Search This Blog

Tuesday 1 November 2022

ZEE LA NYWILA - 5

 





    Simulizi : Zee La Nywila
    Sehemu Ya Tano (5)






    SAA nne usiku. John alikaa chini...mbele ya kompyuta yake iliyo chumbani mwake.



    Kiufupi, John ni mtaalam mno wa masuala ya Kimtandao.

    Aliiwasha haraka, akatafuta eneo ambalo simu yake ipo, kwa kuingiza 'codes' alizozijua yeye, haraka alifahamu ilipo...ilionesha ni maeneo ya Keko, mtaa upi na nyumba pia.



    "Ina maana, wale watoto wa Keko wameniona zoba sana eenh," John aliongea huku anatabasamu, "Kesho wataelewa kuwa Kinondoni, hatuishi mafala kama walivyodhani."



    Na kweli, John Palipokucha tu, aliamka mapema sana, akaelekea kituo cha polisi, huko akatoa taarifa kuwa kuna mhalifu yuko mahala fulani...ikiwezekana aongozane nao akawaoneshe.

    Hakuna polisi anayekataa kukamata mkiuka sheria, walitii.

    Safari ikaanza...



    Walipanda gari za Kariakoo, kufika hapo walichukua ya Temeke...wakaanza kuikatisha barabara ya Nyerere. Mpaka walipofika kituoni, keko. Wakateremka!



    Kwa msaada wa taarifa alizokuwa nazo John, za mtandaoni...walianza kuutafuta mtaa ambao simu yao ilioneshwa, ni mtaa wa Keko Magurumbashi.



    Wakafika hadi kwenye nyumba.

    Dooh, kumbe simu tayari ilishauzwa kwa mtu mwingine.

    Haya, nani kakuuzia?

    Akajifanya kumficha...polisi wakatoa vitambulisho vyao...maana walikuwa wamevaa kiraia tu.

    "Kuna vijana, hapo mtaa wa kati tu" aliwataja mwenyewe.



    Kwa tahadhari ya hali ya juu, walifika eneo waliloelekezwa...huku pua zao zikilakiwa na moshi mzito wa bangi.



    Ile kukunja tu, masela hawa hapa.

    Achana na hao masela sasa, yule jamaa aloyefanana na Abuu, naye alikuwepo.

    John alibaki ameduwaa kwa mara nyingine!



    _____





    WALICHOKOSEA polisi wale ni kitendo cha kuanza kuwakimbiza.

    Masela nao haoo, wakaunga.



    John bado alibaki ameduwa vilevile, "Ina maana huyu jamaa ni mtu kweli? Alikuwa sio mzimu! Au..."

    Kabla mawazo yake hayajamwisha, polisi walirejea, kijasho cha paji kikiwatoka kwa mbali.



    "Daah, tumewakosa b'ana. Hawa vijana inabidi siku tuwaandalie mkakati maalum. Tutawapata tu!"

    Askari mmoja mwenye cheo kushinda wenzake katika msafara ule aliongea huku pumzi zikipanda na kumshuka kwa kasi puani. Hazikuwa mbio za mchezo kabisa!



    ______



    LEO John alipanga kwenda kumtembelea Zainab. Ambaye hali yake haikuwa nzuri tangu kifo cha Abuu kilivyotokea.

    Baada ya msako wake na wale mapolisi kule kwenda mrama, alinyoosha moja kwa moja, nyumbani kwa Zainab.



    Huwa ana tabia ya kupiga simu na kutoa taarifa kwa Zainab ili amwambie mlinzi afungue geti. Lakini kwa siku hii, simu alikuwa hana...aligonga geti.



    Ithna'ashara dakika zilipita, mlinzi alikuja kufungua.

    Mlinzi huyu anamfahamu John, hakukuwa na walakini wowote wakati wa kuingia, aliingia mpaka chumbani kwa mgonjwa.



    "Zainab, unaendeleaje?" John alimsaili huku anaegesha makalio pembezoni mwa kitanda.

    "Salama..a tu!" alijibu kiuchovu huku akihitaji kama kujiinua kutoka alipokuwa amelala.

    "Aah aanh..." John alimzuia, "Acha tu Zainab."

    "Vipi, Harrison na Patrick bado wako hai?"

    Zainab aliuliza.



    Kiufupi, tangu kitokee kifo cha Abuu..., Zainab aliona ni Harrison na Patrick ndiyo sababu kuu ya kifo hiki. Hivyo, kila dakika alitamani kusikia habari za kifo chao pia!



    John jibu alikuwa nalo, ila alikwepesha swali na kuulizia kitu kingine,"Vipi daktari, alikuja kukufanyia vipimo leo asubuhi?"

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Daktari hata akija kila sekunde, haiwezi kusaidia John. Nachotaka kusikia ni kifo cha hawa wapumbavu. Ukishindwa, mlete Abuu."

    Zaina alijibu kwa kituo. Hakuongeza neno.



    Haikuwa vigumu kuamini ukiambiwa na mtu, kuwa msichana huyu amerukwa na akili.

    Mtu aliyekufa na akazikwa atawezaje kurudi?

    Ila ndiyo hivyo, huo ulibaki msimamo wake na hakutaka kuyumba!



    John hakuwa na namna, hakuweza kuongeza neno...akatoka na kwenda zake.

    Hata kama angeweza, Zainab pale alikwisha kumaliza...asingebadili kitu. Anachotaka ni taarifa ya kifo au Abuu aje.



    Hivi, mtu anayeota taarifa ya kifo na kuhitaji kukutana na marehemu...hutegemea nini kwa nafsi yake?

    Ngoja tuone!



    ...



    USINGIZI ndiyo tiba pekee John aliyoiona kwa wakati ule.

    Alipofika tu ndani mwake, alijibwaga juu ya kitanda ili apate usingizi. Ila, usingizi haukuja!



    Alijikuta anatembeza macho yake katika paa, lililokuwa kwa juu ilihali fikra yake ikipapasa matukio magumu na makubwa yaliyomkumba hivi karibuni.



    "Yule ni Abuu?" Aliwaza, akaguna kidogo na kujitoa kasoro mwenyewe, "Sio Abuu bwana, itakuwa ni mawazo yangu tu."

    Alipotezea. Baada ya kuamini kuwa kumuwaza sana Abuu kungeweza kupelekea kupachika watu asiowajua sura zisizo zao.



    Lakini bado suala hili, liliendelea kumtatiza...alimtilia shaka sana, yule jamaa aliyekumbana naye siku ile. Alishuku kuwa yeye ndiye aliyemuibia simu yake siku ile.



    "Akh, wa nini sasa? Simu yangu nishaipata."

    Abuu alijisemea kimoyomoyo.



    Ni kweli, simu yake ilikuwa mikononi mwa polisi, ikiwa laini imeshatupwa. Haijulikani aliyeiba ndiye katenda hivyo au laa!



    Alichofikiri John ni kuusitisha tu mpango wake wa kulipa kisasi. Zainab mwenyewe aliyekuwa anamtegemea ndiyo hivyo...keshavurigikiwa.

    Abuu tayari udongoni keshafukiwa, ya nini sasa kujivika wingi ukiwa?

    Aliamua kuacha na kuanza maisha mapya tu.



    Wazaramo hutuasa, "Ukiuanza mdundiko, kuukoma kati mwiko!"

    John alitakiwa aupige mpaka mwisho...



    Hakutambua ni usingizi ulimpitia tu wakati yuko mawazoni ama ni nini. Ila aliamshwa na sauti ya kugongwa kwa mlango wake.



    Mwanzoni, alihisi ni ndoto tu. Akapuuzia.

    Mara, mlango uligongwa tena, mara hii, ilikuwa ni kwa nguvu zaidi ya awali...akajiinua kitandani, akaelekea mpaka kitasa kilipo, akakisha.

    Alipitisha funguo kisha mlango ukafuatia kufunguka.



    Nje alikutana na sura mbili za kiume. Ngeni kabisa akilini mwake.



    "Habari yako bwana John," alimsaili mwanaume mmojawapo, mwenye sura ngumu, nyeusi na kavu...utafikiri haikuwahi kutabasamu kabisa tangu kuumbwa kwake.

    "Kwema tu, niwasaidie nini," John alijibu,moyoni wasiwasi ukiwa umemtapakaa. Ila alijizuia na kuonesha ujasiri wa hali ya juu.

    "Sisi ni maafisa wa polisi, kutoka kituo cha kati. Unahitajika ili kutoa maelezo kidogo." Mwanaume mwingine, aliyekuwa kushoto kwa yule wa kwanza...alijibu.

    "Kwa kuwa ni haki yangu kisheria, mnaweza kuniambia ni kesi gani hiyo ya kutolea maelezo?" John aliuliza.

    Askari akajibu, "Unatuhumiwa kwa mauaji ya Zainab, Zainab Said...yaliyotokea adhuhuri ya leo."

    ______





    "MAUAJI?" John alishtuka.

    "Hatuna muda kijana. Twende!" Aliamuru yule polisi mwingine.



    Kwakuwa mpaka dakika hiyo, tayari John alikuwa anatambua ana maadui wengi wamuwindao, hakutaka kuzolewa kizembe. Alijituliza kidogo, akawauliza kwa makini. "Hebu ngojeni kwanza. Nitaamini vipi kama ninyi ni mapolisi?"



    "Naitwa Afisa Kicheko Chanini!" Alijibu yule polisi mwenye sura ngumu na kuonesha kitambulisho. John alikitazama vizuri. Akathibitisha!



    "Afisa Dominic Fakayuku!" Mwingine pia alijitambulisha na kutoa kitambulisho chake.

    John hakuweza kukitazama mara hii.

    Tayari alishajua yu-mikononi mwa mapolisi.

    Hilo halikuwa shida kwake...

    Zainabu kauwawa? Kivipi?

    Hilo ndilo lililokuwa linamuweka njia panda.



    "Naona anataka kutupotezea muda huyu..." Yule polisi kauzu, mkavu wa sura, aliongea na kutaka kama kumkwida John suruali yake kwa nyuma.



    "Anh anh...naenda jamani!" John alikataa kitendo kile cha kuhadhirishwa, alikuwa anatambua fika! Kwamba ni haki kisheria mtuhimiwa kutoshurutishwa kama akikubali kutoka kwa hiyari. Kwakua bado haijathibitishwa ni mhalifu.



    John aliomba walau aingie ndani kidogo, alikubaliwa pia kufanya hivyo.

    Akaweka vitu vyake sawa na kuambatana na polisi wale mpaka nje ya nyumba.

    Hapo, kilipaki 'kipira' ambacho John alipandishwa na safari ya kuelekea kituoni, ilianza.



    ______



    MWENDO wa dakika thelathini na sita, uliweza kufanya pua za hawa watu watatu, walioko ndani ya kipira, kuweza kunusa harufu ya shombo ya samaki.

    Walishaikaribia Feri ama Kivukoni, kilipo kituo cha polisi cha kati.



    Gari iliingia ndani ya geti, na kuelekea karibu na jengo kubwa la polisi. Jengo lililokaribiana na ukingo wa bahari ya hindi. Hiki ndiko kituo cha kati... Waswahili hupaita 'Sentro'!



    Kwa mtindo ule ule waliopanda nao. Polisi mmoja alishuka, John akafuata kushushwa kisha akamalizia askari mwingine.



    Eneo hili halikuwa mara ya kwanza kwa John kufika. Kwa kuwa mwanzoni ilikuwa ni kwa wema na siku hii, alifikishwa kwa utuhumiwa...ilikuwa haki yake kibinadamu kutetemeka. Alitetemeka hasa!



    Kiuhalisia, John alikuwa anafahamu kwa asilimia zote kwamba yeye si mhalifu. Na hafahamu chochote kuhusu kosa hilo analotuhumiwa kwalo. Maana ni masaa machache tu, alitoka kuonana na huyo Zainab wanaosema wao kauwawa.

    Ila hilo, halikumfanya kujiamini na kwa kutanuka pindi anaingizwa ndani ya kituo kile...



    Walifika hadi mapokezi. Hapo walimkuta msichana. Alikuwa kavalia mavazi rasmi ya kiaskari. Tofauti na wale waliowasili na John, Afisa Kicheko Chanini na mwezie Dominiki Fakayuku, ambao walivaa mavazi ya kiraia tu.



    "Unaitwa nani?" aliuliza yule askari wa kike, huku akiwa anaandika katika faili lililokuwa mezani kwake.

    "Naitwa John..." John alijibu

    "Taja majina yote!" yule askari wa kike alimuamuru John.

    "John Simon Mbogo!" John aliongea kwa sauti ya chini.

    "Hebu kaza sauti mtoto wa kiume!" yule askari wa kike alifoka huku anapiga kalamu aliyoshika kwenye meza, kuonesha msisitizo.

    "Naitwa John Simon Mbogo!" John aliongea kwa sauti ya juu.

    Yule askari aliendelea kuandika, kisha akamuuliza tena, " Umri wako?"

    "Miaka ishirini na tano."

    "Ni Mtanzania?"

    "Ndi... Ndiyo!" John alijibu kwa mashaka, kitendo kilichomfanya askari amtilie shaka. Akamuuliza swali jingine ambalo hakuwa na umuhimu nalo kabla, " Kabila gani?"

    "Msambaa!" John alijibu.

    "Jinsia yako?" Askari akamuuliza tena, mara hii lilikuwa swali la ajabu sana.

    "Mwanaume!" John alijibu.

    Hakutaka kuwa mkaidi. Alitii na kujibu kila aliloulizwa ili kuthibitisha kutokuwa na hatia kwa lolote lile.



    Je, Utiifu ndiyo kigezo cha kuonesha ukosefu wa hatia?

    Ngoja tuone!



    Baada ya pale, John alichukuliwa mpaka ndani kidogo, huko alifungiwa katika chumba ili asubiri mahojiano yatakayoanza ndani ya muda mfupi.



    Katika chumba hiko, kulikuwa kuna meza moja na viti vilivyowekwa pande mbili tofauti, vikiwa vinatazamana.

    Huku mwanga ukiwa unaingia kwa kiasi kidogo sana.

    Hakikuwa na sauti yoyote inayopenya na kuingia ndanimwe, kutokana na kuta ngumu na nene zilizojenga chumba hiki, Palikuwa tulii.



    Ghafla, mlango ulianza kufunguliwa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hilo si tatizo.

    Ila, huyo aliyekuwa anaingia sasa...

    John alibaki hoi!

    _____



    ALIKUWA ni Patrick. Ukipenda muite Patty, ama 'The master plan'. Mwanaharamu aliyesababisha John aingie katika machungu ya milele. Mtu aliyemfanya akashindwa kuishi kwa furaha katika kipindi cha miaka mingi iliyopita mpaka hivyo.



    Leo amekuja tena machoni mwake. Mbele yake!

    Alivalia nguo za kiaskari na kutembea kwa madaha, mkononi kashikilia daftari na kalamu. Tayari kwa kumfanyia John mahojiano.

    Je, utiifu utamsaidia?

    Ngoja tuone!



    Patrick alitembea mpaka mbele ya ile meza, akakaa katika kiti kilichokuwepo upande mmoja.

    Baada ya hapo, alimuashiria John aketi katika kile kilichokuwepo upande mwingine.



    Muda wote huo, John alihisi macho yake yanaanza kumsaliti sasa.

    Anaonaje sura za watu katika mazingira yasiyowezekana?

    Alijishangaa bila kuelewa.



    Alihisi labda amefananisha tu..

    "Hapana. Patrick, Mtu mchafu kiasi kile...hawezi kuwa katika jeshi la polisi," Abuu alijikosoa kwa ukweli auonao mbele yake.



    "Naomba uketi hapo bwana John!" Patrick aliongea kwa upole. Hata sauti yake, haikuwa ile aitambuayo John.

    John alitii ingawa bado aliendelea kumshangaa yule aliyekuwa mbele yake.

    "Kwa majina, naitwa Sajini Patrick Kamugisha!" Patrick alijitambulisha.

    "Samahani," Kabla Patrick hajaemdelea na lolote, John alimkatisha. "Sajini ndiyo jina lako au?"

    John aliuliza ili apate uhakika. Ingawa jina Patrick Kamugisha... Analifahamu kabisa!

    "Hapana," Patrick alijibu huku akitabasamu. " Jina langu ni Patrick Kamugisha. Sajini ni cheo changu!"

    "Ina maana Patrick wewe ni askari?" John alijibu kwa jazba huku akitaka kusimama.

    Kwa kujiamini sana, Patrick alimpa maneno ya kumfanya akapoa, " Sikiliza kijana, hili eneo lina kanuni na taratibu zake. Labda nikupe kanuni moja tu... Ukitumia nguvu, nasi tunakuiga!"

    John alielewa, ila alihitaji apate uhakika, " Una maana gani?" aliuliza John.

    "Maana hiyo hiyo!" Patrick alijibu kwa dharau.



    Kimya kifupi kilipita, John akiwa anamtafakari aliye mbele yake. Kachanganyikiwa!

    Huku Patrick akifungua kijitabu chake, kwa ajili ya mahojiano kuanza.

    Naam, hatimaye yalianza...

    "Unamfahamu vipi marehemu?" Patrick aliuliza huku kainama chini.

    "Marehemu? Marehemu yupi?" Abuu aliuluza huku akiwa bado katika sintofahamu.

    "Zainabu alikuwa nani kwako?" Patrick aliuliza, wakati huu alikuwa amemkazia macho John.

    " Ni rafiki yangu..." John alijibu. Huku dhoruba ya khofu ikianza kupiga hodi ndani mwake.

    "Majira ya saa sita na nusu mchana. Tulipokea taarifa, kwamba kuna mwili umekutwa maeneo ya Ubungo-Kibangu.

    Taarifa hizo zinaeleza kuwa, marehemu alikutwa na jeraha kubwa la kisu tumboni mwake. Tena akiwa chumbani. Ndani ya nyumba yake. Je, una habari?" Patrick alieleza na kumalizia kwa swali...

    "Sina habari. Ni marehemu yupi?" John nae alijibu akamalizia kwa swali.

    "Hebu acha kuniimbisha ngojera dogo. Kwani mimi mara ya kwanza nilikuuliza nani?"

    "Uliniuliza kuhusu Zainabu."

    "Sasa? Unataka tupelekeshane kipunda au?"

    Japo John hakuelewa hiyo 'kipunda' ni nini, ila kwa namna ilivyoulizwa, alikataa. "Hapana!"



    "Kwa kuwa unajifanya mjinga. Sasa hivi nakuuliza maswali mengine. Nataka majibu ya aina mbili tu. Ndiyo au hapana! Unanisikia?"

    Patrick aliamuru kwa kufoka. Alionesha yu-weledi mno katika kazi yake.

    John aliitikia kuashiria yuko tayari kuhojiwa.

    "Haya. Leo ulikwenda nyumbani kwa Zainabu mida ya saa tano?"

    "Ndiyo!" John alijibu kwa kufuata maelekezo.

    "Uliingia hadi chumbani kwake?" Patrick aliuliza huku akimpa umakini mkubwa anayemuhoji, John.

    "Ndiyo, niliingia ha..."

    John alitaka kuleta maelezo mengi. Kabla hajamaliza, Patrick alimkatisha, " Dogo!"

    "Ndiyo," John alijirekebisha, akajibu tena kiusahihi.

    "Haukakaa sana?" Patrick aliuliza.

    "Ndiyo," alijibu John.

    "Ila siku zote, huwa unakaa sana!"

    "Ndiyo, lakini..."

    "Nimekwambiaje kijana?"

    "Sawa Afande! Sitorudia tena."

    " Huwa unapiga simu kabla ya kuingia ndani?"

    Patrick aliuliza. Hapo ndipo John akabaini maelezo hayo yote ametoa yule mlinzi wa getini.

    "Ndiyo," John alijibu.

    "Ila leo, siku ya mauaji...haukupiga simu!"

    Patrick aliendelea kuuliza maswali ambayo, yalizidi kumdidima John hatiani.

    "Sikupiga kwa kuwa..."

    "Hivi wewe, una akili sawasawa kweli?"

    Kabla John hajatoa maelezo ya kujitetea Patrick alimkatisha. "Nimekwambia sitaki maelezo. Nilikupa nafasi ya maelezo, ukajitia mwendawazimu."

    John alinywea. Hakuwa na la kufanya.

    Patrick akauliza swali jingine, " Umemuua Zainabu?"

    "Hapana!" John alijibu.



    Patrick alimtazama kwa dakika kadhaa machoni, kisha aliinama na kuandika baadhi ya maelezo katika kile kijidaftari chake.



    Baada ya kumaliza, alitoka nje ya chumba kile.

    John, alibaki mulemule ndani akiwa bado kitendawilini.

    Ina maana Zainab kauwawa?

    Na Patrick ni polisi?

    Hakuelewa kitu!



    BAADA ya dakika kadhaa. Patrick alirudi tena mule ndani. Safari hii alikuja kivingine. Hakuwa na daftari mkononi wala kalamu.

    Aliingia akaketi palepale pa mwanzo.



    "Mimi najua kabisa, kuwa unanifahamu John!"

    Patrick aliongea kishkaji. Kwa sauti ile ambayo John pia anaifahamu. Sauti ya kihuni.

    "Ndiyo," John alijibu kwa kufuata maelezo vilevile. Alishaingia woga, akauzoea pia.

    Patrick alicheka kwa nguvu, kisha akamtoa shaka,"Tulia John. Zainabu hajauwawa wala nini. Yuko hai kabisaa!"



    John alishangaa, akamtazama Patrick kwa hasira sana, na kuzungumza, " Sasa mnanifanyia mchezo gani?" aliuliza John kwa sauti kali.



    "Mchezo ulioucheza wewe!" Patrick alijibu kwa fumbo.

    "Mchezo nilioucheza mimi? Mchezo gani?"

    John hakuelewa.

    "Kwani wewe si unajiita G.C.I?"

    "Ndi...yo," John alijibu kwa wasiwasi. Hakujua Patrick kalifahamu vipi jina hili.

    "Basi nataka umrithi ZEE LA NYWILA!" Patrick aliongea kwa kituo.

    "Sijakuelewa bado Afande!" John alikuwa bado yuko katika mtego wa kifikra. Hakuelewa anachotaka kuambiwa na Patrick.

    Patty alicheka sana. Kisha akakikoma kicheko na kuendelea kuongea, "Unajifanya huelewi tu. Okay, kwa kufupisha stori, mimi ni afisa polisi, pia ni mpelelezi wa kiserikali. Nimekuwa nampeleleza Harrison kwa kazi anayoifanya takribani ni miaka kumi na tano sasa. Na tayari nimeshakusanya taarifa za kutosha. Hivi karibuni tu, tutamtia hatiani. Ila, bado kuna kitu...ambacho wewe yakupasa utusaidie."

    "Kitu gani?" John aliuliza. Huku ule wasiwasi wa awali, ambao ulimvaa tangu anaingia humu kituoni ukianza kumpaa.

    "Nafahamu kuwa una uwezo mzuri wa kuchezea mtandao. Au naongopa?"



    Kila alilokuwa anazungumza Patrick kwa John lilikuwa ni la kweli. Hakukosea lolote lile. Liwe ni la siri kwa John ama laa!



    "Ndiyo," John alikubali.



    Patrick aliketi sawa sawa katika kiti na kuanza kuongea, " Iko hivi, nataka uudukue mfumo mzima ambao Harrison anautumia. Ingawa mimi ni rafiki yake, na nimejitahidi kuuzidisha ukaribu kwake ila nimeshindwa kabisa, kwa miaka yote hiyo, kuipata NYWILA yake," Patrick aliongea akaweka kituo kidogo, alimeza funda hafifu la mate na kuendelea, "Nakufahamu. Wewe ndiyo ZEE LA NYWILA halisi. Hakuna Kompyuta inayokushinda!"



    John hakujibu kitu.

    Hakutambua akubali au akatae!



    "Mara ya kwanza uliniambia kuwa ni mchezo." John alijaribu kuhoji.

    "Unataka tuuitaje?" Patrick pia aliuliza.

    "Ina maana kuna kitu kingine pia nyuma yake?" John alizidi kumbana Patrick.

    "Kipo. Ila wachezaji pekee hukijua kitu hiko."

    "Kitu gani?"http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Umekubali kuwa mchezaji?"

    Patrick aliuchomoka uchochoro huo wa maswali aliokuwa amebanwa na John kitaalamu zaidi. Ndiyo taaluma yake. Ni mzungumzaji mzuri mno!

    John hakuwa na la kuongezea.

    Alibaki kimya.



    "Nakuachia kadi ya mawasiliano. Ukiwa tayari naomba unitafute!"

    Baada ya Kuona amemaliza kutoa maelezo yake, Patrick aliiweka kadi hiyo juu ya meza na kutoka nje.



    John alibaki bado ndani ya umande wa kutoelewa kitu.

    "Hivi ni huyuhuyu Patrick nimjuaye?

    Dooh... Walimwengu wana mengi sana," alijisemea John huku anaichukua kadi ile iliyokuwa juu ya meza.



    "Halafuu..." Mara, Patrick aliingia na kumsisitiza kitu. " Uliyoyaona, uliyosikia na kuyaongea humu. Yabakize humuhumu. Nakutakia siku njema!"

    Kisha huyo ak'enda zake...



    Muda kidogo, yule polisi kauzu, aliyejitambulisha kama Afisa Kicheko Chanini, aliingia na kumchukua John.

    Alimrudisha mpaka kwake.



    ________



    ALIFIKA kwake akiwa ana fikra mpya. Zile za kutaka kuacha kulipa kisasi kwa kuwa hana msaada, sasa ziliyeyuka. Zikampotea na zisirudi kamwe!



    Sasa John alipamga mikakati mipya ya kumkomoa Harrison.

    Kifo cha wazazi wake, na dada wa pekee...kilisababishwa na mtu huyo. Hivyo, mwisho wake uliwadia.



    Alitoa ile kadi mfukoni na kutafakari cha kufanya.

    Alipata jibu.

    Kwanza, alihitaji Patrick amtafutie yule kijana anayefanama na Abuu.

    Hilo likitimia, basi atafanya kazi hiyo aliyoombwa.



    Lakini, Tangu kuumbwa kwa dunia, Hakujawahi kutokea mtu alime mpunga akavuna mahindi.



    Kwa John litawezekana kweli?

    ...



    HAKUWA na' simu wakati ule, maamuzi aliyohisi ni sahihi kwake ni kwenda kuiazima kwa majirani, wapangaji wenzake.

    Alijiinua toka pale kitandani alipokuwa amejibwaga, mwili wake uliyumba kidogo mithili ya mlevi, labda ni kutokana na uchovu wa kashikashi za mapolisi alizokumbana nazo kutwa nzima.



    Kutoka nje ya mlango, alihisi hali ya tofauti, tofauti kabisa na siku mbili zilizopita. Chumba cha Ali Sodo leo kilikuwa kiko wazi.

    Tangu walivyopotezana kwenye vurumai la juzi yake, hawakutiana machoni.



    "Ingiaa!" Sauti ya kiume iliitikia kutoka ndani ikimkaribisha. Akaingia.

    Alimkuta Ali Sodo akiwa ameketi kitandani kwake, chumba hakikuwa na hata stuli.

    Vyombo vya vyakula pia havikuwepo, kuashiria aishie humu si mpikaji, zaidi hula kwenye migahawa tu na hapo siku yake ndiyo huwa imekwisha.



    Kwa kujivuta vilevile, huku akili yake ikiwa haielewi kuwa i–ndotoni au katika maisha halisi... John aliketi chini.

    "Enhee, imekuaje kwanza mwenzangu?" Ali Sodo naye aliketi sawa na kumuuliza.

    "Nikuulize wewe... Maana siku ya tatu hii!" John alimjibu.

    "Mbona mi' tangu jana nimerudi?" Ali Sodo alijibu.

    "Tangu jana? Mbona sikukuona Ali?"

    "Sema nilifikia kwa Mudi vyenga."

    Mudi vyenga, si jina halisi, ni mchezaji mwenza wa Ali Sodo katika timu yao.

    John alibaki kimya. Hakuwa pale kimawazo. Aliendelea kufikiri juu ya yale yaliomkumba mchana wa leo hiyo. Jini maamuzi bado aliendelea kumng'ong'a, hakuelewa nini afanye...

    "Mbona unaonekana hauko sawa kaka?" Ali Sodo baada ya kumuona yuko katika hali ile alimuuliza.

    John alikurupuka, mithili ya aliyeshtushwa kutoka usingizini. Kisha akazuga, "Ah, niko fresh tu kaka, kwani vipi?"

    Ali hakujibu kitu, aliendelea kumtazama kwa muda. Halafu akashusha pumzi nzito kidogo. Maongezi yakaendelea...

    "Enhee, tuongee kuhusu wewe, ulikuwa wapi kaka?" Ali Sodo aliuliza.

    "Acha tu kaka, yashapita hayo. Simu yako ina salio?" John alijibu na kuuliza.

    "Ndiyo."

    "Kuna mtu naomba nimpigie!"



    Ali Sodo alichomoa simu yake na kumpatia.

    Nyuso zao wote zilianza kung'aa kwa jasho jembamba lililokuwa likiwatoka kutokana na joto lilikuwepo ndani mule.

    Pamoja na ilikuwa muda wa usiku, ila udogo wa madirisha na namna nyumba zilivyobanana eneo hilo, joto liliweka mizizi yake...halikung'oka!



    John alikitoa kile kikaratasi ambacho Patrick alimpatia mchana, kule kituo cha polisi.

    Akaanza taratibu kuzihamisha ndani ya simu ile na kumpigia.

    Chini ya dakika, baada ya mlio wa muito, simu ilipokelewa.

    "Afande!" Sauti nzito kutoka upande wa pili iliita, si sauti ngeni kwa John, ni ile iliyotoka kumkoromea na kumpa mikwara mchana wa siku hiyo.

    Iweje afande punde tu baada ya kupokea?

    John aliweka mstari chini ya swali hilo kichwani mwake.

    "Hapana. Ni mimi!"

    Ukimya ukatawala upande wa pili. Hakuna jibu wala sauti iliyojaribu hata kukohoa.

    "...ni mimi John, John Simon!"http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Ooowh John, n'ambie John, habari yako kijana?"

    John hakujibu salamu ile, badala yake alienda moja kwa moja kwenye shida yake.

    "Nataka nikwambie kuwa...." Akakwama kidogo, kisha akaendelea, "...lile suala nimelikubali."

    Kicheko hafifu kilisika upande wa pili wa simu ile, alikuwa ni Patrick.

    "Vizuri sana! Huo ndiyo uwanaume! Mwanaume lazima uwe na roho ya fisi. Unaijua roho ya fiki wewe?" Patrick aliongea kisha akauliza swali.

    John hakujibu kitu, huenda hakuwa na la kujibu au swali hakulielewa, au alilielewa akalidharau.

    "Basi ngoja nikwambie leo roho ya fisi ilivyo," Patrick aliongea, akameza mate kwa mbali kisha akaendelea, " Fisi akila nyama, akila kiumbe, haachi kitu! Haijalishi ni mzoga au laa! Na hiyo ndiyo roho ya kiume. Ukianza kitu usiachie kati! Unamuachia nani? Masimba jike nd'o wanafanya hivyo."

    John alitabasamu kwa mbali kusikia maneno hayo, hakuyategemea. Ila aliendelea vilevile kuwa kimya. Alikuwa ni Kama mtu fulani hivi aliyekuwa amepooza ulimi.

    "Nambie John, unahisi tufanye mipango gani?"

    Hapo ndipo akafungua mdomo na kujibu, " Kuna mtu anafanana sana na Abuu, namtaka huyo!"

    Patrick akacheka sana. Kitendo hiko John hakukitegemea, alihisi angeweza kumshtua Patrick kwa kumtajia jina la Abuu.

    "Siyo anafanana John, ndiye yeye!"

    "Tuache utani basi!" John alihisi Patrick alitaka kumletea mzaha.

    "Hebu mpe simu Afande Ali!"

    Hiyo kauli ndo ilizidi kumvuruga. Aliona dunia imekuwa pembenne ghafla!

    Afande Ali? Kivipi?

    Mtungo wenye maswali ya kuvuruga ulimvaa John. Akampatia simu Ali kama Patrick alivyoagiza.

    Ali alizungumza na simu ile kwa dakika kadhaa...akakata, kisha akamwambia John kuna mahali anatakiwa ampeleke muda uleule. Bila kuchelewesha hata sekunde!





    KUNA nyakati namna pekee inayosalia kuepuka kutenda ovu, Ni kulitenda ovu hilo. Haijalishi ni kwa namna gani, njia gani na muda gani. Ila, jambo pekee linalosalia kichwani kwa mtendaji huyo, kuwa atalipiza kwa wema baadaye.

    Wachache sana hukumbuka kujiuliza, vipi baya hilo likizaa baya tena?



    John alikubali kuongozana na Ali Sodo. Muda huo, akiwa anamtambua kama Kamanda Alii.

    Kila hatua waliyokuwa wanaipiga, alikuwa akimtazama usoni kwa kumuiba. Kwa miezi sita yote waliyoishi katika nyumba moja, hakuweza hata kuhisi, sio kuhisi tu, hata kufikiri kuwa Ali Sodo angeweza kuwa ni askari wa jeshi la polisi.



    Waliongoza pamoja mpaka Kinondoni Studio, hapo wakasogea tena mpaka zilipo teksi...

    "Wapi maboss wangu?" Dereva mmoja aliuliza baada ya kuwasogelea kwa kuyaona macho ya uhitaji usafiri.

    "Tunaenda Holiday Inn, bei gani?" Ali Sodo aliongea huku akimtazama dereva yule kwa umakini kiasi.

    "Wapi? Ya Posta pale?" aliuliza dereva huku bashasha ya kazi ikiwa imemjaa mdomoni.



    Kwake John mazungumzo hayo yalikuwa kama kelele fulani zisizo na maana masikioni mwake. Akili yake haikuwa hapo hata kidogo. Moyo wake ulijawa shauku na hamu ya kumuona huyo Abuu aliyehai. Ilihali yeye Abuu alishamzika, na mpaka makaburini mwili unafukiwa kwa udongo alikuwepo.

    Iweje yuko hai?

    Alitamani sana kufahamu.



    "Okay, basi nitakufanyieni kwa elfu kumi na nane!"

    "K'o umegoma kumi na tano?" Ali Sodo aliendelea kubembeleza.

    "Si' unaona kumeshakuchwa ndugu, halafu mjini kule, jioni hii..."

    "Poa basi. Twende zetu..."

    Hatimaye muafaka ulipatikana.



    .....

    Safari ilichukua kama dakika thelathini na tano hivi, walikwisha kuwasili mtaa wa Azikiwe, kulipo hoteli kubwa ya holiday inn.



    Kwa John haikuwa mara ya kwanza kufika eneo hilo. Alifika sana wakati wa enzi za uhai wa Abuu. Mipango yao mingi walikuwa wakiifanyia ndani humo.



    Idadi kubwa ya magari yalioegeshwa eneo la nje yalikuwa ni ya bei kubwa. Kuashiria waliomo ndani hawakuwa watu wa kawaida kiuchumi.



    Kwa maelekezo ya Patrick, walifika mpaka ndani ya mgahawa ambao walikuwemo.

    "Angalia huku 'kaunta'!"

    Patrick alitoa maelezo, yalisikika kupitia simu aliyokuwa nayo Ali Sodo mkononi. Ama Kamanda Alii.

    "Sie tupo kaunta hapa mbona?"

    "Sawa,"

    Kisha simu ikakatwa.



    Walishtushwa kwa kuguswa mabegani mwao. Mshtuko zaidi, ulikuwa ni kwa John, hakuamini kile alichokuwa akikiona baada ya kugeuka, mwanzoni alikuwa akijipa faraja kuwa huenda ni picha zilizokuwa mawazoni mwake tu. Leo Abuu aliyekuwa akifahamu kafariki dunia bado yuko katika uoni wake, yuko hai.

    Mapigo yake ya moyo alihisi yamesimama kwa muda, kisha, yakaendelea kupiga, kwa kasi zaidi ya kawaida.

    "A..buu?!" John alijikaza na kutamka jina hilo...hakuelewa Kama alikuwa akiita au akiuliza.



    Abuu ambaye alikuwa akitazamwa hakuwa na tofauti yoyote akilini mwake, muda wote alikuwa alitabasamu na mara chache kushangaa baadhi ya vitu.

    Alikuwa amevaa kwa unadhifu wa hali ya juu, suti ilimkaa vema mwilini mwake. Vilevile Abuu!

    "Huyu si Abuu bwana!" Patrick alizungumza, mkononi alikuwa kashikilia bilauli ndogo iliyojaa kinywaji kikali.

    Kauli hii ilizama kichwani mwa John na kuukoroga ubongo wake usijue cha kufikiri wala kusema, bumbuwazi likatamalaki. Kimyaa!

    Ni Abuu halafu sio Abuu?

    "...msijali, tutaelezana yote. Naomba tutafute meza tukae." Patrick alizungumza halafu akawa anaongoza ngazi zilizokuwa zinaelekea ghorofa ya juu ndani ya hoteli hiyo ya kifahari ambamo watu waliokuwemo humo kila mmoja alikuwa na la kwake. Kasoro mtu mmoja tu! Alikuwa akifuatilia kwa jicho kali, yote yaliyokuwa yakiendelea kwa kina Patrick.



    ___



    "MNACHOTAKA kuniambia huyu ni pacha wa Abuu tu? Mmefahamu vipi hivyo?" John alihoji, mikunjo ilikuwa imejaa usoni mwake, ilibaki masaa machache tu akili zimruke. Walimchanganya. Muda huo tayari walishakaa katika meza ya pamoja vinywaji vikiwa juu yake.

    "Yeye mwenyewe katuelezea!" Patrick alijibu swali.

    "Umejibu kizembe sana Patrick!" Aliwaka John ambaye hakuhitaji hata kuagiza kinywaji chochote kwa sintofahamu iliyomkumba.

    "Hebu tulia kidogo John..." Yule mtu anayedaiwa ni pacha wa Abuu alimpooza, na hapo ndipo John alimsikia. Sauti yake haikuwa na hata chembe ya kutofautiana na ile ya Abuu.

    Pacha wanafanana mpaka sauti?

    John akatulia, hakutilia sababu ya kutulizwa alifanya hivyo kwa kuishangaa sauti ile...Ni Abuu kabisa!

    "Mimi naitwa Sultani, kabla ya juzi nilikuwa nafahamu sina kaka wala dada... Na wazazi wangu wakiwa wamefariki tangu nikiwa mdogo. Ila, juzi nilikutana na Patrick, yeye pia alihisi mimi ni huyo Jamaa mnayenidhania... Ila mimi ni kibaka tu wa mtaani, maisha yangu ni ya wizi na unyang'anyi... Sina hali! Hivyo huyu kaka hapa... Anahisi mimi na huyo jamaa tu mapacha, ila mimi binafsi Sina hakika. Vilevile, sitaki chochote hapa nilipo zaidi ya pesa, ili nikaendeleze maisha yangu." Aliongea jamaa huyo aliyejitambulisha kuwa anaitwa Sultani, akanyanyua glasi ya kinywaji na kugugumia kisha akaishusha chini haraka na kuwapitishia macho wenzake. John bado aliendelea kumtathmini...akagundua kitu!



    "Nahisi mambo mengine tutaendelea kuelezana, ninachotaka kuwaambia kuwa kesho ninyi wawili mtakwenda Nairobi..." Patrick aliongea.

    "Whaaaat? Nai...?" Kabla hajamalizia John alimdakia, hawakukubaliana kuhusu masuala ya safari. Iweje tena? Halafu, bado alikuwa katika huzuni. Hakutaka kufanya kitu mpaka akili imkae sawa.

    "Nairobi.... Mbona unashangaa?"

    "Imekuwa ghafla mno!"

    "Hakuna kitu kisichotokea ghafla duniani John, mimba yako ilitungwa ghafla, ukazaliwa ghafla na unaishi pia ghafla, kufa pia...utakufa ghafla. Hapo sijakwambia kuhusu kulala, kula, kuamka na kucheka...vyote ni ghafla. John, kumbuka uliniambia uko tayari!" Patrick aliongea kwa hisia ikapelekea mpaka agonge gonge meza iliyokuwa mbele yake.

    "Lakini sio kwa kusafiri kiongozi!" John alilalamika kwa sauti ya wastani.

    "Kumbuka kuwa tumegharimu maisha ya mwenzetu John. Abuu kafariki kutokana na ujinga wetu. Mimi niliweka kazi yangu mbele nikamuingiza katika mikono michafu ya Harrison, mwishowe wakamjeruhi...sikuwa na jinsi ya kumuokoa. Na sifahamu ni nani alimpa Harrison taarifa zake za kumsaliti kupitia wewe. Sifahamu!

    Ulimdanganya kuwa wewe ni Afisa upelelezi ili uweze kulipiza kisasi cha familia yako.

    Okay, Abuu hayupo tena. Hayupo! But God has seen our efforts John...God is there! He has given us another weapon. Why can't we use it? Nakuapia my friend, tukishindwa kulimaliza hili la Harrison, tutaandaliwa cheo cha ukiranja Jehannam...motoni moja hiyo kaka. I swear my friend!" Patrick aliongea maneno ya kuchoma sana na yenye ukweli kwa John.

    Hakuwa na la kumjibu, akageuka kulia na kumuangalia Ali Sodo, akamuangilia na yule aliyefanana na Abuu, Sultani...yeye alikuwa akitabasamu tu huku glasi za kinywaji zikipanda mdomoni mwake na kushuka.

    Abuu mtupu!

    "Sasa tusikilizane jamani, Sultani na John, leo mtalala katika hoteli hiihii, tumewakodishia chumba.

    Kesho asubuhi mtapanda ndege mpaka Nairobi, hoteli na kila kitu mtakuta kule, Kuna mtu wetu atawapokea. Halafu kuhusu kinachofuata tutaelezana. Kiufupi tu, huo ndiyo utakuwa mwisho wa Harrison!"

    Patrick alimaliza kuongea huku akiwatazama wenzake nyusoni.



    Nyuma yao, alikuwepo mtu aliyevalia koti kubwa jeusi, kofia mpaka karibia na pua, alifunika macho yake yasionekane.

    Yeye alikuwa ametegesha vizuri masikio yake kusikia kila kilichojadiliwa. Kufikia hapo, aliinuka akenda zake!



    ....



    ILIKUWA NDANI ya hoteli yenye nyota tano, Hilton Nairobi, nchini Kenya. Hoteli hiyo iko katikati ya jiji hilo la Nairobi. Chumba namba thelathini na tano ndimo John na Sultani waliketi kusubiri simu ambayo Patrick aliwaahidi kuwapigia wakati wowote. Muda huo walikuwa katika mazungumzo ambayo yalikuwa ni ya kufuta kitendawili kilichokuwemo kichwani mwa John.

    "Kwa hiyo unataka kuniambia Zainab anafahamu kuhusu hili?" John aliongea huku akivaa shati lake baada kutoka kukoga.

    "Ndiyo. Ni yeye tu anayefahamu...pamoja na wewe!" Sultani alijibu huku akiendelea kuiweka sawa suti aliyokuwa tayari amekwisha kuivaa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Dah nilipata shida sana Jana usiku kukuelewa, nilishaamini kuwa ni mfanano tu wa watu wawili tofauti. Maana nilihakikisha kabisa ulizikwa Abuu!"

    Yule mwanaume, aliyefananishwa na Abuu. Ambaye muda huu aliitwa Abuu na John, aliishia kutabasamu tu.

    Iweje Abuu tena?



    _____



    SAA saba zilizopita, ndani ya chumba cha Holiday inn hotel, jijini Dar es salaam...



    Walikuwa wamelala ndani ya chumba chenye hadhi ya kifamilia, kila mtu juu ya kitanda chake akitafakari hatma ya kile kitakachokwenda kujiri kesho yake asubuhi.

    "Ikitokea Abuu karudi, ungetamani kumwambia nini?" Sultani alihoji huku akiwa amelala chali, hakuvua fulana yake Kama John ambaye wakati huo alibaki na 'boksa' pekee.

    "Najua haiwezekani!" John alijibu kwa masikitiko.

    "Ni kweli, ila tufanye imewezekana..." Sultani aliongea, safari hii akimgeukia John, John naye akamgeukia na kumuuliza, "Una maana gani?"

    "Nijibu kwanza...!"

    "Nitamuomba msamaha tu. Nafahamu nilimkosea sana, laiti ningemuacha na kutomdanganya mimi ni mpelelezi...asingeshukiwa usaliti na kushambuliwa hadi akajeruhiwa. Inaniuma sana!"

    "Lakini John, lengo lako si halikuwa kumsaliti?"

    "Ndiyo," John alijibu huku miayo ikiwa imemtawala kinywani mwake kumuashiria usingizi umemtinga, "Mimi ngoja nilale Kaka, kesho safari yetu ni asubuhi sana. Ila namchukia sana Harrison, natamani hata kukuche muda huu..."

    "Usilale John. Mimi ni Abuu!"



    John alikuwa tayari keshafumba macho, akafumbua, hapohapo akamgeukia Sultani ambaye wakati huo alikuwa akidai yeye ndiye Abuu.

    "Kaka, sikuelewi..." John alihisi huyo Jamaa anataka amletee uhuni, Kama alivyojitambulisha kwake awali kuwa anataka pesa, aliona ndiyo anataka kumtapeli sasa.

    "Unaikumbuka tatoo ya tumboni mwangu?" Sultani aliuliza huku akimgeukia John.

    "Ipi?" John naye aliuliza, wakati huo akiivuta picha ya 'tatoo' aliyowahi kuiona ubavu wa kushoto wa tumbo la Abuu. akamgeukia. "Ndiyo," akamjibu.

    Wakati huo yule Jamaa asiyemuelewa alikuwa akivua fulana yake, tumboni alikuwa kavaa kitu, ni Kama ngozi hivi, akaibandua. Hapo 'six packs' zikawa zinaonekana.

    Alivaa hivyo kusudi, ili Patrick asiweze kumtambua.

    Rasmi, John alikutana uso kwa uso na Abuu, kwa mara nyingine baada ya kufa.

    Mie naye! Eti baada ya kufa, ilikuwa baada ya kupotea usoni mwake kwa kitambo.

    "Sasa siku ile si ulikufa kabisa kaka!" John aliuliza, uso wake ulijawa hadaa ya kuufanya ututumke, moyo ulihitaji kupasua kifua na umchomoke, damu nayo ikapata baridi na kuuamuru mwili utetemeke, kwenye kitanda akatamani ashuke, ila hazikuwepo nguvu zake, akabaki anashuhudia tu...

    "Usijali John, ondoa hofu. Mimi ni Abuu kabisa. Siku ile moyo wangu ulipata gazi ya sekunde kadhaa tu, haikuwa mara ya kwanza hali ile kunikumba. Tangu kule kwa babu..." Abuu aliongea akaweka kituo kidogo, John aliendelea kumsikiliza, "...Zainab naye alihisi nimefariki, lakini kwa kuwa ananipenda kweli msichana yule, nilivyoshtuka nikamuashiria aendelee kulia vile vile na akatii. Ujanja nilioufanya baada ya wewe kuja, ni kubana pumzi yangu tu. Nawe ukaamini. Kuhusu kuzikwa usishangae, sikuzikwa mimi. Alizikwa mtu mwingine kabisa ambaye tulimtoa hospitali, alikuwa miongoni mwa wale ambao wamekosa ndugu wa kuwazika. Na siri hii ilikuwa ni yangu na Zainab pekee, yeye alikuwa akifahamu kila kitu... Na nilimlazimisha aigize kila kukicha kukulilia mimi ili azidi kukupotezea muelekeo na usiweze kabisa kujua, pia alijifanya hataki kukuona kwake mpaka habari za vifo vya maadui zake ili usitambue kuwa mimi nimo mule ndani. Hivyo wewe ni wa tatu kulifahamu jambo hili..ingawa katika timu yetu kuna watu wanne. Mtu huyo wa nne ninamfahamu mimi peke yangu! Na kesho, lazima Patrick na huyo mpuuzi mwingine waionje adhabu ya dunia." Abuu alimaliza na tusi zito likamtoka!

    "Patrick tena?" John alishtuka.

    "Ndiyo, humfahamu tu Patrick...Ana historia mbovu sana. Na lengo la kufanya kazi hii ni kutaka kujitetea kuhusu uchafu anaoufanya kwa kupitia mgongo wa serikali."

    "Una maana Patrick ni muovu, na anataka kumkamata Harrison ili ajisafishe na kuaminika?" John aliuliza, wakati huo akiwa ameketi na kumpa umakini Abuu.

    "Hapo pigia mstari John. Patrick ni askari...ila kuna shirika kubwa mno la kijasusi duniani analolifanyia kazi. Kazi kubwa ya shirika hilo hapa nchini ni kuwauzia majambazi silaha...na hata kuuza watu wao wa kazi." Abuu alitoa maelezo kwa kujiamini.

    Tamaa ya kujua zaidi ilimshika John na kuuliza. "Una maana gani kwa kusema watu wao wa kazi?"

    "Uliwahi kusikia majambazi wamevamia sehemu wakapambana na askari halafu wakawashinda. Si ushawahi kusikia hivyo?"

    "Ndiyo," John alijibu huku akiwa anarudisha kumbukumbu zake vizuri.

    "Basi hao sio majambazi wa kawaida kaka. Unadhani mtu wa kawaida atamshambuliaje mwenye mafunzo na kumuua? Ni watu wenye mafunzo ya kijeshi kabisa, na wanauzwa kutoka nchi za nje"

    "Wewe umejuaje hivyo?" John alimshangaa Abuu ambaye alikuwa akizungumza mambo nyeti na kuonesha uhakika wa hali ya juu kwa yale atoayo.

    "Kaa nyuma uwaone walio mbele... Pia utaepusha maumivu ya shingo!" Abuu alijibu kwa fumbo.

    "Sijakuelewa,"

    "Utanielewa tu. Ila kiufupi, nami nimeajiri hao watu wa kazi. Ninaye mmoja... Na huyo ndiye mtu wangu wa nne katika timu. Ila sitakuruhusu umfahamu hivi sasa."

    Kimya kikatawala... John alihisi yungali yumo katika ndoto ya ukweli!



    .....



    Hilton Nairobi, Kenya.



    MACHO yao yote manne yaligota mezani kuitazama simu iliyokuwa ikiita. Ni muda mrefu tangu hapo walikuwa wakilisubiri tukio hilo. Kwa mwendo wa haraka, John aliisogelea na kuipokea...

    "Ni simu toka mapokezi hapa, naongea na Mr. Derick?" Ilisikika sauti kutoka upande wa pili kuuliza.

    "Hapana, sio mimi!" John alijibu huku akikunja nyusi zake kwa kushangaa na kumgeukia Abuu, ambaye pia alikuwa akisikiliza maongezi yale kwa makini kabisa.

    "Oowh, samahani kwa usumbufu na nawatakia wakati mwema. Ahsante!" Msichana huyo wa mapokezi akakata simu.

    Wakabaki wanashangaa kwa mara nyingine!



    Lakini ghafla, simu ilikuwa ikiita tena, ni ile ile kutoka mapokezi...

    "Samahani tena kaka, nilichanganya taarifa. Kuna mtu anamuulizia Mr. Sultani...!" Hapo John aligeuka na kumtazama Abuu. Bila shaka alikuwa ni Patrick. Maana hakukuwa na mtu waliyehisi anafahamu wamo hotelini mule zaidi yake.

    "Mleteni chumbani tu." John alijibu baada ya Abuu kumpa ishara ya kumruhusu.

    "Tunaomba radhi, kwa usalama, huwa haturuhusu mgeni kama hivi kuingia vyumbani... Hasa kwa mkutano wa namna..."

    "Wewe dada wee! Kwani nani yuko chumbani?" Hapohapo John alimkatisha kwa kumfokea na kumuuliza swali.

    "Wewe!" Mdada wa mapokezi alijibu.

    "Kama ndivyo, basi mruhusu haraka! Ukiendeleza ujuaji wako, tutaondoka humu halafu pesa uilipe wewe!" John alifoka kwa ujasiri na kuonesha si wa kujaribiwa kwa lolote, akaiweka simu mezani. Abuu wakati huo alikuwa pembeni akicheka tu.



    ____

    MUDA mchache ulivyopita tayari Patrick alikuwa chumbani, kaketi juu ya kiti na pembeni yake alikuwepo John.

    Patrick alimkabidhi John 'laptop' yake ili aifanye shughuli ambayo wamekwisha kupanga.

    Ilihali Abuu tayari alishatoka chumbani mule.



    .....

    Kwa mwendo wake wa madaha, wa kuvutia na muonekano wa kupagawisha, aliingia moja kwa moja katika mgahawa mmojawapo kati ya mitatu iliyokuwemo hotelini mule. Hapo alitakiwa afanye kitu kimoja tu, kumuwinda kimada wa Harrison. Inasadikika msichana huyo anayafamu mengi kuhusu Harrison...ila, inahitajika akili ya ziada kumfanya ayatamke mambo hayo. Wakaamini Abuu au Sultani Kama Patrick anavyomfahamu, angeweza kutokana na muonekano aliokuwa nao.



    .....



    Huko chumbani Patrick alibaki katika koma ya mawazo. Hakuwa akimuamini sana Sultani Kama ilivyokuwa zamani kwa Abuu. Alihisi Sultani hataweza kufanya aliyoweza kuyafanya Abuu.

    Hakufahamu ndiye Abuu mwenyewe. Tumbo lilimpanda joto!

    Kiti kikawa Kama kina misumari, kila saa anainuka na kukaa.

    Wakati huo, John alikuwa akichezea laptop ile na kutuma baadhi ya nyaraka za siri kuhusu Patrick, kwenda kwenye baruapepe yake bila ya Patrick mwenyewe kuliona hilo.



    ....



    Abuu alikaa katika kiti kwa kuinamia, aliambiwa na Patrick kuwa Harrison angaliingia ndani ya mgahawa huo muda mchache ujao.

    Alizidi kusubiri.

    Hatimaye ikawa...



    Harrison aliingia huku kamshikilia kimada wake vizuri, wakaelekea pembezoni kabisa na kuketi. Kisha wakaagiza vinywaji na mazungumzo yakawa yamechukuwa nafasi baina yao, Abuu aliendelea kuwakata jicho la upande tu.

    Harrison ni mgonjwa wa kisukari, hawezi kunywa chochote na kukaa muda mrefu bila ya kutafuta choo kwenda kujisaidia. Na hizo dakika chache ndizo alizokuwa akizisubiri Abuu, alihitaji acheze mchezo wa hatari mno!

    Ndani ya dakika chache, amshawishi mtu ambaye hawakuwahi kuonana, halafu amkubali...mpaka amtajie namba zake za simu. Maana, ilisemekana, nambari tatu za mwisho za simu hiyo ndiyo nywila yenyewe. Namba hiyo, anayeifahamu ni Harrison tu.

    Na ndiyo maana hataki kimada huyo hata aingie Tanzania, badala yake, akimkumbuka humfuata hukohuko Kenya na kula naye bata.



    Haikupita saa, Harrison aliinuka na kuelekea msalani. Hapohapo Abuu naye aliinuka...akazuga kidogo, baada ya kumuona Harrison ameshapotea eneo lile. Moja kwa moja, mpaka kwenye meza, palepale alipokuwa ameketi Harrison.

    Kuketi tu kwa Abuu eneo lile, kukawafanya nzi wote wasopenda harufu nzuri kukimbia na wengine kuzimia.

    Halafu, hakuongea neno...alitabasamu na kubinya jicho la kushoto!

    Wacha kabisa! Wacha wewe!

    Mtoto wa kikenya alianza kuona dunia ndiyo inamchekea mbele yake. Muonekano wa Abuu kwa wakati ule, ungemfanya atoe nguo zote mwilini palepale mbele ya kadamnasi, sembuse namba?

    Haraka, alimpatia Abuu nambari zake baada ya kumuomba. Kisha Abuu huyo, aliinuka na kwenda zake. Msichana yule aliendelea kumtazama huku mwili ukimsisimka kwa hisia kali. Alitamani hata asingekuwepo katika ulimwengu wa kibinadamu na kuwa kuku...wangemalizana palepale tu!

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    _____



    MUDA ulizidi kuyoyoma ndani ya chumba kile ambacho Patrick walibaki na John. Abuu bado hakuwa amerudi. Taharuki ikawachota.

    Imekuwaje?

    "Unajua tena kijana wa mtaani yule, hebu ngoja nimtazame!" John alitoa wazo, Patrick akaafiki na kumruhusu akamtafute.

    Hakujua kuwa amekosea sana! Hakuja hilo!



    Huo ulikuwa ni mpango madhubuti uliopangwa tangu usiku wa jana baina ya watu hao wawili.

    Ikawa zamu ya Patrick kusubiri, alisubiri na kusubiri...hakukurudi mtu!

    Akaamua kutoka nje, holaa! Hakukuwa na mtu hata mmoja kati ya wale awatafutao.

    "Shiiiiiiit!" Alifoka na kupiga chini.

    Akili ilimtuma kurudi katika kompyuta yake, huko ndiko alitamani kuzimia... Kila kitu kilishadukuliwa na John.

    Akafahamu kabisa mwisho wake tayari umekaribia.

    Ooh God!



    ____



    KESHO yake vyombo vya kiusalama nchini Tanzania vilipokea shutuma nzito kuhusu wanaume wawili, Harrison na Patrick.

    Harrison alituhumiwa kwa kushiriki kwake katika kamari haramu ya picha za ngono. Huku Patrick, akituhumiwa kushiriki katika kesi ya biashara haramu pia ya silaha na uingizaji wa majambazi nchini...na ushahidi wote ulitolewa.

    Watuhumiwa walikamatwa ili uchunguzi na mahojiano yafanyike. Huku vyanzo vya habari hizo vikiwa havijulikani!



    ....



    Walikuwa wameketi juu ya vitanda vya mbao, ni jijini Mombasa, macho yao yakibarizi uzuri wa bahari. Vifua vyao viliendelea kumpagawisha kila msichana mkali aliyekuwa akipita karibu yao.

    Hawakuwa na habari na yeyote...walihitaji wajifurahishe kwa siku chache kabla ya kurejea nchini mwao. Maongezi madogomadogo yakisonga baina yao...http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Nakumbuka uliniambia kuwa timu yako ina watu wanne. Huyo wa nne ni nani? Maana mpaka kazi imekwisha, sijamuona." John aliuliza kwa sauti ya kudadisi.

    Abuu akamgeukia na kucheka, kisha akamjibu, "Wanne hakuwa mtu...bali uaminifu wetu. Uaminifu tuliowekeana ndiyo mwanajeshi huyo wa nne. Nafurahi ametusaidia kuishinda vita hii!"

    Abuu aliongea kisha wote kwa pamoja walicheka na kugonga mikono yao.



    Pembezoni kabisa ya fukwe ile, yuleyule mtu aliyekuwa kule katika hoteli ya Holiday Inn jijini Dar, akiwa kavaa vilevile koti lake na kofia iliyoziba macho na pua yake...aliinama, akafungua kidaftari chake, kisha akaweka tiki, akatabasamu na kuondoka zake!



    MWISHO!

    _______

0 comments:

Post a Comment

Blog