Search This Blog

Tuesday, 1 November 2022

ZEE LA NYWILA - 3

 






Simulizi : Zee La Nywila
Sehemu Ya Tatu (3)




Siku zilizidi kuyoyoma, Abuu taratibu aliendelea kupata matibabu, hadi ilipofikia asubuhi moja ya matumaini.

Katika asubuhi hii, Abuu aliweza kukutanisha mboni za macho yake na mwanga wa jua, aliweza kuyaona vizuri mazingira yaliyomzunguka.

Ilikuwa ni ndani ya kajijumba kadogo, juu yake kameezekwa kwa makuti, kutaze zikiwa zimesimamishwa kwa udongo mwekundu uliosindikwa vilivyo.

Hakika Abuu alikuwa ni mithili ya aliyezaliwa upya, dunia ilikuwa ngeni katika uoni wake.



" Usijali kijana wangu, utaendelea kuwa sawa!" Ghafla, alisikia sauti aliyoizoea kuisikia siku zote tangu aingie chumbani humu, akageuza shingo ili amtazame, japo ni kwa tabu sana ila alijikalifu akaweza.

Ni mzee wa makamo, sura yake ikiwa imetapakaa tabasamu lisiloonekana vizuri kutokana na usawajikaji wa ngozi yake.

Huku mdomo wake ukijaa mapengo ya meno machache yaliong'oka na kuvunjika.

Abuu alimtazama shaibu huyu kwa sekunde chache, kabla ya kujikaza na kuufungua mdomo kumuongelesha…

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"Wewe ni nani? Umenitoa wapi? Na nime, nimekaa, nimekaa, hapa kwa mu….mu….muda ga… koh! Koh! Koh!"

Kikohozi kikali kikamkatisha.



Lakini yule mzee alishamuelewa,kwa. utulivu wa hali ya juu alimjibu….

"Kuwa na amani kijana, Mimi ni muuguzi tu wa kijiji hiki cha UHENDE, hapa kisiwani Mafya.

Wiki mbili au tatu zilizopita, uliokotwa na wavuvi wa kijiji, wakakuleta moja kwa moja kwangu. Hawakushindwa kukupeleka hospitali, ila zahanati zetu ziko mbali mno.

Pole sana kijana! Inaonekana ulipata maumivu makali kutokana na kipigo. Kipindi nakupokea, nilitegemea utakufa ndani ya siku tatu tu.

MUNGU katenda maajabu kwako kijana wangu, hatimaye umeanza kuonesha nuru".



Maneno haya machache yenye uzito wa haja, yaliukandamiza mtima wa Abuu kwa hisia Kali. Hakujibu kitu.

Walakini, yalimfanya kuwa katika hali mbili tofauti kwa wakati mmoja.

Kwanza aliwaza kuhusu unyama na uhasidi aliofanyiwa na kina Patrick. Pia, aliuona wema wa hali ya juu aliotendewa na watu wa kijiji hiki.



……

Kadri yaumu zilivyojongea, Abuu alipata nafuu. Aliweza kuongea vizuri, alicheka, akakaa, akaweza kusimama, akatembea hadi kukimbia.

Kiufupi, alirejea uborani mwake.



Ni jioni moja yenye upekee sana, hasa kwa Abuu.

Leo aliamua kuelekea ufukweni, hapahapa kisiwani Mafya, ili apate fursa tulivu ya kuiwaza hatma ya maisha yake.

Aliwaza mengi mno, ikibidi kuacha kabisa aina ya maisha aliyoianza miezi michache iliyopita.Alitamani arudi na kuitwa tena ABUUBAKAR KHALFAN, jina alilopewa na mzaziwe tangu udogoni.

Alitamani hata daima aishi hukuhuku kisiwani.



Ila, upinzani ukatoka chini ya uvungu wa moyo wake.

Ataweza?

Vipi kuhusu mama yake huko mjini alipoondoka? Yuko katika hali gani?

Yote haya yalimjia tafakurini mwake.

Haya ndiyo yalifanya amkumbuke G.C.I, huyu ndiye atakuwa msaada wake mkubwa kama akiamua kurudi Dar.



Isiwe nongwa, kama ni maji tayari mtupu kayakalia. Abuu aliamua arudi tena mjini. Kama ni kifo ameshakikaribia, nini aogope sasa?

Abuu akaweka nadhiri, anarudi kuwa ZEE LA NYWILA zaidi ya mara mbili, na wote waliomfanyia ukatili, atawaonesha ipi ladha ya pilipili.

Aliinuka kutoka alipokuwa ameketi, akasimama juu, alijinyoosha na kuelekea nyumbani, kule kwa yule muuguzi.

Aliwahi akajiandae jioni hii hii , kesho asubuhi na mapema aanze safari ya kwenda kuwaonesha wakina Harrison na Patrick kuwa; Chura waliyempiga teke sebuleni, amedondokea chumbani, tena kitandani.



"Hivi, siku naokotwa, sikukutwa na kitu chochote?"

Abuu alimuuliza yule mzee Muuguzi.



Nyakati za jioni, wawili hawa hupendelea kukaa chini kuzungumza mambo mengi. Mzee huyu alisimulia visa vyake vingi, hasa vya ujanani kwa Abuu.

Abuu nae alihadithia vyake avijuavyo. Ila, alimdanganya vyote. Hakuweza kumueleza ufedhuli anaoufanya. Mzee atamchukuliaje unadhani?



"Hapana. Ulikutwa hata nguo huna. Kama ulivyozaliwa," alijibu yule mzee, macho yake yakiwa yameelekea motoni.

Moto huu waliuwasha uwapatie joto. Kisiwani hapa, usiku huwa hakukaliki nje, kwa baridi kali.



Abuu hakuongeza neno. Bado maumivu makali ya kihisia yalizi kuutafuna mtima wake.

Alizidi kuijutia nafsi. Laiti asingeiruhusu tamaa imtawale. Yote haya angeishia kuyasikia tu. Sasa yamemkuta!



Walaakini, Majuto ni mjukuu, huja baadaye. Lakini, si kwamba ndiyo mwisho wa uzazi. Huenda jitihada mpya, zikaleta kitukuu-faraja.

Abuu alilala usiku huu, ndoto zake zikitiwaliwa na safari ya kesho yake, kuisaka hiyo faraja. Kwa jasho na damu!



***



SAFARI ilikuwa ni ya masaa mengi kidogo. Hatimaye, Abuu aliikanyaga kwa mara nyingine ardhi ya Mzizima.



Mandhari hayakuwa mageni kwake. Bali yeye ndiye aligeuka mgeni kwa mandhari.

Hakuwa hivi mara ya mwisho kuwepo jijini hapa.

Ilikuwa aidha umkute kavaa suti au nguo za kawaida tu...lakini zenye kumpa 'wadhfa' wa hali ya juu.

Leo alikuwa tofauti sana. Hajapendeza hata!



Kwa mwendo wa wastani, alitoka katika lango la Kituo kikuu cha mabasi, Ubungo.



"Naelekea wapi sasa?"aliwaza.



Hakujua wapi aelekee.

"Ni nani atanipokea?"alijisaili.

ZAINAB SAID, lilimjia jina hili.



Zainab. Mrembo wa kipemba huyu, ni mmoja wa wasichana alioruka nao hapo zamani. Msichana huyu alimpenda sana Abuu, sana!



Pamoja na utajiri aliokuwa nao, alikuwa radhi, mali zote amuachie Abuu, kwa penzi tu yani.

Wewe unasema mapenzi yamekuteka? Kuna wenzako yamewatia 'undondocha'.



Zainab alishaolewa, baadae akaachika.

Kitu kilichomfanya asitamani tena, kuja kuitwa mke.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Hata kwa Abuu, alimhitaji waishi tu bila kuona...walifaidi tunda kwa mlango wa nyuma.

Usinielewe vibaya, namaanisha bila kuoana!



Aula ya yote, Zainab haishi mbali na hapo alipokuwepo Abuu. Anaishi Ubungo-Kibangu tu hapo.



Maswali yalibaki kwa Abuu.

Je, bado atakuwa anaishi eneo lilelile?

Kama ndiyo. Atapokelewa? Ilihali, aliwapa mamba ya nguoni, kabla hajaingia mtoni!



Ila, alijipa matumaini. Kama aliweza kumuamini, akamuachia auline mzinga wake wa asali , vipi atafeli kumshawishi ampokee?

Atakubali tu.

Safari ya kwa Zainab ilianza.



Uchovu wa safari, ulimlazimu akodi pikipiki.

Dakika ishirini tu, alishafika nje ya geti kubwa jeusi.

Hapa ndipo kwa Zainab. Akagonga!



Dakika chache, alitoka mwanamume aliyevalia kimasai.



"Nikusaidie nnini!" aliulizia. Lafudhi yake ikiswadiki mavazi aliyokuwa amevaa. Ni Mmasai.



"Tafadhali. Namuulizia Zainab, Zainab Said," Abuu aliongea, huku akionesha unyenyekivu uliojaa taadhima.



Mlinzi yule alimuangalia vizuri, juu mpaka chini, akamuuliza,"Wewe ni nani yako huyo, Sainabu?"



"Zainab, Namuulizia Zainab..."

Abuu alimuweka sawa.



"Ndiyo, kwani nimekujatia nani... Si Sain-nabu unamtaka," Masai aling'ang'ana.



Abuu hapa akaelewa, kuwa ni makosa ya kimatamshi. Aliamua kuitikia yaishe tu, "Ndiyo, ndiyo m'heshimiwa."



"Basi subiri..."

Masai akafunga geti na kuingia ndani.



"Ameenda kumuita au nini?" Abuu alijiuliza. "Ila kasema nisubiri, acha nisubiri."

Alitii.

Huku kichwani akiweka sawa mitambo.

Alipanga anaanzia wapi 'kumseti' mwanamama huyo, mwenye asili ya wavuka bahari, Unguja.



Ghafla, geti lilianza kunguliwa. Akatoka msichana mweusi kwa mbali, mfupi kidogo, mwenye macho ya mviringo...maridadi wa maungo.

Huyo ndiye Zainab. Zainab bint Said



"Abuuuu!" Aliita kwa mshangao.

Hakuamini. Leo Abuu yuko mbele yake?

Alimrukia, akamkumbatia kwa nguvu. Kisha busu zito lilipigwa. Achana na 'mwaah!' Lilikuwa lile la kweli. Eeenh, hilohilo!



Abuu alikaribishwa ndani. Ndani ya nyumba yenye kila kitu. Moja kwa moja, aliingia bafuni kwanza, akaoga, akapewa nguo akavaa.

Naam, Zee la nywila karejea sasa!



Zainab alikuwa ni mwanamke mwenye kujiweza kiuchumi. Tena si kidogo.

Maduka kadhaa ya simu anayomiliki mitaa ya kariakoo, ndiyo yanayompa jeuri ya kusema NITAISHI BILA KUOLEWA.

Wanaume si ndiyo kama hawa. Anawapata tu! Atake nini tena?



Baada ya kujitwaharisha, Abuu alikaa mezani. Maongezi ya hapa na pale yakafuatia.

Abuu hakumficha kitu, alimueleza yaliyomkuta. Ila sababu ya kumtuka hayo, aliibakiza siri moyo mwake.



Ilivyotimu saa mbili usiku, Zainabu aliingia jikoni, akaanda chakula kizuri sana kwa ajili ya Abuu. Bibiye aliandaa wali na rosti la samaki, bila kusahau, bilauri yenye sharubati ya matunda.



Baada ya chakula kuliwa. Wawili hawa walikuwa na njaa bado. Wakakumbatiana, Kikaanza kuliwa chakula kingine.

Nazungumzia chakula hichohicho!



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



MCHEZO uliisha wote wamejilaza kitandani, mashuka pia yaliona aibu yakawakimbia-yako chini.

Walifikajefikaje hapo kitandani?

Hakuna kati yao aliyekumbuka. Kwanza hawakuangaika kukumbuka. Inasaidia nini?

Waliinuka wakaelekea kuoga pamoja.



Hakuna kitu chenye nguvu kama penzi. Ubishe ukatae!

Ila!, Penzi huwa si kitu, jinsi mbili tofauti zikiwa tupu zinatazamana. Vipi jinsi hizo zikiwa tupu zinatazamana na penzi lipo baina yao?

Huko bafuni walishindwa kuvumiliana. Wakasogeleana... Amri ya sita ikavunjwa tena!



Mpaka yatimu saa sita usiku. Zainab tayari alishapitiwa na usingizi.

Ugonjwa wake leo ulipata daktari bingwa. Acha ubingwa tu, mzoefu!

Alilala usingizi mtamu, fofofo!



Tofauti na Abuu. Yeye alijilaza chali, anatafakari mengine kabisa. Atawapataje maadui zake?

Usingizi uligoma kumtembelea. Labda ulimtembelea, akagoma mlango kuufungulia.

Atafanya nini? Alifikiria sana.

Hatimaye, alipata mwangaza.



Usingizi na mafanikio ni maadui walioweka nadhiri kukomoana. Wote wanampa binadamu raha, ila hakuna kati yao anayekurusu ukiwa naye, uwe na mwingine.

Chagua mmoja tu!

Usiku huu, Abuu aliusaliti usingizi kwanza.



Ndani ya chumba cha Zainab, kumepambwa na vitu vingi vya kike. Rangi ya pinki ilichukua nafasi ukutani, kabati la nguo na vipodozi likiwa limesheni urembo wa kila aina.

Lakini vyote hivi, havikuzuia kuwepo na meza ndogo yenye kompyuta pamoja na vitabu vingi vya kibiashara vikiwa pembeni. Mbele ya meza ile kulikuwepo na kiti kizuri kilichonakh'shiwa kwa rangi ya dhahabu.



Achana na hayo mapambo, hayamsaidii kitu mwanaume rijali kama Abuu.

Hivyo vitabu ndiyo hata! Hana mpango navyo kabisaa.

Kilichomuinua kutoka kitandani mpaka akaketi juu ya kiti na kuegemeza mikono yake mezani, ni ile kompyuta.



Haraka aliiwasha. Hakuwa na wasiwasi wa kukutwa na Zainab.

Alishatambua udhaifu wa msichana huyu-anampenda.



Shida ya Abuu hapa haikuwa kubwa, aliingia mtandaoni, akaingiza 'code' anazozifahamu, baada ya muda, kompyuta ile ilimletea nambari za simu, alivuta karatasi iliyopo palepale juu ya meza, akazinakili namba zile.

Kisha akazima kompyuta. Hapo usingizi ulikuja sasa. Alilala!



***

ASUBUHI ilifika. Mboni za Abuu zilikwaana na chai iliyosindikizwa na vitafunwa vilivyokaangwa vikakubali. Pembeni, kulikuwa na supu nzito ya pweza...na glasi ya maziwa ya mtindi.



Abuu alishailewa maana ya chai hii.

Alimtazama Zainab, akatabasamu.

Dooh! Aliharibu. Bora hata asingefanya vile. Tabasamu la ZEE LA NYWILA ni sumaku...mtoto alitamani hata chai isingekuwepo pale kitandani, ili sokomoko liendelee.



Siku hii kuna kitu Abuu alipanga kukifanya. Hakuhitaji kuipoteza kwa mambo mengineyo. Lakini, aliona hatoweza kuyatenda hayo bila msaada kutoka kwa Zainab.

Afanyaje sasa? Amridhishe ipasavyo.

Hivyo tu?

Basi ni kazi rahisi sana hiyo kwa Abuu.



Aliinywa chai na akamnywa mwenye chai. Usiniulize kivipi!



"Zainab, naomba unisaidie simu yako!"

Baada ya kumalizana. Huu ndio muda sahihi Abuu aliona ataweza kumpukusua msichana huyu.



"Huna simu?!" Zainabu aliuliza kwa mshtuko.



"Sina," Abuu alijibu.



"Mmnh, sikujua hilo," alizungumza Zainab kwa kuonesha kuguswa, akaendelea," usijali baby, vaa tutoke sasa hivi. I will register a sim-card for you..."

Kabla hajamaliza kuongea simu yake iliita.



"Haloo..!" Aliipokea na kuongea,"Ndiyo ni mimi...ndiyo...ndiyo...sawa!...Sasa hivi?...Basi sawa nakuja."

Akaikata.



Abuu anaijua saikolojia ya wanawake. Labda Zainab hakulijuwa hilo. Ndiyo maana akazungumza na simu ile mbele yake.

Kitendo kichomfanya Abuu kumsoma vitu vingi.



Kitu cha kwanza, Zainab aliipokea simu ile kwa sikio la upande alioketi Abuu. Baada ya kusikia sauti ya mzungumzaji, alimtazama Abuu usoni, kisha akahamishia sikio jingine.

Kwanini kafanya hivi?

Abuu alishajenga swali kichwani.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Kingine, Yale maongezi ya mwisho, yalikuwa zuga tu. Simu ilikata mapema tu... Baada ya ile 'ndiyo' ya pili. Kwasababu simu ikikatwa, hutoa mwanga...hata ikiwa sikioni. Na ikiwa sikioni huku unazungumza na mtu, mwanga huzima.

Zainab anataka kufanya nini?

Bado Abuu alizidi kujiuliza.



"Ulikuwa unahitaji simu?"

Zainab alimuuliza, kashasahau kuwa alikuwa anazungumzia masuala ya laini. Hapo Abuu alipatwa na walakini mwingine.



Kumuonesha kuwa hajang'amua kitu, Abuu aliipokea simu ile, akatoa kile kikaratasi na kunakili namba. Namba alizochukua usiku uliopita kompyutani.



Cha ajabu, kabla hajamaliza kuzinakili, jina lilitokea kwa chini. Na ndiye mtu ambaye Abuu alihitaji kuwasiliana nae.

Alikuwa ni G.C.I kama Abuu alivyowahi kumsevu, ndivyo alihifadhiwa pia katika simu ya msichana huyu, Zainab.



Zainab amefahamiana vipi na mtu nyeti kiasi hiki, hadi akamsevu kwa cheo chake? Kuna nini kinaendelea hapa?

Au, ndiyo hii ya mbuzi kufia kwa muuza supu?

Abuu hakuna alilolielewa!





KUMPENDA mwanamke ni jambo la kawaida , ila kumuamini ni hatua nyingine kabisa. Hatua inayoweza ikaamua hatma ya maisha yako. Ufanikiwe au Uangamie!



Kama Delila aliweza kumghilibu Samson akaitoa siri. Hawa pia akamfanya Adam aonje lile tunda... Unahisi Abuu ni nani auepuke mtego wa Zainab?

Sidhani!



Baada ya kuliona jina lile linatokea, Abuu aliona atumie mbinu mbadala...

"Aakh! Au basi," alighairi na kumrejeshea Zainab simu.

"Kwanini?" Zainab hakuwa anafahamu kuwa Abuu kuna kitu kashtukia, akajitia kumuuliza, " Au unataka ya kwako baby?"

Alitoa sauti ya kike, sauti chombezaji.



Abuu hakujibu kitu, alitabasamu kisha akataka aivushe mada ile, kuepuka Zainab kung'amua kwamba amejua kitu katika simu yake.



"Ah, ngoja nikaoge, si tunatoka muda huu?" aliongea Abuu huku anainuka kutoka kitandani.

"Mmnh...tukaoge 'ote buanaaaaa..." aliongea Zainab kwa kudeka.

"Hahaha, nisubiri dear!"

Abuu alikataa, haijulikani ni hofu iliyojijenga tayari kuhusu Zainab, au hakutaka 'mdumange' ukatokee tena.



Abuu aliingia bafuni, akachejua taulo, mwili wake mtupu akauacha uloweshwe na maji, maji yalitoka katika bomba lililo juu yake, mithili ya mvua.



Kila tone moja lilipopiga utosini mwake, lilishtua neva moja ya kumbukumbu, aliwaza sana kuhusu Zainab,

Amemfahamu vipi mtu hatari vile?



....



SIKU ILE wakati Abuu anasafirishwa kwenda Ufilipino. Ndipo mkasa kati yake na G.C.I ulipoanzia.



Ilikuwa ni ndani ya ndege, siti ya ubavuni mwa ile aliyokuwa Abuu, alikaa mwanamume mmoja aliyekuwa 'serious' sana. Muda wote huo, tangu safari imeanza, uso wake uliinamia katika kitabu alichokuwa anasoma. Naye, Abuu hakumshughulikia.



Baada ya nusu saa, ndege ikiwa angani, ndiyo mwanaume yule alianzisha mazungumzo kwa namna ya kipekee..

"Mr. Abuu, habari yako?" Yule mwanaume alisalimu huku anazifunga kurasa za kitabu kilicho mikononi mwake.

"Sa-laa-maa..." Abuu aliitikia kwa wasiwasi. " Umenifahamu vipi?" kisha akamuuliza.

Yule mwanaume alitikisha kichwa kwa kusikitika, kicheko kidogo kikafuatia."Serikali inawafahamu raia wake wote kijana," alijibu kisha akaendelea,"Unaenda kujifunza haramu au sio?"



Moyo wa Abuu ulilipuka kwa woga! Moja ya makubaliano yaliyowekwa katika safari ile, ni kubaki siri ya watu watatu tu, yeye, Patrick na Harrison. Iweje huyu wa nne amuulize swali chachu kiasi kile?

Hakuwa na la kujibu Abuu, alibaki kimya anashangaa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



"Usijali dogo..." aliongea mwanaume yule,"Nenda tu kajifunze." alipomaliza akafungua kitabu na kuendelea zake kukisoma.



Kimuhemuhe kilimshika Abuu, siti ilikuwa imegeuka ya moto.



"Wewe ni nani kwani?" Abuu alijakaza na kuuliza. Amani ilimtoka kabisa.



"Kukwambia kuwa hapo ulipo upo chini ya ulinzi, kunaweza kukutosha kunitambua?" Yule mwanaume akajibu kwa swali, macho yake hayakubanduka kitabuni.



Tumbo la kuhara lilimshika Abuu. Alishatambua aliye pembeni yake ni mtu wa aina gani.

Picha ya kuwepo kwake nyuma ya nondo ngumu, huku kavalia nguo zenye rangi ya machungwa, ilimjia tafakurini.

Kuna anayependa jela?

Hakuna!



Wakati abiria wote katika ndege ile wakionekana na furaha ya safari nyusoni mwao, kuna siti ilikuwa imekozwa makaa kwa chini, aliyekaa mahali pale alitamani ainuke na kukimbia. Ila hakuweza!

Abuu mwili mzima uliganda, kama alipigwa 'nusu-kaputi' vile.



Zilipita dakika kadhaa bila ya watu hawa kuzungumzishana, Abuu na yule mwanaume.



"Mimi ni General Commissioner in Investigation... Wengi huniita G.C.I," yule jamaa aliongea huku bado kainamia kitabu. " Hapo ulipo tayari ni mtuhumiwa, hivi unalifahamu hilo?"



"Kwanini?" Abuu aliuliza.



"Hiyo si kazi yangu," yule mwanaume alijibu. Bado wajihi wake hakutaka kuubandua kitabuni. "Nipo hapa kukutoa hatiani, ila ni lazima utufanyie kazi na sisi..."



Ghafla, mawazo ya Abuu yalikatwa na mlango wa bafu kufunguliwa. Alikuwa ni Zainab aliyefanya hivyo.



"Love! Utanikuta nje hapo...am waiting you, Mwaah!" alitoa taarifa kwa Abuu, akamalizia na busu la hewa, Ak'enda zake.



"Nashindwa kumuelewa huyu mwanamke, kuna nini hapa kati!" Abuu aliwaza bila kupata jibu.



Nguo za kiume mule ndani kwa Zainab zilikuwepo, ila si nyingi. Zainab ni mwanamke makini sana. Alizinunua kama akiba tu.

Kama akiba?

Au alizihifadhi kusudi kwa kujua ipo siku Abuu atakuja tu?

Hatufahamu hilo!



Safari ilianza. Walitoka na gari ya Zainab. Huku Abuu akiachiwa aendeshe yeye.

Waliikamata barabara kuu ya Morogoro, moja kwa moja hadi Jangwani, walivyofika mbele kidogo, mitaa ya Fire, ambapo ndipo Zainab hupaki maeneo yale, walisimama. Wakaigesha gari. Kisha 'amzakanuni' ilianza.



Kabla hawajafika mbali...



"Ooh, nimekumbuka. Naomba unisubiri my ... Kuna mtu naingia kuonana naye, juu hapo,"Zainab aliomba akionesha ghorofa lililo pembeni mwao.



"Sawa," Abuu hakufanya hiyana. Alimruhusu.



Zainab alimbusu shavuni, kisha akafanya kama anachangamsha mwendo kuwahi anapoelekea.



" Huyu nitamganda mpaka nifahamu wapi alipo G.C.I, na nikishampata tu G.C.I basi nitafahamu wapi alipo mama yangu..." alijisemea Abuu baada ya kuachwa kwa muda na Zainab.



Mara, alimuona mtu mwenye mfanano na Patrick, m'baya wake wa kutupa.

Haraka Abuu alitafuta chocho kidogo na kujificha.



Akamtazama kwa makini, ndiye, ni yeye. Ni Patrick kabisa. Anaenda wapi? Aliendelea kumfuatilia.

Khee! Alikuwa anasogea upande huuhuu aliokuwepo Abuu.



Patrick alikuja, mpaka nje ya jengo lile ambalo Zainab aliingia mwanzoni. Naye alizama ndani!



"Mmnh, niingie au nisiingie?" Nafsi ya Abuu iliwaza yote hayo. Akachagua asiingie. Alitaka asome mwisho wa Patrick ni upi eneo lile.



Dakika mbili, Patrick alitoka. Huyo, akavuka tena barabara na kurudi kule alikotokea mara ya kwanza.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



"Nimfuate, nisimfuate?" Abuu aliwaza tena bila ya kufanya maamuzi. "Agh! Nitampata G.C.I kupitia huyuhuyu Zainab," alijipa matumaini. Hakumshughulikia tena Patrick. Akamwacha aende.



Dakika zikapita, zikasogea mbele na kutokomea kabisa, Zainab hakurudi. Hapo ndipo Abuu nae aliamua kumfuata ndani. Uvumilivu ulimfika kooni.



Kabla hajapiga hatua nyingi. "Abuu..!" aliitwa kwa sauti ya kiume kwa nyuma. Sauti hii alishawahi kuisikia. Si ngeni masikioni mwake!





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog