Search This Blog

Tuesday, 1 November 2022

MKE WANGU JULIANA - 1

 






IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI



*********************************************************************************



Simulizi : Mke Wangu Juliana

Sehemu Ya Kwanza (1)



Treni ilisimama mwisho wa reli, mkoani Kigoma ambayo ilianza safari yake ya kuelekea huko siku mbili zilizopita kutoka jijini Dar es Salaam.



Wenyeji waliofika mahali hapo kwa lengo la kuwapokea wageni wao, wakaanza kusogea sehemu husika huku wakiangalia kwa makini abiria waliokuwa ndani ya treni hiyo ambapo wengine walikuwa wakichungulia dirishani.



Baada ya sekunde chache, treni ikasimama na haraka sana abiria kuanza kushusha mizigo yao huku wenyeji waliofika mahali hapo kwa lengo la kuwapokea wakianza kusaidiana nao, wafanye haraka na kuondoka stesheni.



Kila mmoja alionekana kuwa na haraka, wengine walipiga simu kwa ndugu zao waliokuwa nje ya jengo la stesheni na kuwaambia waweke magari tayari kwani wageni waliokuwa wamewafuata mahali hapo tayari waliwapata.



Vijana waliokuwa wakijihusisha na kubeba mizigo nao hawakuwa mbali, walikuwa na vitoroli vyao, walisogea karibu kabisa huku wakiwauliza wageni kama walikuwa tayari kusaidia kupeleka mizigo yao nje ya jengo la stesheni na kulipwa kidogo ama la.



“Mama nikusaidie? Utanipoza kidogo tu, hata hela ya maji mama naomba nikusaidie,” alisema kijana mmoja huku akiwa na kitoroli chake kidogo, na tayari alifika mahali hapo huku wenzake wakiwafuata wageni wengine.



Kipindi hicho hali ya hewa ilikuwa ni ya utulivu kabisa, hapakuwa na joto wala baridi, kwa kifupi ilitulia sana hasa mahali hapo ambapo kwa pembeni, kama hatua ishirini za miguu ya binadamu kulikuwa na Ziwa Tanganyika.



Watu wote walivalia nguo zao laini lakini kwa abiria wachache waliokuwa wameingia siku hiyo walikuwa na makoti makubwa, wengine masweta kutokana na hali ya baridi waliyokuwa wamekutana nayo huko njiani.



Wakati abiria wengine wakiendelea kutoka ndani ya eneo hilo, kijana mmoja ambaye kwa kumwangalia tu alionekana kuwa na miaka isiyozidi ishirini na tano akainuka kutoka katika kiti kimoja ndani ya behewa la treni lililotoka jijini Dar es Salaam na kwenda dirishani na kuanza kuchungulia.



Uso wake ulichafuka kutokana na vumbi jingi lililokuwa likipenya mpaka ndani ya treni hiyo kipindi ilipokuwa njiani. Aliwaangalia watu waliokuwa mahali hapo, hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kufika mkoani Kigoma, hakupajua palifafanaje ila kitu alichoambiwa na wazazi wake ni kwamba walitoka mkoani humo.



Aliporidhika na kila alichokuwa akikiangalia, akaanza kutoka ndani ya behewa hilo na kuelekea nje, akashusha ngazi fupi na kukanyaga chini.



Alikuwa abiria lakini hapakuwa na mtu yeyote aliyeshughulika naye, hakuwa na mizigo mingi, alikuwa na mfuko wa Rambo mkononi ambao ndani yake kulikuwa na nguo chache, ukiachana na hayo, muonekano wake ulikuwa kama wabeba mizigo wa maeneo hayo.



“Samahani kaka!” alijikuta akimuita mwanaume mmoja aliyekuwa akipita mbele yake, mtu huyo akamsogelea na kuanza kumsikiliza.



“Nataka kutoka!”

“Unamaanisha nini?”

“Niende nje ya hapa, napita wapi?” aliuliza kijana huyo.



Alionekana kuwa mgeni, mahali hapo kulichanganya kwani japokuwa kulikuwa na jengo kubwa la stesheni lakini pia kulikuwa na njia iliyokuwa ikielekea Kibirizi, yaani kurudi nyuma ambapo treni ilipotoka, na watu wengine walikuwa wakielekea huko.

“Wewe unataka kwenda wapi?” aliuliza mwanaume huyo huku akimwangalia kwa makini.



“Nje ya eneo hili?”

“Kibirizi ama Mwanga?” aliuliza.

“Mh! Nadhani Mwanga!”

“Unadhani! Huna uhakika?”

“Nadhani Mwanga ni pazuri zaidi!” alijibu huku akijitahidi kutoa tabasamu.



Mwanaume huyo alichomwambia ni kwamba alitakiwa kupanda ngazi za jengo la stesheni na kutoka ambapo huko angekutana na barabara ya lami, na kwa mbele kulikuwa na round about, njia ya kulia ilikuwa ikielekea Bangwe, na barabara ya mbele ilikuwa ikielekea mjini, achana na ya hapo karibu na jengo, upande wa kushoto ambayo ilikuwa ikielekea kulipokuwa na jengo la Kampuni ya simu ya TTCL na Shule ya Msingi ya Kiezya.





Jamaa huyo akatoka, akapandisha ngazi na kuelekea nje. Alisimama kwa dakika kadhaa, alikuwa akiangalia huku na kule, hakujua ni njia gani alitakiwa kwenda, kulikuwa na njia nyingi ambazo kulikuwa na moja aliyotakiwa kupita.



Hakutaka kuwa na presha, alitulia, alikuwa kama kocha aliyeanza kuusoma mchezo fulani. Mbali na eneo hilo, hakupajua sehemu nyingine yoyote ile ila kitu alichohitaji ni kufika katika mtaa mmoja wa uswahilini, huko angejua ni kwa namna gani angeweza kuishi.

“Nitafute sehemu kama Tandale, nikajichanganye!” alijisemea.



Hakutaka kupoteza muda, alichokifanya ni kuangalia huku na kule, macho yake yalipotua kwa mwanamke mmoja aliyekuwa akiuza ndizi, akamuita, akanunua ndizi na kumuuliza kuhusu sehemu ya uswahili.



“Kigoma sehemu kubwa ni uswahilini!” alisema mwanamke huyo.

“Ila si kuna uswahili ambayo nyie wote mnajua ni uswahilini?” aliuliza.



“Ndiyo! Kuna Mwanga, Ujiji, Mwandiga....”

“Nataka kufika hapo Mwanga, ni mbali kutoka hapa?” aliuliza huku akimwangalia usoni mwanamke huyo.



“Si mbali sana! Ila chukua daladala!”

“Halafu?”

“Utamwambia akushushe Mwanga Mzalendo!”

“Sawa! Nashukuru mama!”



Mwanamke huyo akaondoka. Hakutaka kuchelewa, ilikuwa ni lazima aondoke mahali hapo, akapiga hatua na kuelekea mbele.

Kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, hakujua ni wapi alitakiwa kuanzia. Alikwenda mkoani Kigoma kwa ajili ya kitu kimoja tu, kutafuta maisha na kurudi zake Dar es Salaam.



Aliishi Dar kwa miaka mingi, alipigwa na maisha, hakuona nafuu hata kidogo. Hakuwa na elimu, hakuwa na pesa, aliishi huko kama mkimbizi, aliteseka na mwisho wa siku kabisa akaamua kwenda huko Kigoma kwa lengo la kujaribu bahati yake kwani wakati mwingine funguo za bahati huwa mikoani na si Dar tu.



Mfukoni mwake alikuwa na kiasi cha shilingi laki tatu tu, alizipata pesa hizo jijini Dar es Salaam na alipanga ndicho kiwe kiasi cha pesa ambacho angeanzia nacho maisha mkoani humo.



Alitembea mpaka alipofika sehemu kulikuwa na daladala ndogo (hiace) ambapo akamsikiliza utingo akiita abiria waliokuwa wakielekea sehemu iliyoitwa Ujiji, akamsogelea.



“Bro! Hii inapitia Mwanga?” aliuliza huku akimwangalia.

“Ndiyo! Ingia! Mwanga mia tatu!” alisema utingo, haraka sana akaingia.



Ndani kulikuwa na abiria wachache, aliwaangalia, alitamani kuuliza zaidi kuhusu hiyo Kigoma, hasa huko Mwanga alipokuwa akienda lakini hapakuwa na mtu aliyeonekana kuwa na utayari wa kuulizwa swali lolote lile na mwanaume huyo, hivyo naye akanyamaza,

Baada ya dakika chache, abiria wakajaa na gari kuondoka mahali hapo.



Alitulia ndani kimya kabisa, kichwa chake kilikuwa kikifikiria maisha yake ya baadaye, hakujua ni kwa namna gani angeweza kufanikiwa na kuwa na pesa kama walivyokuwa watu wengine.



Gari lilitumia dakika kama ishirini akamsikia utingo akisema Mwanga Mzalendo, hakutaka kuchelewa, haraka sana akateremka, akalipa nauli na kusimama barabarani.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Sasa niende wapi hapa?” aliuliza huku akiangalia huku na kule.

Alikuwa mgeni, mahali alipokuwa kulikuwa na idadi kubwa ya watu, hakujua kama alitakiwa kwenda kulia ama kushoto.



Kulia mwa barabara kulikuwa na njia iliyokuwa ikielekea Mtaa wa Kilimahewa, karibu na shule ya Msingi ya Muungano lakini kushoto kwake kulikuwa na njia iliyokuwa ikielekea Mwanga Msufini ambapo kama angeendelea mbele, angefika mpaka Mwandiga ama kushoto ambapo angepanda mlima na kuelekea Mlole, ila kote huko hakuwa akipafahamu.



“Kaka samahani!” alimuita mwanaume mmoja, kwa jinsi alivyomsikia tu, aligundua alitoka jijini Dar es Salaam.



“Mtoto wa mjini!” alisema jamaa huyo.

“Ndiyo nimeingia asubuhi hii! Ninahitaji nionane na dalali, kuna dalali yeyote unamjua?” aliuliza huku akiangalia huku na kule.

“Yeah! Wapo wengi! Unataka chumba ama kiwanja?” aliulia.



“Chumba!”

“Tena una bahati sana!”

“Kwa sababu gani?”

“Mimi mwenyewe nadili sana na ishu za vyumba!”



“Ni dalali?”

“Hapana! Mtoto wa mjini tu! Nifuate!” alisema jamaa huyo huku akiachia tabasamu.





Hakumwamini lakini akafanya kama alivyoambiwa, akaanza kumfuata ambapo wakapita kwenye njia ndogo iliyokwenda kuungana na njia kubwa iliyokuwa ikielekea Mji Mwema na kuanza kuifuata, wakawa wanaelekea Mwanga Makaburini.



Macho yake hayakuacha kuangalia huku na kule, alikuwa akiyasoma mazingira, alihitaji kuyazoea kwa haraka sana kwani aliamini huko ndipo ambapo angepata chumba na kuanza maisha ya kutafuta riziki kama ilivyokuwa jijini Dar es Salaam.



Njiani walikuwa wakipishana na watu mbalimbali, wanawake waliokuwa wakichota maji, watoto waliokuwa wakicheza mpira na hata wanaume waliokuwa wamekaa wakipiga stori.



Walikwenda mpaka Mwanga Makaburini kulipopakana na Gemu ambapo kulikuwa na nyumba zaidi ya kumi na tano zilizojengwa kiswahili ambazo zilikuwa karibu na uwanja wa mpira wa miguu. “Unaitwa nani?” aliuliza jamaa aliyejifanya dalali.



“John!”

“Umetokea Dar?”

“Ndiyo!”

“Umekuja kufanya nini?” aliuliza huku wakiifuata nyumba moja.

“Kutafuta maisha!” alijibu. Jamaa ikambidi asimame na kuanza kumwangalia.

Hakuamini alichoambiwa, yaani mtu atoke jijini Dar es Salaam na kuelekea mkoani Kigoma kwa ajili ya kutafuta maisha tu.



Kwake kilikuwa kitu kisichowezekana hata kidogo kwani watu wote waliamini Dar es Salaam ndipo kulipokuwa na maisha mazuri, sasa iweje mtu aende Kigoma kutafuta maisha hayo.



“Braza unanitania! Umekuja Kigoma kutafuta maisha?” aliuliza jamaa huyo.

“Ndiyo! Nimesikia kuna mashirika ya wakimbizi huku!” alijibu John.



“Ndiyo yapo! Ila umesoma?”

“Nimeishia darasa la saba!”

“Daah! Mshikaji sijui nikwambieje! Ila poa! Una hela ya kupanga kabisa hapo?”

“Hela ipo!”



Wakaingia ndani ya nyumba moja ambapo wakaonana na mwenye nyumba na kumwambia kuhusu John kwamba alihitaji kupanga ndani ya nyumba hiyo.



Hilo halikuwa tatizo, mwenye nyumba akakubali na hivyo kutakiwa kulipa shilingi elfu ishirini ya chumba kimoja alichotakiwa kukaa.



“Naweza kukiona chumba chenyewe?” aliuliza.

“Hakuna shida! Ingieni!” alisema mzee huyo.



Akawachukua wote wawili na kuelekea ndani mpaka kwenye chumba hicho na kumuonyesha. Hakikuwa chumba kikubwa, kilikuwa kidogo, nyavu za kuchanika, ukuta haukupigwa hata plasta, yaani hapo ndipo ambapo alitakiwa kuishi.



Akatoa tabasamu, aliridhika na chumba hicho na hivyo kulipia kodi ya miezi sita na kuandikishiana mkataba na kumlipa jamaa yule pesa ya udalali na kuondoka mahali hapo.

“Huu ndiyo ufunguo wako! Cha msingi kalete vyombo vyako uanze kukaa hata leo!” alisema mzee huyo.



“Nilete vyombo? Hapa ndiyo nina kila kitu!” alisema John.

“Kila kitu kivipi?”

“Sina chochote zaidi ya hizi nguo!” alisema John, hapohapo akauweka mfuko wa nguo zake chini.



“Na umetoka Dar?”

“Umejuaje?”

“Unavyoongea, unachonga sana!”

“Kuchonga ndiyo nini?”

“Aina ya matamshi yenu! Kwa hiyo umekuja Kigoma kufanya nini?” aliuliza mzee huyo.

“Kutafuta maisha!”

“Kutafuta nini?” aliuliza mzee kwa mshtuko.

“Maisha!”



“Oopss!” akashusha pumzi ndefu.

Yeye mwenye hakuwa akiamini kama ilivyokuwa kwa yule dalali, alimwangalia John mara mbilimbili lakini ikabidi akubaliane naye kwamba ni kweli alifika mkoani Kigoma kwa lengo la kutafuta maisha.



Hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kwanza ndani ya mkoa wa Kigoma, ilionekana kuwa sehemu sahihi ya yeye kuishi humo, hakuwa na kimbilio jingine, aliondoka Dar es Salaam baada ya kuona maisha ya huko ni magumu kupita kawaida.



Aliamini kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakifanikiwa mikoani na kule Dar es Salaam walipokuwa wakienda walikwenda kwa lengo la kutumia na kurudi tena mikoani.



Kwa sababu Kigoma ilikuwa Magharibi mwa Tanzania, karibu na mipaka ya kuingia Kongo, Rwanda, Burundi, kulikuwa na idadi kubwa ya wakimbizi na aliamini kama kweli alihitaji kufanya kazi huko ilikuwa ni lazima atafute mashirika ya wakimbizi na kuomba kazi na kama ingeshindikana kabisa basi angekwenda hata bandarini ama kuuza vyombo mitaani, ila mwisho wa siku ilikuwa ni lazima afanikiwe.



Kwa pesa zilizobaki, akanunua jiko la gesi, mchele na unga kwani katika maisha yake alijifunza sana kuwa na chakula ndani, yaani hata kama ingetokea siku moja hakuwa na pesa, asingeweza kushinda njaa kwa kuwa alikuwa na chakula ndani.



“Nitaanza maisha hapa! Nikikosa kazi kwenye mashirika ya wakimbizi, nitaanza hata kuuza vyombo mitaani, ikishindikana kabisa, basi hata kuuza samaki, yaani mwisho wa siku nifanikiwe tu,” alijisemea usiku alipotaka kulala juu ya mkeka aliokuwa ameununua, alichomshukuru Mungu ni kwamba kwa usiku kulikuwa na baridi hivyo hata mbu hawakuwepo kabisa.



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

John akaanza maisha mapya mkoani Kigoma, alipotoka jijini Dar es Salaam alijiapiza ni lazima siku ambayo angerudi tena huko basi angekuwa amefanikiwa na kuwa na pesa nyingi.



Mbele yake aliona giza nene, hakujua ni wapi alitakiwa kuanzia. Siku hiyo hakutaka kubaki ndani, ilikuwa ni lazima kuzoea mazingira ya Mtaa wa Mwanga hivyo akatoka na kuanza kuzunguka huku na kule.



Alipapenda Kigoma, kwa jinsi kulivyokuwa kulimvutia. Hapakuwa na watu wengi kama ilivyokuwa jijini Dar es Salaam, watu walionekana kuwa na utulivu na hapakuwa na rapsha nyingi za huku na kule.



Alitembea kwa miguu mpaka katika uwanja wa mpira wa miguu wa Centre na kuanza kuangalia mechi iliyokuwa ikiendelea mahali hapo.



Alitulia uwanja huo ulikuwa karibu na sehemu iliyoitwa Mwanga Msufini, alitulia kwa dakika kadhaa, baadaye akaamua kuondoka na kuelekea mbele zaidi.



Akafika sehemu iliyokuwa na msufi mkubwa, akaangalia mbele yake, macho yakatua katika kanisa kubwa ambalo kwa mbele liliandikwa T.A.G yaani Tanzania Assemblies of God.



Uso wake ukawa na tabasamu pana, akaanza kupiga hatua kulifuata kanisa hilo. Alipolifikia, kulikuwa na ukimya mkubwa, hapakuwa na mtu yeyote yule, alisimama kwa nje na kuanza kuangalia kwa ndani kupitia dirishani.



Moyo wake ulijisikia huru, amani na wakati mwingine alihisi kabisa alitakiwa kumtumikia Mungu, inawezekana kabisa hakuwa amefanikiwa kwa kuwa alijiweka mbali na Mungu. Akatoka pale na kwenda pembeni kidogo mbali na dirisha lile la kanisa.



“Labda kwa sababu huwa siendi kanisani ndiyo maana Mungu ananisahau sana,” alijisemea huku akiwa amesimama nje ya kanisa hilo.



Wakati akiwa hapo, mara akawaona wanawake wanne walioshika Biblia wakija kule alipokuwa. Aliwaangalia wanawake hao, kwa jinsi walivyovaa, alikiri kwamba walikuwa ni watumishi wa Mungu.



Walivalia magauni marefu, viatu vya saizi na vichwani mwao walikuwa na vilemba. Hawakuonekana kuwa na uwezo mkubwa kipesa lakini walikuwa na furaha kubwa mioyoni mwao, walikuwa wakiongea huku wakitabasamu muda wote.

Wanawake hao wakapita mbele yake, aliyasikia mazungumzo yao, walizungumza kuhusu uwepo wa Mungu, jinsi watu walivyoendelea kutendewa miujiza katika maisha yao, akavutiwa kuendelea kuwasikiliza.



Wanawake wale wakaenda mpaka katika mlango wa kanisa na mmojawapo kufungua mlango na kuingia ndani. Akajikuta akivutiwa na yeye kuelekea humo.



Viti vilipangwa vizuri, aliangalia kwa jinsi kanisa lilivyopangwa humo, alivutiwa nalo na kwa mbele kulikuwa na madhabahu ambayo iliufanya moyo wake kurukaruka kwa furaha.

Kwa mara ya kwanza akahisi moyo wake ukiwa na hali ambayo hakuwanayo hapo kabla, akaanza kupiga hatua kukifuata kiti kimoja na kukikalia.



Wanawake wale wakaanza kufanya usafi, walipomuona, hawakutaka kuwa na shida naye, kila mtu alitakiwa kuingia kanisani, ni kama ilivyokuwa msikitini.



Hapakuwa na mtu aliyekuwa akikatazwa kwani ilikuwa sehemu takatifu, mahali ambapo watu walitakiwa kukutana na kumsifu Mungu muumba mbingu na nchi.



Wakati akiwa hapo, mwanamke mmoja akamsogelea, uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana na alipomfikia tu, akamsalimia na kuhitaji kujua kuhusu yeye.



“Karibu sana kijana wangu!” alisema mwanamke huyo kwa sauti ya chini, iliyokuwa na upendo mkubwa, sauti iliyomfanya John kuhisi amani moyoni mwake.



“Nashukuru sana mama!”

“Bila shaka umekuja kuabudu nasi!” alisema mwanamke huyo.



“Ndiyo! Nimekuja kuabudu nanyi!”

“Ooh! Karibu sana ila leo si siku ya wanaume!” alisema.



“Unamaanisha nini mama?”

“Leo ni siku ya WWK,” alijibu.

“WWK ndiyo nini?”

“Wanawake Watumishi wa Kristo!”



“Bado sijakuelewa!”

“Ni siku ambayo wanawake tunakutana na kuwa na ibada yetu! Ila karibu sana kesho, tutakuwa na ibada mahali hapa!” alisema mwanamke huyo.



“Kwa hiyo niondoke?” aliuliza John, mwanamke huyo hakujibu, akaachia tabasamu pana.



John akasimama na kuanza kuelekea nje, siku hiyo alikuwa na hamu kubwa ya kuabudu kuliko siku yoyote ile.



Alihisi moyo wake ukiwa umebadilika kabisa, inawezekana kwa sababu alikuwa akipitia maisha ya shida hivyo alitaka kumuabudu Mungu ili afanikiwe.



Katika maisha ya vijana wengi makanisa yalikuwa na nguvu yake. Kulikuwa na mialiko kutoka sehemu mbalimbali duniani, mashirika mengi ya wakimbizi yalipeleka ajira kwanza huko na kisha sehemu nyingine.



Kulikuwa na vijana wengi kanisani walikuwa wakifanikiwa kirahisi kabisa. Wengi waliondoka Tanzania na kwenda kusoma Ulaya ama Marekani, makanisa mengi yalikuwa ni nafasi ya kumuondoa kijana mmoja na kwenda sehemu nyingine.



Kulikuwa na ajira nyingi, tena kutoka kwenye mashirika makubwa duniani na ndiyo maana vijana wengi walipenda kwenda kanisani, hasa katika mikoa ambayo ilikuwa karibu na mipaka ya nchi nyingine, waliamini kulikuwa na fursa nyingi, na ndivyo ilivyokuwa.

John akarudi nyumbani kwake, alipofika, akajifungia chumbani, muda huo ilikuwa ni saa kumi na moja jioni.



Hapo chumbani akaanza kuyafikiria maisha yake, alijiona jinsi alivyokuwa akiteseka siku zote katika maisha yake, aliumia mno, aliamini kuna siku angekuja kufanikiwa lakini hakujua ni siku gani.



Alimuomba sana Mungu, hakuwa amesoma hata kidogo ila kila alipoulizwa alisema aliishia darasa la saba kumbe haikuwa hivyo.

Hakuwahi kuingia darasani, kilichomsaidia ni kujifundisha kusoma na kuandika, kuhesabu pesa na mambo mengine madogo.



Hakujua kitu chochote kile kipindi hicho, alijiona boksi kichwani lakini hiyo haikuwa sababu ya kutokufanikiwa, kulikuwa na matajiri wengi ambao hawakusoma kabisa lakini mwisho wa siku walifanikiwa na hivyo kwenda darasani.



“Ila kwanza itanibidi nianze kufanya biashara!” alijisemea.

Akakaa na kuanza kujifikiria tena, kulikuwa na biashara mbili ambazo zilikuja kichwani mwake na ilikuwa ni lazima aifanye moja, hakujua ni biashara gani.



Biashara ya kwanza ilikuwa ni kuuza vyombo mitaani, yaani akanunue vyombo kwa bei ya jumla na kwenda kuuza rejareja mitaani.

Biashara ya pili iliyokuja kichwani mwake ilikuwa ni kuuza samaki, yaani akanunue samaki wa jumla na kuwatembeza mitaani, aliamini angeweza kufanikiwa.



“Ipi niifanye?” alijiuliza.

“Bora nifanye ya samaki! Biashara ya chakula huwa inalipa,” alijijibu.





“Sasa nitanunua wapi samaki? Sipajui wanapouza, nitafanyaje?” akajiuliza tena.

“Ngoja nimuulize baba mwenye nyumba!” akajijibu tena.



Hakutaka kusubiri, kukaa na pesa bila kufanyia biashara ilimaanisha zingetumika kwa matumizi ya hovyo kabisa hivyo ilikuwa ni lazima afanye kila liwezekanalo ziingie kwenye mzunguko.



Akatoka chumbani na kwenda kumgongea baba mwenye nyumba, mzee Alex na kuomba kuzungumza naye. Mzee huyo hakuwa na tatizo, akatoka na kwenda pembeni.

“Nina shida moja,” alisema John huku akimwangalia mzee huyo.



“Shida gani kijana wangu?” aliuliza.

“Ninahitaji nifanye biashara ya samaki!”

“Biashara ya samaki? Kutembeza ama kuuza jumla?” aliuliza.

“Kununua jumla na kuuza kwa rejareja!” alijibu.



“Ni biashara nzuri! Nikusaidie kwenye nini hapo?” aliuliza mzee huyo.

“Ninahitaji kujua mahali wanaponunua samaki!” alisema.

“Oh! Kumbe! Samaki wanapatikana sehemu moja inayoitwa Kibirizi!” alijibu mzee huyo.



“Ndiyo wapi huko?”

“Ni Kibirizi!”

“Ni mbali na hapa?”

“Kiasi! Utatakiwa kuchukua daladala kwenda huko. Ila hebu subiri! Kuna mtu anafanya kazi hiyo unayoitaka, ngoja nitakuunganisha naye,” alisema mzee huyo.



“Leo, si ndiyo?”

“Yeah! Subiri arudi! Nitamuita uongee naye!”

“Anaitwa nani?”

“Jumanne Muuza Samaki! Ila ukimuita Jumanne, inatosha,” alisema mzee huyo huku akitoa tabasamu.



“Sawa!”

Akarudi chumbani kwake na kutulia, alikuwa na presha ya kuonana na huyo Jumanne kwa lengo la kuzungumza naye. Alihitaji kupambana kwa sababu hapakuwa na njia nyingine ya kufanikiwa zaidi ya hivyo.



Alitamani kuwa na magari ya kifahari, nyumba nzuri, pesa nyingi benki, hivyo vyote visingekuja ghafla, ilikuwa ni lazima avipambanie mpaka kuhakikisha vinakuja kwenye maisha yake.



Wakati akimsubiri huyo Jumanne, kichwani mwake kukaanza kupita majina ya watu mbalimbali waliokuwa wamefanikiwa, maneno yao ya kutia moyo.



Watu wote hao walikuwa na neno moja ambalo lilitamkwa na kila mtu, nalo ni kufanya kazi kwa bidii. Hapakuwa na mtu aliyekuwa amefanikiwa katika dunia hii pasipo kufanya kazi kwa bidii.



http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Kulikuwa na matajiri wengi waliotisha kwa utajiri lakini waliposema siri za mafanikio yao ilikuwa ileile, kufanya kazi kwa bidii.



Matajiri wengi hawakulala vya kutosha, wengi walilala chini ya masaa sita, yaani hawakuwa wakilala sana kama masikini. Matajiri walijitoa, waliingiza pesa lakini walifanya kazi kama punda.



“Cha kwanza nitafanya kazi kwa bidii...” alijisemea huku akiwa amelala kwenye mkeka wake akiangalia juu.

“Cha pili nitatakiwa kuchelewa kulala na kuwahi kuamka....labda nitaweza kufanikiwa!” alijisemea.



Alikaa chumbani kwa saa kadhaa, ilipofika majira ya saa tatu usiku akasikia mlango wa chumba chake ukigongwa huku akiitwa jina lake.



Haraka sana akasimama na kwenda kuufungua, macho yake yakatua kwa mzee Alex aliyekuwa na kijana mmoja, hakutaka kujiuliza kama huyo alikuwa ndiye Jumanne ama la, harufu yake ya shombo tu ilimfanya kugundua alikuwa yeye.



“Njoo sasa tuzungumze!” alisema mzee huyo, akamchukua John na kwenda naye nje, wote watatu wakasimama kibarazani.

Mzee huyo akaanza kutambulisha, alipomaliza, akawaacha wazungumze wenyewe.



Walifahamiana na kitu pekee alichokisema John ni kwamba alitaka kuwa muuza samaki mitaani kama alivyokuwa huyo Jumanne.

“Hakuna shida! Nitakusaidia kwa kila kitu!” alisema Jumanne.



“Na changamoto zake?” aliuliza John.

“Zipo! Hasa kwa wewe mgeni kubwa ni kupotea! Huijui Kigoma, unaweza kupotea mtaani ukatangazwa msikitini!” alisema Jumanne na wote kuanza kucheka.



Walizungumza mambo mengi, alichomwambi ni kwamba siku inayofuata angempitia na kwenda wote huko Kibirizi ambapo wangenunua samaki na kuanza kuwatembeza mitaani.



Kwa Jumanne, samaki aliokuwa akiwauza walikuwa ni migebuka, alimwambia John kwamba kwa sababu walitarajiwa kutembea wote, basi yeye auze samaki wadogowadogo mpaka pale ambapo angezoea mitaa ndiyo aanze kuuza samaki wakubwa.

“Haina shida. Kwa hiyo wewe unauza wakubwa tu?” aliuliza John.



“Nauza mchanganyiko ila kwa sababu nitakuwa natembea na wewe, hao wadogo nitakuachia, nitakutambulisha kwa wateja wangu wengine, kama kweli una malengo, utafanikiwa!” alisema Jumanne.

“Nitashukuru sana! Siku nikifanikiwa, sitoweza kukusahau!” alisema John.



Walizungumza na mambo mengine na hatimaye Jumanne kuondoka mahali hapo. Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa urafiki wao, siku iliyofuata akapitiwa, akapewa kapu na kuanza kuelekea huko Kibirizi.



Hawakupanda gari, walitembea kwa mguu mpaka huko, ilikuwa ni umbali kama kilometa nane. Walipofika, John akabaki akishangaa, kulikuwa na wanunuzi wengi wa samaki mahali hapo, kulikuwa na mitumbwi mingi iliyokuwa imepakiwa ziwani, yote hiyo ilitumika kuvua samaki usiku na asubuhi kupakiwa hapo.



“Yule pale ni mzee Buchumi! Mzee mkarimu sana, ndiye ambaye nanunua samaki kwake, ana mitumbwi nane!” alisema Jumanne huku akimuonyesha John mzee fulani aliyekuwa amesimama pembeni na vijana wake akiangalia namna samaki walivyokuwa wakishushwa.



“Na gharama zake zipo vipi?”

“Si sana! Elfu kumi na tano unapata wengi na unaweza kutengeneza hadi elfu arobaini!” alijibu Jumanne.



“Duuh! Mapesa mengi hayo!”

“Ni mengi kweli lakini cha kushangaza sisi wauza samaki huwa hatufanikiwi!” alisema Jumanne.



“Kwa sababu gani?”

“Wanawake! Tunapenda sana wanawake!”

“Daah! Mimi nitapambana mpaka nifanikiwe, sitotaka wanawake hata kidogo!” alisema John.



“Hahah! John bwana! Hata mimi nilisema hivyohivyo, cha ajabu sasa nina michepuko mitatu! Maisha haya ya kijinga sana, kila nikitaka nijitoe, nashindwa kabisa,” alisema Jumanne kwa sauti ndogo, halafu akaangalia chini kama mtu aliyekuwa kwenye masikitiko mazito.



“Pole sana! Ila utafanikiwa tu!”

“Muda unanitupa mkono! Kama ningekuwa na mwanamke mmoja, ningefanikiwa John! Hili jambo limeniangusha sana na ndiyo maana ninakusihi mapema ili na wewe usije kuanguka,” alisema Jumanne.



“Nitafuata ushauri wako!”

“Sawa! Naona mzee Buchumi ameshamaliza, twende tukanunue samaki tukazurure,” alisema Jumanne.



Hilo lilikuwa jambo la kwanza kwa vijana wengi kutokufanikiwa. Wanawake waliwatanguliza mbele, walikuwa wakiingiza kiasi kikubwa cha pesa lakini mwisho wa siku pesa ziliishia kwa wanawake.



Hilo ndilo lililokuwa likimfelisha Jumanne, alitakiwa kufanikiwa kutokana na faida kubwa aliyokuwa akiipata lakini cha kusikitisha kabisa, hakuwa akiendelea, aliligundua tatizo lake lakini kamwe hakuweza kubadilika, ni kama kuhonga kwa sana ukawa ni ugonjwa sugu kwake.



“Deborah...amka..amka mama...unajua unachelewa kazini! Hebu amka kwanza,” ilisikika sauti kutoka nje ya chumba cha msichana mmoja aliyekuwa ndani ya chumba hicho amejifungia kwa ufunguo.



Sauti hiyo ndiyo iliyomuamsha, akayafumbua macho yake na kuangalia huku na kule, akajinyoosha na kuupeleka mkono wake katika kidroo kidogo cha kitanda ambapo akachukua simu yake na kuangalia saa.



“Saa kumi na mbili! Augh! Kwa nini nisijiajiri?” alisema msichana huyo, kwa uchovu mwingi sana akainuka kitandani hapo, akachukua taulo lake, akajifunga kuanzia kifuani mpaka chini kisha kuelekea nje huku akiwa na mswaki mkononi mwake.



Kwa jina aliitwa Deborah Abraham, alikuwa msichana mwenye miaka ishirini na mbili ambaye alikuwa akiishi katika Mtaa wa Mjimwema mkoani Kigoma.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Alikuwa msichana mrembo wa sura, mwenye umbo la kupendeza lililomvutia kila mwanaume aliyepeleka macho kwake, kwa kumwangalia harakaharaka tu, msichana huyo alifanana na wanawake waliokuwa wakisifika kwa uzuri nchini Tanzania.



Alikuwa msichana aliyesoma mpaka kidato cha sita Katika Shule ya Kigoma Sekondari, kabla ya kwenda kuanza masomo ya chuoni mkoani Dodoma miaka hiyo ya nyuma, akatafutiwa kazi katika Kampuni ya Kigoma Fishing Company ambayo ilikuwa na kazi ya kusindika samaki na kuwasafirisha kwenda sehemu mbalimbali nchini Tanzania.



Alitoka kwenye familia iliyokuwa na uwezo wa kati, iliyoishi katika mtaa wa Mjimwema ambao alikuwa akiishi na familia yake, ulikuwa ndiyo mtaa wa watu waliojiweza kwenye mkoa huo ambapo kwa Dar es Salaam ilikuwa ni rahisi kusema Osterbay.



Deborah aliringa, alijijua alikuwa msichana mrembo hivyo hata alipokuwa akitembea barabarani, alijua kuringa na kuwatamanisha wanaume wote waliokuwa wakimwangalia.



Japokuwa msichana huyo alikuwa mzuri wa sura na umbo, kitu ambacho kilimshangaza kila mtu ni kwamba hakubahatika kuolewa japokuwa tayari kulikuwa na wanaume watatu ambao walijitolea kuanza maisha naye lakini mwisho wa siku walikimbia na kumuacha.





Hakujua tatizo lilikuwa nini, katika kipindi hicho shauku yake kubwa ilikuwa ni kuolewa, alitamani sana kuitwa mke wa fulani lakini bahati mbaya sana kwake ni kukimbiwa na wanaume hao.



Moyo wake ulikuwa kwenye majonzi mazito, hilo lilimpa mawazo tele, kuna wakati alijisemea kwamba kwenye maisha yake asingekuja kuolewa kwa sababu tu kila aliyekwenda kujitambulisha kwao na kutoa barua, alikimbia zake na hakurudi tena.



Hilo likamfanya kukosa furaha, alijiona kuwa na mkosi kuliko mtu yeyote katika dunia hii. Kila alipokuwa akienda kanisani, hakujisikia furaha hata kidogo, alishangaa kuona wanawake ambao hawakuwa wazuri kama yeye, wakitoka kwenye maisha ya chini tofauti na yake wakiolewa lakini yeye akiendelea kubaki hivyohivyo.



Mwanaume ambaye alimuumiza mno moyoni mwake kuondoka kwake zaidi ya wengine alikuwa Innocent Nambuo. Huyo alikuwa mmoja wa vijana waliokuwa na sura nzuri katika Kanisa la TAG Msufini.



Alikuwa mtanashati, aliyekuwa na kazi nzuri, aliyependwa na wasichana wengi na kutamani kuolewa naye, mtu ambaye hata kwa kumwangalia mara moja tu ilikuwa ni rahisi sana kusema kwamba angemuoa Deborah lakini kitu cha kushangaza kabisa, alikuja kuahirisha dakika za mwisho na kumchukua msichana mwingine kisha kukimbilia jijini Dar es Salaam kabla ya kuelekea Nairobi nchini Kenya kuendelea maisha na msichana huyo.



Lilikuwa pigo kwa Deborah, moyo wake uliumia, ulisononeka kwa kipindi kirefu sana, alishindwa kuvumilia, chumbani kwake alikuwa na picha nyingi za mwanaume huyo hivyo akaamua kuzitupa kwa kuamini labda hilo lingemfanya kutokuwa na mawazo juu yake.



Haikusaidia, Innocent alimkaa kichwani mwake, siku zilikatika lakini bado mwanaume huyo aliendelea kuganda moyoni mwake, alichukua nafasi kubwa kuliko kitu chochote kile.



“Hivi sasa ningekuwa Nairobi! Innocent, kwa nini ulinifanyia vile?” alijiuliza wakati akiendesha gari alilopewa zawadi na baba yake.





“Kila mwanaume hanitaki, kila mmoja akija, anaondoka bila kunioa, au kwa sababu huwa ninawaruhusu kuugusa mwili wangu kabla ya ndoa? Mh! Hapana bwana, mbona Jackson sikumruhusu lakini bado naye aliniacha! Kwa nini mimi?” alijiuliza bila kupata jibu.



Kwa kipindi hicho hakuwa na mwanaume yeyote yule, alikuwa singo, alitamani sana kupata mwanaume wa kumuahidi kumuoa lakini ilishindikana kabisa.



Wanawaume wengine ambao hawakuwa na uwezo wa kimaisha walimuogopa, kila walipomuona, walipita naye mbali. Kwa muonekano wake ilikuwa ni vigumu kwa mwanaume asiyekuwa na kitu kumfuata, alijiweka kuwa mtu wa gharama na ndiyo maana hata wanaume ambao aliwahi kuwanao walikuwa ni wale waliojiweza mno.



Kutoka Mjimwema mpaka Kibirizi kulipokuwa na kampuni hiyo hapakuwa mbali, alitumia dakika kumi, akafika huko, akateremka na kuanza kupiga hatua kuelekea lilipokuwa jengo la kampuni hiyo aliyokuwa akifanyia kazi.



Sura yake ilikuwa kwenye tabasamu pana, wanaume hawakuacha kumwangalia, kila siku walikuwa naye ofisini hapo lakini cha ajabu kabisa kila walipomwangalia alionekana kuwa mtu mpya kabisa, yaani alionekana kubadilika kila siku katika maisha yake.



“Deborah! My Cleopatra, karibu sana,” alisikika mwanaume mmoja, alikuwa akimwambia Deborah huku akimwangalia, kwa macho yake tu yalionyesha ni kwa namna gani alitamani sana kuwa na msichana huyo.



“Karim! Hujaacha mambo yako tu!” alisema Deborah huku akiachia tabasamu pana.

“Nina mengi sana, yapi hayo?”

“Ya kuniita Cleopatra!”

“Hahah! Sasa hujioni kwa jinsi ulivyokuwa mzuri?”



“Hebu acha maneno yako! Bosi yupo?”

“Bado hajafika! Ila kuna barua zimeletwa kutoka makao makuu huko Dar es Salaam, nimesikia za kuongezwa mishahara!” alisema Karim huku akimwangalia msichana huyo.

“Unasemaje?”



“Taratibu basi bibie! Yaani ushapagawa!” “Hahaha! Yaani wewe acha tu!”

“Pesa za baba hazikutoshi?”

“Nani kakwambia pesa zinatosha, hata ukipewa kiwanda cha kutengeneza pesa, bado kila siku utaendelea kuprinti nyingine,” alisema msichana huyo.

“Hahaha! Kwa hiyo?”

“Kuhusu?”





“Ile dinner yetu! Mbona unanizingua sana? Nataka nikupeleke Hiltop Hotel, tukapigwe na upepo kule kilimani,” alisema Karim huku akimwangalia Deborah, alimtamani sana.



“Nimesema hapana!”

“Kwa nini? Unaogopa nini?”

“Karim hivi unajua shauku yangu ni nini?”

“Kuolewa!”

“Basi ishia hapohapo! Utaweza kubadili dini?” “Kwa ajili yako?”



“Yaap!”

“Nitakuwa tayari!”

“Ila hakuna sex kabla ya ndoa!”

“Sasa jamani nitanunuaje suruali bila kuijaribisha!”



“Hahah! Hakuna kitu kama hicho! Huwezi kunipata kwa sababu sisi ni dini tofauti halafu huwezi kubadili dini kwa ajili yangu, hivyo sahau!” alisema msichana huyo, kama kawaida yake tabasamu lilikuwa usoni mwake, kama alikuwa akielekea kukubaliana na wewe kumbe ndiyo alikuwa akikumaliza taratibu.



Wakati wakizungumza hayo, wafanyakazi wengine walikuwa wakipita, walimwangalia kwa jinsi alivyokuwa, alivyopendeza, alionekana kuvutia kupita kawaida, kila mmoja alitamani kuwa naye lakini ilishindikana kabisa.



Akaingia ofisini kwake na kuwasha kiyoyozi, akajiweka kwenye kiti na kuiwasha kompyuta yake na kuanza kazi.



Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake kila siku, alikuwa na kazi nzuri, mshahara mnono lakini kitu kilichomuumiza mno moyo wake ni kwamba kila mwanaume ambaye alithubutu kuwa naye, kabla ya ndoa ilikuwa ni lazima kukimbia.



Alijitahidi kuwa mtaalamu kitandani, alifanya mautundu yote, alimuonyesha mwanaume mapenzi ya dhati lakini hayo yote hayakuwafanya wanaume hao kubaki, walimkimbia na kwenda kwa wanawake wengine.



“Nisipokuwa makini hii hali kuna siku itakuja kuniletea stress zaidi halafu kuniua, ni lazima niwe makini sana kwani ninaamini bila mwanaume, bado maisha yanaendelea kama kawaida,” alijisemea, alijipa moyo japokuwa maneno hayo hayakuwa na ukweli wowote ule.



“Au niachane na wanaume wa kanisani niende kwa wa mitaani? Ila mh! Hapana! Baba ataniua, kwanza nitaanzaje kumwambia nimepata mwanaume ila si wa kanisani?” alijiuliza, akakosa jibu, akabaki kitini tu ametulia huku akiendelea na kazi zake.







“Binti nikusaidie nini?” ilisikika sauti nzito kutoka kwa mwanaume aliyekaa nyumba ya meza kubwa ya kioo iliyokuwa na kompyuta juu yake na mafaili machache.



“Nimekuja kuomba kazi!” “Umekuja kuomba kazi?”

“Ndiyo!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Kwani huu ndiyo utaratibu wa ofisi hii kwamba unakuja moja kwa moja kwa meneja na kuja kuomba kazi?” aliuliza mwanaume huyo.



“Hapana! Ila niliomba ruhusa ya kuonana na wewe, nimekuja zaidi ya mara saba nikaambiwa umekwenda Dar es Salaam!” “Sawa! Ila huu si utaratibu wetu, kama ofisi huwa kunakuwa na utaratibu wake. Kwanza umeona tangazo kwamba tunatafuta mfanyakazi?” “Hapana! Ila nimekuja kujaribu!”



“Elimu yako?”

“Kidato cha pili!”

“Hukufika kidato hata cha nne?”

“Hapana!”

“Sababu?”

“Mama alikosa ada, akaniambia nibaki nyumbani!” “Pole sana!”



Mwanaume huyo akamwangalia msichana aliyekuwa mbele yake, kwa jina aliitwa Juliana Julius, alikuwa binti wa miaka ishirini na tatu.



Kwa kumwangalia tu lisingekuwa jambo gumu kuyabashiri maisha yake huko nyumbani. Alivalia gauni jekundu lililoanza kufubaa, kichwani alikuwa na kilemba na chini alivalia viatu vya kuchomeka vya kike ambavyo navyo havikuwa na hali nzuri.



Alitoka kwenye maisha ya kimasikini, aliishi na mama yake katika Mtaa wa Ujiji.



Hawakuwa peke yao, pia kulikuwa na wadogo zake wawili ambao kipindi hicho walikuwa wakisoma darasa la tatu katika Shule ya Msingi ya Muungano iliyokuwa Mwanga.



Maisha yaliwapiga kwa pamoja, walichoka, kila siku walikuwa watu wa kuomba msaada tu. Hawakuwa na pesa, hawakuwa na kitu chochote kuonyesha walikuwa na maisha mazuri.



Mama yake, Bi Maria alikuwa mfanyabiashara aliyekuwa akiuza mbogamboga za majani katika Soko la Nazarethi. Pesa alizokuwa akizipata huko ndizo ambazo ziliendesha maisha ya familia.



Alipokuwa akipata, walikuwa lakini pale walipokuwa wakikosa, walishinda njaa kwani hawakuwa na sehemu yoyote ile waliyokuwa wakitegemea kupata chakula.





Maisha yao yalikuwa ni ya shida mno. Juliana alikuwa na kazi ya kuhangaika kutafuta kazi lakini kila alipokuwa akienda, hakufanikiwa kupata kazi yoyote hivyo kurudi nyumbani na kuendelea na maisha yake.



Hakuwa amesoma vya kutosha, hakumlaumu mama yake, mwanamke huyo alijitahidi kwa uwezo wake wote lakini hakufanikiwa kupata ada ya kuendelea kumsomesha mpaka kidato cha nne na hivyo kumwambia abaki nyumbani na kusaidiana naye kazi.



Siku hiyo ambayo alikosa kazi kwa mara ya nane ndani ya wiki mbili moyo wake ulimuuma mno, alisikia maumivu yasiyokuwa ya kawaida.

Akatoka katika ofisi ile huku uso wake akiwa ameuinamisha chini, alijikaza kisabuni, japokuwa alitamani sana kulia lakini hakutaka kufanya hivyo akiwa hapo, alivumilia mpaka pale ambapo angetoka ndani ya eneo la ofisi hiyo ili alie vizuri.



Alipokuwa akipita katika eneo la ofisi hiyo macho yake yalitua kwa wanawake waliokuwa wakifagia, aliitamani kazi hiyo, hakuchagua kazi, hakuwa na elimu ya kutosha hivyo kwake kazi yoyote ambayo ingepatikana na kulipwa mshahara mdogo, alikuwa radhi nayo lakini si kuona akiendelea kuteseka yeye na familia yake.



Alitembea mpaka mbali kabisa ndipo huko alipoanza kulia. Moyo wake uliuma mno, hakuwa na kitu, alimuomba Mungu kila siku lakini hapakuwa na kitu kilichoonekana kubadilika.



Akaanza kutembea kwa miguu kuanzia Bangwe kulipokuwa na ofisi hiyo mpaka kulipokuwa na soko la Nazareth lililokuwa pembeni ya barabara iliyokuwa ikielekea Mwembetogwa.



Alitumia saa moja mpaka kufika huko. Akaelekea mahali alipokuwa ameweka mbogamboga mama yake, alipofika na watu hao kutazamana usoni tu, Bi. Maria akagundua kilichokuwa kimetokea huko kwani sura ya binti yake ilionyesha kukata tamaa.





“Usiniambie kilichotokea huko! Njoo tuendelee kuuza biashara yetu,” alisema mwanamke huyo hata kabla ya salamu, aliyaona maumivu ya binti yake machoni, hakutaka kabisa kuona wakiliongelea hilo.

“Lakini kwa ni.....”



“Juliana! Nimekwambia usilizungumzie suala hilo! Naomba usilie, huna kazi, bado unaishi mwanangu, kukosa kazi haimaanishi unakufa, kuna watu wana kazi lakini wanateseka vitandani, kuna watu wana kazi lakini hawana amani hata kidogo,” alisema mama yake.

“Lakini mama....”



“Hakuna cha lakini! Huwezi kujua kwa nini unakosa kazi! Mshukuru Mungu kwa kila jambo! Cha msingi tuendelee na kazi zetu na jioni twende kanisani, si unajua leo ni Jumatano?”



“Ndiyo mama!”

“Basi tuuze harakaharaka twende huko! Pamoja na umasikini wetu, matatizo yetu lakini bado tunatakiwa kwenda ibadani. Hii pumzi tu tunayoitumia, ni baraka tosha, baraka si nyumba na magari, kuwa na pesa nyingi, kupumua tu napo tunatakiwa kutambua kwamba hii ni baraka, au hujawahi kusikia kuhusu yule tajiri Ruhuza?” alisema mama yake na kuuliza.



“Kwamba?”

“Alijiua!”

“Nakujua!”

“Sasa yule alikosa nini? Jumba kubwa, magari, pesa lakini bado akajiua!”

“Unamaanisha nini?”



“Furaha, amani ya moyo ndiyo kila kitu! Tunaweza kula bamia kila siku lakini tuna amani kuliko yule anayekula kuku nyumbani kwake! Juliana, naomba usiwe na unyonge tena, umesikia binti yangu?”



“Ndiyo mama!”

“Sawa!” aliitikia msichana huyo na kuanza kuchambua mbogamboga za majani zilizokuwa zimewekwa juu ya kiroba kilichotandikwa chini kwa ajili ya wateja waliokuwa wakifika sokoni hapo.

.

.

John hakuwa mzoefu wa mitaa mingi ya Kigoma Mjini hivyo rafiki yake, Jumanne ndiye aliyekuwa akimchukua na kwenda naye huko mitaani kufanya biashara ya kuuza samaki na kurudi nyumbani.



Maisha hayakuwa ya kawaida hata kidogo, kulikuwa na ugumu mkubwa mbele yake, hakukata tamaa, aliamini kuna siku moja angefanikiwa kama watu wengine, na inawezekana kabisa angeweza hata kuagiza gari kutoka Japan na kuliendesha katika mitaa hiyo.



Alipenda kujifunza kwa watu waliokuwa wamefanikiwa zaidi yake, aliamini kwa kufanya hivyo kungemfanya kuwa tofauti na watu ambao hawakuwa wamefanikiwa au hata kutokuwa na ndoto zozote zile za kufanikiwa mbele ya safari.



Alikuwa akitoka nyumbani alfajiri sana na alipokuwa akichukua samaki na kwenda kuwauza, mpaka majira ya saa sita mchana alimaliza na hivyo kutafuta sehemu zilizokuwa na watu waliokuwa wakiweka mijadala mbalimbali na kuanza kusikiliza.



Moyo wake ulikuwa na kiu kubwa ya kufanikiwa, hakutaka kujiona akibaki hapo alipokuwa miaka yote na ndiyo maana alijaribu kuwafuata watu waliokuwa wamepiga hatua na kuwasikiliza kile walichokuwa wamekifanya mpaka kuwa hapo walipokuwa.



Hapo Mwanga, kulikuwa na mzee aliyeitwa Miraji, huyu alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakiishi maisha mazuri. Alikuwa na nyumba nzuri, magari ya kifahari na alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakiishi kama wafalme katika mtaa huo wa uswahilini.



Nyumbani kwa mzee huyo kulikuwa na bomba la maji, watu ambao hawakuwa na mabomba nyumbani kwao walipendelea kwenda hapo na kuchota maji hayo.



Kwa sababu ya umri wake kuwa mkubwa, mara nyingi alikuwa akikaa yeye na wakati mwingine walikuwa watoto wake.

Kila alipomwangalia mzee huyo, alipata picha ya mtu aliyekuwa amefanikiwa.



Kwa muonekano tu aliokuwanao hakuwa kama watu wengine, alionekana kuridhika na kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika maisha yake.



Alihitaji kumsikia akizungumza naye kuhusu mafanikio, alitamani kuweka nae ukaribu ili apate kile alichokuwa akikihitaji wakati huo.



Alikwenda kuchota maji siku ya kwanza, ya pili na ya tatu ndipo alipoanza kuzungumza na mzee huyo. Mara ya kwanza aliposikia lafudhi yake, mzee huyo akagundua John alitoka jijini Dar es Salaam, alimwangalia vizuri kama mtu aliyehitaji kusikia mengi kutoka kwake.



John akakohoa, aliamua siku hiyo kuzungumza na mzee huyo kwani kila siku alikuwa akichota maji na kuondoka, ila kwa siku hiyo alihitaji kujua mengi kuhusu maisha yake kwa ujumla, alivyofanikiwa mpaka kuwa hivyo alivyokuwa.

“Kwa nini unaniuliza hivyo?” aliuliza mzee huyo huku akimwangalia John kwa macho ya kumdadisi.



“Kwa sababu ninataka kujua! Kwa nini umeniuliza kwa kushangaa sana?” alilijibu swali lake, na akauliza swali.

“Ni vigumu sana vijana kuniuliza kuhusu maisha yangu, yaani jinsi nilivyofanya mpaka kufanikiwa!” alijibu mzee huyo.



“Vijana wengi wanakuuliza kuhusu nini?”

“Mabinti zangu tu! Wengi huniambia wanataka kuwaoa!” alijibu mzee huyo na kutoa tabasamu lililomaanisha kwamba vijana hao walimuulizia kuhusu mabinti zake katika hali ya utani tu.



“Hahaha! Mimi ninahitaji kujua zaidi kuhusu njia ulizozitumia mpaka kufanikiwa!” alisema John.

“Zipo nyingi tu! Ila kabla ya yote naomba nikuulize swali?”



“Uliza tu!”

“Umetoka Dar es Salaam mpaka Kigoma kwa sababu gani?”

“Kufanikiwa!”

“Yaani utoke Dar halafu uje Kigoma kisa kufanikiwa tu?”



“Ndiyo! Kwani ni vigumu?”

“Inategemea!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Na nini?”

“Malengo yako! Kama kweli umedhamiria, utafanikiwa japo kwa ugumu sana!”

“Kwa sababu gani? Mbona wewe umefanikiwa ukiwa Kigoma?”



“Nilikuwa na akili ya ziada, nilijitoa kwa kufanya kazi kama mbwa!”

“Na mimi ndicho ninachotaka kufanya!” alisema John.



Walikuwa wakizungumza kuhusu mafanikio, muda mwingi John aliuliza maswali yaliyomfanya mzee huyo kugundua alikuwa akizungumza na mtu aliyekuwa na akili ya ziada.



Waliongea mambo mengi, alimfundisha mambo mbalimbali lakini kwenye hayo yote yalibebwa na kitu kimoja kilichosema ili afanikiwe ilikuwa ni lazima afanye kazi kwa bidii.







ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog