IMEANDIKWA NA : HALFANI SUDY
*********************************************************************************
Simulizi : Penzi Chungu
Sehemu Ya Kwanza (1)
Suto Sutani, alikuwa ni msichana mwenye umri wa miaka 22. Alikuwa msichana mrefu wastani, Suto alikuwa na umbo zuri sana, alikuwa na ngozi nyeupe yenye kupendeza. Katika umri wake wa miaka 22, Suto hakuwa na mpenzi. Hakuwahi kufanya mapenzi, Hakuwahi kupata upendo toka kwa mwanaume yeyote yule duniani. Suto hakupata upendo hata wa baba yake mzazi. Mzee Sutani alimkataa Suto siku ileile aliyozaliwa. Sababu ya kumkataa ilibaki kuwa siri yake.
Bruno Michael, alikuwa kijana mtanashati sana. Alikuwa kijana aliyezaliwa katika familia yenye uwezo kiasi. Alikuwa kijana mwenye uzuri wa umbo na sura, uwepo wa pesa kiasi katika familia yao, vilifanya wanawake wengi sana wamhusudu sana Bruno pale mtaani kwao, Tabata dampo.
Bruno na Suto, walikuwa wanakaa mtaa mmoja, mtaa wa Tabata dampo. Wakati Suto na mama yake walikuwa wamepanga katika nyumba ya mzee Danigo, nyumba yenye vyumba sita na wapangaji sita ndani yake, nyumba ya kiswahili iliyojengwa Kiswahili.
Bruno alikuwa anakaa katika nyumba nzuri ya wazazi wake, nyumba yenye vyumba vitatu, yenye kila kitu ndani, nyumba ya kisasa iliyojengwa kisasa.
Ilikuwa siku ya jumamosi asubuhi, Bruno alikuwa hajaenda chuo siku hiyo. Wazazi wake walikuwa wameenda sokoni kununua mahitaji mbalimbali ya nyumbani kwa gari yao ndogo aina ya Suzuki.
Bruno alikuwa amekaa sebuleni akisoma kitabu cha Riwaya ya Ulaaniwe, riwaya iliyotungwa na Gwiji wa riwaya Tanzania, George Iron Mosenya.
Akili ya Bruno ilikuwa imezama hasa katika riwaya ile yenye kusikitisha sana, huku muziki mwanana wa mwanamziki Ben Pol ukisikika katika spika za redio yake.
Ghafla mlango wa sebuleni uligongwa.
"Karibu" Bruno alisema huku akikiweka juu ya sofa kitabu chake cha riwaya.
"Ahsante " Sauti ya kike ilijibu nje ya mlango ule.
"Sukuma, upo wazi "
Mlango ukafunguliwa.
Aliingia Suto, akiwa amevaa suruali nzuri aina ya jeans na blauzi fupi nyeupe. Mkononi alikuwa ameshika mkanda wa video.
"Kaka Bruno, nimeazima mkanda huu kwa kina Alex, naomba uniwekee niuangalie kidogo" Suto aliomba kwa sauti yake nzuri.
"Sawa, usijari" Bruno aliitikia.
Bruno alikuwa havutiwi kabisa na wasichana, alijiona mzuri, alijiona mtanashati, alikuwa ananata sana pale mtaani. Hakuwapenda wasichana, hakutaka hata kuwa na ukaribu nao. Lakini leo alipatikana, hakuwa na jinsi, walikuwa sebule moja na Suto Sutani.
Bruno aliuchukua ule mkanda mikononi mwa Suto na kwenda kuuweka kwenye deki, na kuzima redio iliyokuwa inaimba. Ulikuwa mkanda wa taarabu . Bruno alirudi sofani na kuendelea kusoma riwaya yake.
Suto akiwa na furaha isiyo na kifani kumuona Mzee Yusuph akiimba kideoni, huku madada wakicheza kwa umahiri mkubwa.
Kidogo kidogo taarabu ikaanza kumuingia kichwani Suto. Mziki wa taarabu ukapenya katika mishipa ya damu yake. Mwili ukamsisimka, Suto alikuwa mpenzi mkubwa sana wa taarabu. Taratibu alianza kutingisha kichwa pale sofani. Bruno alikuwa kazama riwayani, hakumuona Suto alivyokuwa anatingisha kichwa chake.
Taarabu ikachanganya, Suto alijikuta anasimama , akaanza kutingishika mwili wote taratibu. Bruno sasa aliweka kidole kurasa aliyoishia kuisoma, ili isipotee, macho yake yote mawili yapo kwa Suto Sutani.
Suto alikuwa hana habari kabisa. Sasa alikuwa anatingisha nyonga yake barabara. Bruno alibaki kahemewa.
Macho ya Bruno yalipanda kwa wizi, sasa yalitua katika kiuno cha Suto, kilikuwa kiuno kizuri sana. Chenye mviringo unaoeleweka. Bruno alikuwa makini, kiuno kizuri kilikuwa kinafata vizuri ule mdundo wa taarabu. Bruno sasa alikuwa anaangalia dhahiri, sio kiwizi tena.
Kiuno kizuri cha Suto kilikuwa mahiri sana.
Suto alikuwa bize na taarabu, akiwa kasahau kabisa uwepo wa Bruno kwa muda. Bruno alikuwa bize na kiuno cha Suto, akiwa kakisahau kitabu cha riwaya kwa muda.
Bruno naye alisimama taratibu, akawa anamsogelea Suto. Kitabu akikiacha palepale kwenye sofa. Suto alizidi kukatika, na Bruno alizidi kumsogelea. Walikaribiana sana sasa.
Suto kwa mbali alihisi kiuno chake kikishikwa, Bruno alikuwa hajielewi. Akili yake ilihama kabisa. Hakuuona kabisa ubaya wa kumshika Suto namna ile. Sasa alikuwa anamuona Suto ni mzuri zaidi ya Cleopatra. Kiuno kilimchanganya sana, alijikuta ghafla amekipenda kiuno cha Suto, hapana, alijikuta anampenda Suto kutokana na kiuno chake kizuri. Sasa waligusana kabisa, Suto akiwa mbele, Bruno akiwa nyuma.
Mikono ya Bruno ilikuwa kifuani kwa Suto, ikichezea maziwa ya Suto, mdomo wa Bruno ulikuwa sikioni kwa Suto. Walikuwa wananesa kutokana na mapigo ya mziki mzuri wa taarabu. Wote wakiwa hoi kwa hamu ya kitu wasichokifahamu. Pale sikioni mdomo wa Bruno ulijikuta ukisema, maneno yalitoka taratibu kwa sauti ya kukatakata mdomoni.
"Dunia mzi-ma ha-ikupe-ndi Suto. Wa-na-ume wote hawa-kup-endi Suto. Ila mi-mi nimegundua wewe ni mwana-mke mzuri sana. Ndio, Dunia nzi-ma inaku-chukia Su-to. Ila mimi naa-hidi ku-kup-enda kua-nz-ia leo, nit-aku-pen-da siku zote za mai-sha ya-ngu Suto,
Ndio, Nakupenda sana Suto !
Ghafla mlango wa sebuleni ulifunguliwa, hakuna aliyeusikia mlango wakati unafunguliwa, hakuna wala aliyesikia mlio wa gari wakati linapaki kule nje. Wote walikuwa wamezama hisiani.
Wazazi wa Bruno walikuwa wamerudi kutoka sokoni.
Baba na mama Bruno walipigwa na butwaa. Kukuta mtoto wao amemkumbatia Suto namna ile. Ilikuwa picha mbaya sana kwao.
" Bruno ! " mama yake aliita kwa ghadhabu.
"Naam "http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
" Ni nini hiyo ? !"
"Mapenzi mama " Bruno alijibu kwa upole.
"Unasema ! "
"Mapenzi ya kweli Mama"
"Unataka sema, unampenda Suto ?"
"Ndio mama "
"Maajabu haya ! Tangu lini ? "
"Tangu leo Mama "
"Unampenda toka moyoni Suto "
"Nampenda toka moyoni Mama, nataka nimuoe "
"Haiwezekani ! " Baba na mama Bruno walisema kwa pamoja kwa sauti kubwa yenye ghadhabu !
Muda wote huo Suto alikuwa kimya. Alikuwa anasikia kila kitu alichokuwa anasema Bruno. Lakini hakuelewa kabisa. Hakuwahi kumpenda mwanaume tangu azaliwe. Alikuwa anawachukia wanaume wote duniani, sababu kubwa ikiwa ni Simulizi aliyosimuliwa na mama yake, jinsi baba yake akivyomtesa mama yake, kufikia hatua hadi ya kumkataa yeye, mtoto wake. Suto aliwekuwa na kisasi na wanaume wote duniani. Maneno yale ya Bruno yalimtoa Suto machozi.
"Usilie Suto, chozi lako ni la thamani sana kwangu.." Bruno hakumalizia kauli yake.
"Hivi we mtoto umerogwa !" Baba yake alisema kwa sauti ya ukali.
"Nimependa baba " Bruno alisema kwa kujiamini.
Yalikuwa kama maigizo, Bruno mwenyewe hakujua nguvu ya maneno hayo inatoka wapi. Wazazi nao walishikwa na bumbuwazi, Suto alihemewa sana.
Wote hawakujua, mapenzi ni kitu cha ajabu sana, na muda mwengine yanaanza bila sababu maalumu. Bruno hakuwa amerogwa, sasa hakuwa amependa kiuno cha Suto pekee, alimpenda kweli Suto, na dhamira ya dhati toka moyoni mwake alikuwa anataka kumuoa kweli...
Suto Sutani, hakuwa na sura inayopendeza sana machoni mwa watu, hakuwa na mwili unaovutia sana. Lakini Suto alikuwa na upekee na ubora wake. Suto alikuwa na tabia nzuri kwa kila mtu, Suto alikuwa na nidhamu, alikuwa na heshima. Kwa ujumla Suto alikuwa na sifa zote za mwanamke anayepaswa kuitwa mke. Lakini wanaume wengi hawakulijua hilo. Wao walikuwa wanaamini mwanamke ni yule mwenye sura nzuri pekee, yule mwenye umbo zuri sana. Wanaume wengi walikuwa na fikra kama walizonazo baba na mama Bruno. Wao walikuwa wanaamini katika elimu, walikuwa wanaamini katika uzuri, walikosea sana, na wanaume wengi wanaendelea kukosea mpaka leo.
"Bruno unataka kumuoa Suto ?" Mama Bruno aliuliza kama katoka usingizini vile.
" Namaanisha mama !"
" Nipe sababu moja inayokufanya utake kumuoa Suto ?"
"Tabia"
" Sijakuelewa Bruno"
" Suto ana tabia nzuri mama"
"Hoja zako hazijitoshelezi Bruno ! " baba yake alisema kwa jazba.
Bruno alikaa kimya.
"Mimi ni nani yako ? "
"Baba "
"Mimi ni nani yako ?"
"Mama"
Sasa tunasema hivi, huwezi kumuoa Suto hata tukiwa tumekufa !"
"Nipeni sababu moja ya kunizuia kutomuuoa Suto?"
"Siyo chaguo letu" Wote walijibu kwa pamoja.
" Mnataka kunambia mke bora ni chaguo lenu tu, chagua langu Mimi siyo mke bora ?"
"Elimu yako ya sheria isikuvuruge Bruno, wewe ni wathamani, lazima upate mke wa thamani pia... "
"Kama Suto Sutani ! " Bruno alimalizia.
"Karogwaaa huyuuu nakwambia ! " Mama Bruno alipiga kelele kali.
"Ndio nimerogwa, nimerogwa na tabia nzuri ya Suto mama "
"Tabia ipi hasa ?" Mama Bruno aliuliza.
"Hana wanaume huyu, ametulia mama "
"Hahaha, wewe hujui sababu ya Suto kutokuwa na mwanaume ?"
"Najua "
" Ni nini ?"
"Msimamo wake thabiti, wa kutotaka kuchezewa na wanaume waongo ! "
" Bruno unapotea, sura ya Suto ndio sababu" Mama Bruno alisema.
Bruno alikuwa jasiri, hakuwa anampenda kabisa Suto kabla, lakini sasa alimpenda Suto ghafla. Ni kweli Suto hakuwa na mwanaume, ni kweli Suto alikuwa na heshima na nidhamu kubwa sana, lakini kwanini Bruno ameviona leo ? Tena ghafla ?
"Niliapa sitompenda mwanaume katika maisha yangu, nilijengwa hivyo na baba yangu mzazi, baba alimtesa sana mama yangu, alinitekeleza na mimi, alinikataa ningali mtoto mdogo sana. Kwa sababu nisizozielewa mpaka leo.
Labda sipendezi kweli machoni mwenu, lakini kwani mimi nimejiumba ?
Ngoja niwaambie kitu, kosa kubwa wanaolifanya Wanaume wengi, mnaenda kulifanya na ninyi. Ukitaka mwanamke angalia sura, lakini ukitaka mke angalia tabia "
Suto alijieleza kwa kirefu.
Sasa Bruno alipata nguvu mpya.
" Mama na baba, wote mna elimu kubwa sana, lakini kwa hili mnazidiwa busara na Suto ? "
"Unatutukana sasa ! " Baba Bruno alisema kwa hasira huku amekunja ndita.
" Siwatukani wazazi wangu, nawaambia ukweli, hivi inamaana hamjui kama uzuri wa mwanamke ni tabia ? "
" Hatutaki maelezo, sisi tunasema haumuoi Suto !" Walijibu kwa pamoja.
"Namuoa ! " Bruno alijibu kwa nguvu.
"Atanioa ! "Suto nae alipigilia msumari .
Sasa yalikuwa maigizo hasa. Kila mmoja jasho linamtoka. Wote wamekunja ndita.
Wazazi hawataki.
Watoto wanataka.
"Nakupenda Suto "
"Nakupenda sana Bruno"
Baba na mama Bruno walisonya msonyo mrefu. Kwa ghadhabu, wote waliingia ndani.
Pale sebuleni walibaki wawili pekee.
"Sikuwahi kufikiria kama nitakupenda siku moja, sikufikiria kwa kuwa sikuwahi kuwa karibu na wewe, ukaribu wangu huu wa leo, umefanya uniingie moyoni Suto, sitojari dunia inasema nini , nitajari tu moyo wangu unasema nini, nitakupenda Suto, nitakupenda hata kama dunia mzima itanidharau Suto , kuanzia leo nakukabidhi moyo wangu, usiutese, usiunyanyase, naomba unipende Suto ." Bruno alisema kwa sauti ya upole na yenye hisia kali.
Suto hakujibu, majimaji mepesi yalikuwa yanachuruzika katika kifua chake .
Alikuwa analia.
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa penzi hili lililokuja kuwa chungu. Penzi lililoanza kama utani, na kukomaa ghafla, penzi lililokuwa mfano, kati ya kijana mtanashati Bruno na msichana mwenye sura ya kawaida Suto.
Ndani ya nyumba sasa ilikuwa vita, vita kali kati ya Bruno na wazazi wake. Baba na mama yake walichukia sana mahusiano yake na Suto. Taratibu walijikuta hawaelewani na mtoto wao wa pekee Bruno. Ndani ya nyumba moja lakini wakawa hawasemeshani kabisa!
Mtaani ilikuwa ni hatari. Watu walimcheka na kumdharau Bruno. Kijana mtanashati kuzama katika dimbwi la mapenzi kwa Suto. Wengi walihisi karogwa. Penzi hili likazaa chuki nyingine kali kwa Suto. Watu walizidi kumchukia pale mtaani, wakiamini Suto mchawi, karoga ili apendwe na Bruno.
************
Manka Edward, alikuwa ni binti mrembo sana pale mtaani. Alikuwa msichana mrefu wastani, alikuwa mweupe mwenye umbo lililojazia kikike, chini alikuwa na mguu hasa. Mguu unaotoa ruhusa kuvaliwa kwa kimini chochote na binti huyo. Manka alikuwa anajua kuvaa. Tabata nzima hakuna msichana aliyekuwa anamfikia Manka kwa kuvaa nguo nzuri. Alikuwa mwanamke wa kisasa, mwenye kwenda na usasa.
Baada ya matatizo yale, mama Bruno alikuwa anafikiria namna ya kusitisha penzi la Suto na Bruno. Aliamua kutafuta binti pale mtaani ili awe na mwanawe. Ilimradi tu kuvunja penzi lile changa.
Alikaa sana sebuleni, akiwa kashika tama na kutafakari, kichwani mwake lilipita jina moja tu, jina la Manka. Aliamini uzuri wa Manka unaweza kuvunja penzi kati ya Bruno na Suto. Ikapitishwa ndani ya kichwa chake, Manka akawa suluhisho ndani ya kichwa chake.Aliamua kumtumia Manka kuwatenganisha Suto na Bruno. Muda uleule alinyanyuka sofani na kwenda nyumbani kwa Manka kumpa kazi ya kutenganisha penzi la mwanawe na Suto .
***********
Wakati mama Bruno akiwaza hayo na kufikia maamuzi hayo ya kumtumia Manka. Manka Edward alikuwa mbele ya kioo kikubwa chumbani kwake. Alikuwa anautazama mwili wake mzuri, anajitathmini na kujipa maksi mwenyewe.
Mara simu yake iliyokuwa kaitupa tu kitandani iliita.
Aliacha kujiangalia kwenye kioo, kwa mwendo wa madaha alielekea kitandani. Alikaa na kuichukua simu.
Akaipokea.
"Nambie janeth"
"Eeeh nipe huo umbea shoga "http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Unasema "
"Anatoka na Suto Sutani "
"Haiwezekani"
"Itakuwa karogwa, yaani kanikataa mimi mtoto mzuri kamchukua Suto ? Si bure nakwambia "
"Hawezi kumuoa, na sisi twende kwa mtaalamu "
"Sawa kesho"
Simu ikakatwa.
Manka alikuwa anaongea kwa mbwembwe na shoga yake. Lakini baada ya simu kukatwa aliingiwa na majonzi. Ukweli alikuwa anampenda sana Bruno, alitumia mbinu zake zote kumnasa bila mafanikio. Bruno alikuwa na msimamo imara. Siyo kwa Manka tu, hakuwa na msichana mtaani. Hakuwahi kuwa na msichana kabisa hapa duniani.
Manka alinyanyuka, alisogea pale mbele ya kioo chake kikubwa.
Alijiangalia.
Akaivua ile tshirt yake ya pinki.
Akavua ile suruali yake jeans ya bluu.
Juu alibaki na bra tu, nyeupe, chini alibaki na ........ nyeupe. Alianza kuitafuta kasoro katika mwili wake, hakuiona.
Aligeuka nyuma alijiangalia kwa kutumia kile kioo, hakuiona kasoro yoyote katika mwili ule mzuri.
Alikuwa mzuri.
Alikuwa kaumbika.
Alikitazama tena kioo, alijishangaa, alikuwa anatoa machozi....
Chozi lile lilitengeneza chuki mbaya sana, toka kwa Manka kwenda kwa Suto Sutani.
Manka alirudi kitandani, alikaa taratibu. Mawazo mengi yalipita katika kichwa chake. Ila moja lilipitishwa na kichwa chake.
Aliamua kuuwa !
Ndio, aliamua kumuua Suto Sutani.
Alisimama. Aliziangalia nguo zake pale chini. Alizikanyaga kwa miguu yake yote miwili. Alikunja ngumi kwa mkono wake wa kulia. Aliubana mdomo wake kwa meno, kwa hasira. Akawa anapiga ile ngumi kwa nguvu katika kiganja chake cha mkono wa kushoto.
Alipiga ngumi mara tano.
"Lazima nikuuwe Suto Shetani!" Alimpa Suto jina baya ili kuhalalisha dhamira yake mbaya.
Ghafla, mlango wa chumba chake uligongwa.
"Karibu " Alisema kwa sauti yenye mikwaruzo, bila shaka kutokana na hasira.
Mgeni aliingia, alikuwa ni mama Bruno.
Mama Bruno alivyomwangalia Manka alipigwa na butwaa. Manka naye alijiangalia. Akagundua kilichomshangaza mama Bruno, badala ya nguo kuzivaa, yeye alikuwa amezikanyaga.
lakini hakujari kabisa.
"Karibu mama "
"Mbona hivyo Manka ?"
"Suto "
"Suto kafanyaje tena ?"
"Shetani ! "
"Tena jini kabisa " mama Bruno alimalizia kwa hasira.
Baada ya Manka kutulia kidogo. Mama Bruno alimwambia lililompeka. Waligundua wote wana adui mmoja, Suto Sutani.
"We unataka tumfanyaje Suto ?"
" Mimi nataka aachane na mwanangu kabisa"
"Halafu ?"
"Bruno akuowe wewe"
"Ni ngumu sana"
"Kwanini Manka ?"
"Bruno hanitaki !"
"Yule mtoto karogwa haki ya Mungu !"
"La kufanya ni moja tu hapa"
"Lipi Manka ?"
"Kuuwa !"
"Unasema "
"Suto kwenda kuzimu ndio suluhisho pekee!"
"Siyo haki Manka "
"Kila kitu ni haki kwenye mapenzi na vita "
"Hivi unasema kweli Manka"
"Namaanisha "
Mama Bruno alichanganyikiwa. Pamoja na kumchukia sana Suto lakini hakutaka Suto auwawe.
Alikuwa muoga sana kuuwa.
"Nitamuua Suto kwa mkono huu!" Manka alimuonesha mama Bruno ule mkono alioukunja ngumi.
"Nakuomba usimuue Suto !"
"Toka nje mama "
"Manka unanifukuza"
"Kwanini hunielewi Dina" Manka alimwita mama Bruno kwa jina lake halisi.
"Sawa nakubaliana na wewe tumuue Suto '
" Karibu kwenye kochi Mama" Manka alibadirika ghafla.
Sasa walielewana.
**********
Wakati Manka na Mama Bruno wanapanga kumuua, Suto Sutani alikuwa anaosha vyombo nyumbani kwao. Alikuwa anaosha vyombo huku anaimba mashairi ya wimbo wa Rachel, kizunguzungu.
Mara mama yake alirejea kutoka sokoni. Alisikia sauti ya Suto ikiimba tangu yuko nje. Aliingia kimya kimya. Alimkuta Suto ameacha vyombo kabisa, akicheza mziki. Mwimbaji alikuwa yeye.
Mchezaji alikuwa yeye.
Kiuno cha Suto kilikuwa kazini tena.
Ama kweli mapenzi kizunguzungu.....
"Naona una furaha sana mwanangu "http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Kawaida tu Mama "
"Siyo kawaida yako Suto, siku zote umekuwa mtu wa huzuni sana "
"Nimeamua kujikubari Mama, naamini furaha yangu ipo ndani yangu, nikisubiri watu wa nje waniletee furaha, nitakuwa mtu wa kulia siku zote "
"Naona umekuwa sasa Suto, umenifurahisha sana leo"
"Hahaha, mimi nimekuwa zamani sana Mama "
*********
Baba Bruno nae hakuupenda kabisa uhusiano wa Bruno na Suto. Aliona ni dharau kuwa na mkwe kama Suto.
Dharau kwa marafiki zake, dharau kwa wafanyakazi wenzake, dharau kwa ndugu zake.
Alikuwa amekaa ofisini kwake, akiwaza mbinu za kutenganisha penzi lile changa.
Bado alikuwa hajapata suluhisho. Nini afanye kuvunja uhusiano ule.
Mama Suto aliingia ndani akiwa na furaha sana.
Kabla hajatokea Bruno katika maisha yake, Suto alikuwa anapendwa na mtu mmoja tu Duniani, mama yake mzazi. Mama Suto hakumwacha Suto peke yake siku zote. Pamoja na watu wengi kutompenda Suto, lakini mama yake alimpenda sana.
Mara nyingi walikuwa wanalia pamoja Suto anaponyanyaswa. na kucheka pamoja Suto anapofurahi, kama hii leo.
Bruno alikuwa chuoni, alikuwa anasomea sheria katika Chuo kikuu cha Dar es salaam. Tangu asubuhi alivyoenda Chuo mpaka sasa alikuwa anawaza mustakabari wa mahusiano yake na wazazi wake. Aliona sio busara kugombana na wazazi. Akaamua baada ya vipindi awapigie simu wazazi wake, kuwaomba radhi. Lakini pamoja na kuomba radhi alipanga kupinga ushauri wowote utakaohusu kuachana na Suto.
Muda wa vipindi uliisha, Bruno alitoka nje ya darasa. Kabla hajawapigia wazazi wake, simu yake iliita.
Alikuwa Manka.
"Haloo Bruno "
"Nambie Manka"
"Uko wapi ?"
"Sema shida yako Manka"
"Naomba tuonane leo jioni"
" Samahani, sina muda"
"Hivi kwanini unanichukia Bruno kiasi hicho ?"Bruno hakujibu swali lile, nae aliuliza swali.
"Kwa nini umeweka 'loud speaker'....?"
Ghafla simu ikakatwa.
Simu ile alipiga Manka akiwa chumbani kwake na mama yake Bruno, Manka aliweka simu 'loud speaker' ili mama Bruno asikie majibu ya mwanae. Bila kutegemea Bruno aligundua kama simu ile imewekwa loud speaker.
Sasa wanawake wale wawili walikuwa wamehemewa. Wakishangaa Bruno kajuaje kama waliweka 'loud speaker'.
Bruno nae alibaki na maswali mengi.
" Kwanini Manka aweke 'loud speaker ?, na baada ya kumuuliza kwanini akate simu ghafla ? Kwa vyovyote vile, wakati Manka anapiga simu ile alikuwa na mtu, je mtu huyo ni nani ?"
Bruno alibaki na maswali bila ya majibu. Aliamua kumpigia simu Manka ili apate majibu ya maswali yake.
Bruno alipiga simu, mara ya kwanza simu iliita mpaka ikakatika, alipiga tena simu.
Kule chumbani kwa Manka, kulikuwa na mabishano, kati ya mama Bruno na Manka.
"Pokea sasa simu hiyo"
"Nitamwambia nini mama"
"We mwambie sikuweka 'loud speaker' tu "
Walibishana sana, hadi simu ikakatika. Baada ya muda mfupi, simu iliita tena
"Ngoja niwashe redio halafu nimwambie nipo kwenye kelele" Manka alitoa wazo.Hakusubiri kujibiwa.
Aliisogelea redio.
Akaiwasha.
Wimbo wa Ommy Dimpoz, Baadae, ulikuwa unarindima kwenye spika za redio ya Manka.
"Hallo" Bruno aliita.
"Nipo kwenye kelele nitakupigia baadae "
"Sawa "
Simu ikakatwa.
Bruno alitembea kama hatua kumi. Sasa alikumbuka wazo lake la kuwapigia simu wazazi wake, ili awaombe radhi. Alianza kumpigia mama yake.
Simu ikapokelewa.
"Hallo Mama "
"Nipo kwenye kelele nitakupigia baadae"
Simu ikakatwa .
Bruno kengele ya hatari iligonga kichwani kwake.
Aliyasikia maneno yaleyale.
Wimbo uleule.
Toka kwa watu wawili tofauti, alioongea nao muda mfupi sana.
Alivyompigia Manka alisikia vizuri wimbo ule.
"Baadae"
Na sasa kampigia Mama yake. Anausikia tena wimbo uleule.
Mbaya zaidi wote wameongea maneno yaleyale .
Kuna kitu.
"Kuna kitu "
Bruno alihisi kuna kitu, alihisi Manka na mama yake wapo sehemu moja.
"Inawezekana vipi watu waliopo sehemu mbili tofauti, waongee maneno yanayofanana , na usikike wimbo unaofanana
Katika muda unaofanana ". Bruno alikuwa anajiuliza mwenyewe kimoyomoyo.
"Coincidence" Alijijibu mwenyewe pia.
"Coincidence gani hii?"
Hakupata jibu.
'Coincidence ni hali ya vitu viwili au zaidi vinavyofanana kutokea katika muda unaofanana lakini bila kupangwa'
Bruno sasa aliamua kumpigia simu baba yake, ili amuombe msamaha. Baba yake hakuwa anapatikana kwenye simu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Manka na mama Bruno walipanga vizuri mipango yao. Mipango Ikatekelezwa na wao wenyewe. Sasa Manka alikuwa na jukumu la kwenda kuwatafuta vijana wa kumuua Suto kesho yake usiku.
**************
Katika jiji la Dar es salaam, mtaa wa Tandale ni mtaa uliokuwa maarufu sana kwa watu wa hali ya chini. Kutokana na ukosefu wa ajira vijana wengi wa Tandale walijishughulisha na matumizi yaliyokithiri ya bangi na matumizi ya madawa ya kulevya.
Ili kufanikisha azma yao, Manka alienda Tandale ili kutafuta vijana watakaoenda kumuua Suto , mtu waliyetokea kumchukia zaidi Duniani bila sababu za msingi.
Pesa haishindwi kitu !
Manka alifanikiwa kuwapata vijana watatu mahiri katika mauaji.
Vijana ambao hawakuwa na huruma.
Vijana ambao hawakuwahi kuwa na huruma tangu wazaliwe.
Wawe vipi na huruma wakati Dunia haijawahi kuwaonea huruma.
Manka na wale vijana wauaji walipanga usiku wa kesho yake ndio waende kumuua Suto. Kumuua mwanamke yule asiyekuwa na hatia kabisa.
Siku ile waliitumia kufahamu mazingira ya nyumba anayokaa Suto huko Tabata. Vijana wale walirudi Tandale kujipanga ili wajue kwa jinsi gani wataenda kuivamia nyumba aishiyo Suto, na kumuua!
Kinje, Zinja na Dungu ndio vijana waliokodiwa na kina Manka, walikuwa vijana hatari na makatili sana.
Historia ya maisha yao iliwatengeneza wawe hivyo. Walikuwa na historia mbaya katika maisha yao iliyowapelekea kumchukia kila aina ya binadamu duniani. Walikuwa wanatamani kuua hata dunia nzima kwa sababu wakiozijua wao. Leo wamepewa pesa ili wakatekeleze mchezo waupendao, walifurahi sana !
****************
Bruno alirudi nyumbani, alimkuta mama yake amekaa sebuleni. Tofauti na jana, leo mama yake alimchangamkia sana.
Bruno alishangaa.
Muda wa jioni baba yake alirudi. Nae alikuwa na furaha pia. Walikaa sebuleni na kuongea na kucheka kama zamani. Familia hii ilirudi tena kwenye furaha ghafla, bila kujua Kila mmoja alikuwa na siri nzito kichwani mwake.
Wakati mama Bruno akiwa na furaha akijua kesho usiku atapokea taarifa za kifo cha Suto Sutani !
Baba Bruno nae alikuwa na furaha akijua kesho usiku atapokea taarifa ya kifo cha Suto Satani !
Baba Bruno nae aliongea na mtu ili akamuue Suto!
Alikuwa anaitwa Killer, alikuwa jambazi maarufu sana mitaa ya Sinza. Sinza nzima walikuwa wanamjua Killer.
Killer aliupenda sana mchezo wa kuua !
Mchezo wa kuua nao ulitokea kumpenda pia Killer.
Hakika walipendana sana.
Hatimaye ilifika siku ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu na Manka, pamoja na mama na baba Bruno.
Ilikuwa siku jumatano, iliyoambatana na mvua mchana kutwa katika Jiji la Dar es salaam. Mvua ambayo Suto ilimfanya ashinde ndani muda mwingi. Akiwa anachati na mpenz wake Bruno.
Usiku wa siku ile ukaingia. Kutokana na mvua , usiku ule yakatengenezwa mawingu mazito angani. Hakukuwa na mbalamwezi hata kidogo.
Kulikuwa na giza totoro!
Saa saba ya usiku, watu watu walikuwa wanaizunguka nyumba moja mitaa ya Tabata. Walikuwa watu watatu hatari, walikuwa makini na kila hatua waliyokuwa wanapiga.
Kinje alisimama katika kona moja, upande wa magharibi wa nyumba ile, Zinja yeye alisimama katika kona nyingine, upande wa mashariki, huku Dungu yeye alikuwa katika mlango wa kuingia nyumba kubwa ya kina Suto Sutani.
Dungu alikuwa na rundo la funguo bandia. Sasa alikuwa anajaribu funguo wa nne kufungua mlango ule.
Funguo tatu za awali zilikuwa zimekataa.
Nyuma ya nyumba ile, kulikuwa na kivuli kimoja kirefu. Kivuli kile kilikuja muda mrefu pale. Kivuli kiliwashuhudia watu watatu tangu walivyokuja mpaka wakivyoinyatia nyumba ile. Kivuli kile kilikuwa kimeshika kisu kirefu!
Pamoja na kuwa na giza totoro, lakini kisu kile kilikuwa kinameremeta.
Tayari kwa kumchoma mtu yeyote kitakapoamrishwa kufanya hivyo!
Kivuli sasa kilisogea taratibu. Bila kutoa sauti yoyote.
Kilikuwa kinamsogelea yule mtu aliyopo upande wa magharibi wa nyumba ya kina Suto.
Kinje alijibana vizuri pale konani, ingawa hakuwa makini sana. Akili yake yote ilikuwa ipo pale mlangoni, akimwangalia Ngudu akijaribu kufungua ule mlango.
Sasa kile kivuli kilikuwa hatua kama tatu nyuma ya Kinje.
HISIA, Kinje alihisi kuna kitu cha hatari nyuma yake. Aligeuka kwa haraka akiwa kashika panga lake kubwa mkononi.
Alichelewa!
Kwa mkono wake wa kulia kile kivuli kilizamisha kile kisu kwa nguvu katika kifua cha Kinje.
Kisu kilizama kifuani !
Kinje alitaka kupiga kelele, lakini kivuli kilimuwahi. Kinje alizibwa mdomo na kile kivuli. Kivuli kilikuwa kimevaa gloves mkononi.
Kivuli kile, kilikuwa kivuli cha Killer !
Killer aliulaza chini taratibu mwili wa marehemu Kinje. Sasa Killer aliizunguka tena ile nyumba kwa nyuma ili aende upande wa mashariki aliokuwa Zinja.
Killer alilipwa kuuwa mtu mmoja, lakini hakuwa na jinsi. Ilikuwa lazima aue watu watatu hawa, na wengine endapo ikilazimu ili aipate shabaha yake, Suto Sutani !
Killer sasa alikuwa hatua chache sana nyuma ya Zinja. Zinja hakuwa na hisia zozote kama kuna mtu nyuma yake. Alijibana pale mkononi huku akiomba dua mlango akioufungua Dungu ufunguke.
Ghafla! Alizibwa mdomo kwa mkono mpana wa Killer. Kisu kilekile kilichomuuwa Kinje, sasa kilizama tumboni kwa Zinja mara tatu na kutoka. Kilitengeneza jeraha baya sana!
Killer aliulaza pia mwili wa Zinja pale chini. Sasa kwa mwendo wa kunyata alikuwa anamfata Dungu pale mlangoni.
Kule ndani, Suto Sutani aliamka ghafla kutoka usingizini. Alikaa kitandani akikumbuka ni kitu gani kichomuamsha.
Alikumbuka.
Suto alikuwa amebanwa na haja ndogo. Haja ndogo iliyomtoa usingizini na kumleta duniani.
Choo cha nyumba ile kilikuwa cha nje. Ilimlazimu Suto atoke nje usiku ule wa manane, wenye giza la kutisha, ili akajisaidie.
Alinyanyuka pale kitandani na kuelekea nje.
Nje ambako kulikuwa na Dungu, nje ambako kulikuwa na Killer, pia kulikuwa na maiti mbili zenye majeraha mabaya ya kisu !
Suto alitoka taratibu kitandani, huku akiwa na maluweluwe ya usingizi. Alitokea kwenye sebule pana ya nyumba ile. Alichukua funguo Kwenye msumari mrefu uliokuwepo pale sebuleni.
Sasa alielekea kufungua mlango.
Kule nje Killer alikuwa amemkaribia kabisa Dungu. Dungu alikuwa tofauti sana na kina Zinja. Dungu alikuwa mtu hatari sana, aliuhisi ujio wa mtu nyuma yake zamani sana, alijifanya kama hajui kama kuna mtu nyuma yake.
Dungu alijiandaa tayari kwa kwa ujio wa mtu huyo.
Killer alikuwa anavizia, wakati mviziwaji alikuwa ashajua kama anaviziwa!
Kwa mwendo wake wa taratibu Suto alikuwa anaelekea mlangoni, kuufungua ule mlango.
Kule nje, Killer alikuwa nyuma ya Dungu kwa ukaribu wa kama hatua moja. Killer alinyanyua juu ule mkono wenye kisu kirefu kinachomeremeta gizani. Kwa kasi na nguvu kubwa akawa anaushusha shingoni kwa Dungu ule mkono wenye kisu!
Dungu alikuwa anaona kila kitu kwa jicho la pembeni. Kwa kasi naye aliinama, mkono wenye kisu wa Killer ulikosa kwa kupiga, ulipita hewani bila kumpata aliyemlenga.
Kule ndani, Suto alikuwa anaingiza funguo katika kitasa cha mlango. Aliona kuna ugumu kidogo.
Akalazimisha.
Kumbe kule nje Dungu aliacha funguo zake zikining'inia pale kitasani, ghafla zikadondika!
Mlango ukafunguka.
Baada ya kukwepa kile kisu, Dungu aligeuka nyuma, akiacha funguo zikining'inia pale kwenye kitasa.
Sasa Dungu na Killer walikuwa wanatazamana. Killer kashika kisu kwa mkono wake wa kulia, Huku Dungu kashika panga kwa mkono wake wa kushoto!
Suto alikuwa amesimama katikati ya mlango, akiwashuhudia wale majabali wawili wakitazamana. Suto alipigwa na butwaa, hakuweza kutoa sauti yoyote. Na wala hakutoa ishara yoyote.
Alitulia tuli.
Killer alirusha ngumi ya nguvu kwa mkono wake wa kushoto. Ngumi iliyompata Dungu shavuni. Dungu alinesa kidogo, akiwa kwenye ule mneso alirudi kwa nguvu na lile panga, panga lilitua shingoni kwa Killer barabara. Nusu ya panga liliingia pale shingoni, Dungu aliacha lile panga likining'inia shingoni kwa Killer.
Alikimbia mbio!
Suto Sutani, alikuwa kama kapigwa na ganzi pale mlangoni. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake alishuhudia tukio la hatari. Suto alishuhudia binadamu akiwa anakufa huku akimwaga damu mithili ya bomba bovu la maji.
Ghafla, alipata kauli. Alipiga kelele kubwa sana.
Huku akilia kwa woga!
Huku akilia kwa hofu!
Ndani ya dakika tano, watu walikuwa wamejaa. Wenye silaha mbali mbali.
Walifika kwenye ile nyumba akiyokaa Suto Sutani.
Walipofika pale watu wote walipigwa na butwaa. Walikuta picha mbaya sana. Maiti ya mtu ikiwa imedondoka chini, na panga shingoni.
Suto alikuwa analia sana, kila anachoulizwa yeye analia. Mjumbe alipiga simu, kituo cha Polisi Tabata.
Baada ya robo saa polisi waliwasiri.
Polisi waliikagua nyumba yote kuangalia mazingira ya mauaji yale. Ndipo waliikuta miili mengine miwili.
Waliichukua.
Walimchukua na Suto Sutani. Yeye ndiye alikuwa mshtumiwa namba moja katika kesi ya mauaji yale!
Dungu alikimbia sana usiku ule. Alikuwa kama amechanganyikiwa.
Hakuelewa kabisa kimetokea nini?
Hakujua yule mtu ni nani?
Hakuelewa wenzake wake wapi?
Alipofika mbali na nyumba ya kina Suto alisimama, huku anahema, alitoa simu yake mfukoni. Alilitafuta jina la Manka na kumpigia.
"Halloo Bosi"http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Nambie Dungu, mmefanikiwa?"
"Hapana Bosi"
"Kwa nini"
'Mimi sielewi Bosi"
"Dungu! Mbona unanichanganya!"
"Misheni imefeli Manka"
"Kwanini?"
"Suto Sutani analindwa kumbe!"
"Analindwa ??!!"
"Ndio, sijui kama kina Zinja wako salama kweli"
"We uko wapi, nije tuongee maana hata sikuelewi"
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment