Search This Blog

Tuesday 1 November 2022

ZEE LA NYWILA - 4

 






Simulizi : Zee La Nywila
Sehemu Ya Nne (4)




HAKUAMINI uwezo wa macho yake baada ya kugeuka na kumuoana aliyemuita.

"Wewe?" Abuu alimuuliza kwa mshtuko."Hapana..." alishusha pumzi, tabasamu la mbali likinawiri usoni mwake.

"Sikia, nahitaji tuondoke haraka eneo hili. Ni hatari!" yule mwanaume aliamuru, macho yake hayakuwa yanatulia. Kila alipotamka neno, aligeuka kulia na kushoto.

"Twende wapi?" Abuu aliuliza. "Kwanini ni hatari?"

"Hatuna muda huo! Utaenda au?"

"Kuna mtu namsubiri, yuko juu huko?"

"Huyo mtu ni muhimu zaidi ya kujua mama yako alipo?"

Abuu alikosa jibu.



Alitazama huku na kule kwa usalama. Kisha wakaongozana. Waliondoka!

Abuu alimuacha Zainab.

Sasa, kama lengo la kuwa na msichana yule ni Kumpata G.C.I, na G.C.I ndiye huyu yuko mbele yake...amsubiri wa nini tena?



Walipiga hatua za haraka. Hakuna aliyemuongelesha mwenziwe kwa muda ule. Kila mmoja alipambana na utanuaji wa miguu yake ili kuondoka eneo lile. Kama jinsi jamaa alivyodai, ni hatari.



Walivuka barabara, wakasimama kituoni, kituo cha fire. Hapo, walipanda gari ya K/KOO - MABIBO. Ndani ya daladala, hawakuweza kukaa pamoja. Abuu alikosa siti, akasimama. Na mwenzake akapata ya nyuma kabisa. Hivyo hawakuzungumza.



Walipofika kituo cha Magomeni-Usalama, walishuka, wakarudi nyuma kidogo, hapo wakazitafuta gari za Kawe au Makumbusho, zinazotokea Mbagala au maeneo ya Temeke... Ilipatikana ya Kawe. Wakapanda!



Tofauti na awali, katika daladala hii walipata siti ya pamoja.

Abuu alikaa karibu ya dirisha na G.C.I pembeni yake, shimalini mwake.

"Tunaenda kwa mama sio?" Baada ya kuketi tu, Abuu aliuliza...alijawa matumaini makubwa mno moyoni.

"Hapana," alijibu yule jamaa, huku anamtanza Abuu usoni. Kisha akaendelea, "Pole sana kwa yaliyokukuta!"

"Ulipata taarifa kumbe...?" Abuu aliuliza.

"Ndiyo, kabla hayajakukuta!"

"Kabla hayajanikuta!...unamaanisha nini?"

"Mimi ndiye niliyekusababishia," yule jamaa alijibu kwa kituo. Akamtazama tena Abuu usoni.

Ubaridi wa ghafla ulimtembele Abuu damuni. "Sikuelewi bosi, una maana gani?"

"Mimi sio bosi wako. Naomba nisamehe!"

"Wewe sio bosi wangu? Unaomba nikusamehe? Umenifanyia kosa gani kwani?" Abuu alikuwa hamuelewi mtu huyu.

"Yote unayofahamu kuhusu mimi, ni uongo!"



Wakati huo konda alishafika na kudai nauli, Yule jamaa alitoa na kumlipia Abuu pia. Alitoa elfu moja, akarejeshewa mia mbili, aliipokea na kuiweka mfukoni.

Wakati kitendo hiko kinaendelea, mawazo ya Abuu yalihama...yakarudi katika kumbukumbu za siku nyingi zilizopita...



...



Ilikuwa ndani ya ndege. Mtu huyu aliye kushotoni mwake, ndiye aliyekuwa naye siku ile...



"...Harrison na Patrick ni wahalifu. Wewe pia unakwenda kujifunza uhuni. Ili uje kuwasaidia katika kamari," Mwanaume yule alizungumza huku anatazama chini, kitabuni.

"Kamari...!?" Abuu aligatuka.

"Ndiyo. Kamari ya picha za uchi. Mbona unashangaa? Unaigiza hulewi."

"Hapana, hawajaniambia hilo mimi."

"Lakini si unafahamu kuwa ukirudi utatakiwa ufanye kazi ya ngono?"

Abuu alikosa jibu akakaa kimya, kuashiria lililozunguzwa hapo ni sadiki.

Yule jamaa aliendelea,"Sawa, siko hapa kueleza ukubwa wa uovu uliokusudia kwenda kuufanya, ninachotaka kukwambia ni..."

Kabla hajamaliza, Abuu alidakia, " Lakini kiongozi, sijakusudia...ni umasikini tu kaka."

"Umasikini? Unajua Tanzania kuna masikini wangapi?"

Kimyaa! Abuu alikosa jibu.

"...kwahiyo hao wote wakawe majambazi?" yule jamaa aliuliza.



Pamoja na kiyoyozi kilichoko mule ndani ya ndege, bado kijasho cha kwapa hakikuacha kuanza kumkamata Abuu.

"Lakini mimi sio jambazi m'heshimiwa" Abuu alijaribu kujitetea.

"Sawa. Kushiriki kamari haramu, ni uhalifu sio uhalifu?" Jamaa alimpachika swali jingine.

"Uhalifu," Abuu alijibu kiupole.

"Na ujambazi je?"

Abuu alijikuta kanasa tena. Hakujibu kitu.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Yule jamaa akainamisha macho kitabuni mwake tena. Aliendelea kukisoma bila kumtazama Abuu, aliyekuwa amekwisha kuchanganyikiwa. Alishavurugwa tayari.



"Kwahiyo wewe ni askari?" Abuu aliuliza ili apate uhakika.

Sekunde mbili zilipita bila ya jamaa kumjibu, kisha akaongea, "Kuna kitu utahitaji ili nikuthibitishie?"

"Ndiyo," alijibu Abuu kwa wasiwasi.

"Nakusikiliza..." Jamaa aliongea kwa kujiamini.

"Kitambulisho."

Yule jamaa alitoa kitabulisho. Kilionesha cheo chake na jina lake kamili. Pamoja na kitengo cha kiusalama anachofanyia kazi.

Hapo sasa Abuu aliona tayari amekwisha. Kinachoenda kujiri baada, ni maisha ya kusabahiana na manyapara gerezani.



"Sina nia mbaya na wewe Abuu..." Yule jamaa aliongea huku anarejesha kitambulisho kile katika mfuko wa koti jeusi la suti aliyovaa. Abuu hakuongea kitu ila alimgeukia kuonesha anamsikiliza."...Nataka tufanye kazi pamoja, ushirikiane na serikali."

"Kivipi?" Bado Abuu hakumwelewa.

"Unatakiwa ututaarifu kwa kila hatua, kila utakachotumwa."

"Vipi kuhusu usalama wangu?" Abuu alizidi kuhoji, " Wakigundua nawazunguka je?"

"Nikwambie kitu, Katika upelelezi, Imani yako ndiyo angamio lako."

"Sijakuelewa bado."

"Namaanisha, Usimwamini mtu!" Yule mwanaume alizungumza, kisha akasimama kuelekea upande vilipo vyoo.



Abuu alisubiri arejee tena, alikuwa na mengi ya kumuuliza mtu huyu.

Zaidi, mishale ya saa iliendelea kusogea bila ya jamaa yule kurudi.

Aliacha kitabu katika siti. Kitabu kile alichokuwa anakisoma muda wote.



Jalada la kitabu hiki, lilimvutia mno... UKURASA WA 56. Ndivyo kilivyosomeka. Akatazama jina la mwandishi, ni Frank Masai. Moyo ulimlipuka kwa shauku.

Jina la mwandishi huyu si geni kabisa kwake, ni mtu anayemhusudu mno kwa kazi azitoazo. Kwa kuibiaibia, ili asije akakutwa na yule jamaa, Alikifungua kitabu kile.

Mara, alikuta maandishi kwa ndani... Ni dhahiri hayakuwa ya kitabu hiki.

Hapana, si maandishi, zilikuwa ni namba za mawasiliano.



Tangu hapo, hakumtia tena machoni mwake mtu huyu, mpaka ilipofikia leo.

Ingawa, waliwasiliana mara kwa mara mtandaoni.



Hapo hapo, mawazo yake yalifutwa tena kwa sauti...



"Manyanya..." Konda alitangaza kituo.

"Shushaa!" alijibu yule jamaa, akamgeukia Abuu kumuashiria tayari wamekurubia pa kushukia.



Walivyofika, walisogea mbeke kidogo, sehemu palipo na alama ya pundamilia, wakavuka. Bado, macho ya yule jamaa hayakutulia, yalitazama kwa woga huku na kule, kuhofia aidha kuonwa au kufwatiliwa na mtu.

Kitendo hiki, kilizidi kumtia mashaka Abuu, akaona hataa, 'nimechoka kufanywa zwazwa sasa'...

"Hebu sikia, mimi sikuelewi... Unanitia mawazoni ujue ndugu, mara wewe polisi, mara sijui nani, leo tu, nimekuta namba yako kwenye simu ya Zainab. Sielewi imefikaje. Nataka nimtumie Zainab ili nikupate wewe... Wewe unisaidie kumpata mama. Unatokea, unanichukua na kunizungusha kama fala tu huku. Mbona mnanifanya toi kiasi hiki? Kuna nini kinaendelea hapa kati jamani?" Abuu alilalama kwa kufoka.

"Tulia Abuu, tunafika nyumbani sasa hivi, nitakueleza yote. Tukiendelea kuzubaa hapa, tutakamatwa. Ujue tunawindwa!"

"Tunawindwaa...?" Abuu aliuliza kwa mshangao.



____http://deusdeditmahunda.blogspot.com/





"HUJANIELEWA Abuu, nimesema tunawindwa!"

"Ndiyo, na nani?"

"Nd'o maana nakwambia twende nyumbani," yule jamaa aliongea huku bado anaangaza-angaza macho yake kila upande." Trust me Abuu!"

"How can I trust you kizembe?" Abuu alijibu kwa hasira, aliendelea kupayuka, "Umesahau ulichowahi kuniambia? Kuwa imani yangu ndiyo angamio langu?"

"Okay, I know," Yule jamaa aliongea huku akijaribu kushusha sauti yake, ili Abuu naye ashuke. "Najua kuwa sina namna ya kukushawishi, ila jaribu kuusikiliza moyo wako Abuu. Harrison na Patrick wakijua bado uko hai, watakumaliza tu."

Hapo Abuu hakujibu kitu. Ubongo wake pia ulisadikisha yale yaliyotamkwa. Majanga yaliyopelekea akachungulia shimo la kaburi lake, yangeweza kurejea tena na kumsukuma atumbukie.



Abuu alinyanyua nyayo zake na kuendelea kuongezana na mwanaume yule, ambaye mpaka kwa dakika hiyo hakuweza kumuelewa ni mtu wa aina gani na ana nia gani kwake.



Walikatisha njia ya nyuma, iliyokaribiana na msikiti wa Mtambani, wakalivuka soko la Manyanya, mita chache kutoka hapo, ndipo huyu mtu asiyeeleweka kwa Abuu anapoishi.



Ni mitaa ya Kinondoni hii, pilikapilika hazikuwa za kawaida.

Nyumba zilizokaribiana na kutokuwa katika mpangilio stahiki, ndizo zinaakisi uhalisia wa maisha ya watu wa eneo hili.

Si masikini, si matajiri, ni watu wenye kujikimu haja zao kwa wastani.



Ndani ya nyumba moja, ambayo imejaa vyumba vingi vilivyopangishwa, kwa ajili ya makazi ya watu.

Vyumba hivi, vilitenganishwa na korido ndefu inayoishia kwa mlango wa mbele na mlango wa nyuma. Humo, ndimo Abuu alikuwemo na jamaa huyu.



Kitanda cha futi chache, stuli moja, meza ndogo kabisa na kijikabati chakavu kilikojaa vitabu vya kila aina ambavyo havijapangwa vizuri, viliwazunguka watu hawa, Abuu na yule jamaa, huku wao wakiwa katika maongezi...



"Enhee, nataka unieleze, maana unanichanganya yani," Abuu aliongea, huku anarejesha glasi ya maji aliyokuwa anakunywa chini. Mwendo mrefu wa juani haukuwa wa kitoto!

"Labda nianze kwa kujitambulisha, kama hautojali," Yule jamaa aliongea naye, huku akijivuta akae juu ya kitanda na kumuashiria Abuu aketi katika ile stuli iliyokuwepo pembeni.

"Sawa," Abuu alimruhusu ajitambulishe.

"Mimi naitwa John Simon, nimezaliwa hapahapa Kinondoni na nimekulia hapahapa. Ingawa ni kwa ule upande mwingine, Mwananyamala." Yule mwanaume alianza kujieleza.

Wakati huo, Abuu alibaki anamsikiliza.

Jamaa akameza funda jepesi la mate, kisha akaendelea,"Nilisoma shule ya msingi Mwananyamala Kisiwani, Sekondani nilichaguliwa Benjamini William Mkapa. Na kabla sijaingia Kidato cha tano, ndipo majanga yalianza kuniandama."



Abuu hakumkatiza, alibadilisha pozi na kuendelea kumpa umakini kwa ayazungumzayo.

John, kama alivyojitambulisha, aliendelea, " Kiufupi maisha ya kwetu hapo awali yalikuwa mazuri mno, kabla ya Harrison kuja kuyavuruga na kubadilisha hatma yangu, daima!"



"Kivipi?" Hapo Abuu alishindwa kujiziua, aliuliza.



"Usijali Abuu, nitakueleza yote," John alijibu, akavuta bilauri ya maji na kuguguda kiasi kidogo, kisha akaendelea, "Ni hiihii Kamari yao ya picha za uchi."



Hapo Abuu alishtuka kidogo, maana naye kilichomfikisha hapo ni hikohiko kinachotajwa katika historia anayoenda kupewa. Ila hakuongea kitu.



"...Mimi ni wa pili kwetu kuzaliwa. Nikitanguliwa na dada yangu mkubwa, ambaye kwa sasa ni marehemu...na wazazi wangu pia."



"Pole sana!" Abuu aliingilia maongezi na kumpa pole.



"Ahsante, Ni miaka mitano tu iliyopita...



Nakumbuka dada yangu alichumbiwa. Taratibu za ndoa zikafanyika, zikakamilika.



Siku tatu kabla ya tukio lenyewe , yani harusi—zilitumwa picha chafu za dada kwa mchumba wake, huyo aliyekuwa kanuia kumzawiji.



Huwezi kuamini, bwana yule alikatisha nia yake, alikataa kabisa kumuoa dada. Kiufupi, alighairi.

Bora angeghairi pekee, ila alizitumia picha zile kwa wazazi.

Dada alivyopata habari, uamuzi sahihi aliouona ni kujiua.



Uchungu wa aibu iliyomkumba, ukiongeza wa kupoteza mtoto—mama alipandwa na presha, hali ikawa mbaya zaidi, naye alimfuata dada, alifariki.



Hazikupita wiki, baba yangu pia aliwafuata wapendwa wake, umauti ulimkuta.

Nilibaki mimi peke yangu..."

John aliweka kituo kidogo, aliinama chini kwa huzuni iliyomrejea tafakurini mwake.



"Dah, pole sana!" Abuu alimpoza kwa mara nyingine, huku naye hisia taratibu zikianza kumshika, hisia za majonzi. Lakini, haikuzuia kumuuliza, "Kwa hiyo aliyetuma picha hizo chafu ni Harrison?"

"Sina hakika, ila ndiye aliyempiga picha hizo."

"Ulijuaje?"

"Zainab ndiye aliniambia."

"Kwa hiyo, Zainab naye ni polisi kama wewe?"

"Hapana,"

"Sawa. Ni mpelelezi...?"

"Hapana Abuu. Mimi ni raia wa kawaida tu."

"Na Zainab?"

"Yule ni rafiki wa dada yangu kwa kitambo sana. Nipo nae katika mpango..hata pale nilipokukuta, ndiye aliyenigusia taarifa za uwepo wako mahala pale, nikamwambia asitoke nje kabla ya kuja kukufuata."

Hapo Abuu alipata jibu la swali lililokuwa linamsumbua: Zainab anamfahamu vipi G.C.I?

Ila kuna jingine, Alimuona Patrick eneo lile, je yupo pamoja na John?

Swali hili aliliweka pembeni kwanza.



Alimuuliza,"kwanini siku ile ulinidanganya sasa?"http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

John alibaki kimya.

Abuu akaendelea kuuliza mfululizo, "Na kile kitambulisho ulitoa wapi? Ulinijuaje jina? Zile taarifa ulizokuwa unachukua kwangu nazo, ulikuwa unapeleka wapi?"



John alitabasamu kidogo, kisha akajibu, "kitambulisho nilighushi. Taarifa zote nyingine ni kutokana na utaalamu wangu wa kucheza na mtandao. Niliweza kufuatilia mawasiliano yenu nyote!"

"Na taarifa zangu je? Ulikuwa unapeleka wapi?"

"Nilizihifadhi na kuwatumia."

"Kuwatumia...?! Wakina nani?"Abuu aliuliza kwa mshangao.

"Harrison na Patrick." John alijibu huku anatazama mlangoni.



Kulikuwa na mchakato wa nyayo, kisha, mlango ulianza kusukumwa...



Abuu alihisi damu yote inaanza kuwa ya baridi mwilini!



MLANGO haukuweza kufunguka, walikuwa wameufunga kwa kitasa cha ndani.

Macho Abuu yalikuwa yamemtoka pima! Aliutazama mlango na uso wa John kwa zamu. Alihisi kitu cha hatari kinaweza kutokea upande wake.



John alisimama kwa machale sana, akamgeukia Abuu. Alimuonesha ishara ya kuwa na utulivu.



"Nanii?" John aliuliza, huku mwili wake akiuweka tenge na karibu na mlango ule, lolote litakalo kuja alishughulikie.



Kimyaa! Hakuna jibu lolotolewa pale mlangoni.



"Naniii...Zainab?" John aliuliza tena kwa kuotea jina.



"Ndiyo...!" Sauti ya kike ilitokea upande wa nje.



Alikuwa Zainab. John alifungua kidogo na kuchungulia, bado Abuu alikuwa na hofu. Alihisi kuna lolote lingeweza kutokea wakati huo, mpaka pale John alipoufungua mlango zaidi, na msichana mrembo, mtoto wa kipemba, Zainab, alipoingia ndani.

Hapo sasa, alishusha pumzi zake na kumshukuru Mungu!



Zainab alipoingia tu, uso wake ulikutana na uso wa Abuu, alitabasamu kidogo...lakini Abuu aligoma kurejesha tabasamu lile.

Msichana huyu hakulijali hilo, alipita mpaka mbele ya kitanda, akakaa.

Alikaa palepale alipokuwa ameketi John, wakawa wanawajihiana moja kwa moja na Abuu.



"Vipi?" Zainab alianza kumchokoza Abuu.

Abuu hakumjibu kitu, alishamsoma kuwa msichana huyu anamfanyia mzaha tu.



"Okay, Kwa ugeni nilioupata leo..." John alisimama katikati yao na kuanza kuzungumza, "...naomba nikawanunulie vinywaji mvipendavyo, Enhee... Tuanze na Abuu hapa!"

John akaonesha ishara ya kumsikiliza Abuu.



Abuu alijibu, "Mie maji tu yamenitosha haya!"

"Ah, umeanza sasa. Hapa unamuonea aibu nani kwani?" John aliongea kiudaku huku macho anayegeuzia kwa Zainab.

Kuona vile, Zainab aliinama na kucheka kwa chinichini.

Pia Abuu alishindwa kujizuia, "Hahaha, hamna bwana." Abuu alijitetea.



"Basi sawa, najua hakuna atakayechagua kitu. Ngoja niende, nitajua mwenyewe niwaletee nini," John alitamka hivyo na kutoka, "Nani...Zai, njoo ufunge mlango," Aliagaza waufunge mlango kwa ndani, kwa usalama zaidi.



Aliitwa Zainab kufanya hivyo, ila Abuu aliinuka yeye na kwenda kuufunga.



"Hahaha, kumbe una heshima hivyo?"

Zainab alileta utani tena, huku anajichekesha kiuchokozi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Abuu hakuongea lolote, alifunga mlango, kisha akarejea mpaka katika stuli, akaketi kwa mara nyingine.



"Kumbe yote hayo ulikuwa unaniigizia?"

Maneno ya kwanza kutoa Abuu kwa Zainab, yalikuwa ni hayo.

Zainab kicheko kikamkata. "kivipi?" aliuliza.

"Hujui kivipi..!?Wewe na John mna ajenda gani?" Abuu aliuliza, sura ikionesha dhati ya kutaka kupata ukweli.

"Kwani hajakueleza muda wote mliokuwa m'mekaa hapa?" Zainab naye alijibu kwa swali.

"K'o, hukunipenda kweli?" Abuu alijibu kwa swali pia.

"Kwani wewe ulinipenda kweli?" Zainab naye akarudisha swali.

"Sasa utageuka mchezo wa maswali huu," aliongea Abuu huku uso wake ukionesha kukasirishwa na kile anachokiongea msichana huyu aliyekuwa mbele yake.

Zainab akacheka.

"Usicheke!" Abuu alimkataza, "Unaweza kuniambia mama yangu yupo wapi?" alimuuliza.

"Mama yako..."

Zainab alitaka kuongea kitu ila hakuimaliza kauli yake, kigugumizi kilimpata, akatazama pembeni kisha akaendelea, "...ngoja tumsubiri John, anaweza akawa anafahamu zaidi."

Kengele ya hatari ikagonga kichwani mwa Abuu, 'Mbona kapata wasiwasi kunijibu?' alijiuliza.



"Nafahamu hukuwahi kuniambia ukweli...basi naomba leo iwe mara ya kwanza na mwisho. Mama yangu yuko wapi?"

Abuu alihisi Zainab kuna kitu anafahamu kuhusu mamaye ila anamficha, akazidi kum'bembeleza.

"Ukweli gani? Si' nimesema sifahamu jamani?" Zainab hakuisha kujitetea.

"Okay..." Abuu alishusha pumzi ili hasira nazo zimshuke, "...nitajua tu," alimaliza kwa kusema hivyo.

" Mie nimekuja hapa, hofu yangu kubwa...nilihisi umekutana na Patrick kule nilivyokuacha," Zainab aliongea huku akifinyafinya vidole vya mikono yake katika shuka la kitanda alichokalia.

"Nd'o ilikuwa nia yako, sivyo?"

Abuu aliuliza kwa kebehi.

"Hapana."

"Ila?"

"Enh, mbona maswali yanazidi sasa?"

Zainab aliongea na kubinua mdomo...alioneshwa kachoshwa.

Abuu alikaa kimya, alikerwa na Zainab kukataa tena kumueleza suala lile. Alikasirika!



Hapana. Zainab hakupenda Abuu awe katika hali ile. Alitamani amuone Abuu wake akiwa katika furaha masaa yote. Sio masaa tu, maisha yote!

Kwa hakika, alitokea kumpenda mno Abuu, ingawa mwanzoni, ilikuwa ni sehemu ya mpango tu.

"Sawa, ngoja nikwambie..." Zainab alianza kuongea, Abuu akainua macho yake kumtazama, kuonesha anamsikiliza."Nafanya kazi ofisini kwa Patrick, kama kishikio tu. Niko pale ili nimchunguze nyendo zake."

Abuu hakujibu kitu, aliendelea kumtazama. Bado hakuwa anamuamini Zainab mpaka wakati huo.

Alimtathmini macho yake kwa dakika mbili, mikono alivyoiweka, akaangalia jinsi kichwa kinavyotikisika...ndipo alipobaini kuna ukweli katika ayatoayo mdada huyu.



Abuu ni mtaalam wa saikolojia, akikuangalia vizuri, kwa umakini kabisa...laazima atang'amua kuwa usemalo ni la kweli au laa!

Hivyo alimuamini.

Bila ya kuzingatia kwamba, Imani yake ndiyo angamio lake.

Hakujali hilo kwa wakati huo!



Zilipita dakika chache, John alirejea kutoka dukani. Aligonga mlango wakamfungulia.

Mikononi, alishika chupa za soda, zilizofuka mvuke wa ubaridi. Ubaridi ulishindwa kujizuia kutoka, ingawa zilikuwemo ndani ya mfuko mweusi wa nailoni.



"Sikia John," aliita Abuu,"Mie soda yako sijui hiyo, sinywi!... mpaka utakaponijibu maswali yangu matatu."

John aliduwaa kwa sekunde chache huku amesimama, aliziweka chupa mezani na kuketi kitandani, pembeni ya Zainab.



"Maswali yepi tena?"John aliuliza. Wote, yeye na Zainab walimuwemekea nadhari Abuu.



"Pia, sharti jingine, nataka jibu la moja kwa moja, sitaki kuzungushwa!" Abuu aliweka msisitizo.

"Sawa," John alionesha yu-tayari kumsikiliza.

"Mama yangu yupo wapi?" Abuu aliuliza

"Amekufa,"John alijibu.





ABUU alianza kuhisi nguvu zinamuisha kwa kasi isiyo ya kawaida, taratibu alilegea kutoka katika ile stuli aliyokuwa ameketi, mpaka akadondoka chini kwa magoti.

Alitamani hali ile ingekuwa ni ndoto tu. Ila ilabaki hivyohivyo, natamani. Haikuwa ndoto!

"Jikaze Abuu. Na, kwa bahati mbaya hatujamzika. Labda tungesema tukupeleke katika kaburi lake..." John aliongea huku naye akiwa ameshapiga magoti kumtuliza Abuu.

Macho ya Abuu yalilenga machozi. Ya Zainab yalijaa machozi. Zainab alikuwa analia kabisa. Si kwa uchungu wa msiba wa mama yake Abuu, hapana, yeye uchungu ulishamkumba awali. Alilia kwa kujivika hisia za Abuu. Anampenda sana Abuu. Chochote cha Abuu alikiona ni chake, na cha kwake, ni cha Abuu.

Usicheze na mapenzi wewe!



Kwake Abuu, mama ilikuwa ni kila kitu.

Mama ndiye aliyefanya yeye abadilike. Mama ndiye aliyemfanya akubali na kujiita ZEE LA NYWILA. Mama pekee, ndiye aliyemfanya akubali kutembea na kila msichana atakayepangiwa ili apate pesa. Ni mama pekee!

Leo hii hayupo, amekufa. Anataka nini sasa? Maisha yake yana umuhimu gani tena?

Abuu alijiona ana haki zote za kuwa mfu. Hafai kubaki hai katika dunia hii mpweke.

Alilia kwa kugota koo lake. Abuu, Abuu...Abuu alilia kwa kwikwi!



Kisha aliinuka kwa hasira. Hapana, sio hasira pekee...aliinuka kwa hisia kali za uchungu, akaelekea mlangoni atoke nje. Hakutaka kusalia tena mule ndani.

Anasalia ili apate nini hasa?

Mama hayupo. Apate nini?



"Abuu! Harrison na Patrick ndio waliomuua mama yako. Alipigwa sindano ya sumu mpaka umauti ulimfika," John aliongezea.

Kauli hii ilkuwa msumari uliotoka kwenye moto, kisha ukatiwa katika kidonda cha Abuu.

Alikuwa ameshakwisha kushika kitasa, alikiachia. Akapiga hatua za kujishindilia na kurejea mpaka mbele yao, John na Zainab. Hapo, akajiachia mzimamzima na kutulia magoti tena.

Sura yake ilivimba kwa ukakasi wa huzuni, machozi yalitapakaaa juu yake na kuvinjari kila kona.

Wakati huo, Zainab hakuweza kabisa kumtazama Abuu. Hakuweza! Aliinamia chini, nae analia.

John alishindwa kujua am'beleze nani: Mwenye msiba wake au mwanamke asiyeweza kuhimili hisia zake?



Haikuwa ngumu, pia haikuwa rahisi kama John alivyokuwa amefikiria. Kwamba Abuu ni mwanaume hivyo ataweza kuvumilia.

Ni kweli, Sifa ya uwanaume ni ukakamavu. Ila, kufiwa na mama kipenzi kuna ukakamavu?

Hakuna!



John alijikuta anajutia maamuzi yake, lakini angefanyaje sasa?

Waswahili walinena, heri sadiki chungu kuliko uongo, kwa mungu.

Mama alishakufa, yanini ilikuwa kumficha...ukweli ulikuwa ni haki yake.



Kilio kile kikali kilimuumiza mno Abuu, taratibu alianza kuhisi kizunguzungu, mara!, alidondoka chini mzimamzima.

Fahamu zikampotea.



_____



KUJA kufumbua macho yake tena, tayari kulishakuchwa, jua lilishatoa mkono wa kwaheri angani. Giza limechukua nafasi yake.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Kwa taabu sana, aligeuza kichwa chake...hapo, ndipo alimkuta Zainab ameketi katika stuli.

Zainab alikuwa bado anamsubiri Abuu azinduke.



"Abuu uko sawa?" Zainab aliongea na kuinuka, akamuwahi na kumkumbatia, ilihali Abuu akiwa yuko kitandani.



Kwa kiasi fulani, kiasi cha maumivu kilianza kumpungua Abuu moyoni.

Msiba hauzoeleki, ila haubebeki daima...utasahaulika tu. Tena haraka sana!



Ndiyo ilivyokuwa kwa Abuu, muda huu hakulia sana...ila hakuisha mawazo akilini mwake, alim'kumbuka sana mama yake. Mboni yake!



"Zainaa...Zainaaab,"Abuu aliita jina kwa tabu.



"Nakusikiliza love..." Zainab aliitika huku akiwa amepiga magoti pembeni ya kitanda ...mkono wake ukiwa kichwani kwa Abuu.



"Mimi nahisi ni wakati wangu," Abuu aliongea kwa kujiminya...aliongea kwa shida mno!



"Kwa nini?" Zainab aliuliza, moyoni alishtuka...ila kwa kuzingatia hali ya anayezungumza naye, hakuonesha mshtuko ule usoni.

Ndiyo hekima za kiungwana.



Swali hili la Zainab, lilirudisha kumbukumbu za Abuu siku za nyuma kidogo...



...



ULIKUWA ni ule usiku wa mwisho, ambao Abuu aliketi na yule mzee Muuguzi, kule kisiwani alikokuwa ameokotwa.



"Kijana wangu!" aliita mzee yule akimuangalia Abuu kwa umakini. Kumaanisha jambo atakalo kumwambia ni muhimu zaidi.



"Ndiyo babu," Abuu aliitika, naye umakini ule alishauelewa.



"Mjini unarejea kufanya nini?" Mzee yule alimuuliza.



"Naelekea kutafuta ndugu zangu tu," Abuu alijibu kwa kuficha dhamira yake.



"Kweli?" Mzee yule alimuuliza kwa msisitizo, "Mimi mbona naivuta harufu ya kisasi?"



"Hapana," Abuu aliendelea kudanganya,"Mimi kule sina ugomvi na yeyote babu."



"Hayaa..." Babu yule aliongea huku anashusha pumzi, akageuka pembeni kidogo, kisha akarejesha uso wake kwa Abuu. Alimtazama kwa sekunde chache, akamwambia, "Inaonesha una majeraha makubwa bado katika ubongo...jiepushe na ugomvi, unaweza ukatoneshwa. Pia, jiweke mbali na hisia kali...nazo, zinaweza kupelekea maumivu, hata ukapoteza maisha."



....

Hapohapo mawazo ya Abuu yalipea. Pumzi zilipunguza kasi yake kumuingia puani, zikawa finyu.

Moyo ulibadilisha mapigo, macho yakaanza kumtumbuka.

Zainab aliishia kupiga kelele tu.

Abuuu!

John!

Abuuuuuuu!

Joooooooooooohn!

Hakuelewa amuite nani.

Miguu ya Abuu ikaanza kutikisa kitanda, ishara ya roho kutaka kuukimbia mwili.



___________



KAZI ya mungu haina makosa. Walinena wanenaji. Lakini kuna wakati inaumiza zaidi ya kufanyiwa kosa lenyewe. Hasa pale anapoondoka yule uliyehisi ni mwanga wa maisha yako.

Kila kitu utakiona hakifai, kila mtu utahisi yeye nd'o sababu, hakuna utakaloambiwa likakifu na kukidhi ukubwa wa hisia zitakazokukumba muda huo.

Huwa ni zaidi ya maumivu!



Ndivyo ilivyokuwa kwa Zainab wakati huu. Yule aliyekuwa kamkabidhi funguo, funguo ya kufunga milango ya penzi lake na as'ende kwa mwengine, uhai ulikuwa unamtoka mbele ya uoni wake.

Abuu alikuwa yupo katika hatua za mwisho za kuvuta pumzi yake.

Abuu, Zee la nywila, Mr. Password...aliaga dunia palepale.

Abuu alifariki!



Hapanaa...

Zainab alihisi haiwezekani kitu kama kile kutokea, alimpigapiga Abuu aamke, alimtingisha na kumtingisha, aliita na kuita...waapiii, Abuu alishabisha hodi chumba cha akhera, na siti alishakabidhiwa. Chumba ambacho kila mmojawetu lazima ataingia...ila kutoka, ni majaaliwa.

Tayari Abuu alishavikwa cheo kipya, marehemu.



Kilio cha sauti ya chini, chenye unyevunyevu mzito wa maumivu kilimkuta Zainab. Taratibu sauti ikaanza kupanda, juu kidogo, juu tena, juu zaidi...mpaka majirani wasiwasi nao uliwakuta.

Walifika hadi karibu na mlango ule wakaanza kugonga kutambua kipi kimejiri.



Nguvu za kuinuka na kwenda kuufungua mlango Zainab azitoe wapi?

Hakuwa na nguvu kabisa. Yeye aliukumbatia mwili wa marehemu tu. Hakutaka kumuachia.

Kuna nyakati alijaribu kufumba macho yake na kufumbua, huenda ikawa ni ndoto...haikuwa hivyo.

Abuu alikuwa kafariki kweli!



____



MUDA kidogo, John alirejea...alishtushwa na mkusanyiko wa watu nje ya chumba chake.



Watu hawa walikuwa katika majadiliano mazito, wauvunje mlango au wasiuvunje?

Maana, kadiri muda ulivyozidi kuyoyoma, ndipo kilio kilishika kasi.

Walihisi huenda aliyeko ndani angali yupo katika matatizo ila anashindwa kuzungumza, zaidi ya kulia tu.



John akiwa haelewi chochote, alipokewa na macho ya wapangaji wenzake. Wote wakiwa katika mshangao...

Chumba kimefungwa kwa ndani, mbona mwenye chumba yuko nje?

Walijiuliza.

Vipi. Mbona watu wamejaa hivi nje ya nyumba yangu...kunani?

John nae alishindwa kutambua.



"Mwanangu, ndani kuna nani?" Mama mmoja ambaye alionekana ana umri mkubwa kidogo, alimuuliza John.



"Kwanini?" John nae aliuliza huku akijongea mpaka karibu na mlango.



John alianza kusikia kilio. Alimfahamu anayelia ni nani...



"Zainab....Zainab...naomba ufungue mlango!" John aliita.



Wapangaji baada ya kusikia jina la kike, wakaanza kugeukiana kijicho upande...kwa umbea!



Kitendo cha Zainab kulia, kilimpa John fikra ya wasiwasi, maana hali aliyomuacha nayo Abuu haikuwa nzuri.

Aliendelea kumshinikiza Zainab afungue mlango, " Zaii... Zai nisikilize basi."

Haikusaidia kitu! Zai aligoma katakata kuufungua mlango.



Hapo, ndipo walichukua uamuzi wa kuuvunja...walishirikiana watu watatu, John pamoja na wapangaji wawili wakiume, Ali Sodo na Baba Amina.

Ali Sodo, amepewa jina hilo kutokana na umaridadi wake mkubwa wa kusakata kabumbu...yani, kucheza mpira.

Walijitahidi mpaka mlango ulivunjika.



Walipoingia walimkuta bado Zainab yupo ukiwani, analia.

John naye aliishiwa pozi, alisimama. Hakuelewa akae au asimame vilevile. Alichanganyikiwa!

Hakuamini, hakuamini Abuu ndiyo tayari kashafariki.

Daah!



______





WIKI tatu baadaye, mwili wa Abuu ukiwa tayari umezikwa panapostahili. Ilihali Zainab yuko hoi bin taaban...kufikia mpaka akalazwa hospitali. Mahututi!

Aliugua 'gonjwa penzi-kulikosa'.



John alikaa chumbani kwake akitafakari mno. Tayari alishaweka mikakati mikubwa mno...mikakati ya kulipa kisasi akishirikiana na Abuu, halafu Abuu mwenyewe, ndiyo kaiaga dunia.

Mara, alisikia mlango wake ukigongwa...



"Inakuaje blaza!" Alikuwa ni Ali Sodo, alimsaili. Mkononi kashikilia viatu vyake vya michezo. Mwilini 'katupia' jezi zake safi za timu mojawapo kubwa ya mpira wa miguu.

"Ah, safi ndugu..." John alijibu kwa kujivuta. Bado jeraha la kuondokewa na Abuu halikupona mtimani.

"Leo tuna mechi kaka, karibu ukatushangilie vijana wako," aliongea Ali Sodo huku anarusharusha miguu kuonesha makeke yake.

"Ah...mi' siendi," John alijibu kisha akaufunga mlango na kurejea zake ndani.

Kabla hajafika mbali...mlango uligongwa tena...



"Kaka...usikae sana ndani, mawazo ndiyo yatazidi. Twende angalau ukajichanganye na watu ndugu."

Alivyoufungua tena, alikumbana na maneno hayo yaliyotoka kwa Ali Sodo.



Kauli hii ilikuwa ina mantiki kidogo akilini. Alifunga mlango wake wakatoka na kuongozana, Yeye na Ali Sodo...wakaelekea uwanjani.



Uwanja haukuwa mbali sana, ni nyuma tu ya soko la Manyanya, Kinondoni. Ilikuwa ni mechi ya muendelezo wa ligi ya mkoa.

Timu ya hapa sokoni, anayochezea Ali Sodo, dhidi ya timu kutoka wilaya ya Temeke, maeneo ya keko, Al'maarufu kama 'Keko furniture'.



Uwanja ulifurika mashabiki, kila mmoja akiishangilia timu aipendayo. Akili ya John nayo, taratibu ilianza kuendana na kasi yao, ilichangamka.



Baada ya dakika chache, timu ziliingia uwanjani, kipute kikaanza...

Ilikuwa vuta nikuvute, timu zote zikicheza kwa ubora wa hali ya juu.



Ilipofikia dakika ya sabini na sita, mchezaji wa Keko alijiangusha kwa makusudi, katika eneo la hatari, refa akatoa penati.

Weeeh! Unadhani palikalika?

Fujo zikaanza nakwambia, chupa zikaanza kurushwa hovyohovyo. Si refa, si wachezaji, si makocha...wote walikuwa wanatafuta uchochoro wa kuchomokea.



John naye aliunga, alianza kukimbia kunusuru mwili wake usije kujeruhiwa...

Hamadi! Aligongana kwa bahati mbaya na mtu asiyemfahamu...



"Samahani kaka..." Yule kijana aliomba radhi.

Sasa, si nd'o John akaamua amuangalie usoni.

Laahaula! Alikutana na sura ya Abuu.



....



GANZI ya ghafla iliushika mtima wa John. Alitamani kumshika mkono jamaa anayemuona mbele yake, ila alishindwa. Akatamani walau atoe neno, pia alishindwa.



Yule jamaa baada ya kuona hamuelewi, alichomoka mbio na kupotelea mbali. John alibaki palepale, ameganda...haelewi cha kunena wala kutenda.

"Yule ni Abuu?

Abuu lakini si' tumemzika juzi tu?

Ni nani yule? Au nimegotana na jini...

Hapanaa! Ni mauzauza yangu tu. Ila daah... Mbona nimemuangalia vizuri, sio mauzauza bwana, ni nani sasa yule?"

Mawazo yaliuchanganya ubongo wa Abuu...



"Uwiiiii..." alinung'unika mtu aliyekuwa anakatisha mbele ya John. Ni kijana mdogo tu, alikuwa anaugulia maumivu ya kitu kizito kilichondokea kichwani mwake.



Hapo ndipo John alitanabahi kuwa yumo hatarini, akaanza kuzichakata hatua kwa kasi ili aondoke haraka eneo lile, akiitafuta njia ya kuelekea nyumbani kwake.



....

Fikra za yule mtu mwenye sura ya Abuu, hazikuacha kuchora picha akilini mwa John hadi alipofika ndani mwake na kujifungia.



Alijitupa kitandani kwa hasira. Alijuta kwanini kashindwa hata kutamka neno lolote kwa mtu yule...alijuta sana!



"Daah, kwanini sijamuuliza walau jina lake? Ah...huenda sio mtu wa kawaida yule. Ilaa... Jini anaweza akakwaana na binadamu kwa namna ile kweli?"

Aliwaza.



Ghafla, akakumbuka kitu. Ali Sodo yuko wapi? Yu-salama kweli?

Alijiuliza bila ya kupata jawabu lolote kichwani.



Akatoka nje ya chumba chake tena.

Alipiga hatua kadhaa mpaka chumba cha tatu kutoka kilipo chake, na nd'o chumba cha Ali Sodo...mlango ulifungwa kwa cha nje.

Kumaanisha hayupo!



Hayupo?!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Ina maana bado yupo uwanjani?

Anasubiri nini na varangati lote lile?

Hapo Abuu aliweka kituo. Kuna kitu!



Akajaribu atoe simu yake mfukoni ili ampigie...unadhani aliikuta?

Hakukuwa na simu!



Alihisi labda ameiacha chumbani, akarudi kuingalia vizuri...tafuta na kutafuta, hakukuta simu.



"Ina maana wameniibia?" aliwaza. "...ngoja nishughulikie kwanza alipo Ali Sodo. Kisha nidili na huyu mjinga aliyeniingiza mjini."

John alizungumza huku anatoka nje.



...


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog