Simulizi : Dunia Haina Usawa
Sehemu Ya Tatu (3)
Kila mmoja alimuonea huruma Godwin, alisimama pale alipokuwa huku akiiangalia maiti ya ndugu yake iliyokuwa kwenye sanduku kubwa mule mochwari. Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makubwa, aliumia, hakuamini kile alichokuwa akikiangalia mbele yake.
Ndugu yake, dada yake aliyekuwa akimpenda hakuwa pamoja naye, kulikuwa na watu ambao waliamua kumuua msichana huyo. Hakujua walikuwa wakina nani, hakujua sababu ila akajiapiza kwamba ilikuwa ni lazima kumtafuta mtu huyo, atakapomjua amuue kwa mkono wake.
Hawakukaa sana humo mochwari, wakatoka huku hali ya Godwin ikiwa imebadilika kabisa. Muda wote alikuwa akilia, moyo wake ulizidi kuwa na maumivu makali. Kichwa chake kikaanza kukumbuka maisha yake ya nyuma, jinsi alivyopambana na ndugu yake huyo ili maisha yao yakae sawa kama yanavyotakiwa kuwa.
Wazazi wao walikufa, vifo ambavyo viliyabadilisha maisha yao na kuwa ya dhiki zaidi. Hawakupata msaada na mbaya zaidi badala ya kufarijiwa na watu wengine kwa maisha waliyokuwa wakipitia, ndiyo kwanza kukatokea watu ambao kila siku walitamani kuona wakiingia kaburini haraka sana.
Kifo cha Irene kilimuonyeshea njia kwamba mtu aliyetakiwa kufuata baada ya hapo alikuwa yeye mwenyewe. Hakutaka kuona akifa, hakutaka kuona akifukiwa kaburini hata kabla hajamgundua na kumuua mtu aliyesababisha mateso makubwa maishani mwake.
Hakuwa na ndugu yeyote aliyebaki ambaye alimfahamu hivyo mazishi ya Irene yalisimamiwa na marafiki zake pamoja na majirani. Aliumia mno, hakutaka kuona ndugu yake akizikwa kama alivyotakiwa kuzikwa, alitaka kuona akizikwa kiheshima kama wengine lakini hilo halikuwezekana.
Wakati jeneza likiingizwa ndani ya kaburi, Godwin akazidi kulia kwani alijua kwamba baada ya hapo asingeweza kumuona tena ndugu yake huyo.
Watu wakaondoka makaburini, Godwin akaelekea nyumbani na kujifungia ndani. Alikuwa akilia, hakujua maisha yangekuwaje pasipo kuwa na ndugu yake huyo ambaye alimzoea kwa kipindi kirefu.
“Ngo..ngo..ngo..” alisikia mlango wa chumbani kwake ukigongwa. Haraka sana akasimama na kwenda kuufungua, mgongaji alikuwa baba mwenye nyumba ambaye akaingia ndani na kuanza kuzungumza na Godwin.
Hakuwa kwenye hali nzuri, alijua kwamba kama wangemuacha akae peke yake basi angechukua uamuzi mbaya. Hakutaka kuona hilo likitokea na ndiyo maana akaamua kwenda humo ndani na kuzungumza naye.
“Nini kinaendelea?” aliuliza baba mwenye nyumba huku akimwangalia Godwin.
“Dada yangu ameuawa,” alisema Godwin huku akiyafuta machozi yaliyokuwa yakiririka mashavuni mwake.
“Najua! Ila nani yupo nyuma ya haya yote?”
“Sijajua! Ila ni watu waliokuwa wakitutafuta kwa kipindi kirefu sana. Wamefanikiwa kumuua Irene, najua kabisa baada yake mimi ndiye nitakayefuata. Sitaki kuona nikifa kabla ya kuwaua kama kulipa kisasi kwa yote yaliyotokea,” alisema Godwin huku akimwangalia mzee huyo.
“Pole sana! Utatakiwa kuwa makini sana.”
Mzee huyo hakukaa sana ndani ya chumba hicho, akatoka na kumuacha Godwin akiendelea kuomboleza kifo cha ndugu yake aliyekuwa ameuawa kikatili.
****
Kihampa alikuwa na furaha tele, kazi kubwa iliyokuwa mbele yake ilikamilika kwa asilimia zaidi ya sitini. Alitakiwa kuhakikisha Godwin na dada yake, Irene wanauawa kikatilia. Maagizo hayo alipewa na mtu aliyekuwa juu yake, aliwatuma vijana wengi kwa ajili ya kufanya mauaji hayo lakini kitu kilichomuudhi ni pale waliposhindwa kufanya mauaji hayo.
Moyo wake ulikasirika, mkubwa wake alimkaripia lakini mwisho wa siku akafanikiwa kumuua Irene. Alijua kwamba mbele yake kulikuwa na kazi kubwa, kumuua Irene hakukuwa na ugumu wowote ule ila kazi kubwa iliyokuwepo ilikuwa ni kumuua Godwin.
Aliwatuma vijana wake wengi kukamilisha kazi hiyo lakini walishindwa, kitendo cha kumuua ndugu yake, Irene kidogo kikampa uhakika kwamba endapo angeshikilia na kufuatilia kwa ukaribu zaidi kama alivyofanya basi kijana huyo angeuawa ndani ya siku chache.
Akawasiliana na mkuu wake na kumwambia kile kilichokuwa kimefanyika, kwamba alipewa kazi ya kumuua Irene na aliifanya kwa nguvu kubwa na baadaye kuutupa mwili huo pembezoni mwa barabara katika Ufukwe wa Coco.
“Ni kazi nzuri sana, natumaini nikimwambia bosi kwamba kazi imefanyika, atafurahi sana,” alisikika mwanaume mmoja kutoka upande wa pili.
“Nitahakikisha ninafanya kila kitu kadiri ya uwezo wangu mkuu,” alisema Kihampa.
“Safi sana. Bado amebaki mmoja, si ndiyo?” alisikika mwanaume huyo akiuliza.
“Ndiyo!”
“Natumaini pia atauawa ndani ya siku chache zijazo, si ndiyo?” aliuliza mwanaume huyo.
“Ndiyo mkuu!”
“Basi hakikisha anauawa haraka iwezekanavyo,” alisema mwanaume huyo na kukata simu.
Kihampa akashusha pumzi ndefu na nzito, alijiona kufanya kazi kubwa mno. Hakutaka kuona akichukua siku nyingi pasipo kukamilisha mauaji ya Godwin hivyo alichokifanya ni kuwapigia simu Michael na Selemani na kuwaambia kwamba kulikuwa na kazi moja iliyobaki, kazi kubwa ya kumuua Godwin kama ilivyokuwa imepangwa.
“Haina shida! Ila si atakuwa msibani, kwa nini tusifanye msiba ukiisha mkuu?” aliuliza Michael.
“Haina shida. Ninachotaka ni kuona mtu huyo akiuawa, hakuna zaidi ya hilo,” alisema Kihampa na kukata simu.
Aliwaamini vijana wake, alijua fika kwamba kama angefanikiwa katika hilo basi sifa zote kutoka kwenye uongozi wa juu zingekwenda kwake. Mauaji hayakutakiwa kufanyika kipindi hicho lakini kila siku alitakiwa kuwapigia simu na kuwasisitizia kwamba kulikuwa na umuhimu mkubwa wa huyo mtu kuuawa.
Baada ya siku tatu, Michael akampigia simu Kihampa na kumwambia kwamba siku hiyo ndiyo ilikuwa ya kufanya mauaji kama walivyokuwa wamepanga. Kama alivyowaambia kipindi cha nyuma kwamba wamshtue mara baada ya mateka kutekwa, akawaambia tena kipindi hicho na vijana hao kumuahidi kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima kuhakikisha wanamteka na kumpa taarifa.
Ilipofika saa kumi na moja jioni, wakaondoka kuelekea Manzese Midizini huku wakiamini kwamba Godwin alikuwa akiishi katika nyumba ile waliyomkuta msichana Irene akiwa na wanawake wengine. Walikuwa na gari jingine, hawakutaka kuteremka, walikuwa ndani ya gari huku wakiangalia huku na kule.
“Yule pale,” alisema Michael mara baada ya kumuona Godwin akiwa nje, alijiinamia huku akionekana kuwa na mawazo tele.
Haraka sana Selemani akaanza kulisogeza gari kule alipokuwa Godwin, walipanga kwamba mara baada ya kufika mahali hapo, basi Michael ateremke na kumfuata kijana huyo, amuonyeshee bastola na kumteka kama ilivyokuwa kwa Irene.
“Lakini unahisi huu ni muda sahihi?” aliuliza Selemani huku mwenzake akiiandaa bastola yake.
“Wewe unaonaje?”
“Sidhani kama ni muda sahihi! Angalia jinsi watu walivyojazana kwa kule pembeni. Tupo uswahilini hapa, unaweza ukawa na bastola halafu ukapigwa mapanga na bastola yako,” alisema Selemani huku akionekana kuwa na hofu.
“Wewe usiogope! Tufanye yetu halafu utanyoosha moja kwa moja kama kipindi kilichopita,” alisema Michael, hakuonekana kuwa na hofu hata kidogo, moyoni mwake aliamini kwamba wangefanikiwa kwa asilimia mia moja juu yake kile walichotaka kukifanya.
Selemani hakujiamini, bado alikuwa na hofu kwa kuhisi kwamba kama wangefanya tukio la utekaji mahali hapo basi ingekuwa ni rahisi kwa vijana waliokuwa mahali hapo kuwafukuza kwa kuwa tu siku chache zilizopita lilifanyika tukio kama hilo, tena mahali hapohapo.
Huku Selemani akizidi kulisogeza gari kuelekea kule alipokuwa Michael, mara wakaliona gari la takataka mbele yao likiwa limeingia mtaani humo kwa ajili ya kukusanya taka, likaziba barabara hiyo na kuiacha kwa udogo sana kiasi kwamba gari lao lisingeweza kupita kama tu wangetaka kupita.
“Hebu subiri kwanza! Njia imeziba kwa mbele! Hatuwezi kutoka. Tusikilizie gari hilo litoke ndipo tukio lifanyike,” alisema Selemani na kumfanya Michael kuiweka bastola yake kiunoni.
Walisubiri kwa dakika kadhaa, gari hilo lilipomaliza kukusanya takataka, likawashwa na kuanza kuondoka na kuwapa nafasi vijana hao kufanya tukio la utekaji na kutokomea mahali hapo.
“Tukifika pale, simamisha gari, nitatoka kwa kasi, nitamteka, watu wakisogea, nitapiga risasi hewani kuwatisha. Wakikimbia, nitamleta ndani ya gari na kuondoka zetu. Umenielewa?” aliuliza Michael.
“Nimekuelewa!”
“Basi twende,” alisema Michael na gari kuanza kwenda kule alipokuwa Godwin. Michael akaishika bastola yake vilivyo, kilichobaki kilikuwa ni kumteka kijana huyo na kuondoka naye kwenda kumuua kama maagizo waliyopewa na Kihampa.
***
Godwin alikuwa kimya kibarazani, hakujua kama lile gari lililokuja likija kule alipokuwa lilikuwa na watu wabaya. Aliendelea kubaki pale nje huku akionekana kuwa na mawazo tele.
Kichwa chake kilikumkumbuka Irene, hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kuendelea kuishi kwa amani na furaha pasipo ndugu yake huyo. Kila siku alikuwa na mawazo juu ya mtu aliyekuwa nyuma ya matukio yote yaliyokuwa yakiendelea. Alikumbuka kwamba hakukuwa na jambo lolote baya walilolifanya, sasa iweje mtu huyo awatafute, amuue mdogo wake na kutaka kummaliza yeye mwenyewe.
Wakati akijifikiria mambo hayo yote, gari lile likasimama karibu naye, Michael akateremka, Godwin hakujua mwanaume huyo alikuwa nani lakini wakati akijiuliza juu ya mwanaume huyo, ghafla akatoa bastola na kumuonyeshea kisiri.
Godwin akashtuka, akataka kuhamaki lakini Michael akamuonyeshea ishara ya kunyamaza kwani kama angepiga kelele zozote zile basi ilikuwa ni lazima amuue hapohapo alipokuwa.
“Shiiiii…” Michael alionyesha ishara ya kuweka kidole mdomoni na kumtaka Godwin anyamaze vinginevyo angemuua palepale.
Kijana huyo akabaki akitetemeka, alimwangalia mwanaume huyo, hakuonekana kuwa na masihara, sura yake ilitisha na kwa jinsi alivyoonekana, ilikuwa ni rahisi kujua kwamba katika maisha yake alikuwa amefanya mauaji ya watu wengi mno.
Akamtaka Godwin asimame, pasipo ubishi akasimama na kumwambia aingie ndani ya gari kitu ambacho kijana huyo alikubaliana nacho, na bila ubishi wowote ule akaingia ndani ya gari hilo na kuondoka mahali hapo.
Hakukuwa na mtu aliyejua kilichokuwa kikiendelea, wengi waliliona gari lile lakini hawakujua kwamba lilibeba watekaji ambao walitumwa kwa ajili ya kumteka Godwin na kumuua kama walivyoagizwa.
Haikuwa kazi ngumu, walidhani kwamba wangepata wakati mgumu wowote lakini kwa jinsi kazi ile ilivyokwenda, hakukuwa na ugumu wowote ule.
Selemani akaliondoa gari hilo mahali hapo, akaondoka kwa mwendo wa taratibu, hawakutaka kushtukiwa na mtu yeyote yule, walipotoka katika barabara hiyo ya vumbi na kuingia katika barabara ya lami ndipo gari likaendeshwa kwa mwendo wa kasi.
Njiani, Godwin alikuwa akilia, alijua kabisa kwamba kama asingewaomba msamaha watu hao basi wangekwenda kumuua kama walivyomuua ndugu yake, hakutaka kuona hilo likitokea, alitaka kupambana, aendelee kuishi ili mwisho wa siku kumuua mtu aliyekuwa nyuma ya matukio hayo.
“Sijafanya kitu! Naomba mnisamehe niondoke,” alisema Godwin huku akilia.
Alichokifanya Michael ni kuchukua kamba na kumfunga miguu na mikono yake, hakutaka kumuona akileta ubishi wowote au kufanya jambo lolote baya ambalo lingemfanya kutoroka na kutokufanikiwa kumuua kijana huyo.
“Mpigie simu bosi mwambie tushamaliza kazi,” alisema Selemani na Michael kuchukua simu na kumpigia Kihampa kwa ajili ya kumpa taarifa kwamba tayari walikuwa na Godwin mikononi mwao na kilichokuwa kimebaki ni kumuua kama walivyokuwa wameagizwa.
Hilo halikuwa tatizo lolote lile kwa Michael, akachukua simu na kumpigia Kihampa, wala simu haikuchukua muda mrefu ikapokelewa na sauti ya Kihampa kuanza kusikika.
“Mkuu! Tumekwishafanya kazi yenyewe,” alisikika mwanaume huyo kutoka upande wa pili.
“Safi sana. Mnaye hapo?”
“Ndiyo bosi!”
“Anaonekanaje?”
“Kama dada yake tu! Analialia.”
“Subiri nawapigia simu ngoja niwasiliane na mkuu!”
Hawakuwa na wasiwasi hata kidogo, Michael akakata simu na kuendelea na safari yao. Gari lilikwenda mpaka Kinondoni ambapo likaingizwa ndani ya jumba lilelile aliloingizwa Irene na kupelekwa katika chumba kile.
Godwin alikuwa akitetemeka kwa hofu, aliamini kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wake kuvuta pumzi ya dunia hii. Huko, akabaki akimuomba Mungu amuokoe kutoka katika mikono ya watu hao wabaya ambao walikuwa na lengo moja tu, kumuua.
Michael na Selemani masikio yao yalikuwa katika simu yao, walitaka kuona Kihampa akiwapigia na kuwaambia kama alikuwa akija au walitakiwa kumuua hata kama yeye mwenyewe hakuwepo.
Baada ya dakika kadhaa, simu ikaanza kuita, haraka sana Michael akaichukua kutoka mezani alipokuwa ameiweka na kuipokea. Akaisikia sauti ya Kihampa kutoka upande wa pili ikimwambia kwamba walitakiwa kumuacha Godwin aondoke zake.
“Unasemaje bosi?” aliuliza Michael huku akionekana kutokuamini.
“Muacheni aondoke zake!” alisema Kihampa na kisha kukata simu.
Michael alishangaa, ilikuwaje bosi wao huyo atoe maagizo mepesi namna hiyo na kuwaambia kwamba walitakiwa kumuachia Godwin aondoke zake na wakati yeye ndiye aliyekuwa akishadadia kijana huyo atekwe na yeye mwenye kwenda kumuua kama alivyofanya kwa Irene.
Alikuwa bosi wao, hata alipowaambia hivyo, hawakutaka kubisha, walichokifanya ni kwenda mpaka katika chumba kile na kumtoa Godwin na kumwambia kwamba alikuwa huru kuondoka kiasi kwamba yeye mwenyewe alibaki akishangaa.
Godwin hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, alipoambiwa kwamba alitakiwa kuondoka, haraka sana akatoka ndani ya nyumba hiyo na kuanza kukimbia bila kuangalia nyuma kwa kuhisi kwamba angeitwa na kuambiwa arudi ndani ya kile chumba.
Godwin alikimbia mpaka barabarani ambapo akachukua daladala kwa lengo la kuelekea Manzese alipokuwa akiishi, wala hakuchukua muda mrefu, akafika huko ambapo akaingia ndani, akachukua kila kitu alichokuwa nacho na kuondoka mtaani hapo kwenda kutafuta chumba Tandale kwa Tumbo.
Hakutaka mtu yeyote yule afahamu mahali alipokuwa akihamia, alimshukuru baba mwenye nyumba na kumwambia kwamba alikuwa akihama, alipokuwa akihamia ilikuwa siri yake kwa kuamini kwamba kama angemwambia mtu yeyote alipokuwa akihamia basi kuna siku mtu huyo angetoa taarifa kwa wabaya wake na kumwambia alipokwenda.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Huku nyuma, Michael na Selemani walionekana kukasirika, walifanya kazi kubwa kwa kuamini kwamba wangeambiwa wamuue Godwin au kumsubiri Kihampa kumuua kama ilivyokuwa kwa Irene lakini mwisho wa siku wakaambiwa kwamba wamuache aondoke zake.
Wakati wakiwa wanajiuliza sababu ya Kihampa kuamua hivyo, mara wakasikia simu ikianza kuita na walipoangalia jina lilisomeka kama Kihampa hivyo Michael kuipokea na kuiweka sikioni.
“Mmefikia wapi?” alisikika mwanaume huyo akiuliza.
“Kivipi bosi?”
“Mmekwishamteka?”
“Eeeh! Mbona tulikutaarifu bosi mpaka ukatuambia tumuache aondoke zake,” alisema Michael.
“Mmuache aondoke zake?”
“Ndiyo! Si ndivyo ulivyotuagiza?”
“Mimi?”
“Ndiyo bosi!”
“Mimi niliwaambia mmuache?”
“Ndiyo bosi!”
“Hapana! Mpo wapi?”
“Mjengoni!”
“Nakuja!”
Kila mmoja alichanganyikiwa, hawakujua bosi huyo alikuwa akihitaji kitu gani, walikumbuka kwamba aliwapigia simu na kuwaambia kwamba Godwin alitakiwa kuachiwa na wao kufanya mambo mengine lakini kitu cha kushangaza kabisa, bosi huyohuyo akawapigia simu na kuwaambia kwamba alitaka kujua kama walikamilisha mchakato wa kumteka Godwin.
Kihampa hakuchukua dakika nyingi akafika mahali hapo, alichanganyikiwa, kile alichoambiwa kwenye simu alitaka kukisikia kwa masikio yake.
Alipowaona wakina Michael swali lake la kwanza lilikuwa ni kuwauliza kuhusu lile alilowaambia kwenye simu kwamba ilikuaje mpaka yeye mwenyewe kuwaambia kwamba walitakiwa kumuachia Godwin aondoke zake na wakati alikuwa na hamu ya kumuona kijana huyo akifa kama ilivyokuwa kwa dada yake.
Michael akamuelezea Kihampa kila kitu kilichotokea na mpaka akamuonyeshea simu alizokuwa amempigia na kumwambia kwamba alitakiwa kumuacha Godwin aondoke zake.
“Mimi niliwapigia simu?” aliuliza Kihampa.
“Ndiyo bosi! Namba hii hapa,” alisema Michael huku akimuonyeshea namba yake iliyokuwa imempigia na kumpa maagizo hayo.
“Hapana! Sikuwapigia simu!”
“Ulitupigia bosi. Namba hii hapa!”
Kihampa akachukua simu ile na kuangalia namba yenyewe iliyokuwa imempigia Michael na kumwambia kwamba alitakiwa kumuacha Godwin aondoke zake. Alipoiangalia namba, ilikuwa ni yake lakini hakuwa amempigia simu mwanaume huyo na kumwambia kwamba walitakiwa kumuacha Godwin aondoke zake.
Hakujua lipi lilitokea, alihisi kwamba labda kulikuwa na mtu alichukua simu yake na kumpigia Michael na kumwambia kuhusu suala la kumuacha Godwin lakini kila alipokumbuka, hakukuwa na mtu yeyote ambaye aliichukua simu yake, alishinda nayo na hakumpa mtu yeyote yule, je, ni nani alipiga simu hiyo na kuwapa vijana hao ujumbe huo kwamba Godwin alitakiwa kuachwa huru.
“Haiwezekani! Sikuwapigia simu,” alisema Kihampa huku akiendelea kushangaa.
“Sawa! Kama wewe hukupiga, ni nani alipiga?” aliuliza Michael swali lililomfanya Kihampa kubaki kimya kwani hata jibu la swali hilo hakuwa nalo.
“Kuna kitu hapa! Nahisi kuna mtu ametuchezea mchezo,” alisema Kihampa huku akikaa kwenye kochi, alinyong’onyea, kitendo cha Godwin kuondoka, alihisi kabisa kungekuwa na ugumu kumtia mikononi mwao kama ilivyokuwa.
***
Kihampa alikuwa kimya chumbani kwake, moyo wake ulikuwa na hofu kubwa, hakuamini kama kweli namba yake ndiyo iliyotumika kuwasiliana na vijana wake na kuwaambia kwamba wamuache Godwin aondoke zake.
Hakujua ni mtu gani alikuwa nyuma ya tukio hilo. Hakujua ni kitu gani angeambiwa na wakuu wake mara baada ya kuwaambia kwamba Godwin ambaye alikuwa mikononi mwao, aliondoka katika mazingira ya kutatanisha,
Hapo chumbani alipokuwa, alikuwa kimya, alionekana kuwa na mawazo tele na muda mwingi alikuwa akisimama, alitembea huku na kule na kupiga mikono yake kwa hasira.
Alijua kabisa kumpata Godwin haikuwa kazi nyepesi tena kwani iwe isiwe ilikuwa ni lazima kijana huyo aondoke Manzese na kwenda sehemu yoyote kuishi lakini si kuendelea kubaki mahali pale ambapo hakukuonekana kuwa salama kwa maisha yake.
Mawazo hayakumuisha, alijikuta akikesha akimfikiria Godwin na kazi kubwa aliyokuwa nayo mbele yake. Asubuhi ilipoingia, akainuka kitandani alipokuwa amepumzika pasipo kupata usingizi na kuwapigia simu vijana wake na kuwaambia kwamba ilikuwa ni lazima waende kule Manzese kwa ajili ya kumtafuta Godwin na kama ingewezekana atekwe tena na kukabidhiwa mikononi mwake.
Vijana hao wakaondoka, wakaanza kupeleleza huku wakipiga stori na vijana wengine, siku ya pili tu wakapata taarifa kwamba kijana huyo hakuwa akiishi hapo, alihama na alipohamia hakukuwa na mtu aliyepajua.
“Alihama lini?” aliuliza Michael.
“Nimesikia juzi! Ila kuondoka kwake ilikuwa ni kwa magumashi kwani hakukuwa na kubeba mizigo wala nini! Kila kitu alikiacha ndani kwake,” alisema kijana mmoja pasipo kujua alikuwa akizungumza na watu wa aina gani.
Michael na Selemani wakarudi kwa Kihampa na kumwambia kilichokuwa kimetokea kwamba Godwin alihama nyumbani hapo, alipohamia hakukuwa na mtu aliyepafahamu.
Mwanaume huyo akachanganyikiwa zaidi, ule ugumu aliokuwa akiuona mbele yake ndiyo uliojitokeza, kitendo cha Godwin kuhama nyumbani hapo na kutokujulikana mahali alipohamia tayari aliona dhahiri kwamba kumpata tena lisingekuwa jambo rahisi kama kipindi cha nyuma.
“Hatuwezi kujua alipohamia?” aliuliza Kihampa.
“Kiukweli ni vigumu bosi! Dar ni kubwa sana, ila pia anaweza akawa ameondoka kwenda katika mikoa mingine kwa kuhofia kifo,” alisema Selemani huku akimwangalia Kihampa.
“Sidhani kama atakuwa amekwenda mkoani. Hebu nipeni siku moja ya kujifikiria,” alisema Kihampa na kuwaruhusu watu hao kuondoka.
Alikisumbua kichwa chake, hakutaka kutulia, muda mwingi alikuwa akijifikiria juu ya mahali ambapo inawezekana Godwin alikuwa amehamia. Sehemu pekee iliyokuja kichwani mwake ilikuwa ni Tandale.
Aliufahamu mtaa huo, asilimia kubwa ya watu waliokuwa wakiishi huko walikuwa ni wale wa hali ya chini. Hakuhisi kama Godwin alikuwa amehamia Mabibo, japokuwa Manzese na Mabibo palikuwa karibukaribu lakini kutokana na vyumba vya mtaa huo kuwa vya hali ya juu, Godwin asingeweza kwenda huko.
Mbali na Mabibo, pia akapafikiria Tabata, Sinza, Kigogo, Kijitonyama, Mwananyamala na sehemu nyingine, akahisi kabisa sehemu zote hizo maisha yake yalikuwa ya juu ambapo kwa mtu kama Godwin asingeweza kuyahimili hata mara moja.
“Mawazo yangu yananiambia kwamba atakuwa Tandale! Mmh! Au amehamia hapahapa Manzese! Lakini haiwezekani, hawezi kuhama Manzese na kuhamia Manzese, hakuna binadamu wa hivyo hasa kwa mtu anayetafutwa kama yeye. Mwananyamala pia hawezi, kule napo siku hizi watu wanajenga majengo ya maana, haiwezekani kwenda kule, nafikiri atakuwa Tandale tu,” alijisemea peke yake huku akiwa chumbani kwake.
Aliijua vilivyo Tandale, ulikuwa ni mmoja wa mitaa iliyokuwa na watu wengi, japokuwa kulikuwa na mabadiliko makubwa kwamba watu wengi walikuwa wakinunua nyumba, kuzivunja na kujenga nyingine lakini aliamini kabisa kwamba kulikuwa na uwezekano wa Godwin kwenda kuishi huko.
Hakutaka kuchelewa, alichokifanya ni kumpigia simu Michael na kumwambia juu ya hisia zake kwamba kulikuwa na uhakika wa asilimia tisini Godwin kwenda kuishi huko Tandale.
Michael alipoambiwa, naye akahisi kabisa hilo liliwezekana kwani kwa mtu kama Godwin asingeweza kwenda sehemu ambayo ilikuwa na maisha ya juu kwa kuwa hakuwa na pesa za kutosha kupanga chumba cha bei ya juu.
“Ni Tandale, na kama siyo huko, kidogo tujaribuni Temeke na Tandika,” alisema Kihampa.
Hakutaka kuwatuma vijana hao tu bali alichokifanya ni kuongeza jeshi la vijana kwenda huko. Akawatafuta vijana kumi na tano, watano akawapeleka Tandale, watatu akawapeleka Mwananyamala, watatu Tandika, wawili akawapeleka Temeke na wawili akawapeleka Mbagala ili kufanikisha mchakato wake wa kumpata Godwin na kumteka kama ilivyotakiwa kuwa.
Kila siku kazi yake ilikuwa ni kupokea taarifa kutoka kwa vijana wake, alikuwa akiwauliza kama walifanikiwa kumpata kijana huyo au la. Kila mmoja alikuwa na picha yake, isingekuwa kazi kubwa kumteka popote pale atakapoonekana kwani waliamini kwamba kusingekuwa na mtu yeyote wa kuwazuia.
Wakuu waliokuwa wamemtuma Kihampa walikuwa wakimpigia simu mara kwa mara kwa mara kumuuliza alipokuwa amefikia, ilikuwa ni lazima wajue kama alishindwa kazi wamtafute mtu mwingine au angeendelea nayo.
“Mkuu! Naombeni siku kadhaa, nakuhakikishieni kwamba nitafanikiwa katika hili,” alisema Kihampa huku akiwa na hofu, aliwafahamu wakuu wake, walikuwa watu waliopenda kufanyiwa kazi zao mara tu wanapotoa, hawakutaka kuona kama mtu waliyekuwa wakimtuma akiwafanyia longolongo hata kidogo.
“Tukupe muda gani?” ilisikika sauti kutoka upande wa pili.
“Naomba mnipe wiki moja,” alijibu Kihampa.
“Nyingi sana!”
“Mkuu! Yule kijana amehama pale Manzese alipokuwa akiishi, hatujui amehamia wapi na ndiyo maana nimeamua kuwatuma vijana wamtafute kila kona. Naomba unipe wiki moja mkuu,” alisema Kihampa, alivyokuwa akizungumza, ilikuwa vigumu kuamini kama ndiye yuleyule aliyekuwa akiwakaripia polisi.
“Sawa. Tunakupa wiki moja, ukishindwa itakuwa inamaanisha kwamba umeshindwa kufanya kazi na sisi hivyo tutamtafuta mtu ambaye ataifanya kazi hiyo ndani ya siku mbili tu,” alisema mwanaume huyo na kukata simu.
Kihampa akachanganyikiwa, hapohapo akawapigia simu vijana wake na kuwauliza walipofikia, wote aliowauliza walimwambia kwamba hawakuwa wamefanikiwa kumpata Godwin na hawakujua ni mahali gani kijana huyo alipokuwa.
Alihofia, alipenda kuaminika, alikuwa mchapakazi ambaye kila siku katika maisha yake alipenda kuwafurahisha viongozi wake, hata kama kulikuwa na ugumu katika kazi yoyote aliyopewa lakini alihakikisha anaifanya kwa asilimia mia moja tena ndani ya siku chache tu.
Siku zikakatika, hakulala, na hata alipolala, alilala usingizi wa mang’amung’amu, hakuwa na amani hata kidogo. Muda haukumsubiri, baada ya wiki kutimia, akaambiwa aelekee Osterbay kwa ajili ya kuongea na mtu ambaye hakujua alikuwa nani.
Alielekezwa mahali, akaelekea huko huku akiwa na hofu kubwa moyoni mwake. Alichukua dakika kadhaa mpaka kufika katika jumba hilo aliloelekezwa, akaliingiza gari ndani na kuteremka ambapo akaambiwa kuingia ndani mpaka katika chumba ambacho kilikuwa na mwanga hafifu na mbele yake kulikuwa na kioo kikubwa.
“Kaa chini,” alisikia sauti ikimwambia, akatii na kukaa chini huku akiwa na hofu tele moyoni mwake.
“Tukupe siku ngapi?” lilisikika swali kutoka kwa mwanaume huyo aliyekuwa upande wa pili ambaye hakumuona, na sauti yake ilisikika tofauti kabisa, ilikuwa ikisikika ikiwa na mwangwi.
“Mkuu! Naombeni wiki moja,” alisema Kihampa.
“Ni chache sana! Unataka tukupe muda gani?” iliuliza tena sauti hiyo.
“Naombeni mwezi mmoja.”
“Unahisi utafanikiwa ndani ya mwezi mmoja?” iliuliza sauti hiyo.
“Ndiyo! Naahidi nitafanikiwa.”
“Sawa. Tunakupa mwezi mmoja, utakachokihitaji, omba utapewa lakini tunataka uhakikishe huyu kijana anapatikana. Ni mtu hatari sana ambaye kama tutamuacha hai, hakika atakuja kutusumbua sana huko mbeleni,” alisikika mwanaume huyo.
“Sawa mkuu! Nitajitahidi anapatikana!” alisema Kihampa. Hapohapo, ghafla akasikia simu yake ikiwa kwenye mtetemo, ilikuwa ikiita, haraka sana akakiangalia kioo cha simu yake, moyo wake ukapiga paaa kwani jina la mtu aliyekuwa akimpigia alikuwa Michael, kitendo cha kuliona jina hilo, moyo wake ukamwambia kwamba huko tayari Godwin atakuwa amepatikana.
Hakutaka kubaki mahali hapo, haraka sana akachomoka chumbani humo na kwenda chumba kingine kwa ajili ya kuzungumza na Michael, alitaka kufahamu ni kitu gani kilichokuwa kimetokea huko mpaka kumpigia simu.
“Michael…” aliita baada ya kuipokea.
“Good news boss,” (habari njema mkuu) ilisikika sauti ya Michael kutoka upande wa pili.
***
Godwin alikuwa Tandale, moyo wake haukuwa na furaha na hakujua ni kwa jinsi gani angeendelea kuishi pasipo kuonekana na wabaya wake. Mfukoni mwake hakuwa na pesa, hakujua ni kwa jinsi gani angeendelea kuishi, hakujua mahali ambapo angeishi huko Tandale ambapo hakuwa na ndugu yeyote yule.
Maisha yalimpiga na kitu pekee alichokuwa akikifikiria ni kuondoka jijini Dar es Salaam, kama ni kwenda kulima huko mashambani, alikuwa tayari lakini si kuendelea kukaa jijini Dar ambapo hakukuwa na maisha ya furaha hata kidogo.
Kwa kuwa alihitaji pesa ya kula, alichokifanya ni kuanza kuokota chupa za maji, kila siku hiyo ndiyo ilikuwa kazi yake. Ili asigundulike na mtu yeyote yule, aliamua kuchukua kofia chafuchafu na kuivaa, kofia ambayo iliuziba uso wake kwa asilimia kubwa.
Kazi yake kubwa ilikuwa ni kuzunguka huku na kule, mgongoni alikuwa na kiroba kikubwa kilichokuwa na chupa nyingi, maisha yake yalianza kuendeshwa na chupa hizo, aliziokota kila kona na kwenda kuziuza, ilipofika usiku, alikuwa akienda kwenye genge moja hapohapo Tandale kwa Tumbo na kulala.
Wakati akiendelea kuishi maisha hayo, upande wa pili vijana wa Kihampa akiwemo Michael waliendelea kumtafuta. Walikuwa na uhakika kwamba Godwin alikuwa katika mitaa ambayo walihisi kabisa alikuwepo, isingekuwa rahisi kwake kwenda kwenye mitaa ya watu wenye pesa kwa kuwa hakuwa na pesa zozote zile.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Waliendelea kuzunguka huku na kule lakini hawakufanikiwa kumpata na hata walipowasiliana na wenzao waliokuwa katika mitaa mingine, majibu yalikuwa yaleyale kwamba hawakuweza kumuona mtu huyo.
Walikata tamaa, walijua kwamba hata kama wangefanya kitu gani wasingeweza kumpata. Huku nyuma, Kihampa alikuwa akiwapa presha kubwa, aliwasisitizia kwamba mtu waliyetakiwa kumtafuta alikuwa muhimu kuliko hata kitu chochote kile.
“Tutampata tu!” alisema Michael.
“Fanyeni kila liwezekanalo mpaka mumpate,” alisema Kihampa.
Wakaongeza kasi zaidi, hawakuwa na muda mzuri wa kulala, waliendelea kuzunguka na wakati mwingine walikwenda mpaka Tandale. Baada ya kutumia siku kadhaa ndipo wakafanikiwa kumuona Godwin akiwa na kiroba kikubwa kilichokuwa na chupa nyingi za maji.
Alikuwa amevaa kofia kubwa iliyoficha sura lakini hakuweza kuwapotea. Walikwishawahi kumuona, walikwishawahi kuzungumza naye kitendo cha kumuona tena wakamgundua kwamba ni yeye.
Hilo likawa nafuu kwao, hawakutaka kupoteza muda, waliamini kwamba kama wangesubiri mpaka mwanaume huyo aondoke basi ingekuwa vigumu sana kwao kumpata tena. Hapohapo wakamfuata.
Godwin alipowaona, aliwakumbuka vijana hao, walikuwa walewale waliomteka kipindi cha nyuma. Akataka kukimbia, haraka sana Michael akatoa bastola, Godwin alipoiona, akatulia.
Watu wote waliokuwa pembeni walishangaa, hawakuamini kile walichokuwa wakikiona. Ni kweli waliishi na wahuni lakini hawakuwa kuona bastola lakini siku hiyo waliwaona vijana hao wakiwa na bastola huku wakiwa wamemsimamisha muokota chupa.
“Lala chini,” alisema Michael, alikuwa akimwambia Godwin aliyekuwa akitetemeka kwa hofu, aliogopa, hakutaka kubisha, haraka sana akalala chini.
Hakujua sababu ya watu hao kumrudia tena, kipindi cha nyuma walimteka na kumruhusu kuondoka, sasa ilikuwaje watu hao wamrudie tena na kumteka kama walivyofanya.
Michael akamsogelea, akavua mkanda wa suruali yake na kumfunga, akamnyanyua na hapohapo kumpigia simu Kihampa kwa ajili ya kumpa taarifa kwamba kazi waliyokuwa wameambiwa waifanye, ilikamilika kwa asilimia mia moja.
“Nakuja! Mpelekeni Fire, kwenye lile jengo jingine. Msimuache, msije kusema nimewaambia mmuache,” alisema Kihampa, hakutaka kuona lile lililotokea kipindi cha nyuma likitokea tena.
Kihampa hakutaka kubaki ndani ya jumba lile alilokuwa akizungumza na mkuu wake, haraka sana baada ya kutoka akaingia ndani ya gari na kuondoka mahali hapo. Njiani, moyo wake ulikuwa na furaha tele, aliwahakikisha wakubwa zake kwamba angekamilisha mpango huo ndani ya siku chache lakini kwa kuwa Mungu alikuwa upande wake, alikamilisha siku hiyohiyo.
****
“Kihampa! Umefikia wapi?” ilisikika sauti ya mwanaume aliyekuwa amempigia simu Kihampa.
“Kijana tunaye mikononi mwetu! Tunasikiliza maelekezo yenu,” alisema Kihampa.
“Muueni!”
“Tumuue?” aliuliza Kihampa huku akionekana kushtuka.
“Mbona unauliza tena? Umesahau kwamba hakuna kitu kinachotakiwa kufanywa kwa kijana huyo zaidi ya kumuua? Muueni kwa kumuweka ndani ya boksi kisha kalitupeni baharini,” alisikika mwanaume huyo wa upande wa pili.
“Haina shida mkuu! Tutafanya hivyo,” alisema Kihampa na kukata simu.
Alibadilika, Kihampa hakuwa kama alivyokuwa, macho yake yalikuwa mekundu kama mtu aliyekuwa amelia kipindi kifupi kilichopita. Michael na Selemani walibaki wakishangaa, hawakuwahi kumuona mkuu wao akiwa kwenye hali hiyo, tangu walipoanza kufanya naye kazi, alikuwa mchangamfu mno na kila siku aliwasisitizia kwamba ni lazima wampate Godwin na kumuua kama maelekezo kutoka kwa mtu aliyependa kumuita kama mkuu.
“Bosi! Unaonekana haupo sawa,” alisema Miachael huku akimwangalia Kihampa.
“Nipo sawa.”
“Hapana! Ulikuwa unalia?”
“Hapana!”
“Sasa mbona macho mekundu?” aliuliza Michael.
Kihampa hakujibu swali hilo, akabaki kimya, akawaambia vijana wale wachukue boksi na kulipeleka katika chumba alichokuwa Godwin na kumchoma kijana huyo sindano ya usingizi.
Vijana hao wakafanya kama alivyowaambia na yeye kuelekea stoo ambapo akachukua boksi na mfuko mwingine ambao Michael na mwenzake hawakujua ulikuwa na nini.
“Nendeni nje,” aliwaambia.
Hawakubisha, wakaenda nje, Kihampa akabaki ndani na Godwin aliyekuwa katika usingizi mzito, akamchukua na kumuweka ndani ya boksi na kulifunga vilivyo huku akiacha vitundu vidogo kwa juu, baada ya hapo akawaita vijana wake.
“Usiku wa leo anatakiwa kwenda kutupwa baharini, mmenielewa?” aliuliza Kihampa huku akiwaangalia.
“Ndiyo bosi!”
Usiku ulipofika, wakamchukua Godwin aliyekuwa ndani ya boksi na kuanza kuondoka naye. Safari hiyo ilikuwa ni ya kuelekea ufukweni, tayari boti ilikuwa imekwishaandaliwa, walipofika tu, wakaliteremsha boksi na kuliingiza ndani ya boti ile na kuanza kuelekea katikati ya bahari.
Muda wote Kihampa hakuonekana kuwa na furaha, alionekana kama mtu mwenye majonzi makubwa, kama mtu ambaye hakutaka kuona lile lililokuwa likiendelea liendelee kutokea.
Michael na Selemani walishangaa, hawakumuelewa mkuu wao, muda mwingine alikuwa akizungumza peke yake, alionekana kama kuwa na jambo fulani moyoni mwake ambalo hakutaka watu wengine wajue lolote lile.
Walipofika mbali kabisa, mita mia saba kutoka ufukweni wakalitupa boksi lile baharini, hapohapo Kihampa akawaambia warudi wakati boksi hilo likitakiwa kuzama taratibu.
“Ila leo haupo sawa mkuu,” alisema Michael, bado alikuwa na hofu tele.
“Wala usijali! Nitakuwa sawa, nahisi kuumwa sana,” alijibu Kihampa.
“Ndiyo mpaka kulia?”
“Mafua! Yamenibana sana,” alisema Kihampa na kuanza kurudi
Walichukua dakika kadhaa wakafika ufukweni ambapo wakateremka na kuyafuata magari yao, wakayachukua na kuondoka mahali hapo.
Ndani ya gari Kihampa alikuwa akilia kwa uchungu, hakuamini kama yeye ndiye aliyekuwa amefanya mambo yote mabaya yaliyokuwa yametokea katika maisha yake. Alilia sana, alimuomba Mungu msamaha kwani dhambi alizokuwa amezifanya zilikuwa kubwa na alihitaji msamaha hata kabla hajafa.
“Mungu! Nimemuua na Godwin! Mungu naomba unisamehe! Dhambi nilizozibeba ni nzito mno,” alisema Kihampa huku akiwa ndani ya gari lake, alikuwa amelipaki sehemu.
Alipoondoka na kufika nyumbani, akaingia chumbani kwake, bado aliendelea kulia, moyo wake ulikuwa na majonzi tele, siku hiyo alijiona kuwa mtenda dhambi kuliko watu wote duniani. Alilia na kulia, mafua yalimtoka, alitamani kubadilisha kila kitu, wakati mwingine alitamani hata kuwa na uwezo wa kurudisha muda nyuma, arekebishe alipokosea lakini hakuwa na uwezo huo.
Wakati akiendelea kulia, simu yake ikaanza kuita, akaichukua na kuangalia mpigaji. Alikuwa kiongozi wake ambaye alitaka kujua kile kilichokuwa kimetokea.
“Vipi? Umemuua?” ilisikika sauti ya mwanaume huyo.
“Ndiyo! Nimemuua kama ulivyosema, nimemtupa baharini kama ulivyoagiza,” alisema Kihampa.
“Safi sana! Kuna mzigo utaingiziwa kesho kwenye akaunti yako,” alisema mwanaume huyo.
“Wa nini?”
“Kama pongezi.”
“Hapana mkuu! Usijali! Haina haja,” alisema Kihampa, hakutaka kuongea sana, akakata simu. Kitu kilichouumiza moyo wake ni kumuua Godwin, aliona akilaumiwa na dunia nzima kwa kile alichokuwa amekifanya.
Kihampa alikuwa njiani akiwahi kuelekea Fire alipowaambia vijana wake wammpeleke Godwin waliyekuwa wamemteka. Aliendesha gari kwa mwendo wa kasi kuwahi huko kwani hakukuwa na kitu alichokuwa na hamu nacho kama kumuua Godwin.
Alipofika njiani maeneo ya Jangwani, akakumbana na foleni kubwa, mbele kabisa, Fire kulikuwa na ajali iliyotokea ambayo iliziba njia. Alikasirika, mara kwa mara alikuwa akipiga usukani huku akiwa na hasira mno.
Hakutaka kuendelea kubaki, alichokifanya ni kuingia katika upande mwingine wa barabara na kuingia kule kulipokuwa na Uwanja wa Jangwani. Alikuwa akiendesha taratibu kwani napo huko kulikuwa na watu wengi waliokuwa katika mkutano wa injili.
“Huku napo kuna nini?” aliuliza Kihampa kwa hasira.
Mbele yake kulikuwa na gari moja lililokuwa limekwama kwenye shimo, alijitahidi kupiga honi lakini haikuweza kusaidia, hakukuwa na sehemu nyingine ya kupita zaidi ya hapo ambapo gari lilipokuwa limekwamba.
Kwa hasira akateremka na kwenda kule lilipokuwa, yeye mwenyewe alishangaa, kwa nini shimo lilikuwa dogo lakini gari hilo lilikwama. Alijaribu kuwaambia watu hao jinsi ambavyo walitakiwa kuliondoa gari hilo lakini haikuwezekana, kwa hasira, huku akionekana kuvimba akarudi ndani ya gari lake, akaingia, akashusha kioo na kutulia.
Sauti ya mchungaji aliyekuwa akihubiri katika mkutano uliokuwa uwanjani hapo ilikuwa ikisikika, maneno yote yalisikika vema masikioni mwake.
“Mungu anataka kuzungumza na moyo wako, haijalishi wewe ni mtu wa aina gani, haijalishi umeua watu wangapi, haijalishi umelala na wanaume wangapi au wanawake wangapi, jioni ya leo Mungu anataka kuzungumza na wewe. Inawezekana kabisa ukawa na mpango wa kwenda kuua leo, inawezekana una mpango wa kwenda kuzini leo, Mungu wa Mbinguni anakuona, Mungu anataka utubu dhambi zako, Mungu anataka umsogelee kule alipo,” alisikika mchungaji aliyekuwa akihubiri.
Hakuishia hapo, alizidi kuzungumza maneno mengi, maneno yote hayo yalikuwa yakisikika masikioni mwa Kihampa. Hakuamini alichokisikia, ni kama mchungaji huyo aliambiwa kuhusu maisha yake, akauona moyo wake ukianza kupoa, akaona moyo wake ukianza kuumia.
Alishindwa kuyazuia machozi machoni mwake, yakaanza kumtoka na kutiririka mashavuni mwake. Maneno yote hayo yalimuumiza, akajikuta akilia, mauaji aliyokuwa ameyafanya maishani mwake yakaanza kuwa huku nzito moyoni mwake.
Akaanza kusikia sauti za watu wakimlilia, sauti nyingi zilimlaumu kwa kuamua kuwamaliza kabisa. Aliogopa, ndani ya gari alikuwa kama amechanganyikiwa, hakutaka kubaki humo, ni kama alikuwa na mauzauza, akatoka na kuanza kuelekea kule kulipokuwa mkutano ule.
Alitembea, alikuwa akilia kama mtoto, moyo wake ulichoma mno na kitu alichokitaka wakati huo ni kutubu dhambi zake, aanze maisha mapya na Mungu kwani kwa maisha aliyokuwa ameishi kwa kipindi chote yalikuwa machafu mno.
Mchungaji akamkaribisha, mbali na yeye, pia kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakitaka kutubu dhambi zao, wakafanyiwa sala ya toba na kuwa watu wapya, mioyo yao ikaumbwa, wakamrudia Mungu na kuachana na maisha waliyokuwa wakiishi.
“Nifanye nini?” alijiuliza.
Alikuwa na kazi aliyopewa, hakutaka kubaki hapo, akaondoka kwa ajili ya kuifanya kazi hiyo. Moyo wake ulikuwa mzito kufanya mauaji tena, alitubu dhambi zake na hakuwa tayari kuona akifanya dhambi nyingine kwa kumuua mtu.
Hakuchukua muda mwingi akafika alipokuwa akienda, vijana wake wakamwambia kwamba tayari Godwin alikuwa ndani ya jumba hilo katika chumba alichokuwa amehifadhiwa. Alichokifanya ni kumfuata na kumchoma sindano ya usingizi.
Hakutaka kumuua Godwin, alitaka aendelee kuishi. Kama kuua, aliua sana na muda huo ulikuwa ni wa kuishi na Mungu wake na si kuua tena kama ilivyokuwa.
Akachukua boksi, kabla ya kumuingiza humo Godwin, akaelekea stoo ambapo akachukua maboya na kuyaingiza ndani ya boksi lile. Hakutaka kuona Godwin akifa, alitaka kumuokoa na muda wote alikuwa akimuomba Mungu kwamba kwa kile alichokuwa akikifanya basi amlinde na asimuache akifa katika bahari waliyopanga kwenda kumtupa.
Kwa kuwa aliwatoa vijana wake ndani ya chumba kile, akamchukua Godwin na kamuingiza ndani ya boksi lile lililokuwa na maboya, akalifunga na kisha kuwaita vijana wale ambao wakalichukua na kulipeleka ndani ya gari tayari kwa kwenda kulitupa baharini.
Muda wote alikuwa akilia kwa uchungu, moyo wake haukuamini kama yeye ndiye aliyekuwa akifanya yale yote. Baada ya boti kufika baharini, wakalitupa humo na haraka sana kuwaambia waondoke kwani hakutaka wagundue kwamba boksi halikuzama zaidi ya kuelea juu ya maji tu.
****
Godwin alikuwa ndani ya boksi, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea. Usingizi ulimchota baada ya kuchomwa sindano ile ndani ya jumba lile. Boksi lilikuwa likipelekwa huku na kule, halikuwa likielekea nchi kavu bali lilizidi kusonga mbele kabisa kuelekea mbali kabisa na nchi kavu.
Mawimbi yalilipiga lakini halikuzama, liliendelea kuelewa juu ya maji mpaka baada ya saa moja ndipo akaamka kutoka katika usingizi mzito. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuangalia huku na kule, hakuelewa mahali alipokuwa, alichokiona ni kwamba alikuwa ndani ya chumba kimoja kidogo mno ambacho kisingemfanya kuweza kusimama.
Mbali na kuwa humo, akawa anasikia sauti za mawimbi yakipiga, akahisi kwamba alikuwa katikati ya maji. Akaogopa, alipogusagusa pembeni na chini akakuta vitu ambavyo kwa haraka sana akili yake ikamwambia kwamba yalikuwa ni maboya.
Hakutaka kujiuliza sana, akahisi kwamba alikuwa ametupwa baharini lakini kitu kilichokuwa kikimsumbua kichwa chake zaidi ni juu ya kuwekewa maboya hayo, kama kweli watu waliomtupa walitaka kuona akifa, kwa nini walimuwekea maboya?
Hakutaka kupoteza muda, haraka sana akayachukua maboya hayo na kuyavaa kisha kulichana boksi hilo gumu na kubaki akielea juu ya bahari. Hakujua mahali alipokuwa, akaangalia huku na kule, hakukuwa na dalili za nchi kavu, ilikuwa ni usiku lakini hakuona hata mwanga wa taa za nyumba zozote zile.
Hakutaka kupiga mbizi, akakubaliana na hali iliyokuwepo na kuanza kupelekwa huku na kule. Usiku mzima alikuwa juu ya maji, hakuona msaada wowote ule na mbaya zaidi hakuona dalili za kisiwa chochote kile.
Aliendelea kuelea juu ya maji na kitu ambacho kilimtesa sana kwa usiku huo kilikuwa ni baridi kali lililokuwa likipiga. Hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kupona kutokana na baridi kali lililokuwa likimpiga baharini hapo.
“Mungu naomba uniokoe! Naomba usiichukue roho yangu,” alisema Godwin huku akielea juu ya bahari.
Siku hiyo akashinda tena baharini. Hakukuwa na msaada wowote uliofika mahali hapo, alikata tamaa kwani kwa jinsi muda ulivyokuwa ukizidi kwenda mbele ndivyo ambavyo njaa ilivyokuwa ikimuuma mpaka kuhisi kwamba kitu ambacho kingemuua hapo baharini kilikuwa ni njaa tu.
Muda ulizidi kwenda mbele, aliendelea kuelea juu ya maji. Hakuyafumba macho yake, aliendelea kuangalia huku na kule ili kuona kama kungekuwa na msaada wowote ule.
Mchana ukaingia, muda ukazidi kwenda mbele, tumbo likaanza kumuuma, hakujua ni kwa jinsi gani angepata msaada. Mpaka inafika jioni, bado hakupata msaada wowote ule, aliendelea kuelea juu ya maji.
Ilipofika usiku wa saa moja, bahari ikachafuka, akaanza kupiga kelele kuomba msaada, mawimbi makubwa yakaanza kumpiga, yakampeleka huku na kule, hapo ndipo akaona kwamba mwisho wa maisha yake ulikuwa umewadia kwani mawimbi yaliyokuwa yakimpiga yalikuwa makubwa na yenye nguvu ambayo yalimfanya muda mwingine kukosa nguvu kabisa.
Akajilaza juu ya maji, hakuwa na la kufanya zaidi ya kusubiri kifo tu baharini hapo kwani kwa jinsi njaa ilivyokuwa ikimuuma, wakati mwingine akaona kabisa giza likianza kuwa kubwa machoni mwake.
***
Godwin alikata tamaa baharini pale kwani kila alipokuwa akiangalia hakuona msaada wowote ule. Bahari ilichafuka usiku huyo, alipelekwa huku na kule, alipiga kelele kuomba msaada, alilia sana lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyejitokeza kumsaidia na mbaya zaidi kila alipokuwa akiangalia, hakuona meli wala kisiwa chochote kile.
Ukafika muda akakata tamaa, asingeweza kuendelea kuwa baharini pale na wakati hakuwa na kitu chochote kile. Njaa ilimkamata na mwisho wa siku kuendelea kuelea juu ya maji kama kipindi cha nyuma.
Ilipofika majira ya saa nane usiku, huku akiwa amekata tamaa kabisa akashtuliwa na mwanga mkali wa tochi uliokuwa ukimmulika, alishtuka, huo ukaonekana kuwa msaada mkubwa kwake. Akajitahidi kujitingisha mahali pale lakini akashindwa kabisa, akajikuta akiuangalia mwanga wa tochi ile lakini hakufanya lolote lile.
Akasikia watu wakitumbukia ndani ya maji na kuanza kumfuata kule walipokuwa, yote hayo yaliyokuwa yakiendelea aliyasikia vizuri lakini alishindwa hata kujitingisha pale alipokuwa.
Baada ya sekunde chache, watu wawili wakamfikia na kumchukua kisha kumuweka katika boya jingine lililofungwa na kamba kubwa kutoka ndani ya meli na kuanza kuvutwa kuelekea kule.
Mwili wake ulichoka, kila mtu aliyemwangalia alibaki akishangaa, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka kuwa baharini pale. Mara ya kwanza walidhani kwamba meli aliyokuwa amepanda ilikuwa imezama lakini walipoliangalia eneo lile halikuwa na dalili za meli yoyote kuzama.
Walitaka kujua ukweli na waliona kabisa Godwin angewaambia kila kitu kilichokuwa kimetokea. Walipofika karibu na meli, akabebwa na kupakizwa ndani.
Kila mtu alikuwa akimshangaa, wakampa huduma ya kwanza na kumpa muda wa kupumzika. Watu hao hawakuwa Waswahili, walikuwa ni Wajapan ambao walikuwa baharini wakiendelea na shughuli zao za uvuvi na kwa bahati nzuri wakamuona mtu akielea juu ya maji na ndipo wakaamua kumsaidia.
Alikuwa kijana mdogo, mwenye sura nzuri, wakatokea kumpenda, wakamsaidia kwa kumpa chakula na mavazi. Mpaka siku iliyofuata ndipo Godwin akaweza kurudi katika hali yake ya kawaida. Kitu cha kwanza kabisa akabaki akishangaa, watu hao walikuwa wakina nani na walikuwa wakielekea wapi.
Kumbukumbu zake zilimwambia kwamba mara ya mwisho walikuwa baharini, sasa ilikuwaje muda huo awe ndani ya meli kubwa huku akiwa amezungukwa na Wajapan?
“Who are you?” (nyie ni wakina nani?) aliuliza Godwin huku akiwaangalia watu hao kwa macho yaliyojaa hofu.
“We are good people! We are here to help you?” (sisi ni watu wema! Tupo hapa kukusaidia) alisema mwanaume mmoja aliyekuwa na uso wa kutabasamu kila wakati.
Wanaume wale wakajitambulisha kwamba walikuwa wavuvi waliokuwa wakivua samaki hapo baharini, hawakutaka kumficha kitu chochote kile, walimwambia kila kitu lakini cha zaidi ni kwamba walikuwa watu wazuri ambao walimuokoa kutoka baharini.
Watu hao hawakuishia hapo, wakamuuliza kuhusu yeye, ilikuwaje mpaka kuwa baharini katika kipindi kama hicho. Kama kulikuwa na meli ilikuwa imezama, mbona eneo lile halikuonekana kuwa na dalili za meli yoyote ile kuzama?
“Nilikuwa na wenzangu ndani ya meli moja kubwa,” alianza kudanganya Godwin huku watu wote wakiwa kimya kumsikiliza.
“Mlikuwa mnakwenda wapi?”
“Nchini Italia. Tulitaka twende huko kusoma kwani maisha yalikuwa magumu sana huko tulipotoka,” alindelea kudanganya, na kwa jinsi alivyokuwa akionekana, ilikuwa vigumu sana kugundua kwamba kila kitu alichokuwa akikisimulia kilikuwa ni uongo.
“Wewe ni mtu wa wapi? Nigeria, Afrika Kusini au?” aliuliza mwanaume mmoja.
“Tanzania!”
“Kwa Nyerere?”
“Ndiyo!”
Alivyojibu hivyo, mwanaume huyo aliyeuliza swali hilo akawavuta wenzake pembeni na kuanza kuzungumza nao. Aliwaambia jinsi alivyokuwa akiifahamu Tanzania, ilikuwa nzuri iliyokuwa na watu waliokuwa na upendo mkubwa na kubwa zaidi ni kwamba iliwahi kuwa chini ya kiongozi mmoja aliyeheshimika duniani, Julius Nyerere.
“Kwa hiyo ni mtu mwema?”
“sijawahi kumuona Mtanzania mwenye roho mbaya. Nimeishi huko kwa miaka kumi. Ni watu wema sana. Nahisi hata huyu kijana atakuwa mwema,” alisema mwanaume huyo.
Walimwamini, walitaka kumrudisha lakini kwa sababu mwenzao aliwaambia kwamba inawezekana alikuwa mtu mwema, tena alikuwa akienda nchi nyingine kwa ajili ya kusoma na kutafuta maisha, wakapanga kumsaidia kwa kila kitu.
Hu ndiyo ukawa mwanzo wa maisha yake mapya, alilia sana lakini mwisho wa siku Mungu akaonekana katika maisha yake na kuwatuma watu kwa ajili ya kumsaidia. Hakutaka kurudi tena nchini Tanzania, alikuwa akitafutwa sana hivyo kilichofanyika ni kuanza safari ya kwenda nchini Japan tayari kwa kuanza maisha mapya.
Hakutaka kuwa na huzuni tena, alionekana kuwa na furaha, alizungumza na wavuvi wachache waliokuwa wakifahamu Kiingereza, moyo wake ulifurahia kwani kwa jinsi alivyokuwa akicheka na kufurahia, alihisi kabisa kwamba aliipata familia bora ambayo ilikuwa tayari kufanya jambo lolote lile kwa ajili yake.
Hawakutaka kurudi nchini Japan, wakaendelea na shughuli zao za uvuvi, kila siku Godwin alikuwa akifundishwa mambo mengi kuhusu uvuvi, alijisikia vizuri kwani kila mtu aliyekuwa ndani ya meli hiyo akawa kama rafiki yake.
Shughuli hiyo ilichukua wiki nzima ndipo ikakamilika na hivyo kuanza safari ya kurudi nchini Japan. Kutoka katika Bahari ya Hindi mpaka Pasifiki kulikuwa na umbali mkubwa, hawakwenda moja kwa moja nchini humo bali walichokifanya kilikuwa ni kupitia katika baadhi ya nchi kama Indonesia, Thailand na ndipo wakaingia nchini Japan.
Huo ndiyo ukawa mwisho wa safari yao, wote wakateremka na kuanza kuondoka kuelekea majumbani kwao huku wale ambao walihusika katika soko la biashara wa samaki hao wakiwachukua na kuanza kutafuta soko ambalo lilikuwepo muda wote huo.
Kwa Godwin, akachukuliwa na yule mzee aliyezungumzia sana kuhusu Tanzania, akamchukua na kuelekea nyumbani kwake huku akimuahidi kufuatilia vibali vyote ambavyo vingemfanya kusoma nchini Japan kabla ya kuamua ni kitu gani atafanya baada ya elimu hiyo.
“Utaishi vizuri sana! Nitafuatilia kila kitu,” alisema mzee huyo aliyejitambulisha kwa jina la Tokoyo Yokosoko ambaye alikuwa akiishi pembeni kidogo mwa Jiji la Tokyo.
“Haina shida! Nitashukuru sana!”
Hicho ndicho alichokifanya Mzee Yokosoko. Akamtambulisha Godwin nyumbani kwake. Akaiambia familia yake kila kitu kilichokuwa kimetokea baharini, kila mmoja alishtuka, waliifahamu bahari, hakikuwa kitu cha kawaida mtu kupona mara baada ya meli kuzama au kutoswa baharini lakini kwa Godwin, kuokolewa kwake ulikuwa kama muujiza.
Siku iliyofuata, mzee huyo akaanza kufuatilia vibali vya Godwin kumruhusu kukaa nchini humo. Ilikuwa kazi ndogo kwani sheria zao hazikuwashika sana wageni kutoka nchi nyingine, ndani ya siku tano tu, tayari Godwin alipata vibali hivyo na hivyo kuruhusiwa kukaa nchini humo kwa miaka mitano, muda wake ungekwisha, angeamua kama ni kuongeza au kurudi nchini mwake.
“Nashukuru sana!” alisema Godwin.
“Haina shida. Unataka kusomea nini?” aliuliza Mzee Yokosoko.
“Information Technology.”
“I.T?”
“Ndiyo!”
“Sawa. Nitaanza kufuatilia katika Chuo cha Waseda, ni chuo kizuri sana hapa Tokyo naamini kabisa kwamba kama utakwenda kuanza hapo, hakika utafanikiwa sana kwani wataalamu wote wa masuala ya kompyuta wamesoma katika chuo hicho, naamini hata nawe utafanikiwa sana tu,” alisema mzee huyo na siku iliyofuata akaanza kufuatilia.
Alitaka Godwin asome kwa pesa zake, hakutaka kuona akishindwa kwa kitu chochote kile kwani kila alipomwangalia kijana huyo, moyo wake ulimwambia kwamba afanye lolote lile lakini kijana huyo apate elimu bora kwa manufaa ya maisha yake.
***
Godwin alijiandaa kusoma katika Chuo cha Waseda kilichokuwa hapo Tokyo nchini Japan, hakuwa akijiamini, kwa kuwa alikuwa akitafutwa sana nchini Tanzania, akahisi kwamba mpaka nchini Japan watu hao wangeweza kuwatafuta tena.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakutaka kujiachia, hata alipokuwa akipita katika mitaa mbalimbali alionekana kuwa na hofu kubwa. Hakujiamini, hata siku ya kwanza kuingia chuoni hapo kila mtu alikuwa akimshangaa.
Waseda kilikuwa miongoni mwa vyuo vilivyokuwa na Wajapan wengi kuliko watu wa mataifa mengine. Japokuwa kulikuwa na wanafunzi zaidi ya elfu arobaini lakini kitu cha ajabu kabisa chuoni hapo hakukuwa na mwanafunzi mweusi, wengi walikuwa Wajapan, Wachina na Wazungu.
Ubaguzi ulitawala chuoni hapo, kila mwanafunzi mweusi alipotaka kujiunga na chuo hicho, alikataliwa kwa visingizio vingi lakini kwa kuwa Godwin aliombewa nafasi na Mzee Yokosoko ambaye aliheshimika sana hapo Tokyo, akajikuta akiingia na kuanza kusoma katika chuo hicho.
Hakukuwa na mtu aliyekuwa akimpenda, chuoni hapo, watu wengi walikuwa wakimtenga, hawakuamini kama Afrika kungekuwa na mtu aliyekuwa na akili, wengi walihisi kwamba Afrika ilijaza watu wa porini na hata sehemu walipokuwa wakiishi ilikuwa ni rahisi kukutana na simba.
Godwin alikuwa kimya, alijua kwamba kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakimbagua kwa sababu ya ngozi aliyokuwa nayo. Hakutaka kujali, kichwa chake kilifikiria zaidi masomo, alitaka kufanya kila liwezekanalo kwa ajili ya kuwa mtaalamu katika masuala ya kompyuta.
Hakutaka kucheza, hakutaka kuonyesha dharau katika masomo yake kitu kilichomfanya kuanza kusoma sana. Hakutaka kuishia darasani, alikesha akisoma, aliona kwamba kama angefanikiwa kufanya vizuri katika masomoo yake basi hata watu waliokuwa hapo chuoni wangemheshimu na kuacha kumbagua.
Hakupata muda mzuri wa kulala, muda mwingi alikuwa akijisomea, aliingia katika Tovuti ya Google na kutafuta mbinu mbalimbali kuhusu kompyuta. Hakutaka kushindwa kitu chochote kile, alisoma sana, kwa miezi miwili ya kwanza akafanikiwa kujua mambo mengi kuhusu kompyuta.
Akajifunza kutengeneza tovuti, akajifunza kutengeneza virusi kwa kutumia Java na C++. Alitaka kuwa mtu hatari kwa hiyo kukesha kwake ilikuwa ni kujifunza mambo mbalimbali, alitaka kuwa mkali kiasi kwamba kila mtu aogope.
Ingawa alikuwa akibaguliwa sana lakini akajikuta akianza kutengeneza urafiki na kijana mmoja wa Kijapan aliyeitwa Hilahima Takoshima. Huyu alikuwa kijana mrefu, msafi ambaye muda mwingi alikuwa akivaa miwani.
Alikuwa mcahngamfu, alipenda kuzungumza na watu wote chuoni hapo, alipomfuata Godwin na kuzungumza naye, akagundua kwamba kijana huyo alikuwa tofauti na watu wengine. Alijua kuongea, alionekana kama mtu aliyekuwa na vitu fulani kichwani mwake, Takoshima alishangaa, akahisi kabisa kwamba kama angeendelea kuwa kwenye urafiki na Godwin basi kungekuwa na vitu vingi ambavyo angejifunza kutoka kwake.
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa urafiki wao. Wanafunzi wengi walimshangaa Takoshima kwamba aliwezaje kuwa na urafiki na mtu kama Godwin ambaye alikuwa mweusi, mwanaume ambaye kila siku watu walimuita Kegareta, neno la Kijapani lililomaanisha mchafu.
“????????????” (imekuwaje kirahisi namna hii?) aliuliza jamaa mmoja huku akimwangalia Takoshima.
“?,” (nini?)
“?????????????????,” (kwa nini unazungumza naye?)
“??????? ,” (kwa sababu ana akili sana) alijibu.
Hilo ndilo lilikuwa jibu lake kila siku, hakuacha kuwaambia wenzake kwamba kila alipokuwa akizungumza na Godwin alimuona mtu wa tofauti kabisa, kijana huyo alionekana kuwa na akili sana kiasi kwamba kwa mtu yeyote ambaye angezungumza naye asingeacha kufanya hivyo.
Wengi walicheka, hawakuamini kama kungekuwa na mtu mweusi ambaye alikuwa na akili. Walizoea kuambiwa kwamba Waafrika wengi walikuwa wakiishi msituni hivyo hata kuoga hawakuwa wakioga na ndiyo maana miili yao ilikuwa michafu mno.
Pamoja na kuonyeshewa dharau zote chuoni hapo lakini Godwin hakutaka kujali, alichokuwa akikiangalia ni maisha yake ya mbele, angeishi vipi mpaka kufanikiwa kuwa vile alivyotaka kuwa kwa kipindi kirefu.
“Naomba namba ya siri,” alisema Godwin, alikuwa akimwambia Takoshima.
“Ipi?”
“Ya intaneti ya hapa chuoni.”
Takoshima akampa Godwin neno la siri ili aweze kuitumia intaneti ya chuoni hapo. Hakuwa na matumizi nayo bali alitaka kuifunga, hakutaka kuona chuoni hapo watu wakiendelea kuitumia intaneti hiyo, kwa sababu walikuwa wakimbagua, alitaka kuwaonyeshea kwamba alikuwa kiboko.
Hata kabla ya kufanya hivyo, alihitaji kusoma zaidi. Alipenda sana kompyuta na bahati nzuri nayo ikampenda, akafahamu vitu vingi sana na baada ya miezi minne, akaamua kuifunga intaneti ya chuoni hapo.
Hakuwa na pupa, alijua kwamba kama angeifunga kikawaida watu wangegundua hivyo kitu cha kwanza kilikuwa ni kutengeneza virusi vyake ambavyo alitaka viende vikashambulie mafaili kwenye server na kuyaficha kabisa.
Hilo halikuwa tatizo, ilikuwa kazi kubwa lakini alitakiwa kuifanya kwa nguvu zote. Hakuona kama kungekuwa na mtu ambaye angembabaisha katika masuala ya kompyuta kwa wakati huo, alisoma sana, na kwa kuwa alikuwa genius, hakupata ugumu wowote wa kulielewa somo hilo.
Siku hiyo alikesha kwenye kompyuta yake chumbani kwake, hakutaka kula, alikuwa bize kuangalia ni kwa namna gani angeweza kuficha mafaili yote ya chuo hicho yaliyokuwa kwenye server. Alihangaika kwa siku ya kwanza, hakufanikiwa, siku ya pili ikaingia lakini bado hakuweza kufanikiwa.
Hakutaka kumshirikisha mtu, alikuwa akifanya kazi kwa juhudi zote kwani aliamini kwamba angefanikiwa kwa kile alichokuwa akikifanya. Hakuonekana chuoni, wanafunzi walikuwa wakiuliziana mahali alipokuwa lakini hakukuwa na aliyejua.
Wengi wakahisi kwamba alihama chuo kama wengine mara baada ya kubaguliwa lakini kila walipozungumza na Takoshima aliwaambia kwamba Godwin alikuwepo na angerudi chuoni hapo siku si nyingi.
“Kwani amekwenda wapi? Afrika?” aliuliza mwanafunzi mmoja.
“Hapana! Yupo hapahapa Tokyo!”
“Mbona haji chuo?”
“Sijajua! Ila aliniambia kwamba yupo na kuna siku angekuja,” alisema Takoshima.
Alibaguliwa chuoni lakini kitu cha ajabu kabisa alikumbukwa mno kipindi hicho. Kila siku ilikuwa kazi ya Wajapan kuuliza mahali alipokuwa kwani haikuwa kawaida kwa mwanafunzi kukaa nyumbani kwa kipindi chote hicho.
Baada ya wiki moja na nusu kupita ndipo akarudi chuoni hapo, alikuwa na kompyuta yake ya mapajani, uso wake ulikuwa kwenye tabasamu kubwa. Siku zote hizo alikuwa na kazi kubwa ya kujaribu kuficha mafaili yaliyokuwa kwenye server ya chuo, aliifanya kazi hiyo kwa kujitoa sana, alitaka kumuonyesha kila mtu kwamba alikuwa mtu hatari sana katika masuala ya kompyuta.
Hakuzungumza na mtuu yeyote yule, alikuwa kimya mpaka alipokwenda darasani na kutulia ambapo baada ya muda rafiki yake, Takoshima akaingia na kuanza kuzungumza naye.
“Vipi?” aliuliza Godwin.
“Poa! Umesikia kilichotokea?” aliuliza Takoshima huku akimwangalia Godwin.
“Kitu gani?”
“Si unajua kwamba tulitakiwa tuwe na mitihani wiki ijayo?” aliuliza Takoshima.
“Ndiyo!”
“Nimesikia hakuna! Mafaili yote yaliyokuwepo kwenye server yameliwa na virusi,” alisema Takoshima pasipo kugundua kwamba kila kitu kilichotokea kilifanywa na Godwin.
“Mafaili yameliwa?”
“Ndiyo! Walimu wamechanganyikiwa, wamejaribu kuyarudisha, wameshindwa kabisa hivyo wamewapigia simu Mashatikana, kampuni moja ya watu wa kompyuta waje kufanya kila liwezekanalo mafaili yaruri,” alisema Takoshima maneno yaliyomfanya Godwin kutabasamu.
Kila mwanafunzi aliyesikia kwamba mafaili ya chuo yameliwa na virusi alishangaa, hawakutegemea kusikia kitu kama hicho, waliamini kwamba kwa sababu server hizo zilikuwa zimehifadhi data nyingi za chuo basi hata ulinzi wake ungekuwa mkubwa.
Hawakujua nini kilitokea bali walichosubiri ni kuona Kampuni ya Mashatikana ikifika chuoni hapo na kutatua tatizo lililokuwa limetokea.
Walimu wote walichanganyikiwa, mkuu wa chuo alitoka kijasho chembamba, hakujua ni kitu gani kilitokea, alijaribu kuwaita baadhi ya wanafunzi watatue tatizo lakini hawakufanikiwa, na mbaya zaidi hawakujua kama mtu aliyefanya hivyo alikuwa yule kijana wa Kiafrika waliyekuwa wakimuita mchafu kila kona chuoni hapo.
Siwezi kuficha mafaili halafu mtu akayaona, watayatafuta na hawatoyaona mpaka pale nitakapowasaidia,” alijisemea Godwin huku akitoa tabasamu pana.
Watu wa kampuni ya Mashatikana walipofika, moja kwa moja wakaelekea katika ofisi ya mkuu wa chuo ambapo akawachukua na kuwapeleka katika chumba kilichokuwa na server nyingi. Walipofika huko, wakachukua kompyuta zao, wakziwasha, wakaunganisha nyaya na kuanza kufanya kazi hiyo ya kuyarudisha mafaili hayo huku mkuu wa chuo na watu wengine wakiwa pembeni wakisubiri kuona kitu gani kingetokea.
***
Mkuu wa chuo alichanganyikiwa, hakujua zaidi kitu kilichokuwa kimetokea lakini alikuwa na uhakika kwamba watu waliokuja kutoka katika Kampuni ya Matashatikana kwa ajili ya kurudisha mafaili hayo wangefanikiwa kwa kiasi kikubwa zaidi.
Akawaangalia watu hao waliokuwa ndani ya chumba kile kilichokuwa na server, walikuwa bize na kompyuta zao, waliangalia kila kitu, walijua kwamba wao ndiyo waliokuwa wakitegemewa kurudisha mafaili yaliyokuwa yamefichwa. Kitu cha kwanza kabisa walichokigundua ni virusi ambavyo vilivyokuwa vimeficha mafaili hayo.
Virusi hivyo viliitwa Takeshi, vilikuwa virusi vyenye nguvu ambavyo havikuwahi kuonekana kabla. Wataalamu wale walibaki wakiangalia kompyuta zao, walikuwa na ant-virus lakini ilishindwa kabisa kuvishambulia virusi hivyo.
Hawakujua ni kitu gani walitakiwa kufanya. Wakaingia online na kuchukua ant-virus nyingine lakini zote hizo zilishindwa kuvishambulia virusi vile vilivyokuwa vimeshikilia mafaili ya chuo hicho.
Walifanya kazi hiyo kwa saa kumi na moja, kila mmoja alichoka, walihangaika kwa saa nyingi hizo lakini hawakufanikiwa kile walichokuwa wakikihitaji na mwisho wa siku kumwambia mkuu wa chuo, Bwana Tamashi kwamba hawakuwa na jinsi, chuo kilitakiwa kuingia gharama kwa ajili ya kuwaita watu wengine, hasa Wamarekani ambao waliaminika kwa ajili ya kupambana na virusi wagumu kama hao.
“Imeshindikana vipi?” aliuliza mkuu wa chuo, alichanganyikiwa, alichohisi ni kwamba kazi ilikuwa nyepesi lakini mwisho wa siku wakagundua kwamba kazi hiyo ilikuwa ngumu zaidi ya walivyokuwa wakifikiria kabla.
“Ni kazi ngumu!”
“Ugumu wake upo wapi?”
“Kuna virusi vipya. Kuna mtu alivitengeneza na kuvituma katika server yenu iliyohifadhi mafaili,” alisema mtaalamu mmoja kutoka katika Kampuni ya Mashatikana.
“Mtu gani?”
“Hata sisi wenyewe hatujui! Cha msingi hebu jaribuni kuwaita wataalamu wengie kwani kama tukiendelea kuwaondoa, hawa virusi wataingia kwenye kompyuta zetu, na wanaonekana ni hatari sana,” alisema jamaa huyo.
Wakaondoka pasipo kufanikiwa kile kilichowapeleka chuoni hapo. Tamashi alichanganyikiwa, ilikuwa ni lazima afanye juu chini ili mafaili yaliyokuwa yamefichwa yapatikane kwani ndiyo yalihifadhi kila kitu kilichokuwa kimetokea chuoni hapo na mitihani yote chuoni hapo ilihifadhiwa humo.
Akawasiliana na kampuni ya Microsoft ya nchini Marekani, akawaelezea tatizo alilokuwa nalo na watu hao kuahidi kwamba wangefika nchini Japana baada ya siku moja tu hivyo walitakiwa kusubiri. Hilo halikuwa tatizo, aliamini kwamba Microsoft wangeweza kulitatua tatizo hilo kwani ilikuwa moja ya kampuni iliyokuwa ikitengeneza programu nyingi zikiwemo ant-virus iitwayo Microsoft Security Essential.
Baada ya siku moja wataalamu hao wakafika chuoni hapo na kuambiwa kila kitu kilichokuwa kimetokea. Hilo halikuwa tatizo, wakaomba kupelekwa katika chumba kilichohifadhi server za chuo hicho na walipofika huko wakafanya kama walivyofanya watalaamu wa Mashatikana.
Kazi yao kubwa ilikuwa ni kucheza na kompyuta zao, waliviona virusi vya Takeshi vilivyokuwa vimeshikilia mafaili hayo. Walichokifanya ni kuingiza ant-virus zao kwa ajili ya kupambana na virusi hivyo lakini kitu kilichowashangaza zaidi ni kwamba hawakuweza kufanikiwa.
“Tunamuhitaji mtu aliyetengeneza virusi hivi,” alisema Brown, mmoja wa wanaume waliotoka katika Kampuni ya Microsoft.
“Wa nini?”
“Tuzungumze naye. Hii ni biashara kubwa sana, kama tukionana naye natumaini tunaweza kufanya jambo fulani,” alisema Brown huku akionekana kuwa na uhitaji wa kuonana na mtu huyo.
Hakukuwa na mtu aliyejua kama aliyetengeneza virusi hivyo alikuwa Godwin. Mwenyewe alitulia, alikuwa akifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Hakumwambia mtu yeyote yule, kila kilichotokea kilikuwa siri kubwa.
Aliwaona watu walivyokuwa wakihangaika. Kila mwalimu shuleni hapo alichanganyikiwa kwani mitihani yao waliyokuwa wameitunga haikuwa ikionekana. Shule haikufanya usajili tena kwa sababu fomu zote zilikuwa humo na wanafunzi walitakiwa kuingia kwenye mtandao wa chuo kwa ajili ya kujaza fomu hizo.
Taarifa za kufichwa kwa mafaili ya chuo hicho zikaanza kusambaa jijini Tokyo, wataalamu wengi wa kompyuta walipopata taarifa hizo wakafurahi na kuona kwamba hiyo ndiyo ilikuwa nafasi yao ya kwenda kuvuna pesa.
Wengi wakajitolea na kwenda huko lakini bahati mbaya kwao ni kwamba kila walipokuwa wakifika kwa ajili ya kufanya utundu wao na kuyarudisha mafaili walishindwa na hivyo kurudi walipotoka.
Ndani ya wiki nzima chuo kilikuwa kikihangaika kurudisha mafaili hayo. Haikuwa kazi nyepesi hata kidogo, walijitahidi usiku na mchana lakini hakukuwa na mtu aliyekuwa na uwezo wa kupambana na virusi hao.
“Mkuu! Kuna mtu muhimu inatakiwa tuwasiliane naye,” alisema jamaa wa kitengo cha IT kutoka chuoni hapo.
“Yupi?”
“Kuna mzee anaitwa Thierry kutoka nchini Ufaransa, ni mtu hatari sana ambaye kama kweli akifika chuoni hapa, nina uhakika atafanikiwa kwani ana ujuzi wa hali ya juu sana,” alisema jamaa huyo.
“Hakuna shida.”
Hawakuwa na jinsi, walikuwa wakiingia gharama lakini mwisho wa siku walitaka kufanikiwa kwa kile walichokuwa wakikihitaji. Mawasiliano yakafanyika, wakampata Thierry ambaye kitu cha kwanza kabisa ni kutaka kukatiwa tiketi yake, hilo halikuwa tatizo, akakatiwa na kuelekea huko.
Godwin aliposikia mwanaume huyo alikuwa njiani akija chuoni hapo alishtuka, alimfahamu, aliujua uwezo wake, alikuwa mtu hatari sana katika kupambana na watu waliokuwa wakijifanya kuwa hatari katika kompyuta.
Thierry alikuwa mwanaume aliyekuwa amewakamatisha wezi wengi wa mitandao hasa wale waliokuwa wakifanya uhalifu katika mashine za ATM nchini Ufaransa na wakati mwingine mpaka Marekani. Wengi walimchukia kwa kuwa alizika madili ya watu wengi, na wengi walimtafuta wamuue lakini walimkosa.
Hakutaka kuajiliwa, kazi yake kubwa ilikuwa ni kuitwa kufanya kazi huku na kule, kwa lugha nyepesi ya mtaani tungemuita mchezaji wa ndondo. Alipokuwa akiitwa sehemu kwa ajili ya kufanya kazi yake alifanya kwa moyo mmoja, tena kwa nguvu kubwa na kufanikiwa kwa asilimia mia moja.
“Kwa huyu jamaa tutafanikiwa,” alisema Takoshima, alikuwa akimwambia Godwin pasipo kujua maneno hayo yalimuumiza mwanaume huyo kiasi gani.
“Ataweza?”
“Ni mtu hatari sana. Subiri afike, hutoamini,” alisema Takoshima huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.
Siku iliyofuata Thierry akaingia ndani ya chuo hicho. Kila mtu aliyemuona akawa na matumaini kwamba mwanaume huyo angefanikiwa kwani kwa jinsi alivyokuwa akiifahamu kompyuta, alivyokuwa akicheza na data, waliamini kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa matatizo.
Akapelekwa katika chumba kilichokuwa na server, alipofika huko, akaanza kuangalia huku na kule, alionekana kama mtu aliyekuwa na mbwembwe nyingi. Akawaambia watu wote watulie kwani ndani ya dakika chache tu mafaili yangeweza kuonekana.
Akachukua kompyuta yake ndogo, akachukua nyaya kutoka katika server na kuunganisha katika kompyuta yake na kuanza kuangalia huku na kule. Muda wote alikuwa akitabasamu, aliona kazi iliyokuwa mbele yake kuwa nyepesi sana na wakati mwingine alikuwa akishangaa kwamba kwa nini watu walishindwa kazi hiyo na wakati ilikuwa nyepesi sana?
“Ni kazi nyepesi mno. Naombeni soda kwanza ninywe,” alisema huku akiwa ameachia tabasamu, tena akakunja na nne kabisa.
Haraka sana soda ikaletwa na kuanza kunywa taratibu, alikuwa makini kwa kila alichokifanya, aliviona virusi vilivyoshikilia mafaili hayo, vilikuwa virusi hatari ambavyo wakati mwingine mwenyewe aliviogopa.
Aliingia kwa mbwembwe, muda wote tabasamu pana usoni lakini kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda mbele akaanza kubadilika, tabasamu likaanza kupotea taratibu, uso wake ukabadilika, na kilichomshangaza kila mmoja humo ndani ni kwamba mzee huyo akaanza kutokwa na kijasho chembamba hali iliyoonyesha kwamba hata yeye pia, pamoja na utaalamu wakee mkubwa, alianza kuchemka kuyarudisha mafaili hayo.
“Mmh! Huyu aliyetengeneza virusi hivi alitengeneza kwa C++ au java? Mbona naona kama ni virusi ambavyo havijawahi kutengenezwa katika ulimwengu huu?” alijiuliza huku akiikodolea macho kompyuta yake, wakati mwingine alihisi joto kali ingawa ndani ya chumba hicho kiyoyozi kilikuwa kikipiga kwa nguvu kabisa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
***
“Is it done?” (imekamilika?) aliuliza mkuu wa Chuo, Bwana Tamashi huku akimwangalia Thierry aliyeonekana kuweweseka.
“Who did this?” (nani alifanya hivi?)
“We don’t know yet! Is there any possibility of working again?” (bado hatujajua! Kuna uwezekano wa kufanya kazi tena?) aliuliza Tamashi.
“Just give me some minutes,” (nipe dakika kadhaa)
Kulikuwa na dalili zote za Thierry kushindwa kuyarudisha mafaili yale, alihangaika kwa nguvu zote lakini hakuwa amefanikiwa, hakutaka kuwaweka wazi, alikuwa akijulikana kwa kuwakomesha wezi wa mitandao, alijua ‘programing na network’ lakini kuyarudisha mafaili yaliyokuwa yamefichwa na virusi vile ilikuwa kazi ngumu kupita kawaida.
Alichoka mwili, alichoka kiakili, alihitaji kupumzika na hata soda ambayo aliiagiza kwa mbwembwe hakuwa ameimaliza, akatulia huku mtu mzima akitokwa na kijasho chembamba.
Mkuu wa chuo, Tamashi akaona kabisa kwamba kazi ilishindikana, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, hakujua kama kungekuwa na mtu ambaye angeweza kuyarudisha mafaili yale. Kama Thierry, mwanaume aliyejulikana kwa utaalamu wake wa kompyuta duniani alishindwa kuyarudisha, ni nani angeweza kufanya kazi hiyo?
Tamashi aliona dalili za chuo hicho kupata hasara, hakutaka kuona hilo likitokea, serikali ya Japan haikutaka kukubali, kwa kuwa chuo hicho kilikuwa sehemu ya vyuo vya serikali, wakawaita wataalamu kufanya kazi lakini kila aliyefika alivishangaa virusi hivyo, hawakuamini kama kulikuwa na virusi vya kuficha mafaili kwa uwezo mkubwa kama huo.
Wakati kila kitu kikiendelea, Godwin alikuwa ametulia, alitaka kuona mwisho wa yote ungekuwa nini. Alisumbuka kutengeneza virusi hivyo, alishinda usiku kucha kwa siku kadhaa, hakuona kabisa kama kungekuwa na watu ambao wangeweza kuyafichua mafaili yaliyokuwa yamefichwa kwa ufundi mkubwa.
Siku zikaendelea kukatika, wataalamu wote wakashindwa na mwisho wa siku chuo kutangaza kwamba walishindwa, na kama kungekuwa na mtu wa kuyarudisha mafaili hayo, angelipwa kiasi cha dola laki moja (zaidi ya milioni mia mbili) kama pongezi kwake.
“Mimi nataka nikayarudishe! Watanikubalia?” aliuliza Godwin huku akimwangalia rafiki yake, Takoshika.
“Wewe?”
“Ndiyo! Au watanikatalia?”
“Mmh! Utaweza?”
“Unanionaje? Nitaifanya kazi hiyo Jumatatu,” alisema na kuondoka.
Takoshima hakutaka kufuatilia sana, alijua kwamba Godwin asingeweza kuyarudisha mafaili hayo, hivyo akapuuzia japokuwa aliwaambia marafiki zake wengine kama utani kwamba Godwin alitaka kujarabu kuyarudisha mafaili hayo.
Kila mtu aliyesikia akacheka, walimdharau, waliona ni kitu kigumu kwa mtu kama yeye kuyarudisha mafaili hayo. Kama Wazungu, Wajapan na Wachina walishindwa kuyarudisha, ilikuwaje kwa mtu mweusi kama yeye.
Kwa chuoni hapo ilikuwa ni kama kichekesho, kila mtu aliyesikia kwamba Godwin naye alikuwa miongoni mwa watu waliotaka kujaribu walicheka kupita kawaida, hawakuona kama kijana huyo angeweza kubadilisha matokeo.
Japokuwa kulikuwa na watu wengi waliotaka kujaribu lakini gumzo alikuwa Godwin na hata alipokuwa akienda chuo kila mmoja alikuwa akimjadili kwamba angewezaje kuyarudisha mafaili na wakati kulikuwa na watu wengi, tena wataalamu waliokuwa wameshindwa kufanya hivyo.
Hakutaka kujali, alijua fika kwamba kazi ilikuwa nyepesi sana. Siku ambayo alitakiwa kufanya hivyo ilipofika, akaelekea katika ofisi ya mkuu wa chuo na kuanza kuzungumza naye. Alimwambia wazi kwamba alitaka kufanya kazi hiyo na kuwashangaza watu wote ambao walihisi kwamba hawezi kufanya lolote lile.
“Hapana! Unaweza kuharibu hata server zenyewe,” alisema Tamashi, yeye mwenye hakumwamini kabisa Godwin kama angeweza kufanikiwa kwa kile alichokuwa akitaka kukifanya.
“Unaniamini au huniamini?” aliuliza Godwin huku akimwangalia Tamashi.
“Unajua ni watu wangapi wameshindwa?”
“Ni wengi sana. Ninataka nimdhihirishie kila mtu kwamba ninaweza,” alisema Godwin.
“Kwamba unawashinda mpaka wataalamu wa serikali?”
“Unawahusudu sana? Ni kazi ndogo mno. Andaa pesa yangu,” aliseema Godwin huku akimwangalia mkuu wa chuo usoni.
Moyo wake ulimwambia wazi kwamba Godwin hakuweza kuifanya kazi ile, ilikuwa vigumu kwa mtu kama yeye kuifanya na wakati kulikuwa na watu wengi waliokuwa wameshindwa. Hilo hakujali, aliendelea kumwambia mkuu huyo kwamba kama angepewa nafasi basi ilikuwa ni lazima kuifanya kazi hiyo kwa mafanikio makubwa.
Kwa kuwa kulikuwa na wengi waliojaribu na kushindwa, mkuu wa chuo hakuwa na jinsi, akampa nafasi Godwin kujaribu kufanya kile alichotaka kufanya.
“I wanna show them how to do it,” (nataka niwaonyeshe namna ya kulifanya jambo hili) alijisemea wakati akiingia ndani ya chumba kilichokuwa na server.
Wanafunzi wote walikuwa wakisikilizia nje, kila mmoja aliamini kwamba Godwin asingeweza kuyatoa mafaili yale yaliyokuwa yamefichwa. Kwa kuwa alitaka kuwaonyeshea kwamba alikuwa na uwezo wa kuifanya kazi ile, alipoingia tu, akavuta kiti, akatulia na kukunja nne.
“Mbona ni kazi nyepesi sana!” alisema Godwin huku akiwaangalia vijana wa IT waliokuwa humo ndani.
“Wenzako walisema hivyohivyo!”
“Hebu muiteni mkuu wa chuo!”
“Wewe wa nini? Si ufanye tu hiyo kazi!”
Hakutaka kufanya kazi hiyo pasipo mkuu huyo kuwepo ndani ya chumba hicho. Alikumbuka jinsi alivyomdharau na kumuona hajui kufanya chochote kwa kuwa tu alikuwa mtu mweusi. Siku hiyo ilikuwa ni siku maalumu ya kuwaonyeshea watu wote chuoni hapo kwamba kwamba watu weusi hawakuwa watu wa mchezo mchezo.
Mkuu huyo alipopewa taarifa kwamba alihitajika, akaanza kuelekea huko, hakupenda kwenda kwa kuwa tangu aanze kuzungumza na Godwin hakuwahi kumwamini, hakuona kama kijana huyo alikuwa na uwezo wowote ule.
Alipoingia ndani ya chumba kile, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuuliza kama kazi ilifanyika kwani alikuwa na mambo mengi ofisini kwake. Godwin akamwambia kwamba alitakiwa kutulia kwani kulikuwa na kazi ambayo alitaka kuifanya huku mkuu huyo akiwa ndani ya chumba hicho.
“Kwa hiyo haiwezi kufanyika bila mimi kuwepo?” aliuliza Tamashi.
“Yeah! Ngoja nikuonyeshee mbele yako kwamba siku nyingine hutakiwa kuwadharau watu weusi,” alisema Godwin na kuanza kuifanya kazi hiyo.
Haikuwa kazi ngumu kwake, yeye ndiye aliyetengeneza virusi hivyo na alijua jinsi ya kupambana navyo. Kila mmoja alikuwa kimya akimwangalia, hakuonekana kuwa na wasi, alikuwa akiifanya kazi hiyo huku wakati mwingine akiimba Wimbo wa Where is the Love wa Black Eyed Peas.
Hakuchukua muda mrefu, alitumia dakika kumi tu, akasimama na kuwaambia kwamba kazi waliyokuwa wamempa alikuwa ameifanikisha kwa mafanikio makubwa. Mkuu wa chuo, Tamashi hakuamini, akaiwasha kompyuta moja ndani ya chumba kile kwa lengo la kuangalia kama mafaili yalikuwa yamerudi kweli, alipofungua tu mtandao wa chuo, macho yake yakatua kwa mafaili yote yaliyokuwa yamefichwa.
“Haiwezekani! Mafaili yamerudi!” alisema huku akishtuka, tabasamu pana likaonekana usoni mwake, hapohapo akageuza macho yake kumwangalia Godwin, kijana huyo hakuwepo ndani ya chumba hicho.
Wanafunzi walimuona Godwin akitoka ndani ya chumba kile, alionekana kama mtu aliyekuwa na haraka, alikuwa akitembea kwa mwendo wa kasi, kwa jinsi alivyoonekana, kila mmoja akahisi kwamba alikuwa amechemka kama wengine walivyokuwa wamechemka.
Wengi wakaanza kucheka na kumpuuzia, walimuona mjinga fulani ambaye alitaka kufanya jambo chuoni hapo kwa lengo la kutafuta kiki ili azungumziwe kwa mazuri na si kwa mabaya kama ngozi yake ilivyokuwa ikijionyesha.
Wakati Godwin akiwa amefika mbali kabisa, mlango ukafunguliwa na mkuu wa chuo kutoka. Alionekana kuwa mtu mwenye furaha, alikuwa akiangalia huku na kule kama alikuwa akimtafuta mtu au kitu fulani. Akamuona Godwin akiwa mbali kabisa akitokomea, akamuita kwa sauti kubwa, watu wote wakashtuka na kumwangalia mkuu huyo.
Hawakujua kitu gani kilitokea lakini kijana mwingine kutoka katika chumba kile alipoufungua mlango na kupayuka kwamba mafaili yalikuwa yamerudi, kila mmoja akashangaa.
“Mafaili yamerudi! Mafaili yamerudi!” alisema kijana huyo huku akipiga kelele zilizowafanya watu kujiuliza, je, ni Godwin ndiye aliyeyarudisha mafaili hayo au kulikuwa na mtu mwingine.
Japokuwa mkuu wa chuo alikuwa akiita kwa sauti na Godwin kumsikia vilivyo hakutaka kusimama, hakuangalia nyuma, macho yake yalikuwa mbele, alipiga hatua ndefu tena za harakaharaka kusonga mbele na kupotea kabisa.
Gumzo kubwa chuoni hapo lilikuwa ni Godwin tu, kila mtu akaanza kumzungumzia kwa kumsifia na wengi walishangaa, iliwezekanaje mtu mweusi aweze kufanya jambo ambalo watu weupe walihangaika nalo kwa siku nyingi tu.
Kila mmoja akahisi kwamba Godwin alikuwa na kitu cha pekee kichwani mwake, walitaka kujua mengi zaidi, walitamani kuujua uwezo wake ulikuwa ni wa namna gani.
“Is this Ben Carson Jr?” (huyu ni Ben Carson mdogo?) aliuliza Mjapani mmoja huku akishangaa, kwa kile alichokifanya chuoni hapo, kila mtu alistaajabu.
Kila mtu chuoni Waseda alikuwa na hamu ya kumuona Godwin, hawakuamini kama mtu mweusi angekuwa na uwezo wa kuyarudisha mafaili na wakati watu wengi weupe walishindwa kufanya hivyo.
Mkuu wa chuo, Tamashi hakutulia, alitaka kumuona Godwin kwa mara nyingine na kumuomba msamaha kwa yote ambayo aliyasema dhidi yake, kwa dharau aliyomuonyeshea kwamba hakuwa na uwezo wa kufanya jambo lolote lile kwa kuwa tu kulikuwa na wataalamu wengi ambao walishindwa.
Godwin hakuonekana, kila mmoja alijua kwamba kijana huyo aliondoka chuoni hapo, kitu kilichowatia hofu walimu wote chuoni hapo ni kwamba inawezekana kijana huyo akahama chuo kwa kile kilichokuwa kimetokea kwa kipindi kirefu na wakati alikuwa na uwezo mkubwa.
Kupitia Godwin, waliamini kwamba chuo kingetangazwa sana kwamba kulikuwa na mwanafunzi aliyekuwa balaa, mwanafunzi aliyefanya kazi ambayo hata watalaamu kutoka serikalini walishindwa kuifanya.
Taarifa za kile alichokifanya zikaanza kusambazwa kila kona, watu walishangazwa mara baada ya kuzina picha za mwanaume mweusi katika mitandao ya kijamii. Hakukuwa na aliyeamini kwamba mwanaume huyo ndiye aliyefanya jambo hilo lilimuacha mdomo wazi kila mmoja.
Kwa kila kila mmoja alitamani sana kumuona Godwin, wengi wakaanza kutafuta namba yake ya simu kwa ajili ya kuwasiliana naye. Hilo halikuwa tatizo, Takoshima aliwapatia namba kwa lengo la kuwasiliana naye.
Walipiga na kupiga lakini simu haikuwa ikipokelewa, si kwamba Godwin hakuziona namba hizo zilizokuwa zikiingia katika simu yake, aliziona lakini hakutaka kabisa kupokea kwani alijua kabla kwamba angepigiwa sana simu baada ya kufanya jambo kubwa ambalo kila mtu alishindwa kulifanya.
“Mbona simu hapokei?” aliuliza mwanafunzi mmoja, alikuwa amempigia simu zaidi ya mara kumi na tano na zote Godwin hakuwa amepokeea.
“Hata mimi mwenyewe najiuliza. Nimempigia sana simu lakini naona kimya,” alisema mwanaume mwingine.
Godwin alitulia chumbani kwake, moyo wake ulikuwa na furaha kubwa, kwa kila alichokuwa amekifanya kwake kilionekana kuwa ushujaa mkubwa. Alibaki akiwa amejilalia chumbani kwake, kichwa chake kilikuwa na mambo mengi, kwanza kabisa alikuwa na kiu ya kutaka kumfahamu mtu aliyekuwa ameiangamiza familia yake.
Maisha aliyopitia yalimuumiza kupita kawaida, alikuwa na hasira, alijua kulikuwa na kitu kilichokuwa kimetokea, alitaka kujua ukweli juu ya sababu zilizowafanya watu hao kuiangamiza familia yake na sababu ambayo iliwafanya kutaka kumuua mpaka yeye mwenyewe.
“Ila kama walitaka kuniua, kwa nini waliniwekea boya kwenye boksi?” hilo lilikuwa swali jingine kabisa lililokuja kichwani mwake, alibaki akijiuliza sana juu ya kile kilichokuwa kimetokea, kwa nini watu waliotaka kumuua ndani ya boksi walimuwekea boya? Je, hawakutaka kumuona akifa au lile boya liliwekwa na mtu mwingine? Kila alichojiuliza, alikosa jibu.
Wakati akifikiria mambo mengi ndipo akaona simu nyingi zikianza kuingia, akazichukua na kugundua kwamba zilikuwa namba ngeni, alijua kilichokuwa kimetokea, alijua ni kwa jinsi gani watu walitaka kufahamu kila kitu kilichotokea kwamba ilikuwaje mpaka kuweza kuyarudisha mafaili na wakati watu wengine walishindwa.
Hakutaka kujiuliza maswali mengi, akalala na alipoamka, kitu cha kwanza kabisa Mzee Yokosoko akaingia chumbani kwake huku akiwa na simu mkononi, hata kabla hajazungumza lolote lile, akampa ile simu na kumtaka kuangalia kilichokuwa kimeandikwa.
Godwin akaichukua na kuangalia, kulikuwa na taarifa kuhusu kile alichokuwa amekifanya. Kila mmoja alishangaa, hawakuamini kama kungekuwa na mtu aliyekuwa na uwezo wa kufanya kile kilichofanywa.
“Wewe ndiye umefanya hivi?” aliuliza mzee huyo huku akimwangalia Godwin kwa macho yaliyojaa mshangao.
“Oopss! Yaani kila mtu anakizungumzia kitu kidogo kama hiki,” alisema Godwin huku yeye mwenyewe akishangaa, hakuamini kama kila sehemu alizungumziwa yeye tu.
“Ni jambo kubwa sana. Nimepigiwa simu na marafiki zangu wanaofanya kazi katika kampuni kubwakubwa, wanataka kufanya kazi na wewe,” alisema Mzee Yokosoko.
“Wanataka kufanya kazi na mimi?”
“Ndiyo! Achana na hao, nimesikia pia taarifa za chinichini kwamba hata Microsoft na Apple wote wanataka kufanya kazi na wewe. Godwin! Wewe ni mtu wa aina gani?” alisema Mzee Yokosoko na kumalizia kwa swali.
Moyo wake ulifarijika, alikaa na Godwin kwa kipindi kirefu na kuamua kumsomesha, alishangaa kuona kumbe mtu aliyekuwa naye alikuwa na uwezo mkubwa namna hiyo.
Alikuwa akidharaulika na majirani wengi walimlaumu kwa kuamua kuishi na mtu mweusi lakini kwa kile ambacho Godwin alikifanya, kila mtu alimsifia huku wengine wakitamani hata kumfuata na kupiga naye picha.
“Nitahitaji kusoma zaidi,” alisema Godwin huku akimwangalia mwanaume huyo.
“Hutaki kufanya kazi?”
“Si kwa sasa!”
“Unajua kwamba Microsoft na Apple wanakuhitaji! Hutaki pia? Kila mtu anatamani sana kufanya kazi katika kampuni kubwa kama hizo, kwa nini hutaki?” aliuliza Mzee Yokosoko huku akionekana kutokuamini kama Godwin hakuwa na mpango wa kufanya kazi katika kampuni hizo zaidi ya kusoma.
“Hapana! Bado kuna mambo mengi nitahitaji kufanya. Kama kweli unahitaji pesa, hutakiwi kuwa na haraka ya kuzipata. Subira inahitajika ili upate zaidi,” alisema Godwin huku akimwangalia mzee huyo.
Walizungumza mambo mengi, aliendelea kumwambia kwamba hakuwa na lengo la kufanya kazi kwa kipindi hicho. Mzee Yokosoko hakutaka kuumlazimisha, akakubaliana naye na hivyo kumruhusu kuendelea na maandalizi yake ya kwenda chuoni.
****
Tanzania ilibadilika, kila mtu aliyekuwa akikaa nchini humo alikuwa akilalamika kutokana na ugumu wa maisha uliokuwa umetawala kila kona. Masikini walikuwa wakilia, pesa haikuonekana na hata ile kidogo iliyokuwa mitaani ilishikiliwa na watu wenye nguvu.
Uchumi ulishuka, idadi kubwa ya watu waliokuwa wamepigika kipindi cha nyuma, maisha yao yalizidi kuwa mabaya zaidi. Kila mtu alilia, hakukuwa na maisha mazuri tena, kila kona ni malalamiko tu ndiyo yalikuwa yakitawala.
Chama pinzani cha Tanzania National Party kilikuwa katika kazi nzito ya kuhakikisha inawaambia wananchi juu ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Udhaifu uliokuwa ukionekana katika uongozi huo, waliutumia huohuo kuhakikisha kwamba wanashinda katika uchaguzi ujao ambao ulitakiwa kufanyika baada ya miaka mitatu.
Watanzania walichoka, waliamini kwamba uchaguzi ndicho kitu pekee ambacho kingewafanya kuleta mabadiliko lakini hawakuwa na matumaini ya kutosha kwa kuwa tu kwenye kila uchaguzi, chama tawala kilishinda zaidi na zaidi.
Watu walitaka kuongea na Rais Bokasa, hawakujua ni kwa namna gani walitakiwa kufanya ili kumpata. Walipanga namna ya kumfikia rais huyo kwa kutumia maandamano lakini kitu cha ajabu kila walipokuwa wakiandamana, walipigwa vibaya na polisi waliokuwa wakihakikisha maandamano yanayofanyika ni yale yaliyokuwa na vibali tu.
“Kwani kelele zote zinatoka wapi?” aliuliza Bokasa huku akimwangalia Waziri wa Ulinzi, Bwana Edward Ngoshima.
“Eti maisha yamekuwa magumu. Umekaza sana,” alisema Ngoshima huku uso wake ukiwa na tabasamu.
“Kwa hiyo wanataka nilegeze?”
“Sijajua! Ila kwa mtazamo tu wanataka ulegeze, eti kuna watu wanakufa njaa,” alisema waziri huyo.
“Hahaha!”
“Ila tulichokigundua ni kwamba wapinzani ndiyo wanatumia watu hao, hakuna shida yoyote ile mitaani. Mambo yote yapo supa,” alisema waziri huku uso wake ukitawaliwa na tabasamu pana.
Watanzania walilalamika, walipiga kelele kila siku lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote yale. Viongozi waliendelea kula bata huku wakiwasahau watu waliokuwa chini yao. Baada ya kuhangaika sana bila kupata msaada wowote ule ndipo Watanzania wakaanzisha mapambano mapya kupitia mitandao ya kijamii.
Akaunti mbalimbali zikaanzishwa, hizo zote zilikuwa ni za kuisema serikali kwamba kilichokuwa kikiendelea Tanzania hakikuwa kitu kizuri kwani watu walihitaji maisha bora ambayo yalihubiriwa kila siku kwenye majukwaa lakini mwisho wa siku kile walichokuwa wakikipata hawakuwa wakikitarajia.
Huko kwenye mitandao, watu wakaweka dukuduku zao, kurasa nyingi za kuipinga serikali zikaanzishwa lakini baada ya kuweka posti kumi, akaunti hizo zilisimama huku habari za nyuma ya pazia zikisema kwamba wamiliki wa akaunti hizo walikuwa wakiuawa baada ya kutafutwa.
“Mmh! Kwa hiyo hata mimi nikianzisha akaunti yangu ya kuipinga serikali nitauawa?” aliuliza jamaa mmoja.
“Ndiyo! Tena watakusaka kwa nguvu zote,” alisema jamaa mwingine, wakati watu wakijadili ni nani alitakiwa kuanzisha akaunti ya kuizungumzia vibaya serikali ndipo kukaibuka akaunti moja, akaunti iliyoitwa Mabadiliko ya Kweli ambayo kazi yake kubwa ilikuwa ni kuikosoa serikali na kuweka hadharani skendo nzitonzito za viongozi wa nchi hiyo.
***
Watanzania waliishi kwa hofu, kila mmoja aliogopa, maisha yao waliyaona yakiwa hatarini kwa kuhisi kwamba kwa lolote ambalo walitakiwa kulifanya au kuzungumza kinyume na sheria ilikuwa ni lazima watu wakamatwe na wengine kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
Watu hawakuwa na amani na matumizi ya mitandao, wengine waliweka posti zao zilizoirekebisha serikali lakini kwa kuwa ilikuwa na mkono mrefu, wengi wakajikuta wakikamatwa na kupelekwa sehemu ambayo hawakuwa wakiifahamu na kupewa onyo kali kwamba hawakutakiwa kuandika kitu chochote kile.
Kitendo cha akaunti ya Mabadiliko ya Kweli kuibuka ikawachanganya viongozi wengi wa serikali. Akaunti hiyo ilikuwa ikizungumzia maovu mengi waliyokuwa wakiyafanya viongozi huku ikiwa na picha iliyokuwa na ramani ya Tanzania iliyokuwa ikilia machozi ya damu.
Viongozi walichanganyikiwa, wengi wakahisi kwamba kulikuwa na kiongozi mmoja aliyekuwa akiwasaliti kwani wakati mwingine walikuwa wakizungumza mambo ya siri katika simu lakini siku iliyofuata kila kitu kiliwekwa wazi.
Picha zilisambazwa, mawaziri walionekana wakiingia katika hoteli za kifahari na michepuko yao, wakati mwingine video ziliwekwa kuonyesha kwamba mawaziri hao walikuwa katika vyumba vya hoteli na kufanya ufuska na wanawake mbalimbali kitu kilichowaletea aibu kubwa.
Mara kwa mara viongozi walikuwa wakikutana na kuweka vikao, kwa kile kilichokuwa kikiendelea kiliwaumiza vichwa vyao, walitaka kumfahamu mtu aliyekuwa katika mtandao huo ambaye alipata data kwa kiwango kikubwa na kuziweka wazi kwa Watanzania wote ambao walishabikia kutumika kwa mitandao.
Katika kila vikao walivyokuwa wakikaa kwa ajili ya kumzungumzia mtu aliyekuwa akitumia akaunti hiyo, walishindwa kumfahamu, mbele yao waliona giza, viongozi walizidi kuchafuliwa kila siku.
“Jamani! Hii ishu ni siriazi sana, ni lazima tumfahamu mtu anayefanya haya yote. Siri zetu anazipata wapi? Kama si sisi tunaompa, ni nani anampa?” aliuliza waziri mkuu huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Ni kweli mkuu! Hili suala linachanganya sana. Juzi nilikuwa nimeongea na rais kuhusu tatizo langu na kile kimada changu cha Sinza kinachonisumbua. Nimezungumza na rais kwa siri, tena kwenye simu usiku. Saa moja baada ya kukata simu, mazunguzmo yote yamewekwa kwenye ile akaunti. Nani alikwenda kusema? Rais? Hapana! Mimi mwenyewe? Hapana! Sasa nani alikwenda kumwambia?” aliuliza Makamu wa Rais, Bwana Issa Jumanne.
“Hapa kuna kitu! Hebu zungumzeni na vijana wetu wa IT na muwaambie kwamba hii akaunti inatakiwa kufungwa haraka sana,” alisema Rais Bokasa huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Sawa mkuu!”
“Ina wafuasi wangapi mpaka sasa?”
“Laki nane!”
“Ifungeni haraka sana!”
“Saa mkuu!”
Hilo ndilo lililotakiwa kufanyika kwa haraka mno. Mawasiliano yakafanyika, vijana wa IT wakaitwa kwa ajili ya kuifanya kazi hiyo. Kwao, kila kitu kilionekana kuwa chepesi sana hivyo wakaingiza programu zao kwa ajili ya ‘kuihack’ akaunti hiyo na kuifunga.
Matokeo yake yalikuwa ni tofauti na jinsi walivyofikiria kabla, walijua kuwa kuifunga kilikuwa kitendo cha haraka sana kama walivyofanya kwa akaunti za watu wengine. Kwa akaunti hii, walichanganyikiwa, walifanya kila liwezekanalo kwa ajili ya kuifunga lakini hawakuweza.
Hawakuishia kuifanya kazi hiyo wao tu bali waliwashirikisha watu wengine kwa ajili ya kuifunga akaunti hiyo lakini ikawa ngumu kufungika. Viongozi wa chama tawala wakachanganyikiwa, hawakutaka kudili na watu wa vyama pinzani, kwao, walichokuwa wakidili nacho usiku na mchana kilikuwa ni akaunti hiyo ambayo kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele ndivyo siri zao zilivyozidi kuvuja.
“Vijana wanaendeleaje?” alisikika Rais Bokasa.
“Kiongozi! Tumewaambia, wanahangaika nayo!”
“Wiki mbili bado tu?”
“Wanasema ni kazi ngumu mno, tuwape siku zaidi,” alisema waziri mkuu.
“Sawa. Waambie wajitahidi sana!”
Wakati wao wakihangaika kuifunga akaunti hiyo, Watanzania walizidi kuifuata katika Mtandao wa Instagram na ‘kuifollo’ kitu kilichoifanya kuwa na wafuasi wengi kila siku.
Huko ndipo Watanzania walipokuwa wakipata taarifa zote mbaya za viongozi, ndipo ambapo walipokuwa wakijua kiongozi yupi alikuwa akitoka kimapenzi na kiongozi yupi.
Watu wakasahau maisha machungu ya viongozi waliokuwa wakiwanyonya, macho na masikio yao yalikuwa katika akaunti hiyo iliyokuwa ikisema siri zao nyingi kiasi cha kuwachanganya wote.
Watu wa IT baada ya kuona kwamba wameshindwa kuifunga akaunti hiyo wakaanza kupambana kuhakikisha wanajua mahali ilipokuwa ikifunguliwa.
Hilo likaonekana kuwa tatizo pia kwani taarifa walizokuwa wakizipata zilikuwa zikiwachanganya wote. Wakati wakianza kufuatilia, waliona kabisa kwamba mtumiaji kwa kipindi hicho alikuwa Mbagala Zakhem, wakati wakifutailia huko, wakaona kwamba mtumiaji alihama na alikuwa Mikocheni B. Wakageuza gari harakaharaka na kuanza kuelekea huko, wakati wakiwa njiani, ikaonyesha kwamba mtumiaji huyohuyo alihama na kuhamia Kibaha, walichanganyikiwa.
Wakati wakijiuliza nini kilikuwa kikiendelea, ikaonyesha kwamba mtumiaji huyo alikuwa amehama na kuhamia nchini Sweden, tena katika siku hiyohiyo na baadaye kuonyesha kwamba alikuwa nchini Argentina.
Kwa mabadiliko hayo machache wakagundua kwamba walikuwa wakidili na mtu aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kuchezea mitandao. Walichanganyikiwa, hata kuwapa ripoti viongozi wao kwamba walishindwa waliogopa kufanya hivyo.
“Huyu jamaa yupo wapi hasa?” aliuliza kijana mmoja wa IT.
“Inachanganya sana. Eti hapa inaniambia kwamba mtumiaji yupo Ufaransa. Jamani! Huyu mtu ni nani?” aliuliza jamaa mwingine huku kwa kumwangalia tu alionyesha ni jinsi gani alikuwa amechanganyikiwa.
“Umeingia kwenye Mabadiliko ya Kweli leo?’ aliuliza jamaa mmoja.
“Hapana! Si unajua nipo job. Kuna nini?” aliuliza jamaa aliyepewa taarifa.
“Kumbe Spika wa Bunge, Bwana Ramadhani Nyakunyaku alikuwa akimtongoza mke wa Waziri wa Jinsia, Wazee na Watoto, Bi Zubeda,” alisema jamaa huyo.
“Acha uongo bwana!”
“Ndiyo hivyo! Ingia huko uone.”
Hiyo ilikuwa habari kubwa ya siku hiyo ambayo watoto wa mjini walisema kwamba ulikuwa ubuyu wa moto kabisa. Kila Mtanzania hakuamini alichokuwa akikiona, meseji za kimapenzi za watu hao wawili zilikuwa zimewekwa hadaharani, kila mtu aliona kilichokuwa kimetokea, wengi walishangaa kwamba ilikuwaje wawili hao watongozaje kiasi cha spika wa bunge kusema kwamba alikuwa tayari kupoteza kila kitu ila si kulipoteza penzi la mwanamama huyo?
Ilikuwa ni aibu kubwa. Kila mmoja alitoa maoni yake katika mitandao ya kijamii. Wengi walishtushwa na baada ya serikali kuona kiongozi huyo akiingia doa, wengi wakajitokeza na kusema kwamba habari hizo hazikuwa za kweli.
Wakati viongozi mbalimbali wakitetea kwamba zilikuwa ni habari za uongo, hapo ndipo ukaandikwa ujumbe katika akaunti ya Mabadiliko ya Kweli ikisema kwamba kwa kiongozi yeyote aliyekuwa akiona kwamba posti zote kuhusu meseji zile zilikuwa zimetengenezwa aibuke na kusema mbele ya watu ili waanze kudili na mtu huyo kuonyesha hadharani maovu yake ya nyuma ya pazia.
“Mkuu tulisikia kwamba wewe ndiye ulisema kwamba posti zile si za kweli,” alisema mwandishi mmoja wa Gazeti la Uwazi, alikuwa akimhoji waziri mkuu.
“Mimi? Walaaaa! Sijawahi kusema maneno hayo! Kwanza lini? Nilihojiwa?” aliuliza waziri mkuu kwani alijua kwamba kama angesema kuwa yeye ndiye aliyesema hivyo basi kesho tu habari zake zingekuwa katika akaunti ya mtandao huo.
“Kwa hiyo nani alisema?”
“Wala sijui! Naomba msinipakazie! Kwanza hiyo habari si ya kuandika. Mmenisikia? Yaishie hapahapa,” alisema waziri mkuu na kumalizia kwa mkwara mzito.
Hakukuwa na kiongozi aliyejitokeza hadharani kuonyesha kwamba posti zilizokuwa zimewekwa kuhusiana na meseji zile hazikuwa za kweli kwani kila mmoja aliogopa kusema lolote lile kutokana na mkwara uliokuwa umewekwa kwamba kwa yeyote ambaye angejitokeza ilikuwa ni lazima siri zake za nyuma ya pazia ziwekwe wazi.
Wakati watu wakijadili kuhusu mjadaa wa spika wa bunge kumtongoza mke wa waziri ndipo ujumbe mwingine wa neno moja ukaonekana kwenye akaunti ile, ujumbe mfupi uliosomeka ‘Boooom’ kumaanisha kwamba kulikuwa na bomu lililokuwa limelipuka ambalo watu walitakiwa kusubiri ili kujua ni bomu gani hilo ambalo lingewavua nguo viongozi wengi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Jamani tumekwisha!” alisema mkurugenzi wa idara ya mawasiliano, kwa kile kilichokuwa kikiendelea, hakuna mtu aliyekuwa salama.
“Kuna nini?”
“Kuna bomu linalipuliwa huko mitandaoni! Jamani huyu mtu atatuua kwa presha,” alisema mkurugenzi huyo.
“Lini?”
“Kesho! Sijui linahusu nini! Mungu naomba lisinihusu mimi wala kituo changu cha kazi manake nitajinyonga,” alisema mkurugenzi huyo.
Huo ndiyo ubuyu uliokuwa umesambazwa kila kona. Kila mtu alitaka kujua hilo bomu kubwa lililokuwa limeandaliwa, kila mmoja alitaka kufahamu ni bomu gani ambalo lingewavua nguo viongozi wengi.
Kila mmoja alichanganyikiwa, hakukuwa na waziri aliyekuwa na raha, kila mmoja alikuwa na hofu ya kuona kwamba alikuwa ndani ya bomu hilo kubwa. Waziri mkuu hakuwa na furaha, mawaziri wengine mpaka Rais Bokasa wote hawakuwa na furaha, walitamani kuifungia akaunti hiyo lakini kila walichokuwa wamejaribu kufanya, hawakufanikiwa.
“Hakika hili bomu halitomuacha mtu salama,” alisema jamaa mmoja kwenye mtandao wa Facebook huku akitanguliza na ‘emoj’ nyingi za kucheka. Kila mtu akasubiri kuona ni bomu gani hilo lingewekwa katika akaunti hiyo iliyokuwa imefikisha wafuasi milioni moja na nusu.
***
Kila mtu alikuwa akisikilizia akaunti ya Mabadiliko ya Kweli kwenye Mtandao wa Kijamii wa Instagram kuona ni kitu gani kingeandikwa ambacho kingetafsiriwa kama bomu nchini Tanzania.
Watu wakapeana taarifa, kila mmoja alikuwa makini kwenye akaunti hiyo, waandishi wa habari za mitandaoni nao wakajiweka mkao wa kula, walitaka kuona kile ambacho kingeandikwa na kuwekwa katika akaunti hiyo.
Ilipofika majira ya saa saba mchana, watu wakaona kile kilichokuwa kikisubiria, kulikuwa na orodha ya majina ya viongozi waliokuwa wakitoka kimapenzi na wasichana mbalimbali wakiwemo wale wa Bongo Muvi.
Kila mmoja alikuwa na hamu ya kusoma, waliambiwa kwamba kwa kila kiongozi aliyekuwa akitoka kimapenzi na mwanamke wa nje, meseji zao za kimapenzi zingewekwa katika mtandao huo na mtu wa kwanza kabisa ambaye meseji zake zilitakiwa kuweka hadharani katika mtandao huo alikuwa Waziri Mkuu, Godfrey Francis.
Waziri huyo alikuwa akitoka kimapenzi na mwanadada aliyekuwa akitamba kwenye muziki kipindi hicho, Lady Maggy aliyekuwa akiimba RnB. Meseji zao za kimapenzi zikawekwa hadharani, zilionyesha jinsi waziri huyo alivyokuwa akimtongoza Lady Maggy mpaka walipoonana hotelini na kulala pamoja.
Hawakumaliza hapo, waliendelea kwenye uhusiano huku wakati mwingine wakisafiri kwenda Marekani kula raha. Kila uovu wa waziri huyo uliwekwa wazi na kilichowakasirisha watu wengi ni kuona kwamba alimpa mimba msichana huyo na kumwambia autoe.
“Kumbe ile kukemea kwake utoaji wa mimba hata yeye alishindwa kujikemea! Mtu mzima, una mke na watoto lakini bado tu unaendekeza wanawake wa nje, watakusaidia nini?” aliuliza jamaa mmoja, kwa kumwangalia tu alionekana kuwa na hasira mno.
Ilikuwa ni aibu kubwa kwa waziri mkuu, hakuamini alichokuwa akikiona, alijifungia chumbani kwake huku akilia. Mbele yake, hakujua angefanya nini, hata kujitetea alishindwa kwani kwa jinsi posti hiyo ilivyoandikwa katika akaunti ile, ilikuwa na ushahidi wote na hata baadhi ya mambo aliyokuwa akiyafanya, yaliwekwa kuonyesha kwamba hakusingiziwa.
“Siwezi kuishi tena! Hii ni aibu! Nitauficha wapi uso wangu,” alisema waziri mkuu huku akionekana kuchanganyikiwa.
Alishindwa kuvumilia, alikuwa na mke, watoto, ndugu na kubwa zaidi kulikuwa na Watanzania, wangemuonaje? Wangemzungumziaje kwa ule uchafu aliokuwa ameufanya?
Aliendelea kukaa chumbani kwake, hakutaka kutoka, alijifungia na hata mke wake alipogonga kwa ajili ya kuzungumza naye, hakuufungua mlango. Moyo wake ukashindwa kabisa kuvumilia, akafungua droo iliyokuwa kwenye kabati lake, akachukua bastola na kurudi kitandani ambapo akajiwekea kichwani mwake.
“Ni bora nife! Nitauficha wapi uso wangu mimi!” alisema waziri mkuu, hakutaka kuchelewa hapohapo mlio wa bastola ukasikia chumbani kwake.
“Paaaaa…” akaamua kujiua.
****
Kila mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Waseda akamkubali Godwin, alikuwa mwanafunzi mwenye uwezo mkubwa ambaye aliwafanya watu wote kugundua kwamba si watu weupe tu waliokuwa na akili kubwa bali hata watu weusi nao walikuwa balaa.
Hilo lilimpa furaha, akafarijika kwani alibadilisha kila kitu, dharau za Wazungu na Wajapan zikapotea na hivyo kuwafanya hata watu weusi kujisikia fahari kila walipokuwa wakipita mitaani.
Huo ulikuwa mwaka wake wa kwanza. Ulipoingia mwaka wa pili, uwezo wake ukaongezeka maradufu, kila mwanafunzi akatamani kufundishwa na Godwin kiasi kwamba kila alipokuwa watu walimzunguka, kila mmoja alitaka kuona ni kitu gani mwanaume huyo alikuwa akikifanya katika kompyuta yake.
Kila alipokuwa, kompyuta ilikuwa pembeni yake, makampuni mengi yalimfuata yakitaka kumuajiri lakini hakutaka kuangalia pesa, aliamini kwamba zingekuja kama tu angesoma sana na kuijua kompyuta vilivyo.
Wasichana nao hawakuwa nyuma, wale waliokuwa wakimtenga na kumuona si lolote, wakaanza kujigonga kwake, wakachukua namba yake ya simu na kuanza kumsumbua.
Kichwa cha Godwin kilikuwa kwenye masomo yake tu, hakufikiria mapenzi, alijiona kuwa na safari ndefu mbele yake na hivyo ilikuwa ni lazima kupambana kwa nguvu zote.
Alipoingia mwaka wa tatu ndipo akapata wazo kwamba ilikuwa ni lazima apambane kwa ajili ya nchi yake. Kila alipofuatilia katika mitandao ya kijamii alikutana na komenti nyingi za watu wakiilalamikia serikali iliyokuwa chini ya Rais Bokasa kwamba iliwanyonya Watanzania na waliifanya nchi kuwa kwenye kipindi kigumu.
Aliyafahamu maumivu hayo, hakutaka kuona yakiendelea na ndipo hapo alipoamua kufanya jambo kwa ajili ya Tanzania yake, kama viongozi ndiyo waliokuwa wakilalamikiwa kufanya uchafu wote basi ilikuwa ni lazima kupambana nao kupitia mitandao ya kijamii.
“Nitaanzisha akaunti! Nitaiita Mabadiliko ya Kweli, nitakuwa na kazi ya kutoa siri za viongozi. Ila nitapata vipi baadhi ya vitu? Ngoja nitengeneze urafiki na baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii,” aliwaza.
Hicho ndicho alichokifanya, ilikuwa ni lazima kupata namba za simu za viongozi mbalimbali, hakujua angezipata vipi lakini baada ya kupata marafiki kadhaa katika Mtandao wa Kijamii wa Facebook ndipo hapo alipoomba namba za viongozi mbalimbali na kupewa.
Mtu ambaye alikuwa rafiki yake wa karibu katika Mtandao wa Facebook alikuwa Ally Abdul, mmoja wa waandishi wa magazeti ya Siasa nchini Tanzania. Mwanzo alimwambia kwamba yeye mwenyewe alikuwa mwandishi wa kujitegemea ambaye alikuwa akifanya kazi nchini Japan hivyo alikuwa na uhitaji wa kuwa na namba za viongozi wengi kitu ambacho hakikuwa na tatizo lolote lile.
Akapewa namba za viongozi mbalimbali, akazichukua na kuanza kuziingiza katika system yake na ‘kuzihack’, akawa na uwezo wa kuangalia simu zilizokuwa zikitoka na kuingia, alikuwa na uwezo wa kusikia sauti za mawasiliano na kuyarekodi, alikuwa na uwezo wa kusoma meseji zote pasipo wenyewe kufahamu lolote lile.
Hilo lilimsaidia na ndilo lililomfanya kupata mawasiliano ya viongozi hao na kuweka katika akaunti yake ya Mabadiliko ya Kweli iliyokuwa katika Mtandao wa Instagram.
Kwa uwezo wake wa kuwa na digrii ya kwanza katika masuala ya kompyuta, hakukuwa na mtu aliyembabaisha, aliifunga akaunti yake vilivyo, hakukuwa na mtu aliyeweza kuingia kwenye akaunti yake kimagendo na ilikuwa ikibadilisha maeneo kila baada ya dakika kumi kwa ajili ya kuwachanganya watu wengi ambao wangejitolea kuifuatilia.
Kwa kupitia namba hizo ndipo akagundua kwamba kulikuwa na viongozi wengi waliokuwa wakitoka kimapezi na wanamuziki, kulikuwa na matukio mengi ya aibu ambayo aliamini kwamba kama angeyaweka katika akaunti yake, Tanzania ingetikisika, akaamua kuanza na Waziri Mkuu, Bwana Godfrey Francis.
****
Kila mmoja alisikitika baada ya kusikia kifo cha waziri mkuu, hakukuwa na mtu aliyeamini kwamba waziri huyo angechukua uamuzi mkubwa kiasi hicho cha kuitoa roho yake.
Waliokuwa wakitumia mitandao ya kijamii, waliandika maoni yao, wachache walikuwa wakimlaumu mtu aliyekuwa akitumia akaunti ya Mabadiliko ya Kweli lakini wengi walipongeza kwa kile kilichokuwa kimetokea.
Kifo chake kiliwatisha viongozi wengi, wakaogopa kwa kuona kwamba huo ndiyo ulikuwa mwanzo na baada ya yeye kungekuwa na wengine wengi ambao meseji zao zingewekwa hadharani kwa mambo yote waliyoyafanya gizani.
“Sisi tunataka wengine. Watu waovu ni lazima wawekwe wazi kabisa, haiwezekani watu wafanye ujinga kama huu halafu tukae kimya tu,” alisema jamaa mmoja aliyekuwa akikisapoti chama pinzani cha Tanzania National Party.
Hakukuwa na kiongozi aliyekuwa na amani kipindi hiicho, kila mmoja aliogopa kwa kuona kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wao kwani mambo ambayo yalifanyika gizani yalikuwa makubwa mno.
Wakati watu wakihuzunika kwa msiba uliotokea, wakapata taarifa nyingine kwamba hata Spika wa Bunge, Mheshimiwa Ramadhani Nyakunyaku naye alijiua usiku uliopita baada ya meseji zake za kimapenzi akimtongoza mke wa waziri kuwekwa siku mbili zilizopita.
Akaunti ya Mabadiliko ya Kweli ikawa gumzo kila kona, ikazidi kuwa maarufu na kuwafanya hata wale watu ambao hawakujua kilichokuwa kikiendelea huko kutamani kusoma kila siku kilichokuwa kikiendikwa.
Rais Bokasa alichanganyikiwa, aliona kabisa kwamba mwisho wa kila kitu mtu aliyekuwa akitumia akaunti hiyo angeweka mambo yake, hivyo akataka kujilinda kwa kuwaita watu waliokuwa wataalamu wa kompyuta kutoka Afrika Kusini kwa ajili ya kufanya kazi ya kuifuta akaunti hiyo.
Ndani ya siku mbili, wataalamu hao wakafika nchini Tanzania na kupewa rasmi kazi hiyo kwa malipo makubwa. Bila tatizo lolote lile, vijana hao wakaanza kufanya kazi ya kuhangaika kuifuta akaunti hiyo.
“Hii si kazi ngumu! Kitu kama hiki kilitokea nchini kwetu. Kulikuwa na kichaa mmoja alianzisha akaunti kama hii, kutwa nzima alikuwa akimzungumza Nelson Mandela, hakuchukua muda mrefu, ndani ya wiki tu, tukaifuta,” alisema jamaa mmoja, alikuwa akijigamba mbele ya Rais Bokasa.
“Safi sana. Ndiyo maana nimewaita. Ngoja niwaache mfanye kazi yenu,” alisema Rais Bokasa na kutoka ndani ya chumba hicho huku akiwaacha vijana hao wawili wakiwa wanajiandaa kufanya kazi ya kuifuta akaunti ya Mabadiliko ya Kweli katika Mtandao wa Kijamii wa Instagram.
***
Ilionekana kuwa kazi nyepesi mno kabla ya kuifanya lakini baada ya kuianza ndipo wakagundua kwamba haikuwa kazi nyepesi hata mara moja. Vijana wa IT waliotoka Afrika Kusini wakaanza kuhangaika kuifuta akaunti hiyo, ilikuwa kazi kubwa mno, walitumia kila aina ya programu, ujuzi wao wote katika kufuta akaunti hiyo lakini ilishindikana kabisa.
Walihangaika kwa saa kumi na mbili, vijasho vilikuwa vikiwatoka, hawakujua namna ambavyo mtu huyo alikuwa ameifunga akaunti yake, walijaribu kila aina ya mbinu na wakati mwingine kuwasiliana na watalaamu wenzako wa Kiholanzi waliokuwa Uholanzi lakini hawakufanikiwa.
Kwao, tangu waanze kufanya kazi ya kufanya lolote katika kompyuta, iwe kwenye programming au network hawakuwahi kukutana na kitu kigumu kama hicho. Pamoja na kuwa na masters zao lakini hawakufanikiwa kabisa kuifuta akaunti hiyo.
Rais Bokasa aliwaamini vijana hao kwamba wangeweza kufanikiwa kuifunga akaunti hiyo ambayo kila siku ilizidi kuongeza watu waliokuwa wakiifuata kwa ajili ya kupata habari chafu za viongozi wa nchi hiyo.
Alitulia ikulu huku akiwa ameweka miguu juu, alifurahia, alikenua kila wakati huku muda mwingi akiiangalia simu yake kwani alijua kwamba angepigiwa na vijana hao ambao wangempa taarifa kwamba akaunti ile ilifungwa na asingeweza kuiona tena.
Alisubiri simu hiyo kwa saa nyingi, hakuona dalili za kupigwa, akaingiwa na hofu kitu kilichomfanya kuichukua na kuwapigia vijana ambao aliwaacha kusimamia kazi hiyo ambao walimwambia kwamba bado hawakuwa wamefanikiwa.
“Kwa saa kumi na mbili?” aliuliza huku akiwa haamini alichokuwa akikisikia.
“Bado mkuu!”
“Unavyoona kuna dalili za kufanikiwa?”
“Sidhani! Wote naona wanatokwa na jasho jembamba, nahisi hii kazi imekuwa ngumu sana kwao,” alisikika kijana huyo kwenye simu.
Rais Bokasa akakata simu, uso wake ukabadilika, ndita zikaanza kuonekana, moyo wake ulimuuma mno, kwa kipindi hicho hakukuwa na kitu kilichomuuma kama kuona akaunti hiyo ikiendelea kuwa hewani.
Hakuona kama maisha yake yangekuwa na usalama, kulikuwa na mambo mengi machafu aliyokuwa ameyafanya nyuma ya pazia na aliamini kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima mmiliki wa mtandao huo ayapate mambo hayo na kuyarusha hewani kama ilivyokuwa kwa waziri mkuu.
Wakati akiwa chumbani kwake huku akiwa hajui ni kitu gani alitakiwa kufanya, ghafla akashtushwa na mlio wa simu, alichohisi ni kwamba alikuwa akipigiwa na kijana yule kuambiwa kwamba kazi ilifanikiwa, alipoichukua na kuangalia kwenye kioo, macho yake yakatua katika jina Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Selemani Kimwinyi
“Niambie kuna nini” alisema Rais Bokasa huku akiwa ameiweka simu hiyo sikioni kwake.
“Kazi imeanza upya mtandaoni! Kuna tuhuma nyingine nzito, ni nzito zaidi ya zile za waziri mkuu,” alisikika Kimwinyi kwenye simu.
Kabla ya kuzungumza lolote juu ya tuhuma hizo zilizokuwa mtandaoni, Rais Bokasa akanyamaza kwa muda, akahisi mwili wake ukianza kutoka na kijasho chembama, mwili ukakosa nguvu na hapohapo kukaa kochini.
Alijua fika kwamba mtu aliyekuwa ameandikwa kwenye mtandao ule alikuwa yeye na kilichomfanya kuhisi hivyo ni kwa sababu tu alipigiwa simu na mkurugenzi huyo wa usalama wa taifa kwani kama tuhuma hizo zisingemhusu yeye, asingepigiwa simu hiyo kupewa taarifa.
“Subiri kwanza!” alisema rais huyo huku akishusha pumzi zake.
Akakata simu, hakutaka kuendelea kuiacha simu hiyo hewani, alitaka kuona ni kitu gani kilichokuwa kimeandikwa katika akaunti hiyo. Hakutaka kuchelewa, hapohapo, huku akitetemeka akafungua akaunti yake ya siri iliyokuwa kwenye Mtandao wa Kijamii wa Instagram na moja kwa moja kwenda kwenye akaunti hiyo.
Alipoifungua tu, moyo wake ukapiga paaa! Kulikuwa na picha kubwa ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Michael Lazaro ambapo kwa chini kulikuwa na maneno mengi yaliyoeleza kuwa alikuwa mtu aliyejihusisha na mapenzi ya jinsia moja huku pia kukiwa na idadi ya watu ambao amewahi kutembea nao.
“Ni waziri anayelala na wanaume wenzake! Ni mtu mbaya, amelala na viongozi wengi, ila wa kwanza kabisa ambaye nitamtaja ni mtu mliyempa dhamana, Rais Bokasa, ushahidi upo, nawatumia mazungumzo yao katika posti inayofuata. Kama akijitokeza kubisha, nitawawekea na picha zao wakiwa chumbani, yaani wawili tu,” ilisema posti iliyowekwa katika akaunti hiyo.
Bila kutarajia, machozi yakaanza kumtoka rais huyo, hakuamini alichokuwa akikiona, alishindwa kujua afanye nini kwani kila alipoisoma posti hiyo zaidi na zaidi, aliwaona Watanzania wakiwa mbele yake, walimcheka huku wakimdhihaki kwa kile alichokuwa amekifanya.
Wachangiaji kwenye posti hiyo walijitokeza kwa wingi. Waliiamini akaunti hiyo, kila kitu kilichokuwa kikiandikwa kilikuwa na ushahidi wa kutosha, na wengi waliokuwa wakichangia walionyeshwa kuguswa na kile kilichokuwa kikiendelea, yaani rais wa nchi afanye mambo ya kishoga kama hayo, kila mtu alishtushwa kwa posti hiyo.
“Jamani! Dunia inakwenda wapi huku? Kumbe tunaongozwa na rais mpumbavu kama huyu! Yaani nchi inapinga vitendo vya kishoga kila siku kumbe yeye ndiye namba moja kwa kufanya ushenzi huo. Hakika dhambi hii haitomuacha salama,” aliandika jamaa mmoja, kwa jinsi komenti hiyo ilivyoandikwa, alionekana kukasirika mno.
Hilo ndilo likawa gumzo nchi nzima, kila mmoja aliyeiona posti hiyo alimwambia mwenzake, mitandaoni hakukukalika, kila mmoja alionekana kuguswa kwa kile kilichokuwa kimetokea.
Wengi waliumia, hawakuamini kama watu wastaarabu kama wao waliongozwa na mtu mpumbavu kama Rais Bokasa. Kila mmoja alitaka kusikia ikulu ingesema nini juu ya tuhuma hizo kwani mbali na kuweka posti hiyo kungekuwa na ushahidi wa meseji walizokuwa wakiwasiliana
“Jamani mwenzenu napenda abishe ili tuzione hizo picha,” alisema jamaa mmoja.
Viongozi wa Chama Pinzani, Tanzania National Party wakatumia mwanya huohuo kuweka mikutano isiyo rasmi na kuzungumza na wananchi juu ya kile kilichokuwa kikiendelea ambacho kilionekana kuichafua nchi.
Wakati hayo yote yakiendelea, akaunti ya Mabadiliko ya Kweli iliendelea kupata wafuasi wengi, zaidi ya watu laki mbili walikuwa wakiongezeka kwa siku na ndiyo ikawa akaunti ya kwanza kufikisha watu milioni kumi nchini Tanzania.
Vichwa vya watu wengi vilijiuliza juu ya mtu aliyekuwa nyuma ya akaunti hiyo, wengi walihisi kwamba mtu huyo alikuwa mmoja wa viongozi serikali na alikuwa akifanya kazi zake kwa siri sana na ndiyo maana alijua mambo mengi ya siri yaliyokuwa yakiendelea nchini humo.
Hakukuwa na haja ya kumwamini mtu, kila mmoja alijua lazima mhusika wa akaunti hiyo alikuwa ndani ya chama au mtu wa karibu wa viongozi fulani lakini kitu kikubwa kilichokuwa kikiwatatiza watu, ilikuwaje mtu huyo kupata mawasiliano ya simu na wakati mwingine aliweka mpaka sauti za watu waliokuwa wakitongozana.
“Jamani! Hili ni janga la taifa! Rais ajitokeze basi akane tuhuma hizo! Au hataki watu tuone picha?” aliuliza jamaa mmoja aliyekuwa na wenzake, wote wakaanza kucheka.
Siku hiyohiyo baada ya saa moja picha za mawasiliano ya Waziri Lazaro na rais yakawekwa katika akaunti ile, kila mmoja alishangaa, kwa jinsi mawasiliano yale yalivyokuwa, kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba kweli mawasiliano hayo yalikuwa ya watu hao.
Rais Bokasa alikuwa akimshukuru waziri huyo kwa kumwambia kwamba alikuwa mtu muhimu hata zaidi ya mke wake, alikuwa na muonekano mzuri hata zaidi ya mwanamuziki wa Kimarekani, Beyonce. Alimpa sifa kemkem, alimsikifia kana kwamba alikuwa akimsifia mwanamke mrembo aliyewahi kukutana naye mahali fulani.
****
Kikao kizito cha watu sita akiwemo Rais Bokasa kilikuwa kimewekwa ndani ya chumba kimoja kilichokuwa ikulu. Kila mmoja aliyekuwa ndani ya chumba hicho alionekana kutokuwa sawa, wote walionekana kuwa na hofu nzito, nyuso zao zilikuwa na huzuni kubwa kana kwamba walikuwa wamepokea taarifa ya msiba mzito.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wote waliitwa na rais Bokasa kwa ajili ya kujadili ni kitu gani walitakiwa kufanya ili kuhakikisha wanammaliza mtu aliyekuwa na akaunti hiyo. Hawakumfahamu lakini waliona kabisa kwamba kama wangetumia uwezo wao wa kuzaliwa basi wangeweza kumgundua na kumuua mara moja.
Katika kikao hicho, kulikuwa na majina hamsini ya watu kwenye karatasi, walitakiwa kuyasoma majina yote hayo, yalikuwa ni ya watu mbalimbali, wengine walikuwa wanachama wenzao na wengine walikuwa vijana machachari wa chama pinzani ambao walikuwa wakishadadia kila kitu kilichokuwa kikiandikwa katika mitandao ya kijamii.
Wote walitakiwa kuchagua majina ya watu ishirini ambao walihisi kabisa walikuwa wakihusika, watu ambao walitakiwa kuuawa mara moja, kwa kufanya hivyo ingewapa urahisi kumbahatisha kumpata mtu ambaye alikuwa akihusika katika akaunti hiyo.
“Majina hamsini yapo mbele yenu, yachukueni, najua mnawajua wote hao. Akili yangu inaniambia mmojawapo ndiye mhusika wa akaunti hii. Chagua watu ishirini unaowahisi, wale watakaochaguliwa kwa wingi mpaka mwisho ni lazima tuwaue ili tuone kama akaunti ile itaendelea kuandika upuuzi,” alisema Rais Bokasa kwa sauti ndogo kana kwamba hakutaka watu wa vyumba vingine wasikie.
***
Kilikuwa kikao kizito, kila mmoja alikuwa akiyaangalia majina hayo yaliyokuwa yameandikwa katika karatasi zile. Waliona majina ya watu wengi waliokuwa wakituhumiwa kwamba ndiyo watu waliokuwa na mtandao huo.
Hawakumjua mmiliki wa akaunti ile ila kilichokuwa kikifanyika kilikuwa ni kumbashiri mtu ambaye alikuwa nyuma ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Ilikuwa ni kazi nzito kumbashiri mtu ambaye alikuwa akihusika katika akaunti ile.
Kila wakati, wote walikuwa wakishusha pumzi nzito, lilikuwa suala gumu lakini baada ya saa moja, wote waliwabashiri watu wao, wale waliokuwa wamechaguliwa kwenye kila karatasi walitakiwa kuuawa haraka iwezekanavyo.
“Kimwinyi simamia kila kitu,” alisema Rais Bokasa huku akimwangalia mkurugenzi wa usalama wa taifa.
Baada ya kumaliza kikao hicho, wakaruhusiwa kuondoka. Kila mtu ndani ya gari alikuwa na mawazo yake, walijua kwamba kile walichokuwa wamekifanya hakikuwa sahihi kwa kuwa walijua kabisa walikuwa wakienda kuwaua watu wasiokuwa na hatia lakini kwa kuwa mkuu wao ndiye aliyeamua hivyo, hawakuwa na jinsi, utekelezaji ulitakiwa kufanyika haraka iwezekanavyo.
Wakati mipango ikiwa imesukwa kabisa kwamba mauaji hayo yalitakiwa kufanyika haraka iwezekanavyo, wote wakashtuka baada ya kuona kila kitu kilichokuwa kimejadiliwa ndani ya chumba kile kidogo kuwekwa wazi katika akaunti ya Mabadiliko ya Kweli.
Hakukuwa na mtu aliyejua jinsi mawasiliano yale yalivyomfikia mtu huyo kwani walifanya kila kitu kwa siri, hakukuwa na mtu aliyekuwa akifahamu chochote kile zaidi ya wao waliokuwa humo lakini kitu cha ajabu kabisa, ndani ya saa ishirini na nne, kila kitu kilikuwa wazi.
Kila Mtanzania alishangaa, hawakuamini kuona rais wao akiwa ameandaa kikao kile kwa ajili ya kuwaua watu ambao walihisi kwamba walikuwa nyuma ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
Ulikuwa mpango uliozidi kumchafua Rais Bokasa kwani mbali na kutaja tu kuhusu kikao hicho, akaunti ile ilizungumza kila kitu kilichojadiliwa ndani ya kikao hicho mpaka namna ambavyo rais alivyomuachia mkurugenzi wa usalama wa taifa kuhakikisha kwamba watu wote ambao majina yao yalikuwa yamechaguliwa kutakiwa kuuawa haraka sana.
“Kuna mtu anatuuza! Tena mtu huyo alikuwa mulemule ndani, yaani ni mtu ambaye alikuwepo kwenye kile kikao,” alisema Rais Bokasa huku akionekana kuchanganyikiwa.
Hakutaka kupoteza muda, akampigia simu Kimwinyi na kumwambia kwamba alikuwa na kitu cha kujadili naye. Hilo halikuwa tatizo, haraka sana Kimwinyi akakutana na rais huyo ikulu na kuanza kujadili.
Uamuzi wa rais ulikuwa mmoja tu kuhakikisha kwamba watu wote waliokuwa kwenye kile kikao wauawe mara moja pasipo kuangalia nani ni nani na alikuwa na nguvu gani nchini kwani alihisi kwamba mmojawapo kati ya wale watu ndiyo aliyekuwa akihusika kwa kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
“Haiwezekani tuongee kwa siri halafu baada ya saa ishirini na nne kila kitu kiwe wazi, kuna mtu mule alitusaliti, kuna mtu anatusnichi mule,” alisema rais huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Haina shida mkuu! Nitafanya kila kitu utakachoniagiza,” alisema Kimwinyi.
“Ua watu wale wanne tuliokuwa nao kwenye kile chumba,” alisema rais.
“Sawa mkuu!”
Walichokubaliana ndicho kilichofanyika, Kimwinyi akaondoka na kuwaandaa vijana wake kwa kuwapa majina ya watu ambao walitakiwa kufa haraka iwezekanavyo.
Hilo halikuwa tatizo, mtu wa kwanza kabisa kuuawa alikuwa katibu wa Chama Tawala cha Labour party, Mzee Filipo Zabedayo.
Ili kuonekana kwamba hakuhusika kwa kitu chochote kile, Rais Bokasa akaondoka nchini na kwenda Uswisi huku nyuma akiacha mauaji yakifanyika.
Saa kadhaa tu baada ya kuachana na Kimwinyi taarifa zikamfikia hukohuko alipokuwa kwamba Katibu wa Chama, Mzee Filipo alipata ajali mbaya alipokuwa akielekea Dodoma kukutana na mwenyekiti wa kamati ya bunge kuzungumzia kile kilichokuwa kimetokea mpaka spika wa bunge hilo kujiua.
Ilikuwa ajali iliyotengenezwa kwa ustadi mkubwa. Gari lake lilipinduka kwa kile kinachodhaniwa dereva kuendesha kwa mwendo wa kasi huku barabara ikiwa imelowa. Hakukuwa na mtu aliyetoka salama ndani ya gari hilo kwani lilikwenda kugonga mti mkubwa uliokuwa kichakani ambapo miili ya dereva wa Mzee Filipo na yeye mwenyewe kutolewa nje kwa kuwa hawakufunga mkanda.
“Mimi niliiona hii ajali! Ilikuwa mbaya sana! Gari liliseleleka, likaja huku nilipokuwa, likagonga huu mti! Miili yote ikatolewa ndani ya gari! Lawama zote ziende kwa dereva,” alisema jamaa mmoja, kwa kumwangalia ilikuwa rahisi kudhani alikuwa mwanakijiji lakini ukweli ni kwamba alikuwa mmoja wa vijana waliokuwa wametumwa kufanya kazi hiyo.
Ulikuwa ni msiba mzito uliokikumba Chama cha Labour Party, kila mtu alisikitika kwa kile kilichokuwa kimetokea kwani hakukuwa na mtu aliyekuwa akiaminika kwa kufanya kazi kwa kujitolea kama alivyokuwa Mzee Filipo.
Msiba huo ukawa gumzo Tanzania, kila mtu alizungumza lake, wengi walitaka kujua kile kilichokuwa kimetokea kwamba ilikuwa ni ajali kama ajali au kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea.
Kila mmoja macho yake yalikuwa kwenye akaunti ya Mabadiliko ya Kweli, waliamini kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima mtumiaji wa akaunti hiyo aandike kitu chochote kuhusu ajali hiyo ambayo tayari kulikuwa na minong’ono iliyosikika kwamba kulikuwa na mtu aliyehusika katika ajali hiyo.
“Kazi nzuri sana Kimwinyi!”
“Nashukuru mkuu! Kwa jinsi tulivyomuua, hakuna mtu atakayejua!” alisema Kimwinyi.
“Ilikuwaje?”
“Tulimuweka mtu wetu ndani ya gari hilohilo kwa kisingizio cha kuelekea Dodoma kikazi kwa chama. Huyo ndiye aliyefanya kazi ya kuwaua wote wawili ndani ya gari hilo hata kabla halijafika Dodoma, akashikilia usukani, akaenda kuligonga gari hilo kwenye mti, miili tukaitoa kuonyesha ilitoka garini,” alisema Kimwinyi.
“Kazi nzuri sana! Bado wengine,” alisema rais Bokasa.
“Haina shida! Niachie mimi!”
Kila mmoja alikuwa akijipongea kwa kazi nzuri aliyokuwa ameifanya, wale wote waliohusika katika mchakato mzima wa kufanya mauaji hayo wakakutana baa na kuanza kunywa pombe kama ishara mojawapo ya kujipongeza kwa kazi hiyo.
Wakati wakiendelea kunywa tena huku wakicheka ndipo Kimwinyi alipopokea ujumbe kutoka kwa mtu ambaye hakumfahamu, tena namba ngeni iliyomwambia kwamba alijua kila kitu kilichokuwa kimetokea, hivyo asubiri kulipuliwa katika akaunti yake ya Mabadiliko ya Kweli.
“Wewe nani?” aliandika ujumbe Kimwinyi huku akitetemeka.
“Mtetezi wa wanyonge. Mwenye akaunti ya Mabadiliko ya Kweli,” ulisema ujumbe aliotumiwa.
Pombe hazikupanda tena, alichanganyikiwa, hakuamini kile alichokuwa ametumiwa, haraka sana akasimama kutoka katika kiti chake pale baa na kwenda ndani ya gari lake, akauegemea usukani wa gari lake, alikuwa na hofu kubwa kwamba hatimaye naye jina lake lingeenda kuandikwa katika akaunti hiyo kama msuka mipango wa ajali ile iliyokuwa imetokea.
Hapohapo akaingia kwenye akaunti yake ya Instagram, alijua kwamba mtu huyo atakuwa ameandika kuhusu ajali hiyo, alichokikuta humo ni picha ya ajali huku kwa chini kukiwa na maswali matano tata ambayo Watanzania walitakiwa kujiuliza juu ya ajali hiyo. Maswali hayo matano yalikuwa haya:
“Wanasema kwamba gari liliseleleka kwa kuwa barabara ilikuwa imelowa. Kwa siku ya ajali hiyo, hakukuwa na mvua kubwa iliyokuwa imenyesha, yalikuwa ni manyunyu tu, je, iweje ripoti iseme kwamba gari liliseleleka kwa kuwa kulikuwa na maji mengi?”
“Swali la pili ambalo Mtanzania unatakiwa kujiuliza ni kuhusu yule mtu pekee aliyetoa taarifa. Anasema kwamba yeye ni mwanakijiji wa pale lakini kamuulize mwanakijiji yeyote kama anamfahamu, kijiji kizima hakimfahamu, na si kijiji hicho tu bali hata vijiji vya jirani, je, kama kweli mtoa taarifa anasema yeye ni mkazi wa kijiji hicho, kwa nini wanakijiji wote hawamfahamu?”
“Swali la tatu. Gari linapokuwa katika mwendo wa kasi na kugonga sehemu basi ni lazima miili iwe na majeraha makubwa na damu nyingi. Angalia kioo ambacho wanasema miili ilitolewa, kwa jinsi ilivyovunjika, kweli ni rahisi kwa mtu kutoka humo bila hata kuchanika? Inawezekana mmoja asichanike, lakini je, ni rahisi kwa wote kutokuchanika hata damu kutoka?”
“Swali la nne. Wanasema kwamba walitolewa nje kwa kuwa hawakufunga mikanda. Kuna picha nyingi zinaonyesha Mzee Filipo alipokuwa safarini, hata awe anatoka Magomeni kwenda Kinondoni ilikuwa ni lazima kufunga mkanda, zipo picha zaidi ya ishirini zinazothibisha hilo. Sasa iweje leo mzee huyo asafiri kutoka Dar mpaka Dodoma, gari liwe kwenye mwendo wa kasi na asifunge mkanda?”
“Swali la tano. Baada ya ajali kutokea, kitu cha ajabu kabisa wakatokea watu waliodhaniwa kutoa msaada, waliichukua miili harakaharaka kabla watu hawajajaa na kuondoka nayo na kusema kwamba wote walikuwa wamekufa. Je, watu hao walikuwa wakina nani? Na kwa nini wawaondoe haraka sana na wakati tayari walikufa? Kwa nini napo gari liliondolewa haraka sana eneo la tukio? Ukijiuliza maswali hayo yote, utagundua kwamba ajali ilikuwa imepangwa na watu hao walikuwa wameuawa kabla ya tukio hilo.
“Tafuteni mbinu nyingine, hizo zenu zimepitwa na wakati. Kesho nitakwenda kuwaambia Watanzania kila kitu kilichotokea kabla ya hawa watu kuuawa, mpango ulikuwa ni kumuua Mzee Filipo tu. Nitaeleza jinsi kikao cha watu wawili kilichopangwa, badala ya hawa kufa, kuna watu watatu nao wanatakiwa kuuawa haraka iwezekanavyo, sababu yake nitaiweka kesho pia,” ilisema posti hiyo ndefu.
Baada ya kumaliza kuisoma posti hiyo ndefu, Kimwinyi akabaki akitetemeka, mwili ukafa ganzi, akahisi muda wowote ule presha ingepanda na kufariki ndani ya gari hilo.
Godwin alikuwa akiendelea kusoma kama kawaida, kichwa chake kilikuwa na mawazo mengi, alikuwa akifikiria namna ambavyo angeweza kuwawekea chuki kubwa wananchi juu ya viongozi wao waliokuwa wakiwaibia fedha wananchi wao na hata kuwakandamiza masikini.
Hakuacha kudukua mawasiliano yao, kila wakati alikuwa akicheza na kompyuta yake, alijua fika kwamba watu hao walikuwa wakiwasiliana, katika kila meseji walizokuwa wakitumiana wabunge wote nchini Tanzania, alizipata kwani alikuwa ameingiakatika namba zao bila kujua.
Ukiachana na hao, pia kulikuwa na watu wa usalama wa taifa ambao aliamini kwamba kama angefanikiwa kuwa na mawasiliano yao na kufuatilia kila kitu basi angefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Bado aliendelea kukusanya namba za watu mbalimbali, wale waliokuwa na sauti nchini Tanzania. Alifanikiwa kwa kiasi kikubwa sana na ndiyo maana hata kikao kidogo cha watu sita ambacho kiliitishwa ikulu, naye alipata taarifa kwani kila walipopigiana au kutumiana meseji, alikuwa akipata taarifa hizo.
Alishangaa kuona watu hao walikusanyika kwa kuwa walitakiwa kuandika majina ya watu hamsini. Hakujua katika karatasi hizo waliandikwa wakina nani lakini baada ya mkurugenzi wa usalama wa taifa kupigiwa simu na kuambiwa kwamba walitakiwa kufanya mauaji ya watu waliokuwa nao mule ndani, tena kwa kuwataja majina ndiyo akagundua kwamba tatizo kubwa ni kwa sababu aliweka kila kitu kilichozungumziwa katika kikao kile hasa baada ya kudukua mawasiliano ya simu yaliyofanyika baada ya kikao.
Alijua kwamba kulikuwa na mtu mmoja miongoni mwa watu waliokuwa katika kikao kile alikuwa akienda kuuawa, hakujua ni nani na hivyo macho na masikio yake yalikuwa kwenye simu yake ambayo muda wote kazi kubwa ilikuwa ni kudukua mawasiliano ya viongozi hao.
Hapo ndipo akagundua kwamba mtu aliyekuwa akitakiwa kuuawa alikuwa Mzee Filipo, hakuamini macho yake kwani miongoni mwa watu waliokuwa wakiheshimika katika chama tawala alikuwa mtu huyo.
Hakutaka kuzungumza kitu, alitaka kuona kama mauaji hayo yangefanyika au la. Kile alichokuwa akikitegemea ndicho kilichofanyika kwani mzee huyo alikufa katika ajali ambayo mara baada ya kuifuatilia, akapata maswali kadhaa ambayo aliyaandika kwenye akaunti yake Instagram.
Alishangaa, hakuamini kwamba yeye ndiye alikuwa sababu kubwa iliyomfanya mzee huyo kuuawa, hakutaka kuona mauaji yakiendelea, alichokifanya ni kuposti kuhusu mauaji hayo, Watanzania wajue kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
Wakati yeye akitafakari hayo yote upande wa pili Kimwinyi alionekana kuchanganyikiwa, pombe zote alizokuwa amekunywa ziliyeyuka kichwani mwake, ulevi wote ukamuondoka, akaegemea usukani na kuanza kuyafikiria maisha yake.
Alishirikiana na rais kwa kila kitu, walicheza michezo mingi ya mauaji lakini kipindi hicho mambo yalionekana kuwabadilikia, walidili na mtu ambaye hawakujua alikuwa wapi ingawa aliamini kwamba alikuwa na nguvu kubwa.
Mara baada ya kujifikiria kwa muda huku akiwa ndani ya gari, akampigia simu Rais Bokasa na kumwambia kilichokuwa kikiendelea, kwamba alipigiwa simu na mtu asiyemfahamu na kumwambia kwamba alikuwa akijua mchezo mzima na lazima afanye juu chini kuhakikisha majina yao anayaweka katika akaunti ile.
Hilo ndilo lililomchanganya zaidi, pamoja na uovu wake mkubwa lakini hakutaka kugundulika na mtu yeyote yule, kila siku alijifanya mtu mwema, aliwasaidia watu, kitendo cha mtu huyo kusema kwamba angeweka kila kitu hadharani kilimchanganya mno.
“Kwa hiyo tufanye nini Kimwinyi?” aliuliza rais.
“Sijajua! Hii hali inanichanganya sana. Nani anamwambia huyu mtu mambo haya?” aliuliza Kimwinyi.
“Hilo ndilo la msingi kujiuliza. Ila aliponipigia simu, kulikuwa na namba aliyotumia, nadhani tukiitumia hii, tutafanikiwa kumpata,” alisema mwanaume huyo.
“Unayo?”
“Ndiyo!”
“Hebu tuanze kuifuatilia.”
Hilo ndilo lililofanyika, siku iliyofuata Kimwinyi akaondoka kwenda makao makuu ya Mtandao wa Simu wa Tritel ambapo baada ya kufika huko akawapa namba ile iliyotumika kumpigia huku dhumuni lake likiwa ni kujua mahali namba hiyo ilipokuwa mara ya mwisho ilipokuwa ikitumika.
“Hii ndiyo namba yenyewe?” aliuliza dada aliyekaa kwenye meza iliyokuwa na kompyuta.
“Ndiyo!”
Akaanza kuifanyia kazi, akaiangalia kwenye kompyuta yake, muda wote alikuwa kimya, aliikodolea macho kompyuta yake huku Kimwinyi akiwa mbele yake akimwangalia tu.
Msichana yule alihangaika kwa dakika kumi nzima, hakufanikiwa, akaichukua laini ile na kumpatia Kimwinyi ambaye alikuwa na hamu ya kusikia mahali ilipokuwa.
“Hiyo namba bado haijaanza kutumika,” alisema msichana huyo.
“Haijaanza kutumika?”
“Ndiyo! Yaani kwa kifupi bado hatujatengeneza namba ya namna hiyo,” alisema msichana huyo huku akimwangalia Kimwinyi.
“Yaani sijakuelewa. Umesemaje?”
“Tuna namba ambazo tunazitengeneza. Namba zinazoanzia 8 bado hazijaanza kutengenezwa, zipo zinazoanzia na 6 ambazo ndizo tulizofikia,” alisema msichana huyo.
“Kwa hiyo hii namba haipo?”
“Ndiyo!”
“Sasa aliyenipigia mbona ndiyo kaitumia hii?” aliuliza.
“Hebu niione!”
Kimwinyi akampatia simu yake msichana yule ambaye aliiangalia ile namba, kweli ilitumika. Yeye mwenyewe hakujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea, kwa nini namba ile itumike na wakati haikuwa imetengenezwa kwa matumizi.
Kila mtu aliyeulizwa humo, hakujua, vijana wa IT nao walishangaa. Mpaka Kimwinyi akaondoka baada ya kutumia saa mbili makao makuu hapo hakuwa amepata jibu la maswali yake juu ya namba ile.
“Kwa hiyo haipo?”
“Ndiyo mkuu!”
Wakati wao wakijiuliza kuhusu namba, upande wa pili Watanzania walikuwa wakijiuliza kuhusu mauaji ya Mzee Filipo, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mpaka muda huo. Walitaka kusikia taarifa kutoka ikulu juu ya kile kilichokuwa kikiendelea nchini.
“Kumbe Mzee Filipo aliuawa?” aliuliza jamaa mmoja.
“Mmh! Wewe umepata wapi taarifa?”
“Ingia Instagram uone kwenye akaunti ya Mabadiliko ya Kweli ilivyoadikwa,” alijibu jamaa aliyeulizwa swali.
Jamaa huyo alipoingia, kila alichoambiwa ndicho alichokiona, hakuamini macho yake, si yeye tu bali kila mtu aliyeingia na kusoma katika akaunti ile hakuamini kama Mzee Filipo alikuwa ameuawa.
Kulikuwa na maswali ambayo yaliambatana na picha ile iliyowekwa, maswali hayo ndiyo yaliyozua gumzo kubwa hasa la jamaa ambaye alisema kwamba alikuwa mwanakijiji wa kijiji kilichotokea ajali na wakati hakuwa akijulikana na mtu yeyote hapo.
Jinsi maswali yale yaliyoulizwa yalivyokuwa, kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba Mzee Filipo alikuwa ameuawa na kisha ajali ile kutengenezwa ili ionekane kwamba alipata ajali mbaya na kufa.
Vichwani mwa watu wengi walikuwa na hamu ya kujua ni mtu gani alikuwa amehusika katika mauaji hayo. Waliambiwa kwenye akaunti ile kwamba hatimaye mtu aliyehusika angewekwa hadharani lakini pia waliambiwa kwamba kulikuwa na kikao cha watu sita kilichowekwa, kilikuwa kikao muhimu cha kummaliza mtu aliyekuwa na akaunti hiyo, hawakumfahamu, walikuwa wakicheza mchazo wa kubahatisha tu.
“Mimi ninataka kuwajua hao watu waliokuwa kwenye hicho kikao. Ni nani na nani sasa?” aliuliza msichana mmoja aliyekuwa akisoma posti katika akaunti hiyo.
Hilo ndilo lilikuwa hitaji la watu wengi, kila mmoja alitaka kuona majina ya watu waliokuwa kwenye kikao hicho na pia walitaka kujua watu wawili waliokuwa wamepanga mpango wa kumuua Mzee Filipo, tatizo lilikuwa nini na wakati kila mtu ndani ya chama alikuwa akimpenda mzee huyo?
Wakati watu wakihitaji majibu ya maswali yote waliyokuwa wakijiuliza, Rais Bokasa alikuwa na hofu tele, kwa kile kilichokuwa kikiendelea kilimchanganya kichwa chake.
Alitaka kuwaua watu wanne ambao aliamini kwamba kwa namna moja au nyingine mmoja kati ya ndiye aliyekuwa akihusika katika kumiliki akaunti hiyo lakini kitu cha ajabu kabisa, hata alipokaa na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Bwana Kimwinyi watu walijua kile kilichokuwa kimezungumziwa, mipango yao mpaka jinsi mauaji hayo yalivyotakiwa kufanyika.
“Sasa huyu atakuwa nani? Au Kimwinyi mwenyewe? Kama tulipanga mipango wawili tu, mimi na yeye halafu kesho huyu mtu wa mtandao anajua, nani kamwambia kama si yeye? Nina wasiwasi naye, atakuwa anahusika huyu,” alijiuliza Rais Kimwinyi huku akionekana kuchanganyikiwa.
Kama walikuwa wawili tu, wakapanga dili na baadaye kubumbulika, akawa na uhakika kwamba Kimwinyi alikuwa akihusika na akaunti ile na kama si yeye basi alikuwa akimpa mtu huyo kila kitu kilichokuwa kikiendelea, ili aendelee kuwa salama ilikuwa ni lazima amuue huyo Kimwinyi kwani tayari alikuwa na wasiwasi naye kupita kawaida.
Katika harakati za kumuua Kimwinyi hakutaka kumshirikisha mtu yeyote yule, alitaka kila kitu kiwe siri kubwa na kusiwe na mtu yeyote ambaye alitakiwa kufahamu kilichokuwa kikiendelea.
“Ni lazima nimtume aende Nigeria, akifika huko niwasiliane na Boko Haram wamuue,” aliwaza Rais Bokasa, mbinu hiyo ndiyo aliyotaka kuitumia, ilikuwa ni lazima amuue mwanaume huyo ambaye aliamini ndiye aliyemsaidia mtu mwenye akaunti ile Instagram kupata taarifa ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
***
Rais Bokasa hakutaka kukubali, alihisi kabisa kwamba Kimwinyi ndiye alikuwa adui yake namba moja, hakutaka kuona mwanaume huyo akiendelea kuvuta pumzi ya dunia hii, kile alichokitaka ni kumuua kisiri kwa kuamini kwamba baada ya kufanya mauaji hayo basi angekuwa salama kabisa.
Usiku mzima alikuwa na mawazo tele, aliwasiliana na mkuu wa kundi la Boko Haram lililokuwa Afrika Magharibi hasa nchini Nigeria, akamwambia kwamba alikuwa na kazi ambayo ilitakiwa kufanyika haraka sana, kulikuwa na mtu ambaye alitakiwa kuuawa.
Hilo hakukuwa na tatizo kwa Boko Haram, kwa kuwa kundi hilo lilihitaji sana pesa kwa ajili ya kujiendeleza, kazi ambayo waliambiwa kwamba waifanye haikuwa na tatizo lolote lile, wakapanga tarehe, akawatumia picha na kuwapa ratiba kamili ambayo Kimwinyi alikuwa akiondoka Tanzania na kufika nchini Nigeria.
Rais Bokasa akampigia simu Kimwinyi na kumpa taarifa kwamba alitakiwa kuelekea nchini humo kwa ajili ya kuzungumza na baadhi ya viongozi wa huko kuhusu kuidhibiti akaunti mtandaoni ambayo ilikuwa ikisumbua, alimwambia kwamba hakukuwa na mtu aliyekuwa akimwamini katika serikali yake zaidi ya huyo Kimwinyi maneno ambayo yalimfurahisha pasipo kujua kulikuwa na mpango kabambe wa kummaliza hata kabla hajafika hotelini.
“Nashukuru sana kwa kuniamini!” alisema Kimwinyi.
“Haina shida. Wewe nenda Nigeria kisiri na kila kitu tutazungumza ukifika huko,” alisema rais.
“Sawa.”
Wakati wakizungumza hayo mchana siku ya Ijumaa, kwa nchini Japan tayari ilikuwa ni asubuhi ya Siku ya Jumamosi asubuhi. Godwin alikuwa darasani akijisomea, mara akaona kompyuta yake ikimwambia kwamba kulikuwa na mawasiliano yalikuwa yakifanyika kutoka katika namba ya Rais Bokasa aliyokuwa ameidukua.
Haraka sana akachukua ‘hearphone’ zake, akazichomeka na kuanza kusikiliza mawasiliano yao. Simu ilikuwa imetoka kwa rais huyo na kwenda kwa Mkurugenzi wa Usalama wa taifa, Kimwinyi, aliyasikiliza mazungumzo yote na kitu kilichomjia kwa haraka mno kichwani mwake kilikuwa ni mauaji tu.
Alijua kwamba rais huyo alikuwa akijitahidi kufanya kila kitu kuona akaunti ya Mabadiliko ya Kweli inafutika, na kwa sababu alikuwa amemtuma Kimwinyi kumuua Mzee Filipo, basi alitaka kuificha siri hiyo hivyo kumuua Kimwinyi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Saa moja baada ya kuyasikia mazungumzo hayo, Godwin akaingia kwenye akaunti yake na kuweka picha ya Tanzania kisha kuandika R.I.P na chini kuweka maneno machache yaliyosomeka ‘Kuna mtu anakwenda kufa, hatokufa Tanzania, atakufa mbali kabisa ila ni mchezo ambao umechezwa na mtu fulani. Unataka kujua ni nani? Endelea kusubiri tu!’.
Alipomaliza, akaiposti. Kila mtu aliyeiona posti hiyo alishtuka, walimwamini mtu aliyekuwa akiitumia akaunti hiyo, waliamini kwamba kulikuwa na mtu alikuwa akienda kufa na watu wengi wakauliza alikuwa nani lakini hakukuwa na aliyekuwa na majibu ya maswali yao.
Kimwinyi hakuwa akijua lolote lile, alipoambiwa hivyo, ndani ya saa moja akapanda ndege na kuanza kuondoka nchini Tanzania huku akiambiwa kwamba hapo uwanja wa ndege angepokelewa na mkurugenzi wa Usalama wa Taifa wa huko, The National Intelligence Agency (NIA), Bwana Andrew Okafor.
Njia nzima alikuwa na mawazo tele, kama alivyokuwa amechanganyikiwa rais naye alichanganyikiwa hivyohivyo. Muda mwingi alikuwa akiongea peke yake, kichwa chake hakikuwa sawa hata kidogo.
Safari hiyo ilichukua saa kadhaa ndipo ndege ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Murtala Muhammed uliokuwa jijini Lagos. Haraka sana baada ya ndege kusimama, abiria wakaanza kuteremka akiwemo yeye mwenyewe.
Mzigo wake ulipochunguzwa na kuuchukua akaanza kutoka ndani ya jengo hilo ambapo nje akakutana na mwanaume mmoja ambaye alikuwa akimwangalia sana, kwa muonekano wake tu ulionyesha ni ofisa wa usalama wa taifa kitu kilichomfanya kumsogelea.
“My name is Jonas Ogwadugu! I was told to come and pick you up,” (naitwa Jonas Ogwadugu! Niliambiwa nije kukuchukua) alisema mwanaume huyo huku akiwa na tabasamu pana.
“Ooh! Thank you! My name is Kimwinyi! How do you find me?” (Ooh! Asante! Naitwa Kimwinyi! Umenipataje?) aliuliza huku naye akitoa tabasamu.
“I got your picture,” (nina picha yako)
Akamchukua na kuelekea naye katika gari moja la kifahari. Kwa jinsi mapokezi yalivyokuwa, muonekano wa gari ulionyesha kabisa mtu huyo alikuwa ni kutoka katika usalama wa taifa wa Nigeria. Gari likawashwa na dereva wa gari hilo na kuondoka mahali hapo.
Njiani walikuwa wakizungumza mambo mengi, Jonas alionekana kuwa mchangamfu kupita kawaida. Kila wakati uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana na alipokuwa akiongea alionekana kama mtu aliyekuwa na akili kubwa mno.
Alimwambia Kimwinyi jinsi walivyokuwa wakifanya kazi, walikuwa na kikosi hatari sana ambacho kilipambana juu chini kuhakikisha nchi inalindwa kwa ngumu kubwa kuliko kitu chochote kile.
Hakumficha, alimwambia jinsi walivyoguswa kwa kuambiwa kwamba kulikuwa na akaunti ambayo ilikuwa ikiwasumbua. Wao, Nigeria walipita huko zamani, kulikuwa na wataalamu wa kompyuta mitaani, wote baadaye wakaajiliwa serikalini, hakukuwa na mtu aliyekuwa na uwezo mkubwa ambaye alikuwa nje ya serikali ila pamoja na hayo, wangemwambia ni jinsi gani wataweza kuizuia akaunti hiyo.
“Nitafurahi sana! Hakika imetusumbua sana,” alisema Kimwinyi huku akijisikia amani kabisa kana kwamba alipokelewa kupelekwa harusini.
Safari iliendelea, kile alichokitarajia kwamba hotelini alipotakiwa kwenda palikuwa karibuni kilikuwa tofauti na mategemeo yake, gari liliendeshwa kwa mwendo wa kawaida, wakaanza kutoka katika Jiji la Lagos na kuanza kwenda katika Jiji la Ibadan.
Alishangaa, alitamani kuuliza lakini akahisi kama kuingilia jukumu la watu hao hivyo kukaa kimya. Gari lilikwenda mpaka likaacha barabara ya lami na kuanza kuingia kwenye barabara ya vumbi, walikwenda kwa dakika zaidi ya ishirini, gari likasimama nje ya jumba moja kuukuu na kuambiwa kuteremka.
“Tumefika?” aliuliza lakini Okafor hakujibu chochote kile, akateremka kutoka garini.
Hata kabla Kimwinyi hajajua nini kilikuwa kikiendelea mahali hapo, wanaume sita waliokuwa na bunduki aina ya AK47 wakatokea mahali hapo, alishtuka, hakujua kitu chochote kile, akaamliwa kuteremka kutoka garini huku mikono yake ikiwa kichwani, akafanya hivyo huku akitetemeka mno.
“Nimefanya nini jamani?” aliuliza huku akitetemeka.
“Utamuuliza rais wako!”
“Rais wangu? Bokasa ndiye aliyewat...” aliuliza lakini hata kabla hajamalizia swali lake, akapigwa na kitako cha bunduki, akapoteza fahamu, wakamchukua na kuondoka naye.
****
Godwin alikuwa akiandaa ripoti yake ndefu, alitaka kuwaambia Watanzania kila kitu kilichokuwa kikiendelea, tangu mwanzo wa kikao chao mpaka hapo walipofikia, hakutaka kuficha kitu chochote kile, katika ripoti ile aliweka bayana hata ile mipango ambayo ilitakiwa kufanywa baada ya Kimwinyi kuuawa.
Ilikuwa ripoti ndefu na yenye kusisimua sana, aliamini kila Mtanzania ambaye angekwenda kuisoma ilikuwa ni lazima kumchukua rais huyo ambaye alijitahidi kuwaangamiza watu ili mambo yake machafu yasiendelee kutolewa.
Alimini kwamba kwa watu milioni ishirini ambao waliifolo akaunti yake wangeweza kubadilisha kila kitu, aliamini kwamba wengi waliokuwa wamemfolo walikuwa watu wake, waliunga kile alichokuwa akikifanya.
“Ila kweli rais ana mpango wa kumuua Kimwinyi au? Nisije kuonekana muongo!” alijiuliza Godwin, kila wakati macho yake yalikuwa kwenye mitandao mbalimbali nchini Nigeria kuona kama kweli Kimwinyi alikuwa ameuawa kama alivyohisi au la.
Saa ziliendelea kukatika, bado macho na masikio yake yalikuwa yakisikilizia kile kilichokuwa kikiendelea nchini Nigeria. Ilipofika majira ya saa kumi jioni siku ya Jumapili, taarifa aliyokuwa akiisubiri kwa hamu kubwa ikatangazwa.
Mtanzania mmoja alikutwa akiwa ameuawa na mwili wake kutupwa msituni. Japokuwa ilionekana kuwa habari mbaya lakini kwa Godwin ilimfanya kutabasamu sana. Hapohapo akaichukua na kuiweka katika mtandao wake na kuwakumbusha watu kwamba jana yake usiku kwa majira ya Afrika aliandika kwamba kungekuwa na mauaji ambayo yangekwenda kutokea nje ya Tanzania na hatimaye yalikuwa yametokea.
Kila mtu alishangaa, hawakujua ni kwa namna gani mtu huyo aliweza kupata mambo yote hayo. Ni kweli mkurugenzi wa usalama wa taifa alikuwa ameuawa nchini Nigeria ambapo taarifa zilisema kwamba alitekwa na Boko Haram kimakosa kwa kufikiri kwamba alikuwa Mganda, Oseah Mambo waliyekuwa wakimtafuta kwa kipindi kirefu.
“Huu ni mpango na si kwamba walimchanganya! Walijua kwamba walikuwa wakienda kumuua mkurugenzi wa usalama wa taifa, hivyo mnaposikia kwamba walimteka na kumuua kimakosa ni uongo, nitakuwekeeni ripoti kamili ya mambo yote haya” aliandika Godwin katika akaunti yake.
Watanzania wengi wakahisi kama akaunti hiyo ilikuwa ikiendeshwa na malaika kwani mtu huyo alikuwa alikuwa akijua mambo mengi sana, hata kama kulikuwa na mpango mliokuwa mkiufanya chumbani, kesho yake alikuwa akijua kila kitu.
Wengi wakamsifu lakini pia wakatamani kuiona ripoti hiyo ambayo ingezungumzia mambo mengi mno. Mitaani, kila mtu alikuwa akizungumza lake lakini wengi wakabaki na ukweli kwamba Kimwinyi aliyeuawa na Boko Haram ulikuwa ni mpango na si kutekwa kimakosa.
“Nitarudi Tanzania wiki hiihii ndani ya siku tatu! Nikija, nitahakikisha nawapeni mambo mengi zaidi,” aliandika Godwin ambapo watu wengi wakakomenti kwa kumkaribisha kwani hawakuona kama kungekuwa na mtu mwingine wa kuikomboa Tanzania zaidi yake.
“Karibu sana mkombozi wetu,” alikomenti jamaa mmoja. Godwin akajiandaa kurudi nchini Tanzania.
***
Mara baada ya taarifa za kifo cha Kimwinyi kusambazwa katika mitandao mbalimbali, Rais Bokasa akapigiwa simu na rais wa Nigeria na kuambiwa kilichokuwa kimetokea. kwanza akajifanya kushtuka kwa kutokuamini kile kilichokuwa kimetokea. Aliulizwa kama alimruhusu mtu huyo kuelekea nchini Nigeria lakini akakataa katakataka.
Alitaka kujisafisha, alijua fika kwamba kungekuwa na taarifa nyingi ambazo zingeandikwa kuhusu mauaji hayo, alitaka kuyazima mapema hata kabla mitandao ya kijamii haijaweka wazi hisia zao kwa kuhisi kwamba mtu huyo alikuwa ameuawa kimakusudi.
Hakutaka kuchelewa, hapohapo akachukua simu yake na kumpigia mkurugenzi wa televisheni ya taifa ambaye alimwambia kwamba alihitaji waandishi wa habari kwani kulikuwa na mambo aliyotaka kuzungumza.
Hilo halikuwa tatizo, baada ya dakika kadhaa, waandishi hao wakawa ikulu ambapo wakaanza kurusha matangazo moja kwa moja. Hakutaka kujificha, aliwaambia watu hao namna Kimwinyi alivyoondoka, alijifanya kuwasiliana na mawaziri wengine kutaka kujua sababu ya Kimwinyi kuelekea nchini Nigeria lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa na majibu.
“Nilishangaa kupigiwa simu na rais wa Nigeria na kuambiwa kuwa Kimwinyi alitekwa. Alikwenda Nigeria kufanya nini? Nani alimruhusu? Haya ni maswali ambayo nimekosa maj...” alisema lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake, akaanza kulia.
Huo ndiyo ulikuwa ujanja wa kwanza kabisa alioufanya. Hakutaka kugundulika, alihisi kitendo cha kutoa machozi mbele ya waandishi wa habari kingemfanya kila mtu kuamini kile alichokisema, hilo ndilo lilivyokuwa kwani baadhi ya wananchi waliokuwa wakimwangalia katika televisheni hiyo waliamini kwamba hakuwa amefanya jambo hilo.
“Mpaka rais analia! Ameguswa sana jamani halafu kuna mpuuzi mmoja kwenye mtandao kajiunga na kibando chake cha wiki anamchafua rais wetu kwamba kahusika na mauaji hayo. Hivi kweli aliyehusika anaweza kulia?” alihoji jamaa mmoja aliyekuwa akiuza duka.
“Kwani kulia tatizo bwana?” aliuliza jamaa mwingine.
“Unadhani chozi la mwanaume linatoka hivihivi!”
“Mbona wengi wanalia bwana! Tena si kulia, wengine wamefiwa na bado wanacheka msibani,” alisema jamaa mwingine.
Ili kuonyesha kwamba alikuwa ameguswa na msiba huo, Rais Bokasa alikuwa bega kwa bega na familia ya Kimwinyi, alikuwa akijitolea kwa kila hali ili isionekane kama yeye ndiye aliyehusika katika mauaji hayo.
Kulikuwa na misiba mingi iliyokuwa imetokea lakini kwa msiba huo, rais huyo alijitoa kwa nguvu zote kiasi kwamba akaanza kuwalaghai Watanzania kwamba hakuwa amehusika katika mauaji hayo. Wakati akiwa msibani, akasikia simu yake ikiita, haraka sana akaichukua kutoka mfukoni na kuipeleka sikioni.
“Kuna nini?” aliuliza.
“Kumbe yule mtu wa ile akaunti hayupo Tanzania! Nimeona posti yake, amesema kwamba atakuja Tanzania ndani ya siku mbili tatu,” alisema mwanaume huyo.
“Hakikisheni mnaweka usalama wa kutosha katika uwanja wa ndege na mipakani, hakikisheni mnampata huyu mtu,” alisema Rais.
“Sawa.”
Akakata simu. Kichwa chake kilichanganyikiwa zaidi, alitamani kuondoka msibani hapo, hakukuwa na kitu alichokitaka kama kumfahamu mtu aliyekuwa nyuma ya akaunti ile iliyokuwa ikimuumiza kichwa chake. Hakutaka kukaa sana msibani, akaondoka na kuelekea ikulu.
Njiani, alikuwa na mawazo tele, aliongea peke yake, hakuonekana kuwa na raha hata mara moja na mpaka anafika ikulu alihisi kabisa kichwa chake kuwa kziito mno, hivyo akajilaza.
Aliamka majira ya saa tatu usiku, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuchukua simu yake na kumpigia mwanaume aliyempigia kabla na kumpa taarifa kwamba mtu aliyekuwa akitumia akaunti ile angefika nchini Tanzania ndani ya siku mbili tatu, alitaka kujua waliishia wap, alitaka kufahamu kila kitu.
“Mmefikia wapi?”
“Ulinzi umewekwa kila kona mkuu! Kila Mtanzania anayefika ni lazima kuchunguzwa sana!” alijibu mwanaume wa upande wa pili.
“Basi sawa. Ngoja niwaambie kitu kimoja. Mkiwakagua hakikisheni mnawaambia waingie kwenye akaunti zao za Instagram, wasijitoe, hakikisheni mnaangalia akaunti inayotumika ni ipi. Sawa?” alisema na kuuliza.
“Sawa mkuu!”
Hicho ndicho walichokifanya. Polisi na wanausalama wa taifa wakaambiwa kile kilichotakiwa kufanywa. Kila mtu aliyekuwa akiingia nchini Tanzania kupitia mipakani au uwanja wa ndege ilikuwa ni lazima kuchunguzwa yeye kama yeye na pia kuambiwa kufungua akaunti yake ya Instagram kwa ajili ya kuangalia kama wangekuwa watumiaji wa akaunti ya Mabadiliko ya Kweli.
Ilikuwa kazi kubwa lakini ilikuwa ni lazima kufanyika. Kila mtu alikuwa akishangaa, hawakujua sababu ya polisi na wanausalama kufanya kitu kama hicho.
Wakati hali hiyo ikiendelea, Godwin hakuwa akijua lolote lile. Alipanga kurudi nchini Tanzania kwani alisoma na kupata PhD yake katika masuala ya kompyuta. Hakutaka kubaki nchini Japana, akashukuru kwa Mzee Takesh na kurudi nchini Tanzania.
Njiani alikuwa akifikiria kile alichotakiwa kufanya, hakukubali kuona Tanzania ikiendeshwa na rais mmoja kwa miaka mingi, alitaka kubadilisha kila kitu, kama Bokasa aliiongoza Tanzania kwa miaka mingi kwa kuwa tu alibadilisha baadhi ya vipengele kwenye katiba, sasa ulikuwa muda wake kung’oka.
“Habari yako!” alisikia sauti ya msichana mmoja ikimsalimia.
“Salama! Za kwako!”
“Njema tu! Na wewe umetoka Dubai?” aliuliza msichana huyo kwa sauti nyembamba, alionekana kuwa mchangamfu mno.
“Hapana! Nimetoka Uholanzi!”
“Ulikuwa masomoni?”
“Yeah! Jiji Amsterdam!”
“Ooh! Naitwa Manka Msuya!” alisema msichana huo huku akimpa mkono.
“Naitwa Godwin Jr!”
Japokuwa ilikuwa ni mara ya kwanza kukutana lakini kila mmoja alionekana kuwa mchangamfu sana. Walikuwa katika kiti kimoja huku ndege ikiendelea kukata mawingu kuelekea nchini Tanzania. Walizungumza mengi, msichana huyo alionekana kuwa mkweli kwa kila kitu alichokuwa akikizungumza lakini kwa Godwin, hakukuwa hata na kitu kimoja cha kweli alichomwambia Manka.
Baada ya saa kadhaa, ndege ikatua katika Uwanja wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi nchini Kenya. Hawakuteremka, walibaki ndani ya ndege ambapo baada ya muda fulani ikapaa tena na kuelekea nchini Tanzania.
Wote walichoka lakini hakukuwa na mtu aliyekuwa ladhi kulala kwani kwa jinsi stori zilivyonoga, hakukuwa na yeyote aliyekuwa tayari kumuacha mwenzake na yeye kulala.
Baada ya saa chache wakaingia jijini Dar es Salaam ambapo ndege ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Huku wakiwa pamoja kama mke na mume, wakateremka na kuelekea nje ya ndege ambapo wao na abiria wengine wakaunganisha mpaka katika jengo la uwanja huo.
“Mnatakiwa muende kule,” alisema dada mmoja huku akiwaangalia wawili hao.
“Kufanya nini?”
“Ni maagizo ambayo tumeachiwa! Hatujui kufanya nini!” alijibu dada huyo.
“Ni sisi tu?”
“Hapana! Hata wengine pia!”
“Sasa mbona Wazungu wanasepa zao?”
“Ni kwa ajili ya Watanzania tu,” alijibu msichana.
Si Godwin wala Manka aliyejua kilichokuwa kikiendelea kule, walishangaa lakini hawakuwa na jinsi kwani wenzao ambao walikwenda upande ule hawakuwa wakilalamika kwa lolote lile.
Kule, kulikuwa na watu wa usalama wa taifa waliovalia suti zao, walikuwa na wajibu wa kumchukua mtu yeyote na kumpeleka katika vyumba ambavyo walivitenga kwa ajili ya kufanyia kazi yao.
“Kuna nini?” aliuliza Manka.
“Hata mimi sijui! Hebu twende tukawasikilizie. “
“Ila naogopa mwenzio!”
“Hahaha! Kwani umeua Manka! Twende tukawasikilize,” alisema Godwin.
Walipowafikia usalama wa taifa, wakawachukua na kuwaambia kuingia ndani ya chumba kimoja. Godwin akaambiwa asubiri, Manka akachukuliwa na kuingizwa humo. Alikuwa akitetemeka, hakuwa amefanya kosa lolote lile lakini alijiona kama mhalifu.
Alipoingia, akaanza kuhojiwa baadhi ya maswali na kuambiwa kutoa simu yake. Hakubisha, akaitoa na kuambiwa aingie katika akaunti zake za Facebook na Instagram, hilo halikuwa tatizo, akafanya kama alivyoambiwa.
Ofisa mmoja wa usalama wa taifa akachukua simu ile na kuanza kuangalia alichotaka kuangalia. Alichukua dakika tano, alipomaliza, akamrudishia na kumtaka mtu mwingine aingie.
Godwin akaingia, akaambiwa akae kwenye kiti, akakaa na kuanza kuangalia na wanaume hao walioonekana kuwa makini kwa kila kilichokuwa kikitokea ndani ya chumba hicho.
Wakamuuliza maswali kadhaa, Godwin hakuonekana kutetemeka, alijibu kwa usahihi kila swali aliloulizwa, baada ya kila kitu akaambiwa atoe simu yake na kuwakabidhi.
“Ya kazi gani?” aliuliza Godwin.
“Kuna kitu tunataka kuangalia!”
“Kitu gani?”
“Wewe tupe simu yako,” alisema ofisa usalama.
“Hapana! Siwezi kuwapa kirahisi namna hiyo!” alisema Godwin huku akiachia tabasamu kana kwamba kile alichokuwa akikizungumza kilikuwa na utani.
Huo ndiyo ulikuwa msimamo wake, alikataa katakata kuwapa simu yake. Kila mmoja aliyekuwa ndani ya chumba kile akahisi kwamba inawezekana Godwin alikuwa mtu waliyekuwa wakimtafuta.
Walimlazimisha, walipoona amekataa, wakaichukua kinguvu. Wala hakubisha. Walipoichukua, kazi kubwa ilikuwa ni kuifungua simu hiyo. Ilikuwa imefungwa, hakukuwa na mtu aliyejua namba za siri zaidi yake.
“Tupe namba zako za siri!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nitawapa vipi na wakati mmeichukua kinguvu! Itumieni basi,” alisema Godwin, hapohapo akakunja nne, kuonyesha kwamba hakuwa na hofu yoyote ile.
Wakaanza kumpa vitisho ndani ya chumba kile ili aogope. Alihisi kabisa kulikuwa na kitu wanausalama hao walitaka kuangalia na kama akili yake ilikuwa imemwambia kwani akaunti ya Mabadiliko ya Kweli iliyokuwa Instagram haikuwa imetolewa hivyo kama watu wale wangeingia katika mtandao huo, wangekutana na akaunti hiyo.
“Toa namba za siri!” alisema mwanaume mmoja.
“Kutoa siwezi! Kama mna uwezo, futeni kila kitu,” alisema Godwin huku akionekana kumaanisha, mwanausalama yule aliyekuwa akimuhoji na mwenzake wakajiangalia viunoni mwao kuona kama kulikuwa na bastola, zilikuwepo, na pingu nazo, zilikuwepo.
“Tunakupa nafasi ya mwisho! Fungua simu yako!”
“Simu ni yangu, nilinunua kwa pesa yangu, hamkunichangia kwa chochote, iweje niwafungulie? Kufungua siwezi! Mkikasirika, vimbeni mpasuke,” alisema Godwin maneno yaliyowafanya maofisa wale kuvimba kwa hasira.
Wanausalama waliokuwa ndani ya chumba kile walionekana kukasirika mno, walimwangalia Godwin, kwa jinsi alivyokuwa akizungumza nao alionekana kabisa kwamba alikuwa kiburi na kamwe asingeweza kuifungua simu ile na kuwaacha kufanya kile walichotaka kufanya.
Walikasirika, walijiona kuwa na uwezo wa kufanya kitu chochote kile walichotaka kukifanya lakini wakaonekana kuogopa. Mpaka mtu kuwajibu jeuri ilionyesha kabisa kwamba inawezekana alikuwa mtoto wa kiongozi mkubwa au alikuwa mwanasheria ambaye angeweza kuwashtaki na kutaka malipo makubwa.
Wakaangaliana, wakachukuana na kuelekea nje huku wakiwa na simu ile. Huko wakajadili kwa dakika kadhaa, walichokubaliana ni kwamba waendelee kuweka msimamo wao mpaka awakubalie kuifungua simu ile kwani tayari walikuwa na wasiwasi na kijana huyo.
Wakarudi ndani ya chumba kile, kwa jinsi walivyomuacha ndivyo alivyokuwa japokuwa tabasamu lile liliongezeka usoni mwake kuwaonyesha kwamba hawakuwa na ubavu wa kumlazimisha kufungua simu yake na hata kama wangetaka kumpiga, ilikuwa ni lazima kuwafungulia mashtaka.
“Jiandae twende polisi,” alisema mwanausalama mmoja.
“Kwa kosa gani?”
“Kukataa kutufungulia simu yako!”
“Kwani hilo kosa? Mnataka kuingilia uhuru wangu! Mimi ndiye natakiwa kuwashtaki, tena ikibidi mnilipe na pesa si chini ya milioni mia tatu kwa kosa la kunipotezea muda kiboya,” alisema Godwin maneno ambayo yaliwatisha wanausalama wale lakini wakajifanya kutokujali, hawakutaka Godwin ajue kama walianza kuogopa.
Wakaendelea na msimamo wao wa kutaka kufunguliwa simu ile lakini wakati wakiendelea kukaza, wakasikia mlango unafunguliwa na mwanaume mmoja kuingia, alikuwa mwenzao.
“Tumempata!” alisema mwanaume huyo.
“Amepatikana! Ahsante Mungu!” alisema mwanausalama na hivyo kumrudishia Godwin simu yake.
Wakamruhusu kuondoka huku wakimuomba msamaha kwa usumbufu uliojitokeza mahali hapo. Akaondoka huku nao wakielekea kule walipoambiwa kwamba mtu huyo alikuwepo.
Wanausalama wakaelekea huko, wakaingia ndani ya chumba kimoja, macho yao yakatua kwa kijana mmoja aliyekuwa chumbani humo ambaye muda wote alikuwa akilia tu. Alizungukwa, kila mmoja alitaka kujua kile kilichokuwa kikiendelea.
Walimlazimisha kufungua akaunti yake ya Instagram, alipoifungua wakaona akiwa na akaunti mbili, moja ilikuwa yake lakini nyingine ilikuwa ni ya Mabadiliko ya Kweli. Wakaamini kwamba kijana huyo ndiye alikuwa mmiliki wa akaunti hiyo, wakachukua hati yake ya kusafiria ambayo ilisomeka kwamba alitokea nchini Australia.
“Wewe ndiye mmiliki wa akaunti ya Mabadiliko ya Kweli?” aliuliza mwanausalama mmoja.
“Hiyo si akaunti ambayo nyie mnasema namiliki. Hiyo ina wafuasi elfu kumi na tatu, hiyo mnayoitaka ina wafuasi milioni ishirini na mbili. Si akaunti hiyo, niliweka ili nipate wafuasi wengi tu mkuu,” alijibu kijana huyo huku akitetemeka.
Hawakutaka kumuelewa, kila mmoja alijua fika kwamba kijana aliyekuwa akihitajika ndiye alikuwa huyo aliyekuwa ndani ya chumba kile. Walibaki humo huku wakimuhoji maswali mengi, kwa jinsi alivyokuwa akiongea na kujibu maswali yake ilionyesha kabisa hakuwa yeye bali alikuwa mtu mwingine.
Walikaa naye kwa nusu saa nzima, wakapigiwa simu na mkuu wao na kuambiwa kwamba kulikuwa na ujumbe mzito wao katika akaunti ile hivyo waingie na kuangalia. Wakaingia, walipoifungua akaunti ile, wakakutana na picha ya chumba kile walichomuweka Godwin huku chini kukiwa na maneno yaliyosomeka ‘Nimeingia Tanzania salama kabisa. Waliniita ndani ya chumba chao kwa ajili ya kupekua simu yangu. Nilikataa kutoa namba za siri, nikawaogopesha kuwashtaki. Wameniachia, niwaambie tu kwamba nipo salama, kazi inaanza upya.’ Ilisema posti ile.
“Ni yule kijana!” alisema usalama mmoja.
Hawakutaka kubaki ndani ya chumba kile, haraka sana wakatoka na kuelekea katika chumba walichokuwa wakimuhojia Godwin, walipofika huko, hakuwepo, aliondoka huku hata ile simu yake aliyokuwa nayo ikiwa haipo ndani ya chumba kile.
Wakachanganyikiwa. Haraka sana wakatoka na kuelekea nje ya jengo la uwanja ule, wakaanza kuangalia huku na kule, Godwin hakuonekana. Hilo liliwaumiza sana, hawakuamini kama walishindwa kumgundua mtuhumiwa ambaye walikuwa naye.
Walichokifanya ni kwenda katika chumba cha kuhifadhi picha zilizokuwa zikipigwa katika uwanja ule na kuhitaji kuangalia picha za Godwin wakati alipokuwa ameingia. Hilo halikuwa tatizo, kijana wa uwanjani hapo akafungua kompyuta na kuanza kuzitafuta picha hizo.
Halikuwa tatizo sana na hakutumia muda mrefu kuzipata kwani zilipigwa saa moja lililopita. Wakaanza kuziangalia, walijiona jinsi walivyokuwa wakielekea ndani ya chumba kile. Ilionekana kama Godwin alijua kwamba mahali pale kulikuwa na kamera kwani kila alipokuwa akipigwa picha, alificha uso wake mpaka walipoingia ndani ya chumba kile.
“Alijua kwamba kamera zilikuwa zikimchukua,” alisema jamaa mmoja.
Walikuwa na uhakika kwamba yule waliyekuwa wamemuhoji mpaka kukataa kufungua simu yake ndiye alikuwa mtu waliyekuwa wakimuhitaji sana. Walichokifanya ni kwenda katika orodha ya majina ya abiria walioingia kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Fly Emirate ambapo walipopewa majina, wakaambiwa kwamba mtu huyo alikuwa akiitwa Godwin Melkizedek Mapoto.
Kumfahamu alikuwa nani tu iliwapa uhakika kwamba kumpata halikuwa jambo gumu tena. Jina lake halikuwa gumu, walichokifanya ni kuanza kufuatilia ili hata kama watakwenda kumpa taarifa Rais Bokasa basi wajue ni mtu gani alikuwa akisababisha yote hayo.
Walimfahamu baba yake, walihisi kwamba alikuwa mtoto wake hivyo kuanza kufuatilia kwa makini. Ni kweli, alikuwa ndiye yule yule, mtoto wa mwanasiasa mkubwa nchini Tanzania, Bwana Melkizedeki Mapoto ambaye alikufa katika ajali ya gari nchini Marekani alipokwenda kulitumikia taifa kama balozi nchini humo.
“Hebu endeleeni kufuatilia mniambie zaidi, baada ya hapo nini kiliendelea,” alisema mkurugenzi wa usalama wa taifa ambaye alichaguliwa kwa haraka sana, aliitwa Maliki Idrisa.
“Baada ya hapo, familia yake iliendelea kuishi Tanzania, mkewe alipokonywa nyumba katika mazingira ya kutatanisha. Baadaye akafa kwa kugongwa kwa gari, wakabaki wawili, baadaye dada wa huyu aliyeitwa Irene akafariki dunia,” alisema jamaa aliyepewa kazi hiyo.
“Mmh! Nahisi kuna kitu! Hebu naombeni hiyo ripoti nikampe rais,” alisema Maliki na hivyo kuichukua ripoti hiyo.
Hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, ilikuwa ni lazima kumpelekea Rais Bokasa ili ajue kile kilichokuwa kikiendelea. Akampigia simu binafsi na kuomba kuonana naye kwani tayari kwa asilimia kadhaa alifanikiwa kupatikana kwa jina la mtu aliyekuwa akimtafuta usiku na mchana.
Hilo halikuwa tatizo, Rais Bokasa akamwambia kwamba aelekee ikulu ambapo huko akaonana naye na kumpa ripoti ile huku akimwambia kwamba mtoto wa marehemu Mapoto ndiye aliyekuwa akihusika katika kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
“Haiwezekani!” alisema Rais Bokasa huku akihamaki.
“Kwa nini?”
“Kijana huyo alikufa miaka mingi iliyopita. Alikufa baharini!” alisema rais huku akisimama na ripoti yake mkononi.
Alikumbuka kila kitu, yeye ndiye aliyekuwa akiimaliza familia hiyo kwa kuamini kwamba ingetokea siku ambayo wangejua kwamba baba yao, Mzee Mapoto aliuawa hivyo kuifanya nafasi yake ikulu kuwa ngumu.
Alijilinda kwa nguvu zote, alijitahidi kuiangamiza familia hiyo kwa kusudi la kulinda cheo chake ikulu na alikumbuka kabisa kwamba mara ya mwisho mtu aliyetakiwa kuuawa alikuwa Godwin ambaye aliagiza kutupwa baharini akiwa ndani ya boksi, sasa ilikuwaje mpaka mtu huyo awe hai?
“Huyu mtu alikufa! Nakumbuka kwamba niliyemtuma kumuangamiza alikuwa Kihampa! Hakuifanya kazi au?” alijiuliza huku akiiangalia ripoti ile.
Alihitaji kujua ukweli juu ya kilichokuwa kimeendelea, Kihampa alikuwa akijua ukweli kwani yeye ndiye aliyemtuma kwenda kumteka Godwin na kumuua, alikumbuka vilivyo kwamba hata siku hiyo kijana huyo alimpa taarifa kwamba alifanikisha suala hilo.
“Ninamtaka Emmanuel Kihampa!” alisema Rais Bokasa huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Yule mchungaji?”
“Ndiyo! Ninataka mniletee hapa,” alisema rais huyo.
Hayo yalikuwa maagizo ambayo yalitakiwa kufanyika haraka sana. Kihampa alibadilika, tangu siku ya mwisho alipotakiwa kumuua Godwin aliamua kuyabadilisha maisha yake na ndiyo maana hata ndani ya boksi aliweka maboya ili asizame na aweze kuokoka kutoka katika mikono ya rais huyo.
Hilo halikuwa tatizo, haraka sana vijana wakaondoka mpaka nyumbani alipokuwa akiishi, wakamchukua na kumpeleka ikulu. Siku hiyo Bokasa alionekana tofauti, alikuwa na hasira sana, alipomuona Mchungaji Kihampa, kitu pekee alichotaka kujua, je, ni kweli alimuua Godwin siku ile au hakumuua?
“Nilimtupa baharini nikiwa nimemuwekea maboya,” alisema mchungaji huyo.
“Kwa nini ulifanya hivyo?”
“Kwa sababu Yesu Kristo aliyabadilisha maisha yangu! Sikutaka kuua tena,” alijibu Kihampa huku akionekana kutokuogopa hata kidogo.
Rais Bokasa akaingiwa na hasira mno, majibu yale kwake yalionekana kama dharau kubwa. Alimwangalia mchungaji huyo, alikuwa Kihampa yuleyule wa zamani lakini maisha yake yalikuwa yamebadilishwa. Hakujua ni kitu gani alitakiwa kumfanya, kama ni kumuua au kumuachia aondoke zake.
Wakati akijifikiria hayo ni kitu gani alitakiwa kufanya, akasikia mlio wa meseji ukiwa umelia kwenye simu yake. Haraka sana akaichukua na kuanza kuangalia, alitaka kujua ni nani aliyekuwa amemtumia meseji hiyo. Alipoifungua tu akakutana na ujumbe huo uliotoka katika Hospitali ya St. Lucas nchini Marekani uliosomeka
‘Thank you for helping epileptic kids and funding them with 100 million dollars. May the Almighty bless you!’ (asante kwa kuwasaidia watoto wanaougua kifafa kwa kutoa kiasi cha dola milioni mia moja. Mungu akubariki)
“Mungu wangu! Kuna mtu kahamisha pesa zangu zote katika akaunti yangu nchini Uswisi!” alisema Rais Bokasa huku akionekana kuchanganyikiwa. Akahisi presha ikianza kupanda, akakishika kifua chake, akaanguka chini kama mzigo.
***
Godwin hakutaka kuendelea kubaki ndani ya chumba hicho, akaondoka na kuungana na msichana Manka ambapo wakaanza kuelekea nje ya jengo la uwanja huo. Msichana yule alibaki na mawazo mengi, alikuwa akimuuliza maswali ambayo hakupata majibu papo hapo.
Hakujua sababu ya wanaume wale kuchukua muda mrefu kuzungumza na Godwin ndani ya chumba kile zaidi ya watu wengine. Alipomuuliza Godwin, hakumpa jibu zuri zaidi ya kumwambia kwamba walitakiwa kuondoka mahali hapo
Wakaifuata taksi moja na kuingia. Haraka sana dereva aliyekuwa nje ya gari hilo naye akaingia, akawaangalia watu wake, Godwin hakuonekana kuwa katika hali ya kawaida, alionekana kama mtu fulani aliyekuwa na mambo mengi kichwani.
“Niwapeleke wapi?” aliuliza mwanaume huyo.
“Chuichui Hotel,” alisema Godwin, dereva akawasha gari na kuanza kuondoka mahali hapo.
Njia nzima hakukuwa na mtu aliyezungumza lolote, Godwin alikuwa bize na simu yake, huo ndiyo ulikuwa wakati wa kuwaambia wafuasi wake kila kitu kilichokuwa kimetokea uwanja wa ndege ndani ya kile chumba.
Watu wengi walimsifu kwa ujasiri wake, hakuonekana kuogopa, si kama Watanzania wengine ambao mioyo yao ilijawa na hofu kubwa hata pale walipokuwa wakifanyia kitu ambacho sheria haikuruhusu kufanyiwa.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika Hoteli hiyo, haraka sana Godwin akateremka na kuanza kuelekea ndani ya hoteli huku akionekana kumsahau Manka na hata kumlipa dereva.
“Bro...broo..!” dereva akaita huku akiteremka na kumfuata, akamwambia amlipe, hilo halikuwa tatizo, akamuomba msamaha kwa kujisahau kisha kumlipa kiasi cha pesa alichokuwa akikihitaji.
“Naondoka!” alisema Manka huku akimwangalia Godwin.
“Haina shida! Safari njema!” alisema Godwin huku akianza kupiga hatua kuondoka.
“Hukunipa namba ya simu!”
“Usijali Manka! Utanikuta hapahapa. Ukijisikia kunitembelea, unakaribishwa,” alisema Godwin na kuondoka.
Kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, hakuamini kama alifanikiwa kutoka salama katika mikono ya watu hao. Alijipongeza kwa kuonyesha msimamo wake, hakutaka kabisa kuona akikamatwa na wakati bado kulikuwa na kazi kubwa mbele yake ya kuikomboa Tanzania kutoka katika mikono ya watu waliokuwa wakiyaangalia matumbo yao kwa kuwaibia pesa wananchi ambao kila siku walikuwa wakikatwa kodi.
Akaingia chumbani. Alikuwa amefanya kazi kubwa, mbele yake kulikuwa na kazi moja tu aliyotaka kuifanya, nayo ilikuwa ni kumuibia pesa zote Rais Bokasa, pesa ambazo alizificha katika akaunti yake ya Uswisi.
Alijua kulikuwa na kazi kubwa lakini alitakiwa kuifanya pasipo kuogopa kitu chochote kile. Alijua kwamba kulikuwa na viongozi wengi waliokuwa wamejilimbikizia pesa nyingi katika akaunti zao ndani ya benki zilizokuwa nchini humo, alitaka kupambana kwa nguvu zote na hatimaye kuzichukua pesa hizo na kuzipeleka katika taasisi mbalimbali za kusaidia watoto na wagonjwa.
Haikuwa kazi nyepesi kuingia katika data base ya benki za huko, alijua kwamba zilikuwa zikilindwa, watu waliosomea IT ambao walikuwa na uwezo mkubwa ndiyo waliokuwa wakiziendesha benki hizo tena wakati mwingine kubadili ‘codes’ kila wakati.
Hakutakiwa kuogopa, mbele yake hakuamini kama kulikuwa na kitu kigumu. Ugumu wa jambo ulikuwa pale mpaka alipokuwa akifanya na kushindwa ndipo angesema kwamba kitu hicho kilikuwa kigumu, ila kabla ya kujaribu kwa kufanya, hakuamini kama kulikuwa na jambo gumu.
Akaanza kazi, akafungua laptop yake, alichokuwa akikihitaji ni kuingia kwenye ‘data base’ za benki ya Geneva ambayo ilisadikiwa kuwa na akaunti nyingi za pesa kutoka kwa viongozi mbalimbali wa Afrika.
Haikuwa kazi ndogo, yeye mwenyewe alijua kabisa kwamba kulikuwa na kazi kubwa ya kuingia katika data base ya akaunti hiyo, alipofanikiwa kuiona, kuingia na ‘kudownload’ mafaili ilikuwa kazi nyingine.
Alijaribu kila njia, kila faili alilotaka ‘kudownload’ lilionekana kuwa gumu, hakutaka kukata tamaa, alitulia kwenye kompyuta yake, kichwa chake kilikuwa kikifikiria mambo mengi. Alianza kazi hiyo majira ya saa mbili asubuhi lakini mpaka inafika saa kumi na mbili jioni hakuwa amefanikiwa.
Hakutaka kula wala kufanya kitu chochote kile, alikuwa akipambana kwa nguvu zote kuhakikisha kila kitu kinakuwa kama alivyotaka kiwe. Alipoona kwamba ameshindwa kabisa hapo ndipo alipoamua kutumia virusi vyake kwenda katika data base hiyo na kuharibu kila kitu.
Virusi vilevile vya mateshi ambavyo alivitumia kuyaficha mafaili ya chuo ndivyo alivyovitumia kuzivuruga data za benki hiyo. Kila kitu kikafichwa, hakukuwa na mtu aliyeweza kuingia katika ‘data base’ za benki hizo kwa kipindi hicho mpaka yeye mwenyewe atakapoamua kuruhusu mtu mwingine kuingia.
Japokuwa mwili wake ulikuwa umechoka lakini baada ya kufanikiwa kuwaingiza virusi hao na kuvuruga kila kitu, mwili wake ukapata nguvu na kuendelea kufanya kila alilokuwa akilifanya kuhakikisha kwamba anafanikiwa kuchukua pesa hizo.
Kitu cha kwanza akaanza kulitafuta jina la Bokasa katika orodha ya majina ya wateja waliokuwa katika benki hiyo. Alishindwa kuliona jina hilo zaidi ya kuliona jina la Catherine Bokasa ambalo moja kwa moja akajua kwamba hilo ni jina la binti yake, rais huyo alifungua akaunti kwa jina la binti huyo ili asiweze kugundulika mambo yatakapoharibika.
“Anajifanya mjanja! Ngoja nimuonyeshee!” alisema Godwin, akajiweka vizuri, akaisogeza laptop yake karibu naye.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akaangalia taarifa zote za kibenki, alishangaa, rais huyo alikuwa akiingiza kiasi kikubwa cha pesa katika akaunti hiyo kila mwezi, alionekana kuwa bilionea mkubwa, hivyo ili kumchanganya na kumfanya kuwa na presha ilikuwa ni lazima kuzihamisha pesa hizo na kuzipeleka katika Hospitali ya St. Lucas iliyokuwa New York.
Akachukua namba za akaunti ya hospitali hiyo kutoka katika tovuti yao na kisha kuhamisha kiasi chote cha pesa, zaidi ya dola milioni 100 kutoka katika akaunti ya Rais Bokasa.
“It’s done,” (kazi imekamilika) alisema huku akiachia tabasamu pana. Hakutaka kuishia hapo, akaanza kutafuta na majina ya viongozi wengine wa serikali wa Tanzania ambao walikuwa na akaunti katika benki hiyo, alitaka kuhamisha pesa zao kwenda katika miradi na taasisi mbalimbali za kijamii
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment