Simulizi : Furaha Hatimaye
Sehemu Ya Tano (5)
Maisha yake yalijawa na huzuni, hakutamani kuishi na mwanamke tena, mwanamke aliyempenda alikuwa ni Halima tu, mwanamke ambaye alimsaidia na kumtibu mpaka akapona kabisa, lakini baadaye akamgeuka! Pamoja na yote hayo, alimpenda sana!
Rafiki yake Dk. Immanuel pamoja na mkewe Isabela, walikuwa wameketi bustanini wakimsikiliza kwa makini Dk. Othman, aliongea maneno yaliyotia simanzi, kutokana na uchungu wa maneno hayo, wakajikuta wote wakilia!
Machozi yakatawala, kila uso wa mmoja wao ulilowana machozi, pamoja na hayo, wote walikuwa wakisubiri kwa hamu kusikia Dk. Othman alikuwa na matatizo gani. Je, atawasimulia siri hiyo aliyoiomba wamfichie? SONGA NAYO….
Kama angetokea mtu ghafla na kuwakuta bustanini wakilia, asingekuwa na ubishi kuwa walikuwa wamefiwa au kulikuwa na tatizo kubwa lililotokea kati yao. Machozi yaliyokuwa yakibubujika machoni mwao, yalikuwa yanatosha kuonyesha ishara kuwa kulikuwa na tatizo kubwa lililotokea!
Dk. Immanuel alikuwa analia, Isabela naye ndiyo alikuwa hasemeki, Dk. Othman ni kama alikuwa amechochewa kulia. Isabela akainua uso wake juu, kisha akatoa kitambaa mfukoni na kujifuta machozi, alipomaliza akamsogelea mumewe Immanuel kisha akamfuta machozi, alipomaliza akatambaa kwa magoti mpaka alipokuwa amekaa Dk. Othman kisha akamfuta machozi kwa upendo.
“Niache nilie Isabela!” Dk. Othman akasema kwa uchungu.
“Hapana, hupaswi kulia!”
“Kwanini?”
“Kwasababu hujatueleza tatizo, weka wazi naamini kutakuwa na jipya la kufanya utakalopata!”
“Kweli?”
“Niamini shemeji yangu!” Sauti ya Isabela ilikuwa laini iliyotulia, ilitoka taratibu kinywani mwake, ilitosha kabisa kumbembeleza Dk. Othman, kwa kiasi kikubwa akajisikia vizuri.
Alionyesha mapenzi ya hali ya juu sana, alionyesha ni kiasi gani alikuwa anampenda na kumthamini, alimuona sawa na ndugu yake. Wakati mambo yote hayo yakitokea, Dk. Immanuel alionyesha kuwa na huzuni zaidi!
Dk. Othman alinyamaza baada ya kubembelezwa na Isabela, lakini Immanuel aliendelea kulia, akapata kazi mpya ya kumbembeleza Dk. Immanuel.
“Brother Imma, tulia rafiki yangu!” Dk. Othman akasema.
“Inaniuma sana, wewe ni sehemu ya maisha yangu, wewe ni ndugu yangu kwa kila kitu, sasa siwezi kuwa na furaha kama nahisi una matatizo yanayokusumbua, ukweli ni kwamba naumi sana moyoni mwangu!”
“Usijali rafiki!”
“Enhee…unaweza kuendelea kunihadithia?”
“Hilo linawezekana ila…”
“Ila nini tena?”
“Iwe siri, nawaombeni muitunze siri hii!”
“Usihofu!”
Dk. Othman akainama chini kwa nukta kadhaa kisha akainua tena uso wake, kisha kwa huzuni wa hali ya juu ambayo kwa hakika hapakuwa na kipimo cha kupima huzuni hiyo, Dk. Othman akaanza kuelezea.
“Ni hadithi ndefu kidogo, hadithi yenye machungu na kila aina ya mateso, ni lazima muwe wavumilivu na mjiandae kusikia hadithi ambayo kwa hakika itawatoa machozi!”
“Tupo tayari, naweza kusema tumzoea kulia sasa!” Isabela akajibu.
Hapakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kuanza kuwaelezea kila kitu, hakuwaficha alikuwa wazi kwa kila kitu kuanzia mwanzo mpaka mwisho, maisha yake yalitia simanzi, akawaeleza kila kitu kuhusu Halima. Isabela hakuweza kuvumilia, muda wote Othman aliokuwa akisimulia alikuwa akilia! Machozi yalitoka na kukauka zaidi ya mara sita! Hali ilikuwa mbaya sana, huzuni ikatawala nyumbani kwa Dk. Immanuel.
“Kwa hiyo ndio hivyo ndugu zangu, huyu mwanamke hafai kabisa, ni yeye ndio aliyesababisha leo hii niitwe Albert Mkambila badala ya jina langu la Othman. Ameharibu maisha yangu!”
“Pole sana Othman!”
“Nashukuru lakini ni changamoto katika maisha yangu!”
“Ni kweli ila sasa unapaswa kufanya uamuzi mwingine!”
“Uamuzi gani?”
“Unatakiwa kusahau yote yaliyopita na kufungua ukurasa mwingine!”
“Ni vigumu sana Immanuel!”
“Hakuna ugumu wowote, ni wewe kuamua!”
“Hakuna mwanamke ninayempenda duniani kama Halima, sasa sijui kama nitaweza kuwa na mwingine tena!”
“Fanya yote yamepita, halafu fungua ukurasa mwingine kama nilivyokuambia, kila kitu kinawezekana!”
“Naumia…moyo wangu una makovu, siwezi kuwa na mwanamke mwingine ila…”
“Ila nani sasa?”
“Labda Halima, ingawa alinitesa sana!”
“Futa mawazo hayo kichwani mwako!” Isabela akasema.
“Kwanini Isabela, kumbuka kuwa nampenda sana!”
“Pamoja na hayo, lakini ni mtu hatari sana kwa maisha yako, hutakiwi kukumbuka kitu chochote kuhusu yeye tena, anza kufikiria maisha yako!”
“Ok!” Dk. Othman akajibu kwa kifupi sana. Mazunguzo yakaendelea mpaka usiku, Dk. Othman akasahau kuwa alitakiwa kwenda nyumbani.
“Sidhani kama ni lazima sana kwenda nyumbani leo!” Dk. Othman akasema.
“Kwanini?” Immanuel akadakia.
“Nimechoka, nahitaji kupumzika sasa, naona nilale hapa hadi kesho, halafu isitoshe kesho ni siku yangu ya kupumzika!”
“Hakuna tabu rafiki yangu, hapa ni nyumbani kwako!” Ndivyo ilivyokuwa, Dk. Othman hakuondoka, alilala nyumbani kwa Dk. Immanuel.
*********
Ulikuwa usiku usioweza kusahaulika katika maisha yake, ni usiku alioutumia kumfikiria zaidi Halima, ni kweli alimtesa sana moyoni mwake, lakini pamoja na hivyo, moyo wake ulikuwa na doa, doa ambalo halikuwa rahisi kusahaulika, dawa pekee ya moyo wa Othman ilikuwa ni Halima pekee!
“Ni kweli, Halima ni mtu mbaya sana katika maisha yangu, lakini nashindwa kujizuia, nampenda Halima, anautesa sana moyo wangu!” Aliwaza huku akijigeuza geuza kitandani.
Kwa saa kadhaa alitulia kitandani huku macho yake yakiwa juu ya Luninga iliyokuwa chumbani mwake, mawazo yakazidi kutawala kichwa chake, akiwa anaendelea kuwaza, simu yake ikaita!
Lilikuwa jambo la kushangaza, kwanza alidhani alikuwa ndotoni, akayatupa macho yake kwenye saa iliyokuwa ukutani, ikasomeka kuwa ni saa nane na ushee za usiku, akapuuza. Dakika moja baadaye simu ikapigwa kwa mara nyingine, safari hii hakutaka kupuuza kama ilivyokuwa awali, akasimama kisha akapiga hatua za kivivu mpaka ilipokuwa simu yake, akaichukua haraka na kuangalia jina la aliyekuwa akipiga, moyo wake ukazidisha kasi, alikuwa ni Dk. Ringo, haraka akaipokea.
“Habari za huko rafiki yangu?”
“Nzuri, habari za Tanzania!”
“Salama…tena sana!”
“Kwanini unasema hivyo ndugu yangu?”
“Nina habari nzuri sana kwa ajili yako!”
“Habari nzuri? Habari gani hizo rafiki yangu?”
“Hutakiwi kuwa na haraka, amini kuwa nina habari nzuri kwa ajili yako, unatakiwa kufanya jambo moja tu, kwa sasa!”
“Jambo gani hilo Dk. Ringo?”
“Safari… Anza kupanga safari ya kurudi Tanzania, mambo mengine utayajua huku!”
“Hapana, ni lazima nijue kwanza!”
“Kuna nafasi ya kazi hapa Hospitalini, nimeshazungumza na mkuu na kuelewana naye vyema, kwa hiyo unatakiwa uje kuanza kazi mara moja!”
“Siamini!”
“Amini rafiki, kila kitu kinawezekana, njoo tuwe pamoja!”
“Ni hapo hapo Ifakara?”’
“Ndiyo!”
“Ila lazima tuwe makini na jambo moja muhimu!”
“Jambo gani hilo Dk. Othman?”
“Ni juu ya jina langu, lazima nibaki kuwa Dk. Mkambila na siyo Dk. Othman, hilo litabaki mioyoni mwetu wenyewe!”
“Bila shaka!”
“Unadhani unaweza kuchukua muda gani?”
“Ni baada ya mwezi mmoja tu, kutoka sasa!”
“Hakuna tatizo, nitaanza kukutafutia nyumba mapema!”
“Nashukuru sana!” Furaha ikarudi kwa kasi katika moyo wa Dk. Othman (Mkambila), hakupenda kuishi katika nchi ya ugenini, alitamani sana siku moja arudi tena nyumbani Tanzania, aliota hilo siku zote na wakati wa kutimiza ndoto yake ulikuwa umeshafika.
Mwezi mmoja baadaye, Dk. Mkambila akarudi Tanzania, moyo wake ulikuwa na furaha sana. Saa mbili na nusu za usiku Ndege ya Shirika la Ndege la Nairobi, ilitua katika Uwanja wa Mwalimu Nyerere, Dk. Mkambila akashuka taratibu kabisa, uso wake ukiwa na miwani meupe iliyompendeza bara-bara. Haikuwa rahisi kumtambua kuwa alikuwa ni Dk. Othman ambaye ilifahamika kuwa alikuwa ameshakufa.
Alichokifanya ni kuchukua taxi na kumwambia dereva ampeleke katika hoteli nzuri ya kulala. Baada ya makubaliano, safari ya kwenda hotelini ikaanza. Akamlipa pesa zake, kisha akaenda moja kwa moja mpaka mapokezi. Baada ya kuandikisha, akaonyeshwa chumba chake cha kulala, akataka kuondoka. Kabla hajafanya hivyo, akageuka nyuma, akakutana na mtu ambaye alimtilia mashaka.
Ni mtu ambaye alikuwa akimfuatilia kuanzia Uwanja wa Ndege! Aliposhuka tu kwenye ndege alikuwa akimfuatilia kwa nyuma, alipoingia kwenye taxi na kuondoka, aliifuata gari hilo mpaka hotelini, na hata alipoandikisha jina naye alitokea! Ni jambo lililomtaka awe makini sana. Taa nyekundu ikawaka ubongoni mwake.
“Mh! Ni lazima niwe makini na mtu huyu, kuna kitu kinataka kufanyika hapa, kitu kibaya ambacho kinaweza kuharibu kila kitu katika maisha yangu, lazima niwe makini!” Akawaza.
Hata hivyo alipuuza inagawa akili yake ilimtaka kuwa makini na mtu huyo, akaziendea ngazi na kupandisha ghorofa ya tatu kulipokuwa na chumba chake, hakutaka kuoga akavaa suti za usiku, kisha akaenda katika chumba maalumu cha vinywaji, akaagiza maji ya matunda na kuanza kuburudika huku akipanga ratiba ya siku iliyokuwa mbele yake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kuletewa kinywaji na kunywa fundo moja tu, mtu aliyekuwa akimfuatilia, akaingia akaketi meza ya nne kutoka alipokuwa ameketi yeye. Akili yake ikapata kazi ya ziada, umakini ukasisitizwa kwa mara nyingine.
“Ni nani huyu? Kwanini ananifuatilia? Au yupo na mambo yake?” Kichwa chake kilipata maswali mengi yasiyojibika, kimsingi alijua wazi kuwa kulikuwa na matatizo!
Alichokifanya ni kunywa kinywaji chake haraka kisha akarudi chumbani kwake. Akautafuta usingizi kwa shida sana lakini hakufanikiwa! Baada ya muda kidogo akasinzia, usingizi ulipompitia, akasikia kama mlango wa chumba chake ulikuwa ukigongwa! Akafikiri alikuwa kwenye njozi, lakini alipojitahidi kuamka na kukaa kitandani, akasikia mlango wake ukigongwa, hakuwa na maswali zaidi, ni kweli mlango wa chumba chake ulikuwa ukigongwa!
Akayatupa macho yake kwenye saa yake ya ukutani iliyosomeka kuwa ni saa saba za usiku, akili yake ikarudi kwa mtu aliyekuwa akimfuatilia!
“Atakuwa ni yeye tu, hakuna mwingine!” Akawaza huku akitetemeka.
Akatulia kwa muda, lakini aliyekuwa akigonga mlango akaendelea, tena safari hii aligonga kwa kasi ya ajabu kama alikuwa akitaka kuuvunja! Akasimama akitetemeka kwa woga.
“Nina nani wewe unayegonga?” Akauliza kwa woga.
“Fungua mlango haraka!” Sauti hiyo aliifananisha kama aliisikia saa chache zilizopita, haja ndogo ikaanza kumtoka!
****
Safari Hotel, ilikuwa nzuri iliyoheshimika sana jijini Dar es Salaam, ilikuwa ni kati ya hoteli kubwa zilizokuwa na wateja wengi hasa watalii kutoka nchi mbalimbali. Mmiliki wa hoteli hiyo Novathus Kangunga, alikuwa na marafiki wengi wenye uwezo mkubwa ambao kila wakati alipokuwa na matatizo huwa msaada mkubwa sana kwake.
Jumamosi hiyo, kama ilivyo kawaida ya siku za mwisho wa wiki vyumba vyote vilikuwa vimejaa! Ulikuwa usiku wa saa sita na dakika kadhaa, vyumba vyote vilikuwa tulivu, ingawa katika sehemu ya Baa ya Hoteli hiyo ilikuwa imechanganka sana kutokana na baadhi ya wateja kuendelea kuburudika na vinywaji pamoja na muziki uliokuwa ukiporomoshwa na Dj maarufu Da-Kalimu!
Watu hawakuwa na wasiwasi na maisha yao yajayo, kwao ilikuwa ni kuponda raha kwa kwenda mbele. Sehemu ya baa ya hoteli hiyo ilikuwa ipo katika ghorofa ya kumi na tisa, watu waliendelea kuponda raha!
“Say yeaah!” Dj wa siku hiyo akasema.
“Yeaah!” Watu wakaitikia.
“Nimewarusha sijawearusha?”
“Umeturusha!”
“Nimewamba sijawabamba?”
“Umetubamba…”
“Tuendelee au tusiendelee?”
“Tuendeleeee…”
“Nikaumue au nisikamue?”
“Kamua…” Kila mtu alikuwa na furaha ya ajabu, kelele ziliendelea mpaka saa nane za usiku. Wakiwa wanaendelea kuburudika na muziki pamoja na vinywaji, ghafla wakasikia harufu ya nyaya za umeme zinazoungua! Mwanzoni hawakujali, wakahisi huenda ni harufu ya vyombo vya umeme baada ya kufanya kazi muda mrefu.
Dakika moja baadaye, moto ukaanza kuwaka katika chumba cha Dj, kelele zikaanza kusikika, kila mtu akawa anamkanyaga mwenzake, hakuna aliyekuwa tayari kufa. Kelele zikapigwa na watu wakawa wanashuka kwa kasi kupitia ngazi. Waliogopa kutumia lifti wakifofia shoti ya umeme.
Baada ya dakika tano hakuna mtu aliyekuwepo katika chumba hicho wote walikuwa wakishuka chini kwa kasi ya ajabu ili kuokoa maisha yao. Wanaume kwa wanawake wote walitimua mbio kwa ajili ya kuogopa kufa! Wenye roho ndogo, walifikia hatua ya kujirusha kuanzia ghorofa ya juu kwa nia ya kujiokoa lakini walifika chini wakiwa wameshakufa.
Ghorofa nzima ikashika moto, kadri muda ulivyozidi kwenda jengo la hoteli hiyo liliendelea kuungua kuelekea juu na chini! Baada ya kugundulika jengo lilikuwa linaungua, magari ya zimamoto yaliitwa wakati huo huo, wageni wote waliokuwa vyumbani waligongewa wakiamriwa kutoka vyumbani.
Lilikuwa jengo lengo ghorofa ishirini na tano!
Kuanzia ghorofa ya pili hadi ya kumi na tano ndiyo ilikuwa na vyumba vya kulala wageni. Walinzi walipita haraka na kuwagongongea wageni ili waamke kabla moto haujawafikia.
*********
Woga ukatanda katika moyo wa Dk. Albert Mkambila, (Dk. Othamn) hakuweza kuelewa ni nani hasa aliyekuwa akigonga mlango wa chumba chake, lakini kwa haraka kitu kilichoingia akilini mwake ni kwamba mtu huyo alikuwa adui yake. Sauti ya mtu huyo ilitosha kabisa kumthibitishia kuwa ni yule aliyekuwa akimfuatilia kuanzia Uwanja wa Ndege.
Haja ndogo ikaanza kumtoka mfululizo, ni jambo lilimfanya aamini kuwa maisha yake yalikuwa yakielekea hatarini! Akasimama kisha akawasha taa, baada ya hapo akauliza kwa sauti ya unyonge sana.
“Ni nani wewe unayegonga?”
“Nimekwambia fungua!”
“Kivipi sikuelewi….siwezi kufungua kama hutaniambia wewe ni nani!”
“Kama unataka kufa, basi endelea kubaki huko, hoteli inaungua!” mtu huyo akasema kisha hakusikika tena akitoa kauli.
Kitendo cha kuambiwa kuwa hoteli ilikuwa inaungua, kilimshangaza sana na halikuwa jambo la kuliamini haraka kiasi hicho, akili yake ilimtuma kuwa mtu huyo hakuwa mwema kwake na alitumia moto kama chambo cha kumtoa chumbani ili amdhuru.
Akiwa bado anawaza akasikia sauti ya watu na vishindo, kama walikuwa wakikimbia, bado hakutaka kuamini kama alichokisikia kilikuwa sahihi, akili yake ilimtuma aamini kuwa ni ndoto! Harufu ya moto ikamfikia!
“Inawezekana ni kweli!” Akajisemea mwenyewe kisha akafungua mlango, alichokutana nacho hakuamini!
“Mungu wangu, ni moto!” Haraka akarudi chumbani kwake kisha akavaa na kuchukua begi lake na kushuka ngazi kwa kasi ya ajabu. Alipofika chini akawakuta wageni wengine wengi wakiwa wametoka vyumbani mwao.
“Nini chanzo cha moto huu?” Dk. Mkambila akamwuliza mtu mmoja aliyekuwa pembeni yake.
“Shoti ya umeme!”
“Imeanzia wapi?”
“Ghorofa ya kumi na tisa, sehemu ya baa!”
“Kulikuwa na watu mpaka saa hizi?”
“Ndio!”
“Mh! Kweli watu wanapenda starehe!”
“Tena nasikia kulikuwa na muziki, watu walikuwa wanacheza bila wasiwasi, wanasema moto umeanzia kwenye chumba cha Dj!”
“Mh! Hakuna watu waliokufa?”
“Wapo, kuna waliojirusha, na wengine wameshindwa kutoka!”
“Kwahiyo wameungulia huko huko?”
“Ndiyo!” Wakati mazungumzo hayo yakiendelea magari ya zima-moto yalikuwa yakiendelea na kazi za kuzima! Hata hivyo hawakufanikiwa kuzima sehemu kubwa ya jengo hilo.
Kilichofanyika ni kuwahamisha wageni wote katika hoteli nyingine ya jirani. Dk. Mkambila hakuweza kulala usiku, aliutumia kumshukuru Mungu kwa kumuokoa na janga hilo. Kwa bahati nzuri alifanikiwa kutoka akiwa salama pamoja na mizigo yake yote.
“Nina kila sababu ya kumshukuru Mungu wangu, kama siyo yeye sasa hivi ningekuwa na jina lingine!” Akajisemea mwenyewe.
Hakuwa a muda wa kupoteza zaidi, alichokifanya ni kumpigia Dk. Ringo simu na kumtaarifu juu ya safari yake ya Ifakara ambapo alimuahidi kusubiri kituoni. Akapanda gari asubuhi hiyo hiyo na kuondoka kwenda Ifakara.
Kitu cha kwanza kufanya alipofika Ifakara ilikuwa ni kumweleza jinsi alivyonusurika katika ajali ya moto ya hoteli ya Safari.
“Pole sana rafiki yangu!”
“Ahsante sana Dk. Ringo!”
“Karibu sana Dk. Mkambila, kila kitu kitakuwa sawasawa, hakuna atakayekufahamu, utaishi hapa bila matatizo!”
“Nashukuru kusikia hivyo, kwakweli nina kila sababu ya kukushukuru, kwasababu kama siyo wewe maisha yangu yangeshafika mwisho!”
“Usiseme hivyo Mkambila, ni Mungu peke yake ndiye anayetakiwa kushukuriwa kwa kuwa bila nguvu zake leo hii ungekuwa gerezani!”
“Ni kweli na tumshukuru pamoja ! ”
“Amen!”
Asubuhi ya siku iliyofuata wakaongozana mpaka hospitalini ambapo mambo yalikwenda kama yalivyopangwa! Wiki moja baadaye, Dk. Mkambila akaanza kazi katika hospitali aliyokuwa akifanyia kazi Dk. Ringo. Akahamia katika nyumba iliyoandaliwa tangu alivyokuwa nchini Uingereza.
Maisha yakaendelea kama kawaida, alikutana na watu wengi sana aliowafahamu, lakini hawakujua kuwa yeye ndiye Dk. Othman, walimtambua kama Dk. Mkambila, hiyo ilibaki kuwa siri kubwa katika ya Othman na Dk. Ringo. Ilikuwa vigumu sana kuishi na siri hiyo, lakini hakuwa na jinsi, ilikuwa lazima akubaliane na ukweli halisi uliokuwepo.
********
Blandina alikuwa kimya akimsikiliza kwa makini Dk. Mkambila, muda wote aliokuwa akihadithiwa, alikuwa akilia. Haikuwa rahisi kuamini jambo hilo. Kutokana na hisia kali zilizomkumbusha machungu Dk. Mkambila, alijikuta akilia kila wakati.
Baada ya kugundua kuwa aliyekuwa mbele yake ni Dk. Othman na sio Mkambila, alichanganyikiwa, hakutegemea kama siku moja angekutana naye. Siku zote aliamini Dk. Othman alikuwa amekufa.
“Siamini…” hatimaye Blandina akasema.
“Kwanini usiamini, kila kitu kinawezekana kwa uwezo wa Mungu!”
“Lakini mimi ndiyo chanzo cha mateso yote hayo, naomba unisamehe Othman tafadhali!”
“Usiniite Othman!”
“Samahani…”
“Ngoja nikuambie kitu kimoja, nilijua kuwa lazima siku moja ningekutana na wewe, nilijua pia kuwa siku mopja dunia ingekunza, naamini umejifunza. Nataka kukuambia kitu kimoja muhimu sana!”
“Kitu gani?”
“Nakupenda Halima!”
“Mimi? Unaweza kunipenda tena mimi?”
“ Ndiyo maana siku zote sikuoa mwanamke mwingine, nilijua ningekutana na wewe, na ningekuoa ! ”
“ Huwezi kuishi na mimi Othman, huwezi ! ” Blandina alisema huku machozi yakitiririka machoni mwake.
“Bado nakupenda, naamini muda wangu wa kuishi na wewe sasa umefika, sioni sababu ya kuishi na mwanamke mwingine zaidi yako! Nimeumbwa kwa ajili yako!” Haikujulikana ilivyokuwa, wakati Dk. Mkambila akizungumza hayo, ghafla Blandina (Halima) akaanguka chini kama mzigo! Akaanza kutokwa na mapovu mdomoni na puani na mdomoni.
Dk. Mkambila akachanganyikiwa!
Baada ya Genesis mtoto wa Blandina kuruhusiwa hospitalini, walirudi nyumbani kwa Dk. Mkambila. Kila mmoja aliamua kumhadithia mwenzake historia ya maisha yake. Alianza Blandina na baadaye Dk. Mkambila akafuata.
Alikuwa na historia ya kusikitisha sana. Alimweleza kila kitu kilichotokea katika maisha yake. Ni hapo sasa Blandina alipogundua kuwa aliyekuwa mbele yake ni Dk. Othman! Akashtuka sana na kuomba msamaha, Dk. Mkambila alikuwa anampenda sana Blandina, akamwambia kuwa alikuwa akimpenda na alitaka kuishi naye!
Hilo lilikuwa kosa kubwa sana kwa Dk. Mkambila, Blandina akaanza kuhema kwa kasi, kisha machozi yakafutia, baada ya hapo akaanguka chini kama mzigo! Nini kitaendelea SONGA NAYO...
Kila kitu kiliharibika, Dk. Mkambila alichanganyikiwa sana, baada ya kuona Blandina ameanguka chini. Alichokifanya ni kuinama na kusikiliza mapigo yake ya moyo, alipogundua kuwa yalikuwa yanapiga, akatikisa kichwa kwa furaha. Alijua kilichotokea, pia alijua alitakiwa kufanya jambo gani ili aweze kuokoa maisha yake.
“Lazima niwe makini, vinginevyo nitampoteza!” Akawaza, kisha haraka akaanza zoezi la kumwagia maji mwili mzima! Alifanya hivyo kwa muda mrefu, kisha baadaye kidogo Blandina akashtuka akiwa anahema kwa kasi ya ajabu.
“Pole!” Dk. Mkambila akamwambia Blandina.
“Ahsante!”
“Usijali!”
“Lazima nijali!” Blandina akasema huku machozi yakichukua nafasi katika macho yake.
“Kwanini?’
“Mimi ndiyo chanzo cha matatizo yote hayo!”
“Usiseme hivyo, mambo hayo nilishayasahau siku nyingi!”
“Lakini najiona mwenye makosa makubwa sana kwako, ni lazima unisamehe!”
“Hakuna tabu, sasa fanya kitu kimoja kwanza!”
“Kitu gani?”
“Nenda kabadili nguo chumbani, halafu urudi hapa!”
“Sawa!” Blandina akatoka huku machozi yakiendelea kububujika machoni mwake, alijua ni kiasi gani alikuwa mkosaji kwa Dk. Mkambila, kuomba samahani lilikuwa jambo la lazima, ambalo aliamini kurudia kila wakati ingesaidia kumpunguza Dk. Mkambila machungu.
Dk. Mkambila akabaki sebuleni akiwa na mawazo tele kichwani mwake. Ilikuwa siri kubwa sana katika maisha yake, aliificha siku zote na aliyekuwa akifahamu juu ya siri hiyo ni Dk. Ringo pekee! Dk. Ringo ndiye aliyekuwa akifahamu kuwa Dk. Mkambila alikuwa ndiye Dk. Othman.
Dk. Ringo alikufa akiwa na siri hiyo moyoni mwake. Akaendelea kuwa na siri hiyo, lakini siku hiyo hakuona sababu ya kuendelea kuificha katika moyo wake. Hata hivyo kulikuwa na kitu kilichomfanya aamue kuifichua siri hiyo. Mapenzi, alimpenda sana Blandina (Halima), ilikuwa lazima afanye kila awezalo ili aweze kuishi naye, kitu cha kwanza ambacho aliamini kingeweza kumpa nafasi nyingine kwa Blandina! Kitu hicho kilikuwa ni kumfahamisha ukweli halisi wa maisha yake, akijitambulisha kuwa yeye ndiye Dk. Othman badala ya Mkambila kama alivyofahamika na kila mtu!
Alibaki akiwa amejishika tama, mawazo tele yakichukua nafasi kubwa akilini mwake, alitamani sana kuishi naye kwa mara nyingine kama mke wake. Dakika nne baadaye, Blandina alirudi sebuleni akiwa amebadilisha nguo. Hakuweza kuyazuia machozi yake, aliendelea kulia bila kukoma.
“Nyamaza Blandina tafadhali!”
“Naamini kulia ni haki yangu!”
“Huna haki ya kufanya hivyo!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kwanini?”
“Kwasababu nimeshakuambia kuwa mambo hayo, nimeamua kuachana nayo, kwahiyo kuendelea kulia ni sawa na kunikumbusha mambo yaliyopita!”
“Siamini kama wewe unaweza kuwa Othman halisi, kila mtu alijua umeshakufa!”
“Kwa habari yote niliyokupa unapaswa kuamini kuwa mimi ndiye, ni lazima uniamini, usiponiamini mimi utamwamini nani?”
“Hebu vua tena hiyo sura ya bandia?” Blandina akamwambia kwa sauti ya taratibu sana.
Mkambila hakuwa na kitu cha kufanya, alitaka kumthibitishia ili aamini kuwa yeye ni mzima na hajafa kama wengine wanavyofahamu! Haraka akavua sura ya bandia iliyokuwa usoni mwake.
“Siamini!”
“Sasa unapaswa kuamini, mimi ndiye Dk. Othman!”
“Nakupenda Othman, naomba unisamehe, sikutegemea haya yaliyotokea kama yangetokea, Gerald ni mtu mbaya sana katika maisha yangu, ni yeye ndiye aliyesababisha mateso haya katika maisha yangu. Yeye ndiye chanzo cha matatizo yote haya!”
“Usijali, sahau yote yaliyopita, tufungue ukurasa mpya. Ngoja nikuambie kitu kimoja!”
“Kitu gani?”
“Wewe ndiye mke wangu, naamini hilo ndiyo maana mpaka leo hujaolewa wala mimi sijaoa, hilo linatosha kabisa kunithibitishia!”
“Nakupenda pia Othman!”
“Nataka nikuoe!”
“Nini?”
“Kwani hujasikia vizuri?”
“Ni kama sijasikia...”
“Nimesema kuwa, nataka kukuoa!”
“Na mwanangu?”
“Mtoto wako sio tatizo, kwakuwa nimekupenda wewe, hata mwanao pia nampenda, utakuwa wangu, Genesis atakuwa chini ya uangalizi wangu, nakuomba shaka ondoa, upo katika mikono salama!”
“Nimefurahi sana kusikia hivyo!”
“Niruhusu nikuambie kitu kingine!”
“Niambie tu!”
“Nataka tufunge ndoa ndani ya mwezi mmoja!”
“Mh! Jamani siamini Othman!”
“Amini Blandina wangu, haya yote yanawezekana kwa sababu nakupenda, hivyo tu!”
“Mh! Ahsante sana mpenzi!” Wakakumbatiana kwa furaha. Huo ulikuwa mwanzo mpya wa maisha mapya, huku furaha ikiwa imetawala katika nyumba yao.
Blandina akaenda Dar es Salaam, kwa ajili ya kuchukua vitu vyake kisha akahamia nyumbani kwa Dk. Mkambila, wakaishi kama mtu na mkewe ingawa hawakuwa na ndoa, walipanga kufanya hivyo baada ya mwezi mmoja. Siku zote Othman aliitwa Mkambila, jina la Othman lilitumika chumbani tu, tena usiku wakati wakiwa wamelala, muda mwingine aliitwa kwa jina lake bandia la Mkambila.
*********
Hawakutaka kupoteza muda, kila kitu kilifanyika haraka-haraka, Mkambila na Othman wakafunga safari mpaka Morogoro nyumbani kwa akina Halima. Mzee Mohamed na mama yake Halima walishangaa sana, hawakutaka kuamini kama mwanao siku moja angerudi nyumbani. Ingawa alirudi akiwa na hali mbaya kidogo kiafya.
Afya yake haikuwa ya kuridhisha! Baada ya Halima kubadilisha dini kwa ajili ya Gerald, alitengwa na familia yake, miaka ikasonga mbele bila kufahamu kilichokuwa kikiendelea katika maisha yake. Hata hivyo hawakutaka kufahamu kitu chochote kwa sababu alikataa kubaki nyumbani na kubadilisha dini ambayo mzee Mohamed, hakuikubali.
“Habari zenu?” Mama yake Halima akauliza.
“Nzuri tu mama!”
“Pole sana mwanangu, lakini nilikuambia mwanzoni, Gerald ni muuajii, hakuwa mwanaume ambaye angekufaa katika maisha yako!”
“Naomba msamaha mama, sasa nimejifunza!” Mazungumzo yakaendelea, lakini baadaye Dk. Mkambila akatambulishwa kama mchumba wake. Kitu cha kwanza mzee Mohamed kuuliza ilikuwa ni dini.
“Ni dini gani?”
“Muislam!”
“Kama ni hivyo, sawa kabisa!” Mzee Mohamed akafurahi sana, mipango yote ikakamilika, barua ya posa ikatumwa na siku ya ndoa ikapangwa. Hata hivyo, siri ya Dk. Mkambila kuwa ndiye Othman ilibaki kuwa siri yao wenyewe, hawakutaka kivujisha siri hiyo.
Siku ya ndoa ikafika, ndoa ya Kiisalam ikafungwa na baadaye ikafuatiwa na sherehe kubwa sana. Baada ya ndoa hiyo iliyofungwa Morogoro, wakarudi nyumbani kwao Ifakara. Mwezi mmoja tu, baada ya ndoa yao, Dk. Mkambila akapata uhamisho, kutoka hospitali aliyokuwa akifanyia kazi Ifakara, kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Wote walifurahia sana uhamisho huo, wakaenda kuanza maisha mapya Dar es Salaam. Maisha yakawa mazuri, lakini mara nyingi madaktari wa siku nyingi wa Hospitali ya Muhimbili, walishangazwa sana na sauti ya Dk. Mkambila, ilifanana sana na ya Dk. Othman aliyekufa muda mrefu uliopita, kama walivyofahamu, haakujua kuwa Dk. Othman alikuwa mzima.
“Dokta uliwahi kuwa na ndugu yako aliyefanya kazi hapa zamani?” Dk. Kweka, rafiki mkubwa wa Dk. Mkambila alimuuliza siku moja walivyokuwa hotelini wakipata chakula cha mchana.
“Anaitwa nani?”
“Othman!”
“Hapana! Kwani siku hizi yupo wapi?”
“Alijinyonga!”
“Alijinyonga?”
“Ndiyo!”
“Kwanini?”
“Ni habari ndefu sana!”
“Unaweza kunisimulia?”
“Bila shaka!” Dk. Kweka akaanza kumhadithia kila kitu, hakutaka kumficha kitu chochote, akamhadithia kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Dk. Mkambila alikuwa makini sana kumsikiliza. Hapakuwa na kitu chochote asichokijua, kila kitu alikifahamu, kwasababu aliyekuwa akiongelewa alikuwa ni yeye!
“Simfahamu!” Baadaye akaitikia.
“Anafanana sana sauti na wewe!”
“Sauti?”
“Ndiyo, tena sio sauti tu, hata kutembea na mwili, tofauti iliyopo kati yenu ni sura tu!”
“Mh! Basi hayo maajabu!” Akasema kwa sauti huku akitabasamu. Baada ya chakula wakarudi ofisini. Kitendo cha Dk. Kweka kuanza kumfananisha kilimtia wasiwasi sana Dk. Mkambila, lakini hakutaka kulipa nafasi kubwa sana jambo hilo akilini mwake.
Jioni akaondoka na kurudi nyumbani kwake Mikocheni. Alipofika nyumbani, kwa mbali akashangaa kuona magari mengi yameegeshwa nje ya nyumba yake. Jambo lingine lililomshangaza ni uwingi wa watu waliokuwa nje ya nyumba yake. Alitetemeka kwa hofu, kuna jambo moja liliingia akilini mwake kwa haraka, alihisi kulikuwa na msiba! Kama sio mkewe amefariki basi mwanaye Genesis!
Machozi yakaanza kutiririka machoni mwake kama mfereji mdogo wa maji! “Lazima kuna matatizo!” Akawaza.
Hakutaka kuingia ndani, akaegesha gari lake nje ya geti, kisha akaingia ndani haraka. Hakuwa tayari kukabiliana na tatizo alilokuwa akihisi lipo mbele yake. Kila nukta moja ilipoondoka ndipo mapigo ya moyo wake yalivyozidi kubadilisha kasi!
****
Mkuu wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika, mama Gibson alimpenda sana Genesis, alithamini uwezo wake wa ajabu katika masomo. Aliumia sana baada ya kupata taarifa kuwa Genesis alikuwa ametekwa katika fukwe za Miami, Marekani. Hata hivyo hakuwa na jinsi, ilibidi akubali ukweli huo, ingawa alikuwa na kazi ya ziada ya kukabiliana na matusi pamoja na lawama kutoka kwa Blandina.
Hilo liliendelea kumtesa kwa miaka saba mfululizo mpaka alipoona kwenye luninga yake, Genesis alikuwa amepatikana! furaha yake iliongezeka zaidi baada ya kusikia kuwa Genesis angewasili Tanzania, ambapo angefikia Ikulu kwa ajili ya sherehe, na baadaye katika shule yake ambapo alipanga kufanya sherehe pia!
Tofauti na matarajio yake, hilo halikuwezekana, baada ya sherehe hizo, alisikia Genesis amepelekwa Ifakara.
Siku zote alijaribu kumfuatilia lakini hakuweza kuelewa alikuwa mahali gani Ifakara. Hakutaka kuona mtoto huyo mwenye kipaji akisoma katika shule za kawaida, alikuwa tayari hata kumlipia ada lakini asome katika shule yake, alifahamu wazi kuwa kama mtoto huyo angemaliza katika shule yake, basi angeipatia sifa kubwa shule yake. Akaendelea kumtafuta kwa bidii zote bila mafanikio.
Siku moja, alifanikiwa kumuona Genesis akiwa nje ya nyumba yao Mikocheni, kwanza alihisi amemfananisha, lakini baadaye alipomuangalia kwa makini aligundua ni kweli alikuwa ni Genesis! Akasimamisha gari na kumuita.
"Hujambo?"
"Sijambo, shikamoo mwalimu!" Genesis akaitika na kumsalimia mwalimu wake.
"Mh! Kumbe unanikumbuka?"
"Kwanini nikusahau?"
"Kwani mimi ni nani?"
"Mkuu wa Shule wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika!"
"Siamini kama umeweza kunikumbuka?"
"Kwanini?"
"Ni muda mrefu sasa umepita!"
"Lakini sio rahisi kukusahau mtu kama wewe!"
"Kwanini unasema hivyo Genesis?"
"Wewe ni muhimu maishani mwangu, walimu wote ni muhimu pia!"
"Kwaheri, nitakuja kukusalimia wakati mwingine!"
"Sawa!" Walizungumza na Genesis kwa zaidi ya dakika tano, alionekana mchangamfu, mwenye uelewa na mwenye kumbukumbu za kutosha. Ni jambo hilo ndilo lililomfanya Mama Gibson aendee Wizara ya Elimu, kuomba msaada wa kuwashinikiza wazazi wa Genesis wamrudishe shule, ni kweli alifanya hivyo na alipewa ushirikiano wa kutosha.
Mipango ikapangwa kimya kimya na siku ya kwenda nyumbani kwa akina Genesis ikafika. Waliamua kwenda bila kutoa taarifa, kilichofanyika ni kuandaa watu maalum watakaokwenda nyumbani kwa akina Genesis. Wizara ikatoa wawakilishi watatu kisha Mkuu wa Shule mama Gibson, akaandaa walimu watano, na wanafunzi kumi, kisha wakaenda nyumbani kwa akina Genesis.
Baada ya kufika nyumbani kwao Mikocheni, walikaribishwa, kutokana na ufinyu wa nafasi baadhi yao waliamua kubaki nje, wakaingia watu watatu tu ndani, ambao ni Mkuu wa Shule mama Gibson, Mwalimu wa Nidhamu na mwakilishi mmoja kutoka Wizara ya Elimu. Mipango yote ilikwenda sawa, walifanikiwa kumshawishi Blandina kwa kiwango kikubwa sana.
"Mwanao ana akili sana, lazima asome, hapaswi kuendelea kukaa nyumbani!" Mkuu wa Shule ya Tanganyika mama Gibson alisema.
"Tena ni hazina ya Taifa, atakuja kuisaidia nchi yetu hapo baadaye, kwa sasa hivi hatuwezi kuona umuhimu wake, lakini baadaye utaonekana!" Akadakia mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu.
"Ni kweli kabisa, kila kitu kinawezekana, lakini siwezi kuamua jambo hili peke yangu, mpaka baba yake aje!"
"Yupo wapi?"
"Kazini, na huu ndio muda wake wa kurudi, bila shaka nusu saa kutoka sasa anaweza akatokea, labda kuwe na dharula ofisini!"
Kwani anafanyia wapi kazi?"
"Yupo Muhimbili!"
"Kama?"
"Daktari!"
"Aisee hongera sana, naamini una mume muelewa sana, kwa hiyo hakutakuwa na matatizo katika hilo!"
"Naamini hivyo!"
"Kwani sasa hivi Genesis anasomea wapi?"
"Anasoma kwenye shule ya hapa mtaani, ila walimu wanasema ana uwezo mkubwa sana, japokuwa wameshamrusha madarasa mpaka amefika darasa la saba, walimu wake wanashauri aendelee na masomo ya sekondari!"
"Mh!" Mmoja wao akaguna.
"Mbona unaguna?"
"Nastaajabu uwezo wake, ana uwezo mkubwa sana!"
"Kwahiyo, acha sisi tuondoke, lakini mzee akija, usisahau kumpa ujumbe huu!"
"Lakini mimi nilikuwa nashauri msubiri, huu ndiyo muda wake na hana desturi ya kuchelewa nyumbani!"
"Basi vizuri!"
*********
Hakuwa tayari kuamini kuwa nyumbani kwake kulikuwa na msiba, hakuishi na mtu mwingine zaidi ya mwanaye pamoja na mke wake Halima. Kilichovamia akili yake kwa haraka ni matatizo. Matatizo ambayo hakujua kama angeweza kukabiliana nayo.
Akapiga hatua za kinyonge huku mapigo ya moyo yakibadilisha kasi, akamvuta mtu mmoja pembeni kwa ajili ya kumuuliza kilichokuwa kikiendelea nyumbani kwake.
“Habari yako?”
“Nzuri!”
“Samahani naweza kukuuliza?”
“Ndiyo!”
“Kuna nini kimetokea hapa?”
“Hakuna tatizo, ni watu wa Wizara ya Elimu pamoja na uongozi wa Shule ya Tanganyika wamefika hapa!”
“Kufanya nini?”
“Ni kuhusu Genesis!”
“Amefanyaje?”
“Wanataka asome katika shule yenye kiwango kikubwa!”
“Ni hilo tu!”
“Ndiyo, kwani vipi?”
“Hakuna tatizo, ahsante!” Dk. Mkambila hakutaka kuuliza maswali zaidi, alichokifanya ni kuingia ndani moja kwa moja. Tayari wasiwasi aliokuwa nao ulishaondoka!
Alipomkuta mkewe pamoja na mwanaye wameketi sebuleni, alifurahi sana, akawakumbatia kwa furaha, kisha akaketi. Mke wake akaonyesha tabasamu maridhawa kabisa usoni mwake, akamwangalia mume wake kisha akawageukia wale watu na kuwaangalia kwa zamu kabla hajaongea.
“Jamani, huyu ndiye mume wangu mpenzi. Anaitwa Dk. Albert Mkambila, ndiye baba wa mwanangu Genesis!” Akawaambia huku akitabasamu.
“Tumefurahi sana kumfahamu!” Wakasema.
“Hata mimi pia!” Mkambila naye akasema. Baada ya hapo Blandina akamgeukia mumewe huku akitabasamu, ni wazi kuwa alikuwa na jambo alilotaka kumwambia.
“Mume wangu mpenzi, hawa ni wageni wetu, kutoka Wizara ya Elimu na Shule ya Kimataifa ya Tanganyika!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Oh! Nimefurahi sana kupata ugeni wao!”
Wote wakatabasamu. Baada ya muda, wakamweleza kila kitu, Mkambila, ni kama walikuwa wamechelewa kumweleza, Mkambila alifurahi sana na hakupingana na maombi yao.
“Hata mimi nilikuwa na wazo hilo, hakuna tatizo!” Mkambila akajibu.
Ilikuwa furaha sana nyumbani kwake, kila mmoja aliungana na wazo hilo, kila kitu kikawa katika mipango iliyofikiriwa awali! Wageni wakaondoka, akabaki Genesis, Blandina na Mkambila.
“Mwanangu Genesis sasa unarudi kusoma katika shule bora tena!” Blandina akamwambia mwanaye.
“Sawa, lakini...”
“Lakini nini?” Mkambila akadakia.
Genesis hakujibu, kilichofuata ilikuwa ni kimya cha muda mfupi, kisha baadaye machozi yakaanza kumiminika machoni mwake.
“Genesis kuna nini mwanangu?” Blandina akauliza. Genesis hakujibu, akaendelea kulia. Hawakuweza kuelewa tatizo lililompata.
****
Machozi katika maisha yao, ni kitu kilichosahaulika kwa muda mrefu wakati huo, kila kitu kwao kilikuwa ni furaha, waliishi maisha ya amani huku furaha ikiwa imechukua nafasi kubwa katika familia yao! Lakini siku hiyo Genesis alileta simanzi, simanzi ambayo ilishatoka katika familia yao.
Genesis hakuongea kitu chochote zaidi ya kuendelea kulia! Hakuna aliyefahamu sababu ya yeye kulia, tena mfululizo! Hata alipotakiwa kueleza sababu, jibu lake lilikuwa ni kuendelea kulia.
Blandina na mumewe wakabaki wakiwa na maswali mengi vichwani mwao, kwa haraka walidhani Genesis hakuwa tayari kuendelea na masomo. Wakaangaliana kwa macho yenye kuonyesha wasiwasi wa jambo fulani.
“Genesis mwanangu una nini?” Blandina akauliza.
“Mama niache!”
“Sikiliza mwanangu mpenzi, wewe ndiye tegemeo letu, si unajua hatuna mwingine zaidi yako! Kulia kwako, kunamaanisha na sisi tuanze kulia. Tueleze kuna matatizo gani?” Dk. Mkambila akamwambia Genesis.
“Au hutaki kwenda shule?” Blandina akadakia.
“Hapana...”
"Sasa kumbe nini?"
"Kuna jambo linalonisumbua kwa muda mrefu sasa!"
"Jambo gani hilo?" Blandina akauliza.
"Mnajua..."
"Tunajua?"
"Ndio!"
"Kivipi mbona hatukuelewi?"
"Mnanielewa. Naomba mniambie ukweli wa jambo moja!"
"Sema tu, tunakusikiliza!"
"Nataka kufahamu kuhusu baba yangu! Sitakwenda shule bila kumfahamu baba yangu, mnadhani sifahamu, lakini najua vizuri kuwa Dk. Mkambila siyo baba yangu wa kunizaa, ni baba wa kufikia! Nataka kumfahamu baba yangu halisi!" Wakati Genesis akisema maneno hayo, machozi mfululizo yalitiririka machoni mwake.
Hakuna aliyeweza kutoa jibu la moja kwa moja. Wote wakainamisha vichwa vyao chini, simanzi ikatawala mioyo yao, ni jambo ambalo Blandina hakutaka kukumbushwa kabisa.
"Mwanangu baba yako ni mtu mbaya sana, huna haja ya kumfahamu, huyu ndiye baba yako kwa sababu amekukubali ulivyo na ametuokoa katika mateso!"
"Najua...lakini nataka kumfahamu tu!"
"Sipendi umjue, angekuwa anakupenda na kukujali kama wewe, angekutafuta, lakini kwa kuwa ni kinyume chake, achana naye, usiweke kumbukumbu zako kwake!"
"Lakini mama nina haki ya kumfahamu!"
"Ni kweli mwanangu, ila..."
"Ila nini, niambieni ukweli kuhusu baba yangu!"
"Hivyo tu?" Blandina akamwuliza.
"Ndiyo!"
"Lakini mwanangu, ni mapema sana wewe kujua mambo haya!"
"Kwanini?"
“Wewe ni mdogo sana kufahamu mambo haya!”
“Nani kasema? Kama mnaniambia, niambieni, kama hamtaki pia mniambie!”
Blandina hakuwa mbishi tena, akaamua kumweleza ukweli wa kila kitu. Hakutaka kumficha, akamweleza kuanzia mwanzo alivyokuwa na uhusiano na Gerald mpaka alipokutana na Dk. Othman (Mkambila).
Hakuna kitu alichofanya siri, alimweleza pia kuhusu Gerald alivyomfanyia ukatili kwa kumfanyisha mapenzi na Abedayo, ambaye alimsababishia ujauzito! Baada ya kuzaliwa Genesis akiwa katika hali mbaya akamkataa. Muda wote Blandina aliokuwa akisimulia alikuwa akilia machozi!
Dk. Mkambila naye hakuweza kuvumilia uchungu aliokuwa nao moyoni mwake, naye alikuwa akilia kama mtoto mdogo! Wakati Blandina anaendelea kusimulia, alipofikia mahali akasema, Adebayo alimkataa, machozi ya Genesis yakaongezeka!
“Inatosha mama, usiendelee kunisimulia zaidi!”
“Kwanini?”
“Inatosha mama. Sihitaji kumfahamu mtu huyo zaidi ya hapo, yaani alinikataa?”
“Ndiyo maana nilikuambia kuanzia mwanzo kuwa mtu huyo hutakiwi kumfahamu kabisa!”
“Sasa nimeamini mama, wewe ni mama yangu, na huyu ni baba yangu, nyie ni wazazi wangu halisi, nashukuru kwa kuwa naamini kuwa mnanipenda, nawapenda pia!” Wote wakakumbatiana kwa furaha.
Wakaendelea na mazungumzo mengine, wakipanga jinsi ya kuishi maisha yao kwa furaha. Hakuna aliyehoji wala kutaka kusikia habari za Abedayo tena, kwao alikuwa mtu mbaya asiyepaswa kuzungumzwa kabisa na familia hiyo.
“Mama muda unakwenda, hivi kuna nini jikoni?” Genesis akauliza.
“Usijali mwanangu, nilishapika kitambo, lakini nataka kukuliza swali moja!”
“Uliza tu, mama!”
“Shule utakwenda?”
“Uliza swali lingine, hilo lina jibu lake!” Wote wakacheka.
Blandina akaingia jikoni, kisha akaandaa chakula mezani na kujumuika na familia nzima kula kwa furaha. Maisha yakaendelea kuwa matamu kwao, machungu, huzuni na machozi kwao vilitoweka.
*********
Upasuaji aliofanyiwa nchini Japan, ulimsaidia kwa kiwango kikubwa sana kuweka sura ya Genesis vizuri, ingawa haikuwa nzuri sana. Tatizo alilobaki nalo ni la kudumaa! Alionekana mdogo sana, lakini umri wake ulikuwa mkubwa, uwezo wake pia wa kuelewa mambo uliwachanganya watu.
Wiki ya kwanza tu, aliyoingia darasani katika Shule ya Kimataifa ya Tanganyika, alifanya maajabu makubwa. Mwezi mmoja baadaye akarukishwa madarasa! Vitu vingi alikuwa akivifahamu kabla ya kufundishwa, ndani ya mwaka mmoja alishavukishwa mpaka darasa la saba! Mtihani wa mwisho alifaulu masomo yote vizuri! Hakuna swali hata moja alilokosa!
Alishika nafasi ya kwanza Tanzania nzima, rais akaagiza Genesis na wenzake walioshika kumi bora kwenda Ikulu kwa ajili ya tafrija fupi ya pongezi. Kila mtu alishikwa na butwaa kuona uwezo mkuwa aliokuwa nao Genesis, kuweza kushika nafasi ya kwanza, tena msichana ilikuwa maajabu sana kwao!
“Huyu mtoto ana uwezo wa ajabu sana, hawezi kuendelea kusoma hapa!” Balozi wa Japan, alimwambia rais.
“Kwanini?”
“Anahitaji kuulizwa anapenda kufanya nini ili apelekwe katika vyuo maalum ka ajili ya kusomea fani anayoipenda!”
“Wazo zuri sana, lazima tuzungumze naye, unadhani akasomee nchi gani?”
“Kwa kuwa ana uwezo mzuri katika somo la Sayansi, nadhani ni bora akasomee kompyuta!”
“Wapi?”
“Japan...nitashughulikia kila kitu mimi!”
“Sawa basi, wacha tuzungumze naye kwanza!” Ndivyo ilivyokuwa, hapakuwa na kitu cha kufanya zaidi ya kuagiza aitwe kwa ajili ya mazungumzo zaidi.
Kitu kilichowashangaza, ni kwamba baada ya kumuuliza juu ya kompyuta alikubali haraka na tayari alikuwa na vitu vingine anavyovifahamu juu ya kompyuta!
“Napenda sana, naweza pia, ningependa kusomea fani hiyo!”
“Basi hakuna tabu, wiki moja kutoka sasa, utajulishwa, mipango inaendelea!”
“Ahsante sana!”
Baadaye wazazi wa Genesis wakaitwa Ikulu, wakapewa taarifa hiyo, hakuna aliyepingana nao. Sherehe ikafikia ukingoni, watu wakatawanyika. Kwa Blandina kila kitu kilikuwa kama miujiza.
“Mwanagu wewe ndio faraja yangu, unanipa heshima, najivunia sana kuwa na wewe!” Blandina akamwambia Genesis.
“Ni kweli mama, lakini unapaswa kumshukuru Mungu zaidi kuliko mimi!”
“Ni kweli mwanangu, na tumshukuru Mungu pamoja!”
“Amen!”
*********
Wiki moja baadaye wakapokea simu kutoka Ofisi ya Rais, wakapewa taarifa iliyowafurahisha sana, mipango ya safari ya chuo ilishakamilika, alitakiwa kwenda nchini Japan, kwa ajili ya mafunzo malum ya kumpyuta.
Siku tatu baadaye kila kitu kilikuwa sawa, Blandina, Dk. Mkambila na Genesis wakaingia katika gari kisha safari ya kwenda Uwanja wa Ndege ikaanza. Wakiwa wanasubiri muda wa kuondoka ili Genesis aingie kwenye ndege, Dk. Mkambila na mkewe walikuwa hawaishi kumsihi Genesis akasome kwa bidii, walijua hapakuwa na msaada mwingine wowote zaidi ya elimu.
“Ukasome kwa bidii mwanangu!”
“Najua mama, nina wajibu wa kufanya hivyo, hakika sitawaangusha!”
“Tunashukuru sana kusikia hivyo, masomo mema!”
“Nawashukuru wote pia, lakini nitawamisi sana jamani!”
“Lazima ukubaliane na jambo hilo mwanangu!”
“Nitajitahidi!”
Muda wa kuingia kwenye chumba malum cha ukaguzi kabla ya kuingia kwenye ndege ukafika, Genesis hakuwa na kitu cha kufanya, ilikuwa lazima aondoke. Alichokifanya ni kuwakumbatia wazazi wake kisha akawabusu na kuwaaga. Blandina alishindwa kuvumilia, alijikuta akitokwa na machozi machoni mwake.
“Nitawezaje kuishi bila wewe?” Blandina akamwambia Genesis.
“Usijali mama, safari sio kifo, ni kwa ajili ya masomo tu, Mungu akipenda tutaonana!”
“Nashukuru kusikia hivyo mwanangu!” Moyo wa Blandina ukawa mzito ghafla, kuna wakati alikuwa akifikiria kuhairisha safari ya mwanaye, alihisi kama alikuwa akikifuata kifo chake. Hata yeye alishindwa kuelewa sababu ya hisia hizo kuingia moyoni mwake.
“Baba Genesis, au arudi tu!”
“Nani?”
“Genesis!”
“Unamaanisha nini?”
“Asisafiri tena!”
“Kwanini?”
“Moyo wangu unakuwa mzito!”
“Achana na mawazo hayo, mwache mtoto akasome!”
“Mh! Lakini...”
“Hakuna cha lakini!” Blandina hakuwa na maswali zaidi, akakubali matokeo, wote wakampungia mkono alipokuwa akipanda ngazi kuingia kwenye ndege. Baada ya muda mfupi ndege ikaruka! Blandina akaendelea kuipungia ndege mpaka ilipopotelea mawinguni, hakujali kama alikuwa akimuona au hakumuona. Blandina na Dk. Mkambila wakarudi nyumbani, Genesis akawa angani kwa safari ya kwenda Japan.
********
Genesis alifika Japan salama, akaanza masomo mara moja! Kama kawaida yake, aliwashangaza sana walimu na wanafunzi wenzake kwa uwezo mkubwa aliokuwa nao. Kila mtihani alikuwa anafaulu katika kiwango kikubwa. Kwa muda wa miezi sita tu, alishakuwa fundi mzuri wa kompyuta, pia alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kubuni programu mbalimbali za komputa.
Sifa zake zilifika mpaka Tanzania ambapo vyombo vyote vya habari vilitangaza juu ya uwezo wa ajabu wa Genesis!
Siku moja Blandina alikwenda posta kuchukua barua zao, baada ya kuzichukua, akaondoka haraka mpaka kwenye gari lake. Akaingia kisha akafunga mlango, akaanza kukagua bahasha moja baada ya nyingine ili kujua zilikuwa zimetokea wapi. Akiwa anachagua bahasha, akaona moja iliyotokea Japan. Kwanza alishtuka, haikuwa kawaida kupokea barua kutoka Japan! Mara nyingi alipigiwa simu!
Akili yake ikamwambia aifungue haraka, tayari taa nyekundu zilishaanza kuwaka akilini mwake. Kwa vyovyote kulikuwa na tatizo lililotokea!
Huku mapigo ya moyo wake yakizidisha kasi, akaaza kusoma mstari mmoja baada ya mwingine, ghafla akaukunja uso wake, akahisi kizunguzungu, kisha machozi yakaanza kulowanisha mashavu yake! Hakuamini alichokisoma. Alidhani alikosea kusoma, lakini alivyochunguza, ilikuwa sawa!
Kuna wakati alihisi alikuwa kwenye ndoto, akatingisha kichwa chake kwa nguvu, kuhakikisha kama ilikuwa yakini! Ni kweli hakuwa kwenye ndoto, alichokisoma ndivyo kilivyokuwa!
“Noooooooooooooo!” Akapiga kelele.
Genesis msichana mwenye umbile lililodumaa lakini mwenye uwezo mkubwa sana kiakili, anafanya majabu katika masomo yake kiasi cha kupata afasi ya kwenda kusomea Kompyuta nchini Japan. Akiwa huko, anaonyesha maajabu katika kunasa masomo aliyokuwa akifundishwa.
Wazazi wake walipata taarifa zote juu ya maendeleo ya mtoto wao, yalikuwa matokeo yaliyowafurahisha sana. Siku moja Blandina alikwenda Posta kuangalia barua, baada ya kuzichukua na kwenda garini, akaona moja iliyotoka Japan. Ni barua iliyomshawishi aifungue haraka na kuanza kuisoma.
Alipomaliza kuisoma barua hiyo, machozi yalianza kumtoka machoni mwake. Nini kimeandikwa kwenye barua hiyo? SONGA NAYO...
Historia ya Blandina (Halima) ilihuzunisha sana, kila alipokumbuka mambo aliyofanyiwa na Gerald, alikosa raha kabisa, alikuwa mwanaume mbaya sana katika maisha yake, alimfananisha na nyoka na siku zote alimlaani! Kila alipojitahidi kumsahau alishindwa kwa sababu kila alipomwangalia mwanaye Genesis, picha nzima ya tukio la kubakwa na Abedayo lilijirudia upya akilini mwake.
Gerald alikuwa mtu hatari sana katika maisha yake! Maisha yake yaliharibiwa na mwanaume huyo ambaye alimwachia majeraha makali katika moyo wake. Machozi yakazidi kumtoka kila alipoendelea kusoma barua iliyotokea Japan. Hakuweza kuamini kilitokea chuoni alipokuwa akisoma Genesis.
Barua hiyo iliyoandikwa na Mkuu wa Chuo, ilikuwa ikieleza kuwa Genesis amehitimu masomo yake na kupata alama za juu kuliko wanafunzi wote chuoni hapo, kwa hiyo alipata ofa ya mkataba wa kufanya kazi na kampuni kubwa ya kutengeneza Kompyuta nchini Marekani kwa miaka kumi! Hiyo ilikuwa furaha ya ajabu sana kwa Blandina. Furaha hiyo ilisababisha machozi kumtoka machoni mwake.
Aliondoka na kwenda nyumbani kwao Mikocheni ambapo mumewe alivyorudi jioni kitu cha kwanza kumweleza ilikuwa ni juu ya taarifa za Genesis kufaulu vizuri sana mtihani wake wa mwisho.
“Nilishindwa kuamini mpenzi!”
“Kwanini?”
“Ni maajabu mpenzi wangu, lakini namshukuru Mungu kwa kunipigania!”
“Kwa hiyo, umesema amepata alama nyingi zaidi ya wanafunzi wote chuoni?” Dk. Mkambila akauliza.
“Huo ndiyo ukweli!”
“Ukweli ambao nashangaa sijui ni kwanini nashindwa kuuamini!”
“Ngoja kidogo…” Blandina akatoka moja kwa moja na kwenda chumbani ambapo alichambua barua alizozihifadhi kwenye kabati kisha akarudi akiwa na moja mkononi mwake.
“Hiyo hapo, soma uone mwenyewe!” Blandina akamwambia mumewe kisha akamkadhi bahasha iliyokuwa na barua kutoka Japan.
Dk. Mkambila alionekana kutoamini kabisa alichokisoma kwenye barua, alirudia zaidi ya mara tatu kusoma ili kuhakikisha kama alichokuwa akisoma kilikuwa yakini. Ni kweli alikuwa akisoma kitu yakini kisicho na chembe ya maruweruwe!
“Yah! Ni kweli kabisa, lakini nimeudhika na kitu kimoja!”
“Kitu gani mpenzi?”
“Hawakumpangia muda wa kuja kupumzika kwanza nyumbani!”
“Hilo sio tatizo, furaha yetu ni yeye kupata ajira tena inayoeleweka!”
“Ni kweli!”
Furaha ikaendelea kutawala katika maisha yao, wakamshukuru Mungu kutokana na mambo makuu aliyowatendea katika familia yao. Machozi ya Blandina sasa yalifutika! Alimshukuru Mungu kumkutanisha na mwanaume mvumilivu kama Dk. Mkambila.
*********
Tangu siku ya kwanza tu, alipoingia ofisini kwake katika Kiwanda cha kutengeneza Kompyuta cha Techno Computers LTD, alionyesha maajabu, uwezo wake uliwashangaza wengi kwa muda mfupi tu alijikuta akijenga heshima kwa wafanyakazi wenzake na viongozi wa juu. Uwezo wake uliwashangaza wengi sana.
Alifanya kazi kwa kujiamini na aliweza kubuni progamu mbalimbali kiasi cha kuwashangaza viongozi wake wa juu. Hiyo ilitosha kabisa kumpandisha mshahara kila wakati, kwa muda wa miaka mitatu, aliyokuwa kazini alishapandishwa mishahara zaidi ya mara saba! Genesis aliendelea kumshukuru Mungu kwa kumjalia uwezo wa uelewa, aliendelea kufanya kazi kwa bidii kubwa huku lengo lake likiwa ni kujenga kiwanda kikubwa cha kompyuta nyumbani kwao Tanzania.
Siku moja asubuhi alipoingia tu kazini, akakutana na barua mezani kwake, iliyomtaka kuonana na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni! Ni barua iliyomshtua sana ingawa alijua wazi hapakuwa na kitu kibaya kilichokuwa mbele yake! Siku zote alifanya kazi kwa kuzingatia kanuni na alipendwa na kila mtu kazini kwao.
Alizoea wito wa aina hiyo kwa meneja wake ambaye alimtegemea sana katika kurekebisha matatizo madogo madogo ya kiufundi. Hakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kuondoka na kwenda moja kwa moja mpaka ofisini kwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni.
“Karibu Genesis!” Mkurugenzi alimkaribisha baada ya kuingia ofisini kwake.
“Nashukuru shikamoo...”
“Mar-haba, habari za kazi?”
“Nzuri sana!”
“Hata mimi naona ni nzuri sana, nimekuita kwa jambo moja muhimu!”
“Jambo gani hilo?”
“Usijali, ni jambo jema tu, lakini kubwa zaidi ni kukupongeza!”
“Nashukuru kusikia hivyo!”
“Unafanya kazi zako vizuri sana, sasa kwa kuwa Kampuni imeona uwezo wako ni mkubwa, tumeamua kukupandisha cheo! Kuanzia sasa utakuwa Mkuu wa Kitengo cha ubunifu wa progaramu hapa kiwandani, barua yako inakuja baada ya muda kidogo!”
“Nakushukuru sana Mkurugenzi, ahsante!”
“Usijali binti, ni haki yako, una kipaji cha ajabu sana!”
“Nashukuru kusikia hivyo!”
“Kazi njema!”
“Nawe pia!”
Zilikuwa habari za kufurahisha sana, kwa Genesis, aliona mipango yake inazidi kwenda vizuri, hakusita kuendelea kumshukuru Mungu kutokana na maajabu aliyokuwa akimfanyia katika maisha yake, ilikuwa yakini lakini ilimchukua muda mrefu sana kuamini kilichotokea!
“Nakushukuru sana Mungu wangu, najua haya yote unayafanya kwa makusudi maalum!” Aliwaza akilini mwake.
Wazo la kufungua kiwanda kikubwa cha Kompyuta nchini Tanzania likaingia kwa kasi sana akilini mwake, alitamani kumiliki kiwanda nyumbani kwao, aliamini angeweza kuipatia heshima kubwa serikali yake na kujenga heshima katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.
“Lazima siku moja nitakuwa na kiwanda nyumbani Tanzania, lazima...” Wazo hilo liliendelea kujirudia akilini mwake.
*********
MIAKA SABA BAADAYE
Kila kitu kilichoendelea nchini Marekani Blandina na Dk. Mkambila walikuwa wakipata taarifa zote! Waliona ni miujiza ya ajabu sana iliyokuwa ikitokea katika maisha yao, siku zote walimuombea mtoto wao apate mafanikio makubwa katika kazi yake.
Wazo la kufungua kiwanda cha Kompyuta nchini Tanzania, walikubaliana nalo kwa asilimia zote, mipango ikafanyika taratibu, Genesis akiwa nchini Marekani, alituma fedha kwa ajili ya kununua eneo kubwa linalotosha kujenga kiwanda. Haikuwa kazi kubwa, Dk. Mkambila akampa tenda Mkandarasi aliyeitwa Mr. Tulo, ambapo kiwanja kilipatikana katika eneo la Mbagala na ujenzi ukaanza mara moja!
Genesis alituma ramani kupitia waraka pepe, ambapo Mr. Tulo alianza usimamizi haraka iwezekanavyo. Baada ya mwaka mmoja kila kitu kilikuwa tayari, Genesis akatumiwa picha za kiwanda chake, aliporidhika akaacha kazi Marekani kisha akaenda nchini Tanzania kwa ajili ya kufungua kiwanda chake. Kilikuwa kiwanda cha kihistoria nchini Tanzania. Hakuna aliyewahi kufungua kiwanda cha kutengeneza Kompyuta na Programu zake Afrika Mashariki nzima, Genesis alikuwa wa kwanza.
Mgeni rasmi katika ufunguzi wa kiwanda chake alikuwa ni rais wa nchi ambaye aliongozana na Balozi wa Japan. Sherehe ya ufunguzi ilipoisha alirudi nyumbani kwao, huku mipango ya kuanza kazi mara moja ikiwa inaendelea.
“Wewe ni shujaa mwanangu!” Blandina alimwambia mwanaye siku moja walipokuwa mezani wakipata chakula cha jioni.
“Kwanini mama?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Umeniletea heshima mwanangu, wewe ni mwanamke wa pekee!”
“Usijali mama, lakini nina wazo lingine!”
“Wazo gani?”
“Nahitaji kuwajengea nyumba nyingine nzuri zaidi ya hii, halafu pia nataka kuwahamisha bibi na babu kule wanapoishi, huu sio wakati wa kupata mateso wakati uwezo wa fedha ninao. Nina imani utajiri wangu ni kwa ajili ya ukoo wetu wote!”
“Ni kweli kabisa mwanangu, hilo halina ubishi!” Ndivyo ilivyofanyika, kila kitu kilifanyika haraka haraka, miezi mitatu tu, ilitosha kusimamisha nyumba mbili kubwa za kisasa ambazo, moja walihamia bibi na babu wa Genesis na nyingine walihamia yeye na wazazi wake.
Kiwanda kikaanza kufanya kazi, sifa zake zikaenea kila mahali Tanzania na nchi za jirani za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Maisha yao yakabadilika, wazazi wake wakastaafu kazi, lakini waliendelea kufurahia maisha, baada ya Genesis kuwaokoa na utajiri wake.
Jumapili moja jioni, familia nzima ilikuwa sebuleni wakizungumza, kila mmoja alikuwa akionyesha sura iliyojaa furaha, hakuna aliyekuwa na uso uliokunjamana, maisha yao yalijawa na furaha na amani tupu. Ghafla simu ya mezani ikaita, ilikuwa ikitokea kwa mlinzi getini.
“Unasemaje Jamali?” Blandina ndiye aliyepokea simu.
“Kuna mgeni wako mama!”
“Anaitwa nani?”
“Abedayo!”
“Nani?”
“Abedayo!”
“Mwambie aondoke haraka sana nyumbani kwangu!” Akasema kwa hasira kisha akakata simu, Hakuna aliyeelewa ni kwanini alijibu kwa hasira kiasi hicho na kukata simu. Uso wake ulionyesha wazi kuwa na hasira.
“Mama ni nani huyo?” Genesis akauliza.
“Huna haja ya kumfahamu!” Baada ya kumjibu tu, mwanaye simu ikaita kwa mara nyingine, akaamua kuipokea, alikuwa ni mlinzi wa getini amempigia kwa mara nyingine.
“Ameshaondoka?” Blandina akauliza.
“Hajaondoka na amesema hawezi kuondoka kabla hajajua utaratibu wake na mwanaye Genesis unavyoenda!” Mlinzi alimwambia. Ni maneno yaliyoingia sawasawa masikioni mwake na kupenya mpaka ubongoni, lakini yalisababisha hasira kali sana moyoni mwake.
Picha nzima ya siku aliyobakwa na Adebayo ikamjia, akaanza kutetemeka kwa hasira, kisha akafungua mlango na kutoka nje.
“Mama kuna nini?” Genesis akauliza.
“Niache...”
****
Siku Abedayo aliyombaka Blandina ikajirudia upya, ilikuwa siku mbaya sana katika maisha yake, alishasahau kabisa mtu anayeitwa Abedayo, lakini sasa picha nzima ilijirudia! Machozi yakaanza kumtoka machoni mwake mithili ya maji ya mfereji.
Kwa kasi ya ajabu akatoka nje kwa ajiili ya kwenda getini kwenda kupambana naye, alikuwa mwanaume ambaye alimpa machungu na mateso makali sana katika maisha yake, hakuwa tayari kumsikiliza kwa jambo lolote, hakuwa na thamani tena katika maisha yake. Alikuwa mwanaume katili kuliko wote aliowahi kukutana nao maishani.
Dk. Mkambila alijua wazi kuwa kulikuwa na kitu kibaya ambacho kingetokea mbele ya Blandina, hakuwa tayari kukabiliana na matatizo, alichokifanya ni kuamka haraka na kumfuata Blandina aliyekuwa akikaribia kufika getini.
“Blandina, naomba urudi tafadhali!”
“Siwezi, siwezi kurudi!”
“Kwanini?”
“Huyu ndiyo chanzo cha maisha yangu kuharibika, nimepata mateso akiwa hajui, leo hii anakuja kuulizia mwanaye, hivi ana kaili kweli?”
“Usiseme hivyo mpenzi wangu, kumbuka sisi ni watu wazima sasa, na siku zote mambo kama haya humalizika kwa mazungumzo na sio hasira, kwanini usirudi ndani tukamwita kwa ajili ya mazungumzo?”
“Mazungumzo?”
“Ndiyo?”
“Siwezi kuzungumza na huyo mpuuzi!”
“Sawa basi, lakini naomba urudi ndani!”
“Twende!”
Wakarudi kwa pamoja mpaka ndani, walipofika sebuleni, Dk. Mkambila akamvuta Blandina chumbani, hakubisha, wakaingia.
“Mke wangu sisi ni watu wazima sasa, hatuna haja ya kujiabisha, kama umeshafahamu kuwa mtu hana nia nzuri na wewe ni bora ukaachana naye!”
“Sawa nimekuelewa!”
Wakaendelea kuzungumza mambo mengine ya maisha yao, dakika kumi na tano baadaye, Blandina akatoka sebuleni. Akili yake ilishafanya kazi zaidi ya uwezo wake, alishapata kitu cha kufanya!
“Unakwenda wapi?”
“Mume wangu jamani, nakwenda kuzungumza na mtoto sebuleni!”
“Sawa, wacha mimi nipumzike!”
“Hakuna shida mume wangu!”
Alivyofika tu, sebuleni akapiga simu kwa mlinzi, alitaka kujua kama Abedayo bado alikuwa anamsubiri, akili yake ilimtuma amwagize mwanaye akazungumze naye. Aliamini kwa kufanya angeweza kuibuka mshindi. Akili yake ilifanya kazi kama umeme, alijua ni kitu gani Abedayo alikuwa akikitaka kutoka kwa mtoto wake, hapakuwa na kitu kingine zaidi ya utajiri! Ni utajiri pekee ndiyo uliokuwa ukimfanya Abedayo ajitokeze nyakati za mwisho akidai Genesis alikuwa ni mwanaye.
Kwa mateso aliyompa katika maisha yake, alimfananisha na mnyama, tena hakustahili kabisa kuonja hata senti moja ya utajiri wa mwanaye. Ni yeye peke yake ndiye aliyehangaika na mwananye mpaka kufikia mafanikio aliyokuwa nayo, mwingine ambaye alionyesha moyo wa dhati alikuwa ni Dk. Mkambila. Akachukua mkonge wa simu kisha akabonyeza namba za kibandani kwa mlinzi.
“Bado yupo?”
“Ndiyo!”
“Anataka nini lakini?”
“Kama nilivyokuambia mwanzo!”
“Kwamba?”
“Anataka kujua mustakabali wa mwanaye!”
“Umemuuliza mwanaye anayemuulizia ni nani?”
“Ndiyo!”
“Akasema ni nani?”
“Genesis!” Balndiana alihisi kizunguzungu baada ya kusikia kauli hiyo kutoka kwa mlinzi. Hasira zikampanda maradufu, alihisi kuua!
“Sikiliza, ingia naye, lakini mfikishe kwenye nyumba ya wageni, baada ya hapo nipigie simu!”
“Sawa mama!”
Ndivyo ilivyokuwa, baada ya kukata simu tu, mlinzi akamruhusu Adebayo aingie ndani. Kwake ulikuwa mwanzo mzuri, hakujua kuwa alikuwa akifuata matatizo! Macho yake yalikutana na nyumba nzuri ya kifahari, nje kulikuwa na bwawa la kuogelea, bustani nzuri na mabanda ya mifugo.
Kwa kuangalia tu, alijuwa wazi kuwa Blandina alikuwa akiishi maisha ya kifahari sana. Nyumba ya wageni ilikuwa mwanzoni kabisa baada ya kuingia getini, ilikuwa nyumba ndogo iliyokuwa na kila kitu ndani. Sebule ya kisasa na vyumba vya kulala sita!
Wageni wote ilikuwa lazima waishie hapo kwanza kabla ya kuingia ndani kwa Blandina. Waliishi maisha ya kisasa sana! Abedayo alishangaa sana kuiona nyumba iliyoitwa ya wageni ikiwa katika hadhi ya juu kiasi kile, kila kitu kilikuwa ndani, kulikuwa na sehemu malumu ya kuhifadhia vinywaji vya kila aina. Wahudumu wawili kwa ajili ya kazi hiyo waliajiriwa!
Ni maisha ambayo Abedayo hakuwaza kama siku moja angeishi, lakini kwa wakati huo aliamini kulikuwa na uwezekano mkubwa sana wa yeye kuishi katika nyumba hiyo. Mlinzi akamwangalia kwa macho ya udadisi kisha akampa taratibu za kuwepo katika nyumba hiyo.
“Mkubwa!”
“Naam!”
“Upo katika nyumba ya Bwana na Bibi Albert Mkambila, lazima ufuate taratibu za hapa, vinginevyo utakuwa mahali pabaya!”
“Kwanini unasema hivyo?”
“Kwa sababu unaonekana una matatizo!”
“Kijana fanya kazi yako, na sio kunikashfu!”
“Ninachokuambia ni sehemu ya kazi yangu!”
“Kuwa?”
“Ukae hapo ulipo kwa utulivu, wahudumu watakusikiza kwa kila kitu, kuanzia vinywaji na vipindi uvipendavyo kwenye Stesheni za Redio na Televisheni!”
“Ok!” Abedayo akajibu, hakuwa na jinsi, ilikuwa lazima akubaliane na masharti aliyopewa. Dakika moja haikupita, msichana mmoja mrembo aliyejitambulisa kwa jina la Tatu alifika alipokuwa amekaa! Alikuwa msichana ambaye alikuwa na kila aina ya sifa anazotakiwa kuwa nazo msichana mrembo.
“Habari yako?”
“Salama zako je?”
“Njema pia, naomba nikuhudumie!”
“Maji ya mataunda yanatosha!”
“Matunda gani?’
“Maembe!”
“Hakuna tabu, nakutayarishia, baada ya dakika kumi na tano itakuwa tayari!”
“Hakuna tabu!” Kila kitu kilikuwa kigeni kwa Abedayo, pamoja na kutembelea sehemu mbalimbai na uwezo mkubwa wa fedha aliowahi kuwa nao, lakini kwa Blandina alitulia! Hapo sasa alikiri kuwa kweli pesa ilikuwa na kiburi kibaya sana!
Robo saa baadaye bilauri lenye maji ya matunda ya maembe pamoja na glasi kubwa iliyochongoka chini vilikuwa mezani kwake.
“Karibu ufurahie kinywaji!”
“Ahsante sana dada!” Hazikuisha dakika mbili baada ya kupewa juisi, Genesis akaingia katika nyumba hiyo ya wageni, uso wake hakuonyesha furaha hata kidogo.
“Shikamoo mzee!” Alimsalimia kabla ya kuketi kwenye sofa kubwa.
“Mar-haba binti, hujambo?”
“Sijambo, naomba nikusaidie!”
“Nashukuru!” Abedayo akajibu huku woga ukiwa umemjaa usoni mwake.
“Nakusikiliza!”
“Unanifahamu mimi?” Abedayo akauliza.
“Hapana... kwani wewe ni nani?”
“Mimi naitwa Abedayo, hujawahi kusikia jina hilo?”
“Nimewahi, kwahiyo unasemaje?”
“Sikiliza...mbona sikuelewi, wewe si ni Genesis?”
“Ndiyo mimi?”
“Sasa hujui kuwa mimi ni b....” Kabla hamalizia kauli yake, tayari Blandina alishaingia katika nyumba hiyo. Alikuwa amevimba kwa hasira. Alivyofika, hata kukaa hakutaka, akashika kiuno chake kwa mbwembwe kisha akamwangalia kwa hasira sana.
“Unataka nini kwangu wewe?”
“Mwanangu!”
“Nini?”
“Mwanangu!”
“Una mtoto hapa wewe, hebu ondoka kabisa katika nyumba yangu, mateso uliyonipa ni makubwa sana ambayo siwezi kuyaelezea kabisa!”
“Hata kama, lakini huu ni muda wa kukaa na kuzungumza na sio kurushiana maneno!”
“Ungekuwa unajua hilo, usingefanya uliyonifanyia!”
Mzozo ulikuwa mkubwa sana, kiasi Dk. Mkambila alisikia kelele, akaamka na kwenda katika nyumba ya wageni.
“Mama Genesis kuna nini mke wangu?”
Kuna huyu mjinga-mjinga hapa anafanya fujo hapa nyumbani!”
“Anaitwa nani?”
“Adebayo!”
“Hebu sogeeni pembeni!” Dk. Mkambila akasema kisha akamsogelea Abedayo akiwa amekunja uso wake kwa hasira.
“Nakuomba uondoke nyumbani kwangu haraka sana!”
“Siondoki!”
“Unasemaje?”
“Siondoki!”
“Sasa, endelea kusubiri uone!” Dk. Mkambila akaondoka kwa hasira, akakimbilia katika nyumba kubwa. Dakika moja na sekunde kadhaa baadaye alirudi akiwa na bastola mkononi mwake.
“Sogeeni hapo nimmalize!” Akasema kwa hasira kisha mlio wa risasi ukasikika Paaaaaaaaaaa!
Abedayo akapiga kelele!
****
Dk. Mkambila alikuwa na hasira sana, hakutaka kuona Genesis akichukuliwa kirahisi, kitendo cha Abedayo kung’ang’ania kuwa Genesis alikuwa mwanaye kilimuuma sana, hakutaka kumpa nafasi hiyo. Alimfananisha na mnafiki. Kwa maisha ya shida aliyoishi Genesis bila msaada wa Abedayo aliona hakustahili kabisa kula matunda ya Genesis.
Adhabu pekee ambayo aliona ilikuwa ikimfaa ilikuwa ni kifo! Alidhamiria kumuua, hakufanya makosa akakimbia ndani haraka kisha akachukua bastola yake na kurudi katika nyumba hiyo ya wageni. Hasira aliyokuwa nayo haikuweza kufananishwa na kitu chochote! Tayari moyo wake ulishaingia doa, kilichokuwa mbele yake ilikuwa kumuondoa Abedayo duniani!
Akanyanyua mkono wake kisha akahakikisha risasi imesogea mdomoni mwa bastora, baada ya hapo akaingiza kidole chake katika sehemu ya kufyatulia, kisha akafyatua risasi. Kiasi cha sekunde thelathini Blandina aliupiga mkono wa baba yake risasi ikatua ukutani badala ya mwili wa Abedayo.
“Kwanini unafanya hivyo?”
“Hapana baba usimuue tafadhali!” Genesis akasema.
“huyu anastahili kifo!”
“Kwanini?”
“Hawezi kuja kutuharibia amani kwenye nyumba yetu, wakati ulipokuwa unateseka alikuwa hayupo, hakukujali wala hakujua kama wewe ni mwanaye, alikuchukia wewe na mama yako. Mkaishi maisha ya shida bila msaada wowote , leo tuna maisha mazuri ndio anasema yeye ni baba yako tena aondoke hapa!” Dk mkambila alisema kwa hasira huku akitetemeka, mara moja akatoka akifuata bastola iliyodondoka chini.
Blandina alishahisi matatizo, alijua wazi kulikuwa na dalili mbaya mbele yao, ni jambo ambalo hakutaka litokee.
“Genesis !” Blandina aliita huku akiwa amemshika Dk. Mkambila.
“Abee mama!”
“Chukua hiyo bastola nenda kaifiche ndani!”
Genesis hakuongea kitu chochote zaidi ya kuokota bastola na kuondoka moja kwa moja kukimbilia kwenye nyumba kubwa. Alipofika huko akaingia chumbani kwake kisha akaiweka bastola uvunguni mwa kitanda chake, baada aya hapo akarudi mbio mpaka walipokuwa wazazi wake.
“Baba...”
“ Unasemaje?”
“Bado tunakupenda sana!”
“Najua mwanangu!”
“Sasa kama unajua kwanini unataka kuua?”
“kwani nikimuua ndiyo nitakuwa sionyeshi kuwa nawapenda? Tena basi naamini kwa kumuua huyu mshenzi nitakuwa nimejitoa kwa ajili yenu nakuonyesha mapenzi ya kweli!”
“Hapana baba, Serikali ipo macho, utaozea Gerezani!”
Yalikuwa maneno makali sana yaliyowachoma wote, ghafla macho ya blandina yakabadilisha rangi yakawa mekundu, sekunde chache baadaye machozi mithili ya mfereji yakaanza kuchuruzika machoni mwake. Blandina akamsogelea Dk. Mkambila kisha akamkumbatia.
“Mume wangu mtoto ameongea mambo ya msingi sana, ni vizuri tukayazingatia!”
“Kwahiyo unasemaje?”
“Nafikiri tuzungumze naye!”
“Sawa...” Wakamkaribisha Adebayo katika nyumba kubwa, hapakuwa na njia nyingine ya kutatua tatizo lililokuwepo zaidi ya kuzungumza.
“Sasa tunazungumza pamoja, ni lazima nyote muwe wakweli sitapenda kuona mmoja kati yenu anaongea uongo!” Dk. Mkambila alisema huku akiwatupia macho kwa zamu.
“Sawa!” Wote wakaitika kwa pamoja.
Kwa ujumla ilikuwa siku mbaya sana kwa familia yao, ilikuwa Ijumaa mbaya kuliko zote zilizopata kutokea katika maisha yao. Blandina alikuwa na uchungu sana moyoni mwake, kila alipojaribu kuifuta siku aliyobakwa na Adebayo alishindwa, machozi yakazidi kutiririka machoni mwake. Alimuona mwanaume mbaya sana katika maisha yake, ni yeye ndiye aliyemsababishia matatizo katika maisha yake, hakumtamani hata mara moja!
Mazungumzo yakaanza, kilichotakiwa kujulikana ni ukweli kuhusu mtoto Genesis! Pamoja na kwamba Genesis alikuwa akifahamu kuwa Dk. Mkambila hakuwa baba yake, lakini alikuwa akifahamu wazi kuwa alikuwa na baba yake mwingine, ambaye aliambiwa kuwa alikuwa akiitwa Gerald! Kutokea kwa Abedayo kulimchanganya sana!
“Sasa wewe, kwahiyo unasema huyu mtoto ni wako sio?”
“Ndiyo!”
“Una uhakika gani?”
“Ninao, siku zote nilikuwa nafutilia maisha yenu ijapokuwa sikuwa karibu na nyie!”
“Kama ulikuwa unafuatilia na ulikuwa ukifahamu, kwanini hukuja kumtembelea mwanao?”
“Sikuwa hapa nchini!”
“Ulikuwa wapi?”
“Nigeria!”
“Sawa, sasa ukiambiwa uthibitishe kuwa huyu ni mtoto ni wako, utathibitisha vipi?”
“Nafahamu kuwa ni wangu, lakini pia kama hamuamini, twendeni hospitalini tukapime Kipimo cha Diribonucleacacid au DNA, kwa kipimo hicho tutajua ukweli juu ya uhalisi wa huyu mtoto!”
Blandina hakuwa na jibu la haraka, akaonekana akiwa kimya ghafla, hata hivyo kila alipojaribu kufikiria kwa makini, hakuweza kujua ni nani hasa kati ya Gerald na Abedayo alikuwa baba wa mtoto wake. Hilo lilisababishwa na kuwa na uhusiano na wanaume hao wawili kwa wakati mmoja.
“Kwani mtoto ni wa nani hasa?” Dk. Mkambila akauliza.
“Ukweli ni kwamba sifahamu, unajua nilikuwa nikikutana kimwili na Gerald mara nyingi, baadaye ndio wakanifanyia mchezo mchafu, sifahamu ni nani kati yao ni baba halisi wa mwanangu!”
“Ndiyo maana nikasema kuwa hilo litafahamika baada ya kufanya vipimo, kwanini hutaki kukubali?” Adebayo akasema.
“Sawa tupange siku ya kwenda kupima!”
“Sawa!” Adebayo akajibu.
Muda wote waliokuwa wakizungumza, Genesis alikuwa akilia, alitamani sana kumfahamu baba yake halisi alikuwa ni nani! Ingawa aliishi na Dk. Mkambila pamoja na mama yake kwa heshima kama wazazi wake. Lilikuwa wazo zuri lakini Dk. Mkambila alilichukulia kwa ukubwa zaidi. Akili yake ilifanya kazi zaidi ya zawaida, alikuwa na wazo jipya lililoingia akilini mwake kwa kasi.
“Suala hili sio dogo kama mnavyofikiria, lazima kitu fulani kifanyike!” Hatimaye akasema.
“Kitu gani?”
“Lazima tumshirikishe mwanasheria!”
“Ni wazo zuri sana!” Adebayo akajibu. Hakuwa mbishi wala hakupinga mawazo yanayotolewa na Dk. Mkambila au Blandina. Mipango yote ikapangwa, wakakubaliana kukutana jutatatu asubuhi kwa safari ya kwenda kwa wakili!
*********
Baada ya Adebayo kuondoka, Blandina na Dk. Mkambila walikuwa na kazi ya kumbembeleza Genesis, alikuwa akilia wakati wote, hakutamani kuendelea kuishi katika mazingira ya kutokumfahamu baba yake.
Pamoja na kubembelezwa sana, lakini hakutaka kunyamaza, aliona kama alikuwa na mkosi katika maisha yake.
“Lakini mama nahitaji kumfahamu baba yangu halisi!”
“Sawa mwanangu, hilo litafahamika baada ya vipimo kufanyika!”
“Kwa hiyo unataka kuniambia kuwa hufahamu baba yangu ni nani?”
“Swali gumu sana hilo mwanangu!”
“Ugumu wake ni nini?”
“Ni swali linalonikumbusha mbali sana, nasikia uchungu sana katika moyo wangu kutokumfahamu baba yangu!”
“Kimsingi sina uhakika ni nani baba yako halisi kati ya Gerald na Adebayo, lakini hilo litajulikana jumatatu!”
“Ok!” Genesis akajibu. Baada ya hapo aliondoka na kwenda chumbani kwake kulala. Blandina na Dk. Mkambila nao waliingia chumbani kwao kulala. Ilikuwa siku mbaya sana kwao, ni siku ambayo ingeweza kusababisha matatizo katika siku zote za maisha yao.
“Kwahiyo tutakwenda kwa wakili gani?” Blandina akamwuliza Dk. Mkambila.
“John Nondo ni wakili mzuri sana, tutampigia simu kabla ya kwenda huko!”
“Sawa!” Muda huo huo, Dk. Mkambila akachukua simu kisha akampigia Nondo simu na kumweleza ukweli juu ya kila kitu kilichotokea. Nondo akamuahidi kumsaidia.
“Mambo yatakuwa sawa mke wangu, tulale tu, usijali!”
“Hakuna tabu mpenzi!” Wakalala.
*********http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nondo Advocate & CO, ilikuwa Kampuni kubwa ya Mawakili iliyojijengea heshima kubwa sana miongoni mwa jamii. Kesi nyingi kubwa, zilikuwa zinaisha kwa usaidizi wa Kampuni hiyo. John Nondo ndiye aliyekuwa Wakili Mkuu wa Kampuni hiyo na Mkurugenzi.
Jumatatu asubuhi na mapema, Abedayo, Blandina, Dk. Mkambila na Genesis walikuwa pamoja kwa safari ya kwenda kwa wakili Nondo. Kwa bahati nzuri walifanikiwa kumkuta wakili ofisini kwake. Baada ya maelezo ya kutosha, Nondo aliwaandikia barua ya kwenda kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya kwenda kufanya kipimo cha DNA! Baada ya kipimo hicho ukweli ungekuwa wazi.
“Nendeni na hii barua, bada ya vipimo nahitaji majibu hapa!”
“Tunashukuru sana!” Hawakuwa na kitu cha kusubiri zaidi, safari ya kwenda kwa Mkemia Mkuu ikaanza.
Walipofika walimpa barua ya Wakili kisha wakatoa maelezo mengine ya ziada. Hawakumficha kitu chochote, ingawa Blandina aliumia sana. Ilikuwa ni siri ya maisha yake ambayo siku zote hakutaka iwe hadharani. Mkemia akaelezwa kuhusu Gerald na Abedayo. Mkemia Mkuu alikuwa makini sana kumsikiliza, kisha badaye akaonekana kuwa kimya kwa muda kabla ya kuanza kuzungumza.
“Hakuna tatizo, ukweli utajulikana, lakini pia ni vizuri kama Gerald naye angepatikana!” Mkemia Mkuu akasema.
“Kwanini?”
“Tunahitaji kupata majibu ya uhakika, sasa ni lazima Gerald apatikane!”
Wote wakachanganyikiwa, hakuna aliyejua mahali alipokuwa anaishi Gerald, ni muda mrefu sana ulipita bila kuwa na mawasiliano naye. Hawakuwa na la kufanya, wakabaki wanatazamana!
*****
Kutokana na machungu aliyoyapata katika maisha yake, siku zote alimchukia sana Adebayo, alimwona ndiye chanzo cha maisha yake kuharibika! Hakutamani siku moja ibainike kuwa mtoto wake alikuwa wake, ingawa hata yeye alishindwa kufahamu ukweli kuwa kati ya Adebayo na Gerald ni nani hasa aliyekuwa baba wa mwanaye.
Kitu pekee ambacho kingeanika ukweli huo, ni kipimo cha DNA, hicho pekee ambacho kingeweka ukweli hadharani. Kila kitu sasa kiliharibika, hawakuweza kuelewa wangewezaje kumpata Gerald. Kila mmoja akaelekeza macho yake kwa Mkemia Mkuu. Adebayo ambaye alionekana alikuwa na shauku sana na kipimoi hicho, alikuwa wa kwanza kumuuliza Mkemia Mkuu.
“Lakini kwani kuna umuhimu gani hasa wa Gerald kuwepo? Inamaana kipimo changu na huyu mtoto hakitoshi kuonyesha kuwa kama ni wangu au sio wangu?”
“Inaewezekana kabisa, lakini lengo ni kutaka kupata ukweli wa moja kwa moja ambao hautakuwa na ubishi wowote!”
“Mh!” Dk. Mkambila akaguna, kisha akamgeukia Geneisis ambaye machozi machoni mwake yalikuwa yakitiririka!
“Nahitaji kumfahamu baba yangu. Kwanini asipimwe huyu kwanza ili kama siye niamini kuwa Gerald ndiye baba yangu ili nimtafute?”
“Tulia binti, kila kitu kinafanywa kwa utaratibu, sasa ni lazima Gerald apatikane kwanza. Kwani Blandina, hukuwahi kuwa na wanaume wengine zaidi ya Gerald na Adebayo?’
“Ndiyo, sikuwa na wengine ni hawa wawili tu!”
“Unadhani ni nani anaweza kuwa baba wa mtoto wako?”
“Ni swali gumu sana kwangu, hakika sipendi kukumbuka mambo yaliyopita, naamini baada ya vipimo ukweli utakuwa wazi!”
“Bila shaka, lakini hayo yote yanaweza kuwa wazi ikiwa Gerald atapatikana!” Mkemia akasema bila kuongeza neno lingine mbele yake.
Hawakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kuondoka na kurudi nyumbani. Safari yao iliishia nyumbani kwa akina Blandina. Walipofika wakaegesha gairi lao, kisha Abedayo naye akapaki gari lake na kuingia ndani.
Kwa ujumla Blandina alichukizwa sana na hali iliyojitokeza, uso wake ulionyesha hasira alizokuwa nazo. Alipofika sebuleni hakuzungumza kitu chochote zaidi ya kwenda kukaa kimya kwenye kiti cha kubembea!
“Abedayo!” Blandina aliita.
“Nakusikia!”
“Hivi kwanini unamfuata-fuata mwanangu?”
“Kwani hujui sababu?”
“Sijui, ndiyo maana nakuuliza!”
“Sababu ni moja tu!”
“Gani?”
“Genesisi ni damu yangu, ni mwanangu kwa hiyo ni lazima ifahamike hivyo!”
“Eti Genesis ni mwanao, mbona mwanzoni ulimkataa na kunikimbia? Niache na mwanangu tafadhali, mimi ndiye niliyehangaika naye mpaka kufikia sasa, wewe sema umefuata mali, lakini sio mtoto!”
“Wewe ndiyo umesema hivyo, lakini mimi nia yangu ni kumfuata mwanangu ambaye nampenda!” Yalikuwa maneno makali sana ambayo kwa hakika yalizidi kumchoma moyo Blandina, hakuwa na kitu cha kufanya ingawa moyo wake ulikuwa ukizidi kuumia.
“Sawa basi, ukweli utajulikana baada ya Gerald kupatikana!”
“Ok! Mimi nakwenda zangu!”
“Siku njema!” Abedayo akaondoka, akawaacha Blandina, Dk. Mkambila pamoja na Genesis wakiwa wameketi sebuleni. Blandina hakufurahishwa hata kidogo na kitendo cha Abedayo kumfuatilia mwanaye. Hilo liliendelea kumwumiza sana.
*********
Kama kuna mtu Blandina alikuwa akimchukia basi ni Abedayo, alikuwa na sababu nyingi sana za kumchukia, kwanza alifanya naye mapenzi bila ridhaa yake, halafu kitu kingine kichomchukiza zaidi ni kitendo chake cha kumtelekeza akiwa na mwanaye kwa kuwa alikuwa na kasoro.
Aliomba yatokee maajabu, Genesis awe mtoto wa Gerald, hilo aliendelea kumwomba Mungu siku zote! Pamoja na Gerald kumfanyia mabaya, lakini alikuwa na mema mengi pia aliyomfanyia katika maisha yake, alihisi kumpenda Gerald.
Kitu kilichofanyika ni kwenda nyumbani alipokuwa akiishi Gerald, asubuhi ya siku iliyofuata. Alipofika aliegesha gari lake nje kisha akaingia ndani.
“Habari za hapa?” Blandina alimwuliza msichana mmoja aliyekuwa anaosha vyombo kwenye karo uani.
“Salama tu, shikamoo!”
“Mar-haba!”
“Karibu!”
“Ahsante sana, hata hivyo mimi sio mkaaji!”
“Kwanini?”
“Nina shida muhimu sana, nina imani unaweza kunisaidia hata nikiwa nimesimama!”
“Nakusikiliza, hakuna tabu!”
“Unamfahamu Gerald?”
“Ndiyo!”
“Nimemkuta?”
Yule msichana aliyejitambulisha kwa jina la Lucy, alibaki kimya, uso wake ukajenga makunyanzi madogo, kwa hali aliyoionyesha ni wazi kulikuwa na tatizo lililotokea, ni kwamba alikuwa na habari mbaya ambazo hakuwa tayari kuzitoa. Aliinamisha kichwa chake chini akifikiria jambo ambalo Blandina hakuweza kuligundua.
“Vipi?” Blandina akauliza.
“Hapana, unajua....”
“Niambie tu binti, kuna nini kimetokea?”
“Gerald alihama siku nyingi sana na mke wake!”
“Wamehamia wapi?” Blandina akauliza akiwa na woga kidogo.
“Marekani! Hawaishi hapa nchini tena!”
“Mh! Ilikuwaje?”
“Kwakweli sijui, ila ninachojua walihamia Marekani miaka miwili iliyopita!” Blandina hakuuuliza swali lingine, hakuwa na uhakika kama alikumbuka kumuaga msichana huyo. Alichokifanya ni kuondoka moja kwa moja mpaka nyumbani kwake, ambapo alikwenda kuzungumza na mumewe juu ya yaliyotokea, kwa ujumla kitu kiliharibika. Hawakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kwenda kwa Mkemia Mkuu kwa mara nyingine kwa kumpa taarifa iliyokuwepo. Wakampigia simu Abedayo kisha wakamweleza hali halisi, ambapo walikubaliana kwenda kwa Mkemia Mkuu siku iliyofuata.
Ndivyo ilivyokuwa, siku iliyofuata asubuhi na mapema walikutana ofisini kwa Mkemia Mkuu.
“Huyu bwana hajapatikana, tena haishi hapa nchini tena!” Blandina akasema.
“Yupo wapi?”
“Marekani!”
“Taarifa hizi mmezipata wapi?”
“Alipokuwa akiishi zamani wametueleza hivyo!”
“Basi hakuna kitu kingine ya kufanya zaidi ya kuwapima Genesis pamoja na Adebayo, ikiwa vipimo vitaoana, basi Abedayo atakuwa ndiye baba wa mtoto, lakini kama ni kinyume chake basi baba wa mtoto atakuwa ni Gerald!”
“Hakuna tabu!” Wote wakakubaliana.
Abedayo, Genesis na Mkemia Mkuu wakaongozana mpaka maabara, kisha vipimo vikafanyika!
*********
Siku zote alimchukia sana Adebayo, hakutaka awe baba wa mtoto wake, alikuwa mwanaume katili ambaye alimfanya aishi maisha ya shida sana na mwanaye. Aliendelea kumwomba Mungu amsaidie ili majibu yawe mtoto sio wake, hilo aliendelea kuomba kimoyomoyo bila kukoma.
Alitamani hata kama majibu yalikuwa ni mtoto wake, lakini yabadilke! Kimsingi alimchukia sana Abedayo.
“Mume wangu!”
“Unasemaje mpenzi?’
“Yaani ninavyomchukia huyo Adebayo, yaani sitaki kabisa awe baba wa Genesis!”
“Hilo litajulikana baada ya vipimo!”
“Kwahiyo kama ikionekana ni mtoto wake itakuwaje?’
“Hakutakuwa na kitu cha kufanya zaidi ya kukubaliana na ukweli huo!”
“Lakini utakuwa ukweli utakaoniumiza sana!”
“Usiseme hivyo mpenzi! Unapaswa kujifunza kukubali ukweli siku zote, hiyo ni silaha muhimu katika maisha mpenzi wangu!” Waliendelea kuzungumza mpaka Genesis na Adebayo walivyotoka. Waliambiwa wasubiri kwa muda mfupi nje, wakati vipimo vikiendelea.
Kila mmoja alikuwa na hamu ya kutaka kujua ni nani hasa alikuwa baba wa Genesis, hata Genesis naye alikuwa na hamu sana ya kumfahamu baba yake mzazi alikuwa ni nani! Aliamini baada ya muda mfupi, angeweza kuufahamu ukweli halisi! Kiasi cha saa mbili, kila mmoja akiwa na maswali mengi kichwani mwake, Mkemia Mkuu alitoka nje.
“Karibuni ndani tafadhali, majibu yapo tayari!”
“Tunashukuru sana!” Wote wakaingia ofisini kwa Mkemia Mkuu wakitaka kujua ukweli halisi ulivyokuwa.
“Karibuni sana!”
“Tunashukuru!”
“Bila shaka mpo tayari kwa majibu nitakayoyatoa!” Lilikuwa swali gumu kidogo kwao, aliyeonekana kuwa tayari kujibu ni Genesis pekee! Wengine walisita.
“Tunasikilizana lakini?”
“Ndiyo!”
“Majibu yameshakamilika, ila kabla sijayatoa, nilitaka kufahamu kama mpo tayari kwa majibu hayo!”
“Tupo tayari!” Hatimaye wote wakajibu.
Mkemia Mkuu, akafungua kadi iliyokuwa mkononi mwake, kisha akawatizama wote kwa zamu, majibu alikuwa nayo, lakini alisita kuyatoa.
“Naomba utuambie tujue kinachoendelea!” Blandina akamwambia.
“Ok! Hakuna tabu, majibu yanaonyesha kuwa Genesis .....” Kabla hajamalizia sentesi yake, tayari macho ya Blandina yalishalowanishwa na machozi, yaliyotiririka mashavuni mwake. Hakujua ni nani kati ya Adebayo na Gerald angekuwa baba wa mtoto wake, pamoja na hilo alitamani sana awe Gerald!
Adebayo anaingia Tanzania akitokea nchini Nigeria kwa ajili ya kazi moja tu, kuhakikisha kuwa Genesis anatambulika kama mwanaye. Huko anakutana na kazi ya ziada baada ya kupambana na Dk. Mkambila aliyemkosakosa kumuua kwa bastola!
Hata hivyo baadaye wanazungumza kisha wanaenda kwa Wakili ambaye anaawaandikia barua ya kwenda kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya kipimo cha DNA! Vipimo vinatolewa na majibu yanakuwa tayari, wanaitwa ndani kwa ajili ya kupewa majibu yao! Je, majibu yataonyesha Genesis ni mtoto wa Adebayo? SONGA NAYO...
Kilichokuwa kichwani mwa Adebayo ni kuambiwa kuwa Genesis alikuwa mtoto wake! Hicho ndicho kitu pekee kilichokuwa akilini mwake kwa wakati huo. Alifahamu vizuri sana uwezo wa kifedha aliokuwa nao Genesis, alijua ni kiasi gani angekuwa katika hali nzuri kiuchumi, ikiwa angekuwa pamoja na mwanaye, akaomba kimoyomoyo kuwa majibu yathibitishe yaliyokuwa akilini mwake.
Moyo wa Blandina ulizidi kuuma, hakutamani hata mara moja mwanaye awe mtoto wa Adebayo, kwa vyovyote ilivyokuwa, lakini hakumpenda hata kidogo mwanaume huyo. Macho yake yakawa kwa Mkemia akiwa tayari kusikia chochote kitakachotoka kwa daktari. Genesis, ndiyo alikuwa makini zaidi kumfuatilia Mkemia ili kujua ukweli kuhusu baba yake, hilo lilikuwa jambo lililomuumiza sana kichwa chake usiku na mchana.
"Tafadhali Mkemia, unatuweka roho juu, kama majibu unayo ni vizuri ukayatoa. Majibu hayawezi kubadilika hata ukiyachelewesha, tafadhali tunaomba utuambie ukweli!" Blandina akamwambia daktari.
“Hakuna tabu, ila mnapaswa kufahamu kuwa kila kitu kinafanyika kwa utaratibu, hata hivyo muda wa kutoa majibu yenu sasa umefika!”
“Tunakusikiliza!” Adebayo akadakia.
“Vipimo vinaonyesha kuwa Genesis hana uhusiano wowote na Adebayo!” Mkemia Mkuu akasema. Kila mmoja akapigwa na butwaa isipokuwa Blandina peke yake aliyeonekana kufurahia majibu hayo. Genesis aliinamisha kichwa chini akaonekana kama ana mawazo mengi kichwani mwake.
“Haya majibu siyo sahihi! Kama mmenifanyia njama, mimi siyo wa kudhulumiwa haki yangu!” Adebayo alisema kwa hasira kisha akatoka nje.
Moyo wa Adebayo ulimwambia kitu, alihisi kulikuwa na mchezo mchafu aliokuwa akichezewa, hasira ikampanda, hakutaka kuamini kuwa Genesis hakuwa mwanaye! Safari ya kwenda Tanzania akitoa Nigeria ilikuwa ni kwa ajili ya Genesis, lakini sasa ndoto hiyo ilianza kuzimika taratibu. Alitoka moja kwa moja mpaka nje ambapo aliketi kwenye kiti nje akiwasubiri. Walipotoka tu, walikutana na uso wa Adebayo uliojenga makunyanzi, huku hasira ikiwa haijifichi.
“Najua mnanichezea mchezo mbaya, ninachojua mimi ni kwamba Genesis ni mwanangu, siyo zaidi ya hivyo!” Adebayo alisema kwa hasira huku akitetemeka.
“Hivi kwanini unamng’ang’ania mwanangu? Huyu ni mtoto wa Gerald na siyo wako!”
“Nini?”
“Ulivyosikia ndivyo ilivyo!”
“Usijaribu kunidhulumu haki yangu. Hii ni damu yangu!” Adebayo akasema kwa uchungu.
“Hudhulumiwi ndugu yangu, kama ni vipimo vimefanyika na majibu yameonyesha ukweli, sasa unataka kubishana na vipimo kaka?” Dk. Mkambila aliyekuwa kimya muda mwingi alisema.
“Hivi vipimo siviamini!”
“Kwahiyo?”
“Kuna kitu kingine cha kufanya!”
“Kitu gani?”
“Twende kwenye hospitali nyingine sasa hivi, hospitali ambayo hakuna mmoja wetu anayefahamika!” Adebayo akasema.
“Kwani hapa kwa Mkemia Mkuu kuna mtu anafahamiana naye? Si tumeagizwa na Wakili?”
“Pamoja na hayo, lakini nasema kuwa sina imani na hapa, kama ni kweli hamna nia mbaya, basi twende hospitali nyingine!”
“Hivyo tu!” Blandina akauliza.
“Baada ya hapo roho yangu itatulia, vinginevyo tutaonana wabaya!” Adebayo akasema.
“Hakuna tabu, tuingieni garini twendeni Ocean Road Hospital!” Blandina akasema.
“Ok!” Wakakubaliana, kisha wakaingia kwenye magari yao na safari ya kwenda Ocean Road Hospital ikaanza.
*********
Safari yao iliishia moja kwa moja katika Hospitali ya Ocean Road, iliyokuwa pembeni mwa Bahari ya Hindi, jijini Dar es Salaam. Walipofika Mapokezi, wakaomba kuonana na Daktari Mkuu wa Hospitali hiyo. Wakapewa maelekezo kisha wakaenda ofisini kwake.
Kwa bahati nzuri, walimkuta Daktari Mkuu, Profesa Dan Khajij akiwa hana wageni, hivyo kupata nafasi ya kuhudumiwa mapema.
“Poleni sana jamani!” Profesa Khajij akasema.
“Tunashukuru sana Profesa!” Wakaitika kwa pamoja.
“Naomba niwasikilize!”
“Tuna shida ya kufanya Kipimo cha DNA!” Adebayo akawa wa kwanza kusema.
“Hakuna tabu, nitawashughulikia!”
Hawakuchukua muda mrefu, vipimo vilitolewa na baada ya muda mfupi majibu yalikuwa tayari. Kama ilivyokuwa kwa Mkemia Mkuu, majibu ya Profesa Khajij yalionyesha kuwa Adebayo hakuwa na uhusiano na Genesis!
Kwa upande wa Dk. Mkambila na Blandina ilikuwa furaha lakini kwa Adebayo ilikuwa machungu na huzuni moyoni mwake, hata hivyo hakuwa na jinsi hakuweza kubadilisha ukweli uliokuwa wazi. Lakini bado hakuwa na imani na majibu hayo, akaleta kipingamizi kwa mara nyingine.
Adebayo alikuwa wa kwanza kutoka katika chumba cha daktari, akaingia katika gari na kufunga mlango kwa nguvu kisha akainamisha kichwa chake chini kwa mawazo. Baada ya muda Dk. Mkambila, Blandina na Genesis wakatoka. Alivyowaona tu, akashuka garini haraka.
“Sasa umeamini majibu ya vipimo?” Blandina akamwuliza.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Bado! Hata hivyo sina imani na hospitali za Tanzania, kama ni kweli mnataka kujua ukweli, twendeni tukapime Nairobi!”
“Hakuna tabu, popote utakapotaka tutakwenda lakini ukweli hauwezi kubadilika!” Blandina akasema kwa kujiamini.
Hakuna aliyekuwa na pingamizi, mipango ikafanyika, siku mbili baadaye wakaenda katika Hospitali ya Kenyata iliyopo Nairobi nchini Kenya kwa ajili ya kurudia vipimo vya DNA. Majibu yalikuwa yale yale, Genesis hakuwa mtoto wa Adebayo.
Baada ya majibu hayo, hakuwa na maswali zaidi, akili yake ikamtuma kuamini kilichojulikana, hakuona sababu za kubishana na vipimo vya kitabibu! Majibu yakawa hivyo, wote kwa pamoja wakakubaliana nayo! Hawakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kurejerea Tanzania, ambapo wiki moja baadaye Adebayo alikwenda Nigeria kuendelea na shughuli zake. Mjadala wa Adebayo na Genesis ukafungwa!
*********
Maisha yaliendelea kama kawaida, Blandina alifurahishwa sana na majibu ya mtoto wake, siku zote hakuwa na uhakika mtoto wake alikuwa ni wa nani, lakini kwa wakati huo alishafahamu ukweli halisi juu ya mwanaye. Pamoja na yote hayo, alifurahi sana kusikia kuwa mtoto wake alikuwa wa Gerald, mwanaume aliyekuwa akimpenda kwa maisha yake yote.
Furaha yake ikaongezeka! Lakini kwa upande wa Genesis hali ilikuwa tofauti sana, siku zote alionekana ana mawazo sana, furaha yake ya awali ikatoweka! Kwa wiki nzima baada ya kupata majibu ya mwisho katika Hospitali ya Kinyata alishinda na kulala nyumbani kwa wazazi wake! Hakutamani kwenda nyumbani kwake kuishi peke yake.
Hali yake ilibadilika taratibu, kiasi wazazi wake wakaanza kuwa na wasiwasi naye. Jioni moja wakiwa mezani wakipata chakula cha usiku, Blandina aliamua kumuuliza ili kupata ukweli wa mambo kutokana na jinsi alivyoona mabadiliko ya mwanaye.
“Genesis mwanangu, una matatizo gani?”
“Nipo sawa!” Genesis akajibu kwa kifupi sana.
“Siyo kawaida yako kuwa katika hali hii, ninaamini kuna tatizo, naomba uniambie mwanangu, mimi ndiyo mama yako mzazi, unadhani usiponiambia mimi utamwambia nani? Kuwa wazi, nini kinakusumbua mama?” Blandina akaongea kwa upole sana.
“Nimekwambia sina tatizo, lakini kama unadhani ninalo, niambie...” Sasa Genesis aliongea kwa ukali kidogo.
“Lakini mwanangu, sisi tunakufahamu vizuri ulivyo, haupo katika hali yako ya kawaida, tuambie Genesis binti yetu, sisi ndiyo wazazi wako, ni sisi ndiyo wenye uwezo wa kukusaidia!” Dk. Mkambila akasema.
“Ndiyo, ni kweli nina tatizo!”
“Tatizo gani?”
“Nahitaji kumwona baba yangu mzazi!” Wakati akizungumza maneno haya machozi machoni mwake yalijaa.
“Usilie mwanangu, ukweli ni kwamba baba yako ni Gerald, na hivi sasa hayupo hapa nchini, jambo la kufanya ni kutangaza katika Internet, inaweza kusaidia kumpata!” Blandina akasema.
“Niachieni kazi hiyo!” Genesis akasema kisha akainuka na kwenda chumbani kwake kulala.
Asubuhi na mapema ya siku iliyofuata, aliamka kisha akaingia katika gari lake akaenda zake mjini. Kubwa zaidi lililompeleka mjini ni kwenda kuandika taarifa katika Mtandao wa Internet. Kitu cha kwanza kufanya asubuhi hiyo ilikuwa ni kwenda Internet.
Alipofika kazi yake kubwa ilikuwa ni kutangaza kumtafuta baba yake Gerald! Alihakikisha anatangaza taarifa hiyo katika vyombo vya habari na tovuti mbalimbali za Kimataifa. Alipokamilisha kazi hiyo, akaamua kufungua akaunti yake ya waraka pepe.
Katika akaunti yake kulikuwa na waraka pepe tano ambazo hakuzisoma! Akafungua kisha akaanza kusoma mmoja baada ya mwingine. Alipofika wa tatu, alisoma taarifa zilizomshtua sana! Akaanza kusoma haraka haraka, lakini kabla hajafika hata nusu ya waraka, tayari blauzi yake ilishakuwa chapachapa kwa machozi!
Kila alichokisoma alifananisha na simulizi ya kitabu, mpaka anamaliza kusoma, macho yake yalishakuwa mekundu, zilikuwa taarifa zilizomshtua sana, haikuwa rahisi kuamini haraka. Akapiga meza kwa nguvu puuuu!
****
Siku zote aliishi maisha ya shida, mpaka kufikia umri huo alishakumbana na mambo mengi ya hatari katika maisha yake! Hata hivyo alimshukuru sana Mungu kwa kumpa uwezo wa ajabu katika ubongo wake. Pamoja na yote maisha yake yalikosa kitu kimoja muhimu, baba yake mzazi! Hilo ndilo hasa lililomfanya akawa katika chumba cha mtandao wa Internet muda huo akimsaka baba yake.
Zoezi alilikamilisha, kilichokuwa mbele yake kwa wakati huo ilikuwa ni kusubiri majibu, kama baba yake angeweza kupata taarifa hizo popote alipo duniani. Lakini alipoamua kufungua anuwani pepe yake ndipo alipohisi moyo wake ukipigwa shoti ya umeme. Kwa muda mrefu aliendelea kurudia kusoma ujumbe mara mbili-mbili, lakini kilichoandikwa ndicho kilivyokuwa. Machozi yakamtoka akiwa haamini kabisa kilichotokea. Ulikuwa ujumbe wa ajabu sana katika maisha yake.
Sehemu ya ujumbe huo ulisomeka hivi; “Genesis natambua uwezo wako kiakili ulivyo tangu tulipokuwa pamoja huku chuoni Japan. Wewe ni mwanamke wa pekee kati ya wanawake niliowahi kukutana nao katika maisha yangu. Kubwa zaidi ni uvumilivu na ukarimu wako, amini wewe ni mwanamke shujaa.
Nina imani unafahamu ni kiasi gani familia yetu ilivyo na uwezo mkubwa kifedha, pamoja na hilo niliamua kusoma kwa kuwa nafahamu fika kuwa bila elimu maisha hayawezi kwenda sawa! Genesis hivi sasa nina ofisi yangu hapa Japan na kwakweli inaendelea vizuri sana.
Kwa ujumla naweza kusema nina kila kitu, lakini kuna kitu kimoja ambacho kimekosekana, mke! Nahitaji kuishi na msaidizi sasa, msaidizi ambaye atanisaidia kwa kila hali. Nilifikiria jambo hili kwa muda mrefu sasa, nikajaribu kukumbuka wanawake ambao nilipata kukutana nao katika maisha yangu, wewe Genesis ukaingia ubongoni mwangu, nikafuatilia maisha yako ya Tanzania, nikagundua kuwa una maendeleo makubwa sana.
Hilo linatosha kabisa kukufanya uwe wangu! Amini nakupenda sana Genesis, nahitaji kuishi na wewe, uwe mke wangu, niwe mume wako! Amini maneno haya yanatoka moyoni mwangu. Nakutakia mafanikio mema, nikiamini kuwa utanijibu.
Ni mimi, Doy Nasake,
Japan.
Hakuwahi kufikiria kama angetokea mwanaume atakayemtamkia kuwa anampenda, sura yake na umbo lake dogo lilimvunja moyo akiamini aliumbwa kwa ajili ya kuishi peke yake, siku hiyo ilikuwa siku ya furaha kwake, machozi ya furaha yakabubujika machoni mwake. Doy ni kijana mzuri, mpole, mwenye uwezo mkubwa sana darasani na mbunifu!
Alimkumbuka vizuri sana kijana huyo wa Kijapan, aliyekuwa akipishana naye maksi chache kila wanapokuwa katika majaribio. Ilikuwa ni bahati kubwa sana katika maisha yake, pale pale alipokuwepo akaanza kumshukuru Mungu, kutokana na miujiza aliyoanza kumuonyesha katika maisha yake. Hakukaa sana katika Mgahawa huo, akatoka kisha akaenda katika gari lake, akapanda na safari ya kwenda nyumbani kwake ikaanza.
*********
Siku hiyo ilikuwa ya aina yake katika maisha ya Genesis, ilikuwa ni siku mpya katika maisha yake, siku ambayo isingeweza kufutika katika siku zote za maisha yake! Alifurahia sana waraka alioupata kutoka kwa Doy, lakini haikutosha kumsadikisha kuwa Doy alikuwa yakini kwa yale aliyoyaandika. Kitu pekee ambacho kingeweza kumpa uhakika katika hilo, ilikuwa ni kumpigia simu.
Hakufanya makosa, alipokuwa akisoma ujumbe ule katika anuwani pepe yake alichukua namba za simu za Doy. Alipofika nyumbani, hakutaka kukaa sebuleni na house girl wake kama ilivyo kawaida na badala yake akakimbilia chumbani kwake.
“Dada, mbona leo una furaha sana?” Msichana wake wa kazi akamwuliza.
“Usijali mdogo wangu, kuna kitu kimenifurahisha sana, siku chache zijazo utajua!”
“Siwezi kujua sasa hivi?”
“Ni mapema sana mama, usijali muda ukifika utajua!”
“Ni lini sasa?”
“Muda ukifika!”
“Sawa!”
“Usiku mwema!”
“Kwahiyo ndiyo unakwenda kulala?”
“Ndiyo!”
“Mbona mapema sana?’
“Najisikia kulala mapema leo. Sihitaji kuangalia filamu!”
“Usiku mwema!”
“Nawe pia!”
Ilikuwa kawaida yake kila siku kuangalia Filamu za Kinigeria, lakini siku hiyo hakutamani kukaa sebuleni kuangalia kama ilivyokuwa kawaida yake, alipanga ajifungie chumbani afikirie vizuri waraka wa Doy.
Akaingia chumbani ambapo alijitupa kitandani mwake akiwa na simu yake mkononi mwake. Alichokifanya kwa haraka ilikuwa ni kubonyeza namba za Doy, akiwa na matumaini makubwa kuwa angeweza kuzungumza naye kwa kirefu. Akabonyeza namba za Doy, kisha akaweka simu sikioni kwa ajili ya kusikiliza. Kwa bahati nzuri simu ikaita.
“Habari za saa hizi Doy!” Genesis akasema kwa lugha ya Kiingereza
“Salama tu, naongea na nani?”
“Genesis!”
“Oh! Genesis? Siamini!”
“Ndiyo, kwanini huamini?”
“Kwasababu nimekutafuta kwa muda mrefu sasa mpaka nilipofanikiwa kupata anuwani pepe yake. Nina imani umepata ujumbe wangu!”
“Ndiyo, lakini nina swali moja kwako!”
“Swali gani?”
“Kwanini umenipenda mimi Doy na sio mwanamke mwingine yeyote?”
“Nakupenda Genesis, nikisema nianze kuorodhesha sababu, pengine muda hautatosha, lakini fahamu kuwa wewe ni mwanamke wa pekee ambaye moyo wangu umekuchagua wewe!”
“Ahsante, nimefurahi sana kusikia hivyo!”
“Kitu kizuri zaidi ni kwamba wazazi wangu wanafahamu juu ya jambo hili na wamenipa baraka zote. Nahitaji kukuoa Genesis!”
“Ahsante sana Doy, naomba ahadi zako ziwe za kweli!”
“Nakuahidi!” Baada ya hapo wakakata simu zao. Genesis alilala usingizi mzuri sana huku usiku mzima ukiwa umetawaliwa na Doy, kijana ambaye hata yeye alikiri kumpenda.
Siku iliyofuata baada ya kutoka kazini alikwenda kwa wazazi wake, ambapo aliwaeleza kila kitu kuhusu Doy.
“Nimefurahi sana kusikia hivyo mwanangu, huwezi kuishi peke yako siku zote, ni vyema upate mwenzako, lakini ana tabia nzuri?” Blandina, mama mzazi wa Genesis alimuuliza.
“Kwa hilo mama nakuhakikishia, kwa sababu nilisoma naye chuoni, namfahamu vizuri, hana matatizo!”
Mazungumzo yakaendelea, furaha ikaongezeka katika familia yao. Kila mmoja alimshukuru Mungu kwa ajili ya Genesis! Mipango ikaendelea kufanyika, Doy na wazazi wake wakaenda Tanzania kwa ajili ya kumchumbia Genesis! Hapakuwa na kipingamizi.
Mzee Nasake Kebuy baba mzazi wa Doy, alifurahishwa sana na kitendo cha mwanaye kuamua kuoa na kuachana na maisha ya kibachela, kilichomfurahisha zaidi ni kutokana na mwanaye kuchagua mwanamke mwenye elimu na mtafutaji. Mzee Nasake alikuwa na uwezo mkubwa sana kifedha nchini Japan, alikuwa na jina na heshima kubwa miongoni mwa matajiri wakubwa nchini Japan.
Kwa mwanga aliouonyesha Genesis aliamini uwezo wa familia yake kiuchumi utaendelea kuwa juu, hata kama siku moja ikitokea amekufa.
Familia zikaungana, mzee Nasake hakutaka kuvuta mambo, akawaomba wazazi wa Genesis wakubali kufunga ndoa mapema kabla ya kurudi Japan, hakuna aliyepinga, mipango ikapangwa na siku ya ndoa ikafika. Ndoa ikafungwa nyumbani kwa wazazi wa Genesis na hatimaye sherehe kubwa ikafanyika katika Ukumbi wa Nice Club uliopo Upanga jijini Dar es Salaam.
*********
Gerald akiwa katika moja ya Mgahawa wa Internet katika mji wa Manhattan nchini Marekani, akaingia katika mtandao wa Google, kisha akaanza kuandika jina la Blandina na kutafuta habari zake. Katika hali ya kushangaza sana, ikaonyesha kuwa ana mtoto anayeitwa Genesis ambaye ni tajiri mwenye uwezo mkubwa kifedha, pia anamiliki kampuni kubwa ya kutengeneza kompyuta.
Akiwa anaendelea kutafuta habari zaidi, akashangaa kuona kuwa alikuwa anatafutwa na Genesis kwa madai kuwa alikuwa baba yake. Zilikuwa habari mpya kwake, akiwa anaendelea kusoma zaidi, akaona kuwa Genesis alikuwa akijiandaa kuolewa na kijana wa Kijapan ambaye pia wana uwezo mkubwa kifedha.
“Hii ni bahati ya pekee, hakika lazima jambo fulani haraka sana, bado siku mbili tu anaolewa, lazima niwahi, lazima!” Gerald akajisemea mwenyewe kisha akaondoka muda huo huo na kwenda nyumbani kwake.
“Nimepata safari ya ghafla mke wangu, lazima niende Tanzania kesho asubuhi!” Gerald akamwambia mkewe.
“Kuna nini?”
“Kuna tenda ya kazi, isitoshe mwisho ni keshokutwa, ingawa nimechelewa lakini lazima niende!”
“Sawa!” Maandalizi yakafanyika na siku ya pili akawa safarini kwenda nchini Tanzania.
Hakupata shida kuulizia, akafika mpaka nyumbani kwa Blandina, akashangazwa sana na mandhari nzuri ya nyumba yake. Hakukuta mtu nyumbani zaidi ya mlinzi wa getini.
“Wenye nyumba wapo wapi?” Gerald akauliza.
“Wapo kwenye sherehe!”
“Ya…”
“Harusi, Genesis amefunga ndoa leo, na hivi ninavyokuambia watu wapo ukumbini wanasherehekea!”
“Ukumbi gani huo?”
“Nice Club!” Hakuwa na maswali zaidi, alichokifanya ni kuondoka haraka hadi ukumbini.
Kulikuwa na kitu kimoja kilichoutatiza ubongo wake, hakuweza kujua angewezaje kuingia bila kadi ukumbini? Lilikuwa swali gumu kwake lakini alijipa moyo. Akafika Nice Club, magari yalikuwa mengi yameegeshwa nje ya ukumbi. Akashuka kisha akamkabidhi dereva tax pesa yake, akapiga hatua kuelekea lango kuu la kuingilia ndani. Kabla hajaufikia mlango, akasikia sauti ya mtu akizungumza kwa lugha ya Kiingereza.
“Nawashukuru sana wazazi wenzangu kwa kumzaa mkwe wangu Genesis, ambaye leo hii wamekuwa kitu kimoja na mwanangu Doy. Kwa kuonyesha furaha yangu natoa zawadi ya dola mia tano kwa kila mmoja mzazi, yaani baba na mama!” Maneno hayo aliyasikia vizuri sana, aliweza kugundua kuwa alikuwa ni baba wa bwana harusi!
Dola mia tano zikajirudia akilini mwake, akazitamani, alijua wazi kuwa ni yeye ndiye baba halisi wa Genesis, hivyo fedha zile zilikuwa haki yake kwa asilimia mia moja.
Alipofika getini akazuiwa kuingia ndani, mabaunsa walikuwa wakali waliofanya kazi yao ipasavyo, hawakutaka kufanya uzembe. Gerald akajitahidi kujieleza lakini hakueleweka.
“Kama huna kadi ondoka hapa, usizidi kutupotezea muda!” Mmoja wa mabaunsa akamwambia.
“Siondoki hapa, lazima niingie ndani, hii ni harusi ya mwanangu mwenyewe, kama mnabisha nendeni mkaulize huko ndani Gerald ni nani, kama hamtaambiwa mniruhusu niingie!”
“Kazi hiyo sisi hatufanyi, tunakuomba uondoke kabla ya kuanza kutumia nguvu!”
“Mimi siondoki, hapa!”
“Bwanaee, huyu mtu tunamkawiza sana, ngoja nimfunze adabu ili siku nyingine aheshimu ofisi za watu!” Ganga Man, mmoja wa mabaunsa akasema huku akimvuta Gerald na kumpiga mateke, dakika mbili baadaye mabaunsa wote wakamzunguka Gerald na kuanza kumpiga huku wakimtoa karibu na lango kuu la kuingia.
Gerald alilia kwa maumivu makali, alipiga kelele lakini haikusaidia, mabaunsa waliendelea kumpiga.
****
Hakuna aliyeelewa kilichokuwa kikiendelea, ni Blandina, Dk. Mkambila na Genesis pekee ndio waliokuwa wakifahamu kilichokuwa kikiendelea, kila mmoja alipigwa na butwaa! Hata baba wa Doy alishangaa pia, kwa nukta kadhaa alisita kuongea kitu chochote! Minong’ono ikaanza ukumbi mzima.
“Kuna nini?” Mmoja wa waalikwa alimwuliza mwenzake.
“Hata mimi sielewi, mbona wanasimama wawili?”
“Hii kali, sijawahi kuona tangu nizaliwe!”
“Au huyu mtoto ana baba wawili?”
“Sijui!” Waliendelea kuulizana maswali bila kupata majibu.
Baadaye mzee Nasake Kebuy alianza kuzungumza tena; “Nashindwa kuelewa ni nani ni baba wa Genesis kati ya hao wawili, hivyo kutokana na hilo itabidi mama mzazi wa Genesis apokee zawadi ya baba wa Genesis halafu yeye atajua ni nani kati ya hao wawili ndiyo baba wa bibi harusi!” Lilikuwa wazo zuri sana hakuna aliyepingana nalo, vigelegele na makofi vilitawala ukumbi mzima.
Ratiba zingine zikaendelea kama kawaida, baadaye watu waliruhusiwa kwenda mbele kwa maharusi kwa ajili ya kutoa mikono ya pongezi. Watu waliunga foleni kwenda kuwapongeza maharusi. Tangu mwanzoni mwa sherehe Genesis alionekana akiwa na furaha sana lakini baada ya Gerald kuingia ukumbini alionekana akiwa na furaha zaidi ya mwanzoni.
Watu walijipanga kwa wingi, ilipofika zamu ya Gerald, Genesis aliongeza tabasamu zaidi, alijiandaa sawasawa kwa ajili ya kusalimiana na baba yake kwa mara ya kwanza, ilikuwa siku ya furaha kuliko zote zilizowahi kutokea katika maisha yake! Kwake ilikuwa zaidi ya harusi. Ilikuwa siku muhimu kwa kuwa alikutana na baba yake kwa mara ya kwanza.
Siku zote alisikia kuwa ana baba, lakini hakuwahi kumuona, pamoja na kuhangaika kumtafuta katika mitandao ya Internet lakini hakufanikiwa kumpata, katika vitu ambayo vilimuuma sana ni kuolewa bila baba yake kuhudhuria katika harusi yake, lakini sasa furaha iliongezeka baada ya kumuona baba yake ingawa alipigwa sana.
Ilikuwa kama mchezo wa kuigiza, Gerald akaanza kupanda ngazi taratibu sana, macho yake yalikuwa usoni mwa mwanaye, Genesis naye alimwangalia baba yake kwa hisia kali sana huku machozi yakianza kumtiririka machoni mwake. Badaye akamfikia, akamkumbatia huku machozi yakimtoka! Waling’ang’aniana kwa zaidi ya dakika tano!
“Genesis mwanangu!”
“Baba!”
“Naomba unisamehe mwanangu!”
“Baba naomba uelewe kuwa nakupenda sana!”
“Nafahamu hilo mwanangu!”
“Kama unafahamu hilo, fahamu kuwa nilishakusahe tangu siku nyingi kabla, ni mimi ndiye niliyemwambia mama akuruhusu uingie ndani, harusi yangu isingekuwa na maana kama wewe ungekosekana, nathamini sana mchango wako, wewe ndiye baba yangu ninayekupenda na kukuthamini, usijali baba!” Maneno hayo yalimtoka Genesis mfululizo huku machozi kama mfereji wa maji yakichuruzika machoni mwake.
“Nashukuru kusikia hivyo mwanangu, nakupenda pia!”
“Hunishindi mimi baba, namshukuru sana Mungu wangu kwa kunijalia akili na uwezo wa kuelewa masomo yangu vizuri kiasi cha kufaulu na kufikia mafanikio makubwa niliyonayo hivi sasa, usijali baba nimekwishakusamehe!”
Watu walibaki wameduwaa, zaidi ya dakika tano walikuwa bado wamekumbatiana huku wakilia pamoja. Baadaye Gerald alirudi mahali alipokuwa amekaa. Genesis akamuomba mshereheshaji wa siku hiyo ampe nafasi azungumze kidogo, aliporuhusiwa alisimama na kuanza kuongea.
“Nina furaha sana siku ya leo, furaha yangu inasababishwa na vitu vitatu muhimu. Kwanza nina furaha kwa sababu nimeolewa tena na mwanaume ninayempenda....” ukumbi mzima ukazizima kwa vigelegele na makofi. Badaye kidogo Genesis akaendelea kuongea.
“Kitu cha pili kinachonifanya niwe na furaha ni kutokana na wageni wote tuliowaalika kukubali wito na kuungana nasi katika siku hii muhimu, hakika bila nyie sherehe yetu isingependeza kwa kiasi hiki. Kubwa zaidi ambalo linanifanya niwe na furaha ni kutokana na baba yangu mzazi ambaye sikuwahi kumuona tangu kuzaliwa kwangu kuhudhuria, hakika kwa hilo nafarijika sana!” Vigelegele na makofi vikatawala ukumbini.
Sherehe iliendelea mpaka saa saba za usiku ambapo watu walitawanyika, maharusi walikwenda kulala katika hoteli waliyopangiwa kwa maandalizi ya kwenda nchini Mexico kwa ajili ya fungate la ndoa yao.
Siku iliyofuata jioni kukafanyika kikao katika hoteli waliyokuwa wamelala Genesis na mume wake. Kikao hicho kilihudhuriwa na Gerald, Dk. Mkambila, Blandina, Genesis na Doy. Kubwa zaidi katika kikao hicho ilikuwa ni kumzungumzia Gerald.
“Nadhani kila mmoja anafahamu historia yangu na Gerald, labda mkwe wangu Doy pekee ndiye hafahamu, alinifanyia mengi mabaya ambayo kila nikiyakumbuka machozi yananitoka! Leo amekuja anasema Genesis ni mtoto wake, inaniuma sana na hakika siwezi kumpa nafasi hiyo kabisa!” Blandina alisema kwa uchugu mwingi sana.
“Usiseme hivyo mama, kama huyu ni baba yangu atabakia kuwa hivyo tu, mambo yaliyopita tusiyaruhusu katika maisha yetu, tuachane nayo, tugange yajayo!” Genesis akasema.
“Blandina mke wangu, kumbuka kuwa Mungu hukusamehe makosa yako, kwanini usimsamehe Gerald, mkaishi kwa amani?”
“Naweza kufanya hivyo, lakini nitajuaje kama yeye ndiye baba halisi wa mwanangu?”
“Hilo siyo tatizo Blandina, atafanya kipimo cha DNA ukweli utajulikana!”
“Ni kweli kabisa, hata mimi nilikuwa na wazo kama hilo!” Genesis akadakia.
Hapakuwa na kitu kingine cha kujadili, siku hiyo hiyo wakaenda hospitalini na kufanya kipimo cha DNA, majibu yalipokuja ilijukana kuwa Gerarld ndiye baba halisi wa Genesis!
Gerald alifurahi sana.
“Nimefurahi sana baba, sikutegemea siku moja ningekutana na wewe!”
“Usijali ni mipango ya Mungu!”
Wote wakakumbatiana kwa furaha. Wakasameheana na kusahau yaliyopita, wakafungua ukurasa mpya. Genesis na Doy wakaenda zao Mexico kwa mapumziko ya mwezi mmoja ya fungate lao. Gerald akabaki nyumbani kwa Blandina.
*********
Utajiri ukaingia katika maisha ya Gerald, ni kweli baada ya kushinda bahati nasibu na kwenda kuishi Manhattan nchini Marekani alikuwa na uwezo mkubwa sana kifedha, lakini kitendo cha kupata dola milioni tano, tena ghafla kiasi kile kulimchanganya sana, alifurahi kumfahamu Genesis, uwezo wake wa fedha ulimpa faraja kuwa siku zote angekuwa akipata misaada kutoka kwake.
Alifurahia pia msamaha lakini ilikuwa lazima afanye jambo moja muhimu sana ili kuonyesha kweli alijutia makosa yake, alitamani sana kuonyesha dunia nzima kiasi gani alivyoumizwa na makosa aliyomfayia Blandina na Genesis!
“Nimekumbuka...lazima niende kwenye Kituo cha Televisheni kwa ajili ya kufanya kipindi!” Aliwaza. Hakutaka kupuuza siku hiyo hiyo akaenda katika Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, huko akakutana na Mtangazaji maarufu wa Kipindi cha Evening Talk, Steven Ngassa na kumueleza nia yake.
“Kwa hiyo ndio hivyo ndugu yangu, nahitaji ulimwengu mzima ufahamu jinsi ninavyojuta kutokana na kosa nililolifanya kwa mama na mtoto wake!” Gerald akasema.
“Hakuna shaka ndugu yangu, hiki ni kipindi maalum kabisa kwa ajili hiyo!”
“Nashukuru kusikia hivyo!”
“Sasa ni lini utakuwa tayari?”
“Baada ya wiki mbili, Genesis ambaye ndio huyo binti yangu atarudi nchini, hivi sasa yupo Mexico kwa ajili ya fungate!”
“Hakuna shida, tutawasiliana!”
Gerald aliendelea kubaki na siri hiyo moyoni mwake kwa ajili ya kuwashtukiza hapo baadaye. Ndivyo alivyofaya, siku moja tu baada ya Genesis na mumewe kufika Tanzania, Gerald akawaeleza nia yake. Hakuna aliyeleta pingamizi.
Siku ya kipindi ikafika, ilikuwa ni siku ya Alhamisi, majira ya saa 2.30 za usiku, kwakuwa kipindi hicho kilikuwa maarufu kinachosisimua sana, watu wengi sana walikuwa nyuma ya TV zao kuangalia kipindi hicho.
Kila mtu alikuwa na hamu ya kujua kitu kitakachoendelea katika kipindi hicho, katika kipindi hicho kilichoongozwa na Mtangazaji nyota Steven Ngasa, kulikuwa na Blandina, Dk. Mkambila, Gerald, Genesis na Doy. Baada ya salamu na matangazo mafupi, Gerald alipewa nafasi ya kuanza kusimulia.
Hakuna alichoficha, alizungumza kwa uchungu sana na kuomba dunia imsamehe kutokana na kosa alilolifanya. Hakuweza kuvumilia kuzungumza bila kutoa machozi, robo ya muda aliokuwa akizungumza alikuwa akilia! Alikuwa akiongea maneno makali sana kiasi Blandina na Genesis nao walijikuta wakilia. Baadhi ya watazamaji hasa wanawake walikuwa wakilizwa na historia yao iliyojaa machungu na mateso ya kila aina.
“Nina imani Blandina alishanisamehe, Genesis naye amenisamehe pia, lakini bado nafsi yangu inaumia, kila nukta moja inapopita nazidi kujiona mkosaji, naomba Watanzania wote mnaoniangalia sasa hivi katika Kipindi hiki mnisamehe pia!” Gerald alisema huku akilia.
Ilikuwa ni historia ya kuhuzunisha sana katika maisha yao, Blandina na Genesis ndiyo waliokuwa wanafahamu ni kiasi gani waliteseka, siku hiyo walisameheana, Gerald alimini hiyo ilikuwa njia pekee ya kuwaonyesha Genesis na mama yake jinsi alivyoumizwa na kitendo alichowafanyia na kuomba msamaha wa kweli!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wote kwa pamoja wakatengeneza duara, kisha wakakumbatiana huku machozi yakiwatoka! Machozi yao yalikuwa na sababu, maisha yao yalijaa vizingiti na mateso ya kila aina, lakini siku hiyo kila kitu kiliishia pale.
“We are happy at last!” (Hatimaye tuna furaha) Wakatamka maneno hayo kwa pamoja.
Pazia la maisha mapya likafunguliwa, kila kitu kilichotokea katika maisha yao ya nyuma, kikabaki kama historia. Hatimaye furaha ikarejea katika maisha yao.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment