Search This Blog

Tuesday, 1 November 2022

MKE WANGU JULIANA - 4

 






Simulizi : Mke Wangu Juliana

Sehemu Ya Nne (4)





Deborah alilia sana, alihuzunika, maisha yake yalikuwa ya majonzi kupita kawaida, alikonda mno, aliteseka lakini wazazi wake hawakutaka kujali kabisa.

Alitia huruma, kila mtu aliyekuwa akimwangalia alimsikitikia kwani hakuonekana kuwa kama yule Deborah wa kipindi cha nyuma, huyu alikuwa mwingine kabisa.

Mawazo yakawa makubwa, akaanza kupata vidonda vya tumbo vilivyoanza kumtesa na kumpa maumivu makali, akaanza kuchagua aina ya vyakula ambavyo alitakiwa kula, vingine aliambiwa asile, hasa vile vilivyokuwa na asidi.

Wazazi wake walimuonea huruma lakini kamwe hawakutaka kujutia kile walichokifanya, waliamini kilikuwa kitu kizuri kwa sababu walifanya kila lililokuwa bora, hawakutaka binti yao aangukie kwenye mikono ya mwanaume ambaye angeshindwa kumfanyia kitu chochote hasa kumpa maisha ambayo aliyahitaji.

Walizungumza naye kila siku, kila walipoongea naye, alionekana kuwa na majonzi mazito, hasira kali dhidi ya wazazi wake.

Alitamani kuufumbua mdomo wake na kuwaambia ni kwa namna gani alikuwa akiwachukia lakini alishindwa kufanya hivyo kwa kuwa tu aliwaheshimu, ila moyoni mwake aliwachukia kupita kawaida.

Hakuonana na John, mwanaume huyo alifukuzwa kazi, hakupata hata muda wa kwenda nyumbani kwake, kila alipokuwa, mama yake alikuwepo, alikuwa kama mlinzi kwake, alitakiwa kurudi nyumbani mara tu anapomaliza kazi.

Kwa kuwa waliamini kitendo cha kumuona John kingemfanya kurudi tena nyuma, wakaamua kuhama kanisa, yote hayo ni kwa sababu hawakutaka kuona binti yao akiungana na mwanaume huyo tena.

Maisha yalikuwa ni ya mateso mno, hakuyapenda lakini alitakiwa kuyaishi kila siku katika maisha yake. Siku ziliendelea kukatika na baada ya miezi saba ya kuwa na maisha yenye maumivu makali ndipo akapata mwanaume aliyemwambia alikuwa akimpenda mno.

Mwanaume huyo aliitwa Jericho Michael, mmoja wa kijana aliyetoka kwenye familia iliyokuwa na uwezo mkubwa kama wao.

Jericho hakumpata hivihivi, aliwatumia wazazi wake ambao walikwenda kuzungumza na wazazi wa Deborah na wao wakazungumza na binti yao na hatimae wawili hao kuwa wapenzi.

Maisha hayakuwa kama yalivyokuwa kwa John. Japokuwa John hakuwa na kitu lakini alimfanya kuwa mwanamke spesho maishani mwake.

Alimpa furaha, alipenda sana kumchekesha, kumtania na mambo mengine tofauti na alivyokuwa akifanya Jericho, muda mwingi mwanaume huyo alikuwa siriazi sana, yaani ni kama mtu ambaye hakupenda utani.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Hilo Deborah alilizoea, hata wanaume aliowahi kuwa nao kabla ya John walikuwa hivyohivyo, wakali, siriazi sana, hawakuwa na matani kwa kuwa tu walijua walikuwa na pesa hivyo ni vigumu kukimbiwa na wanawake.

Maisha hayakusubiri, waliendelea kuwa pamoja mpaka pale ambapo sasa waliona ni muda sahihi wa kuoana. Lilikuwa jambo gumu kwa Deborah kwa kuwa bado moyo wake ulikuwa kwa mwanaume mmoja ambaye mpaka mwaka unakatika hakuweza kumona tena.

Alimwambia Jericho alihitaji muda, hakutakiwa kukurupuka kwenye suala la kuingia kwenye ndoa kwani alihitaji mambo fulani kuyaweka sawa.

Kijana huyo akaamua kuzungumza na wakwe zake ili wamuwekee mambo vizuri, hakutaka kumkosa Deborah, alimpenda na alitamani sana kuwa mke wake.

“Tatizo nini Deborah?” aliuliza mama yake.

“Bado moyo wangu haupo sawa!” alijibu.

“Kwa sababu gani?”

“Namuwaza sana John! Ninampenda kupita kawaida,” alimjibu mama yake.

Mwanamke huyo akakaa kimya, hakuamini alichokisikia, kilimkera lakini hakutakiwa kuonyesha hasira zozote, akaachia tabasamu kama mtu ambaye aliguswa na kile alichoambiwa.

“Usijali! Kuna siku utamsahau tu!” alisema.

“Hivi mama kwa nini mliamua kuniachanisha na John?” aliuliza huku akimwangalia mama yake.

“Kwa kuwa hakufai kabisa.”

“Ni kwa sababu masikini?” aliuliza.

“Hilo ndilo kubwa zaidi!”

“Uliolewa na baba akiwa tajiri?”

“Hapana!”

“Ikawaje wazazi wako walikubali uolewe naye?” aliuliza.

“Deborah! Acha maneno hayo. Tunahitaji uolewe na Jericho,” alisema mama yake kwa hasira na kutoka ndani ya chumba hicho.

Maneno ya binti yake yalimgusa, ni kweli kile alichokizungumza. Aliolewa na Abraham wakati kijana huyo akiwa masikini wa kutupwa lakini baadaye walipambana wote na kupata maisha waliyokuwanayo kipindi hicho.

Kama yeye alikubali kuolewa na Abraham akiwa masikini, kwa nini wao walikataa binti yao kuolewa na John kwa kuwa alikuwa masikini?

Hilo lilimuuma sana, akahisi akihukumiwa moyoni mwake, alitokwa na jasho jingi, alionekana kuogopa sana. Mumewe aliporudi, hakutaka kukaa kimya, alimwambia ukweli kila kitu kilichotokea.

“Kwa hiyo yeye anataka kuwa kama sisi?” aliuliza mzee Abraham huku akionekana kuwa na hasira.

“Ila alichoongea kina maana kubwa!”

“Hakina maana! Usimpe nafasi ya kuulaghai moyo wako!” alisema mzee Abraham.

Mzee Abraham alikuwa na msimamo uleule, alichokitaka ni kuona binti yake akiolewa na mwanaume aliyekuwa na pesa kwani hakupenda kuona binti yake akipitia maisha yaliyojaa mateso makubwa.

Baada ya miezi miwili mbele, hatimaye Deborah na Jericho wakawa mume na mke, harusi ambayo ilifungwa katika Kanisa la KKKT. Hiyo ndiyo ilikuwa ndoto ya wazazi wao, kuwaona wakiona na kuwa mume na mke.

***

Mama yake Juliana alikuwa na furaha tele baada ya kuona binti yake akiwa amefanikiwa kumpata John, ni kweli alikuwa kijana masikini, asiyekuwa na uwezo lakini moyo wake ulionyesha kuwa mwanaume mpambanaji kupita kawaida.

John aliendelea kufanya biashara ya samaki, alitia huruma, hakuwa na maisha mazuri lakini alitakiwa kupambana kwa sababu tu alihitaji kufunga ndoa na mwanamke aliyekuwa akimpenda mno kipindi hicho.

Siku zilikatika, alizidi kuweka akiba mpaka kufikia kiasi cha shilingi milioni moja. Haraka sana akawaandaa watu kwa ajili ya kwenda kutoa mahari.

Mama Juliana hakuhitaji kitu, alizungumza hivyo hata na kaka zake ambao walikuwa wajomba wa Juliana na kuwaambia hakuhitaji kitu chochote kutoka kwa John kwa kuwa alikuwa mwanaume masikini aliyekuwa akiyapambania maisha yake.

Wakakubaliana, wakawaruhusu watu hao waingie kwenye mchakato wa ndoa na hatimaye baada ya miezi mitatu mbele, watu hao wakaoana na kuwa mume na mke.

Maisha yalikuwa ya furaha, hawakuwa na pesa nyingi lakini walikuwa na amani tele, waliyafurahia maisha hayo, walikuwa watu wa kupambana na kwa sababu John alipata pesa kidogo alizokuwa ameweka akiba, akamwambia mke wake ni lazima akafungue biashara ya kufanya.

Juliana akaanza kufuatilia biashara ya kuuza vitenge kutoka nchini Kongo na kupeleka hapo Kigoma. Ilikuwa ni biashara nzuri, akaridhia kuifanya na hivyo kumwambia mume wake.

Halikuwa tatizo, wakawekeza kwenye biashara hiyo na hatimaye kuanza huku wakichukua fremu sokoni mjini ambapo huko ndipo alipokuwa akiuza vitenge hivyo.

Ilikuwa biashara nzuri, iliyokuwa ikiingiza kiasi kikubwa cha pesa. Maisha yao yakaanza kubadilika na kitu cha kwanza alichokisema John ni lazima wadogo wa mke wake wahamishwe shule, watoke kwenye shule ya chini na kupelekwa kwenye shule ambayo ilikuwa na hadhi kidogo.

Hilo likamfurahisha mkewe na mkwewe, japokuwa alikuwa na uwezo wa kukataa lakini familia ya mke wake ilikuwa kitu cha kwanza kabisa katika maisha yake.

Aliendelea kuuza samaki huku upande wa pili mke wake akiendelea kuuza vitenge. Maisha yalibadilika kwa kiasi kikubwa mno.

Wakahama Mwanga na kuamia Mlole, mlimani kabisa mbapo walikuwa na uwezo wa kuuangalia mtaa wote wa Mwanga na Mjimwema.

Ilikuwa ni furaha kwao, mafanikio hayo ni kwa sababu tu waliamua kupambana, hawakulala, walifanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanafanikiwa na kupiga hatua.

Baada ya wiki kadhaa hatimaye Juliana akamwambia mumewe kuhusu suala la ujauzito, tayari aliziona dalili zilizoonyesha alikuwa na mimba.

Ilikuwa ni furaha kwao, kila mmoja alionekana kulifurahia jambo hilo hivyo kitu walichokifanya ni kumsubiri mtoto kwa hamu kubwa, walikuwa na presha kupita kawaida.

Kila wakati John alikuwa akilibusu tumbo la mke wake, alifurahia, alitamani kuona mtoto akizaliwa mapema hata kabla ya kuzeeka.

Kwa kuwa alikuwa na presha, baada ya miezi kadhaa wakaamua kwenda kuangalia ili kujua jinsia ya mtoto, walipokwenda huko akaambiwa mke wake alikuwa na ujauzito wa watoto mapacha

“Unasemaje?” alimuuliza daktari huku akiwa haamini.

“Watoto mapacha!” alijibu daktari huku akionyesha sura ya tabasamu pana, hakuishia hapo, vilevile akawaonyesha kwenye karatasi gumu ambalo lilipiga picha humohumo tumboni.

Kila mmoja alikuwa na furaha, John akazidi kutafuta zaidi kwani aliamini kuwalea watoto mapacha halikuwa jambo dogo, ilikuwa ni lazima ujitoe kwa kiasi kikubwa mno.

Maisha yalikuwa na furaha tele, ile mimba ikawafanya kupendana zaidi na zaidi. Miezi ikakatika, waliendelea kwenda kliniki pamoja, baada ya miezi nane kutimia, wakaenda hospitalini kuangalia hali ya watoto tumboni.

Walipofika huko, Juliana akachukuliwa na kupelekwa kwenye chumba maalumu na kuanza kuangaliwa. Kila mmoja alipigwa na mshtuko baada ya kuona wale watoto mapacha wakiwa tumboni huku wakiwa wameungana.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Daktari alishangaa, aliangalia zaidi na zaidi, alitoa macho, katika maisha yake hakuwahi kuona watoto wa namna hiyo zaidi ya kuwasoma kwenye makala mbalimbali, kwa mfano wa Abby na Brittany, watoto wa Kimarekani waliokuwa wameungana mpaka ukubwani kwao.

“Mungu wangu!” alisema kwa mshtuko.

John na Juliana walionyeshwa picha hizo, hawakuamini, pale alipokuwa amelala, Juliana akaanza kulia, hakuamini kama tumbo lake lilibeba watoto mapacha walioungana.

Aliumia mno, John alikosa nguvu na kujikuta akikaa kwenye kiti, alihuzunika lakini baadaye akagundua kufanya hivyo ilikuwa ni ujinga kwa kuwa yeye ndiye aliyetakiwa kumpoza mke wake na si kuonyesha huzuni.

Akasimama na kumsogelea mke wake aliyekuwa kitandani na kuanza kumbembeleza, mwanamke huyo alikuwa akilia, moyo wake ulimuuma kwani hakuamini kwa maisha ya mateso aliyokuwa amepitia, bado Mungu aliwapa jaribu jingine, watoto mapacha waliokuwa wameungana.

“Nyamaza mke wangu!” alisema John.

“Watoto wetu wameungana! Watoto wetu wameungana mume wangu,” alisema Juliana huku akilia kitandani pale.



Moyo wa Juliana ulikuwa na huzuni mno, hakuamini kama yeye ndiye aliyekuwa akipitia maisha hayo, yalimuumiza, yaani walipewa umasikini, uliwasumbua maisha hayo yote na baada ya kuanza kufanikiwa tayari Mungu aliwapa tatizo jingine, lililoonekana kuwa kubwa kuliko hata uwezo wao.

John aliendelea kumfariji mke wake, aache kulia kwani machozi yake yasingebadilisha kile kilichokuwa kimetokea, kama watoto kuungana tumboni, wangeendelea kuwa hivyohivyo.

Baada ya hapo wakarudi nyumbani, kila mmoja alikuwa kimya, bado Juliana aliendelea kuhuzunika na machozi kutiririka mashavuni mwake.

Walipofika, John akawa na muda mwingine wa kumfariji mke wake na kumwamba hapakuwa na tatizo lolote lile, alitakiwa kupumzika na kusahau kilichokuwa kimetokea.

Maisha yaliendelea, John akawa bize na mkewe, hakutaka kumpa nafasi ya kuwa peke yake kwa kipindi kirefu kwa sababu hali hiyo ingemfanya kuanza kufikiria kilichokuwa kimetokea.

Alimwambia hakutakiwa kuwa na majonzi kwani bado Mungu alikuwa na makusudi na maisha yao, hivyo kila kitu kilichotokea walitakiwa kumshukuru Mungu.

“Tumshukuru Mungu kwa kila kitu,” alisema John huku akimwangalia mkewe.

“Kuna wengine hawana watoto, wanatamani hata kupata watoto walioungana lakini imeshindikana, sisi tunapewa watoto hao, kwa nini tusimshukuru Mungu?” aliuliza John huku akimwangalia mke wake.

Siku ziliendelea kukatika, John hakutaka kukaa kimya, alikuwa na uwezo wa kipesa kiasi hivyo alichokifanya ni kuzungumza na mchungaji wake, alimwambia kila kitu kwani kwa jinsi hali ilivyokuwa, siku ya kujifungua ingefika walitakiwa kuelekea jijini Dar es Salaam ili ajifungue salama.

“Ni miezi mingapi imebaki?” aliuliza mchungaji.

“Mwezi mmoja!”

“Una pesa za safari ya kuelekea Dar es Salaam?” aliuliza mchungaji.

“Pesa ninazo, hilo si tatizo!”

“Ila bado kuna kitu kinatakiwa kufanyika. Watoto wako wameungana wapi?” aliuliza mchungaji swali lililomfanya John kuvuta kumbumbuku ya picha aliyoonyeshwa.

“Makalioni!”

“Bado wanaweza kutenganishwa!” alisema mchungaji.

“Kutenganishwa?” aliuliza John huku akionekana kushangaa.

“Ndiyo! Kuna watoto walizaliwa na kutenganishwa, huwa inafanyika hivyo ila si kwa Tanzania, ni lazima watoto wasafirishwe na kupelekwa nchini India ambapo huwa wanatenganishwa huko, nadhani hapa utatakiwa kutumia pesa zaidi!” alisema mchungaji.

“Kiasi gani?”

“Sijajua! Ila si chini ya milioni arobaini!” alijibu mchungaji.

John akabaki kimya, kile alichoambiwa kilimtisha kwani kiasi kilichotajwa kilikuwa kikubwa mno ambacho hakuwahi kufikiria kabla.

Akaondoka na kurudi nyumbani, alichokifanya ni kuzungumza na mke wake, hakumficha, alimwambia kila kitu kwamba siku chache kabla ya kujifungua walitakiwa kwenda jijini Dar es Salaam ambapo wangepanga chumba huko na kulipia kodi na kusubiri siku ya kujifungua.

Halikuwa tatizo, wakakubaliana na wiki moja kabla ya kujifungua, wakaondoka na kuelekea jijini Dar es Salaam na walipofika wakapanga chumba maeneo ya Kijitonyama.

Baada ya siku kadhaa, Juliana akaanza kujisikia uchungu hivyo John kumchukua na kuelekea naye katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Akapokewa na kuingizwa katika chumba kwa ajili ya kujifungua. Kabla ya kuanza kazi hiyo John akamuita daktari na kumwambia kuhusu watoto wale.

Dokta alishangaa, hakuwahi kumzalisha mwanamke mwenye watoto wa namna hiyo. Akaenda kwenye kile chumba cha leba na kuongea na wenzake, akawaambia kuhusu kile alichoambiwa.

Wote walishangaa kama yeye alivyoshangaa, walikuwa na hamu ya kuwaona watoto wa namna hiyo kwani walisikia tu sehemu mbalimbali na hawakuwahi kuwaona kwa macho.

Muda huo bado Juliana alikuwa akiendelea kulia uchungu wa kujifungua, pale kitandani alipokuwa alijikunjakunja huku na kule, na kuna wakati alihisi kama angeweza kufa kitandani hapo.

Baada ya dakika kadhaa madaktari wakaanza kazi yao, na kwa sababu waliambiwa watoto hao waliungana, madaktari wengine wakaongezekana kuhakikisha mwanamke huyo anajifungua salama.

John alikuwa nje ya chumba hicho, hakutulia, kulikuwa na benchi lakini hakukaa, muda wote alikuwa akitembea huku na kule akimuomba Mungu, alihitaji kuona mkewe akijifungua salama.

Alikuwa nje ya chumba hicho kwa zaidi ya saa moja, akaanza kusikia sauti za watoto wakilia kutoka ndani ya chumba kile. Akashtuka, akapiga magoti na kumshukuru Mungu.

Machozi yalikuwa yakimtoka, Juliana alijifungua lakini mpaka muda huo hakujua kama mkewe alikuwa mzima ama alifariki, akawa na hamu ya kutaka kulifahamu hilo.

Aliendelea kubaki hapo kwa dakika kadhaa, mlango ukafunguliwa na daktari kutoka. Haraka sana akamfuata na kuanza kuongea naye, alijua watoto wake walikuwa salama, alihitaji kuijua hali ya mke wake.

“Daktari! Mke wangu anaendeleaje?” aliuliza John huku akimwangalia daktari huyo.

“Naomba twende ofisini tukaongee!”

“Hapana daktari! Naomba uniambie kwanza hali ya mke wangu!” alimwambia daktari huyo.

“Twende ofisini!”

“Unataka kunitoa hapa ili muitoe maiti yake muipeleke mochwari?” aliuliza John, tayari mashavu yake yakaanza kujawa machozi yaliyoanza kutiririka kutoka machoni.

“Twende ofisini!” alisema daktari, hakutaka kumpa jibu hapo kuhusu mkewe.

John akahisi akiishiwa nguvu za miguu, kinyonge akaanza kuongozana na daktari huyo kuelekea katika ofisini yake ambayo haikuwa mbali kutoka hapo.

“Pole sana...mkeo amefariki wakati wa kujifungua,” aliisikia sauti hiyo kutka moyoni mwake, sauti iliyosema maneno yaliyomuumiza kupita kawaida.

***

Maisha ya ndoa kati ya Deborah na Jericho yalikuwa yakiendelea. Mwanaume huyo alimpenda mkewe kupita kawaida, alimsikiliza, kumuheshimu na kumpa kila aina ya maisha aliyokuwa akiyahitaji kwa kipindi hicho.

Kwa Deborah, alikubaliana na kila kitu lakini hakuacha kumkumbuka John. Mwanaume huyo alikuwa mtu wa tofauti kuliko wanaume wote ambao aliwahi kukutana nao kipindi cha nyuma.

Jericho alilifahamu hilo, alijua ni kwa jinsi gani mkewe alimpenda John hivyo alijitahidi kufanya kila kitu kumfurahisha ili amsahau lakini haikuwezekana kabisa.

Ni mwaka na nusu ulipita lakini bado Deborah alikuwa na mawazo tele juu ya John, na kilichomfanya kuwa katika hali hiyo ni kwa sababu tu wazazi waliamua kumuachanisha naye na wakati moyo wake ulikuwa ukimuhitaji kupita kawaida.

Siku ziliendelea kukatika, maisha yalikuwa ya kawaida. Mume wake alikuwa akifanya kazi katika Shirika la Ndege la ATCL. Wao wote kwa pamoja walikuwa na maisha mazuri, walipendana na kuheshimiana kwa kila kitu.

Baada ya mwezi mmoja shirika hilo likahitaji kupunguza wafanyakazi kwa sababu halikuwa likiingiza pesa kama kipindi kingine kutokana na mashirika mengine ya ndege kuongezeka.

Kwenye orodha ya watu ambao walitakiwa kupunguzwa kazi haraka sana, naye Jericho alikuwa miongoni mwao. Ilikuwa ni taarifa ya ghafla sana, hakuwa amejipanga na siku ambayo alikabidhiwa barua hiyo, hakuamini macho yake, alikuwa akitetemeka huku moyo wake ukiwa na huzuni kupita kawaida.

Akaondoka na kuelekea nyumbani, alitaka kumpigia simu kumwambia Deborah kuhusu kitu hicho lakini akasita, hakutakiwa kumwambia kwenye simu, jambo hilo lilikuwa siriazi, hivyo alitakiwa kumwambia ana kwa ana.

Usiku ulipoingia, Deborah akarudi nyumbani, alimkuta mumewe akiwa kwenye hali ambayo hakuitegemea hata kidogo, alibadilika, hakuwa na furaha kabisa.

Akamuuliza, jibu ambalo alilitoa ni kumpa barua ile Deborah, akaichukua na kuanza kuisoma, hakuamini alichokiona, alibaki akitetemeka, kijasho chembamba kikianza kumtoka.

“Umefukuzwa kazi?” aliuliza Deborah huku akimwangalia mume wake.

“Ndiyo! Shirika halina pesa, mashirika ya ndege yamekuwa mengi sana,” alijibu Jericho huku akimwangalia mke wake.

Akamuinua kutoka pale alipokaa, akamkumbatia na kumwambia kufukuzwa kazi haikuwa mwisho wa kila kitu, kama kweli walipendana, basi hawakutakiwa kuangalia kazi ama kitu chochote kile.

Jericho akaanza kuwa kwenye hali ya majonzi, kitendo cha kufukuzwa kazi kilimfanya kutokuwa na furaha hata kidogo. Maisha hayakuwa magumu kwa kuwa mke wake alikuwa akiendelea kufanya kazi na kulipwa vizuri.

Deborah hakuwa na dharau, alimpa kila kitu mume wake, alimuheshimu kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma. Wazazi wa pande zote mbili wakajua kilichotokea, walimuonea huruma Jericho lakini hawakuwa na cha kufanya.

Kwa kuwa alikuwa na vyeti vizuri kwa mambo ya akaunti, ikambidi Deborah akazungumze na bosi wake, mzee Masako ili kama itawezekana basi mwanaume huyo apate kazi katika kampuni hiyo kwa kuwa bado kulikuwa na upungufu.

Mzee huyo alimwambia Deborah hapakuwa na nafasi ya kazi yoyote ile ila alitakiwa kuangalia katika makampuni mengine.

Deborah hakutaka kukubali, alijua kabisa kampuni hiyo ilikuwa na nafasi ya kazi hivyo alichokifanya ni kuzungumza na uongozi mkuu uliokuwa jijini Dar es Salaam ambapo walimwambia wangeangalia kama kuna uwezekano basi mwanaume huyo apewe kazi.

Alihangaika kwa ajili ya mume wake, hakutaka kuona akielekea kazini na wakati mume wake alikuwa nyumbani tu. Alimpambani kwa kipindi cha mwezi mzima bado hakupokea majibu kutoka jijini Dar es Salaam.

Alichokifanya ni kwenda kuomba ushauri kwa baba yake, alihitaji kufahamu kama inawezekana basi aende Dar es Salaam ambapo huko angekwenda yeye mwenyewe.

Alichoshauriwa ni kwenda huko, alitakiwa kuomba ruhusa kazini kuonyesha kama baba yake alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa hivyo kwenda huko Dar.

“Inakupasa uende, haina jinsi! Ninafurahi sana kuona unapambana kwa ajili ya mume wako,” alisema baba yake huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.

“Nadhani hata John ningempambania hivi, ila hamkutaka kunielewa,” alisema maneno yaliyomfanya mzee huyo kuwa kimya.

Baada ya siku mbili, akasafiri na kwenda Dar es Salaam. Alipofika huko, akachukua chumba katika Hoteli ya Cat iliyokuwa Kariakoo ambapo akatulia na siku iliyofuata akaondoka kuelekea huko makao makuu ya kampuni hiyo.

Alipewa maelekezo yote, mtu ambaye alitakiwa kuonana naye siku hiyo, alipofika, akawasiliana naye na hivyo kukutana ofisini na kuanza kuongea.

“Wewe ndiye Deborah?” aliuliza mwanaume huyo, alikuwa meneja kwenye kampuni hiyo.

“Umenijuaje?”

“Uliomba kuja kuonana nami kutoka huko Kigoma, ama si wewe?” aliuliza.

“Ndiye mimi!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Walizungumza, alimwambia kuhusu hali ya mume wake, alifanya kazi kwa miaka sita, alikuwa mtu mwenye sifa nzuri katika kampuni hiyo, hivyo waliongea mambo mengi na meneja huyo, Bwana Kinyora alimwambia angefanya kila juhudi mume wake aajiriwe kwenye kampuni hiyo.

“Nitajitahidi kwa hali na mali!” alisema mwanaume huyo.

Baada ya kumaliza mazungumzo hayo, akatoka na kurudi hotelini, alipofika njiani, akaamua kununua Gazeti la Nipashe ambapo kulikuwa na taarifa ya mwanaume mmoja aliyekuwa akitafuta msaada wa watoto wake walioungana kupelekwa nchini India kwa ajili ya kutenganishwa.

Aliiangalia habari hiyo, hakuona picha ya mwanaume huyo wala watoto hao walioungana lakini alipoangalia namba ile ambayo walitakiwa wasamaria wema watume pesa, aliifahamu vilivyo, ilikuwa namba ambayo haikuwahi kutoka kichwani mwake.

“John!” alijikuta akisema kwa mshtuko, akaamua kuipiga, mwanaume huyo akapokea.

“Halooo!” aliita.

“Halo John!” aliita msichana huyo.

“Deborah?”

“Ndiyo! Ni mimi hapa!” alijibu Deborah! Tayari machozi yakaanza kumtoka, kile alichokuwa amekisoma kwenye gazeti kilimuumiza kupita kawaida.

Yule John, kijana masikini alikuwa akihitaji kiasi cha shilingi milioni hamsini na tano ili watoto wake walioungana wakatenganishwe nchini India.





 John alikuwa akitetemeka, moyo wake ulikuwa na hofu kupita kawaida, ile sauti ya moyoni mwake iliyomwambia mke wake alifariki dunia iliendelea kusikika kichwani mwake. Ilimtisha na kumfanya kulia kama mtoto mdogo, mashavu yake yalilowanishwa na machozi yaliyokuwa yakiendelea kumbubujika kama kawaida. Baada ya sekunde kadhaa, wakaingia ndani ya ofisi ya daktari yule, akakaa kwenye kiti na kuanza kuzungumza naye. Alimwambia hali halisi, mkewe alijifungua watoto walioungana, wote walikuwa wa kiume lakini hakuwa kwenye hali nzuri, walitakiwa kumuacha apumzike kwani hakujifungua kwa hali ya kawaida, alifanyiwa upasuaji. “Pole kwa matatizo!” alisema daktari. “Mke wangu amepona?” “Ndiyo! Tulimfanyia upasuaji!” alijibu daktari. John akatoka kwenye kiti, akapiga magoti na kuiinua mikono yake juu, akaanza kumshukuru Mungu kwani kile kilichotokea kwake kilikuwa muujiza mkubwa. Alishindwa ni kwa namna gani alitakiwa kumwambia Mungu ahsante kwani hata neno lenyewe aliona kama halikutosha kumshukuru kwa yote aliyokuwa amemfanyia. “Mungu wewe ni mwema kwetu, umetupa watoto walioungana, nilishukuru kwa hilo, nilipohisi mke wangu amefariki, bado ukamponya. Ninakushukuru Mungu, wewe ni Mungu muumba mbingu na nchi, ni Mungu ambaye matendo yako ni makuu mno, nashukuru sana kwa kumpa mke wangu nafasi ya kuishi te.....” alishukuru pale alipopiga magoti, hakumalizia maneno yake, akaanza kulia kwa uchungu uliochanganyikana na furaha nzito. Daktari akasimama alipokuwa na kumfuata, akamuinua na kuanza kumbembeleza kwani kwa jinsi alivyokuwa akilia, hakuonyesha kama angenyamaza. “Pole sana John!” “Usinipe pole. Ninamshukuru Mungu kwa matendo yake. Si kwamba nyie ndiyo mmemponya mke wangu na kujifungua salama, ni Mungu, miujiza yake ni mikubwa sana daktari...” alisema John. “Mshukuru sana Mungu!” “Nitamshukuru mpaka ninaingia kaburini!” alisema John. Baada ya kuzungumza machache wakiwa wamesimama, wakakaa kwenye viti na kuendelea. Daktari alimwambia kuhusu hali za watoto wake, jinsi walivyoungana kulikuwa na nafasi kubwa ya kutenganishwa na kuwa kama watoto wengine.





“Kuna aina nane za watoto kuungana! Hivi ni vitu muhimu sana ambavyo ningependa sana uvifahamu na ujue watoto wako wapo kwenye kundi gani,” alisema daktari huku akimwangalia John. “Sawa,” aliitikia kwa unyonge. “Kundi la kwanza linaitwa Cephalopagus. Hawa ni wale mapacha ambao wameungana kwa mbele, yaani wameungana kuanzia tumboni, kifuani mpaka kichwani, na ukiwaangalia kwa jinsi uso ulivyo unaweza kusema ni uso wa mtu mmoja, ila ukiwaangalia vizuri utagundua ni watu wawili kwani muonekano wa huwa tofauti na watu wengine,” alisema daktari na kuendelea: “Kundi la pili linaitwa Thoracopagus. Hawa ni mapacha walioungana kwa kuangaliana. Wameungana sehemu za tumboni, kwa maana hiyo hawa watu wanachangia utumbo mmoja, inawezekana hata kuwatenganisha ikawa vigumu,” alisema na kuendelea: “Kundi la tatu linaitwa Omphalopagus. Kundi hili ukiliangalia fufanana na kundi hilo la mwanzo ila hili kuungana kwao kuanzia tumbo mpaka kifuani huwa ni kwa kiasi kikubwa sana,” alisema na kuendea: “Na kundi la nne limaitwa Ischiopagus. Hili kundi huwa baya sana kwani watoto wanaungana na huwa na muonekano kama kenge ama mamba, wengi wakiungana kwa namna hii, hawachukui muda mwingi huwa wanakufa,” alisema huku akimpa kikaratasi kilichokuwa na picha ya watoto wote walioungana. “Kundi la tano linaitwa Parapagus. Hili kundi watoto wanaungana kuanzia kiunoni kwenda chini. Huwa wanachangia miguu miwili tu waliyokuwanayo, huwa hawana miguu minne, huwa na miwili tu,” alisema na kuendelea: “Kundi la sita huitwa Craniopagus. Hili kundi watoto huungana vichwa kwa kuangaliana, yaani paji la nyuso zao, kuwatenganisha huwa vigumu kwa sababu wanashea misuli ya vichwa vyao, hivyo huachwa hivyohivyo,” alisema. “Kundi la saba huitwa Pygopagus. Hili kundi watoto huwa wameungana kwenye makalio kwa nyuma, ni kundi jepesi kuwatenganisha, ila hadi kwa watalaamu,” alisema na kuendelea:



“Kundi la mwisho huitwa Rachipagus. Kundi hili watoto huwa wameungana makalioni kwa nyuma mpaka migongoni mwao. Ni vigumu kuwatenganisha kwa kuwa huchangia uti wa mgongo mmoja,” alisema daktari. “Watoto wangu wapo kundi gani kati ya haya?” “Hilo la saba!” alijibu daktari, John akashusha pumzi. “Pygopagus?” “Ndiyo! Wanaweza kutenganishwa, ila mpaka kwa watalaamu, kwa hapa Tanzania hatuna kwa sababu huwa na misuli mingi hapo kwenye makalio,” alijibu. “Kwa hiyo wasafirishwe?” “Ndiyo! Wapelekwe nchini India.” Huo ndiyo ulikuwa uamuzi wa hospitali hiyo, ilikuwa ni lazima watoto hao wasafirishwe na kuelekea nchini India kwa ajili ya kutenganishwa kama alivyoshauri daktari. Kazi kubwa ambayo ilikuwa mbele ya John ni pesa za kuwasafirisha kwenda huko, aliuona ugumu mbele yake, hakuwa na pesa za kutosha, ilikuwa ni lazima atafute pesa hizo kama tu alitamani kuona watoto wake wakitenganishwa na kuwa tofauti. Kwenye akaunti yake alikuwa na kiasi cha shilingi milioni saba ambazo alizidunduliza mpaka kufikia kiasi hicho ukiachana na milioni sita ambazo zilikuwa katika akaunti ya mkewe. Hakujua ni kwa namna gani angeweza kupata kiasi kilichobaki. Alizungumza na daktari, alimwambia kuhusu ugumu uliokuwa katika kufanikisha kuzipata pesa hizo, na kitu pekee alichomwambia ni kutafuta msaada kwa wananchi. “Niende nikaombe mitaani?” aliuliza John. “Hapana! Taarifa itolewe kwenye magazeti, weka namba yako na watu wakitaka kukusaidia, watakusaidia,” alisema daktari huyo. Hilo ndilo lililofanyika, siku iliyofuata haraka sana John akaondoka nyumbani na kuelekea katika ofisi za magazeti ya Nipashe na alipofika huko, akawapa habari hiyo, hivyo waandishi wakaondoka na kuongozana naye mpaka Muhimbili ili kupata uhakika wa kile alichokuwa amekisema. Walipofika huko, wakaonana na daktari ambaye aliwaambia kweli watoto wa mwanaume huyo walitakiwa kusafirishwa mpaka nchini India ambapo gharama zake ingekuwa kiasi cha milioni hamsini na tano. Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kutoa taarifa hiyo gazetini mpaka Deborah kukutana na tangazo hilo na namba ya John na kumtafuta.





 “Unaishi wapi?” aliuliza msichana huyo. “Nipo Kijitonyama, ila muda mwingi nipo hospitali!” alijibu. “Unamaanisha mkeo alijifungua mapacha walioungana ama nimesoma vibaya?” aliuliza Deborah, ukimya kidogo ukaingilia, Deborah akaita. “Ndiyo! Mungu ametujalia watoto ila kwa mapenzi yake ikawa hivyo!” alijibu John, sauti yake tu ilisikika kama mtu aliyekuwa na maumivu makali. “Naomba nije hospitali kukuona!” “Sawa. Nitashukuru!” alisema John. Simu ikakatwa na haraka sana msichana huyo kuelekea hospitali kuonana na John. Njiani alikuwa na mawazo tele, kichwa chake kilikuwa na mawazo, hakujua nini kingetokea mara baada ya kuonana na mwanaume huyo aliyempenda kwa moyo wa dhati ambapo ilipita miaka mingi pasipo kuonana. Moyo wake ukaanza kurudi tena kwa John, akaanza kukumbuka mambo mengi yaliyowahi kutokea kipindi cha nyuma baina yake na John, akahisi yale mapenzi yakirudi kwa kasi na ni kama yalifufuliwa kwa kasi kubwa. Baada ya dakika kadhaa akafika hospitali na kuanza kwenda alipoelekezwa na mwanaume huyo. Akafika huko, macho yake yalipotua kwa John tu, akahisi mapenzi mazito yakija moyoni mwake. Akashindwa kuvumilia, akamkimbilia na kumkumbatia na kumwagia mabusu mfululizo. Hakutaka kujali kama kulikuwa na watu, alikuwa mke wa mtu na John alikuwa na mke, alichokijali ni kuuridhisha moyo wake tu. “John!” alisema Deborah, kwa jinsi alivyochanganyikiwa kwa furaha, machozi yakaanza kumtoka. “Naam Deborah!” “Umekonda sana!” alisema msichana huyo. “Ni matatizo!” “Pole sana. Mungu ndiye anapanga kila kitu, imekuwaje kwani?” aliuliza msichana huyo. Hapo ikabidi wote wakae kwenye benchi na kuanza kumsimulia kila kitu kilichokuwa kimetokea tangu walipoachana. Deborah alikuwa kimya akimwangalia John, alimsikiliza kwa makini, kile alichokuwa akikizungumza kilimuhuzunisha na moyo wake ukakiri kwamba John aliletwa duniani kwa ajili ya kuteseka tu, hapakuwa na kitu kingine. “Kwa hiyo inahitajika milioni hamsini na tano?” aliuliza Deborah. “Ndiyo! Ila nina milioni kumi na tatu, kwa maana hiyo imebaki kama milioni arobaini na mbili!” alijibu John.





 “Mh! Ni kiasi kikubwa sana, ila nitajitahidi nipate hata nusu yake,” alisema Deborah kwa sauti ndogo mno. Haraka sana akachukua simu yake na kumpigia baba yake, alihitaji kumsikia katika hilo. Hakutakiwa kumficha, ilikuwa ni lazima amwambie ukweli kila kitu kilichokuwa kimetokea, jinsi John alivyokuwa na tatizo mpaka kufikia hatua hiyo. Baba yake alimsikiliza kwa makini, alichokiamini ni kwamba angemsaidia ama kumpa kiasi chochote kile lakini kitu cha ajabu kabisa, mzee huyo akamkatalia. “Baba! Yaani unashindwa kutoa hata milioni tano na pesa zote hizo ulizokuwanazo?” aliuliza Deborah huku akiwa na uchungu. “Kwanza kwa nini umekwenda kuonana na John?” lilikuwa swali lake la kwanza. “Mkewe ni mgonjwa!” “Hilo jibu halijaniridhisha! Unahisi mume wako atajisikiaje akisikia umekwenda kuonana na mwanaume huyo?” aliuliza. “Baba! Hayo yote yametoka wapi? Umesema hauna pesa, ninajua unazo ila hauna moyo wa kusaidia. Bado una chuki sana na John, sijajua kwa nini! Ila ninaamini nitamsaidia, nitauza hata kiwanja changu ila ni lazima nimsaidie!” alisema Deborah huku akionekana kumaanisha. John alikuwa kimya, mawazo yalimjaa na alishangaa ni kwa namna gani baba yake alikuwa na hasira juu yake na wakati aliachana na Deborah kama alivyokuwa ametaka. Alipomaliza kuongea naye, alimwambia John kila kitu, alichomwahidi ni kwamba angeuza kiwanja chake kilichokuwa Kilimahewa kwa lengo la kumsaidia. “Ninashukuru sana Deborah! Ninashukuru sana,” alisema John huku akitaka kupiga magoti, msichana huyo akamzuia. Walizungumza mengi na mwisho msichana huyo akaondoka zake. Akiwa njiani akakumbuka kuhusu Bwana Kinyora, meneja wa makao makuu ya kampuni yao ambaye alizungumza naye siku hiyo kuhusu ajira ya mumewe.





Aliamini kwa jinsi mwanaume huyo alivyokuwa na roho nzuri angeweza kufanya jambo lolote lile kwa ajili ya John. Akampigia simu na kuomba kuonana naye, halikuwa tatizo, mzee huyo akakubali na hatimaye kuonana na kuanza kuzungumza. Alimuhadithia kwa uchungu kuhusu John, alihitaji kumwambia ukweli kwani ndiyo ilikuwa njia mojawapo ya kupata msaada kwa kile kilichokuwa kimetokea. Mzee huyo alimsikiliza kwa makini mno, maneno aliyomwambia yalimgusa moyo wake, hakuamini kama kulikuwa na watu walikuwa wakipitia maisha ya mateso kama aliyokuwa akipitia mwanaume huyo. “Pole yake sana! Wewe kama Deborah utajitahidi kutoa kiasi gani?” aliuliza mwanaume huyo. “Nadhani milioni kumi!” “Kwa nini udhani?” “Kwa sababu nina milioni tano! Nitakwenda kuuza kiwanja changu kwa shilingi milioni tano, jumla nitakuwa na kumi!” alijibu. “Kwa hiyo imebaki milioni thelathini na mbili!” alisema mzee huyo. “Sawasawa!” “Kwa kuwa sisi pia tuna mfuko wetu, nitaongea na wafanyakazi, hiyo pesa tutamsaidia tu ili mradi watoto hao watenganishwe! Nadhani Mungu atatulipa kwa wakati wake,” alisema Bwana Kinyora. Ni kama Deborah hakuamini alichokuwa amekisikia, akahisi moyo wake kama ukichomwa na kitu kikali, haraka sana machozi yakaanza kumtiririka mashavuni mwake, hakujua kama yalikuwa machozi ya furaha ama uchungu. Akajikuta akisimama na kumkumbatia mwanaume huyo. Alimpenda sana John, ni kweli alitenganishwa naye lakini hakutegemea kuona mwanaume huyo akipata mateso, alikuwa radhi kumsaidia kwa lolote lile. Hasira yake ilikuwa kwa baba yake, alimchukia, hakuamini kama kweli mzee huyo alishindwa hataka kutoa milioni moja kumsaidia John, alikuwa na pesa nyingi lakini hakupenda kuambiwa lolote kuhusu mwanaume huyo. Akarudi hospitalini, akaonana na John ambaye alimpa taarifa kuhusu michango ya wananchi ilivyokuwa ikiingia kwenye simu yake mfululizo. Watu waliguswa na matatizo aliyokuwa akipitia, hilo lilimtia uchungu mno Deborah, kama watu ambao hawakumjua John, walimchangia ili watoto wake wasafirishwe na kupelekwa nchini India, ilikuwaje kwa baba yake ambaye aliwahi kuonana na mwanaume huyo na kuongea naye?





“Chuki dhidi ya baba yangu imeongezeka maradufu,” alisema Deborah.

Muda haukuwa rafiki, haraka sana akaondoka na kuelekea Kigoma kwa ndege, njia nzima alikuwa na majonzi tele, alijiuliza maswali juu ya hali aliyokuwanayo John lakini alishindwa kupata majibu.

Hakujua Mungu alikuwa na mpango gani kwake, alipitia matatizo makubwa mno, hakuwahi kupata furaha hata kidogo, kila alipokuwa akijiuliza kuhusu mwanaume huyo, moyo wake uliendelea kuwa na uchungu kupita kawaida.

Alipofika Kigoma, akaonana na wazazi wake, aliwaambia kuhusu roho mbaya waliyokuwanayo lakini hawakuonekana kujali kitu chochote kile kana kwamba huyo John aliwahi kuwafanyia jambo baya kupita watu wote.

“Mungu atawalipia kwa mabaya mnayofanya,” aliwaambia na kuondoka zake huku akiwa na hasira tele.

Mpango uliokuwepo ulikuwa ni kuuza kiwanja chake lakini asingeweza kufanya hivyo bila kumshirikisha mume wake. Usiku wa siku hiyo akamuita na kuongea naye, alihitaji ushauri juu ya kile alichohitaji kukifanya.

Jericho alimsikiliza mkewe, alivyokuwa akiongea alionekana kuguswa kwa kile kilichokuwa kimetokea. Alimwangalia Deborah, ni kweli alionyesha kuguswa na hali ya John na alihitaji kumsaidia kwa moyo mmoja.

“Pole sana! Kama tuna nafasi ya kusaidia! Tumsaidie,” alisema Jericho bila wivu wowote ule.

Wakati akizungumza hayo, simu ya Deborah ikaanza kuita, haraka sana akaichukua na kuipokea, ilitoka kwa Bwana Kinyora ambaye alihitaji kuzungumza naye.

“Mungu ni wa ajabu sana,” alisema mzee huyo kwenye simu, Deborah akawa na hamu ya kusikia ni kitu gani alitakiwa kuambiwa.

“Kwa sababu gani?”

“Nilizungumza na wafanyakazi, wamekubali kumsaidia John kwa pesa zao wenyewe, wakatwe kwenye mishahara yao,” alisema mzee huyo.

“Unasemaje?” aliuliza Deborah huku akiwa haamini alichokuwa akikisikia.

“Wamekubali! Wamesema watachanga kiasi cha shilingi milioni sitini kwa ajili ya John!” alisema mzee huyo.

“Un...as..ema..j..e..” Aliuliza Deborah, hakuamini alichokisikia, akaanza kulia hapohapo.

“Mungu ni mkuu Deborah! Kiwanja chako umeshakiuza?” aliuliza, Deborah hakujibu, alikuwa akilia kwa uchungu, hakuamini kile alichokuwa amekisikia.

Alibaki kwenye hali hiyo kwa dakika nzima ndipo akamwambia kwamba hakukiuza ila alizungumza na mumewe, wote wakakubaliana wauze kiwanja kwa lengo la kupata pesa hizo.

“Mumeo akakubali?”

“Bila kinyongo! Ndiyo nilikuwa nazungumza naye, wewe ukapiga simu!” alisema Deborah.

“Mungu ambariki sana. Ninakuhakikishia wiki hii ataanza kazi hapohapo Kigoma,” alisema mzee huyo, hapohapo akakata simu.





Matangazo yaliendelea kuwekwa kwenye magazeti mbalimbali, michango ilifanikiwa, wananchi waliokuwa na wema, kuguswa walichanganya mpaka kufikia milioni kumi.

Kilikuwa kiasi kikubwa cha pesa, haraka sana mchango kutoka katika kampuni iliyokuwa ikiendeshwa na Bwana Kiyora ikawasilisha mchango wake katika hospitali ya Muhimbili na hatimaye John, mkewe na watoto wao kujiandaa kwa safari ya kwenda nchini India.

Wakati John akipewa taarifa za michango hiyo alikuwa pembeni ya mkewe aliyekuwa kimya. Hakuongea kitu chochote kile japokuwa mume wake huyo alizungumza maneno mengi likiwa la kumshukuru kwa kumzalia watoto wawili hata kama walikuwa wameungana.

Juliana alikuwa akilia tu kitandani pale, maneno ya mume wake yalimgusa kupita kawaida kwani yalionekana kutoka ndani ya moyo wake kabisa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Baada ya dakika chache, daktari akaingia na kuwapa taarifa kwamba pesa zilipatikana, zilikuwa nyingi zaidi ya zile zilizokuwa zimechangwa hivyo walitakiwa kuanza safari haraka sana.

Hilo halikuwa tatizo, wakajiandaa, mawasiliano baina ya Muhimbili na Hospitali ya Ganga kutoka nchini India yakafanyika na hatimaye wakakubaliana watoto hao wapelekwe haraka sana.

“Kila kitu kipo tayari! Tunatarajia kuanza safari kesho,” alisema dokta, alikuwa akizungumza na John.

“Nashukuru sana! Na sisi tupo tayari!” alisema John.

John akampigia simu Deborah na kumshukuru kwa wema wake kwa kumwambia kwamba kila kitu kilifanikiwa kwa sababu yake, hakujua ni kwa namna gani alitakiwa kumshukuru ila alimwambia kungekuwa na zawadi nzuri ambayo angempa, zawadi ambayo hapakuwa hata na siku moja angeifikiria kuipata kutoka kwa mtu yeyote yule.

Wakaondoka, wakiwa ndani ya ndege ndipo Juliana akaanza kuongea japo kwa sauti ya chini. Alimwambia mume wake jinsi alivyompenda, alivyopenda watoto wake na kuwa tayari kwa kila kitu, hakuacha kumwambia ni kwa namna gani alimshukuru Mungu kwa yote yaliyokuwa yametokea katika maisha yake.

“Hilo ni la muhimu sana! Ila ninaomba unisamehe mke wangu!” alisema John huku akimwangalia mke wake.

“Hujanikosea mpenzi!”

“Hapana! Nimekukosea sana!”

“Kwa lipi?”

“Nilitaka kucheza kamari, nimeicheza mno na ndiyo imenigharimu sana,” alisema John huku akimwangalia mke wake.

“Sijakuelewa!”

“Najua ni vigumu kunielewa! Ila cha msingi naomba tumshukuru Mungu kwa kila kitu!” alisema John.

Mkewe akakubaliana naye lakini bado moyo wake ulikuwa na maswali mengi kuhusu kamari aliyoicheza mume wake huyo. Ndege ilichukua saa kadhaa ikafika nchini India ambapo tayari gari la wagonjwa kutoka katika Hospitali ya Ganga likawa mahali hapo. Wakapakizwa na kuelekea huko.

Kitu cha kwanza kabla ya yote kilikuwa ni jopo la madaktari kuonana, walikuwa na jambo la kuzungumza na pia kuipitia ripoti ya wagonjwa kutoka katika Hospitali ya Muhimbili.

Waliijadili na kukubaliana utenganisho wa watoto ufanyike kwani ilikuwa vizuri sana kwa kuwa bado walikuwa wadogo, hawakuona kama kungetokea tatizo lolote lile.

John hakujua Kiingereza, aliongea na daktari aliyetoka naye nchini Tanzania ambaye yeye ndiye alikuwa mkalimani wake.

Ripoti hiyo ndiyo ambayo iliwaambia ni wapi walitakiwa kuanzia, kwao, hilo halikuwa suala kubwa ila kitu walichokitaka ni kuwa makini zaidi kwa kuwa mahali pale walipoungana kulikuwa na misuli mingi ya damu.

“Dk. Rajiv utasimamia upasuaji! Kuwa na madaktari sita ndani ya chumba hicho,” alisema Dk Patel ambaye ndiye alikuwa kiongozi wao ndani ya kikao hicho.

Wakakubaliana na hivyo siku iliyofuata madaktari hao wakajipanga na hatimaye kwenda ndani ya chumba hicho kwa lengo la kufanya upasuaji huo.

Kabla ya kitu chochote kile, John na mkewe, Juliana wakapelekewa karatasi za kusaini ambazo zilimaanisha kwa lolote litakalotokea ndani ya chumba kile basi walikuwa tayari kulipokea.

***

Mzee Abraham alikuwa akitetemeka ofisini kwake, hakuamini karatasi alizokuwa ameletewa na watu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, TRA. Aliuona mwisho wake, biashara zake alizokuwa akiziendesha zilimfanya kuwa na malimbikizo makubwa ya kodi.

Ulikuwa mchezo wake, alijua kuucheza, alicheza na vigogo wakubwa kwa kujificha kulipa kodi kwa kuwa alikuwa akizichanga na watu wengine kutoka serikalini mpaka pale ambapo watu wa TRA walipogundua mchezo uliokuwa ukifanywa.

Walishangazwa ni kwa namna gani hawakumbaini mzee huyo, malimbikizo yake ya kodi yalikuwa makubwa mpaka kufikia bilioni mbili lakini hawakugundua kwani mbali na vigogo aliokuwa akicheza nao, pia kulikuwa na watumishi kutoka katika mamlaka hiyo ambao walistaafu.

Walimchachamalia, walimtaka kulipa kiasi hicho cha pesa vinginevyo biashara zake zingefungwa na kupelekwa mahakamani.

Pale ofisini alipokaa alichanganyikiwa, aliona kama dunia imemuelemea, alihitaji msaada na hakujua ni kwa namna gani angeweza kusaidiwa.

Alijisahau, alishindwa kuchanga karata zake vizuri na leo hii alikuwa akiingia kwenye matatizo makubwa kwa sababu tu ya madeni makubwa aliyokuwa akidaiwa na serikali.

Biashara zake zikafungwa na kutaifishwa na serikali na kumtaka kulipa kiasi hicho cha pesa, walimpa siku saba tu afanikishe malipo hayo vinginevyo wangempokonya nyumba zake tatu, magari na kumuacha mikono mitupu.

Pale ofisini alihisi kama presha ikipanda, mwili ulikuwa ukitoka jasho jingi na wakati kiyoyozi kilikuwa kimewashwa chumba kizima.

Akasimama na kuanza kuzunguka huku na kule, hakujua ni kitu gani kingetokea baada ya kunyang’anywa kila kitu, akaunti zake za benki kufungwa, yaani kiasi ambacho alibaki nacho mikononi ndicho ambacho kingeendesha maisha yake.

Akachukua simu yake na kupiga upande wa pili, mtu aliyempigia alikuwa mkurugenzi wa TRA ambaye kwa kipindi hicho alistaafu na nafasi yake kuchukuliwa na mtu mwingine.

Akazungumza naye na kuhitaji msaada wake kwani maji yalimfikia shingoni na hakuona kama angeweza kunusurika katika janga lililokuwa mbele yake.

“Hivi hukulipa tena tangu mwaka ule?” aliuliza mzee huyo, aliitwa Salumu.

“Ndiyo! Nilijisahau! Sijajua kwa nini nilijisahau namna ile,” alisema mzee Abraham.

“Ila ulitakiwa kulipa. Kipindi kile nilikusamehe kwa sababu tulifanya mambo makubwa sana, kumbe ukahisi ingekuwa hivyohivyo? Ndugu yangu, sijui nikusaidie nini!” alisema mzee huyo maneno yaliyokuwa mwiba mkali kwa mzee Abraham.

“Naomba uzungumze na mkurugenzi!”

“Huyu aliyeingia?”

“Ndiyo!”

“Haiwezekani! Nimesikia jamaa ni mkali sana, hana masihara hata kidogo! Anafuatilia malimbikizo yote ya kodi, kwenye hili janga haupo wewe tu bali mpaka wafanyabiashara wengine,” alisema mzee huyo.

“Kwa hiyo imeshindikana?”

“Ndiyo! Kwani wamekwambia ulipie kiasi gani?”

“Bilioni mbili!”

“Daah! Wamekuonea huruma, wenzako wameambiwa bilioni kumi halafu walikuwa na malimbikizo madogo kushinda wewe,” alisema mzee Salumu.

Bwana Abraham akakata simu, shati lake lililowanishwa na jasho jingi kwani alihisi kabisa huo ndiyo ungekuwa mwisho wake. Hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya.

Aliomba ushauri kwa watu wengine lakini hapakuwa na msaada wowote ule walioweza kumpa zaidi ya kumlaumu kwa kutokulipa kodi mpaka kufikia kiasi hicho cha pesa.

Hakufanya kazi tena, kila kitu alichokuwanacho kilinyang’anywa, akaunti zake benki zilifungwa, magari yake, kampuni yote yakachukuliwa na serikali.

Alidata, akawa anaongea peke yake kama kichaa. Ofisini hakukukalika, akatoka na kurudi nyumbani kwake. Kwa jinsi alivyochanganyikiwa mpaka akataka kupata ajali ya kizembe kabisa.

Alipofika nyumbani kwake, akaingia chumbani na kutulia. Mkewe alimwangalia, alijua kulikuwa na tatizo, haikuwa kawaida kwa mume wake kuwa na muonekano huo, alichanganyikiwa na hivyo kumuuliza.

Hakuwa na jinsi, kwa kipindi hicho alitamani kupata ushauri wa mtu yeyote yule hivyo akamwambia mkewe kila kitu.

Kama alivyochanganyikiwa mumewe na yeye akachanganyikiwa, alimwangalia mume wake, kwa jinsi alivyokuwa na presha alijua kungekuwa na tatizo hivyo akampigia simu Deborah ambaye akafika nyumbani haraka sana.

“Kuna nini?” aliuliza msichana huyo huku akimwangalia baba yake.

“TRA!” alijibu mama yake.

“Wamefanya nini?”

“Wanachukua kila kitu!”

“Kisa?”

“Malimbikizo ya kodi!” alijibu mama yake.

Deborah hakuamini alichokisikia, alichanganyikiwa, kwake, kila kitu kilichokuwa kimesikika masikioni mwake kilikuwa kama ndoto, akauliza mara kadhaa, majibu yakawa hivyohivyo kwamba ni malimbikizo ya kodi ndiyo ambayo yatafanya kupokonywa kila kitu.

“Mpaka nyumba?” aliuliza.

“Ndiyo! Wameanza na magari ya kampuni, wamezuia akaunti za benki, yaani kila kitu na baada ya siku saba wanavipiga mnada! Tutakuwa wageni wa nani sisi?” aliuliza mama yake na kuanza kulia kama mtoto mdogo.

Deborah akasogea pembeni na kuanza kulia kivyake, hakuamiani, alihisi kama alikuwa ndotoni, kila kitu kilichokuwa hakikuwa halisi.

Akamsogelea baba yake na kumwangalia. Kumbukumbu za John zikaanza kujirudia kichwani mwake, hakutaka kumficha, alimwambia kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika maisha yake kilikuwa ni malipo ya ubaya aliokuwa ameufanya.

Hawakumuelewa mpaka pale alipowaambia kuhusu John. Walimnyanyasa kijana huyo, pale alipohitaji kazi, akafanya figisu afukuzwe, alipohitaji msaada kwa watoto wake, alikuwa na uwezo wa kumsaidia lakini hakufanya hivyo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Kwa mara ya kwanza maneno ya Deborah kuhusu John yakaanza kumuingia kichwani mwake, akaanza kujuta, alitamani kumtafuta John na kumuomba msamaha lakini alichelewa kwani huyo John alisafiri kuelekea nchini India siku tatu zilizopita.

TRA hawakuwa na utani hata kidogo, kwa kuwa kulikuwa na malimbikizo makubwa ya pesa, wakaamua kuzifunga biashara zake, kuchukua kila kitu na nyumba zake tatu zote ziliingia kwenye mnada.

Deborah hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, akajaribu kuwasiliana na mzee Kayore na kumuhadithia kila kitu ili kama kulikuwa na uwezekano wa kuzungumza na watu wa TRA afanye hivyo lakini mzee huyo hakuweza kufanya hivyo.

“Ni vigumu sana Deborah! Nilitamani nimsaidie baba yako, ila haitowezekana!” alisema mzee huyo.

Kila alipopiga simu, hakupata msaada, alibaki na maumivu moyoni mwake. Baada ya siku saba, nyumba hizo zikapigwa mnada, zikanunuliwa na mfanyabiashara mmoja kutoka mkoani Mwanza, mwanaume aliyekuwa na pesa nyingi na hivyo wao kutakiwa kuhama humo ndani.

Bila kupenda Deborah akawahamisha wazazi wake na kuwapangia nyumba nzima katika Mtaa wa Kilimahewa, sehemu ambayo walitakiwa kuanza maisha upya.

Afya ya mzee Abraham ilikongoroka, alikonda kwa kipindi kifupi tu, yaani kila kitu kilibadilika, bosi yeye, leo hii alikuwa amepangiwa nyumba na mtoto wake, kila pesa ambayo alikuwanayo, ilipotea.

Aliishi huko na mkewe kwa mwezi mzima, heshima aliyokuwanayo mjini ikaondoka, mbaya zaidi kila mtu alijua kilichokuwa kimetokea.

Watu ambao walikwenda kumuona nyumbani kwake hawakuamini kama alikuwa yeye, alikonda, kitambi cha pesa kikawa kama tumbo la mtu aliyekuwa akiumwa kwashakor.

Kwa kupitia pesa za mtoto wao wa mume wake walikula vizuri lakini mzee huyo hakurudi katika hali ya kawaida, kila siku alikuwa mtu wa mawazo mazito, aliona aibu na muda mwingi alijiilaumu kwa kutokulipa kodi, kitu kilichochangia kuanguka kwake.

Mwezi wa pili ulipoingia ndipo binti yao, Deborah akawapigia simu na kuwaambia kulikuwa na mgeni aliyetaka kuwaona, alihitaji kuonana nao, wazungumze, na kuwaomba msamaha kwa yote yaliyokuwa yametokea.

“Ni nani?” aliuliza mzee huyo.

“John! Huu ndiyo muda wa kumuomba msamaha!” alijibu Deborah.

“Nikimuomba msamaha nitapata kila kitu nilichokuwanacho kabla?” aliuliza mzee huyo kwa jeuri.

“Hapana! Lakini si ulimkosea! Baba, kuomba msamaha si kitu kigumu, ni jambo dogo tu, kwani ugumu upo wapi? Inawezekana akawa masikini lakini bado anapokosewa anatakiwa kuombwa msamaha!” alisema Deborah.

Haikuishia hapo, mkewe naye alizungumza naye na kumwambia kuhusu suala la msamaha, yeye kama mama alikuwa tayari kuomba msamaha kwani kwa hakika kile walichomfanyia John hakikuwa kitu kizuri kabisa.

“Nipo tayari kuomba msamaha! Mume wangu! Tuombe msamaha!” alisema mke wake.

“Sawa,” aliitikia kwa unyonge.

Baada ya siku mbili John na mkewe Juliana wakiongozana na Deborah aliyekuwa na mume wake, Jericho wakaingia ndani ya nyumba hiyo, walionekana kuwa na afadhali ya maisha tofauti na kipindi cha nyuma.

Sura zao zilionyesha tabasamu pana lilionyesha kabisa roho zao zilikuwa safi kabisa, hapakuwa na mateso kama kipindi cha nyuma, yaani kwa kipindi hicho, mkono wa Mungu ulikuwa juu yao.









John na familia yake walikaa nchini India kwa muda wa wiki moja na nusu, madaktari walifanikiwa kwa asilimia mia moja kuwatenganisha watoto wao.

Ilikuwa ni furaha ya kila mmoja, japokuwa walitumia kiasi kikubwa cha pesa za michango ya watu lakini mwisho wa siku kile walichokuwa wakikihitaji na kumuomba Mungu kila siku hatimaye kilifanikiwa.

Waliwasiliana na Deborah wakiwa hukohuko, walimshukuru kwa wema wake kwani bila mwanamke huyo wasingeweza kupata msaada mkubwa kama walioupata hasa baada ya kwenda kuzungumza na Bwana Kayore.

Baada ya wiki ya pili kuingia, wakaondoka na kurudi nchini Tanzania. Safari ilikuwa nzuri, njiani walikuwa wakicheka kwa furaha, hawakuamini kama kile walichokuwa wamekifuata nchini India kilifanikiwa kwa asilimia mia moja.

Watoto wao walikuwa na sura nzuri, walifanana nao, waliwapa majina mazuri ya Godlove na Godson, yote yakiwa na maana ya upendo mkubwa wa Mungu aliowapa na kuwakabidhi watoto hao mikononi mwao.

Baada ya saa kadhaa wakafika nchini Tanzania ambapo wakapokelewa na madaktari na kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo waliwashukuru na watoto wale kupumzishwa kwa siku moja na kisha kuondoka kurudi Kijitonyama ambapo walipanga nyumba nzima.

“Ninakupenda mke wangu,” alisema John huku akimwangalia mke wake.

“Nakupenda pia!” alisema mwanamke huyo.

Maisha yakawa na furaha tele, walikaa jijini Dar es Salaam kwa wiki mbili kisha kurudi mkoani Kigoma kuendelea na maisha yao.

Walipofika huko, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuonana na Deborah na mumewe na kuwashukuru kwa wema wao, waliwaambia wazi kwamba bila wao basi inawezekana kabisa watoto wao wangefariki, ila kwa msaada wao mkubwa, walitenganishwa na kuwa wazima wa afya.

“Na sisi tunakushukuru sana, kupitia matatizo yenu, mume wangu amepata kazi,” alisema Deborah huku akimwangalia John.

“Ni Mungu! Ninajifunza mambo mengi sana katika ulimwengu huu, kama unapofanya ubaya tunasema malipo ni hapahapa duniani, basi amini hata unapofanya mema malipo huwa hapahapa,” alisema John huku akiwaangalia watu hao wawili.

Walizungumza mambo mengi, baada ya kumaliza, Deborah na mumewe wakaaga na kuondoka huku mioyo yao ikiwa na furaha tele.

Baada ya kumaliza kuzungumza nao, wakampigia simu mchungaji wao na kuwaambia kila kitu kilichotokea. Mwanaume huyo hakuwa na la kusema, katika maisha yake siku zote aliwaambia kuhusu kumtumaini Mungu kwani alikuwa muweza wa kila kitu.

“Kwa Mungu hakuna kinachoshindikana!” alisema mchungaji huyo.

“Kabisa!”

“Matatizo yetu yote, magonjwa yalimalizwa pale msalabani Goligotha alipoteswa na kufa Yesu Kristo, hatutakiwi kuwa na hofu tena, kwenye kila kitu, ni lazima tuamini matatizo yetu yaliishia pale,” alisema mchungaji huyo.

Jumapili iliyofuata, John na mkewe wakaelekea kanisani wakiwa na watoto wao. Kila mmoja alijua kilichokuwa kimetokea, kuwaona tena kanisani humo ilikuwa ni furaha ya kila mmoja.

Mama yake Juliana kila siku alikuwa mtu wa kulia tu, kilichokuwa kikiendelea kilimpa furaha ya ajabu, alimshukuru Mungu kiasi kwamba alijiona alifanya hivyo kuliko mtu yeyote katika dunia hii.

Aliwapenda wajukuu zake zaidi ya kitu chochote kile, aliacha kufanya mambo yake, muda mwingi alikuwa na wajukuu hao ambao walimpa furaha ya ajabu.

John na Juliana wakaanza kutoa ushuhuda kanisani hapo, kila kitu kilichokuwa kimetokea katika safari yao ndefu ya kuwauguza watoto wao.

Waliongea mambo mengi lakini kwenye yote hayo yalibebwa na neno moja lililoitwa shukrani, yaani kumshukuru Mungu kwa mambo yote, waliamini yeye ndiye aliongea na Deborah, yeye ndiye aliyewagusa watu kuwa na moyo wa huruma na kuwasaidia kwa mambo yote yaliyotokea.

“Kwenye maisha yako, mtu anapokuwa na tatizo, wewe msaidie tu,” alisema John huku akiwaangalia washirika wa kanisa, walikuwa kimya wakimsikiliza.

“Unapomsaidia mtu, hujui ni kwa namna gani Mungu atakurudishia malipo ya wema wako. Inawezekana ukawa unasumbuliwa sana na magonjwa, lakini baada ya kuanza kuwasaidia watu wenye matatizo, magonjwa yanapotea mwilini mwako. Malipo ya Mungu si pesa tu, kuna wakati anafanya miujiza katika maisha yako kupitia afya yako!

“Unaweza kuona huumwi kama watu wengine, mambo yako yanafanikiwa, kumbe bila kujua, Mungu anakulinda kwa sababu tu unatenda wema kwa watu wenye matatizo,” alisema John huku akianza kulengwa na machozi.

“Leo kuna watu wametusaidia bila kutujua! Wamesikia tuna matatizo, wametusaidia tu. Mtu anayekusaidia si lazima awe anakufahamu, na usitake kila unayemsaidia lazima umfahamu, hapana!

“Unapoguswa kumsaidia mtu fulani, saidia, usiangalie dini, kabila ama cheo cha mtu, kuna masikini wengi wana mahitaji, wasaidie, wengine wana nguo nyingi kabatini, wanajisifu kuwa na nguo lukuki, ni ajabu wanapopita mitaani wanawaona watu wana nguo zilizochakaa na bado hawawasaidii.

“Inawezekana kuna wengine mambo yenu hayafanikiwi kwa sababu hamsaidii watu, umesoma, una vyeti vimekaa tu ndani lakini hupati kazi, yote ni kwa sababu kwa kidogo ulichonacho hutaki kuwasaidia wasivyonavyo.

“Huu ndio moyo niliotaka sana kuuona kwa kipindi kirefu, nilihitaji kujua ulimwengu wa pili watu walikuwa wakiishi vipi. Unapokuwa kwenye ulimwengu huu, watu wanakuchukuliaje! Sikuwahi kuishi maisha haya niliyokuwa nikiishi kwa miaka miwili, nilikuwa nayasikia tu kwa sababu nilizaliwa kwenye familia ya kitajiri, baba yangu ni bilionea.

“Kwenye maisha yake aliniambia kuna siku nitatakiwa nijifunze maisha ya upande wa pili, niwe na njaa kama wengine, niteseke ili siku mtu akija na kuhitaji msaada, basi nijue aliteseka kwa kiasi gani,” alisema John na kuwafanya watu kuwa makini kanisani hapo, si hao tu bali hata mke wake.

“Nilipokwenda India kwa ajili ya watoto wangu, baba na mama yangu walikuja kutoka nchini Australia wanapoishi na kufanya biashara zao. Waliponiona, wakanisogelea na kunipongeza, waliniangalia machoni, sikuwa John yule wa kipindi cha nyuma, nilichakaa mno, nilikonda, hilo ndilo jambo ambalo walikuwa wakilitaka sana, kunifundisha mtoto wao maisha ya upande wa pili, jinsi masikini wanavyo...” alisema John, hakumalizia sentensi yake, akanyamaza na kuanza kulia.

Kila mmoja alimshangaa John, maneno aliyoyasema hayakuaminika, mchungaji ni kama alipigwa na butwaa, yaani kanisa zima lilikuwa likimshangaa, hawakuamini maneno aliyokuwa akiyaongea mwanaume huyo.

“Au ndiyo kamari aliyoniambia alikuwa akiicheza?” alijiuliza mke wake.

Alizungumza mambo mengi mno, historia ya maisha yake, sababu iliyomfanya kwenda mkoani Kigoma na mambo mengine mengi aliyowahi kukutana nayo.

“Mpaka sasa hivi sijaelewa,” alisema jamaa mmoja.

“Kwa nini?”

“Yaani huyu John ni bilionea! Kivipi yaani mbona kama amenichanganya?” aliuliza jamaa huyo, maneno hayo yote yaliwafanya watu kumshangaa tu.

“Sisi kama watu wenye kitu kidogo ni lazima tuwasaidie wale ambao hawana kitu, leo mtu akishiba, ukimwambia kama hapa duniani kuna njaa, atakataa kwa sababu yeye ameshiba. Tunapopata tunachokitaka ni lazima tuwasaidie wale ambao hawana,” aliendelea kusema na kuendelea:

“Mungu na malaika ni roho, tunapoomba kuwaona, haimaanishi watakuja kwa njia ya roho, wanatufuata kwa njia ya mwili, inawezekana njiani ulimuona malaika anaomba akiwa kwenye mwili wa mwanaume aliyechakaa na ukampita bila kumsaidia kwa lolote lile na wakati ulikuwa na pesa nyingi tu,” alisema na kuendelea.

“Kuna wanawake wengine wanauza mbogamboga mitaani, umetoka kununua vyakula vya kupika nyumbani vya laki mbili kwa wiki nzima, unakutana na mwanamke huyu, anauza fungu la mchicha shilingi mia tatu, bila aibu unaanza kumshusha akuuzie kwa mia mbili! Tena unalalamika kabisa,” alisema John, akanyamaza, machozi yaliendelea kutitika, akachukua kitambaa chake na kuanza kujifuta.

Baada ya kumaliza wakarudi kukaa. Yeye na mke wake walikuwa wakilia tu, Juliana hakuamini alichokisikia kwa mume wake, aliamini siku zote walikuwa masikini wa kutupa kumbe haikuwa hivyo, John alikuwa na sababu zake kufanya hivyo, baba yake alimshinikiza kwa sababu alimtaka kuyajua maisha ya upande wa pili.

Baada ya ibada kumalizika, akampigia simu Deborah na kuhitaji kuonana naye, alihitaji kuzungumza naye mambo mengi mbele ya wazazi wake kabla ya kuondoka na kwenda kuishi Dar es Salaam.

“Kwenda kuishi Dar es Salaam?” aliuliza Deborah.

“Ndiyo!”

“Kwa nini unahama Kigoma?”

“Nakwenda kuishi kwangu!”

“Sijakuelewa!”

“Naomba nionane na nyie wote, wazazi wako, nitahitaji kuzungumza nao leo hii,” alisema John.

Hilo halikuwa tatizo, baada ya kukubaliana jioni ya siku hiyo wakaondoka na kuelekea nyumbani kwa mzee Abraham. Alipofika na kumwangalia, hakuamini macho yake, mzee Abraham alikonda mno, hakuwa kama alivyokuwa, hakushangaa kwa sababu alijua kila kitu kilichokuwa kimetokea.

“TRA si mchezo!” alisema John, alikuwa akimwambia Deborah.

“Umejuaje?” aliuliza, John hakujibu, akaachia tabasamu tu.

Wakasalimiana na kuanza kuzungumza nao. Hakutaka watu hao waombe msamaha, yeye ndiye akajifanya kuwa na kosa, si kwamba alikosewa bali yeye ndiye aliwakosea.

Deborah alishangaa, hakujua John alijuaje hayo yote. Akakaa chini na kuwaangalia watu hao, aliporidhika akaanza kuzungumza nao.

“Naomba mnisamehe kwa sababu sikutaka kuishi kama ambavyo nilitakiwa kuishi, inawezekana ndiyo sababu ya nyie kunichukia,” alisema John.

“Unamaanisha nini?” akauliza mama yake Deborah.

“Naomba niwahadithie kidogo historia ya maisha yangu, baada ya hapo nitakujibu swali hilo uliloniuliza,” alisema John na hapo ndipo akaanza kuwasimulia watu hao historia ya maisha yake mpaka kufikia hatua ya kwenda mkoani Kigoma.





MIAKA KADHAA NYUMA

Hali ya hewa ilibadilika kwa kiasi fulani, lile jua lililokuwa likiwaka kipindi kifupi kilichopita likafunikwa na mawingu mazito yaliyoanza kutanda angani kitu kilichoonyesha muda wowote ule mvua kubwa ingenyesha ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Kijana John Marcela alikuwa ofisini kwake, aliiona saa ikienda taratibu kwa sababu siku hiyo majira ya saa tatu alitakiwa kuwepo kwenye ukumbi wa Twiga uliokuwa Makumbusho kwa ajili ya kuhudhuria sherehe ya harusi ya rafiki yake kipenzi Cosmas Lyaruu.

Alikuwa na hamu ya kuwaona watu hao wawili wakiwa pamoja. Alikuwa na furaha mno, alimkumbuka rafiki yake huyo ambaye alikuwa mbishi mno kila alipokuwa akimwambia kuhusu kuoa.

Waliweka madau kwamba kila mmoja angekuwa wa mwisho kabla ya mwenzake kuamua kufunga ndoa. Kila walipokutana walikumbushiana ahadi yao lakini bila kutarajia, baada ya Cosmas kukutana na msichana aliyeitwa kwa jina la Cindy Masanja, hakuwa na ujanja tena, akajikuta akiamua kufunga naye ndoa.

John alitamani kumuona Cosmas akiwa na mke wake, hakujua ni kwa namna gani angecheka kiutani na kumwambia yeye alikuwa mshindi wa ahadi ile waliyokuwa wameiweka kwa kipindi kirefu.

Muda mwingi macho yake yalikuwa kwenye saa yake ya ukutani. Alikuwa mtoto wa trilionea mkubwa aliyekuwa na utajiri unaokadiriwa kuwa kiasi cha shilingi trilioni ishirini na nane.

Baba yake, mzee Marcela alikuwa akimiliki makampuni matano, matatu yakiwa nchini Tanzania na mawili yakiwa nchini Afrika Kusini. Yeye ndiye alikuwa mzalishaji mkubwa wa mbao, mkaa, nafaka nchini Tanzania.

Alikuwa akipewa tenda mbalimbali na serikali kama kuleta kompyuta kwenye mashule, kuingiza pembejeo na mambo mengine mengi, kwa kifupi alikuwa mtu mwenye pesa ndefu.

Kwa kuwa alikuwa na utajiri huo, aliamua kumuita kijana wake, John na kuzungumza naye, alichomwambia ni kwamba alitamani sana siku moja aone akisimamia kampuni yake mwenyewe na si zile za familia kama ilivyokuwa.

Alitamani sana kumfundisha kuhusu biashara, alikuwa na mtoto mmoja tu hivyo aliwekeza muda wake na utajiri wake kwa John huyohuyo.

Maisha ya John hayakuwa ya kuridhisha, alijua baba yake alikuwa trilionea mkubwa, aliisha maisha aliyokuwa akiyataka kipindi hicho. Alipenda sana wanawake, alilala na mwanamke yeyote aliyekuwa akimtaka kulala naye.

Alijua kuzitumbua pesa za baba yake, hakuwa mlevi, hakuwahi kwenda klabu, kuvuta bangi wala sigara ila alipenda sana kulala na wanawake.

Wanawake aliokuwa akilala nao walikuwa ni kutoka katika familia za kitajiri. Hakuwa akilala na mwanamke aliyetoka kwenye maisha ya kimasikini, hakuwapenda kwa kuwa aliamini wengi ambao wangemkubali wangefanya hivyo kwa sababu ya pesa tu, hivyo akaamua kuwafuata wanawake waliokuwa wakitoka kwenye maisha kama aliyokuwa akiishi.

Baada ya baba yake kuona akipotea kwa kutumia sana pesa, akaamua kumuuliza ni kitu gani alitamani sana kuona akimfanyia. Hilo lilikuwa swali gumu kwa John, akaomba muda, angemjibu kwani alitamani sana kumwambia kitu ambacho kingekuwa na msingi mkubwa kwa maisha yake.

Haraka sana akamvutia waya rafiki yake, Cosmas na kumuuliza kwa staili ya kuomba ushauri na ndipo kijana huyo akamwambia amuanzishie kampuni.

“Kampuni gani?” aliuliza John.

“Kusindika samaki! Yaani uwe msambaji mkubwa wa samaki kutoka Kigoma na Mwanza kwa hapa Dar,” alijibu mwanaume huyo.

“Kwa hiyo niwe muuza samaki?” aliuliza.

“John! Sio muuza samaki bali ni mkurugenzi wa kampuni ya kusindika samaki!” alisema Cosmas.

John akakaa kimya kwa muda, akajifikiria sana lakini mwisho wa siku akakubaliana na rafiki yake huyo na hatimaye kumwambia baba yake.

Haraka sana mzee Marcela akafungua kampuni hiyo jijini Dar es Salaam huku ikiwa na matawi mkoani Kigoma na jijini mwanza ambapo kwa huko Kigoma iliitwa Kigoma Fishing Transport na Mwanza kuitwa Mwanza Fishing Transport, yalikuwa kama matawi ya kampuni yake iitwayo Fishing Company iliyokuwa na makao makuu jijini Dar es Salaam.

Matawi hayo yalitakiwa kuwaajiri wavuvi na kuwapa boti kwa lengo la kwenda ziwani kuvua samaki na kuwapeleka katika kiwanda cha kampuni hiyo ambapo waliandaliwa na kisha kusafirishwa kuelekea jijini Dar es Salaam na hapo wengine kusafirishwa kuelekea nchi mbalimbali.

Ilikuwa ni biashara kubwa kipndi hicho, ilionekana kuingiza kiasi kikubwa cha pesa. Makao makuu ya kampuni hiyo yalikuwa Tabata jijini Dar es Salaam lakini yeye akataka ofisi yake iwe Posta.

“Siwezi kukaa uswahilini kule,” alisema alipoulizwa na baba yake kuhusu ofisi yake kuwa Posta.

Wakati John akifikiria hayo yote huku akiwa ofisini kwake, mara simu yake ikaanza kuita, haraka sana akakurupuka na kuichukua kutoka mezani na kuangalia kioo.

“Peter...” alisema na kisha kuipokea.

“John! Unakuja muda gani?” lilikuwa swali kutoka kwa kijana huyo.

Hapo ndipo alipokumbuka kwamba alitakiwa kuonana na Peter na baadhi ya marafiki zake kwa kuwa walikuwa wamemuandalia zawadi Cosmas kama marafiki zake.

Hakukumbuka hilo, alipoambiwa, akakumbuka kila kitu na hivyo kumwambia muda huo walitakiwa kuonana Serena Hotel kwa lengo la kuzungumza.

“Nakuja Serena!” alisema John.

“Poa! Tunakusubiri! Ila acha gari! Kuna bonge la foleni!” alisema Peter.

“Siwezi kutoka hapa Posta ya Zamani mpaka hapo na gari! Natembea kwa miguu tu,” alisema John na kukata simu.

Hakutaka kubaki humo, haraka sana akasimama na kuondoka zake. Alipanda lifti na kuteremka. Kila mtu aliyekuwa akimwangalia, alimuheshimu, alikuwa kijana mdogo lakini mwenye pesa nyingi.

Akatoka getini na kuelekea nje, alipofika huko akaunganisha na lami kutoka upande wa bandari ya Azam ilipo, akawa anakwenda kule kulipokuwa na Hoteli ya New Africa.

Alitembea kwa mwendo wa taratibu kuelekea Posta Mpya, alipofika karibu na Sanamu la Askari macho yake yakatua kwa msichana fulani aliyekuwa amevalia gauni refu jekundu huku kichwani akiwa amezibana nywele zake.

John akasimama kwa sekunde chache na kuanza kumwangalia msichana yule, alivutia, alikuwa mpole tu kwa kumwangalia, alibeba mkoba wake huku akiwa na simu yake mfukoni.

Alikuwa mzee wa wanawake, aliwajua wanawake kama aliwazaa yeye. Mwanamke aliyekuwa msafi, alijua kwa kumwangalia tu, hata aliyekuwa mchafu wa mwili, hata kama alioga na kupaka mafuta yote duniani bado alimjua.

Akakatisha safari yake na kuanza kumfuata. Akaanza kushika barabara iliyokuwa ikienda katika Chuo Cha IFM, alikazana zaidi mpaka alipolipita duka la SH Amon, akavuka barabara na kuelekea sehemu iliyokuwa ikiuzwa vitabu mbalimbali, msichana akasimama hapo. Naye akamfuata.

Akasimama pembeni yake, meza ya vitabu iliyosimama ilikuwa mbele yake, walikuwa wakiviangalia vitabu vile kana kwamba na yeye alikuwa mteja. Alitamani kumuongelesha lakini akasita, akaona kama angeonekana kuwa na haraka sana, hivyo alikuwa akimvutia pumzi kwanza.

“Unapenda sana kusoma vitabu?” akaamua kuuliza baada ya sekunde kadhaa bila hata salamu.

“Yeah!” alijibu msichana huyo kwa kifupi huku akiwa bize kuchukua kitabu kimoja baada ya kingine.

“Safi sana! Kuna mambo mengi yanafichwa kwenye maandishi! Naweza kukununulia kitabu ukasome?” aliuliza, msichana huyo akashtuka na kuanza kumwangalia.

“Uninunulie kitabu?”

“Ndiyo! Ila kama inawezekana!”

“Unataka kuninunulia vingapi?”

“Wewe unahitaji vingapi?”

“Meza nzima!”

“Haina shida!” alisema John na kutoa tabasamu pana.

Naye msichana huyo akatoa tabasamu.

“By the way! Naitwa John Mtoto wa Uswahilini!” alisema huku akimwangalia msichana huyo na kumpa mkono.

“Naitwa Amanda!”

“Unaelekea wapi?”

“Kuna watu nakwenda kuwaangalia hapo chuo!”

“Unasoma hapo?”

“Hapana nafanya kazi!”

“Wapi?”

“Hapo Mafco!”

“Oh! Kwenye jengo la Benjamini Mkapa?”

“Yaap!” alijibu msichana huyo.

John akashusha pumzi, ni kama aliishiwa maneno, alitulia na kuanza kujifikiria ni kwa namna gani alitakiwa kuendeleza stori na msichana huyo.

Hakutaka kumuacha, ilikuwa ni lazima aendelee kuzungumza naye, amzoee na mwisho kabisa kumuomba namba zake.

“Naomba nikununulie vitabu viwili Amanda,” alisema John.

“Si meza nzima tena?”

“Ukitaka napo hakuna shida!”

“Sawa. Nahitaji viwili nikasome!”

“Unahitaji kipi na kipi?”

“Dili la Dola Bilioni Nne na Damu ya Mwanamwali Kitandani,” alijibu msichana huyo.

“Hakuna shida.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Akamsogelea muuzaji, mzee fulani wa makamo na kumpa kiasi cha pesa kilichohitaji na kisha kuendelea na safari, muda huu wakawa wanaongozana na kuongea pamoja.

Kila mmoja alionekana kuwa na furaha isiyo kifani, John alijisikia fahari mno, hakuamini kama hatmaye alikuwa akitembea na msichana mzuri kama Amanda.

“Naomba nichafue kitabu chako kimoja,” alisema John huku akimuomba kitabu, akapewa, akatoa kalamu yake na kuandika namba yake ya simuu.

“Naomba unitafute ukipata nafasi!” alisema huku akimrudishia.

“Sawa! Nikipata nafasi! Ahsante kwa vitabu!” alisema Amanda huku akitoa tabasamu.

“Usijali!” alisema John.

Akageuza na kuendelea na safari yake. Yaani msichana mrembo aliisitsha safari hiyo kwa muda. Ni kawaida ya wanaume wote duniani hasa wanapokutana na wanawake wazuri.











ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog