Search This Blog

Tuesday 1 November 2022

MKE WANGU JULIANA - 5

 





    Simulizi : Mke Wangu Juliana

    Sehemu Ya Tano (5)





    John alikutana na marafiki zake na kuanza kuongea kuhusu zawadi ambayo walitakiwa kwenda kumpa Cosmas katika sherehe yake ya ndoa ambayo alitarajiwa kufunga na mchumba wake mrembo.

    Kwa kuwa alipenda sana kucheza game, wakapanga kumwandalia zawadi ya Play Station 4 itakayomfanya kuwa bize katika kipindi cha wikiendi, aache kwenda kuzurura kama kawaida yake.

    Wakati wakizungumza hayo yote kichwa cha John kilikuwa na mawazo tele, alikuwa akimfikiria msichana aliyekutana naye muda mfupi uliopita. Alimwachia namna yake ya simu lakini hakuwa na uhakika kama angeweza kumpigia ama angemsubirisha kwa siku kadhaa.

    Kila wakati alikuwa akiiangalia simu yake, moyo wake ulikuwa na presha kubwa, alipoisikia ikiita, haraka sana akaichukua na kuangalia kioo, alipokuta aliyekuwa akipiga si Amanda, uso wake ulikuwa na hasira mno.

    Baada ya kumaliza kikao hicho kifupi, akarudi ofisini kwake ambapo akachukua gari lake na kurudi nyumbani. Mawazo hayakumtoka, yaliendelea kumvuruga kichwa chake kiasi cha kuona muda wowote ule angeweza kukonda hata kama alikuwa na pesa nyingi kiasi gani.

    Ilipita siku ya kwanza, ikawa kimya, ikapita ya pili, ya tatu mpaka ya nne ndipo akapokea ujumbe kutoka kwa msichana huyo, haraka sana hakutaka kusubiri, akampigia na kuanza kuzungumza naye.

    “Amanda...” aliita huku uso wake ukiwa na tabasamu.

    “Niambie John!” alisema msichana huyo.

    “I’ve missed you a lot,” (nimekukumbuka sana) alimwambia kwa sauti laini kabisa, ile ya kubembeleza.

    “I’ve missed you too!” (nimekukumbuka pia)

    “Why didn’t you check on me?” (kwa nini hukunitafuta?) aliuliza.

    “I’ve been busy the whole week! By the way! How are you doing?” (nimekuwa bize wiki nzima! Unaendeaje lakini?) alisema msichana huyo.

    Wakaanza kupiga stori, moyo wa John ulikuwa na furaha tele, hakuamini kama msichana huyo angeweza kumpigia simu na kuzungumza naye.

    Alikuwa na hamu ya kumuona, muda mwingi alikuwa akiiangalia namba ya msichana huyo, picha yake iliganda ubongoni mwake na haikutaka kutoka hata kidogo.

    Akashindwa kuvumilia, akamuomba kuonana naye katika Hoteli ya Hyatt ambapo msichana huyo akakubaliana naye na siku hiyo wakaonana.

    Ilikuwa ni kwa mara ya pili, alimwangalia jinsi alivyokuwa mzuri, alivyopendeza, kwake alionekana kuwa msichana mrembo kuliko wote ambao aliwahi kukutana nao.

    Waliongea na kucheka, walifurahia kupita kawaida. Kwa kuwa msichana huyo alikuwa mchangamfu sana, hakutaka kuona akiondoka, akamuomba sana kama itawezekana basi siku hiyo wakae pamoja mpaka asubuhi.

    “No!” (hapana) alisema Amanda.

    “Kwa sababu gani?”

    “Ninaishi na wazazi wangu! Itakuwaje nikilala nje ya nyumba yetu?” aliuliza.

    John akanyamaza, kile alichokizungumza msichana huyo kilikuwa sahihi kabisa, kuamua kulala naye na wakati alikuwa chini ya wazazi wake haikuwa adabu hata kidogo.

    Akamwambia kama ingewezekana basi waende pamoja mpaka kwao, akaombe ruhusa yeye mwenyewe. Lilikuwa suala la kijinga mno lakini kwa sababu alimpenda sana msichana huyo, alikuwa tayari kwa kila kitu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Amanda akakataa na kumwambia siku nyingine lingekuwa suala zuri ila si kwa siku hiyo. Wakaachana na jambo hilo na kuendelea kupiga stori kuhusu mambo mengine.

    “Unaniangalia sana mpaka najisikia aibu!” alisema Amanda huku akiangalia chini.

    “Najaribu kuutafakari uzuri wako! Nimeanza kushikwa na wasiwasi na vitabu vyetu vya dini,” alisema John.

    “Kwa sababu gani?”

    “Kwamba sisi wote tumeumbwa! Ni kweli tumeumbwa wote ama wengine wameshushwa tu hapa duniani?” aliuliza huku akitoa tabasamu pana, naye Amanda akatabasamu.

    “Hebu acha masihara bhana na wewe!” alisema Amanda.

    “Nisikilize Amanda. Kuna kitu ninahitaji kukwambia!”

    “Ila kisihusu mapenzi?”

    “Hahaha! Kwa sababu gani?”

    “Nimeshaanza kuziona dalili! John! Sipendi mapenzi!”

    “Kwa sababu gani?”

    “Yanatesa sana!”

    “Unamaanisha wanaume wote ni watesaji?” aliuliza.

    “Ndiyo! Nyie wanaume mnafanana!”

    “Amanda.....”

    “Unasemaje! Una la kujitetea?”

    “Unajua kama Adolf Hitler aliwaua Wayahudi zaidi ya milioni mia moja?” aliuliza huku akimwangalia.

    “Ndiyo! Nilisoma kwenye historia!”

    “Sawa! Mpaka leo baba yako ameua watu wangapi?” aliuliza.

    “Mh! Kwa nini unauliza hivyo?”

    “Wanaume wote tunafanana kumbuka!”

    Amanda hakujibu kitu, hapohapo akaanza kucheka, alijua John alimaanisha nini, alitegwa bila kujua kabla alichokuwa akimaanisha mwanaume huyo.

    “Wanaume hatufanani, wanaume wote si wabaya! Leo kuna wanawake wanasema wanaume wanafanana lakini kila siku wanaongoza kuhudhuria harusi za wenzao! Sasa wale wanaoolewa, wanaolewa na akina nani?” aliuliza John, Amanda akabaki kimya.

    John akaanza kumpa somo la mahusiano ambalo msichana huyo hakuwahi kulisikia kwa mwanaume yeyote yule. Alimwambia mambo mengi kuhusu hayo mahusiano na mwanaume ambaye alitakiwa kuwa naye.

    Amanda alikuwa kimya, ni kama alikuwa darasani huku akimsikiliza mwalimu ambaye alimfundisha somo ambalo baadaye lingekuja kumsaidia kufaulu mitihani yake.

    “Binadamu wote tunakosea, lakini wote tuna nafasi ya kujirekebisha! Inawezekana kabisa nikawa mwanaume mbaya sana kwako, ila haimaanishi nitakuwa mbaya hivyo milele, hakuna mtu anayetaka kuwa mbaya, ubaya unakuja ghafla, wakati mwingine unaondoka,” alisema John huku akimwangalia msichana huyo.

    “Hujawahi kuona siku moja umechukua uamuzi mbaya wa kumuumiza mtu fulani halafu unaanza kujuta? Hutokea kwenye maisha yetu, na kama kungekuwa na mtu ambaye anakuona wakati unamfanyia mtu huyo ubaya huo, angesema wewe ni mbaya, kumbe ni hali tu ambayo imetokea na baadaye ulijuta kwa nini ulifanya hivyo,” alisema John.

    “Unamaanisha nini?”

    “Kitu cha kwanza unachotakiwa kujua ni kwamba mwanaume hajakamilika, sisi ni binadamu na si malaika. Mwanamke unapoamua kuingia kwenye uhusiano na sisi, unategemea kupata maisha mazuri milele bila kujua kuna wakati ubinadamu unatuingia na kuanza kufanya maamuzi ya kijinga kabisa,” alisema John.

    “Unamaanisha usaliti?”

    “Usaliti, wivu, hasira na mambo mengine ni ukamilifu wa binadamu. Leo nikikusaliti haimaanishi mimi ni mbaya sana kwa kuwa utampata mwingine naye atakusaliti vilevile. Kuna makosa tukiyafanya yanadhihirisha kwamba sisi ni binadamu,” alisema John.

    “Mh!”

    “Hakuna ndoa ambayo wanandoa hawatofautiani! Ni lazima hilo litokee, wanaonyesha ukamilifu wao kama binadamu. Inawezekana sisi tungekuwa malaika tusingekuwa na mambo kama hayo!” alisema John.

    “Unamaanisha na wewe pia unaweza kusaliti?”

    “Hahaha! Amanda! Kwenye ndoa usaliti upo, ila si unasaliti mpaka mwenzako anajua kwamba unamsaliti!” alisema John.

    “Mh! Wanaume nyie!”

    “Nisikilize Amanda! Mwanaume anaweza kusaliti na mke usijue, ila mwanamke anaposaliti anataka mwanaume wake ajue, huwa hamsaliti kwa kupenda, wakati mwingine mnafanya kwa makusudi kabisa, ili tujue, tuumie halafu muone tutafanya nini,” alisema John.

    “Nyie wanaume si watu wa kuwaamini kabisa.”

    “Ndiyo! Upo sahihi! Mimi mwenyewe sitaki uniamini tukiwa kwenye uhusiano!” alisema John.

    “Kwa sababu gani?”

    “Nichukulie kama binadamu, kwamba naweza kukusaliti, kukuumiza au kufanya upuuzi mwingine wa kijinga. Ukitaka uniamini kwa kuniona mimi ni malaika, jua siku ambayo nitakusaliti ama kukufanyia ubaya mwingine ni lazima utajiua kwa sababu uliniamini kupita kawaida,” alisema John.

    “Mh!”

    “Na ndiyo maana hata wanafunzi wanajiua baada ya kufeli!”

    “Yaani weweeee...”

    “Kwa kuwa tangu kidato cha kwanza walikuwa wanafunzi wa kwanza darasani, waliamini hawatokuja kufeli, hawakujua kwamba nao ni bindamu kama wengine. Inapotokea wanafeli, wanachukua uamuzi mbaya, kwenye maisha yao hawakuwa na neno kufeli, waliishi na neno kufaulu tu,” alisema.

    “Aya baba nimekuelewa. Yote hayo unamaanisha nini?”

    “Ninakuhitaji!”

    “Unanihitaji mimi?”

    “Ndiyo! Ninakuhitaji baada ya kukupenda sana!”

    “Kwa nini mimi?”

    “Hahaha! Ushawahi kuambiwa hivyo na mwanaume mwingine?”

    “Ndiyo!”

    “Ulijiuliza kwa nini wewe tu?”

    “Hapana!”

    “Unahisi kwa nini mwanaume huyo alikwambia wewe na tena na mimi nimekuja kukwambia wewe kwa mara nyingine?” aliuliza John, swali aliloulizwa, akaligeuza.

    “Yaani sina hata jibu.”

    “Kwa sababu ni mzuri! Unajiheshimu, unaonekana kuwa msichana tofauti sana unapokuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Umejuaje?”

    “Unaonekana tu, ila ninahitaji nijue kama nipo sahihi na ndiyo maana nimekufuata na kuhitaji kwenye uhusiano na wewe,” alisema John.

    Amanda alibaki kimya kwa muda, alimwangalia John, muda wote huo mwanaume huyo alikuwa akizungumza huku tabasamu likiwa usoni mwake.

    Kumkataa mwanaume kama huyo lilikuwa jambo gumu, alikuwa na akili na maisha yake yalionekana kuwa mazuri kuliko hata wengine waliowahi kumfuata.

    Na hicho ndicho alichokifikiria sana, kumuacha mwanaume kama huyo apite lilionekana kuwa kosa kubwa hivyo akajifanya kugomagoma lakini mwisho kabisa akakubaliana kuwa naye.

    Kwa John ilikuwa ni furaha, hakuamini kama alikubaliwa na msichana huyo. Alimpenda, moyo wake ulimwambia kwamba kuna siku moja angemuoa na kuwa mke wake wa ndoa.

    Huku akifikiria maisha ya raha tu mbele yake, hakufikiria kuhusu maumivu ambayo yangekuja hapo baadaye. Kwa zaidi ya dakika hamsini, akatokea kumwamini Amanda kwamba angempa furaha, hakukumbuka maneno aliyoyasema dakika chache zilizopita kwamba binadamu hakukamilika, alikuwa na mapungufu kwa kuwa hakuwa malaika.

    Hakuhisi kama kungekuwa na maumivu kwenye upande wa pili wa mahusiano yao, alichokuwa akikifikiria ni furaha ambayo angekuwa nayo baada ya kuwa na Amanda.





    “Tina upo wapi?”

    “Nipo huku Samaki Samaki, Mlimani City!”

    “Unafanya nini mbona mapema hivyo?”

    “Kuna jamaa nimekuja kumuona, ila ananiweka sana! Wewe upo wapi?”

    “Nipo hapa Mwenge ITV tunaweza kuonana?”

    “Kuna ishu gani?”

    “Njoo tuongee mara moja, halafu nitakutoa.”

    “Mh! Aya nakuja!”

    Yalikuwa ni mazungumzo kwa njia ya simu baina ya wasichana wawili, Amanda na Christina. Wasichana hao wawili walikuwa marafiki wakubwa, ilikuwa kazi ngumu sana kumuona mmojawapo pasipo mwingine.

    Walimaliza wote Chuo cha IFM mwaka huo na katika kipindi hicho walikuwa wakitafuta ajira katika taasisi mbalimbali kwa ajili ya maisha yao.

    Ukaribu wao ulikuwa mkubwa, kwa siku za karibu hawakuwa wameonana kutokana na maisha yao kuwa na changamoto nyingi za ajira.

    Amanda aliamua kumpigia simu rafiki yake huyo kwa lengo la kuonana na kuzungumza. Kulikuwa na jambo muhimu ambalo alihitaji sana ushauri wake kabla ya kufanya maamuzi yake binafsi.

    Walikubaliana waonane Mwenge, ITV na ndani ya dakika kadhaa walikaa kwenye kimgahawa kidogo na kuanza kuzungumza.

    Alichohitaji kusema Amanda ni kuhusu John, alikutana na mwanaume huyo, alimuelewa kwa sababu alikuwa mzuri wa sura, alimpagawisha zaidi kwa sababu alikuwa na pesa.

    Amanda akamwambia Christina kuhusu John, msichana huyo alibaki kimya akimsikiliza mwenzake. Kile alichokisikia hakuamini, moyo wake ulichoma kwa sababu kila siku rafiki yake huyo ndiye alikuwa akifuatwa na wanaume wazuri, wenye pesa tofauti na yeye.

    Alimsikiliza kwa makini. Ushauri ambao aliuhitaji muda huo ni kuhusu huyo John na mwanaume mwingine aliyeitwa kwa jina la Martin.

    Martin alikuwa jamaa yake tangu walipokuwa chuoni, walipanga mambo mengi likiwemo la kuishi pamoja hapo baadaye. Alimpenda sana kijana huyo, walifanya mambo mengi lakini kubwa zaidi likiwa ni kumtambulisha kwa wazazi wake kwamba alikuwa mpenzi wake ambaye alipanga kuoana naye.

    Alimpenda, ndiyo, lakini mwanaume ambaye alimfuata kipindi hicho alikuwa tofauti. Achana na uzuri wake, zile pesa alizokuwanazo zilimchanganya akili yake kupita kawaida.

    Akakaa kati, akawa kama fisi, tamaa ikamuingia, alitamani wanaume wote awamiliki lakini alishindwa, mmojawapo alitakiwa kuwa bora zaidi ya mwingine.

    “Sasa hapo unataka nikushauri nini?” aliuliza Christina huku akimwangalia rafiki yake, alikuwa na wivu mkali lakini uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana kana kwamba alifurahia alichokuwa akiambiwa.

    “Niwe na nani hapa?” aliuliza Amanda.

    “Wewe unampenda nani?”

    “Nawapenda wote!”

    “Wa zaidi?”

    “Martin jamani! Si unajua tumeanzia mbali! Hivi nikimuacha itakuwaje?”

    “Sasa hapo ni kumpenda ama kumuonea huruma?” aliuliza Christina.

    “Yaani hata sijui nisemeje!”

    “Na huyo mwingine?”

    “Ana pesa sana. Jana kanichukua kunipeleka pale Hyatt, ilikuwa balaa, sijui yule kaka anamliki visima vya mafuta!” alisema huku akijifanya kujifikirisha.

    “Kwani wewe katika maisha yako unahitaji nini hasa?” aliuliza Christina huku akimwangalia rafiki yake huyo.

    “Maisha mazuri!”

    “Basi kuwa na huyo mpya!”

    “Ila sasa...daah! Martin....” alijisemea.

    “Basi achana na huyo jamaa mpende Martin, si ndiye unampenda kwa moyo wa dhati!” alisema Christina.

    Amanda akanyamaza, ni kweli mbele yake kulikuwa na mtihani mzito, hakujua ni uchaguzi gani alitakiwa kufanya. Alimpenda Martin lakini kijana huyo hakuwa na maisha yoyote yale.

    Alimaliza naye chuo, na wakati huo kama alivyokuwa yeye hata kijana huyo alikuwa akitafuta ajira, aajiriwe na kuendelea na maisha yake lakini hiyo ilikuwa tofauti na John.

    Mwanaume huyo alionekana kuwa na maisha mazuri, alikuwa na pesa na alikuwa akifanya alichokuwa akikitaka kwa wakati wowote ule.

    Kitu kilichokuwa kikimsumbua moyoni mwake ni kuujua ukweli wa John, ni kweli alikuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati ama alihitaji kumfunua na kuondoka zake.

    Alitakiwa kufanya uamuzi sahihi lakini kabla ya yote alitakiwa kufanya uchunguzi kwa hali ya juu. Alipofika hatua hiyo ndipo akajilaumu kwa nini alimwambia Christina mapema hivyo.

    Alitakiwa kujiamulia mwenyewe kwamba ni uchunguzi ndiyo uliotakiwa kufanyika na mambo mengine yaendelee. Walizungumza mengi na baada ya kumaliza akachukua elfu thelathini na kumpa rafiki yake huyo.

    “Hizi alikupa yeye nini?”

    “Yaani wewe acha tu! Alinipa laki mbili za matumizi ya wiki hii!” alijibu Amanda.

    Moyo wa Christina ukazidi kuuma, aliumia kwa kuwa mwenzake alikuwa na mwanaume mwenye pesa ambaye angemaliza matatizo yote aliyokuwanayo.

    Wakati mwenzake akiwa na bahati hiyo, yeye alikuwa akihangaika usiku na mchana kutafuta wanaume wa namna hiyo. Aliishia kuchukuliwa na kutumiwa usiku mmoja na wanaume wenye vipesa na kumuacha kwenye mataa.

    Aliagana na Amanda huku akiwa na hasira moyoni mwake, moyo uliwaka kwa wivu mkali uliomfanya mpaka kuhisi kama muda wowote ule angeweza kufariki dunia.

    Hakutaka kukubali, hakutaka kuona mwenzake akiwa na mwanaume mwenye pesa halafu yeye abaki na wale kapuku, alitaka kupambana kuhakikisha anampata mwanaume huyo na kumpa kila kitu alichokihitaji, yakiwemo mapenzi matamu kitandani ili aachane na Amanda.

    Hakujua ni kwa namna gani angeweza kupata namba yake ya simu. Hakutaka kujua alikuwa na sura gani, doa gani lakini kuwa na sifa ya kuwa na pesa tu kwake ilitosha kabisa kulala na mwanaume huyo.

    Akajifanya kuwa karibu zaidi na rafiki yake, Amanda huku kila siku akionekana kucheka kumbe moyoni mwake akiwa na wivu mkali uliokuwa ukimtafuna kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele.

    Wakati yeye akiwa kwenye hali hiyo kwa Amanda ilikuwa tofauti kabisa, msichana huyo aliendelea kujiona kuwa mtu mwenye bahati, mbele yake alikuwa na wanaume wawili, wote walikuwa wakimpenda kwa mapenzi ya dhati na wakati huo ilikuwa ni uamuzi wake ni yupi ambaye alitakiwa kuwa naye.

    John alimpenda sana Amanda, alimuhitaji msichana huyo, mara kwa mara alikuwa akimpigia simu na kumjulia hali, hakutaka kuomuona akiwa kwenye hali ya huzuni, alitamani kumpa kila kitu kilichokuwa kikihitajika kwa msichana huyo.

    “Natamani sana kupendwa kama ninavyokupenda,” alisema John kwenye simu.

    “Nitakupenda kama unavyotaka!”

    “Nitashukuru sana! Naomba nikuulize kitu!”

    “Uliza tu mpenzi!”

    “Kuna mtu una-date naye kwa sasa?” aliuliza.

    Swali hilo hakulitegemea hata kidogo, lilimshtua, hakuwa amepanga jibu la haraka haraka la kumpa. Kumwambia alikuwa aki-date na mtu fulani ilimaanisha huo ungeweza kuwa mwisho wao.

    Alijiona kuwa msichana asiyekuwa na akili hata kidogo kama tu angekubaliana naye ndiyo kulikuwa na mwanaume mwingine, angezipata vipi pesa hizo? Yale maisha mazuri angeyapata wapi? Akaamua kumdanganya.

    “Hapana! Nipo singo now! Nyie wanaume wabaya sana ndiyo maana sitaki kuwaamini tena,” alisema Amanda.

    “Ila naomba uniamini!”

    “Sawa haina shida. Ila kwa nini umeniuliza hivyo?”

    “Ninahitaji kufahamu kabisa kama kuna mtu, haimaanishi nitakwambia uachane naye, hapana, sitokwambia ila nitatakiwa kujua kuna mtu mwingine hivyo nina kila sababu ya kumuonyesha mtu huyo nampenda mpaka niuteke moyo wake kwa asilimia mia moja kabisa na huyo mwingine atoke moyoni mwake,” alisema John.

    “Mh!”

    “Ndiyo hivyo! Kila mwanamke mzuri unayemuona ana mwanaume, hivyo tunapofanikiwa kumpata mwanamke wa mtu basi tumpende kwa dhati, tumuonyeshe mapenzi makubwa, yule mwingine ataachwa tu,” alisema John.

    “Kumbe!”

    “Ndiyo! Kama mtu kwenye uhusiano wake kila siku anapigwa, anadharauliwa, ananyanyaswa na kufanyiwa mambo ya kishenzi halafu wewe ukaingia na kumuonyesha mapenzi ya dhati, ukamjali, kumsikiliza na mambo mengine, kwa nini usiuteke moyo wake? Ni rahisi Amanda,” alisema John.

    “Nimekuelewa!”

    “Na kitu gani hupendi kufanyiwa na mpenzi wako?” aliuliza.

    “Mengi! Zaidi kusalitiwa!”

    “Sawa! Sitokusaliti!”

    “Na wewe?”

    “Sipendi kudanganywa! Ujinga wote unaanzia kwenye uongo. Mtu anapotaka kusaliti ni lazima aanze kudanganya, ajifanye anapenda sana kumbe nyuma ya pazia kuna kitu kingine. Uongo ndiyo dhambi ya kwanza duniani, si unalijua hilo?” alisema John na kuuliza.

    “Ndiyo!”

    “Basi ndiyo maana uongo ninauchukia sana. Inawezekana kama yule nyoka asingemdanganya Hawa pale bustanini na kuwafanya wale tunda, leo hii tungekuwa tunakula bata tu,” alisema John na kuanza kucheka.

    “Yaani wewe!”

    “Amanda mpenzi! Naomba usinidanganye, hata kama kitu kitaniumiza sana, naomba usinidanganye kwa sababu nikiujua ukweli baadaye na wakati umenidanganya, nitaumia sana,” alisema John.

    “Usijali! Sitokudanganya!”

    “Una uhakika?”

    “Ndiyo mpenzi!”

    ***

    Christina alikuwa akipambana kivyakevyake, ilikuwa ni lazima mwisho wa siku afanikiwe kwa kile alichokuwa akikihitaji, kuwa na John na kumfanya mwanaume wake.

    Kipindi hicho alikuwa bize sana lakini baada ya kuambiwa na Amanda kulikuwa na mwanaume mwenye pesa aliyekuwa naye akaamua kurudi na kuwa naye karibu kama ilivyokuwa chuoni.

    Kila siku walikuwa wakionana na kuzungumza mambo mengi, alichokuwa akikihitaji ni namba ya mwanaume huyo tu. Alijua jina lake aliitwa John, japokuwa kulikuwa na John wengi lakini aliamini baada ya kuliona jina hilo na namba angejua tu ndiye mwenyewe.

    Kama walikuwa wapenzi basi John huyo ndiye aliyekuwa akiongoza kupigiwa ama kupiga hivyo ilikuwa rahisi sana kuipata namba hiyo.

    Siku moja wakiwa chumbani kwa Amanda na msichana huyo kuitwa na mama yake ndiyo ilikuwa siku ambayo aliichukua simu yake na kuichukua namba hiyo.

    Haikuwa kazi kutoa loki ya simu hiyo, aliijua kwa kuwa walikuwa karibu, akaiandika namba hiyo na kuisevu kwa jina jingine kabisa na sasa kazi ikabaki kwake, kuhakikisha anafanikiwa kulichukua penzi la mwanaume huyo.

    Alivumilia, hakutaka kuingia kwa pupa, aliamini tu kwamba baada ya kukaa na Amanda kwa kipindi fulani angejua mengi kuhusu John.

    Na hilo ndilo lililotokea, bila msichana huyo kujua akamwambia kuhusu ofisi yake ilipokuwa na mambo mengine.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hiyo ndiyo nafasi ambayo msichana huyo alihitaji kuitumia, hakutaka kufanya jambo jingine zaidi ya kumfuata John huko Posta alipokuwa akifanya kazi.

    Hakuwa akijuana naye, aliamini baada ya kuonekana mbele ya macho yake angekuwa mtu mpya na kama angekuwa kama wanaume wengine inawezekana mwanaume huyo angeusha ndoano yake na kuhitaji penzi lake.

    Siku hiyo alivalia vilivyo, akaamua kuelekea huko. Kwa kuwa alikuwa na kiwowowo cha kishkaji, akavalia kisketi cha kubana kilichoishia juu ya magoti, blauzi na viatu virefu kidogo.

    Kila alipokuwa akipita, alivutia, alionekana kama msichana fulani aliyekuwa na pigo za hatari mno. Wanaume wote waliokuwa wakipishana naye walikuwa wakiangalia nyuma kuangalia kijungu chake.

    Hilo likampa uhakika wa kumpata John, kama kulikuwa na wanaume wengi waliokuwa wakigeuka na kumwangalia basi alikuwa na uhakika wa kumpata pasipo tatizo lolote lile.

    Alipofika nje ya jengo la ofisi ya John, kwanza akampigia simu Amanda, alihitaji kujua alikuwa mahali gani, hakutaka kugundulika, alizungumza naye na kumwambia aliagizwa na mama yake kwenda Mbezi Beach.

    “Oh! Basi sawa kipenzi changu,” alisema Christina.

    “Ulikuwa unahitaji nini my sweatie?”

    “Nijue kama upo nyumbani nije! Basi tutaonana baadaye bestie!”

    “Sawa love! Baadaye!” alisema Amanda na kukata simu.

    Christina akashusha pumzi ndefu na kuingia ndani. Alikuwa hajiamini hata kidogo. Hapo getini akamuulizia John, akaambiwa yupo na hata alipoangalia pembeni, Range nyeupe ilikuwa imepaki, aliamini alikuwepo kwa kuwa ni gari hilohilo ndilo aliloambiwa na Amanda alikuwa akilimiliki.

    Akapelekwa mpaka mapokezi, alipofika hapo akaomba kuonana naye kwani kulikuwa na kitu muhimu alihitaji kuzungumza naye, kilikuwa cha kiofisi zaidi.

    Haraka sana sekretari akapiga simu kwa bosi wake, John akapokea na alipoambiwa hivyo, akamruhusu msichana huyo aingie ndani.

    Akainuka na kupelekwa huko. Alipoufikia mlango, akashusha pumzi ndefu na kuingia ndani. Mlango ulipofunguliwa na sekretari, akashusha pumzi ndefu, mwanaume mzuri wa sura alikuwa nyuma ya meza iliyokuwa na iMac na mafaili kadhaa.

    Kwa jinsi alivyokuwa akionekana, alivyovalia Christina alishindwa kuamini kama kulikuwa na mwanaume mzuri namna hiyo, aliaminishwa wanaume waliokuwa na sura za hivyo walikufa kwenye Vita vya Pili vya Dunia mwaka 1945 lakini cha ajabu leo alikuwa amekutana naye.

    “Mungu wangu mbona natetemeka hivi?” alijiuliza huku akimwangalia John ambaye akasimama, akamkaribisha na kumpa mkono.

    Walipogusana tu, akahisi kama mwili wake ukipigwa shoti ya umeme, kijasho chembamba kikaanza kumtoka na wakati humo ofisini kulikuwa na kiyoyozi kilichokuwa kikipuliza mfululizo.

    “Karibu sana!” alisema John huku akimwangalia kwa tabasamu pana, hakujua kama lile tabasamu tayari jamaa alidata naye au ilikuwa kawaida yake kuwaonyesha wageni waliokuwa wakija ofisini mule.

    “Nashukuru!” aliitikia kwa sauti nyembamba, nyororo ambayo aliamini hakuwahi kuitumia kwa mwanaume yeyote yule.







    John alimwangalia msichana mrembo aliyekuwa mbele yake, ni kweli alipendeza na kuvutia, kila alipomwangalia na kujaribu kuweka kasoro zake, hakuona, alionekana kukamilika kwa asilimia mia moja.

    Kama mwanaume akaingiwa na tamaa za kumtaka Christina lakini alipoikumbuka sura ya mpenzi wake, Amanda, ghafla tamaa hiyo ikamtoka.

    Alimkaribisha kwa mbwembwe na msichana huyo kumwambia alikuwa na biashara alitaka kuifanya na kitu muhimu ambacho kilimpeleka hapo ni kutafuta network ya watu ambao walikuwa na uwezo wa kumsaidia na kumfanya kufika mbali.

    Alijielezea kwa ustadi mkubwa kabisa kiasi kwamba John hakugundua kama msichana huyo alikuwa na mipango yake mingine. Kama mfanyabiashara akaanza kumwambia jinsi ya kukabiliana na changamoto zilizokuwa mbele yake, kama kweli alihitaji kufanya biashara basi lingekuwa jambo zuri sana kutafuta network kubwa kama alivyotaka.

    “Ila hujaniambia ni biashara gani!” alisema John.

    “Nataka nifungue biashara ya juisi, ila niwe nawapelekea watu mwenyewe ofisini kwao,” alisema John.

    “Sijaona kama ni tatizo! Ninakuahidi kukusaidia kutafuta wateja, mimi nitakuwa namba moja, namba mbili watakuwa wafanyakazi wangu,” alisema John.

    Hilo lilimpa furaha Christina, aliamini kabisa hakugundulika na John aliongea kwa roho nzuri kama kumsaidia kutoka hapo alipokuwa.

    Walizungumza mambo mengi, kama saa moja na hatimaye msichana huyo kuondoka zake. Aliridhika na John, ni kweli alikuwa na sura nzuri, pesa, na alipomwambia alikuwa na wafanyakazi wake akachanganyikiwa zaidi, akagundua kweli mwanaume huyo alikuwa na pesa za kutosha.

    Hakutaka kumuonyesha Amanda kitu chochote kile, ilikuwa ni siri kubwa ambayo ilikuwa moyoni mwake siku zote. Walikuwa wakikutana, walizungumza kwa furaha pasipo kujua kwamba tayari mpenzi wake alianza mawasiliano ya kawaida na rafiki yake huyo.

    Christina alihitaji kuwa na John, hakutaka kutumia nguvu kubwa sana, alimuingia kama mtu aliyetaka kufanya biashara ya kuuza juisi katika ofisi mbalimbali, ili kuonyesha kwamba kweli alikuwa na lengo hilo, akaanza kutengeneza juisi hizo na kuzipeleka huko, akaongezewa na watu wengine na hatimaye kuanza kuingiza pesa.

    Alichogundua ni kwamba kweli kukutana na watu waliofanikiwa inaweza kukufanya kufanikiwa kama ilivyoanza kuonekana kwake, kwa kipindi cha wiki moja tu, alitumia kiasi cha shilingi elfu hamsini tu lakini akaingiza zaidi ya laki tano.

    Biashara ya juisi ilikuwa ndogo lakini aliuza kwa watu wengi. Hakuangalia kuhusu mafanikio hayo, hakuridhika nayo hata kidogo, lengo lake kubwa lilikuwa ni kumpata huyo John kwa kuamini angeingiza pesa nyingi kuliko kwenye biashara zake.

    John hakuacha kuwasiliana naye, aliyaona mabadiliko kwa msichana huyo, alikuwa akifanikiwa taratibu na kila walipokuwa wakizungumza kwenye simu, alimtia moyo kwamba alitakiwa kupambana usiku na mchana.

    “Christina! Biashara huwa zinaanza hivi! Cha msingi endelea kutafuta network ya watu wengine, nitaendelea kukupigania. Napenda sana kumuona msichana akipambana kama wewe,” alisema John.

    “Nashukuru sana!”

    “Usijali! Karibu!”

    Christina alivumilia sana lakini baada ya mwezi mmoja akapiga moyo konde, hakutaka kuona akiendelea kuteseka kisa mapenzi, kama kweli alimpenda John basi ilikuwa ni lazima amwambie ukweli.

    Alitaka kufanya mambo hayo kwa kuanza ishara ndogo tu, kuanza kumtumia emoj za makopa na mambo mengine. Kwa John alishangaa lakini hakutaka kuonyesha dhahiri juu ya mshangao wake, alimchukulia Christina kama msichana fulani aliyekuwa na uhuru wa kupenda, ila kwake, hakuwa radhi kumwambia kitu chochote cha mapenzi.

    Baada ya wiki nyingine kukatika ndipo msichana huyo alipoanza kumwambia ukweli juu ya jinsi alivyokuwa akijisikia. Alimueleza kwa makini kila kitu kwenye simu.

    John hakushangaa, alilitegemea hilo kwani hata wakati mwingine alipokuwa akizungumza naye na kuchati, msichana huyo alimuonyesha ishara fulani ambazo kwa mtu mzima kama yeye, alizielewa kabisa.

    Alichomwambia ni kwamba alichelewa, tayari alikuwa na msichana wake, aliyekuwa akimpenda na kisingekuwa kitu kizuri kama angeanza kumsaliti na wakati hakuwahi kufanyiwa kitu kama hicho.

    Hapo, Christina alitamani kumwambia kuhusu huyo Amanda kwamba alikuwa na mwanaume mwingine na yeye alipendwa kwa ajili ya pesa zake tu.

    Kila alipotaka kusema hivyo, akasita, halikuonekana kuwa jambo zuri, yaani alitakiwa kutumia nguvu zake, kumpata mwanaume huyo pasipo kumtaja Amanda kwenye ishu yoyote ile.

    “Najua John kwamba una mwanamke mwingine,” alisema Christina.

    “Umejuaje?”

    “Mwanaume mzuri kama wewe huwezi kukosa mwanamke,” alijibu.

    “Ndiyo hivyo! Sitoweza kuwa na wewe! Samahani!”

    “Lakini John! Hivi huoni jinsi ninavyokupenda?”

    “Naona, unajitahidi lakini mpenzi wangu Amanda ananipenda hata zaidi ya unavyonipenda, huwezi kujua hilo tu!” alisema John.

    Alipolisikia jina la Amanda moyo wake ukamchoma mno. Alikuwa akimchukia msichana huyo kwa kuwa tu alikuwa na mwanaume aliyekuwa na pesa, alihisi kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake.

    Hakuacha kumwambia maneno ya kimapenzi, kila siku alitumia muda wake mwingi kumpigia simu na kumtongoza kumnunulia zawadi na vitu vingine kuonyesha alivyokuwa akimpenda lakini mwanaume huyo hakutaka kuelewa.

    Siku zilikatika! Hatimaye mambo yote aliyokuwa akiyafanya yakamchosha, hivyo John akaamua kumualika kwenye chakula cha usiku, siku hiyo alipanga kumuonyesha sapraizi, awepo pamoja na mpenzi wake ili Christina aone tu sababu zilizomfanya kumkataa kila alipokuwa akimwambia kuhusu mapenzi.

    “Leo una ratiba gani mpenzi?” aliuliza John, alikuwa akizungumza na Amanda.

    “Nitakuwepo nyumbani!”

    “Naomba tuonane, nataka kula chakula cha usiku na wewe...” alisema John.

    “Wapi mpenzi?”

    “Kilimanjaro hotel!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sawa!”

    Zilipita siku nyingi kidogo hawakuwa wamepata chakula cha usiku pamoja. Siku hiyo ambayo aliambiwa walitakiwa kula chakula cha usiku pamoja alipanga kwenda kulala kwa mpenzi wake, Martin.

    Hakujua ni wapi alitakiwa kuchagua. Alikaa kwa kujifikiria sana na ndipo akaamua kwenda kula chakula cha usiku na John lakini endapo angemwambia suala la kwenda kulala naye, akatae kwa kisingizo cha mama yake kuumwa, ili tu apate muda wa kwenda kulala na Martin.

    Siku hiyo ilimfanya kuwa na furaha kama siku nyingine, alitamani kumpigia simu Christina na kumwambia lakini akauona moyo wake ukiwa mzito kufanya hivyo, hakutaka kujali sana, akaacha na hivyo kujiandaa kwa ajili ya usiku wa siku hiyo.

    Kwa John, alichokifanya ni kumpigia simu Christina na kumwambia kuhusu chakula cha usiku ambacho alitamani sana kula naye siku hiyo.

    Kwa msichana huyo ilikuwa kama ndoto, hakuamini kama kweli John angempa nafasi hiyo adhimu, hiyo ilionyesha kwamba alikubaliana naye, ila alitaka kuitumia nafasi hiyo kumuonyesha ni kwa namna gani alikuwa akimpenda.

    “Can I ask you something?” (naweza kukuuliza kitu?) aliuliza Christina.

    “Just go on...” (uliza tu)

    “Is it a date?” (ni mtoko wa kimapenzi?) aliuliza.

    “No! Just outing,” (hapana! Ni mtoko tu) alijibu John.

    Japokuwa mwanaume huyo alimwambia hivyo lakini akajipa moyo kwamba ulikuwa ni mtoko wa kimapenzi ila hakutaka kumwambia ukweli tu.

    Alichokifanya ni kumpigia simu Amanda na kumwambia alikutana na mwanaume ambaye alimpenda na siku hiyo alipanga kutoka naye mtoko wa kimapenzi.

    Hakumwambia kuhusu hoteli, alimpa taarifa ya chakula cha usiku tu ili hata kama kuna siku ingetokea msichana huyo akajua kilichokuwa kikiendelea basi aseme kwamba hakujua kama huyo alikuwa mpenzi wake.

    “Mungu akubariki! Sasa ndiyo utulie shoga yangu...” alisema Amanda kwa utani.

    “Nitatulia tu! Si kama wewe, mara Martin, mara John!” alisema Christina.

    “Yaani wewe acha tu! Yaani kama leo nimepata mtihani! John na Martin wote wanataka nikalale nao usiku wa leo!” alisema msichana huyo.

    “Kwa huyo ukaamua nini?”

    “Nitakutana na John mara moja ila kulala nitalala kwa Martin,” alisema.

    “Safi sana! Wa kwanza ni wa kwanza tu,” alisema Christina huku akicheka na kukata simu.

    John alikuwa akijiandaa, ilipofika majira ya saa moja, akampigia simu Christina na kumwambia ajiandae kwani angempitia baada ya kutoka kazini.

    Hilo halikuwa tatizo, akampitia na hatimaye kumchukua, kwanza alitaka kwenda naye huko hotelini, lakini akaahirisha na kumpeleka nyumbani kwao.

    Huko akakutana na wazazi wake, akamtambulisha rasmi kwamba alikuwa mchumba wake, mwanamke ambaye alitaka kumuoa na kuishi naye maisha yake yote.

    Kwa Amanda ilikuwa ni furaha tele, hakuamini kama kweli alipata nafasi kama hiyo, kutambulishwa kwa wazazi wa mpenzi wake kilikuwa kitu kikubwa kuliko vyote alivyowahi kufanyiwa.

    “Mnapendana kweli?” aliuliza baba yake John.

    “Ndiyo! Tunapendana na tunachokipanga ni kuoana na kuwa pamoja,” alijibu John huku akiwa na tabasamu pana.

    Wazazi hao wakawapa baraka zote na kisha kuondoka zao. Ilikuwa ni majira ya saa mbili usiku. Ndani ya gari walikuwa wakiongea mambo mengi, Amanda alimwambia John jinsi alivyokuwa akijisikia muda huo, hakuamini kama kweli alimtambulisha kwa wazazi wake.

    Walitumia dakika kadhaa wakafika katika Hoteli ya Kilimanjaro na kuteremka, wakaenda kwenye meza moja mgahawani na kutulia hapo. Haraka sana John akampigia simu Christina ambaye alimwambia yupo njiani.

    Waliagiza chakula na kuanza kula, walikuwa wakizungumza mambo mengi tu, baada kama ya nusu saa, tayari Christina alifika mahali hapo na hivyo kumpigia simu John

    “Njoo huku kwenye mgahawa!” alisema John.

    “Sawa love!”

    Ni ndani ya sekunde chache, Christina akatokea mahali hapo. Alipowaona watu hao, akashtuka, akabaki akimwangalia Amanda kwa mshtuko, hakuamini kile alichokuwa akikiangalia wakati huo.

    Amanda alibaki akiwa amekodoa macho, hakuamini kumuona rafiki yake huyo mahali hapo, alichanganyikiwa. Alikumbuka namna alivyozungumza naye na kumwambia alikuwa na miadi ya kuonana na mpenzi wake, kitendo cha kuwa hapo kilimfanya kuhisi mwanaume aliyekuwa akimzungumzia alikuwa John.

    John hakugundua kama wawili hao walikuwa wakishangaana, alichokifanya ni kusimama na kumkaribisha Christina mahali hapo, msichana huyo akakaa huku akiwa haelewi ni kitu gani kilikuwa kikiendelea kwani aliamini John angekuwa peke, asingekuwa na Amanda mahali hapo.

    “Si alisema anakwenda kwa Martin?” alijiuliza.

    Mtoko ukabadilika, ni kama roho zao zikaingiwa nyongo. Amanda alimwangalia Christina kwa hasira, akahisi kabisa rafiki yake huyo alikuwa akimuibia mpenzi wake bila kujua kitu kilichomuumiza mno.

    “Christina! Huyu ndiye huyo mwanaume uliyeniambia?” aliuliza Amanda huku akimwangalia Christina.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    John alishangaa, kitendo cha msichana huyo kutajwa jina na mpenzi wake kilimshtua kupita kawaida. Hapo akahisi wawili hao walikuwa wakifahamiana.

    “Mnafahamiana?” aliuliza John kwa mshtuko.

    “Ndiyo! Ni rafiki yangu! Aliniambia kwamba leo anakwenda kuonana na mwanaume anayempenda, kumbe ndiye wewe!” alisema Amanda, hata sahani ya chakula akaisogeza pembeni kabisa.

    “Kwani wewe si uliniambia utakwenda kulala kwa Martin, kwa nini upo hapa?” aliuliza Christina, sasa aliamua, rafiki yake alimwaga ugali, yeye akaamua kumwaga mboga.

    John alinyamaza, kile alichokisema Christina kilimuumiza mno, hakuamini kama mpenzi wake huyo alikuwa na ratiba nyingine ya kwenda kulala na mwanaume mwingine.

    Akashusha pumzi, Amanda akanyamaza, akaangalia chini, alihisi rafiki yake suala hilo angelifanya siri lakini kwenye hali ya kushangaza, akalimwaga mbele ya John.

    “Kulala kwa Martin? Martin ndiye nani?” aliuliza John huku akimwangalia Christina.

    “Ndiyo umuulize huyo! Nashangaa ananilaumu na wakati hakuwahi kuniambia kuhusu wewe,” alisema Christina, akajiweka upande mwingine kimaongezi kuonyesha hakuwa na kosa.

    “Amanda! Martin ndiye nani?” aliuliza John, hakutaka kuonyesha kukasirika, kwa mbali tabasamu lilionekana usoni mwake.

    “I was about to talk to you, so sorry!” (samahani, ndiyo nilipanga kuongea nawe) alijibu msichana huyo.

    “Really? What is it about?” (Kweli? Kuhusu nini?) aliuliza John.

    “Martin...”

    “Who the hell is he?” (ndiye nani?) aliuliza John.

    Amanda akanyamaza, kujibu lilikuwa jambo gumu mno. Rafiki yake huyo alimuharibia, hakutaka kumpoteza John kwani tayari mwanaume huyo alionyesha mapenzi ya wazi juu yake na kubwa zaidi ni kuwa alikwenda kumtambulisha mpaka kwa wazazi wake.

    Amanda hakuwa na ujanja, akaanza kumwamboa John kuhusu Martin, ni kweli alikuwa mpenzi wake na alipanga kuachana naye kwa kuwa alionyesha nia naye.

    “Kuachana naye?”

    “Ndiyo!”

    “Kivipi na wakati uliniambia huna mwanaume yeyote yule?” aliuliza John.

    “Naomba unisamehe!”

    “Amanda! Kama kweli uliweza kunidanganya kwa jambo hili, utaweza kuniambia ukweli kwa mengine? Leo ulipanga kwenda kulala kwa huyo Martin, hivi kuna kuachana hapa kweli? Amanda! Hapana kwa kweli!” alisema John, hapohapo akasimama, akamuita mhudumu na kuomba bili yake mezani.

    Muda huo Amanda alikuwa akilia tu, hakuamini kama kweli rafiki yake huyo alimpotezea mpenzi wake aliyekuwa na mapenzi ya dhati kwake.

    Christina hakujali, kwake kila kitu kilikuwa poa kabisa. Hakujiona kuwa na kosa kwani hata kama angeulizwa, angesema tu kuwa alikutana na mwanaume njiani, akamtongoza na ikawa hivyo, kosa la Amanda ni kwamba hakuwahi kumuonyesha mpenzi wake, hivyo hakujua.

    John alikuwa kimya, alijizuia kutokupiga kelele, hoteli hiyo ilikuwa na watu wenye heshima zao, hivyo hataka kama angetiwa hasira kwa namna yoyote ile asingethubutu kupayuka.

    Moyo wake ulimuuma mno, hakuamini mwanamke aliyekuwa akimuonyesha mapenzi yote, kumbe usiku huo alipanga kwenda kulala na mwanaume mwingine, moyo ulichoma kupita kawaida. Mhudumu akaleta bili yake, akaichukua, akaisoma na kumlipa.

    “Twende nikurudishe nyumbani!” alisema John huku akisimama na kuelekea ndani ya gari lake, Amanda akafuata.

    John hakuzungumza kitu, japokuwa msichana huyo alikuwa akiomba sana msamaha ndani ya gari lakini hakuongea chochote kile. Alichokigundua msichana huyo hakumpenda, alikuwa na mwanaume mwingine, kama kweli alipanga kwenda kulala naye, basi mapenzi hayakuwa kwake kabisa.

    Walitumia dakika kadhaa mpaka kufika kwao, akasimamisha gari na kumtaka ateremke.

    “Naomba unisamehe John mpenzi! Najua nimeko....”

    “Naomba uteremke garini! Tutaongea kesho!” alisema John, tayari macho yake yalikuwa mekundu mno.

    Kwa upole, Amanda akateremka ndani ya gari! John hakutaka kubaki, akaondoka zake mahali hapo, Amanda akaanza kulia kama mtoto, hakuamini kama John aliamua kumuacha, lawama zake zote zikawa kwa rafiki yake, hata urafiki wenyewe ukawa na dalili ya kufa.





    John alisimulia mambo mengi ambayo alikutana nayo kipindi cha nyuma kabla ya kwenda mkoani Kigoma. Deborah na wazazi wake walikuwa wakishangaa, hawakuamini kama kweli kile alichokuwa akikizungumza kilikuwa kilichotokea maishani mwake ama alikuwa amekitunga.

    Alionekana kuchoka, fukara asiyekuwa na kitu, ile stori iliyozungumziwa mbele yao ilionekana kama filamu fulani hivi ambapo baada ya muda wangeambiwa imemalizika.

    Juliana alikuwa kimya, alimwangalia mume wake, hakuamini yote hayo aliyokuwa ameyasikia kutoka mdomoni mwake. Kumbe John hakuwa kama alivyofikiria, alikuwa mwanaume wa kitajiri aliyekuwa na maisha mazuri mno.

    Alitamani kucheka, kulia kwa pamoja, hakujua ni kitu gani hasa alitakiwa kufanya kwa wakati huo. Mzee Abraham alikuwa akiangalia chini kwa aibu, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya.

    Alichoka, dharau zake zilimtokea puani kipindi hicho, alipoteza kila kitu kwa kuwa tu aliidhulumu serikali lakini aliamini hayo yote yalitokea kwa kuwa alimnyanyasa huyo John, kilichokuwa kikimshangaza zaidi, kumbe kampuni ambayo ilimfukuza kijana huyo ilikuwa yake!

    “Nashukuru sana Deborah kwa kuniamini siku zote,” alisema John huku akimwangalia msichana huyo.

    “Najua ulinipenda sana ila bahati mbaya wazazi wako hawakutaka uwe nami. Si kosa lako, kwenye maisha kuna mambo ambayo yanatokea kwa sababu ya makusudi ya Mungu. Huwezi kujua ni kitu gani kingetokea baada ya mimi kuwa na wewe, inawezekana Mungu akawatumia wazazi wako ili nisiwe na wewe, niwe na Juliana ambaye inawezekana kutokana na uvumilivu wake Mungu alimwandalia mwanaume kama mimi,” alisema John huku akimwangalia Deborah.

    “Nimeishi Kigoma kwa miaka miwili, nimepazoea sana, ni kama nyumbani ila nitatakiwa kuondoka na kwenda kuishi Dar es Salaam! Umenitendea wema sana wewe na mumeo, naomba niseme kitu kimoja, kesho nitaita kikao ofisini, nitakutangaza kuwa meneja mkuu wa kampuni yangu,” alisema John huku akimwangalia msichana huyo.

    Deborah akashtuka, hakuamini alichokisikia, ni kama alikuwa akiota vile, yaani mfanyakazi yeye wa kawaida kuchukua nafasi ya kuwa meneja badala ya mzee Masako, hakika ilikuwa ndoto ambayo hakuwahi kuiota hata siku moja.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Najua elimu yako si kubwa sana kama mzee Masako, ila utatakiwa kuwa meneja na mzee huyo nitamfukuza kazi ama kumshusha chini, huwezi kuwa na kiongozi ambaye anawasikiliza watu wengine wampangie maamuzi ya kuwafukuza watu kazi,” alisema John na kuendelea:

    “Baada ya kuwa meneja, utatakiwa kusoma, nitahakikisha unakwenda nchini Sweden kusomea japo kwa mwaka mmoja, kama utakwenda peke yako ama na mume wako, hakuna tatizo, nitahakikisha nasimamia kila kitu. Kama familia mtaamua nyie wenyewe,” alisema John na kuendelea:

    “Sifanyi haya kwa sababu una akili sana, au mfanyakazi mkubwa, ninafanya haya kwa sababu ya wema wako, kama ubaya hulipwa hapahapa duniani basi hata wema nao hulipwa hapahapa!” alisema na kumgeukia mzee Abraham.

    “Najua ni kwa namna gani umeghafirika sana, umechanganyikiwa, umekonda kupita kawaida. Ni maisha, huwa tunapita katika matatizo mengi sana. Na katika hili ninaamini utakuwa umejifunza sana. Unadaiwa bilioni mbili na TRA, nakuahidi nitazilipa. Ni kiasi kikubwa lakini nitajitahidi hata kulipa kidogokidogo na mwisho upate kila kitu chako kilichochukuliwa!” alisema John na kuendelea:

    “Sifanyi haya kwa kuwa umestahili sana, ninafanya kwa sababu ninataka kuwaonyesha watu kwamba tunaweza kulipa ubaya kwa wema, lakini pia ninafanya hivi kwa ajili ya binti yako. Ninahitaji kumuona akifurahia, yeye kuwa meneja huku baba yake akiwa kwenye hali mbaya, umeneja hauwezi kumpa furaha maishani mwake. Ninahitaji afurahie kila kitu na ndiyo maana nimeamua kufanya hayo yote,” alisema John.

    Mzee Abraham alikuwa kimya, kile alichoambiwa hakikuaminika masikioni mwake, macho yake yakaanza kuwa mekundu na baada ya sekunde kadhaa machozi yakaanza kumtitirika.

    Maneno aliyoongea John yalikuwa makubwa, yenye faraja lakini kwa msaada aliokuwa ameutoa kwake na kwa binti yake hakika hakuwa na uwezo wa kulipa wema huo hata siku moja.

    Pale kochini alipokaa, akajikuta akisimama na kutaka kupiga magoti mbele ya John, haraka sana mwanaume huyo akamuwahi na kumuinua na kumuomba kutofanya hivyo.

    “Ni Mungu pekee ndiye anayetakiwa kupigiwa magoti,” alisema John.

    Mzee Abraham alitamani kuongea lakini kilio kilikuwa kifuani mwake, akashindwa kuufumbua mdomo wake kuzungumza kitu chochote kile.

    Mke wake naye akasimama, akamsogelea John na wote kukumbatiana kwa kile alichokuwa amekifanya kwa familia hiyo.

    Baada ya dakika kadhaa, John na familia yake wakaaga, wakaondoka nyumbani hapo na kuelekea walipokuwa wamepanga. Muda wote huo Juliana alikuwa na maswali mengi, alikuwa akijiuliza kuhusu mume wake, ni kwa namna gani hakuwahi kumwambia kuhusu maisha yake halisi na wakati aliona kabisa walivyokuwa wakipigwa na maisha.

    Hilo akabaki nalo moyoni mwake lakini baada ya kufika nyumbani tu, kitu cha kwanza kilikuwa hicho. Kabla ya kujibu John akatoa tabasamu pana, akamsogelea mke wake na kumshika mikono.

    “Nilikuwa natafura mwanamke atakayenipenda kwa jinsi nilivyo!” alijibu John.

    “Lakini tayari tulioana, kwa nini hukuniambia?”

    “Kuoana si tatizo! Unaweza ukaoa, baada ya mwanamke kuona anateseka, anakimbia ndoa, hutokea kwa watu wengi sana, mnakubaliana kuishi kwenye shida na raha, ila shida zikiongezeka tu, wanakimbia,” alijibu John.

    “Nakupenda mume wangu!”

    “Nakupenda pia!” alisema John na kukumbatiana.

    Siku iliyofuata John akajiandaa na kwenda katika kampuni yake, alipofika huko, kwanza mlinzi akataka kumzuia lakini kwa jinsi mwanaume huyo alivyokuwa amevaa, alionekana kuwa tofauti na siku nyingine, akaamua kumuacha tu.

    Alikwenda mpaka mapokezi, sekretari alipomuona, alishtuka, hakuamini kumuona mwanaume huyo kwa mara nyingine tena, huku akiwa na muonekano mwingine kabisa.

    “Agnes! Nahitaji kumuona bosi!” alisema John huku akimwangalia dada wa mapokezi.

    “Haina shida! John! Mbona umebadilika?” aliuliza Agnes huku akimwangalia mwanaume huyo.

    “Nimepata bingo!”

    “Hahaha! Bingo gani tena na wewe?” aliuliza.

    John hakujibu zaidi ya kutoa tabasamu tu. Agnes akachukua simu yake na kupiga mpaka kwa sekretari wa meneja wake na kumwambia kulikuwa na mgeni alifika mahali hapo kwa lengo la kuonana na mzee Masako.

    Hakumwambia alikuwa mgeni gani ila akakubaliana naye na kwenda huko. Alipofika, naye sekratari akashangaa, hakuamini kumuona mfagia ofisi akiwa amerudi tena ofisini hapo akiwa na muonekano mwingine kabisa.

    “John! Ni wewe ama naota?” aliuliza msichana huyo.

    “Ni mimi Upendo! Mzima lakini?” alijibu John na kumjulia hali.

    “Wa afya tele!”

    “Ofisi yenu haikunitaka tena kisa demu!” alisema John huku akicheka.

    “Hahaha! Eti kisa demu! Halafu si unajua Deborah aliolewa?”

    “Ndiyo! Na mbaya zaidi hata hamkunialika nije kula ubwabwa! Mna roho mbaya sana nyie,” alisema John na wote kuanza kucheka.

    Walipiga stori kwa dakika chache na kumwambia kilichompeleka mahali pale. Alihitaji kuonana na mzee Masako, kwanza msichana huyo alisita kumruhusu kwa kuwa alimfahamu mzee huyo, alikuwa mtu wa lawama, hakupenda kuona akifanyiwa kitu ambacho hakupenda kufanyiwa.

    “Usiwe na hofu Upendo!” alisema John baada ya kumuona msichana huyo akionekana kuwa na hofu.

    “Basi subiri!” alisema.

    Akachukua mkonga wa simu na kumpigia mzee huyo, aliposikia John ndiye aliyefika mahali hapo, haraka sana akatoka ndani na kumfuata hapohapo mapokezi, hakutaka hata kuingia ofisini kwake.

    “John! Umefuata nini?” aliuliza mzee huyo bila hata salamu.

    “Kukusalimia tu mzee wangu! Shikamoo!” alisema John, alisimama na kumpa mkono huku akitoa tabasamu.

    “Marahaba! Nikusaidie nini? Au umekuja kunitambia kwamba maisha yako yamekuwa mazuri?” aliuliza mzee huyo huku akimwangalia John kuanzia juu mpaka chini.

    “Hapana mzee! Tunaweza kuingia ofisini tukaongea mara moja?” aliuliza John huku akimwangaliaangalia Upendo kumaanisha kitu alichotaka kuzungumza hapo msichana huyo hakutakiwa kusikia.

    “Hapana! Tuongee hapahapa! Nipo bize kidogo!”

    “Bosi! Naomba tu tuongee kidogo ndani!” alisema John.

    “Kuna ishu gani hasa?”

    “Ya muhimu sana! Nikuombe msamaha pia, ikiwezekana unirudishe kazini! Nilikwenda kusoma, nadhani sasa naweza kupata ngazi ya juu kidogo!” alisema John huku akitabasamu.

    “Kupata kazi hapa?”

    “Ndiyo!”

    “Cha kwanza hilo haliwezekani! Cha pili zungumza hayo mengine!”

    “Mzee Masako......”

    “Zungumza hapahapa!” alisema kwa hasira kidogo.

    “Utakuwa huru?”

    “Haina shida! Wewe zungumza!”

    Wakakaa kwenye kochi, mzee Masako alikuwa akimwangalia John, hakujua alibadilikaje kipindi hicho, alimshangaza kupita kawaida.

    John akaanza kuzungumza naye, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumpa tahadhali juu ya maamuzi aliyokuwa akiyafanya, kumfukuza mtu kazi kwa sababu tu aliambiwa na mtu fulani kufanya hivyo.

    “Kwa hiyo umekuja kuninanga na kunifundisha kazi?” aliuliza mzee huyo kwa ukali kidogo.

    “Hapana! Nimekuja kukupa taarifa moja tu!” alisema John.

    “Taarifa gani?”

    “Subiri!” alisema.

    John akatoa simu yake na kumpigia Deborah na kumuhitaji kufika mahali hapo. Ni ndani ya dakika moja, msichana huyo alifika hapo, kitu cha kwanza alichokitamka baada ya kumuona John ni neno ‘Bosi’.

    Mzee Masako alibaki akishangaa, hakujua kilichokuwa kikiendelea. John hakutaka kuzungumza lolote lile, alimwambia Deborah amwambie kila kitu kilichokuwa kikiendelea, na mwisho wa siku amwambie zaidi kuhusu mpango wa mkurugenzi juu ya mzee huyo, alipomaliza, akaondoka zake.

    Deborah akabaki kimya kidogo, alimwangalia mzee huyo, alionekana kuwa na hofu lakini hakuwa na jinsi, akaanza kumwambia yote kuhusu huyo John, mwanaume ambaye alimfukuza kazi kwa kuwa aliambiwa na baba yake kufanya hivyo.

    Mzee Masako alitulia akimsikiliza Deborah, kulikuwa na kiyoyozi lakini kwa maneno aliyokuwa akiambiwa, akaanza kuweweseka na kijasho chembamba kuanza kumtoka, alichoambiwa kilikuwa kama ndoto.

    “John ndiye mwenye kampuni hii?” aliuliza mzee Masako.

    “Ndiyo!”

    “Mzee huyo hakutaka kukubali, haraka sana akarudi ofisini kwake na kuangalia management nzima ya kampuni hiyo, alichoambiwa alihisi ni sahihi kwani mkurugenzi wa kampuni hiyo alijulikana kwa jina la Josephat Malecela.

    “Deborah! Njoo mara moja,” alisema mzee huyo, haraka sana Deborah akafika ndani ya ofisi hiyo.

    “Huyu anaitwa Jihn nani?”

    “John Malecela!”

    “Mungu wangu!” alisema mzee huyo na kukaa kwenye kiti.

    Aliona dunia yote ikiwa imemgeuka, hakuamini alichokuwa akikiona, aliuona mwisho wa maisha yake ukiwa umefika, kwa kile alichokuwa amemfanyia John aliamini kabisa angechukua uamuzi wa kumfukuza kazi.

    Alijuta, alitulia kwenye kiti chake, alihisi kabisa presha ikianza kupanda mpaka Deborah kuanza kuogopa. Ilipofika majira ya saa saba mchana muda wa chakula kukawa na kikao cha wafanyakazi wote.

    Wakaitwa na mtu ambaye aliyehitaji kuzungumza nao alikuwa John. Wote walishtuka na baada ya kujitambulisha wakashangaa, hawakuamini kama mwanaume huyo ndiye alikuwa mkurugenzi wa kampuni hiyo.

    Alianza kuongea nao, aliwashukuru kwa yote yaliyokuwa yakiendelea ndani ya kampuni hiyo, jinsi wafanyakazi walivyokuwa wakijitoa kufanya kazi usiku na mchana. Alimshukuru kila mmoja ambaye alijitahidi kuiendeleza kampuni hiyo mbele zaidi.

    Baada ya kuongea mengi, akawaahidi kitu kimoja kwamba ni lazima aboreshe mishahara yao zaidi, kwenye mambo mengi aliyoongea, hilo likawafanya watu wote wapige makofi na kushangilia.

    “Nitazungumza nanyi zaidi. Ila ofisi inafikiria kuwashusha baadhi ya wafanyakazi na kuwapandisha vyeo baadhi ya wafanyakazi. Naomba tuvumiliane kwa mabadiliko yoyote yatakayotokea,” alisema John na kufunga kikao, wafanyakazi wakatakiwa kwenda kuendelea na kazi zao.





    John na familia yake hawakukaa mkoani Kigoma, walichokifanya baada ya siku kadhaa ni kurudi jijini Dar es Salaam na kuanza maisha yao upya,

    Siku ambayo walifika nyumbani hapo Juliana alibaki akishangaa tu, hakuamini kama yeye ndiye ambaye aliolewa na mwanaume aliyekuwa akimiliki jumba kubwa na la kifahari kama lile alilokuwa akiliona mbele yake.

    Alibaki akiliangalia tu, hakuamini, kwa mwendo wa taratibu akamsogelea mume wake na kumkumbatia, hatimaye masikini yeye, mwanamke aliyekuwa kwenye maisha ya kimasikini kama yeye alikuwa akitarajiwa kuishi katika jumba hilo la kifahari.

    John alimwangalia Juliana, alimpenda, kwake alijivunia kuwa na mwanamke mzuri kama alivyokuwa mwanamke huyo. Alibaki akitabasamu na mara zote alitamani kumwambia ni kwa namna gani alimpenda, alimthamini kuliko mwanamke yeyote katika dunia hii.

    Kwenye eneo la maegesho ndani ya nyumba hiyo kulipaki magari ya kifahari, ya gharama kubwa ambayo yalimfanya mwanamke huyo kupigwa na mshangao kupita kawaida.

    John akamchukua na kumpeleka ndani. Mwanamke huyo alipoingia, alizidi kuchanganyikiwa, kwenye kila kitu alichokuwa akikiona ndani ya nyumba hiyo kilimfanya kutokuamini kwamba hatimaye alikuwa akitarajia kuishi humo.

    Maisha yalianza ndani ya nyumba hiyo, waliamua kusahau kila kitu kilichokuwa kimetokea. John hakuridhika, alitamani kuwa na utajiri mkubwa, alifungua biashara nyingine nyingi zilizomuingizia kiasi kikubwa cha pesa.

    Alikuwa kijana mdogo lakini mwenye mafanikio makubwa. Alihitaji mwanamke ambaye angempenda kwenye maisha yake ya shida aliyokuwanayo, akampata huyo Juliana ambaye alimuahidi angeishi naye mpaka siku wanaingia kaburini.

    Watoto wao wazuri waliendelea kukua bila matatizo kabisa. John akawa na daktari wa familia ambaye kila siku alikuwa na jukumu la kufika nyumbani hapo na kuwaangalia watoto hao wadogo.

    Kwa upande wa Deborah, aliendelea na maisha yake, kuna wakati mwingine alikuwa akiwalaumu wazazi wake moyoni kwa kuwafanya kutokuwa na John lakini pia kuna wakati mwingine alimshukuru Mungu kwa kuamini kila kitu kilichokuwa kimetokea kilikuwa katika mipango yake.

    Yeye na mume wake waliishi kwa furaha na upendo, walipendana mno. Maisha ya Deborah yalibadilika na hata siku ambayo alitakiwa kuanza kazi kama meneja wa kampuni hiyo, hakuamini, alikikalia kiti, akayafumba macho yake na kuanza kumshukuru Mungu.

    Ili kuonyesha hakuwa na tatizo lolote wala kisasi, John akamuhamisha mzee Masako na kwenda kusimamia kampuni yake iliyokuwa jijini Mwanza, akamlipa mshahara mzuri ila kitu ambacho alimtahadharisha ni kuwachukia watu wengine kwa sababu ya cheo chake.

    “Kuna watu wenye sifa nyingi kama zako, ni kitendo cha kuwaita tu, wakaja na kufanya kazi, ila ninaamini bado wewe ni binadamu na unaweza kubadilika,” alisem John, alikuwa akizungumza na mzee Masako aliyekuwa upande mwingine wa simu.

    “Nashukuru kwa nafasi nyingine bosi!”

    “Usijali!” alisema John na kukata simu.

    Stori ya maisha yake ikawa gumzo Kigoma nzima, hapakuwa na watu waliokuwa wakiamini kwamba yule kijana aliyekuwa akiishi kwenye maisha ya kimasikini, John alikuwa tajiri kama alivyokuwa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wapo waliokuwa wakibisha ambao walichukuliwa na kupelekwa mtaani kwake ambapo huko watu waliwajibu kwamba ni kweli kile walichokuwa wakikisikia ndicho kilikuwa ukweli wenyewe.

    Wengi walibadilika, waliokuwa na dharau dhidi ya watu masikini wakaanza kuwaheshimu watu hao kwani waliamini kama mzee Masako ilimtokea yale yaliyomtokea basi kulikuwa na uwezekano hata wa kuwatokea wao.

    Maisha yake yaliwabadilisha watu wengi. Vijana wengi wakajifunza, mabosi wakabadilika, masikini wakaheshimiwa. Kuanzia mwaka 2017 ambapo John alianza kuishi mkoani Kigoma, mpaka leo hii historia ya maisha yake ilibaki kuwa vichwani mwa watu wengi.



    MWISHO




0 comments:

Post a Comment

Blog