Search This Blog

Tuesday, 1 November 2022

DUNIA HAINA USAWA - 1

 






IMEANDIKWA NA : ERIC SHIGONGO



*********************************************************************************



Simulizi : Dunia Haina Usawa

Sehemu Ya Kwanza (1)





“Mume wangu! Naomba unisamehe!”

“Nikusamehe! Mara ngapi? Nahisi hunijui! Sasa subiri.”

“Mume wangu naomba unisamehe! Sitorudia tena!”

“Eti hutorudia! Unanifanya mimi mjinga! Leo nataka nikuonyeshee, utajua kwa nini Mungu alianza kumuumba Adamu kabla ya Hawa.”

Zilikuwa ni kelele kutoka katika nyumba moja chakavu iliyokuwa katika Mtaa wa Tandale kwa Tumbo jijini Dar es Salaam. Watu waliokuwa wakipita nje ya nyumba hiyo, walisimama na kusikiliza kile kilichokuwa kikiendelea.

Hiyo haikuwa mara ya kwanza, kila siku kulikuwa na fujo ndani ya nyumba hiyo waliyokuwa wakiishi watu wawili tu, Godwin Mapoto na mwanamke mrembo aliyewahi kutikisa kutokana na urembo wake, Winfrida Michael.

Kelele zile ziliendelea kuwakusanya watu wengi nje ya nyumba hiyo. Wale waliokuwa ndani ya nyumba zao, wakatoka na kwenda kusimama karibu kabisa na nyumba hiyo.

Hakukuwa na mtu aliyediriki kuingia ndani kugombelezea kwani walimfahamu Mapoto, japokuwa alionekana kuwa mwanaume dhaifu, mwenye mwili mwembamba lakini alivuma kutokana na ubabe wake mtaani hapo.

Alikuwa mwanaume wa fujo, aliyetikisa kuanzia Kwa Tumbo, Kwa Mtogole, Yemen mpaka Mwananyamala kwa Manjunju. Watu wengi walikuwa wakimuogopa, jina lake lilikuwa likivuma sehemu kubwa kuanzia Tandale, Mwananyamala mpaka Magomeni Kondoa.

Alikuwa mbabe wa mtaa kiasi kwamba watu walihisi kwamba asingekuja kuwa na mwanamke mrembo kutokana na ubabe wake, lakini kitu kilichowashangaza ni kwamba alifanikiwa kumnasa msichana aliyekuwa na sura nzuri, ya kipole, umbo matata, Winfrida Michael, msichana aliyekuwa akikubalika katika Chuo cha St. Joseph alipokuwa akisomea biashara.

Chuoni hapo, Winfrida alitingisha kwa uzuri, kila mwanaume alikuwa akimzungumzia yeye, alipokuwa akitembea, watu walimfananisha na twiga huku macho yake yakiwa na mvuto mithili ya mwanamke aliyekula kungu.

Hakuwa msichana mwepesi, alikuwa mgumu, wanaume walimfuata na kumtaka kimapenzi lakini Winfrida hakukubaliana nao hata kidogo. Kila walipokuwa wakizungumza naye, alionyesha tabasamu kubwa kiasi kwamba liliwapa matumaini wanaume wengi lakini jibu lake halikufanana na tabasamu alilokuwa akilitoa usoni mwake.

“Nimekuelewa,” alisema Winfrida.

“Sawa. Kwa hiyo?” aliuliza mwanaume mmoja, kama walivyokuwa wengine, na yeye alimfuata msichana huyo kwa lengo la kumtaka kimapenzi.

“Kwa hiyo nini Ibrahim? Nimekwishakwambia kwamba sikutaki! Kwa nini hutaki kusikia?” aliuliza Winfrida huku akionekana kuchukizwa na uwepo wa mwanaume huyo mbele yake.

“Winny! Ninakupenda sana. Wewe ni mwanamke wa ajabu sana mbele ya macho yangu, ni mwanamke mzuri sana. Nakuomba uwe nami, nakuahidi kwamba kamwe sitokuumiza, ninaapa kwa viapo vyote, kamwe sitokuumiza,” alisema mwanaume huyo, kwa kumwangalia tu, macho yake yalionyesha kumaanisha alichokuwa akikizungumza lakini kwa msichana kama Winfrida, ilikuwa ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa.

“Haiwezekani!”

Huyo hakuwa mwanaume wa kwanza kumfuata, wengi walifuata. Wengine walimwendea na gari kwa kuhisi kwamba msichana huyo angenasa katika mitego yao lakini waligonga mwamba, hakutaka kumuelewa mtu yeyote yule kiasi kwamba wanaume wengi wakajiuliza juu ya kitu alichokuwa akikihitaji msichana huyo.

“Labda gari?” alisema jamaa mmoja.

“Haiwezekani! Godwin alimfuata akiwa na gari!”

“Ikawaje?”

“Akapigwa cha mbavu!”

“Mh! Labda mkwanja!”

“Hata nao hauwezekani! Idris alimfuata akiwa na mkwanja wa kutosha, akamtamanisha lakini wapi! Labda tujaribu kuwa watumishi wa Mungu,” alisema jamaa mwingine.

Walikuwa wakizungumza mambo mengi kuhusu Winfrida, walianzisha mbinu nyingi za kumpata msichana huyo lakini hakukuwa na mtu aliyekubaliwa kitu kilichoendelea kuwaumiza mioyo yao.

Baada ya kumaliza mwaka wa kwanza, tena huku Winfrida akiwa kwenye chati kubwa machoni mwa wanaume wengi, akakutana na Godwin maeneo ya Makumbusho, mahali ambapo mwanaume huyo alipokuwa akifanya kazi ya kupiga debe.

Macho ya Winfrida yalipotua kwa Godwin akashtuka, mapigo yake ya moyo yalimuenda mbio, hakuamini kama siku hiyo angekutana na mwanaume kama huyo.

Alimvutia! Mwili wake uliojazia ambao ulionekana vilivyo ulimchanganya msichana huyo kiasi kwamba akabaki akimkodolea macho tu kiasi cha kumshangaza Happiness, rafiki yake aliyekuwa naye pembeni.

“Dada mnakwenda? Dada vipi hapo?” aliuliza Godwin huku akimwangalia Winfrida na Happiness, hakutaka kuridhika, akawafuata na kuwashika mkono na kuwavutia kwake kama walivyokuwa wakifanya wapiga debe wengine.

Japokuwa alishikwa kibabe lakini Winfrida akachanganyikiwa, mapigo ya moyo wake yakapiga kwa nguvu, akahisi mwili wake ukipigwa na shoti ya umeme, mguso ule ulimchanganya na kujikuta akiachia tabasamu pana.

“Unakwenda dada? Ingia! Twende dada! Kuna siti za kumwaga, utakaa na ukichoka utalala,” alisema Godwin.

Hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kwanza kuonana na Godwin. Moyo wake ulichanganyikiwa, aliporudi nyumbani, alijilaza kitandani na kuanza kumfikiria mwanaume huyo. Alionekana kuwa mvuta bangi, aliyepigwa na maisha lakini kwa Winfrida hakujali, alimpenda, kwa jinsi alivyokuwa, kwa muonekano wake uleule, moyo wake ukamkubali kwa asilimia mia moja.

Safari za kwenda Makumbusho hazikuisha, kila siku alikuwa akielekea huko hata kama hakuwa na kitu chochote kile. Alipofika, hakupanda kwenye daladala yoyote ile, alisimama pembeni na kumwangalia Godwin jinsi alivyokuwa akiita abiria, moyo wake ulimuonea huruma lakini hakuwa na jinsi.

“Mbona unapata tabu hivi! Hutakiwi kupata tabu hata kidogo,” alisema Winfrida huku akimwangalia mwanaume huyo.

Moyo wake ukafa na kuoza, penzi likaingia moyoni mwake kwa kasi kubwa. Darasani alipokuwa akisoma, hakusoma kwa raha, aligubikwa na mawazo tele na muda mwingine alikuwa akizungumza peke yake kama kichaa.

Happiness aliligundua hilo, alijaribu kumuuliza Winfrida kilichokuwa kikiendelea lakini msichana huyo hakuwa radhi kumwambia zaidi ya kumdanganya kwamba alikuwa na matatizo ya kifamilia.

“Kweli?”

“Ndiyo Happy! Siwezi kukuficha chochote kile,” alisema Winfrida huku akimwangalia rafiki yake usoni, ili kumdanganya zaidi, akamtolea tabasamu pana.

Happiness hakuhoji sana, alimuacha Winfrida ambaye aliendelea kuteseka kila siku moyoni mwake. Safari za kwenda Makumbusho ziliendelea huku lengo lake kila siku likiwa lilelile la kumuona mwanaume huyo ambaye tayari aliingia moyoni mwake, akavuta kiti na kutulia kabisa.

Aliteseka sana, baada ya miezi miwili, hakutaka kuteseka zaidi, alichokifanya ni kuamua moyoni mwake kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima amfuate mwanaume huyo na kumwambia ukweli, jinsi alivyokuwa akimpenda na kumtesa kila siku usiku.

Siku hiyo alijipanga, alioga vizuri na kuvaa nguo maalumu, alitaka kuonekana kama malkia machoni mwa Godwin ambaye wala hakuwa na habari naye. Alipofika chuo, alisoma ingawa kichwa chake kilikuwa kikimfikiria zaidi mwanaume huyo.

Hakukuwa na siku ambayo aliona masaa yakienda taratibu kama siku hiyo. Kila wakati alikuwa akiangalia saa yake, walimu walipokuwa wakiingia, alisonya, aliona muda ukienda taratibu sana, alitamani kuondoka chuoni hapo haraka iwezekanavyo kwani moyo wake ulishindwa kuvumilia, alijiona akiingia katika ulimwengu mwingine wa mahaba.

“Hebu niambie kitu,” alisema Happiness.

“Kitu gani?”

“Una nini?”

“Sina kitu!”

“Hapana! Hebu niambie ukweli. Unapokuwa na matatizo ninajua kipenzi, umekuwa ukiniambia kila kitu kinachokusibu, miezi hii unaonekana kutokuwa sawa kabisa. Hebu niambie ukweli! Nini kinaendelea?” aliuliza Happiness huku akimwangalia Winfrida.

Msichana huyo hakuzungumza kitu, akanyamaza na kuangalia chini. Kumwambia Happiness halikuwa tatizo lolote lile lakini alianza kujifikiria ni kwa jinsi gani msichana huyo angehisi mara baada ya kumwambia kwamba alikuwa kwenye mapenzi mazito na mwanaume aliyemuona kituoni.

“Niambie!” alisema Happiness.

“Sawa. Ishu ni kwamba moyo wangu upo kwenye mapenzi mazito! Hilo tu,” alisema Winfrida huku akimwangalia Happiness ambaye alionekana kushtuka.

“Upo kwenye mapenzi mazito?”

“Ndiyo!”

“Mwanaume gani tena huyo mwenye bahati? Edmund? Shedrack? Rahman? Hebu niambie,” alisema Happiness, uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana, masikio yake akayatega vizuri kusikia majibu kutoka kwa Winfrida.

“Unakumbuka siku ile tuliyokwenda Makumbusho?” aliuliza Winfrida.

“Siku gani?”

“Siku ile mpaka yule kaka akaja kutuvuta?”

“Ndiyo! Nakumbuka! Yes! Nishapata jibu! Au ndiye yule mwanaume uliyekuwa umekaa naye kwenye daladala?” aliuliza Happiness.

“Hapana!”

“Kumbe yupi?”

“Yule aliyetuvuta mikono!”

“Unamaanisha yule mpiga debe?”

“Hapana! Namaanisha yule mume wangu wa baadaye,” alijibu Winfrida huku akionekana kukasirika kwani hakutegemea kama Godwin angeitwa jina la Mpiga Debe.

Happiness akabaki kimya, alishtuka, akashusha pumzi, akamwangalia shoga yake, hakummaliza. Alimwangalia vilivyo machoni kuona kama kweli alimaanisha kile alichokuwa amekizungumza au la. Kwa jinsi Winfrida alivyoonekana, alionekana kumaanisha kila kitu alichomwambia msichana huyo.

“Imekuwaje tena?” aliuliza.

“Mapenzi!”

“Sawa. Lakini kwa yule?”

“Ndiyo!”

“Hapana! Utakuwa umechanganyikiwa Winny!”

“Bila shaka nimechanganyikiwa. Tena nimechanganywa na mapenzi mazito niliyokuwa nayo kwa yule kaka,” alisema Winfrida. Hakutaka kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kusimama na kuondoka.

Hakutaka kuingiliwa, aliamua kupenda kwa moyo wote, kwake, Godwin alionekana kuwa mwanaume wa ajabu, mwenye uzri wa ajabu kuliko wanaume wote katika dunia hii.

Akaondoka mpaka Makumbusho. Siku hiyo alijipanga, hakutaka kuona akiendelea kuteseka moyoni mwake. Aliamua kumwambia ukweli kwani kama kuteseka, aliteseka sana na alitaka kuwa huru.

Alipofika Makumbusho, akateremka kwenye daladala na kwenda kusimama pembeni kabisa. Alisimama huku akimwangalia Godwin aliyekuwa bize kuita abiria.

Ilipofika saa 8:16 mchana, muda ambao mwanaume yule alielekea katika kibanda cha mama ntilie kula, naye Winfrida akasimama na kumfuata mwanaume huyo.

Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kupita kawaida. Alipofika katika kibanda kile, akakaa kwenye benchi, wanaume wote waliokuwa mahali pale walimshangaa, iliwezekanaje msichana mrembo kama yeye akae mahali hapo?

Hakuzungumza kitu, kwa sababuu hakuwa amekaa mbali na Godwin, akayageuza macho yake kisiri na kumwangalia mwanaume huyo, kitu kilichomshtua ni baada ya kugonganisha macho na Godwin. Moyo wake ukalia paaa! Mbaya zaidi mwanaume huyo akatoa tabasamu pana. Winfrida akahisi baridi kali, mwili ukaanza kumtetemeka na kijasho chembamba kumtoka.

“Mungu nitie nguvu,” alijikuta akisema huku akiendelea kuangalia na Godwin ambaye hakuwa na taarifa yoyote kupendwa na msichana huyo.





Mapigo ya moyo wa Winfrida yalikuwa yakidunda kwa nguvu, hakuamini kama siku hiyo ndiyo ilikuwa maalum kwake kuzungumza na Godwin, mpiga debe ambaye kila siku aliuendesha moyo wake puta.

Hapo kwa mama ntilie alipokuwa, Winfrida hakuzungumza kitu, mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kwa nguvu, alitetemeka huku akiwa na hofu, alimpenda mwanaume huyo na alikuwa mahali hapo kwa ajili ya kuzungumza naye lakini kitu cha ajabu kabisa, maneno yote aliyokuwa ameyapanga yalipotea na hivyo kubaki kama bubu.

“Dah! Wewe dada mzuri kinoma,” alisema mwanaume mmoja, hakutaka kunyamaza, uzuri wa Winfrida ulimchanganya kila mtu aliyekuwa mahali hapo.

Winfrida hakusema kitu, akaachia tabasamu tu na kumwangalia mwanaume huo aliyemsifia. Tabasamu lake lilimchanganya kila mtu aliyekuwa mahali hapo, si wanaume hao tu bali hata mama ntilie aliyekuwa akiwauzia chakula alichanganywa na uzuri wa Winfrida.

“Halafu msichana bomba kama huyu, anakuja kuchukuliwa na boya fulani hivi! Mapenzi yanakera sana, wewe unafikiri atachukuliwa na mshikaji fulani wa kishua, anachukuliwa na mtu asiyejielewa,” aliingilia mwanaume mwingine huku naye akimwangalia Winfrida.

Mpaka dakika hiyo Godwin hakuzungumza kitu, aliyatuliza macho yake usoni mwa msichana huyo. Aliudadisi uzuri wake, alikuwa msichana mwenye uzuri wa ajabu kiasi kwamba hakukumbuka kama aliwahi kumuona msichana wa namna hiyo maishani mwake.

Wenzake waliendelea kumsifia lakini macho yake hatakutoka usoni mwa Winfrida, msichana huyo kila alipokuwa akimwangalia Godwin, aligonganisha macho naye kitu kilichomfanya kuangalia chini huku aibu ya kikekike ikimuingia.

“Kuna siku nitampata msichana kama huyu,” alisema Godwin maneno yaliyomfanya Winfrida kushtuka.

“Hahah! Mzee wa Tandale umpate mtoto kama huyo! Utarogwa! Demu mkali kama huyu unafikiri ataweza kukanyaga Tandale, kwanza kwa ardhi gani? Labda mmuwekee kapeti la kukanyagia,” alisema jamaa mwingine kwa utani na wote kuanza kucheka.

Walizidi kuongea mambo mengi huku yote ikiwa ni kumsifia Winfrida kwa uzuri aliokuwa nao. Msichana huyo hakuzungumza kitu, alibaki kimya huku muda mwingi akiangalia chini.

Winfrida hakutaka kula, hata alipoambiwa chakula kipi alichohitaji alimwambia mama ntilie kwamba hakuhitaji chakula, alihitaji kupumzika mahali hapo ila kama malipo, alitaka kuwalipia wateja wote waliokuwa katika kibanda hicho.

“Hayo ndiyo maneno! Tungekuwa na madada wanne kama hawa hapa kituoni, mwezi tu tungetoka vitambi!” alisema Godwin huku akionekana kuwa na furaha tele.

Japokuwa kabla ya kufika mahali hapo alikuwa na maneno mengi ya kumwambia Godwin lakini hakuzungumza kitu, kila alichokuwa amepanga kumwambia mwanaume huyo kilipotea kichwani mwake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Hakujua sababu iliyoufanya moyo wake kuwa mzito namna hiyo. Baada ya kukaa kwa dakika thelathini, wanaume hao wakaaga na kuondoka, kama kawaida, Godwin akaenda kuendelea na shughuli zake.

Macho ya Winfrida hayakutoka kwake, alibaki akimwangalia. Alimpenda jinsi alivyo, japokuwa alionekana kuwa mchafumchafu lakini moyo wake ulimpenda hivyohivyo. Hakujua jina lake, aligundua kwamba kama angelifahamu jina lake basi isingekuwa kazi kubwa kumpata, na mtu pekee ambaye angemwambia jina hilo hakuuwa mwingine, alikuwa huyohuyo mama ntilie.

“Yule anaitwa nani?” aliuliza Winfrida.

“Yupi?”

“Mwenye jezi ya Manchester?”

“Anaitwa Godwin! Mwanaume mtata sana! Ana hasira za karibu mno,ukimzingua kakuzingua,” alijibu mwanamke huyo, alimuongezea na majibu mengine ambayo maswali yake hakuulizwa.

“Mmh! Mbona anaonekana mpole sana?”

“Ndivyo alivyo! Kama angekuwa anavaa suti na kushika Biblia, kesho tu ungependa kwenda kanisani kwake kuombewa! Ila ndiye mtata kuliko wote. Hapa wanamuogopa mno,” alisema mwanamke huyo.

Hilo halikumtisha Winfrida, aliwafahamu wanaume, wengi walikuwa wakorofi lakini kwa wanawake walishindwa kufanya kitu. Wao ndiyo walikuwa udhaifu wao, hata kama mwanaume alikuwa mkorofi kiasi gani kwa mwanamke angekuwa mpole na kufanyiwa kitu chochote kile.

Siku hiyo akaondoka, ilikuwa ni siku ya mateso mno moyoni mwake. Hakukuwa na siku ambayo alimfikiria sana Godwin kama siku hiyo. Alikaa kitandani, moyo wake ulikuwa ukijilaumu sana, alijipanga kwa mwezi mzima lakini siku ambayo alitakiwa kuzungumza na mwanaume huyo hakufanya hivyo japokuwa alipata nafasi kubwa ya kufanya hivyo.

Alitamani kupafahamu mahali alipokuwa akiishi, amfuate usiku huohuo na kuzungumza naye. Alikumbuka kwamba aliambiwa ni Tandale, hakufahamu vizuri mtaa huo hivyo alishindwa kwenda.

Alivumilia kwa usiku huo, hakutaka kuwa na haraka kwa kuamini kwamba angefanikiwa kwa kile alichokuwa akikihitaji. Siku iliyofuata hakutaka kwenda chuo, kitu cha kwanza kilikuwa ni kwenda katika Kituo cha Daladala cha Makumbusho kwa ajili ya kuonana na Godwin ambaye aliutesa moyo wake na kumfanya kutokuishi kwa furaha.

Alipofika huko, akamuona akiendelea kuita abiria. Siku hiyo alipiga moyo konde, huku akiwa na hofu kubwa moyoni mwake, akaanza kumsogelea, alipomfikia tu, akamsalimia.

Godwin akamwangalia Winfrida, alimkumbuka, alikuwa msichana yule aliyekuwa amemuona jana yake na ndiye ambaye aliwalipia chakula. Akamchangamkia, wakazungumza kwa muda mchache na kuagana.

Huo ndiyo ukawa mwanzo wa wawili hao kuzungumza, Winfrida hakutaka kuacha kwenda Makumbusho, na kila alipokuwa akielekea huko, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumtafuta mwanaume huyo na kuanza kuzungumza naye.

Wakati wakiwa wamezoeana na kuzungumza kwa kipindi kirefu, ndipo Winfrida akagundua kitu cha tofauti kwa mwanaume huyo. Kila alipokuwa akiongea, aliingizia maneno mengi ya Kiingereza na hata wakati mwingine kuzungumza sentensi zaidi ya tano kwa Kiingereza tu.

Winfrida alishangaa, hali hiyo ilimpa maswali mengi kwani mbele yake, mwanaume huyo alionekana kuwa mtu wa tofauti. Alikuwa mpiga debe ambaye aliamini kwamba hakuwa ameingia darasani, sasa ilikuwaje azungumze Kiingereza kizuri kama alivyokuwa akizungumza?

“Wewe ni mpiga debe kweli?” aliuliza Winfrida huku akimwangalia Godwin kwa macho ya mshangao.

“Ndiyo! Kila siku unanikuta napiga debe! Inakuwaje unaniuliza kama mimi ni mpiga debe?” aliuliza Godwin huku akimwangalia Winfrida.

“Unaonekana tofauti!”

“Kivipi?”

“Unazungumza Kiingereza kizuri sana, kunishinda mimi! Inakuwaje uwe mpiga debe tena ukionekana kuwa na maisha ya kimasikini sana?” aliuliza Winfrida huku akiendelea kushangaa.

Godwin hakujibu kitu, akanyamaza, akakiinamisha kichwa chake chini, alipokiinua, macho yake yalikuwa mekundu na baada ya sekunde kadhaa machozi yakaanza kumtiririka mashavuni mwake kuonyesha kuchomwa na swali alilouliza Winfrida.

“What has happened to you?” (nini kimetokea?) aliuliza msichana huyo.

“I will tell you!” (nitakwambia)

“When?” (lini?)

Godwin hakujibu kitu, alichomwambia Winfrida ni kumuacha kwani alitakiwa kuendelea na kazi yake kama kawaida. Msichana huyo alikuwa na maswali mengi, akahisi kulikuwa na kitu kikubwa kilichotokea kwa mwanaume huyo.

Alitaka kufahamu, kila alipokutana naye swali lake lilikuwa lilelile kwamba ni kitu gani kilitokea mpaka kuishi maisha aliyokuwa akiishi. Godwin hakumjibu kitu, kila siku alimwambia kwamba angemwambia japokuwa hakumwambia siku ambayo angemueleza ukweli kuhusu maisha yake.

Baada ya kuwa karibu kwa miezi miwili huku kila siku msichana huyo akimuuliza swali hilohilo, hatimaye akamwambia kwamba alikuwa tayari kumuhadithia kila kitu ambacho kilitokea kwenye maisha yake.

Akamchukua na kumpeleka katika kibanda kimoja chakavu, akakaa naye mahali hapo. Winfrida alikuwa na kiu ya kutaka kusikia kile kilichokuwa kimetokea katika maisha ya mwanaume huyo.

“Godwin! Niambie ukweli! Nini kimetokea mpaka kuwa mpiga debe na masikini hivyo?” aliuliza Winfrida huku akimwangalia Godwin ambaye hapohapo akaanza kufungua vifungo vya shati lake na kisha kumuonyeshea maneno yaliyoandikwa kwa tattoo ya korosho, maneno yaliyosomeka ‘I WANT TO KNOW WHO KILLED MY DAD, MOM AND SISTER’ (ninataka kumjua aliyemuua baba, mama na dada yangu)

Winfrida alipoyasoma maneno hayo, akashtuka, akahisi kabisa kwamba kulikuwa na simulizi ndefu juu ya maisha ya mwanaume huyo. Akajiweka vizuri na kumuuliza kama alikuwa tayari kumwambia kuhusu kile kilichotokea katika maisha yake.

“Nitakwambia! Nitakuhadithia kila kitu,” alisema Godwin, akaingiza mkono mfukoni na kutoa kitambaa kichafu na kuanza kuyafuta machozi yake. Akajiweka sawa kwa lengo la kumuhadithia msichana huyo kila kitu kilichotokea, historia kali iliyomchoma moyo wake kila siku.

***

25/10/1998, Dar Es Salaam

Hakukuwa na utulivu nchini Tanzania, kila mtu alikuwa kwenye presha kubwa juu ya uchaguzi mkuu ambao ulikuwa ukienda kufanyika mwaka huo.

Kila mtu mitaani alikuwa akizungumza lake, wapo waliokuwa wakikipenda chama tawala, Labour Party ambacho kilisimamisha mgombea wake mashuhuri, Ibrahim Bokasa lakini pia wapo waliokuwa wakikipenda chama cha upinzani, Tanzania National Party ambacho kilimsimamisha mwanaume mwenye nguvu, mvuto, aliyependwa kila kona, Melkizedek Mapoto.

Kwa mwaka huo, uchaguzi ulikuwa na nguvu kuliko miaka mingine ya nyuma, kila mtu alikuwa na uhakika kwamba huo ndiyo ungekuwa mwaka wa mwisho kwa chama tawala kuwa madarakani, kila mmoja aliamini kwamba Bwana Mapoto ndiye angekuwa rais mpya wa Tanzania kwani kila kona, jina lake lilikuwa likiimbwa huku watu wakipeperusha bendera ta chama chake.

Kila mtu aliyekuwa katika chama tawala aliogopa, waliuona mwisho wao, wananchi ambao kila siku walikuwa wakiwapigia kura kwa mwaka huo wakabadilika, hawakutaka kuongozwa na chama tawala tena, walihitaji kuwa na mabadiliko na hakukuwa na mtu ambaye alionekana kuwa na nguvu ya kuwaletea mabadiliko zaidi ya Bwana Mapoto.

Kila alipokwenda mikoani kwa ajili ya kampeni, alipokelewa vizuri, wakinamama walitandika kanga chini na kumtaka kukanyaga juu, wazee wa kimila hawakukubali, wao, walimchinjia ng’ombe na kumtabiria kwamba yeye ndiye angekuwa rais mpya wa nchi hiyo kwani watu walichoka kunyanyaswa na kwa kipindi hicho hakukuwa na kingine walichokihitaji zaidi ya mabadiliko tu.

Watu wengi wa Chama cha Labour wakajitoa kwenye chama chao na kujiunga na Chama cha Tanzania National Party ambapo waliamini kwamba kulikuwa na mabadiliko ya kweli ambayo yangewatoa katika maisha ya umasikini waliyokuwa wakiishi na kuwapeleka katika nchi ya maziwa na asali.

Hali ilikuwa ni ya mvurugano ndani ya Chama cha Labour, hakukuwa na aliyeona dalili za ushindi mbele yao, Bwana Mapoto alitisha, alikuwa akitikisa kila sehemu na kwenye kila kona ya nchi ya Tanzania, jina lake liliimbwa kwa shangwe huku wengine wakisema kwamba hatimaye Mungu alisikia kilio chao na kumleta mtu aliyeahidi kuleta mabadiliko na kuipeleka Tanzania kuwa nchi yenye nguvu barani Afrika.

“Nimechanganyikiwa kwa furaha! Leo nimemgusa Mapoto,” alisema mwanaume mmoja, alikuwa amevalia kofia ya chama hicho, fulana, kwa jinsi alivyoonekana kuwa na uzalendo na chama hicho, alikuwa kama mtu aliyekunywa maji ya bendera.

“Natamani sana na mimi nikamguse. Huyu ndiye mgombea wa ukweli, ndiye rais wetu ambaye ataweza kututoa hapa tulipokuwa. Maisha yamekuwa magumu sana kisa Labour Party! Huu ndiyo mwisho wao, yaani nikifika kwenye chumba cha kupigia kura, lazima niwachinje,” alisema jamaa mwingine huku akionekana kuwa na kiu ya kuhitaji mabadiliko.

Chama tawala kikachanganyikiwa, hawakuamini kile kilichokuwa kikiendelea. Hawakuona mahali pa kutokea, walizoea kwenda vijijini ambapo waliamini kwamba huko wangechukua watu wengi, kwa mwaka huo kila mmoja aliwashtukia, na walipokanyaga mguu tu, walikuwa wakizomewa na wakati mwingine kupigwa mawe.

“Jamani! Hali imebadilika, hebu zungumza na rais mstaafu,” alisema mwenyekiti wa kampeni, Bwana Edward Mrope.

Simu ikapigwa kwa rais aliyemaliza muda wake, alipewa taarifa juu ya hali ilivyokuwa imebadilika. Kule vijijini ambapo ndipo walikuwa wakipategemea, palibadilika na kila walipokanyaga, ni jina la Mapoto tu ndiyo lililokuwa likisikika.

“Unasemaje?” aliuliza rais mstaafu.

“Huku hali ni mbaya, kila kona Mapoto, Mapoto, Mapoto tu,” alisema mwenyekiti wa kampeni maneno yaliyomfanya rais huyo kushtuka.

“Haiwezekani!”

“Huo ndiyo ukweli mkuu! Tufanye nini?”

“Nipigie simu baada ya dakika tano,” alisema rais mstaafu na kukata simu.

Alichanganyikiwa, hakuamini, hali ilikuwa imebadilika, moyo wake ulijuta kwani kwa mambo aliyokuwa ameyafanya, mambo ya ubabe, ya kujiona kwamba yeye ndiyo yeye ndiyo ambayo yalikuwa yakikigharimu chama hicho na kuona hawafai kabisa.

Hakutaka kukubali, hakutaka kuona chama kikimfia mikononi mwake, kwa haraka sana akachukua simu yake na kumpigia katibu wa chama hicho, Bwana Idrisa Awadh na kumwambia kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima kuhakikisha kwamba chama chao kinapata ushindi kwa namna yoyote ile.

“Hakuna tatizo! Hilo suala niachie mimi! Wewe wala usiwe na hofu na wananchi, sisi ndiyo tunaishikilia nchi hii na kujua ni wapi pa kufanyia kazi,” alisema katibu huyo.

“Nakuamini!”

“Siwezi kukuangusha mkubwa. Kama ulivyoniamini mwaka 1993, unatakiwa kuniamini na sasa hivi,” alisikika katibu huyo.

Kidogo moyo wake ukapata ahueni, alimwamini katibu wake, alikuwa mtu machachari aliyeweza kucheza na masanduku ya kura, kwake, hiyo ilikuwa ni kazi ndogo na kama alivyofanya mwaka 1993 ndivyo ambavyo angefanya mwaka huo.

Chama cha Tanzania National Party kiliendelea kusonga mbele, kwa kipindi hicho walijizatiti vijijini, waliamini kwamba watu wote wa mjini walikuwa watu wao kwani kila kona kulitawala bendera zao na kila mtu aliyekuwa akiuliza, alionyesha ishara ya mabadiliko kwamba alihitaji ladha mpya ya chama na si ileile ya miaka yote.

Bwana Mapoto akaonekana kuwa mwiba mkali kwa chama tawala, kila alipopita, watu walipomuona, wengine walizimia, kwenye kila mkutano wa kampeni watu walijaa huku neno mabadiliko likisikika kila kona.

“Nu nene ndinghaya uyu ng’wenekele (na mimi namtaka huyuhuyu) alisema mwanamke aliyekadiriwa kuwa na miaka themanini, hata naye alihitaji mabadiliko.

“Nu nene mama nanoga na kikalile iki,” (hata mimi bibi! Nimechoka na maisha haya) alisema msichana mmoja huku wakimwangalia Mapoto aliyekuwa jukwaani katika Uwanja wa CCM Kirumba alipokuwa akihutubia.

Kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele, hali iliendelea kuwa ngumu kwa chama tawala, hata kabla siku ya kupiga kura haijafika, tayari walijiona kushindwa na ilitakiwa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba wanaubakiza urais huo mikononi mwao.

“Nimekuja na sera moja tu ya kutaka mabadiliko. Mmekuwa hampati maisha mazuri kwa kipindi gani? Nchi yetu imekuwa ikichekwa kwa kipindi kirefu, tuna kila sababu ya kuwa na uchumi mkubwa, tuna madini ambayo hata sehemu nyingine hakuna, tuna vyanzo vingi sana vya mapato. Mungu hakuwa mjinga kutupa mbuga za wanyama, madini na vitu vingine, alikuwa na maana ila kwa sababu ya watu wachache tu, nchi haikusonga mbele. Huu ni muda wenu kuchagua, kama mngependa kunywa chai bila sukari au kula asali,” alisema Bwana Mapoto kwa sauti kubwa.

“Tunataka asaliiiiiiiiiiiiiii…” uliitikia uwanja mzima.

“Basi msifanye makosa tarehe 19!” alisema Bwana Mapoto na kuibua makofi ya shangwe uwanjani hapo.



“Mke wangu, unaamini kwamba tunakwenda kukaa ikulu?” aliuliza Bwana Mapoto huku akimwangalia mke wake aliyekuwa akimwangalia muda wote.

“Naamini hilo! Ila sidhani kama hawa wa chama tawala watakubali,” alisema mkewe, mwanamke mrembo aliyeitwa kwa jina la Rosemary.

“Watakubali tu! Kwa kipindi hiki tutawazuia kwa kila hali kuhakikisha hakuna wizi wa kura, tutaziba njia zote ambazo zinaonekana kutoa mwanya mkubwa wa wizi wa kura.”

“Kama mtaziba njia zote, naamini kwamba tutaingia huko,” alisema Rosemary huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.

“Ninaumia sana nikiwaona Watanzania wanateseka, wanaishi katika maisha yenye maumivu makubwa. Mungu si mpumbavu kutuzawadia madini, mbuga za wanyama na mlima Kilimanjaro, naamini kwamba alitaka watu wanufaike na kujivunia maisha yao, lakini cha kushangaza, nchi hiyohiyo yenye kila kitu ndiyo nchi masikini. Nitapambana! Nitapambana mke wangu!” alisema Mapoto huku akionekana kuwa mtu mwenye maumivu makubwa moyoni mwake.

Alimaanisha alichokuwa akikizungumza, alihitaji kuibadilisha Tanzania, aliyaona maumivu ya Watanzania, jinsi walivyokuwa wakiteseka, hakutaka kuendelea kuangalia maumivu hayo, alitaka kupambana kwa hali na mali kuhakikisha kwamba kila kitu kinakuwa vizuri na Watanzania waanze kujivunia nchi yao.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Mbali na kuwafikiria Watanzania, aliwafikiria watoto wake wawili, Godwin na Irene waliokuwa na miaka saba. Alitaka kuwapa maisha bora, alijua kwamba kupitia wao angepata wajukuu ambao aliamini kwamba kama angeyatengeneza maisha yao basi hata hao wajukuu wangekuja kuishi vizuri.

Alikuwa katika mapambano makubwa, hakutaka kushindwa, hakutaka kurudi nyuma, mbele yake aliyaona mafanikio makubwa, aliona jinsi Watanzania walivyokuwa wakimuunga mkono, aliamini kwamba Watanzania wote hao wangempigia kura kwa sababu kila mtu kwa kipindi hicho alihitaji mabadiliko.

“Nitapambana kwa ajili ya Godwin na Irene,” alisema Mapoto.

Wakati akizungumza na mkewe, watoto wake walikuwa shuleni, walikuwa miongoni mwa watoto waliokuwa wakisoma katika shule ya watoto matajiri na viongozi serikalini, St. Marie iliyokuwa Masaki jijini Dar Es Salaam.

Alitaka watoto wake wapate elimu bora kwa ajili ya maisha yao ya baadaye na kila siku dereva wao alikuwa na jukumu la kuwapeleka shule na kuwarudisha nyumbani.

Kila siku Mapoto alipata muda wa kukaa na watoto wake na kuzungumza nao. Aliwapenda, alijitahidi sana kuwaweka karibu nao kwani aliamini kwa kufanya hivyo ingekuwa rahisi kugundua matatizo waliyokuwa wakikutana nayo kila wanapokuwa shuleni au sehemu nyingine.

Urafiki mkubwa ukatawala, watoto wake walikuwa kila kitu katika maisha yake. Alijiahidi kwamba ni lazima ailinde familia yake, hakutaka mtu yeyote yule aiingilie, aliithamini na kuipa nafasi ya kwanza maishani mwake.

Wakati Irene akiwa mzungumzaji sana, mtundu lakini ilikuwa tofauti kwa Godwin, alikuwa kijana mpole, mkimya ambaye hakuwa mzungumzaji kabisa. Kila wakati alionekana kama mtoto aliyekuwa na mambo mengi kichwani mwake, alipokuwa akionewa au hata kukasirishwa, hakuwa akikasirika, alipendwa na wazazi wake kwa sababu ya hali ya upole aliyokuwa nayo.

“Godwin! Unataka kuwa nani ukikua?” aliuliza baba yake.

“Nataka kuwa mchungaji!” alijibu.

“Kwa nini?”

“Nataka niombee watu wapone kama Reinhard Bonnke,” alijibu Godwin huku akitoa tabasamu pana.

Hicho ndicho alichokuwa akikitaka, kila siku walipokuwa nyumbani, baba yake aliwawekea televisheni ya Praise And Worship kwa ajili ya kuangalia mahubiri na kujifunza neno la Mungu.

Kila alipokuwa akimuona Mwinjilisti Reinhard Bonnke akihubiri, moyo wake ulisisimka, alifurahia huku naye akitamani sana kuwa kama mwinjilisti huyo ambaye alikuwa akivuma sana duniani miaka hiyo.

“Na wewe Irene?”

“Niongee jukwaani kama wewe!”

“Unamaanisha mwanasiasa?”

“Eeeh!”

“Wote mtafanikiwa. Mtakuwa kama mnavyotaka kuwa,” alisema Mapoto huku akiwaangalia watoto wake.

Kampeni hazikuisha mitaani, mara kwa mara alikuwa akizungumza na wananchi na kuwaomba kura zao kwani alikuwa na ndoto za kuingia ikulu na kuibadilisha Tanzania ambayo kadiri miaka ilivyozidi kwenda mbele ndivyo ilivyokuwa ikiharibika kutokana na viongozi wengi kutumia nafasi zao kupiga madili makubwa ya pesa.

Viongozi wa Chama cha Labour Party hawakutaka kutulia, waliweka vikao vingi wakijadili namna ya kumzuia Mapoto ambaye alionekana kuwa mwiba wa kuotea mbali.

Kwenye kila kikao walichokuwa wakikaa na kupanga mipango, walishtukia kuiona mipango yao katika magazeti na masikioni mwa watu hali iliyowaonyeshea kwamba kulikuwa na watu ndani ya chama ambao walikuwa wakishirikiana na Chama cha Tanzania National Party ambao walitoa kila mipango waliyokuwa wakiipanga.

Rais mstaafu aliliona hilo hivyo alichokuwa akikifanya ni kumuita katibu wa chama na mwenyekiti wa kampeni na kuzungumza nao. Walipanga mipango lukuki lakini mpango mkubwa ambao ulitawala vichwani mwao ni namna ya kuiba kura kwani waliamini kwamba kama wasingefanya hivyo basi Mapoto angeweza kuingia ikulu.

“Kuna mchezo nitaucheza,” alisema Hawadh.

“Upi?”

“Sisi si ndiyo tutakaotoa fedha za kutengeneza karatasi za kupigia kura?”

“Ndiyo!”

“Basi tutacheza na karatasi hizo na matokeo utayaona,” alisema Awadh.

Huo ndiyo ulikuwa mpango uliotakiwa kufanywa, walijua dhahiri kwamba wasingeweza kushinda uchaguzi huo kutokana na Watanzania wengi kumkubali Mapoto hivyo walichokitaka ni kucheza na karatasi za kura tu.

Siku zikakatika mpaka siku ya mwisho ya uchaguzi ambapo watu wengi wakajitokeza katika vituo vya kupigia kura huku idadi kubwa wakiwa na dhamira ya kukiondoa chama tawala madarakani.

Kura zikapigwa, kwa sababu kila mtu aliogopa kura kuibwa, wapo waliokesha huku wakifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea, mpaka kura zilipopakizwa ndani ya magari na kuondolewa katika maeneo ya kupigia kura, kila mmoja alikuwa akifuatilia.

Siku hiyo, Mapoto na viongozi wengine wa Chama cha Tanzania National Party walikuwa makao makuu wakifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Waliwasambaza vijana wao sehemu mbalimbali na kila kura za vituo zilizokuwa zikitangazwa waliwatumia matokeo haraka sana.

Kila mmoja akaona kwamba hiyo ndiyo nafasi waliyokuwa wakiisubiri kwani kwa maeneo ya mijini, hakukuwa na wasiwasi, waliamini kwamba walifanikiwa kwa asilimia mia moja, kazi kubwa ilikuwa ni kwa vijijini ambapo waliamini kwamba kama wasingekuwa makini, basi huko wangeweza kupigwa vibaya.

“Vipi huko?” aliuliza Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania National Party, Bwana Luzukumi.

“Huku poa. Mwanza nzima tumekimbiza! Tena taarifa zinasema Kanda ya Ziwa yote tumetoka kidedea,” aliongezea mtoa taarifa huyo.

“Safi sana!” alisema Luzukumi pasipo kufahamu kwamba upande wa pili, chama tawala walikuwa makini mno, walikuwa tayari kupoteza uchaguzi wowote ila si wa mwaka huo, hivyo walijipanga vilivyo. Wakati wao wakipigia mahesabu 12345 wenzao walihesabu ABCDE.

“Tumeuangangusha mbuyu,” alisikika katibu wa Chama cha Labour Party akimwambia rais mstaafu.

“Unasemaje?”

“Fungua televisheni uanze kufuatilia,” alisema Awadh huku uso wake ukiwa na tabasamu tele. Harakaharaka rais akafungua Global TV na kuanza kufuatilia.





Hakukuwa na mtu wa Chama cha Labour Party ambaye alikuwa radhi kuona nchi ikienda upande wa wapinzani, walikuwa tayari kupoteza kila kitu, hata familia zao ziteketee lakini si kukubali kuona nchi ikichukuliwa na chama pinzani.

Wakati chama pinzani cha Tanzania National Party wakihangaika na wananchi kwamba wafanikiwe kuichukua nchi ya Tanzania wenzao walichokifanya ni kucheza na karatasi za kura.

Walijua kwamba serikali ndiyo ingesimamia mchakato mzima, kwao, chama chao ndicho kilikuwa serikali yenyewe hivyo walichokifanya ni kuamuru zitengenezwe karatasi ambazo zitazifanya kura za wapinzani wote ziende upande wa pili, zifanye hivyo baada ya dakika thelathini.

Hilo halikuwa tatizo, Wachina wakaingia mchezoni na kufanya kazi hiyo ambayo kwao haikuwa na ugumu wowote ile. Waliifanya ndani ya siku tatu, yale masanduku yaliyokuja na karatasi za kupiga kura yakachomwa moto na kuletwa mengine, hayo yote yalifanyika kisiri na hakukuwa na mtu aliyejua.

Siku ilipofika, watu wakaingia vyumbani, wakapiga kura kwa nguvu zote na kila walipotoka walionyesha alama ya kuchinja kama ishara ya kuwachinja Tanzania Labour ndani ya chumba kile pasipo kugundua mchezo mzima uliokuwa umechezwa.

“Nimemchinja! Sikuwa na huruma. Nilipofika, nikamwangalia Ibrahim Bokasa na kumwambia kwamba sasa hivi na wewe unatakiwa kuwa raia wa kawaida kama mimi, baada ya hapo, nikapiga tiki ya uhakika kwa Mapoto,” alisema jamaa mmoja, si yeye tu, kila mtu alisema kwamba ndani alimpa kura Mapoto kwani ndiye aliyeonekana kuwa mtu sahihi.

Mchakato wa kura ukafanikiwa na hatimaye baada ya siku mbili watu kujiandaa kupokea matokeo yao. Kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba hiyo ilikuwa siku yao ya ukombozi kwani kila mtu alikuwa amechoka na kwa moyo mmoja alitaka kusikia Mapoto akitangazwa na kuwa rais wa nchi hiyo.

Kila mmoja akawasha televisheni na kuanza kumwangalia mkurugenzi wa tume ya uchaguzi jinsi alivyokuwa akitangaza matokeo. Alizungumza kwa sauti ya upole, tabasamu pana lilikuwa usoni mwake hali iliyowapa matumaini wananchi kwamba siku hiyo ndiyo ilikuwa siku ya ukombozi ambayo ingekuwa historia kizazi mpaka kizazi.

Matokeo yalianza kutangazwa, kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele, hali ya hewa ilizidi kubadilika, katika majimbo yote makubwa ambayo yalikuwa na watu wengi, Bokasa aliongoza kwa asilimia nyingi na kummwaga mpinzani wake kwa kura zisizokuwa na idadi.

Kila mmoja alikunja sura yake, wengine wakahisi labda matokeo yaliyokuwa yakitangazwa na mkurugenzi wa tume yalikuwa ya uongo lakini hawakujua chanzo kilikuwa nini, hawakujua kwamba mchezo huo ulichezwa hata kabla ya masanduku ya kura kumfikia mkurugenzi huyo.

“Haiwezekani! Haiwezekani kushindwa uchaguzi huu!” alisikika jamaa mmoja akipayuka, aliongea kwa sauti kama mtu aliyekuwa amechanganyikiwa na kile alichokuwa akikisikia.

Si yeye tu, kila mtu aliyekuwa mahali hapo alichanganyikiwa. Kwa jinsi matokeo yalivyotangazwa, kwa Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na mikoa mingine mikubwa, ni Chama cha Labour Party ndicho kilichokuwa kimeongoza kwa kura nyingi.

Watu hawakukubali, hawakutaka kuona wakishindwa, hawakukubali kabisa kuona Chama cha Labour Party kikiendelea kuongoza nchi na wakati kila mtu hakuwa akikitaka, kila mmoja alitaka kuona kikiondoka madarakani kama vyama vingine katika nchi nyingine.

Vijana wakajipanga, walitaka kuingia mitaani kwa ajili ya kuandamana, hawakutaka kukubali, waliyataka mabadiliko kwa karatasi lakini ilishindikana na kitu pekee walichokitaka ni kuyaleta mabadiliko kwa kupitia silaha.

Polisi walipewa taarifa juu ya maandamano makubwa yaliyotaka kufanyika, japokuwa watu walitangaziwa kutokufanya hivyo lakini hawakutaka kukubali, wakajipanga vijana zaidi ya elfu mbili na kuingia mitaani.

Wote walikuwa na kaulimbiu ya kuitaka nchi yao. Hawakuogopa polisi, walisonga mbele kuelekea ikulu kwamba hata kama hawakupewa nchi yao basi ilikuwa ni bora kukosa wote, kama vipi wachome moto ikulu.

“Watu wote mnatakiwa kurudi nyumbani, hamruhusiwi kusogea mbele zaidi,” ilisikika sauti kwenye kipaza sauti, aliyekuwa akizungumza alikuwa Kamanda Mkuu Kanda ya Dar es Salaam, Abou Ishimeri.

“Tunataka nchi yetu! Yaani msituzingue kabisa. Leo ndiyo mtakiona,” alisema mwanaume mmoja, mkononi mwake alikuwa na kidumu kilichokuwa na mafuta ya petroli.

Kila mmoja alikuwa na nia moja moyoni mwake, kwa kipindi hicho hakukuwa na aliyejali kama polisi waliokuwa mbele yao walikuwa na mabomu ya machozi na risasi za moto, kitu walichokiangalia ni kufanya maandamano ya kuelekea ikulu na kuichoma moto.

“Tufanye nini?” aliuliza polisi mmoja.

Simu ikapigwa mpaka kwa Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Andrew Kizota na kumwambia kile kilichokuwa kikiendelea ambapo kamanda huyo akawaambia kwamba huo ulikuwa ni muda wa kutumia mabomu ya machozi, na kama kungekuwa na ulazima wa kutumia risasi za moto basi ziwe kupiga hewani na si kuwapiga raia.

Hilo ndilo lililofanya, zikapigwa risasi tatu hewani na kupigwa mabomu manne ya machozi kuelekea kwenye kundi lile la watu. Kila mtu aliogopa, milio ya risasi ikawachanganya na kwa jinsi moshi mkubwa ulivyokuwa ukitanda ndiyo ukawavuruga kabisa na kuanza kukimbia hovyo.

Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi ya polisi kufanya kile walichotakiwa kufanya, wakawafuata raia na kuanza kuwapiga hali iliyoanzisha mtafaruku mkubwa mahali hapo.

****

Mapoto na viongozi wengine wa Chama cha Tanzania National Party walichanganyikiwa, hawakuamini kile kilichokuwa kimetokea kwamba waliangushwa vibaya katika uchaguzi ule na wakati walikuwa na idadi kubwa ya watu waliotaka mabadiliko, watu waliojitoa kwa ajili yao, kupambana mpaka tone la mwisho la jasho.

Walikaa ndani ya jengo la makao makuu ya chama chao na kujifikiria walishindwa wapi. Walisikia kwamba waliongoza kwenye mchakato mzima wa kupiga kura mikoani lakini mwisho wa siku wakaambiwa kwamba walishindwa uchaguzi huo.

“How?” (kivipi?) aliuliza Mapoto huku akimwangalia kila mmoja ndani ya chumba walichokuwa.

Hakukuwa na mtu aliyejibu kitu, kila mmoja alichanganyikiwa, hakukuwa na maboksi ya kura za wizi waliyokuwa wameyakamata, walihakikisha kila kona kunakuwa na ulinzi lakini cha kushangaza, walishindwa uchaguzi, walishindwaje? Ilikuwaje? Nini kilitokea? Je, kweli wananchi waliwabadilikia? Kila kitu walichokuwa wakijiuliza mahali hapo, walikosa jibu kabisa.

Wakati kila mmoja akiwa na huzuni mahali hapo tena huku ukimya ukiwa umetawala kwa muda mrefu, mara simu ya Mapoto ikaanza kuita, hakutaka kuipokea kwani alikuwa amechanganyikiwa kupita kawaida, kila mtu alikuwa akimwangalia kwa mtazamo wa kumtaka angalie simu yake kuona nani alikuwa akimpigia, akaingiza mkono mfukoni na kuitoa simu hiyo.

Jina la Bokasa lilikuwa likionekana kwenye kioo cha simu yake. Hasira kali ikamkamata usoni mwake, akamwangalia kila mtu mule ndani na kuwaonyeshea simu ile ambapo wote kwa pamoja wakamwambia kwamba angepokea na kusikiliza mwanaume huyo alitaka kuzungumza naye nini.

“Halo!” aliita mara baada ya kupokea simu hiyo.

“Halo! Pole sana Mapoto. Najua unajisikia vibaya, najua umeumia sana, hizi ni siasa ambazo tunatakiwa kuachana nazo kwa muda na kuziweka akili zetu kukubaliana na kilichotokea,” alisikika Mapoto.

“Niambie nikusaidie nini?”

“Ninataka kuonana na wewe. Ninataka tuzungumze. Tusizungumze kama wapinzani, hebu tukutane na tuzungumze kama Watanzania! Nchi hii ni kubwa, pasipo mimi na wewe kudumisha urafiki, Watanzania watakuwa kwenye hali mbaya sana. Ninataka tukubaliane kitu kimoja,” alisikika Bokasa.

“Tukubaliane kitu kimoja?”

“Ndiyo!”

“Wewe na mimi?”

“Ndiyo!”

“Inawezekana vipi?”

“Ni kwa sababu sisi wote ni Watanzania, sisi wote ni ndugu. Ninataka tulifanye hili kwa faida ya taifa na si mimi na wewe,” alisema Bokasa.

“Bokasa…”

“Nakuomba Mapoto, naomba nionane nawe. Kuna jambo nataka kulizungumza,” alisema Bokasa.

“Nitaangalia,” alisema Mapoto na kukata simu.

Jambo hilo likazua mjadala mahali hapo, walikuwa kwenye maumivu makali, waliamini kwamba waliibiwa kura japokuwa hawakujua hizo kura ziliibwa kwa mtindo gani.

Kitendo cha Mapoto kutakiwa kuonana na Bokasa kilizua gumzo mahali hapo kwa kuhisi kwamba mtu huyo alitaka kumuua ili kuizima nyota ya upinzani ambayo ilionkana kuwa tishio kubwa.

“Ninahofu watakuua!” alisema katibu wa chama hizo, Bwana John Pondamali.

“Acha tu niende!”

“Sawa. Ila hutakiwi kunywa maji wala chai! Hutakiwi kufanya chochote kile ukifika huko zaidi ya kumsikiliza,” alisema mwenyekiti wa chama hicho, Bwana Edward.

“Sawa. Ila ningependa kwenda na walinzi hata wawili!” alisema Mapoto.

“Haina shida!”

***

Kila mmoja alikuwa na hofu, waliamini kabisa kwamba kulikuwa na kitu ambacho Bokasa alitaka kukifanya, hasa kumuua Mapoto ambaye alionekana kuwa mwiba wa kuotea mbali.

Viongozi wa Chama cha Tanzania National Party walikubaliana naye lakini ilikuwa ni lazima aende huko akiwa na vijana wengine, walihisi kwamba kungekuwa na mchezo mchafu ambao ungeweza kuchezwa kitu ambacho hawakutaka kuona kikitokea.

Aliporudi nyumbani, Mapoto alionekana kuwa na mawazo tele, kichwa chake kiliuma mno, hakuamini kama kweli alikosa urais, alikubalika kila kona, kila alipopita, jina lake liliimbwa, alionekana kuwa tumaini la mwisho kwa wananchi wa Tanzania kwani chama ambacho kilikuwa madarakani kipindi hicho hakikufanya kitu, yeye aliutaka urais kwa kuwa aliamini kwamba angeibadilisha Tanzania kiuchumi na kuifanya kuwa na hadhi kubwa kama ilivyokuwa kipindi cha Mwalimu Nyerere.

Mkewe, Rosemary akamfuata na kuanza kumfariji kwa kumwambia kwamba kukosa urais si mwisho wa kila kitu, iliwezekana kwamba Mungu alikuwa akimwandaa kwa miaka mitano ijayo na si kwa kipindi hicho, kama alipangwa kuwa mtetezi wa Watanzania, mtetezi wa wanyonge basi ilikuwa ni lazima kutokea hata kama isingekuwa kipindi hicho.

“Hutakiwi kuwa na hofu! Wewe bado ni mtetezi wa wanyonge, naamini Mungu anakuandaa, unachotakiwa kufanya ni kuvuta subira,” alisema Rosemary huku akimwangalia mume wake alioyeonekana kuwa na mawazo tele.

“Naamini mke wangu!”

“Basi jitie nguvu! Bado wewe ni mshindi,” alisema Rosemary.

Moyo wake ukawa na nguvu, akasimama na kumkumbatia mke wake, japokuwa alikuwa na marafiki wengi lakini mkewe ndiye aliyekuwa kila kitu, kwenye matatizo, alikuwa faraja yake, kwenye maumivu ya moyo, alikuwa furaha yake na hata kwenye hasira, alikuwa tabasamu lake.

Wakati hayo yakiendelea, Bokasa akampigia simu Mapoto na kumwambia kwamba wangekutana mara baada ya kuapishwa kwani kulikuwa na mambo mengi waliyotaka kuzungumza kwa faida ya Watanzania kitu ambacho kwa Mapoto hakikuonekana kuwa tatizo lolote lile.

“Dad! What is wrong with you?” (baba! Una nini?) aliuliza Godwin huku akimwangalia baba yake.

“I have nothing! It is time to sleep,” (sina kitu! Ni muda wa kulala) alisema Mapoto.

“Can you read for me a story about rabbit and the Queen Leah?” (unaweza kunisomea hadithi ya sungura na Malkia Leah?) aliuliza Godwin.

“Okey! Let me take you to bed,” (sawa! Ngoja nikupeleke kitandani)

Akambeba Godwin na kumpeleka kitandani ambapo huko akaanza kumsomea kitabu cha hadithi za watoto mpaka pale alipolala na Mapoto kutoka chumbani.

Japokuwa walikuwa na umri mdogo lakini Godwin na dada yake, Irene walikuwa watoto wenye akili sana darasani. Walikuwa na uwezo mkubwa kiasi kwamba hata walimu wenyewe walikuwa wakishangaa.

Shuleni, hawakuwa wakishika nafasi zaidi ya mbili za juu. Katika kipindi chote walikuwa wakipokezana kushika nafasi ya kwanza. Katika kipindi hiki aliposhika Godwin, kipindi kijacho alishika Irene.

Walikuwa na upinzani mkubwa, walisoma sana kiasi kwamba walimu walihisi kabisa maisha ya mbele ya watoto hao yangekuwa yenye mafanikio makubwa. Hakukuwa na somo ambalo hawakufanya vizuri, kwenye Hesabu, Kiingereza na masomo mengine walikuwa moto wa kuotea mbali.

Wazazi wao walijisikia faraja, kila walipokuwa wakienda shule kwenye vikao vya wazazi walipokea sifa mbalimbali kuhusu watoto wao jinsi walivyokuwa wakifanya vizuri na kuwashangaza walimu wao.

“They are very bright,” (wana akili sana)

“Are you sure?” (una uhakika?) aliuliza mwalimu mwingine.

“Yes! Apart from their brightness, they speak fluent English,” (Ndiyo! Ukiachana na akili zao, wanazungumza Kiiingereza kizuri sana) alisema mwalimu huyo.

Kila kona shuleni hapo sifa zilikuwa kwa watoto hao, walikuwa na uwezo mkubwa sana darasani, walifanya vizuri katika kila masomo kiasi kwamba kila mwalimu alitamani kuona watoto hao wakiwa watoto wao.

Katika somo la Hesabu, walijua kuhesabu kwa haraka zaidi ya wanafunzi wengine, walikuwa wanafunzi wa kwanza kujua kusoma kuliko wanafunzi wengine. Uwezo wao wa akili uliwachanganya walimu wengi mpaka kujidharau kwa kuhisi kwamba watoto hao hawakustahili kabisa kuzaliwa nchini Tanzania.

Baada ya wiki moja, Bokasa akaapishwa na kuwa rais wa Tanzania. Si watu wote waliofurahi, zaidi ya asilimia themanini ya Watanzania walichukia kwa kuwa waliamini kwamba mtu huyo asingeweza kuwaletea mabadiliko waliyokuwa wakiyataka.

Wengi walilalamika lakini hakukuwa na mtu aliyekuwa na uwezo wa kubadilisha matokeo, Bokasa akawa rais wa Tanzania kitu kilichozungumzwa sana barani Afrika kwamba iliwezekanaje mtu aliyekuwa na mashabiki wengi kama Mapoto akose nafasi hiyo.

“Mkuu! Hali naona si nzuri kwa chama pinzani,” alisema mshauri wa Rais Bokasa.

“Najua watu wanalalamika sana ila ninachoshukuru hakuna mtu anayejua ni kwa jinsi gani mchezo umechezwa. Ninahitaji kufanya kitu kimoja, kama Mapoto ataendelea kubaki hapa Tanzania, anaweza kujijenga zaidi na kuleta upinzani mkubwa mwaka 2003. Nahisi kuna kitu ninahitaji kufanya,” alisema Rais Bokasa.

“Kitu gani?”

“Nataka nimpe ubalozi nchini Nchini India! Akawe balozi huko, akasahaulike katika vichwa vya Watanzania ili hata mwaka 2003 usiwe wa upinzani mkubwa,” alisema Bokasa huku akimwangalia mshauri wake.

“Ni wazo zuri ila sidhani kama atafurahi kuwa balozi nchini humo,” alisema mshauri huo.

“Wewe unahisi wapi ataweza kukubaliana napo?”

“Marekani!”

“Basi haina shida.”

Rais Bokasa akampigia simu Mapoto na kuomba kuzungumza naye, hilo halikuwa tatizo, kabla ya kwenda huko Mapoto akatoa taarifa kwa viongozi wa chama hicho ambao walimpa vijana wawili na kwenda nao ikulu.

Walipofika, akaomba kukaa naye sehemu, wawe wawili, wazungumze kile ambacho alikuwa amemuitia. Hilo halikuwa tatizo, wakaelekea katika bustani iliyokuwa hapo ikulu na kuanza kuzungumza.

Alimgusia suala lote la kuwa balozi nchini Marekani. Mara ya kwanza kwa Mapoto ilikuwa ngumu kukubaliana naye, hakutaka kuondoka nchini Tanzania, alijua kwamba yeye ndiye angekuwa rais wa nchi hiyo miaka mitano mbele, hivyo alitaka kuendelea kubaki ili ajiimarishe kwa miaka hiyo.

“Mapoto! Najua unatamani, lakini kumbuka kwamba sasa hivi ni kipindi cha kuijenga nchi yetu. Naomba, ninakuheshimu sana, wewe ni kichwa, nimeangalia watu wengi, hawana uwezo kama wako, una akili sana na ndiyo maana nimeamua kukupeleka Marekani na wengine kuwapeleka sehemu nyingine,” alisema Bokasa.

Alikuwa akimsifia Mapoto, alimfanya kujiona yeye alikuwa mtu muhimu, mwenye akili kuliko Watanzania wote, kumfanya kujiona kwamba hakukuwa na mtu mwingine aliyetakiwa kuwa balozi nchini Marekani zaidi yake.

Hilo likaulegeza moyo wa Mapoto na mwisho wa siku kukubaliana naye, hakujua kwamba kwa kufanya hivyo ndiyo ilikuwa njia moja ya kumpoteza kisiasa, hakuangalia mbele, kwake, kuwa balozi nchini Marekani ilionekana kuwa heshima kubwa.

“Una uhakika hili litakusaidia?” aliuliza mke wake.

“Ndiyo! Naamini kwamba litasaidia. Najua jinsi watu wanavyonipenda, haijalishi kama nitakuwa nchini Marekani au wapi, nitakachokifanya ni kuendeleza mapambano hukohuko na ninakuhakikishia mpaka mwaka 2003 nitakuwa na nguvu hiihii,” alisema Mapoto huku akiwa na uhakika kwa kile alichokuwa akikizungumza.

“Sawa.”

Baada ya siku mbili, Mapoto akatangazwa kama balozi nchini Marekani. Hilo likaibua maneno mengi, watu wakakasirika, wengine wakatukana kwani walijua kabisa kwamba Bokasa alitumia njia hiyo kama kumzima Mapoto kisiasa.

Watu wakamuona Mapoto kama msaliti kwani hawakutaka kuona akiwa balozi, kitendo cha kumpeleka Marekani kingemfanya kutokuonekana, kumdhoofisha kisiasa na hivyo kupotea kabisa.

Maneno mengi mitaani, lawama zote hazikuweza kubadilisha kitu chochote kile kwani baada ya wiki mbili, yeye na watoto wake wakaondoka kuelekea nchini Marekani. Mke wake, Rosemary hakwenda naye, aliendelea kukaa nchini Tanzania akiendelea na kazi yake ya ualimu katika Shule ya Wasichana ya Azania alipokuwa akifundisha.

“Nakutakia safari njema! Usisahau kuendelea kuwafundisha watoto wetu kuhusu kumjua Mungu,” alisema Rosemary wakati akiagana na mumewe katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

“Usijali katika hilo.”

“Nakupenda sana mume wangu!”

“Nakupenda pia,” alisema Mapoto, wakakumbatiana na kuagana huku muda wote Rosemary akilengwa na machozi. Alitamani kumzuia mume wake lakini alishindwa kabisa.





Ndege kubwa ya Shirika la Ndege la American Airlines ilikuwa ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JFK uliokuwa jijini New York nchini Marekani. Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Bwana Mapoto kufika katika jiji hilo kubwa la biashara, achilia mbali na Los Angeles, Texas ambapo alikuwa akifika huko mara kwa mara.

Hali ya hewa ilikuwa nzuri, hakukuwa na baridi kali, kulikuwa na dalili ya mawingu huku kwa mbali jua likianza kuzama. Walipoteremka kwenye ndege pamoja na abiria wengine, Mzee Mapoto akaanza kuangalia huku na kule, alilishangaa jiji hilo, lilikuwa kubwa na lililokuwa na majengo makubwa, kwa kifupi lilionekana kuvutia kuliko Los Angeles.

“Karibu sana mkuu,” alisema mwanaume mmoja aliyekuwa mahali hapo kwa ajili ya kuwapokea.

“Nashukuru sana!”

Wakaingia kwenye gari na safari ya kuelekea katika mtaa wa kitajiri wa Lenox Hill kuanza. Muda wote macho yao yalikuwa yakiangalia nje, jiji hilo lilionekana kuwa na mvuto mno na hakuamini kama alikuwa amekwenda kuanza kazi huko.

Alisahau mambo ya siasa kwa muda, akasahau kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wakimuhitaji sana nchini Tanzania, kitu alichokifikiria sana kwa kipindi hicho ni namna ambavyo angefanya kazi yake ya ubalozi nchini humo.

Walichukua dakika thelathini mpaka kufika katika mtaa huo ambapo gari likasimama nje ya jumba moja kubwa la kifahari na geti kuanza kujifungua na gari kuingizwa.

Hakukuwa na aliyeamini kama wao ndiyo wangekwenda kuishi ndani ya jumba hilo kubwa. Lilikuwa na bwawa kubwa la kuogelea, bustani iliyokuwa na maua mazuri, mbuga ndogo ya wanyama na sanamu kubwa la Mwalimu Julius Nyerere huku katikati kukiwa na bendera ya Tanzania.

“Karibuni sana,” alisema dereva huyo na kuwafungulia milango.

Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa maisha yao nchini Marekani. Kila mmoja alionekana kuwa mwenye furaha tele. Bwana Mapoto hakuacha kuwasiliana na mkewe, majukumu makubwa aliyokuwa nayo nchini Tanzania ndiyo yaliyomfanya kutokwenda pamoja naye.

Mbali na watoto wake aliokuwa nao ndani ya nyumba hiyo, pia kulikuwa na wafanyakazi wake wawili wa kike ambao walikuwa wakisaidia kazi za ndani.

Akaanza kazi huku akimwagiza kijana ambaye alikuja kumpokea kumtafutia shule nzuri kwa ajili ya watoto wake. Hilo halikuwa na tatizo lolote kwani baada ya siku moja tu, akapewa orodha ya shule bora za watoto zilizokuwa hapo New York.

“Kuna hii St. Monica! Ni shule ya watoto ambayo ninaamini ni bora kabisa. Watoto wengi wanaosoma hapo ni wa matajiri na viongozi wa serikali, ni shule inayotoa elimu bora kabisa,” alisema James, kijana ambaye alimwambia afuatilie masuala yote ya shule.

“Kama ni nzuri! Basi acha wakaanze hapo.”

St. Monica haikuwa mbali na mahali alipokuwa akiishi, ilikuwa ni mwendo wa dakika kumi kwa gari. Kila siku James ambaye alikuwa na dereva wake alikuwa na kazi ya kuwapeleka watoto hao shuleni na kwenda kuwachukua mchana.

Siku ya kwanza kuingia shuleni, watoto wengi walikuwa wakiwashangaa, hakukuwa na mtoto mweusi hata mmoja shuleni hapo, wao ndiyo walikuwa watoto weusi wa kwanza kusoma ndani ya shule hiyo.

Watu wengi walikuwa wakijiuliza kuhusu Godwin na Irene, walionekana kuwa watoto wachangamfu ambao kila mmoja alitamani kuzungumza nao. Darasani, hawakuwa wazungumzaji, kila mmoja alikuwa kimya huku wakionekana kutaka kuyazoea mazingira ya shuleni hapo.

Wazazi waliokuwa wakifika shuleni hapo na kuwaona watoto hao, walishangaa, waliwauliza walimu kuhusu watoto hao, ilikuwaje kuanza masomo katika shule hiyo na wakati walikuwa watoto weusi.

“Ni watoto wa balozi!” alijibu mwalimu mmoja.

“Balozi wa nchi gani?”

“Tanzania!”

“Afrika?”

“Ndiyo!”

Walitaka kufahamu mengi kuhusu watoto hao, waliwadharau kwa kuwa hawakuamini kama kungekuwa na mtu mweusi ambaye alikuwa na akili zaidi ya Mzungu.

Siku zikakatika, japokuwa Godwin na Irene walikuwa wageni shuleni hapo, waliyakuta masomo katikati lakini walionekana kuwa hatari sana katika masomo yote.

Walijua kusoma vizuri Kiingereza, waliweza vizuri sana somo la hesabu kiasi kwamba hata walimu wenyewe walishangaa na kubaki kujiuliza juu ya uwezo waliokuwa nao watoto hao.

“Haiwezekani! Mbona wana akili hivi?” aliuliza mwalimu Wilbert huku akionekana kushangaa.

“Hata mimi nashangaa! Wanaonekana ni hatari sana. Wana akili za kuzaliwa, haiwezekani kwa mwanafunzi kufahamu mambo kama haya, ni mapema mno lakini cha ajabu, wao wanafahamu sana,” alisema mwalimu mwingine huku uso wake ukiwa kwenye mshangao mkubwa.

Huyo ulikuwa mwezi wa kwanza, uwezo wao darasani uliendelea kujionyesha shuleni hapo na hata kipindi cha mitihani ya mwisho wa mwaka kilipofika, waliweza kushika nafasi ya kwanza kitu kilichowachanganya walimu wengi.

“Wamefaulu vizuri sana, zaidi ya wanafunzi wengine,” alisikika mwalimu mmoja, hakuamini kile alichokuwa akikiona.

“Wakina nani?”

“Wale watoto wa Kiafrika!”

“Godwin na Irene.”

“Hebu nione!”

Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mabadiliko, shuleni, walikuwa wanafunzi hatari, hata mwaka huo ulipokatika na mwingine kuingia, bado walikuwa moto wa kuotea mbali.

Wale waliokuwa wakiwadharau watu weusi, wakaacha dharau zao kwani watoto hao wawili walizisafisha akili zao na kugundua kwamba si Wazungu peke yao waliokuwa na akili kuliko watu weusi, hata watu weusi wenyewe walikuwa na akili kuliko hao Wazungu.

“Ninaamini kwamba mnaweza kufanya vizuri zaidi ya hapa. Watoto wote mnaosoma nao, hakuna mtoto mwenye akili zaidi yenu. Hebu waonyesheeni kile ambacho Mungu amekiweka vichwani mwenu,” alisema Bwana Mapoto huku akiwaangalia watoto wake.

“Ninataka kuwa mchungaji baba,” alisema Godwin huku akimwangalia baba yake, kila siku katika maisha yake, hakukuwa na kitu chochote alichokuwa akikihitaji kama kuwa mchungaji kama alivyokuwa Reinhard Bonnke ambaye kila siku alimuona kama ‘role model’ wake.

Wakati hayo yote yakiendelea nchini Marekani, nchini Tanzania hali ilikuwa imebadilika, kila mtu alionekana kukata tamaa ya maisha, hawakuamini kama kweli huo ndiyo ungekuwa mwisho wa Bwana Mapoto ambaye aliondoka na kuelekea nchini Marekani ambapo maisha yake yote yangeendelea kuwa huko.

Watu waliompenda, walimchukia, mioyo yao iliyokuwa na upendo mkubwa juu yake ilibadilika na chuki nzito kuanza kuchipua kwani kwa kitendo cha kumkubalia Rais Bokasa kuwa balozi nchini Marekani kilimaanisha kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wake.

Chama cha Tanzania National Party na viongozi wake wakachanganyikiwa, waliona kabisa kwamba kama Bwana Mapoto angeendelea kuishi nchini Marekani basi uchaguzi wa mwaka 2003 wasingeweza kuchukua, hivyo ilikuwa ni lazima kumlaghai.

“Ni miaka mitano tu, niamini kwamba nitakaporudi nitakuwa na nguvu ileile,” alisema Bwana Mapoto wakati akizungumza kwenye simu na mwenyekiti wa chama chake, Bwana Edward.

“Hapana! Ni kipindi kirefu sana. Naomba ufanye kitu kimoja, andika barua ya kuacha kazi,” alisema Edward.

“Unahisi hilo litasaidia?”

“Ndiyo! Huku kila mtu anakuhitaji wewe, kitendo chako cha kwenda huko ni kujipoteza kisiasa, fanya juu chini, andika barua ya kuacha kazi na urudi huku Tanzania tuje tulisukume gurudumu hili na kuuchukua urais uchaguzi ujao,” alisema Edward.

“Hakuna shida. Nitafanya hivyo!”

Hilo ndilo walilokubaliana lakini kabla ya kufanya uamuzi wowote ule ilikuwa ni lazima kuwasiliana na mkewe na kushauriana kama lingekuwa jambo sahihi kufanya kama alivyoambiwa.

Akampigia simu na kuzungumza naye, alichoambiwa, mkewe naye akamuunga mkono kwamba alitakiwa kuacha kazi kwani kila mtu nchini Tanzania alikuwa akimlalamikia kwa kitendo alichokifanya, aliwasaliti, ili kuwafurahisha ilikuwa ni lazima kuachana na kazi ya ubalozi na kurudi nchini Tanzania.

“Naandika barua leo hiihii…” alisema Bwana Mapoto.

“Sawa.”

Hakutaka kuchelewa, akawasha kompyuta yake ya mapajani, bila kupoteza muda akaanza kuandika barua hiyo kwa njia ya barua pepe kwa ajili ya kuituma kwa Rais Bokasa na kumwambia kwamba hakutaka tena kufanya kazi ya ubalozi nchini Marekani, alibadilisha maamuzi yake na kitu alichokuwa akikihitaji ni kurudi nchini Tanzania.

Alipomaliza, akaisoma, aliporidhika, akapeleka kasa katika kitufe cha kutuma barua pepe hiyo lakini hata kabla hajaibonyeza, simu yake ya mezani ikaanza kuita. Akaacha kuituma, harakaharaka akachukua mkonga wa simu na kuupeleka sikioni, alichokisikia ni sauti ya mwanamke iliyokuwa ikilia.

“What is going on?” (nini kinaendelea?)

“Don’t tell him that she has died,” (usimwambie kama amekufa) alisikia sauti ya mtu aliyekuwa pembeni ya mtu aliyepiga simu hiyo kutoka shuleni walipokuwa wakisoma watoto wake. Kijasho chembamba kikaanza kumtoka.

“Who has died?” (nani amekufa?) aliuliza lakini hata kabla hajajibiwa, simu ikakatwa. Akachanganyikiwa kupita kawaida. Kilichomjia akilini ni binti yake Irene tu.

***

Ofisini hakukukalika tena, Mapoto alichanganyikiwa, kwa simu aliyopigiwa, alihisi kabisa kulikuwa na tatizo shuleni hasa kwa mtoto wake Irene. Akachukua koti lake, hata kuuweka mkonga wa simu sehemu husika hakukumbuka, akatoka, hakumuaga ‘secretary’ wake, akatoka na kwenda nje ambapo akaingia ndani ya gari lake.

Dereva hakuwemo garini, alikuwa katika mgahawa uliokuwa hapo ofisini akinywa kahawa. Hakutaka kusubiri na wala hakutaka kumuita, akachukua ufunguo mwingine aliokuwanao, akaliwasha na kuondoka mahali hapo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Alichanganyikiwa, hata uondokaji wake haukuwa wa kawaida, watu wote waliouona uondokaji ule wakawa na wasiwasi kwamba kulikuwa na kitu kimetokea.

Njiani, aliendesha kwa mwendo wa kasi, akaingia katika barabara iliyokuwa ikiruhusu magari kwenda kwa mwendokasi kuanzia 90 na kuendelea, akakanyaga mafuta kwa kasi, alichokuwa akikihitaji ni kuwahi huko, alitaka kuona ni kitu gani kilitokea.

Alichukua dakika kumi mpaka kufika shuleni ambapo geti likafunguliwa, hata hakuzima gari, akateremka na kuelekea katika ofisi ya mwalimu mkuu, alitaka kujua ni kitu gani kilitokea.

Alipofika huko, macho yake yakatua kwa mtoto wake, Godwin ambaye baada ya kumuona, akainuka kitini, akamkimbilia na kumkumbatia huku akilia mno.

“Kuna nini?” alimuuliza lakini Godwin hakujibu zaidi ya kuendelea kulia tu.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo akamkaribisha, hakutaka kuzungumza kitu chochote kuhusu Irene, alimwangalia Mapoto, kwa jinsi alivyoonekana, alionekana kuwa na hofu kubwa.

“Mtoto wangu yupo wapi?” aliuliza Mapoto.

“Kuna kitu inabidi tuzungumze,” alisema mwalimu mkuu.

“Kitu gani? Kwanza niambieni mtoto wangu yupo wapi,” alisema Mapoto kwa sauti kubwa iliyowafanya walimu wawili kuingia humo kwani walihisi kwamba kulikuwa na fujo.

“Ndiyo tunahitaji kuzungumza kuhusu hilo,” alisema mwalimu mkuu.

“Ila yupo hai?”

“Ndiyo! Yupo hai! Cha msingi nisikilize kwanza,” alisema mwalimu huyo.

Hakutaka kumficha, alimwambia ukweli kwamba mtoto wake, Irene hakuwa kwenye hali nzuri. Wakati wakiwa darasani, alipanda juu ya kiti huku akicheza na wenzake lakini kwa bahati mbaya alidondoka baada ya viatu vyake kuteleza.

Lilikuwa tukio baya, japokuwa kuteleza kulionekana kuwa kwa kawaida kwa watoto wengi shuleni hapo lakini kitu ambacho kilionekana kuwa kibaya kwake ni kwamba alipoanguka, aliangukia kichwa na kukipigiza kwenye marumaru kisogoni hali iliyosababisha damu kutoka na kupoteza fahamu hapohapo.

“Nilisikia kwamba amekufa!” alisema Mapoto huku machozi yakianza kumtoka.

“Nani alikwambia?”

“Nilisikia kwa masikio yangu kwenye simu, mmoja wa walimu alisema hivyo!” alisema Mapoto.

“Hapana! Ila wote walihisi kwamba amekufa kutokana na mazingira yaliyokuwa yametokea ajali hiyo,” alisema mwalimu mkuu.

Hawakuongea sana, kitu alichokitaka Mapoto ni kumuona mtoto wake hivyo mwalimu mkuu alimwambia kwamba ni lazima waondoke na kuelekea katika Hospitali ya St. Monica Medical Center ambayo haikuwa mbali na mahali hapo.

Wakaondoka, njiani, Godwin alikuwa akilia tu, alitaka kumuona dada yake, alikuwa kwenye tukio, kila alipokumbuka jinsi Irene alivyoanguka na kuumia vibaya kichwani, moyo wake ulimuuma mno.

Hawakuchukua muda mwingi wakafika hospitalini hapo na kuanza kuelekea katika chumba kile alicholazwa Irene, walipofika, hawakuruhusiwa kwani mgonjwa hakuwa kwenye hali nzuri, alihitaji muda mrefu wa mapumziko.

“Dokta! Mtoto wangu atapona?” aliuliza Mapoto huku akionekana kuumia moyoni mwake.

“Tunamwamini Mungu!”

“Kwa hiyo atapona?”

“Hebu nifuateni ofisini!”

Wakamfuata daktari huyo mpaka ofisini ambapo wakakaa na kuanza kuwaelekezea tatizo alilokuwa nalo Irene. Lilikuwa tatizo kubwa ambalo huwatokea watu wengi, wakati Irene alipoanguka chini, alikipigiza kichwa chake kwenye sakafu na hivyo kushtua mishipa ya fahamu hali iliyompelekea kupoteza fahamu na kuwahishwa hospitalini.

“Atarudiwa na fahamu zake?” aliuliza Mapoto.

“Ndiyo japokuwa anatakiwa kuwa chini ya uangalizi wetu kwani tatizo ambalo amekutana nalo ni kubwa sana, kama itachukua muda mrefu zaidi na hakuna mafanikio basi itabidi afanyiwe upasuaji wa kichwa,” alisema daktari huyo aliyekuwa na kichuma kifuani mwake kilichoandikwa Dr. Phellips.

Hilo ndilo waliloambiwa na daktari, hawakutakiwa kumuona Irene kipindi hicho kwa kuwa tu hali yake haikuwa nzuri na baada ya kutolewa kwenye chumba cha upasuaji, haraka sana akahamishwa na kupelekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Hilo lilimuuma sana Mapoto, hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kukabiliana na hali hiyo ambayo ilikuwa ni yenye kuumiza sana, mbali na hayo yote, pia hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kumwambia mke wake juu ya lile lililokuwa limetokea.

Alimfahamu Rosemary, aliwapenda sana watoto wake, kwake, hao walikuwa kila kitu katika maisha yake, alijua kwamba kama angempa taarifa moja kwa moja basi hali ingekuwa mbaya zaidi na angeweza kumsababishia matatizo.

“Nitamwambia tu, ila sitotaka kumpa taarifa akiwa nchini Tanzania, ni lazima aje huku,” alisema Mapoto.

Siku hiyo walikaa hospitalini hapo, hawakuruhusiwa kumuona mgonjwa mpaka ilipofika majira ya saa 2:00 usiku ndipo wakaruhusiwa na kwenda katika chumba maalum alicholazwa mtoto huyo.

Walipomuona kitandani, kila mmoja alionekana kuumia mno. Irene alikuwa kimya kitandani pale, mdomoni alikuwa na mashine ya oksijeni iliyokuwa ikimsaidia kupumulia huku pembeni kukiwa na mashine nyingine ambayo ilikuwa ikionyesha mapigo ya moyo kwa jinsi yalivyokuwa yakidunda.

Mapoto na Godwin wakamsogelea Irene pale kitandani alipokuwa, walipomfikia, wakasimama na kumwangalia. Alikuwa kimya kabisa kiasi kwamba ilikuwa ni rahisi kusema kuwa tayari aliaga dunia, walikuwa kama wakimwangalia mtu ambaye tayari alikuwa amekwishafariki dunia.

“Irene…We came for you, open your eyes and look at us,” (Irene…tumekuja kwa ajili yako, fumbua macho yako utuangalie) alisema Mapoto huku akimwangalia mtoto wake kitandani pale.

Walihuzunika, waliendelea kukaa ndani ya chumba kile kwa saa mbili ndipo wakaondoka na kurudi nyumbani. Hakukuwa na mtu aliyelala, kila mmoja alikuwa kimya, walimkumbuka Irene, kitendo cha kutokuwa ndani ya nyumba ile kiliwapa mawazo mazito mno.

Ilipofika asubuhi, majira ya moja, tayari walikuwa hospitalini kwa ajili ya kumjulia hali, kama walivyokuwa wamemuacha usiku uliopita ndiyo alikuwa vilevile, walihuzunika, walilia sana kwani kuna kipindi walihisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa Irene, pale kitandani alipokuwa asingeweza kuinuka wala kufumbua macho yake.

“Ni lazima niwasiliane na Rosemary,” alisema Mapoto.

Hakutaka kujiuliza mara mbilimbili, hapohapo akachukua simu yake na kumpigia mkewe, hakutaka kumpa taarifa moja kwa moja, ilikuwa ni lazima amdanganye kwamba kuna kitu ambacho kingemfanya kusafiri na kwenda nchini Marekani haraka sana.

“Rosemary! Tumekukumbuka sana mke wangu,” alisema Mapoto mara baada ya kumpigia simu mkewe.

“Nimewakumbuka pia. Mnaendeleaje huko?”

“Huku sisi ni wazima sana. Watoto wapo shuleni, wamekukumbuka mno, kila siku wanakuulizia, ninahitaji uje huku, uwaone, uwafanyie sapraizi kwanza. Halafu pia kuna kitu,” alisema Mapoto.

“Kitu gani?”

“Kuhusu kujiuzulu. Kuna jambo nimelifikiria, ninataka uje tuweze kulizungumzia,” alisema Mapoto.

“Mmh!”

“Mbona unaguna sasa?”

“Hatuwezi kulizungumzia kwenye simu?”

“Hapana! Uje huku kwanza, uwaone watoto waliokukumbuka, halafu kuna sehemu tutakwenda, ni sehemu nzuri sana, huko, tutazungumza mambo mengi. Nadhani umekwishasikia Jiji la Hollywood!”

“Yeah!”

“I just want to take you there,” (nataka nikupeleke huko!)

“Ooh! Sawa. Ngoja niombe ruhusa. Ila naomba nisichukue mwezi kukaa huko!”

“Hilo usijali my Juliet,”

“Nashukuru my Romeo.”

Moyo wake ulimuuma, kuzungumza na Rosemary pasipo kumwambia ukweli kile kilichokuwa kimetokea kilimfanya kujihukumu sana moyoni mwake. Akakata simu, akaelekea pembeni ukutani na kuanza kulia kama mtoto.

Alijitahidi kujifanya kama mtu mwenye furaha kuzungumza na Rosemary lakini moyo wake ulimkatalia kabisa, hakufarijika na hata maumivu aliyokuwa nayo moyoni hayakupungua hata mara moja.

“Itakuwaje akifika? Itakuwaje kama akigundua nimemdanganya? Atafanyaje? Mungu naomba umtie nguvu asipate tatizo lolote lile baada ya kupokea taarifa kuhusu Irene,” alisema Mapoto, akamchukua Godwin na kukaa naye kwenye kiti kilichokuwa nje ya chumba kile na kuanza kulia, kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele, mioyo yao iliwaka moto kwa maumivu makali.





Moyo wa Rosemary ulikuwa na shauku kubwa ya kutaka kuwaona watoto wake, aliwapenda sana na kilipita kipindi kirefu pasipo kuwatia machoni mwake, alifurahi kwa kuwa alijua baada ya saa kadhaa, ndege ingetua na kuwaona watoto wake hao.

Aliona ndege ikienda taratibu, alikuwa na hamu kubwa ya kuwaona kwa mara nyingine, hakufikiria kama kulikuwa na jambo baya lililotokea ambalo lingemuumiza sana moyo wake.

Ndani ya ndege, alikuwa akiwasiliana na mume wake kwa kutumia barua pepe, kila sehemu alipofika, ilikuwa ni lazima amtumie barua pepe kuonyesha kwamba alikuwa njiani na muda wowote ule angefika nchini Marekani.

“Tumefika Heathrow nchini Uingereza, muda wowote ule tunaondoka kuja huko,” alisema Rosemary mara baada ya kupata muda wa saa mbili kupumzika kabla ya ndege kuendelea na safari.

“Ooh! Tunakusubiri kwa hamu kubwa. Kila mtu hapa nyumbani amekukumbuka sana,” alisema Mapoto, kwa jinsi sauti ilivyosikika, ilikuwa vigumu kugundua kwamba kulikuwa na jambo baya lililokuwa likiendelea.

Saa 4:45 usiku wakapanda ndege kuelekea nchini Marekani. Muda mwingi alikuwa akiwasiliana na mumewe kwa barua pepe, alitamani kufika nchini Marekani haraka sana kwani kilipita kipindi kirefu tangu siku ya mwisho kuwaona watoto na mume wake.

Upande wa pili, Mapoto alikuwa na mawazo tele, mke wake alikuwa njiani akielekea nchini Marekani, mpaka kipindi hicho hakuwa amemwambia ukweli juu ya kile kilichokuwa kimetokea.

Moyo wake ulikuwa mzito, alimfahamu mkewe, alikuwa na presha, alijua kwamba kama angemwambia waziwazi basi angeweza kupata tatizo zaidi na hata kufariki kutokana na mshtuko mkubwa.

Baada ya saa kumi, akaondoka nyumbani kwake na kuelekea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JFK uliokuwa hapohapo jijini New York. Alipofika, akatulia na kuanza kumsubiri mkewe.

Ubao ulisomeka kwamba ndege aliyopanda Rosemary ambayo ilikuwa ikitoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Heathrow ingeingia mahali hapo majira ya saa saba mchana hivyo alitakiwa kusubiri.

Moyo wake haukuacha kumuomba Mungu, alitaka amtie nguvu mkewe mara baada ya kugundua kitu kilichokuwa kimetokea, hakutaka kumuona akipata tatizo lolote lile, alitaka kumuona akiwa kwenye hali ya kawaida japokuwa kile alichotaka kumwambia kilikuwa kitu kibaya, chenye kuumiza ambacho kwa mwanamke yeyote, mwenye mapenzi na watoto wake asingeweza kuvumilia.

Ilipofika saa saba, ndege hiyo ikaanza kutua katika uwanja huo, aliiona ikitembea ardhini, haraka sana akakimbilia bafuni, akanawa uso wake, hakutaka michirizi ya machozi ionekane, ilikuwa ni lazima kumuonyeshea mke wake furaha kubwa ili asiweze kugundua kitu chochote kile.

Alipotoka huko, akaelekea sehemu ya kuwasubiri wageni wanaoingia, alipomuona mke wake, akamsogelea na kumkumbatia kwa nguvu, hakutaka kuona akiondoka mikononi mwake.

“Nimekukumbuka mke wangu!” alisema Mapoto huku akiwa amemkumbatia zaidi.

“Nimekukumbuka pia mume wangu! Watoto wapo wapi?” aliuliza Rosemary.

“Unakumbuka nilikwambia nini?” aliuliza Mapoto huku akiachia tabasamu pana ambalo liliyaficha maumivu mazito yaliyokuwa moyoni mwake.

“Sapraiziiiii…” alisema Rosemary na kuachia kicheko.

“Yeah! Nataka washtuke kwa furaha kukuona,” alisema Mapoto huku akionekana kuwa na furaha mno.

Wakatoka nje ya jengo la uwanja huo na kuingia ndani ya gari, aliamua kuendesha yeye mwenyewe kwani alihitaji kujiweka bize na asiweze kumfikiria mtoto wake.

Njiani, walikuwa wakizungumza mambo mengi, kila mmoja alionekana kuwa na furaha mno. Hawakuchukua muda mrefu wakafika nyumbani ambapo Mapoto akaliingiza gari mpaka ndani na kumfungulia mlango mkewe.

Nyumba ilikuwa kimya, wakaelekea ndani na kumuita mfanyakazi ambaye tayari alimtengeneza kwa kile kilichokuwa kikiendelea, alichokifanya ni kumwambia akawaite watoto.

“Daktari alikuja na kumchukua Irene, alikuwa akilalamika kuumwa kichwa,” alisema mfanyakazi wa ndani.

“Nilijua tu! Jana amecheza sana! Na hii si mara ya kwanza,” alisema Mapoto, aliongea kama utani ili mkewe asiweze kufikiria kitu kibaya.

“Na Godwin?”

“Yule asingeweza kubaki. Wale watoto wanavyopendana! Ni hatari! Ngoja tujiandae twende tukamuone na kuwachukua. Naamini akikuona tu, na kichwa kitapona,” alimwambia mkewe ambaye hakuonekana kuwa na hofu yoyote ile.

Wakaondoka na kuelekea bafuni, huko, Rosemary alimkumbatia mumewe, kwa kipindi kirefu hakuwa amekutana naye, alilikumbuka joto lake, alitamani sana afike na kuonana na mume wake huyo japo wachangie kitanda kama ilivyokuwa nchini Tanzania.

Mapoto hakuwa na hamu yoyote, hisia zote za kufanya mapenzi ziliondoka mwilini mwake, alipokuwa akimwangalia sana mkewe, taswira ya Irene aliyokuwa amelala kitandani ilimjia kichwani mwake, machozi yalipoanza kutiririka, akafungua bomba la mvua na kuyaruhusu maji kummwagikia.

“Una nini?” aliuliza Rosemary huku akionekana kuwa na wasiwasi.

“Sina kitu chochote.”

“Hebu uruhusu mwili wako! Utanifanya nijisikie vibaya kwamba una mwanamke mwingine,” alisema Rosemary huku akimwangalia mumewe usoni.

Hakuwa na jinsi, hakuwa na hamu yoyote ile lakini ili kumridhisha mkewe ilikuwa ni lazima afanye kile alichotaka kifanyike. Wakakumbatiana, walikaa kwenye hali hiyo kwa dakika kumi na tano kisha kutoka bafuni.

Wakajiandaa na kisha kuondoka nyumbani hapo kwa ajili ya kwenda hospitalini kumuona Irene aliyekuwa amelazwa kwa kupoteza fahamu baada ya kuanduka kutoka kwenye kiti.

Hawakuchukua muda mrefu wakafika huko, wakamuona daktari na kuzungumza naye, kwa kuwa na yeye alikuwa akijua kilichokuwa kikiendelea, akawaita ndani ya ofisi yake na kuwaambia kwamba mtoto wao hakuwa amepata tatizo, lilikuwa dogo sana la kichwa.

“Huwa anakuwa anaumwa kichwa mara kwa mara?” aliuliza daktari.

“Ndiyo! Huwa anaumwa mara kwa mara, tena hasa baada ya kuja kuishi huku, nahisi ni matatizo ya kubadili hali ya hewa” alidakia Mapoto kwani alijua kama asingeingilia, mkewe angekataa hilo.

“Sawa. Ndiyo maana! Tumempa chumba apumzike kwanza. Mkitaka kumuona, mnaruhusiwa, ila mtatakiwa kuwa kimya, amepumzika,” alisema daktari.

“Sawa.”

Wakatoka ndani ya ofisi hiyo na kuanza kuelekea katika chumba alicholazwa Irene. Mapigo ya moyo wa Mapoto yalikuwa juu kwa kiwango kikubwa, alikuwa na hofu kubwa kwa kuhisi kwamba inawezekana mkewe angegundua kile kilichokuwa kimetokea Irene mara baada ya kumuona kitandani hapo.

Walipokifikia chumba hicho, wakaufungua mlango na kuingia ndani. Irene alikuwa kimya kitandani, waliambiwa kwamba alikuwa amepumzika hivyo hata Rosemary alivyomuona mtoto wake kitandani pale, hakuonekana kuwa na hofu kabisa.

“Nafikiri baadaye atakuwa kwenye hali ya kawaida,” alisema daktari.

“Tunashukuru sana!”

Mpaka kufikia hapo, wakawa na uhakika kwamba walifanikiwa kuutuliza moyo wa Rosemary, hakuonekana kuwa na presha, aliamini kile alichokisema mume wake. Wakatoka na kukaa kwenye viti vilivyokuwa nje ya chumba kile, walikuwa wakizungumza huku Mapoto akijitahidi sana kujiweka katika hali ya kawaida.

Baada ya dakika kadhaa, dereva wake, James akafika hospitalini hapo akiwa na Godwin. Alipomuona mama yake, akamkimbilia, alipomfikia, wakakumbatiana huku Godwin akilia kwa maumivu makali kiasi kwamba Rosemary alishangaa.

“Unalia nini?”

“Irene…Irene…”

“Amefanya nini?” aliuliza Rosemary.

“Anaumwa kichwa tu. Godwin njoo kwa baba,” alisema Mapoto huku akimchukua Godwin.

“Hebu subiri kwanza. Godwin, Irene amefanya nini?” aliuliza.

“Atakufa! Mwalimu amesema Irene atakufa, alianguka darasani,” alisema Godwin huku akimwangalia mama yake, Rosemary aliposikia maneno hayo, akahisi kama alipigwa na shoti ya umeme, akayapeleka macho kwa mume wake, Mapoto alibadilika, machozi yakaanza kumlenga, akayainamisha macho yake chini kwani hata kukutanisha macho na mkewe aliogopa.

“Irene alianguka darasani? Atakufa? Alianguka darasani au anaumwa kichwa?” aliuliza Rosemary huku akimwangalia mume wake.

“Nisamehe mke wangu!”

“Niambie! Ukweli ni upi?”

“Ire..Irene…Iren…”

“Niambie amefanya nini?” aliuliza mke wake kwa sauti ya juu, tayari machozi yalianza kumtoka, maumivu aliyoyasikia moyoni mwake kipindi hicho hayakuweza kuelezeka.

“Alianguka!”

“Alianguka? Alianguka? Ina maana atakufa? Irene mtoto wangu atak…” alisema Rosemary, hata kabla hajamalizia sentensi yake, presha ikapanda, akadondoka chini.

“Rose…Rose…Rose mke wangu,” aliita Mapoto huku akilia, manesi wakafika mahali hapo haraka sana, mapigo yake ya moyo yalianza kushuka, wakambeba na kumuweka kwenye machela, mwili wake ulimlegea, alionekana kama tayari alikwishakufa. Manesi wenyewe wakatingisha vichwa vyao kushoto na kulia kuonyesha kwamba inawezekana huo ulikuwa mwisho wa mwanamke huyo.

***

Mapoto alijipa moyo kwamba mtoto wake angeweza kupona na kurudi katika hali ya kawaida. Moyo wake ulikuwa na huzuni kubwa, kila alipokuwa akiikumbuka sauti ile ambayo aliamini kwamba ilikuwa ni sauti ya shetani, alijikuta akichukia moyoni mwake.

Hakuwa na tumaini jingine zaidi ya Mungu wake aliyekuwa akimuabudu. Kila saa alimwambia mke wake washikane mikono na kuanza kusali kwani aliamini kwamba Mungu angekwenda kufanya muujiza na hali waliyokuwa wakiipitia ilikuwa ni jaribu ambalo lilikuwa ni lazima walishinde.

“Mke wangu! Hili ni jaribu. Namuamini Mungu wangu, hawezi kukupa jaribu kubwa zaidi ya uwezo wako! Hili ni jaribu linalolingana na uwezo wetu, hatuna budi kulishinda,” alisema Mapoto huku akimwangalia mke wake ambaye macho yake yalikuwa mekundu mno kuonyesha ni kwa jinsi gani alikuwa amelia sana.

“Amen!” alijibu mkewe, hakutaka kuzungumza maneno mengi kwani kila alipotaka kufanya hivyo, moyo wake uliuma zaidi.

Upasuaji ukaanza, baada ya kukichana kichwa cha Irene, wakaanza kutoa kipande cha fuvu ambacho kitaalamu huitwa Bone Flap na kisha kukiweka pembeni kwa ajili ya kuangalia ndani ya ubongo kuona kulikuwa na nini.

Wakati wakiendelea kufanya upasuaji huo bado walikuwa wakizungumza huku wakikiangalia kichwa hicho kwa makini kabisa ambapo huko wakaliona donge la damu likiwa limeganda katika ubongo wake, tena kwa kujificha ndani ya ubongo kwa mbali.

“Ooh my God!” (Ohh Mungu wangu) alisema Dk. Phillips huku akionekana kushtuka kwani donge lile lilionekana kuwa kubwa tofauti na walivyodhani.

“What is it?” (kuna nini?) aliuliza nesi mmoja.

“This is brain hemorrhage,” (damu imevuja kwenye ubongo) alijibu Dk. Phillips japokuwa alijua kwamba aliwaambia hilo kabla.

Kila mmoja alishtuka, hawakuamini kusikia kwamba damu ilikuwa imevilia katika ubongo wa Irene kwa kiasi kikubwa. Lilikuwa tatizo kubwa ambalo kwa watu wengi waliokuwa wakipata tatizo hilo, asilimia themanini walikuwa wakifa kwani damu huwa na kawaida ya kusambaa kwa haraka sana katika ubongo kuliko sehemu nyingine yoyote ile.

Waliogopa, waliuona mwisho wa Irene ukiwa mikononi mwao kwani hata kama angepona ilikuwa ni lazima kupata matatizo mawili, iwe ugonjwa wa kusahau kila kitu kilichotokea katika maisha yake yote au nusu ya maisha lakini pia ilikuwa ni kupata ugonjwa wa kupooza ambao ungeyatesa maisha yake kitandani.

Japokuwa walikuwa wakisali kimoyomoyo lakini baada ya kugundua hilo, kila mmoja akatulia, wakaanza kuangalia, damu ilikuwa kwenye ubongo na kwa bahati nzuri sana kwa Irene ni kwamba lilikuwa donge moja la damu lililotulia ndani ya ubongo paspipo kusambaa.

“We have to remove it without soring a brain,” (ni lazima tuiotoe damu pasipo kuutonesha ubongo) alisema Dk. Phillips huku akiliangalia donge lile la damu.

“We have ten hours to perfom this craniotomy,” (tuna saa kumi za kufanya upasuaji huu wa kichwa) alisema Dk. Phillips, na mpaka kipindi hicho, tayari zilikuwa zimepita saa saba.

Upasuaji ulikuwa ukiendelea, Dk. Phillips na wenzake hawakutoka ndani ya chumba kile, walijua kwamba nje kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakisubiri kuona ni kitu gani ambacho kingetokea ndani ya chumba kile.

Donge la damu halikutoka kirahisi, kila walipoligusa kwa maana ya kulitoa, lilihama na kuhamia sehemu nyingine kitu kilichowapa usumbufu mkubwa kwani mpaka wanakamilisha kulitoa, tayari walitumia saa sita na hivyo kuanza kurudishia fuvu taratibu.

Mpaka wanamaliza, walichukua saa kumi na mbili, walichoka, hawakuwa na matumaini kama Irene angepona kwani kila walipokuwa wakiangalia mashine ya Mult Parameter Monitor mapigo yake ya moyo yalionyesha kushuka kwa ghafla na kupanda.

“We have to pray for her,” (inabidi tumuombee) alisema Dk. Phillips.

Hawakuwa na jinsi, kadiri walivyomwangalia Irene kitandani pale walikiri kwamba mtoto huyo alikuwa akienda kufa. Hali yake ilitisha na kila walipomwangalia, mioyo yao iliwaambia kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa wake kuvuta pumzi ya dunia hii.

Baada ya kumaliza kusali, wakatoka na moja kwa moja Dk. Phillips kuwaita wazazi Irene ofisini kwake kwa ajili ya kuzungumza nao. Hakuwaficha, aliwaambia ukweli juu ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea kwamba binti yao alikuwa kwenye hali mbaya na kama wasingemuomba Mungu basi angeweza kufariki dunia kitandani hapo.

“Hatuna ujanja zaidi ya kusali sana, tukishindwa, basi atakufa kwani nisingependa kuwaficha, watu wanaopata tatizo hili, wengi hufa japokuwa kwa Irene tunajaribu kupambana,” alisema Dk. Phillips japokuwa alikuwa akizuiliwa kuwaambia ndugu wa wagonjwa maneno kama hayo lakini hakuwa na jinsi.

***

Rais Bokasa akarudi hotelini, alikuwa amechanganyikiwa, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, ni kweli alifika nchini Marekani kwa ajili ya kuzungumza na Mapoto na kumwambia kuhusu kile alichotaka kukifanya lakini jambo baya kwake ni kwamba mtu huyo hakuweza kuzungumza chochote kwa kuwa alikuwa kwenye matatizo makubwa.

Alimuonea huruma lakini hakuwa na jinsi, alitakiwa kumalizana naye, aachane na barua hiyo na aendelee kufanya kazi kama balozi kwani kurudi kwake nchini Tanzania kungemaanisha kwamba upinzani ungepata nguvu na kujipanga tena kwa ajili ya uchaguzi ujao.

“Ni lazima nikae naye chini na kuzungumza. Hatakiwi kujiuzulu, nitamshawishi hata kwa kumlipa mshahara mnono,” alisema Rais Bokasa huku akiwa kitandani kwake.

Siku iliyofuata, haraka sana asubuhi akaelekea hospitalini kuonana na Mapoto, bado hakuwa sawa, alijitahidi kumchangamsha lakini mwanaume huyo hakuchangamka kabisa, alionekana kukata tamaa na kila alipomkumbuka mtoto wake, jinsi alivyokuwa amelala kitandani, moyo wake ulimuuma mno.

Godwin alikuwa mtu wa kulia tu, alikuwa na majonzi mazito, alitamani kumuona dada yake akisimama na kuzungumza tena, hali aliyokuwa nayo kitandani pale ilimuumiza mno.

Alizoea kuwa naye kila siku, kwenda shuleni pamoja, kucheza wote na kufanya mambo mengi lakini kwa kipindi hicho hali ilikuwa mbaya, kwani kwenda shuleni kwenyewe alikwenda peke yake na hata kurudi, alirudi peke yake bila Irene kitu kilichomfanya kukosa furaha kabisa.

“Mama! Nataka nimuone Irene,” alisema Godwin huku akifuta machozi yake.

“Utamuona! Daktari amesema kesho tutaingia na kumuona, ila utatakiwa kwenda shule kwanza. Umesoma nini leo?” aliuliza Rosemary swali ambalo lilionyesha ni kumtaka Godwin asiendelee kuuliza kuhusu Irene.

Wakati hayo yote yakiendelea nchini Marekani, Edward na viongozi wengine hawakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea nchini humo. Waliambiwa na Mapoto kwamba angewaandikia barua ya kuomba kujiuzulu lakini kitu cha ajabu kabisa mpaka kipindi hicho alikuwa kimya kabisa.

Wakawa na hofu kwa kuhisi kwamba mwanaume huyo aliwabadilikia, wakajaribu kuwasiliana naye, simu yake haikuwa ikipatikana, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea.

Rais Bokasa alipopata safari ya kuelekea nchini Marekani, wakajua kabisa kwamba mwanaume huyo alikuwa akienda kuonana na Mapoto, wakajua kabisa kwamba walibadilikiwa, mtu ambaye walimwamini kwa moyo mmoja, mtu ambaye walimpa dhamana kubwa ya kugombea urais kupitia chama chao, hatimaye aliamua kuwabadilikia na kuungana na chama tawala kinyemela.

“Huu ni usaliti! Sisi kama Tanzania National Party hatutoweza kukubali, ni lazima tulifute jina lake kama mwanachama wa chama hiki,” alisema Edward, alionekana kuwa na hasira sana.

Hilo halikupingwa, kila mmoja akamuunga mkono kwamba ni lazima Mapoto afutwe katika chama hicho. Hawakujua ni hatua gani alizokuwa akipitia nchini Marekani, hawakujua kama mwanaume huyo alikuwa kwenye hali mbaya, kwamba mtoto wake mpendwa, Irene alikuwa hoi kitandani.

Taarifa ya kufutwa kwake uanachama ikatangazwa kwenye vyombo vya habari na baada ya siku mbili, jina lake likakatwa. Kila mtu akahuzunika, wengi hawakuamini kama mwanaume huyo waliyemwamini aliamua kuwasaliti na kujiunga na chama tawala.

Chuki dhidi yake ikaingia mioyoni mwa kila mmoja, kila mtu akamchukia, kuanzia watoto, vijana mpaka wazee wote walionyesha chuki dhidi yake, hawakumpenda, walimuona kuwa msaliti mkubwa, hata habari ya kuumwa kwa Irene hawakuwa wakiijua. Kila mmoja alikubaliana na viongozi wa chama hicho kwamba jina lake lifutwe.

“Yule ni nyoka, ni mtu mbaya sana ambaye huwezi kuvumilia kuwa naye, kama ukiishi naye, anaweza kukuua,” alisema mwanaume mmoja, kwa kipindi hicho, hasa miaka hiyo hakukuwa na mitandao ya kijamii, watu walitegemea taarifa kutoka kwenye televisheni na magazeti, waandishi wa vyombo hivyo hawakujua kilichokuwa kikiendelea, hilo likawafanya wananchi kutokujua lolote lile kuhusu mtoto Irene.

***

Kila kona nchini Tanzania kulikuwa na tetesi kuhusu kuandika barua ya kujiuzulu ya Bwana Mapoto, kila mtu aliyepata taarifa hiyo alimwambia mwenzake kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa mwanaume huyo kuwa balozi nchini Marekani na baada ya siku chache angerudi nchini Tanzania.

Mtu wa kwanza kupewa taarifa alikuwa Bwana Edward ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Tanzania National Party, kitendo cha kuwaambia viongozi wenzake tu, tayari taarifa hizo zikaanza kusambaa kila kona na ndani ya saa chache watu wengi wakajua kile kilichokuwa kikiendelea nchini Marekani.

Kila mmoja alikuwa na hamu ya kumuona Mapoto akirudi nchini Tanzania, watu walimpenda na waligundua kwamba mbinu za Rais Bokasa zilikuwa ni kumpoteza kisiasa kwa hiyo kitendo cha kuandika barua ya kujiuzulu kilikuwa ni kama kuwaambia kwamba alikuwa tayari kurudi katika uwanja wa vita mpaka kieleweke.

Viongozi wa chama tawala walichanganyikiwa, kwa kutumia usalama wa taifa ambao walikuwa mitaani, waliwapa mamlaka ya kuchunguza suala hilo kama lilikuwa na ukweli wowote, hilo halikuwa tatizo, wakaingia mitaani, wakachunguza kwa kina na kupeleka majibu kwamba kila kitu kilichozungumzwa kilikuwa ni cha kweli kabisa.

“Kwa hiyo?”

“Tumpeni taarifa rais,” alisema Waziri wa Mambo ya Ndani, Bwana Amani Kizutu.

Hakutaka kupoteza muda, haraka sana akampigia simu rais na kumwambia kilichokuwa kimetokea, rais mwenyewe hakuamini kama kweli jambo hilo lingeweza kutokea kwani aliamini kwa kumpa ubalozi Mapoto basi kila kitu kingekwenda kama kilivyotakiwa kwenda.

Alichanganyikiwa, huo ndiyo aliuona kuwa mwisho wa chama chake kwani aliamini kuwa kama mtu huyo angemwandikia barua ya kujizulu basi ingekuwa tatizo sana kwake.

Alichokifanya ni kumpigia simu, alitaka kuzungumza naye mambo mengi likiwa hilo la kutaka kujizulu kwa kumwandikia barua. Mapoto alipopokea simu, alimwambia kwamba hakuwa tayari kulizungumzia hilo kwani alikuwa kwenye matatizo makubwa kipindi hicho.

“Matatizo gani?”

“Mtoto wangu anaumwa sana. Naomba umkumbuke katika maombi yako,” alisema Mapoto huku sauti yake tu ikisikika kama mtu aliyekuwa kwenye maumivu makali mno.

“Pole sana!”

Rais Bokasa hakutaka kubaki nchini Tanzania, hakutaka kulipuuzia jambo hilo, alichokifanya siku iliyofuata ni kuondoka nchini Tanzania na kwenda Marekani, alihitaji kuzungumza na Mapoto, alitaka kufahamu sababu iliyompelekea kutaka kufanya maamuzi hayo.

Ndani ya ndege, rais huyo alikuwa na mawazo lukuki, kichwa chake kilichanganyikiwa mno, alikuwa kimya, safari hiyo ilionekana kuwa ndefu na yenye kuchosha kuliko safari yoyote ile aliyowahi kufanya katika maisha yake.

Mara baada ya kufika jijini New York nchini Marekani, akaelekea katika Hoteli ya Bavarian iliyokuwa na hadhi ya nyota saba na kutulia huko. Usiku wa siku hiyo hakutaka kuwasiliana na Mapoto, kwa kuwa alimwambia juu ya hospitali waliyokuwepo, kesho yake akaelekea huko na kukutana naye.

“Pole sana! Jitie nguvu, natumaini Irene atapona na kurudi katika hali yake ya kawaida,” alisema Rais Bokasa huku akimkumbatia Mapoto.

“Nashukuru sana!”

Matibabu yaliendelea hospitalini hapo, watu wengi walikuwa wakifika mahali hapo na kumpa pole. Kila mmoja alionekana kumuonea huruma balozi huyo, hatua aliyokuwa akipitia katika maisha yake ilikuwa ngumu kupita kawaida.

Mke wake, Rosemary ambaye alipoteza fahamu baada ya kupewa taarifa juu ya mtoto wake kupata tatizo la kichwa hakuwa amerudiwa na fahamu huku tayari zikiwa zimepita saa arobaini na nane.

“Daktari! Mke wangu anaendeleaje?” aliuliza Mapoto huku akimwangalia mkewe aliyekuwa kimya kitandani, tena huku akisaidiwa kupumia kwa kutumia mashine ya oksijeni.

“Anaendelea vizuri! Natumaini atakwenda kuwa mzima wa afya ndani ya siku hizi chake,” alijibu Dk. Phellips.

Baada ya saa kadhaa, mke wake akarudiwa na fahamu, kitu cha kwanza kabisa kuuliza kilikuwa ni mtoto wake. Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuamini kama kweli Irene, mtoto wake aliyekuwa akimpenda mno alikuwa kwenye hali hiyo.

Kitandani pale alikuwa akilia tu, alimwangalia mume wake huku muda wote akiwa anamlaumu juu ya sababu iliyomfanya kutokumpa taarifa tangu alipokuwa nchini Tanzania.

“Ilikuwa vigumu kufanya hivyo mke wangu! Najua ni jinsi gani unawapenda watoto wetu, kama ningekwambia wakati upo Tanzania, ungepata tatizo zaidi. Naomba unisamehe Rose,” alisema Mapoto huku akimwangalia mke wake.

Hali ya Irene haikuweza kubadilika kitandani hapo, japokuwa shuleni alionekana kuumia kidogo lakini alionekana kuwa na tatizo kubwa kichwani mwake kwani ilionekana kwamba alipokuwa ameanguka, kichwa chake kiliumia vibaya kwa ndani na kuifanya damu kuingia na kuvilia katika ubongo kitu kilichoonekana kuwa kibaya sana hasa kwa mtoto kama yeye.

“We must perfom craniotomy surgery,” (ni lazima tumfanyie upasuaji wa kichwa) alisema Dk. Phillips huku akiwaangalia madaktari wenzake.

“Will they agree with us?” (watakubaliana nasi?) aliuliza nesi mmoja.

“There are no other options,” (hakuna njia nyingine) alijibu Dk Phellips.

Hilo ndilo walilokubaliana, ilikuwa ni lazima Irene afanyiwe upasuaji wa kichwa kwani kulikuwa na donge dogo la damu lililovilia kwenye kichwa chake na kuganda.

Dk. Phellips akamuita Mapoto na mkewe na kwenda nao ofisini, walipofika huko, kwanza akawaelezea ugumu waliokuwa wakikutana nao, aliwaambia kuhusu donge dogo la damu na kwamba ilikuwa ni lazima wamfanyie upasuaji wa kichwa vinginevyo Irene angeweza kufa kitandani pale.

“Dokta....”

“Hakuna kitu kingine tunachoweza kufanya zaidi ya hicho! Hatuna jinsi, ni lazima tufanye kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba Irene anapona kabisa,” alisema daktari huyo.

Hawakuwa na jinsi, walitamani kumuona mtoto wao akirudi katika hali yake ya kawaida. Walijua kwamba kulikuwa na hatari kubwa katika kufanyiwa upasuaji wa kichwa kwa mtoto wao lakini wakakubaliana na daktari huyo.

Hakukuwa na muda wa kupoteza, siku iliyofuata, Dk. Phellips na timu yake wakajipanga vilivyo kwa ajili ya kazi hiyo ambayo ingechukua saa ishirini na mbili mpaka kukamilika.

Wakaweka kikao na kuanza kumjadili Irene, wakapitia ripoti ya tatizo lake lote na walipoona kamba wamepitia kila kitu, wakapanga muda wa kuanza upasuaji huo.

Si Mapoto wa Rosemary aliyeonekana kuwa na furaha, wote walikuwa na majonzi tele mioyoni mwao, kila walipokuwa wakimfikiria Irene na tatizo alilokuwa nalo wakahisi kabisa kwamba wangeweza kumpoteza mtoto wao kitu ambacho kingewauma mno.

Ilipofika saa 3:05 asubuhi, mlango wa chumba kile alicholazwa mtoto wao ukafunguliwa na kitana alicholazwa Irene kutolewa. Hawakuweza kubaki mahali walipokuwa, wakainuka na kukisogelea kitanda kile, wakainama na kumwangalia Irene.

“Irene mtoto wangu! Mungu akulinde, ninaumia moyoni, siamini kama wewe ndiye unayepitia hatua hii ngumu. Binti yangu, moyo wangu unaniuma sana, siwezi kuzuia jambo hili, siweza kufanya lolote lile zaidi ya kukukabidhi mikononi mwa Mungu aliye hai,” alisema Rosemary huku akibubujikwa na machozi.

“Mke wangu! Irene atapona. Ninamuamini Mungu wangu! Kama aliweza kumuokoa Daniel katika shimo lenye simba, kama aliweza kumfufua Lazaro, kama aliweza kumbadilisha Paulo kutoka kwenye ubaya mpaka utakatifu, amini hili ni jambo dogo sana kwa Mungu, ninaamini atamponya,” alisema Mapoto huku akimtoa mke wake kutoka katika kitanda alichokuwa Irene.

“Ninaumia mume wangu! Moyo wangu unachoma, moyo wangu unauma,” alisema Rosemary, machozi yake hayakukata.

“Mungu atamponya tu,” alisema Mapoto na kumkumbatia mke wake.

Alimwamini Mungu wake aliyekuwa akimwabudu, alijipa nguvu moyoni mwake. Manesi wale wakakisukuma kitanda kile mpaka katika chumba cha upasuaji na kisha mlango kufungwa.

“Unahisi Mungu wako atamponya? Umesikia lini mtu anayefanyiwa upasuaji wa kichwa akapona kirahisi namna hii? Huo ndiyo mwisho wa mtoto wako, hatoweza kuamka tena, atakufa na kulala kaburini milele,” ilisikika sauti moyoni mwa Mapoto, kila alipoikemea sauti ile, iliendelea kuzungumza moyoni mwake kitu kilichomtia hofu kubwa.

“Hatokufa…mtoto wangu hatokufa..” alisema kimoyomoyo kuijibu sauti ile.

“Endelea kujidanganya,” iliongezea sauti ile.

***

Mwandishi wa Gazeti la Siasa la Kioo, Samuel Matamshi alikuwa akifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Moyo wake ulihuzunika sana, hakuamini mtu kama Mapoto angeweza kufanya kitu kama kile, kuhamia katika chama tawala na wakati nyuma yake kulikuwa na idadi kubwa ya watu waliokuwa wakihitaji kumuona akiwa rais wa nchi hiyo.

Imani yake ilimwambia kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea, isingekuwa rahisi kwa mtu kama Mapoto kufanya uamuzi kama huo ambao ulikuwa mwiba mchungu kwa Watanzania wengi masikini.

Alitaka kufahamu kilichokuwa nyuma ya pazia, alisikia kwamba Mapoto aliachana na chama hicho, hizo zilikuwa tetesi lakini hakukuwa na taarifa iliyoandikwa kwenye gazeti lolote kuthibitisha ule uvumi uliokuwa ukiendelea kusikika.

Hakutaka kubaki nchini Tanzania, akazungumza na viongozi wake kwamba alitaka kuelekea nchini Marekani kufuatilia kile kilichokuwa kikiendelea kwa Mapoto nchini humo.

Hilo halikuwa tatizo hata kidogo, akaruhusiwa, akatafuta viza na vibali vingine vya kusafiria na alipotimiza masharti yote ya kuingia nchini Marekani, akaelekea huko kwa ajili ya kufanya kazi.

Waandishi wenzake walitaka kusikia taarifa kutoka kwake, walitaka kufahamu ni kitu gani kilichokuwa kimetokea, kwa kiasi fulani nchi haikuwa imetulia, kila kona ni jina la Mapoto tu ndilo lililokuwa likitajwa, halikukauka midomoni mwa watu na watu wengi waliokuwa wakilitaja, walilitaja kwa mabaya na si kwa mazuri.

Baada ya saa ishirini na tatu akaingia nchini Marekani, kipindi hicho kilikuwa ni cha baridi kali, akanunua koti kubwa na kuelekea katika hoteli ambayo aliweka oda ya chumba. Alipofika huko, akatulia kitandani na kupumzika kwani kesho yake alikuwa na jukumu zito la kumfikia Mapoto na kufanya naye mazungumzo huku akitaka kujua kila kitu.

Usiku ulipofika akalala, asubuhi na mapema akaamka na kuchukua teksi ambayo alihitaji impeleke katika ubalozi wa Tanzania hapo Marekani. Hilo likafanyika, dereva akampeleka huko ambapo baada ya kufika, akateremka kutoka garini na kulifuata geti.

“Tukusaidie nini?” aliuliza jamaa mmoja mweusi, alikuwa Mtanzania.

“Ninahitaji kumuona balozi.”

“Wewe ni nani?”

“Mwandishi! Samuel Matamshi!” alijibu huku akimuonyeshea kitambulisho.

“Ooh! Kumbe ndiye wewe? Nimefurahi kukuona, huwa ninasoma sana makala zako, hakika ni nzuri! Unafanya kazi safi sana, Mungu akubariki,” alisema jamaa huyo ambaye alikuwa mlinzi ubalozini hapo.

“Nashukuru sana.”

“Umesema umekuja kumuona balozi?”

“Ndiyo!”

“Ana wiki nzima hajafika ofisini!”

“Kwa nini?”

“Mtoto wake ni mgonjwa, juzi tu ametoka kufanyiwa upasuaji wa kichwa na hali yake si nzuri,” alijibu mlinzi yule.

Mlinzi huyo alimwambia Matamshi kila kitu kilichokuwa kimetokea. Mwandishi huyo akabaki kimya, alimwangalia mlinzi yule huku akionekana kutokuamini kile alichoambiwa.

Hapo ndipo alipogundua kwamba mwanaume huyo alikuwa kimya kutokana na matatizo aliyoyapata. Hakukuwa na mtu yeyote aliyejua hilo nchini Tanzania, kila mtu alimlaumu kwa kumuona msaliti aliyestahili kupigwa mawe na kufa kabisa.

Hakutaka kubaki hapo, alitaka kumsikia Mapoto mwenyewe, muda huohuo akapanda taksi na kuelekea katika hospitali aliyolazwa Irene. Njiani, kichwa chake kilichanganyikiwa, aliwalaumu viongozi wa Chama cha Tanzania National Party kwa kuamua kumfuta uanachama mtu huyo pasipo kujua kwamba kitu kilichomfanya kutokuandika barua ya kujiuzulu ni kwa sababu mtoto wake alikuwa kwenye matatizo makubwa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Hakuchukua muda mrefu akafika katika hospitali hiyo. Akamlipa dereva na kuelekea huko. Aliliona kundi la wanafunzi wengi wakiwa hospitalini hapo, hakujua kama wanafunzi wote hao walifika hospitalini hapo kwa ajili ya kumjulia hali mwanafunzi mwenzao, Irene ambaye alikuwa katika hali mbaya hospitalini hapo.

Akaelekea mpaka mapokezini ambapo baada ya kuuliza, akaelekezwa chumba alicholazwa Irene na kwenda huko. Nje, macho yake yakatua kwa Mapoto, mkewe, mtoto wake, Rais Bokasa na walimu waliokuwa hapo nje. Akawasogelea, akamsalimia Mapoto na mkewe ambao walikuwa kwenye majonzi mazito.

“Pole sana Mapoto,” alimwambia huku akimkumbatia.

“Nashukuru sana Matamshi. Nashukuru sana kwa kuja kuniona,” alisema Mapoto huku akimwangalia akiwa amekumbatiana na mwanaume huyo.

“Sitoweza kuzungumza kwa sauti. Hebu niambie huku tukiwa tumekumbatiana. Mbona hukuandika barua ya kujizulu?” aliuliza Matamshi.

“Twende chooni, nitakwambia yote,” alijibu Mapoto.

“Sawa!”

Wawili hao wakaondoka kuelekea chooni. Rais Bokasa alibaki mahali hapo huku akionekana kuwa na hasira, hakutegemea kuona mwandishi huyo akifika nchini Marekani kuzungumza na Mapoto, alitaka kuona kila kitu kikiendelea kuwa siri, kama kweli Watanzania waliamini kwamba mtu huyo alikuwa amewasaliti, alitaka jambo hilo liendelee kuwa hivyohivyo.

Kule chooni, wakasimama na kuanza kuongea mengi. Mapoto hakutaka kuficha, alimwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea kwamba aliandika barua hiyo kwa ajili ya kumtumia rais lakini bahati mbaya hata kabla hajaituma, alipokea simu kuhusu hali aliyokuwa nayo mtoto wake hivyo kuachana nayo.

“Kwa hiyo suala la kujiuzulu lipo palepale?”

“Ndiyo! Nitajiuzulu hali ya mtoto wangu ikiwa sawa. Kama nitajiuzulu sasa hivi inamaanisha kwamba nitarudishwa Tanzania. Sasa nikiwa kule, nitamuhudumia vipi mtoto wangu? Ni bora niendelee kubaki katika nafasi hiyo. Akipona tu, natuma barua,” alisema Mapoto huku akimwangalia mwandisshi huyo.

“Basi sawa!”

Walipomaliza wakatoka ndani ya choo hicho na kurudi kule walipokuwa. Muda wote Rais Bokasa alionekana kuwa na hasira mno, alijua fika kwamba mwandishi huyo angerudi nchini Tanzania na kuwaambia watu ukweli juu ya barua ile. Hakutaka kuona hilo likitokea, ilikuwa ni lazima amzibe mdomo mwandishi huyo kwani pasipo kufanya hivyo hali ingekuwa ya hatari zaidi.

Matamshi alikaa nchini Marekani kwa siku tatu tu, aliiandika habari kamili na kisha kuituma kwa barua pepe yake huku akitaka itolewe siku ambayo atakapokuwa nchini Tanzania.

Alipomaliza kila kitu, akapanda ndege na kurudi nchini Tanzania. Ndani ya ndege, alijiona kuwa mwanaume shujaa, alijisifia kwa kufanya kazi kubwa ambayo isingeweza kufanywa na mwandishi yeyote yule.

Hapo alipokaa kwenye ndege alikuwa na mwanaume mmoja, alikuwa mtu mzima kidogo, walianza kupiga stori na kuzungumza mambo mengi. Walichangamkiana na mzee yule aliposikia kwamba alikuwa mwandishi wa habari, alifurahi zaidi.

“Nitataka kuanzisha gazeti langu la siasa, nadhani nitafanya mawasiliano na wewe ili uje kunipa mawazo juu ya nini cha kufanya,” alisema mzee huyo huku akiwa kwenye tabasamu pana.

Wakakubaliana, walipofika Dar es Salaam, ndege ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Iliposimama, wakainuka na kuanza kuelekeea nje.

“Nina mizigo mingi sana, unaweza kunibebea mmoja hadi nje?” aliuliza mzee huyo.

“Hakuna shida.”

Wakaelekea sehemu ya kuchunguzia mizigo yao, walipoichukua, mzee yule akampa begi lake Matamshi ili amsaidie mpaka nje ambapo angechukua teksi na kuelekea nyumbani.

Huku akiwa na begi lile na kupiga hatua nje, ghafla akashtuka akisimamishwa na polisi wawili waliokuja mbele yake. Mzee yule hakusimama, aliendelea kupiga hatua kwenda mbele, na hata alipoitwa, hakugeuka.

“Simama hapo,” alisema polisi mmoja.

“Kuna nini?”

“Tunahitaji kukuchunguza!”

“Ili?”

“Tunahisi umebeba madawa yya kulevya!”

“Nimebeba madawa ya kulevya?”

“Ndiyo! Twende kwenye chumba kile,” alisema polisi mmoja na polisi wengine watatu kuongezeka.

Matamshi hakuonekana kuwa na hofu, alijua kabisa kwamba hakuwa muuzaji wa madawa ya kulevya, hakuwahi kuyatumia, hakutaka kupinga, akaondoka nao na kwenda kwenye chumba kimoja na kukaa huko.

Polisi wale wakaanza kuangalia mizigo yake, hakukuwa na kitu. Hapo ndipo walipoanza kulipekua begi lile alilopewa na mzee yule. Muda wote Matamshi alikuwa akitabasamu, alijijua kwamba alikuwa mtu msafi na hakuhusika kabisa na biashara hiyo haramu.

“Umejitetea sana kwamba hujabeba madawa ya kulevya, na haya ni nini?” aliuliza polisi mmoja huku akitoa mfuko wa madawa ya kulevya, Matamshi akapigwa na mshtuko, hakuamini kuona mzigo wa madawa ya kulevya ukitolewa ndani ya begi.

“Hapana! Huo mzigo siyo wangu! Ni wa mzee aliyeniambia nimbebee,” alijitetea huku macho yakiwa yamemtoka.

“Hahah! Wenzako wote wanaokamatwa husema hivyohivyo! Upo chini ya ulinzi,” alisema polisi mmoja na polisi mwingine kuchukua pingu na kumfunga mwanaume huyo.

“Jamani! Mimi siyo mzigo wangu huo!” aliendelea kujitetea huku akianza kulia.

“Sawa. Ila si ndiyo begi jingine ulilokuwa nalo!”

“Nilikuwa namsaidia yule mzee. Jamani! Nisikilizeni, mimi sihusiki na madawa, sijawahi kutumia wala kuuza. Jamani! Mimi ni mwandishi wa habari!” alisema Matamshi huku akilia kama mtoto.

“Utamwambia hakimu mahakamani! Ila miaka ishirini inakuhusu,” alisema polisi mmoja huku wakimchukua na kuondoka naye ndani ya chumba hicho.



Mapoto aliendelea kumuuguza mtoto wake, Irene aliyekuwa hoi kitandani. Kila siku katika maisha yake ilikuwa ni siku ya maombolezo, hakuacha kulia, alifarijiana na mkewe kwa kuamini kwamba kuna siku mtoto wao angesimama tena lakini kikafika kipindi mioyo yao ikakata tamaa kwa kuhisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa kumuona mtoto wao akiwa hai.

“Hivi kweli Irene atapona?” aliuliza Mapoto huku akimwangalia Dk. Phillips.

“Tunaamini hivyo!”

“Imani ni jambo la kiroho zaidi. Hebu niambie kibinadamu, kweli mnahisi atapona?” aliuliza Mapoto.

“Tunajitahidi sana kumrudisha katika hali ya kawaida, na ukweli ni kwamba atarudiwa na fahamu japokuwa hatujajua ni kwa muda gani. Hutakiwi kuwa na hofu, tumuachieni Mungu, kuna siku mtoto Irene atafumbua macho tena,” alisema Dk. Phillips.

Siku ziliendelea kwenda mbele, kitandani pale Irene hakuonyesha mabadiliko yoyote yale, alikuwa vilevile kama siku ya kwanza. Kula kwake, alikula kwa kutumia mipira huku hata kupumua alipumulia mashine ya oksijeni.

Kila siku walimu na wanafunzi wenzake walikuwa wakifika hospitalini hapo kumjulia hali. Godwin hakuwa na furaha tena, alitawaliwa na majonzi, kila alipokuwa akimuona dada yake akiwa kitandani alikuwa akilia tu.

Hakuacha kuwauliza wazazi wake juu ya Irene, alitaka kujua ni siku gani ambayo dada yake angeamka lakini hakukuwa na mtu aliyempa majibu ya kuridhisha na hivyo kuhisi kwamba inawezekana Irene angekufa kitandani pale.

“Will she open her eyes again?” (atayafumbua macho yake tena?) aliuliza Godwin huku akimwangalia baba yake.

“Yes!” (ndiyo)

“When?” (lini?)

“Very soon.” (hivi karibuni)

Hakuwa na jinsi, kila alipomwangalia Godwin alimuonea huruma, kila siku alikuwa akilia, kama yeye na Rosemary walivyokuwa wamekata tamaa basi hata naye Godwin alikuwa amekata tamaa.

Alimfariji, alimdanganya kwamba Irene angefumbua macho hivi karibuni japokuwa hakuwa na uhakika juu ya hilo. Siku zikaendelea kukatika, baada ya mwezi mmoja kidogo hali ya Irene pale kitandani ikaanza kuonyesha mabadiliko, vidole vyake vikaanza kuchezacheza kitandani pale.

“Vidole vyake vimeanza kuchezacheza,” alisema nesi aliyekuwa akimuhudumia kila siku.

“Kweli?” aliuliza Dk. Phillips.

“Ndiyo!”

Daktari huyo akatoka ndani ya ofisi yake na kuelekea katika chumba kile. Alikuwa akikimbia kiasi kwamba hata Mapoto na familia yake waliokuwa nje ya chumba kile wakashangaa na kuhisi kwamba ndani kulikuwa na tatizo.

Dk. Phillips akaingia ndani ya chumba kile, alionekana kuchanganyikiwa kwa furaha, ni kweli Irene alianza kutingisha vidole vyake kuonyesha kwamba alikuwa amerudiwa na fahamu. Alisimama na kuumwangalia mtoto huyo kitandani, kwa mbali sana akaanza kuyafumbua macho yake kwa kuangalia huku na kule.

Hawakuamini, baada ya kukaa kitandani kwa mwezi mzima, hatimaye leo mtoto huyo alikuwa amefumbua macho na kuwaangalia. Alionekana kushangaa, ni kama hakujua sababu iliyomfanya kuwa mahali hapo, alimwangalia daktari, hakujua walikuwa wakina nani.

“I want to see my Godwin,” (nataka kumuona Godwin wangu) alisema Irene kwa sauti ya chini huku akimwangalia Dk. Phillips ambaye uso wake ulitawaliwa na tabasamu pana.

“Doctor…tell us what is going on…you freaking us out…” (daktari tuambie ni kitu gani kinaendelea…umetutisha…) alisikika Mapoto nje ya chumba kile huku akigongagonga mlango, alionekana kuwa na hofu kubwa kwani kitendo cha kumuona daktari yule akikimbia kuelekea ndani ya chumba kile, alihisi kulikuwa na tatizo.

“Welcome back to the world,” (karibu tena duniani) alisema Dk. Phillips huku uso wake ukiwa na furaha tele.

***

Rais Bokasa alichukia, kitendo cha kumuona mwandishi Matamshi akielekea chooni na Mapoto alihisi kabisa kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea. Moyo wake uliwaka kwa hasira na muda wote alikuwa akimwangalia mwandishi huyo huku akionekana kuwa na hasira kupita kawaida.

Hakukuwa na jambo jingine la kufanya zaidi ya kumuua mwandishi huyo kwani aliamini kwamba kama angemuacha akafika nchini Tanzania na kupelekea taarifa juu ya kile kilichokuwa kikiendelea basi hali ingekuwa ya hatari na watu wangeshinikiza mwanasiasa huyo kuandika barua ya kujiuzulu.

Ilikuwa ni lazima amuue, hakukuwa na jingine ambalo lingetakiwa kufanyika zaidi ya hilo. Akawapanga watu wake kwa ajili ya kummaliza kwa sababu tu alitaka kutetea kiti chake cha urais.

“Mkuu! Hatutakiwi kumuua! Nilikuwa na wazo moja,” alisema kijana wake aliyekuwa amempa kazi hiyo.

“Lipi?”

“Tumfunge. Tukifanikiwa katika hilo, basi tumemuweza. Kama tukimuua, kuna watu watahisi kwamba wewe ndiye umehusika, huyu ni lazima tumfanyie kitu ambacho kitawafanya watu kutokugundua kitu chochote kile,” alisema kijana huyo aliyeitwa kwa jina la Edson Pius.

“Sawa. Tutamfunga vipi?”

“Tumuwekee mzigo wa madawa ya kulevya, akifika uwanja wa ndege, akamatwe!” alishauri.

“Tutamuwekeaje?”

“Hapo ndiyo uniachie mimi!” alisema Edson.

“Sawa.”

Alimuamini kijana huyo, alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa na uwezo mkubwa wa kufikiria, kazi hiyo akaiacha mikononi mwake kwa kuamini kwamba ingefanikiwa haraka iwezekanavyo.

Edson akamuandaa mwanaume mmoja ambaye alitakiwa kuondoka nchini Tanzania na kwenda Marekani haraka sana, huko alikuwa na kazi ya kurudi na mzigo mdogo wa madawa ya kulevya.

Hilo halikuwa tatizo, mtu huyo aliyetumwa akaelekea huko. Alikuwa mzee wa makamo ambaye alikuwa rahisi sana kuaminika na mtu yeyote yule. Alipofika, mzigo wa madawa ya kulevya ulikuwa umeandaliwa na kupakiwa katika mfuko mmoja wa mzee huyo ambaye alipitishwa sehemu ya VIP kwa kuwa na kitambulisho kilichoonyesha ni mfanyakazi kutoka katika ikulu ya Tanzania.

Alipoingia ndani ya ndege, akamtafuta Matamshi na kwenda kukaa naye. Alihitaji kumchangamkia ili asimkatalie kwa kitu chochote kile ambacho angemwambia mwisho wa safari.

Kwa kipindi kifupi tu wakawa marafiki wakubwa kana kwamba waliwahi kuonana kipindi kirefu nyuma. Matamshi hakugundua kama mzee huyo alikuwa na mambo yake, alimzoea kama abiria wengine na hata walipofika Dar es Salaam na kumwambia amshikie begi lake, mwandishi huyo hakuwa na hofu naye kabisa, alipofanya hivyo, akajikuta akikamatwa na polisi.

Polisi waliendelea kumshikilia Matamshi, wakamchukua na kuelekea naye katika kituo cha polisi kilichokuwa hapohapo uwanjani. Alikuwa akilia, aliendelea kuwaambia polisi kwamba hakuwa amehusika na madawa yale ya kulevya bali alikuwa amemsaidia mzee mmoja ambaye ndiye aliyempa begi lile lililokuwa na madawa hayo.

“Atakayekuamini, nina hakika huyo atakuwa binadamu wa kwanza duniani kuwa mpumbavu,” alisema polisi mmoja huku akimwangalia Matamshi.

Kukamatwa kwa Matamshi ndiyo ilikuwa habari ya mjini, watu waliomuona akiwa mikononi mwa polisi hawakujua ni kitu gani kilikuwa kimemtokea, walimfahamu kama mtu mzuri ambaye hakuwa na uchafu wowote ule, alionekana kuwa mtu mwema kwa kuwa aliifanya kazi yake kwa ufasaha mkubwa kwa kuwahabarisha watu kila kitu kilichokuwa kikitokea nchini Tanzania.

Taarifa za kukamatwa kwake zikasambazwa, kila mtu aliyesikia alishangaa, hawakujua sababu iliyopelekea kukamatwa kwake hivyo watu kuanza kufuatilia na kugundua kwamba alikuwa amebeba mzigo wa madawa ya kulevya.

“Nini?”

“Eti alikuwa amebeba mzigo wa madawa ya kulevya!” alisema jamaa mmoja huku akionekana kushangaa.

Walimfahamu mwanaume huyo, hakuwahi kujihusisha na biashara hiyo haramu, hawakujua nini kilitokea mpaka mwanaume huyo kubeba madawa ya kulevya na kukamatwa uwanja wa ndege.

Wengi walihisi kwamba kulikuwa na mchezo mchafu ulikuwa umechezwa, hawakujua mazingira ya mchezo huo na mtu pekee ambaye waliamini kwamba angewaambia ukweli ni Matamshi pekee ambaye alikuwa sero akilia.

Hakukuwa na mtu aliyeruhusiwa kumuona, si wafanyakazi wenzake wala familia, alishikiliwa huku akiandaliwa kupandishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kubeba madawa ya kulevya yaliyokuwa yakimkabili.

“Kazi imefanyika mkuu!” alisema Edson huku akionekana kuwa na furaha.

“Safi sana! Hicho ndicho nilichotaka kifanyike!” alisema Rais Bokasa kwa kuamini kwamba alimfunga mdomo mtu huyo na kusingekuwa na mtu yeyote ambaye angejua kile kilichokuwa kimetokea Marekani, hakujua kama habari iliandikwa hotelini na kutumwa kwa barua pepe.

***

Dk. Phillips akatoka ndani ya chumba kile, Mapoto na mkewe, Rosemary wakawa wakimwangalia kwa macho yaliyoonyesha walitaka kufahamu kile kilichokuwa kimeendelea ndani ya chumba kile.

Sura yake ilionyesha tabasamu pana, alionekana kuwa tofauti na siku nyingine, kwa muonekano huo tu ulionyesha kwamba kila kitru kilichokuwa kikiendelea ndani ya chumba kile kilikuwa salama.

“Kuna nini?” aliuliza Mapoto huku akimwangalia daktari huyo usoni.

“Mungu ametenda!”

“Imekuwaje? Amepona? Irene amepona?” aliuliza Rosemary huku akiwa amechanganyikiwa kwa furaha.

“Amefumbua macho, amepata nguvu na anazungumza,” alisema Dk. Phllips huku tabasamu lake likiendelea kuonekana usoni.

Mapoto akashindwa kuvumilia, palepale aliposimama akapiga magoti, akanyanyua mikono juu na kuanza kumshukuru Mungu.

Mwezi mzima walikuwa hospitalini hapo, alishindwa kufanya kazi zake, alikata tamaa kwa kuona kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa kumuona binti yake akiwa mzima tena lakini kwa nguvu za Mungu, hatimaye alipona na kuanza kuzungumza.

Hawakuamini kwa kusikia, waliona kwamba kulikuwa na uhitaji wa kuona kile walichoambiwa hivyo kumwambia Dk Phillips kwamba walitaka kumuona binti yao na kumsikia kwa masikio yao.

Hilo halikuwa tatizo, wakapelekwa ndani ya chumba kile. Wakapiga hatua mpaka katika kile kitanda alicholala Irene na kuanza kumwangalia. Walichoambiwa ndicho walichokiona, binti yao alikuwa amefumbua macho, na alipowaona, aliwatambua kwamba walikuwa wazazi wake.

Rosemary akashindwa kuvumilia, akaanza kutokwa na machozi ya furaha, alijisikia nguvu mpya moyoni mwake, hakutegemea kumuona mtoto wake akirudi katika hali aliyokuwa nayo.

Hiyo ilikuwa hatua ya kwanza Irene, aliendelea kulala kitandani hapo huku akiendelea kupata nafuu kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele. Moyo wa Mapoto ukafarijika, ukaanza kurudi katika hali yake ya kawaida, mawazo yakaisha na huo ukawa muda wa kurudi kazini kuendelea na kazi.

Alikutana na barua ile aliyotaka kuiandika kwa ajili ya kujiuzulu, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, ni kweli alitaka kufanya hivyo lakini tatizo lilikuwa moja tu, kama angejiuzulu inamaanisha kwamba angetakiwa kurudi nchini Tanzania.

Afya ya binti yake haikuwa imetengemaa, kama angerudi na kwenda kutibiwa nchini Tanzania, aliamini kwamba asingepata matibabu mazuri kama aliyokuwa akiyapata nchini Marekani, hivyo akaahirisha kwa muda zoezi lake la kujiuzulu.

“Rosemary! Nimeamua kuahirisha zoezi la kujiuzulu kwa ajili ya familia yangu,” alisema Mapoto, alikuwa akizungumza na mkewe walipokuwa nyumbani.

“Kwa nini?”

“Nimefikiria sana kuhusu matibabu! Kama tutarudi nchini Tanzania huku Irene akiwa kwenye hali hii, tunaweza kumpoteza, ni bora niendelee kubaki kama balozi kwa ajili ya Irene,” alisema Mapoto.

Wakakubaliana kwamba huo haukuwa muda wa kujiuzulu, akaachana na barua ile aliyokuwa ameiandika. Waliendelea kumuuguza Irene mpaka aliporudi shuleni na kuendelea na masomo na Rosemary kurudi nchini Tanzania.

Bado waliendelea kuwa vichwa darasani, walikuwa na akili nyingi mno, walimu hawakuisha kuwashangaa, kila siku watoto hao kwao walionekana kuwa na uwezo wa hali ya juu hali iliyowafanya Wazungu hao kushika vichwa, tena wakati mwingine walikuwa wakiumia kwa kuwa watoto waliokuwa wakiwaongoza walikuwa Waafrika na si Wazungu kama walivyotaka iwe.

***

“Ni kweli uulibeba madawa ya kulevya?” aliuliza mwanasheria wa kujitegemea wa Matamshi aliyeitwa Edwin Mwendapole.

“Hapana! Sikubeba madawa. Ningebeba vipi madawa na wakati siijui biashara hiyo? Sijui hata wateja wake ni wakina nani? Mwendapole, sikuwahi kubeba madawa,” alijitetea Matamshi.

“Sawa. Ila wanasema walikukuta na begi lenye madawa ya kulevya mikononi mwako,” alisema Mwendapole.

“Najua. Ngoja nikuhadithie ilivyokuwa,” alisema Matamshi na kisha kuanza kuhadithia.

Moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kama safari yake ya kuelekea nchini Marekani ingemfanya kuwa katika hali hiyo. Alikuwa akilia, alihadithia huku akiwa na maumivu makali moyoni mwake, kila kitu kilibadilika, alikuwa na ndoto za kuwa mwandishi mkubwa barani Afrika lakini mwisho wa siku safari yake ya kwenda Marekani ikamfanya kuwa gerezani.

Kukamatwa kwake kwa madawa ya kulevya ikawa stori kila kona nchini Tanzania, wapo watu waliosema kwamba alipakaziwa lakini pia walikuwepo watu waliosema kwamba kweli alibeba mzigo wa madawa ya kulevya kwa kuwa mshahara wake haukuwa ukitosha.

“Hii Tanzania bwana! Hata mchungaji utakuta naye anabeba madawa, ndiyo sembushe mwandishi wa habari!” alisema jamaa mmoja.

“Umeona! Yaani hakuna kumuamini mtu kwa sasa, ukimwamini hata baba yako, kuna siku utajuta wallahi!” alisema jamaa mwingine.

Walichokifanya waandishi wa habari ni kuandika habari kuhusu Matamshi. Hawakuficha, waliandika kila kitu kilichokuwa kimetokea ndani ya ndege, iliandikwa kwa mfumo wa makala ambapo watu walipoisoma, wakahisi kulikuwa na kitu, mzee huyo alikuwa ametumwa na mtu ambaye hakufahamika.

Ilikuwaje mtu huyo apite bila kukamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JFK? Ilikuwaje mtu huyo asionekana wakati akiingia? Ilikuwaje polisi wamtilie shaka sana Matamshi na wakati alikuwa mwandishi wa habari mkubwa tu? Mbali na hayo, kwa nini Matamshi alipokuwa akimuita mzee yule, polisi hawakumfanya kitu mzee huyo na matokeo yake kumchukua na kumpeleka katika chumba cha uchunguzi?

Kila swali ambalo watu walikuwa wakijiuliza, mwisho wa siku wakagundua kwamba huo ulikuwa ni mchezo uliopangwa, madawa ya kulevya yalipandikizwa kwa sababu fulani.

Uchunguzi ukaendelea kufanyika, watu walitaka kufahamu kile kilichokuwa kimetokea. Kwa kipindi hicho, suala hilo la madawa ya kulevya lilikuwa gumzo kila kona, kila mmoja alitaka kufahamu.

Gazeti la Kioo halikuishia hapo, likaandika kila kitu kilichotokea nchini Marekani kwamba Mapoto alitaka kuandika barua ya kutaka kujiuzulu lakini bahati mbaya mtoto wake alianguka na kupoteza fahamu, alishindwa kuandika kwa kuwa tu alikuwa kwenye hali ngumu ya kumuuguza mtoto wake.

Siku ambayo Matamshi alielekea hapo hospitali kumuona Mapoto, alikutana na Rais Bokasa ambaye alikuwa akimwangalia kwa jicho la chuki, na hiyo iliwezekana kuwa sababu kubwa ya kutaka kumpoteza mtu huyo kwa kuamini kwamba angesema ukweli juu ya kile kilichokuwa kikiendelea nchini Marekani.

“Huyu rais magumashi washikaji! Yeye ndiye atakuwa amehusika katika hili,” alisema jamaa mmoja huku akionekana kuwa na uhakika juu ya kile alichokuwa amekizungumza.

Hali ya hewa ikabadilika mitaani, kila mmoja akaanza kumshutumu rais kwamba alihusika katika shutuma ya usafirishaji wa madawa ya kulevya iliyokuwa ikimhusu mwandishi mashuhuri nchini, Matamshi.

Kelele zilikuwa nyingi kila kona, hata kabla mwandishi huyo hajapelekwa mahakamani tayari kukawa na tetesi kwamba wananchi walipanga kufanya fujo, kuchoma magari moto wakishinikiza mwandishi huyo aachiwe huru kwani kesi iliyokuwa ikimkabili ilikuwa imepandikizwa.

“Wananchi wanataka kuandamana na kufanya fujo,” alisema Waziri Mkuu, Bwana Donatius Marango.

“Wana nini hao wananchi?”

“Kivipi mkuu!”

“Wana bunduki?”

“Hapana.”

“Mabomu?”

“Hapana!”

“Sasa mnaogopa nini? Waambie polisi wawashambulie. Katika hili msilete kabisa mzaha, mtu yeyote akiingia mtaani kwa ajili ya kupambana, pambaneni naye, hii serikali yangu si ya masihara hata kidogo,” alisema Bokasa, alionekana kukasirika mno.

“Lakini mkuu…..”

“Marango! Unaogopa? Kama unaogopa acha niliambie jeshi liingie.”

“Hapana mkuu! Siogopi! Nitafanya hivyo! Nitawaambia polisi wafanye hivyo!”

Hiyo ilikuwa ni amri, hakukuwa na mtu wa kuipinga, kila alichokitaka Rais Boksa ndicho ambacho kilitakiwa kufanywa mahali hapo. Polisi wakajipanga, nao wananchi wakaingia mitaani katika siku hiyo ambayo mwandishi huyo alikuwa akipelekwa mahakamani, hawakutaka kuona wakionewa, kila mtu alitaka haki na waliamini hakukuwa na haki bila kupambana, ili upate kile unachokihitaji ilikuwa ni lazima kupambana.

“Waziri mkuu amesema tupambane nao. Ikiwezekana tuue pale kunapotakiwa kufanya hivyo,” alisema IGP, alikuwa akiwaambia wenzake.

“Unasemaje?”

“Nadhani umenisikia. Waambie polisi wajipange asubuhi hiihii. Yeyote atakayeonekana na silaha yoyote karibu na uwanja wa mahakama, huyo halali yetu,” alisema IGP.

“Sawa mkuu!” wakaitikia kwa pamoja. Japokuwa mikwara ilitangazwa kila kona na polisi hao lakini wananchi hawakusikia, walichokitaka ni kuona mwandishi huyo akiachiwa huru. Hivyo wakaingia mitaani.

***

Polisi walikuwa wakitoa tangazo kwamba wananchi wote waliokuwa karibu na viunga vya mahakama walitakiwa kuondoka haraka iwezekanavyo lakini hakukuwa na mtu aliyeelewa.

Hakukuwa na mtu aliyeonekana kuogopa kitu chochote kile, walichokuwa wakikitaka mahali hapo ni kumuona mwandishi nguri wa habari za siasa nchini, Matamshi akiachiwa huru au hata kwa dhamana kwani kesi iliyokuwa ikimkabili haikuwa ya kweli bali kulikuwa na watu waliotaka kumuweka kifungoni kwa maslahi yao na si kwamba alisafirisha mzigo wa madawa ya kulevya kutoka nchini Marekani.

Polisi waliendelea kutangaza zaidi na zaidi lakini hakukuwa na mwananchi aliyeelewa, kwao, waliamini zaidi katika maandamano, walijua kabisa kwamba serikali isingeweza kuwakubalia kitu chochote kile kama tu wasingeandamana.

Magari ya polisi yaliyokuwa na maji ya kuwasha yakafika mahali hapo, polisi wakaongezeka huku wakiwa na bunduki zao zilizokuwa na mabomu ya machozi, walisimama imara huku wakisubiri kupewa ruhusa ya kufanya kile walichotakiwa kufanya mahali hapo.

Wakati tangazo la kuondoka mahali hapo likiendelea kutolewa, basi kubwa la gerezani likaanza kuingia katika viunga vya mahakama hiyo na liliposimama, washtakiwa wakaanza kuteremka kutoka ndani ya basi lile.

Kitendo cha watu kumuona Matamshi, wakaanza kupiga kelele za shangwe huku wakiwataka polisi kumuachia mtu huyo, msafi ambaye hakuonekana kuwa na kosa lolote lile. Matamshi alikuwa kimya, alipowaona watu hao wakipiga kelele huku wakilitaja jina lake, akawaangalia, akatoa tabasamu pana kisha kuwapungia mikono.

“Mbona mnaonea sana, si mmuache na kama hamna kazi za kufanya mkalale,” alisikika mwananchi mmoja kwa sauti kubwa.

“Mwachieniiiiiiiiiii……mwachieniiiiiiii huyooooo,” walisikika watu kadhaa wakipiga kelele za kumtaka mtu huyo aachiwe huru.

Wananchi waigoma kabisa kuondoka mahali hapo mpaka pale Matamshi alipoingizwa mahakamani kwa ajili ya kujibu tuhuma zilizokuwa zikimkabili. Polisi hawakuchoka, waliendelea kuwahimiza watu hao waondoke mahali hapo lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyeelewa, walitaka kushuhudia mtu huyo akiachiwa huru kwa kile kilichokuwa kimetokea.

Waandishi wa habari waliendelea kubaki mahali hapo, waliwajua polisi, waliona kabisa kukitokea fujo mahali hapo, walitaka kupiga picha kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.

Hawakutaka kuishia kupiga picha, walipata nafasi ya kuwahoji baadhi ya waandamanaji ambao hawakuficha hisia zao, walisema wazi kile walichokuwa wakiikiona juu ya mwanaume huyo ambaye alikuwa akipambana usiku na mchana kwa ajili ya kufichua uovu wa serikali.

“Hapa hatuondoki. Huu uonevu umezidi! Za chinichini zinasema kwamba walimtumia yule mzee kwa ajili ya kumkamatisha Matamshi kuhusu uuzaji wa madawa ya kulevya, hii siyo fea,” alisema mwanaume mmoja.

“Kwa hiyo hamuondoki!”

“Hata kama wewe mwandishi! Unaanzaje kuondoka?”

Baada ya kukaa kwa dadkika thetahini, polisi wakaanza kupiga mabomu ya machozi mahali hapo huku wakiwamwagia maji ya kuwasha. Hakukuwa na mtu aliyebaki mahali hapo, wakaanza kukimbia kurudi katika Barabara ya Kawawa kwani kadiri mabomu yalivyozidi kupigwa mahali hapo, kila mmoja alihisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wake.

***

Rais Bokasa alikuwa kimya katika kiti chake, akili yake haikuwa sawa hata kidogo, hatua alizopitia katika uongozi wake zilimnyima raha, muda mwingi alionekana kuwa na mawazo tele.

Aliona kulikuwa na mambo mengi ya kufanya mbele yake, hakujua ni mahali gani alitakiwa kuanzia na kuishia. Wakati mwingine aliwaona watu wakiwa wamemzunguka, wakimzomea kwa kila kitu alichokuwa akikifanya.

Serikali ikaanza kukosa fedha, kodi zilizokuwa zikikusanywa kwa kiasi kikubwa zikapungua, akashikwa na hofu na wafanyabiashara kwa kuhisi kwamba walikuwa wakimzunguka, hawakuwa wakilipa kodi kama ilivyotakiwa kuwa.

Aliandaa mikutano na wafanyabishara mbalimbali na kuwaambia umuhimu wa kulipa kodi lakini hawakutaka kuelewa kwani kama wao wangeendelea kulipa kodi kama ilivyotakiwa basi kusingekuwa na shida yoyote ile.

Nchi ikaanza kuyumba kiuchumi, pesa ikakosekana mitaani, kila mtu aliyekuwa akiulizwa kuhusu pesa, alisema kwamba hakuwa nayo. Aliwalalamikia wafanyabiashara wengi, bado hofu yake ilikuwa ni kuhusu ulipaji wa kodi, aliamini kuwa wafanyabishara walikuwa wakikwepa ulipaji wa kodi hiyo.

Mahospitalini, watu walikosa dawa, vyuoni, idadi ya wanavyuo waliokuwa wakipelekwa ilipunguzwa na mikopo ikafungwa. Nchi ilikuwa kwenye hali ya hatari lakini alifanya hivyo kwa kuwa tu alitaka serikali ibaki na fedha, abane matumizi yaliyokuwa makubwa kwa ajili ya nchi yake.

Baada ya kufikiria sana, akagundua kwamba hata mabalozi waliokuwa katika nchi za nje ambao walikuwa wakiwasomesha watoto wao huko kwa kutumia pesa za serikali, walitakiwa kuwarudisha nchini na kusoma katika shule za hapahapa Tanzania.

Hakutaka kupokea ushauri juu ya jambo hilo, akawaita waandishi wa habari ikulu na kuwaambia kile kitu ambacho alikifikiria kwamba watoto wa mabalozi ambao walikuwa wakisoma nje ya nchi walitakiwa kurudishwa nchini Tanzania kwa kuwa tu nchi haikuwa na pesa ya kutosha.

“Warudi Tanzania?” aliuliza Mapoto, alikuwa akipewa taarifa na mkewe.

“Ndivyo alivyosema.”

“Daah! Kweli?”

“Ndiyo!

Mapoto alipokea taarifa hiyo kutoka kwa mke wake, alishtuka, hakutegemea kupta taarifa kama hiyo. Aliwapenda watoto wake, alitaka wapate elimu bora ambayo ingewafanya kuwa watu fulani huko baadaye, walikaa nchini Marekani kwa miaka minne na muda huo ulikuwa ni wa kurudi nchini Tanzania.

Hakupenda lakini hakuwa na jinsi, akamwambia mke wake kwamba Godwin na Irene wangerudi nyumbani nchini Tanzania haraka iwezekanavyo na hivyo ndivyo ilivyofanyika, wakarudishwa.

Huko, kwa kuwa bado familia ilikuwa na pesa, wakapelekwa katika shule ya watoto wa matajiri kwa ajili ya kusoma darasa la saba na kuendelea. Uwezo wao haukushuka, bado waliendelea kuongoza darasani kitu ambacho kila mwalimu alikuwa akiwashangaa.

Wazazi wao waliwekeza katika elimu yao, waliamini kwamba ili watoto wawe na maisha mazuri ilikuwa ni lazima wasome katika shule nzuri na kufanya vizuri na ndiyo maana walifanya kila liwezekanalo kuhakikisha watoto wao wanapata elimu bora.

“Do you still want to be a pastor?” (bado unataka kuwa mchungaji?) aliuliza Rosemary huku akimwangalia Godwin.

“Yes! I will preach the world of God around the globe,” (Ndiyo! Nitalihubiri neno la Mungu dunia nzima) alijibu Godwin.

Hakuwa na ndoto nyingine maishani mwake zaidi ya kuwa mchungaji. Alimpenda Mungu, alitaka kumtumikia katika maisha yake yote hapa duniani.

Kila siku alikuwa mtu wa kusali tu, alipenda kujifungia chumbani kwake na kusali kama kawaida. Shuleni alipokuwa akisoma, kwenye begi lake ilikuwa ni lazima kuwa na Biblia, pale alipokuwa akipata nafasi alikuwa akisoma kitu kilichowafanya wanafunzi wengine wa darasa la saba kumuita kwa jina la mchungaji.

Rosemary alifarijika, moyo wake ulikuwa na furaha tele, alimpenda sana mtoto wake, Godwin. Kitendo cha kushika sana dini kilimfanya kuwa na mapenzi makubwa kwake.

Siku ziliendelea kukatika. Baada ya watoto wake kumalizia mtihani wa darasa la saba, siku moja akiwa sebuleni amekaa na watoto wake wakiangalia televisheni, akapigiwa simu na mtu ambaye hakumfahamu aliyekuwa nchini Marekani.

Aliipokea simu hiyo na kuanza kuongea na mtu huyo ambaye alimwambia kwa kifupi kwamba kulikuwa na taarifa mbaya kutoka nchini humo.

“A bad news?” (taarifa mbaya?) aliuliza huku akionekana kushtuka.

“Yes mom!” (ndiyo mama)http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“What is it?” (habari gani?) aliuliza huku kijasho kikianza kumtoka na mwili kumtetemeka.

“Please calm down,” (tulia tafadhali)

“Just tell me about it….please tell me,” (niambie tu kuhusu hiyo habari….niambie tafadhali) alisema Rosemary kwa sauti iliyojaa hofu kubwa.

***

Wananchi wengi walijeruhiwa vibaya kwa sababu tu waliamua kuandamana kwa kuitaka mahakama kumuachia huru mwandishi mashuhuri Matamshi ambaye alikuwa ameshikiliwa kwa tuhuma za kuingiza madawa ya kulevya nchini Tanzania.

Baada ya kupigwa sana na polisi, huo ndiyo ulikuwa mwisho wa maandamano hayo, Kwa siku hiyo, kesi hiyo ilisikilizwa na mwandishi huyo kurudishwa rumande na hivyo kutakiwa kurudi mahakamani hapo baada ya wiki mbili.

Hiyo ilikuwa kesi nzito iliyotingisha sana katika vyombo mbalimbali vya habari, kwenye kila kona, watu walikuwa wakiizungumzia kesi hiyo, magazeti hayakutoka bila kuandika kuhusu tuhuma hizo nzito, waandishi wa habari wakaungana na hata kwenye televisheni, habari kubwa ilikuwa ni ya mwandishi Matamshi huku kila mmoja akiituhumu serikali kwa kushindwa kumsikiliza mtu huyo alipokuwa akiwaambia ukweli kwamba hakusafirisha madawa ya kulevya.

“Basi apimwe kwa mkemia mkuu wa serikali kuona kama anatumia madawa hayo,” alishauri waziri mkuu.

Serikali ilikuwa na presha kubwa, kwa jinsi wananchi walivyoonekana kuchachamaa walijua kabisa kwamba suala hilo lilionekana kuwa dogo lakini kwa upande wa pili lilikuwa kubwa mno.

Walitaka kumuachia mwanaume huyo huru lakini hawakutaka kumuachia hivihivi bali kilichofanyika ni kumpima na mkemia mkuu kujiridhisha kwamba Matamshi hakuwa akitumia madawa ya kulevya.

“Kwa hiyo?”

“Kesi iahirishwe, kwanza akae rumande hata miezi sita halafu ndiyo aachwe huru,” alisema rais alipokuwa akizungumza na waziri mkuu.

“Sawa.”

Hilo ndilo lililofanyika, Matamshi aliendelea kusota rumande na kila alipokuwa akipelekwa mahakamani, kesi yake iliahirishwa na kutakiwa kusikilizwa tena siku nyingine.

Alihangaika, waandishi waliendelea kumtetea mwandishi mwenzao kwa kutumia kalamu zao na baada ya miezi sita, mwandishi huyo akashinda kesi kwa kuonekana kwamba kweli si yeye aliyekuwa akiingiza madawa ya kulevya.

“Umeshinda kesi, ukijaribu kuishitaki serikali, utapotea katika mazingira ya kutatanisha,” alisikika mwanaume kwenye simu, alikuwa akimwambia Matamshi.

“Sawa. Sitofanya hivyo!” alisema Matamshi huku akionekana kuogopa, kwa jinsi serikali ilivyokuwa na mkono mrefu, alijua tu kwamba kama asingefanya kile walichokitaka, kweli wangempoteza.

***

Baada ya familia yake kurudi nchini Marekani, Mapoto hakuonekana kuwa na furaha hata kidogo, upweke ukamuingia kwani aliizoea familia yake na alitamani kuwa nayo miaka yote.

Alikuwa akiwasiliana nao kama kawaida, aliwapenda na kwake walikuwa kila kitu. Aliendelea kumsisitiza mke wake kwamba watoto wao walitakiwa kupata elimu bora kwa ajili ya maisha yao ya baadaye na ndiyo maana baada ya kufika nchini Tanzania, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuwapeleka katika shule ya watu wenye fedha na kuwataka wasome hapo.

“Najua elimu ndiyo kitu pekee ambacho kitakuja kuwasaidia hapo baadaye,” alisema Mapoto wakati akiongea na mkewe kwenye simu.

“Nitahakikisha wanapata elimu bora,” alisema Rosemary.

Maisha yaliendelea kama kawaida, kila siku alikuwa na jukumu la kuamka asubuhi na mapema na kuelekea ofisini mwake na kufanya kazi zake kama kawaida.

Siku ya Jumatatu ya tarehe 07/10/2002, kama kawaida yake Mapoto akaamka asubuhi na mapema kwa ajili ya kwenda kazini. Siku hiyo alitaka kuwasiliana na mwenyekiti wa Chama cha Tanzania National Party, Edward na kumwambia mpango wake wa kurudi nchini Tanzania mwezi wa kumi na mbili kwa ajili ya kufanya kampeni za uchaguzi mkuu wa Tanzania uliotakiwa kufanyika mwezi Juni mwaka 2003.

Alipokuwa ndani ya gari, akampigia simu na kumwambia kwa kifupi juu ya kitu ambacho walitakiwa kuzungumza kwa kirefu kwani asingeweza kuendelea kubaki nchini Marekani na wakati alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi nchini Tanzania na kuwa rais wa nchi hiyo.

“Sawa. Ukifika ofisini niambie. Huku kwetu ni jioni sasa nafikiri nitapata muda mzuri wa kuongea nawe,” alisema Edward.

“Haina shida.”

Baada ya kuzungumza kwa kifupi, akaendelea na safari, hakuchukua muda mwingi akafika ofisini ambapo kitu cha kwanza kabisa kukifanya kilikuwa ni kuinua simu yake ya mezani na kumpigia Edward.

Siku hiyo walizungumza mambo mengi, walipanga vitu mbalimbali juu ya kuiteka tena Tanzania, kuwaambia wananchi kwamba huo ndiyo ulikuwa muda sahihi wa ukombozi.

Bado Watanzania walihitaji mabadiliko, kila mtu alijiandikisha kwa ajili ya kupiga kura kwani kitendo cha kuwa na kadi ya kupiga kura ilimaanisha kwamba ungepiga kura na kumchagua kiongozi uliyekuwa ukimtaka, na wengi waliaidi kumwangusha Bokasa na kumchagua kiongozi wa chama pinzani.

“Mwaka ujao tunashinda, cha msingi ni kuziba mianya yote ya wizi wa kura na kuwataarifu watu juu ya upigaji kura ili tusije kuchezewa mchezo kama mwaka ule,” alisema Edward.

Alifanya kazi zake kama kawaida, ilipofika mchana, muda wa kurudi nyumbani akaingia ndani ya gari lake na kuanza kurudi nyumbani. Wakati gari likiwa linaingia katika barabara kubwa ya Lansdowne, ghafla wakakutana uso kwa uso na gari moja kubwa ambalo lililigonga gari lao, na kwa sababu lilikuwa kwenye mwendokasi, gari la balozi Mapoto likaharibiwa vibaya kiasi kwamba ilikuwa ni vigumu kuamini kama ndani ya gari hilo kungekuwa na mtu ambaye angetoka salama.

“Mungu wangu!” alisema mwanaume mmoja aliyekuwa kwenye gari jingine.

Kila mtu alishtuka, ajali iliyokuwa imetokea ilikuwa mbaya mno, gari la balozi Mapoto liliharibika vibaya na watu waliposogea kuangalia, kulitapakaa damu na hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akitingishika kuonyesha kwamba alikuwa hai.

Ulikuwa ni uzembe mkubwa mno kwani gari la balozi Mapoto lilikuwa katika njia yake lakini gari kubwa ambalo liliwagonga halikuwa kwenye njia yake, lilihama kutoka kati magari yanayoelekea upande wa Mashariki na kuhamia katika upande wa magari yanayokwenda upande wa Magharibi.

Ilikuwa ni ajali mbaya mno, kila mmoja aliyeiona, aliogopa, alitetemeka kwani katika histori ya ajali za barabarani hasa katika Jiji la New York, hakukuwa na ajali mbaya ya magari kugongana ambayo iliwahi kutokea kama ilivyokuwa ajali hiyo.

Hakukuwa na sababu ya kuyasubiri magari ya wagonjwa yafike mahali hapo, watu waliokuwa na magari binafsi wakajitolea kuibeba miili ile iliyokuwa ndani ya gari lile na kuipeleka katika Hospitali ya St. Monica Medical Centre ambayo haikuwa mbali kutoka mahali ilipotokea ajali hiyo.

“Vipi?” aliuliza nesi mara baada ya kuipokea miili hiyo.

“Ajali!”

“Ya ndege?” aliuliza huku akionekana kushangaa kwani kwa jinsi miili ile ilivyokuwa, ilikuwa vigumu kuamini kama ilikuwa ni ajali ya gari.

“Hapana! Gari!”

“Gari?”

“Ndiyo!”

Watu waliokuwa hospitalini hapo hawakuamini kile walichokuwa wakikiona, waliogopa, picha iliyokuwa ikionekana ilimtisha kila mmoja. Ni kweli kwamba waliwahi kuona ajali mbaya zilizokuwa zikitokea lakini kwa miili ile waliyokuwa wakiiona, walijua kabisa kwamba hiyo ilikuwa ajali mbaya ambayo hawakuwahi kuiona jijini hapo.

Miili ile ikachukuliwa, haikupelekwa katika chumba cha upasuaji, moja kwa moja ikapelekwa mochwari kwani hakukuwa hata na mtu mmoja aliyeonekana kuwa mzima.

Ilikuwa ni vigumu kuzitambua maiti zile ila kilichowafanya watu kugundua kwamba alikuwa ni balozi wa Tanzania, Mapoto ni namba za gari alizokuwa akizitumia.

“Kumbe ni balozi!”

“Huyu aliyekufa?”

“Ndiyo!”

Polisi walikuwa na taarifa hiyo, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuwasiliana na serikali ya Tanzania na kuwaambia kile kilichokuwa kimetokea lakini pia ilikuwa ni lazima kuitaarifu familia yake na hivyo kuchukua simu ya balozi MApoto na kumpigia mkewe kwa ajili ya kumpa taarifa.

“Mumeo amefariki!” ilisikika sauti ya upande wa pili.

“Mume wangu amefariki?”

“Ndiyo!”

Miguu ya Rosemary ikakosa nguvu, hapohapo akakaa chini na kuanza kulia kama mtoto.



Rosemary alilia kwa uchungu, moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kile alichoambiwa kwenye simu kwamba mume wake mpendwa, Mapoto alikuwa amefariki dunia.

Hakuishia kulia tu, baada ya muda akapoteza fahamu na mtu wa kwanza kabisa kumsaidia alikuwa mfanyakazi wa ndani ambaye akawaita majirani zake na walipofika, wakambeba na kuondoka naye kuelekea katika Hospitali ya Upendo wa Mungu iliyokuwa Masaki jijini Dar es Salaam.

Godwin na Irene walikuwa na hofu, hawakujua ni kitu gani kilitokea kwa mama yao, waliogopa, wakati mwingine nao walikuwa wakilia kwa kuamini kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa mama yao mpendwa.

Hospitalini hapo, mfanyakazi wa ndani hakutaka kuwaambia kilichokuwa kimetokea, alihisi kwamba mwanamke huyo alikuwa amefariki na kama angewaambia watoto hao ilikuwa ni lazima kulia sana kitu ambacho hakutaka kabisa kukiona kwani moyo wake uliwaonea huruma.

Rosemary aliwekewa dripu, aliendelea kulala hospitali na baada ya saa moja, akayafumbua macho yake na kuanza kuangalia huku na kule. Hakuelewa alikuwa wapi, ilikuwaje mpaka dripu kuning’inia juu yake lakini baada ya kukumbuka kilichokuwa kimetokea, akaanza kulia tena, kumbukumbu juu ya mume wake zikamrudia kitu kilichomfanya kuwa kwenye huzuni kubwa.

“Mume wangu amekufa…” alisema huku akimwangalia nesi ambaye alionekana kushtuka.

“Mumeo amekufa?”

“Ndiyo! Nilipigiwa simu na kuambiwa hivyo. Mungu! Kwa nini umemchukua mume wangu?’ aliuliza Rosemary na kuanza kulia tena.

Kitendo cha nesi yule kuambiwa hivyo, akatoka ndani ya chumba kile na kuelekea katika ofisi ya daktari na kumwambia hali aliyokuwa nayo mgonjwa. Nesi huyo hakuishia hapo, akachukua simu yake na kuwaambia marafiki zake kwamba Balozi Mapoto alikuwa amefariki dunia nchini Marekani.

“Amefariki! Wewe nani kakwambia huyo ubuyu?” aliuliza rafiki yake kwenye simu.

“Mkewe.”

“Umeonana naye?”

“Amekuja hapa hospitali akiwa amepoteza fahamu, na yeye ndiye aliyesema kwamba mumewe amefariki,” alisema nesi huyo.

“Jamaniiii! Huyo ndiye niliyetaka kumpa kura yangu mwaka kesho,” alisema rafiki yake huyo.

Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kusambazwa kwa taarifa hiyo, kupitia marafiki zake aliokuwa amewapigia, nao wakawapigia marafiki zao na hatimaye taarifa hiyo kuwafikia waandishi wa habari.

Waandishi hawakutaka kuchelewa, walitaka kujua ukweli juu ya kile kilichotokea hivyo kwenda katika hospitali hiyo na kuhitaji kuonana na Rosemary. Hilo lilionekana kuwa jambo gumu, daktari mkuu wa hospitali hiyo hakuruhusu jambo hilo kwani mgonjwa wake alihitaji muda wa kupumzika.

“Ila sisi tunataka kujua ukweli. Yaani aseme ndiyo tu, halafu kujaza gazeti tuachie sisi,” alisema mwandishi wa habari kutoka katika Gazeti la Kumekucha.

“Hapana!”

“Dokta! Yaani kuzungumza naye kidogo tu! Tunakuomba dokta, Watanzania wangependa kusikia kuhusu hili,” alisema mwandishi huyo lakini daktari hakutaka kukubaliana naye, alimwambia kwamba yeye na wenzake walitakiwa kusubiri mpaka Rosemary atakapopumzika vya kutosha.

Hawakuwa na jinsi, walitakiwa kusubiri mahali hapo. Hawakuondoka kwani Mapoto alikuwa mtu mwenye nguvu nchini Tanzania, aliheshimika na kila mmoja aliamini kwamba mwaka unaofuata mwanaume huyo angekuwa rais wa Tanzania kwani kila mmoja aliiandaa kura kwa ajili yake.

Walisubiri kwa saa mbili ndipo wakaruhusiwa kuzungumza na mwanamke huyo. Aliwaambia ukweli kwamba alipigiwa simu kutoka nchini Marekani na kuambiwa kwamba kweli mumewe alikuwa amefariki dunia.

“Kwa hiyo huna uhakika?” aliuliza mwandishi wa habari.

“Sijajua! Sijui chochote kile.”

“Basi subiri! Utajua ukweli!”

Walichokifanya baadhi ya waandishi ni kupiga simu nchini Marekani na kuwaambia marafiki zao kwamba walitakiwa kufuatilia kile kilichokuwa kimetokea. Hilo halikuwa tatizo, marafiki hao wakafuatilia mpaka katika hospitali ambayo waliamini kwamba inawezekana mwili wa Balozi Mapoto ungekuwa umefikishwa huko, walipofika, wakapewa taarifa juu ya mwili uliokuwa umeletwa kwamba ulikuwa ni wa balozi wa Tanzania nchini humo.

“Kweli amekufa!” alisema mwanaume aliyetumwa.

“Mwili upo hospitali gani?”

“St. Monica Medical Centre.”

Hiyo ilitosha kabisa kuandika habari hiyo iliyosisimua. Kesho, magazeti yakawa na taarifa ya kifo cha Balozi Mapoto. Watu hawakuamini, kitu cha kwanza kabisa walichohisi ni kwamba serikali ilihusika katika kifo chake lakini baada ya kuambiwa kilichotokea, jinsi kifo kilivyokuwa, wakagundua kwamba ilikuwa ni ajali tu, kitu ambacho hakukuwa na mtu wa kupewa lawama.

“Ni ajali! Ila nasikia ilikuwa mbaya sana,” alisema mwanaume mmoja.

“Wacha weee….”

Katika kipindi hicho cha mwaka 2002, mitandao ya kijamii iliyokuwepo kama Yahoo na Bearshare haikuwa na nguvu hivyo ilikuwa ni vigumu kupata taarifa kutoka katika mitandao ya kijamii, kila mmoja alitegemea magazeti na televisheni.

Tanzania ikanyamaza, ikaomboleza, kifo cha Balozi Mapoto kilimsisimua kila mmoja. Vilio vilitawala kila kona, hakukuwa na mtu aliyekuwa na furaha kwani mtu ambaye alikuwa amekufa alikuwa mtu wa watu, tumaini jipya kwa Watanzania, mtu ambaye alikuwa mabadiliko sahihi kwa Watanzania wote.

Rosemary hakutaka kubaki nchini Tanzania, akapanga kuondoka na kuelekea nchini Marekani, alitaka kwenda kuuona mwili wa mume wake hospitalini lakini hata kabla hajafanya hivyo, akapigiwa simu na rais na kuanza kuzungumza naye.

Kwanza akampa pole kwa kile kilichotokea, akamfariji katika kipindi kigumu alichokuwa akipitia lakini pia alimwambia kwamba serikali yake ingefanya kila liwezekanalo kuupeleka mwili wa Balozi Mapoto nchini Tanzania.

Hilo ndilo lililofanyika, siku mbili baadaye, mwili wa mwanaume huyo ukaingia nchini Tanzania. Uwanja wa ndege watu walijaza kupita kawaida, wengi hawakuamini kama kweli mwanaume huyo alikufa nchini Marekani, walitaka kujionea wenyewe, walitaka kuona kama kweli aliyekufa alikuwa Balozi Mapoto waliyekuwa wakimpenda au mtu mwingine.

“Inauma sana, ni bora angekufa ndugu yangu yeyote yule kuliko Mapoto,” alisema mwanaume mmoja, alionekana kuguswa sana na msiba wa Mapoto.

“Wewe ni kama mimi. Huu ni msumari wa moto moyoni mwangu na sidhani kama utaweza kupoa. Kweli mapoto amekufa! Kweli nimeamini Mungu anataka Watanzania tuendelee kuteseka milele na milele, sijui tumemkosea nini sisi,” alisema mwanamke mmoja, kama alivyokuwa mwanaume yule wa kwanza, hata naye alikuwa na maumivu makali moyoni mwake.

Nyumbani kwake kulikuwa na idadi kubwa ya watu, vilio vilitawala kila kona, kila aliyekuwa mahali hapo sura yake ilionyesha majonzi makubwa, hakukuwa na aliyeamini kama huo ndiyo ulikuwa mwisho wa mwanaume huyo aliyedhamiria kuibadilisha Tanzania.

Watoto wake, Godwin na Irene walilia mno, mioyo yao iliwauma kupita kawaida, walionekana kuwa na huzuni mno. Japokuwa ndugu zao wengine walikuwa wakiwabembeleza na kuwataka kunyamaza lakini hawakunyamaza, waliendelea kulia zaidi.

Kila mtu aliyekuwa nyumbani hapo alikuwa akizungumza lake, wengine walisema kwamba inawezekana marehemu aliuawa lakini watu wengine walibisha hilo kutokana na mazingira ya kifo jinsi yalivyokuwa.

“Kuna gari lilifika na kuligonga gari lake, unadhani kuna mtu atakuwa amemuua?” aliuliza jamaa mmoja.

“Huwezi kujua lakini!”

“Hakuna kitu kama hicho! Halafu nchi kama Marekani, utapanga vipi mipango ya kumuua mtu kwa ajali halafu nchi isijue? Ni ajali, tukubali kwamba ni ajali na tugange mambo yajayo,” alisema mwanaume mwingine huku akiwaangalia watu wachache waliokuwa wamemzunguka.

Hicho kilikuwa kipindi kigumu mno, kilikuwa kipindi cha masikitiko kwa kila mtu aliyetamani mabadiliko nchini Tanzania. Msiba huo ulihudhuriwa na watu wengi, viongozi mbalimbali kutoka katika nchi nyingi walifika Tanzania kwa ajili ya kumzika balozi huyo ambaye alikuwa mtu aliyedhamiria kuibadilisha Tanzania.

Rais Bokasa alikuwa kwenye majonzi makubwa, hakuamini kile kilichotokea. Kwake, Mapoto alikuwa mtu wa nguvu, mwenye kufanya kazi kwa kujitolea japokuwa alikuwa mtu aliyesimama katika chama tofauti na chama alichokuwa.

Msibaki hapo alishindwa kuyazuia machozi yake, aliumia moyoni na hata macho yake yalikuwa mekundu mno kuonyesha kwamba kabla ya kufika msibani hapo alikuwa amelia vya kutosha.

Kila mtu aliyemwangalia, alimuonea huruma, ilikuwa vigumu kumuona rais huyo akilia, kila mmoja aliamini kwamba alikuwa na roho mbaya, ambaye kila siku alitamani lolote baya litokee kwa Balozi Mapoto, lakini siku hiyo, kila mmoja hakuamini alichokuwa akikiona.

“Mpaka rais imemuuma! Huu msiba umegusa watu wengi sana,” alisema jamaa mmoja huku akimwangalia Rais Bokasa ambaye alishindwa kabisa kuyaficha majonzi yake.

Baada ya siku mbili, mwili wa Balozi Mapoto ukazikwa katika Kijiji cha Matombo mkoani Morogoro. Ilikuwa ni siku ya masikitiko mno, Rosemary alishindwa kuvumilia, akalifuata kaburi la mumewe na kuanza kugalagalaga juu yake, moyo wake ulimuuma kupita kawaida na kila mtu aliyemwangalia mwanamke huyo, moyo wake ulimuonea huruma.

“Mume wangu! Kwa nini unaniacha? Nitabaki na nani? Nani atakuwa mfariji wangu? Kwa nini umeondoka mume wangu? Kwa nini Mungu amekuchukua mapema hivi? Nitaishi na nani mimi?” aliuliza Rosemary huku akilia kama mtoto juu ya kaburi la mume wake.

***

Ulikuwa ni msiba mzito uliotokea nchini Tanzania, kila mtu alihuzunika, furaha ikatoweka mioyoni mwa Watanzania wengi. Mtu ambaye walimwamini kwamba angeweza kuyabadilisha maisha yao, aliondoka, Mungu alimchukua hata kabla hajapata nafasi hiyo.

Vijana wengi wakakata tamaa, walitamani kuona Tanzania ikiingia katika mabadiliko ya kweli, hawakukipenda Chama cha Labour Party, hawakumpenda Rais Bokasa kwa sababu hakujua kitu chochote kile kuhusu uongozi, aliongoza ilimradi tu kitu kilichowafanya watu wengi kuumia.

Ilikuwa imebaki miezi kadhaa kabla ya kuingia katika uchaguzi mkuu. Kuanzia kipindi hicho maisha yakawa magumu zaidi, serikali ikabana fedha kwa ajili ya kuitumia katika kipindi cha uchaguzi. Wananchi wakakosa pesa, mitaani hakukuwa na pesa tena hali iliyofanya hata matendo ya kikatili, wizi kuongezeka.

“Hakuna hela!” alisema kijana mmoja.

“Ndiyo! Rais amezibana eti kwa sababu ya uchaguzi wa mwaka kesho! Hii siyo haki kabisa,” alisema jamaa mwingine.

“Nyamaza! Ukisikiwa tu, msala. Hutakiwi kumwamini mtu yeyote yule, jikaze kisabuni kwani usalama wamemwagwa kila kona,” alisema jamaa mwingine na kumfanya jamaa aliyeanzisha mazungumzo hayo kunyamaza.

Hakukuwa na unafuu, Watanzania wenyewe waliichukia nchi yao, wengine wakadiriki hata kukimbia na kwenda nje ya nchi, matajiri hawakutaka kukaa nchini humo, walichokifanya wao na familia zao kuondoka na kuelekea Dubai, Oman, Marekani na sehemu nyingine kuendelea na maisha yao.

Kila kitu kikawa shaghalabaghala, ugumu wa maisha ukatawala kila kona, masikini walilia, kwa kile kiasi kidogo walichokuwa nacho ikawa kama wamenyang’anywa, ili upate pesa ilikuwa ni lazima ufanye kazi kwa nguvu, pesa iliyokuwa ikipatikana kwa urahisi, haikupatikana tena.

Maisha ya Rosemary na watoto wake yalibadilika, hakukuwa na furaha tena, kila siku kwao ilikuwa ni majonzi mazito. Kifo cha mapoto kilibadilisha maisha yao yote, kwa watoto wake, Godwin na Irene, nyumbani hawakuwa na furaha tena, hawakuwa kama zamani kwani baba yao ambaye ndiye alikuwa furaha kubwa mioyoni mwao hakuwa nao tena, baba yao ambaye kila siku aliwauliza kuhusu ndoto zao aliondoka maishani mwao.

Matokeo ya darasa la saba yalipotoka, walifaulu vizuri na hivyo kutakiwa kujiunga katika shule za sekondari, Godwin alichaguliwa kujiunga na Shule ya Wavulana ya Azania huku dada yake, Irene alitakiwa kujiunga na Shule ya Wasichana ya Jangwani alipokuwa akifundisha mama yake.

Bado walikuwa na fedha, Rosemary hakuona kama shule hizo zilikuwa sahihi kwa watoto wake, kama alivyokubaliana na mumewe kwamba Godwin na Irene walitakiwa kupata elimu bora, akaamua kuwapeleka katika shule nyingine ya watoto wa matajiri na viongozi serikalini iliyoitwa Kingston iliyokuwa Mikocheni B jijini Dar es Salaam.

Huko, masomo yalianza, hawakubadilika, bado walikuwa na uwezo mkubwa darasani, walijua kuzungumza Kiingereza kizuri, walipendwa shuleni hapo, walifanana na hata uwezo wao darasani ulikuwa mkubwa kiasi kwamba hata walimu wa shule hiyo walitamani sana kuona watoto wale wakiwa watoto wao.

“Hawa ndiyo watoto wa Balozi Mapoto?” aliuliza mwalimu mmoja.

“Ndiyo!”

“Mmh! Hawa watoto wana uwezo wa ajabu sana. Ni magenius, wana akili kupita kawaida,” alisema mwalimu huyo huku akionekana kushangaa.

Huo ulikuwa mwaka wao wa kwanza katika shule hiyo, walisoma bila tatizo lolote lile na hata mwaka ulipokwisha, walifanya vizuri na kuongoza kwa wanafunzi wote wa kidato cha kwanza.

Kufaulu kwao vizuri ilikuwa ni kama zawadi kwa baba yao ambaye kila siku aliwaambia kuwa walitakiwa kusoma kwa bidii kwani kusingekuwa na kitu chochote ambacho kingewatoa pale walipokuwa mbali na elimu. Mwaka huo ukamalizika, ulipoingia mwaka wa pili na kuendelea na masomo yao ndipo matatizo yalipoanza rasmi.

“Mama! Kuna karatasi imetoka Benki ya Watu,” alisema mwanaume mmoja aliyekuwa amemfuata Rosemary shuleni alipokuwa akifundisha.

“Kutoka benki?”

“Ndiyo!”

“Inasemaje?”

“Sijajua!”

“Na wewe nani?”

“Mleta barua kutoka hapohapo benki!” alijibu kijana huyo, hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, akaondoka zake.

Rosemary akawa na hofu, hakujua ni kitu gani kilichokuwa kimetokea, hakujua sababu iliyomfanya kupokea barua hiyo, hakujua ilikuwa ni barua ya nini, akaifungua bahasha ile na kuanza kuisoma.

Ilikuwa ni barua fupi iliyompa taarifa kwamba alitakiwa kunyang’anywa nyumba aliyokuwa akiishi kwa kuwa mume wake aliiweka kama dhamana alipokwenda kuchukua mkopo wa shilingi milioni mia tano benki.

“Mkopo? Mume wangu alichukua mkopo? Lini?” alijiuliza swali hilo bila kupata jibu.

Alichanganyikiwa, hakuamini kama huo ulikuwa ukweli, alimfahamu mume wake, walipanga mipango pamoja, waliambiana kila kitu kilichokuwa kikiendelea, ilikuwa vigumu kwa mume wake kuchukua mkopo benki pasipo kumwambia, akahisi kwamba kulikuwa na kitu, alichokifanya ni kuwasiliana na mwanasheria wake.

“Umepokea barua kutoka Benki ya Watu?” aliuliza mwanasheria huyo aliyeitwa kwa jina la Emmanuel Makange.

“Ndiyo!”

“Inasema kwamba mumeo alichukua mkopo wa milioni mia tano kwa kuiweka dhamana nyumba yenu?” aliuliza Makange.

“Ndiyo!”

“Hebu niione!”

Akapewa barua hiyo na kuanza kuiangalia, ni kweli ilitoka katika benki hiyo, kulikuwa na sahini ya mkurugenzi wa benki hiyo na muhuri, ilionekana kuwa barua halisi iliyotoka katika benki hiyo.

Alichokifanya mwanasheria huyo ni kuondoka na kuelekea huko benki, alitaka kupata ukweli juu ya barua hiyo, alipofika, akaomba kuonana na mkurugenzi na kumwambia kile kilichokuwa kimetokea na mkurugenzi huyo kuthibitisha kwamba kweli Bwana Mapoto alichukua mkopo na aliahidi kurudisha mwezi huo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Hapana! Mzee asingeweza kufanya kitu pasipo kumshirikisha mama,” alisema Makange.

“Labda alifanya hivyo kwa ajili ya kimada wake, angemshirikishaje mama?” aliuliza mkurugenzi huyo.

“Hapana! Hakuwa mtu wa hivyo!”

“Wewe ni mwanaume! Hivi kweli inawezekana kuwa na mtu aliyekosa kimada? Usiusemee moyo,” alisema mkurugenzi huyo.

Hakuishia mahali hapo, ili kumuaminisha kwa kile alichokuwa amemwambia, akamtolea na nyaraka nyingine nyingi ambazo zilionyesha kwamba Bwana Mapoto alichukua mkopo huo ndani ya benki hiyo.

Hawakuishia katika nyaraka zilizokuwa kwenye makaratasi tu bali akamchukua na kumpeleka katika kompyuta na kumuonyeshea kila kitu ambacho alitakiwa kukiona.

Emmanuel alichanganyikiwa, aliangalia sahini, ilikuwa ni ya Bwana Mapoto. Akarudi nyumbani kwa Rosemary akiwa hana nguvu kabisa, alichoka, alichokiona kule benki kilimshtua sana.

“Imekuwaje?”

“Mama! Hali ni ngumu sana!”

“Lakini si huwa kitu kama hiki kunakuwa na mwanasheria. Ningependa nionane na huyo mwanasheria ambaye alimsimamia katika hili,” alisema Rosemary huku akionekana kuchanganyikiwa hasa.

Hilo halikuwa tatizo, kwa sababu katika karatasi zile aliandikwa mwanasheria aliyemsimamia katika hilo, akatafutwa na alipoulizwa, alimwambia Rosemary kwamba kweli alikuwepo siku hiyo na yeye ndiye aliyemsimamia Mapoto kupata pesa hizo, na uzuri ni kwamba walikwenda kuandikisha mpaka mahakamani.

“Mpaka mahakamani?”

“Ndiyo!”

Rosemary hakutaka kukubali, alitaka kujua kila kitu kilichokuwa kimetokea, akaelekea mahakamani, kweli, alipofika akaonyeshewa nyaraka zote alizosaini mume wake kama kukamilisha kuuchukua mkopo huo mkubwa.

Miguu yake ikakosa nguvu, palepale mahakamani alipokuwa, akapiga magoti na kuuficha uso wake, akaanza kulia kama mtoto mdogo kwani alihisi akiwa amebeba dunia nzima, alijiona kuwa mtu mwenye mikosi kuliko watu wote duniani.

Hakujua angekimbilia wapi, hakujua angefanya nini kuzilipa fedha hizo, kilikuwa kiasi kikubwa sana ambacho asingeweza kulipa, na kama angeshindwa kulipa, inamaana kuwa angepokonywa nyumba aliyokuwa akiishi.

“Haiwezekani! Mungu! Mume wangu hawezi kufanya ujinga huu! Hapa kuna kitu, ninamuamini mume wangu, ni mtu makini, tulishirikiana kwa kila kitu, hawezi kufanya hivi,” alisema Rosemary huku akiwa amekiinamisha kichwa chake, alikuwa akilia kama mtoto.

Watu wote waliokuwa mahali hapo walimshangaa, walimfahamu, alikuwa mke wa mtu aliyekuwa na nguvu sana nchini Tanzania, hawakujua ni kitu gani kilitokea mpaka kumwaga machozi namna ile hapo mahakamani. Hawakukubali, wakawapigia simu waandishi wa habari na kuwapa taarifa kile kilichokuwa kinaendelea mahali hapo.

Ni kama Rosemary alijua, hakutaka kukaa sana mahakamani hapo, akaingia ndani ya gari lake na kuondoka huku akiendelea kulia kama kawaida. Baada ya dakika kadhaa, waandishi wakafika mahali hapo wakiwa na kamera zao, walitaka kuhakikisha kile walichokuwa wameambiwa.

“Yupo wapi?” aliuliza mwandishi mmoja.

“Ameondoka!”

“Mna uhakika kwamba ni yeye?”

“Sasa sisi tutakupa taarifa ya uongo bwana! Kwani hatumjui?” aliuliza jamaa mmoja.

“Inawezekana mkawa mmemchanganya. Si mnajua duniani wawiliwawili!” alisema mwandishi huyo.

“Mtafuteni. Ila alikuwa akilia kama mtoto!”

“Kweli?”

“Habari ndiyo hiyo!” alijibu mtoa taarifa, waandishi wa habari wakaondoka na kuanza kuelekea nyumbani kwa Rosemary huku wakiwa na kiu ya kutaka kufahamu ukweli juu ya kitu kilichokuwa kikimliza mahakamani?

“Hii ishu inaweza kuwa habari kubwa sana,” alisema mwandishi mmoja.

“Ndiyo hivyo! Halafu siku nyingi hajasikika, kama tukiiandika, inaweza ikawa kiki kubwa ya kutupatia wasomaji wengi,” alisema mwandishi mwingine.

“Kweli kabisa. Hebu tuwahi nyumbani kwake kabla ya waandishi wengine hawajajua kuhusu hii taarifa,” alisema mwandishi mmoja, safari ikaanza.

***

“Ni kweli?” aliuliza mmoja wa waandishi wa habari waliokwenda kuonana naye.

“Kuhusu nini?”

“Kuhusu benki kuitaka nyumba yako kwa deni la milioni mia tano unalodaiwa?”

“Naomba mniache kwanza.”

Rosemary hakutaka kulizungumzia hilo, alitaka kuachwa kwani kwa kipindi hicho akili yake haikuwa sawa kabisa. Alijua fika kwamba mumewe hakuchukua huo mkopo, mumewe hakuwahi kufanya jambo kimyakimya pasipo kumtaarifu lakini hakujua mambo hayo yalisababishwa na nini kwani kama kufariki, alifariki na alichokijua ni kwamba kila kitu kilianza upya.

Akawasiliana na Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania National Party, Elibariki Edward na kumwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea. Mwenyekiti huyo hakuamini, alichomwambia ni kwamba angeonana naye na kulizungumza hilo kwani naye kwa jinsi alivyomfahamu Mapoto, asingeweza kufanya jambo kama hilo.

“Nakuja!”

Ndani ya nusu saa, mwanaume huyo alikuwa nyumbani kwa Mapoto kwa ajili ya kuzungumza na Rosemary. Alikuwa mwanamke mjane aliyehitaji msaada kwa hali na mali. Alizungumza naye, akamwambia jinsi alivyoletewa barua ile na mwanasheria wake kufuatilia kila kitu mahakamani na kuambiwa kwamba kile alichokiona ndicho kilivyokuwa.

“Inawezekana vipi?” aliuliza Edward huku akishangaa.

“Sijajua! Nimechanganyikiwa, sijajua ni kitu gani natakiwa kufanya. Huu ni uonevu, kwa nini jambo hili wasingelisema wakati mume wangu akiwa hai? Kwa nini wamesubiri mpaka afe?” aliuliza Rosemary.

Hakukuwa na kitu kilichobadilika, bado msimamo wa Benki ya Watu ulimwambia kuwa alitakiwa kulipa kiasi cha pesa alichokuwa akidaiwa mume wake vinginevyo nyumba yake ambayo iliwekwa dhamana ingechukuliwa na benki hiyo kisha kupigwa mnada.

Hakuwa na kiasi hicho cha fedha, alikuwa tayari kwa kila kitu. Waandishi wa habari ambao walikwenda kufanya naye mahojiano wakaitoa habari ile katika magazeti. Kila mtu aliyeiona, alishtuka, hawakuamini kama Mapoto angeweza kufanya kitu cha kipumbavu kama kile.

Maneno yakaibuka, wengi wakasema kwamba serikali iliingiza mkono katika jambo hilo kwa ajili ya kumfilisi mwanamke huyo kwa kuhisi kwamba naye angeweza kuingia katika Chama cha Tanzania National Party na kuleta upinzani mkali.

“Serikali inajihami tu! Nina uhakika Mapoto hajawahi kufanya jambo kama hili,” alisema mwanaume mmoja.

“Wewe ni kama mimi! Yule ni mtu makini sana, nahisi kuna kitu ila siku si nyingi tutakijua tu,” alisema jamaa mwingine.

Rosemary alipewa muda wa kulipa deni alilotakiwa kulilipa. Hakuwa na furaha tena, ile kidogo ambayo ilianza kurudi moyoni mwake ikapotea, majonzi yakautawala moyo wake, kila alipokuwa alionekana kuwa na mawazo mno kitu kilichowafanya hata watu wengine waliokuwa wakimwangalia kumuonea huruma.

“Mom! What is going on?” (mama! Nini kinaendelea?) aliuliza Irene huku akiwa amemsogelea mama yake.

“Nothing my daughter!” (hakuna kitu binti yangu)

“But you look so upset!” (unaonekana huna furaha!)

“Me? No! I am happy Irene. Have you already eaten?” (mimi? Hapana! Nina furaha Irene. Tayari umekula?) aliuliza Rosemary kwa lengo la kumtoa Irene katika mambo aliyokuwa akimuuliza.

“Yes!” (ndiyo)

“Where is your brother?” (kaka yako yupo wapi?)

“He is already sleeping” (amelala)

Akamchukua Irene na kumpeleka chumbani kwake na kumlaza kisha na yeye kuelekea chumbani kwake. Hakupata usingizi, hakukuwa na kipindi kilichokuwa kigumu kwake kulala kama kipindi hicho.

Alikuwa na mawazo tele, ubongo wake ulikuwa ukifikiria kupita kawaida. Alipewa muda wa mwezi mmoja kukamilisha deni alilokuwa akidaiwa, hakujua ni mahali gani ambapo angepata kiasi kikubwa namna hiyo na kukilipa.

Alijaribu kuwasiliana na ndugu zake wengine, wote walipogundua tatizo alilokuwa nalo, hata simu hawakuwa wakipokea. Hakuchoka, aliendelea kuwatafuta lakini majibu yalikuwa yaleyale.

Wakati zikiwa zimebaki siku kumi, akajaribu kumpigia simu Edward kwa ajili ya kumuomba msaada wa kisheria zaidi lakini kitu cha ajabu kabisa, mwanaume huyo hakuwa anapokea simu zake na hata alipokuwa akimtafuta ofisini kwake, mwanaume huyo alijifanya kuwa bize na kutokuwa na muda wa kuzungumza na mtu yeyote yule.

Hilo lilimuuma mno moyoni mwake. Edward, mwanaume ambaye kila siku alimwambia kwamba angepigana naye kwa moyo mmoja leo hii hakutaka kupokea simu zake na mbaya zaidi hata alipokwenda kumuona ofisini kwake, hakutaka kabisa kuonana naye.

Hakujua cha kufanya, akarudi nyumbani kwake na kutulia sebuleni. Kila alipokuwa akiwaona watoto wake, mawazo yake yalikuwa ni juu ya maisha ambayo wangeishi baada ya nyumba hiyo kupigwa mnada.

Alikitegemea kiasi cha shilingi milioni mia mbili kilichokuwa kwenye akaunti yake, akahisi kwamba hicho kingemsaidia kuyaendeleza maisha yake, angenunua nyumba ya kawaida kuendelea na maisha yake na watoto wake.

“Mama nimerudi tena!” alisema mwanaume mmoja aliyemfuata nyumbani kwake.

“Eeh! Jamani! Kuna nini tena?”

“Nimekuletea barua!”

“Nyingine?” aliuliza huku akionekana kushangaa.

“Ndiyo! Hii hapa!”

Mwanaume yule akampa barua hiyo. Rosemary alibaki akitetemeka, hakujua ni kitu gani ambacho angekutana nacho katika barua ile. Alipoifungua, maneno ya kwanza aliyokutana nayo ni kuhusu kufungwa kwa akaunti yake ya benki ya mume wake.

“Nini? Wanafunga akaunti?” alijiuliza huku akishtuka kupita kawaida.

Akasoma maelezo kwa kirefu. Benki hiyo iliyokuwa ikimdai mumewe ilieleza kwamba kwa kiasi cha shilingi milioni mia mbili kilichokuwa benki kilitakiwa kuchukuliwa chote na kisha nyumba hiyo kuuzwa kwa bei ya kawaida kwa ajili ya kupata hata nusu ya fedha walizokuwa wakimdai.

“Mungu wangu! Kwa nini wananifanyia hivi? Nimewakosa nini?” aliuliza Rosemary na kuanza kulia.

Hakupata faraja, siku hiyo ndiyo iliyomuumiza mno, maisha yake yalikuwa ni sawa na karatasi nyeupe ambayo haikuandikwa kitu chochote kile, hakujua angeanzia wapi, hakujua angefanya nini ili kupata haki zake za msingi.

Alijua kwamba kulikuwa na mchezo mchafu uliokuwa ukichezwa na serikali, alijua kabisa kwamba serikali hiyo iliamua kufanya hayo yote kwa kuwa tu mumewe alionyesha upinzani mkubwa hivyo walifanya hayo yote kama kuipoza mioyo yao kwa majeraha makubwa waliyokuwa wameyapata.

Akawashirikisha walimu wenzake ambao aliamini kwamba ndiyo walikuwa watu pekee ambao wangeweza kumfariji. Walimu hao wakamshauri kwamba lingekuwa jambo jema kama angewasiliana na Rais Bokasa na kumwambia kilichokuwa kikiendelea.

“Mmh! Itawezekana kweli?” aliuliza Rosemary.

“Jaribu! Tunaamini kwamba anaweza kukusaidia,” alisema mwalimu mwenzake.

“Lakini nahisi serikali inahusika, sasa kama inahusika, itakuwaje rais kunisaidia?” aliuliza.

“Hebu kwanza wasiliana naye. Usitake kuingiza hofu na wakati bado hujawasiliana naye. Akikataa, basi jua kwamba umeshindwa,” alisema mwalimu mwingine.

Hakutaka kusubiri, siku zilikuwa zimekwenda sana hivyo akatafuta mawasiliano ya Rais Bokasa na kumpigia. Alipoisikia sauti ya mwanaume huyo tu, Rosemary akaanza kulia, moyo wake ulimchoma kupita kawaida, alijua kwamba mtu huyo ndiye alikuwa wa mwisho kumsaidia na kusingekuwa na mtu yeyote ambaye angeweza kumsaidia.

Akamwambia Rais Bokasa kila kitu kilichokuwa kimetokea. Rais huyo alihuzunika mno, hakuamini kama benki hiyo ingeweza kumfanyia mwanamke huyo mambo ya kijinga kama hayo. Akamwambia kwamba angemsaidia kwa hali na mali.

“Nitakusaidia, nitazungumza nao, ila jua utashinda tu,” alisema Rais Bokasa maneno yaliyomfanya Rosemary kushukuru sana.

Moyo wake ukarudisha tumaini, akafarijika na kuwaambia walimu wenzake kwamba rais huyo aliahidi kumsaidia na hivyo alitakiwa kusubiri. Siku ya kuondolewa ndani ya nyumba hiyo, hakuondolewa kitu kilichompa uhakika kwamba tayari rais huyo alizungumza nao na kumalizana.

Siku ziliendelea kukatika, baada ya wiki mbili kupita baada ya siku ile ya kuondolewa ndani ya nyumba, akashangaa akipigiwa simu kwa namba ngeni wakati akiwa shuleni na kuambiwa aende nyumbani kwake kwani kuna watu walifika na kuanza kuipiga mnada nyumba hiyo.

“Wanaipiga mnada? Kivipi? Mimi ndiye nina hati ya nyumba!” alisema Rosemary huku akionekana kuchanganyikiwa.

“Sidhani kama unayo! Wahi kuja hapa, vinginevyo utakuta mtu kaipandia dau,” ilisikika sauti ya mwanaume aliyempigia simu. Rosemary hakutaka kufanya kitu chochote, akaingia ndani ya gari lake, akaliwasha na kuondoka shuleni hapo kwa mwendo wa kasi, hata kuaga akasahau, wanafunzi na walimu wote wakabaki wakimshangaa.



Rosemary alichanganyikiwa, aliendesha gari kwa mwendo wa kasi ili kuiwahi nyumba yake hata kabla haijapigwa mnada. Hakujua ni kitu gani kilikuwa kimeendelea kwani alizungumza na Rais Bokasa na kumwambia kwamba angezungumza na benki hiyo ili nyumba yake isipigwe mnada na hata kiasi cha fedha alichotakiwa kutoa kama malipo ya mkopo ambao aliuchukua mumewe kisichukuliwe.

Aliendesha gari huku akilia, akaanza kuyafikiria maisha yake bila kuwa na fedha, watoto wake walimuumiza kichwa na hakujua ni kwa jinsi gani wangeweza kuishi bila kuwa na pesa hata kidogo.

Kama angefilisiwa kila kitu alichokuwa nacho inamaanisha kwamba angekwenda kuishi mitaani huku watoto wake wakiachishwa shule ile ya watoto wa matajiri na kwenda katika shule nyingine za kawaida kitu ambacho hakutaka kabisa kuona kikitokea.

Foleni zilimchelewesha, zilikuwa nyingi na alitumia muda mwingi kukaa katika foleni hizo. Mpaka anafika nyumbani kwake, alichukua saa moja, akafika mahali hapo, idadi kubwa ya watu iliyokuwa mahali hapo ilionyesha kabisa kwamba kulikuwa na kitu kinaendelea.

“Mbona mnaipiga mnada nyumba yangu? Kwa nini?” aliuliza Rosemary huku machozi yakiendelea kumtiririka mashavuni mwake, alikuwa akizungumza na kijana mmoja aliyevaa shati jeupe na tai nyekundu.

“Kamuulize bosi!”

“Yupo wapi?”

“Yule pale,” alisema kijana huyo huku akimnyooshea mwanaume aliyesimama pembeni kabisa huku akiwa na makaratasi mikononi mwake.

Akamfuata mwanaume huyo na kumuuliza swali lilelile, akamjibu wazi kwamba alishindwa kulipa fedha walizokuwa wakidaiwa na ndiyo maana nyumba ilikuwa ikipigwa mnada na hata pesa zilizokuwa kwenye akaunti ya mumewe, zilizuiliwa.

“Ila niliongea na rais,” alisema Rosemary.

“Kwani sisi tulimkopa rais? Hoja yako haina mashiko mama!” alisema mwanaume huyo, kwa kumwangalia tu, uso wake ulitosha kuonyesha ni kwa jinsi gani alikuwa na chuki kali dhidi ya Rosemary.

Rosemary hakutaka kukubali, hapohapo akachukua simu yake kwa lengo la kumpigia rais lakini simu ilipopokelea, akaambiwa kwamba rais alikuwa safarini kuelekea nchini Ujerumani.

Moyo wake ulimuuma, ulimchoma kupita kawaida. Akashindwa kujizuia, akakaa chini na kuendelea kulia kama kawaida. Kila mtu aliyemwangalia alimuonea huruma, alionekana kuwa mtu aliyekuwa akipitia matatizo makubwa mno, kwa jinsi mume wake alivyokuwa kipenzi cha watu, kwa jinsi alivyokuwa akipendwa kila siku, hakustahili kuwa katika hali aliyokuwa nayo kipindi hicho.

Rosemary akakumbuka kwamba alikuwa na hati ya nyumba, haraka sana akasimama na kuelekea ndani, alipofika, akafungua kidroo cha kitanda kwa ajili ya kuangalia hati ya nyumba, akaikuta lakini alichokishangaa, haikuwa hati ya nyumba orijino, ilikuwa ni nyingine kabisa ambayo hata sahihi zilizokuwa zimeandikwa, hazikuwa zake na za mumewe.

“Haiwezekanai!”

Akatoka chumbani huku akiwa amechanganyikiwa, akaelekea nje na kumfuata mwanaume yule huku akiwa ameshika ile hati ya nyumba ambayo ilikuwa feki. Alimwambia mwanaume huyo kwamba kulikuwa na mchezo umechezwa, kulikuwa na mtu aliingia chumbani kwake na kuchukua hati orijino na kumuachia feki.

“Mama! Ulishaambiwa kabla kwamba mumeo alichukua mkopo benki, unadhani angepewa bila kuwa na hati ya nyumba ambayo aliiweka kama bondi?” aliuliza mwanaume huyo huku akimwangalia Rosemary.

“Lakini ilikuwepo mpaka jana nimeangalia, ilikuwepo,” alisema Rosemary.

“Utakuwa umechanganyikiwa mama! Nenda kwanza kapumzike tufanye yetu,” alisema mwanaume huyo, akageuka upande wa pili na kuendelea na kazi yake.

Rosemary akashindwa kuzuia, siku hiyo nyumba yake ikapigwa mnada. Yalikuwa ni maumivu makali moyoni mwake, hakuamini kama angeweza kupoteza nyumba hiyo, na mbaya zaidi hata kwenye akaunti ya mumewe, fedha zote zilizokuwepo humo, zikachukuliwa kama kukamilisha malipo ya fedha aliyokuwa akidaiwa mumewe.

***

Miongoni mwa matajiri waliojitolea kukisaidia Chama cha Tanzania National Party alikuwa bilionea Adam Matiku. Huyu alikuwa miongoni mwa mabilionea wakubwa nchini Tanzania. Alimiliki kiasi kikubwa cha fedha, alikuwa na kampuni nyingi za usafirishaji, migodi ya dhahabu iliyokuwa Shinyanga na Mererani mkoani Arusha.

Hakuwa mtu wa siasa lakini hakuwa akiipenda serikali ya Chama cha Labour ambacho kilikuwa madarakani ambacho kazi yake kubwa kilikuwa ni kuwabana wafanyabiashara kwa kuwaongezea kodi.

Alikichukia chama hicho na hivyo kuwekeza nguvu zake kukisaidia chama pinzani cha Tanzania national Party kilichokuwa kimemuweka mwenyekiti wa chama hicho, Edward kuwa mgombea wa chama hicho.

Hawakushinda, walishindwa vibaya na hivyo Bokasa kuendelea kuiongoza Tanzania kwa miaka mingine mitano. Alikasirika, hakutaka kukiona chama hicho kikiendelea kuwa madarakani, aliwaandaa watu wake kwa ajili ya kufungua kesi ili kuyapinga matokeo hayo katika mahakama ya kimataifa lakini ilishindikana na hivyo kuamua kuachana na siasa na kufanya biashara zake.

Kila kitu kilichokuwa kikiendelea kwa Rosemary alikifahamu, moyo wake ulimuuma mno, alijua fika kwamba Mapoto hakuwa amekopa fedha hizo bali kulikuwa na mchezo ambao serikali ulitaka kuucheza, kumfilisi mwanamke huyo na kumuacha akiwa hana kitu kabisa.

Hakutaka kuona hilo likitokea, na hata nyumba ilipopigwa mnada, yeye ndiye aliyeinunua kwa kumtumia rafiki yake, Othman Ngolisho ili kusiwe na mtu yeyote ambaye angegundua kwamba yeye ndiye aliyeinunua nyumba hiyo.

Hakuishia hapo bali alichokifanya ni kupanga mikakati ya kumsaidia Rosemary kwa kila kitu. Alijua kwamba kama angemuweka ndani ya nyumba ileile ilikuwa ni lazima serikali kufahamu kilichotokea hivyo aliamua kuachana naye lakini mwisho wa siku amsaidie kumtunza na kumfanyia mambo mengine.

Wakati Rosemary hajui ni kitu gani kingeendelea katika maisha yake, akamtuma kijana wake kwa ajili ya kumpa taarifa mwanamke huyo kwamba kulikuwa na nyumba iliyokuwa Kimara Stop Over ambayo alikuwa ameandaliwa kwa ajili ya kuishi na familia yake.

“Ni ya nani?” aliuliza Rosemary.

“Bosi wangu!”

“Nani?”

“Si lazima umfahamu! Ila ni yeye ndiye ameamua kukusaidia,” alisema kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Juma Hassani.

“Sawa.”

Wakati Juma akizungumza na Rosemary, kulikuwa na wanaume watatu waliokuwa wakimfuatilia, walijua kwamba kulikuwa na kitu, walihisi hivyo kwa sababu kila walipomwangalia, kijana huyo alikuwa akiangalia huku na kule.

Wakati Juma akiondoka, wanaume wale hawakutaka kumfuatilia kwa ukaribu, walichokifanya ni kutulia ndani ya gari lao kisha kumwacha mpaka atakapoingia ndani ya gari lake, alipofanya hivyo, wakaanza kumfuata.

“Kuna kitu!” alisema jamaa mmoja.

“Hata mimi nahisi! Hebu tumfuatilie, atatuambia ni kitu gani kinaendelea!” alisema jamaa mwingine.

Juma hakuwa na habari kama alikuwa akifuatiliwa kwa nyuma, akaingia kwenye barabara ya lami na kuondoka huku akielekea maeneo ya Namanga huku lengo lake likiwa ni kutaka kuelekea Kinondoni alipokuwa akiishi.

Wakati akiwa amekwishafika maeneo hayo ya Namanga, karibu na kona ya kuelekea ubalozi wa Marekani, akashtukia gari moja aina ya Range SUV jekundu likija na kusimama mbele yake.

“Kuna nini?’ alijiuliza lakini hata kabla hajajijibu, milango miwili ya gari lile ikafunguliwa, wanaume wawili waliokuwa na bastola mikononi mwao wakateremka na kumfuata Juma.

“Shuka chini,” alisema jamaa mmoja huku akiwa amevunja kioo.

“Nimefanya nini?”

“Paaa…” risasi ikapigwa hewani, watu wote waliokuwa wakishangaa huku wakitamani kujua kitu gani kinaendelea, wakaanza kukimbia.

“Jamani msiniue!”

“Basi teremka.”

“Sawa!” alisema Juma huku akitetemeka.

Akateremka, wakamchukua, wakamuingiza ndani ya gari lao na kuondoka naye mahali hapo. Watu wote waliokuwa wamejificha, wakaanza kujitokeza huku wengine wakilaumu kwamba kwa nini polisi wa Kituo cha Osterbay hawakutokea na wakati hawakuwa mbali na mahali ambapo risasi ilipigwa?

“Wale ni majambazi?” aliuliza jamaa mmoja.

“Majambazi! Majambazi gani wanavaa suti?” aliuliza jamaa mwingine, wakati huo gari lile lilifika ubalozini, likakata kulia na kuanza kuelekea Mikocheni huku muda wote huo Juma akilia kuomba msamaha japokuwa hakujua alifanya nini.

***

Bilionea Adam Matiku alikuwa nyumbani kwake ametulia, alichokuwa akikisubiri ni ripoti kutoka nyumbani kwa Mapoto ambapo nyumba ya marehemu huyo ilikuwa ikipigwa mnada huku akiwa amemuandaa rafiki yake, Othman Ngolisho kwa ajili ya kuinunua nyumba hiyo.

Hakusubiri kusikilizia suala hilo tu bali pia alitaka kufahamu kilichokuwa kimeendelea kati ya kijana wake aliyemtuma kuzungumza na Rosemary, kijana mtanashati aliyeitwa kwa jina la Juma.

Alitaka kupata taarifa juu ya kila kitu. Hakutaka kuona Rosemary akionewa kisa tu mumewe alifariki dunia, alitaka kuona akimsaidia kwa kuwa alikuwa mke wa mwanaume aliyekuwa na nguvu sana nchini Tanzania hivyo hakuona kama kulikuwa na sababu ya kumuacha mwanamke huyo pasipo kumpa msaada.

Alikuwa akimsubiri Juma, kijana aliyemtuma kwa ajili ya kuzungumza na Rosemary na kumwambia kila kitu kilichokuwa kimepangwa lakini cha kushangaza, kijana huyo hakupiga simu, na hata alipompigia haikupokelewa.

Matiku akakasirika mno, alitaka kusikia kila kitu hata kabla mnada haujamalizika na watu kuondoka mahali hapo. Alipoona kimya sana ndipo akampigia simu mwanaume aliyekuwa amemtuma kununua nyumba hiyo, Othman ambaye alimwambia kwamba alimuona Juma kipindi fulani akizungumza na Rosemary, baada ya hapo, akaondoka zake.

“Hujajua ameelekea wapi?” alimuuliza.

“Hapana! Ila aliondoka!”

Matiku hakutulia, muda wote alikuwa akimpigia simu kijana huyo lakini hali haikubadilika, iliendelea kuwa vilevile kwamba simu haikuwa ikipokelewa na baada ya kupiga sana, ikaisha chaji, alipoendelea kumpigia, haikuwa ikipatikana.

Akashikwa na hofu, akahisi kulikuwa na jambo baya lilikuwa limemtokea Juma, akawasiliana na vijana wake wengine ili wachunguze na kujua kilichokuwa kimetokea, walipoingia mitaani, wakarudi na taarifa kusema kwamba Juma alitekwa na watu wasiojulikana.

“Alitekwa?” aliuliza Matiku kwa mshtuko.

“Ndiyo mkuu! Ametekwa, waliomteka wala hawajulikani,” alijibu kijana wake.

“Wapi?”

“Namanga!”

Hilo likamchanganya zaidi, hakujua ni watu gani waliokuwa wamemteka, hakugundua kwamba watu hao walitumwa, alihisi kwamba baada ya kumuona na gari la kifahari wakadhani kwamba alitoka kwenye familia ya kitajiri na ndiyo maana walimteka kwa kuitaka familia yake kutoa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kumuokoa ndugu yao.

Akawapigia simu polisi na kuwaambia kilichotokea, polisi walishangaa kwani mazingira ya utekaji hayakuonyesha kama watekaji walitoka sehemu ya mbali au walihitaji gari lake kwani kama ingekuwa hivyo ilikuwa ni lazima kulichukua na kuondoka nalo.

“Waliomteka walimtaka yeye na ndiyo maana wameacha gari,” alisema polisi mmoja.

“Sawa. Ila kwa nini wamemteka?”

“Labda wamejua kwamba ametoka katika familia ya kitajiri! Kuendesha V8 kwa nchi kama yetu si jambo la kitoto mkuu,” alisema polisi mmoja.

“Hebu fuatilieni! Watu walioshuhudia tukio wamesema kwamba watekaji waliondoka na huyo kijana njia ya kwenda Mikocheni, sasa kwa jinsi ninavyowajua, inawezekana wamekwenda naye Kawe. Fuatilieni huko,” aliagiza mkuu wa polisi katika Kituo cha Polisi cha Osterbay.

Hilo ndilo lililofanyika, gari moja la polisi likaondoka kituoni hapo huku kukiwa na polisi watano waliokuwa na bunduki, waliunganisha na kuanza kwenda Mikocheni na Kawe huku wakiwasiliana na wenzao na kuwataarifu tukio lililokuwa limetokea.

Mbali na watu waliokuwa wameshuhudia tukio hilo pale Namanga hakukuwa na watu wengine waliojua kwamba gari lililoondoka mahali hapo lilikuwa na mateka kwa ndani hivyo watu wengi kutokujua jambo lolote lile.

“Twendeni ufukweni! Ni lazima tuhakikishe huyu mateka anapatikana vinginevyo Matiku akiamua kuwaambia ngazi ya juu, halitokuwa jambo jema,” alisema polisi mmoja huku tayari gari hilo likiwa linakata kulia kwenye Kituo cha Sanaa kuelekea ufukweni.

***

Juma hakunyamaza, aliendelea kuomba msamaha, hakuwajua watu hao walikuwa wakina nani, hakujua walikuwa wakihitaji nini kutoka kwake. Alitetemeka, alilia kama mtoto mdogo huku akiwaambia watu hao wasimuue kwani alikuwa na familia iliyokuwa ikimtegemea.

Wanaume hao ni kama hawakuwa wakimsikiliza, walikuwa wakiendelea kuzungumza huku katika mazungumzo hayo wakijadili ni kwa namna gani walitakiwa kumuua Juma baada ya kuliegesha gari sehemu husika.

Gari lilizidi kusonga mbele, mwendo wao ulikuwa wa kawaida sana, walipofika Kawe karibu na Uwanja wa Tanganyika Parkers, wakaliingiza gari hilo humo na kwenda kulificha nyuma ya jengo moja ambalo zamani lilitumika kama kiwanda cha nyama.

Japokuwa kulikuwa na watu wengi waliloliona gari hilo lakini hakukuwa na mtu aliyekuwa na wasiwasi nalo. Hiyo haikuwa mara ya kwanza magari kufika mahali hapo, kulikuwa na magari mengi yaliyokuwa yakiingia katika uwanja huo, hasa magari ya wachezaji mpira na watu waliokuwa wakienda kutazama mechi mbalimbali.

“Hapa panatosha,” alisema mwanaume mmoja.

“Jamani naomba mnisamehe! Sijafanya lolote lile,” alisema Juma huku akivikutanisha viganja vyake kama ishara ya kuomba msamaha.

“Sawa. Tutakuacha kama tu utatuambia ukweli!” alisema mwanaume mwingine.

“Hakuna shida mkuu! Nitawaambia kila kitu. Haki ya Mungu nitawaambia kila kitu!” alisema Juma huku akitetemeka.

“Ni nani amekutuma ndani ya nyumba ile kuzungumza na yule mwanamke?” aliuliza jamaa mmoja huku akiwa na bastola mkononi mwake.

“Nimetumwa na bosi wangu!”

“Hana jina?”

“Matiku. Adam Matiku!”

“Alivyokutuma alikwambiaje?”

“Aliniambia kwamba nimwambie mwanamke yule kwamba amemtuma mtu anunue ile nyumba halafu atamsaidia kwa kila kitu,” alisema Juma.

“Nadhani unatuchezea mpaka unatudanganya,”alisema mwanaume mmoja kwa lengo la kuambiwa zaidi.

“Haki ya Mungu tena! Siwadanganyi! Naapia, wallahi tena,” alisema Juma.

“Kingine?”

“Ni hayo tu!”

“Sawa.”

Mwanaume mmoja akateremka kutoka ndani ya gari na kupiga simu sehemu fulani, ndani ya sekunde kadhaa akawa anazungumza na mwanaume mmoja kutoka kutoka upande wa pili na kumwambia kila kitu ambacho Juma aliwaambia baada ya kumteka.

“Kumbe ndiyo hivyo! Sawa. Sasa fanyeni kitu kimoja,” alisikika mwanaume huyo.

“Ndiyo bosi!”

“Muueni na muuache mwili wake hapohapo,” alisikika mwanaume huyo.

“Sawa. Hakuna tatizo!”

Jamaa yule akarudi ndani ya gari na kuwapa ishara wenzake juu ya kile kilichotakiwa kufanywa. Juma hakujua lakini kwa namna wanaume wale walivyokuwa wamebadili mikao yao akajua tu kwamba kulikuwa na kitu kinataka kutokea.

“Jamani! Nimewaambia ukweli! Naomba mniruhusu niondoke,” alisema Juma.

“Boka! Kazi kwako!” alisema mwanaume mmoja, mwenzake aliyeitwa Boka akatoa kitambaa kutoka mfukoni mwake na kumkamata Juma na kumziba pua na mdomo kwa kutumia kitambaa kile.

***

Moyo wa Rosemary ukawa na amani tena, alifurahia lakini kilichokuwa kikimsumbua ni juu ya mwanaume huyo aliyekuwa ameahidi kumsaidia, hakumfahamu, hakujua alikuwa nani lakini kwa mawazo yake, akagundua kwamba alikuwa Rais Bokasa ambaye hakutaka kugundulika kama alikuwa akimsaidia.

Hakuacha kumpigia simu, alipoona haipatikani, akamtumia ujumbe mfupi wa kumshukuru kwa kile alichokuwa amemfanyia kwani alikata tamaa na kuamini kama ndiyo ungekuwa mwisho wake lakini kwa kutumia fedha zake aliweza kumsaidia kulimaliza suala la nyumba.

Kila siku alikuwa akitumiwa kiasi cha fedha, hakujua kilipotoka lakini kila alipokuwa akiangalia kwenye akaunti yake benki, aliona akiwa ameingiziwa kiasi kikubwa cha fedha.

Hicho ndicho kilichoyaendeleza maisha yake, hakutaka kuona watoto wake wakipata tabu, alitaka kuona wakiendelea kusoma katika shule nzuri na za gharama kwa kuwa tu alikuwa na fedha ambazo aliamini kwamba zilitoka kwa Rais Bokasa.

Siku zikaendelea kukatika, baada ya miezi miwili ya msaada wa kifedha, ghafla msaada huo ukakatika, hakukuwa na fedha zilizoingizwa katika akaunti yake. Hakujua sababu iliyomfanya Rais Bokasa kuchukua uamuzi huo, akajipa moyo kwamba labda kulikuwa na vitu vimeingilia hivyo kusubiri na kusubiri lakini hali haikubadilika, hakikuingia kiasi chochote cha fedha katika akaunti yake.

Hilo likamtia hofu, hakujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea na wakati huku akiendelea kusubiri kuona nini kingeendelea, kapokea notisi ya kuhama ndani ya nyumba hiyo.

“Nihame? Nihamie wapi? Ila si niliambiwa nitakaa miaka yote?” alijiuliza pasipo kupata jibu.

Hakutaka kuondoka, alitaka kupata jibu la mtu aliyekuwa amemuagiza kukaa ndani ya nyumba hiyo. Hakuondoka, baada ya wiki moja, wanaume wawili wakafika nyumbani hapo huku wakiwa wameongozana na polisi na kumwambia kwamba siku hiyohiyo alitakiwa kuondoka ndani ya nyumba hiyo.

“Niende wapi?”

“Hiyo haituhusu! Unachotakiwa ni kuondoka humu,” alisema mwanaume mmoja.

“Hapana! Sina pa kwenda, nitakuwa mgeni wa nani mimi?” aliuliza Rosemary.

“Hilo nalo halituhusu! Chukua kila kitu kilichokuwa chako. Tukifunga milango, hutoingia tena ndani ya nyumba hii,” alisema mwanaume mwingine huku akionekana kumaanisha.

“Hapana!”

“Mama! Fanya kama unavyoambiwa, utajuta!” alisema polisi, kidogo Rosemary akaona kwamba watu hao hawakuwa na utani hata kidogo.

Kwa mwendo wa taratibu akaingia ndani ya nyumba yake, akachukua baadhi ya vitu na kutoka nje ambapo watu wale wakafunga milango ya nyumba ile. Hakuamini macho yake, nyumba ambayo aliijenga na mumewe, leo hii ilikuwa ikiondoka mikononi mwake.

Alilia na kulia, hakuondoka mahali hapo, akabaki kibarazani akiwasubiria watoto wake, Godwin na Irene ambao walikuwa shuleni kipindi hicho. Waliporudi, wakashangaa kumuona mama yao akiwa nje ya nyumba ile akilia.

“Mom! Why are you crying?” (mama! Kwa nini unalia?) aliuliza Godwin.

“We have to leave?” (tunatakiwa tuondoke)

“Where to?” (kwenda wapi?) aliuliza Irene huku akionekana kushangaa.

“I don’t know but we have to,” (sifahamu ila tunatakiwa kuondoka) alijibu mwanamke huyo huku akilia kama mtoto.

***

Shughuli zilikuwa zikiendelea katika Uwanja wa Tanganyika Parkers kama kawaida. Hakukuwa na mtu aliyejua kama kulikuwa na tukio la kutisha lilitokea katika jengo bovu lililokuwa mahali hapo. Waliokuwa wakicheza mpira, kama kawaida waliendelea, waliokuwa wakifanya shughuli zingine, nao waliendelea kama kawaida.

Baada ya siku mbili kupita ndipo watu wakahisi kitu cha tofauti, pua zao zikaanza kuhisi harufu mbaya na kali ya mzoga ambapo mara ya kwanza walihisi kwamba alikuwa paka au mbwa lakini kadiri muda ulivyokwenda, harufu hiyo ilikuwa kali tofauti na harufu za mizoga ya wanyama hao.

Kila mmoja akawa na wasiwasi, wengi wakahisi kwamba huo ulikuwa ni zaidi ya mzoga wa wanyama hao hivyo walichokifanya ni kuanza kutafuta ni kitu gani kilikuwa kimesababisha harufu kali namna hiyo.

“Harufu inatokea kwenye jumba,” alisema mwanaume mmoja.

“Twendeni!”

Wakaacha kucheza mpira na kuelekea huko, kila mmoja alitaka kuona ni kitu gani kilichokuwa kimesababisha harufu kali namna hiyo. Walipoingia ndani ya jumba hilo, harufu ikaongezeka zaidi, wakaziba pua zao na kusonga mbele na baada ya kwenda katika pembe moja ya jumba hilo, wakashtuka baada ya kuiona maiti ya mtu ikiwa chini huku imeharibika vibaya.

Wakashtuka, hawakuamini walichokuwa wakikiona, hawakutaka kuchelewa, wakapiga simu katika Kituo cha Polisi cha Kawe ambacho hakikuwa mbali kutoka mahali hapo na kufika katika uwanja huo kwa lengo la kuuchukua mwili huo.

“Imekuwaje?” aliuliza polisi mmoja.

“Tumeshtukia kuiona maiti! Hatujui kitu chochote mkuu!” alijibu mwanaume mmoja huku akiwaangalia polisi waliofika mahali hapo.

“Hakuna watu waliokuja kuitupa hii maiti?”

“Hakuna mkuu! Kuna magari mengi huwa yanakuja na kuondoka, hatujui chochote kile,” alijibu jamaa mmoja.

Polisi hao waliwauliza maswali kadhaa watu waliokuwa mahali hapo, walipomaliza, wakaondoka na mwili wa Juma. Nyuma wakaacha minong’ono ya watu, kila mmoja alikuwa akilizungumzia tukio hilo.

Walishangaa, ilikuwaje mwili ukae siku zote hizo mpaka kuharibika halafu kusiwe na mtu yeyote aliyegundua kama kuna mtu aliuawa? Hakukuwa na mtu aliyemfahamu mtu aliyeuawa kwani mwili ulikuwa umeharibika kupita kawaida.

Taarifa hizo zikawafikia waandishi wa habari ambapo kituo cha taifa kikaitangaza taarifa hiyo kitu kilichomfanya Bilionea Matiku kuhisi kwamba maiti iliyokuwa imeokotwa ilikuwa ya kijana wake, Juma.

Akaifuatilia, aliyakumbuka mavazi aliyokuwa amevaa, saa ya gharama aliyomnunulia, alipofika huko hospitalini ilipohifadhiwa maiti ile, akaomba kuiona.

“Hakuna shida mkuu!”

Akaelekea katika chumba cha kuhifadhia maiti ambapo akaanza kufunguliwa kila droo iliyokuwa na maiti kwa ndani. Akaanza kuziangalia, aliangalia moja baada ya nyingine na alipoona kulikuwa na ugumu wa kuiona maiti ya Juma, akawaambia mahali ilipokuwa imetolewa.

“Kumbe yule aliyeuawa Tanganyika Parkers?”

“Ndiyo!”

Akachukuliwa na kupelekwa katika droo za mwisho kabisa ambapo zikaanza kufunguliwa na kuiona maiti ya Juma. Hakukuwa na ugumu wa kuitambua japokuwa ilikuwa imeharibika vibaya, alipoziona nguo tu, akagundua kwamba alikuwa yeye.

“Polisi wa kituo gani walimleta mahali hapa?” aliuliza Matiku huku akionekana kuchanganyikiwa.

“Sijajua! Ila kama aliokotwa Kawe, basi ni polisi wa huko ndiyo waliomleta,” alijibu kijana aliyekuwa na jukumu la kuzipokea maiti na kuzihifadhi hapo mochwari.

Matiku akaondoka hospitalini hapo, alitaka kujua kitu kilichokuwa kimetokea Juma, alijua kwamba kulikuwa na watu walimuua, alitaka kuwajua watu hao kwani mara baada ya kumteka, walionyesha kabisa kwamba hawakutaka kitu chochote kutoka kwake zaidi ya roho yake.

Alichukua dakika thelathini mpaka kufika katika Kituo cha Polisi cha Kawe ambapo akahitaji msaada wa ripoti kuhusu maiti iliyokuwa imeokotwa na polisi kumwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea.

Hakuridhika, alitaka kumjua mtu aliyefanya mauaji hayo. Ilimuuma moyoni mwake kwani Juma alikuwa mtu muhimu kwake, dereva aliyemwamini kwa kila kitu na wakati mwingine kumpa siri zake nyingi kuhusu wanawake aliokuwa akitembea nao.

“Jamani! Naomba mchunguze hiki kifo, si kawaida. Yaani mtu aende pale uwanjani na kufanya mauaji! Tena huku watu wakiwepo halafu asionekane! Naomba mchunguze jamani!” alisema Matiku.

***

Hakukuwa na siri tena, watu wa serikalini wakagundua kwamba mtu aliyenunua nyumba ya Mapoto hakuwa Othman kama ilivyojulikana bali alikuwa Bilionea Matiku ambaye hakutaka kujulikana.

Hilo lilionekana kuwa tatizo, watu ambao walitaka kumuona Rosemary akiteseka hawakutaka kubaki kimya, walichokifanya ni kumuita Othman kwa ajili ya kuzungumza naye.

Walitaka kufahamu utajiri wake mkubwa aliokuwa nao mpaka kununua nyumba hiyo. Biashara zake hazikuwa kubwa, hawakuamini kama angeweza kununua nyumba hiyo kwa bei kubwa. Alipofuatiliwa zaidi kuhusu biashara zake akagundulika kwamba hakuwa mnunuaji wa nyumba hiyo.

Akakamatwa na kuwekwa selo, huko, akalazimishwa kusema mtu aliyekuwa nyuma ya mpango wa kununua nyumba ile. Waliomuuliza ni kama hawakuwa wakifahamu lakini ukweli ni kwamba walifahamu kila kitu, walijua kwamba Bilionea Matiku ndiye aliyetoa kiasi cha fedha kununua nyumba hiyo.

Walikasirika, walitaka kumuonyesha Matiku kwamba walikuwa na nguvu hivyo walichokifanya ni kuanza kumsumbua katika biashara zake. Magari ya kampuni zake yalikuwa yakikamatwa hovyohovyo, alipandishiwa kodi kubwa bila sababu maalumu. Kila alipokuwa, alikuwa akifuatiliwa, kila alichokuwa akikifanya ripoti ilipelekwa katika kitengo cha juu.

Baada ya siku kadhaa, polisi wakatumwa kwenda kumkamata kwa kisingizio cha kufahamu kwamba alikuwa akifahamu kuhusu mauaji ya Juma yaliyokuwa yamefanyika Kawe.

“Hamuwezi kuja kunikamata kiholelaholela tu kama mmekuja kumkamata mbeba mizigo sokoni,” alisema Matiku huku akiwaangalia polisi waliofika nyumbani kwake.

“Unafikiri mabilionea wapo juu ya sheria?” aliuliza polisi mmoja.

“Arrest warrant yenu ipo wapi?” aliuliza Matiku.

“Hii hapa!’

Matiku akaichukua na kuanza kuangalia, akaisoma na kukubaliana nao kwamba alitakiwa kwenda nao kituo cha polisi. Hata kabla hajafika mbali akawasiliana na mwanasheria wake kwa ajili ya kufika kituoni ili hata kama kingetokea kitu chochote kile, ajue nini cha kufanya.

Njiani, hakukuwa na mtu aliyezungumza lolote lile, kila mmoja alikuwa kimya. Kumkamata Bilionea Matiku ilikuwa ni amri kutoka ngazi ya juu hivyo walitakiwa kumkamata kwa gharama yoyote ile.

Alipofikishwa katika Kituo Kikuu cha Polisi, akapelekwa katika chumba maalum cha mahojiano na kuanza kuhojiwa, kwa kuwa lengo lao lilikuwa ni kumlaza kituoni hapo, wakamlaza.

Matiku alijua kwamba kulikuwa na mtu nyuma aliyekuwa akifanya mambo hayo yote, aligundua kwamba sababu ya mambo hayo ni kwa sababu tu alimsaidia mwanamke mjane wa Mapoto ambaye alikuwa akichukiwa na serikali iliyokuwa madarakani kipindi hicho.

Kukamatwa kwake ikawa ni stori kubwa, kila mtu akaanza kulizungumzia jambo hilo, wengi waliona kabisa kwamba polisi walitumwa kwani kwa sababu iliyowekwa wazi kwamba ndiyo iliyosababisha bilionea huyo kukamatwa haikuonekana kuwa na mashiko hata kidogo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Huu ni uonevu ujue,” alisema jamaa mmoja.

“Kwani geni lipi? Au umetusahau Waafrika?” aliuliza jamaa mwingine.

Wakati Bilionea Matiku akisota sero ndicho kipindi ambacho Rosemary alikuwa nje na watoto wake, hakujua ni sehemu gani alitakiwa kwenda. Moyo wake ulikuwa kwenye majonzi mazito, hakuamini kile kilichotokea, aliwapenda watoto wake, alitamani sana wapate elimu bora lakini kila kitu kilionekana kubadilika.

Akasimama pale alipokuwa, aliwaangalia watoto wake, Irene na Godwin, moyo ulimuuma mno lakini hakuwa na la kufanya. Akawashika mikono na kuondoka nao mahali hapo huku akiwa na kadi yake ya benki ambayo ilikuwa na kiasi cha shilingi milioni tano tu.

“Mama! Tunakwenda wapi?” aliuliza Godwin huku akimwangalia mama yake ambaye mashavu yake yalilowanishwa na machozi.

“Tunakwenda sehemu nyingine,” alijibu.

“Na hapa nyumbani vipi?”

“Twendeni! Nitawaambia kila kitu!”

Hawakuwa na jinsi, mama yao ndiye alikuwa kila kitu, wakaondoka mpaka walipofika Msasani ambapo Rosemary akaingia katika kibanda cha ATM na kutoa kiasi cha shilingi laki tano na kuondoka mahali hapo.

Safari yao iliishia Tandale Kwa Mtogole. Alihitaji chumba cha kuishi na watoto wake. Hawakuwa na fedha za kutosha hivyo alijua kwamba kama angechukua chumba katika mtaa wa watu wenye uwezo mkubwa ni lazima angeshindwa kulipia au kukwamba katika baadhi ya matumizi na ndiyo maana akaamua kwenda Tandale.

“Unataka chumba? Vipo vingi sana! Unahitaji cha kiasi gani?” aliuliza dalali.

“Hata efu arobaini!”

“Sawa. Twende!”

Huo ndiyo ukawa mwanzo wa maisha mapya yeye na watoto wake. Kutoka kuishi maisha ya kifahari Masaki mpaka Tandale yalikuwa ni mabadiliko ya haraka sana, kutoka juu na kushuka chini kwa kasi kubwa.

Wakakabidhiwa chumba, hakikuwa kikubwa sana, kilikuwa kidogo ambacho kilikuwa katika nyumba iliyokuwa na wapangaji wengi.Kabla ya kufanya kitu chochote kile, Rosemary akakaa chini, akaikunja miguu yake na kukiingiza kichwa katikati ya miguu hiyo na kuanza kulia.

“Mungu! Kwa nini? Kwa nini imekuwa hivi? Mbona ghafla sana?” aliuliza Rosemary huku akilia. Mbele ya maisha yake aliliona giza kubwa likiwa limetanda.



Mpaka muda huo Bilionea Matiku hakujua ni mtu gani alikuwa nyuma ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Moyo ulimuuma, alijuta kwa kile alichokuwa amekifanya, alijua kwamba kila kitu kilisababishwa na wema wake wa kumsaidia Rosemary na ndiyo maana mwisho wa siku jambo hilo lilitokea.

Nje, watu hawakunyamaza, kila mmoja alizungumza lake. Wapo waliodai kwamba serikali ilikuwa nyuma ya kila kitu lakini pia wapo waliosema kwamba inawezekana kweli bilionea huyo alihusika katika mauaji hayo.

Baada ya siku kadhaa akafikishwa mahakamani, watu wengi walijaa, walitaka kusikia ni kitu gani kilichokuwa kimetokea. Upande wa jamhuri ukasimamisha mashahidi wake na kwa upande wa Bilionea Matiku akasimamisha mashahidi wake ambao walikuwa mahali hapo kwa ajili ya kumtetea tu.

Waandishi wa habari hawakukosa, walikuwepo mahakamani hapo, walikuwa na hamu kubwa ya kutaka kufahamu kitakachotokea siku hiyo. Kama ilivyokuwa kawaida, kwa siku ya kwanza, kesi ikasikilizwa na kurudishwa rumande ambapo aliendelea kushikiliwa.

Mitaani, kelele hazikuisha, kila mtu alikuwa akizungumza lake, kelele za kuilaumu serikali ziliendelea kusikika kila kona kiasi kwamba kila mmoja akajua serikali ilikuwa imehusika katika tukio hilo.

Baada ya wiki mbili, kesi ikarudishwa tena. Iliendelea kama kawaida, mashahidi walisimama lakini baada ya kuzungushwa sana hatimaye mwisho wa siku Matiku kushinda kesi hiyo.

“Nilisingiziwa, najua nini cha kufanya,” alisema Matiku huku akionekana kuwa na hasira mno.

Wiki moja baada ya kutamka maneno hayo akapigiwa simu na mtu asiyemfahamu ambaye alimwambia kwamba alitakiwa kuachana na kila kitu kilichokuwa kimetokea na mbaya zaidi aliambiwa kuachana na Rosemary kwani vinginevyo angepata tatizo kubwa katika biashara zake.

Aliogopa, alijua kabla kwamba kumsaidia mwanamke huyo ndipo kulipokuwa na tatizo kubwa hivyo akaachana naye na kufanya mambo yake kwa kuamini kwamba watu aliotaka kupambana nao walikuwa na mkono mrefu.

Rosemary hakupokea tena misaada. Hakuwa na pesa za kutosha kwa maana hiyo asingeweza kuendelea kuwasomesha watoto wake katika shule za kitajiri na hivyo kuwapeleka katika shule nyingine za watu wa chini, na shule ambayo ilimjia kichwani mwake kipindi hicho ilikuwa ni Royal Land, shule binafsi iliyokuwa Manzese jijini Dar es salaam.

Maisha yalikuwa tofauti, yalibadilika kwa kasi kubwa, kila alipokuwa akiwaangalia watoto wake, hakuamini kama alishuka kwa kasi kubwa na kuwa hapo alipokuwa.

Hakuacha kulia, aliumia sana na hata kazini alipokuwa akifanya kazi, walimu wenzake walimuonea huruma na kila siku wakawa na kazi ya kumfariji kwa kumwambia kwamba huo haukuwa mwisho, kama ni majaribu, Mungu alimuwekea mlango mwingine wa kutokea.

Uwezo wa Godwin na Irene haukuishia katika shule ya matajiri walipokuwa wakisoma bali uliendelea mpaka katika shule hiyo waliyokuwa wamehamia. Ilikuwa ni shule ya watu wa chini maarufu kama Kayumba, hakukuwa na wanafunzi waliokuwa na uwezo mkubwa kuzungumza Kiingereza, kitendo cha wao kuzungumza lugha hiyo kwa ufasaha kiliwafanya wanafunzi wengine kuwaona watu wa ajabu na wenye uwezo mkubwa.

“Mmejifunza wapi Kiingereza?” aliuliza mwanafunzi mmoja aliyejulikana kwa jina la Amina.

“Tulipotoka!” alijibu Godwin.

“Aisee mnaongea vizuri sana. Nifundishe na mimi!”

“Nitakufundishaje sasa Amina? Huwezi kufahamu lugha pasipo kuiongea, wewe tuongee na utaifahamu mbele ya safari,” alijibu Godwin ambaye kwa kumwangalia, alionekana kuwa kijana mpole kupita kawaida.

Maisha yalikuwa ni tofauti, walizoea kula chakula kizuri katika shule waliyotoka lakini ndani ya shule hiyo, maisha yalionekana kuwa magumu mno. Hawakuviona vyakula walivyokuwa wakila walipotoka, kila chakula walichokitaka ilikuwa ni lazima kulipia tofauti na kule ambapo gharama zilijumuishwa katika ada yao ya mwaka.

Mbali na kufahamu Lugha ya Kiingereza, pia walikuwa hatari katika somo la Kiswahili na Hisabati. Walifanya vizuri, walifaulu katika majaribio waliyokuwa wakipewa kila wiki.

Wakawa maarufu shuleni hapo, watu waliwafahamu kutokana na uwezo wao mkubwa waliokuwa nao kwenye masomo. Wanafunzi wengi waliwafuata na kuhitaji kufundishwa, hawakujiona, walijiona kuwa sawa na wanafunzi wote waliokuwa shuleni hapo.

Wakati hayo yote yakiendelea, bado Rosemary alijiona kuwa kwenye wakati mgumu, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea katika maisha yake. Moyo wake ulimuuma mno, kupoteza kila kitu lilikuwa pigo kubwa ambalo hakulitegemea kabisa.

Baada ya mwezi mmoja tangu ahamie Tandale hatimaye akapoka barua kutoka kwa mwalimu mkuu ambaye alipewa na serikali ambayo ilimfuta kazi ya ualimu shuleni hapo.

Alipoipokea na kuisoma, hakuamini kama kweli yeye ndiye aliyeandikiwa barua ile. Iliandikwa kwamba hakutakiwa kufundisha shuleni hapo, hakukuwa na sababu yoyote ya maana, ila kwa kifupi iliandikwa kwamba kulingana na matumizi makubwa, serikali iliamua kupunguza wafanyakazi wake.

“Nini? Nimefukuzwa kazi?” aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.

Hakutaka kukubali, hapohapo akatoka ofisini na kwenda katika ofisi ya mwalimu mkuu, alipofika, akaambiwa asubiri kwenye benchi. Ndani ya dakika tano, akaambiwa aingie ndani.

Alikuwa akilia, mashavu yake yalilowanishwa na machozi yaliyokuwa yakimtoka. Alimwangalia mwalimu mkuu, alikuwa akitia huruma mno, alishindwa kuzungumza, alikuwa kimya huku akiendelea kulia, kila alipotaka kuzungumza, alibanwa na kilio cha kwikwi.

Mwalimu mkuu akapata kazi ya kuanza kumbeleza, hakujua kilichokuwa kikimliza Rosemary kwani yeye alipelekewa barua na kumuagiza mwalimu ampe, hakujua ndani ya barua kuliandikwa nini na hata ishu ya kufukuzwa kazi, yeye kama mwalimu mkuu hakuambiwa lolote lile.

“Madam Rosemary, kuna nini?” aliuliza mwalimu mkuu, hapohapo Rosemary akaiweka barua hiyo mezani na mwalimu huyo kuanza kuisoma.

Alianzia juu mpaka mwisho. Yeye mwenyewe alishangaa, aliujua uwezo mkubwa aliokuwa nao Rosemary, miongoni mwa walimu waliokuwa wakipendwa kutokana na kufundisha vizuri basi alikuwa mwanamke huyo.

Hakujua sababu iliyowafanya watu wa ngazi ya juu kuamua jambo hilo. Alimwangalia Rosemary huku yeye mwenyewe akihisi maumivu makubwa moyoni mwake, aliyafahamu maisha ya mwanamke huyo, alifahamu hali aliyokuwa amepitia katika maisha ya shida na mateso, ilikuwaje leo afukuzwe kazi huku akiwa na watoto? Wangeishi vipi? Kila alichojiuliza, akakosa jibu.

“Rosemary! Haya ni maisha, hili ni jaribu kubwa sana kwako! Hutakiwi kuhuzunika sana, hutakiwi kulia kwa sababu kwenye kila jaribu Mungu anaweka mlango wa kutokea,” alisema mwalimu mkuu huku akimwangalia Rosemary.

“Inaniuma! Nimefanya nini? Kwa nini wamuamua hili? Kwa nini wamenifukuza kazi? Kweli hawajui maisha yangu niyoishi? Kweli hawajui jinsi ninavyohangaika na watoto wangu?” aliuliza Rosemary huku akilia kama mtoto.

Pamoja na kulia sana, pamoja na kuhuzunika sana ndani ya ofisi ya mwalimu mkuu haikuweza kubadilisha kitu, ukweli ukabaki palepale kwamba alifukuzwa kazi na alitakiwa kuacha kufundisha shuleni hapo mara moja.

Hakuridhika, mchana huohuo akaamua kwenda kumuona Waziri wa Elimu, Bwana Samson Massatu kwa ajili ya kumwambia kile kilichokuwa kimetokea. Alipofika, akaanza kumuhadithia kila kitu, jinsi alivyokuwa akiishi kwa mateso, alivyokuwa na wakati mgumu wa kuihudumia familia yake.

“Umefukuzwa kazi? Inawezekana vipi?” aliuliza Bwana Massatu.

“Sijajua! Sijui chochote kile. Nimekuwa nikionewa, hakuna anayenionea huruma, sijajua ni kwa sababu gani mambo haya nafanyiwa mimi. Kila siku mimi tu,” alisema mwanamke huyo huku akiendelea kulia.

“Nitafuatilia mama! Nakuahidi kwamba nitafuatilia!” alisema Bwana Massatu.

“Nitashukuru!”

Rosemary akaondoka ofisini kwa waziri wa elimu huku akiwa na matumaini ya kusaidiwa. Njiani, hakuacha kulia, kila alipokuwa akiiangalia barua ile moyo wake ulikuwa na maumivu makali mpaka kuhisi kama kulikuwa na kitu chenye ncha kali kilichokuwa kikimchoma.

“Mungu! Mbona kila siku hivi? Ni nani yupo nyuma ya mambo haya yote? Na kwa nini kila siku ni mimi tu? Mungu! Kuna kitu nimekukosea? Kuna kitu nimekifanya hakipo sawa na umeamua kunipiga namna hii? Mungu, hili jaribu limekuwa kubwa sana kwangu, siwezi kulibeba, nitie nguvu ya kusonga mbele, nionyeshe njia kwani bila nguvu zako, siwezi, nitashindwa kusimama na kusonga mbele,” alisema Rosemary huku akiwa ameinama chini ndani ya daladala, machozi yaliendelea kumtiririka mashavuni mwake kama maji.

***

Hakukuwa na maisha ya raha wala furaha, majonzi ambayo alikuwa nayo tangu mumewe afariki dunia ndiyo yaliendelea kila siku. Umasikini ukaanza kumnyemelea Rosemary na familia yake.

Alijaribu kuwafuata ndugu zake na ndugu wa mume kwa ajili ya kuwaomba msaada lakini wakati huo kila mmoja alimkimbia, hakutaka kumsaidia, hawakukumbuka wema waliokuwa wakifanyiwa na familia ya Mzee Mapoto, kwao, chuki na majivuno yalitawala moyo yao.

Hilo lilikuwa pigo kubwa kwa Rosemary, hakuwa na pesa ya kutosha na ilikuwa ni lazima ailee familia yake, watoto wake waliokuwa kidato cha tatu waendelee kusoma lakini hakujua angepata vipi pesa.

Alipokwenda benki kuchukua pesa zilizobaki, akakuta akaunti yake ikiwa imefugwa na alipouliza, hakupewa majibu ya kuridhisha hata kidogo. Mkononi hakuwa na kitu, alikuwa mweupe kabisa, shilingi elfu ishirini aliyokuwa nayo ndiyo fedha pekee iliyobaki ambayo ilitakiwa kuyaendesha maisha yake na familia yake.

Alilia, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya. Kwa kuwa alikuwa uswahilini, akaanzisha genge siku hiyohiyo. Ulikuwa ni uamuzi wa haraka, watu walimshangaa, waliomfahamu, walimuonea huruma kwani alishuka chini kabisa na kuanza maisha ambayo hakuwahi kufikiria hata siku moja kwamba angeyaishi.

Godwin na Irene waliporudi nyumbani, walishangaa, mama yao alibadilika zaidi, walijua kwamba alikuwa na mawazo tele, moyo wake uliumia lakini siku hiyo alionekana kuwa tofauti kabisa.

Godwin akamfuata mama yake na kumuuliza kilichofanya kuwa katika hali hiyo lakini mwanamke huyo hakumjibu chochote zaidi ya kutoka nje na kwenda gengeni.

“Hili genge ni letu?” aliuliza Godwin huku akionekana kushangaa.

“Ndiyo!”

“Umelijenga leo?”

“Ndiyo!”

Godwin aliumia mno, hakuongea tena, akaelekea ndani na kulala kitandani. Moyo wake ulimuuma mno, aliyakumbuka maisha ya raha waliyokuwa wakiishi zamani, aliyakumbuka maisha ya nchini Marekani baba yake alipokuwa hai, kitendo cha kutoka katika maisha yale na kuwa na maisha waliyokuwa nayo yalikuwa ni mabadiliko ya haraka ambayo hakuamini kama kungekuwa na mtu mwingine duniani ambaye angekuwa na mabadiliko ya maisha kwa haraka kama waliyokuwa nayo.

Moyo wake ukawaka kwa hasira, alijua dhahiri kwamba kulikuwa na mtu aliyesababisha hayo yote. Roho ya kichungaji aliyokuwa nayo, ikatoka, akagubikwa na hasira nzito, hasira ya kisasi ambayo aliamini kwamba ni lazima ahakikishe wale waliowafanya kuwa katika hali ile wanakufa mara moja.

Hakutaka kuwa na huruma tena, aliikumbuka mistari kadhaa ya Biblia iliyohusu ghadhabu kali ya Mungu kwa mtu atakayelipiza kisasi, alijua fika kwamba kisasi chochote kile kilitakiwa kuachwa kwa Mungu aliye hai. Hakutaka kukubali, aliona kama Mungu akichelewa kulipa kisasi, iwe isiwe ilikuwa ni lazima kulipa kisasi kwa mikono yake mwenyewe.

“Mungu! Nimekutumikia tangu nikiwa mdogo, nilitamani sana niwe mchungaji kama Bonke, ila siwezi, sitaki kuwa mchungaji tena, ni lazima niwe muuaji kwa kila mtu aliyemfanya mama yangu kuwa katika hali hii,” alisema Godwin kwa hasira huku machozi yakimtoka.

Walipaswa kumsaidia mama yao kazi ya kuuza genge. Kila walipokuwa wakitoka shuleni, walifikia kuuza genge. Mwanzoni walijisikia aibu lakini kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele, walizoea na hatimaye kukubaliana na hali halisi kwamba yale yalikuwa maisha yao.

“Amina! Natakiwa kurudi nyumbani haraka sana,” alisema Godwin, alikuwa akimwambia rafiki wake wa kike aliyeitwa Amina.

“Ila si mara moja tu! Tunakwenda halafu tutawahi kurudi!” alisema msichana huyo.

“Hapana! Tufanye siku nyingine. Siwezi kumuacha mama akiuza genge peke yake,” alisema Godwin.

“Lakini Irene si yupo?”

“Haijalishi! Na yeye pia anatakiwa kupumzika Amina,” alisema Godwin.

“Please!” (tafadhali)

“Am I understood?” (nimeeleweka?)

“A little bit,” (kidogo tu)

Amina alisimama akimwangalia Godwin, alimpenda mvulana huyo lakini alishindwa kumwambia ukweli. Alikuwa kijana mpole ambaye hakuonekana kuzungumza jambo lolote kuhusu mahusiano ya kimapenzi.

Alijaribu kumuonyeshea ishara zote kwamba alikuwa akimpenda lakini Godwin hakuonekana kabisa kuelewa. Alikuwa bize na masomo, maisha ya nyumbani kwao yalikichanganya mno kichwa chake.

Siku hiyo ya Jumamosi Amina alimwambia kwamba alitaka kwenda naye katika Ufukwe wa Coco lakini kijana huyo hakutaka kabisa kumuelewa. Alimwambia wazi kwamba alitakiwa kurudi nyumbani baada ya mitihani ya wiki kumalizika,

Amina aliumia lakini hakuwa na jinsi kwani hata Godwin alivyokuwa akionekana, ilionyesha kabisa hakuwa sawa. Hakumbishia, akabaki akimwangalia wakati Godwin akiungana na Irene kurudi naye nyumbani.

Njiani, kila mmoja alikuwa kimya, walisoma tu kwa sababu walihitajika kusoma lakini ukweli wa mambo ni kwamba vichwa vyao havikuwa sawa kabisa.

“Irene!” aliita Godwin.

“Abee!”

“Kuna mtu amesababisha haya yote, katika kila kitu kinachotokea, kuna mkono wa mtu,” alisema Godwin huku akimwangalia Irene.

“Kwa nini unasema hivyo?”

“Maisha yamebadilika kwa kasi sana. Hakuna mabadiliko yanayotokea kwa kasi namna hii! Umesoma historia, ni nani alikuwa na maisha yenye mabadiliko ya kasi kama yetu? Hakuna kabisa, nina uhakika hapa kuna mkono wa mtu,” alisema Godwin huku akimwangalia Amina.

“Tumuachie Mungu tu!

“Tumuachie Mungu? Yaani Mungu ashuke aje kudili na watu hao?” aliuliza Godwin.

“Sasa tutafanyaje?”

“Irene! Tutachelewa! Sijaona sababu ya kumsubiri Mungu na kudili na watu hao na wakati ametupa nguvu, akili, sasa unahisi Mungu ametupa za nini? Kukaa nazo tu?” aliuliza Godwin.

“Sijakuelewa unamaanisha nini?”

“Ni lazima tuue!”

“Tuue?”

“Irene! Hiyo ndiyo njia rahisi ya kufanya. Ili amani ipatikane, ni lazima tuue kama kisasi kwa kile tulichofanyiwa!” alisema Godwin huku akimwangalia Irene.

“Tumeokoka lakini!”

“Sizungumzii wokovu! Nazungumzia mauaji!

“Godwin!”

“Irene! Wakati mwingine amani inatakiwa kupatikana kupitia vita! Utakuwa tayari kuua?” aliuliza Godwin.

“Siwezi kuua!”

“Mimi nitaua! Nitakapomgundua mtu aliyesababisha haya yote, nitaua!” alisema Godwin.

Irene hakumuunga mkono Godwin, alibaki kimya huku akimwangalia. Alimuona Godwin ambaye hakumzoea kabisa katika maisha yake, alibadilika, roho ya kutamani kuwa mchungaji iliondoka moyoni mwake na kuingiwa na roho ya kutamani kuua.

Kila alipokaa, alifikiria ni kwa jinsi gani angefanya mauaji. Alijua dhahiri kwamba kwa kila kitu kilichokuwa kimetokea, kulikuwa na mtu aliyesababisha hayo yote.

Irene hakutaka kumwambia mama yake, alinyamaza huku kila alipokuwa akimwangalia Godwin manano yale aliyomwambia yaliendelea kujirudia kichwani mwake.

Maisha yaliendelea, walizidi kupigika, wakati mwingine biashara ya genge ilikuwa ngumu, walilala bila kula, walivumilia kwa kuamini kwamba kuna siku maisha yangekuwa na uafadhali kama kipindi cha nyuma lakini hilo halikuweza kutokea.

Baada ya kuishi kwa miezi sita, hatimaye kodi ya nyumba ikamalizika na hivyo mwenye nyumba kumuita Rosemary na kumpa taarifa kwamba alitakiwa kulipa.

“Nitalipa mwisho wa mwezi huu!” alisema Rosemary.

“Sawa. Usiniangushe basi!”

“Haina shida baba!”

Hakujua ni kwa namna gani angepata kodi hiyo, biashara ilikuwa ngumu na kila alipoifanya, pesa aliyoipata ilikuwa ni ya kula tu. Aliamini kwamba ni lazima angefukuzwa nyumbani hapo na famiia yake hakutaka hilo litokee, alitamani kulizuia lakini hakuwa na jinsi.

Baada ya mwezi kumalizika, baba mwenye nyumba akamfuata na kuhitaji pesa yake ya kodi, hakuwa nayo na hivyo kuwapa saa arobaini na nane kuondoka nyumbani hapo.

Hawakuwa na pa kwenda, Rosemary aliyafikiria maisha yake baada ya hapo. Saa arobaini na nane ambazo ni sawa na siku mbili zilipomalizika, wakafukuzwa nyumbani hapo.

Rosemary alilia, aliomba msaada wa kuongezewa siku lakini mwenye nyumba hakutaka kuwaelewa. Watu walikusanyika, waliwaonea huruma lakini hawakujua ni kwa jinsi gani wangeweza kumsaidia.

Hawakuchukua kitanda, walichukua baadhi ya vyombo vyao vya chakula na kuondoka nyumbani hapo. Waliviinamisha vichwa vyao, kila mmoja alikuwa akilia. Godwin alizidi kuwa na hasira tele, maisha waliyokuwa wakiyapitia yalimfanya kuwa na hasira zaidi juu ya mtu aliyesababisha wao kuwa mahali hapo.

“Nitamuua! Nitamuua mtu yeyote aliyesababisha haya!” alisema Godwin, wakati huo walikuwa njiani wakielekea Mwananyamala, hawakujua ni mahali gani walitakiwa kwenda kuishi. Waliamini kama wangefika huko, wangejua sehemu ya kuishi, hata kama ingekuwa barabarani, kwao kusingekuwa na shida yoyote ile.

***

Rosemary akiwa na watoto waliendelea na safari ya kuelekea Mwananyamala. Japokuwa walikuwa wakipita barabarani, hakukuwa na mtu aliyegundua kwamba walikuwa wao. Walichoka, maisha yaliwapiga kupita kawaida.

Walikuwa na utofauti mkubwa na wa zamani, walionekana watu dhaifu waliopitisha siku nyingi bila kula. Ilikuwa ni aibu kwa Rosemary, wakati mwingine alikuwa akichukua khanga yake na kuufunika kidogo uso wake.

Safari yao hiyo iliishia Mwananyamala karibu kabisa na hospitali ambapo kwa pembeni kulikuwa na mti mkubwa huku kukiwa na watu waliokuwa wakitengeneza masofa.

Wakatulia chini ya mti huo, hawakutaka kugundulika hivyo muda wao mwingi walificha sura zao. Walitaka kulala pembeni ya ukuta wa hospitali hiyo, hawakuwa na sehemu ya kwenda, kutoka katika maisha ya kifahari na kutamani hata kulala nje ya hospitali hiyo kwao yalikuwa mabadiliko makubwa mno.

Wakati wakiwa mahali hapo, muda mwingi watu waliokuwa wakipita karibu na eneo hilo walikuwa wakiwaangalia sana. Walishangaa, kwa eneo hilo haikuwahi kutokea hata siku moja watu wa mitaani au hata machokoraa kwenda kukaa mahali hapo.

Rosemary akagundua kwamba kama wangeendelea kukaa mahali hapo ilikuwa ni lazima wagundulike kama walikuwa wao, hivyo walichokifanya ni kuondoka huku tayari ikiwa saa kumi na mbili jioni.

Walipotaka kwenda ilikuwa ni Mikocheni. Rosemary alikumbuka kwamba zamani alipokuwa akipita kwa gari huko aliwaona wanawake wakiwa na watoto wao wakiishi mitaani kwa kujenga kibanda na kuendelea kuishi. Kama walivyokuwa watu hao, na yeye alitaka kwenda huko na watoto wake kwa ajili ya kuyaanza maisha hayo.

Kutoka Mwananyamala mpaka Mikocheni ilikuwa ni umbali mrefu, walipita katika njia ya Mtaa wa Mama Zakaria ambapo waliunganisha nayo mpaka Makumbusho.

Hapo, wakasonga mbele mpaka walipofika Sayansi ambapo wakachukua njia inayoelekea Rose Garden ambapo kwa mbele kidogo wakaachana na barabara ya lami na kuchukua barabara ya vumbi ambayo iliwapeleka mpaka sehemu iliyokuwa wazi, majani mengi kidogo ambapo hapo ndipo walipotaka kuyaanza maisha yao upya.

“Hapahapa panatosha,” alisema Rosemary huku akiliweka chini begi lake la nguo.

“Mama! Tunafanya nini hapa?” aliuliza Godwin.

“This is our new home,” (hapa ni nyumbani kwetu kupya!)

“A new home?” (nyumbani kupya?)

“Ndiyo!”

Hiyo ndiyo ilikuwa nyumba yao mpya, hawakubishana na mama yao, alikuwa mwanamke shupavu ambaye alikuwa tayari kupambana kwa ajili ya watoto wake hao.

Kwa kuwa giza lilikwishaanza kuingia, Rosemary akatandika kanga chini kwa lengo la kulala. Hakukuwa na mtu aliyelala, kila mmoja alikuwa akiyafikiria maisha yake, jinsi walipotoka mpaka kuwa mahali hapo.

Yalikuwa ni maisha yaliwaumiza, yaliyowasikitisha ambapo kwa Godwin kila siku alijiapiza kwamba ni lazima alipe kisasi, hata kama ingechukua miaka mingapi.

Walikesha, ilipofika asubuhi, wakatoa vyombo vyao vya kupikia. Kila mtu aliyekuwa akipita mahali hapo aliwashangaa, watu wengine, matajiri waliokuwa wakielekea kazini walisimamisha magari yao na kuanza kuiangalia familia hiyo.

Hilo liliwashangaza kila mmoja. Huo ulikuwa mtaa wa matajiri, kila jumba lililojengwa lilikuwa la kifahari, hawakujua watu hao walitoka wapi na kwa nini waliamua kuhamia hapo na wakati kulikuwa na sehemu nyingi za watu masikini ambapo wangeweza kwenda.

Hakukuwa na mtu aliyejua kwamba hiyo ilikuwa familia ya Mapoto. Kila walipokuwa wakimwangalia Rosemary, alijitahidi sana kuuficha uso wake, hakutaka mtu yeyote agundue kama wameanza maisha mapya.

Hakukuwa na shule tena, Irene na Godwin walitakiwa kusahau kila kitu kuhusu kusoma na kilichokuwa kimefuata ni kuendelea kuishi maisha ya mtaani huku wakitakiwa kutoka nyumbani na kwenda mitaani kuomba kwa ajili ya pesa za kumsaidia mama yao.

“Irene! Tumekuwa ombaomba mitaani! Kweli?” aliuliza Godwin, alikuwa amechanganyikiwa kupita kawaida.

“Godwin! Kila kitu kinatokea kwa sababu, hujui ni sababu gani imemfanya Mungu kuamua kutupa maisha haya, cha msingi ni kumshukuru kwa kila jambo,” alisema Irene.

“Mungu hakutuumba kwa ajili ya kuwa watoto wa mitaani, hakutuumba ili tuwe ombaomba mitaani, kuna mtu au watu ambao wamesababisha sisi kuwa katika hali hii! Ni lazima tupambane na tutoke huku! Ni lazima turudi kule tulipokuwa,” alisema Irene.

Wakati wakizungumza hayo walikuwa katika Barabara ya Ali Hassani Mwinyi wakiomba. Hakukuwa na mtu ambaye aliwagundua, wakati baba yao alipokuwa na jina kubwa nchini Tanzania, walikuwa wadogo sana. Waliokuwa na pesa waliwasaidia lakini wala ambao hawakuwa na kiasi chochote kile, waliwapita kama hawakuwaona.

“Jamani! Kwa nini hampo darasani?” aliuliza mwanamke mmoja, alikuwa akizungumza na Irene.

“Sisi ni masikini mama!”

“Mbona mnaonekana wakubwa hivyo! Wazazi wenu wapo wapi?” aliuliza mwanamke huyo, alikuwa kwenye gari lake, Land Cruiser nyeusi.

“Baba alikufa! Mama yetu masikini! Hana pesa ndiyo maana tunaomba kumsaidia,” alijibu Irene huku akimwangalia mwanamke huyo usoni.

“Sawa.”

Mwanamke huyo aliwaonea huruma, alimwangalia Irene, akamwangalia Godwin, walikuwa watoto wazuri walioonekana kuwa na akili sana. Alitamani kuwasaidia, si pesa tu, alitamani kuwapa maisha mazuri lakini kitu pekee alichokuwa akikihitaji ni kuonana na mzazi wa watoto hao.

“Ninahitaji kuwasaidia, huwa mnapatikana wapi?” aliuliza mwanamke huyo.

“Hapahapa!”

“Sawa. Wiki ijayo nitakuja kuzungumza nayi kwa kirefu. Mmesikia?” aliuliza mwanamke huyo.

“Ndiyo mama!”

Mwanamke huyo akaingiza gia na kuondoka mahali hapo. Kichwa chake kilichanganyikiwa. Aliolewa na mumewe, aliishi katika ndoa kwa miaka kumi na tano na hakubahatika kupata watoto.

Kitendo cha kuwaona watoto hao kilimfanya kujisikia huruma mno moyoni mwake. Alitamani nyumbani kwake kuwe na watoto, alitamani sana kuwachukua watoto wa ndugu zake na kuishi nao lakini ndugu haohao ndiyo waliokuwa na gubu, kumsema kila siku hiyo kuachana na watoto wao.

Moyo wake ukatua kwa Godwin na Irene, akajiwekea nadhiri moyoni mwake kwamba ni lazima awasaidie watoto hao kama watoto wake. Alitaka kufanya hivyo baada ya kumshauri mumewe, alijua jinsi mwanaume huyo alivyokuwa na kiu ya kuwa na watoto ndani ya nyumba yake, aliamini kabisa kwamba kama angemshirikisha, hakika asingekataa.



“Huyu chizi vipi?” aliuliza jamaa mmoja, alikuwa muuza duka katika mtaa wa Mikocheni.

“Hata mimi nashangaa! Halafu amekuja kuweka makazi hapa! Kweli huu ni mtaa wa machizi jamani?” aliuliza jamaa mwingine.

Macho yao yalikuwa yakimwangalia mwanaume asiyekuwa na akili ambaye alikuwa akitangatanga katika Mtaa wa Mbuni, Mikocheni. Kila mmoja alishangaa, huo waliuita mtaa wa matajiri, hawakuwa na historia ya kumuona kichaa akirandaranda mitaani, hawakujua kichaa huyo alitoka wapi kwani hata kumsogelea waliogopa kwa kuwa mkononi mwake alikuwa na fimbo ndefu.

Kila mmoja alitamani kumfuata kichaa huyo na kumfukuza lakini hakukuwa na mtu aliyethubutu kumfuata. Hawakumpenda, walimjadili kila siku lakini hawakupata jibu juu ya kitu gani walitakiwa kumfanya.

Mbali na kichaa huyo pia waliwaangalia Rosemary na watoto wake, kama ilivyokuwa kwa kichaa yule, hata mwanamke huyo hawakupenda kumuona mahali hapo. Hiyo haikuwa sehemu ya kuwaweka ombaomba wa mitaani wala vichaa lakini walishindwa kujua wafanye nini.

“Tuanze na kichaa au huyu mwanamke?” aliuliza jamaa mmoja.

“Kichaa kwanza! Yule mwanamke na watoto wake tuachane nao, wanatafuta maisha, ni masikini. Ila huyu kichaa tumtoeni mtaani kwetu,” alisema jamaa mwingine.

Hawakujua sababu ya kichaa yule kuwa mahali hapo, hawakujua alitoka wapi, walichokiangalia ni kuona kichaa huyo akiondolewa mahali hapo mara moja.

Wakaitana vijana wote wa mtaani, wakaweka nguvu za kutaka kuhakikisha mtu huyo anaondolewa mahali hapo pasipo kujua kwamba kichaa huyo alikuwa ni ofisa wa Usalama wa Taifa ambaye alifika hapo kwa kazi maalumu ambayo hawakuijua.

***

“Kuna taarifa gani kuhusu yule mwanamke?” ilisikika sauti kutoka upande wa pili.

“Kila kitu kipo kama kilivyopangwa. Anapigwa na maisha!”

“Safi sana! Inatakiwa tufuatilie kila kitu kitakachoendelea katika maisha yake. Ninahitaji vijana zaidi wamfuatilie kila hatua, hatakiwi kuyafurahia maisha, ninataka ale matunda ya kazi aliyoifanya mumewe,” iliendelea kusikika sauti ya mwanaume huyo.

Huo ndiyo ulikuwa mpango uliopangwa, ilikuwa ni lazima kuhakikisha kwamba Rosemary na watoto wake wanaishi kwenye maisha ya tabu kwa kuwa hawakustahili kuishi maisha ya raha hata siku moja.

Hilo ndilo lililofanyika, vijana wakaandaliwa na kuanza kufanya kazi waliyotumwa. Rosemary na familia yake walipokuwa Tandale, vijana hao nao wakaenda huko, wakapanga vyumba na kutulia huko.

Walitakiwa kupeleka ripoti kila baada ya siku mbili ili wakubwa wajue ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea. Wakati mwingine vijana hao waliwaonea huruma lakini hawakutakiwa kujali, ilikuwa ni lazima kuhakikisha anaishi maisha ya tabu kwa sababu tu walipewa maagizo ya kufanya hivyo.

Walikuwa nao hatua kwa hatua, walipohama Tandale na kuhamia mtaani huko Mikocheni, hawakuweza kuwafuatilia bali walipeleka ripoti kwamba mwanamke huyo na familia yake walihamia huko na hivyo kulitakiwa kupelekwa mtu wa kuendelea kuwafuatilia.

Waliamini kwamba kama wangewaweka vijana wa kawaida, basi watu waliokuwa wakiishi mahali hapo wangeweza kuwashtukia hivyo walichokifanya ni kumuweka kijana aliyeonekana kuwa kama kichaa kwa ajili ya kuendelea kumfuatilia mwanamke huyo na familia yake.

Hilo halikuwa tatizo, baada ya siku kadhaa, mwanaume mmoja, mwendawazimu akaanza kuonekana mtaani hapo. Kila mmoja alihisi kwamba alikuja na kuondoka lakini kilichowashangaza ni kwamba maisha yake yakaanzia hapo, wakati Rosemary akiwa na familia yake upande mmoja, mwenyewe aliweka kijiwe chake upande mwingine.

Ilikuwa ni vigumu kugundua kama mwanaume huyo alikuwa na akili timamu, muonekano wake ulikuwa kama kichaa, alitembea na fimbo na alionekana kuwa mkali hasa.

Pembeni yake kulikuwa na mifuko kadhaa, ilionekana kama takataka, alivaa nguo za kuchakaa lakini kiunoni alikuwa na bastola yake ya kujilindia kama kungekuwa na tatizo lolote lile.

Wakati vijana wa mtaa huo wakijiandaa kumfuata kwa ajili ya kumuondoa mahali hapo, aliwaona, alitulia, akachukua fimbo yake na kusimama, akawaangalia watu hao ambao walionekana kuwa na dhamira ya kutaka kumuondoa mahali hapo.

“Vipi sasa?” aliuliza jamaa mmoja, alionekana kuogopa kwani kwa jinsi kichaa yule alivyosimama na fimbo yake, aligundua kabisa kwamba kungekuwa na hatari mahali hapo.

“Tumsogeleeni!”

“Mmh! Tutamuweza jamani?” aliuliza jamaa mwingine.

Walikuwa wakijiuliza, kumuondoa kichaa huyo mtaani kwao likaonekana kuwa zoezi kubwa na gumu ambalo kulifanya ilihitajika nguvu za ziada. Walimwangalia, naye alikuwa imara akiwaangalia kwa hasira kubwa.

Waliogopa, hawakuwa radhi kuumia hivyo walichokifanya ni kupiga hatua kurudi nyuma na kumwacha akiendelea na mambo yake. Alionekana kuwa kero lakini hawakuwa na la kufanya, waliwasiliana na serikali ya mtaa lakini nao walishindwa kumtoa kichaa huyo mahali hapo.

Rosemary hakujua kama alikuwa akifuatilia yeye na familia yake. Maisha yake yaliendelea na kila siku alikuwa akiteseka. Hakuwa na muda wa kwenda kutafuta pesa, alijulikana na watu wengi hivyo kuhisi kwamba kama angekwenda huko angeweza kuonekana na waandishi wa habari na kumripoti katika vyombo vyao vya habari.

Watoto wake ndiyo walikuwa kila kitu kwake. Walipokuwa wakirudi nyumbani, walimgawia kiasi cha fedha ambacho walikipata mitaani na maisha kusonga mbele.

“Tumekutana na mwanamke mmoja hivi,” alisema Irene huku akimwangalia mama yake, alikuwa na shauku kubwa ya kumwambia kuhusu mwanamke waliyekutana naye.

“Nani?”

“Sijui! Ila amesema kwamba anataka kutusaidia!” alisema Irene.

“Kuwasaidia? Kivipi?”

Irene akaanza kumuhadithia kila kitu kilichotokea barabarani, jinsi mwanamke huyo alivyowaona na kuwaonea huruma kwa hali waliyokuwa nayo. Rosemary alimsikiliza kwa makini, hakumfahamu mwanamke huyo lakini kitendo cha kusema kwamba awachukue watoto hao na kuondoka kwenda kuishi nao lilionekana kuwa jambo gumu mno.

“Haiwezekani!” alisema Rosemary.

“Mama! She is a good woman!” (mama! Ni mwanamke mwema.)

“No! You can’t leave me here? I just want to live with you both,” (hapa! Hamuwezi kuniacha! Ninataka kuishi na nyie wote wawili).

Huo ndiyo ukweli, hao walikuwa watoto wake, kwake, walikuwa kila kitu katika maisha yake. Hakutaka mtu yeyote aje na kuwachukua, aliwapenda, japokuwa hakuwa na kitu, japokuwa alikuwa masikini mkubwa sana lakini suala la kuwaacha watoto wake lilikuwa gumu mno.

Hakutaka kumwamini mtu yeyote katika maisha yake, hakumjua mbaya wake alikuwa nani, alihisi kwamba inawezekana huyo mbaya wake alikuwa akimfuatilia, aliamini kwamba kama angeruhusu watoto wake waondoke mikononi mwake basi wasingekuwa salama.

Alitaka kuendelea kuishi nao ili hata kama ingetokea kufa basi afe akiwa mikononi mwao. Kukataa kwa mama yao kuliwaumiza mno mioyoni mwao. Hakukuwa na kitu walichokitamani wakati huo kama kusoma, waliamini kwamba kama wangekwenda kwa mwanamke huyo ilikuwa ni lazima kuwasomesha kama walivyokuwa wakifanya zamani.

Walihuzunika lakini hawakutaka kumuonyeshea mama yao huzuni zao. Walitamani kumuona akiwa na furaha muda wote, walitamani kumuona akisahau kila kitu kilichokuwa kimetokea na kuishi maisha ya kawaida.

Siku iliyofuata, kama kawaida wakaamka asubuhi na mapema na kuelekea mitaani kama kawaida. Hayo yalikuwa maisha yao ya kila siku na jioni walipokuwa wakirudi walikuwa na kiasi cha fedha cha kutosha ambacho walimpa mama yao.

Baada ya wiki moja, wakafanikiwa kukutana na mwanamke yule ambaye alijitambulisha kwa jina la Angelina, ila alipenda sana kuitwa kwa jina la Madam Angelina. Akawaambia kwamba alitaka kuonana na mama yao kwa ajili ya kuzungumza mawili matatu kwani bado mpango wa kwenda kuishi nao.

“Ila mama alikataa!” alisema Irene, wakati huo Godwin alikuwa kimya kabisa.

“Wala usijali! Nina uhakika atakubali! Nitazungumza naye tu,” alisema mwanamke huyo.

Akawaambia waingie ndani ya gari, wakafanya hivyo na kuondoka mahali hapo. Kitendo cha kuwa humo tu, mawazo yao yalianza kukumbuka mbali, siku ambayo baba yao alikuwa akiwafuata shuleni na kuwachukua kisha kuondoka nao.

Mule garini, walikuwa wakitokwa na machozi kwani hawakukumbuka mara ya mwisho kupanda gari ilikuwa lini. Madam Angelina aliwaonea huruma, kila alipowaangalia, walikuwa watoto wazuri ambao walistahili kupewa maisha mazuri, hawakutakiwa kuwa mitaani, walitakiwa kuwa shuleni wakisoma.

Hawakuchukua muda mrefu wakafika mahali walipokuwa wakiishi, wakateremka na kisha kukifuata kibanda chao ambapo mara baada ya kuingia, mwanamke yule akapigwa na mshtuko, hakuamini yule aliyemuona ndani ya kibanda kile, alimfahamu, alikuwa Rosemary, mwanamke mpole, mke wa mwanasiasa mkubwa sana nchini Tanzania.

“Rosemary!” aliita huku akionekana kushtuka.’

“Ndiyo mimi!”

“Nini kimetokea?”

Rosemary hakujibu kitu zaidi ya kulia tu. Moyo wake ulimuuma, swali hilo likaanza kuyarudisha mawazo yake nyuma, tangu siku za kwanza alipoanza kunyanyaswa mpaka kufikia hatua ya kufukuzwa nyumbani kwake.

Moyo wake ulimuuma mno. Madam Angelina akaanza kumbembeleza akimtaka kunyamaza. Baada ya kunyamza akaanza kumuhadithia mwanamke huyo kila kitu kilichokuwa kimetokea kwenye maisha yake.

Madam Angelina aliumia moyoni, yeye mwenyewe akahisi kabisa kwamba kulikuwa na mtu aliyekuwa amehusika katika maisha ya mwanamke huyo, ila alimuahidi kumpa msaada wa hali na mali.

“Nitakusaidia mpaka unapata kila kitu chako,” alisema Madam Angelina huku akimwangalia Rosemary.

“Nitashukuru sana!”

Hata suala lililokuwa limemleta nyumbani hapo hakulizungumzia, alikuwa na maumivu makali hivyo kuondoka. Akaingia ndani ya gari lake, kabla ya kuliwasha, akaegemea usukani na kuanza kulia kama mtoto, maisha ya Rosemary na watoto wake yaliugusa moyo wake vilivyo.

Alikaa kwenye hali hiyo kwa dakika kadhaa, akawasha gari na kuondoka mahali hapo. Wakati akiwa kwenye barabara ya lami maeneo ya Rose Garden, akashtukia magari mawili yakifunga breki mbele yake, wanaume wawili waliokuwa na bunduki wakateremka, watu wakashangaa, wanaume hao wakapiga risasi juu, kila mmoja akakimbia.

Wakalifuata gari lile, wakapiga kioo kwa bastola, kikavunjika, wakaufungua mlango na kumshusha Madam Angelina kisha kuanza kumpeleka lilipokuwa gari lao.

“Naomba msiniue! Nitawapeni kiasi chochote cha fedha,” alisema Madam Angelina huku akilia.

“Hatuhitaji pesa zako! Tunachotaka ni roho yako tu,” alisema mwanaume mmoja na kumuingiza ndani.

Kila kilichokuwa kikiendelea, watu walikuwa wakishuhudia kwa kujificha. Ilionekana kama muvi fulani ya mapigano ya Kimarekani.

***

Kazi waliyokuwa wametumwa waliifanikisha kwa asilimia sabini. Waliambiwa wamteke Madam Angelina kwa kuwa alikuwa kimbelembele kumsaidia Rosemary ambaye hakutakiwa kupata faraja yoyote ile, hakutakiwa kusaidiwa kwa kitu chochote.

Mawasiliano yakafanyika na kuwaambia watu waliowatuma kwamba tayari mwanamke huyo alikuwa mikononi mwao na walisubiri kuambiwa ni kitu gani walitakiwa kufanya wafanye.

Mtu kutoka upande wa pili akawaambia kwamba mwanamke huyo alitakiwa kufa, hakutakiwa kuachwa kwani kwa kile alichokuwa amekifanya kiliwachanganya mabosi na hakutakiwa kuachwa hai hata mara moja.

“Sawa mkuu!”

Safari ilikuwa ikiendelea, Madam Angelina alikuwa akilia ndani ya gari, hakujua ni kitu gani alikuwa amekifanya, alihisi watu hao walikuwa majambazi, walimteka kwa sababu walihitaji pesa lakini alipowaambia suala la kuwapa pesa, wakakataa na kumwambia kwamba walichokihitaji kilikuwa ni roho yake tu.

Alikiona kifo, bastola walizokuwa wamezishika wanaume wale ziliwaogopesha na kuona kwamba mwisho wake ulikuwa umekaribia. Alitamani kumpigia simu mumewe na kumwambia kile kilichomtokea lakini alishindwa kufanya hivyo kwani simu yake ilikuwa ndani ya gari lake.

“Naomba msiniue…naomba msiniue,” alisema Madam Angelina huku akilia kama mtoto.

“Tumesema tuna kazi na roho yako! Hata ulie machozi ya damu jua kwamba wewe kuiona kesho ni vigumu sana,” alisema mwanaume mmoja kwa jeuri huku akimwangalia Madam Angelina.

Kilio chake hakikusaidia kitu, wanaume wale walikuwa na lengo moja tu, kumuua na kuutelekeza mwili wake. Safari iliendelea mpaka walipokaribia katika Msitu wa Pande.

Kilio cha Madam Angelina kiliongezeka zaidi, aliufahamu msitu huo, kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakiuawa huko na miili yao kutelekezwa, akajua kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wake na wanaume wale walipomwambia kwamba lazima afe walimaanisha na walichokuwa wakikisema.

Gari likakata kona kulia, likatoka katika barabara ya lami na kuingia katika msitu wa Pande. Madam Angelina aliendelea kulia, alivikutanisha viganja vyake na kuanza kusali kwani hakuona kama kungekuwa na dalili za kuachwa salama humo.

Gari lilipita msituni, liliendelea mbele mpaka lilipofika sehemu kulipokuwa na nyasi nyingi, likasimama na kisha kumteremsha na kumuweka chini. Mwanaume mmoja akachukua bastola yake na kuikoki tayari kwa kumfyatulia Madam Angelina risasi.

“Yule wa siku ile kule Tanganyika Parkers ulimuua wewe, leo huyu wangu,” alisema mwanaume huyo.

“Haina shida. Ua fasta tusepe!”

“Na mwili wake?”

“Tuuacheni hukuhuku!”

“Tukiwa tumeuzika?”

“Tuuzike? Tunauzikaje kwa mfano? Ndege watakula wapi? Ni dhambi kuua ila ni thawabu kuwapa ndege chakula chao,” alisema jamaa mmoja.

“Sawa. Let me kill her,” (sawa. Acha nimuue) alisema jamaa huyo ambapo akachukua bastola yake na kumnyooshea Madam Angelina na kumuua kama walivyofanya kwa Juma.

****

Matumaini yalianza kurudi tena, kila mmoja akaona kabisa kwamba siku chache zijazo maisha yangekuwa nafuu, kusingekuwa na harakati zao za kuombaomba mitaani. Walimwamini Madam Angelina, kwa jinsi alivyokuwa ameongee nao, walikuwa na uhakika wa kupata maisha mazuri.

Walikumbuka shule, walitamani kurudi darasani na kusoma kama ilivyokuwa zamani, hawakutaka kuendelea kuishi mitaani kwani waliamini kwamba kwa staili yoyote ile ilikuwa ni lazima kurudi darasani na kuendelea kusoma, kwa jinsi maisha yao yalivyokuwa, hawakuona kama walistahili kuwa mitaani kama walivyokuwa.

Walimsubiri Madam Angelina, siku ya kwanza ikakatika, ya pili ikaingia na kukatika lakini bado hawakupata mawasiliano kutoka kwa mwanamke huyo. Hilo hawakuwa na hofu nalo, hawakujua kama kulikuwa na kitu kibaya kilitokea, kitu pekee ambacho walikiamini ni kwamba alikuwa akijiandaa kuwasaidia, na kama hakuwa akionekana basi alikuwa akifuatilia shule ambazo walitakiwa kwenda kusoma.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Wiki ya kwanza ikakatika, hawakupata taarifa zozote kutoka kwa mwanamke huyo, hawakukata tamaa, kwa jinsi Madam Angelina alivyojitolea kuwasaidia, alivyowaambia maneno matamu ya matumaini walikuwa na uhakika kwamba angerudi tena.

Wiki ya pili ilipoingia ndipo wakagundua kwamba mwanamke huyo asingeweza kurudi tena. Walimsubiri, kama kweli alikuwa na lengo la kuwasaidia ilikuwa ni lazima kuwarudia na kuwapa kila kitu alichowaambia kabla.

“Will she come back?” (atarudi?) aliuliza Irene huku akimwangalia mama yake, macho yake tu yalionyesha jinsi alivyochoka kusubiri.

“I don’t know! We have to wait!” (sijajua! Tunapaswa kusubiri) alijibu mama yake.

Hawakuchoka kusubiri, hawakuwa na msaada wowote kutoka sehemu yoyote ile zaidi ya kwa Madam Angelina ambaye hawakujua alikuwa wapi. Walikuwa wavumilivu na mpaka mwezi unakatika, mwanamke huyo hakutokea, na si hivyo tu bali hata dalili za kutokea tena hazikuwepo.

****





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog