Search This Blog

Tuesday 1 November 2022

NIKUITE NANI? - 5

 





    Simulizi : Nikuite Nani? 
    Sehemu Ya Tano (5)






    Usiku wa saa tano tukaianza safari. Ndani tukiwa na mmoja wa madaktari, maalumu kwa ajili ya huduma ya kwanza kwa baba na shangazi. Ambao muda wote walitokwa na machozi kuonyesha uchungu walionao.



    Awamu hii tulipitia barabara ya Songea kuelekea Mbeya. Hivyo tulikata miji mbalimbali, midogo kwa mikubwa, huku saa zikizidi yoyoma. Tulivyoingia mjini Tunduru tulipokelewa na wingu zito lililotanda moshi na harufu ya moto. Kuna mahali palikuwa panaungua. Tena si pa dogo. Sehemu kubwa, ilyochukua hekari za kutosha.



    Sababu tulikuwa na mambo yetu hatukutilia sana maanani tukio hilo. Tukazidi kuchanja mbuga. Huku tukitoa pole na manung’uniko kimoyomoyo kwa mtendewa.



    Tulivyowasili jijini Mbeya tulipokelewa na habari kuhusu tukio tulilokutana nalo mjini Tunduru. Lile la moto.



    Maskini! Kumbe ni majengo ya kliniki ya baba. Ndiyo yaliyokuwa yameteketea. Iliniuma sana. Kwani niliona azma ya kuwasaidia watanzania wenziye ishakoma. Haraka. Nikapeleka tuhuma kwa mzee Namahala. Kuwa ndiye muhusika mkuu wa tukio hilo. Katuma watu. Achilia mbali wale wa Mangaka.



    Nikajikuta nafikiria namna timu ilivyo. Nikaiona kuwa ni pana. Tena pana mno. Na alifanya hivyo, ili tu, mipango yake isiyumbe. Baadaye nikawazua malipo aliyofanya ni ya aina gani. Ila kwa haraka, yalionesha ni makubwa, kiasi kwamba, watendaji wameshawishika kwa wepesi ndiyo maana wametekeleza.



    Siku zijazo wapendwa wangu wakaanza kupatiwa matibabu. Ila aibu iliwasumbua. Kwa kile walichotendewa. Hata ongea yao haikuwa ya amani. Walidhihirisha wanahitaji wawepo wao pekee. Wasionwe na mtu yeyote. Siri ibaki kuwa siri.

    “Tunatamani leo hii ungelikuwa mwisho wa uwepo wetu duniani. Kwa sababu aibu tutayoenda kukutana nayo ni kubwa mno,” walisema kwa pamoja. Wakati huo tupo nyumbani kwa bwana jela. Na ndiko waliko kuwa wanapatiwa matibabu.



    Afya zao zilivyokuja kutengemaa wakaanza mazoezi machache ya kujiimarisha, wakati huo wakibadilisha mazingira ya uono wa mboni zao. Wakawa wanatoka siku mojamoja.



    Walivyoimarika zaidi ndipo wakapatiwa taarifa kuhusu kuungua kwa kliniki na taarifa chache wanazozifahamu juu ya mzee Namahala na Jamila.



    Hawakuonesha mshangao wowote kuwahusu. Waliwafahamu. Ndiyo maana hawakuwashangaa.

    “Mzee Namahala na Jamila, ndiyo wasadikiwao kuhusika katika matukio yanayowahusu. Hivyo jeshi la polisi linafuatilia nyendo zao kwa ajili ya kuwaweka chini ya ulinzi. Wasaidizi wao, hasa wa mzee Namahala, baadhi yao wanashikiliwa kituo cha polisi kwa maelezo zaidi,” alisema afande Mzee. Akimaanisha afande Madevu na Chitoko. Kwamba wako kituo cha polisi baada ya kuwatoa mule chumbani.



    Vilevile, mmoja wa wale vijana waliofanya uhalifu Mangaka. Yule niliyempiga na jiwe. Naye alikuwa anashikiliwa na jeshi la polisi. Kwani tulisafiri naye hadi Mbeya.

    “Nawafahamu hao. Zaidi ya ninyi mnavyowafahamu,” alisema baba. Kauli iliyotushangaza sote tumsikilizao. Na kutoa ulizo kwa kila mmoja anawafahamu vipi? Ila kabla hatujafungua kingo za midomo yetu kuuliza, alitukatisha kwa endelezo lake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “…mtu hatari, kati ya hao wawili ni Jamila. Jamila ndiye mtu wa kumwekea nguvu za ufuatiliaji. Kuliko huyo munayemuani ana nguvu kubwa. Kisasi cha mzee Namahala, ni cha kawaida sana. Kuliko kisasi alichonacho Jamila. Jamila ana kisasi dhidi ya serikali, kwa sababu, haikumtendea haki angali mdogo. Hivyo kisasi chake kikubwa ni kuliangamiza taifa. Na kashaanza hiyo kazi. Kwa kusambaza vurusi vya ukimwi kwa wanaume kupitia shughuli aifanyayo…

    “…nimemfahamu Jamila angali mdogo. Alivyozulumiwa haki yake, kwa kosa la mauaji ya mama na kubakwa kwake na watu waliodhaminiwa na mzee Namahala. Ijapokuwa mzee Namahala, alijinasibu kumsaidia. Lakini, hakumpa msaada, zaidi ya matatizo.

    “Kisasi alichonacho dhidi ya mzee Namahala, ndicho humpa uficho dhidi ya kisasi na serikali. Kudhihirisha kuwa kisasi alichonacho kwa serikali ni kikubwa, kabla ya kupata upevu, nilikutana naye. Nikamuhoji baadhi ya mambo. Na akanijibu vyema kabisa kuhusu historia ya maisha yake. Kisha, nami nikampa ndoto nitamaniayo siku zote. Kuona gonjwa sugu linateketea kwa namna yoyote hapa duniani. Ila ndoto yangu ilikuwa umizo kwake. Kiasi kwamba akanitolea jicho la shari kuonesha haafikiani na ndoto niliyonayo.

    “Huyu ndiye Jamila. Msichana asiyepaswa kuwa na jina lolote lile lenye kumtambulisha.”

    “Kwa nini?” tukauliza kwa pamoja.

    “Kila jina haliendani kwake. Na endapo mukipata nafasi, jaribuni kumuuliza mumuite nani? Kwani, ana uficho mwingi wenye utatanishi. Pia jiulizeni, kwa nini anafanya vitu kwa kujiamini?

    “Ila…” shangazi akamkatisha.

    “Nini?”

    “Mwanao anahitaji kumfanya mwanamke mwenye nguvu hapa duniani. Atayeondokana na kebehi za watu kuhusu uuzaji aufanyao.”

    “Si jambo baya. Je, ataweza kubadili fikra zake? Kwani ayafanyayo, lipo moja lililojificha. Anatumiwa na yule mfungwa wa kisiasa, aliyeko jela miaka saba sasa. Akitumikia hukumu yake ya kifungo cha maisha. Na hiyo, ndiyo njia nyingine aitumiayo kuliangamiza taifa. Si munafahamu historia ya kifungo cha yule mfungwa jinsi ilivyo?” aliuliza baba na kututumbulia macho utadhani ni wadeni wake.

    “Umeyafahamu vipi hayo?” nikauliza.

    “Kila siku jumamosi. Lazima atembelee nyumbani kwa yule mfungwa. Kukutana na mmoja wa watu wamtembeleao mfungwa gerezani.”



    Tukaduwaa!



    Kwa upande wangu ni zaidi ya sana. Sikuamini nilichosikia. Fikra za Jamila zikaanza kuniambaa ambaa kwa ujirani. Lile swali alilotuambia baba likawa nalirudia rudia kujiuliza kama namuuliza Jamila akiwa kasimama mbele yangu. Nikuite nani?



    Sikuishia hapo. Nikapeleka fikra mbali zaidi. Kwa utaratibu. Kuanza kumdadavua Jamila. Nilianza, viungo viumbavyo mwili wake. Vile vya nje, kimoja baada ya kingine. Baada ya hapo nikahamia kwenye tabia. Tabia alizonazo na uhalisia wa matamshi yake pindi tuna maelewano.



    Hakika! Nilipaswa kufahamu undani wake. Lile swali la nikuite nani? Lilikuwa sahihi kuulizwa. Naye kuwa na wajibu wa kulijibu haraka iwezekanavyo, ili kuondoa mkanganyiko nafsini.



    Baadaye nikapatwa na hisio juu ya matendo yetu kipindi cha awali. Naam! Niliyakumbuka sana. Kiasi kwamba machozi hayakuniacha salama Nililengwa, huku akili ikiwa mbali kwa fikirio.

    “Nini hitajio la mwisho wa maisha yako?” nilijiuliza. Kana kwamba nimeketi na jamila ananisikiliza.



    Si, mara moja pekee. Nilijiuliza zaidi ya mara tatu, machozi yakizidi kunitiririka. Sikuwa na budi. Nikajikuta nafungua kingo za mdomo wangu nazungumza. Na kuvuta hisia za watu nilionao.

    “Dah! Nakumbuka, ni upendo. Upendo wangu ndiyo uliopelekea kila mmoja awe mbali na mwenziye kwa sasa. Hali inayopelekea niharibu furaha ya moyo. Na hatimaye kuzalisha huzuni. Huzuni ichangiayo kutokwa na machozi. Hadi nahisi napoteza uzito mwingi kwa ajili yako.

    “Abdul, una malengo gani juu ya maisha?”



    Nakumbuka. Jioni moja ulipata niuliza hivyo. Siku ile nilivyokutembelea, punde nilivyotaarifiwa hauko sawa kiafya. Ajabu, sikukupatia jibu, zaidi ya kukutazama na mwishowe kuishia kutabasamu. Naamini nilikuumiza sana kwa kutojibu swali lako, uliumia haswa, kwani baada ya kutoka pale ulinitumia ujumbe mwingine uliosomeka;

    “Nini maana ya kimya chako, ama hilo ndiyo jibu la swali langu?”



    Nakumbuka hata ujumbe huu sikuujibu pia. Ndipo nikazidi kukuchanganya nini maana yangu. Taratibu, furaha yako ikaanza kutoweka na kila tukutanapo hukuisha kuwa mnyonge.



    Nakumbuka. Yote haya yalijitokeza kabla hatujapatanishwa, kisha ukaanza kunipatia darasa la wema ndani ya ubongo wangu. Lakini sikutambua, kama una yako mengi mengineyo.



    NIKUITE NANI? Sina budi kukuuliza, na ikiwezekana nitumie swali hilo kuwa jina lako kwa sasa hadi pale utaponipatia majibu ya ujumbe wangu. Sijajua ni muda gani utachukua ujumbe huu kukufikia, ila punde tu baada ya kukufikia na kupata kuusoma nakuomba uujibu,” Nilihitimisha. Chozi likiwa limetiririka vya kutosha na kulowanisha sehemu kubwa ya shavu na shati nililovaa.



    Nilivyotuliza mboni zangu na kuanza kuangaza kwa wenzangu, ambao muda wote walikuwa wamenitumbulia macho pima kunishangaa, nikakumbuka kauli za bwana jela. Nikaanza kufikiri upya. Serikali inanihitaji kwa lipi? Kwa sababu ya Jamila? Mzee Namahala? Ama mtu mwingine. Hasa huyo mfungwa wa kesi ya kisiasa.



    Nilijiuliza pasi na jibu. Japo dhanio halikukosekana. Kwamba, naenda kupambana na mfungwa wa kesi ya kisiasa. Mbunge. Wa jimbo la Mbugwe. Kupitia mgongo wa Jamila.



    Mnamo saa tatu usiku baada ya mazungumzo mengi nikapelekwa kwenye moja ya nyumba iliyoko maeneo ya New forest. Nyumba yenye mahadhi ya kifahari, na kila sifa itambulishayo, anayeishi ni mtu wa namna gani. Si mlala hoi!



    Uwepo wangu ulisindikizwa na afande Mzee pamoja na bwana jela. Mwenyeji wetu akiwa ni Mkuu wa mkoa wa Mbeya. Baadaye ukaja ugeni mwingine, ugeni mzito ulionishangaza na kuendeleza kuniaminisha kuna kazi kubwa nayopaswa kuifanyia serikali.



    Ikanibidi niwazue kwa kina. Tatizo la waziwazi liikumbalo serikali dhidi ya wananchi. Lakini sikuwa mwepesi wa kutambua kama kuna tatizo. Niliona mambo yako sawa. Mwishowe nilizinduliwa na sauti nzito ya mgeni aliyekuja baada yetu. Mheshimiwa Rais. Rais wa serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania.



    Ujio wake ukionekana kuwa wa siri mno. Uliotambuliwa na viongozi wachache wa mkoa. Hata wale wahusikao na ulinzi hawakuleta mbwembwe pindi watumiapo barabara. Hasa zile za kuliza ving’ora.

    “Naamini utaweza kutufanyia kile tukitakacho. Kwani tunahitaji amani ndani ya taifa letu. Ila kuna watu, wachache wanaleta ukinzani wenye maslahi binafsi. Serikali tunahitaji ukatukatie mizizi inayochipukia huko mtaani,” alisema Rais. Nahonyo Liumba. Tukiwa tumeketi viti jirani nyuso zikitazamana.

    “Kwa namna ipi?” niliuliza.

    “Kuna watu wamejaa dhamirio la kuvunja moja ya sheria iliyopo ndani ya katiba. Wanahitaji kuingiza u—magharibi, kisha wapoteze mila zetu zitutambulishazo kama taifa.”

    “Niwekeni wazi, napaswa kufanya kazi gani?”

    “Kuna watu inabidi waondoke kwenye uso wa dunia…” alisema rais na kuweka tuo kwa muda. Akaingiza moja ya mkono kwenye mfuko wa koti alilovaa akatoa picha ya mnato, akanikabidhi. “…hawa wanatakiwa waondoke,” aliendelea kusema. Punde alivyonikabidhi huku akinisaili nachukuliaje maongezi yake.



    Ile picha ilikuwa ya mbunge wa jimbo la Mbugwe. Dkt. Aman Ngumije. Pamoja na Jamila. Wakiwa wamekumbatiana kama wapenzi.



    Nikashtuka!



    Kiasi kwamba wote waliona mshituko wangu.

    “Huyu mzee ana dhamira gani? Mtu aliyenitendea wema kwa kunifanya mwerevu leo hii nimuue? Hapana. Ila...nikikataa si utakuwa mwisho wa maisha yangu? Maana hawatokuwa radhi nifahamu dhamira yao halafu waendelee kuniacha nikiranda randa mtaani,” nilijisemeza.

    “Tumtoe huyu chambo, ili wengine tuwatengenezee maisha utakayo,” alisema rais Nahonyo. Macho yake pima kwangu.









    Nami nikaishiwa pozi. Nitaruhusu vipi Jamila auwawe wakati alishanitendea mema? Ijapokuwa nilipatwa na fikra za upande wa pili kumuhusu, mpango wake na Dkt. Aman.



    Mwishowe nilipatiwa karatasi nisaini. Kuonyesha kuna makubaliano baina yangu na serikali. Si serikali, bali baina yangu na rais Nahonyo.



    Rais Nahonyo alitumia mwavuli wa serikali kunitumikisha. Kwani, nakumbuka. Ni yeye, ndiye katoa amri ya Dkt. Aman akamatwe na jeshi la polisi pindi yuko Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa. Leo hii kautwaa urais, anataka ammalize kabisa.



    Nakumbuka, chanzo. Kilichopelekea Dkt. Aman awe hatiani ni mwanzo aliohamasisha wananchi wapokee kwa mikono miwili mapenzi ya jinsia moja. Yeye ndiye mtu wa kwanza kutoa mapendekezo hayo. Huku akijinasibu kuwa dunia inaheshimu uhuru wa faragha, hivyo taifa linapaswa libadilike, kwa kuendana na matakwa ya nchi nyingine pasipo angalia matokeo yatayopatikana mbeleni.



    Kitendo hicho kikajenga chukizo kwa serikali. Hasa kwa Nahonyo. Ambaye kwa wakati huo alikuwa waziri mwenye mamlaka yahusuyo mambo ya nje. Tamaduni ngeni iingiapo nchini basi naye huwa sehemu ya uridhiaji wa kutumika. Ila kwa hili hakuwa ridhaa.



    Hivyo Nahonyo, na waandamizi wachache wa serikali wakamuundia tume Dkt. Aman, ya kumuasa aachane na mambo yatayoliingiza taifa matatizoni. Tume iliyoundwa kwa siri, na mkutano wao dhidi ya Dkt. Aman ulikuwa wa siri. Ila Dkt. Aman hakuitunza siri hii. Mara kikao kilivyohairishwa akaanza kusambaza kilichotendeka. Jambo lililowachukiza zaidi wanakamati, mwishowe wakampatia tuhuma kuhusu uraia wake. Na ndiyo imempeleka gerezani.



    Nakumbuka! Tuhuma hii ilisukwa vilivyo. Na ikasukika. Kiasi kwamba Dkt. Aman alishindwa kufurukuta.



    Hakika! Alikuwa raia wa Tanzania. Ila wenye mamlaka walionesha uwezo wao tu. Kuwa wanaweza kiasi gani. Pasipo kujali jamii itawachukuliaje.



    Nakumbuka. Wanaserikali waliziba sikio. Kwa kutosikiliza wananchi wanazungumza nini na wanafanya nini. Kwani achilia mbali maandamano ya amani, walifanya maandamano haribifu ya miundombinu na sehemu nyinginezo nyeti za serikali.



    Mwishowe wanaserikali waliibuka kidedea. Dkt. Aman akaonekana mkosaji. Akaonekana si raia wa Tanzania. Uraia wake ukasomeka nchini Rwanda. Kisa tu, mmoja miongoni mwa wazazi wake ana asili ya taifa hilo kwa upande mmoja. Mama!



    Ni jambo la kusikitisha. Lakini hakukuwa na budi kwa sababu ndiyo maamuzi ya wao. Kwa wakati ule. Nilikuwa mmoja kati ya watu wamchukiao Nahonyo. Kutokana na maamuzi haya dhidi ya Dkt. Aman.



    Tena alichukiwa na wengi. Huku tukishindwa kutambua nia yake ya kukataa kuingiza utamaduni wa kigeni nchini. Si mnafahamu, baya moja lina uwezo wa kufuta mema kumi.



    Leo hii yule niliyemchukia. Aliyemfutia mtanzania mwenziye uraia na kuonekana mnyarwanda kisha akampatia kesi ya kukutwa na nyara za serikali anahitaji nimpatie msaada zaidi kwa kutaka kumfuta yule niliyeamini yuko juu zaidi yake.



    Yule, niliyegeuka muumini wake kwa kufuata kauli, huku nikisahau mila na desturi zetu, kisa, dunia imebadilika kwa teknolojia. Lakini, mbona hayo mataifa makubwa, bado yanatambulika kwa tamaduni zao? Iweje huku kwetu ukiwa muumini wa tamaduni asilia unaonekana mshamba, na mpitwa wakati?



    Nilitatizwa na hili!



    Na kunipa shinikizo la kuafiki alichodhamiria rais Nahonyo wa kupinga tamaduni ngeni ije iathiri taifa letu. Pia. Nilijiaminisha hiyo inaweza kuwa nafasi pekee ya kuwapigania wale wote wafanyao biashara ya kuuza utu wa miili yao kuwa kitega uchumi, kuwa wenye nguvu mtaani. Kwa kupata heshima sawa na yule asiyejishughulisha na kazi hiyo.



    Kwa niaba ya utaifa. Nilisaini ile karatasi. Ambayo ilikuwa na maelezo machache tu. Nilivyomaliza akafuatia rais Nahonyo naye akasaini.



    Kauli ya u—taifa ilinihalalisha kuridhia matendo ambayo kisheria hayapaswi kutendeka. Kauli itumiwayo na wanaserikali kutenda unyama.

    “Jamila, nakupenda sana. Sipo radhi uondoke duniani, mimi nikiwa chanzo. Nitafanya kila jitihada kuhakikisha unapata badiliko. Lakini huyu mwalimu wako, lazima alambe mchanga kwa manufaa ya wengi,” nilijisemeza. Wakati huo tukielekea kwenye moja ya gari safari ya kurudi nyumbani kwa bwana jela.



    Tulivyorudi nyumbani ikanibidi nianze kuwadadisi. Kulikoni? Rais, kiongozi wa kitaifa afanye dili nami.

    “Kuna muda, kiongozi yeyote lazima ajirudi kwa watu wake mambo yaendavyo hovyo. Sisi tulipatiwa kazi. Tumtafute mtu toka gerezani atayefanya hiki alichokuambia. Tukaona unaweza kwa sababu una weledi mkubwa kwa ajili ya jamii yako,” alisema afande Mzee kwa unyenyekevu mkubwa.

    “Mulijuwaje naweza?”

    “Hata shangazi yako alituhakikishia hili. Ndiyo maana alitolewa gerezani baada ya siku chache tu. Ila isivyo bahati, hakufanikisha kwa sababu ya kutekwa.”

    “Tukiwazima hawa itakuwa rahisi kufanikisha kile ukitakacho pia. Kwani nia ya mheshimiwa, ni kuhakikisha anazima tamaduni inayopigiwa debe iingie nchini na kutokomeza biashara ya uuzaji utu wa kimwili kiholela,” bwana jela naye alichangia hoja. Iliyoniongezea mwangaza kichwani mwangu.

    “Acha nasi tulitambulishe taifa, kuwa tuna desturi isiyovunja misingi ya kidini.”

    __________



    Siku hii, ilipita kwa lepe la usingizi kulisikia kwa jirani. Kwangu halikupatikana hadi panapo mapambazuko. Kikubwa, nilikuwa nawazua namna nitavyofanikisha kazi niliyopatiwa. Kuondoa uhai wa binadamu wenzangu. Kazi ambayo sijawahi ifanya hata siku moja.

    Naanzaje? Na kwa namna ipi?



    Lilikuwa swali ngumu kwangu kulipatia jibu. Ila nililazimika, kwa uficho tu wa wengi. Kwani hata hao nitaowaondoa si wapo sehemu ya wengi?



    Kikubwa, kingine kilichonipatia wakati mgumu wa kumuondoa mtu nimpendaye. Mtu aliyenifanya mwerevu na mwenye maono.

    Sikuishia hapo. Nilienda mbali zaidi kwa kufikiria matokeo ya tukio nitalofanya.

    “Watu wengi wataandamana sana. Maana yule kiongozi ana nguvu na bahati ya kupendwa kutokana na kusimama kwenye misingi ya sheria na haki.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Siku iliyofuata nikafanya matembezi ya hapa na pale katika hatua za kuchangamsha akili yangu nisahau kwa muda yale niliyokabidhiwa. Zoezi nililolianza asubuhi, ya saa tatu na kuhitimisha saa nane mchana. Huku nikiwa na mengi niliyojifunza.



    Mengine, ni yaleyale niliyojifunza toka kwa shangazi na Chitoko. Kama mjuavyo. Kauli zinaumba na kuumbua.



    Pindi nikiwa na uelekeo wa kurudi nyumbani kwa bwana jela, nilivyofika maeneo ya Mabatini, nikabahatika kukutana na Jamila. Katika moja ya upenyo pasi na matarajio.

    “Jamila!” niliita. Nikiwa na wingi wa mshangao kumwendea. Fuadi ukilipuka hofu, kwamba nitamwambia nini msichana huyo akanielewa.

    Maana nijuavyo. Wasichana wenye tabia kama yake hujiona, mithili wao ndiyo wa pekee duniani. Hamna mtu mwingine kama wao. Imani inayowapeleka puta kwa kushindwa kufikiri maisha ya baadaye ukiachana na muda waliopo.



    Hata jibu la wito wangu liliendana na tabia husika iliyomkithiri. Lilijaa kebehi, kana kwamba nampatia kinyaa mdomoni mwake.

    “Ushawahi kufikiri maisha yako baada ya hapa?” nilimuuliza. Mboni zangu zimetumbua mwilini mwake kumsaili alivyo. Maana alijaa mabadiliko kibao yaliyodhihirisha anapitia wakati mgumu. Wakati wa kuhitaji msaada nje ya jamii iliyomzunguka kitabia.

    “unaniuliza ewe kama nani?” aliniuliza. Kingo za mdomo kazibinua kwa kupindisha. Moja ilielekea upande huu, nyingine upande ule.

    “Picha unionyeshayo tofauti na ile ya awali. Umekuwa mpinga mema, kiasi kwamba nashindwa kukutambua ewe ni mtu wa aina gani.”

    “Nani kakuambia kuna mtu mwema dunia hii? Duniani hamna mtu mwema. Wote ni wa katili, kwa sababu kila mmoja ana mnyonge wake. Niache nifanye kazi yangu. Hujui niliyoyapitia. Hao, wanaohubiri amani na wema leo hii, ndiyo waliohalalisha unyama kipindi cha nyuma. Sasa unawezaje kuwafuata? Wakati huohuo, unaamini msemo kuwa mchovya asali hachovi mara moja? Kaa mbali. Na endapo utabahatika kuonana tena nami, nione mtu mwenye sura mbili. Mtu nisiyepaswa kuaminiwa na kutambulika.



    Na nakuahidi, lazima nitimize azma yangu. Ya kukifuta kizazi hiki kijimilikichasho umalaika.”

    “Acha kujifanya nunda. Unatafuta kifo chako. Na ukicheza ovyo, nitakuua, ili tubaki na kizazi salama,” niling’aka. Kwa hasira ya hali ya juu, kwa kuwa nilichukizwa na kauli zake. Huku nikiwa na ujasiri uliomshtua Jamila. Nimepata wapi kiburi cha kuzungumza hivyo.



    Iweje mkosaji hujiona sahihi?



    Hili ni tatizo. Kwa nini haitaji kusaidika? Kisasi kinashindwaje kutambua thamani ya msamaha? Kama Mwenyezi Mungu husamehe, vipi sisi tuliopo duniani kwa mamlaka yake?



    Uwepo wetu pamoja ulihitimishwa pasi na maelewano. Baada ya hapo kila mmoja akaendelea na safari yake. Mimi, nilielekea nyumbani kwa bwana jela kama nilivyojipangia awali. Kichwani nikiwa na mafikirio dhidi yake kupitia maongezi tuliyofanya.



    Inawezekana kumdhuru umpendaye kwa maslahi ya wengi?



    Ni moja ya swali lililokosesha amani wangu fuadi.







    Mipango ya ufanikishaji ikaanza. Awali, nilipatiwa mafunzo ya utumiaji wa silaha. Hasa bunduki. Yalikuwa mafunzo ya gizani. Niliyopatiwa usiku wa kiza kikali. Na sehemu yenye uficho iliyowazuia watu wengi wasitambue kiendeleacho.



    Si bunduki aina zote. Hapana. Ni bunduki chache tu, ndizo nilipatiwa mafunzo yake. Hasa bastola na baadhi zenye uwezo mkubwa. Jamii ya SMG. Pasi na kusahau, aina ya mitindo nayopaswa kuketi wakati wa upigaji. Kama vile, pigo la kusimama. Natakiwa nisimamaje, pigo la kupiga goti na pigo la kulala.



    Kwa muda mfupi tu. Nikiwa na maana ya siku chache. Nikawa mjuzi, kama sio mjuvi. Nikalowea katika utumiaji. Baada ya hapo nikasubiri siku tu, ya kutekeleza tukio husika.

    Shauku ikichipua, itakuaje hiyo siku.



    Usiku wa siku ya mwisho ya kuhitimisha mazoezi yangu. Ambayo asilimia kubwa nilikuwa napatiwa na afande Mzee tukafikiwa na taarifa iliyotuvumbua Jamila kaanza kuonesha upande wa pili wa sura yake.



    Taarifa ya kifo!



    Moja ya kigogo ndani ya wizara ya fedha. Miongoni mwa wahamasishaji wa mambo ya maendeleo kwa vijana. Vilevile ni mpingaji mkuu kati ya wakuu wakataao ingizo la tamaduni ngeni nchini. Al haji Zuberi. Ndilo jina maarufu alilozoeleka nalo.



    Tulipata taarifa kupitia mtandao wa kijamii. Facebook! Kwenye moja ya blogu. Ikieleza mazingira ya kifo chake. Kwamba ni kifo tata kilichotokea mazingira ya kutatanisha. Kafia chumba cha hoteli. Lakini hawakueleza mkasa mzima. Nahisi walitaka kutunza heshima aliyopata kuwanayo.

    “Huyu ndiyo yule tuliyoambiwa,” alisema afande Mzee.

    “Sahihi! Nami alipata kunihakikishia kuwa ana sura mbili. Hivyo hana utambulisho maalumu.”

    “Kwa hiyo anastahili kifo.”

    “Dhahiri shahiri!” nilisema. Baada ya ufikirio mfupi. Kama kaanza kuua watu waliojaliwa hekima za kiuongozi na maono yenye manufaa ya wengi, kwa nini aachwe?



    Kabla hatujahitimisha majadiliano yetu, simu ikaita. Simu yangu. Simu niliyokabidhiwa, maalumu kwa ajili ya mawasiliano na rais. Na kwenye orodha ya namba hakukuwa na namba nyingine zaidi yake.



    Simu hii nilipatiwa usiku ule wa makubaliano. Simu ndogo ya mkononi. Aina ya Nokia 105. Sikusita. Chap, nikasogeza dole gumba la moja ya mkono kwenye kitufe cha kipokeleo.

    “Ndiyo mheshimiwa.”

    “Kazi imeanza. Usiku huu, yule mtu kafanya mauaji ndani ya hoteli ya Naf beach mjini Mtwara. Kifo cha moja ya waumini wapingao tamaduni ngeni kuingia nchini. Hii inatoa ishara, pambano ni kali. Na nia nzima ya pambano.”

    “Usihofu kiongozi. Mimi niko tayari. Nasubiri siku tu.”



    Sikuwa na namna zaidi ya kumuhakikishia utendaji. Nitaendeleaje kumtunza asiyetunzika? Na asiyetambua nini maana ya shukrani.



    Simu ikakatwa .

    __________



    Kweli! Jamila alikuwa kadhamiria. Jinsia na atendayo hayakulandana japo chembe. Kisasi chake alikitengeneza kuwa kisichohitaji msamaha. Hakuhitaji kusamehe. Mbali na kisasi, aliungana na Dkt. Aman ili kujihakikishia urahisi wa ulipaji. Kwani biashara aifanyayo endapo ingelihalalishwa, basi ingelimpatia wepesi wa malipizi.



    Na mtu pekee wa kumfanyia wepesi huo ni Dkt. Aman pekee. Ndiyo maana kaamua kushirikiana naye kupitia mmoja wa watu wa karibu wa Dkt. Aman, amtembeleaye gerezani. Kisha humpatia maelezo nini kifanyike. Ikiwa njia ya kuhalalishwa matakwa yake, na kujibu alichotendewa.



    Alihitaji tamaduni ngeni. Na biashara ya uuzaji wa utu wa kimwili kwa wanawake, itambulike rasmi kama biashara zingine.



    Na njia pekee. Ni kuwaondoa washupavu wote wasimamiao jambo lao lishindikane.



    Hivyo Jamila, akapatiwa idadi kadhaa ya majina ya watu wanaopaswa kuondoka katika sura ya dunia. Miongoni mwao, ni Al haji Zuber. Wakafuatia vigogo wengine wa kiserikali. Toka wizara na idara mbalimbali.



    Pasi na sahau viongozi wa dini!



    Hawa. Walikuwa kwenye orodha ya watao shinikizwa. Kufungwa kingo za midomo yao, wasizungumze chochote kuhusu mpango wao.



    Njia kuu itumikayo ikawa ni mapenzi. Jamila alijitongozesha kwa watu hawa, nao kwa ukosefu wa ujasiri mbele ya ngozi ya kike wakawa wanajiingiza kwa pupa. Mwishowe hukutwa na mauti. Katika orodha aliyokabidhiwa, aliitekeleza ipasavyo kwa asilimia tisini.



    Wote waliuwawa. Kwa njia ileile aliyoitumia kwa Al haji Zuber. Wote walifia ndani ya vyumba vya hoteli. Miji tofauti tofauti, hali iliyozua taharuki kwa wananchi. Ila sio kwa wenye mamlaka ya kuliongoza taifa na vyombo vya ulinzi.



    Walilipotezea. Ukizingatia wengi waliouwawa ni watu wa serikali, ama walio karibu na viongozi serikalini.



    Waliuwadahaa tu umma, kwamba wanafuatilia, lakini hakukuwa na umaanani wowote. Kuna kitu walikikwepa. Si mnafahamu, kinga ya kisiasa ilivyoenea siku hizi kwa waovu wa kichama?



    Serikali walijizuia. Lengo kuniachia nafasi yangu. Nikipiga, isibainike. Kwamba wao, wanahusika kwa namna moja ama nyingine.



    Kwa upande wa viongozi wa dini. Wao walisalimika. Hasa Mufti Mkuu na kiongozi wa maaskofu wote nchini. Sina hakika, walifanyiwa nini. Ila walikatwa kauli. Hawakuwa na uchangiaji wowote uhusio mgeni apiganiwaye kwa mgongo wa sheria za umoja wa mataifa.

    “Mtu pekee aliyehusika na mauaji ya hawa watu ni Jamila. Hapaswi kusamehewa. Ndiyo maana nimeridhia kupoteza wachache kwa ajili ya kulinda wengi. Kwani, sheria za umoja wa mataifa ndizo huanza kuongoza nchi yetu? Si tunaanza na zetu za ndani ndizo hufuata za mbali?” aliuliza rais Nahonyo. Pindi tuko ndani ya moja ya chumba nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.

    “Sasa nimeamini, dhahiri hapaswi msamaha, kama mwenyewe hatambui thamani ya kusamehe.”

    “Ijumaa. Wiki ijayo tunamtoa yule mtu. Kiongozi wao. Hakikisha, huzembei. Nataka asili ya taifa letu ibaki ilivyo pasi na kuathiriwa. Tuwe na tamaduni za kujivunia. Na si kujivunia zilizoasisiwa na mataifa ya nje.”

    “Ila mkuu…”

    “Nini tena?”

    “Kinacho tuathiri, ni huu uhuru wa kuazima. Mataifa mengi barani Afrika yana uhuru usio huru.”

    “Kwa nini wazungumza hivyo?”

    “Kuna taifa laitwa Tuleane. Ni moja ya nchi zilizoathiriwa na uhuru huo. Mwisho wa hii kazi, nitakupatia kitabu cha hadithi kielezeacho uhuru wa namna hiyo. Kilichoandikwa na Hassan Mboneche.”

    “Itakuwa vyema sana.”

    “Sahihi. Na kitakuvumbua kwa mengi.”

    “Sawa. Kumbuka, ijumaa, saa kumi jioni, ndiyo muda ataotolewa yule mtu. Gereza kuu Arusha. Lililoko maeneo ya Kisongo.

    __________



    Ijumaa. Saa tisa alasiri, nilishawasili jijijni Arusha. Nikiwa na begi dogo la mgongoni nililohifadhia zana za kazi kwa ajili ya kile kilichonisafirisha. Kuuondoa uhai wa Dkt. Aman. Sambamba na Jamila, ambaye naye alihisiwa kuwepo eneo la tukio. Ili tuzime ndoto za wafuasi wao kwa matakwa ya wazi ya tamaduni ngeni, zinazokinzana na misingi ya dini.



    Ijapokuwa, ajabu ya leo, misingi ya dini si chochote kwenye matakwa ya kisheria katika mataifa mengi.



    Baadaye nilipanda bodaboda hadi kituo cha daladala Kilombero. Huko nilipanda moja ya daladala zielekeazo gerezani kisha nikasubiri muda tu wa kuondoka. Kwenda eneo husika. Daladala ilivyojaza safari ya kuelekea gerezani ikaanza. Sikumbuki tulitumia muda gani. Tukawasili, kisha abiria tukaanza kuteremka nje ya lango la kuingilia uwanja wa ndege.



    Langoni palikuwa na askari wa kampuni moja ya ulinzi. Ambao kazi yao kubwa ni kufungua geti na kushikia watu baadhi ya vitu visivyoruhusiwa kuingia navyo gerezani.



    Nami nikawa mmoja miongoni mwa walioingia ndani ya uga wa uwanja wa ndege. Nikaangaza angaza, maana kulikuwa na nyomi ya watu utadhani wanasubiri ugeni unaowasili kwa njia ya ndege.



    Wingi wa watu ulianzia getini hadi liliko jengo la utawala wa uwanja wa ndege, karibu tu, na gereza kuu la Arusha. Baadhi wakiwa wamekamatia mabango yenye jumbe mbalimbali.



    Kwa hisia zangu za haraka, nilitambua wengi kati yao ni wenyeji wa mkoani Arusha. Na baadhi waishio mkoa jirani, hasa Manyara. Kwa miji ya jirani, kama vile Minjingu na Magugu.



    Kazi yangu hapa ilikuwa moja tu. Kusoma mazingira kabla sijafanya tukio. Ijapokuwa tukio lilipaswa kutendeka sehemu nyingine nje ya mkoa wa Arusha, ili ipotezwe dhana ya serikali kuhusika kwenye tukio.



    Naam! Niligeuka kibaraka wa matakwa yangu. Na mkono wa serikali pia.



    Nilivyojiridhisha kwa kile nikitakacho, nilifunga safari kurejea mjini. Nako niliunga safari hadi mjini KIA. Sababu ulikuwa ni mpango ulioandaliwa kwa uficho. Nilienda kwenye moja ya jengo mjini hapo ambalo liliandaliwa maalumu kwa ajili ya kufanyia shambulizi.



    Kwa wepesi nilioshindwa kukadiria muda, nilifunga zana ya shambulizi, bunduki. Aina ya 90 mm kisha nikaenda kuketi sehemu ya kushambulia. Juu ya paa ya nyumba hiyo. Kwani nilikwisha fahamishwa mara baada ya kutolewa gerezani, atasafirishwa hadi uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro, ambako atalazimika kupanda ndege na kuondoka nchini baada ya notisi iliyomtaka aondoke ndani ya saa tano toka atavyotolewa gerezani. Hivyo saa mbili usiku alipaswa kuondoka kabla hazijachukuliwa hatua kali dhidi yake.



    Bahati iliyoje. Mnamo saa moja usiku msafara wake uliwasili KIA. Msafara uliosindikizwa na pikipiki mbele, yakafuata magari kadhaa, takribani tano. Ambapo kati ya hayo, alipanda moja wapo. Huku kuna baadhi ya watu walikuwa wanakimbiza msafara pembeni muda wote wakitoa shangwe.



    Sina hakika. Kama shangilio lao lilikuwa linahusiana na kitendo cha kutolewa gerezani, ama kwa sababu ya kuanza kuingiwa na imani kwamba kile alichokuwa anapigania siku zote kinaenda kutimia. Japo hakuwa na nafasi tena ya kuendelea kuwepo nchini.



    Walivyoifikia njia panda ya kuelekea uwanja wa ndege wakaweka tuo. Kwa, muda, huku wakiendelea kufanya pambio lililoonekana linatoka kwa dhati moyoni mwao. Hakika alishangiliwa. Kiasi kwamba nami nikaingiwa na huruma na kutamani niingie katikati ya kundi hilo niyamwage.



    Msaada wa mwanga ukanisaidia. Kuangaza vyema, kila tukio hali iliyonifanya nipembue pumba na kupata kichele kilicho bora. Dkt. Aman, akasomeka kwenye rada zangu. Kwa ufasaha wa hali ya juu pasi na shaka.



    Wapi ujuvi. Nikauvaa utakavyo. Moja ya mkono wangu, hasa wa kuume nikakamatia kishikio cha nyuma cha bunduki. (pistol grip) mwingine uliosalia nikakamatia mshikio wa mbele (fore hand grip) wakati huohuo kiwiko cha mkono wa kushoto nimekikita juu ya paa la bati, nyama ya mkono nimegandamiza sawia kwenye kisanduku cha risasi, ikiwa ni lengo la kupoteza ama kupunguza kidogo myumbisho husababishwao na presha ya utokaji wa risasi. Pasi na sahau kwapa, nimezibana kiasi.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sikusahau vilengeo. Nikavioanisha vyema. Nikafuatia kubana pumzi, kisha kidole cha shahada juu ya kifyatulia risasi. Nikakiminya kiasi. Pasi na nguvu, kikagota kidogo. Ishara iliyonitambulisha hiyo ni sehemu ya kwanza ya kifyatulia risasi (trigger 1) halafu nikaongeza nguvu tena, hapo nikapata kifyatulia namba mbili (trigger 2). Ambayo, ndiyo huruhusu mfumo mzima wa utokaji risasi.



    Kichwa cha risasi kikapasua anga. Kwa safari ya kufuata lengo nililolilenga. Huku ganda likidondoka chini. Kuashiria mwisho wa matumizi yake ushafika. Baada ya kuhifadhi baruti kwa muda mrefu tangu ilivyotengenezwa kiwandani.









    Cha kushangaza!



    Pigo langu halikuwa na madhara. Kichwa kilienda kapa hadi mwisho wa ukomo wake wa masafa. Ijapokuwa sina hakika. Kwa kuwa, yawezekana kilikutana na kizuizi cha kupunguza kasi. Lakini, mlengwa alipatwa na pigo toka sehemu nyingine. Alipigwa, sehemu ambayo sikuilenga. Na kunipa picha, kuna mtu mwingine zaidi yangu aliyefanya tukio hilo.



    Nani?



    Sikumfahamu. Ila nilivyojaribu kuchunguza kwa umakini wa hali ya juu, niliambulia tawanyiko la watu waliokosa ujasiri na kusalia wachache waliotaka kujiridhisha kilichomsibu kiongozi wao. Nilivyopeleka mboni kwa Dkt. Aman, nilimuona akitokwa na damu nyingi, waliomzunguka wakijitahidi kumpatia huduma.



    Uwepo wangu kule juu ukaishia hapo. Chap! Nikateremka. Nikaokota ganda la risasi, nikafuatia kufungua bunduki na kuhifadhi kwenye kibegi nilichohifadhia awali kisha nikapiga hatua kuondoka.



    Sikukawia kufika kituo cha kupanda gari. Kilikuwa mkabala na pale lilipotokea tukio la shambulizi la Dkt. Aman. Watu wakawa wamekusanyika kwa wingi. Kiasi kwamba walitengeneza foleni na kuleta ugumu wa magari kupita. Ila sikulitilia mkazo. Niliendelea na mambo yangu, huku nikiruhusu fikra za nani kafanya shambulizi.



    Kuna muda nilihisi, yumkini walionipa kazi hawakuniamini, wakaamua kujipanga kazi wenyewe. Ila hisia hii ilikata ghafla, nilivyoingia ndani ya gari. Kosta! Itokayo Arusha kuelekea Moshi. Mboni zangu zikaruhusu uono wa msichana, pasi na shaka, msichana niliyemfahamu. Jamila!



    Kidogo, ikanipa ulizo. Iweje awe hapo kwa muda huo. Nikahisi jambo. Tena kwa mavazi aliyovaa, yalinipa shaka zaidi kuhusu ulizo nafsini mwangu.

    “Kwa nini hayupo kwenye mapokezi ya mkuu wake? Ama kaondoka baada ya kushambuliwa?” nilijiuliza. Taratibu nikipiga hatua kwenda kuketi.



    Nikaenda kuketi siti jirani naye. Ila ilikuwa kama chukizo kwake. Kwani, alifunga ndita kama hanitambui. Nadhani hakuhitaji niketi jirani naye. Ama hakufurahishwa na uwepo wangu ndani ya gari. Ijapokuwa hana umiliki.



    Sekunde chache baadaye toka nilivyoketi nikafukizwa na harufu fulani iliyonishutua na kunishinikiza kumpiga jicho kali. Sina hakika kama naye alifukizwa na harufu ile toka kwangu. Kwani tulijikuta tumetumbuliana macho, huku tukijenga ulizo na dhanio akilini.



    Waarabu wa pemba hujuana kwa viremba!



    Ndicho kilichotushinikiza kutumbuliana macho. Takribani sekunde kumi, kisha kila mmoja akaendelea na angaza nyingine.



    Harufu ya baruti. Baruti ya risasi. Ndiyo iliyotufukiza. Na kutupa shinikizo kwa kile nilichofanya.

    “Ina maana huyu ndiyo kamuua Dkt. Aman?” nilijiuliza. Takribani zaidi ya mara tatu. Wakati huo nikipiga jicho la wizi kumwangalia na kumchambua. Ni mtu wa namna gani.



    Bado, alikuwa mtu asiye na umaalumu wa jambo. Mwenye walakini na mengi yaliyosheheni utata.

    __________



    “Naamini ewe ndiyo umemuua Dkt. Aman,” nilisema. Kumwambia Jamila, pindi nimeongozana naye, tukiwa tuna ambaa ambaa na barabara itambulikayo double road mara baada ya kuteremka garini kituo cha mabasi mjini Moshi.



    Ila hakuonesha kujali kauli yangu. Si kauli tu, hadi ujali wake kwa ujumla haukuwa mzuri kiasi kwamba akanipandisha hasira, iliyonifanya nimkamate moja ya mkono wake kwa nguvu kisha tukasimama.

    “Niache. Unahitaji nini kwangu?” aliluliza Jamila kwa sauti ya nguvu. Iliyosikika hadi kwa watu jirani walioketi kwenye kijiwe fulani wakituliza tumbo zao kwa mlo. Kwani, mwisho wa ulizo wa Jamila, niliwasikia wale vijana wakipaza sauti zao kutupa jumbe kwangu.

    “Mapenzi hayalazimishwi.”

    “Mapenzi ya sasa hutegemea uchumi wa mfukoni, kama haujitoshelezi, using’ang’anie wanawake usiokuwa na uwezo nao.”

    Jumbe zao zilinighafirisha. Zikanipa mhemko nisio utaraji na hatimaye kuniondoa relini kwa kiasi. Soni haikuniacha. Kwamba natazamikaje mbele ya uso wa wengi ingawa sifahamiki.

    “Niweke wazi. Umehusika na lile tukio?”

    “Kipi cha ajabu kikushangazacho? Yule si mwanasiasa, moja ya watu waliobarikiwa utashi wa uchongani. Huwa na kawaida, hutambua umuhimu wa mtu kwa maslahi mengi binafsi. Kwani ushawahi ona wanasiasa wenye itakadi tofauti wanasifiana?



    Hivyo nililazimika kumuondoa, ili niendelee kutunza umuhimu wangu kabla haujadhalilishwa. Yule angelinitumia tu. Halafu baadaye angeliniacha mithili ya taka jaani.”

    “Huoni kuwa unaenda kuipatia picha mbaya serikali ilhali hawajahusika?”

    “Ni wajibu wao kuvaa uovu wa wananchi. Kwani walivyonitenda, hawakuona wanaenda kutengeneza picha mbaya? Iweje kwao iwe picha mbaya, halafu watendeapo wengine mubariki picha nzuri wakati dhamira ya tukio ni moja?

    “Unahitaji upatiwe nini? Uweze kutulia, na usiwasumbue wote walindao maono mema kwa manufaa ya wengi?”

    “Nani kakuambia watu wa namna yetu hununulika kwa hadaa za kipumbavu? Unafahamu, u—mimi ndiyo jadi yetu, sasa tutaanzaje kurudisha majeshi nyuma na kupoteza nguvu kubwa ya umma? Nakusihi. Tukikutana tena, basi tambua, maisha ya mmoja wetu yatakuwa rehani. Au watu wa muhimu na karibu waliopo nyuma yetu,” alisema Jamila na kuanza kupiga hatua taratibu kuendelea na safari. Huku akiniacha nimesimama palepale kutafakari kauli zake.



    Dhahiri! Kazungumza yaliyo jadi yetu. Naamini kwa dunia nzima, kwa sababu sote ni binadamu tofauti yetu ni rangi tu. Daima, kama ewe ni muumini au mfuasi mzuri wa misemo haya hutoweza yakana.



    Nilitumia takribani dakika nne kusimama eneo lile. Huku nikimsindikiza kwa kuruhusu mboni zangu zirubuniwe na muonekano wa umbile la nyuma. Kwa kiasi, alikongoroka. Ila haikumfanya apoteze sehemu ya urembo aliobarikiwa. Alikuwa na urembo wa kuzaliwa nao. Urembo usiohitaji matumizi ya makemikali yaguse ngozi yake.



    Alivyopotea mbele ya mboni zangu ndipo nami nilichanganya nyayo zangu safari nakopaswa kufikia. Marangu shine! Nilifikia hapo. Kwa ajili ya mapumziko ya siku kadhaa kabla sijaendelea na ratiba zilizofuata.



    Usiku huu nao ukawa wa shida kidogo kwangu. Nilikuwa mwingi wa fikirio, kumchambua Jamila na kauli zake. Zilizonitatiza zaidi zihusuzo watu wa karibu, ikiwa na maana baba na shangazi.

    “Bado ana dhamira ya kuwatokomeza,” nilijisemeza kimoyomoyo nafsini mwangu.



    Asubuhi ya siku iliyofuata, vyombo vingi vilitawaliwa na habari zimuhusuzo Dkt Aman. Kwamba alikwishaaga dunia. Kwa risasi moja iliyoenda kuharibu mfumo wa moyo. Sikushangazwa. Kwa sababu nilifahamu, hilo lingetokea. Kilichonistaajabisha, Jamila kapatia wapi ujuzi wa kutumia bunduki. Tena kwa mazingira niliyomkutanayo ile siku, yanaonesha aliandaliwa kila kitu. Yeye akahusika kwenye upigaji tu, baada ya hapo akaacha bunduki palepale akaondoka zake.



    Kuna mtu mwingine nyuma yake!



    Nilipatwa na wazo hilo. Kisha nikaelekeza mbali kwa namna nilivyoamini nina ndoto ya kufanya mabadiliko pasipo kutambua kuna kitu kiitwacho njozi ambayo wengi hushindwa kutofautisha.



    Ya kwangu ilikuwa njozi kwa Jamila. Ya kumbadilisha toka kisabaluu kuwa mwanamke mwenye nguvu atayeheshimika na mtu wa aina yeyote. Sasa nikawa radhi, kwa kutoitimiza, na kuibadili akili kuweka nguvu kwa watu wangu wa karibu alionihadhari nao. Niwasaidie, ili waende kukomboa maisha ya wengi kwa msaada wa serikali. Kupitia mgongo wa rais Nahonyo. Ndivyo tulikubaliana kwenye ule mkataba niliosaini ile siku. Nimfanyie kazi yake, atanilindia wapendwa wangu kwa namna yoyote.

    “Watu wa aina ya Jamila, hawapaswi kuchukuliwa poa kwa kila wafanyacho. Lazima wahadhibiwe kujenga heshima. Hivyo sipaswi kumchekea chekea huyu mtu. Yanipasa nile naye sahani moja.”

    __________



    Kutengana na mtu aliyeko ndani ya fuadi huacha donda kubwa kwa sababu ya kushindwa kuruhusu usahaulifu. Inakuwa ngumu kumsahau. Ndicho kilichonitokea kwa Jamila. Alibahatika kuuteka moyo wangu. Moyo uliruhusu upendo dhidi yake japo si ule wa kimapenzi.



    Lakini, sasa ilinilazimu kuruhusu usahaulifu, ili nitimize hitajio. Kumwendekeza, ni sawa na kuhalalisha matendo atendayo.



    Nilikaa Moshi takribani muda wa wiki moja. Hadi vuguvugu la kifo cha Dkt. Aman kilivyopoa, ndipo nami nikafunga safari kurejea jijini Mbeya. Afya ya wapendwa wangu kilikuwa kitu cha msingi kukitambua kabla sijaendelea na ratiba zingine.



    Nilivyojiridhisha, wako imara, ratiba ikaendelea kama ilivyo ada. Kumuondoa Jamila. Ambaye sikufahamu baada ya kuondoka kule mjini Moshi kaelekea wapi.

    “Hapaswi kuchukua muda mrefu kuanzia leo,” ilisikika sauti ya rais Nahonyo. Ikipasua viwambo vya sikio pindi tukizungumza kwa njia ya simu.

    “Ila kuna mengi yanayo tatiza.”

    “Yapi tena?”

    “Yupo mwingine aliyeko nyuma ya Jamila.”

    “Kwa nini?”

    “Yeye ndiye alihusika na mauaji ya Dkt. Aman.”

    “Acha utani!”

    “Sikuongopei. Dhahiri, yule mwanamke ndiye kamuua. Mimi sikufanikiwa. Aliwahi kufanya shambulizi dhidi yangu.”

    “Hayo mafunzo kapatia wapi?”

    “Swali gumu kwangu. Kwa sababu sina jibu la kukupatia.”

    “Ndiyo maana awali, nilikwisha kuambia lazima auwawe. Kwa sababu yapo mengi ninayoyafahamu dhidi yake.”

    “Kama yapi tena?”

    “Mimi ndiye, nilikuwa jaji wa kesi imuhusuyo Jamila kipindi cha nyuma,” alisema Rais Nahonyo kisha simu ikakata.



    Nilivyojaribu kutafuta mawasiliano kwa mara nyingine sikufanikiwa. Mtandao ulisumbua, kiasi kwamba ukanifanya nighafirike na niishiwe nguvu nifanye jambo gani. Kumsaidia rais, ambaye alihusika kumweka Jamila katika mazingira magumu kutokana na uamuzi wake hapo awali. Ama nimsaidie Jamila. Niliyeaminishwa kuwa mbaya kwa jamii yetu, ilhali analipa kwa kile alichotendewa.









    Kauli ya Rais Nahonyo ilinipunguzia nguvu. Na kunifanya nianze kumuona ni mkatili zaidi ya yule waliyeniaminisha kuwa katili.



    Hata wapendwa wangu, ikabidi niwachukie. Yapo waliyonificha, si yeye tu. Hata afande Mzee na bwana jela. Msaada wao kwangu, ulikuwa na uponzaji mwingi. Heri ningelibaki na msimamo wa awali. Na nisingelipokea msaada.



    Hamna kitu kikosacho athari!



    Huu msemo nilikuja uamini hapa. Athari ya msaada wa rais Nahonyo kwa mgongo wa serikali ulijitokeza. Ina maana alinisaidia kwa lengo la kujilinda binafsi na si umma kama alivyonihadaa. Alitumia umma kama kificho. Na kama ilivyo kwa Jamila. Alivyoutumia u—kisabaluu kuficha kisasi chake.



    Nilivyokuja wakumbuka afande Mzee na bwana jela kwa lengo la kuwahoji kiundani, napo nilikwishachelewa. Sikuwakuta nyumbani. Si wao tu, hata baba na shangazi. Hawakuwepo tena nyumbani kwa bwana jela. Ikanipa walakini. Na kutengeneza picha hatarishi kichwani mwangu.

    “Nahisi mambo yashaanza kwenda mrama. Kuna baya linalotengenezwa kwangu,” nilijisemeza. Pindi nikiwa na mihangaiko ya kuzunguka huku na kule ndani ya vyumba mule ndani.

    “Wako wapi hawa?” nilijiuliza. Huku nikivuta rununu, kwenye moja ya mfuko wa suruali niliyovaa, niweze kuwasiliana nao nifahamu walipo.



    Lakini, hatua hii haikuwa na msaada kwangu pia. Kila namba niliyopiga, mtandao haukuonesha kutoka. Ilikata, kwa watu wote niliohitaji kuwasiliana nao. Nikarudi kumtafuta Rais Nahonyo kwa mara nyingine, naye sikufanikiwa kumpata. Mara hii si kama mtandao ulisumbua, bali kila nilivyojaribu kupiga nilijibiwa kuwa namba haipo.



    Baadaye nilipoteza imani na nyumba niliyopo pia. Ikanilazimu kupiga hatua kwenda kuwauliza majirani kama wana chochote walichokiona juu ya kutowepo kwa niwatafutao. Nikapandisha jazba na mori ya utambuzi. Nikapiga hatua kwa kasi. Nilivyoifikia sebule pindi naelekea lango la kutokea, nikakuta kikaratasi kidogo kilicho na maandishi mezani. Kimezuiliwa na kitako cha bakuli lililobeba maua ya urembo.



    Nikasogeza pembeni na kuvuta kile kikaratasi. Kwa uharaka, niliokosa ubashiri wa muda nilitumia, nikapepesa mboni hadi kwenye maandishi machache yaliyoandikwa kwa wino wa bluu.

    “Naomba tusamehe mwenetu.” Ndiyo maneno niliyokutana nayo. Na kunifanya niwe na shinikizo la kutambua chanzo cha msamaha.



    Baada ya hapo nilipiga hatua hadi moja ya nyumba jirani. Kwa bahati, nilifanikiwa kumkuta mwenyeji. Nikamsalimu, kisha nikaenda moja kwa moja kwenye hitajio.

    “Wazee wako wameondoka muda mchache uliopita. Na gari aina ya Toyota IST yenye rangi nyeusi,” alisema jirani.



    Jibu lililozidi kuniweka mshangaoni kuhusu kiendeleacho.

    “Rais Nahonyo kanizunguka. Kaenda tofauti na yale makubaliano. Yote, kwa sababu ya hofu kuhusu hadithi aliyonieleza,” nilijisemeza. Taratibu nikiondoka nyumbani kwa yule jirani.



    Hatua tano toka nyumbani kwa jirani simu yangu ikaita. Nikaitoa nilikoihifadhi, nikaangalia jina la mpigaji, nikaona namba ngeni.



    Kidogo, ikanipa ulizo. Nipokee ama lah! Ulizo lililochukua sekunde chache kisha nikapata uamuzi wa kipi nachopaswa kufanya.



    Nikapokea!

    “Unachopaswa kukaa kimya. La sivyo, familia yako itaenda kupatwa na tatizo,” ilisikika sauti ikichana vyema viwambo vyangu. Sauti ya Rais Nahonyo. Tena ikizungumza kwa mkazo kana kwamba nina u—hatari mkubwa kwake.

    “Lakini kwa nini umeenda tofauti na mkataba tuliosaini?”

    “Nimeona una kila dalili za kwenda tofauti mara baada ya kukufahamisha kwa uchache uhusiano uliopo baina yangu na Jamila,” alisema kisha akakata simu.



    Kauli zake zilikuwa kama onyo. Nifunge kingo za mdomo wangu kuhusu kitu chochote kimuhusucho. La sivyo atafanya chochote kuhakikisha ananidhibiti. Nikajikuta nimeduwaa. Akili ikalala kwa muda, kuja kuzinduka, ilinichukua dakika moja, mara baada ya kupigiwa honi ya gari kwa nguvu.

    “Inaweza ikawa, naye alipita kwa Jamila,” nikajisemeza, huku nikisogea pembezoni mwa barabara kupisha ile gari.

    __________



    Haya ndiyo maisha tuishiyo. Tumetawaliwa uficho. Ilhali mboni zetu huonesha mng’aro uvutiao. Mng’aro huu ndiyo huficha yasiyopaswa kutamkwa. Ama kufanyika kwa namna yoyote.



    Hii ikanifanya nihakikishe kauli za shangazi kuwa sahihi. Na zitaendelea kuwa sahihi kila uchao. Na kupata nyongeza. Ukatili, roho ngumu ndiyo mwanzo wa mafanikio ya wengi. Hivyo kuipata amani ya kweli itakuwa sawa na njozi ya mchana.



    Baada ya kuondoka kwenye uga wa nyumba ya jirani nilikoenda kupata msaada wa ufahamu nilifunga safari hadi Mwanjelwa. Sehemu kubwa ya safari nikiwa nimetawaliwa mawazo tele. Hasa ya jambo nalopaswa kufanya kwa wakati huo ili nijitengenezee uhuru. Uhuru wa nafsi utaoniweka huru na matatizo yasiyo na msingi. Maana matatizo ya ufichoni huumiza kuliko yale ya wazi.



    Mwanjelwa, niliishia kwenye moja ya banda la uuzaji magazeti. Nikanunua gazeti moja, kisha nikaweka tuo kwa minajili ya usomaji kwenye benchi karibu tu na banda la uuzaji.



    Nilivyoingia shauku ya kufunua kuanza kusoma, taarifa ya mchuuzi wa magazeti ikanisitisha.

    “Eh! Bhana eh! Kuna watu wameuwawa huko kinyama,” alisema. Akiwahadithia baadhi ya wanunuzi waliozingira meza kupangusa ubongo kwa ajili ya kupata yaendeleayo nchini.

    “Wapi tena?”

    “Maeneo ya Nanenane hapo. Kuna ki—IST kimeshambuliwa kwa bunduki watu wote waliomo ndani wameuwawa.”



    Nikashtuka! Na kusimama. Kisha nikatega sikio kwa makini kusikia anenacho.



    Chap! Nikapeleka fikra kuwakumbuka baba na shangazi. Yumkini ni wao. Ndiyo wameshambuliwa, hisia zilizonihimiza nifike eneo la tukio muda huohuo nijionee ukweli wa jambo.



    Kwa uharaka, nikatafuta usafiri utaonifikisha Nanenane. Kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani. Tukio likiwa limefanyika mita chache toka hapo. Nikapata daladala! Nikaingia ndani ya gari, safari ilivyoanza moyo ukapata nafuu ya hofu kwa kufikiria picha ya tukio nitayoenda kukutana nayo.



    Juu ya simama simama ya gari kwa ajili ya kuteremsha na kupakiza abiria, lakini tukafanikiwa kuwasili ndani ya muda. Nikateremka. Na kutafuta uelekeo wa tukio ulipo.



    Hapo niliishughulisha miguu yangu. Moja, mbili hadi eneo husika, ambapo nilikuta mambo bado yako moto kwa watu kuingiwa na shauku ya ushuhuda wakasambaze vyema maneno waishiko.



    Nami sikujiacha nyuma. Nikakatiza katikati ya watu nifike mbele nijionee kwa uzuri. Lakini sikufanikiwa. Hatua saba tu, za kutafuta nafasi ya kupita, nikajikuta navutwa shati toka nyuma. Nilivyogeuza macho kumuangalia ni nani. Mboni zangu zikagongana na sura ya Jamila.

    “Nifuate,” alisema. Huku akiendelea kunivuta nisipingane na kauli yake.



    Sikuonesha ubishi. Niligeuza kumfuata. Tukapiga hatua hadi nje kidogo ya kusanyiko la mashuhuda tukasimama. Kikapita kimya kifupi, takribani sekunde kumi na tano ndipo Jamila akafungua kingo za mdomo kunena yaliyo nafsini mwake.

    “Inabidi tuungane. Kumteketeza aliyefanya hivi,” alisema Jamila, mboni zake kanitumbulia mithili ya mtoto aliyefika kunako mchezoni.

    “Kwa nini?”

    “Wana serikali wamefanya yao kwa wazazi wako.”

    “Eti?”

    “Eeh! Ni wao. Kama utahitaji kuafiki ombi langu, hii ni kadi ya mawasiliano, nitafute tutawasiliana,” alisema Jamila huku akinikabidhi kadi paswa.









    Nikapokea, kisha akatokomea eneo lile kama moto wa nyika.



    Hakika! Waliopatwa na tukio walikuwa wazazi wangu. Kweli, ni wao. Walifariki, palepale, chanzo kikiwa shambulizi la risasi.

    “Ina maana Rais Nahonyo ana watu wengine awatumiao kufanya uovu?” nilijiuliza, baada ya kutambua afande Mzee na bwana jela nao wameshambuliwa.

    “Kama kawaida yake ni hivi, si hata huyo mtu akimaliza jukumu alilokabidhiwa si atauwawa?” niliendelea kujiuliza. Na kujaza fikirio namna tukio lilivyotendeka.



    Sikuwa na jinsi. Zaidi ya kuruhusu umivu litawale mwili wangu. Kuanzia siku ya tukio hadi pale walipofanikiwa kuhifadhiwa kwenye jumba za milele.



    Wakati huo wote niliamini Rais Nahonyo ndiye kafanya tukio hilo. Ikiwa ni njia ya kunionesha uwezo wa nguvu alionao. Huku akisahau nyadhifa alizonazo ni kitu tu cha mpito. Ule msemo kuwa kuna maisha mengine baada ya kile ukifanyacho kwake aliona hauna mantiki.



    Umivu lilivyopotea ndipo nikamkumbuka Jamila. Nikafanya jitihada za mawasiliano, nikafanikiwa, na baada ya siku kadhaa nikaenda aishiko. Sikumbuki jina la mtaa vyema, ila nakumbuka vichochoro nilivyokatiza hadi nyumba aishiyo.



    Nilivyowasili langoni. Lango la kuingilia ndani ya jengo nikapokelewa na maongezi. Maongezi ya Jamila na mtu wa upande wa pili, ambaye alikuwa anawasiliana naye kwa njia ya simu.



    Nikasita kwa muda. Nikatega sikio na kuvuta azungumzayo. Alikuwa anazungumza maneno makali mno. Yaliyonichoma na kunifanya niketi chini pasipo mapendo. Akili ikafubaa kwa muda. Hata nguvu, nazo zilitoweka kwa kasi huku ubaridi ukichipua.



    Kwa wakati ule, ningeliambiwa niuwe sisimizi nisingeliweza. Kwani nguvu hazikuwepo kabisa. Nikahisi upoozi unaninyemelea.

    “Kiongozi. Nishatekeleza vyema majukumu yangu. Wale watu tayari washazikwa sasa nimebakiza mtu mmoja tu. Rais Nahonyo. Mwanaume aliyechangia dhulumio la haki yangu mahakamani. Akishirikiana na mzee Namahala japo walikuja tengana baadaye kwa sababu ya maslahi. Na nakuhakikishia lazima nimuuwe. Japo anatumia mwavuli wa serikali kuficha mabaya yake.



    Nikupe uhakika, wote walioshiriki dhuluma ya haki yangu angali niko mdogo lazima nile nao sahani moja.”

    “Sasa mbona umewauwa wazazi wa Abdul?”

    “Hawa niliona wanaenda kushirikiana na huyu mzee. Ndiyo maana imenilazimu niwaondoe mapema kabla hawajakomaa kuwa watumwa wa fikra za mtu. Niliona picha zote za hawa watu kutumika kumsafisha yule mtu.”



    Niliisikia vyema sauti ya Jamila. Ila kwa yule aliyoko upande wa pili sikuitambua. Kwa sababu ya ungeni ndani ya viwambo vyangu. Ilikuwa mara ya kwanza kuisikia.

    “Huyu ndiye kawauwa? Mbona ile siku ya tukio alijikomba sana kwangu? Ama lengo ni kuficha hili?” nilijiuliza. Maswali niliyokosa jibu, na kunipandisha hasira.



    Ilinichukua takribani dakika mbili ndipo nilianza rudiwa na nguvu kwa uchache iliyonisukuma niamke pale nilipoketi na kupiga hatua hadi ndani. Bado nilimkuta akiendelea kuzungumza. Ila alivyoniona tu, akakata na kunitumbulia macho mithili ya mwana mkiwa.



    Tukaishia kutazamana!



    Kwa muda mrefu tu, kila mmoja akikosa neno la kumwambia mwenziye.

    __________



    Uchungu ukanipanda kwa kasi. Mtu aliyeko mbele yangu hakuwa rafiki tena kama nilivyojiaminisha. Alikuwa adui nambari moja. Aliyechangia nishindwe kuangalia maisha binafsi yatakuaje.



    Hakika yangu. Haya ndiyo malipo wapatiwao wengi watendao mema kwa watu wenye chembe za uovu. Wachache sana hupata malipo yenye uridhisho. Jamila ni mmoja miongoni mwa waabudiao dhana hii.

    “Yakupasa uwe jasiri. Ili uweze kukabiliana na hatari yoyote iliyoko mbele yako. La sivyo, kamwe hautokuja kufanikiwa,” nilipata kumbukizi. Moja ya kauli alizowahi niambiaga shangazi awali. Shangazi Janeth. Ambaye alibadili dini kwa ufanikishaji wa dili zake. Katika makabiliano ya ulipizi wa kisasi.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ikanibidi nianze kupambanua hatua nayopaswa kuchukua dhidi yake. Kila niliyoifikiri nikaiona haiko sawa. Kwa sababu niliona kama najiingiza matatizoni kwa kujitakia. Ilhali sikuhitaji, kwa wakati huo. Nilichohitaji niwe mwana amani, sikutaka shari ikiwa hatua ya kuelekea kutengeneza maisha yangu ya baadaye.



    Nikiwa katikati ya fikirio nikashtushwa na msukumo wa ghafla uliofanywa na Jamila. Alinisukuma, kupitia kiwiko cha moja ya mkono wake. Nikapepesukia pembeni kidogo, karibu nianguke, ila nikajidhatiti kwa kujishikiza sofani.



    Nilivyokuja kukaa sawa nikawa nimesalia pekee ndani. Jamila alikwisha toka na kupotelea nje. Nilivyopiga hatua kwenda kumuangalia, niliambulia patupu. Kila pande niliyoangalia nilikutana na nyuso za wengine tofauti na ile niliyotaraji.

    “Kaenda wapi?” nilijiuliza. Taratibu nikikatiza hapa na pale pasipo mafanikio.



    Swali hili, likawa desturi kwangu. Kwani toka siku ile, sikubahatika kumuona Jamila. Wala kuwasiliana naye. Mawasiliano niliyokuwa naye kumuhusu hayakupatikana, na nilivyobahatisha kutembelea vijiwe alivyokuwa anapenda kufanyia biashara sikufanikiwa kupata habari zake.

    “Huyo mtu kwa sasa hayupo hapa kijiwe. Ni muda mrefu tu, kiasi kwamba hata shoga zake washatengeneza hofu dhidi yake,” nakumbuka nilishapata jibiwa hivi. Na moja kati ya watu aliokuwa anafanya nao biashara.



    Huo ukawa mwisho baina yangu na Jamila. Hatimaye zikakatika siku, hadi panapo miezi. Zaidi ya saba, ndipo nikaja pata taarifa zake, za kuhusika katika shambulizi la rais Nahonyo. Shambulizi lililotokea mjini Tunduma, pindi rais Nahonyo akifanya mkutano na wananchi wa mji huo.



    Ukurasa wa Jamila nikaufunga hapo rasmi. Urahisi wa sababu zake ulinifanya nimuone mtetewa japo hakustahili. Hadhi. Ile niliyohitaji kumtunuku nikaiondoa na kujenga picha ya usawa wa tabia.



    Hapa niligeuka muathirika wa kuamini jambo pasipo uthibitisho. Mafundisho ya shangazi niliyasahau, nikajaza mengi ya vijiweni. Yatamkwayo kwa uhitaji wa kufurahisha genge, na kujikomba kwa ujuaji wa mengi yasiyo na chanzo sahihi cha habari.

    __________



    Ndugu wasikilizaji, haya ndiyo machache niliyopitia maishani mwangu. Msemo wa wanaume tumeumbiwa mateso, kwangu ulichukua nafasi. Nilionesha uhodari kama tunavyoamriwa kwenye vitabu vya dini, lakini mlengwa hakutambua. Yumkini moyoni mwake alikuwa na utofauti mkubwa juu yangu ila mimi sikumuelewa.



    Hadi leo hivi, sijajua yeye ni mtu wa aina gani. Hasa nikikumbuka mauaji aliyoyafanya kwa wazazi wangu. Kisa tu, anachukia umma kwa kushindwa kumpigania pindi anapoteza haki utotoni.



    Sijajua ni umma wa namna gani alihitaji wampiganie. Kwamba mamia ya watu? Ama mtu mmoja. Na kama ni mmoja, mbona mimi nilijitolea halafu akashindwa kutambua juhudi zangu? Au dhamira ya moyo wake ulishakithiri kisasi, hivyo hayo mengine aliyaweka wazi kwa kutaka kuficha hili?



    Wapo wengi kama Jamila duniani. Na naweza sema, kila mtu ni kama huyu kitabia. Endapo tunaamini misemo. Vilevile hata kama hatuamini misemo. Kwa sababu ya uumbaji wetu. Sote ni binadamu. Hakuna aliyekamilika. Hivyo makosa ni jadi yetu.



    Ila. Jadi hii isiwe kinga. Ya kujilinda, kwa imani ya kukosa bahati ilhali umetenda kwa makusudi. Nasaha hizi, zifike kwenu. Na yule niliyekosa kupata uwakilishi wake. Yule aliyefanya ndoto yangu kuwa hayawani.



    Nathubutu, kusema. Nilipoteza ndoto yangu. Ila inaweza kuendelea endapo atafanikiwa kupata ujumbe huu na kunijibu. Daima huaswa, tusikate tamaa. Hivyo nami sijakata tamaa. Hakika yangu, ipo siku huko alipo atainuka na kujionesha yupo.



    Tena atajitokeza kwa muonekano safi tofauti na ule niliouzoea. Atakuwa msafi, mwenye kila jema, huku akiwa kinara wa upingaji wa kile alichokuwa anatenda awali.



    Mabadiliko, kwake ni muhimu. Na wote wenye tabia kama zake ama wahitajio kuwa kama yeye. Ila endapo lengo letu ni kuhalalisha uovu, basi haina haja ya kukesha majukwaani kutapika maneno yanayonasibu amani.



    Nikuite nani? Nairejea kauli hii, na kuitengeneza kuwa utambulisho. Si kwake tu, na watu wote wa namna yake. Pia kutoa tahadhari, tunapaswa kuwaangalia kwa jicho la tatu. Jicho kodo, lisilo na ulegevu tuweze kunyoosha.



    Nanena haya, kwa kuwa naihitaji amani. Ya nafsi yangu na wote. Ijapokuwa ni jambo ngumu kuja kutokea. Tukitengeneza amani za nafsi zetu, migogoro ya kila uchao itakoma.



    Vurugu hizi, hazina msingi. Hasa zipelekeazo upotevu wa uhai wa maisha ya watu wasio na hatia. Tujenge tamaduni, ya kuvaa huruma juu ya matatizo ya wenzetu. Lakini yasiyo ratibiwa makusudi na mtu aliyekumbwa. Ila kwa mtu aliyeundiwa, hatuna budi kuunganisha nguvu zetu na kutengeneza mseto.

    __________



    Ukimya ukapita kwa muda, mfupi tu. Huku Abdul akiivua miwani yake, akapikicha macho kisha kuirejesha. Wasikilizaji, wakawa bado wanashauku ya ufahamu kama historia inaendelea ama inaishia hapo kutokana na nasaha alizozitoa.



    Kipindi cha subira kama kuna endelezo hakikukosa kuambatana na nong’onong’o. Wengi, walipiga kwa yale waliyoyasikia na kuingia vilivyo nafsini mwao. Historia iliwakosha. Kupitia huzuni na msisimko mchache uliojitokeza ndani yake.

    “Dah! Jamaa mvumilivu sana. Anastahili kutunzwa.”

    “Na ana kila sifa ya kuwa mwanaume. Koromeo lake linadhihirisha kiasi cha uvumilivu alichonacho. Si unaona namna lilivyomtoka?”



    Ni machache kati ya mengi yaliyosikika toka kwa wasikilizaji. Abdul alivyorejea kwenye ukawaida ikawabidi watulie. Baada ya hisio la mwendelezo walilomuona nalo. Hasa baada ya hangaika yake ya muda ya upangaji wa karatasi alizoandikia historia ahadithiayo.

    “Ndugu wasikilizaji, katika machache niliyohadithia, lipo la mwendelezo. Ambalo nililifuata, kama sio lilinifuata lenyewe. Hivyo tuendelee kuwa wavumilivu pindi tukielekea kwenye hitimisho la zoezi letu.”

    __________



    Baada ya kukaa kwa muda mrefu hadi panapo miaka tano maisha yangu yakaanza kubadilika. Badiliko kidogo lenye unafuu. Kwani nilijihangaisha huku na kule hali iliyonineemesha kwa riziki za kusongesha maisha.



    Shughuli kuu, niliyohangaika nayo kwa kipindi hicho ni u—kuli. Muda mwingine kazi za usafi wa sehemu za biashara za wafanyabiashara mbalimbali ili mradi nipate shilingi. Za ununuzi wa chakula na mavazi ya mitoko kwa baadhi ya siku. Suala la makazi, halikuwa shida. Nilikuwa naishi nyumbani kwa shangazi. Pale nilipokuwa naishi awali.



    Baadaye nikaanza sumbuliwa na hisia. Hisia za ki—utu uzima zioneshazo urijali wangu. Nikatamani, kama sio hitajio. Ipate tokea siku nipate mwenza. Si wa kuoa kwa siku hiyo. Bali wa kuelekea kwenye uoaji pale tutapoendana.



    Hangaiko likanivaa!



    Mithili ya kijana aanzaye balehe. Kila msichana apitaye niliona halali yangu. Hivyo nikawa naita sana pasi na mpangilio, hadi nikatengeneza kero kwa waitwa. Laiti kama wote niliowaita wangelikuwa wanaishi mtaa mmoja wangelikuwa wanahadithiana namna niwasumbuavyo.



    Mafanikio lazima huyahangaikie!



    Nilitii kauli hii na kujipa moyo wa kuifanyia kazi. Hakika nilifanya kazi ya ziada. Ilyonichukua siku nyingi tu, ndipo mwanga wa mafanikio ukaanza kujitokeza.



    Ijumaa. Saa kumi na moja jioni, ndipo nuru ilianza kutapakaa taratibu moyoni mwangu. Punde, windo la uitaji lilivyotiki kwa moja ya wasichana niwaitao. Scolastica! Ndivyo alivyonitambulisha yule dada, mara baada ya kumtupia swali lenye lengo la utambulisho.



    Ni msichana mzuri. Avutiaye, na aliyebarikiwa kila sifa ya urembo. Japo hakukosa kasoro ndogondogo. Kwangu, kasoro zake sikuziona kwa uharaka. Na niliamini, Mwenyezi Mungu kamkamilisha, hivyo ile dhana tuaminiayo kuwa hamna binadamu aliyekamilika kwake niliipuuza.



    Kidume sikujiacha nyuma. Suala la tafakari sikulipa nafasi. Nililipotezea, hisia zilinikithiri. Na kunipa ushinikizo wa kutamka nilichonacho pasi na kuchelea. Hofu ya ugonjwa nayo niliiweka kando, nilitanguliza matokeo ya starehe ambayo uzuri wake niliufahamu kupitia stori za vijiweni. Tena nilivyokumbuka jitihada za kila leo zihusishwazo na umalizaji wa kutokomeza ugonjwa sugu utetemeshao wengi, ndiyo nazidisha morali ya kutupa neno.

    “Kinga na tiba iko njiani yaja,” nilijisemeza, wakati huo tumetawaliwa na ukimya, baina yangu na Scolastica uliochukua takribani dakika mbili.

    “Hupaswi kuwa na hofu dhidi yangu. Kwani hamnaga mahusiano yafikiayo kuiva tu, pasipo kupitia hatua hii ya leo. Niamini. Kwa muonekano na kauli pia. Kauli zangu ni zenye uaminisho wa tendo, hazina chembe ya uongofu wenye kukupa shaka, hakika! Nakupenda,” ilikuwa moja, miongoni mwa kauli nilizotupa kwa Scolastica, akiwa kasimama mbele yangu. Jicho la aibu likimtawala hadi nikahisi maneno yamemkuna na kumpa msisimko fulani mwilini mwake. Kwani, baadaye nilimuona akikenua kingo za mdomo zilizozalisha tabasamu kisha akatoa neno.





    “Una maneno mazuri, matamu yaliyojaa ushawishi wenye kuvuta kwa wepesi. Litakuwa jambo la heri kama na matendo yako yanaendana na utamkacho,” alisema Scolastica. Kauli ambayo ilinipa mwanga na ufunguzi kwa kiasi kidogo, kwamba sina uhitaji wa kutumia nguvu kubwa ya bembelezo. Kwa sababu tayari moyo wake ushaanza kunielewa.



    Kweli! Siku kadhaa baadaye Scolastica akawa mpenzi wangu. Tukaanza mahusiano, tena kwa nguvu sana hadi ikawa kero kwa majirani pale niishipo.



    Raha ya mahusiano yetu ilikuwa inapatikana nyumbani pekee. Pasipo kujali muda, kila ninapohitaji nilijitwalia chakula. Hakuwa mchoyo. Labda, apatwapo na tatizo, ndipo tutapata mapumziko, zaidi ya hapo, kazi yetu ni kunoa tu makali. Usipatikane ubutu.

    “Ama kweli nimekawia kufaidi mengi yenye utamu hapa duniani,” nilisema, Scolastica kaegesha kichwa juu ya kifua changu, moja ya mkono wake akifanya papaso la hapa na pale lililoniacha na msisimuko uliokosa kipimo.



    Scolastica aligeuka sehemu ya faraja maishani mwangu. Nikamtunuku na wadhfa kuonesha kiasi cha umuhimu wake. Ishara tosha ya kumthibitishia nilichozungumza awali pindi tunaanza mahusiano sikuzungumza kwa lengo la kujifurahisha ama kumfurahisha. Kwa kiasi fulani, niliamini yeye ndiye atayeziba pengo la kiasi cha furaha nilichopoteza mara baada ya kuwapoteza wapendwa wangu.



    Si kwa tabia, bali hata kwa umbile lake. Vilinisahaulisha machungu niliyopitia. Maana…si kwa madoido na maufundi niliyojionea. Ijapokuwa wana vijiwe hunena, mtu mwenye ufundi mwingi, basi kafanya mazoezi mengi. Ama ile inenayo wanawake wote ni sawa. Wana akili finyu. Sikuzitilia maanani. Kwa sababu, nishawahi jionea, moja ya kijana wa kiume akitamka kauli hizo huku wiki inayofuata ana zoezi la kufunga ndoa.



    Kinachonishangaza, wapo wasomi pia. Wengi tu, wakeshao kueneza dhana hizi kiasi kwamba napata ulizo, yeye kazaliwa na nani? Upi umuhimu wa kusherehekea siku ya mwanamke kwa kumtukuza mama huku ukiwa muumini wa zana nilizozitamka?



    Dhana za misemo nilizikana. Hasa ziletazo ubaguzi na unyanyasaji wa kijinsia.

    Kadri siku zilivyozidi kusonga mbele ndivyo uhusiano wetu ulivyozidi kuchipua na kuimarika. Mpaka akaja pata ujauzito. Uliobadilisha historia ya maisha yangu kwa kuwa baba kijacho.



    Furaha ikaongezeka maradufu. Kana kwamba mimi ndiye mwanaume pekee shababi. Ujauzito ulivyofikia miezi sita akahamishia makazi nyumbani. Na kugeuka rasmi mama wa nyumba ijapokuwa taratibu za kuhalalisha mahusiano angali bado.



    Jumatatu. Asubuhi ya saa kumi na mbili, kama ilivyo ada nilielekea kwenye shughuli zangu. Siku hii niliondoka na uchovu. Uchovu mwingi ulionipa hata ushawishi wa kutokwenda kazini kwa kuhofia sitofanya kazi kwa ufasaha unaotakikana.



    Ila nililazimika, kwa sababu sikuwa na kiasi chochote cha pesa kitachotuwezesha kupata mlo. Ningelikuwa pekee, insingelinipatia tabu. Ningelipitisha siku, lakini Scolastica, alinifanya nitambue umuhimu wa kutafuta. Ukizingatia na ugeni ujao, ndiyo kuzidi. Ilinibidi kuwa mtafutaji haswa. Nisipoteze heshima yangu na yake kama wanafamilia.



    Sikuhitaji akongoroke kwa namna yoyote juu ya uzao wake.



    Juu ya mvutano wa kwenda au nisitishe safari, mwishowe nilipiga moyo konde na kujisogeza kijiwe. Bahati iliyoje, mapema tu baada ya kuwasili nikapata ulaji. Wa kuteremsha gunia za viazi toka kwenye moja ya lori iliyotoka shamba. Kazi niliyofanya na wenzangu watatu na kufanya jumla kuwa wanne.



    Haikuwa kazi nyepesi. Ilikuwa ngumu na nzito. Kwani ilituchukua zaidi ya saa tatu kumaliza. Baada ya hapo tukapata ujira wetu kisha nikaondoka zangu. Sikuona haja kuendelea kuwepo, angali afya haikuwa poa sana. Kidogo nilichopata nilijiaminisha kitakidhi mahitaji yetu kwa siku kadhaa.



    Mwendo ukawa wa taratibu. Kama niliotembea asubuhi hadi nilivyofika nyumbani. Ambako nilipokelewa na ukimya ulionipa shaka. Kutaka kufahamu kulikoni, nilipaza sauti kumuita Scolastica, lakini wito wangu haukuitikiwa ishara iliyonitanabaisha hayupo ama yuko chumbani kalala. Au sehemu ya jirani ambayo sauti niliyoitoa haijamfikia.



    Sikujalisha sana. Nikapiga hatua hadi chumbani kujihakikishia. Ila matokeo yakawa tofauti na nitarajiayo. Scolastica hakuwepo. Nyumba ilikuwa tupu, hali iliyonipa ulizo la ufahamu.

    “Kaelekea wapi?” nilijiuliza, nikiwa natupa macho huku na kule kwa usaili zaidi wa mazingira mule chumbani.



    Angaza yangu ikawa yenye manufaa. Nilivyopiga jicho kitandani nikakutana na picha nyingi za mnato, sambamba na karatasi zilizoandikwa jumbe mbalimbali. Shauku ikanikimbiza kwenye picha. Nikazikwapua kwa wepesi na kuanza kuangalia moja baada ya nyingine.



    Nikashikwa na butwaa!



    Nilivyoifikia picha ya tatu. Ilikuwa picha ya mtu ninayemfahamu. Akiwa katika mavazi ambayo daima namuhasa Scolastica awe anayavaa sababu humfanya azidi kuonekana mrembo. Hata nilivyoendeleza picha zingine, zilikuwa za yuleyule ninayemfahamu. Ikanipa tabu, kama si kuongeza mashaka.

    “Hawa wanafahamiana?” nikajiuliza. Mboni zangu nimezitumbua kuelekeza pichani.



    Kabla sijapata hitimisho, nikashuhudia mlango wa chumba nilichopo ukifunguliwa, likaongoza kutokeza tumbo na baada ya muda ndipo wajihi wa muhusika ukajidhihirisha. Scolastica!



    Naye akapatwa na mshituko wa ghafla alivyoniona nimekamatia zile picha mkononi. Niliuona mshituko wake, lakini akawa mahiri wa kuupoteza kwa haraka.

    “Kipenzi changu, pole na majukumu,” alisema na kunipa kumbatio la tabu. Huku akizitupa zile picha mkononi mwangu.

    “Lazima niufahamu ukweli wa hili,” nilijisemeza. Akili ikenda mbali kwa tafakuri. Mbinu nitayoitumia kuufahamu ukweli.

    “Nimerudi mapema mpenzi wangu, kwa sababu nime—miss kukuona ukiwa mtupu…” nilisema baada ya kukumbuka jambo. Yule nimdhaniaye ana doa sehemu fualani ya ngozi yake ambayo mara pengi huzuiliwa kwa mavazi.

    “Ina maana unahitaji penzi langu ilhali nina ujauzito mkubwa hivi?”

    “Sahihi.”

    “Abdul, si nishakupa taarifa, kwa hii miezi niliyofikia sipaswi kufanya mapenzi hadi nijifungue na nitavyokuwa sawa kiafya hapo baadaye?”

    “Natambua hilo. Lakini hisia zimenizidi,” nilimuongopea.

    “Aaah! Hapana. Siko tayari kufanya hilo jambo.”

    “Mmmh!...hata ukibana, lazima nifanye kila ghururi nifanikishe nitakacho,” nilijisemeza kimoyomoyo, huku nikimtua na kunyanyuka pale kitandani.

    __________



    Kituo cha ondoko langu mule chumbani lilikuwa nje. Nikaenda kuketi kwenye gogo fulani lililo jirani na nyumba kisha nikaanza upya kutafakari kuhusu zile picha. Hasa kuanzia ya tatu na zilizofuata. Zilikuwa picha za Jamila. Jamila Namahala! Akiwa katika mitoko ya aina tofauti tofauti.



    Kilichonifanya niwe na tafakuri, iweje picha zake ziwe mikononi mwa Scolastica? Ama Scolastica ndiyo Jamila? Au wana undugu?

    Nilikesha kujiuliza pasi na jibu.



    Kidogo! Amani na furaha iliniponyoka. Naanzaje kuwa na amani kwenye utata wa utambuzi?



    Sauti ya Scolastica ndiyo ilinishtua toka kwenye lindi la tafakuri. Iliyonitaka niende ndani nikapate chakula. Nikafanya hivyo. Huku nikijivika uchangamfu kana kwamba sina linitatizalo.

    “Kama ni Jamila, nitakuwa na nguvu ya kumfanya jambo gani ikiwa kabeba damu yangu?” nilijuliza. Taratibu nikirusha miguu yangu huku na kule kupiga hatua za uharaka kusonga mbele.

    “Karibu chakula mpenzi wangu,” alisema, pindi nilivyoufikia uwanja wa maakuli.

    “Ahsante. Ila naomba tukapate maji kidogo kwa ajili ya kuondoa jasho ndipo tuje kula.”

    “Hee! Chakula si kitapoa?”

    “Haina shida. Si unakumbuka, tangu tuwe na mahusiano hatujawahi oga pamoja? Hivyo ni vyema leo tufanye zoezi hilo ishara ya kuongeza uchangamfu katika uhusiano wetu.”



    Kauli yangu ikampa uzito wa maamuzi. Akaishia kunitumbulia macho na kuzalisha ukimya nisioutaraji.

    “Leo umekuwa na mabadiliko. Nini tatizo?” aliufukuza ukimya.



    Kutokana na ukimya alioutengeneza nikapata dhanio dhidi yake. Kahisi jambo. Kupitia zile picha. Hivyo kabla sijamjibu, alikenua kingo za mdomo akaendelea kutokwa na kauli.

    “Zile picha ndizo zimekufanya uwe hivyo? Unamfahamu yule dada? Kama unamfahamu, si ungeliniuliza iweje nina picha zake?” ilikuwa kauli iliyojaa maswali. Niliyoshindwa nianze kujibu lipi.



    Naam! Zile picha ndizo zilinifanya niwe nilivyokuwa kwa wakati huo. Ila sikuhitaji kuweka bayana. Nilijitia ukomavu kwa kukana, ilhali wajihi ukiniumbua kwa uhalisia nilionao moyoni mwangu.

    “Huyu ndiye Jamila. Lakini mbona ana muonekano wa tofauti?” nilijiuliza, huku nikivuta kumbukizi ya kupambanua maungo yake. Kuanzia yale yaonekanayo kwa uwazi, hadi yazuiliwayo. Ijapokuwa, yazuiliwayo sikuwahi yaonaga kwa muda mrefu.



    Sikukosa utata wa uhakika. Kilichonitatiza, ni rangi na umbo kwa kiasi fulani.

    “Yumkini kafanyiwa upasuaji wa kubadili muonekano wa sura. Ila, ana uwezo gani wa kumudu gharama za upasuaji?” niliendelea kujiuliza. Akili ikiendelea kupambanua mbinu nitayotumia kujihakikishia niwazayo.



    Nilikuwa na njia moja tu. Ya kumshawishi awe mtupu nijionee sehemu moja ya paja la mguu.



    Nilihitaji nimuone sehemu hii, kwa sababu, nilikwisha karirigi sehemu moja ya paja lake, ile siku alivyonitolea radhi kwa kuniruhusu nijionee maumbile aliyobarikiwa. Moja ya paja. Hasa la kushoto, lilikuwa na kovu, lililonibainisha kakua nalo. Lipo tangu utoto wake.

    “Kama kajifanyia mabadiliko, hawezi kubadili muonekano wa maumbo yote. Kule uliko mji wa dhahabu lazima kuwe kulivyo mwanzo,” nilijisemeza, taratibu nikimsogelea alipo. Nikamkamata mkono na kumshinikiza tuelekee chumbani.



    Mbano niliompatia hakuweza kufurukata. Japo hakuacha kuleta usumbufu wa hapa na pale. Wa kutaka ajiondoe mikononi arudi uwanja wa maakuli.

    “Nahitaji kuoga nawe muda huu,” nikapaza sauti, nikiwa nimemtua kitandani huku nikitweta kwa hofu. Kutokana na nguvu niliyotumia pindi namshinikiza tuongozane.



    Ubabe ukaanza kutumika. Kwani Scolastica hakuwa mwepesi wa kutoa mavazi yake. Nikaanza kuhusika katika uchojoaji. Pasi na ridhaa yake. Nilimvua. Huku nikiambatanisha kauli za kimyakimya zenye kashfa kumuhusu.



    Akili ikalala kwenye uvuaji. Nikakosa fikra ya upande wa pili. Kwamba anaweza kufanya jambo.



    Na ndivyo ilivyokuwa !



    Pindi nahangaika kumvua, mwenzangu akakamata kitu kifananacho na kisu akakielekeza tumboni mwake.

    “Niache!” alipaza sauti na kuweka tuo, kama sekunde tano kisha akaendelea. “…la sivyo namwaga damu iliyoko tumboni mwangu.”



    Nikasita, na kuacha haraka. Hofu ya kifo ilinikamata. Naanzaje kuwa mfungwa kwa mara nyingine kwa kosa nisilolitenda? Sikuhitaji iwe hivyo. Mwishowe nikatii takwa lake. Nilimuacha na kuipa kazi akili ya kumfuatilia, nifahamu matokeo ya kile alichonitendea ni nini.



    Alinikodolea macho tu! Wakati huo nilikwishafanikiwa kumvua nguo za juu. Ilisalia hatua chache nikamilishe za chini, ila mbinu aliyotumia, ilikuwa kinga ya kunipa zuio. Na ilikuwa kinga nzuri kwake, kwani hitajio la moyo, la kutohitaji kuona damu ikimwagika nikiwa chanzo lilinifanya mzembe wa kushurutishwa.

    “Mapenzi ya aina gani hayo unayoyafanya? Yako wapi yale maneno? Mbona hayaendani na hiki ulichofanya leo,” alipaza sauti ya kasiriko. Hadi nikajihisi vibaya. Nikaona kosa langu kwake. La kutotambua thamani aliyonayo kisa tu, nina mamlaka ya kumwongoza namna ya kuishi.

    “Huyu ndiye Jamila,” nilijisemeza, nikipiga mguu nyuma yake kufuata uelekeo aendao.



    Nikajikuta nina uhakika kwa hisio la mgomo alioutenda.





    __________



    Kuanzia ile siku nguvu ya upendo na furaha ikapotea baina yetu. Scolastica, alinipa badiliko, ambalo halipaswi kuoneshwa sehemu yoyote. Si sababu mtoto wa kiume, kwamba napaswa kusamehewa mapema. Hapana, nina wajibu wa kufanyiwa hivyo kwa kuwa nimetenda kosa. Ila si vyema, kwa watu waishio pamoja. Tena kwa kuchangia shuka. Ukizingatia, kuna matokeo makubwa yaletayo matumaini ya kuongeza faraja kwa kila mmoja tuliyokuwa tunayasubiri.

    “Asiniletee ujinga. Akishajifungua tu, nampiga chini. Kwa sababu atakuwa ashaniletea mwana, hatokuwa na thamani yoyote tena kwangu,” nilijisemeza kimoyomoyo jioni moja nikiwa natoka shughulini.



    Nilifikia hatua ya kuwaza hivi, kwa kuwa, imani juu ya Scolastica ilipungua. Vitu vyote nilivyowekeza kwa nguvu nilivipunguza baada ya jitihada zake za kutotaka nitimize nilichokihisi. Naamini naye aligutuka jambo, niko kwenye uchunguzi kumuhusu.

    “Na endapo dhanio hili litakuwa sahihi, hatokuwa na nafasi tena. Nitamfanyia vitendo kama paka mwizi, pasipo kujali dhamana ya damu aliyonibebea.”



    Scolastica, alinigeuza kuwa mtambuzi wa uchungu. Kwa matendo ovu yafanywayo na mwanadamu. Sikuwa na haja tena ya kumuonesha ule upendo, ambao niliamini kwa wakati huo ni mahususi kwake kwa sababu ya kuziba pengo la wale nilioweka haja ya kuwapatia kutokana na malezi yao kwangu.



    Japo alinikosesha uhakika, lakini aliendelea kunipa imani, naishi na adui. Aliyezima ndoto ya maisha yangu.



    Namlipa nini kwa yale aliyonitenda?

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Niliwazua pasi na jibu. Na kilichonikosesha zaidi, damu aliyoibeba. Kuna haja ya kudhuru damu isiyo na hatia?



    Lilikuwa swali lingine. Lililonifanya mwenye tafakuri zaidi muda mwingi. Huku, imani ya misemo ikiwa sehemu kubwa ya utawala wa akili yangu.

    “Haina haja. Hana hatia. Hivyo sipaswi kumdhuru,” nilijisemeza. Kwa minajili ya kuondoa roho ya kisasi kwa mwana aliye tumboni ijapokuwa kabebwa na mwanaharamu, mwanadhambi anayestahili kupata idhinisho la hukumu ya kila mmoja duniani.



    Hatimaye siku zilizidi kusonga mbele. Huku tukiishi kwa uongofu mwingi kwa ku—uhadaa umma, kuwa ni wana mahusiano mazuri yapaswayo kuigwa.



    Kwani juu ya utofauti mkubwa tuliouzalisha lakini hatukuuonesha nje. Maisha ya ndani yalibaki kuwa ndani. Tulidumisha dhana halisi ya umoja wetu kama wana mahusiano.



    Kutokana na uchungu ulionikithiri hatimaye nilisahau viapo vyote nilivyojiapiza juu ya Jamila. Na kunishinikiza kuwa mtu wa tafakuri, toa hii, weka ile katika kutafuta mbinu wezeshi itayomfaa Scolastica, ambaye nilishamfahamu fika kuwa Jamila. Alijibadili, yumkini kwa nia ya kupata gia ya kuniingilia, kwani nikivuta kumbukumbu, naipata taswira yake mara kibao ikikatiza eneo nifanyialo kazi. Si asubuhi, mchana wala jioni. Nilimuona akijipitisha.

    “Yumkini naye alikuwa mawindoni.”



    Ya kunitafuta, niingie himayani mwake ikiwa sehemu ya kuomba msamaha. Ila alishindwa kutamka tu, kujieleza uhalisia wake. Kwa imani, ingelikuwa ngumu kwangu kumuelewa. Hivyo ikamlazimu aanzishe mahusiano kutengeneza urahisi baadaye.



    Hakuna mkate mgumu mbele ya chai. Jamila aliishi kwa msemo huu. Kwamba, sitokua na la kuamua mbele ya penzi lake. Aliamini harufu ya fahari ya mji wa dhahabu, juu ya ku—uruhusu katika uwekezaji wa uchimbaji holela, usiozingatia umri, bado una thamani.



    Na kweli! Una thamani. Na utaendelea kuwa na thamani, hata kama una matatizo kiasi gani. Ukiachana na tatizo sugu lisilo na mwenye kulidhibiti. Ukimwi! Scolastica akanipa fumbo hapa. Kama kweli yeye ni Jamila, Jamila ni muathirika, vipi kuhusu usalama wa afya yangu kwa muda tulioishi?



    Kizungumkuti!



    Jamila nilihitaji awe moja ya mwanamke mwenye nguvu nchini, kama si dunia kwa ujumla. Naanzaje kutimiza hili? Ilhali ashaniingizia hofu nafsini juu ya afya yangu. Kubwa zaidi, mauaji aliyofanya.



    Kuna haja ya kumsamehe muuaji na kumtekelezea ahadi niliyojiapiza dhidi yake? Alinipa wakati mgumu!



    Hakika, alinipatia wakati mgumu. Wakati ulionifanya nishindwe kutambua aina ya utu nayopaswa kuwanayo. Mtu wa namna gani.



    Kuna haja ya kulipiza mema kwa mtu aliyekutenda? Tena kwa athari zisizoweza kuisha mpaka mwisho wa maisha?

    __________



    Jumapili. Jioni, nilisitisha shughuli zangu na kurudi nyumbani mara baada ya kupata simu iliyonitambulisha kuwa ya dharura toka kwa mpigaji. Ambaye sikumfahamu ni nani. Kwani, namba ilikuwa ngeni, na nilivyoitafakari sauti yake kama nishawahi isikia sehemu sikung’amua. Ilikuwa sauti mpya kabisa ndani ya viwambo vya masikio yangu.

    “Fanya haraka, nyumbani pana matatizo,” nilikumba sauti ya mpigaji. Ikiniamuru, kwa sauti iliyojaa mashaka, wakati huo nikikazana kupishanisha miguu yangu niwahi kufika. Ukizingatia, nami aliniambukiza hofu, iliyonifanya kila sekunde iendayo nijiulize kulikoni? Pasi na jibu.



    Kuna wakati nikawa namfikiria Scolastica, sambamba na hali aliyonayo. Tena huyu ndiyo alinifanya nimfikirie zaidi, kulinganisha na kitu chochote kilichopo nyumbani.

    “Kapatwa na nini?” ghafla nikapatwa na uaminisho pasi na chembe ya shaka kumuhusu. Sijui imani hii ilitokea wapi. Iliyonisahaulisha nyumba na samani zilizopo ndani. Nilisahau, kama hivi navyo vinaweza kukumbwa na adha ya ulazima inayohitaji muhusika kupata wito wa dharura.



    Maana kuna nyumba kuungua, kubomoka au vyombo kuibiwa. Haya yote niliyasahau. Fikra zangu zililala kwa Scolastica pekee. Sijui shinikizo lipi lilizalisha hali hii. Ila sikuwa na budi, nililipokea na kulipa nafasi ya kutamalaki litakavyo, huku nikishindwa kukumbuka kuwa nazidisha kudidimiza afya yangu.



    Nilivyowasili nyumbani, mboni zikaruhusu mapokezi ya uono wa watu lukuki waliosimama makundi makundi. Baadhi wakiweka bidii katika uzungumzaji, nikahisi labda ni wale walioshuhudia tukio tangu lianzapo. Ama waliojitolea kushauri kutokana na mguso wa tukio lililotokea.



    Hali hiyo ikaniongezea mashaka. Na mshawasha usiopimika wa ufahamu kilichojiri. Hatimaye nikakatiza hapa na pale, huku nikijitahidi kusukumiza watu waniachie nafasi ya kupita.



    Wakafanya hivyo!



    Nikapata nafasi, na nikaitumia taratibu hadi langoni. Ilinibidi nitembee taratibu, kwa kuhofia kutotengeneza bughuza, hasa ya kuwakanyaga kanyaga watu. Waliotoa muda wao kwa minajili ya msaada. Kwa mwana mpotevu. Mvumilivu avumiliaye uchungu usiopaswa kuvumiliwa. Yumkini, kwa sababu ya imani kidini.



    Nina hofu ya Mungu!



    Matone na lundo jingi la damu yakawa sehemu ya mapokezi pale langoni. Achilia mbali, wapokezi wa kiserikali. Mjumbe wa serikali ya kijiji na mwenyekiti wake. Ambao waliketi pembezoni kidogo mwa damu, huku wakiwa wenye kuteta taratibu.



    Matone ya damu yakaniongezea hofu. Tena nilivyoona mlango wa kuingilia umefungwa, nikazidisha maradufu, kutokana na imani hasi, niliyoshindwa kutambua imewezaje kuniathiri kirahisi.

    “Scolastica, mzima huko uliko?” nilijiuliza. Mboni zangu zikiwa pima kusaili ile damu.



    Dhahiri! Ilinichanganya akili. Kwani niliamini ndani kutakuwa na kiwango kikubwa tofauti na kile nikionacho nje.

    “Ewe ndiye mwenye nyumba?” ilisikika sauti ya mwenyekiti wa kijiji.

    “Ndiyo. Ni mimi,” nilijibu. Kwa wasiwasi mkubwa. Ulionihimiza nisimpatie nafasi mwenyekiti wa kijiji aendelee kuzungumza jambo lingine. Kwa hofu, ya kunizalishia presha.



    Hata kama, Jamila alikuwa na ubaya. Ila si ubaya wa kuhitajika kuchukiwa kwa maisha yote. Ililazimika ifike mahali, apatiwe msamaha, atambue, dunia inampenda tofauti na namna afikiriavyo.



    Pia aende mbali kwa utambuzi. Hupaswi kulipa mabaya kwa mabaya. Pasi na kupima ubaya huo una kiasi gani. Yafaa kumshukuru akutendaye, kwa sababu tayari kashakuonesha njia mwanzo tu, hata kabla hamjafika mbali kimahusiano.

    “Scolastica! Kwa nini umeamua kuondoka? Mbona mimi sikuchukii kiasi hicho?” nilijisemeza, wangu fuadi ukiendelea kunitafuna taratibu.



    Nilipata udhoreteshaji kwa muda. Wa ki—akili na mwili kwa ujumla. Huku akili ikiendelea kunipa kikwazo cha mapokezi ya kauli ya mwenyekiti wa kijiji.

    “Pole sana kijana. Ewe ni mtoto wa kiume, huna budi kuvumilia. Hiki kilichotokea leo, ni njia ya kukufikisha sehemu nzuri. Kuwa mvumilivu, piga moyo konde, maisha yasonge mbele,” alisema mwenyekiti. Huku akinikabidhi bahasha ndogo yenye rangi ya khaki, iliyo na mtuno kiasi ulioashiria uwepo wa kitu ndani.



    Nami pasi na hiyana, kwa mikono miwili, huku nikiweka utiifu wa kukunja miguu kidogo, niliipokea. Nikafahamu fika kilichopo ndani ni barua, toka kwa Scolastica. Iliniuma sana! Kwani japo ya kuwa na fikra kwamba yeye ni Jamila, na kahusika katika matendo ya uangamizaji wa uelekeo wa maisha yangu fuadi uliruhusu chembe ya upendo kwake.



    Uchungu, kisasi na kila lililo baya linalomuhusu lilianza kupungua. Nahisi kutokana na umati wa watu uliokuwepo, ambao walihangaika kumsaidia mtu aliyezima maono ya uchu wa uchimbaji holela wa mji wa dhahabu.

    “Niwekeni wazi, kimetokea nini? Naona munazunguka sana. Niwekeni bayana tu,” nilisema nikiwa mwenye hamaniko tele.

    “Aaaah!...mkeo karuhusu onesho la damu hadharani. Lililopelekea kudhuru watu kadhaa, ambao walifanya bidii ya kutaka kumuokoa.”

    “Una maanisha nini?”

    “Mkeo alitaka kujiua,” alisema mwenyekiti na kutulia. Mboni zake zikinisaili kwa shauku ya uhitaji wa kutambua mapokeo ya kauli aliyoitamka.



    Hakika! Nilikosa ustahimilivu. Nikawa na mapokeo ya katisho la furaha na ondoko la amani nafsini mwangu. Sikuwa na la kuamua, zaidi ya kuruhusu huruma initawale dhidi ya Scolastica.



    Nilivyokuja kupoa ndipo nikapatiwa nafasi ya kuingia ndani. Nijionee mazingira yalivyo.

    Yalikuwa kinyume na fikra zangu!



    Hakukuwa na dosari ya aina yoyote. Ila nikapatwa na ulizo, wapi pana lundo kubwa la damu nikianchana na lile nililoliona.

    “Yumkini limefichwa na yale makundi ya watu,” nikajisemeza, wakati huo nikitoka ndani. Pembeni yangu alikuwepo mwenyekiti, aliyeongozana nami kwa lengo la kunisindikiza, na kuhakikisha usalama zaidi kwa upande wangu. Nisije jidhuru!

    “Kijana, upande wetu kama serikali ya kijiji tunaishia hapa. Panapoendelea, papo chini ya mamlaka ya juu zaidi yetu. Ukifika huko, utafahamu, hali ya mkeo, na lipi lifuatalo,” alisema mwenyekiti wa kijiji kwa sauti ya unyenyekevu, iliyoniashiria nisichukue maamuzi mabaya katika hili. Nitulize konde moyo wangu. Niache kupaniki, pasi na kujali kiasi cha umivu nipatacho.



    Inawezekanaje?



    Kikubwa kilichonizidisha kuwa hivyo, ni damu yangu. Kwani kifo cha Scolastica, ni sawa na kuhalalisha kifo cha kiumbe alichobeba ndani ya tumbo lake. Nililazimika kuumia, kwa namna yoyote, huku nikijaribu kutafuta tulizo. Ambalo lilinitumikisha kila dakika pasi na kulipata sahihi.

    “Kwa sasa atakuwa wapi?” niliuliza.

    “Awali, alichukuliwa na kupelekwa kituo cha polisi. Huko aliandikiwa kibali maalumu cha kumruhusu apatiwe matibabu hospitalini, ilhali mipango mingine ikiendelea. Kama vile ufunguzi wa kesi na mengineyo. Hivyo hakika yangu, atakuwa hospitalini. Ila kwa uhakika zaidi, unalazimika kufika kituo cha polisi cha kati utapatiwa maelezo yenye utoshelezo.”



    Tukaagana!



    Na wengine waliokuwa wamesalia pia wakaanza kuondoka. Dakika kumi na tatu tu, toka mwenyekiti wa kijiji alivyoondoka, zilitosha kuufanya uga wa nyumba yangu kuwa mweupe, nikisalia pekee. Hapo ndipo nikapata wasaa wa kumbukizi, bahasha niliyokabidhiwa, iliyobeba karatasi ya ujumbe ndani, ulioandikwa na Scolastica.



    Chap! Nikapiga papaso la mkono wa kushoto hadi nilikoihifadhi. Ndani ya mfuko wa suruali niliyovaa. Upande wa kono la kuume.



    Sikuremba. Nikafanya hima kuitoa na kuifungua pia. Ilikuwa karatasi iliyochanwa kwenye daftari. Imekunjwa vyema, mithili ya mpelekewa ni mtu mwenye heshima iliyotukuka ulimwenguni. Ilhali ni kapuku tu, asiye hata na chembe ya nguvu ya kushawishi kaya tano.



    Ila sikujalisha hayo sana. Nikaenda moja kwa moja kwenye uhitaji wa nafsi kwa wakati huo. Kufahamu kilichoandikwa.



    Niliikunjua, na kukutana na maandishi mengi, makubwa kwa madogo, yalikolezwa wino na yasiyokolezwa, na kunipa ufahamu wa kutopuuzia. Ufahamu huu ulitokana na maneno yaliyoandikwa kwa herufi kubwa na kukolezwa wino. Ishara ya kunipa msisitizo.



    Taratibu kidume nikabinua kingo za mdomo wangu na kupitia neno moja baada ya lingine.



    Kwako, Abdul mpendwa.



    Awali nikupe pole na pongezi, kwa kuthamini muda na kutambua maana ya kujitambua. Yafaa kutunzwa kwa hili. Kama si toka serikalini, basi hata mtu mmoja mmoja aonaye jitihada zako.



    Abdul! Ewe ni mwanaume wa mfano. Unayepaswa kuigwa. Kwa sababu nilichokigundua kwa muda mfupi tulioishi pamoja, maishani mwako, huruhusu dhana ya mtu ikutawale. Unaishi kwenye dhana zako, huku zile za nje huzitumia kuongeza kwa uchache kama sehemu ya maboresho. Hongera sana!



    Leo nimeamua kukamata kalamu na kumwaga wino kwa sababu hustahili kutendwa. Ewe ni mtu unayepaswa kutendewa mema, ili yapitie kwako kama daraja kisha yaende kutoa manufaa kwa wengine.



    Mimi Scolastica. Nadiriki, kwa huruma yangu, nikuondoe kifungoni. Ulichojizalishia mara baada ya kumuona mtu aliyekutenda. Na kukupotezea dira ya maisha yako kwa namna moja au nyingine.



    Abdul! Nahitaji nikupe uhuru wa nafsi, ila kwa AHADI, kwa kile nitachokuomba.



    Kwanza; naomba unisamehe. Kwa kuwa sehemu ya watu wasiotambua vitu nilivyozungumzia aya za mwanzo, kutokana na kukithiri kwa imani potofu, nilizoamini ni za kishujaa nitendapo. Pili; na mwisho, naomba tena MSAMAHA. NISAMEHE, NIMEKOSA.



    Msamaha huo ujumuishe mabaya yote niliyokutendea tangu tufahamiane. Abdul, Scolastica aliye mwaga wino hapa, si yule unayemfahamu kwa muonekano wa sura ulalanapo kitanda kimoja. Scolastica wa hapa, ni yule umuhisiye…



    Abdul! Mimi ni…Jamila. Na si Scolastica kama nilivyokutambulisha awali. Nililazimika kujibadili, ili iwe njia rahisi kwangu kukufikia. Kwani, niliamini, ningelikuja na sura halisi, pangelichimbika.



    Nimelazimika kuja kitofauti, na kufanya hayo yote, ili nipate msamaha wako. Nikurejeshee furaha, hata kama sitofanikiwa kuiziba ile niliyoipoteza kwa mikono yangu. NATUBU, mimi ndiye nimewauwa wazazi wako. Ikiwa sehemu ya kulipiza kisasi kwa maisha niliyopitia. Nimepitia maisha magumu udogoni mwangu, yote kwa sababu ya HILA za mtu tu.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Naumia sana nikumbukapo. Na niwakumbukapo hao watu. Hivyo nilivyoona wanasaidiwa, ilinizidishia umivu. Wakati mimi nilipoteza msaada ijapokuwa taarifa ya tukio langu lilivuma kila pande ya nchi yetu. Na kilichonizidisha, katu, hawakufanya TOBA.



    Abdul! Sahau yaliyopita. Na naomba unipe nafasi. Rudisha moyo nyuma. Mwenzio NAJUTA kutenda kosa. Najuta kwa kukupoteza, ila kwa sasa, naamini kwako ndipo sehemu salama pekee iliyosalia maishani mwangu.





    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog