Search This Blog

Sunday 20 November 2022

KASRI YA MWINYI FUAD - 3

 

    Simulizi : Kasri Ya Mwinyi Fuad

    Sehemu Ya Tatu (3)





    Walifuatana mguu kwa mguu mpaka kondeni kwa Kondo na walimkuta anapiga matuta.



    “Leo nimekuja kwa kazi muhimu sana,” Marijani alianza kusema. “Mambo tayari na silaha zote zinatakiwa ziwe zishafika mjini leo.”



    “Leo?” Kondo aliuliza.



    “Ndiyo leo. Tena sasa hivi kazileteni maana gari nimekuja nalo. Njiani askari wameshaanza kisiran’ chao na magari yote yanayotoka shambani yanapekuliwa. Sisi tumejitolea na askari yo yote atakayetusimamisha hatutasimama Kama mmoja atatufanyia matata basi tutamponda; haidhuru na liwe litakalokuwa.”



    “Silaha ziko tayari twendeni tukazichukue,” alisema Kondo.



    Wote watatu walifuatana na kwenda msituni mpaka sehemu moja palipokuwa pamewekwa lundo la makuti ya minazi.



    “Ondoeni hayb makuti,” Kondo aliamuru.



    Vuai na Marijani waliondoa makuti. Chini yake palikuwa na shimo kubwa na ndani yake mlikuwa na mapanga, visu, miundu na silaha nyinginezo. Walizichukua kidogo kidogo na kuzipeleka garini mpaka zikamalizika.



    Baada ya kumaliza kufanya kazi hiyo, wote watatu walisimama pembeni mwa lile gari. Vuai alimtazama yule dereva akamtambua kuwa ni yule yule aliyomleta pale Dambwe kwa lile gari dogo bovu mara ile ya kwanza baada ya kutoka kwa Fuad



    “Sasa sikilizeni vizuri mipango ya kesho; mana’ke kesho ndiyo siku ya siku,” Marijani alisema. “Kesho patapigwa magoma ya kienyeji hapo Kisiwandui na wakulima na wafanyakazi wote wanatakiwa wafike kwenye magoma hayo. Madhumuni yenyewe siyo kupiga magoma, ni kuweza kuwapata wanamapinduzi wote kutoka sehemu mbali mbali za mashamba na kuja mjini. Ndiyo sababu tumeona bora tupigishe magoma ili watakapokuwa wakija mjini magoma yawe ndiyo kis’ngizio. Baada ya magoma hayo kwisha. wote wale wanaohusika wataarifiwa ni wapi watazikuta silaha zao. Usiku huo huo tutaanza mapinduzi kwa kulichukua boma la askari wa serikali ya kisultani hapo Mtoni. Mipango yote kuhusu jinsi boma hilo litakavyochukuliwa imekwisha tayarishwa na mtaambiwa huko huko mjini.” Marijani aliendelea na maelezo yake



    “Tumefahamu sawa sawa na tutawaarifu wenzetu wote,” Kondo alisema.



    “Basi sasa kwa herini na tunatumai m’shajiandaa na kwamba nyote mtafika hapo Kisiwandui kesho usiku. Angalia msifuatane nyote pamoja, au sivyo, maaskari pale Mwera watawatilia shaka. Njooni mmoja mmoja au wawili wawili.” Marijani aliwatahadharisha.



    Marijani alikuwa ametulia na hakuwa na wasi wasi hata kidogo. Uso wake ulidhihirisha imani yake kuwa mapinduzi yatafanikiwa.



    “Basi kwa herini tutaonana kesho. Kondo utapofika Kisiwandui usiwe na haja ya kuonana na mtu yo yote pale. Kila kikundi kina mtu wa kukifahamisha mipango yote na mimi ndive nitakayekuwa na dhamana ya kukifahamisha mipango yote kikundi cha huku Dambwe.” Marijani alimgeukia Vuai na kumwambia, “Wewe utawatafuta wale jamaa wa Koani uwapashe habari za mipango yote. Wamekwishapashwa habari za ngoma na iliyobaki ni kuwajulisha wale wanaohusika kazi zao ngoma ilakapoiva.”



    Baada ya kumaliza hapo, Marijani aliingia ndani ya lile gari na hapo hapo lilitiwa moto na kuondoka mbio.
    http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Kwa bahati hawakusimamishwa pale Mwera. Walipita bila ya taabu yo yote. Gari lao likiwa limesheheni mapanga na mashoka. Walikwenda moja kwa moja mpaka Wengiwape na wakazitia silaha zote ndani ya kijumba kidogo.



    Kila kitu kilikuwa lazima kifanywe bila ya kuacha alama yo yote ambayo ingemfanya mtu kutia shaka. Kwa hiyo, pale Wengiwape palipoteremshiwa silaha palikuwa na watu maalum ambao walipewa kazi ya kuzifagia alama za mipira ya ile motokaa kutoka pale nyumbani mpaka kufika barabarani. Kazi hiyo ilifanywa mara moja baada ya lile gari kuondoka.



    Siku ile ilikuwa ya kujiandaa kwa kila mwanamapinduzi po pote pale alipo. Huko mjini cheti cha ngoma kilikuwa kimeshakatwa na banda kubwa lishajengwa. Kila mtu alikuwa anajiandaa kuja ngomani, tena ngomani kweli. Siku ile ilikuwa siku ya wakulima na wafanyakazi, siku walipoamua kuleta mabadiliko katika maisha yao kwa kuondoa dhuluma ya kame.



    Tokea asubuhi wakulima kutoka sehemu mbali mbali za mashamba walianza kuteremkia mjini wengine kwa magari wengine kwa miguu. Wengine walikuwa wanakuja ngomani kweli; wanamapinduzi tu ndio waliojua vizuri mwisho wa ngoma ile.



    Si wanamapinduzi wote waliotakiwa wafike hapo ngomani na kwa hivyo baadhi ya wanamapinduzi walipata amri ya kukaa katika nyumba maalum mpaka utakapofika wakati.



    Usiku huo asiyekuwa na mwana alibeba jiwe. Mamia ya wakulima walifika magomani, waliokuwamo na wasiokuwamo. Waliokuwamo walijua vizuri nini kilichowapeleka mjini na wasiokuwamo walikwenda ngomani.



    Kisiwandui ilikuwa inang’ara siku hiyo kwa mataa ya umeme. Hewa ya hapo ilichafuka kwa vumbi lililokuwa likitimuliwa na wacheza ngoma. Lilikuwapo ‘gombesugu’, yalikuwapo ‘maumbwa, ‘gonga’ na ngoma nyingine za kienyeji. Mchanganyiko wa ngoma namna mbali mbali ziliizokuwa zikipigwa hapo ulisababisha kelele kubwa. Watu walistarehe kwa ngoma mpaka saa sita ya usiku.



    Baada ya kuvunjika ngoma, taratibu watu walianza kupungua ngomani pale. Akina mama walikuwa wanakimbilia majumbani kupika daku. Waliwacha nyuma yao nuru ya mataa ya umeme iliyokuwapo ngomani pale na kujitosa ndani ya kiza cha vichochoro vya ng’ambo kwa safari za mitaani kwao kulikojaa vijumba vya udongo vilivyosongamana kwa kujengwa bila ya mpango. Misitu na vichaka vilivyokuwapo katika sehemu hiyo waliyokuwa wakiishi wafanya kazi wa Unguja, makaburi yaliyotapakaa katika takriban kila pembe ya sehemu hiyo pamoja na imani ya hadithi mbali mbali za kubuni juu ya mashetani, wanga na wachawi walizokuwa nazo watu - hayo yote yaliwafanya wakimbilie makwao mbio usiku ule kwa khofu wasiyokuwa na hakika nayo.



    Ulikuwa usiku wa kuamkia Januari 12, na watu walikuwa wamo katika kumi la mwanzo la mwazi wa Ramadbani. Wanamapinduzi wote walikuwa wanaelewa vizuri dhamana waliyokuwa nayo siku ile. Kutoka ngomani kila mmoja wao alishika njia yake, kuelekea kwenye mkutano ‘Wengiwape’.



    Chonjo alikuwa wa mwanzo kufika penye kijumba kilichofichiwa silaha. Alimkuta Pongwe amejibanza pembeni ya kijumba kile tumbo wazi kama mtu aliyekuwa akivizia kitu na panga lake mkononi. Alipomwona tu Chonjo, Pongwe aligutuka na kuuliza kwa sauti ya ukali, “Nani wewe?”



    “Mimi”

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    “Wewe nani? Huna jina?”



    “Mimi Chonjo”



    Pongwe alimjongelea Chonjo taratibu na alipofika karibu naye alimwuliza kwa sauti ya chini. “Wengine wako wapi?”



    “Watakuja sasa hivi. Nenda kanitafutie panga zuri uniletee.”



    “Nenda kachague mwenyewe.”



    Kijumbani humo mlikuwa kiza totoro. Miembe na mizambarau mikubwa iliyokizunguka kijumba hicho ilikizidisha kiza hicho. Chonjo aliingia ndani, akajaribu kuyalazimisha macho yake apate kuona katika kiza kile lakini yalikataa katakata. Aliutia mkono ndani ya suruali yake ya khaki na kutoa kibiriti. Aliwasha kijiti cha kwanza lakini mara kilizimika kwa upepo uliopepea ghafla kutoka uani.



    “Ala, wewe namna gani bwana! Usiwashe kibiriti; hapatakiwi mwangaza hapa!” kwa sauti ya hamaki Pongwe alimwambia Chonjo. “Ingia hicbo chumba cha mkono wa kushoto vita vyote vimo humo.”



    Chonjo alipapasapapasa mpaka akaugusa mlango wa chumba alichoelekezwa. Alisukuma ule mlango akaingia chumbani humo na kunyemelea kidogo kidogo. Bila ya kutumainia alikwaa chungu ya silaha zilizokusanywa humo. Alipotaka kuinama na kuchagua silaha aliyopenda katika kiza kile alimsikia Pongwe akizungumza na mtu mwingine. Chonjo aliinuka na kutaka kusikiliza ni mtu gani yule lakini mara alimsikia mtu yule akiingia ndani. Mara moja alijua kuwa yule alikuwa mwanamapinduzi mweazake. Aliinama tena na kuanza kuchagua silaha. Yule mtu naye aliingia chumbani mle na aliposikia parakacha parakacha aliuliza, “Je nani mwenzangu?”



    “Mimi Chonjo. Je, wewe nani?”



    “Mimi Marijani. Upesi chagua silaha; wengine wanakuja sasa hivi. Na tutapotimia tutakwenda zetu; wakati ushakuwa mkubwa.”



    Kila mtu alichukua panga ambalo alilihisi zuri na kutoka nje.



    Wanamapinduzi waliendelea kuja mmoja mmoja. Kila aliyefika alichukua silaha aliyoipata, mwenye panga, mwenye rungu, mwenye shoka na wote baadaye walijikusanya mbele ya kijumba kile. Pongwe aliingia ndani na kuvaa shati. Na baada ya wote kutimia Marijani alianza kutoa amri.



    “Ndugu, saa ya kitendo imefika. Sasa sote tunaelekea Mtoni, kufa na kupona - lakini mambo yote tuyabadili leo. Haya, safari ndugu.”



    Ilikuwa kiza totoro. Hali ya hewa ilikuwa shwari na miti imetulia tulii. Ari ya kimapinduzi ilikuwa imetawala ndani ya nyoyo za akina Shomari na wenzake.



    Walipita njia za porini kwa hadhari. Hapana aliyekuwa akizungumza na mwenzake mpaka walipolikaribia boma. Walipofika hapo Shomari alitoa shauri, “Sasa sote tulaleni chini. Tutatambaa mpaka tuzifikie seng’enge. Kundi moja litabujumu kutokea mlango wa mbele wa boma na kundi jingine litahujumu kwa upande wa pili.



    Bomani kulikuwa kimya. Askari wa jeshi la Sultani walikuwa wamelala. Mataa makali ya umeme yalimulika kila pembe bomani hapo. Mlangoni mbele ya boma palikuwa na askari mmoja aliyekuwa akishika zamu. Alikuwa akiranda huku na huku na bunduki yake mkononi.



    Wanamapinduzi walitambaa mpaka wakazifikia seng’enge na walipofika hapo walitulia tulii wakingojea amri ya kushambulia.



    Kikundi kimoja kilinyemelea kwa kutambaa maguguni mpaka wakafika karibu na alipo yule mlinzi. Alisituka kidogo aliposikia parakacha parakacha lakini pale pale alilia komba na hapo wasiwasi ulimtoka na kufikiri parakacha parakacha ile ilikuwa ni yule komba aliyckuwa akichupia minazi. Lakini hakwenda hata hatua mbili alijishtukia amevamiwa na kutiwa kabari na kabla hajawahi kupiga kelele alishindiliwa kisu eha shingo na kuanguka chini kimya. Alikufa hapo hapo.



    Hapo tena ulisikika ukelele Wa Marijani - “Tayari ndugu!”



    Waliingia ndani ya boma kama umeme. Baada ya muda mchache walilikamata boma na kufungua chumba cha silaha. Askari wa serikali ya kisultani hawakuwa na moyo wa kupigana. Baada ya kuona kishindo tu walitimka na kukimbia.



    Baada ya masaa machache tu boma la Ziwani nalo pia lilitekwa. Na baada ya hapo, hatua kwa hatua, wanamapinduzi walianza kuvikamata vituo muhimu na klkundi kimoja kikaelekea kwenye kituo cha radio.



    Kiza kilikuwa kimeutawala usiku wa siku ile na vivuli vya miembe mikubwa mikubwa iliyoizunguka Raha Leo nzima vilizidisha kiza kile kukawa kweusi tititi.



    Mbele ya jumba kubwa la manjano lililozungukwa kila pembe na vibanda vya udongo vilivyoezekwa makuti, koplo Paulo na askari mwenzake walikuwa wamezama katika soga lililowaza kuvunja machofu ya ulinzi wa usiku kucha wa kituo cha radio kilichokuwemo ndani ya jumba hilo.



    “Basi nikamfata toka Kidongochekundu mpaka Miembeni,” Koplo Paulo aliendelea na soga lake.



    “Enhe!”



    “Kila nikimwuliza hali hanijibu, kila nikimwuliza hali hanijibu, Shoti ananukia kama jini.”



    “Enhe!”



    Halafu nikajiuliza mwenyewe moyoni. mwanamke huyu anaringa nini hasa?”



    “Enhe!”



    “Nilivyomwona hanijibu nikaona bora nimkaribie zaidi na nilipofika karibu yake nikamshika mkono.”



    “Enhe!”



    “Nilipomgusa tu alinigutua mkono wangu. E, mwanamke anaringa yule, lakini mwa...... “Mara koplo Paulo aliyakata mazungumzo na kurejesha kiti alichokua amekalia nyuma. Alionyesha amestuka sana na bila ya kusema chochote au kumwambia mwenzake lolote alikupuka mbio.



    Yule mwenzake Koplo Paulo alibabaika na alipogeuka nyuma aliona kundi la watu linamkaribia. Alianza kujiuliza na kujijibu, “Nikimbie? Ah, hata nikikimbia sitofika popote. Nipigane nao? Ah, hata nikipigana nao wataniua bure. Bora nijisalimishe.”



    “Nani wewe?” iliuliza sauti moja kutoka katika kundi lile kwa ukali.



    “Mimi askari!”



    “Unafanya nini hapa?”



    “Nipo kazini!”



    “Aa, msipoteze wakati bwana! Mchinjeni tu!” ilisema sauti nyingine kwa hamaki zaidi kuliko ile sauti ya kwanza.



    “Ngojeni, msimwue bure, ngojeni kwanza,” alisema mwingine kwa sauti ya kuamrisha.



    Yule askari alikwisha fadhaika haelewi kinachotokea Alihisi amekabiliwa oa mauti na alikata tamaa kabisa kwani kundi lililomzunguka lilikuwa m kundi la watu waliokasirika kila mmoja na silaha mkononi. Bahati yake nzuri kiza cha usiku ule kilificha mandhari ya kutisha ya watu wale ambao nguo zao zilijaa damu na nyuso zimezungukwa na manywele na madevu yasiyoshughulikiwa kwa muda wa siku nyingi sana.



    “Wewe nani?” iliuliza sauti katika kundi.



    “Mimi askari.”



    Pale pale alitoka mtu katikati ya kundi lile na kumpiga kofi hata akaona vimurimuri badala ya shangwe lile lililomzunguka.



    “Ebo, sisi tunakuuliza wewe nani tokea saa ile wewe umeshika askari, askari. jina lako nani?”



    “Mcha, Mcha Hamadi.” alijibu mbio mbio huku bado maruirui ya kofi alilopigwa yanamtaabisha.



    “Ah, Mcha, mwacheni, hawezi kufanya tabu, mlinzi mwenye funguo yuko wapi?”



    “Yuko pale! Nyumba ile!” alijibu Mcha huku sauti inamtetemeka kwa hofu na wasiwasi, miguu inamtetemeka, nywele zimemsimama.



    “Haji, nenda kachukue funguo halafu..wengine watakwenda kumlafuta fundi mitambo, nani anajua anakokaa?”



    “Mimi nakujua! Twendeni nikupelekeni!” Mcha aliruka na kusema haraka haraka.



    “Twende, sisi tutakuchukua kwa amani lakini ukijaribu kuleta shari njiani utakiona cha mtema kuni,” ilisema sauti moja kutoka katika kundi lile la watu waliokuwa tayari kufanya chochote kile, kizuri au kibaya.



    Kundi lile lilijigawa sehemu mbili, kundi moja lilibaki Raha leo na kundi jingine likafuatana na yule askari na kukiandama kiza cha usiku ule. Mcha bila ya hata kujua njia aliyoipita alijishtukia ameshafika mbele ya nyumba ya fundi wa mitambo, “anakaa hapa, ngojeni nimgongee dirisha.”



    “Ngoja kijana, usiwe na pupa, sisi tunamjua zaidi kuliko wewe,” ilisema sauti moja kwa utulivu.



    Dirisha liligongwa, kabla ya aliegongewa dirisha hajafungua, dirisha la nyumba ya pili lilifunguliwa na ilisikika sauti ikiuliza, “Nani ana......”



    Kabla hajamaliza kusema alilolitaka risasi ya ghafla iliyotoka katika bunduki mojawapo ya watu waliokuwemo kundini mle ilipiga pale pale ilipotokea ile sauti na sauti hiyo haikusikika tena.



    “Mwamba!” iliita sauti moja.



    “Hallo!” alijibu Mwamba aliyeonyesha yu macho.



    “Tayari!”



    “Tayari sio? Nakuja.”



    Mwamba alifungua mlango wa nyumba kwa haraka na kutoka nje. Vunge la fungilo lilikuwa mfukoni mwake na kutoka hapo walifululiza moja kwa moja mpaka kwenye kituo cha radio.



    Zogo lilizidi na makundi ya watu yalianza kumiminika Raha Leo kila mmoja silaha mkononi. Mwamba alipousogelea mlango wa kituo cha radio macho ya watu wote waliokuwa na hasira za siku nyingi yalimwangalia yeye. Mwamba alilifungua lango kubwa lililochongwa kwa nakshi nzuri na bila ya kujali chochote alifululiza moja kwa moja mitamboni. Watu watatu walokuwa na bunduki za aina ya ‘Mark 4’ walimfuata nyuma yake.



    Ijapokuwa alfajiri ilikuwa ishaanza kubisha hodi, kiza kilichochanganyika na mwanga mdogo kilimlazimisha Mwamba kuwasha taa na baada ya kufanya hivyo alianza kuchokora mitambo iliyokuwemo ndani ya chumba cha matangazo. Mara alibinya kifungo kile, akabinya swichi hii. Mara alichomoa waya na kuupachika pengine halafu aliingia na mmoja wa wale watu mpaka kwenye chumba cha kusemea na kumweka juu ya kiti, “Sasa sema,” alimwambia.



    “Ndugu wananchi, serikali ya Ki-Sultani tushaipindua, tunawaomba wananchi wawe watulivu. Tunawataka askari wote wa Sultani wajisalimishe na wote wale wenye silaha wazisalimishe silaha zao kwa wanamapinduzl.”http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Baada ya tangazo hilo matangazo kem kem yalifuatia. Ilipofika asubuhi mapinduzi yaliendelea.



    Hiyo ilikuwa kweli ni siku ya siku. Wanamapinduzi waliranda katika kila pembe ya kisiwa cha Unguja wengine kwa miguu wengine kwa magari waliyoyateka. Waliuranda mji wa Unguja kila mmoja bunduki mkononi, kwani sasa haikuwa mapanga ‘na mashoka tena. Walipigana kila walipolazimu kupigana na vikosi vya serikali ya Ki-Sultani na vibaraka wao.



    Mapigano makali yalitokea hapo penye kituo cha polisi cha Malindi. Wanamapinduzi walipigana kishujaa kabisa na askari wa serikali ya Ki-SuItani, ambao walikuwa na kinga nzuri ya kujificha. Wakati wa mapigano ndani ya kituo hicho waliweza kuwaona wanamapinduzi waliokuwa wametawanyika katika uwanja uliokuwa wazi kabisa mbele ya kituo hicho. Wengi katika wanamapinduzi waliteketezwa hapo. Lakini bila ya kujali kifo, wanamapinduzi hao walisonga mbele, na baada ya mapigano ya muda mrefu, walikiteka kituo hicho.



    Kwa Sultani mambo yalikuwa ya moto. Yeye na watu wake kwa mara ya kwanza iliwabidi waende mbio huku majoho na makanzu yakiwazonga miguuni. Walikimbia huku wakipita wakianguka. Bahati yao waliwahi kutoroka katika meli iliyokuwa bandarini, wao na baadhi ya wafuasi wao.



    Mjmi na mashamba mambo yote yalimalizika wakati wa magharibi. Radio ya Mapinduzi ilitangaza kuundwa kwa serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar iliyoongozwa na Chama cha Afro-Shirazi - wakombozi wa wananchi.



    Serikali ya Ki-Sultani iliyowapa kila haki na uwezo mabwana shamba na mabepari ilipinduliwa, kwa mara ya kwanza katika historia ya visiwa vya Unguja na Pemba, ikaundwa serikali inayoongozwa na wakulima na wafanyakazi.

    MWEZI mmoja baada ya kufaulu kwa mapinduzi serikali mpya ilitangaza kutaifishwa kwa ardhi yote na baada ya muda ilianza kugawiwa miongoni mwa wakulima. Wasiwasi uliochanganyika na chuki ulimjaa Fuad.



    “Wallahi shamba langu hawalichukui!” Fuad alianza kusema peke yake.



    Wakati wote Fuad alikuwa ameghadhibika. Lakini hivi sivyo alivyokuwa kama vile akimghadhibikia Mkongwe au mfanyakazi wa shambani mwake, la. Ghadhabu hii ilikuwa pia na woga mkubwa, na kwa hiyo, ilimkera sana moyoni.



    Masikini Kijakazi hakujua nini kimetokea nchini ila kuwa wakati wote Bwana Fuad alikuwa asnekasirika na mnyonge. Kijakazi alimwonea huruma sana na alitamani kumsaidia na kumtoa katika shida aliyokuwa nayo lakini ndiyo hakuwa na uwezo.



    “Siku nyingi anatafuta mchumba; labda hajapata mchumba anayemtaka?” Kijakazi alijiambia kimoyomoyo.



    Asubuhi moja kama saa mbili na nusu magari mawili yalisimama mbele ya mlango wa nyumba ya Fuad. Watu watatu kutoka katika kila gari walishuka wakapiga hodi na Fuad aliyekuwa amekaa ukumbini peke yake alitoka kuja kuwaona wageni hao.



    “Tumekuja tunataka kuonana na wewe,” mmoja wao alisema.



    “Mnataka kuonana na mimi. Tafadhali, karibuni; piteni ndani!” Fuad alijibu huku akijidai kujichekesha kicheko kil’chochanganyika na chuki.



    Kijakazi aliyekuwa amesimama kwa mbali aliweza kuwaona watu hao wakiongea na Fuad lakini hakujua wakiongea kitu gani.



    Fuad aliwakaribisha wote ukumbini na kuwataka wakae juu ya viti.



    Wote wale sita walikuwa wamevaa nguo zilizochafuka. Wawili wao walivaa viatu vya mpira na wengine walikuwa miguu wazi. Hii ilikuwa ni ajabu kubwa kwa Kijakazi. Maisha yake yote, tangu uhai wa Bwana Malik, hakupata kuona watu kama wale wakiingia ukumbini mle mlimopambwa kwa mapambo ya kila aina. Miguu ya wale watu ililichafua lile zulia zuri lililotandikwa juu ya sakafu ya ukumbi huo.



    Baada ya kukaa vitini wale wageni wasiojulikana kwa yule waliyemtembelea, kwanza walitazamana na mara mmoja wao akaanza kusema.



    “Nafikiri unaelewa kuhusu sheria mpya ya ardhi?”



    “Sheria ya ardhi? Sheria gani?” Fuad aliuliza huku roho ikimwenda mbio.



    “Sheria inayosema kwamba ardhi yote ni mali ya serikali.”



    “Naam! Nimeisikia, Bwana!” Fuad alijibu, wakati umemgeukia na sasa naye anajua kuita ‘Bwana’.



    “Basi sisi tumekuja kukujuvya kwamba, ijapokuwa wewe mwenyewe utakuwepo hapa, inakupasa ujue kwamba ardhi yote ile iliyokuwa chini ya milki yako ni mali ya serikali. Kwa hivi sasa unaweza kuendelea na kazi zako mpaka tutakapokuletea taarifa nyingine,” alieleza yule mtu.



    “Nimesikia, Bwana! Nimesikia!”



    “Basi sisi tumekuja kukuarifu tu tunakwenda zeut.”



    Wale watu walitoka na kuingia ndani ya magari yao wakaondoka.



    Baada ya kuondoka tu. Fuad alitoka nJe ya nyumba. yake amekasirika sana, uso umemwiva mwekundu kama papai akinung’unika peke yake.



    “Wezi wakubwa!” alijisemea.



    Ilikuwa wakati wa asubuhi kiasi ya saa nne. Kijakazi alikuwa anafagia uwanja ulioko mbele ya jumba la Fuad. Fuad alikuwa chumbani mwake amelala na mara ilifika gari moja mbele ya nyumba yake.



    Ilikuwa ni moja katika zile gari mbili zilizokuja siku ile. Baada ya kufika tu gari hiyo, alishuka mtu mmoja na kumwuliza Kijakazi, “Fuad tumemkuta?”



    “Bwana? Si ... sijui, ngojea nikamtazame ndani.” Kijakazi alijibu.



    Fuad aliyekuwapo chumbani mwake alimsikia yule mtu alipokuwa akiuliza na mara alitoka nje mbio.



    “Nipo! Nipo Bwana! Je mnataka kuonana na mimi?” Fuad aliuliza huku akijifunga vizuri kikoi cha Jabir alichokuwa amevaa wakati ule.



    “Tuna haja ya kuonana na wewe kidogo,” alisema yule mtu.



    “Karibuni, piteni ndani!” Fuad alijibu huku akijidai kucheka kama mtu aliyefurahi kweli kufikiwa na wageni wale.



    Watu wengine wawili waliteremka kutoka kwenye lile gari na wote watatu waliingia ukumbini kwa Fuad pamoja na Fuad mwenyewe.



    Kijakazi hakuwa mbali na aliweza kusikia wazi wazi yaliyokuwa yakizungumzwa.



    “Je, khabari za toka siku ile?” aliuliza mmoja wa wageni wale.



    “Nzuri! Nzuri Bwana!” Fuad alijibu.



    “Tumekuja kuonana na wewe kuhusu ile habari tuliyozungumza siku ile. Je unakumbuka tulizungumza nini?”



    “Nakmbuka! Nakumbuka vizuri!”



    “Basi tunapenda kukueleza hivi,” alianza yule kijana, “kama unavyojua, serikali ya Ki-Sultani tumeipindua na siasa ya serikali ya kimapinduzi ni kujenga ujamaa. Tunajua kwamba hiki ni kitu kipya kwako ambacho hukupata hata kukisikia. Au je, unaelewa maana ya ujamaa?”



    “Sielewi, Bwana, na itakuwa vizuri ukinifahamisha!” Fuad alijibu.



    “Hayo ndiyo madhumuni ya kaja hapa,” aliendelca yule kijana. “Sisi tutakuzungumza wewe kuhusu ardhi tu. Siku ile tulikwambia kwamba ardhi yote imechukuliwa na serikali lakini hii baina maana kuwa ardhi ni ya serikali tu, basi. La! Ardhi ni ya serikali lakini itagawiwa miongoni mwa wakulima. Katika sehemu nyingine jambo hili limekwishatendeka na sasa ni zamu ya sehemu hii. Kila mkulima anayeishi katika eneo hili atagawiwa ardhi na baada ya hapo kuna mipango ya kuanzisha ukulima wa kijamaa, yaani kuanzisha mashamba ya ushirika. Maana yake m kwamba shamba lako pia itabidi ligawiwe na wewe mwenyewe utapewa sehemu yako ili nawe uwe na kitu cha kukuendeshea maisha yako. Utapatiwa ardhi inayokutosha, lakini itakubidi uilime wewe mwenyewe kwani hutapata mtu wa kukutumikia tena.”



    “Mimi niko tayari! Niko tayari kabisa! Wako majirani hapa naweza kushirikiana nao katika kazi kama hiyo. Wapo akina Pandu, Haji, Makame na majirani wengine chungu nzima ambao naweza kushirikiana nao. Mimi mwenyewe nitafanya kazi bila shaka; kwani nyinyi mnafikiri mimi siwezi kushika jembe?. Naliweza vizuri” Fuad alisema huku akijidai kucheka na kufanya masihara.



    Kutoka alipokuwa amesimama Kijakazi aliyasikia vizuri yaliyokuwa yakizungumzwa, lakini hakuna alichokielewa Mambo ya ujamaa hakuyaelewa hata kidogo. Aliona yote yale hayakumhusu yeye. Jambo lililomshangaza ilikuwa kule kumsikia Fuad akiwataja watu kama Pandu, Haji na Makame - kama majirani zake; watu ambao, hapo zamani, hakuwa na mahusiano nao yo yote. Watu hao walikuwa wakiishi hapo Koani lakini walikuwa m katika mafukara wa kutupwa.



    Baada ya mazungumzo yao kumalizika wale watu walitoka nje wakaingia ndani ya gari lao na kuondoka. Kama kawaida baada ya kuondoka tu, Fuad alikuwa mkali kama moto.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Siku nyingi zilipita; Kijakazi hakujua kinatokea nini pale walipokuwa na katika nchi kwa jumla. Taabu na wasiwasi wake ilikuwa kule kumwona Bwana wake alivyokasirika siku wale watu walipokuja.



    Siku moja Kijakazi alikuwa amekaa peke yake chini ya mti nyuma ya nyumba ya Fuad. Hapo alianza kujiuliza maswali, “Jamani huu ujamaa ndiyo nini hasa? Hawa watu wanataka nini hasa kwa Bwana Fuad. Haweshi kuja kumkera maskini.”



    Ijapokuwa hakuweza kupata jawabu lo lote katika maswala aliyokuwa akijiuliza, alitia shaka kwamba lazima kuna jambo linataka kutendeka.



    Vuguvugu la mapinduzi ya kumiliki ardhi lilianza kutapakaa katika kila sehemu ya Unguja. Mabwana sbamba walishikwa na wasiwasi mkubwa. Kila njia za kutaka kuharibu mipango ya serikali ya kimapinduzi walizifanya.



    Fuad alikuwa amekaa ukumbini pamoja na mabwana shamba wengine watatu ambao walikuja kumtembelea siku ile, Khalfan, Swelum na Khator.



    “Hapa pako washakuja?” Khator aliuliza.



    “Washakuja! Ati wanataka kuligawa shamba langu madhalim wale!” Fuad alijibu hamaki zimemjaa moyoni mwake.



    “Hata mimi walipokuja shambani kwangu walinambia maneno hayo hayo! Hawa watu wana wazimu? Hawajui kama ni dhambi kubwa kumnyang’anya mtu mali yake?” Swelem naye aliingia kati.



    “Ati wanataka kujenga ujamaa; ujamaa, ujamaa, hawana lao moja wanaloliweza hawa!” Khalfani naye alisema.



    Mazungumzo baina ya Fuad na mabwana shamba wenzake yalichukua muda mrefu na baada ya kuzungumza kila mmoja alishika njia na kwenda zake.



    Kila siku iliyopita, wasiwasi ulimzidi Fuad. Kijakazi aliyaona haya na mara alikuwa akimwona Fuad akificha vitu. Mara humwona akificha mbatata, mara akificha sukari, mara akificha vitunguu. Almuradi alikuwa ni mtu aliyejaa wasiwasi.



    Kijakazi hakuweza kuelewa nani aliyekuwa akifichwa vitu hivi lakini alihisi kama kuna maadui kutoka mbali wanataka kumnyang’anya Fuad shamba lake zuri. Tena alihisi kuwa maadui hao ni watu wenye nguvu. Alistaajabu kuona hakuambiwa chochote kuhusu mambo yaliyokuwa yakitokea lakini aliamini kwamba huu ujamaa na kuishi kijamaa ni mambo ya laana kubwa kwa vile alivyomwona Fuad akighadhibika anapozungumza habari hiyo......



    Ilikuwa wakati wa jioni, Fuad ametoa kiti chake cha kulala uwanjani mbele ya nyumba yake anapunga upepo. Alikuwa akivuta sigara moja baada ya moja huku kichwa chake kinatazama juu. Mara alipita Mkongwe. Alipomwona tu, Fuad hakuweza kujizuia na mara alimwita.



    “Mkongwe hebu njoo nikwambie!”



    “Unambie nini?” Mkongwe aliuliza.



    “Wewe njoo tu halafu utasikia nini nataka kukwambia!” Fuad alisema huku sigara yake iko mkononi.



    “Usinishughulishe mimi, sasa hivi n’na kazi,” Mkongwe alijibu.



    ‘Njoo mara moja tu,” Fuad alimwomba Mkongwe.



    “Eh! Husikii nakwambia n’na kazi; sitaki basi!” Mkongwe alijibu na hapo hapo alielekea kule kwenye banda la ng’ombe na kwenda zake.



    “He! Hata Mkongwe naye siku hizi amekuwa jeuri. Ama kweli mambo yamebadilika!” Fuad alisema peke yake huku amej nyosha juu ya kile kiti cha kulala.



    Mkongwe alikuwa hashughuliki tena na kazi. Alikuwa akipuuza kila kitu. Hata huyo Fuad alikuwa hampi heshima kama ile heshima anayotaka apewe - heshima ya bwana shamba mwenye kumiliki ardhi na kila kinachoishi katika ardhi hiyo, tokea mimea mpaka watu. Yeye al’elewa vizuri nini kinatokea kwani Umari alikwisha mdokeza kuhusu mipango mipya ya serikali ya kimapinduzi.

    http://pseudepigraphas.blogspot.com/

    Wafanyakazi wa shambani kwa Fuad walikuwa wakisubiri tu lini wao watagaiwa ardhi ili wao pia wapate kuishi kijamaa kwani hii ilikuwa ndio njia ya pekee itakayoweza kuwaokoa kutoka katika ule unyonge waliokuwa nao kwa muda mrefu.



    Fuad alimtilia shaka kila mfanyakazi katika shamba lake kwani siku hizo hakuna tena hata mmoja aliyemjali.



    Mabwana shamba kutoka sehemu mbalimbali waliendelea kuja kumtembelea Fuad. Walikuja kutaka nasaha lakini hakuna aliyeweza kutoa nasaha zo zote kwa mwenzake, na kwa hiyo, mazungumzo yao yalikuwa ni yale yale ya kulaani ujamaa na kuutemea mate chini. Waliwaita wakuu wa serikali mpya kila jina baya, wajinga, wahuni watu wasiosoma, wezi na kadhalika.



    Wajumbe wa serikali ya kimapinduzi walikuja tena kuonana na Fuad. Kama kawaida, Fuad aliwakaribisha ukumbini na mara hii aliwatengenezea kahawa. Alitoa pakti ya sigara na kuizungusha duru na kila aliyekuwa mvutaji alichukua moja. Mazungumzo yalikuwa yale yale - ardhi - kilio cha wakulima kwa miaka. IIlkuwa ni siku ya, furaha kwa wafanyakazi wa shambani kwa Fuad kwani kila walipokuja wajumbe wale, wafanyakazi hao walikuwa wakifurahi sana wakiwa na matumaini ya kukombolewa kutokana na mateso ya siku zote za nyuma.



    Kinyume na wafanyakazi wenzake, Kijakazi alikuwa akielemewa na unyonge mkubwa alipowaona watu wale ambao hakujua walitoka wapi au walitaka nini. Alihisi walimlctea bwana wake kero na hili hakulipenda. Alipowaona wale watu alikuwa akizunguka huku na kule akitafuta kazi ya kufanya karibu na ukumbi wa nyumba ya Fuad ili alau asikie nini kinazungumzwa.



    Katika kupitapita pale alisikia sauti ya mmoja wa wale wageni ikisema,



    “Sasa Fuad unasemaje? Sisi tumekwisha anzisha kilimo cha pamoja, na tunataka kukiendeleza mpaka sehemu hii ya shamba lako.”



    “Fikra nzuri!” Fuad aliruka na kusema. “Mimi nakubaliana moja kwa moja na fikra hizo. Najua vizuri kwamba hilo ni jambo zuri na naliunga mkono kwa moyo wangu wote. Niko tayari kabisa kuishi kijamaa.”



    Hiyo ilikuwa ni sauti ya Fuad na Kijakazi aliweza kuitambua hata kama ingelikuwa miongoni mwa sauti elfu nyinginezo. Kijakazi alisita hapo chini ya dirisha ili aweze kusikia zaidi yaliyokuwa yakizungumzwa. Aliyoyasikia yalikuwa ni maneno ya ajabu. Hakupata kumsikia Fuad hata siku moja kusema kwamba yeye anataka kuishi kijamaa. Alilojua yeye m kwamba hao waliozungumza habari hizo za kuishi kijamaa ni makafiri wakubwa na ilikuwa ni mara yake ya kwanza kusikia Fuad akisema maneno kama yale.



    “Hivyo haya maneno aliyoyasema Bwana mimi nimeyasikia vizuri au masikio yangu yananidanganya? Au huyu Bwana, masikini, amekwishatekwa akili na hawa watu wanaokuja hapa?”



    Kijakazi alisimama kusikiliza zaidi mazungumzo yale yaliyomshitua.



    “Si muhimu ikiwa wewe unaunga mkono au huungi mkono, sisi tumekuja kukwambia tu ikiwa m katika mipango yetu, tusije tukafanya jambo halafu ukasema, ‘eh, wamefanya hivi wamefanya vile!” Mbaruku alisema.



    Wenzaka wote walinyamaza kimya wakivuta sigara tu na kila walipomaliza basi Fuad alikuwa tayari kuwakaribisha nyingine.



    Mbaruku aliendelea na mazungumzo yake na kusema, “Basi wapo vijana hapa, watoto wa wakulima, washaanza kazi hiyo ya kulima pamoja na wanaelekea huu upande wako, ukiona wamefika sehemu hii nd’o ujue tena, wamo kazini.”



    Kijakazi aliyekuwa amejibanza pale dirishani alimsikia Fuad akisema tena, na mara hii kwa sauti ya juu zaidi.



    “Vijana? Walete hapa kwangu, mimi nitawafahamisha kila kitu, mana’ke nankiri wao bado vijana hawana ujuzi wa kazi hizi za kulima.”



    “Wao hawana haja ya kufundishwa kulima, wao ni wakulima tokea babu wa babu zao,” Mbaruku alisema.



    “Sisi tunachotaka ni kwamba tutakapofika sehemu hii utuonyeshe kila kilichomo ndani ya shamba,” aliendelea Mbaruku.



    “Msitie wasiwasi mimi nitakuonyesheni kila kitu na mimi mwenyewe nitachukua dhamana ya vitu hivyo!” Fuad alisema, amehamaki, lakini hawezi kuonyesha, akijidai kucheka anaposema kitu, ingawa ukweli ni kwamba hana kicheko. Joto la hamaki lilikuwa likifukuta ndani ya kiwiliwili chake na alikuwa akitoka kijasho chembamba ilhali ya kuwa upepo mzuri ulikuwa ukiingia ukumbini humo.



    Mazungumzo ya Fuad na wale watu yalimshangaza Kijakazi na hasa yaliyomshangaza zaidi ni maneno ya bwana wake Fuad. Kule kusema kwa Fuad kwamba yuko tayari yeye mwenyewe kushiriki na kuwafunza hao vijana wakulima ilikuwa ajabu kubwa. Zamani watoto kama hao Fuad hakutaka hata kukaribiana nao acha kushirikiana nao na kuwafundisha cho chote. Kijakazi alifikiri labda bwana wake amepotelewa na akili.



    Mara Kijakazi alimsikia Fuad akiagana na wale watu naye akaondoka pale alipokuwa amejibanza.



    “Basi mnaweza kuja siku yo yote ile, mimi mtanikuta tu hapa,” alisema Fuad alipokuwa anaagana na akina Mbaruku, amesimama mlangoni.



    “Mambo makubwa haya!” Kijakazi alinong’ona peke yake, “Masikini Bwana! Lakini nafikiri atabadili fikra zake!”



    Kwanza Kijakazi aliyaamini aliyoyasema Fuad kwa kuhisi kuwa akili zake zilikwisha tekwa. Lakini hakumwona na furaha yo yote na hii ilimfanya awe na wasi wasi kwamba huenda Fuad anayasema yale kwa kuzidiwa nguvu. Kila alipofikiri hivyo alifurahi kidogo kwani hakutaka Fuad achanganyike na watu wale.



    Baada ya kwisha kuagana na akina Mbaruku Fuad alibaki pale pale mlangoni jasho linamtoka, hamaki zimemjaa. Mara Kijakazi alipita na mtungi kichwani anaelekea kisimam kuteka maji. Kumwona tu, mnyonge wake alianza kumfokea kama kwamba yeye ndiye aliyefanya mapinduzi.



    “We, wewe, kazana! Unakwenda kama huna miguu! Kwanza nani aliyekutuma maji? Basi kazi kwenda kuchezea maji tu huko kisimani?”



    “Nakwenda kuwapa ng’ombe maji haya!” Kijakazi alijibu.



    Kwa kweli Fuad hakuwa na haja yo yote ya kumhimiza Kijakazi lakini hakuwa na mwingine ye yote wa kuweza kumhamakia isipokuwa yeye tu. Kijakazi alikaza mwendo na kwa ajili ya uzee wake atikuwa akiyumba njiani ungedhani ataanguka wakati wo wote.



    Fuad hakuwa na la kufanya. Hakuwa na njia yo yote ya kuyazuia yaliyokuwa yakitokea. Kila siku akisikia matangazo ya mapinduzi katika redio, matangazo ya kuohukuliwa mali za mabepari, kudhibiti biashara ya nje na ya ndani na matangazo mengine mengi ambayo yalidhamiria kuzuia kabisa unyonyaji wa mabepari na mabwana shamba. Yeye hakuwa na la kusema isipokuwa kulaani na kutukana tu na hayo hayakumsaidia cho chote. Kila siku hatua zaidi za kimapinduzl zilichukuliwa.



    Siku nyingi kidogo zilipita kabla ya Fuad kusikia. cho chote kuhusu ile mipango aliyoambiwa na Mbaruku. Jambo hili lilimpa moyo mkubwa akifikiri yamekwisha au labda wale watu wamemsahau.



    Halafu bila ya kutumaini, siku moja aliona watu wawili waliovaa nguo zilizochakaa wakija nyumbani kwake. Alipowaona tu alinong’ona peke yake, “Hao washakuja tena, sijui wanataka nini? Mungu awashinde!”



    Lakini mara aliigeuza sura yake iliyokuwa imekasirika. na kujifanya kama aliyefurahi kuwaona.



    “Je, nini khabari za siku nying’? Naona mmenitupa siku hlzi hamnipiti kabisa?” Fuad aliuliza.



    Wale watu hawakutaka kujijulisha, na Fuad mwenyewe alikwisha tambua wanapokuja wageni kwake huwa wametoka wapi.



    Fuad aliamkiana na wale watu na kuwapa mkono lakini wao hawakumwambia kitu cho chote. Mmoja wao alitia mkono mfukoni na kumpa barua. Fuad aliisoma ile barua na mara aliruka.



    “Mnataka lile trakta? Kachukueni! Kachukueni! Hapana wasiwasi wo wote; tena ile ni mashine nzuri sana, mali ya M’ngereza ile!”



    Fuad aliwachukua wale watu mpaka lilipokuwa lile trekta na mmoja katika wale watu wawili alilipanda na kulitia moto.



    “Barabara!” alisema yule dereva.



    Fuad alipeana mikono na wale watu wakaagana na hata aliwasindikiza kidogo, wao wakiwa juu ya trekta na yeye akitembea kwa miguu.



    Kabla ya lile trekta halijafika njia kuu, Kijakazi ambaye umbea wa kutaka kujua nini hasa kinachotokea ulikuwa umemshika alimwona Fuad akirejea ameghadhibika. Aliivua kofla aliyokuwa ameivaa na kuitupa chini halafu akaikanyagakanyaga kwa miguu huku akisema kwa sauti kubwa,



    “Basi huu si wizi huu? Huu ni wizi dhahiri. Wanaiba kimacho macho!” Alipiga makelele huku akilaani na kutukana. Makelele yalikuwa makubwa hata ng’ombe waliokuwa wakila majani bandani walisituka.



    Kijakazi hakujua lililokuwa likitokea. Alipigwa na mshangao kuona watu wanakuja na kuanza kuchukua vitu vya bwana wake. Lilikuwa trekta jipya alilonunua siku zile zile aliponunua liIe gari lake la aina ya Rambler.http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Alisimama karibu ya Fuad na kukunja mikono yake huku akimwonea huruma. Puad alipomwona tu Kijakazi amemsimamia mbele yake alimrushia teke kali lakini Kijakazi alijirusha upande na teke hilo halikumpata. Hata hivyo, kwa ajili ya kutokuwa na nguvu kwake kuliko sababisbwa na utu uzima, Kijakazi alianguka chini lakini mara alijizoazoa na kusimama.



    “Mbuzi we! Unataka nini hapa? Kwani huna kazi ya kufanya?” Fuad alimpigia makelele Kijakazi.



    Kijakazi alijiburura hivyo hivyo, mbio na kukimbilia bandani kwa ng’ombe.



    Kutoka pale, Fuad alifutuka moja kwa moja mpaka kwenye banda la matrekta na magari na alipofika hapo alisimama kati kati na kuanza kupiga kelele kama mtu aliyepandwa na wazimu, “Wezi wakubwa, wallahi ntayaharibu.” Alilitazama gari lake la kupelekea karafuu mjini ambalo kwa muda wa miezi miwili lilikuwa limelala kwa kukosa mipira ya nyuma.



    Aliranda huku na buku halafu alisimama mbele ya trekta lake moja lililobakia, “Na hili hawalipati ng’o,” aliendelea kupiga kelele huku jasho linamtoka kwa hamaki zilizochanganyika na joto la bandani mle.



    Alitazama huku huku na halafu alitoka bandani mle na kurejea nyumbani kwake na kuingia katika vyumba vyote kama mtu asiyejua la kufanya na mwisho aliingia ndani ya ghala yake ya chakula. Alifungua gunia la sukari na kuijaza sukari hiyo ndani ya kikapu tele, halafu akarejea tena kule kwenye banda la magari na kikapu chake cha sukari mkononi.



    “Hawalipati; na hata wakilichukua litakuwa halina faida yoyote. kwao,” aliendelea kusema huku akifungua kifuniko cha tangi la petroli la gari lile. “Na atakayekuja kulitia moto injini itampasukia,” aliendelea huku akimimina ile sukari ndani ya tangi lile la petroli.



    Fuad alimimina sukari nyingine ndani ya tangi la petroli la trekta halafu alifungua pale penye mashine na kukatakata waya.



    Alipoondoka bandani hapo hakusimama mpaka bandani kwa ng’ombe na kufungua mlango kwa vishindo vikubwa na kumsitua Kijakazi ambaye alikuwa amekaa amejinamia, mnyonge, kama aliyefiwa na baba yake. “Toka mbele ya macho yangu kisirani mkubwa we!” Fuad alimpigia kelele, na baada ya ukelele huo Kijakazi aliinuka na kuanza kukimbia mbio huku akisepetuka na kushikilia viguzo asije akaanguka.



    Bandani humo Fuad alianza kuvunjavunja mabao na vitu vingine na vishindo vilivyokuwamo bandani humo viliwasitua hata ng’ombe wakaanza kupiga kelele ovyo kama walioingiliwa na chui zizini mwao. Fuad aliangaza huku na huku na halafu aliuvuta ubao uliokuwa karibu naye na kushangaa nao mkononi halafu akamrembea nao ng’ombe mmoja na kumpigia kelele, “Na nyinyi nyote nitakufungulieni mtokomee huko mkatafute huo ujamaa wanaojenga ng’ombe wenzenu.”



    Alipotoka bandani humo alifululiza mpaka nyumbani kwake, akajitupa chali juu ya kitanda huku akipumua kama mtu aliyeshikwa na ugonjwa wa pumu kwa ghafla. “Mungu atawalaani! Mungu atawashinda makafir hawa!” alipiga makelele.



    Fuad tafrani zilimzidi. Asubuhi baada ya kwisha kunywa chai tu alivalia kwa safari ya mjin’. Alitia gari lake moto na kuondoka mbio. Hakusimama po pote mpaka Shangani kwa rafiki yake Nasoor. Alipofika nyumbani kwa Nassor hakushuka ndani ya gari ila alibakia humo humo na kupiga honi ya gari. Nassor, ambaye alijua vizuri sauti ya honi ya gari ya Fuad, alichungulia dirishani.



    “Vaa twende!” Fuad aliamuru.



    “Wapi?” Nassor aliuliza.



    “Twende zetu tukaupige!” Fuad alijibu.



    Bila ya kuchelewa Nassor alival’a na waliondoka pamoja mpaka bar ya marikiti. Walipofika tu walianza kwa ‘vikali’. Hapakuwa na mazungumzo yo yote isipokuwa yale ya Fuad kutaka kuchukuliwa shamba lake. Ijapokuwa Fuad alikuwa na nishai, hakuweza kuzungumza kwa kelele kwa kuchelea asije akasikika akiisubu serikali ya kimapinduzi ambayo wananchi wote waliikaribisha kwa mikono miwili.



    Walilewa mpaka usiku na walipomaliza walianza kutafuta panapo starehe.



    “Sasa leo wapi?” Fuad aliuliza.



    “People’s” Nassor alijibu.



    “People’s nd’o wapi?” Aliuliza Fuad.



    “Densini hapo Mnazimmoja!” Nassor alijibu.



    “Densini? Twende zetu!” Fuad alisema.



    Waliingia ndani ya gari mpaka mnazi mmoja hapo People’s Club.



    Ndani humo mlikuwa na kivumbi. Mziki ulikuwa umekolea na wananchi walikuwa wakicheza densi huku nyoyo zao zimejaa furaha. Zamani fursa kama ile walikuwa hawawezi kuipata kwani kabla ya mapinduzi klabu ile ilikuwa m ya mabwenyenye tu; wafanyakazi na wakulima waliiona kwa nje tu. Wakati huo ilijulikana kwa jina la Karimjee Club. Baada ya mapinduzi jumba hilo zuri lilichukuliwa na serikali na pakawa ni pahala maarufu ambapo wafanyakazi na wakulima huenda kujipumzisha baada ya kazi.



    Fuad hakupendezwa na mandhari ya humo ndani. Aliona waliomo humo wote ni kama wale watumishi wake ambao zamani akiwatuma kama anavyotaka yeye mwenyewe.



    “Hawa wanajuaje kustarehe hawa? Mimi nakwenda zangu. Siwezi fujo kama hii!” Fuad alimwambia Nassor.



    Alitoka nje peke yake na kumwacha Nassor anastarehe na mziki. Aliingia ndani ya gari lake na kuondoka. Alikuwa amelewa sana na alipofika hapo Mikunguni aliligonga gari kwenye mti. Katika ajali hiyo pale pale fahamu zikampotea.



    Kijakazi alijawa na wasiwasi mkubwa. Siku zote Fuad al pokwenda mjini basi Kijakazi hakupata usingizi mpaka alipolisikia gari la Bwana wake limerudi. Lakini siku hiyo mpaka saa sita ya usiku Fuad alikuwa bado hajarudi. Alikaa, macho muda mrcfu lakini Fuad hakutokea.



    “Sijui amefikwa na maafa gani maskini?” Kijakazi alijiuliza huku amekaa juu ya kitanda chake cha mayowe.



    Kucha Kijakazi hakupata usingizi na kila usiku ulipozidi kuwa mwingi bila ya kumwona bwana wake wasiwasi ulimzidi. Alitoka usiku ule mpaka kibandani kwa Mkongwe na kubisha hodi.



    “Mbona saa hizi, Kijakazi, kumezidi nini?” Mkongwe aliuliza.



    “Bwana Fuad hajarudi mpaka saa hizi sijui amefikwa na nini” Kijakazi alisema kwa sauti ya unyonge.



    “Na wewe nawe na Fuad wako? Mimi nikifikiri umefikwa na jambo gani sijui; kumbe hujalala mpaka saa hizi kwa sa’oabu Fuad hajarudi?”



    “Maana yake si kawai...”



    Kabla Kijakazi hajamaliza kusema Mkongwe alimkatiza maneno yake na kusema:



    “Sikiliza shoga; kama lililokuleta hapa ndilo hilo basi bora ondoka uniwache mimi nipumzike, mana’ake nimejichokea hapa niiipo.”



    Kijakazi hakuwa na ‘a kusema. Aliondoka na kwenda zake, wasiwasi umemjaa.



    Asubuhi iliingia, Fuad hakutokea. Kijakazi alikaa mbele ya mlango wa nyumba ya Fuad ameshika tama hajui la kufanya. Mara gari la hospitali liliingia na Kijakazi aliruka kutoka pale alipokaa. Kwa hakika hakujua ni gari gani lile alifikiri Fuad amenunua gari jingine kubwa zaidi lakini alishtushwa alipoona nyuma ya gari hilo ukifunguliwa mlango na watu wanne wakitoka na machera wamcmbeba Fuad.



    “Jamani niwahini! Niwahini jamani! Masikini Bwana wangu!”



    Kijakazi aliangusha kilio; alilia na huku akiomboleza kama mwanamke aliyefiwa na mumewe. Wafanyakazi wenzake wote walifika pale lakini hapana aliycouyesha majonzi wala huruma. Wote walikuwa wakimtazama Kijakazi alivyokuwa akimiminikwa na machozi.



    Aliwaongoza wale waliochukua machera mpaka chumbani kwa Fuad na walipofika humo walimlaza juu ya kitanda.



    “Usilie mama hakuumia sana,” mmoja katika wale waliokuwa wamechukua machera alimwambia Kijakazi. Alimbembeleza kidogo na baada ya kumwona yumo katika kupiga makelele tu alimpuuza. Waliingia ndani ya lile gari la hospitali na kurejea mjini.



    Kijakazi alimwonea huruma Fuad mfano wa mama anavyomwonea huruma mtoto wake mchanga wakati akiwa mgonjwa. Kila Fuad alipoondoka na gari lake dua ya Kijakazi ilikuwa “Mungu mrejeshe salama” lakini leo amerejea hali ile, majeruhi.



    Fuad aliumia kichwa na mguu wa kulia. Kichwa kilizungushiwa kitambaa cheupe na mguu ulikuwa ndani ya gamba la chokaa.



    Ajali hii ilimlaza Fuad kitandani muda wa miezi miwili. Mguu ulianza kupona lakini Fuad alikuwa mkaidi hatulii; wakati mwingi alifanya mambo ya kitoto labda kwa ajili ya athari ya kichwa aliyoipata.



    Siku moja jioni Kijakazi alikuwa anakwenda jikoni kuchukua kigongo cha kusukumia mkate. Fuad alikuwa chumbani amejinyosha kitandani na alipomwona Kijakazi alimwita bila ya kufikiri.



    “Kijakazi! Kijakazi! Njoo unikande mguu!”http://pseudepigraphas.blogspot.com/



    Fuad alionyesha mguu wake uliovikwa gamba la chokaa. Kijakazi alisita na kupigwa na mshangao. Alitazama chumbani kwa Fuad kwa hofu kwani hakupata hata siku moja kufikiri kwamba iko siku Fuad atamwita chumbani mwake.



    “Kijakazi!” Fuad aliita tena kwa sauti ya upole, “nimekwambia uje unikande mguu.”



    Kijakazi aliingia chumbani taratibu huku akinyemelea pale kitandani alipolala Fuad kama paka anavyomnyemelea panya anapotaka kumkamata.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog