Search This Blog

Tuesday, 1 November 2022

KICHAA WA MTAA - 1

 






IMEANDIKWA NA : ALEXIS WAMILAZO



*********************************************************************************



Simulizi : Kichaa Wa Mtaa
Sehemu Ya Kwanza (1)
 Katika kijiji cha Mwasanda mkoa wa Simiyu wilayani Bariadi, anaonekana kichaa akitembea kuelekea kwenye makaburi ya kijiji hicho. Kichaa huyo hakuwa mwingine bali ni Nyogoso, kijana ambaye alikumbwa na ugonjwa wa akili baada kutoka Dar es salaam na kukuta mama yake amefariki pasipo kumuomba msamaha juu ya yale aliyomfanyia. Moja ya mambo hayo ni kuamua kuondoka Dar es salaam na kumuacha mama yake peke yake ilihali akijua kabisa yeye ndio tegemezi kwake kwani tayari alikuwa amekula chumvi nyingi. Licha mama yake kumkataza lakini katu Nyogoso hakuweza kumuelewa, alilazimisha safari ya kuelekea jiji Dar es salaam pasipo mama yake kulidhia. Huko alikumbana na tabu shida mbali mbali, aliishia maisha mgumu. Kazi pekee iliyomlea jiji Dar es salaam ilikuwa ni kuzoa takataka, kazi ambayo mwishowe ilimpelekea kuzama kwenye penzi la mtoto watajiri Dominic atwae Mazoea. Vita ilikuwa kali sana baina ya mama Mazoea na Nyogoso, mama huyo hakutaka binti yake atoke kimapenzi na Nyogoso mzoa takataka. Na siku ambayo ilikuwa mbaya kwa Nyogoso ni siku ile aliyohukumiwa jela baada kuzushiwa kesi ya kuiba, kesi ambayo nguvu ya pesa ndiyo iliyotumika ni pale kufumaniwa na wazazi wa Mazoea ambapo waliamua kumzushia kesi hiyo iliyomuhukumu jela maika sita. Msamaha wa rais ndio ukamtoa Nyogoso jela, hiyo nayo ikawa siku nyingine ya toafu kwake. Alipambana vya kutosha, alifanya kazi ngumu ambazo zilitumika nguvu sana mpaka akapata nauli ambayo ilimrejesha kijijini kwao. Na ndio siku hiyo hiyo ambayo alikumbwa na uwendawazimu baada kuambiwa kuwa mama yake ameshafariki.

"Kwanini umefariki? Hukutaka kungoja mwanao nikuombe msamaha? Kwanini mama?", ndilo swali la mwisho ambalo Nyogoso alijiuliza, na punde akawa kichaa.

Ilikuwa jioni, kichaa Nyogoso akiwa na furushi lake begani. Furushi lililojaa mazagazaga, alizipiga hatua kuelekea makaburi kwa dhumuni la kulitafuta kaburi la mama yake ili alisafishe lakini pia aweze kuomba msamaha akiamini kuwa huwenda mzimu wa mama yake akamtokea ukampa msamaha. Kichaa Nyogoso alizunguka huku na kule akilisaka kaburi la mama yake, wingi wa makaburi malaloni hapo yalimpelekea kushindwa kutambua mahali lilipo kaburi la mama yake. Pumzi alishusha huku akiangaza macho yake kulia na kushoto, mbele na nyuma. Alichoka akakaa kwenye moja ya kaburi kisha akasema "Mama umelala wapi? Nataka nione nyumba yako mama yangu. Sema uko wapi", alidondosha chozi Nyogoso alipokwisha kusema maneno hayo. Mwishowe alinyanyuka kwenye kaburi hilo akarejea kijijini kichwa chini mzigo wa mazagazaga yake ukiwa begani. Taharuki inazuka kijijini Mwasanda. Wanakijiji walistuka kumuona Nyogoso mtoto wa mama Nyogoso akiwa mwendawazimu. Sintofahamu ilichukua nafasi mioyoni mwa wanakijiji waliomfahamu Nyogoso, lakini mbali na hilo kichaa Nyogoso alikuwa kama mfano wa kujifunzia juu ya vijana waliokuwa na hurka ya kukurupuka kwenye maisha. Vijana wengi wa kijiji hicho walijijengea utamaduni kuwa Dar es salaam ndio jiji la kutafutia maisha, ila walipotazama maisha ya Nyogoso hamu ya kuelekea ndani ya jiji hilo ilipotea haraka sana iwezekanavvyo. Wazee wa busara ndani ya kijiji hicho walishauriana ni namna gani ya kumsaidia Nyogoso, ilikuwa jioni moja. Kijiweni walikusanyika wazee kupata chai ya tangawizi sambamba na vibumunda huku birika lenye tangawizi nalo likiwa katikati yao. Zogo lilinoga,utani wa hapa na pale ulitawala. Waligusia maendeleo ya kijiji chao, lakini pia waligusia siasa na kandanda. Vyote hivyo vikipambwa na chai ya tangawizi pia kahawa. Hakuweza kuishi hapo, wazee hao walienda mbali zaidi kumgusia kichaa Nyogoso. Jambo hilo liliwasikitisha sana wazee hao katika kilinge hicho. Mzee mmoja aliyeitwa Bushiri alisema "Wazee wenzangu. Ukweli hili ni suala la kuzungumza kwa kina ili tujue tutawezaje kumsaidia huyu kijana. Ukweli anasikitisha sana"http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"Kazi ngumu sana hiyo", aliongea mzee wa pili, huyo aliitwa Busara.

"Kwanini unasema hivyo?", mzee Bushiri alimuuliza Busara huku akiwa akimtazama.

"Kwa sababu hatujui chanzo chake kilicho mpelekea kukumbwa na balaa hilo",alijibu mzee Busara. Baada jibu hilo, kimya kilitanda katika kilinge hicho. Punde kimya hicho kilitoweka, mzee Bushiri kwa kudai aongezewe andazi ili amalize chai yake.

"Nipatie andazi kwanza", aliongea mzee Bushiri. Alipatiwa alicho hitaji lake. Mzee mwingine aliyeitwa Mabula alisema "Hata mimi naunga mkono jambo alilo lizungumza mzee mwenzangu hapo, kumbukeni kwamba Nyogoso aliondoka kijiji hapa miaka isiyopungua mtatu kama sio minne. Alirudi kijijini akiwa mzima akiwa na akili zake timamu kabisa lakini baada ya siku mbili tatu ndio anaonekana akiwa katika hali ile. Mimi na nyinyi hatujui huko alikotoka alifanya kitu gani, huwenda aliiba mali ya watu. Mwenye mali akaamua kumfanyia kitendo kile aidha kuna dhambi nyingine tofauti alifanya mpaka ikampelekea kuwa vile. Wazee wenzangu, mshahara wa dhambi siku zote ni mauti. Hivyo basi chonde chonde tusije tukafanya kitu juu yake tukaangamia wote ", alisema mzee Mabula kwa msisitizo na vitisho. Wakati huo mzee Bushiri naye alionekana kujiandaa kujibu kile alichokiongea mzee Mabula. Lakini kabla mzee huyo hajafungua kinywa chake, alitokea kichaa Nyogoso akiwa na furushi lake lenye mazagazaga begani. Nyogoso aliongea mahali hapo kilingeni, alipofika alitua mzigo wake chini kisha akatoa salamu kwa wazee hao. "Habari zenu wangu, shkamoni. Ila kabla hamjaitikia salamu, nipeni kwanza chai na maandazi sita. Matatu nitakula mimi na mengine matatu nitampelekea mama yangu kaburini.", alisema Nyogoso kisha akaangua kicheko. Wazee walitazamana, hawakuweza kumuelewa kichaa Nyogoso alimanisha nini aliposema kuwa maandazi matatu atampelekea mama yake kaburini.

" Mpe hayo maandazi, pesa nitalipa mimi ", aliongea mzee Bushiri. Nyogoso kwa mara nyingine tena akaangua kicheko baada kupewa alicho kihitaji. Alipohitimisha kicheko chake akasema "Hii nchi ya ajabu sana, utakuta mwanamke anadai haki sawa ilihali toka mwanzo Mungu alishabainisha kuwa sisi wanaume hatuwezi kwenda sawa na wanawake na ndio maana tunauwezo wa kuoa mwanamke zaidi ya mmoja ilihali wao hawawezi kuolewa na mwana zaidi ya mmoja. Mungu fundi bwana. Hahahahah hahahah! Alijua mwanamke ni kiumbe dhaifu sana. Eti haki sawa! Mnaijua haki sawa nyinyi?. ", kichaa Nyogoso akaurudia kaungua kicheko. Alicheka sana halafu akaendelea kusema." Nakumbuka babu aliwahi kuniambia, mjukuu wangu mwanamke akili yake haina tofauti na akili ya kuku. Hahahah hahahahah.. Nilicheka sana kiukweli na baadaye nikamuuliza kwanini babu? Akanijibu, hapo sasa nyie wazee naombeni mnisikilize kwa umakini. Babu akanijibu kwamba, mwanamke ni kiumbe ambacho kinamfanya makosa kwa kujirudia rudia kama ilivyo kuku", wazee hao waliokuwa kwenye kilinge waliangua kicheko walipoyasikia maneno ya kichaa Nyogoso. Utulivu ulichukua nafasi yake, walikaa kimya kumsikiliza ingawa kila mmoja moyoni akisikitika kwa namna yake. Kichaa Nyogoso alikohoa kidogo kisha akahitimisha kwa kusema "Lakini pia mbali na hayo,akaniambia kuwa mwanamke anamasikio matatu. Kuna sikio moja usipo usipo lichokonoa vizuri, katu hatakaa akakuheshimu", alipokwisha kusema hivyo alinyanyuka akachukua mzigo wake wa mazagazaga akayaweka maandazi yale matatu aliyosema kuwa anampelekea mama yake kaburini kisha akaondoka zake huku akiendelea kujisemea "Eti utakuta mwanaume mzima unasimama unawaambia wanaume wenzie, tena kwa kujinasibu. Kuna binti nilimtoa bikira, najua hatonisahau. Hahahah hahahah. Huu ni ujinga uliopitiliza kipimo, wamesahau anasahau kwamba ili mwanamke asikusahau dawa pakee ni kumzawadia mimba na sio vingenevyo ". Gumzo anaacha kichaa Nyogoso kilingeni. Maneno yake yaliwashangaza wazee hao, walibaki midomo wazi na hata wasijue ni kwanini Nyogoso ananena maneno hayo hasa hasa akiwazungumzia wanawake. Alifika malaloni, aliangaza macho yake huku na kule kulisaka kaburi la mama yake huku akipasa sauti ya kumuita na kusema "Uko wapi mama, mwanao nimekuletea chakula mama yangu",maneno hayo Nyogoso kila alipokua akiyaongea, macho hayakua mbali na mboni za macho yake, yalimtoka vilivyo hasa ukipat uchungu kwa kulikosa kaburi la mama yake.

Lakini pia mbali na gumzo lile aliloacha kichaa Nyogoso kilingeni, mwishowe taharuki ilileta huzuni mahali hapo. Simanzi kubwa ilitanda, kila mzee aliyekuwepo hapo kilingeni alimuona huruma Nyogoso. Kichaa huyo nguo zake zilionekana kuchakaa sana, suruali yake imekatwa miguu kwa kuzidiana urevu vile vile kichwa chake kikionekana kuchakazwa na nywere ndefu zilizojisokota mithili ya rasta.

"Hii ndio Dunia, bila shaka aliyemroga huyu kijana huwenda ameshakufa", aliongea mzee Bushiri kisha akainuka kutoka kwenye benchi akaelekea nyumbani kwake, giza tayari lilikua limetanda.

Hayo ndivyo yalikua maisha ya mwendawazimu Nyogoso, kichaa mstarabu muongeaji. Kutokana na maneno yake alijikuta akipigwa vikali na wanawake, lakini kitendo hicho kamwe hakikuweza kumfanya aogope kuwapa ukweli uliokua moyoni mwake. Na wakati maisha ya yakiendelea kwa Nyogoso, upande wa mwingine ndani ya jiji la Dar es salaam. Suzani. Yule binti aliyeokotewa pochi na Nyogoso alizidi kukosa usingizi kila alipomkumbuka mzoa takataka. Dharau ile aliyomuonyeshea iliuumiza moyo wake, alijiona mkosefu na hivyo kila wakati amani ndani ya moyo wake ilitoweka. Lakini pia Suzani mbali na kutaka kumuomba radhi Nyogoso kwa kile alichomfanyia, vile vile moyo wake ulitokea kuvutiwa naye punde tu alipoonyesha ukalimu uaminifu mbele ya mboni zake. Alimpenda, hali hiyo ilimpelekea kutumia muda mwingi sana kumuwaza kuliko kufikiria masomo yake. Ghafla alijikuta akifeli mitihani yake chuoni, alikonda sana kwa usongo wa mawazo ya kumuwaza kijana mzoa takataka Nyogoso ambaye kwa sasa ni mwendawazimu..



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Hali hiyo Suzani kumuwaza Nyogoso mara kwa mara ilimpelekea kuharibika kisaiklojia, hakupenda tena kujisomea kama alivyokuwa akifanya hapo mwanzo. Suzani sasa aliamua kuzulula sokoni kila wakati akidhania kuwa huwenda akabahatika kumuona Nyogoso,ila kamwe hakuweza kupata bahati hiyo kwa sababu Nyogoso hayupo tena jijini Dar es salaam amesharejea kijijini kwao ambapo huko nako amekumbwa na wendawazimu. Maisha hayo yalikua endelevu kwa Suzani, kila siku furaha kwake ilikua ndoto.

Kichaa Nyogoso makazi yake yalikua makaburini, huko ndipo alipoona panamfaa kuishi. Ilkua asubuhi moja, siku hiyo alichelewa kuamka. Alijinyoosha kisha akachukua mfuko wake wa mazagazaga tayari kwa safari za kutembea huku na kule, kwa sababu ndio yalikua maisha yake. Ilipotimu mchana wa jua kali, alihisi kiu hivyo alizipiga hatua kuelekea kisimani. Alipofika aliwakuta wanawake wanne wakichota maji, aliwasalimu "Habari zenu jamani",wanawake hao waliposikia sauti hiyo waligeuka kutazama upende ule ilipotokea. Walistuka kumuona kichaa ilihali muda huo huo Nyogoso akasema "Samahani kwa usumbufu naomba nisaidieni maji, maana nina kiu sana"

"Mshenzi wewe. Jamani huyu ni mbakaji tukimbie", mmoja ya wanawake waliokuwepo hapo kisimani aliongea kwa sauti ya juu huku akiwaasa wenzake wamkimbie Nyogoso. Nao waliogopa sana, haraka kwa pamoja walitimua mbio huku wakipiga mayowe. "Jamani mbakajiiii.. Mbakaji jamaniii.." , kichaa Nyogoso alistaajabu kuwaona wanawake hao wakimkimbia,alitikisa kichwa akisikitika kisha akachukua kata akachota maji kisimani akanywa yaliyobakia akajimwagia kichwani. Alipokwisha kukata kiu, alibeba mazagazaga yake akarudi kijijini kuendelea na safari zake zisizo na faida. Lakini wakati yupo njiani, alikutana na jopo la vijana wa kijiji. Walikua vijana wasio pungua sita, na nyuma yao walionekana wale wanawake waliomkimbia Nyogoso kisimani.

"Ndio huyu mwendawazimu mwenyewe,alitaka kutubaka", aliongea mwanamke mmoja kati ya wale waliokuwepo mahali hapo. Kichaa Nyogoso alitaharuki kusikia tuhuma hiyo, alirudi nyuma hatua kadhaa wakati huo vijana hao wa kijiji walimzunguka huku mikono wakiwa wameshika fimbo.

"We kichaa. Unawajua hawa wanawake?", kijana mmoja aliuliza kwa sauti ya mkazo. Nyogoso hakujibu, alibaki kuwashangaa huku akiwa ameushika vema mfuko wake wenye mazagazaga.

"Hatutaki utuharibie sifa za kijiji chetu, sasa ngoja tukupe onyo mjinga mkubwa wewe", kijana wa pili alidakia kwa kusema hivyo na punde si punde walianza kumpiga fimbo mfululizo sehemu mbali mbali za mwili wake. Alipigwa bila huruma kichaa Nyogoso, machozi yakimtiririka ingawa aliyafuta kwa kutumia shati lake kukuu iliyozagaa viraka vya kila rangi. Hatimaye alipiga magoti akiwaomba msamaha hao vijana, ila katu haukuweza kueleweka. Alipigwa sana wakati huo huo wanakijiji baadhi walikusanyika kwenye tukio. "Kafanya nini huyu mtu mpaka mumuadhibu kiasi hiki?.", mmoja kati ya wanakijiji waliokuwa wakishuhudia tukio hilo aliuliza.

"Huu wendawazimu wake unampeleka pabaya sana huyu mtu, si alitaka kuwabaka mama Saulo, mama Sarai na mama Peto?. Sasa hiki tunacho kifanya ni kumpa onyo ili ajue kabisa alichotaka kukifanya sio sahihi", alijibu kijana mmoja kati ya wale sita waliokuwa wakimpiga Nyogoso.

"Yani mpaka mke wangu? Basi ngoja tumuadabishe mwanahidhaya mkubwa huyu", aliunga mkono mtu huyo aliyehitaji kufahamu kisa hasa kinachompelekea Nyogoso kupigwa. Alikata fimbo kubwa zaidi, akiwa na wingi wa hasira alimpiga Nyogoso fimbo ya kichwani ambayo ilimpelekea kuanguka chini kisha pumzi ikakata. Taharuki inazuka mahali hapo, kila aliyekua mahali hapo alikimbia kupitia nyia yake. Walijua wamemuuwa Nyogoso. Yule mtu aliyempiga fimbo kichwani, aliogopa sana kwani tayari mzigo wa walama alitwishwa yeye. Aliitwa Kilemoni. Akiwa na wingi wa hofu alifika nyumbani kwake, akachukua akiba ya fedha aliyokua nayo ndani kisha akakimbia sehemu isyojulikana huku akiwa ameacha mke na mtoto mmoja. Si yeye tu bali kila aliyehusika kumpiga Nyogoso alikimbia kijiji hicho kukwepa zahma ya kukutwa na hatia ya mawaji.

Masaa yalizidi kutaladadi Nyogoso akiwa bado amepoteza fahamu, lakini ilipotimu mnamo saa moja usiku alizinduka. Alijaribu kujinyanyua ila alishindwa sababu wakati huo mwili wake haukua na nguvu ya kuweza kujinyanyua, hivyo alilala hapo hapo mpaka pale nguvu ilipomrejea ambapo tayari ilikua yapata saa sita usiku. Alinyanyuka pole pole huku akilalama maumivu, hatimaye alisimama kidete akachukua mfuko wake wa mazagazaga akazipiga hatua kuelekea makaburini ambako huko ndipo yalipokua malazi yake. Alipofika alikaa kwenye kaburi lililojengewa wigo, machozi yalimtoka huku akiangaza macho yake kutazama kulia na kushoto mbele na nyuma. Pumzi ndefu alishusha kisha akasema "Ukowapi mama yangu? Hivi huko uliko unaona jinsi mwanao ninavyonyanyaswa bila kosa? Napasa sauti hii nadhani utakua unanisikia tu kwa sababu laiti ningejua mahali ilipo nyumba yako, ningeti pembezoni mwako ili nidondoshe machozi haya mbele yako",kwa uchungu huku akitokwa na machozi, kichaa Nyogoso alinena maneno hayo peke yake kwenye makaburi ya kijiji cha Mwasanda mkoani Simiyu wilayani Bariadi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Kesho yake asubuhi kichaa Nyogoso alikurupuka kutoka usingizini, alijinyoosha viungo vya mwili wake kisha akachukua furushi lake akazipiga hatua kuondoka hapo makaburini. Lakini kabla hajafika mbali, aligeuka nyuma alisimama akatazama eneo lote la makaburi halafu akasema "Siku zote akufukuzae hakwambii toka. Mama kwaheri mwanao naondoka ili kulinda uhai wangu, roho inaniuma kukuacha peke yako ila sina budi kuchukua hatua hii. Ubaki salama", Nyogoso alipokwisha kusema maneno hayo aliondoka huku akiwa ameinamisha uso chini, mzigo wenye mazagazaga begani chozo nalo likimtiririka. Aliona haina haja ya kuendelea kuishi kijijini hapo. Akiwa njiani aliokota pingili za miwa na kisha kuzila akipoza njaa. Safari sio kifo, Nyogoso akafika Bariadi. Hapo akaweka makazi ambayo nayo hayakua ya kudumu,kwa sababu alipigwa vikali akawa anaishia bila amini. Ndipo jioni moja alidadia Lori la mizigo pasipo wahusika kujua, hatimaye akafika Kahama. Ni jambo ambalo lilimfurahisha mno kichaa Nyogoso, kwa sababu aliishi kwa amani pasipo kubuguziwa na wala yeye pasipo kumbuguzi mtu. Aliweza kujizolea umaarufu kwa muda mchache sana tangu afike mjini Kahama,kichaa mstarabu ndilo jina aliokua akitambulika. Hakua mkorofi wala mwizi, na cha ajabu zaidi aliwapenda watoto na mara kadhaa alionekana akicheza nao. Lakini siku moja wakati yupo mtaani akitembea, alifika stendi ya mabasi yaendayo mikoa mbali mbali. Kigoma, Dar es salaam Mbeya Mwanza na mikoa minginayo. Ghafla macho yake yakagonga kwenye basi ambalo aliwahi kulipanda miaka kadhaa nyuma, basi liendalo Dar es salaam. Aliachia tabasamu baada kuliona basi hilo, punde akalisogolea akaendelea kulitazama huku akilizunguka,alicheka aliimba na kucheza huku akionekana kituko kwa wakazi wa hapo stendi. Mwishowe akashusha pumzi kisha akaenda kuketi kando ya nyumba wanayolala abiria. Alfajiri palipo pambazuka, honi ya basi hilo ililia ishara ya kuwaamsha abiria ili safari ianze. Kichaa Nyogoso alistuka akachukua furushi lake lenye mazagazaga akaingia ndani ya gari.

"Unakwenda wapi? Hebu shuka haraka sana kabla sijakuvuruga", aliweka mkazo konda wa basi hilo. Lakini kichaa Nyogoso katu hakuweza kuogopa, aling'ang'ana kuingia ndani kitendo ambacho kilizua mzozo mkubwa baina yake na kondakta. Konda alimtaka Nyogoso ashuke ilihali Nyogoso naye akigoma huku kwa mbali taswira ya Mazoea ikimjia akili mwake jambo ambalo lilimfanya kichaa Nyogoso kuzidi kuweka kizungumkuti, patashika nguo kuchanika ikawa imepamba moto. Lakini wakati zogo hilo liliendelea, ilisikika sauti ya mzee mmoja wa makamo akisema "Muache usimfukuze, huyu ni kichaa mstarabu. Nitamlipia nauli mpaka mwisho wa safari yake"





Kondakta alipopewa nauli ya Nyogoso alitulia ingawa alionekana kukasirika, ilihali muda huo kichaa Nyogoso naye alionyesha utulivu wa hali ya juu. Lakini utulivu huo haukua wa kudumu, punde alipasa sahati akasema "Dunia hii inawatu wenye roho mbaya sana, na ndio maana heri kuishi na wanayama kuliko kuishi na wadamu. Unataka kunishusha kwenye gari lako eti kisa mimi kichaa? Hahaha hah hahahahah. Sasa basi kama Mungu ananisikia naomba gari hili lipinduke, tufe ili kila mmoja avune alichopanda" alisema Nyogoso. Maneno hayo yaliwashangaza abaria waliokuwemo ndani ya basi hilo. Minong'ono ilisikika huku baadhi ya abaria wakimkodolea macho kichaa huyo. Muda mfupi sauti ya kike ilisikika ikisema "Dereva simamisha gari huyu mwendawazimu ashuke,simama Dereva", alisisitaza binti huyo. Lakini Dereva hakuweza kufanya hivyo, gari tayari ilikua imekolea mwendo. Kitendo hicho cha Dereva kukaidi maneno ya yule binti kilipelekea kuzuka wingi wa abaria kuendelea kushinikiza Nyogoso ashushwe ila kichaa Nyogoso alikatataa katu katu.

"Nani ashuke? Naongea ukweli kutoka moyoni. Na kama wewe unakwepa kifo basi huna imani na yale uyafanyayo ya kumpendeza meenyezi Mungu", alisema Nyogoso huku akimtazama binti yule aliyesikika akimuamuru Dereva asimamishe gari.

"Kaa kimya kichaa usijielewa wewe mwanahidhaya mkubwa", kwa hasira binti yule aliongea. Hakuisha hapo tu, bali aliendelea kumwagia Nyogoso maneno machafu kedekede kiasi kwamba gari nzima alisikika yeye peke yake. Nyogoso alimtazama binti yule kisha akacheka. Alipohitimisha kicheko chake akasema "Unaonakana mzuri wa sura mbaya wa roho, siku zote mwanaume kubishana na mwanamke ni kumkosea Muumba aliyetutunuku kuwaamiliki. Sina cha kuongea na wewe ila nataka nikupe onyo ili hata siku nyingine uwe na adabu. Binti. Unaongea kwa nyodo huku sauti yako ukiwa umeibana vema lakini tambua kuwa mke wa raisi wa nchi ya Marekani anapewa mahitaji yote ayatakayo, ila hajawahi kumdharau wala kumkashifu mtu aliyemzidi kipato au asiyekua nacho. Lakini wewe unayevaa wigi moja wiki nzima, wigi chafu kama nywere zangu unalinga sana na kuiona tayari umemaliza. Acha ujinga pumbafu kuwa na heshima ".

" Wewe unanitukana mimi?.. ", binti yule alikasirika kusikia maneno hayo aliyoyasema kichaa Nyogoso, punde alinyanyuka kutoka kwenye siti kwa dhumuni la kutaka kumpiga kichaa huyo. Alizuiwa wakati huo akitulizwa hasira alizokua nazo. Lakini mbali na kutulia ila aliendelea kumtupia Nyogoso maneno machafu wakati huo huo baadhi ya abiria wakijiuliza maswali mengi kuhusu kichaa huyo.

"Mmmh huyu kweli kichaa au anaigiza?..", moja ya abiria alijiuliza wala asiishi hamu kumtazama Nyogoso.

Baada hayo kupita, kimya kilitawala ndani basi hilo. Binti yule aliyekua akimtolea Nyogoso maneno machafu alikaa kimya huku akipandisha kwikwi shauri ya kaungua kilio, maneno ya kichaa huyo yalimuumiza sana. Akajikuta akililia moyoni huku machozi yakimbubujika katika mboni zake. Muda wote alijiinamia kwenye siti, na mara kadhaa aliona haibu pindi abiria wenzake walipokua wakimuangalia. Lakini baadaye kimya hicho kilipotea baada kichaa Nyogoso kuimba akilitaja jina la marehemu mama yake,abiria walitaharuki, wengine wakiona kero anayoifanya kichaa Nyogoso ila bahati nzuri muda huo basi lilifika Dodoma, ilikua yapata saa kumi na mbili jioni. Hapo gari ilipumzika kabla kesho safari haijaendelaea kuelekea jiji Dar es salaam. Abaria yule aliyejitolea kumlipia kichaa Nyogoso nauli, vile vile hakusita kumnunulia chakula. Alipokwisha kufanya hivyo alimuaga huku akimtakia safari njema. Mtu yule alisema.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"Kichaa mstarabu, mimi safari yangu imekomea hapa. Bila shaka wewe safari yako bado inaendelea. Nakusihi uwe na moyo huo huo, usiwe mkorofi utapendwa na kila mtu".

"Ahsante sana ndugu, Mungu akubariki. Huu ndio maana ya uanaume, amini kwamba laiti ulimwenguni pasingelikua na hawa viumbe dhaifu basi wanaume wote tungeingia peponi", alijibu Nyogoso.

"Unamaana gani sasa?..", aliuliza mtu yule.

"Maana yangu ni nyepesi sana kuielewa. Ndugu yangu mwanamke ndio kiumbe pekee aliyeonana na shetani. Ndio maana nawaaamini sana wale walio sema wanawake ni mashetani wa pili, kwa sababu hutujui mbali na shetani kumshawishi Eva kula tunda, hatujui ni maneno gani mengine waliyokubaliana. Ila tu, ninacho kusihi, ishi nao vizuri kwa sababu kuishi nao inahitaji maarifa kuliko kitu chochote ulimwenguni ", alisema kichaa Nyogoso kisha akaangua kicheko. Wote kwa pamoja wakacheka na punde si punde mtu yule aliyemlipia nauli Nyogoso aliondoka zake huku akitikisa kichwa ishara ya kukataa jambo fulani.

Kesho yake asubuhi safari iliendelea, jioni ya saa kumi na moja basi lilifika jijini Dar es salaam. Abiria wote walishuka ndani ya basi hilo akiwemo na kichaa Nyogoso ambaye alionekana kubeba begani mzigo wake wenye mazagazaga. Furaha isiyo kifani ilitawala ndani ya moyo wake alipoliona jiji kwa mara nyingine tena, kwa mbali ndani ya fikra zake picha ya sura ya Mazoea ilimrudia. Jambo ambalo lilimpelekea kuimba na kucheza, akiwa kituo kituko stendi ya ubungo. Wakati anacheza na kuimba, mbele ya macho yake chini aliona kitumbua. Haraka sana alikiokota akakifuta vumbi kwenye flana yake chakavu kisha akakila iilihali muda huo huo alizipiga hatua kutoka stendi na kuelekea mahali asipo pajua huku begani ukining'inia mzigo wake wenye mazagazaga.

Maisha ya kichaa Nyogoso ndani ya jiji la Dar es salaam yalikua ya kutangatanga huku na kule, alilala majalalani na kula makombo yaliyotupwa. Lakini wakati maisha hayo yakiendelea kuwa tegemezi kwa kichaa huyo, upande wa pili Suzani naye alizidi kukosa furaha moyoni mwake. Akili yake ilizidi kumfikiria kijana mzoa takataka. Mwishowe binti huyo aliamua kutembea majalala mbali mbali akidhania kuwa atafanikiwa kumuona huko ila kila siku aliambulia patupu. Hakumuona mzoa takataka Nyogoso ambaye tayari ni mwendawazimu. Suzani alilia sana, siku zote hakuijua furaha. Maisha yake yalikua ya huzuni wakati wote. Na roho ilizidi kumuuma kila alipoiona pochi yake aliyomuokotea Nyogoso pindi alipoidondosha bila kujua. Lakini Nyogoso alipohitaji kumkabidhi, Suzani alijikuta akimtolea maneno machafu ya dharau na kebehi pasipo kujua dhumuni la Nyogoso aliyekua mzoa takataka. Pochi lilikua na vitu vya thamani sana, ila Nyogoso hakupunguza kitu hata kimoja. Na alipomkabidhi hakungoja shukrani kwani maneno aliyoambiwa yalimtosha. Jambo hilo ndilo lililoendelea kumtesa Suzani mbali kumtaka kimapenzi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Suzani alisafa, ilihali upande wa pili ndani ya hospital ya Muhimbili alionekana mama Mazoea akiwa na wingi wa tabasamu. Uso wake ulionyesha kuna jambo limemfurahisha.

"Dokta! Kweli amefumbua macho?...",aliuliza mama Mazoea.

"Ndio, ila jitihada bado zinaendelea", Doktari alijibu. Jibu hilo bado mama Mazoea hakutaka kuliamini, kwa sauti ya mshangao huku machozi yakimtoka alisema "Ina..ina.. Inamaana yupo hai?.."





Alikua na furaha isyokifani, muda wote mapigo ya moyo wake yalienda mbio. Machozi ya furaha nayo hayakua mbali na mboni zake, yalimtoka huku akiinua macho na mikono yake juu akimshukuru mwenyezi Mungu kwa kufanikisha jambo hilo la miujiza. Habari hiyo njema aliwaambia kila ndugu jamaa na marafiki pia, nao hakuamini kwani wengi wao walikua wameshakata tamaa na kujua kuwa Mazoea amefariki. Na hata taarifa ambayo ilisambaa kwa kasi zaidi, ilieleza kwamba Mazoea amefariki. Lakini siku hiyo wanapokea jumbe fupi kwenye simu zao, zikieleza kuwa Mazoea kafumbua macho.

Wakati hayo yakijili upande wa familia yakina Mazoea, upande wa pili kichaa Nyogoso alionekana kuyafurahia maisha ya jijini Dar es salaam. Makazi yake ni jalalani huku chakula alichotegemea ni makombo yanayotupwa na mama ntilie, ni chakula ambacho hakikuweza kumletea madhara yoyote. Hakuwahi kutokea siku ambayo aliumwa ugonjwa wa mlipuko, Mungu alimsaidia kulingana na maisha harisi aliyonayo kijana huyo. Siku zilisonga, hayo yakiwa ndio maisha ya kichaa Nyogoso. Siku moja asubuhi mapema, jiji la Dar es salaam liligubikwa na mawingu mazito angani. Punde si punde manyunyu ya mvua yakaimwagilia vilivyo jiji hilo wakati huo huo kichaa Nyogoso alikua bado amelala kando ya jalala maeneo ya Kinondoni. Ghafla alistuka kutoka usingizini, manyunyu ya mvua yaliukatisha usingizini wake na hapo ndipo aliposimama akainyoosha huku akipiga mwayo. Alipomaliza zoezi hilo akazipiga hatua kuingia jalalani kutafuta kiporo kilicho tupwa asubuhi hiyo, kwa sababu tayari tumbo lake lilihisi njaa. Lakini hakubahatika kupata, licha ya kutafuta kwa umakini wa hali ya juu.

"Loh! Yani viporo vyote vimeliwa na panya au ndio kusema watu jana hawajala?. Hii sio kawaida bwana", alijisemea kichaa Nyogoso wakati huo akitoka katika jalala hilo. Alipofika kando ya jalala, alichukua mfuko wake wenye mazagazaga kisha akaondoka zake hapo jalalani, akaingia mtaani kutafuta cha kuokota ili apoze njaa kali aliyoamka nayo asubuhi hiyo.

Alitembea huku na kule, hatimaye alifika Mwananyamala. Kwa mbali aliona mgahawa mbele yake, aliachia tabasamu huku akiamini kuwa tayari njaa yake imepata tiba. Hivyo kichaa Nyogoso aliusogelea mgahawa huo, lakini mama ntilie aliyekuoa akitoa huduma kwenye mgahawa ho alipomuona kichaa Nyogoso alisimama kidete kisha akasema "Unakuja wapi? Sitaki kukuona hapa, hebu ondoka mwanaharamu mkubwa wewe", mama ntilie huyo alimfukuza Nyogoso huku akimtupia maneno makali. Haraka sana kichaa Nyogoso aliondoka zake mahali hapo, hatua mbili mbele alistuka baada kumwagiwa maji machafu. Aligeuka kutazama nyuma, akamuona mama ntilie yule aliyemtimua ndio aliyemwagia maji hayo machafu.

"Kosa langu nini mpaka animwagie maji machafu?",alijiuliza kichaa Nyogoso wakati huo akimtazama yule mama ntilie kwa machozi ya huzuni, alisikitika sana chozi lilimtoka kisha akaendelea na safari yake na hata asiseme neno lolote na mama ntilie yule mwenye gubu.

Kipindi hayo yanajili kwa kichaa Nyogoso, kwingeneko hali ya Mazoea iliendela kuimalika. Jitihada za utalamu wa jopo la madaktari zilipelekea kuokoa uhai wa binti huyo ambaye awali ilisemekana kuwa amefariki baada kunywa sumu siku ile ambayo alipata habari kuwa mpenzi wake Nyogoso mzoa takataka amehukumiwa miaka sita jela.

Roho ilimuuma sana, aliamini kwamba yeye ndio chanzo cha Nyogoso kufungwa jela. Lakini sio shauri yake bali ni moyo wake ambao ulivutiwa naye pasipo kujali maisha aliyokuwa nayo kijana huyo. Alitamani amuombe msamaha, ila nafasi hiyo alikosa kwa sababu wazazi wake walimzibiti vilivyo kuhakikisha Mazoea hapati hata wasaa wa kusema naye huku wakitumia nguvu ya pesa kumfunga Nyogoso jambo ambalo Mazoea aliona heri kujiua akiamini kwamba atapata kupona maumivu makali anayo yahisi moyoni mwake. Hapo ndipo alipoamua kunywa sumu.

Mama Mazoea alifurahi sana kumuona binti yake hali yake imezidi kuimalika,alishangilia sana. Na hapo ndipo yeye pamoja na mumewe walipoamua kukubaliana kumuacha binti yao afanye kile anacho kiona kinamfaa,ingawa baba Mazoea kwa alionekana kutokubalina na suala hilo kwa asilimia zote ila alikubali tu kumlidhisha mkewe.

"Lakini mke wangu, kwa hali hii unafikiri Mazoea atasoma kweli?..", aliuliza Mr Dominic. Baba Mazoea.

"Mume wangu, tayari binti yako ameshayajua mapenzi. Tukiendelea kumzuia mwishowe siku moja tutamkuta kajinyonga", alijibu mama Mazoea kwa sauti ya upole iliyojaa huzuni ndani yake. Mr Dominic alikaa kimya kidogo, mkono shavuni. Baadaye alivunja kimya hicho kisha akasema "Hakika huu ni msiba"

"Kabisa mume wangu, wala hujakosea", aliuunga mkono mama Mazoea. Alifadhaika sana moyoni mwake kwa sababu alijua binti yake anaharibikiwa. Alitamani Mazoea aweke akili yake kwenye masomo na sio mapenzi kama afanyavyo. Aliwaza sana mwishowe alishusha pumzi ndefu kisha akasema "Eeh Mungu wangu unakusudi gani kwa mwanangu? Mbona kabadirika kiasi hiki?..", maneno hayo alijisemea huku uso wake akiwa ameuinua juu, punde alishusha akamtazama binti yake kitandani. Wakawa wamekutana uso kwa uso, muda huo machozi yakimtiririka Mazoea kwenye pembe za macho yake. Kwa sauti ya chini iliyojaa huzuni ndani yake alisema "Mama nomba nisaidie"

"Nikisaidie nini mwanangu?",mama Mazoea alimuuliza binti yake.

"Kama upo tayari mama, nisaidie. Mtoe gerezani yule mkaka mzoa takataka,kwa sababu nampenda sana naombeni mnielewe tafadhal", kilio kilifuata baada Mazoea kuongea maneno hayo yaliyojaa simanzi ndani yake. Hakika mama Mazoea naye chozi lilimtoka hasa akimuangalia binti yake. "Mazoea. Wewe ndio mwanangu pekee ninaye kutegemea,kwahiyo sitarajii kuipoteza furaha yako. Hebu nyamanza, mama yako nipo hapa. Subir ukiruhusiwa kutoka hapa hospital, nakuahidi nitamleta mpenzi wako", alijiapiza mama Mazoea. Maneno hayo yalimfanya Mazoea kuachia tabasamu pana lililochanganywa na wingi wa machozi. Alishusha pumzi ndefu halafu akasema "Nitashkuru sana mama yangu"

*********

Wiki mbili baadaye, hatimaye Mazoea aliruhusiwa kurudi nyumbani. Hali yake sasa ilionekana thabiti ingawa aliapewa dawa za kuendelea kunywa akiwa nyumbani ili kumaliza dozi. Lakini pia mbali na hilo, daktari aliwasihi mama na baba yake Mazoea kutomkasirisha binti huyo kwa sababu Mazoea tayari kisaiklojia hayupo sawa, penzi la mzoa takataka ambalo lilikumbwa na misukosuko ya hapa na pale lilimpelekea kukumbwa na hali hiyo. Wazee hao Mr Dominic na mkewe walikubali ushauri wa daktari. Walipofika nyumbani, Mazoea aliendelea kumkumbusha mama yake juu ya suala la kumtoa Nyogoso gerezani. Mama Mazoea aliona haina haja ya kupoteza wakati. Siku moja alimpigia simu Afande Daniel kwani ndio mtu wake wa karibu, nia na madhumuni ni kutaka washirikiane kwa vyovyote vile kumtoa Nyogoso jela. Ni muda mrefu sana tangu Nyogoso atoke jela kwa msamaha wa raisi, hivyo ilimuwea vigumu Afande Daniel kuweza kumkumbuka kwa haraka mtu huyo aliyemuulizia mama Mazoea. Hapo ndipo mama Mazoea alipoanza kumkumbusha baadhi ya matukio aliyowahi kushirikiana naye kipindi cha nyuma. Daniel aliangua kicheko sana baada kumkumbuka, alipokatisha kicheko chake akasema "Anhaa yule kijana? Doh! Mbona zamani sana ameshatoka jela? Msamaha wa raisi naye ulimkumba bwana"http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"Unasemaje? Mungu wangu. Nitamwambia nini sasa Mazoea?..", alitaharuki mama Mazoea,ghafla kijasho chembamba kikimtoka. Alijihisi kujiona mdogo sana mithili ya ya sisimizi.

Na wakati mama Mazoea alipokua kwenye hali hiyo ya sintofahamu, upande mwingine alionekana Suzani. Ilikua jioni eneo la sokoni akinunua mahitaji mbali mbali. Punde alijikuta akistuka kumuona Nyogoso. Akajiuliza ndani ya nafsi yake "Yule sindio mkaka mzoa takataka aliyeniokotea pochi yangu au nimemfananisha", macho ya Suzani yalimkodolea kichaa Nyogoso huku taharuki nzito nayo ilitamalaki moyoni mwake wakati huo huo akizipiga hatua kumfuata huku akijsemea "Mungu kajibu maombi yangu, hatimaye ile ndoto ya kukutana na huyu mkaka inakwenda kutimia. Sijui kama atakua bado ananikumbuka. Lakini nitamkumbusha tu na atanikumbuka. Akinikumbuka tu basi kila kitu kitakua kimekwisha,nitamuomba msamaha vile vile nitamwambia ukweli wa hisia zangu juu yake, hakika nitambadirisha atakua kidume mzuri wa kuvutia machoni mwa watu",alimaliza kwa tabasamu bashasha mrembo Suzani wakati huo akiendelea kumfuata Nyogoso ambaye naye alionekana akitembea pole pole akirudi maskani kwake jalalani...





ITAENDELEA 

0 comments:

Post a Comment

Blog