Simulizi : Penzi Chungu
Sehemu Ya Pili (2)
Dungu alimuelekeza Manka alipo. Usiku wa manane Manka aliamka na kumfuata Dungu. Ajue kilichowasibu.
Mambo sasa yaliwaendea kombo. Tofauti na wakivyotarajia kabisa.....
Suto Sutani alifikishwa kituo cha Polisi Tabata usiku, hakuhojiwa.
Aliwekwa selo.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Suto kupelekwa Polisi, Ilikuwa ni mara ya kwanza pia kwa Suto kuingizwa selo. Ulikuwa ni usiku mbaya sana kwake. Ndani ya selo kulikuwa na mazingira magumu sana kwa mtu kuishi. Kilikuwa ni chumba kidogo sana, chenye dirisha moja juu. Chumba chenye hewa nzito iliyoambatana na harufu ya damu iliyokauka.
Pamoja na Jiji la Dar es salaam, kuwa na hali ya mvua, ambayo ilipooza hali ya joto na kuigeuza kuwa ya baridi, lakini mbu hawakukoma katika selo ile. Kulikuwa na mbu waumao na wenye kuleta kelele mbaya masikioni.
Suto aliwakuta watuhumiwa watatu ndani ya ile selo. Walikuwa wamekonda na majeraha kwenye miili yao. Suto alihisi walikuwa mateja au wanywaji wa pombe za kienyeji, waliodhulumiana na kuamua kupigana. Wote walikuwa wamelala usingizi nzito.
Suto nae alichagua kona moja ya selo ile. Akaiegemea, akawa anajikokota chini taratibu kwa kutumia mgongo.
Suto alijiburuza mpaka akajipweteka chini, alikunja miguu na kuiweka sura yake juu ya magoti yake.
Alikuwa analia..
Kule Tabata, Manka na Dungu walikutana. Dungu alimueleza kila kitu kilichotokea usiku ule. Manka hakuamini kabisa, alijua ni hila tu za Dungu ili asiitekeleze kazi yake. Mwishowe waliagana wakiwa wamekubaliana watakutana kesho yake saa nne. Kulijadiri vizuri jambo lile.
Nyumbani kwa kina Suto kulikuwa hakueleweki. Kulikuwa na kelele za kilio toka kwa mama Suto. Mama Suto alimlilia sana mwanae, huku akimlaani mtu aliyeua na kumsababishia balaa lile mwanae.
Usiku uleule Manka alienda nyumbani kwa kina suto. Aliyoyakuta, yalimshangaza sana. Alikuta kuna umati mkubwa wa watu, alimvuta mwanamke mmoja pembeni na kumuuliza kilichotokea pale.
"Kuna watu watatu wameuliwa na dada mmoja anakaa ndani humu"
"Ziko wapi maiti zao?"
"Zishapelekwa hospitali"
"Huyo dada yuko wapi sasa?"
"Dada amechukuliwa na polisi, amewauwa kinyama kweli, sijui hata walimkosea nini....?"
Yule dada aliendelea kuongea, lakini Manka hakuendelea kumsikiliza. Alihisi kelele kichwani kwake kama kuna watu wanagonga vyuma.
Kwa kifupi alichanganyikiwa !
Muda uleule, alichukua simu yake, na kumpigia mama Jfloux.
Mama Bruno na baba Bruno walikuwa wamelala kitandani. Walilala huku wakitarajia kupigiwa simu. Wakati mama Bruno akiitarajia simu kutoka kwa Manka, baba Bruno alikuwa akiitarajia simu kutoka kwa Killer. Simu zenye ujumbe sawa. Toka kwa watu wawili tofauti.
Ujumbe, wa kifo cha Suto Sutani !
Simu ya mama Bruno ndio ilianza kuita...
Mama Bruno akiwa na sura yenye furaha sana alienda bafuni kuipokea ile simu aliyotarajia ina habari za kufurahisha toka kwa Manka.
Alienda kwa furaha, lakini alirudi na huzuni kuu.
Bruno alikuwa amelala chumbani kwake akiwa hana habari yoyote iliyotokea duniani. Alikuwa njozini, akiota jinsi penzi lake jipya na Suto jinsi likivyochanua. Penzi lao lilikuwa linazidi kukomaa, likichagizwa na meseji wakizotumiana mara kwa mara.
Hakujua kabisa, wakati yeye akiota ndoto nzuri, Suto Sutani alikuwa katika selo moja chafu sana, katika kituo cha Polisi Tabata.
Mama Bruno alirudi toka bafuni, alifika kitandani, alikaa kitako pembeni kabisa mwa kitanda. Alishika tama na kuanza kuichambua habari ile mbaya aliyopewa na Manka kwa njia ya simu.
Baba Bruno alikuwa amejifanya amelala, lakini alikuwa hajalala kabisa. Alikuwa macho Akisubiri simu toka kwa Killer. Baba Bruno, alikuwa anazishuhudia pilikapilika zote za mkewe usiku ule. Lakini hakuelewa nini kimemsibu mke wake. Na wala hakumuuliza.
Mtu na mkewe walikesha macho siku ile.
Asubuhi na mapema bila kujua hili wala lile, Bruno alijiandaa kuelekea chuoni.
Akiwa njiani, alimuona kijana mmoja akiuza magazeti. Bruno alimuita kijana muuza magazeti kwa lengo la kununua gazeti. Vichwa vya habari vya magazeti yale yalimstua sana Bruno.
Alilichagua gazeti litokalo kila siku, gazeti pendwa la Dumizo lililokuwa na kichwa cha habari...
'Muuaji katili wa kike aibuka Tabata !'
Bruno akiwa ndani ya daladala alianza kuisoma habari ile. Kila alivyoendelea kuisoma habari ile mwili wake ulimuingia baridi.
Jinsi mwandishi wa kike, Veronica Baro, alivyoisimulia habari ile ilikuwa inasisimua sana, alieleza jinsi walivyoukuta mwili wa marehemu ukiwa na panga shingoni.
Mwishoni akiishauri serikali impe adhabu kali muuaji, huku akimtaja kwa jina muuaji kuwa ni Suto Sutani!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Veronica Baro, kwa kutumia kalamu yake, aliiaminisha jamii kwamba, muuaji wa watu wale ni Suto Sutani.
Wakati anamaliza kusoma Jfloux machozi yalikuwa yanamdondoka. Aliamua kugairisha safari ili aende Tabata, kwa Suto. Kuthibitisha habari zile. Hakuamini kabisa kama Suto anaweza kuuwa kikatili namna ile.
Suto alikuwa mwoga, hakuweza hata kuua panya !
Kule selo, Suto aliendelea kuteseka hadi asubuhi. Hakulala kabisa. Mbu na harufu vilimtesa sana.
Lilikuja gari la gereza la Segerea, Suto aliingizwa kwenye karandinga na kupelekwa kwenda kuanza maisha mapya gerezani.
Alitolewa pale Polisi bila ya kuhojiwa chochote, haukuwa utaratibu kabisa, lakini Suto alifanyiwa hivyo. Huku akipandishwa kwenye karandinga kwa mateke na mangumi toka kwa askari Polisi mmoja. Suto alimuangalia kwa jicho kali sana yule askari, alirushwa kwa nguvu na kujipweteka kwa nguvu nyuma ya lile gari. Akiwa kalala chini, Suto alimwangalia tena askari yule.
Utajuta !
Macho ya Suto yalieleza hivyo.
Kule kwa baba Bruno, Mzee Boe na mama Bruno waliamka wakiwa hoi, wote walikuwa hawajalala, wote walificha siri nzito vifuani mwao. Hakuna aliyemshirikisha mwenzie.
Baba Bruno alikuwa anapiga simu kila mara, simu Ilikuwa haipatikani.
Killer alikuwa hana tabia ya kufanya kazi hatari kama zile akiwa na simu. Huwa anazima na kuiacha nyumbani. Anajua madhara ya kwenda kufanya mauaji akiwa na simu.
Sasa Killer ameuwawa, na simu yake ikiwa haipatikani.
Baba Bruno jasho lilimtoka.
'Ulale salama Shangazi'
Upande wa mama Bruno nae aliamka akiwa anawasiliana na Manka kwa njia ya meseji.
"Lazima tuhakikishe Suto anafia jela" mama Bruno aliandika.
"Kweli maana hatujui kama kina Zinja walitutaja au vipi?"
"Tutamuuaje sasa ?"
"Tutajua tukikutana"
"Sawa"
Wanawake hawa hawakuwa na huruma kabisa. Walipania kumuua Suto Sutani, kwa hali yoyote ile, kwa namna yoyote ile .
******************
Habari nzuri husambaa taratibu, lakini habari mbaya husambaa haraka sana !
Habari za mauaji ya kikatili ya watu watatu Tabata, yalisambaa haraka sana Tanzania nzima.
Yaliishangaza nchi hasa baada ya kugundulika kuwa muuaji wa watu hao alikuwa ni mwanamke. Kama habari ilivyoandikwa kwa uhakika mkubwa na mwandishi wa habari wa gazeti la Dumizi, Veronica Baro.
Veronica Baro hakuandika tu habari, alihukumu pia, tena bila uhakika.
Bila kufanya uchunguzi wa kina.
Tanzania nzima sasa ikawa inamlaani Suto Sutani !
Bila kujua undani wa sakata hili. Bila kujua chanzo halisi cha mauaji yale.
Mwandishi ni mtu anayeaminiwa sana kwa kila anachokiandika, Watanzania wengi walimwamini Veronica Baro. Kalamu ya Veronica Baro ikamsulubu vilivyo Suto Sutani.
Tanzania nzima wakawa wanaimba, anyongwe.... anyongwe, Suto muuaji !
**********
Bruno alienda nyumbani kwa Suto Asubuhi ile. Hakumkuta Suto, wala mama yake Suto. Aliwakuta majirani wachache, baada ya kuulizia aliambiwa Suto na mama yake, wameenda kituo cha Polisi Tabata.
Bruno nae alienda kituo cha Polisi akiwa na mawazo tele. Huku habari iliyoandikwa na Veronica Baro ikijirudiarudia kichwani mwake.
Alifika Polisi, majibu ya askari Polisi yalimchosha kabisa, walimwambia Suto amepelekwa mahabusu, Segerea.
Bruno alikaa huku kashika tama kwenye benchi la pale kituo cha Polisi.
Alichoka kabisa.
Segerea, Suto alikaribishwa vibaya sana. Askari magereza, Wafungwa na mahabusu wenzake walimchukia sana Suto. Walikuwa wanamuona ni mwanamke muuaji.
Hawakumpenda, walimtenga na kumnyanyasa sana. Wakisahau kabisa kama nao walipelekwa pale kwa makosa mbali mbali. Wakisahau kama kama Suto alikuwa Mtuhumiwa tu, mahakama ilikuwa haijamtia hatiani bado.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Saa nne kamili asubuhi, Manka na Dungu walikutana, ilikuwa katika mgahawa mdogo uliopo Magomeni. Hawakutaka kukutania Tabata.
Sasa walipanga vizuri mpango wao, walitaka kuhakikisha Suto Sutani anaozea jela, au anafia jela. Waliamua kutumia Pesa. Kumhonga yeyote yule ili Kuhakikisha adhma yao inakamilika!
Walipanga mipango, mipango ikapangika!
Bruno alitoka pale kituo cha Polisi kichwa chini, mikono nyuma, alirudi nyumbani kwao kwa mwendo wa taratibu.
Alipofika nyumbani, aliwakuta wazazi wake wakiwa kimya sebuleni. Naye alichagua kochi moja, akakaa.
Bruno aliuvunja ukimya !
"Wazazi wangu, Suto amepatwa na matatizo makubwa..!"
"Matatizo gani?" Baba Bruno aliuliza kwa fadhaa.
"Suto, amekamatwa na Polisi"
"Unasemaaa!" Baba Bruno hakutarajia taarifa hiyo. Yeye alikuwa anatarajia kupokea taarifa ya kuuwawa kwa Suto.
"Suto amekamatwa babaa" kwa mara ya kwanza tangu sakata hili litokee, Bruno alidondosha chozi.
Mama Bruno alibaki midomo inamtetemeka. Ilikuwa habari anayoijua lakini hakupenda kabisa kuisikia...
Ilikuwa taharuki ndani ya nyumba ile. Mipango hasi ya Baba na mama Bruno sasa ilileta taharuki kuu katika familia ile. Wote watatu walikaa pale sebuleni wamechoka mwili, wamechoka na akili.
***********
Kule gerezani, Suto sasa alibatizwa jina kwa baba mpya, badala ya Sutani, jina la baba yake mzazi, sasa alipewa jina la baba anayeitwa muuaji.
Sasa aliitwa Suto muuaji !
Gerezani pia Suto aliendelea kuwa na damu ya kunguni. Suto hakupendwa na watu wote mle gerezani, lakini kuna watu wawili walimchukia zaidi Suto, watu hao walikuwa ni askari magereza wa kike, Beji na Zura.
Beji na Zura, walikuwa ni askari makatili sana katika Gereza la Segerea. Beji na Zura walihakikisha wanapeleka mateso makali sana kwa Suto.
Sababu ya kumtesa Suto waliijua wao, labda ni chuki tu ndizo zilisababisha mateso hayo kwa Suto.
Beji na Zura walimpa Suto kila aina ya mateso waliyoyafikiria, walikuwa wanamyima Suto chakula, wanampiga na kumgomea.
Suto maisha yake siku zote yakawa ya kulia mle gerezani.
************
Siku ya jumapili, Bruno alitoka nyumbani kwao na kwenda katika Gereza la Segerea, ili kumuona mpenzi wake Suto.
Siku hiyo mlangoni ilikuwa zamu ya kulinda ya Beji. Ingawa ilikuwa siku ya kuwaangalia mahabusu na wafungwa, lakini Beji alimkatalia katakata Bruno kuingia gerezani kumuona Suto. Bruno alipambana sana bila mafanikio, mwishoni aliamua kurudi nyumbani. Bruno alirudi nyumbani akiwa na mawazo tele, aliyakumbuka sana maneno ya askari yule kuwa eti hawezi kumuona Suto kwa kuwa alikuwa muuaji. Wakihofia usalama wa Bruno.
Bruno alifika nyumbani kwao. Alikaribishwa na maneno makali toka kwa mama yake mzazi.
"Ndio ulienda kwa huyo muuaji wako, utajitia hatiani mwanangu, Suto siyo mtu wa kukaa nae karibu kwa sasa !"
Sasa maneno ya yule askari, Beji, kule gerezani yaliunganika na maandishi ya mwandishi mahiri wa gazeti la Dumizi, Veronica Baro, yakipewa nguvu nzito na mama yake mzazi, kidogo kidogo Bruno mbegu ya chuki ilianza kujengeka kifuani kwake.
Alianza kumchukia Suto!
Baadae jumapili ileile, mama yake Suto alienda kumwangalia Suto gerezani. Mtu wa kwanza Suto kumuulizia ni Bruno, hata mama Suto ilimshangaza sana taarifa ya kuwa Bruno hakuwahi kufika gerezani kumuangalia Suto. Mama Suto aliahidi, ataenda kumtafuta Bruno.
***********
Baba Bruno alipata taarifa ya kifo cha Killer, kijiweni Sinza. Ilikuwa taarifa ya kushangaza sana masikioni mwa baba Bruno.
Hakuamini .
Hakutegemea.
Taarifa ya Killer kuuwawa na mtoto wa kike ilikuwa taarifa ya kushangaza sana. Haikuingia kichwani kwa mtu yeyote pale Sinza.
Killer hakuwa mtu lelemama kabisa, alikuwa mbabe kweli. Hadi umauti ule mbaya unamkuta, Killer alishauwa watu wengi sana pale Sinza. Ni Polisi gani Sinza ambaye alikuwa hamjui na kumuogopa Killer ?. Killer alikuwa mtemi, alikuwa jasiri, alikuwa mbabe.
Nani atakubali kwa anayemjua Killer umwambie ameuliwa na mtoto wa kike, eti Suto Sutani!
Suto Sutani sasa akaingia katika orodha ya watu hatari sana nchini Tanzania.
Kifo cha killer sasa kilimtia kiwewe baba Bruno. Alianza kumfikiria Suto kwa fikra zingine.
Alianza kumuogopa Suto !
Mtu wa kuweza kupambana na wanaume watatu, tena wauaji na kuweza kuwauwa kinyama vile. Lazima umwangalia katika jicho la tatu.
************
Hatimaye siku ikiyosubiriwa kwa hamu, siku ya kesi ya Suto Sutani ilifika.
Ilikuwa jumatatu tulivu ndani ya Jiji la Dar es salaam. Kama kawaida ya Jiji, kulikuwa na joto kali sana lililotokana na jua kali lichomalo.
Karandinga la Gereza la Segerea, lilikuwa njiani kuelekea Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu. Ndani ya gari hilo, katika kiti cha mwisho kilikaliwa na Suto Sutani. Mwili wa Suto ulikuwa umedhoofika sana, kwa kukosa chakula bora na malezi mazuri huko gerezani.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Waliwasiri viwanja vya Mahakama ya Kisutu saa mbili kamili asubuhi. Mahakama ilikuwa na umati mkubwa wa watu. Umati uliotokana na umaarufu wa kesi ya Suto.
Hatimaye, Suto alishuka katika gari lile kubwa la kijani la Magereza ya Segerea.
Mguu wake ulivyogusa ardhi tu, Suto alivamiwa.
Waandishi wa habari walimvamia huku wakisukumana wao wenyewe. Angalau tu wapate nafasi ya kumpiga picha Suto, Suto muuaji!
Kukosa picha za Suto ilimaanisha kutouza magazeti yao kesho yake asubuhi.
Suto alikuwa maarufu sana.
Alivyoingia Mahakamani, Suto hakumuona mtu yeyote anayemfahamu zaidi ya mama yake mzazi. Hata Bruno mwanaume aliyetokea kumpenda sana hakumwona Mahakamani. Muda wa kupandishwa kizimbani Suto ulifika, huku chozi la uchungu lilimtirika pale Kizimbani. Alisomewa mashtaka yake, na Hakimu alimwambia Suto asijibu chochote. Uchunguzi wa kesi ile ulikuwa bado unaendelea.
Suto alirudishwa kwenye gari, huku akifatwa nyuma na rundo la waandishi wa habari. Suto aliwashangaa waandishi wale. Kwanini walikuwa wanamfata yeye tu.
Miongoni mwa waandishi wale, alikuwepo mwandishi mahiri wa Gazeti la Dumizi, Veronica Baro.
Veronica alimfata dirishani Suto na kumuuliza kwa sauti kubwa.
"Kwanini uliua wewe binti ?"
Suto alimwangalia mwandishi yule kwa jicho kali sana....
Lakini Suto hakumjibu, alikaa kimya. Baada ya kesi za mahabusu wengine, Suto na mahabusu wenzake walirudishwa gerezani, Segerea.
Jumanne asubuhi magazeti yote yaliandika habari kuhusu kesi ya Suto Sutani. Magazeti mengi yaliandika habari hiyo katika kurasa zake za mbele kabisa, zikiambatanishwa na picha za Suto Sutani akiwa anashuka katika karandinga la Segerea.
Veronica Baro wa gazeti la Dumizi nae hakuwa nyuma, kama kawaida yake alipata cha kuandika kuhusu Suto. Kichwa cha habari katika gazeti la Dumizi kilisomeka hivi.
"Suto Sutani ni Muuaji Kiburi na jeuri ! "
Kwa kiasi kikubwa katika habari ile Veronica Baro alikuwa anazungumzia kutojibiwa swali lake na Suto Sutani pale kwenye dirisha la gari la Segerea.
Suto sasa alipachikwa sifa nyingine mpya, sifa ya kiburi na sifa ya jeuri. Huku ile sifa ya uuaji ikiendelea kumng'ang'ania.
*************
Upande wa kina Bruno walisahau kabisa habari kuhusu Suto. Sasa Bruno alizama katika dimbwi la mapenzi na Manka. Aliendelea na Chuo kama kawaida. Huku akiamini suto aliua kweli, na kusubiri kwa hamu kusikia adhabu kali atakayopewa Suto.
Kwa upande wa baba na mama Bruno, maisha yaliendelea vizuri, kwa kuwa adui yao alikuwa jela. Upendo ulirudi kama zamani, huku wakifurahi sana kuwa na mkwe mzuri kama Manka.
*************
Kule gerezani, maisha ya Suto yaliendelea kuwa magumu.
Sababu kuu ikiwa Beji na Zura, Askari hao sasa walikuja na mpango mpya, walikuwa wanataka Suto Sutani abakwe na kuuwawa mlemle gerezani !
Ulikuwa usiku wa giza totoro. Ndani ya Gereza la Segerea, kulikuwa kimya, wafungwa wote wamelala, askari wachache walikuwa doria. Wakizunguka ndani na nje ya Gereza.
Katika lango kuu kulikuwa na askari wawili, Beji na Zura. Walikuwa wameweka sawa mipango yao, ya kumpitisha mtu kwa siri ili akambake Suto, ili akamuue Suto Sutani.
Banda, alikuwa mlevi maarufu katika vilabu vya Tandale. Yeye ndiye alikuwa amepewa kazi maalumu, kazi ya kwenda kumbaka na kumuua Suto, ilipangwa itekelezwe na Banda chini ya usimamizi wa
Beji na Zura, Beji na Zura walikuwa ndio wasimamizi wa jambo hilo.
Kule ndani ya selo, Suto alikuwa amejikunyata katika kona moja ya selo ile.
Suto akiwa amelala usingizi nzito.
Kwa kushirikiana na kina Beji, Banda aliingia kwa siri ndani ya selo ya Suto. Beji alimfungulia mlango wa selo na kumfungia kwa nje ili Banda atekeleze kilichopangwa. Kule kwenye geti kuu alibakia Zura, akiwa makini kulinda usalama.
Sasa ndani ya selo ile, kulikuwa na watu wawili, Suto Sutani akiwa amelala, na Banda Mlevi akiwa anamnyatia Suto....
Banda alikuwa anamsogelea Suto taratibu pale chini.
Tayari kwa kubaka.
Tayari kwa kuuwa.
Banda alimkaribia Suto kabisa. Kwa kutumia mkono wake wa kulia alimziba Suto mdomo na pua kwa nguvu, na mkono wake wa kushoto aliishika sketi aliyoivaa Suto.
Suto alipata mstuko mkubwa sana, mstuko uliomuamsha toka usingizini. Sasa alikuwa anafurukuta kwa kukosa pumzi, bila kutoa sauti yoyote. Banda alikuwa mlevi mahiri, lakini alikuwa na mabaki ya nguvu katika mwili wake.
Alimbana Suto kisawasawa!
Suto alijaribu kuutoa mkono wa banda bila mafanikio. Sasa aliamua kufanya kitu. Na yeye aliamua kumkaba Banda ili ajiokoe katika kisanga kile. Alimshika banda shingoni kwa mikono yote miwili, Ilikuwa patashika ya kimya kimya ndani ya selo, sketi ya Suto Sutani ikiwa imeshuka nusu, hadi magotini.
Mizizi ya chuki moyoni kwa Suto ilikuwa imeshaanza kutamalaki, chuki na ulimwengu, chuki na walimwengu, chuki ambayo ilizidisha hasira zake, chuki ambayo ilimpa nguvu Suto ambazo hakuwa nazo kabla, Suto alipata nguvu za ghafla, kwa kutumia dole gumba lake alianza kulibinya koromea refu la Banda.
Ilikuwa ni picha mbaya sana kuangalia.
Macho ya Banda yalikuwa yametoka nje, mithili ya kijusi kabanwa na mlango.
Suto alimbinya Banda kwa nguvu zake zote zilizobakia.
Kule getini wale maaskari wawili, wenye roho mbaya walikuwa wanasubiri taarifa ya furaha kwao, taarifa ya kifo cha Suto Sutani.
Walikaa robo saa, ilikuwa kimya, Banda alikuwa hajarudi , ndipo Beji alikwenda kule selo, akitegemea Banda itakuwa kashatekeleza kazi waliyomtuma.
Alijidanganya.
Suto sasa alibadirishwa na mazingira , Suto alianza kuwa katili taratibu, mazingira yakiwa ndio mwalimu wa ukatili wa Suto Sutani, na sasa alikuwa amefuzu.
Beji alifungua geti la selo aliyowekwa Suto. Alimulka kwa tochi yake ndogo, iliyotoa mwanga hafifu, alichokikuta ndani ya selo, kilimuacha mdomo wazi.
Alikuta mwili wa Banda ukiwa umelala chini, huku Suto akiwa amesimama wima, jasho linamtoka !
"Umefanya nini Suto?" Beji aliuliza kwa sauti ndogo.
"Nimemuuwa jamaa yenu" Suto alisema bila wasiwasi wowote.
"Suto!" Beji alisema akiwa na uwoga mkubwa sana.
Beji aliingiwa na wasiwasi, maana endapo Banda itakuwa amefia ndani ya gereza, wao walikuwa na chakujibu kuwa ameingia vipi ndani ya gereza, na wao ndio walikuwa zamu usiku ule ?
Alisogea pale ulipo mwili wa Banda na kumwangalia mapigo yake ya moyo.
*************
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Huko nje, maisha yaliwaendea vizuri sana baba Bruno, mama Bruno, Manka na Bruno. Walikuwa wanaishi kwa furaha sana, huku wote wakiwa wamesahau kabisa habari kuhusu Suto.
Baada ya kutoka gerezani siku ile mama Suto alienda kwa kina Bruno, ila alijibiwa majibu ya kejeri, dharau na kebehi, toka kwa Bruno na mama yake. Mama Suto aliondoka kichwa chini. Aliumia sana moyoni, lakini angefanya nini?
Beji aligusa kifuani kwa Banda, alisikia mapigo ya moyo kwa mbali. Ishara kwa Banda alikuwa hajafariki bado. Beji alishusha pumzi ndefu..
Beji alirudi mbio mpaka getini. Akamuekeza Zura kila kitu kilichotokea, kwa kushirikiana na Zura walimtoa Banda kwa usiri mkubwa sana.
Banda hakufanikiwa kubaka wala kuuwa.
Banda alifanikiwa kukabwa na Suto Sutani mpaka kuzimia.
Suto Sutani, alielewa kwamba zile zilikuwa ni njama za Beji na Zura, sasa alikuwa makini zaidi. Alielewa kwamba askari wale walikuwa na nia mbaya sana na yeye.
Upelelezi wa kesi ya mauaji ikiyomkabiri Suto uliendelea. Inspekta wa kike, Jasmine, ndiye alipewa jukumu la kuipeleleza kesi ile.
Inspekta Jasmine alikuwa askari hodari sana katika jeshi la Polisi, jasiri na mtu anayetumia akili nyingi sana katika kuvumbua sababu za vifo vya kutatanisha. Taifa lilikuwa linamtegemea sana,hasa katika kipindi kama hiki ambacho mpelelezi namba moja Tanzania, Daniel Mwaseba, alikuwa mapumzikoni nchini Ujerumani. Baada ya kufanya kazi kubwa sana ya kuwakamata maadui wa nchi yetu waliokuwa na Mpango wa Siri. Inspekta Jasmine sasa aliingia kazini mzima mzima, akidhani hii ni kesi rahisi sana, laiti angejua atakayokutana nayo......
Inspekta Jasmine tangu alipopewa tu jukumu la kupeleleza kesi hii, hakuwa amepiga hatua yoyote.
Alishawahoji mama Suto, Suto na majirani wawili. Alijumuisha maelezo yao na kujikuta yupo palepale.
Pamoja ya kuwa majirani walikuwa hawampendi Suto lakini hawakusita kutaja sifa nzuri za Suto, mbele ya inspekta Jasmine.
Jumatatu ya leo ilimkuta Inspekta Jasmine mlangoni kwa jirani wa tatu wakina Suto.
Alikuwa anaitwa mama Siyawezi.
"Habari mama" inspekta Jasmine alisalimia.
"Nzuri mwanangu" mama Siyawezi alijibu huku akimwangalia Inspekta Jasmine kwa macho ya udadi.
"Mimi ni afisa wa jeshi la Polisi" Inspekta Jasmine alisema huku akionyesha kitambulisho.
"Nimefanya nini tena jamani ?" Mama Siyawezi alisema kwa sauti ya woga.
"Usiwe na wasiwasi mama, kuna vitu vya kawaida tu nataka kukuliza"
"Mwenzenu mimi nikisikia Polisi tu roho inaniruka, nawaogopa sana Polisi"
"Walikufanya nini Polisi hadi uwaogope kiasi hicho ?"
"Wala hawajanifanya kitu, mimi nikiona mavazi yenu tu yale yaani nachanganyikiwa, bora wewe hujayavaa, ningekukimbia hapa" Mama Siyawezi alisema huku akicheka.
"Hahaha tuendelee na kilichonileta mama"
"Sawa, nakusikiliza " Mama Siyawezi alitulia sasa.
"Unaitwa nani mama?"
"Jina nililopewa nyumbani ni Asha Msigeze, ila sahivi wananiita Mama Siyawezi, kwa kuwa nini mtoto wa kike anaitwa Siyawezi, lakini yupo Kisiju kwa bibi yake"
"Sawa mama, ulikuwa unamfahamu Suto?"
"Nisimfahamu Suto mimi, kazaliwa hapa hapa, kakulia hapa hapa, na kaulia hapa hapa!"
"Kamuua nani Suto?"
"Yaani, we askari halafu huna habari, Suto kawaua vijana watatu hapa, mwezi uliopita. Wawili kwa kisu, na mmoja kwa panga. Yule wa panga alikatwa vibaya sana. Ile picha inajirudia Kila mara nikilala, kumbe Suto alikuwa katili sana yule"
"Una hakika Suto aliwauwa wale vijana wale?"
"Nakubali sikusoma, ila picha nazielewa vizuri sana, ukiangalia mazingira tu ya siku ile, unapata jibu....Suto anahusika katika mauaji....au anawajua vizuri sana wauaji !" Mama Siyawezi alipigia msumari wa mwisho katika kaburi la Suto.
"Sawa mama Siyawezi, hivi ni nani aliyekuwa rafiki mkubwa wa Suto?"
"Mama yake" mama Siyawezi alijibu bila kufikiria.
"Hakuwa na rafiki mwengine?"
"Rafiki wa Suto ni mama yake mzazi......aaaaah lakini juzijuzi alipata rafiki mpya wa kiume"
"Ni nani?"
"Kwa jina sijui, lakini ukienda kumuuliza mama Suto atakwambia."
"Nashukuru mama, ahsante kwa ushirikiano wako"
Inspekta Jasmine alitoka nyumbani kwa mama Siyawezi na kuelekea kwa mama Suto. Nia ni kumjua huyo rafiki mpya wa Suto.
Angejua kitakachotokea, ni bora asingetoka ndani ya nyumba ile.
Alivyotoka Inspekta Jasmine, mgeni mpya wa kiume aligonga hodi katika nyumba ya mama Siyawezi, Mama Siyawezi alidhani Inspekta Jasmine amerudi tena. Alifungua mlango kwa haraka, kumbe alikuwa anaharakia kifo. Alipofungua tu mlango, alitazamana na kisu !
Jicho la kwanza la mama Siyawezi alikitazama kisu, tazamo la pili alijiangalia upande wake wa kushoto wa kifua chake. Pale unapokaa moyo. Nusu ya kile kisu kirefu alichokitazama mara ya kwanza kilikuwa kimezamishwa katika upande wake wa kushoto wa kifua na mkono imara wa mwanaume. Mama Siyawezi, alianguka chini huku akijiangalia kifuani. Akishuhudia damu nyingi zikibubujika katika kifua chake, ilikuwa ni kama bomba linalopitisha maji yenye kasi kali limekatika ghafla, ilikuwa ni picha mbaya na ya kutisha sana, mama Siyawezi alikata roho pale chini, bila kuijua sababu sahihi ya kuchomwa kisu kile, alikufa na kisu kifuani.
kwa mwendo wa kasi, mgeni yule wa kiume mwenye roho inayopaswa kuitwa mbaya, alitokemea mtaani.
Kwa kutumia gari yake ndogo, aina ya Rav 4 nyeusi, Inspekta Jasmine alifika nyumbani kwa mama Suto. Alikuwa anagonga hodi katika mlango wa nyumba ya kina Suto Sutani mara ya tatu sasa, lakini hakujibiwa.
Alijaribu kuusukuma ule mlango,
ukafunguka!
Aliingia sebuleni kwa tahadhari kubwa sana, macho ya Inspekta Jasmine yalikutana na majimaji ya ajabu katika kapeti zuri la pale sebuleni, maji maji mekundu, damu!
Damu ile ilikuwa inaelekea au kutokea chumbani. Inspekta Jasmine aliifata, huku akiwa kaishikilia bastola yake mkononi, tayari kwa kukipiga kiumbe chochote kibaya kitakachotokea mbele yake.
Michirizi ya damu ilimfikisha Inspekta Jasmine hadi chumba cha mama Suto,
Alipigwa na butwaa !
Alikuwa anatazamana na mwili usio na roho wa mama Suto! huku ukiwa na jeraha baya sana kifuani, juu kidogo ya ziwa lake la kushoto. Damu nyingi zilikuwa zimetapaa sakafuni. Bila shaka mama Suto aliuwawa sebuleni na kuburuzwa mpaka chumbani. Inspekta Jasmine aliichunguza nyumba yote kwa umakini mkubwa, hakukuwa na mtu yeyote ndani ya nyumba ile, watu wote waliikimbia nyumba ile baada ya tukio la siku ile usiku, tukio lililompeleka Suto Sutani Segerea.
Inspekta Jasmine alipiga simu Polisi, walifika pale kwa gari yao baada ya dakika kumi. Baada ya taratibu za kipolisi mwili wa mama Suto ulipakiwa na kupelekwa hospitali ya Amana. Baada ya Inspekta Jasmine kuchunguza mazingira ya ile nyumba, akihusianisha na tukio lile, hakupata jibu sahihi.
Alitoka nje ya nyumba ile. Alipofika nje, alipigwa na butwaa !http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alikutana na waandishi wa habari wameshafika eneo lile, wakiongozwa na mwandishi wa habari mahiri wa gazeti la Dumizi, Veronica Raymond Baro.
Waandishi wale walimvamia Inspekta Jasmine, kila mmoja na swali lake lake.
Inspekta Jasmine hakujibu swali hata moja, haukuwa muda wa kujibu maswali, ulikuwa ni muda wa kutafuta majibu ya maswali lukuki yanayotokana na visa vya ajabu tena mfululizo vya kesi ile, aliwaangalia tu waandishi wale kwa macho yake madogo. Alipenya kwa nguvu katika kundi lile kubwa la waandishi wa habari, aliingia kwenye gari yake, akaling'oa kwa kasi kubwa sana, akiwa hajui anaelekea wapi ?
Baada ya kuzunguka kwa muda mrefu na gari bila uelekeo maalumu. Sasa alipata mawazo mawili yakiyokinzana. Aende hospitali ulipopelekwa mwili wa mama Suto, au arudi Tabata kwa mama Siyawezi.
Inspekta Jasmine hakujua kwanini nafsi ilimwambia arudi Tabata, kwa mama Siyawezi, nafsi ilishinda aliamua kwenda huko.
Alipaki gari yake vizuri barazani kwenye nyumba ya mama Siyawezi. Akawa anaelekea mlangoni kugonga mlango. Inspekta Jasmine aligonga sana mlango ule, lakini haukufunguliwa. Alijaribu kuusukuma, ilikuwa kama mlango wa mama Suto, nao ulifunguka bila kizuizi chochote, Alichokiona pale chini ya sakafu Inspekta Jasmine kilimstua sana. Aliukuta mwili wa mama Siyawezi umelala katika dimbwi dogo la damu.
Alichoka sana !
Alishusha pumzi ndefu, sasa, Inspekta Jasmine aliona maji yamezidi unga.
Sasa alijua kwamba anapambana na watu wanaozijua nyendo zake zote. Bila shaka walimwona wakati kaja kwa mama Siyawezi, na walijua pia ataenda kwa mama Suto.
Inspekta Jasmini aliwapigia tena askari Polisi. Waliwasiri baada ya muda mchache, waliuchukua mwili wa marehemu mama Siyawezi na kuupeleka hospitali nao, Inspekta Jasmine nae alielekea huko kwa gari yake...
Walifika katika hospitali ya Amana. Mwili wa mama Suto uliingizwa katika chumba maalumu cha kufanyia uchunguzi. Daktari Boniface Mperu ndiye alikuwa na jukumu la kuuchunguza mwili wa mama Suto, na daktari huyohuyo ndiye aliyehusika katika uchunguzi wa maiti ya mama Siyawezi muda mfupi uliopita.
Inspekta Jasmine na askari wengine wawili walikaa nje ya chumba ambacho Dokta Boniface akifanyia uchunguzi wakimsubiri Dokta Boniface amalize, ili wajue watapata nini katika uchunguzi huo kitakachowasaidia katika upelelezi wao.
Katika benchi moja la wagonjwa la pale hospitali ya Amana, lilikaliwa na watu wengi sana, wagonjwa pamoja na waliokuja kuwaona wagonjwa wao. Miongoni mwa watu hao, kulikuwa na kijana mmoja asiyetulia. Akipepesa macho huko na kule, akiwa makini na nyendo za Inspekta Jasmine na wale askari wawili.
Kijana huyu ndiye yuleyule aliyekuwa mgeni wa mama Suto muda mfupi uliopita.
Alimuua kinyama sana kwa kutumia kisu chake kikali, alimuuwa mama Suto kwa sababu akizozijua yeye .
***********
Kule gerezani Suto Sutani, alipewa taarifa za kifo cha mama yake mzazi kwa dharau kubwa sana. Beji na Zura walionesha dharau kubwa sana. Hawakuonesh kujari kabisa kifo cha mama Suto. Hawakujari kabisa hisia za Suto Sutani juu ya msiba wa mama yake mzazi.
"Nyang'au mwenzio kashakufa huko!"
Beji alimwita Mama Suto Nyang'au, bila kujua Suto ana hisia gani juu ya mama yake, Suto anampenda vipi mama yake.
Neno nyang'au lilibadirisha hisia za Suto. Kuuwawa kwa mama yake kulimbadirisha kabisa Suto!
Sasa alihama, alihama rasmi toka kuitwa Suto Sutani hadi kuuitwa Suto muuaji kweli! Kama mwandishi wa habari mahiri wa gazeti la Dumizi, Veronica Baro alivyomwita.
Kifo cha Mama yake kilimtoa Suto kutoka katika hali ya u binadamu, na kumpeleka kwa kasi katika hali ya unyama. Suto sasa hakuwa na cha kupoteza Duniani. Mtu pekee aliyekuwa anamjari na kumthamini hapa duniani alikuwa kauwawa. Suto alikuwa anatamani kufa na yeye, lakini atakufa vipi ilihali watu waliomsababishia matatizo makubwa katika maisha yake walikuwa bado wanaishi?
"Nitawauwa mmoja baada ya mwengine!!!!!!!!"
Suto alitoa kauli hiyo akiwa peke yake, chozi la uchungu likitiririka katika mashavu yake, na kudondoka chini, katika sakafu mbovu ya jela, kwa kauli hiyo Suto Sutani alikuwa anamaanisha. Na alikuwa amepania kuuwa kweki ili kulipa kisasi cha mama yake mzazi !
**************
Baada ya saa moja, Dokta Boniface alitoka katika chumba cha uchunguzi. Akawanyooshea mkono kina Inspekta Jasmine ili wamfate ofisini kwake. Bila kusema neno, askari wale watatu walimfata daktari yule kijana, lakini hawakuwa watatu walioitikia wito ule wa Daktari kama waliyokuwa wanajiona, walikuwa wanne, na yule kijana alinyanyuka taratibu pale kwenye benchi nae alifata kwa nyuma kusikiliza walichoitiwa askari wale...
Wakati wakina Inspekta Jasmine wakiingia ofisini kwa dokta Boniface, yule kijana alikaa katika benchi, nje ya ofisi ya dokta Boniface. Alitega kwa umakini masikio yake yote mawili na kusikiliza maongezi ya kule ndani kwa umakini.
"Eeh dokta Boniface, tupe ripoti ya uchunguzi wako ulioufanya" Inspekta Jasmine alianzisha mazungumzo walipoingia tu ndani.
"Mambo yote nimeandika katika faili, ila la msingi ninalotaka mjue, marehemu hawa wamekufa muda mmoja, wamepishana sekunde chache sana. Alianza yule mwanamke aliyeletwa mara ya kwanza, akafatiwa na huyu mlimleta sasa. Wauaji inaonesha ni wazoefu na makini sana, hawajaacha alama zozote katika miili ya maiti zile, lakini habari zaidi zipo humo katika ripoti zao za uchunguzi"
"Inawezekana muuaji akawa mmoja daktari?"
" Hiyo kazi yenu Afande, kupeleleza kwa umakini chanzo cha vifo vyao, na kuwajua wauaji halisi. Sisi kwa vipimo vyetu hatujaligundua hilo, mengine mengi yameelezwa kwenye hizo ripoti za uchunguzi wa vifo vyao." Dokta Boniface alisema huku akiionesha kwa kidole ile ripoti aliyoishika Inspekta Jasmine.
"Sawa, tunashukuru sana dokta"
"Karibuni sana Afande"
Walipeana mikono.
Inspekta Jasmine na wale askari wawili walitoka nje ya ofisi ya Dokta Boniface, wakimpita pale yule kijana bila hata ya kumwangalia usoni. Hawakuwa na tahadhari yoyote. Walitembea katika ile korido ndefu na kutoka nje ya hospitali, hawakujua kabisa kama kuna kijana anayewafata, nia ya kijana yule ni kuzipata zile ripoti kwa njia yoyote ile. Ripoti zilizokuwa katika bahasha mbili kubwa, mikononi mwa Inspekta Jasmine.
Waliingia ndani ya gari ya Inspekta Jasmine na kuondoka. Yule kijana alichukua pikipiki na kuanza kuwafata kwa nyuma. Wakiwa ndani ya gari walikuwa hawana hili wala lile. Walikuwa hawajui kabisa kama wanafatwa.
Inspekta Jasmine hakuzipa uzito uliostahili ripoti zile ripoti za uchunguzi toka kwa Dokta Boniface, wao walikuwa wameridhika na maneno ya dokta Boniface. Lakini kwa upande wa yule kijana, pamoja na kusikia baadhi ya maneno ya Dokta Boniface, lakini nia ya kuzipata ripoti zile ilikuwa palepale, alijua dokta Boniface alikuwa anaficha baadhi ya vitu, ndio maana aliwasisitizia sana wale askari wakazisome zile ripoti za uchunguzi.
Kule hospitali, ndugu wa mama Siyawezi waliruhusiwa kuichukua mwili wa ndugu yao, tayari kwa maandalizi ya kwenda kuzika.
Hakukuwa na zuio lolote la kuzuia miili ile, maana kama uchunguzi ulikuwa umishafanyika.
Mwili ule muhimu sana kwa mustkabali wa kesi hii ulichukuliwa.
Huku mwili wa mama Suto ukichukuliwa na wasamaria wema, waliojitolea kwenda kuuhifadhi katika makazi yake ya milele. Mazishi ya mama Suto yalienda kufanyika, bila uwepo wa mtoto wake kipenzi Suto Sutani....
Inspekta Jasmine na wale askari wawili walikuwa wanaelekea kituo cha Polisi cha kati. Hawakujihangaisha kabisa kufungua zile ripoti za uchunguzi.
Walipofika kwenye mataa walisimama ili kusubiri taa ziruhusu gari yao kuendelea na safari.
Inspekta Jasmine alikuwa ametulia kwenye usukani, akiwa ameshusha kioo mpaka chini, ili kupambana na joto la Jiji la Dar es salaam. Askari mmoja alikaa pembeni yake, na yule askari mwengine alikuwa amekaa nyuma ya Inspekta Jasmine. Ile bahasha yenye ripoti za uchunguzi za vifo za mama Suto na mama Siyawezi, zikiwa katikati ya mapaja ya Inspekta Jasmine. Askari wote kwenye gari walikuwa kimya. Kila mmoja akitafakari lake.
Ghafla mkono mwembamba ulipenya katika dirisha la dereva, na kutua katika mapaja ya Inspekta Jasmine, na kuitwaa ile bahasha yenye ripoti muhimu sana. Mkono ule ulirudishwa kwa haraka sana ukiwa na bahasha. Kilikuwa kitendo cha haraka sana, mithili ya kufumba macho na kufumbua.
Yule kijana mwenye pikipiki alifanikiwa kuichukua ile bahasha muhimu sana mbele ya askari watatu na kuondoka nayo.
Askari wote walibaki wameduwaa. Kwanza hawakuelewa kilichotokea, na baada ya kuelewa hawakuamini kabisa kilichotokea. Walikuwa wanaangaliana tu wakati pikipiki ile ikipenya katikati ya magari na kutokomea kusikojulikana.
Askari wale walihemewa, sasa wakawa wanatafuta jinsi ya kugeuza gari ili wakaangalie uwezekano wa kupata ripoti nyingine za uchunguzi kwa Dokta Boniface.
************
Kule gerezani, Suto Sutani alikuwa na mambo mengi kichwani, sasa alikomaa, alikomazwa na maswahibu na madhila makubwa yaliyomkuta.
Suto sasa alibadirika !
Akawa kiburi, haogopi, hajari, na mtukutu hasa. Matatizo yaliibadiri tabia nzuri ya Suto Sasa akatawaliwa na wazo moja tu kichwani mwake, kutoroka gerezani na kwenda nje kulipa kisasi !
***********
Inspekta Jasmine na askari wenzake walifika katika hospitali ya Amana, na moja kwa moja walienda kwenye ofisi ya Dokta Boniface, Dokta hakuwepo. Walikaa nje kwenye benchi kumsubiri. Benchi lilelile alilokaa yule kijana aliyewapora bahasha yenye ripoti muhimu za uchunguzi.
Baada ya robo saa, Dokta Boniface alirejea. Alishangaa kukutana tena na wale askari pale. Kabla ya salamu, Inspekta Jasmine alisema;
"Dr we lost a report!"
"Whaaat?"
"Ndio hivyo dokta, kuna dereva bodaboda mmoja katupora aisee, sijui alidhani kuna hela mle"
"Kaichukua, yule kijana itakuwa kaichukua "
" Mbona sikuelewi Dokta"
Dokta Boniface alitulia, akameza funda kubwa la mate, kisha aliwakaribisha ofisini na kuanza kuwaelezea habari nzito kuhusu yule kijana mwendesha pikipiki....
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Dr Boniface aliongea maneno yaliyowaacha hoi kina Inspekta Jasmine na wale askari wengine.
"Leo asubuhi, ilivyokuja ile maiti ya kwanza kabla sijaifanyia uchunguzi kuna kijana alikuja ofisini kwangu. Alidai yeye ni ndugu wa marehemu mama Suto na alitaka nimpe ripoti ya uchunguzi ya kifo cha mama Suto kwa siri. Aliniahidi pesa nyingi sana.
Alisema anataka kumshughulikia mtu aliyemuua dada yake. Nilimkatilia katakata, nilimwambia huo sio utaratibu wetu hapa hospitali. Aliondoka kwa ghadhabu, huku akiniahidi atahakikisha anaipata ripoti ya uchunguzi kwa njia yoyote ile . Mimi nilimpuuza lakini
tangu muda ule nilikuwa makini sana kwa kila hatua niliyokuwa ninapitia, nikijiahidi kutunza ripoti kwa hali yoyote ile.
" kwani ripoti ilikuwa ina lipi la maana Dokta, si yaleyale uliyotueleza?"
"Hapana Inspekta!" Dokta Boniface alisema kwa sauti kubwa huku akigonga meza kwa kiganja chake.
"Kuna nini sasa?"
"Alama ya macho ya muuaji!"
"Unasema?"
"Ndio, pamoja na muuaji kuvaa gloves mikononi, lakini alijisahau, taswira yake ilionekana dhahiri katika macho ya marehemu mama Suto. Na na na marehemu wote wawili ilitokea taswira moja!"
"Sasa kwanini hukutuambia kabla maneno hayo, ili tuwe makini kuilinda ile ripoti, na hayo yaliwezekana vipi kwa muda mfupi kama ule ?"http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Ilikuwa kwa ajiri kwa usalama Inspekta, niliamua kutosema pale, ili kama kuna mtu anatusikiliza kwa siri aidharau ripoti ile, kuhusu muda mfupi aliotumia muuaji, hata mimi inanishangaza Afande "
"Sasa tushaipoteza ripoti muhimu za uchunguzi, zenye macho ya muuaji, tunaomba ukafanye tena uchunguzi, nitalipia mimi gharama zote."
"Mmechelewa Inspekta, ndugu wa marehemu washachukua maiti zao"
"Afanalekiii !"
Miguu ya Inspekta Jasmine iliishiwa nguvu, akawa anadondoka chini taratibu, wale askari wawili wakamdaka na kumketisha kitini.
Kama maji yalikuwa yamepita shingoni, sasa yalikuwa yanamzamisha kabisa Inspekta Jasmine, hakutegemea kabisa kama atapata vikwazo katika kesi hii. Kesi aliyoiona nyepesi sana, sasa ilimkalia shingoni.
*************
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment