Simulizi : Utanikumbuka Tu!
Sehemu Ya Tatu (3)
Ghafla Edga akaingiwa na wazo, aliona hana cha kupoteza zaidi ya kuchukuwa fedha hizo ili apate nauli ya kuelekea Dar es salaam kumtafuta dada yake. Akiwa na wingi wa hofu, alizichukuwa fedha hizo na wala hakutaka hata kuzihesabu hima alirejea sebuleni moja kwa moja akatoka ndani ambapo nje alikutana na mlinzi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"We vipi, kwema huko?..", aliuliza mlinzi akimtilia shaka Edga ambaye kwa wakati huo alionekana kuwa na hofu.
"Hapana..hakuna hakuna tatizo babu", alijibu Edga kwa sauti ya woga wakati huo akifungua geti, alifunga kisha akatimua mbio kuelekea stendi ya mabasi. Alilala hapo hapo stendi, kesho yake alfajiri alipanda basi liendalo Dar es salaam. Alishusha pumzi Edga, hakuamini kama ameponyoka salama kwenye msala huo mzito wa kuiba fedha. Safari sio kifo, salama wa salimini Edga aliwasiri jijini saa ya jioni. Hakujua aeleke wapi, mpaka jua linazama Edga alikuwa bado hajajua muelekeo wake na hivyo ilimlazimu alale kwenye jumba la abiria. Lakini kesho yake asubuhi alistuka kujikuta mfukoni amebakia na shilingi elfu mbili tu kati ya fedha zote alizoiba, Edga alihaha kuzitafuta mfukoni pasipo kufanikiwa kuziona.
"Laah! Tayari wajanja wameondoka nazo", alijisemea baada kuzikosa, na hapo ndipo alipoanza kuwaza namna gani ataishi mjini pasipo kuwa na dira. Akiwa katika hali hiyo ya sintofahamu, ghafla alisikia sauti ikisema "Wale wa Kariakoo panda juu ukazibe, Kariakoo siti zipo za kumwaga. Mjini kariakoo twendeni", ilikuwa sauti ya kondakta akipiga debe. Edga alichomoa mfukoni shilingi elfu mbili aliyoasalia nayo kisha akazipiga hatua kuisogelea ile daladala.
"Konda, nauli bei gani?..", aliuliza Edga mara baada kumkaribia kondakta.
"Mia mia tatu, panda tuondoke", alijibu konda. Haraka sana Edga aliingia ndani ya dala hiyo punde safari ikaanza. Aliposhuka, alishangaa sana kuona majengo marefu huku wingi wa watu nao ukimuacha mdomo wazi. Jioni ilipoingia, alijikuta akitaharuki kuona watu wakilala nje ndipo naye hakuwa na budi kuungana na hao watu walalao nje. Hayo ndiyo yakawa maisha ya Edga ndani ya jiji, yalikuwa maisha magumu sana ambayo yalimpelekea kushindwa kufanya kile kilicho mleta jijini badala yake akajikuta akisaka sarafu ili apate mkate wa kila siku.
Maisha hayo yalikuwa endelevu mpaka anafikisha miaka kumi na tisa, alitegemea kuishi kwa kamali. Mchezo ambao ulimpa umaarufu mkubwa kwa wahuni wenzake, aliitwa Master. Jina ambalo alibatizwa baada kuonekana bingwa wa kuwala wenzake kwenye mchezo huo uliofahamika kwa jina karata tatu. Siku moja Edga akiwa na vijana wenzake wakicheza kamali kwenye moja ya uchochoro, ghafla waliona gari ndogo aina ya Rav4 limesimama. Punde si punde ndani ya gari hilo walishuka wanaume wawili wakiwa wamevalia makoti maeusi na miwani meusi pia. Edga na kundi lake walistuka, amri ikatoka kwa watu wale wawili "Hapo hapo malipo mikono juu", walisema wakati huo tayari wakiwa wamechomoa bastora.
"Chuchumaa chini", waliongeza kusema kwa amri baada kuwafikia. Hofu iliwatanda vijana hao wakiamini kuwa wamevamiwa na jeshi la polisi, lakini wakati wapo kwenye hofu hiyo mtu mmoja kati ya wale wawili aliangua kicheko kisha akasema "Acheni woga nyie watoto wa mama, yani koti kubwa na miwani mnatishika?.."
"Aaah sio poa mkuu, au wewe huoni kama mishe zetu hizi tunaishi kama kunguru?.." alisema Edga.
"Kweli kabisa wasi wasi mwingi", aliunga mkono mtu wa pili.
"Wasi wasi ndio akili ma-braza, acheni kukaa kiboya. Hebu tuachane na hayo kwanza,kuna habari njema nimewaletea. Lakini nataka kujua mko tayari?.."
"Habari gani hiyo?..", Edga alihoji.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Hapa sio sio sehemu sahihi ya kuzungumza, aliyetayari twende".aliongeza kusema mtu huyo aliyevalia koti jeusi. Edga na wenzake walikaa kimya huku kila mmoja ndani ya ubongo wake akijishauri,jambo ambalo liliweza kuzua ukimya. Lakini baadaye ukimya huo ulitoweka, Edga akasema "Mimi nipo tayari".
"Vizuri sana, tunaweza kwenda?.."
"Ndio",Edga alibali.
"Naitwa Ndama,na huyu mwenzangu anaitwa Dominic", alijitambulisha mtu huyo na pia akamtambulisha na mwenzake.
"Mimi naitwa Edga".
"Ahahahaha safi, Edga amini kwamba utajiri upo mkono mwako endapo kama utakubali dili hili", aliongea Ndama kisha wakaambatana na Edga kuelekea kwenye gari. Sasa safari ikaanza, Kinondoni Studio walifika. Waliingia kwenye moja ya jumba bovu ambalo ndani palikuwa na vijana wakivuta bangi wengine wengine wakinywa pombe.
"Safi sana Ndama kwa kuongeza jopo,sasa kundi limetimia lakini sio rahisi kihivyi kumkubali huyu dogo mpaka tumpe mtihani kidogo" aliongea mtu mmoja ambaye alionekana kuwa ndio kiongozi wa kundi, aliitwa Boko.
"Sawa, hilo sasa lipo juu yenu", Ndama alijibu kisha akarejea ndani ya gari akaondoka zake. Sasa Edga anajikuta anaingia mkononi mwa Boko muhuni wa jiji, Boko na watu wake ni wezi. Kazi hiyo wanaifanya nyakati za usiku. Hivyo Edga baada kuungana na kundi hilo, alipewa mtihani wa kuvamia moja ya duka kubwa la nguo Kinondoni. Alifanikiwa, walimpongeza sana. Boko aliamini kuwa amepata mtu sahihi lakini baadaye Edga akapoteza sifa zake baada kumgomea Boko amri aliyotoa ambayo upande wake aliona ni vigumu kuweza kutekeleza. Ilikuwa jioni sana pindi wawili hao walipokuwa wakipanga mkakati kabambe wa kupora.
"Oya! Naombeni mnisikilize kwa umakini", Boko aliongea. Ukimya ukatawala kwa vijana wake akiwemo na Edga.
"Edga, kuna dili lipo mbele yetu, dili ambalo lipo kando na kile tunacho kifanya ila nina uhakika endapo kama hili dili litakwenda vema basi sisi wote hapa ni matajiri. Unatakiwa ukachukue nyaraka kwenye nyumba ya Mr Omon. Hili ni dili kubwa sana, na sisi tumekuteua wewe ili ulikamilishe..", alisikika akisema Boko kiongozi wa kundi,maneno hayo alikuwa akimwambia Edga.
"Hii nyumba ngumu sana, kuingia na kutoka pia. Hivyo basi umakini unahitajika ili dili hili liweze kulikamilisha. Kila sehemu kuna ilinzi, tena ulizi madhubuti", aliongeza kusema.
"Lakini nitawezaje wakati mimi bado mgeni katika mambo haya? Ni heri tungeshirikiana hata wawili braza", alijibu Edga kwa sauti ya woga. Boko alikasirika kusikia maneno hayo, alimtazama kwa hasira kisha akasema "Usinipangie kazi, unataka kusema miezi hii mitatu uliyojiunga nasi bado hujazoea? Hiki ni kipimo cha maisha, na kuishi ni kuchagua siku zote ukitaka kuruka sharti uagane na nyonga".
"Hapana bro, kwa hilo sipo tayari", alikacha Edga, akikataa agizo la kiongozi wake, kitendo ambacho kilimkera sana Boko. Na tangu siku hiyo maelewano baina yake na yao yakawa ya kususua huku kwa mara kadhaa wakimtenga kwenye ufanyaji wao wa kazi.. Edga alishusha pumzi ndefu baada kukumbuka hayo, alimgeukia Kayumba kwa sauti ya upole iliyojaa huzuni ndani yake akasema "Hivyo ndivyo ilivyokuwa Kayumba, maisha ni kuchangua. Mimi niliona yale ndio maisha,ingawaje mazingira ndio yaliyonishawishi baada dhumuni langu la kumtafuta dada yangu kuzimika ghafla kama mshumaa. Kayumba hapa nilipo sijui na wala sielewi kama dada yangu bado mzima au amepoteza maisha ", chozi lilimtoka Edga alipokwisha kusema maneno hayo. Kayumba alimsogelea akamgusa bega kisha akasema." Braza Edga pole sana kwa mitihani lakini hupaswi kukata tamaa, wewe ni shujaa. Ukijikwaa nyanyuka endekea na safari. Lakini pia siku zote kaa ukijua, milima haikitani lakini binadamu hukutana. Wasaka.."
"Tongee.." aliitikia Edga japo kwa sauti ya chini sana. Muda huo tayari ilikuwa yapata saa sita usiku, Edga na Kayumba walilala kwa dhumuni la kesho kuwahi kazini.
Siku iliyofuata ilikuwa siku njema sana, anga lote la jiji lilionekana kung'aa. Hali hiyo ilionyesha fika kuwa kuna dalili chache ya mvua kuonyesha. Edga aliachia tabasamu kisha akasema "Siku njema huonekana asubuhi"
"Naam! Abadani hujakosea", alijibu Kayumba kisha kila mmoja akaelekea kwenye kiwanja chake cha riziki. Edga alienda kubeba mizigo (Kuli) ilihali Kayumba naye alikwenda kuuza madafu.
Ilipotimu mnamo saa sita jua kali, anaonekana Kayumba akivuta kwama lake liliosheheni madafu, jasho la chumvi lilimvuja kichwa chini mikono nyuma. Punde si punde mlio wa honi ya gari ulisika wakati huo huo gari ndogo aina ya Noah yenye rangi nyeusi ilisimama mbele yake. Kayumba alikereka sana, akapayuka kwa hasira "Hii ni dharau", alisema huku akiliacha kwama lake nyuma na kisha kumfuata dereva ili ampe ya moyoni. Lakini alipo ukaribia mlango, kioo kilishushwa. Kayumba akamuona ni yule mrembo aliyemsaidia siku ya jana alipoporwa mkoba wake.
"Aah kumbe ni wewe mrembo", aliongea Kayumba kwa tabasamu bashasha..
"Ndio habari yako.. Ammh madafu unauza bei gani?.."
"Madafu mia nane tu", Kayumba alitaja bei. Mrembo huyo alihitaji dafu moja akatoa noti ya shilingi elfu kumi na wala hakuta kurudishiwa chenji. Kayumba alistaajabu sana, hakuamini macho yake aliamini kuwa wadada wazuri kama hao huwa na kasumba hasa kwa masikini kama yeye. Hivyo aliona kuna haja ya kufahamu jina lake, kwa tabasamu bashasha Kayumba akasema "Ni mara mbili sasa tunakutana, sio mbaya kama tukifahamiana hata kwa majina. Jina langu naitwa Kayumba", mrembo huyo binti wa kiarabu aliyevalia hijabu nyeusi aliachia tabasamu na akasema "Naitwa Najrat, kaa ukijua nametokea kukupenda", kwisha kusema hivyo akawasha gari akaondoka huku nyuma Kayumba akibaki mdomo wazi, maneno ya mrembo Najrat yakijirudia mara mbili mbili kichwani mwake ilihali tabasamu pana likitawala uso wake..
"Au ni jini? Kama hilitokuwa zali kwa mentali? .", alijuliza Kayumba..
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kayumba alibaki na taharuki, alihisi huwenda amsekia vibaya kile alichokiongea Najrat. Lakini yote kwa alishusha pumzi akarejea kwenye kwama lake, akaendelea na mihangaiko ya kusaka shilingi. Mnamo sana kumi na mbili jioni, mzigo ulikuwa umekwisha. Kayumba alirejea maskani, punde si punde Edga naye alifika na baada ya kusalimiana Kayumba akasema "Leo mambo yamekwenda kama yalivyo pangwa"
"Ahahahah hahahaha", Edga aliangua kicheko kisha akahoji "Kwanini umesema hivyo, sijakuelewa ujue?.."
"Najua huwezi kunielewa lakini maana yangu ndogo sana, Edga mzigo umekwisha", alijibu Kayumba kwa furaha. Wawili hao walicheka sana, baada ya vicheko hivyo Edaga akasema "Kweli waliosema siku njema huonekana asubuhi wala hawajakosea,braza leo magari ya mzigo yamekuwa mengi mno kiasi kwamba tulibagua bosi yupi mwenye mtonyo wa kutosha. Kwahiyo hapa nilipo pochi imetuna"
"Ahahahah", Kayumba aliangua kicheko kwa mara nyingine tena kisha akaongeza kusema "Tukiachana na hayo, nina habari njema nyingine..."
"Ipi hiyo?..", alihoji Edga wakati huo akiwa makini kumsikiliza Kayumba. Kayumba akajibu "Nadhani unakumbuka niliwahi kukwambia kwamba kuna binti nilimsaidia baada kuporwa mkoba wake"
"Ndio nakumbuka"
"Enhee.. Basi leo wakati napamabana na mkokoteni wangu, nipo hoi jasho mpaka kwenye kisigino jua kali, mara ghafla nikasikia bleki ya gari mbele yangu, nikainua uso nikaiona Noah nyeusi. Unajua mimi nikiwa kazini huwa sipendi dharau, kwa hasira nikamfuata dereva wa ile gari ili nimpe makavu, lakini braza mwili wangu ulijikuta ukinyong'onyea baada dereva kushusha kioo uso kwa uso nikamuona yule mrembo huku akiachia sabasamu. Tuliongea mengi sana ila alicho nishangaza ni baada kununua dafu akatoa noti ya shilingi elfu halafu akakata chenji, na mwishowe wakati anaondoka akaniambia kwamba ametokea kumipenda ", aliongea Kayumba.
" Kweli!?.. ", kwa taharuki ya aina yake Edga alimuuliza Kayumba.
" Basi ndugu yangu hupaswi kulemba mwandiko kwa mrembo huyo wa kiarabu, na ndio maana nilikwambia kwamba wewe unanyota ya utajiri. Kwa maana hiyo basi usijipendekeze kwake, vuta subira kama amekupenda atakutafuta kwa udi na uvumba..."
"Lakini Edga mimi kwa sasa nayaogopa sana mapenzi, sitaki tena kulia kisa mapenzi"
"Kayumba rafiki yangu, naomba unielewe, anayekupenda kwa dhati katu hatapenda kukuona unalia.
" Sawa, hebu tuachane na hayo. Leo pesa ipo mshkaji wangu kwahiyo twende tukale chakula cha nguvu.."
"Hilo tu ndilo lililobakia.." aliongea kwa furaha Edga. Hayo ndio yakawa maisha ya vijana hao, Kayumba na Edga. Maisha ya furaha sana ingawaje waliishi kwa nguvu na kula kwa utepe ila kwa furaha haikuweza kukauka. Walifanya kila jitihada kuhakikisha furaha haipotei kwenye nyuso zao, kwenye magumu walitiana moyo na kwenye furaha walifurahi zaidi. Naam! Hao ndio wasaka tonge.
Siku zilisonga, Kayumba hakubahatika tena kukutana na mrembo Najrat. Hakuliwazia sana suala hilo sababu alimchukulia Najrat kama mpita njia na sio vinginevyo, hivyo Kayumba alifanya kazi kwa juhudi zake zote. Hatimaye alisahau kama aliwahi kukutana na Najrat, lakini siku moja alipokea karatasi kutoka kwa kijana mmoja ambaye alifahamu kutokana na kazi anayoifanya. Kijana huyo alikuwa muuza duka, ambapo wakati Kayumba akakikokota kwama lake alisikia sauti ikimuita, haraka sana alitii wito.
"Habari yako bwana mkubwa".
"Salama tu vipi kwema?..", alijibu Kayumba.
"Kwema, naona unapambana". Aliongeza kusema kijana huyo muuza duka.
"Naam! Nautafuta utajiri." Kayumba alijibu huku akijifuta jasho usoni kwa flana yake.
"Vizuri, kuna ujumbe wako hapa nimeachiwa. Na kibaya zaidi aliyeniachia hakutaka nikutajie jina", alisema kijana huyo huku akimkabidhi Kayumba kipande kidogo cha karatasi. Kayumba alipokea karatasi hiyo, akiwa na shauku ya kutaka kujua kilichoandikwa aliifungua.
"Mambo Kayumba, naomba kesho saa nne asubauhi tukutane Seline Hotel nina maongezi zaidi ya kuzungumza na wewe, nakutakia kazi njema mpenzi", Kayumba alisoma kile kilichoandikwa kwenye karatasi hiyo. Ghafla akajikuta akiachia tabasamu wakati huo akiitazama mara mbili mbili hiyo karatasi.
"Sawa ahsante bwana", alimshukuru mwenye huyo kijana aliyempatia karatasi, na sasa alizipiga hatua kurudi kwenye mkokoteni wake. Lakini kabla hajapiga hatua mbili, alisikia sauti ya kijana huyo ikisema "Chukuwa hii fedha", Kayumba aliposikia maneno hayo aligeuka akakutana na mkono wa huyo kijana ukiwa umeshika fedha,na kabla hajazipokea alihoji "Za nini hizo?.."
"Aliyeacha huo ujumbe ameniambia nikukabidhi", alijibu kijana huyo. Kayumba alipigwa na butwa. Alistaajabu sana kila akitazama kiasi hicho cha fedha, zilikuwa fedha nyingi mno. Alizipokea kisha akarudi kwenye mkokoteni wake akaendelea na kazi huku akiahidi kufika Seline Hotel pasipo kuchelewa. Jioni aliporejea maskani, alikuwa ni mtu mwenye wingi wa furaha. Hata pia alipomueleza Edga, naye pia alifurahi zaidi.
"Nilikwambia mimi, amini ndugu yangu siku zote Mungu hamtupi mja wake...", alisema Edga kwa furaha.
"Hakika nimeamini, na kuanzia sasa naweza kusema maisha ya kulala nje baaasi. Hii laki tatu aliyonipa huyu mrembo, inatosha kupanga chumba na chenji inarudi. Naomba unipe ramani mahali ilipo hiyo Hotel ili wakati mimi naelekea huko, wewe ubaki unatafuta chumba ", alisisitiza Kayumba.
" Hahaha ah.. Wasaka.. "
" Tongeeeee ", walitaniana kama ilivyo ada. Na pindi furaha ikiwa imatamaraki kwa wasaka tonge hao, upande wa pili Catherine alionekana kukosa furaha. Usiku huo hakupata usingizi, aliona Dunia inamtenga hasa hasa kila alipoitazama picha kubwa iliyokuwa ukutani. Picha ya kijana msomi mwenzie atwae Johnson. Catherine kitanda alikiona kidogo, kila mara alikuwa akijipundua huku na kule huku nafsi yake ikiwa imefura giza la maumivu ya kusalitiwa na Johnson mwanaume aliyempenda kwa dhati na kuthubutu kumkana Kayumba.
"Johnson wa kunifanyia mimi hivi? Johnson kweli amedhutu kunidhihaki kiasi hiki? Mbona hakuniambia kama anampenzi mwingine! Nakuchukia sana Johnson sikupendi tena", alijisemea Catherine na punde akaangua kilio. Tangu awali hakujua ya kuwa Johnson ni mwanaume asiye dumu na mwanamke mmoja,kijana huyo alipendelea sana kuwachezea mabinti na kuwaacha kwenye mataa. Catherine akajikuta akiingia kwenye mkumbo huo wa wale mabinti wanaotumia na kuachwa, sasa anaachiwa maumivu makali ya usaliti. Jambo hilo linamfanya anamkumbuka Kayumba, aliona ni heri arudishe hisia zake kwa Kayumba akiamini kuwa huwenda akapata faraja ya moyo wake pasipo kujua kuwa Kayumba ameshamsahau.
"No! Lazima nimfuate Kayumba wangu kijijini, nitamuomba radhi kwa kile nilichomtendea",alijisemea Catherine huku akipandisha kwikwi baada kulia kwa muda mrefu. Lakini wakati Catherine akiwaza suala hilo la kumfuata Kayumba, upande wa pili hivyo hivyo Najrat alionekana kukosa usingizi. Mawazo yake yote alimuwaza Kayumba huku akitamani pawahi kukukucha ili aweze kuonana naye kama alivyomuasa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku iliyofuata ilikuwa siku nzuri sana, hali ya hewa ilionekana kuwa shwari kabisa. Kayumba na Edga waliamka, mabox yao wakayahifadhi pema tayari kwa safari ya kuelekea kufanya kile walichokipanga usiku wa jana.
"Kama nilivyo kwambia, sio mbali saana ila nina imani utafika tu", alisema Edga huku akijinyoosha.
"Hilo ondoa shaka, jitahidi upate chumba kizuri", alijibu Kayumba.
"Ahahhah hahahahah", Edga aliangua kicheko, alipokatisha kicheko chake akatania kwa kusema "Usijali mume wa Najrat",
"Hahahahah..", Kayumba alifurahia utani huo wa Edga. Ndio maisha waliyokuwa wakiishi, na hivyo sasa alianza safari kuelekea Soline Hotel akitii wito la mrembo Najrat huku asijue mrembo huyo anakipi hasa anataka kumueleza. Hatimaye alikaribia kufika,kwa mbali aliliona gholofa la Hotel hiyo ambapo ingemlazimu kuvuka barabara ili aelekee upande wa pili mahali ilipo hiyo Hotel. Lakini wakati anavuka barabara kuelekea upende wa pili, ghafla aligongwa na gari.
Gari iliyomgonga ilikuwa taksi nyeupe iliyopigwa mstari wa njano, punde ndani ya gari hilo walishuka watu wawili. Walimnyanyua Kayumba kutoka chini alipoangia baada kugongwa, akivuja damu mdomoni huku akiwa amepoteza fahamu walimuingiza ndani ya gari kisha wakaondoka naye. Mnao saa kumi na moja jioni, Kayumba alitikisa mguu baada kupoteza fahamu kwa muda mrefu. Akastuka kujikuta yupo Hospital, alijiuliza amefikaje mahali hapo wakati huo huo wodini aliingia kijana mmoja mtanashati mwenye umbile la urefu , alivaa mavazi ya kitenge shati mpaka suruali uso wake ulijaa tabasamu pana huku akikisogelea kitanda alicholazwa Kayumba "Habari yako", kijana huyo alimsalimu Kayumba. Kayumba alikaa kimya kwa sekunde kadhaa kisha akashusha pumzi ndefu akajibu "Habari yangu nzuri"
"Ammh pole sana, jina langu naitwa Ikene. Sio raia wa hapa Tanzania ila huwa nakuja mara moja moja kufanya kufanya show, mimi ni mwanamuziki huwa naimba naimba kwenye kumbi mbali mbali hapa Dar es salaam. Ammh!..leo wakati naelekea kuandaa nyimbo yangu mpya, dereva wangu hakuwa makini barabani bahati mbaya akakugonga. Na hata hivyo hatukutaka kukuacha pale pale ukiteseka, kisingekuwa kitu cha kiungwana na ndio maana tukakuleta hapa Hospital ili utibiwe ", alisema Ikene kijana wa Nigeria, mwanamuziki ambaye mara kwa mara alifika Nchini kusaka riziki kwa kuimba kwenye kumbi mbali mbali jijini. Maneno hayo aliyaongea kwa chini rafudhi yake nayo ikionyesha dhahiri ni si Mtanzania.
" Kwahiyo ulitaka kuniuwa?..", aling'aka Kayumba.
"Haiko haja ya mimi na wewe kugombana, mimi ni kijana mzuri sana ndio maana sikuweza kukuacha", aliongeza kusema Ikene. Kayumba hakuongeza neno lolote zaidi ya kutokwa machozi kwenye kona ya macho yake. Kimya kilitanda wodini humo, lakini punde si punde kimya hicho kilitoweka Ikene akasema "OK! Mimi naondoka, nimeshaagiza chakula kuna mtu atakuletea hivi punde. Nitarudi baadaye kukujulia hali, sawa braza?.."
"Sawa", kwa sauti ya unyongea Kayumba akaitikia,na ndipo Ikene akanyanyuka kutoka kwenye kitanda hicho alicholazwa Kayumba, akausogelea mlango akaufungua. Kabla hajaondoka aligeuka nyuma kumtazama Kayumba, aliachia tabasamu bashasha kisha akaondoka zake.
Upande wa pili, alionekana Edga akiwa maskani. Tayari alishapata chumba, na sasa alirejea maskani kumsubiri Kayumba ili aambatane naye kuelekea kwenye makazi mapya. Lakini mpaka giza linatanda Kayumba hakuweza kutokea, ghafla Edga akaingiwa na hofu moyoni mwake, ila baadaye alijipa tumaini kwa kujisemea "Sio bure yawezekana Najrat amemtunuku tunda, ngoja nilale kidogo", kwisha kujissemea hayo akajilaza kwenye balaza, muda mchache baadaye alisinzia. Alfajiri palipo kucha, bado Kayumba alikuwa hajarejea, ndipo hofu dhofu lihali ilipozidi ndani ya moyo wake. Hakutaka kuamini kama amelala na Najrat, bali aliingiwa na imani ya kwamba huwenda rafiki yake amekutwa na tatizo. Alimama wima, mikono aliweka kiunoni huku uso akiwa ameinamisha chini. Alijiuliza "Kakutwa na nini Kayumba? Je, kanitoroka au ameuliwa? Loh! Kayumba? Hapana huwezi kunitoroka, usahau ulikotoka,wewe ni kama pacha wangu. Bila shaka utakuwa umekumbwa na tatizo" aliwaza Edga huku akiwa na sintofahamu nzito kuhusu Kayumba.
Upande wa pili, Hospital. Asubuhi ya siku hiyo aliletewa chai na binti yule yule aliyepewa jukumu na Ikene,jukumu la kumletea Kayumba chai, chakula cha mchana mpaka jioni. Mama ntilie huyo anaitwa Diana.
"Kaka habari ya asubuhi", akiwa na tabasamu bashasha Diana alimsabahi Kayumba.
"Salama dada karibu", alijibu Kayumba huku akiinuka na kisha kuegemea mahali anapolaza kichwa akiutanguliza mto ili asiumie mgonga. Diana alimimina chai kwenye kikombe, ilikuwa chai ya maziwa ambayo alimpatia pamoja na chapati tatu.
"Karibu chai", Diana alimkalibisha Kayumba kwa tabasamu pana.
"Haya Ahsante, samahani unaitwa nani?..", aliuliza Kayumba kwa sauti ya chini ilihali uso wake ukilijibu vema tabasamu aliloonyesha Diana.
"Naitwa Diana", alijibu binti huyo.
"Anhaa, unajina nzuri kama wewe ulivyo", alisifu Kayumba, Diana akacheka huku uso wake akiwa ameinamisha chini kwa haibu.
"Ahsante. Ila mimi naondoka. Naenda kuendelea na majukumu mengine, nitarudi baadaye kuchukuwa vyombo", alisema Diana wakati huo akimuonea haya Kayumba.
***************
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Manamo saa sita mchana, jua kali jijini. Edga, kijana msamalia mwema aliyejitolea kumsaidia Kayumba baada kuonekana hana pakwenda. Siku hiyo ilionekana kuwa mbaya sana upande wake, alimzoea sana Kayumba hasa hasa akikumbuka utani mbali na ushauri wa kutiana moyo kwenye maisha ya kusaka tonge. Hakika Edga alisafa, alijihisi kukosa nguvu, hakusikia kiu ya maji wala njaa. Lakini wakati hali hiyo ikiendelea upande wa Edga, upande wa pili Kayumba naye alishindwa kunywa ile chai aliyoletewa na Diana. Nafsi yake ilishiba kama ilivyo kwa Edga, kukaa mbali na mshkaji wake ilimsikitisha sana. Kayumba alitambua umuhimu wa Edga, hasa akifikiria maisha magumu waliyopitia tangu siku ile atoswe na Catherine. "Mmh Edga rafiki yangu, ungejua kilicho nikuta basi natumaini moyoni usingelikuwa na mpweke. Najua popote ulipo umejaa na sintofahamu, na itaniuma sana endapo kama tutapotezana", aliwaza Kayumba, chozi lilimtoka kwa huzuni lakini alifanya hima kulifuta ilihali punde si punde Diana aliingia wodini. Alistaajabu kukuta chai ikiwa bado imejaa kwenye kikombe na wala chapati zisiguswe. Kwa mshangao Diana akamuuliza Kayumba "Mbona hujanywa chai?.."
"Daah! Diana we acha tu, yani ukweli sijisikii kula kiti chochote", alijibu Kayumba.
"Mmh! Pole jamani, basi kwa kuwa chai hujanywa ngoja nikakuletee wali, ujilazimishe kula ili dawa zifanye kazi vizuri, hofu ondoa kabisa Ikene kalipia mpaka cha usiku", aliongeza kusema Diana kisha akaondoka huku akimuacha Kayumba akiwa ameshika tama akimfikiria Edga. Baada ya dakika kumi Diana alirejea akiwa na chakula kwenye kikapu chake cha kubebea, hima imuandalia mgonjwa lakini Kayumba alikataa kula jambo ambalo lilimpelekea Diana kumbembeleza ili ale hali ya kuwa moyoni alijisemea "Ama kweli Mungu anaumba, mkaka mzuri kweli yani ghafla nimekupenda", kwisha kujisomea maneno hayo aliachia tabasamu huku bado akiendelea kumbembeleza Kayumba ale chakula. Na wakati Diana akiendelea na zoezi hilo, ghafla wodini aliingia nesi akasema "Sinsia kuna mtu anakuita nje mara moja", Diana aliposikia wito alinyanyuka akamtazama Kayumba kisha akatii huo hali ya kuwa huku nyuma Kayumba akibaki na taharuki.
"Sinsia!?..", alijuliza Kayumba kwa mshangao wa hali ya juu.
Alijiuliza Kayumba, akakumbuka kuwa rafiki yake aliwahi kumwambia kuwa anadada yake kapotezana naye miaka kadhaa nyuma. Naye anaitwa Sinsia.
"Inamana ndio huyu Sinsia?..", bado aliendelea kujiuliza Kayumba. Lakini wakati akiwa na sintofahamu kuhusu Diana, punde mlango wa wodi ulifunguliwa. Akaingia Diana, alikisogelea kitanda kwa mwendo wa madaha aliketi kisha akaendelea kumbembeleza ale chakula, mwishowe Diana alifanikiwa. Kayumba alikula ingawaje mawazo yake yote yalikuwa yakimfikiria Edga. "Ahsante kwa chakula", alishukuru Kayumba huku akinawa mikono yake.
"Jamani mbona hivyo? Kula bwana ili dawa ifanye kazi isavyo",kwa sauti ya kubembeleza Diana alisema.
"Hapana dada, tarayari nimetosheka. Endapo kama nitajilazimisha basi nitatapika, kuwa na amani mimi nimeshiba", alijibu Kayumba huku Diana akimsikiliza kwa umakini na wala asiishiwe hamu kumtazama. Diana alivutiwa mno muonekano wa Kayumba, alipenda namna alivyo mrefu kiasi, sura nzuri na kifua chake cha kiume kilicho chanika balabala. Diana hoi kwa Kayumba,alimuuliza jina lake ili apete kufahamu "Samahani, jina lako nani?.."
"Mimi naitwa Kayumba", Kayumba alijibu.
"Ooh, wewe ni mwenyeji hapa Dar es salaam?..", alihoji Daiana.
"Hapana, mimi wa kuja. Lakini wewe umenidanganya jina lako,huitwi Diana. Wewe unaitwa Sinsia bwana"
"Hapana hilo ni jina ambalo watu wengi hupenda kuniita"
"Kwanini wakuite jina hilo badala ya jina lako? Hebu kuwa mkweli,Mungu hapendi uongo ujue".
"Ukweli ni huo Kayumba, Sinsia hili ni jina ambalo bosi wangu ninaye mfanyia kazi alinibatiza. Nilijaribu kumuuliza kwanini uniite Diana? Akanijibu kwamba mdogo wake na fanana naye kila kitu. Kwahiyo ndio maana akaamua kunipa hilo jina,nami nimelizoea sasa "
" Anhaa sawa, mimi sina neno katika hilo"
"Enhee kwahiyo unaishi wapi hapa mjini?.." aliuliza Diana.
"Mimi ni msaka tonge", Kayumba alijibu.
"Unamaana gani kusema hivyo", kwa mshangao Diana alihoji. Kayumba kabla hajajibu alishusha kwanza pumzi kisha akajibu "Maana yangu ni kwamba, sina sehemu maalumu ingawa nina kazi maalumu naishi na mshkaji wangu"
"Anhaa, unamaana kwamba wewe na rafiki yako ni moja ya watu ambao mnalala nje si ndio?.."
"Ahahahah", aliangua kicheko Kayumba kisha akajibu "Ndio maana yake"
"Doh! Pole sana jamani, lakini uliwezaje kuja jiji hili pasipo mipango maalumu?..", aliongeza kuhoji Diana, yote hayo yakuwa moja ya maongezi baada Kayumba kumaliza kula.
"Ni hadithi ndefu sana dada", alijibu Kayumba kwa sononeko.
"Unaweza kunisimulia?..tafadhali niambie basi", aliongea Diana kwa sauti ya chini huku akimtazama Kayumba usoni. Kayumba alikaa kimya kidogo, kwa mara nyingine tena akaishusha pumzi yake kisha akasema "Diana, kitu pekee kilicho nifanya nikafunga safari kutoka kijijini kwetu kuja ndani ya jiji hili, ni binti mmoja aliyeitwa Catherine. Huyu ni binti ambaye tulikuwa wapenzi angali wadogo mpaka tunafikia umri wa utu uzima. Nilipofeli elimu ya darasa la saba, yeye alipata nafasi ya kuendelea mpaka sekondari. Ila katu sikutaka Catherine wangu asononeke, hakuwa na wazazi na hivyo nilimpa kila alichotaka ili kuhakikisha furaha inadumu kwenye penzi letu.. Lakini baadaye nilikumbwa na matatizo, huwezi amini Diana nilifungwa jela kwa ajili yake, baada kuiba ili nipate fedha itakayo endeleza elimu yake. Ila baada kifungo changu kumalizika, nikasikia habari Catherine anaishia Dar es salaam. Sikutaka kuchelewa nilifanya kila lililowezekana na hitamaye jijini nikaingia, ramani niliyopewa iliyokuwa ilionyesha mahali anapoishi Catherine niliitunza vema huku moyoni nikiamini kwamba Catherine atakapo niona lazima atafurahi. Diana, nilicho Kitana nacho sikuweza kuyaamini masikio yangu. Catherine alinikataa akidai kuwa sina elimu, yeye ni msomi kwahiyo lazima aolewe na msomi mwenzie. Nilitaharuki sana, nikajiuliza inawezekana vipi Catherine asahau mchango wangu kwenye elimu yake? Majibu nilikosa, na dakika ya mwisho Catherine alinitimua kama mbwa nyumbani kwake. Hapo sasa ndipo nilipowaza nitaishije jijini ikiwa sina ndugu wala fedha ya kunirudisha kijijini kwetu. Mungu si Athumani, nikabahitika kupata kijana mwenzangu msamalia mwema ambaye alinisaidia mpaka kufikia hatua fulani ya kuweza kumsahau Catherine... "alisimulia Kayumba.
" Na hapa nimepata ajari hajui chochote ", aliongeza kusema Kayumba kwa sononeko. Na wakati Diana na Kayumba wakiwa kwenye maongezi, upande wa pili alionekana Edga akiwa amepoa, aliondoka hapo maskani akiwa mnyonge huku sintofahamu nzito ikiendelea kutawala kichwani mwake. Kichwani chini mikono nyuma, ghafla alisikia sauti ikimuita "Alooh! We kijana", Edga aligeuka kutazama kule ilipokuwa ikitokea sauti hiyo. Aliona gari ndogo aina ya taksi ikiwa imesimama kando kidogo ya barabara, mzee wa makamo ndiye aliyemuita.
"Mimi?", alihoji Edga.
"Ndio wewe!", alijibu mzee huyo, na mara moja Edga akatii wito.
"Bwana mdogo hebu sikia, duka langu sio sehemu ya kustili masikini kama nyinyi. Kwa maana hiyo basi, nakuomba wewe na ndugu yako tafuteni sehemu nyingine pakulala la sivyo tusije tukalaumiana", aling'aka mzee huyo ambaye alimtaka Edga na Kayumba kuondoka mahala pale wanapolala kila iitwayo leo. Mzee huyo alipokwisha kusema maneno hayo alipandisha kioo kisha akaliondosha gari lake kwa kasi huku nyuma akimuacha Edga akilisindikiza kwa macho na hata asiseme chochote. Edga alishusha pumzi ndefu, machozi yalimtoka aliamini sasa huo ndio mwanzo wa kupotezana na swahiba wake wa karibu. Rafiki yake kipenzi ambaye walipambana kwenye shida na raha. Hakika roho ilimuuma sana Edga, alimeza mabunda ya mate mfululizo, ndani ya nafsi yake akajisemea "Maisha ni kama kitabu, ni kweli Kayumba wa Najrat leo hii nakuacha kwenye ukurasa wa nyuma!? Niliamini tutaendelea kuwa pamoja kukimaliza kitabu hiki lakini mipango imeota mbawa. Mbali ulipo mchizi wangu, msaka tonge mwenzangu ila kinacho nipa hofu ni juu ya uhai wako, je upo salama ama umekubwa na tatizo. Kayumba Kayumba Kayumba.. Nina imani ipo siku tutakuna, kama sio hapa hapa ulimwengu basi hata baradiso huku tukitabasamu.. ", aliyafuta machozi Edga, aliyaondoa macho yake upande ule aliokuwa akilisindikiza gari la yule mzee aliyemfukuza maskani, na sasa Edga alitazama mbele akazipiga hatua kichwa chini mikono nyuma huku mboni za macho yake ziliendelea kububujika machozi ya kumpoteza Kayumba.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Pole sana kwa yote yaliyokukuta Kayumba, na pia nina ombi moja kwako", upande wa pili alisikika Diana akimwambia Kayumba mara tu alipomsimulia ufupi wa story ya maisha yake.
"Ombi gani?..", aliuliza Kayumba kwa sauti ya chini iliyojaa huzuni ndani yake. Daina hakujibu papo hapo, alikaa kimya kidogo kwa dakika kadhaa kisha baadaye akajibu "Naomba tukaishi pamoja nyumbani kwangu, na pia tutashirikina kwa pamoja kumtafuta rafiki yako. Vile vile nakupa hongera kwa kumsahau Catherine wako", aliongeza kusema Diana. Kayumba alistuka kusikia suala hilo la kwenda kuishi na binti huyo. Na wakati ikiwa na taharuki, Diana aliendelea kusema "Na huyo rafiki yako anaitwa nani?.."
"Anaitwa Edga..", Kayumba alijibu.
"Edga?..", alistuka Diana..
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment