Simulizi : Kilio Cha Nafsi
Sehemu Ya Pili (2)
Mazungumzo hayo yakawa kama chachu kwa Samweli kuanzia siku hiyo akawa mtu mwingine kabisa alianza kujifunza kwa bidii sana hakuwa na muda wa kucheza kama vijana wenzake japo alikuwa mpenzi wa mpira wa miguu lakini alilazimika kuacha kabisa kufatiria vitu hivyo. Mwisho wa mwaka alijikuta akifanya vyema hivyo akawa amefankiwa kuingia kidato cha chatu.
“Sasa umezidi kunifurahisha sana Samweli kwa haya matokea yako mazuri lazima ufanikishe kile ulichokuwa umekidhamiria toka mwanzo.”
“Baba nitazidi kukufurahisha na hata kujifurahisha mimi mwenyewe ili tu niweze kuwa kama wenzangu.”
“Safi sana na kidato cha tano nitakupeleka Tanganyika Intanetional school nadhani utaipenda sana.”
“Ahsante baba.”
Yalikuwa ni mazungumzo kati ya Samweli na baba yake mara baada ya matokea yake ya kidato cha nne kutoka akiwa amefanya vizuri. Matoke hayo pia yalipelekea ndugu zake wakubwa kumpongeza sana na kuahidi kumsaidia kwa lolote ile mbegu ya upendo iliyokuwa imepandwa toka wakiwa wadogo ilizidi kuwaunganisha watoto hao. Kila mwanafamilia alifurahishwa na ushindi mzuri wa samweli tabasamu na vicheko ndivyo vilivyotawala ndani ya nyumba hiyo kila siku kwao ilikuwa ni sherehe.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Miezi kadhaa ilikakatika hatimaye Samweli akawa amejiunga na kidato cha tano katika shule ya kimataifa ya Tanganyika iliyopo jijini Dar es salaam shule iliyokuwa ikifahamika sana kwa utoaji mzuri wa elimu kuanzia chekechea hadi kidato cha sita. Ilikuwa ni furaha isiyofichika moyoni mwa kijana huyo aliyekuwa mwembamba kiasi maji ya kunde na mrefu. Uwepo wa shuleni hapo ulionesha dhahiri adhima yake ya kuwa Daktari ilikuwa ikianza kusogea kadiri siku zilivyokuwa zikizidi kusonga mbele.
“Mambo kaka?”
“Poa vipi wewe?”
“Salama naitwa Rose je naweza kukufahamu japo kwa jina kama hutojari.” Alizungumza msichan a huyo mwenye asili ya kihindi ile ongea yake tu ilipelekea uzuri wake wa asili uliokuwa haufichi kuonekana wazi.
“Naitwa Samweli.”
“Oooh! Samweli mtu mashushuri ndani ya Bibilia nafurahi kukufahamu,” Rose aliongea huku akinyosha mkono wake wa kulia kuelekea kwa Samweli aliyekuwa amesimama na kujiegemeza ukutani lakini hakuupokea akabaki akimtazama msichana huyo na kumuuliza swali.
“ Umemjuaje Samweli Rose?”
Baadala ya kuupokea mkono huo alijikuta akimuuliza swali msichana huyo aliyekuwa gumzo kwa uzuri wake shuleni hapo mara baada ya kujiunga na kidato cha tano miezi michache nyuma.
“Mimi mkristo wa kanisa katoriki hivyo naifahamu sana Bibili wala usiahangae.”
“Ooooh! Na ninyi? Mimi hudhani wahindi hamuwezi kuwa wakristo,” Samweli alisema huku akitoa tabsamu la kwanza toka ajiunge na shule hiyo siku mbili nyuma.
“Hahahahaha! Wapo mimi nimezaliwa ndani ya hiyo dini na je unachukua mchepuo upi?”
“PCB nataka kuja kuwa Daktri hapo kwa baadae wewe je?” Samweli alimuuliza Rose huku akimtazama kwa macho ya wiziwizi kuanzia juu hadi chini.
“Nami kama wewe na tupo darasa moja kwani hujawahi kuniona?”
“Hapana.”
“Tatizo uk….”
Rose hakuweza kumaliza sentensi yake mara baada ya kengere ya kuelekea darasani kugongwa wote waliondoka eneo hilo bila kusemeshana lolote zaidi ya Rose kumtazama sana Samweli aliyekuwa akitembea kwa mwendo wa haraka haraka kana kwamba alikwa amechelewa sana. Muda wa mapumziko Rose alijitahidi kumtafuta Samweli ili tu aweze kuzungumza naye hakufahamu kwanini moyo wake ulitaka kuzungumza na mvulana huyo . Mazungumzo hayo yalizalisha wawili hao kuwa marafiki walioshibana kila aliokoonekana Rose na Samweli nyuma walishi kama mapacha na kusaidizana kwa kila kitu hadi wanahitimi kidato cha sita walikuwa marafiki walioshibana sana.
“Samweli natamani urafiki wetu ungeendelea zaidi.”
“Kwani unataka kuuvunja?” Samweli alimuuliza huku akikaa juu ya kiti kidogo siku chache mara baada ya matokeo yao ya kidato cha sita kutoka na siku hiyo walikutana shuleni hapo kwa lengo la kupokea vyeti vyao.
“Simanishi hivyo Samweli.”
“Ila?”
“Toka tumalize shule huonekani kabisa na…nana..nanaa..”
“Naa…na… nani? Niambie kabla ya kungia ndani ya ofisi naona mkuu ametokea.”
“Natamani siku moja tungeishi sote.”
Rose alijikuta akizungumza kitu kilichokuwa kikimuumiza kwa muda mrefu toka macho yake yamuone Samweli kitu mapenzi ndani ya moyo wake kilizaliwa alishindwa kufikisha hisia zake kwa kijana huyo aliyeonekana makini sana katika masomo hakuwa kama vijana wengine aliowahi kuwaona. Japo alikuwa akitumia njia mbalimbali zikiwemo za kumpatia zawadi ndogo zenye kufikisha ujumbe huo lakini Samweli alikuwa mgumu sana kumuelewa.
“Tuishi wote kiaje?” Alimuuliza huku akimtazama machoni. Macho yenye kuonesha mabadiriko mara baada ya kusikia neno hilo. Ule mkazo wa macho ya Samweli ulipelekea Rose kukosa ujasiri wa kuzungumza zaidi alibaki kuzitafuna kucha zake za mkono wake wa kushoto na kuziondoa kabisa
“Naukuliza Rose.”
“Haa…pana hakuna kitu ila tambua kuna mtu anakupenda sana,” Rose aliongea huku akiondoka eneo hilo na kumuacha Samweli akiwa haelewi chochote. Alitembea taratibu huku akili yake yote ikimfikiria Samweli hakuweza kumuelewa kuwa alikuwa mwanaume wa aina gani, vitu vingi alikuwa amemfanyia lakini ahakuonesha mabadiliko yeyeote kwa Rose.
“Labda ana msichana mwingine?” Akajiuliza peke yake huku akizidi kutembea polepole kuelekea ndani ya ofisi ya mkuu wa shule hiyo.Mara baada ya kufanya utaratibu wote alikabidhiwa cheti chake na kutoka akiwa na mawazo sana hakutaka tena kuzungumza na Samweli aliona kufanya hivyo ilikuwa ni moja ya njia ya yeye kujiumiza sana, moyo wake ulikuwa ukiumizwa sana na Samweli kila alipomuona.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Matokeo mazuri ya Samweli yaliifanya familia yake kuzidi kufurahi zaidi toka kijana wao aanze maisha yake ya elimu hakuna hata siku moja aliyowahi kuwaangusha juhudi zake binafsi zilikuwa moja ya njia ya mafanikio kwake.Haikuwa familia yake tu bali hata Daktari wake aliyekuwa akimtibu naye alifurahi sana na ili kuonesha furaha hiyo alifanya mpango wa Samweli kwanda kusomea shahada ya kwanza ya udaktari nchini Marekani.Ilikuwa ni taarifa njema sana masikioni mwa kijana huyo siku aliyomuita ofisini kwake na kuzungumza naye, hakuamini kama mtu huyo angejitolea kumfanyia kitu hicho japo hakuwa akitoa pesa za yeye kwenda kusoma huko lakini kitendo cha yeye kumtafutia nafasi ya kwenda kusomea huko ilikuwa ni moja ya upendo wa dhati kwa Samweli.
“Acha niongee na Rose kwanza nadhani atafurahi sana kusikia taarifa hii.”
Hapo hapo alichukua simu yake iliyokuwa juu ya kitanda na kutafuta jina la Rose aliweka simu sikioni mara baada ya kupiga.
“Hallo Samweli habari za Bunju.”
“Safi kwema huko?”
“Huku poa vipi ulikubali ombi langu?”
“Aaaah! Hilo potezea sema nini nina habari njema sana.”
“Ipi hiyo unaleta barua ya posa nyumbani?”
“Unapenda kuolewa wewe subili,”akanyamaza kimya huku simu ikiwa bado sikioni, mapigo ya moyo yakaongezeka ghafla akajikuta akipoteza ujasili aliokuwa nao mwanzo, mwili wote ukaanza kutetemeka akishindwa kumueleza kile alichokuwa amekidhamiria.
Alishindwa kuzungumza kile alichokuwa amekidhamiria ujasili wote aliokuwa nao uliyeyuka mithili ya mshumaa, akabaki kimya kama dakika mbili kisha akakohoa kikohozi kikavu na kutazama pembeni kana kwama alikuwa akitafuta kitu.
“Wewe vipi?”upande wa pili ukamshtua, kiasi kashtuka na kujiweka sawa.
“Namwambia namwambia,”akateta na moyo wake kisha akazungumza.
“Utafurahi ama utachukia au utalia?”
“Kwani nini Samweli,”Rose akauliza huku akihisi mapigo ya moyo yakikosa uvumilivu wa kile kilichokuwa kikienda kuzungumzwa.
“Unaharaka wewe!”
“Eeeh…Ujue nitapenda siku ukileta barua kwetu sijui nitakupa nini wewe!”
“Tatizo lako unawaza mapenzi tu mimi nakwenda kusomea nje ya nchi Bongo sisomi tena.”Akamwambia huku akicheka cheka.
“Nini? Ina maana… unania…” Rose alishindwa kuzungumza vizuri alichofanya ni kukata simu kisha alikimbilia chumbani kwakwe chumba kilichokuwa na kila kitu alipitiliza moja kwa moja bafuni ndani ya dakika saba alikuwa ameshamaliza kuvaa na kutoka akikimbia, kwa kuwa nyumbani alikuwa yeye na mfanyakazi wa ndani nafasi ya kuondoka ilikuwa wazi.
“ Sitaki kutumia gari nitachelewa hapa nachukua pikipiki,” aliwaza ndani ya ubongo wake huku akitoka ndani ya nyumba yao alinyosha moja kwa moja hadi kituo cha waendesha pikipiki alimarufu kama bodaboda.
“Dada tunaenda?”
Mmoja wa vijana hao alisema mara baada ya kumuona Rose akitembea kwa mwendo wa haraka sana.
“Nipeleke Bunju.” Alisema huku akikaa juu ya pikipiki hiyo.
“Ushafika Dada,” akamjibu huku akiwasha pikipiki hiyo na kuondoka eneo hilo akitimua vumbi jingi sana.
Njia nzima Rose alikuwa kimya akili yake ilikuwa ikimfikiria Samweli hakujua ni kwa nini kijana huyo alikuwa hamuelewi kile alichokuwa akikiongea , mapenzi yake ya dhati kwake yalikuwa shubiri hadi wanasimama mbele ya geti Rose alikuwa ndani ya mawazo.Akiwaza na kuwazua bila kupata jibu sahihi la kile alichokuwa akikiwaza alitamani kumuona siku moja Samweli akiwa mume wake.
“Kwanini unanifanyia hivi Samweli?” Aliongea mara baada ya kukaribishwa ndani hata kabla ya kukaa mikono yake akiwa amekishika kiuno chake huku uso wake ukionesha hali ya kutofurahishwa kabisa na maneno ya Samweli.
“Karibu ukae mrembo mbona unakuwa mkali kama mbogo?”Akazungumza huku akinyanyuka kitini hapo na kutembea hadi eneo alilokuwa amesimama Rose, akamshika mkono na kumuongoza hadi kwenye kochi na kumkalisha kisha akasimama karibu yake mguu mmoja ukiwa umekanyanga mkono wa koshi hilo na kuugemeza mguu wake, macho yake makubwa kiasi yakawa yanamtazama Rose aliyekuwa ameiinamisha shingo yake huku kope zake zikilowana na machozi.
“Kwa…kwa…nini unanifanyia hivi S…”
“Huna sababu ya kulia mrembo mbona kila kitu kitaenda sawa?” Akamwambia akimuinua kichwa chake.
“Nina haki ya kufanya haya kwanini inakuwa hivi Samweli”
“Kwani kunanini chaurembo Rose?” Samweli aliuliza akiwa hana wasiwasi kabisa hata alijikuta akishangazwa na maneno ya Rose achilia mbali ujio wake asubuhi hiyo.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Si nishakueleza nakupenda sana Samweli kwanini hutaki kunielewa.”
“Ni kweli unanipenda tena kwa dhati ila naomba hayo yaendelea mara baada ya sisi kumaliza safari yetu ya masomo huko tunakokwenda ndiko kugumu zaidi siko tayari kufanya kile unachokitaka.” Aliongea kwa kujiamini bila kujali kama maneno hayo yalikuwa mwiba mkali ndani ya moyo wa msichana huyo aliyekuwa akimpenda kwa dhati toka siku ya kwanza kumuona.
“Kwahiyo Samweli hunitaki?” Alimuuliza huku kope zake zikiendelea kulowana kwa machozi, hakuamini kama kweli Samwel alikuwa hamtaki kila alipojiangalia hakuwa na kasoro yeyote kama sura alikuwa nayo tena iliyokuwa ikiwasumbua wanaumwe wengi, kama umbo alikuwa nalo tena la kuvutia kipi kilipelekea Samweli kutompenda ama yeye kuwa na asili ya kihindi! Na kama mapenzi alikuwa nayo tena ya dhati kwa asilimia kubwa sana alijiaminisha mwenyewe kuwa hakuwahi kumpenda mwanaume mwingine kama alivyokuwa akimpenda Samweli.
“Samweli utanifanya ninywe sumu siku moja sitoweza kuvumilia nikikuona ukiwa na mwanamke mwenzagu ili hali mimi nakupenda sana nakupenda kwa muda mrefu na nimejitolea maisha yangu kuwa na wewe kwanini hunitaki?”
“Mmmmmh! Unakotaka kufika siko kabisa kufa kwa ajili ya mwanaume?”
“Ndio!Bora nikaondoka duniani lakini si kuendelea kuteseka namna hii, huyajui mapenzi Samweli hukujui kupenda kwani wote wanaojiua ama kuua wanapenda?Ni mapenzi ya dhati wanajiona hawana thamani yeyote hapa duniani, wanajiona wenye mikosi sana leo unaniliza nawe ipo siku utalizwa na utayaamini maneno yangu waninyoshea kwa kidole kimoja lakini tambua vinne vyakutazama Sameli…samweliii,”Rose akashindwa kuendelea kuzungumza na kuanza kulia hali iliyompa wakati mgumu sana Samweli kuhakikiasha anamnyamzisha.
“Usiseme hivyo Rose. Tambua wewe ni msichana tena msichana mmoja mzuri sana, msichana anajitambua na kujithamini msichana mmoja mrembo mno na ni zaidi ya neno lenyewe ila ninachokuomba usikimbilie mapenzi kwa wakati huu yatakuharibia kila kitu,” alisema huku akimfuta machozi ili kumuweka sawa pia alifanya hivyo ili kuzuia mambo mengine kutokea. Wosia wa wazazi wake aliokuwa akipatiwa kila siku hakutaka kuupuuzia kwani hata yeye mwenyewe alikuwa akiona jinsi vijana walivyokuwa wakiharibikiwa mipango yao ya mbele mara baada ya kujiingiza katika mapenzi kabla ya umri sawa.
“Basi naondoka ila usiste kunijuza ni chuo kipi utaenda kusomea sawa.” Akamwambia huku akinyanyuka na kuanza kutembea bila kumtazama Samweli.
“Kwanini haraka hivyo?”
“Yanibidi kufanya hivyo,” akamjibu akigeuza shingo yake na kuizuia miguu yake macho yake yakiwa yakikitazama kifua cha kijana huyo, dakika mbili za yeye kusimama eneo hilo alirudi kwa haraka na kwa kushtukiza na kumkumbatia Samweli kwa nguvu akiendelea kulia kwa kwikwi.
Samwel hakuamini kitendo cha msichana huyo moyoni hakuwa na mapenzi kabisa alichokuwa akikiwaza yeye kwa wakati huo ni kwenda kusoma basi habari ya mapenzi kwake kilikuwa kitu kingine kabisa ikabidi atumia akili ya kuzaliwa ya kumkubalia ombi lake ili aweze kuondoka kifuani kwake.
“Kweli unanipenda?”
“Ndio!Ila mpaka tutakapo maliza masomo yetu.”
“Ndio utaishi na mimi?”Akamuuliza akiwa hayaamini maneno ya kijana huyo aliona kama ni ndoto hakuamini kama siku moja angekuja kuyasikia maneno mazuri tena yenye kuufurahisha moyo wake kutoka kwa mtu aliyekuwa akimpenda kupita maelezo.
“Usiste kunijuza sawa bebi wa mimi!”
“Wewe tena lazima ufahamu.”
Walisimama na kutoka ndani ya nyumba hiyo huku wakizungumza kwa furaha na hata vicheko vilitokea.Rose akiwa ameridhishwa na maneno ya Samweli na kuyaamini kwa asilimia kubwa sana.
****
University of Califonia Los Angeles ni moja ya chuo kikuu na vikongwe sana nchini Marekani. Chuo hiki kinapatikana ndani ya jimbo la Califonia ni chuo kinachosifika sana nchini humo kwa utoaji mzuri wa elimu.Chuo hiki ni bora sana katika Nyanja nyingi zikiwemo isimu, udaktari biashara na fani zingine. Chuo hiki ndicho Samweli alikuwa amechanguliwa kujiunga kwa shahada yake ya kwanza ya udaktari, hakuamini kama alikuwa akienda Marekani kwa mara ya kwanza kwenda kujiunga na chuo hicho ambacho kilikuwa cha gharama sana, si kwa ada tu lahasha! Hata maisha ya chuoni hapa yalikuwa ya gharama sana. Ile juhudi yake katika masomo toka akiwa mtoto mdogo hadi alipohitimu kidato cha sita na kufanikiwa kufauru daraja la kwanza ilipelekea wazazi wake kumsomesha huko bila kujari gharama hizo.
“Mimi si nilikueleza lazima uje uwe zaidi yangu nataka kukuona ukiisaidia Tanzania siku moja, nataka kukuona ukiokoa maisha ya watu wanaofariki kila siku kwa matatizo ya moyo.”
“Ni kweli Dokta nitahakikisha nafanya hivyo na ninakuahidi siku moja watanzania hawatakwenda tena India kutibiwa mimi nitakuwa mkombozi wa matatizo yao ya moyo.”
“Safi sana ila nakusistizia ujihadhali na mapenzi sawa?”
“Hilo ondoa hofu.”
“Nakutakia maisha mema na ya mafanikio huko uendako ukifika usiache kunijuza.”
“Ondoa hofu kila kitu kitakuwa salama kama tulivyopanga.”
Walishikana mikono kwa ukakamavu huku wote wakisimama ishara ya kuagana kisha Samweli aliondoka ofisini kwa Dk. Godfrey Gerevas ambaye alikuwa rafiki yake mkubwa na huyu huyo ndiye aliyefanya mpango wa yeye kwenda kusomea Marekani.
***
Siku kumi na nne mbele Samweli aliondoka Tanzania akiwa na furaha sana alitamani kufika mapema sana chuoni hapo ili aanze kuchukua masomo aliyokuwa akiyapenda toka akiwa mtoto mdogo.
“Kweheri Tanzania kwaheri nchi yangu, nitarudi kwa ukombozi wa watu wako Mungu nitangulie,” aliongea ndani ya moyo wake mara baada ya ndege kutoka shirika la duniani Emirates kuiacha aridhi ya Tanzania akiwa amekaa juu ya kiti macho yake akiwa ameyafumba akizungumza na moyo wake.
Ilikuwa ni safari yenye furaha sana ndani ya moyo wa Samweli kila alipojitazama hakuamini kama kweli alikuwa akienda nchini Marekani kwa ajili ya masomo tena masomo aliyokuwa akiyapenda toka utoto wake ile ndoto yake ya miaka mingi sasa ilitimia.
“Nahakikisha kujifunza sana na zaidi ili nije kuiokoa nchi yangu na matatizo ya ugonjwa wa moyo ambao ni tishio sana kwa watanzania wenzangu,” aliendelea kuwaza akiwa ndani ya ndege moyo wake ukijawa furaha ya hali ya juu picha ya yeye akiwa daktari mkubwa nchini kwake alianza kujengeka ndani ya kichwa chake hali iliyopelekea kuaanza kutabasamu peke yake. Katika waza waza hiyo alijikuta akipitiwa na usingizi mzito uliomchukua masaa mengi sana, alikuja kushtuka ndege ikihangaika kutua ndani ya kiwanja cha nchi hiyo.
Mara baada ya kukamilisha taratibu zote ndani ya uwanja huo alitoka nje huko alichukua tax iliyompeleka moja kwa moja ndani ya kituo cha mabasi yaliyokuwa yakifanya kazi za kuelekea chuoni hapo umbali wa kilomita kadhaa aliingia ndani ya basi hilo na kuketi siti ya nyuma kabisa na kutulia huku macho yake akiyaruhusu kulitazama jiji hilo ambalo ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kufika huko, hadi basi hilo linasimama eneo maalumu alikuwa akishangaa shangaa madhari ya mji huo mara baada ya kufika stendi hapo akashuka na kuchukua mizigo yake kisha akaelekea chuoni mita chache kutoka eneo liliposimama basi hilo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Chuo hicho kilichokuwa kikubwa sana na chenye idadi kubwa ya wanafunzi kutoka nchi mbalimbali duniani.Siku ya pili yake Samweli alianza kuingia darasani mara baada ya kukamilisha taratibu zote zilizokuwa zinahitajika chuoni hapo hivyo akayaanza maisha ya chuoni hapo akiwa na shauku la kujifunza kile kilichokuwa kimempeleka huko.
Mwezi mmoja wa yeye kuwa chuoni hapo alipokea barua kutoka kwa Rose akimsistizia kusoma kwa bidii kwani naye alikuwa mmoja wa wanafunzi waliokuwa wakitazamiwa kujiunga na chuo hicho siku chache zijazo. Siku hiyo alishinda vibaya sana hakupenda msichana huyo awe eneo hilo alijua vyovyote lazima mambo yangeharibika kwa asilimi kubwa kama hakuwa makini na mwanamke huyo ambae alimuona kama nuksi kwake.
“Mbona huyu msichana ananisumbua sana?”alijiuliza mara baada ya kumaliza kuisoma barua hiyo huku akiwa anayatazama maadishi yaliyokuwa yameandikwa katika karatasi nyeupe na chini yake kulichorwa moyo uliokuwa na mkuki katikati.
“Moyo wangu haupo tayari kuwa na Rose na nahisi kutompenda japo ni msichana mzuri kupita maelezo.”aliendelea kuwaza kisha alisimama na kuedelekea na safari yake ya darasani kwa ajili ya kujisomea. Toka aanze safari yake ya masomo hakuna siku moja masomo yalikataa kuingia kama siku hiyo taswila ya Rose ilizidi kuisumbua akili yake aliuona usumbufu wa masichana huyo na hata alijiona jinsi atakavyopeteza muda kwa ajili ya msichana huyo.
“Mbona kinanisumbua sana?Na kikija nitakikomesha nakikaushia mpaka kikome,” akazungumza akiiuma kalamu yake kwa uchungu wa hali ya juu hakuweza tena kuendelea kusoma hivyo alitoka na kelekea chumbani kwake kwa lengo la kujipumzisha lakini nako hakuweza kulala ikabidi atoke na kuelekea uwanjani kwa mara ya kwanza toka afike chuoni hapo kitendo kilichowashangaza wanafunzi wenzake mara baada ya wao kumuona akiwa eneo hilo.
Kweli baada ya mwezi kupita Rose naye alifanikiwa kujiunga na chuo hicho kitu kilichomchukiza sana Samweli, uwepo wa Rose chuoni hapo ungepelekea yeye kutofanya vizuri katika masomo yake kwani aliamini mapenzi ni moja ya sumu kali katika masomo yake. Kama alivyojisema ndivyo ilivyokuwa Samwel hakupenda kuambatana na Rose hata siku moja, alijitahidi kumkwepa na kujificha sehemu alizokuwa akizifahamu hali iliyokuwa ikimuumiza sana msichana huyo.
“Samwel kwanini hutaki kunielewa?” Rose alimuuliza Samwel siku moja mara baada ya wanafunzi wote kutoka mazoezi majira ya asubuhi.
“Kukuelewa kiaje?”
“Toka nikiwa kidato cha tano nimekuwa nikikupenda lakini wewe hutaki kunielewa kwanini?Kosa langu ni nini? Ama hunipendi?”
“Mmmmmh!” Alishusha pumzi ndefu kisha aliikunja vyema tsheti yake ya mazoezi iliyokuwa ya mikono mirefu na kumtazama Rose.
“Sikiliza Rose mapenzi ni makubaliano kati ya watu wawili ama mioyo ya watu wawili inapoamu kufanya kitu fulani, ua…”
“Samweli nimechoka kusikia ngojera zako na mashairi yako wewe ni mwanaume wa aina gani nikufanyie nini ili uelewe kuwa nakupenda? Nikupe nini ili uniamini tazama nimeamua kuja huku si kwa ajili ya masomo pekee ila ni kwa ajili yako siwezi nikaishi mbali na wewe hata siku moja kwanini lakini hutaki kuniamini?” Rose alizungumza huku akikaa chini bila kujali hali ya unyevunyevu iliyokuwepo eneo hilo, kila alipomfikiria Samwel hakuweza kumuelewa ni mwanaume wa namna gani,muda mwingine alimfikiria Samwel labda alikuwa na msichana mwingine lakini kila alipolifikiria hilo hakuliamini kabisa kwani toka amfahamu hakuwahi kumuona na msichana yeyote zaidi yake.
“Hutakiwi kuongea maneno mengi kiasi hicho?Kwanini huna subila?”
“Subila! Subila? Ya namna gani ni miaka mingapi nimekusubiri kama hunipendi niambie lakini si kunifanyia hivyo au kwa sababu mimi Mhindi?”akasema huku akibubujikwa na machozi mithili ya chemchemi.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Samweli akapatwa na wakati mgumu mno, akili ikazidi kuchanganyikiwa kila kilichokuwa kikitoke kwa wakati huo alikiona kama mtihani mgumu mno maishani mwake, hakufahamu chochote kuhusu mapenzi kila kitu kwake kilikuwa ni kigumu mno. Akanyanyua sura yake na kumtazama kisha akazungumza.
“Hapana Rose wewe ni msichana mzuri sana unayezivutia mboni za macho yangu msichana mzuri na mwenye mapenzi ya dhati nafahamu unanipenda sana ila muda wa sisi kufanya hivyo bado, nakuomba tumalize masomo yetu ndipo tufanye kile unachokitaka sawa mpenzi.”
Saweli alizumngumza huku akiwa anapiga magoti mbele ya Rose aliyekuwa akilia ndani kwa ndani bila kutoa sauti kitu pekeee kilichoneka kwa nje ni michirizi ya machozi iliyokuwa ikiyachora mashavu yake.Moyoni hakuwa na hata chembe ya mapenzi kwa masichana huyo ila hakupenda kumueleza ukweli alijua kufanya hivyo kungepelekea msichana huyo kufanya kitu kibaya, pia aliyafahamu mauvimu ya kutendwa hivyo hakuwa tayari kumtamkia neno hilo.
“Kama mimi ni mrembo kwanini hutaki kunielewa?”
“Nakuelewa sana ila tambua masomo yetu ni magumu sana tukichanganya vitu viwili hatutavuna kile tulichokipanda, tupo huku kwa ajili ya kuwaokoa watazania wanaoteseka na magonjwa mbalimbali naomba tusome kwanza miaka mitatu siyo mingi sana,tukimaliza tu shahada ya kwanza nitakuwa tayari kuwa na wewe sawa mamy,”alizungumza huku akimbusu shavuni kisha alinmyanyua akanyanyuka kivivu vivu na kujidekeza kwa Samweli ili tu kuwaonesha wasichana waliokuwa wakimtamani Samweli na kumsifia kwa uzuri wa sura yake umbo na hata ucheshi pamoja na upole wake.
“Sawa nimekuelewa nitafanya hivyo kama ulivyosema,” akazungumza huku akiendelea kujidekeza na kujifanya ameumizwa sana na matendo ya Samweli hakufahamu kama mwenzake alikuwa katika wakati mgumu sana matendo na maneno ya Rose yalikuwa shubiri ndani ya mtima wake kwani kila alipojaribu kujifanya anampenda msichana huyo moyo wake ulikataa kabisa.
“Pole mrembo ila jaribu kuzingatia kile kilichokuleta huku mapenzi yapo tu masomo ni nguzo kwako daima ila mapenzi hufa na kupotea kabisa na umdhaniaye anaweza kuwa siye.”
“Unasema nini Samweli?” Akamuuliza huku akiunyanyua uso wake na kumtazama kwa macho ya mshangao sana.
“Usizalishe maneno na mawazo potofu ndani ya kichwa chako kutokana na maneno yangu ila nimezungumza kwa wema kabisa mpenzi Rose.”
“Ooooh!Inamana wewe siye sahihi kwangu Samweli?”
“Mpenzi Rose wewe u mwanamke mrembo katika wanawake ambao mboni za macho yangu zimewaona, unamapenzi ya dhati ambayo ni baadhi ya wanawake wachache sana ambao wanayo, unanifanya niishi kama mfalme ndani ya sayari hii najivunia upendo wako,” akazungumza huku akitabasamu na mikono yake ikiishika mikono ya Rose ambayo ilikuwa imeikaba tsheti yake eneo la shingo.
“Samweli!”
“Naam malkia wangu.”
“Unanipenda?”
Rose akauliza swali hilo hali iliyopelekea Samweli kukaa kimya akimtazama msichana huyo kwa macho ya kutofahamu kile atakachokwenda kukizungumza, akakiinamisha kichwa chake chini akifikiria ni nini angeenda kukizungumza kwa msichana huyo.
Lilikuwa ni swali gumu sana kwa Samweli kutoka mdomoni mwake hakufahamu ajibu vipi kwani kujibu ndio aliamini angeweza kujiingiza katika matatizo mengine tena yangepelekea yeye kujiingiza kitanzini, kukataa nako aliaamini angempelelka Rose katika matatizo mabaya sana na hata angepelekea kufanya kitu kibaya sana kwake.
“Niambie Samweli usinifiche chochote kweli unanipenda?” Akauliza tena huku mkono wake wa kulia ukikishika kidevu cha Samweli na kuuinua uso wake macho yao yakagongana na Rose akaachia tabasamu, akiuuma mdomo wake wa chini akiambatananisha na kulikonyeza jicho lake la kulia hali iliyozidi kumtesa sana Samweli.
“Niambie usinifiche.”
“Ndio tena zaidi ya neneo lenyewe kwani vipi?”
“Ndio nini?”
“Nakupenda!”
“Kwanini unaniambia maeneo hayo?” Akazungumza uso wake ukiwa umebadilika na kukunja ndika mithili ya mtu aliyekuwa anataka kupigana.
“Daima mwanamke mrembo huwa hachukii na akichukia uzuri wake huongezeka mara dufuu…u waridi ndani ya maisha yangu, mwanamke mwenye mapenzi hata shetani anayaogopa nakupenda Rose mwaaaah!” Akamtuliza huku akiambatanisha na busu la kwenye shafu hali iliyomfanya Rose kutabasamu kidogo na kumkumbatia Samweli kwa nguvu zake zote akimshushia mvua ya mabusu usoni mwake kitendo kilichokuwa kikiuchukiza sana moyo wa Samweli. Japo alilitoa jibu hilo lakini moyoni hakuwa na hata chembe ya mapenzi kwa msichana huyo.
Waliondoka eneo hilo kwa furaha sana kila mtu alikuwa ameridhika na majibu ya mwenzake, vicheko na michezo ya watu walioashiria kuwa wapenzi ndivyo vilivyokuwa vikiendelea kati ya watu hao hadi Rose anamfikisha Samweli hosteli kwao ndipo alipogeuka na kurudi hosteli kwake akiwa na furaha sana. Kuanzia siku hiyo Rose hakumsumbua tena Samweli zaidi ya kumchunga kila alikokwenda kukichukua hakupenda kumuona Samweli akiwa karibu na msichana yeyote zaidi yake.Alimpatia zawadi mbalimbali na kadi kibao kila alipojisikia kufanya hivyo , siku za mwisho wa wiki alikuwa akiomuomba kutoka lakini Samweli hakukubali kufanya kitendo hivyo kwani aliamini kilichompelekea huko ni masomo na si kingine.
Miaka mitatu likatika hivyo Samweli na Rose wakawa wamehitimu shahada ya kwanza ya udaktari kitu kilichomfurahisha kila mtu, hawakutaka kubaki tenaMarekani walirejea moja kwa moja Tanzania walikopokelewa kwa furaha sana, kila mzazi alimpongeza mtoto wake hatua aliyokuwa ameifikia.
“Ahadi yetu leo imetimia ninachotaka ni ndoa.”
“Jamani Rose kwanini unapenda kuharakisha mambo kiasi hicho tunatakiwa kupumzika kwanza na kujipanga kwa hilo.”
“Kujipanga kwa njia ipi?”
“Nitakueleza muda ukiwadia ila siyo kwa sasa vipi maombi yako ya kazi yanendeleaje?”
“Nahisi kuanzia kesho ama kesho kutwa nitakuwa nimeeanza kazi.”
“Safi sana nakuombe.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Wewe je?”
“Bado bado nitakueleza kitakachofuata,” Samweli hakutaka kuzungumza siri iliyokuwa moyoni mwake kwani alipanga kurudi chuoni mara baada ya chuo kufunguliwa kwa shahada yake ya pili ya udaktari hakupenda kuanza kazi mara moja, mara baada ya wao kurejea nyumbani alimsistizia Rose kutafuta kazi ili tu aweze kupata nafasi nzuri ya yeye kusoma vizuri. Kwa kuwa walikuwa na tabia ya kutembelea kila siku siku hiyo waliiamu kuitumia kuzunguka kila kona ya jiji la Dar es salaam na jioni Samweli alimrudisha Rose nyumbani kwao.
***
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment