Search This Blog

Tuesday, 1 November 2022

SIPASWI KUSAMEHEWA - 5

 







    Simulizi : Sipaswi Kusamehe

    Sehemu Ya Tano (5)







    Siku moja Esmile akiwa anatoka kituo cha Polisi kufuatilia mwenendo wa kesi ya kifo cha mzee wake, alikuwa na mmoja kati ya wafanyakazi wake ambae alimuacha sehemu na gari kwa ahadi ya kukutana eneo la Posta.

    Baada ya kumaliza kilichompeleka huko, alitoka akiwa yupo kwa miguu akielekea Posta ili kukamilisha miadi yake na mfanyakazi mwenzie. Njiani akamuona mrembo anaemkumbuka.

    Hakukumbuka ni wapi alimuona lakini alikiri kumuona sehemu, alimvutia kweli mdada huyo ambae alikuwa kituo cha Station akisubiri daladala. Akamtamani, hakuwa amempenda, ni tamaa tu ikamfanya hivyo naye akajibanza kituoni pale hadi ilipofika daladala yule dada akaingia na Esmile naye akaingia.

    Gari waliopanda ilikuwa ni ya Mwananyamala – Station, ilikuwa imejaa kwenye siti za mbele ila siti ya mwisho ilikuwa na nafasi chache hivyo wote wakakaa siti ya nyuma lakini kulikuwa na mtu mwingine katikati yao. Binti yule kifupi alizishika akili za Esmile.

    Esmile alimsalimia na kutazama mbele, kama kawaida umbali mchache mbele, konda wa daladala hiyo akapita kwa ajili ya kukusanya nauli, Esmile ndio alikuwa wa kwanza kudaiwa, akalipa ya watu wawili, yake na ya yule binti.

    Binti aliona na kujidai kama vile hajaona lolote, Konda akamueleza kuwa tayari amelipiwa, alishukuru na kulipa tena, hivyo konda ikamlazimu kumrejeshea Esmile nauli yake.

    Baada ya kama vituo kadhaa, wakafika Magomeni Kanisani, binti akashuka na Esmile hakujiuliza, nae akaliachia gari hapohapo na kuanza kumfuatilia tena. Wakakatisha barabara kuu na kuingia mtaa wa ndani kidogo kisha binti akaingia kwenye kigrocery na kuagiza bia ya kopo.

    Esmile nae akaingia na kuagiza maji ya baridi akiwa ameketi kwenye kiti kinachotazamana na kiti cha yule binti ila ni mbali kidogo, akatoa simu na kumuelekeza mfanya kazi wake pale alipo.

    “Nifuate huku kama umemaliza unachofanya, ikiwa bado kwa sasa basi nitatumia Taxi, niambie.” Alipenda kuishi na wafanya kazi wake kama familia, kutokana na kuwapa uhuru kwa muda ule mchache, nao walimchukulia kama mwenzao tu.

    Jamaa akamwambia bado hajamaliza hivyo wakaamua kwamba jamaa akimaliza apeleke gari nyumbani kwao Esmile moja kwa moja.

    Wakati akiongea na simu, muhudumu alikuwa pembeni akisubiri malipo, utaratibu wa Glosary ile ni kulipa kabla hujatumia, hivyo Esmile akatoa shilingi 10,000 kwa ajili ya malipo ya maji ila akaagiza na kinywaji alichokuwa akinywa yule binti. Muhudumu alipofikisha kinywaji, akamwambia akate na pesa ya kinywaji anacho kunywa binti yule (huku akimuonesha kwa kidole) kisha ampelekee na ile nyingine.

    Mjumbe hauwawi, akafanya kama alivyoambiwa, akamsogelea na kuongea nae

    “Nashukuru, mwambie bia hii nimeisha ilipia, pia mimi huwa nakunywa bia moja tu hivyo hii mrudishie, mwambie asante sana, ameonesha anajali!” aliirudisha na Esmile akampa muhudumu bia ile ainywe yeye.

    Alikwama kwa wazo la kwanza, akajiuliza kuhusu plan B, na kupata wazo lingine ambalo aliona linafaa. Akamuita tena muhudumu na kumwambia anaomba amuitie mtu wa jikoni.

    Alipofika akamulekeza kwa binti yule tena na kumwambia aende kumuuliza atakula nini, jamaa akafurahi kwa kujua sasa atatengeneza pesa nzuri, kwa kufanya biashara, hasa ukizingatia muonekano wa binti Yule, alijua vema kuwa lazima atataka chips na kuku kama si samaki.

    Ujumbe ulifika, akarudi mjumbe huku akiwa ametabasamu na kumwambia Esmile kuwa amesema ‘hataki!’ kwa aibu Esmile akatabasamu na kumwambia amfungie yeye mwenyewe chips kavu na ndizi, akidhamiria kumpelekea mama yake.

    Jamaa wa jikoni alipoondoka tu, yule binti alinyanyuka na kuelekea alipo Esmile. Bia yake ikiwa mkono wa kushoto, mkono wa kulia akavuta kiti na kuketi mbele ya Esmile.

    “Kaka kwenye daladala ulitaka kunilipia nauli, nikakataa na kukushukuru! Hapa pia umeniagizia pombe nimekataa, bado tena unaniletea mtu wa jikoni kuchukua order, hivi kaka yangu, unafikiri nilipanda ile gari bila nauli au unaamini niliingia hapa Glocery bila pesa za vinywaji? Naomba uwe mstarabu, usipende kuharibu starehe za watu, jiheshimu utaheshimiwa!” maneno kuntu kabisa kwa Esmile.

    Lakini hata kabla hajajibu, binti akanyanyuka na kurudi kwenye meza yake ya awali na kumuacha Esmile amepigwa na butwaa, maana hakutegemea jambo lile kutokea.

    Akajifikiri kidogo na kuona sasa ni vema nae amfuate binti yule pale alipokaa kwa mtindo uleule aliokuja nao yeye. Alisogea na kuvuta kiti, alipoketi tu akaanza kuchombeza…

    “Samahani binti kama nimekukwaza naomba unisamehe, sikuwa na nia hiyo, ilikuwa ni ukarimu tu wa Kitanzania…”

    “Sikia kaka kuna watu wengi sana mitaani wanahitaji msaada na huo ukarimu unaousema, nashangaa wewe unataka kutoa msaada baa tena kwa mtu anaelewa, hivi una busara kweli? Mi naona kama unanipotezea muda wangu bure tu,” kauli ile ilikuwa ni ya mwisho kwa yule binti na kunyanyuka akimuacha Esmile akiwa amebaki peke yake kama aliemwagiwa maji.

    Muhudumu akasogea tena ili kuondoa mabaki ya kinywaji alicho kiacha binti yule, huyu aliekuja alikuwa ni msichana pia, akamwambia kwamba yeye anamjua yule binti na huja pale mara kwa mara.

    Akamueleza sehemu anayopatikana na siku ambazo huja pale, ila jina hata nae alikuwa halifahamu.

    Sehemu ambayo alimwambia anaishi wala haikuwa mbali sana na pale Glocery, Esmile akamshukuru na kumuacha msichana Yule na kifuta jasho kidogo na kurejea nyumbani.

    Kampuni yake ya uwakili ikaanza kupata jina mjini hasa pale alipoamua kutekeleza kazi nyepesi mbili za watu wasiojiweza kuhusu malipo ya mawakili, kama ambavyo alivyokuwa amedhamiria.

    Akaagiza wafanyakazi wake waende kwenye Magereza kutembelea katika mikoa tofauti. Akateua mikoa yenyewe kuwa ni Dodoma, Arusha, Kigoma, Tanga na Mbeya.

    Akawawezesha safari ya uhakika akiwa amewapa pesa kwa ajili ya nauli kwenda na kurudi, alilipia gharama za malazi kwa siku tano za kazi, pia akawapa Trip allowance yenye kuridhisha akiamini anawekeza tu, na kuna siku lazima itakuja kumlipa tu.

    Wote walifurahi kutokana na mwenendo ama tuseme mwanzo mzuri wa tabia alio ionyesha bosi wao, hivyo nao wakajitoa kwelikweli kuiboresha kazi yao huku kila mmoja akijiapiza kufanya kazi bora zaidi, wakasambaa kila mmoja akiwa tayari kutekeleza jukumu alilo lipokea.

    Wakati wao wakiwa safarini, yeye huku nyuma aliendela kuumizwa na muuaji wa baba yake na pia alikuwa akitamani sana kumuona Mam ili aweze kutimiza ahadi aliyomuahidi.

    Ahadi ya kumfikisha mbele ya sheria yule aliembaka na kumuathiri kisaikolojia, ambae sasa Esmile anaamini ndio alimuambukiza Virusi vya Ukimwi.

    Mishemishe za kumtafuta Mam zilikwamishwa na mawasiliano.

    Wakati huohuo alikuwa akikosa kabisa ushirikiano kutoka jeshi la Polisi alipokuwa akifuatilia kesi ya Mzee wake, hadi sasa, bado hakuwa na fununu yoyote juu ya muuaji wa Mzee wake.

    Ilimchukua miezi miwili kumtia mikononi mwake binti yule ambaye baadae alikuja kumjua jina lake kuwa ni Layla. Hakuwa amemfananisha wala nini, bali jicho lake tu liona kama vile limemuona Mam, kwani walifanana kiasi Fulani.

    Rasmi sasa akaingia ndani ya mapenzi, mapenzi amabyo aliamini hatoweza kuyapata popote tofauti na kwa Mam, lakini mapenzi yake yakawa motomoto kama kawaida yake anapojitoa kupenda, anapenda kweli.

    Wafanyakazi wake wote walirejea na maelezo ya kila mmoja yakachujwa lengo ni kupata watu wawili watakaowasaidia. Mchujo wa awali ulipita yakabaki majina matatu yaliyoleta kizaazaa baina ya wafanyakazi wenyewe kwa wenyewe.

    Esmile aliingia na kukuta ubishani mkubwa sana miongoni mwa wafanyakazi wake akawaambia waumalize mzozo huo kitaalam huku wakilinda vigezo walivyo jipangia wenyewe, na wakishindwa wamfuate ofisini kwake.

    Hawakusubiri, kwa kuwa tayari walikuwa wameisha tumia muda mrefu kwenye kufanya maamuzi, wakanyanyuka wote na kuingia ofisini, akawataka wamueleze tatizo nini.

    Wakamueleza uzito wa kesi zile tatu wakianza na kesi ya huko Dodoma ambapo kijana Denis alichoma basi la tajiri mmoja wa kiarabu baada ya kumgonga mama yake na kumuua hali ya kuwa amekaa nje ya nyumba yake.

    Mwarabu hakutoa msaada wowote kwa kijana huyo wakati alipomfuata na zaidi akatishiwa kuuawa. Ajabu walipokwenda kwenye sheria, kesi wala haikusomwa kwa muda mrefu mno.

    Hata ilipokuja kusomwa, jibu likawa ni tofauti kabisa na mategemeo ya watu wote, hapo ndio kijana alipopatwa na hamaki na hasa baada ya kuambiwa ule ulikuwa ni uzembe wa mama yake. Jazba ikampelekea kulichoma gari lile lililomgonga mama yake na kumuua.

    Na ndio sababu iliyofanya kijana kufungwa miaka 15 jela.

    “Hii ya kwanza muanze nayo haraka iwezekanavyo,”

    Kesi ya pili ilikuwa ikimuhusu mwanaume wa makamo aitwae John, huyu alikuwa ni mkulima anaemiliki shamba huko maeneo ya Kigamboni, alihusishwa na kutuhumiwa kushirikiana na majambazi.

    Chanzo kikiwa John aliekuwa shambani kwake akiwa amelala kwenye kichaka baada ya kuchoka kwa kilimo, walifika majambazi wawili na kuficha mzigo fulani kisha wakakimbia huku yeye akiwaona.

    Si hatua nyingi sana wakakamatwa na kuuawa na wananchi wenye hasira kali. Ghafla wananchi waliokuwa na silaha za asili, wakavamia shambani kwake na kuanza kutafuta, wakidhani bado kuna wengine, akaona atauawa, kwa kujitetea, akaona akimbie, maana wangempata mle shambani wasingeamini kama yeye si jambazi, ni mmiliki wa shamba.

    Haraka akatokomea mbele ili kutetea maisha yake amabyo kabisa aliona yapo htarini bila kujua kuwa anafanya kosa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku ya pili alirudi kujua usalama wa shamba lake, kumbe askari walikuwepo pale na kumkamata na kumpa kesi hiyo, maneno haya alimueleza wakili huyo wa kujitegemea kutoka kampuni ya ‘The Chambers’ hakuwahi kumueleza yoyote, si ndugu jamaa wala Hakimu, maana aliamini hatosaidiwa.

    “Madenge, utashughulikia hii kesi ikusafishie nyota, najua ni kesi ndogo sana hii, kazi kwako” alitoa maelekezo Esmile huku akimkabidhi madenge file hiyo na kuuliza







    “Kuna la ziada?” karibu wote walitabasamu na kusimama huku wachache wakijibu kwamba hakuna la ziada.

    Kwa kuwa walikuwa akihitaji kesi mbili tu, hakutaka kuisoma ile ya tatu, akagawa wafanyakazi wawili wawili katika kila kesi, kisha akabaki msichana mmoja tu kati ya wafanyakazi wake na kumwambia yeye atabaki pale ofisini na atapangiwa kazi nyingine.

    Kati ya wafanyakazi wake 6 alio waajiri, mmoja hakuwa akijihusisha na mambo mengine yoyote zaidi ya mambo ya ukatibu muhtasi, watano ndio walikuwa ni mawakili wake.

    Walipotoka Esmile akawa hana cha kufanya akaamua aipitie tu na ile kesi ya mwisho iliobaki mezani kwake wakati akivuta muda wa kutoka ofisini kwake kwenda kwenye mambo yake mengine.

    Alifunua file ile kizembezembe tu akiwa amejilaza na kuanza kuisoma, kiukweli hakuwa na nia sana ya kujua kilichomo mle ndani, bali alichotaka ni kupeleka muda mbele hadi wakati autakao utakapofika.

    Baada ya kufunua, kesi ile ilikuwa ni ya mauaji na ilimuhusu mwanamke mmoja muathirika wa VVU aliyemuua mumewe kwa stuli kutokana na unyanyasaji wa kijinsia, bado haikumvutia kabisa.

    Chanzo chake kilivyo andikwa mle kilikuwa hivi;

    Siku ya tukio mume wa dada ambae ni mtuhumiwa kwa sasa, aliingiza mwanamke ndani ya nyumba yao na kumtaka mkewe akalale sebuleni, kwa kuwa alijijua ni dhaifu na hana uwezo wa kupambambana na mumewe, akalala.

    Asubuhi mumewe akamuamsha ili awawekee maji ya kuoga, mumewe na yule hawara yake, mwanamke huyo alijizuia jazba isimpande, akatekeleza alivyotaka mumewe.

    Ila walipotoka kuoga mumewe na hawara yake, ikamlazimu Yule mwanamke kufanya kitendo ambacho hakikutarajia yeyote, maana walipokwenda kuoga tu, huku nyuma yeye aliketi kwenye kochi na kujikuta kapitiwa na usingizi kutokana na kukosa usingizi usiku kwa sababu ya kulala chini kwenye sakafu.

    Mumewe alipotoka kuoga, akaanza kumuita, bahati mbaya usingizi ukawa umemchukua, akanyanyua mguu na kumkanyaga pajani ili kumuamsha huku Yule mwanamke mwingine akicheka.

    Aliposhtuka tu mumewe akamuuliza kama amewatengea chai, alipojibu kwamba bado hajatenga, mumewe akaanza kumsulubu kwa makofi na mateke, kila alipotaka kukimbia mumewe alifunga mlango na kuendeleza kichapo kikali.

    Kibaya zaidi Yule mwanamke aliekuwa pale alikuwa akicheka hadi anakaa chini, hivyo nae kama binadamu mwenye hisia, aliamua kuchukua stuli na kujikinga nayo, baada ya kukosa msaada wowote.

    Kwa bahati mbaya wakati akiinua stuli juu mumewe huyo alikuwa ameruka kumpiga kichwa hivyo akapiga kichwa chake kwenye stuli na kuanguka, damu zikaanza kumwagika yule mwanamke mwingine akatoka na kutimua mbio huku akipiga kelele.

    Hapo sasa ule mkao wa kizembezembe ukaondoka na umakini ukamtawala, alihisi kuguswa na habari ile japo hakujua lolote wala kumfahamu muhusika, ila tu alihisi dhulma imefanyika kwa binti huyo.

    Akaendelea kuisoma habari ile ambayo iliandikwa na mmoja wa mawakili wake aliemtuma gereza la Maweni kuangalia kesi mojawapo ya kuishughulikia. Iliendelea kusema kuwa mwanamama huyo alikuwa akiomba msaada na majirani akisema kuna mauaji huku akionesha chumba alichopo mtuhumiwa. Watu walijaa, wengine walipiga simu na kuita Polisi, baadhi walikuwa na shughuli za kupiga picha na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii, ila walikuwepo wachache wenye akili ya kufanya jitihada za kumpeleka hospitali.

    Juhudi zilifanikiwa lakini walichelewa kwani mwanaume yule alivuja damu nyingi sana na alifia njiani wakati akipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Tanga, maarufu kwa jina la Bombo Hospital.

    Habari hii alipoisoma akashusha pumzi na kujiuliza inakuwaje mtu unakuwa na roho ya ajabu kiasi hicho? Akaangalia mwanzo tena ili kujua kama kesi ile imekwisha ama Inaendelea?

    Kesi ilikuwa bado ikiendelea Kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga, hukohuko jijini Tanga, hakika ilimvutia sana Esmile, hasa jina la mtuhumiwa alikuwa akiitwa Maryam Mahmoud.

    Alijaribu kuvuta picha ya Mam, ila hakufanikiwa kabisa kuipata picha kamili. Akahisi huenda ni majina tu yamefanana na si Mam yule anaemfahamu. Hata hivyo akawaita tena vijana wake na kuwaambia kesi ile pia ishughulikiwe haraka, wajipange wenyewe wawezavyo ili na ile ipate watu wa kuisismamia.

    Muda wake wa kurejea nyumbani ukawa umewadia na akapanga kurejea tu nyumbani kuimaliza siku akiwa na mama yake ambae aliamini anamtegemea yeye kwa kila kitu, kwani ndio mtu pekee alie baki kama furaha yake, maana mumewe ambae ndio baba wa Esmile ameisha toweka kwenye sura ya Dunia.

    Aliporudi nyumbani akaenda moja kwa moja chumbani kwa mama yake alipokuwa amejipumzisha, akamsalimia na kupiga nae story kidogo, kisha akaelekea chumbani kwake kujipumzisha.

    Ilikuwa ni mida ya alasiri bado, alilala hadi saa moja kasoro za jioni, ndio akaamka na kwenda kujiswafi. Wakati anavaa nguo zake baada ya kuoga, taswira fulani ya ile file yake ya ofisini, ikamuijia kichwani na kuna kitu akakikumbuka.

    Moja kwa moja akaelekea hadi kabatini, kabati ya nguo, kwenye sehemu ya kwanza anapotunzia nguo, juu kabisa akateremsha nguo zote, haikuchukua muda akakipata kile alichokuwa akikitafuta, ilikuwa ni pete ya Mam aliyoitupa mara ya kwanza alipomuona.

    Alijitupia kitandani akimuwaza Mam kwa robo saa nzima, ile kesi nayo ikamjia akilini na kuanza kulinganisha matukio hasa akikumbuka kwamba Mam nae alikuwa muathirika, lakini hakutaka kuamini kwamba Mam alikuwa ameolewa katika kipindi hicho cha miaka takriban mitatu na kunyanyasika kiasi kile.

    Akaazimia kesho aanze kumsaka Mam kila sehemu, akapanga mikakati kama akili yake ilivyo muongoza, jambo la kwanza ilikuwa ni kutoka mle ndani na mama yake, wawe wawili tu nje ya pale ndani japo hata mle ndani wanaishi wawili.

    Alinyanyuka na kumalizia kuvaa, akatoka na kumfuata mama yake ili kumuomba mama yake watoke pamoja kwa chakula cha jioni, mwanzo mama yake alikataa, ila baadae akakubali baada ya Esmile kumueleza kwamba alipanga watoke wao wawili tu kwani kuna jambo la muhimu wanapaswa kuliongea wao tu.

    “Sasa si tuongee hapahapa? Kwani kuna nani mwingine ambae unamuogopa hapa?” aliuliza mama yake na Esmile akamjibu kwamba alipanga iwe ni nje ya pale, mama akasema kama ni nje ya pale basi na Layla nae awepo.

    “Mama sasa Layla wa nini wakati mambo mengine yapo kifamilia zaidi?”

    “Unataka kuniambi akuwa Layla hahusiki kwenye familia yetu?”

    “Sina maana hiyo mama yangu!”

    “Sawa, sasa una maana gani?”

    “Basi mama nimekubali yaishe, tutaenda wote pamoja na Layla,”

    Hapo akachukua simu na kumtafuta Mpenzi wake, baada ya muda alimtumia ujumbe wa simu kwa kuwa simu yake ilikua haipokelewi.

    Layla alipoiona msg ya Esmile, hakuweza kukataa, aliomba tu muda kidogo wa kujiandaa, huku nao wakaingia garini na kuondoka kwa nia ya kumpitia Layla nyumbani kwao.

    Walimkuta Layla akiwa anawasubiri nje ya nyumba yao, akungana nao na kuelekea maeneo ya Escape One, huko ndio Esmile aliona panafaa kwa kile alichokiandaa kuzungumza na mama yake.

    Mazungumzo yalianza taratibu kabisa yakiwa ni yale mazungumzo ya kawaida, amani iliwatawala sana, wote walikuwa na furaha, na hicho ndio kitu pekee ambacho Esmile alikuwa amemuahidi mama yake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Siku zote mama yangu ninapenda mno uwe na furaha, wakati wowote nitahakikisha unakuwa na furaha mama, popote nitakapokuwepo, amini nitakuwa faraja kwako,”

    “Ni kweli mwanangu, ila unasema hivyo kwa sasa kwa kuwa majukumu bado hayajakubana sawasawa, wewe ni faraja sana kwangu, ila baadae huwezi kuwa name wakati wote,”

    “Nini unamaanisha Mama?”

    “Nitapata faraja zaidi iwapo utakuwa na Layla ndni ya nyumba yangu, japo nae ni mfanyakazi, lakini si msafiri kama ulivyo wewe,” mazungumzo yalipamba moto hasa, mama akamuuliza mwanae kuhusu suala la ndoa.

    Esmile akamwambia mama yake kuwa hilo ndio suala alilotaka kuongea nae, lakini kabla ya kulizungumzia hilo, kuna masuala mawili yanamchanganya sana, yakiisha hayo tu, basi kila kitu kitakuwa sawa.

    Mama yake alipomuuliza ni matatizo gani hayo yanayomchanganya? Esmile akajibu,





    Mama ninafikiri unafahamu fika kuhusu suala la Mam na ahadi aliyomuahidi ya kumsaka aliyembaka na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria…” aliuliza huku akiwa amemshika mama yake mkono wake wa kushoto kwa mikono yake yote miwili, alionesha mapenzi makubwa mno kwa mama yake.

    “Ndio ninakumbuka vizuri tu”

    “Lakini moyoni kuna jambo linguine nalo ni muhimu sana mama yangu kabla ya hilo la ndoa, japo hili linaweza kuendelea hata nikiwa ndani ya ndoa,”

    “Lipi hilo Esmile?” aliuliza kwa shauku mama yake.

    “Nataka nimtafute aliemkatisha maisha baba yangu kipenzi, kisha baada ya hapo nitakuwa nimetulia na sasa itakuwa ni wakati muafaka kwa mimi kutulia na Layla wangu tule maisha nawe mama tukiwa ni wenye furaha na amani tele,” alijibu Esmile

    “Sasa mwanangu, unasema kweli lakini kazi zote hizo zikichukua miaka mitano je, Layla atakaa anakusubiri wewe tu siku zote hizo?”

    “Hapana mama yangu, kesho ninakwenda Tanga kwa ajili ya suala hilo hilo, nitaanza na suala la Mam, naomba uniamini mama, jambo hili halina hata miezi 6 mbele, kila kitu kitakuwa safi. Layla nitakaa nae na kuliweka sawa jambo hili kiundani, maana halielewi, eti Layla?” alimuuliza huku akimpigapiga mikononi, akaitikia kwa kutikisa kichwa huku akiona aibu.

    Waliondoka saa tano usiku kurudi kwao wakianza kwa kumuacha Layla nyumbani kwao kisha nao wakarudi Upanga. Alipofika ndani akachukua simu na kuongea na Layla kwa takriban saa nzima akimueleza kila kitu kuhusu Mam, hadi kile alichomuahidi Mam cha kumfikisha Mahakamani aliembaka na kumuambukiza Ukimwi.

    Pia alimueleza juu ya mauaji ya baba yake na hatua aliyofikia wakati ule. Layla alimuonea huruma sana na kumpa moyo akimuahidi kuwa nae pamoja katika kipindi chote hiki cha mihangaiko ya kufikia malengo, hadi siku ya mwisho.

    Asubuhi ya siku ya pili Esmile alifika ofisini na kuwaaga kuwa anakwenda Tanga, akawauliza walivyo jipanga kuhusu kesi ya Tanga, wakasema wamejipanga kesi hiyo itasimamaiwa na Naima ila hawajajua ni nani atakuwa pamoja na Naima. Naima ni msichana mrembo sana ambae alikuwa na umbo zuri mno, ni msichana aliemaliza elimu yake ya sharia hivi karibuni, lakini kitambo akiwa na uzoefu kiasi Fulani na kesi za madai, hiyo ikawa ni nafasi ya upendeleo kwake kuajiriwa na Esmile kwenye kampuni ya The Chambers.

    Sasa ndio alikuwa amechaguliwa na wenzie kuongoza kazi hii ambayo inakuwa ni kazi ya kwanza kwake, ilimtia hofu na mwenyewe akajisalimisha kwa mkuu wake wa kazi kumueleza ugumu wa kazi.

    Esmile alimsikiliza na kumtoa hofu akimwambia kuwa hata wanasheria wakubwa hukwama, lakini pindi wanapouliza kwa wenzao ama kupitia vitabu vya sheria, basi hupata muafaka,

    “Nani nitakuwa nawe bega kwa bega ili kumsaidia Maryam wa Tanga, sawa Naima?” alipotoa kauli hiyo Naima akafurahi na kusimama akiaga.

    “Sawa, lakini mimi nilitaka tuondoke leoleo, vipi itawezekana kweli? Ama mimi nitangulie?” aliuliza Esmile huku akitazama saa.

    “No boss! Nisubiri tu nikapack vitu vyangu, hakika sitachelewa,” wakati akisema hivyo akawa ameshika mlango kutoka, Esmile akamrushia funguo ya gari na kumwambia awahi.

    Saa moja lilifuata tayari walikuwa wakiwaaga wenzao ofisini na safari ikaanza mdogo mdogo kuelekea Tanga ikiwa ni saa tano asubuhi, njiani Esmile alipiga simu hoteli ambayo alikuwa akifikia mara kwa mara ili kuweka order ya vyumba viwili.

    Waliwasili Tanga mida ya saa 11 alasiri na gari yao ndogo, wakaelekea hotelini moja kwa moja ambapo tayari walikuwa wametuma maombi ya kuwekewa vyumba.

    Kila mmoja aliingia chumbani mwake na hawakutoka hadi usiku wakati Esmile alipompigia simu Naima na kumwambia yeye anatoka kwa miguu, hivyo nae kama atapenda kutoka, afuate funguo ya gari kabla hajatoka.

    Akiwa ni mwenye furaha tele, akatoka chumbani kwake hadi sehemu alipokuwa Esmile na kuchukua funguo za gari akiwa tayari na kuanza kuzunguka jiji la Tanga huku bosi wake akiwa ameelekea Makorora.

    Hakuwa mgeni tena kwenye nyumba ile, hii sasa ilikuwa ni mara ya tatu anafika pale. Aligonga mlango na kupokelewa vizuri na kukirimiwa, waliompokea walionyesha furaha ya hali ya juu kwa kumuona, wakamkaribisha kwenye sofa na kusalimiana, baada ya maongezi machache, Esmile akauliza alipo Mam

    Mama na baba Mam wakatazamana, mtazamo ulioonyesha kuwa jibu la swali lake lilikuwepo, ila mtoaji wa hilo jibu lililopo, ndio hakuwepo.

    “Vipi wazee wangu...? (Huku akiwasogelea) ...kuna tatizo? Niambieni...” hofu ilimvaa moyoni Esmile, sura nayo ikaonesha hivyo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hapana Esmile, kwa kweli…” hapa akasita Mzee Mahmoud kisha akaendelea

    “Mam alifungwa, Mam yupo Gereza la Maweni kwa kesi ya Mauaji Esmile,”

    “Ha! Mam... Mam huyu nimjuae mimi?” huku akihisi mwili kumsisimka, aliuliza Esmile kwa mshangao mkuu

    “Ndio mwanangu” alijibu Mama yake Mam kwa huzuni ambayo Esmile ilimuumiza nafsi yake.

    Aliwapoza na kuahidi kuwasaidia kumuweka Mam huru tena, lakini angependa kujua Mam alimuua nani na kwa sababu gani. Mzee Mahmoud hakuon haja ya kuficha chochote, hasa akifikiria ukarimu wa familia ya kina Esmile tangu uhai wa mzee Hanson, aakaamua kufunguka kila kitu

    “Baada ya Mam kutoroka kipindi kile akiwa nawe, alikwenda Gairo na kukaa kwa mdogo wangu, hadi baada ya miezi mitatu tukamfuata tukiwa tayari tumeikubali hali yake, maana hiyo ndio ilikuwa ni hali halisi.

    Tukakaa nae huko Dar kama mwezi mmoja hivi, akaja siku moja mchana na kusema amekutana na Alfred na anataka kumuoa, wamekutana Muhimbili kwenye foleni na wote wawili... (Mzee Mahmoud alinyamaza kidogo, kisha akaendelea) …walikuwa tayari wameathirika. Na baada ya miezi miwili wakafunga ndoa bomani kulekule Dar...” alinyamaza Mzee ili kumeza mate.

    Esmile alikuwa ametulia kwa umakini wa hali ya juu akisikiliza, Mzee akaendelea

    “Hawakudumu sana kwenye ndoa yao, ikawa ni vurugu kila siku, mara Alfred kampiga Mam, wakati mwingine anakuja kalewa na siku zingine akileta mahawara zake hadi nyumbani, tulimkanya sana pande zote mbili, yaani wazazi wake yeye Alfred na sisi pia, lakini hakuelewa,” akatulia tena Mzee Mahmoud ili kujua kama Esmile anaenda nae sawa. Kama mtu aliejua kuwa ule ni mtego, akauliza

    “Kwa hiyo nyinyi kama wazazi mkachukua hatua gani hapo?”

    “Kwa kuwa hii nyumba ya Marehemu mama ilikuwa ni tupu hakuna anaeishi hapa, tukafikiri kwa pamoja na kuamua wahamie huku Tanga huenda akatulia,” hapa akameza funda la mate kisha akaendelea…

    “Kumbe huku ikawa ndio balaa kabisa, walifikia hapahapa wakiwa wao wawili tu, Alfred akawa hashikiki, tena inasemekana ikawa ni nafuu ya Dar kuliko huku...” Ndio hapa sasa Mzee akamuhadithia kile kisa Esmile alichokisoma kwenye jalada akiwa ofisini, moyo ukapiga mshindo, japo alihisi tangu mapema, lakini alikuwa akitamani asiwe Mam huyu ndio Mam muhusika wa kesi ile.

    Roho ilimuuma sana, chozi likamdondoka na kutamani kumuona usiku uleule lakini ikawa ni jambo ambalo haiwezekani. Ikawa ni huzuni tu, aliwaza mbali sana, aliona ugumu wa kesi, lakini aliona kuna upenyo wa kuchomoka hapa, akawaahidi wazee wake kuwa yeye atamsaidia Mam kwa gharama yoyote, ile, na jambo la kwanza atakalofanya ni kumuwekea Wakili wa kujitegemea.

    Hawakumuelewa alimaanisha nini hadi pale alipowajulisha kuwa atamuweka mtu atakae msaidia Mam kwenye kesi ile. Wao wakaona kama vile atapoteza bure tu pesa zake, akasikitika moyoni kwa kuona wazee tayari wamekata tama, lakini yeye akawaambia wasijali kwani hayo ndio matumizi ya pesa.

    Baada ya mazungumzo hayo Esmile pia aliwaeleza juu ya msiba wa Baba yake nao walimpa pole japo walikuwa wamepata taarifa kupitia vyombo vya habari ila hawakuwa na mawasiliano na Esmile wala mama yake kuweza kuwapa pole...

    Aliondoka pale saa sita usiku kurejea hotelini akiwa amewaacha wazazi wa Mam wakiwa na faraja kiasi fulani hasa pale alipowaambia wajiandae atawaijia asubuhi ya siku ifuatayo kwenda gereza la Maweni ili wakaongee na Mam.

    Wakamtazama kwa tabasamu, halikuwa tabasamu la furaha, bali lilikuwa ni la huzuni, mama akamjulisha kuwa hawataruhusiwa kumuona siku ya katikati ya wiki, kwani walijulishwa hivyo. Akawajibu kuwa tayari watakuwa na wakili na wataruhusiwa.

    Kwa muda ule aliofika hotelini alikuta Naima amelala, akamtaka radhi baada ya kumgongea, kisha akamweleza juu ya yale aliyokutana nayo huko japo hakumgusia juu ya uhusiano uliokuwepo kati yao.

    “Hivyo kwa kuanzia mimi kesho nitakupeleka kwa kina Mariam nikiwa kama mdhamini nawe ukiwa kama wakili wa kujitegemea, nisingependa wajue lolote juu ya uhusiano wetu wa kikazi uliopo,” wakakubaliana na kila mmoja akaingia chumbani kwake.

    Waliwapitia mapema sana wazazi wa Mam, bahati mzur nao waliwakuta wakiwa tayari wakiwasubiri, waliondoka na kuwasili Magereza saa tatu asubuhi na kuomba kuonana na Mkuu wa Gereza, waliporuhusiwa, wakafanya hatua zote zinazopaswa kufanya pindi unapotaka kufanya mambo ya kisheria.

    Baada ya kukamilisha taratibu zote, wakaruhusiwa kuonana na Mam, kwanza walianza wazazi wake ambao walipewa dakika tano za kuongea nae, kisha wakaingia Esmile na Naima.

    Hakuna alieamini kumuona mwenziwe, Esmile na Mam wote walilia, hakuna aliejali mwenzie amevaaje walikuwa wamekumbatiana japo Esmile alikuwa amevaa suti nzuri na ghali huku Mam akiwa kwenye nguo ambazo hazikuwa kwenye ubora wala usafi wowote.

    Muonekano wake ulitia huzuni sana hata kwa Naima japokuwa hakujua machozi yale yaliwatoka wale watu wawili kwanini ila nae yakamtoka.

    Askari aliekuwepo pale akaja na kuwatenganisha kwa huzuni na kuwakumbusha kuwa muda waliopewa unakwenda bure nao hawajaanza hata maongezi yao. Wakaketi na Esmile akamtambulisha Naima kwa Mam kama rafiki, kisha akamgeukia Mam na kumwambia yule ni wakili wa kujitegemea, anaitwa Naima na yupo pale kwa ajili ya kumsaidia yeye.

    Wakati huo Naima alikuwa akiandaa baadhi ya vitu muhimu ambavyo alikuwa akivihitaji kwenye mahojiano yake na Mam, alitoa tape na diary pia kalamu akiwa tayari tayari.

    Mam alimtazama Esmile na kuanza kulia kwa dukuduku huku akimlaumu Esmile kwa kumdhalilisha

    “Esmile unajua fika kuwa wazazi wangu hawana hata uwezo wa kunihudumia baadhi ya huduma muhimu ninazo zikosa hapa magereza, watawezaje kumlipa dada huyu aweze kusimamia kesi yangu? Kama si udhalilishaji ni nini hiki?”

    “Mam hilo wala lisikupe tabu, kila kitu kinaratibiwa na Kampuni yangu, jambo la msingi ni kuwa muwazi kwetu bila kutuficha ili tujuwe ni wapi pa kuanzia, ama sio Naima?” Esmile aliuliza huku akimtazama Naima





    “Yes boss!” Naima aliitika huku akijiweka vizuri kwenye kiti alichokaa, kalamu yake ikiwa mkononi. Lakini Mam aligoma na kusema hastahili kupata msaada mwingine wowote kutoka kwa Esmile.

    Hapo kwenye ‘msaada mwingine’ ndio Naima alishtuka na kujiuliza kuwa watu hawa wanajuana sana? Ina maana si urafiki tu wa kawaida kama alivyofikiria yeye, ina maana kuwa ni marafiki wa karibu sana kama si wa muda mrefu.

    Walijaribu kumbembeleza lakini wapi, Mam alishikilia msimamo wake uleule kuwa hahitaji msaada na anaikubali hali ile, ikafikia hatua hadi Naima akakasirika na kumtaka bosi wake waondoke.

    Mam akamtazama Naima kwa jicho la kusanifu huku akimtazama kuanzia viatu alivyovaa hadi nguo alizovaa akapanda hadi kichwani alipoweka wigi lake kisha akasema kwa sauti ya upole mno

    “Wakili najua nimekuudhi, naomba unisamehe, huyu unaemuita Boss amenifanyia mengi sana mema, sio moja wala mawili, bali ni zaidi ya mambo matatu, nami hadi leo sijamlipa hata moja, bali ni uovu mtupu, sasa anataka kunisaidia tena, hivi unafikiri mimi nitamlipa nini? Tena ni lini hiyo siku ya kumlipa huo wema wake? Hebu tazama upande wa pili wakili..?”

    Naima alishusha pumzi na kumtazama Esmile, walikutanisha macho yao na Esmile akakwepesha, akayaelekeza kwa Mam, kwani maneno yale yalimuingia vema, yalikuwa ni maneno kuntu, Esmile akajitutumua na kusema

    “Umenilipa furaha Mam, sijawahi kuwa na furaha kama kipindi kile nilichokuwa nawe Mam, naomba unikubalie Mam, tafadhali…” aliongea Esmile kwa hisia kali, lakini bado Mam akagoma. Wakaamua wamuache hadi siku ifuatayo warudi kwa mara nyingine.

    Waliporudi kwa Mkuu wa Gereza ili kuaga, walimjulisha kuwa watarudi siku ifuatayo kwa mahojiano zaidi. Akawauliza hatua waliyofikia, wakamwambia si njema. Esmile akamuhadithia nae akasikitika na kuahidi kuwasaidia.

    Wakatoka na kuwarejesha wazazi wa Mam nyumbani kwao nao wakiwa ni wenye majonzi hasa baada ya kujua kuwa Mam amekataa kutoa ushirikiano juu ya jambo hilo ambalo kwa siku ile limekula muda wao.

    Siku iliyofuata wakiwa wao wawili tu, yaani Esmile na Naima, bila kuwa na wazazi wa Mam, saa mbili na nusu asubuhi walifika tena kwa Mkuu wa Gereza na aliwapokea, aliwajulisha juu ya yeye kuongea na Mam baada ya wao kuondoka siku iliopita;

    “Amekubali kutoa ushirikiano ila inaonyesha ana siri nzito mno moyoni, nendeni mkaongee nae, lilikuwa ni tatizo la kisaikolojia…” wakatoka. Siku ile walifanikiwa kuongea nae kwa zaidi ya saa nne huku Naima akimrekodi mazungumzo yao.

    Alitoa ushirikiano hasa, leo alionekana kama mtu ambae alikuwa akiwasubiri waje ili aweze kuongea nao, kila swali alailoulizwa alilijibu lilivyo stahili, hivyo aliafanya kazi ya mahojiano kuwa ni nyepesi.

    Walimaliza na kuondoka kwenda kufanya maandalizi mengine kwa ajili ya kuja kamili kamili kuivaa kesi ile, walipita kwa mkuu wa gereza ili kujua siku ya kesi ya Mam, alipowaambia wakamuaga na kumshukuru kisha wakaondoka.

    Walipomaliza yale ya Tanga wakarudi Dar na kukaa jopo zima la mawakili wa kampuni ya Esmile, The Chambers kutafakari juu ya zile kesi walizochukua watazikabili vipi. Walitoa rekodi zao na kuzisikiliza wote kwa pamoja huku wakishirikiana kutoa maoni haya na yale.

    Kila lililoonekana la muhimu liliandikwa na kuhifadhiwa, kisha wakaendelea kushughulika na mengine hadi kesi waliokuwa wakiijadili ilipo kamilika wakaanza nyingine.

    Baada ya kuzimaliza kuzipitia kesi zile zote, jopo lile liliweka nukta muhimu kwa kila kesi na kumkabidhi muhusika, kwa msaada na ushauri waliokuwa wakipeana mara kwa mara, walifanikiwa kuzimaliza zile kesi mbili za awali kwa haraka na mafanikio makubwa, ikiwepo ya kijana Denis kulipwa fidia ya mamilioni ya fedha.

    Mzee mwenye shamba naye aliachiwa huru bila sharti lolote. Watu wote hawa wawili walishukuru sana na kijana Denis alitoa milioni 25 kwa kampuni ya The Chambers kama shukran kwa msaada wao. Uongozi wa kampuni nao ukatoa shilingi milioni 5 kama pongezi kwa mawakili wali endesha kesi ile na kuwapa milioni moja moja wafanyakazi wote waliosalia kama motisha.

    Kesi ikawa imebaki moja na ni ngumu hasa ukizingatia ni ya mauaji. kesi ikasomwa kwa mara ya kwanza baada ya kujitokeza kwa mawakili wa upande wa mtuhumiwa, na kuahirishwa siku ile, hali ilikuwa ni hivyo hadi siku ya utetezi ilipotimia. Naima akasimama mbele ya jopo la Majaji na kumtetea Mam kwa kiwango cha juu huku akitoa mifano mingi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mmojawapo alioutumia ni ule wa Uchokozi. Kwa mujibu sheria za nchi hii, kuchokozwa kunapunguza kosa la mauaji ya kukusudia hadi kufikia kuwa ni mauaji ya bila kukusudia.

    “Uchokozi ni kitendo cha kiovu ambacho mtu yeyote akifanyiwa, humfanya mtu ashindwe kujizuia na kujitawala hivyo hufanya kitu chochote pasi na kufikiria matokeo yake na hatimaye hata kusababisha mauaji kama ilivyotokea kwa mteja wangu Maryam” kisha akaendelea…

    “Waheshimiwa Majaji kufanyika zinaa ndani ya nyumba yako na wakati huo huo unafanyiwa dhihaka, katika hali ya ubinadamu ni lazima ukasirike, na kwa hali hiyo basi, bi Maryam alichokozwa na kama tulivyoona hapo nyuma Sheria ilivyotafsiri uchokozi, hivyo ninaiomba Mahkama ipunguze uzito wa kosa lake kufikia kuua bila kukusudia,”

    Mahakama iliendelea kwa wiki nzima na kuwadia siku ya hukumu, siku iliyokuwa ni ngumu kuliko siku zote kwa Mam, maana hii ilikuwa ni ngumu kuliko hata ile siku ya kwanza kukamatwa na kutuhumiwa kwa mauaji, siku ambayo alipigwa sana na askari Polisi.

    Hiyo ni siku amabyo alilaumiwa na kila mtu, siku hiyo alizodolewa na jamii yote, wanaomjua na hata wasio mtambua wote waliungana na kumuita ni muuaji.

    Mam akaketishwa kizimbani, pamoja na kuwepo watu wachache pale kizimbani, yeye aliweza kuona ni mamilioni ya watu wamejazana.

    Majaji waliingia huku watu wote wakisimama, itifaki ikazingatiwa na kisha wakaketi. Mmoja wa majaji akaanza kusoma marudio ya kesi ile tangu mwanzo wa kesi hadi pale ilipofikia, akaanza kupitia vifungu vya sharia. Akalizungumzia jambo hilo hivi;

    “Katika kulitazama suala hili Mahakama Kuu imekuwa macho sana, maana mauaji yanapaswa kufanyika katika hali ya hasira kubwa (Heat Of Passion) na kusiwe na muda kati ya kuchokozwa na kuua,”

    Hapa tena Jaji akatoa mifano kadhaa ikiwepo ya Niko aliekua ndani ya basi alipotukanwa na Salim ambae alikuwa ni abiria mwenzie ndani ya basi asubuhi ya siku ya tukio, ila jioni ya siku hiyo hiyo Niko akaenda kumpiga Salim na kumsababishia kifo, hapa Mahakama moja kwa moja ilimuhukumu kifo ndugu Niko kwa sababu alipata muda wa kutosha kabisa kwa yeye kupoa.

    “Pia huwezi kulipiza kisasi kwa mtu tofauti na yule aliekuchokoza na ndio tumeona hapo kabla, Maryam hakumpiga mwanamke aliyekuwa na mumewe, bali yeye alimpiga mumewe moja kwa moja, kwa kuwa mumewe ndiye aliyemnyanyasa na kumpiga hapa sharia ya nchi yetu nayo inambeba mtuhumiwa,”

    Zaidi ya yote Maryam alishikwa na hasira ya kudhalilishwa mbele ya macho yake, hicho ni kitendo kiovu kilicho kinyume na sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo si kitu kinachoruhusiwa kisheria, naam.

    “Labda nitoe mfano katika kesi ya bwana Kufa Kunoga aliporudi nyumbani kwake usiku na kumuona bwana Kabila Ndogo akikimbia kutoka nyumbani kwake, shati likiwa begani na huku ameshikilia suruali yake iliyokuwa ikionekana kudondoka, bwana Kufa Kunoga akampiga risasi iliyomuua palepale bwana Kabila Ndogo. Mahakama ya rufaa ya Afrika Mashariki, ikasema mauaji hayo hayakuwa ya kudhamiria ingawa Bwana Kufa Kunoga hakumkuta Marehemu katika hali ya kimapenzi na mkewe, ila ile hali ya mwenendo wa Marehemu, baada ya kushtuliwa pale nyumbani, ilionyesha kuwa ni kweli ngono ilikuwa ikitendeka. Na ni lazima mume angekasirishwa na tendo hilo na kufanya kitendo kiovu ambacho kingeweza kufanya mshitakiwa asiweze kuitawala hasira yake, basi Mahakama ikampunguzia hatia, kutoka kwenye kesi ya mauaji ya kukusudia na kuwa ni mauaji ya kutokukusudia na kufungwa miaka mitano tu.”

    Jaji akatulia na kuwatazama watu waliokuwemo mle ukumbini kisha akaendelea…

    “Kwa kitendo kile cha marehemu Alfred kufanya ngono na mwanamke mwingine asiyekuwa mkewe mbele ya mkewe hicho chenyewe ni kitendo ambacho ni cha kidhalilishaji na pia kumkanyaga kanyaga sehemu za mwili ni tendo linguine kumdhalilisha mkewe, katika hali ya kibinaadamu ni lazima upandwe na hasira kama ilivyotokea kwa bi Maryam na kupelekea kifo cha mumewe,” akafunua karatasi na…

    “Sasa kupitia vifungu kadhaa vya sheria tulivyopitia, pia ushahidi wa mshitakiwa ambae amekuwa akisaidiwa na wakili wake, sisi kama jopo la majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, baada ya kupitia mambo yote na vifungu vya sheria tumeona kuwa bi Maryam ana kesi ya kuua bila kukusudia, kama ilivyotokea huko India kwa Abdul v/s Nizar mwaka 1974”

    Hapo tena akapumua na kutoa nafasi ya watu kutathmini maneno asemayo, akawatazama waliopo mle ndani kisha akaweka miwani sawa na kuendelea…

    “Kwa hiyo basi kupitia kanuni ya adhabu ya Mahakama ya Afrika Mashariki namba 405 kifungu cha 201 cha kanuni ya adhabu, Mahakama ya Rufaa ya Tanzania inamuhukumu Bi Maryam Mahmoud kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela, na hii inaanza tangu alipohukumiwa na Mahakama Kuu, na kwa kuwa ameshatumikia adhabu hiyo kwa kipindi ambacho mahakama hii inakiamuru kwa mujibu wa sheria hai za nchi hii…” hapa Jaji Mkuu akanyamaza na kuwatazama walio mbele yake na kuteremsha miwani huku akitembeza macho yake kule na huku, kisha akaipadndisha tena miwani na kushika karatasi yake na kusema







    “…hivyo Mahakama inapenda kumwambia bi Maryam kuwa..

    YUPO HURU TANGU SASA.” kisha ikasikika sauti ikisema

    KOORT! Watu wote wakasimama na kusubiri Majaji watoke, Mam alizimia hakuelewa kilichoendelea, hata wengi wao waliokuwepo pale walishikwa na bumbuwazi, ni Esmile na Naima tu ndio wakajua wafanye nini.

    Wazazi wake Mam nao walibaki na butwaa. Esmile alisogea pale alipoanguka Mam huku akisaidiana na jamaa wachache aliowaomba wamsaidie kumuingiza garini na kumuwahisha hospitali. Wakati Naima akimalizia hatua za mwisho pale Mahakamani.

    Hali haikuwa mbaya maana ulikuwa ni mshituko tu alio upata, hivyo alipata matibabu na kuruhusiwa kurejea nyumbani japo hali yake haikuwa njema sana lakini hiyo ilisababishwa na ugonjwa wa Ukimwi alionao na kutokana na kukosa matunzo mazuri wakati akiwa gerezani.

    Hasa ukizingatia kwamba alikuwa bado alikuwa ni mwanzoni tu tangu aathirike na dawa zenyewe ndio kwanza alikuwa ameanza kutumia, ikamlazimu kuziacha hasa baaa ya utaratibu kubadilika kuytokana na kule kukamatwa kwa ghafla na kuwekwa rumande.

    Ilikuwa ni vigumu sana kusikilizwa juu ya kuletewa vidonge vya ARV mahabusu, hivyo ndio taratibu dozi ilivyokata.

    Ilikuwa ni furaha nyumbani kwa kina Mam, Naima alipokamilisha mambo yote kule Mahakamani akampigia Esmile kumuuliza alipo na akamwambia yupo kwa kina Mam ila atakwenda hukohuko Mahakamani amsubiri. Akatoka pale nyumbani kwa kina Mam na kuahidi kurudi jioni.

    Safari yake ilielekea moja kwa moja Mahakamani, alipofika akamkuta Naima akiwa na baadhi ya mawakili wenziwe wakimpongeza, Esmile aliwasalimia na kuwapa mikono, wakataniana kidogo, akamchukua Naima na kuondoka.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakapita mjini kwenye duka la simu na kununua simu moja ya kisasa na kisha wakarejea hotelini ili kubadili mavazi na pia kujiweka tayari kwa ajili ya kutoka ili kwenda nyumbani kwa kina Mam.

    Saa moja usiku Naima alimpigia simu bosi wake akitaka kujua kama yupo tayari. Esmile alimjibu kuwa yeye yupo tayari na anamsubiri katika bar ya hoteli waliofikia, Naima akacheka na kumwambia yeye yupo garini tayari, Esmile akashuka na msafara ukaanza kwenda nyumbani kwa kina Mam.

    Walipokelewa kwa kina Mam kama chakula kwa mtu mwenye njaa, bado palikuwa na msongamano wa watu waliokuja kumpa pole Mam, hata Mam alipowaona waokozi wake, aliwaacha watu wengine na kuwapokea Naima na Esmile.

    “Esmile kwa mara ya pili unaniokoa mimi…” akaangusha kilio tena, hilo wala halikumsumbua Esmile, aliisha mjua Mam kuwa ni bingwa wa kulia na kufanya maamuzi ambayo ni ya kujidhuru, akamtuliza taratibu akiwa amemkumbatia.

    Wazazi wa Mam nao wakaja na kuongea hadi nao saa tano usiku, hawakuacha kuwashukuru kila dakika kwa msaada wao, msaada ambao ulimliza Mam kila mara, waliaga na kuruhusiwa, wakasindikizwa na Mam hadi garini.

    Esmile akavuta draw ya gari na kutoa simu mpya na kumpatia Mam akimwambia tayari amemfanyia kila kitu, Mam hakuamini, akaangua kilio tena badala ya kufurahi.

    Ikabidi Naima amchukue na kumrudisha ndani, wao wakaondoka, wakiwa njiani ndio Naima akamuuliza bosi wake ni kwanini amekuwa mwema sana kwa Mam? Esmile akatabasamu na kumwambia ni habari ndefu mno, waiache kwa muda huo.

    “Kuna siku tu utajua ni kwa nini ninafanya hivi Naima,” tayari walifika hotelini na wakaingia kila mtu kwake na kupanga safari yao ya kurejea Dar kesho yake asubuhi.

    Ulikuwa ni usiku wa furaha sana kwa Mam, kwani ulikuwa ni usiku wa kwanza tena kuwa uraiani baada ya kuwa hana imani ya kuja kuliona jua la nyumbani.

    Pamoja na furaha hiyo, hakuwa na amani kwa kufikiria ni nini atamlipa Esmile? Maana imekuwa kila siku anamtendea jema jipya, sasa imefikia hata hawezi kumlipa tena, afanyeje? Ndio hilo lililomnyima amani.

    Akashika simu yake na kuanza kuibonyeza ikiwa ni saa 11 alfajiri, kwa hakika siku ile Mam alikesha, hakupata hata lepe la usingizi.

    Japo ni muda mrefu, alipoona namba fulani aliikumbuka, akaipiga. Wakati ikiwa inaita ndio akagundua kuwa hajafanya jambo jema hata kidogo, kumpigia simu mtu alfajiri vile bila kuwa na ahadi nae si vema, akakata.

    Kumbe mtu wa upande wa pili alikuwa tayari ameisha amka na kutaka kupokea, mtu huyo hakuwa mwingine bali ni Esmile. Simu ile ilipokatika tu, Esmile akaenda yeye hewani.

    Mam nae akaanza kujishauri apokee ama aache, ilivyoita sana akapokea, akaanza kwa kumtaka radhi Esmile kwa kumsumbua alfajiri, ila lengo lake lilikuwa ni kumshukuru tena na tena. Akamwambia wala asijali na ataendelea kumsaidia zaidi na zaidi hasa katika kipindi hiki ambacho ni kigumu kwake.

    Akamwambia kuwa wanapaswa kumshukuru Mungu kuwa hilo moja limeisha, sasa bado kuna lingine lipo njiani. Waliongea hadi saa moja asubuhi ndio wakaagana na Esmile akaanza kujitayarisha kwa safari.

    Mungu alikuwa pamoja nao tena, maana walifika Dar mapema, Esmile akamuacha Naima kwake na akaelekea nyumbani kwao na kupokelewa na mpenzi wake Layla pamoja na mama yake ambao waliokuwa wakimsubiri kwa hamu na shauku. Na wote walitaka kujua kiurefu yote yaliyojiri kule.

    Wakakaa bustanini Esmile akawahadithia kiurefu kila kitu na kuwafanya nao kuwa na furaha wakiamini kuwa ndoto zote za Esmile zitatimia karibuni, walimalizia siku yao palepale bustanini, usiku wakaagana kwa Layla kuchukua gari na kwenda nayo kwao akimuahidi Esmile atampitia asubuhi kumpeleka kazini.

    Usiku ulikua mrefu mno kwa Esmile ambaye mara kwa mara alikuwa akichati na Mam wakipeana habari mbalimbali za hapa na pale. Kwa upande wa Leyla yeye alikuwa na furaha tu kwa kuona mambo yanakaribia kuiva kwa upande wake.

    Siku ya pili Naima aliwahi kazini kuliko Esmile ambaye alichelewa kwa sababu ya kumsubiri Layla. Kule ofisini ilikuwa ni pongezi tu kwa Naima, baadhi ya magazeti yalitoa picha za Mam, Naima na mavazi yake ya uwakili na hata ofisi za The Chambers. Radio zilitangaza tukio lile na hata TV zilionyesha ilikuwa ni fahari kwa wana Chambers.

    Hilo hasa ndio lilikuwa lengo la Esmile, hakutaka kutumia mamilioni kujitangaza kupitia vyombo vya habari, bali alitaka kutumia utu kujiweka mahali ambapo jamii imtambue, na alifanikiwa kwa hilo.

    Mam alishapiga simu mara kadhaa kwa Esmile, pia aliongea na Mama Esmile. Na wakati huohuo Esmile alipokea simu nyingi sana za pongezi kwa kampuni yake, ikafikia sasa akajua tayari kile alichokuwa akikitaka kimeanza kuwa. Alipokuwa akianza kutoka na Layla, simu yake ikaita

    “Hellow Mam,”

    “Yes boss, mambo?”

    “Poa za mida?”

    “Safi nipo njiani nakuja Dar, nimefika Kibaha, naomba unitafutie hotel, samahani kwa usumbufu boss!” alisema akimtania tu Esmile kwa kumuita Boss kama afanyavyo Naima. Akamuitikia kimatani na kumwambia wala asijali yeye aje tu.

    Esmile kweli alijua ni utani, akamueleza Layla Mpenzi wake, Leyla akamwambia asichukulie ni utani, huwenda ikawa ni kweli. Akampigia simu Naima na kumwambia juu ya ujio wa Mam, Nae hakuamini pia hadi pale boss wake alipomwambia aende akamchukulie chumba katika hoteli moja eneo la Magomeni.

    “Boss wala usihangaike, kwani nyumba ninayoishi ina vyumba vitatu nami nipo peke yangu, nitakaa nae, ama hatokubali?”

    “Mh, haya Mama, kwa hiyo nimwambie?”

    “Hapana ninampigia mimi mwenyewe sasa hivi!”

    Wakatoka Esmile na Layla akiwa hajui wanaelekea wapi. Waliingia ofisini na kuwakuta wafanyakazi wote wakiwa pale, baada ya salamu na pongezi za hapa na pale, Esmile akawaita wote kwa kikao cha dharula na kuwaambia jioni ya siku ile kutakuwa na sherehe ndogo nyumbani kwake, wote wanakaribishwa na waje wawili wawili.

    “Ambae anaruhusiwa kuja peke yake ni Naima tu kwani yeye atamkuta muhusika wake hukohuko kwangu, ila nyie wengine hakuna anaetakiwa kuja peke yake, anaejijua yupo peke yake ni heri asije tu, abaki nyumbani na familia yake wanacheza mdako,” walicheka kutokana na masihara ya boss wao kisha Esmile akatoka na Layla kuelekea mjini kwa ajili ya maandalizi ya sherehe.

    Waliingia madukani, maduka tofauti na kupeana robo saa wawe wamekutana pale garini. Kama walivyopanga, kila mmoja alijinunulia kile atakacho na kukutana garini ili kurudi nyumbani.

    Kama nilivyosema kule mwanzo, unaweza kumzuia mtu mwenye akili nyingi asiondoke, lakini katu, huwezi kuuzuia muda. Wakati ukawadia watu wakaanza kujimwaga uwanjani.

    Walipokelewa kwa furaha na kulikuwa hakuna mshereheshaji yaani MC katika hafla hiyo, ila alikuwepo msemaji ambae ni Esmile, saa moja kamili usiku aliwakaribisha walikuwa kama watu 21 hivi na kuwaaambia ile ni sherehe ya kuvishana pete ya uchumba kati yake na mpenzi wake.

    Pia ilikuwa ina sehemu ya kupongezana kwa sababu ya kushinda kesi zote tatu walizochukua kuwasaidia watu. Na bahati mzuri mmojawapo kati ya wale walioshinda kesi, yupo hapohapo.

    Kipindi watu wakiingia pale, Naima alikuwa ameongozana na Mam, lakini alipofika pale, Esmile akamwamuru Naima ashuke peke yake kwenye gari na amuache Mam huko ili asionekane na mtu yeyote.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Hivyo ni Naima pekee kati ya watu wa ofIsini aliekuwa akijua uwepo wa Mam pale na ndio pekee pia aliekuwa akimtambua, hivyo Naima alipewa ishara na Esmile akamfuata Mam.

    Alirejea pale akiwa na Mam, wote walikuwa wakimtazama, japo ni mgonjwa na hajarudia hali yake lakini dhahiri alionekana kuwa ni mrembo matata sana. Hata Layla alishtuka, Mam alianza kupita na kuwasalimu kwa kuwapa mikono, baadae Esmile alimtambulisha kwa watu wote kuwa ni rafiki ambae ni zaidi ya rafiki, kauli iliyowachanganya kidogo, kisha akampa nafasi ya kuongea kidogo.

    Mam alitumia nafasi ile kuishukuru The Chambers Na wafanyakazi wake hasa Naima aliesimama kidete, pia akampa shukran za kipekee kwa Mkurugenzi wao yaani Esmile. Alimaliza kwa kilio kama kawaida yake Mam.

    Baada ya tukio hilo la kumtambulisha Mam na kumsikia kauli yake kukamilika, likafuata la pili la kuwapongeza wafanyakazi wote kwa kufanikiwa kuvuka hatua zote tatu kwa mafanikio, hivyo akatoa zawadi kwa wafanyakazi wote ili kuwatia morali, maana alitambua kuanzia sasa wafanyakazi wake watawindwa kwa nguvu zote na makampuni nguli ambayo yataona thamani yao kwa sasa.

    Hatua iliyokuwa imesalia sasa ni uchumba, Pete ya uchumba, Esmile akatoa pete moja ambayo si mpya na kumuita Mam, wote walishtuka, wakihisi huenda huyu ndio amechaguliwa kuvishwa pete ile ya uchumba? Aliposogea Esmile akasema;

    “Naomba ushike pete hii, uniambie je unaitambua?” akakana Mam

    “Basi naomba umuulize kila mtu aliemo humu ndani,” Mam akazunguka nayo pote nyumba nzima kwa waliokuwepo wote wakaikana, Esmile akasema akitabasamu

    “Ndugu zangu mmiliki wa pete hii yupo humuhumu, naomba ajitokeze,” bado ikawa kitendawili, Esmile akaomba mabinti waijaribu, mwenywe lazima itamkaa sawa.

    Walijaribu wote ikawagoma, ila ilipoingia kwenye vidole vya Mam, japo alikuwa amekonda, pete ikanasa, ajabu Mam akaikana, Esmile akamfuata na kusimama na mbele, wote wakimshuhudia

    “Mam unaweza kuikumbuka pete hii?”

    “Hapana Esmile, sio tu kwamba siikumbuki bali pia wala siijui” Esmile akatumia muda ule kumkumbusha Mam tangu mara ile ya kwanza kuonana, alihadithia mwanzo mwisho, Mam alikumbuka na kumrukia Esmile na kumkumbatia. Watu wote sasa wakawa wameelewa uhusiano uliopo kati ya Esmile na Mam.

    Naima akatikisa kichwa ishara ameridhika sasa, maana swali lake leo limejibiwa, huku napo chozi lilimtoka kwa mbali Mam na kumuomba Esmile amuachie pete ile iwe ni kumbukumbu yake, hakumnyima akamwambia pete ile ni yake na ana uwezo wa kuifanya lolote, akashukuru na kwenda kuungana na waalikwa wengine.

    Mam, Mama Esmile, Layla na hata Naima na walikwa wote hawakujua ni nani anavalishwa pete ile kati ya Mam na Layla. Esmile akatoa kiboksi cha pete na kumuangalia Naima, kisha Mam na mwisho Layla. Akawaita wote watatu, akawapanga Mam kulia, Naima mbele yake na Layla kushoto, kisha akasema akimtazama Mam huku Naima amekishika kiboksi

    “Samahani Layla...” kisha akamgeukia Mam

    “Mam unajua ni jinsi gani nilivyokupenda, ninaamini fika unajua kwamba bado nakupenda sana na daima itakuwa hivyo, lakini pia nahisi unatambua kuwa kwa sasa mimi nawe hatuwezi kuwa wapenzi tena… (Mam alitikisa kichwa kukubali hilo) nilipenda hapo awali nitakachokifanya hivi punde, nikifanye kwako, lakini hilo limeshindikana, ama nimekosea?”

    “Hapana Esmile, upo sawa mno,”

    “Basi Mam nakuruhusu, uende ukakae!” huku akimuonesha waalikwa, Mam akamkumbatia, kisha akamkumbatia na Layla na kumbusu, wakashikana mikono na Naima na kuondoka pale mbele.

    Esmile alimvisha pete Layla na sherehe zikaenda kama zilivyopangwa, kufikia saa nne usiku wakamaliza sherehe yao na kila mmoja akaelekea kwake, siku hiyo Layla alilala pale ila Mam na Naima waliondoka na moja ya magari ya Esmile.

    **********



    Maisha yaliendelea na siku kadhaa baadae kabla Esmile hajakaa na Mam kuzungumzia suala la kumfikisha mbele ya sharia mtu aliembaka, hali yake ikawa si njema, akaomba arudishwe kwao Tanga, ila alipomuuliza juu ya mtu huyo, Mam akamuomba aachane nae, maana ndie aliemuua baba yake pia.

    Esmile alishtuka sana na kuvuta picha ya watu wote waliokuwepo pale miaka kadhaa iliopita, aliweza kupata taswira za watu waliokuwepo, lakini akashindwa kumjua mtu huyo ni nani, kifupi sasa aliona umuhimu wa Mam.

    Akashindwa kabisa kupata jibu akaamua kusubiri kidogo Mam apate nafuu kisha ndio ataongea nae kwa nafasi. Mam aliondoka Dar kwa kushindikizwa na Naima hadi Tanga kwa kutumia gari ya ofisi. Naima aligeuza siku ya pili japo hali ya Mam bado haikuwa nzuri.

    Wiki moja baadae Mam alimpigia simu Esmile na kumwambia yeye hawezi kuendelea kuishi kwa sasa, anahisi hana tena muda wa kuendelea kuwepo hapa duniani.

    Alijaribu kumpa moyo lakini haikusaidia kabisa. Mam alishikilia msimamo uleule na zaidi akamuomba Esmile aende Tanga pamoja na Mama yake, mchumba wake na Naima.

    Akasema anataka kuwaona wote kwa mara ya mwisho, kauli ambayo ilimsikitisha sana Mama Esmile alipoisikia toka kwenye kinywa cha Esmile na kumwambia mwanawe waondoke siku ifuatayo.

    Tayari Naima, alitokea kuwa ni rafiki mkubwa wa Mam, akakubali kujiunga nao safarini, mara tu alipojulishwa juu ya wito kutoka kwa Mam.

    “Lakini mimi nimeongea nae na hajaniambia Boss!” alisema Naima kwa mshangao.

    “Sawa, lakini mimi ameniambia mkuu!” Alipenda sana utani Esmile, Naima akasema sawa, yupo tayari, akaambiwa ajiandae siku ifuatayo watampitia mapema ili kwenda Jijini Tanga kumsikiliza Mam ni kipi alicho waitia watu wote.

    **********



    Mam alifurahi sana alipowaona ila hali yake ilikuwa ni mbaya sana japo tabasamu lilionekana, alikaa nao kwa nusu saa na kumwambia Naima kuwa siku ile haitaisha salama kwake, ila anafurahi kuwa amewaona.

    Alikuwa amelazwa hospitali ya Bombo na aliwekwa chumba maalum, kwa kuwa walikuwa wameingia wote kwa pamoja, akawaomba Esmile na mama yake watoke nje, wakabaki wazazi wake na kuongea nao.

    Aliwaambia kuwa waapaswa kuendeleza mahusiano kwa ukaribu na familia ile, kwani wamekuwa ni wema sana kwao kiasi ambacho hata wafanyeje wao hawawezi kuwalipa japo familia hiyohiyo ndio imemfikisha hapo alipo.

    Hakufafanua zaidi, akawaacha njia panda na kisha akawaomba nao watoke nje waingie Layla na Naima, kwani nao anataka kuzungumza nao kwa wakati wao tofauti.

    Wakatii na kutoka nje kuwapisha Naima na Layla, hawa walitumia muda mchache zaidi na baadae kidogo nao wakatoka bila kujua ni kipi walichoambiwa, walipofika nje wakamnyanyua Esmile na mama yake.

    Hawa pia Mam aliwaambia kuwa hana maisha marefu kwa sababu tayari ameisha athirika kwa kiwango kikubwa sana na hatopona hata ifanyike juhudi gani.

    Esmile hata nae sasa alikubali matokeo kutokana na hali ilivyombadilikia Mam, akamuuliza amfanyie nini ili iwe kumbukumbu? Mam akamwambia amsamehe yote aliyomkosea na amuombee kwa Mungu pia.

    Vilevile akamgeukia Mama Esmile na kusema maneno hayohayo. Maneno ambayo yaliwafanya kutazamana na mama Esmile akamwambia Mam kuwa hakuna alilomkosea na wala asitie shaka.

    Esmile akamuwahi Mam kwa kumwambia, amweleze mtu ambae amesababisha hali ile, maana mtu huyu aliembaka ndio aliemuathiri, Mam akamuuliza Esmile

    “Utanisamehe nikikwambia mtu mwenyewe?”

    “Ndio Mam, wewe nitakusamehe ila yeye nitamfikisha Mahakamani,” Mam akaguna na kumgeukia Mama Esmile na kusema..

    “Mama ninaomba tena unisamehe, pia wasamehe wote waliotangulia, msamehe hata Mzee kwa makosa yake aliyotenda akiwa hai…”

    Mama Esmile akamkatisha maneno yale ya huzuni kwa kumwambia tayari amewasamehe wote waliomkosea ila ana hakika Mam hajamkosea, hivyo asiwe na shaka yoyote. Kwa majonzi makubwa Mam akasema huku akiwatazama kwa zamu yeye akiwa kitandani;

    “Samahani sana, nawaambia nyie kwa niaba ya jamii nzima, nitakayosema hapa nitakuwa nimeyasema wakati muafaka, kwanza ninaomba mnisamehe, pia nawaomba muwasamehe wote waliotangulia, mama umsamehe Mzee kwa makosa yake aliyotenda akiwa hai. Mama na Esmile, samahani sana, nimekaa na siri hii kwa muda mrefu sana, sasa sina muda tena na ninapaswa kukiri hadharani mbele yenu ili mnisamehe, japo najua itawaumiza sana…” alinyamaza kidogo kisha akaendelea

    “Kuna makosa mengine binadamu tunafanya kwa hiyari yetu, ila kuna mengine tunalazimika kuyatenda kutokana na historia ya nyuma ya mtu alichofanyiwa, huenda kilimkwaza ama kumuuumiza kabisa, ndio mana name leo naungama mbele yenu, kwani kuna mengi sana mema mmenitendea, kiasi siwezi kuwalipa hata nikiishi miaka 100 mingine...” sauti yake ilikuwa ikizidi kuwa dhaifu “Ninapoomba msamaha kwa kosa langu, sina mamlaka ya kuwalazimisha mnisamehe, ila nia yangu ya dhati ni kuwa nife nikiwa msafi, nife nikiwa na radhi yenu, radhi itakayosababisha hata Mola Mtukufu anipokee, ila mi mwenyewe nikitazama wema mlionifanyia na uovu niliowalipa, nakiri kabisa…

    …SIPASWI KUSAMEHEWA”

    Bado Mam alizidi kuwaweka njia panda Esmile na mama yake, mama akamsogelea karibu zaidi na kumuinamia huku akimuuliza ni kitu gani hasa kinachomsukuma kuomba radhi ambayo anaona kama haistahili kwa muda wote huo anaosema? Akajitahidi Mam kuongea

    “Mama na Esmile, samahani sana, nimekaa na siri hii kwa muda mrefu sana, sasa sina muda tena wa kuendelea kuificha, na ninapaswa kukiri hadharani mbele yenu ili mnisamehe, japo mi naona na ninarudia kuwa sipaswi kusamehewa,” Esmile akapitisha mkono wake kwenye kichwa cha Mam na kumtazama kwa jicho la matumaini, kisha Mam akaendelea







    “Najua nyote mnatambua kuwa mimi nilibakwa, lakini hamtambui ni nani alienibaka,” kwa shauku wote wakatikisa kichwa ili aendelee kuongea, nae kama aliejua kuwa watu wale wana shauku, akasema

    “Mzee Hanson ndie alinibaka na kuniambukiza ugonjwa huu wa Ukimwi, ambao sasa unaniua,” wote walishtuka na kujishika vichwa, Mam hakutoa nafasi ya kuwaza zaidi maneno aliyosema, bali akaendelea;

    “Naomba sasa hapa nisamehewe, maana huko kwingine nadhani nyinyi si wahusika sana, hapa panapofuatia ndio panawahusu nyinyi…” sasa akawatazama kwa zamu na kunyanyua mdomo huku chozi likionekana kuchungulia kwa mbali

    “Ni mimi huyuhuyu ndie niliemuua Mzee Hanson,” kama walioambiana, wakaguna na kushusha pumzi kwa nguvu, Mama yake akakaa chini

    Ukimya ukaingia na kuwashtua waliokuwepo nje, nao bila kuitwa wakaingia ndani kwa pamoja kama vile wameitwa, na kukuta kila mtu yupo kivyake, Esmile kasimama kaegamea ukuta, Mama yake kakaa chini na Mam yupo kitandani. Hali ilikuwa ni tafauti kabisa.

    Wakati huo muda wa kuona wagojwa ulikuwa umekwisha… hivyo nesi nae alikuwa ameingia wodini na kuwaeleza watu wote watoke nje ili taratibu zingine za kitabibu ziendelee.

    Walioingia ndani hawakujua nini kimetokea na hawakuwa na nafasi ya kuhoji kwa kuwa kengele ya ya kuwatoa nje ilikuwa imeshalia.

    Waliishia kumuaga tu na kuahidi kukutana kwenda kumuona siku ifuatayo, wote walimshika mkono kumuaga Mama yake na Baba yake Mam walimuaga pia na kuanza kutoka lakini kabla hawajapiga hatua Mam akawauliza Esmile na mama yake kama wamemsamehe.

    “Mama na Esmile, mmenisamehe jamani?” Aliwauliza Mam kwa sauti ya chini sana, sauti ya kukata tamaa

    “Mam kwanini usiseme tangu awali? Ona sasa matokeo yake…” alisema Mama Esmile kisha Esmile akadakia

    “Mama hupaswi kusema hivyo, hatuna muda tena wa kulaumu, tunalazimika tu kujibu swali lake alilotuuliza Mam na si kingine,” huku machozi nae yakimlenga, kwa huzuni mama Esmile akasema

    “Sawa Mam, mi nimekusamehe kutoka moyoni kwangu kabisa…”

    “Je wewe Esmile?” aliuliza Mam hali macho yamejaa ukungu wa machozi

    “Mam kwanza nakusifu kwa ushujaa wako, umekuwa ni zaidi ya mfano kwangu, kuwa ninaweza kuishi na mtu ambae amenikosea bila walio nje yangu kujua, nashukuru mno kwa somo lako Mam ambalo nasikitika kuwa umenifundisha bila kunipa habari kuwa ninasoma, zaidi ya yote nafurahi kukujulisha kuwa mimi nimekusamehe, kesho tutaongea zaidi Mam…” Uso wa Mam ukang’ara kwa tabasamu, akashukuru na kuwaaga kwa ahadi ya kuonana kesho yake.

    Hakika aliwaacha wote katika fadhaa kubwa, Naima na Layla aliwaambia siri nzito ambazo wote walikuwa wakizitafakari. Esmile na Mama yake nao walikuwa katika dimbwi zito la mawazo juu ya kile walichoelezwa na Mam.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kila mmoja alitaka kufahamu zaidi ilikuwaje Mam akabakwa na ilikuwaje akamuua Mzee Hanson wote walipania kwenda kumuona kesho kwa mazungumzo zaidi.

    Kila mmoja alikuwa na usiku mrefu sana kutokana na mawazo mengi juu ya yale waliyoyasikia, maana yalikuwa ni mapya kwao,

    Usiku ule pia ulikuwa ni usiku wa maumivu makali kwa Mam, hakuweza kuumaliza kama alivyo ahidi kwa Naima, saa mbili usiku hali yake ilibadilika na kuwa ni mbaya sana.

    Ilipofika saa nane usiku hali ikawa mbaya zaidi, madaktari na wauguzi waliokuwepo zamu walijitahidi sana kunusuru maisha yake lakini haikuwa hivyo kwani saa 11 alfajiri Mam aliaga dunia.

    Asubuhi ilipofika Esmile alikuwa wa kwanza kufika hospitali, lakini hakuruhusiwa kumuona mgonjwa kwa kuwa hakwenda na chochote na kwa utaratibu wa kawaida mida ya asubuhi vile wanakwenda watu wanaopeleka kifungua kinywa.

    Baadae watu wengine walifika Mama yake Mam alikuwa na chupa ya uji na vitafunwa. Wote walizuiliwa kuingia kwa maelezo kwamba mgonjwa anafanyiwa vipimo na daktari.

    Baadaye daktari akawaita Esmile na Baba yake Mam pembeni, akawaeleza ukweli wa kilichotokea, akawajulisha kwamba, Mam hayupo Duniani tena! Walichanganyikiwa ghafla japo hali waliyomuacha nayo usiku uliopita, haikushangaza kusikia jibu hilo.

    Wote wakapata habari za msiba na taratibu za kuutoa mwili zikaanza, yote yalifanyika na Esmile na watu wake waliongeza siku za kukaa Tanga ili kuhakikisha wanamaliza msiba wa mpendwa wao Mam.

    Walikaa Tanga kwa siku nne zaidi kisha wakarejea Dar. Walipewa pole kila sehemu kuanzia ofisini hadi mitaani. Majonzi yaliwatawala sana karibu wafanyakazi wote wa The Chambers, wakikumbukia siku ile moja ya furaha kule Upanga nyumbani kwa bosi wao.

    **********



    Siku hazigandi na mambo lazima yaendelee, mipngo ya harusi ya Layla na Esmile ilianza na kushika kasi lakini wakati huo wote si Leyla wala Naima aliyewahi kusema alichoambiwa na Mam, na wala Esmile na Mama yake nao hawakuwahi kusema walichoambiwa.

    Siku moja wakiwa kwenye kikao cha mwisho cha harusi, Naima alimvuta Esmile pembeni na kumwambia kuna ujumbe aliachiwa na Mam, Esmile alishtuka, Naima akamtoa shaka

    “Siku ile aliyotuita ndani mimi na Layla, akatuambia tumuombee msamaha kwani kuna kosa kubwa aliwafanyia na kibaya zaidi nyinyi hamjui na kinachomsikitisha ni wema mliomfanyia”

    “Alikuambia kosa lenyewe?”

    “Ndio aliniambia,”

    “Alisemaje?”

    “Ni yeye ndio alimuua Mzee Hanson kupitia Alfred, yaani alimpa kazi Alfred ya kumuua baada ya kubakwa kwa Mzee wako kwa sababu alimkataa kimapenzi na siku aliyombaka alimfuata shule kwa kuwa Mzee wako alikuwa akitoa sana misaada shule, wala hakumuhofia,” alinyamaza Naima

    “Ok! Kwa hiyo alikwenda huko na kumchukua mtoto wa watu na huenda alimwambia atampa lift tu,”

    “Inawezekana ilikuwa hivyo,”

    “Ok Naima nashukuru sana, sote mi na mama tumemsamehe kabisa,” walimaliza maongezi yao na kuagana kila mmoja akiendelea kushika hamsini zake.

    **********



    Siku moja kabla ya ndoa yao, Layla alimuita Esmile na kumpa ujumbe toka kwa Mam, ujumbe ni uleule wa Naima, ila huu wa Layla ulizidi kidogo, kuna maneno binafsi aliachiwa na Mam..

    “Aliniambia hajawahi kupenda, kama alivyokupenda wewe, na kamwe nisije kufanya kosa la kukuacha, kwani watu wenye mapenzi ya kweli na ya dhati kama wewe ni wachache mno chini ya jua,” Esmile akatikisa kichwa kusikitika. Hakuongeza neno lolote akaondoka.

    Aliporudi nyumbani wageni walikuwa ni wengi akamuita mama yake chumbani na kumpa ujumbe toka kwa Layla alioachiwa na Mam, mama yake akasikitika na kusema

    “Masikini Mam, baba yako hakumtendea haki kabisa mtoto wa watu, tena yeye akiwa anajijua kabisa kuwa ni muathirika, akambaka… hilo ni kosa la kwanza, kosa la pili kumbaka bila hata ya Condom, na ndio maana alikuwa hataki kabisa ukaribu wowote baina yako na Mam, alijua mambo yatakuwa wazi…”

    “Ah basi mama tuwasamehe wote, japo kisheria Mam nae ni muuaji, ila hata baba pia, cha kufanya kwa sasa ni kuwaombea wote kwa Mola awasamehe,”

    “Sawa mwanangu, vipi tayari umeongea na Sheikh?”

    “Ndio Mama nimeongea na ustadh Mnela ndio atafungisha ndoa hii,”

    “Haya mwanangu, nenda kapumzike,”

    Alipoingia ndani mwake hakulala, hilo ni suala ambalo alilitarajia, akampigia simu Layla na kuongea nae. Hata Layla alimwambia pia nae hana hata lepe la usingizi, anajisikia hofu na hajui ilipotoka.

    Wakapeana moyo kuwa jambo linalotarajiwa kufanyika kesho sio kifo bali ni tendo la furaha kwao na jamii nzima iliyo wazunguka.

    Layla sasa akapata usingizi isipokuwa Esmile yeye bado hali ilikuwa ni tete, hatimaye alfajiri kabisa ndio akapata usingizi baab kubwa na hata akamuota Mam nae yupo kwenye sherehe ile. Akashtuka na hakulala tena hadi jua lilipochomoza. Akatoka na kuungana na watu waliokuja kwenye shughuli.

    Ndoa ilifungwa kama ilivyopangwa na kufuatiwa na sherehe ndogo iliyohudhuriwa na watu takriban 100. Wazazi wa Mam nao walikuwepo kama wana familia na ndugu wa Esmile, wakishirikiana nao tangu mwanzo wa shughuli hadi mwisho wakiwa bega kwa bega, wakiwa wamefikia palepale Upanga.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hadi wakati huu, Esmile bado yupo na mkewe Layla wakiwa na mtoto mmoja aitwae Lulu, kampuni yake ya THE CHAMBERS ni jina kubwa nchini, kila apatapo muda hukaa na kukumbuka story ya Mam na mambo yake mengi katika siku walizofahamiana, zaidi pia alikumbuka kauli yake, kauli ambayo Esmile anaichukulia kama ni kauli ya mwisho mwisho anatafakari zaidi na chozi linamtoka pindi akifikia kuikumbuka kauli hiyo …



    ‘SIPASWI KUSAMEHEWA’



    Mwisho.


0 comments:

Post a Comment

Blog