Search This Blog

Tuesday 1 November 2022

NIKUITE NANI? - 3

 






Simulizi : Nikuite Nani? 
Sehemu Ya Tatu (3)








Ubaridi mchache ulitamalaki ndani ya chumba. Harufu ya kemikali mbalimbali zikakerehesha nafsi yangu, sambamba na vitu vilivyopo ndani ya chumba hicho. Kila nilivyotupa macho huku na kule mazingira hayakuwa yanifurahishayo, yalikuwa mazingira yanichukizayo kila leo na ambayo daima siyatamanigi kuwepo.



Niliweza kuyatambua kwa uharaka kwa sababu ya harufu ifukizayo na vile nivionavyo. Vitanda vilivyotandikwa vyema shuka nyeupe zenye maandishi yaliyosomeka msd. Nilivyoangaza yaliyonizunguka kwa ukaribu, nami nikafahamu fika, niko kwenye moja kati ya vitanda vilivyopo mule chumbani. Huku baadhi ya sehemu ya viungo vya mwili wangu umefungwa bandeji, dripu ya maji nayo ikitiririsha vyema maji kuelekea mwilini mwangu.

“Nini kinisumbuacho?” nilijiuliza. Ila kabla sijajijibu, taswira ya Jamila ikaambaa ambaa machoni. Nayo haikuchukua muda mrefu, nikajikuta niko na kumbukizi nyingine, iliyotukutanisha baina yangu na shangazi. Nikakumbuka maongezi yetu.

“Abdul…”

“Naam!” niliitikia, lakini hakuwa mwepesi wa kuufanyia kazi wito wangu. Alisita kwa muda, takribani sekunde hamsini ndipo akaendeleza.

“…kama wewe ni mmoja miongoni mwa wafuasi waaminiao kila mnyonge na mnyonge wake kama mimi, basi tambua hakuna binadamu mwenye huruma hapa duniani.”



Mwisho wa kumbukizi hii nikavuta taswira ya kitendo nilichofanyiwa na Jamila. Hakika! shangazi alikuwa sahihi, tena kwa asilimia zote, ijapokuwa ile siku sikumuelewa amaanichasho. Angali alinipatia kazi pia ya kufanyia tafiti kauli yake.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Hali ya kumbukizi ilistopishwa punde viwambo vyangu vya sikio vilivyoruhusu usikiaji. Muungurumo wa vishindo vya viatu sakafuni. Si kiatu cha mtu mmoja, watu wengi ambao nilikosa dhanio la kadirio wako kiasi gani. Ila walivyoingia wodini, pasi na kukawia, nilianza utambuzi wa idadi yao, nilivyomfahamu; nilihamia kwenye suala la kutambua ni kina nani kupitia muonekano wao.



Wazi, wengi wao hazikuwa sura ngeni mbonini mwangu. Walikuwa askari, wale waliokuja ile siku nyumbani kwa kina Jamila, ijapokuwa baadhi hawakuvaa sare. Nilivyohamishia akili kwenye suala la sura kwa sura, nilimfahamu yule kiongozi wao sambamba na mzee Namahala ambaye waliambatana naye.



Moja kwa moja wakaja kukizingira kitanda changu, mithili ya wanagenzi watokao chuoni kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo. Nyuso zao zikitamalaki shari zilizopelekea kunipa kumbusho la jambo. Maongezi baina yangu na shangazi!

“…hupaswi kumwamini mtu umsaidiaye…” nilikumbuka kauli hii. Na kunifanya nimkumbuke Jamila pia. Mwishowe, nikajidharau, kwanini sikuifanyia kazi.



Sekunde zilikatika pasipo wale watu kufungua kingo za midomo yao kuzungumza. Kila mmoja nilimuona akihangaika huku na kule kusaili namna nilivyolazwa pale kitandani, muda mwingine husogeleana kunong’onezana.

Ukimya ulifukuzwa takribani sekunde mia moja tisini baadaye toka walivyokuja. Huku yule kiongozi wao ndiye aliyefanya jambo hilo baada ya kumuuliza mzee Namahala.

“Kwa hiyo unataka kutuambia huyu kashirikiana na mwanao kumuua mkeo?” aliuliza askari huyo. Niliyemtambua kwa jina la Afande Tumainiel Madevu.



Pasi na tegemeo, wangu fuadi ukalipuka hamaniko. Na fikra mbalimbali zilizonipeleka kwenye maulizo niliyoshindwa jijibu.

“Nimeua?...ina maana nimeunganishwa kwenye tukio alilofanya Jamila?” nilijiuliza, huku macho yangu yakiwa ng’amu ng’amu kuwasaili waendeleacho kufanya.



Pindi nikiwa kwenye tafakuri hiyo, nikagutushwa na jibu la mzee Namahala.

“Sahihi afande, huyu kashirikiana naye kwenye tukio. Kwani ndiye rafikiye mkubwa hapa mjini,” alisema mzee Namahala. Wajihi ukiwa umefura ndita tele za shari kwangu. Alimaanisha alichozungumza!

“Basi yafaa kuwa chini ya ulinzi mkali asije toroka.”

“Sahihi! Na atatusaidia kumpata mwenziye,” alisema mzee Namahala. Kauli ambayo ilinishinikiza kuugulia kilio cha chinichini.



Dhahiri! Nilishindwa kuizuia hiyo hali. Ilinilazimu kufanya, nikiwa na imani nitaondoa fukuto la uchungu lililonianza kuchipukia punde kutokana na kauli waongeazo. Ijapokuwa ongea yao ilitawaliwa na upotezaji mwingi kama si muongelewa.



Baada ya kukamilisha walichothubutu kufanya kwangu uhitaji wa uwepo wao ukatoweka. Wakaondoka! Ila waliniachia wakati mgumu sana wa uamuzi. Wakati ulionishinikiza niendelee kulia, tena awamu hii, kilio cha nguvu kilichowaibua hadi wagonjwa waliopo jirani yangu. Si wao pekee, hata baadhi ya wauguzi na madaktari waliopo wodi jirani waliofikiwa na sauti ya kilio nitoacho hawakusita kunijia pale kitandani.

“Kulikoni?” ndiyo kauli yao ya kwanza kuitoa, huku wakisaili saili vifaa tiba vyao kama vipo sahihi sambamba na sehemu iliyokuwa inapatiwa tiba mwilini mwangu. Kama ina athari ipelekeayo kutoa kilio.



Kabla sijainua kingo za mdomo wangu kwa ajili ya kuwajibu nikapata kumbusho la kauli ya shangazi.

“…wengi wetu binadamu, hatunaga akili zenye msimamo…” sikumalizia. Nikakatishwa na midundo ya viatu vilivyokuwa vinaingia wodini. Nikainua kichwa kuchungulia. Nikambaini ni mganga mkuu, tembea yake ikionekana kuwa ya shari tele kwangu.

“Maendeleo yake yapoje?” aliuliza pasi na salamu.

“Anaendelea vyema kiongozi.”

“Kilio nilichosikia kimetokana na nini?”

“Sijajua, ndiyo tulikuwa tunamfanyia tafiti tufahamu.”

“Fanyeni hima kisha mnijuze. Maana huyu kuanzia sasa yuko hatiani kwa kufanya mauaji ya kukusudia. Hivyo hapaswi kuondoka hospitalini kwa idhini yetu hadi amri ya jeshi la polisi.”

“Hamna shida kiongozi.”



Ki—ujumla kauli zao hazikuwa zenye matumaini kwangu. Zilijaa umivu, tena umivu tele lisilovumilika. Yote kwa sababu ya upendo. Upendo wangu umeniponza, kwa yule niliyehitaji nimfanye awe huru mbele ya jamii yetu asisemangwe semangwe ovyo.



Hakika nilijuta. Upendo! Ndiyo ulionifanya nifikie hapa. Tena ni upendo madhubuti toka ndani ya moyo wangu. Sina budi kuweka wazi kwa sababu hata uvumilivu umechipua hisia za ushindwa.



Baadaye yule mganga mkuu akaondoka. Wakafuatia wengineo, mmoja mmoja, hadi akasalia muuguzi wa zamu. Akinisogelea zaidi pale kitandani akaanza nihoji.



Mahojiano yake hayakuwa marefu. Yalikuwa ya muda mfupi tu, baada ya hapo akaondoka na kuniachia wasaa wa kufanya tafakuri.

Awamu hii nikakumbuka kwa uzuri ile kauli ya shangazi ambayo ilikatishwa na kishindo cha viatu vya mganga mkuu.

“…wengi wetu binadamu hatunaga akili zenye msimamo. Tumekuwa na akili za uyumbaji ndiyo maana wanasiasa hutufanya kama watoto wadogo. Wanatuendesha watakavyo mithili ya kima ahadiwaye na maembe. Hivyo ili uwe imara, ni lazima uondokane na dhana hii. Kama umeamua kufanya jambo, fanya pasipo kujali unakutana na changamoto za aina gani. Kamwe, usidiriki KUKATA TAMAA!”



Kumbukizi hii ikafunua matumaini mapya moyoni mwangu. Kwamba sipaswi kumkasirikia yule aliyesababisha niwe matatizoni na kuacha kufanya kile nilichodhamiria. Imani ilianza niaminisha hatua iliyoko mbele yangu ni nzuri kuliko ya sasa. Kuhakikisha hilo kuwa timilifu, nilipiga sala kisha nikatulia.

__________



Jitihada za madaktari zilichukua wiki mbili kuponya tatizo nililonalo. Nikawa vyema, ijapokuwa haikutengemaa sawia kama awali. Lakini muda huo wote nilikuwa chini ya ulinzi mkali wa askari polisi. Askari wanne ambao walikuwa wanafanyiana zamu.



Baada ya wiki mbili na siku nne nikaruhusiwa kuondoka pale hospitalini. Ondoka yangu, haikuwa ya kwenda nyumbani, bali kituo cha polisi kuanza hatua za mashtaka niliyotuhumiwa. Mwendo kutoka hospitalini, ulikuwa wa dakika nane tu. Tulivyofika nikaingizwa kaunta, nikaamriwa kuvua vitu vihisivyo kuashiria hatari nikakabidhi kwa askari wa zamu, nikafuatia kuandika maelezo kisha nikaingizwa mahabusu kusubiri hatua inayofuata. Kwenda mahakamani!



Taswira ya Jamila ndiyo kitu cha kwanza kilichoambaa ambaa akilini mwangu. Nikaenda mbali kwa kukumbuka namna nilivyojitoa kwa ajili yake, lakini kabla sijahitimisha, nikapatwa na taswira ya mzee Namahala. Huyu akabadili hali ya hewa. Nikamuona kama chui ama mkuki uliotolewa motoni na kwenda kukitisha moyoni. Sikuacha kumtofautisha na mnyama yeyote aliyetawaliwa sifa na tabia kali ziogopwazo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Wawili hawa waliteka akili yangu barabara. Tena nikifikiria juu ya kifungo cha maisha, huwa naishiwa nguvu zaidi mithili ya mgonjwa aliyoko mahututi. Ndoto yangu nayo, naiona inateketea motoni. Katika moto mkali niuonao umeibuka ghafla.



Mafikirio hayo nilisitisha punde nilivyoguswa na kiganja cha mkono, kisha nikapatiwa wito kwamba nahitajika chumba cha mahojiano. Sikupinga, nilinyanyuka pale nilipoketi na kuelekea sehemu niliyohitajika punde mlango wa mahabusu ulivyofunguliwa na mmoja wa askari aliyoko zamu.



Nikiwa njiani kuelekea, akili yangu ikakesha kuwaza namna mahojiano yatavyoendeshwa. Na askari ambaye niliamini atakuwa na mwili uliojazia na sura mbaya kama wacheza filamu za mizuka. Picha ya kupigwa vikali na kutapakaa kwa damu ikatawala vya kutosha, huku kipigio kikiwa kitu fulani kama chuma kilichosheheni vipini vidogo vidogo.



Fikirio likaenda mbali, kwamba wakati narejeshwa mahabusu sitokuwa na jiweza kwa chochote kutokana na kipigo nitachopatiwa.



Ajabu! Wazo hili lilikatika ghafla, punde nilivyomuona mtu aliyeketi kwenye kiti cha mhojaji. Alikuwa yule muuguzi, ambaye aliniuliza maswali ile siku mara baada ya mganga mkuu kuondoka.

“Nipo kwa ajili ya msaada wako,” alisema, pindi nikiwa hima kuketi kitini macho yangu pima kwake kwa kutoamini nikionacho.

“Majibu ya kile unachojiuliza kipo katikati ya majibu utayonipatia kupitia maswali yangu,” aliendelea kusema, kiasi kwamba akanipa utata wa kufahamu dhamirio lake ni lipi.

“Wewe ni nani?” nilijikuta namuuliza pasipo tarajio. Kwani lilikuja ghafla nilivyopatwa taswira ya mzee Namahala na kumbukizi za maafisa wa ulinzi na usalama watumiavyo pandikizi zao kuwapeleleza watuhumiwa wao.

“Mbona unaonekana kama hauna akili timamu. Muda huu tu, ushanisahau?” alisema yule muuguzi. Kauli ambayo ilijaa ukereheshaji kwangu. Nikachukia!

“Nimekuuliza, wewe ni nani? Jibu kulingana na namna nilivyokuuliza si…” nilisema nikiwa na hamaniko lakini sikumalizia kauli yangu nikakatishwa.

“Akili yako haipo sawa. Unahitajika kupatiwa vipimo…” naye alisema kwa ukali, ila baadaye akapoa na kuzungumza taratibu. Akaninong’oneza… “hiyo ndiyo nafasi pekee ya kuokoka toka kwenye tuhuma hii. Hamna namna nyingine, la sivyo utasota mpaka…” alisema kisha akanyanyuka pale kitini. Akatembea hatua kadhaa na kusimama.

“Jina langu ni Chitoko Chindume. Kama utabahatika kunihitaji siku yoyote kabla hujapandishwa kizimbani toa taarifa kwa askari zitanifikia,” aliendelea kusema. Hali iliyonifanya nishindwe kumtambua yeye ni mtu wa aina gani? Kaingiwaje huruma juu yangu? Na nini dhamirio lake kwangu?



Aliniacha hayawani. Kwa kushindwa kumtambua kama ni mtu wa msaada kwangu, ama nia yake aniingize chaka ili askari wapate wepesi wa kushughulika nami.

__________









Siku mbili baadaye yule muuguzi alirejea tena kituoni. Siku ambayo nilikesha kukereheka kwa sababu ya afya yangu kuiona haiko vyema, halafu nikiwaambia askari walioko zamu hunitolea maneno ya shombo kama sio binadamu mwenziye.



Kama ilivyo ada, nikapata wasaa wa kukutana naye. Kwenye kilekile chumba cha awali huku akiwa na muonekano tofauti. Muonekano uliojaa hasira, kiasi kwamba akanipa ambukizo la uogofyaji.

“Nina hakika umefanyia kazi ujumbe wangu,” alisema, punde baada ya kusabahiana.

“Ndiyo, ila siwezi kutoa jibu kwa kuzungumza.”

“Unataka kwa njia ipi?”

“Maandishi!”

“Ina maana nikuletee kalamu na karatasi?”

“Litakuwa jambo jema,” nilidhamiria kufanya hivyo, mara baada ya kumbukizi kadhaa ambazo dhahiri hazimuachi mtu salama hata kama alikuwa na nia ovu juu yako.

“…ukiwa katika mazingira magumu, fanya jambo litalomshawishi yule akuleteaye mazingira hayo alainike.” Niliikumbuka kauli ya shangazi.



Vitu nilivyoomba viliwasilishwa sekunde sabini baadaye toka ombi lilivyotolewa. Nikakabidhiwa, nikavikagua huku na kule, nilivyojihakikishia viko vyema nikaanza kutiririka yakereheshayo wangu fuadi. Ijapokuwa hadi kufikia muda huo sikuwa na imani, kama Chitoko ni mtu mwema kwangu. Ila kupitia maandishi, nilijiaminisha atavaa huruma ya lazima pasipo mapendo yake.



“Asalam alleykhum!



Nikupe pole kwa kazi uliyojivika, ila ni wajibu wako kwa sababu wote ni watu wa taifa moja. Huna budi kuvaa huruma, na moyo wa msaada kama ilivyo kwangu, japo leo hii vimeniponza. Mimi sina tofauti nawe. Japokuwa sikuamini hata chembe. Nakufananisha na hao watumiao jengo hili kutoa huduma. Ambao siku zote hujiona kama uzao wao ni wa kuteremshwa huku wakisahau wamepitia mapajani mwa mwanamke.



Juu ya mashaka niliyonayo kukuhusu, sina budi kuweka hisia zangu wazi kwako ili ukipendezwa tujumuike katika kutatua lile nilipigialo kelele nafsini mwangu litoweke mbele ya jamii yetu. Kwani siku zote wataalamu hunena, hakuna harakati za mtu mmoja katika jitihada za kufikia maendeleo. Hivyo kama nawe ni muumini wa dhana hii yafaa ujiunge nami ili tuitengeneza jamii yenye kutazamika.



Naamini ujumbe wangu hautoupuuzia, utaufanyia kazi, na kufuta dhana yangu ya tamanio kuwa hitajio thabiti. Nia yangu ya dhati, ni kuifanya ile sehemu aliyoko Jamila, inatoweka machoni mwa watu kisha kuwapa dhana itayowafumbua maisha yanawezekana pasipo kuutumia mwili wao kama sehemu ya biashara. Kwa sababu madhara yake unayafahamu.



Hebu vuta taswira, kisha iambae ambae machoni mwako kwa muda mrefu, mama yako yupo katika hiyo kazi. Halafu watu wasasambuao fahari yake ni vijana wenye umri mdogo. Acha kujisikia vibaya, huo ni mfano tu, ila ndiyo ukweli kwa jamaa wenye watu wa namna hiyo.



Njoo tuungane ili tulete heshima. Ila ruhusa hii usiitumie kama mchepuko ajivikaye hati miliki ya mahusiano.”



Nilivyohitimisha nikakamkabidhi ile karatasi, kalamu nikaitua mezani. Hakukawia! Akaanza isoma, alitumia takribani dakika moja na sekunde nne tu kutamatisha, akafuatia kuichana chana na kutupia kwenye kapu la taka. Ila muonekano wake ukaonekana kubadilika ghafla, maneno yalimchoma. Lakini hakuweza kuzungumza jambo, aliishia kunitazama kwa jicho la shari kisha akapiga hatua kuondoka.



Hazikupita sekunde tano, mmoja wa askari walioko zamu akanifuata. Akanibeba mzobe mzobe kunirudisha mahabusu huku nikimwazia Chitoko namna atavyoyafanyia kazi maneno yangu.

“Yamemfika, na nina hakika atatambua nimaanichacho kama ana akili timamu,” nilijisemeza, taratibu nikiyatanguliza makalio yangu chini niweze kuketi.

“Chitoko ni mwerevu asiye na fikirio. Anataka kunifanya ni mjinga kwa hisio la kutokwenda shule basi anaamini uelewa umenipitia kushoto,” niliendelea kujisemeza, macho yangu yakiangaza paa lililotandwa na buibui. Baada ya hapo nikapitiwa na usingizi.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Sauti ya mzee Namahala iliyokuwa inaunguruma kaunta ndiyo iliyonizindua. Kiza kikianza kufukuza mwanga mule chumbani na kunifanya nitambue huo ni usiku, usiku mchanga usiorutubishwa vyema. Pasipo kuchelea nikajiinua, nikapikicha macho na kukaa sawa. Masikio sikuyapeleka mbali, nikayaweka kwa ukaribu ninyake kile azungumzacho mzee huyo.

“Enhee!...huyu ndege wangu ashahojiwa?” alisikika mzee Namahala. Akiwauliza askari wa zamu.

“Bado. Maana mpaka muda huu hatujapatiwa taarifa ya daktari toka hospitalini kuonyesha afya yake imetengemaa zaidi na kama tunaweza anza kumuhoji,” alijibu mmoja miongoni mwa wale askari. Askari wa kike, ambaye tamka yake ya matamshi nilimuona ni mtu mwenye weledi wa juu zaidi ya mzee Namahala juu ya uzee wote alionao.

“Kwanini mnamchelewesha hivyo? Wakati ni sasa, huyu inabidi akae ndani pamoja na yule mpuuzi wake ili waniachie amani yangu huku uraiani.”

“Usihofu mzee, mambo yatakaa vyema kwa mujibu wa sheria…” alisema yule askari wa awali, ila hakumalizia kauli yake akakatishwa na mzee Namahala.

“Kwa mujibu wa sheria? Sheria hiyo itajadili nini ilhali washatenda tukio?”

“Hapana. Wana wajibu na haki zote kama ilivyo kwa mshitaki. Pungua jazba, weka moyo sawa, mambo yatanyooka tu.”



Kauli za mzee Namahala zilinipa utambulisho wa kiasi cha shari alichonacho. Si kwa Jamila tu, bali na kwangu pia, kwa imani aliyojijengea kwamba kuna vitu ninavyovifahamu vinavyomhusu. Tena si vitu vimleteavyo sifa njema, hapana, sifa mbaya, zaidi ya zile zilizomzunguka Jamila.



Picha la mapambano mapana likajijenga akilini mwangu. Namna ya kupambana na Jamila, mzee Namahala na jeshi la polisi. Kuna muda nikawa najiona niko juu ya mapambano hayo, nikiwa na maana ni mshindi. Lakini badiliko hujitokeza ghafla nipatwapo wazo la hadhi, ulinganifu wa hali ya kiuchumi na mvuto. Naishiwa pozi, kwa sababu mwenzangu hali zao ziko vyema tofauti nami. Kwa upande wa mzee Namahala, ni mfanyabiashara hivyo ana nguvu ya pesa, Jamila, ana nguvu ya mvuto kupitia jinsia yake. Kwa upande wangu hakukuwa na chochote chenye kuleta urubuni. Hapo ndipo naliona anguko langu.



Mazingira ya jela nikawa nayaona kwa ukaribu mbele yangu!

__________



Usiku ulivyokuwa mwingi, na mara baada ya mzee Namahala kuondoka, Chitoko akawasili. Nilitambua ujio wake kupitia mazungumzo aliyofanya baina yake na askari waliopo kaunta. Kitendo hiki kikanishangaza, kwani haikuwa kawaida kutembelea mahali hapa tangu nilivyoletwa.



Katikati ya mshangao wangu, nikaongezwa mshangao mwingine, niliitwa, na kuhitajika kumfuata mtoa wito, ambaye ni mmoja kati ya askari walioko kaunta. Maongozano yetu yakaishia hapo, nilivyopiga jicho huku na kule kwa haraka nikatambua idadi ya watu tuliopo. Watu wanne, askari wawili pamoja na Chitoko. Lakini kuna askari wengine walikuwepo nje wakidumisha ulinzi. Askari wa ulinzi!

“Mbona wito usiku usiku kulikoni?” nilimuuliza Chitoko, sura yangu ikitamalaki ashirio la kutopendezwa na kitendo hicho.

“Unahoji hoji nini? Wewe si mtuhumiwa? Hupaswi kuhoji, wajibu wako ni kufuata maelekezo unayopatiwa,” alisema yule askari aliyenifuata mahabusu pindi akiketi kitini. Kauli iliyonifanya nijawe na ghazabu lisilotawalika. Na viapo vya ajabu ajabu kwa askari.

“Eeeh!...bhana eh! Muacheni mteja wangu,” alisema Chitoko huku akinipiga begani na moja ya mkono wake kuashiria nimfuate aelekeako. Nikamfuata! Wakati huo mkononi nimefungwa pingu na yule askari aliyenitoa chumba cha mahabusu.



Hatua zetu zikawa fupi fupi hadi nje ya jengo, muda wote akili yangu ikimfikiria Chitoko ni mtu wa aina gani kwa kuwa muda wote yupo kiraia na anapata wasaa wa kuzungumza na mtuhumiwa wa mauaji. Si kuzungumza tu, hata kufanya jambo lingine lolote ajisikialo.

“Huyu ni askari, wale wasiovaa sare,” nilijisemeza nikiwa naigamia bodi ya gari, aina ya Toyota Vanguard. Wakati huohuo nikimtathmini alivyononoka.

“Ingia ndani ya gari tuondoke,” alisema.

“Tunaelekea wapi?”

“Hospitalini!”



Nikatii kauli yake. Nilifungua mlango kisha nikapanda ndani ya gari. Naye akazunguka upande wa pili, akafungua mlango na kupanda.



Sekunde kadhaa baadaye safari ikaanza. Akili yangu ikikosa uvumilivu wa kufikiria. Naenda kufanyiwa nini tuendako. Sikuishia hapo, nilifikiria na visa vingine pia, mwishowe nikajikuta najirushia lawama baada ya kukumbuka maongezi yangu yote na Chitoko kuna sehemu nilimzungumzia Jamila. Hii ni picha kamili kwao, na inawapa nguvu ya kuwaaminisha tuna ukaribu.

“Hivi nini maana ya mchepuko mwenye hati miliki ya mahusiano?” aliuliza Chitoko. Swali lililovunja fikirio langu.



Sikutoa jibu kwa uharaka, nilianza kupiga jicho kumtathmini alivyovaa ndipo nikafungua kingo zangu kumjibu.

“Wewe si umeolewa?”

“Hapana! Sijaolewa.”

“Ila una mahusiano na mwanaume?”

“Ndiyo, mbona maswali mengi halafu hujibu kile nilichokuuliza?”

“Naelekea kukujibu. Huyo mwanaume uliyonayo ni mwanaume halali ama ni mume wa mtu?” niliuliza na kumtupia jicho, naye akafanya vivyo hivyo. Alinikodolea macho pima mithili ya mtu agundulikaye maovu yake.



Kikapita kimya, takribani sekunde kumi na saba huku tukitengeneza shauku ndani ya mioyo yetu ya kuzungumza.

“Yeah! Ni mume wa mtu,” alijibu huku akinikazia jicho kusubiri kauli yangu ijayo.

“Basi nawe ni mmoja kati ya wanawake wenye tabia hiyo. Wanawake, waishio na waume za watu hujiaminisha wao ni bora na wako juu zaidi ya wake wa wanaume husika. Hebu vuta kumbukumbu, unakuwa katika hali gani ukutanapo na mke wa mwanaume unayetembea naye?”



Swali hili pia alikosa wepesi wa kunijibu. Aliishia kunitumbulia macho akijifanya yuko bize na udereva. Nami sikutaka kumghasi, nilijua namna lilivyo mgonga ndiyo maana yuko katika hali hiyo. Ila nikakazia jambo.

“Hiyo si kwa wanawake tu, hata wanaume pia.”



Nilivyohitimisha tu kauli hiyo tukawa tumewasili eneo la maegesho ya vyombo vya usafiri hospitali husika. Ileile nilivyolazwa mwanzo. Tukateremka na kuongozana kwenye moja ya chumba. Akawasha taa, mwanga ukatupa nuru ya kuona sehemu za kuketi. Nikatumia wasaa huo kusaili vilivyo ili nijibu baadhi ya fikirio. Kweli! Nilivyo angaza huku na kule katika mavazi aliyovaa nilionao bandiko la utambulisho, bandiko dogo ambalo alilivaa kwenye bwela suti lenye rangi nyeusi likiwa na bendera ya taifa na maandishi kadhaa.



Nilivyoangaza yale maandishi niliona neno WP, mbele yake kukawa na namba zilizofutika futika hivyo sikuzitambua vizuri ni namba gani. Lakini kupitia neno la awali nililoliona, niliweza kumtambua fika. Kwamba huyo ni askari polisi. Kazi kubwa aliyonayo kwangu ni kunipeleleza.



Hamad! Hayakuwa matarajio yangu. Kwa sababu nilimpa nafasi ya kumuamini kiasi. Yumkini angeliweza kunisaidia kile nikitakacho.

“Kwanini umediriki kuhusika na mauaji ya mke wa mzee Namahala?” ilikuwa kauli ya kwanza toka kwa Chitoko. Kauli ambayo sikuwahi dhania kama itapata tokea siku akaniuliza. Kwa sababu maongezi yake siku zote hayakuegemea huko.



Dhahiri Nilishangazwa. Tena mshangao wangu ulizalisha simanzi pale nipatapo hatua ya mwisho ya hicho kinachonikabili. Kifungo cha maisha na katisho la ndoto yangu. Niliumia sana. Umivu kali ambalo siwezi lielezea.

Picha kamili likajijenga akilini mwangu, niko mikononi mwa maharamia wenye dhumuni la kuhalalisha haramu.

“Sipaswi kuwachekea,” nilijisemeza huku nikifikiria kitu cha kumjibu Chitoko. Na hasira ikipasua kifua kwa kasi kwenda kukaba koo.

“Kumbe nawe huna tofauti na waumini wajipimao uzuri kupitia sehemu ya nyama za paja. Na wale waaminiao mng’aro wa picha za mnato huchangia ubora wa mng’aro wa akili,” nilisema kwa jazba na kunyanyuka kitini kwa kasi, lengo nitoke nje nirudi kituoni kwa sababu nilihisi kuna kitu kinaweza tokea.



Naye hakutaka hilo litokee. Akainuka kwa uharaka pale kitini akanifuata nilipo na kunishika mkono. Huku moja ya mkono wake, wa kushoto kakamatia rununu.

“Hupaswi kuondoka humu ndani hadi…” alisema, lakini hakumalizia kauli yake. Muito wa rununu ukamsitisha. Kwa pupa, tukajikuta tumetolea macho kwenye skrini. Tukakumbana na jina la mpigaji. Jamila!



Hatimaye tukajikuta tunashangaana, mshangao uliochukua takribani sekunde kumi na tatu, tulivyorudisha akili sawa ili tuendelee na mada ya tukio tulilonalo, tukazuiwa na tukio la mlango wa chumba tulichopo ukifunguliwa. Sura za afande Tumainiel Madevu, mzee Namahala na askari mwingine aliyechafukwa kwa sura zikajibainisha.

“Hujatosheka na tukio moja la mauaji ulilofanya? Hivyo unataka kutuulia askari wetu?” aliuliza afande Madevu. Macho pima kwangu.

“Huu ndiyo mwisho wangu,” nilijisemeza, taratibu ulegevu ukinichukua na kuenea katika viungo vyote mwilini.

__________









Kilichofuata baada ya pale sikukielewa. Kwani nilifunikwa boshori iliyotobolewa tundu tatu, usawa wa machoni mawili, lingine usawa wa pua na mdomo.



Lengo la tundu hizi, niweze kuona, kupumua na kuzungumza. Ila ajabu sikupata wasaa huo. Kwani punde tu nilivyovishwa nilipatwa na harufu fulani iliyokata mawasiliano yangu yote ya utambuzi. Mwishowe nikaishiwa fahamu!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Sikumbuki nilichukua muda gani kuwa hivyo. Maana hata nilivyorejewa na fahamu, awali fahamu yangu haikukaa sawa mpaka nilipozinduliwa na maji ya baridi yaliyotolewa muda si mrefu jokofuni.

“Upo himayani mwetu. Huna budi kuendana na matakwa tuyatakayo,” alisema afande Tumainiel Madevu. Mkononi kakamatia rungu, huku viganjani kavaa glavu kuzuia kuacha alama kwenye rungu na ngozi yangu.



Nilivyopiga jicho huku na kule kusaili mule chumbani, ambapo achilia mbali watu tuliomo, wanne, vingine vilivyomo ni kiti, kilichokaliwa nami pamoja na meza kubwa iliyo mbele yangu. Wale watu wengine walikuwa wamesimama kunizunguka. Ambao ni afande Tumainiel Madevu, mzee Namahala pamoja na yule askari mwingine wa kiume mwenye umbo lililotisha tisha.



Mule chumbani mulitamalaki mwanga hafifu wa mshumaa, hivyo kunifanya mazingira ya kuta nisiyatambue vyema, ila yalikuwa na kila dalili za ubaya kutokana na harufu ya uvundo wa vitu vilivyooza.

“Eeh!...leo nimeingia pabaya…” nilijisemeza na kutulia kwa muda. Takribani sekunde tano kisha nikaendelea… “…usalama wangu wa kuendelea kuishi ni mdogo. Yote ni kwa sababu ya kutaka kuitakasa ile jamii, hapo ubaya uko wapi? Ama mpaka leo hii bado wanaamini malipo ya wema ni ubaya?”



Ulizo langu la nafsi lilikosa jibu. Nikaishia kupiga sala kumuomba Mwenyezi Mungu aninusuru na balaa hilo.

“Wamenileta hapa wanitese ili nikubaliane na hii tuhuma yao. Nini kilichopo kwa mzee Namahala hadi…” nilijisemeza baada ya kuhitimisha sala. Lakini sikumalizia kauli, baada ya kuingiwa na kumbukizi imuhusuyo Chitoko. Nikajiuliza, yuko wapi? Yule mwenye jina la Jamila aliyempigia ni nani? Kwanini alishtuka nilivyoliona? Nikapata picha, yumkini ni Jamila yule nimfahamuye. Wana ushirikiano, ushirikiano wa kuniangamiza ili wapate wasaa wa kufanya mambo yao. Wapambane na mzee Namahala.



Mawazo haya yalisumbua akili yangu, mwishoni nikapatwa na uaminisho ulionishinikiza nijawe na hamu ya kufahamu picha kati ya mzee Namahala na Jamila litaishaje. Picha ambalo askari polisi nao wameingizwa kwa maslahi binafsi ya kujinoofisha.

“Tunamchelewesha,” alisema mzee Namahala. Kauli ambayo ilisisimua viungo vya mwili wangu na kuruhusu akili ipambanue kipigo nitachopatiwa ni cha aina gani.



Haikuchukua muda mrefu, toka mzee Namahala atamatishe ile kauli nikaanza kushukiwa na kipigo kikali kutoka kwa yule askari mwenye sura ya kitisho pamoja na afande Tumainiel Madevu. Kila mmoja alinipiga palipomfaa, ijapokuwa nilikuwa najaribu kutumia mikono yangu kujikinga nayo lakini ilivyozidiwa na maumivu niliiteremsha na kuzipa nafasi rungu zielekee kule walikokusudia.



Walitumia takribani dakika tano kufanya hilo shambulizi la awali. Ambalo lilikuwa kama ‘briefing' katika kufikia hatua ya kina. Kidogo ikawa hauweni kwangu, ilhali nikigugumia maumivu na kutafakari kijacho baada ya hapo.



Baada ya muda mchache yule askari mwenye utisho alitoka mule chumbani. Ondoko lililozalishwa na unong’ozi alioufanya afande Tumainiel Madevu. Hakuchelea, sekunde chache baadaye alirejea. Akiwa kakamatia bahasha mkononi. Alivyoifikia meza alitoa kilichomo ndani kisha akatupia pale mezani. Karatasi! Zilizojaa maandishi ya mkono. Afande Tumainiel akakazia kwa kunisogezea usawa niliopo. Hazikuwa pekee, aliambatanisha na kopo la wino maalumu wa muhuri. Pasi na sahau kalamu ya wino.

“Weka saini hapo uokoe maisha yako,” alisema yule askari mwenye utisho. Macho akinitumbulia kudhihirisha aongeacho, hajaongea kwa majaribio.



Kauli yake ikanifikirisha nisiyowahi yadhania. Kwamba sina epuko lolote litalojitokeza mbele yangu. Kifungo gerezani kinanihusu. Hivyo nisaini, nisi—saini basi lazima kile walichodhamiria kitatimia. Hapo nikakumbuka filamu mbalimbali za kimapigano, hasa zile za kivita. Mateka akamatwapo hawanaga mzaha naye. Kama atafanikiwa kutoroka, atatoroka huku akiwa na kovu lisilofutika maishani mwake. Na kama atauwawa, vivyo hivyo atafunga safari ya duniani akiwa na kovu. Nami nikaamini nitaondoka mahali hapo, au nitamaliza tuhuma hiyo nikiwa na kovu kubwa ambalo sitolisahau.



Baadaye nikapeleka akili yangu kwenye vitu vilivyopo juu ya meza. Nikajitia ujuaji, kwa kutaka kusoma kilichoandikwa kwenye moja ya karatasi ila kabla sijaanza kufanya hivyo, nikapigwa pigo moja kali kwenye jicho la kushoto huku mpigaji akiambatanisha na kauli zenye lengo la kunipa onyo.

“Tumekuambia weka saini, na sio kusoma. Mpumbavu mkubwa weee…!!” alisema. Wakati huo mikono yangu yote nimeielekezea kwenye jicho lililopigwa kwani maumivu niliyokuwa nayapata hayakuwa ya kawaida.



Sikuwa na budi, ukizingatia uvumilivu wa kugugumia maumivu ulishaaanza kupungua, nilianza kutoa kilio cha nguvu, kutoa uchungu lakini hakikufika mbali kwa sababu ya chumba jinsi kilivyo. Kilikuwa chini ya ardhi. Hivyo sauti ilikuwa haifiki nje.



Katikati ya kilio changu nikaongezwa kipigo kingine. Cha kwenye taya, kilichopigwa na afande Tumainiel huku aking’ang’aniza kukunjua mikono yangu ili aipeleke kwenye kopo la wino wa muhuri nichovye na kuweka alama ya dole gumba kwenye karatasi.

“Atatupotezea muda huyu tukicheka naye,” alisikika pindi akifanya kile kitendo.

“Hivi, ninyi mupo kwa ajili ya ulinzi ama dhuluma za mtu asiye na hatia?” nilijikuta naropoka.

“Wewe mwanahizaya unasema sisi ni wadhulumu?” alidakia yule askari mwenye utisho. Huku akiniparamia kwa makonde mfululizo.



Makonde ya awamu hii yalikuwa yenye nguvu haswa na kipigo chao kilichukua muda mrefu. Taratibu nguvu nazo zikaanza niishia, hali ya ukataji roho kwa mbali nikaanza ishuhudia kiasi kwamba wenyewe wakaingiwa na wasiwasi.

__________



Februari 12, 2008.



Siku hii ndiyo mara yangu ya kwanza kuingia viunga vya mahakama. Tena ni mahakama kuu kanda ya Mbeya baada ya mahakama ya hakimu mkazi kushindwa kushughulikia kesi yangu kwa mujibu wa sheria. Wakati huo ulemavu ukiwa sehemu ya mwili wangu. Kwani sikuwa na vidole viwili mkono wa kuume. Jicho la kushoto nalo lilikosa nguvu ya kuona kwa ufasaha, muda mwingine halikuwa likiisha kutoa machozi. Nilivaa hali ya kuonewa huruma, lakini haikuwa hivyo kwa watu wasimamiao sheria. Wajibu wao ulikuwa mmoja tu, kuhakikisha nahukumiwa.



Kweli! Shitaka likaendeshwa puta, huku vitisho vikinijia kila uchao, kwamba nisivyofanya wakitakacho, basi nitakitafuta kifo cha maumivu. Yaani wataharibu kiungo changu kimoja baada ya kingine hadi kufikia hatua ya mwisho.



Ndani ya miezi kumi na nne tu, kesi ikamalizika. Huku nikila hukumu ya kifungo cha maisha kwa kufanya mauaji ya kukusudia. Utetezi wangu ulikosa nguvu, mashahidi wa kupandikizwa walifanya yao, sambamba na wale wasimamiao sheria. Kwa hadaa ndogo ambayo hairefushi muda wa kuishi.



Sare ya rangi ya chungwa haikuniepuka. Iliyojaa maandishi urekebishaji na kazi ngumu zote katika kutumikia kifungo changu. Nilikosa amani, furaha, lakini sikuwa na jinsi kwa sababu ilishatokea. Yamkini kwa sababu ya uzembe wangu wa kutofahamu sheria ama uchovu wa kimaisha nilionao. Ndoto na mipango yote niliyonayo iliishia kwenye kuta refu ya mawe iliyozunguka gereza. Gereza la Karanga lililopo mjini Moshi. Ndipo nilipelekwa baada ya kuhukumiwa.



Wazo, kwamba ipo siku nitakuwa huru uraiani sikuwanalo. Kwa sababu kila nilivyojichunguza sikuona mtu mwenye nguvu aliye jirani yangu mwenye uwezo wa kutengua hukumu.

“Shangazi! Mpango niliokuahidi unaenda kufeli. Yule niliyekuwa namsaidia kakataa msaada na hatimaye kanigeuka kwa kuona nambughuzi hatofanikisha alichodhamiria. Leo hii, nami niko kule uliko. Nimezungukwa na kuta kubwa za mawe, ambazo zinaninyima nafasi ya kuona mazingira ya nje zaidi ya wingu,” nilijisemeza, nikiwa ndani ya chumba nilalacho. Kwa mbali chozi jembamba likinitiririka.

__________



Jumatano, ya wiki ya pili tangu nilivyoletwa gerezani kuna ugeni ukawasili. Wa waziri wa mambo ya ndani, Mhe. Dkt. Lukia Awadh, akiambatana na waandamizi mbalimbali wa wizara ya mambo ya ndani na majeshi. Jeshi la magereza, jeshi la polisi na idara ya uhamiaji. Dhumuni la ujio wao ni katika ziara ya kutembelea magereza kuangalia hali ya wafungwa kwa nyanja zote. Hivyo wakachaguliwa wafungwa kadhaa kama wawakilishi wa kuonyesha mazingira tuishiyo. Miongoni mwa wafungwa hao, nami nilikuwa mmoja wao.



Uwakilishi wetu ulikuwa wa kutathminiwa baadaye huulizwa maswali kadhaa kuhusu mwenendo wa mashtaka mahakamani na wajibu wa polisi katika kushughulika na kesi. Hatua ambayo tulikuwa tunatumia maandishi kuelezea.

“Unajua kusoma vizuri?” lilikuwa swali toka kwa mmoja miongoni mwa waandamizi wa jeshi la polisi aliyeongozana na msafara wa waziri.



Sauti yake haikuwa ngeni masikioni mwangu. Kiasi kwamba baada ya kuhitimisha swali lake nilimtumbulia macho ya ufananisho kwa sekunde kadhaa kisha nikaingiwa na wajibu wa kutaka kujibu swali lake lakini kabla sijafanya hivyo, akakazia kauli nyingine.

“Ni wewe? Una muda gani humu ndani? Na ulifanya tukio gani?” aliniuliza maswali mengi hadi nikashindwa nianze lipi kulijibu.

“Hadithi ndefu,” nilimjibu huku akinikabidhi karatasi mbili za kujieleza kuhusu dhamira ya ujio wao.

“Chukua na hii, utatumia kunihadithia mkasa uliokukuta hadi ukawa hapa,” alisema. Ni yule askari aliyenikabizigi kadi ya utambulisho siku niliyomtembelea shangazi kituo cha polisi. Mzee Selemani.



Sikusita, nikatumia wasaa huo ipasavyo kwa kuamini unaweza kuwa upenyo wa kufikisha machungu yangu katika kufikia hatua ya ukombozi. Nilihitaji ukombozi wa hali na mali, kwa sababu sikuwa mhusika wa tuhuma niliyohukumiwa nayo. Kwa uharaka mno, nikacharaza muandiko kuhusu hali ya uchunguzi wautakao baada ya hapo nikahamia kwenye mkasa wangu. Huku niliandika mkasa mzima, ila kwa ufupi nisimpatie msomaji uchosho.



Niliandika kuanzia awali. Lengo nililojipangia, mahusiano baina yangu na familia ya kina Jamila, mwishowe matokeo ya harakati zangu katika kile nilicholenga. Nilienda mbali kuelezea taratibu walizotumia askari kufanikisha hatua za upelelezi. Walivyonipiga na kunisababishia ulemavu hadi hatua ya mwisho waliyosalia nayo.

“Kwa sasa huko mtaani kuna vita kali, baina ya mzee Namahala na Jamila. Nia yao kuonyeshana ubabe kwa yale waliyotendeana. Tamanio langu, tukio hili nilishuhudie, na kinachonipa shinikizo la hamu hiyo ni kitendo cha askari wa jeshi ulilopo kujiingiza kwa kila pande wakiwa na nia ya kutoa msaada pande walizopo,” nilitamatisha kwa namna hiyo. Huku nikijenga imani atanielewa nimaanichasho.



Nilivyojihakikishia iko vyema nilimpelekea. Nikimuambatanishia maneno machache ya kumpa mkazo.

“Kama una uwezo, naomba nisadie kutoka humu ndani, kwa sababu natumikia kifungo kisichonihusu,” niliongea kwa unong’ozi wengine waliyeketi jirani naye wasisikie. Baada ya hapo nilipiga hatua kuelekea sehemu nyingine.



Mwisho wa zoezi ulikuwa saa tisa alasiri. Ugeni ukaondoka, nasi tunaelekea kwenye majukumu yetu ya kila siku. Muda huo ulikuwa mahususi kwa kupata chakula kisha kutimkia vyumbani kuifukuzia siku ifuatayo.



Tukio la mchana likanifukuzia mawazo mengine na kusalia pekee akilini. Sikuyapa nafasi, hata kama yalijitokeza, basi ni kwa sekunde chache tu. Kikubwa, kuhusu mafanikio. Nilikuwa najiuliza kama ujumbe wangu unaweza kumshawishi afande Mzee. Hakika! Mpaka panapo kiza cha usiku mnene, lepe la usingizi nililisikia kwa jirani. Kwangu halikubisha hodi, kope zilikesha kusimama muda wote kama nina ugomvi nazo.

“Afande Mzee, ni muda sasa nimejawa na tamanio. Sio tamanio tu, bali ni hitajio la dhati toka ndani ya moyo wangu nipate kumuona Jamila akitamkwa kwa mema na maelezo yenye heshima na sio yamjengeayo kashfa na uchafu kila uchao. Hili ni dhihirisho la dhati, kutokana na kiasi kingi cha upendo kumhusu. Si upendo wa mahusiano ya kimapenzi. La, hasha! Ni upendo wa kirafiki ujengao undugu wa msaada. Kwani, majina aitwayo Jamila huko mtaani, si sahihi kwangu kuyatamka, kwa sababu nahisi nitamvunjia heshima kulingana na kile alichonitendea chenye kunineemesha,” nilijisemeza. Taswira za Jamila na afande Mzee Seleman zikiambaa ambaa usoni.



Siku iliyofuata, punde baada ya kuamka na kufanya usafi wa hapa na pale, kuanzia mwili na mazingira, shughuli za gerezani zikaanzwa kupanga kama ilivyo ada. Kwa asilimia kubwa shughuli hizi zilikuwa hazinihusu. Muda mwingi nilikuwa mtu wa mazingira ya ndani ya gereza. Kama kutoka nje, basi huwa chini ya ulinzi mkali wa askari magereza wakiwa na bunduki SMG (Sub—machine gun) iliyo na kisanduku kilichojazwa risasi thelathini na kisanduku kingine cha akiba, nacho kikiwa na risasi thelathini.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Yote ni kwa sababu ya hukumu niliyonayo. Askari magereza waliaminishwa mimi ni nunda niliyeshindwa mara kibao na jeshi la polisi ndiyo maana nina makovu makubwa. Hivyo wakanichukulia kama mtu mmoja hatari, mithili ya Osama Bin Laden ama wapigaji wa Mungiki watokao nchini Kenya ambao walisumbua kanda ya kaskazini. Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro. Walifanya matukio mengi ya kiuhalifu, hasahasa wizi wa pesa benki ulioondoa uhai wa askari kadhaa wa jeshi la polisi.







Ajabu, siku hii nilitolewa. Na kupewa jukumu la kufanya usafi mazingira yazungukayo ofisi ya bwana jela. Kidogo, ikawa haueni kwangu. Kwa sababu nilikuwa nimebadili mazingira kwa kiasi.



Shughuli ya usafi nikawa naifanya taratibu, mithili ya mtoto mdogo afunzwaye jambo. Japokuwa askari magereza hakubanduka jirani yangu kwa lengo la usimamizi. Sikumbuki nilitumia muda gani kuhitimisha. Ila kumbukizi yangu ipo kwa kitendo kilichofuata baada ya kumaliza. Nilihitajika ofisini kwa bwana jela. Yule askari aliyenisimamia ndiye alinipatia taarifa hii.



Wasiwasi haukuacha kujijenga, kwa sababu ya dondoo fupi nizipatazo kutoka kwa wafungwa wenzangu, kwamba, wengi wahitajikao kwa bwana jela huwa wametenda kosa. Ikanibidi nijifikirishe, nimetenda kosa gani, kiasi kwamba fuadi ukapoteza nuru ya amani ya kunishinikiza nifungue kingo za mdomo wangu kuzungumza.



Jibu la fikirio langu lilipatikana tulipolikaribia lango la kuingia ofisini. Tena ni jibu ambalo lilinizidishia amani kutoweka zaidi.

“Yumkini wale walionileta huku ndiye waliochangia wito huu. Wanataka nizidi kunyamaza zaidi, ili wao waendelee na mambo yao kwa amani na kila aina ya starehe. Ewe Mwenyezi Mungu…” nilisema, ila nilishindwa kuimalizia kauli yangu baada ya kuhisi neno nalohitaji kuhitimisha nalo si zuri. Neno la lawama, kumwendea Mwenyezi Mungu jambo ambalo si vyema kulifanya.



Tulivyoifikia ofisi, yule askari aligonga kisha tukaingia. Tofauti na matarajio yangu, mule ndani mulikuwa na watu wawili, bwana jela na mgeni, ambaye nilivyomuona tu, amani ikaanza kurejea kwa kasi kuziba pengo. Alikuwa afande Mzee Seleman.

“Abdul keti hapo, ewe askari unaweza kusubiri nje,” alisema bwana jela.



Kabla mazungumzo ya kusabahiana na mengineyo hayajaanza, ukapita ukimya takribani sekunde kumi na tano, ulionisukuma kupata kumbukizi ya jambo. Yale maelezo yangu.

“Itakuwa yalimfika,” nilijisemeza, huku nikipiga jicho kumsaili afande Mzee.

Bwana jela akafukuza ukimya!

“Kijana. Kuna mgeni wako hapo, unamfahamu?”

“Ndiyo namfahamu.”

“Basi ana jambo la kuzungumza nawe.”

“Sawa,” nilisema huku nikitingisha tingisha kichwa kuashiria niko tayari kwa mazungumzo.



Muda wote huo afande Mzee alikuwa kimya akitusikiliza tulivyokuwa tunahangaisha ulimi na kingo zetu kuumba maneno. Alikuja kuanza kuzungumza alivyopatiwa wasaa na bwana jela, ndipo naye akadiriki kufungua kingo za mdomo wake kutema yaliyomleta.

“Nimekuja unieleweshe vyema yaliyokukuta,” alisema afande Mzee.



Kabla sijachangia jambo kuhusu hiyo kauli, nilijikohoza kidogo kulainisha koo na kufukuzia mbali vikohozi vichache vilivyoashiria dalili tosha za kutaka kupunguza nguvu ya maneno nitayoyatamka.

“Nahitaji msaada wako nitoke humu ndani. Maana…” nilisema na kuweka tuo baada ya kuhisi jambo ghafla. Kuhusu bwana jela.



Jambo hilo lilinichukua sekunde kadhaa kulifikiria hadi wale nilionao wakapatwa mshangao uliowapa ugumu wa kuniuliza. Kwa sababu hawakufahamu kama nishamaliza kauli yangu ama nilikuwa na nia ya kuiendeleza. Ila afande Mzee aliufukuza ukimya alipoona unazidi kuongezeka.

“Mbona umepoa ghafla? Ama…” naye hakumalizia kauli yake. Nikamkatisha!

“Natamani mazungumzo haya tuyafanye tukiwa wawili pekee,” nilisema, kwa sababu nilikuwa na wasiwasi na bwana jela. Kwamba yumkini ni kibaraka wa wale watu walionileta, hivyo kufanya maongezi mbele yake ni sawa na kufanya mazungumzo mbele yao.

“Hapana, zungumza tu. Huyu mzee hana tatizo lolote,” afande Mzee alinitoa hofu.



Kauli hiyo ikanipa matumaini. Kwamba yale tutayoyazungumza yatabakia mulemule chumbani. Hakuna mtu atayethubutu kuyavusha upande mwingine kwa nia ya kujizolea umaarufu kwamba ni hodari wa kufukunyua taarifa mbalimbali.

“Nduguyo natumikia kifungo pasipo kutenda kosa. Nateseka bure, na matumaini ya kuachana na mateso haya siyaoni. Nahitaji niwe huru kama nilivyokuambia kwenye maelezo yangu awali, ili niendeleze maisha yangu kwa ustadi utukukao.”

“Nani wahusika wa haya?” aliuliza afande Mzee.

“Mzee Namahala, afande Tumainiel Madevu, Chitoko Chindume (Askari wa kike) na Jamila. Wote wapo ulikokuwa unafanyia kazi awali.”

“Mmmh! Pole sana ndugu. Haya ndiyo maisha, yana changamoto nyingi sana, ambazo muda mwingine hukuaminisha hauwezi zitatua hadi mwisho wa maisha yako. Nikupe ahadi, nitafanyia kazi ombi lako mapema iwezekanavyo.”

“Nashukuru sana. Nakuombea kwa Mwenyezi Mungu mipango iende vyema ili nduguyo ninusurike na hii adhabu. Nusura hii haitokuwa kwangu tu, hata kwa wale niliotaka kuwakomboa. Nafahamu, endapo nikitoka, nitaendeleza zile harakati. Nahitaji ile jamii ipate mfano kupitia Jamila. Kule kudhihakiwa na makundi ya wanawake kwa wanaume kufutike, badala yake waonyeshwe kama mfano katika kuchangia maendeleo binafsi.

“Nahitaji wapitapo mahali waitwe jina moja lenye heshima, lililohalalishwa na kumfanya muitaji awe na hofu atamkapo, ya kumpa shinikizo la upambanaji.”

“Usihofu kuhusu hilo, kwa upande wako utalitimiza, labda, litashindwa kuwa timilifu kwa yule utayemsaidia.”

__________



Wiki tatu baadaye toka tulivyokutana na afande Mzee, mipango ya rufaa ikaanza. Kulekule mkoani Mbeya, nilikoanza somewa shitaka awali. Afande Mzee alijivika huruma kuhakikisha mwana apotezwaye narudi sehemu yangu. Sikuwa na budi kufurahi, ijapokuwa upande wa pili niliamini naenda kutengeneza vita kali yenye mapambano ya muda mrefu katika kumfikia mshindi.



Hatua hii haikuwa nyepesi, si kwangu tu, hata kwa afande Mzee naye niliona naenda kumtengenezea mazingira hatarishi na watumishi wenziye. Waliojitengenezea ulaji, sasa kitendo cha kuthubutu kujiingiza ni sawa na kuwatibulia ulaji wao. Hawawezi muacha salama!

“Nitahakikisha haki inasimama upande wako,” alisema afande Mzee, mapema siku ya kwanza pindi tunaingizwa ndani ya ukumbi wa mahakama kwa ajili ya kuanza kusomewa mashtaka.



Wasaa ulivyowadia jaji akaanza kutekeleza wajibu wake. Tena shitaka langu lilikuwa la mwanzo baada ya hapo yakafuatia ya watu wengine.

“Ondoa uoga na hofu. Hapa unapambania maisha yako, hivyo hupaswi kuwatazama maadui zako watakuchukuliaje,” afande Mzee aliniasa. Lengo nampa ushirikiano madhubuti wa kuhakikisha mafanikio yanajitokeza.



Punde hairisho la mahakama lilivyotolewa tukarudishwa mahabusu. Gereza la Luanda, lililoko mkabala na kambi za FFU. Kichwa kikiwa na mengi niwazayo, kiasi kwamba sikuikwepa hofu niwakumbukapo maadui zangu.



Picha pekee iliyo ambaa ambaa usoni mwangu ni kuhusu yale niwazayo. Na kuona chumba kiko tupu, watu wengine waliomo kimo chao niliona sawa na sakafu iliyobomoka bomoka na kupamba chumba tulichopo.

“Hey! Dogo…” mzee mmoja aliyoko jirani yangu alinishtua.



Nikazinduka!



Mithili ya mtu aliyemwagiwa maji ya baridi. Chozi jembamba likitiririka shavuni ilhali sikuwa na kilio cha aina yoyote.

“Vipi unataka kunitambulisha ugeni?” nilijikuta naropoka kutokana na wenge. Taratibu nikipikicha macho kufuta machozi.

“Nimekuona ukilia ndiyo maana nikakushtua.”

“Dah! Ni mawazo tu mzee wangu. Sina tatizo lolote. Na huu ugeni?” nilimuuliza, baada ya kuona idadi yetu imeongezeka mule chumbani.

“Acha utani dogo. Kwani hujamuona pindi analetwa? Si kaletwa na bwana jela akiambatana na mkuu wa kituo cha kati?”

“Eti? Kaletwa muda gani? Naye kaua?” nilimuuliza kwa pupa, pasi na kumpa mpangilio wa swali gani aanze kujibu.



Na hakupata wasaa huo, kwani punde nilivyohitimisha ulizo langu, sauti ya wito iliyoniamuru kuelekea mlangoni ilisikika. Sikukawia, nilitii, huku nikiishia kupiga jicho kwa mzee niliyemuuliza na yule mtuhumiwa mwingine ambaye fikra zangu moja kwa moja ziliniaminisha kuwa ni kibaraka wa wale watu. Ama yumkini naye kabambikiwa tuhuma, ila hisia hii sikuipa nguvu sana.



Hatimaye niliongozana na mtoa wito hadi kwenye moja ya chumba. Kikuukuu, akaniacha humo, na sekunde chache baadaye aliingia afande Mzee, hali iliyonipa sintofahamu na bumbuwazi kwa kutoamini kitokeacho mbele yangu. Alijitokeza wakati sahihi. Wa kujibu yale maswali niliyomuuliza mzee mule chumbani.



Nikamvaa kwa maongezi pasi na salamu.

“Wameanza kazi. Kiasi kwamba sasa naishi kwa wasiwasi tele wa kupoteza maisha yangu,” nilisema, nikiwa nimemkamata afande Mzee mkono wake wa kuume macho yangu pima kwake.

“Kina nani?”

“Hakika! Mwisho wa uhai wangu nauona uko karibu. Sina matumaini ya kuendelea kuwepo. Kwani wale jamaa…” nilisema, ila sikuimalizia kauli. Akanikatisha!

“Mbona sikuelewi?”

“Usichonielewa nini? Wakati nimekuambia wale watu washaanza mapambano?”

“Kivipi?”

“Kuna mtuhumiwa wamemleta muda mfupi uliopita. Sina imani naye yule mtu, moyo wangu unanisukuma ana dalili tele zilizojaa ubaya kunihusu,” nilisema nikiwa nimemkazia macho na sauti pia.

“Hapana. Yupoje huyo mtu?” aliuliza afande Mzee akiwa mwingi wa hamaniko. Kama kuna mbinu fulani anazozifahamu ambazo mara pengi hutumiwa na waandamizi wa jeshi la polisi ama magereza kwa ubaya. Muonekano wa wajihi ulionesha ufahamu wa siri nzito ambayo ilishawahi tokea hapo awali.

“Nashindwa kukueleza anafananaje, ila kwa muonekano ni mwingi wa ukatili.”

“Nisubiri kwanza,” alisema na kuniponyoka chap. Nikasalia chumbani na maulizo yasiyo hesabika.



Sekunde chache baadaye mlango wa chumba nilichopo ukafunguliwa. Kitendo hiki kikanihimiza kuinua kichwa na kuyaongoza macho yangu mlango ulipo. Sikuamini! Hofu ikanikumba, haja ndogo ikanikaba pasipo kutaraji, sura niliyoishuhudia ilinifanya niwe hivyo. Yule mtuhumiwa mgeni niliyehitaji utambulisho wake kule chumbani.



Yale niliyohisi sasa nilianza yaona karibu. Nilivuta picha namna watu watavyohangaika na maziko ya mwili wangu, ambayo nilijiona nimejitakia mwenyewe kwa sababu ya kuingilia mambo ya watu.

“Yale yote nayofanya, nafanya kwa ajili ya jamii kuwa sawa. Napambania heshima ya jamii yangu, hivyo sina budi na hapa kupambana na huyu mtu ili hitajio libaki kuwa hitajio na timizo siku zijazo,” nilijisemeza huku nikimtumbulia macho yule mtu. Maana alikuwa na muonekano wa kuogopwa kama yule askari mwenye utisho.



Sikutaka kupuuzia, niliutaarifu mwili kuwa nipo kwenye makabiliano, kisha nikanyoosha viungo na kufanya subira kumsubiri adui nione atafanyaje. Muda wote macho yakawa kwake. Hivyo ikanipa urahisi wa kuona akitendacho.

Taratibu akawa ananisogelea, nami nikawa narudi nyuma kwa nia ya kumkimbia, tukafanya mizunguko miwili tu, baadaye kasi ikaongezeka na kufanya purkushani izidi mule chumbani.

“Unataka uonywaje ewe mtoto ili uwe mwelevu?” aliuliza yule mtu. Swali nililoshindwa kulijibu, kwa sababu niliipa akili fikirio imekuaje mtu huyo akawa mahali hapo.



Katumwa na nani? Nani aliyemfungulia mule chumbani? Ndiyo maswali niliyokesha kujiuliza huku nikihangaika na suluhu ya kutaka kujiokoa. Sikuhitaji nitumie mlango kutokea, kwa sababu angelinikamata mapema kutokana kuwa ni mgumu kufunguka. Aliurudishia! Na kuubamiza kwa nguvu kweye fremu yake.



Mtafutano wetu ukawa wa kuzunguka zunguka mule chumbani. Huyu akienda kule mimi naenda huku, mwishowe, jamaa akaniwekea tego la mguu lililonifanya nilivae vae hatimaye akanikwida vyema na kunisogeza karibu na usawa aliopo.

“Acha kuharibu mipango ya watu. Hufahamu mabilioni mangapi yamewekezwa katika miradi hiyo,” alinena yule jamaa. Huku akishindilia makonde ya nguvu mwilini. Na kunipata barabara, na kushindwa kupata nafasi ya kujitetea.



Sikuwa na budi, nikaanza angua kilio!



Lakini hakikuweza kuwa msaada kwangu. Kutokana na namna chumba kilivyotengenezwa. Kilitengenezwa sehemu ya kipekee, huku kikiwa na tundu chache na ndogo maalumu kwa ajili ya kuingiza hewa na mwanga. Hakitofautiani na chumba cha mateso!



Sekunde, dakika zilikatika. Kipigo kikiendelea kunishukia, kipigo cha nguvu kana kwamba kimehalalishwa kisheria. Kila nilivyojaribu kufurukuta huku na kule sikupata upenyo wa kunyofoka mikononi mwa huyo jamaa. Zaidi ya kukwepesha sehemu tu za kupigwa. Yaani akinipiga hapa, mara inayofuata anapiga kiungo kingine. Mambo yakawa changanyikeni!



Nafuu yangu ilipatikana punde mlango wa chumba tulichopo ulivyosukumwa kwa nguvu kuashiria kuna mtu anataka kuingia. Fikra zikanituma ni afande Mzee, na kweli ikawa hivyo. Alikuwa afande Mzee, aliingia mzobe mzobe kwa lengo la kukabiliana na yule jamaa ambaye hadi muda huo hakuniachia mpaka pale alivyozibuliwa kofi moja shavuni. Alijiaminisha ana nguvu za kutumudu, pia fikra zilimtuma aliyeingia yupo sehemu ya upande wake. Alifanya kosa kutomuangalia pindi akiingia.



Hatimaye mambo yakabadilika. Kipigo kikahamia upande wake, tena cha mtungo kutoka kwangu na afande Mzee, ambaye alionekana mwingi wa mapigano ya mkono.

“Nani kakutuma?” tuliropoka kwa pamoja, huku tukipeleka makonde mfululizo.

“Hakuna aliyenituma. Nimejituma mwenyewe, kwa sababu nia yenu si thabiti upande wetu,” alisema. Kingo zikitiririsha damu toka mdomoni.

“Kwanini sio thabiti? Ilhali sisi tunafanya kwa ajili ya jamii yote?”

“Wengine watakula wapi ikiwa wote tupo sawa? Lazima tuwe na madaraja ya utofauti ndiyo mambo yataenda vizuri. Endapo tukiwa sawa, tutapoteza kitu kiitwacho heshima.”

“Huamini kuwa tukiwa sawa ndiyo tunajenga heshima? Na kukiwa na utofauti tunajenga dharau?”

“Labda kwa imani zenu.”









Kauli zake zikatupunguza nguvu ya kuendelea kumshambulia. Tulizembea! Naye akatumia wasaa huo kujikakamua kisha akatusukumia pembeni na kupata nafasi ya kukimbia. Tulipokuja pata wazo la kumkimbiza, hasa afande Mzee, tayari alishajisimamia kwa mbio kali.

“Naweza sema hii ni vita,” alisema afande Mzee.

“Tena ihusishayo wapiganaji hodari sana. Wasiotaka kupoteza japo chembe ya sekunde katika ushambuliaji.”

“Mmmmh!...sheria haiwezi kuamua hili. Kwa sababu wanasheria wamo ndani yake.”

“Nasubiri msaada wako wa uamuzi.”

“Lazima nikutane na wote wanaojihusisha.”

“Itaafaa sana. Maana wao ndiyo chanzo cha haya nipatayo.”

“Ondoa shaka, naamini ushindi utasimama upande wako.”

“Amina!”

__________



Jiji lilitamalaki kiza. Nuru za taa za barabarani zilishindwa kufanya kazi yake, kutokana na hitilafu ya transfoma iliyolipuka punde baada ya mvua kubwa kumalizika. Na kuchangia pitapita za watu watembea kwa miguu kuwa hafifu, kwa sababu ya uogofyaji, na wale watembeao kwa pikipiki ama magari wakawa wa nadra pia. Hofu ya uhalifu ilitamalaki, japo kwa wale waliothubutu kutembea muda huo walijivika ushujaa uliochangamana na hofu ndani yake. Na kufanya jiji kuzizima kwa ukimya. Jiji la Mbeya! Al—maarufu jiji la vumbi walivyopenda kuliita baadhi ya watu, hasa wageni waishio ukanda huo.



Wakati huo, afande Mzee naye alikuwa mmoja miongoni mwa watembea kwa miguu. Akipita kando kabisa, karibu na mwisho wa kingo ya barabara maeneo ya Mwanjelwa. Muonekano wake ulipambwa kwa mavazi tatanishi, kama sio hatarishi. Mavazi ambayo daima hutumiwa na watu ovu kuficha uhalisia wao.



Alipambwa kwa koti kubwa jeusi, boshori nyeusi pia, pasi na sahau suruali na buti nazo zilikuwa za rangi hii. Suruali, aliichomekea ndani ya buti, kama ilivyo kawaida ya waavao vazi liitwalo kombati, mwendo ukawa wa wastani akili ikiwa mbali kwa usaili wa jambo.



Alivyofika usawa wa baa ya New City, alipiga tuo kwa sekunde kadhaa, akaangaza huku na kule, kuangalia kama kuna chombo chochote cha usafiri kiko karibu naye kwa utumiaji wa barabara. Alivyojiridhisha hamna, akaanza upya kupiga mguu kuvukia upande wa pili wa barabara.

“Chitoko Chindume!” alijisemeza, akizidi kuchanja mbuga kwa utaratibu, kauli iliyoashiria mwendo wake unamuhusu mtu aliyemtamka.



Alivyofika usawa wa jengo la FINCA, akaweka tuo kwa mara nyingine. Akaangaza huku na kule kisha akavukia upande wa pili. Huko akaweka kituo kwa muda mrefu akilisaili jengo la FINCA na maeneo jirani yazungukayo jengo hilo.



Sekunde chache baadaye!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Alishuhudia moja ya tukio lililomshinikiza kuingiza mkono wake wa kuume na kutoa kamera katika mfuko wa koti alilovaa, maalumu kwa ajili ya urekodiaji wa picha ya video pamoja na picha ya mnato. Kwa uharaka, aliiwasha na kuielekezea mbele ya jengo la FINCA.



Zikapita sekunde saba tu, toka alivyoitoa kamera, kwa muono hafifu, akabahatika kumuona mtu mwenye umbo la kike akitoka kwenye banda litumiwalo na askari kwa ajili ya ulinzi. Nyuma ya mtu huyo alifuatia mwanaume aliyebeba bunduki mgongoni kwa mtindo wa muzzle down (mtutu huelekea chini) kana kwamba hana habari nayo.

“Huu ndiyo wasaa wa ufanikishaji,” alijisemeza huku akibonyeza kitufe kimoja wapo kilichoruhusu mwanga mkali kutoka kwenye kamera uwamulike wale watu kwa sekunde na kuzima. Alipiga picha ya mnato!



ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog