Simulizi : Dunia Haina Usawa
Sehemu Ya Tano (5)
Halima alikuwa msichana mrembo, aliyekuwa na mvuto wa kumfanya mwanaume yeyote yule amfuate na kumchombeza kwa maneno matamu. Alikuwa mzungumzaji, alikuwa akizungumza na kila mtu aliyekuja mbele yake. Watu wengi walimpenda kwa kuwa tu hakuwa akijiona, alikuwa msichana ambaye alitoa tabasamu kwa kila mwanaume aliyesimama mbele yake.
Wanawake wengi wa Tandale wakatokea kumchukia, uzuri wake uliwachanganya na wengine kuhisi kwamba msichana huyo angewachukulia wanaume wao. Hawakutaka kumsalimia lakini hilo wala halikuwa tatizo kwa msichana huyo, kitu pekee alichokuwa akikiangalia kilikuwa ni kumpata mtu aliyemfanya kuwa hapo, Godwin.
Wanaume wakapeana taarifa, kama ilivyokuwa kwa mitaa mingine kwamba msichana mrembo anapohamia mtaani basi mitaa mingine wangejua nivyo ilivyotokea kwa Tandale. Wanaume kutoka Manzese, Mwananyamala na Magomeni wakafika mtaani hapo kwa ajili ya kumuona Halima ambaye alikuwa na sifa za kuwa msichana mrembo mno.
Kila aliyemuona, hakujutia muda wake aliopoteza, hakutaka kujuta kwa hatua aliyochukua ya kutoka mtaani kwake mpaka Tandale kwani msichana ambaye alibahatika kumuona siku hiyo aliingia ndani ya kichwa chake na kukiri kwamba Halima alikuwa msichana mrembo mno, msichana ambaye wengine walisema kwamba hakutakiwa kuishi Tandale bali Masaki kulipokuwa na wanaume wenye pesa.
Hakukuwa na mtu aliyejua sababu ya msichana huyo kuwa mahali hapo, wengi wakatamani kujua kwani kila siku asubuhi, alikuwa mtu wa kukaa ndani, hakutoka kwenda sehemu nyingine yoyote, hakuwa akifanya kazi kitu kilichowapa watu maswali mengi.
Vijana wengine wakajitoa kumfuatilia msichana huyo, walitaka kujua alikuwa nani na kwa nini aliamua kwenda kuishi mtaa huo na wakati alikuwa na uzri wa ajabu. Katika kufuatilia kwao wakagundua kwamba msichana huyo alikuwa kimada cha bwana mmoja mwenye pesa ambaye aliamua kumpangishia maeneo ya Tandale kwa kuwa tu hakutaka binti huyo achukuliwe na mwanaume yeyote mwenye pesa.
Mchana alionekana sista duu lakini kwa usiku alikuwa mtu mwingine kabisa, alitulia katika chumba chake huku akiwa na laptop yake akiangalia ni kwa jinsi gani angeweza kumtafuta mtu huyo.
Kazi yake kubwa ilikuwa ni kuwasiliana na maofisa wa Usalama wa Taifa nchini Uswisi, FIS ambao walikuwa wakimwambia kitu gani cha kufanya na mahali ambapo walikuwa na wasiwasi wa kuwepo kwa mtu huyo.
“Umefikia wapi?” lilikuwa swali la kwanza kabisa.
“Bado ninaendelea kupeleleza, nahisi nitafanikiwa kumpata tu kwani bado nazoeana na watumbalimbali wa mtaa huu,” alisema Halima.
“Sawa. Jitahidi mpaka tufanikiwe.”
“Haina shida!”
Hakuacha kupeleleza huku na kule, alijitahidi kuendelea kuwapeleleza watu wengine ili afahamu mahali mwanaume huyo alipokuwa hapo mtaani. Wakati hayo yote yakiendelea ndipo akatokea kuzoeana na msichana mmoja mrembo ambaye alikuwa akifika sana hapo Fogo, Tandale.
Wakaanza kuzungumza, kwa muonekano, msichana huyo alionekana kuwa msomi kwani kila alipokuwa akifika huko, alikuwa na laptop yake katika begi kitu kilichowafanya kuanza kuzoeana kwa kuwa tu mara ya kwanza walipokutana, walionekana kuvutiana wenyewe.
“Unaitwa nani?” aliuliza msichana huyo.
“Naitwa Angelica,” alidanganya Halima.
“Ooh! Sawa. Mimi naitwa Winfrida!”
“Unaishi huku au?”
“Hapana! Huwa ninakuja kutembelea mpenzi wangu, nyumba hiyo hapo mbele. Anaitwa Godwin. Unamfahamu?” aliuliza Winfrida huku akitoa tabasamu pana.
Halima alipolisikia jina hilo, akashtuka, hakuamini kama kweli Winfrida alilitaja jina la mtu aliyekuwa akitafutwa sana ambaye alimfanya kufika mahali hapo. Alimwangalia msichana huyo mara mbilimbili huku akijiuliza kama lile jina la mtu aliyekuwa ametajwa mbele yake alikuwa ndiye aliyekuwa akimtafuta au mwingine.
“Angelica! Mbona umeduwaa?”
“Ooh! Samahani! Unajua nilikuwa na mpenzi wangu mwenye jina kama la mpenzi wako! Alifariki kwa ajali ya gari mwaka jana,” alisema Halima hapohapo kuyavuta machozi kwa nguvu zake zote na kuanza kulia kiasi kwamba Winfrida akamkumbatia kumpoza pasipo kujua ni kwa jinsi gani msichana huyo alijisikia baada ya kugundua kwamba mtu aliyekuwa akimtafuta, alikuwa mpenzi wake.
****
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania National, Bwana Kambili akawaita wenzake na kuanza kuwaambia kila kitu kilichokuwa kimetokea. Alikuwa na ushuhuda mkubwa kwamba kwa kila kitu walichokuwa wakikiona kikitokea katika kipindi hicho kilikuwa kimesukwa na mtu aliyeitwa Godwin ambaye alikuwa akitafutwa kila kona duniani.
Wengi hawakumwamini, kwanza walitaka kujua sababu ya kuachiwa kwake na polisi, yeye mwenyewe hakujua zaidi ya kuambiwa kwamba IGP Ng’osha aliamuru atolewe na waandishi wa habari kupewa taarifa. Kila mmoja alishangaa, wengi walimjua Ng’osha, alikuwa mwanaume mwenye roho mbaya kwa watu wa chama pinzani.
“Kwa nini aliruhusu kuondoka, yaani kirahisirahisi tu?” aliuliza katibu wa chama hicho, Bwana Walusanga Ndani.
“Sijajua! Mimi mwenyewe nilishangaa sana! Ila ukiachana na hayo, nimepigiwa simu na mtu anaitwa Godwin,” alisema Kambili.
Hapo ndipo alipoanza kuwaambia kila kitu kilichokuwa kimetokea na maneno aliyokuwa ameambiwa na mtu aliyempigia simu ambaye alijitambulisha kwa jina la Godwin. Kila mmoja alishangaa, hawakuona kama hilo lingekuwa jambo rahisi kutokea kwani pamoja na yeye kumiliki akaunti ile, pia alimwambia kwamba ndani ya siku chache Rais Bokasa angejiuzulu au kupinduliwa na wao kuchukua uongozi.
“Haiwezekani!”
“Jamani! Mimi ndiyo nimeambiwa hivyo! Tujipangeni kwa ajili ya kuichukua nchi hii,” alisema Kambili.
“Kuna ishara gani ambayo inaweza kutufanya tumuamini?” aliuliza Ndaki, alitaka kuamini baada ya kuona na si kuamini baada ya kuambiwa.
Kambili akawaambia kwamba kesho kungekuwa na kiongozi mmoja ambaye angewaita waandishi wa habari na kuwaambia kwamba hakuwa na imani na rais na hivyo kujitoa katika uongozi huo. Hakutakiwa kuwaambia ni kiongozi gani ila walitakiwa kujua kwamba kungekuwa na mtu ambaye angewaita waandishi wa habari na kuwaambia hivyo.
Hilo kidogo likawafanya viongozi hao kusubiri kuona kama jambo hilo lingetokea ili waanze kuamini. Siku hiyo ilipofika, wakaambiwa kwamba Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Bwana Noel alikuwa amewaita waandishi wa habari Habari Maelezo kwa kuwa kuna jambo alitaka kuzungumza nao.
Kilichotokea ndicho kilichowafanya kuamini kama Godwin angeweza kuwapeleka mpaka ikulu kwani kwa maneno tu kutoka kwa Kambili hawakuwa wameamini lakini kwa kile ambacho waliambiwa na kutokea, waliamini kwamba walikuwa wakienda ikulu, tena njia ilikuwa nyeupe kabisa, ishu ilikuwa ni kwao tu kujipanga na kwenda huko.
“Jamani! Iteni mikutano mzungumze na watu, waambieni kwamba tunakwenda ikulu. Kama tutakamatwa na kuuawa, acha tuuawe lakini tukawaambieni kwamba tunajiandaa kwenda ikulu,” alisema Kambili huku akiwaangalia wenzake kwa umakini kabisa kwani kwa jinsi alivyopigwa na macho yake kuvimba, hakuwa akiona vizuri.
“Tutafanya hivyo! Nadhani napo ni muda wa kupanga nani atakuwa makamu wa rais na nani atakuwa waziri mkuu!” alisema Ndani huku akionekana kuwa na hamu ya madaraka.
“Hilo tutapanga tukionana naye! Nadhani ni njia moja ya kufanikiwa katika hili. Nitawasiliana naye, nitapokea maelekezo kutoka kwake!” alisema Kambili.
****
Rais Bokasa alikuwa amechanganyikiwa, hakuamini kilichokuwa kimetokea, moyo wake ulimuuma, ulichoma kama mkuki, mtu ambaye alimwamini kwa nguvu zote, ambaye alikuwa akijua siri kubwa kutoka ikulu alikuwa amemkataa, hakutaka kufanya naye kazi kwa kuwa hakuwa na imani naye.
Hakutaka kukubali, alichokijua ni kwamba kulikuwa na mtu mwingine nyuma ya pazia ambaye alimshawishi kufanya jambo kama hilo, kwa sababu wanawake walikuwa na nguvu kwa waume zao, akataka kumtumia mkewe, Bi Stela kwa ajili ya kumshawishi mumewe na hatimaye kurudisha moyo nyuma.
Akamtuma Waziri mkuu mpaka nyumbani kwa Noel kwa lengo la kuzungumza naye lakini baada ya kufika huko akapewa taarifa kutoka kwa vijana wa Usalama wa Taifa waliokuwa wakilinda nyumba huyo kwamba hiyo ilikuwa siku ya pili mwanamke huyo hakuwa ameonekana.
“Amekwenda wapi?”
“Hatujui! Mumewe hataki kuzungumzia suala hilo hata kidogo,” alisema Andrew.
Waziri mkuu hakutaka kubaki nje, alichokifanya ni kuingia ndani kwa lengo la kuzungumza na Noel. Akakaribishwa mpaka ndani ambapo dada wa kazi akaenda kumuita bosi wake ambaye ndani ya dakika mbili, tayari alikuwa sebuleni.
Kwa jinsi macho yake yalivyoonekana, alionyesha kulia sana, yalikuwa mekundu huku kila wakati akivuta mafua yake kwa ndani. Waziri mkuu alibaki akimshangaa, hakujua kilichokuwa kikiendelea ila alihisi kwamba kulikuwa na jambo.
“Kuna nini?” aliuliza.
“Mheshimiwa Godson! Moyo wangu unaniuma sana,” alisema Noel huku akimwangalia waziri mkuu huyo.
“Kuna nini? Niambie kijana wangu. Umefanya maamuzi ya ghafla sana, niambie kuna nini,” alisema Bwana Godson.
“Ninaipenda sana familia yangu! Nadhani unajua hilo!” alisema.
“Ndiyo!”
“Nilikuwa tayari kufanya kila kitu kwa ajili yao.”
“Ndiyo!”
“Familia yangu siioni, sijajua ipo wapi! Ni ghafla tu siioni ndani, walinzi walisema aliondoka, alipokwenda, hakurudi, nimechanganyikiwa sana,” alisema Noel, akaanza kulia tena.
“Imetekwa?”
“Sijajua! Sijui chochote kile.”
“Niambie ukweli!”
“Sijui mkuu!”
Walizungumza mambo mengi, Bwana Godson alimuomba sana Noel arudi katika nafasi yake lakini mwanaume huyo alikataa na kusema kwamba siku zote angeendelea kubaki na msimamo wake, hakutaka tena kusikia kuhusu uongozi huo.
“Ni nani yupo nyuma yako?”
“Hakuna mtu, ila kurudi, siwezi kwa kweli,” alisema Noel.
Hakukuwa na kitu cha kumbadilisha, alibaki na msimamo wake kwamba kusingekuwa na kitu chochote cha kumrudisha kwani aliamini kwamba kama angefanya hivyo basi familia yake ingeweza kuuawa. Aliogopa na alipanga kubaki kwenye msimamo wake uleule mpaka pale ambapo angeona ni kitu gani kingeendelea baada ya hapo.
Baada ya siku mbili kupita huku kila mtu akiwa na maswali mengi juu ya uamuzi alioufanya Noel, mara waandishi wa habari wakapigiwa simu na Bilionea Kizota na kuambiwa kwamba walitakiwa kuonana naye nyumbani kwake kwani kulikuwa na mambo mengi alitaka kuzungumza nao.
“Bilionea Kizota? Kuna nini tena?” aliuliza mwandishi mmoja.
“Hatujui! Ila twendeni jamani. Si unajua yule ndiyo ameshikilia uchumi wa wafanyabiashara wengi. Twendeni,” alisema mwandishi mmoja, zaidi ya waandishi hamsini kutoka kwenye magazeti, mitandao na sehemu nyingine wakaanza kwenda huko, kila mmoja alikuwa akijiuliza ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, walittaka kujua kama ni yaleyale kama ya Noel au yalikuwa mengine.
Kila mtu alitaka kufahamu kile kilichokuwa kikitaka kuzungumzwa na Bilionea Kizota. Huyo alikuwa mwanaume mwenye pesa nyingi kuliko wote nchini Tanzania, maisha yake yalikuwa ya siri sana kiasi kwamba kuna watu wengine hawakuwa wakifahamu alifananaje.
Ilikuwa vigumu kumuona katika magazeti, televisheni au sehemu nyingine, alikuwa mzee aliyeishi kisiri sana kiasi kwamba kuna wengine hawakuwa wakiamini kama mzee huyo alikuwa mwembamba, mwenye sura ya kimasikini kuliko vitu alivyokuwa akimiliki.
Baada ya saa moja, tayari waandishi wa habari walikuwa nje ya jumba lake la kifahari lililokuwa Osterbay jijini Dar es Salaam. Haikuwa rahisi kuingia hivihivi, waliambiwa mmoja mmoja kwenda kusimama sehemu moja kulipokuwa na taa ya rangi ya bluu ambayo iliwaonyesha kila kitu walichokuwa nacho.
Nyumba ilikuwa na ulinzi mkubwa sana, waandishi wa habari wote walichunguzwa lakini hakukuwa na mtu aliyeonekana kuwa na silaha yoyote ile. Wakaruhusiwa kuingia ndani na kupelekwa sehemu fulani iliyokuwa na viti pamoja na hema na kuambiwa wasubiri hapo.
Wakatulia na kuanza kufunga mitambo. Walikuwa wakimsubiri bilionea huyo ambaye alikuwa akijiandaa tayari kwa kuzungumza na waandishi hao. Alitaka kuzungumza mambo fulani ambayo yalikuwa ni siri sana, mambo ambayo hakukuwa na mtu aliyekuwa akiyafahamu.
“Bro! Nimefika,” alisema mwanaume mmoja aliyekuwa na kaera, wakati waandishi wa habari wenzake wakiwa wameingia ndani, yeye ndiyo kwanza alikuwa akifika.
“Wewe nani?”
“Mwandishi kaka!” alijibu mwanaume huyo huku akimuonyeshea kamera aliyokuwa ameishika.
“Kutoka wapi? Kitambulisho chako kiko wapi?’ aliuliza mlinzi huku akimwangalia mwanaume huyo.
Hapohapo akachukua kitambulisho na kumuonyeshea mlinzi, kitambulisho kilichomuonyesha kwamba alikuwa mwandishi wa habari kutoka katika Mtandao wa Omen ambao ulikuwa ukitikisa kipindi hicho.
Akaambiwa aende kusimama katika taa ile ya kuwachunguzia watu ili kuonekana kama hakuwa na silaha yoyote ile, akaenda, akasimama na kummulika kisha kuruhusiwa kuingia ndani.
Mwandishi huyo alikuwa Godwin. Alifika mahali hapo kwa kuwa alitaka kufanya kitu kingine kabisa. Alitembea kwa kujiamini, hakuwa na hofu hata kidogo na kila mtu aliyemwangalia, kwa jinsi alivyokuwa alionekana kuwa mwandishi kweli.
Alikwenda mpaka walipokuwa wenzake na kutulia hapo. Baada ya dakika kadhaa, Bilionea Kizota akafika mahali hapo. Kwa jinsi alivyoonekana, alikuwa amekonda, ilikuwa ni vigumu kuamini kama mtu mwenye pesa ambaye siku chache zilizopita alikuwa na mwili wa kawaida leo hii alikuwa vile.
Kichwa chake kilimpa mawazo, kila mwezi alikuwa na uwezo wa kuingiza bilioni tatu lakini kitu cha ajabu kabisa, alikuwa mtu wa mawazo mengi kuliko hata mtu masikini ambaye alilala pasipo kuwa na chakula chochote.
Waandishi wa habari wakaanza kumpiga picha tangu alipokuwa akiingia mpaka alipokwenda kukaa. Godwin hakutulia, kama walivyokuwa wenzake, naye alikuwa akishughulika sawa na wao na kutulia sehemu yake.
Alimwangalia bilionea huyo, alitia huruma, alipoteza mwili wake mkubwa, kwa kumwangalia mara moja, ilikuwa ni vigumu kuamini kama mtu huyo alikuwa bilionea. Akatulia kwenye kiti, kabla ya kuzungumza chochote kile, akaanza kuwaangalia waandishi hao.
“Nimefurahi sana kuwaona mahali hapa. Najua wengi mnashangaa jinsi nilivyopungua. Ndugu zangu, kuna wakati unakaa na kuingiza pesa nyingi lakini hiyo haitoshi kuonyesha kama umefanikiwa,” alisema Kizota huku akiendelea kuwaangalia watu waliokuwa mahali hapo.
“Siamini pesa ndiyo inaweza kumfanya mtu kuwa tajiri. Tajiri pekee ni yule ambaye ana vitu ambavyo pesa haiwezi kununua kama furaha, faraja, amani. Mimi ni masikini, nina pesa lakini haziwezi kununua furaha, kuna haja gani ya kuwa na pesa?” aliuliza Kizota, alivyokuwa akizungumza, alionekana kuwa na jambo kubwa moyoni mwake.
Alizungumza mambo mengi mno lakini mwisho kabisa aliwaambia kile kitu kilichoujaza moyo wake kwamba kuna wakati alitamani kufa, kuondoka katika dunia hii kwa kuwa kuna jambo ambalo halipo sawa kabisa.
“Jambo gani?” alidakia Godwin, hakutaka kuchelewa.
“Siipendi serikali hii, simpendi rais hata kidogo. Ninamchukia kwa sababu yeye ndiye amekuwa chanzo cha mambo yote, yeye ndiye amekuwa sababu ya mimi kukosa furaha,” alisema Kizota, machozi yakaanza kumlengalenga.
“Kwa nini?” Godwin akadakia tena kiasi kwamba mpaka baadhi ya waandishi wakaanza kushangaa kwani hakukuwa na mwandishi wa habari aliyeonekana kujiamini kama yeye.
“Nilitishiwa maisha kwa sababu ya serikali hii. Jana tu Noel alijiuzulu nafasi yake, najua inawezekana kuna kitu kimemtokea ambacho hata mimi kimenitokea. Jifikirie kwa nini yanatokea haya yote? Jibu ni jepesi kwamba rais ndiye anayesababisha haya, bila rais kuwa na serikali ya kipuuzi haya mambo yote yasingeweza kutokea. Kama wananchi wanapata wanachokitaka, unahisi haya yote yangetokea? Kama rais angekuwa siyo muuaji unafikiri haya yote yangetokea? Hakuna kitu kama hicho. Rais ndiye katunyima furaha, katufanya tutekwe. Kama Noel alisema wazi hamuungi mkono rais, hata mimi pia simuungi mkono hata kidogo,” alisema Kizota.
Hakuogopa, moyoni mwake alikuwa na mzigo mkubwa lakini baada ya kufunguka kwa kirefu na kutoa dukuduku lake, moyo wake ukawa na amani, akahisi kama alikuwa ameutua mzigo mzito aliokuwa ameubeba.
Kila mwandishi alikuwa akishangaa, hawakuamini kama bilionea huyo angezungumza maneno kama hayo tena akiwa laivu kabisa. Wengi wakahisi kwamba kungekuwa na kitu kibaya ambacho kingetokea mahali hapo kwani kama kila mtu alikiona kipindi hicho, rais Bokasa asingekubali kuona akichafuliwa, kwa kutumia cheo chake, mabavu yake basi angetuma polisi kwenda huko na kumkamata.
Walichokuwa wakikihisi ndicho kilichotokea, huku bilionea huyo akiendelea kuzungumza na waandishi, magari mawili ya polisi yakafika nyumbani hapo, kwa mwendo wa kijeshi polisi wakaingia ndani na kumkamata mzee huyo ambaye muda wote alikuwa akisema kwamba ilikuwa ni bora kukamatwa kuliko kuendelea kuishi huku akiwa hana amani moyoni mwake.
“Hata kama kufungwa nitakuwa tayari! Ninachokitaka ni kuwa na amani moyoni mwangu tu. Inatosha,” alisema bilionea huyo wakati amechukuliwa na kupandishwa ndani ya gari na kuondolewa mahali hapo.
Waandishi wa habari hawakuwa na nongwa, walichokifanya ni kuendelea kupiga picha kila kitu kilichokuwa kikitokea mahali hapo. Kwa hilo, Watanzania wengi walikasirika, chuki dhidi ya Rais Bokasa ikazidi kuongezeka kwani kwa kile alichokizungumza bilionea huyo kilikuwa kitu cha kawaida, alitoa dukuduku lake na hakutakiwa kukamatwa kama ilivyokuwa imetokea.
“Ila Kizota alikuwa na haki kabisa. Kwani katukana? Kwani kasingizia? Alichokizungumza ndiyo ukweli wa mambo,” alisema jamaa mmoja alipokuwa akizungumza na wenzake maskani.
“Shiiiii! Sasa hivi Usalama wa Taifa kila kona, unaweza kudakwa, hayo mambo kalalamikie chumbani ukiwa na mkeo,” alisema jamaa mwingine, kwa jinsi hali ilivyokuwa nchini, hakukuwa na haja ya kumwamini mtu yeyote yule.
***
Ndani ya siku chache tu, tayari urafiki baina ya Halima na Winfrida ulikuwa mkubwa. Walikuwa wakikutana na kuzungumza mambo mengi, alimpenda msichana mwenzake huyo kwa kuwa alikuwa na sura nzuri, msikivu na aliyeonekana kufahamu mambo mengi mno.
Halima alihisi kwamba alikuwa kwa mtu sahihi, aliamini kwamba Godwin aliyekuwa amezungumziwa ambaye alikuwa mpenzi wa Winfrida ndiye ambaye walikuwa wakimtafuta kwa udi na uvumba.
Baada ya kuzoeana sana ndipo Winfrida akaamua kumkaribisha Halima nyumbani kwake. Hiyo ikaonekana nafuu kwa msichana huyo kwani aliamini kwamba mara baada ya kufika huko angepata nafasi ya kumuona huyo Godwin na kupanga mikakati juu ya kumkamata mwanaume huyo.
Siku ambayo alikwenda nyumbani hapo alishangaa, hakukuonekana kuwa pazuri hata kidogo. Kulikuwa na godoro chini, chumba kibovu na humo ndani hakukuwa na kitu chochote kilichoonekana kuwa na gharama yoyote ile.
Halima alibaki akishangaa, alipoondoka nchini Somalia aliambiwa kwamba mwanaume aliyekuwa akienda kupeleleza huko alikuwa na uwezo mkubwa wa kuchezea kompyuta lakini pia alikuwa amehamisha kiasi kikubwa cha pesa kutoka benki lakini kwa jinsi alivyokuwa akikiangalia chumba hicho, hakikufanana na zile sifa za mtu huyo ambazo aliambiwa.
Akavumilia, alichokitaka ni kumuona mwanaume mwenyewe, alifananaje na alikuwa na uwezo gani hata kwenye kuzungumza. Hilo halikuwa tatizo lolote kwani baada ya saa mbili, Godwin akafika nyumbani hapo, alikuwa ametoka katika mkutano aliouandaa Bilionea Kizota kwa ajili ya kuzungumza na waandishi wa habari.
Alipofika nyumbani hapo na Halima kutambulishwa kwamba alikuwa mpenzi wa Winfrida aliyeitwa Godwin, hakuamini kama kweli mwanaume huyo ndiye ambaye alikuwa akiwasumbua Usalama wa Taifa wa Uswisi, FIS kwani muonekano wake ulikuwa wa kimasikini mno, alichoka na alionekana kutokuwa hata na shilingi mia tano mfukoni.
“Huyu ndiye mpenzi wako?” aliuliza Halima, hakuwa akiamini.
“Ndiye yeye! Yupoje kwani?”
“Mmh! Hakuna kitu! Ni mwanaume mzuri sana,” alijibu Halima.
Alichokifanya msichana huyo ni kuchukua miwani yake ya macho na kuivaa. Ilionekana kama miwani lakini ukweli wa mambo haikuwa miwani ya kawaida bali ilikuwa na kamera ambayo ilipiga picha moja kwa moja na kuzipeleka nchini Uswisi.
Ili kuwapa taarifa wenzake akamwambia Winfrida kwamba alitaka kwenda chooni kujisaidia haja ndogo, alipoonyeshewa, akaelekea huko, alipofika, akavua miwani ile na kuanza kuiangalia, kamera ndogo ikaanza kumpiga.
“Nimefanya kazi kwa kipindi kichache, nimempata Godwin ambaye sidhani kama ndiye yeye,” alisema Halima huku akitumia simu yake aliyoiunganisha na bluetooth ambayo ilipeleka taarifa kupitia miwani ile.
“Ndiye yule uliyempiga picha?”
“Ndiyo! Na pale ndipo anapoishi!”
“Yaani kwenye lile jalala?”
“Kile ni chumba!”
“Hapana! Atakuwa si huyo. Huyo tunayemtafuta ni yule aliyechukua pesa benki, yule ambaye anaisumbua serikali yetu mpaka ya huko Tanzania,” alisikika Bwana Kom.
“Kwa hiyo huyo si yeye?”
“Sijajua! Hebu endelea kuchunguza zaidi, nenda kampige picha zaidi,” alisema Kom.
“Sawa,” aliitikia Halima, hapohapo akaivaa miwani ile, akaufungua mlango, akashtuka, macho yake yakatua kwa Godwin ambaye naye alikuwa mlangoni hapo na dalili zilionyesha kwamba alisikia kila kitu kilichokuwa kimezungumzwa ndani.
“Ooh My Gosh....” alijikuta akisema huku macho yake yakitazamana na macho ya Godwin aliyekuwa amesimama karibu naye kabisa kwenye mlango wa choo.
***
Tangu Godwin alipoingia ndani ya chumba chake na macho yake kutua kwa msichana Halima, akawa na hofu kwamba inawezekana msichana huyo alikuwa mbaya kwani kwa muonekano alioonekana, hakuonekana kama msichana aliyekulia maisha ya Tanzania, ngozi yake, muonekano wake ulimtia shaka kupita kawaida.
Walikaa na kuzungumza, muda mwingi alikuwa akimwangalia Halima kiwizi, bado moyo wake ulikuwa na hofu na msichana huyo, alihisi kabisa kwamba alikuwa mtu mbaya ambaye hakutakiwa kabisa kuwa karibu naye.
Halima alizungumza mambo mengi chumbani pale mpaka alipotaka kuelekea chooni. Haraka sana naye Godwin akaaga kwamba alikuwa akienda nje, alipofika huko, alikuwa akihesabu sekunde huku akikadiria kwamba muda huu Halima alikuwa amekwenda chooni au bado.
“Atakuwa amekwenda, hebu subiri niende,” alisema Godwin.
Hakutaka kuchelewa, haraka sana naye akaelekea chooni kwani hakuamini kama kweli msichana huyo alikuwa ameshikwa na haja kweli au la. Alipofika huko, akanyata na kusogea karibu na mlango na kuanza kuisikiliza sauti ya msichana huyo ambaye alikuwa akizungumza na mtu mwingine kwa simu.
Mazungumzo yote aliyasikia, akapata uhakika kwamba Halima hakuwa msichana wa kawaida kama alivyosema Winfrida, akapata uhakika kwamba msichana huyo alifika mahali hapo kwa ajili ya kumpeleleza na kujua kama alikuwa ndiye yeye au si yeye.
Halima alipotoka chooni, macho yake yakagongana na Godwin ambaye alijifanya kutokujua kitu chochote kile kilichokuwa kikiendelea, alimwangalia msichana huyo, hapohapo akaanza kutoa tabasamu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Umemaliza?” aliuliza Godwin.
“Kumalizi nini shemeji?”
“Kujisaidia ili na mimi niingie manake tumbo limeanza kunivuruga,” alisema Godwin huku akiachia tabasamu pana lililokuwa na lengo la kumsahaulisha msichana huyo, asijue chochote kama kweli mwanaume huyo alikuwa Godwin aliyekuwa akimtafuta.
“Nimemaliza!” alisema Halima, akateremka ngazi ndogo na kuelekea chumbani. Godwin akaingia chumbani kwake, moyo wake ulikuwa na hofu, alijua dhahiri kwamba kama asingefanya lolote liwezekanalo basi msichana huyo angeweza kumkamata kizembe sana. Alichokihitaji kwa wakati huo ni namba yake ya simu tu.
Alipokaa kwa dakika kadhaa, akarudi chumbani ambapo akaungana na wasichana hao na kuanza kupiga nao stori. Alimuonyeshea Halima hali ya kumzoea sana, hakutaka msichana huyo awe na hofu yoyote ile, mwisho kabisa wakati akiaga, akamuomba namba ya simu ambapo kwa Halima halikuwa tatizo lolote lile, akamgawia ili kumfanya kuwa karibu naye.
“Amekwisha!” alisema Godwin.
Halima aliyejulikana kwa jina la Angelica akaondoka huku Winfrida akimsindikiza, haraka sana Godwin akachukua kompyuta yake ya mapajani na kuiwasha, alitaka kufanya vitu kwa haraka, kuingilia mawasiliano ya msichana yule.
Akaiingiza namba ile katika kompyuta yake na kisha kuifungua progamu yake iitwayo SpyGd ambayo aliitengeneza yeye mwenyewe na hakuwa ameisambaza sehemu yoyote ile. Akaiingiza namba ile, kompyuta ikaanza kumuonyeshea sehemu iliyoandikwa download ambapo kwa mbele kulikuwa na asilimia zilikuwa zikisogea mbele.
Ilipofika asilimia mia moja, ikabadilika na kujiandika searching, ikaanza kuitafuta simu ile na ilipoipata, ikaanza kuonyesha asilimia nyingine zikipanda huku kukiwa na neno lililoandikwa Hacking process.
Mpaka inafika mia moja, tayari alikuwa na uwezo wa kuingia katika simu ya Halima. Aliangalia meseji zote, aliona mawasiliano yote na kulikuwa na namba moja kutoka nchini Uswisi ambayo alikuwa amepigiwa na kupiga.
Alichokifanya ni kukata mawasiliano baina ya namba yake na namba ile ya Uswisi na kisha kuiingiza namba yake kwa namba ile na kuiiba kisha kuingia Google, akatafuta picha ya mwanaume mweusi kisha kuandika ujumbe kwenda kwa Halima huku akitumia namba ile ya Uswis, ujumbe uliosomeka:
“We have found his picture,” (tumeipata picha yake) aliandika.
Ujumbe huo ukaenda kwa Halima, alipoupata, haraka sana akaandika ujumbe wa kuomba kutumiwa picha hiyo ili aone kama kweli yule aliyekuwa amempata alikuwa ndiye yeye au mwingine.
“Send it to me,” (nitumie)
Hapohapo Godwin akamtumia picha ya mwanaume yule aliyoitoa Google. Ilikuwa picha ya mwanaume mweusi, Halima alipoiona na kuikumbuka sura ya Godwin ambaye alikutana naye, vilikuwa vitu viwili tofauti.
“Is he the one you found?” (ndiye yeye uliyempata?) aliuliza Godwin pasipo Halima kujua kama alikuwa akiwasiliana na mwanaume huyo.
“No! This is another one,” (hapana! Huyu mwingine kabisa) alijibu Halima.
Msichana huyo alichanganyikiwa, alijipa uhakika kwamba hatimaye Godwin alikuwa amepatikana lakini ujumbe wa simu alioupata kutoka nchini Uswisi tena huku ukiambatanisha na picha ya huyo Godwin aliyekuwa akitafutwa, ukamvunja moyo na kuona kwamba kazi kubwa aliyokuwa ameifanya haikuwa na faida yoyote ile.
Huo ndiyo ukawa mwisho wa kuelekea kwa Godwin kwani aliamini kwamba hata kama angekwenda huko na kudumisha urafiki na Winfrida bado kungekuwa na ugumu wa kumpata kwa kuwa yule aliyefikiri kwamba alikuwa Godwin, hakuwa mwenyewe.
Akaiprinti picha ile, akawa nayo kila alipokuwa akienda. Akaanza kumtafuta mwanaume huyo hapo Tandale. Hakujua kama hiyo ilikuwa picha ya mtandao ambayo ilitolea huko nchini Ghana. Kila siku alipokuwa akilala, aliiweka picha hiyo pembeni yake, alikuwa akiiangalia sura ile na kuikariri na kesho yake alikuwa akiingia mtaani na kuanza kumtafuta.
Ilikuwa kazi ngumu, aliuona ugumu mkubwa mbele yake, hakutaka kukata tamaa, aliendelea kupambana kwa ajili ya kuhakikisha anampata mtu huyo na kumkamata kama ilivyotakiwa kuwa.
Wakati Godwin akiwa ameidukua namba ya Bwana Kom kule Uswisi, pia aliidukua namba ya Halima, kwa maana hiyo Kom alipokuwa akimtumia ujumbe Halima, mtu aliyekuwa akijibu alikuwa Godwin na hata alima alipokuwa akimtumia Bwana Kom ujumbe, mtu aliyekuwa akijibu alikuwa huyohuyo Godwin.
“Umefikia wapi?” aliuliza Kom kupitia ujumbe mfupi wa meseji.
“Bado naendelea kumtafuta, nimejaribu kuwashirikisha baadhi ya watu na wamesema kwamba mtu huyo yupo, si mgeni machoni mwao,” alijibu Godwin na kwa Bwana Kom ilionyesha kama Halima ndiye aliyeituma meseji hiyo.
****
Rais Bokasa alichanganyikiwa, hakuamini kilichokuwa kikiendelea kwamba hata yule bilionea mkubwa, Bwana Kizota hakuwa akimkubali na alisema wazi kwamba alikuwa akimchukia kwa kuwa yeye ndiye alikuwa mtu aliyechangia kwa Tanzania kuwa kama ilivyokuwa.
Moyo wake ukawa na hasira kali, hakutaka kuchelea, hapohapo akampigia simu IGP Ng’osha na kumwambia kwamba ndani ya dakika kumi tu alitaka kuona bilionea huyo akikamatwa kitu ambacho kilifanyika ndani ya dakika saba tu.
Mambo yalianza kuharibika, hali ya nchi ilianza kusumbua, ilimuumiza kichwa na kuhisi kwamba watu hao walikuwa wakitumiwa na mtu fulani, alihisi kwamba alikuwa Godwin lakini baadaye akaona kwamba kijana huyo asingeweza kuwatumia watu hao, mkurugenzi wa Usalama wa Taifa na Bilionea Kizota, hakika kilikuwa kitu kisichowezekana.
Kwenye mitandao, kila mtu alikuwa akizungumza lake, watu wengi walifurahi kwani hawakumpenda rais huyo hata kidogo. Wakati mwingine watu waliona hiyo miezi miwili mpaka rais huyo kujiuzulu au kupinduliwa ilikuwa mingi mno, kila mmoja alitamani kuona jambo hilo likitokea hata muda huo.
Hakuwa na kimbilio, aliogopa, wakati mwingine aliitwa na marais wenzake wa Afrika kwa lengo la kwenda huko na kupumzisha akili lakini alikataa kabisa kufanya hivyo kwa kuhisi kwamba kama angeondoka nchini basi angeweza kupinduliwa huku nyuma.
“Bado kuna mambo mengi napambana nayo, siwezi kuja huko, nataka nipambane mpaka nitakapoona mwisho wake nini,” alisema Rais Bokasa.
Huo ndiyo ulikuwa ukweli wenyewe, hakutaka kuondoka nchini Tanzania, aliendelea kubaki huku akisimamia msimamo wake kwamba kamwe asingeweza kuondoka kwani kama angefanya hivyo basi huo ndiyo ungekuwa mwisho wa kila kitu.
Alitamani kuwa rais milele, hakutaka kuachia madaraka kwa kuamini kwamba kwa yale yote ambayo aliyafanya, ingetokea siku moja kutoka madarakani basi angeweza kushtakiwa kwa uchafu wote aliokuwa ameufanya katika kipindi chake cha madaraka.
“Ila nini kitatokea kama siku nikipinduliwa kama anavyosema Godwin kwenye mitandao? Inawezekana amewaandaa watu kwa ajili ya kufanya hivi! Nitafanya nini?” alijiuliza huku akiwa chumbani kwake.
Hapo ndipo alipopata wazo kuwasiliana na mtu aliyeitwa kwa jina la Mikel Ludovic, mwanaume aliyekuwa akiishi nchini Urusi ambaye alikuwa miongoni mwa wanajeshi waliokuwa wakitengeneza mabomu ya nyuklia nchini humo.
Akataka kuonana naye, yaani mwanaume huyo asafiri mpaka nchini Tanzania na kuzungumza naye. Hilo halikuwa tatizo, mwanaume huyo akasafiri na kuingia nchini Tanzania kisiri huku watu wakiwa hawajui kama Ludovic alikuwa nchini.
Wakakutana na kuzungumza mambo mengi, alichokuwa akikihitaji rais huyo ni gesi aina ya nitrogen trioxide iliyokuwa na sumu kali. Alimwambia kwamba alitaka aandaliwe sumu hiyo kwa kuwa alikuwa na kazi kubwa alitaka kuifanya.
“Haina shida. Nitakuletea ujazo wa kutosha kabisa,” alisema Ludovic na kuondoka.
Ulikuwa mpango wa siri ambao alikuwa ameuandaa na mwanaume huyo, hakutaka kitu chochote kile kijulikane kwani hata watu wa hapo ikulu walimuona Mzungu huyo akiingia lakini hakukuwa na aliyejua sababu ya mwanaume huyo kufika nchini na kuonana na rais huyo.
“Hakuna mtu atakayeweza kukaa ikulu. Ama zangu ama zao,” alisema Rais Bokasa huku akionekana kudhamiria hasa kuhakikisha anabaki ikulu mpaka kifo chake.
Ludovic alikuwa ndani ya ndege, moyo wake ulikuwa na furaha tele, katika maisha yake, hakukuwa na kitu alichokuwa akikichukia kama watu waliokuwa na ngozi nyeusi. Alikuwa akitengeneza mabomu ya nyuklia huku kila siku akimsisitiza rais wake kwamba kama inawezekana waende Afrika na kuhangamiza bara zima ili weusi wasiendelee kuwepo tena.
Kitendo cha kuitwa na rais huyo na kuambiwa kwamba alitakiwa kusafirisha gesi kwa ajili ya kufanya mauaji hayo, kwake alikuwa na furaha tele, tena wakati mwingine alimshukuru Mungu kwa kuwa alikisikia kilio chake.
“Hiki ndicho nilichokuwa nikikitaka. Ameagiza ujazo wa lita kumi. Mimi nitamtumia ujazo wa tani moja kabisa. Yaani ikiwezekana nchi nzima aiangamize kwa sumu hiyo,” alisema Ludovic huku ndege ikikata mawingu kuelekea Moscow nchini Urusi.
***
Jenerali Ojuku alikuwa chumbani kwake, kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, aliikumbuka familia yake ambayo mpaka kipindi hicho hakujua mahali ilipokuwa. Moyo wake ulijawa na hasira tele, hakuamini kama kweli mwanajeshi yeye, mwenye cheo kikubwa nchini Tanzania ambaye nyuma yake kulikuwa na vikosi vyote vya jeshi alichezewa mchezo kama ule.
Alihuzunika, wakati mwingine alikuwa akisimama na kutembea huku na kule, aliumia moyoni mwake na hakujua ni kitu gani ambacho angefanya ili kuipata familia yake hiyo ambayo kwake ilikuwa kila kitu.
Wakati amekaa hapo, simu yake ya mkononi ambayo ilikuwa mezani ikaanza kuita, hakuifuata na kuipokea, aliiacha iendelee kuita mpaka ilipokata na baadaye kuanza kuita tena. Kwa kuwa ilikuwa ni kelele, akaifuata na kuangalia kioo, hakuiona namba bali maneno yaliyoandikwa ‘Private call’, akaipokea kwani alimjua mpigaji.
“Hallo!” aliita mara baada ya simu kuiweka sikioni.
“Nisikilize kwa makini sana. Leo inaweza kuwa siku yako ya mwisho kwa familia yako kuvuta pumzi ya dunia hii,” alisikika Godwin.
Ojuku akashusha pumzi ndefu, hakukuwa na maneno yalilouchoma moyo wake kama kuambiwa maneno mabaya kuhusu familia yake, akajua kabisa kwamba huyo mwanaume alitaka kufanya kitu fulani, hivyo akabaki akimsikiliza.
“Ninataka ufanye kitu kimoja.”
“Kitu gani mkuu?”
“Uite waandishi wa habari, useme kwamba humuamini rais na hivyo utamtaka aondoke madarakani haraka sana,” alisema Godwin.
“Unasemaje?”
“Una saa tano za kufanya hivyo! Usipofanya, utazikuta maiti za familia yako ufukweni,” alisema Godwin na kukata simu.
“Halo..halo..halo..” aliita Ojuku lakini tayari simu ilikuwa imekatwa.
Hakuamini kile alichokuwa ameambiwa, kwake, aliona mawenge, alichanganyikiwa kupita kawaida kwani katika maisha yake yote hakuamini kama ingetokea siku ambayo angeambiwa maneno kama hayo.
Kwake, familia yake ilikuwa bora zaidi lakini kile alichokuwa ameambiwa kilimchanganya sana kichwa chake. Pale kochini alipokuwa amekaa alipaona kama padogo, akasimama na kuanza kufikiria kwa makini kila neno aliloambiwa.
Hakuwa na jinsi, kama alitaka kuiokoa familia yake alitakiwa kufanya kile alichoambiwa kwani hata alipojifikiria sana, rais huyo hakuwa akipendwa, kila mtu alitamani kuona siku yoyote ile akiondoka madarakani.
Hapohapo akachukua simu na kumpigia Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally na kumwambia kwamba alitaka kuonana na waandishi wa habari kutoka katika Kampuni ya Magazeti ya Global Publishers, baada ya hapo, akavipigia simu vyombo vingine vya habari kwamba alikuwa akitaka kuzungumza nao maneno kuhusu hali iliyokuwa ikiendelea nchini.
Waandishi walipopewa taarifa, haraka sana taarifa hizo zikarushwa katika mitandao ya kijamii ambapo huko kila mtu akabaki na maswali, hali iliyokuwa ikiendelea nchini ilimfurahisha kila mmoja kwani kitu ambacho hawakuwa wakikipenda kuona kikiendelea ni kitendo cha rais huyo kuendelea kuiongoza Tanzania.
“Naye anataka kumkataa rais au?” aliuliza jamaa mmoja.
“Mmh! Kwa Ojuku? Hakuna kitu kama hicho!”
“Sasa kwa nini naye amewaita waandishi wa habari?”
“Labda anataka kuwaeleza kuhusu msimamo wake kwamba jeshi la wananchi litamuunga mkono rais mpaka mwisho,” alisema jamaa mwingine.
“Hebu tusubiri tuone!”
Kila mtu masikio yake yalikuwa huko, watu ambao walikuwa bize na mambo yao, wakaachana nayo na kuanza kusikiliza kile kilichokuwa kikiendelea huko. Mitandao mingi ya habari ikaanza kurusha kila kitu kilichokuwa kikiendelea huko.
Hakukuwa na mtu aliyejua kile kilichokuwa kikiendelea, hata Meja Jenerali naye hakujua kitu chochote kile na hata alipokuwa akimpigia simu mkuu wake kumuuliza kile alichotaka kuzungumza, hakumwambia kitu chochote kile.
Zaidi ya waandishi wa habari themanini walikusanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee kwa ajili ya kusikiliza kile walichokuwa wameitiwa mahali hapo. Baada ya dakika ishirini, magari ya kijeshi yakaanza kuingia mahari hapo na wanajeshi zaidi ya ishirini wakateremka huku wakiwa na bunduki zao kana kwamba walikuwa wakielekea vitani.
Gari alilokuwa Jenerali Ojuku likasimama, mwanaume huyo akasimama na moja kwa moja kuanza kuelekea katika ukumbi huyo huku waandishi wa habari wakimpiga picha mfululizo na wengine wakichukua video.
Alipofika ndani, akaelekea mahali ambapo paliandaliwa kwa ajili yake na kutulia hapo. Hakuzungumza kitu kwanza, akaanza kuwaangalia waandishi waliokuwa ndani ya ukumbu huo ambapo baada ya dakika kadhaa akaanza kuzungumza.
“Najua nyie wote mtakuwa mnafahamu mambo yanayoendelea ndani ya nchi hii! Ni mambo ya ajabu sana ambayo yaliwapelekea watu wengi kuona kwamba Rais Bokasa ananyanyasa watu na kujiona kwamba yeye ni rais wa milele,” alisema Ojuku, akanyamaza kidogo na kuendelea.
“Hili ni jeshi la wananchi, tunapoona mambo hayaendi sawa, chuki ya wananchi inakuwa kubwa, ni lazima tujiulize ni wapi tumekosea. Nimekaa na kujifikiria na mwisho wa siku kugundua kwamba nchi yetu inapotea, watoto na wajukuu zetu wataishi vipi kama sisi wenyewe hatutotengeneza mazingira mazuri kwa ajili yao?” aliuliza Ojuku na kuendelea:
“Jeshi la wananchi limekaa chini na kuamua kitu kimoja tu kwamba hatumuungi mkono Rais Bokasa na hivi ninavyoongea, ninampa saa moja kukusanya kila kitu kilicho chake ikulu na aondoke haraka sana,” alisema Ojuku.
Kitu ambacho hakikutegemewa na mtu yeyote ndani ya ukumbi ule, waandishi wa habari wote wakaanza kupiga makofi huku wengine wakishangilia. Tais huyo hakupendwa, kila mtu alitaka kuona akiondoka haraka sana madarakani kwani aliiharibu nchi na kujifanya mungu mtu ambaye hakusikia la mtu yeyote yule nje ya ikulu.
Ojuku hakuongea sana, alipomaliza akasimama na kuondoka zake huku nyuma akiacha shangwe ambazo hazijawahi kusikika kabla. Kwenye mitandao, kila mtu alikuwa akizungumza lake, hakukuwa na mtu ambaye hakuunga mkono msimamo wa jeshi la wananchi, kila mmoja alipongeza kwa hatua kubwa ambayo jeshi hilo limeliona, haraka sana waandishi wa habari wakaondoka hapo na kuelekea ikulu, walitaka kupiga picha kila kitu kilichokuwa kikiendelea huko, walitaka kumuona rais huyo akiondoka madarakani kwa agizo la Jenerali Ojuku au kama alishindwa, basi jeshi liingie kumtoa kinguvu.
***
Wiki moja ilipita tangu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Noel kuamua kujitoa kumuunga mkono. Moyo wake ulikuwa umevurugwa na kitu pekee alichokuwa akikisubiria kipindi hicho kilikuwa ni gesi ya sumu ambayo aliiagiza kutoka nchini Urusi ifike na yeye kufanya kile alichokusudia kufanya.
Hakutaka kuondoka madarakani, alilewa, alitaka kuona akiendelea milele na wakati mwingine alikuwa akijilaumu kwamba kwa nini hakufanya yale ambayo wananchi walitakata kuona akiyafanya, alijiona kuwa mjinga, lakini pamoja na hayo yote, hakutaka kuona akiondoka ikulu pasipo kufanya jambo lolote lile.
Akaendelea kuwasiliana na Ludovick ambaye alimwambia kwamba tayari mzigo wa gesi ya sumu ulitumwa kutoka nchini Urusi kwa kutumia meli na muda wowote ule mzigo ungewasili nchini Tanzania.
“Nimekutumia tani nzima,” alisema Ludovick kwenye simu.
“Nashukuru sana kwa kunijali. Nitakuingizia pesa zako,” alisema Bokasa na kisha kuzihamisha pesa kutoka kwenye akaunti yake na kumtumia Ludovick aliyekuwa nchini Urusi kama malipo yake.
Baada ya siku mbili akawatuma vijana wake kwenda nbandarini ambapo huko wakachukua mitundi minne ya gesi na kwenda nayo ikulu. Hakutaka kumwamini mtu yeyote, alitaka kufanya jambo ambalo aliamini kwamba lingeweka historia nchini Tanzania.
Baada ya siku kadhaa kupita na kusikia kwamba Jenerali Ojuku aliita waandishi wa habari kwa ajili ya kuzungumza nao, alijua kabisa kwamba naye alikuwa akienda kwa ajili ya kumkataa kwani kama angekuwa mtu wake, angempigia simu na kumwambia kile ambacho alikuwa njiani kuwaambia waandishi wa habari.
Alifungulia redio na kusikiliza kila kitu na familia yake. Moyo wake ulimuuma kupita kawaida, akaona kwamba alibaki yeye peke yake hivyo alitakiwa kupambana yeye kama yeye. Aliposikia kwamba alipewa saa moja tu kwa ajili ya kuondoka, akaiambia familia yake kwamba walitakiwa kuelekea nje ambapo wangechukua gari na kuondoka zao kwenda uwanja wa ndege.
“Na wewe?” aliuliza mkewe.
“Nitakuja tu! Nitakimbia Kenya. Nyie nendeni kwanza,” alisema Bokasa na familia yake kuondoka.
Ikulu nzima alibaki peke yake, alikuwa akijifikiria namna ya kuanza. Akachukua mitudi ile ya gesi na kuanza kunyunyizia katika kila chumba, alitaka kumuua mtu yeyote ambaye angeingia ndani ya jumba hilo kubwa. Alipulizia kwenye kila chumba na alipomaliza, akachukua simu yake, akaenda kwenye akaunti ya serikali na kuhamisha pesa zote zaidi ya dola trilioni kumi na kuzipeleka katika akaunti yake ya siri nchini Ubelgiji.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Yeyote atakayeingia, hakika atakufa,” alisema Bokasa, akatoka nje ambapo akachukua gari, likampeleka ufukweni kisiri, akapanda boti na kuanza safari ya kuelekea Mombasa huku akiwa ameacha sumu ya kutosha ndani ya jumba lile.
Baada ya saa moja kutimia, Jenerali Ojuku akawaambia wanajeshi wake kwenda ikulu na kuvamia ili hata kama rais huyo alikuwa ndani ya jumba hilo basi waweze kumchukua na kuondoka naye.
Hiyo ilikuwa ni amri ambayo moja kwa moja ikapokelewa na wanajeshi hao na kuanza kuelekea huko. Walipofika, wanajeshi ishirini wakaanza kuingia ndani huku wengine wakibaki nje.
Wakaingia ndani mpaka sebuleni ambapo hapo wakaanza kuelekea kwenye vyumba vingine. Walipoanza kufungua tu, wanajeshi hao wakaanza kuanguka kama mizigo, gesi kali yenye sumu ikawapata na hivyo kuwapukutisha kama kuku.
“This is insane,” (huu ni wendawazimu)
“Boss! We have to wait for a little bit,” (bosi! Tusubiri kidogo)
“For how long?” (kwa muda gani?)
“Atleast two weeks.” ( Hata kwa wiki mbili)
Bwana Kom alichanganyikiwa, hakuelewa ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea nchini Tanzania, kwake, Godwin alikuwa mtu mdogo sana ambaye hakutakiwa kutumiwa nguvu kumtafuta lakini kitu cha ajabu, Halima alikuwa mtu wa tatu kutumwa huko lakini hakukuwa na mafanikio yoyote yale.
Hakutaka kusikia jambo lolote lile kwa wakati huo, kitu alichokuwa akikihitaji ni kuona mwanaume huyo akikamatwa tu. Alihamisha kiasi kikubwa cha pesa kutoka katika Benki ya Geneva, kitendo cha kushindwa kumkamata kilimaanisha kwamba wateja wasingekuwa na imani na benki hiyo kubwa duniani ambayo ilikuwa na wateja wengi kipindi hicho.
Aliamini kwamba mtu aliyekuwa akiwasiliana naye alikuwa Halima, kila alipomtumia meseji, alijibu kwa kumwambia kwamba hali ilikuwa ngumu, mategemeo makubwa aliyokuwa nayo ya kumkamata mtu huyo hakuwa nayo tena kwani kila alipokuwa akimtafuta, hakuambulia kitu chochote kile.
Siku zilikatika, hakupata majibu chanya, hiyo ilimsikitisha na wakati mwingine kuona akifanya uzembe mkubwa mno. Alisubiri zaidi majibu kutoka kwa msichana huyo lakini kila siku majibu yalikuwa yaleyale.
Akawasiliana na mkurugenzi wa Benki ya Geneva, alitaka kujua kama akaunti zile zilizohamishiwa pesa hizo zilirudishwa au la, alipowasiliana naye, akaambiwa kwamba hakukuwa na pesa yoyote iliyorudi.
Hilo lilimchanganya, vijana wa IT katika benki hiyo walipambana vya kutosha lakini hakukuwa na mtu aliyefanikiwa, waliziona pesa lakini kila zilipotakiwa kutoka, hazikutoka na mbaya zaidi, baadaye zikahamishwa kwenda nchini Marekani kisha kupelekwa katika akaunti nyingine ambayo hawakuifahamu.
Wakati Bwana Kom akipambana kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Godwin anapatikana, Godwin mwenyewe alikuwa akihangaika kumuondoa Rais Bokasa kutoka madarakani. Alihakikisha anaitumia akaunti yake ya Mabadiliko ya Kweli kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata taarifa ambazo wasingeweza kuzipata sehemu yoyote ile.
Watu walitembelea huko, kwa siku zaidi ya watumiaji milioni thelathini walikuwa wakiingia kuona ni kitu gani kilikuwa kikiendelea huko. Akaunti ile ilizidi kupata nguvu na watu wengi kutamani kumuona huyo mtu aliyekuwa akiiendesha akaunti hiyo, alifananaje na kwa nini alikuwa akipata data nyingi kiasi kwamba mpaka viongozi wenyewe walikuwa wakishangaa.
Winfrida hakujua ni mwanaume wa aina gani alikuwa naye, alipenda sana kutembelea akaunti hiyo iliyokuwa katika Mtandao wa Kijamii wa Instagram, alipenda kila kitu kilichokuwa kikiandikwa humo lakini hakujua kama mwanaume aliyekuwa naye ndiye aliyekuwa akihusika na akaunti hiyo ambapo alikuwa akiandika kwa kupitia simu yake ambayo aliificha na wakati mwingine kutumia kompyuta yake.
“Nimesikia Jenerali Ojuku anaita waandishi wa habari kwa ajili ya kuzungumza nao, naye kuna jambo anataka kufanya au?” aliuliza Winfrida huku akimwamsha mpenzi wake aliyekuwa amelala.
Haraka sana Godwin akashtuka kutoka usingizini, kitendo cha kusikia kwamba mtu aliyekuwa amezungumziwa alikuwa Jenerali Ojuku, alitaka kusikia kile kilichokuwa kikiendelea. Alimpigia simu kabla na kumwambia kwamba alitakiwa kutokumuunga mkono Rais Bokasa, kitendo cha kuita waandishi wa habari kilimaanisha juu ya kile alichotakiwa kukifanya.
Akawasha kompyuta yake na kuanza kumwangalia, kwa jinsi alivyoonekana, hakuonekana kuwa na amani, moyoni mwake alikuwa na jambo kubwa alilotaka kuzungumza mahali hapo, waandishi wa habari kutoka katika vyombo mbalimbali vya habari walikuwa mahali hapo kwa ajili ya kuripoti kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
Alizungumza kwa marefu lakini mwisho wa siku akaweka wazi kila kitu kwamba hakuwa akimuunga mkono Rais Bokasa na alimalizia kwa kumpa saa moja tu la kuondoka ikulu kwani nchi ingekuwa chini ya jeshi kwa siku kadhaa.
Winfrida akabaki akitabasamu, hakuamini alichokuwa amekisikia, kitu ambacho kila siku alimuomba Mungu ni kumuona rais huyo akiondoka madarakani. Alikuwa kiongozi mbaya, aliyetumia kiasi kikubwa cha pesa kwa matumizi yake binafsi lakini pia alihakikisha kila mtu anayekuwa waziri anakuwa na roho ya tamaa kama aliyokuwanayo na ndiyo maana nchi haikusonga mbele, hakukuwa na kiongozi aliyekuwa na uchungu na nchi yake.
Alipomaliza, Godwin akafungua programu yake kwa ajili ya kuangalia simu ya Rais Bokasa, alijua fika kwamba rais huyo alikuwa amepanga mipango siku hiyo kwa ajili ya kukimbia nchi na kwenda sehemu nyingine. Alipoingiza namba hiyo na kuangalia, akaona kitu ambacho kilichomshtua sana.
Akaona mawasiliano yaliyokuwa yakifanyika baina yake na mtu aliyejulikana kwa jina la Ludovick kutoka nchini Urusi. Haraka sana akaingia Google na kuangalia kuhusu mwanaume huyo, alitaka kujua ni nani na alikuwa akijihusisha na jambo gani.
Alichokiona ni kwamba mwanaume huyo alikuwa mtengeneza mabomu ya nyuklia nchini Urusi aliyekuwa na uwezo mkubwa kiasi kwamba hata Marekani wenyewe walikuwa wakimuhofia. Aliyaona mazungumzo yao kwa njia ya meseji, akaingia katika barua pepe yake pia ambapo huko akaona kukiwa na ujumbe kuhusu sumu ya gesi ambayo ilitakiwa kuingizwa nchini Tanzania na kuipulizia katika kila chumba ikulu.
“Mungu wangu! Kumbe sumu iliagizwa tangu juzi!” alisema Godwin huku akionekana kushtushwa na kile alichokuwa akikiona.
Haraka sana akampigia simu Ojuku kwa lengo la kumweleza kile kilichokuwa kimetokea kwamba kama inawezekana akawasiliana na wahusika kuzuia watu kuingia ndani ya ikulu kabla ya watalaamu wa masuala ya gesi kwenda kupulizia gesi nyingine kwa ajili ya kuitoa sumu hiyo.
Kila alipompigia simu Ojuku, haikupokelewa. Hiyo ilimpa presha kubwa, akaona kwamba kama angechelewa basi kungekuwa na waathirika wa sumu hiyo, akavaa nguo zake haraka sana, hakutaka kubaki mahali hapo, piga ua ilikuwa ni lazima kuhakikisha kwamba hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kuingia ndani ya ikulu hiyo.
“Vipi tena?” aliuliza Winfrida, kila alipomwangalia mpenzi wake namba alivyokuwa akibadilisha nguo harakaharaka, hakumwelewa.
“Kuna kitu natakiwa kukiwahi.”
“Kitu gani?”
“Subiri! Nitakuja, nitakwambia,” alisema Godwin, hakutaka kuendelea kubaki chumbani humo, akaondoka kuelekea huko.
Njiani, hakuacha kumtafuta Jenerali Ojuku kwenye simu, kama kawaida mwanaume huyo hakuwa akipokea simu, iliendelea kuita zaidi na zaidi kitu kilichomfanya kutokufanikiwa kwa kile alichokitaka.
“Unajua kuendesha pikipiki kwa kasi kama ndege?” aliuliza Godwin huku akimwangalia dereva bodaboda.
“Hilo wala usijali! Una moyo wa kuvumilia?” aliuliza dereva bodaboda kwa kujiamini.
“Ndiyo maana nikauliza unajua!”
“Ninajua! Hata ukitaka niendeshe kama Air Force One, wewe tu,” alisema dereva huyo.
“Niwahishe Magogoni.”
“Mjini?”
“Ndiyo!”
“Huko wanakataza bodaboda kuingia!”
“Hata kwa malipo ya laki moja bado hutaki kuingia?”
“Kama ni hivyo poa. Kalia mchuma nikisanue,” alisema dereva huyo kwa lugha ya kihuni, Godwin akapanda na kuondoka mahali hapo.
Kasi waliyoondoka nayo kila mtu alishangaa. Muda wote Godwin macho yake yalikuwa kwenye saa yake, muda aliokuwa ametoa Ojuku zilibaki dakika mbili tu kabla ya wanajeshi kuingia ndani ya ikulu hiyo na kumuondoa rais huyo kinguvu.
Hakukuwa na foleni iliyowababaisha, walipenya katikati ya magari, kwa kasi kubwa na hata pale kulipokuwa na mataa kama Magomeni, Fire walipita kana kwamba walikuwa majambazi waliotoka kuiba benki.
Walichukua dakika tano tu mpaka kufika Magogoni ambapo dereva aliposimamisha tu pikipiki yake, Godwin akateremka pasipo hata kuzungumza na dereva huyo. Akaanza kupiga hatua kwenda getini ambapo kulikuwa na wanajeshi zaidi ya ishirini waliosimama wakiwa na bunduki zao.
“Wewe nani? Simama! Hutakiwi kusogea huku,” alisema mwanajeshi mmoja huku akimwangalia Godwin.
“Kuna kitu! Humo kuna sumu!” alisema Godwin huku akisogea kwa kasi.
“Nimesema simama!”
“Huko kuna sumu! Rais ameacha sumu vyumbani,” alisema Godwin huku akiwasogelea wanajeshi wale waliokuwa wakimnyooshea bunduki.
“Paa....paa...paa...” ilisikika milio ya risasi zilizokuwa zimepiga chini, karibu kabisa na miguu yake kumtaka kusimama. Akatii na kusimama.
“Unataka nini? Umetoka wapi? Wewe ni nani?” yalikuwa maswali matatu mfululizo yaliyotoka kwa mwanajeshi mmoja aliyekuwa na kitambaa kilichoandikwa MP mkononi.
“Rais amecha sumu ya gesi, naomba asiingie mtu, huyu rais anataka kummaliza kila mtu atakayeingia humu,” alisema Godwin huku akiwaangalia wanajeshi hao waliokuwa wakimshangaa.
Hata kabla hajaeleza zaidi kile kilichokuwa kimetokea ndani ya vyumba vya ikulu ile, wanajeshi wakashangaa kuwaona wenzao wakianza kutoka nje huku wakikimbia, wengine wakaanza kuanguka huku wakikohoa, damu zilikuwa zikiwatoka midomoni, puani, machoni na masikioni.
Kila mmoja alishangaa, hawakujua kilichokuwa kikiendelea mpaka wanajeshi hao kuwa katika hali hiyo. Wakaogopa, hapohapo Godwin akawaambia kwamba walitakiwa kuondoka katika eneo hilo, ikulu haikukalika, kulikuwa na gesi yenye sumu iliyokuwa imepulizwa humo ndani.
“Sogeeni, sumu inasogea huku. Tokeni huko,” alisema Godwin hali iliyowafanya wanajeshi hao waliokuwa wamesimama hapo getini kusogea.
Waliwaona wenzao wakihangaika, wakiomba msaada, sumu ilikuwa ikiwateketeza, iliwamaliza lakini hakukuwa na mtu aliyesogea, kila mmoja alikuwa akiogopa. Moyo wa Godwin uliuma, hakuamini kama Rais Bokasa angeweza kufanya upumbavu kama ule.
Kwa kuwa yeye ndiye aliyeleta taarifa kuhusu sumu ile, walichokifanya wanajeshi hao ni kumuweka chini ya ulinzi, walitaka kufahamu baadhi ya vitu, yeye alikuwa nani? Alijuaje kama ndani ya ikulu ile kulikuwa na sumu iliyowamaliza wanajeshi wenzao?
“Mimi ni msamaria mwema. Niliweza kubamba mawasiliano ya Rais Bokasa na mtu anayejulikana kwa jina la Ludovick kutoka nchini Urusi,” alisema Godwin.
“Unatudanganya. Utakuwa umehusika katika upandikizaji wa sumu hii ndani ya hii ikulu. Mchukueni, mpelekeni kambini. Ninataka kusikia ukweli baada ya uso wake kupendeza na kuonekana mnene, akikataa, mpeni kaoshi avae,” alisema mwanajeshi huyo kwa hasira, aliposema kwamba uso wake upendeze, alimaanisha apigwe sana mpaka avimbe, na aliposema akutwe amevaa kaoshi alimaanisha kwamba akatwe mikono kama tu hatosema ukweli juu ya kile kilichokuwa kimetokea.
Hapohapo wanajeshi wanne wakambeba msobemsobe na kumuingiza ndani ya gari. Hata kabla gari halijawashwa, tayari alianza kushushiwa mkong’oto hali iliyomfanya kulia kama mtoto, akajua tu kwamba huko alipokuwa akipelekwa, hakukuwa sehemu ya amani hata kidogo.
***
Kila mtu alikuwa na huzuni tele, hawakuamini kile kilichokuwa kimetokea kwamba wanajeshi zaidi ya ishirini walikufa walipokuwa wameingia ikulu. Kila mmoja alishangaa, hakukuwa na mtu aliyejua kama humo kulikuwa na sumu ya gesi, wengi wakahisi kwamba Rais Bokasa aliamua kuweka uchawi wake ambao ulimwangamiza kila mtu aliyeingia ndani.
Kwenye mitandao, kila mtu alikuwa akizungumzia lake, wengi walikasirika, walionyesha hasira zao waziwazi, hawakupenda kuona lile lililotokea, malalamiko yalikuwa mengi mno kiasi kwamba IGP Ng’osha akapiga mkwara kwamba hakukutakiwa na mtu yeyote aliyetakiwa kulizungumzia jambo hilo katika mitandao ya kijamii.
Wakati hayo yakiendelea, hakukuwa na mtu aliyeruhusiwa kuingia ndani ya jengo hilo tena, hali ilikuwa ni ya hatari na baada ya kugundua kwamba humo kulikuwa na gesi, walitakiwa kwanza kuwasiliana nao na watu wa kitengo cha gesi ili kufika mahali hapo na kueleza hiyo ilikuwa ni gesi ya aina gani na ilitakiwa kuondolewa namna gani.
Jenerali Ojuku alikasirika, kuwapoteza wanajeshi wake kwa dakika kadhaa ilimuuma moyoni mwake, alikasirika na muda mwingine alipokuwa akiongea, alionekana kuumia mno. Alitaka kujua mahali Bokasa alipokuwa, hata kama alikuwa amekimbia, ilikuwa ni lazima kumpata na kupelekwa mahakamani na kushitakiwa kwa kile alichokuwa amekifanya.
“Ni lazima atafutwe haraka sana,” alisema Ojuku huku akiwa amevimba.
“Sawa mkuu! Ila kuna mtu tumempata, nahisi naye alihusika katika hili,” alisema mwanajeshi mmoja.
“Yupo wapi?”
“Kambini!”
Hakutaka kuchelewa, hakukuwa na muda wa kupoteza. Hapohapo akaondoka kuelekea kambini. Njiani, alikuwa na hasira, kila kitu kilichotokea kwake ilikuwa ni aibu kubwa kwamba kwa nini katika uongozi wake litokee jambo la kijinga kama hilo? Hakutaka kuona akishindwa, ilikuwa ni lazima kupambana mpaka kuhakikisha kwanza Bokasa anapatikana haraka iwezekanavyo.
Alipofika kambini, akateremka na kuanza kuelekea ndani ya jengo moja ambalo ndipo alipoambiwa kwamba kijana huyo alikuwemo. Wanajeshi wote waliokuwa wakipishana naye walimpigia saluti kama kumuonyeshea heshima. Hakuwa na muda wa kujibu saluti hizo, alichokuwa akikitaka ni kuonana na kijana huyo tu.
Akatembea mpaka katika chumba kimoja kilichoandikwa Goligotha mlangoni, akaufungua mlango, alipoingia, macho yake yakatua kwa Godwin aliyekuwa kwenye kiti. Kwa kumwangalia tu ilikuwa vigumu kuamini kama mtu huyo alikuwa hai au tayari alikuwa amekufa.
Uso wake ulivimba, upande mmoja wa jicho ulikuwa mkubwa, mashavu yake yaliumuka huku damu zikiwa zimetapaa katika uso mzima. Alikuwa ametulia tu tena akiwa uchi wa mnyama. Akamsogelea kijana huyo na kumuinua uso wake, yeye mwenyewe alibaki akisikitika, hakusikitika kwa kuwa alimuonea huruma, alisikitika kwa sababu adhabu zote alizokuwa amepewa, alipewa wakati yeye akiwa nje ya chumba hicho.
“Imekuwaje? Huyu anajua aliyehusika?” aliuliza Ojuku huku akimwangalia Godwin.
“Ndiyo! Tumezungumza naye kirafiki, amesema hausiki na ndiyo maana tukamgusagusa kidogo tu,” alijibu mwanajeshi mmoja aliyekuwa pembeni, yaani pamoja na Godwin kupigwa vile kama adhabu ya kutakiwa kusema ukweli juu ya upandikizaji wa gesi ile ikulu lakini alidai kwamba walimgusagusa tu.
Ojuku alitaka kuzungumza naye, aliamini kwamba Godwin alikuwa akijua kila kitu. Alichokuwa akikihitaji ni kumpata Bokasa ambaye alihisi kwamba hakuwepo nchini kwa kipindi hicho. Akahitaji Godwin achukuliwe na kupelekwa sehemu kwa ajili ya kupumzika kwanza huku wakimfanyia matibabu kidogo ilimradi tu aweze kuzungumza.
Hakutaka kuondoka mahali hapo, ilikuwa ni lazima kuhakikisha kwamba Bokasa anapatikana haraka sana. Akawasiliana na jeshi la anga, maji na nchi kavu, kote huko aliwaambia kuweka ulinzi wa kutosha mpaka mwanaume huyo kukamatwa lakini cha ajabu, hakukuwa na mtu yeyote aliyetoa taarifa kama mwanaume huyo alinaswa sehemu fulani.
Alisubiri kwa saa saba ndipo Godwin akaanza kupata nafuu. Kwanza akapewa chakula, akala kwa tabu, alipomaliza, akachukuliwa na kupelekwa katika chumba kingine kwa lengo la kufanyiwa mahojiano na jenerali mwenyewe.
“Ulijuaje?” aliuliza huku akimwangalia usoni.
“Nilinasa mawasiliano yake kwa njia ya barua pepe. Aliagiza sumu kutoka nchini Urusi kwa mtu anayeitwa Ludovick,” alisema Godwin kwa sauti ndogo.
“Hebu nionyeshe!”
“Sina simu.”
Hilo halikuwa tatizo, akaletewa simu yake ambapo akaingia na kuanza kumuonyeshea barua pepe hiyo. Yeye mwenyewe alishangaa, hakuamini kama rais huyo angefanya kitu cha kipumbavu kama hicho.
Mbali na hiyo, pia Godwin akamuonyeshea barua pepe nyingine zilizokuwa zimeingia humo kwenda kwa rais wa Kenya, Bwana Onyango na kumwambia kwamba alikuwa njiani kuelekea nchini humo kwa ajili ya kujificha kabla ya kuelekea nchini Ubelgiji.
“Yupo njiani kwenda Kenya. Anakwenda kwa njia gani? Hajafafanua kama ni gari, ndege au meli,” alisema Ojuku huku akionekana kuchanganyikiwa.
Tayari alimuona Godwin kuwa kijana mzuri ambaye angeweza kumsaidia kupata vitu vingine. Alichokifanya ni kuagiza kupatiwa matibabu haraka sana kwani kulikuwa na vitu vingi alitakiwa kusaidiana naye.
Akawataka wanajeshi wote wa anga, maji na ardhi kuwa makini kwani iwe isiwe ilikuwa ni lazima mwanaume huyo akamatwe hata kabla hajafika nchini Kenya bila kujali ni kwa usafiri gani alikuwa akiutumia kwenda huko.
Polisi wa barabarani hawakutakiwa kukaa huko, walikaa wanajeshi ambao walikuwa wakipekua kila gari lililokuwa likipita barabarani kuelekea mikoani. Kila kona walipokuwa wakimtafuta mwanaume huyo, hawakuweza kumpata, walishangaa, kama hakuwa ameondoka kwa ndege, sasa kulikuwa na ugumu gani wa kumpata?
“Bado hajapatikana?” aliuliza Ojuku.
“Ndiyo mkuu! Ila tutampata tu kwani mipaka yote imefungwa, hakuna anayeruhusiwa kuingia au kutoka nchini,” alisema mtu aliyekuwa upande wa pili.
“Basi endeleeni kupambana.”
Rais Bokasa alikuwa njiani kuelekea nchini Kenya. Ilikuwa saa 1:00 usiku. Alikuwa ndani ya boti yake ya kawaida sana ambayo hakuwa amewaambia watu kuhusu boti hiyo kwa kuamini kwamba kuna siku jambo kama hilo linalotokea lingetokea.
Alimwambia nahodha wake aendeshe taratibu, hakutaka kabisa kugundulika kama yeye ndiye alikuwa ndani ya boti hiyo. Hakukuwa na mizigo, humo, kulikuwa na begi lake ambalo ndani kulikuwa na nguo za mkewe, manukato na wigi, yote ilikuwa ni kuhakikisha kwamba anabadilisha muonekano wake.
Wakati safari ikiendelea, akachukua begi lile, akalifungua, akatoa nguo za mkewe na kuanza kuzivaa. Akachukua wanja, akaupaka, akausafisha uso wake vilivyo na kupaka lipstiki, akavaa viatu vya kike na nguo nyingine kuweka kwenye makalio yake kuonyesha kwamba alikuwa na wowowo.
Alibadilika kwa asilimia kubwa na kwa kumwangalia tu ingekuwa vigumu kugundua kama huyo alikuwa Rais Bokasa akiwa kwenye harakati zake za kuikimbia nchi hiyo. Boti ilikuwa ikiondoka kuelekea mbali kabisa, hawakutaka kupita katika upande wa Tanzania bali walichokifanya ni kuelekea katika upande wa kimataifa kwa ajili ya kusafiri kwa raha bila kubughudhiwa.
Wakati wakiwa wanakaribia katika eneo la kimataifa baharini, wakashtuka kuona boti moja ya kijeshi ikija kwa kasi kubwa kule walipokuwa huku mtu mmoja akisema kwenye kipaza sauti kwamba walitakiwa kusimama haraka sana.
“Tufanyeje?” aliuliza kijana wake.
“Simama! Wakikuuliza, waambie unakwenda kuvua na mama yako. Si uliweka nyavu kama nilivyokwambia?” aliuliza Rais Bokasa.
“Ndiyo!”
“Basi waambie hivyohivyo!”
Hawakuwa na uhakika kama wangeondoka salama, boti ikasimamishwa, haraka sana kijana yule akachukua nyavu na matenga mawili ambayo aliyaandaa kabla na kuyaweka tayari. Ndani ya sekunde kadhaa, boti hiyo ya kijeshi ikawafikia na wanajeshi wawili kusimama, wakarukia ndani ya boti ile.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nyie ni wakina nani?” lilikuwa swali la kwanza kutoka kwa mwanajeshi mmoja aliyeshikilia bunguki aina ya Ak-47
“Wavuvi, tunakwenda kuvua na mama yangu!” alijibu kijana yule, kwa jinsi muonekano aliokuwa nao, ilikuwa vigumu kukataa kama hakuwa mvuvi.
“Mama yako yupi?”
“Yule kule,” alisema kijana yule, mwanajeshi alipopiga macho kwa mtu aliyeonyeshea, yalitua kwa mwanamke mrembo, mwenye wowowo ambaye alikuwa ameinama huku akiwa amewapa mgongo, alikuwa akiweka vizuri nyavu.
“Wewe mwanamke!” aliita mwanajeshi huyo. Hapohapo Rais Bokasa akageuka na kuanza kuwaangalia huku akitabasamu.
Kila kitu, kuanzia uso mpaka muonekano mwingine alionekana kama mwanamke fulani mrembo kabisa. Alimuuliza maswali kadhaa huku akiwa amesimama kwa mbali, kwa jinsi alivyokuwa akijibu, sauti yake ya kike haikusikika sana kwani kulikuwa na mawimbi yaliyokuwa yakipiga ambayo yalisababisha kelele mahali hapo.
“Huyu ni kijana wako?” aliuliza mwanajeshi kwa sauti ya juu kabisa ambayo aliamini angeweza kusikika.
“Ndiyo baba! Tunakwenda kuvua kidogo. Wazima lakini? Mbona bunduki tena mpaka mnatutisha? Hatuvui kwa baruti jamani,” alisema Bokasa kwa sauti ya kike.
“Usijali mama! Tunajaribu kuhakikisha ulinzi mahali hapa,” alisema mwanajeshi huyo.
“Nashukuru baba yangu!” alisema Bokasa na mwanajeshi huyo kuondoka.
Akaingia ndani ya boti yao na kuondoka mahali hapo. Macho yake hayakutoka kwa mwanamke yule, alikuwa akimwangalia, hakuamini kama kulikuwa na mwanamke duniani aliyekuwa na umbo matata kama alilokuwa nalo yule aliyemuona ndani ya boti ile.
“Jamani kuna watu wameumbika, nadhani Mungu alipokuwa akiumba, aliacha kazi zake zote na kumuumba yule mama,” alisema mwanajeshi yule.
“Mama gani?”
“Yule aliyekuwa kwenye boti. Amevimba kama kala amira. Mama huyo, katuna katuna kweli, yaani ni shida, yule ukiwa naye ndani, haki ya Mungu unaomba likizo ya mwaka mzima, ukiondoka tu, baba mwenye nyuma kakuibia,” alisema mwanajeshi yule, alichanganyikiwa kiasi kwamba hakujua ni kwa jinsi gani alitakiwa kumsifia mwanamke yule, alimdatisha, mbaya zaidi, hakujua kama yule ndiye mtu waliyekuwa wakimtafuta kwa udi na uvumba. Meli ikaingia katika eneo la kimataifa na safari ya kuelekea Mombasa ikaendelea.
***
Kitendo cha wanajeshi wale kuondoka mahali hapo kilimpa uhakika kwamba wangefika salama Mombasa nchini Kenya na hivyo kuendelea na safari yake ya kuelekea nchini Ubelgiji.
Japokuwa alikuwa mlemavu wa miguu lakini alijitahidi mpaka kujiweka sawa kwa muda kiasi kwamba mwanajeshi yule hakugundua kabisa kilichokuwa kikiendelea.
Hakuonekana kuwa na hofu tena, alikuwa ameingia katika eneo la kimataifa, sehemu ambayo aliamini kwa namna moja ama nyingine asingeweza kukamatwa na mtu yeyote yule, kichwa chake kilikuwa kikifikiria maisha mapya ambayo angekwenda kuishi nchini huko kwani kama kufanya ubaya, aliufanya sana na kipindi hicho kilikuwa ni cha kuondoka na kwenda kuishi huko mbali.
Safari iliendelea kama kawaida, moyo wake ulikuwa na amani tele. Waliendelea na safari huku wakipiga stori nyingi, boti iliendelea na safari na kwa sababu boti hiyo ilikuwa ikikimbia kwa mwendo wa kasi usiku kucha, wakafanikiwa kutumia saa tisa mpaka kufika huko.
Akapokelewa pembezoni mwa Bandari ya Mombasa, vijana wa Rais Onyango wa hapo Kenya, akaanza kuzungumza nao kidogo na kupewa maelekezo kwamba alifuatwa yeye mahali hapo hivyo kukubaliana nao na kuondoka mahali hapo.
Njiani, alikuwa akiwasiliana na rais huyo, alimshukuru kwa kila kitu kilichotokea ila angemshukuru sana kama angemfanyia mipango ya kuondoka na kuelekea nchini Ubelgiji ambapo angeanza maisha mapya kwani tayari alihamisha kiasi kikubwa cha pesa kwenda katika moja ya benki nchini humo.
Walitumia saa kadhaa mpaka kufika Jijini Nairobi ambapo akapokelewa, akalala mahali hapo na kwa sababu Rais Onyango alipanga kusafiri kuelekea nchini Ubelgiji kama moja ya mipango yake ya kumsafirisha Bokasa nchini humo, siku iliyofuata wakaanza safari kuelekea uwanja wa ndege tayari kwa kupanda ndege na kuelekea nchini Ubelgiji.
"Tanzania wanasemaje? Sikupata taarifa yoyote ile," aliuliza Bokasa huku akionekana kuwa mwenye furaha tele.
"Wanarukaruka tu. Hivi kwanza imekuwaje kuhusu ile gesi, na mimi nataka siku niitumie nikizinguliwa nchini mwangu," alisema Rais Onyango.
"Rahisi sana! Kuna mtu nitakupa namba zake, anaitwa Ludovick."
"Yule Mrusi?"
"Ndiyo huyohuyo. Yule jamaa ni shida sana. Yaani anakupa kitu nachulo kabisa, ukiweka tu, mambo yanajipa," alisema Bokasa na wote kuanza kucheka.
"Daah! Huyo jamaa hatari sana!"
"Kwani imekuwaje? Ilijibu? Sikufuatilia habari!"
"Hahah! Wanajeshi ishirini palepale."
"Kweli?"
"Ndiyo! Watu wamemkimbiza rais, halafu wanaogopa kuingia ikulu. Hahaha!" alisema Rais Onyango na kucheka kwa sauti kubwa, hawakuishia hivyo, wakagongesheana mpaka mikono.
Siku hiyo haikuwa kama siku nyingine, taarifa za safari zote za Rais Onyango zilikuwa zikitangazwa katika televisheni mbalimbali lakini kwa safari hiyo, hakukutakiwa mtu yeyote yule afahamu. Ilikuwa ikifanyika kimya kimya na hakukutakiwa kuwa na mwandishi wa habari wa aina yoyote ile.
Baada ya saa ishirini na mbili, ndege hiyo ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Brussels uliokuwa hapohapo katika Jiji la Brussels. Wakateremka na kuanza kupiga hatua kuelekea katika mlango wa VIP ambapo wakapita pasipo watu wengine kugundua kwamba kwenye msafara ule wa rais huyo kulikuwa na rais mwingine ambaye alikuwa akitafutwa kwa udi na uvumba nchini mwake.
Japokuwa Bokasa alikuwa katika kiti chake cha matairi, hakukuwa na mtu aliyekuwa na hofu naye kabisa kwani huo haukuwa msafara wa kwanza wa rais kuingia nchini humo huku ukiwa umeongozana na mlemavu kama alivyokuwa Bokasa.
Wakatoka nje, wakaingia ndani ya magari yaliyokuwa yakiwasubiri na kuondoka. Mpaka kufika hatua hiyo, Bokasa akawa na uhakika wa kuwa salama maisha yake yote. Hakutaka kabisa kuisikia kuhusu Tanzania, aliichukia nchi hiyo, kwake, ilionekana kama Jehanamu ambapo hakutaka kurudi maisha yake yote.
Wakaelekea katika Hoteli ya Catalonia Grand Place na kuchukua vyumba huko. Maisha yakabadilika, kwa kuwa alikuwa nchini humo alihitaji kununua jumba la kifahari na kuanza maisha yake mapya hapohapo Brussels huku akiisubiri familia yake ambayo aliamini kwamba Rais Onyango angeifanyia mipango ya kwenda kujumuika naye huko alipokuwa.
"Utaishi vipi?" aliuliza Onyango.
"Nitaishi kwa amani na furaha. Niliiba pesa zote za serikali kiasi cha dola trilioni kumi na kukihamishia katika akaunti yangu kwenye benki kuu ya hapo Ubelgiji," alisema Bokasa huku akionekana kuwa na furaha tele.
"Dola trilioni kumi?"
"Ndiyo!"
"Basi wewe ni tajiri namba moja duniani. Ni pesa nyingi sana. Kama Bill Gates ana dola bilioni 89, wewe una dola trilioni kumi, basi wewe ndiye tajiri namba moja duniani," alisema Onyango na wote kuanza kucheka kwa furaha.
Kwa muda wa miezi sita ya misukosuko, hakukuwa na siku ambayo Bokasa alilala kwa amani na furaha kama siku hiyo. Alijiona kuwa bilionea mkubwa, kiasi cha pesa ambacho alikihamisha kutoka katika akaunti ya serikali nchini Tanzania kingemfanya kuyafurahia maisha yake mpaka kifo chake.
Siku iliyofuata hakutaka kubaki hotelini, akaondoka na kuanza kuelekea katika jengo kubwa la benki hiyo, alipofika, akakaribishwa. Wahudumu wa benki walipomuona tu, wakaanza kuzungumza kimya kimya kuhusu yeye, walimfahamu, alikuwa miongoni mwa marais wasiopendwa nchini Tanzania.
Hakutaka kujali, kwa kuwa alitaka kuangalia usalama wa pesa zake zilizokuwa zimeingia siku chache zilizopita, akaandika akaunti yake kwa lengo la kuangalia kama pesa zake zilikuwa salama.
"Mara ya mwisho kulikuwa na kiasi gani?" aliuliza dada aliyekuwa akimhudumia, walimchukulia kama rais wa kawaida.
"Dola trilioni kumi."
"Kweli?"
"Ndiyo!"
Dada yule akabaki akiiangalia kompyuta yake, hakuelewa kama mwanaume aliyesimama mbele yake alikuwa akizungumza kweli au alikuwa akimdanganya kwani kila alipokuwa akiangalia kwenye akaunti ile, hakukuwa na pesa yoyote ile, yaani salio lilisoma 0.00.
"Una uhakika uliweka humu?"
"Sasa dada yangu! Kwa nini nikudanganye? Kwani mimi siijui akaunti yangu?" aliuliza Bokasa huku akimwangalia msichana huyo.
"Sawa. Hebu pita huku kwanza, nisubiri katika kiti kile," alisema msichana huyo.
Hilo halikuwa tatizo hata kidogo, kitu pekee alichokuwa akikihitaji ni usalama wa pesa zake tu, akaondoka na kumsubiri msichana huyo, alipomfuata, akamchukua na kuelekea naye kwa meneja huku akiwa na karatasi kadhaa mikononi mwake.
Wakaelekea katika chumba kilichoandikwa General Manager na kuambiwa kusubiri hapo. Napo, wala hakuleta ubishi, akasubiri huku akiwa na wasiwasi, alihisi kulikuwa na kitu kilichokuwa kimetokea kwani ishu ya kuangalia salio lake katika akaunti yake hakukuwa na ubaya wowote ule.
Baada ya dakika kadhaa, akaitwa na sekretari na kuingia humo huku akikikokota kiti chake cha matairi. Alipofika, muonekano aliomkuta nao huyo meneja ulionyesha dhahiri kwamba kulikuwa na tatizo kubwa lililokuwa limetokea.
"Kabla ya yote! Kuna nini?" aliuliza Bokasa hata kabla ya salamu.
"Usijali! Karibu."
"Sawa. Ila kwanza ninataka kujua, nini kinaendelea kuhusu pesa zangu?" aliuliza huku akimwangalia meneja huyo.
Alionekana kuwa na presha kubwa, kwa kuwa hakutaka kumuona akianzisha ugomvi wowote ule, akampa karatasi ile na Bokasa kuanza kuisoma. Aliisoma taratibu, mapigo ya moyo yalikuwa yakimdunda.
"Hakuna pesa?" aliuliza huku kijasho chembamba kikianza kumtoka.
"Ndiyo kama unavyoona. Una uhakika uliweka katika akaunti hiyo?" aliuliza meneja.
"Ndiyo! Niliweka humu. Pesa zangu zipo wapi? Pesa zangu zipo wapi?" aliuliza huku akianza kulia, wakati akijiuliza swali hilo, ndipo jina la Godwin likaanza kugonga kichwani mwake.
"Huyu ni Godwin! Huyu ni Godwin," alisema Bokasa huku akitetemeka, alijua tu kwamba mchezo huo aliufanya kijana yuleyule aliyemfanyia umafia katika akaunti yake iliyokuwa katika Benki ya Geneva nchini Uswisi. Hata kabla hajazungumza zaidi, hapohapo akaanguka na kupoteza fahamu.
****
Godwin ndiye alikuwa mkombozi wao, yeye ndiye alikuwa na uwezo wa kuwaambia mahali alipokuwa mtu waliyekuwa wakimtafuta. Walimwambia kwamba alitakiwa kufanya kitu chochote kile mpaka kuhakikisha mtu huyo anajulikana mahali alipokuwa.
Hilo halikuwa tatizo kwa Godwin, alichokifanya ni kuanza kucheza na kompyuta yake, haikuwa kazi nyepesi hata kidogo kuipata simu ya mtu huyo kwani kule alipokuwa, hakukuwa na network, hakukuwa na mawasiliano yoyote yale na ni mara chache tu ilikuwa ikija na kutoka.
Huku akiwa na kompyuta yake, majira ya saa mbili usiku ndipo akapata majibu juu ya mahali alipokuwa Bokasa. Mnara wa simu ukasoma kwamba alikuwa baharini akiendelea na safari ya kuelekea Mombasa.
Akawaambia kwamba mwanaume huyo alikuwa safarini kuelekea nchini Kenya, haraka sana Jenerali Ojuku akakipigia simu kikosi chake cha majini ambacho alikiambia kwamba mtu waliyekuwa wakimtafuta alikuwa huko akielekea nchini Kenya.
"Mkuu! Tumezunguka bahari nzima lakini hatukuweza kumuona mtu huyo," alisikika mwanaume mmoja kwenye simu.
"Mna uhakika?"
"Ndiyo mkuu!"
"Kwa hiyo hamkuiona boti yoyote ile?"
"Tuliiona moja tu, kijana mmoja alikuwa akienda kuvua samaki na mama yake," alisema mwanajeshi huyo.
"Alikuwa akienda kuvua samaki na mama yake?"
"Ndiyo!"
"Hivi mna akili nyie? Ni mvuvi gani anaweza kwenda kuvua samaki na mama yake? Hiyo ndiyo boti aliyokuwa huyo rais. Huyo mwanamke mliongea naye?"
"Ndiyo mkuu!"
"Mlimsogelea?"
"Hapana mkuu! Alikuwa bize na kukunjua nyavu!"
"Mmefanya kosa kubwa sana! Huyo alikuwa Bokasa, rudini baharini mkaiangalie tena hiyo boti," alifoka Ojuku na kukata simu kwa hasira.
Alichanganyikiwa, akamwambia Godwin kile kilichotokea kwamba vijana hao walifanya kosa kubwa kuiruhusu boti iondoke na wakati alikuwa na uhakika kwamba ilikuwa ikiendeshwa na mtu waliyekuwa wakimtafuta kwa udi na uvumba.
"Kwa hiyo anaondoka kuelekea Ubelgiji?" aliuliza Ojuku.
"Ndiyo! Kwa maelezo yake aliyokuwa akimwambia Onyango, atakuwa anakwenda huko. Subiri," alisema Godwin.
Wazo likamjia kichwani mwake, akahisi kwamba kama kweli rais huyo alikuwa akikimbilia nchini Ubelgiji ilikuwa ni lazima kuhamisha pesa hivyo ni kuanza kuichunguza simu yake ili kama kweli alikuwa amehamisha pesa basi angepata kila kitu humo.
"Yes! Nilijua tu. Mungu wangu, kakomba pesa zote za serikali! Huyu mpumbavu sana," alisema Godwin huku akiangalia ujumbe wa meseji uliokuwa katika simu ya Bokasa, akamwambia Ojuku.
"Ameiba pesa za serikali?"
"Ndiyo! Dola trilioni kumi. Basi kama ameiba, ngoja tuzichukue pesa zetu. Au unaonaje swahiba?" aliuliza Godwin, alikuwa akiongea kijana zaidi.
"Haina shida, " alisema Ojuku na Godwin kuanza kuifanya kazi hiyo, yaani pesa zote alizoiba kiongozi huyo zilitakiwa kurudishwa haraka sana, tena si pesa hizo tu, hata pesa zake nyingine zilizokuwa humo, zilitakiwa kurudi katika akaunti ya serikali.
"Yes! Nimemuachia balansi ya 0.00, hiyo itamtosha kufanya shopping huko," alisema Godwin huku akicheka, hata maumivu ya mwilini wake hakuyasikia tena.
***
Moyo wa Godwin ukawa na amani, alifanya kazi kubwa ambayo alitakiwa kuifanya kwa kipindi kirefu. Alikaa katika chumba kile alichoambiwa kukaa huku uso wake ukiwa na tabasamu pana, kitendo cha kufanikisha kuzirudisha pesa zile katika akaunti ya serikali kulimfanya kujiona kuwa mkombozi wa Tanzania.
Jenerali Ojuku alipumua huku akionekana kuwa na furaha tele, kitendo cha Godwin kuifanya kazi ile kilimfanya kumuona kijana huyo kuwa muhimu kuliko mtu yeyote yule nchini Tanzania. Akawasiliana na Meja Jenerali na kumwambia kwamba haraka sana wataalamu wa gesi waende ikulu kwa lengo la kutoa sumu ile kitu kilichofanyika haraka sana.
“Cha kwanza sumu itolewe ikulu ndiyo mambo mengine yafanyike,” alisema Ojuku.
Hilo halikuwa tatizo hata kidogo, baada ya saa mbili akapigiwa simu na kuambiwa kwamba watu wale aliokuwa akiwataka kwenda ikulu walikwenda na kufanya kile alichokuwa akikitaka. Akawa na amani zaidi na kuanza kuzungumza na Godwin.
Alitaka kumfahamu kijana huyo, alikuwa nani na kulikuwa na kitu gani kilichokuwa kikiendelea. Godwin hakutaka kumwambia ukweli, akamdanganya kwamba alikuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye moyo wake ulikuwa na uchungu wa kuona mabadiliko yakifanyika nchini mwake.
“Safi sana. Kuna kazi nataka unisaidie!” alisema Ojuku.
“Kazi gani?”
Akamwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea kuhusu mtu aliyekuwa ameiteka familia yake. Alimwelezea kwa makini kila kitu kilichokuwa kimetokea kwamba familia yake ilitekwa na mtu asiyemfahamu na mpaka kipindi hicho hakujua familia hiyo alikuwa wapi. Alichokiamini ni kwamba Godwin aliyejitambulisha kwa jina la Denis angeweza kumsaidia kwa kile kilichokuwa kimetokea.
Hilo, kwake halikuonekana kuwa tatizo lolote lile, akazungumza naye na kumwambia ampe siku mbili na angemwambia mahali familia yake ilipokuwa kitu kilichomfurahisha mno Ojuku. Godwin hakukaa sana kambini, akaruhusiwa kuondoka, akapakizwa ndani ya gari la jeshi mpaka Magomeni aliposema anaishi na kuteremshwa.
“Nashukuru sana,” alisema Godwin huku akiwaangalia wanajeshi walimpeleka mahali pale.
Baada ya kuhakikisha kwamba lile gari limeondoka, akachukua bodaboda mpaka Tandale ambapo akateremka na kwenda alipokuwa akiishi. Alipoufikia mlango, akafungua na kuingia ndani. Kitendo cha Winfrida kumuona, akasimama na haraka sana akamfuata na kumkumbatia.
Machozi yalikuwa yakimtoka, kwa siku moja hakumuona mpenzi wake huyo, hakujua mahali alipokuwa na hata muonekano aliokuwa nao kupindi hicho ulionyesha dhahiri kwamba alikuwa katika matatioz makubwa kwani uso wake tu ulikuwa umevimba.
“Nini kimetokea?” aliuliza Winfrida huku akimwangalia mpenzi wake.
“Hakuna kitu!”
“Hakuna kitu kivipi na wakati umevimba uso? Niambie ni kitu gani kimetokea,” alisema Winfrida huku akimwangalia mpenzi wake huyo.
Godwin hakumwambia ukweli, aliendelea kusisitiza kwamba hakukuwa na kitu chochote kile cha hatari kilichokuwa kimetokea. Winfrida hakuridhika lakini hakuwa na jinsi, akaachana naye na kuendelea kufanya mambo yake.
Godwin hakutaka kuchelewa, hapohapo akachukua simu yake na kumpigia bilionea Kizito na kumwambia kwamba aiache familia ya Jenerali Ojuku. Si huyo tu bali aliwapigia watu wote waliokuwa wakizishikilia familia za wenzao na kuwaambia waziachie huru kwani kile kitu alichokuwa akikihitaji, tayari kilifanyika.
“Na picha zangu?” aliuliza Kizito.
“Nakuhakikishia hakuna mtu yeyote atakayejua kitu chochote kile, nitakufa na siri hii moyoni,” alisema Godwin.
“Nikupe kiasi gani kwa kukushukuru kwa wema wako? Nikulipe kiasi gani kwa kuitunza siri hii zaidi?” aliuliza bilionea Kizito, kwa jinsi sauti ilivyosikika tu, ilikuwa kama mtu ambaye hakuwa akiamini kilichokuwa kikiendelea.
“Hakuna haja ya pesa. Nakuhakikishia kwamba hakutokuwa na mtu yeyote atakayefahamu kitu chochote kile,” alisema Godwin kwa msisitizo uliomfanya bilionea huyo kumuamini.
Tanzania ikabadilika, haikuwa ile ya huzuni tena, kila kona watu wote walikuwa na furaha tele. Hakukuwa na mtu aliyeamini kwamba hatimaye Rais Bokasa alitimuliwa na nchi yake kuwa mikononi mwa wanajeshi. Amani ikarudi na bila kupoteza muda, Godwin akampigia simu Kambili na kuzungumza naye, akamwambia wazi kwamba uchaguzi mkuu ulitakiwa kufanyika, mawaziri wote wavuliwe nyadhifa zao, na kwenye uchaguzi huo, Chama cha Labour Party kikatakiwa kufutwa haraka sana, msajili wa vyama akapigiwa simu na Jenerali Ojuku na kuambiwa kwamba chama hiko hakikutakiwa kiwepo na hata wale mawazilri wote ambao walikuwa katika utawala uliopita walitakiwa kukamatwa na polisi na kufanyiwa mahojiano maalumu ambayo yangehusu zaidi mali walizokuwanazo.
****
Meneja wa Benki ya Brussels alishangaa, alibaki akimwangalia Bokasa ambaye alikuwa chini, presha ilimkamata baada ya kuambiwa kwamba kwenye akaunti yake hakukuwa na pesa yoyote ile. Akampigia simu sekretari wake ambaye akafika mahali hapo, wote wawili wakasaidiana kumbeba na kumpeleka nje ambapo wafanyakazi wengine wakawapokea na kuondoka naye kuelekea nje kwa ajili ya kumuwahisha hospitalini.
Njiani, hakuwa amefumbua macho, alikuwa kimya huku kila mmoja akiwa na hofu kwamba inawezekana mtu huyo alikuwa amefariki dunia. Safari hiyo ilichukua dakika kadhaa ndipo wakafika hospitalini ambapo moja kwa moja machela ikaletwa, akapakizwa na kuanza kusukumwa kuelekea ndani.
Kila nesi aliyekuwa akimwangalia alibaki akishangaa, walitaka kujua kitu kilichotokea kwa mtu huyo, alikuwa mlemavu, nini kilitokea? Kila aliyejiuliza alikosa jibu.
Akaingizwa katika chumba cha upasuaji na kuanza kufanyiwa uchunguzi mdogo kwa ajili ya kugundua ni kitu gani kilichokuwa kimetokea. Wakampima presha yake, ilikuwa imepanda kwa kiasi kikubwa sana kiasi kwamba walibaki wakishangaa.
“Jamani! Nini kimetokea? Mbona presha imepanda hivi?” aliuliza daktari huku akiwaangalia manesi waliokuwa wameisukuma machela ndani ya chumba kile na kumlaza kitandani.
“Ndugu zake wamemleta, hatujui chochote kile,” alijibu nesi mmoja huku macho yake yakiwa kwa Bokasa aliyekuwa hoi kitandani.
Walichokifanya ni kumuhudumia kwa nguvu zote kuhakikisha wanayaokoa maisha yake. Walipambana kwa nguvu zote, kidogo hali yake ikaanza kupata nafuu kwani baada ya saa moja kuhudumiwa, akayafumbua macho yake, akaanza kuangalia huku na kule na kitu cha kwanza kabisa kilichokuja kichwani mwake ni pesa zake.
“Where is my money?” (pesa zangu zipo wapi?) aliuliza huku akimwangalia daktari aliyekuwa amesimama karibu naye.
“Which money?” (pesa gani?)
“Someone stole my money! Godwin stole my money,” (kuna mtu ameniibia pesa zangu! Godwin ameniibia pesa zangu) alisema Bokasa maneno yaliyomfanya kila mtu kumshangaa.
Bokasa alikuwa akipiga kelele tu ndani ya chumba kile kiasi kwamba kila mtu alikuwa akishangaa. Hawakumjua mwanaume huyo, hawakujua kitu chochote kilichokuwa kikiendelea katika maisha yake, walishangaa, hizo pesa alizokuwa akizizungumzia zilikuwa zipi na aliibiwa na nani?
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ojuku aliambiwa kwamba Bokasa alikuwa nchini Ubelgiji, hakutaka kuona mwanaume huyo akikimbia na kujificha kama ilivyokuwa kwa marais wengine wa Afrika, hivyo akaagiza watu kuondoka kuelekea nchini humo kwa ajili ya kujua mahali alipokuwa na kumkamata.
Hilo halikuwa tatizo, wanaume hao wakaondoka kuelekea huko, walipofika, wakaanza kuulizia sehemu mbalimbali kuhusu mwanaume huyo, walikuwa na uhakika kwamba alikuwa hapohapo Brussels hivyo hawakutaka kutoka kwenda sehemu nyingine yoyote ile.
Walimtafuta kimyakimya tena kwa kuulizia kwa siku mbili mfululizo lakini hawakufanikiwa kitu kilichowafanya kumpigia simu Ojuku na kumwambia kilichokuwa kimetokea. Hilo tayari likaonekana kuwa tatizo, hakujua ni kwa jinsi gani wangeweza kumpata mwanaume huyo.
Wakati akiwa anafikiria sana ndipo jina la Denis likamjia kichwani mwake, hakutaka kuchelewa, hapohapo akampigia simu na kumwambia kilichokuwa kimetokea kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima kujua mahali alipokuwa Bokasa.
Denis, ambaye ndiye Godwin akaondoka mpaka kambini na kukutana na Ojuku na kuanza kuzungumza naye kwa undani. Alimwambia lengo lao la kumpata Bokasa, kwa yote aliyokuwa ameyafanya nchini Tanzania, alitakiwa kushtakiwa na kufungwa gerezani.
“Watu wetu wapo Ubelgiji, hawajui mahali alipo,” alisema Ojuku.
“Si tatizo. Ngoja nimtafute.”
Kitu pekee alichokifanya ni kuanza kumtafuta kwa kutumia simu yake. Aliingiza namba ya simu yake katika kompyuta yake na kuanza kumtafuta kila kona. Hiyo ilikuwa kazi yake, alizoea kuifanya kila siku hivyo hakukuwa na shida yoyote ile, baada ya dakika chache, akapata majibu kwamba mtu huyo alikuwa katika Benki ya Brussels.
“Atakuwa benki! Una uhakika?” aliuliza Ojuku.
“Simu yake ipo huko, na bila shaka inawezekana alikwenda kwa ajili ya kutoa pesa. Cha msingi watume waende huko, hata kama hayupo basi kutakuwa na watu wanaojua mahali alipo,” alisema Godwin.
“Sawa. Hakuna shida,” alisema Ojuku, hapohapo akachukua simu yake na kuwapigia watu hao na kuwaambia waende katika Benki ya Brussels ambapo walikuwa na uhakika kwamba mtu huyo anaweza kuwa huko.
“Haina shida. Tunakwenda,” alisema jamaa aliyekuwa huko na safari ya kwenda katika benki hiyo kuanza.
***
Kila mtu alitaka kuiona Tanzania mpya, matumaini na furaha ya Watanzania ambayo ilikuwa imepotea mioyoni mwao ikaanza kurudi, mpaka kipindi hicho hakukuwa na kitu chochote kilichobadilika lakini tayari Watanzania waliona tayari wameanza kupata maisha mazuri ambayo kila mmoja alikuwa akiyatamani.
Godwin alifanya kazi kubwa sana kupitia akaunti yake ya Mabadiliko ya Kweli, kila mtu nchini Tanzania alitaka kumuona mtu huyo, alikuwa nani na alikuwa na muonekano gani? Hilo likawafanya watu kutengeneza umoja waliouita ONYESHA SURA YAKO ambao ulikuwa na kazi ya kupanga mikakati ya kuandamana kutaka kumuona mwanaume ambaye alichangia kuiweka Tanzania hapo ilipokuwa, na hata kumuondoa Rais Bokasa madarakani.
Hakukuwa na mtu aliyemjua mtu huyo, kila mmoja alikuwa na hamu, watu wengi waliomba kumuona huku wengine wakienda mbali na kutaka kuona mtu huyo akiwa rais wa Tanzania lakini hilo halikuwezekana, Godwin hakufikiria kuwa rais wa nchi hiyo, kitu pekee alichokuwa anakitamani kila siku ni kumuondoa Bokasa madarakani kitu ambacho alifanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Watu hawakuishia kulalamika mitandaoni tu bali baada ya siku kadhaa, wakajikusanya mitaani na kuanza kuandamana maandamano ya amani ya kumtaka Godwin kujitokeza hadharani huku wengine wakitaka hata kuona akizungumza lolote tangu alipoanzia mpaka pale alipofikia.
Kila kitu kilichokuwa kikiendelea, Godwin alikuwa akikifuatilia na wakati mwingine kukusanyika na waandamanaji hao na kuandamana pamoja nao pasipo kugundua kwamba alikuwa miongoni mwao.
“Kesho nitahitaji kuzungumza na watu kupitia akaunti hii, nitasema mimi ni nani, nimeibukaje, nitaeleza kila kitu ila sitohitaji sura yangu ionekane,” aliandika Godwin kwenye mtandao, maneno ambayo kidogo yakawafanya watu waliokuwa wakitaka kuandamana tena kuacha kufanya hivyo.
Kama alivyokuwa ameahidi ndivyo alivyofanya, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kwenda katika Hoteli ya Atriums iliyokuwa Africasana, moja ya hoteli iliyokuwa na ukimya mkubwa, akachukua chumba ambapo humo ndani akaanza kujirekodi video huku akisimulia historia ya maisha yake.
Wakati mwingine alikuwa akilia, hakutaka kuiacha sura yake ionekane, aliiacha ionekane mwisho mdomoni kushuka chini na kuendelea kuhadithia. Alianza tangu siku ya kwanza alipokuwa na ufahamu, aliwaambia watu kwamba yeye alikuwa mtoto wa Mzee Mapoto, mwanasiasa maarufu nchini Tanzania ambaye alitokea kupendwa kuliko mtu yeyote katika ardhi ya Tanzania.
Akaelezea kifo cha baba yake ambaye alichaguliwa kama balozi nchini Marekani, aliwaeleza kwamba hata kifo chake hakikuwa cha bahati mbaya kama watu waliyovyohisi bali nyuma yake kulikuwa na mkono wa Rais Bokasa ambaye alitaka kuitekekeza familia nzima kwa kuhisi kwamba ingemletea matatizo hapo baadaye.
Hakutaka kuficha kitu, alisimulia kifo cha mama yake, ndugu yake, Irene, jinsi alivyokuwa akitafutwa mpaka alipowekwa katika boksi na kutupwa baharini huku akitakiwa kufa ila mtu mmoja aliyeitwa Kihampa hakutaka kuona hilo likitokea.
Akaelezea namna alivyookolewa na wavuvi wa Japan na kupelekwa nchini humo ambapo alisomea kompyuta na kuwa mkali katika Chuo cha Waseda. Alisimulia kila kitu mpaka alipokuwa akihamisha pesa za viongozi, jinsi alivyowasumbua FIS na kuhakikisha kwamba hapatikani.
Hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kuwaambia Watanzania kwamba yeye alikuwa nani, kila mtu alishangaa, wengine wakashindwa kuvumilia kwani mateso na shida alizopitia mwanaume huyo hakika hakukuwa na mtu aliyeamini kwamba kuna binadamu angeweza kupitia maisha hayo.
“Nilitaka kulipa kisasi, na kisasi pekee kilikuwa ni kumuondoa madarakani na kuwapa Watanzania nchi yao. Nimefanikiwa sana,” alisema Godwin hali iliyowafanya Watanzania wengi kufurahi.
“Wengi wanasema kwamba nichukue nafasi ya urais. Ndugu zangu, sikuwa na ndoto za kuwa rais, sikuhangaika kumuondoa madarakani Rais Bokasa ili nije kuwa rais, nilifanya hivyo kwa kuwa nilihitaji kuona Tanzania ikiongozwa na mtu sahihi. Kwangu mimi, nadhani Kambili ni mtu sahihi, mtu mwenye uchungu, mtu ambaye anaweza kufanya kila liwezekanalo sisi kufika kule tunapotaka kufika,” alisema Godwin na kuendelea:
“Ninamshukuru Jenerali Ojuku, kuna mengi amepitia ila ninamwambia kwamba kazi yake ilionekana, nilicheza michezo mingi ya hatari, sikucheza kwa lengo baya, nicheza kama njia ya kumsukuma kunisaidia kumtoa rais huyu madarakani, na kweli imewezekana. Nashukuru kwa wote. Hii akaunti haitofutwa, kwa viongozi wote ambao waliweka pesa zao katika akaunti za Uswisi, nimefunga akaunti, na hata wale viongozi wenye pesa hapa Tanzania, nimezuia pesa zao mpaka kesi zao zitakapokwisha. Kufunga akaunti hizo si kazi ya benki tu, nilifanya hivyo ili kuwasaidia. Nashukuru sana. Karibuni kwenye Tanzania mpya,” alimalizia Godwin, huo ndiyo ukawa mwisho wa video yake iliyogawanywa katika vipande thelathini na mbili.
***
“Sir! We have got a video,” (mkuu! Tumepata video) ilisikika sauti kutoka upande wa pili.
“What is it about?” (kuhusu nini?)
“Godwin! He has released a video,” (Godwin! Ametoa video) alisikika mwanaume huyo.
Kitendo cha Bwana Kom kusikia jina la Godwin akasikia moyo wake ukipiga paa. Hakuamini, hapohapo akamwambia mwanaume huyo kwamba amtumie video hiyo lakini akaambiwa kwamba ilikuwa katika mtandao wa Instagram ambapo alipoingia katika Akaunti ya Mabadiliko ya Kweli, akaiona video hiyo.
Haikuwa ya Kiingereza, ilikuwa ni ya Kiswahili kitu kilichomfanya kumtafuta mkalimani ambaye alikuja kumfafanulia kila neno lililozungumziwa katika video hiyo.
Hapo ndipo alipojua ukweli kwamba mwanaume huyo hakuwa mhalifu kama alivyokuwa akihisi bali alifanya hivyo kwa kuwa alikuwa akipambana na viongozi waliokuwa wakiihujumu nchi yao na hata kuzichukua zile pesa zilizokuwa zimeibwa nchini mwao.
Aliposikia kila kitu, akakifuata kiti chake na kutulia, akaegemea na kuweka mikono kichwani mwake. Hakuamini kama alikuwa akipambana na mtu aliyekuwa akiipigania nchi yake na kuwatokomeza mafisadi waliokuwa wakiwanyonya kila siku.
“Make a call to Halima! Tell her to leave him alone,” (mpigie simu Halima! Mwambie amuache) alisema Kom na hapohapo Halima kupigiwa simu.
***
Wakati simu kutoka kwa Kom ilipokuwa ikiingia, Godwin alikuwa akiiona, alijua kwamba kulikuwa na kitu mwanaume huyo alitaka kumwambia msichana huyo. Alichokifanya ni kuiunganisha mpaka kwa Halima ambapo msichana huyo alipopokea, akampa taarifa kwamba alitakiwa kuachana na Godwin kwani kwa kile alichokuwa akikifanya, hakuwa mtu wa kutafutwa na kushtakiwa kwa kuwa kulikuwa na jambo jingine la msingi alilokuwa akilipigania kwa ajili ya nchini yake.
Kwa Halima, hiyo ikaonekana kuwa nafuu, alikuwa amehangaika kwa kipindi kirefu kumtafuta mwanaume huyo lakini hakuwa amempata, kitendo cha kuambiwa kwamba alitakiwa kurudi, akanyanyua mikono na kumshukuru Mungu.
Alikwishawahi kufanya kazi nyingi lakini kwa ile ya kumtafuta Godwin ilikuwa ni ngumu kuliko zote alizowahi kufanya katika maisha yake. Hakutaka kuchelewa, aliona kama Bwana Kom angeahirisha na kumwambia kwamba aendelee kupambana kumtafuta, siku iliyofuata ukawa mwisho wa kukaa nchini Tanzania, akapanda ndege na kurudi zake nchini Somalia kuendelea na majukumu yake mengine.
Kwa Godwin, maisha yalikuwa ni furaha tele, akawa anaendelea kuishi na Winfrida, hakumwambia alikuwa nani, aliishi kisiri, kila kitu kilichokuwa kimetokea alikifanya kuwa siri kubwa mno. Kazi yake ikawa ni kuwasiliana na Kambili, alimwambia kwamba kila kitu kilikuwa tayari na aliamini kwamba baada ya siku kadhaa yeye ndiye angekuwa rais wa nchi hiyo.
“Nashukuru sana,” alisema Kambili.
“Usijali! Ila usifanye kama Bokasa.”
“Sitoweza kufanya. Naomba uniamini! Sitoweza kufanya jambo lolote lile baya. Nimepigana kwa ajili ya nchi hii kwa miaka mingi, nitaonekana sina akili kama tu nitaanza kufanya vitu tofauti na vile ambavyo Watanzania wanavitaka kila siku,” alisema Kambili, aliamini kabisa kwamba alikuwa akienda kuchukua nafasi ya urais kwa kuwa Godwin aliamua kufanya hivyo.
Hakuishia hapo, alichokifanya ni kuwasiliana na Jenerali Ojuku na kumuomba msamaha kwa yote yaliyokuwa yametokea, kuiteka familia yake, halikuwa lengo lake ila alifanya hivyo kwa kuwa alihitaji mabadiliko kwa nguvu kubwa na yote yalifanyika.
“Haikuwa kwa faida yangu, ilikuwa ni kwa faida ya Watanzania, faida ya watoto na wajukuu zako,” alimwambia Ojuku kwenye simu.
“Nashukuru sana. Najua niliumia sana, sikuwa nimelijua lengo lako, si baya, ni zuri ambalo ninaliunga mkono kwa asilimia mia moja,” alisema Ojuku kwenye simu.
“Nashukuru kwa kulifahamu hilo!”
“Ila hutujawahi hata kuonana. Ningependa nimuone huyu shujaa ambaye ameifanya Tanzania kurudi katika heshima yake na kuondokana na udikteta,” alisema Ojuku.
“Tulikwishaonana! Tukazungumza na kufanya mambo mengi sana,” alisema Godwin maneno yaliyomshtua Ojuku.
“Tulishawahi kuonana?”
“Ndiyo! Niliisaidia Tanzania hata kuhamisha pesa za Bokasa alizozituma Ubelgiji,” alisema Godwin.
“Inamaanisha wewe ndiye yule kijana aliyeitwa Denis?”
“Ndiye mimi!”
“Ni kijana mdogo mno!”
“Najua! Ni kijana mdogo lakini mwenye kiu ya kupambana. Nashukuru kwa msaada wako,” alisema Godwin.
“Nashukuru pia. Naomba tuonane japo tule chakula cha mchana!”
“Ningefurahi sana kama ningepata nafasi hiyo. Lakini sina jinsi, hutoweza kuniona tena. Nimefanya kazi ambayo nilitakiwa kuifanya kwa uwezo wangu wote. Popote nitakapokuwa, utakuwa na namba yangu, tutawasiliana, kama kutatokea tatizo lolote lile, naomba uniambie, kama kuna pesa zimeibwa, nijulishe nizirudishe,” alisema Godwin.
“Haina shida. Nakutakia maisha mema!”
“Nashukuru pia kiongozi,” alisema Godwin na kukata simu.
Alimaliza kuzungumza na Ojuku, mtu mmoja wa kipekee aliyetamani sana kuonana naye alikuwa Mchungaji Kihampa. Huyo ndiye aliyekuwa amemuokoa, mtu aliyemuweka kwenye boksi, japokuwa alitakiwa kuuawa lakini mwanaume huyo alimuokoa kwa kumuacaha hai na kuokolewa na Wajapan.
“Ni lazima nimtafute huyu mtu. Ni muhimu sana, siwezi kumuacha,” aliseema Godwin, akasimama na kuanza kujiandaa kwenda kumtembelea mchungaji huyo.
***
Maofisa wa Usalama wa Taifa wakafika mpaka katika Benki ya Brussels kwa lengo la kwenda kumkamata Bokasa ambaye alikuwa akihitajika sana nchini Tanzania. Walipofika hapo, wakataka kuonana na uongozi wa benki hiyo kwani hapo ndani kila walipoangalia huku na kule, hawakuweza kumuona mtu huyo japokuwa mashine yao ya GPS ilionyesha kwamba simu ile ilikuwa humo ndani.
Kuhusu kuonana na meneja wa benki hiyo hakukuwa na tatizo lolote lile, akapigiwa simu na kuambiwa kwamba kulikuwa na watu waliotaka kuonana naye. Wakaruhusiwa na kwenda ndani ambapo moja kwa moja wakaanza kuzungumza naye.
“Sijawaelewa vizuri! Mmesema rais?” aliuliza meneja huyo huku akiwaangalia kwa mshangao.
“Ndiyo! Picha yake hii hapa!” alisema jamaa mmoja huku akimpa picha yya Bokasa.
“Ooh! Kumbe mnamzungumzia huyU! Mmesema kwamba ni rais! Wa wapi?’ aliuliza meneja huku akishangaa na hapohapo kumwambia kwa kifupi kilichotokea.
Hilo halikuwa tatizo, wakaambiwa kwamba mwanaume huyo hakuwa mahali hapo bali aliiacha simu yake ambayo aliihifadhi katika droo ila mwanaume huyo alikuwa hoi hospitalini.
Hawakutaka kuondoka pasipo kumuona hivyo wakaomba kupelekwa huko kwa lengo la kuonana naye. Wakachukuliwa mpaka hospitalini ambapo kwa ruhusa ya daktari wakapelekwa mpaka katika chumba alichokuwa amelazwa.
Walipofika, wakabaki wakimwangalia. Mwanaume huyo alikuwa akitia huruma kitandani pale, alikuwa kimya, alionekana kuwa na hofu kubwa na hapo kitandani alikuwa akipumulia mashine ya oksijeni tu. Walichokifanya ni kumwambia kwamba alikuwa chini ya ulinzi na alitakiwa kusafirishwa mpaka nchini Tanzania kwa ajili ya kushtakiwa kwa kila kitu kilichokuwa kimetokea pamoja na ubadhilifu wa pesa.
“Daktari! Huyu mgonjwa atatakiwa kupelekwa nchini Tanzania haraka sana!” alisema jamaa mmoja.
“Hapana! Ni mapema sana. Mpeni miezi sita kwani bado hali yake si nzuri kabisa,” alisema daktari kiasi kwamba mawasiliano yakafanyika mpaka nchini Tanzania ambapo wakakubaliana kumpa mtu huyo miezi hiyo kwa ajili ya kupatiwa matibabu na hali yake irudi na kuwa kawaida.
“Haina shida! Kwa kuwa ndiyo utakuwa muda wa uchaguzi, mleteni kipindi hicho, ila awe chini ya uangalizi!” alisikika Jenerali Ojuku.
“Haina shida kiongozi!”
***
Tangu Kihampa aliposikia sauti moyoni mwake ikimwambia kwamba alitakiwa kuyabadilisha maisha yake, akaamua kubadilika na kumtumikia Mungu kwa moyo mmoja. Hakutaka tena kushiriki katika mauaji yoyote yale, moyo wake ulibadilika na ni kitu kimoja tu ndicho kilichokuwa kikimfurukuta moyoni mwake, kumtumikia Mungu katika roho na kweli.
Baada ya kumuweka Godwin ndani ya boksi lile na kulitupa baharini huku akiwa ameweka maboya ndani yake, akaondoka, hakutaka kurudi tena na hivyo kumpigia simu Rais Bokasa na kumwambia kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wake wa kutumikishwa kufanya mauaji mbalimbali.
Akaanza kumuabudu Mungu, akajiunga katika Kanisa la Praise And Worship lililokuwa Tabata Bima. Hakutaka kusikia kitu chochote kile mbali na kumuabudu Mungu, akaanza kuwa mshirika wa kanisa hilo, akajiunga na kikundi cha vijana cha kuhubiri Injili sehemu mbalimbali nchini Tanzania na baada ya miaka miwili ya huduma hiyo akaamua kwenda kusomea uchungaji katika Chuo kilichopo mkoani Dodoma.
Moyo wake ukaendelea kubadilika, akaendelea kumuhubiri Mungu sehemu mbalimbali na alipomaliza kusomea masomo ya kichungaji ndipo akakabidhiwa kanisa lililokuwa Magomeni Mapipa jijini Dar es Salaam.
Hapo ndipo ambapo Godwin alitaka kwenda kwa ajili ya kumshukuru kwa kila kitu alichokuwa amemfanyia, aliamini kwamba bila mwanaume huyo basi angekuwa marehemu kwani alikuwa na nguvu zote za kummaliza lakini kitu cha ajabu kabisa ambacho hata yeye mwenyewe alikishangaa, aliyakuta maboya ndani ya boksi na wakati alitekwa na mtu huyo huku akipewa amri ya kummaliza.
Alipofika kanisani hapo kulipokuwa na ibada iliyokuwa ikiendelea, akaelekea nyuma kabisa ya kanisa na kutulia hapo. Macho yake yalikuwa yakiangalia mbele, kulikuwa na kwaya iliyokuwa ikiimba kanisa hapo lakini macho ya Godwin yalikuwa kwa mchungaji huyo aliyetulia katika kiti chake huku akisikiliza kwaya iliyokuwa ikiendelea kumuimbia Mungu.
Hakuwa na haraka, aliendelea kusubiri mpaka pale ibada ilipokwisha ambapo moja kwa oja akamfuata mchungaji huyo kwa lengo la kuzungumza naye na kumwambia kile kilichokuwa kimempeleka mahali pale.
“Bwana Yesu Asifiwe mchungaji,” alisalimia Godwin huku akimwangalia mchungaji huyo ambaye baada ya macho yake kutua usoni mwa Godwin, alihisi kuwahi kumuona sehemu fulani.
“Amen! Hujambo mtumishi wa Mungu?” aliuliza huku akimwangalia kwa mtazamo uliomaanisha kwamba alitaka kukumbuka mahali alipowahi kumuona mwanaume huyo.
“Nashukuru Mungu ni mzima kabisa.”
Bado mchungaji Kihampa alikuwa akiendelea kukumbuka, kichwa chake kilikuwa kikifikiria mbali kabisa, aliendelea kujaribu kuikumbuka sura hiyo lakini alishindwa kabisa. Alipoona kwamba haikuwezekana, akamuuliza ambapo bila tatizo lolote lile Godwin akajitambulisha.
“Godwin?” aliuliza huku akiendelea kumwangalia vizuri kabisa.
“Ndiyo mchungaji!”
“Godwin yupi?”
“Wa boksi lililotupwa baharini miaka mingi iliyopita,” alisema Godwin.
Maneno hayo ndiyo yakamfanya mchungaji huyo kuanza kukumbuka kila kitu kilichokuwa kimetokea, hakuwa mgeni tena, alimkumbuka, yeye ndiye alikuwa mtu pekee aliyemuokoa katika mauti kwa kumuweka maboya kadhaa ndani ya boksi alilokuwa amefungwa na kutupwa baharini.
Hapohapo Kihampa akamsogelea zaidi Godwin na kumkumbatia, moyo wake ukawa na furaha tena kwani kwa kipindi chote hicho hakuwa na uhakika kama kijana huyo alinusurika baharini kama alivyokuwa amekusudia alikuwa alikuwa amekufa baharini.
Hapo ndipo Godwin alipoanza kusimulia kila kitu kilichokuwa kimetokea, ilikuwa ni stori ileile ambayo aliisikia sana midomoni mwa watu mara baada ya kusoma katika mitandao ya kijamii.
“Wewe ndiye huyu Godwin msumbufu aliyeitoa Tanzania katika mikono ya Bokasa?” aliuliza Kihampa.
“Ndiyo! Ninamshukuru Mungu kwamba nilipambana kwa nafasi yangu, alinipigania sana, na ninashukuru kwa sababu bila yeye nadhani nisingeweza kumkimbia Bokasa,” alisema Godwin huku akimwangalia mchungaji huyo.
Walibaki na kuzungumza mambo mengi mno, walifurahi na kucheka pamoja kiasi kwamba hata baadhi ya washirika wa kanisa hilo walikuwa wakishangaa, hawakuwahi kumuona mchungaji wao akiongea na mtu mmoja kwa kipindi kirefu kama ilivyokuwa kwa kijana huyo.
Walitumia dakika kadhaa na walipomaliza, Godwin akaondoka kurudi nyumbani ambapo huko akawasiliana na Kambili na kumwambia kwamba alitakiwa kujiandaa kwani uchaguzi mkuu ungeitishwa na yeye kuwa miongoni mwa wagombea ambao walitakiwa kugombea, kwa hiyo alitakiwa kuwaahidi wananchi vile tu ambavyo atavifanya katika uongozi wake, asivyoviweza, aachane navyo.
“Haina shida! Ila kuna siku ningependa sana kukuona,” alisema Kambili.
“Usijali! Kuna siku utaniona, tutazungumza sana, ila bahati mbaya hutonijua kama ndiye mimi,” alisema Godwin kwenye simu.
“Kwa nini unataka kujificha kila siku?”
“Kwa sababu vita vizuri ni kupambana na mtu asiyekujua. Nipo kwa ajili ya Watanzania, tukiongea na kuonana mara kwa mara, utajenga urafiki nami, siku ukifanya ujinga, sitokufanya kitu kwa kuwa wewe ni rafiki yangu, ila ili niwe na nguvu ya kukufanya lolote lile, ni lazima nisiwe rafiki yako, ili siku nikikupiga, nimpige mtu asiyekuwa rafiki yangu,” alijibu Godwin.
“Haina shida! Nitahakikisha napambana kufanya kila kitu ambacho Watanzania wengi wamekuwa wakihitaji kutoka kwangu,” alisema Kambili.
“Nashukuru sana.”
Japokuwa hakuwa na cheo chochote kile lakini Jenerali Ojuku alikuwa akimheshimu mno Godwin, kila alipokuwa akimpigia simu, kwa jinsi alivyokuwa akizungumza naye alizungumza kiheshima, alionekana kama kiongozi wake kiasi kwamba kwa lolote lile ambalo angelisema mwanaume huyo angemuunga mkono kwa asilimia mia moja.
Siku zikaendelea kukatika, miezi sita ilipokatika watu wakawa na hamu ya kuingia katika uchaguzi mkuu ambao haukufanyika nchini humo ngazi ya rais kwa takribani miaka kumi na ishirini, kila mtu alitaka kushuhudia kile ambacho kingetokea.
Wagombea waliokuwa wakigombea nafasi hiyo waliendelea kupiga kampeni ya kuzunguka kila kona nchini Tanzania kuhakikisha kwamba wanachaguliwa na kuiongoza nchi hiyo. Kambili hakuwa na tabu, aliamini kwamba jina la Godwin lingeweza kumpa nafasi hiyo na kila alipokuwa akisimama jukwaani, alisema wazi kwamba angeiongoza nchi hiyo kwani hata Godwin alimuamini kwamba anaweza kufanya yale ambayo Watanzania wote wangependa ayafanye kwa miaka mitano ya kwanza.
“Naombeni mnipe dhamana! Nitahakikisha Tanzania mpya inarudi, kama Godwin ameniamini, kwa nini usiniamini? Nawaahidi wote kwamba sitawaangusha,” alisema Kambili alipokuwa akizungumza na wananchi
“Umepita baba!” alisikika mwanamke mmoja akisema kwa sauti.
“Nimepita?” aliuliza.
“Ndiyoooooo!” watu wote waliitikia kwa sa
Kampeni zilikuwa zikiendelea kila siku, katika kila mkoa ambao Kambili alikuwa akisimama na kuzungumza, Godwin alikuwa kwenye umati wa mkutano huo. Hakukuwa na mtu aliyemfahamu, alikuwa akisikia mauoni ya watu mbalimbali na kila mtu ambaye alimzungumzia Kambili, alisema wazi kuwa kura yake ingekwenda kwa mtu huyo kwa sababu tu Godwin alimwamini.
“Nitampa jamaa kura yangu kwa kuwa Godwin amemwamini! Kama Godwin amekukubali, kwa nini mimi nisikukubali? Ni lazima nikukubali kwani yule jamaa ndiye mkombozi wetu,” alisema mwanaume mmoja huku akionekana kuwa na furaha tele.
***
"Mpo wapi?"
"Nairobee! Kuna lolote the big boss?" ilisikika sauti ya mtu mwingine.
"Mnaweza kuja huku Mombasa mara moja!"
"Hakuna shida, tunakuja!"
"Sawa. Nawasubir! Njooni haraka sana hapa white house," alisema mwanaume mmoja.
"Okay!"
Yalikuwa mazungumzo baina ya watu wawili waliokuwa wakiwasiliana kwa njia ya simu. Mmoja alikuwa Mombasa na mwingine jijini Nairobi nchini Kenya. Mazungumzo yao hayakuwa marefu sana, wakakata simu na kila mtu kuendelea na mambo yake.
Mwanaume aliyevalia suti alikaa nyuma ya meza yake katika ofisi yake iliyokuwa ndani ya jumba moja kubwa ambalo kila mtu hapo Mombasa aliliita kwa jina la White House kama ilivyoitwa ikulu ya Marekani. Muda wote mwanaume huyu alikuwa na sigara kubwa aina ya sigar mdomoni mwake, alikaa kwa kujiachia na mezani kwake kulikuwa na mafaili mengi pamoja na cd ambazo ni yeye tu ndiye alijua humo kulikuwa na nini.
Mwanaume huyu aliitwa Stephano Olotu, alikuwa miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa nchini Kenya. Alimiliki utajiri wa dola bilioni mbili ambazo zilikuwa ni zaidi ya shilingi trilioni 4, alikuwa na migahawa mingi jijini Nairobi, migodi ya dhahabu na pia alimiliki kisima cha mafuta nchini Nigeria.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Japokuwa alikuwa mfanyabiashara aliyekuwa na mafanikio makubwa na hata kufanya biashara za halali kabisa lakini nyuma ya pazia mwanaume huyo alikuwa na michezo mingi ya hatari. Alijishughulisha na uuzaji wa madawa ya kulevya, maisha yake yalikuwa ni kutanua na wanawake mbalimbali Afrika nzima. Kwa kuwa alikuwa na jina kubwa alilitumia vilivyo kuweka mikakati kabambe kuzoeana na marais wengi ili kuweza kufanya biashara zake za madawa ya kulevya.
Miongoni mwa marais waliokuwa wakipiga naye mishemishe alikuwa Rais Bokasa, alitumia kiasi kikubwa cha pesa kuwekeza nchini Tanzania, huko, aliwatafuta wafanyabiashara wenzake ambao walikuwa wakifanya biashara haramu ya madawa ya kulevya kwa kupitia mgongo wa rais huyo.
Hakuwa akiwafahamu wafanyabiashara hao, Bokasa alikuwa mjanja, alimwambia kwamba mzigo ulitakiwa kufika kwake kwanza na yeye kuwafikishia hao wafanyabiashara wengine ambapo ulipokwisha, alichukua asilimia kumi na tisini ya pesa iliyolipwa kwenda kwa Olotu.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake. Katika kipindi chote hicho Bokasa hakutaka kumruhusu Olotu kuwafahamu wafanyabiashara wengine aliokuwa akifanya nao biashara hiyo kwani alijua kwamba kama angeruhusu hilo basi kusingekuwa na ulazima wa Olotu kumtafuta na kuwauzia wenzake mzigo mkubwa ambao alikuwa akiutuma nchini humo.
Bokasa aliondolewa madarakani huku akiwa bado hajakabidhi pesa alizokuwa ameuza mzigo mkubwa uliokuwa na thamani ya shilingi bilioni mia tatu. Olotu alichanganyikiwa, hakuamini kama kweli pesa zake asingezipata kwa kuwa tu rais huyo alikuwa ameondolewa madarakani.
Kwa kipindi hicho alihitaji pesa hizo, hakuwa na njia nyingine za kupata mzigo huo zaidi ya kumuuliza Bokasa juu majina ya wafanyabishara aliokuwa akiwauzia kwani alifanya siri lakini kwa hatua aliyokuwa amefikia, hakukuwa na siri tena, alitaka kuambiwa ili awafuate na kudai pesa zake.
Kumpata Bokasa halikuwa jambo jepesi, mwanaume huyo alikuwa nchini Ubelgiji akiendelea kupata matibabu, hakukubali kuona akifa pasipo kumwambia ukweli juu ya mzigo wake hivyo kitu pekee alichokiamua ni kuwasiliana na vijana wake, wasafiri mpaka nchini huko na kumuuliza juu ya wafanyabisahara hao, na kama hataki kuwaambia ukweli basi wamteke, waondoke naye mpaka nchini Kenya ambapo angefanya kitu kimoja tu, kumuua ili kuiridhisha nafsi yake kwa dhuluma aliyokuwa akifanyiwa.
Baada ya saa mbili, vijana wale aliowapigia simu wakafika Mombasa na kuanza kuzungumza nao, aliwaambia hitaji lake kwamba alitaka wao wasafiri mpaka nchini Ubelgiji ambapo huko wangekwenda mpaka katika hospitali aliyolazwa na kumteka huko.
Mipango ikapangwa ndani ya jumba hilo kubwa na hivyo kutakiwa kwenda nchini humo kwa ajili ya kuhakikisha mwanaume huyo anapelekwa haraka sana mikononi mwake na kufanya kile alichotaka kukifanya.
"Hana ulinzi?" aliuliza kijana mmoja, huyo aliitwa Wilson.
"Sijajua! Ila nina uhakika hana ulinzi, atakuwaje na ulinzi na wakati hapendwi? Ninachokitaka ni kujua majina ya wafanyabiashara aliokuwa akifanya nao biashara yangu," alisema Olotu.
"Basi haina shida."
Baada ya siku tatu wanaume wawili, Wilson na Okotee wakaondoka nchini Kenya na kwenda Ubelgiji kwa ajili ya kukamilisha kile walichoambiwa. Hawakuona kama wangepata tabu kwani tayari waliambiwa kuwa Bokasa alikuwa katika Hospitali ya Clinique Saint Jean iliyokuwa katika Jiji la Brussels akiendelea kupatiwa matibabu kutokana na tatizo la presha alilokuwa amelipata.
"Tukifika, ni kumchukua na kurudi naye, sidhani kama tutashindwa. Cha msingi ndege ya rais binafsi iandaliwe kwa ajili ya kuondoka naye," alisema Wilson, kwao, kitendo cha kumchukua Bokasa na kwenda naye nchini Kenya hakukuwa na tatizo lolote lile, ilikuwa ni kama kumsukuma mlevi katika mteremko wa mlima.
Wakati vijana hao wakiwa njiani, alichokifanya Olotu ni kumpigia simu Rais Onyango wa hapo Kenya na kumwambia kuhusu lengo lake. Alimwambia ukweli kuhusu mzigo wa madawa ya kulevya ambao kipindi hicho hakujua uliuzwa kwa wafanyabiashara gani nchini Tanzania, ilitakiwa mtu huyo achukuliwe kutoka Ubelgiji na kupelekwa Kenya kwa lengo la kuwajua watu hao.
"Si tatizo! Unataka nikusaidie nini Olotu?" aliuliza Rais Onyango.
"Ndege yako kwenda kumsafirisha kutoka Ubelgiji kuja huku!" alijibu Olotu.
"Una uhakika ataweza kutolewa hospitalini?" aliuliza.
"Hilo si tatizo!"
"Unajua kama kuna ulinzi huko?"
"Ulinzi gani?"
"Tanzania imetuma ulinzi, kuna watu wanamlinda usiku na mchana mahali hapo."
"Haina shida! Watu niliowatuma ni hatari sana. Hata kama utaweka ulinzi wa Kimarekani, mwisho wa siku tunapata tunachokitaka," alitamba Olotu.
"Basi sawa. Wasiliana nao, waulize siku gani huyo mtu atakuwa mikononi mwao kwa lengo la kumchukua na kumsafirisha!"
"Haina shida. Ila nafikiri baada ya siku tatu. Yaani Jumatano kila kitu kitakuwa sawa."
"Haina shida."
***
Bokasa alikuwa kitandani, aliendelea kupumulia mashine ya hewa ya oksijeni, hakuwa na nguvu kitandani pale na kila muda macho yake yalikuwa yakiangalia huku na kule. Alipewa taarifa kwamba kulikuwa na maofisa wa Usalama wa Taifa ambao walikuwa hapo kwa lengo la kumlinda na kuhakikisha wanasafiri naye kuelekea nchini Tanzania mara baada ya kupata nafuu.
Hakutaka kurudi Tanzania, alitamani kuendelea kubaki nchini humo, alijua dhahiri kile kilichokuwa kikienda kutokea mara baada ya kufika huko. Hakutaka kwenda, hakutaka kuona akifungwa gerezani kwa maovu yote aliyokuwa ameyafanya katika kipindi alichokuwa rais wa nchi hiyo.
Kwa kuwa kulikuwa na kazi kubwa, wakaongezwa maofisa wa Usalama wa Taifa wengine ili wawe wanabadilishana mpaka pale ambapo mwanaume huyo angepata nafuu na kupelekwa nchini Tanzania.
"Doctor! There is something we have to discuss," (dokta! Kuna kitu nataka tujadili) alisikika msichana fulani kutoka kwenye simu, alimpigia simu daktari mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Thump.
"Who are you?" (wewe nani?)
"Amanda Kalulu."
"What is it about?" (kuhusu nini?)
"About my uncle!" (kuhusu mjomba wangu)
"Who is that?" (nani huyo?)
"Bokasa!"
Alipolitaja jina hilo tu daktari akajua ni mtu gani alikuwa akizungumziwa. Hakumjua msichana huyo aliyempigia simu ambaye alitaka sana kuonana naye. Hilo halikuwa tatizo, akamwambia kwamba kama inawezekana basi waonane na kuzungumza kuhusu mwanaume huyo.
Baada ya saa mbili wakaonana ndani ya hospitali hiyo na kuanza kuzungumza. Mwanamke mrembo alikuwa katika kiti cha wageni ndani ya ofisi ya daktari huyo, alifika mahali hapo kwa ajili ya kuzungumza naye kuhusu mgonjwa aliyekuwa ameletwa ambaye alisema kwamba alikuwa mjomba wake.
Walikaa na kuzungumza mambo mengi, alimwambia kuhusu rais huyo kwamba alikuwa mjomba wake kabisa na alisikitishwa kwa taarifa ya ugonjwa aliokuwa nao ambao ulisababisha kupelekwa ndani ya hospitali hiyo.
"Lengo lako ni nini?" aliuliza Dk. Thump.
"Tumekaa kama familia na kuamua jambo moja!" alisema.
"Lipi?"
"Kumpeleka mgonjwa wetu nchini Ufaransa. Anateseka na tunaona kabisa matibabu ya hapa si mazuri kama ambavyo yanatakiwa kuwa. Miezi sita ni mingi sana," alisema mwanamke huyo.
Dokta Thump alibaki akimwangalia mwanamke huyo, kwa jinsi muonekano wake ulivyokuwa ilikuwa vigumu mno kugundua kwamba hakukuwa na uhusiano wowote ule baina yake na mgonjwa aliyekuwa amelazwa ila kwa kuwa alikuwa akiongea kwa huruma sana na wakati mwingine machozi kumtiririka, daktari akajihisi hukumu kubwa moyoni mwake.
Wakati wakizungumza, mara simu ya mwanamke yule ikaanza kuita, hakutaka kuchelewa, akaipokea na kuanza kuzungumza na mwanaume wa upande wa pili, kwa jinsi mazungumzo yao yalivyokuwa, ilionyesha kabisa kwamba aliyepiga simu alikuwa ndugu yake ambaye naye alitaka kufahamu hali aliyokuwa nayo Bokasa.
"Ni mgonjwa mno. Kama ndugu tulivyokubaliana, inabidi asafirishwe na kuelekea nchini Ufaransa," alisema mwanamke huyo.
"Sawa. Nakuja na familia yangu kumuona," alisikika mwanaume huyo wa upande wa pili.
Hicho ndicho kilichofanyika, ndani ya nusu saa, mwanaume mwenye ndevu nyingi akafika hospitalini hapo na moja kwa moja kuonana na Dk. Thump huku akiwa na familia yake ya watu sita.
"Kaka anaendeleaje?" aliuliza mwanaume huyo huku akimwangalia Amanda.
"Ni mgonjwa sana, miezi sita ni mingi mno, hatutokuwa tayari kusubiri kipindi chote hicho," alisema Amanda huku akimkumbatia ndugu yake huyo aliyejitambulisha kwa daktari kwa jina la Sebastian Gambole.
Ilikuwa ni vigumu sana kugundua kwamba huo ulikuwa mchezo uliokuwa umepangwa, watu hao walikuwa mahali hapo kwa lengo la kumtorosha Bokasa na kuelekea nchini Kenya ambapo tayari walikutana na Wilson na mwenzake na kupanga ni kwa jinsi gani mwanaume huyo alitakiwa kusafirishwa kuelekea huko badala ya Ufaransa kama walivyokuwa wamemwambia daktari.
Kitu cha kwanza walichohitaji ni kuonana na mgonjwa wao, hilo halikuwa tatizo, wakapelekwa katika wodi ile na kuonana naye ambapo huko wakampiga picha na kumtumia Wilson ambaye alithibitisha kwamba huyo ndiye mtu aliyetakiwa kusafirishwa.
"It is him!" (ndiye yeye!)
"Okay!" (sawa)
***
Ilikuwa kazi ambayo ilitakiwa kufanyika haraka sana kabla ya watu kujua kile kilichokuwa kikiendelea. Walichokifanya mara baada ya kumpiga picha na Wilson kusema kwamba alikuwa ndiye mtu aliyehitajika, wakaondoka hospitalini hapo na kwenda kupanga mikakati ya kumtoa mwanaume huyo katika hospitali hiyo pasipo mtu wale walinzi kutoka Tanzania kufahamu chochote kile.
Mpango waliokubaliana ilikuwa ni lazima wajifanye madaktari ili iwe rahisi kuingia na kuondoka humo na mtu huyo lakini pia kwa Wilson na Okotee walitakiwa kujifanya madaktari waliokuwa wakizungumziwa kutoka nchini Ufaransa ambao walifika mahali hapo kwa lengo la kumchukua Bokasa.
“Na itakuwaje kuhusu Dk. Thump?” aliuliza Amanda.
“Ni kazi nyepesi sana. Kwa kuwa amekubaliana nanyi, hakuna tatizo, kitakachotakiwa ni kumlazimisha kufanya kile tunachokihitaji au vinginevyo tumuue,” alisema Wilson.
“Sawa. Haina shida kama ni hivyo!”
Walitakiw akujiandaa, Dk. Thump hakutakiwa kuhusika, aliambiwa kwamba ndugu wa mgonjwa ndiyo waliokuwa wakishughulikia kila kitu na wao ndiyo waliokuwa wakijia ni hospitali gani mgonjwa wao alitakiwa kwenda.
Hilo halikuwa tatizo, kitu pekee alichokiandaa ni ripoti kuhusu ugonjwa wa Bokasa ambayo ndiyo walitakiwa kupewa madaktari na hivyo kuondoka naye. Ndege ikaandaliwa tayari kwa kuanza safari ya kuelekea nchini Kenya, kitu pekee kilichobaki ni kuona kama kungekuwa na uwezekano wa kuondoka mahali hapo pasipo wale Usalama wa Taifa wa Tanzania kujua kilichokuwa kikiendelea.
“Hivi kile chumba hakina mlango wa nyuma?” aliuliza Okotee.
“Unao! Niliangalia tulipokwenda kumuona, tuliuona mlango wa nyuma,” alisema Amanda.
“Basi itakuwa vizuri kama tukiutumia huo,” alisema Wilson.
Walipanga mipango yao, ilipokamilika, siku iliyofuata Amanda na wenzake walitakiwa kwenda huko kwa ajili ya kukamilisha mipango midogomidogo iliyokuwa imebaki. Walipofika katika hospitali hiyo wakawasiliana na Dk. Sebastian na kumwambia kwamba madaktari kutoka nchini Ufaransa ambao walikuwa wameandaliwa na familia waliwasili nchini humo.
“Nitatakiwa kuonana nao na kuwapa ripoti kuhusu mgonjwa huyo,” alisema.
Hilo halikuwa tatizo, wakasubiri na ilipofika majira ya saa nane mchana, Wilson na Okotee wakaenda mpaka hospitalini hapo na kuanza kuzungumza naye. Walizungumza Kiingereza kizuri kabisa huku wakati mwingine wakichanganya na Kifaransa ili kuvuta uasilia wa kile walichokuwa wakikitaka mahali hapo.
“Ripoti inasemaje?” aliuliza Wilson huku akimwangalia Dk. Sebastian.
“Ana tatizo la presha, hilo tu!”
“Basi sawa.”
Walijifanya kuwa bize kukagua ripoti hiyo na baada ya muda wakamwambia kwamba walitakiwa kumuona mgonjwa wao ili wajue ni kwa namna gani walitakiwa kufanya kazi ya kumsafirisha na kumpeleka nchini Ufaransa.
Walipoingia ndani ya chumba hicho, umakini wao haukuwa kwa mgonjwa, walikuwa wakiangalia mazingira ya chumba hicho na ule mlango walioambiwa kwamba ulikuwa humo. Walipojiridhisha, wakawaambia watu wote watoke ili wamchunguze kwa umakini?
“Mpaka sisi?” aliuliza Wilson.
“Ndiyo! Kila mtu!” alijibu Wilson huku akijifanya kama mtu aliyekuwa makini kwa kile alichokifanya.
Manesi waliokuwa humo, madaktari kutoka katika hospitali hiyo wakatoka ndani, ilikuwa ni lazima wamchunguze mgonjwa zaidi, lakini lengo la kufanya hivyo ilikuwa ni kama kumuandaa kwa safari pasipo walinzi kufahamu chochote kile.
Maofisa wale wa Usalama wa Taifa hawakutakiwa kuingia ndani, ulinzi wao waliufanya nje ya chumba kile, walisimama imara pasipo kuzungumza na mtu yeyote yule, kila kitu kilichokuwa kikiendelea walikuwa wakikiangalia kwa umakini kabisa na hawakuyatilia ulakini kwa kuwa walikuwa wakishirikiana na madaktari wa hospitali hiyo.
Kitendo cha Amanda na wenzake kutoka nje ulikuwa ni mpango ambao uliandaliwa, hawakukaa hapo, wakaondoka mpaka nje ya hospitali hiyo ambapo huko wakaandaa gari lao, wakazunguka kwa nyuma mpaka ulipokuwa mlango ule wa nyuma wa kuingilia ndani ya chumba kile na kuanza kugonga.
Wilson na Okotee wakajua kwamba hao walikuwa watu wao, wakaufungua mlango, wakaanza kukisukuma kitanda kile kupitia mlango ule na kukitoa nje huku Bokasa akiwa kitandani akishangaa, hakupewa taarifa juu ya kilichokuwa kikiendelea, aliona kama kulikuwa na mchezo uliokuwa ukifanyika.
Hawakutakiwa kugundulika hivyo Amanda na mwenzake wakaondoka na kuwaacha Wilson na mwenzake wakiisukuma machela kule nje. Kila mtu aliyekuwa akipishana naye hakuwa na wasiwasi nao, muonekano wao kuanzia mavazi, miwani waliyoivaa ilionyesha kabisa kwamba walikuwa madaktari hivyo kumpeleka Bokasa kwenye gari walilokuwa wamekuja nalo.
Hakukuwa na mtu aliyehoji kitu chochote kile, kitu cha ajabu hata manesi wengine waliokuwa wakikiona kitendo kile waliona ni kawaida sana, imani yao ilikuwa kubwa kwa madaktari hivyo kuhisi kwamba wale walikuwa madaktari wa hospitali hiyo na iliwezekana mgonjwa huyo alikuwa akihamishwa hospitali kwa matibabu zaidi.
Hawakuzungumza kitu, wakaingia ndani ya gari ambapo likawashwa king’ora na kuondoka mahali hapo kuelekea uwanja wa ndege. Kazi hiyo mara ya kwana ilionekana kuwa kubwa mno lakini baada ya kuifanya wakagundua kuwa ilikuwa kazi nyepesi mno ambayo isingeweza kuwasumbua hata kidogo.
“Kumbe ni nyepesi hivi! Haki ya Mungu tumemsukuma mlevi kwenye mteremko wa mlima,” alisema Wilson huku akimwangalia mwenzake kwa furaha kwani kile walichokuwa wamekifanya kilionekana kuwa kitu chepesi kuliko vyote walivyowahi kuvifanya.
Wakati hayo yakiwa yametokea, Dk. Sebastian alikuwa ofisini kwake, kitu pekee ambacho alijua ni kwamba madaktari wake walikuwa wakishughulika na mgonjwa ambaye alikuwa akiandaliwa tayari kwa kusafirishwa na kupelekwa nchini Ufaransa kwa ajili ya matibabu.
Baada ya dakika kadhaa, akaamua kutoka ndani na kuelekea kule. Huko, akaanza kuhisi kulikuwa na kitu kinaendelea kwani alipofika hapo, alishangaa kuwaona manesi wakiwa nje ya chumba kile pamoja na walinzi.
Hilo halikuwa jambo la kawaida, akawasogelea na kuwauliza sababu ya kuwepo hapo nje ambapo walimwambia kwamba wale madaktari walikuwa ndani ya chumba kile wakimwangalia zaidi mgonjwa wao.
“Wapo ndani wakimwangalia mgonjwa wao?” aliuliza Dk. Sebastian huku akiashangaa.
“Ndiyo!”
“Kivipi? Mbona hili ni jambo tofauti sana na utaratibu wetu!?” aliuliza Dk. Sebastian huku akiwaangalia kwa mshangao mkubwa.
Akaufuata mlango kwa lengo la kuufungua, alipofanya hivyo, mlango haukufunguka. Alishangaa, ilikuwaje madaktari hao wawe ndani huku manesi wake wakiwa nje? Ila jambo jingine ambalo lilimshangaza, kwa nini ndugu wa mgonjwa huyo hawakuwa mahali hapo?
“Na ndugu zao?”
“Waliondoka!”
Alipopewa jibu hilo tu akahisi kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea, akaugonga mlango, haukufunguliwa, akaugonga zaidi na matokeo yakawa vilevile hali iliyomtia hofu. Hawakuwa na jinsi, kama hali iliendelea hivyo ilikuwa ni lazima kuuvunja mlango, kitu walichotaka ni kujua kilichokuwa kikiendelea ndani ya chumba hicho.
Mlango ukavunjwa na walipoingia, hawakuwakuta madaktari, na mbaya zaidi hata mgonjwa hakuwa akionekana kitandani hapo hali iliyomshangaza kila mmoja.
Wakaitana, kila mtu aliyekuwa akiangalia kilichokuwa kimetokea, alishangaa. Usalama wa Taifa walipopewa taarifa, wakachanganyikiwa hivyo kuanza kuwatafuta watu hao hapo hospitalini. Walikuwa wamekwishachelewa kwani hata walipouliza walinzi wa getini waliwaambia kwamba kuna gari la wagonjwa liliondoka kama dakika ishirini na tano zilizopita.
“Kuna gari liliondoka? Lina namba zipi?” aliuliza Dk. Sebastian! Akili yake iliruka.
“Bel89J0,” alijibu mlinzi.
“Hatuna gari hilo! Ni la hapa hospitali?”
“Hapana! Hilo sikuwahi kuliona. Na tulishindwa kuuliza chochote kwa kuwa tulijua kwamba ni madaktari ambao mlikubaliana nao kumchukua mgonjwa!” alisema mlinzi maneno yaliyomchanganya zaidi Dk. Sebastian.
Hakutaka kukubali, hakukukalika, akachukua simu na kukipigia kitengo cha ulinzi wa barabarani, akawaambia kwamba kulikuwa na tatizo limetokea, gari moja la wagonjwa liliondoka hospitalini huku likiwa na mgonjwa, hawakujua ni wapi lilielekea lakini baada ya kutaja namba zake, akaambiwa kwamba kamera za barabarani zililinasa gari hilo likielekea uwanja wa ndege.
“Unasema?”
“Kamera zinaonyesha hivyo!”
Hakutaka kuchelewa, haraka sana akawapigia simu polisi wa uwanja wa ndege. Alichanganyikiwa, kitendo cha mgonjwa huyo kuibwa hospitalini hapo kilionyesha kabisa kwamba angekuwa kwenye matatizo makubwa na angeweza hata kufukuzwa kazi, alipopiga huko, akaambiwa kwamba gari hilo lilikuwepo kwani liliingia mpaka ndani kabisa ya uwanja huo.
“Hebu lizuieni. Kuna mgonjwa humo ameibwa. Lizuieni,” alipiga kelele Dk. Sebastian huku akivua koti lake tayari kwa kwenda huko uwanjani.
“Mkuu! Kuna taarifa kutoka nchini Ubelgiji!” alisikika mwanamke akizungumza kwenye simu.
“Taarifa gani?” aliuliza Ojuku.
“Bokasa ametoroshwa hospitalini!” alisema mwanamke huyo.
Ojuku akashtuka, akasimama pale alipokuwa, akauliza tena juu ya kile alichoambiwa, alihisi kama hakusikia vizuri, kilekile alichoambiwa ndicho akaambiwa kwa mara nyingine kwamba Bokasa alikuwa ametoroshwa hospitalini na kulikuwa na taarifa kwamba gari lililokuwa limemsafirisha lilionekana uwanja wa ndege.
Hakutaka kusikia lolote lile, haraka sana akapiga simu mpaka nchini Ubelgiji na kuzungumza na waziri mkuu wa nchi hiyo na kumwambia kilichokuwa kimetokea, waziri huyo yeye mwenyewe alishangaa kwani kitu kama hicho hakikuwa kutokea nchini mwake, ilikuwaje mpaka mgonjwa atoroshwe huku madaktari wakiwa hawafahamu chochote kile.
Simu ikapigwa mpaka hospitalini ambapo akathibitishiwa taarifa hiyo na hivyo kuzungumza na kamanda mkuu wa jeshi la polisi nchini humo na kumwambia kwamba alitakiwa kupambana mpaka kuhakikisha anafahamu mahali mgonjwa huyo alipopelekwa.
Ndani ya dakika kumi tu akapewa taarifa kwamba gari lililokuwa limemchukua lilionekana uwanja wa ndege hali iliyoonyesha kwamba mtu huyo alitakiwa kusafirishwa kuelekea nchi fulani.
“Mtafuteni hapo! Jueni hilo gari limempeleka hapo kwa lengo la kwenda wapi! Hakutakiwi ndege yoyote kuondoka mpaka tujue huyo mgonjwa alikuwa akipakizwa ndani ya ndege gani. Hakikisheni hakuna ndege inayoondoka muda huu!” alisikika kamanda mkuu wa jeshi la polisi nchini humo.
“Sawa mkuu!”
***
Wilson akawasiliana na Olotu na kumwambia kwamba mtu waliyetumwa waende kumchukua tayari alikuwa mikononi mwao na wakati huo walikuwa njiani kuelekea uwanja wa ndege. Hiyo ilikuwa taarifa nzuri, na kwa sababu ndege ya rais ilikuwa imekwishafika katika uwanja huo, akawaambia kwamba hakukuwa na tatizo lolote lile, walichotakiwa ni kufika uwanjani hapo na kuondoka na mtu huyo.
Walipofika, gari likapitishwa mpaka ndani kabisa ya uwanja huo, walipewa taarifa kwamba kulikuwa na ndugu wa rais ambaye alipelekwa katika hospitali moja hapo Brussels kutibiwa na alikuwa amepona hivyo kutakiwa kurudishwa nyumbani. Hata Bokasa alipoteremshwa huku akiwa kwenye kiti chake, hakukuwa na mtu aliyekuwa na hofu kwa kuhisi kwamba huyo alikuwa ndugu wa rais wa Kenya.
Hakukuwa na muda wa kupoteza, kila kitu kilikuwa tayari na kilichofanyika kilikuwa ni kuingia ndani ya ndege na hapohapo kuwashwa tayari kwa kuondoka nchini Ubelgiji. Kila mmoja akashusha pumzi, kazi nzito waliyokuwa wamepewa waliikamilisha kwa kiasi kikubwa na hapo walikuwa wakielekea nchini Kenya kwa ajili ya kumkabishi Bokasa katika mikono ya Olotu aliyehitaji kujua kitu kimoja tu, majina ya wafanyabiashara waliokuwa wamepewa mzigo mkubwa wa madawa ya kulevya.
“Koh koh, koh! Nyie ni wakina nani?” alikohoa Bokasa na kuuliza, alikuwa akiwaangalia wanaume hao, mpaka kipindi hicho hakujua kilichokuwa kikiendelea, aliwaona watu wakiwa wameingia ndani ya chumba kile kama madaktari, wakamchukua, wakampakiza ndani ya ndege na kuondoka.
“Utatufahamu! Kwa kifupi ni kwamba tumetumwa kuja kukuchukua,” alijibu Wilson huku akimwangalia mwanaume huyo.
“Na nani?”
“Olotu! Unamfahamu?” alidakia Okotee huku akiwa amemsogelea Bokasa karibu na kitanda chake.
Alimfahamu mtu huyo, alikuwa mmoja wa marafiki zake ambao alikuwa akishirikiana nao katika mambo yake machafu. Kitendo cha kumchukua kule Ubelgiji hakikuwa kumpenda sana bali kulikuwa na jambo jingine kabisa ambalo alitaka kulifanya kwa ajili ya kupata kitu fulani kutoka kwake.
Hakuwa na furaha, alijua dhahiri kwamba alitoka mikononi mwa maofisa wa Usalama wa Taifa lakini katika mikono aliyokuwa ameangukia, hakukuwa na amani hata mara moja. Akabaki kimya, akaanza kuyakumbuka majina ya watu aliokuwa akiwauzia madawa ya kulevya, aliyakumbuka majina yote matatu ambayo alitakiwa kuyataja kama tu angefika nchini Kenya na kuulizwa kuhusu watu hao.
***
Gari la wagonjwa lilikuwa likionekana katika uwanja wa ndege, kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba inawezekana mtu waliyekuwa wakimtafuta alikuwa ndani ya gari hilo. Polisi wanne wakalisogelea huku wakiwa na bunduki mikononi mwao, walipofika, wakafungua mlango, ndani hakukuwa na mtu yeyote yule.
Hilo likawachanganya, hawakubaki mahali hapo, wakaondoka mpaka katika ofisi ya meneja wa uwanja huo na kumuuliza kilichokuwa kimetokea kwamba waziri mkuu alisema kwamba hakukutakiwa ndege yoyote kuondoka kwa kuwa kulikuwa na mtu aliyekuwa akitoroshwa, kwa nini sasa mtu ateremshwe kutoka mule, apandishwe ndani ya ndege na kuondoka?
“Tangazo lilichelewa kutoka. Nilipigiwa simu saa 7:30, wakati nikipigiwa simu hiyo, ndege iliyomchukua ndugu wa rais kutoka katika gari lile iliondoka saa 7:15. Sasa ningefanyaje?” alihoji meneja huku akiwaangalia polisi waliokuwa wameingia ofisini kwake.
Tatizo halikuwa kwake, alifanya kile alichoagizwa kufanya ila tatizo hilo likahamia kwa Dk. Thump ambaye yeye na madaktari wenzake walifanya uzembe mkubwa mpaka kutokuona wakati Bokasa akiondolewa ndani ya chumba kile na kupelekwa uwanja wa ndege.
Uzembe huo ukaanza kutangazwa kila kona, watu wakatoa taarifa katika mitandao ya kijamii kwamba Bokasa aliyekuwa rais wa Tanzania alitoroshwa nchini Ubelgiji kwa kutumia ndege ya rais wa Kenya na kupelekwa sehemu isiyojulikana.
Taarifa za ndege ya rais kutumika katika utoroshaji wa Bokasa nchini Ubelgiji zikapingwa vilivyo na msemaji wa ikulu ambaye aliwataka watu wote wasiziamini taarifa hizo kwa kuwa kulikuwa na ugomvi uliokuwa ukiendelea chini chini baina ya Kenya na Ubelgiji.
“Hakuna kitu kama hicho. Ni stori ambazo zimesambazwa kwa kuwa kuna kitu kinaendelea! Hatuwezi kumtorosha mtu, tumtoroshe kwa maslahi ya nani?” alihoji msemaji wa ikulu kauli iliyofanya watu kuhisi kwamba hakukuwa na kitu cha kweli kama hicho.
***
Ulikuwa ni kama ugomvi baina ya Tanzania na Kenya, hakukuwa na kitu ambacho Ojuku alikuwa akikihitaji kipindi hicho kama Bokasa aliyekuwa akisubiri kusafirishwa kupelekwa nchini Tanzania na kusomewa kesi yake iliyokuwa ikimkabili.
Mawasiliano yalifanyika baina ya nchi hizo, bado Kenya walikuwa wakisisitiza kwamba taarifa zilizokuwa zimetolewa hazikuwa za kweli, kulikuwa na mtafaruku uliokuwa ukiendelea baina ya Kenya na Ubelgiji baada ya nchi hiyo kuamua kubinafsisha mashamba yaliyokuwa yakimilikiwa na Wabelgiji hapo Kenya.
“Hapana! Kutakuwa na kitu! Haiwezekani taarifa hizo ziwe za uongo na wakati ndege imepigwa mpaka picha,” alisema Ojuku.
“Hutakiwi kuamini kila kitu unachokiona kwenye mitandao!” alisikika Rais Onyango.
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Hebu rudia nisikie tena!”
“Hutakiwi kuamini kila kitu unachokiona kwenye mitandao!” alisema kwa mara nyingine.
“Basi sawa. Ila usije ukaamini kitu kingine kinachotokea huko kwenye mitandao. Kuna siku utaniuliza, nitakwambia maneno hayohayo uliyoniambia! Umesikia?” alisema Ojuku na kuuliza swali.
“Nimesikia! Ila hutakiwi kuamini kamwe!” alisema rais huyo kwa kebehi na kisha kukata simu.
Ojuku akatulia, kichwa chake kilikuwa kikimuuma, moyo wake ulichanganyikiwa, Watanzania hawakutaka kusikia kitu chochote kile, mtu waliyekuwa wakihitaji kumuona nchini mwao hakuwa mwingine bali ni Bokasa tu ambaye mpaka kipindi hicho hakujulikana mahali alipokuwa.
Hakujua kipi alitakiwa kufanya. Wakati akiwa amekaa akifikiria mambo mengi mara akasikia simu yake ya mkononi ikipigwa, haraka sana akaichukua na kuangalia mpigaji, namba ilikuwa ngeni, hapohapo akaipokea.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Halo!”
“Unazungumza na Godwin hapa,” alisikika mwanaume wa upande wa pili.
“Godwin! Umepiga simu wakati sahihi kabisa. Kuna kitu nataka unisaidie!” alisema Ojuku.
“Haina shida. Kabla hujaniomba, nimekwishajua hivyo nitakusaidia,” alisikika Godwin maneno yaliyomfanya Ojuku kushtuka kwani aliamini kwamba kila kitu alichokuwa amekizungumza kwenye simu kilikuwa baina yao watu wawili, iweje mwingine asikie kila kitu.
“Umesikia nini?”
“Nataka rais wa Kenya asiamini kila kitu anachokiona kwenye mitandao. Unaonaje?” aliuliza Godwin.
“Sawasawa. Ninataka maneno aliyoniambia ndiyo nimwambie,” alisema Ojuku.
“Basi sawa. Nipe saa kumi, kabla ya ndege kufika nchini Kenya, tayari kuna mambo yatatokea hapo Kenya, atagundua kwamba anacheza na watu hatari sana. Kama Usalama wa Taifa wa Uswisi walisumbuka sana, Wakenya watajificha vipi mpaka wasisumbuke. Nipe saa kadhaa tu! Kila kitu nitakiweka wazi,” alisema Godwin na kukata simu.
***
Ndege ilikuwa ikiendelea na safari kuelekea nchini Kenya, kila mtu alikuwa na amani moyoni mwake, walikuwa na uhakika kwamba wangefika salama nyumbani. Ndani ya ndege walikuwa wakiongea yao huku wakijipongeza kwamba walifanya kazi nzuri.
Marubani wawili, Sosi Omog na Amrani Neta walikuwa wakiendesha ndege huku wakifanya mawasiliano na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai kwa ajili ya kufika hapo, kuweka kituo kwa dakika kadhaa, kujaza mafuta na kuendelea na safari yao mpaka jijini Nairobi nchini Kenya.
Ndege ilichukua saa kadhaa mpaka kuficha Dubai ambapo ikatua, wakapumzika, wakajaza mafuta na kuondoka mahali hapo huku wakitakiwa kuunganisha moja kwa moja mpaka katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta nchini Kenya.
Ndege ilikuwa ikikata mawingu. Kila mmoja alitegemea kuingia jijini Nairobi baada ya saa kumi lakini kitu cha kushangaza kabisa, mpaka saa kumi na mbili zinakatika ndege haikuwa imetua katika uwanja huo jijini Nairobi.
Hilo likawatia wasiwasi Wilson na Okotee, wakajua kwamba kulikuwa na tatizo lililokuwa limetokea, walitaka kujua sababu ambayo iliwafanya rubani kuwa wazembe mpaka ndege hiyo kutokutua kwa wakati katika uwanja huo.
Wakawafuata na kuanza kuzungumza nao lakini watu hao wakawaambia kwamba kila kitu kingekwenda kama kinavyotakiwa, baada ya dakika kadhaa wangetua katika uwanja wa ndege.
“Sawa,” aliitikia Wilson.
Baada ya dakika arobaini na tano wakaambiwa wafunge mikanda yao kwani ndege hiyo ilikuwa ikijiandaa kutua katika uwanja wa ndege, wakafanya hivyo haraka sana na ndege hiyo kuanza kutua katika uwanja huo.
“Hatimaye tumefika. Mungu ni mwema,” alisema Wilson wakati ndege ikitembea katika ardhi ya uwanjani hapo na mbele kabisa kusimama.
Wakanyanyuka, mhuhdumu mmoja akaufungua mlango, gari lililokuwa na ngazi kubwa ya kushukia likasogea pale mlango wa ndege ulipokuwa, ukafunguliwa na kila mmoja kutakiwa kutoka ndani ya ndege hiyo. Wakamchukua mtu wao na kwenda mlangoni, walipoangalia nje, kulionekana kuwa tofauti, haukuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta walioufahamu bali ulikuwa uwanja mwingine kabisa.
“Bumba Airport,” alisema Wilson huku akiwa amesoma ubao mmoja mkubwa ulioandikwa maneno hayo kiasi kwamba wakabaki wakishangaa.
“Bumba?” aliuliza Okotee huku naye akisogea mlangoni kuangalia kile alichokisikia.
“Ndiyo! Mbona tumeletwa Kongo badala ya Nairobi?” aliuliza Wilson huku akishangaa, hapohapo akaanza kuelekea kule mbele kuwauliza marubani ni kitu gani kilikuwa kimetokea, walipofika kule, cha kushangaza wakawakuta marubani wote wawili walikuwa wakilia kama watoto wadogo.
***
Godwin aliona kazi kubwa mno mbele yake, kichwa chake kilitakiwa kufanya kazi ya ziada kuhakikisha kwamba Bokasa anapatikana haraka iwezekanavyo. Kitu cha kwanza kabisa alichokuwa akihitaji kufanya ni kuhakikisha kwamba anapata majina ya marubani wa ndege ile ya raisi kwa ajili ya kufanya kazi aliyokuwa akiitaka.
Akawasiliana na Ojuku na kumuomba namba ya Rais Onyango, hilo halikuwa tatizo, namba hiyo ilikuwepo na hapohapo akampa. Godwin akachukua kompyuta yake na kuiingiza namba ile katika kuifungua prorgamu yake aliyoitengeneza kwa ajili ya kudukua namba za simu.
Alipoiingiza, likatokea neno ‘download’ huku mbele yake kukiwa na asilimia zilizokuwa zikipanda. Zilipanda na kupanda, kuanzia 0, 20, 37, 79 mpaka kufikia mia moja na hapohapo likatokea neno jingine yaliyosomeka ‘hacking process’ ambapo mbele yake kulikuwa na asilimia kama zile zilizokuwa zimepita.
Ilipofika mia moja, neno sehemu ile ikajiandika ‘hacking completed’ na hapohapo kuingia katika simu ya Rais Onyango na kuanza kuangalia kila kitu kilichokuwa humo. Akasoma meseji zote zilizoingia na kutoka, akagundua ukweli kuwa mpango mzima wa kumtorosha Bokasa haukuwa chini ya Onyango tu bali kulikuwa na mtu aliyeitwa Olotu, bilionea aliyekuwa akiishi kifahari Mombasa ambaye alimtaka mtu huyo kwa kuwa kulikuwa na wafanyabiashara aliofanya nao biashara ya kuuza madawa ya kulevya hivyo alihitaji majina ya watu hao.
Mpaka kufika hapo akapata uhakika wa kukamilisha kazi hiyo, akachukua simu yake na kumpigia Ojuku, akampa taarifa juu ya kile alichokuwa amekisoma kwenye meseji zile kwamba mtu aliyekuwa katika mpango mzima alikuwa Olotu ambaye aliitumia ndege ya rais kwa makubaliano maalumu.
“Ninamfahamu mtu huyo. Ni bilionea mkubwa sana, ana nguvu mno hapo Kenya,” alisema Ojuku kwenye simu.
“Huyo ndiye aliyehusika kwa kila kitu,” alisema Godwin.
“Duh! Sawa. Na vipi kuhusu kumpata mtu wetu?”
“Nipe saa moja kila kitu kitakuwa tayari,” alisema Godwin na kukata simu.
Bado kompyuta yake ilikuwa katika simu ya Rais Onyango. Alikuwa akiangalia kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Akaenda kwenye majina ambapo huko akakuta majina mawili yakiwa yameandikwa Pilot Sosi na nyingine iliandikwa Pilot Amrani, akajua kwamba hao walikuwa marubani wa ndege yake.
Hakutaka kuchelewa, akazichukua namba zao na kuanza kuzidukua kwa kuingia kwenye kompyuta. Haikuwa kazi kubwa, ndani ya muda mchache akaingia ndani ya simu zao na kuchukua namba za wake zao, akaziunganisha na namba yake, akazidukua kwa lengo la kuwachezea mchezo mmoja hatari.
“Winfrida! Kuna kitu nataka unisaidie,” alisema Godwin huku akimwangalia mpenzi wake.
“Kitu gani?”
“Kuna watu nataka uzungumze nao. Ninahitaji udanganye kwamba wewe ni wake zao, uzungumze nao huku ukilia kwamba umetekwa na watu waliokuwa na bunduki ambapo kama hawatofanya kitu wanachokitaka basi unaweza kuuawa,” alisema Godwin.
“Kwa nini sasa?”
“Utajua baadaye! Unaweza kufanya hivyo?”
“Ndiyo!”
“Kwa lafudhi ya Kikenya, na wakati mwingine zungumza Kiingereza, usitoke nje ya biti! Yaani uwe kama Mkenya!” alisema Godwin.
“Hakuna tatizo!”
Alimuandaa Winfrida kwa ajili ya kuifanya kazi hiyo, hakuwa na hofu, alijua kwamba kwa namna moja au nyingine ilikuwa ni lazima kwa marubani wale kuamini kwamba walikuwa wakizungumza na wake zao. Kilichofuata ni kuanza kuwapigia simu, katika kila nchi waliyokuwa wakipita walikuwa na namba zao, Godwin alizichukua, na kwa kuwa aliambiwa muda ambao ndege hiyo iliondoka nchini Ubelgiji, akajua muda ambao ingetua Dubai na hivyo kujiandaa kuwapigia simu wakati ndege hiyo itakapotua nchini humo na kuzungumza nao.
Kila wakati alikuwa akipiga simu zao kujua kama walikuwa wamefika au la. Aliendelea hivyohivyo huku msichana wake akiwa pembeni yake akiwa amejiandaa kabisa kufanya kazi aliyotakiwa kuifanya. Dakika zilikatika, baada ya saa kadhaa alipojaribu kupiga simu ya Sosi, ikapokelewa na mwanaume huyo.
“Halo mke wangu!” alisikika mwanaume huyo kimapozi kabisa.
“Mume wangu njoo utuokoe! Mume wangu tunakufa, wanatuua...they want to kill us...pleasee come to save us...” alisema Winfrida kwa lafudhi akihitaji msaada wa kuokolewa kutoka kwa watu waliowateka, tena hakuzungumza hivihivi, alijifanya kulia kiasi kwamba ilikuwa vigumu kugundua kwamba hakuwa yeye.
“Nani amekuja wateka? Mke wangu! Who kidnapped you?” aliuliza Sosi huku akiwa amechanganyikiwa, hata kabla hajajibiwa kile alichokitaka, simu ikakatwa.
Alichanganyikiwa, akapiga simu kwa mke wake, kwa kuwa tayari Godwin alikuwa amekwishaidukua simu hiyo, ilipopigwa kwenda kwa mke wa Sosi, ikaingia kwake, akaipokea na kuipeleka sikioni.
“Halo! Mke wangu...mke wanguuuuu...” aliita Sosi.
“Nisikilize bwana mkubwa. Tupo na mke wako, tunamuua. Si yeye tu bali tupo na watoto wako pia, wote tunawaua. Ukifika huku, utakuta vichwa vyao katika jokofu na runingani kote wataitangaza habari hii,” alisema Godwin na kukata simu, alichokifanya ni kuifunga simu ya Sosi ili isitoke kwenda kwenye simu nyingine yoyote ile.
Hakuishia hapo, alipomalizana na Sosi akahamia kwa rubani Amrani na kumwambia vilevile. Marubani wote hao walichanganyikiwa, hawakujua kilichokuwa kikiendelea. Walizipenda familia zao, kwao, hizo zilikuwa kila kitu.
Walikuwa ndani ya ndege, maisha yao yalikuwa humo, walisafiri kwenda nchi mbalimbali na hata katika safari hiyo waliagizwa na rais kwa kuwa kulikuwa na mtu waliyetakiwa kwenda kumchukua, hivyo wakaenda peke yao pasipo watu wa rais ambao mara kwa mara walikuwa wakisafiri nao.
Kila mmoja akajua kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa kuziona familia zao, wakawapigia simu, hazikutoka, wakati wakijifikiria ni kitu gani walitakiwa kufanya, mara simu ya Sosi ikaanza kuita na alipoipokea, Godwin akaanza kusikika.
“Nisikilizeni. Kuna jambo moja tu mtatakiwa kufanya ili kuzikuta familia zenu zikiwa salama kabisa,” alisema Godwin.
“Jambo gani? Tuambie, kitu chochote kile tutafanya. Kitu chochote kile,” alisema Sosi, Amrani akaona kama angeulizwa sababu ya yeye kutokuuliza, na hivyo kuuliza kama mwenzake.
“Ipelekeni ndege nchini Kongo katika Uwanja wa Ndege wa Bumba ambapo huko mtatakiwa kusubiri kuona kitakachotolewa. Mkiifikisha ndege huko tu, familia zenu zitakuwa salama ila mkileta mchezomchezo, mtavikuta vichwa vyao katika jokofu,” alisema Godwin kwa mkwara mzito.
“Sawa. Tunafanya hivyo!”
Hilo lilikuwa agizo, walijua kwamba ndege ilikuwa ni ya rais wa Kenya lakini ilikuwa ni lazima ipelekwe nchini Kongo kama tu walihitaji kuziona tena familia zao zikiwa salama kabisa. Hakukuwa na haja ya kujadili kitu chochote kile, hawakuwaambia Wilson na mwenzake kilichotokea bali walichokifanya ni kuwasha ndege na kuelekea nchini Kongo.
Njiani, kila mmoja alikuwa na huzuni, waliogopa, walihisi kabisa kwamba mtu aliyekuwa amewapigia simu kulikuwa na uhakika kwamba alikuwa Al Shaabab hivyo kama wasingefanya kile kilichotakiwa kufanywa basi wote wangeuawa kama walivyoambiwa.
Safari ikawa chungu, ikaendelea mpaka walipofika katika uwanja huo ambapo watu wa anga walionekana kuwa na taarifa kwamba ndege ya rais wa Kenya ingetua katika uwanja huo kitu kilichowashangaza kwamba kwa nini isingekwenda kutua Kinshasa au Lubumbashi mpaka wakaamua kwenda Bumba?
Ndege ilichukua saa kadhaa, ikaanza kutua katika uwanja huo wa ndege ambapo hata kabla Wilson na Okotee hawajateremka wakaona kundi la wanajeshi zaidi ya hamsini kutoka nchini Tanzania wakiingia na bunduki katika uwanja ule huku wakiifuata ndege ile.
“Washeni ndege tuondoke! Kwa nini mmeileta ndege hii huku?” aliuliza Wilson huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Kwa sababu ya familia zetu. Tumefanya hivi kuziokoa familia zetu,” alijibu Sosi huku mashavu yake yakiwa yamelowanishwa kwa machozi yaliyokuwa yakimtoka mfululizo.
“Familia zenu?”
“Ndiyo! Tusingefanya hivi, zingeuawa,” alijibu Amrani, hapohapo wakawasikia wanajeshi wale wakianza kupandisha ngazi za ndege ile na kuingia ndani. Wakawekwa chini ya ulinzi na Bokasa kuanza kuteremshwa huku akiwa katika kitanda maalumu.
“Bokasa! Karibu sana katika mikono ya Watanzania. Upo salama, tunakupeleka nchini kwako, kuna kesi nyingi zinakusubiri,” alisema mwanajeshi mmoja aliyekuwa na kofia iliyokuwa na rangi ya damu ya mzee.
“Jamani! Mbona sielewi?”
“Utaelea tu baada ya kufika katika Mahakama ya Kuu! Mpelekeni chini,” alisema mwanajeshi huyo na hapohapo kuanza kushushwa kibabe.
****
Godwin ndiye aliyeanzisha maneno maneno katika Mtandao wa Instagram, aliandika kwamba ndege ya Rais wa Kenya ilikuwa imepotea katika mazingira ya kutatanisha na tayari ilionekana angani ikienda katika nchi fulani Afrika.
Habari hiyo ndiyo iliyoanza kusambaa mpaka ilipowafikia Usalama wa Taifa nchini kenya ambao moja kwa moja wakawasiliana na Rais Onyango na kumwambia kilichokuwa kimetokea.
Hilo lilimchanganya mno, hakuamini kilichokuwa kimetokea, alihisi kwamba ulikuwa ni uongo, akawapigia simu watu wa anga uwanja wa ndege ili kupata taarifa ya ndege hiyo na wao kumwambia kwamba hakukuwa na dalili za ndege hiyo kutua siku hiyo kwani kama kulikuwa na ratiba hiyo basi wangepewa taarifa wakati ndege ikiondoka Dubai.
“Tanzania!” hilo ndilo jina lililomjia kichwani mwake. Haraka sana akachukua simu na kumpigia Ojuku, akagundua kabisa kwamba mwanaume huyo alifanya kitu kimoja mpaka ndege hiyo kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Simu ilipopokelewa, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumwambia kilichokuwa kimetokea na alikuwa na uhakika kwamba alihusika katika hilo.
“Kwani taarifa hizo umezipata wapi rafiki yangu?” aliuliza Ojuku.
“Watu wangu wamezipata Instagram kwenye akaunti ya Mabadiliko ya Kweli!” alijibu Rais Onyango huku akitetemeka.
“Nisikilize Onyango. Hutakiwi kuamini kitu chochote unachokiona katika mitandao. Au umesahau hilo?” aliuliza Ojuku swali lililomfanya Rais Onyango kupandwa na hasira kali.
***
Rais Onyango alikasirika, jibu alilopewa na Ojuku kumwambia kwamba hakutakiwa kuamini taarifa zilizokuwa katika mitandao lilimkera. Hakutaka kuendelea kusikiliza dhihaka kutoka kwa Ojuku, alichokifanya ni kukata simu.
Alichanganyikiwa, kwa tukio lililotokea, hakuamini kama Usalama wa Taifa walishindwa kugundua mahali ndege hiyo ilipokuwa. Mawasiliano yalifanyika kutoka katika uwanja wa ndege mmoja mpaka mwingine lakini cha ajabu hakukuwa na taarifa zozote ambazo zilisema mahali ndege hiyo ilipokuwa.
Wakenya walishangaa, hawakuamini kile kilichotokea, ilikuwaje ndege ya rais wao ipotee katika mazingira ya kutatanisha? Taarifa mbalimbali zilizokuwa zikiandikwa katika Akaunti ya Mabadiliko ya Kweli kwenye Mtandao wa Kijamii wa Instagram zilionyesha kabisa mtu aliyekuwa akiandika posti hizo alijua mahali ndege hiyo ilipokuwa.
Hakutaka kupoteza muda, hapohapo akampigia simu Olotu kwa lengo la kumwambia kile kilichokuwa kimetokea. Wala hazikupita sekunde nyingi simu ikapokelewa.
“Nilitaka nikupigie. Niambie kiongozi,” alisikika Olotu kwenye simu.
“Umeona kilichotokea?” aliuliza Rais Onyango.
“Nimeona! Nimechanganyikiwa. Ndege imekwenda wapi?” aliuliza Olotu huku kwa kuisikia sauti yake tu halikuwa jambo gumu kugundua kwamba alikuwa amechanganyikiwa.
“Hata sisi hatujui! Ila mkuu wa majeshi nchini Tanzania anajua mahali ndege ilipo,” alisema Olotu huku akionekana kuwa na uhakika.
Taarifa hizo ziliendelea kuwashangaza kila watu duniani, lilikuwa jambo lisilowezekana hata kidogo kwa ndege ya rais yeyote kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Simu zilipigwa katika viwanja vyote vikubwa, hawakuwa na taarifa juu ya ndege hiyo, kila sehemu walisema kwamba ndege haikuwa imeonekana.
“Kwa hiyo imepotea kama ndege ya Malaysia?” alihoji mwandishi wa kituo cha Televisheni cha NBC nchini Kenya.
“Hakuna anayjua, Usalama wa Taifa hawazungumzi kitu chochote kile, nahisi katika hili kuna mtu ndani ya serikali anajua kinachoendelea,” alisema mwandishi mwingine.
Kila mmoja alijua kabisa kwamba Tanzania ilikuwa ikijua mahali ndege ilipokuwa, maneno kwenye mitandao ya kijamii yalikuwa yakiwachanganya Wakenya lakini wengi wao walikuwa wakiuamini ukurasa wa Mabadiliko ya Kweli ambao kwa kipindi hicho ulizidi kushika kiki mpaka kufikisha wafuasi milioni sabini huku Wakenya nao wakiwa wengi kuufuatilia.
“Ndege ipo Afrika, nchi fulani hivi! Ila kwa sababu ilitumika vibaya, itafunguliwa yote na itakwenda kuundwa katika nchi moja huko Asia, itauza huko na pesa kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu nchini Kenya. Hiyo itakuwa fundisho kwa serikali nyingine za Afrika ambazo zinaifanya ndege ya rais kuingia katika kazi nyingine ambayo haikupaswa kuingia. Hayo ni matumizi mabaya ya serikali,” aliandika Godwin katika akaunti ile kitu kilichowafanya watu wengi kutokuwa na uhakika kama ndege itapatikana.
“Hebu tuambie ukweli! Kwa hiyo ndege haitoonekana?” aliuliza jamaa mmoja kwenye posti hiyo.
“Ndiyo! Hivi ninavyoongea, ndiyo inafunguliwa yote na vifaa vyake kusafirishwa,” alijibu Godwin kisha kutuma emoj ya mtu anayecheka sana.
Serikali ya Kenya ikachafuka, hakukuwa na mtu aliyeamini kama kitu hicho kilifanyika katika nchi hiyo ambayo iliaminika kuwa na ulinzi wa hali ya juu. Walijua kwamba ndege hiyo ilikuwa sehemu fulani lakini kitu cha ajabu kabisa walipiga simu katika nchi zote za Afrika na kuambiwa kwamba ndege hiyo haikuwepo katika nchi hizo.
“Burundi, Kongo, Namibia, Senegal, Nigeria na nchi zote tumepiga simu na kuambiwa kwamba ndege hiyo haipo,” alisema waziri mkuu wa nchi hiyo.
“Tanzania! Itakuwa katika Uwanja wa Ndege wa JFK, tuma watu waende Tanzania,” aliagiza Rais Onyango huku akionekana kuchanganyikiwa zaidi.
Hakukuwa na muda wa kupoteza, haraka sana Usalama wa Taifa wakatumwa huko huku baadhi ambao walijifanya kuwa kama wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakitangulia katika uwanja huo kwa ajili ya kuchunguza kama kulikuwa na ndege hiyo.
Walipofika huko, haraka sana wakaanza kufanya uchunguzi. Lilikuwa jambo gumu mno kuipata, hakukuwa na mtu aliyekuwa akijua kama ndege hiyo ilikuwa nchini Kongo na wakati huo ilikuwa ikifunguliwa kwa ajili ya vifaa vyake kusafirishwa kwenda kuuzwa nchini Japan.
Walichunguza kwa siri, tena kwa kila eneo lakini hawakuweza kuiona ndege hiyo kitu kilichomchanganya zaidi Rais Onyango.
“Huu ni uadui! Hatuwezi kukubali aibu hii! Lazima tuivamie nchi yako,” alisema Onyango kwenye simu, alikuwa akizungumza na Ojuku.
“Kisa?”
“Ndege yetu ipo wapi?”
“Kwani nani kaichukua?”
“Tuambieni ndege yetu ipo wapi?”
“Hatujui! Kwa kuwa suala hilo ulilipata katika mitandao ya kijamii, hebu nenda kaulize hukohuko, wanaweza kukupa majibu,” alisema Ojuku na kukata simu.
Wakati hayo yakiendelea, ndege hiyo ilikuwa ikifunguliwa, ilikuwa ni lazima isafirishwe, hayo yalikuwa maagizo ya Godwin, alikuwa na hasira, alipompa Ojuku maagizo hayo, hakupinga bali alikubaliana naye kwani kwa kipindi hicho ukimzungumzia Godwin, ilionekana kama unamzungumzia malaika aliyetumwa kuilinda nchi hiyo.
Yeye mwenyewe akafanya mawasiliano na rafiki yake aliyekuwa nchini Japan, Yokoshima Inamoto ambaye alisoma naye, katika kipindi hicho alikuwa akifanya kazi ya udalali katika mitandao mbalimbali ikiwemo Alibaba, Amazon na mitandao mingine mingi duniani.
Akamwambia kwamba kulikuwa na mzigo alitaka kumpelekea kwa ajili ya kuuza kwa matajiri waliokuwa wakitaka, alipouliza, akajibiwa kwamba ilikuwa ndege ya Rais wa Kenya ambayo ilikuwa ikitafutwa kila kona.
“Hakuna shida. Mmekwishaitenganisha?” aliuliza Inamoto.
“Ndiyo kazi hiyo inafanyika, ikiwa tayari, tutaituma huko kwa kutumia meli yetu, itafungwa katika makontena,” alisema Godwin.
“Sawa. Iwe kiasi gani?”
“Dola bilioni nne.”
“Nitaiuza kwa dola bilioni tano, moja ya dalali hapa,” alisema Inamoto kijana aliyejua kutafuta pesa kupitia mali za watu.
“Haina shida.”
***
Ojuku aliwasiliana na rais wa Kongo, Bwana Boniphace Kaposhoo na kumwambia kuhusu ndege ambayo ilitakiwa kusafirishwa haraka sana kuelekea nchini mwake. Hilo lilikuwa jambo gumu sana kukubali, alikataa lakini kutokana na maneno matamu aliyoyatumia mwanaume huyo, mwisho wa siku Kaposhoo akakubaliana naye ila kwa sharti kwamba ndege hiyo haikutakiwa kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa Kinshasa bali ilitakiwa kupelekwa Bumba.
Hilo halikuwa tatizo, Ojuku akamwambia Godwin ambaye aliwapigia simu marubani na kuwaambia ni kitu gani kilitakiwa kufanyika wakati huo. Kila kitu kilikamilika na hiyo kuitwa wataalamu wa kuifungua ndege na kuanza kufanya kazi yao ambayo iliwachukua saa sita, ilipokamilika, wakaipakiza katika lori lililokuwa mahali hapo na kuondoka kuelekea nchini Tanzania kupitia mkoani Kigoma huku likiwa chini ya ulinzi wa wanajeshi.
Wakati hayo yakiendelea, Wilson, Okotee na marubani walichukuliwa, wakaingizwa ndani ya gari na wao kuanza kusafirishwa kuelekea nchini Tanzania. Kila mmoja aliogopa, walijua kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wao kwani kwa jinsi wanajeshi wale walivyoonekana, walionekana kutokuwa na masihara hata kidogo.
Baada ya saa chache wakafika mkoani Kigoma ambapo hapom wakapandishwa ndege na kupelekwa nchini Tanzania wakiwa na Bokasa ambaye alikuwa akitafutwa kwa udi na uvumba.
“Mkuu! Tutakuwa huko ndani ya saa chache, ndiyo tunaondoka Kigoma,” alisema mkuu wa kikosi cha Leopard ambao walikwenda nchini Kongo kwa ajili ya kufanya oparesheni waliyokuwa wamepewa.
Bokasa alikuwa kimya, moyo wake ulijisikia uchungu mno, hakuamini kama kweli alikuwa amepatikana kizembe na kupelekwa nchini Tanzania. Aliamini kwamba kama angeendelea kukaa Ubelgiji basi maisha yake yangekuwa na amani na hata Watanzania waliokuwa wakimtafuta wangesubiri mpaka miezi sita ipite ndiyo wamsafirishe kwa kuwa tu waliheshimu maamuzi ya madaktari.
Kwa kutumia ndege ya kijeshi, walichukua saa moja tu wakafika jijini Dar es Salaam ambapo wakachukuliwa na kuingizwa ndani ya gari na kuondolewa mahali hapo. Hakukuwa na mtu aliyekuwa akijua juu ya uwepo wa Bokasa nchini Tanzania, alipelekwa kimyakimya na kuondolewa mahali hapo hivyohivyo.
Hakukuwa na waandishi wa habari, tukio hilo lilikuwa la siri sana kwani waliamini kama Wakenya wangejua basi wangekuwa na uhakika kwamba Tanzania ndiyo iliyofanya mpaka ndege hiyo kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
“Tufanyeje ili wasijue kwani ni lazima Bokasa apandishwe mahakamani!” alisema Meja Jenerali.
“Bado sijajua! Hapa tunatakiwa kufanya kitu kimoja cha hatari sana. Au tuseme kwamba ndege ilitekwa na watu halafu tukaiokoa na kumchukua mtu wetu?” aliuliza Ojuku.
“Hapana! Watauliza hiyo ndege ipo wapi waifuatilie!”
“Basi tuseme kwamba ililipuka!”
“Watauliza Bokasa kaponaje!”
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Sijui! Labda tuendelee kujifikiria zaidi!”
“Subiri! Nadhani Godwin anajua nini cha kufanya, ngoja nimpigie simu,” alisema Ojuku, hakutaka kumaliza, hapohapo akampigia simu Godwin kwa ajili ya kuzungumza naye.
Alimwambia wazi kwamba akili yao ilifika mwisho, hawakujua ni kitu gani walitakiwa kufanya ili watoke katika tukio hilo la kuhisiwa kwamba wao ndiyo walifanya kila liwezekanalo kuhakikisha ndege hiyo inapotezwa.
“Ni kazi rahisi sana!” alisema Godwin.
“Ndiyo maana nimekupigia simu! Tufanye nini?”
“Kuna msemo mmoja wa Kiingereza unasema hivi; ‘Enemy of my friend is enemy of mine’ ukimaanisha kwamba adui wa rafiki yangu ni adui wangu pia’” alisema Godwin.
“Unamaanisha nini?”
“Ngoja nifanye jambo moja! Wewe sikiliza kitakachotokea Kenya. Hakuna atakayejua kama Tanzania imehusika katika tukio hili. Nataka washikane uchawi wao kwa wao,” alisema Godwin.
“Utafanya nini?”
“Subiri! Tega masikio utasikia kitakachotokea huko,” alisema Godwin na kukata simu. Macho na masikio ya Ojuku yakawa nchini Kenya, akataka kuona ni kitu gani ambacho Godwin angefanya mpaka watu hao kushikana uchawi wao kwa wao.
Hakukuwa na utulivu nchini Kenya, kila mtu alitaka kujua mahali ndege ya rais wao ilipokuwa. Wabunge wakapata cha kujadili, kila mmoja hakufahamu ukweli, rais wao alisema kwamba Tanzania ilihusika katika upotevu wa ndege hiyo lakini kitu cha ajabu, walipoulizwa Tanzania walisema kwamba hawakuhusika kabisa.
Hilo liliwachanganya, waliwatuma watu wao kuchunguza kila kona lakini hakukuwa na majibu yoyote yale. Hilo likawapa wasiwasi kwamba ndege hiyo ilipotezwa kama ilivyopotea ndege ya Malaysia na hivyo isingeweza kuonekana tena.
Wakati wakijiuliza sana kuhusu ndege hiyo wakapata taarifa kutoka kwenye mtandao wa Instagram katika Akaunti ya Mabadiliko ya Kweli ambayo ilisema kwamba ingetoka taarifa ambayo ingewafanya Kenya kufahamu mahali ndege yao ilipokuwa lakini endapo tu wangekuwa tayari kuambiwa mahali ndege ilipokuwa kwani aliyehusika katika upoteaji wa ndege hiyo alikuwa akijulikana.
Hilo ndilo lililowafanya Wakenya kidogo kuwapenda Watanzania, wakaanza kuiweka taarifa hiyo katika mitandao mbalimbali kwamba Tanzania ilijua mahali ndege ilipokuwa mpaka mtu aliyehusika katika kuipoteza alikuwa akijulikana.
Haraka sana Rais Onyango akampigia simu Ojuku na kuzungumza naye. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumuomba msamaha kwa kila kitu kilichokuwa kimetokea lakini lengo lake kubwa lilikuwa ni kuambiwa mtu aliyekuwa amehusika katika lile lililokuwa limetokea.
“Tumegundua kosa letu, tusameheane tu kwa kuwa wote ni watu wa ukanda mmoja,” alisema Rais Onyango kwa sauti ndogo na ya huruma kabisa.
“Sawa. Haina tatizo! Nikusaidie nini?” aliuliza Ojuku.
“Kujua mahali ndege ilipokuwa. Hata tukimfahamu mtu aliyehusika, litakuwa jambo jema pia,” alisema mwanaume huyo.
“Hakuna shida! Tutazungumza! Utafahamu kila kitu!” alisema Ojuku, yeye mwenyewe hakufahamu ni kitu gani Godwin alitaka kukifanya, ila aliamini kuwa kuna kitu kikubwa sana ambacho Godwin angekifanya na Wakenya kuchanganyikiwa.
***
Godwin alikuwa bize, hakutaka kuzungumza na mtu yeyote, alitulia chumbani kwake huku akiwa na kompyuta yake mapajani mwake. Alitaka kucheza mchezo hatari ambao ungemfanya kila mtu kushangaa na kustaajabu.
Mtu ambaye alitaka kumtumia kipindi hicho alikuwa bilionea Olotu, alichokifanya kwa kutumia simu ya Rais Onyango aliipata simu yake na hatimaye kuanza kuanza kuidukua. Hiyo wala haikuwa kazi kubwa kwake, alifanikiwa na moja kwa moja kutengeneza meseji ambazo zingekuwa ngumu kuonyesha kama zilikuwa zimetengenezwa.
Akaandika ujumbe kwa namba zilezile, ujumbe uonekane kama ulikuwa umetoka katika simu ya Olotu na kwenda kwa mtu aliyejulikana kwa jina la Ibrahim Omeng, Mkenya aliyekuwa nchini Afrika Kusini, mtu ambaye naye alikuwa karibu sana na bilionea huyo.
Akaweka mawasiliano ya siri kwamba wawili hao walikuwa wakiwasiliana kwamba walitaka kucheza mchezo mmoja hatari, kujifanya kama wanamtaka Bokasa lakini lengo kubwa likiwa ni kuipoteza ndege ya rais nchini Kenya.
“Kwa hiyo tufanyeje?” ilikuwa ujumbe ulioonekana kutoka katika simu ya Omeng.
“Nitajifanya namtaka Bokasa, niitumie ndege yake, halafu ikifika huko, itasafirishwa kupelekwa nchini Uganda kisiri, huko itafunguliwa vipandevipande na kwenda kuviuza,” ulisomeka ujumbe kutoka katika simu ya Olotu.
“Hawatotushtukia?”
“Hakuna kitu kama hicho!”
“Halafu huyo Bokasa tumfanye nini?”
“Tukamtupe katika mpaka wa Tanzania na Kenya. Halafu sisi tunaondoka kwani lengo letu litakuwa ni ndege. Nina kisasi moyoni, tukimaliza suala la ndege, tunafanya mikakati ya kuichoma moto ikulu, tutamtumia mtu mmoja wa karibu ambaye ataifanya kazi hiyo kiuaminifu kabisa,” ulisomeka ujumbe.
“Basi sawa. Ndege tukaiuze kiasi gani?”
“Iuzwe kwa dola bilioni mbili. Ni pesa nyingi sana hizo!”
“Haina shida! Ila kuwa makini ili Rais Onyango asijue kama unamtumia kwa ajili ya kuipoteza ndege yake!”
“Hilo usijali!”
Alizitengeneza meseji hizo na kisha kuzipiga picha. Ilikuwa vigumu kugundulika, baada ya hapo akaziweka katika Akaunti ya Mabadiliko ya Kweli na kuandika kwamba ukweli ungekwenda kujulikana kwa mtu aliyeucheza mchezo huo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kitendo cha watu kuziona meseji hizo katika akaunti hiyo tena zikiwa zimepigwa picha, kila mtu alishangaa, Wakenya walichanganyikiwa. Walimjua bilionea Olotu, alikuwa mwanaume makini aliyekuwa akifanya vitu vyake kisiri na kila siku alisema kwamba alikuwa akiipenda sana Tanzania.
Wakenya waliendelea kushangazwa, hawakuamini kile walichokiona, kila siku waliilaumu Tanzania kwamba ilihusika katika upoteaji wa ndege ya rais wao kumbe nyuma ya pazia kulikuwa na mtu aliyekuwa amehusika katika mpango mzima.
Godwin hakuishia hapo, alichokifanya ni kuzitumbukiza meseji zile katika simu za watu hao wawili ili zionekane kuwa ndizo walizokuwa wakichati na mbaya zaidi akaziwekea virusi wakati alipokuwa ameviweka ili kama itatokea wawili hao kutaka kuzifuta, zisifutike, ziendelee kubaki humohumo.
Rais Onyango alisikia kile kilichotokea, akapigiwa simu na kuambiwa kwamba mbaya wake haikuwa nchi ya Tanzania bali rafiki wake wa karibu, Olotu ambaye alicheza mchezo mzima kwa kujifanya kumshirikisha kumbe nyuma ya pazia alikuwa akitaka kukamilisha mambo yake.
Hilo lilimhuzunisha mno, hakuamini, akajifungia chumbani na kuanza kulia, aliumia moyoni mwake, hakuamini kwamba moyo wote wa wema aliojaribu kumuonyeshea mwanaume huyo kwa kukubaliana naye kwenda Ubelgiji kumleta Bokasa kumbe ulikuwa ujanja wa kuipoteza ndege yake.
“Kwa nini amefanya hivi?” alijiuliza huku akionekana kustaajabu, kwake, kilichokuwa kimetokea kilionekana kuwa kama kitu cha muujiza sana.
Hakutaka kupoteza muda, alichokifanya ni kuchukua simu yake na kupiga Mombasa kwa kuwataka polisi wamkamate Olotu haraka sana kitu ambacho ndani ya dakika thelathini akaambiwa kwamba mwanaume huyo alikuwa mikononi mwa polisi na alikuwa njiani kwenda kufanyiwa mahojiano.
***
Bilionea Olutu alikuwa ndani ya jumba lake la kifahari, moyo wake ulikuwa na mawazo tele, alikuwa akimfikiria Bokasa ambaye aliambiwa kwamba alikuwa njiani kupelekwa nchini Kenya. Baada ya saa kadhaa akapewa taarifa za kupotea kwa ndege, alichanganyikiwa, hakuamini kirahisi kama ndege inaweza kupotezwa kirahisi kama ilivyokuwa.
Haraka sana akawasiliana na Rais Onyango na kuanza kuzungumza naye, walipanga mikakati kwamba piga ua ilikuwa ni lazima ndege ipatikane na hatimaye kumpata mtu wake aliyekuwa akimtaka kwa kipindi kirefu.
Akaambiwa kwamba bado Usalama wa Taifa walikuwa wakipambana usiku na mchana kuhakikisha kwamba ndege inapatikana, aliendelea kuambiwa kwamba mawasiliano yalikuwa yakifanyika katika nchi moja na nyingine kujua kama ndege ilikuwa huko au la.
Majibu hayakumridhisha, akaliacha jambo hilo mikononi mwa rais huku naye akiendelea kufanya mambo mengine. Baada ya siku moja na saa kumi na nane, akapokea taarifa kutoka kwa vijana wake kwamba kulikuwa na mtu kwenye mitandao alisema kuwa yeye alihusika katika upotevu wa ndege na alifanya hivyo kwa kuwa alitaka kulipa kisaisi kwa Rais Onyango.
Kwanza akashangaa, hakujua sababu ya taarifa hizo kutolewa na wakati hakukuwa na ukweli wenyewe, akataka kuangalia ili aone kama kweli taarifa hizo zilitolewa au la. Alipoingia, kitu cha ajabu kabisa alichokutana nacho ni meseji ambazo zilionekana akiwa anachati na rafiki yake aliyekuwa Afrika Kusini.
“Mmh!” alishangaa.
Alikumbuka kwamba hakuwa amewasiliana na mwanaume huyo kwa meseji kama zile, zilitoka wapi? Wakati akijiuliza zaidi, akasikia akiambiwa kwamba polisi walikuwa wamefika nyumbani kwake na hivyo kutaka kumchukua.
“Nimefanya nini?” aliuliza.
“Wanasema kwamba meseji zilizokuwa zimetuma na kutumiwa katika simu yako,” alijibu mlinzi aliyekwenda kumpa taarifa kuhusu polisi hao.
Polisi wakaingia ndani, waliagizwa kumchukua bilionea huyo, hawakutaka kuchelewa, wakamfunga pingu na kuondoka naye. Njiani alikuwa akishangaa, kila kitu kilichokuwa kimezungumzwa kilikuwa ni uongo mtu na alikuwa na uhakika kwamba hakuwa amewasiliana na mwanaume huyo kwa kupitia namba yake.
Hakutaka kusema kitu, akanyamaza mpaka alipofikishwa katika kituo cha polisi hapo Mombasa ambapo akachukuliwa na kuingizwa sero huku tayari waandishi wa habari wakiwa wamekwishafika katika kituo hicho.
Kitu cha kwanza walichokifanya polisi ni kuanza kupekua katika simu yake ili kuona kama meseji hizo zilikuwepo, walipoifungua sehemu ya kuhifadhi meseji, wakazikuta meseji hizo zikiwa zimetumwa na kuingia katika namba ya jamaa yuleyule aliyekuwa Afrika Kusini.
“Olotu! Hii kesi ngumu sana, kumbe meseji zenyewe hata kufuta hukufuta,” alisema mkuu wa kituo cha polisi huku akimwangalia mwanaume huyo aliyekuwa sero.
“Meseji gani?”
“Zile ulizochati na huyo mwanaume. Zote zipo tena zikielezea mipango kabambe mliotaka kufanya kuhusu kuipoteza ndege,” alijibu mkuu huyo ambaye alikuwa akilipwa pesa kwa ajili ya kumlinda mwanaume huyo.
“Meseji kwenye simu yangu?”
“Ndiyo! Zipo zote, tena zilezile zilizokuwa zimeandikwa katika mitandao ya kijamii!” alijibu.
Olotu hakuamini, akahitaji kuziona meseji hizo, kisiri akaletewa simu yake ambayo hakuwa ameiangalia na kuonyeshewa meseji zile. Hakuamini alichokuwa akikiona, alipigwa butwaa, alikumbuka kwamba hakuwa amechati na mwanaume huyo kuhusu jambo hilo, meseji hizo zilifikaje katika simu yake?
Alipagawa, akajaribu kuingia sehemu ya kuzifuta, hakuwa na uwezo wa kufanya hivyo, zilionyesha kabisa kwamba zilizuiliwa kwa kila kitu. Alibaki akilia kwani ilikuwa ni lazima kesi ifikishwe mahakamani na kitu cha kwanza kabisa kuangalia kilikuwa ni simu yake ili kuona kama kulikuwa na meseji hizo ambazo hazikuweza kufutika.
“Hapana! Sikuwa nimechati na huyu mtu!” alisema huku akiwehuka.
“Sasa hizi meseji aliandika nani?”
“Sijui! Lakini sikuwahi kuchati na huyu mtu!”
“Olotu! Niliahidi kukutetea, lakini umefanya uzembe sana, yaani hata meseji umeshindwa kufuta?”
Alichanganyikiwa mno, meseji hazikuwa zikifutika, ndani ya saa moja, polisi kutoka jijini Nairobi wakafika hapo, wakamchukua na kuanza kwenda naye huko huku wakiwa na simu yake. Njiani, alikuwa akilia kama mtoto, alijitetea kwamba hakukuwa na meseji alizokuwa amechati na mtu huyo bali kulikuwa na mtu aliyefanya jambo hilo.
“Sikuchati na mtu yeyote yule,” alisema kwa sauti akiwa ndani ya gari la polisi.
“Hiyo utakwenda kusema kwa mahakama,” alisema polisi mmoja kwa lafudhi ya Kikenya.
Waandishi wa habari walipewa taarifa kuhusu Bilionea Olotu aliyekuwa njiani kutoka Mombasa kuelekea Nairobi. Waandishi hao kutoka katika mitandao ya kijamii, magazeti, redio na televisheni wakakusanyika kituoni hapo kwa ajili ya kuchukua habari na kupiga picha kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.
Kila mtu alitaka kuwa na picha ya bilionea huyo aliyekuwa gumzo kubwa nchini Kenya, kila mtu alitaka kuona kile ambacho kingetokea kwamba ilikuwaje mpaka bilionea huyo apange mipango ya kuweza kuiteka ndege ya rais kwa lengo la kwenda kuiuza? Kila mmoja alikuwa akijiuliza maswali mengi ambayo walikosa majibu kabisa.
Ilipofika majira ya saa tisa alasiri, gari la polisi kutoka Mombasa likaanza kuingia katika Kituo Kikuu cha Polisi. Waandishi wa habari ambao waliambiwa wasimame mbali kabisa wakaanza kupiga picha kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.
Bilionea Olotu akateremka huku akiwa na pingu mikononi mwake, alitia huruma, alionekana kuwa mnyonge sana kiasi kwamba kila mtu akaamini kwamba kweli mwanaume huyo alikuwa amefanya kile kitu kilichokuwa kimetangazwa sana katika mitandao ya kijamii.
Akaingizwa ndani, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kutaka kuonana na wakili wake, alijua kwamba alikuwa na kesi nzito iliyokuwa ikimkabili ambayo kwa namna moja au nyingine asingeweza kuchomoka salama, alihitaji kuzungumza na wakili huyo kwa lengo la kumwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea na kwamba ujumbe uliokuwa ukionekana katika simu yake, haukuwa wake na hakuwahi kuandika ujumbe wa namna ile.
“Sikuwahi kufanya kitu kama hiki,” alisema Olotu wakati wakili wake alipofika mbele yake. Alizungumza naye huku akilia, hakuamini kama mwisho wa siku ungekuwa namna hiyo, mipango yote ambayo ilielezewa katika simu yake haikuwa sawa kabisa.
“Lakini wanasema kwamba meseji zilionekana kwenye simu yako, ni kweli?’ aliuliza wakili, alitaka kujua ni kwa namna gani angeweza kumalizana naye katika kesi ile.
“Ni kweli?”
“Sasa inakuwaje unaposema kwamba si meseji zako?”
“Hata mimi nashangaa, sikuwahi kuandika meseji za namna hiyo! Inakuwaje sasa mpaka zipatikane katika simu yangu?” alihoji huku akionekana kuchanganyikiwa.
Wakili mwenye alishangaa alipoambiwa kwamba hizo meseji zilikutwa katika simu ya mteja wake. Hakuamini kama kungekuwa na mtu ambaye angetuma meseji za namna hiyo na kuziacha katika simu yake. Akahisi kwamba kulikuwa na kitu nyuma ya pazia na jambo kubwa kabisa alilokuwa amelifikiria ni kwamba inawezekana mwanaume huyo alimuachia mtu mwingine simu yake ambaye aliitumia kutuma meseji hizo.
“Sikumwachia mtu!”
“Sasa inakuwaje meseji hizo kukamatwa katika simu yako?” aliuliza wakili.
“Hata mimi nashangaa!”
Wakati hayo yote yakiendelea Rais Onyango alikuwa ikulu, alipewa taarifa kwamba bilionea yule alikuwa mikononi mwa polisi, moyo wake ukaingiwa na hasira, hakuamini kama kweli kungekuwa na mtu ambaye angejitolea kumsaidia kwa asilimia mia moja na mwisho wa siku kutaka kumgeuka kama alivyokuwa amefanya.
Akataka kumpoteza, akataka kummaliza kwa kila kitu alichokuwa nacho. Akawaambia polisi kwamba ilikuwa ni lazima mwanaume huyo afungwe gerezani kwa kile alichokuwa amekifanya, maelekezo yakatolea na siku iliyofuata kufikishwa mahakamani kusikiliza kesi yake.
Hakukuwa na kesi ambayo ilifautilia sana nchini Kenya kama ilivyokuwa kwa kesi hiyo. Kila mtu alitaka kufahamu kwa kile kilichokuwa kikiendelea. Wengi walilaani, wanasiasa walimwandama Olotu kwamba hakuwa ametenda haki kwa kuwa alihitaji msaada, akasaidiwa lakini kumbe nyuma ya pazia kulikuwa na jambo lake alilotaka kulifanya.
Kesi hiyo iliunguruma kwa wiki kadhaa na hatimaye akaonekana kuwa na kesi ya kujibu na hivyo kuhukumiwa miaka kumi na tano gerezani. Hapo, Wakenya wakaridhika, ni ghafla sana wakatokea kumchukia mwanaume huyo kwa kuwa alitaka kuwaingiza katika uhasama mkubwa na Watanzania ambao walionekana kama ndiyo waliokuwa wameiteka ndege hiyo na kuipoteza.
Japokuwa Olotu alihukumiwa lakini ndege haikuonekana. Wakenya walijaribu kuitafuta kila siku lakini hakukuwa na mafanikio yoyote yale, hawakujua kama ndege ilisafirishwa nchini Japan, ikauzwa huko na fedha kwenda kuingizwa katika akaunti ya Godwin ambayo hata watu wa benki wenyewe hawakujua akaunti hiyo ilikuwa na kiasi gani kwani ilionekana kama imefungwa na wakati kila siku kulikuwa na fedha zilizokuwa zikiingia na kutoka.
***
Ojuku aliamua kuwaita waandishi wa habari kwa lengo la kuzungumza nao, aliwaambia kwamba hatimaye Bokasa alikuwa amepatikana na hivyo ilikuwa ni lazima kushitakiwa kwa kila kitu alichokuwa amekifanya. Hakukuwa na mawakili wenye nguvu wa kumtetea kwani kila mmoja alikuwa akimchukia.
Aliua wanajeshi kadhaa kwa kuwapulizia sumu ikulu, hilo lilimfanya kuchukiwa na kila mtu kutamani kuona mwanaume huyo akihukumiwa kifo huko gerezani.
“Bora akahukumiwe kifo,” alisikika mwanaume mmoja akiwaambia wenzake.
“Kweli kabisa! Yule hafai! Yaani ni bora aondoke katika dunia hii,” alisema jamaa mwingine huku akimwangalia mwenzake.
Kesi hiyo iliunguruma kila siku na baada ya miezi miwili, akahukumiwa kufungwa kifungo cha maisha baada ya kupona ugonjwa aliokuwa akiumwa. Familia yake ambayo aliipanga kutoroka, ikakamatwa na kurudishwa nchini Tanzania, hawakutakiwa kuondoka, walitakiwa kuendelea kubaki nchini kwani bado walihisiwa kupanga njama mbaya za kuweza kufanya matukio ya kutisha Tanzania.
“Naomba nisamehewe kwa kila kitu kilichotokea,” alisema Bokasa huku akilengwa na machozi.
Waandishi wa habari wakamsogelea, japokuwa haikuwa ruhusa kwa mtu aliyehukumiwa kuzungumza na waandishi wa habari lakini yeye akapewa nafasi hiyo ya dakika tano kwa kuzungumza mara ya mwisho na Watanzania, kuwaomba msamaha kwa kila kitu alichokuwa amekifanya.
Alizungumza huku akilia, alijuta katika maisha yake kufanya mambo machafu, alijiona kuwa mjanja, mwerevu lakini mwisho wa siku akagundua kwamba alikuwa mjinga ambaye alitaka kuwaangamiza zaidi Watanzania.
Kila mtu aliyesikia jinsi alivyokuwa akiongea, alimuonea huruma, alisinyaa, hakuonekana kama alikuwa rais aliyepita nchini humo, alionekana kuwa dhoofu kiasi kwamba watu wengine walihisi kuwa kama angefika gerezani basi angeweza kufa kutokana na mawazo aliyokuwa nayo.
Alichukua dakika nne kuzungumza na waandishi wa habari, akachukuliwa na kisha kupelekwa gerezani huku akiwapungia mikono watu waliokuwa mahakamani hapo.
“Godwin! Umefanya kazi kubwa sana! Hebu tuonane kwanza tusherehekee,” alisema Ojuku wakati akizungumza na Godwin kwenye simu.
“Haina shida. Nafikiri nimemaliza kila kitu!” alisema Godwin.
“Ndiyo! Hebu kwanza tukutane kwanza tusherehekee, bila wewe basi Tanzania ingepotea,” alisema Ojuku.
Hilo halikuwa tatizo, baada ya saa kadhaa wawili hao wakakutana katika Mgahawa wa Manjumat uliokuwa Masaki. Ojuku alipomwangalia Godwin, hakuamini, alikuwa kijana mdogo mno, sawa na mtoto wake lakini kwa kitu alichokifanya kwa ajili ya Tanzania, yeye mwenyewe alishangaa.
Hata kabla ya kuzungumza kitu, akasimama na kumkumbatia kijana huyo, akamshukuru kwa kazi kubwa aliyokuwa ameifanya ambayo mwisho wa siku iliifanya nchi ya Tanzania kuwa huru kama ilivyokuwa kipindi hicho.
“Na wale marubani mmewafanya nini?” aliuliza Godwin.
“Tuliwarudisha kwao hukuu tukiwapa mikwara mizito kwamba kama kuna siku wangesema ukweli, basi tutawaua,” alisema Ojuku.
“Na wale vijana?”
“Tumewamaliza na kuwatupa baharini huku miili yao ikiwa imefungwa kwa vyumba vizito vya matairi ya gari kwani hatukutaka maiti zao zionekane, acha zikawe chakula cha samaki,” alisema Ojuku huku akimwangalia mwanaume huyo.
“Safi sana!”
“Wewe ni mtoto wa Bwana Mapoto?” aliuliza Ojuku.
“Ndiyo!”
“Aisee! Pole sana kwa kila kitu kilichotokea, hakika umepitia maisha ya shida sana mpaka muda huu kuwa hapa. Ila kwa ulichokifanya, hakika ni kisasi ambacho hakitoweza kusahaulika katika maisha yote ya watu waliowahi kukuumiza!” alisema Ojuku huku akimwangalia Godwin.
“Nashukuru sana!”
Walikaa hapo na kuzungumza kwa kipindi kirefu, watu wengine waliokuwa pembeni walishindwa kugundua kwamba mtu aliyekuwa akizungumza na Jenerali Ojuku alikuwa Godwin ambaye kila siku walitamani kumfahamu. Baada ya dakika arobaini, Godwin akasimama, akamuaga na kumwambia kwamba siku chache mbeleni angemualika kwa ajili ya kuhudhuria harusi ambayo angekwenda kufunga na msichana Winfrida.
“Kweli?” aliuliza.
“Hakika! Karibu sana!”
Godwin akatoka nje, akalifuata gari alilokuwa amekuja nalo lakini hata kabla hajaufikia mlango na kuufungua, akasikia akianza kuitwa kwa sauti kubwa kutoka nyuma yake. Hakujua mtu aliyekuwa akimuita lakini kwa jinsi alivyokuwa akiisikia sauti hiyo, ilionyesha kwamba ni ya mtu aliyekuwa akimfahamu kabisa.
“Godwin! Godwin!” aliendelea kuita mtu huyo.
Watu wote waliokuwa mahali hapo wakageuka na kumwangalia mtu aliyekuwa akimuita Godwin. Hapohapo akasimama na kuyapeleka macho yake kwa mtu aliyekuwa akimuita, alipomwangalia tu, hakuwa mgeni, alimfahamu mtu huyo, uso wake ukajawa na tabasamu, mtu yule akamsogelea.
“Godwin! Ni wewe kweli? Mungu wangu! Za masiku? Mbona ulipotea? Ni wewe kweli au naota?” aliuliza mtu huyo huku akihema kwa nguvu, Godwin akabaki akishangaa tu japokuwa alimfahamu vilivyo mtu huyo.
***
Godwin alibaki akimwangalia mwanamke aliyesimama mbele yake, sura yake haikuwa ngeni machoni mwake, alikumbuka kwamba aliwahi kumuona sehemu fulani japokuwa hakukumbuka ilikuwa wapi.
Alimkazia macho, mwanamke yule alikuwa akimwangalia huku akionekana kuwa na furaha mno. Wakati akizungumza naye, mwanaume mmoja naye akatokea na kumsabahi Godwin ambaye bado alionekana kushangaa tu.
“Unanikumbuka?” aliuliza mwanamke huyo huku tabasamu likiwa usoni mwake.
“Sura inakuja na kupotea,” alijibu Godwin.
Akamkumbusha jina lake kwamba aliitwa Rachel. Alivyolitaja jina hilo tu, Godwin akakumbuka kila kitu kwamba mwanamke huyo alikuwa yule wa Coco ambaye alimpenda, alimthamini na kumpa kila kitu alichokihitaji lakini mwisho wa kumuona ilikuwa ni katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Kumbe ni wewe!” alisema Godwin na kumkumbatia.
Alipomwangalia mwanaume yule aliyesimama karibu na Bi Rachel alimkumbuka, alikuwa mumewe, mwanaume ambaye alimtetea alipokwenda kumtembelea Bi Rachel katika hospitali hiyo.
Akamsalimia na kumshukuru kwamba kama si yeye basi polisi kipindi kile wasingeweza kulifuatilia gari lililokuwa limemteka na kutoweka katika mazingira ya hospitali.
“Ulikuwa wapi?” aliuliza Bi Rachel huku akionekana kuwa na furaha, japokuwa alikuwa na umri mkubwa zaidi ya kipindi cha nyuma lakini bado moyo wake haukumwambia kitu kwa Godwin.
“Niliondoka! Nashukuru sana kwa msaada wako, nashukuru kwa kila kitu,” alisema Godwin huku akiachia tabasamu pana.
Hawakuzungumza sana, akaondoka huku akiendelea kushangaa kwamba mwanamke huyo alimgunduaje na wakati kilipita kipindi kirefu pasipo kuonana.
Hakutaka kujali sana, akaondoka na kurudi nyumbani. Alipofika huko, akamwambia Winfrida kila kitu kilichotokea, kwamba alikutana na mwanamke yule ambaye alimsaidia sana kipindi cha nyuma ila mbali na hilo, akamsisitizia kwamba ni lazima waoane baada ya rais mpya kuapishwa.
Siku iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu iliwadia, kila mtu alikuwa na presha, muda wa kampeni ulikuwa umekwisha na kilichobaki kilikuwa ni kwa wananchi kupiga kura na kumchagua rais ambaye angewaongoza kwa muda wa miaka mitano.
Japokuwa Kambili alikuwa na uhakika wa kuchukua nafasi hiyo lakini alikuwa na wasiwasi mkubwa, hakuona kama alitakiwa kujiamini kwani binadamu wengi walibadilika, ilikuwa ni rahisi kukubaliana leo lakini baada ya siku kadhaa kubadilika na kujifanya kama hakuwa mtu uliyeelewana naye.
Alilijua hilo, hakuwa na amani hata kidogo. Aliondoka na kundi lake kuelekea katika kituo cha kupiga kura na kupiga huko huku waandishi wa habari wakiwa kila kona kwa ajili ya kuchukua matukio mbalimbali yaliyokuwa yakitokea siku hiyo.
Alipomaliza, akapigwa picha nyingi na kurudi katika makao makuu ya Chama cha Tanzania National Party ambapo huko akaanza kusikilizia kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
Kwa kipindi hicho hakutaka kumwamini mtu yeyote yule, kila aliyekuwa akimwangalia, alihisi kama hakumpigia kura. Alibaki mahali hapo kwa dakika thelathini ndipo akaamua kumpigia simu mke wake na kuzungumza naye.
Huyo ndiye alikuwa faraja yake, alimpenda, ndiye mtu aliyekuwa akimfariji hata katika kipindi alichokuwa na matatizo mengi. Alizungumza naye kwa dakika kadhaa, akakata simu na kutulia kimya.
Hakutaka kuzungumza na mtu yeyote yule, alikuwa na presha, aliwaza vitu vingi kwamba kama asingefanikiwa kuwa rais nini kingetokea? Nani angemuonyeshea upendo kama alivyokuwa akimuonyeshea kipindi cha nyuma?
Wakati mwingine alitamani kumpigia simu Godwin na kumwambia afanye kila linalowezekana ili kubadilisha matokeo kwani kwa kipindi hicho yalikuwa yakihesabiwa kwa kutumia kompyuta.
“Hivi nitashinda kweli? Mbona sijiamini? Mbona kila mtu namuona kama amebadilika, ana wasiwasi, hivi kweli nitakuwa rais au ndiyo itakuwa kama miaka mingine?” alijiuliza huku akionekana kutokuwa na furaha kabisa.
Alihitaji muda wa kukaa peke yake kwanza, kila mtu aliyemwangalia aliuona wasiwasi wake aliokuwa nao, alitetemeka kana kwamba kulikuwa na baridi kali, akasimama na kuelekea katika chumba kimoja kilichokuwa wazi na kutakiwa kubaki humo.
Kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Godwin tu, alijua kwamba kijana huyo alikuwa na nguvu ya kubadilisha matokeo yale, kama wangezungumza kwa kirefu basi angecheza na kompyuta, matokeo yale angayachezea na mwisho wa siku kushinda kwa asilimia kubwa.
Alimfahamu kijana huyo, alipambana kwa nguvu zote, katika vitu ambavyo hakuwa akivipenda ni kumpendelea mtu. Alikuwa akipigana kwa kila hali lakini mwisho wa siku haki ipatikane. Hakuona kama lilikuwa jambo sahihi kumshirikisha kijana huyo katika jambo kubwa kama hilo.
Wakati amekaa katika chumba hicho, akaiona simu yake ikianza kuita, akakiangalia kioo, namba ilikuwa mpya kabisa, akabaki akijiuliza kama ilikuwa sahihi kuipokea namba hiyo hasa katika kipindi kama hicho au la. Akapiga moyo konde na kuipokea.
“Halo!” aliita kwa hofu kubwa.
“Mbona unaitikia kinyonge hivyo?” lilikuwa swali la kwanza alilouliza mpigaji simu.
“Kawaida. Nani? Godiwn?’ aliuliza.
“Ndiyo!”
“Mungu wangu! Nilikuwa nakufikiria wewe hapa,” alisema Kambili huku kidogo uso wake ukianza kuonyesha tabasamu la mbali kabisa.
Hakutaka kumficha, akamwambia kila kitu kilichokuwa kikiendelea kwamba moyo wake ulikuwa na hofu kubwa kwamba angeweza kushindwa katika uchaguzi huo kwani hakumwamini mtu yeyote yule.
Badala ya kumuondoa wasiwasi aliokuwanao, Godwin akaanza kucheka kwa sauti kitendo kilichomshangaza Kambili kwani hakutegemea kumsikia mwanaume huyo akicheka na wakati alikuwa akimwambia kitu kilichomfanya kukosa furaha kabisa.
“Unacheka nini?”
“Una wasiwasi sana. Umeshinda uchaguzi kwa silimia tisini, asilimia ambazo hazikuwahi kufikiwa na mtu yeyote yule,” alisema Godwin huku sauti ya kicheko chake ikianza kupungua.
“Unasemaje?”
“Umeshinda uchaguzi. Nilikuwa nataka nikupe habari hiyo tu,” alisema Godwin, hakutaka kuendelea kuzungumza naye, akakata simu.
Kambili alibaki akiwa amesimama tu, hakuamini aichokuwa amekisikia, aliiangalia simu yake huku kutetemeka kule kukianza kuisha. Hakuamini, aliita kuona kama Godwin alikuwa hewani lakini hakusikia sauti yoyote ile.
Moyo wake uliokuwa umekata tamaa ukaanza kurudi katika hali ya kawaida, haraka sana akatoka chumbani mule na kwenda walipokuwa wenzake, akaanza kurukaruka kwa furaha kitendo kilichomshangaza kila mtu kwamba nini kilitokea mpaka kiongozi wao kuwa kweye hali ya furaha kiasi kile.
“Tumeshinda uchaguzi,” alisema Kambili huku akionekana kuwa na furaha kupita kawaida.
Kila mtu alimshangaa, hawakuamini kile alichowaambia kwani matokeo hayakuwa yametangazwa, ndiyo kwanza kura zilipelekwa katika kompyuta tayari kwa kuhesabiwa, ilikuwaje aseme kwamba alikuwa ameshinda uchaguzi huo?
Kila mmoja akatamani kuuliza swali hilo, hata kabla hawajapata jibu Kambili akawaambia kuwa kila mmoja alitakiwa kuamini kwamba alikuwa ameshinda uchaguzi huo na kilichokuwa kikisubiriwa ni matokeo kutangazwa tu.
Wakatulia na kusikilizia kile kilichokuwa kikiendelea. Hawakuondoka, kila mtu mtaani alitaka kujua kilichotokea, kila mmoja alitamani kumuona Kambili akishinda uchaguzi huo kwani alihangaika kwa kipindi kirefu kuipigania nchi hiyo, katika uchaguzi mwingine alikuwa akishinda lakini kura ziliibwa na ushindi kupewa mtu mwingine.
Siku iliyofuata Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi, Bwana Hidifonce Kipunde akaanza kutangaza matokeo ya uchaguzi huo ambayo yalikuwa yakisubiriwa kwa hamu kubwa na kila mtu. Jina lake na chama chake ndivyo vilivyokuwa vikitawala, alipata kura nyingi mno kiasi kwamba kila mtu alishangaa.
Matokeo yalitangazwa kwa saa kadhaa na kufungwa huku akiwa ameshinda kwa asilimia tisini kama alizoambiwa na Godwin. Moyo wake ukafurahi, baada ya kupambana kwa miaka kadhaa kwa ajili ya kuiongoza nchi hiyo hatimaye alifanikiwa kuwa rais wa nchi hiyo.
Ilikuwa shangwe mitaani, kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba Kambili angewafikisha kule walipokuwa wakitaka kufika kwa sababu tu aliaminiwa na Godwin aliyekuwa akipendwa na kila mtu kutokana na umaarufu mkubwa aliokuwa amejiwekea katika kufanya yale ambayo kila mtu alitaka kuyaona yakifanyika nchini kwake.
“Hatimaye nimekuwa rais! Siamini mke wangu,” alisema Kambili huku akimkumbatia mkewe.
Taarifa hizo zilitangazwa kila kona, watu wengi walifurahi kuona upinzani ukiwa umechukua nchi baada ya mapinduzi ya kumtoa Bokasa kufanyika kwa nguvu kubwa. Shukrani za kila Mtanzania zilikuwa kwa Godwin ambaye hawakujua hata alifananaje.
Baada ya kukaa wiki moja na nusu, hatimaye Kambili akaapishwa mbele ya Watanzania lakini moja waliokuwa uwanjani na milioni ishirini waliokuwa katika televisheni zao na hivyo kuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo kutoka katika chama cha upinzani.
“Nitaanza upya kila kitu, nitafanya mambo mengi ambayo hayakufanywa. Nitachagua viongozi wengi makini. Tunamshukuru Godwin kwa kila kitu. Yeye atakuwa waziri wa ulinzi kivuli asiyeonekana, kazi yake kubwa ni kutuambia kila kitu kinachoendelea kutoka kwa maadui zetu ambao bila shaka watakuwa wakiwasiliana kupitia simu na kompyuta,” alisema Rais Kambili maneno yaliyoibua shangwe kubwa uwanjani hapo.
“Kila kitu kitakwenda kama kinavyotakiwa. Uchumi utapanda, pesa itaongezeka,” alimaliza kusema Kambili maneno ambayo pia yalipokelewa kwa shangwe kubwa kila kona ya Tanzania.
***
“Nitapambana mpaka nihakikishe Tanzania imebadilika na kuwa ile ambayo kila mtu anatamani sana kuiona! Kuna watu wengi wamenyonywa, wengine wameteswa, wengine wamekimbia nchini kwa kuhofia kufa njaa, umasikini uliwaua, ninawahakikishia kwamba kila kitu kitakwenda kama kinavyotakiwa kuwa,” alisema Kambili huku akiwaangalia watu wote waliokusanyika kushuhudia kuapishwa kwake.
Aliongea mambo mengi jukwaani kipindi cha kuapishwa kwake. Moyo wake uliamua kujitoa asilimia mia moja kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania ambao walimpa kura zao kwa ajili ya kuona mabadiliko yakitokea nchini.
Alidhamiria kuibadilisha Tanzania, miziz ya utawala uliokuwa umepita, alitaka kuing’oa na kutengeneza Tanzania mpya ambayo aliamini kwamba kila mtu angeipenda. Alitaka kurahisisha maisha, Watanzania wale waliokuwa wamepigika maishani mwao alitaka kuwapa tumaini jipya, alitaka kuwaona wakiyafurahia maisha yao kana kwamba waliishi peponi.
Alipomaliza kuzungumza, akashuka jukwaani na kwenda kukaa sehemu yake. Macho yake yalikuwa yakiwaangalia wananchi waliokuwa wamekusanyika katika Viwanja vya Jangwani, kwa jinsi watu walivyoonekana, nyuso zao zilikuwa na matumaini makubwa kwamba kila kitu kingekwenda kuwa kama kilivyotakiwa kuwa kipindi hicho.
Baada ya kumaliza sherehe za kuapishwa kwake, watu wakatawanyika huku wakiwa na nguvu mpya kwamba hatimaye Tanzania mpya ilikuwa njiani kutengenezwa. Mitaani, bado sherehe zilikuwa zikiendelea kama kawaida, watu walirukaruka kwa furaha huku kila mmoja akijaza matumaini makubwa moyoni mwake.
Kambili alipoanza kazi yake ofisini, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuzifunga zile akaunti za mawaziri ambao walijitajirisha kwa kutumia pesa za serikali, mali zao zikachukuliwa na kila kitu walichokuwa nacho kikarudi mikononi mwa serikali.
Mikataba mipya iliyokuwa imesainiwa, ikaanza kupitiwa upya, kila kitu kilichokuwa kimefanyika kwa ajili ya kumpendalea mtu fulani muda huo ulikuwa ni wa kukirekebisha na kuwekwa vile kilivyotakiwa kiwepo.
Pesa za serikali ambazo Bokasa alikuwa amezihamishia nchini Ubelgiji na hatimaye Godwin kuzirudisha, zikaingia katika akaunti ya serikali na hata zile za mawaziri wengine ambazo zilihamishwa kutoka katika Benki ya Geneva, zote zikaingizwa katika akaunti ya serikali.
Mfumo wa utozaji kodi ukakaguliwa na kupangwa upya, kila kitu kilichokuwa kimefanyika kwa kusudi la kuwanyonya wananchi kikarekebishwa na kuwa kama kilivyotakiwa kuwa kipindi hicho.
Mabadiliko makubwa yakafanyika, hata kabla ya kuwachagua mawaziri Kambili alihakikisha anarekebisha kila sehemu iliyoonekana kuwa na uozo mkubwa. Ilikuwa kazi ngumu na kubwa kwani kila kitu alichokuwa akikigusia kilionekana kuwa uozo mkubwa na kilifanywa na msururu wa watu wengi.
Watu wote waliokuwa wamejilimbikizia mali wakapokonywa na kuanza kufuatilia namna ya walivyofanikiwa kuzipata mali hizo. Hakukuwa na tajiri aliyebaki salama, wengi walionekana kujipatia pesa kwa njia ambazo hazikuwa halali kabisa.
Kila kitu alichoanza kufanya Kambili alionekana kuwa mkombozi wa taifa hilo, hakuwa akifanya kazi nyingine kwa kipindi hicho zaidi ya kurekebisha pale kote kulipokuwa na uozo mkubwa. Wananchi wakampenda na kuona kwamba huyo ndiye alikuwa mtu aliyekusudiwa kuwaongoza japokuwa alichelewa sana kufika.
Kwa upande wa Godwin, kazi yake ilikuwa ni kufuatilia mawasiliano ya watu waliokuwa karibu na viongozi waliotoka madarakani, alitaka kuangalia kama kulikuwa na kitu chochote kile kilichokuwa kikiendelea.
Alikuwa bize lakini muda mwingi alikuwa na nafasi ya kuzungumza na Winfrida, alimpenda msichana huyo na kila siku alimsisitizia kwamba ilikuwa ni lazima kumuoa kwani hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa naye kwa karibu kama ilivyokuwa kwake.
Akawasiliana na mchungaji wa Kanisa la Praise God lililokuwa Mwenge jijini Dar es Salaam na kumwambia kuhusu hitaji lake la kutaka kufunga ndoa na msichana huyo. Hilo halikuwa tatizo, kitu pekee walichotakiwa kufanya ni kuanza kuhudhuria mafunzo ya ndoa ndani ya kanisa hilo kitu ambacho hakikuwa tatizo hata kidogo.
Baada ya mwezi mmoja wa mafunzo, wakafunga ndoa ndani ya kanisa hilo huku kukiwa hakuna mtu hata mmoja aliyegundua kama Godwin huyo ndiye yule shujaa aliyekuwa akisifika Tanzania nzima, mwanaume ambaye kila mtu alitamani sana kumuona.
Kwenye harusi hiyo, marafiki zake walikusanyika kwa wingi, hawakuamini kama kweli dsiku hiyo rafiki yao alikuwa akiolewa. Happiness, msichana ambaye alikuwa naye tangu siku ya kwanza alipoonana na Godwin kituoni alibaki akimshangaa Winfrida kwani mpaka kufikia kitendo cha kuolewa na mpiga debe, kilimaanisha kwamba alikuwa na mapenzi ya dhati moyoni mwake.
Winfrida hakujua mahali Godwin alipopata pesa lakini baada ya kufunga ndoa, wakahama Tandale na kuhamia Masaki katika jumba moja kubwa la kifahari na kuanza maisha hapo. Alimfahamu kama mipiga debe tu, ilikuwaje mpaka awe na kiasi hicho cha pesa, kwa mbali moyo wake ukaanza kuwa na hofu kwamba inawezekana mumewe huyo alikuwa jambazi au mtu yeyote wa madili.
“Nahisi kuna mengi unanificha,” alisema Winfrida huku akimwangalia Godwin.
“Hakuna. Umejua mengi kuhusu familia yangu, wazazi wangu na kila mtu niliyewahi kuwa naye, hutakiwi kuhofia lolote lile,” alisema Godwin huku akimwangalia mke wake huyo.
“Kwa hiyo unajua mahali kaburi la mama yako lilipo?”
“Ninafahamu! Nitakwenda nawe siku yoyote ile, nilitamani sana katika maisha haya niwe na Irene, dada yangu niliyempenda kwa moyo wote. Hakika hakustahili kufa, alikuwa mdogo mno,” alisema Godwin huku akimwangalia mke wake machoni, alionekana kuumizwa sana na kile alichokuwa akimwambia.
Siku iliyofuata, wakaondoka na kuelekea makaburini, ilipita miaka mingi pasipo kuona makaburi hayo, moyo wake ulimuuma mno alipoyaona kwa mara ya pili. Aliyaangalia huku kumbukumbu zake zikirudi nyuma kabisa tangu walipotoka nchini Marekani baada ya kifo cha baba yake aliyekufa katika ajali ya kupangwa.
Kilichofanyika ni kuwasiliana na mafundi kwa ajili ya kuyatengeneza makaburi hayo ili yawe ya kisasa na yasipotee kwani kwa jinsi yalivyokuwa kipindi hicho, muda wowote ule yasingeweza kuonekana tena.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakuacha kuwasiliana na Rais Kambili, yeye ndiye aliyemuweka mwanaume huyo katika madaraka japokuwa hawakuwahi kukaa pamoja na kuzungumza, mtu pekee ambaye kwa mara chache sana alikuwa akionana naye alikuwa Ojuku, walikuwa wakiyapanga mambo mengi na namna ya kuilinda nchi hii dhidi ya maadui ambao walikuwa wakitumia mitandao ya kijamii, barua pepe na hata kwa kutumia simu, alitaka kuhakikisha kila kitu kinakuwa salama mahali pote na ili kuwaongeza wataalamu wengine, akashauri wapelekwe vijana kwenda kusoma katika Chuo cha Waseda nchini Japan kwa ajili ya kusomea mafunzo ya kompyuta kwa miaka kadhaa ili hata kama kuna siku atakufa basi nchi iendelee kuwa salama kabisa katika masuala yote ya kompyuta.
Hakukuwa na kitu kilichoharibika, kila kitu kilikwenda kama kilivyotakiwa kwenda na baada ya mwaka mmoja, Godwin na mkewe wakafanikiwa kupata mtoto wa kike na kumpa jina la Irene kama kumbukumbu ya dada yake aliyeuawa miaka mingi iliyopita.
“Nitawapenda miaka yangu yote na nina hakika kwamba hakutokuwa na mtu yeyote atakayenitenganisha nanyi,” alisema Godwin huku akiwakumbatia wote kwa pamoja.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment