Search This Blog

Tuesday, 1 November 2022

FURAHA HATIMAYE - 4

 






Simulizi : Furaha Hatimaye

Sehemu Ya Nne (4)





Dk. Ringo alikuwa wa kwanza kuamka asubuhi iliyofuata, usiku mzima hakuweza kupata usingizi wa kutosha, muda mwingi alitumia kuwaza jinsi ya kuanza kumtafuta Genesis, alifahamu ni kiasi gani Blandina alikuwa akiumia kutokana na kukosekana kwa mwanaye. Alichokifanya mara baada ya kuamka tu ni kumgongea Blandina mlango ili aamke.

Blandina hakuwa amelala usingizi, hivyo Dk. Ringo alipogonga mara moja tu, aliitika na baada ya muda mfupi walikutana sebuleni kisha wakaanza kupanga mipango ya kumpata Genesis.

“Mimi nafikiri baadaye twende wizarani tukapate ushauri!” Dk. Ringo akashauri.

“Sawa Dk., nashukuru sana, naheshimu sana mchango wako katika maisha yangu, sisi sasa ni ndugu wa damu!”

“Nashukuru kwa kutambua hilo!” Baada ya hapo Blandina alimhimiza msaidizi wake wa ndani aandae kifungua kinywa¸ambapo baadaye walijumuika pamoja mezani na kula!

Saa nne na nusu za asubuhi, walikuwa ofisini kwa mmoja wa Ofisa wa Waziri wa Elimu, macho ya Blandina yalizungumza alichokifuata.

“Poleni sana jamani!”

“Tunashukuru, lakini tulikuja na wazo moja ambalo tunahitaji msaada wenu!”

“Wazo gani hilo?”

“Nataka kufuatilia suala hili mwenyewe Marekani!”

“Utaweza kweli?”

“Naamini hivyo!”

“Kwanini usiwaachie watu wa usalama wakafanya kazi yao?”

“Pamoja na hilo, lakini nataka kiuonana na uongozi wa Marekani!”

“Hakuna tabu!”

“Nashukuru kusikia hivyo, ila nahitaji msaada wenu zaidi!”

“Msaada gani?”

“Fedha. Nahitaji fedha za kunifikisha huko!”

“Suala lako linashughulikiwa ndani ya masaa 48 utakuwa safarini!”

“Nashukuru kusikia hivyo!”

“Nawatakia kazi njema!”

“Nawe pia!”

*********

Siki mbili baadaye Blandina alikuwa Uwanja wa Ndege tayari kwa safari ya kwenda Marekani. Dk. Ringo alimsindikiza mpaka uwanjani, alionyesha kuwa na majonzi sana, alimuonea huruma sana Blandina, kwa mateso aliyokuwa nayo, aliona hakustahili kabisa kupata aliyonayo, Balndina alikuwa mwenye historia iliyosikitisha sana.

“Nakutakia safari njema yenye mafanikio!”

“Nashukuru sana Dokta, nasisitiza kukuambia kuwa wewe ni ndugu yangu wa damu, nitakuheshimu na kukupenda siku zote za maisha yangu!”

“Nashukuru sana kusikia hivyo!” Ikiwa zimebaki dakika saba kabla ndege haijaruka, Blandina na Dk. Ringo walikuwa bado wamekumbatiana, moyo wa Blandina ulikuwa mzito sana, alihisi huenda kulikuwa na jambo la hatari lililotaka kutokea mbele yake!

Kila aliporudisha macho yake na kuyatuliza usoni mwa Dk. Ringo, alihisi tukio baya mbele yake, kwa mbali akaanza kufikiria kuahirisha safari lakini alijikaza na kumuachia Dk. Ringo kisha akaingia kwenye chumba cha ukaguzi kabla ya kuingia kwenye ndege tayari kwa safari.

Blandina hakupata shida alipofika Marekani, uwanjani kulikuwa na mtu kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, aliyekwenda kumpokea. Alipokelewa vizuri kisha akapelekwa moja kwa moja Ubalozini.

**********http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Marekani ilichanganyikiwa sana kupata taarifa za mauaji ya majangili yaliyotokea katikati ya msitu wa Marakon, halikuwa jambo la kawaida, kwao walihisi kulikuwa na tatizo kubwa sana nyuma ya pazia, walijua kuna mtu aliyeharibu mpango mzima!

Ndani ya chumba kidogo, kulikuwa na kikao cha kikundi cha majangili wakijadilina juu ya hali iliyojitokeza. Hawakutaka kuamini mara moja kilichotokea, taarifa za vifo ziliwashtua sana.

“Hivi ni kitu gani hiki? Haijawahi kutokea hata mara moja katika historia ya nchi yetu!”

“Kwa kweli ni maajabu, ila tunapaswa kufanya jambo fulani ili kujua kilichosababisha, huenda waliomuiba mtoto ni wa hapa hapa nchini na hawajafika mbali bado!”

“Inawezekana kwa sababu taarifa za uwezo wa akili wa huyo mtoto zilisambaa kila mahali!” Kila mmoja alikuwa ana mawazo yake. Kimsingi mipango ya Marekani ilivurugika, walipanga kumtumia mtoto huo kuvumbua vitu vingi kutoka na uwezo wake mkubwa kiakili.

Wakiwa wanaendelea na mkutano wao, akaingia mmoja wa wapelelezi wa Marekani, akiwa ameshika bahasha ya khaki mkononi mwake, alipofika alikwenda moja kwa moja mpaka kwa Mkuu wa Majangili na kumkabidhi. Baada ya kuifungua na kuisoma, alionyesha kupigwa na butwaa!

“Kuna nini?”

“Mama yake na huyo mtoto yupo ofisini kwa Mkuu wa Upelelezi!”

“Unamzungumzia huyu Genesis aliyetekwa?”

“Ndio!”

“Amekuja lini?”

“Sijui, ila amefika leo kwa mara ya kwanza ofisini, anataka serikali ifuatilie kwa makini!”

“Mh! Kweli hapo kazi ipo!”

****

Kila mmoja alishtuka sana, hawakuweza kuelewa kitu kilichokuwa kikiendelea. Zilikuwa taarifa mbaya sana kwao, kupoteza wapiganaji waliokuwa wakiwategemea, wakati huo huo Genesis, lilikuwa pigo kubwa sana! Vichwa viliwauma, hakuna hata mmoja aliyezungumza. Ukimya ukatawala ghafla katika Chumba cha Mkutano, ghafla mmoja wao akafungua kinywa na kuzungumza.

“Amekuja saa ngapi?”

“Sijui!”

“Anataka nini hasa?”

“Ni kuhusu mtoto wake, anashindwa kuelewa mazingira aliyopotea!”

“Kwa hiyo?”

“Hakuna cha kufanya ila yatupasa tuwe makini kuna kitu kibaya mbele yetu kinakuja, lazima tujiandae!”

“Ni kweli kabisa mkuu!”

Hapakuwa na kitu kingine mbele yao zaidi ya kujipanga upya kuwatafuta watu waliohusika kumteka Genesis. Kwa mbali sasa walianza kuhisi Japani au China ilikuwa inahusika na kumtorosha Genesis, pamoja na hisia hizo hawakutaka kupasisha hilo moja kwa moja, ilikuwa lazima wafanye uchunguzi wa kutosha kwanza. Kikao kiliisha bila kupata ufumbuzi wa moja kwa moja juu ya vifo vya majangili pamoja na kutoroshwa kwa Genesis katika mazingira ya kutatanisha.

*********

Mkuu wa upelelezi alikuwa makini kumsikiliza Blandina, alionyesha kuwa na huzuni sana moyoni mwake kila alipozungumza neno moja machozi yalimlengalenga kuna wakati alishindwa kuzungumza na kuishia kulia!

“Usilie tafadhali, haya mambo yataisha, mradi yamefika kwangu ondoa shaka!” Mkuu wa Upelelezi Deogratius Steven alizungumza kwa unyenyekevu. Kwa kiasi fulani aliingiwa na maneno ya Blandina mama yake Genesis.

“Ni lazima nilie! Nina haki ya kulia, haiwezekani mwanangu apotee katika mazingira haya!”

“Kwanini unasema hivyo?”

“Kwanini yeye? Mbona walikuwepo watoto wengi tu, nahisi kuna kitu!”

“Kitu gani?”

“Kitu kibaya!”

“Unafikiri inaweza kuwa nini?”

“Hizo ni hisia zangu, siwezi kuziweka wazi!” Blandina alilia sana, alimlilia mwanaye kwa uchungu mkubwa, furaha yake ilikuwa imepotea kwa muda mrefu, ingerudishwa na Genisis pekee, ambaye alionyesha mwanga wa kurejesha furaha hiyo.

“Sawa… ila kipo kitu cha kukusaidia!”

“Kitu gani?”

“Tutatuma jeshi wamfuatilie popote alipo, hata hivyo tutatangaza katika vyombo vyote vya habari na atakayempata tutampa zawadi nono, naamini kwa kufanya hivyo tutafanikiwa!” Blandina akatabasamu kidogo, ingawa alikuwa na mawazo kichwani lakini alihisi juhudi za kumpata mwanae zilikuwa zimeanza kufanyika.

Kwa kiasi fulani alianza kuwa na matumaini ya kumpata mwanaye, hisia za kwamba Marekani walihusika kumtorosha mwanaye zikaanza kutoweka taratibu. Kimsingi Deo alikuwa mjanja mwenye maneno matamu aliyekuwa na uwezo wa kushawishi jambo lolote likasikilizwa, kwa mtu kama Blandina asingeshindwa kumuweka sawa kwa maneno matamu.

“Nitashukuru sana kaka Deo, ni lazima nimpate mwanangu!”

“Nakuahidi!”

“Nashukuru sana, lakini tutatumia utaratibu gani?”

“Kesho saa tatu kamili asubuhi nitakuhitaji hapa ofisini kisha tutaongozana pamoja katika vyombo vya habari!”

“Kazi njema kaka Deo!”

“Nashukuru ila samahani naomba nikuulize kidogo!” Deo akamwambia Blandina, huku uso wake ukionyesha wasiwasi wa atakachomwambia.

“Nini tena?” Blandina akapatwa na wasiwasi kidogo, lilikuwa swali gumu kwake, lililomfanya maswali mengi kujirudia akilini mwake.

“Usishtuke ni mambo ya kawaida tu!” Ubongo wa Deo ulifanya kazi zaidi ya kawaida alishawaza kitu, japokuwa alipanga kumsaidia Blandina lakini alifahamu ni kiasi gani kazi iliyokuwa mbele yake ilivyokuwa ngumu. Ili kupunguza ugumu wa kazi hiyo ilikuwa lazima ajenge ukaribu baina yake na Blandina, kwa maana hiyo hatua ya kwanza ilikuwa ni kufahamu alipofikia.

“Sawa niambie basi!“

“Umefikia Hoteli gani?”

“Hills Hotel”

“Unaweza kunipatia mawasiliano yako?”

“Bila shaka Deo!” Ndivyo ilivyokuwa, Blandila akatoa kipande cha karatsi ngumu kilichokuwa na namba za simu za Hoteli aliyofikia, baada ya hapo wakaagana.

Kwa mbali Blandina alianza kuwa na wasiwasi, hata hivyo wasiwasi huo hakuwa na nguvu sana, alihisi Deo alikuwa na nia ya kumsaidia. Hata hivyo Deo hakuwa na mawazo kama aliyofikiria Blandina. Akaondoka akiwa na mawazo tele kichwani mwake, ulikuwa usiku mgumu kuliko siku zote zilizowahi kutokea katika maisha yake. Usiku Deo alimpigia simu akamsisitizia kuwahi siku inayofuata asubuhi.

Kitu cha kwanza kufanya baada ya kuamka asubuhi hiyo, ilikuwa kujitayarishia kifungua kinywa kisha kujiandaa tayari kwa safari ya kwenda ofisini kwa Mkuu wa Upelelezi. Alipofika alipokelewa na Deo kwa furaha, hakuwa na muda wa kupoteza wakaingia ndani ya gari kisha wakaanza kwenda katika vyombo mbalimbali vya habari.

Sehemu ya kwanza waliyokwenda ilikuwa katika Kituo cha Televisheni cha CNN, baada ya hapo wakaenda Sky News na vituo vingine ikiwa ni pamoja na magazeti ya nchini Marekani. Tangazo la kupotea kwa Genesis likasambazwa na zawadi nono ikatangazwa kutolewa.

Huo ulikuwa mwanzo wa furaha kwa Blandina, aliamini kwa matangazo yote waliyofanya lazima Genesis angepatikana. Pamoja na hivyo Marekani ilikuwa tayari kutumia gharama yoyote ili waweze kumpata Genesis lakini walipanga wakimpata wamtumie kwa manufaa yao na siyo kumrudisha kwa mama yake. Hiyo ilbaki kuwa siri kwa Marekani. Hatimaye Blandina alirudi nyumbani kwao Tanzania akiwa na matumaini ya kumpata mwanaye wa pekee aliyempenda Genesis.

*********

Safari ya Majangili wa Japan iliishia katika jumba moja kubwa la Utafiti wa Sayansi lililokuwa pembeni kidogo mwa jiji la Tokyo. Hapo ndipo mahali walipoona panamfaa Genesis. Muda wote Genesis alikuwa akilia na kumtaja mama yake. Majangili hawakujali, waliopomfikisha walimwingiza katika chumba maalum kwa ajili ya kusubiri maelezo zaidi kutoka kwa uongozi wa juu.

“Tumefanikiwa mkuu!” Mkuu wa Majangili alimpigia simu Waziri wa Mambo ya Ndani kumfahamisha juu ya taarifa hiyo.

“Vizuri sana, mmekuja naye?”

“Ndio!”

“Mmefikia wapi?”

“Kama mlivyotuelekeza, tumefikia katika Jumba la Utafiti wa Sayansi!”

“Vizuri sana, endeleeni na kazi nyingine kama kawaida, ila lazima muwe makini, Marekani wanaweza kufutilia suala hili kwa ukaribu!”

“Hakuna tatizo, ila kuna jambo nataka kufahamu!”

“Jambo gani hilo?”

“Nini kinachofuata sasa hivi?”

“Maagizo yote nimemwachia Dk. James Rusheshe, kwani hayupo hapo?”

“Yupo!”

“Basi mwambie atimize majukumu yake!” Kama alivyoagizwa na mkuu wake wa kazi ndivyo alivyofanya, alizungumza na Dk. Rusheshe ambaye mara moja alimchoma Genesis sindano ya kumpotezea kumbukumbu pamoja na ya usingizi, dakika tano baadaye Genesis akapotelea usingizini.

“Kazi imekamilika!”

“Kweli kabisa, haiwezekani Marekani wapate hazina hii muhimu wakati sisi tupo!” Walikuwa wakizungumza kwa furaha huku wakipongezana kukamilisha kazi hiyo ngumu.

*********

Siku mbili baadaye Genesis aliamka akiwa mchovu sana, hakuwa alikumbuka kitu chochote tena ingawa alikuwa na ufahamu wa kawaida. Kilichofanyika ni kumtafutia mwalimu aliyekuwa akifika kumfundisha masomo yote muhimu. Uwezo wake wa kuelewa uliwashangaza wengi.

Baada ya wiki tatu tu, aliweza kuzungumza vizuri sana lugha ya Kiingereza na Kijapan, kila mmoja alishangazwa sana na uwezo wake wa akili, wakati mwingine ilibidi mwalimu amvukishe masomo kwa kuwa alikuwa ameshayaelewa kabla hata ya kumfundisha. Miaka miwili baadaye, walishangaa Genesis akipenda sana kucheza na kompyuta, alipoletewa mwalimu wa kumfundisha ni wiki mbili tu zilitosha yeye kufahamu mambo yote muhimu ikiwa ni pamoja na kugundua programu mpya za komyuta. Kila mtu alistaajabu sana, Japan ilipata faida nyingi kutokana na Genesis kugundua programu mbalimbali za kompyuta.

Siku moja walishangaa kumuona Genesis akilia sana, hakutaka kusikia kitu chochote kutoka kwa mtu yeyote, hakuna aliyeelewa sababu ya kulia kwake. Muda wote alitumia kumtaja mama yake, alimtaka mama yake tu, hakutaka kitu kingine. Kwao ilikuwa maajabu sana kwa sababu ilishapita miaka mitatu akiwa hapo tena aligundua programu mbalimbali za kompyuta, kumtaja mama yake wakati walijua alishasahau iliwashtua sana.

Baada ya kumbembeleza kwa muda mrefu bila mafanikio, wakaamua kumwita daktari wake kwa ajili ya kumwangalia alikuwa na tatizo gani.

“Genesis unasumbuliwa na nini?” Daktari alimwuliza.

“Namtaka mama yangu!” Genesis alimjibu. Lilikuwa jibu lililotosha sana kufahamu kulikuwa na kitu gani kilichokuwa kikiendelea. Alifahamu vizuri sana kuwa sindano aliyomchoma iliisha nguvu, hakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kumchoma sindano nyingine.

Baada ya hapo hali ikawa shwari, Genesis hakulia tena wala kumtaja la mama yake, kilichoendelea ni kugundua programu zaidi za komyuta. Japan ilitajirika sana kupitia mtoto huyo, hata hivyo walitumia muda mwingi kumbadisha sura yake ili angalau ivutie ikiwa ni pamoja na kuhakikisha anapata elimu ya kutosha.

Wakati hayo yote yakiendelea, mashirika mbalimbali ya habari yaliendelea kutangaza zawadi kwa yeyote atakayempata Genesis. Baada ya miaka saba, Japan iliridhika na faida walizopata kutokana na Genesis, hawakuona sababu ya kuendelea kuwa naye, hasa kutokana na ukweli kuwa siku moja wangeweza kujulikana walikuwa wakimtumia mtoto huyo, jambo ambalo lingetia doa taifa lao.

“Hatuna sababu ya kuendelea kuwa naye tena!” Mkuu wa Wizara ya Ndani alisema, siku moja walipokuwa na kikao.

“Kwa hiyo tufanye nini?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Mrudisheni mlipomtoa!”

“Unamaanisha porini? Kwa hiyo tutakuwa tumemsaidia kweli, kwa sababu kama msaada kwa nchi yetu ameutoa mkubwa sana!”

“Namaanisha Hawaii, mkamtelekeze ufukweni, kwa kuwa anatafutwa, mtu atakayemuona atatoa taarifa kwa vyombo vya habari ili akapatiwe zawadi, bila shaka mama yake atampata!”

“Ni kweli kabisa, kwa hiyo tufanye hivyo lini?”

“Sio jambo la haraka, subirini mpaka sindano itakapoisha, akianza kulia mnampakia kwenye ndege na kumrudisha!”

“Hakuna tatizo mkuu!” Kama walivyokubaliana ndivyo ilivyokuwa, siku nane baadaye Genesis alipoanza kulia na kumtaja mama yake, wakajua tayari dawa ilishaisha mwilini, hivyo wakamchukua na kumpakia kwenye ndege, safari ya kwenda Marekani ikaanza.

Saa tisa na dakika ishirini walifika mjini Hawaii, bila kupoteza muda wakaingia katika gari lililoandaliwa, kisha wakaenda moja kwa moja mpaka ufukweni Miami. Genesis aliendelea kulia lakini hawakuwa na njia yoyote ya kumsaidia. Kama walivyopanga, walipofika walimuacha peke yake ufukweni akilia.

“Kazi yetu sasa imekwisha!”

“Tena tuondoke kabla mambo hayajaharibika!” Majangili wakamuacha Genesis peke yake ufukweni usiku wa manane.

****

Genesis alilia sana, hakuwa na kitu chochote cha kufanya ufukweni, ulikuwa ni usiku wa manane wenye upepo mkali na baridi, alipata mateso makubwa kuliko kawaida. Genesis ambaye kwa muda huo alishafikisha miaka kumi na moja, lakini kutokana na umbo lake kuwa dogo alionekana kama mtoto mdogo!

Hakuna aliyesikia kilio chake, alichokifanya ni kusogea karibu na mwavuli mkubwa wa makuti uliokuwa pembeni mwa ufukwe, pembeni mwa mwavuli huo kulikuwa na viti, alipofika kwa taabu sana akakaa kisha akayatupa macho yake ufukweni.

Ghafla macho yake yakatua katikati ya bahari, akajaribu kufikiria kwa muda, ni kama alihisi kitu, baada ya muda kidogo akili yake ilipofanya kazi ipasavyo, akakumbuka kuwa mahali alipokuwa aliwahi kufika siku nyingi kabla! Haikuwa kazi kubwa sana kufikiria kwa mtu mwenye akili kama yeye! Akafumba macho yake kisha akasafiri kiakili, alipofumbua tayari alikumbuka kila kitu!

Ni mahala hapo ndipo walipokuwa na wanafunzi wenzake wa Tanganyika International School, miaka kadhaa iliyopita, walipofika hapo kutembelea vivutio vya Marekani! Sasa akakumbuka kila kitu bara-bara, kuwa alitekwa na watu asiowajua, baadaye akapelekwa katika jumba asilolijua baada ya hapo hakukumbuka kitu kingine zaidi!

Muda wote aliokuwa nchini Japan, alikuwa akiishi kwa nguvu ya dawa, dawa iliyokuwa ikimpotezea kumbukumbu zote na kuwa mpya, ni dawa hizo ndizo zilizomfanya ashindwe kufahamu kilichokuwa kikiendelea. Alikumbuka kitu kimoja tu, kuwa aliwahi kufika hapo akiwa na wanafunzi pamoja na mwalimu wake Ngatengwa!

“Imekuwaje? Mbona sielewi, kuna nini lakini?” Akawaza. Lilikuwa swali gumu, lakini gumu zaidi kujibika kuliko ugumu wa swali lenyewe!

Wakati akiwa katika hali ya simanzi, upepo mkali ukawa unavuma kutoka baharini kuelekea nchi kavu, ghafla akasikia muungurumo mkali sana, baadaye mvua ikaanza kunyesha, mwanzoni ilianza kama manyunyu ambayo yangekatika baada ya muda mfupi lakini muda ulivyosonga, ndivyo mvua ilivyoongeza kasi na kuonyesha dalili ya kutokukatika kabisa.

Hakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kulia! Aliamini kulia ndio lilikuwa suluhisho la mwisho kwake, akasimama huku akitetemeka kwa baridi kali kisha akaanza kutembea ufukweni akifuata taa, zilizokuwa mbele yake. Hakuwa na matumaini ya kufika salama mahali hapo, alihisi baridi kali na viungo vyote vilikuwa vimekufa ganzi. Akiwa anatembea kwa woga ufukweni, mawimbi nayo yakija kwa kasi ya ajabu sana, kwa mbali akahisi kama muungurumo mkubwa uliombatana na upepo mkali, alipotazama kwa makini, alijua kilichokuwa kikitokea, maji yalikuwa yanarudi!

Kwa kasi ya ajabu akaanza kukimbia kutoka ufukweni, kupanda juu zaidi ili kukwepa hatari iliyokuwa mbele yake! Kwa baridi aliyokuwa akiisikia, mvua kubwa iliyokuwa ikimnyeshea akahisi kizunguzungu kikali, akiwa hatua chache kufika juu ambapo haikuwa rahisi maji kufika, akaanguka chini kisha akahisi vitu kama nyota nyota mbele yake! Maji yakawa yanakuja kwa kasi!

*********

Kila siku saa kumi kamili za Alfariji ilikuwa lazima walinzi wapite ufukweni Miami kuangalia usalama ulivyoendelea! Ilikuwa ni kawaida ya walinzi wa ufukwe huo kufanya hivyo kila siku! Siku hiyo pia walifanya hivyo, wakiwa walinzi sita wenye silaha wakagawana majukumu, watatu wakapita upande mwingine na wengine watatu wakapita upande wa pili!

Wakiwa wanaendelea na doria, wakaona kama kuna mtoto mdogo aliyekuwa akikimbia kwa kasi ufukweni, walishtuka sana, kila mmoja akashindwa kuelewa kilichokuwa kikiendelea mbele yao , ingawa kuna walioamini kuwa alikuwa ni mwanga anayepita au jini.

“Ni nini kile, kama mtu?” Mmoja akauliza.

“Lakini mbona kama ni mtoto? Inawezekana vipi mtoto mdogo kuwa huku saa hizi?”

“Labda ni jini, sio kimbwengo kile?” Mwingine akadakia.

“Inawezekana, lakini mbona anakimbia? Kuna kimbwengo anayekimbia?”

“Acha kuchekesha walionuna, kwanini asikimbie? Labda uulize kuhusu sababu za yeye kukimbia!”

“Lakini pamoja na yote, hebu tumfuatilieni!”

“Yule ni mtu…lazima iwe hivyo, kwa sababu nahisi anakimbia maji yanayorudi, sasa kama angekuwa ni kimbengo, alikuwa na haja gani ya kukimbia?”

“Ni kweli, hebu twende!”

Wote kwa pamoja wakatoka wakikimbia kumfuata, wakiwa karibu kabisa na kumfikia, yule mtoto akaanguka, wakati huo huo, maji yakawa yanaendelea kuja kwa kasi ya ajabu sana. Kama wangechelewa dakika tatu tu, wasingefanikiwa kumpata. Kwa kasi ya ajabu mlinzi mmoja akakimbia kisha akambeba juu juu na kukimbia naye nchi kavu, maji yalikuwa yanakuja kwa kasi, akafanikiwa kuyakimbia!

Wakatoka mpaka kwenye mwavuli mmoja kisha wakakaa na kumchunguza vizuri.

“Ah! Ni huyu mtoto?” Mmoja wao akashtuka.

“Kwani ana nini? Au unamfahamu?”

“Kwani wewe humfahamu?”

“Hapana!”

“Huyu ni Genesis anayetangazwa na vyombo vya habari kila siku kuwa alipotea hapa ufukweni na atakayempata aliahidiwa zawadi nono!”

“Ahaaaaa! Kweli bwana anafanana naye sana!”

“Sio suala la kufanana tu, bali huyu ndiye!”

“Sasa?”

“Sasa nini? Huu ni uchache!”

“Tunafanyeje sasa?”

“Hakuna kitu cha kufanya zaidi ya kwenda kutoa taarifa kwa Uongozi wa Hoteli kwanza kisha kwenda naye hadi kituo cha polisi ambapo tutapewa utaratibu wa kupata pesa zetu!”

“Sawa hakuna tabu!”

Walichokifanya ni kuwasiliana na wenzao waliokuwa upande wa pili ambao waliwaomba wawasubiri ili wamuone kama ndiye. Walionyesha kutoamini kabisa kuwa walifanikiwa kumpata Genesis, kutokana na kitita cha fedha kilichoahidiwa, Genesis alikuwa utajiri tosha!

Muda mfupi baadaye wakafika!

“Hebu tumuone, mmesema ni Genesis?”

“Ndio!” Wakawasha tochi kumuumulika usoni ili kuhakikisha, hawakujali mvua kubwa ya mawe iliyokuwa ikiendelea kunyesha!

“Ni kweli kabisa, ni yeye!”

“Sasa acha tuondoke!’

“Mnaelekea wapi?”

“Kwanza tunaenda kwa Mkuu wa Hotel, halafu baadaye tutaelekea polisi!”

“Sawa, kinachofuata?”

“Nini tena zaidi ya kupewa zawadi zetu?”

“Hilo tunafahamu, lakini vipi na sisi tutanufaika?”

“Tutakapopata hizo fedha tutajua!”

“Msitutenge bwana!”

“Hakuna tabu ndugu zetu, maadamu tulikuwa katika lindo moja, lazima nayi mpate sehemu yenu!”

Hawakuwa na muda wa kupoteza zaidi wakaondoka mpaka kwa Mkuu wa Hotel kisha wakaruhusiwa kuondoka na kwenda naye polisi! Kila mmoja alipingwa na butwaa!

“Mmmempata wapi?”

“Ufukweni!”

“Lakini mbona kama hajakua? Ni muda mrefu sasa amekuwa akitangazwa!”

“Ni kweli lakini umesahau kuwa walitangaza kuwa ni mgonjwa?”

“Tunashukuru sana kwa msaada wenu, tunaamini wazazi wake watafurahi sana kumpata mtoto wao tena, isitoshe heshima ya nchi yetu mtakuwa mmeirejesha!”

“Hiyo ni kweli, lakini vipi kuhusu zawadi yetu?”

“Msijali ndugu zangu, kesho jioni mfike hapa, kitu cha kufanya ni kutuachia majina yenu kisha kesho mje, kila kitu kitakwenda sawa, hiyo ilikuwa ahadi na ahadi siku zote ni deni!”

“Tunashukuru kwa kutambua hilo!”

Ndivyo ilivyokuwa, wakaacha majina yao kisha wakaondoka, Genesis akapelekwa hospitalini, ambapo alitibiwa mpaka asubuhi hali yake ilpokuwa sawa, hakuwa akikumbuka kitu chochote zaidi ya kumtaja mama yake!

Mashirika mbalimbali ya habari yakafika na kuzungumza na Genesisi, habari zikaenea kote duniani. Ndani ya saa kumi na nane tu, dunia nzima ilifahamu juu ya kupatikana kwa Genesis, hakuna aliyefahamu jinsi mtoto huyo alivyopatika! Kila mmoja alisema lake, ingawa wengi waliamini kuwa kulikuwa na mambo ya kishirikina!

*********

Kama ni machozi alishalia mpaka yakakauka! Alishafuatilia vyombo vya habari mpaka akachoka, hakuwa na matumaini ya kumpata Genesis tena! Kwake ulikuwa msiba mzito sana lakini uliopita! Aliamua kulikubali hilo kwa moyo wote, hakutaka kujipa presha tena!

Blandina alijua mwanaye alikuwa ameshakufa! Usiku wa kuamkia siku hiyo alikuwa na mawazo sana, alishangazwa na ndoto mbaya za kutisha alizoota usiku huo, alipoamka alikuwa mchovu sana, hakujua ni kwanini lakini alijikuta akitamani sana kuangalia TV asubuhi hiyo. Ndivyo alivyofanya, akatoka moja kwa moja mpaka sebuleni, alipofika akawasha TV yake kisha akatulia kwenye sofa na kuangalia kwa makini.

Dakika tatu tu, baada ya kufungua TV yake, Taarifa ya Habari ya Kituo cha CNN ikaanza kusomwa, habari ya kwanza kusomwa ilikuwa ni juu ya kupatikana kwa mwanaye Genesis. Mwanzoni hakuamini kama aliyezunguzwa alikuwa mwanaye, lakini alipoona picha ya Genesis akaamini! Zilikuwa habari za furaha zilizoleta huzuni kwa wakati mmoja!

“Nani Genesis mwanangu amepatikana? Siamini…” Akapaza sauti yake kisha akajikuta machozi yakitiririka machoni mwake.



Blandina alishazoea kuishi bila mwanaye, kila kitu aliamua kumuachia Mungu! Hakujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea kaika maisha ya mwanaye Genesis, hayo yote alimua kuachana nayo na kufanya kama sehemu ya historia ya maisha yake!

Mfariji wake mkubwa alikuwa ni Dk. Ringo, yeye ndiye aliyefanya maisha yake yawe yenye furaha bila mwanaye. Lakini siku moja, kikatokea kitu cha ajabu sana katika maisha yake, akiwa yupo sebuleni anaangalia TV akaona habari zilizounganishwa na kituo cha CNN kuwa Genesis alipatikana ufukweni Miami.

Furaha aliyokuwa nayo haikuwa rahisi kuainishika! Kitu cha kwanza kufanya ilikuwa ni kumpigia simu Dk. Ringo na kumweleza, baada ya hapo akapigiwa simu na Mkuu wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika ambaye alimpongeza, kisha baadaye akaenda Wizara ya Elimu, ambao bila kusita walimpa tiketi ya kwenda Marekani kwenda kumfutilia mwanaye.

Akiwa amezungukwa na vyombo mbalimbali vya habari vya Kimataifa, Blandina anakutanishwa na mwanaye tena! Macho yake yanabubujikwa na machozi, Genesis naye analia!wakakimbiliana ili wakutane katikati! Nini kitaendelea? SONGA NAYOÖ



Kila mtu alikuwa akiwaangalia Blandina na mwanaye Genesis kwa masikitiko makubwa sana! Hakuna aliyekuwa tayari kuamini kuwa ni kweli Genesis alipatikana na mama yake alikuwa nchini Marekani kwa ajili ya kumchukua! Baadhi ya watu hasa wakinamama walishindwa kuvumilia na kujikuta wakuungana na Blandina kulia. Ilikuwa furaha ambayo maelezo yake hayakuwepo!

“Mama!” Genesis akaita.

“Mwanangu!”

“Siamini mama!”

“Unapaswa kuamini mwanangu!”

“Siamini kama siku moja ningeweza kuonana na wewe tena!”

“Wewe huwezi kuamini, lakini Mungu anaweza kupanga kila kitu na hakuna binadamu ambaye anaweza kupanga tofauti! Najua umechoka na umeteseka sana, huu ni wakati wako wa kufurahi tena, usijali mwanangu, mimi mama yako ninayekupenda nitakuwa nawe mpaka mwisho wa maisha yako!”

“Nashukuru mama kusikia hivyo!”

“Hata mimi pia!”

“Mama!”

“Bee mwanangu!”

“Kuna kitu nataka kukuambia!”

“Kitu gani hicho mwanangu?” Macho ya Blandina yaliongea anachomaanisha. Alikuwa na woga uliongia moyoni mwake ghafla. Kuna kitu alianza kuhisi, kitu kibaya! Hakika kulingana na kauli ya mwanaye alikuwa na kila sababu ya kuhisi kuwa kulikuwa na kitu kibaya kilichokuwa mbele yake.

“Nakupenda sana mama!”

“Nashukuru kusikia hivyo Genesis wangu, nina imani kama kungekuwa na darubini ya kuangalia ndani ya moyo wangu, bila shaka mapenzi niliyonayo dhidi yako yangeonekana, ila kwa sababu hakuna, nakuomba uamini kuwa nakupenda, shahidi wa hili ni Mungu wa Mbinguni peke yake!” Blandina alizungumza kwa sauti ambayo ilitia huruma sana.

“Ahsante mama!”

Wakati hayo yote yakitokea, Waandishi wa Habari walikuwa makini sana kuchukua kila kitu, zilikuwa habari kubwa sana kwao, ilikuwa lazima wafanye kazi yao kwa umakini mkubwa sana, ili kuweza kupata vichwa vya habari vitakavyotalawala katika vyombo vyao.

Kila kitu kilirekodiwa, maneno yote waliyokuwa wakizungumza Blandina na mwanaye Genesis yalirekodiwa na vinasa sauti maalum. Pilikapilika zikaendelea, hatimaye Balozi wa Tanzania nchini Marekani, akakaribishwa kuzungumza mawili matatu.

“Kwanza kabisa napenda kumpa pole sana mama Genesis, pia kumpongeza kutokana na uvumilivu wake, sitakuwa na mengi ya kusema zaidi ya kuwashukuru viongozi wa Serikali ya Marekani kuweza kumtafuta mtoto huyu kwa nguvu na bidii zote mpaka matokeo haya yaliyopatikana leo kuonekana!

“Kwa niaba ya wenzangu namkabidhi Blandina mwanaye Genesis leo, na ninamuahidi kuwa Serikali ya Tanzania, bado itaendelea kumpatia elimu kama ilivyokuwa ikifanya awali kabla ya kutekwa katika fukwe za Miami.

“Hakuna kitu cha zaidi, nina imani hata Waandishi wa Habari wameshatimiza kile walichokusudia kukifanya tena kwa ukamilifu wa hali ya juu! Genesis na mama yake, watakuwa hapa kwa mapumziko ya siku mbili kabla ya kurejea nyumbani Tanzania baada ya siku hizo, kutokana na hilo dakika kumi na tano kutoka sasa, nitaondoka nao kwenda ubalozini kwa ajili ya mapumziko hayo!” Alimaliza kuzungumza Balozi wa Tanzania nchini Marekani aliyeitwa Ramadhani Babotwa.

Msafara wa kwenda Ubalozi wa Tanzania nchini humo ukaanza.

*********

Maandalizi ya mapokezi ya Genesis na mama yake Blandina yaliendelea nchini Tanzania, Serikali na Wizara ya Elimu ilikuwa na hamu kubwa sana ya kumuona tena mtoto mwenye kipaji cha hali ya juu nchini Tanzania, Genesis alikuwa utajiri wa Tazania! Kumpata kulimaanisha utajiri uliopotea ulikuwa umerejea!

Upande wa Tanganyika International School waliandaa mapokezi makubwa sana kwa ajili yao, lakini mapokezi makubwa zaidi yalikuwa ya kitaifa ambapo ilikuwa lazima wapitie Ikulu kabla ya kufanya kitu chochote! Maandalizi yakaendelea kama kawaida! Ikiwa ni siku moja kabla ya Blandina na mwanaye kufika nchini Tanzania, kulikuwa na kikao cha uongozi wa wizara ya elimu juu ya ujio wao. Kilikuwa kikao kizito sana!

“Kesho wanakuja, kama tulivyokubaliana ni lazima tuhakikishe mipango yetu inaenda kama kawaida!” Mwenyekiti wa Mkutano huo Moses Alhendo alisema.

“Hakuna tabu Mwenyekiti, kila mmoja anafahamu majukumu yake, vinginevyo kuwe na ratiba nyingine mpya, kama ni ile ile basi itaenda kama ilivyopangwa!”

“Nashukuruku sana kusikia hivyo, bila shaka hakuna asiyefahamu umuhimu wa mtoto huyo katika nchi yetu, sasa hatuna budi kuonesha ni jinsi gani tunavyomthamini na kumpenda nchini mwetu!”

“Ni kweli kabisa Mwenyekiti!”

Ndivyo ilivyokuwa, vombo mbalimbali vya habari nchini Tanzania na nchi nyingine, zilitangaza juu ya kupatikana kwa Genesis lakini pia vilitangaza juu ya ujio wao nchini Tanzania, kila Mtanzania alikuwa na hamu kubwa sana ya kuona mapokezi ya mtoto mwenye kipaji Genesis.

Maandalizi yalipokamilika walikaa tayari kuwasubiri wageni wao.

********

Furaha aliyokuwa nayo Blandina haikuweza kuelezeka kirahisi! Hapakuwa na kitu kingine chochote ambacho kingeweza kurudisha furaha yake kama Genesis, kupatikana kwake kulimaanisha furaha kurudi upya! Kila alipokuwa akimwangalia mwanaye machozi yalitiririka machoni mwake, alimpenda kuliko kitu chochote duniani, kwake alikuwa ni kila kitu!

Walifanyiwa sherehe kubwa sana ubalozini kisha wakaanza maandalizi ya safari ya kurejea nyumbani Tanzania ambako pia kulipangwa kufanyika sherehe kubwa zaidi . Balozi na wafanyakazi wengine wa ubalozini walifurahi sana.

“Lakini kwa anavyosema, anakumbuka alipokuwa?” Balozi akamuuliza Blandina.

“Hapana hakumbuki kitu chochote!”

“Yaani kwa miaka yote hiyo saba, hajajua kitu chochote?”

“Hata mimi nashangaa, nahisi kuna kitu kibaya kilikuwa kinafanyika!” Blandina alisema huku machozi yakianza kumlengelenga machoni mwake!”

“Huna sababu ya kufikiria hivyo, unapaswa kutulia na kumuomba Mungu, ni yeye peke yake mwenye uwezo wa kukufunulia kila kitu kinachotokea, huna haja ya kupaniki!”

“Nashukuru sana Balozi!”

“Nashukuru pia kwa kuwa mvumilivu mpaka wakati huu, hakika wewe ni mvumilivu sana, Mungu amekupa moyo wa uvumilivu, moyo ambao ni wanawake wachache sana wanaoweza kuwa nao!”

Sidhani kama ndivyo, ila kama ndivyo basi Mungu ahimidiwe!” Ilikuwa ni siku ya kihistoria kwao, walizungumza mpaka saa sita usiku, kila mmoja akiwa na shauku na ya kuzungumza na Genesis, kwa balozi ilikuwa kazi ya kitaifa aliyopaswa kuifanya kwa uangalifu wa hali ya juu sana. Hatimaye ilipotimu saa saba na nusu Blandina na Genesis wakaingia chumbani kwao kulala!

Saa kumi na mbili na dakika arobaini na tisa Blandina aliamka, alichokifanya ni kumuamsha mwanaye na kumuandaa kisha kuandalia kifungua kinywa na kujumuika mezani. Saa mbili kamili walikuwa barabarani wakienda Uwanja wa Ndege tayari kwa safari ya kwenda Tanzania.

“Mfike salama!” Mmoja kati ya wafanyakazi wa Ubalozi waliowasindikiza alisema.

“Ahsante sana, mbaki salama pia!”

“Ahsante Mungu akipenda tutaonana wakati mwingine!”

“Amen!” Bila kupoteza muda wakaingia katika Chumba cha Ukaguzi kabla ya kuingia ndani ya ndege kwa safari.

Saa tatu kasorobo ndege iliacha ardhi ya Hawaii na kupaa tayari kwa safari ya kuelekea nchini Nairobi kabla ya kupanda ndege nyingine itakayowafikisha Dar es Salaam.

Kwao ilikuwa safari ya ushindi! Machozi yao yalifutika, Kilichokuwa mbele yao ni kumshukuru Mungu kutokana na mambo makuu ambayo yametokea katika maisha yao. Walitumia muda mwingi kuzungumza kwa furaha, lakini wakiwa katikati ya safari, Blandina alisinzia, baadaye kidogo akapitiwa na usingizi kabisa!

Muda wote Genesis alikuwa macho, akamwangalia mama yake kwa macho yaliyojaa simanzi, baadaye akashangaa kuona kitu cha ajabu sana kwa mama yake.

Shingo ya Blandina iliangukia upande mmoja, kisha ute mwepesi ukaanza kutoka mdomoni mwake! Genesis akashtuka sana, akaanza kumuamsha.

“MamaÖmamaÖmama!” Aliita lakini Blandina hakushtuka!

“Kuna nini?” Genesis akawaza.

“Hapana kuna tatizo hapa!” Baadaye akajijibu mwenyewe.

“MamaÖmamaÖmamaaaaaaa!” Akazidi kupaza sauti lakini Blandina hakushtuka.

“Kuna nini?” Mhudumu wa ndege akamuuliza Genesis.

“Mama yangu!”

“Amefanyaje?”

“Njoo umuone!” Haraka Mhudumu akaenda mpaka walipokuwa wamekaa Blandina na Genesis. Alipofika akamwangalia kisha akaonyesha kushtuka sana.

“Mungu wangu!” Akasema na kukimbia kumfuata muhudumu mwinmgine ili wasaidiane!

*****

Alipoangalia saa iliyokuwa kwenye simu yake ya mkononi ilionyesha kuwa ilikuwa tayari imeshafika saa nane na dakika ishirini za usiku, jasho lilizidi kumtoka kwa hofu, alishatembea umbali mrefu bila kumuona mwanaye, moyo ukazidi kwenda mbio, ilikuwa lazima ampate mwanaye, maisha yake bila yeye yasingeweza kukamilika, ni yeye pekee ndiye angeweza kurejesha furaha iliyotoweka katika maisha yake.

“Haiwezekani, lazima nimpate, hata kama ni usiku na mapori yote haya, lakini nitahakikisha nampata mwanangu!” Aliwaza.

Hakuchoka kutembea, ingawa alisikia milio ya ajabu ajabu ikisikika kutoka kila kona ya msitu huo hatari, alikuwa katikati ya msitu wa Ambuje uliopo nje ya mji wa Kigoma, hakuweza kuelewa mahali amabapo angempata mwanaye.

Huyu ni Blandina aliyekuwa akimsaka mwanaye mpenzi Genesis, ilikuwa lazima ampate. Hakukata tamaa, ingawa alimtafuta kila mahali bila mafanikio. Baada ya kupewa taarifa kuwa alikuwa amepatikana Kigoma, aliamua kumfuatilia na akabahatika kumpata. Kwa furaha aliyokuwa nayo akaamua aende naye akatembee katika uoto wa asili wa msitu wa Ambuje. Huko ndipo aliposhangaa kuona Genesis akipotea ghafla!

Machozi yakazidi kumtoka, ingawa alikuwa akimtafuta kuanzia saa kumi na mbili za jioni alipotoweka bila mafanikio, lakini aliendelea kuifuata njia nyembamba iliyokuwa katikati ya msitu akimsaka mwanaye bila mafanikio!

Akiwa amekwishakata tamaa kabisa, akaamua kuketi chini ya mti mmoja mrefu sana, ikiwa ni dakika moja tu tangu alipokaa, akaamua kufumba macho kwa nia ya kujipumzisha kidogo. Ghafla akahisi kama kuna kitu kinatembea jirani na mahali alipokuwepo. Akafumbua macho mara moja, heeh! Akashtuka sana!

“Usishtuke, subiri hivyo hivyo!” Sauti yenye mngurumo kutoka kwa bibi aliyekuwa mbele yake ilisikika.

Haikuwa rahisi Blandina kutoshtuka, ilikuwa lazima ashtuke kutokana na hali halisi iliyokuwa mbele yake, hakuwahi kukutana na bibi mzee kama aliyekuwa mbele yake, alishtuka sana, hakuweza kumuangalia mara mbili usoni mwake, alikuwa mzee aliyevalia gauni refu jeupe, uso wake ulipambwa na tabasamu maridhawa lililomfanya Blandina azidi kuchanganyikiwa.

“Wewe ni nani?” Blandina akauliza kwa tabu.

“Huwezi kunijua!”

“Kwanini?”

“Kwasababu huwezi!”

“Unafanya nini hapa?”

“Hapa ni kwangu, tena mimi ndio ninayetakiwa kukuuliza wewe unafanya nini hapa kwangu, huku ni kwangu!”

“Siwezi kukuambia!”

“Hata kama usiponiambia tayari nimeshajua kilichokufanya uwe hapa!”

“Unaweza kuniambia?”

“Ndio!”

“Ni nini?”

“Unamtafuta mwanao Genesis!”

Moyo wa Blandina ukapiga kwa nguvu puuu! Hapo sasa ikabidi asimame ili amuulize zaidi, aliamini kwa namna yoyote, yule bibi angeweza kumsaidia! Akamsogelea taratibu, kisha akapiga magoti chini yake, akiwa anahema kwa kasi.

“Kwanza naomba unisamehe kwa kukuingilia nyumbani kwako bila taarifa, lakini bibi nahitaji sana msaada wako!”

“Msaada gani?”

“Nahitaji kumpata mwanangu!”

“Hakuna tabu, najua mahali yupo, nifuate!” Alipomaliza kusema maneno hayo tu, yule bibi akaanza kupiga hatua kuelekea katikati ya msitu, hapakuwa na mtu yeyote waliyekutana naye, zaidi ya fisi na wanyama wengine wakali, lakini kitu cha ajabu ni kwamba hawakuwagusa kabisa.

“Bibi, mbona kuna wanyama wakali lakini hawatugusi?”

“Ondoa shaka, hawa wote ni wangu!”

“Unamaanisha nini?”

“Hawawezi kutugusa kwa sababu siku zote naishi nao hapa porini!” Blandina hakuwa na maswali zaidi, wakazidi kusonga mbele mpaka walipoona nyumba moja kubwa iliyokuwa katikati ya msitu, kwanza hakuamini kama ndani ya pori kama lile kungeweza kuwa na nyumba nzuri kama ile.

Kitu cha ajabu zaidi, nje ya nyumba kuliwaka makarabai makubwa yaliyomulika eneo lote la nyumba hiyo, walipoikaribia nyumba hiyo, bibi akasimama na kumgeukia Blandina.

“Mwanao yumo humo ndani!”

“Anafanya nini?”

“Wote hatujui, kwa hiyo tuingie tuone!”

“Hakuna tatizo!” Mara moja wakaingia, walipoingia ndani tu, Balndina akashangaa kutoona nyumba tena, kulikuwa na eneo kubwa ambalo halikuweza kuonekana mwisho wake. Mwanga ulikuwa hafifu ambao haikuwa rahisi kuona kitu kilichopo mbele yako.

“Bibi!” Alipomwita akasikia sauti yake upande wa pili kama mwangwi.

“Unasemaje?” Sauti ya bibi ikageuka ya kiume, tena nzito iliyotisha.

“Mbona hivyo?”

“Si unamtaka mwanao, simama hapo hapo!” Akasimama, ghafla akaona watu wanne wanakuja eneo walilosimama na Bibi yule, wakiwa wamembeba mtoto mdogo, ghafla akasikia sauti ya Genesis ikiita kwa sauti kubwa.

“Mama!”

“Genesis mwanangu!” Kabla hajateremshwa chini, Blandina akataka kwenda kumchukua, kabla hajafanya hivyo akapigwa kibao kimoja katikati ya uso wake na kuanguka chini.

Alipofumbua macho akamuona mwanaye akilazwa chini, baada ya muda kidogo panga lenye makali pande zote likapita katikati ya koo la mwanaye, Blandina akasisimkwa moyo sana, machozi yakamtoka machoni mwake.

“Noooooooooo! Hamuwezi kufanya hivyo….” Blandina akasema kisha akawasogelea wale watu waliokuwa wakimchinja Genesis, tayari damu zilishaanza kumwagika, kabla hajafanya hivyo, naye akashikwa na kufungwa kamba mikononi na miguuni kisha akalazwa chini, punde panga lenye makali pande zote mbili, likawa linashuka kwenye koo lake.

“Nakufaa…..” Akapiga kelele, lakini wachinjaji wakaendelea.

*********

Pilikapilika za kuwapokea Genesis na Blandina ziliendelea kama kawaida nchini Tanzania, walikuwa na hamu kubwa sana ya kuonana na Genesis tena, alikuwa ndio faraja pekee kwa nchi ya Tanzania, waliamini kwa kutumia akili yake angeweza kufanya mambo makubwa sana.

Maandalizi yalikuwa makubwa sana, Ikulu iliandaliwa kwa ajili ya kumpokea shujaa, kila mmoja alikuwa na furaha sana, matangazo yalitangazwa katika vyombo vya habari yakihimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Ndege kumpokea Genesis, watu walihamasika na walikuwa tayari kumpokea Genesis akiwa na mama yake.

Kati ya watu waliokuwa Uwanja wa Ndege wakimsubiri Genesis kwa hamu alikuwa ni Mama Gibson, Mkuu wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika akiwa na Mwalimu Ngatengwa ambaye ndiye alikuwa mkuu wa msafara wa safari ya wanafunzi walipokwenda nchini Marekani.

“Nina hamu sana ya kumuona Genesis mwalimu!” Mwalimu Ngatengwa alisema.

“Hata mimi!” Mama Gibson akadakia.

“Kama asingepata matatizo, sasa hivi angekuwa ameshafika darasa la sita!”

“Kweli kabisa mwalimu, miaka saba ni mingi sana!”

“Tusubiri, si wamesema saa moja ijayo watakuwa wamefika!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Hata mimi nimesikia hivyo!”

Wakaendelea kusubiri wakiwa na hamu ya kuonana tena na Genesis, alipanga kufanya sherehe kubwa shuleni. Lakini kabla ya sherehe ya shule haijafanyika, ilikuwa lazima sherehe kubwa ianzie Ikulu.

*********

Genesis aliendelea kulia huku akimtingisha mama yake kwa huzuni, muda huo huo, wakatokea wahudumu wawili waliokuwa na machela, wakamlaza na kumkimbiza katika chumba cha huduma ya kwanza. Walimpofikisha tu, haraka daktari akaanza kumpima ili kuangalia kilichompata, lakini ghafla Blandina akashtuka na kupiga kelele.

“Noooooooo!”

“Kuna nini?” Mhudumu mmoja akamuuliza. Blandina hakuweza kujibu, bado alikuwa ameduwaa.

“Yuko wapi Genesis wangu?”

“Huyu hapa!” Wakamwonyesha. Alichokifanya ni kumkumbatia Genesis huku akitetemeka kwa hofu, akajaribu kumkagua shingoni mwake kama alikuwa na alama za panga, lakini hazikuwepo. Ni muda huo huo, aligundua alikuwa katikati ya ndoto ya kutisha.

“Unajisikiaje?”

“Mh…mhhhmmm!” Blandina akaendelea kupumua kwa kasi, hakuamini kama mwanaye alikuwa mzima.

“Mama!”

“Mwanangu!”

“Nini kilikupata?”

“Nilikuwa kwenye ndoto kali!” Kila mmoja alishangaa.





Hatimaye furaha ya Blandina ilirejea tena, ni Genesis ndiye aliyerejesha furaha yake iliyokuwa imetoweka! Mateso aliyoyapata katika maisha yake yalikuwa yanatosha, hakutamani kuendelea kuteseka zaidi! Pamoja na maisha ya kifahari aliyokuwa akiishi Masaki lakini hakuyafaidi bila mwanaye!

Baada ya kupewa mtoto wake nchini Marekani, safari ya kwenda Tanzania ilianza. Baada ya mazungumzo ya muda mrefu safarini, hatimaye baadaye alisinzia kisha akalala na kuangusha shingo yake upande mmoja, ute ukawa unachukuruzika kinywani mwake.

Hali hiyo ilimshtua sana mwanaye Genesis ambaye haraka aliwaita wahudumu ambao walimpeleka ndani ya Chumba cha Huduma ya Kwanza, ikiwa ni nukta chache tangu daktari aanze kumpima ili aweze kujua nini kimempata, Blandina akazinduka na kupiga kelele! Hakuna aliyejua kilichotokea, ila Genesis alipomuuliza alimwambia alikuwa katika ndoto mbaya! Nini kitatokea? SONGA NAYO…



Wahudumu wa Ndege na daktari walibaki wamesimama wakishangaa kilichotokea, Blandina alikuwa katika hali mbaya, kwa alivyoonekana mwanzoni alihitaji huduma ya kitabibu haraka sana, lakini wakashangazwa na kitendo cha kushtuka tena akiwa analia machozi. Alikuwa kama amepigwa bumbuwazi, haikuweza kueleweka mara moja alipatwa na nini.

Genesis alikuwa ubavuni mwa mama yake huku akilia kwa uchungu, kila Blandina alipomwangalia mwanaye machozi yalizidi kumiminika, ndoto aliyoota ilimshtua sana, hakutaka mwanaye afe kifo cha aina ile, alimpenda sana Genesis, alikuwa kila kitu katika maisha yake.

“Mama tafadhali, naomba uniambie, kuna nini?” Genesis alimsisitiza mama yake amweleze ukweli wa kilichotokea.

“Hakuna kitu mwanangu!”

“Hapana mama, lazima utakuwa mgonjwa!”

“Niamini siumwi mwanangu!”

“Sasa kama huumwi, mbona ulikuwa umezimia na ulikuwa huongei?”

“Sikuzimia mwanangu!”

“Sasa kumbe nini?” Genesis alikuwa na maswali magumu sana. Mama yake akamwangalia kwa macho yaliyojaa huzuni kisha akamwambia;

“Geneses!”

“Mama!”

“Wewe ni mdogo sana kufahamu kinachoendelea, fahamu kitu kimoja tu, nilikuwa kwenye njozi mbaya!”

“Sawa…” Genesis alikubali ingawa upande mmoja ulimwambia kitu fulani. Hata hivyo kwa umri wake na uwezo wake wa akili halikuwa jambo la ajabu sana kwa Genesis kuhisi kuwa kulikuwa na kitu kilichoendelea ambacho mama yake alificha.

Baadaye kidogo, daktari aliwataka wahudumu na Genesis watoke nje ya chumba hicho ili aweze kupata nafasi ya kuzungumza naye. Hakuna aliyebisha, wote walitoka nje na kuwaacha daktari na Blandina pekee.

“Vipi unajisikiaje sasa?”

“Najisikia vizuri!”

“Una ugonjwa wa kuzimia?”

“Hapana, sijawahi kuzimia tangu kuzaliwa kwangu!”

“Sasa ni nini kilitokea?”

“Ni njozi mbaya tu, siwezi kukuhadithia, kwa sababu inatisha sana, hakuna zaidi ya hilo!”

“Pole sana!”

“Nashukuru!”

“Ila unahitaji kupumzika kwa muda kidogo, mpaka utakapokuwa sawa!”

“Ahsante sana Dokta!”

Baada ya daktari kuridhika na hali ya Blandina, alimpatia kitanda kwa ajili ya kupumzika kwa muda mpaka hali yake itakapokuwa nzuri. Muda mfupi baadaye Blandina alitulia na kuwa katika hali ya kawaida! Hakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kurejea kwa kwa mwanaye.

“Lakini mama, ni ndoto gani hiyo ambayo huwezi kunisimulia?”

“Nitakusimulia tukifika nyumbani!”

“Nitafurahi kufahamu!”

*********

Saa nne na dakika ishirini na tano za asubuhi, Ndege ya Shirika la Ndege la Kenya, ilikuwa inatua katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, tayari maandalizi ya kumpokea shujaa Genesis yalikuwa yamekamilika, kila mmoja alikuwa na furaha na hamu ya kutaka kumuona mtoto huyo wa ajabu.

Kabla ya abiria wengine kuanza kushuka, alitangulia Genesis kisha akafuata mama yake, Blandina, vigelegele na makofi ya furaha yalitawala, Waandishi wa Hahari hawakutaka kupitiwa na tukio hata moja, kamera zilikuwa tayari kunasa kila kila kilichoendelea.

Aliposhuka moja kwa moja alielekezwa kwenye gari la wazi ambapo maandamano ya kwenda Ikulu yalianza. Njia nzima alikuwa akipungia watu mikono, shangwe kila mahali gari lilipopita zilitawala, kila mmoja alishangalia!

Kitu kilichowachanganya wengi ni kutokana na umbo la Genesis kutokuwa kubwa, hakuwa na mabadiliko yoyote zaidi ya mwonekano wa sura yake kuanza kuwa na mvuto kidogo tofauti na zamani, ilikuwa kazi ya Japan, baada ya kumwingiza katika Jumba la Utafiti wa Sayansi, walimkarabati sura yake! Hilo liliwashangaza wengi.

Njia nzima alikuwa na kazi ya kupunga mikono kwa watu waliojipanga barabarani kumshangilia. Dakika arobaini na tano baadaye, waliingia Ikuku. Kulikuwa na viongozi wa juu wa serikali pamoja na wa ngazi za chini, walimu wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika na viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali walioalikwa walikuwa ndani ya Ikulu kwa ajili ya tafrija fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya Genesis.

“Tunayo furaha kubwa sana kumpata shujaa wetu aliyepotea, alipotea katika mazingira tatanishi sana, lakini tunaamini kutokana na nguvu za Mungu amepatikana tena!” Alikuwa ni Mkuu wa Nchi akizungumza na waalikwa.

“Yaliyotokea hayaanishi kukatisha tulichokusudia kufanya katika maisha ya Genesis, bado ataendelea kusoma, ila atakuwa chini ya uangalizi mkali wa serikali. Huyu ni shujaa wa nchi, ni kiongozi hodari wa kesho, lazima tumlinde kwa nguvu na uwezo wetu wote!” Ukumbi mzima ukashangilia kwa furaha.

Ilikuwa furaha isiyokuwa na maelezo, sherehe ziliendelea mpaka usiku ambapo watu walitawanyika, Genesis na mama yake walipelekwa nyumbani kwao Masaki kwa gari maalum. Walipofika hawakuwa na kitu kingine zaidi ya kulala, walikuwa wamechoka sana.

Siku iliyofuata, Blandina aliamka asubuhi na mapema kisha akaanza kufanya usafi na kuandaa kifungua kinywa. Baadaye akaamua kuketi sebuleni kuangalia TV. Akiwa hapo, ghafla mawazo yake yakahama, yalikwenda mpaka Ifakara ambapo alianza kumkumbuka Dk. Ringo, katika hali ya ajabu sana moyo wake ukaanza kwenda mbio, akahisi kuna jambo limetokea.

Alichokifanya ni kupiga simu yake ya nyumbani, lakini haikupokelewa, muda huo huo akajaribu kupiga simu yake ya mkononi, nayo pia haikupatikana! Akahisi jambo.

“Kuna nini?” Akajiuliza bila kupata jibu.

“Wacha nimpigie Dk. Mkambila anaweza kuniambia jambo fulani, haiwezekani mwanangu aje nchini halafu asifahamu!” Akawaza kisha akabonyeza namba za Dk. Mkambila, kwa bahati nzuri simu yake ilikuwa inapatikana.

“Habari za asubuhi Dk. Mkambila!”

“Salama dada Blandina, habari za Dar es Salaam!”

“Ni nzuri, huna tarifa kuwa jana nilikuja na mwanangu?”

“Nimesoma kwenye magazeti, si mlikuwa na sherehe Ikulu jana?”

“Ndio, mbona hukuja kutupokea?’

“Mambo yaliingiliana dada yangu!”

“Hata kunipigia simu?”

“Nilipitiwa, naomba unisamehe!”

“Usijali, vipi kuhusu Dk. Ringo?”

“Amekwenda kufanya Utafiti wa Malaria!”

“Wapi?”

“Malugiro!”

“Kurudi!”

“Alisema atarudi leo, lakini mpaka sasa bado hajafika!”

“Leo hii jioni nitakuwa huko, nahitaji kuonana naye!”

“Karibu sana, nitakupokea kituoni!”

Ndivyo ilivyokuwa, muda mfupi tu, baada ya kukata simu akaenda chumbani kwa Genesis kumuamsha. Alionekana mchovu sana, lakini usoni mwake kulijaa tabasamu pana sana.

“Shikamoo mama!”

“Mar-haba malaika wangu, unajisikiaje?”

“Furaha! Nina furaha sana mama. Furaha ya kuwa na wewe tena, nahisi kama nipo kwenye njozi!”

“Amini mwanangu, sasa nikuambie kitu utakachokifurahia?”

“Niambie mama yangu mpenzi!”

“Leo tunakwenda kwa Uncle Ringo Ifakara, nimemkumbuka sana, ni muda mrefu sijaenda kumwangalia!” Blandina alisema huku akitabasamu.

“Kweli mama? Nimefurahi sana kusikia hivyo!” Genesis akasema. Hawakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kujiandaa. Saa tatu na nusu tayari walikuwa ndani ya basi la Kedikose kwa safari ya kwenda Ifakara.

*********

Kama Dk. Mkambila alivyoahidi ndivyo ilivyokuwa, waliposhuka kwenye basi aliwapokea kwa furaha, wakaenda moja kwa moja mpaka nyumbani. Mkambila alifurahi sana kumuona Genesis tena. Kwa kuwa Dk. Ringo hakuwepo, ilibidi waende nyumbani kwa Dk. Mkambila.

“Karibu sana dada!”

“Nashukuru sana, kwa hiyo huenda akaja leo!”

“Kama itakuwa kama alivyoahidi!”

“Nitafurahi sana kumuona!” Walizungumza mambo mengi mpaka muda wa kulala ulivyofika na kuingia vyumbani kupumzika.

Usiku wa saa tano mlango wa Dk. Mkambila ulikuwa unagongwa, Dk. Mkambila hakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi kufungua, baada ya kufungua mlango alikutana na Dk. Ringo akiwa na hali mbaya sana, alikuwa akihema kwa kasi huku jasho jingi likimchuruzika!

“Kuna nini Dk.?”

“Naumwa!”

“Nini?”

“Malaria!”

“Pole sana, ngoja nimuamshe Blandina twende hospitalini!”

“Blandina? Amekuja lini?”

“Leo, tena amekuja na Genesis!”

“Fanya hivyo haraka tafadhali, hali yangu inazidi kuwa mbaya!” Dk. Mkambila hakuwa na kitu kingine zaidi ya kuingia ndani haraka na kumuamsha Blandina haraka, alipotoka hakuamini hali aliyomkuta nayo Dk. Ringo. Hali yake ilizidi kuwa mbaya na hakujiweza kabisa. Hata kuongea kulimshinda!

Kitu kilichokuwa mbele yao ni kumfikisha hospitalini haraka, walimuaga msichana wa kazi wa Dk. Mkambila na kuondoka haraka kwenda hospitalini.

Walifika hali ya Dk. Ringo ikiwa mbaya zaidi, alikimbizwa moja kwa moja mpaka katika chumba cha wagonjwa maalum, lakini nusu baadaye Daktari aliyekuwa akimshughulikia alitoka nje na kuwakuta Blandina na Dk. Mkambila wamekaa kwenye benchi. Uso wake ulionyesha huzuni sana.

“Hebu njoo kidogo ndugu yangu!” Dk. Akilimali akamvuta pembeni Dk. Mkambila.

“Huyu mgonjwa ni nani yako?”

“Ni rafiki yangu wa karibu sana!”

“Na yule dada ni mkewe?”

“Hapana, ila ni ndugu yake! Kwani kuna nini?”

“Wewe ni mwanaume, huna budi kukubalina na kilichotokea, kwa sababu hata hivyo hatuwezi kubadilisha ukweli huo!”

“Kuna nini? Niambie basi!”

“Dk. Ringo ame….”

“Amefariki, haiwezekani….” Dk. Mkambila hakutaka kumpa nafasi Dk. Akilimali amweleze kilichotokea. Kwa jinsi alivyoanza sentesi yake, aliamini Dk. Ringo alikuwa ameshakufa.

****

Katika ubongo wa Dk. Mkambila, kulishatawaliwa na matatizo! Alijua tayari mambo yalishakuwa mengine, haikuwa hali ya kawaida kuitwa na daktari pembeni tena kwa sauti ya kusihi kama kunakuwa hakuna matatizo makubwa. Kwa uzoefu wake yeye, aliamini kuwa habari ambazo angepewa zisingeweza kusikilizika!

Kwa kuyatizama tu macho ya Dk. Akilimali, alishajua kulikuwa na matatizo, lakini kubwa zaidi lililomchanganya ni kuambiwa kuwa yeye ni mtoto wa kiume kwa hiyo asishtushwe na habari ambazo alipanga kumwambia.

“Nooooooo! Haiwezekani dokta, hebu niambie vizuri, nini kimempata Dk. Ringo?”

“Naomba utulie dokta, kubaliana na ukweli uliopo kwa kuwa hata hivyo hatuwezi kuubadilisha ukweli wenyewe, Dk. Ringo amefariki dunia!”

“Amefariki?” Dk. Mkambila akauliza kwa sauti kubwa.

“Ndio, naomba ujikaze, najua ni kiasi msiba huu ulivyo mkubwa kwako lakini piga moyo konde ndugu yangu!”

Dk. Akilimali aliendelea kumsihi Mkambila apunguze jazba na akubaliane na matokeo, kutokana na sauti yao kuwa kubwa, Blandina aliweza kusikia baadhi ya maneno, lakini neno moja ambalo aliweza kulinasa vizuri ni kuwa Dk. Ringo alikuwa amefariki! Alichokifanya mara moja ni kuondoka haraka mahali alipokuwa ameketi na kuwafuata Dk. Alimali na Mkambila.

“Daktari hebu niambie vizuri, nimesikia kama mkizungumza Dk. Ringo amefariki, ni kweli?”

“Huo ndio ukweli dada yangu, lakini nawasihi mtulie, hakuna jinsi!”

“Ringo amefariki? Mungu wangu, hakustahili kufa mapema kisi hiki kabla hajamuona mwanangu aliyepotea kwa miaka yote saba? Kwa nini Mungu umemchukua jamani…” Blandina alipiga kelele huku machozi yakitiririka machoni mwake kama mfereji mdogo wa maji.

Hapakuwa na kitu kingine zaidi ya kukubalina na ukweli halisi uliokuwepo! Wakaongozana pamoja mpaka ndani, ambapo walimwangalia Dk. Ringo akiwa amelala kitandani, alikuwa amefumba macho yake, hajigusi wala hatingishiki! Dk. Ringo alikuwa amekufa!

Baadaye wakaondoka na kurudi nyumbani, kila mioyo yao ilitawaliwa na huzuni, hakuna aliyekuwa tayari kukubaliana na ukweli kuwa Dk. Ringo alikuwa amefariki dunia. Walilia mpaka wakachoka na hatimaye wakaamua kuukubali ukweli!

Siku iliyofuata, Dk. Mkambila akatoa taarifa kwa ndugu wa Dk. Ringo waliokuwa wakiishi pale Ifakara. Zilikuwa taarifa za kushtua sana, shangazi yake na Dk. Ringo alilia sana, hakutaka kumpoteza ndugu yake kirahisi kiasi hicho! Hata hivyo ukweli ulibaki pale pale kuwa Dk. Ringo alikuwa marehemu.

“Nini zaidi?”

“Malaria!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Malaria?”

“Ndio, alikuwa amekwenda kufanya utafiti wa malaria Malugiro, ndipo alipopata maambukizi!”

“Mungu wangu, wiki mbili zilizopita alikuja hapa nyumbani na kuniaga, kumbe alikuwa akiniaga moja kwa moja…” Shangazi yake na Dk. Ringo alisema huku akilia.

Taarifa zikatolewa kwa ndugu wote walioishi Ifakara na nje ya Ifakara, haraka michango ikafanyika kisha safari ya kwenda Marangu kwa maziko ikapangwa! Siku mbili baadaye ndugu wote waliokuwa wakiishi mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam, walikuwa Ifakara tayari kwa safari ya pamoja kutokea huko kwenda Marangu.

Huko Marangu hali ilikuwa mbaya sana, ndugu wa Dk. Ringo walilia sana, walimpenda sana ndugu yao, lakini hapakuwa na jambo la kuutengua ukweli uliokuwepo. Siku ya mazishi ikafika, watu wakahudhuria mazishi yake ambapo alizikwa Marangu Mtoni.

*********

Baada ya mazishi, ndugu na jamaa wa karibu waliendelea kukaa kwenye msiba mpaka siku ya tatu ambapo walianua matanga. Ilikuwa siku iliyowahuzunisha watu wengi, huzuni ilitawala zaidi kuliko hata siku ya mazishi ilivyokuwa. Mama yake na Dk. Ringo pamoja na ndugu zake wa karibu walianza kulia upya!

Kulikuwa na kazi kubwa sana ya kuwatuliza ndugu wa marehemu walioonekana kulia zaidi. Blandina naye alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakilia zaidi, alikuwa na sababu za kufanya hivyo, Dk. Ringo alikuwa muhimu sana katika maisha yake, alishamsaidia mambo mengi sana, moyo wake ulichukua muda mrefu sana kuamini kilichotokea.

Ikiwa ni siku tatu baada ya matanga, Genesis akaanza kuugua ghafla, hakuwa na hali mbaya sana, lakini alilalamikia maumivu makali ya kichwa. Kilichofanyika ni kumfikisha katika Hospitali ya Gubilo iliyokuwa karibu na Chuo cha Ualimu cha Marangu.

“Anasumbuliwa na nini?”

“Kichwa!”

“Kimemuanza lini?”

“Tangu jana usiku, analalamika kuwa kinamuuma sana!”

“Poleni sana!”

“Ahsante!”

“Mpeleke maabara wakamchukue vipimo halafu tutajua kitu cha kufanya baada ya kupata majibu!” Dk. Kessy akajibu kisha akawapatia cheti kilichokuwa na maelezo.

Dk. Mkambila, Blandina pamoja na ndugu wawili wa Dk. Ringo waliokuwa wamewasindikiza wakaenda moja kwa moja mpaka maabara, Genesis akapimwa na kupatiwa majibu, kisha wakayarudisha mpaka kwa daktari.

“Anaonekana hana tatizo, ila kuna dawa nitamwandikia za kupunguza maumivu!”

“Sawa dokta!” Blandina akajibu.

Baada ya kuchukua dawa, wakarudi nyumbani. Kwa hali aliyokuwa nayo Genesis hakuna aliyeamini kuwa alikuwa hana ugonjwa unaomsumbua. Ndugu waliokuwa wakiishi mbalimbali walianza kurudi majumbani mwao kwa ajili ya kuendelea na kazi kama kawaida. Dk. Mkambila na Blandina nao pia walikuwa wakijiandaa kwa safari ya kwenda Ifakara. Kabla ya kuanza safari Blandina alitaka kujua hali ya afya ya mwanae, hapo akaamua kumuuliza.

“Unajisikiaje sasa mama?”

“Nina nafuu!”

“Kweli mwanangu?”

“Ndio mama!”

“Tunaweza kurudi nyumbani leo!”

“Wapi Dar es Salaam au Ifakara?”

“Nataka turudi Ifakara kwanza na Uncle Albert, halafu baada ya siku mbili tatu tutarudi nyumbani Dar es Salaam!”

“Hakuna shida mama!” Ndivyo ilivyokuwa, siku hiyo hiyo safari ya kwenda Ifakara ikaanza. Walisindikizwa mpaka Njia Panda-Himo, ambapo walipanda basi mpaka Dar es Salaam kabla ya kupanda basi lingine la Ifakara. Walifika usiku wa saa nne.

Hawakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kulala, usiku huo Genesis hakulala, aliendelea kulalamika kuwa alikuwa akiumwa sana na kichwa. Blandina alijitahidi kumbembeleza lakini haikusaidia kitu, alilia sana! Kilichofanyika ni Blandina kwenda kumgongea Dk. Albert Mkambila ili amweleze hali halisi inavyoendelea.

“Hali ya Genesis mbaya sana, analia!”

“Mh!”

“Sasa tufanyeje kaka Albert!”

“Jiandae tumpeleke hospitali tena kazini kwangu ili aweze kushughulikiwa kwa undani zaidi. Blandina akaondoka haraka na kurudi chumbani kwake, hali aliyomkuta nayo Genesis ilimchanganya.

Genesis alikuwa akitokwa damu puani, hali yake ilitisha, aliishia kulia muda wote! Dakika kumi baadaye, walitoka nje na kuchukua tax iliyowapeleka hadi hospitalini. Walipofika, Dk. Albert Mkambila alitoka kisha Blandina akatoka na Genesis, hawakupita mapokezi, walikwenda moja kwa moja hadi wodini, kila kitu kilifanyika huko! Haraka akachukuliwa vipimo kwa ajili ya uchunguzi. Muda wote matibabu yalipokuwa yakiendelea kufanyika, Blandina alikuwa amekaa nje, akisubiri kusikia kinachoendelea kutoka kwa madaktari waliokuwa wanamshughulikia Genesis.

Akiwa amejiinamia kwa uchungu, akimfikiria mwanaye anayempenda, ghafla Dk. Mkambila akatoka nje akiwa ameongozana na daktari mwenzake, mkononi mwake akiwa na faili. Nyuso zao zilionyesha wazi kulikuwa na kitu kilichotokea.

“Mama yake ndio huyu?” Dk. Makombora aliyekuwa ameongozana na Dk. Mkambila akauliza. Blandina alisikia vizuri sana kauli hiyo! Taa nyekundu zikaanza kuwaka ubongoni mwake.

“Ndio!”

Blandina akshtuka sana!

*****

Uso wa Dk. Makombora ulionyesha jambo fulani, ni wazi kuwa kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea. Akawatupia macho kwa zamu bila kupata majibu, akili yake ilishafika mbali zaidi, alijitoa thamani ya maisha, akajiona ameumbwa kwa ajili ya kupata mateso duniani.

Dk. Makombora akafika mahali alipokaa Blandina kisha akamsalimia na kumtia moyo. Kwa alivyoonekana, alionyesha wazi kukata tamaa kabisa ya mwanaye kupona.

“Habari yako dada!”

“Nzuri tu Dk. Pole na kazi!”

“Ndio majukumu yetu, usiwe na shaka!”

“Naweza kujua hali ya mwanangu?”

“Hana hali mbaya sana, ingawa hali yake hairidhishi pia!”

“Unamaanisha nini?”

“Usijali dada yangu, tutajitahidi kadri ya uwezo wetu kuhakikisha anapona, ondoa shaka!”

“Nashukuru kusikia hivyo, lakini naomba uniambie kitu kimoja!”

“Kitu gani hicho?”

“Atapona?”

“Ndio maana nimekuambia kuwa tuache tujitahidi, ila kitu cha msingi zaidi ni kumuomba Mungu!”

“Naweza kukuliza jambo lingine?’

“Ndio!”

“Anasumbuliwa na nini?”

“Bado vipimo vinaendelea, tutakujulisha baadaye!”

“Nashukuru sana Dokta!”

“Nashukuru pia!” Kwa maelezo na maswali ya Blandina, alionesha ni mwanamke anayemjali sana mwanaye, alimpenda na kumthamini, hakuweza kuishi bila yeye, alionyesha ni kiasi gani mwananye alivyo muhimu katika maisha yake!

Hayo yalimfanya Dk. Makombora amuhurumie sana Blandina. Baada ya mazungumzo hayo, Dk. Makombora na Dk. Mkambila waliondoka wakifuata korido kuelekea ofisini kwa Dk. Makombora. Walionyesha kuwa makini na kuhakikisha hali ya mgonjwa wao inakuwa sawa sawa!

“Vipi Dokta kuna usalama?” Dk. Mkambila akamwuliza Dk. Makombora, mara baada ya kuingia ofisini.

“Usalama upo, lakini lazima tuhakikishe tunakuwa makini!”

“Vipimo vinasemaje?”

“Ana matatizo ya mifupa!”

“Mh!”

“Lazima tumwanzishie dozi mara moja!”

“Hakuna tatizo ila kumbuka kitu kimoja!”

“Kitu gani hicho?”

“Huyu ni ndugu yangu, lazima tuwe makini tuokoe maisha ya mwanaye!”

“Hata kama asingekuwa ndugu yako, kumuhangaikia ni wajibu wetu dokta, ondoa shaka!”

“Nashukuruku kusikia hivyo, hebu twende tukaendelee na matibabu!”

*********

Mateso na huzuni vilitawala katika maisha yake, alihisi kama aliumbwa duniani kwa ajili ya kuteseka kabla ya kurejea mbinguni, maisha yake yalitawaliwa na simanzi na huzuni. Blandina alikumbana na mitihani mingi sana ya maisha.

“Kwani nini mimi, kwanini nakumbwa na matatizo makubwa kiasi hiki? Nina mkosi gani katika maisha yangu mimi jamani?” Aliwaza alipokuwa ameketi kwenye benchi, nje ya chumba alichoingizwa mwanaye.

Ubongo wake ulitawaliwa na huzuni tupu, aliamini mwananye alikuwa amekufa ila alikuwa akidanganywa, hilo liliendelea kuusumbua ubongo wake. Akiwa anaendelea kukumbuka mambo mbalimbali yaliyopata kutokea katika maisha yake, akaona taswira ya Gerald, mwanaume wa maisha yake, alipatwa na hasira ya ghafla na hakuona sababu ya kuendea kupata mateso hayo!

Alimpenda sana Gerald, lakini alimfanyia mambo ya ajabu sana! Alimsaliti na kumsababishia matatizo makubwa katika maisha yake, thamani ya maisha yake ikaondoka! Hakuona sababu ya kuendelea kuishi, kwake maisha aliyafananisha na gereza lenye mbu na kunguni wengi! Alikata tamaa kabisa.

“Au ninywe simu nife! Kwanini niendelee kusumbuka na dunia hii yenye shida na mateso?” Akawaza akilini mwake, lakini muda huo huo akamfikiria mwanaye Genesis, alifahamu alivyo muhimu kwake, akajaribu kufikiria kama akifa, mwanaye angeishi katika mazingira gani, akajua wazi kuwa lazima angeteseka sana, hakutaka kuendelea kuumiza kichwa zaidi, akatulia kisha akaegemeza kichwa chake kwenye ukuta.

“Mungu ndiye atakayepanga, wacha nitulie!” Hatimaye akaamua kutulia. Lakini kila alipozidi kufikiria maisha yake machozi yalizidi kutiririka machoni mwake.

Akiwa bado anaendelea kulia, ghafla Dk. Mkambila na Dk. Makombora wakatokea, walihuzunishwa sana na hali waliyomkuta nayo Blandina.

“Vipi, mbona unalia?” Dk. Albert Mkambila akauliza.

“Mwanangu! Nina uchungu sana na mwanangu!”

“Najua, lakini huna sababu ya kulia, jikaze tafadhali!”

“Kwanini mimi lakini? Kwani nimeumbwa kwa ajili ya mateso?” Akasema kwa sauti huku akilia.

“Ukisema hivyo utakuwa unakufuru, tafadhali tulia, ondoa mawazo hayo mabaya!”

“Nitajitahidi kufanya hivyo!”

“Naomba usubiri hapo kwa dakika tano, sasa hivi tutakuja kukuchukua ili ukae na mwanao wodini!”

“Sawa!” Dk. Mkambila na Dk. Makombora wakaondoka taratibu kuingia katika wodi maalum aliyokuwa amelazwa Genesis. Walipokaribia kufika, walishangazwa na hali waliyoikuta kitandani mwa Genesis! Jopo la madaktari watatu walikuwa wamezunguka kitanda cha Genesis huku kila mmoja akionyesha kuwa na wasiwasi sana!

Hali ya Genesis ilitia shaka!

“Vipi Dokta, mgonjwa anaendeleaje?” Dk. Mkambila akauliza kwa hofu.

Hakuna aliyejibu, kutokana na sababu hiyo aliamua kuinama kisha kumuwekea kifaa maalum cha kupima mapigo ya moyo wa Genesis, alipomaliza zoezi hilo, akasimama macho yake yalionyesha jambo fulani, huzuni na majozi.



Dk. Mkambila alikuwa na wasiwasi sana kutokana na hali ya Genesis, aliwaangalia madaktari wenzake kwa zamu kisha akainama kwa mara nyingine na kumwangalia Genesis. Hakika alikuwa na hali mbaya sana!

“Dk. Tunahitaji msaada zaidi!”

“Msaada wa…!”

“Mganga Mkuu!”

“Sasa muda huu anakuwaga ofisini kwake?”

“Tunaweza kumpigia simu akaja, hii ni dharula na bila yeye kwa kweli Genesis anaweza kupoteza maisha!” Hakuna aliyebisha kuhusu jambo hilo, haraka Mganga Mkuu akapigiwa simu na kuelezwa hali ya mgonjwa ilivyo.

“Nini hasa kinamsumbua?”

“Anasumbuliwa na mifupa!”

Nipeni saa moja, nitakuwa hapo!”

“Haiwezekani ukawahi zaidi ya hapo?”

“Ok! Basi nipeni nusu saa!”

“Jitahidi Mkuu!”

“Hakuna tabu!” Alikuwa ni Dk. Mkambila akizungumza na Filbert Ngonde, akimsisitizia kuwahi kutokana na hali ya mgonjwa kuwa mbaya.

Nusu baadaye Dk. Ngonde aliegesha gari lake kisha akashuka haraka na kwenda katika wodi maalum aliyokuwa amelazwa Genesis. Baada ya hapo aliagiza vifaa mbalimbali abavyo vilitumika kumpima na kufahamu kinachomsumbua.

“Ni kweli ana matatizo katika mifupa yake, hebu muanzishieni hii dozi haraka, mpaka asubuhi mtanipa maendeleo yake!” Dk. Ngonde akasema huku akionyesha kadi aliyoandika aina ya dozi ya dawa alizotakiwa kutumia Genesis.

Baada ya hapo Blandina aliitwa, akakabidhiwa mgonjwa wake. Baada ya muda kidogo, madaktari wote wakaondoka, wakamuacha Dk. Mkambila na Blandina pekee wakiwa katika wodi hiyo.

“Hebu niambie Dokta nini kinaendelea?”

“Hali yake sasa ni nzuri, ingawa ana matatizo kidogo katika mifupa yake!”

“Sasa?”

“Kuna dozi ambayo tumemuanzishia, tunaamini mpaka asubuhi atakuwa na nafuu kubwa sana!”

“Hakuna tatizo Dokta!”

“Ok! Usiku mwema acha nirudi nyumbani kesho asubuhi nitakuja kuangalia hali yako!”

“Ahsante sana!”

*********

Siku iliyofuata saa nne asubuhi Dk. Mkambila alikuwa katika wodi aliyolazwa Genesis, alikuwa akitamani sana kujua hali ya mgonjwa wake. Alipoingia tu, wodini akakutana na sura ya Blandina ikiwa imejaa tabasamu pana!

“Karibu Dokta!”

“Ahsante vipi, naona hali ya mgonjwa imekuwa nzuri!”

“Mungu mkubwa!” Genesis alikuwa amepata nafuu kubwa sana, tayari alikuwa ameshazinduka ana aliweza kukaa mwenyewe kitandani. Baada ya hapo Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo alimkabidhi Dk. Mkambila amhudumie Genesis mpaka atakapopona kabisa.

Ndivyo ilivyokuwa, alikuwa makini sana kuhakikisha hali ya Genesis inarudi katika hali ya kawaida! Siku tano baadaye Genesis alipata nafuu kabisa. Mama yake alifurahi sana, tabasamu likawa halipotei usoni mwake! Ilikuwa furaha kubwa kwa Dk. Mkambila pia.

Siku moja akiwa wodini, Dk. Mkambila aliingia na kuangalia hali ya Genesis, kimsingi alikuwa akiendelea vizuri sana, jambo hilo lilimfurahisha, aliona ni kiasi Mungu alivyo mkubwa na kusimamia matibabu ya Genesis.

“Vipi Blandina unaendeleaje na mtoto?”

“Hali yake ni nzuri sana sasa!”

“Nimefurahi sana kusikia hivyo, ila kuna jambo moja nataka kukuambia!”

“Jambo gani hilo?”

“Hivi baba yake na Genesis ni nani?”

“Unamaanisha jina lake?”

“Ndio!”

“Anaitwa Gerald!”

“Yupo wapi?”

“Dar es Salaam!”

“Huwa anakuja kumuangalia mtoto?”

“Ndio, ila mara chache, ana kazi nyingi sana mjini!”

“Lakini mbona kama unanidanganya? Sijawahi kumuona hata siku moja!”

“Mama acha uongo!” Genesis akamwambia mama yake, ni kama alikuwa akimshtakia!

“Sawa Dokta, wacha nikueleze ukweli, lakini tafadhali naomba usimwabie mtu yeyote juu ya siri hiyo, nina siri kubwa katika maisha yangu, ambayo hakuna ambaye ataamini, hata hivyo niahidi jambo moja!”

“Jambo gani hilo?”

“Kuwa hutamwambia mtu yeyote!”

“Nakuahidi Blandina!” Dk. Mkambila akajibu. Alikuwa anatamani sana kufahamu historia ya Blandina, kwa jinsi alivyoielezea alionekana wazi kuwa ilikuwa ya kusisimua sana.

Blandina alikuwa msichana mwenye sura na umbo zuri la kuvutia, ila kutokana na matatizo aliyokutana nayo alikuwa anaonekana mchafu na aliyechakaa, hata hivyo alikuwa hajapoteza uzuri wake wa awali aliozaliwa nao. Akaanza kumweleza historia nzima ya maisha yake.

Alimweleza kuwa familia yao ilikuwa yenye uwezo mkubwa sana kifedha, akamweleza kuhusu uhusiano wake na kijana Gerald ambaye baada ya kwenda Uingereza kwa wazazi wake alikutana na Daktari aliyeitwa Othman, akawa katika uhusiano wa kimapenzi lakini mwisho wa siku aliporudi Gerald kutoka Uingereza akamkataa Dk. Othman na kuamua kurudiana na mpenzi wake wa zamani Gerald.

Blandina alikuwa akizungumza kwa sauti ya upole na hisia kali sana, aliumizwa na historia aliyokuwa akiisimulia, ilikuwa historia iliyohuzunisha sana. Hakuna jambo alilolificha katika maisha yake.

“Pole sana Blandina, wewe ni mwanamke shujaa, hakika hakuna mwanamke mvumilivu kama wewe, ila nataka kukuahidi jambo moja!”

“Jambo gani hilo Dokta?”

“Siku moja utapumzika na furaha itarejea tena katika maisha yako!”

“Unamaanisha nini?”

“Huwezi kuelewa juu ya jambo hili kwa sasa, ila ukiruhusiwa nitakuambia ni kwanini nimekuambia hivyo!”

“Sawa, nashukuru kwa kunitia moyo!”

“Mungu akubariki sana!”

“Amen!”

“Wacha niendelee kupitia wagonjwa wengine, leo ni zamu yangu ya kupita round!”

“Kila la kheri!” Dk. Mkambila akaondoka na kumwacha Blandina akiwa na maswali mengi kichwani mwake yasiyo na majibu yakinifu.

*********

Siku mbili baadaye Genesis akaruhusiwa kutoka hospitalini akiwa na mama yake Blandina, Dk. Mkambila akamwomba warudi nyumbani kwake badala ya nyumbani kwa Dk. Ringo walipokuwa wakiishi awali. Blandina hakutegemea kama mwanaye angepona, akili yake ilishafikiria kuwa mwanaye alikuwa wa kufa, kitendo cha kupona kilimpa faraja kubwa sana. Jioni walipokuwa mezani wanapata chakula pamoja, Blandina alianzisha mazungumzo na Dk. Mkambila.

“Kaka Albert kuna jambo nataka kukuambia!” Blandina alimwambia Dk. Mkambila.

“Jambo gani hilo?”

“Nina hamu sana ya kujua historia yako, lakini uliniahidi ungeniambia baada ya kutoka hospitali!”

“Sawa hakuna tatizo, acha nikuhadithie!” Kuanzia hapo akaanza kumpa historia ya maisha yake yote. Blandina alikaa kimya kumsikiliza kwa makini.

“Mimi nilizaliwa Dar es Salaam miaka 46 iliyopita, wazazi wangu walijitahidi sana kunisomesha mpaka nikafanikiwa kuwa Daktari. Maisha yangu hayakuwa mabaya, nilianza kufanya kazi katika hospitali moja jijini Dar es Salaam.

“Kuna mambo mengi sana ambayo yalitokea katikati, lakini sitapenda kuyataja yote, nadhani ni vizuri kama nikakumbia yale yaliyo muhimu zaidi!” Dk. Mkambila akaanza kwa kumwambia maneno hayo. Blandina alikuwa makini sana, lakini kubwa zaidi ni kwamba siku hiyo alikuwa makini sana kusikiliza sauti yake pamoja na kumwangalia kwa makini alama za mikono yake! Sauti yake ilifanana sana na ya Dk. Othman ambaye alikuwa mpenzi wake zamani, kisha akamkataa baada ya Gerald kurudi Uingereza.

Ni jambo lililomchanganya sana, ilikuwa lazima amwuulize ili aweze kupata ukweli!

“Lakini unafanana sana na Othman?”

“Othman, Othman gani?”

“Aliyekuwa mpenzi wangu wa zamani!”

“Mimi?”

“Ndio, yaani kila kitu, sura tu ndio tofauti! Hata hivyo alishakufa siku nyingi, ndio maana nastaajabu jambo hili!”

“Duniani wawili wawili Blandina, wacha niendelee kukusimulia!”

“Sawa, endelea…!”

****

Blandina alikuwa makini sana kumsikiliza Dk. Mkambila, historia yake ilikuwa ya kusikitisha sana, pamoja na hayo, kitu kikubwa zaidi kilichomchanganya ilikuwa ni kuhusu kufanana karibu kila kitu na Dk. Othman, pamoja kumuuliza kila wakati lakini aliendelea kusisitiza kuwa, hakuwa Othman bali Dk. Mkambila.

“Enhee endelea kunisimulia nakusikiza!”

“Hakuna tatizo, ila lazima uniahidi jambo moja kwanza!”

“Jambo gani hilo?”

“Kuwa kila nitakachokuambia itakuwa siri yetu!”

“Usijali, itakuwa siri yangu!”

“Ok!”

“Sasa basi, nikiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, alikuja msichana mmoja aliyekuwa akiitwa Halima, alikuja akiwa na matatizo, lakini nilijitahidi sana kumtibu mpaka hali yake iliporejea kawaida. Wakati namtibu, nilijikuta nikimpenda sana binti huyo, hivyo nililazimika kuanzisha naye uhusiano!”

“Kwa hiyo mkawa wapenzi?”

“Ndio!”

“Baada ya hapo!”

“Baada ya hapo, uhusiano wetu ulikuja kuharibika baada ya mpenzi wake wa zamani kurudi kutoka Uingereza ambapo Halima alinikataa, niliumia sana kwa kweli, siwezi kuelezea ni kiasi gani niliumia lakini niliumia sana! Kwa kweli sikukubali kuumizwa kiasi hicho, hasa ukizingatia kuwa nilikuwa nampenda sana Halima.

“Kwa bahati nzuri, huyo mpenzi wake aliyekuwa akiitwa Gerald, aliletwa hospitalini Muhimbili kutibiwa, sikutaka kumuona akiendelea kuishi, ni yeye ndiyo alikuwa chanzo cha mimi kukataliwa na Halima, sikuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kufikiria jinsi nitakavyokatisha uhai wake ili niweze kuishi na Halima!” Mkambila alikuwa akizungumza kwa hisia kali sana na mara nyingi uso wake ulizingirwa na machozi. Blandina alionyesha wasiwasi kidogo baada ya kusikia jina la Gerald, alimfahamu Gerald vizuri sana, aliwahi kuwa mpenzi wake, ingawa alimpenda sana lakini alimfanyia unyama ambao haikuwa rahisi kabisa kuweza kuusahau!

Gerald alikuwa mwiba katika maisha yake. Kwanza alitulia kimya, baadaye akainamisha kichwa chake chini, akakumbuka miaka kadhaa iliyopita, machozi yakazidi kumtoka, alipoinua kichwa chake akakutana na uso wa Dk. Mkambila uliojaa hasira na machozi mengi.

“Mbona unalia?” Blandina akauliza.

“Ni lazima nilie!”

“Kwanini unasema ni lazima?”

“Nakumbuka mambo mengi!”

“Lakini nimekusikia ukizungumzia kuhusu Gerald!”

“Ndio!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Ni nani huyo hasa? Mbona kama historia yako inataka kufanana na ya maisha yangu? Tofauti iliyopo hapo wewe ni Dk. Mkambila na huyo aliyekuwa mpenzi wangu alikuwa akiitwa Dk. Othman, kwa kweli nilimkosea sana, alikuwa mwanaume mzuri sana kwangu, sikupaswa kumtenda vibaya kama nilivyomfanyia!”

“Pole sana Blandina, kwani bado unampenda Dk. Othman?”

“Sana, kama ingekuwa inawezekana kufufua wafu, ningemfufua kwa gharama zozote!”

“Hilo haliwezekani, wacha niendelee kukusimulia; Gerald alipokuwa hospitalini, niliamua kumuua, kabla sijatimiza lengo langu nilikamatwa kisha nikapelekwa polisi, lakini kuna rafiki yangu aliyenisaidia! Ilikuwa kesi mbaya sana kwangu, rafiki yangu akafanya mpango, akaongea na Mkuu wa Kituo, ikaonekana nimekufa, lakini nilikuwa mzima kabisa ambapo nilitoroshwa na kwenda Uingereza!”

“Ilikuwaje?”

“Ni historia ndefu sana, dunia nzima inafahamu kuwa mimi nimeshakufa, lakini nipo hai na ninaishi kama kawaida, lakini mambo yote haya yametokea kwa sababu ya mwanamke ninayempenda!”

“Nani?’

“Halima, nilimpenda sana Halima na bado nampenda mpaka sasa, kwa kweli najisikia vibaya sana kumkosa!” Mkambila alisema huku akijitahidi kufuta machozi machoni mwake.

“Pole sana, usilie tafadhali!”

“Nina haki ya kulia!”

“Hapana huna haki ya kufanya hivyo, unapaswa kumshukuru Mungu kwa jambo hilo!”

“Sawa lakini nataka kukumbia jambo fulani muhimu sana, sijui kama utaweza kuvumilia?”

“Kuvumilia? Unaanisha nini?”

“Ni jambo zito ambalo linaweza kukuchukua muda mrefu sana kuliamini, lakini ndio ukweli halisi!”

“Niambie tafadhali!”

“Umesema kuwa uliwahi kuwa na mwanaume aliyeitwa Othman?’

“Ni kweli kabisa!”

“Pia umesema ameshafariki?”

“Ndio!”

“Nikikuambia kuwa hajafa utaamini?”

“Siwezi kuamini wakati kila mtu anafahamu kuwa alishakufa, unajua ni nini kilipata?”

“Hapana!”

“Alijinyonga, kesi yake ilikuwa ngumu sana, asingeweza kutoka, kwa hiyo aliamua kupanda juu ya dumu kisha akafunga shati lake juu ya paa, akaingiza kichwa chake na kulisukuma dumu pembeni, akafariki! Vyombo vyote vya habari viliandika hivyo, isitoshe maiti yake ilionyeshwa ingawa iliharibika sana sura!”

“Basi hakufa, yupo!”

“Mbona sikuelewi!”

“Kwa sasa huwezi kunielewa, lakini baadaye kidogo utanielewa!”

“Unaniweka njia panda, akili yangu haipo sawa, tafadhali naomba uniweke wazi!”

“Mimi ndiye Dk. Othman!”

“Unasemaje?”

“Mimi ndiyo Dk. Othman!”

“Haiwezekani hata siku moja, Dk. Othman namfahamu vizuri sana, hawezi kuwa wewe, isitoshe alishafariki!”

“Huamini sio?”

“Siamini…”

“Subiri!” Kilichoendelea baada ya hapo ilikuwa ni Dk. Mkambila kushika kichwa chake kuanzia shingo ilipoanzia na nywele zilipoanzia, akawa kama anavuta kitu fulani, muda ulivyozidi kwenda ndivyo ngozi ya sura yake ilivyoonekana kusinyaa kwa mbali. Ghalfa kikaonekana kitu kama kinamenyeka!

Punde ngozi ya uso wa Dk. Mkambila ikabanduka, ikaonekana ngozi nyingine, ni kweli alikuwa ni Dk. Othman!

“Dk. Othman?”

“Ndiyo ni mimi, tulia tafadhali niendelee kukuhadithia!” Dk. Mkambila akasema. Hali ikawa tofauti kabisa na alivyofikiria. Macho ya Blandina yakajawa na machozi, akamwangalia kwa hisia kali, kisha ghafla akaanguka chini kama mzigo!

Dk. Mkambila (Othman) akajitahidi kumtingisha kwa nguvu huku akimuita jina lake lakini hakujigusa, alishafahamu kilichotokea, alichofanya ni kumlaza chini kisha akamwagia maji baridi mwili mzima.

Blandina alischanganyikiwa, hakutaka kuamini kuwa Dk. Othman alikuwa mzima, alichojua yeye ni kwamba Dk. Othman alikufa kwa kujinyonga na sio vinginevyo! Lilikuwa jambo lililomshtua sana kiasi cha kupoteza fahamu!

Dakika kumi baadaye Blandina akafumbua macho huku akihema kwa kasi. Dk. Mkambila akamwangalia kwa macho yaliyojaa huruma sana.

“Blandina naomba utulie kwanza, sikiliza mimi ndio Dk. Othman, mwanaume niliyekupenda kwa moyo wangu wote, napenda kukumbia kuwa bado nakupenda!”

“Unasema?”

“Bado nakupenda!”

“Sistahili kupendwa na wewe Dk. Othman, mimi ni mwanamke mbaya sana kwako, sistahili hata kuzungumza na wewe muda huu, nilikukosea sana!”

“Yote haya nilijua yatakufika, nilitaka dunia ikufundishe, lakini siku zote hizo nimeishi bila mke kwa sababu yako!”

“Umaanisha nini?”

“Niliamini mke wangu ni wewe, nilijua siku moja ungerudi na kuwa wangu, ndivyo maana sijaoa!”

“Unaweza kunioa mimi tena?”

“Nakupenda kama ulivyo, nakupenda wewe na mwanao, sina kinyongo na wewe, siku zote nimejaribu kuvumilia jambo hilo lakini sasa imenibidi nikufahamishe!”

“Nashukuru sana kusikia hivyo!”

“Nitakuoa na nitaishi na wewe siku zote za maisha yangu, ndio maana nilikuambia kuwa wewe ni mwanamke jasiri siku moja utapumzika! Nilikuambia hivyo kwa kumaanisha na sasa wakati wako wa kupumzika umefika!”

“Nashukuru sana kusikia hivyo!” Baada ya kukubaliana, Dk. Albert Mkambila akairudishia tena sura yake ya bandia kisha akamgeukia Blandina.

“Lazima uifiche siri hii moyoni mwako!”

“Hilo halina tabu, lakini nataka kufahamu kitu kimoja!”

“Kitu gani hicho?”

“Dunia nzima inafahamu ulikufa, tena ulijinyoga ukiwa mahabusu, nini kilitokea mpaka sasa hivi upo hai?” Lilikuwa swali gumu sana kwa Dk. Mkambila, akayagandisha macho yake usoni kwa Blandina kwa nukta kadhaa kisha akainamisha kichwa chake chini, machozi yakaanza kutiririrka machoni mwake kama mfereji wa maji. Hakuweza kuzungumza kitu!





Dk. Mkambila alimsimulia Blandina kila kitu kilichotokea katika maisha yake, hakumficha kitu chochote! Alimweleza jinsi alivyokuwa akifanya kazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jinsi alivyopelekwa polisi baada ya kugundulika alikuwa katika jaribio la kumuua Gerald!

Ilikuwa historia ya kusikitisha sana, lakini zaidi ya kusikitisha ilikuwa ikifanana karibu kila kitu na historia iliyowahi kutokea katika maisha yake. Muda mwingi aliokuwa akimsikiliza Dk. Mkambila, aliutumia kulia! Alijitahidi kumsihi Dk. Mkambila amweleze ukweli juu ya historia yake, lakini alisisitiza kuwa hakuwahi kumfahamu Gerald wala Dk. Othman.

Baada ya mazungumzo ya muda mrefu, hatimaye Dk. Mkambila aliamua kumweleza ukweli kuwa alikuwa ndiye Dk. Othman! Zilikuwa taarifa za kushtua sana kwa Blandina, hakukubali kabisa jambo hilo, lakini Mkambila alipobandua sura yake ya bandia, ndipo alipogundua kuwa ni kweli alikuwa ni Dk. Othman.

Blandina akachanganyikiwa, akaanguka chini na kupoteza fahamu! Dk. Mkambila akamwagia maji baridi na baada ya muda akazinduka!

Hakuwa tayari kuamini jambo hilo, lakini hakuwa na sababu za kubisha kutokana na kuona sura halisi ya Dk. Othman, akataka amweleze kilichotokea! Dk. Mkambila (Othman) akaendelea kumuhadithia! Nini kilitokea? SONGA NAYO…



Dk. Ringo alikuwa rafiki mkubwa sana wa Dk. Othman, hakuwa tayari kuona rafiki yake anafungwa kirahisi, kila kitu kilikuwa kama ndoto, kwa wema wa Dk. Othman hakuwa tayari kumuona anafia jela, kesi yake ilikuwa kubwa sana, ilikuwa lazima afungwe kifungo cha maisha kama sio kuhukumiwa kunyongwa! Jela ndio kitu kilichokuwa kikijirudia kila wakati akilini mwa Dk. Ringo.

“Hapana, lazima jambo fulani lifanyike ili niweze kumuokoa rafiki yangu, nisipomsaidia mimi, nani atamsaidia?” Akawaza Dk. Ringo alipokuwa ofisini kwake, siku hiyo kazi hazikufanyika vizuri, akili yake ilikuwa ikifanya kazi zaidi ya uwezo wake, alipaswa kuhakikisha Dk. Othman anatoka basi!

Muda huo huo akatoa simu yake kisha akabonyeza namba za simu za Mkuu wa Kituo alichokuwa amewekwa Dk. Othman. Nukta chache baadaye, alikuwa akizungumza na Mkuu wa Kituo Lusele Mwakatego.

“Natumaini nazungumza na Mkuu wa Kituo!”

“Ndio ni mimi bwana Mwakatego, wewe ni nani mwenzangu?”

“Dk. Ringo!”

“Ndio Dokta!”

“Nina shida ndugu yangu, kuna rafiki yangu ameletwa hapo kwako, anaitwa Dk. Othman, nafiki una taarifa naye!”

“Ndio!”

“Nahitaji sana msaada wako!”

“Juu ya nini?”

“Nahitaji atoke!”

“Mh!” Mkuu wa Kituo akaguna.

“Mbona unaguna?”

“Shauri lake ni gumu sana, sio rahisi kutoka!”

“Inawezekana, kuna vitu vya kufanya ambapo atatoka bila mtu yeyote kufahamu, isitoshe nitakufurahisha!”

“Kivipi?’

“Sema kiasi chochote cha fedha nitakupatia, ila shida yangu ni kumuona Dk. Othman akiwa nje!”

“Njoo ofisini tuzungumze!”

“Nusu saa tu, nitakuwa hapo!” Hakuwa na muda wa kupoteza, akatoka ofisini kwake mbio kisha akaingia ndani ya gari lake na safari ya kwenda Kituo cha Polisi ikaanza!

Nusu saa baadaye Dk. Ringo alikuwa ofisini kwa Mkuu wa Kituo bwana Mwakatego. Dk. Ringo alikuwa kimya mwenye kuonyesha nia ya dhati ya kuhakikisha rafiki yake mpenzi anatoka!

“Natamani sana kukusaidia, lakini ni jambo lako ni zito sana, serikali inafahamu vyema huyu bwana yupo hapa, na anatakiwa kupandishwa mahakani, sasa nitaeleza nini?”

“Kipo kitu cha kufanya!”

“Kitu gani?”

“Tunahitaji kuzungumza na Dk. Othman juu ya mpango huu, kinachotakiwa kufanyika ni kwamba Dk. Othman anatakiwa ajinyonge, lakini kabla ya kutimiza hilo atokee mtu wa kumuokoa, lakini baada ya hapo ionekane kuwa alikufa kwa kujinyonga!”

“Sawa, sasa wakihitaji maiti yake itakuwaje?”

“Hiyo ni kazi yangu, nitaiba maiti moja mochwari, halafu tutadanganya ni yeye!”

“Huoni kuwa atakuwa na sura nyingine?”

“Hilo sio tatizo, nitamwagia tindikali usoni ili kuharibu sura yake, halafu tutaivalisha nguo za Dk. Othman, huoni hapo mambo yatakuwa yameisha?”

“Hilo linaweza kuwa sawa, lakini akionekana mitaani?”

“Hawezi kuishi Afrika tena, nitafanya mipango ya kumtorosha, ataishi nje ya nchi sio hapa!” Ilimchukua muda mrefu sana Mwakatego kuelewa na kukubaliana na aliyoambiwa na Dk. Ringo, muda mwingi alionekana ametulia kimya akijaribu kuwaza jinsi itakavyokuwa.

Hata hivyo Dk. Ringo alijitahidi kumwelesha kwa nguvu zake zote, kwa kutumia ahadi ya kiasi kikubwa cha fedha, Mwakatego alikubaliana na Dk. Ringo. Pamoja na hayo, ulikuwa mpango wa hatari sana, ambao ulihitaji umakini wa hali ya juu sana.

“lakini naona jambo hili lazima ashirikishwe na mahabusu mwingine mmoja!”

“Ni kweli!” Bila kupopoteza Mkuu wa Kituo akaondoka mwenyewe kisha akachukua funguo za chumba cha mahabusu kisha akaingia.

Akajaribu kuangaza macho yake huku na huko kisha akanyoosha mkono wake na kuufinya kwa ishara ya kumwita mahabusu mmoja aliyeokena mtu mzima kidogo.

“Mimi?” Mzee huyo akauliza.

“Ndio!”

Haraka akainuka alipokuwa amekaa chini kisha akamfuata Mkuu wa Kituo mpaka ofisini kwake, kila mmoja alishangazwa sana na kitendo cha Mkuu wa Kituo kwenda katika chumba cha mahabusu mwenyewe! Baada ya muda mfupi walikuwa ndani ya ofisi ya Mkuu wa Kituo.

“Umeletwa lini hapa?”

“Leo asubuhi!”

“Kwa kosa gani?”

“Wamenisingizia nimeiba mbuzi!”

“Unaitwa nani?”

“Musa!”

“Sikiliza Musa, nataka kukutoa ila kuna kazi nataka utusaidie!”

“Kazi gani hiyo afande?”

“Subiri…” Alivyotamka maneno hayo, kwa mara nyingine akaondoka kwenda katika chumba cha mahabusu ambapo aliporudia alikuwa na Dk. Othman.

Dk. Othman akashangaa sana kuona hali hiyo, hakuweza kujua kuna kitu gani kilichokuwa kikiendelea. Alipokutanisha macho yake na Dk. Ringo alikuwa akilia kwa uchungu.

Kila kitu kikapangwa, mpango mzima ukawekwa wazi, ilitakiwa Dk. Othman ajifanye anataka kujinyonga, lakini kabla ya kufanyika jambo hilo Musa alitakiwa kumuokoa, lakini baadaye ionekane alikufa! Ndivyo ilivyokuwa na wote wakakubaliana hivyo.

“Ila Musa, lazima uwe msiri sana wa jambo hili, baada ya hapo na wewe tutakuachia huru!”

“Hakuna tatizo afande!”

Wote wakatawanyika, wakabaki Dk. Ringo na Mwakatego ofisini. Kwa mbali Mkuu wa Kituo alianza kuingiwa na woga, lakini kutokana na ushawishi wa Ringo pamoja na pesa nyingi aliamua kukubaliana na kila kitu. Dk. Ringo akaondoka kurudi kazini ambapo mipango ya kutafuta maiti ikaanza.

Kwa bahati nzuri kulitokea ajali moja mbaya sana ya daladala iliyogongana na lori, majeruhi walikuwa wengi na wengine walikufa! ilikuwa furaha kubwa sana kwa Dk. Ringo.

“Safi sana, lazima nipate maiti moja hapa!” Akasema kisha akapiga hatua za haraka kuelekea mochwari, hakuwa na la kufanya ilibidi azungumze na mhudumu wa mochwari, akamweleza kila kitu!

“Sawa Dokta, hakuna tatizo!”

“Sawa basi, naona huyu hapa atanifaa!” Akasema huku akimwonyesha maiti moja iliyokuwa ilazwa kwenye jokofu. Alichokifaya baada ya hapo ni kumwagia tindikali usoni, sura yake ikaanza kubadilika taratibu kisha ikababuka kama iliyoungua.

“Mbona unafanya hivyo?”

“Lazima nifanye hivyo ili asitambulike!”

Dk. Ringo alipotoka hapo moja kwa moja alikwenda ofisini kwake, kisha alipofika tu, akabonyeza namba za Mwakatego na kuzungumza naye. Tayari muda huo ulishafika saa tatu za usiku!

“Vipi Dokta?”

“Kila kitu kipo tayari ni wewe tu!”

“Unaamanisha tayari umeshapata maiti?”

“Nilikuambia hilo ni suala dogo kwangu, sio tu kupata ila nimeshamuunguza na tindikali!”

“Kweli wewe ni master, sasa?”

“Sasa nini tena, kazi imebaki upande wako, kila kitu kipo tayari nakusubiria wewe!”

“Hakuna tatizo!” Wakakata simu zao, Dk. Ringo akakaa akisubiria simu ya Mkuu wa Kituo, Mwakatebo, ambayo ingempa taarifa nzuri.

*********

Chumba cha mahabusu kilikuwa kidogo kisicho na madirisha makubwa, kulikuwa na madirisha madogo mawili tena yaliyokuwa juu kabisa ya selo. Hapakuwa na choo, walitumia dumu kwa kujisaidia haja kubwa na ndogo, hali ya hewa ilikuwa chafu sana.

Kama ukiingizwa kwa mara ya kwanza unaweza usiamini kuwa kuna binadamu wanaoweza kuishi katika mazingira magumu kiasi hicho. Palikuwa pachafu sana! Tayari ilishatimu saa saba na nusu za usiku, mahabusu wote walikuwa wamelala isipokuwa Othman na Musa, walikuwa na sababu ya kufanya hivyo, walikuwa wakisubiria muda ufike ili wafanye jambo waliloagizwa walifanye. Baada ya muda huo kufika, Musa alimshtua Othman.

Alijua alitakiwa kufanya jambo gani, alichokifanya ni kuvua shati lake kisha akalizungusha na kupanda juu ya dumu lenye kinyesi kisha akaingiza shingo yake katika shati hilo na kuning’nia juu!

“Mamaaa, nakufa….!” Alipopiga kelele, mahabusu wote wakashtuka, mlango wa mahabusu ukafunguliwa haraka kisha tukio lile likapigwa picha! Mpiga picha alipiga kuanzia katikati ya miguu ya Othman na shingo iliyokuwa ikining’inia, kilichofuata baada ya hapo ilikuwa ni Musa kupiga teke dumu la kinyesi.

Kinyesi kikatapakaa chumba kizima! Mahabusu wakashtuka, walikuwa na hofu sana, hakuna aliyefahamu kichotokea!

“Kuna nini?” Mmoja wa mahabusu akapiga kelele.

****

Baada ya Dk. Othman kujitundika kwa shati na kusukuma dumu la kinyesi, askari mmoja aliingia kwa kasi ya kisha akapiga picha ya tukio hilo, hakuna aliyekuwa akifahamu kilichoendelea, ni baadhi ya askari pamoja na Musa na Dk. Othman pekee! Kila kitu kilikuwa kinafanyika kisanii, siri hiyo ilikuwa moyoni mwa watu wachache pekee.

Kwa nukta chache Dk. Othman akavumilia maumivu makali ya kamba iliyokuwa ikipita katikati ya shingo yake! Ilikuwa lazima Musa afanye kazi aliyoagizwa mapema, vinginevyo Dk. Othman ilikuwa lazima afe! Kwa kasi ya ajabu, akaruka juu akiwa na chuma chenye ncha kali kisha akakata shati, Dk. Othman akaanguka chini kama mzigo!

Tayari mahabusu walishaamka kuangalia kilichotokea. Wengi walikuwa bize kujinasua kwenye kinyesi zaidi ya kuangalia kilichompata Dk. Othman, hata hivyo kuna ambao walitaka kufahamu kilichompata.

“Nini kimempata?” Mmoja wa mahabusu akamwuliza Musa.

“Sijui!”

“Hujui?”

“Ndio sifahamu, nilisikia akitoa kilio, niliposhtuka nikamuona akiwa amening’inia, nafiki ana matatizo!”

“Halafu ishu yake kubwa sana, inawezekana ameamua kuwahi ili kukwepa kifungo cha maisha!”

“Hilo linawezekana pia!” Yalikuwa mazungumzo kati ya Musa na mahabusu mwingine.

Kilichofuata baada ya hapo ni Dk. Othman kujifanya anakoroma kwa kasi! Haukupita muda mrefu, Dk. Othman akatolewa haraka nje, kisha akapakizwa katika gari la polisi kisha akapelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbuli. Kila kitu kilifanywa haraka-haraka.

*********

Dk. Ringo hakulala kabisa siku hiyo, ingawa alikuwa amepangwa zamu usiku, lakini huwa anapata muda japo kidogo wa kusinzia, lakini kwa siku hiyo alikuwa macho akisubiri rafiki yake mpenzi Dk. Othman afikishwe hospitalini.

Kila wakati alikuwa akimpigia simu Mkuu wa Kituo, akimuuliza kinachoendelea. Akiwa ameshikwa na hasira, akaamua kumpigia kwa mara ya mwisho. Akaichukua simu yake kisha akapekua katika kitabu chenye orodha ya majina kisha akatafuta jina la Mwakatego, na kubonyeza kitufe cha kupiga!

Simu haikuita kama alivyotarajia, alikutana na jibu tofauti kabisa na matarajio yake. Aliambiwa simu aliyokuwa akiipiga ilikuwa inatumika. Hapo akachanganyikiwa zaidi.

“Nini tena? Au anataka kunifanyia sanaa?” Akasema kwa sauti ya taratibu, kilichomchanganya zaidi kichwa chake ni kwa sababu alikuwa amekwishamlipa pesa walizokuabaliana.

Akarudia kumpigia kwa mara nyingine, jibu likawa la aina ile ile! Hasira ikaongezeka maradufu! Alijua mambo yalishaharibika. Alichokifanya ni kwenda katika sehemu ya kuandika ujumbe mfupi wa maneno ‘sms’ kisha akaandika ujumbe uliosomeka; ‘Kumbuka kuwa nina uchungu sana na rafiki yangu, hiyo ndio sababu pekee iliyonifanya nipange mpango huu na kukupatia kiasi hicho kikubwa cha fedha! Lakini kwa hali ninayoiona mwisho wetu hautakuwa mzuri, napenda kukuhakikishia kuwa, ikiwa hutatimiza makubaliano yetu tusilaumiane…’

Alirudia kuisoma sms hiyo mara mbili mbili ili kuhakikisha alichokiandika kama kilikuwa sawasawa, baada ya kuridhika akabonyeza katika sehemu ya kutuma, kisha akatafuta jina la Mwakatego, akiwa anakaribia kulipata, simu yake ikaita!

Akayatupa macho yake juu ya kioo cha simu, akakutana na jina la Mwakatego, kabla hajamtumia meseji aliyopanga kuituma, akapokea.

“Vipi mshirika, mbona unaniangusha?” Sauti ya Dk. Ringo iliyoonyesha dhahiri kuwa na jazba, ilisikika katika ngoma za masikio ya Mwakatego.

“Kazi hii ni ngumu kaka, sio rahisi kama unavyofikiria, lakini hata hivyo mambo ni mazuri!”

“Mazuri?”

“Ndio mazuri!”

“Unamaanisha nini kusema hivyo?”

“Kazi imeshaisha!”

“Sijakusikia vizuri…”

“Kazi uliyonipa nimeshaimaliza!”

“Yupo wapi Dk. Othman?”

“Ratiba yetu haijabadilika, wanamleta na gari hapo hospitalini!”

“Hakuna tatizo, mimi ndiyo nipo zamu kwa hiyo kila kitu kitakwenda sawa!”

“Nashukuru sana ila lazima uwe mwangalifu sana, hii ni kazi ya hatari!”

“Hakuna tabu, ila unapaswa kufahamu jambo moja muhimu!”

“Jambo gani?”

“Mimi ni daktari, tena sio wa kubabaisha, nimesomea nje ya nchi. Ni msomi niliyekamilika!”

“Nakuamini kaka!”

“Kila la kheri!” Baada ya kukata simu, Dk. Ringo alibaki ameishika simu yake kwa takribani dakika nzima, akiwaza huku meno yake yakiwa nje. Alikuwa na furaha ambayo haikuwa rahisi kuelezeka! Alipiga meza kwa nguvu kisha akateki katika kiti chake cha kuzunguka.

“Mimi ni mwanaume kamili, lazima nionyeshe uanaume wangu kwa jambo muhimu na hatari kama hili, huu ni ujasiri, ni jambo ambalo haliwezi kufutika katika kumbukumbu za maisha yangu!” Akawaza.

Alichokifanya baada ya hapo ni kutoka nje haraka kisha kuangalia huku na huko kabla ya kurudi tena ofisini kwake. Alikuwa akisubiri gari lililomleta Dk. Othman.

*********

Kiasi cha dakika kumi baada ya kumaliza kuzungumza na Mwakatego kwenye simu, ofisi ya Dk. Ringo ikagongwa, hakuwa na wasiwasi wala haja ya kutaka kujua ni nani alikuwa akigonga, alijua ni askari waliomleta Dk. Othman.

Alipowaruhusu waingie, ndivyo ilivyokuwa! Wauguzi wakamlaza kwenye machela kisha Dk. Ringo akajifanya kumpima vipimo mbalimbali.

“Nini kilimpata?” Dk. Ringo akauliza.

“Alikuwa anafanya jaribio la kujiua!”

“Kwanini?’

“Hatujui, ila kwa kutokana na uzito wa kesi yake inawezekana akaamua kufanya hivyo ili kukwepa kunyongwa au kifungo cha maisha!” Dk. Ringo alijisikia vibaya sana moyoni mwake, Othman alikuwa anatia huruma sana. Haikuwa rahisi kuamini kuwa aliyekuwa amelala kwenye machela alikuwa ni yeye!

“Mnaweza kusubiri nje nimfanyie uchunguzi kwanza!”

“Hakuna tabu ila ni lazima awe na pingu, ni mtu hatari sana huyo!” Mmoja wa askari waliokuwepo katika chumba cha daktari alisema.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Hakuna tabu, yupo salama ila akiingizwa wodini mtamfunga pingu!”

“Sawa dokta!”

Walipofunga mlango tu, akamtingisha rafiki yake, Dk. Othman alikuwa anaonyesha hali ya woga sana. Alijua ni kiasi gani jaribio lililokuwa linafanyika lilivyokuwa hatari.

“Sikiliza kamanda wangu, sipo tayari kukupoteza, ndio maana nafanya haya yote, sasa lazima uwe mjanja, ukipoteza stepu moja tu tunaumbuka! Tulia, nakufunika shuka na kukufunga kama maiti, kisha utapelekwa mochwari!”

“Mh!” Dk. Othman akaguna.

“Mbona unaguna?”

“Mochwari? Kweli kazi ipo! Baada ya hapo!”

“Kila kitu kipo tayari, watu watajua umekufa, vyombo vya habari vitatangaza hivyo, lakini wewe utaondoka kesho usiku kwenda Uingereza, kila kitu kipo tayari, mambo mengine tutazungumza usiku huu!”

“Hakuna tatizo ndugu yangu!” Walikuwa makini kuliko kawaida, kila kitu kilifanyika haraka kuliko maelezo. Kilichofanyika baada ya hapo ni kujinyoosha kisha kumfunika mashuka meupe. Haikuwa kazi ngumu kwa Othman, alishazoea kuona maiti kila wakati, sio kuona tu, bali kuna waliokufa mikononi mwake. Kila kitu kilipokamilika, Dk. Ringo akatoka nje akionekana kuwa na huzuni sana.

“Nini kimetokea?”

“Othman amefariki!”

“Nini?” Muuguzi mmoja akauliza kwa hamaki.

“Dk. Othman amefariki!” Hakuna aliyekuwa tayari kukubaliana na Dk. Ringo, wakaingia katika chumba cha daktari haraka kisha wakamkuta Dk. Othman akiwa amelala kimya kwenye machela. Kilichofanyika ni kumfunua usoni, alikuwa kimya akiwa amezizuia pumzi zake ipasavyo.

Kila mmoja alilia kwa uchungu. Askari wakarudi kituoni wakiwa na fomu ya taarifa za kifo cha Dk. Othman. Hiyo ilikuwa siri kubwa kwa Dk. Ringo, Othman, Mkuu wa Kituo na Musa. Wauguzi na wafanyakazi wote wa Hospitali ya Muhimbili, waliamini Dk. Othman alikufa!

Mwili wa Dk. Othman ukasukumwa katika machela ya magurudumu kuelekea mochwari.

*********

“Mambo vipi?”

“Safi, mambo bado?”

“Kwani wewe umeshajitayarisha?”

“Kila kitu kipo tayari nakusubiria wewe!”

“Usijali, kila kitu kipo sawa, wauguzi wanamleta Othman huko kwako sasa hivi, hakikisha unafanya zoezi hilo haraka, usisahau kumbadilisha nguo!”

“Hakuna tatizo!” Yalikuwa mazungumzo kati ya Dk. Ringo na muhudumu wa Mochwari.

Haukupita muda mrefu, wauguzi walifika katika chumba cha kuhifadhia maiti wakiwa na mwili wa Dk. Othman. Walivyofika tu, jambo la kwanza kuzungumza ilikuwa ni kumpa taarifa za msiba!

“Huwezi kuamini Dk. Othman amefariki!” Mmoja wao akasema.

“Amefia wapi, kituoni?”

“Hapa hapa hospitali, hii ni maiti yake!”

“Haiwezekani yaani Dk. Othman amefariki?”

“Ndiyo, kwanini hutakiwa kuamini?”

“Nini kilimpata?”

“Alijinyonga!”

“Alijinyonga?”

“Ndio…” Gebeshi muhudumu wa mochwari akaonyesha kushtushwa sana na taarifa hizo, laiti wauguzi wangejua kilichoendelea moyoni mwa Gebeshi, haijulikani ingekuwaje! Walipoondoka tu, akamfungua Dk. Othman mashuka kisha akamwambia avue nguo.

Bila kupoteza muda Dk. Othman akafanya hivyo, baada ya hapo akaivua nguo maiti iliyokuwa chini kisha akampa Dk. Othman akazivaa!

“Maagizo yote ninayo usijali, subiri kwanza niivishe nguo hii maiti, ni lazima watu wajue umekufa!”

“Hakuna tabu!” Dk. Othman alikuwa na hofu sana, hakuamini kilichotokea, aliona kila kitu kama ndoto. Kabla Gebeshi hajaanza kuivisha nguo ile maiti, akasikia mlango wa mochwari ukigongwa kwa nguvu! Wote wakatetemeka!





Baada ya Dk. Othman kufikishwa kituoni na kuwekwa mahabusu akisubiri kupandishwa mahakani, mipango ya kumtoa ikafanyika! Ni Dk. Ringo ndiye alifanya mipango hiyo. Kwa kushirikiana na Mwakatego Mkuu wa Kituo alichokuwa anashikiliwa Dk. Othman, ikafanyika mipango, Dk. Othman akaonekana kama amejinyonga!

Akapelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matatibabu, lakini kwa njama walizokuwa wamepanga, akaonekana amekufa! Kilichoendelea ilikuwa ni kupelekwa mochwari. Akiwa na muhudumu wa mochwari Gebeshi, mlango wa mochwari unagongwa! Ni nani huyo aliyekuwa anagonga mlango? SONGA NAYO…



Mapigo yao ya moyo yakaongezeka kasi, walijua kila kitu kilishaharibika! Ilikuwa lazima wafikirie kitu cha kufanya ili waweze kuepukana na balaa ambalo lilikuwa linaanza kunukia! Wafanye nini sasa? Hakuna aliyejua. Wakabaki kimya wamejikunyata, mlango ukazidi kugongwa. Akili ya Gebeshi ikafanya kazi zaidi ya kawaida, ilikuwa lazima afikirie jinsi ya kujinasua na balaa hilo.

“Itakuwaje?” Dk. Othman akamwuliza Gebeshi.

“Sijui!”

“Unadhani anaweza kuwa nani?”

“Wote tupo ndani, unadhani ninaweza kufahamu ni nani ambaye anagonga mlango?”

“Ila lazima kutakuwa na tatizo!”

“Hilo halikwepeki, lakini ni lazima tufikirie kitu cha kufanya ili tuweze kuepuka!”

“Sawa, nakusikiliza. Wewe ndio mtaalam, una wazo gani?”

“Fuata kila nitakachokuambia!”

“Hakuna shida!”

“Utaweza kuvulimia kulala ndani ya jokofu kwa muda?”

“Mh!”

“Mbona unaguna?”

“Hakuna kitu kingine cha kufanya?”

“Unadhani itakuwa ni nini?”

Wote wakabaki kimya, hakuna aliyeweza kujibu. Wakadumu na ukimya huo kwa muda mrefu kidogo, kisha Gebeshi akaonekana akihangaika kutafuta kitu fulani ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti. Baada ya kujizungusha kwa muda mrefu, aliita kwa sauti ya chini sana.

“Dokta!”

“Naam…!”

“Njoo huku!” Akamwita alipokuwa amekaa karibu na sehemu maalumu ya kuoshea maiti.

“Nakuja!” Hakuwa na kitu kingine cha kufanya, kwa wakati huo Gabeshi alikuwa ndiye kiongozi wa kila kitu, kila alichokisema ilikuwa lazima akisikilize na kukifuata.

Alipomfikia, akashangaa akimwonyeshea kwa vitendo jeneza la kusafirishia maiti.

“Unamaanisha nilale ndani yake?”

“Hilo ndiyo jibu lake!”

“Mh!”

“Mbona unaguna!”

“Naogopa!”

“Sasa unaogopa kulala ndani ya jeneza au unataka tukamatwe?” Swali hilo lilimfanya anyong’onyee kwa woga, hakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kuingia ndani ya jeneza, akalala kisha likafunikwa na mfuniko wake. Gebeshi akatoka haraka na kwenda mlangoni, akiwa anahema kwa kasi akafungua.

Hakuamini macho yake! Alikutana na Dk. Ringo akiwa na mzinga mkubwa wa pombe aina ya konyagi.

“Vipi Dokta?”

“Poa, mbona unahema hivyo?”

“Umenishtua sana rafiki yangu, nilijua picha imeshaungua!”

“Usijali, jamaa yupo wapi?”

“Ingia ndani umuone!” Akamshika mkono na kuingia naye ndani, Dk. Ringo alikuwa amekolea kilevi sawa-sawa! Mkononi mwake alikuwa na chupa kubwa ambayo bado alikuwa akiendelea kuinywa bila kuchanganya na kitu chochote. Ni muda huo ndipo Gabeshi alipofanikiwa kuona chupa ya pombe mkononi mwa Dk. Othman.

“Vipi Dokta, mbona unakunywa pombe kali?”

“Ni lazima nifanye hivi!”

“Kwanini?”

« Furaha. Nina furaha sana kuona rafiki yangu amekuwa huru tena !

Gabeshi hakuwa na maswali zaidi, akamshika mkono mpaka mahali ambapo jeneza lilipokuwepo ! Alipofika akafungua mfuniko wa jeneza, Dk. Ringo akashtuka sana.

« Kwani amekufa ? »

« Hapana ! »

« Sasa mbona umemuweka humu ? »

« Ilikuwa lazima nifanye hivyo ! » Gebeshi akaanza kumweleza jinsi ilivyokuwa mpaka walipoamua Othman aingie ndani ya jeneza. Dk. Ringo akazidi kuhuzunika. Akamtoa rafiki yake kisha wakatoka taratibu nje ya chumba cha kuhifadhia maiti, kilichoendelea hapo ilikuwa ni kwenda kuchukua gari lake kisha akamwingiza garini. Kitu kilichofanyika ni kufunga vioo vyote ambavyo hata hivyo vilikuwa vyeusi, kisha akaliegesha mahali pake.

« Pumzika humu ndani ya gari, usijaribu kukaa, lala tu ! Namsubiri Dk. Masakamla aje anipokee, kisha tutaondoka ! »

« Hakuna tabu rafiki yangu ! » Dk. Othman akajibu kwa upole sana. Kwa ujumla alitia huruma sana.

Dk. Ringo akaondoka kuelekea ofisini kwake, akaendelea na kazi huku kichwa chake kikimuwaza rafiki yake mpenzi. Aliendelea kuwahudumia wagonjwa lakini akili yake ilikuwa ni kumtorosha rafiki yake, hakutaka kuona rafiki yake anafungwa au ananyongwa, aliamua kujitoa kwa ajili yake! Alikuwa akifanya jambo la hatari sana lakini hakuwa na jinsi, ilikuwa lazima afanye hivyo kama ni kweli alikuwa na nia ya kumuokoa rafiki yake.

*********



Mahabusu na maaskari wote walijua Dk. Othman alikuwa ameamua kujinyonga! Kila mmoja alikuwa akihuzunika sana, siri hiyo ilikuwa kati ya Mkuu wa Kituo Mwakatego, Dk. Ringo, Musa aliyekuwa mahabusu na askari wengine wawili, wote kwa pamoja walikubaliana kutovujisha siri hiyo baada ya kugawana kiasi kikubwa cha pesa.

Ikiwa ni saa Saa tisa na nusu za usiku, mlango wa Ofisi ya Mwakatego ukagongwa! Kwanza haikuwa kawaida yake kukaa usiku ofisini kwake, ila alikuwa akifanya hivyo mara chache, tena kwa sababu maalum! Haraka akili yake ikafanya kazi kuliko kawaida, alishajua kilichotokea, alijua wazi alikuwa akiletewa habari za msiba, habari ambazo alijua ni bandia na alijiandaa kuzipokea.

Alipowaruhusu kuingia, wakaingia askari wawili, wakionyesha hali ya majonzi sana.

“Mambo yameharibika afande!”

“Yamekuwaje?”

“Yule mahabusu amefariki!”

“Duh! Na kweli alidhamiria kufa, hakupaswa kufa!”

“Lakini ndio hivyo yameshatokea!”

Hapakuwa na kitu kingine cha kufanya, zaidi ya kukubaliana na ukweli ambao hata hivyo alishaujua kabla. Askari wale wakaondoka, Mwakatego akabaki peke yake ofisini kwake. Akajibembeza katika kiti chake cha kuzungukazunguka!

“Mjini shule, ukiwa mjanja kila kitu kinakwenda sawasawa, na kula pesa yangu nzuri kwa kazi ndogo ya kutumia akili!” Akawaza huku akicheka taratibu. Taarifa zikasambazwa kila mahali, mpaka vyombo vya habari vikaripoti kifo chake.

Asubuhi yake taarifa za kifo cha Dk. Othman kujinyonga zikasambaa kila mahali! Watu wakaamini hivyo, ukweli uliokuwa umefichwa ulijulikana na wachache. Kama alivyoahidi, siku hiyo hiyo alimwachia huru Musa. Pamoja na kuachiwa huru, aliambiwa aitunze siri hiyo moyoni mwake.

“Taarifa hizi zikisikika mahali popote, tutajua ni wewe, kitakachofuata… »

“Hapana siwezi kufanya hivyo!”

“Naomba iwe hivyo!” Mwakatego alimwambia Musa ili asije akajaribu kutoa siri hiyo. Kutoa siri hiyo kulimaanisha kazi yake kuwa mashakani.

********

“Kaka tuondoke!” Dk. Ringo alimwambia Dk. Othman, alipotoka zamu ya usiku baada ya kupokewa na Daktari mwingine saa kumi na mbili za asubuhi.

“Hakuna shida!” Dk. Ringo akatoa kofia ya chepeo aliyoiandaa kwa ajili ya Dk. Othman kisha akampa na kuivaa. Safari yao ikawa ni ya moja kwa moja hadi Masaki nyumbani kwa Dk. Ringo.

Walipofika alimwingiza katika chumba maalum alichomwandalia kisha wakaanza kupanga mipango ya safari.

“Kila kitu kipo tayari rafiki yangu, itabidi utoroke hapa Tanzania!”

“Hiyo ni sawa, kwenda wapi?”

“Mi’ nafikiria uende Uingereza, huko utafanya kila kitu kwa upya ili uwe mpya, hakuna kitu kingine zaidi ya hicho!”

“Kivipi?”

“Naamanisha ukaweke sura ya bandia na kubadilisha uraia, uishi huko huko, usome upya ili baadaye uje kufanya kazi Tanzania kama Daktari mwingine kabisa!”

“Mh! Una akili sana rafiki yangu, hayo yote yanawezekana, ila si unajua kuwa sina pesa za kutosha?”

“Usijali nipo na wewe kwa kila hali!”

“Sawa, hakuna tabu!” Mipango ikafanyika hara-haraka, Dk. Othman akampa Dk. Ringo kadi yake ya Benki, akaenda kuchukua pesa zote zilizokuwa kwenye akaunti, baada ya hapo wakajiandaa kwa safari ya Uingereza siku inayofuata.

*********

Vituo vyote vya Redio na Televisheni, vilitangaza juu ya kifo cha Dk. Othman, kila mmoja alihuzunika sana hasa kutokana na historia yake kuhuzunisha. Picha iliyopigwa alipokuwa amening’inia juu ya paa! Hakuna aliyekuwa na ubishi na kifo chake, iliaminika hivyo!

Saa moja na nusu, gari la kisasa aina ya Range Rover lilikuwa linapita Magomeni likitokea barabara ya Kawawa. Ndani ya gari hilo kulikuwa na Dk. Othman akiwa na Dk. Ringo. Wote walikuwa wamevalia suti nyeusi na kofia aina ya pama. Hati ya kusafiria na vitu vyote muhimu ikiwemo fedha za kutosha, Dk. Othman alikuwa nazo.

Kilichokuwa mbele yake ilikuwa ni safari ya Uingereza basi! Magazeti yote ya siku hiyo yalipamba kurasa zao za mbele kwa kutumia picha ya Dk. Othman iliyoonesha akiwa amejitundika! Kila wakati Dk. Othman na Dk. Ringo walikuwa wakigongeana mikono huku wakicheka. Walijiona washindi!

“Kaka wewe si umekufa? Mbona upo hapa?” Dk. Ringo akamwambia Othman huku akicheka.

“Hata mimi nashangaa!”

Foleni iliyokuwa katika taa za usalama haikuwa kubwa sana, kwa bahati nzuri kulikuwa na askari aliyekuwa akiongoza magari. Muda mfupi baadaye wakawa wamevuka katika taa hizo. Dakika tatu baadaye walifika katika taa nyingine zilizokuwa katika eneo la Karume. Foleni ya pale ilikuwa ndefu kidogo.

Baada ya kusubiri kwa muda, taa zikaruhusu, kabla hawajavuka katika taa hizo, zikazima na kuwaka za rangi nyekundu. Hiyo ilimaanisha walipaswa kusubiri! Dakika moja baadaye askari wanne wenye bunduki mikononi mwao wakaonekana kutilia mashaka gari la Dk. Ringo, walionekana wakiliangalia kwa muda mrefu huku wakiwa wanajadiliana! Punde wakalifuata. Walipolifikia, wakamwambia Dk. Ringo apaki gari pembeni.

“Kuna nini tena jamani? Nina haraka nampeleka mgonjwa uwanjani anatakiwa aende Uingereza kwa matibabu! Naomba nieleweke hivyo!” Dk. Ringo akasema kwa hofu. Alishampa ishara Dk. Othman ajilaze kwenye kiti na kuiangusha pama usoni mwake.

“Paki gari pembeni hatuhitaji maelezo!” Mmoja wa askari hao akamwambia.

“Naomba mnielewe, kwani nimefanya nini? Mimi ni Dokta au niwaonyeshe kitambulisho changu!” Dk. Ringo akasema huku akitoa kitambulisho chake.

« Hatuna haja na kitambulisho chako, ila tunataka upaki gari pembeni na ukiendelea kubishana na sisi, dakika moja ijayo utakuwa na jina jingine ! »

****

Kitu pekee kilichokuwa akilini mwa Dk. Ringo ilikuwa ni hatari, alijua wazi kuwa kulikuwa na hatari iliyokuwa mbele yake. Kuwaruhusu maaskari wakague gari lake kulimaanisha kuonekana kwa Dk. Othman jambo ambalo lingesababisha wote kuishia jela! Akavuta pumzi ndefu sana kisha akazishusha taratibu.

“Mimi ni Daktari wa Muhimbili jamani, mbona hivyo?” Alisema kwa sauti ya chini huku macho ayke yakisoma woga aliyokuwa nao.

“Hatuna haya ya kujua kazi yako!”

“Bali?”

“Tunataka upaki gari lako pembeni kwa ajili ya ukaguzi!”

“Huu ni ukaguzi wa aina gani kwa gari langu pekee, kwani hakuna magari mengine ya kukaguliwa zaidi ya hili?”

“Usitufundishe kazi, kwanini unazidi kubisha?”

“Kwa sababu nimeshawaambia kuwa nachelewa ndege, mgonjwa wangu anatakiwa kusafiri haraka kwa ajili ya kwenda kufanyiwa upasuaji!”

“Unapaki gari pembeni au nipasue tairi la gari lako?” Mmoja wa maaskari alisema huku akilenga tairi la mbele la gari la Dk. Ringo kwa bunduki.

Hapo sasa akajua hapakuwa na utani katika jambo hilo, ilikuwa lazima afikirie jambo la kufanya haraka, hakuwa na jibu la kuwapa maaskari wale walioonekana kuwa makini na kazi yao. Punde taa zikaruhusu magari kupita, lakini kwa kuwa hakuruhusiwa kuondoka akasababisha foleni ndefu ambapo honi zilisikika zikilia kwa sauti kubwa.

“Tafadhali naomba mniruhusu!”

“Wewe ni mjanja sio?”

“Hapana!”

“Basi, paki gari pembeni!” Hakuwa na ujanja tena, akakata kulia kisha akaegesha gari pembeni. Tayari watu walikuwa wameshazunguka eneo la tukio kuangalia kilichokuwa kikiendelea.

Askari mmoja akaingia ndani ya gari na kuanza upekuzi kila mahali garini. Dk. Ringo akaamriwa afungue buti, kisha ukaguzi ukaendeelea.

“Shuka chini!” Askari mmoja akamwambia Dk. Ringo.

“Hakuna tabu!” Dk. Ringo akashuka akionyesha huzuni, uso wake ulionyesha wasiwasi sana. Hakuwa na kitu kibaya ndani ya gari lake, lakini tatizo lilikuwa ni Dk. Othman ambaye magazeti yote ya siku hiyo, yalikuwa yameandika kuwa alikuwa amejinyonga. Hilo aliliomba kwa sauti ya chini, alijua ni kiasi gani mambo yangeharibika kama Dk. Othman angeonekana akiwa katika gari lake. Akiwa amekaa kimya akisubiria kuambiwa chochote kutoka kwa maaskari waliokuwa wakikagua gari lake, akasikia sauti ya ukali kutoka kwa askari mmoja.

“Mwambie na mwenzako ashuke!”

“Huyo ni mgonjwa hataweza!”

“Sasa anawezaje kusafiri peke yake mpaka Uingereza?”

“Haendi peke yake, nasafiri naye, lakini uwanjani kuna mtu atakayerudisha gari nyumbani!” Ukaguzi ukaendelea kwa dakika tatu, hawakukuta kitu kibaya! Hatimaye wakamruhusu Dk. Ringo kurudi kwenye gari, akapanda na kuwasha kisha safari ya kuelekea Uwanja wa Ndege ikaendelea.

*********

Kila wakati Dk. Ringo alikuwa akiangalia nyuma kupitia vioo vya pembeni vya gari lake kuangalia kama alikuwa akifuatiliwa na gari la polisi, hakuamini kuwa ni kweli alikuwa ameachiwa baada ya ukaguzi na rafiki yake hakugundulika! Huo ulikuwa ukweli ambao hakuwa tayari kuuamini haraka.

“Siamini!” Dk. Ringo alimwambia Dk. Othman.

“Hata mimi pia!”

“Hakika Mungu ni wa ajabu sana!”

“Sana, tena apewe sifa!”

“Kazi iliyobaki ni moja Tu!”

“Ipi?”

“Kufika Uingereza!”

“Ni kweli kabisa, kwa uweza wa Mungu hilo linawezekana!” Hawakuwa na jambo lingine la kufanya zaidi ya kuendelea na safari ya kwenda Uwanja wa Ndege. Baada ya muda mfupi kidogo wakafika uwanjani, kwa kuwa kila kitu kilikuwa tayari, hawakuwa na muda wa kupoteza.

Muda ulipowadia, Dk. Othman akajiandaa kuingia katika chumba maalum cha ukaguzi kabla ya kuingia kwenye ndege. Akamwangalia Dk. Othman mara mbilimbili, machozi yakaanza kumlengalenga machoni mwake.

“Sijui nikushukuru kiasi gani rafiki yangu?”

“Usijali…kuniambia ahsante tu, inatosha!”

“Nashukuru kusikia hivyo!”

“Safari njema, ila ukifika tu, lazima uwasiliane nami!”

“Hakuna shida!”

“Emmanuel atakupokea uwanjani, atakuwa mwenyeji wako kama nilivyokuambia, maagizo yote nimeshampatia, kwa hiyo unapaswa kumsikiliza yeye kwa kila kitu!”

“Hakuna tabu!” Wakakumbatiana kwa furaha na kuagana. Othman akaingia katika chumba maalum cha ukaguzi, baadaye akaingia ndani ya ndege. Dk. Ringo alisubiri mpaka ndege ilipopaa na kuishilia angani.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

*********

Dk. Othman aliposhuka tu, uwanjani, akaona bango kubwa lililoandikwa ‘Karibu Uingereza Dk. Mkambila’, Othman alishafahamu kuwa ni yeye ndiye aliyekuwa akisubiriwa! Jina la Mkambila ni jina jipya ambalo walikubaliana kulitumia kuanzia akiwa Tanzania. Mara moja akamfuata mtu aliyekuwa amebeba bango hilo, akamsalimia na kujitambulisha.

“Habari yako ndugu!”

“Njema sana!”

“Naitwa Othman!”

“Naitwa Emmanuel, karibu sana Uingereza!”

“Nashukuru sana!” Wakaondoka moja kwa moja mpaka kwenye gari lake, safari ya kuelekea nyumbani kwa Emmanuel ikaanza. Hapakuwa mbali sana na uwanjani, kiasi cha dakika thelathini na tatu tayari walishafika katika nyumba nzuri iliyovutia, nyumba aliyokuwa akiishi Emmanuel.

“Karibu sana ndugu yangu!”

“Ahsante sana, nyumba yako nzuri sana!”

“Ahsante, hata hivyo sio yangu ni nyumba ya shirika!”

“Pamoja na hivyo ni nzuri pia!”

“Nashukuru sana!” Wakaingia ndani, akakaribishwa katika sebule nzuri ya kisasa.

“Naomba nikuletee kinywaji!” Msichana wa kazi wa Emmanuel alimwambia Othman.

“Nashukuru sana, niletee maji ya matunda!” Yule msichana hakuuliza swali lingine, alitoka moja kwa moja mpaka kwenye jokofu kubwa, akatoa maji ya matunda ya mananasi.

“Karibu ufurahie kinywaji!”

“Ahsante sana!”

Ilikuwa nyumba nzuri sana ya kuvutia, geti imara na mlinzi ilifanya nyumba hiyo kuwa na ulinzi wa kutosha. Emmanuel alikuwa ni Daktari, alisoma na Dk. Ringo miaka ya nyuma, urafiki wao ulikuwa kwa kasi, kiasi wakawa kama ndugu. Alikuwa akifanya kazi katika Hospitali moja ya Mifupa iliyokuwa jijini London Uingereza.

Baada ya kumaliza kupata kinywaji, mazungumzo yakaendelea. Dk. Othman akamweleza kila kitu bila kumficha. Historia yake ilitisha, ingawa alishaelezwa kila kitu na Dk. Ringo lakini kumsikia moja kwa moja akisimulia mkasa unaomuhusu yeye mwenyewe, ulimshtua sana.

“Pole sana ndugu yangu!”

“Nashukuru!”

“Usijali, kila kitu kitakuwa sawa, hapa kuna wataalamu wazuri sana wa kubadilisha sura za bandia, utakuwa mtu mwingine saa chache zijazo!”

“Kweli?”

“Kabisa…hakuna atakayekutambua tena, utakuwa mwingine na jina lako litakuwa lingine pia, kitu cha kufurahisha zaidi, uraia wako pia utabadilika, nitakutafutia uraia wa hapa Uingereza!”

“Nitafurahi sana!”

“Anza kufurahi sasa hivi!”

“Nashindwa kuelewa namna ya kukushukuru!”

“Usijali ndugu, sisi wote ni wanaume na mambo kama haya yanaweza kumkuta mtu yeyote, ni bora uishi kama mtu mwingine sasa hivi, kuliko kuishia jela au kunyongwa!”

“Ni kweli kabisa!” Mazungumzo yakaendelea, kila mmoja akimuuliza maswali mwenzake kwa ajili ya kufahamiana zaidi!

Ikiwa ni dakika arobaini na tano tu baada ya Dk. Othman kuingia katika nyumba ya Dk. Emmanuel, akatokea msichana mmoja mrembo sana, alikuwa akitokea katika mlango kubwa wa kuingilia ndani. Kwa alivyoonekana hapakuwa na ubishi kuwa alikuwa akitokea kazini! Alikuwa mrembo sana, lakini urembo aliokuwa nao, haukumfanya Dk. Othman ashtuke, ila kuna jambo lingine lililotaka kuharibika!

Alimfahamu vizuri sana msichana huyo, kitendo cha msichana huyo kugundua kuwa Dk. Othman alikuwa Uingereza, kulimaanisha maisha yake kurudia jela. Akamwangalia kwa macho yaliyojaa huruma na wasiwasi, woga ukiwa umemjaa moyoni mwake! Hakuweza kujua mara moja ni kitu gani kitakachotokea mbele yake, ila aliwaza jambo tu, hatari!



Dk. Othman alifanikiwa kutoroka polisi, kwa msaada wa Dk. Ringo. Mipango ikafanyika safari ya Uingereza ikakamilika, ingawa walipata matatizo walipokuwa safarini kuelekea Uwanja wa Ndege lakini Dk. Othman alifika salama Uingereza ambapo alipokelewa na Dk. Immanuel, rafiki mkubwa wa Dk. Ringo.

Ikiwa ni saa chache baada ya kuingia katika nyumba ya Dk. Immanuel, akatokea msichana aliyesababisha mapigo ya moyo wa Othman kubadilisha kasi! Ni kweli alikuwa mrembo sana, lakini sio urembo wake uliomshitua, kuna kitu kingine zaidi! Alihisi angeozea gerezani kama sio kunyongwa! Msichana huyo ni nani? SONGA NAYO…



Alitamani sana kilichokuwa mbele yake ibaki kuwa ndoto, hakutaka iwe kweli, msichana huyo alikuwa na uwezo mkubwa wa kumpeleka jela au hata kunyongwa kutokana na kesi iliyokuwa ikimkabili. Dk. Othman akabaki ameduwaa bila kujua kitu cha kufanya. Akiwa ameyatuliza macho yake juu ya uso wa msichana huyo ambaye aliketi kwenye sofa kubwa kimya, Immanuel alishangazwa sana na hali iliyotokea ghafla nyumbani kwake.

Akawaangalia kwa zamu, Dk. Othman na msichana huyo, kisha akatingisha kichwa kuonyesha kuwa alisikitishwa na hali iliyokuwepo.

“Othman!” Dk. Immanuel aliita.

Dk. Othman hakuitika.

“Hivi kuna nini?” Dk. Immanuel akauliza akiwa na wasiwasi wa wazi kabisa machoni mwake.

Dk. Othman akarudisha kumbukumbu zake miaka miwili iliyopita.

*********

Ilikuwa asubuhi njema sana machoni mwa Dk. Othman, aliamka akiwa mwenye furaha na ari ya kufanya kazi kwa bidii. Ilikuwa ni siku ya mvua za rasharasha, hivyo alilazimika kuvaa koti kubwa jeusi kutokana na baridi iliyoambatana na upepo iliyokuwepo asubuhi hiyo.

Alipomaliza kufanya jambo hilo, haraka akatoka na kwenda kupanda katika gari lake, kisha safari ya kwenda kazini kwake Hospitalini Muhimbili ikaanza. Alishangazwa sana na furaha aliyokuwa nayo ingawa hakuitamani huzuni iingie katika moyo wake.

Alipofika ofisini kwake, akajiandaa kuwaona wagonjwa. Aliporidhika na maandalizi, akamuagiza Muuguzi awaruhusu wagonjwa waingie. Baada ya kuwadumia wagonjwa watatu, akaingia msichana mmoja mrembo sana, alipata kazi kidogo kuvumilia uzuri wa binti huyo aliyevutia.

“Karibu sana dada!”

“Ahsante Dokta!”

“Habari za kazi?”

“Nzuri tu!”

“Dokta nina shida!”

“Usijali, ndiyo maana nikawa hapa, nipo kwa ajili yenu!” Dk. Othman akajibu kwa upole sana, lakini kila dakika moja ilipoondoka ndipo kumbukumbu za msichana huyo zilivyozidi kuja.

Kwa kumwangalia tu, usoni aligundua kuwa msichana huyo naye alikuwa akijaribu kuvuta kumbukumbu zaidi ili aweze kumwuliza jambo. Hata hivyo hakuridhishwa na hisia zake moja kwa moja, alichokifanya ni kumsikiliza kwa makini mgonjwa wake kisha kumpatia matibabu yakinifu. Baada ya muda kidogo, msichana huyo akaangalia juu kwa nukta kadhaa, kisha aliporudisha macho yake chini, akawa kama amekumbuka kitu!

“Samahani Dokta!”

“Bila samahani!”

“Tumewahi kukutana sehemu yoyote kabla?”

“Nahisi hivyo, lakini kila nikijaribu kuvuta kumbukumbu sikumbuki sawasawa!”

“Oh! Yes…sasa nimekumbuka!”

“Nikumbushe tafadhali!”

“Wewe si ni Othman!”

“Ndio!”

“Ok! Mimi ni Isabela!”

“Isabela?”

“Ndio!”

“Makungi Sekondari Mbeya!”

“Hujakosea kitu!” Walikumbuka kila kitu, walisoma pamoja katika Shule ya Sekondari Makunga iliyopo Mbeya. Baada ya kumaliza kidato cha nne kila mmoja alipangiwa shule tofauti, hawakuonana tena mpaka siku hiyo.

Walizungumza mambo mengi sana kuhusu maisha, kila mmoja alikuwa na furaha kukutana na mwenzake.

“Mh! Hongera sana, umekuwa Daktari!”

“Ahsante, lakini kawaida, kazi zetu ngumu sana!”

“Usijali ila umekupendeza sana!”

“Kwanini?”

“Unapendeza kuwa daktari!”

“Nashukuru kusikia hivyo! Hivi bado upo na Richard?”

“Yale yalikuwa mambo ya shule Othman, sasa hivi nina mchumba mwingine, anaishi Uingereza, tunafunga ndoa mwezi wa kumi na mbili!”

“Hongera sana Isabela, umesema yupo Uingereza, anafanya kazi gani huko?”

“Anafanya kazi kama yako!”

“Unamaanisha daktari?”

“Ndio!”

“Siamini, naweza kujua jina lake?”

“Hakuna tatizo, anaitwa Dk. Immanuel!” Wote wakacheka na kugongeana mikono.

*********

Alichojua Dk. Othman ni kwamba kwa alivyofahamiana na Isabela, ilikuwa lazima awe anajua kila kitu kuhusu yeye! Kujua huko kulimaanisha kutoboa siri hiyo, hali ambayo ingesababisha kukamatwa. Kichwa chake kikawa kizito, machozi yakaanza kumtoka.

“Vipi Albert?” Dk. Immanuel akamwambia Othman.

“Hilo sio jina lake, anaitwa Othman!” Isabela akasema kwa sauti kubwa, ni hapo sasa ndipo Othman alipogundua kuwa Isabela alikuwa anamkumbuka kiasi cha kutosha.

“Kwani unamfahamu huyu?”

“Sana!” Isabela akajibu. Lilikuwa jibu lililomshtua zaidi Dk. Othman, kwake ilikuwa ni sawa na mambo kuharibika moja kwa moja. Hakutegemea kama angekutana na mtu mwingine zaidi ya Dk. Immanuel kama alivyoelezwa na rafiki yake Dk. Ringo. Kwa ujumla hilo lilimchanganya sana, lakini hakuwa na kitu cha kufanya zaidi ya kukubaliana na ukweli.

Isabela alikuwa akimfahamu vizuri sana Dk. Othman, hata habari za kufanya jaribio la kumuua Gerald alikuwa nazo, alifahamu ni kiasi gani Dk. Othman alivyokuwa akitafutwa! Kilichomshangaza zaidi ni kukutana na Dk. Othman wakati habari zinazojulikana dunia nzima alijinyonga.

“Lakini mbona vyombo vya habari vilitangaza kuwa ulikufa?” Isabela akauliza.

“Ni habari ndefu Isabela, ila naomba ufiche siri hii!” Hapo sasa Dk. Immanuel akapata picha, alichokifanya ni kumvuta pembeni Isabela kisha akazungumza naye.

“Huyu ni rafiki yangu anaishi Tanzania, ndiye mwenye matatizo niliyokueleza awali, yupo karibu sana na Dk. Ringo, ni lazima tumsaidie na tulinde siri hii, unajua tayari ameshaogopa baada ya kukuona!”

“Hakuna tabu mpenzi, mimi namfahamu zaidi yako, nilisoma naye shule moja ya Sekondari!”

“Kweli?”

“Ndiyo!”

“Basi kama nilivyokuambia, huu ni wakati wa kuwa naye karibu, anahitaji sana ukarimu wetu!”

“Ni kweli kabisa mume wangu!” Wakarudi sebuleni kisha wakazungumza sana na Dk. Othman, wakamtoa wasiwasi juu ya kuvuja kwa siri hiyo. Wote wakafurahi sana.

*********

Wiki mbili baadaye, kila kitu kilikamilika, Dk. Othman alifanyiwa usajili mpya, akanunua uraia wa Uingereza. Kubwa zaidi lililofanyika ilikuwa ni kubadilisha sura pamoja na jina. Kuanzia hapo jina la Albert Mkambila likaanza kutumika. Haikuwa rahisi hata kidogo kukutana naye umtambue kuwa yeye sio Mkambila bali Dk. Othman.



Kilichofanyika baada ya hapo ilikuwa ni kutafuta chuo ambapo aliamua kusomea udaktari kwa mara nyingine ili aweze kupata vyeti akiwa na jina la Albert Mkambila. Masomo hayakuwa magumu kwake, alikuwa akifanya kama marudio tu, alisoma masomo aliyowahi kusoma kabla.

Waliishi maisha mazuri sana kwa Dk. Immanuel, gharama zote za Chuo na matumizi zilitolewa na Dk. Ringo. Baada ya masomo yaliyomchukua miaka minne, aliajiriwa katika hospitali ya utafiti wa mifupa iliyokuwepo London Ungereza. Maisha yake yalibadilika sana, akaishi maisha ya furaha yenye uhakika.

Alipendwa na kila mtu katika hospitali aliyokuwa akifanyia kazi, ndugu zake pekee nchini Uingereza walikuwa ni Dk. Immanuel na Isabela, msichana aliyesoma naye shule ya sekondari miaka mingi iliyopita. Alipanga nyumba na kununua vitu vya thamani. Hiyo ilikuwa furaha kubwa sana kwa rafiki yake mpendwa Dk. Ringo.



Haikuwa rahisi kuamini kuwa alikuwa ni Dk. Othman, Jina hilo alikwisha lisahau siku nyingi, Dk. Mkambila likawa ndio jina lake lilifahamika kwa watu wengi nchini Uingereza. Hiyo ilibaki kuwa siri moyoni mwake na rafiki zake wakaribu. Maisha yake yaliendelea kama kawaida, Dk. Ringo akawa anakwenda kumtembelea rafiki yake kila wakati, alifurahishwa sana na maisha aliyokuwa akiishi Dk. Othman.

Pamoja na maisha ya Dk Othman kuwa mazuri Immanuel na mkewe Isabela walishwangazwa sana na kitu kimoja, Othman kutokuwa na mke! Hilo liliwashangaza sana, wakapanga siku moja wazungumze naye, siku hiyo hiyo wakampigia simu na kumtaka jumapili inayofuata afike nyumbani.

“Mbona ghafla sana kuna nini?” Dk. Othman akauliza kwa mshangao.

“Usijali kaka, kuna mazungumzo muhimu!” Dk. Immanuel alisema.

“Huwezi kuniambia kwenye simu?”

“Hapana…”

“Mambo yameharibika nini?”

“Mh! Umefika mbali, jambo la msingi ni wewe kufika hapa nyumbani juma pili!”

“Hapana, leo jioni nitakuwepo nyumbani jumapili ni mbali sana Dokta!”

“Basi itakuwa vizuri zaidi!” Ndivyo ilivyokuwa, jioni ya siku hiyo baada ya kutoka kazini Dk, Othman alikwenda nyumbani kwa Dk. Immanuel. Alipokelewa kwa furaha sana, tofauti na siku zote alizokuwa akifika pale, siku hiyo alikaribishwa bustanini.



Walipokaa, Dk Immanuel alitabasamu hali iliyomfanya Dk. Othman naye atabasamu.

“Karibu sana, Dk. Othman!”

“Ahsante, naomba unieleze ulichoniitia kuniondoa wasiwasi!”

“Unahisi ni kitu gani?” Dk. Immanuel aliuliza, akiendelea kutabasamu.

“Sijui, naomba unitoe hofu yangu ? ”

“ Subiri shemeji yako aje ! ”

“ Yaani mpaka shemeji aje, kwani kuna nini ? ”

Dk. Othman hakuwa na swali lingine zaidi, alichokifanya ni kusubiri, dakika mbili baadaye Isabela akaja akiwa amebeba chano chenye glasi tatu za maji ya matunda.

“Karibuni jamani ! ”

“ Ahsante ! ” Wote wakaitika. Baada ya muda kidogo, Dk. Immanuel akaanzisha mazungumzo.

“ Dk. Mkambila, maisha yako yamekuwa mazuri sasa, kila kitu unapata lakini kuna kitu kimoja ambacho naamini unakikosa, kitu ambacho ni muhimu katika maisha yako…. ” Kabla hajamalizia kuongea Dk. Othman akamkatisha.

“ Ni kitu gani hicho ? ”

“ Mke ! ” Isabela alidakia.

Lilikuwa jambo lililomuudhi sana Dk. Othman, ghafla akakunja uso wake kisha akaangalia chini, alipoinua uso wake, macho yake yalikuwa yamefunikwa machozi.

“Kuna nini ? ” Dk. Immanuel akauliza, huku akimbembeleza rafiki yake.

“ Sihitaji kuwa na mke !”

“ Kwanini ? ”

“ Yupo mwanamke mmoja pekee ambaye nilimpenda, lakini mambo aliyonifanyia yananifanya nisitamani kuwa na mwanamke mwingine yoyote katika maisha yangu, nilimpenda sana lakini penzi langu kwake likageuka tanuru la moto, sipendi mapenzi ! ”

“ Ni nani huyo ? ” Dk. Immanuel aliuliza.

“ Nashindwa kukueleza rafiki yangu ? ”

“ Kwanini ? ”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“ Sina uhakika kama utaweza kunitunzia siri hii kubwa ! ”

“Kama nimeweza kukutunzia siri hii nitashindwa kukutunzia hiyo nyingine, tafadhali niambie rafiki yangu, sipendi uteseke na kitu moyoni mwako ! ” Dk Immanuel aliongea kwa sauti ya upole akimsihi rafiki yake amueleze ukweli, alitamani sana kumuona rafiki yake akiishi na mke.

“ Niahidi jambo moja ! ”

“ Jambo gani ? ”

“ Kuwa utaitunza siri hiyo ! ”

“Nakuahidi ! ” Kilichofuata hapo, ilikuwa ni machozi machoni mwa Dk. Othman, kila mmoja akishangaa, Isabela akaanza kulia. Nukta chache baadaye, Dk. Immanuel naye alianza kulia.







ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog