IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI
*********************************************************************************
Simulizi : Penzi Ama Kaburi
Sehemu Ya Kwanza (1)
“Shadya! Wewe ni msichana mzuri sana, mrembo, msichana ambaye ninajisikia fahari sana kuwa nae,” ilisikika sauti ya mwanaume mmoja aliyekuwa amejibanza kwenye ukuta wa chuo cha madrasa ya Al Munira Siraja kilichokuwa katika Mtaa wa Michenzani huko Zanzibar.
Shadya alikuwa kimya, macho yake aliyatuliza usoni mwa kijana aliyesimama mbele yake. Alivalia kanzu ndefu nyeupe, kichwani alikuwa na kofia aina ya baghalashia na mkononi mwake alishika tasbih, chini alikuwa peku.
Hapo waliposimama ilikuwa ni rahisi kusikia sauti za wanafunzi waliokuwa wakijifunza koran ndani ya madrasa hiyo.
Kijana aliyekuwa akizungumza aliitwa kwa jina la Ngwali Shangali, alikuwa mwalimu wa madrasa hiyo ambaye alipewa jukumu la kuwafundisha watoto wadogo waliotakiwa kuishi katika misingi ya kumtumikia Mungu.
Shadya alikuwa kimya, alimwangalia kijana huyo, maneno aliyokuwa akiyazungumza yalimgusa kupita kawaida. Alimpenda, alimthamini, katika maisha yake hapakuwa na mwanaume aliyekuwa akimpenda kama huyo.
Kwa kumwangalia, Shadya alikuwa msichana mrembo mno, alivutia, alikuwa na asili ya Pemba, mweupe, macho ya goroli na kila alipokuwa akicheka ama kutabasamu ilikuwa ni rahisi sana kuviona vishimo vidogo mashavuni mwake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Weupe wake ulimfanya kuvutia, sura ya kitoto ilimfanya kupendwa na kila mtu katika mtaa huo wa uswahili.
Wanaume wengi walimfuata tangu alipokuwa na miaka kumi na tatu, walihitaji nafasi ndani ya moyo wake, alikuwa mdogo lakini urefu wake ulimfanya kila mmoja kuhisi alikua, alifaa kulalishwa kitandani na kuvuliwa nguo.
Wengi walimmendea, walimtolea macho huku wakitamani hata kuiona miguu yake, ilifananaje, ule weupe uliokuwa ukionekana usoni ulikwenda mpaka miguuni na mapajani, tumboni ama la.
Japokuwa hapo Unguja lilikuwa jambo gumu kwa mwanaume kumsimamisha mwanamke waziwazi na kuongea naye stori za kimapenzi lakini kwa Shadya walishindwa kuvumilia kabisa, hivyo wakajikuta wakianza kufanya hivyo.
Mpaka anafikisha umri wa miaka ishirini na moja Shadya alimvulia nguo mwanaume mmoja tu, naye alikuwa Ngwali ambaye alisimama mbele yake muda huo.
Kukutana kwao ilikuwa ni humohumo chuoni, wakati Shadya alipokwenda kujiunga na madrasa hiyo, Ngwali alichanganyikiwa, alijitahidi kuwa naye karibu, kumsaidia na mwisho wa siku kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi.
Sheria za dini hazikuruhusu, hata sheria za madrasa hiyo hazikuruhusu hivyo walifanya mambo yote kwa siri huku wakiwa makini kwenye kuepuka siku za hatari kwa msichana huyo.
Japokuwa watu wengi wa huko hawakuamini kama msichana alitakiwa kusoma kipindi hicho lakini mzee Hamduni alikuwa na jukumu la kumsomesha binti yake ili siku moja aje kuwa na maisha yake, apate kazi nzuri na kulipwa mshahara mnono.
Alimkazania kila siku, alitumia pesa zake kuhakikisha anasoma, tena kwa kufaulu vizuri huku wakati mwingine hata wao wenyewe kama wazazi wakijinyima.
Mbali na huyo Shadya pia kulikuwa na kijana wao mwingine, alikuwa pacha wa Shadya, kijana huyo aliitwa Rahim.
Kwa kumwangalia harakaharaka, Rahim alifanana sana na Shadya, alibarikiwa kuwa na uzuri, wasichana wengi walimpenda, wakatamani kulala naye lakini hakukuwa na kitu alichokuwa akikiogopa kama kulala na mwanamke, kama ni kidume basi aliitwa ‘Joka la Kibisa.’
Pamoja na kuwa na umri wa miaka ishirini na moja lakini Rahim aliogopa wanawake waliokuwa wakijipeleka kwake kimahaba, hakutaka kusikia lolote kuhusu wanawake hao na hata walipokuwa wakimwambia kuwa walimpenda, hilo halikumuingia kabisa akilini.
“Rahim niangalie kwanza,” alisema mwanamke mmoja huku akimwangalia Rahim aliyekuwa kwenye kochi. Siku hiyo alishindwa kuvumilia, alimpenda sana kijana huyo kiasi kwamba alikuwa tayari hata kuvunja ndoa yake lakini mwisho wa siku alale naye.
Alivizia muda ambao mume wake alikwenda kazini ndipo akamleta kijana huyo ndani na kumuweka kwenye kochi. Alivua juba lake na kubaki na sketi fupi laini iliyoifanya miguu yake kuonekana mpaka juu ya magoti kidogo na kumwangalia Rahim ambaye hata kusisimka hakusisimka.
“Naomba unipoze kiu,” alisema mwanamke huyo ambaye alikuwa kwenye ndoa kwa miezi sita, hata kifua chake kilionekana kichanga, yaani kilisimama dede.
“Allah hapendi!” alijibu Rahim huku akitetemeka.
Mwanamke huyo hakutaka kukubali, akamsogelea pale kwenye kochi na kumshika mkono, Rahim akahisi kama amepigwa shoti ya umeme, kijasho kilikuwa kikimtoka.
“Kwani unaogopa nini jamani?” aliuliza mwanamke huyo huku akianza kuitoa nguo yake ya juu, sasa akabaki kifua wazi.
Japokuwa alikuwa na mvuto wa aina yake lakini kwa Rahim ulikuwa si kitu, hakutamani, hakusisimka, hakuwehuka, hakudata, yaani alipokuwa akimwangalia mwanamke huyo, ni kama alikuwa akimwangalia mwanaume mwenzake, yaani hata suruali yake maeneo ya zipu haikupanda juu.
“Rahim...” aliita mwanamke huyo kwa sauti ya mahaba tele lakini ilikuwa ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa acheze na wakati hata kukata viuno hakujua.
“Naomba niondoke!” alisema Rahim.
“Kwa hiyo hutaki kula?”
“Naomba niondoke nitapiga kelele!” alisema mwanaume huyo.
Ilishangaza, ikamshtua sana lakini hakuwa na la kufanya, hivyo akakubaliana naye, akavaa nguo na Rahim kuondoka zake.
Haikuwa kwa mwanamke huyo tu, kwa wengi walifanya kama hivyo lakini hawakuambulia kitu, hawakujua kama Rahim alikuwa na tatizo, jogoo wake hakuwa akiwika na taratibu hisia zake zilianza kuhama, kuhamia upande mwingine kabisa.
Kila alipokuwa akipiga stori na wanaume wenzake walikuwa wakimtania kwamba alifanana na Shadya, alikuwa mwanamke kwa asilimia tisini na tisa ila Mungu alijisahau na kumuumba akiwa mwanaume, hakutakiwa kuwa hivyo.
Walimtania lakini maneno yale yakawa yanajijenga kichwani mwake, akayaamini kwamba kweli Mungu alikosea, alitakiwa kuwa mwanamke kama dada yake.
Hilo likawa kosa, akabadilika na kuanza kuwatamani wanaume wenzake. Lilikuwa jambo baya mno, lilikuwa siri lakini baada ya kupita kipindi fulani, wale ambao walifanikiwa kuwa naye wakatoa siri na hivyo kila mmoja kugundua hilo.
“Umeanza lini?” aliuliza mzee Hamduni kwa ukali.
“Baba nisamehe!”
“Sawa! Ila umeanza lini?”
“Zamani! Walianza kuniambia eti mimi ni mwanamke kama Shadya!” alijibu Rahim huku akionekana kuogopa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mzee huyo hakuwa na jinsi, aliumia moyoni mwake, alijua hata kama angemwadhibu Rahim asingeweza kumbadilisha hivyo kuonana na madaktari na kuanza kumpa matibabu na hata ushauri.
Ilisaidia kidogo, alianza kubadilika lakini kila alipokuwa chumbani peke yake alitamani kuwa na mwanaume, ilikuwa dhambi kubwa iliyokuwa ikimtafuna kila siku.
Japokuwa alikuwa katika hali hiyo lakini Rahim alikuwa kijana mwenye akiili mno, alikuwa na uwezo mkubwa darasani. Tangu alipoanza darasa la kwanza mpaka kidato cha sita alikuwa akishika nafasi ya kwanza na dada yake kushika nafasi ya pili.
Na muda huo wawili hao walifaulu vizuri hivyo wazazi wao kuomba uhamisho ili wapelekwe jijini Dar es Salaam na kusoma katika Chuo Kikuu.
Uhamisho ulikubaliwa kwa haraka sana mpaka wakashangaa. Siku chache kabla ya kuondoka kuelekea huko ndipo Shadya akaonana na Ngwali na kumuaga, alimwambia alikuwa akienda Dar es Salaam kusoma.
“Nitakupenda maisha yangu yote,” alisema Ngwali.
“Nitakupenda pia!”
“Naomba usinisaliti!”
“Sitokusaliti! Ninakuahidi hilo!” alisema Shadya huku akiwa na uhakika wa kutokumsaliti mpenzi wake hata kama angetokea mwanaume mzuri kiasi gani.
“Una uhakika?”
“Mbona unaogopa hivyo mpenzi?”
“Dar es Salaam! Jiji la maovu, jiji la ngono! Nalichukia sana. Liliwahi kuniharibia dada yangu, wakamtia mimba, wakamuacha,” alisema Ngwali huku akionekana kuwa na majonzi tele.
Ni kweli alikuwa na hofu, Dar es Salaam ilikuwa Dar es Salaam kweli. Watu walikuwa bize kutafuta pesa ila kwa upande mwingine walikuwa bize kutafuta mapenzi.
Wanaume walipokuwa wakimfuatilia msichana fulani walimfuata kwa uwezo wao wote, walifuatilia kana kwamba walifuatilia kazi TRA, kwa wasichana waliokuwa wakitoka Zanzibar na mikoani wengi waliishia mikononi mwa watu hao, walifanya walichokuwa wakitaka kufanya.
“Sitokusaliti!” alisema Shadya kwa sauti ya chini, iliyomaanisha alichokuwa akikisema.
“Kabisa mpenzi?”
“Niamini! Kama nilivyokuwa bega kwa bega na wewe, nilivyokuwa muaminifu nina hakika nitakuwa hivyo mpaka huko!” alisema.
“Ila ile ni Dar es Salaam baby!”
“Hata ingekuwa Marekani! Shadya na Ngwali milele!” alisema msichana huyo, moyo wa Ngwali ukawa na amani, sasa akaanza kuamini kama kweli mpenzi wake angekuwa mwaminifu katika kipindi chote cha miaka mitatu kusomea masomo ya Uandishi wa Habari.
Baada ya kuzungumza na mpenzi wake, Shadya akaondoka kuelekea nyumbani. Alipofika huko akajifungia chumbani na kuanza kuifikiria safari yake.
Hakuamini kama alikuwa akienda Dar es Salaam, yaani kwenda kusoma huko. Wakati mwingine alihisi kama alikuwa akiota na muda mfupi angeamka na kujikuta akiwa kitandani.
Alitamani kwenda kuishi huko. Ni mara chache kipindi cha likizo alikuwa akielekea kwa shangazi yake aliyekuwa akiishi Ilala hukohuko Dar.
Aliyapenda mazingira ya huko, alipenda kila kitu, mpaka vyakula ambavyo vilipikwa tofauti na watu wa Zanzibar.
“Eti nimsaliti Ngwali! Haiwezekani! Yaani hata kwa dawa,” alijisemea.
“Ila kumbuka ile Dar! Kule kuna watu wenye uwezo wa ajabu sana,” aliisikia sauti yake ikimwambia moyoni.
“Hata kama siwezi!”
“Una moyo huo?” Iliendelea kuuliza.
“Utaona!”
“Si unakumbuka Nusrat alipata mimba!”
“Ni yeye! Ila si mimi.”
“Kweli?”
“Kabisa. Wewe subiri utaona. Hizo siku elfu moja ni chache sana. Nitabaki hivihivi mpaka nitakaporudi Zanzibar na kufunga ndoa na Ngwali!” aliijibu sauti ile.
Na baada ya siku mbili, Shadya na Rahim wakaanza safari kuelekea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza maisha mapya, kusoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, moja ya sehemu kulipokusanya watu wa kila aina. Wapole, wababaishaji, mabishoo, masista duu na hata wanaume waliokuwa tayari kuachana na vipindi darasani ila mwisho wa siku wafanikishe misheni zao za kumnasa msichana fulani.
Ndani ya boti Shadya alionekana kuwa na mawazo tele, alikuwa akimfikiria mpenzi wake, Ngwali ambaye alimuacha huko Unguja. Moyo wake ulimpenda kijana huyo kwa asilimia mia moja na muda wote ambao alikuwa humo kwenye boti, alijiambia ilikuwa ni vigumu kumsaliti mwanaume kama huyo.
Mbali na kumfikiria Ngwali, pia alikuwa akifikiria masomo yake, alitamani mno kuwa mwandishi wa habari, alikuwa akijisikia wivu sana kila alipokuwa akiwaona waandishi wadogo wa kike kama yeye wakitangaza kwenye televisheni na redio, kupata umaarufu na kuingiza pesa nyingi.
Alitamani kuwa kama wao, hakutaka kuona akiendelea kuishi kwa wazazi, kwa kipaji cha utangazaji ambacho aliamini alikuwanacho, ilikuwa ni lazima apambane mpaka kuona akitimiza ndoto zake na kuwa mwandishi mkubwa.
“Nitatimiza ndoto zangu halafu nitafunga ndoa na Ngwali,” alijisemea kipindi hicho boti ilikuwa ikiendelea na safari zake.
Baada ya saa tatu, yaani saa tisa alasiri tayari boti ya Azam Marine ilifika katika bandari ndogo ya jijini Dar es Salaam na watu kuanza kuteremka. Hali ya hewa haikuwa na mabadiliko yoyote yale, ilikuwa ni joto kama ilivyokuwa huko walipotoka.
Hapo walipokewa na mjomba wao ambaye aliwachukua na kuanza kuondoka nao kuelekea Ilala alipokuwa akiishi. Mazingira yalikuwa vilevile, hapakuwa na mabadiliko yoyote yale, ilikuwa ni kama walivyokuwa wakija katika siku za nyuma.
Japokuwa Unguja ilikuwa kwao lakini moyo wake ulikuwa na mapenzi ya dhati na Dar es Salaam, alilipenda jiji hilo kwa kuwa aliamini mara unapokuwa humo, mzunguko mkubwa wa pesa unakufanya na wewe kuwa mchakarikaji kama watu wengine.
Kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakitoka mikoani na kuelekea Dar es Salaam, walipofika huko, walifanikiwa kwa sababu kulikuwa na idadi kubwa ya watu, kulikuwa na nafasi nyingi za kazi, maeneo ya kufanya biashara zako na mambo mengine mengi, yaani kwa kifupi, Tanzania nzima ilikuwa ikipatikana jiji hapo.
“Mbona shangazi hajaja kutupokea?” aliuliza Shadya huku akimwangalia mjomba wake aliyekuwa mbele akiendesha gari.
“Nimemuacha akifanya baadhi ya kazi nyumbani, ila alitamani sana aje,” alijibu mjomba.
“Nimemkumbuka!” alisema Rahim.
“Amewakumbuka pia! Kwanza hongereni kwa kufanya vizuri kwenye masomo yenu,” alisema mjomba huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.
“Tunashukuru! Allah ndiye kila kitu!”
“Ila someni sana, mnajua kwamba nyie ndiyo vichwa vyetu vilivyobaki, yaani sisi hatujasoma, nadhani mnajua hilo, shangazi, baba zenu wadogo kwa wakubwa wote hawajasoma, tunaomba msituangushe,” alisema mjomba huyo.
“Sisi tutasoma sana, tena sana yaani!” alisema Shadya.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Walikuwa wakizungumza haya na yale na baada ya nusu saa wakafika Ilala ambapo wakateremka na kwenda ndani. Siku hiyo ilikuwa ni ya furaha tele, kila mmoja alipenda kuwaona mahali hapo.
Hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kwanza kufika hapo Ilala baada ya kumaliza masomo yao, walionekana kuwa na furaha mno, kwa uzuri wa Shadya, wanaume waliokuwa mtaani hapo hawakuacha kumwangalia kwa macho ya matamanio, walimpenda na waliamini alikuwa mmoja wa wasichana waliokuwa warembo mno.
Japokuwa alipenda sana kuvaa mavazi makubwa na marefu kama dela, mabaibui lakini hayo yote hayakulifanya umbo lake zuri kuonekana, alivutia, kiwowowo chake kilikuwa kama pembe la ng’ombe, yaani hata kama kilifunikwa vipi ilikuwa ni lazima kionekane tu.
Wanaume hao hawakuacha kumuita, alivutia lakini Shadya hakuwa na habari nao, alifika Dar es Salaam kwa ajili ya kusoma tu, ukiachana na hivyo, alikuwa na mpenzi wake ambaye hakutaka kabisa kuona akimsaliti, alikuwa tayari kujitoa uhai lakini si kumvulia nguo mwanaume yeyote yule.
“Nimekwishakukumbuka mpenzi,” alisema Ngwali kwenye simu. Pumzi zake zilikuwa zikisikika masikioni mwa Shadya.
“Nimekukumbuka pia!” alisema Shadya.
“Umekumbuka nini kutoka kwangu?” aliuliza Ngwali.
“Sauti yako!”
“Kingine?”
“Muonekano wako!”
“Kingine?”
“Tabasamu lako!”
“Kingine?”
“Jinsi unavyojua kuuchezea ulimi wako mwilini mwangu,” alisikika Shadya.
“Kweli?”
“Kabisa! Huwa ninahisi kuweweseka sana kila ninapokuona mpenzi! Nilikwishasema kwamba huu mwili ni wako, peke yako na hapatotokea mwanaume mwingine wa kuweza kuushika kama ulivyokuwa ukiushika!” alisema Shadya.
“Ila upo Dar kumbuka!”
“Hata ningekuwa Marekani! Bado msimamo wangu utabaki kuwa hivyo,” alisema Shadya.
Walikuwa wakizungumza kila siku, ilikuwa ni lazima kwa wawili hao kuongea usiku, walikuwa wakiambiana jinsi walivyokumbukana, jinsi uhusiano wao huo ambavyo ungedumu na mwisho wa siku kuja kufunga ndoa na kuwa mume na mke.
Siku zilikatika na baada ya kukamilisha kila kitu kwenda kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hatimaye wakaenda huko na kuanza masomo katika chuo hicho.
Hawakutakiwa kurudi Ilala kwanza, walichukua mabweni ya huko, ndani ya chuo hivyo kama walitaka kurudi Ilala walitakiwa kusubiri mpaka wikiendi.
Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kilikuwa na wasichana warembo mno, waliokuwa wakijua kuvaa, wasichana ambao mara unapokutana nao kwa mara ya kwanza basi ingekuwa ni rahisi kuhisi umekutana na msichana mrembo kuliko wote katika dunia hii.
Walijua kuvaa, kutembea, kuongea kwa sauti ya kumuibia mwanaume, walijua kumgusa mwanaume, kumpapasa, kumrembua macho na kufanya ujinga wote ambao hata kama angefanyiwa mwanaume aliyejiita kuwa mgumu, mwisho wa siku angeingiza mkono mfukoni na kutoa pochi yake iliyokuwa na pesa.
Wengi wao hawakufikiria masomo, walifika hapo huku wakiwa na mambo mengine kabisa, walifikiria vitu vingine lakini si hasa kile kilichokuwa kimewapeleka mahali hapo.
“Wewe ni wa mwaka wa kwanza?” alisikika msichana mmoja akimuuliza Shadya, walikuwa katika sehemu ya kulia chakula.
“Ndiyo!”
“Oh! Nimejua tu!” alisema msichana huyo huku akiachia tabasamu pana.
“Umejuaje?”
“Unavyovaa!”
“Kwani vibaya?” aliuliza Shadya huku akijiangalia.
“Si vibaya! Ila kama unakwenda kuswali!”
“Eh! Jamani!!!”
“Usijali! Hata mimi nilikuwa hivyo mwaka wa kwanza. Ukifika wa pili, au hata wa kwanza mwishoni utaona mabadiliko makubwa sana,” alisema msichana huyo aliyekuwa akimwangalia Shadya, naye msichana huyo akamwangalia, alivalia sketi fupi na kuyaacha mapaja yake wazi, kwa juu alivaa kiblauzi fulani ambacho kilionyesha nyamanyama za matiti yake.
“Kama yapi?” aliuliza.
Msichana huyo hakumjibu, alikuwa na mambo mengi ya kumwambia lakini hakutaka kufanya hivyo kwa sababu aliamini raha ya ngoma, ingia mwenyewe uicheze.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Masomo yalikuwa yakiendelea, uzuri wa Shadya ulionekana wazi, kila mwanaume aliyekuwa akimwangalia, alipenda sana kuyaweka macho yake kwake tu.
Alikuwa na urembo wa asili, alivutia, alikuwa akinukia vizuri, mikono laini na kila alipokuwa akiangalia na mwanaume yeyote na kugonganisha macho, alijisikia aibu, hivyo kuangalia chini.
Wanaume aliokuwa akisoma nao hawakuacha kumfuata, walitamani sana kuzungumza naye, walihitaji kuisikia sauti yake kwani kwa jinsi alivyokuwa mrembo, waliamini alikuwa na sauti ya kumtoa nyoka pangoni.
Alipokuwa akifuatwa, hakukataa, alijumuika nao na kuongea nao mambo mengi, hasa masomo waliyokuwa wakifundishwa.
Shadya akamuona kila mwanaume ni rafiki yake, hapakuwa na yeyote ambaye alimwambia jambo lolote la mapenzi, walikuwa wakijadili kuhusu masomo kana kwamba wanaume wote hao walikuwa majoka ya kibisa.
Hilo likampa amani, akahisi kabisa kweli watu walikuwa bize kusoma kumbe upande wa pili wanaume walikuwa wakitafuta nafasi nzuri ya kumuingia, mahesabu yao hayakutaka kuishia hapo, walihitaji hata kumpeleka mitaani walipokuwa wakiishi, kwa jinsi Shadya alivyoonekana kuwa mrembo, waliamini hata majirani ambao wangediriki kumuona msichana huyo, wangeshangazwa na uzuri wake.
Hapo chuo akafanikiwa kupata marafiki kadhaa wa kike ila rafiki yake mkubwa akatokea kuwa Diana. Alikuwa mmoja wa wasichana wakimya, alikuwa mwaka wa kwanza lakini alifanya kosa moja kubwa ambalo kwa kipindi hicho hakuona kuwa kosa, pale alipoanza urafiki na msichana aliyeitwa kwa jina la Bupe aliyekuwa mwaka wa pili.
“Ila wewe ni mzuri sana,” alisema Diana huku akimwangalia Shadya.
“Nani?”
“Wewe hapo! Yaani u mzuri mpaka unaboa!” alisema msichana huyo huku akicheka, macho yake yalionyesha kumaanisha alichokuwa akikizungumza.
“Mbona nipo kawaida!”
“Yeah! Hata Malkia Cleopatra naye alikuwa akijiona kuwa kawaida, ni jambo la kawaida pia,” alisema Diana huku akimwangalia Shadya.
“Nashukuru jamani! Ila hujafika Unguja, kuna wanawake wazuri kuliko mimi,” alisema Shadya, akaachia tabasamu la aibu.
Huo ulikuwa ni mwezi wa kwanza chuoni hapo. Mambo yalikuwa moto! Alikipenda sana chuo hicho kwa kuwa kilimchangamsha na kumfanya kuonekana kuwa tofauti kabisa.
Wakati yeye akipata marafiki wapya hata ndugu yake, Rahim naye alipata marafiki wapya kila siku. Alijitahidi sana kujizuia, hakutaka watu wajue kama alikuwa mshirika mzuri wa mapenzi ya jinsia moja.
Alijikaza, kila alipokuwa akitembea, alitembea kiume na wakati mwingine alijilazimisha kuongea sauti nzito.
Yalikuwa ni kama mateso kwake, hakuzoea lakini ilikuwa ni lazima kujikaza ili watu wasijue kama alikuwa na tabia zipi. Siku zikakatika, mpaka mwezi wa pili unaingia, Rahim alijikaza kuonyesha uanaume wake na Shadya alionyesha umwamba wake wa kuwa muaminifu kwa Ngwali aliyekuwa huko Unguja.
“Shadya...” alisikika mwanaume mmoja akiita kwa nyuma kwa sauti ya taratibu.
Shadya aliyekuwa amekaa katika Ukumbi wa Nkurumah, akageuka na kumwangalia mtu aliyemuita.
Alikuwa ni rafiki wake, waliyekuwa kwenye kundi moja la kujisomea, mwanaume mweusi, aliyenyoa kwa staili ya panki kwa mbali, aliyevalia mavazi nadhifu, kijana aliyejua mno kutabasamu, mwenye sura ya upole, aliitwa Gibson.
“Oh! Gibson...” aliita Shadya, akasimama na kumkaribisha mwanaume huyo.
“Mzima lakini?”
“Nipo poa!”
“Nimekupigia sana simu, hupatikani!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mimi?”
“Yaap!”
“Mbona napatikana!”
“Hapana! Hupatikani!” alisema Gibson, hapohapo Shadya akatoa simu yake na kuangalia, ilikuwa imejizima kwa kuishiwa chaji.
“Oh! Kumbe ilizima!”
“Bado unatumia hiyo simu?” aliuliza Gibson huku akiachia tabasamu.
“Gibson sipendi! Ushaanza utani wako!”
“Sasa huoni jinsi hizo simu watu wanavyozikashifu mitandaoni jamani! Kweli msichana mrembo kama wewe unatumia hiyo simu! Kweli jamani!” alisema Gibson huku akianza kutoa kicheko cha chini.
“Kwani kuna tatizo gani?”
“Inashusha hadhi yako! Yaani ni sawa na kumuoa mwanamke mzuri halafu hazai!” alisema.
“Jamaniiiiiiiiiii.....” “Ndiyo! Hebu fikiria umealikwa na rais, halafu kwenye kuchukua namba yako ukatoa simu hiyo! Hahaha...”
“Jamaniiiii! Hebu usitutanie!”
Baada ya utani huo wakaanza kuzungumza mambo mengi, Gibson alionekana kuwa kama kijana safi ambaye hakuwa na papara zozote zile, na alionekana kutokuwa na lengo lolote baya kwa msichana huyo.
Baada ya kuongea kwa robo saa nzima, hatimaye Gibson akaamua kumwambia kitu fulani Shadya ili ampe kazi ya kumanya kutafakari siku nzima.
“Nikwambie kitu Shadya....” aliuliza Gibson, akautoa uso wa masihara na kuuweka ule wa usiriazi.
“Kitu gani!”
“Unazijua gari fulani zinaitwa Range?”
“Ndiyo! Zile za hela nyingi?”
“Yaap! Unaonaje siku moja ukaliona Range kaliiii halafu lina matairi ya Vitz?”
“Unamaanisha nini?”
“Hujajibu! Utaonaje?”
“Nitashangaa....”
“Basi ndivyo ambavyo hata sisi tunashangaa!” alisema Gibson, akasimama kutoka kwenye kiti.
“Unamaanisha nini?”
“Naomba niondoke, tutaonana siku nyingine,” alisema na kuanza kuondoka.
“Gibson! Unamaanisha nini?”
“Nitakwambia next time.....” alisema kijana huyo na kupotea zake.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Shadya akabaki na maswali mengi, hakujua kijana huyo alifikiria vipi, alijiuliza maana halisi ya maneno yale lakini hakuambulia kitu.
Cha kushangaza! Akaanza kuwa na hamu ya kuonana na mwanaume huyo tena na kumwambia maana halisi ya maneno yale.
Alitamani kumpigia simu lakini haikuwa na chaji, alichanganyikiwa, kufuata chaji mpaka bwenini alihisi ni mbali mno.
Hakusoma tena, kila alipojitahidi kufanya hivyo, alishindwa kwani ni Gibson tu ndiye aliyekuwa kichwani mwake, alifikiria zaidi kile alichokuwa amemwambia.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment