Search This Blog

Tuesday 1 November 2022

MACHUNGU YA USALITI - 1

 





IMEANDIKWA NA : JUMA HIZA



*********************************************************************************



Simulizi : Machungu Ya Usaliti

Sehemu Ya Kwanza (1)





Simulizi hii naitoa maalum kama zawadi kwa wote waliowahi kuumizwa mapenzini, wale ambao waliwaamini sana wapenzi wao ingawa walikuwa wakisalitiwa pamoja na wale wote ambao walijua thamani ya mapenzi ingawa wao kamwe hawakuonyeshwa thamani hiyo na hivyo wakatokea kuyachukia mapenzi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Niseme poleni sana, amini Mungu yu pamoja nanyi katika kipindi chote.



ANZA NAYO…



Hali ya hewa ilikuwa shwari katika jiji la Dar es Salaam. Ndani ya chuo cha Usimamizi wa Fedha IFM kilichokuwepo maeneo ya Posta mtaa wa Shaaban Robert, msichana mrembo aliyejulikana kwa jina la Evelyne alionekana akitoka darasani huku akiwa anakimbia, machozi yalikuwa yakimtoka kwa wakati huo na kutiririka mashavuni mwake.

“Evelyne! Evelyne! Evelyne,” ilisikika sauti ya msichana mmoja akimuita, muda huo alikuwa akimfuata huku akimkimbilia.

Evelyne aliongoza moja kwa moja mpaka kwenye kimbweta, alipofika mahali hapo aliketi na kuanza kulia huku akiwa amejiinamia.

“Evelyne kuna nini mbona sikuelewi?” aliuliza msichana huyo huku akionekana kutofahamu kitu kilichokuwa kimetokea mpaka kusababisha hali hiyo.

“Hapana Happy siwezi kuendelea kuwa eneo hili, acha niondoke zangu,” alisema Evelyne kwa sauti iliyoandamana na kilio cha kwikwi.

“Unaondoka unaenda wapi sasa na wakati darasani kuna kipindi?” aliuliza Happy huku akimtazama Evelyne ambaye muda huo hakunyamaza, aliendelea kulia huku machozi yakitiririka mashavuni mwake.

“Narudi zangu nyumbani.”

“Unajua sikuelewi Evelyne, kwani kuna nini?” aliuliza Happy huku akisubiria jibu lakini katika hali ya kushangaza Evelyne aliinuka na kuondoka mahali hapo. Happy alibaki akimtazama Evelyne kwa mshangao huku asijue ni nini kilichokuwa kimetokea.

Wasichana hao wawili walikuwa ni marafiki wakubwa sana chuoni hapo, walikuwa wakisaidiana mambo mengi, walishiriki kusaidiana katika masomo na hata katika mipango yao ya kimaisha.

Happy alimfahamu vyema rafiki yake tangu walipoanza kusoma katika chuo hicho mpaka kufikia katika kipindi cha mwaka wa mwisho ambao ndiyo waliubakiza. Walikuwa wakisomea Uhasibu.

Walikuwa ni marafiki waliyoshibana na walikuwa wakiishi pamoja katika chumba kimoja walichokuwa wamepanga maeneo ya Kigamboni.

***

Wakati Happy akiwa bado amesimama huku akishangaa tukio la Evelyne kuondoka ghafla! ilisikia sauti ya kiume ikimuita nyuma yake, haraka sana akageuka na macho yake kutua kwa mwanaume mmoja ambaye ndiye aliyekuwa akimuita kwa wakati huo, mwanaume huyo alijulikana kwa jina la Richard.

“Niambie Shem.”

“Poa tu.Vipi mbona Evelyne ametoka darasani, kuna nini?”

“Mimi mwenyewe sijui, nimeshangaa kuona akiondoka.”

“Kwani yuko wapi?”

“Ameondoka zake, ameniambia hawezi kuendelea kubaki hapa chuoni hivyo amerudi nyumbani.”

“Mbona sielewi?”

“Richard kwani kuna kitu gani kimetokea kati yenu?”

“Hakuna kitu.”

“Mbona sasa Evelyne amebadilika baada ya kukuona.”

“Mimi mwenyewe sielewi chochote.”

“Una uhakika?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Ndiyo Happy inamaana huniamini?”

“Nakuamini,” alijibu Happy huku akionekana kuwa na wasiwasi na mwanaume huyo.

Richard alikuwa ni kijana aliyetokea katika familia ya kitajiri. Alikuwa ni mtanashati, mwenye sura nzuri iliyomvutia kila msichana aliyekuwa anamtazama katika chuo hicho.

“There’s something I want to tell you,” (Kuna kitu nataka kukuambia,) ilikuwa ni sauti ya msichana mmoja aliyeitwa Monalisa, muda huo alimtoa chemba Richard na kuanza kuzungumza naye.

Alipomtazama mwanaume huyo usoni, macho yake yalionyesha wazi kwamba kulikuwa kuna kitu ambacho kilikuwa kikiutesa mtima wake ila alishindwa kumwambia.

“What’s that Monalisa?” (Kitu gani hicho Monalisa?) aliuliza Richard huku akiyatupa macho yake kwa Monalisa ambaye alikuwa akijing’atang’ata kucha za vidole vyake kwa aibu.

“But I feel like I’m going to make a mistake,” (Lakini nahisi kama nitakukosea,) alijibu huku akijishtukia, macho yake alianza kuyalegeza.

“No, tell me don’t be afraid,” (Hapana niambie usiogope,) alisema Richard huku akiwa makini kumsikiliza msichana huyo ambaye alionekana kuwa na mengi mazito ya kumweleza.

Kwa muonekano ambao aliuona kwa Monalisa akilini mwake alikwisha fahamu ni kitu gani ambacho msichana huyo alitaka kumwambia lakini hakutaka kuwa na papara ya kukurupukia mambo, alihitaji kumpa nafasi msichana huyo ya kujieleza ili asahili kile alichokuwa akikifikiria kichwani mwake kwa wakati huo.

“Richard I love you so much and I’m ready to do anything for you, please say yes don’t let my kid,” (Richard ninakupenda sana na nipo tayari kufanya lolote kwa ajili yako, tafadhali sema ndiyo usinikatalie ombi langu,) alisema Monalisa huku akianza kumsogelea Richard kwa lengo la kutaka kumbusu shavuni.

“No, don’t do that,” (Hapana usifanye hivyo,) alisema Richard huku akimzuia Monalisa, kwa kufanya hivyo ikaonekana kama amefanya kosa kubwa, msichana huyo akahisi kutopendwa, hakika alijisikia vibaya mno moyoni mwake.

Monalisa hakuwa msichana wa kwanza wala wa mwisho kumsumbua Richard, kila msichana chuoni hapo alitamani kuwa naye kimapenzi na huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kupokea usumbufu kila kukicha lakini hakukuwa kuna msichana aliyewahi kuipata nafasi hiyo katika moyo wake.

Kwa upande wa Richard moyo wake ulizama katika dimbwi la mapenzi na msichana mmoja ambaye ndiye alikuwa ameishikilia nafasi hiyo na kuwazibia wasichana wengine wote waliyokuwa wakiitamani kuipata.

Hakukuwa na mtu ambaye alitaka kuamini Evelyne, msichana aliyeonekana kuwa na uzuri wa kawaida kwamba ndiye ambaye alifanikiwa kuwa katika uhusiano wa kimapenzi na Richard.

Wengi wao waliamini kwa muonekano wa kuvutia aliyokuwa nao mvulana huyo pamoja na kutokea katika familia ya kitajiri basi ni lazima angekuwa na msichana ambaye alitikisa chuo kizima kwa uzuri wake au aliyetokea katika familia ya kitajiri kama ilivyokuwa kwa upande wake lakini haikuwa hivyo, hilo liliwashangaza sana.

“Huyu kinyago ndiyo anatuzibia riziki yetu,” alisema Monalisa huku akiwaambia marafiki zake, wakati huo walikuwepo hostel, wote walikuwa wakitamani kuwa na Richard kimapenzi.

“Hivi ndiye huyu Evelyne?” aliuliza Adela.

“Ndiyo hivi ana uzuri gani yule msichana wakunishinda mpaka atembee na Richard kama sio mchawi ni nini?” alisema huku akiuliza Monalisa, muda huo alikuwa ameubetua mdomo wake.

“Kweli atakuwa mchawi sio bure,” alidakia Penina maneno yaliyowafanya wote wakaanza kucheka kwa sauti kubwa huku wakigongeana.

Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuibuka kwa chuki kati ya wasichana hao na Evelyne, walitokea kumchukia sana msichana huyo, hapa ni baada ya kugundua alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na Richard.

Hilo lilizidi kumuumiza kila msichana ambaye aliwahi kumtamkia neno nakupenda au kuibuka kwa chembechembe zozote za kimapenzi kwa mvulana huyo aliyetokea kuipagawisha mioyo ya wasichana wengi chuoni hapo.





Monalisa ndiye msichana ambaye alionekana kumpenda zaidi Richard kuliko wasichana wengine pale chuoni, licha ya Richard kumkatalia ombi lake la kuwa wapenzi lakini bado hakutaka kukubali hilo, aliamini kwa vyovyote iwezekanavyo ni lazima mvulana huyo angefanikiwa kummiliki.

Kuna kipindi kichwani mwake yalimjia mawazo ya jinsi ambavyo alivyofanikiwa kumpata Richard kisha wakawa wanayafurahia mapenzi yao katika ufukwe wa bahari ya Hindi, alizidi kulifurahia hilo katika moyo wake maradufu na hata pale mawazo hayo yalipomtoka kichwani alionekana kukasirika mno, hakutaka kuamini kama kweli alikuwa akiwaza kwa wakati huo.

Moyo wa mapenzi ukazidi kumuendesha vilivyo, alikuwa amezama katika dimbwi la mapenzi ya Richard mvulana ambaye na yeye moyo wake ulikuwa umekufa umeoza kimapenzi na msichana mwingine chuoni hapo, Evelyne.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Kwa nini Richard anashindwa kunikubalia hivi inamaana sina uzuri wa kumvutia au?” aliuliza Monalisa huku akiwatazama kwa huruma marafiki zake, hii ilikuwa ni siku nyingine ambapo alionekana kuumizwa na kile kilichokuwa kikiendelea kati ya Richard na Evelyne. Hakupenda kuwaona wakiwa pamoja na kuyafurahia mapenzi yao, moyo wake ulilipuka kwa wivu.

“Sio kwamba humvutii isipokuwa Richard ameshatekwa na Evelyne,” alijibu Penina huku akionekana kuwa bize na simu yake.

“Sitaki kumsikia huyo mpumbavu tena nitamkomesha mwanaharamu yule,” alisema Monalisa huku akionekana kuchukia mno baada ya kulisikia jina la Evelyne likitajwa katika masikio yake.

“Shoga yangu mimi nimeshachoka kumfuatilia huyo Richard kwani hakuna wavulana wengine hapa chuo kwani yeye ni nani?” aliuliza Mary huku akionyesha kukata tamaa ya kumfuatilia mwanaume huyo ambaye alimchanganya kila msichana chuoni hapo kutokana na uzuri aliokuwa nao.

“Jamani Richard ni handsome, mimi mwenyewe bado sijaona mvulana mwingine wa kumfananisha naye, hakuna anayemfikia kwa uzuri,” alisema Adela, msichana aliyeikamilisha hesabu yao ya wanne, muda huo ambapo walikuwa hostel.

“Lakini lazima nitampata tu, ipo siku nitafanikiwa kuwa naye,” alisema Monalisa huku akijiapiza kumpata mwanaume huyo kwa udi na uvumba.

“Utatumia njia gani?” aliuliza Mary huku akimtazama Monalisa kwa umakini wa hali ya juu. Alihitaji kufahamu mambo mengi kutoka kwa rafiki yake huyo ambaye moyo wake ulikufa kwa mwanaume, Richard.

“Nitajua tu! Lakini lazima nimpate, nitahakikisha Richard anakuwa mali yangu na sio kuendelea kumuona akiwa na yule kinyago,” alisema Monalisa huku muda huo hasira zikiwa zimempanda.

Hakukuwa kuna kitu kingine alichokuwa akikihitaji Monalisa katika maisha yake zaidi ya Richard, alichokuwa akikihitaji ni kuona anafanikiwa kummiliki mwanaume huyo ambaye moyo wake ulikufa kwake ukaoza.

Kila kitu alichokuwa akikifanya, alikifanya huku malengo yake makubwa yakiwa ni siku moja kuona akifanikiwa kummiliki Richard.

Miongoni mwa wasichana ambao waliwahi kumtamani Richard kimapenzi kutokana na muonekano wake kuwa mzuri alikuwa ni Adela, Mary pamoja na Penina.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Wasichana hawa wote mioyo yao iliwahi kufa na kuoza kwa Richard lakini kutokana na msimamo aliyokuwa nao mvulana huyo hawakuweza kuambulia hata busu bandia.

Kila mmoja alishaanza kukata tamaa ya kufanikiwa kulipata penzi la mvulana huyo, walitumia kila aina ya njia walizoziona zinafaa kumteka Richard kimapenzi lakini hakukuwa na njia hata moja iliyomkamata mtegoni.

Hilo lilizidi kuwasononesha mioyo yao mno, ilifikia kipindi hata wakati wa kula chakula kila mmoja alishindwa kula kwa nafasi yake, moyo wake ulikuwa ukiumia kwa sababu ya kulikosa penzi la Richard.

“Sitaki kuamini na sitaamini kama nimelikosa penzi la Richard,” alisema Monalisa huku akionyesha kutokubaliana na hali halisi.

“Hutaki kuamini nini sasa wakati mwenzako ameshapendwa,” alisema Penina huku akimcheka Monalisa wakati huo walikuwa darasani, tukio hilo lilizidi kumuumiza mno moyo wa Monalisa, hakutaka kuamini licha ya kuupoteza muda wake wote katika kumfukuzia Richard lakini mwisho wa siku aliambulia patupu.

“Nadhani kuna kitu natakiwa kufanya hapa,” alisema Monalisa huku akionyesha kung’amua wazi fulani kichwani kwake.

“Kitu gani?” aliuliza Penina huku akimpa nafasi ya kujieleza.

“Ni mapema mno kukuambia kwa wakati huu, subiri kwanza.”

“Nisubiri mpaka lini? Wewe niambie usinifiche.”

“Usijali nitakuambia muda ukifika,” alisema Monalisa kisha hakutaka kuendelea kuzungumza muda huo.

Kichwani mwake lilimjia wazo, lilikuwa ni wazo la kufanya kitu kwa ajili ya Richard ili afanikiwe kumpata kimapenzi na ni katika wazo hilo ambapo hakutaka kuyawaza au kuyapima maumivu ambayo angeweza kumpata Evelyne, msichana ambaye tayari alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na Richard.

***

Moyo wake bado uliendelea kumuuma mno, kila alipokuwa akimuona Richard darasani alijihisi kuwa na sababu milioni mia moja za kuwa naye kimapenzi.

Kuna kipindi alipokuwa akimtazama Richard pamoja na muonekano wake mzuri alijaribu kumlinganisha na Evelyne msichana ambaye alimuona kuwa na uzuri wa kawaida sana, hakustahili kabisa kuwa na Richard kimapenzi. Lilipokuja suala la uzuri kati yake na Evelyne alipokuwa akijiremba kwenye kioo alikiri fika alimzidi msichana huyo kwa uzuri wala hakukuwa na upinzani katika hilo.

“Sasa kwa nini Richard asinipende mimi?” alijiuliza swali ambalo lilizidi kumfanya ajione kuwa na mapungufu mengi katika mwili wake, kuna muda pia alijiona kuwa miongoni mwa wajinga na wapumbavu wa kumkosa Richard.

“Lazima nifanye kitu kwa ajili yako Richard, sitokubali na siwezi kamwe kukubali kuona ukiendelea kuutesa moyo wangu kila siku kiasi hiki, nakupenda sana na ninahitaji ulifahamu hilo,” alisema Monalisa siku moja majira ya usiku alipokuwa amelala.

Usiku wa siku hiyo ulikuwa mrefu sana kwake na aliutumia katika kumfikiria Richard tu, kichwani mwake jina la Richard lilitawala sehemu kubwa sana.

Alichokuwa amepanga kukifanya Monalisa ni kutengeneza mazingira ambayo yangeweza kumuonyesha kuwa yeye na Richard kuwa ni wapenzi, alilifikiria wazo hilo huku akiamini kama kweli angeweza kufanikiwa kuyatengeneza mazingira hayo basi ni lazima Evelyne angeingiwa na wivu kiasi cha kuumia sana moyoni mwake, hilo ndilo alilokuwa anahitaji kuliona likitokea kwa msichana huyo, hakumpenda wala hakutaka kumuona akiendelea kuwa karibu na Richard mvulana ambaye tayari alikuwa ameshauteka moyo wake wa kimapenzi.

“You must be mine,” (Lazima utakuwa wangu,) alijisemea Monalisa huku akitabasamu, ulikuwa ni wakati ambao wazo hilo lilimjia kichwani mwake.





Maisha ya chuo yaliendelea huku Monalisa kila siku akizidi kuumia, kuna kipindi alitamani kutengeneza mazingira ya kumfanya Evelyne afukuzwe chuo na yote hayo aliwaza ilimradi afanikiwe kumpata Richard.

Siku moja Monalisa alijaribu kutafuta nafasi ya kuzungumza na Richard mpaka akafanikiwa kuipata.

“Kwa nini hutaki kuwa na mimi?”

“Hapana siwezi.”

“Kwa nini?”

“Nipo katika uhusiano wa kimapenzi na msichana mwingine.”

“Richard kwa nini unapenda kunifanyia hivyo lakini, kwa nini unapenda kuutesa moyo wangu kiasi hiki?”

“Sio kama nakutesa Mona tatizo tayari moyo wangu upo kwa msichana mwingine na sipendi nimuumize.”

“Nikuulize kitu?”

“Yeah…niulize.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Hunipendi?”

Hilo lilikuwa ni swali gumu mno lililomfanya Richard ashindwe kutoa jibu la haraka, akabaki akimtazama Monalisa huku asijue ni nini alitakiwa kumjibu kwa wakati huo.

Macho yake yalipotazamana na macho ya Monalisa kuna kitu alikigundua kilikuwa kikiendelea kwa wakati huo, aliyashuhudia machozi yakianza kumtoka na kutiririka mashavuni mwake, hakutaka kuamini kile alichokuwa akikishuhudia, kitendo cha kumuona msichana mrembo kama huyo akiyadondosha machozi mbele yake hakika kilimuumiza mno, kuna muda alianza kujiona kuwa na makosa makubwa mno kwa kuendelea kuutesa moyo wa msichana ambaye alionekana kumpenda kuliko kitu chochote kile.

Alichoamua kukifanya alikitoa kitambaa katika mfuko wa suruali yake kisha akamfuta machozi Monalisa, kitendo hicho kilimfanya Monalisa ashangae, hakutaka kuamini kama machozi yake yalimgusa Richard kiasi kwamba akafikia hatua ya kumfuta.

“Richard,” alimuita.

“Niambie,” alisema Richard.

“Unaweza kweli kuendelea kuishuhudia nafsi ambayo inateseka, inasononeka, inaumia kila siku kwa sababu yako?” aliuliza Monalisa.

“Hapana siwezi,” alijibu Richard.

“Sasa kwa nini hutaki kunifikiria hata mara moja, nimekusumbua sana, nimetumia kila njia ilimradi niwe na wewe lakini imeshindikana basi naomba unisaidie kitu kimoja tu kama hutojali,” alisema Monalisa kwa sauti ya utulivu.

“Kitu gani hicho?” aliuliza Richard huku akimtazama Monalisa.

“Nalihitaji penzi lako, naomba nitumie kuwa na wewe ndani ya usiku mmoja nahisi nitakuwa nimeuridhisha moyo wangu maana kila siku unaishi kwa kuteseka kwa sababu yako,” alisema Monalisa.

Maneno ya Monalisa yalimuweka Richard kuwa katika wakati mgumu sana, hakutaka kuamini kile alichokuwa akikisikia kutoka kwa msichana huyo ambaye alikuwa na kila sifa za kumteka mwanaume rijali, bado hakutaka kuamini kile alichokuwa amekisikia kutoka kwa msichana huyo, ilibidi amuulize ni nini alichokuwa amefikiria lakini kabla hajafanya hivyo ghafla! Monalisa aliweza kumzuia asizungumze lolote kwa kumuwekea kidole katika lips zake.

“Don’t say no please say yes,” (Usiseme hapana tafadhali sema ndiyo,) alitamka maneno haya Monalisa wakati ambao alikuwa amemuwekea kidole kwenye lips Richard.

Richard alishindwa la kufanya, alikosa la kuamua kwa wakati huo. Ni kweli Monalisa alikuwa na sifa zote za kumchanganya mwanaume rijali na kupitia udhaifu huo aliweza kumchanganya Richard mwisho akajikuta akili yake ikianza kumfikiria.

“Ok right but let’s make it a secret between us,” (Sawa ila naomba tufanye iwe ni siri kati yetu,) alisema Richard huku akionekana kukosa uvumilivu kabisa.

“Don’t worry about it I will keep that secret,” (Usijali kuhusu hilo nitaitunza siri hiyo,) alisema Monalisa huku akimtoa hofu Richard.

“Don’t go against our agreement,” (Usiende kinyume na makubaliano yetu,) alisema Richard.

“Don’t worry,” (Usijali,) alisema Monalisa huku akitabasamu.

Monalisa hakutaka kuamini kama kweli alifanikiwa kwa asilimia zote mpango wake, aliamini huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kumpa maumivu Evelyne, maumivu ambayo alikuwa akiyapitia kila siku.

Siku hiyo aliporudi hostel hakukuwa na kazi nyingine aliyoifanya zaidi ya kuwasiliana na Richard, alisahau mpaka kusoma kwa sababu ya Richard mvulana aliyeutesa sana moyo wake lakini mwisho wa siku alifanikiwa kuwa naye.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Mbona unafuraha sana leo?” aliuliza Penina wakati huo alikuwa akisoma kitabu.

“We acha tu shosti yani huwezi kuamini,” alisema Monalisa huku furaha ikionekana kumtawala.

“Kuhusu nini?” aliuliza Penina.

“Kuhusu Richard,” alijibu Monalisa.

“Amefanyaje?”

“Amekubali kuwa na mimi.”

“Unasemaje?”

“Ndiyo amekubali kuwa na mimi,” alijibu Monalisa jibu lililowashangaza wasichana wote pale ndani, kila mmoja hakutaka kuamini kama kweli Monalisa aliweza kukubaliwa na mvulana huyo.

****



ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog