Simulizi : Jeraha La Moyo
Sehemu Ya Nne (4)
Siku iliyofuata majira ya saa nne asubuhi. Jeni aliingia nyumbani kwa kina Cecy. Alimkuta Anita akiwa bize akiendelea na shuhuli zake. Akamsalimu kisha akapitiliza ndani ya nyumba hiyo. Moja kwa moja mpaka chumbani kwa Cecy. Alifungua mlango na kuzama ndani. Huko alimkuta Cecy akishusha mkono wake ulioshika simu yake ukitoka sikioni kwake akiwa amejilaza kitandani. Bilashaka alitoka kuongea na mtu kwenye simu.
“Karibu bi dada” Cecy aliongea hayo huku akijiinua pale kitandani. Akajivuta hadi ubavuni mwa kitanda na kukaa hapo. Jeni akamsalimu, Cecy akarudisha majibu. Akaenda kukaa kwenye stuli iliyokuwa ndani humo huku muda huo Cecy akijiinua pale kitandani kwaajili ya kwenda kujiswafi. Maana ndio anainuka muda huo kutoka usingizini baada ya kushtuliwa na simu yake iliyokuwa ikiita.
Dakika kadhaa akarudi akiwa tayari ameshajifanyia usafi kila sehemu ya mwili wake. Akaliendea kabati lake la nguo la kulifungua. Akachukua nguo ambayo itaipitisha siku hiyo kwa kuustiri mwili wake.
“Nilidhani nikifika huku utakuwa tayari ushamaliza kila kitu”Jeni aliongea hayo huku akiwa bize na simu yake.
Wakati Cecy anataka kumjibu Jeni. Sauti ya mama yake ilisikika kwa nje ikimuita. Akakaa kimya kusikiliza nini mama yake atasema. Anita alimuambia Cecy atoke nje akamalizie kazi alizoziacha yeye kuna pahali anataka kwenda muda huo. Cecy akajibu sawa.
Alipomaliza kuvaa na kujiona yupo sawa. Wakatoka nje ambapo Cecy aligundua mama yake alishaondoka. Akatafuta ni kazi gani hasa mama yake aliyoibakiza, lakini hakuona. Sebuleni palikuwa safi, nje palikuwa safi hata chumbani kwake pia palikuwa safi. Alipokagua kote huko na kukuta pako safi. Akarudi sebuleni na kwenda kukaa.
“Wewe! Si umeambiwa na mama umelizie kazi alizoziacha?” Jeni alimuliiza baada ya kuona Cecy amerudi kukaa ilhali alisikia akiambiwa na mama yake amalizie kazi.
“We nawe! Kwani humjui mama alivyo. Hapo alitaka nitoke nje tu baada ya kuona nimelala sana.... Embu kwanza niangalie mambo ya ‘breakfast’ naona tumbo lishaanza kulia ‘alarm’”. Cecy aliinuka pale alipokaa na kwenda jikoni. Dakika moja alirudi akiwa na chupa ya chai na bakuli kubwa. Akaviweka mezani na kuenda tena jikoni. Aliporudi alikuwa amebeba bakuli jengine na vikombe vya chai. Akaviweka mezani kisha akakaa.
“Unajua nini Jeni. Njoo kwanza tunywe chai then mambo mengine yataendelea” Cecy aliongea hayo huku akiandaa-andaa pale mezani. Jeni alikataa akidai huko atokako alishakunywa. Lakini Cecy akamuambia hawezi kunywa pekeake bila ya ‘saport’ yake. Tena aliondoka pale mezani na kurudi kukaa kwenye sofa.
“Haya mama twende” Jeni aliongea hayo huku akicheka. Cecy aliinuka na kurudi pale mezani akifuatiwa na Jeni. Walitumia dakika kumi kunywa chai kisha wakaenda pale kwenye masofa na kuweka kambi hapo.
“Cecy, fanya yakuisha basi, saa nane natakiwa niwe home unajua” Jeni aliongea hayo. Cecy akainuka na kuingia chumbani kwake. Alipotoka alikuwa amebeba ‘laptop’ mkononi kwake. Akaenda pale alipokaa Jeni na kukaa karibu yake. Akamkabidhi Jeni ‘Laptop’ na yeye akawa mtazamaji.
“Inabidi tu-‘connect’ na simu yako, ndio itakuwa rahisi zaidi” Jeni alisema. Cecy akachuku ‘USB’ na kuichomeka kwenye simu kisha na kwenye ‘Laptop’. Kisha hapo akatulia aone nini kitafuata.
“Aaaa nimekumbuka kitu. Kuna juisi niliitengeneza jana. Subiri nikaichukue tushushie” Cecy aliongea hayo na kunyanyuka.
Wakati analiendea friji dogo lililokuwa mahala hapo. Jeni alikuwa akiipekuwa simu ya Cecy kwenye ‘Laptop’. Alionekana kama kuna kitu anatafuta. Akaona amuulize Cecy baada ya kuhisi anaweza akazunguka sana kupekuwa halafu asifanikiwe kuona hicho anachokitaka. Haikujulikana ni kipi hasa wanachotaka kufanya muda huo. Baada ya kumuuliza, Cecy alimuambia aingie kwenye faili la ‘Whatsapp’.
Lakini muda huo, Jeni alishaingia kwenye faili la picha. Bahati mbaya akaziona picha ambazo Cecy amepiga na Rommy. Akazitazama moja baada ya nyengine mpaka alipozimaliza zote. Akaguna huku akitabasamu, kisha akasikitika.
“Kwahiyo Cecy. Umeamua umrudie Rommy?” Jeni alimuuliza huku akimtazama Cecy ambae muda huo alikuwa ameshafika hapo akimkabidhi glasi yenye shurubati ya embe. Cecy akamaizi kuwa Jeni alishaziona zile picha. Akatabasamu na yeye kisha akakaa.
“Kwani kuna ubaya?” Cecy aliuliza katika hali ya kutahariza.
“Yeah Cecy. Kwani wewe huuoni?”
“Hapana. Sioni kama kuna ubaya wowote. Kwanza yule alishawahi kuwa mpenzi wangu kabla hata ya Ramah. Sasa huo ubaya unatoka wapi?” Jeni alizidi kushangazwa na Cecy kwa hayo maamuzi aliyoyachukua.
“Kwahiyo Ramah hana nafasi tena?” Jeni alizidi kuhoji katika hali ya kutaharuki.
“Pengine labda! Kwasababu nimegundua hakuwa chaguo langu na niliishi nae tu kwasababu fulani.” Jeni alitaharuki zaidi mpaka kupelekea kuziba kinywa kwa vigana vyake huku akimtolea macho Cecy.
“Haki vile sitaki kuamini kama umeingia tena mikononi mwa yule mshenz...”
“Wee! Tena koma kumuita Rommy mshenzi. Juzi nilikuwa nakutazama tu unavyoongea pumba zako. Mwenye maamuzi ya mwisho ni mimi na si mtu mwengine. Kwasababu mimi ndie ninaependa. Achana na hizi mambo, ukiendelea nazo utanifanya nimchukie Ramah bila sababu za msingi. Tuendelee na kile kilichotuweka hapa na si vinginevyo” Cecy aliwaka kwa jazba kiasi ambacho kilimuacha mdomo wazi Jeni.
“Nitakutafuta baadae tuongee, nahisi muda huu haupo sawa...”
“Labda hiyo baadae unitafute kwa mengine lakini sio haya. Na kama pia hutaki kunifanyia hii ishu, acha nitatafuta mwengine wa kunifanyia” Cecy aliongea kwa kisirani. Jeni akawa mpole na kufanya kile walichokuwa wanataka kufanya.
Muda wote Jeni alikuwa mnyonge baada ya kuwakiwa na rafiki yake kitendo ambacho hakikuwahi kutokea hata mara moja. Pamoja na yote hayo. Alijiahidi kumuweke chini Cecy ili walizungumze hilo na ikiwezekana amkumbushe yale aliyofanyiwa na Rommy miaka nane iliyopita walipokuwa darasa la saba. Dakika arobaini na tano kazi waliyokuwa wakiifanya iliisha kisha Jeni akamuaga Cecy kuwa anaelekea kwao muda huo.
“Jeni wewe nenda tu, tutakutana baadae ama kesho. Leo hata sikutoi nimechoka sana.” Cecy aliongea hayo huku akiipokea ‘Laptop’ kutoka kwa Jeni. Jeni akajibu sawa na kuufuata mlango kwaajili ya kutoka. Akageuka kule alipo Cecy.
“Cecy...?” Jeni aliita. Cecy alipogeuka kule alipo, akaendelea. “Usiusahau uwanamaji kwa hila za nahodha. Utaangamia majini ungali kuishi watamani” Jeni alionge hayo. Cecy akacheka kicheko kikubwa muda huu Jeni akiwa ameshapotea mahala hapo.
“Nenda huko na maneno yako ya wazee. Na wewe pilipili usoila yakuwashia nini?. Eeee hata mimi nayaweza hayo maneno ya wazee wenu” Cecy aliongea kwa kejeli akipaza sauti ili maneno yake yamfikie Jeni.
Yakamfikia!.
* *
Majira ya jioni, maeneo ya Mkwakani kwenye ‘Cafe’ moja iliyokuwa maeneo hayo. Alionekana Ramah akiwa amekaa mahala hapo huku kila mara akiangalia saa yake ya mkononi aliyoivaa. Alionekana kuwa na miadi na mtu ambae alikuwa akimsubiri muda huo. Dakika nne mbele, Cecy aliingia mahala hapo na moja kwa moja akaenda kukaa pale alipokuwa amekaa Ramah. Ramah alimtazama kwa udadisi na kugundua Cecy hakuwa sawa. Ikabidi amuulize ni kipi kimtatizacho?
“Sikutaka kuwa mahala hapa muda huu, ila imenibidi tu” Cecy alijibu kwa dharau hafifu. Ramah akaguna na kuzidi kumtazama usoni. Akavuta kiti na kuisogelea meza zaidi.
“Unajua Cecy niliona mabadiliko fulani kutoka kwako tangu juzi. Na kila kukicha ndio yanazidi hari yake. Kwani Cecy unatatizo gani hasa? Embu nieleze leo.”
“Kwanza sijui ni mabadiliko gani hayo uliyoyaona kwangu. Pili sijui ni kueleze kipi wakati mwenyewe ushayaona mabadiliko kama usemavyo. Sina cha kukueleza eti” Cecy alijibu hivyo. Ramah akamtazama kwa wasiwasi. Akataka kusema kitu lakini akaghairisha. Akaendelea kumtazama usoni.
“Hee! Mbona unanitazama kama sanamu la maonyesho wewe?” Cecy alimuuliza kwa jeuri. Ramah akataka kujibu lakini akashindwa baada ya kuhisi akipandwa na hasira kutokana na majibu ya Cecy. Akataka kuongea kitu ila alikatishwa na simu ya Cecy iliyokuwa ikiita. Cecy akaitazama simu yake, akatabasamu, kisha akaipokea.
“Nipo Mkwakwani huku...” Akaongea baada ya kusikiliza kwa dakika moja. “Ok” Akamaliza kisha akashusha simu baada ya kukatwa upande wa pili. Akamtazama Ramah bila tabasamu wala kicheko.
“Nadhani nilikuambia mwanzo kuwa sikupendezwa kuwa mahala hapa, ila ilinibidi tu kwasababu ni wewe ndie ambae umeniita. Pamoja na kukupa heshima hiyo lakini naona inazidi kukupa kiburi cha kuniuliza maswali ambayo hayana kichwa wala miguu. Endelea kukaa mwenyewe hapa uzidi kuwashangaa wenye magari yao wanavyopita hapo barabarani. Au kama utakuwa na mtu mwengine utakae muita na akaja hapa akaziba nafasi yangu, pia unaweza muita mkajumuika pamoja. Acha mimi nikuache” Cecy aliongea hayo kisha akabeba mkoba wake mezani. Akainuka na kuanza kuondoka mahala hapo.
“Cecy una nini wewe? Wapi unaenda sasa?” Ramah alimuuliza huku nae akiinuka pale alipokaa. Lakini asifanye jitihada zozote za kumfuata.
“Naenda kwa wanaojua kupenda” Cecy alijibu kwa sauti kidogo kwasababu alikuwa mbali. Kisha akapotelea kwenye kona.
Ramah akabaki mdomo wazi asielewe ni nini kimemkuta Cecy. Amesema anaenda kwa wanaojua kupenda ama ni kutenda, ama ni vipi labda? Mbona sijamuelewa vyema? Ramah alijiuliza huku akiitazama ile njia aliyopotelea Cecy. Anamapepo huyu! Aliendelea kuwaza. Taratibu kabisa alikaa kinyonge kwenye kiti akiwa bado anatazama kule nje alipopotelea Cecy. Alitabasamu huku akijipa matumaini huenda Cecy kwa kipindi hicho hayupo sawa.
Lakini ni nini kinachomfanya asiwe sawa? Ndio swali lililokuwa likimtatiza.
Cecy alipotoka pale alipomuacha Ramah. Moja kwa moja akafika Hostel. Akaenda kukaa kwenye uzio mfupi ulioizunguka bustani ya Uhuru Park. Kila mara alikuwa akitazama sehemu zote mpaka pale alipoona gari alilozoea kumuona nalo Rommy likisogea mahala pale. Akatabasamu na kuinuka. Kisha akaanza kulifuata baada ya gari lile kusimama pembeni kidogo ya bustani ‘Garden’ ile. Mlango wa nyuma wa gari lile ukafunguliwa na yeye akazama ndani.
Kwenye siti za nyuma za gari lile alikuwapo Rommy pekee. Huku siti za mbele upande wa dereva akiwapo Paskali na upande mwengine akiwapo Assu. Cecy aliwasalimia wakina Paskali nao wakaitikia salamu yake. Kisha akamgeukia Rommy. Mara hii hakuwa na hofu tena maana alishaambiwa na Rommy kuwa watu hao ni walinzi wake. Na akapewa uhuru kabisa wa kufanya chochote, lolote hata wakiwa karibu na watu hao. Hata muda huo hakuona haya wala soni kumpiga busu la mdomo Rommy.
“Umpendeza sana mumy, ulikuwa wapi kwanii?” Rommy alimuuliza hayo baada ya kupatikana utulivu. Cecy akajibu kuwa alikuwa yupo maeneo hayo hayo na rafiki yake ambae walikutaniana Mkwakwani kwenye mgahawa mmoja uliokuwa eneo lile. Rommy akamuuliza tena kwamba huyo rafiki yake ni wakiume ama wakike? Nae akajibu ni wakike.
“Sasa umemuacha wapi?” Rommy alimuuliza. Akajibu kuwa ameendelea na safari zake, kwasababu hata yeye alikuwa na miadi na mtu mwengine.
“Ok. Leo nataka nikupeleke ukapaone ninapoishi. Sijui utapendezwa na hili?” Rommy aliuliza kimtego. Lakini Cecy alilifurahia jambo lile na kujibu haraka kuwa yupo tayari hata muda huo. Rommy akamuambia Paskali waelekee huko. Paskali akatii na kuwasha gari.
Wakiwa wanaendelea na maongezi yao ambayo walikuwa ni wao wenyewe wawili tu. Simu ya Rommy ikaingia ujumbe kutoka kwa Paskali. ‘Huyu Manzi unampeleka home. Je na yule wa kule hom utamuweka wapi muda huo?’ Ujumbe wa Paskali ulisomeka hivyo akimaanisha Cecy atamficha vipi ilhali kule nyumbani kuna Siwema. ‘Nitajua nitacheza vipi. We mwenyew si unaniaminia niwapo uwanjan huw sifanyi makosa’ Rommy akajibu hivyo na Paskali alipousoma ujumbe wake. Akatabasamu na kuhamisha mawazo yeke kwenye usukani.
Upande wa Ramah mambo hayakuwa mambo kabisa. Mpaka muda huo hakuwa akiamini kama ni kweli Cecy ametoweka mahala pale kwa kiburi. Akajaribu kumpigia simu, lakini simu ikawa inakatwa kila ikiita. “Duh! Hata kama alishawahi kunifanyia dharau lakini hii ya leo kubwa aisee” Ramah aliongea hayo huku akiipiga tena namba ya Cecy. Mara hii akamaizi amewekwa kwenye ‘blacklist’.
Alibaki mdomo wazi huku akiitazama namba ya Cecy ikimalizia kukata yenyewe. “Yani Cecy umefikia hatua ya kuiweka namba yangu kwenye orodha nyeusi?” Alijisemeza hayo huku akiitazama simu yake. Akajipa moyo kwa kutabasamu huku akiwaza pengine Cecy yupo kwenye utani. Lakini huu ni utani gani unaolekea kwenye ukweli kabisa? Hapana kwa kweli, Cecy hakufikia hatua ya kunitania kiasi hiki. Ipo namna hapa.
Aliinuka pale alipokuwa amekaa. Akazivuka meza zilizokuwa mbele yake na kupotelea nje. Huko akauendea usafiri wake uliomfikisha mahala pale na kuupanda. Mdogo mdogo akaanza kuondoka mahala hapo huku kichwani akiwa na mawazo mengi sana juu ya Cecy.
Majira haya walikuwa ndio wanaingia yalipo makazi yao. Gari ikaegesha pembeni na wote wakashuka. Lakini kabla ya kufika hapo, Rommy alishamtumia ujumbe Paskali ya kwamba atangulie ndani akamuangalie Siwema yupo wapi ili ajue afanye nini. Baada ya kufika tu, Paskali akawa wa kwanza kuingia ndani huku Rommy akitumia muda huo kumuonyesha mazingira ya nyumba hiyo Cecy.
“Hii nyumba ni ya kwako ama?” Cecy alimuuliza Rommy akiwa bado anaonyeshwa mazingira ya nyumba hiyo.
“Yeah! Ni milki yangu” Rommy alijibu kwa fahari akitegemea kumteka zaidi Cecy.
“Jamaani! Rommy unajua tayari maisha unayo. Mi nataka ukimaliza kusoma tu unioe. Sitaki mapenzi yetu yaishie hapa tu” Maskini Cecy hakujua kama kijana huyo amekubuhu kwa ulaghai. Nyumba hiyo ilikuwa ni ya kwake ndio. Lakini hakuweza kumaizi ni lipi hasa limepangwa na kijana huyo juu yake. Rommy akacheka sana mpaka Cecy akashangaa. Akahoji ni kwanini amecheka baada ya yeye kuongea hayo.
“Unajua nini Cecy. Nimeamini muda mwengine mawazo yanaweza kulandana baina ya watu wawili, hasa hasa wale wenye kufanana hisia. Hata mimi niliwaza kukuambia hayo lakini nikaona ni mapema sana. Nikahisi labda huenda ukanihisi vibaya ama vipi. Lakini ulipoyatamka hayo ya kuoana nikawa sina budi kufurahi tu...” Akamtazama usoni Cecy huku akitabasamu. “Sio lazima mpaka nimalize kusoma ndipo nikuoe. Mbona hata sasa naweza fanya hivyo. Ila acha kwanza nirudi tena Nairobi nikaongee na baba kuhusu hilo. Kisha mambo mengine yatafuata”
Cecy alifungua kinywa kwa taharuki huku akitabasamu baada ya kusikia maneno hayo. Mbio mbio alikwenda kumkumbatia Rommy kwa furaha. Alikuwa na furaha isiyo na kifani baada ya kuhisi kwamba anapendwa sana. Akamuahidi kumpenda, akamuahidi kutulia, mpaka akamuahidi visivyo haidika chanzo kikiwa ni ile furaha aliyokuwa nayo.
Simu ya Rommy iliingia ujumbe kutoka kwa Paskali aliemjulisha ya kuwa, Siwema muda huo alikuwa chumbani kwake amelala. Rommy akamtaka Cecy waingie ndani ya nyumba hiyo. Wakaongozana taratibu mpaka sebuleni. Cecilia akabaki kuyashangaa mandhari ya sehemu hiyo. Akatembeza macho yake kila pahali huku akiwa na tabasamu. Sehemu ambayo baba yake aliuliwa na mzazi wa Rommy kisa mama yake. Hata hivyo hakuwa akifahamu chochote, na si yeye tu, hata Rommy hakuwa akifahamu lolote.
Shauku ya kuishi ndani ya nyumba hiyo ama pengine popote pafananapo na hapo ikamjaa. Akatamani hata muda huo awe mke halali wa Rommy. Muda wote Rommy alikuwa akimtazama vile anavyoshangaa mazingira ya hapo. Ghafla tu Cecy alipiga siyahi kubwa baada ya furaha kumzidia. Alikatishwa na Rommy kwa kuambiwa ndani ya nyumba hiyo kuna mgonjwa. Cecy aligwaya aliposikia hayo huku akiziba kinywa chake kwa viganja vyake.
“Nani mgonjwa?” Akauliza kwa sauti ndogo.
“Twende huku ukamuone” Rommy alisema kisha akamshika mkono kumuongoza kilipo chumba chake.
Akafungua mlango na kumtaka Cecy atangulie ndani. Cecy akazama ndani huku akiwa na hofu kiasi. Lakini ikawa tofauti na vile alivyotarajia yeye kukuta mtu akiwa kitandani akiwa hajiwezi. Alipokelewa na kitanda kikubwa kilichotandikwa vyema. Chumba kikubwa kilicho safi kabisa kilichoyavutia macho yake. Hapakuwa na vitu vingi zaidi ya kabati kubwa la nguo na meza ndogo ya kioo iliyoweka baadhi ya vitu vidogo vidogo.
Pamoja na kutokuwa na vitu vingi, lakini chumba kilionekana cha thamani kutokana na vitu ghali vilivyoweka ndani humo kwa mpangilio mzuri. Rommy akamkaribisha Cecy kitandani. Lakini Cecy akajifanya amenuna. Rommy akamuuliza kwanini amenuna ghafla?
“Kwani uniongopee?” Cecy alimuuliza kwa deko. Rommy alitabasamu na kumfuata pale aliposimama. Akapitisha mikono yake kwenye kiuno bambataa cha mnyange huyo na kumvutia kwake.
“Cecy, kitanda changu kibovu kile, nimekuita wewe fundi wangu uje unitengenezee walafu usiku wa leo nipate kulala usingizi mororo” Rommy aliongea hayo akiwa anamtazama usoni. Cecy akaona aibu na kutazama chini kisha kichwa chake akakiegemeza kwenye kifua cha Rommy.
“Natumai leo tutafungua ukurasa wa mapenzi yetu rasmi huku kitanda hiki kikiwa shahidi wa hilo” Rommy alizidi kuchombeza. Cecy akiwa bado ameegemeza kichwa chake kifuani kwa Rommy huku sura yake akiangaliza chini. Alimuambia Rommy kuwa haitowezekana kwa siku hiyo kwasababu alikuwa katika siku zake.
“Nimekuelewa mpenzi, lakini naomba tukalale tu hata kwa dakika tano ili siku nyengine utakapokuja kulalia kitanda hiki usiwe mgeni nacho” Rommy alisema kisha akamtoa Cecy kifuani kwake. Akamvuta taratibu mpaka kitandani. Akamlaza kama mtoto alazwapo na mamae kisha na yeye akafuatia.
Pamoja na kuwa alishajifanya kumuelewa Cecy alipomuambia yupo katika siku zake. Lakini alianza uchokozi ambao Cecy alijua ni wa kawaida. Lakini upande wa Rommy haukuwa kama vile alivyodhani yeye. Rommy alikuwa akiuchezea mwili wa Cecy kila pahali alipojiskia. Kichwani, shingoni, kifuani mpaka kiunoni kiasi ambacho alimlegeza mtoto wa watu. Akawa hajiwezi kabisa.
Yote hiyo ilikuwa ni janja ya kutaka kuthibitisha maneno ya Cecy. Taratibu kabisa akiwa bado hajaacha kucheza na mwili wa Cecy. Alipenyeza mkono wa kushoto mpaka kwenye maungo ya Cecy ili kuthibitisha aliyoambiwa. Ghafla Cecy alizinduka huko alipokuwa na kurejewa na fahamu zake za kawaida. Akauzuia mkono wa Rommy usiendelee mbele zaidi na kuurusha pembeni. Akajiweka sawa na kukaa kitandani akiwa amenuna.
“Inamana hukuniamini nilipokuambia nipo katika siku?” Cecy alihoji kwa hasira huku akimtaza Rommy akiwa na uso mkavu usio na tabasamu. Rommy akajua ameyatibua tayari. Alilazimika awe mpole ili amani irejee. Nitakuomba msamaha hiyo basi tu. Lakini wala sikupaswa. Rommy aliwaza hayo akiwa na yeye anamtazama.
“No Cecy sio kwamba sikukuamini. Bali nimejikuta tu nikifika huko lakini haikuwa dhumuni langu wala kusudio. Akili yangu haikuwa hapa bali nakiri kwa kukuomba msamaha kwamba unisamehe” Rommy alibadili sauti, sio sauti pekee mpaka sura pia aliiweka kimaigizo zaidi. Cecy alimtazama kwa kitambo kisha akatabasamu.
“Uwe muelewa siku nyengine. Usipandishe mashetani ikiwa hakuna mganga karibu” Cecy aliongea hayo huku akijisogeza karibu na Rommy.
Siku yake ilibadilika ghafla mithili ya mvua kipindi cha kiangazi. Aliiona siku hiyo ikiwa ni chungu sana mithili ya shubiri, japokuwa ilianza kwa utamu mithili ya asali. Alihisi kuchanganyikiwa pasi na mfano kila akikumbuka aliyofanyiwa na mtu ambae yeye alimuamini kwa kiasi kikubwa na hakutegemea wala kuwaza hata siku moja kwamba atakuja kumfanyia dharau kama alizomfanyia siku hiyo.
Majira hayo ya saa moja jioni alikuwa amejilaza kitandani kwake Ramah kimya mfano wa mgonjwa wa homa. Kichwa kilikuwa kizito kwa kumfikiria Cecy hasa hasa kwa kitendo alichomfanyia siku hiyo. Hata mamae alipomuuliza ni kwanini amerudi nyumbani muda huo ilhali sio kawaida yake, alimjibu kwamba hakuwa akijisiia vyema siku hiyo na alihitaji kupumzika kwanza.
Kwa huruma ya mzazi wake alimtengea uji ambao aliupunguza kidogo alipokuwa akitaka kusonga ugali. Alimpoozea vyema na kumpelekea chumbani kwake. Ramah aliekuwa amejikunyata kitandani kama kitoto kidogo aliamka baada ya kusikia sauti ya mama yake akimuita. Akamuwekea ule uji mezani na kumuambia anywe kisha hapo watafanya mipango mengine ya dawa. Kisha hapo akatoka nje kuendelea na shuhuli nyengine.
Pengine asingekuwa katika hali hiyo kama asingetumiwa ujumbe ulioumiza moyo wake kutoka kwa Cecy. Kwa mara nyengine aliinua simu yake na kuingia upande wa jumbe. Akautafuta ujumbe ule na kuusoma tena utadhani kama hakuuelewa ama alitaka kuthibitisha vizuri kama umetumwa na Cecy. ‘Sikilza Rafa nikuambie, naomba kwa leo usinisumbue maana nip katika starhe ya nafsi. Waweza nitafute kesho na sio leo. Then mama akikpigia simu akikuuliz kuhus mm mwambie nip na wewe. Nakutkia usku mwema mpendwa’. Akaiweka simu pembeni baada ya kumaliza kuusoma tena. Kisha akajifunika shuka na kulala tena.
“Sasa Cecy si unaelekea home kwenu saa hii? maana ishafika saa mbili hivi sasa”
“Muda bado bana, home mpaka saa tatu ama saa nne hivi” Cecy aliongea hayo huku akichezea simu ya Rommy.
“Hivi unakijua unachoongea ama? We si uliniambia mwisho wa kuwa nje ya nyumba yenu ni saa moja usiku. Sasa hiyo saa nne huoni kama itakuwa ni hatari?” Rommy aliongea hayo huku akimtazama Cecy kwa mshangao. Cecy aliacha kuchezea simu na kumuangalia kisha akatabasamu.
“Mpaka nimeongea haya ujue kipo cha kujitetea. Kwahiyo usihofu mpenzi” Rommy akashusha pumzi akiwa bado anamtazama. Dah muda wote huo tulioupoteza kama tungekuwa kwenye mchezo ingekuwa raha raha yani. Ramah aliwaza hayo.
“Ok. Tuelekee mezani tukale kwanza. Kisha tutarudi tena” Rommy aliongea. Wakanyanyuka na kutoka chumbani humo.
Walifika mezani ambapo waliwakuta wakina Paskali wakiwa tayari kwa kuanza kula. Walikaa na wao tayari kwa kula. Mara hii Siwema alipokuwa akiandaa chakula, macho yake yaligongana na ya Cecy. Wakatazamana kwa dharau hasa hasa Cecy aliebenjua na midomo pembeni na kuifanya midomo ile ifananiane na nguo iliyotonoka lastiki. Kisha akamtazama Rommy usoni na kukuta kijana huyo akiwa bize na kuangalia chakula hicho.
Rommy alishamaizi kilichotokea kwa mabanati hao na wala yeye hakujishuhulisha nao hata kidogo. Siwema akaondoka mahala hapo huku akipigwa jicho na Cecy mpaka pale alipopotea kwenye upeo wa macho yake. Akarudisha macho mbele na kukuta kila mmoja akiwa bize na chakula.
Siku hiyo mezani palikuwa kimya. Hakuna ambae alimuongelesha mwenzake, haikujulikana ni kwanini imekuwa hivyo. Hata pale Rommy alipomaliza kula, aliwaaga wenzake na kuingia chumbani kwake. Cecy nae akaacha kula na kumfuata Rommy kule kule ndani. Alipofika alikuta chumba kitupu. Lakini alimaizi kuwa yupo chooni anaoga kutokana na sauti za maji zilizosikika yakimwagika. Akakaa kitandani na kutulia.
Dakika kadhaa Rommy akatoka kule chooni akiwa anajifuta maji na taulo. Alifika mpaka pale alipokuwa Cecy na kukaa karibu yake. Cecy muda huo alikuwa amenuna na isijulikane ni kipi hasa kilichomnunisha. Rommy alimuita jina lake na kumuuliza kwanini amekuwa katika hali hiyo.
“Yule mwanamke kule ni nani?” Cecy aliuliza kwa kisirani.
“Alaa! Yule si mfanyakazi. Ama hujaona pale akituandalia chakula?” Rommy alijibu kwa mtindo wa kuuliza.
“Sawa. Lakini mbona ameniangalia kwa jicho la dharau?”
“Sio yeye tu. Hata wewe pia ulimuangalia. Labda mimi ndio nikuulize wewe kwanini umemuangalia ama mmeangaliana vile” Rommy alijibu kwa upole kiasi ambacho Cecy alikosa cha kusema tena.
“Nirudishe nyumbani” Baada ya kimya kingi, akasema hayo. Rommy akaangalia saa na kukuta ni saa tatu kasoro.
“Mbona mapema hivyo?” Rommy akamuuliza. Cecy akajibu kuwa Mama yake amemtafuta sana kwenye simu na mara ya mwisho alipompigia alimjibu kuwa yupo njiani anaelekea nyumbani. Rommy akajibu sawa kisha akavaa nguo. Baada ya hapo wakatoka mpaka sebuleni. Rommy akawaambia wakina Paskali kuwa anamsindikiza Cecy nyumbani kwao kisha wakatoka nje sehemu ambayo kuliegeshwa magari. Akazama kwenye gari moja Cecy nae akaingia. Kisha Rommy akalirudisha nyuma taratibu mpaka pale alipopata nafasi nzuri ya kutoka. Akatoka nje baada ya geti kufunguliwa.
Dakika kumi na nane wakafika karibu na nyumba anayoishi Cecy. Leo hii Cecy alimuambia Rommy wasifike kabisa nyumbani kwao maana mama yake kama atamuona anashuka kwenye gari lazima atamuhoji. Rommy alifuata kile alichoambiwa. Wakaagana kisha Cecy akashuka kwenye gari na kuanza kuifuata njia ya nyumbani kwao.
Wakati Cecy anaelekea nyumbani kwao. Kuna gari jengine lilifika pale aliposimamisha gari Rommy. Paskali akashuka kwenye lile gari lililofika mahala hapo punde tu na kuliendea lile gari alilokuwamo Rommy, kisha akazama ndani, mbele upande wa kushoto.
“Mbona leo manzi umemfikisha hapa?” Paskali alihoji huku akijiweka vyema kitini.
“Ndivyo alivyotaka na mimi sina muda wa kuhoji sana” Rommy aliongea hayo huku akianza kuliondoa gari mahala hapo. Gari likatembea huku nyuma likifuatiwa na lile jengine lililofika hapo punde tu.
“Hivi Cecy...” Cecy aliekuwa akitembea kuufuata mlango wa kuingilia ndani kwao, alishtuliwa na sauti ya mamae na kugeukia kule alipo. “Huu mchezo uliouanzisha wa kurudi nyumbani muda unaotaka bila taarifa yoyote umeuanza lini?” Mama yake alimuuliza hayo wakati akitoka kwenye chumba fulani walichotumia kama jiko. Cecy akawa kimya.
“Na tena nakupigia simu hupokei. Yani hupokei simu zangu kwavile umekuwa sasa waoga chooni” Mama Cecy alizidi kuwaka. Cecy akaona ajitetee maana kimya kingi ni ishara ya kukubali hayo.
“Mama hapana. Simu sikuwa nayo karibu na ndio maana sikuweza kupokea. Ila nisamehe mama”
“Unatoka wapi kwanza?” Mama yake alimuuliza akiwa bado yupo katika hali ya hasira. Nae akajibu alikuwa na Ramah. Mama yake alimtazama kwa ghadhabu kiasi ambacho Cecy alihisi huenda Ramah ameshaharibu kila kitu. Hofu ikazaliwa nafsini kwake baada ya kuhisi hivyo.
“Mbona hata yeye hakuwa akipokea simu kila nilivyompigia? Ama mlipanga kutopokea simu zangu?” Cecy alishusha pumzi za hofu baada ya kumaizi kumbe hata Ramah hakupokea simu. ‘Chap chap’ akatafuta uongo mwengine ambao utamuacha mama yake asiwe tena na maswali juu yake.
“Kwa kweli mama kwa upande wake sijui. Ila leo sikumuona na simu, pia sijabahatika kumuhoji kuhusu hilo” Mama Cecy kwa jibu hilo hakuwa na cha kuhoji tena.
“Nenda ndani kisha urudi hapa uje kumalizia kupika hizi mboga” Mama yake alimuambia hivyo na yeye akapotelea ndani.
* *
Majira haya ya saa tatu asubuhi ikiwa ni siku mpya kabisa ambayo haikuwahi kujiri ndani ya ulimwengu zaidi ya ufanano wa jina tu. Jumatano. Ndio, ilifanana jina na Jumatano zilizopita lakini ilikuwa tofauti kwa matukio na haikuwa na mfanano wowote ulionasibika na hizo zilizopita.
Majira hayo Ramah alikuwa akiingizana kwenye viunga vya nyumba ya kina Cecy. Alimkuta mama Cecy kwenye uga wa nyumba hiyo akiwa amejipumzisha chini ya mti uliokuwa ukitoa ladha safi ya hewa na upepo mororo na kumfanya hata kiusingizi kumyemelea. Ramah alifika mahala pale alipoweka makazi mama Cecy na kumsalimu. Mama Cecy aliitikia kwa bashasha kama kawaida yake huku akijiinua kwenye mkeka ambapo alikuwa amejilaza.
“Nyumbani hawajambo baba?”
“Hawajambo wote, twamshukuru muumba kwa kutuafu na kutuamsha tukiwa na siha njema” Ramah alijibu kisha akauliza uwepo wa Cecy nyumbani hapo. Mama Cecy akamjibu kuwa Cecy yupo, amtazame sebuleni maana mara ya mwisho alimuacha mahala huko. Ramah akashukuru na kuanza kuondoka mahala hapo. Lakini kabla hajafika mbali, alishtuliwa na sauti ya mama Cecy, akageuka nyuma na kumtazama mama huyo.
“Hivi jana mlikuwa wapi? Niliwapigia simu mkawa nyote hampatikani. Aaaa hampokei simu zenu?”Mama Cecy alihoji. Ramah ukimya ukachukua nafasi upande wake. Akaukumbuka ule ujumbe aliotumiwa na Cecy siku iliyopita kuwa atakapopigiwa simu na mamae kumuulizia yeye. Basi ajibu yupamoja nae. Inamaana Cecy anatumia kivuli changu kufanya mambo yake? Ramah alijiuliza.
Lakini akawaza kumtetea Cecy kisha hapo akamuhoji kuhusiana na hilo. Akaweka tabasamu kisha akajibu kuwa alikuwa mbali na simu hivyo hakuweza kusikia pindi ilipoita. Mfanano wa ule aliojibu Cecy siku iliyopita pindi alipoulizwa swali hilo na mamae. Mama hakutaka kumuhoji sana badala yake akamruhusu aende. Ramah akaufikia mlango wa kuingilia Sebuleni kisha akaufungua na kuzama ndani.
“Nilidhani utanichoma. Ila nashukuru kwa kunitetea” Alipoingia mahala hapo, alipokelewa na sauti hiyo iliyotoka kwa Cecy. Ramah hakujibu wala kusema chochote, alibaki kimya akiwa anamtazama Cecy aliekuwa akicheza na simu yake. Baada ya kusimama kwa muda mrefu, alienda kukaa akiwa bado anamtazama Cecy.
“Yani hiyo tabia yako ya kunitazama sana hata sijui umeitoa wapi. Utafikiri ndio unanijua sasa bwana” Cecy aliongea hayo kisha akainuka na kuingia chumbani kwake. Dakika moja akatoka na kwenda kukaa pale alipokuwa amekaa mwanzo.
“Enhee! Niambie, unataka nini?” Cecy alimuuliza kwa jeuri akiwa macho makavu bila kupepesa kope.
“Sina chochote kikubwa nitakacho kutoka kwako...... Zaidi nahitaji unieleze kwanini umebadilika sana siku mbili hizi?” Ramah aliongea kwa upole mithili ya kitoto kiombae msamaha kwa mamae kwa kosa kilichotenda.
“Nimebadilika? Nimekuweje? Mweusi, au mweupe zaidi? Mfupi au mrefu zaidi?...” Cecy aliongea hayo kwa kejeli huku akimtazama Ramah usoni. “Nitakutafuta baadae” Akainuka pale kuufuata mlango wa chumba chake. Alipoufikia, aliusukuma kwa ndani na wala asiingie. Badala yake aligeuka kule alipo Ramah na kukuta kijana huyo akiwa anamtazama kwa mshangao.
“Zingatia niliyokuambia. Usinitafute, nitakutafuta mimi” aliongea hayo kisha akazama ndani. Mlango ukafungwa na kimya kikafuata.
Kinywa cha Ramah kilikuwa nusu kufumba, nusu wazi. Alikuwa akiutazama mlango wa chumba cha Cecy utafikiri umechangia kumuondosha Cecy mahala hapo. Akarudisha macho yake taratibu mpaka pale alipokuwa amekaa binti huyo mwanzo. “Ana nini lakini huyu?” Alijiuliza. Akataka kuinuka, miguu ikamsaliti kusimama. Akatulia pale pale.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Aagrh..” Akapiga kite cha hasira kwa kitendo cha kushindwa kuinuka. Pengine miguu yake haikuwa bado ikiamini kitendo alichokifanya Cecy na ilihitaji uthibitisho wa kina. Dakika nne zikapita Ramah akiwa bado mahala hapo. Akasimama baada ya kuhisi miguu yake kupata nguvu mpya. Akatoka kinyonge ndani humo mpaka nje akiwa anatembea kichwa amekiinamisha chini.
“Baba mbona mapema hivi?” Ramah alipepesuka kwa mshtuko baada ya kugutushwa kwenye lindi la mawazo na Mama Cecy. Alishtuka haswaa si mas'hara pindi sauti ya Mama Cecy ilipogota kwenye ngoma za masikio yake.
“Aaaa! Hapana... Hakuna, aliniambia.. Alisema, nimepita tu kumjulia hali, naelekea hapo mbele, nimemuacha ndani huko” Ramah alibabaika kuongea kama mtu aliefumaniwa na mke wa mtu. Mama Cecy hakutaka kuhoji sana, akamruhusu aende kisha yeye akajilaza vyema pale mkekani.
Kichwa kilimuuma ghafla. Miguu aliihisi ikizidiwa uzito na mwili. Alihisi kushindwa kutembea. Hata hivyo alijikaza vivo hivyo walau afike nyumbani kwao. Napaswa kuwa jasiri, huenda akawa ananitega aone msimamo wangu juu yake. Ramah alijiliwaza kwa hayo. Alijilazimisha kutabasamu ili walau ajizidishie imani yake ya kwamba. Pengine Cecy anamtega.
Walau miguu ikapata nguvu mpya. Lakini kichwa ni kama alikianzishia ugonjwa wa ghafla. Maumivu ya kichwa bado aliyahisi. Alipita duka la dawa na kununua dawa za maumivu ya kichwa ili walau apunguze maumivu. Kisha hapo akaendelea na safari yake ambayo mwisho wake ilikuwa ni kwao. Alipitiliza mpaka chumbani kwake na kwenda kujilaza kitandani.
Pamoja na kumeza dawa za kutuliza maumivu, lakini kichwa hakikukoma. Mama yake aliingia ndani humo punde tu na kumkuta Ramah akiwa amejilaza kitandi chali akilitazama dari.
“Kama hicho kichwa kinauma sana, ni bora uende tu hospitali Rafael, lakini sio kujitesa namna hiyo” Mama yake aliongea hayo kwa sauti iliyojaa huruma ya mwana. Ramah aliinua kichwa kumtazama mama yake kisha akakilaza tena. Mwanzo hakuwa amemuona wala kuhisi uwepo wake humo. Pengine ni msongo wa mawaozo ndio uliosababisha hayo.
“Nimeshapitia duka la dawa na nimenunua dawa za kutuliza maumivu. Acha kwanza nikisikilizie kama kitaendelea kuuma basi kesho nitaenda hospotali Mama”
“Pia ni sawa. Lakini umekula umeshiba ama ndio unaleta udenguaji wako mpaka kwenye maradhi?” Ramah alitabasamu baada ya kusikia maneno ya mamae.
“Mama, sinakumbukumbu kama nilishawahi kudengua kwenye kula. Na hilo hata wewe unalithibitisha. Na kama huamini, niletee msosi mwengine hapa nikuonyeshe” Tabasamu likachanua kwenye uso wa mama yake baada ya Ramah kutamka maneno hayo.
“Pumzika kwanza utakula baadae. Usije ukajiovadozi bure kwa shibe na kusababisha dawa zisifanye kazi ipasavyo” Mama Ramah alisema hayo kisha akatoka akimuacha Ramah akiwa anacheka.
“Dah! Kama huyu mwanamke atakuwa ‘serious’ kabisa. Bora mapenzi niyahamishie kwa mama yangu maana yeye hachoki kunipa furaha” Ramah aliongea hayo akiwa anatabasamu.
Majira ya saa kumi na mbili na robo jioni. Ramah aligutushwa usingizini na mlio wa simu yake iliyokuwa ikiita. Akajiinua pale kitandani akiwa na mawenge ya usingizi. Akaifuata simu yake iliyokuwa juu ya meza na kuichukua. Kwenye kioo cha simu jina la Cecy lilionekana akiwa yeye ndie mpigaji. Akaipokea na kuiweka sikioni.
“Nakupigia simu mara ya pili hii hupokei, au unahisi nina shida na wewe sana ama?” Sauti ya Cecy ilisikika ikiyanena hayo. Moyo wa Ramah uliripuka kwa hofu na isijulikane hofu hiyo imetoka wapi ama imetokana na nini. Akaitoa simu yake sikioni na kuitazama kwenye kioo. Kisha akairudisha tena sikioni baada ya kuthibitisha kwamba Cecy ndie aliempigia simu na ndie alieongea hayo.
“Lakini Cecy kwanini siku hizi umekuwa na kisirani hivi? Inamaana hukuweza kunihoji kwa upole kwanini sikupokea simu ya...”
“Eee eee! Mwanaume usiniletee maneno yako ya khanga hapa. Njoo Kaskaravila majira haya na ukichelewa hunikuti” Cecy alimkatisha Ramah kuongea kisha akamuambia hayo. Simu ikakatwa huku Ramah akibaki na taharuki.
Cecy muda huo alikuwa ndani ya baa ya Kaskaravila. Alikuwa amekaa pekeake kwenye meza moja iliyokuwa eneo hilo. Alishusha simu yake chini taratibu mpaka pale sikio lake lilipobaki tupu.
“Sikupaswa kumfanyia dharau hizi Ramah. Ananipenda kweli lakini nimegundua simpendi. Na sina budi kumthibitishia hilo ili abaki huru na mimi niwe huru. Ramah na Rommy ni ndugu hawa na mimi hisia zangu zimetua kwa Rommy moyo wangu shahidi wa hilo. Ni vipi nitamlaghali Ramah kuwa nampemda ilhali sio. Acha niwe na Rommy naamini ataliziba pengo la nduguye. Ni lazima Ramah aujue ukweli na siwezi kumtamkia kwa kinywa changu kwasababu lazima ataumia. Lakini vitendo vinatosha kuthibitisha hilo. Ee Mungu nisimamie mwana wako”
Cecy aliongea hayo kwa masikitiko huku chozi likimtoka kwenye jicho lake moja. Sipendi Ramah ateseke kwajili yangu. Sitaki Ramah ajiumize kwa mapenzi yangu feki. Lazima ukweli aujue ili awe huru nami nibaki huru. Cecy aliwaza hayo kisha akaichukua simu yake kwaajili ya kumpigia Ramah. Hata pale alipopiga namba ya Ramah alisikia mlio wa sauti ya simu ya Ramah ikiita maeneo hayo. Akageuka nyuma na kumuona Ramah akijongea maeneo hayo aliyopo. Alikata simu na kutulia.
Ramah akafika pale alipo na kuvuta kiti kisha akakaa. Kimya akimtazama Cecy usoni akiwa haelewi aanze vipi kumuongelesha. Baada ya kutazamana sana usoni bila kuzungumzishana lolote. Cecy akahamia kwenye simu akawa bize huko.
“Cecy..?” Ramah aliita na Cecy akamtazama. “Ningependa kujua ni kipi hasa kilichokufanya mpaka ukawa hivi ulivyo. Tena ghafla tu na wala haikuwa ni tabia yako huko mwanzo?” Ramah alimuuliza. Cecy akatabasamu kisha akarudisha macho yake kwenye simu. Alionekana hakuwa tayari kuzungumza na Ramah. Sasa kivipi ilhali ni yeye ndie amemuita eneo hilo muda huo?
Haikujulikana!
Pengine labda ni kiburi tu!.
Hzi sasa dharau. Ramah aliwaza hayo huku akimtazama Cecy. Ghafla tu aliipora simu ya Cecy kitendo ambacho kilimfanya Cecy kuhamanika. Alianza kuropoka akidai kurudishiwa simu yake, na Ramah wala asiwe na shuhuli nae zaidi ya kutazama kile alichokuwa akikifanya Cecy muda wote kwenye simu yake.
“Unayoyataka utayapata. Endelea kukaa na hiyo simu” Cecy aliongea kwa kiburi kisha akaifunganisha mikono yake kwenye kifua chake akimtazama Ramah.
Ramah moyo ulianza kumuenda mbio mbio baada ya kugundua kile alichokuwa akikifanya Cecy. Cecy alikuwa akichart na mtu aliemsavu ‘Dear Rommy’. Zilikuwa ni jumbe za mapenzi dhahiri. Na aligundua pia kuwa watu hao walishakutana ama kuwa pamoja siku iliyopita baada ya kukuta ujumbe uliotumwa na huyo mtu uliosema kuwa, siku hiyo iliyopita alimuacha katika hali mbaya na anamuhitaji kwa siku nyengine wafanye kile kilichoshindikana siku hiyo.
Ebwana eee!.
Alimtazama Cecy kwa gadhabu huku mashavu yakimcheza cheza kudhihirisha hasira alizokuwa nazo. Hata Cecy pia aliogopa baada ya kumuona Ramah akiwa katika hali hiyo ambayo hakuwahi kumuona nayo hata mara moja. Lakini maji alishayavulia nguo, hakuwa na budi kuyaoga. Na yeye akamtazama Ramah kwa dharau.
“Inamaana... Aargh! Huyu mtu ndie anaekufanya uniletee dharau mimi?... Rommy ni nani.....? Ni huyu Rommy nimjuae mimi ama ni mwengine....? Nijibu wewe usinitolee mimacho yako!” Ramah aliongea kwa hasira na mwisho alipiga meza kwa gadhabu huku akimtazama. Cecy alishtuka baada ya Ramah kupiga meza. Akajiweka sawa na kusema.
“Eee eee! Mwanaume tusitishane saa hizi. Yanini kutaka kuvunja meza ya watu kwa mahasira yako yasio na kichwa wala miguu? Acha...”
Cecy aliacha kuongea baada ya kumuona Ramah akiondoka mahala hapo baada ya kumuwekea simu yake juu ya meza. Cecy akatabasamu. Tabasamu ambalo liligeuka kicheko kilichochukua dakika nzima. Kisha akanyamaza na kuivuta simu yake.
“Kumbe Ramah akiwa na hasira anageuka Mbogo? Hah hah hahaaha!” Cecy aliongea hayo kisha akainuka na kuondoka mahala hapo.
Alifika nyumbani kwao na moja kwa moja aliingia chumbani kwake. Ni wazi alichanganyikiwa kama sio uchizi kumuanza kabisa. Kila alichotaka kufanya kwa wakati huo aliona hakifai. Aliishika simu yake na kuitazama tu isijulikane anataka kufanya nini. Akaingia upande wa majina na kulitafuta jina la Rommy ambae alimsevu kama Ethan. Akapiga simu. Lakini bahati mbaya simu haikuwa ikipatikana muda huo. Akatafuta jina la Jenifa na kupiga, kisha akaweka simu sikioni.
“Heloo Ramah, vipi” Sauti ya Jeni ilisikika kwenye spika ya simu ya Ramah.
“Ona Jeni. Natakaaa.. Naomba uniambie unajua yapi kuhusu Cecy?” Ramah aliongea kwa wahka huku akiurusha-rusha mkono wake wa kushoto ambao ulibaki huru huku wakulia ukiwa umeshikiza simu sikioni.
“Nini Ramah! Mbona sikuelewi?”
“Unanielewa Jeni ila sema unafanya kusudi kwasababu nyote lenu ni moja. Na unayajua anayofanya mwenzako. Tafadhali naomba uniambie”
“Sasa nikuambie kitu gani?” Jeni aliuliza kwa mashaka.
“Ok..ok. Acha nikuambie. Cecy anatembea na ndugu yangu na wewe unalijua hilo na wala usiniambie chochote”
“Haaaa! Unajua Rafael sijakuelewa. Anatembea na ndugu yako? Jay, ama?”
“Jay wapi! Ethan! Humjui Ethan wewe? Unayajua ila sema unafanya kusudi kujifanya huyajui. Ila asanteni sana”
“Sikiliza Ramah....” Sauti ya Jeni ilikatishwa baada ya simu kukatwa.
Ramah aliona akigeukwa na watu wote. Aliiweka simu pembeni na kujiinamia. Bongoni kwake kulipishana mawazo ya kila namna na asijue ni amuzi lipi achukue. Sauti ya simu yake iliyokuwa inaita iliyakatisha mawazo yake. Akaitazama kama sio simu yake ama hakuwa na haja ya kuipokea simu hiyo. Akakuta ni Jeni ndie ambae anapiga. Akatulia kwa sekunde kadhaa huku akiwa bado anaitolea macho simu. Kisha hapo akaipokea.
“Sikiliza nikuambie kitu Ramah. Wewe unavyonishutumu kwamba nayajua anayoyafanya Cecy unakosea kwasababu si kila alifanyalo Cecy lazima na mimi aniambie. Hata hayo unayoniambia hivi sasa kuwa anatembea na ndugu yako sijui ni nani huko ndio kwanza unaniambia wewe. Ila mi nitajaribu kumtafuta nimuulize kuhusu hayo na kama yana ukweli basi nitajua nafanya nini?” Ramah alikuwa kimya akisikiliza yale anayoambiwa na Jeni. Kisha hapo akajibu sawa na simu ikakatwa.
Baada ya kukatika simu ya Jeni. Ramah simu yake ikaita tena. Akaitazama kiuvivu na ghafla moyo ukaanza kumuenda mbio. Alikuwa Rommy ndie ambae anaempigia muda huo. Akaitazama simu yake kwa muda kisha akaipokea.
“Habari ndugu” Sauti ya Rommy ilisikika akiyanena hayo. Ramah alibaki kimya ni kama vile hakusikia salamu hiyo ama alikuwa akifikiria ajibu vipi. Ilichukua sekunde zaidi ya kumi mpaka Ramah kuja kuijibu salamu hiyo. Ramah aliongea kwa sauti ya kawaida tu kama vile hakuna kitu chochote cha tofuati kilichotokea.
“Etahn, samahani sana ndugu yangu. Kesho kama utukuwa na muda naomba tuonane” Ramah alizungumza hayo baada ya kujuliana hali.
“Sawa kaka. We niambie ni muda gani na ni mahali gani” Ramah akatulia kimya akitafakari. Kisha akaibuka na jibu kuwa, itapendeza zaidi kama watakutana sehemu yoyote ile tulivu muda wa jioni. Rommy akajibu poa kisha simu ikakatwa baada ya Rommy kumtaka Ramah awasalimie wote wa hapo nyumbani.
“Nakwenda kupigania penzi dhidi ya ndugu yangu. Sidhani kama Ethan anatambua kama natoka na Cecy. Lakini hata hivyo ni muda mfupi sana tangu Ethan arejee huku. Sasa ni vipi amekutana na Cecy kwa muda huu mfupi, wakazoeana mpaka kuanzisha uhusiano? Tena na kukutana juu na bilashaka walikutaniana sehemu ya faragha... Inamaana Cecy amekuwa mrahisi hivi mpaka kumuamini mtu kwa muda mfupi namna hii, na wakakutana sehemu faragha?..” Ramah alikuwa akiyaongea hayo kwa sauti ya chini huku akiutazama mlango wa chumbani kwao. Alikuwa kama vile akiyasoma maneno hayo kwenye mlango ule, maana hakubandua macho yake mahala hapo.
“Mmmh! Hapana! Cecy nimjuae mimi sio huyu wa sasa aisee. Amebadilika sana. Tena kwa muda mfupi sana. Muda ambao hata nikimuelezea mtu jinsi Cecy alivyobadilka lazima ashangae tena kwa kicheko juu akinicheka kwa dhihaka. Lazima ahisi ni uongo tu. Lakini hata hivyo najua Cecy lazima ajirudi na atayatambua makosa yake. Nami bilashaka nitampokea tena....” Ramah aliendea kuzungumza mazungumzo ambayo alijizungumzisha mwenyewe.
Hata pale Jay alipoingia ndani humo kupitia pale pale mlangoni ambapo Ramah alipakodolea macho bila kutazama popote. Lakini pia hakuweza kumuona. Jay alishangazwa na hali hiyo aliyomkuta nayo Ramah. Kuongea pekeake huku akitazama sehemu moja bila kupepesa macho. Alimtazama kwa muda akimtafakari kisha akatabasamu. Lakini tabasamu likazima ghafla baada ya kuona chozi likitoka kwenye jicho moja na Ramah.
Vipi huyu? Alijiuliza huku akimtazama kwa taharuki. Ramah chozi lile lilimtoka kwasababu macho yake aliyaacha wazi bila kupepesa kwa muda mrefu na kufanya upepo uzame kwenye mboni na kusababisha chozi kutoka. Hata hivyo bado hakuwa amegundua uwepo wa Jay mahala hapo.
“Oyaa....?” Jay alimuita huku akimtazama. Ramah akageuza kichwa taratibu kumtazama. Akarudisha kichwa nyuma kwa mshtuko huku akimkodolea macho. Kisha tabasamu la mbali likachanua usoni kwake.
“Vipi dogo? Mbona unaonekana unawaza sana?” Jay alimuuliza hayo huku akimtazama kwa udadisi. Ramah aliangalia pembeni kisha nae akauliza.
“Kwani vipi?” Jay bado alikuwa akimtazama. Akakiendea kitanda na kukaa, lakini bado asiache kumtazama Ramah.
“Vipi kuhusu nini? Nakuuliza kwanini upo katika hali hiyo na wewe unaniuliza maswali yako ya kibwege. Unatoka michozi machoni, unaongea pekeako. Unatatizo gani kwani?”
Muda huu sasa Ramah ndio aling'amua kwamba alikuwa akitokwa na machozi baada ya kusikia maneno ya Jay na kuthibitisha mwenyewe kwa kupeleka kiganja chake cha mkono machoni. Alifuta chozi lile lililokuwa likimtoka pasi na yeye kujua. Kwani nilikuwa nikilia? Alijiuliza mawazoni. Akamtazama Jay usoni huku akitabasamu. Hakuwa tayari kumuambia lolote Jay kuhusiana na yale yaliyotokea akihisi labda ni kwa muda tu kisha hapo mambo yatakuwa sawa.
“Au ulikuwa unafanya mazoezi ya hisia nini?” Jay alimuuliza baada ya kuona Ramah akiwa kimya. Ramah aliposikia swali hilo, lile tabasamu likazidi na kuwa ni kicheko. Jay akasonya akihisi ni katika matani tu ya nduguye.
* *
Majira haya ya mchana ikiwa ni siku mpya baada ya ile iliyopita kupita. Jeni na Cecy walikuwa wapo kibarazani nyumbani kwa kina Cecy. Walikuwa mahala hapo wakipiga soga zao ambazo hazikuwa na maana sana kuandikwa mahala hapa. Jeni muda wote alikuwa akitafuta namna ya kumuingilia Cecy kwa kumuuliza ama kumuambia yale aliyotoka nayo nyumbani kwao.
“Unajua Ramah jana mida ya usiku alinipigia simu akanilalamikia sana” Jeni alinena hayo na isijulikane kama ameyanena kwa nia gani. Pengine ndio ameonelea aanzie hivyo. Cecy alimtazama usoni na wala asiongee chochote. Jeni akaendelea.
“Cecy unanifanya nionekane mbaya kwa Ramah. Maana alinihisi nayajua hayo unayoyafanya hata pale ulipoanzisha mahusiano upya na Rommy alihisi hata mimi natambua hilo..”
“Kwahiyo?” Cecy alimkatisha kwa kumuuliza hivyo. Jeni akaachia tabasamu kisha akamtazama Cecy usoni. Akataka kuongea lakini kicheko kifupo kama mguno fulani kikachukua nafasi. Akaacha kutabasamu kisha akauvaa uso wa ‘serious’ na kusema.
“Unajua Cecy mimi na wewe ni marafiki sana. Tena mpaka ukabadilika na ukafikia hatua ya undugu. Nakujua, naijua historia yako japo si yote. Lakini kwahili lazima nikushangae sana Cecy, hili la kuanzisha uhusiano na Rommy ilhali upo na Ramah. Hata sijui ni kipi hasa kinachokufanya umuingize tena moyoni mwako Rommy wakati alishawahi kukuumiza, na sio kukumiza tu, mpaka kukudhalilisha mbele za watu. Mi nakumbuka sana hata kama unajifanya hukumbuki kwasababu hata mimi ile aibu ilinipata kwasababu mimi ndio nilikuwa rafiki yako mkubwa kuliko wote. Sasa sijajua ni vipi Rommy ameweza kukushawishi mpaka ukalainika mtoto wa kike mpaka ukasahau yote na kumrudia tena..... Sawa. Haiwezekani kuingilia maamuzi yako lakini ushauri yafaa kukuambia kama rafiki yako...” Jeni baada ya kuongea sana, akanyamaza kwanza aone ni kwa kiasi gani Cecy amemuelewa. Cecy alitabasamu kisha akasikitika. Akacheka kidogo na kutazama pembeni huku na huko. Kisha akamgeukia Jeni akiwa hata lile tabasamu hana tena usoni kwake.
“Kwahiyo ulitaka nikusaidiaje labda? Ama niwasaidiaje?” Cecy alimuuliza kwa dharau utafikiri Jeni wakati anamuambia alimuambia kwa jeuri. Jeni aliongeza tabasamu baada ya kumaizi kuwa Cecy amekasirishwa na maneno yake.
“Kwangu haitonifaa kitu, ila ni kwaajili yako wewe. Na ndio maana nikawahi kukuambia kuwa siwezi ingilia maamuzi yako ila ushauri nafaa kukupa kama rafiki yako. Tambua Ramah anakupenda lakini Rommy nina hakika hakupendi, amekutamani tu kwa mara nyengine baada ya kukuona ulivyobadilika na umeyafurahisha macho yake. Hakika yupo kwaajili ya kukutumia tu na akishamaliza hashki zake atakuacha ukilia kama kipindi kile. Muda mwengine unapaswa kujiongeza Cecy. Embu fikiria, mtu mwenyewe amekuja huku likizo tu baada ya muda mfupi atarudi huko atokapo atakuacha mwenyewe. Ikiwa unaharibu kwa Ramah unadhani baada ya kuondoka Rommy utamuangalia vipi Ramah? Haki Ramah anakupenda na mwenyewe walitambua hilo. Amefanya majambo mengi kwaajili yako na si kwa chochote zaidi ni kutokana na upendo alionao kwako...”
“Unajua Jeni unaongea sana lakini sikuelewei hata moja. Unanishauri ili iweje labda? Natambua Ramah ananipenda na amefanya mengi kwangu, lakini mi simpendi sasa. Kwahiyo unataka nijilazimishe kuwa nae ilhali simtaki? Yanini ni nimdanganye ikiwa uwezo wa kumuambia ukweli ninao? Simpendi wala simtaki Ramah na moyo wangu ni shahidi wa hilo” Cecy aliongea kwa kumaanisha. Muda wote kinywa cha Jeni kilikuwa wazi kwa butwaa asiamini anayosema Cecy.
“Hivi kweli ni akili yako Cecy ama unaanza kuchanganyikiwa? Ok. Unatambua kama Ramah na Rommy ni ndugu?” Jeni alisema kwa hofu na mwisho alimuuliza swali hilo akitegemea kuona mshtuko kwa Cecy. Lakini aliyotegemea ni tofauti na aliyoyaona. Cecy alicheka sana mithili ya Malkia aliyepewa taarifa ya kupendeza na bwana Mfalme wake.
“We unayajua leo...? Basi mi mwenzako nayajua muda tu na ndio maana si umizwi kumuacha Ramah na kuwa na Rommy kwasababu wote ni ndugu. Zaidi nitafurahia kuwa na Rommy kwasababu yeye ndie wa kwanza kunijua mimi kabla ya Ramah...”
“Haki vile Cecy umechanganyikiwa wewe na nilikosea kusema unaanza kuchanganyikiwa. We umeshachanganyikiwa Cecy. Yani huoni hatari yoyote kuwachangaya ndugu kwenye mapenzi?” Jeni alizidi kushangazwa na maneno ya Cecy kiasi ambacho alihisi ni kweli Cecy ameshachanganyikiwa.
“Hatari nimeiona na ndio maana nipo katika harakati za kuachana na Ramah ili niwe huru na Rommy. Halafu ona Jeni. Kama huna cha maana cha kuzungumza achana na hii habari. Tutakosana hivi punde na sitojali lolote, chochote kuhusiana na sisi. Kama unamuonea huruma sana Ramah kuwa nae wewe basi. Sitaki kubugudhiwa na maamuzi yangu. Alaa!” Cecy aliwaka mithili ya moto wa kifuu. Lakini hata hivyo Jeni hakutaka kumuacha Cecy akiamini anapotea kurudisha upya uhusiano na Rommy ilhali huko nyuma alishatendwa vibaya.
“Lakini Cecy mi...”
“Eee eee! Baki mwenyewe hapa maana nahisi unataka nikuachie Rommy uwe nae wewe kwasababu hata kipindi kile twasoma ulikuwa pia ukimtaka. Pumbavu wewe mtaka waume za watu...” Akamalizia na msunyo kisha akainuka kwa kisirani na kuingia ndani akimuacha Jeni mdomo wazi.
Majira ya jioni ikiwa ni muda ambao Ramah na Rommy walipanga kukutana kwaajili ya kuzungumza kama Ramah alivyomtaka Rommy uliwadia. Kwenye mgahawa ulioko maeneo ya soko la Mgandini. Ramah alikuwa ndani humo akimsubiri Rommy. Hata hivyo haikuchukua muda sana, Rommy akaonekana akiingia eneo hilo. Alipofika ndani ya mgahawa huo alienda mpaka pale alipokuwa amekaa Ramah. Ramah alipomuona alisimama na kupeana mikono kisha wakakumbatiana. Baada ya hapo wakakaa kwenye viti kwaajili ya kuzungumza.
“Mbona sijawaona wale majamaa zako?” Ramah alimuuliza akimaanisha kina Paskali.
“Wapo mbona! Hawawezi kuniacha wale, popote niendapo lazima wawepo. Mmoja yule pale kwenye ile meza na wale wengine wapo nje kule kwenye gari” Rommy alimuambia na kumuonyesha Paskali aliekuwa amekaa kimya kwenye meza iliyokuwa mbali kidogo na walipo wao. Ramah akatazama kule alipoonyeshwa na kumuona, akataka kuuliza ameingia muda gani mtu huyo ikiwa yeye hakumuona. Lakini akapotezea baada ya kukumbuka kuwa alimuona mtu huyo akiingia mahala hapo kabla ya kuingia kwa Rommy lakini hakumtilia maanani.
Wakazungumza mengi ikiwa ni kukumbushiana ya nyuma na kupanga mipango yao kama ndugu. Huku Rommy akimuahidi kwa mara nyengine kumsaidia Ramah kimaisha. Maana mali zile alizozirithi kutoka kwa baba yake marehemu Antony Magasa, hata Ramah pia alihusika. Ila ndio hivyo tu hakuwa ametajwa kwenye kurithi mali hizo. Baada ya kuzungumza zaidi ya nusu saa. Ndipo Ramah alionelea muda huo utafaa zaidi kuzungumza kile kilichopelekea mpaka kumuita Rommy mahala hapo.
“Kuna mwanadada flani anaitwa Cecy, unamfahamu?” Ramah alimuuliza akiwa katika hali ya kawaida ili asizue taharuki kwa nduguye maana alihisi angeonekana waajabu kuzungumzia maswala hayo ilhali ni mara ya pili tu wanaonana. Ethan akatuliza kichwa kutafakari kisha na yeye akaibuka na swali.
“Nadhani unamzungumzia mtu alieko ndani ya jiji hili, maana isingekuwa rahisi kuniuliza hivyo ikiwa mtu mwenyewe yupo nje ya mji huu.... Mi namfahamu mwanamke mmoja tu kwa jina hilo ambalo ubini wake ni Ally, ama sivyo?” Ramah alitingisha kichwa kukubali.
“Ni nani yako yule ama unamfahamu fahamu vipi?” Ramah alimuuliza tena. Maswali ambayo yalianza kujenga hoja bongoni mwa Rommy. Lakini akawa mpole aone mwisho wa maswali hayo utakuaje.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Aaaa! Kama ndie, basi binti huyo nilianza kumfahamu kipindi nipo msingi nilipohamishiwa shule aliyokuwa akisoma yeye. Tukajenga mazoea mpaka ikafikia hatua tukawa wapenzi. Lakini bahati mbaya tulikuja kuachana, nikimaanisha tulitofautiana. Mpaka naondoka ndani ya mji huu, nchii hii na kuhamia Kenya kwaajili ya masomo hatukuwa bado tumepatana. Majuzi kati hivi nikiwa ndani ya mji huu. Nikiwa katika matembezi nilikutana nae SuperMaket moja nimeisahau jina. Tukabadilishana namba za simu ndipo mapenzi yakaanza upya.” Rommy alieleza kwa ufasaha mwanzo mwisho. Nia na malengo ni kujua lengo la Ramah kumuuliza hayo kuhusiana na mtu huyo.
Ramah alishusha pumzi, mapigo yake ya moyo yakienda mbio mbio huku sasa pumzi zikienda hobwe hobwe na kinywa kisijue kitamke nini. Macho yalimlegea mithili ya banati alietafuna kungu huku pua zikimcheza cheza. Inamaana Cecy alianza kujuana na Ethan kabla yangu? Akajiuliza swali hilo mawazoni kwake. Rommy alikuwa akimtazama muda wote na asijue ni kwanini Ramah amekuwa mpole ghafla.
“Kwani vipi kaka?” Akauliza. Ramah akajichekesha kimbea ili kupotezea hali iliyomkumba punde tu. Lakini hata hivyo Rommy alishaelewa kwamba nduguye ana jambo.
“Hakuna kitu. Bali nilataka tu kujua, kwasababu binti yule ni rafiki yangu sana na... na alinieleza habari zako. Nikashangazwa sana ndipo nikaona nikuulize mwenyewe ili niamini”
“Uamini nini?” Rommy alihoji akiwa makini akisubiri jibu kwa Ramah. Hata hivyo Ramah alilichelewesha jibu kwa sekunde kadhaa. Kisha hapo akajibu kwamba. Aamini kwamba kweli ni shemeji ya nduguye. Rommy akatabasamu lakini alishamaizi kwamba ameongopewa.
Ramah baada ya kupata kile alichokitaka. Akabadili mada maana alishaona inaweza ikabainika adhma yake huko mbeleni kama ataendelea na mada hiyo hiyo. Walikaa wakizungumza mpaka kigiza kilipoingia. Ramah akasema kwamba, kwa siku hiyo wafanye inatosha watakakutana tena siku nyengine na kuzungumza zaidi. Rommy hakupinga kisha wakainuka wote na kutoka nje ya mgahawa huo. Huko waliagana na Rommy akaingia kwenye gari na kupotea mahala hapo.
Ramah alirudi ndani ya mgahawa huo akiwa na mawazo mengi kichwani kwake. Alihisi kuchanganyikiwa. Kuchanganywa na yale aliyoelezwa na nduguye. Akakaa pale alipokuwa amekaa mwanzo akiwa mwingi wa mawazo. Hata kama lakini Cecy bado anabaki kuwa ni msaliti kwangu. Kwani alishindwa kumueleza Ethan kama ana mtu mwengine? Aliwaza.
Akatoa simu yake na kumpigia Jeni. Simu ilipopokelewa akamuuliza Jeni yupo wapi muda huo. Jeni akajibu yupo barabara ya ishirini kwa shangazi yake na muda huo alikuwa akijiandaa kurudi nyumbani kwao. Ramah akamuomba afike mahala hapo muda huo kama ataweza. Jeni akakubali na kumuahidi ndani ya dakika kumi atakuwa hapo. Ramah akakata simu akimsubiri Jeni. Kutoka barabara ya ishirini mpaka hapo alipo Ramah. Hapakuwa na umbali wowote hata kwa kutembea kwa miguu tu.
Dakika kumi na tano mbele, Jeni alifika mahala hapo ambapo alimkuta Ramah akiwa katika hali ya fadhaa. Uso wake ulisawijika kwa huzuni, alieonekana kama mtu aliekutwa jambo kubwa na asijue alitatue vipi. Alifika mahala pale na kukaa huku muda wote akimtazama Ramah usoni kwa mashaka huku Ramah yeye akimtazama kwa huzuni. Wakatazamana!.
Lakini katika hali tofauti.
“Vipi Ramah! Mbona hivi tena?” Jeni alihoji baada ya kimya kifupi kupita. Ramah akashusha pumzi nzito ambazo zilifanya kifua chake kupanda kisha kushuka.
“Uliniahidi utakaa na Cecy umuhoji vyema kuhusiana na yale niliyokuambia jana. Nini kimeendelea?” Ramah aliongea kwa upole utafikiri alilazimishwa kuzungumza. Jeni soni ikamvaa moyoni. Akaona haya hata kumuelezea yale yaliyotukia siku hiyo alipomfuata Cecy na kuzungumza nae. Unadhani angemueleza nini ilhali hata yeye alisuswa na Cecy mpaka kuachwa pekeeake nje? Akashindwa kumueleza!.
Jeni akajibu kwa kudanganya kwamba, siku hiyo hakupata wasaa mzuri wa kuzungumza na Cecy baada ya mama yake kumtaka aende barabara ya ishirini kwa shangazi yake kwenda kumjulia hali maana alikuwa akiumwa. Lakini akamuahidi kuwa siku inayofuata lazima atatafuta muda mzuri na ataenda nyumbani kwa kina Cecy kwaajili ya kuzungumza nae.
Ramah akamuelewa kisha akamueleza yote kuhusu undugu wake na Ethan ambae Jeni alishatambua kuwa kwa jina lengine anamjua kama Rommy. Akamueleza yale aliyoelezwa na Rommy kwamba alikutana na Cecy shule ya msingi ambayo hata yeye (Jeni) alikuw akisoma hapo. Ramah akamuuliza kumtambua Ethan na Jeni akajibu ndio. Akamuuliza tena kuutambua uhusiano wa Cecy na Ethan wa kipindi hicho na Jeni akajibu ndio. Hapo Ramah akathibitisha kwa uhakika yale aliyoambiwa na nduguye.
“Lakini kabla ya kumaliza shule waliachana, tena kwa chuki. Nashangaa sasa unaponiambia kuwa wamerudiana tena” Jeni akamueleza.
“Embu naomba unielezee waliachana-achana kivipi yani” Ramah aliongea. Jeni akamueleza yote tangu uhusiano wao ulipoanza mpaka pale walipoachana. Pia hakusahau kumueleza kashfa na dharau alizofanyiwa Cecy na Ethan mpaka kupelekea kudhalilishwa darasani na kupatwa na aibu kuu ambayo yeye (Jeni) alisema hatokuja kuisahau. Akamalizia kwa kusema kwamba anamchukia sana Rommy kwa vitendo vyake kisha akamuaomba msamaha Ramah kwa kumchukia nduguye akisema hana namna yoyote nyengine zaidi ya kuwa hivyo.
Ramah alishikwa na hasira za ghafla juu ya ndugu yake baada ya kuisikiliza historia hiyo ambayo Rommy alimtenda vibaya Cecy kipindi hicho. Lakini ni vipi awe na hasira juu ya nduguye ilhali kipindi hicho hakuwa bado akimfahamu Cecy? Pengine ni hasira za kupokonywa tunda lake na nduguye hata kama alishawahi kuwa nalo kabla yake.
Ramah akamuambia Jeni waondoke mahala hapo warudi majumbani kwao, lakini wakutane ama wawasiliane siku inayofuata baada ya Jeni kuzungumza na Cecy kama ambavyo Jeni alimuambia atazungumza nae. Wakapanda usafiri aliokuja nao Ramah wa pikipiki kisha hapo safari ya kuelekea kule wanapotaka kuelekea ikaanza.
Majira ya saa nne usiku Cecy akiwa ameshamaliza shuhuli zake zote za siku hiyo na hapo alikuwa akijiandaa kulala. Simu yake iliita. Akatazama nani ampigiae muda huo, akatabasamu baada ya kumaizi ni Rommy ndie mpigaji. Akaipokea huku akijilaza kitandani kwake ili apate nafasi nzuri ya kuzungumza nae. Hata baada ya salamu kukamilika. Rommy akaingia kwenye jambo lililomfanya ampigie simu Cecy muda huo.
“Unamfahamu Rafael ama Ramah” Rommy alimuuliza swali hilo kwa kushtukiza na kumfanya Cecy mapigo yake ya moyo yaanze kwenda mbio kwa hofu. Hakujua Rommy alimuuliza hivyo akiwa na maana gani. Huenda Ramah ameshaharibu tayari! Cecy alijiwazia. Akajibu ndio kwa upole.
“Ni nani yako yule?” Rommy alimuuliza tena baada ya lile swali lake la kwanza kupata jibu. Cecy alianza kutetemeka na hata isijulikane ni nini kimtetemeshacho. Akajibu kwa kulalamika kuwa ni mara ya pili sasa anamuambia Rommy kwamba Ramah ni rafiki yake tu. Hapo Rommy akakumbuka kwamba alishawahi kumuuliza swali hilo Cecy kipindi kile walipokutana kwa mara ya pili.
“Hapana Cecy unanidanganya. Embu niambie ukweli. Usinifiche maana kuna mambo makubwa ameniambia kuhusu wewe. Sasa unaponiambia ni rafiki yako naona dhahiri unanidanganya” Cecy baada ya kusikia hayo moyo wake ukapiga sambasoti kwa hofu. Mambo makubwa kuhusu mimi? Akajiuliza.
“Mambo yepi hayo aliyokuambia?” Akauliza kwa kiroho akisahau kwamba alitakiwa aeleze ukweli kama Rommy alivyomtaka. Rommy alicheka kidogo ili kumtoa hofu binti huyo kisha akamuambia atamuambia endapo yeye atakapomueleza ukweli. Hata hivyo Rommy alitaka kumuweka Cecy katika hali ya kumueleza yote anayoyajua kuhusu Ramah. Maana alishaingiwa na mshaka akihisi kuna jambo ambalo yeye hakuwa akilijua. Hata vile kumuambia Cecy kwamba kuna mambo makubwa ameambiwa na Ramah kuhusu yeye, ilikuwa ni danganya toto tu ili Cecy aeleze yote akitarajia na yeye ataelezwa hayo makubwa.
Cecy akafunguka!.
“Iko hivi. Ramah alikuwa akinitaka kitambo sana, lakini mimi sikumkubalia. Aliendelea na mambo yake hayo hayo kila siku huku akinisisitiza kwamba ananipenda na anahitaji kuwa nami. Pamoja na ushawishi wote alioutumia ili anipate mimi, lakini ilishindikana. Mi sikuwa nampenda lakini yeye aliendelea na usumbufu wake mpaka hivi leo lakini mimi namkatalia bado” Cecy aliongea hayo kwa sauti kavu akimaanisha aongeayo. Pamoja na uzuri wote ule aliokuwa nao Ramah halafu uniambie ati umemkatalia? Ananidanganya huyu. Rommy alijiwazia hayo baada ya kusikiliza maelezo ya Cecy. Pengine labda! Yote yanawezekana!.
“Mlikutana wapi?” Rommy alimuuliza.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Shule! Tulikuwa tukisoma shule moja, ila yeye alinizidi kitado kimoja” Cecy alijibu hivyo. Ukimya ukatawala kwa kila mmoja. Kisha Cecy akaibuka na swali.
”Ok. Nieleze alichokuambia kuhusu mimi”
“Sikiliza Cecy. Hakuna chochote alichoniambia kibaya ama kikubwa kuhusu wewe. Bali nilikuwa natafuta kiki ya wewe kunieleza kama hayo uliyonieleza hivi punde... Pamoja na hayo, tambua kwamba Ramah ni ndugu yangu”
Wakati Cecy akiwa anazungumza na Rommy kwenye simu. Muda huo Ramah alishapiga zaidi ya mara tatu kwa dakika tofauti tofauti simu ya Cecy na majibu aliletewa kwamba simu hiyo ilikuwa ikitumika. Alionelea ni bora alale tu maana kutumika kwa simu ya Cecy muda mwingi kunazidi kumuongezea mawazo na kumfanya ahisi kuchanganyikiwa tu muda wote.
--------------
Yakiwa ni majira ya asubuhi tena ikiwa ni siku nyengine. Muda huu wa saa moja na nusu, Ramah alijaribu kupiga tena namba ya Cecy baada ya kumkosa usiku wa siku iliyopita. Mara hii simu ilikuwa ikiita na Ramah alikaa katika pozi zuri ka kuzungumza. Sekunde kadhaa simu ikapokelewa lakini Cecy asiongee lolote. Ramah akajitutumua na kumsalimu. Kisha hapo akamuuliza kwa utaratibu kwamba imekuwaje simu yake itumike sana muda mwingi? Alikuwa akizungumza na nani?
“Kwahiyo siku hizi twapangiana muda wa kuongea na simu? Kwanza we ni nani mpaka uniulize hivyo? Umeninunulia simu wewe ama umeweka vocha humu? Acha ushamba mwanaume, ongea kilichokufanya ukanipigia simu muda huu wa asubuhi na sio kuniuliza maswali yako ya kibwege. Alaa!” Ramah akanywea ghafla. Kinywa kikawa kizito kutoa maneno huku koo likipishana kumeza mate hata yale ambayo yalikuwa magumu kupita yalisikika. Baada ya kimya cha sekunde kadhaa, akataka kuongea lakini akawahiwa na Cecy.
“Sikiliza nikuambie Rafael. Pema pasipo pema, paki pema si pema tena. Unakuwa kama mtoto mdogo aelekezwae kila jambo. Waswahili husema, mwerevu habishani, lakini nakushangaa unang'ang'ania tawi ambalo waona kabisa dhahiri laenda kukatika. Achia utakuja kuvunjika kiuno likija kuanguka. Usiwe mjinga kiasi hicho mpaka ukondwe konzi utosini ndipo maarifa yakurejee. Vitu vyengine unapaswa tu kutazama kwa macho sio mpaka uje kufumbuliwa masikio na shazia ndipo uelewe. Kwamba, Aaaa! Hapa sasa pameshafika kikomo. Wewe ni mtu mzima jielewe utakuja kuaibika siku moja ukiendelea kuwa na akili za kuku. Mi nakuambia kwasababu nakupenda, na sio kwangu tu hata kwa mwengine yaweza kuwa hivi hivi. We ni mkubwa jitambue, ohooo!” Cecy aliuponda kabisa moyo wa Ramah kwa maneno yake. Mwili mzima uliingiwa na ubaridi kama amebandikwa na mabonge ya barafu.
“Lakini si kirahisi kama udhaniavyo wewe! Mi nakupenda na naamini hata wewe wanipenda ila sijui ni kipi kimekubadilisha ghafla hivi...”
“Najua si kirahisi, na natambua kwamba unanipenda lakini utausemeaje moyo wangu kwamba ati na mimi nakupenda kama unipendavyo? Mi sikupendi Ramah! Na hilo nimelithibitisha muda tu lakini sikujua ni jinsi gani nitakueleza kwasababu umeshanizoea. Lakini muda huu nimepata nafasi sina budi kukuambia ukweli ili niwe huru. Halafu nikushauri kitu kakaangu. Unapompenda mtu usimuonyeshe kwamba unampenda moja kwa moja. Utakuja kunyanyasika kama hivi unyanyasikavyo. Si kwamba nakudhihaki! Laaa! Bali nakuambia ukweli uliopo. Ulinionyesha unanipenda sana mpaka nikawa naona haya kukuonyesha kwamba sikupendi. Lakini bado nilijihisi mnafiki kuuongopea moyo ilhali sipo vile unionavyo. Kwa wema kabisa nawa mikono ridhika na matokeo..."
“Lakini Cecy yote uyaongeayo mi siyaelewi. Nachojua unanipenda na sivinginevyo na huyo ni shetani tu amekuingia na....” Ramah alikatishwa na sauti kali ya Cecy.
“Unaniudhi Rafa, kwahiyo mimi nina mapepo? Unanikosea heshima ikiwa nimekueleza kwa upole. Anhaa! Maneno yangu ya busara umeyachukulia kama ngonjera zisizo maana. Usiniudhi mwanaume na asubuhi yote hii. Sikupendi na nishakuambia hivyo, lakini naona unataka sasa nitumie lugha ya matusi. Ok..ok. Nimeshajua, unanibabaisha na vitu vyako vidogo vidogo ulivyonipatia, unahisi labda sina uwezo wa kukurudishia? Ok. Baadae njoo home uchukue ama nitakutumia pesa zako zote ulizo gharamia vitu vyako, mjinga wewe....”
“Hapana Cecy tusifikie huko! Pia sikuwa na maana hiyo mimi. Tafadhali naomba kuonana na wewe ili tuyaongee vyema haya. Kwenye simu hatutoweza elewana Cecy.” Ramah alinung'unika kama kitoto kidogo kilichonyimwa ukoko wa wali na mamae.
“Tutaongea yepi Ramah? Mi na wewe tumeshayamaliza, halafu sipendi tuachane kwa shari, lakini naona wewe unalazimisha iwe hivyo. Ok. Bado nakumbuka fadhila zako, si kwa upendo, bali ni kwa fadhila. Kwa sasa sina muda, na si leo tu, hata kesho pia. Labda unicheki keshokutwa na si vinginevyo. Nadhani umeniskia. Nakutakia siku njema na maisha mema bila ya mimi” Cecy akakata simu utafikiri ni yeye ndie aliepiga.
“Nani tena huyo unaemtolea maneno makali namna hiyo?” Sauti ya Mamae ilimtoa kwenye lindi la hasira. Akamtazama huku akiiweka simu yake pembeni.
“Aaaa! Mama kuna watu wasumbufu sana” Cecy alisema hivyo na asifafanue vyema.
“Sawa. Njoo nje huku unisaidie kazi. Utafikiri sina mtoto wa kike bwana! Embu njoo huku” Anita alisema hayo kisha akatoka nje ya chumba cha Cecy.
Upande wa Ramah mambo hayakuwa mambo kabisa. Mwili mzima ulimtetema, kila kiungo alikihisi hakina nguvu. Kinywa kilibaki wazi na si kwa taharuki. La hasha! Ni kutojielewa tu kwa muda huo. Aliishika simu yake lakini hakuwa akiihisi kabisa kuishika. Maumivu ya kichwa yalizidi kuliko yale aliyokuwa akiyahisi mwanzo.
“Hata kama hukuwa ukinipenda lakini usingenitamkia waziwazi namna hii. Ni bora ungeendelea kunificha vile vile Cecy” Kinywa kilipopata uhai kilinena hayo. Kisha kikafumba ikawa zamu ya macho kutoa machozi. Uuguapo mtima, macho hudhihirisha uchungu kwa kumwaga machozi.
Ndio! Ramah machozi yalimtoka bado asiamini yanayoendelea. Lakini haamini kivipi ilhali ni Cecy mwenyewe ndio ametamka hayo? Pengine alitaka kuthibitisha kwa macho yake kinywa cha Cecy kikitamka kama yale aliyoyatamka punde tu. Hata hivyo kuthibitisha kwa macho ndio kutaondoa uchungu? Hapana!.
Zaidi maumivu yatazidi pengine kuliko yale ayahisiyo sasa. Japo hakutoa sauti, lakini machozi yalitangaza maumivu ya moyoni mwake. Ghafla tu alijiona asie na thamani tena kama Cecy ataendelea na msimamo wake huo huo. Alitamani kumpigia tena simu amuombe msamaha lakini akakumbuka kwamba hakuna alichomkosea. Sasa ni vipi ampigie simu?
Akatamani kumtumia ujumbe amueleze ni kiasi gani aumiavyo. Lakini aliona Cecy hatoweza kuyatasfiri maumivu hayo kama vile ambayo ayahisivyo yeye. Sasa ni nini afanye zaidi ya kulia, kulalamika mwenyewe? “Sikuwahi kuwaza hata kwa sekunde chache kama unaweza kubadilika kwa ghafla namna hii Cecy. Hata nikiusemea moyo utulie, pengine unanipima tu nikupendavyo kisha hapo utarejea kwa huzuni huku ukiniomba msamaha kwa haya. Bado sitaki kuamini kwasababu sauti ni yako iliyotamka hayo. Pumzi ulizo hema ndio zile zile uhemazo ukiwa nami. Sitaki kujiaminisha kwamba si wewe. Leo hii nimekosa thamani kwako kiasi ambacho hata muda wa kuzungumza nami mpaka ujifikirie hivyo? Aargh! Hapana Cecy si kihivyo!”
Kipindi ambacho Ramah anaugulia mwenyewe maumivu yake. Jeni muda huu ndio alikuwa akiitafuta namba ya Cecy kwenye simu yake kwaajili ya kumpigia. Maana alivyoachana nae siku iliyopita wakiwa wamepishana kiswahili, ndio hadi muda huo hakuwa amezungumza nae. Yeye alihisi Cecy anaweza kumtafuta na kujirudi baada ya kugundua alipokosea. Lakini ikawa tofauti. Hata ujumbe wa salamu kutoka kwa Cecy kwenye simu yake haukuingia.
Akaipiga namba ya Cecy na mara hii simu ikawa inaita. Akasubiri kwa sekunde kadhaa na simu ikapokelewa. Akamsalimu kwa bashasha rafikiye kama ilivyo ada yake. Lakini ikawa tofauti na alivyotarajia. Cecy aliitikia ki kawaida sana kama mtu aliechukizwa na jambo fulani. Ikabidi Jeni amuhoji nini tatizo. Hata hivyo Cecy alijibu kwamba yupo sawa tu.
“Hapana Cecy! Mi nakujua ukiwa sawa na hata ukiwa na jambo...”
“Kwahiyo unanilazimisha niwe utakavyo wewe ama?” Cecy alihoji kwa kisirani. Hata hivyo Jeni hakujali sana. Akajaribu kumuuliza kama ni yale ya jana ndio yamemfanya awe katika hali hiyo. Cecy akajibu hapana. Jeni akaibuka na swali jengine lililomuudhi Cecy mpaka kupelekea kukatwa kwa simu yake. Alimuuliza kama alishazungumza na Ramah kwa siku hiyo? Cecy akawaka kwa shari huku akimtamkia maneno ya kuudhi Jeni kisha akakata simu.
“Haki vile Cecy tunamkosa sasa. Eeeh Mungu mnusuru na lile jinamizi maana ndio linalomtia kichaa” Jeni aliongea hayo baada ya kujua kwamba amekatiwa simu na Cecy.
Tunda jema halikawii mtini. Lakini pia, si kila king'aacho ni dhahabu. Haitokuwa sawa ulimwengu kutenda wema kila jogoo akemapo. Kwasababu wazee walinena. Ulimwengu si mbaya, bali binadamu ndio wabaya. Pia wakaongezea kwa kunena kwamba, Tenda wema nenda zako, usingoje shukurani. Pengine walimaizi fika ya kwamba, si wote katika binadamu wenye kutunukiwa shani ya kulipa fadhila.
Majira ya jioni iliwakuta Rommy na Cecy mahala fulani tulivu wakifurahisha nyoyo zao. Mara hii Cecy alikuwa huru kwa Rommy kiasi cha kufanya lolote akiwa nae. Alijihisi yu ndoani na kijana huyo na hapo alishatunukiwa cheo cha mke, kichwa cha pili cha nyumba. Pengine Rommy alimpenda kweli binti huyo maana alionekana kufanya lolote ili kumfurahisha. Hakika kwa hilo alifanikiwa.
“Siamini Rommy kama nipo na wewe tena” Cecy aliongea hayo akiwa amejilaza begani mwa kijana huyo wakitazama mandhari iliyoko mbele yao.
“Kwanini unasema tena?” Rommy alihoji.
“Kwasababu tulikuwa wote mwanzo, tukatengana na sasa tupo pamoja tena” Rommy akatabasamu baada ya kusikia hayo. Cecy akaongea tena.
“Unajua Rommy. Nimeamini upendo wa kweli haufi. Pamoja na kutengana kule, lakini huezi amini mi nilikuwa bado nakupenda sana. Niliwaza sana ni lini tutaonana tena na kuja kuyaendeleza mapenzi yetu kama hivi..” Akajitoa begani kwa Rommy na kumtazama usoni, Rommy nae akaacha kutazama mbele na kutazamama nae. “Unajua kwamba Rommy nakupenda sana! Pamoja na kuwa kwa msemo unaosema ukimpenda mtu basi usimuonyeshe unampenda sanaa. Lakini kwako nashindwa, nashindwa kuzizuia hisia zangu na kujikuta nikikuonyesha moja kwa moja kwamba nakupenda na pia najua wanipenda kama nikupendavyo”
“Kwanini wamesema kwamba ukimpenda mtu usimuonyeshe kwamba unampenda?” Rommy alimuhoji.
“Kwasababu ukimuonyesha mtu kwamba unampenda sana, anaweza kuja kuutumia upendo wako kukuadhibu nao. Ukabaki unalia pekeako pasi na kupata wa kukufuta machozi huku yule unaemlilia yupo sehemu nyengine anafurahi na mwengine na wala hakuwazi wewe...” Cecy akakatishwa na kicheko kikali kilochomtoka Rommy baada ya kuongea hayo. Akamuuliza kwa mshangao kwanini anacheka?
“Unajua Cecy. Nimegundua mapenzi yanawaendesha wengi sana. Wengi wao hutumbukia pahali sipo na mwisho huibuka na maumivu mengi sana. Hao hao unaosema kwamba wamesema ukimpenda mtu usimuonyeshe, ndio hao hao waliosema ukipendwa pendeka, utakuja kupenda usipopendwa. Na ndio hao hao waliosema ukipenda unakuwa kipofu. Hakika hawakukosea hata kidogo kusema hayo. Kwasababu mtu anapendwa lakini yule anaempenda wala hampendi, anakuja kumpenda mwengine asiempenda yeye na huenda hata huyo aliempenda yeye kuna mwengine anampenda. Na hapo hapo wanakuja kusema tena kwamba usijilazimishe kumpenda usiempenda. Hapo sasa ndio utaona mapenzi yanachanganya sana. Watu tupendane tu lakini kila mmoja ana siri kubwa juu ya mwenzake na hataki aijue”
* *
Ni siku ya nne sasa yu ndani tu, chumbani kwake. Hata kazi zake alizisimamisha kutokana na hali yake ilivyo. Maumivu ya kichwa yalianza kama mzaha tu na hata pale alipotumia dawa, bado yaliendelea kuwa nae. Maumivu yataishaje ilhali kila mara ni mtu wa kuwaza tu? Mtu wa kusononeka na kunung'unika pekeake.
Kichwa nacho kikazidi kumuuma!.
Ramah alionekana kama mgonjwa wa muda mrefu kwasababu ya kudhohofika kwa muda fupi sana. Hakuijua raha tangu siku ya kwanza ya mabadiliko ya Cecy. Mabadiliko ambayo yalimpelekea muda mwingi awe ni mwenye kuwaza. Kuwaza ambako kulianzisha maumivu ya kichwa ambayo mwanzo aliyahisi ni ya kawaida sana, lakini hivi sasa yalizidi na kupelekea kuonekana mgonjwa wa muda mrefu.
Yakiwa ni majira ya jioni, muda ambao Cecy na nduguye Rommy, walikuwa pahala wakila raha. Raha ambazo zilimsahaulisha Cecy kama kuna mtu aitwae Rafael, na hakuweza kujua kwamba yu hali gani juu yake. Jeremiah aliingia katika chumba ambacho Ramah alikuwapo. Chumba ambacho pia kilikuwa ni chumba chao wao. Sawa, alijua kwamba nduguye ni mgonjwa. Lakini kilichomshangaza yeye, ni ugonjwa gani uliomdhohofisha muda mfupi hivi?
Akamtazama kwa huruma nduguye aliekuwa pale kitandani amejilaza kwa kujikunyata. Hapana kwa kweli. Haya si maradhi ya kawaida!. Jay alijiwazia huku akimtazama Ramah. Akapiga hatua ndogo ndogo mpaka pale kitandani. Akakaa na kugeuza shingo kule alipojilaza Ramah. Bado hakuacha kumtazama kwa huruma nduguye. Akanyanyua mkono wake na kumgusa kwenye paji la uso.
“Oyaa..?” Jay alimuita kwa sauti ndogo kiasi. Ramah akageuza shingo na kumtazama. “Hivi ni kichwa tu ndio kinauma ama kuna zaidi?” Jay alimuuliza. Na alimuuliza hivyo baada ya kuona joto lake halikuwa kali sana tofauti na hali yake ilivyo. Ramah akalaza tena kichwa chake na baada ya sekunde kumi. Akaamua ainuke kabisa na kukaa kitandani.
Sura ilikunjamana kwa kukosa tabasamu muda mrefu. Pengine na kulala kwa muda mwingi pia kulichangia hilo. Akavuta kamasi kwa ndani alilohisi likibugudhi tundu za pua yake kisha akameza na mate. Ni nani mwengine wa kwanza afaaye kumuambia haya niliyonayo zaidi ya yeye? Alijiwazia Ramah. Lazima nimuambie ili nijue atanisaidia vipi. Akavuta pumzi ndani na kuzitoa kwa mkupuo nje. Kisha akamgeukia nduguye tayari kumueleza yote. Akamueleza!.
Jay alishusha pumzi baada ya kusikiliza yote aliyoambiwa na Ramah yaliyochukua zaidi ya dakika tano. Kisha hapo akamtazama Ramah aliekuwa akifuta machozi huku akivuta kamasi. Akataka kusema kitu, lakini akashindwa. Hakujua aanze na neno lipi ambalo yeye atahisi ni sahihi katika kumshauri ama kumfariji nduguye.
“Inamaana ndugu yako Ethani ndio amekufanyia mchezo huo?” Jay alionelea aanze na swali hilo na si kwamba hakuelewa vyema maelezo ya Ramah. Bali tu alitaka aanzie hapo. Ramah akatingisha kichwa kukubali. Kisha akasema.
“Pamoja na hayo, lakini sidhani kama anatambua kama natoka na Cecy. Naamini Cecy ndio chanzo cha yote haya na si yeye” Ramah aliongea hayo kisha akafuta chozi lililokuwa likitoka kwenye jicho lake la kushoto.
“Sikulaumu sana, lakini hata wewe pia unamakosa. Kwasababu kama hiyo siku uliyokutana na Ethan na mkazungumza kuhusu Cecy. Na hata pale alipokuuliza wewe na Cecy mkoje. Naamini kama ungemuambia ukweli, pengine muda huu angekwisha achana nae. Kwasababu, kama Ethan aliwahi kuwa kwenye mapenzi na Cecy huko nyuma kabla ya wewe kukutana nae. Na waliachana kwa shari, na wamekuja kukutana tena hivi karibuni tu baada ya Ethan kurejea huku. Naamini kama ungejieleza vyema kwa Ethan angekuelewa na kukuachia mtu wako. Lakini hata hivyo bado hujachelewa. Mtafute tena na umueleze yote, mi naamini atakuelewa tu” Jay alishauri.
“Sawa. Ila kesho kutwa nitaanza na Cecy. Asiponielewa ndio itabidi nimfuate Ethan”
“Pia sio mbaya. Lakini usijiweke katika hali hii. Jua unamnyima raha mama kila akikuona katika hali hiyo. Kila siku anahangaika kukutafutia madawa halafu kumbe ni mawazo tu ndio yanakuweka katika hali hiyo. Wewe kwa sasa usimfikirie Cecy wala Ethan kwasababu wao ndio wanaokunyima raha. Poteza nao mawasiliano kwa hizi siku mbili mpaka pale utakapoona sasa unauhitaji wa kuzungumza nao ndio uwatafute kila mmoja kwa wakati wake. Usijiumize sana na mawazo” Jay alimaliza hivyo na Ramah akatingisha kichwa kukubali kwamba ameelewa.
Basi hapo Jay alimtaka nduguye ajiandae waelekee pahali kwaajili ya kuipa utulivu akili. Yote hiyo Jay alifanya kwaajili ya kumtoa upweke nduguye. Japo alikuwa na ratiba nyengine ambazo alipanga azifanye kwa siku hiyo. Lakini alionelea azivunje zote na kufanya jambo hilo ili kumuweka sawa ndugu yake. Ramah alijiinua kiuvivu pale kitandani na kupepesuka kidogo kutokana na kuwa muda mwingi alikuwa ni mwenye kulala tu. Kisha hapo akatoka nje kwaajili ya kwenda kuoga ili arejeshe nguvu pindi maji yatakapo usawili mwili wake.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Dakika kumi alirejea chumbani mule ambapo alimkuta Jay akiwa bize na simu yake yeye. “Ebwana kumbe hii foto unayo bado kwenye simu yako..?” Jay alimuuliza hayo huku akimuonyesha picha ambayo iliwaonyesha wao wawili wakiwa juu ya gogo sehemu ambayo ilionekana kama ufukwe hivi. Ramah akatabasamu. Tabasamu ambalo lilileta faraja moyoni mwa Jay. Dah! Ndugu yangu umzuri sana sasa sijui ni kwanini unajiweka katika hali hiyo mpaka uzuri wa wajihi wako unapotea. Jay alijiwazia hayo pale alipoona tabasamu la Ramah. “Nakumbuka hii ilikuwa ni Amboni” Akamaliza hivyo na kuirejesha tena simu ile kwenye macho yake akimuacha Ramah akibadili nguo.
Dakika sita Ramah alimaliza na kuwa tayari kutoka. Akamshtua Jay aliekuwa bize na simu na kumuambia tayari. Jay akaacha kucheza na simu na kumtazama yeye. “Dah! Mwanangu huo mtindo ukiuweka kwenye nywele zako unatokelezea ile ile aisee. Ila mi siwezi kuweka hivyo hata kidogo” Jay alimsifia Ramah baada ya kumuona akiwa amezibana nywele zake kwa nyuma zilizo nyingi. Nywele ambazo zilimeremeta kwa kupakwa mafuta mazuri ambayo pia, hayakuzipendezesha nywele zake tu. Bali yalikuwa na harufu nzuri.
“Hata mwenyewe napenda sana kuzifunga hivi ila wanga wengi mtaani, hawakawii kuniroga” Ramah aliongea hivyo na wote wakacheka. Wakatoka nje ambapo walimuaga mama yao kwamba wanatoka kidogo. Mama yao alifarijika sana baada ya kumuona Ramah akiwa amerejesha tabasamu lake tofauti na siku zilizopita.
“Wenyewe ndio mpendavyo hivyo. Huyo Ramah mwenyewe ameridhika kabisa nywele ziwe katika hali hiyo... Lakini sikufichi mwanangu umependeza sana japokuwa siyapendi hayo manywele. Sipati picha mkwe wangu Cecy akikuona atakavyo chachawa. Maana hata yeye hupenda sana uziweke katika hali hiyo hizo nywele.” Wakati Mama yao alipokuwa akiyaongea hayo. Wote walikuwa katika tabasamu, lakini pale alipotaja jina la Cecy, Ramah alipoteza tabasamu ghafla na kitendo hicho Jay alikishuudia. Akamminya mkono Ramah ishara ya kuwa asionyeshe tofauti yoyote mbele ya mama yao, maana hawakutaka mama yao ayatambue hayo mapema yote hiyo. Ramah akarudisha tabasamu kisha wakaondoka. Hawakutaka kutumia pikipiki zao kwenda huko walipotaka waende zaidi walipanga kukodisha usafiri mwengine.
Walifika maeneo fulani tulivu ambapo walionelea hapo patawafaa kutuliza akili zao. Palikuwa pamechangamka japo hapakuwa na watu wengi sana. Walitulia mahali tulivu sana ambapo hapakuwa na rabsha za watu. Waliagiza vinywaji laini kwaajili ya kusindikiza soga zao.
“Unajua nini Rafael...” Katikati ya soga zao, Jay alichomeka maneno hayo. Ramah akatulia kusikiliza ni kipi hasa nduguye atasema. “Kila mmoja hupenda sana kuwa na furaha kwasababu furaha ndio mwanzo wa kutimia kwa kila jambo zuri. Na utaona mzazi anafanya kila awezalo hata vyengine vipo nje ya uwezo wake ili mradi tu mwanawe awe ni mwenye furaha kila wakati. Mfano mzuri mama yetu. Hata wewe shahidi wa hilo. Mama anafanya vitu vingi sana ilimradi sisi wanae tufurahike, tufurahie uwepo wake, muda mwengine anafanya hata yale yaliyo magumu mpaka wenyewe tunamuonea huruma. Kwavile yeye hufanya mengi kwaajili yetu. Hatuna budi na sisi kama wanae kufanya mengi zaidi kwaajili yake japo hatutoweza yafikia yale aliyoyafanya yeye kwaajili yetu...” Akaweka kituo na kuinua glasi ambayo ndani yake ilikuwa na kinywaji na kuigida kidogo. Kisha akaitua chini na kuisikilizia ladha iliyobadilisha hali ya ulimi wake kutoka hali ya kawaida mpaka kuwa katika hali ya utamu. Kisha akaendelea. ”Embu fikiria Rafael. Mimi baba yangu simjui na inasemekana amekufa ningali mwanamchanga. Nimeishia kuona kaburi lake tu na alichoniachia ni urithi wa jina la ubini tu. Sijui yeye alikuwa yupoje, ila ninachojua alikuwa mwema kama mama anavyonipa sifa zake. Mwaka wa pili baada ya uzao wangu. Mama akapata mimba yako na ndani ya mwaka huo huo akajifungua wewe. Tukawa tupo wawili, na sio wawili tu. Bado sote tungali wachanga tuhitajiwo kunyonya ziwa lake. Nikikuambia kwamba mama yetu anatupenda, basi pakuthibitisha ni hapo. Kwasababu hakuniachisha mimi kunyonya kisha akakupa wewe wala hakukuachisha kunyonya kisha akanipa mimi. Wote tulinyonya maziwa yake. Tena bilashaka muda mwengine huenda sote tulikuwa na njaa na yeye akatunyonyesha sote wakati huo huo. Kama huo si upendo mkubwa na wa dhati nini sasa?” Ramah akatingisha kichwa kuafiki. Jay alitazama kinywaji cha Ramah na kukiona kikiwa bado kingi ilhali kikipungua ubaridi. Akamkumbusha kunywa kisha nae Ramah akanywa kidogo na kuwa tayari kumsikiliza tena nduguye.
“Ninapozungumza yote haya maana yangu ni moja tu. Kwamba, mama yetu anatupenda na anahitaji tumlipe upendo pengine zaidi ya huu atupatiao yeye. Hizi siku mbili tatu ambazo wewe ulikuwa ukiugua. Nimeona mabadiliko makubwa sana kwa mama. Mama hakuwa na furaha hata kidogo kila akuonapo upo ndani tena kitandani umejikunyata muda wote. Haki vile nakuapia mdogo wangu sikuiona furaha ya Mama hata kidogo. Muda mwingi nilimuona akihangaika kutafuta dawa kwaajili yako ili mwanae upate siha njema. Siha yako iwe thabiti kama ilivyo mwanzo. Halafu kumbe ndugu yangu hukuwa ukiumwa sana kiasi kile, kumbe ni mawazo tu yaliyokufanya uwe vile. Sikulaumu wala sikudhihaki kwasababu najua umependa. Lakini ifikie hatua umuangalia na yule aliekuleta duniani nae anaumia vipi kwaajili yako. Cecy ni mwanamke kama wanawake wengine, hata yeye anaweza kuja kuitwa mama kama waitwavyo wanawake wengine. Labda haya nisiyazungumze sana, lakini kama utajaribu kumuweka chini kwa mara nyengine na ukaona hayupo pamoja na wewe. Kama kaka yako na ndugu yako wa pekee nakushauri achana nae na yule nduguyo atabaki kuwa nduguyo tu, wala mwanamke asiwatenganishe...”
Hakika kitendo cha Ramah kupoteza furaha yake kisa Cecy kilimuuma sana Jay. Japo walipanga wafike mahala hapo kwaajili ya kuipa akili utulivu. Lakini pia alionelea ampe ushauri walau arejeshe ujasiri wake uliopotea ghafla tu. Ramah akakiri kuyaelewa yale aelezwayo na nduguye na kumuahidi kuyafuata.
Yakiwa yameshatimia majira ya saa moja jioni. Jay alimuambia Ramah kwamba, wakaimalizie siku hiyo kwenda kutazama sinema katika ukumbi wa Majestiki Cinema.
Wakati wao wakipanga kwenda kutazama sinema ambayo inatarajia kuanza saa mbili usiku. Upande wa Rommy na Cecy pia walipanga waelekee mahala huko. Wakajitoa mahala hapo walipokuwa na kwenda kupakia kwenye magari yao waliyofika nayo hapo. Gari moja walipanda Rommy na Cecy huku dereva wao akiwa ni Paskali. Na lile jengine walipakia Zumo na Assu. Msafara wa magari mawili uliondoka mahala hapo kuelekea katika ukumbi wa sinema.
---------
Nusu saa ilitosha kuwafikisha mahala hapo. Wakashuka kwenye usafiri uliowaleta na kumpatia ujira wake dereva wa chombo kilicho waleta. Kisha dereva akaondoka na wao wakawa wanasubiri magari yapungue barabarini ili wavuke upande wa pili. Wakati wakiwa mahala hapo wakisubiri kuvuka barabara. Magari mawili yaliingia kwenye maegesho ya ukumbi huo wa sinema. Kisha wakashuka watu kwenye lile gari la pili na wakashuka wengine kwenye lile gari la kwanza.
Muda wote Ramah aliekuwa upande wa pili alikuwa akiyatazama magari yale. Ndio, alikuwa akilifananisha lile la kwanza ama alilifahamu kabisa. Ndio hili hili Ethan alilokuja nalo nyumbani. Ramah aliwaza hayo huku akilikodolea macho lile gari la kwanza kufika mahala pale.
Hakika hakukosea kabisa na alithibitisha baada ya kumuona Rommy akishuka kisha akaenda kufungua mlango uliokuwa upande wa kushoto mwa gari hilo. Huko alishuka Cecy ambae alikuwa amependeza haswa huku akichagiza uzuri wake na tabasamu murua. Kule upande wa pili Ramah alibaki mdomo wazi asiamini macho yake. Huyu sie Cecy kweli? Hapana bwana, Cecy hata aweje mi nitamjua tu.
Alijiwazia!.
Ramah alikuwa akijiuliza hayo katika hali ya kutaharuki kiasi ambacho Jay alivuka na wala yeye asilitambue hilo. Jay alipofika upande wa pili alishangazwa baada ya kutomuona Ramah pembeni yake. Akatazama kule watokapo na kumuona akiwa bize kutazama mlangoni pa kuingilia ukumbini mule. Akatazama na yeye na kukuta watu wawili wa jinsia tofauti wakimalizikia kuingia ndani mule. Hakuwatilia maanani sana badala yake akageuka kule alipo Ramah.
Alimuona bado akiwa ameduwaa, ikabidi ampigie kelele ndipo Ramah akagutuka na kugundua kuwa Jay alishavuka muda tu. Akavuka barabara kwa pupa bila kutazama popote. Honi za magari zilimsindikiza huku zikichagizwa na matusi aliyopatiwa na madereva wa magari hayo kwa kitendo chake cha kuvuka barabara bila kuwa makini.
“Nini kaka, mbona ulikuwa umeduwaa muda wote?” Jay alimuuliza.
“Tuingie” Ramah alijibu kiufupi na kuanza kupiga hatua kuufuata mlango huku Jay akifuata nyuma.
Walikata tiketi mlangoni na kuelekea pahali ambapo walitakiwa waonyeshe tiketi zao ndipo waruhusiwe kuingia. Nao wakafanya hivyo kisha wakapita. Baada ya kuingia ndani, Ramah macho yake hayakutulia sehemu moja. Alifananiana na mlinzi jinsi alivyokuwa. Mara huko, mara kule. Mara atizame mbele, mara nyuma. Mpaka pale aliposhtuliwa na Jay aliemtaka watafute mahali wakae wasubiri muda muafaka wa sinema kuanza.
Wakatulia sehemu lakini bado Ramah hakutulia mpaka pale alipowashuhudia anaowatafuta. Roho ilimuuma huku moyo ukijawa na maumivu ya ghafla kama umepitishiwa kisu cha moto. Macho yake yaliwashuhudia Rommy na Cecy wakiwa wamekaa kimahaba zaidi katika mtindo wa kukumbatiana. Hakuweza kujizuia kutowatazama huku kiroho cha wivu kikimuenda mbio mbio.
Jay alikosa ushirikiano hata pale alipokuwa akimsemesha nduguye. Akamtazama kwa mshangao na kumuona akiwa anatazama sehemu moja tu. Akayaagiza macho yake yaelekee kule alipokuwa akitazama Ramah. Hata yeye alishtuka baada ya kuwaona Rommy na Cecy wakiwa ndani ya ukumbi huo. Kumeshaharibika tayari hapa. Aliwaza huku akirudisha macho yake kwa nduguye.
“Rafael ushinde moyo wako. Kumbuka tumekuja kutazama sinema na si vinginevyo” Jay aliyanena hayo akiwa amemshika bega Ramah. Ramah akageuka kinyonge kule alipo Jay na kumtazama usoni. Jay aliushuhudia uso wa Ramah ukiwa si wenye tabasamu kama mwanzo. Furaha yote ilipeperuka na isijulikane imepotelea wapi.
“Najua Ramah. Najua ulivyo kwa wakati huu. Lakini huna budi kujivika moyo wa ujasiri mithili ya mwanajeshi katikati ya kundi la maadui. Tuliza moyo wako yakumbuke niliyokushauri. Achana nao kwa sasa mpaka pale utakapo hisi unauhitaji wa kuzungumza nao. Tena kila mmoja kwa wakati wake. Ili nijaribu tu hakika utalishinda” Jay aliyaongea hayo akiwa amelishika bega la Ramah.
Kama pia haitoshi. Akaonelea ahamie ile sehemu ambayo alikaa Ramah kisha akampisha Ramah pale alipokuwa amekaa yeye. Lakini hata hivyo Ramah hakuacha kutazama kule walipo wakina Rommy. Muda wa kuanza sinema ukawadia na video ikaanza kuonyeshwa. Akiwa yeye hana furaha yoyote huku waliomkosesha furaha akiwaona wakiwa na furaha tele. Ilimuumiza! Ilimuhuzunisha na ilimsikitisha si mas'hara.
Hata pale sinema ile ilipokuwa akiendelea. Ramah hakuweza kuelewa lolote zaidi ya kutawaliwa na maumivu tu. Kuna muda alitamani akafanye fujo kwa Rommy lakini alimuomba Mungu aishinde nafsi hiyo.
Sinema ile iliisha baada ya saa moja na nusu kupita. Watu wakaanza kutoka mmoja mmoja ndani humo. Bahati mbaya Ramah alipotezana na kina Rommy na kujikuta hawaoni tena kutokana vurugu za watu ambao wote walitaka kutoka. Jay alimshika mkono Ramah baada ya kuona akipagawa kuwatafuta watu wale maana alihisi wanaweza poteana na wao.
Baada ya watu wengi kiasi kutoka nje huku waliobakia ndani wakiwa ni wachache. Jay akaona huo ndio muda mzuri wa wao kutoka. Wakajitoa kwenye viti na kuanza kupiga hatua ndogo ndogo kuuendea mlango wa kutokea. Wakiwa mlangoni, Ramah aligeuka nyuma baada ya kuhisi ameshikwa bega. Moyo ukapiga paah! Huku taharuki ikimkumba baada ya kukutanisha uso kwa uso na Rommy ambae nyuma yake alikuwapo Cecy aliekuwa bize na simu.
Kitendo hicho kilipata kushuhudiwa na Jay. Cecy aliekuwa bize na simu muda wote, aliinua sura na kutazama mbele baada ya kuona Rommy amesimama. Alipotazama mbele macho yake yaligongana na ya Ramah lakini wala hakuonyesha mshtuko wa aina yoyote. Zaidi aliongeza mwendo kwenda mbele na kuwaacha watu hao nyuma.
“Nilikuona muda mwingi tu ila sikuwa na uhakika kama ni wewe. Nambie ndugu yangu” Rommy aliongea hayo kisha akampa mkono Ramah. Ramah aliutazama ule mkono kwa sekunde kadhaa kisha akaupokea huku akijilazimisha kutabasamu.
“Safi tu. Mi sikuwa nimekuona, kumbe na wewe upo humu” Ramah alinena hayo. Rommy akampa salamu na Jay kisha hapo wakapiga hatua za taratibu kutoka mahala hapo ili wawapishe wengine waliokuwa wakitaka kutoka.
Nje kabisa waliweka kambi kwa muda ili wazungumze vyema. Muda huo Cecy alikuwa ameshaingia kitambo ndani ya gari, hakutaka kuzungumza na Ramah chochote kwasababu alihofia kuharibiwa. Rommy aliwauliza ni wapi wanaelekea muda huo na wao wakajibu wanaelekea nyumbani. Akawauliza tena kama wamekuja na usafiri wao binafsi na wao wakajibu hapana.
“Sio mbaya, tukaingia kwenye gari tukawa ‘drop home’. Imekuwa ni bahati kukutana mida hii” Rommy aliwaambia.
“Usijali kaka, kuna jamaa tumeshampigia simu anakuja saa hii kutuchukua. Kwahiyo kuhusu usafiri usiwaze, nyie nendeni tu kwasababu pia sisi kuna sehemu tutapitia kwanza kabla ya kufika home” Jay alisema hayo ili tu wajitetee wasiingie ndani ya magari aliyokuja nayo Rommy. Kwasababu alijua ni jinsi gani Ramah hali yake ilivyo kwa muda huo.
Rommy hakuweza kuwalazimisha sana kuhusu hilo. Waliagana kisha Ramah na Jay wakaondoka mahala hapo. Wakati wakiwa wanaondoka, Ramah alipiga jicho kwenye gari alilofika nalo Rommy na kukutanisha macho yake na ya Cecy. Wakatazamana kwa kitambo kidogo kisha Cecy akageukia na pembeni.
“Oya, tupande Bajaji turuke chap home, maana Mama naona anapiga simu saa hii” Jay alimtoa kwenye mawazo Ramah baada ya kumuambia hayo. Wakajitosa kwenye usafiri wa Bajaji ambayo ilikuwa imepaki nje ya ukumbi huo. Wakamuelekeza dereva ni wapi wanataka kwenda na dereva akawasha chombo baada ya kuelewana bei.
“Sasa mpenzi, si tunaelekea nyumbani ama?” Rommy alimuuliza Cecy walipokuwa ndani ya gari.
“Hapana, nipelekeni nyumbani maana sikumuaga Mama kama nitachelewa kurudi” Rommy akamjuza Paskali ni wapi wanatakiwa kwenda muda huo. Kisha Paskali akawasha gari kwaajili ya kuelekea nyumbani kwa kina Cecy.
“Lakini kesho si tutakuwa wote?” Rommy alimuuliza.
“Ndio, nilishamuambia Mama kuhusu hilo. Na ndio maana leo nataka niwahi kurudi ili kesho asiwe mgumu wa kunipa ruhusu kamili”
Kimya kikachukua nafasi ndani ya gari. Ni Paskali pekee ndie ambae alikosa utulivu kwasababu yeye alikuwa akicheza na usukani muda wote. Dakika kadhaa wakafika karibu na nyumba ya kina Cecy. Cecy akaomba kushushwa mahala hapo na gari zikasimama. Wakaagana kwa minijali ya kuonana siku inayofuata kisha Cecy akashuka kwenye gari. Akampungia mkono Rommy huku gari zile zikiondoka mahala hapo.
“Manzi huyu naona umekaa nae sana, ama una malengo nae nini?” Paskali aliongea hayo wakati huo akicheza na usukani. Rommy alicheka kidogo kisha akasema.
“Kaka mkubwa huyu mwanamke anajifanya mgumu, kwani mara ngapi namlazimisha tufanye lakini aishiwi na sababu. Jeuri yake itaisha hivi punde, subiri kwanza nimlee maana nahisi hana imani nami kwasababu nilishawahi kumtema kipindi hiyo” Paskali alicheka na Rommy akasaidizana nae kucheka.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nastaajabu ati maana si kawaida yako kulaza maiti ya kiarabu. Nimezoea kukuona una ‘approach’ leo kesho unatafuna, kesho kutwa unatema. Aisee kijana mtata wewe!”
“Ni kweli usemayo, sikuwahi kulaza maiti ya kiarabu, ila huyu muache kwanza, kesho tuiende hiyo safari tukirudi namgusia. Akijifanya anamsimamo wake huo huo natishia kumkataa, naamini hawezi chomoka yule” Rommy aliongea hayo na wote wakacheka.
* * * *
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment