Search This Blog

Tuesday 1 November 2022

MKE WANGU JULIANA - 2

 






Simulizi : Mke Wangu Juliana

Sehemu Ya Pili (2)







Mafanikio haikuwa bahati, hakuna mtu aliyefanikiwa kwa bahati. Kufanikiwa si kama kucheza bahati nasibu, ili ufanikiwe ilikuwa ni lazima upambane, ujinyime kwa kufanya mambo mengi ya anasa na mwisho wa siku kupata kile ulichokuwa ukikihitaji.



Ukimuona mtu amefanikiwa, haimaanishi alibahatika, hapana, kufanikiwa ilikuwa ni matokeo ya kufanya kazi kwa bidii, yaani ni sawa na kufaulu mitihani ilikuwa ni lazima usome, huwezi kusema husomi halafu mtihani wa mwisho ufaulu, hakuna kitu kama hicho.



Hiyo ndiyo ilikuwa ni sawa na mafanikio. Wakati mzee huyo akisema hayo yote John alikuwa kimya akimsikiliza kwa makini kana kwamba mwisho wa siku kulikuwa na maswali angeulizwa.



Mzee huyo aliongea kwa dakika zaidi ya arobaini na baada ya hapo, akajiinua kutoka kwenye kiti na kuanza kuelekea ndani pasipo kuaga.



“Umeongea mengi sana, mwisho kabisa unaondoka bila kuniaga!” alisema John huku akitabasamu kwa mshangao.



“Nakuja! Unajua kusoma?”

“Ndiyo!”

“Kiingereza unakijua?”

“Hapana!”



“Hata kidogo?”

“Ndiyo! Sijui hata kidogo!”

Mzee Miraji akatoa tabasamu na kuingia ndani.



John akabaki mahali hapo huku akiangalia jinsi watu walivyokuwa wakiendelea kuchota maji. Aliona namna wengi wao walivyovaa, walionekana kutokuwa na maisha mazuri kabisa, inawezekana yeye alikuwa na maisha mabovu lakini kulikuwa na wengine walikuwa na maisha mabovu kushinda yeye.



Baada ya dakika kadhaa mzee Miraji akarudi akiwa na kitabu mkononi mwake, akamsogelea John na kumkabidhi, kitabu hicho kiliandikwa Rich Dad Poor Dad kilichoandikwa na mwandishi aitwaye Robert Kiyosaki.

“Kiingereza sifahamu!” alisema John haraka sana baada ya kuona kava.



“Umeniambia! Ila hicho kimeandikwa kwa Kiswahili. Unajua hapa Tanzania tuna wahuni wengi sana, wanavichapisha hivyo kwa lugha ya huku na kuuza kisiri,” alisema mzee Miraji, John akakifungua, kweli kiliandikwa kwa lugha ya Kiswahili.

“Kinahusu nini?” aliuliza.





“Ni maisha ya kijana aliyekuwa na baba wa aina mbili, mmoja alikuwa tajiri na mwingine masikini. Hao watu walikuwa na mawazo mawili tofauti waliyokuwa wakimpa kijana huyo. Kakisome, mwisho wa siku utaibuka na kitu kikubwa sana,” alisema mzee Miraji.

“Nashukuru sana!” alisema John, akasimama na kuaga.



“Ila kumbuka kitu kimoja!”

“Kipi?”

“Kufanya kazi kwa bidii! Usipende kulala, kumbuka usingizi rafiki yake umasikini!” alisema mzee huyo. John akatoa tabasamu na kuondoka zake.



Akafika chumbani kwake, kitu cha kwanza kilikuwa ni kufungua kitabu kile na kuanza kukisoma, alivutiwa nacho, kwenye kila mstari ambao aliupitia ulikuwa ukimgusa mno.



Alikaa na hicho kitabu kwa siku mbili, alikisoma kwa ufasaha mpaka Jumamosi ambapo akamrudishia mzee huyo, akamwambia alichojifunza na kumuahidi angeyafanyia kazi mambo yote na mwisho kufanikiwa kama watu wengine.



Hilo lilikuwa jambo zuri hivyo akaondoka zake. Siku ziliendelea kukatika na ilipofika Jumapili, asubuhi na mapema akajiandaa na kwenda kanisani, katika Kanisa la TAG Mwanga Msufini ambalo alikwenda siku kadhaa zilizopita.



Aliingia kanisani hapo akiwa mgeni kabisa, kila mtu aliyekuwa akimwangalia, hakumfahamu hata mmoja. Alivalia kawaida, vijana wengi waliokuwa humo walipendeza, walivalia nadhifu na walionekana kuwa na mafanikio makubwa.



Alikaribishwa na mwanamke mtu mzima aliyekuwa mlangoni mwenye cheo cha shemasi na kuonyeshwa kiti alichotakiwa kukaa, akakisogelea na kutulia hapo.



Moyo wake ulifarijika, ilipita miaka mingi hakuwa ameingia kanisa kiasi kwamba aliamini hakuwa akifanikiwa kwa sababu alijiweka mbali na Mungu.



Alitulia kitini hapo, alionekana kuwa na hofu moyoni mwake, na hata ibada ilipoanza, alitumia muda mwingi kuwa kimya na kuangalia huku na kule.



Ilipofika majira ya saa 3:35 asubuhi, akaanza kusikia watu wakiongea kwa nyuma, akageuka na alipopitisha macho yake, yakatua kwa msichana mmoja mrembo mno, aliyevalia vizuri na kuzibana nywele zake vilivyo.





Alimwangalia msichana huyo, alishtuka, hakutegemea kumuona ndani ya kanisa hilo. Akaachana na ibada kwanza, aliyagandisha macho yake kwa sekunde kadhaa huku akionekana kama kupigwa butwaa.

Alikuwa Deborah!



Msichana huyo baada ya kuongea na kusalimiana na mwanamke aliyekuwa mlangoni, akaingia ndani.



Uzuri wake ulikuwa tishio, wanaume wakageuka na kumwangalia.

Kila alipokuwa akipita, hapakuwa na utulivu wa macho, watu wengi walikuwa wakimwangalia yeye, alionekana kutokujali, akatafuta kiti na kukaa, kitu cha kwanza kilikuwa ni kusali kwa kumshuruku Mungu kufika salama kanisani hapo.



Muda wote huo John hakuacha kumwangalia msichana huyo. Alikuwa mzuri, aliyevutia lakini alionekana kuwa mnyenyekevu mbele za Mungu, hakuringia uzuri wake, inawezekana aliringia huko nje lakini ndani ya kanisa, alionekana kuwa mnyenyekevu kupita kawaida.



“Mwanamke mzuri halafu mnyenyekevu kwa Mungu! Sijawahi kuona,” alijisemea John wakati Deborah akisimama na kwenda mbele kabisa na kuanza kucheza pamoja na waimbaji, alicheza bila kujali uzuri wake, mavazi yake, alipokuwa mbele za Mungu, alicheza kadiri awezavyo kama Mfalme Daudi.



Ibada iliendelea, wageni walijitambulisha na watu walipomsikia John ametoka jijini Dar es Salaam, wakahitaji kufahamu mengi kuhusu sehemu hiyo kwani wengi walikuwa wakipasikia tu.



Ibada ilipomaliza, vijana wakamfuata na kumsalimia kwa shangwe, walimkaribisha kwani alisema kuwa amehamia kwenye kanisa hilo, maisha yake yote yangekuwa mkoani Kigoma.



Wakati akisalimiana na washirika wengine, akili yake ilikuwa kwa Deborah, msichana huyo aliuteka moyo wake ghafla sana, alichanganyikiwa, alijiona kuwa na uhitaji mkubwa wa kuwa na Deborah.



Labda amuoe! Akaona kuwa jambo gumu kwa sababu kwa jinsi alivyovaa tu ilionyesha kutoka kwenye familia ya kitajiri tofauti na alivyokuwa.



Alimwangalia msichana huyo aliyekuwa akiongea na watu, moyo wake ulivurugika kabisa, alisubiri kufuatwa na Deborah ili aende kumsalimia na kumkaribisha lakini hakupata nafasi hiyo, akaamua kwenda yeye mwenyewe.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Alipomfikia, akaonyesha tabasamu, naye msichana huyo akafanya hivyohivyo na kumpa mkono kwa lengo la kumsalimia. Walipogusana, John akahisi kama akipigwa shoti moja ya hatari!



“Karibu sana mgeni! Nilisikia umetoka Dar es Salaam!” alisema msichana huyo huku akiachia tabasamu pana.

“Ndiyo! Nimetoka huko!”

“Na umekuja huku kufanya nini? Kutembea?”



“Hapana! Nimekuja kutafuta maisha!”

“Kigoma?”

“Ndiyo! Nimebarikiwa sana na huduma yenu, hakika sijawahi kuiona kwenye makanisa mengi!” alisema John.



“Usijali! Tunapokuwa mbele za Mungu huwa hatutakiwi kujiona kitu, hatutakiwi kuyaangalia mavazi yetu, ni kama ilivyokuwa kwa Mfalme Daudi, mbele za Mungu alicheza mpaka nguo zikamvuta, hakuangalia ufalme wake,” alisema msichana huyo.



“Nimebarikiwa kwa kweli!”

“Oh! Utukufu kwa Mungu!” alisema Deborah, wakapiga stori mbili tatu, msichana huyo akamuaga.



“Ila hujaniambia unaitwa nani!” alisema John.

“Naitwa Deborah!”



“Oh! Asante kwa kukufahamu!”

“Karibu!”

Deborah akasalimiana na watu wengine na kuwachukua wadogo zake, wakaingia ndani ya gari na wazazi wao kisha kuondoka kanisani hapo.



John alibaki akiwa amesimama, aliliangalia gari lilivyokuwa likiondoka machoni mwake. Alitamani kulisimamisha , azungumze tena na Deborah kwani alivurugwa mno.



Huku akiwa kwenye hali hiyo, mara akashikwa bega kwa nyuma, haraka sana akageuka, macho yake yakagongana na ya msichana mmoja aliyekuwa kwenye tabasamu pana, mavazi yake yalikuwa ya kawaida, si kama Deborah.



“Karibu sana mgeni!” alisema msichana huyo huku akimpa mkono.



“Nashukuru sana!”

“Naitwa Juliana!” alisema.

“Oh! Naitwa John!”

“Karibu mpendwa!” alisema msichana huyo huku akiwa na tabasamu.



“Asante sana!” aliitikia na msichana huyo kuondoka, haraka sana akageuka ili aliangalie tena lile gari, lilipotea machoni mwake.

“Deborah! Deborah! Deborah! Nitapambana kwa ajili yako, nifanikiwe na kukutolea mahari!” alijisemea kwa sauti ndogo, moyo wake ukatekwa vilivyo na msichana huyo.



John alichanganyikiwa, akili yake iliruka, hakuamini kama angekutana na msichana aliyekuwa mrembo wa sura kama alivyokuwa Deborah.



Moyo wake ni kama ulipigwa ganzi, sura ya msichana yule iliendelea kukisumbua kichwa chake. Alibaki kanisani akiongea na watu wengine lakini akili yake haikuwa hapo kabisa.



Alitamani kuuliza kuhusu msichana huyo zaidi, alihitaji kufahamu mahali alipokuwa akiishi, aende kuzungumza naye na kumwambia alikuwa mzuri lakini alishindwa kufanya hivyo.

Alikaa kanisani kwa dakika kadhaa kisha kurudi nyumbani.



Sura ya Deborah iliendelea kuwa kichwani mwake, alipaangalia Kigoma, alimkumbuka msichana yule, moyoni alijiambia kabisa hakustahili kuishi huko, alitakiwa kwenda kuishi jijini Dar es Salaam katika mtaa wa watu wenye pesa, Osterbay.



Njia nzima ya kwenda nyumbani aliendelea kumfikiria msichana huyo, alikuwa na mawazo mengi mno mpaka alipofika nyumbani ambapo akajifungia chumbani kwake.



Alitulia humo kwa dakika kadhaa, akachukua kitabu chake ambacho alikuwa na kazi ya kuandika kila kitu kilichokuwa kikiendelea (diary) na kuandika kuhusu msichana huyo.



Jumapili, 14/08/2016: Nilimuona msichana mrembo wa sura, nikampenda, ni msichana wa aina yake ambaye ninaamini ni lazima siku moja atakuja na kuwa mke wangu wa ndoa. Kwa jina anaitwa Deborah.



Baada ya kuandika hivyo, akatulia chumbani hapo mpaka jioni ambapo akatembeatembea na usiku ulipoingia akaingia chumbani na kulala.



Asubuhi ilipofika, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumkumbuka Deborah, hakuacha kuchanganyikiwa, alitamani siku hiyo amuone tena lakini hakujua ni mahali gani alipokuwa akiishi.



Alfajiri hiyo akaondoka na kuelekea Kibirizi kuchukua samaki na rafiki yake, Jumanne. Njiani walikuwa wakizungumza mambo mengi kuhusu maisha huku kwenye kila neno alilokuwa akizungumza Jumanne alimsisitizia ni lazima awekeze sana na kuachana na wanawake.



“Mimi sipendi wanawake!” alisema John.

“Ni vizuri sana kama ndiyo hivyo, utafanikiwa!”



“Ila nampenda mwanamke mmoja tu!” alisema.

“Mwanamke gani?”

“Anaitwa Deborah!”

“Yupo Dar?”

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Hapana! Nilimuona jana kanisani!” Jumanne akasimama na kumwangalia rafiki yake, ni kama alimshangaa sana, hapohapo akaanza kutoa kicheko kikubwa na kumpigapiga begani mwake.



“Rafiki yangu! Hawa mademu wasikuchanganye sana,” alisema Jumanne huku akimwangalia John na kuendelea kucheka.



“Ila ninataka kumuoa!”

“Kwani yupo vipi?”

“Ni mrembo! Halafu anaonekana ana pesa sana,” alijibu.

“Ana pesa?”

“Ndiyo!”



“Sasa atakukubali muuza samaki?”

“Ushaanza kunishusha sasa!”

“Si hivyo! Unajua hawa mademu wa sasa hivi wanapenda sana pesa!” alisema Jumanne.

“Ila yule ameokoka!”



“Nani kakwambia waliookoka hawapendi pesa? Kuna wachungaji matapeli kichizi,” alisema Jumanne.



“Kwa hiyo nifanyeje?”

“Umempenda kweli?”

“Sana tu!”

“Basi mwambie!”

“Mh!”



“Usigune! Mfuate na umwambie ukweli! Au unaogopa?”

“Sikuwahi kuzungumza naye ujue, yaani tulisalimiana tu!” alisema John huku akimwangalia rafiki yake huyo.



“Haijalishi! Mfuate na uzungumze naye!”

Wakafika Kibirizi, wakachukua samaki na kwenda kutembeza kama kawaida yao. Siku nzima kichwa cha John kiliendelea kumfikiria Deborah, alitamani kumtafuta na kumwambia kama alivyoambiwa na Jumanne lakini alishindwa kufanya hivyo.



Alijipa moyo kwamba inawezekana Jumatano msichana huyo angekuwepo ibadani hivyo siku hiyo ilipofika, akaelekea kanisani jioni. Muda wote macho yake yalikuwa yakiangalia huku na kule, kila aliposikia mtu akiingia kanisani, aligeuka na kuangalia.



Deborah hakufika kanisani, alichanganyikiwa lakini alijipa moyo kwamba ilikuwa ni lazima ajue mahali msichana huyo alipokuwa akiishi ama kufanya kazi.



Ibada ilipokwisha, akasalimiana na washirika wenzake, akamfuata kijana mmoja ambaye kidogo alizoeana nae na kuanza kumuuliza kuhusu Deborah.



“Yupo vipi?”

“Ni mweupe kidogo, anapendeza, alikuja na familia yake na kuondoka nayo kwa gari,” alijibu John.



“Unamzungumzia Deborah!”

“Yeah! Halafu ndiye yeye bwana! Sijui kwa nini sikukutajia jina lake!” alisema John na kuanza kucheka.

“Amefanya nini?”

“Kwani anaishi wapi?”

“Mji Mwema!”



“Mji Mwema! Kule ushuani?”

“Yeah! Anafanya kazi kwenye kampuni ya kusindika samaki!” alijibu kijana huyo.

“Oh! Sawa! Mji Mwema sehemu gani?”

“Unazijua kota za Posta?”





“Ndiyo!” alijibu japokuwa hakuwa akizijua.

“Basi kwenye kota zile, nyumba ya juu! Zamani walikuwa wakiishi Wakongoman, hapo ndipo anapoishi!” alisema kijana huyo.

“Kumbe ni pale?”



“Yeah!”

Alielekezwa, akaridhika na siku iliyofuata huku akiwa na kapu lake la samaki akaanza kwenda huko Mji Mwema. Alipitia njia ya makaburi ya Mwanga, akatokea Mtaa wa Game ambapo akaunganisha mpaka kwenye barabara iliyokuwa ikielekea Mji Mwema na kuanza kupandisha kilima kidogo.



Majumba yaliyojengwa huko yalimdatisha kupita kawaida, alibaki akiyaangalia, yalivutia machoni mwake. Alipandisha na nyia hiyo mpaka kwenye kota tatu za Posta ambazo zilikuwa zimezungushiwa fensi ya seng’enge na kuziangalia.



“Niliambiwa kwa juu! Kwa hiyo ili kufika upande wa pili inabidi nipitie na hii barabara mpaka huko!” alijisema na kuanza kuifuata narabara ya upande wa kulia, mbele kidogo akapandisha ya upande wa kushoto na kuachana na ile iliyokuwa ikielekea jeshini na kuunganisha mpaka Bangwe kulipokuwa na nyumba ya mkuu wa mkoa.



Akapandisha juu mpaka alipokutana na njia panda ambapo akakata kushoto na kukutana na nyumba kadhaa zilizoonyesha kumilikiwa na watu wenye pesa.



Aliifuata nyumba ya kwanza, alipofika getini, akaanza kugonga, wala hazikupita sekunde nyingi, mlango ukafunguliwa na mlinzi mmoja aliyekuwa na bunduki yake kubwa.

“Samahani!” alisema mara baada ya salamu.

“Bila samahani!”



“Hapana ni kwa akina Deborah?” aliuliza huku akimwangalia mlinzi huyo.

“Hapana! Ni nyumba hiyo inayofuata!” “Sawa.”



Akatoka na kwenda katika nyumba hiyo, alipofika, akagonga hodi, geti likafunguliwa na mlinzi na kuanza kuzungumza naye. Alimuulizia Deborah, akaambiwa hakuwepo.

“Yupo nani?” aliuliza.



“Mfanyakazi na mama yake!”

“Sawa! Aliniambia nilete samaki hapa!”

“Nani?”



“Deborah! Nimetoka kazini kwake akasema nilete hapa,” alisema John.

“Sawa! Ngoja nimuite dada wa kazi!” alisema mlinzi na kuondoka.



Baada ya dakika mbili, akarudi akiwa na mfanyakazi aliyekuwa na sufuria ndogo, akamwambia kama alivyomwambia mlinzi na kisha kumpa samaki wadogo na kisha kuondoka zake.





Alijihesabia hasara lakini hilo hakutaka kulitia akilini kabisa, alichokuwa akihitaji ni kuwa na huyo Deborah tu. Aliendelea na biashara zake na alipomaliza, akarudi zake nyumbani na kuendelea na ratiba zake nyingine.



*** Deborah alikuwa kazini kwake akiendelea na kazi yake kama kawaida. Alikuwa na furaha tele kwa sababu barua za kuongezwa mishahara zilifika ofisini na hivyo kusaini mkataba mwingine.



Muda wote moyo wake ulikuwa na furaha tele, hakuamini kama kweli dau lake lilipanda na hivyo kuyafanya maisha yake kuwa mazuri zaidi.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Alifikiria mambo mengi lakini kubwa zaidi lilikuwa ni kujenga nyumba yake mwenyewe. Baba yake alimpa zawadi ya kiwanja kilichokuwa hukohuko Mji Mwema na kitu ambacho alitakiwa kufanya ni kujenga nyumba yake tu.



Huku akiendelea na kazi yake, akaona simu yake ikiita, haraka sana akaichukua na kuangalia kioo, alikuwa mama yake, akaachia tabasamu na kuipokea.



“Mama huwezi kuamini!” alisema Deborah hata kabla ya salamu.

“Kuna nini tena?”

“Eti tumeongezewa mishahara!” alisema huku akionekana kuwa na furaha.



“Ndiyo maana ukatuagizia samaki, tule tujidai?” aliuliza mama yake.

“Kuwaagizia samaki?”

“Ndiyo! Si umemwambia muuza samaki alete samaki hapa nyumbani?” aliuliza mama yake.

“Mimi?”



“Ndiyo!”

“Hapana mama!”

“Ila muuzaji alisema umemuagiza, na kawaacha hapa ndiyo tunawatengeneza!” alisema mama yake.

“Oh! Samaki? Yeah! Nilimwambia awalete, kumbe aliwaleta?”



“Ndiyo!”

“Sawa mama! Kesho nitaagiza wengine,” alisema na kisha kukata simu.

Akaanza kujifikiria, alimwambia mama yake kwamba kweli alimwagiza mtu apeleke samaki lakini ukweli ni kwamba hakufanya hivyo.



Alijifikiria ni mtu gani alimwambia muuzaji apeleke samaki nyumbani kwao lakini akashindwa kupata jibu.

Alikaa kwa dakika nyingi akiwa na mawazo ndipo akahisi inawezekana mtu aliyemtuma muuza samaki apeleke samaki nyumbani kwao alikuwa akimtaka.

“Huu uzuri huu! Yesu nisaidie!” alisema Deborah.



Alifanya kazi mpaka jioni, akarudi nyumbani na kuendelea na mambo yake. Bado suala la muuza samaki lilimsumbua moyo wake, alijifikiria sana na kusubiri kama angeona namba ikimpigia na kumwambia kuhusu suala la samaki lakini hapakuwa na simu yoyote iliyoingia.



“Sasa atakuwa nani? Mh! Hawa wanaume wana shida sana,” alijisemea na kuanza kucheka, jambo la samaki akaamua kulipuuzia.



*** Juliana alikuwa na shida nyingi, matatizo mngi ya kifamilia, yalimsononesha na kumkata maini lakini hayo yote hayakumfanya kuacha kumfikiria mwanaume ambaye alimuona kanisani, John aliyetoka jijini Dar es Salaam.



Moyo wake ulimpenda mara ya kwanza tu alipomuona, alisalimiana naye na alipogusana naye mikono, alihisi hali ya ajabu ikiwa imepita mwilini mwake.



Alihisi huyo ndiye ambaye angekuja kuwa mume wake wa baadaye, alikuwa na hisia hizo lakini hakujua ni kwa namna gani angezibadilisha hisia hizo na kuwa kweli.



Alitoka jijini Dar es Salaam, bila shaka alikuwa na pesa za kutosha. Hakutaka kuangalia pesa, alichokuwa akikiangalia ni penzi lake moyoni mwake, amuoe na hatimaye kuishi naye mpaka kifo chake.



Hakujua alikuwa akiishi wapi lakini aliamini angezidi kumuona zaidi kwa kuwa alisema hapo Kigoma alihamia na angeishi maisha yake yote.



Alitamani kumwambia mama yake juu ya mwanaume huyo lakini alishindwa, kwanza angeanzia wapi, angemwambiaje ili apate kueleweka na kuonekana mtu aliyekuwa akijielewa.



Ikambidi anyamaze tu, hivyo kuendelea na maisha yake. Hali ilikuwa mbaya nyumbani kwao, hawakuwa na nafuu hata kidogo, kila siku kupata ilikuwa majaliwa lakini kukosa ilikuwa ni kawaida sana.





Waliteseka, hawakuwa na kimbilio jingine lakini kila siku mama yake aliamini kuna siku wangefanikiwa, wangekuwa na maisha mazuri kama waliyokuwanayo watu wengine.

Hakuacha kuwaambia hivyo watoto wake, Juliana alimuunga mkono lakini kila alipoangalia mbele, hakuona dalili za kuwa na maisha hayo hata kidogo.

Alikubaliana na mama yake kwa sababu tu hakutaka kumkatisha tamaa lakini ukweli ni kwamba moyo wake haukuamini hata kidogo.

Siku ziliendelea kukatika, maisha yaliendelea kuwa mabovu kiasi kwamba hata ada ya mtoto ilikosekana na hivyo kurudishwa nyumbani kwanza.

Hilo lilionekana kuwa pigo kwa familia nzima, walikuwa na mawazo lakini hawakutaka kukata tamaa, waliendelea kufanya biashara ndogondogo ya mboga za majani sokoni kwani ndicho kitu walichokuwanacho kipindi hicho.

“Juliana! Unajua nakupenda sana,” alisikika mwanaume mmoja, alikuwa mwanaume mwenye umri wa miaka thelathini, aliyekuwa akijiheshimu, maisha mazuri, alikuwa na kila kitu kilichomfanya kuonekana mwanaume mwenye mafanikio.

Alikuwa na pikipiki tatu alizowapa vijana ambao kazi yao ilikuwa ni kumpelekea pesa ya hesabu kila Jumapili. Hakuwa na shida hata kidogo, alikuwa na kila kitu alichokihitaji.

Mwanaume huyo aliitwa Sangiwa Machebe. Alikuwa kijana mtanashati ambaye alipendwa na wasichana wengi kwa kuwa maisha yake yalikuwa ni ya mafanikio makubwa.

Alipapatikiwa na kila mtu lakini kwake mtu aliyekuwa akimpenda kwa moyo wake wote alikuwa huyo Juliana. Alijitahidi kumnunulia zawadi nyingi, kumwambia kwamba alikuwa akimpenda lakini msichana huyo hakutaka kuelewa kabisa.

Hilo lilimuumiza Sangiwa, alihitaji kuyabadilisha maisha ya msichana huyo lakini yeye mwenyewe alionekana kutokuwa radhi kukubaliana naye.

Kila siku aliambiwa kwamba moyo wake haukuwa kwake, ni kweli alikuwa na mafanikio makubwa lakini kwa msichana huyo alionekana kuwa si lolote lile.

“Juliana! Kwani tatizo nini?” aliuliza Sangiwa huku akimwangalia msichana huyo.

“Ni kwamba moyo wangu haupo kwako!” alijibu kwa sauti ya upole.

“Upo wapi sasa?”

“Sijajua kabisa.”

“Kwa mwanaume mwenye pesa kuliko mimi?” aliuliza.

“Hapana!”

“Mwenye elimu kuliko mimi?”

“Hapana Sangiwa!”

“Au mwenye kazi nzuri kuliko mimi?” aliuliza tena.

“Sangiwa! Naomba unielewe tu kaka yangu, nitaendelea kukuheshimu kama kaka yangu!”

“Kaka yako?”

“Ndiyo! Sangiwa naomba unielewe! Kuwa na wewe halafu moyo wangu ukawa haupo kwako, unahisi ni kitu kizuri?” aliuliza msichana huyo.

“Ila si unaweza hata kunipenda mbele ya safari! Ninahitaji kuwa nawe,” alisema Sangiwa, kwa jinsi alivyokuwa akionekana usoni, alimaanisha alichokuwa akikisema.

Hilo halikukubalika kwa Juliana, ni kweli Sangiwa alikuwa na maisha mazuri, kila kitu ambacho kilihitajika kwa mwanamke yeyote yule lakini jambo la ajabu kabisa, kwa msichana huyo hakuwa moyoni mwake hata kidogo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Wanawake wengi walijua ni kwa namna gani Sangiwa alimpenda Juliana, waliona wivu, walimshangaa msichana huyo, walitamani kumshawishi akubaliane naye lakini kwa Juliana lilikuwa jambo lisilowezekana hata kidogo.

Mama yake alifahamu hilo lakini hakutaka kumuingilia binti yake, aliamini msichana huyo alikuwa na uhuru wa kumchagua mwanaume yeyote wa maisha yake lakini si kumlazimisha awe na mtu fulani kwa kuwa alikuwa na pesa.

Alimsisitizia kila siku Juliana kwamba mwanaume ambaye angekubali kuwa naye basi awe amempenda kwa moyo wake, na si kumpenda kwa sababu ana kitu fulani katika maisha yake.

“Kama si chaguo lako, achana naye,” alisema mama yake, alikuwa akimzungumzia Sangiwa.

“Najua mama! Ila ananing’ang’ania sana!”

“Hata akisema nini, hutakiwi kwenda kinyume na moyo wako! Binti yangu hebu sogea hapa,” alisema mama yake na kumtaka asogee. Akaendelea:

“Mungu amekuandaliwa mume mwema maishani mwako, ni lazima ujue moyo wako unahitaji nini, kama mtu hayupo, usiyalazimishe mapenzi kwani kuna wengi wanajuta mpaka leo hii.

“Kuna wanawake wanalia kwenye ndoa, waliangalia pesa, umaarufu, vikawadanganya, hawakufuata mioyo yao, tamaa iliwaingia na wakati mwingine wanajuta kwa nini wapo kwenye ndoa,” alisema mama yake na kuendelea.

“Ni lazima ujue kila mwanamke unayemuona hapa duniani, Mungu amemuandalia mume mzuri ambaye utaishi naye kwa upendo na amani maisha yako yote, hata mkigombana, mtakuwa wepesi mno kusameheana na kusahau mliyotendeana, ila ukijilazimisha kumfuata fulani kisa pesa, kuna siku utalia na kujuta maisha yako yote,” alisema mwanamke huyo.

Maneno ya mama yake yakaingia moyoni mwake, yakamjenga na kurudi nyuma kutoka kwa Sangiwa. Yalimfungua na kumshukuru kwani alihisi endapo angemkubali mwanaume huyo, kuna siku isiyokuwa na jina angekuja kuumia mno moyoni mwake, na inawezekana matatizo yakawa makubwa mpaka kujimaliza, hivyo hakutakiwa kuwa na haraka.

Hapo, alitamani kumwambia mama yake kuhusu huyo John ila hakujua ni kwa namna gani angemuanza. Alihisi mama yake angemwambia kwamba kwa sababu alitoka jijini Dar es Salaam ndiyo maana alimpenda kumbe haikuwa hivyo.

Hakutaka kumwambia kwa wakati huo lakini alijiahidi kwamba siku moja ilikuwa ni lazima kumwambia kuhusu moyo wake, jinsi ulivyompenda mwanaume huyo ambaye hakujua aliishi wapi, alichokijua ni kwamba alikuwa akisali naye kanisa, hilo tu.

***

Jumatatu, 15/08/2016: Nilimpelekea Deborah zawadi ya samaki nyumbani kwao lakini kwa bahati mbaya sikuweza kumuona, hivyo nikaiacha zawadi hiyo mahali hapo.

Bado moyo wa John ulikuwa kwa msichana Deborah, kwake mtu huyo alionekana kuwa kila kitu, alimpenda na alikuwa tayari kufanya lolote lile kwa ajili yake.

Sura ya msichana huyo haikutoka akilini mwake, alivumilia mpaka siku ya Jumapili ambayo alikwenda kanisani lakini lengo lake kubwa likiwa ni kuonana na msichana huyo.

Alipofika, akasali, na huku ibada ikiwa inaendelea, msichana Deborah akafika na kuingia kanisani. Alikuwa vilevile, urembo wake ulikuwa ni wa juu kabisa, alionekana kupendeza na kuvutia kupita kawaida.

Wanaume kwa wanawake wakageuka na kuanza kumwangalia msichana huyo aliyekuwa akipiga hatua kuelekea sehemu ya kukaa na kama kawaida akapiga magoti na kuanza kumshukuru Mungu kwa kumfikisha salama kanisani hapo.

Macho ya John hayakutulia, alibaki akimwangalia Deborah tu, alitamani kumfuata na kuzungumza naye lakini alishindwa. Moyo wake ulikufa ganzi, alikuwa na mawazo tele na aliiona hiyo kuwa nafasi yake.

“Ngoja ibada iishe! Leo lazima niongee naye tena,” alijisemea huku akiendelea kumwangalia msichana huyo.

Ibada iliendelea huku kila wakati macho ya John yakiwa kwa Deborah, alimpenda kwa moyo wa dhati na alitamani sana muda ufike amfuate na kuzungumza naye lakini aliona kama akicheleweshwa kufanya hivyo.

Baada ya saa kadhaa, ibada ikamalizika na akasimama nje huku akimsubiri msichana huyo mrembo. Alisimama kwa dakika kadhaa, akashtuka kuona msichana mmoja akija mbele yake huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana. Alikuwa Juliana.

“Bwana Yesu asifiwe!” alimsalimia msichana huyo huku lile tabasamu likiendelea kuwepo usoni mwake.

“Amen!” aliitikia lakini macho yake hayakuwa radhi kumwangalia Juliana muda wote, alikuwa akichunguliachungulia kanisani.

“Umependeza sana leo!”

“Nashukuru mno! Utukufu kwa Mungu aliye hai!” alijibu.

“Hivi unaishi wapi?”

“Nani? Mimi?” aliuliza.

“Ndiyo!”

“Nipo hapo mbele, karibu na makaburi!”

“Mwanga Makaburini?”

“Ndiyo! Nyum....” alisema Juliana lakini hata kabla hajamalizia sentensi yake, John akaingilia.

“Samahani kidogo!” alimwambia baada ya kumuona Deborah akiwa ametoka kanisa.

Akamfuata na kumsalimia.

Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kwa nguvu, hakuamini kama alikuwa amesimama mbele ya msichana huyo kwa mara nyingine tena.

Uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana, kwake, kile kilichokuwa kikiendelea kilionekana kama muujiza fulani hivi. Hakujua ni kitu gani alitakiwa kumwambia, alimsimamisha, akamsalimia lakini hakujua ni kipi kingine alichotakiwa kuzungumza.

“Umependeza sana,” alimwambia.

“Nashukuru sana!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Juzi nilikuletea samaki, sijui ulipata?” aliuliza, hakutaka kuchelewa, ilikuwa ni lazima amfanye msichana huyo ajue kwamba yeye ndiye ambaye alipeleka wale samaki.

“Oh! Kumbe ni wewe?”

“Yeah! Ni mimi! Ulipata?” aliuliza.

“Ndiyo! Nashukuru sana Mungu akubariki!” alisema Deborah, akatoa tabasamu pana ambalo liliuvuruga moyo wa John kabisa.

“Amen.”

“Unauza samaki?” aliuliza.

“Ndiyo!”

“Una mtumbwi ama?” aliuliza.

“Hapana! Rejareja tu! Nanunua na kuwauza mitaani!”

“NA nilisikia umetoka Dar es Salaam!”

“Yeah! Ushawahi kufika?”

“Mara moja tu! Mwaka juzi, na sikukaa sana!”

“Oh!”

“Yeah! Nilikuwa huko kikazi kidogo, kwenye semina!” alijibu.

“Semina gani? Kampuni gani?”

“Kigoma Fishing Company,” alimjibu, John akashtuka.

“Kigoma Fishing Company?”

“Ndiyo! Unaijua?”

“Ndiyo! Mungu wangu kumbe unafanya kazi kwenye kampuni hiyo?” aliuliza John huku akijifanya kutokuamini.

“Ndiyo!”

“Mungu wangu!”

“Kwani kuna nini?”

“Ops! Siamini! Unafanya kazi kwenye kampuni hiyo?” aliuliza tena na tena.

Hilo likamfanya Deborah kushtuka zaidi, akajikuta akiingiwa na shauku ya kutaka kufahamu ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea kwenye kampuni hiyo ambayo alijitolea kwa nguvu zote kufanya kazi usiku na mchana.

John hakutaka kumwambia sababu siku hiyo, alichomwambia ni kutafuta muda ambapo watakaa pamoja na kuzungumza kuhusu kampuni hiyo na sababu iliyomfanya kushtuka namna hiyo.

“Mh! Ila kuna nini?” aliuliza Deborah!

“Usijali! Nitakwambia! Kumbe kwenye kampuni hiyo? Aiseee!” alisema, maneno ambayo yalizidi kumtia msichana huyo kwenye maswali mengi.

Hiyo ilikuwa njia ya kwanza ambayo alitamani sana kumzoea msichana huyo. Hapakuwa na jambo lolote lile, alijua kwamba endapo angejifanya kuwa na kitu kuhusu kampuni hiyo basi msichana huyo angehitaji kujua na hivyo kumwambia waonane ili wazungumze zaidi.

Hilo ndilo alilolitaka, alihitaji kuzoeleka na msichana huyo, hiyo iwe mwanzo na mwisho kabisa wawe wapenzi kama alivyotaka iwe.

Alichokifanya ni kumuomba namba ya simu ili siku akiwa na muda ampigie, waonane na kumwambia mengi. Kwa kuwa Deborah alikuwa na hamu kubwa ya kutaka kujua, akamwachia namba yake na hivyo kuondoka zake.

Muda wote huyo Juliana alikuwa pembeni, macho yake hayakutoka kwa wawili hao, aliwaangalia, kwa jinsi John alivyoonekana tu ilionyesha ni kwa namna gani alimvutiwa na Deborah, hata ongea yake ilikuwa na maana kubwa sana kwa kile kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake.

Baada ya kumaliza kuzungumza na John, Deborah akaomba kuondoka, akaruhusiwa na hapohapo Juliana kumfuata John ambaye alibaki akiwa amesimama akimwangalia msichana huyo.

“John!” aliita. John akageuka na kumwangalia Juliana.

“Naam!”

“Umeniacha solemba!”

“Oh! Samahani! Hivi unaitwa nani vile?”

“Juliana!”

“Oh! Sawa dada! Ulikuwa unasemaje?” aliuliza John huku kwa macho ya kuibia akimwangalia Deborah aliyekuwa akiingia ndani ya gari na kuondoka mahali hapo na familia yake.

“Nilitaka kukusalimia tu!”

“Oh! Ahsante sana dada yangu!” alisema John.

“Sawa. Mungu akubariki! Tutaonana Mungu akipenda!” alisema msichana huyo, akamuaga na kuondoka zake.





John alikuwa na namba ya simu ya Deborah, kilikuwa kitu kizuri ambacho alitamani kuwa nacho kwa kipindi kirefu mno. Moyo wake ulikuwa na furaha tele, hakuamini kwamba hatimaye alikuwa akienda kufanikisha kile alichokuwa akikifikiria kila siku.

Hofu yake ilikuwa ni muonekano wake tu. Yaani yeye na Deborah hata kama walikuwa wakisimama pamoja walionekana kuwa watu wawili tofauti. Msichana huyo alikuwa wa kishua, aliyetoka kwenye familia ya kishua, msichana ambaye alikuwa na uwezo wa kumchagua mwanaume aliyekuwa akimtaka.

Hofu yake hiyo ilianza kutoweka baada ya kukumbuka kwamba alitoka jijini Dar es Salaam. Kilichoaminika ni kwamba wasichana wengi waliokuwa wakiishi mikoani waliwaona wanaume wa Dar kuwa tofauti fulani kuliko wa huko.

Wengi walihisi wana pesa, muonekano mzuri, jinsi walivyoongea waliongea vizuri na mambo mengine ambayo kila siku waliendelea kujidanganya nayo.

Hilo likamfanya kuhisi kwamba angeweza kumdaka msichana huyo ila alipokuja kukumbuka kwamba yeye alikuwa muuza samaki tu, mnuka shombo, moyo wake ukafa ganzi.

Akaondoka kanisani, alipofika nyumbani akatulia, akachukua simu yake iliyofungwa na ruber band na kuanza kuiangalia namba ya msichana huyo.

Moyo wake ulikuwa na shauku ya kumpigia na kuzungumza naye, hata asikie sauti yake tu ili moyo wake uridhike. Alivuta pumzi kwa dakika chache tu, hatimaye akaamua kumpigia simu msichana huyo.

Wakati simu ikianza kuita, moyo wake ulikuwa na presha kubwa, ulikuwa unadunda kwa nguvu kama ulitaka kuchomoka kutoka kifuani. Baada ya sekunde chache, ikapokelewa.

“Bwana Yesu asifiwe!” ilikuwa salamu ya kwanza aliyoitoa, alifanya hivyo kwa makusudi kabisa, alihitaji kumuweka sawa ili ajue alikuwa akiwasiliana na mwanaume aliyeokoka.

“Amen! Habari yako!” alisikika msichana huyo.

“Nzuri tu! John hapa!”

“John yupi?”

“Wa kanisani!”

“Oh! Mdar es Salaam!”

“Yeah!” alisema John huku akijisikia fahari kuitwa hivyo.

Wakaanza kuzungumza. Lengo kubwa la kumpigia simu msichana huyo lilikuwa ni kumzoea, kabla ya mambo mengine kuendelea kwanza ilibidi wawe karibu kwa kipindi fulani ili hata kama kitakuja kipindi cha kumwambia kwamba alimpenda kusiwe na tatizo lolote lile.

Alikuwa mcheshi, alimchekesha msichana huyo, hakumpa pumzi ya kuongea sana kwa sababu watu wengi walipenda kuwasikia watu wa Dar es Salaam kwa jinsi walivyokuwa wakiongea kwa mapozi, kama cherehani.

“Umenifurahisha sana!” alisema Juliana.

“Ni wajibu wangu kukufurahisha!” alisema.

“Na Dar ulikuwa unaishi sehemu gani?” aliuliza.

“Tandale!”

“Tandale?”

“Ndiyo! Ushawahi kufika?”

“Hapana! Huwa nikienda nafikiaga Mwenge kwa baba mdogo!” alijibu.

“Oh! Basi ninaishi huko! Kwa wajanja!”

“Kwa akina Diamond?”

“Yeah! Alikuwa jirani yangu, yaani nyumba yao ile kule, yetu hii,” akajiongeza kidogo.

Wakazungumza kwa dakika kadhaa na walipomaliza, simu ikakatwa na kuendelea kufanya mambo yake. Hapo kidogo moyo wake ukatulia, akawa na furaha, alijiona kuwa mshindi na pia ua ilikuwa ni lazima msichana huyo aingie mikononi mwake.

Wakati akijifikiria hayo, mara simu yake ikaanza kuita, haraka sana akahisi ni Jumanne, akaichukua, kuangalia jina, akashangaa kuona ni Deborah. Moyo ukaanza kudunda tena.

“Niambie bosi wangu!” alisema.

“Eti bosi wangu! Sasa nina ubosi gani?” aliuliza msichana huyo huku akicheka.

“Wewe ni bosi tu! Nimewaona wanawake wengi Kigoma, ila kwako, daah! Mungu kakubariki sana,” alisema.

“Hahaha! Aya ahsante! Nimekupigia kutaka kukuuliza kitu!” alisema.

“Kitu gani?”

“Kuhusu kampuni yetu!”

“Oh! Husahau! Sasa hatuwezi kuongea kwenye simu!”

“Mpaka?”

“Tuonane!”

“Basi nitakutafuta baadaye! Ama utakuwa bize?” aliuliza msichana huyo.

“Hapana! Nitakuwa na muda!”

“Sawa!” alisema na kukata simu.

Furaha aliyokuwanayo haikuweza kuelezeka hata kidogo. Moyo wake ulichanganyikiwa, hakuamini kama kweli Deborah alihitaji kuzungumza na yeye.

Haraka sana akakurupuka kutoka kwenye godoro lake na kuufungua mfuko wake wa nailoni na kuanza kuangalia nguo zake, alihitaji kuvaa nguo fulani maridadi kwa lengo la kumvutia msichana huyo.

“Hii hapana! Nitaonekana wa kuja!” alijisemea na kuiacha.

Alikuwa na mtihani mkubwa wa kuchagua mavazi ya kuvaa huo muda ambao angekutana na Deborah. Alifanya uchaguzi kwa dakika kumi na tano ndipo akajua ni mavazi gani ambayo alitakiwa kuyavaa.

“Haya yanafaa!” alijisemea.

Ilipofika majira ya saa 10:15 jioni akapigiwa simu na msichana huyo, haraka sana akaipokea na kuanza kuzungumza naye. Alimwambia alikuwa tayari kama vipi walitakiwa kuonana sehemu na kuzungumza.

Hilo halikuwa tatizo, wakapanga kuonana katika mgahawa wa Bijou uliokuwa Mjini karibu na Shule ya Msingi ya Kigoma ambapo hapo wangekaa na kuzungumza.

Baada ya nusu saa wakaonana huko. Kwa jinsi Deborah alivyovaa, John akabaki hoi, alimwangalia msichana huyo, alivutia, alikuwa mrembo kupita kawaida. Akachanganyikiwa na mapenzi juu yake yakazidi kuongezeka zaidi na zaidi.

Watu walikuwa wakimwangalia, hawakuamini kama kulikuwa na msichana mrembo kama alivyokuwa huyo Deborah. Ni kama alikamilika, alionekana na sifa zote ambazo alikuwanazo mwanamke aliyeitwa kwa jina la mrembo.

Akasimama, akamsogelea na kumsogelea kisha kumkumbatia, alinukia vizuri, alitamani kumng’ang’ania ili na yeye aichukue harufu ya manukato ya msichana huyo.

“Unanukia vizuri!” alisema John.

“Nashukuru sana!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Akamvutia kiti na kukaa. Hakuzungumza kitu, alibaki akimwangalia tu, alinoga kupita kawaida, muda wote huo Deborah alikuwa akiachia tabasamu pana.

“Wewe ni mrembo sana!” alisema John huku akimwangalia Deborah.

“Oh! Nashukuru sana!”

Kabla ya kuzungumza kile kilichowafanya kuwa mahali pale, wakaanza kuzungumza mambo mengine kabisa. John aliamua iwe hivyo kwa sababu alihitaji kumzoea kwanza, wawe marafiki wa kutosha na ndipo wazungumze mambo mengine ya msingi.

Walikuwa katika hilo kwa dakika kadhaa ndipo hasa wakaanza kuzungumza kile kilichowafanya wapigiane simu na kuitana mahali hapo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Kuna nini kwenye kampuni hii?” aliuliza Deborah.

John hakuwa na jibu zuri la kumpa ila alichokifanya ni kuanza kumwambia kuhusu mambo mengine tu ya kuunga unga, jinsi alivyowahi kwenda kwenye kampuni hiyo kuomba kazi, akatolewa nje kwa sababu tu hakuwa na muonekano mzuri.

“Yaani kisa muonekano?” aliuliza Deborah.

“Ndiyo! Niliumia vibaya mno, nadhani ndiyo moja ya sababu iliyonifanya nije Kigoma kutafuta maisha!” alisema John huku akimwangalia Deborah, sura yake aliiweka katika hali ya kuonewa huruma.

“Umekuja Kigoma kutafuta maisha?” aliuliza Deborah.

“Ndiyo! Na bahati nzuri nimekutana na wewe,” alisema John.

Deborah alishangaa lakini hakutaka kugundulika, akampa pole kwa mambo yote yaliyokuwa yametokea huko Dar es Salaam na alimtia nguvu kwamba alitakiwa kupambana kwani maisha yalikuwa popote pale.





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog