Search This Blog

Tuesday, 1 November 2022

PENZI CHUNGU - 4

 






Simulizi : Penzi Chungu

Sehemu Ya Nne (4)







Alisema kwa sauti kubwa. Mzee yule kwa mwendo wa haraka alienda nyumbani kwa mtendaji wa kijiji, muda uleule ikapigwa mbiu. Wanakijiji wote walikusanyika. Wakaambiwa taarifa ya kuonekana muuaji kijijini kwao. Taarifa iliyowastua sana. Huku wakisisitizwa wawe makini sana. Eti muuaji kaingia kijijini kwao.

Afisa mtendaji akapiga hatua moja mbele zaidi, alipiga simu kituo cha Polisi Mkuranga, kuomba msaada wa Polisi.

OCD wa Mkuranga aliipokea taarifa ile kwa hofu sana. Naye alipiga simu makao makuu ya Polisi, makao makuu wakamtaarifu askari anayehusika na kesi ile, Inspekta Jasmine yupo njiani. Kutoka kwa Inspekta Jasmine taarifa zilimfikia Veronica Baro, kutoka kwa Veronica Baro taarifa zikawafikia kina Kulwa na Doto. Wakati Inspekta Jasmine akiwa ndani ya gari lilikuwa linaenda kwa kasi kuelekea Mwanambaya. Kulwa, Doto na Dungu, nao walikuwa kwenye gari wakielekea huko kwa kasi kubwa zaidi.

Wote wakimuwahi Suto Sutani. Kina Kulwa kwa lengo la kumuua, wakati Polisi kwa lengo la kumkamata...



Gari ya kina Kulwa ilikuwa inaendeshwa kwa kasi sana. Nyuma ya usukani alikuwepo kijana wa kihuni, na akiendesha gari kihuni pia, alikuwa anaitwa Dungu, na alikuwa analitungua gari.



Suto Sutani, kwa mwendo wa taratibu alielekea kwenye ficho lake jipya. Bila kujua kuna hatari kubwa sana iliyokuwa inamkimbilia kwa kasi. Jambo usilolijua......

Aliingia katika kibanda chake , na kujilaza.



Kule kijijini Mwanambaya kulikuwa na taharuki kubwa sana. Wanakijiji walikuwa na hofu kubwa sana. Suto sasa alikuwa tishio. Wanakijiji wengi walikuwa wamekaa kwa mafungu wakimuongelea Suto Sutani huku wakionesha uwoga wao dhahiri.



Ghafla gari ya kina Dungu iliingia kwa kasi kubwa na kufunga breki kali, gari ile ilizidisha hofu kwa wanakijiji. Walianza kupiga kelele hovyo na kukimbia. Kelele zile zilitua moja kwa moja katika masikio ya Suto Sutani kule porini.



"Hapa siyo sehemu salama tena"

Alisema kwa sauti ndogo. Hakujishauri mara mbili, alibeba begi lake na kutokomea porini zaidi.



Kule kijijini ilikuwa patashika, Kulwa, Doto na Dungu walileta patashika kijijini. Waliingia kwa Mtindo mbaya, Mtindo ambao uliwafanya wakose ushirikiano toka kwa wanakijiji. Kila mmoja na bastola yake, walikuwa wanamtafuta Suto Sutani kwenye nyumba za watu.



Muda mfupi, vilisikika ving'ora kwa mbali, ishara kuwa Inspekta Jasmine na askari wengine walikuwa wanawasiri kijijini pale. Hali ya taharuki iliongezeka Mwanambaya !



Sasa kina Dungu nao iliwaingia hofu, walikimbia mbio na kupanda katika gari yao, waliifata barabara inayoelekea Mkuranga. Wale askari nao kufika Mwanambaya waliikuta taharuki kubwa, huku vumbi likiwa hewani, wanakijiji wote wakionesha kwa kidole njia inayoelekea Mkuranga. Bila kuuliza zaidi gari la Polisi lilielekea huko wakijua ndipo alipoelekea Suto Sutani.

Gari ya kina Dungu ilikuwa inaenda kwa kasi kubwa sana. Liliiacha mbali sana gari ya Polisi.

Dungu alikuwa mtoto wa kihuni mwenye kujua kweli kuliendesha gari kihuni. Walipokaribia jaribu, walipunguza mwendo wa gari. Na walipofika kijijini Jaribu, walisimamisha kabisa gari. Wakalipaki huku wenyewe wakikaa pembeni. Baada ya dakika kumi, waliliona gari ya Polisi ikipita kwa kasi kubwa sana. Huku king'ora cha hatari kikilia. Wakina Dungu walitabasamu, walipanda kwenye gari yao na kurejea kijijini Mwanambaya.

Walikaribia kijiji cha Mwanambaya, waliliacha gari na kuelekea Mwanambaya kwa miguu. Safari hii walibadiri mbinu, walikuwa wapole sana. Walikutana na mwanakijiji mmoja aliyawaeleza kila kitu kuhusu Suto Sutani, na mahali inaposemekana yupo kule porini. Kina Dungu, Kulwa na Doto walielekea huko.



Dungu na wenzake waliingia porini. Huku wakijilaumu kwa mbinu mbaya waliyoitumia mwanzoni walipofika pale kijijini. Porini kulikuwa na Giza la kutisha sana, la kumuogopesha mtu yeyote wa kawaida. Lakini Dungu, Kulwa na Doto hawakuwa watu wa kawaida kama mimi na wewe. Walikuwa manunda, walikuwa wameshindikana, walikuwa hawaogopi lolote, walisonga mbele kule porini bila wasiwasi wowote.



Inspekta Jasmine, pamoja na Polisi wake sasa walikuwa wanaingia Kibiti. Kwa kasi ileile na king'ora chao chenye sauti kali sana. Hawakubahatika kuliona gari lolote, kwa mara nyingine tena walihisi Suto Sutani kawazidi kete. Wao walikuwa wanajua mbio zile wanamkimbiza Suto. Walipofika Kibiti kijijini walisimama, waliwauliza watu na kuambiwa kuwa haijapita gari yoyote kijijini hapo, Inspekta Jasmine alifura kwa hasira. Alitamani kumkaba yule mtu aliyewapa taarifa ya kutoonekana kwa gari walilohisi anaendesha Suto Sutani. Waliamua kurejea Mwanambaya.



Wakati kina Dungu wakihangaika kule porini, Inspekta Jasmine na mapolisi wakihangaika kule Kibiti, Suto Sutani alikuwa Tandika. Alitembea kwa miguu pori kwa pori usiku ule akatokea Kisemvule, Kisemvule alipanda daladala iliyomteremsha Mbagala. Ulikuwa usiku hakukuwa na mtu aliyekuwa makini na Suto ndani ya gari. Kwa kutumia faida ya giza alipanda na kutulia katika gari ya Mbagala inayoelekea tandika bila kujulikana na mtu yeyote. Na sasa alikuwa amekaa katika darasa moja la shule ya Sekondari Maarifa.



Kule porini kina Dungu hawakumuona Suto. Walitafuta sana, lakini hawakumuona kabisa Suto. Waliamua kurejea kijijini.

wakati ule wakati kina Dungu wanaamua kurejea kijijini, kina Inspekta Jasmine nao ndio walikuwa wanaingia kijijini Mwanambaya.



Kina Dungu walikuja taratibu, walipokaribia kijijini waliona kitu kilichowastua sana.

Askari !

Askari zaidi ya kumi walikuwa wanakuja upande waliokuwa wao, kule porini. Kwa kasi ya ajabu vijana wale waliingia vichakani, walijificha.

Inspekta Jasmine na askari wake walipita pale bila kuhisi kitu chochote na kuelekea porini, askari walivyopita kina Dungu wao walinyanyuka na kuelekea kijijini. Walipofika waliongoza kule walikoliacha gari yao, walilichukua na kurejea mjini. Walifanikiwa kuwakwepa Polisi, lakini hawakufanikiwa kumkamata Suto Sutani ambaye ndiye alikuwa dhamira yao kuu...





Mapolisi nao walitafuta sana kule porini, hawakufanikiwa kumpata Suto. Ilikuwa kama hakuwahi kuwepo sehemu ile. Maaskari walirejea kijijini. Wakiwa mikono mitupu. Waliamua kuacha askari wawili kulinda kijijini pale, huku Inspekta Jasmine na askari wengine wakirejea mjini.



Alfajiri Suto Sutani ilimkuta mle darasani, aliupitisha usiku wa siku ile mlemle.

Aliamka.

Kutokana na mateso aliyoyapitia usiku ule dhamira yake ya kulipa kisasi ilizidi kushamiri. Aliteseka sana kule porini, aliteseka sana pale darasani. Aliamua kuyarejesha mateso aliyoyapata kwa waliomsababishia mateso hayo. Aliwakumbuka, Beji na Zura, askari Polisi waliomtesa sana gerezani, askari waliochangia kwa kiasi kikubwa kumpandikiza roho mbaya ya kikatili aliyokuwa nayo leo. Suto sasa aliamua kwenda kuwaonesha Beji na Zura matokeo ya kazi waliomfundisha. Aliamua kwenda kuwauwa Beji na Zura hukohuko Segerea. Alinunua kanga pale Tandika sokoni, akaongeza na idadi ya visu. Alivyovihifadhi vizuri katika begi dogo.

Alijifunga zile kanga mbili mwilini, kiunoni na kifuani, kanga iliyomsaidia kumfunika hadi kichwani. Sasa Suto alibadirika sana, alikuwa na taswira nyingine, taswira ya kimama, tofauti kabisa na taswira waliyokuwa nayo wakina Inspekta Jasmine na Polisi wenzie.



Aliingia katika daladala na kuelekea Segerea.

Gari liliondoka kwa mbwembwe nyingi za dereva pale Tandika sokoni. Safari ya kuelekea Segerea ilianza.



Walipofika njiani walikutana na askari wengi sana barabarani. Wakiosimamisha kila gari linalopita.

Na gari alilopanda Suto nalo lilisimamishwa. Kule ndani ilikuwa taharuki kubwa sana kwa Suto. Alipata mstuko mkubwa sana, alijua arobaini zake zimefika. Suto alianza kulia kwa uchungu, kilio kilichotokana na kushindwa kutekeleza kwa aliyoyapanga. Aliona huu ndio ulikuwa mwisho wa kisasi chake kwa watu waliomsababishia mateso makali sana duniani. Hakuwa anahofia kukamatwa Suto, ila alihofia kukamatwa kabla hajakamilisha kisasi chake, na hilo ndilo lililokuwa linamliza kwa uchungu mkubwa, kukamatwa kabla hajaimaliza orodha yake ya kifo !

Sasa askari walikuwa wanalisogelea gari alilopanda Suto Sutani....





Askari mmoja alilisogelea lile gari alilopanda Suto Sutani. Alienda upande wa kulia anaokaa dereva, na kuongea nae kidogo, kwakuwa Suto Sutani alikuwa amekaa katika siti za nyuma za ile daladala hakusikia lolote. Wakati yule askari akiongea na dereva alimuona askari mwengine akielekea ulipo mlango wa daladala ile.

Aliingia ndani !.

Suto Sutani aliinamia kiti, akijifanya amelala usingizi mzito. Askari alisogea hadi siti za mwisho za daladala ile. Akawa amesimama jirani kabisa na Suto Sutani, aliyekuwa ametopea katika usingizi mkali wa kuigiza huku jicho moja likiona kila kitu kinachoendelea.

Daladala ile ilisogezwa pembeni na kupaki, na kuzimwa kabisa na dereva.

Askari wengine wawili walilifuata daladala lile.



Ghafla!, msafara mkubwa wa magari ulipita, Suto Sutani kwa kutumia jicho lake moja aliushuhudia msafara ule. Gari la nne katika msafara ule ndio lililorejesha matumaini katika moyo wa Suto Sutani, alimuona Raisi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania akiwa na mkewe, wakiwa wametulia katika siti za kati za gari lile la kifahari. Suto sasa akaijua sababu ya kusimamishwa, kumbe msafara wa Raisi wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa anapita katika njia ile. Suto alipumua pumzi ndefu sana, huku akimshukuru Mungu kimoyomoyo. Baada ya msafara wa raisi kupita,waliruhusiwa kuendelea na safari. Laiti trafki wangeijua dhamira iliyopo katika moyo wa Suto Sutani, wasingeiruhusu daladala ile iendelee na safari yake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Daladala ilimfikisha Suto Sutani Segerea, aliwaona watoto wa maaskari wakicheza mpira wa manailoni katika uwanja mdogo wenye mchanga mwingi, Suto alimuita mtoto mmoja na kumuuliza.

"Hujambo mtoto"

"Sijambo, shikamoo"

"Ngoja nikuulize kitu mtoto mzuri, Dada Beji na Zura wanakaa nyumba gani?"

"Ngoja nikuitie Bakari mimi siwajui"

Mtoto ambaye aliyetambulika kama Bakari aliitwa, alikuwa mtoto mwenye umri mkubwa kidogo tofauti na yule aliyemuuliza Suto awali.

"Eti Bakari,Dada Beji na Zura wanakaa nyumba gani?"

"Walihama hapa siku nyingi, ila leo nimemuona Beji kwa mkuu wa gereza. Moyo wa Suto uliruka sarakasi !



Suto alimuaga harakaharaka yule mtoto, na kuelekea mahali ilipokuwa ofisi ya mkuu wa Gereza. Alikuwa anaijua vizuri sana ofisi hiyo.



Beji alikuwa ameleta malalamiko yake ya madai ya mafao kwa mkuu wa Gereza. Alishayapeleka katika Wizara ya mambo ya ndani, na nakala aliileta kwa mkuu wa Gereza la Segerea. Gereza alilokuwa anafanyia kazi. Kabla ya kisanga kile cha usiku kilichoondoka na kazi yake, kilichoondoka na mafao yake.

Beji na Zura hawakukubali!



Kazi kama hii ya kuleta nakala ya madai aliifanya Zura siku iliyopita. Ingawa sheria zilikuwa wazi kwa mtu aliyefukuzwa kazi, lakini Beji na Zura walikuwa vichwa ngumu!



Sasa Beji alikuwa anatoka katika ofisi ya mkuu wa Gereza baada ya kumkabidhi ile nakala.

Walikutana na Suto Sutani katika korido ndefu ya kutoka kule ofisini kwa mkuu wa Gereza. Beji hakumtambua kabisa Suto Sutani, wakati Suto alimtambua Beji vizuri sana. Huku akificha kwa ile kanga aliyovaa alikiweka kisu chake vizuri, kikiwa amekishika imara kwa mkono wake wa kulia. Huku lile begi lake lenye visu likibembea katika bega lake la kushoto.

Korido yote ilikuwa kimya. Msuguo wa viatu vya watu wawili tu ndio vilikuwa vinasikika, viatu vya Suto Sutani na msuguano wa viatu vya Beji. Walikaribiana kabisa sasa, walikuwa na tofauti kama ya hatua mbili hivi.



Mara, kwa kasi ya ajabu na nguvu zake zote Suto alipiga hatua kubwa kumkaribia Beji na kukididimiza kile kisu kirefu shingoni kwa Beji. Beji alistuka sana, alipata maumivu makali na mstuko mkubwa sana!. Suto aliishusha kabisa ile kanga iliyomfunika kichwani. Sasa alionekana vizuri sana.

"Suto ume-ni-u--a..." Beji aliongea kwa sauti ya kukatakata. Suto alipiga kofi la nguvu juu ya ule mpini wa kisu! Beji alitoa ukelele dhaifu wa kukata tamaa.

"Ndio, naitwa Suto Sutani!"

Suto Sutani alivaa vizuri ile kanga yake na kurudi kwa kasi kule alikotoka.

Akijua tayari kashaua!.



Beji hakutegemea kabisa kitendo alichofanyiwa na mwanamke yule katili. Kwa taabu alijishika pale shingoni kilipoingizwa kisu,

alistaajabu!.

Aliushika mpini tu wa kisu, kisu chote kilikuwa kimezama ndani ya shingo yake!

Beji alikosa nguvu, aliyumba, akajiegemeza katika ukuta wa Gereza lile, damu sasa ikawa inatoka shingoni mithili ya chemchem ya maji. Beji alijitahidi kupiga kelele, lakini alijisikia mwenyewe, sauti haikutoka kabisa. Mara aliona macho yake yamekuwa mazito, macho yalikuwa yanajifumba yenyewe taratibu huku yakishuhudia kwa mbali damu nyingi sana pale ukutani.

Beji alizimia !



Wakati Beji akipitia katika mateso makali na hatimaye kuzimia, Suto Sutani alikuwa katika daladala inayoelekea kariakoo. Alikuwa amesimama hakupata siti ya kukaa. Alikuwa mtulivu sana kama hajafanya tukio la kutisha sana dakika chache zilizopita. Alikuwa anaelekea kariakoo, akiamini wingi wa watu wa Kariakoo utakuwa faida kwake na kutokamatwa kwa urahisi na askari.



Akiwa amesimama wima, ghafla macho yake yakatua kwa kondakta wa daladala ile.

"Ndiye mwenyewe" Suto alisema kimoyomoyo, kondakta wa daladala ile alikuwa Banda mlevi. Mlevi aliyejaribu kutaka kumuua na kumbaka kwa mara ya kwanza Suto Sutani pale gerezani Segerea, pamoja na Giza la usiku ule haikuwa sababu ya Suto kutomtambua, alikumbuka vizuri sana umbo la mtu aliyepambana nae usiku gerezani, alikumbuka vizuri....



Suto alijipongeza sana kwa kupanda daladala ile. Daladala iliyomkutanisha na mmoja wa maadui zake!

Daladala ilienda huku ikishusha abiria na kupandisha wengine kama ilivyo kawaida. Hatimaye Suto Sutani naye alipata siti ya kukaa, katikakati ya daladala ile. Alikaa huku akiwa amepakata mkoba wake wenye vitendea kazi, visu vya kutosha kwa kazi maalum. Daladala ilipokaribia kariakoo yule abiria aliyekaa dirishani katika ile siti aliyokaa Suto alinyanyuka. Suto akasogea ile siti ya dirishani sasa, akajifanya amelala usingizi mzito.

Daladala ilifika mwisho, abiria wote walishuka, alibaki Suto Sutani pekee amelala ndani ya daladala.



Kondakta Banda aliangalia siti za gari yake, alimuona abiria mmoja amesalia, bila shaka amelala, alienda kwa mwendo wa haraka huku akipiga kelele za kumuamsha Suto.



"Oyaa utalipa na hela ya kitanda hapa!"



Suto alijifanya kama hasikii, kumbe maneno yote yalipenya vizuri sana katika masikio yake. Banda alimkaribia sasa, taratibu Suto alichomoa kisu katika begi lake, alikishika imara kile kisu kwa mkono wake wa kulia. Banda alimuinamia Suto, kwa lengo la kumtikisa ili amuamshe, alimpigia kelele kali huku akiwa anamtikisa bega kumuamsha, lilikuwa kosa kubwa sana alilolifanya Banda kondakta. Ghafla! Kwa nguvu zake zote Suto alizamisha kile kisu katika tumbo la Banda. Lilikuwa ni tendo la haraka ambalo Banda hakulitarajia, na atalirarajia vipi wakati hakuwa anamjua kwamba yule ndiye Mfungwa aliyetumwa kwenda kumuua! Alitumwa kazi usiku, alienda kuitekeleza usiku. Banda alitoa mguno hafifu wa maumivu, alijaribu kupeleka mkono katika tumbo lake, lakini haukufika, akajitupa pale kwenye kiti, huku akiruhusu damu nyingi sana zichafue siti za daladala ile. Macho yaliangalia juu ya kipaa cha gari, yamemtoka pima mithili kaiona ndoto ya jaha. Wakati dereva wake akiwa nje ya ile gari, ndani ya gari konda aliuwawa ndani ya gari.

Ndio, Banda aliuwawa!

Taratibu Suto alinyanyuka, na begi lake lenye kisu, na kushuka nje daladala, bila wasiwasi wowote, kama abiria wengine. Alijichanganya kwenye kundi kubwa la watu pale sokoni Kariakoo. Huku akiacha dhahma kubwa ndani ya ile daladala....



"Suto amebadirika!"



Kule gerezani Segerea kwa Beji hali ilikuwa ya taharuki kubwa sana!. Askari wengi walikuwa wamemzunguka Beji, wakiwa hawaelewi ni kitu gani kilichomtokea. Beji alikuwa ametapakaa damu mwili mzima, kasoro kichwa tu. Hata sehemu sahihi iliyopata jeraha ilikuwa haijulikani. Ilikuwa damu tupu!



Ni mkuu wa Gereza mwenyewe ndiye aliyekuwa wa kwanza kuuona mwili wa Beji pale chini. Alikuwa anatoka ofisini kwake ili kwenda haja ndogo, alishangaa sana kuuona mwili wa askari wake wa zamani ukiwa umelala hoi huku umeegemea ukuta. Aliusogelea taratibu.

Aliona Damu !

Aliushangaa mwili ule ulivyotapakaa damu, hakuelewa kabisa Beji amekumbwa na nini. Alipiga simu polisi kuwataarifu juu ya tukio lile la kutisha sana, kuwahi kutokea katika Gereza la Segerea. Wakati wanawasubiri askari Polisi ndipo askari wengine walijaa katika eneo lile. Wote walipigwa na butwaa, hawakuelewa kabisa kilichomkumba askari wa zamani Beji.



Baada ya nusu saa askari Polisi waliwasiri, wakiwa pamoja na daktari. Baada ya uchunguzi wa daktari uliochukua nusu saa, mwili wa Beji ulichukuliwa na kukimbizwa haraka hospitali. Kwa bahati nzuri Daktari aligundua kuwa Beji alikuwa hajafa, ila mapigo yake ya moyo yalikuwa chini sana.



Wakati hayo yanatokea huko Segerea, Inspekta Jasmine alikuwa ameketi ofisini kwake, akitafakari mwenendo wa kesi ya Suto Sutani, hakuelewa kabisa Suto anaupata wapi uwezo wa akili wa kuwakimbia Polisi waliopitia mafunzo namna ile. Historia yake ilionesha kwamba Suto hakumaliza hata darasa la saba, Siyo! Suto hakuanza hata darasa la kwanza. Historia hiyo ilizidi kumtia hasira Jasmine, askari msomi, anayeheshimika sana na viongozi wa juu Serikali na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kwa weledi wake, kwa umakini na uchapakazi wake, leo hii anazidiwa ujanja na Suto? Ilikuwa ni dharau kubwa sana.



Wakati Akiwaza hayo simu yake ya mezani iliita, simu ilitoka kwa yule askari Polisi aliyeenda kule Segerea, alimpa taarifa ya kuchomwa kisu kwa Beji!

Inspekta Jasmine alihamanika sana!

Dakika tano baadae alipokea tena simu, ilikuwa inatoka sokoni Kariakoo, simu yenye taarifa ya kuchomwa kisu kondakta wa daladala na kuuwawa!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Inspekta Jasmine hakuelewa, aende Kariakoo ama Amana hospitali ulikopelekwa mwili wa Beji?

Hakika alichanganyikiwa sana !



"Ngoma nzito kwa Inspekta Jasmine! "





Inspekta Jasmine alitoka nje ya ofisi yake. Alichukua pikipiki yake, aliiondosha kwa kasi kubwa lakini akiwa hana uelekeo maalum, hajui aende Amana hospitali ama Kariakoo sokoni. Lakini akiwa juu ya pikipiki alipata maamuzi, aliamua kwenda Amana hospitali, alijua mwili wa huyo mtu aliyeuwawa Kariakoo nao utapelekwa Amana tu.



Baada ya kufanya mauaji yale ya kikatili, Suto Sutani aliona Kariakoo siyo mahali salama tena kwake, alijua muda mchache ujao kariakoo itajaa maaskari wakimsaka muuaji wa kondakta yule. Hakutaka kabisa kukutana na Polisi wakati bado hajamaliza alichopanga kufanya, Suto Sutani alipanda daladala inayoelekea Mwenge kutokea Kariakoo.

Suto bado alikuwa na hela za kutosha, zile shilingi laki mbili za yule mvamizi kule gerezani bado zilimlinda. Alijua askari sasa itakuwa wameacha kumtafuta Hotelini. Alifika Mwenge na kuchukua chumba katika hoteli iitwayo Ocafona inn, chumba namba 41. Kuingia tu ndani alilala usingizi mzito sana sofani, maana alikuwa hajalala vizuri kwa siku mbili mfululizo.



Wakati Suto Sutani akilala katika hoteli Ocafona inn. Inspekta Jasmine alikuwa anateremka katika pikipiki yake, aliwasiri katika hospitali ya Amana, iliyopo Ilala. Moja kwa moja Inspekta Jasmine alienda ofisini kwa dokta Boniface, kujua hali ya mgonjwa mpya aliyeletwa, Beji.



"Za siku nyingi dokta"

"Safi, vipi za kazi?"

"Kazi imekuwa kazi kweli, vipi huyo mtu aliyepigwa kisu anaendeleaje?"

"Mgonjwa yuko ICU, kile kisu kiliingia sana shingoni, na kapoteza damu nyingi sana"

"Umeongea na mgonjwa hata kidogo dokta, anasema nini kilitokea dokta?" Inspekta Jasmine aliuliza kwa wahka mkubwa.

"Mgonjwa hajibu chochote anachoulizwa, yeye anasema neno moja tu tena kwa sauti dhaifu, Suto Suto Suto basi, nadhani anamzungumzia yule mwanamke muuaji.

Taarifa hizo zilimchosha kabisa Inspekta Jasmine, kabla hawajaamua wafanye nini simu ya dokta Boniface iliita.



" Nakuja sasa hivi" Dokta Boniface alijibu baada ya kuisikiliza simu, alitoka mbio huku akimwacha Inspekta Jasmine kapigwa na butwaa. Naye alitoka nje kinyonge. Alivyotoka nje aliona mwili wa mtu mwengine ukiwa umebebwa katika machela, na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti, baada ya kuuliza, Inspekta Jasmine aliambiwa ulikuwa mwili wa kondakta aliyeuwawa Kariakoo, Inspekta Jasmine akajua sasa mambo yamekuwa mambo.



Akiwa kasimama palepale ghafla alishikwa bega, Inspekta Jasmine alistuka sana. Aligeuka nyuma kwa haraka, mkono wake wa kulia ukiwa umeshafika kiunoni kuitoa bastola yake.



Alikuwa anatazamana na Dokta Boniface.

"Beji amefariki !"

"Unasema.."

"Alipoteza damu nyingi sana, amefariki Afande"

Chozi la hasira lilimtoka Inspekta Jasmine. Alikuwa anatumaini atapata kila kitu kutoka kwa Beji.

"Siku ya kukukamata Suto utajuta, utalipa damu ya watu hawa, nakwambia utalipa Suto, na nitakukamata tu Suto, hakuna marefu yasiyo na ncha, hakuna Suto, wewe ua, nami nitakipasua vibaya sana kifua chako kwa bastola hii Suto. Nitakuuwa baada ya kukupa mateso makali sana, chozi hili utalilipa Suto....."



"Vipi Inspekta mbona unalia?" Inspekta Jasmine alikatisha anachoongea na kumwangalia aliyemuita, alistuka sana, alikuwa ni Daniel Mwaseba !

Mpelelezi namba moja nchini Tanzania, kijana shupavu, jasiri, mwerevu, anayetumia akili nyingi sana katika kukamata wahalifu. Kijana asiyeogopa misukosuko katika kukamata wahalifu. Ni nani asiyemjua Daniel Mwaseba nchini Tanzania. Kijana aliyelisaidia Taifa katika mipango mingi mibaya iliyopangwa na maadui wa Taifa hili. Daniel Mwaseba alikuwa anatabasamu mbele ya chozi mwanana la Inspekta Jasmine.



"Hatukufunzwa kulia kutokana na matatizo, tulifunzwa kutatatua matatizo, iweje akulize Mhalifu afande, ni udhaifu na aibu pia" Daniel Mwaseba alimwambia Inspekta Jasmine.

"Afadhali umekuja Daniel, afadhali" Inspekta Jasmine ilikuwa kama hajayasikia maelezo ya Daniel, alikumbwa na furaha iliyoambatana na fadhaa, kumuona Daniel kwake ilikuwa ni kuisha kabisa kwa kesi anayoifatilia.



"Eeh nambie Inspekta, tatizo hasa nini?"

"Suto Sutani! "

"Suto" Daniel aliuliza kwa sauti kubwa.

"Unamjua Inspekta?"

"Anyway, tutafute sehemu nzuri tuongee"

"Twendeni mukaongelee ofisini kwangu" Dokta Boniface alitoa ushauri wake.

"Sawa dokta" Walikubaliana nae.



Askari wale wawili walienda ofisini kwa dokta Boniface. Waliketi vizuri vitini na kuanza kuongea.



"Eeh Daniel unamjua Suto?"

"Mmh simjui sana, lakini nipo hapa kwa ajiri ya kumjua Suto, na kujua vitu zaidi kuhusu Suto Sutani"

"Unataka kujua nini zaidi ya kukwambia Suto Sutani ni muuaji hatari zaidi kuwahi kutokea hapa Tanzania" Inspekta Jasmine aliongea kwa msisitizo.

"Ngoja nikwambie kwanini nimemfata Suto hapa"

Inspekta Jasmine alitulia tuli, na Kumsikiliza Daniel ambaye alimsimulia mambo mapya kabisa yanayoihusu kesi ile....





"Nimewasiri jana toka Ujerumani. Baada ya kuwasiri tu katika ardhi ya Tanzania, IGP aliniita. Nilitoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Juliuas Nyerere moja moja kwa moja nilienda kituo kikuu cha Polisi. Niliwakuta watu watatu ofisini, wote wamekaa wameshika tama. Wakiwa wamezongwa na mawazo.

Nilimkuta Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, nilimkuta mkuu wa majeshi, pamoja na mkuu wa Polisi Tanzania.

Kwa jinsi nilivyowakuta wamekaa nikajua kuna tatizo kubwa sana lililokuwa linawakabiri.

Mkuu wa Polisi, kamanda John Rondo ndiye aliyenikaribisha na kuniamuru nikae kwenye kiti, nilikaa nikiwa na hofu sana. Sikujua ni kitu gani kilichowakutanisha wakuu wale wakubwa wa nchi, tena wakiwa katika hali ya wasiwasi namna ile, IGP John Rondo alianza kuongea, kabla hata ya kusubiri nitulie vizuri kitini.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Alinambia mambo makubwa sana, mambo ambayo yalikuwa rahisi sana kuingia katika masikio yangu, lakini yalikuwa magumu sana kuyaelewa. Hata John Rondo mwenyewe hakuwa na uhakika sana na alichokuwa anakieleza, lakini mwishoni alinielekeza kwa mtu ambaye anaweza kunifafanulia mambo hayo, alinambia niende kwa usiri mkubwa sana, na nitumie ushawishi mkubwa sana ili aweze kunambia mambo hayo. Ni yeye aloyeyashuhudia mambo hayo, huku akionywa kutotoa siri ya mambo hayo, kutoa siri ni kuweka rehani maisha yake. Mtu huyo ni mwanamke, anaitwa Magdalena Zomba, lakini watu wengi wanamtambua kama mama Suto. Nilitoka pale kituo cha Polisi na kuelekea Tabata, nyumba akiyoishi mama Suto, niliwakuta majirani wachache, walionieleza kuwa mama Suto amefariki siku kadhaa, sasa nikajua kazi imeanza. Ndio nimekuja hapa moja kwa moja kuulizia ripoti ya uchunguzi wa kifo cha mama Suto iko wapi, nami nianze kazi yangu"



Inspekta Jasmine mwili wote ulikuwa unamtetemeka, alikumbuka alivyoidharau na kuipoteza ripoti zile za daktari kizembe, kumbe ripoti zile hasa ya Mama Suto ilikuwa na umuhimu mkubwa sana, ripoti ambayo ingetoa njia kwa kukamatwa kwa hao watu, wenye nia mbaya lakini isiyoeleweka wazi kwa wakuu wale wa Polisi na mkuu wa jeshi.



"Ripoti zilipotea Daniel" Inspekta Jasmine aliingea kwa sauti yenye kitetemezi.

"Zimepotea vipi Inspekta?"

"Kuna kibaka aliiba tukiwa katika foleni, na kufanikiwa kukimbia nazo"

"Come on Inspekta, hatufanyi mambo kiurahisi namna hiyo, alikukimbia vipi kibaka Inspekta ?."



Inspekta Jasmine hakuwa na la kusema, alimuomba radhi Daniel, huku akimuomba taarifa ya kupotea kwa ripoti asiipeleke kwa IGP.

"Sasa insp...." Daniel hakumalizia alichotaka kusema, simu ya Inspekta Jasmine ilikuwa inaita.

Akaipokea.

"Mnafanya kazi gani Inspekta, raia wenye hatia wanaendelea kuuwawa, au unataka tuandike kwamba jeshi la polisi ni wazembe kuliko taasisi yoyote Tanzania" Bila salamu Veronika Baro aliwaka kwenye simu.

"Come down mwandishi, tunalifanyia kazi"

"Hadi lini Afande, tuandikaje sasa kwenye magazeti, tuandike nini zaidi ya uzembe wa jeshi la Polisi ?." Inspekta Jasmine hakutaka kuendelea Kumsikiliza mwandishi yule alikata simu.

Mara, simu yake ilianza kuita tena, hakuipokea, alikuwa anaitazama tu mithili ya mtoto akiungalia kwa makini mdoli wake.



Daniel alimwangalia kwa huruma askari mwenzie, akajua kesi imemshinda, kwa mkanganyiko uliokuwepo katika kesi ile. Inspekta Jasmine aliendelea kuiangalia tu simu yake iliyokuwa inaita.



"Lete simu" Daniel alimwambia Inspekta Jasmine.

Bila kipingamizi wala ubishi wowote Inspekta alimpa simu yake Daniel Mwaseba.

Daniel aliipokea ile simu na kuongea kwa kujiamini.



"Naitwa Daniel Mwaseba, unahitajika leo katika kituo cha Polisi cha kati saa kumi jioni" Lengo la Daniel kusema hivyo ilikuwa ni kumfanya Veronica aiogope na kuiheshimu dola, lakini kauli ile ilipokelewa tofauti sana na Veronica.

"Daniel Mwaseba, umerudi?"

"Ndio, na nakuhitaji kwa mahojiano saa kumi jioni kituo cha Polisi kati" Daniel alisema bila kubabaika. Ghafla! Simu ya upande wa pili ilikatwa!

"Kuna kitu itakuwa anakijua huyu mwandish wa habari " Daniel alisema huku akimwangalia Inspekta Jasmine usoni.

"Sikuelewi Daniel"

"Hujaisikia sauti ya huyu mwandishi, baada ya kujua tu anaongea na mimi ameingiwa na woga, woga huo unajidhihirisha pia katika sauti yake, kwa nini aniogope, kama yeye ni mwandishi wa habari mzuri mwenye lengo la kupata habari tu ?"

Inspekta Jasmine alianza kuelewa sasa.

"Huyu mwandishi anaitwa nani?" Daniel aliuliza.

"Veronica, Veronica Baro"

"Sawa, mweke kwenye orodha yetu ya watu wa kutupeleka kwenye lengo"

"Sawa Daniel"

"Hapa hamna cha kusubiri, twende kituoni tuone kama Veronica Baro atakakuja, akija tutajua mbivu na mbichi baada ya kufanya nae mahojiano, asipokuja tutajiridhisha na tunachokihisi"

"Sawa Daniel"



Inspekta Jasmine alianza kuuhusudu uwezo wa Daniel Mwaseba. Siku ya kwanza tu kuingia Daniel katika kesi hii walianza kupiga hatua muhimu sana...



Kule upande wa pili kwa mwandishi wa habari nguli wa gazeti la Dumizi hali ilikuwa mbaya. Veronica Baro alikuwa anatetemeka, hajui lipi afanye, hajui lipi aache.

Mara nyingi sana alikuwa anamsifia Daniel Mwaseba katika makala zake mbalimbali gazetini. Alikuwa anaufahamu sana uwezo wa Daniel Mwaseba, kwa kuusikia uwezo wake na yeye kuuandika kwenye gazeti kwa umahiri mkubwa sana. Sasa leo hii alikuwa anaitwa kituo cha Polisi ili akahojiwe na Daniel Mwaseba.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Aliikumbuka vizuri sana makala yake moja aliyoiandika katika gazeti la Dumizi, miaka mitatu iliyopita. Makala yenye kichwa cha habari.

" Daniel, Mwanaume Hatari Zaidi Duniani" Makala hiyo ilimpa heshima sana Veronica Baro na kwa kiasi kikubwa ilichangia kupata tuzo ya mwandishi bora wa kike kwa mwaka huo. Tangu mwaka huo, Veronica aliendelea kuitwaa tuzo hiyo.

Veronica alikumbuka kuwa tamaa ya pesa ndiyo iliyomponza. Pesa za mama Bruno zilifanya Veronica Baro aitumie kalamu yake vibaya. Amkandamize Suto Sutani, ashindwe kabisa kuweka uwiano katika habari zake kuhusu Suto Sutani.

Sasa maji yalikuwa shingoni kwake.



Saa kumi kasoro dakika kumi na tano, Veronica Baro aliwasiri kituo cha Polisi cha kati. Alipokelewa na askari mmoja aliyemkuta kaunta. Baada ya kujieleza kuwa alikuwa na miadi na Daniel Mwaseba, alikaribishwa katika kiti kilichokuwepo pale mapokezi. Veronica Baro alionesha uwoga dhahiri usoni mwake, sura yake ilikuwa mithili ya mwanafunzi aliyekuwa anasubiri adhabu ya bakora toka kwa mwalimu anayemuogopa sana. Moyoni sasa roho ilimpwitapwita, miguu ilimtetema, alikuwa na hofu, hofu ya kukutana na Daniel Mwaseba!.

Saa kumi kamili ilifika, Veronica akiwa amekaa palepale, lakini Daniel Mwaseba alikuwa hajawasiri bado pale Polisi.

Saa kumi na nusu, Veronica ilimkuta amekaa palepale kitini,



Mara alinyanyuka kwenye kiti, muda huohuo Inspekta Jasmine aliingia akiwa katika sare zake safi za jeshi la Polisi. Kwa ishara ya mkono alimuashiria Veronica akae, bila kutafakari Veronica Baro alijipweteka tena kitini. Inspekta Jasmine alisalimiana na yule askari aliyekuwepo pale kaunta na kuingia ndani. Woga wa Veronica ulirejea kwa kasi zaidi safari hii. Kutosalimiwa na Inspekta Jasmine ilionesha kuna tatizo ndani yake. Sasa tumbo lilianza kumuunguruma. Ishara mbaya zaidi kwa mtu mwenye woga.

Inspekta Jasmine alirudi tena. Kwa mwendo wake wa madaha, kofia yake ya kipolisi ikiwa kaishika mkononi. Alimkaribia kabisa Veronica Baro, kisha akamuonesha ishara kuwa asimame, Veronica alisimama. Inspekta Jasmine alitoka nje akimwacha Veronica amesimama vile vile.



"Hivi ndivyo anavyopaswa kufanyiwa mwandishi wa habari?" Veronica Baro alimuuliza kwa hasira askari aliyekuwepo pale kaunta.

"Hapana....Hiyo ni namna sahihi ya kuwafanyia wahalifu!" Inspekta Jasmine alikuwa anaongea kumjibu Veronica huku alikuwa anaingia tena ndani.

Veronica Baro alistuka sana, lakini akajivisha ujasiri wa bandia.

"Nani mhalifu Inspekta Jasmine, kauli zitakuponza" Veronica Baro alimtisha kidogo Inspekta Jasmine.

"Kama wewe zilivyokuponza pesa" Inspekta Jasmine alimjibu bila kumwangalia usoni.

Kusikia kauli hiyo, moyo wa Veronica ulipiga kwa nguvu, akajua ameshajulikana, alihisi kama kavuliwa nguo zote, tena akiwa katikati ya soko.



Inspekta Jasmine alipatia, ni kweli pesa zilimponza Veronica, ingawa yeye ilimtoka tu hiyo kauli, hakukusudia.

"Nifate" Inspekta Jasmine aliongea huku akiiondoka, huku Veronica Baro akisimama na kumfata Inspekta Jasmine mithili ya mkia. Wakaingia katika ofisi moja pale kituoni. Kwa haraka Veronica Baro alifanikiwa kusoma kilichoandikwa juu ya mlango ule. Maneno makubwa yaliyonakshiwa kwa rangi nyeusi yalisomeka.



OFISI YA UPELELEZI WA MAKOSA YA JINAI.



Alipoingia ndani alimkuta Inspekta Jasmine ameshakaa tayari, kwenye kiti kilichokuwepo nyuma ya meza pekee iliyokuwemo mle ofisini. Meza iliyojaa mafaili na makaratasi mbalimbali.



"Karibu mwandishi bora nchini Tanzania"

Veronica Baro hakujibu, ajibu nini wakati mambo yalimuendea kombo kwa haraka sana. Hata hela zake alizopewa alikuwa hajazitumia vizuri. Leo hii anaingia matatani.



Veronica alikaa kitini, macho yake makubwa akiyainamisha chini kwa aibu.



Mara simu ya Inspekta Jasmine iliingia ujumbe, ujumbe toka kwa Daniel Mwaseba.



"Usimhoji chochote huyo Mwandishi, mruhusu tu aondoke"



Inspekta Jasmine aliushangaa sana ujumbe ule, alitamani kumuhoji Veronica kwa sababu aliona kila dalili kuwa Veronica Baro kuna vitu anavijua katika sakata lile. Hiyo ndio sababu iliyomfanya atamani kuupinga ujumbe wa Daniel lakini hakuweza. Kumpinga Daniel Mwaseba ni kumpinga Raisi wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyempa dhima hiyo Daniel Mwaseba.

Veronica Baro aliruhusiwa kuondoka bila ya kuhojiwa chochote pale kituoni.....



"Nini lengo la Daniel Mwaseba? Tuwemo wote katika sehemu inayofuata..







"Ni nini hii afande ?" Veronica Baro aliuliza kwa hamaki.

" nimekwambia ondoka! Au unataka kulala ndani?"

Veronica aliushangaa sana uamuzi ule wa Inspekta Jasmine.

Lakini hakuwa na jinsi, alitoka nje ya kituo kile kikubwa cha Polisi akiwa na wasiwasi mwingi.

Alisogea mbele kidogo ya kituo, alikodi teksi iliyokuwa inampeleka nyumbani kwake.

Ilivyotoka tu ile teksi, na gari nyingine iliyokuwa imepaki pale pembeni kituo cha Polisi nayo iliifuata teksi ile, na kuanza kuifuata ile teksi aliyopanda Veronica Baro. Bila kutambua kama anafuatwa Veronica alitulia katika siti za nyuma za ile teksi.



Dereva wa gari lile likilofuata nyuma ile teksi aliyopanda Veronica Baro alikuwa makini sana. Akihakikisha hatoi nafasi kwa ili gari ya mbele aliyopanda Veronica Baro kujua kama inafuatwa kwa nyuma. Na alifanikiwa kwa hilo.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Teksi aliyopanda Veronica Baro ilipaki katika Mgahawa. Na ile gari ikiyofuata kwa nyuma ilipaki kwa mbali kidogo. Dereva wa gari lile alimshuhudia Veronica Baro akishuka katika ile teksi, na kumuona akimlipa ujira wake dereva wa teksi ile.



Yule jamaa alikuwa ametulia tuli katika sukani ya ile gari. Akiangalia kila hatua aliyokuwa anapiga Veronica Baro. Alimshuhudia Veronica Baro akiingia kwenye ule Mgahawa baada ya kumlipa dereva wa teksi. Veronica Baro alitulia katika meza moja iliyokuwa pembeni ya Mgahawa ule.



Ilichukua muda mfupi, Mhudumu wa ule mgahawa alikuja na Veronica aliagizia kinywaji aina ya red bull, aliletewa na yule Mhudumu kwa kasi ileile, wahudumu walikuwa wanaijua sana kazi yao. Veronica alitulia na kuanza kunywa taratibu ile red bull.



Kule nje, yule jamaa alishuka katika ile gari. Kigiza mwanana cha saa moja kilikuwa kinaanza kuingia, kigiza ambacho kilimsaidia yule jamaa asionekane kabisa na macho ya Veronica Baro. Yule jamaa alichagua kiti kimoja kilichokuwa mbali kidogo na kile kiti alichokaa Veronica, naye akakaa. Mhudumu alienda kumulizia huduma anayoitaka, jamaa aliagiza maji makubwa ya Kilimanjaro. Akawa akayafungua na kuyaacha wazi bila kuyanywa.



Veronica Baro alikuwa hajatulia kabisa. Akiangaza macho Huku na huko, akaona kuna usalama, alitoa simu yake na kuiweka sikioni, aliongea kama dakika tano. Alimaliza na kuiweka simu yake katika mkoba mdogo mweusi. Akaichukua ile red bull yake na kupiga funda refu sana, ilimparia kidogo na nyingine kudondokea katika T-shirt yake nyeupe aliyokuwa ameivaa. Fulana Iliyoandikwa kwa mbele kwa maneno yaliyokolezwa kwa wino mweusi, DUMIZI.



Macho ya yule jamaa yalikuwa makini kuangalia katika mlango wa mgahawa ule. Ukimtathmini kila mtu anayeingia ndani ya mgahawa ule.



Kule nje nako pikipiki kubwa aina ya Baja ilipaki katika Mgahawa uleule, waliokuwemo Veronica Baro na yule jamaa. Katika ile pikipiki alishuka kijana mmoja, mrefu wastani, mwenye mwili wa kimazoezi. Alikuwa amevaa T-shirt nyeusi yenye mistari meupe mabegani na suruali ya bluu aina ya jeans.



Kijana huyo aliyeshuka kwenye pikipiki, kwa majina alikuwa anaitwa Daniel Mwaseba.

Kumbe yule dereva teksi aliyopanda Veronica Baro alikuwa shushushu wa jeshi la Polisi. Aliyewekwa kwa lengo maalum.

Wakati anarudi njiani alimpigia simu Daniel na kumuelekeza mahali alipomuacha mwandishi yule wa kike. Moja kwa moja Daniel aliwasha pikipiki lake na kuelekea katika Mgahawa ule. Alishuka katika lile Baja na kuingia katika mgahawa ule. Alielekea upande ule ule alioelekea yule jamaa aliyekuja awali.

Upande ule ulikuwa mzuri zaidi kwa mtu anayetaka kujificha. Yule jamaa na Daniel walikaa sehemu tofauti kwa meza kama tatu.

Ilikuwa inakaribia saa mbili usiku sasa.

Wote wawili wakiwa kwa mbali walimwona Veronica Baro akiangalia saa yake mara kwa mara. Ishara kuwa akitarajia mtu ama watu mahali pale.



Masaa matatu yalipita. Watu wale watatu walikuwa wamekaa vile vile. Hakukuwa na mgeni yeyote wa Veronica Baro aliyewasiri.



Mara, Veronica Baro alisimama na kuelekea nje ya mgahawa, huku akiiangalia simu yake, bila shaka akisoma ujumbe fulani. Daniel na yule jamaa nao waliinuka kwa muda tofauti katika viti vyao, walitoka nje nao. Lakini kule nje hawakumuona Veronica. Kila mmoja alijaribu kuangaza lakini Veronica hakuwepo kabisa.

Veronika Baro alikuwa ametoweka !





Daniel ndiye alikuwa wa kwanza kugundua kuwa, walikuwa wanamtafuta mtu mmoja yeye na yule jamaa. Daniel alimsogelea yule jamaa taratibu.



"Habari yako" Daniel alimsalimia yule jamaa huku akimwangalia kwa umakini mkubwa.

"Safi kaka, mambo?"

"Safi, samahani kaka mimi naitwa Daniel, Daniel Mwaseba..." Yule jamaa alimtolea macho Daniel kusikia jina hilo. Bila shaka hakutegemea kulisikia katika maisha yake.

"Mimi naitwa Bruno" Bruno alijitambulisha kwa sauti ya uwoga kidogo.

"Nimekuona umetoka nje kwa kasi, bila shaka ulikuwa unamfuata yule mwanamke?"

"Ndio Daniel, namsaka veronica Baro, namsaka nimuue!" Sasa sauti ya woga toka kwa Bruno ilipotea, aliongea akimaanisha.

"Umuue, kwanini umuue Veronica Baro Bruno?"

"Veronica Baro ni mwandishi wa habari mahiri sana, lakini mahiri pia kuitumia kalamu yake vibaya, ndio! anaitumia vibaya sana kalamu yake, ingawa watu wengi hawajui"

"Kivipi Bruno ? Sijakuelewa kabisa yaani"

"Hapa siyo sehemu nzuri ya kuongelea hili. Ni hadithi ndefu sana, hatuwezi kuiongea tukiwa tumesimama namna hii, turudi mgahawani nikakusimulie"



Daniel na Bruno walirudi tena katika ule mgahawa.



"Ee hebu nambie vizuri unavyomjua mwandishi Veronica Baro" Daniel alichokoza.

"Ni hadithi ndefu sana kama nilivyokwambia awali Daniel. Hapo mwanzo nilikuwa namsikia tu Veronica Baro. Nikimtambua kama mwandishi wa habari mahiri sana Tanzania. Mwandishi wa habari wa kumtolea mfano miongoni mwa waandishi katika fani hiyo. Nilikuwa sijui kabisa upande wa pili wa Veronica Baro. Nilianza kumjua vizuri zaidi Veronica baada ya mpenzi wangu kupata kesi.."

"Anaitwa nani huyo mpenzi wako?" Daniel aliuliza kwa shauku kubwa.

"Anaitwa Suto Sutani" Bruno alilitaja jina hilo akitegemea mstuko toka kwa Daniel, lakini Daniel hakustuka kabisa.

"Eeh" Daniel aliitikia kwa upole, ingawa alistuka kusikia jina la Suto Sutani lakini hakutaka kuuonesha kabisa mstuko wake.

"Mpenzi wangu alikabiliwa na kesi ya mauaji, siyo alikabiliwa, anakabiliwa na kesi ya mauaji mpaka sasa, anatafutwa kwa udi na uvumba usiku na mchana, lakini na uhakika Suto siyo muuaji!, wanamsingizia Suto wangu!" Bruno machozi yalikuwa yanambubujika. Lakini alikuwa analia kimya kimya bila kutoa sauti.

"Unajua sijakuelewa kabisa Bruno, hebu nyoosha maelezo kaka"

"Suto alikuwa mpenzi wangu Daniel, nilimpenda sana, alinipenda sana, kwa hakika tulipendana !

Lilikuwa penzi tamu sana, utamu wa penzi uliodumu kwa muda mfupi sana.



Siku ya kwanza tu ya Penzi hilo lilipata pingamizi, penzi lilikataliwa na watu wawili muhimu sana katika maisha yangu. Penzi langu na Suto Sutani lilipingwa na baba, lilipingwa na mama, penzi lilikataliwa katakata na wazazi wangu wapendwa.

Lakini mimi sikuwa tayari kumuacha Suto Sutani, mwanamke niliyempenda kuliko kitu chochote duniani, sikuwa tayari kulivunja penzi langu na Suto Sutani.

Kukataa huko kulivunja penzi hilo kulizua jambo, kukataa kwangu kulitengeneza chuki ! Chuki kali sana kati yangu na wazazi wangu wapendwa.

Tulikuwa na mgogoro mkubwa sana na wazazi wangu, mgogoro ulioanza siku yetu ya kwanza tu ya uhusiano wangu na Suto Sutani.

Lakini mimi nilikuwa mbishi, nilikuwa naamini mapenzi ya kweli kati yetu, mapenzi yatokayo moyoni ndio cha kuang'ang'ania penzi hilo. Nilimpenda sana Suto Sutani.



Siku tatu za Penzi lile zilikuwa chungu sana. Chungu, chungu, chungu sana. Chungu kuliko shubiri, chungu kuliko mwarobaini, chungu kuliko kitu chochote kile unachokijua kichungu.

Ndio zilikuwa chungu kwakuwa Suto alisingiziwa amewauwa wanaume watatu nyumbani kwao usiku !

Daniel, inakuingia akilini Suto Sutani kuweza kumuuwa mtu? Nakwambia Suto alikuwa muoga ! Alikuwa anaogopa hata kuuwa mende, kwa mtu mwoga namna hiyo inakuingia akilini Daniel eti Suto Sutani auwe wanaume watatu, tena usiku wenye giza kali. Kwanza Suto mwenyewe hilo giza alikuwa analiogopa. Kama Suto Sutani alikuwa anaogopa kuuwa mende kwa kiatu, ataweza vipi kuuwa mtu kwa shoka?

Hapana ! Walimsingizia Suto Sutani.



Suto alipelekwa Polisi, na hatimaye gerezani, Segerea. Suto aliingizwa kwenye gereza lile linalofanana na kiwanda cha mbu, Suto aliingia kule kwenye watu wenye roho mbaya kabisa. Watu makatili, watu waliyoyashinda maisha, huku maisha yenyewe yakiwa yana hasira na wao...." Bruno aliacha kuongea, alifuta machozi kwa kutumia shati lake lake. Akavuta kamasi nyepesi kwa ndani. Upande wa Daniel alikuwa makini kusikiliza kila kitu akichosema Bruno. Na kurekodi kwa siri bila Bruno kujua.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"Veronica Baro, mwandishi mshenzi kabisa kuwahi kutokea Tanzania, hapana...ni mwandishi mshenzi kuwahi kutokea duniani. Veronica Baro alijitahidi kumwandika vibaya sana Suto Sutani. Alitumia vibaya kalamu yake kuithibitishia dunia kwamba Suto Sutani alikuwa muuaji ! Hivi wewe Veronica ulikuwepo Wakati Suto anauwa? Una hakika Suto Sutani ni muuaji? Uliupata wapi ushahidi?









ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog