu wa manufaa ya wengi? Badala yake wanajiangalia wao kwanza?”

“Ndiyo dunia ya leo. Wacha tujaribu bahati yetu, yumkini tutawazuia.”

__________



Usiku! Saa tatu. Tukazuru pale sheli. Kwa mnyapio, toka nyuma ya jengo. Ambako kulijengwa ukuta wa kimo cha kati. Ajabu, ama msaada kwetu. Muda huo hakukuwa na taa yoyote iwakayo. Sijajua kama umeme ulikata ama palikuwa na hitilafu ya kiufundi wahusika wameshindwa kushughulikia.



Hivyo kukawa na kiza. Tena kikali, kwa sababu eneo jirani kulipambwa na mikorosho iliyofungamana. Mmoja, mmoja. Kwa utaratibu usioleta makelele, tulipanda ukuta na kuteremkia upande wa pili. Usawa wa vyoo. Kisha tukaambaa ambaa na ukuta hadi pembe iliyotuwezesha kuona mazingira ya mbele yalivyo. Kulikuwa na kitu tu. Kitumikacho na mlinzi kuketi. Tulivyotega sikio kwa makini, tukasikia michako ndani ya jengo. Ya mtu akitembea na minong’ono.

“Hapa pana ulinzi. Ila nahisi ni wa kawaida. Hauna nguvu sana,” alisema bwana jela.



Na kweli! Sekunde chache baadaye tulimshuhudia mzee mfupi akiwa kabeba bunduki. Aina ya gobori iliyompita kimo akitoka ndani na kwenda kuketi kwenye kile kiti.

“Mzee tunataka tuanze kazi. Hivyo usiruhusu mtu kusogelea jirani,” ilisikika sauti toka ndani ikimuhasa yule mlinzi.

“Ondoeni shaka. Hili ni eneo rafiki kwenu.”

Kauli iliyosikika ndani ikatuaminisha, tuliowafuata, kweli wamo. Na wanaenda kufanyikiwa kile tulichoelezwa. Na nani? Hatukufahamu. Kwa sababu, tuliamini Jamila, ama mzee Namahala hawezi kusafiri umbali mrefu kuja kutekeleza mauaji. Kuna watu walitumwa. Na ndiyo walikuwemo ndani!



Baadaye tukaanza kusikia purkushani. Kidogo hizi zilikuwa zenye ushindo mkubwa. Zilizoashiria kuna ushindani baina ya watendewa na mtendaji.

“Mtaondoka duniani kwa aibu. Ninyi wenyewe ndiyo mtahusika na vifo vyenu. Kwani usiku huu, tunaenda kuweka historia isiyokuwa sahaulifu kwenu. Makacho, washa kamera, halafu ewe Kitabu vua nguo zao tushughulike,” ilisikika sauti mule ndani. Iliyotufanya, nami na bwana jela tutazamane kwa mshangao na ulizo.

“Wanaenda kubakwa kwanza,” tulisema kwa pamoja. Ila kwa sauti ya unong’ozi.



Kilichofuata ni purkushani za nguvu zaidi ya zile tulizosikia awali na minong’ono isiyoisha. Hadi mlinzi akaanza kuingiwa na wasiwasi alivyohisi anaweza kutembelea mtu akasikia yatendekayo. Akatengeneza hofu na kibarua chake!

“Jamani punguzeni makelele yanasikika kwa nguvu huku nje,” alisema yule mlinzi. Akiwa usawa wa dirishani chumba walicho watesi.



Alivyorudi kuketi. Bwana jela akaambaa ambaa na ukuta, kwa usaidizi wa kiza na mnyapio usio sikika. Alikuja kushtakiwa alivyomkaribia mlinzi. Mlinzi aliruka kwa hofu. Na kukumbuka bunduki yake alikohifadhi ila haikumsaidia. Kwani, alikuwa kaivaa. Mtutu ukielekea chini, huku kitako cha bunduki kikizidi urefu wa bega kidogo. Na kumpatia wakati mgumu wa kuivua ili aiweke katika mtindo mzuri utaomwezesha aiweke kimapigano.



Chap! Bwana jela akapeleka moja ya mkono usawa wa mtutu na kuikamata kwa nguvu. Mlinzi akaishia kushikwa na butwaa. Japo hakuacha kufanya purkushani za kujiokoa na kuifikirisha akili afanye nini apate usalama zaidi.



Maana akiruhusu kupiga makekele ingelikuwa shida kwake pia. Watu wangelijaa, kwa nia ya kutoa msaada halafu ingelikuwa tatizo kwa wale waliopo ndani. Watu wa usalama wakishawasili. Na ilikuwa lazima wawasili.



Purkushani walizozalisha watu wa ndani walizisikia. Na kujawa shauku ya kutaka kufahamu nini kimemkabili mlinzi. Wakapaza sauti kwa kiasi kuhoji.

“Mzee kulikoni? Umepatwa na tatizo gani?” waliuliza. Mmoja wao akifungua mlango taratibu kuchungulia.



Alivyojionea kuna mtanange, akapiga hatua kwenda kutoa msaada. Ila kabla hajawafikia niliokota kipande cha jiwe chenye uzani kiasi na kulenga usawa wa mbele aendao.



Shabaha ikawa upande wangu! Akakumbana na lile jiwe hadi akatoa mguno wa nguvu. Uliowashinikiza waliosalia ndani watoke na ulizo.

“Huko nje kuna nini? Mbona munataka tuharibiane?”

“Kumeharibika wanangu,” alijibu yule niliyempiga. Taratibu akienda chini kuugulia maumivu. Viganja vya mikono yake, kaikumbata kwenye moja ya jicho. Alipopigwa na jiwe!



Pasi na mpangilio. Waliomo ndani wakakurupuka na kutoka mbio kila mmoja akipita pande yake kupotelea kichakani. Yule niliyempiga jiwe, alivyojaribu, nikamuwahi. Nilimkimbilia na kumkamata asifanye chochote japo hakuacha kutafuta nusura ya uokozi.

“Tulia. Ukileta mchezo nakuchakaza sasa hivi,” nilimgombeza. Kwa sauti ya ngurumo yenye kuashiria ubabe.



Bwana jela akamzimisha mlinzi. Konde kadhaa alizopiga sehemu hatarishi. Kisha akakimbilia ndani akajionee hali iliyopo.



Hakukutamanika!



Watu aliowakuta, walikuwa uchi. Aliwakuta kama walivyozaliwa. Huku wamechafuliwa vilivyo kwa manii. Alishuhudia kupitia mwanga hafifu toka kwenye simu punde alivyoiwasha. Pembeni yao kukiwa na stendi ya kamera.



Aliowakuta, walikuwa watu sahihi tuliowafuata. Baba na shangazi. Siha zao zikiwa mbaya kwa michubuko. Midomo walifungwa na kuna vingine vingi vya ajabu walitendewa ambavyo havikuoneka kwa haraka.



Hakusita! Aliwafungua. Akawarushia mavazi yao, wakavaa .Baada ya hapo akawasaidia taratibu kutoka nje.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Tumeingiliwa, huku tukiwa tunarekodiwa,” walisema kwa pamoja. Kwa sauti dhoofu iliyotupatia nasi unyonge.



Kama ilivyo ada. Baadaye tuliomba muongozo kwa afande Mzee. Nini kifuatacho kwa hatua tuliyofikia.

“Unakuja msaada hivi punde,” alisikika afande Mzee.



Hakika! Kauli ya afande Mzee ikawa ya uhakika. Dakika mbili tu baadaye, gari ya wagonjwa imilikiwayo na kituo cha afya Mangaka ikawasili.



Hapo ndipo nikaamini, kuna mpango naopaswa kutumikia serikalini.





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog